Supplementary Questions from Hon. Sylivia Francis Sigula (20 total)
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa majibu mazuri ya Wizara lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imerahisisha upatikanaji wa vifaa, lakini pia tumeona vijana wengi wamejitokeza na wamehamasika kuingia katika sekta ya uvuvi na wengi wameunda vikundi, lakini hawajapatiwa mafunzo, lakini pia hawana vifaa vya kisasa vya kuvulia.
Je, ni lini kauli ya Serikali kwa vijana ambao wamejiunga kwenye vikundi na wamekidhi vigezo lakini awajapatiwa vifaa vya kuvulia na mikopo?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili tunaona kabisa kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba mahitaji ya wavuvi wa Tanzania na yaliyopitishwa ikiwa ni 2.6 bilion lakini hela iliyotolewa ni milioni 500 plus ambayo hii ni chini ya asilimia 25.
Je, ni nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha tunaongeza kipato hiki hili wavuvi wakaweze kupata tija na uvuvi uweze kuwa na tija kwa nchi hii kwa kuongeza ajira kwa vijana na kipato cha Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylivia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uniruhusu pia nimpongeze Mheshimiwa Sylivia kwa umahiri na uhodari wake wa kufuatilia masuala ya wavuvi hasa vijana wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya mafunzo na uwezeshaji wa makundi haya ya vijana yaliyokwisha kuanzishwa, tunacho chuo chetu cha uvuvi kilichopo pale Kigoma Mjini kwa maana ya Kibirizi, nataka nimhakikishe ya kwamba tutahakikisha chuo kile kinayafikia makundi yote haya, namuomba Mheshimiwa Mbunge aniwasilishie vikundi vile vya Ziwa Tanganyika kimoja baada ya kingine tutakifia kwa mafunzo na tutakifikia katika kukiwezesha hasa kupata mashine ya boti, hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni juu ya kuongeza mikopo kwa tasnia hii ya uvuvi. Serikali hususani Wizara ya Mifugo na Uvuvi tulifanya jitihada ya makusudi ya kuanzisha Dawati la Sekta Binafsi na sasa limefanya kazi kubwa kabla ya kuanzishwa kwa Dawati la Sekta Binafsi Idara ya Uvuvi ilipata mikopo sawa na sifuri kwa wavuvi wadogo na baada ya kuanzishwa tumeipandisha mpaka kufikia milioni 560.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wanawakilisha wavuvi katika Bunge hili Tukufu kwamba mkakati wetu ni kuimarisha zaidi Dawati la Sekta Binafsi kimkakati, kwa ajili ya kuweza kuiwezesha sekta hii iweze kupata pesa zaidi, maandiko ya vikundi hivi vya wavuvi tutayapitia na kuyawezesha yaweze kuweza kushawishi benki kuweka pesa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini na mkakati wetu wa pili ni bima ya wavuvu; pamekuwa na mgogoro wa muda mrefu juu ya kuweza kupata bima kwa ajili ya wavuvi na wafungaji. Dawati la Sekta Binafsi tumefika mahala kuzuri hivi sasa Shirika letu la Bima la Taifa linakwenda kutupelekea kupata bima ya wavuvi na bima ya mifugo ili sasa mabenki yaweze kuwa na appetite ya kutoa pesa zaidi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa ni jukumu la Serikali kukuza, kuibua na kuendeleza sanaa nchini, tunatambua kuna vijana wengi sana nchini wana vipaji, lakini wanashindwa kuvitumia vipaji vyao kulingana na mazingira magumu yaliyopo ya kufanya vipaji hivyo na huenda vipaji hivyo vingeweza kuwapatia ajira.
Je, ni nini mpango wa Serikali wa kuibua, kuendeleza na kusimamia vipaji hivi vya vijana walioko katika nchi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunatambua kwamba kuna taasisi na watu binafsi wanaofanya matamasha ya kuibua vipaji: -
Je, ni nini kauli ya Serikali katika kuwaidia hizi taasisi au watu binafsi wanaofanya matamasha na jitihada za kusaidia kuinua vipaji Tanzania?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylvia kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na maswali ya msingi ambayo yalijieleka moja kwa moja kwenye swali la kwanza ambalo limeulizwa kama swali la nyongeza, Wizara yetu inajipanga vyema kutafuta vijana wenye vipaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwataarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba mimi na wasaidizi wangu tumejipanga kupita katika kila mtaa ili kuweza kutafuta vijana wenye vipaji mbalimbali. Pia, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali imejipanga vizuri; na Mheshimiwa Rais tayari ameshaanzisha mfuko maalum ambao utawasaidia vijana wenye vipaji.
Kwa hiyo, tutapita kila mtaa, kila kijiji, kila wilaya, kila halmashauri katika kila mkoa kuhakikisha kwamba tunawasaka vijana wenye vipaji na kuweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili linalozungumzia matamasha yanayofanywa na baadhi ya watu na taasisi, sisi kama Wizara hatutakuwa na jambo dogo. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Wizara haitakuwa na jambo dogo, kila jambo litakuwa na uzito wake. Kwa hiyo tutashiriki katika kila kitu kinachofanyika kinachohusu utamaduni, sanaa na michezo ambacho wenzetu katika taasisi mbalimbali wamekuwa wakitusaidia Serikali.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwanza kwa majibu mazuri ya Wizara, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Katosho wamepisha eneo la ujenzi wa bandari ya nchi kavu kwa zaidi ya miaka sita sasa na majibu haya ya usanifu yamekuwa yakitolewa kwa zaidi ya miaka sita na kuwaumiza sana wananchi: Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuharakisha huu upembuzi yakinifu ili eneo hilo lifanyiwe kazi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ili bandari ya nchi kavu iweze kuwa na tija kwa Taifa lazima kuwe kuna miundombinu wezeshi ikiwemo uwepo wa reli, uwepo wa meli, uwepo wa mabehewa ya kutosha na barabara za uhakika. Ukizingatia Mkoa wa Kigoma bado tuko nyuma sana kimiundombinu: -
Mheshimiwa Spika, nini mpango wa Serikali kuhakikisha miundombinu wezeshi inatekelezeka ili bandari hii iwe na tija?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba bandari hii imechukua muda mrefu, lakini tangu mwaka 2019 tulijenga uzio ama ukuta wa eneo hili. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Kigoma kwamba ifikapo Aprili mwakani 2023 upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unakwenda kukamilika na tayari tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bandari hii.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili angependa kufahamu miundombinu wezeshi katika kufanikisha bandari yetu kavu na miundombinu hiyo wezeshi ni pamoja na reli, barabara na kupata mzigo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, bandari hii kavu tayari ipo karibu kabisa na bandari nyingine ya Kigoma, pia ipo karibu kabisa na barabara kuu inayokwenda Kigoma Mjini. Pia tumewaelekeza mamlaka ya bandari nchini pamoja na TRC, wapo kwenye majadiliano kwa ajili ya kupeleka reli ili iwe rahisi kupeleka mzigo utakaokuwa unahudumiwa na nchi rafiki na nchi jirani kati ya Congo, Rwanda, Burundi pamoja na Zambia. Ahsante.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tatizo la MSD kutokuleta dawa kwa wakati katika Mkoa wa Kigoma, hata wakileta wanaleta chini ya asilimia 50.
Je, nini kauli ya Serikali katika kutatua changamoto hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli anachosema Mheshimiwa Mbunge na kama nilivyosema jana na nimerudia leo kwamba shida siyo fedha ni pale MSD Idara ya Manunuzi kumekuwa na tatizo ambalo Wabunge mmekuwa mkielezea.
Mheshimiwa Spika, siyo Kigoma tu nilikwenda Mkoa wa Lindi waliomba madawa 102 lakini ziko item 55 wakapewa Tano, kwa hiyo kuna tatizo kwenye eneo la manunuzi na ndilo ambalo mmekuwa mkizungumzia.
Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na wenzetu tutaenda kulishughulikia. (Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kibondo hakina hadhi ya kituo cha wilaya maana ni kidogo sana lakini pia ni chakavu mno. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo hicho ili kiwe na hadhi ya wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunafahamu kituo cha Kibondo ni kidogo kwa size lakini pia ni chakavu kinahitaji kufanyiwa ukarabati. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Jeshi la Polisi mpango wa kukarabati kituo hicho kimewekwa katika Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2023/2024 kwa hiyo ukae kwa subira kwamba mwaka ujao tukipitisha bajeti hapa kituo hicho pia kitakuwa kimezingatiwa.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Kigoma Mjini wameahidiwa mradi mkubwa wa maji kukamilika tangu mwaka 2020 na sasa tuko mwaka 2023 na mradi haujakamilika.
Je, ni nini kauli ya Serikali kwa wananchi wa Kigoma Mjini kuhusu mradi huo mkubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sylvia, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mradi Kigoma Mjini, mimi mwenyewe nimefika mwezi Novemba, mradi upo kwenye hatua za mwisho kabisa na maji yataanza kutoka hivi punde.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tatizo sugu la kukatika katika kwa umeme Mkoani Kigoma hasa katika Wilaya ya Kigoma Mjini na Kigoma Vijijini, mara zote umeme unakatika bila hata taarifa na kusababisha hasara kwa wananchi.
Je, ni nini maelekezo ya Serikali katika kutatua changamoto hiyo ili kupunguza hasara kwa wananchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sylvia Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma ni mmojawapo ya Mikoa ambayo haijafikiwa na gridi ya Taifa, lakini ziko njia tatu zinazopeleka umeme wa gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kigoma na mojawapo ilielekezwa na Kiongozi wa Kitaifa Mheshimiwa Makamu wa Rais, kwamba ifikapo Oktoba mwaka huu iwe imekamilika ambayo ni ya kutoka Tabora kupita Uhuru - Nguluka kwenda mpaka Kidahwe.
Mheshimiwa Spika, kazi hiyo inaendelea kufanyika na tunataratijia kabla mwaka huu haujaisha kazi hiyo itakuwa imeisha, tunatarajia itaweza kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wetu wa Kigoma badala ya kutumia zile mashine za mafuta ambazo ziko kwa sasa na zinashindwa kuzalisha umeme wa kutosha kwa wananchi wetu wa Kigoma na hivyo mambo yatakuwa mazuri kabisa.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Wizara, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; uchumi wa vijana wengi wa Mkoa wa Kigoma unategemea sana uvuvi, na sasa hivi tunashukuru kwa sababu tumeanza usafirishaji wa samaki kutoka ndani kwenda nje. Lakini kumekuwa na changamoto, pamoja na kuwa na hiki chuo bado kuna tatizo kubwa la ubora wa samaki wetu kukidhi kwenye masoko ya nje na ndani na chuo hiki kinatoa kozi moja.
Je, Serikali haioni sasa ni muda mwafaka wa kuongeza kozi ya fish processing, quality assurance and marketing ili tuweze kupata wataalam wengi wa kusimamia ubora wa samaki wetu ili kupunguza hasara kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri yuko tayari kuongozana na mimi au Mbunge wa jimbo husika kwenda katika chuo hiki kuona hizi changamoto yeye mwenyewe? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua umuhimu wa vijana kuingia katika tasnia hii ya uvuvi hasa vijana wa Mkoa wa Kigoma kwa sababu ya mazingira waliyonayo ya Ziwa Tanganyika. Chuo chetu hiki cha Kibirizi kiko kwenye eneo dogo na sisi kama Wizara tunachukua hatua za makusudi kutafuta eneo lingine kwenye Manispaa hiyo hiyo ya Kigoma ili tuweze kukipanua chuo hiki kiweze kutoa mafunzo zaidi kwa vijana hawa ikiwa ni pamoja na kozi aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la kufika Kigoma ili kuweza kuona mazingira halisi, niko tayari kuambatana naye.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu suala la elimu ni suala nyeti katika Taifa letu, ni muda sasa Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa mapitio na watoto wetu wanaendelea kutumia mtaala huu ambao hauna tija kwao. Ni lini hasa utekelezaji utaanza rasmi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, vijana wengi wameathiriwa na mfumo huu ambao hauna tija, wengi wapo mtaani na wanashindwa afanye nini kwa elimu walioipata. Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuwasaidia vijana hawa ambao tayari ni wahanga wa mfumo wetu huu wa elimu pale tutakapobadilisha mfumo rasmi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylvia, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishaeleza kwenye majibu ya swali la msingi kwamba kwa upande wa upitiaji wa mitaala Serikali tayari tumekamilisha rasimu ya mitaala pamoja na sera yetu, hivi sasa tupo katika hatua za kurudisha tena kwa wadau lakini vilevile katika mamlaka mbalimbali ambazo zitathibitisha au zita- approve mitaala hiyo. Mara tu mchakato huo utakapokuwa umekamilika tunataraji mitaala hii itaanza kutumika rasmi kwenye ngazi zote za elimu hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili, anazungumzia kwamba tayari kuna wananfunzi ambao walitumia mitaala ile ya zamani. Naomba nimuhakiishie tu Mheshimiwa Mbunge, utaratibu wa upitiaji wa mitaala pamoja na sera ni suala endelevu ni suala ambalo linatokea mara kwa mara pale tunapoona tu kuna mahitajji ya mabadiliko ya mitaala pamoja na sera, Serikali imekua ikifanya hivyo ili elimu inayotolewa ilingane au iendane na mazingira halisi ya kazi au mazingira halisi ya dunia inavyokwenda. Vilevile utaratibu wetu au sera yetu ya elimu inampa wasaha yule mhitimu kuweza kujiendeleza au kwenda maeneo mengine na kupata elimu zaidi ambayo itaendana na mazingira yale ambayo anafanyia kazi. Ninakushukuru sana.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni ukweli usiofichika kwamba SIDO zetu nyingi zinafanya kazi chini ya kiwango na hiyo ndiyo maana unaona hata idadi ya wanufaika ni wachache. Je, nini mpango wa Serikali wa kuziwezesha SIDO hizi ili ziweze kuwanufaisha wajasiriamali wengi zaidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wajasiriamali wengi wanashindwa kumudu gharama za mafunzo haya. Je, Serikali iko tayari kuweka wazi na kutoa maelekezo kwa SIDO zote nchi nzima kutoa mafunzo haya bure na kuweka mwongozo wazi wa namna gani mafunzo haya yanafanyika katika SIDO zetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kweli, niungane na hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna changamoto ya bajeti kidogo kwa Shirika letu la SIDO lakini sasa ni mpango wa Serikali kuona baada ya kuongeza katika sekta nyingine, ni dhahiri tutakuja kwenye sekta hii ya viwanda ambapo SIDO ni wadau muhimu sana kuhakikisha wanaendeleza na kufanya kazi zao kwa weledi wakiwa na bajeti ya kutosha. Kwa hiyo, Serikali imejipanga kuongeza fedha ili waweze kuongezewa SIDO waweze kufanya kazi zao zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni kweli tungeweza kutoa bure mafunzo lakini lazima kuna gharama ndogo ambazo wajasiriamali wanatakiwa kuchangia. Hoja kubwa hapa ni kuona namna gani tunawawezesha SIDO ili wawe na fedha za kutosha na gharama za wajasiriamali kuchangia kupata mafunzo ziwe chini zaidi au hatimaye yaweze kutolewa bure kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tangu mwaka 2010 tuliahidiwa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Nyarubanda, lakini zaidi ya miaka 12 mpaka leo ujenzi haujaanza: Nataka kujua, ni lini hasa ujenzi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huu katika Kata ya Nyapanda utaanza kadiri ya upatikanaji wa fedha. Tutaangalia katika bajeti hii ambayo inakuja ya 2023/2024 kama haijatengewa, basi tutaangalia kutenga fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mkoa wa Kigoma ni kati ya Mikoa iliyobarikiwa kuwa na vyanzo vikubwa vya maji lakini bado suala la umwagiliaji halijapewa kipaumbele. Nataka kujua, wananchi wa Kasulu, Buhigwe na Uvinza ni lini watanufaika na miradi hii ya umwagiliaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba yetu ya bajeti kiambatisho namba tano tumeyatamka mabonde 22 ambayo tunakwenda kuyafanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya umwagiliaji. Bonde mojawapo ni Bonde la Mto Malagarasi ambalo lina hekta 7000 na litahudumia eneo la Buhigwe, Kasulu pamoja na Uvinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika eneo la Kasulu tuna miradi miwili pale ambayo tunaifanyia kazi katika mwaka ujao wa fedha mradi wa Ahsante Nyerere na Kilimo Kwanza ambayo ina jumla ya hekta 3,500 ipo ndani ya mpango itafanyiwa kazi na wakulima wa Kigoma watafanya kilimo cha umwagiliaji.
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali na niishukuru kwa majibu mazuri. Tunashukuru kwa hizo milioni mia tano kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Wilaya ya Kibondo kata ya Nyaruyoba hakuna Kituo cha Afya na wananchi wanahangaika. Tumeahidiwa milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa wodi.
Je, ni lini Serikali itatuletea milioni 200 hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili Wilaya ya Buhigwe kata ya Mbanga na Kata ya Mhinda hakuna Vituo vya Afya, wananchi wanatembea umbali mrefu kupata huduma.
Je, ni lini Serikali itajenga Vituo vya Afya katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Sigula; la kwanza hili la Nyaruyoba kule Wilayani Kibondo milioni mia mbili, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuwasiliana na idara ya afya katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kuona fedha hizi zilizo ahidiwa zinaweza kwenda mara moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya kule Wilayani Kibondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili, tutafanya tathmini kule Wilayani Buhigwe na kuona vituo hivi vya afya alivyoviomba Mheshimiwa Sigula kama vina kidhi vigezo vya kuweza kupandishwa hadhi na kuwa vituo vya afya ili tuweze kutenga fedha katika mwaka wa fedha unaofata kwa ajili ya kuanza ujenzi wake mara moja.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini kutokana na majibu ya Serikali utaona kabisa bado tuko kwenye asilimia 31.5 ya utekelezaji, hii inaonesha bado kazi inatakiwa kufanyika. Nataka kujua ni nini mkakati maalum wa Serikali, kuhakikisha wanawake wengi na vijana wengi wanapata uelewa na umuhimu wa masuala haya ya SACCOS ili waweze kujiunga wajikwamue kiuchumi?
Swali la pili, kulikuwa na VICOBA vingi vya wakinamama na vijana. Je, Serikali iko tayari kuviwezesha vitambulike rasmi ili viingie kunufaika kwenye mikopo ya asilimia 10 katika mfumo huu mpya unaokuja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylvia Sigula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza la mkakati maalum wa Serikali kwa ajili ya kutoa elimu kwa wingi zaidi ili kufahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya na Majiji na Halmashauri za Miji, zina utaratibu na watumishi waliokuwa kule Maafisa Biashara, Maafisa Maendelo ya Jamiii pamoja na Maafisa Ushirika. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba wanasajili vikundi vingi zaidi au SACCOS nyingi zaidi kwenye maeneo yao na kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa SACCOS hizi. Hivyo basi, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaelekeza tena Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya hapa nchini kuhakikisha hawa niliowataja Maafisa Biashara, Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Ushirika wanafanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuweza kutoa elimu juu ya umuhimu kuwa na SACCOS na kusajili SACCOS nyingi ambazo zinakidhi vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la VICOBA kutambuliwa zaidi na kupewa mikopo. Hili linategemeana vilevile na wao VICOBA kukidhi vigezo vile vya masharti ya mikopo ile ya asilimia 10. Hata katika mapitio yanayofanyika kwa maelekezo yake Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, juu ya utoaji wa mikopo hii bado mikopo hii itakuwa ni ya vijana, wanawake na walemavu. Kinachofanyika ni review ya namna ya utoaji wa mikopo ile, siyo ubadilishwaji wa namna mikopo ile inavyotolewa kwa watu. Kwa hiyo, kama vikundi hivi vitakuwa vinakidhi vigezo, VICOBA hivi kwamba vina vijana, vina wanawake na walemavu, vinatakiwa pia kunufaika na mikopo ile inayotolewa. Kwa hiyo, tutazingatia hili pia katika timu ile inayofanyia mapitio haya ili waweze kuongeza SACCOS nyingi zaidi. (Makofi)
MHE. SLYVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Wizara na tunashukuru kwa kupata hizo shilingi bilioni mbili tunaishukuru sana Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uhaba wa mafuta ulioko nchini na hamasa iliyofanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wananchi wa Kigoma wamehamasika sana katika kuingia kwenye zao la michikichi lakini kumekuwa na uhaba wa upatikanaji wa miche ya michikichi inafikia hatua mche mmoja unauzwa hadi shilingi 5,000.
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kutoa ruzuku ya miche ya michikichi katika vyama hivi vya ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Slyvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kwamba tutoe miche bora ya michikichi kwa wakulima wa Mkoa wa Kigoma ili kuongeza uzalishaji na ninavyozungumza ni kwamba zoezi hili linaendelea katika Kambi ya JKT Bulombola, lakini vilevile pamoja na Gereza la Kitwanga ambapo jumla ya mbegu zilizozalishwa mpaka hivi sasa ni milioni tisa na miche iliyopo kwenye viriba ambayo bado kugaiwa milioni moja, lakini kwa wananchi tumeshagawa miche 970,000 ikiwa ni elekezo la Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge haya ni maelekezo ya wananchi hawa watapatiwa miche hii bure, isipokuwa tu kwa sharti la kwamba lazima wawe katika mashamba makubwa ili tuweze kui-trace miche hii na kuona inaleta tija katika nchi yetu.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ukanda wa Ziwa Tanganyika yaani Mkoa wa Kigoma, Rukwa na Katavi tumesubiri kwa muda mrefu ukarabati wa meli ya MV Liemba. Je, ni lini Serikali itakamilisha ukarabati wa meli ya MV Liemba ili kunusuru usafiri huo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimwa Mwenyekiti, Serikali ya awamu ya sita imejipambanua katika kutenda. MV Liemba ni kiungio kubwa la Ziwa Tanganyika na wananchi wote wanaotumia ziwa hilo. Tumekwishasaini mkataba mwaka jana mwezi Novemba na ndani ya mwaka mmoja tutakuwa tumeshakamilisha ukarabati na ili Wananchi wa Kigoma na maeneo jirani wasubiri kwa hamu tunakwenda kukamilisha meli yao.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ukanda wa Ziwa Tanganyika yaani Mkoa wa Kigoma, Rukwa na Katavi tumesubiri kwa muda mrefu ukarabati wa meli ya MV Liemba. Je, ni lini Serikali itakamilisha ukarabati wa meli ya MV Liemba ili kunusuru usafiri huo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimwa Mwenyekiti, Serikali ya awamu ya sita imejipambanua katika kutenda. MV Liemba ni kiungio kubwa la Ziwa Tanganyika na wananchi wote wanaotumia ziwa hilo. Tumekwishasaini mkataba mwaka jana mwezi Novemba na ndani ya mwaka mmoja tutakuwa tumeshakamilisha ukarabati na ili Wananchi wa Kigoma na maeneo jirani wasubiri kwa hamu tunakwenda kukamilisha meli yao.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa majibu mazuri. Vile vile naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia. Wote ni mashahidi, tumeona juzi amefanya kazi kubwa sana ya kukabidhi boti zaidi ya 160, haijawahi kutokea! Hakika hii ni kubwa na Mama apewe maua yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri utaona kabisa Ziwa Tanganyika wamewezeshwa boti tisa, na Ziwa Tanganyika linahudumia mikoa mitatu; Kigoma, Katavi na Rukwa. Uwiano huu ni mdogo sana: Je, nini mkakati wa Serikali wa kuongeza boti katika ukanda wa Ziwa Tanganyika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Ziwa Tanganyika tuna uhaba wa vizimba; je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuwapatia wavuvi wa Ziwa Tanganyika vizimba ili kuboresha Sekta ya Uvuvi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na hili la mpango wa Serikali wa kuongeza vizimba na maboti yote yanakwenda kwa pamoja. Ni kweli kwamba Ziwa Tanganyika ni Ziwa kubwa linalohudumia mikoa mingi na idadi ya boti zilizotoka mpaka sasa ni chache. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshatoa maelekezo kwamba wale wote wanaohitaji boti na vizimba waendelee kuomba na Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo waendelee kuomba Wizarani na Wizara iko tayari kuwahudumia, kuwagawia boti hizo kupitia benki yetu ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale wenye uhitaji, wanahamasishwa kwenda kuonana na Maafisa Uvuvi, wawasaidie kuandika maandiko mazuri yatakayowawezesha kupata hiyo mikopo ili waweze kujiendeleza kwenye Sekta yao ya Uvuvi. Ahsante.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Wilaya ya Nkasi, Kata ya Itete ina vijiji vinne na havina kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Kata ya Itete?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, tulikwishaelekeza halmashauri kuainisha maeneo ya kimkakati ya kata zile ambazo zinakidhi vigezo vya kuwa na vituo vya afya kwa kuzingatia idadi ya wananchi, umbali kutoka kituo cha afya cha Jirani, lakini pia hali ya kijiografia ya eneo hilo. Kwa hiyo, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutawasiliana na Halmashauri ya Nkasi na Mkoa wa Rukwa tuweze kuona kama wanakidhi vigezo, baada ya hapo tuweke mipango ya ujenzi wa kituo hicho, ahsante
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali na naishukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, bado kuna changamoto kubwa ya ucheleweshwaji wa mizigo bandarini. Kuna wakati unakuta zaidi ya meli 20 ziko zinasubiri kushusha mzigo. Je, Wizara hii kwa kuwa inahusika na wafanyabiashara, haioni kama kuna haja ya kukaa na TPA na mwekezaji kuona namna nzuri ya kutatua hii changamoto ya ucheleweshaji wa mizigo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunaipongeza sana Serikali kwa uboreshaji wa Bandari. Ukanda wa Ziwa Tanganyika tunaona kuna Bandari ya Kalema, tunaishukuru sana Serikali, lakini Wizara hii haioni kuna haja ya kuwa na mpango maalumu wa kuwaandaa wafanyabiashara vijana, wakulima na wavuvi ili kuitumia Bandari hii ya Kalema kufanya biashara ili kuingiza pato kwa Taifa na pato la mtu mmoja mmoja? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Sylvia Francis, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli hivi karibuni baada ya kupata uteuzi, niliamua kukaa na wafanyabiashara kubaini changamoto zao. Miongoni mwa jambo ambalo walibainisha ni suala hilo kwamba mizigo sasa hivi inachelewa. Hata hivyo, Serikali hivi sasa ina mchakato mpana, hili ni jambo la mpito tu, siyo muda mrefu watu wataona kuna transformation kubwa sana inafanyika na shughuli za usafirishaji mtaona zimeboreka sana katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hata juzi nilipotembelea Bandari ya Tanga, wengine wanaanza kusema sasa hivi kuna mabadiliko makubwa yanapitia katika Bandari ya Tanga. Kwa hiyo, naomba kuwahakikishia Watanzania kwamba kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Uchukuzi na Serikali kwa ujumla, siyo muda mrefu mtaona mapinduzi makubwa katika suala zima la usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima la Kalema kwamba ni jinsi gani tutahamasisha vijana kuletewa utaratibu mzuri, ni jukumu letu hili. Naomba niwaombe Watanzania kwamba, hivi karibuni tumeamua sasa kuja na mpango mkubwa sana na hasa mpango huu utahusisha makundi mbalimbali ikiwemo makundi ya vijana. Kwanza, suala zima la kuweka programu kwanza ya viwanda, lakini kuhakikisha kurahisisha mchakato wa kusafirisha mizigo maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Watanzania, hili jambo tutalibeba kwa nguvu zote na muda siyo mrefu sana mtaona tunakuja na kazi kubwa sana ya kuwasaidia Watanzania. Lengo letu ni kwamba tufanye reform katika maeneo mbalimbali ambayo itawasaidia Watanzania katika viwanda na halikadhalika katika biashara na hasa katika hii milango yetu ya bandari tulizokuwanazo za baharini na katika maziwa yetu tuliyokuwanayo. Ahsante sana. (Makofi)