Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. John Danielson Pallangyo (35 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niseme kidogo kuhusu Mpango huu wa Serikali ambao umeletwa mbele ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri na watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wanafanya. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana ya kusimamia mapato pamoja na kupanga mipango ambayo imetufikisha mahali tulipofika. Niseme pia hata huu Mpango ambao wameuleta 2020/2021 ni mzuri na naunga mkono a hundred percent. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiona Mawaziri wanafanya vizuri, watendaji wakuu wa Serikali wanafanya vizuri, ujue kwamba nyuma yao kuna kiongozi wao. Nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, ambaye anafanya kazi nzuri mno na ndiyo maana Mawaziri nao wanafanya kazi nzuri. Tumeshuhudia mambo mengi yanafanyika hapa nchini kwenye sekta nyingi; afya, elimu, nidhamu Serikalini, vita dhidi ya rushwa, umeme na kadhalika lakini kwa kipekee miradi mikubwa ya kimkakati; reli ya kisasa, Mradi wa Kufua Umeme Stiegler’s Gorge, kufufua Shirika la Ndege Air Tanzania kwa kununua ndege nane mpaka sasa. Sina haja ya kuyazungumza sana haya kwa sababu kila mmoja anayaona, kila mmoja anayafahamu lakini itoshe kusema kwamba tunampongeza Rais kwa kazi nzuri na tunamuombea maisha marefu na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ni- comment kidogo kwenye Mpango huu na nianze na kilimo. Kilimo ndicho kimebeba Watanzania katika ajira kwani idadi kubwa ya Watanzania wanategemea kilimo na toka tunapata uhuru tumekuwa tunaimba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu. Yamepita maazimio mengi; Azimio la Iringa (Siasa ni Kilimo) na baadaye juzijuzi likaja Azimio la Kilimo Kwanza mpaka magari ya Wabunge na Mawaziri yakaitwa kwa jina hilo la Kilimo Kwanza lakini pamoja na hivyo bado kilimo hakijakaa sawa ni kwa sababu hatujaweka msukumo unaostahili kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani pale mwanzoni tulidhani kwamba mechanization alone ingetusaidia lakini kumbe kilimo cha kutegemea mawingu, kutegemea mvua hakitatufikisha mahali. Ndiyo maana mpaka leo toka tumepata uhuru kilimo chetu bado kinasuasua na niseme sasa wakati umefika kwenye Mpango huu wa 2020/2021 Wizara iangalie namna ambayo itaweka msukumo mkubwa kwenye irrigation. Tunaomba Serikali iwekwe nguvu nyingi kwenye miundombinu ya irrigation ili tubadilike tuache kungojea mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mazao ya traditional cash crops, kahawa, pamba, tumbaku, wenzangu wamesema yamedorora. Kule kwetu kahawa ndiyo kabisa, tulikuwa tunaitegemea zamani lakini kahawa imekwisha kabisa kabisa na sababu kubwa ni pamoja na population boom. Yale mashamba ambayo yalikuwepo wamezaliwa watoto wengi badala ya mashamba sasa ni plots, kwa hiyo hakuna mahali pa kulima kahawa. Badala yake wananchi vijana wame-resort kwenye hot cultural farming. Nilipata faraja kubwa sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo juzi aliposema kwamba wanaleta Muswada wa kuanzisha mamlaka ambayo tunaamini ita-coordinate na ku-promote hot cultural farming. Suala hilo ni la msingi na lifanyike haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeshuhudia vijana wanalima mboga mboga zao ukifika wakati wa kuvuna yale mazao yanaozea shambani kwa sababu barabara zimeharibika. Barabara za vijijini ni za kutengeneza, kwa hiyo msukumo mkubwa upelekwe katika kutengeneza miundombinu ya kufuata yale mashamba ambayo vijana wanahangaika, wanalima karoti, wanalima nyanya na pilipili hoho na kila kitu lakini mwisho wa siku yale mazao yanaoza kwa kukosa usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya kazi nzuri sana kwenye miundombinu, barabara, madaraja na hata miradi mikakati ambayo imeshatekelezwa imefanyika vizuri. Nilisikia siku moja Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi akasema, sera sasa hivi imelenga kuunganisha mikoa kwa barabara za lami tu, lakini nikasema kwamba sera siyo static ni dynamic inaweza ikabadilishwa kidogo pale ambapo barabara inaonekana inaweza ikastawisha wananchi mradi utekelezwe. Hapa nitoe mfano, barabara ya King’ori – Malula kwenda King’ori Madukani kwenda Maruvango, kwenda Ngarenanyuki, Ngabobo, Uwiro inakwenda mpaka Oldonyo Sambu, barabara hii iko kilomita mbili kutoka junction ya KIA na mpaka wa Arusha na Kilimanjaro. Barabara hii inaunganisha barabara kuu ya Arusha – Moshi – Dar es Salaam na barabara ya Arusha kwenda Namanga – Nairobi na inazunguka Mlima Meru. Wale wananchi wote pale walikuwa wameachwa hawana miundombinu ambayo inaeleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, barabara hii iko kando kando ya hifadhi ya Arusha National Park, barabara hii ikijengwa kwa kiwango cha lami itatusaidia, itaongeza idadi ya watalii ambao wataingia pale Arusha National Park na kuongeza kipato cha Taifa kupitia utalii. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye Mpango huu wa 2020/2021 asiisahau hii barabara, ina umuhimu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kweli imefanya kazi nzuri sana katika kuwapa wananchi maji lakini miradi ya maji tumeona inachukua muda mrefu, mingine mpaka Mheshimiwa Waziri anakuja anaingilia kati, anavunja mikataba ile, kwa hiyo usimamizi wa ile mikataba kidogo umekuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba huku tunakoelekea tujaribu kubadilisha mfumo, tutumie Force Account kwa sababu nimeona, nimeshuhudia kazi ikifanyika kwa mafanikio makubwa sana kwenye sekta ya afya. Vituo vingi vya afya vimejengwa kwa kutumia Force Account na ile miradi imetekelezwa vizuri kwa haraka haraka bila kupoteza muda na bila kutoa nafasi ya price variation.

Kwa hiyo nisema tu kwamba huku tunakokwenda hasa kwenye eneo la sekta ya maji, tubadilike kidogo tutumie Force Account ambayo ni...

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Pallangyo kwa mchango wako.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo kwenye hii hoja ambayo iko mezani. Nianze kwa kumshukuru Mungu mwingi wa rehema ambaye ndiye ametuweka hapa, lakini pia niwashukuru sana wananchi wa Arumeru Mashariki ambao waliniamini wakanichagua kwa kura nyingi na kunifanya niwepo hapa leo hii. Waungwana wanasema kwamba ukiaminika unakuwa ni mdeni; kwa hiyo niseme tu kwamba mimi ni mdeni wao kwa hiyo ninawahakikishia kwamba nitajitahidi kuwatumikia kwa kadiri Mungu atakavyoniwezesha.

Mheshimiwa Spika, kipekee sana nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye anafanya kazi nzuri sana na ya heshima kwa nchi hii. Anatekeleza ilani ya uchaguzi kwa umahiri mkubwa, na niseme kwamba anaziishi ahadi zake alizozitoa majukwaani mwaka 2015. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende Wizarani. Mheshimiwa Lukuvi nakupongeza sana Ndugu yangu. Nakupongeza wewe na Naibu wako, Makatibu Wakuu na watumishi wote wa Wizara hiyo, mnafanya kazi nzuri na ya heshima. Wenzangu wanakuita kinara wa kutatua migogoro, ni kweli nakubaliananao. Nilikuwa nakufuatilia kwa karibu, mara leo uko Bukoba, kesho Kilombero, kesho kwetu, Jumapili Kilimanjaro; hakika umefanya kazi nzuri unastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ni Serikali makini sana, inajali Watanzania na ndiyo maana tuliamua kwa makusudi kutenga asilimia nne za ecosystem ya Selou ili tuweze kujenga kinu cha kuzalisha umeme unaotumia nguvu ya maji ili Watanzania waondokane na giza na pia wapate nyenzo muhimu ya kuzalishia bidhaa kwa kuanzisha viwanda vidogovidogo na vikubwa.

Mheshimiwa Spika, ardhi ni rasilimali muhimu sana kwa wananchi, naamini Mheshimiwa Lukuvi analijua hilo. Ninamuomba, wiki iliyopita lilizungumzwa jambo la Kata ya Ngarenanyuki, Kijiji cha Olkung’wado, kwamba kuna tatizo, lakini Waziri wa Maliasili akasema pale hakuna tatizo. Baada ya pale nilipata ujumbe kwamba kweli bado tatizo linaendelea, na nimefuatilia nikakuta wananchi kuna ardhi walikuwa wanaitumia kwa ajili ya maisha yao, ekari 960, zilikuja zikachukuliwa kihalali na Arusha National Park, kisheria, lakini badaye wakakaa chini wakakubaliana wakapunguza pale wakawapa wananchi ekari 360. Nilivyozungumza nao wakasema bado kuna tatizo, na watu wanateseka wamenyang’anywa uhai wao.

Mheshimiwa Spika, sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri, nikusihi sana, tulia kidogo uzungumze na Waziri wa Maliasili na Utalii ili muone ni namna gani kwa spirit ileile ambayo tumetenga four percent ya ecosystem kwa ajili ya manufaa ya wananchi, uende pale Momela uzungumze na wananchi uchukue lile eneo ambalo limechukuliwa na TANAPA, ekari zote 960 zirudishwe kwa wananchi ili wakawage na waweze kuishi. Ardhi ni rasilimali ya msingi sana na ndio utajiri mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa muda huu mfupi. Naunga mkono hoja percent 100. (Makofi).
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwa kifupi hoja iliyoko mezani.

Naomba nitangulie kwanza kuwa kumpongeza sana Waziri Mkuu na Waziri na Naibu Waziri walioko chini yake pamoja na watendaji wote kwa wasilisho zuri na kazi nzuri inayofanyika Wizarani.

Mheshimiwa Spika, kipekee niruhusu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanyia Watanzania tangu walivyomchagua mwaka 2015. Lakini pia nichukue nafasi hii kukupongeza kwa dhati kabisa kwa jinsi ambavyo umeliongoza Bunge letu tukufu kwa umahiri mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nitajikita kwenye maliasili na utalii na afya kwenye mchango wangu huu.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba Waziri Mkuu atusaidie mgogoro wa mpaka kati ya wananchi wa Kitongoji cha Momela na Hifadhi ya ANAPA utatuliwe kwa hekima kama ilivyo dhamira ya Mheshimiwa Rais kwa kuunda jopo la mawaziri nane. Historia inaonesha wananchi wa eneo hilo wamekuwa victim wa kuchomewa nyumba na kutaka kuhamishwa tangu mwaka 1951.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Momela kiko katika hatari ya kufungwa kwa sababu ya tatizo dogo sana la ownership. Tulikwenda pale na Naibu Waziri wa Afya akatoa maelekezo isainiwe MOU ya PPP ili status quo ya kituo iwe maintained pamoja na kupandisha hadhi kituo kiwe charitable hospital. Hayo hayajafanyika mpaka sasa na matunda yake wananchi wa eneo hilo ambalo liko mbali na Hospitali ya Wilaya wanakosa huduma muhimu ya afya bila sababu za msingi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa 100%.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kidogo kwenye hii hoja iliyoko mezani. Nitangulie kwanza kumshukuru Mungu, Baba yetu wa Mbinguni ambaye ndiye ametuamsha salama na kutukutanisha hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mpango. Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana pamoja na Naibu wako na Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo mmekuwa mnafanya, pia kwa bajeti nzuri ambayo mmetuleta ambayo naweza nikai-brand kwamba ni reconciliatory budget. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imegusa mioyo ya wananchi wengi ambayo ilikuwa imeinama kwa kukumbana na kero nyingi katika kufanya shughuli zao kwa kuondoa tozo 54 na kuweka checks and balances kwenye kodi, kwa kweli bajeti ni nzuri na inastahili kuungwa mkono hundred percent. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukiona Wizara inafanya vizuri, ina mila ya utendaji wa mamlaka iliyoko juu. Kwa maana hiyo, nasema nampongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye amekuwa ni msukumo mkubwa kwenye utekelezaji wa mradi na mambo mengi mazuri ambayo yanaendelea hapa nchini. Amekuwa anatekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa umahiri mkubwa, amekuwa anasukuma utekelezaji wa miradi mikubwa ambayo mwisho siku itaacha historia kubwa sana hapa nchini kwetu; Stiegler’s Gorge, SGR na ununuzi wa ndege Air Tanzania. Haya mambo siyo madogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napata shida kidogo nilipokuwa nasikia Waheshimiwa wengine wanasema kwamba haya ni maendeleo ya vitu badala ya watu. Nikajiuliza, hivi mtu ukijenga nyumba yako nzuri utasema ni maendeleo ya nyumba au ya nani? Nadhani kuna haja ya kujitathmini kidogo kwenye haya mambo kabla hatujasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo juu ya kilimo. Kilimo bado ni mwajiri mkubwa kwa Watanzania, lakini mpaka sasa sidhani kama tumeweka nguvu ya kutosha. Tumekuwa tunategemea hali ya hewa na hali ya hewa inabadilika mara kwa mara. Matunda yake, wananchi wetu wanalima, wanapata mavuno kidogo. Basi niseme kwamba wakati umefika sasa hivi wa kuweka programu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Programu ya mwisho kufanyika ilikuwa ni pragramu ya Kilimo Kwanza. Nadhani wakati umefika sasa wa kuanza pragramu ya Irrigation Kwanza, Kilimo cha Umwagiliaji, tuache kutazama mawingu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine Ilani ya Uchuguzi ya mwaka 2015 ililenga katika kukuza soko la ajira. Katika hilo ilikuwa ni kulinda taasisi zetu. Wizara hii ya fedha ina taasisi nyingi. Nilikuwa napitia makabrasha hapa nikakuta taasisi ya mamlaka ya bima (TIRA). Kazi yake hii ni kukuza soko la bima na kulinda migongano ndani ya walengwa na ndani ya wadau. Nimeshuhudia siku za karibuni na taasisi hii players wake ni mashirika ya bima, brockers, loss adjusters na mawakala.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibu nimeona kwamba hii taasisi, TIRA wanatoa leseni za u-brocker kwa mabeki. Hii nikaona kama siyo sawa, kwa sababu mabenki watafuta ma-bocker. Mabenki hawawezi wakashauri wateja kwamba ni bima ya namna gani ambayo inatakiwa ichukuliwe. Kwa ajili hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri regulations ziangaliwe ili benki ziwe restricted wasipewe u- brocker, waishie kwenye u-agent tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliza, naomba, kuna somo ndani ya Biblia linamhusu mtoto mpotevu, aliomba haki yake kwa baba yake akapewa akaondoka, akaenda kuzurura mjini, akatumia ile haki yake akamaliza akafilisika, akapata shida, mwisho akaanza kushiriki chakula na nguruwe, akaamua kurudi kwa baba yake kwenda kuomba msamaha; na siku amefika alipokelewa na baba yake vizuri akachinjiwa kondoo na ng’ombe mnono sana akafanyiwa sherehe kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu kule Arumeru Mashariki kwa muda mrefu sana barabara zake hazijatengenezwa, hazipati matengenezo stahiki na ya wakati. Kwa hiyo, matokeo yake ni kwamba yake sasa hivi hazipitiki. Naomba unipe ruhusa nimwombe Waziri wa Fedha aangalie namna atakavyomwezesha Waziri wa Ujenzi na TAMISEMI ili ifanyike pragramu ya barabara, opesheni barabara kule Arumeru Mashariki barabara zile zibadilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanajisikia vibaya wakitoka pale Kibaoni King’ori wakifika Bomang’ombe kuna barabara lami inakwenda milimani, wakifika kwa Sadala kuna barabara ya lami, inakwenda milimani; wakifika Machame kuna barabara ya lami inakwenda milimani; wakija Kibosho kuna barabara ya lami inakwenda milimani; pale Meru hakuna barabara ya lami. Mheshimiwa Mpango nakuomba, nakusihi lile Jimbo sasa hivi ni Jimbo mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeomba kibali unipe nizungumzie hilo kwa sababu nimetoka kwenye lile Jimbo na ninajua hali yake ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, naomba kuunga hoja mkono kwa percent mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais akifungua rasmi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dodoma, tarehe 13 Novemba, 2020 naomba kutoa mchango wangu wa maandishi baada ya kubaini kwamba wachangiaji wamekuwa wengi na naomba niseme kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma hotuba zote mbili ya mwaka 2015 na ya 2020; kama Mheshimiwa Rais alivyotuasa Wabunge kwamba lengo la kufanya hivyo ni ili tuweze kupima utekelezaji wa vipaumbele alivyokuwa navyo Mheshimiwa Rais katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ni dhahili kwamba Mheshimiwa Rais amewafanyia Watanzania kazi nzuri mno na ni utendaji uliotukuka ambao umekiinua chama chetu (CCM) na hata kutubeba Wabunge tulioshinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 na kuwepo Bungeni leo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Ilani ulikuwa wa ufanisi mkubwa kila sekta; kwanza, utawala bora. Tumeweza kuwa nchi ya kwanza Afrika katika kupiga vita rushwa. Pia tumekuwa nchi ya 28 kati ya 136 duniani katika matumizi mazuri ya fedha za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, uchumi umekuwa kwa 7% na kufanya pato ghafi kupanda toka shilingi trilioni 94.349 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 139.9 mwaka 2019 na Taifa kupanda chati kiuchumi na kuwa Taifa la uchumi wa kati 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, umeme wa REA toka vijiji takribani 2000 mwaka 2015 na kufikia vijiji 9000 mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, upatikanaji wa maji safi na salama kuongezeka kutoka 47% mwaka 2015 hadi 70.1% mwaka 2020 kwa vijijini na kwa mjini toka 74% hadi 84%.

Mheshimiwa Naibu Spika, tano, barabara za lami zimejengwa, madaraja yamejengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sita, watoto wetu wameendelea kupatiwa elimu bila malipo darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Kila sekta Serikali imefanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, saba, miradi mkakati imeendelea kutekelezwa, mfano Bwawa la Mwalimu Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha umeme megawati 2115 linaendelea kujengwa na mradi unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaendelea vizuri na section ya Dar es Salaam/Morogoro itamalizika mwaka huu wa 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, ATCL; ndege zimenunuliwa nane na zinaruka; tatu ziko njiani; kwa kifupi mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kipindi cha kwanza cha miaka mitano (2015 – 2020) ni makubwa sana na pongezi na shukrani nyingi zimuendee Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa uongozi uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais ya Novemba 13, 2020, kimsingi kwenye hotuba hii ameweka dira kwa Taifa kwamba ni mambo gani amepanga kutekeleza na ameweka wazi kwamba itakuwa ni utekelezaji Ilani ya Uchaguzi yenye kurasa 303 na ahadi alizotoa majukwaani wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mengi ya kuboresha maisha ya Watanzania lakini naomba kuchangia kwenye mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara; zitajengwa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 2500 na lengo ni kufikia kilometa 6006 kuunganisha Wilaya na Mikoa yote nchini. Nashauri utekelezaji uanze na ahadi za Mheshimiwa Rais alizozitoa hadharani kwa mdomo wake na mbele ya wapiga kura wengi ukizingatia kwamba pia mikutano yake ilikuwa na watu wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Meru aliahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Malula Kibaoni kwenda King’ori; Maruvango, Leguriki hadi Ngarenanyuki na mpaka Oldonyosambu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; kwenye hotuba ya Rais kilimo kitaboreshwa na kubadilishwa sura kiwe kilimo cha biashara ili kuongeza uzalishaji. Nashauri Wizara ya Kilimo iongeze nguvu kwenye miundombinu ya umwagiliaji ili tuondokane na kilimo cha kutegemea hali ya hewa ambapo mvua zikikosekana basi wakulima wanapata hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eleimu; elimu itaendelea kuboreshwa na mpango ni kujenga shule za sayansi za wasichana moja kila Mkoa. Huu mpango mzuri na kule Meru kuna shule ya wasichana ilibuniwa na aliyekuwa Mbunge wetu kwa tiketi ya CCM Marehemu Jeremiah Solomon Sumari ambaye alitangulia mbele ya haki Januari, 2012 kabla ndoto yake haijatimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni shule hiyo ijengwe maana ilishaanza tayari na eneo la ujenzi lipo. Nilikwenda kutembelea mradi huo nikaridhika na kuamua kwamba nitaishawishi Serikali iendelee na mradi huo kumuenzi ndugu yetu huyo ambaye mema yake sasa yanaingia kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2021 – 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kusema kidogo kuhusu huu Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Nchi yetu. Nimepitia makabrasha yote ya Mpango huu na hotuba mbili za Mheshimiwa Rais, ya 2015 pamoja na hii ya mwaka 2020 ambayo tulisomewa tarehe 13 Novemba hapa wakati wa kuzindua Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uhakika kabisa Mpango huu wa Tatu nina hakika utafanikiwa na unakwenda kutuinua kwa viwango vya juu zaidi na kuboresha maisha ya mwananchi wetu. Hii inatokana na kwamba Mpango wa Pili wa Maendeleo pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ambao ulisimamiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, umefanikiwa sana kwa hali ya juu. Kwa mafanikio yale nina hakika kabisa kwamba Mpango huu unakwenda kuinua maisha yetu na utaboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nita- comment kwenye maeneo mawili; miundombinu; tulishuhudia barabara zikijengwa, madaraja yakijengwa, lakini barabara zetu zikishamalizika kujengwa, kule zinakopita unakuta ukihama barabarani mita mbili tairi linazama. Kwa hiyo niruhusu nilishauri Bunge hili na Serikali yetu kwamba kuanzia sasa tutakwenda kujenga barabara nyingi sana ambapo tumelenga kujenga barabara kilomita 6,600 ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miradi hiyo kila barabara itakayojengwa tufanye extension kwenye vijiji na kata ambazo zitakuwa zimepakana na zile na barabara kwa kiwango cha kilomita tano kila kijiji kiweze kufaidi. Hali hiyo niliweza kuiona kwenye nchi fulani nilikwenda kutembelea, nikaona kwamba ilifungua sana maisha ya wananchi ambao wako kwenye vijiji ambavyo vimepakana na zile barabara. Nikaona hilo jambo ni zuri na niishauri Wizara ya Ujenzi iliweke kwenye sera zetu ili barabara zote zitakazojengwa kuanzia sasa zifanye extension, zifanye matawi kwenda kwenye vijiji na tunaamini kwamba itafungua maisha na maendeleo ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais alitoa ahadi nyingi sana, nishauri kipaumbele kipelekwe kwenye ahadi za Mheshimiwa Rais. Hii itaondoa minong’ono ambayo nimekuwa naisikia mara kwa mara kwamba ooh ahadi za kisiasa tu, ahadi za kutafuta kura na kadhalika, lakini zile ahadi alizitoa mbele ya wananchi wengi kwa hiyo nashauri kwamba zipewe kipaumbele kwenye huo Mpango wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia niseme kitu kwenye kilimo. Tangu nasoma kulikuwa kuna kitengo cha umwagiliaji kule Wizara ya Kilimo, lakini mpaka leo bado hatujaweka nguvu kubwa kwenye umwagiliaji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Shukurani sana kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru san ana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sikusimama Bungeni kutoa mchango wangu wa kawaida naomba nichagie kidogo kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Engineer Elias Kwandikwa, Katibu Mkuu na watendaji wote Wizarani pamoja na Mkuu wa Majeshi (CDF) pamoja majeshi yetu kwa kazi nzuri wanazofanya za ulinzi wa Taifa letu, lakini pamoja na majukumu mengine wanayoagizwa na Amiri Jeshi Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi letu linafanya vizuri sana na linasifika hata nje ya mipaka yetu. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamechangia mengi mazuri kuhusu bajeti iliyoletwa kwetu na mimi naomba nichangie jambo moja tu ambalo naliona ni la muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida wanajeshi wanatekeleza majukumu yao kwa amri na amri zote ni halali. Ni kwa ajili hiyo mataifa mengine mengi yanatumia majeshi yao kama nyumba ya kufanyia tafiti za kisayansi kwa sababu ya nidhamu ya kijeshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nchi yetu nayo ni sehemu ya dunia ya leo ya ki-TEHAMA, nashauri Serikali iangalie ni namna gani tunaweza kutumia majeshi yetu kama nyumba ya kufanyia tafiti za kisayansi (atomic, molecular, medical etc) na hata ujenzi wa viwanda vya kutengeneza magari ya kisasa na vifaa tiba na vya kijeshi pamoja na vifaa vya ujenzi wa miundombinu. Hili linaweza kufanyika kwa kutenga fedha na kuchukua vijana wetu wenye vipaji maalum watunzwe na kuhakikishiwa maisha mazuri na kutengenezewa maabara za kisasa kwa ajili ya tafiti ambazo tunazihitaji kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya kisayansi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na kwa sababu ya ufinyu wa muda naomba niende moja kwa moja nizungumzie matatizo yaliyoko kwenye jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, barabara ya King’ori inaanzia Malula kwenda King’ori kwenda Malulango, kwenda Leguluthi hadi Ngarenanyuki, sasa hivi iko kwenye hali mbaya sana sana na hivi karibuni nilipata picha kutoka jimboni ya hiyo barabara, nilikwenda kwa Waziri wa Ujenzi akaitizama, akaniambia ni kweli hii siyo barabara tena imekuwa shamba. Hii barabara nimeiongelea mara nyingi sana, lakini kwa bahati mbaya sana hata kwenye ilani haipo, hata kwenye mpango haipo.

Nilikwenda kumwona Waziri Mkuu tukazungumzia hilo jambo akaniambia niandike barua kwa Waziri wa Ujenzi niliandika. Kwa hiyo, naomba sana TAMISEMI waikumbuke barabara hii, iingie kwenye mpango na itengenezwe haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni nilipata jibu la swali langu namba 42 ambalo niliuliza TAMISEMI kwamba zilitengwa shilingi bilioni 1.259 kwa ajili ya kukarabati kwa kiwango cha changarawe ili ipitike mwaka mzima, lakini hizo fedha hazijapelekwa. Matokeo yake barabara ile imeharibika na haipitiki, wananchi wanateseka, wanashindwa kufuata mahitaji yao ya muhimu, wanashindwa kwenda kutafuta huduma zao za afya. Naomba sana, sana, hatua zichukuliwe. Hilo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napongeza Serikali imefanikiwa sana kuwafikia wananchi Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro ukitizama barabara zinatoka barabara kuu kwenda mlimani, barabara inayotoka Boma Ng’ombe kwenda Sanya Juu ni lami, barabara ya Kwa Sadala kwenda Masama ni lami. Ukienda barabara ya Machame kutoka Bashinituzi kwenda Machame ni lami, barabara ya Kibosho ni lami, KCMC kwenda Huru lami, KCMC kwenda Mweka lami, barabara ya Kawawa lami, barabara ya kwenda Marangu lami, barabara kwenda Mwika lami, hayo mafanikio, tunaomba wahamishe wapeleke Mlima Meru, Mlima Meru Terei inafanana na Mlima Kilimanjaro wananchi wengi wako kwenye mteremko, kwa hiyo, barabara zile huwa zinaharibika sana kila mvua zikinyesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ya hospitali ya wilaya ni mbaya, yale majengo yalijengwa miaka 60, tunaomba sana TAMISEMI watupie jicho pale, wakarabati yale majengo na watusaidie kumalizia mortuary ambayo tuliianza kwa nguvu za wananchi kufikia mahali na imebaki kidogo tu, kama tukipata fedha kidogo tutamalizia ile mortuary, tuweze kuwa na mortuary pale Arumeru Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna upungufu wa Vituo vya Afya; tuna upungufu wa vituo 19, tuna vituo saba tu wilaya nzima, tunaomba TAMISEMI iliangalie hilo na kutujengea vituo vya afya, najua wananchi wanaangaika kujenga vituo vya afya, lakini wanahitaji msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, kuna Kituo cha Afya Momela, kilikuwa kinafanya kazi vizuri. Kwa bahati mbaya kwa sababu ilitokea sintofahamu mwaka 2019, wale wa hisani Africa Amini Alama ikabidi waondolewe kukiendesha kile kituo. Baada ya hapo huduma zimedorora sana, hakuna mashine X-Ray na ile iliyopo hakuna wataalam wa kusoma. Tunaomba Serikali ifanye juhudi iboreshe huduma za afya pale na kama ikiona ni shida sana, wale wahisani wako pale pale wanaendesha huduma za tiba mbadala, waitwe kile kituo kiendeshwe kwa mpango wa PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niyaseme hayo machache. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo kwenye hoja ambayo ipo mezani.

Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PIC, Kamati ambayo ni mtambuka, kwa hiyo moja kwa moja niseme kwamba naunga mkono hoja zote tatu za PIC, PAC na LAAC. Pia, nichukue nafasi hii kupongeza sana Wenyeviti wetu kwa jinsi ambavyo wamewasilisha taarifa hizi; na kwa sababu ya ufinyu wa muda na mimi nitazungumza kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TANAPA; kuna mwenzetu ameshalizungumzia lakini nongezee. Mwaka 2020 tulipitisha sheria hapa, Sheria ya Fedha Namba Nane ambayo ilipelekea makusanyo yote yanayokusanywa na mashirika haya ya uhifadhi kukusanywa na mamlaka ya mapato. Pamoja na nia njema ya Serikali kuhakikisha kwamba haya mashirika hayaathiriki na athari za UVIKO – 19 ambayo ilisababisha kukawa na upungufu wa watalii nchini lakini hatua ile imefanya mashirika haya ambayo yanafanya kazi kwenye mazingira magumu ya porini kushindwa kutekeleza majukumu yake sawa sawa, hasa kwenye miundombinu ambayo kwa sababu ya hali ya mazingira huwa inaharibika haribika hasa kwenye barabara na sehemu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunashauri kwamba ili kutatua tatizo hilo Serikali iangalie namna ya kuwaruhusu wa-retain, kuwe na retention yale makusanyo wabaki nayo moja kwa moja bila ya kungojea kwenda kuomba fedha Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Dar es Salaam iliyopo chini ya Mamlaka ya Bandari ndilo lango kuu la uchumi wa landlock countries za DRC, Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi, Zambia, Zimbabwe na Sudan ya Kusuni. Wingi wa shehena ambazo zinapitia pale bandarani zinafanya bandari hii inaelemewa. Sasa hivi Bandari ya Dar es Salaam inafanya upanuzi lakini bado upanuzi ule hautakidhi uzito wa kuelemewa na shehena ambazo zinapitia pale. Kuna mradi wa ujenzi wa Bandari Kavu Kwala ambao sahivi umefikia percent 98 kumalizika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashauri Serikali iharakishe na ihakikishe kwamba mradi ule unamalizika haraka kwa sababu bandari ile itakapoanza kufanya kazi itapunguza mzigo wa shehena pale bandarini kwa percent 30; lakini pia kuna mpango wa kujenga Bandari mpya ya Mbegani Bagamoyo ambayo sana sana itatumika kwa ajili ya kushushia makontena. Bandari ile nayo ni muhimu sana, hivyo mradi ule utekelezwe haraka ili kunusuru Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya itekeleze majukumu yake kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya ufinyu wa muda, hayo ndiyo niliyokuwa nataka kusema. Niseme naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniona niweze kuchangia kidogo kwenye bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kumung’unya maneno nitangulie kusema kwamba Serikali imefanya kazi nzuri sana kwenye sekta hii ya maji. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa kazi nzuri Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Watendaji wote pamoja na Wakuu wa Taasisi ambazo zipo chini wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita nilipiga kelele kidogo kusema kwamba miundombinu ya maji kwenye Kata za Akeri imeharibika lakini nilipokuja kufungua hotuba ya Waziri nikakuta ametoa majibu, kuna mradi wa maji Patandi ambapo ndipo shinda ilikuwepo wa Sh.461,300,000 unajumlisha na Vijiji vya Patandi, Akeri, Kimundo, Ndoombo Nkoarisambu na Ndoombo Mfulony, tunasema ahsante sana kwa mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji Nshupu wenye thamani ya shilingi 269,427,924 utatekelezwa, tunasema ahsante sana kwa Serikali. Mradi wa Maji Olmulo ambao unapitia Losinyai, Enoti, Milongoine, Orjoro, Mbuguni, Laroi, Terati, Kisima ya Mungu and Enjoro umetengewa kiasi cha shilingi 350,000,000, tunashukuru sana kwa mradi huo. Nikumbushe tu Mheshimiwa Waziri kwamba mradi huo utapita Mbuguni na Shambarai Burka msisahau kupeleka matawi kwa ajili ya wananchi wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa maji Mbaseni, Maji ya Chai, Kitefu wa thamani ya Sh.300,000,000, tunashukuru sana kwa kutukumbuka. Kuna mradi wa maji Kikwe, Nambala, Maweni na Karangai wa Sh.287,049,450, tunasema ahsante mno kwa kutukumbuka. Kuna mradi wa maji Kikatiti, Maroroni, Kitefu na Samaria umepewa Sh.287,049,430, tunashukuru Serikali kwa kutukumbuka. Mradi wa maji Sura, Ushiri, Poli, Kwaugoro, Valeska, Patanumbe, Makiba, Kisimili Juu, Msitu wa Mbogo umepewa Sh.50,000,000, tunashukuru sana kwa kutukumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nitoe angalizo kwamba hivyo vijiji vilivyotajwa hapa viko mbali sana; Sura na Ushiri viko mlimani wakati Valeska na Patanumbe ni chini karibia na Mbuguni, sidhani kama hizi fedha zilizotengwa zitatosha, naomba waangalie namna ya kubadilisha. Pia kule Akeri kuna chanjo cha Kwa Saibala ambacho kimeharibika kinahitaji ukarabati na ndicho ambacho kinapeleka maji kwa watu wengi. Naomba chanzo hicho Wizara ikiangalie, watume RUWASA wakakikague, kikarabatiwe kwani sasa hivi kinatoa maji machafu na wakati mwingine hakuna maji kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia chanzo cha Makilenga, Mheshimiwa Waziri nadhani atakuwa anakumbuka alikuja akamfuta mtu kazi pale, kile chanzo ni cha kukarabatiwa. Sasa hivi kinatoa maji machafu yanahitaji kutibiwa ili kuondoa fluoride na wadudu hatarishi kwa maisha ya watu. Naomba mtukumbuke kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwenye hotuba ya Rais aliahidi kwamba kwenye Mpango wa Miaka Mitano ijayo tutaelekeza nguvu katika kuvuna maji ya mvua. Kule Shambarai Burka kuna korongo la Mto Nduruma, hii ni sehemu ya Mradi wa Maji wa Bonde la Mto Pangani. Korongo lile lilifukiwa katika harakati za kuendeleza mashamba kwenye miradi ambayo inaendelezwa pale, baada ya kufukiwa kila msimu wa mvua maji yanaondoka kwenye korongo yanakwenda kwa wananchi yanaharibu mali zao na hata kuvunja nyumba zao na barabara zinakuwa zimejaa maji zinakuwa kama mito. Tunaomba Wizara ifanye utaratibu ama wa kwenda kulichimbua lile Korongo au kujenga bwawa sehemu inaitwa Marurani ili yale maji yakija yasiende tena kusumbua wananchi yakawa laana yahifadhiwe na baadaye yatumike kwa ajili ya umwagiliaji na kwa matumizi ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikia kengele imelia, nakushukuru sana kwa kuniona, nampongeza Waziri na timu yake, ahsanteni sana na naunga mkono hoja. (Makofi
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu kwa maandishi na kwa kifupi kabisa.

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu naomba nianze kwa kumpongeza Waziri Ummy na Naibu wake Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu na watendaji wote Wizarani kwa kazi nzuri sana wanayofanya. Lakini kipekee naomba kwa dhati kabisa, nimshukuru na kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri na jinsi anavyotubeba Watanzania kama vile mama anavyobeba familia yake. Ni kwa sababu ya uongozi wake mahiri Mawaziri wanatekeleza majukumu yao kwa umakini . Pamoja na salamu zangu za pongezi naomba kuweka mezani changamoto zifuatazo kwenye Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -

Kwanza kuna upungufu mkubwa wa vituo vya afya jimboni na hata vile vilivyopo havikidhi viwango na mfano mzuri ni Kituo cha Afya Makiba ambacho Naibu Waziri alikitembelea.

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya miundombinu imechakaa inahitaji ukarabati mkubwa. Mwaka jana tuliletewa shilingi 500,000,000 ambazo zilirudishwa Serikalini kabla ya kutekeleza kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie kidogo kwenye hii bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ambayo ni Wizara nyeti kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Watendaji wote, Katibu Mkuu pamoja na Wakuu wa Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara, kwanza kwa kazi nzuri sana ambayo wanafanya kutandika barabara za lami nchini, lakini pia na hotuba nzuri ambayo Mheshimiwa Waziri ameitoa hapa Bungeni. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hiyo ina walakini, kwa sababu nimeipitia yote sijaona Arumeru Mashariki ikipewa hata mita moja ya barabara. Kwa hiyo nasema ina kasoro pamoja na kwamba nimempongeza Waziri lakini bado hotuba yake ina kasoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja na kuchangia na nianze na ukarabati wa kawaida (routine maintenance). Kwa muda mrefu nimekuwa na-observe, natazama ukarabati wa barabara zetu ambazo zimejengwa kwa fedha nyingi sana, lakini ukarabati unachelewa na baadaye kama unafanyika, unafanyika kwa utaratibu ambao ndivyo sivyo, kiholela holela tu. Wanafanya part works, wanarudia part works, mwisho barabara zetu zinakuwa nundu, uendeshaji unakuwa ni mgumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wwizara, irudie utaratibu wa zamani. Ilikuwa ukifanya part works miaka miwili unafanya surface dressing, unapiga layer moja ya lami barabara inakuwa mpya. Turudie kama tulivyokuwa tunafanya zamani kwenye ukarabati wa barabara zetu baada ya kuzijenga, maana yake tunatumia fedha nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wananchi wetu wengi wanaoishi kwenye miteremko ya milima mirefu, hususani Nyanda za Juu Kusini, Nyanda za Juu Kaskazini wameachwa, hawajapelekewa barabara nzuri, maisha yao yanaendelea kuwa duni. Tunaishauri Serikali sasa ichukue hatua mahsusi ifanye special program ya kujenga barabara za lami kwenda milimani kwenye wananchi wengi ili waweze kuishi maisha ya kawaida na wao waweze kupata neema ya barabara nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu, kuna barabara inaitwa Barabara ya Mbuguni, inaanzia Tengeru kwenda Mererani inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara. Barabara hii ni muhimu sana kwa maana ya kwamba inafungamanisha uchimbaji wa Tanzanite kule Mererani na masoko ambayo yapo Mjini Arusha. Barabara hii ina kilometa 27, ikijengwa kwa kiwango cha lami itafupisha safari ya sasa hivi kutokea Mererani kupitia KIA kwa ajili ya kupeleka Tanzanite sokoni ni kilometa karibia 80. Badala ya kwenda kilometa 80 kupitia barabara ya Mererani – Tengeru – Arusha unakwenda kilometa 30 na itachochea sana biashara ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya King’ori; barabara hii huwa naiongea mara kwa mara. Barabara hii iko kilometa tatu kutoka kwenye mpaka wa Kilimanjaro na Arusha. Barabara hii inazunguka mlima Meru kwa upande wa mashariki, Mto Meru pamoja na Hifadhi ya Arusha inapandisha Kaskazini inakwenda kutokea Oldonyo Sambu kuelekea Namanga. Barabara hii ikijengwa kwa kiwango cha lami itakuwa kama by-pass. Kwa hiyo niishauri Serikali ifanye kama mradi mkakati ijengwe kama by-pass kwa kiwango cha lami. Itainua kiwango cha maisha ya wananchi wanaoishi eneo lile hususani Kata nane za Malula, King’ori, Maruvango, Leguruki, Ngarenanyuki, Uwilo, Oldonyo-Wass, Angabobo. Pia itakuwa kichocheo itafanya accessibility kwenda Hifadhi ya Arusha kuwa rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jimbo letu limesahaulika sana. Mheshimiwa Waziri aki-check kwenye kumbukumbu zake atakuta kwamba kwenye barabara Arumeru Mashariki haijaguswa kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita. Bahati mbaya kwenye mpango, kwenye Ilani ya Uchaguzi hatukupata hata mita moja ya lami, lakini Mungu akatukumbuka, Marehemu aliyekuwa Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipokuja kwenye kampeni alituahidi kujenga ile barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe Waziri kwamba, maneno ya Rais ni decree, maneno ya Rais ni kama sheria, lakini bahati mbaya rais huyo ameondoka, tunaye rais mwingine ambaye amesema kwamba yaliyosemwa na ambaye yalikuwa yamedhamiriwa na marehemu tutayatenda, ni wosia. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akumbuke hili jambo na kuhakikisha kwamba safari hii, hii barabara inajengwa, tunaomba sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukipata hizo barabara mbili, Arumeru Mashariki nchi itabadilika ile. Wananchi watafanya kazi zao vizuri, wananchi watatulia, wananchi walitupa kura nyingi sana kwa sababu tulisema habari ya barabara na kwa Wabunge wote mnasema kwamba barabara ndio bidhaa ambayo ilikuwa inatuuza sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sikupata nafasi ya kuchangia hoja hii ndani ya Bunge naomba niwasilishe mchango wangu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitangulie kwanza kumpongeza Waziri Mheshimiwa Lukuvi, Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula, Katibu Mkuu na watendaji wote Wizarani pamoja na taasisi zilizoko chini Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya. Nadiriki kusema bila kumumunya maneno kwamba Waziri Lukuvi ni mmoja wa Mawaziri wenye uwezo mkubwa ndani ya Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze Waziri kwa kufuta hati ya shamba la Valeska kule Arumeru Mashariki na kwamba sasa yuko tayari kwenda Meru na kukabidhi shamba hilo Halmashauri na wananchi wa Meru.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo sasa nachangia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, upimaji na umilikishaji na kupanga matumizi bora ya ardhi; nilipokuwa nahudumu kwenye Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Waziri aliwahi kutuahidi kwamba kila inchi ya nchi yetu itapimwa na kuwekewa mpango bora wa matumizi. Mpaka sasa zoezi la upimaji wa ardhi linafanyika kwa kususua sana. Nashauri Wizara ije na mpango kabambe wa kuharakisha upimaji na umilikishaji wa ardhi nchini kote ili tuondokane na janga la ujenzi holela ambao unapelekea miji yetu kuwa squatters. Lakini si hivyo, ardhi iliyopimwa na kumilikishwa ni chanzo cha kuaminika cha mapato. Serikali iangalie eneo hili kwa jicho tofauti na kulifanyia kazi kwani zoezi hili linaweza kuwa mwarobaini wa tatizo sugu la ufinyu wa bajeti ya ujenzi wa barabara na sekta zingine ambazo ni muhimu na zinahitaji fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya ardhi; Serikali ibadilike sasa na kuacha kunyang’anya wananchi ardhi bila ustaarabu kwa kisingizio cha kupisha miradi ya kitaifa/ uwekezaji. Nikisema hivyo siyo kwamba napingana na Serkali katika utekelezaji wa miradi muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Tatizo liko kwenye namna ya utekelezaji wa zoezi zima la kuwaondoa wananchi kwenye mashamba ambayo yamekuwa earmarked kubadilisha matumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba wananchi washirikishwe kikamilifu kabla ya kuwaondoa kwenye mashamba husika. Mfano mzuri ni mashamba ya Malula upande wa Meru na Hai jirani na KIA. Wananchi walioko kwenye mashamba hayo waliambiwa siku nyingi wangeondolewa na kulipwa fidia kwa lengo la kuwawezesha wakapate mashamba sehemu nyingine ukizingatia kwamba wamekua pale kihalaii kwa miaka zaidi ya 40. Baada ya miaka takribani kumi tangu watangaziwe kwa mara ya kwanza kwamba wangeondolewa kupisha mradi wa industrial park na bandari kavu hivi karibuni Serikali ilikuja kwa ukali kwamba ardhi hiyo ni mali ya Serikali. Matisho hayo si sawa kwa sababu ardhi yote nchini ni mali ya Serikali na hata pale penye nyumba yangu ya kuishi ni mali ya Serikali, lakini ninaamini Serikali ikipahitaji itaniondoa kwa utaratibu fulani. Iko mifano mingi nchi nzima lakini itoshe kusema kwamba tuondokane na migogoro ya ardhi kwa kuwatendea wananchi haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu migogoro ya mipaka; nashauri Wizara ije na mkakati wa kumaliza migogoro yote ya mipaka kati ya wananchi na hifadhi ikiwa ni pamoja na mpaka wa kitongoji cha Momella na ANAPA (Hifadhi ya Arusha). Pia kuna migogoro kila leo kwenye mpaka wa Arumeru na Hai na Siha. Naomba Waziri atenge muda kidogo aje Arumeru na Siha aone ni jinsi gani matatizo yaliyoko kule yataondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya machache, nakushuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya ufinyu wa muda naomba kuwasilisha kwa maandishi maeneo ambayo nilitaka kuyasema jana lakini muda wangu ukaisha kabla ya kusema.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuhusu ujenzi wa barabara ya Akheri kutoka Sangis hadi Ndoombo; ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya kuanzia Sangis kwenda Akheri hadi Ndoombo ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyoitoa mwaka 2012 wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wetu Marehemu Jeremiah Solomon Sumari. Ujenzi wa barabara hii umeanza lakini kazi inaenda kwa kusuasua sana licha ya kwamba kipande kilichopatiwa fedha mwaka huu wa fedha 2022/2023 ni kilometa 1.2 tu. Maoni yangu ni kwamba urefu wa kipande kilichopatiwa fedha ni kidogo mno ukizingatia kwamba ahadi hii imechukua muda mrefu zaidi ya miaka kumi kutekelezwa. Nashauri Serikali iongeze fedha kwa TARURA barabara hii imalizike ndani ya uhai wa Bunge hili la Kumi na Mbili.

Pili ni kuhusu ujenzi wa vivuko; mwaka 2020 wakati wa Bunge la Bajeti Serikali iliahidi kutoa fedha kutoka kwenye Mfuko wa Maafa ili kujenga upya madaraja na vivuko vilivyosombwa au kuharibika kipindi cha mvua nyingi za mwaka 2019/2020. Kata nyingi kule Arumeru Mashariki mipaka yake ni mito na vivuko vingi vilisombwa. Naomba pia Serikali itekeleze ahadi yake kwa kuipatia TARURA fungu maalum kutoka kwenye Mfuko wa Maafa ili vivuko vilivyosombwa vijengwe upya.

Tatu; utekelezaji wa ahadi za viongozi; ahadi za viongozi wakuu: -

(a) Barabara ya Akheri kutoka Sangisi hadi Ndoombo iliyotolewa mwaka 2012 (kazi inaendelea);

(b) Ujenzi wa barabara kilometa tano kwa kiwango cha lami Usa River iliyotolewa mwaka 2015 (utekelezaji bado); na

(c) Ujenzi wa barabara ya Kingori kwa kiwango cha lami kilometa 33 ilitolewa mwaka 2020 (utekelezaji bado).

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuchangia kidogo kwenye Wizara hii ya Nishati ambayo kimsingi ni Wizara ya kazi, kimkakati na maendeleo na bajeti nzima percent 98 ni maendeleo tu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Katibu Mkuu na watendaji wote kwenye Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanafanya pamoja na taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ukiangalia jinsi ambavyo mambo yanakwenda sasa hivi kuhusu hii bidhaa ya umeme nchini utaona kwamba kuna tofauti kubwa sana. Kabla ya mwaka 2015 ukitaka kupata umeme ilikuwa ni kizungumkuti lakini siku hizi ukitaka umeme unafungiwa na unaelewa ufuate hatua gani ili uweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeza sana Waziri, naungana na ndugu yangu Mheshimiwa Elibariki kwa kweli Waziri Kalemani na Manaibu wake ni watu wastaarabu, wapole, unazungumza nao na wanaonyesha kabisa wana kiu ya kufikia malengo yao. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia pia mafanikio kwenye Bwawa la Nyerere, nilikwenda kule mwaka juzi mwishoni nikiwa chini ya Wizara ya Maliasili na Kamati yetu kazi ambayo ilikuwa imefanyika ni kidogo sana. Sasa hivi bwawa limetengenezwa kwa kiwango cha percent 52, ni kazi kubwa napongeza sana Wizara.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, naomba sasa nizungumzie kidogo habari ya jimbo langu kuhusu umeme wa REA. Kuna mafanikio makubwa sana over all ni percent 86 lakini ukija kwenye jimbo langu zipo percent 43 tu za kazi iliyofanyika. Kwa faida ya Wizara na Waziri naomba nitaje vijiji ambavyo viko gizani, jimbo upande wa Mashariki na Kusini liko gizani; Kata ya Kingori, Vijiji vya Muungano, Oldonyongilo, Ngonoheri, Mboleni, Ngosio, Nsengoni viko gizani. Kata ya Malula; Vijiji vya Kolila, Ndumangeni, Malula, Ngajisosia, viko gizani. Kata ya Maruwango; Vijiji vya Mowaro, Maruwango yenyewe, Mbasenyi, Nombele, Songambele viko gizani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kata nyingine ni Kata ya Ngarinanyuki iko gizani kabisa, Olukung’wado pale mjini wana umeme kidogo sana. Kata ya Uwilo; Kijiji cha Kimosonu wako gizani, Ngwandua Kijiji cha Nkoavele wako gizani. Kata ya Songolo; Vijiji vya Ulisho, Songoro, Malula, Kilinga wako gizani. Kata ya Kikatiti; Sakila Juu, Sakila Chini, Njeku, Nashori Kikatiti wako gizani. Kata ya Maroroni; Migadini, Kwaugoro, Samaria wako gizani. Kata ya Ngwalusambu; Kijiji cha Mfuloni, Ngwalusambu yenyewe, Kimundo wako gizani. Kata ya Maji ya Chai; Vijiji vya Maji ya Chai, Kitefu, Lerai, Ngurudoto wapo gizani. Kata ya Mbuguni; Kambi ya Tanga, Kikileto, Migungani wako gizani. Kata ya Shabarahi; Bulka na Karangai wako gizani. Kata ya Kwikwe; Luwainyi na Malala wako gizani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi pamoja na kwamba over all kazi iliyofanyika ni nzuri lakini kwa kweli jimboni kwangu hali si nzuri. Hivi vijiji viko karibu karibu kama Wizara ingejipanga vizuri ile kazi isingekuwa ngumu sana. Nadhani kuliwa kuna tatizo kidogo wakati wa kuanza kazi hii nakumbuka walileta nguzo sehemu zingine wakachimba mashimo wakayaacha wazi, wakaacha nguzo zikaendelea kuoza pale, kuna hadithi nyingi ambazo kwa kweli hazifurahishi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu hii bei ya kuunganisha umeme wa REA Sh.27,000, bado ni kizungumkuti. Kuna watu ambao walikwenda wakajaza fomu wakitegemea kwamba wanaunganishiwa kwa Mpango wa REA wakapelekewa bili kubwa badala ya Sh.27,000 anapelekewa bili ya Sh.337,000, kiwango ambacho kimekuwa kigumu sana kwa wao kuweza kufungiwa umeme.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, naskuhukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya ufinyu wa muda sikuweza kumaliza mambo machache ambayo nilitaka kuyasema hususan mahitaji ya visima virefu, kwa hiyo, kwa ridhaa yako naomba maandishi haya yawe sehemu ya mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, tuna uhitaji mkubwa wa visima virefu katika vijiji vfuatavyo; Kijiji cha Oldonyongiro ambako pia kuna kituo kipya cha afya cha Mareu Kata ya Kingori; Kijiji cha Ngyani Kata ya Nkoaranga; Kijiji cha Nkoaranga; Kijiji cha Kilinga; na Kijiji cha Poli.

Mheshimiwa Spika, miundombinu ya kuwapatia maji wananchi walioko katika vijiji ambavyo bomba kubwa la mradi mkubwa wa shilingi bilioni 520 Mradi wa AUWSA linapita Makiba, Mbuguni, Msitu wa Mbogo, Karangai Maweni, Kikwe na Nambala.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nichangie kwa ufupi hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii. Nianze moja kwa moja kwa kutoa pongezi zangu kwa kazi nzuri ambayo inafanywa na Wizara. Kusema kweli Waziri, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro; Naibu wake, Mheshimiwa Mary Masanja; Katibu Mkuu, Dkt. Allan Kijazi; Wakuu wa Taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake apewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na salam zangu za pongezi, nizungumzie tatizo la mipaka. Wabunge wenzangu wameshazungumzia jambo hili kwa kirefu na kwa undani zaidi, lakini nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba kule kwenye Jimbo langu Arumeru Mashariki kuna tatizo la mpaka kati ya Arusha National Park na Kitongoji cha Omela. Arusha National Park walichukua ekari takriban 960 mwaka 2017 na baadaye wakarudisha ekari 360. Baada ya kuchukua lile shamba waliwaacha wananchi wakiteseka hawana mahali pa kufanyia kilimo ambacho ndio ajira kubwa kwa wananchi wetu wa Tanzania. Kwa maana hiyo waliwaacha wananchi wakiwa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara kupitia Waziri, watumie busara kidogo waangalie ekari zilizobaki ekari 640 sio tatizo kubwa kwa Taifa hili na sio tatizo kwa hifadhi. Wapime faida ambayo hifadhi inapata na hasara ambazo wananchi wameingia katika kunyang’anywa yale mashamba. Ikiwezekana zile ekari zirudishwe kwa wananchi waweze kuendelea na maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme kidogo kuhusu Sekta ya Nyuki. Taifa hili tangu tumepata Uhuru, tumesomesha wataalam wengi sana kwenye sekta ya nyuki na kama tungetumia sekta hii vizuri, mazao ambayo yanatokana na nyuki yana uwezo wa kuingizia Taifa hili fedha nyingi tu hasa fedha za kigeni. Hata ile sumu ya nyuki ina soko sana nje ya nchi. Rai yangu kwa Wizara, iongeze nguvu kwenye sekta ya nyuki iweke kipaumbele ili hatimaye sekta hii nayo iweze kuchangia kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, wenzangu walizungumza kuhusu kuwekeza kwenye cable cars; ni kweli kabisa kwamba sisi Tanzania utalii tunaofanya kwenye milima ni utalii wa kupandisha watalii milimani kwa miguu. Tukubaliane kwamba kupanda mlima ni zoezi na jinsi watu wanavyozidi kuzeeka mazoezi yanakuwa ni tabu kidogo kuyafanya, huwezi kupanda mlima baada ya kufikisha miaka 80. Kwa hiyo, niseme kwamba Wizara iangalie, ifungue mlango kwa wawekezaji waweze kujenga miundombinu ya cable cars kwenye milima yetu hususan Mlima Kilimanjaro, Mlima Meru na kule Kitulo ambako mwenzangu, ndugu yangu Mheshimiwa Festo Sanga alisema kwamba miundombinu hiyo ikijengwa itaweza kutuingizia fedha nyingi sana za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kutembelea nchi fulani, South Africa Cable mountains ni ngumu sana kupanda, lakini nilishuhudia jinsi ambavyo cable cars ambayo imejengwa pale inavyoingiza fedha nyingi kwa nchi ile. Nina uhakika kabisa kabisa kwamba…

T A A R I F A

MHE. CONSTANTINE J KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu.

MHE. CONSTANTINE J KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nataka kumpa taarifa Mheshimiwa anayechangia kwamba Nchi ya Thailand inapata watalii milioni 16, lakini asilimia zaidi ya 80 ya watu wanaokwenda Thailand wanakwenda kwenye cable car na hawana milima mirefu kama Mlima Kilimanjaro. Wana milima ya kawaida tu ambayo wameiunganisha na cable car lakini ndiyo inayopeleka watalii wengi ambao ndio wanakwenda kutembea.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Pallangyo unapokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono 70. Ni kweli kwamba cable cars zina-supplement sana income kutokana na tourism. Ukiangalia fedha zinazoingia pale cable mountains utasema ni kwa nini hatufanyi hivyo na sisi. Niseme kwamba ninavyozungumza sasa hivi kuna ndugu yangu yupo Marekani alinidokeza kwamba ikiwezekana nirushe hiyo karata mezani kwako ili Wizara ilichukue halafu tuangalie namna gani tunaweza tukakaribisha wawekezaji waweze kuja kushirikiana na Taifa hili kujenga ile miundombinu kwa sababu pia nayo ile ni gharama, lakini ni njia mojawapo ambayo ingeweza kusaidia kutengeneza fedha nyingi sana za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, nakushukuru kwa muda ulionipa na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sikupata nafasi ya kuchangia kwa kuongea Bungeni, naomba nitoe mchango wangu kwa maandishi kwa kifupi sana.

Kwanza naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri iliyofanyika na inayoendelea kufanyika. Nilipata neema ya kutembelea miradi inayotekelezwa wakati wa ziara ya Kamati; SGR, Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam, Mwendo Kasi Dar es Salaam, Bandari Kavu Kwala, Bandari ya Kalema - Katavi, Daraja la Busisi, ujenzi na ukarabati wa meli vivuko na chelezo na kadhalika. Kwa kweli Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na shukurani na pongezi zangu, nasikitika kusema kwamba Serikali haitekelezi ahadi za viongozi wakuu ipasavyo. Kuna ahadi nyingi za viongozi wakuu ambazo zilitolewa mbele ya wananchi wengi ambazo bado hazijatekelezwa licha ya ukweli kwamba anachokisema mkuu wa nchi ni decree na inapaswa itekelezwe.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa kwenye Jimbo la Arumeru Mashariki ni barabara kwa kuwa sehemu kubwa ya jimbo ni Mlima Meru ambako wako wananchi wanaoishi kwenye miteremko ya huu mlima. Terrain si rafiki kwa barabara za udongo na changarawe.

Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kwamba jimbo hili lilikuwa limesahaulika kwa muda mrefu halijawahi kupewa hata mita moja ya barabara ya lami, lakini mwaka 2020 tulipata bahati ya kupewa ahadi ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kingori inayoanzia Malula Kibaoni hadi Ngarenanyuki iungane na barabara ya Usa River hadi Oldonyo Sambu.

Mheshimiwa Spika, ahadi hii ikitekelezwa tutakuwa na ring road ya kimkakati ambayo itaweka katikati vivutio vya utalii vya Hifadhi ya Taifa Arusha na msitu wa Mlima Meru, lakini pia itafupisha safari ya kutoka Moshi hadi Namanga kwa kilometa 33 na kuinua uchumi na ubora wa maisha ya wananchi wengi wa kata nane ambako imepita.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ifanye kila linalowezekana ahadi itekelezwe hasa ukizingatia kwamba tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambao tunauanza mwakani kwa Serikali za Mitaa. Wabunge tunapata mzigo yanapokuja maswali ya ahadi za Rais kutoka kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya ujenzi wa barabara ya Sangis kwenda Akheri hadi Ndoombo ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyoitoa mwaka 2012; hii imeanza kutekelezwa lakini inafanyika kwa kusuasua sana. Nashauri Serikali iongeze nguvu hapa ikiwezekana imalizike kabla ya mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya ujenzi wa barabara urefu wa kilometa tano Mjini Usa River aliyotoa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mwaka 2025 bado nayo inangojea utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mbuguni kuanzia Tengeru inaunganisha Mikoa ya Arusha na Manyara, nasikitika haijaongelewa kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru upembuzi yakinifu umeanza lakini nashauri Waziri aiongelee wakati wa kuhitimisha kwa sababu ilisahaulika kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru sana kwa kuniona ili nipate kuchangia kidogo kwenye bajeti hii ya Serikali ambayo ipo mezani kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kumshukuru Mungu sana mwingi wa rehma ambaye ametupa uhai na nguvu hata nikaweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu hili siku ya leo, lakini namshukuru zaidi kwa ajili ya kulipenda sana taifa letu hili. Tumeshuhudia mambo makubwa Bunge hili la 12. Tulianza kushuhudia aliyekuwa Rais wetu Hayati Dkt, John Pombe Magufuli akiapishwa tarehe 5 Novemba, 2020 baadaye na sisi tukaja tukaapishwa, tarehe 13 Novemba, 2020 akaja akazindua Bunge akatoa hotuba nzuri sana. Kwa kiwango kikubwa bajeti hii ya Wizara ya Fedha, bajeti hii ya taifa imebeba maono yaliyokuwa kwenye ile Hotuba ya Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii, baada ya yale matukio kwa upendo wa Mungu Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan alichukua kijiti, na tumeshuhudia akifanya mambo yake kwa umahiri mkubwa. Alitupitisha kwenye taharuki ambayo tulipata baada ya kuondokewa na kipenzi chetu, Rais wa Wwamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alifariki tarehe 17. Alitupitisha kwenye ile taharuki kwa umahiri mkubwa sana na ameendelea kuijenga Serikali na sasa hivi tunaendelea kupaa. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana, anafanya kazi nzuri na kila mmoja anaamini hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu wake Mheshimiwa Engineer Masauni, Katibu Mkuu na watendaji wote kwenye Wizara hii ya fedha kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kufanya.

Tumeshuhudia uchumi wa nchi yetu ukipanda kwa percent 6.9, lakini pia na hali ya umasikini kupungua kutoka percent 28.2 hadi percent 26.4; haya ni mafanikio makubwa sana. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo anaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na baada ya hayo machache sasa niseme kidogo kuhusu hii bajeti ambayo imeletwa mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Wizara imekuwa inasikiliza hoja za Wabunge na hatimaye fedha zimetolewa milioni 500 kwa kila Jimbo kwa ajili ya kuiwezesha TARURA ili wajenge barabara za vijijini. Kwakweli kwa hilo ninaishukuru sana Serikali yetu, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo; kwa sababu Wabunge tumelalamika muda mrefu hapa kwamba hali ya barabara za vijijini ni tatizo na fedha hazitoshi. Kwa kuanzia ameamua kutoa hizo milioni 500, tunaamini kwamba itapunguza yale makali na kelele ambazo tulikuwa tunazipata kutoka kwa wananchi kwa sababu ya ubovu wa baarabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye sekta ya kilimo. Kama tunadhamiria kweli kweli kuhakikisha kwamba tunakuwa na uchumi wa kijani, kama kweli tumeamua kwamba tufanye kilimo cha uhakikani lazima tuachane na kutazama mawingu, ni lazima turudi sasa tujenge miundombinu ya umwagiliaji ili tuweze kufanya kilimo kinachoeleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo imeajiri Watanzania takribani percent 65 lakini mchango wake kwenye Pato la Taifa ni chini ya percent 25, hiyo hali haina uwiano kabisa na kusema kweli tunapaswa tubadilishe hiyo hali na namna pekee ya kubadilisha na kuhakikisha kwamba nchi inakuwa ya kijani na kwamba tunavuna sawasawa ni tuhakikishe kwamba tunatengeneza miundombinu ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaishi milimani kule Arusha Wilaya ya Arumeru. Kule kuna mvua za kutosha na kila mwaka kunatokea na mafuriko. Mafuriko haya yanakwenda yanaharibu mashamba na miundombinu sehemu za tambarare . Rai yangu kwa Serikali, tuhakikishe kwamba tunavuna maji haya na kuyatumia kwa ajili ya kumwagilia mashamba yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu ahadi za Mheshimiwa Rais. Kwenye hotuba ya Rais ya tarehe 13 Novemba, 2020 alisema atatoa vipaumbele kwenye ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni. Nimkumbushe Mheshimiwa Waziri atenge fedha kwa ajili ya kutekeleza ahadi zile, maana sasa hivi zile ahadi ni wosia, na usipotekeeza wosia unapata laana, na haya maneno si yangu, aliyazungumza Rais wetu mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati akiapisha viongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kwamba Halmashauri zetu nyingi zimeendelea kufanya kazi kwa shida kwa kuwa hazina mapato ya ndani. Kwa mfano Halmashauri ya Arumeru mwaka juzi ilikuwa imetengewa fedha kwa ajili ya mradi wa kituo cha mabasi lakini fedha zile zilirudishwa, sijaelewa kwanini ule mradi ulikatizwa. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aliangalie hili sasa. Kwamba ili Halmashauri zifanya kazi vizuri zinapaswa ziwezeshwe, watekeleze miradi mkakati kwa kule Halmashauri ya Meru tunahitaji bado kile kituo cha mabasi lakini pia kuna soko la Tengeru, lile soko la Tengeru linatoa huduma kwa wananchi wengi; linatembelewa hata na wananchi kutoka nchi za jirani kuja kufanya biashara na kuja kununua mazao pale. Niombe Serikali iliangalie ili hilo soko liweze kujengwa na kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanafanya biashara zao vizuri kwa ajili ya kuboresha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nipo kwenye ahadi za Mheshimiwa Rais, nakumbushia barabara ya King’ori na nitaendelea kuikumbusha, kila nikisimama nitaendelea kuikumbushia; na hizi ni pamoja na ahadi ya kilometa tano ambazo Marehemu aliitoa pale USA River tarehe 6 Oktoba, 2015. Kwa bahati mbaya mpaka leo hakuna hata mita moja iliyojengwa pale USA River pamoja na kwamba ule mji ulishatangazwa kwamba Mamlaka ya Mji Mdogo. Niombe Serikali iendelee kuwazia Mji wa USA River ili uingizwe kwenye ule mpango ule mradi wa TACTIC angalau nao miundombinu yake ijengwe kwa sababu ule mji ni Makao Makuu ya Wilaya ya Arumeru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa muda mfupi huu. Yako mengi yakusema lakini niishie hapa; nashukuru kwa muda ulionipa naunga mkono hoja (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsantse sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi nimesimama kuunga mkono hoja zote mbili, ukizingatia pia kwamba mimi ni mjumbe wa Kamati ya PIC, lakini pia nimekuwa wa ili kutoka mwisho kuchangia, kwa hiyo, mengi yameshazunguzwa na Wabunge wenzangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze sana wenyeviti wote wawili kwa hotuba zao nzuri ambazo zimejaa na zimesheheni kila tulichokuwa tunakihitaji. Lakini pia nikupongeze wewe na Mheshimiwa Spika kwa kuaminiwa na chama chetu na majina yenu yakarudi hapa nasi tukafanya kweli, na sasa hivi ninyi ndio viongozi wa kuu wa huu mhimili muhimu wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee sana nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana mama yetu na kumpongeza kwa kazi nzuri ambazo Mheshimiwa Rais anawafanyia Watanzania, kwa uongozi mahiri. Kwa kweli amefanya makubwa. Mwaka jana ametengeneza historia kwa Watanzania, madara 15,000 kwenye sekta ya elimu si jambo dogo; lakini pia kule Arumeru Mashariki nasi tulipata madara 70 ambayo kwakweli ametua mzigo mkubwa sana kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, si sekta ya elimu tu, hata sekta nyingine alifanya kazi nzuri mno, zile fedha za UVICO 19 alizotuletea na kuzisambaza kwa uwazi mkubwa zimeweka historia kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hizo salamu za pongezi naomba sasa nirudi kwenye hoja, na nitazungumzia mambo mawili kwa ufupi sana. Nazungumzia changamoto za bodi za wakurugenzi za mashirika na taasisi zetu za umma. Lakini pia nitazungumzia upungufu wa mitaji kwa taasisi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekutana na mashirika kadhaa ambayo yalikuwa na matatizo ya bodi, kwamba bodi haipo na kama ipo composition yake ina matatizo. Kwa mfano EPZA na TIC, na TIC haikuwa na bodi, lakini pia watendaji wakuu na waliokuwa wameshika nafasi zile nyeti walikuwa wanakaimu. Sasa hii kukaimu na kutokuwa na bodi kunafifisha utendaji kazi wa hizi taasisi zetu. Tunaomba Serikali iangalie kwa jicho tofauti kidogo maeneo haya na kuhakikisha kwamba taasisi hizi zinakuwa na utawala ambao ni timilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upungufu wa mitaji, tulishuhudia kwamba kuna taasisi na mashirika kadhaa ambayo hayana mitaji ya kutosha. Kwa mfano TTCL, TPDC, TADB pamoja na EPZA. Mashirika haya yameanzishwa na Serikali na yalitegemea kuwa funded fully kwa sababu umiliki ni wa Serikali kamili. Mashirika haya, kwa mfano EPZA kwa miaka mitatu Serikali haijatoa fedha. Matunda yake ni kwamba EPZA imekuwa inafanya kazi zake kwa kusuasua. Zone pekee ambayo inaonekana inafanya kazi vizuri ni ya Benjamin William Mkapa iliyoko kule Mabibo, huku kwingine kote wanasuasua na sehemu nyingine kwa sababu wana nguvu ya kisheria ya kuchukua ardhi ya wananchi na kuwafidia, wameshindwa kuchukua lakini wakasababisha taharuki, kwamba wanachukua lakini hatimaye hawapi fedha lakini wameshatia doa kwenye maisha ya wananchi kwamba wananyang’anywa maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali itazame vizuri na kuhakikisha kwamba taasisi hizi wakati zinaanzishwa ziwe funded fully, pamoja na TADB lakini tunashukuru na tunaipongeza Serikali kwamba iliweza kutoa shilingi bilioni 208 mwezi Disemba.

NAIBU SPIKA: Malizia Mheshimiwa.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia kengele imelia, basi niseme tu kwamba naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa muda nimeshindwa kusema mengine ambayo nilitamani niyaseme katika mchango wangu katika bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Maliasili na Utalii bado kuna tatizo la mpaka kati ya ANAPA na Kitongoji cha Momela na eneo lenye mgogoro lilikuwa sehemu ya mashamba Na. 40 na 41 na ukubwa wake ni ekari 604. Walikuja kwangu akina mama kutoka eneo husika wakilia na kulalamika wameolewa na kuishi eneo hilo kwa takribani miaka wamezaa na watoto wao kuolewa na sasa wanaambiwa wahame bila kuelekezwa waende wapi na Meru hakuna tena ardhi iliyo wazi.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Rais kwa huruma yake kama mama aruhusu wananchi wale waendelee kuishi kwenye makazi yao hata kama ni kwa masharti ya kihifadhi kama WMA.

Pili ni kuhusu Ujenzi na Uchukuzi; ahadi za Rais; Arumeru Mashariki tuna ahadi kadhaa za viongozi wakuu ambazo hazijafanyiwa kazi; kwanza barabara ya Kingori kuanzia Malula Kibaoni hadi Ngarenanyuki kujengwa kwa kiwango cha lami ni moja ya ahadi alizotoa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa mwezi Oktoba, 2020 pale Usa River mbele ya maelfu ya wananchi wa Arumeru. Nakumbuka Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan - Rais wa Awamu ya Sita katika hotuba yake kwa Baraza lake la Kwanza la Mawaziri aliahidi kutekeleza yote yaliyokuwa kwenye mipango ya mtangulizi wake aliyerehemika akiwa kazini ikiwa ni pamoja na ahadi zote alizotoa kwa Watanzania, naomba tamko la Serikali kuhusu ahadi hii.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hoja hii ambayo ipo mezani. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya PIC. Kwa hiyo nitajikita zaidi kwenye Kamati hiyo.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kukupongeza wewe kwa kazi nzuri ambayo unafanya, unaongeza Bunge hili kwa umahiri mkubwa, hadi IPU imekuona; hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nisiishie hapo, nimshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuandika historia kwenye Jimbo langu. Ametuletea fedha nyingi za maendeleo. Hapa si mahali pa kuzizungumzia sana, lakini itoshe kusema nashukuru mno, ameandika historia kwenye Jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nichukue nafasi hii, kupongeza Wenyeviti wa Kamati hzi tatu PAC, PIC na LAAC, pamoja na wajumbe na wote kwa kazi nzuri ambayo wamefanya na hatimaye hizi taarifa zikaja mezani kwako.

Mheshimiwa Spika, Serikali kama baba ambavyo anahangaika kutafuta resources huku na kule, mikopo ya bei nafuu, misaada, yote hii ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba anatuletea maendelo wananchi wake. Fedha hizi Serikali imeamua kwamba, pamoja na mambo mengine tutumie resources zote kuziweka kama mitaji kwenye kampuni na taasisi zake.

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu ilipewa jukumu la kuchambua na kubaini ufanisi wa uwekezaji huu ambao Serikali inafanya, ambao ni uwekezaji mkubwa sana. Hadi kufikia tarehe 30 Mwezi wa Sita mwaka 2021 Kamati ilibaini kwamba Serikali ilikuwa imewekeza kwenye taasisi na kampuni zake shilingi trilioni 67.95. Hizi ni fedha nyingi sana. Pia, katika uchambuzi, tumebaini kwamba, TR alieka maotea; ali-project kufanya makusanyo ya returns za uwekezaji wa takribani bilioni 930.3, lakini halisi iliyokusanywa ni bilioni 637.66.

Mheshimiwa Spika, tukiendelea kuchambua yale makusanyo ambayo yanatakiwa yakusanywe, kwa maana ya gawio percent 15 ya mapato ghafi ya Serikali na kampuni hizi, urejeshaji wa mikopo, urejeshaji wa TTMS na makusanyo mengine; tumeona kwamba kulikuwa na mapungufu. Kwa mfano, gawio, maoteo ya TR yalikuwa ni bilioni 408 lakini halisi ilikuwa ni bilioni 308.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo ufanisi hapa ilikuwa ni percent 75.61. Percent 15 ya makusanyo ya kisheria, maoteo ilikuwa bilioni 365.4 makusanyo halisi ilikuwa bilioni
202.2. Kwa hiyo ufanisi hapa wa mtaji ulikuwa percent 51.

Mheshimiwa Spika, tuliendelea kuchambua na kuangalia kwamba ni sababu gani zimepelekea haya mashirika na taasisi za Serikali zikashindwa kufikia malengo. Tukachambua changamoto, tukatazama mashirika yale ambayo yalikuwa yamelengwa, tukaona kulikuwa na matatizo kidogo. Moja, kulikuwa na shida kubwa, taasisi zile zinakuwa hazina Bodi za Wakurugenzi kwa muda mrefu, lakini pia, taasisi zile zilikuwa hazina vibali vya kuajiri wataalum, kwa hiyo vibali vinachelewa sana, matunda yake ufanisi unakwenda ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Spika, pia, tuligundua kwamba kuna mwingiliano wa majukumu kati ya taasisi na taasisi. Kwa mfano TANROADS na TIA; ukijaribu kuangalia majukumu yake utakuta yanafanana; lakini TIA wamepewa umiliki, hawaangaliii ujenzi, wao wamepewa jukumu la kuangalia matengenezo ya kazi ambayo imefanywa na mtu mwingine; kwa hiyo, quality ya kazi hawaijui. Lakini pia kulikuwa na tatizo la kuajiri wataalamu. Tumekuta bodi nyingi sana hazina Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi, au watumishi wana kaimu. Hilo ni tataizo kubwa sana kwa sababu hatimaye maamuzi hayafanyiki on time (kwa wakati).

Mheshimiwa Spika, lakini pia, kulikuwepo na tatizo la mitaji. Utakuta Serikali inanzisha taasisi na kuahidi itatoa mtaji kamili, mfano mzuri ni Benki ya TADB ambayo ilikuwa inahitaji mtaji wa Shilingi bilioni 760. Hadi mwaka jana ilikuwa imepata bilioni 208, zikaongezeka bilioni 60. Kwa kweli tunaona kwamba uchelewaji wa mitaji au kutokuwa na mitaji kuna athiri performance za hizi taasisi za Serikali ambazo zimeanzishwa kwa lengo zuri tu la kuhakikisha kwamba fedha zinazungushwa na faida ipatikane, iweze kwenda kuhudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, pia, kuna taasisi ambazo zilianzishwa lakini zina madeni chechefu; kwa mfano TIB na TCB. Hizo ni benki ambazo vitabu vyake vinaonyesha kwamba kuna madeni makubwa ambayo hatimaye hatuamini kama yatalipika. Wazo letu kama Kamati ni kuwa utaratibu ufanyike ili hao madeni yaangaliwe namna ya kufutwa bila kuathiri ukusanywaji wa yale madeni ambayo yanalipika.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo mafupi, Kamati ilikaa ikatoa maoni yake, ikatoa mapendekezo yake na maazimio. Kwa kulinda wakati, niseme kwamba, mimi kama Mwanakamati wa hii Kamati ya PIC, naungana na Mwenyekiti na Wajumbe wote kuunga mkono mapendekezo, maoni na maazimio ambayo yapo kwenye taarifa.

Mheshimiwa Spika, nisiishie hapo, pia nimesoma hizi taarifa za Kamati zingine; zinaeleweka, nako niseme kwamba pia naunga mkono yale maoni, mapendekezo na maazimio ambayo yamewekwa kwenye zile taarifa

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, niseme nashukuru sana kwa nafasi hii naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kutoa mchango wangu kwa hoja hii ambayo ipo mezani. Nitangulie kwa kuungana na wenzangu waliozungumza hapa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai, afya na nguvu hata tukaweza kukutana hapa leo. Napenda pia kuendelea kuwashukuru wananchi wangu kule Arumeru Mashariki kuendelea kuniamini na niwahakikishie kwamba kazi inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa nachukua nafasi hii kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa Bashungwa na Manaibu wake wawili Mheshimiwa Dugange na Mheshimiwa Silinde kwa kazi nzuri sana ambayo wanafanya. Ni vijana wema, wasikivu na ndiyo maana wameimudu hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nisipowashukuru na kuwapongeza watendaji wakuu kuanzia Katibu Mkuu na watendaji wengine, nitakuwa sijatenda haki. Nawapongeza watumishi wote kwenye hii Wizara. Ukisoma vizuri hii hotuba ya Waziri wa TAMISEMI, utakubaliana nami kwamba ile reflection ya siku 365 za Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan akiwa ofisini. Ni kipindi hiki ambacho tumeona utekelezaji wa Ilani chini ya uongozi mahiri wa Mama ukifanyika kwa umahiri mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni katika kipindi hiki, kila Jimbo lilipata shilingi bilioni moja na nusu kwa ajili ya barabara kwa kupitia TARURA. Nasi tulipata hivyo hivyo, tunavyozungumza sasa hivi barabara ya King’ori ambayo nilikuwa naizungumzia hapa mara kwa mara, imefunguka, ni barabara. Nashukuru sana na ninaipongeza Wizara kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi za viongozi wakuu wa nchi ambazo zilitolewa, hazijatekelezwa. Mwaka 2012 Januari wakati wa maziko ya aliyekuwa Mbunge wetu, Marehemu Jeremiah Sumari, tulipewa ahadi na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, kwamba barabara inayoanzia Sangisi kwenda Keri hadi Ndoombwe ingejengwa kwa kiwango la lami. Leo hii ni miaka 10 na ushee, bado ile ahadi haijatekelezwa. Naomba wakati wa kuhitimisha Mheshimiwa Waziri atoe tamko kuhusu barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye suala la afya bado kuna ahadi nyingine. Mwaka 2020 Rais wa Awamu ya Tano, Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli alitoa ahadi mbele ya wananchi wengi sana pale Usa River kwamba barabara ya King’ori kuanzia maeneo ya Kibaoni hadi Ngare Nanyuki kwa kupitia King’ori Madukani - Maruvango - Leguruki ingejegwa kwa kiwango cha lami. Ninaamini Mheshimiwa Waziri katika kuhitimisha pia atatoa tamko kuhusu ahadi hiyo ya Rais, kwa sababu pia hata kwenye maelezo ya hotuba yake amesema haya mambo ni ilani na ahadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya niseme pia kwamba, ni kwa kipindi hiki cha siku 365 ambapo tumeshuhudia vituo vya afya vinajengwa vingi, nchi nzima. Kule Meru pia nasi tumepata Kituo cha Afya cha King’ori, lakini niseme pia kwamba tuna matatizo ya vituo vya afya. Vituo vingi vya afya kule zilikuwa zahanati, ni maboma yaliyochoka, Mheshimiwa Waziri ukumbuke, ukipata nafasi twende tukatembee uone hali ilivyo kwenye vituo vya afya. Tunashukuru sana tulipata Kituo cha Afya na tulipata pia fedha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kujenga Emergence Unit pale kwenye Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni katika kipindi cha siku 365 tuliweza kupata madarasa 70 ndani wa wiki nane. Ndani ya miezi miwili tulipata madarasa 70 kule Meru, kwa kweli tunapongeza Serikali kwa hilo. Tunashukuru sana, imetupunguzia mzigo, wananchi hawauzi tena kuku wakikimbizana kujenga maboma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kwamba kuna shule nyingi kule Jimboni ambazo zinahitaji ukarabati. Naomba Wizara ilitazame hilo ili ije na operation ya kukarabati zile shule, kwa sababu miundombinu imekaa vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu pia kuwatetea Madiwani. Kwakweli Madiwani wanafanya kazi kubwa sana kwenye Majimbo yetu, lakini ukiangalia stahiki zao hazitoshelezi. Wanapata sitting lakini wanahangaika huku na kule kusimamia miradi ambayo inatekelezwa kwa fedha za ndani, lakini pia na fedha ambazo zinatoka Serikali Kuu. Wakati umefika sasa tuangalie maslahi yao. Wabunge wamesema nadhani Mheshimiwa Waziri utaliangalia hilo ili Madiwani wetu wapate ahueni kwenye bajeti inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nitoe mchango wangu huo kwa ufupi sana. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa ruhusa na ridhaa yako niwasilishe mchango wangu kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi alivyosimamia kidete miradi mikubwa ya kimkakati;

(a) Ujenzi wa SGR ambapo sasa lot II za Dar es Salaam – Morogoro na Morogoro – Dodoma zimekamilika na kubadilisha kabisa taratibu za usafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma na kufanya uchumi wa Dodoma kupaa ghafla.

(b) Ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao sasa umefikia 96% na sasa mgao wa umeme haupo tena nchini.

(c) Kufufua na kulijenga upya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na sasa ATCL ina ndege 16, ikiwepo ndege moja kubwa ya mizigo.

(d) Kupeleka fedha nyingi, kwa ajili ya miradi ya maendeleo sekta zote majimboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, naomba nitoe ushauri juu ya mambo muhimu machache ya kuzingatiwa katika mpango unaopendekezwa .

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kilimo. Hii ndiyo sekta inayoajiri Watanzania wengi (70%), lakini mchango wake katika pato la Taifa uko chini 30% licha ya mipango na kauli mbiu nyingi; uti wa mgongo, siasa ni kilimo, kilimo kwanza na kadhalika. Nchi yetu bado ina eneo kubwa la ardhi ambayo inaweza kuzalisha chakula na mazao mengine ya kibiashara, lakini bado tunashindwa kufikia malengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, mpango unaopendekezwa nashauri uelekeze nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea hali ya hewa. Pili, mpango unaopendekezwa nashauri uelekeze nguvu kujenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua yatumike kufanya kilimo cha umwagiliaji na matumizi mengine ya kibinadamu na tatu, mpango unaopendekezwa nashauri uelekeze nguvu katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao yanayolimwa, ili hatimaye kilimo chetu kiwe ni kilimo cha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nishati. Mpango unaopendekezwa nashauri uelekeze nguvu nyingi katika kuhakikisha gesi asilia tuliyonayo inavunwa, ili azma ya Mheshimiwa Rais ya matumizi ya nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira kwa kiwango cha 80% ifikapo Mwaka 2034 inatimia, ikiwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme ambao utahitajika kwa wingi kukidhi mahitaji yatokanayo na umeme wa REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu ya barabara. Mpango unaopendezwa nashauri uhakikishe ahadi zote zilizotolewa na viongozi wakuu wa nchi, za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, zinatekelezwa. Mpango pia, uzingatie hali ya majimbo kijiografia, ukubwa na terrain katika ujenzi ama kwa lami au zege kwa maeneo ya milimani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wameshasema mengi ya muhimu kwa hiyo, kwa haya machache ninaomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo kwenye hoja hii ambayo ipo mezani; na nijielekeze moja kwa katika pongezi. Nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso na Naibu wake pamoja na watendaji wote pale Wizarani, nikianza na Katibu Mkuu, Wakurugenzi lakini pia Mtendaji Mkuu wa RUWASA, Injinia Clement kwa kweli wameonesha wanatekeleza shughuli zao vizuri sana na wanastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kuangalia taarifa ya utekelezaji kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hali ya upatikanaji wa maji lengo mpaka 2025 kwa upande wa vijini ni asilimia 85 lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza Wizara imeshafanikiwa kwa kiwango cha Asilimia 74.5 upatikanaji wa maji safi na salama vijijini; lakini pia asilimia 86.5 kwa upatikanaji wa maji salama mijini. Haya ni mafanikio makubwa sana, tunaendelea kuwapongeza Waziri na timu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio katika utekelezaji wa miradi mpaka tunavyozungumza sasa hivi kwa mwaka wa fedha tunaoumalizia, Wizara imekwishatekeleza miradi kwa kiwango cha percent 95. Hayo ni mafanikio makubwa sana, na tunaipongeza wizara kwa kazi nzuri hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisoma Pugu miaka ya nyuma hiyo, wakati nasoma pale A level tatizo la maji lilikuwa nightmare. Lakini mwezi Machi nilikwenda kule nikiwa kwenye ziara ya Kamati yetu nikakuta Wizara imetekeleza mradi, pale Kisarawe kuna tanki la lita milioni 10 na kuelekea upande wa Pugu kuna tanki la lita milioni mbili maana yake ni kwamba lile tatizo la maji Pugu limemalizika. Nilifurahi mno, nilibubujika furaha; nichukue nafasi hii kwa kweli kipekee kabisa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na watumishi wote wizarani kwa kazi nzuri ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mafanikio ya wizara hayakuishia Pugu hata kule jimboni kwangu mambo ni mazuri. Kuna mradi ambao unaendelea sasa hivi katika Kata ya Keri na kwa Lusambu mradi wa maji Kijiji cha Patandi wenye thamani ya shilingi bilioni 2.7, Mkandarasi yupo kazini. Tunashukuru sana na tunapongeza Serikali kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, kuna mradi wa milioni 379 Kijiji cha Nshupu wa uboreshaji, kazi inaendelea tunaishukuru sana Serikali na kumpongeza Waziri. Pia kuna Mradi wa Kijiji cha Nkure milioni 502 wa fedha za UVIKO utekelezaji unaendelea, tunaishukuru na kuipongeza Serikali. Aidha, wakati Waziri walivyokuja kwenye ziara jimboni kwangu kukabidhi Kituo cha Utafiti wa Kuondoa Madini ya Fluoride kwenye Maji ambapo ilikuwa kinakabidhiwa Chuo cha Maji, Mheshimiwa Waziri ali-initiate mradi wa kuboresha upatikanaji wa maji Kijiji cha Kiwawa na Ngongongare na akatoa Shilingi milioni 100 kama fedha za awali. Mradi ule ni Shilingi bilioni, 1.6. Kazi inaendelea na RUWASA na AUSA wanashughulikia hiyo kazi. Tunashukuru na kuipongeza Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Imbasen, Kikatiti na Maji ya chai wa gharama ya Shilingi bilioni nne. Nasikia sasa hivi utekelezaji bado upo kwenye stage ya manunuzi. Tunashindwa kuelewa ni kwanini huo mradi umechelewa sana kwa sababu ulikuwa unapaswa uanze wakati mmoja na mradi wa Patandi. Niweke angalizo kwamba inaelekea RUWASA wanakumbatia sana sana taratibu za manunuzi, hawajaweza kuzi-delegate chini kwa Mamlaka za Mkoa na Wilaya. Ni vizuri wakafanya delegation ili hizi kazi zikafanyika haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mafanikio ya wizara si bure, ni reflection ya kazi nzuri ambayo inafanywa na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. Nichukue nafasi hii kipekee kabisa na kwa dhati ya moyo wangu kumpongeza kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, anatubeba Watanzania kama watoto wake. Hata ukiangalia anavyohangaika; juzi tulizindua Filamu ya Royal Tour ambayo kimsingi imekuja kuitangaza nchi yetu hasa kwenye utalii. Yote kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watanzania tunatoka hapa tulipo tunakuza utalii kwa maendeleo ya nchi hii. Lakini pia mwaka jana alituletea fedha za maendeleo nje ya bajeti ambapo hivi fedha milioni 502 ambazo na sisi tumepata Kijiji cha Nkure zilielekezwa kutoka kwenye lile fungu Shilingi trilioni 1.3.; tunamshukuru na tunampongeza tunamuombea maisha marefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi ya kuzungumza lakini nasiki kengele imeshalia, basi nichukue nafasi hii kukushukuru sana naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ilio nichangie kwenye hii Wizara ambayo ni Wizara muhimu sana iliyotubeba sisi Wabunge, Wizara ya TAMISEMI chini ya Ofisi ya Rais, lakini ambayo inasimamia Tawala za Mikoa, halmashauri zetu na kule kwetu tunakotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kwanza kushukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi ambayo anawafanyia Watanzania. Anatubeba Watanzania kama watoto wake, kama mama anavyobeba watoto wake. Amesambaza fedha majimboni, kila jimbo, ukijaribu kufuatilia kila Mbunge akisimama anazungumzia habari ya mabilioni mabilioni na sisi kule Arumeru Mashariki pia tumepata hiyo neema ya kupokea mabilioni. Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kipekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Dada yetu Mheshimiwa Angellah Kairuki pamoja na wasaidizi wake Mheshimiwa Dkt. Dugange na Mheshimiwa Deo Ndejembi ambao kusema kweli wanafanya kazi nzuri. Kwa dhati kabisa niseme kwamba hawa vijana wawili ni vijana wema sana lakini Mheshimiwa Waziri naye ni mwema sana, kila Mbunge amesema kwamba akipigiwa simu anapokea, kama asipopokea anarudisha ujumbe kwamba nitakupigia. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema tumepokea fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo Jimboni kwangu. Naomba niseme machache kisekta kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jimboni kwangu changamoto kubwa sana ni miundombinu ya barabara. Ni ngumu kwa sababu lile jimbo letu sehemu kubwa limebeba Mlima Meru, kwa hiyo wananchi wanaishi kwenye miinuko, miteremko ya Mlima Meru na kwa hiyo miundombinu barabara huwa zinaharibika sana kila msimu wa mvua na barabara nyingi ni za udongo na changarawe. Kwa hiyo tuna shida kubwa ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niseme kwamba TARURA wamekuwa wanafanya kazi nzuri. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mtendaji Mkuu Engineer Seif, kwa kazi ambayo anafanya. Ni kijana mzuri ambaye ukimpigia simu anapokea na anachukua hatua saa hiyo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu nina barabara ambazo ni ahadi za Viongozi Wakuu. Barabara ya King’ori ni ahadi ya Rais kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, lakini mpaka sasa hiyo ahadi haijatekelezwa. Hiyo barabara inaanzia Malula – Kibaoni - Ngarenanyuki lakini inapitia King’ori. Kutoka Ngarenanyuki iko chini ya TANROADS, lakini ni barabara muhimu Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri. Ile barabara ikijengwa kwa kiwango cha lami itakuwa bypass ya mashariki ambayo itasaidia sana utalii kwenye lile jimbo na kuchangia uchumi kwa kuwa itazalisha ajira kwa kata nane ambako inapita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana waifikirie ni ahadi ya Rais na ahadi ni deni na kusema ukweli ahadi za Viongozi Wakuu zinatusumbua na ziko nyingi. Nilitoka kuzungumza na Naibu Waziri Mheshimiwa Silinde akaniambia inatakiwa ifanyike operation ya kuondoa madeni haya ya ahadi za Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA wamepata shilingi bilioni 855. Fedha hizi kila tukizichambua bado ni kidogo. Bajeti ya TARURA iko chini kwa sababu wanahangaika na barabara za vumbi, changarawe ambazo huwa zinaathiriwa sana na hali ya hewa. Kwa hiyo tuiombe TARURA waongezewe fedha na kule kwetu ambako barabara zinapanda milimani na siyo kwetu tu, maeneo yote ambayo yana milima TARURA wanapata shida sana. Waongezewe fedha, sisi kwa mwaka tunapata kama shilingi bilioni mbili kama na nusu. Hizo fedha ni kidogo, tungepata kama shilingi bilioni tano, ungeona Wabunge wangekuwa watulivu. Wangeona kwamba kazi zinafanyika na zinaonekana. Kwa sasa hivi nakiri kwamba Bajeti ya TARURA iko chini. TARURA wanafanya kazi vizuri lakini hawapati fedha za kutosha, muhimu waongezewe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafuatilia pia kupanga na kusema kwamba tunatoa fedha kiasi Fulani, ni suala moja lakini kutekeleza kwa maana ya kutoa fedha miradi itekelezwe ni suala lingine. Taarifa nilizonazo ni kwamba sisi tulipata shilingi bilioni 2.1 kwa mwaka huu wa fedha ambao tunamaliza kesho kutwa, lakini mpaka sasa tumepata shilingi bilioni moja na chenji. Utekelezaji unafanyika umeshafikia 46% peke yake. Tunaomba fedha zitoke kwa wakati ili miradi ambayo imepangwa kutekelezwa itekelezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali. Toka kipindi cha miaka miwili ya Mheshimiwa Rais aliyokaa madarakani, Sekta ya Afya tumepata fedha nyingi. Nimepata Kituo cha Afya cha Mareu, kazi iliyofanyika ni nzuri sana, lakini niseme kwamba tulipata ahadi ya vituo vitatu vya kimkakati kwa kila tarafa. Sasa namuuliza Mheshimiwa Waziri, nimepata kituo kimoja, vile viwili viko wapi? Pale Karangai kuna eneo tumetenga kwa ajili ya kuweka kituo cha afya naomba wakumbuke mwaka huu wa fedha tupate kituo kingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana, kengele imeshalia.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni ya kwanza, si bado ya pili?

MWENYEKITI: Mheshimiwa ni ya pili hiyo.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi nichangie kwenye bajeti hii ya Wizara ya Maji, Wizara ambayo ni muhimu sana kwa Watanzania kwa kuwa maji ni uhai.

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu kwanza kutoa shukrani zangu na pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa kweli anatufanyia Watanzania kazi nzuri sana na amedhamiria kwa dhati kabisa kuinua ubora wa maisha ya Watanzania, siyo kwenye sekta ya maji tu, lakini sekta zote. Na wewe pia Mheshimiwa Spika nakupongeza sana kwa kazi nzuri unaendesha hili Bunge kwa umahiri mkubwa. Sasa niende kwa Waziri, Waziri tunakupongeza, Waziri, Naibu Waziri na timu nzima pale Wizarani ni Pamoja na watendaji Wakuu kwenye Mkoa mnafanya kazi nzuri sana, kuhakikisha kwamba azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani inatimia; ile ndoto inatimia.

Mheshimiwa Spika, katika jitihada zenu na sisi kule Arumeru Mashariki tumeopata neema, kuna miradi mingi ambayo inaendelea. Miradi ambayo inandelea sasa hivi ina takribani bilioni 12. Mradi wa Patandi unaendelea vizuri, mradi wa Nkure umemalizika wananchi wanakunywa maji na wanaoga mara tatu sasa kwa siku. Mradi wa Imbaseni Maji ya Chai ambao una bilioni sita, pamoja na Kikatiti unaendelea vizuri. Mradi wakule Uwiro bilioni nne, uko kwenye taratibu za manunuzi na taratibu zinaendelea vizuri. Kwa kweli nakupongeza na nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo niweke angalizo, tumeshuhudia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, wakati ukame ulipotokea maji yalikosekana kabisa kule Meru. Hata Mheshimiwa Waziri wa Habari alikuwa pale Kili Golf alishangaa kuona kwamba, hakuna maji Meru na mlima uko jirani pale unatoa maji mengi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba, kwa kuwa maji yale yanakwenda kwa gravity, kuwe na matenki makubwa kwenye vyanzo vya kuhifadhi yale maji yasipotee hovyo, lakini pia matanki ya ku-reserve yawe mengi kwenye main line kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, pressure inakuwa sawasawa mpaka kule mwisho kwenye vijiji vya mwisho. Mheshimiwa Waziri, kipekee kabisa nikushukuru, tarehe 27 Februari, 2022 alikuja Arumeru Mashariki, tukafanya kikao pale kwa DC, nikampelekea kilio cha Korongo la Mpeduwima ambalo lilikuwa limepotea kwamba, linahitaji kufukuliwa.

Mheshimiwa Spika, Waziri hakuchelewa akatuma wataalam wa Bonde la Mto Pangani tukaenda kufanya survey na badaye ile kazi ilifanyika na alikuja kuzindua. Kwa kweli, lile korongo sasa hivi limerudi kwenye hali yake. Takribani kilometa 18 lile korongo linaonekana, mvua za mwaka huu hazijaleta matatizo. Namshukuru sana ndugu yangu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kawaida ukishasafiri safari ya kwanza inaita safari ya pili. Baada ya yale maji sasa kwamba, yamepelekwa kule mwisho, yamekwenda kuishia Kata ya Majengo, sasa Kata ya Majengo ndio inateseka, maji yanakwenda kutuama kule yanawanyima wananchi kuishi kwa furaha na amani. Nimwombe Waziri sasa aweke kwenye mipango yake, tuje tujenge bwawa pale Kata ya Majengo yale maji yakusanywe pale yaunganike na mifereji ambayo itajengwa kwa kuanzia kule Kimweli Malula kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua na mafuriko ambayo yanatokea. Hata juzi kuna mafuriko yalitokea mpaka yakasomba gari. Yale maji yakusanywe yapelekwe kwenye bwawa ambalo litajengwa pale Majengo, hayo maji yatumike kwa ajili ya mifugo na kwa ajili ya irrigation. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nilikuwa nataka kuongeza lingine, lakini kwa haya machache, kwa leo nasema ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Nishati ambayo ndiyo hasa inatupeleka kwenye maendeleo nchi hii. Pamoja na shukrani hizo nichukue nafasi hii pia kuungana na wenzangu kukuombea uso wa Mungu upatane nawe katika hiyo safari ambayo unaiendea. Tunaamini kabisa kwamba unaweza. Kwa namna ambavyo unaendesha hili Bunge kwa umahiri mkubwa, huko unakokwenda ni shaihi kabisa. Tunakuombea Mungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anatufanyia kazi Watanzania. Pamoja na fedha nyingi sana ambazo ameweza kupeleka majimboni mabilioni kwa mabilioni, lakini pia ameendelea kutekeleza miradi mkakati mikubwa na mfano mzuri kabisa ni hili Bwawa la Nyerere ambalo linakuja kutuongezea umeme mwingi sana kwenye grid ya Taifa, megawati 2,115. Kazi inayofanyika ni nzuri na sasa hivi kazi imefikia asilimia 86.89; kwa kweli tunamshukuru na kumpongeza.

Mheshimiwa Spika, lakini kipekee nimpongeze Waziri Januari Makamba na Naibu wake Stephen Byabato lakini pia Katibu Mkuu Eng. Mramba na Naibu wake Bwana Butuka na watendaji wote pale Wizarani, kazi ni nzuri inaonekana. Waliobahatika kufika kwenye mabanda ya maonesho ya wiki ya nishati, wanaweza kukubaliana na mimi kwamba Wizara inafanya kazi nzuri na mmejipanga vizuri. Kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba muendelee vivyo hivyo; ari hiyo hiyo, nguvu hiyohiyo, msirudi nyuma kwa sababu hii kazi ya kusambaza nishati kwa Watanzania ndiyo maendeleo yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa na pongezi hizo kwa Wizara nizungumzie kidogo kuhusu REA. Tunashukuru kwamba REA wanafanya kazi vizuri lakini kuna mapungufu. Waheshimiwa Wabunge wamesema, kwamba bado vijiji vingi havijapata umeme, vitongoji ndivyo vingi zaidi; lakini pia hat akule kwangu kule Arumeru Mashariki hali sio shwari sana. Kuna kata, vijiji na vitongoji ambavyo bado havijapata umeme. Hivi ni kama vile Kata za Uwiro, Marurango, King’ori na Majengo, kuna vijiji na vitongoji ambavyo havijapata umeme wa REA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na niseme kwamba, tatizo kubwa sana ni kwamba, hawa wakandarasi ambao wanapewa hii kazi wanapokuja majimboni wanakwenda moja kwa moja site bila kuwasiliana na mamlaka. Wanapaswa wakifika waripoti kwa DC, waripoti Halmashauri, lakini pia na Ofisi ya Mbunge kwa sababu Mbunge ndiye anayefuatilia hizi fedha. wanapokuja halafu wanakwenda moja kwa moja site kunakuwa kuna maswali mengi kwamba, kazi inaendeleaje, lakini kama wakipitia kwenye hizi ofisi nilizosema tukakaa chini wakatueleza mpango kazi inakuwa ni rahisi kuwafuatilia na kujua kwamba, kazi inaendeleaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kule Korogwe ambalo limezungumzwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati ni mfano halisi, kwamba kuna mapungufu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia, niseme kwamba bei ya kuunganisha umeme bado haiko clear. Nadhani ni wakati umefika Serikali iwe wazi iseme sasa kwamba, utaratibu uko hivi, shilingi 27,000/= zitatumika maeneo fulani na kulipia nguzo itakuwa maeneo fulani, ili tuache kuuliza maswali ambayo tunakutana nayo kwa wananchi na hatimaye na sisi tuwe na amani.

Mheshimiwa Spika, nilisema kwamba, kazi ni nzuri inayofanyika na Wabunge wote wamepongeza. Na niseme kwamba, Mheshimiwa Waziri endeleeni kufanya kazi vizuri, msimamie hapohapo, Watanzania wanawaona na wanawaelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye bajeti hii ya Maliasili na Utalii, Wizara ambayo kwa kweli ni nyeti, ambayo inachangia percent 25 ya fedha zote za kigeni pia percent 17.5 Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa, Naibu wake, Mheshimiwa Mary Masanja pia na Naibu Katibu Mkuu na Katibu Mkuu, kwa kazi nzuri ambayo wanafanya Wizarani pamoja na watumishi wote ambao kwa kweli wote wanachangia katika kazi nzuri ambazo zinafanywa na Wizara hii, ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, nilibahatika kutembea wakati wa ziara za Kamati kukagua miradi, tulikwenda Ngorongoro, tulikwenda TANAPA kule Mkomazi, tulikwenda TANAPA Rubondo. Kwa kweli kazi zinazofanyika ni za uhakika. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo mnafanya, wewe tunakufahamu, ni mtu mwema pia ni mchapakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijikite kwenye Hifadhi ya Arusha. Hii hifadhi ilianzishwa mwaka 1960, mwaka mmoja kabla hatujapata Uhuru wetu. Nimekuwa nashangaa kwamba ni kwa nini hii hifadhi ilitwa Arusha mpaka leo inaitwa Arusha, lakini kumbe hifadhi yenyewe ni sehemu ya Msitu wa Mlima Meru. Watalii wengi wanakuja wanapanda ule Mlima, nikaona heri leo nishauri Mheshimiwa Waziri ile hifadhi badala ya kuiita Arusha National Park, kuanzia leo ibadilike uiite Hifadhi ya Taifa ya Mount Meru (Mount Meru National Park). Nakuomba ikiwezekana leo wakati wa kuhitimisha hapa utangaze kwa Watanzania kwamba sasa ile hifadhi itakuwa ni Hifadhi ya Taifa ya Mlima Meru.

Mheshimiwa Spika, kwenye ile hifadhi kuna mgogoro. Niliwahi kufika kwenye ofisi ya Waziri nikamwambia kwamba tupange angalau tende kule Jimboni aende azungumze na wananchi, bahati mbaya ile timu ya Mawaziri Nane ambayo ilizunguka nchi nzima haikuweza kufika pale hifadhini iweze kuzungumza na wananchi. Kwa hiyo nakuomba ile agenda ya kwenda Momela ukazungumze na wananchi wa kile kitongiji usiiache. Upange twende ukazungumze na wale wananchi kwa sababu ule mgogoro ulianza siku nyingi na ulitokana na mashamba mawili, Na. 40 na Na. 41 kutwaliwa na Serikali ambayo mashamba haya yalikuwa yanamilikiwa na wawekezaji, mwekezaji wa kwanza akafa, akachukua mwingine baadaye yakamshinda akaya-abandon akayaacha pale.

Mheshimiwa Spika, wakati ulipokuja mpango wa vijiji na vijiji vya ujamaa, wananchi waambiwa wajipange kule wajikimu na kufanya kazi za kilimo na ufugaji. Mwaka 2017 Serikali iliwatoa kwa nguvu na baada ya pale hakuna kilichofanyika, wananchi wale wameachwa wanateseka wametupwa kwenye lindi la umaskini, niseme ukweli kwamba Serikali ina haki ya kuchukua ardhi yake kwa sababu ndiyo yenye mamlaka, lakini inavyotoa wananchi bila kujua wanawapeleka wapi, kidogo hiyo haiko sawa. Naamini kabisa kwamba Serikali ina nia njema, haiko hapa ku-displace wananchi wake lakini inapaswa ifanye relocation. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuamini wewe ni mtu mwema hili tatizo nina uhakika utalimaliza.

Mheshimiwa Spika, pia nadhani nilishawahi kuzungumza tena hapa kuhusu cable cars. Wakati unabadilisha jina la ile hifadhi uweke pia na cable car pale kwenye lango la kuingia hifadhini ambayo itakwenda mpaka Miliakamba. Nakuhakikishia ukiweka hiyo cable car idadi ya watalii wa ndani itaongezeka mara dufu. Nakuomba uliweke kwenye mpango ili tuweke huo mpango wa cable car.

Mheshimiwa Spika, naona unataka kunisemesha, basi niseme tu kwamba nakushukuru sana kwa muda huu mfupi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafsi hii nichangie hii bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2023/2024. Nianze kwanza kwa kuungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anawafanyia Watanzania, juhudu zake tumeziona katika kujenga Diplomasia ya Uchumi, Royal Tour na mambo haya yamefanya nchi yetu sasa imepanda ilikuwa Namba Sita kiuchumi Afrika, tumeondoka kwenye dola bilioni 69.9 mwaka 2021 na sasa tumefikia dola bilioni 85.4 kufika mwezi Aprili, haya ni mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anategemea sana wasaidizi wake wa karibu na kwa ajili hiyo nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake Mheshimiwa Chande pia na Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Mkuu pale Wizarani wote, hawa wanafanya kazi nzuri, ndiyo wametufikisha hapa tulipo kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuja na bajeti ya trilioni 44.39 fedha ambazo zinatakiwa zikusanywe na kutumika kwa mwaka huu wa fedha, sina mashaka kwamba hizo fedha zitapatikana kwa sababu nimesoma mikakati ya kuzitafuta lakini pia na mikakati ya usimamizi. Nimpongeze sana Waziri kwa kujipanga sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salamu hizo za pongezi naomba nizungumze kidogo kwenye Wizara za Kisekta nikianzia kilimo. Wenzangu wamesema kwamba Kilimo kinaajiri Watanzania wengi lakini mchango wake kiuchumi bado uko chini sana. Mimi nipongeze kwa kweli juhudi za Serikali katika kukiboresha na kukiinua kwa kuongeza bajeti kutoka bilioni 294 mwaka juzi sasa tuko bilioni 970 ambazo zimependekezwa hapa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinakuwa cha kisasa, kwa maana ya mbegu bora, pembejeo lakini pia na kuhakikisha kwamba tunaachana na kilimo cha kutegemea mvua. Nirudie kusema tena kwamba kwa kweli tutafanikiwa tu kama nchi hii tutaachana na kufanya kilimo cha kukaa na kusubiri mawingu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, kule Arusha Meru Tarafa za King’ori na Mbuguni kwa miaka mingi zimekuwa ndiyo kapu la chakula kwa ajili ya Jiji la Arusha na viunga vyake lakini pia hata kwa nchi za Jirani. Lakini sasa hivi Tarafa zile zimeathiriwa sana na mabaliliko ya tabianchi, na kwa hiyo nishauri Serikali ichukue hatua za haraka yajengwe mabwawa kwenye Tarafa hizo na kujenga skimu za umwagiliaji sambamba na kuendelea kutoa mbegu bora na pembejeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani sana miaka ya 1970 kule Kisimiri Juu tulikuwa tunalima Pareto na tulikuwa na Kiwanda cha Pareto kule Arusha, yale mashamba yalifungwa na siku hizi yale mashamba wananchi wanalima bangi. Kwa hiyo, Serikali imekuwa inahangaika sana kupambana na kilimo cha bangi kule Kisimiri Juu. Ushauri wangu kwa Serikali, tufufue Kilimo cha Pareto kule Kisimiri Juu, hali ya hewa inakubali kwa ajili ya kilimo cha Pareto nina taarifa kwamba Iringa wameanza ujenzi wa Kiwanda cha Pareto kama sijakosea, lakini kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba tunafufua kile kilimo cha Pareto ili wananchi waachane kilimo cha bangi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Serikali imekuja na mipango mingi tu, nimshauri Waziri, kule abeleke hii program ya BBT zile familia ziunganishwe, wasaidiwe kimtaji na kuhakikisha kwamba hicho Kilimo cha Pareto kinafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mashamba ya maua ambayo yalikuwa yanaongeza sana Pato la Taifa, yalikuwa yanatuingizia fedha nyingi za kigeni. Haya mashamba yamefungwa na wananchi wafanyakazi kule wamebaki wanahangaika kutafuta ajira, lakini pia wamekuwa maskini. Nishauri pia kwamba Serikali ije na mpango wa BBT kwenye yale mashamba ya maua, wale watumishi waliokuwa kwenye yale mashamba waunganishwe wachanganywe na vijana, wapewe pesa kazi iendelee na maisha yawe bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kupongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuja na mpango wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam. Sasa hivi Serikali inajenga SGR ambayo tunahakika kabisa kwamba itakuwa na uwezo mkubwa sana wa kubeba mizigo lakini kama bandari ile isingeboreshwa ile Reli ingebakia kama white elephant, jambo ambalo lingekuwa si zuri kwa sababu soko la huduma za bandari kwa nchi yetu ni kubwa sana. Bandari ya Dar es Salaam ina soko kubwa sana ya kutoa huduma landlocked counties za Malawi, Zambia, DRC, Burundi, Rwanda, Uganda na wakati mwingine Msumbiji. Kwa hiyo, uboreshaji wa ile bandari ni kama ni lazima ifanyike kazi kubwa ya kuiboresha na nashukuru Mungu kwamba Serikali imeshaanza mchakato kwa kusaini mkataba wa EGA kati ya Tanzania na Dubai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu nilikuwa na Waziri Mkuu juzi kule Jimboni kwangu alizungumza vizuri sana na kusema ile kweli alinisaidia sana mimi kama Mbunge kule kwa sababu sitakuwa na kazi kubwa sasa ya kwenda kuelimisha wananchi kuhusu hilo la bandari. Alizungumza alikaa kama Mwalimu akafundisha na watu wote waliomsikiliza waliondoka pale wana amani kwamba kumbe nchi haiuzwi, bandari haiuzwi bali inafanyiwa maboresho ili iweze kufanya kazi efficiently.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi kwa sababu ya muda na mimi naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi nichangie kwenye hotuba hii ya bajeti ya Maliasili na Utalii na moja kwa moja niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anawafanyia Watanzania hakika tumeshuhudia akihangaika huku na kule akituhangaikia sisi kama mama anavyohangaikia familia yake tunampongeza sana. Lakini amekwenda mbali zaidi akaamua kutengeneza filamu ya Royal Tour ambayo kimsingi imekuja kufungua nchi yetu kwenye biashara ya utalii na tunaamini kabisa kwamba sasa hivi tutapata watalii wengi na nimedodosa kule Arusha kuna makampuni mengi ya utalii wanasema booking zipo nyingi sana ni juu yetu sasa kujipanga kwa ajili ya kupokea wageni wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais na kumpa nafasi ya juu kwenye Wizara hii kama Waziri. Lakini pia nimpongeze Naibu Waziri Mheshimiwa Mary Masanja kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais akambakiza kwenye nafasi yake ya Unaibu Waziri kwenye Wizara hii, hawa wote viongozi wetu hawa wanafanya kazi nzuri wanatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sasa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu watendaji wote pale Wizarani kwa kazi nzuri ambayo wanafanya hakika tunawaona tunashuhudia, hata ukisoma hotuba ya Waziri mapato yatokanayo na maliasili nyuki wenyewe tu inachangia percent 3.3 kwenye pato la Taifa, si hivyo tu inachangia percent 5.9 kwa biashara ya nje ya nchi hii lakini biashara ya utalii inatupatia kwenye pato la Taifa percent 17 lakini pia percent 25 ya fedha kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ni kazi nzuri nilibahatika nilipata neema ya kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro mwezi wa tatu nikiwa na Kamati yangu pamoja na Hifadhi ya Mkomazi kwenye mradi wa faru kazi zinazofanyika kule zinafurahisha tunaamini kabisa kwamba uhifadhi na utalii unakwenda kukua kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kupongeza Wizara, lakini pia niseme kwamba kwa jinsi utalii unavyokua nchini mwenzangu asubuhi alizungumzia kuhusu cable cars, hakika milima yetu kuna milima miwili Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru ni vivutio vikubwa sana kwa utalii nchini hapa. Nilipata neema ya kwenda South Africa nikashuhudia jinsi ambavyo cable cars zinafanya kazi naamini kabisa kama huku tunakokwenda tutajenga hizo cable cars kwenye Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru tutasomba watu wengi kule mjini ambao watakwenda kupanda mlima na kushuhudia vivutio vya utalii, lakini pia kuingiza na kuongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na salamu zangu hizi za pongezi, kule kwenye jimbo langu kuna changamoto ya mpaka wa Kijiji cha Olkung’wado na Hifadhi ya Arusha. Changamoto hii ilisababishwa na TANAPA kununua mashamba mawili yaliyopo kwenye Kitongoji cha Momella na inavyoelekea ni kwamba Serikali ya Kijiji na wananchi hawakuhusishwa vizuri matunda yake ni kwamba sasa hivi kuna sheria mbili zinafanya wananchi wanapata shida, wanateseka kidogo. Sheria ya Uhifadhi inawafanya wananchi pamoja na kwamba kile kijiji yale mashamba walikuwa wanaishi pale, wamezaliwa pale wanaonekana kwamba wamevamia. Kwa hiyo, wahifadhi wakiwaona wakiwa palepale kwenye mashamba yale wanawaona kama wameingilia hifadhi. Pia Sheria ya Ardhi inaona kama wame trespass, wamevamia sehemu ambayo si ya kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nishauri Sheria ya Ardhi ina sehemu ambayo inasema kwamba yaani inatoa mwanya kwamba kama mwananchi amekuwa kwenye ardhi kwa zaidi ya miaka 12 anaweza akapewa kwa kutumia kipengele cha address possession.

Mheshimiwa Spika, nasema kwamba Wizara hizi mbili Maliasili na Wizara ya Ardhi wakae chini, waangalie ni wapi makosa yalifanyika kwa sababu kile kijiji kina Mwenyekiti wakati mashamba haya yananunuliwa alikuwepo Mwenyekiti na Mwenyekiti ardhi ipo chini yake sijui kama aliridhia hayo manunuzi. Kwa hiyo, kwa kweli nashauri kwamba Waziri wa Maliasili na Waziri wa Ardhi wakutane waone ukweli wa hili jambo kwa sababu ukifuatilia mgogoro huu wananchi wanavurugwa mara kwa mara, wanapigwa mabomu wakati mwingine, wanafukuzwa, mifugo yao inafukuzwa, lakini pia mashamba yao yanaharibiwa na jambo hilo si sawa ni tofauti na ni kinyume kabisa na azma ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo inazungumzia maisha bora kwa Watanzania wote, hilo ni ombi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matukio yaliyotokea mwaka 2017/2018 hayafurahishi hata kidogo na ndiyo maana nilisema niliseme hili kwa sababu wahifadhi wana element ya kupenda wanyama na misitu yao kuliko binadamu na hilo si kosa ndiyo kazi waliyopewa, lakini pia tukubali kwamba na binadamu wana value yao na tunataka wananchi wafurahie maisha yao katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa muda na idadi kubwa ya wachangiaji kwenye bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kwa ridhaa na ruhusa yako nitoe mchango wangu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na pongezi; awali ya yote naomba kumpongeza Waziri Mheshimiwa Mchengerwa kwa hotuba nzuri, lakini pia kwa kazi nzuri anayofanyia Taifa hili pamoja na wasaidizi wake Naibu Mawaziri Mheshimiwa Dkt. Dugange na Mheshimiwa Zainab Katimba pamoja na watendaji wote Wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa naomba kutoa shukrani na pongezi nyingi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha nyingi (mabilioni ya fedha za Kitanzania) katika kipindi kifupi cha miaka mitatu ya uongozi wake kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta zote za maji, elimu, (tumepata madarasa mengi na shule mpya saba), barabara, afya, nishati (umeme wa REA), kilimo na kadhalika, na wakati tukipokea fedha nyingi jimboni miradi ya kimkakakati kitaifa ya Bwawa la Nyerere, SGR na uboreshaji wa Shirika la Ndege la Tanzania kazi imekuwa inaendelea kwa ufanisi wa hali ya juu bila kusimama kwa sababu ya muda naomba kutoa shukrani na pongezi hizi bila takwimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto; pamoja na shukrani na pongezi hizo hapo juu naomba kuwasilisha changamoto tulizo nazo jimboni Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Kwanza ni kuhusu barabara; changamoto kubwa tuliyonayo Arumeru Mashariki ni barabara na hii inatokana na hali ya kijiografia ambayo siyo rafiki kwa barabara za vumbi na changarawe. Tiba pekee ni barabara za lami au teknolojia nyingine ya tabaka gumu. Aidha, tunaishukuru Serikali imeanza kutujengea barabara ya lami inayotokea Sangis kwenda Akheri hadi Ndoombo. Tatizo ujenzi unaendelea kwa kusuasua sana, tunaenda kumaliza mwaka wa pili na kazi iliyomalizika mpaka sasa ni mita 900 na mkandarasi anaendelea na mita 700 zilizotengewa fedha mwaka huu wa 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri TARURA waongezewe fedha ili waweze kutekeleza mradi huu kwa wakati. Aidha, tunaomba pia barabara zifuatazo ziwekwe kwenye mpango:-

(a) Leganga kwenda Mulala hadi Songoro;
(b) Sangisi hadi Seela; na
(c) Barabara ya mchepuko (ring road) toka Peace point (daraja la Mto Nduruma kupitia Nkoanrua, Akheri, Seela, Poli, Nkoaranga, Mulala hadi Ngurdoto).

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi za viongozi wakuu; zifuatazo ni barabara zilizoahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na viongozi wakuu nyakati tofauti walipofanya ziara jimboni ambazo ni kilometa tano za barabara za lami Mji Mdogo wa Usa River (Hayati Dkt. Magufuli mwaka 2015); kilometa 33 za barabara King'ori kuanzia Malula Kibaoni hadi Ngarenanyuki (Hayati Dkt. Magufuli mwaka 2020); na kilometa saba za barabara kutoka Kikatiti hadi Sakina (Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa mwaka 2023).

Mheshimiwa Naibu Spika kwa upande wa miradi ya kimkakati; Halmashauri ya Meru mpaka sasa haina mradi wowote wa kimkakati kwa ajili ya kuongeza mapato. Mwaka 2019 mradi wa stendi ya mabasi eneo la Madira uliondolewa dakika za mwisho kabla ya kuanza utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu michoro kwa ajili ya mradi wa soko la kisasa eneo hilo hilo la Madira imewasilishwa Wizarani tangu mwaka 2023. Nashauri mchakato wa kutekeleza mradi huo uharakishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hoja ambayo iko mezani bajeti ya Wizara ya Fedha pamoja na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na kwa jinsi anavyoongoza Taifa hili kwa ufanisi na umahiri mkubwa. Pia, nichukue nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wetu wawili hapa Dkt. Mwigulu Nchemba na Prof. Kitila, Naibu Mawaziri wake Mheshimiwa Chande na Mheshimiwa Nyongo kwa kazi nzuri ambayo wanafanya na hotuba inayoeleweka, bila kusahau watendaji kwenye hizi Wizara mbili kuanzia Katibu Mkuu na watumishi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ambayo tumeona mafanikio makubwa kwenye utekelezaji wa mambo mengi hapa nchini. Miundombinu inaendelea kutekelezwa, usafirishaji, SGR sasa hivi imefikia 96 percent kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora, lakini pia Bwawa la Mwalimu Nyerere ujenzi wake umefikia asilimia 98 na sasa hivi umeshatupa kwenye Grid ya Taifa Megawatts 470.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia bajeti ya kilimo ikipanda sasa hivi ni zaidi ya trilioni na uzalishaji wa chakula umevuka asilimia 124, pia matumizi ya mbegu bora na mbolea umeongezeka na maeneo ya umwagiliaji yameongezeka imefikia hekta 730,000. Haya mafanikio siyo kidogo, kwa hiyo niseme moja kwa moja kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo mafanikio nina machache ya kusema hasa kuhusu barabara. Barabara zimejengwa sana, sasa hivi tumefikia kilometa 181,600 lakini mafanikio haya sioni kama yamekuwa na impact kwenye Jimbo langu. Kwa hiyo, niseme wazi kwa Waziri wa Fedha na Mipango kwamba waweke mpango wananchi kule Arumeru Mashariki wa-feel mafanikio haya ya ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wengi kule Arumeru Mashariki wako milimani na wanafanya kilimo cha viazi na carrot, baada ya kuvuna mazo yao wanashindwa kuyapeleka sokoni kwa sababu ya shida ya barabara. Najua kwamba kuna mradi unaotekelezwa Nyanda za Juu Kusini wa Agri-connect. Sasa niishauri Serikali ifikirie namna gani italeta mradi kama ule kule Nyanda za Juu Kaskazini ili wananchi wanaolima milimani waweze kupeleka mazao yao sokoni. Mradi wa Nyanda za Juu Kusini unatekelezwa na wadau wetu wa maendeleo, sasa nasi tujiongeze kidogo tuanzishe huo mpango tuutekeleze locally.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 13 Novemba, 2020 Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. Magufuli kwenye hotuba yake ya kuzindua Bunge alisema dira yake ya utekelezaji wa majukumu yake ingeongozwa na Ilani ya Utekelezaji, Mpango lakini pia na ahadi. Tarehe 22 Aprili, 2021, Rais wa Awamu ya Sita hapa ndani akasema mambo hayo hayo akarudia na akasema ndiyo urithi ambao amechukua, lakini sasa nimekuwa nasema hapa ahadi ahadi toka mwaka 2020 mpaka leo hakuna ahadi hata moja kule Jimboni imetekelezwa. Niishauri Serikali itekeleze zile ahadi kwa sababu ndiyo urithi ambao Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua kwa Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanikiwa sana kwenye kilimo lakini kule kwetu Arumeru Mashariki tuna Mashamba ya Kili Flora ambayo yamechukuliwa na Serikali baada ya mwekezaji kuyatelekeza. Niishauri, lile shamba la Kili Flora ambalo liko chini ya Wizara ya Fedha lifanywe kama mradi wa BBT, kuna vijana wengi hawana kazi kule Jimboni waweze kuingia kwenye hilo shamba wajikimu na kujiendeleza kimaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia kengele ya kwanza sitaki unipigie tena ya pili, nakushukuru kwa nafasi hii naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, mimi nakushukuru kwa kunipa hii nafasi nichangie kwenye hii hotuba ya Wizara ya Ujenzi; Wizara ambayo ina kazi nzito ya kubadilisha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitangulie pia kumshukuru Mungu kwa kunisimamisha hapa leo lakini nimshukuru na kumpongeza sana Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo ameendelea kuongoza nchi hii kwa umahiri mkubwa ili atufikishe next level. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kipekee nimpongeze sana Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Naibu wake Mheshimiwa Engineer Kasekenya, Katibu Mkuu Balozi Engineer Aisha Amour pamoja na watumishi wote wanaofanya kazi Wizara hii pamoja na taasisi ambazo ziko chini ya Wizara. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana na nzito. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kupitia TANROADS pamoja na barabara zingine, inasimamia barabara zenye urefu wa kilometa 24,889 za mikoa. Katika hizo, kilometa 26 ni barabara ya Mbuguni kutokea Tengeru kwenda Mererani. Barabara hii nimekuwa naipigia kelele kwa muda mrefu sasa takriban miaka miwili na Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Kasekenya amekuwa ananiahidi itajengwa, itajengwa, nikimuuliza vipi? Ananiambia inafanyiwa usanifu, upembuzi yakinifu, kila leo, usanifu, upembuzi yakinifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nimepitia majedwali haya sijaona chochote kinachogusa Arumeru Mashariki. Nikitoka hapa nina pressure sijalala usingizi, nawaza nakuja kuondoa shilingi kwenye bajeti yako na wewe ni kijana wangu. Ni mtu mzuri, mwema, mpole, Innocent kama jina lako linavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuja kupata ahueni kidogo leo nilivyokuta kwamba bado inafanyiwa upembuzi yakinifu. Sasa niombe, kwa sababu kuna wenzetu walisema kwamba kipindi kile cha Serikali kutafakari mjadala wa bajeti zote za Wizara, tuangalie namna gani tunaweza tukawaongezea hela. Kwa hiyo, hili lichukue, barabara ya Mbuguni, kuanzia Tengeru hadi Mererani, ni barabara muhimu sana maana inakwenda kwenye machimbo ya Tanzanite. Ni fedha nyingi zinatoka pale kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii lakini zaidi inaunganisha mikoa miwili, Manyara na Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana isikosekane kwenye bajeti ya mwaka huu. Mheshimiwa Waziri ukumbuke kwamba siasa sasa hivi za majimboni ni barabara. Kila ukizunguka ni barabara, kila ukipita hapa barabara. Kwa hiyo, tafadhali nakuomba sana hiyo barabara isikosekane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi tena, kuna ahadi za viongozi wakuu kule jimboni kwangu ambazo hazijatekelezwa. Kuna barabara inatokea Usa River kwenda Oldonyosambu kwa kupitia Arusha National Park. Imejengwa mpaka pale kwenye lango la kuingia ANAPA, inapaswa iendelee Ngarenanyuki iende mpaka Oldonyosambu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna barabara ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. Magufuli, ya kutokea Malula mpaka Ngarenanyuki inaungana na hiyo barabara. Naomba uichukue hiyo barabara ya King’Ori kutoka Malula kwenda Ngarenanyuki mpaka Oldonyosambu ili nayo ijengwe kwa kiwango cha lami maana ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, ni ahadi ya viongozi wakuu wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna ahadi ya kilometa tano pale Usa River ilitolewa mwaka 2015, zijengwe kwa kiwango cha lami. Nimesubiri niambiwe sasa mnaanza, sijasikia. Nakuomba nalo ulichukue, kilometa tano Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli alisema pale Usa River kwamba atatoa kilometa tano za lami kwa ajili ya mji wa Usa River, naomba nazo uzichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kengele ya kwanza imelia eeh?

WABUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, bado.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, bado. Nadhani ni hayo niliyokuwa nataka niyaseme kwa ajili ya jimbo langu. Barabara ya Mbuguni, barabara ya King’Ori – Malula – Oldonyosambu na kilometa tano za mji wa Usa River. Pia, kuna kilometa tano za barabara ya Kikatiti kwenda Sakila alitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameingia sasa hivi, mwaka jana tukiwa kwenye …nayo ichukue pia. (Makofi)

SPIKA: Sasa mbona unamsemelea? Mheshimiwa Mbunge ngoja kwanza, ameingia sasa hivi akitokea wapi? (Makofi, Kicheko)

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, yuko hapa ndiyo kaingia.

SPIKA: Hapana yupo Bungeni, Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo Bungeni.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nashukuru sana. Basi na hilo ulichukue Mheshimiwa Waziri, tafadhali sana.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii ili nami nichangie kwenye hii Hotuba ya Wizara ya Ardhi. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri. Kwa kweli nikiri kwamba anaitendea haki nafasi yake na ninamfahamu sana Mheshimiwa Jerry Silaa, alikuwa Mwenyekiti wangu kwenye Kamati ya PIC. Kazi anayoifanya hapa hata Mheshimiwa Rais ameiona akamkubali na akasema anaitambua. Nisimsahau naibu wake kwa sababu hawa wanafanya kazi pamoja, wakiwa pamoja na watumishi wote katika Wizara hii, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ardhi ni mali, ardhi ni utajiri, ardhi ni commodity ambayo haipungui thamani, siku zote thamani yake inaongezeka. Kwa hiyo mwenye ardhi ana utajiri.

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa leo kuchangia kwa kifupi sana. Nikiri kwamba wenzangu wameshazungumza sana maneno mazuri na ya msingi. Niseme kwamba nataka kutoa ombi maalumu. Kwa kuzingatia na kwa kukiri kwamba ardhi ni mali; kule Meru kuna matatizo makubwa sana ni ya ardhi. Ukienda kwa DC pale utakuta mara kwa mara kuna watu wamekwenda kulalamika kwa sababu ya migogoro ya ardhi. Kwa hiyo nimesimama kuomba Serikali iangalie ni namna gani italinda huu utajiri kwa wale ambao tayari wana ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa KIA walioondolewa kwenye eneo la KIA wameondolewa wakalipwa fidia ambazo hazitoshi chochote, hazimsaidii kitu mwananchi aliyeondolewa. Kwa ajili hiyo niombe Wizara iangalie na ikiwezekana ilete sheria hapa Bungeni, kwamba kabla ya kumtoa mwananchi kwenye ardhi ambayo ameikalia ambayo ni mali yake ihakikishe kwamba kuna ardhi mbadala ambayo imetengwa.

Mheshimiwa Spika, kwa wananchi ambao sasa hivi wameondolewa pale eneo la KIA; kuna shamba la TPC limerudishwa Serikalini, tunaomba Wizara iangale ili wale wananchi ambao wameondolewa kwenye maeneo yao wapatiwe ardhi mbadala ili waweze kuendelea kuishi. Si eneo la KIA tu, hata eneo la Momera ambako wananchi wameondolewa kwenye maeneo yao ili kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Arusha. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili.

Mheshimiwa Spika, hawa wananchi wote waliopoteza ardhi tusiwafanye wakawa maskini, tusiwafanye maisha yao yakaenda yakawa miserable, tuangalie ni namna gani tutalinda utajiri wao ili waendelee kuishi; kwa sababu wengine wamekaa kwenye yale maeneo waliyoondolewa kwa miaka 40. Kwa mfano pale KIA kuna watu ambao wamekaa na wamejenga kwa kushiriki kuchanganya zege; lakini leo wanaondolewa na kuitwa ni wavamizi. Kwa kweli sidhani kama kuwaita wavamizi ni sahihi, ni kwamba tuna eneo limetengwa kwa ajili ya maendeleo ya kiwanja. Kwa hivyo tunaomba Mheshimiwa Waziri aliangalie sana hilo.

Mheshimiwa Spika, pia kuna shule tumejenga pale Shambarai Burka; ile shule tuliijenga lakini eneo lile halitoshi. Ombi langu, kuna wananchi ambao wamelizunguka lile eneo la shule, wao wako tayari kupisha ili waende mahali pengine lakini kwa kupatiwa ardhi mbadala.

Mheshimiwa Spika, kule kwenye lile shamba la TPC kuna maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya huduma za jamii. Tunaomba sana kwenye lile eneo tupate pale kama heka kumi lipatiwe sekondari ya Shambarai Burka ili libadilishwe sasa na wale wananchi ambao wamezunguka ile shule wao wahamie kule kwenye lile eneo ambalo litakuwa limetengwa kwenye lile shamba na yale maeneo yao yakabidhiwe shule ili shule iendelee kujengwa vizuri na kuwekwa infrastructure ambazo ni za muhimu. Hili ndilo ombi langu na nimesimama mahususi kwa ajili ya kutoa ombi hili.

Mheshimiwa Spika, baada ya ombi hili nina uhakika kabisa Mheshimiwa Waziri ameyachukua haya. Ninaomba kumalizia hapa na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)