Contributions by Hon. Michael Mwita Kembaki (8 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili, napenda kuchukua nafasi hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ili leo niweze kusimama hapa na niweze kuchangia katika Mpango huu ambao umeletwa katika Bunge letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wanananchi wa Tarime, wapiga kura wangu kwa kura nyingi walizonipa ili niweze kuwakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Najua wana imani kubwa na Chama cha Mapinduzi lakini pia wana imani kubwa na mimi, niwahakikishie kwamba nitawatendea haki kuwawakilisha vyema kuhakikisha kwamba mji wetu unaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nichukue nafasi hii kushukuru chama change, Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini na kuniteua kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi na hatimaye tukapata ushindi mnono katika jimbo ambalo lilikuwa limekaa upande wa pili kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Nikianza upande wa elimu, Serikali imefanya kazi kubwa ikiwemo ujenzi wa miundombinu muhimu katika shule zetu zaidi ya 3,904 kwa mwaka 2019/2020. Vilevile imetoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari na imetoa pesa nyingi kugharamia masomo hayo ambayo imewezesha watoto wetu kupata elimu kwa wingi katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu mchango wangu nitauelekeza sana upande wa ukusanyaji wa mapato. Ili nchi iweze kusimama na iweze kutekeleza miradi ambayo imepangwa katika kipindi cha mwaka huu au miaka inayokuja lazima iwe vizuri katika ukusanyaji wa mapato ili uweze kupata fedha ya kutosha kujiendesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mashaka kidogo kuhusiana na ukusanyaji wa mapato katika nchi yetu na hii nipeleke kwa TRA. Mfano katika Jimbo letu la Tarime Mjini hakuna mahusiano mazuri kati ya TRA na wafanyabiashara. Mfano cement katika Mji wetu wa Tarime inauzwa Sh.24,000 ambapo cement inayotoka katika nchi jirani ya Kenya inauzwa Sh.16,000. Kipato cha watu wa Tarime bado kipo chini na wanahitaji kujenga na ukiangalia cement inayotoka katika nchi jirani inauzwa bei ya chini tofauti ya Sh.8,000. Hivyo basi, naomba Mamlaka ya Mapato na Bunge hili Tukufu tuangalie namna gani tunaweza kufanya ili hizi kodi ambazo ni kubwa zinazopelekea wafanyabiashara kukwepa kodi ziangaliwe upya. Waziri Mpango aweze kuleta hoja hapa ili hizi kodi ziweze kuangaliwa upya ziweze kusababisha wafanyabiashara walipe kodi bila kukwepa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachonisikitisha ni kwamba badala ya TRA kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kwa wananchi inatumia nguvu kukusanya kodi. Mfano kama mfanyabiashara au wale wanaoendesha bodaboda amekwenda kuchukua cement moja Kenya anaileta huku, wanatumia gharama kubwa kufukuza vijana hawa na mwishoni vijana hawa wamekuwa wakiumia na wengine hata kufariki wakitumbukia kwenye mitaro na kujigonga pembezoni mwa barabara. Naamini njia pekee ambayo tungeweza kufanya ni TRA kukaa chini na wafanyabiashara waone umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari bila kufukuzana nao. Pia kutoa elimu kwa wananchi, mfano, ukienda kununua spear dukani unaambiwa bei mbili; ya kwanza unaambiwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Kengele imegonga Mheshimiwa.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge hoja mkono lakini pia nina mambo mengi ya kusema. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Afya ambayo ni muhimu sana katika Taifa letu. Mtu yeyote asipokuwa na afya nzuri hawezi kuzalisha au kuwa na amani kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa sababu wameweza kujenga zahanati zaidi ya 423 na vituo vya afya zaidi ya 449 na Serikali imeweza kukarabati Hospitali za Halmashauri zaidi ya 22 na Hospitali za Rufaa zaidi ya 23. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 102.9 kwa ajili ya kukarabati na kujenga Hospitali za Rufaa katika Mikoa ya Geita, Katavi, Njombe, Simiyu na Mara. Kwa hivyo, ninayo sababu ya kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya katika kipindi hiki cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ninayo machache ambayo napenda kuishauri au kuisemea Serikali ili iweze kufanya marekebisho. Kwa mfano, katika Jimbo langu la Tarime Mjini tunayo hospitali moja ya Halmashauri, kituo cha afya kimoja na zahanati tatu, ukilinganisha na idadi ya watu iliyopo na jiografia ilivyo bado vituo hivi vya afya havikidhi mahitaji katika kuhakikisha kwamba watu wa Tarime wanakuwa na afya nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika Hospitali ya Bomani mara nyingi kilio kinakuwa hakuna dawa, hakuna siku mgonjwa atakwenda pale aweze kupata dawa na matibabu yaliyostahili lakini sababu kubwa ya ukosefu wa huduma hii nzuri ni kama zifuatazo. Moja, tulihitaji madaktari zaidi ya 16 katika hospitali ile lakini madaktari waliopo ni watano peke yake na unajumlisha pamoja na DMO. Sasa ukiangalia idadi ya watumishi hawa haitoshelezi, mtu anafanya kazi usiku na mchana kiasi kwamba anachoka hata kuhudumia, wagonjwa wanapata wakati mgumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ipo changamoto, kwa kipindi hiki ambapo barabara imekatika na mawasiliano ya barabara hayapo, unakuta hakuna zahanati za kutosha ambazo zinaweza zikahimili watu kupata huduma kwa karibu. Kutokana na hali hiyo watu wengine hufia njiani na akina mama hujifungulia njia kwa kukosa huduma ya afya kwa karibu. Kwa hivyo, nashauri tupate zahanati katika kila kata kwa mfano Kata za Kebaga, Ketare, Nyandoto, Bomani, Nyamisangura, Kenyamanyori pamoja na Sabasaba. Zahanati hizi zitaweza kutoa huduma karibu badala ya watu wote kusongamana katika Hospitali ile ya Bomani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine inayopelekea huduma kuwa siyo nzuri katika hospitali ile ni kutokana na hospitali ile kuwa kongwe, toka miaka mingi iliyopita ni hospitali ambayo Halmashauri zaidi ya tatu zimetoka pale: Hamashauri ya Rorya, Halmashauri ya Tarime Vijijini imetoka pale na Tarime Mjini. Watu wana imani sana na hospitali ile na hivyo basi wengi wanakuja kutibiwa pale, kwa hiyo, dawa zinazokuja katika hospitali ile zinachangiwa na Halmashauri zote tatu. Naomba hospitali ile ikiwezekana ipandishwe daraja iweze kuwa Hospitali ya Kanda ili at least iweze kupata dawa na madaktari wa kutosha ili watu wetu waweze kupata huduma inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika hospitali ile unakuta hakuna damu na sababu kubwa si kwamba watu wa kuchangia damu hawapo isipokuwa damu inapopatikana pale lazima ipelekwe Bugando ili iweze kupata vipimo na iweze kurejeshwa. Hata hivyo, ili majibu yaweze kurudi inachukua zaidi ya mwezi mmoja na kusababisha damu kukosekana katika hospitali yetu ya Tarime. Naomba Waziri aweze kutujengea kituo pale Mkoani ili huduma hii ya kupima damu iweze kupatikana kirahisi hatimaye kusiwepo na upungufu wa damu katika hospitali zetu. Hii si kwa Mkoa wa Mara peke yake ninaamini katika nchi nzima damu bado ni changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu huduma inayotolewa kwa akina mama wajawazito, wazee pamoja na watoto. Hii imekuwa ni kero na kila Mbunge anayesimama hapa anaongelea kuhusu suala hili. Mimi nilikuwa naona kama Mheshimiwa Waziri huduma hii hawezi kuitoa vizuri basi tuangalie namna nyingine ambayo tunaweza kufanya ili wazee, akina mama wajawazito na watoto waweze kupata huduma kama inavyostahilli. Wanakwenda pale wanaandikishwa lakini bado hawapati dawa na hatimaye wanarudi nyumbani bila kupata matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nizungumzie kuhusu huduma inayotolewa na watumishi wetu. Kwa mfano, katika Hospitali yetu ya Tarime hakuna wahudumu wanaotosheleza inafikia hatua mpaka wagonjwa wanafanya usafi. Mimi nikifika jimboni kila mtu ninayekutana naye analalamika kuhusu hospitali, tafadhali sana Mheshimiwa Waziri tunaomba sana uangalie hospitali yetu kwa jicho la pekee at least watu wale wapate huduma inayostahili, watu wengi wanafia pale kwa kukosa huduma inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho naependa kukizungumzia na kuishauri Serikali ni kuhusu kuongeza watumishi. Ukiangalia katika vituo vingine ambavyo vipo pembezoni bado watumishi hawatoshelezi kutoa huduma katika vituo au zahanati zile zilizo pembezoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu katika ustawi wa uchumi wa nchi yetu. Nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kuhakikisha kwamba, wanapunguza malalamiko na kero ambazo zinakabili Watanzania katika idara hii ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusoma majukumu ya Wizara hii ambapo miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na kutatua migogoro ya ardhi na nyumba. Mengine ni kupima ardhi na kutayarisha ramani; kusimamia Shirika la Nyumba la Taifa, pamoja na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza kwa kusema haya kwa sababu katika Jimbo letu la Tarime Mjini ipo migogoro ya ardhi ambayo imechukua muda mrefu. Miongoni mwa migogoro hii ya ardhi ni pamoja na ile ya Nyagesese, lakini pia ile ya Mlima Nkongore. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyojua, mtu akitaka akuondoe utu au akufanye uwe ombaomba ushindwe kutekeleza majukumu yako ipasavyo ni pale anapokunyima uhuru wa kumiliki ardhi. Unapokuwa huna ardhi maana yake utakuwa mhamiaji, utakuwa kibarua na vilevile utakuwa ombaomba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo letu la Tarime wapo wakazi zaidi ya kaya 10 ambao sasa hivi wanaishi maisha ya hofu, hawana shughuli za kufanya, wamekuwa vibarua katika mashamba ya wengine kwa sababu ardhi yao imechukuliwa. Ningependa nitaje hizi kaya 10 ambazo ardhi yao imechukuliwa na sasa hawafanyi shughuli zozote na wamebaki ombaomba katika ardhi ambayo wamezaliwa. Wamezaliwa pale, baba zao wamezaliwa pale na wameoa pale na sasa hivi wana wajukuu, lakini sasa hivi ardhi ile hawawezi kuimiliki kwa sababu imechukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kaya hizi ni pamoja na Kaya ya Girimu Aryuva Kisiri, Kaya ya Maro Muniko Kisiri, Mkami Marwa Mkami, Lewis Cosmas Mwita, Marwa Girima Ngendo, Marwa Kirumwa Mkirya, Nyamuhanga M. Nyasebe, Matiko Mturu, Rugumba G. Ngendo na Chacha Mukami George. Kaya hizi sasa hivi hazina sehemu ya kulima kwa sababu eneo lao limechukuliwa kwa kisingizio kwamba wanalinda Hifadhi ya Mlima Nkongole.
Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza, mwaka 2018 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ilienda katika Mlima Nkongole na waling’oa bangi pale, baada ya kung’oa bangi wakaja kwamba wanalitaifisha lile eneo ili wasiendelee kulima bangi. Toka wakati huo, mwaka 2018 wananchi hawa ambao wanaishi katika Mlima Nkongole hawana sehemu ya kulima na walikuwa wanategemea kulima katika eneo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile miji yao wengine wamejenga nyumba pale nyumba za kudumu, miji yao beacon imewekwa kwamba sasa wanatakiwa wahame katika eneo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba vitu vingine vinaumiza moyo kwa sababu watu walikuwa wanaendelea na shughuli zao za kila siku, ghafla wanasimamishwa. Ninapozungumza sasa hivi kuna watu wawili wako ndani wamekamatwa kwa sababu wameonekana wakipita pale; na huyu ni Lugumba G. Ngendo. Kwa sababu jukumu la Wizara hii ni kutatua migogoro ya ardhi, ninamwomba Waziri, mimi ninakuaminia sana Mheshimiwa kwa uchapa kazi wako mzuri, naomba utatue tatizo hili la mlima Nkongole ili watu wale wapate haki waendelee kufanya shughuli zao za kila siku kama walivyokuwa wanaendelea hapo mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza swali hili siku chache zilizopita na majibu niliyopewa hayakuridhisha kwa sababu niliambiwa kwamba Serikali ichukue eneo lile ili kulinda mazingira, lakini kigezo cha kulinda mazingira wananchi wale walikuwa wanalima, lakini waliopewa kulinda eneo lile, vile vile wanalima. Sasa najiuliza, kama walionyang’anywa eneo walikuwa wanalima na hawa waliopewa wanaendelea kulima: Je, ni nani sasa anatunza mazingira hapa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika maeneo mengi, kwa mfano ukienda Milima ya Uluguru utakuta watu wanaishi pale na ile milima kwanza ni chanzo cha maji lakini watu wanaendelea kuishi na wanaendelea kufanya shughuli zao kama kawaida; lakini ukija katika Mlima Nkongole, hata panya ukimtafuta humpati kwa sababu hakuna chochote ambacho unachoweza kuhifadhi pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana sana Mheshimiwa Waziri anaposimama kumalizia, tafadhali aje na majibu ya namna gani wananchi wa Nkongole watapata haki yako ya kuendelea kufanya shughuli zao za kila siku ili maisha yaendelee, wasiwe watumwa na wasiwe wahamiaji katika ardhi ya baba zao ambao wamezaliwa pale siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kuzungumzia nyumba za National Housing ambazo zipo katika Jimbo letu la Tarime Mjini. Kwa sababu majukumu ya Wizara ni kusimamia Shirika la Nyumba, ukienda katika nyumba zile za National Housing ni aibu sana, watu wanaziba mpaka na makaratasi ya nylon juu ili wasinyeshewe, wengine wanaweka mawe ili vile vigae visidondoke. Naomba Waziri tafadhali sana macho yako yafike pale katika nyumba zile za National Housing ili watu wale wapate kuishi mazingira rafiki kama ilivyo, lakini pia mapato ya Serikali yasipotee hivi hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nakushukuru kwa kunipa nafasi, Mungu akubariki sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika bajeti yetu hii ya mwaka 2021/2022. Nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti ambayo kwa kweli imekoza kila mtu. Imegusa wafanyabiashara, wamachinga, wakulima, wafanyakazi, wafugaji na wavuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya yote, Mheshimiwa Rais wetu Mama yetu ameweza kufanya jambo lingine la kipekee kwa kutoa shilingi milioni 500 kwa kila Jimbo. Tayari fedha ile imeingia, nimefanya mazungumzo na Meneja wa TARURA kuongeza Kilometa moja ya lami katika Mji wetu wa Tarime Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nitakuwa sina fadhila kama sitampongeza na kumshukuru kwa shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari katika Jimbo letu la Tarime Mjini ambapo tulikuwa hatuna Sekondari katika Kata ya Saba Saba, sasa inakwenda kujenga. Nampongeza na ninatoa shukrani sana kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na watalaam wote katika Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, kuhakikisha kwamba wanatuletea bajeti ambayo imeshiba. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Nchemba pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Masauni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kutoa mchango wangu kwa upande wa tozo au ushuru kwa bidhaa zinazotoka nje. Ukienda katika nchi jirani ya Kenya unapokuwa unatoa bidhaa hapa unapeleka Kenya, kwa mfano kama sasa hivi juice hizi za Azam zinavuka sana kwenda Kenya, wewe unavusha tu hamna usumbufu wowote unaopatikana katika upande ule. Wafanyabisahara wanaovusha bidhaa zile wanapita custom kawaida, wanapita wanalipa ushuru na bidhaa zao wanafanya biashara kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukitolea mfano mwingine ng’ombe wanatoka Tanzania kwa wingi sana wanapita tena pale mpakani bila shida yoyote wanavuka na wanaenda wanauza bila shida yoyote. Sababu kubwa inayosababisha biashara hii iweze kufanyika vizuri ni kwa sababu ushuru wa Kenya uko chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuchukue mfano katika Mji wetu wa Tarime nyumba zinajengwa kila siku, wakati wanajenga wanatumia simenti, mabati, misumari, na kadhalika lakini sasa tuchukulie mfano wa simenti inayozalishwa Tanzania inauzwa shilingi 22,000 mpaka shilingi 24,000 ilhali simenti ambayo inatoka Kenya inauzwa shilingi 16,000 mkapa shilingi 17,000, sasa kwa mkulima au mtu wa kawaida pale Tarime kununua simenti shilingi 22,000 na huku anajua kwamba, kuna simenti hapa inauzwa shilingi 17,000 inakuwa ni ngumu kidogo. Nini kinafanyika sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika sasa vijana wanaamka wanaanza kufanya wanapita njia panya road kupitisha ile simenti na matokeo yake Serikali inapoteza mapato makubwa sana. Mimi ningeshauri Serikali waangalie, wajifunze kutoka katika nchi ya Kenya walifanyaje ili wafanyabisahara waweze kulipa kodi kwa hiyari badala ya kufukuzana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale kuna vifo vinatokea mara kwa mara pale na hivi vinatokana na vijana ambao wanasomba hizi bidhaa au magendo kutoka nchi ya Kenya kuanguka au kugongwa pale ambapo wanafukuzana, hii inatokana na kwamba, anapopita alipe ushuru kawaida ushuru ule unakuwa ni mkubwa zaidi kiasi kwamba, hawezi kupata faida, lakini iwapo kama ushuru huu ungekuwa wa kawaida kama nchi jirani…
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kembaki kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Abdullah Mwinyi.
T A A R I F A
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ningependa tu kumpa taarifa mchangia mada taarifa ya kwamba, simenti ya Kenya kwa mujibu wa Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikija Tanzania haitozwi kodi na simenti ya Tanzania ikienda Kenya haitozwi kodi, taarifa.
NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana. Mheshimiwa Kembaki unapokea taarifa hiyo?
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mimi naona inatozwa na ndiyo maana wanafukuzana. Kwa hiyo, nikipokea na ilhali kuna kufukuzana na inakamatwa na hivi juzi punde tu TRA imegawa zaidi ya simenti 150 kwa shule za sekondari na msingi ambazo zimekamatwa kutokana na hii biashara ambayo wafanyabiashara ambao wanafanya magendo katika barabara hii ya Sirari.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, sipokei hiyo taarifa. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Sasa ili taarifa zetu rasmi za Bunge zikae vizuri, hao wamepokonywa kwa sababu ya kodi au wamepokonywa kwa sababu ya magendo?
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wananunua simenti Kenya wanaileta Tarime. Kwa hivyo, wakati wanaleta wanakamatwa.
NAIBU SPIKA: Wanaileta kwa njia ya magendo ama wanaileta kwa njia halali?
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, wanaileta kwa njia ya magendo, kwa jina maarufu njia za panya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, kwa njia hii kumbe kuna haja ya Serikali kutoa elimu kwa wafanyabiashara elimu ambayo itasaidia wafanyabiashara kujua hizi namna ya kupitisha au namna ya kuagiza bidhaa kutoka nchi nyingine ili kuepuka ukwepaji kodi au hii bidhaa kupita kwa njia ya magendo. Ukweli ni kwamba, Serikali ikifanya hivi kwa kutoa elimu ya kutosha pia kuhakikisha kwamba, hizi tozo au ushuru unakuwa wa chini kwanza itahamasisha watu kulipa kodi wenyewe kwa hiyari, lakini pia itasababisha Serikali kupata mapato yake bila usumbufu wowote ikilinganishwa kwamba, mipaka ya nchi yetu na wafanyakazi walioko TRA hawatoshi kudhibiti haya mazingira ya ukwepaji au utoroshaji wa bidhaa ambazo zinaingia nchini. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia, Serikali ifanye utafiti wa kina ni kwa nini viwanda vyetu au bidhaa zinazozalishwa nchini zinauzwa kwa bei ya juu ikilinganishwa na bidhaa zinazotoka nje. Bila kufanya hivi bado ukwepaji kodi utaendelea, vilevile hatutapata suluhu ya nchi yetu kuwa tegemezi. Ningependa sana utafiti huu ufanyiwe kazi na baada ya utafiti huu kupatikana tutafute majibu namna gani tunaweza kutatua changamoto hizi ambazo zinasababisha bidhaa zinazozalishwa nchini kuuzwa kwa bei ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Ahsanteni sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika mada hii. Kwanza ningeanza kumshukuru Rais wetu, Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika kulijenga taifa letu la Tanzania. Kazi kubwa imefanyika katika Jimbo letu na katika nchi nzima amefanya kazi kubwa ambayo imetukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeanza kwa kusema katika Jimbo letu la Tarime Mjini kuna jambo ambalo haliko vizuri ambalo ningependa kulisemea kabla ya kuchangia mchango wangu. Katika Mji wetu wa Tarime kumetokea tatizo pale Mgogoro wa Bugosi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Mgogoro ule umepelekea ng’ombe wanafuga pale wanakamatwa, na wale ambao wanachunga wanapigishwa mazoezi kweli kweli. Mmoja wao aliniambia siku hizi amenunua buti ili akitoa ng’ombe nje aweze kufanya mazoezi, ameshaanza kuwa mwanajeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wananchi wanaishi pale na walipaswa walipwe fidia waondoke ili waweze kuendelea na shughuli zao. Sasa kama mtu anaishi pale, anafuga mifugo yake lakini mifugo haipaswi kutoka nje kwa sababu itakamatwa; na pale ambapo inakamatwa wanalipishwa faini siyo chini ya shilingi laki tano. Ningeomba Serikali ione namna gani ya kutatua tatizo hili kwa kuwalipa fidia wananchi wale ili waondoke katika eneo lile ili Jeshi liendelee na sehemu yao kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile imetolewa pesa ya kujenga barabara na Halmashauri yetu imepokea zaidi ya shilingi milioni 450 kwa ajili ya kujenga barabara. Tayari wakandarasi wamesaini mkataba na mpaka sasa barabara zile hazijaanza kujengwa. Ningeomba Serikali sasa iingilie kati ili hao wakandarasi ambao wana-sign mikataba alafu hawaingii site kujenga barabara wachukuliwe hatua ili barabara zile, kwa nia njema ya Serikali ya kutaka barabara zijengwe basi hiyo dhamira itimie kwa kuwabana hawa wakandarasi waweze kujenga barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuelekeza mchango wangu mwingine upande wa kuajiri wafanyakazi. Taswira ya taasisi ama kampuni yoyote ni wafanyakazi wake. Wafanyakazi namna wanavyofanya kazi, lugha wanayoitumia, namna wanavyojitoa katika kufanya kazi lakini pia namna wanavyojitoa kuhudumia wateja wao inaonesha taswira kamili ya taasisi husika. Na ndipo watu wanaweza kusema kwamba taasisi hii ni nzuri au taasisi hii ina tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi Watanzania tujiulize, kwamba watumishi wa Serikali na watumishi wanaoajiriwa na Serikali wakoje? Hali ikoje katika taasisi za kiserikali? Katika hospitali watumishi hawa wakoje? Shuleni na Katika taasisi zingine kama TANESCO watumishi hawa wakoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha zinazotumika katika taasisi hizo za Serikali ikiwemo hospitali haziridhishi; na hii inasababishwa na nini? Hebu turudi nyuma namna watu wanavyoajiriwa Serikalini. Kwa mfano waliomaliza elimu mwaka 2014/2015 wamekuwa nyumbani tangu 2015 mpaka 2021 walipoajiriwa. Katika kipindi hiki chote watumishi hawa ambao wameajirwa walikuwa wanaendesha bodaboda, wengine walikuwa wafanyabiashara. Sasa wanapokuja kuajiriwa baada ya miaka sita miaka mitano unakuta knowledge yake, ufahamu wake, ujuzi wake haupo tena anaenda kuanza upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inasababisha utendaji kazi kwa watumishi katika Serikali yetu unakuwa chini ya kiwango; lakini pia hata lugha zile ambazo wanatumia unakuta tayari wameingia wengine unakuta ni bodaboda, wengine ni machinga; kwa hiyo anapoenda pale anaanza kujifunza upya. Mimi ningependa kushauri itungwe sheria, kwamba wahitimu wote wanaotoka elimu ya juu wajitolee katika Idara za Serikali kulingana na idara waliopo. Kwa mfano, kama ni Madaktari wakirudi kwao waanze kujitolea katika hospitali, kama ni Walimu warudi kujitolea shuleni, kama ni Ma-engineer warudi kujitolea katika maeneo yao ili kuwasaidia ku-gain ujuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujitolea kunasaidia mtu kuweza kuongeza na kukuza maarifa. Kujitolea ni tendo la huruma, ni tendo la kuonesha fadhila kwa taifa. Lakini vile vile tukitunga sheria hii, Serikali itaondokana na uhaba wa wafanyakazi uliopo katika taasisi zetu. Kwa mfano katika Mji wetu wa Tarime madaktari sita tu kati ya 15 wanaohitajika. Lakini kuna madaktari wengi ambao wako nje ambao wamehitimu elimu lakini hawana kazi. Kwa hivyo wakijitolea, Serikali kwanza itakuwa imepata nguvu kazi itakayosaidia kulijenga taifa letu pamojan na kupunguza matatizo wanayokabiliana nayo kwenye upungufu wa watumishi katika idara mbali mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vijana wengi wanaohitimu elimu ya juu unakuta wametumia gharama ya Serikali kama mikopo lakini hawapati nafasi ya kurudisha ile mikopo kwa sababu hakuna ajira. Wakijitolea ninaamini watakuwa wamelipa fadhila kwa kodi ya wananchi wameitumia wakati wanasoma… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE: MICHAEL M. KENDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kutoa pongezi kwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuongoza Wizara hii muhimu katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa niseme kidogo kuhusiana na kazi kubwa ambayo inafanywa na viongozi wetu wa kitaifa. Wakati nikiwa mdogo mama ndiye alikuwa tegemeo kubwa katika familia, alikuwa akienda kusenya kuni akiuza ndipo tunapata riziki ya kula. Familia ilikuwa inategemea jitihada za mama, kusomesha, kula na kila kitu. Leo hii wana Tarime tunaona jitihada kubwa za mama yetu mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kulijenga Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza tayari soko ambalo lilikuwa ni tatizo kubwa katika mji wetu wa Tarime tayari limejengwa liko katika asilimia 75 ili liweze kukamilika wapate sehemu ya kufanyia biashara. Vilevile kubwa zaidi ni ule mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria. Mji wetu tulikuwa tunapata shida kubwa sana. Maji tuliyokuwa tunatumia yamechanganyikana na tope, magonjwa ya bilharzia na Magonjwa ya kuhara yalikuwa ni sehemu ya Maisha yetu. Sasa mradi huu wa maji utakuwa ni ukombozi wa wana Tarime. Kwa hiyo nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu kwa kutupa fedha za kutosha kwa ajili ya kuleta maji katika mji wetu wa Tarime.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuwapongeza mawaziri wote kwa kazi nzuri wanazozifanya, lakini niwaombe wasiwe wanakwenda kwenye majimbo yetu kimya kimya, na wakati mwingine wanakwenda bila kutoa hata taarifa kwa Wabunge. Ni matarajio ya wananchi kuona Mawaziri wakizungumza nao na kueleza mambo makubwa ambayo Serikali imefanya kupitia kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine Mawaziri wanaenda pale kinyemela kinyemela, unashtukia tu anaenda kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya, wananchi wanaambulia kuona misafara na vimuli muli vinapita. Tungependa waweze kufanya mikutano, waweze kuzungumza matendo makubwa ambayo yanafanyika kupitia Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya kazi kubwa sana kwa upande wa madarasa, vituo vya afya na kujenga hospitali. Kwa mfano, kwa kipindi cha kuanzia 2021 mpaka sasa hivi kumejengwa hospitali zaidi ya kumi za rufaa za mikoa. Vile vile hospitali 102, vituo vya afya 487 na Zahanati 1,198. Upanuzi wa vituo hivi, na madarasa unahitaji wafanya kazi ambao wanahitajika kufanya kazi katika vituo hivyo, zahanati hizi pamoja na shule ambazo zimejengwa mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini takribani wafanyakazi watumishi waliopo katika Serikali yetu ni takribani laki saba ambayo kwa ujumla kila Mbunge anayesimama anaongelea kuhusu upungufu wa watumishi katika majimbo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri jambo moja. Kila mwaka wahitimu wanahitimu katika vyuo vyetu, na wahitimu hao wanapotoka katika vyuo vyetu wanaenda kufanya shughuli ambazo haziendani na kazi walizosomea. Kwa mfano mtu amesomea udaktari ameenda kufanya kazi ya kupiga debe stendi; sasa amefanya kazi ya kupiga debe ndani ya miaka sita mfululizo. Kwa mfano ajira zilizotoka hivi juzi akaajiriwa mpiga debe ambaye amefanya kazi kwa miaka sita akaenda kutibu mgonjwa. Kama tunavyojua mtu akikaa muda mrefu bila kuendeleza taaluma yake kile anachokifanya kinaingia kichwani mwake na anaendelea kukifanya. Ni nini tunategemea basi? Hatima yake ni kwamba hatutegemei atoe huduma iliyo bora, hata kauli atakayokuwa anatoa haitakuwa kauli ya taaluma aliyoisomea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile ningependa kusema hili. Ukiangalia sasa hivi wale wanao ajiriwa loan board inaenda kuwadai walipe mikopo, na ukiangalia mishahara yao especially wale wanao ajiriwa katika sekta binafsi unakuta mtu anapata mshahara wa laki tatu, mshahara wa laki nne, anadaiwa alipe makato yote pamoja na mkopo huu wa loan board. Hii inapelekea apate kitu kidogo sana ambacho hakiwezi kustahimilisha maisha yake ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nishauri kuwepo utaratibu, sera madhubuti iandaliwe, ambayo itaruhusu wahitimu wote walio hitimu waweze kwenda kujitolea katika sehemu zao walikotoka. Kama ni madaktari waende kwenye hospitali, zahanati na vituo vya afya vilivyo katika maeneo yao. Hii itapunguza gharama za maisha kwa sababu atakuwa anatoka nyumbani anaenda kufanya kazi. Lakini vile vile wakati anajitolea Serikali ipange utaratibu mzuri waweze kuwalipia mikopo hiyo kidogo kidogo kwa sababu wanafanya kazi, ili atakapokuwa wameajiriwa at least ipunguze makali ya makato ambayo huwa wanakatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujitolea kunajenga mtu aweze kupata uzoefu, ajenge na kuwa na uzalendo wa nchi yake na pia kujitolea ni tendo la upendo. Kwa hiyo tutakuwa tumejenga uzalendo katika nchi yetu, kwamba watu wakimaliza elimu yao vyuoni watakwenda kujitolea, kwa hivyo tutakuwa na watumishi wengi, jambo ambalo litapunguza uhaba wa madaktari, walimu na watumishi katika idara zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, hili nilishalisema, lakini ninarudia kusema kwa sababu ninaona kwanza huduma zinazotolewa katika taasisi na idara zetu za Serikali wakati mwingine zinakuwa ni chini ya kiwango kwa sababu watu waliotoka pale ni wametoka direct kutoka kupiga debe, kuendesha boda boda, wakulima na ile fani ambayo waliisomea hata imesha yeyuko kutoka kwenye akili zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ichukue hili kwa u-serious ili iweze kulifanyia kazi na tuondokane na tatizo la upungufu wa watumishi katika idara zetu. Lakini vile vile itasaidia kujenga uzalendo na vijana wetu kupata ujuzi wa kufanya shughuli zao kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,ukiangalia katika Sekta ya elimu, kwa mfano kwa mwaka 2020, utafiti uliofanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya BEST ilibainisha kwamba kuna upungufu wa watumishi katika idara ya elimu zaidi ya 50,993, hiyo ni miaka hiyo kabla ya madarasa hayo kujengwa na shule kupanuliwa. Kwa hiyo sasa hivi kutakuwa na uhitaji mkubwa wa watumishi katika sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuondokana na tatizo hili, ambalo ni kubwa na ni sugu katika nchi yetu. Najua kwamba si Tanzania peke yake, ni nchi nyingi, ningependa sana Serikali kupitia Wizara hii wafanye mchakato wa kuandaa sera ya kuhakikisha kwamba wale wahitimu wanaotoka katika Vyuo vyetu wanapata nafasi ya kujitolea katika maeneo yao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika sekta hii ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyoelewa nchi yetu asilimia kubwa ya wananchi wetu wanategemea kilimo ili kujipatia kipato cha kila siku, matatizo mengi yanaweza kutatuliwa kupitia sekta hii ya kilimo ikiwemo chakula, pesa za kigeni, malighafi katika viwanda vyetu na ajira kwa vijana wetu. Majibu ya matatizo haya yanayoikabili nchi yetu yanaweza kutatuliwa pale ambapo Serikali itawekeza na kuipa kipaumbele sekta hii ya kilimo ambapo itaweza kutatua changamoto ya ajira katika nchi yetu lakini pia kupata malighafi za kutosha katika viwanda vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya kazi nzuri na kuwekeza pesa nyingi katika upande wa utafiti. Kama unavyojua ili kilimo chetu kiweze kufanya vizuri Serikali inapaswa iweke pesa nyingi katika utafiti, maana utafiti utaweza kuleta majibu ni wapi tunaweza tukalima mazao mazuri na yakafanya vizuri. Pamoja na kuwekeza pesa nyingi katika utafiti, umwagiliaji bado tija ni ndogo sana, hauleti majibu ambayo yanatosheleza. Kwa mfano, tunavyo vituo vingi vya utafiti katika nchi yetu mfano tunavyo vituo vikuu ambavyo ni TARI Kihinga, Ilonga, Tumbi, Buyola, Makutupola, Seyani, Ukiriagulu, Naliendele Mlingano, lakini pia tunavyo vituo vidogo ambavyo ni TARI Mikocheni, Tengeru, Naruku, Dakawa, Ifakara, Hombolo na Kifyulilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na vituo hivi vyote, Serikali imekuwa ikipeleka pale pesa nyingi, utafiti umekuwa ukifanyika na majibu yanapatikana. Mfano, tulitembelea Kibaha tulipata watafiti wamefanya kazi nzuri sana, kuna muhogo mkubwa ambao ni zaidi ya kilo tano uko pale na umekuwa kama maonyesho katika kituo kile. Pia wataalam wale wamegundua wadudu rafiki ambao wakitumika badala ya kutumia viuatilifu ambavyo ni hatari kwa afya ya binadamu, lakini pia wamegundua hazina kubwa ya tafiti ambazo ni za udongo ambao unafaa na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti hizi ambazo zinagunduliwa na wataalam wetu haziwafikii wakulima wetu. Ni masikitiko yangu kwamba, pale katika Jimbo langu la Tarime Mjini, tumeshaacha kulima zao la muhogo, kwa sababu wadudu wanashambulia muhogo na haufanyi vizuri. Vilevile kuna ugonjwa ambao unashambulia migomba na wataalam hawa wamegundua mbegu nzuri ambayo wakulima wakilima haishambuliwi na magonjwa, lakini bado wakulima hawafikiwi na tafiti hizi ambazo zinafanywa na wataalam wetu. Pamoja na kwamba Serikali inatoa pesa nyingi katika tafiti lakini haifikishi kwa wakulima, hivyo haina tija kwa sababu walengwa wakubwa ni wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa niseme hakuna haja ya kutoa fedha kwa watafiti ambapo tafiti hizi zinawekwa kwenye madroo na zinawekwa kwenye makabrasha badala ya kuchukuliwa na kupelekwa kwa wananchi. Nitoe ushauri wangu kwa Serikali wanapokuwa wanatenga fedha kwa ajili ya utafiti, watenge fedha kwa ajili ya kupeleka ujumbe au matokeo ya tafiti zinazopatikana kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivi, kwa sababu kazi yote tunayojadili hapa, hoja zote zinazotolewa na Wabunge hapa, lengo lake ni wakulima ambao wengi wao wako vijijini hawako mjini. Mara nyingi wanapofanya maonyesho, wanafanya mjini wanaacha wakulima pale vijijini. Ningependa Waziri wa Kilimo kaka yangu, ahakikishe fedha zitengwe kwa ajili ya kuwafikia walengwa ambao ni wakulima, wapate taarifa sahihi. Kwa kufanya hivi wakulima…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana kwa mchango mzuri, mengine andika.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu.
Kwanza kabisa ningependa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anawajali wana wa Tarime. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana kwa sababu kulikuwa na tatizo kubwa sana katika Jimbo letu la Tarime Mjini ambapo kulikuwa na madai ya muda mrefu ya fidia katika Mtaa wa Kinyambi na Bugosi ambapo kulikuwa na mgogoro kati ya Jeshi na Wananchi wa Mtaa ule. Mheshimiwa Rais alitoa pesa na wale wananchi wakalipwa. Kwa niaba ya wana wa Tarime nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo aliweza kusikiliza kilio chao na kuweza kuwalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tulikuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa soko katika Mji wetu wa Tarime. Ametoa zaidi ya shilingi bilioni 9.5 na ujenzi ule sasa unaelekea kukamilika na sisi tunategemea wafanyabiashara wa Tarime wapate sehemu ya kufanyia biashara ambayo ilikuwa ni tatizo kubwa katika kipindi cha muda mrefu. Hizi ni baadhi ya mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya katika kipindi cha miaka mitatu cha uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nichangie Mpango kuelekea katika upande wa vijana. Ukizingatia kwamba vijana ni wengi katika nchi hii na vijana wengi hawana ajira, ningependa niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Fedha kwa namna ambavyo wamekuja na Mpango mzuri ambao umezingatia vile vile vijana kwa upande wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shabaha ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2024/2025 ulikuwa umelenga kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi ambao ni jumuishi unaopunguza umasikini, unaozalisha ajira kwa wingi, unaotengeneza utajiri na unaochochea mauzo ya bidhaa nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningependa nilenge sana upande wa ukosefu wa ajira kwa vijana. Tatizo la ajira katika Nchi yetu ni kubwa sana na ni kubwa, kubwa, kubwa, kubwa. Imekuwa tatizo kubwa mpaka watu wanapoanza kuomba ajira wanadanganya kwamba ni walemavu ili waweze kupata upendeleo wa kupata ajira. Mwaka uliopita waombaji kazi 419 walidanganya kwamba ni walemavu ili waweze kupata ajira na hii inadhihirisha ni namna gani tatizo hili ni kubwa katika Nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walioomba kazi walikuwa 171,916 na waliopata kazi katika upande wa walimu walikuwa 13,130. Katika upande wa Afya waliopata kazi walikuwa ni 5,319. Kwa hivyo jumla ya waliopata ajira kati ya 171,916 walikuwa 18,449. Kwa hivyo waliobaki 153,512 hawa walibaki bila ajira wakienda mtaani. Jumla mwaka 2014 watu 1,000,000 kwenda kuomba kazi katika idara ya uhamiaji na huku watu 70 ndiyo walikuwa wanahitajika kwa mwaka huo. Kwa hivyo watu 930 walitoka pale bila ajira na walienda mtaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umasikini Tanzania (REBOA) ya mwaka 2019, vijana 1,000,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali na uwezo wa Serikali pamoja na Sekta Binafsi wa kutengeneza ajira ni 2,500. Unaweza kuangalia namna tatizo hili lilivyo kubwa ndiyo maana tunao machinga wengi mitaani, tunao boda boda wengi ambao hawapendi kufanya ile kazi lakini kwa sababu hawana kazi ndiyo maana wamejiingiza katika kazi ile ili waweze kupata at least kipato cha kuwaweka waendelee kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo letu la Tarime Mjini wapo watu waliojiwekeza kuchimba madini wadogo wadogo. Katika kuchimba wanapokuwa wametoka shimoni wamechimba madini yao, wanapotoka nje tayari wanatozwa ushuru bado hawajauza lakini bado hata hawajapata chochote kutokana na wanatozwa kulingana na udongo waliopata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna vijana ambao wanatoa bidhaa Kenya wanakuja kuuza Mji wa Tarime. Kutokana na kwamba bidhaa nyingi ambazo zinatoka Kenya kuja Tarime pale at least bei yao inakuwa chini. Anapokuwa amepita na cement 10 kwamba aje auze Tarime hawezi kulipa kodi kwa sababu mfumo hauruhusu kulipa kodi bidhaa ndogo ndogo. Hii inasababisha vijana wale wapite kwa njia ya magendo na Serikali inapoteza fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili ndilo lililosababisha Serikali ikaja na Mpango wa Maendeleo 2024/2025 na katika Mpango huu kuna Program ya Taifa ya kukuza ujuzi Nchini lakini pia kuna Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Ningependa nizungumzie Program ya Taifa ya Kukuza Ujuzi Nchini. Program hii iliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali pamoja na Sekta Binafsi kwamba waweze kutoza fedha kwa ajili ya kugharamia kukuza ujuzi wa vijana wetu kwa lengo la kuzalisha ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, makubaliano yalikuwa kwamba asilimia moja ya tozo hizo iweze kupelekwa kwa ajili ya kuendeleza ujuzi wa vijana. Kwa mwaka 2021 na 2022 makusanyo halisi yalikuwa shilingi bilioni 291 na kwa asilimia moja ilipaswa shilingi bilioni 97 ziende kuendeleza ujuzi wa vijana wetu lakini mambo yalikuwa tofauti. Mwaka 2015/2016 walipeleka shilingi bilioni 15, 2016/2017 walipeleka shilingi bilioni 15, 2017/2018 walipeleka shilingi bilioni 15, 2018/2019 walipeleka shilingi bilioni 15, 2019/2020 walipeleka shilingi bilioni 18, 2020/2021 walipeleka shilingi bilioni 18. Kuanzia 2021 mpaka 2022 walipeleka shilingi bilioni tisa, 2022/2023 wamepeleka shilingi bilioni tisa. Hii imesababisha vijana ambao walikuwa wananufaika 42,000 imeshuka sasa mpaka vijana 12 peke yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na Mpango, vijana 681,000 walipaswa wanufaike na Mpango huu ndani ya miaka mitano lakini kwa namna ambavyo wanapeleka…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)