Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Neema Kichiki Lugangira (47 total)

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa jitihada kubwa za kuboresha miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Conchesta kwamba tayari kazi ya kuboresha barabara ile inaendelea ili iweze kupitika ambapo sasa hivi wanafanya kazi za kuchepua maji, kuweka mawe na changarawe. Vilevile napenda kumfahamisha Conchesta kwamba mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini tumeshawasiliana na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na barabara hii itafanyiwa kazi kwa kuzingatia mpango kazi uliowasilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kuwa umuhimu wa kipande hicho cha barabara unafanana na barabara ya Kanazi - Kyaka kupitia Katoro, ni lini barabara hiyo nayo itatengewa fedha na kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Lugangira, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuboresha miundombinu ya barabara ikiwepo barabara hii ya Kanazi, Kyaka kupitia Katoro. Kimsingi tathmini na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kujenga barabara hizi unaendelea. Mpango umeandaliwa kwa ajili ya kufanya tathmini lakini kuhakikisha kwamba barabara hizi zinatafutiwa fedha ili ziweze kujengwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutekeleza mipango yake hii ya kufanya tathmini lakini pia kutafuta fedha ili barabara hizi ziwezwe kujengwa na kusogeza huduma kwa wananchi.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri na ya kina. Maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo: Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kanzidata kwa kutumia TEHAMA ili kuhakikisha kwamba wanaonufaika ni wale ambao wanakidhi vigezo vilivyowekwa na pia kuondoa mianya ya watu wanaonufaika kusajiliwa mara mbili kwenye maeneo tofauti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni je, sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba kaya ambazo hazikunufaika awali sasa zitanufaika katika hii Awamu ya TASAF III, hususan wazee siyo tu wa Bukoba Manispaa, Mkoa wa Kagera bali wa Taifa kwa ujumla? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mpango huu wa kuanzisha kanzidata ya walengwa wote wanaopokea fedha za TASAF imeanza. Mwanzo ilianza katika halmashauri 19 nchini lakini hadi hivi ninavyoongea tayari imekwenda katika halmashauri 39 na tayari tunaanza kuweka mfumo kwa ajili ya kuunganisha na NIDA, kuunganisha na mitandao yetu ya simu ili walengwa hawa badala ya kupokea fedha hizi dirishani kwa wale wanaokwenda kugawa, fedha hizi ziende moja kwa moja kwenye simu zao. Tutafanya hivi ili kuhakikisha kwamba hakuna kwanza double payment katika suala hili, kwa sababu kuna maeneo ambayo watu huwa wanalalamika mtu anapokea mara mbili au mtu akiwa hayupo watu wengine wanachukua zile fedha. Sasa ili kudhibiti hilo ndiyo maana tunakwenda sasa katika ku-roll out hii katika halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na tuta- roll out katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali lake la pili, kwamba ni lini Serikali sasa itatanua mpango huu kwa wazee ambao hawakuingia na kaya ambazo hazikuingia. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge yeye wa Viti Maalum anafahamu anatoka Kagera, lakini hata wa Jimbo la Bukoba Mjini Mheshimiwa Byabato anafahamu kwamba sasa kaya zote katika Awamu hii ya Pili ya TASAF zinakwenda kuingia kwenye mpango huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwatoe mashaka Wabunge wote wa Majimbo humu ndani na wa Viti Maalum kwamba mpango huu unakwenda kwenye kaya 1,400,000 ambayo ni sawasawa na watu milioni saba wanakwenda kunufaika na Mpango huu wa TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Hapa ningependa kuikumbusha Serikali, kwamba si mara moja, mara mbili, mara tatu; na hata hivi karibuni tarehe 25 Agosti tulimsikia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akilisemea eneo hili la ucheleweshaji wa kesi kufikia hukumu na idadi kubwa ya mahabusu. Vilevile, tulishamsikia Jaji Mkuu wa Mahakama zetu hapa nchini akilisemea pia suala hili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hivi sasa idadi ya mahabusu ni 17,000 ukilinganisha na idadi ya wafungwa ambayo ni 14,000; na wakati huo huo Serikali haitoi bajeti ya aina yoyote kwa ajili ya chakula; kwa sababu Magereza imepewa maelekezo kwamba ijitegemee kwenye chakula, sasa wale wafungwa 14,000 wanazalisha chakula kwa ajili ya kujilisha wao wenyewe na pia kulisha wale mahabusu 17,000. Je, Serikali haioni ipo haja ya kupitia upya Sheria ile ili itafute namna ya kuwawezesha hawa mahabusu angalau wazalishe chakula chao wenyewe wanachokula?

Mheshimiwa Spika, na swali langu la pili, kwa kuwa majibu ya Serikali wamesema kwamba viko vyombo mbalimbali ambavyo vinahusika kwenye kutoa hukumu hizi za kesi. Je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuweka ukomo wa muda ambao utatumika kuanzia upelelezi mpaka kutolewa kwa hukumu kwa kulingana na uzito wa kesi zenyewe? Kwa sababu, ukweli ni kwamba, tuchukulie mfano mtu amebaka halafu kesi yake inaendelea kwa miaka 10...

SPIKA: Mheshimiwa Neema inatakiwa swali. (Kicheko)

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, sawa. Kwa hiyo swali langu ni kwamba, je, Serikali haioni sasa ipo haja ya kupitia upya mfumo mzima wa Mahakama na kuweka ukomo wa muda wa upelelezi mpaka kutoa hukumu? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Lugangira kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hili la kupitisha sheria ili mahabusu waanze kufanya kazi wakati wakisubiri kesi zao kimsingi ni jambo ambalo tutakuwa tunavunja vile vile haki za binadamu. Kwa sababu wakati mtu anasubiri upelelezi wake wa kesi hajahukumiwa kuwa mfungwa, ukianza kumfanyisha kazi maana yake umemhukumu kabla ya wakati wake. Kwa hiyo, mahabusu huwa wanafanya kazi ndogo ndogo tu za usafi wa mazingira waliyopo, lakini si kuwafanyisha kazi kama wafungwa. Kwa sababu, mfungwa kifungo chake kinamruhusu sasa kufanyishwa kazi kwa ajili ya kurekebishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu hili suala la ukomo wa upelelezi, tunao ukomo wa upelelezi kutegemeana na mazingira ya kesi yenyewe. Kwa mfano, kesi nyingine zimepewa siku 60, kesi nyingine zina miezi sita, lakini kesi nyingine kulingana na mazingira yake zinaweza zikaenda muda mrefu; kwa mfano kesi za mauaji. Kwa hiyo hili linatekelezwa Kisheria.

Mheshimiwa Spika, isipokuwa kama nilivyotoa maelezo yangu kwenye jibu la msingi, kuvitaka vile vyombo vinavyohusika na michakato kuharakisha michakato. Hiyo itasaidia sana kupunguza baadhi ya kesi ambazo kimsingi zinapelekwa pale lakini zinakuwa hazina mashiko ya kuendelea kuwa Mahakamani. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa uhitaji wa stendi kuu ya mabasi uliopo kule Makete unafanana kabisa na uhitaji wa Stendi ya Mabasi ya Bukoba Mjini. Ningependa kupata kauli ya Serikali; je, sisi Bukoba Mjini tutapata lini stendi mpya ya mabasi hususan ukizingatia kwamba Wilaya ya Bukoba Mjini ndiyo reception ya Mkoa wetu wa Kagera na inaunganisha Kagera na nchi ambazo tunapakana nazo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Stendi ya Mabasi ya Mji wa Bukoba ni miongoni mwa stendi ambazo Serikali imeziwekea kipaumbele cha kutosha kwa kuhakikisha kwamba kinatafutiwa fedha; lakini pia nitaangalia kwenye miradi ile ya kimkakati ya TACTIC kama Halmashauri ya Mji wa Bukoba imo ili tuweze kujiridhisha kwamba stendi ile itakuwa sehemu ya ule mradi ambao utakwenda kuhudumiwa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Lugangira, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Steven Byabato, Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa Bukoba Mjini kwa kazi kubwa ya kufuatilia stendi hii na mambo mengine; na kwamba nimhakikishie, sisi kama Serikali tutashirikiana nao Waheshimiwa Wabunge wote kutekeleza miradi hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika nashukuru, pamoja na jitihada kubwa na nzuri za Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, bado wavuvi wadogo hususan wa kutoka Mkoa wa Kagera, Geita, Mwanza, hawanufaiki ipasavyo hususan katika uuzwaji wa samaki aina ya sangara. Nasema hivi kwa sababu, mvuvi anapouza sangara kwenye viwanda vya kuchakata wanauza sangara pamoja na mabondo ambayo yanakuwa ndani ya sangara kwa Sh.4,500 mpaka Sh.8,000 kwa kilo. Mabondo haya yana wastani wa bei kidunia kati ya Sh.1,000,000 mpaka Sh.2,000,000 kwa kilo. Kwa hiyo ningependa kufahamu, je, ni lini Serikali itaweka kisheria kuhusiana na bei ya sangara na bei ya mabondo iwe tofauti ili wavuvi wadogo wa kutoka kata…

SPIKA: Mheshimiwa Neema K. Lugangira mabondo ni nini?

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, mabondo ni mfuko wa hewa ambao unakuwa ndani ya mdomo wa samaki unamsaidia samaki kuelea, lakini mabondo hayo yanatumika kama chakula kwa wenzetu kule wa Asia, lakini pia mabondo haya yanatumika kutengeneza vipuri vya ndege, yanatumika viwandani, inatengeneza mpaka nyuzi kwa ajili ya operesheni au mtu anapoumia. Zaidi ya hapo, mabondo hayo pia yanatumika kutengeneza plastiki mbalimbali, ndio maana yanakuwa na thamani kubwa sana.

Mheshimiwa spika, kwa hiyo kwa jinsi sheria ilivyo sasa hivi, mvuvi anapokwenda kuuza samaki aina ya sangara, anauza sangara pamoja na mabondo yake ndani kwa bei ya Sh.4,500 mpaka Sh.8,000. Wakati haya mabondo peke yake yanaingizia Serikali kiwango kikubwa cha fedha kwa sababu bei ya kidunia kilo moja ya mabondo ni kati ya sh.1,000,000 mpaka Sh.2,000,000. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa kuangalia suala hili kisheria ili yule sangara anapouzwa bei iwe tofauti kwa sangara na bei iwe tofauti kwa mabondo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni kwamba katika sekta ya uvuvi lipo kundi maalum la wanawake. Wanawake wana mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa Taifa letu, lakini bado kumekuwa na changamoto kubwa ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake wanaojihusisha na sekta hii ya uvuvi. Wengi wao tukiwaliuza wanasema changamoto hii inatokana na kwamba wanawake hawana mitaji ya kutosha ya kuendesha kambi. Kule kwenye kambi wanakuwepo wanawake wanajihusisha na shughuli za uvuvi, lakini kuna ukatili wa kijinsia mkubwa sana unaoendelea.

Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kuiuliza Serikali, je haioni iko haja ya kutenga angalau asilimia 20 kutoka Mfuko wa Kuendeleza Uvuvi Nchini kwa ajili ya wanawake wanaojihusisha katika zao la samaki? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Lugangira, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mabondo ni kweli, ni boya, lililoko tumboni mwa samaki linalo msaidia katika zoezi zima la kuelea. Kwa miaka ya hivi karibuni biashara ya mabondo imekuwa ni biashara mpya, ambayo imeonekana kuwa na soko kubwa katika Nchi za Asia. Sheria na Kanuni tulizonazo hivi sasa, mabondo ni zao linalotokana baada ya kuchakatwa samaki. Kwa hiyo, kiwanda ambacho kinachakata samaki anapelekwa samaki akiwa mzima mzima.

Mheshimiwa Spika, kwa Mujibu wa Sheria za Usalama wa Chakula na Ubora wake, ni lazima yule samaki anavyofikishwa pale kiwandani apelekwe akiwa mzima mzima katika umbile lake lote. Kwa hiyo, baada ya kumchakata, ndio sasa yanapatikana mabondo na mazao mengine ambayo yote sisi katika Sheria ya Uvuvi tunayatambua ikiwemo ile skeleton, lakini vilevile kichwa, mikia, ngozi na hata mafuta ya samaki yanayopatikana katika mwili wake.

Mheshimiwa Spika, mabondo yanachukua kati ya asilimia 1.8 mpaka asilimia 2.0 ya uzito mzima wa yule Samaki. Kwa hiyo, ili upate kilo moja ya mabondo inakuhusu uwe na samaki zaidi ya mmoja, watatu, wanne hadi watano, ndio utapata kilo moja ya mabondo. Yenyewe ukubwa wake yanatokana na ukubwa wa yule samaki mwenyewe. Hata hivyo, niseme tu kwamba, rai na ushauri wa Mheshimiwa Neema Lugangira ni mzuri. Kwa kuwa sasa tupo katika utaratibu wa kuboresha sheria yetu, jambo hili ni jema, tunalichukua na sisi Serikalini tutakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, amezungumzia juu ya wanawake wachakataji na wafanyabiashara ya samaki na ukatili wanaofanyiwa katika shughuli zao hizo.

Kwanza, Sheria yetu ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003, Kipengele cha 29 kinakubali na kinatoa mamlaka kwa Wizara kuunda Mfuko wa Kusaidia Uvuvi, kwa maana hiyo pia, vilevile, sera yetu ya Uvuvi ya mwaka 2015, tumeiboresha na katika kuboresha kwetu tumeweka jambo maalum la kuwasaidia wanawake na kwa hiyo, tutakuwa na jukwaa la kusaidia wanawake. Vilevile kama hiyo haitoshi, tutatambua moja kwa moja wanawake hawa wachakataji wa samaki.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimpongeze vilevile Mheshimiwa Neema Lugangira kwa kuwa akinamama hawa wanaoshughulika na shughuli za uvuvi na uchakati na wafanyabiashara wa samaki ni miongoni mwa wapiga kura waliopiga kura kuhakikisha kwamba yeye na Wabunge wengine akinamama wanaingia humu Bungeni na kwa hivyo amechukua jukumu la kutukumbusha kama Serikali na tutalifanyia kazi ipasavyo. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, sheria zilizopo bado kuna changamoto kubwa sana katika eneo hili na ndiyo maana hata Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kimeliona hili na kimeahidi kwamba kitaelekeza Serikali kwenye ukurasa wake wa 145 inasema hivi; “Chama cha Mapinduzi kitaelekeza Serikali kuimarisha huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na matunzo kwa watoto.” Kwa msingi huu naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, je, Serikali haioni saa ipo haja ya kurekebisha sheria zilizopo ili gharama ya matunzo ya watoto iendane na hali ya uchumi wa sasa na maisha ya sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili kwa kuwa vitendo vya masuala ya familia vimezidi kushamiri; je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuanzisha Mahakama ya Familia (Family Court) kama walivyofanya kwenye Mahakama ya Ardhi ili masuala haya ya matunzo ya watoto yaweze kubebwa kwa uzito unaostahili na kupanua wigo wa haki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaungana na Mheshimiwa Mbunge kuwa kuna haja ya chombo maalum kitakachokuwa kinashughulikia masuala ya familia. Ushauri wake tumeupokea na tutaufanyia kazi kulingana na sheria zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali iweke kiwango cha matunzo kitakachozingatia hali ya uchumi ya sasa kusaidia matunzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi kuwa huduma za matunzo ya watoto umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kifungu cha 44(a) na (e) sheria hii imeipa mamlaka Mahakama kufanya maamuzi ya kuzingatia mambo yafuatayo; kuangalia kipato cha wazazi wote wawili, ulemavu wowote na uwezo wa kipato cha mzazi katika jukumu la kutunza mtoto, wajibu wa majukumu ya mzazi katika kutoa matunzo kulinganisha na majukumu ya kutoa matunzo kwa watoto, gharama za maisha katika eneo ambalo mtoto anaishi na haki nyingine za kisheria ambazo mtoto anahitaji kupatiwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nashukuru sana Serikali kwa majibu mazuri. Sasa nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni ipo haja ya kufanya tathmini ya mifuko hii ya uwezeshaji kwa kuzingatia muda mfuko ulipoanzishwa, jumla ya mikopo iliyotolewa, ruzuku na dhamana pamoja na hali ya marejesho. Na tathmini hii pia iangalie hasara na faida ili kwa kufanya hivyo, Serikali iweze kuja na mikakati ya kuimarisha utendaji wake na iwe na tija kwa maendeleo ya wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni kutokana na changamoto kubwa za ajira kwa vijana, je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuweka vipaumbele vya kutoa startup capital kwa wahitimu wa vyuo maana mara nyingi vijana hawa wanakuwa na bankable ideas lakini wanashindwa namna ya kupata mikopo, ruzuku na dhamana zenye riba na vigezo nafuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA
NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa sababu amekuwa mfuatiliaji kwa wakati wote katika masuala haya yanayohusu maendeleo ya vijana lakini pia wanawake na Watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna haja kubwa ya kufanya tathmini ya muda kuhusiana na masuala ya ruzuku na dhamana ambazo zimekuwa zikitolewa kila wakati ili kuangalia kama inaleta tija. Katika hatua hiyo, Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa tayari tumekwishakuanza kufanya zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya mifuko yote 54 na ile mitatu ambayo ipo chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tayari tumekwisha kuanza kufanya zoezi hilo ili kuweza kuangalia namna gani ambavyo itakuwa na tija zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ambayo baadhi ya hayo ambayo tumeyabaini, ukiacha kazi ya timu ambayo bado inaendelea, tumebaini kwamba katika fedha hizi nyingi zinatolewa wakati mwingine vikundi vinakuwa havijaunganishwa vizuri zaidi na tumeenda kwenye hatua ya kuona kwamba lazima sasa kuwe na tija ya kutoa mafunzo kabla ya kutoa mikopo hii. Vilevile kuweza kufanya na kuangalia yale maandiko ya mpango kazi au mpango wa biashara kwa maana ya zile business writeups ambazo zinazletwa kwa ajili ya wao kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hatua nyingine pia tunaangalia namna ya kuweza kutanua wigo wa kutoa mikopo hii au fedha hizi na uwezeshwaji huu kwa makundi mengi zaidi na kuona jinsi gani ambavyo inaweza ikaenda kwa mtawanyo kwa maana ya uwiano mzuri katika mikoa lakini pia katika Majimbo na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tumebaini jambo jingine ambalo katika mikopo hii ambayo imekuwa ikitolewa, na tutakubaliana kwamba fedha hizi zimekuwa zikitolewa katika mifumo mbalimbali. Ukiangalia kwenye Halmashauri kuna ile 4:4:2 kwa maana ya fedha ambazo ni asilimia 4 kwa wanawake, 4 kwa vijana na 2 kwa watu wenye ulemavu. Fedha hizi zimekuwa zikitolewa nchi nzima lakini kwa sehemu kubwa utaona kwamba marejesho yamekuwa ni hafifu sana. Kwa hiyo, tulitegemea kwamba fedha hizi zikitolewa, vijana hawa waweze kuzifanyia kazi na wa-graduate waende kwenye hatua ambayo watawaachia wengine waweze kukopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaenda kwenye hatua nyingine ambayo bado ipo katika hatua ya mashauriano kuona kama tutaweza kutoa asilimia 50 ya vifaa na 50 iwe fedha kwa ajili ya operational cost kwa sababu ili tuweze kama ikitokea wameshindwa kulipa, tumewapa trekta au mashine za kushona nguo ama tumewapa vifaa vitendea kazi labda mashine za kufyatua tofali na ilikuwa mkopo labda wa milioni 10; tukawapa milioni 5 gharama za mashine na milioni 5 nyingine wakapewa kama fedha taslimu maana yake ni kwamba hata wakishindwa kurejesha walau tunaweza tukarejesha ile mashine ya kufyatua tofali ikawasaidie vijana wengine kuliko sasa hivi mfumo wa returns umekuwa mgumu na halmashauri zimekuwa zikihangaika wakati mwingine kulazimika kuwapeleka mahakaman. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa la kuona namna gani ambavyo tunaweza tukatengeneza startup capital kwa wanafunzi wahitimu wa vyuo vikuu ni pamoja na mpango mzuri ambao tumekuwa nao katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu…

MWENYEKITI: Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri utajibu hapo kwa ufupi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA
NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ni pamoja na mpango huu ambao tumeanza kuona bado lipo katika kuona namna gani ambavyo vijana wa vyuo vikuu tutawaingiza kwa programu tatu ambazo zipo. Kwa sasa tumeanza na programu ya uanagenzi ambayo kimsingi inatumika kwa wale ambao hawajamaliza chuo kikuu lakini tuna programu maalum ya internship ambayo tayari tunawachukua vijana hawa na kuwaunganisha kwenye maeneo ya ajira. Sambamba na hilo, tunatoa mafunzo pia na kuwasaidia kuweza kupata mikopo kwenye maeneo ya halmashauri lakini pia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaotolewa na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo pia tumelichukua na tutalifanyia kazi, nakushukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, hitaji la wakulima kuunganishwa na wawekezaji wa nje na ndani lililopo kule Mikoa ya Kusini linafanana kabisa na hitaji la wakulima wa zao la vanilla kutoka Wilaya za Bukoba, Misenyi, pamoja na Muleba Mkoani Kagera, ningependa kufahamu Serikali ina mpango gani wa kuunganisha wakulima wa zao la vanilla na wawekezaji wa kutoka nje na ndani ya nchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli zao la vanilla linalimwa katika Mkoa wa Kagera, vilevile ni moja kati ya zao linalokua katika Mkoa wa Kilimanjaro. Nikiri tu hapa kwamba miongoni mwa Wabunge ambao wamekuwa wakilifuatilia zao hili mmojawapo ni Mheshimiwa Neema na Mheshimiwa Saasisha Mafuwe, Mbunge wa Mwanga - Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka tu niwahakikishie tumeanza mazungumzo na local exporters wa zao hili la vanilla ili tuanze kutengeneza mfumo wa contract farming moja kwa moja na mikataba. Mheshimiwa Shigongo naye ni mmoja kati ya waathirika wa zao hili, ili tuhakikishe zao hili linakua kwenye ramani, hili ni high value commodity na Wizara tumeanza kuwekeza kwenye research and development.

Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge ni zao jipya ambalo limeanza kuchukua nafasi na tunalitazama kwa ukaribu sana na kuwaunganisha na masoko. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, kwa kuwa matatizo na changamoto ambazo wanapitia wanawake kwenye masuala haya ya kifamilia yamezidi kukithiri, na tarehe 6 Oktoba, 2021 Mheshimiwa Rais alilikazia hili, na hata Jaji Mkuu alielezea umuhimu wa kuwa na Mahakama ya Familia. Ningependa kuiuliza Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria. Je, ni lini ambapo itakuja na Mahakama ya Familia ili masuala yote haya ya mirathi matunzo na kadhalika yaweze kuangaliwa kwa utaratibu na haki iweze kutolewa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa mapendekezo mbalimbali yalitolewa kwa ajili ya kuanzisha Mahakama ya Familia, na bado tunaendelea kufanyia kazi, kwa sababu ni taasisi ambayo inahitaji kuwa kwenye muundo sasa wa utendaji kama zilivyo Mahakama nyingine. Kwa hiyo, ni imani yangu kwa kuwa tunakwenda sasa katika kurekebisha sheria yenyewe na muundo wake tunadhani tutakapokuwa tunakuja tutakuja na sura sasa ya kuwa na mahakama hii ambayo itashughulikia masuala ya mirathi. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika nashukuru. Nami napenda kuiuliza Serikali: Ni lini itaimarisha utoaji wa huduma kwa magonjwa yale ambayo yalikuwa hayapewi kipaombele; magonjwa ya kitropiki, kwa maana ya neglected tropic diseases kwenye hospitali hii ya Kanda ya Kusini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, kwanza ukisikia tunaanzisha specialists mbalimbali, tunazungumzia magonjwa yote hayo. Ukisikia tunasema tunaongeza watumishi, ni kwa kuzingatia hayo. Ndiyo maanda unaona sasa kuzunguka nchi nzima, utaona kila Mkoa sasa unafanya wahamasa kuhusu magonjwa ambayo ameyazungumzia. Juzi Arusha nilimwakilisha Waziri wa Afya kwenye kuzindua swala hilo kitaifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nami niungane na Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya sekta ya Asasi za Kiraia, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Wizara hii mpya mahususi ambayo inalenga kusimamia masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, na kwa kuwa tunafahamu sisi waswahili tunasema anayemlipa mpiga zumali ndio anayechagua wimbo, sasa kwa mustakabali huo na kwa kutambua kwamba NGOs nyingi zinapata fedha ambazo zimetengwa na Serikali za nje; je, Serikali haioni ipo haja ya kuona namna gani ambavyo pia itatenga fedha kwa ajili ya NGOs za ndani ili kuepusha baadhi ya NGOs kwenda na kufanya kazi ambazo zinakwenda kinyume na maadili na malengo ya Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa hali ya sasa ipo changamoto kubwa sana kwa upande wa TRA na namna ambavyo inaangalia hizi NGOs. Pale ambapo inatokea NGO inapata rasilimali fedha na inakwenda kutekeleza mpango ule kutoka mwaka mmoja kwenda wa pili, TRA wanatoza kodi ya mapato kwenye hizi NGOs kwenye zile fedha ambazo zinakuwa zimebaki mwisho wa mwaka, lakini zinakwenda kutekeleza mradi mwaka unaofuata. Nwa kwa mantiki hiyo TRA inafanya hivyo kana kwamba NGOs zinafanya biashara wakati hazifanyi biashara, zinatoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali haioni haja ya kuleta hizi sheria, kanuni na haya maelezo mbalimbali ambayo yanatoa fursa kwa TRA kufanya hivyo ili iletwe Bungeni ifanyiwe maboresho ili kuimarisha mazingira wezeshi kwa hizi Asasi za Kiraia ili ziweze kuendelea kufanya kazi kwa tija na kuendelea kuchangia maendeleo ya jamii ambayo kimsingi ili Wizara hii itekeleze malengo yake ni lazima ifanye kazi kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa nyingine niweze kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Neema Lugangira.

Mheshimwa Mwenyekiti, nianze na sehemu ya kwanza, kwamba Serikali ina mpango wa kutoa fedha kwa ajili ya Mashirika haya Yasiyo ya Kiserikali. Niseme kwamba Serikali imekuwa ikifanya hivyo tangu miaka ya nyuma kwenye baadhi ya taasisi chache ile zile NGOs ziweze kuchangia maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni CCBRT, ile ni hospitali yetu ambayo inawanufaisha akinamama na watoto na watu wengine wenye magonjwa mbalimbali ya ulemavu. Imekuwa ikipeleka fedha kule tangu miaka ya 2000 na
kikubwa katika mwelekeo huo, pamoja na hili andiko tunalolifanyia kazi, bajeti ya mwaka 2022/2023, Serikali inajielekeza kuanza kutekeleza mpango wa ruzuku kwenye baadhi ya hizo NGOs zitakazokuwa zimeonekana zina vigezo na tutawasilisha kwenye kipindi cha bajeti, mtaweza kuona mwelekeo huo wa Serikali.

Mheshimwa Mwenyekiti, aidha, katika kipengele kingine cha pili cha swali, maboresho ya kanuni na sheria ili kuzifanya hizi NGOs zetu ziweze kufanya kazi kwa kujiamini na kuwa na uendelevu baadaye. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu alishaelekeza, andiko limeanza kuandikwa lakini tayari tumeanza kutekeleza kupata maoni kutoka kwenye NGOs mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilifanyika kikao Arusha; Mashirika 200 yalikaa yakatoa maoni na tarehe 5, hapa Dodoma kinafanyika kikao kingine, NGOs nyingine zimealikwa, zitakuja kutoa maoni na baadaye tunakwenda Mwanza Kanda ya Ziwa, tunafunga. Yale maoni ndiyo tutayafanyia kazi na kuyachakata kuona tunaendaje katika suala zima la kuhakikisha sheria na kanuni zote zilizopo zilizopitwa na wakati ziweze kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo hatua tuliyonayo. Lengo kubwa la Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona NGOs hizi zilizo ndani yetu zinapunguza utegemezi, zinakaa vizuri na kushiriki kuwa wanufaika wa Serikali yao kupitia National Cake. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru; kwa kuwa leo ni Siku ya Saratani Duniani, ningependa kuiuliza Serikali, ina mkakati gani wa kuzuia wenye viwanda ambao wanachepusha machi yenye kemikali ambazo si salama? Maji haya yanakwenda kwenye Mto Msimbazi na ndiyo maji hayo hayo ambayo hawa wakulima wa mbogamboga wanatumia katika kuzalisha na kumwagilia mbogamboga hizi, hivyo kuhatarisha usalama wa chakula (food safety) na hatimaye usalama wa hali ya afya ya wananchi na hivyo uwezekano wa kuchangia katika saratani ni mkubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumebaini kuwa kuna baadhi ya shughuli nyingine za kibinadamu zinasababisha uchafuzi wa mazingira, zikiwemo hizo ambazo amezitaja, za viwanda na nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali kupitia Ofisi ya Makamu Rais, Muungano na Mazingira tunazo jitihada Madhubuti ambazo huwa tunazichukua katika kuhakikisha kwamba tunazuia mambo haya ili kuweza kuzuia athari kwa wananchi, ikiwemo hiyo milipuko ya maradhi, yakiwemo ya kansa na mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tunaendelea kutoa taaluma kwa hawa wanaofanya shughuli hizi za kibinadamu, lakini la pili kuna wakati tunatoa hata faini ili waweze kuacha na iwe funzo kwa wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile huwa tunafanya operations za mara kwa mara kwenye haya maeneo ya uzalishaji, lengo na madhumuni ni kwamba wanaozalisha wajue kwamba wanazalisha lakini wananchi nao wanaathirika. Lakini zaidi tunafika hatua mpaka tunazuia. Inafika wakati kuna kiwanda kinafanya visivyo, kuna shell inafanya isivyo, kuna migodi inafanya visivyo. Kisheria, kwa mujibu wa utaratibu tunazuia uzalishaji ili sasa shughuli nyingine au taratibu nyingine za uhifadhi wa mazingira ziweze kuendelea. Nakushukuru.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Japokuwa Serikali imekuwa ikiweka jitihada kubwa kwa kuhakikisha kwamba vijiji vya Mkoa wa Kagera vinapata umeme kupitia REA, lakini ukweli ni kwamba hata kabla ya mgao huu Mkoa wetu wa Kagera umekuwa ukikaa gizani siku mbili, tatu mpaka nne kila wiki na hii inatokana na kwamba bado Mkoa wa Kagera haujaungwanishwa kwenye Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha mwaka 2021 hapa Bungeni niliuliza suala hili na Serikali waliahidi kwamba mwaka 2022 Mkoa wa Kagera utaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Kwa hiyo, napenda kupata kauli ya Serikali: Je, ni lini Mkoa wa Kagera utaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa ili tuondokane na adha ya kuwa gizani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera unazo Wilaya saba na Wilaya mbili tu za Biharamuro na Ngara ndiyo zinapata umeme wa gridi. Wilaya tano zilizobaki zinapata umeme kutoka Gridi ya Taifa la Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada kubwa sana ambazo zinafanywa na Serikali ni kuhakikisha kwamba Mkoa wa Kagera unaunganishwa na Gridi ya Taifa kwa kutoa umeme katika eneo linaitwa Benako kwa kuchota kwenye line inayotoka katika mradi wetu wa Rusumo kwenda Nyakanazi. Tayari eneo la kupitisha kilometa 179 za line kubwa ya Kilovolt 220 zimeshatengenezwa, survey imeshafanyika na umeme ule utaletwa katika kituo chetu cha kupooza umeme cha Kyaka na Mkoa wa Kagera katika muda mfupi wa miaka miwili utakuwa umeunganishwa katika Gridi ya Taifa. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na Mwanasheria Mkuu natambua kwamba mwaka jana tulibadilisha sheria ya kuzuia ukamataji kabla ya kukamilisha upelelezi, lakini jambo hili bado halitekelezeki na ndiyo maana hata hivi karibuni Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amelisemea na amelitolea maelekezo; kwa mantiki hiyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali haioni umuhimu wa kurekebisha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) ili kuweka ukomo wa upelelezi kama ambavyo wenzetu wa upande wa Zanzibar wamefanya na nchi jirani za Kenya, Uganda, Malawi na kadhalika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka masharti nafuu ya dhamana kwa watu ambao hawana mali kwa sababu hivi sasa masharti ya dhamana ni makubwa kuliko makosa hivyo ni kana kwamba tunakomoa wananchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Neema Lugangira swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika majibu ya msingi wakati najibu swali la Mheshimiwa Enosy Swalle nilieleza hatua mbalimbali ambazo Serikali imekuwa inaendelea kuzifanya kuboresha ili dhana nzima ya haki jinai na pia nimeeleza katika Bunge lako kwamba katika moja ya hatua kubwa ambayo imefanyika ni mashirikiano na taasisi mbalimbali zisizo za Kiserikali, Asasi za Kiraia na Taasisi za Dini na Vyuo vinavyotoa elimu ya sheria juu ya andiko lililotolewa kutafuta maoni ya watalaam hawa ili tuweze kufikia sehemu ya kujadili mambo yote ya msingi yanayoambatana na issue za haki jinai.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria zetu zipo wazi kabisa juu ya masuala ya haki jinai na katika eneo hilo la haki jinai ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tuna pande mbili kuna wanaotenda jinai na wanaotendewa jinai. Sasa kama mpango mzima utakuwa ni kuwatetea waliotenda jinai uelewe upande wa pili kuna waliotendewa jinai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tulikuwa tuna tatizo la panya road, sasa inasemwa hapa kama vile polisi wasikamate mpaka upelelezi upatikane na ndiyo maana tulipotunga hii sheria mwaka huu nafikiri tuliweka wazi kwamba kwa baadhi ya makosa ya kawaida ambayo hauoni sababu ya haraka ya kwenda kumkamata mtu kama upelelezi haujakamilika tunaweza tukasema yawe hivyo, lakini kwa kweli ni lazima tujue kwamba watu wanaotendewa makosa ndiyo wanaotakiwa kuonewa huruma zaidi na kusaidiwa kuliko wanaotenda makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niombe rai kwamba twende hivyo kwasababu kwa kufanya hivyo ndiyo maana nchi ipo salama hata leo hii. Vinginevyo tukibadilisha jurisprudence hapa tunaweza tukaharibu kabisa haki jinai ikawa ni tatizo, lakini haki jinai inapande mbili. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kufahamu hivi karibuni Makamu wa Rais alivyokuwa pale Bukoba Mjini aliwasilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwamba Bukoba Mjini sasa tutajengewa stendi kuu ya mabasi. Kwa hiyo, ninataka kufahamu ni lini hiyo ahadi itatekelezwa na Bukoba tutapata stendi kuu ya mabasi ili kufungua Mkoa wetuwa Kagera na nchi za jirani? (Makofi)
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Neema Lugangira Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa ambacho Wabunge wote wanapaswa kufahamu wakiwemo Mheshimiwa Neema Lugangira ni kwamba ahadi zote za Viongozi zipo katika hatua ya utekelezaji. Kikubwa tumeshaziainisha, tumeshazipa vipaumbele, jukumu letu sasa hivi ni kutafuta fedha kuhakikisha hizo ahadi zinatekelezeka.

Kwa hiyo, pesa itakapokuwa imepatikana hii ahadi ya Makamu wa Rais na yenyewe itatekelezeka kama ambavyo ameahidi. Kikubwa ni kwamba ahadi zote za viongozi zitatekelezwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Spika, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo; Je, Wizara ya Kilimo ina mpango gani wa kuhamasisha na kuimarisha uwekezaji kwenye zao la vanilla kwa Mkoa wa Kagera? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Lugangira kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama Wizara zao la vanilla halikuwa kwenye map ya Serikali na kuonekana kama ni zao ambalo lina-attract na kuweza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, nataka tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge baada ya kujitokeza wanunuzi na wakulima wengi either kutapeliwa au kufanya nini, tumeanza kuchukua hatua sasa hivi na tunavyoongea sasa hivi timu yetu ya Wizara ya Kilimo iko Mkoa wa Kagera na wengine wameelekea Mkoa wa Njombe kwa ajili ya kuweza kuangalia map na kuweza kulitambua vizuri na kulitengenezea mkakati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuanzia mwaka ujao wa fedha baada ya mwaka mmoja kutakuwa na mkakati rasmi wa nchi kuhusu zao la vanilla. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali kwa kwanza; kwa kuwa tayari ipo Sheria ya Mbegu ya Mwaka 2003 ambayo ilifanyiwa maboresho mwaka 2014, je, kwa nini Serikali ianzishe upya mchakato wa kuleta sheria mpya badala ya kuongeza kwenye hii Sheria ya Mbegu iliyopo ya mwaka 2003 utambuzi wa mbegu za asili kwa kuwa sheria hii inatambua mbegu za kisasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; naipongeza Serikali imeanzisha hiki Kitengo cha Taifa cha Kuhifadhi Vinasaba vya Mimea ikiwemo mbegu za asili, lakini tokea mwaka 2005 zaidi ya miaka 15, Sheria ya National Plant Genetic Resource Act bado haijawahi kupitishwa, kwa hiyo kitengo hiki kimsingi hakina meno wala hakiwezi kutambua wala kulinda mbegu za asili ikiwemo na hivi vinasaba na ikiwemo pia kulinda hakimiliki ya mbegu zetu za asili…

NAIBU SPIKA: Swali.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Je, Serikali itailleta lini Bungeni Sheria hii ya National Plant Genetic Resource ili tuweze kuhakikisha kwamba kitengo hiki kinafanya kazi ipasavyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anakuwa mfuatiliaji mzuri wa masuala haya, lakini swali lake la kwanza ni kwamba, tumepokea wazo lake la maboresho ya sheria iliyopo lakini pamoja na hiyo sheria aliyouliza katika swali lake la nyongeza ni sheria ambayo ndio itakuja hasa kuja kuzitambua na vilevile kuzungumzia usajili wa mbegu za asili, ambao sheria hii mpaka hivi sasa ipo katika ngazi ya IMTC. Tunaamini kabisa taratibu zinaendelea vizuri na sheria hii italetwa hapa Bungeni ili iweze kupitishwa na basi tuwe tuna sheria ambayo itakuwa inatambua lakini vilevile ambayo itakuwa ina usajili mbegu za asili kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia yameendelea kukithiri hapa nchini, je, ni lini Serikali italeta Muswada wa Sheria ya Ukatili wa Kijinsia hapa Bungeni kama ambavyo Tanzania iliridhia katika Mkutano wa 44 wa Bunge la SADC (SADC Parliamentary Forum)?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, tutajipanga Wizara pamoja na Wizara mtambuka ambazo tunatengeneza miamala hii ya miswada kwa pamoja ili kuweza kuifikisha pale panapohitajika, ahsante sana.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya wanafunzi kupewa adhabu kali ya viboko shuleni inayosababisha majeraha, kuzimia, kulazwa na hivyo kushindwa kuhudhuria shule ipasavyo.

Je, Serikali haioni ipo haja ya kuweka adhabu kali kwa waalimu wanaofanya vitendo hivi ili kuwalinda watoto wetu shuleni?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nipenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la adhabu zisizo na kiasi kwa wanafunzi kule shuleni, na kwamba anaomba adhabu kali zitolewe kwa waalimu wale ambao wanachukua sheria mkononi; kimsingi limekuwa ni tatizo. Kila siku naona kwenye mitandao hatua ambazo walimu wanachukua. Mimi niwasihi, hasa walimu, kwa sababu tunayo sheria ya elimu inayotoa utaratibu wa adhabu kwa watoto wetu. Pale mtu anapochukua sheria mkononi atashtakiwa kama mhalifu mwingine yeyote ambaye ametumia nguvu katika kutoa adhabu kwa watoto wetu.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kuimarisha soko la zao la vanila mkoani Kagera? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli zao la vanila hivi sasa limeanza kupata muamko mkubwa na wakulima wengi wamehamasika kulima zao hili na sisi kama Serikali tumeendelea kufatilia hatua kwa hatua kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira bora na wezeshi kuwafanya wakulima wetu waweze kunufaika na zao hili.

Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni sehemu pia ya mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunatengeneza miundombinu rafiki na mazingira rafiki ili wakulima wetu waweze kunufaika na uzalishaji wa zao la vanila.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ningependa kuuliza Serikali, Je, ni lini itapeleka fedha za kukamilisha ujenzi na kununua vifaatiba kwa ajili ya hospitali za Wilaya za Biharamulo, Bukoba DC, Karagwe na Kyerwa ili ziweze kukidhi viwango vya kuwa hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba hospitali zetu za Halmashauri zikiwemo hizi za Biharamulo, Bukoba, Kyerwa na maeneo mengine lakini nchini kote tuna upungufu wa baadhi ya vifaatiba na ndiyo maana katika bajeti zetu zote tumeendelea kutenga fedha na bajeti ijayo tumetenga Shilingi Bilioni 69. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha tunazipa vipaumbele hospitali hizo.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuwa sera ya Wizara ya Elimu inatambua umuhimu wa kuwa na walimu wanaotoa ushauri wa nasaha kwenye shule zetu.

Je, Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii ina mpango gani wa kuhakikisha ya kwamba jambo hili linatekelezeka na kwenye shule zetu kunakuwa na walimu wanaotoa ushauri nasaha kwa watoto wetu hususan ukizingatia kwamba kuna wanafunzi wengi wanaohitimu masomo ya saikolojia na kwa kuanzia wanaweza kuanza kwa njia ya kujitolea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa wanasaikolojia hao. Kwa hiyo Serikali ipo katika kujipanga na kuhakikisha kwamba pale tunapopata nafasi za ajira basi wataalamu hao tutawaajiri na kushirikiana na Afisa wa Maendeleo ya Jamii kuwapa elimu wananchi wetu. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wazee wa Mkoani Kagera walipewa vitambulisho ambavyo vinawaruhusu kwenda kupata matibabu bure. Lakini vitambulisho vile havitambuliki pale ambapo wanakwenda kwenye hospitali au vituo vya afya. Vilevile wakiandikiwa dawa, huwa wanaandikiwa dawa ambazo bado wanaambiwa hawawezi wakapewa pale hospitali au kituo cha afya, inabidi wakanunue nje.

Je, Serikali ina mpango gani kudhibiti hayo maeneo mawili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikia ni Mzee mwenye kitambulisho chake, maana yake ni mzee ambaye tayari ameshatimiza vigezo vyote ambavyo vinatakiwa apate huduma. Kwa hiyo, kimsingi anatakiwa apate huduma. Lakini kuna hilo tatizo sasa kwamba anapewa huduma lakini anapofika dirisha la dawa, dawa inayohihitajika kupata haipatikani haipo kwenye dirisha la dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesikia hapa nyuma tukiwa tunazungumza masuala ya MSD na upatikanaji wa madawa kwenye vituo vyetu. Nguvu nyingi sasa tunaelekeza kuhakikisha hakuna dawa inayokosekana kwenye vituo vyetu ili wazee wetu waliotimiza vigezo wakienda kwenye dirisha la dawa wapate dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Jumamosi tulikuwa na Wabunge wenzetu wa Kamati ya Huduma za Jamii, kwa ajili ya Muswada wa Bima ya Afya kwa wote. Sasa tutaenda kutoa semina kwa Wabunge wote likija Bungeni basi tulisimamie hilo kwa sababu ndiyo litakuwa suluhu la kudumu. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya kutia moyo ya Serikali, shule za msingi 459 za Wilaya za Misenyi, Ngara, Biharamulo, Bukoba Vijijini pamoja na Muleba katika Mkoa wa Kagera hazijaunganishwa na maji safi na salama. Kwa hiyo ningependa kupata commitment ya Serikali ni nini itakwenda kufanya kuhakikisha shule hizi zinaunganishwa na maji safi na salama ili kutoendelea kuweka hatari afya za watoto zaidi ya laki nne wanaosoma kwenye shule hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mtaa wa Kisindi na Kashenye katika Kata ya Kashai, Bukoba Manispaa ina changamoto kubwa sana ya maji. Je, Wizara hii itakwenda kufanya nini kupata ufumbuzi wa haraka ili kutua ndoo akinamama ambayo ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Neema kwa ufuatiliaji mzuri. Suala la maji mashuleni, kwenye vituo vya afya, kama nilivyoongea kwenye maswali mengine, hili ni agizo ambalo Wizara imetoa kwa watendaji wote mikoani. Hivyo nitarajie mabadiliko makubwa sana katika shule zote za Mkoa wa Kagera zitafikiwa na maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji katika mitaa aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kuona kwamba watu wote wanafikiwa na maji safi na salama na ya kutosha, hivyo mitaa hii pia naamini kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha, wataweza kupatiwa huduma ya maji safi na salama na ikiwezekana basi kufikia mwaka ujao wa fedha pia zoezi litaendelea ili kuona maeneo yote yanapata maji safi na salama.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, ni mara ya tatu au zaidi nauliza hili swali nilitaka kufahamu ni lini Mkoa wa Kagera utaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari fidia imeshafanyika katika njia ya kutoka Benako kuja Kyaka kwa ajili ya kupitisha umeme utakaotoka Nyakanazi na Rusumo kuja katika Mkoa wa Kagera na Serikali kupitia BADEA imepata fedha za utekelezaji wa mradi huo, kwa hiyo, siku sio nyingi mambo yataanza kufanyika katika eneo la site.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali ni vyema tutambue kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaweka jitihada kubwa sana kuimarisha mazingira wezeshi na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na hiyo imeenda sambamba kabisa na Mheshimiwa Rais kuamua kuchukua jukumu la uwekezaji na kuweka chini ya Ofisi ya Rais, pamoja na kuteua Katibu Mkuu wa Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Blueprint imeelekeza kwamba ili kuimarisha mazingira wezeshi lazima tuwe tuna ardhi inayojulikana kwa ajili ya uwekezaji kwa maana ya kwamba ardhi hiyo ipimwe na iainishe ni uwekezaji gani ambao uatafanyika sasa je, mpaka hivi sasa Serikali imepima kiwango gani cha ardhi na ramani ya ardhi hiyo kwa ajili ya uwekezaji inapatikana wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pamoja na kwamba Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 2022 ilipitishwa ndani ya Bunge lako Tukufu kwenye blueprint imeelekeza zaidi ya sheria 20 ambazo zinatakiwa zifanyiwe maboresho.

Kwa hiyo ningependa kufahamu kutoka kwa Serikali, je, ni lini Serikali italeta hizo sheria zingine zaidi ya 20 ili zifanyiwe maboresho ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha mazingira wezeshi hapa nchini na hivyo kuunga mkono na kutokufifisha jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha na kuleta wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi tumeshaanza kutekeleza MKUMBI au Blueprint na moja ya utelekezaji huo ni kuhuisha au kutunga Sheria mpya ya Uwekezaji lakini pia ninyi ni mashahidi katika Bunge liliopita tumepitisha maboresho ya sheria mbalimbali zaidi ya 19 ambazo ziligusa sekta tofauti tofauti.

Kama nilivyosema utekelezaji wa MKUMBI au blueprint sio kitu cha siku moja, kwa hiyo tunaendelea kutekeleza moja ya maeneo ambayo Mbunge ameyasema ni hayo ya kupitia baadhi ya sheria na kanuni lakini pia kuboresha baadhi ya taratibu ambazo zipo na tunazoona ni changamoto au kero kwa ajili ya kuboresha uwekezaji hapa nchini, nakushukuru.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Kwa kuwa swali la msingi linauliza kuhusu ongezeko la kansa, mimi nilitaka kufahamu: Je, Serikali imefikia wapi katika kufanya tafiti kwenye mikoa ya kanda ya ziwa na suala zima la ongezeko kubwa la magonjwa ya kansa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, hatua tuliyoifikia tayari tumeshachukua sample kwa watu mbalimbali zaidi ya 700, na sasa ziko kwenye maabara kwa ajili ya kuchambua kwenye level ya genetics ili kuona hasa ni nini tatizo linalosababisha hali hiyo kule kanda ya ziwa.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na kwa kutambua jitihada kubwa ambazo anaweka Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza: Je, Serikali haioni ipo haja ya kufanya mapping katika nchi za nje ili kujua katika kila nchi tunataka kuwauzia nini na pia kujua kutoka kila nchi sisi tunataka kuwauzia nini ili tuweze kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na sekta binafsi na pia kuziwezesha balozi zetu za nje kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi pamoja na balozi za nje hapa nchini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Wizara ya Mambo ya Nje iko tayari kuandaa mfumo ambao utaweza kufanya tracking ya utekelezaji wa mafanikio yaliyoainishwa yanayotokana na ziara ya viongozi wetu kimataifa, kwa sababu utekelezaji wake haufanywi moja kwa moja na Wizara hii ya mambo ya nje, bali unafanywa na Wizara nyingine pamoja na taasisi nyingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kusaidiana na sekta binafsi katika kufanya mapping ya fursa ambazo zipo katika nchi mbalimbali huko nje. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Wizara ya Mambo ya Nje inafanya kazi kwa karibu sana na sekta binafsi. Kwanza sekta binafsi pia hushiriki katika ziara za viongozi wetu mbalimbali huko nje, ambapo Wizara hizo huwafungulia milango na kujua fursa mbalimbali za uwekezaji. Pia kupitia mabalozi wetu wa nchi mbalimbali, tumekuwa tukiwaunganisha na sekta binafsi ili kujua fursa mbalimbali ambazo ziko huko.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ufuatiliaji wa yatokanayo na safari za viongozi wetu, hili ni suala muhimu sana, nasi tuna wajibu sana wa kufuatilia kwamba ziara za viongozi wetu zinaleta matunda ipasavyo. Hivyo, uko mfumo maalum wa kuhakikisha kwamba sekta zote ambazo zinaguswa na ziara hizo tunakaa pamoja, tunafanya mkutano na kuainisha utekelezaji wake ili kujua changamoto na faida zake ili kupatiwa ufumbuzi ipasavyo, ahsante sana.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ningependa kufahamu je, Serikali ipo tayari kupitia upya posho kwa ajili ya vikao vya Madiwani kwa kuzingatia umbali wanakotoka kwa sababu kama Wilayani Muleba tunazo Kata tano Boziba, Kerebe, Rubale, Ikuza na Mazinga ambazo ni za visiwani lakini Waheshimiwa Madiwani wakienda kwenye vikao wanalipwa posho sawa na wale ambao wanatoka pale pale mjini wakati wao wakienda kwenye vikao inawalazimu walale kutokana na umbali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishatoa mwongozo wa posho za kujikimu kwa Waheshimiwa Madiwani wanapohuduhuria vikao vya mabaraza na mwongozo ule ulizingatia wale ambao wanatoka mbali wanahitaji kulala, rate zao zilikuwa ziko tofauti na wale ambao wanatoka eneo la jirani hawahitaji kulala rate zao ziko tofauti.

Kwa hiyo, nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwasisitiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Halmashauri zote kuzingatia mwongozo ambao uko very clear na unaelekeza wanaotoka mbali wanatakiwa kulipwa kiasi gani na wale wanaotoka jirani wanatakiwa kulipwa kiasi gani, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Ninataka kufahamu Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa stendi mpya ya mabasi Bukoba Mjini? Ahsante. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa stendi katika Mkoa wa Kagera, Bukoba tutawasilina na wenzetu TAMISEMI ambao wanasimamia jambo hili na naamini katika bajeti yao mwaka huu huenda wamepanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa stendi hii. Ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa, Malabo convection inaweka msingi wa Makosa ya Mtandao, Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na Biashara ya Mtandao, na kwa kutambua fursa zinazotokana na Soko Huru la Afrika la Biashara ya Mtandao; Je, ni lili sasa Serikali italeta azimio hapa Bungeni la kuridhia mkataba huu wa Malabo ili Tanzania isiendelee kuchelewa kupata fursa zinazotokana na soko huru hili la biashara Barani Afrika.

Swali la pili, kwa kuwa tayari Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi imeanza kutumika. Je, ni lini sasa Serikali itatunga kanuni kwa ajili ya sheria hiyo ili kuendelea kulinda Ulinzi wa Taarifa Binafsi ikiwemo changamoto kubwa ya ukatili wa kijinsia mtandaoni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Lugangira kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Neema Lugangira ambaye amekuwa mdau mkubwa sana katika sekta yetu hii ya mawasiliano.

Kwanza kabisa nianze na swali dogo la pili kuhusiana na Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Mheshimiwa Waziri tarehe 6 Mei, 2023 alisaini kanuni hizo ambazo ziko tayari kwa ajili ya kutumika. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge anaweza akapata fursa ya kuzipitia na kuona namna gani zinaenda kujibu hoja baadhi ya maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge ameligusia kuhusu maazimio kuletwa Bungeni. Tayari tuko kwenye mchakato huo na mchakato una hatua kadhaa lakini katika hizo hatua kuna hatua ya kuleta Bungeni. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tuko katika hatua nzuri kabisa na zikishakamilika hatua hizo za awali pale ambapo itahitaji sasa kuileta Bungeni tutaileta kulingana na utaratibu unavyotuelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ni dhahiri kwamba viko visababishi ambavyo vinapelekea mama kujifungua mtoto njiti ikiwemo mahitaji ya lishe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inaimarisha huduma za lishe kwa akina mama wajawazito ili waweze kufikisha full term yaani mtoto azaliwe ndani ya umri anaotakiwa kuzaliwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu ameshaelekeza, kumekuwepo na makongamano mengi, kumekuwepo na semina nyingi ambazo zinazungumzia suala zima la lishe. Sasa badala ya kufanya makongamano na semina fedha hizo zitaelekezwa kununua vitamini ambazo zina multiple vitamin na akina mama wajawazito wote wanapewa hizo vitamin. Lakini niendelee kuwaomba Wabunge wa kike na wa kiume mojawapo ya sababu za Watoto Njiti ni stress. Sisi wote tunapofika mahali kina mama wajawazito wanakuwepo tuhakikishe mazingira yao ya kufanya kazi lakini sisi wanaume tuwe karibu nao ili kuondokana na mambo mengine yanayoweza kuzuilika yanayosababisha uwepo wa Watoto Njiti.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ucheleweshaji sio la Biharamulo, kwa sababu Biharamulo walishawasilisha Mkoani na Mkoani wanaleta moja kwa moja TAMISEMI. Jengo la Halmashauri ya Biharamulo, liko kwenye miradi ya kimkakati ya Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa. Swali la kwanza, maombi yalikuwa ni bilioni 3.4 lakini Serikali imetenga bilioni 2.7 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 lakini kwa uchumi wa Biharamulo haitaweza kupata hiyo milioni 700 inayosalia.

Je, Serikali ina mpango gani waku-top up kiasi hicho cha fedha tukifika wakati huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali tayari imeshaweka commitment na ahadi kwamba itatenga hiyo bajeti ya bilioni 2.7; je, bado kuna haja tena ya kuandika maombi haya au hakuna haja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum ambayo ameuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la msingi bila kujali vimechelewa wapi ni suala la kwamba jengo la utawala la Halmashauri litatengwa kwenye mwaka wa fedha 2023/2024. Lakini kiasi ambacho kimeombwa ni Bilioni 3.475 lakini mpango wa Serikali tumefanya standardization ya majengo yetu yote ya halmashauri ili kuepukana na variation ya majengo ambayo yamekuwa yanajengwa kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sasa Halmashauri zote zitakuwa na mchoro mmoja na kila halmashauri itapata bilioni 2.7, kwa hiyo hatuna haja ya kuongeza fedha hiyo, hiyo ndiyo fedha kulingana na mchoro huo ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na standardization. Lakini pale ambapo tutalazimika kuwa na variation ya mchoro kulingana na mazingira, basi tutaona namna ya kufanya.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwa mujibu wa takwimu za Serikali ya mwaka 2016 zinaonesha kwamba ni asilimia 19 tu ya wanawake ambao wanamiliki ardhi wakati wanachangia takribani asilimia 54 ya uzalishaji katika kilimo ambao ndiyo uti wa mgongo wa uchumi. Nina maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Je, Serikali imeweka kipaumbele gani kuhakikisha kwamba umiliki wa ardhi kwa wanawake unaongezeka kwa kuipa uhai na meno Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mila, tamaduni na desturi ni kati ya sababu kubwa ambazo zinachangia kutokumiliki ardhi kwa wanawake. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba sheria za kimila za umiliki ardhi, pamoja na sheria zingine ambazo zinakinzana na Sheria Na. 4 na 5 haziwi juu ya hii Sheria Mama ya Umiliki wa Ardhi wa Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza, ni kweli idadi ya wanawake ambao wanamiliki ardhi hapa Tanzania bado ni ya chini na hiyo haisababishwi na sheria, inasababishwa na mtazamo wa jamii, inasababishwa na mila na desturi zetu ambazo ni lazima sasa tushirikiane kati ya Serikali na Asasi za Kiraia, kati ya Serikali na Wadau wote kutoa elimu kuhusu haki ya mwanamke kumiliki ardhi kwa mujibu wa Katiba kama ambavyo imeelezwa kwenye Ibara ya 24, lakini pia kama ambavyo imeelezwa katika Sheria ya Ardhi, Kifungu cha 3(2).

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili, Sheria hizi za kimila zimekuwepo toka zamani lakini ni wazi kama ambavyo Mheshimiwa Neema amesema zinakinzana na haki za wanawake ambazo zimeelezwa kwenye Katiba na Mikataba mingine ya Kimataifa ambayo tumesaini. Hivyo basi, sisi kama Serikali tumejipanga kuzipitia upya sheria hizi ili kuweza kupendekeza mabadiliko na endapo Bunge lako litaridhia, basi kadhia hii itaweza kuondoka kabisa.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ni dhahiri kwamba viko visababishi ambavyo vinapelekea mama kujifungua mtoto njiti ikiwemo mahitaji ya lishe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inaimarisha huduma za lishe kwa akina mama wajawazito ili waweze kufikisha full term yaani mtoto azaliwe ndani ya umri anaotakiwa kuzaliwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu ameshaelekeza, kumekuwepo na makongamano mengi, kumekuwepo na semina nyingi ambazo zinazungumzia suala zima la lishe. Sasa badala ya kufanya makongamano na semina fedha hizo zitaelekezwa kununua vitamini ambazo zina multiple vitamin na akina mama wajawazito wote wanapewa hizo vitamin. Lakini niendelee kuwaomba Wabunge wa kike na wa kiume mojawapo ya sababu za Watoto Njiti ni stress. Sisi wote tunapofika mahali kina mama wajawazito wanakuwepo tuhakikishe mazingira yao ya kufanya kazi lakini sisi wanaume tuwe karibu nao ili kuondokana na mambo mengine yanayoweza kuzuilika yanayosababisha uwepo wa Watoto Njiti.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufanya rejea kwenye zana nzima ya local content ambayo imeweka takwa la kisheria kwamba, katika miradi wakandarasi kwa maana fursa za zabuni pamoja na ajira ziweze pia kupatikana kwa wale wanaotoka kwenye maeneo ya mradi (host community). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika hao 42 waliowasilishwa hapa na Serikali ambao amesema kwamba ni wakandarasi pamoja na watoa huduma. Ukweli ni kwamba hao 42 ni watoa huduma (local suppliers) na siyo wakandarasi (local contractors). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali langu la kwanza. Je, Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya kina, kuweza kuainisha maeneo na fursa ambazo wakandarasi wa Mkoa wa Kagera wanaweza wakapewa kinyume na ilivyo hivi sasa? Fursa zingine wamepewa wakandarasi kutoka mikoa mingine, kama Mwanza ili hali Mkoa wa Kagera wanao wakandarasi wanaoweza kufanya kazi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali kupitia Wizara ya Nishati wapo tayari kuja Mkoa wa Kagera ili kukaa na Uongozi wetu wa Mkoa wa Kagera chini ya Mkuu wa Mkoa wetu Mheshimiwa Fatma Mwasa, kujadili na kuona namna bora ya kuhakikisha kwamba Wakandarasi wa Mkoa wa Kagera wanapata fursa (local contractors), jambo ambalo litaweza kuhakikisha ulinzi wa mradi (host community) kinyume na ilivyo hivi sasa jambo ambalo linasikitisha, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Neema Kachiki Lugangira, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kufanya tathmini, kwa kuwa Mradi huu wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Chongoleani Tanga umefikia 32.6%. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunavyoendelea kwenye utekelezaji wa mradi, tutahakikisha wakandarasi wadogo ambao wanatokea maeneo ambapo mradi unatekelezeka wanaendelea kupewa fursa, kadri ambavyo tunaendelea na utekelezaji wa mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kutemebelea Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie, tutakuja ili kuweza kuona ni namna gani tunaweza tukashirikiana kwenye masuala haya ya msingi ambayo tunaamini yanagusa jamii ya watu wa Kagera. Lakini vilevile kwa kwa jamii zote ambazo mradi unatekelezeka tutahakikisha tunafanya hivyo kwa maslahi ya wananchi vile vile kwa maslahi ya utekelezaji wa mradi, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mradi wa Maji Awamu ya Pili wa Jimbo la Bukoba Mjini unaohudumia Kata tano; Kata ya Buhembe, Nyanga, Kashai, Kahororo na Nshambya umekwama tokea mwaka jana japokuwa mkandarasi yuko site.

Je, Serikali ipo tayari kupeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 253 kwa dharula ili wananchi wa kata hizi tano waweze kupata maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Lugangira, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi unaendelea kutekelezwa ndiyo maana umeweza kusema yule Mkandarasi yuko pale lakini suala la kupeleka fedha milioni 253 ni jukumu la Wizara nikuhakikishie Mheshimiwa Neema hizi fedha zitapelekwa ili kazi ziweze kuendelea. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika teknolojia. Pia, kwa Serikali kutambua kwamba zipo faida za kutumia akili mnemba kwa maana ya artificial intelligence, lakini zipo athari kubwa hasa tukiangalia kwenye maeneo ya uchaguzi, hata kwenye maeneo ya elimu ambapo wanafunzi wanaweza wakatumia akili mnemba kuandaa research zao.

Sasa je, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya teknolojia kwa maana ya akili mnemba (artificial intelligence) yupo tayari kutumia mamlaka yake ya kutumia kanuni kuona ni namna gani ambavyo sheria zitalinda Watanzania dhidi ya matumizi hasi ya artificial intelligence? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Lugangira, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, suala la faida na hasara la artificial intelligence haliwezi kushughulikiwa kwa sheria moja na ndiyo maana hata wakati wa mjadala wa Sheria ya Uchaguzi tulisema hebu tupeni muda tutengeneze kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutatumia sheria zaidi ya moja kulishughulikia na juzi tumefanya mabadiliko hapa ya Sheria ya Miamala ya Kielektroniki na mengine, lakini bado kama Serikali tuko tayari na mimi kama Waziri nipo tayari kutumia mamlaka ya kisheria kutengeneza kanuni wakati tukisubiri hayo mabadiliko makubwa. Tutengeneze kanuni ili jamii yetu iendelee salama pia ifaidike na matumizi ya akili bandia. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza mara kwa mara hapa Bungeni kuhusu nini mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika kuimarisha kilimo cha vanilla ili wakulima wa vanilla wa Mkoa wa Kagera waweze kunufaika na zao hili? Kwa hiyo, ningependa kupata kauli thabiti ya Serikali, ni nini itakwenda kufanya ili kuhakikisha kilimo cha vanilla kinanufaisha wakulima wa Mkoa wa Kagera? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Wizara ya Kilimo sasa hivi tuna mpango wa kuwaita wadau wote wa sekta ya vanilla wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, wakulima pamoja na wafanyabiashara ili tuweze kukaa pamoja na kujadiliana kuona namna bora ambayo tunaweza tukasaidia kukuza kilimo cha vanilla. Miongoni mwa mipango tuliyonayo ni pamoja na kutafuta masoko na kuongeza bei ya vanilla ili wananchi wetu waweze kunufaika zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kufahamu ni nini mkakati wa Serikali kuweka utaratibu wa kuuza vanila, hususani mkoani Kagera? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mkakati wa Serikali wa sasa ni kwamba zao la vanila tumeliingiza kati mnada wa TMX kwa maana linauzwa kwa mnada na kwa mfano tulikuwa kule Kyela pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulienda kuzindua msimu wa ununuzi wa vanila kupitia mfumo wa TMX. Kwa hiyo, mfumo ule siyo tu utatumika Kyela ni kwamba utatumika katika maeneo yote wanayozalisha mazao ya vanila ikiwemo Kagera, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuiuliza Serikali, kituo cha polisi kilichopo Kata ya Kashai kimepewa chumba kimoja katika Ofisi ya Kata na tukizingatia kwamba Kata ya Kashai ndani ya Jimbo la Bukoba Mjini ina wakazi zaidi ya 33,000. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Kashai? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Lugangira, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Kata ya Kashai ina wananchi wengi, kama alivyotamka Mheshimiwa Mbunge, kwa hiyo namhakikishia kwamba kwa kuwa ina wananchi wengi na pia kunakuwa na hatari ya kuwa na wizi au matukio mbalimbali. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa kata yake aliyoitaja ya Kashai na yenyewe tumeichukua na tutaiingiza kwenye mpango kwa ajili ya kujengewa Kituo cha Polisi, ahsante sana.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa kuwa Wizara ya Maji inalo jukumu la kufikisha huduma ya maji kwenye taasisi ambazo zinatoa huduma kwenye jamii: Je, Serikali itafikisha lini huduma ya maji kwenye shule ya sekondari iliyopo Kata ya Kagondo, Bukoba Mjini, shule ya msingi iliyopo Kata Kaharoro, Shule ya Msingi Kibeta, Shule ya Msingi Rwamishenye, Shule ya Sekondari Nyanga, Kituo cha Afya Nyanga pamoja na Kituo cha Afya Ijuganyondo ili wananchi na watoto wetu wa Jimbo la Bukoba Mjini waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua maji ni msingi wa uhai wa binadamu na engine ya maendeleo kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameiongelea, kwa sababu iko ndani ya mipango ya Serikali. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, na kwa namna ambavyo anaendelea kuisemea, nasi Serikali tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba wanafunzi, vituo vya afya na taasisi nyingine zote zinapata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Bukoba Mjini inahitaji walimu wa sayansi 386 lakini hivi sasa kuna walimu 146, hivyo tuna upungufu wa walimu wa sayansi 240.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba Bukoba Mjini tunapata walimu wa sayansi wa kutosha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Bukoba Mjini ni moja ya halmashauri ambazo katika ajira zote za walimu zilizopita pia walipata walimu wa masomo ya sayansi, lakini ni kweli kwamba walimu wale bado hawatoshelezi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kila ajira zitakapojitokeza tutahakikisha tunaipa kipaumbele Halmashauri ya Bukoba Mjini ili walimu wa sayansi waweze kupatikana na kuboresha ikama katika shule zetu zote, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maelezo mazuri ya Serikali na natambua kwamba Kanuni za Maadili ya Uchaguzi huwa zinaandaliwa mwaka wa uchaguzi, lakini kwa kuzingatia unyeti na upekee wa makosa ya ukatili wa kijinsia katika uchaguzi yaliyoongezwa ningependa kujua, je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa kanuni hizi mapema zaidi ili wananchi wapate muda wa kutosha wa kuelimishwa kuhusu kanuni hizi na wale ambao watakuwa wanagombea wajue ni hatua gani za kuchukua pale ambapo wanapitia matukio ya ukatili wa kijinsia katika uchaguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Neema kwa namna ambavyo amelisema suala hili la ukatili wa kijinsia. Pia nimwambie kwamba ushauri wake tumeupokea, tutaendelea kuufanyia kazi. Pia niwatoe wasiwasi Watanzania kwamba tupo vizuri na tutaendelea kuhakikisha kwamba kanuni hizi zinafahamika kwa wananchi wote. Vile vile tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, Asasi za Kidini, vyombo vya habari na maeneo tofauti tofauti ili kuweza kutoa elimu.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Changamoto ya madeni ya wazabuni wa chakula shuleni inasababisha kuathiri moja kwa moja upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi na ubora wa chakula hicho hivyo kuathiri elimu kwa maana ya uwezo wa watoto kusoma. Sasa, ningependa kufahamu, Mei mwaka huu nilichangia hapa Bungeni kwenye Wizara ya Elimu kuhusu suala hili na Agosti; Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Zainab Katimba, alisema kwamba TAMISEMI imewasilisha Wizara ya Fedha madeni ya wazabuni wa chakula takribani shilingi bilioni 21.7. Sasa, je, uhakiki huo utakwisha lini? Kwa sababu nikitoa mfano kwenye Jimbo la Bukoba Mjini kuna shule sita za sekondari za Serikali ambazo zinaidai Serikali jumla ya shilingi milioni 935, na madeni hayo ni kati ya mwaka mpaka miaka sita.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baadhi ya wazabuni malipo yao hayajakamilika na hayajawafikia, lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyoendelea kusema, kadri mapato yatakavyoendelea kupatikana ndivyo wazabuni wetu watakavyolipwa. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ningependa kufahamu, je, Serikali kupitia Wizara ya Maji haioni kuna uhitaji na sababu kubwa ya kuweka bei pungufu ya kuunganisha maji kama ilivyofanyika kwenye umeme kwa sababu nikitolea mfano kwenye Jimbo la Bukoba Mjini, Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kuna upatikanaji wa maji, lakini gharama ya kuunganisha wakazi ili waweze kunufaika na maji hayo bado ni kubwa sana.

Je, Serikali haioni ipo haja ya kuweka bei elekezi ambayo itakuwa ni gharama nafuu ili kuhakikisha kwamba kaya zote zinanufaika na maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Neema Lugangira, anaendelea kuwasemea wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ina mambo matatu ambayo imejikita nayo; la kwanza, upatikanaji wa huduma bora, lakini pia muda wa upatikanaji wa huduma yenyewe, lakini na gharama ambayo mwananchi anatakiwa kununua huduma hiyo ya maji. Kikubwa ni kwamba Wizara yetu kupitia Mheshimiwa Waziri, alishatoa mwongozo na mwongozo huo ni kulingana na aina ya uzalishaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aina ya maji ambayo tunayapata kwa njia ya mserereko, kuna aina ya maji tunayopata kwa njia ya umeme wa solar na kuna aina ya maji ambayo uzalishaji wake unatokana na umeme wa TANESCO. Kwa hiyo, ukiangalia uzalishaji wake na gharama zake zitakuwa tofauti. Kwa mfano, kwa sasa umeme wa TANESCO ndiyo umeme ambao uzalishaji wake unakuwa na gharama kubwa hivyo hata mtumiaji wa mwisho atapata kwa gharama kidogo ambayo imechangamka, lakini umeme wa solar kidogo inashuka kidogo, mserereko unakuwa chini kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ni nini? Kikubwa ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kupeana elimu ya kujua kwamba maji haya kuna gharama fulani ambazo zimehusishwa mpaka mtumiaji wa mwisho anaenda kuyapata hayo maji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tutaendelea kulitazama kama Serikali pale ambapo tutaona kwamba inaruhusu kupunguza gharama tutafanya hivyo kwa manufaa ya Watanzania, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kufahamu ni nini mkakati wa Serikali kuweka utaratibu wa kuuza vanila, hususani mkoani Kagera? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mkakati wa Serikali wa sasa ni kwamba zao la vanila tumeliingiza kati mnada wa TMX kwa maana linauzwa kwa mnada na kwa mfano tulikuwa kule Kyela pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulienda kuzindua msimu wa ununuzi wa vanila kupitia mfumo wa TMX. Kwa hiyo, mfumo ule siyo tu utatumika Kyela ni kwamba utatumika katika maeneo yote wanayozalisha mazao ya vanila ikiwemo Kagera, ahsante. (Makofi)