Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sylivia Francis Sigula (12 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami ikiwa ni mara yangu ya kwanza kuongea katika Bunge hili tukufu, nianze kwa kumshukuru Mungu Mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa kibali kuiona siku ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee sana, nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kinachoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kutuamini vijana na kutupa uwakilishi katika Bunge hili tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nimepata bahati ya kuipitia hii Hotuba ya Mheshimiwa Rais zaidi ya mara tatu. Naomba nikiri katika Bunge hili Tukufu, kama kuna hotuba nilizowahi kuzisoma ambazo ni bora, hii ni hotuba nambari moja. Hotuba hii imebeba dira, maono, matarajio na matamanio makubwa sana ya vijana na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukianzia ukurasa namba moja mpaka ukurasa wa 41, utaona kabisa Mheshimiwa Rais amegusia sekta zote na zote hizo anamlenga kijana. Unapozungumzia viwanda, unazungumzia wanufaika ambao ni vijana; unapozungumzia nishati, wanufaika wa kwanza ni vijana; unapozungumzia mikopo, wanufaika wa kwanza ni vijana. Kwa hiyo, wakati Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake anazungumzia utengenezaji wa ajira zaidi ya milioni nane, naona ni jambo ambalo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijielekeze katika ukurasa wa 37 ambapo Mheshimiwa Rais ameelezea kukuza sekta ya sanaa, michezo na utamaduni. Ni wazi kabisa tunafahamu michezo ni ajira na ni kipato; katika kuelezea sekta hii Mheshimiwa Rais amesema kabisa kwamba ataanzisha mfuko ambao utawawezesha wasanii kimafunzo na mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hapa; kwanza naipongeza Serikali kwa kuanzisha Taasisi ya Sanaa ambapo zamani kilikuwa ni Chuo cha Sanaa Bagamoyo. Taasisi hii inatoa kozi, lakini kozi zinazotolewa pale ni chache. Tukisema tuwezekeze katika sekta ya sanaa tutatengeneza ajira nyingi sana kwa vijana. Tunajua sanaa ipo kwa upana wake mkubwa lakini tunaona sanaa hizi zinawatoa vijana wengi na kuwatengenezea kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mdogo tu. Juzi tulitembelewa na vijana hapa, tunaweza tukawatengeneza vijana wa aina ile zaidi. Tunaweza tukawatengeneza akina Manula na Boko wengi kutoka kwa vijana wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa huu wa 37 naomba kunukuu. Rais anasema: “Tutahuisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili kuwasaidia wasanii wetu ikiwemo kupata mafunzo na mikopo.” Napenda nijikite hapa, kipengele hiki ni kikubwa sana na kama tutakifanyia kazi vizuri, basi tutatengeneza ajira nyingi kwa vijana. Kwa sababu sekta ya sanaa tukisema tuwekeze kwa nguvu kubwa, itaweza kuwainua vijana wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mdogo tu wa mkoani kwetu Kigoma. Tunaelewa kabisa Mkoa wa Kigoma ndiyo kitovu cha sanaa za hapa Tanzania. Ndiyo maana ukifanya tathmini ya wasanii wengi wa Tanzania utaona wengi wanatokea Mkoa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, naiomba sana Wizara husika ione ni namna gani ya kuboresha na kuwekeza katika sekta hii ya sanaa. Sawa tumeanzisha Taasisi hiyo ya Sanaa lakini bado tuna vijana wengi wa Kitanzania wenye vipaji ambao wakipewa fursa wanaweza wakafanya vizuri. Changamoto katika sekta hii ya sanaa, vijana wengi hawana mitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tuna chuo hicho kimoja lakini naiomba Serikali kama itawezekana tuweze kuongeza vyuo hivi hata kwa level ya kanda. Itakuwa rahisi kuwahudumia vijana wengi kwani watapata mafunzo pale, lakini hii mikopo ambayo ameisema Mheshimiwa Rais ikawasaidie hawa vijana wajiendeleze. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda umeisha.

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana lakini mada yangu nitaiwasilisha vizuri kwa sababu iko katika mapana yake. Nakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii. Nianze moja kwa moja kwa kuchangia mapendekezo ya Mpango uliopo mbele yetu. Nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha. Kwa kweli ukiusoma mpango utaona kabisa dhamira ya dhati ya kutupeleka katika uchumi imara tunaoutarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kwa ajili ya muda nijielekeze katika Sekta ya Uvuvi. Tunapoteza sana mapato katika Sekta ya Uvuvi. Nasema hivi kwa sababu Tanzania tumebarikiwa. Tuna maziwa ambayo tungeweza kuyatumia yakatusaidia kutengeneza ajira nyingi lakini pia kukuza uchumi. Kwa sababu tukiangalia vipaumbele vyetu tunasema kipaumbele ni kukuza uchumi na pato la Taifa, lakini kwenye Sekta hii ya Uvuvi tunapoteza mapato mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hapa naona kwamba tutapanua Bandari za Kigoma na Tanga lakini pia kuboresha miundombinu. Nitoe mfano mdogo tu; tumekuwa na tatizo, japo limeahidiwa kwenye ilani, Meli yetu ya Liemba, kuanzia mwaka 2017 haifanyi kazi. Kwa kweli tumepata hasara na uchumi umezorota. Kwa hiyo maboresho haya yatakwenda sambamba na kuipatia Serikali mapato lakini pia tutatengeneza ajira nyingi kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Meli yetu hii ya Liemba na Ziwa Tanganyika, linawanufaisha watu wa Kigoma, Katavi pamoja na Rukwa. Kwa hiyo kuwepo kwa fursa hii ya meli kutaweza kuchochea maendeleo kwa haraka, lakini pia kukuza kipato na uchumi. Pia tukiangalia Ziwa letu Tanganyika hili tunashirikiana na wenzetu wa Burundi na Kongo. Kwa hiyo kuwepo kwa meli hii kutachochea sana kipato na uchumi, lakini pia Serikali itaweza kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia pia naona kabisa kutokuwepo kwa meli hii kumezorotesha uchumi. Vijana wengi wamekosa ajira lakini pia hata usafirishaji wa mazao ambayo yanapatikana Kigoma, Katavi na Rukwa umekuwa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali katika mpango wetu huu ni Mpango mzuri sana na ukiupitia Mpango mzima unaona kabisa tutatoka hapa kwenda level nyingine. Niombe marekebisho haya ya bandari hizi, upanuzi huu ufanyike kwa haraka ili Serikali isiendelee kupoteza mapato yanayotokana na Sekta hii ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais nilijielekeza katika Sekta ya Sanaa na kwa sababu muda ulikuwa mchache nilishindwa kusema; siyo vibaya sana kujifunza kwa wenzetu wanaofanikiwa. Nimepata kusoma Makala moja, tunaambiwa wenzetu wa Nigeria mwaka 2013 suala la Sanaa lilichochea maendeleo sana na liliweza kuchangia zaidi ya robo ya bajeti yao katika Serikali yao. Kwa hiyo na sisi tunaweza tukatengeneza fursa nyingi kupitia huko, lakini tukubali kujifunza kwa waliofanikiwa, siyo dhambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye hotuba hii Mheshimiwa Dkt. Mpango amekiri kwamba pamoja na mengine tuliyoyafanya kumekuwa na changamoto. Nimeona kuna baadhi ya Wabunge wamefanya kama kebehi, lakini niseme tunapokubali changamoto au unapokiri changamoto siyo udhaifu ila ni uimara, kwa sababu changamoto ndizo zinazokujenga. Kwa hiyo wanaobeza naomba tu niseme wanakosea kwa sababu kukiri changamoto pia kunakuimarisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niendelee hapo, kwa sisi watu tunaopakana na maziwa haya, nikiizungumzia Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria, tunaona kabisa kupitia maziwa haya tunaweza tukatengeneza viwanda vikatusaidia kuwaajiri vijana wengi. Hata hivyo, lazima tukubali, lazima niishauri Serikali na Wizara husika; lazima tuwekeze katika Sekta hii ya Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto, hatuna vifaa imara vya kuvulia. Bado tuna changamoto vifaa tulivyonavyo haviwezi kutusaidia kuendesha viwanda hivi vya uvuvi. Kwa hiyo niombe sana, bado tuna kazi ya kufanya, lazima tuwekeze ili tuweze kupata matunda bora sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Waziri Mkuu kwa namna ambavyo amewasilisha hotuba yake vizuri, hotuba ambayo imebeba matarajio makubwa sana, hasa kwa sisi vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda moja kwa moja kujielekeza kwenye hotuba, ukurasa wa 34 ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelezea kuhusu suala la uvuvi. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali inakwenda kufufua Shirika la Uvuvi (Tanzania Fisheries Corporation), napenda kupongeza jitihada hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kufufua Shirika hili la Uvuvi, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameongelea pia ujenzi wa bandari na ujenzi wa meli za uvuvi. Napenda sana kuongelea hapa; pamoja na kufufua Shirika hili la Uvuvi, pamoja na kujenga bandari hizi, pamoja na kujenga meli, lazima tuangalie Sheria yetu ya Uvuvi ya mwaka 2003 na kupitia upya Kanuni zetu za Uvuvi, bado si rafiki sana kwa wavuvi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Tanzania tumebarikiwa sana kuwa na vyanzo vingi vya maji na wakati sisi tunasoma tulikuwa tukisoma kwamba Ziwa Tanganyika ni miongoni mwa maziwa yenye kina kirefu duniani na ni la pili kwa kina kirefu likiwa na kina cha kilometa 1.47. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulitarajia sasa katika urefu huu wa kina cha Ziwa Tanganyika na umaarufu wake basi utuneemeshe sisi Watanzania, hasa tunaotokea Kanda ya Ziwa Tanganyika, lakini matarajio yetu yamekuwa ni tofauti. Najiskia vibaya kusema hivi lakini Ziwa Tanganyika tumesahaulika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukianza kabisa tunaona kwamba sekta ya uvuvi hii kama ingewekezwa vizuri ingeweza kutengeneza ajira nyingi sana kwa vijana. Wizara hii ya Waziri Mkuu ni Wizara ambayo inabeba dhamana ya kushughulikia ajira za vijana. Kwa hiyo niiombe sana Wizara hii ipige jicho mbele zaidi kuona namna ambavyo tunaweza kuwekeza katika Sekta ya Uvuvi na tukaleta tija kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ajira limekuwa la kidunia, limekuwa suala la Kitaifa. Hatuwezi kutatua changamoto hii nzito ya vijana kwa kutegemea asilimia nne za vijana. Kwa hiyo naomba Wizara hii itie nguvu katika sekta ya uvuvi, iwekeze katika vyombo vya kisasa vya uvuvi. Ni aibu mpaka leo Ziwa Tanganyika halina vyombo vya kisasa vya uvuvi; ni aibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ajabu sana katika Kanuni zetu hizi, tunaona leo tunahamasisha vijana wajiingize katika uvuvi, wafanye biashara ya uvuvi, lakini sheria zetu bado ni kandamizi kwa vijana. Leo hii ukitaka kupata leseni ya kusafirisha samaki nje, kwanza kila aina ya samaki lazima uwe na leseni tofauti. Tafiti zilizofanywa na shirika la utafiti zimesema Ziwa Tanganyika lina aina zaidi ya 400 za samaki. Sasa leo ukitaka kusafirisha sangara uwe na leseni yake, ukitaka kusafirisha mgebuka uwe na leseni yake, ukitaka kusafirisha kuhe uwe na leseni yake; jambo hili ni kandamizi kwa wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ziwa Tanganyika hili kutokana na utafiti uliofanywa, tumesema tuna aina zaidi ya 400 na katika idadi hii tuna samaki pia wa mapambo ambao wangekuwa ni kivutio kikubwa sana kwa watalii wetu, lakini Wizara yetu ya Uvuvi ipo kimya. Niombe sana Wizara hii ya Uvuvi iwekeze katika utafiti, tujue hawa samaki wa mapambo tunanufaika nao vipi, hasa sisi tunaotokea Ukanda wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na samaki hao wa mapambo, Ziwa Tanganyika hili lina samaki ambao wanaweza kuzalisha umeme na kwa utafiti uliofanywa ni hadi kufikia volti 900; ni umeme mkubwa sana huo. Niombe sana Wizara hii ya Uvuvi ijitahidi sana kuwekeza katika tafiti, maana tafiti hizi zimefanywa na zipo na Wizara inazijua na inazo. Kwa hiyo niombe sana suala hili liweze kuangaliwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunajaribu kuongea na wavuvi, wana changamoto nyingi sana. Wavuvi wanafanya kazi katika mazingira magumu na hali ikiwa wenyewe ndio watu wa kwanza wanaotoa kura kwa Serikali hii. Wavuvi wametupatia kura nyingi lakini wamesahaulika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijielekeza katika Kanuni zetu hizi za Uvuvi, leo hii mimi kijana nikitaka kujiajiri kwenye sekta ya uvuvi, nikisema nataka kusafirisha samaki, kwanza Ukanda wa Ziwa Tanganyika hatuna maabara ya kupimia sample ya samaki. Lazima samples hizo tukazipime Mwanza na kipimo cha sample kwa mwezi kwa leseni moja, nimesema kila aina ya samaki ana leseni yake, leseni moja ni shilingi 150,000 kwa mwezi, kwa mwaka ni shilingi 1,800,000, hiyo ni kwa leseni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukiwa na leseni tatu au nne imagine itakuwa ni shilingi ngapi. Tunaua biashara ya vijana wetu, tunaua malengo na matarajio ya vijana wetu. Niombe sana Wizara husika waone namna ya kufanya ili hizi leseni ziwekwe pamoja. Niombe sana Wizara iingilie kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu, Wizara hii ndiyo inasimamia ajira, lazima iwe na wivu na maeneo yote ambayo yanaweza yakatoa ajira. Lazima yenyewe iwe ya kwanza kushirikiana na hizi Wizara nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye kipengele kingine; wakati tunasema kwamba tutaanzisha viwanda ni wazi kwamba hatuwezi kuanzisha viwanda kama hatuna raw materials. Kwa hiyo lazima tuwekeze kwenye kupata malighafi ili viwanda vyetu viweze kupata malighafi hizo. Sasa hatuwezi kuanzisha viwanda kama tumeshindwa kuwekeza kwenye malighafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019 wakati wa ziara ya Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli Mkoani Katavi, aliahidi kiwanda cha kusindika samaki. Mpaka leo Serikali iko kimya hatuoni dalili zozote na sisi vijana tunatamani maana tunajua kwamba kiwanda kile kikifunguliwa vijana tutapata ajira. Sasa leo zinatoka takwimu hapa kuna viwanda kadhaa, tunajiuliza hawa vijana wanaoajiriwa wako wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana Wizara husika, twendeni site, twendeni tukaongee na wavuvi, twendeni tukapokee kero za wavuvi ili sekta hii iweze kutupatia ajira nyingi za kutosha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Sasa hapa nilikuwa najiuliza; mvuvi mwenye leseni ya mgebuka halafu akavua kuhe, anamrejesha ziwani ama anaondoka naye? Hebu tusaidie hilo.

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni leseni ya kusafirisha, kama unataka ku-export.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia na kwa sababu ya muda moja kwa moja naomba nijielekeze kuzungumzia Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, katika Jeshi la Polisi kozi mbalimbali zinatolewa na tunafahamu wazi kwamba kozi hizi ni nzuri kwa sababu zinawajenga askari wetu. Hata hivyo, kuna hii refresher course kwa ajili ya kuwajenga uwezo askari na utaratibu wa sasa hivi ni kwamba ni lazima ifanyike kwenye vyuo vya askari ambavyo viko Zanzibar, Moshi pamoja na Kidatu.

Mheshimiwa Spika, kozi hizi ni nzuri lakini utaratibu unaotumika sasa hivi si rafiki sana na hauleti tija. Katika kozi hizi askari wanajitegemea chakula na tunafahamu kabisa mishahara ya askari au watumishi mingi ni midogo lakini pia inakuwa na makato mbalimbali. Askari wetu wengi wanategemea sana posho lakini wanapokuwa kwenye mafunzo haya inawalazimu kukatwa Sh.7,000 kwa siku kwa ajili ya chakula.

Mheshimiwa Spika, jambo hili si jambo rafiki sana kwa sababu kwanza linazuia tija ya kozi ile badala ya askari ku- concentrate na kozi anakuwa anawaza kwamba anatakiwa achangie pesa hiyo na inakatwa moja kwa moja kwenye posho. Tunafaahamu kwamba kwa siku posho ya askari anapewa shilingi 10,000, kwa hiyo, tunapokata shilingi 7,000 tunamlazimisha abaki na shilingi 3,000 ili aweze kuitumia na familia yake. Kwa hiyo, jambo hili linamfanya awe na mawazo lakini pia atashindwa ku-concentrate kwenye mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe tu ushauri, utaratibu wa zamani ulikuwa ni mzuri, hizi refresher course zilikuwa zinafanyika kwenye mikoa husika kwa maana kwamba zilikuwa hazina makato ya gharama za chakula.

T A A R I F A

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa endelea.

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa mchangiaji kwamba kozi hiyo inaitwa ya utayari na ilianza kutolewa kwa muda wa wiki mbili, wiki tatu, mwezi mmoja sasa hivi inatolewa kwa muda wa miezi mitatu. Akimaliza kozi hiyo baada ya wiki moja imeanzishwa tena kozi nyingine, kwa hiyo, ni tabu kidogo. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa unapokea taarifa hiyo?

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo kwa sababu hiyo miezi mitatu kama askari akiwa kozi atakatwa Sh.7,000 kila siku.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naendelea na utaratibu wa zamani ambapo kozi hizi zilikuwa zinafanyika kwenye mikoa husika hizi gharama za chakula hazikuwepo. Askari wali-concentrate kwenye kozi kwa sababu mwisho wa siku walirudi nyumbani kwenye familia zao. Kwa hiyo, naishauri Serikali aidha utaratibu huu wa zamani ufuatwe au basi kama itawezekana Serikali ichukue gharama hizi za chakula kwa sababu haiwezekani tumpe mafunzo polisi halafu ajigharamie chakula. Kwa hiyo, naomba kuishauri Serikali aidha ichukue changamoto hii ya chakula igharamie au urudishwe mfumo ule wa zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niipongeze sana Wizara pamoja na Kamati imetoa ushauri mzuri lakini bado kuna changamoto kubwa ya vitendea kazi pamoja na stationeries.

Hivi navyoongea sasa hivi Kituo cha Polisi Kigoma Mjini hakina gari la askari. Sasa unaweza ukaona ufanisi utatoka wapi kama vitendea kazi vinakuwa adimu hasa tukijua kabisa Kigoma Mjini pale kuna bandari, benki na mambo mengi ambayo yangehitaji ulinzi wa raia na mali zao lakini mpaka sasa hatuna gari la askari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini imekuwa ni utamaduni bajeti hizi zinazotengwa hazitoshelezi kuendesha haya magari ya askari. Leo hii ukipata tatizo ukipiga simu polisi utaambiwa gari haina mafuta, mbovu au haipo. Kwa hiyo, napenda kuishauri sana Wizara iingilie kati jambo hili hasa kwenye mfumo wa bajeti ya mafuta ili askari wetu hawa wawezeshwe vizuri na tutakapokuwa tunahitaji huduma tuzipate kwa wakati kwa sababu imekuwa ikileta shida sana kwa wananchi wanapotaka huduma ya kipolisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 12, ameeleza namna ambavyo wanashughulikia makosa na taarifa zinazotolewa Polisi, lakini kumekuwa na mlundikano mkubwa sana wa mahabusu katika Vituo vya Polisi. Utaratibu huu tunaona ni kinyume na sheria. Sheria inatutaka tusizidishe masaa 48 mtu awe ameshafikishwa Mahakamani, lakini utaratibu huu haufwatwi, vijana wanawekwa ndani, ukiulizia unaambiwa upelelezi unaendelea au unaambiwa maelezo hayajachukuliwa. Kwa kweli hali hii inawatesa sana wananchi. Kwa hiyo, naiomba Wizara ione namna nzuri ya kushughulikia jambo hili, kupunguza msongamano wa mahabusu katika Vituo vya Askari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona kabisa na ni wazi kwamba katika majeshi mengine kumekuwa na utaratibu mzuri wa kuwa-handle hawa Askari wa kike, wamekuwa wakipatiwa fedha ya kujikimu katika mazingira yao ya kike hasa ya hizi pads, lakini katika Jeshi la Askari Polisi, Askari wa kike hawapatiwi. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara, kama yote ni majeshi, kwa nini wengine wapatiwe, wengine wasipatiwe? Kwa hiyo, naomba sana jambo hili liweze kuchukuliwa serious, kwani Askari hawa wanafanya kazi ngumu, nzito na pia wanafanya kazi ambayo inaleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

MHE. NEEMA F. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa Neema, endelea.

T A A R I F A

MHE. NEEMA F. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kutoa taarifa kwamba jambo hili la uhitaji wa taulo za kike siyo tu kwa watumishi maskari wanawake, pia kwa wafungwa na mahabusu wanawake.

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekuwa ikitenga bajeti ndogo kwa ajili ya kuwawezesha wafungwa na mahabusu wanawake, lakini bajeti hii imekuwa haitoki na matokeo yake hawa wanawake walio mahabusu na wafungwa wanatumia magodoro na magazeti wanapokua kwenye siku zao jambo ambalo ni hatarishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Kabla Mheshimiwa Sylivia hujaendelea, hii inanikumbusha wakati wa vita vya Kosovo na Herzegovina palikuwa na vita moja kule Yugoslavia ya zamani ambayo ilikuwa mbaya sana. Sasa baada ya vita ile kwisha, wakawa wanamhoji mtu mmoja, raia wa kule kwamba katika vita hii, kitu gani kilikuwa ni shida kubwa sana katika kipindi cha vita? Yule mtu akasema, yaani hebu imagine wakati ule kulikuwa hakuna toilet paper. Yaani kwake katika shida kubwa wakati wa vita, kulikuwa hakuna toilet paper kabisa. Sasa you can imagine matatizo makubwa kama haya! Endelea Mheshimiwa Sylivia. (Kicheko)

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naipokea taarifa.

SPIKA: Nafikiri siyo kwa Polisi peke yake, itakuwa na Magereza, Uhamiaji na Zimamoto labda. Ahsante, endelea. (Makofi)

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nimalizie kama nilivyokuwa naeleza. Kwa hiyo, jambo hili linabidi lichukuliwe kwa uzito wake, wanafanya kazi ngumu, lakini pia mazingira siyo Rafiki.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kabisa, kwenye hizo stationary, sisi tunaotokea mikoa ya pembezoni, mgao huu wa stationaries unachelewa kutufikia. Leo Kigoma na mikoa mingine ya pembezoni, nafikiri hata na Rukwa, tunachelewa kupata vitendea kazi (stationary). Unakuta hizi log book pamoja na mambo mengine havitufikii kwa wakati. Tunaomba sana Wizara izingatie mgawanyo huu, hat sisi wa mikoa ya pembezoni tuzipate basi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunapozungumzia suala la vitendea kazi ambavyo nimesema, ilikuwa ni ajabu sana, juzi nilipigiwa simu na mwananchi, amefika Kituo cha Polisi hajapata PF3, anaambiwa zimekwisha, akatoe copy nje. Nadhani tuweke utaratibu mzuri, kama hizi document… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia. Nianze kwa kuiongeza Wizara, hasa kumpongeza Waziri na timu yake. Wakati uliopita nilitoa kero zangu hapa kuhusu wavuvi wa Ziwa Tanganyika, lakini Waziri alifika Kigoma akaongea na wavuvi na baadhi ya kero akazitatua. Wavuvi wa Kigoma na wavuvi wa Mwambao mwa Ziwa Tanganyika wanaipongeza sana Serikali Sikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nitakuwa na uchangiaji mdogo sana; na leo nina kero chache ambapo naamini Serikali yetu ni sikivu itakwenda kuzifanyia kazi. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati wa majumuisho aweze kutupatia ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nachangia nilieleza umuhimu wa Ziwa Tanganyika. Kwa tafiti zetu zilizofanyika, nilisema Ziwa Tanganyika lina kina kirefu ambacho ni mita 1,470. Masikitiko yangu makubwa ni kwamba hili Ziwa Tanganyika ni kama Serikali hailioni. Naongea haya nikiwa na masikitiko makubwa kwa sababu moja. Ziwa Victoria lina urefu wa kina cha mita 120, na Ziwa Tanganyika ni mita 1,400 lakini tunaona kwamba kuna kanuni kandamizi kwa wavuvi wetu wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tafiti zilifanywa na TAFIRI zinasema kwamba uwezo wa samaki kuishi, oxygen inayopatikana ni mita 150 kutoka kwenye water surface (kina kile cha juu). Leo wavuvi wa Ziwa Tanganyika wanaruhusiwa kutumia nyavu ambazo zinakwenda kwa mita saba tu. Mbali ya kuwa na kina kirefu, wavuvi wa Ziwa Victoria wanaruhusiwa kwenda mpaka mita 16. Hii siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Wizara watueleze sisi wavuvi wa Ziwa Tanganyika, watuambie ni vigezo gani vinavyotumika ili sisi wavuvi tujue, maana tunaona kwamba hiki kitu siyo sahihi. Kwa hiyo, wavuvi wa Ziwa Tanganyika wanaomba angalau waweze kupatiwa nyavu ambazo zitaweza kwenda hata mita 20 au 25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero namba mbili ya wavuvi wa Ziwa Tanganyika, wanatumia taa lakini kanuni zinawataka wasitumie taa zinazozidi watt tano; na kwa chombo kimoja zisizidi watt 50. Sasa kulingana na urefu wa kina cha Ziwa Tanganyika, hiyo taa ya watt 50 kwa chombo inaweza kwenda chini, yaani light intensity kwenda chini ni mita 20 tu. Sasa hao samaki ambao tunasema wako kwenye mita kuanzia moja mpaka 150 tunawapata vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Wizara iingilie kati jambo hili kwa sababu linakuwa ni kikwazo na linasababisha upatikanaji mdogo wa samaki katika Ziwa Tanganyika. Leo hii ukienda Kigoma, kilo moja ya dagaa ni shilingi 28,000/= mpaka shilingi 30,000/=. Hebu ona, mwananchi wa kawaida huyu masikini hatakuwa na uwezo wa kula dagaa ilhali wanavuliwa wanapoona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Wizara itueleze mambo haya wakati wa majumuisho kwamba ni kwa nini tunawazuia wavuvi wasitumie taa ambazo zitaweza kuangaza chini sana? Mapendekezo ya wavuvi wanasema, angalau wapatiwe ruhusa ya kutumia taa ambazo zinaweza kwenda hata mita 200. Kwa hiyo, naomba sana, wavuvi wanasema kama watatumia taa zenye watt 200 wanaweza kwenda chini kuona mpaka mita 70 au 80. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara, Waziri wewe ni msikivu na Naibu Waziri wako pia ni msikivu, tunaomba sana jambo hili liangaliwe kwa umakini mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa sababu leo sikuwa na mambo mengi. Wavuvi wa Ziwa Tanganyika wana masikitiko makubwa sana. Mbali ya kuwa ziwa la pili duniani lenye kina kirefu, lakini wamesahaulika. Waziri amesema kwamba Serikali imepeleka zaidi ya shilingi milioni 505 katika Ziwa Victoria, lakini ni aibu, Serikali haijapeleka hata shilingi 100/= kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika. Sasa tuambiwe: Je, wavuvi wa Ziwa Tanganyika ni sehemu ya nchi hii au siyo sehemu ya nchi hii? Kwa sababu tunaona hawanufaiki na Ziwa hili Tanganyika ilhali wanaliona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu mimi ni mwakilishi wa vijana na wanaojishughulisha na uvuvi, wengi ni vijana. Nisiposema haya nitakuwa sijawatendea haki vijana wenzangu. Nitaomba sana Mheshimiwa Waziri, atuambie kwa sababu kwa taarifa nilizonazo, mbali ya kupatiwa hiyo shilingi milioni 505 plus, bado kuna vikundi 20 vya Ziwa Victoria tayari uthamini umekamilika na muda wowote wanapewa mikopo hiyo. Ila Ziwa Tanganyika hatuoni. Kama shida ni vigezo, mtuambie tufanye nini ili tu-qualify kupata hiyo mikopo. Haiwezekani tuachwe ilhali tunateseka na sisi ni Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Wizara, watakapokuja kufanya majumuisho, watupatie majibu hayo. Kama sitaridhika na majibu hayo, kwa kweli nakusudia kutoa shilingi kwenye mshahara wa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kidogo sana kuhusu mifugo. Mkoa wetu wa Kigoma una mifugo mingi, lakini huwezi kusikia inasemwa kokote kwa sababu moja tu. Miundombinu ya Mkoa wa Kigoma ni hafifu. Kigoma kuna ng’ombe wengi, lakini leo nikitaka kumsafirisha ng’ombe kumpeleka sokoni ni gharama, yaani ng’ombe mmoja naweza nikatumia zaidi ya shilingi 200,000/=. Kwa hiyo, kama nitamnunua ng’ombe Kigoma kwa shilingi 300,000/= ili nimpeleke sokoni, nitahitaji kuongeza shilingi 200,000/=, mpaka anafika sokoni ni shilingi 500,000/. Je, mimi sokoni nitamuuza kwa shilingi ngapi? Kwa hiyo, siyo kwamba Kigoma hakuna mifugo; ipo, lakini miundombinu siyo rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni kulikuwa kuna mabehewa yanabeba ng’ombe, lakini leo mabehewa yamekufa. Kwa hiyo, naomba kwa sababu jambo hili ni mtambuka, Wizara zishirikiane; Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Mifugo, tutakapokuwa na miundombinu ya uhakika tutasafirisha mifugo yetu, tutasafirisha samaki wetu na pia tutaweza kuongeza mzunguko wa fedha katika Mkoa wetu wa Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni wakati Waziri anawasilisha, alielezea vizuri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimwia Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa na mimi kuingia katika taarifa ya nchi hii ya kuchangia bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha Kaka yangu Mwigulu kwa hotuba nzuri sana yenye kuleta matumaini makubwa. Naomba nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mama yetu mpendwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazozifanya na kuona umuhimu wa vijana na kufanya kikao kikubwa na vijana Jijini Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe pongezi zangu kwa Serikali kwa kuhusu suala zima hili la bodaboda, kwa kweli kitendo cha kutoa faini ya bodaboda kutoka shilingi 30,000 mpaka kufika shilingi 10,000 vijana tumefarijika sana. Lakini tutakuwa hatujafanya vizuri kama tutaishia tu kupunguza faini hii kutoka shilingi 30,000 kwenda shilingi 10,000 bado kwenye bodaboda changamoto ni kubwa tunafahamu wazi kwamba dhamira ya Serikali ni nzuri sana ya kuwatengenezea mazingira vijana ili waweze kufanya kazi vizuri lakini bado changamoto ni kubwa. Mbali ya kuwa na hii shilingi 10,000 kama faini na tusipoitumia vizuri hii shilingi 10,000 kama faini tutatengeneza tatizo lingine. Nasema hivi kwa sababu moja, matatizo mengi ya bodaboda yanahusiana na suala zima la kuwa hawana leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu leo kijana wa bodaboda ili aweze kupata leseni lazima awe na shilingi 70,000. Kwa hiyo, matatizo mengi na faini nyingi hizi wanapigwa kwa sababu hawana leseni. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali na nimuombe Waziri pamoja na kupunguza hii faini basi tuangalie pia utaratibu huu wa leseni. Kama itampendeza Mheshimiwa Waziri angalau hata iwe shilingi 20,000 kwa mtu mmoja. Kwa sababu, leo haiwezekani kijana wa bodaboda atoe shilingi 70,000 pia na watu wenye magari watoe shilingi 70,000 haiwezekani Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri, Rais wetu mpendwa, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, wakati anaongea na vijana wa Taifa hili kupitia vijana wa Mwanza aliongea na vijana wa bodaboda na katika hotuba yake ya vijana wa bodaboda alisema anatamani kuona vijana wa Taifa hili wanamiliki bodaboda zao wenyewe. Nasema hivi kwa sababu, mwanzoni bodaboda ilifikiriwa kuwa ni ajira kwa watu ambao hawajasoma lakini naomba nikupe taarifa hii, leo hii asilimia kubwa ya vijana waliomaliza vyuo vikuu leo wanafanya kazi ya kuendesha bodaboda, yote hii ni kwa sababu kuna changamoto kubwa ya ajira, vijana wameamua kujipatia ajira kupitia bodaboda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ili uingize bodaboda hapa nchini, kumekuwa na kodi nyingi na hizi kodi zinawanyima fursa vijana kumiliki bodaboda zao wenyewe ndiyo maana wanatumia bodaboda za watu na kuwaingizia utajiri watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nikitaka kuingiza bodaboda kwanza lazima nilipe import duty ambayo ni 20 percent pia lazima nitalipa excise duty asilimia tano, nitalipa VAT asilimia 18. Ukiangalia tozo zote hizi anayezilipa mtu wa mwisho ni yule mnunuzi, kwa hiyo hii inawafanya vijana wengi wanashindwa kumiliki bodaboda zao wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri, tunasema kabisa kwamba, maagizo ya viongozi wakubwa tunasema ni maagizo. Sasa Rais amesema natamani kuona vijana wanamiliki bodaboda zao wenyewe. Nilitarajia kuona mkakati wa Wizara ni namna gani vijana wataenda kumiliki bodaboda zao wenyewe. Hapa naomba nitoe ushauri kidogo tu kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na uhamasishaji wa vijana wengi kwamba wajiunge kwenye vikundi na vikundi hivi tumekuwa tukivielekeza kwenye Halmashauri zetu bado tuna Mifuko ya uwezeshaji wa vijana na akina mama chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, niombe Mheshimiwa Waziri kwamba tunaweza tukaratibu vikundi hivi ama kupitia Halmashauri zao au kupitia usajili wao wa vikundi angalau tukaona tukapunguza hizi kodi hasa VAT.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe Mheshimiwa Waziri tunaweza tukaratibu vikundi hivi either kupitia halamashauri zao au kupitia usajili wao wa vikundi. Angalau tukaona tukapunguza hizi kodi hasa VAT. Tukisema kama tutatoa hii asilimia 18 tutakuwa tumewafanyia ahueni vijana wengi, na vijana wataweza kumiliki bodaboda zao wenyewe. Lakini leo ukisema vijana waende benki, tunajua zipo benki zinazotoa mikopo ya bodaboda, wanasema ni riba nafuu lakini Riba hizo sio nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni kijana, nafahamu benki si rafiki kwa vijana wengi kwa sababu hawana hati za nyumba, viwanja wala mitaji kwa hiyo wakifika watakosa vigezo hivyo. Kwa hiyo nilikuwa napenda sana kuishauri Wizara, kwamba either wawape mamlaka halmashauri zetu hizi, kama itawezekana waondolewe hii VAT watakapokuwa wanaagiza bodaboda kwa vikundi ambavyo vimesajiliwa vipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda ni mchache lakini naunga mkono hoja, ahsante kwa kunipa fursa ya kuingia kwenye record ya Taifa hili kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza na mimi niungane na wenzangu kumpongea Rais wetu mpenda Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutuletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimepitia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inayohusiana na vijana, ajira na watu wenye ulemavu; na mimi ningependa sana nijikite kwenye ajira. Changamoto kubwa ya vijana ni ajira na sisi wawakilishi wa vijana ajenda yetu namba moja ni suala la ajira kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kabisa kuwa hatuwezi kutatua matatizo au kero ya ajira kwa kutegemea asilimia nne za mikopo ya halmashauri, haiwezekani. Kwa hiyo Wizara hii imepewa jukumu kubwa la kusimamia ajira za vijana. Nilitarajia kuona tuna mpango maalum wa namna gani tunakabiliana na hii changamoto ya ajira kwa vijana (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 62 wa Hotuba ya Waziri Mkuu, anasema kwamba asilimia 87.8 ya vijana wana ajira; ajira rasmi na ajira zisizo rasmi, either wamejiajiri au wameajiriwa. Sasa utaona kama asilimia 87 wana ajira na waswahili wanasema no research no right to speak nadhani wataalam wataelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumzia nini hapa? Unaposema asilimia 87 wana ajira ninaamini kabisa ajira ambazo zinakuwa nyingi hapa ni ajira zisizo rasmi. Unapozungumzia ajira zisizo rasmi ziko nyingi, kuna ajira nyingi bodaboda, kuna mama ntilie, kuna baba ntilie, kuna mmachinga na wafanyabiashara wengine wadogo, hawa wanaingia kwenye ajira zisizo rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina ushauri kwa Serikali. Kwamba, tunapotaka kukabiliana na hii changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana natamani sana kuona tunawekeza nguvu kubwa katika ajira zisizo rasmi kwa sababu ndizo zinazoajiri watu wengi. Ninaonge haya na nitatoa reference kwa kutumia bodaboda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodaboda ambazo tumeingiza nchini kuanzia 2017 mpaka leo 2022 ni bodaboa Milioni 1,279,455 na tumeweza kuipatia Serikali zaidi ya bilioni 117. Hapa nataka kuzungumza nini, ukifanya takwimu ya vijana ambao wamejiari kwenye bodaboda kwa Mkoa wa Dar es Saalam tu wako vijana 136,431. Ukija Mkoa wa Mwanza wako vijana 86,218. Ukija Mkoa wa Dodoma wako vijana 58,316. Ukija Mkoa wa Kigoma wako vijana 36,411. Sasa, unapofanya rafli ya hawa vijana wa bodaboda nchi nzima ni zaidi ya 2,090 na kuendelea huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sekta hii inaweza ikaajiri vijana wengi namna hii, naona ni muda mwafaka sasa wa Serikali kuweka kipaumbele katika sekta hii. Sekta hii ya bodaboda imeachwa, imeachwa vijana hawanufaiki wanateseka lakini imeachwa Serikali pia haipati mapato kupitia bodaboda. Na hapa nataka nielezee kitu gani? Unapozungumzia vijana milioni 2,092 ambao wamejiajiri kupitia bodaboda hawa ni vijana mchanganyiko; wako vijana ambao wana elimu na ambao hawana elimu.

Hapa kinachotokea kitu gani? Changamoto yao kubwa ni suala la leseni. Ili kijana apate leseni anahitaji kuwa na 83,000. Hali mtaani ni ngumu vijana wanalia, ajira hakuna, abiria hakuna, hiyo 83,000 anaipata wapi huyu kijana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kukosa hiyo 83,000 lakini anapokuwa hana hiyo 83,000 hana leseni lakini hajapaki yuko barabarani. Nini kinatokea hapa? Badala ya Serikali kukusanya mapato kupitia hizo leseni Serikali haipati mapato na kijana anaishia kutoa elfu tano tano, elfu mbili mbili kwa Askari ili aendelee kuwa barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali is either tupunguze hii bei ya leseni ni kubwa sana, tunaweza kufanya leseni ikawa 40,000 na Serikali ikapata mapato kuliko hivi tunavyofanya sisi, kuwaachia wenyewe wajifanyie. Au tunaweza tukatengeneza mfumo hawa vijana wakalipia leseni kwa installment na Serikali ingeweza kupata mapato mengi na vijana wangeweza kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Tax Administration Act inamtambua mlipa kodi. Unapokuwa na biashara inayoingiza zaidi ya milioni nne unatakiwa usajiliwe kama mlipa kodi. Lakini wapo watu wanafanya biashara hizi za bodaboda, ana bodaboda tatu mpaka nne; lakini kwa sababu Serikali imeacha wazi hawa watu hawalipi kodi na Serikali inazidi kupoteza mapato na vijana wengi wanaendelea kunyanyasika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ustawi wa taifa letu ukisoma ukurasa wa 55 unatambua kabisa kwamba vijana ndio nguvu kazi ya taifa hili kwa asilimia 55. Sasa kama vijana ni nguvu kazi, embu tuwasaidie kuwaokoa na hali wanayopitia. Bodaboda kwa sababu wameachwa wazi tunapata majeruhi wengi Serikali inaingia gharama kuwatibu lakini inaendelea kupoteza nguvu kazi ya taifa. Kwa kuwa tumeshindwa kusimamia suala la bodaboda Serikali inapoteza mapato na bodaboda wanazidi kuteseka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua Serikali imetoa bilioni tano kwa ajili ya machinga lakini tunatoa bilioni tano kwa ajili ya miundombinu. Je, tunashindwa kuwapatia mikopo hiyo miundombinu tunayoianzisha ni nani atakayeenda kuitumia kama vijana hawa hawana mikopo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusidanganyane hapa hatuwezi kuhamasisha vijana wajiari kama hatutawapatia mikopo. Vijana wanahitaji mitaji ili waweze kujiari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia sasa hivi ukiangalia hospitali nyingi zina wodi maalum kwa ajili ya majeruhi wa bodaboda. Mimi niiombe Ofisi ya Waziri Mkuu isimamie sekta hizi. Bado Wizara ya Mambo ya Ndani haijafanya kazi yake vizuri zaidi ya kutengeneza ugomvi kati ya bodaboda na Askari. Lakini pia kuna haja ya Wizara ya Uchukuzi kusimamia jambo hili ili kutengeneza kwa sababu hata bodaboda hii iko sehemu ya uchukuzi. Uchukuzi siyo ndege tu na meli… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Bunge lako hili Tukufu. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa hai na kuiona siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kuipongeza Kamati ya Sheria Ndogo; kiukweli wamefanya kazi kubwa na ninawapongeza sana. Pia ninampongeza Mwenyekiti wetu kwa namna alivyowasilisha vizuri taarifa ya kamati yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajielekeza kwenye mambo machache ya upande wa sheria ndogo. Tumebahatika kuchambua sheria nyingi, na ni ukweli usiofichika bado sisi kama Bunge hili tuna kazi ya kufanya. Tumekasimu madaraka haya kwa baadhi ya taasisi zenye uwezo wa kutunga hizi kanuni lakini tunaona bado changamoto ya hizi sheria ndogo ni nyingi mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ndogo nyingi zinakosa uhalisia, hazitekelezeki na zinaleta changamoto sana kwa maisha ya wananchi. Ukiangalia sheria ndogo ya usafi wa mazingira ya Wilaya ya Misungwi ya mwaka 2022 inatoa katazo la watu kufanya shughuli yoyote ya maendeleo kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa nne asubuhi kwa lengo la kufanya usafi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo linaweza likawa zuri la kufanya usafi lakini kutoa katazo la kufanya shughuli yoyote ya maendeleo, hili si sawa. Sisi tunadhani kama taifa tulitakiwa tufikirie kwenda mbele na si kufikiria kurudi nyuma. Kama lengo likiwa ni kufanya usafi tuondoe hili zuio la kusema shughuli za maendeleo zozote zisifanyike kwa masaa haya matano. Sheria hii inaleta usumbufu sana kwa wananchi. Jiulize, wewe eneo la biashara kila siku uko hapo unafanya biashara, ni usafi gani huo utakaohitaji kuufanya kwa masaa matano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu ambao wanaweza wakafanya usafi kwa nusu saa, waruhusiwe kuendelea na shughuli zao za maendeleo. Wapo watu ambao wanaweza wakafanya usafi kwa muda wa saa moja, waruhusiwe kuendelea na shughuli zao za maendeleo. Kuna mama zetu hawa ambao wanafanya biashara ndogo ndogo. Mama anapika vitumbua, biashara yake anatakiwa afanye asubuhi. Unapomwambia kuanzia saa 12 mpaka saa nne asifanye shughuli yoyote tunarudisha uchumi nyuma wa Watanzania hawa masikini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii haiko tu Misungwi, sheria hii iko maeneo mengi; na moja ya maeneo ambayo sheria hii inatumika, hata hapa Dodoma sheria hii inatumika. Sheria hii inatumika Ikungi, Nsimbo na maeneo mengi ya nchi yetu. Sisi kama Kamati tunaona sheria hii imepitwa na wakati, tunarudisha nyuma maendeleo ya wananchi wetu kwa kuweka sheria hii ambayo ina usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiitazama sheria ndogo hii kwenye utekelezaji wake, haiwezekani. Hata kwenye practice huko mitaani watu hawaendi kufanya usafi kama tulivyotarajia; wanachokifanya ni kufunga biashara zao ifike saa nne waweze kufungua ili wasikamatwe na kupigwa faini. Sasa tujiulilze, sisi kama taifa tunataka nini? Tunataka usafi au tunataka watu wafunge biashara kusubiri saa nne ndipo wafungue?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe, kama kamati ilivyoshauri jambo hili kamati imekataa na haikubaliani nalo. Ukija sheria Ndogo ya Usafi wa Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi inazungumzia ni kosa kwa abiria kutupa takataka nje ya chombo cha usafiri. Kweli kila mtu anakubaliana na jambo hilo; lakini kusema tukio hilo au kosa hilo litachukuliwa kama limefanywa na mmiliki wa chombo hicho, hiyo siyo sawa. Kwanza ni kinyume cha sheria, ni kinyume cha misingi ya sheria lakini pia kinapingana na sheria mama. Ukisoma kifungu cha 40 cha Sheria ya Mazingira kinazungumzia principle ya mtu aliyefanya kosa ndiye awajibike. Haiwezekani leo abiria atupe takataka, faini alipe mwenye basi, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama kamati tumeshauri, kama kosa litafanywa na abiria, basi awajibishwe abiria, kama kosa litafnywa na kondakta, basi awajibishwe kondakta na kama kosa litafanywa na mwenye chombo, basi awajibishwe mwenye chombo; huo ndio uliokuwa usahuri wa Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi ndogo sisi kama Bunge tunazipitisha hapa; na tumetoa mamlaka, ukisoma Cap 1 kifungu kile cha 37 kinatoa mamlaka ya sheria hizi kuanza kutumika kabla hazijapitishwa na Bunge. Shida kubwa ya changamoto hii inaanzia hapo. Kwa kuwa tumeruhusu sheria hizi zianze kutumika kabla hazijapitishwa na Bunge, hicho ndicho kimekuwa kichaka cha wananchi wetu kuteswa na sheria hizi mbovu, kukandamizwa na kanuni hizi mbovu na mwisho wa siku zinaletwa tayari wananchi wameshaumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nina ombi kwa Bunge hili. Kama itakupendeza kuna haja sisi kama Bunge kufanyia marekebisho Kifungu cha 37 cha Sheria ya Tafsiri. Kifungu cha 37 kiondoe ile hali ya kuiruhusu sheria hizi kuanza kutumika kabla hazijapitiwa na Bunge. Kwa sababu unaona changamoto hizi, unapozungumzia Misungwi wana sheria hii.

Pia Halmashauri ya Nsimbo ime-copy sheria hizi nao wana sheria hizi hizi. Kwa hiyo ukifanya tathmini utagundua kuna sheria nyingi ndogo mbovu zinazoumiza wananchi na bado zinaendelea kutumika zikisubiri mpaka Bunge lije liziite, lizichambue na lizipitishe. Kwa hiyo mimi niombe Waheshimiwa Wabunge, kama itawapendeza kuna haja ya Serikali kuleta sheria ili sisi tuifanyie marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimalizie kwa kusema yafuatayo. Mwaka 2019, sisi kama Bunge tulipitisha sheria ndogo, na sheria hiyo ilikuwa ni kanuni ya kukataza mifuko ya plastic. Leo ni takribani miaka mitatu tu tangu zuio hilo litokee lakini naomba nikupe taarifa, mifuko ya plastic sasa iko mitaani na inatumika, na Serikali iko kimya haitoi tamko lolote kuhusu kitendo hicho kinachoendelea. Sasa hii inashangaza. Sisi kama Bunge tunakaa hapa, tunapitisha sheria, tunatoa maazimio yetu lakini utekelezaji wake ndio unakuwa na changamoto hizo. Mimi niombe, niiombe Serikali. Kwanza inajukumu la kufanya kujua kwamba taarifa ya mifuko inayo au haina.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi? Mheshimiwa Ramadhan.

T A A R I F A

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji dada yangu Sylvia na mwanakamati mwenzangu kwamba Zanzibar ilipitisha kanuni kama hiyo anayoisema ya kuzuia mifuko ya plastic, leo Zanzibar mifuko ya plastic ni historia. Kama wenzetu wanataka kwenda kujifunza waende Zanzibara wakajifunze, wao wamewezaje, huku tushindwe tuna nini?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sylvia unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo taarifa kwa mikono miwili, si jambo baya kujifunza kwa waliofanikiwa. Kwa hiyo hata sisi kama tumeona changamoto ya utekelezaji wa mifuko hii ya plastic bado tuna nafasi ya kwenda kujifunza kwa wenzetu, kwa hiyo siyo jambo baya kujifunza kwa waliofanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimalizie kwa kusema, ninaipongeza Kamati; lakini nilikuwa na ombi maalum kama Kamati itaona inafaa kuongeza azimio kwenye Maazimio ya Kamati tuitake Serikali ilete sheria cap 1, interpretation of laws act, ije hapa tuifanyie marekebisho hicho kifungu cha 37. Kwa sababu kifungu hicho ndicho kinacholeta changamoto zote hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja za Kamati zote mbili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba hii iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha leo kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, pia kwa namna ya pekee sana naomba nimpongeze na nimshukuru Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kututeulia watu makini wanaoijua Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na muda naomba nijielekeze moja kwa moja kuchangia Fungu Namba 64 linalohusu masuala ya uvuvi, kuanzia ukurasa wa 68. Tunafahamu kabisa uvuvi na ufugaji hii ni sekta ya uzalishaji nasi kama vijana tunaamini sana sekta hii ingewekezwa vizuri ingetatua changamoto nyingi za vijana ikiwemo ajira lakini ikiwemo kutufanya vijana tuweze kufanya biashara kutokana na mazao ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana nimekuwa nikisimama kwenye Bunge hili mara nyingi, nikielezea na nikiomba Serikali itupe ufafanuzi wa namna ambavyo wanawekeza kwenye Ziwa Tanganyika. Majibu yamekuwa ni utafiti, utafiti, utafiti, utafiti unaendelea! Sasa hili ni jambo la aibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumebarikiwa Mungu ametujaalia tuna maziwa mengi, tuna Ziwa Tanganyika, tuna Ziwa Nyasa, tuna Ziwa Rukwa, tuna Ziwa Victoria pia tuna Bahari. Ni aibu kuona leo sekta hii ya mifugo na uvuvi inachangia kwa asilimia ndogo sana kwenye Pato la Taifa, ni aibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu tunawalaumu viongozi, lakini Serikali kwa kiasi kikubwa imefanya mchango wa uvuvi usionekane. Leo tukienda huko kwa Maafisa Uvuvi hali zao ni mbaya sana. Ukiangalia Mkoa wa Kigoma, ukiangalia Mkoa wa Katavi, ukiangalia Mkoa wa Rukwa vitendeakazi, miundombinu bado ni hafifu sana. Bado tunategemea sekta hiyo ya uvuvi izalishe, inazalishaje? Labda kama tunataka miujiza, lakini hatuwezi kuzalisha, hatuwezi kuona tija ya sekta hii kama hatutafanya uwekezaji wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea haya kwa sababu leo hii ukiangalia Mkoa wa Kigoma, Wilaya zinazofanya uzalishaji, Wilaya zinazofanya uvuvi ukiwaambia hata vitendeakazi wanafikaje site? Hawana magari, hawana hata pikipiki za kuwafanya wafanye movements za kwenda kufuatilia. Sasa unataka kuniambia kwa mazingira hayo ni namna gani sekta hii italeta tija kwa Taifa letu? Kwa hiyo, kuna haja kubwa sana ya Serikali kuwekeza katika sekta hii ili tuone tija yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilitamani kulizungumza kwenye sekta ya uvuvi, wamezungumza hapa Wabunge wengi vizuri sana na mimi naungana nao. Sisi watu wa Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi, uchumi wetu kwa asilimia 90 unategemea Ziwa Tanganyika. Tumekuwa tukiongea hapa tuna masikitiko kwa sababu tunaona Serikali ni kama haitambui umuhimu wa Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani leo hii bado siku Nane, Wawakilishi wa Wananchi hatuna taarifa rasmi kuhusu kufungwa kwa Ziwa! Bado siku Nane! Haiwezekani maamuzi makubwa kama haya, maamuzi ya kuwakosesha ajira watu wetu, ndani ya Mikoa mitatu bila kuwashirikisha wananchi…

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sylvia kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kilumbe.

TAARIFA

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, wakati Serikali yetu na Serikali hizo nyingine zimefanya makubaliano katika jambo hilo, ukiingia kwenye internet Bunge la Congo limekataa hoja ya kufunga Ziwa Tanganyika, kwa maana hiyo na leo tuko kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunazungumza nasi tunakataa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sylvia taarifa unaipokea? Endelea na mchango wako.

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa ninaipokea kwa mikono miwili. Sisi Wawakilishi wa Wananchi hasa tunaotoka Ukanda wa Ziwa Tanganyika jambo hili hatukubaliani nalo kwa asilimia zote. Tutakubaliana nalo tu endapo Waziri atakapokuja atatuambia njia mbadala ya watu wetu ndani ya miezi mitatu hii wanaishije? Kama kuna vizimba kwa ajili ya watu wetu tutakubaliana nalo. Tunamuomba Waziri uandae majibu mazuri, kwamba ndani ya miezi mitatu hii tunapofunga Ziwa, wavuvi wetu, wafanyabiashara wadogo ambao wanategemea mazao ya samaki na sisi wananchi ambao tunategemea tupate kitoweo, tunaishije ndani ya miezi hii mitatu? Tunaomba tupate alternative ndiyo hapo tutakapounga mkono jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza hii ni Serikali yetu na ni Serikali sikivu, kama jambo hili ni kwa manufaa wavuvi kwa nini tusiambiwe mapema? Kwa nini msisikilize ushauri wetu? Kwa nini msitake maoni yetu? Kwa hiyo mimi niseme tu, Mheshimiwa Waziri wewe ni Kaka yangu na ninakuheshimu sana na wewe unajua mimi nakuheshimu sana, lakini katika jambo hili la kufunga Ziwa bila kutushirikisha wananchi, hapana hatuko tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana jioni tumesikia maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, mwaka jana Tarehe 03 Novemba, Mheshimiwa Waziri Mkuu alizuia suala la herein, ukisoma taarifa ya Wizara utaona Tanzania ni ya pili Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, lakini ukifuatilia kwenye suala la uuzaji wa mifugo yetu nje, Tanzania tunazidiwa na nchi ambazo hata haziko kwenye top 10. Hii yote inatokana na sababu mifugo yetu bado haina quality ya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa kama tuko kisiwani, Waziri Mkuu kaongea vizuri na mimi ningependa niishauri Serikali kwamba changamoto ya hereni ilikuwa ni bei ya hereni, lakini kama Serikali itafanya utaratibu mzuri ambao hautakuwa na changamoto kwa wafugaji, jambo hili lina tija ili kuongeza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema, ameongea hapa Mheshimiwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, watu wa Tanganyika, watu wa Ziwa Tanganyika, watu wa Mkoa wa Kigoma, Rukwa na Katavi tunaomba Serikali ichukulie jambo hili kwa uzito sana, tunaomba Serikali ije na majibu mazuri itueleze ni amna gani tunaenda kumaliza suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Uwekezaji Viwanda na Biashara. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha leo kusimama katika Bunge lako Tukufu. Kwa namna ya pekee sana namshukuru Rais wetu, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyopambana kutengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji wetu wa ndani na nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na mambo mawili tu ambayo ningependa nichangie asubuhi ya leo. Tunapoiangalia Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara sisi wawakilishi wa vijana tunaziona ajira, tunaona ndiye mkombozi wa changamoto zetu sisi vijana. Nitaongelea kuhusu ubunifu kidogo.

Mheshimiwa Spika, bado tunaona kuna changamoto katika Wizara hii. Bado hatuna mikakati, wala mpango ambao unawezesha vijana wetu wabunifu na wavumbuzi. Nasema haya kwa sababu moja, mbili au tatu. Katikati hapa, miaka miwili, mitatu hii, kumetokea vijana wavumbuzi wengi. Tumeona vijana wamevumbua local radios, wamevumbua magari, matrekta na ubunifu mbali mbali, lakini bado hatujaona mwendelezo wa bunifu zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Mkoa wetu wa Kigoma kuna kijana amevumbua local radio, lakini hatuoni mwendelezo wa ubunifu wa kijana yule. Hatuoni Serikali inapoingia kumsaidia kijana yule kuendeleza ubunifu wake. Bado Serikali haijaweka mikakati mizuri ya kuwasaidia wabunifu wetu wa ndani. Hapa Waheshimiwa Wabunge wameongea vizuri, kama ambavyo wabunifu wa pombe wameelezwa, na kama ambavyo wabunifu wa magari wameelezwa, lakini bado hatuna mikakati ya kuendeleza bunifu zao.

Mheshimiwa Spika, naongea haya kwa sababu, ilitokea hapa mwaka 2021, kuna kijana mmoja alivumbua radio, lakini cha kushangaza, badala ya kusaidiwa kwenda mbele zaidi, tukasikia kijana yule kapelekwa Form Five na Six. Sasa unajiuliza, kwa kijana mbunifu, kijana ambaye amekaa, ametengeneza wazo, nini kilipaswa kufanyika? Kumwendeleza katika wazo lake, au kumpeleka shule akasome Form Five na Six ambayo haimsadii sana kama wangeendeleza ubunifu wake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili napenda kushauri, sisi kama Wizara tuje na mkakati wa incubation centers. Tunaposema incubations centers, hivi viwe vituo vya wavumbuzi na wabunifu. Tukiwachukua hawa wavumbuzi na wabunifu tukawaweka pamoja, kwanza inakuwa rahisi kuwapa elimu, kuwaendeleza na pia hata tukiamua kuwapa uwezeshaji wa kimitaji ni rahisi kuwa- manage na kuwafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, incubation centers hizi zitatusaidia. Wizara inapokuja kutoa taarifa, inaweza kutuambia, katika miaka miwili hii tumepokea wabunifu sita, tumewaendeleza hivi, wamefikia hapa, na mchango wao kwa Taifa ni huu. Leo Wizara inaweza isiwe hata na database ya wabunifu kwa sababu bado mikakati na mipango hatujaiweka vizuri. Kwa hiyo, nashauri sana Serikali kuhusu suala la incubation centers. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ukisoma ukurasa wa 11 na wa 10 wa Hotuba ya Waziri, ameeleza vizuri namna ambavyo Serikali imejitahidi sana kuwasaidia wazalishaji wa zabibu. Nami nachukua nafasi hii kuwapongeza, kwa ambacho mmekisema mmewasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo moja, ukiangalia wazalishaji wa zabibu, hata kama Serikali inasema imewapatia soko kwenye viwanda vidogo vya hapa Dodoma, bado changamoto ya soko ni kubwa sana. Nasema haya kwa mambo makubwa mawili; sijui kama Mheshimiwa Waziri ana taarifa, viwanda hivi vidogo ambavyo mnasema Serikali imewasaidia wakulima wa zabibu, kwamba bado vinashindwa kuwalipa wakulima wa zabibu kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mkulima wa zabibu analima mwenyewe, akimaliza kulima anapeleka kiwandani zabibu zake, lakini inamchukua zaidi ya miezi nane mpaka mwaka kuweza kupata pesa yake. Pesa yenyewe anaipata kwa awamu na kidogo kidogo. Leo mkulima huyu amepeleka kiwandani zabibu za shilingi milioni mbili, anaambiwa leo anapewa shilingi 200,000, anaambiwa uje baada ya miezi miwili upewe shilingi 300,000, uje baada ya mwezi upewe shilingi 100,000. Kwa mazingira hayo, wakulima hawawezi kupenda kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nini kifanyike hapa? Pamoja ya kuwa mmewatafutia soko kwa viwanda hivyo, bado viwanda haviwalipi wakulima kwa wakati. Ukiongea na wamiliki wa viwanda, changamoto yao ni uwezo mdogo. Kwa hiyo, kwa sababu changamoto ni uwezo mdogo, hawawezi kuchukua zabibu zote na kuwalipa kwa wakati. Nini kifanyike? Kwanza naishauri Serikali iweze kuwasaidia hawa wamiliki wa hivi viwanda vidogo iweze kuwapatia mikopo ya uwekezaji. Hatuwezi kuwasaidia viwanda hivi kama tutawapa mikopo ya kibiashara, haiwezekani. Kwa sababu mikopo ya kibiashara ina riba kubwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iingilie kati jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuliko kutumia nguvu kubwa kuanzisha mashamba mapya, ni bora kutumia nguvu hiyo kwenda kuwawezesha watu ambao tayari wapo site, wanafanya shughuli hizo. Hii itawasaidia waone umuhimu wa kilimo na kuhamasisha wengine. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, nguvu kubwa inayotumika kuanzisha mashamba mapya ni bora itumike nguvu hiyo kuwasaidia watu ambao tayari wapo site na wana changamoto ya kukuza mitaja yao ili waweze kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda sana niongelee SIDO, kwa sababu sisi kama vijana tulitamani na tulifikiria ingeweza kuwa mkombozi wetu, lakini Mheshimiwa Waziri bado una haja ya kupitia hizi SIDO, kwani nyingi hali zao ni tete. Sisi Kigoma pale na Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni alienda pale kuzindua kiwanda cha kuchakata mafuta, lakini ukikiangalia kiwanda kile utaona, bado kiwanda kile hakina level ya kiwanda cha kisasa. Bado mzunguko wake ni mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hatutawekeza nguvu kubwa kwa SIDO, kama hatutatoa pesa kuwekeza SIDO, bado tutaendelea kuagiza vitu nje, bado tutaendelea kuagiza mashine nje na SIDO haitakuwa na umuhimu tena. Leo ninavyoongea hivi, Watanzania wengi hawafanyi biashara na SIDO tena, wanaenda zao kuagiza vitu nje. Kuliko niagize kitu SIDO, kitu chenyewe bado ubunifu wake au teknolojia yake ni ya kizamani, bora niagize zangu kitu tu nje kwa haraka na gharama nafuu, lakini pia kinakuwa kiko updated. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iwekeze nguvu sana katika SIDO ili vijana wengi wapate ubunifu huko na itusaidie kupata mashine nyingi, vijana wengi waweze kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, ukiona mtu mzima analia, ujue kuna jambo. Jana nimesikiliza michango ya Wabunge wa Mkoa wa Tanga, na nimesikiliza michango ya Wabunge wengi, nikajiuliza kunani Tanga? Ikabidi nifuatilie. Nimeenda kusoma hukumu ya Fair Competition Tribunal nikabaki najiuliza. Hivi kweli katika nchi inayoongozwa na sheria, nchi inayofuata mifumo ya sheria, nchi kama hii ya kwetu, hivi chombo cha Serikali kinapata wapi ujasiri wa kupingana na maamuzi ya Mahakama? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana atakapokuja Mheshimiwa Waziri atuweke wazi, aondoe hii sintofahamu iliyokuwepo, atuelezee jambo hili ili tuweze kulielewa. Pia kuna haja sana ya sisi kama Watanzania kufuata sheria zetu. Tumeweka za nini kama tuna sheria na bado hatuwezi kuzifuata? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mungu Mwingi wa Rehema kwa kuniwezesha kusimama katika Bunge lako hili tukufu. Nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri kaka yangu Masauni na Naibu Waziri, kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana na tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kuipongeza Serikali. Sasa hivi askari wetu wanapokuwa kwenye mafunzo haya ya refresher course mambo ni mazuri. Serikali imechukua suala lile la chakula na sasa hivi inaligharamia Serikali. Tunaipongeza sana Serikali na waendelee kufanya hivyo ili askari wetu wafanye kazi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ulinzi wa raia na mali zao tumewapa jukumu hili Jeshi la Polisi. Ni ukweli usiofichika Jeshi la Polisi wanafanya kazi kubwa sana, lakini mazingira yao ni magumu mno. Leo ukienda Mkoa wa Kigoma, ukienda Wilaya ya Kibondo ukaambiwa hizi ndizo nyumba za askari, utatoa machozi, lakini utaungana na mimi Wabunge hapa wanasimama kila mmoja anaelezea makazi ya askari, makazi ya askari. Mimi naomba nikuombe Mheshimiwa Waziri, utakapokuja kumalizia hapa hebu tupe mkakati wa Serikali ni namna gani tunaenda kukabiliana na hili jambo la nyumba za askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuchangia kuhusu hii inaitwa Police General Order (PGO). Kama kuna changamoto ambayo polisi wanakutana nayo basi ni hii PGO. PGO hii imeanzishwa zaidi ya miaka kumi iliyopita, na huenda lengo lake lilikuwa zuri, kuwapa motisha askari, lakini jambo hili kulingana na mazingira ya sasa limekuwa tena halina uhalisia na hivyo ni wakati mwafaka sasa wa kufanya mapitio yahii PGO. PGO hii ni sheria zinazoongeza Jeshi la Polisi, na zimekuwa zimeeleza mambo mengi sana. PGO hii ina kurasa zaidi ya 900 lakini mimi nitaomba nijielekeze kwenye PGO namba 132. PGO hii namba 132 inazungumzia posho za askari. PGO hii imeeleza posho nyingi ambazo askari anastahili kupewa. Kuna posho ya pango, kuna posho ya mavazi, kuna posho ya upelelezi, kuna posho ya utaalam lakini kuna posho nyingine nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini masikitiko yangu ni kwamba posho hizi haziendani na uhalisia wa sasa kwa mfano, ukizungumzia posho ya pango inasema askari atapewa asilimia kumi ya mshahara. Huenda kwa kipindi hicho ilikuwa ina maana sana. Leo kwa askari anayepata mshahara wa laki tano asilimia kumi ni shilingi elfu 50, sasa uniambie ni nyumba gani askari atapata kwa shilingi 50,000? Hii haiwezi kukubalika. Lakini PGO hii haijaeleza ni namna gani hii posho wanapewa. Sasa ninashauri Serikali tufanya mapitio, tupitie hii ili tutoe utaratibu rasmi ni namna gani askari wanapata posho hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunazungumza hapa, unapozungumzia suala la posho ya mavazi, maisha yamebadilika kila mmoja anafahamu. Miaka kumi iliyopita leo uhalisia ni tofauti…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE.SYLVIA F. SIGULA: …leo unampa posho ya mavazi askari, unasema posho ya mavazi apewe shilingi 30,000, kwa mavazi gani atakayo nunua?

Mheshimwia Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe, ni wakati sasa Mheshimiwa Waziri wa kufanya mapitio ya hii PGO kwa sababu ina mambo mengi mengi sana ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la rushwa kwa askari polisi. Mimi nilikaa nikatafakari sana, lakini nikaona kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya rushwa kwa askari na uhaba au ufinyu wa mishahara yao. Haiwezekani leo upate mshahara ambao hauwezi kukidhi mahitaji yako. Kitakachofanyika ni nini? Kwa hiyo mimi niombe Mheshimiwa Waziri, ni wakati sasa wa kuboresha maslahi, ni wakati sasa wa kuboresha mishahara ya askari ili nao waweze kufanya vizuri. Tusikae kuwalaumu rushwa, rushwa, rushwa wakati maslahi yao ni madogo. Mwaka jana ilitembea video hapa ya askari amechukua elfu kumi kama rushwa …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia.

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti,lakini askari yule ile video ilinitoa machozi. Askari yule elfu kumi ile alipewa adhabu kali, alifukuzwa kazi lakini leo ukisoma ripoti ya CAG kuna wezi wa mabilioni bado wako ofisini. Hili jambo haliwezekani. Kwa hiyo mimi niombe Mheshimiwa Waziri, askari wanafanya kazi kubwa sana na wanafanya kazi ngumu sana hebu ifikie hatua tuwape thamani yao. Ikitokea kesho askari wakagoma ndio utaelewa kwa nini askari ni muhimu katika nchi hii.

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, malizia.

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Tuna amani sasa kwa sababu askari wanafanya kazi yao vizuri. Naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu Mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa wazima wenye afya na tuko hapa tunajadili bajeti ya Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kutuletea maendeleo Watanzania. Nisibaki nyuma, nimpongeze Naibu Waziri Mkuu ambaye ni Waziri wa Nishati kwa kweli amefanya kazi kubwa sana, hotuba ni nzuri hata sisi wenyewe wachangiaji tunaona kama hotuba imesheheni kila kitu. Kwa namna ya pekee sana nampongeza Naibu Waziri wetu, Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge kijana, Mbunge mahiri, Mbunge msikivu, anapokea simu, anajibu message na anatusikiliza sana Waheshimiwa Wabunge wenziwe. Nampongeza sana Mheshimiwa Judith Kapinga, sisi vijana wenzake ametuheshimisha, tunamupongeza sana, sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najielekeza kwenye mchango wangu na nitachangia maeneo mawili. Nitachangia upande wa gesi asilia, lakini pia nitachangia eneo la umeme. Kwenye gesi asilia hapa, nitazungumzia mambo mawili, nitazungumzia gesi ya magari, lakini pia nitazungumzia gesi ya majumbani. Mheshimiwa Rais alianzisha kampeni ya kumtua mama kuni kichwani, kampeni ambayo Wizara waliitendea vizuri, tumeona matamasha makubwa yamefanyika. Wananchi wamegawiwa mitungi ya gesi, Waheshimiwa Wabunge hapa, kila mmoja jimboni kwake ameenda kugawa mitungi ya gesi. Hakika hilo ni jambo kubwa sana ambalo limefanyika tunampongeza Mama Samia na pia tunawapongeza Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilikuwa na ushauri kwenye hii gesi ya majumbani. Tunafahamu kabisa vipato vya Watanzania ni vidogo sana na tunafahamu kabisa wananchi wamehamasika na wako tayari kutumia nishati safi ya kupikia. Changamoto yao ni moja, kwanza, ni gharama ya hizi gesi. Pia, huko mitaani gunia la mkaa ni shilingi 20,000 mpaka shilingi 30,000. Leo ukienda mtaani kuna mkaa wa shilingi 2,000, ule mkaa wa shilingi 2,000 unatosha kupikia siku nzima. Naishauri nini hapa Wizara? Sisi kama Wizara inabidi twende mbele zaidi, kwa sababu Watanzania wamehamasika kutumia gesi. Tunatamani kuona tunakuja na mpango ambao hautamlazimisha mtumiaji wa gesi awe na shilingi 25,000 apate mtungi wa kilo sita. Tunatamani kuona mpango ambao hautamlazimisha mtumiaji wa gesi awe na shilingi 58,000 aweze kupata mtungi wa kilo 15. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani kuona, kama ilivyo kwa magari, leo mtu mwenye gari siyo lazima aweke full tank, unaenda petrol station na shilingi 15,000 unaweka mafuta ya shilingi 15,000, mafuta ya shilingi 20,000, mafuta ya shilingi 30,000. Tunatamani kuona tunakuja na mpango ambao tutapata ujazo tofauti tofauti ili watu wote, leo nikiwa na shilingi 3,000 nyumbani kwangu niweze kwenda kununua gesi ya shilingi 3,000 nipikie ikiisha nikanunue tena. Ukichukua hii shilingi 25,000 kwa mtungi wa kilo sita ni wastani wa shilingi 4,000 kwa kilo moja. Sasa kama mtu anaweza akawa na shilingi 4,000 akaenda kuweka kilo moja na akaweza kupikia hiyo itaturahisishia sana sisi Watanzania kuondokana na matumizi mabaya ya nishati na kwenda kwenye nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye gesi za magari, tumeona Watanzania wamehamasika na naipongeza Wizara tumeona kwenye hotuba zaidi ya magari 3,000 yamebadilisha mfumo wa gesi. Tunasema, Watanzania wanatamani kuendelea kutumia gesi kwenye magari yao kwa sababu gesi ni gharama nafuu. Changamoto inakuja, tumeona mna mpango wa kuongeza vituo lakini bado vituo ni vichache, foleni inakuwa kubwa kusubiri gesi. Pia, bado vifaa vya kubadilishia mifumo ni gharama sana ambavyo vinafanya ubadilishaji wa mifumo uwe bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiwa na gari yako unataka kubadilisha mfumo kwenda kwenye mfumo wa gesi siyo chini ya shilingi milioni mbili, kwa hiyo, gharama hizi bado ni kubwa. Kwa hiyo, naishauri Serikali ione namna nzuri ya kufanya ili Watanzania wengi magari yao yafunge mfumo wa gesi. Tunaweza tukapunguza kodi kwenye vifaa hivi vya kubadilishia mfumo. Tunaweza kuwashirikisha wadau wa sekta binafsi wakawekeza katika mifumo hii ya kubadilisha magari yetu kwenda kwenye mfumo wa gesi, ili magari ya watu wengi yabadilishwe kwenda kwenye mfumo wa gesi, wapunguze matumizi ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejiuliza hapa, sijaona Serikali kama yenyewe ndiyo inasema inasimamia jambo hili, hamasa ipi inatupa kama Serikali? Wao kama Serikali ni magari mangapi ambayo tayari yana mfumo wa gesi? Wao kama Serikali wameanza kitu gani kutuonesha kwamba now wako serious na jambo hili. Kwa hiyo, ningependa sana kuona jambo hili linachukuliwa kwa uzito wake hasa na Wizara na Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia pia kuhusu umeme. Tumekuwa na phase nyingi za mabadiliko ya matumizi ya umeme. Tulianza na mafuta, tukaja na gesi kwa zaidi ya 65%, sasa hivi tumeenda kwenye maji, lakini ukiangalia gharama za umeme bado ziko juu. Leo kwa zaidi ya miaka mitano unit moja ya umeme bado bei ni ile ile. Tulitarajia kwa kuwasha mitambo hii ambayo imewashwa basi gharama za umeme zingepungua walau hata kidogo. Leo mwananchi ananunua unit moja kwa shilingi 350 lakini tulitarajia kwa sababu gharama za uzalishaji zimepungua, tunatarajia kuona na gharama za umeme zinapungua ili kuleta unafuu kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaambia vijana wajitokeze, wafanye biashara, waanzishe viwanda vidogo vidogo, wanahamasika lakini bado gharama za umeme ziko juu. Kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati waliangalie jambo hili kwa kina. Tunatamani kuona vijana wengi wanafanya biashara, wanajiajiri, tunaomba waliangalie jambo hili kwa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuendelea pia kwenye suala la umeme, umeme wa REA. Tumeona hapa kila Mbunge anayesimama anasema REA, wanafanya kazi nzuri lakini mimi binafsi nasimama hapa kwa masikitiko makubwa. Sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa bado jambo hili halijafanyika vizuri. Sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa bado tuna vijiji havijafikiwa na umeme. Sasa haiwezekani Wabunge hapa wanasema kwamba umeme umefika, tuna umeme mwingi mpaka mashine zinazimwa lakini bado sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuna vijiji havijafikiwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkandarasi Rukwa tumempa vijiji 141 na mkataba wake ulikuwa uishe tarehe 30 Mwezi Desemba, 2023. Mpaka inafika Mwezi wa Desemba bado hajakamilisha vijiji 40. Akaomba aongezewe muda, tumemwongezea muda mpaka Mwezi Machi, Mwezi Machi umefika bado vijiji vile 40 havijafanyiwa kazi. Sasa hivi tena kaomba aongezewe muda mpaka Mwezi Juni. Sasa haiwezekani, huyu mkandarasi JV Pomy Engineering and Qwihaya Enterprises wanatukwamisha sana Wanarukwa. Haiwezekani leo wananchi wanaambiwa umeme upo, umeme unatosha lakini kuna vijiji bado havijafikiwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma maoni ya Kamati ya tangu mwaka jana na mwaka huu wanapendekeza hawa wakandarasi ambao hawafanyi vizuri Serikali ione namna nzuri ya kushughulika nao. Sisi wananchi Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu wala hatujui chochote tunachotaka ni umeme. Hatujui wao hawajalipana, tunachotaka ni umeme. Sasa huyu Mkandarasi tangu mwaka jana hajamaliza, ameongezewa muda hajamaliza. Wananchi mpaka leo hawana matumaini kama huo Mwezi Juni umeme utakuwepo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sylvia unaweza kuhitimisha tafadhali.

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu atakapokuja kutoa majibu ya hitimisho, sisi wananchi wa Rukwa tunataka kujua hatma ya hivi vijiji 40, ni lini hasa tutakuwa tumepata umeme wa uhakika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)