Primary Questions from Hon. Sylivia Francis Sigula (14 total)
MHE. VUMA A. HOLLE K.n.y. MHE. SYLIVIA F. SIGULA aliuliza:-
Je, nini Mpango wa Serikali kuhakikisha kuwa Timu ya Taifa Stars inafanya vizuri katika Michezo ya Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa Timu za Taifa ikiwemo Taifa Stars zinafanya vizuri katika mashindano mbalimbali, kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imeendelea kuboresha maandalizi ya timu zetu kwa kutenga fedha za kuzihudumia timu hizi. Mipango mingine iliyowekwa na Serikali ni ile ya muda mrefu na muda mfupi. Mipango ya muda mfupi ni pamoja na:-
(a) Kushirikiana na TFF katika maandalizi ya kambi za Timu ya Taifa ndani na nje ya nchi.
(b) Kuongeza motisha kwa kutoa posho na bonasi kwa wachezaji na benchi la ufundi la Timu ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya muda mrefu ni pamoja na:-
(a) Kuwekeza katika michezo ya UMITASHUMTA, UMISSETA.
(b) Kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo nchini.
(c) Mazungumzo yanaendelea kati ya Wizara yetu na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha fedha hizi zinatengwa.
(d) Kuanzisha shule maalum za michezo katika kila mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango mingine ya Serikali iliyopo ni ushirikiano kati ya Wizara yangu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya TAMISEMI juu ya uendeshaji bora wa michezo nchini na mipango ya uanzishaji wa tahasusi za kidato cha Tano zenye somo la michezo.
MHE. SYLIVIA F. SIGULA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wavuvi wa Ziwa Tanganyika wavue kisasa ili kupata kipato zaidi na kutoa ajira kwa vijana?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiaw Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Sylivia Francis Sigula, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika juhudi za kusaidia na kuwezesha wavuvi wadogo kuvua kisasa, Serikali imerahisisha utaratibu wa kupata zana za kisasa za uvuvi. Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vingi vya uvuvi ikiwemo engine za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu, nyavu za uvuvi na vifungashio kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2011 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato ya mwaka
2014 ili kuwasaidia wavuvi kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vilevile, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ili wavuvi wapate mikopo ya masharti na riba nafuu kutoka katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa maana TIB. Aidha, Wizara kupitia Dawati la Sekta Binafsi imeviunganisha vyama vya ushirika vya wavuvi na taasisi za fedha ambapo mikopo iliyoombwa na kupitishwa ni shilingi bilioni 2.6 na mikopo iliyotolewa ni shilingi milioni 560.7. Pia Wizara imehamasisha Benki ya Posta kuanzisha na kuzindua Akaunti ya Wavuvi kwa ajili ya mikopo na bima mahususi kwa wavuvi hususan wavuvi wadogo.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali wa kutoa ajira rasmi na zisizo rasmi kupitia tasnia ya Sanaa?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu katika Wizara hii mpya ya Utamaduni Sanaa na Michezo, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mjawa wa kadiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini kwa mara nyingine na kuniteua katika Wizara hii. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Rais kwamba Wizara yetu hii pamoja na watendaji wa Wizara tutajipanga kweli kweli ili matamanio yake aliyokusudia katika Wizara hii yaweze kutimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, kwanza kwa kutambua mchango wake kwa vijana. Amekuwa na mchango mzuri kwa vijana, nasi kama Wizara tunampongeza sana kwa kuwasemea vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kutambua kwamba swali lake ni la msingi na la muhimu sana, ili kuwavutia wadau hasa vijana kujiajiri katika Sekta ya Sanaa, mpango wa Serikali ni kuendelea kuboresha mazingira ya kazi za sanaa kwa kufanya mambo kadhaa. Moja ya mambo makubwa ambayo tunakwenda kuyafanya ni: -
Kwanza, ni kuhakikisha vifaa na vitendea kazi vya sanaa vinapatikana kwa bei nafuu kwa kufanya mapitio kwenye kodi za vifaa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tutakwend kupitia upya tozo kwenye Kanuni za BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu Tanzania ili ziwe rafiki kwa walipaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, tutakwenda kuanzisha mifumo mbalimbali ya kieleketroniki ya usajili, ambayo mingine tunayo lakini tutakwenda kubuni na kuendeleza mingine ya maombi ya vibali na leseni pamoja na mfumo rasmi wa ukusanyaji mirabaha kutoka kwa watumiaji wa kazi za sanaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, tutakwenda kujenga miundombinu ya sanaa kama vile Arts Arena, National Art Gallery na One Stop Center, ambayo tayari tunayo inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tunakwenda kuanzisha Mfuko ambao utakaokuwa ni suluhisho la kimitaji na mafunzo kwa wadau wa Sekta ya Sanaa.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Bandari Kavu katika Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Bandari Kavu umepewa kipaumbele katika Mpango Kabambe wa Mamlaka ya Bandari Tanzania ulioanza 2009 na utaisha 2028. Mpango huo umeziainisha Bandari Kavu za King’ori iliyoko mkoani Arusha, Ihumwa (Dodoma), Inyala (Mbeya), Shinyanga (Isaka), Fela (Mwanza), Katosho (Kigoma), Kwala (Pwani) na Songea kuwa bandari za kipaumbele kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa shehena katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia TPA imetenga fedha kwa ajili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa bandari hizo ikiwemo ya Katosho ilioko mkoani Kigoma. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2023. Kukamilika kwa kazi hiyo kutapelekea manunuzi ya Mkandarasi wa ujenzi wa bandari hiyo ambayo ni muhimu kwa kuhudumia shehena za nchi jirani za ukanda wa Ziwa Tanganyika. Ahsante.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa madarasa katika Kampasi ya Chuo cha Uvuvi Kibirizi utaanza?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kupitia kampasi ya Kibirizi ulianza kutoa mafunzo ya muda mrefu ya tasnia ya uvuvi mwaka 2013/2014 kwa kutumia majengo ya kilichokuwa Kiwanda cha Mashua Kigoma ambacho kilikuwa katika eneo la Kibirizi. Hivyo, kwa sasa kampasi ya Kibirizi inatoa mafunzo ya teknolojia ya ukuzaji viumbe maji (aquaculture technology) katika ngazi za Astashahada na Stashahada kwa kutumia madarasa yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha Kampasi ya Kibirizi kwa kujenga madarasa mapya na kuipatia vitendea kazi ili iweze kutoa mafunzo zaidi ikiwemo masomo ya sayansi na teknolojia ya uvuvi (fisheries science and technology) na usimamizi wa uvuvi (fisheries management) ngazi za Astashahada na Stashahada, ahsante.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea na mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, sambamba na mapitio ya Mitaala ya Elimu katika ngazi zote.
Mabadiliko haya ya Sera na Mitaala yamelenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za kazi, stadi za maisha za karne ya 21 ambazo ni fikra tunduizi, ubunifu, ushirikiano, uongozi pamoja na stadi za mawasiliano na teknolojia ya habari kwa lengo la kuwajengea uwezo wahitimu kukabiliana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali upande wa Vyuo vya Kati na Vyuo vya Ufundi Stadi, Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTVET) linaendelea na maandalizi ya Occupational/Professional Standards ambazo zitatoa mwogozo katika mabadiliko na maandalizi ya mitaala inayokidhi mahitaji ya sasa na baadae. Vilevile, kwa upande wa Elimu ya Juu tayari Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) inaendelea kukusanya maoni ya wadau kuhusu ubora wa elimu inayotolewa na Vyuo Vikuu pamoja na kutoa mafunzo kwa Wahadhiri katika maandalizi ya mitaala inayozingatia mahitaji ya ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia ujuzi na mafunzo?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (SIDO), lenye ofisi katika Mikoa yote nchini hadi kufikia Februari 2023, imeratibu na kutoa mafunzo na ujuzi kwa wajasiriamali wapatao 12,091, ambapo wanaume walikuwa 5,082 sawa na asilimia 42 na wanawake 7,009 sawa na asilimia 58 kupitia kozi 519 katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na uendelezaji wa biashara na shughuli za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kutoa mafunzo na ujuzi katika nyanja mbalimbali kwa wajasiriamali nchini. Aidha, Serikali imepanga kuongeza wigo wa kutoa mafunzo ya biashara na ufundi pamoja na ushauri kwa kutumia TEHAMA. Nakushukuru.(Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, lini SACCOS 130 za wanawake na vijana zitaanzishwa katika mikoa 16 ikiwemo Kigoma kama ilivyoainishwa katika Ilani ya 2020/2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, ninaomba kujibu swali Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imewezesha kuanzishwa kwa jumla ya SACCOS 41 kwenye Mikoa 16 zikiwemo SACCOS 03 za Mkoa wa Kigoma. SACCOS hizo ni Kasulu Women SACCOS yenye wanachama 100 ikiwa na mtaji wa milioni 44, Vijana Kidahwe SACCOS yenye wanachama 20 ikiwa na mtaji wa milioni 14, na Amani Wanawake SACCOS yenye wanachama 33 ikiwa na mtaji wa milioni 21.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha Mikoa ikiwemo Mkoa wa Kigoma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kuanzisha na kuzisimamia SACCOS kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ili ziendelee kutoa huduma inayokusudiwa.
MHE. SLYVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, ni lini Vyama vya Maendeleo ya Ushirika vya zao la mchikichi vitaanza kufanya kazi katika Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Slyvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma una Vyama vya Msingi vya Ushirika wa Kilimo na Masoko 14 (AMCOS) vya zao la michikichi katika Halmashauri za Wilaya za Kigoma vipo tisa, Kigoma Manispaa viwili, Uvinza viwili na Buhingwe kimoja ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendeleza zao la michikichi.
Mheshimiwa Spika, vyama hivyo vimeshaanza kufanya kazi na kwa sasa vipo katika hatua ya kupata mkopo wa shilingi bilioni 2.9 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) utakaowezesha kuboresha mashamba ya wakulima, miundombinu ya uhifadhi mikungu ya michikichi, mashine za uchakataji na ukamuaji wa mafuta ya mawese.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza:-
Je, Wavuvi wangapi Ziwa Tanganyika wamewezeshwa na shilingi ngapi zimetumika kuwawezesha?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatekeleza mradi wa kukopesha vyombo vya uvuvi kwa wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi katika maeneo yote yenye uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na Ziwa Tanganyika. Mradi huu unalenga kuwawezesha wavuvi boti za kisasa na vifaa vyake ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi, kipato chao na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya kwanza ya mradi huo, kwa upande wa Ziwa Tanganyika, makundi yaliyowezeshwa boti za kisasa ni vyama vya ushirika viwili vyenye idadi ya wanachama 169, vikundi viwili vyenye idadi ya wanachama 17 na wavuvi binafsi watano ambapo wamekabidhiwa jumla ya boti tisa zenye thamani ya shilingi 596,762,192.72.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga vipi kuendana na kasi ya uboreshaji Bandari ya Dar es Salaam?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara, pamoja na majukumu mengine iliyonayo, ina majukumu mahsusi ya kusimamia maendeleo ya viwanda na biashara, kuendeleza miundombinu ya viwanda na kukuza mauzo ya bidhaa nje na ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kufuatia uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kama ifuatavyo: -
(i) Kuimarisha na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mahitaji ya usafirishaji wa bidhaa za mazao kwenda sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi;
(ii) Kuimarisha Kamati za Pamoja Mpakani na Asasi za Wafanyabiashara ili kurahisisha ukaguzi wa pamoja wa bidhaa na mazao;
(iii) Kutoa usaidizi kwa wafanyabiashara wadogo wanaonufaika na itifaki ya Soko la EAC, SADC na AfCFTA ili kuharakisha ufanyaji biashara mipakani; na
(iv) Kuanza maandalizi ya Mpango Kabambe wa Ujenzi wa Viwanda kwa Mwaka 2025/2026 hadi 2030/2031 wenye lengo la kuhamasisha uwekezaji nchini.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi zitasaidia kuharakisha ufanyaji wa biashara kupitia usafirishaji na kuhakikisha kwamba uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na miundombinu mingine ikiwemo Reli ya SGR italeta faida kubwa za kiuchumi na kijamii hapa nchini, ahsante sana.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. SYLVIA F. SIGULA aluliza: -
Je, nini chanzo cha ongezeko la wagonjwa wa figo nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la magonjwa ya figo hapa nchini kwa sasa yanachangiwa zaidi na sababu zifuatazo: -
(i) Ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza hususani shinikizo la damu pamoja na kisukari;
(ii) Matumizi holela ya dawa hasa zile za maumivu;
(iii) WAVIU wasiokuwa na ufuasi mzuri wa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI;
(iv) Kutozingatia mtindo wa maisha unaofaa hususani matumizi makubwa ya chumvi, tabia bwete na matumizi ya vilevi hasa pombe na tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuielimisha na kuiasa jamii kuhusu kujikinga kwa kubadili mtindo wa maisha ambao unajumuisha ulaji usiofaa hususani matumizi makubwa ya chumvi, vyakula vyenye sukari nyingi au nafaka zilizokobolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imeimarisha huduma za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza pamoja na matibabu ya UKIMWI ili kuzuia madhara haya yasijitokeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka vizimba Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika ziwa huanza kwa kuainisha maeneo yanayofaa kwa kuzingatia vigezo vya kitaalamu na kisheria kwa lengo la kulinda ikolojia ya ziwa. Mpaka
sasa Serikali kwa kushirikiana na taasisi ya The Nature Conservancy imeainisha maeneo matano yanayofaa kwa ufugaji wa samaki kwa vizimba katika Ziwa Tanganyika. Maeneo hayo ni Katabe, Kalalangabo, Kirando, Kimbwela na Kigalye. Aidha, katika mwaka 2023/2024, Wizara imetenga kiasi cha jumla ya shilingi 233,500,000 kwa ajili ya kuendelea kuainisha maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) itatoa mkopo wa masharti nafuu kwa vizimba 29 kwa vikundi na watu binafsi walioomba na kukidhi vigezo. Mgawanyo wa vizimba hivyo ni kama ifuatavyo: Kigoma vizimba 25, Rukwa vizimba viwili na Katavi vizimba viwili.
Mheshimiwa Spika, aidha, zoezi hili ni endelevu ambapo katika mwaka 2024/2025, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo itaendelea kutoa mikopo kwa vikundi na wananchi ambao wataomba na kukidhi vigezo vya mkopo wa vizimba.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DEUS C. SANGU K.n.y. MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza:-
Je, Serikali inawasaidia vipi wakulima ambao mazao yao yameharibiwa na mafuriko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapenda kuwapa pole waathirika wote wa mafuriko yaliyotokana na mvua za El-Nino zilizonyesha katika msimu wa mwaka 2023/2024 katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Mikoa ya Manyara, Morogoro, Pwani na Mbeya. Kufuatia athari hizo, Serikali imechukua hatua za haraka na za muda mfupi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kusaidia waathirika kwa kuwapatia msaada wa kibinadamu ikiwa ni pamoja na chakula. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2024, Serikali ilisambaza jumla ya tani 1,043.34 za mahindi ya chakula katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya awali ilionesha takribani ekari 75,594 za mazao ziliharibiwa katika mikoa iliyoathirika na mafuriko, ili kuwezesha wakulima katika maeneo hayo kuendelea na shughuli za kilimo, Serikali kwa kushirikiana na wadau imetoa msaada wa pembejeo ikijumuisha tani 70 za mbolea, tani 5.6 za mbegu bora za mahindi, maharage, ngano na alizeti. Maandalizi ya kusambaza mbegu za mahindi tani 748.4 na mpunga tani 449 yanaendelea kwa ajili ya Halmashauri za Wilaya ya Kibiti na Rufiji kwa msimu wa 2024/2025. Serikali itaendelea kufuatilia hali ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na usalama wa chakula katika maeneo yote na kuchukua hatua stahiki. (Makofi)