Answers to Primary Questions by Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew (98 total)
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza:-
Je, ni lini minara ya simu itajengwa katika Kata za Endahagichen – Ndamilay, Mewadan – Magong na Endaghadat – Qamtananat katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambazo hazina mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni siku yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa katika Bunge lako hili tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini ili nikatetee na kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Jimbo la Bariadi. Pia naomba niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Bariadi kwa kunichagua kwa kishindo na hakika hawajapoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuniamini na kuniteua kuwa msaidizi wake katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote pamoja na wadau wengine wa sekta ya mawasiliano ina jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya vijijini na mijini yasiyo na mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa jumla ya kata 633 zimekwishapata huduma za mawasiliano nchi nzima ambapo ujenzi unaendelea katika kata zingine 361 kupitia ruzuku ya Serikali. Watoa huduma kwa uwekezaji wao wamefikisha huduma za mawasiliano katika kata 1,692.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tarehe 25 Januari, 2021 tuliwekeana sahihi ya mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 59 zenye vijiji 166 katika zabuni ya awamu ya tano. Vilevile mwezi huu tunatarajia kutangaza zabuni nyingine ya awamu ya sita ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 74 zenye vijiji 206.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) una miradi 15 katika Jimbo la Mbulu Vijijini katika kata 13. Kata zenye miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano ni pamoja na Yaeda Ampa, Yaeda Chini, Maghang, Masieda, Bashay, Eshkesh, Geterer, Gidihim, Hayderer, Maretadu, Masqaroda, Endamilay, na Tumati. Jumla ya minara 14 imekamilika kujengwa katika kata 12 kati ya minara 15 inayopaswa kujengwa, hii ni sawa na asilimia 87.5 (87.5%) ya utekelezaji wa miradi hiyo. Bado mnara mmoja ambao unatarajiwa kujengwa na Shirika letu la Mawasiliano Tamnzania (TTCL) ambao utakamilika kabla ya mwezi Juni, 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado kuna takribani kata 1,365 kati ya Kata 3,956 zilizopo Tanzania Bara zikiwemo kata za Jimbo la Mbulu Vijijini na wadi 16 kati ya wadi 111 zilizopo Zanzibar ambazo bado zina changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inavifanyia tathmini vijiji vingine vyote Tanzania Bara na Visiwani vikiwemo Vijiji ambavyo viko katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambavyo ni Endahagichen – Ndamilay, Mewadan – Magong na Endaghadat – Qamtananat, na hatimaye vijiji husika vitaingizwa katika orodha ya vijiji ambavyo vitajumuishwa katika kutangaza zabuni katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano ya simu katika Kata ya Uru Shimbwe Jimbo la Moshi Vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote inatambua changamoto ya ukosefu wa huduma za mawasiliano katika Kata ya Uru Shimbwe yenye Vijiji vya Shimbwe Chini na Shimbwe Juu. Tathmini katika Kata hii ilifanyika mwezi Machi mwaka 2021 na kubainika kuwa vijiji hivi vina changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano. Hivyo, Vijiji hivi vya Kata ya Uru Shimbwe vitaingizwa katika zabuni zijazo za kupata mtoa huduma wa kuvifikishia huduma za mawasiliano. Nashukuru.
MHE. AMINA ALI MZEE Aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuhamasisha vijana nchini kujiunga na biashara mtandao?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbali mbali katika kuweka mazingira wezeshi nchini ya kuvutia wananchi wengi kujiunga na biashara mtandao hususan vijana. Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala ya kielektroniki inayofanyika kimtandao.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inapitia Sheria na tozo mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa vijana, wabunifu wa TEHAMA na wale wanaochipukia (start-ups) ili kuweka mazingira wezeshi ya vijana kushiriki kwenye biashara mtandao. Hii hatua inakwenda sambamba na maboresho yanayoendelea ya kupunguza tozo za leseni za maudhui mtandaoni, kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2021.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Posta Tanzania imeanzisha jukwaa la kutangaza na kuuza bidhaa na huduma kwa njia ya mtandao ambapo maduka 270 ya kuuza na kununua bidhaa yamesajiliwa na jukwaa hili ambalo linapatikana kupitia tovuti https://www.postashoptz.post. Jukwaa hili limeunganishwa na mtandao wa vituo 670,000 duniani. Jukwaa hili linatoa fursa kwa wafanyabishara ikiwemo vijana kutumia mtandao huo kufanya biashara mtandao kwa kuunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa na huduma ulimwenguni. Ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano ya simu katika Jimbo la Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imetekeleza miradi ya ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu katika maeneo mbalimbali Wilaya ya Lushoto. Mpaka sasa kuna miradi 16 ya ujenzi wa minara katika Wilaya ya Lushoto katika kata 15 ambapo tayari miradi 8 imekamilika na miradi mingine 8 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi hiyo iko katika Kata za Baga, Kwai, Kwekanga, Malibwi, Malindi, Manolo, Mayo, Mbaramo, Mgwashi, Mlola, Mponde, Rangwi, Shume, Ubiri na Vuga. Miradi ya ujenzi wa minara katika Kata za Kwekanga, Kwai, Malindi, Manolo, Mbaramo, Mayo, Mponde na Mlola imekamilika na tayari inatoa huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa minara ya mawasiliano unaendelea katika Kata za Shume, Ubiri, Rangwi, Mgwashi, Vuga, Baga, Kwai na Malibwi. Ujenzi wa minara hii utakamilika mwezi Disemba 2021. Aidha, Kata zilizobaki Mfuko utazifanyia tathmini na zitaingizwa katika zabuni zijazo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika Kata za Masisiwe, Nyanzwa, Irole na Ibumu ambazo zina shida kubwa ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Serikali ya Awamu ya Sita, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. Sambamba na hilo, naomba niwapongeze wanawake wote wa Tanzania, kwa sababu wameendelea kuonesha mfano wa kuigwa, tukishuhudia katika Awamu ya Nne, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Katika Awamu ya Tano, alikuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kuwa Makamu wa Rais na katika Awamu ya Sita, amekuwa mwanamke wa kwanza katika Nchi yetu ya Tanzania kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuniamini kumsaidia katika nafasi ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kilolo lina Kata 24 ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeishakamilisha utekelezaji wa miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata tatu ambazo ni Lugalo ambapo ina mnara wa Halotel, Udekwa ambapo kuna mnara Vodacom na Ukwega ambapo kuna minara miwili ya Tigo na Halotel.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizi za Serikali baadhi ya kata za jimbo hili zinachangamoto za upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kama vile Kata za Masisiwe, Nyanzwa, Ibumu na baadhi ya maeneo ya Kata ya Irole. Jiografia ya jimbo hili ni ya milima na miti mirefu ambapo kwa kiasi kikubwa sana inaathiri upatikanaji wa huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Irole kuna baadhi ya maeneo yanapatikana huduma za mawasiliano kupitia mnara wa mawasiliano wa HTT, uliobeba watoa huduma watatu ambao ni Airtel ambayo inatoa teknolojia ya 2G, Vodacom ambapo wanatoa teknolojia ya 2G na 3G na Tigo ambao wanatoa 2G na 3G. Pamoja na uwepo wa huduma za mawasiliano kutoka kwa watoa huduma niliotaja, bado kuna maeneo ndani ya Kata ya Irole yana changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliifanyia tathmini Kata ya Ibumu na hatimaye kukijumuisha Kijiji cha Ilambo katika zabuni ya awamu ya tano ya mradi wa kufikisha mawasiliano mipakani na kanda maalum. Mradi huu unatekelezwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambapo mikataba ya utekelezaji wa mradi huo ilitiwa saini tarehe 6 Julai, 2020. Mradi huu utakapokamilika utaweza kuhudumia Vijiji vya Ibumu, Kilala, Kidewa, Ilambo na Kilumbwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote UCSAF itavifanyia tathmini vijiji vya Kata za Masisiwe, Nyanzwa na baadhi ya vijiji vya Kata ya Irole ambavyo huduma ya mawasiliano imekuwa changamoto kwa kiasi kikubwa sana. Huduma inatolewa na mnara wa HTT uliopo na hatimaye vijiji husika vitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-
Je, ni lini changamoto ya mawasiliano ya simu Wilayani Nanyumbu itamalizika katika Kata za Likokona, Mkonona, Nangomba, Nandete, Napacho, Lumesure, Michiga na Chipuputa?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ina jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya vijijini na mijini yasiyo na mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa kupitia tumeshafikisha miradi 1,057 ambapo miradi 686 imeshakamilika na miradi 371 inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali bado kuna maeneo mengi yakiwemo maeneo ya Jimbo la Nanyumbu ambayo hayana huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, umevifanyia tathmini vijiji vya Kata ya Likokona, Mkonona, Nangomba, Nandete, Napacho, Lumesure, Michiga na Chipuputa katika Jimbo la Nanyumbu. Vijiji vya Kata hizi vimeingizwa katika Mradi wa Mpakani na Kanda Maalum awamu ya sita ambapo zabuni tarajiwa kutangazwa kabla ya kwisha kwa mwaka wa fedha 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Jimbo la Nanyumbu vilivyoingizwa katika zabuni hiyo inayotarajiwa kutangazwa ni kama ifuatavyo:-
1. Kata ya Likokona Vijiji vya Misawaji, Namaka, Msinyasi, na Likokona;
2. Kata ya Mkonona Vijiji vya Nambundu, Waniku and Namaromba;
3. Kata ya Nandete Vijiji vya Chivikikiti na Nakole;
4. Kata ya Lumesure Kijiji cha Lumesure;
5. Kata ya Michiga Kijiji cha Makong’ondera; na
6. Kata ya Chipuputa Vijiji vya Mpwachia, Nakatete na Ngalinje.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Vijiji vya Kata za Nangomba na Napacho vitaingizwa kwenye awamu nyingine ya miradi ya kufikishiwa huduma za mawasiliano kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano ya simu kwenye Vijiji vya Igalula ambavyo havina mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ina jukumu la kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini ambayo hayana mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa Mfuko wa Mawasiliano umeshatekeleza miradi 686 na bado kuna miradi katika kata 371 ikiwa inaendelea na utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Igalula lina kata 11 ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza miradi sita ya mawasiliano katika Jimbo la Igalula ambapo imejengwa minara sita ambayo imetolewa na watoa huduma katika Kata tano ambazo ni Kizengi, Loya ambayo ina Miradi miwili, Lutende, Miswaki pamoja na Tura.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata zenye watoa huduma wa mawasiliano katika Jimbo la Igalula ni 10 ambazo ni Igalula yenyewe, Kigwa, Loya, Lutende, Miswaki, Kizengi, Miyenze, Tura, Goweko pamoja na Nsololo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada za Serikali, Kata ya Mmale na baadhi ya maeneo ya Jimbo la Igalula bado yana changamoto ya mawasiliano na kupitia Mfuko wetu wa Mawasiliano tunaendelea kufanya tathmini, ili tujiridhishe specifically kwamba kuna changamoto katika maeneo yapi ili yaingizwe katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika siku za usoni kadri upatikanaji wa fedha utakapokuwa unaruhusu. (Makofi)
MHE. YAHYA ABDULWAKIL AHMED aliuliza: -
Je, Shirika la Posta Zanzibar halioni umuhimu wa kuchimba kisima katika Jimbo la Kwahani katika Kitongoji kilichopo karibu na Ofisi hiyo ili kukuza ujirani mwema?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Abdul Wakil Ahmed Mbunge wa Kwohani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania ni taasisi ya Kimuungano ambapo kwa upande wa Zanzibar ina jumla ya Ofisi tisa, kati ya Ofisi hizo, Unguja kuna Ofisi tano ambazo zipo Kijangwani, Shangani, Mahonda, Jambiani na Makunduchi; na Pemba kuna Ofisi nne zilizopo Chakechake, Wete, Mkoani na Kengeja.
Mheshimiwa Spika, Shirika limekuwa na utaratibu kila mwaka wa kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii kwa kuzingatia mtiririko wa fedha na bajeti ya mwaka husika. Kwa kipindi cha miaka mitatu yaani 2018 hadi 2020 Shirika katika kuchangia huduma za kijamii kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – SMZ imefanya yafuatayo: -
(i) Mwaka 2018, Shirika lilitoa vifaa mbalimbali katika Kituo cha wazee cha Amani ili kusaidia matunzo ya wazee katika kituo hicho.
(ii) Mwaka 2019, Shirika lilitoa vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Mnazi Mmoja ili kusaidia akinamama wanaojifungua.
(iii) Mwaka 2020, Shirika lilitoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kusaidia wazee wanaotunzwa katika kituo cha kulelea Wazee cha Welezo kilichopo Unguja.
Mheshimiwa Spika, Shirika linaendelea na utaratibu wake wa huduma kwa jamii kulingana na bajeti. Shirika litaangalia uwezekano wa kuchangia uchimbaji wa kisima katika kitongoji kilichopo karibu na ofisi katika kuendeleza ujirani mwema kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu, ahsante.
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka Mawasiliano ya Simu yenye usikivu katika Kata ya Litehu, Ngunja na Mkwiti Wilayani Tandahimba?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani Mbunge wa Tandahimba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi saba katika kata sita za Jimbo la Tandahimba kupitia Mradi wa Awamu ya nne na tano . Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Chaume, Mdimba Mnyoma, Mkoreha katika Kijiji cha Chikongo, Ngunja. Kuna miradi miwili mmoja uko Kijiji cha Ngunja na mwingine Namindondi Juu, lakini katika Kata ya Mihambwe, na Namikupa utekelezaji wa mradi uliopo katika hizo Kata unaendelea.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado kuna maeneo mengi ya Jimbo la Tandahimba ambayo yana changamoto za mawasiliano. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano imevifanyia tathmini vijiji vya Kata za Litehu, Ngunja na Mkwiti katika Jimbo hilo.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba zinaingizwa katikazabuni ya mradi wa mipakani na kanda maalumu ya Kanda Maaalum awamu ya sita yaani Border and Special Zone Phase six Mradi huu unatarajiwa kutangazwa kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano katika Kijiji cha Matinje Ikombandulu ambalo ni eneo la machimbo na lina idadi kubwa ya watu ili kurahisisha biashara katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi mitatu katika Jimbo la Manonga. Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Igoweko; mnara huu unahudumia pia Kata ya Uswaya, Sungwizi pamoja na Ngulu. Utekelezaji wa miradi katika Kata hizi umekamilika.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itakifanyia tathmini Kijiji cha Matinje Ikombandulu na hatimaye kijiji hiki kitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika mwaka wa fedha 2021/22, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Kijiji cha Kintanula Kata ya Mwamagembe katika Jimbo la Manyoni Magharibi mawasiliano ya uhakika ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi minne katika Kata mbili za Jimbo la Manyoni Magharibi. Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Mgandu ambapo kuna miradi miwili na Idodyandole miradi miwili. Utekelezaji wa miradi yote miwili katika Kata ya Mgandu na mradi mmoja katika Kata ya Idodyandole umekamilika. Utekelezaji wa mradi mmoja katika Kata ya Idodyandole katika Kijiji cha Mbugani bado unaendelea.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itakifanyia tathmini Kijiji cha Kintanula Kata ya Mwamagembe na hatimaye kijiji hiki kitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Je, ni lini Kata 16 zisizo na mawasiliano ya simu katika Wilaya ya Urambo zitapatiwa mawasiliano ya simu na kuwaondolea wananchi adha ya kutokuwa na mawasiliano kwa muda mrefu?
Je, ni kwa nini kuna maeneo yenye minara ya mawasiliano ya simu lakini kuna matatizo ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Urambo lina jumla ya Kata 18 ambapo Kata zote zina huduma ya mawasiliano isipokuwa vijiji baadhi katika Kata Tisa za Kiloleni, Itundu, Imalamakoye, Ugalla, Vumilia, Nsondo na Uyogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Utundu na Ukondamoyo zitafikishiwa huduma za mawasiliano na kampuni ya simu ya Vodacom ifikapo Oktoba, 2021, Kata za Nsondo na Uyogo zitafikishiwa huduma za mawasiliano na kampuni ya Airtel ifikapo Oktoba, 2021, Kata ya Vumilia itafikishiwa huduma za mawasiliano kupitia kampuni ya simu ya Halotel ifikapo Septemba, 2021 pamoja na Kata ya Ugala itakayofikishiwa huduma na kampuni ya simu ya TTCL ifikapo Septemba, 2021. Aidha Kata za Kiloleni na Imalamakoye zitaingizwa kwenye miradi ya mfuko itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha kukosekana huduma ya mawasiliano kwenye maeneo yenye minara ya simu ikiwa ni pamoja na hali ya kijiografia ya eneo husika kama vile uwepo wa milima, mabonde na uoto wa asili wenye miti mirefu ambayo huzuia huduma za mawasiliano. Hali ya kukosekana kwa nishati ya umeme wa uhakika pia inaweza kusababisha minara kushindwa kutoa huduma za mawasiliano. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -
Je, Serikali haioni uamuzi wa kutaka ifikapo tarehe 1 Mei, 2021 wasajili wa namba za simu za mkononi mitaani (freelancers) wawe katika maduka unaweza kufuta ajira zaidi ya 40,000 na kudhoofisha lengo lake la ajira milioni nane ifikapo mwaka 2025?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tarehe 16 Februari, 2021 Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliwaelekeza watoa huduma kutekeleza takwa la kikanuni la usajili wa laini za simu kibayometria kwa kuwatumia mawakala wanaokidhi vigezo kwa mujibu wa Kanuni ya 10 ya Kanuni za Usajili wa Laini za Simu ya 2020 (The Electronic and Postal Communications (SIM Card Registration) Regulations, 2020 GN No. 112 ya 2020.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa freelancers kwenye sekta, kiuchumi na katika kulinda ajira zao, tarehe 14 Aprili, 2021 Serikali ilisitisha zuio kwa watoa huduma kutowatumia freelancers katika usajili wa laini za simu kibayometria, kwa kutoa taarifa kwa umma na kwa kuwaandikia watoa huduma barua ya kuondoa zuio hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma imetengeneza rasimu ya mwongozo wa kuwatambua na kuratibu kazi za freelancers ili kuondoa mapungufu yaliyojitokeza na kuweka bayana uhusiano kati ya watoa huduma na freelancers, ahsante.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -
Je, Serikali ina mikakati gani ya ziada ya kudhibiti tatizo la utapeli na wizi wa kimtandao kupitia simu za mkononi?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imechukua hatua za kuweka mazingira salama kwa wananchi hususan kwenye mitandao kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Makosa ya Mitandao kwa lengo la kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao ili kuweza kuchukua hatua stahiki yanapobainika makosa hayo; na vile vile, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mitandao chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa ya kimitandao ikiwemo wizi wa aina yoyote kwenye mtandao na kuandaa majalada ya kufungulia mashtaka kwa kusaidiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Watuhumiwa wanaokamatwa kutokana na matumizi mabaya ya mitandao huchukuliwa hatua stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Februari, 2021 Serikali imeunda Kamati ya Taifa ya Kusimamia Utatuzi wa Matumizi Mabaya ya Huduma na Bidhaa za Mawasiliano ambayo inahusisha Wizara na taasisi zote zinazohusika katika kushughulikia makosa ya mtandao. Kamati hiyo ni Kamati ya kudumu na inaishauri Serikali namna ya kutatua changamoto za mitandao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Watoa Huduma wa Simu za Mkononi imeanzisha mfumo kupitia namba 15040 wa kupokea na kuzifungia namba ambazo zimeripotiwa na kuthibitika kutuma ujumbe au kupiga simu za utapeli. Baada ya kuthibitisha namba hizo kufanya vitendo hivyo, namba husika hufungiwa na kitambulisho cha NIDA kilichotumika kusajili namba hiyo kufungiwa pia, lakini vile vile hata kifaa ambacho kimetumika pia(simu) kinafungiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali itaendelea kuongeza jitihada za kuelimisha Umma matumizi mazuri na sahihi ya TEHAMA kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ahsante. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu katika Kata ya Litapunga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufatia mabadiliko aliyoyafanya katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na baadaye kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuniteua na kuniapisha kuendelea kuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Taknolojia ya Habari.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata ya Litapunga ina jumla ya vijiji nane ambavyo ni Kaburonge “A”, Kaburonge “B”, Kambuzi “A”, Kambuzi “B”, Kambuzi Halt, Bulembo, Lukama pamoja na Litapunga.
Mheshimiwa Spika, Kata hii imekuwa ikipokea huduma za mawasiliano kutoka kata Jirani za Katumba na Kanoge zenye huduma ya mawasiliano ya Mtandao wa Halotel na Vodacom.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini ya kiufundi ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata ya Litapunga ili kupata uelewa wa pamoja na ukubwa halisi wa changamoto ili kuelekeza ufumbuzi unaoendana na changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Spika, iwapo tathmini hiyo itabainisha kuwa utatuzi wa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano iliyopo unahitaji kuwa na mnara katika kata hiyo, basi Serikali itaingiza kata hii katika zabuni zitakazotangazwa katika siku za karibuni kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano wa Halotel katika Kata ya Chilangala ambapo mkataba ulisainiwa mwaka 2020 lakini mpaka Septemba, 2021 mradi huo haujaanza?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARl alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika zabuni ya awamu ya nne ya kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini, iliingia mkataba wa kufikisha huduma ya mawasiliano ya simu katika Kata 114 ikiwemo Kata ya Chilangala na Kampuni ya Halotel (Viettel) mnamo tarehe 24 Januari 2020. Utekelezaji wa mkataba huo ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi tisa yaani tarehe 23 Oktoba 2020. Lakini kutokana na changamoto ya UVIKO-19 utekelezaji wa mradi huo ulichelewa.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi huo ulipelekea watoa huduma wengine kuboresha huduma za mawasiliano katika kata hiyo ambapo Kata ya Chilangala ina mawasiliano ya Mtandao wa Tigo ambao wana minara miwili katika Vijiji vya Chilangala na Namdimba. Hivyo basi, Serikali haitojenga mnara huo katika Kata ya Chilangala, na hivyo kuzielekeza fedha hizo katika maeneo mengine yenye changamoto zaidi za mawasiliano. Ahsante.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha usikivu wa Radio ya Taifa (TBC) katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiboresha usikivu wa TBC kwa kutenga fedha katika bajeti ya maendeleo kila mwaka ili kuyafikia maeneo yasiyo na usikivu wa TBC kwa nchi nzima yakiwemo maeneo ya Zanzibar. Miradi iliyotekelezwa na TBC ni pamoja na kufunga mitambo ya kurushia matangazo ya redio katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, aidha, miradi ya upanuzi wa usikivu wa TBC inaendelea kutekelezwa katika Mikoa mipya ya Songwe, Njombe na Simiyu. Vilevile upanuzi huo unaendelea kwa upande wa Visiwa vya Unguja na Pemba. Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo Machi, 2022.
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuiwezesha TBC ili maeneo yote nchini ambayo hayana usikivu yakamilike ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM (2020 – 2025) Ibara ya 125 (f). Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la mawasiliano ya simu katika maeneo ya Bukiko, Chabilungo, Kitale na maeneo mengine yenye tatizo hilo Visiwani Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, eneo la Bukiko lina mnara wa Halotel uliojengwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Eneo la Chabilungo linapata huduma za mawasiliano kupitia watoa huduma ambao ni Tigo, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) pamoja na Vodacom.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini kwa mara nyingine katika maeneo ya Chabilungo, Bukiko, Kitale na maeneo mengine katika Jimbo la Ukerewe ili kubaini mahitaji halisi ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo hayo, Ahsante.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: -
(a) Je, ni lini Serikali itafanya maboresho ya mawasiliano ya simu katika Jimbo la Tabora Mjini hususan kwenye kata za pembezoni?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka minara ili kuondoa changamoto hii hasa katika kata ya Itetemia ambayo ina changamoto kubwa ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum - Tabora, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ilifanya tathmini katika Jimbo la Tabora Mjini na kubaini kuwa kata 12 za pembezoni zilikuwa zinahitaji wa kufanyiwa maboresho ya huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imefikisha huduma za mawasiliano ya simu katika kata tatu za pembezoni ambazo ni Kabila -mtoa huduma ni Halotel; Kalunde na Uyui - mtoa huduma ni Vodacom ndio wamefikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo hayo yenye teknolojia ya 2G pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ipo katika maandalizi ya awali ya kutangaza zabuni ya kuboresha miundombinu ya minara iliyopo ili iweze kutoa huduma za mawasiliano zenye kutumia teknolojia ya 2G/3G na 4G. Aidha, ujenzi wa minara katika teknolojia ya 2G/3G na 4G unaendelea katika kata tatu za Ndevela, Tumbi pamoja na Itetemia kupitia mtoa huduma Halotel.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Itetemia; Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iliitangaza kata ya Itetemia katika zabuni ya awamu ya nne na kupata mtoa huduma ambae ni Kampuni ya Simu ya Halotel kwa ajili ya kifikisha huduma za mawasiliano ya simu katika kata hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mnara huo wa simu upo katika hatua za mwisho na unatarajiwa kuanza kutoa huduma kabla ya mwezi Julai, 2022 na utakuwa na teknolojia ya 2G/3G na 4G.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawezesha upatikanaji wa mawasiliano ya simu katika Kata ya Likawage na vijiji vyake vya Likawage, Nainokwe na Liwiti?
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa na kwa unyenyekevu kabisa naomba upokee salamu za pongezi kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Bariadi kwa wewe kuchaguliwa kwa kishindo kabisa kuwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tulibaini uwepo wa changamoto ya mawasiliano ya simu katika Kata ya Likawage na vijiji vyake vyote. Hivyo, Serikali ilitangaza kata hii katika zabuni ya awamu ya tano ya mwaka 2021.
Mheshimiwa Spika, kata hiyo ilipata mtoa huduma wa Kampuni ya Tigo iliyokamilisha ujenzi wa minara miwili mnamo mwezi Oktoba, 2021. Ujenzi wa minara hiyo umetatua tatizo la mawasiliano lililokuwepo katika Kata ya Likawage na vijiji vyake. Nakushukuru.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga mnara wa mawasiliano ya simu katika Kata ya Mtego wa Noti ili wananchi waweze kupata huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilifanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa kutembelea Kata ya Mtego wa Noti mnamo tarehe 19 Disemba, 2021 na kubaini kuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Mtego wa Noti imeainishwa ili kuingizwa katika zabuni ijayo ya kufikisha huduma za mawasiliano ya simu inayotarajiwa kutangazwa katika mwaka huu wa fedha 2021/2022. Aidha, ujenzi wa mnara huo utaanza mara baada ya kupatikana mtoa huduma na hivyo wananchi wa kata hiyo watarajie kupata huduma za mawasiliano ya simu mara baada ya kukamilika ujenzi huo, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -
Je, ni lini Mtambo wa matangazo ya TBC Taifa na TBC FM utafungwa katika Mji wa Itigi ili Wananchi wapate matangazo hayo muhimu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare Mbunge wa Manyoni Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenekiti, Serikali kupitia Shirika lake la Utangazaji la Taifa (TBC) mkakati wake ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya matangazo ya redio nchi nzima ifikapo Mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Mwaka 2022/2023 TBC imepanga kuwasilisha maombi katika Bunge lako tukufu kuidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni saba zitakazotumika mahsusi kwa ajili ya upanuzi wa usikivu katika Wilaya 14 nchini ikiwemo Wilaya ya Manyoni. Mkakati ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika wilaya ambazo hazipati matangazo ya TBC Taifa na TBC FM zinapata ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenekiti, TBC imeendelea kuboresha usikivu katika maeneo ambayo hayana usikivu ama usikivu wake ni hafifu. Miradi inayotekelezwa kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 ni katika Wilaya na maeneo 24 ya nchi ikiwemo maeneo ya mpakani ambayo ni Ngara, Karagwe, Kasulu, Tanganyika, Same na Nkasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ni Kilombero/Mlimba, Kahama, Sikonge, Bunda, Ngorongoro, Uvinza, Makete, Ruangwa, Kyela, Morogoro Vijijini/Kisaki, Kilwa, Serengeti, Songwe, Njombe, Simiyu, Unguja na Pemba. Miradi hii iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika yote na kuzinduliwa ifikapo Julai, 2022. Miradi hii ikikamilika usikivu wa TBC utafikia asilimia 83, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya udanganyifu mkubwa kwenye mikataba ya Ushuru wa kampuni za Simu na wenye maeneo pale panapojengwa minara ya simu kiasi cha kusababisha ushuru kwenda kwa watu wasiohusika?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeir Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kwa mtumiaji wa mwisho huwezeshwa na minara ambayo kwa kiasi kikubwa hujengwa ardhini, lakini pia husimikwa katika majengo marefu, hususan katika maeneo ya miji mikubwa. Ardhi ambayo hutumika katika ujenzi wa minara humilikiwa na wananchi ama taasisi za umma au taasisi za kijamii ambapo hupangishwa kwa mtoa huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, katika kubaini eneo linalopaswa kujengwa mnara wa mawasiliano vigezo mbalimbali vya kitaalam hutumika kama vile uimara wa ardhi, eneo linalowezesha mnara husika kuwasilisiana na minara mingine na maeneo yanayoweza kufikiwa na mawasiliano kupitia mnara husika. Vigezo hivi na vingine ndio vinaweza kuamua mahali sahihi ambapo mnara unaweza kujengwa. Kwa utaratibu uliopo sana, eneo likibainika kukidhi vigezo vya kitaalam, mtoa huduma hufanya mawasiliano na mmiliki wa eneo husika pamoja na Serikali ya eneo hilo ili eneo hilo liweze kujengwa mnara wa mawasiliano. Mtoa huduma huingia mkataba na mmiliki wa eneo ambapo mmiliki huyo hulipwa fedha ya pango la ardhi kulingana na makubaliano yaliyofikiwa ambayo ndiyo huwekwa katika mkataba.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya minara ya mawasiliano ikiwemo kufuata taratibu katika upangishaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa minara. Vilevile Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umetoa maelekezo katika mikataba wanayoingia na Kampuni za Simu kufuata taratibu zote katika kukodi ardhi ambapo minara hiyo hujengwa kupitia halmashauri husika. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu Kata ya Jangwani na Mtawanya Manispaa ya Mtwara Mikindani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata ya Jangwani iliyopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani inapata huduma za mawasiliano kutoka kwa Kampuni za Tigo, Airtel na Vodacom. Vile vile maeneo ya Kata ya Mtawanya yanapata huduma hafifu za mawasiliano kutoka kwa watoa huduma wa Airtel, Vodacom na Tigo kupitia minara iliyojengwa katika Kata ya Likombe juu ya Mlima wa Lilungu.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itavifanyia tathmini na uhakiki wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano maeneo yote yaliyopo katika Kata za Jangwani na Mtawanya na kuchukua hatua stahiki mara moja ili kuimarisha na kuboresha huduma endapo utatuzi hautahitaji ujenzi wa minara mipya.
Mheshimiwa Spika, endapo tathmini hiyo itabaini utatuzi wa changamoto zilizopo unahitaji ujenzi wa minara mipya, maeneo husika katika kata hizi yataainishwa na kuingizwa katika zabuni za kufikisha huduma ya mawasiliano zitakazotangazwa katika mwaka wa fedha 2023/2024. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika Kata za Jimbo la Ludewa pamoja na kuongeza nguvu kwa minara iliyopo iwe 4G?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius kamonga Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Seriakili kupitia Mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF inaendelea kutatua changamoto za mawasiliano katika Jimbo la Ludewa kwa kushirikiana na watoa huduma wa mawasiliano kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Airtel ambao sasa tayari imewasha minara mitatu katika Kata za Madiru Kijiji la Ilawa, Kata ya Madope Kijiji cha Lusitu na Kata ya Mkongobaki katika Kijiji cha Mkongobaki.
Mheshimiwa Spika, kampuni ya tiGo ambayo imejenga minara katika Kata ya Lupanga, Kijiji cha Lupanga, Kata ya Mkomang’ombe Kijiji cha Mkomang’ombe na Kata ya Ludewa Kitongoji cha Ngalahawe ambapo mnara unafika katika Kijiji cha Nindi. Aidha, kampuni ya simu ya tiGo ipo katika hatua za kutekeleza mradi wa kufikisha huduma ya mawasiliano katika Kata ya Lupingu na Mkwimbili ambapo changamoto kubwa imekuwa ni namna ya kusafirisha vifaa vya ujenzi wa mnara na kuvifikisha katika eneo la mradi.
Mheshimiwa Spika, pia Halotel inatoa huduma katika Kata zote za mwambao wa Ziwa Nyasa zikiwemo Makonde, Kimata, Nsele, Ndowa na Igalu. Hata hivyo, Serikali inatambua changamoto kubwa ya mawasiliano inayowakabili wananchi wote wa kandokando ya Ziwa hususa ni Tarafa ya Jua. Kwa upande mwingine, TTCL inatoa huduma katika Kata ya Ibumi japo bado kuna changamoto hasa katika Kijiji cha Masimalavafu. Serikali inatambua kuwa mradi wa uchimbaji wa madini ambao kwa namna moja au nyingine utachangia pato la uchumi kwa nchi yetu. Hivyo, Serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF inatumia wataalam wake kwenda kata ya Ibumi na kuangalia namna gani ya kutatua changamoto ya mawasiliano hususa ni katika eneo la uchimbaji wa madini.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na nguvu ya minara kwenda teknolojia ya 4G. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeanza kutekeleza mradi wa kuongeza nguvu kwenye minara yote nchini iliyokuwa na teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G. Hivyo, minara iliyopo Jimbo la Ludewa itaingizwa katika mradi huo. Ahsante sana.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza programu ya kuunda na kurusha setilaiti?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwa na Setilaiti, hivyo, mwaka huu wa fedha Serikali imeanza utaratibu wa awali utakaowezesha kuunda na kurusha setilaiti angani. Ili kuwezesha kufikia azma hiyo, Serikali tayari imeandaa andiko dhana na kuunda timu ya wataalam watakaoshauri aina ya setilaiti tutakayorusha angani itakayoendana na mahitaji halisi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio kuwa timu hiyo itakamilisha kazi ya uchambuzi kisha kuwasilisha mapendekezo yake Serikalini kwa hatua za kimaamuzi ndani ya mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuboresha minara ya mawasiliano ya simu katika Kata za Makurunge na Fukayosi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imezijumuisha Kata za Makurunge na Fukayosi katika Mradi wa Tanzania ya Kidigitali unaotekelezwa kwa fedha kutoka Benki ya Dunia ambapo zabuni ya mradi huo imeshatangazwa tarehe 24 Oktoba, 2022.
Mheshimiwa Spika, kata hizo zitapata huduma za mawasiliano kwa teknolojia za 2G, 3G na 4G. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya mikataba ya minara ya simu kati ya kampuni za simu na Kijiji cha Namuchinka Kata ya Kapele?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Namchinka kina minara miwili iliyojengwa na Kampuni ya Tigo na Halotel. Minara hiyo imesimikwa katika ardhi inayomilikiwa na watu binafsi na siyo kijiji. Hivyo, watoa huduma hulipa malipo ya pango la ardhi kwa wamiliki hao kulingana na makubalino katika mikataba waliyoingia.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu nitoe maelekezo kwa watoa huduma wote kuhakikisha kuwa wanashirikisha Serikali ya Wilaya na Kijiji wanapotaka kujenga minara ya mawasiliano katika Kijiji husika ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza ya namna hii. Vilevile, watoa huduma wahakikishe waingie mikataba ya ulinzi wa minara na Serikali za Vijiji ili kuwa na ulinzi wa uhakika katika minara ya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nitoe rai kwa wananchi kuwa wazalendo na kutoa ushirikiano kwa watoa huduma wakati wa ujenzi na ulinzi wa miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinakuwa endelevu kwenye maeneo yetu.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano ya simu katika Kata ya Karitu na Ikindwa – Bukene?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliifanyia tathmini Kata ya Ikindwa iliyopo katika Wilaya ya Nzega na kubaini kuwa ina changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na hivyo kata hiyo imejumuishwa katika zabuni iliyotangazwa tarehe 24 Oktoba, 2022 kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kata ya Karitu, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote itaifanyia tathmini kata hiyo ili kubaini mahitaji ya mawasiliano na kuiingiza katika zabuni zitakazotangazwa na Mfuko katika awamu zifuatazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -
Je, ni lini Kata za Kiangamanka, Ukata, Kipololo na Kijiji cha Kiwombi zitapelekewa mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kipololo inapata huduma za mawasiliano kutoka kwa Kampuni ya Halotel iliyojenga mnara katika Kijiji cha Lunoro. Kata ya Ukata inapata huduma za mawasiliano kutoka kwa Kampuni ya Vodacom iliyojenga mnara katika Kijiji cha Ukata na vile vile kutoka Halotel iliyojenga mnara katika Kijiji cha Litoho. Minara hii imejengwa kati ya mwaka 2017 na 2019 kwa ruzuku ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata ya Kiangamanka na Kijiji cha Kiwombi, Serikali itafanyia tathmini ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kata hii na kijiji hiki Katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023. Tathmini hiyo vile vile itahusisha uhakiki wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo yote yaliyopo katika Kata za Ukata na Kipololo, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -
Je, ni lini mnara wa mawasiliano ya simu utajengwa Kata ya Mamba Kusini Jimbo la Vunjo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mamba Kusini inaundwa na Vijiji vya Mkolowony, Lekura, Kiria, Kimbogho na Kimangara. Katika jitihada za Serikali za kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na watoa huduma, Kampuni za Tigo na Vodacom zinatoa huduma za mawasiliano katika kata hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali itafanya tathimini katika Kata hii ya Mamba ili kubaini changamoto zilizopo za mawasiliano ya simu na kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuyaingiza maeneo ya kata hii yatakayobainika kuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya uhakika katika orodha ya vijiji vitakavyoingizwa katika zabuni zijazo. Ahsante.
MHE. JOHN M. SALLU aliuliza: -
Je, ni lini minara ya simu itajengwa katika maeneo ambayo hayana mawasiliano katika Jimbo la Handeni Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma ya mawasilianao katika Jimbo la Handeni Vijijini katika Kata za Kwamatuku ambapo umejengwa mnara wa Tigo katika Kijiji cha Kwamatuku; Kwamkonje ambapo umejengwa mnara wa Tigo katika Kijiji cha Kwamkonje; na Misima ambapo imejengwa minara miwili ya TTCL katika Vijiji vya Kibaya na Msomera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya tathmini ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika Jimbo la Handeni Vijijini katika Kata za Kang’ata, Kwamgwe, Kwamkonje, Kwaruguru, Kwasunga, Mazingara, Mgambo, Misima, Ndolwa na Sindeni pamoja na vijiji vyake vyote. Ilibainika uwepo wa changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano ambapo utatuzi wake unahitaji ujenzi wa minara ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia matokeo ya tathmini hiyo, Serikali imeziingiza kata hizi katika zabuni ya mradi wa Tanzania ya kidigitali iliyotangazwa na imefunguliwa tarehe 31 Januari, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -
Je, lini minara ya mawasiliano itapelekwa Kata za Nyamtukuza, Nyabibuye, Gwarama, Kasuga, Rugenge, Gwanumpu, Katanga na Magunzu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Vodacom imetekeleza miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Nyamtukuza, Nyabibuye, Gwarama, Gwanumpu, Rugenge na Mugunzu. Miradi hii imetekelezwa kati ya mwaka 2016 na 2019 ambapo ujenzi wa minara katika Kata hizi umekamilika na inatoa huduma kwa teknolojia ya 2G na 3G.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kata ya Katanga na Kasuga, Serikali itafanya tathmini ya hali halisi ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano Kata hizi katika mwaka wa fedha 2023/2024, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je, ni lini Minara yenye Kasi Kubwa itajengwa Kata za Nhwande, Kanoge, Uyowa, Silambo, Makingi, Ichemba, Igombemkulu na Mwongozo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Babari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetekeleza miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata tano ambazo ni Kata ya Kanoge, ambapo kuna mnara wa Airtel umejengwa katika eneo la Ulanga, Uyowa katika eneo la Uhindi, Ichemba eneo la Ichemba yenyewe, Igombemkulu katika eneo la Imara na Mwongozo katika eneo la Mwanditi ambapo minara hii imekamilika na inatoa huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Minara ya Kata za Kanoge, Ichemba, Igombemkulu na Mwongozo inatumia teknolojia ya 2G/3G hivyo inatoa huduma za mawasiliano yenye kasi kubwa; na mnara huu uliopo Kata ya Uyowa unatumia teknolojia ya 2G pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Uyowa imengizwa kwenye mpango wa kuboreshewa huduma za mawasiliano yenye kasi na zabuni yake itatangazwa katika awamu ijayo kulingana na upatinaji wa fedha. Aidha, Serikali itafanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu yenye kasi kubwa katika Kata za Nhwande, Silambo, na Makingi katika mwaka wa fedha 2023/2024, ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu na TBC Redio katika Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
(a) Kuhusu Ujenzi wa Minara ya simu, Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Kata za Bunyambo, Murungu na Nyaruyoba ambazo zimebainika kuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Jimbo la Muhambwe. Zabuni ya minara hiyo itatangazwa kabla ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 kukamilika.
(b) Kuhusu TBC Redio, mtambo wa masafa ya FM katika Jimbo la Muhambwe, Mwezi Machi, 2022 mtambo huo ulipigwa na radi iliyoharibu vipuri vyake. Vipuri hivyo vimeshaagizwa na tayari vimeshawasili nchini. Kazi ya kufunga vipuri hivyo itakapokamilika, na kuwashwa na kufanyiwa majaribio ya kiufundi kabla ya tarehe 30 Mei 2022 hivyo kurejesha usikivu wa TBC katika Jimbo la Muhambwe na maeneo ya jirani. Ahsante. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafikisha mawasiliano ya simu katika Kata ya Kinungu, Isakamaliwa, Mtungulu, Kining’inila na Itumba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Kinungu, Isakamaliwa, Mtungulu, Kining’inila na Itumba katika Jimbo la Igunga mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Mheshimiwa Spika, Zabuni ya miradi hii itatangazwa kabla ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 kukamilika. Ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Minara katika maeneo yasiyo na minara na kutatua matatizo ya mawasiliano katika maeneo yenye Minara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatekeleza miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata tatu za Ugalla, Itundu na Vumilia Wilayani Urambo ambapo ujenzi wa minara unaendelea na utakamilika ifikapo Julai 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imepanga kufikisha huduma za mawasiliano ya simu Kata za Kiloleni, Kasisi, Itundu na Uyogo katika mwaka wa fedha wa 2022/ 2023 baada ya kubaini uwepo wa changamoto za mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya vijiji katika kata hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata hizo zimejumuishwa katika zabuni inayotarajiwa kutangazwa kabla ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 kukamilika kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali. Utekelezaji wa miradi hii ya usimikaji wa minara ya mawasiliano utahusisha uboreshaji wa mawasiliano ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa huduma za intaneti katika Kata za Songambele na Imalamakoye asante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Ofisi ya Posta katika Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukuaji wa teknolojia ya TEHAMA na mabadiliko yanayoendelea ndani ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) katika utoaji wa huduma kwa njia za kielekitroniki kupitia mawakala, Shirika halijapanga kujenga Ofisi ya kutolea huduma bali litatumia mawakala katika kutoa na kufikisha huduma zake kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania limepanga kutumia Kituo cha TEHAMA kilichopo Micheweni kinachomilikiwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kutoa huduma za Posta kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni kwa kutumia wakala. Shirika tayari limewasilisha maombi ya kupatiwa nafasi katika Kituo hicho na kukubaliwa. Shirika linakamilisha taratibu ili huduma za posta zianze kutolewa kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 kukamilika.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kufunga mtandao wa Wi-Fi maeneo yote nchini kufuatia jamii kuhamasika na matumizi ya teknolojia?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kufunga mtandao wa Wi-Fi maeneo yote ya umma nchini kufuatia jamii kuhamasika na matumizi ya teknolojia katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa utekelezaji wa kufunga mtandao wa Wi-Fi umefanyika katika vituo sita ambavyo vinatoa huduma ya internet ya wazi (Internet hotspot) katika maeneo mbalimbali. Maeneo hayo ni Stendi ya Nanenane, Dodoma; Buhongwa, Mwanza; Kiembesamaki, Unguja; Chuo Kikuu cha Dodoma, Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu (CIVE) na Soko la Tabora, na Chuo cha Ustawi wa Jamii Lungemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji huo utaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutegemea upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -
Je, ni upi mkakati wa kurahisisha matumizi ya Kibenki kwa njia ya Simu kwa kutumia bando za simu badala ya salio la simu la kawaida?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kurahisisha matumizi ya Kibenki kwa njia ya Simu kwa kutumia Bando za Simu badala ya salio la Simu la kawaida, utaratibu umewekwa kwamba unapokuwa na kifurushi cha data unaweza kutumia huduma za kibenki zinazotumia programu tumizi kama SIM Banking App na nyinginezo ili kuweza kupata huduma za kibenki.
Mheshimiwa Spika, pale ambapo mtumiaji anatumia namba fupi fupi (USSD) ambazo ni huduma za ziada, mtumiaji anaweza kulipishwa ama kutolipishwa gharama za ziada; suala hili linategemea makubaliano kati ya benki na watoa huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza wigo wa matumizi ya fedha, Msimamizi wa huduma za kifedha anaweza kuwaelekeza watoa huduma za kifedha kuingia mikataba na watoa huduma za mawasiliano, badala ya kuwalipisha wanaotumia namba fupifupi kwenye huduma za kifedha.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Minara ya simu katika Kata za Kikolo, Mbangamao, Kitanda na Kagugu - Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma ya mawasiliano nchi nzima. Aidha, kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Kata ya Kitanda imejumuishwa katika utekelezaji wa mradi huo ambapo utekelezaji wake umeanza.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa upande wa kata zilizowasilishwa kuwa na changamoto ya mawasiliano ambazo ni Kata za Kikolo, Mbangamao na Kagugu, zitafanyiwa tathmini na kuchukua hatua stahiki, ahsante.
MHE. MAULID SALEH ALI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti utapeli unaofanywa kwa kutumia namba za simu za nje?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Saleh Ali, Mbunge wa Jimbo la Welezo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, utapeli ama kwa lugha nyingine ni udanganyifu unaofanywa kwa kutumia simu za nje hudhibitiwa kwa kushirikisha Mamlaka za Udhibiti kwenye nchi ambako namba zinazotumika zimegawiwa. Mamlaka hizo huchukua hatua stahiki kwa kadri wanavyopokea taarifa zinazohusiana na utapeli huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni Mwanachama wa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kama vile ATU, EACO, CRASA, CTO, ITU, UPU, PAPU na kadhalika. Ushirikiano uliopo kupitia Jumuiya hizi husaidia sana kwenye utatuzi wa masuala mengi yakiwemo yanayohusu utapeli unaofanyika kwenye mitandao ya simu.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza: -
Je, ni lini umeme utafungwa kwenye mnara wa halotel uliopo kata ya Ngujini Wilayani Mwanga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Jukumu la kuunganisha umeme kwenye minara ya mawasiliano ya simu nchini, ikiwemo ile iliyojengwa kwa ruzuku ya Serikali, ni jukumu la watoa Huduma, hii ni pamoja na gharama za kuunganisha umeme na kuendesha minara husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia huduma za mawasiliano nchini kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi matakwa ya leseni zinazotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO aliuliza: -
Je, ni lini Kituo cha Posta kilichopo Kengeja kitafanyiwa ukarabati na kutumika?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania linaendelea kufanya ukarabati wa majengo yake nchi nzima kwa kutumia fedha zake za ndani kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 – 2025/2026. Kutokana na mpango huu, ofisi ya Kengeja imepangwa kufanyiwa ukarabati kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. FROLENT L. KYOMBO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaongeza minara au kuboresha mawasiliano katika kata zote 20 za Wilaya ya Misenyi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI, alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frolent Laurent Kyombo Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza miradi ya mawasiliano iliyokamilika katika kata 10 za Wilaya ya Missenyi. Kufikia mwezi Machi, 2023 tayari ujenzi wa minara 13 imekamilika na inatoa huduma katika teknolojia ya 2G na 3G.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali Serikali imeshapata watoa huduma wa kufikisha huduma za mawasilioano katika Kata za Bugorora, Kasambya, Mutukula na Kakunyu ambapo tayari zimeshapata watoa huduma, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA K.n.y. MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua changamoto za mawasiliano ya simu Kata za Milepa, Zimba, Kaengesa na Lusaka?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilibaini kuwepo kwa changamoto katika Kata za Lusaka, Milepa, Kaengesa pamoja na Zimba. Hata hivyo, Kata ya Lusaka imepata mtoa huduma wa kufikisha huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata za Milepa, Zimba pamoja na Kaengesa zitafikishiwa huduma za mawasiliano kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali kupitia UCSAF itapeleka minara ya mawasiliano Wilaya ya Malinyi kwa kuwa maeneo mengi ya wilaya hiyo hayana usikivu wa mawasiliano na data?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Jimbo la Malinyi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka wa fedha 2015/2016 na 2020/2021 Kata za Biro, Sofi, Ngoheranga na eneo ilipo Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi zimenufaika na Miradi ya huduma za mawasiliano ya simu kupitia ruzuku ya Serikali. Aidha, ujenzi wa minara katika Kata ya Ngoheranga na eneo ilipo ofisi ya Mkurugenzi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia mradi wa Tanzania ya kidigitali imeainisha Kata za Igawa na Njiwa ambazo tayari zimepata mtoa huduma wa kuzifikishia huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa minara hii ikikamilika itatoa huduma za mawasiliano katika teknolojia ya 3G na 4G.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je, kwa namna gani Serikali inatekeleza Kanuni ya Kimtandao ya Network Neutrality katika utoaji na upatikanaji wa huduma za jamii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya Network Neutrality ni hali ya kuweka usawa katika huduma zote zinazopatikana kwenye mtandao wa intaneti bila kuathiri kasi, gharama wala upendeleo wa tovuti fulani au maudhui ya aina fulani mtandaoni. Serikali inasimamia Sekta ya Mawasiliano kwa kuzingatia kikamilifu Kanuni ya Kimtandao ya Network Neutrality ambapo mtoa huduma yeyote wa mtandao wa intaneti anaruhusiwa kutoa huduma ya mtandao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa. Aidha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeweka utaratibu wa kuwezesha watoa huduma kutoza gharama za data bila kujali ni ya matumizi ya mitandao gani ya kijamii, tovuti au programu tumizi mbalimbali.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -
Je, lini Kata za Miyombweni, Malilo, Songwe na Luhanga zitawekwa anuani za makazi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Februari, 2022 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi ufanyike kwa njia ya operesheni kwa usimamizi wa Wakuu wa Mikoa na kwamba utekelezaji wake ukamilike mwezi Mei, 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ulifanyika kwa tija na ufanisi mkubwa ambapo hadi Mei, 2022 Halmashauri, Kata, Vijiji, Mitaa, Shehia zote nchini zilikuwa zimefikiwa. Aidha, utekelezaji ulifanyika kwa kuzingatia miongozo iliyopo ikiwa ni pamoja na kutotoa anwani za makazi maeneo ambayo ni hatarishi yasiyoruhusiwa kwa makazi mfano, mabondeni, kwenye vyanzo vya maji, maeneo oevu, maeneo ya hifadhi, maeneo ya wazi na maeneo ya hifadhi ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya Kata za Miyombweni, Malilo Songwe na Luhanga zipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, lini Serikali itahakikisha tatizo la kutokuwepo mawasiliano ya simu ya uhakika katika maeneo mengi ya Jimbo la Sumve linatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasasali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Jimbo la Sumve kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imefikisha huduma za mawasiliano katika Kata za Bugando, Lyoma, Mwandu, Ngulla na Sumve.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itafanya tathmini katika Jimbo la Sumve ili kubaini maeneo ambayo bado yana changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano ili yatafutiwe fedha kwa ajili ya kutatua changamoto hizo.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza:-
Je, ni minara mingapi ya mawasiliano ya simu itasimikwa Uyui kati ya minara 780 itakayojengwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP), Serikali imeainisha kata tisa zilizopo Uyuyi ambazo zimepatiwa watoa huduma (Airtel, Halotel na TTCL) hivyo kufanya idadi ya minara tisa itakayojengwa na tunatarajia vijiji 26 vilivyopo katika kata hizo vitanufaika na huduma baada ya kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wilaya ya Uyui ni miongoni mwa Wilaya zinazonufaika na Miradi ya Mawasiliano kupitia UCSAF, ambapo idadi ya minara 28 imejengwa na imekamilika katika kata 25 zilizopo wilayani humo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa upande wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Kata za Igulungu, Kalola, Ufuluma, Nsimbo na Upuge zimefanyiwa tathmini na sasa Serikali kupitia UCSAF inamtafuta mtoa huduma atakayefikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo hayo.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza ujenzi wa minara kumi katika kata 10 ambazo ni kati ya kata 18 za Wilaya ya Urambo, ambapo minara tisa imekamilika katika Kata za Imalamakoye, Kasisi, Songambele, Itundu, Ukondamoyo, Nsenda, Uyogo, Vumilia, Ugalla pamoja na Uyumbu.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika baadhi ya Vijiji vya Kata ya Kasisi na Kiloleni na tayari imekwisha wapata watoa huduma wa kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata hizo. Kwa upande wa kata za Kapilula, Kiyungi, Mchikichini na Muungano, Serikali kupitia UCSAF itafanya tathmini ili kupata hali halisi ya changamoto ya mawasiliano katika maeneo hayo.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:-
Je, lini huduma ya Mawasiliano ya Simu itapelekwa Kata za Bwawani, Oldonyowas, Laroi, Mwandet, Oljoro na Oldonyosambu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Saputu, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini ili kubaini changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata za Bwawani, Oldonyowas, Laroi, Mwandet, Oljoro na Oldonyosambu zilizopo Jimbo la Arumeru Magharibi, tathmini hii itasaidia kufahamu ukubwa wa tatizo na mahitaji halisi ili hatimaye yaweze kuingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha na kutangazwa katika zabuni zijazo, ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y. MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu yenye usikivu katika Kata za Litehu, Ngonja na Mkwiti Wilayani Tandahimba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmadi Katani, Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, vijiji vilivyopo katika Kata za Mkwiti, Litehu na Ngonja vitafanyiwa tathmini kujua mahitaji halisi ya huduma ya mawasiliano na hatimaye kuingizwa katika orodha ya miradi ya Serikali itakayotekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -
Je, kwa kiasi gani Mkongo wa Taifa umesaidia kuboresha na kupunguza gharama za mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano nchi nzima ambao unafanyika kwa awamu mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, ni kweli uwepo wa muundombinu huu umeboresha huduma za mawasiliano na kusaidia kupunguza gharama za mawasiliano kwa kupunguza gharama za uwekezaji kwa watoa huduma za mawasiliano ambao wangepaswa kujenga muundombinu kama huu kuboresha miundombinu na huduma zao. Hii imesaidia kupunguza gharama za mawasiliano (cost of backhaul transport bandwidth) kwa asilimia 99 na kufanya gharama za maunganisho kwa watoa huduma kupungua kutoka shilingi 157 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi mbili mwaka 2022.
Mheshimiwa Spika, kupungua kwa gharama hizi kumesaidia kushuka kwa gharama za huduma kwa mtumiaji wa mwisho kutoka shilingi 147 kwa dakika mwaka 2009 hadi shilingi 30 kwa dakika mwaka 2022, sawa na asilimia 79.6; hii ni pasipo kutumia vifurushi.
Mheshimiwa Spika, matokeo makuu ya kushuka kwa gharama hizi kupitia miundombinu wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni kuongezeka kwa matumizi ya huduma za mawasiliano kwa wananchi na Serikali kwa ujumla. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -
Je, ni lini minara ya simu itajengwa maeneo ya Endahagichang, Tumati Juu, Qalodaginwe, Aidurdagawa, Qamtananat na Migwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Endahagichang imeingizwa katika mpango wa kufikisha huduma ya mawasiliano kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali, ambapo vijiji vitakavyonufaika ni Endadubu, Miqaw na Endahagichan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafanya tathmini katika maeneo mapya yaliyowasilishwa na Mheshimiwa Mbunge ambayo ni Tumati Juu, Qalodaginwe, Aidurdagawa, Qamtananat na Miqaw ili kubaini changamoto za huduma za mawasiliano zilizopo.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilifanya tathmini na kubaini changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na imekwisha wapata watoa huduma watakaofikisha huduma za mawasiliano katika Kata za Alailelai, Alaitolei, Engaresero, Mundarara, Ngoile, Olbalbal na Ololosokwan. Aidha, Serikali itayaingiza maeneo mengine yaliyobaki yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya simu katika Kata za Masisiwe, Udwekwa na Nyanzwa Wilayani Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilibaini changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata za Udekwa, Nyanzwa na Masisiwe ambapo tayari imekwishawapata watoa huduma wa kufikisha huduma za mawasiliano katika kata za Masisiwe na Nyanzwa wakati Kata ya Udekwa itaingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga minara ya simu maeneo yasiyo na mawasiliano hususan Kata za Ipwani, Miyombweni na Igava?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilibaini changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali yakiwemo Ipwani, Miyombweni na Igava ambapo Serikali imempata mtoa huduma wa kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata ya Ipwani kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigitali. Aidha, Kata za Miyombweni na Igava zitaingizwa katika miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza:-
Je, ni lini Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Pamoja na Malabo Convention vitahuishwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha utungwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act, 2022) iliyosainiwa Novemba, 2022 na kutangazwa katika gazeti la Serikali tarehe 2 Desemba, 2022. Sheria hiyo imeanza kutumika rasmi tarehe 1 Mei, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuweka mazingira wezeshi zaidi ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusiana na TEHAMA nchini ikiwemo kufanikisha kufikia azma ya uchumi wa kidijitali, Serikali kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) inaendelea na zoezi la mapitio ya Sera, Sheria, na Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa inayohusu TEHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zinazofanyiwa mapitio kwa ajili ya kuhuishwa ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015. Vilevile mikataba ambayo utaratibu umeanza kwa ajili ya kuridhiwa ni pamoja na Mkataba wa Malabo.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza:-
Je, ni lini Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa utapelekwa katika Wilaya 14 ikiwemo za Mjini Magharibi na Kusini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum Zanzibar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Miundombinu ya Mawasiliano Zanzibar imefikisha huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar. Mjini Magharibi inapata huduma kupitia vituo vilivyopo maeneo ya Jamhuri Garden, Fumba na Ofisi za Miundombinu ya Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) na Kusini Unguja inapata huduma kupitia kituo kilichopo Paje.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa jumla ya Wilaya 43 nchini zimefikiwa na Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa. Kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya Wilaya mpya 23 zitafikiwa na hivyo kuwa na jumla ya Wilaya 66 nchini zenye huduma ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuwa Wilaya zote nchini zitafikiwa na huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ifikapo mwaka 2025. Mwaka wa fedha 2022/2023 Wilaya zingine mpya 15 zitafikiwa na hivyo kuwa na jumla ya Wilaya 81. Wilaya zinazobaki zitafikishiwa huduma za Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa kwa kipindi kinachobaki kufikia 2025 kama ilivyopangwa. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu katika baadhi ya Kata Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imepanga kufikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Busangwa, Itilima, Masanga, Mwakiponya, Mwamalasa, Shagihilu na Talaga ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 ili kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu katika kata hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kata hizo zimejumuishwa katika zabuni inayotarajiwa kutangazwa kabla ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 kukamilika kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -
Je, lini Tanzania itajiunga na Mkataba wa Budapest ili kujiimarisha na mapambano dhidi ya makosa ya kimtandao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkataba wa Budapest ni Mkataba ulioandaliwa mwaka 2001 na Baraza la Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Makosa ya Mtandao. Mkataba huu ulianza kufanya kazi Julai Mosi mwaka 2004 na hadi sasa ni nchi 66 kutoka maeneo tofauti duniani ambazo zimejiunga na Mkataba huo, ambapo kati ya nchi hizo nchi 12 ni kutoka Bara la Afrika. Tanzania si miongoni mwa nchi ambazo zimejiunga na Mkataba huo. Aidha, katika hatua ya kutunga Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kwa sehemu kubwa maudhui ya Mkataba wa Budapest yametumika, kwa kuwa yanaakisi kwa mapana na usahihi mazingira ya kisheria dhidi ya uhalifu wa kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kuna jitihada za kuandaliwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya makosa ya mtandao ambao unahusisha nchi zote duniani na una mawanda mapana kuliko Mkataba wa Budapest. Hivyo, baada ya kufanya tathmini tumebaini kuwa hakuna haja ya Tanzania kujiunga na Mkataba wa Budapest na badala yake tutajiunga na Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Makosa ya Mtandao utakaokuwa tayari kuanzia mwaka 2025.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Mnara wa TBC – Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kujenga mnara wa redio Wilayani Kiteto katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2024, ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaimarisha Mawasiliano ikiwemo Minara ya Simu na usikivu wa Radio ya Taifa (TBC) – Kondoa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wakishirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) imekamilisha ujenzi wa majengo ya mitambo ya redio pamoja na miundombinu ukiwemo mnara wa redio wilayani Kondoa ambapo kwa sasa TBC wanasubiria vifaa ambavyo vipo katika hatua ya manunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini katika jimbo la Kondoa Mjini na kuona maeneo yaliyobaki yenye changamoto za mawasiliano na kuviingiza vijiji husika katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya simu katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imepata mtoa huduma wa kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata ya Ntobo yalipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala. Kampuni ya Simu ya Vodacom ndiyo ilishinda zabuni ya kujenga mnara huo kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Vodacom inaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji wa ujenzi wa mnara huo.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -
Je, lini Tanzania itajiunga na Mkataba wa Budapest ili kujiimarisha na mapambano dhidi ya makosa ya kimtandao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkataba wa Budapest ni Mkataba ulioandaliwa mwaka 2001 na Baraza la Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Makosa ya Mtandao. Mkataba huu ulianza kufanya kazi Julai Mosi mwaka 2004 na hadi sasa ni nchi 66 kutoka maeneo tofauti duniani ambazo zimejiunga na Mkataba huo, ambapo kati ya nchi hizo nchi 12 ni kutoka Bara la Afrika. Tanzania si miongoni mwa nchi ambazo zimejiunga na Mkataba huo. Aidha, katika hatua ya kutunga Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kwa sehemu kubwa maudhui ya Mkataba wa Budapest yametumika, kwa kuwa yanaakisi kwa mapana na usahihi mazingira ya kisheria dhidi ya uhalifu wa kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kuna jitihada za kuandaliwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya makosa ya mtandao ambao unahusisha nchi zote duniani na una mawanda mapana kuliko Mkataba wa Budapest. Hivyo, baada ya kufanya tathmini tumebaini kuwa hakuna haja ya Tanzania kujiunga na Mkataba wa Budapest na badala yake tutajiunga na Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Makosa ya Mtandao utakaokuwa tayari kuanzia mwaka 2025.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuliwezesha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kujiendesha kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linatekeleza majukumu yake kikamilifu kama chombo cha utangazaji cha umma. Serikali ipo katika mkakati wa kukamilisha utungaji wa Sheria ya TBC ya mwaka 2023, itakayowezesha kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato. Aidha, TBC inazo chaneli za kimkakati kwa ajili ya kuongeza mapato ikiwemo TBC2, TBC Online, TBC FM na Radio za Jamii Dodoma na Arusha, ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Je, lini Kata za Ruvu, Msindo, Mshewa, Vudee, Mhezi, Tae na Suji - Same zitapelekewa mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeainisha Kata Sita kati ya Kata Saba za Jimbo la Same Magharibi zenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Vudee, Suji na Ruvu zitafikishiwa huduma ya mawasiliano kwa kupitia Kampuni ya Horora PLC (TiGo), wakati Kata ya Mshewa itafikishiwa huduma za mawasiliano kupitia kampuni ya simu ya Airtel. Kata ya Msindo itafikishiwa huduma za mawasiliano na kampuni ya simu ya TTCL na Kata ya Mhezi itafikishiwa huduma ya mawasiliano ya simu kupitia kampuni ya simu ya Halotel.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kata ya Tae, USCAF itaifanyia tathmini Kata hiyo ili kubaini mahitaji halisi ya huduma za mawasiliano na hatimae kuiweka katika mpango wa zabuni zijazo zitakazotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu Kata ya Masaka – Kalenga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliingiza Kata ya Masaka katika zabuni ya kufika huduma ya mawasiliano Vijijini kupitia Mradi wa Tanzania ya Kiditali, ambapo Kampuni ya Simu ya Vodacom ilishinda zabuni hiyo ya kufikisha huduma hiyo katika Kata ya Masaka yenye Vijiji vya Kaning’ombe, Saadani pamoja na Makota. Mpaka sasa Vodacom inaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji katika ujenzi wa mnara huo.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya mawasiliano ya simu Micheweni, vijiji vya Sizini, Dodeani, Michungani, Mapofu, Msuka na Makangale?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolijia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Sizini kipo katika mradi wa awamu ya sita ambapo mnara katika kijiji hicho unajengwa na mtoa huduma ambaye ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL). Mnara huo upo katika hatua mbalimbali za ujenzi, ambapo utakamilika na kuwashwa ifikapo Aprili, 2024. Aidha, Serikali imetekeleza ujenzi wa mnara katika kijiji cha Dodeani kupitia mradi wa awamu ya nne ya UCSAF ambapo mnara ulijengwa katika Shule ya Dodeani.
Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali itavifanyia tathmini vijiji vya Michungani, Mapofu, Msuka na Makangale kuangalia mahitaji halisi ili kuvifikishia huduma ya mawasiliano.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti matumizi mabaya ya Akili Mnemba, kutumia Akili Mnemba kuchangia ukuaji wa uchumi nchini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya akili mnemba yameendelea kuongezeka siku hadi siku hapa nchini katika kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya akili mnemba, Serikali imechukua jitihada za kutosha kujenga uwezo wa wataalam na kuandaa miongozo ya kisera na kisheria ambayo italinda na kuchochea matumizi sahihi na salama ya teknolojia zinazoibukia ikiwemo akili mnemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tayari Serikali imetoa ufadhiri wa masomo ya muda mrefu na muda mfupi kwa watumishi wa umma 500 kwenye maeneo ya teknolojia zinazoibukia ikiwemo eneo la matumizi ya akili mnemba. Kati ya watumishi 500, watumishi 20 tayari wameanza masomo ya kozi ya muda mrefu na nafasi 480 zilizobaki tayari Serikali imetangaza nafasi hizo na mchakato wa kupokea maombi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeanza taratibu za ujenzi wa chuo mahiri cha TEHAMA kitakachojengwa Nala Dodoma kwa lengo la kuzalisha wataalam watakokidhi mahitaji yaliyopo kwa sasa ikiwemo hitaji la akili mnemba. Ujenzi wa chuo hiki unaenda sambamba na ujenzi wa vituo vya ubunifu vinane kwenye maeneo ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mbeya, Arusha, Lindi pamoja na Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha Wizara imeboresha sera ya TEHAMA ya mwaka 2016 kwa kuandaa rasmu mpya ya sera ya mwaka 2024 ambayo itajumuisha maeneo ya akili mnemba. Sambamba na hilo Wizara imekamilisha mkakati wa miaka 10 ya uchumi wa kidigiti unaoainisha maeneo muhimu ya matumizi ya akili mnemba katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidigitali. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafunga mitambo ili wananchi wa Tarafa ya Kilolo wapate matangazo ya Redio ya Taifa (TBC)?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Kilolo ni miongoni mwa maeneo yaliyo katika miradi ya maendeleo yaliyopangwa kutekelezwa kwa mwaka 2023/2024 ambayo utekelezaji wake umeishaanza kwa hatua za utafiti wa kitaalam, kutangazwa na kufanyiwa tathmini kwa zabuni za ujenzi wa vituo na ununuzi wa mitambo ya vituo 14 ikiwemo Kilolo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utatekelezwa katika Eneo la Ipugulu, Kijiji cha Lulanzi Kata ya Mtitu katika Tarafa ya Kilolo na umepangwa kukamilika ifikapo Juni, 2024.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, ipi kauli ya Serikali juu ya kutokamilika kwa Miradi ya Maji katika Jimbo la Kibamba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa miradi mitatu ya usambazaji wa maji kutokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi Bagamoyo (2B-2F), Mshikamano na Kitopeni ambapo miradi hiyo inanufaisha wakazi wapatao 210,876 wa Jimbo la Kibamba.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji Kusini mwa Dar es Salaam (Bangulo) ambapo utekelezaji wake umefikia 25% na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024. Mradi huo ukikamilika utanufaisha wakazi wapatao 271,863 wa Jimbo la Kibamba.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kukamilisha utekelezaji wa miradi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Jimbo la Kibamba.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Mradi wa Maji ya Mserereko katika Milima ya Nongwe kwa wananchi wa Gairo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi ya maji miwili ya Gairo na Njungwa kwa kutumia vyanzo vya Mserereko vinavyopatikana kwenye Safu za Milima ya Nongwe na Mamiwa Wilayani Gairo. Kazi zinazotekelezwa kupitia miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa ukarabati wa madakio matano (intakes), ujenzi wa matanki matano yenye jumla ya ujazo wa lita 2,300,000, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 90 na ujenzi wa vituo 58 vya kuchotea maji.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi hiyo umefikia wastani wa asilimia nane na inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024 na kunufaisha wananchi wapatao 87,134 waishio kwenye Kata nane za Rubeho, Msingisi, Gairo, Ukwamani, Magoweko, Chakwale, Kibedya pamoja na Mandege.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika kuendelea kuboresha hali ya huduma ya maji Wilayani Gairo, Serikali ina mpango wa kujenga miradi mitatu ya Nongwe, Lukinga na mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji Gairo Mjini kwa kutumia chanzo cha mto Chagongwe kinachopatikana kwenye Milima ya Nongwe katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji katika Kijiji cha Chemchem – Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Chemchem unaohusisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 135,000 kwenye mnara wa meta sita, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 16.5, ujenzi wa vituo 14 vya kuchotea maji, ujenzi wa ofisi ya CBWSO, ujenzi wa nyumba ya kuendeshea mitambo (pump house), kufunga mfumo wa umeme jua (solar system) pamoja na ujenzi wa mbauti ya kunyweshea mifugo (cattle trough).
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 85% na umeanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo; Shule ya Msingi Chemchem, Shule ya Sekondari Chemchem na Zahanati ya Chemchem. Utekelezaji wa mradi huo unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2024 na kunufaisha wananchi wapatao 6,010 wa Kijiji cha Chemchem, ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza: -
Je, lini kibali cha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kyerwa, Nyaruzumbura, Nyakatuntu, Kamuli kitatolewa ili ujenzi uanze?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha za utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji utakaonufaisha vijiji 57 wilayani Kyerwa ikiwemo Kyerwa Mjini, Nyaruzumbura, Nyakatuntu hadi Kamuli kwa kutumia chanzo cha Mto Kagera. Aidha, katika mpango wa muda mfupi, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji itakayonufaisha vijiji 27 vya Nkwenda, Rwabwere, Karongo, Nyamiaga, Nyakatera, Kagu, Masheshe, Nyamweza, Kaikoti, Iteera, Muleba, Chanya, Kimuli, Rwanyango, Chakalisa, Kikukuru, Omukitembe, Karambi, Rwele, Rubilizi, Mukunyu, Kitwechenkura, Rukuraijo, Makazi, Kibimba, Nyakatete na Mabira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali katika mwaka wa fedha 2024/25 itachimba visima katika Vijiji vya Omuchwenkano, Businde, Nyaruzumbura, Bugara, Rukiri, Nyakatuntu, Kyerere, Kamuli, Ibamba na Rukuraijo ili kuongeza vyanzo vya maji. Kukamilika kwa miradi hiyo kutaboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji wilayani Kyerwa kufikia wastani wa 80.3% mwezi Juni, 2025. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 utaanza kutekelezwa katika Wilaya ya Rorya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Rorya - Tarime kwa kutumia chanzo cha maji ya Ziwa Victoria. Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa dakio (intake) yenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 29 kwa siku, ujenzi wa miundombinu ya kutibu maji (water treatment plant) yenye uwezo wa kutibu maji lita milioni 28 kwa siku, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 110, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (booster station) pamoja na ujenzi wa matanki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 12.5% na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2025 na utanufaisha wakazi wapatao 460,885 waishio kwenye Wilaya za Rorya, Tarime pamoja na Mji wa Sirari.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -
Je, ni lini wananchi wa Kijiji cha Mtila Kata ya Matola Njombe Mjini watapelekewa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma ya maji katika Kijiji cha Mtila Kata ya Matola Njombe Mjini, Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 imetenga fedha kwa ajili ya kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi pamoja na kuchimba kisima kirefu ili kupata chanzo cha maji. Aidha, baada ya kupatikana kwa chanzo hicho cha maji Serikali itafanya usanifu wa miundombinu ya usambazaji maji kwa ajili ya kunufaisha wananchi wa Kijiji cha Mtila, ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kuanzisha Mamlaka ya Maji Mkoa wa Pwani ili kuondoa changamoto ya maji maeneo mengi ya mkoa huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya huduma majisafi na salama katika Mkoa wa Pwani ni wastani wa 79.8% kwa vijijini na 90% kwa mijini ambapo huduma hiyo inatolewa kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa upande wa vijijini na kwa maeneo ya mijini huduma hiyo inatolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaridhishwa na taasisi zinazotoa huduma ya majisafi na salama katika Mkoa wa Pwani ambapo maeneo yote ya mijini yanapata huduma za maji safi kwa viwango mbalimbali. Hata hivyo, Serikali ipo tayari kufanya mabadiliko yoyote yanayolenga kuboresha eneo la utoaji huduma ya maji katika Mkoa wa Pwani pindi itakapoonekana inafaa. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza:-
Je, lini Serikali italipa fidia kwa Wananchi waliopitiwa na bomba la maji la Mto Ruvuma – Mtwara Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma hadi Manispaa ya Mtwara – Mikindani na baadhi ya maeneo ya Lindi na Mtwara, vikiwemo vijiji vilivyopo pembezoni mwa bomba kuu. Kwa sasa Serikali inaendelea na mapitio ya usanifu wa mradi huo ili kujiridhisha na mawanda yake. Kazi hiyo ikikamilika, maeneo yote yanayopitiwa na miundombinu ya maji yataainishwa na kisha daftari la tathmini litaandaliwa kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi wote ambao maeneo yao yatapitiwa na miundombinu hiyo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha Miradi ya Maji ya Mpasa na King’ombe, Wilayani Nkansi, Mkoa wa Rukwa na inatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi. Kwa sasa skimu hizo zinasimamiwa na chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) cha Chipiruka kwa ajili ya uendeshaji na matengenezo. Skimu hizo zinahudumia jumla ya watu 11,267 waishio kwenye vijiji vitatu vya King’ombe, Mpasa pamoja na Mlambo kupitia vituo 42 vya kuchotea maji, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-
Je, lini Serikali itatenga fedha kumalizia usambazaji wa maji safi na salama Kata ya King’ori, Wilayani Meru hususani katika Vijiji vya Meru kwa Philipo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Maleu, eneo la kwa Philipo, Kata ya King’ori, Wilayani Meru kinapata huduma ya maji safi na salama kupitia Skimu ya Maji ya Makilenga ambayo kwa sasa haitoshelezi mahitaji kutokana na kuhudumia vijiji 22 vyenye mahitaji ya jumla ya lita 4,931,000 za maji kwa siku wakati uzalishaji ukiwa lita 2,465,500 kwa siku. Katika kuboresha huduma ya maji katika kijiji hicho, Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 itashirikiana na Shirika la Korea International Cooperation Agency (KOICA) kutekeleza mradi wa usambazaji maji safi na salama katika vijiji sita kikiwemo Kijiji cha Maleu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zitakazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa vyanzo vya maji na uboreshaji wa mitambo ya maji. Muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miezi 18 ambapo kukamilika kwake kutanufaisha wananchi wapatao 16,584 waishio katika vijiji sita vya Maleu, Oldonyongiro, Shambarai Burka, Msitu wa Mbogo, Sakina Chini na Sakina Juu.
MHE. HAMISI S. TALETALE aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka maji Kata ya Tununguo katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Tununguo ina jumla ya wakazi 11,924 katika vijiji vinne vya Mlilingwa, Dete, Kisanga Stendi na Tununguo. Kati ya vijiji hivyo, vijiji vitatu vya Dete, Kisanga Stendi na Tununguo vinapata huduma ya maji kupitia visima sita vya pampu za mkono. Aidha, ukarabati wa Bwawa la Mlilingwa unaendelea kwa gharama ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Kijiji cha Mlilingwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mrefu, Serikali imeanza kufanya usanifu wa mradi mkubwa wa kutoa maji Mto Mvuha kwenda Tarafa za Ngerengere na Mvuha. Usanifu huo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024 na utekelezaji wake kuanza katika mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo utanufaisha vijiji 35 vya Tarafa hizo vikiwemo vijiji vinne vya Kata ya Tununguo.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -
Je, lini Serikali itamaliza tatizo la maji Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisau, Mbunge wa Jimbo ka Kiteto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kiteto ni wastani wa 64%. Katika kuboresha huduma ya maji Wilayani Kiteto na kufikia malengo ya 85%. Serikali imekamilisha utekelezaji wa miradi 11 ya Kibaya, Bwagamoyo, Majengo Mapya-Kaloleni, Sunya, Ndirgish, Mdunku, Wezamtima-Bwawani, Matui, Engongungare, Magungu-Nhati na Ostet. Vilevile utekelezaji wa miradi tisa unaendelea katika vijijini 14 vya Nchinila – Engusero, Njiapanda, Chang’ombe-Njoro, Orkine, Ilera-Esekii, Laiseri – Dongo, Kimana, Ngipa, Nasetani, Lembapuri, Esuguta, Kiperesa, Ndotoi na Enguserosidani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2025 na kunufaisha wananchi wapatao 69,825 waishio kwenye vijiji hivyo na kufanya jumla ya vijiji 60 kufikiwa na huduma ya majina salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji ili kuwezesha vijiji vilivyobaki kufikiwa na huduma ya maji safi na salama.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Je, lini Mkandarasi anayejenga Mradi wa Maji Kata ya Mabaranga - Kilindi atakamilisha kazi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji Mabalanga uliopo Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga. Mradi huo unahusisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 135,000, ujenzi wa tanki la kukusanyia maji (sump well) lenye ujazo wa lita 25,000, ujenzi wa vituo 12 vya kuchotea maji, ulazaji wa mabomba yenye umbali wa kilometa 6.62, ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house), ujenzi wa ofisi CBWSO, ukarabati wa machujio ya maji, ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua pamoja na ufungaji wa pampu.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024 na kunufaisha wananchi wapatao 6,021 waishio katika Kijiji cha Mabalanga. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza changamoto ya maji Wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi ina jumla ya vijiji 90, ambapo kati ya hivyo vijiji 66 vinapata huduma ya majisafi. Katika kuboresha huduma ya maji wilayani humo Serikali imekamilisha utekelezaji wa miradi minne inayohudumia Vijiji vya Lyazumbi, Kacheche, Masolo pamoja na Itindi. Aidha, utekelezaji wa miradi mitatu itakayohudumia Vijiji vya Korongwe, Isale na Matala inaendelea, ambapo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024 na kunufaisha wananchi wapatao 52,192 wa vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, imepanga kutekeleza miradi ya maji itakayonufaisha Vijiji vya Ninde, Kipili, Kalila, Mkombe, Mpenge, Mandakerenge, Bumanda, Isaba Kazovu, Utinta, Uhuru, Kasanga, Kisambala, Msamba pamoja na Izinga. Pia, mwezi Juni, 2024 washirika wa maendeleo USAID watatekeleza miradi itakayonufaisha vijiji saba vya Wampembe, Kizumbi, Katenge, Lyapinda, Ng’anga, Mwinza na Kasapa; wakati vijiji vinne vya Mbwendi, Kalundi, Lyele na Ng’undwe vitachimbiwa visima na kujengewa miundombinu kupitia programu ya visima 900. Kukamilika kwa miradi hiyo, kutawezesha kuboresha huduma ya maji Wilayani Nkasi kutoka wastani wa 50.3% ya sasa na kufikia wastani wa 87.1% ifikapo Juni, 2025.
MHE. DKT. THEA M. NTARA K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -
Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupeleka gari RUWASA Wilaya ya Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inaendelea kutatua changamoto za uhaba wa vitendea kazi ikiwemo magari katika mikoa 25 na Wilaya 128 Tanzania Bara zinazohudumiwa na Taasisi hiyo. Katika kutekeleza azma hiyo, RUWASA katika mwaka wa fedha 2023/2024 imeshalipia ununuzi wa magari mapya 35 na yanatarajiwa kupokelewa hivi karibuni kwa ajili ya kusambazwa kwenye mikoa na wilaya zenye uhitaji nchini ikiwemo Wilaya ya Nyasa.
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -
Je, lini chanzo cha uhakika cha maji ya Ziwa Tanganyika kitatumika katika Vijiji vya Mwambao wa Ziwa na maeneo mengine Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya Serikali ni kutumia vyanzo vya maji vya uhakika katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini ikiwemo mito na maziwa. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali tayari imeanza na inaendelea kutumia vyanzo hivyo kwa ajili ya kusambaza maji, huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Rukwa, chanzo cha Ziwa Tanganyika kimenufaisha wananchi wapatao 47,349 waishio kwenye mwambao wa ziwa hilo kupitia utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Kipwa, Kapele Wilayani Kalambo, Kabwe, Kabwe camp, Udachi, Mkinga, Majengo, Ntanganyika, Kalungu, Mtakuja, Kamwanda, Kichangani na Itete Wilaya ya Nkasi. Vilevile Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kuajiri mtaalam mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina (feasibility study and detailed design) kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji utakaotumia chanzo cha Ziwa Tanganyika kwa lengo la kuhudumia mikoa ya Rukwa na Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itatekeleza miradi ya maji kwa kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika itakayonufaisha vijiji 16 vya Kazovu, Kisambala, Mandakerenge, Msamba, Uhuru, Utinta, Kalila, Isaba, Izinga, Kala, Kasanga, Muzi, Kisala, Samazi, Pamoja na Kipanga na Katili.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha utekelezaji wa Mradi wa Maji Makonde?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Makonde kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28. Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 26 kwa siku, ujenzi wa matanki manne yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 13 na ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 81.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 31% ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2025 na kunufaisha wananchi waishio kwenye Wilaya za Newala, Tandahimba pamoja na Mji wa Nyanyamba. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka mita za maji kama za LUKU ili kuwawezesha wananchi kulipa bili za maji kulingana na matumizi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeendelea na ufungaji wa dira za malipo ya kabla (pre paid water meters) ambapo hadi kufikia mwezi Juni, 2024 jumla ya dira 14,914 zilikuwa zimefungwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini pamoja na RUWASA ambapo kati ya hizo, dira 11,861 zilifungwa kwa Mamlaka ya Maji Safi na Miji Mikuu ya Mikoa, dira 325 zilifungwa na Mamlaka za Miradi ya Kitaifa, dira 692 zilifungwa na Mamlaka ya Maji ya Miji Mikuu ya Wilaya na dira 50 Mamlaka za Miji Midogo. Vilevile kwa upande wa vijjijni jumla ya dira 1,986 zilifungwa kwa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imekamilisha uandaaji wa andiko dhana (concept note) pamoja na mpango mkakati sambamba na kutengeneza mfumo wa ankara wa kuendesha dira za malipo ya kabla ifikapo Julai, 2025. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia, kusisitiza na kuziwezesha Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira pamoja na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha zinaongeza kasi ya ufungaji wa dira za malipo ya kabla ili kuwawezesha wananchi kulipa ankara za maji kulingana na matumizi na kuboresha usimamizi wa mauzo na makusanyo.
MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza:-
Je, upi mkakati wa Serikali kuhakikisha miradi ya maji katika Jimbo la Mbarali inakamilika kwa wakati ili kuondoa changamoto ya maji iliyopo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama Wilayani Mbarali umeongezeka kutoka wastani wa 54% mwaka 2023 na kufikia 58.4% mwaka 2024. Hali hiyo imechagizwa kutokana na kukamilika kwa utekelezaji wa miradi ya maji Kibaoni, Matebete, Luduga - Mawindi, Mkunywa Awamu ya Kwanza, Miyombweni na Utengule - Usangu. Kukamilika kwa miradi hiyo kumesaidia wananchi wapatao 70,582 waishio kwenye maeneo hayo kupata huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji Chimala, Ruiwa na Igurusi Awamu ya Kwanza ambapo miradi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024 na kunufaisha wananchi 79,653 wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaanza utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Ilongo Group Awamu ya Kwanza, Mbuyuni Awamu ya Kwanza, Itamboleo Awamu ya Pili, Iwalanje, Warumba, Vikaye, Isunura - Ikanutwa na Igunda - Muungano wilayani Mbarali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati mahususi wa Serikali ni kuhakikisha inapeleka fedha zinazohitajika kwa wakati sambamba na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini ikiwemo Wilaya ya Mbarali ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi kukamilisha miradi ya maji mikubwa na midogo nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kupitia bajeti ya 2024/2025 jumla ya miradi 1,095 inatarajiwa kutekelezwa vijijini na miradi 247 mijini. Miradi hiyo inatekelezwa ili kufikia malengo ya Serikali ya kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha miradi ya maji yote mikubwa na midogo iliyopangwa kutekelezwa na inayoendelea na utekelezaji nchini inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi. Mkakati mahsusi wa Serikali ni kuhakikisha inapeleka fedha zinazohitajika kwenye utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati sanjari na kusimamia utekelezaji wake.
MHE. ESTHER N. MATIKO K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji uliokwama kwa muda mrefu katika Kijiji cha Mang’ola Juu Wilayani Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji Kijiji cha Mang’ola Juu Wilayani Karatu. Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa matenki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita 270,000, ulazaji wa mtandao wa mabomba umbali wa kilometa 30, ujenzi wa vituo 25 vya kuchotea maji, ujenzi wa Ofisi ya CBWSO, ujenzi wa nyumba ya kuendeshea mitambo (pump house) na ujenzi wa mbauti tatu za kunyweshea mifugo (cattle trough).
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 30% ambapo umeanza kutoa huduma kwenye baadhi ya maeneo kupitia vituo saba vilivyokamilika wakati utekelezaji ukiendelea. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024 na kunufaisha wananchi 5,616 waishio kwenye vijiji cha Mang’ola Juu, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kukamilisha mradi wa maji kutoka Ziwa Tanganyika na kusambaza katika Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum Rukwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira inaimarika katika Mkoa wa Rukwa, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa awali wa kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika ambacho ni cha uhakika. Hadi sasa, taratibu za manunuzi za kumpata mtaalam mshauri wa usanifu wa kina wa kutoa maji Ziwa Tanganyika na kuyapeleka katika Mikoa ya Rukwa, Katavi mpaka Kigoma zimeanza na zitakamilika katika mwaka 2024/2025.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza kujenga Mradi wa Maji Lutale Langi kwa kuwa usanifu umekamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa Mradi wa Maji Lutale Langi na hatua za kumwajiri Mkandarasi atakayetekeleza mradi huo zinaendelea. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Agosti, 2024 ambapo utatekelezwa kwa muda wa miezi 24.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chanzo (intake), ujenzi wa mtambo wa kutibu maji (treatment plant), ujenzi wa matanki mawili yenye jumla ya ujazo wa lita 3,000,000, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 122.5 na ujenzi vituo 90 vya kuchotea maji. Kukamilika kwa mradi huo kunatarajia kunufaisha wananchi wapatao 77,794 waishio katika Vijiji tisa vya Lutale, Langi, Kageye, Itandula, Ihushi, Sese, Matale, Shilingwa na Ihayabuyaga Wilayani Magu.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Je, lini utekelezaji wa mradi mkubwa wa Maji wa Kyerwa, Nyaruzumbura, Nyakatuntu hadi Kamali utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuanza ujenzi wa Mradi mkubwa wa Maji wa Kyerwa, Nyaruzumbura, Nyakatuntu hadi Kamali katika mwaka wa fedha wa 2025/2026. Vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni pamoja na Kyerwa, Nshunga, Milambi, Nyaruzumbura, Omukiyonza, Nyakatuntu, Rukiri, Kishanda A, Kishanda B, Kyerere, Kasoni, Kamuli, Rwabigaga na Ruhita.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuimarisha hali ya huduma ya maji Kyerwa, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa mitano ya Runyinya – Chanya, Kikukuru, Kimuli – Rwanyango – Chakalisa, Kaisho – Isingiro na Mabira. Jumla ya vijiji 30 vinatarajiwa kufikishiwa huduma ya majisafi na salama pale ambapo miradi hiyo itakapomalizika.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, lini Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana wenye thamani ya shilingi bilioni 6.6 utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana kwa mujibu wa mkataba umekamilika. Kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa bomba kuu kwa umbali wa kilometa 33.65, ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 100,000 katika Kijiji cha Lagana, Ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji katika Kijiji cha Lagana na ulazaji wa bomba la usambazaji maji umbali wa kilomita 7.86 katika Kijiji cha Lagana ikijumuisha matoleo ya maji (offtake) sita katika Vijiji vya Igaga, Isagala, Mwamashele, Busongo/Mwamanota, Bubinza na Mwamadulu. Katika Vijiji vya Mwamashele na Mwamadulu, Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana unatoa huduma kwa wananchi wapatao 3,040 wa Kijiji cha Lagana.