Primary Questions from Hon. Maryam Azan Mwinyi (19 total)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI Aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kuwa na Mtaala mmoja kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne kati ya Tanzania Bara na Zanzibar? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana vizuri na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika masuala mbalimbali ikiwemo suala la elimu hususan katika utekelezaji wa mitaala na kutoa elimu bora kwa watoto wa kitanzania.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mitaala ya elimu kati ya Tanzania Bara na Visiwani, pande zote mbili hutumia mtaala mmoja kuanzia Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Sita. Ahsante.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha uzalishaji wa zao la Vanila nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la vanila hulimwa kwa wingi katika Mikoa ya Kagera, Morogoro, Tanga, Mbeya, Arusha na Kilimanjaro ambapo uzalishaji umekuwa ukiongezeka kutoka tani 229 mwaka 2015 hadi kufikia tani 1,949 mwaka 2020. Katika kuhamasisha uzalishaji wa zao la hilo, Wizara ya kilimo imefanya tathmini ya kutambua wadau na masoko ya vanila ndani na nje ya nchi na kuzifahamu changamoto zinazokabili zao hilo ikiwemo upatikanaji wa mbegu bora. Wadau wakubwa wa vanila ni pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu Umoja wa Wazalishaji wa Viungo (Tanzania Spice Producer Association), Chama cha Wakulima wa Viungo vya Amani, Chama cha Maendeleo ya Wakulima (MAYAWA), Taasisi ya Kilimo Endelevu SAT, Ushirika wa Wazalishaji Viungo wa Mtamba lakini Kiwanda cha Natural Extract Limited kilichopo Mkoani Kilimanjaro na Chama cha Wazalishaji wa Vanila Mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali itaongeza upatikanaji wa miche bora ya vanila nchini kwa kuhamasisha wazalishaji wa ndani na kuandaa utaratibu wa kuingiza miche bora kutoka nje ya nchi. Pia Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhamasisha uendelezaji wa zao la vanila na mazao mengine ya viungo kwa kutoa mbinu bora za kilimo cha vanila ili kujadili maendeleo ya tasnia ya viungo. Hadi kufikia Machi, 2021 jumla ya wakulima 1,387 wa zao la vanila wamepatiwa mafunzo ya kanuni na mbinu bora za uzalishaji. Aidha, katika kuimarisha huduma za ugani kwa zao hilo, Maafisa Ugani 20 wamepatiwa mafunzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Utafiti cha TARI – Tengeru kinafanya utafiti wa mazao ya bustani likiwemo zao la vanila na viungo. Kituo hicho kimeanza ukusanyaji wa vinasaba vya mazao likiwemo zao la vanila kwa ajili ya kufanya utafiti wa aina bora za vanila ili kuboresha uzalishaji. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha International Trade Centre imeandaa mfumo maalum wa kutambulisha mazao ya viungo yanayozalishwa Tanzania katika masoko ya nje. Vilevile, Serikali itaendelea kusimamia mikakati yote inayolenga kuongeza uzalishaji tija na kuboresha mazigira ya biashara ya zao la vanila na mazao ya viungo.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia wavuvi elimu ya uelewa kuhusu madhara ya uvuvi haramu ili wasifanye aina hiyo ya uvuvi na kuharibu mazingira ya maziwa na bahari nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii ya kujibu maswali, lakini kwanza naomba nami nimshukuru Mwenyezi Mungu; na pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini katika Wizara hii kwa nafasi hii ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo ya shukrani, naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kuwa ni muhimu sana kuwapatia wavuvi elimu kuhusu madhara ya uvuvi haramu ili wasifanye uvuvi haramu na tuweze kulinda rasilimali za uvuvi nchini. Katika kutekeleza jukumu hili, Serikali imekuwa ikitoa elimu hiyo kupitia vipindi vya redio, runinga, mikutano, vipeperushi, semina na maonesho mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wataalam wa Wizara wamekuwa wakitoa elimu kwa kuwafikia wavuvi na wadau wengine moja kwa moja katika maeneo yao ambapo kwa mwaka 2021/2022 mikoa ambayo tayari imefikiwa ni mikoa ya Tanga, Pwani, Mwanza, Mara, Kagera na Katavi. Ahsante sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuunda Kikosi Kazi kuratibu Mikataba ya mazingira na mabadiliko ya Tabianchi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Kusini Pemba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa mikataba mbalimbali ya Kimataifa ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira ambayo inaratibiwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, utaratibu unaotumika katika kuratibu masuala ya mikataba ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wa kushirikiana katika majadiliano ya pamoja na kushiriki katika mikutano ya Kimataifa na utekelezaji wa Mikataba hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutekeleza program na miradi mbalimbali ya hifadhi na usimamizi wa mazingira inayotekelezwa chini ya mikataba husika.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuwapatia vifaa vya kisasa wananchi wanaofanya shughuli za kukausha dagaa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inatarajia kujenga vichanja 80 vya kukaushia dagaa (drying racks), kununua mitambo minne ya umeme ya kukaushia dagaa (electric drier) na Solar Tents 15 katika Halmashauri za Kilwa, Mafia, Pangani na Bagamoyo katika mwaka wa fedha 2023/2024. Pia Wizara itaendelea kuwahamasisha na kuwaunganisha Wajasiriamali wa Sekta ya Uvuvi ili waweze kupata mikopo nafuu kupitia TADB itakayowawezesha kununua zana bora na za kisasa za kuendesha uvuvi endelevu, biashara yenye tija ya mazao ya uvuvi na matumizi ya vifaa vya kisasa vya kukaushia dagaa.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa adhabu kali kudhibiti vifo vya akina mama vinavyosabishwa na waume au watoto wao?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Kanuni ya Adhabu imeweka adhabu ya kosa la mauaji ya kukusudia kuwa ni kunyongwa hadi kufa. Aidha, kwa makosa ya mauaji bila kukusudia Mahakama inaweza kutoa adhabu nyingine yoyote kulingana na mazingira na namna kosa lilivyotendeka. Hata hivyo kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia sheria imeweka adhabu ya juu ya kifungo cha Maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Adhabu ya Kunyongwa hadi kufa ndiyo adhabu kali kuliko zote hapa nchini pamoja na ulimwenguni kote. Ahsante.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakomesha shughuli za ukataji miti, kilimo na ujenzi karribu na vyanzo vya maji ili kulinda vyanzo vya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya mwaka 2009. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imekamilisha uandaaji wa Mipango ya Muda Mrefu ya Kuhifadhi Vidakio vya Maji (Catchment Conservation Plans) katika mabonde yote tisa nchini. Mipango hiyo imeweka dira, vipaumbele na utaratibu mzuri wa utunzaji wa vyanzo vya maji katika maeneo ya vidakio vya maji na mipango hiyo itatekelezwa hadi mwaka 2035.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuhakikisha inakomesha shughuli za ukataji miti kilimo na ujenzi karibu na vyanzo vya maji, hadi sasa jumla ya vyanzo vya maji 191 vimewekewa mipaka ikiwa ni hatua za kuzuia shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivyo na vyanzo 44 vipo katika hatua ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali ili vilindwe kisheria. Vilevile, jumla ya Jumuiya za Watumia Maji 162 zimeanzishwa katika maeneo ya vyanzo vya maji ili kuwashirikisha wananchi katika shughuli za utunzaji wa vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji itaendelea kutolewa kwa wananchi ili wafanye shughuli za kiuchumi katika maeneo ambayo hayana athari kwa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakarabati upya Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkoani Pemba pamoja na nyumba za kuishi askari wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Jengo la kituo cha Polisi cha wilaya ya Mkoani, mkoa wa kusini Pemba ni chakavu na halifai kwa matumizi ya kutoa huduma za Polisi. Mwezi Disemba 2022 Serikali imetoa kiasi cha fedha shilingi milioni 700 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi kipya cha Daraja B eneo hilo. Taratibu za ujenzi zimeshaanza na ujenzi unatarajia kukamilika mwezi Agosti, 2023.
Mheshimiwa Spika, tathimini ya uchakavu kwa ajili ya kufanya ukarabati wa nyumba ya makazi ya askari ya kuishi familia nne ambayo iko eneo la kituo imeshafanyika na kubaini kwamba shilingi milioni 46.27 kinahitajika kwa ajili ya kubadilisha paa, dari, miundombinu ya maji safi, maji taka na umeme, kuziba nyufa na kupaka rangi. Fedha hizo zitaombwa kutoka kwenye mfuko wa tuzo na tozo katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga upya na kufanyia ukarabati nyumba zilizo katika Makambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na kuboresha miundombinu mbalimbali kwenye vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, ikiwemo ukarabati wa makambi na nyumba za makazi kwa Maafisa na Askari. Ukarabati wa makambi ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2020, na unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na vipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya ukarabati inahusu nyumba zilizonunuliwa kimakundi nje ya makambi ya Jeshi, ikiwemo magorofa ya Mwenge, Keko, Nyumba za makazi za Masaki, Kitangili, Nyegezi, Nyamanolo, Tabora, Tanga, Shinyanga na Mtwara. Aidha, ukarabati huu umeanza kutekelezwa katika magorofa ya Mwenge Dar es Salaam na Tanga. Inategemewa ifikapo Desemba, 2023, ukarabati wa awamu hii utakuwa umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati awamu ya pili utahusisha nyumba zilizopo makambini kwa kuzingatia kanda mbalimbali kwa kuanza na Kanda ya Mashariki, Zanzibar, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kusini, Kanda ya Ziwa na kumalizia ukarabati Kanda ya Magharibi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID K.n.y. MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, lini Serikali itafanya uhakiki ili kuwarejesha walengwa 2,500 waliosimamishwa kupokea ruzuku ya TASAF?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuanza utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF, mwaka 2019 na 2021 Serikali iliagiza kufanyika uhakiki wa walengwa wote wa TASAF ili kupata taarifa sahihi ya walengwa wote waliomo katika kanzidata. Zoezi la uhakiki lilifanyika katika maeneo yote nchini na baadhi ya kaya zilibainika kukosa vigezo vya kuwa kwenye orodha ya walengwa na hivyo kusimamishwa kupokea ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaya ambazo zilithibitika kuwa na vigezo zimepewa nafasi ya kukata rufaa kwa mujibu wa sheria na taratibu na zilizobainika kuwa ni kweli zilikuwa na vigezo vya kuendelea kuwa kwenye mpango zilirejeshwa.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufuatilia mila potofu za kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama hasa Manyara na Arusha?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi kuhusu mpango gani Serikali tunao kufuatilia mila potofu za kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama hasa mikoa ya Manyara na Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa kuna mila zenye faida ambazo zinapaswa kuendelezwa na mila zenye kuleta madhara ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziita “Mila potofu” ikiwemo mila ya kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama. Mila hii ina madhara kwa kuwa inachochea ukatili wa kihisia, ndoa za utotoni na ina mnyima mhusika haki yake ya msingi ya kumchagua mwenza wa kuishi naye umri utakapofika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutokomeza mila za aina hiyo, Serikali imeandaa utaratibu wa kufanya majadiliano kuhusu masuala ya kimila na majadiliano haya yanahitaji umakini mkubwa katika kuyajadili. Hivyo basi, Wizara imeandaa mwongozo wa Taifa wa uendeshaji majadiliano kuhusiana na mila na desturi zenye madhara kwa jamii wa mwaka 2022. Majadiliano hayo yanakuwa ni jumuishi yanayohusisha viongozi wa mila, viongozi wa dini, wazee maarufu na wataalam waliopo katika ngazi ya jamii ili kuja na ujumbe mahsusi wenye lengo la kutokomeza mila zenye madhara ikiwa ni pamoja na kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa Wataalam wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii waliopo ngazi za Jamii kuandaa majukwaa ya kuongoza majadiliano haya kuhusu mila hiyo yenye madhara na kuja na ujumbe mahsusi utakaotumika kutoa elimu ikiwa ni kwenye nyumba za ibada pia na kwenye redio mbalimbali. Ahsante.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza:¬-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kikundi maalum kuweza kutathmini hewa ukaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Pemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeshaweka mipango thabiti ya kusimamia na kutathimini hewa ukaa. Ofisi ya Makamu wa Rais, imetoa Mamlaka kwa Kituo cha Uratibu na Usimamizi wa Kaboni (NCMC) kilichopo Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kwa ajili kuratibu, kutathmini na kutoa utaalam wa masuala yote yanayohusu gesijoto na biashara ya hewa ukaa nchini. Aidha, katika kuhakikisha biashara ya hewa ukaa inakuwa biashara rasmi hapa nchini, Ofisi ya Makamu wa Rais, imeandaa kanuni na mwongozo wa kusimamia na kudhibiti biashara ya kaboni za mwaka 2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kushirikiana na wadau wengine kwa kuhakikisha kwamba masuala haya ya hewa ukaa yanaeleweka kwa kila mdau na Watanzania wote kwa ujumla. Nakushukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, ni kwa nini hadi sasa Wilaya ya Chakechake ina kituo kimoja cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Chakechake ina kituo kimoja cha polisi. Sababu ya hali hiyo ni kwamba, Wilaya ya Chakechake ilikuwa na idadi ndogo ya matukio ya uhalifu na hivyo kituo hicho kilionekana kinatosheleza.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu pamoja na shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imepanga kujenga vituo vya polisi katika maeneo ya Vitongoji, Pujini, Wesha na Gombani. Tayari Idara ya Ardhi imetoa eneo la mita za mraba 1,496 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi eneo la Vitongoji. Serikali itaanza kujenga kituo hicho kulingana na mpango wake wa ujenzi hususani katika mwaka wa fedha 2023/2024. Nashukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani kuhakikisha NEMC na ZEMA zinasajiliwa kwenye Mfuko wa GCF?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mkakati uliopo ni kuhakikisha NEMC, ZEMA pamoja na taasisi nyingine zilizoomba au zitakazoomba usajili chini ya GCF zinapata usajili katika Mfuko wa GCF. Hivyo, kwa sasa Serikali inaendelea na mawasiliano, majadiliano na mazungumzo ya kuhakikisha usajili kwa taasisi mbalimbali za Serikali unakamilika.
Mheshimiwa Spika, NEMC tayari imeshaomba na kuanza mchakato wa usajili (accreditation) tangu mwaka 2021, na kwa upande wa ZEMA ilikuwa bado haijawasilisha maombi ya usajili kwenye Mfuko wa GCF. Hata hivyo, Serikali itaendelea kuhakikisha taasisi zote zilizoomba usajili katika Mfuko wa GCF zinapata usajili ili kunufaika na faida za mfuko huo, ahsante sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kuwasaidia wahanga wanaopata mimba kutokana na matukio ya ukatili wa kijinsia kama ubakaji na udhalilishaji?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mipango na mikakati ya kuwasaidia waathirika na manusura wa vitendo vya ukatili kwa kuhakikisha wanapatiwa huduma muhimu zinazolenga kuwasaidia kukabiliana na athari zinazotokana na vitendo hivyo. Aidha, huduma zinazotolewa ni pamoja na huduma za afya, huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia na kijamii. Huduma za hifadhi, chakula na malazi kupitia Nyumba Salama na Urejeshaji wanafunzi shule kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vile ubakaji na udhalilishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, Serikali imeendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 na mikopo ya wanawake kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake (WDF) kwa lengo la kusaidia wanawake kujiinua kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu, ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, ni mikataba mingapi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambayo watumishi wake wanatoka Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imeridhia mikataba 12 ya kimataifa na kikanda kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Utekelezaji wa mikataba hii hufanyika kwa ushirikiano na uratibu baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira - Tanzania Bara pamoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Tanzania - Zanzibar. Hivyo, utekelezaji wa mikataba hii hujumuisha watumishi wote wa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi zetu mbili zimekuwa zikishirikiana kwa pamoja kwenye vikao vya maamuzi vya mikataba hii. Pia pande zote mbili za Muungano zinanufaika na utekelezaji wa mikataba hii hususani kupitia, programu na miradi inayoratibiwa kupitia mikataba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa maslahi mapana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kukabiliana na changamoto za kimazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi, nakushukuru. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, lini Serikali itawasilisha Marekebisho ya Sheria ya Mazingira ili kuipa NEMC uwezo wa hadhi ya mamlaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Mwinyi Azan, Mbunge Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Pemba, najibu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Ofisi ya Makamu wa Rais ipo katika mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191. Katika marekebisho hayo, kubadili muundo wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) ni moja ya masuala yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho ili NEMC iweze kuwa Mamlaka.
Mheshimiwa Spika, ni matumaini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwamba hadi kufikia Juni 2024, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 uwasilishwe katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nakushukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kusimamia uhifadhi wa misitu ikizingatiwa kwamba imeandaa na kuzindua biashara ya hewa ya ukaa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina takribani hekta za misitu milioni 48.1 ambayo inajumuisha misitu ya Serikali Kuu, misitu ya halmashauri, misitu ya vijiji na misitu binafsi. Aidha, kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kama kilimo cha kuhamahama, uchomaji moto kwenye misitu na ufugaji, nchi yetu inapoteza takribani hekta 469,000 kwa mwaka na hivyo kuchangia kuzalisha gesi joto na hatimaye uwepo wa mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya kaboni ni mojawapo ya mkakati wa Kimataifa wa kusaidia kupata fedha za uhifadhi wa mazingira na misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeweka mikakati ya kulinda misitu iliyopo na kuongeza upandaji miti nchini. Serikali imefanya hivyo kupitia mikakati na miongozo mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Kuongoa Misitu wa mwaka 2024, Makakati wa Mianzi wa mwaka 2024, Mwongozo wa Kitaifa wa Uandaaji na Utunzaji wa Kitalu cha Miche ya Miti wa mwaka 2024 pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Kilimo Mseto wa mwaka 2024. Hivyo, nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuzingatia sheria za uhifadhi zilizowekwa na kutojishughulisha na shughuli za uharibifu wa misitu.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza:-
Je, lini Serikali itaweka vifaa tiba katika majengo ya huduma za mama na mtoto kwenye halmashauri mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2023/2024, jumla ya shilingi bilioni 186.3 zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vikiwemo vifaa vya huduma ya mama na mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2024/2025, Serikali imetenga shilingi bilioni 66.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ambapo kipaumbele kimewekwa kwenye vifaa tiba vya huduma za mama na mtoto kwenye vituo vyenye upungufu mkubwa zaidi kote nchini. Ahsante.