MHE. JANEJELLY J. NTATE K.n.y. MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:-
Je, utekelezaji wa Azimio la kuwa na Sarafu moja ifikapo 2024 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI (MHE. DENNIS L. LONDO) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kujibu swali kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Spika, pia, namshukuru Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani yake kwangu. Vile vile nakushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Bunge lako kwa malezi na usimamizi wangu.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Tarimba Gulam, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sarafu ya Afrika Mashariki ni moja ya kati mambo muhimu ya utekelezaji katika hatua za Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliojikita katika nguzo nne ambazo ni Soko la Pamoja, Umoja wa Forodha, Umoja wa Fedha na Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika, kupitia utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi wanachama zilikubaliana kutekeleza mpango wa miaka 10 ili kufikia azma ya Umoja wa Fedha na Sarafu Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ifikapo 2024. Katika kipindi cha miaka 10 kabla ya kufikia umoja wa fedha na sarafu nchi jumuiya zilitakiwa kutekeleza kikamilifu hatua za awali za mtangamano ambazo ni ushirikiano katika soko la pamoja na umoja wa forodha.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuanzisha taasisi muhimu za kusimamia utekelezaji wa umoja wa fedha na kutimiza au kufikia vigezo vya kuoanisha uchumi mpana. Vigezo vya kuoanisha uchumi mpana vilivyokubalika ni kiwango cha juu cha mfumuko kisizidi asilimia nane; kiwango cha juu cha nakisi ya bajeti kisizidi asilimia tatu ya pato la Taifa; kiwango cha juu cha deni la Taifa kisizidi 50% ya pato la Taifa; na akiba ya fedha za kigeni ya kutosheleza mahitaji ya miezi minne na nusu.
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako, tathmini ya mwaka 2022 ilionesha kuwa, nchi Jumuiya za Afrika Mashariki bado zilikuwa hazijatekeleza kikamilifu hatua za awali za mtangamano. Aidha, tathmini hiyo ilibainisha kuwa nchi nyingi zilishindwa katika vigezo vya kuoanisha uchumi mpana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, hadi sasa Tanzania ni nchi pekee katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokidhi vigezo vinne kati ya vitano vya kuoanisha uchumi mpana ambavyo vimekubaliwa na Jumuiya hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko na changamoto za kiuchumi duniani na uhaba wa miundombinu muhimu, nchi wanachama zimeshindwa kufikia malengo ya kuwa na sarafu moja katika mwaka uliopita 2024. Kutokana na tathmini hiyo, mpango wa awali umehuishwa na muda wa utekelezaji umeongezwa hadi ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)