Supplementary Questions from Hon. Maryam Azan Mwinyi (37 total)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, nina swali moja dogo la nyongeza:
Mheshimiwa Spika, kwa vile sasa Wizara ipo kwenye mchakato wa kukusanya maoni ya kurekebisha mtaala. Je, Serikali haioni sasa kuwa ipo haja ya kuweka mtaala mmoja wa elimu ya msingi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar? (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Maryam nakupa nafasi tena, sasa uulize swali lako ukiniangalia, usipige chabo. (Kicheko)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwa vile Serikali sasa ipo kwenye mchakato wa marekebisho ya mtaala. Je, Serikali haioni kwamba ipo haja sasa ya kuweka mtaala mmoja wa elimu kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Bara? (Makofi/ Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa upande wa Elimu ya Msingi kuna tofauti ya mitaala kati ya Tanzania Bara na Visiwani. Kwa sababu kwa upande wa Tanzania Bara tunawapeleka watoto shule miaka saba kwa upande wa shule za msingi, lakini kwa wenzetu wa Tanzania Zanzibar wao wanakwenda kwa kipindi cha miaka sita. Kwa hiyo kuna utofauti wa namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na nilitaarifu tu Bunge lako Tukufu kwamba, Taasisi yetu ya Elimu Tanzania (TET) na ile ya Zanzibar (ZIE) zinafanya kazi kwa karibu sana kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mitaala unakwenda sawasawa lakini na majadiliano ya karibu kuhakikisha kwamba changamoto zote zinazotokea kwenye utekelezaji wa mitaala zinapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli pasipokuwa na shaka kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza sasa kufanya mapitio ya Sera ile ya Elimu ya Zanzibar ya mwaka 2016 na wataangalia sasa namna gani tunaweza kuhusianisha miaka hii ya Elimu ya Msingi kuhakikisha kwamba tunakwenda sawasawa.
Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu kwamba tuna mjadala mpana wa kitaifa kuhakikisha kwamba mwenendo au mfumo wa elimu yetu uwe vipi.
Kwa hiyo, katika majadiliano haya tunaamini changamoto hizi zote anazozungumza Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge humu ndani zinaenda kupata ufumbuzi ikiwemo na hili la kuwa na mtaala mmoja kuanzia Elimu ya Msingi.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa vile wanawake ndiyo wanaoshughulika sana katika kilimo hiki cha vanila lakini mitaji, elimu na ujuzi wao pia ni mdogo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuviwezesha vikundi hivi vya akina mama?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, Serikali imefanya tathmini gani ya bei hapa nchini kwetu na nchi za nje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali ina mkakati gani kuwapatia uwezo wa kifedha vikundi vya akina mama ama wajasiriamali waliopo kwenye zao la vanila na mazao mengine ya kilimo. Kwanza, nitumie nafasi hii kuhamasisha Halmashauri zote za Wilaya ambazo zao la vanila na mazao mengine ya kilimo yanapatikana, ni vizuri asilimia 10 ya kukopesha akina mama na vijana ikaelekezwa kwenye maeneo ya uzalishaji ili kuweza kusaidia mitaji yenye gharama nafuu kwa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tutaendelea kuwasiliana na Serikali za Mitaa ili waweze kutusaidia katika hilo na tumepeleka mapendekezo Wizara ya Fedha namna ya kutumia cess inayopatikana kwenye mazao iweze kurudi kwenye uzalishaji badala ya kufikiria kukopesha bodaboda na vitu vya namna hiyo. Hatua ya pili kuhusu financing, Waziri wa Kilimo hivi karibuni ameunda committee ya kuangalia namna gani tunaweza tukapata mitaji katika sekta ya kilimo ambayo inaendana na sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kipengele cha pili, Taasisi yetu ya Tengeru inaendelea kufanya utafiti ambao utatoa majibu halisi ya bei. Naomba nitumie Bunge hili kusema kwamba maeneo kama ya Mbeya ambapo kuna watu wanapita kuwapotosha wakulima kuwaambia kwamba kilo moja ya vanila ni zaidi ya Sh. 150,000 – Sh. 200,000 sasa hivi katika soko, sio kweli, bei iliyopo sasa hivi haizidi Sh. 20,000 – Sh. 25,000. Kwa hiyo, wasiwapotoshe wakulima kwa kuwapa matumaini ambayo siyo sahihi. Wizara ya Killimo sasa hivi tunafanya tathmini na tutatoa taarifa kwa umma kuwaonesha masoko na bei halali za mazao hayo katika masoko ya nje na masoko ya ndani.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa vile Serikali imetoa majibu mazuri sana, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Je, Serikali imefanya tathmini katika elimu inayotoa, kama kusaidia kupunguza uvuvi huu haramu ambao bado tunauona unaendelea?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Maryam Azan Mwinyi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wote tumekuwa tukifanya tathmini na ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge ya kwamba pamoja na elimu tunayoitoa, bado tatizo la uvuvi haramu liko pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Serikali tumekubaliana; la kwanza, elimu ni jambo endelevu, kwa hiyo, tutaendelea nalo. La pili, ni kupanua wigo na kufanya ushirikishaji zaidi ili kusudi tuweze kupambana na vita hii ya uvuvi haramu kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie ya kwamba wavuvi walio wengi wanaelewa sana ya kwamba hiki ni sahihi na kipi kisicho sahihi. Tunazo changamoto za msingi sana ambazo zinawapelekea wakati mwingine baadhi yao; aidha kwa makusudi au kwa au kwa bahati mbaya wanaingia katika vitendo hivi haramu. Miongoni mwa changamoto hizo ni ongezeko la mahitaji ya hizi rasilimali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Serikali tunafanya tathmini na tunaendeleza mikakati ya kuhakikisha tunafanya uendelevu wa rasilimali zetu.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mashirikiano haya hayapo kisheria: Je, Serikali haioni haja ya kuwa na utaratibu wa kisheria ili kuwezesha ushiriki wa Zanzibar kuwa bora zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Je, mpaka kufikia Julai, 2022, Zanzibar imenufaika na miradi gani ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Pemba, Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ushirikiano na majadiliano ambayo huwa tunafanya yanayohusiana na mikataba ya Kimataifa, ya mazingira na kukabiliana na mazingira ya tabia ya nchi, ni ya kisheria. Maana yake, yako kisheria. Hata ukienda ukisoma Katiba ya Jamhuri kwenye fungu lile la Foreign Affairs utakuta kumeelezwa namna ambavyo inatakiwa tushirikiane kwenye mahusiano yanayohusu masuala ya mikataba ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, hata ukienda kwenye sheria yetu ya mazingira, imeeleza, Waziri anayehusika na mazingira kwa upande wa Jamhuri ya Muungano, basi anatakiwa akae na ashirikiane na Waziri anayehusika na mazingira kwa upande wa Zanzibar. Kwa hiyo, majadiliano haya hasa mikataba ya Kimataifa yanakuwa yapo kisheria zaidi.
Mheshimiwa Spika, ipo miradi ambayo imetekelezwa na inaonekana. Kwa mfano, kuna ujenzi wa kuta ama kingo za kuzuia maji Wete kule Sepwese, hiyo ipo; pia kuna miradi ya kurejesha ardhi iliyoathirika na mabadiliko ya tabia ya nchi, hii iko maeneo ya Kiuyu, Shumba Viamboni, Shumba Mjini, Maziwa Ng’ombe maeneo mingine miradi hii ipo na imepita.
Mheshimiwa Spika, pia upo mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi maeneo ya Kaskazini A, Unguja katika Mkoa wa Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa swali la nyongeza. Tunaipongeza Wizara kwa jitihada yake inayofanya kwa ajili ya TEHAMA. Kwa wale wanafunzi wanaoona watapewa vishikwambi: Je, kwa wale wanafunzi wenye uono hafifu Serikali itawasaidiaje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Mwinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada zake za kuhakikisha kwamba watoto wote wakiwemo na wale wenye uono hafifu na wenye ulemavu wa aina mbalimbali wanaweza kupata vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina takwimu sahihi za wanafunzi hawa na tutahakikisha nao vilevile katika eneo hili tunakwenda kuwapatia vifaa vya kuwasaidia na wao kuweza kujifunza somo hili muhimu la TEHAMA. Ahsante.
MHE. MARIAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza ni gharama sana. Je, Serikali wanasaidia vipi wananchi kwenye gharama hizi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwa mwaka mmoja, Serikali inatumia bilioni 670 kwa exemption yaani kwa maana na hasa asilimia kubwa ya fedha hizo zinaelekea kwenye kuwasaidia hawa wenzetu ambao wana matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza, zinatumika hizo fedha kwa ajili ya exemption.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Muswada wa Bima ya Afya, unakuja hapa ndani, hilo ndiyo litakuwa suluhisho na mnajua pamoja na kwamba tuna Muswada wa Bima ya Afya, Rais wetu ametenga bilioni 149.77 kwa ajili ya kuwapatia bima wale wasiojiweza. Kwa hiyo, mikakati ndiyo hiyo ya kwenda kuboresha na kuhakikisha watu wanapata huduma.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa wanawake wengi ndiyo wanajishughulisha na ukaushaji wa dagaa, je, Serikali ina mpango gani maalum wa kuwasaidia kwa haraka wanawake hawa ili kupata tija zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango maalum tulionao, la kwanza Serikali imejikita katika kulitangaza zao la dagaa kuwa ni zao la kimkakati na lengo na dhamira ya Serikali ni kulipa thamani zao hili kulifungulia masoko na kuweza kuwahakikisha hata mabenki yaweze kuwa na utayari wa kuwakopesha akinamama wanaojishughulisha na shughuli hizi za ukaushaji wa dakaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kufungua masoko ya duniani na hivi tunavyozungumza zao la dagaa limekuwa na thamani kubwa sana katika soko la dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kuwawezesha kupata mikopo kupitia Benki yetu ya kilimo na kuhimiza halmashauri zetu kupitia ile asilimia nne ya akinamama, kuwasaidia na kuwakopesha zaidi akinamama wazalishaji hasa kundi hili la wavuvi linalokausha dagaa na kufanya biashara hii ya dagaa. Ahsante.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kituo cha Polisi kilichopo wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba kipo katika hali mbaya.
Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati kituo hicho japo kwa dharura?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Mwinyi Kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba maeneo ya Pemba vituo vyake vingi vya Polisi vimechakaa vinahitaji kufanyiwa marekebisho au kiujengwa vipya. Tumeanza na majengo ya Kamanda wa Polisi wa mikoa miwili ya Pemba, lakini tutaendelea kujenga hivi vya ngazi ya wilaya na vingine vidogo ili hatimaye maeneo yote yaweze kupata vituo vinavyostahiki. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ziara nitakayoifanya huko Pemba, moja ya maeneo ni kuzingatia maeneo haya ambayo hayana kabisa vituo vya Polisi ili na wao waweze kupatiwa vituo hivi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi Kengeja ambacho kipo Mkoani Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kituo hiki cha Kengeja kipo isipokuwa ni chakavu sana. Nimekitembelea katika ziara yangu ya mwezi uliopita nikajiridhisha kwamba ni kituo chakavu na Wizara kupitia Jeshi la Polisi imekiweka kwenye mpango wa ukarabati katika bajeti ya mwaka 2023/2024.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza;
Kwa kuwa watuhumiwa wa matukio haya wanaachiwa huru kwa kigezo kwamba ushahidi haujapatikana.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha kitengo cha ushahidi na uchunguzi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nini mpango wa Serikali wa kuzuia mauaji haya ili kuwanusuru wanawake hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza linaonesha kwamba kumekuwa na muda mrefu wa kesi hizi zikiwa na visingizo vya kupatikana kwa ushahidi wa haraka. Kesi za mauaji zina utaratibu wake katika upelelezi wake. Walio wengi wanafikiri ni jambo la mara moja katika kufikia maamuzi ya upelelezi unaohusisha mauaji, lakini kwa namna yeyote ile muda uliowekwa na mahakama na vyombo vya upelelezi umekuwa ukizingatiwa sana katika masuala ya kesi hizi za mauji na hivyo hatuna kumbukumbu sahihi za watu ambao wamekaa magerezani muda mrefu kuliko kile kipindi ambacho tumekiweka kama dhamirio la kuwapa nafasi wapelelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu namna ya kuzuia mauaji haya; hili ni jambo la kijamii. Mambo haya mengi yamekuwa yakitokea kwenye jamii zetu na sisi wanajamii ndio tunastahili kuyakemea maana ni maisha yetu ya kila siku ambayo yanasababisha mauaji haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kumpa maelezo muuliza swali; ni kwamba si mauaji tu kwa kina mama na watoto ukienda pale Njombe, nimetembelea Gereza la Njombe, asilimia 75 ya akina mama waliopo mle jela wakisubiri hizo kesi wanahusishwa na mauaji ya kuwaua waume zao. Kwa hiyo unaweza ukaona jinsi ambavyo mauaji haya yanajiografia zake; na mengine yote haya yanayojitokeza kweye jamii zetu wakemaji namba moja lazima tuwe sisi wenyewe wanachi katika maeneo yetu.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Je, Serikali haioni iko ya haja ya udhalilishaji na ukatili wa wanawake na watoto kuwa ajenda ya kitaifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Maryam, ushauri wake tumeupokea na tutaufanyia kazi kwa sababu vitendo vya ukatili ni vya jamii na jamii yote tunatakiwa tushirikiane kwa pamoja ili kuungana na kupinga vitendo vya ukatili nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM A. MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kijiji cha Vujini, Wilaya ya Mkoani kina matokeo ya uhalifu sana. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi katika kijiji hicho ili kupunguza matukio hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa hali ya usalama Zanzibar. Niombe tuendelee kushirikiana ni kweli kwamba baadhi ya maeneo ya Zanzibar ikiwemo kijiji alichokitaja kina hayo matukio ya uhalifu, lakini Jeshi la Polisi linafanya misako na doria kule ambako hakujawa na kituo ili kuhakikisha kwamba usalama unakuwepo. Kwa hiyo tutawasiliana na wenzetu wa upande wa Zanzibar kama maeneo yamepatikana na wananchi wako tayari kutoa ushirikiano, basi kituo hicho kinaweza kuanza kujengwa kwa siku za usoni.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na sheria zote zilizonukuliwa katika Ofisi ya Waziri. Je, Ofisi hiyo inashirikiana vipi na Ofisi ya TAMISEMI, Ardhi, Kilimo na Mifugo katika kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinahifadhiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini Serikali isianzishe tuzo maalum kwa ajili ya vijiji na Kamati za Maji zinazohifadhi vyanzo hivyo kikamilifu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tayari Wizara tunashirikiana na hizi wizara ambazo tunaingiliana kimajukumu na hili tumeendelea kulifanya hasa katika ziara ya Wizara za Kisekta tumekuwa tukiendelea kutoa elimu ya pamoja.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na tuzo maalum kama nimemsikia vizuri. Tuzo maalum ni moja ya vitu ambavyo tunavitoa kwenye Jumuiya za Watumia Maji. Tunatoa tuzo kwa maana ya kuwapa motisha ili kuona kwamba wananchi wanashiriki moja kwa moja kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji. Vilevile kama ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, kwa niaba ya Waziri, naomba niseme nimepokea, tutaendelea kuongeza nguvu. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Je, Serikali inachukua hatua gani ya kudhibiti udanganyifu badala ya kusubiri udanganyifu ndiyo mnatoa adhabu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maryam kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyozungumza kwenye majibu yangu ya msingi jukumu letu kama Wizara, jukumu letu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatoa elimu ya kutosha ya athari za udanganyifu wa mitihani kwa wasimamizi vilevile kwa wale wanafunzi ambao kwa namna moja au nyingine wanaathirika kwa kiasi kikubwa kwenye zoezi hili. Kwa hiyo, jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunatoa elimu watu wasifanye udanganyifu katika mitihani kwa sababu athari zake ni kubwa kwa wao wenyewe binafsi lakini na kwa Taifa kwa ujumla. Nakushukuru sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, Serikali inachukua hatua gani kwa matapeli wanaotumia lane za ndani ambazo zimesajiliwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA
YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema tuna mfumo unaoitwa Tele Traffic Management System, kwanza kabisa tunabaini simu ambazo zinafanya mambo ambayo hayastahiki na mpaka sasa tunatumia mfumo huo ambao unatumia simu za majaribio (Test Calls) na tukitumia baadae tunabaini na tangu Julai mwaka 2022 mpaka sasa ni takribani simu 826,951 zilibainika kufanya mambo ambayo yasiyostahili lakini kati ya hizo tayari tumeshachukua hatua na bahati mbaya sana tunapochukua hatua katika mambo haya huwa hatuyatangazi kwa sababu tunakuwa tumepeleka kwenye mamlaka ambayo yanatakiwa kutoa hukumu na katika mchakato huo bado kunakuwa na ukusanyaji wa taarifa na evidences ambazo zitafanya kwamba hukumu iweze kutoka vizuri, ndiyo maana huwa hatutangazi lakini Serikali imejizatiti kuhakikisha kwamba jambo hili linaendelea kukomeshwa, ahsante sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza, nina swali moja la nyongeza. Kwanza napenda niipongeze Serikali kwa majibu yake mazuri. Je, Waziri yuko tayari kwenda kukikagua Kituo hicho cha Polisi ambacho Waziri amesema kitamalizika Agosti, 2023?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, nimewahi kukitembelea kituo hiki na kuona kasi ya ujenzi unavyoendelea, inanitia moyo kwamba inaweza ikamalizika. Hata hivyo, kwa vile hakuna zida mbovu, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge kukamilika ili kwenda kuangalia maendeleo ya ujenzi na kujiridhisha kwamba kitakamilika katika muda uliopangwa, nashukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, Serikali itapeleka lini magari katika Mkoa wa Kusini, Pemba ambao una uhaba wa magari hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kurejea jibu langu la msingi kwamba, mara tutakapopokea magari yatakayonunuliwa kwa bilioni 15 tulizopewa na Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Kusini Pemba pia ni moja ya maeneo yatakayogawiwa magari hayo. Namwondoa mashaka Mheshimiwa Maida kwamba Mkoa wake pia utapata gari, ahsante.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa jeshi letu limekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha ulinzi wa nchi na mipaka yake; je, ni maeneo gani kwa Zanzibar ambayo yatapewa kipaumbele katika ujenzi huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mahanga katika kambi hapa nchini? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Maryam Mwinyi kwa kufuatilia mambo haya ya msingi kwa ustawi wa majeshi yetu. Nimhakikishie, kwenye majibu yangu ya msingi nimeeleza kwamba kwenye ukarabati wa makambi ya awamu ya pili, Zanzibar imo katika vipaumbele. Ninapozungumzia Zanzibar, ni Unguja na Pemba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwenye awamu ya pili upande wa Zanzibar pia ni kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili kuhusu mahanga, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali hili. Wizara itafanya tathmini ya mahitaji ya mahanga kote nchini na kuhakikisha katika utekelezaji wa ujenzi wa mahanga pia upande wa Zanzibar wanapewa kipaumbele, ahsante sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kuozesha mtoto bila ridhaa yake ni unyanyasaji wa kijinsia; je, ni lini mwangozo huo utamalizika?
Swali la pili, je, kwa nini jambo hili lisiingizwe kwenye sheria? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo huu umeshakamilika na kinachofuata ni kuzindua. Kwa swali lake zuri la leo tutaenda kuzindulia Manyara hukohuko au Arusha na tutamualika na yeye awepo ili awe Balozi kabisa wa kubeba ujumbe huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili kuhusu masuala ya sheria, ni kweli naona umuhimu huo, kwa sababu bado tunaendelea na mchakato wa maboresho ya Sheria ya Mtoto nimelipokea tutaliwasilisha kwenye Kamati waone itifaki ya kisheria kwa sasa kama inaweza kuingizwa au kunahitaji tafiti zaidi kisha tutawasilisha taarifa. Ahsante.(Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza; je, Serikali ipo tayari kugawa vifaa kwa wavuvi ili waweze kutumia hiyo mobile app? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Mwinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza tangu awali kwenye majibu yangu ya msingi kwamba Serikali tupo tayari, ilikuwa kwanza ni kuangalia namna gani tunaweza tukawafanya wavuvi wetu waweze kunufaika na mazao ya bahari au mito na maziwa kwa kufanya huo utafiti na kupata hiyo application ambayo ni maalum inayosaidia wao kuweza kujua mazalia ya samaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu mpango ni pamoja na utaratibu wa kuweza kuwafundisha, kuwapa elimu, na pia utaenda sambamba na kuwapa vifaa. Zaidi hapa watatumia simu zao za mkononi tu kuweza kujua mazalia ya samaki na kupata taarifa zaidi. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana nao na kuwawezesha kiutaalamu, kielimu, na kiujuzi katika kuhakikisha kwamba tunapata tija iliyokusudiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kukuza sekta ya uvuvi. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifanyia ukarabati nyumba za Polisi zilizopo Madungu Wilaya ya Chake Chake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea eneo la Chake Chake na kubaini mbali ya uchakavu wa Kituo cha Polisi cha ngazi ya Wilaya, vile vile nyumba za Askari zimechakaa sana. Hata hivyo, Serikali imeanza kujenga hanga moja ambalo litachukua Askari lakini tutaendelea kuzikarabati nyumba hizo kadiri tunavyopata fedha ili Askari wote waweze kukaa kwenye makazi yenye hadhi stahiki, nashukuru. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa vile tayari Serikali imeshatenga bajeti ya kutoa kifungua kinywa katika shule. Je, ni vipi Serikali itaangalia kwa uangalifu zaidi vifungua vinywa hivyo ambavyo vitatolewa katika shule hizo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza. Kwanza Serikali siyo kwamba imetenga bajeti kwa ajili ya vifungua kinywa, nilichokisema kwenye majibu yangu ya msingi ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Elimu, imetoa mwongozo wa namna gani ya kupata lishe ikiwemo wazazi wa maeneo husika kuchangia katika kupata lishe watoto hawa wakiwa shuleni.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tayari Wizara imeshatunga katika kanuni na miongozo ya biashara ya hewa ukaa. Je, ni jitihada gani ya Wizara katika kutoa uelewa wa biashara hii kwa jamii hasa wanawake? (Makofi)
Swali langu la pili, je, Zanzibar inanufaika vipi kutokana na fedha inayotokana na faida ya biashara hii ya hewa ya ukaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, najibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Maryam pamoja na Wabunge wote kwa kuwa na hamu sana ya kutaka kujua faida na fursa mbalimbali ambazo zinapatikana kwenye biashara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar sasa muda wowote inakwenda kuanza kunufaika kutoka na biashara hii, tulichokuwa sasa tunakisubiria ni kwanza tunasubiri tumalize utafiti. Zanzibar tunayo misitu kwa upande wa Pemba tunao Msitu wa Ngezi lakini kwa upande wa Unguja tunao Msitu wa Jozani na kama unavyojua kwamba biashara hii inavunwa kwenye misitu hasa misitu ya asili. Kwa hiyo, tutakapokamilisha utafiti wetu Zanzibar inakwenda kunufaika kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa tulisema wacha tuendelee kutoa taaluma kwa wananchi hasa kwa upande wa Zanzibar, tumeshaanza kushirikiana idara ya mazingira tumeanza kutoa taaluma, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi tumeanza kuwapa taaluma. Kwa hiyo, muda wowote kuanzia sasa Zanzibar inakwenda kuanza kunufaika na biashara hii ya hewa ukaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa jitihada ambazo zimechukuliwa ni kwamba, tumeunda kikosi kazi na kikosi kazi hichi kimekuwa kinashirikiana na TAMISEMI katika kuzunguka nchi yote kuhakikisha kwamba tunawafundisha wananchi. Tayari tumeshaanza kwenye baadhi ya Halmashauri za Mkoa wa Tabora, Simiyu, Katavi, Manyara na maeneo mengine. Kwa hiyo, taaluma hii tutahakikisha kwamba inaenea kote na juzi tulikuwa na Kamati za Wabunge kuwapa taaluma hii ya biashara ya hewa ukaa. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ina vituo Vinne vya Polisi ambavyo vina gari moja ambalo lilipatikana mwaka 1980. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea gari nyingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu wakati najibu swali la msingi kwamba tunao mpango wa kuimarisha usafiri kwenye maeneo yote ambayo yana changamoto ya usafiri ikiwemo Mkoa wa Kusini Pemba. Kwa hiyo, kulingana na vipaumbele na mahitaji ya magari, magari tutakayoyapata mapema iwezekanavyo yale 78 Mkoa wa Kusini Pemba pia utazingatiwa. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tatizo la Mkongo wa Mawasiliano lilipo Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja halitofautiani na tatizo la Kaskazini Pemba na Kusini Pemba. Nini kauli ya Serikali kuhusu mawasiliano katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa kwa upande wa Zanzibar umeshafika katika Wilaya zote kwa upande wa Zanzibar. Kwa hiyo labda tu tutaendelea kutoa elimu na ili kuwajulisha namna gani Mkongo wa Taifa huu unatoa huduma na kuwaonyesha vituo ambavyo vinatoa huduma hiyo. Nakushukuru sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa vile wanaojishughulisha sana na zao la Mwani ni wanawake. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa wanawake hao nyenzo za kisasa kwa ajili ya kilimo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tulishakwisha kuanza kutoa zana kama vile Kamba na ipo zana inaitwa taitai na hilo zoezi tutaendelea nalo ikiwa ni pamoja na matarajio yetu ya kununua boti ambazo zitakwenda kwa ajili ya wavuvi lakini na vikundi vya akina mama kwa ajili ya wakulima wa Mwani kuweza kuyafikia maeneo yale pale maji yanapokuwa mengi na uvunaji wa ule Mwani. Ahsante sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara imepata ardhi ya kujenga Kituo kimoja cha Polisi; je, ina mkakati gani wa kupata ardhi kujenga vituo vitatu vilivyobaki?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, eneo la Pujini ni miongoni mwa maeneo yenye uhalifu sana; je, Serikali haioni? Ichukue uharaka wa kujenga kituo hicho cha polisi, ili kulinda mali na usalama wa raia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, ardhi inahitajika na kupitia Bunge lako tukufu nimtake Kamishna wa Polisi Zanzibar awasiliane na mamlaka ya ardhi katika Wilaya ya Chakechake ili waweze kumpangia ardhi kwa ajili ya kujenga kwenye maeneo hayo niliyoyabaini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu eneo lenye changamoto ya uhalifu, niseme kwamba kwa sasa kwa sababu hakuna fedha za kujenga Kituo cha Polisi, basi Polisi Wilaya ya Chakechake waimarishe doria ili kudhibiti makundi yote ya uhalifu kwenye eneo hilo. Nashukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni hatua gani zinazotumika mpaka uungwe kwenye Mfuko huu wa GCF?
Swali la pili, kutokana na uhitaji wa miradi ya mazingira Zanzibar; je, ni lini ZEMA wataanza mchakato wa usajili kwenye Mfuko wa GCF? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Dada yangu Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hatua zilizokuwepo ni kwamba taasisi mbalimbali nchini mwetu ambazo Ofisi ya Makamu wa Rais ni mratibu zinawasilisha nia hiyo na mwishowe mchakato huo unaenda sasa katika mfuko huo. Mwisho wa siku ni kwamba, taasisi hiyo baada ya mchakato utakapokamilika basi inakuwa imekidhi viwango.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kumekuwa na changamoto katika mchakato huo kwa sababu zaidi ya taasisi sita nilizozipeleka hivi sasa bado hazijafanikiwa. Kwa hiyo, tumeendelea kufanya kazi hii kubwa ya kuhamasisha jinsi gani wenzetu waweze kukubali maombi yetu, kwa lengo kwamba taasisi zetu ziweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, upande wa swali la pili ni kweli, upande wa Zanzibar kuna changamoto kubwa za kimazingira. Hata hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, inaendelea kushirikiana kwa dhati.
Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge ni kwamba hivi sasa tunatekeleza baadhi ya miradi. Kwa mfano, ukienda kule Sipwese - Pemba, tunajenga ukuta pale wa Bahari, ukienda Kaskazini A na maeneo mbalimbali. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaendelea kushirikiana lengo kubwa ni pande zote mbili za Muungano ziweze kupata fursa miradi maendeleo hususani katika hususan katika sekta hii ya mazingira, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; kwa kuwa mimba zinazotokana na ubakaji, ni mimba zisizotarajiwa hasa kwa walengwa; je, Serikali imeweka adhabu gani kwa wanaofanya kitendo hiki? (Makofi)
Swali langu la pili; je, Serikali ina mkakati gani wa kuwabaini watoto wote wanaozaliwa kutokana na mama zao kubakwa ili kuwapa huduma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAUME NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza Serikali imeweka adhabu kali ikiwemo kifungo kwa ajili ya udhalilishaji, ukatili na ubakaji, kwa lengo la kupunguza vitendo vya ukatili katika jamii na mimba za utotoni. Pia inaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha kwamba vitendo hivi vya ukatili vinakwisha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, Serikali itaendelea kutoa huduma za kijamii kwa wahanga waliofanyiwa vitendo vya ukatili na ubakaji ili kuwabaini watoto hawa, wale waathirika wa vitendo vya ukatili na waliobakwa, tunawaomba wanapokwenda kuripoti katika vituo vya afya, basi kesi zao jinsi zinavyokwenda ndipo tutakapojua jumla ya watoto ambao wamezaliwa kutokana na ubakaji na kuwapa huduma zinazostahiki. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa vile Serikali ina mpango wa ukarabati wa vyuo vikuu hapa nchini. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati vyuo vikuu vilivyopo kule Zanzibar? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Mwinyi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, mkopo huu wetu wa HEET (Higher Education for Economic Transformation) unakwenda kuboresha maeneo yote ya vyuo vikuu vya umma vikiwemo na vile vya Zanzibar. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi chuo chetu kile cha SUZA Zanzibar kimepata gawio katika gawio hili la mradi wetu wa HEET lakini taasisi yetu ile ya Marine Science ya Zanzibar ambayo inasimamiwa na Chuo chetu cha Dar es Salaam nayo vilevile sio tu inakwenda kuboreshwa bali inakwenda kujengwa upya. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Zanzibar nayo tumeizingatia kwenye mgao huu na tutahakikisha kwamba kazi hii inakwenda kufanyika kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninampongeza sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni haja ya kuwa na Mratibu Msaidizi kutoka Zanzibar ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha miradi ya mazingira inamalizwa kwa wakati ili iwanufaishe walengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Maryam kutoka Mkoa wa Kusini Pemba kwa kazi nzuri anayoifanya hasa kwenye suala la mazingira na athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi hasa katika Mkoa wa Kusini Pemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunafanya kazi zetu kwa kushirikiana, lakini Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais - Zanzibar kwenye jambo la mazingira tunafanya kazi kwa kushirikiana. Sasa jambo la kutafuta mratibu ambaye atakuwa anasimamia haya mambo kwa sababu mambo mengi tumekuwa tunafanya kama taasisi, Wizara na Wizara, hatufanyi kama mratibu na mratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wazo lake na fikra yake aliyoipendekeza tunaichukua, tutakwenda kufanyia kazi kwa sababu hata wakati tunakwenda kusaini mikataba ya adaptation fund, hatukwenda kama mratibu na mratibu, tulikwenda kama taasisi na pande zote mbili tulishiriki. Tunakwenda kusaini mikataba ya EBA, tulikwenda kusaini mikataba ya miradi mbalimbali tulikwenda kama Wizara kutoka pande zote mbili. Lakini jambo la kutafuta mratibu atakayekuwa msaidizi tunalichukua na tunakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kijiji cha Pujini kilichopo Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba ni kijiji ambacho kina matukio ya uhalifu siku hadi siku, je, ni lini Serikali itajenga kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Mwinyi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, Serikali ina mkakati wa kujenga vituo vya kata nchi nzima, nadhani takribani kata 4,434 zimebaki. Kama nilivyosema, vinajengwa kwa awamu, havijengwi mara moja, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kituo alichotaja kitawekwa kwenye mpango ili kiweze kutengewa fedha kwa miaka inayokuja na kujengewa kituo cha polisi katika eneo lake, ahsante sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je baada ya mabadiliko ya sheria, majukumu ya mameneja wa kanda wa NEMC yatabadilika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika marekebisho hayo je, mna mkakati gani wa Serikali ZEMA na NEMC kufanyakazi kwa pamoja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa mujibu wa sheria hii ya NEMC tumeteua mameneja wa kanda ambao wanasimamia kwenye kanda zao zikiwemo Kanda za Ziwa, Kanda za Kusini na Kanda ya Dar es Salaam na kanda nyingine.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii hapa mbele ya Bunge lako Tukufu niwapongeze sana mameneja wetu wa kanda zote za NEMC kwa kufanya majukumu yao na kusimamia vizuri. Majukumu haya yanaweza yakaongezeka lakini pia yanaweza yasibadilike kikubwa itategemea sheria hii itakavyopendekeza. Hatujajua Wabunge na wadau wengine watakuja na mapendekezo gani lakini kikubwa majukumu yao ni kusimamia sheria, majukumu yao ni kutoa elimu kwa jamii na kufanya majukumu mengine yatakavyoelekezwa kama sheria itakavyotaka. Kwa hiyo, nadhani sheria itakapokuja ndivyo itakavyoonyesha mabadiliko ama kuongezeka kwa majukumu hayo.
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili niseme tu kwamba ZEMA na NEMC wamekuwa ama tumekuwa tukifanya kazi ya ushirikiano wa karibu kwa muda mrefu lakini hata mabadiliko haya ya sheria yatakapokuja moja ya miongoni mwa msisitizo wake katika sheria hii yatasisitiza ZEMA na NEMC, ama ZEMA na NEMA kufanyakazi kwa pamoja zikiwemo kazi za utoaji wa elimu na kazi za usimamiaji wa sheria na kazi nyingine za masuala ya usimamizi na uhifadhi wa mazingira, nakushukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa biashara ya kaboni, je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha biashara hiyo ya kaboni Tanzania Bara na Zanzibar?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na kampeni endelevu ya upandaji miti nchini, je, kampeni hii inakidhi utunzaji wa mazingira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba elimu hii inatolewa, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa na jukumu la kusimamia jambo hili na kwa mahsusi kabisa Kituo cha Taifa cha Uratibu wa Usimamizi wa biashara hii inafanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wananchi na kama mnavyofahamu tayari Serikali ilitunga kanuni za usimamizi na udhibiti wa biashara ya kaboni ya mwaka 2022. Niwaombe wadau wetu wapate fursa ya kutembelea kwenye kituo chetu cha Taifa cha Uratibu na Usimamizi ili kupata taarifa za msingi za jinsi ya kuweza kushiriki kwenye biashara hii.
MHE. MARYAM AZAN. MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa bado kuna baadhi ya hospitali wakinamama wanapokwenda kujifungua huwa wanaambiwa watoe hela kwa ajili ya vifaa je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili vifaa bila watumishi bado kazi bure, upi mpango wa Serikali kuhusu kutoa ajira kwa watumishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya vituo vya huduma za afya kote nchini kutoza gharama za vifaa na hasa grooves na vifaa vingine kwa wajawazito wanapofika kupita huduma za afya ya mama na mtoto. Serikali kupitia Sera Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tulikwisha elekeza kwamba huduma kwa kinamama wajawazito zinazohusiana na masuala ya kujifungua na watoto wenye umri chini ya miaka mitano zinatolewa bila malipo yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kauli ya Serikali naomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri kote nchini, Waganga Wakuu wa Halmashauri na Waganga Wafawidhi kuhakikisha wanasimamia maelekezo ya Sera, lakini pia wanasimamia maelekezo Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kuwa na Vifaa Tiba vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kinamama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano ili huduma hizo zitolewe bila malipo yoyote kama ilivyo maelekezo ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuajiri Watumishi wa Sekta ya Afya wa kada mbalimbali na kuwapeleka kwenye Vituo vya Afya vyote vya huduma ya afya msingi. Katika kipindi cha miaka mitatu zaidi ya watumishi 18,876 wameajiriwa na hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora alishatangaza kutolewa kwa kibali cha watumishi wengine wa afya karibu elfu kumi. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba mara ajira hizo zikitangazwa tutahakikisha watumishi wanapelekwa kwenye vituo vyetu vyote. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia posho japo kidogo kwa wanafunzi hawa ili kuhakikisha wanabaki shuleni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Maryam Mwinyi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Maryam anashauri kwamba tuangalie namna gani ya kuweza kutoa posho kidogo. Hatuwezi kusema moja kwa moja jambo hili utekelezaji wake unakuwaje na kwa namna gani katika miongozo ya Serikali, lakini tubebe kama ushauri na twende tukaufanyie evaluation au tathmini tuweze kuangalia kama namna gani tunaweza kutekeleza au laa.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni juzi tu mtoto mwenye ulemavu wa ualbino Sengerema amenusurika na kifo. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu jambo hili ambalo linaanza kutoa mizizi mikubwa katika nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kumjibu Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi kwa kumwambia kwamba, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa alitoa taarifa ya Serikali. Serikali imekwishatoa maelekezo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa yote na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba, wanaimarisha ulinzi na usalama kwa watu wenye ualbino.
Mheshimiwa Spika, lakini tuseme tunaendelea kuwapa elimu Watanzania kuwathamini na kuwajali watu wenye ualbino, ili wasiwadhuru. Sisi tutaendelea kufuatilia kwa ukaribu jambo hili na tunawataka pia, walezi waendelee kuwa karibu na watoto hawa. Ahsante. (Makofi)