Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. John Danielson Pallangyo (82 total)

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Barabara hii inapita kata nane huko kuna wananchi ambao wanafanya shughuli nyingi sana za kiuchumi lakini pia kuna taasisi hata shule iliyokuwa ya kwanza kitaifa iko eneo hilo.

Je, ni kwanini Serikali isione kwamba kuna umuhimu sasa wa kuipandisha hadhi ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami? Kwa sababu pia iko kilomita mbili kutoka mpaka wa Kilimanjaro na Arusha.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba hii barabara ina changamoto lakini Mheshimiwa Mbunge hapa anaomba kama barabara inaweza ikapandishwa hadhi, kupandishwa hadhi ni mchakato maana yake unaitoa barabara kutoka TARURA kwenda TANROAD ambayo ni Wizara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge jambo hili inabidi lianzie kwenye halmashauri yake liende kwenye ngazi ya mkoa kwenye kikao cha halmashauri cha barabara halafu walete kwenye ngazi nyingine ya kitaifa tutaona namna ya kufanya kama inakidhi vigezo basi itapewa hadhi hiyo ili iweze kupata fedha za kutosha na iweze kutengenezwa na wananchi wa eneo hilo waweze kupata huduma kama ambavyo ndiyo matarajio Serikali.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Hivi karibuni Mheshimiwa Rais alizindua mradi mkubwa sana wa maji kule Arumeru Magharibi, lakini wakati huohuo Arumeru Mashariki kuna shida kubwa ya maji kiasi kwamba wananchi wanaoga na kunywa maji ya shallow wells. Je, ni nini mkakati wa Serikali kutatua changamoto hii? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ni kwamba baada ya uzindizi wa mradi ule ambao ni mradi mkubwa sana wa maji katika Jiji la Arusha na viunga vyake likiwemo eneo la Arumeru Mashariki. Mikakati ya Serikali ni kutekeleza mradi huo ambao umeanza kutekelezwa mwaka huu wa fedha ambao utakamilika mwaka 2022 na vilevile kuweka mkazo kwenye uchimbaji wa visima virefu vya maji kwenye eneo la Uwanja wa Ndege na eneo la Magereza ambalo litatosheleza kabisa maji katika Jiji la Arusha na viunga vyake, likiwemo Jimbo la Arumeru Mashariki. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona na mimi.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizoko kule Kwela, zinafanana sana na kule Arumeru Mashariki hususan Kitongoji cha Momela ambacho kimepakana na Hifadhi ya Arusha National Park.

Je, Serikali inasemaje kuhusu ule mgogoro ambao umedumu kwa miaka kama mitano sasa hivi, wananchi walikuwa wanaishi kwenye yale mashamba, baada ya ukomo wa umiliki kumalizika, baadae wakaja kuondolewa kwa nguvu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema awali kwamba Serikali kwa kutambua umuhimu wa wananchi wake na jinsi ambavyo kumekuwa na migogoro ya ardhi hasa upande wa mipaka ya hifadhi, iliteua Kamati ya Mawaziri nane ambao walitembelea maeneo yote ya hifadhi nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hii tayari imeshamaliza mchakato wake na tumeshaanza kukaa kwa ajili ya kuangalia namna ya kutatua migogoro hii. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Pallangyo awe na subira maana Kamati hii tayari imeshaanza kazi na baada ya Bunge lako tukufu hili utekelezaji wake sasa utaanza. Kwa hiyo, sehemu zote ambazo zina migogoro ya mipaka inaenda kutatuliwa na pale ambapo kuna migogoro mipya itakayoibuka, basi Serikali itaona ni utaratibu gani mwingine ambao itafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu rai kwa maeneo mengi nchini ambayo yanakutana na hii changamoto ya mipaka na migogoro ya hifadhi, mara nyingi kumekuwa na tatizo kubwa sana la wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi. Maeneo haya kwa asilimia kubwa ni njia za wanyama (shoroba). Kwa hiyo, migogoro mingi tunaianzisha kwa maana ya wananchi kupewa maeneo, lakini kwa upande wa pili tena tunaanzisha mgogoro mwingine wa wanyama wakali kupambana na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tuwe na hiyo tahadhari pia kwamba tunapokuwa tunayaachia maeneo, lakini tunakuwa tumeanzisha mgogoro mwingine tena kati ya wanyama na binadamu. Maana wanyama siku zote wanapita maeneo yale yale ambayo walizaliwa nayo mwanzo na waliwaacha mabibi na mababu zao pale. Kwa hiyo, hili tatizo litaendelea kuwepo tu kama wananchi wenyewe hawatakubali uhifadhi ubaki kuwa hifadhi na maeneo mengine ya wananchi yaendelee kutumika kwa wananchi wa kawaida. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali bado kuna tatizo. Wengi wa wateja waliokuwa wa benki hii ambayo ilifutiwa leseni pamoja na wanahisa ni wanyonge, ni watu ambao wasingeweza kusubiri kwa muda mrefu wakisubiri amana zao zilipwe. Pamoja na kwamba kuna ambao walilipwa 1,500,000/= kwa kupitia DIB naona kwamba suala la muda ni changamoto. Wateja wengi hawataweza kusubiri kwa muda mrefu kiasi hiki, sasa hivi ni miaka mitatu na miezi mitatu tangu benki hii ifutiwe leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itamke bayana, je, ni lini itamaliza tatizo hili kwa kulipa amana zote kwa wana hisa na wateja ambao walikuwa wa benki hii?

Mheshimiwa Naibu Spika na ninaomba hapa ni- declare interest, kwamba mimi mwenye nilikuwa mwanahisa wa benki hii nasubiri hiyo pesa kwa miaka mitatu sasa, ningeipata ningenunua hata ng’ombe. Naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa John kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, Bodi ya Bima ya Amana bado inaendelea na zoezi la ufilisi wa mabenki na itakapokamilisha ufilisi wateja wote waliozidi zaidi ya shilingi 1,500,000/= watalipwa fedha zao kulingana na mapato yaliyokusanywa na kupatikana kutokana na benki husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge, changamoto ambazo wanazipata katika benki ya amana mpaka sasa hivi ni wale ambao waliokopeshwa fedha hizo bado wanaendelea kuwa na ugumu wa kulipa. Hata hivyo Serikali inaendelea kutafuta taratibu nyingine ili kuhimiza wale waliokopeshwa kulipa madeni hayo ili wateja wanaodai fedha zao katika benki hiyo waweze kulipwa kwa haraka. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona, tatizo lililoko kule Momba linafanana sana na kule Arumeru Mashariki maeneo ya Kia kwenye mashamba ya Malula. Wakulima wa eneo lile walipewa notice na Serikali kwamba wataondolewa lakini wangefidiwa. Hata hivyo, kabla ya zoezi hilo kufanyika kukazuka mgogoro na wawekezaji hawajaonekana pia Serikali inasema kwamba wakulima wale wako pale kimakosa na mashamba yale yalikuwa ni ya Serikali. Je, ni lini Serikali itatoa tamko kuhusu wakulima wale kwamba watafidiwa au la au wataendelea na kufanya kazi zao za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo kumekuwa na migogoro kati ya wawekezaji na wananchi maeneo mengi ambayo yana migogoro ni yale ambayo wawekezaji walipewa na wakayatelekeza mashamba yao matokeo yake wananchi wakawa wameingilia pale. Kisheria ni kwamba kama mtu amekaa pale kwa muda wa miaka 12 bila kusumbuliwa anakuwa na uhalali wa kuendelea kumiliki eneo lile kama katikati hapakuwa na mawasiliano ya kuweza kujua kwamba anadai eneo lake limevamiwa au namna gani. Sasa pale kama Serikali ilishaingia na kuwatambua kwamba wananchi wana haki basi hilo kwa sababu ndio nimelipata hapa, naomba nilichukue ili nifanye ufuatiliaji wa karibu kuweza kujua uhalisia wa kile anachokisema na hali halisi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia katika maswali haya hasa katika mashamba yaliyotelekezwa ni jukumu pia la mamlaka zenyewe za upangaji kufanya ufuatiliaji kuweza kufanya ukaguzi kuona mashamba yote yale ambayo yanamilikiwa na wawekezaji au hata kama ni mtu binafsi lakini amelitelekeza kwa maana ya kukiuka masharti yaliyoko kwenye hati yake, utaratibu wa kuanza kutaka kumnyanganya unaanzia kwenu kama halmashauri.

Kwa hiyo, wakishaleta sisi kazi ya Waziri ni kumshauri Mheshimiwa Rais kufuta pale ambapo anakuwa amekizi vigezo. Kwa hiyo, nitoe rai kwa halmashauri zote kule kuliko na mashamba pori ni jukumu la halmashauri sasa kuanza kufanya ufuatiliaji, ku-save notice, kutoa maonyo na mwisho wa siku wakipendekeza kufutwa Wizara itakuwa tayari kushirikiana nao kuhakikisha taratibu zinafuatwa, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Changamoto zilizoko Tunduru zinafanana sana na changamoto zilizoko kule Arumeru Mashariki, hususan Kata za Maruvango, Kikatiti, Malula na Majengo. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya afya kwenye hizo kata ambazo nimezitaja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilijibu katika swali la msingi kwamba kwa kadri Serikali tutakavyokuwa tunapata fedha ya kutosha na bajeti yetu tutakavyokuwa tunaitenga, tutaendelea kujenga. Kwa hiyo, hata maeneo ya Arumeru Mashariki nayafahamu na ninajua umbali wake. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri fedha itakavyopatikana basi tutazingatia na maeneo husika. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Halmashauri ya Meru nayo ilikuwa victim ya withdraw ya mradi mkakati ambayo ilikuwa imetengenezwa mwaka ule wa 2019. Naomba kuuliza: Je, Serikali sasa iko tayari kuja kutekeleza ule mradi?

Mheshimiwa Spika, Mradi huo uko eneo la Tengeru mahali panaitwa Sadak, ulikuwa umeshatengenezwa na Serikali ilikuwa imeshachakata lile andiko na nilipofika kule Hazina nikakuta karibia pesa zinatoka, kuja hapa Bungeni nikaambiwa mradi umekuwa withdrawn: Je, ni hatua gani zinazoendelea kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Meru nayo inawezeshwa, kwa sababu sasa hivi inashindwa kuhudumia wananchi kwani haina mapato ya kutosha?Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ni kweli mwaka 2019/2020 Serikali ilijaribu kusitisha kwa muda miradi yote ile ambayo ilikuwa inasuasua. Sasa hivi nikuhakikishie kwamba, Serikali imejipanga na tumekubaliana tui-review; na miradi yote ile ambayo ilisitishwa, ile miradi ya kimkakati katika Halmashauri zote ambazo zilikuwa zimepangiwa awali, inakwenda kufanya kazi. Ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Changamoto zilizopo kule Busega zinafanana sana na changamoto ambazo tunazo Arumeru Mashariki. Wananchi Kata za Kikatiti, King’ori, Majengo, Gabobo na Kikwe, wanahangaika kila leo kujenga zahanati wenyewe lakini hatujaona Serikali ikija kutusaidia. Je, Serikali ina mpango gani wa kuja kutupa msaada na sisi tuweze kupata huduma za afya kikamilifu?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wananchi wa Arumeru Mashariki wameendelea kuchangia nguvu zao kujenga maboma ya zahanati na vituo vya afya. Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wale wanaungwa mkono kwa juhudi zao ambazo wanazionesha katika kuwekeza katika miundombinu hii ya huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo pamoja na maboma hayo mengine ambayo Mheshimiwa Dkt. Pallangyo ameyasema, nimhakikishie kwamba, kwanza katika mwaka huu wa fedha ambao tunaendelea, 2020/2021, shilingi milioni 150 kwa ajili ya maboma matatu, kuhakikisha kwamba yanakamilishwa, zimetengwa na zitafikishwa kabala ya tarehe 30, Juni, mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha, 2021/21, Serikali pia imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya maboma matatu katika Jimbo hili la Arumeru Mashariki. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Pallangyo kwamba tutahakikisha tunaendelea kutenga fedha za kuchangia nguvu za wananchi kukamilisha maboma ya zahanati na vituo vya afya ili tuendelee kusogeza huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, amekuwa mfuatiliaji wa karibu sana kwa ajili ya wananchi wa Arumeru Mashariki, amehakikisha anasimamia miradi mbalimbali ikiwemo miradi hii ya huduma za afya. Na sisi tumhakikishie kwamba tutaendelea kushirikiana kwa karibu sana na wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, lakini pia na Mheshimiwa Dkt. Pallangyo kuhakikisha kwamba tunahudumia wananchi wetu kwa karibu zaidi.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nami kuniona. Changamoto zilizopo katika Jimbo la Singida Magharibi hasa kwenye miundombinu ya maji zinafanana sana na zile zilizoko Arumeru Mashariki, hususani Kata ya Keri ambayo ina taasisi nyingi za Serikali:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuja kukarabati ile miundombinu na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama kwenye kata hiyo pamoja na Embaseni, Maji ya Chai, Kikatiti, Maroroni na Majengo? Nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwani amekuwa mfuatiliaji mkubwa hususan wananchi wake wa Arumeru. Tunachotaka ni kujenga commitment katika Wizara yetu ya Maji kupitia bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni makubwa ya Waheshimiwa Wabunge tumeyazingatia, nataka nikuhakikishie maeneo ambayo ameyaeleza tutayafanyia kazi kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini bado niseme kwamba Arumeru Mashariki kuna shida nyingi sana hususan katika sekta ya afya. Wananchi wanahangaika sana kujijengea zahanati wenyewe, mimi mwenyewe tangu nianze harakati za kurudisha jimbo kwenye jengo, nimezunguka kwenye jimbo kushoto, kulia, kusini, magharibi, kaskazini kuhakikisha kwamba, wananchi wanajua kwamba tunahangaika nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana nami kwamba Wabunge hatupitwi na changizo lolote jimboni, kwa hiyo, kila zanahati inayojengwa kila kituo cha afya kinachojengwa Mbunge anahusika.

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali, je, ni lini Serikali itaingilia kati ujenzi wa Zahanati iliyoko Katiti, Zahanati ya Kolila, Zahanati ya Zengon, Zahanati ya Majengo na sehemu nyingine nyingi jimboni. (Makofi)

Pili, je, Waziri yuko tayari kuambatana na mimi baada ya Kikao hiki cha Bajeti tukakague aone ninalolizungumza hapa kama ni la kweli au la? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge amejaribu kulieleza ili Serikali iweze kutoa ufafanuzi, ni kwa namna gani Serikali inatoa mchango katika maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakianzisha ujenzi, hususan wa maboma ya afya; na ameainisha baadhi ya maeneo ikiwemo Kikatiti, Kolila na maeneo mengineyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana Serikali katika mwaka huu wa fedha tumeamua kutenga shilingi milioni 150 mpaka 200 kwenye kila jimbo ili kwenda kusaidia kumalizia zahanati ambazo zimeanzishwa na wananchi. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kulingana na fedha tunazopata na tutaendelea kuzingatia mchango mkubwa ambao unatolewa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali dogo la pili la nyongeza lilikuwa, kama niko tayari kuongozana naye Mheshimiwa Mbunge; nimhakikishie, nipo tayari na nitaifanya hiyo kazi kwa uaminifu mkubwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Changamoto zilizoko Maswa Mashariki kuhusu barabara zinafanana sana na changamoto ambazo ziko Arumeru Mashariki. Kuna barabara inayoanzia Tengeru kwenda Mererani, inaunganisha Mkoa wa Arusha na Manyara, lakini pia ni kiungo muhimu kwa shughuli za uchimbaji Mererani na soko ambalo liko Mjini Arusha. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii ni muhimu sana na Mheshimiwa Pallangyo amekuwa akiifuatilia sana, lakini bado tunasema nia ya Serikali ni kujenga hizi barabara ambazo zimeainishwa na zinarahisisha maisha ya wananchi kama zitajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Pallangyo, Serikali inaendelea kutafuta fedha na fedha ikipatikana basi hii Barabara ya Tengeru kwenda Mererani, sehemu ambayo kuna machimbo ya tanzanite itajengwa ili kuweza kuboresha maisha na kupandisha uchumi, lakini pia kurahisisha biashara ya tanzanite kule Arusha. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Naibu Waziri ya kuvipatia huduma ya maji Vijiji vya Nkonekoli, Nkure, Njani, ambayo aliitoa wakati alipozuru jimboni kwetu mwezi Disemba kuelekea sikukuu za Christimas? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ahadi ni deni, kwa sababu tumeahidi lazima tuje tutekeleze. Mara baada ya utaratibu mzima wa upatikanaji wa fedha kwenye eneo lako, lazima wataalamu waje na ni lazima maji yapatikane kwenye Jimbo lako la Arumeru, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nitaomba kuuliza swali moja la nyongeza, ila naomba pia kwamba Serikali isiwe inatoa majibu tu kwa ajili ya kutuliza Wabunge, lakini kwa kweli ije na kutekeleza yale ambayo wanayasema kwenye majibu yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu; jiografia ya Jimbo langu la Arumeru Mashariki ni ngumu, kwa maana ya kwamba Mlima Meru ambao ni mlima mrefu wa pili hapa nchini uko katikati ya jimbo na kuwafanya wananchi walioko Mashariki na Kaskazini mwa mlima huo, kupata shida kufuata huduma ambazo zinapatikana Kusini mwa mlima pamoja na kufika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Je, sasa hivi Serikali haioni kwamba ni muhimu sasa kujenga Mahakama ya Mwanzo Kata ya Ngarananyuki ili wananchi walioko Kaskazini mwa mlima huo waweze kupata huduma za Mahakama? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, tuko kwenye mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2025/2026 nchi nzima itakuwa imefikiwa na Mahakama za Mwanzo kwenye ngazi za Makao Makuu ya Tarafa zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Ngarananyuki kupata Mahakama, tunalichukua ingawa katika kipindi hiki cha fedha ambacho tunakijadili sasa kilishapita, tutalipa umuhimu kwenye kipindi kijacho cha fedha. Ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tena kwa kunipa nafasi. Kwanza niseme naishukuru sana Serikali na kuipongeza kwa kazi nzuri ambayo inafanya kwa kuhakikisha kwamba inawasha umeme kwa vijiji vyote na vitongoji nchi nzima. Hata hivyo, hivi karibuni tulipata orodha ya wakandarasi ambao wamekuja kwa ajili ya kufanya kazi ya kumalizia zoezi la kuwasha umeme REA III.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Arusha Mkoani amekuja kandarasi mmoja tu na kule Longido, nakuwa na mashaka kwamba ahadi ya Serikali kwamba mwaka kesho watakuwa wametimiza ahadi yao ya vijiji vyote nchi nzima kuwa vimeshapata umeme; nakuwa na mashaka kwamba tutaweza kufanikisha hilo zoezi. Swali langu, je, wana mpango gani wa kuhakikisha kwamba wanaongeza idadi ya wakandarasi ili hiyo kazi na ahadi ya Serikali iwe ya kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru kwa kutambua juhudi za Serikali za kuendelea kuwahudumia watanzania kwa kuwapelekea umeme katika maeneo yao na ni commitment ya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwamba kufikia Disemba, 2022, tutakuwa tumekamilisha upelekaji wa umeme katika maeneo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wiki kama mbili zilizopita Mradi wa REA III, round II, ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Waziri katika eneo la Longido na mkandarasi anayefanya kazi katika Mkoa wetu wa Arusha anaitwa SAGEMCOM na yuko kazini tayari na alikuwa amepewa maeneo matatu ya Longido, Karatu na Monduli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na upana wa Mkoa wa Arusha, Wizara imeona ni vema kuongeza mkandarasi mwingine, aende akafanye kazi katika Jimbo la Arumeru Mashariki, Mgharibi lakini pia na Ngorongoro. Kabla ya mwezi Julai haujaisha mkandarasi atakuwa ameripoti kazini kwa ajili ya kuendelea kufanya kazi ili ile ahadi iliyotolewa na Serikali ya kufikisha umeme kwa wananchi wote ifikapo Disemba mwakani iwe imekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwa sababu baada ya hapa tunatawanyika kwenda kwenye maeneo yetu basi wakawe mkono wa kwanza kabisa wa kushirikiana na
wakandarasi kutimiza azma ya kupeleka umeme kwa wananchi kwa kuwasimamia kwa karibu na kuwa pamoja na sisi ili kuweza kufikisha hiyo ahadi. Nashukuru.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili niliuliza kwa sababu kuna kata nyingi sana kule ambazo hazijapata umeme hususani Kata ya Uwilo kuna vijiji kama viwili vile Lukulu Skimosoni na kule Maruhango pia kuna vijiji maruhango kwenye hakuna umeme je, niulize ni lini hasa vijiji hivyo vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Pallangyo na nimshukuru kwa ufuatiliaji na uvumilivu kwa sababu jimbo lake ni moja ya majimbo ambayo mkandarasi alichelewa kupatikana kwa sababu ya taratibu ya kimanunuzi. Lakini kama nilivyosema kwenye swali na jibu la msingi ni kwamba kufikia Disemba mwaka huu kwa mujibu wa mkataba kata zote ambazo hazina umeme ambazo ni vijiji kwakwe ni vijiji 12 ndiyo havina umeme vitakuwa vimepatiwa umeme kwa kadri ya mkataba tuliokuwanao.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Je ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi katika ujenzi wa zahanati za Nsengoni, Gaisosya, Kikatiti na Samaria? Wananchi wamehangaika kuzijenga zahanati hizi kwa miaka mingi lakini hawaoni support ya Serikali.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kweli swali la msingi, mwaka wa fedha uliopita zaidi ya shilingi 27,750,000,000 zilipelekwa ili kukamilisha maboba 555, lakini katika mwaka wa fedha huu wa 2021/2022 zaidi ya shilingi bilioni 28.2 pia zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha maboma 564 ya zahanati.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ambaye aliitoa mwaka 2012 ya kuijenga barabara ya Sangisi - Akeri hadi Ndorombo kwa kiwango cha lami. Ahadi hiyo aliitoa wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wetu Marehemu Jeremiah Sumari? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja na kwa kuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Awamu ya Nne, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tutalichukua kwa uzito mkubwa na ikiwezekana baada ya kipindi hiki cha Bunge tukutane tuone kwa nini imechukua muda mrefu ili tuweze kuona namna ya kutimiza ahadi ya Kiongozi wa Taifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Buguni kuanzia Tengeru sokoni kupitia Kikwe hadi Mererani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ni barabara ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa eneo hilo na Serikali ina mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami. Ikishakamilisha usanifu wa kina barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi unaohusu wananchi wa Kata ya Malula na Majengo walioko katika eneo linalozunguka uwanja wa KIA?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Pallangyo, Mbunge wa Arumeru, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tutakapokuwa tumemaliza Bunge hili, nitaomba kuongozana pia na Mheshimiwa Pallangyo ili twende tukazungumze na wananchi wale tuweze kujua undani wa tatizo lenyewe na baada ya hapo tuweze kutafuta suluhu ya pamoja katika kuleta maendeleo katika maeneo yetu ya Arumeru. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa ujenzi wa vizimba vya kufugia samaki katika Ziwa Duluti kwa lengo la kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kule Arumeru Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo, Mbunge wa Arumeru, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ilitenga kiasi cha Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya kuanza mradi maalum wa vizimba vya Samaki. Vilevile tunao mradi kwa ajili ya maeneo ya ufugaji samaki nje ya vizimba kwa maana ya mabwawa. Naomba niseme tu kuwa Ziwa Duluti tutalifanyia tathmini ikiwa kama ni katika maeneo yenye kuweza kufanyiwa shughuli hizi za vizimba katika mwaka mwingine wa fedha tutaliwekea mpango na lenyewe, kwa sababu siyo kila mahali tunaweza kujenga vizimba kulingana na taarifa za kitaalam. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi; elimu ya ufundi ni nyenzo muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yoyote.

Je, Serikali haioni sasa kwamba ni muhimu kubadilisha utaratibu, badala ya kujenga hivi vyuo kiwilaya ijenge kijimbo kwa sababu, kuna Wilaya nyingine ambazo zina majimbo mawili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kada hii ya ufundi ni muhimu, naomba tuchukue ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, hivi sasa tumeanza katika ngazi ya kanda, mikoa pamoja na ngazi ya Wilaya. Tuangalie baadaye namna gani tunaweza tukafika katika ngazi ya jimbo kama Mheshimiwa Mbunge anavyoshauri.

Kwa hiyo, tunaubeba ushauri wako tunakwenda kuufanyia kazi na tufanye tathmini ya kina. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi katika Kata ya King’ori?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pallangyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tupo tayari kushirikiana na Mbunge na wadau wengine wa Kata ya King’ori kuona kiwango cha ujenzi kinachotakiwa kumaliziwa ili tuweze kutengea fedha kituo hicho kiweze kukamilishwa. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLAGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.

Je, ni lini Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Tengeru kwenda Holili ambayo ni sehemu ya mradi wa barabara ya Afrika Mashariki unaoanzia Sakina. Barabara hii ujenzi wake ulisimama takribani sasa hivi miaka Minne.

Je, ni lini ujenzi utaendelea kwa sababu barabara ile sasa hivi ina magari mengi sana na ajali ni nyingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii inayotoka Arusha kwenda Holili ipo kwenye mpango, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tunategemea mwaka wa fedha unaoanza kujenga kati ya Tengeru na Usa River, barabara nne, lakini daraja la Kitafu litajengwa na barabara za Moshi Mjini zitajengwa katika huu mpango. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, barabara ya USA River kwenda Oldonyo Sambu kwa kupitia Hifadhi ya Arusha imejengwa kwa kiwango cha lami hadi Getini Ngongongare.

Je, ni lini Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kutoka ngare na nyuki Kwenda Oldonyo Sambu na kuunganisha Barabara ya Kwenda Namanga na Moshi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ipo kwenye ilani na Mpango wa Serikali ni kuijenga kwa kiwango cha lami barabara aliyoitaja. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa jimbo lake kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuijenga barabara hiyo.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri.

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuzijenga na kukarabati Mahakama za mwanzo za Nkwaranga na West Meru, kama ilivyoahidi mwaka wa fedha uliopita 2021?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Pallangyo tuwasiliane ili niweze kumpa mkakati halisi, lakini mpango kazi wote umeshakamilika katika kukarabati na kujenga majengo mapya ya maeneo ambayo hayana mahakama. Kinachokosekana hapa ni kumbukumbu sahihi tu, kwa sababu swali linakuwa limekuja kwa sasa hivi. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Barabara ya Guguni inaanzia Tengeru Sokoni hadi Mererani, inaunganisha mikoa miwili ya Arusha na Manyara.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pallangyo Mbunge wa Meru, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri barabara hii naifahamu, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ipo kwenye mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami na tukizingatia inakwenda kwenye migodi yetu kule Tanzanite. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini mazingira pale kwenye lile soko na fedha zinazobadilishwa wakati wa biashara pale ambazo ni nyingi sana zinahitaji kuweka miundombinu ikae vizuri kidogo.

Je, Serikali iko tayari kwenda kujenga shade kama machinga complex ya Dodoma pale kwa ajili ya kunusuru akina mama ambao wanachomwa na jua wakati wa jua kali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Halmashauri ilitumia takribani Milioni 11 kwa ajili ya kuweka stendi ndogo pale ambayo inaweza ikaingiza mabasi 12. Je, Serikali haioni kwamba ni muhimu sasa kuingilia kati na kujenga ile barabara ya kutokea kwa sababu kibali cha kutumia ile stendi bado hakijatoka kutokana na barabra kutokukidhi viwango. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufatilia suala la soko lile la Tengeru, lakini utaratibu wa Serikkali ni kwamba tumetafuta eneo jingine kubwa zaidi haina maana kwamba tunaliacha kabisa lile eneo ambalo tayari kwa sasa linatumika kama gulio. Kwa hiyo, ninatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hii ili watenge fedha kwenye mapato ya ndani kuboresha soko hilo, kwa maana kuweka miundombinu rafiki kwa wafanyabiashara, pia kupitia TARURA Halmashauri hii watenge fedha kwa ajili ya kuboresha barabara hiyo ambayo itawezesha kujenga uwezo wa wananchi kufanya biashara kwa ufanisi mkubwa zaidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itamaliza mgogogro wa mpaka kati ya TANAPA na wananchi wa Momela ambao unatokana na TANAPA kutwaa mashamba Namba 40 na Namba 41 bila kushirikisha Serikali ya Kijiji.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pallangyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuahidi Mbunge tutaenda kuzungumza na wananchi nikishirikiana na wataalamu tupate maelezo ya kutosha.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, changamoto zilizoko kule Same zinafanana sana na changamoto za Meru ambako barabara nyingi zinakwenda mlimani na barabara ni za vumbi.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuongeza bajeti ya matengenezo ya barabara ili tuweze kuwa na barabara ambazo ni za hard surface?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaona haja hiyo ya kuongeza fedha kwa ajili ya bajeti za matengenezo na ujenzi mpya na ndio maana kila mwaka imekuwa ikiongeza bajeti. Kwa hiyo, sisi tulishukuru Bunge kwa kutuongezea na tutafanya hivyo kuhakikisha barabara za jimboni kwako na Tanzania nzima kwa ujumla zinapitika wakati wote, ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kunipa nafasi niulize swali la nyongeza nalo liko hivi.

Mheshimiwa Spika, baada ya wafadhili waliokuwa wanaendesha kituo cha afya Momela kujiondoa watumishi pia ambao walikuwa wanalipwa na wale wafadhili Afrika waliondoka. Sasa hivi huduma zimedorora; Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi na wataalam kwa ajili ya kufanya huduma zikae vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dokta Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba kuna upungufu wa watumishi katika kituo hicho cha afya na nimhakikishie kwamba tutaendelea kupeleka watumishi pale ili waendelee kutoa huduma za afya na tutaangalia katika ajira hizi na zinazofuata ili tuhakikishe kwamba kituo kile kinatoa huduma bora kwa wananchi.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi na kwanza nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri ambaye wakati alipokuwa jimboni kwangu mara ya mwisho alitoa maelekezo ya namna ya kutatua changamoto ya mafuriko yanayosababishwa na kufukiwa korongo la Mto Nduruma na kutesa wananchi wa Kata za Shambarai Burka, Mbuguni, Majengo na Makiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya ziara ya wale wataalam ambao walitumwa...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Pallangyo swali.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: ...kimya kimetanda. Swali sasa, je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha kwa ajili ya kwenda kutatua ile changamoto ya mafuriko?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimefanya ziara katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge la Arumeru Mashariki na moja ya ahadi ni kuwapatia fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshatoa fedha mwezi huu, shilingi milioni 100, kwa ajili ya uanzaji wa kazi ile. Mheshimiwa Mbunge unaweza ukafuatilia katika hilo. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Barabara inayoanzia USA River kupitia Arusha National Park kwenda mpaka Oldonyo Sambu imejengwa kwa kiwango cha lami hadi kwenye lango la kuingia hifadhini.

Je, Serikali inampango gani wa kumalizia kipande kilichobaki kuanzia Ngarenanyuki kwenda Oldonyo Sambu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kukamilisha hicho kipande ambacho kimebaki lakini ukamilishaji wake pia utategemea na upatikanaji wa fedha na kwa kuwa tuko kwenye kipindi cha bajeti naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira tuone kama tutakuwa tumependekeza nini katika bajeti ambayo tunaiendea kuileta mbele ya Bunge lako.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Vijiji vingi katika Kata za Narurango, King’ori, Majengo bado havijapata Umeme wa REA na Mkandarasi anavyofanya kazi yake wala haeleweki, analeta nguzo, anaondoka…

SPIKA: Swali!

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Umeme wa REA utafika kwenye hizo kata ili vijiji vyote vipate umeme kulingana na ahadi ya Serikali kwamba mwisho wa mwaka huu vingepata umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumetoa ahadi ya Serikali, tutahakikisha kwamba wakandarasi wote wanaotekeleza mradi wa REA III Round II kufikia Desemba mwaka huu kazi hizo zitakuwa zimekamilika katika maeneo ambayo yanapelekewa umeme kwenye kata, vijiji na vitongoji ili wananchi waweze kunufaika na hiyo huduma ya umeme ambayo iko katika huo mradi mkubwa wa mwisho wa kupeleka umeme katika vitongoji na vijiji.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuzijenga Mahakama za Mwanzo za West Meru Mkwaranga na Ngerenanyuki ambazo ziliachwa tu zikaharibika kabisa sasa hivi yamebaki magofu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, naomba nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Pallangyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mpango wetu wa ujenzi na ikarabati wa mahakama katika mwaka huu wa fedha tunategemea kukarabati na kujenga Mahakama 60 za mwanzo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika Mkoa wake pia Arumeru tumeweka Mahakama za kukarabati tutampatia list ataona Mahakama zake kama zinahitaji kukarabatiwa.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara ya Mbuguni inayounganisha Mikoa ya Arusha na Manyara kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ilishaahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, na tayari tumeshakamilisha usanifu. Sasa hivi Serikali inaendelea kuweka mipango ili tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira tuangalie kwenye bajeti tunayokwenda kuileta mbele yenu, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; hospitali hii ni ya siku nyingi sana na majengo yake yamechakaa sana kiasi kwamba mengine yatalazimika kuvunjwa na kujengwa upya, lakini pia kuna changamoto ya eneo. Kwa Hiyo tunaona kwamba ni busara kuanza sasa kuwaza kwenda kujenga majengo ya ghorofa.

Je, Serikali pamoja na kwamba imetupatia shilingi milioni 900 ambazo tunashukuru sana, je, Serikali haioni kuwa ni muhimu kujipanga kwa ajili ya kujenga maghorofa kwa maana ya kwamba fedha ziongezwe? Hilo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; hospitali hii haina
mortuary siku zote tangu imejengwa. Tumejitahidi tumejenga mortuary pale na mpaka sasa haijapata majokofu. Je, ni lini Serikali itatupatia majokofu ili ile mortuary ianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hospitali hii ni kongwe, ni ya siku nyingi na mwezi mmoja uliopita nilifanya ziara pale nikishirikiana na Mheshimiwa Mbunge, lakini tulikubaliana kwamba kwa sababu imekwishaingizwa kwenye Mpango wa Hospitali Kongwe 31 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi ndio maana mwaka wa fedha 2023/2024 imetengewa Milioni 900. Sasa dhamira ya kujenga hospitali mpya ndani ya halmashauri wanaweza wakakaa na kuleta mapendekezo Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili na sisi tuweze kuyatathimini na kuona kama yanaweza kutekelezeka ama vinginevyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, niwapongeze kwa kujenga jengo la kuhifadhia miili ya marehemu (mortuary) lakini jokofu liko ndani ya uwezo wa halmashauri kupitia Bohari ya Dawa (MSD). Kwa hiyo, nielekeze Mkurugenzi wa Halmashauri hii kuhakikisha kwamba wanaomba jokofu Kupitia akaunti ya MSD ili waweze kutoa huduma kwa wananchi. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa fursa hii. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga Kituo cha Polisi katika Kata ya King’ori kama ilivyoahidi mwaka jana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyowahi kujibu kwa nyakati tofauti, ujenzi wa Vituo vya Polisi ngazi ya Kata ni jukumu la jamii kwa maana ya halmashauri na wananchi wake, lakini pale ambapo tunakuta juhudi hizo zimefanyika Wizara huunga mkono kupitia Jeshi lake la Polisi. Nimwombe Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, najua juhudi zake kwenye hili, waanze na sisi tutakuja kuwaunga mkono, ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Akheri inayoanzia Sangisi kwenda Ndoombo ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne kujengwa kwa kiwango cha lami miaka kumi iliyopita. Mwaka jana barabara hiyo imeanza kujengwa: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimalizia mwaka huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Akheri – Sangisi ambayo ameitaja Mheshimiwa Dkt. Pallangyo hapa ambayo tayari imeshaanza kuwekewa lami itaendelea kuwekewa lami kwa sababu ni ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kadri ya upatikanaji wa fedha na tutaendelea kuitengea bajeti kwenye miaka ya fedha ambayo inafuata.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii; je, ni lini Serikali itajenga bwawa na mifeji kwa ajili ya umwagiliaji katika Kata za Shambalaiguruka na Majengo kwa lengo la kupunguza athari za mvua na mafuriko ya Mto Nduruma na Mto Chiplepa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti yetu inayokuja tumetangaza kwamba tunaenda kujenga mabwawa 100 ambayo yatagusa takriban maeneo yote nchi nzima. Hivyo katika wilaya ya kwake Mheshimiwa Mbunge tunakwenda kuangalia maeneo ambayo amaeyataja. Kama si hayo basi tutaichukua kama sehemu pia ya kuifanyia kazi ili katika wakati mwingine ujaotuweze kuyajenga pia.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Mradi mkubwa wa maji uliogharimu takribani shilingiza bilioni 520 za Kitanzania kule Arusha sasa hivi karibu unamalizika. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga miundombinu ya kusambaza maji katika vijiji ambavyo bomba kuu limepita?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi huu tuko mwishoni kabisa na tayari vijiji vingi vimenufaika, tayari maji haya kutoka kwenye mradi yameingizwa kwenye laini ambazo zina-exist. Vilevile maeneo yote ya vijiji hivyo alivyovitaja na vingine vyote ambavyo vimepitiwa na bomba kuu vinakwenda kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika,ahsante kwa kunipa nafasi sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza, nishukuru sana kwamba Serikali ina mpango wa kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko la kisasa eneo la Madiira, lakini ningependa kujua kwamba huo mradi utaanza lini?

Pili, soko hili la Tengeru tunalolizungumzia hapa ni soko maarufu sana la wafanyabiashara hasa akina mama wanafanya biashara zao kwa mateso makubwa wakati wa mvua, kwa sababu wanafanya kwenye matope na mvua nyingi lakini pia wakati wa jua wanaungua jua.

Je, Serikali haioni sasa ni busara kuliboresha soko hili kwa kujenga hanga kama Machinga Complex ya Dodoma? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali yake mawili Mheshimiwa Pallangyo kwanza kuhusu mradi huu utaanza lini?

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, mradi huu utaanza pale ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Meru itawasilisha michoro yake Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili na sisi tuweze kuipitia na kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukafanya marekebisho na baadae tukaipeleka Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupata fedha kwenye miradi ya kimkakati kama Halmashauri nyingine zinavyopata.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la kuboresha eneo la soko hili. Hizi zinatakiwa pia ziwe jitihada za Mkurugenzi wa Halmashauri pale ya Meru. Tumeona hapa katika mradi anaoutaja wa Jiji la Dodoma ilikuwa ni mradi wao wenyewe wa Jiji na wametumia mapato yao ya ndani kama Jiji la Dodoma, tumeona katika Halmashauri nyingine nchini kama Shinyanga ambapo wamejenga soko la machinga wadogo wadogo hawa kwa hela zao wenyewe za ndani na maeneo mengine ya Halmashauri zetu hapa Tanzania. Hivyo basi, nichukue nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru kuhakikisha anatenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa soko kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kuelekea mwishoni mwa mwaka jana Serikali ilichukua hatua za kuweka mipaka ya kudumu eneo linalozunguka Uwanja wa Kimataifa wa KIA kwa lengo la kuweka miradi ya kimkakati. Je, ni miradi mingapi ya kimkakati na ni ya namna gani ambayo itajengwa kwenye eneo lile kwa sababu imechukua eneo kubwa sana takribani square kilometer 110? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni kweli lengo la Serikali ya Awamu ya Sita, kama nilivyosema chini ya Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuona tunaongeza uwekezaji, kuvutia mitaji katika uwekezaji, uwekezaji wa ndani, lakini pia uwekezaji kutoka nje. Jambo hili linataka maeneo mahususi ambayo yameshaandaliwa tayari ili kupunguza ukiritimba na urasimu wa kutokupata maeneo ya uwekezaji kwa wawekezaji katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo hili la KIA linafanyiwa tathmini ili kuona miradi mahususi ya kimkakati ambayo itawekezwa katika eneo hili ambalo mwanzoni lilikuwa kidogo na changamoto ya kuingiliwa na watu. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuona miradi mahususi ambayo itawekezwa katika eneo hili la KIA, nakushukuru sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itaanza upya mchakato wa ujenzi wa stendi ya kisasa eneo la Madira, mchakato huo ambao ulisitishwa mwaka 2019 ghafla wakati umefikia hatua ya utekelezaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nilichukue hili suala la stendi hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja kule Arumeru tuone kwa nini ilisitishwa ghafla mwaka 2019, na hatua zipi zimechukuliwa kuondoa changamoto hiyo ili lengo la Serikali kuwahudumia wananchi kwa kujenga stendi hiyo liweze kukamilika kwa wakati.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Changamoto za mawasiliano zilizopo Arumeru Magharibi zinafanana sana na hali ilivyo kule kwetu Mashariki.

Je, ni lini Serikali itaondoa kabisa changamoto za mawasiliano katika Kata za pembezoni Ngarenanyuki, Leguruki, Maruvango, King’ori na Malula? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inawapenda Watanzania na kwa sababu inataka Watanzania wote washiriki katika uchumi wao wa kidigitali na ni lazima wawasiliane kwa kutumia mifumo ya TEHAMA na sisi kama Serikali ambao ni wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, najitolea kuhakikisha kwamba nitaenda katika Jimbo la Arumeru Mashariki ili tukajionee changamoto ilivyo na tuchukue hatua na hakuna cha kwamba ni kata moja tu, tutahakikisha maeneo yote ambayo yana changamoto kulingana na upatikanaji wa fedha tutafikisha mawasiliano, ahsante sana. (Makofi)
MHE.JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri kutoka Serikalini lakini napenda kuuliza swali moja la ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya uvuvi inaonekana kama sasa hivi ina mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi. Je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kujengwa mabwawa maeneo ya Malula na maene ya Majengo ambako kila mwaka mvua zinaleta mafuriko, yale maji yavunwe yajengwe mabwawa kwa ajili ya kufugia Samaki?
NAIBU WAZIRI WA UVUVI NA UFUGAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Kwanza nibampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua mchango wa Uvuvi katika uchumi wetu na hata maoni ambayo Mheshimiwa Mbunge ameeleza hapa kwamba tuanze sasa kujenga mabwawa kwa ajili ya kuboresha sekta ya uvuvi ni sehemu ya mpango tulionao sasa hivi. Kwa hiyo, tunachokifanya sasa hivi ni kutafuta fedha ili kuhakikisha kwamba tunafika kwenye maeneo yote hususan maeneo ambayo hayana maji mengi kwa maana ya Maziwa na Bahari, ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Mbuguni kwa kiwango cha lami ambayo inaanzia Tengeru hadi Mererani?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge, ni ya kimkakati ambayo inakwenda machimbo ya Tanzanite. Mheshimiwa Mbunge atakuwa shahidi kwamba mpaka sasa hivi tunaendelea kukamilisha usanifu wa kina na baada ya hapo Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga sasa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Sehemu kubwa ya Jimbo la Arumeru Mashariki liko kwenye miteremko ya Mlima Meru, kwa hiyo barabara zake kwa mwaka mzima zinakuwa ni mavumbi au mifereji wakati wa mvua. Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha kwa ajili ya kuzijenga kwa kiwango cha lami au tabaka gumu la namna nyingine kwa teknolojia nyingine yoyote? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo la barabara zake hizi za Arumeru Mashariki kwamba, Serikali imeweka commitment kubwa kwa kuiongezea fedha TARURA kuhakikisha barabara nyingi zaidi zinatengenezwa kwa kuwapa bajeti mara tatu ya ile ambayo Dkt. Samia Suluhu Hassan aliikuta mwaka 2021. Sasa tutakaa na Mheshimiwa Dkt. Pallangyo tutazidi kuangalia ni namna gani TARURA inaweza ika-fast track utengenezaji wa barabara hizi ambazio wananchi wa Arumeru Mashariki wanazihitaji.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara za lami huwa unaboresha sana mazingira na mandhari ya nchi yetu kule inakopita. Barabara hii pale inapoanzia kuna soko la Tengeru ambalo hali yake ni mbaya kimazingira na miundombinu, lakini tunajua kwamba, miradi mikubwa hii ina-component ya CSR.

Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia Halmashauri ya Meru kuboresha soko hili kwa kutumia CSR yake?

Swali la pili, kwa kuwa, mradi huu uko kwenye hatua ya usanifu na upembuzi yakinifu, Serikali haioni ni busara kuweka uboreshaji wa soko hili katika usanifu huo? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili kwa pamoja ya Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwenye miradi hii mikubwa kunakuwa na component ya CSR. Ninachoweza kumuomba Mheshimiwa Mbunge, tumelipokea ombi lake la kuboresha hiyo miundombinu ya soko la Tengeru pamoja na barabara inayoingia, lakini tu pengine nishauri ni vyema tukapata maombi rasmi ili tuweze kuyaratibu kabla Mhandisi Mshauri hajakamilisha, basi iwe ni sehemu ya mpango wa kuijenga hiyo barabara ikiwa ni pamoja na kujenga hiyo barabara ndogo ya kuingia kwenye soko na kuboresha hilo soko, ahsante. (Makofi)

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara hii inaunganisha Mikoa miwili, Arusha na Manyara pia ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa. Sasa barabara hii kwa unyeti wake iko busy na imekuwa ni changamoto kubwa sana ya afya kwa wanachi walioko katika barabara hii kwa sababu ya vumbi. Naomba commitment ya Serikali kwamba; Je, ni lini ujenzi utaanza kwa sababu kuna fedha nyingi, kuna mpango wa RISE, kuna Agri - connect. Je, Serikali haiwezi ikafanya utaratibu barabara hiyo ianze kujengwa mara moja baada ya usanifu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna ahadi nyingi sana za Serikali, Viongozi Wakuu za ujenzi wa barabara kwa viwango vya lami, na mojawapo ni barabara ya King’ori kutoka Malula hadi Ngarenanyuki. Naomba niulize barabara ya King’ori kutoka Malula hadi Ngarenanyuki lini itajengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu ni ahadi ya Viongozi Wakuu wa Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, commitment ya Serikali imeshaonekana na ndiyo maana tayari tumeshaanza taratibu za kujenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami tukitambua kwamba inaenda kwenye sehemu muhimu sana ya kiuchumi eneo la mgodi wa Mererani lakini pia inaunganisha kama alivyosema Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara. Isingekuwa rahisi kufanya chochote kabla ya kukamilisha usanifu. Kwa hiyo, kama fedha inaweza ikatokea yoyote katika kipindi hicho tutafanya, vinginevyo ni kwamba baada ya kukamilisha usanifu basi tutaipangia bajeti kwa mwaka ujao wa bajeti kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu hii barabara aliyoitaja. Ni kweli barabara ya King’ori – Ngarenanyuki ilikuwa inatengenezwa na wenzetu wa TARURA tumekasimiwa, kwa hiyo tunaendelea kutafuta fedha ili tuweze kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami kwa sababu inapita kwenye maeneo makubwa sana ya uzalishaji wa wenzetu ambao ndiyo wanalisha Mji wa Arusha. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami kipande cha barabara kinachoanzia Ngarenanyuki hadi Oldonyo Sambu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja inachangiwa kipande na barabara yetu ya TANROADS, pia kuna kipande ambacho wenzetu wa TARURA wanakifanya. Kwa upande wetu wa TANROADS tayari tumeshafanya usanifu na tunachofanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba hii barabara inapitika kwa muda wote wakati tukiendelea kutafuta fedha ili kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Changamoto za barabara Arumeru Mashariki zinasababishwa na hali ya kijiografia ambayo sio rafiki wananchi wengi wako milimani. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo ya barabara hizi kwa kiwango cha lami au kwa teknolojia nyingine yoyote ambayo itafanya barabara hizi zihimili mafuriko wakati wa mvua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Pallangyo kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa Jimbo la Arumeru Mashariki. Pia nimhakikishie kwamba tunafahamu na tumefanya tathmini ya barabara ambazo ziko milimani katika Jimbo la Arumeru Mashariki na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tumeweka mpango kazi wa kutenga fedha kulingana na uhitaji. Kuna maeneo yenye milima yenye mvua nyingi na changamoto kadhaa. Kwa hiyo bajeti zetu sasa pamoja na vigezo vingine itazingatia sana hali ya hewa, lakini pia na uhitaji mkubwa wa barabara hizo. Kwa hiyo nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili tunalifanyia kazi.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitenga fedha nyingi kwaajili ya miradi ya maji kule Arumeru Mashariki mwaka huu wa fedha lakini kuna mradi ambao hatujajua hatma yake.

Je, ni lini mradi wa maji Kata ya Ibaseni, Maji ya Chai na Kikatiti utaanza kutekelezwa kwa maana ya kwamba upo kwenye miradi inayopaswa kutelezwa mwaka huu? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge yeye mwenyewe kazi kubwa tuliyoifanya jimboni kwake, nimekwenda na tumetembelea miradi yote ambayo ilikuwa ni historia maji kufika tayari unafahamu maji yanatoka. Hivyo, katika mradi huu ulioutaja endapo mwaka huu wa fedha utaisha utekelezaji utakuwa haujakamilika mwaka ujao wa fedha ni lazima maeneo haya yote tuje tuendelee kufanyia kazi na kuhakikisha maji yanapatikana. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha kata zilizoko Mashariki na Kaskazini mwa Mlima Meru kwa kujenga barabara itakayounganisha barabara kuu ya Moshi na barabara kuu inayokwenda Namanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara hizi ambazo zinaunganisha Kata za Mashariki ya Meru na Moshi na maeneo mengine yote ni miongoni mwa barabara ambazo Serikali imeweka mpango, kwanza wa kuziainisha, kuzifanyia upembuzi yakinifu, lakini kutenga bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ukamilishaji wa barabara hizo. Lakini jambo la msingi hapa Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na Meneja wa TARURA katika Halmashauri hii ya Arusha wafanye tathmini ya barabara muhimu zaidi ambazo zinatakiwa kupewa kipaumbele ili Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hizo, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru pia Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha Shilingi Bilioni Moja mwaka jana ambazo ndizo zimetumika kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Spika, swali, barabara hii ni moja ya ahadi ya Mheshimiwa Rais ili ijengwe kwa kiwango cha lami. Je, Serikali inasemaje kuhusu hilo, ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hatua ya awali ni hii ambayo tunarekebisha hii barabara ili walau iweze kupitika kipindi chote wakati ambapo tunatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza hiyo ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itatekeleza ahadi yake kwa vitendo. Ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha kata zilizoko Mashariki na Kaskazini mwa Mlima Meru kwa kujenga barabara itakayounganisha barabara kuu ya Moshi na barabara kuu inayokwenda Namanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara hizi ambazo zinaunganisha Kata za Mashariki ya Meru na Moshi na maeneo mengine yote ni miongoni mwa barabara ambazo Serikali imeweka mpango, kwanza wa kuziainisha, kuzifanyia upembuzi yakinifu, lakini kutenga bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ukamilishaji wa barabara hizo. Lakini jambo la msingi hapa Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na Meneja wa TARURA katika Halmashauri hii ya Arusha wafanye tathmini ya barabara muhimu zaidi ambazo zinatakiwa kupewa kipaumbele ili Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hizo, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza nalo liko hivi; je ni lini Serikali itatua mgogoro kati ya Arusha National Park na wananchi wa Kijiji cha Lukungw’ado ambao unatokana na Serikali haikununua bila kushirikisha Serikali ya Kijiji mashamba Namba 40 na Namba 41 ambayo wananchi walikuwa wanategemea kujikimu nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza na Mheshimiwa Pallangyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti suala la kutatua migogoro ni wajibu wa Wizara ya yale maeneo ambayo hatujayafikia ni mhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakuja kuyatatua, na ukizingatia maeneo mengi yalikuwa kwenye vijiji 920, lakini kwa yale maeneo ambayo hayakuingizwa kwenye vile vijiji 920, na migogoro yao ni mipya tumeshaelekeza wananchi kupitia wawakilishi wao watuletee malalamiko haya ili tupite katika maeneo hayo tuweze kutatua migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro mingine ni ya kufika sisi kama viongozi, kukaa na wananchi tukaisikiliza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaambatana katika Jimbo lake ili tuweze kutatua mgogoro huu.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona; je, nini kinakwamisha ujenzi wa stendi mpya eneo la Madira kule Jimbo Arumeru Mashariki ambao mradi huu ulisitishwa katika hatua za mwisho katika utekeleza mwaka 2019?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ndiyo nimepata taarifa hii kwamba huo mradi umekwama naomba nilichukue hili baada ya session hii ya maswali na majibu nikae na Mheshimiwa Dkt. Pallangyo tujuwe hiyo stendi kwa nini imekwama na sisi tutatumia wataalamu wa Wizara kufanya tathimini lakini kukwamua mkwamo ambao hupo katika stendi hiyo. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru pia Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha Shilingi Bilioni Moja mwaka jana ambazo ndizo zimetumika kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Spika, swali, barabara hii ni moja ya ahadi ya Mheshimiwa Rais ili ijengwe kwa kiwango cha lami. Je, Serikali inasemaje kuhusu hilo, ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatua ya awali ni hii ambayo tunarekebisha hii barabara ili walau iweze kupitika kipindi chote wakati ambapo tunatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza hiyo ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itatekeleza ahadi yake kwa vitendo. Ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa tena nafasi niulize swali la nyongeza, kwanza nitoe shukurani nyingi kwa majibu mazuri ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Jerry Silaa ambaye alikuwa Mwenyekiti wangu Kamati ya PIC, nimpongeze kwa kuwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu majibu yake yapo sawasawa lakini watendaji wakati wa kutekeleza huwa hawaweki bayana sheria inasemaje badala yake wanakuja wanakuambia jamani hili eneo linachukuliwa kwa ajili yakazi hii na hii ya Serikali ninyi mnatakiwa muondoke, mtapata fidia kwa maendelezo ambayo mlikuwa mmefanya.

Je, Serikali haioni sasa kwamba ni muhimu wakati wa kuhamisha wananchi kwenye maeneo yao watoe maelekezo kwamba watapata nini na nini kulingana na eneo ambalo linachukuliwa either kwa uhifadhi au utekelezaji wa miradi?

Pili, swali langu ni je, Waziri utakuwa tayari kuambatana na mimi tuende tukafanye mkutano uwaeleze wananchi maeneo ya Momela pamoja na KIA ambao wanatakiwa wahame?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa majibu kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa John Danielson Pallangyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, naomba kutumia Bunge lako tukufu kuagiza Wathamini wote na Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali kuhakikisha inatoa elimu stahiki kwa wananchi pindi ambapo maeneo yao yanatwaliwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Wananchi waelezwe wazi takwa la sheria kwa wale wanaotaka kuchukua fedha taslimu kwa niaba ya ardhi yao na kwa wale ambao wanataka kutafutiwa ardhi mbadala.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, pamoja na kwamba niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo lakini eneo la KIA na eneo la Momela ni maeneo ambayo yanaangukia kwenye vile vijiji 975 ambapo wananchi walikuwa wameingia kwenye maeneo ya hifadhi na wengine wameingia kwenye eneo la Uwanja wa Ndege wa KIA. Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iliona ni busara kuwafidia kwa yale maendelezo waliyoyafanya, maeneo haya fidia yao wanayolipwa haihusishi ardhi ambayo wamekuwa wakiikalia. Baada ya Bunge hili Mheshimiwa Dkt. Palangyo tutaongozana pamoja kwenda kutoa elimu kwa wananchi wa Jimbo lako, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa hii fursa. Tatizo la mpaka lipo kule kwetu kati ya Wilaya ya Arumeru Mashariki, Hai na Siha, eneo lile linasemekana ziko GN kama tatu. Je, Serikali inasemaje kuhusu mpaka halisi wa Arumeru Mashariki, Siha na Hai?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Utaratibu wa mipaka unaainishwa kwa mujibu wa GN zinazotambullika rasmi na Serikali. Kiutaratibu GN ya mwisho ndiyo GN ambayo inatambulika, GN ambayo imepitishwa kwa mara ya mwisho ndiyo GN ambayo ina-sound kwa kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue jambo hili la Mheshimiwa Pallangyo ili tuweze kuongea na Mkuu wa Mkoa wa Arusha lakini na Kilimanjaro ili waweze kuona namna nzuri ya kwenda na wataalamu kusoma GN uwandani, kutafsiri mipaka ya Wilaya ya Hai, Siha Pamoja na Arumeru Mashariki ili wananchi watambue mipaka hiyo lakini pia waweze kufanya shughuli zao kwa amani zaidi, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Mradi wa Maji wa Patandi unaotekelezwa katika Kata ya Keri umeacha vitongoji vinne katika Kata ya Gwarusambo ambako ndiko vyanzo vya maji vinapatikana.

Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuambatana nami kwenda site kutatua hizo changamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nimeshafika Jimboni kwa Mheshimiwa Dkt. Pallangyo na tumefanya kazi nzuri, maeneo ambayo hayakupata maji kwa miaka mingi sasa hivi yanapata. Hivi vitongoji vinne vilivyobaki navyo vinaenda kwenye mwaka ujao wa fedha na vitapata maji. Suala la mimi kufika Jimboni kwa Mbunge, asijali kama ambavyo nilikwenda nikimaliza maeneo ambayo sijafika, nitarudi tena.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Changamoto zilizoko Iramba Mashariki zinafanana sana na Changamoto zilizoko Arumeru Mashariki katika Sekta ya Afya. Je, ni lini Serikali itakuja kuboresha Kituo cha Afya Makida ambacho majengo yake yamekuwa magofu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue hoja ya Kituo cha Afya cha Makida ambacho ni chakavu na kinahitaji ukarabati ili tuweze kutuma wataalam wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI lakini pia Mkoa wa Arusha kufanya tathmini na kutuletea makadirio ya gharama zinazohitajika ili tutafute fedha kwa kupitia mapato ya ndani lakini mahususi kupitia Serikali Kuu ili tuweze kukarabati kituo hiki cha afya kiweze kutoa huduma vizuri, ahsante.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa hii nafasi. Halmashauri ya Meru iliwasilisha michoro ya soko la kisasa TAMISEMI mwaka jana mwezi Novemba, kwa maana ya mwaka 2023; soko hili linategemewa kujengwa Eneo la Madira; je, ni lini ujenzi wa soko hili utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pallangyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tulikuwa na utaratibu wa kuwasilisha miradi ya kimkakati lakini tunafanya tathmini na upembuzi kuona kama fedha kwanza ya Serikali ipo, na pia kama halmashauri zenyewe zinaweza zikagharamia kupitia mapato ya ndani. Kwa hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anatoa taarifa kwamba limeshawasilishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba tulichukue suala, tutalifanyia kazi tufuatilie, andiko liko wapi, limefikia hatua gani, ili tuweze kuona namna gani tunafanya ili kwenda kujenga soka la kisasa katika eneo hili la Madira, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa na ridhaa yako kwa dhati kabisa naomba nitoe shukrani zangu kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutuletea miradi ya maji ya mabilioni ya fedha Jimboni Arumeru Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo mradi wa maji wa Kata za Imbaseni, Maji ya Chai, Kikatiti hadi Samaria unatekelezwa kwa kusuasua sana. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu huyo miradi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote uliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, mimi na wewe tumekwenda ziara na shughuli zinafanyika tumeshuhudia sisi wote. Miradi kukamilika tutaendelea kupeleka fedha ili kuona kwamba Wakandarasi wanafanya kazi na miradi hii inakamilika wananchi wananufaika na majisafi na salama.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Natambua kwamba Barabara ya Mbuguni imekuwa inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu; na kwamba kazi hiyo ilimalizika mwishoni mwa mwaka jana 2023. Je, ni lini sasa ujenzi wa kuijenga kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada kukamilisha usanifu wa kina tunategemea kwamba barabara hiyo sasa itaingizwa kwenye mpango wa bajeti huu ambao tunaendelea ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu ndio kwanza tunaanza kuandaa bajeti zetu.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Usa River kwenda mpaka Oldonyosambu ujenzi wake ulisimama kwa muda mrefu baada ya kufika lango la ANAPA. Je, ni lini Serikali itaendelea na ujenzi huo kutoka Ngarenanyuki hadi Oldonyosambu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusaidiana na wenzetu wa TAMISEMI, barabara hii ni kweli ilisimama, lakini tunaendelea kutafuta fedha ili mvua itakapokatika, basi tuendeleze kuijenga hiyo barabara. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa hii nafasi, je, ni lini ujenzi wa Chuo cha VETA kinachojengwa Kata ya Uwiro, Arumeru Mashariki utamalizika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nikiri kwamba kuna ujenzi ambao unaendelea katika Jimbo la Mheshimiwa Pallangyo, kule Arumeru na mimi mwenyewe nimeshafanya ziara zaidi ya mara mbili kwenye eneo lile kuangalia maendeleo ya chuo kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, malengo yetu ni kuhakikisha kwamba mpaka kufika mwezi Oktoba, mwaka huu vyuo hivi katika awamu ya kwanza viwe vimekamilika ili mwezi wa Novemba tuweze kuanza kutoa zile kozi za muda mfupi na Januari mwakani tuweze kuanza kutoa zile kozi za muda mrefu.

Kwa hiyo, hayo ndio malengo yetu tutahakikisha kwamba, ifikapo mwezi Oktoba, vyuo hivi vimekamilika, nakushukuru.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi. Je, Serikali imefikia hatua gani katika mchakato wa kujenga Soko la Kisasa katika eneo la Madira ambalo michoro yake tumeshawasilisha Wizarani? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze Halmashauri ya Meru kwa kupitia Mheshimiwa Mbunge Pallangyo kwa kuandaa michoro na kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama maelekezo ya Serikali yalivyopelekwa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa tutafanya tathmini kuona gharama hizo zinazohitajika na kuona vyanzo vya fedha kupitia Serikali Kuu, lakini pia kupitia mapato ya ndani ili tuanze kujenga soko hilo kwa awamu. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa hii fursa. Shule ya Sekondari Indoombo ina walimu watano tu. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha ili kukidhi uwiano unaokubalika kitaifa na kimataifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu mwaka huu tuna ajira mpya za walimu, kwa hiyo, katika mgao ule tutaangalia kipekee pia kwenye jimbo lake naye aweze kupata mgao wa walimu hao.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa mwenyekiti, changamoto za barabara za Mlimani kule Same Magharibi zinafanana sana na hali ilivyo kule kwetu Meru na nimeishalisema hapa mara nyingi. Kwa hiyo, sasa niulize Serikali inatoa tamko gani kuhusu barabara za milimani kule Arumeru Mashariki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akipambania sana suala la Ujenzi wa barabara kwa viwango vitakavyodumu hasa katika Jimbo lake ambalo lina milima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari tumeshazungumza na suala tayari lipo kwenye michakato na fedha tayari zimeshatengwa, nikuhakikishie Serikali itakuja kujenga barabara, itatenga fedha kila mwaka kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara hizi na hasa katika jimbo lako ambalo ni la milima. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali na nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kwa juhudi kubwa ambayo tunaiona jimboni ya kutaka kumaliza kabisa tatizo la maji. Tunavyozungumza sasa hivi mtambo wa kuchimba maji visima virefu kwa ajili ya kufuata maji ya ardhini huko jimboni na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna shida kubwa sana ya maji katika Tarafa ya King’ori ambayo imebeba Kata za Kikatiti, Majengo, Malula, King’ori, Maruvango, Leguruki, Ngarenanyuki, Uwiro na Ngabobo. Pia eneo hilo maji yana- fluoride...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, swali.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza changamoto hizi za maji eneo hilo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi kuona Mheshimiwa Mbunge anatambua kazi kubwa ambayo inafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kweli mtambo upo na kama ambavyo nilijibu katika majibu mengine, mitambo hii sasa wataalamu tayari wameshapatikana wanaingia site kuhakikisha kwamba visima vinaanza kuchimbwa. Pamoja na hilo, Skimu ya Makilenga inahudumia takribani 50% ya Tarafa ya King’ori. Kwa hiyo, tumwombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba changamoto hii inaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa pia Serikali inashirikiana na mdau wa maendeleo kutoka Korea kuhakikisha kwamba kuna madini ya fluoride katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameongelea na madini hayo sasa tunaenda kufanya mchakato wa kuyaondoa na kuchuja na kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo lile wanapata maji ambayo hayatokuja kuwa na madhara katika afya zao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Serikali tayari imeshaanza kufanya kazi hiyo, nakushukuru sana.
MHE. DKT. JOHN J. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya barabara za vumbi iliyoko kule Jimboni Kawe inafanana sana na hali ilivyo jimboni kwangu ambapo barabara nyingi zinapanda mlimani, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuongeza bajeti ili kuondoa hiyo changamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akisemea sana mazingira ya jimbo lake na hasa kwa sababu ya mazingira ya kuwa katika milima. Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari tumekuwa tukiwasiliana mimi na wewe. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha tunatengeneza msukumo ili kuweza kupatikana bajeti ya kutosha ambayo itakuja uhudumia barabara katika jimbo lako. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa vipande vya barabara kutoka Sangisi – Akeli hadi Ndoobo na Sangisi – Chuo cha Jeshi Duluti hadi Nelson Mandela? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikikarabati na kujenga barabara zetu hizi za TARURA kwa awamu. Mheshimiwa Mbunge katika jimbo lake barabara hizi za Wilaya ambazo zinasimamiwa na TARURA zimekuwa zikiendelea kutengewa fedha kila mwaka wa bajeti. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itahakikisha barabara hizi alizozitaja katika jimbo lake zinaweza kukarabatiwa na kujengwa.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; eneo hili la Kikatiti liko Tarafa ya King’ori ambayo ina Kata 10 zenye watu 124,000, pia eneo hilo ndilo kapu la chakula kwa Jiji la Arusha na viunga vyake. Kikatiti yenyewe ina watu .....

SPIKA: Swali Mheshimiwa Pallangyo.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, swali langu ni je, kwa takwimu ambazo zipo katika Sensa ya Mwaka 2022, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka benki hizi zifungue matawi pale?

Mheshimiwa Spika, kama ni ngumu sana, ni kwa nini benki hizi zisifungue mashine za kutolea fedha (ATM’s) Eneo la Maji ya Chai, Kikatiti yenyewe na King’ori Madukani? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Pallangyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, takwimu aliyotaja ni kweli inaleta ushawishi kufungua tawi la benki huko, lakini jukumu la Serikali kama nilivyojibu ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji. Kwa hiyo, naomba tu Benki za NMB, CRDB na nyingine waende kuangalia hiyo fursa ili ikiwezekana wafungue tawi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni ushauri, naomba tuchukue na tunaenda kuufanyia kazi.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tuliwasilisha michoro kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa soko la kisasa eneo la Madiira kule Arumeru Mashariki mwaka jana mwezi Novemba, je, ni lini ujenzi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Halmashauri ya Arumeru na Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Mheshimiwa Dkt. Pallangyo waliwasilisha andiko la kimkakati la soko la kisasa. Nimhakikishie tu kwamba tayari ilishapitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI na ilishafanyiwa tathmini na tuko hatua za ngazi ya Wizara ya Fedha kuona uwezekano wa kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji. Kwa hiyo naomba uwe na imani kwamba Serikali inalifanyia kazi suala hilo na wananchi watambue kwamba tumelichukua na tunalishughulikia. Ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mradi wa Maji unaogusa Kata za Imbaseni, Maji ya Chai, Kikatiti hadi Samaria umesimama na mkandarasi amekimbia site kwa ukosefu wa fedha. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kule kwa ajili ya kukamilisha mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Pallangyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa na tayari Serikali kupitia Wizara ya Maji tumeanza ku-engage na mkandarasi. Pia, tumeshakaa na wenzetu Wizara ya Fedha sasa tuweze kuanza kutoa fedha. Tayari kwa kipindi hiki tumepokea bilioni 16 kutoka National Water Fund na jana tumepokea bilioni tisa. Pia, tumeanza kupokea kutoka Serikali Kuu, tumepokea exchequer ya bilioni 105. Kwa hiyo, tunaamini kabisa miradi ambayo ilikuwa imekwamba pamoja na wakandarasi ambao walikuwa bado wanadai sasa wakati umefika wa kuanza kuwalipa ili warudi site na kuendeleza miradi ambayo ipo katika hatua mbalimbali.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; eneo hili la Kikatiti liko Tarafa ya King’ori ambayo ina Kata 10 zenye watu 124,000, pia eneo hilo ndilo kapu la chakula kwa Jiji la Arusha na viunga vyake. Kikatiti yenyewe ina watu .....

SPIKA: Swali Mheshimiwa Pallangyo.

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, swali langu ni je, kwa takwimu ambazo zipo katika Sensa ya Mwaka 2022, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka benki hizi zifungue matawi pale?

Mheshimiwa Spika, kama ni ngumu sana, ni kwa nini benki hizi zisifungue mashine za kutolea fedha (ATM’s) Eneo la Maji ya Chai, Kikatiti yenyewe na King’ori Madukani? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Pallangyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, takwimu aliyotaja ni kweli inaleta ushawishi kufungua tawi la benki huko, lakini jukumu la Serikali kama nilivyojibu ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji. Kwa hiyo, naomba tu Benki za NMB, CRDB na nyingine waende kuangalia hiyo fursa ili ikiwezekana wafungue tawi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni ushauri, naomba tuchukue na tunaenda kuufanyia kazi.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii. Kwanza naipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambayo imeifanya kule Arumeru Mashariki, kwa ajili ya kusambaza umeme wa REA. Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, ukanda wa mashariki, hususan Tarafa ya King’ori, bado vitongoji vingi viko gizani. Je, ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa umeme wa REA kwenye ukanda huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kuhusu hii ya kupeleka umeme huku King’ori; namhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutapeleka umeme katika vitongoji hivi, kwanza kupitia mradi wa vitongoji 15 na pia, tutaendelea kupeleka kupitia miradi ya REA ambayo tunayo kwa Mwaka huu 2025 na kuendelea. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hii nafasi. Ninatumia pia nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuweza kujenga kwa kiwango cha zege kipande cha barabara eneo Ndoombo ikiwa ni sehemu ya barabara ndani ya barabara inayoanzia Sangisi - Akheri hadi Ndoombo.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka wa kuendelea na zoezi hilo la kujenga kwa zege barabara zote ambazo zinapanda milimani kule Meru, tukianza na eneo la Ulong’a - Kata Nkoanrua, eneo la Sela - Kata ya Seela Sing’isi, Sura - Kata ya Poli na Songoro - Kata ya Songoro? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, hakika mimi na yeye tumekuwa tukizungumza mara kwa mara kuhusiana na ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya barabara katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na barabara hizi za milimani ambazo kwa kweli amekuwa akizizungumzia mara nyingi sana hapa Bungeni, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumekwishaanza. Hii ni hatua ya kwanza na kila mwaka tutakuwa tunatenga fedha ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kuziboresha barabara hizi ili ziwe katika hadhi ya zege ambayo ina uimara zaidi na inayostahimili mazingira ya milimani.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Akheri kuanzia Sing’isi hadi Ndoombo ambayo ujenzi wake unakwenda kwa kusuasua sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameshawahi kunieleza kuhusiana na umuhimu wa barabara hii na nirejee makubaliano tuliyozungumza kati ya mimi na yeye kumhakikishia kwamba, barabara hii itajengwa ili iweze kuwanufaisha wananchi wake.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali fupi la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo Makambako, inafanana sana na changamoto ambayo tunayo kule Arumeru Mashariki, hususani mpaka wa Jimbo letu la majimbo mawili ya upande wa Mashariki kwa maana ya Siha na Hai. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu changamoto hiyo ya mpaka? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee kwamba ni Serikali inashauri mamlaka husika kwa maana ya DCC na RCC kukaa na kutoa mapendekezo, lakini mipaka ya Majimbo inatolewa pia na ya Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, naomba wafuate taratibu hizo kuleta maoni yao ambayo yamefuta sheria na kanuni za mwongozo ulivyo ili tuweze kuona namna gani mamlaka husika zitachukua hatua kurekebisha changamoto hizo ikiwa inawezekana kufanya hivyo, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa mwenyekiti, changamoto za barabara za Mlimani kule Same Magharibi zinafanana sana na hali ilivyo kule kwetu Meru na nimeishalisema hapa mara nyingi. Kwa hiyo, sasa niulize Serikali inatoa tamko gani kuhusu barabara za milimani kule Arumeru Mashariki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akipambania sana suala la Ujenzi wa barabara kwa viwango vitakavyodumu hasa katika Jimbo lake ambalo lina milima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari tumeshazungumza na suala tayari lipo kwenye michakato na fedha tayari zimeshatengwa, nikuhakikishie Serikali itakuja kujenga barabara, itatenga fedha kila mwaka kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara hizi na hasa katika jimbo lako ambalo ni la milima. (Makofi)