Primary Questions from Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu (22 total)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa bila malipo huduma za uzazi wa mpango na za afya kwa Wajawazito na Watoto chini ya umri wa miaka mitano kama Sera ya Afya inavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara ya kwanza kusimama hapa mbele, nitumie fursa hii kumshukuru Mungu, kushukuru Chama changu, kumshukuru Rais wetu kwa kutupa nafasi hii. Pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Siha kwa kuendelea kuniamini lakini nimshukuru mke wangu kwa kuendelea kunipa ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Sera ya Afya ya mwaka 2007, ukurasa wa 19, kifungu 5.3.4 ambacho kinahusu Afya ya mama na mtoto na Tamko la Sera Kipengele (c) Sehemu ya (i), inaelekeza huduma bila malipo kwa Huduma za Afya ya Uzazi na Watoto chini ya miaka mitano. Baadhi ya maeneo wamekuwa wakifanya kinyume na tamko la kisera na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa pale wananchi wanapotoa taarifa. Katika kipindi cha mwaka 2015-2020, Serikali ilitoa huduma kwa wenye uhitaji bila malipo likiwemo kundi hili zenye thamani ya bilioni 880.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Wizara inawaagiza Waganga Wakuu na Mikoa na Wilaya ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa utekelezaji wa sera na miongozo ya afya katika ngazi ya mkoa na halmashauri kutimiza kikamilifu majukumu yao kwa kushughulikia haraka kero na malalamiko ya wananchi pia utekelezaji wa suala hili ambalo siyo tu ni tamko la kisera lakini pia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho chama kilichounda Serikali. Ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa kimkakakti wa machinjio Iringa Ngelewala ili kuwekezaji huo uanze kuleta tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilianza ujenzi wa machinjio ya Ngelewala katika mwaka wa fedha 2008/2009. Hadi Juni, 2018 kiasi cha shilingi milioni 928.99 kilikuwa kimetumika ikiwemo shilingi milioni 550 kutoka Serikali Kuu, shilingi milioni 108 mapato ya ndani ya Halmashauri, shilingi milioni 101 kupitia programu ya kuendeleza kilimo nchini ASDP na shilingi milioni 169 kutoka UNIDO.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 mradi huu ulijumuishwa kwenye miradi ya kimkakati ya Halmashauri inayotekelezwa ili kuziongezea Halmashauri uwezo wa kutoa huduma na kukusanya mapato. Miundombinu ambayo tayari imejengwa ni pamoja na mabwawa ya maji machafu (oxidation ponds), zizi la kuhifadhia mifugo kabla ya kuchinjwa, shimo la kutupa nyama isiyofaa kuliwa na binadamu, jengo la utawala, uzio eneo la shughuli za dobi, kichomea taka, maabara na jengo la kubadilishia mavazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mradi kukamilika kwa kujenga miundombinu yote, utagharimu shilingi bilioni 1.147. Mkandarasi anaendelea na ujenzi na anatarajiwa kukamilisha mradi ifikapo tarehe 1 Agosti, 2021.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itarekebisha tatizo la Hospitali ya Frelimo ambayo inapata mgao kama Kituo cha Afya wakati ni Hospitali ya Wilaya ya Iringa tangu mwaka 2013?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwemo Hospitali za Halmasahuri hupatiwa mgao wa fedha za ruzuku kwa ajili ya uendeshaji na ununuzi wa dawa na vitendanishi na vifaa tiba kwa kuzingatia vigezo maalum vilivyowekwa. Vigezo hivyo ni pamoja na idadi ya watu wanaopata huduma katika eneo husika, umbali kilipo kituo, pamoja na idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano katika Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, utofauti wa mgao baina ya vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo Hospitali ya Frelimo na Hospitali nyingine za Halmashauri hutokana na vigezo hivyo. Hospitali ya Manispaa ya Iringa Frelimo ilisajiliwa tarehe 25 Julai, 2013 kama Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na ilianza kupokea mgao wa ruzuku ya fedha za uendeshaji kama Hospitali kuanzia Agosti, 2013 ambapo kwa mwaka huu wa fedha mpaka Machi imepokea kiasi cha shilingi 53,32.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu iliyopo katika Hospitali ya Frelimo ni pamoja na jengo la Utawala, jengo la Huduma za Wagonjwa wa Nje, jengo la huduma za Maabara, jengo la huduma za Mionzi, jengo la Ufuaji na jengo la Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto. Miundombinu inayokosekana katika Hospitali hii ni pamoja na jengo la upasuaji, Wodi za kulaza wagonjwa, jengo la kuhifadhia maiti, na jengo la kutunzia dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuongeza majengo kwenye Hospitali hii ili kuboresha huduma zinazotolewa. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea TARURA fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kuzingatia ukuaji wa kasi wa Miji na Halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/ 2022, Serikali imeitengea TARURA shilingi bilioni 400 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja. Bajeti hiyo ni ongezeko la shilingi bilioni 124.97 kutoka bajeti ya shilingi bilioni 275.03 iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja katika Mwaka wa Fedha 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, sambamba na kuipatia TARURA fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja, Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu katika miji inayokua kupitia mipango mbalimbali kama vile Mpango wa Uboreshaji wa Miji Mikakati ambayo ilihusisha Majiji na Manispaa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati (TSCP), Programu ya Kuimarisha Halmashauri za Miji 18 (ULGSP) ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP).
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na maandalizi ya Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Mijini (TACTIC) na Mradi wa Uendelezaji wa Miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam, awamu ya pili (DMDP II) kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, madaraja, stendi za mabasi na masoko.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Utalii Nyanda za Juu Kusini katika eneo la Kihesa – Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali iko kwenye hatua za awali za ujenzi wa jengo la kituo cha utalii katika eneo la Kihesa -Kilolo Mkoani Iringa, kupitia mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania - REGROW. Hadi kufikia mwezi Julai, 2021, Wizara imeajiri Mshauri Mwelekezi ambaye anaendelea na kazi ya kutengeneza Mpango wa Biashara na upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa awali wa kituo hicho. Aidha, Mshauri Mwelekezi ameshawasilisha taarifa ya awali.
Mheshimiwa Spika, lengo la kituo hicho ni kutoa huduma za utalii ikiwa ni pamoja na vibali vya kuendesha utalii, kutoa taarifa zinazohusiana na maeneo ya uwekezaji wa utalii na pia kuweka jukwaa kwa sekta binafsi kukaa pamoja na kujadiliana fursa na changamoto mbalimbali katika Sekta ya Utalii ikiwa ni pamoja na kupeana uzoefu kwenye kutoa huduma kwa watalii katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha kipengele cha “moving expenses” kilichotolewa ili watumishi walipwe fedha za nauli wakati wakisubiri mafao mengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Kanuni J(1) na J(8) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 pamoja na Waraka wa Utumishi Na. 5 wa mwaka 2008, kipengele cha moving expenses hakijaondolewa. Hivyo, Serikali imekuwa ikigharamia usafiri yaani nauli kwa watumishi wa umma kwa kuzingatia utaratibu ulioelezwa kwa kuzingatia Kanuni tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni J(6)(1) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 Mtumishi wa Umma hulipwa gharama za usafiri yaani nauli, yeye, mwenza wake na watoto au wategemezi wasiozidi wanne wenye umri chini ya miaka 18 pale anapoajiriwa, anapohama au utumishi wake unapokoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya kila mtumishi anapostaafu kulipwa gharama za usafiri kurudi mahala atakapoishi baada ya kustaafu, ni wajibu wa kila mwajiri kuhakikisha anatenga fedha za “moving expenses” kwenye bajeti. Hivyo, nitumie nafasi hii kuwakumbusha na kuwataka waajiri kutenga fedha hizi na kutekeleza wajibu wao. Aidha, nichukue fursa hii kuwataka waajiri wote kuandaa orodha ya watumishi wanaokaribia kustaafu na hivyo kurahisisha kubaini gharama halisi zitakazohitajika kuwasafirisha na kuzitenga kweye bajeti kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Kanuni J(8) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 pamoja na Waraka wa Utumishi Na. 5 wa mwaka 2008 kuhusu usafirishaji wa mizigo yaani personal effects ya watumishi wa umma, imeeleza namna ya kusafirisha mizigo ya mtumishi wa umma pale anapohama au utumishi wake unapokoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kulipa gharama za kusafirisha watumishi wa umma, familia zao pamoja na mizigo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali ipo tayari kuanzisha shule maalum kikanda ili kusaidia watoto walioathirika na ukatili wa kijinsia?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwasaidia Watoto manusura wa ukatili, ambapo imeweka mifumo mbalimbali ikiwemo; Kamati za Jamii za Ulinzi wa Wanawake na Watoto; Madawati ya Jinsia kwenye Vituo vya Jeshi la Polisi na Magereza; Vituo vya Mkono kwa Mkono kwenye Hospitali; Madawati ya Jinsia Vyuo Vikuu na Kati; Madawati ya Ulinzi wa Watoto Shule za Msingi na Sekondari; pia Nyumba Salama kwa ajili ya Manusura kupata huduma jumuishi.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kutochelewesha vibali vya kuruhusu umeme kupita kwenye hifadhi za misitu ili kuwahisha usambazaji umeme vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Misitu Sura ya 323 haijazuia upitishaji wa nguzo za umeme katika Hifadhi za Misitu hapa nchini. Kupitia Kifungu cha 26 cha Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002, utaratibu umewekwa kwa taasisi au mtu anayetaka kufanya shughuli mbalimbali ndani ya Hifadhi ya Msitu na utaratibu huo unamtaka mtu huyo au taasisi kuwa na kibali kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kinachomruhusu kufanya shughuli husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TFS kwa nyakati tofauti imekuwa inashirikisha Wizara za kisekta kukamilisha miradi ya kimkakati ya kupeleka umeme vijijini bila kuchelewa.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kurudisha uoto wa asili wa milima ya Iringa ili kuendelea kutunza mazingira yake na vyanzo vya maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Maiznigra, naomba Kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imebaini kuwepo kwa uharibifu wa mazingira unaotokana na uvamizi wa wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye milima na vyanzo vya maji katika Wilaya ya Iringa Mjini pamoja na Wilaya nyingine Mkoa wa Iringa. Kutokana na changamoto hiyo, Mkoa wa Iringa umeanzisha programu ya upandaji miti kwenye maeneo yaliyoharibiwa ambapo kila Kata imepanda miti 1,000 kwa mwaka ili kuokoa maeneo yaliyoharibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, programu hii imeimarishwa zaidi na uzinduzi wa kampeni ya ‘Soma na Mti’ iliyozinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mheshimiwa Dkt. Selemani Saidi Jafo tarehe 25 Januari, 2022 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iringa. Kampeni hii imehamasisha shule za Msingi na Sekondari za Mkoa wa Iringa kupanda miti takribani 27,656 katika maeneo mbalimbali ikiwemo shule vyanzo vya maji, mabonde, miteremko ya milima na kandokando ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha mazingira ya milima na vyanzo vya maji katika Mkoa wa Iringa yanastawi Ofisi ya Mkoa wa Iringa inaendelea kuotesha vitalu vya miche Laki Tatu kila mwaka na kuwapatia wananchi wa mkoa wa Iringa kuipanda katika maeneo yao. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, lini Serikali itapitia upya masharti ya fomu za bima ya afya ili kuondoa upotevu wa fedha za Vituo vya Afya kwa kushindwa kujaza fomu hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini na Balozi wa Afya ya Akili kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, makato ya madai ya bima ya afya kwa watoa huduma za afya hayasababishwi na vipengele vilivyoainishwa katika fomu za bima ya afya (Fomu 2A na B). Sababu za Makato ya madai husababishwa na: -
(i) Kutozingatiwa kwa miongozo ya Tiba nchini inayotolewa na Wizara ya Afya;
(ii) Baadhi ya watoa huduma kuwasilisha madai yenye udanganyifu katika utoaji wa huduma;
(iii) Kutozingatiwa kwa bei zinazoainishwa katika Mkataba wa Huduma baina ya Mfuko na Watoa Huduma; na
(iv) Kutozingatiwa kwa taratibu za uwasilishaji wa madai ulioainishwa na Mfuko kwa mujibu wa Mkataba.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali imejipanga vipi kushughulikia malalamiko kuhusu kikototoo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitangaza matumizi ya kanuni mpya ya mafao ya kikokotoo ya pensheni kuanzia tarehe 1 Julai, 2022 kupitia Gazeti la Serikali Na. 357 Toleo la Tarehe 20 Mei, 2022. Kanuni hiyo iliandaliwa kwa kuzingatia haja ya kuboresha, kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya Mifuko ya Pensheni kuwa endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua wajibu wa kuwaelimisha wananchi hususan waajiri na wanachama wa Mifuko ya Pensheni kuhusu Kanuni mpya ya Mafao ya Pensheni, elimu imeendelea kutolewa na Mifuko ya Pensheni kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA). Hadi kufikia tarehe 28 Februari, 2022, Mifuko iliweza kutoa elimu kwa jumla ya waajiri 2,927 (PSSSF), waajiriwa 318 na NSSF waajiriwa 2,609 ambapo wanachama 71,836 wa PSSSF wakiwa 19,656 na NSSF 52,180 walifikiwa na mafunzo hayo. Mifuko inaendelea kutoa elimu kama sehemu ya majukumu yao ya kila siku, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, kwa kodi ya mapato kwa wachimbaji wadogo wa madini isiunganishwe na Mineral Market Management Information System (MMMIS)?
WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze sana Taifa Stars jana kwa kutuandikia historia kubwa sana. Kiongozi akiwa na baraka malango yote yanafanyika, kila linalofanyika kwa sababu ya baraka za Mama Samia linakubali tu ndiyo maana hata Yanga tukaingia makundi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya awali, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuzitaka taasisi za umma kuhakikisha mifumo yote ya mapato na matumizi inasomana, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kuunganisha na kufungamanisha mifumo yake ya usimamizi wa mapato na mifumo ya taasisi nyingine ikiwemo mifumo ya Mineral Market Management Information System.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Tume ya Madini zimeingia makubaliano ya kubadilishana taarifa ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi. Aidha, kodi ya mapato kwa wachimbaji wadogo wa madini inakusanywa katika masoko ya madini chini ya usimamizi wa Tume ya madini kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, lini Kituo cha Utalii Kihesa Kilolo chini ya Mradi wa REGROW kitaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha taratibu zote za usanifu na makadirio ya ujenzi ikiwemo michoro ya usanifu (Detailed Design), kabrasha la zabuni (Tender Document), makadirio ya gharama za ujenzi na michoro (BOQ). Kwa sasa tunasubiri kibali cha Benki ya Dunia ili taratibu za manunuzi zianze. Tunatarajia ifikapo Julai, 2023 tuwe tumempata Mkandarasi.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbolea nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi vikiwemo viwanda vya Minjingu Mines and Fertilizer Limited na ITRACOM Fertilizers Limited kuhakikisha uzalishaji na upatikanaji wa mbolea hapa nchini unaimarika na kupunguza utegemezi wa kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi. Kupitia mpango huo, uwekezaji unaofanywa na kiwanda cha ITRACOM unatarajiwa kufikia uzalishaji wa takribani tani 1,000,000 za mbolea ifikapo Desemba, 2024. Vilevile kiwanda cha mbolea cha Minjingu kinafanya upanuzi ili kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka tani 100,000 hadi kufikia tani 300,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2023/2024 Serikali imepanga kuiwezesha Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kuipatia mtaji wa takribani Shilingi Bilioni 40 utakao iwezesha kununua na kusambaza mbolea kwa wakulima. Serikali kwa kushirikiana na kampuni za mbolea na Vyama vya Ushirika imepanga kuongeza vituo vya mauzo ya mbolea nchini ili kuwezesha wakulima kupata mbolea kwa urahisi na kwa wakati.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kugawa mizinga ya nyuki ili kubadili shughuli za kiuchumi zinazoharibu mazingira kama kukata miti na mkaa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ugawaji wa mizinga na vifaa vingine ni mojawapo ya mikakati ya Serikali katika jitihada za kuwezesha makundi mbalimbali ya kijamii kushiriki katika shughuli za ufugaji wa nyuki hapa nchini. Zoezi la ugawaji wa mizinga lina lengo la kuchochea ufugaji nyuki kwa jamii hasa zile zinazoishi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa ili ziweze kujipatia kipato na kuachana na shughuli zinazoharibu mazingira kama kukata miti na kuchoma mkaa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha uhifadhi wa maeneo mbalimbali ambapo kupitia Mradi wa REGROW imetoa elimu ya Ufugaji nyuki kwa jamii ya Tungamalenga na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kuwagawia mizinga 50 kwa kikundi cha Subira kilichopo Wilaya ya Iringa. Vilevile elimu ya ufugaji nyuki imeendelea kutolewa kwa jamii zinazozunguka hifadhi ambapo kupitia elimu hiyo wananchi wamefundishwa namna bora ya kufanya shughuli za ufugaji nyuki kwa tija.
Mheshimiwa Spika, mathalan kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara ilitoa mizinga 269 yenye thamani ya shilingi milioni 26.9 kwa vikundi 19 vya wafugaji wa nyuki katika Wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi. Vilevile Mfuko wa Misitu Tanzania umetoa ruzuku ya shilingi millioni 20 kwa vikundi viwili vya ufugaji Nyuki vilivyopo Wilaya ya Iringa. Pia, wadau wa maendeleo wametoa mizinga 260 kwa wafugaji nyuki katika Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo, itaendelea kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu bora za ufugaji nyuki ili jamii iweze kufuga nyuki kibiashara. Aidha, Mfuko wa Misitu Tanzania umekuwa ukitoa tangazo na kupokea maombi ya ruzuku zitolewazo kwa wadau wa misitu na ufugaji wa nyuki. Hivyo, Mfuko unaendelea kupokea maombi ambayo yanachakatwa ili waombaji waweze kunufaika na ruzuku hizo ikiwemo kupatiwa mizinga ya kufugia nyuki.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, ni lini ombi la kubadilishana Hospitali ya Mkoa na ya Wilaya litafanyiwa kazi kuruhusu upanuzi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, hivyo mwezi Julai 2022 timu ya wataalamu itakwenda Mkoani Iringa ili kuja na ushauri wa kitaalamu wa namna ya kutekeleza suala hili bila kuathiri mfumo wa utoaji wa huduma za afya katika Mkoa, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzisaidia Community Banks kama MUCOBA Bank Iringa ili kukuza uchumi wa Wananchi wa hali ya chini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kimfumo ili kuziwezesha benki za biashara na za kijamii (Community Banks) kukua na kushamiri, ikiwemo benki ya MUCOBA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ni pamoja na kutafuta mwekezaji mpya wa MUCOBA ambaye ni Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ); kurekebisha kanuni za usajili wa wakala wa benki kwa kuondoa kigezo cha uzoefu wa miezi 18; kuanzisha mfuko maalum wa shilingi trilioni 1 kwa ajili ya mikopo kwa benki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa wakulima kwa riba ya asilimia 3 kwa mwaka; kutoa unafuu wa kiasi cha amana ambacho benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuweka Benki Kuu kwa benki zinazota mikopo kwa sekta ya kilimo; kupunguza kiwango cha riba kinachotolewa katika akaunti za wateja wa watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi kuwa sawa na riba za amana za sekta ya benki; na kudhibiti uwiano wa gharama za uendeshaji wa benki na pato la benki usizidi asilimia 55 na mikopo chechefu isizidi asilimia 5 ya mikopo yote, ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO K.n.y. MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, lini watumishi wa umma watarekebishiwa madaraja hasa walimu waliopandishwa na kunyang’anywa mwaka 2016 - 2018 kupisha uhakiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 Serikali ilisitisha mambo mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo upandishaji vyeo ili kupisha zoezi la uhakiki wa taarifa za kiutumishi na vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua changamoto zilizojitokeza kutokana na sitisho hilo mwaka 2021/2022 Serikali ilianza kutekeleza zoezi la kuwarejesha watumishi wa umma wa kada mbalimbali kwenye nafasi na vyeo vyao stahiki kwa njia mbalimbali ikiwemo msawazo wa vyeo na mserereko wa madaraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa jumla ya watumishi 375,904 wamepandishwa vyeo wakiwemo watumishi 85,471 walioathirika na zoezi la uhakiki. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 81,503 wakiwemo walimu walioathirika na zoezi la uhakiki.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Utalii Kihesa, Kilolo chini ya mradi wa REGROW?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 26 Januari, 2024 Wizara ya Maliasili na Utalii ilisaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utalii katika eneo la Kihesa Kilolo, Mkoani Iringa kupitia Mradi wa REGROW. Aidha, tarehe 27 Januari, 2024 mkandarasi alikabidhiwa eneo la ujenzi na kuanza kazi. Mkataba huo ni wa miezi 12 na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2025. Hadi kufikia mwezi Mei, 2024 ujenzi wa jengo hilo umefikia 15% na ujenzi unaendelea.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuwahusisha vijana waliomaliza mafunzo ya JKT waliopo katika vikosi na waliohitimu katika Mpango wa Block Farming?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, udahili wa vijana wa BBT unahusisha vijana kati ya miaka 18 hadi 40, katika awamu ya kwanza vijana 120 walioshiriki mafunzo ya JKT walikuwa miongoni mwa vijana 812 wanufaika wa Programu ya BBT. Pia, kutokana na umuhimu wa Mafunzo ya JKT, vijana wote wa BBT ambao awali hawakuwa wameshiriki mafunzo ya JKT, wamepata mafunzo hayo kwa kipindi cha miezi miwili kwa lengo la kuwajengea ukakamavu na uzalendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu huo wa kuwa na vijana wenye uzalendo, tarehe 8 Agosti, 2023 Wizara ya Kilimo iliingia makubaliano (MOU) na JKT, ambapo JKT watatoa si chini ya 30% ya vijana watakaodahiliwa na 70% watatoka katika nafasi zitakazotangazwa. Hivyo, awamu zinazofuata udahili wa vijana katika Programu ya BBT utazingatia makubaliano hayo. Aidha, kwa wale waliokwishaanza wenyewe na kuwa na changamoto ya mikopo, tunawahimiza kuwasiliana na Mfuko wa Pembejeo ambao hutoa mikopo hiyo, nakushukuru.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, ni muda gani Hazina hulipa malipo ya katikati ya mwezi kwa Wastaafu kwa Mfuko ulioanza mwaka 1992 kwa kuwa hawalipwi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha inahusika kulipa michango ya mwajiri kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (PSSSF, ZSSF, WCF na NHIF) kila mwezi pamoja na malipo ya nyongeza ya pensheni. Aidha, Wizara ya Fedha hulipa pensheni za kila mwezi pamoja na mafao ya hitimisho kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina. Ahsante sana.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-
Je, ni muda gani Hazina hulipa malipo ya katikati ya mwezi kwa Wastaafu kwa Mfuko ulioanza mwaka 1992 kwa kuwa hawalipwi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha inahusika kulipa michango ya mwajiri kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (PSSSF, ZSSF, WCF na NHIF) kila mwezi pamoja na malipo ya nyongeza ya pensheni. Aidha, Wizara ya Fedha hulipa pensheni za kila mwezi pamoja na mafao ya hitimisho kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina. Ahsante sana.