Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Michael Mwita Kembaki (19 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI Aliuliza: -

Serikali ilichukua eneo la Mlima Nkongore ambao ndani yake kulikuwa na makazi ya wananchi na kuliwekea beacon na kusababisha kaya zaidi ya 10 zilizochukuliwa maeneo hayo kuishi kwa hofu.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzilipa fidia Kaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mlima Nkongore uliopo katika Halmashauri ya Mji Tarime una eneo lenye ukubwa wa ekari 266.65. Wananchi wanaozunguka eneo hilo walikuwa wakiutumia Mlima Nkongore kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ukataji kuni, uchomaji mkaa na kilimo kinyume na taratibu za Mamlaka ya Upangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Mlima Nkongore ni moja ya eneo lililokuwa limekithiri kwa shughuli haramu ikiwemo kilimo cha bangi. Hivyo, mwezi Novemba, 2017 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime ilikabidhi eneo hilo kwa Jeshi la Magereza ili kuhakikisha kuwa eneo hilo linalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 58(1) na (2) ambacho kinazuia kufanya shughuli zozote zinazoweza kusababisha hifadhi ya mlima kuharibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira inakamilisha taratibu za kulifanya eneo la Mlima Nkongore kuwa hifadhi. Hivyo, eneo la Mlima Nkongore litaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Magereza hadi taratibu zitakapokamilika na kulitangaza kuwa eneo la hifadhi, ahsante.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaupatia ufumbuzi mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wa kazi wa Mtaa wa Kinyambi na Bugosi katika Halmashauri ya Mji wa Tarime?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali na kwa ruhusa yako naomba nimshukuru Mungu kwa afya na kuniwezesha kusimama hapa. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais mama yetu mama Samia Suluhu Hassan kwa kuniacha niendelee kutumika kwenye Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kama Waziri. Baada ya shukrani hizo naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kambaki Michael Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wananchi waliokuwepo kabla ya eneo kuchukuliwa na Jeshi hawajalipwa fidia. Uthamini uliofanywa na Halmashauri ya Tarime ulikamilika na ambapo kiasi cha shilingi 1,651,984,692.76 zilihitajika. Jedwali lilipelekwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali mwezi Machi 2020 kupata idhini na lilirejeshwa Tarime kwa marekebisho.

Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2021 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliwasiliana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na majibu yaliyotoka ni kwamba, uthamini huo utarejewa kwa kuwa ulifanywa kwa muda mrefu na pia baadhi ya nyaraka zilikosekana kuhalalisha fidia hiyo.

Mheshimiwa Spika, Wananchi wa Mtaa wa Kinyambi na Bugosi wanaombwa wawe na Subira katika kipindi hiki ambacho Halmashauri inafanya taratibu za kurejea uthamini huo. Utaratibu wa uthamini utakapokamilika Serikali italipa fidia kwa wananchi hao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, ni sheria ipi ambayo ilitumika kuchukua ardhi ya Mlima Nkongore kutoka kwa wananchi na kulipatia Jeshi la Magereza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi. Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mlima Nkongore upo katika Halmashauri ya Mji Tarime na una eneo lenye ukubwa wa ekari 266.65. Eneo hilo halina mchoro wa mipango miji na halijamilikishwa. Wananchi wanaozunguka eneo hilo walikuwa wakiutumia Mlima Nkongore kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ukataji kuni, uchomaji mkaa na kilimo, shughuli ambazo zilikuwa zinahatarisha mazingira ya Mlima Nkongore.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Novemba, 2017 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime ilikabidhi eneo hilo kwa Jeshi la Magereza ili kuhakikisha kuwa eneo hilo linalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 kwa maana ya Environmental Management Act, 2004; kifungu cha 58(1) na (2) ambacho kinazuia kufanya shughuli zozote zinazoweza kusababisha hifadhi ya mlima kuharibiwa. Halmashauri ya Mji Tarime kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inakamilisha taratibu za kulifanya eneo la Mlima Nkongore kuwa hifadhi. Hivyo, eneo la Mlima Nkongore litaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Magereza hadi hapo taratibu zitakapokamilika na kulitangaza kuwa eneo hilo kuwa hifadhi.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kuharakisha utoaji wa matokeo ya tafiti za ndani za tiba asilia za kutibu maradhi mbalimbali kama inavyofanya kwenye tafiti za nje ya nchi kwa kuziundia Tume ya Jopo la Wachunguzi mapema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa taarifa za utafiti mbalimbali zinazohusiana na dawa za asili zilizofanywa kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zinazolenga kuonyesha ufanisi na usalama wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili mpaka Septemba 2021, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi ya NIMR, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC, zilitekeleza utafiti wa ufuatiliaji wa ufanisi wa dawa saba za asili zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa lengo la kupambana na maambukizi ya UVIKO-19. Matokeo ya utafiti huu yalitolewa na kutangazwa kwa umma kupitia vyombo vya habari mbalimbali. Ahsante. (Makofi)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, kwa nini darasa la saba wanafanya mtihani wa Taifa mwezi Septemba, wakati mtaala unaelekeza masomo yakamilike mwisho wa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala wa elimu unaelekeza mwanafunzi kutumia siku 194 za mwaka kwa masomo. Aidha, mtaala wa elimu pamoja na masuala mengine umezingatia muda wa kufanyika kwa mitihani ya ndani na ile ya Kitaifa. Hivyo, kukamilika kwa ufundishaji na ujifunzaji wa maudhui ya muhtasari kwa darasa la saba hutegemea zaidi mpango kazi wa Mwalimu. Kwa msingi huo, hadi kufika mwezi wa Septemba walimu wa darasa la saba hupaswa kuwa wamekamilisha kufundisha mada zilizobainishwa katika muhtasari ili kutoa nafasi ya ufanyikaji wa mitihani ya Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanyikaji wa mitihani ya kitaifa ya darasa la saba mwezi Septemba unasaidia kutoa nafasi kwa zoezi la usahihishaji na utoaji wa matokeo kwa wakati ili kutoa nafasi kwa wazazi na walezi kufanya maandalizi ya kuwawezesha watoto wao kujiunga na masomo ya ngazi nyingine za elimu ambapo masomo yanaanza Januari mwaka unaofuata. Ninakushukuru.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha matokeo ya tafiti za kilimo yanawafikia wakulima?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha matokeo ya tafiti za kilimo yanawafikia wakulima, Taasisi za Utafiti na Idara ya Ugani hutumia njia mbalimbali kufikisha taarifa za utafiti na matumizi ya teknolojia ambazo ni pamoja na kufungua mashamba darasa na mashamba mfano katika maeneo ya kilimo, kutengeneza na kusambaza majarida ya tafiti za kilimo, uwezeshaji wa shughuli za ugani, kuwepo kwa siku ya mkulima, warsha kwa wadau, ushirikishwaji wa wakulima kwenye tafiti na kukusanya takwimu za kiutafiti.

Mheshimiwa Spika, vilevile, safari za mafunzo, vituo mahiri na atamizi vya uhaulishi teknolojia katika viwanja vya Nanenane, maonesho ya kilimo na biashara, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii. Vilevile simu za kiganjani, maandiko ya kisayansi na machapisho.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Taasisi za Utafiti zimeshiriki katika maonesho ya Nanenane yaliyofanyika Kitaifa Jijini Mbeya katika Kiwanja cha John Mwakangale na Viwanja vingine vya Kikanda.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, ni lini chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime TC kitaanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Magena kilichopo Halmashauri ya Mji wa Tarime kimekwishakamilisha ujenzi wa Jengo la kuhifadhia maiti. Aidha, Halmashauri inaendelea na taratibu za ununuzi wa jokofu la kuhifadhia maiti baada ya kupokea fedha za ununuzi wa vifaatiba shilingi milioni 150 kutoka Serikali Kuu katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani kuondoa tatizo la wanafunzi kusoma kwa zamu katika Halmashauri ya Mji Tarime?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime imeshatenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ili kuondoa msongamano wa wanafunzi pamoja na kuondoa tatizo la wanafunzi kusoma kwa zamu. Baadhi ya maeneo tayari wananchi wameanza kujenga shule, mfano Kata ya Turwa, Chirya, Kenyamanyori.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jitihada hizo za wananchi, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, hii itasaidia kuongeza madarasa katika shule za msingi na hivyo kuondokana na msangamano wa wanafunzi darasani.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, kwa nini ujenzi wa barabara ya Tarime – Nyamwaga – Serengeti umeanzia katikati badala ya kuanzia Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandaasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Singida kuanzia Sabasaba – Sepuka – Ndago – Kizaga yenye urefu wa kilometa 77.6 amepatikana na mkataba wa ujenzi unatarajiwa kuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023, ahsante.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023, Serikali kupitia Mradi wa SEQUIP ilitoa shilingi bilioni 1.054 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za Gicheri na Nyagisese zenye miundombinu yote ya madarasa, maabara, jengo la utawala na chumba cha kompyuta. Shule hizo zitakapokamilika zitaongezewa miundombinu ya mabweni ili ziweze kudahili wanafunzi wa kike.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kutatua kero zinazowakabili wachimbaji na wasafirishaji wadogo wa dhahabu Mgodi wa Kebaga?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Kebaga kilichopo Wilaya ya Tarime kina madini ya dhahabu ambayo wachimbaji wadogo wanachimba.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wachimbaji hao wanafanya shughuli zao ipasavyo, Wizara kupitia Tume ya Madini imeanzisha kituo kidogo cha ununuzi wa dhahabu katika eneo la Kebaga ambapo wachimbaji huuza madini yao. Aidha, Tume ya Madini hufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji na wachenjuaji wa dhahabu wanafanya kazi hizo kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Madini na kushughulikia kero zozote zinazowasilishwa na wachimbaji wa mgodi huo, ahsante sana.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye mitaa 61 katika Mji wa Tarime?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Mji wa Tarime ina jumla ya mitaa 81. Kati ya Mitaa hiyo, Mitaa 53 ina umeme na Mitaa 28 haijapata huduma ya umeme. Mitaa minne ya Nyamiobo, Kogesenda, Itununu, na Nguku itapatiwa huduma ya umeme kupitia Mradi wa ujazilizi (Densification 2C) unaotarajiwa kuanza mwezi Agosti, 2022. Mitaa mingine 24 iliyobaki inaendelea kupatiwa huduma ya umeme na TANESCO kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kufikisha umeme katika mitaa yote katika kipindi kifupi kijacho.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza michango kwa Wanafunzi wanaojiunga Kidato cha Kwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Waraka wa Elimu Namba 5 wa mwaka 2015 iliamua kutoa Elimu Msingi kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Nne bila malipo. Azma hii ya Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ambayo ina lengo la kuhakikisha kwamba watoto wote wa Kitanzania wenye rika lengwa la Elimu Msingi wanapata elimu bila kikwazo chochote ikiwemo ada au michango.

Mheshimiwa Spika, michango inayoendelea shuleni kwa sasa ni michango ya lishe ambayo imepata kibali cha Mkuu wa Wilaya baada ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi. Michango hii ni kwa wanafunzi wote wa Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Nne.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza michango kwa Wanafunzi wanaojiunga Kidato cha Kwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Waraka wa Elimu Namba 5 wa mwaka 2015 iliamua kutoa Elimu Msingi kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Nne bila malipo. Azma hii ya Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ambayo ina lengo la kuhakikisha kwamba watoto wote wa Kitanzania wenye rika lengwa la Elimu Msingi wanapata elimu bila kikwazo chochote ikiwemo ada au michango.

Mheshimiwa Spika, michango inayoendelea shuleni kwa sasa ni michango ya lishe ambayo imepata kibali cha Mkuu wa Wilaya baada ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi. Michango hii ni kwa wanafunzi wote wa Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Nne.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza michango kwa Wanafunzi wanaojiunga Kidato cha Kwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Waraka wa Elimu Namba 5 wa mwaka 2015 iliamua kutoa Elimu Msingi kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Nne bila malipo. Azma hii ya Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ambayo ina lengo la kuhakikisha kwamba watoto wote wa Kitanzania wenye rika lengwa la Elimu Msingi wanapata elimu bila kikwazo chochote ikiwemo ada au michango.

Mheshimiwa Spika, michango inayoendelea shuleni kwa sasa ni michango ya lishe ambayo imepata kibali cha Mkuu wa Wilaya baada ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi. Michango hii ni kwa wanafunzi wote wa Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Nne.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kwa mawe Korongo la Starehe ambalo linahatarisha maisha ya wananchi wa Kata ya Nyamisangara, Tarime?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itatenga shillingi millioni 280 kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ajili ya ujenzi wa Korongo la Starehe lililopo Mji wa Tarime.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani kumaliza migogoro kati ya bajaji na daladala katika miji mingi nchini inayotokana na routes kugongana?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajaji ni miongoni mwa vyombo vya kukodi vinavyodhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kupitia Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (magari ya kukodi) za mwaka 2020 (TS 78). Daladala ni miongoni mwa vyombo vinavyodhibitiwa na LATRA kupitia Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria) za Mwaka 2020 (TS 76).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa vyombo vingine vinavyodhibitiwa chini ya Kanuni za magari ya kukodi, bajaji huwa hazipangiwi njia (route) ya kutoa huduma kama daladala. Badala yake, hupangiwa vituo vya maegesho kwa ajili ya kusubiri abiria ili wakodi na kupelekwa maeneo mbalimbali na kurejea kwenye vituo hivyo kusubiri abiria wengine. Aidha, kanuni ya 15 (h) ya Kanuni za magari ya kukodi inakataza vyombo vinavyodhibitiwa chini ya Kanuni za Magari ya Kukodi, kuingilia huduma za daladala au mabasi ya masafa marefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia LATRA imekuwa ikitoa elimu na kufanya ufuatiliaji kuhakikisha migogoro hii inakoma. Aidha, kwa sasa LATRA inahimiza madereva wa bajaji na pikipiki kuungana kupitia SACCOS kwa lengo la kuongeza elimu na usimamizi wa kundi hili. Tayari SACCOS inayojulikana kama KIBOBAT SACCOS imesajiliwa mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kufanya majiribio ya mpango huu kuanzia mwezi Februari, 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu, napenda kuchukua nafasi hii kuiagiza LATRA kuongeza udhibiti wa vyombo hivi kwa kuharakisha jitihada za kuwaunganisha madereva wa pikipiki na bajaji kupitia SACCOS kwa lengo la kuongeza udhibiti wao. Aidha, niwaombe viongozi wa Serikali kwenye maeneo mbalimbali nchini kuungana na LATRA kuhakikisha bajaji zinatoa huduma kwa mujibu wa sheria ili kuepusha madhara ya kiuchumi na kijamii tunayoyashuhudia sasa.
MHE. MWITA M. WAITARA K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italipa fidia au kurejesha maeneo ya wananchi katika Mlima Nkongore yaliyochukuliwa na Jeshi la Magereza – Tarime?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kikao cha tarehe 11 Novemba, 2017 cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya kilichojadili masuala mbalimbali ya ulinzi likiwemo suala la kilimo haramu cha zao la bangi na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti katika maeneo mbalimbali likiwemo eneo la Mlima Nkongore. Kupitia kikao hicho, eneo la Mlima Nkongore lilikabidhiwa kwa Jeshi la Magereza kwa lengo kuuhifadhi na kuulinda ili kuepusha uharibifu wa mazingira kwa kukata miti na kilimo cha zao haramu la bangi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004, kifungu cha 58(1) na (2) kinazuia kufanya shughuli zozote zinazoweza kupelekea hifadhi ya mlima kuharibiwa. Hivyo kutokana na sheria hiyo, taratibu za umiliki maeneo ya milima zinazuia kumilikishwa mlima kwa mtu yeyote, hivyo hapatakuwepo na fidia au kurejeshwa kwa eneo la Mlima Nkongore kwa wananchi, nashukuru. (Makofi)

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani kuzuia uingizaji wa bidhaa bandia kutoka nje ya nchi ambazo ni hatari kwa watumiaji?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Serikali kupitia Tume ya Ushindani (FCC) inachukua hatua mbalimbali ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na uingizaji wa bidhaa bandia kama ifuatavyo:-

(i) Kuimarisha ukaguzi katika bandari na mipaka ikiwa ni pamoja na ufunguaji wa Ofisi mpya katika Kanda ya Magharibi (Kigoma) na Kanda ya Kusini (Mtwara);

(ii) Kuimarisha shughuli za ufuatiliaji katika soko na utoaji wa elimu kwa wadau ili kutambua na kuondoa bidhaa bandia sokoni;

(iii) Kushughulikia malalamiko juu ya uwepo wa bidhaa bandia sokoni kwa kufanya kaguzi za kushitukiza katika maeneo na maduka yanayodhaniwa kuwa na bidhaa bandia;

(iv) Kuimarisha ushirikiano na wadau wa biashara, ikiwa ni pamoja na Jumuiya za Wafanyabiashara hususan katika Soko la Kariakoo, wasambazaji na wauzaji ili kuunda umoja dhidi ya bidhaa bandia; na

(v) Kuimarisha mfumo wa kisheria unaohusiana na hatua za kudhibiti bidhaa bandia ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya sheria iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia uzalishaji na uingizaji bidhaa kwa kuzingatia ubora, usahihi wa alama na mahitaji ya nchi ili kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi na jamii, nakushukuru.