MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunafahamu kabisa shughuli ya usafirishaji ni moja kati ya sekta zinazotoa ajira nyingi kwa vijana, hasa bodaboda. Pia kumekuwa na tabia hii ya askari wetu wa Jeshi la Polisi kuwakimbiza vijana wetu wa bodaboda pale wanapovunja sheria za barabarani, hali inayosababisha ajali na vifo kwa bodaboda pamoja na abiria:-
Je, ni lini Serikali itatoa tamko kwa Jeshi la Polisi kuhusu namna nzuri ya udhibiti wa sheria hizi badala ya mfumo huu wa kuwakimbiza ili kupunguza idadi ya ajali na vifo kwa bodaboda na abiria? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylivia, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bodaboda ni miongoni mwa vyombo vya usafiri vinavyotumia moto, kwa maana ya mtambo ambao unatumia moto katika kuendesha chombo hicho. Vyombo vyote vya moto vimewekewa kwenye sheria katika uendeshaji wake. Kwanza kila dereva lazima awe na leseni; lakini pili, chombo hicho lazima kiwe na bima. Kwa chombo kama bodaboda dereva anatakiwa kuwa amevaa helmet ili aweze kuendesha. Hayo ni matakwa ya kisheria na wasimamizi wa sheria ni hawa makamanda wetu wa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, sasa nimemsikia Mheshimiwa Mbunge akisema wanawakimbiza, sina uhakika sana na hilo la kukimbiza, lakini yapo matukio kwa kamanda mmoja mmoja, inategemea na mazingira hayo yaliyowafikisha katika kukimbizana, lakini hakuna utaratibu wa kuwakimbiza madereva hata pale ambapo wanatenda makosa. Tumeweka utaratibu wa makamanda kufanya ukaguzi na ili ufanye ukaguzi wanatoa alama ya kumsimamisha yule dereva ili ajiridhishe kama vigezo vyote hivi ameweza kuvifikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunatambua watu wanaposimamishwa na makamanda wetu wengine wanapita. Sasa wanapopita hawa wanakuwa na mawasiliano na anapopita anajua anavunja sheria, kwa hiyo utakuta mtu anaongeza moto anakimbia akidhani anakimbizwa kumbe anakimbia mwenyewe halafu anapata ajali. Sasa hilo nalo pia halikubaliki sana kama imetokea mmoja akaamua kumkimbiza dereva, lakini muhimu zaidi tunahitaji madereva wote wanaoendesha vyombo vya moto kuzingatia sheria ambazo ziko na sisi Wabunge tumezitengeneza hapa na wasimamizi wetu ni hao askari polisi ambao ni trafiki.
Mheshimiwa Spika, muhimu zaidi tuendelee kutoa wito kwa waendesha bodaboda kuzingatia sheria. Serikali imeridhia bodaboda hii iwe chombo cha usafirishaji na ni fursa kwa vijana wetu kutumia kama sehemu ya mradi, kama biashara kusafirisha abiria hapa na pale; wazingatie sheria hizi ili wafanye kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumeweka utaratibu mzuri sana ambao hauhitaji vijana hawa wawe wanakurupushwa huko maeneo mbalimbali. Halmashauri zetu tumezipa maelekezo kuwakutanisha hawa vijana, kuwaandalia mazingira mazuri, kuwapa elimu na Jeshi la Polisi liko kulekule kwenye wilaya na lenyewe lihusike katika kuwapa elimu na kuona namna nzuri ya kuwahudumia ili wafanye kazi hiyo ya kusafirisha abiria na waendelee kupata mitaji yao.
Nimeona katika halmashauri mbalimbali kupitia Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi, wakiita vikao vya madereva bodaboda kuwaanzishia umoja wao, kuwaelimisha namna ya kuendesha biashara zao ili kuondokana na hayo malalamiko yanayojitokeza ya askari kukimbizwa. Hata hivyo, pale ambapo inatokea polisi anamkimbiza bodaboda, huo siyo utaratibu, badala yake ni muhimu kuendelea kutoa elimu. Tunatoa agizo kwa maaskari wetu kuendelea kutoa elimu kwa vijana wetu wanaofanya biashara ya bodaboda na wote wako kwenye maeneo hayo ili tuwe na uelewa wa pamoja katika kutekeleza sheria hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi likitimiza wajibu wake wa kutoa elimu na kusimamia sheria, lakini hawa kwa sababu ni wengi na wengi wanaanza kujifunza na wanaingia kwenye biashara, wakipata hiyo elimu nao wazingatie haya ili kupunguza hizo ajali. Nadhani tukifanya hilo tutafika mahali pazuri pa kila mmoja kufanya kazi yake kwa weledi mkubwa; Jeshi la Polisi lifanye kazi yake, bodaboda afanye kazi yake, kila mmoja atimize wajibu wake. Ahsante sana. (Makofi)