Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew (392 total)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mbulu Vijijini tumepata minara sita ambayo imejengwa. Mwingine umejengwa 2017, mingine inayofuata imejengwa mpaka juzi hapa lakini sasa minara hii sita haifanyi kazi.
Je, Mheshimiwa Waziri ana mpango kuwafuata au kuwaona wakandarasi ili wawashe minara hii sita ambayo sasa wananchi wanaisubiri mpaka leo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa amesema kata hizi atazipelekea mawasiliano na kujenga minara; je, kata zilizobaki lini zinakwenda kupata hiyo minara ambayo amekwishaisema?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulingana na changamoto ambayo ilikuwepo ya masuala ya ujenzi, kata hizo zilikuwa zimechelewa kukamilishiwa miradi hiyo. Hata hivyo, hivi navyoongea wataalam wetu tayari wameshaanza kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba kutumia fursa hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna hatua mbili katika ujenzi wa minara; kuna hatua ambayo inatokana na ujenzi wa mnara wenyewe ambao tunaita passive equipment na hatua ya pili ambayo sasa ni kuweka vile vifaa ambavyo tunaita kwamba ndiyo active equipment.
Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa hivi tumekutana na changamoto ya wakandarasi wetu ambao walikuwa wamepewa majukumu ya kukamilisha miradi hii kwa sababu wanatumia sana vifaa kutoka nje na mwaka jana tulikumbana na changamoto ya Corona, hivyo tukaona kwamba tuwaongezee muda ili waweze kukamilisha ujenzi wa minara hii. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, suala hili tayari tunalifanyia kazi na hizi kata ambazo amezisema tayari wataalam wetu wameshafika site kwa ajili ya kujua nini kinafanyika ndani ya muda ambao unatakiwa. Ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naomba kuuliza Wizara ya Mawasiliano swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa vijiji vitatu katika Kata ya Ziginali, Kisawasawa na Kiberege havina mawasiliano ya simu kabisa. Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi hawa huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba Serikali iko katika mpango wa kufanya tathmini katika Kata nyingine 1,392 ambazo zimebaki Tanzania Bara ili tuweze kuona namna gani tutaziingiza katika Mpango wa Utekelezaji katika Bajeti ya 2020/2021. Hivyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sambamba na hilo tutahakikisha kwamba tunawasiliana naye kwa ukaribu sana ili kujua changamoto ziko katika maeneo gani ili tuhakikishe kwamba mawasiliano katika Kata hizo yanafika kwa ukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Tatizo lililopo katika Jimbo la Mbulu Vijijini ni sawa kabisa na changamoto iliyoko katika Jimbo la Kalenga. Kata ya Kihanga, Ulanga, Ifunda katika Vijiji vya Mibikimitali na Kata ya Mgama iliyoko katika Vijiji vya Lupembewasenga, kuna changamoto ya mawasiliano.
Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo ya mawasiliano ili waweze kufanya shughuli zao za kawaida?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto tuliyonayo kwa sasa, labda nitoe maelezo kidogo. Ni kwamba kuna baadhi ya sehemu ambazo mawasiliano au minara ilipelekwa ambapo uhitaji wake inawezekana walikuwa watu 5,000 ambao walikuwa wanaweza kutumia huduma hiyo. Kwa sababu ya ongezeko la watu katika eneo husika, kwa hiyo, ile minara yetu inashindwa kuwa na uwezo wa kuhudumia watu wengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, kwa kugundua hilo, tumeagiza mobile operator wote wafanye tathmini, wafanye research za kutosha ili waongeze uwekezaji katika maeneo hayo, aidha kwa kuongeza minara au kwa kuongeza capacity katika minara ambayo tayari ipo katika maeneo husika ili kuhakikisha kwamba wananchi wote wanafikiwa na mawasiliano hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali la nyongeza ambalo lina vipengele viwili.
Mheshimiwa Spika, kwanza, katika Kata ya Uru Shimbwe kuna shida kubwa sana ya huduma ya mawasiliano ya Radio hasa kwa Redio yetu ya Tanzania na Television yetu ya Taifa. Pili, kuna shida ya huduma ya internet na imesababisha Kata ya Uru Shimbwe ishindwe kutuma taarifa kupitia kwenye zahanati yetu kwenye Shirika la Bima la Afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba huduma hizi zinaboreshwa kwenye eneo la Uru Shimbwe?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Patrick Alois Ndakidemi Mbunge wa Moshi Vijijini kwa sababu masuala haya tumekuwa tukiwasiliana na jiografia ya eneo husika tayari ameshanieleza jinsi ilivyo. Hata hivyo, kupitia mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma za mawasiliano vijijini zikiambatana na usikivu wa redio katika maeneo husika tayari Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeshaanza kufanya tathmini katika maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika eneo ambalo ameongelea kuhusu upatikanaji wa data, Serikali tayari imeshatoa maelekezo kwa watoa huduma wote, sehemu yoyote ambapo tutapeleka mradi wowote ule, lazima mradi huo ukajengwe wa kutoa huduma ya kuanzia 3G maana yake ni kwamba, ni lazima sasa Tanzania tutakuwa na miradi au minara ambayo itakuwa inatoa huduma ya internet. Nasema hivyo kwa sababu hapo kabla tulikuwa tunaangalia tu angalau kila Mtanzania aweze kupata mawasiliano, lakini kwa sasa tunalazimika kwa sababu ya mahitaji ya kuelekea kwenye digital transformation maana yake kwamba mahitaji ya internet ni makubwa zaidi ikiambata na eneo la Mheshimiwa Patrick, Moshi Vijijjini. Nashukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote una jukumu kubwa la kuboresha mawasiliano hususan kwenye sehemu za vijijini ambazo hazina mawasiliano ya simu ya kutosha, lakini juzi juzi tumeshuhudia hapa Mfuko huu ukizindua studio za kisasa za TBC wakati bado kuna sehemu hususan za vijijini hazina mawasiliano ya simu ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua ni nini hasa vipaumbele vya Mfuko wa huu wa Mawasiliano kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa ni jukumu la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano maeneo ya vijijini, lakini sio maeneo ya vijijini peke yake maeneo yote ambayo hayana mvuto wa kibiashara, kwa sababu kuna maeneo ambayo watoa huduma wengine hawawezi kwenda kuwekeza kwa sababu zao za kibiashara.
Mheshimiwa Spika, vilevile tunapoongelea kufikisha mawasiliano ni pamoja katika maeneo ambayo ni ya mipakani. Pamoja na maeneo ya mipakani, kuna maeneo ya hifadhi, kuna maeneo ambayo kwa kweli ukiangalia katika ramani vizuri ni kwamba hakuna wakazi wengi, lakini hao wakazi waliopo pale wana haki ya kupata huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, nasema hivyo, kwa sababu huduma ya mawasiliano tunaichukulia kama ni sehemu ya usalama, sehemu ya huduma ya msingi ya kila Mtanzania na kubwa zaidi ni uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu mawasiliano yanaenda kuwa moja ya njia kuu ya uchumi wa nchi yetu. Hivyo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote utaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote ambayo bado yamebaki nyuma kimawasiliano ili yaweze kufikishiwa mawasiliano. Nakushukuru sana.
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hatua zipi zinachukuliwa na Serikali kuwawezesha vijana wanaofanya biashara mtandao ili kuwezesha mapato ya Taifa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu na mikopo ili kuwezesha upatikanaji wa ajira ya ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali kazi yake ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira wezeshi kwa vijana ili waweze kufanya biashara hiyo. Sambamba na hilo kupitia biashara zozote za kimtandao Serikali imeweza kurasimisha shughuli hizo kwa kuanzisha sheria ya makosa ya kimtandao maana yake kwamba kijana ili aweze kujua mipaka ya namna gani biashara yake akaifanye.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya Mwaka 2010, hii yote inatoa guidelines za namna gani kijana anaweza kuingia katika biashara hiyo.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa sababu unapofanya biashara lazima kuna transactions zitakuwa zinafanyika, ili sasa kumlinda katika zile transactions Serikali pia ilichukua jukumu la kuanzisha Sheria ya Miamala ya Kieletroniki ambayo sasa transaction yoyote inakuwa inatambulika, anapokuwa anafanya hizi biashara.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kupitia Wizara yetu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia vijana hawa, Serikali ina mpango mzuri wa kutoa elimu ambapo vijana watakuwa wanajua namna gani na sehemu zipi wanaweza kuwa wanapata mikopo kwa ajili ya kujiongezea kipato na hatimaye tunaongeza pato la Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kwa kweli nimehakikisha mwenyewe kwamba kazi inaendelea.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kama unavyojua jiografia ya Wilaya ya Lushoto ni ya milima na mabonde ambayo husababisha kutopata huduma katika maeneo mbalimbali hasa Makanya, Mavului, Mbwei na maeneo mengine ya Mazumbai. Je, ni lini sasa Serikali itaenda kujenga minara ile ili kuondoa kadhia wanayoipata wananchi wa Wilaya ya Lushoto?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Wilaya ya Lushoto ina changamoto ya usikivu wa Radio ya Taifa yaani TBC na hili suala nilikuwa naliongelea mara kwa mara lakini mpaka leo hii hakuna majibu yoyote wala hakuna mnara wowote uliojengwa. Je, ni lini Serikali itaenda kujenga minara ya habari ndani ya Wilaya ya Lushoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hatua ambazo Serikali inazichukua kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwanza kabisa ni kujiridhisha na ukubwa wa tatizo wa eneo husika. Ukubwa huo unaweza ukategemea na tatizo lenyewe, inawezekana katika maeneo fulani mawasiliano hakuna kabisa; maeneo mengine mawasiliano ni hafifu; lakini kuna maeneo mengine ambapo unakuta kwamba mawasiliano yako hapa hayako hapa; kunakuwa na dark sport za kutosha. Sasa Serikali inapofanya tathmini ni kujiridhisha pia na ukubwa wa tatizo ili kujua teknolojia gani ambayo tunaweza kwenda kuitumia pale ili kutatua tatizo la eneo husika kulingana na tathmini iliyofanyika.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri tumekuwa na mawasiliano mazuri na amekuwa akiwapambania kweli wananchi wa Jimbo lake na sisi kama Serikali kwa sababu ndio jukumu letu na kupitia Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, ibara ya 61(f) na (g) inaeleza kabisa kwamba ni jukumu la Serikali kwenda kufikisha mawasiliano kwa wananchi wote, kwa hiyo, suala lake litaangaliwa baada ya tathmini kufanyika.
Mheshimiwa Spika, vilevile suala la usikivu ni jambo lilelile ambalo pia kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanaendelea na kufanya tathmini katika maeneo yote pamoja na maeneo ya mipakani kuhakikisha kwamba palipo na changamoto ya usikivu basi Serikali inafikisha mawasiliano katika maeneo husika.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri ambayo yanatoa matumaini kwenye maeneo yale ambayo kumewekwa ahadi za kuweka minara. Hata hivyo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Kata ya Masisiwe na Kata ya Udekwa hakuna mawasiliano kabisa na tayari watu wawili wameanguka kutoka kwenye miti wakijaribu kutafuta mtandao na kuumia na kulazwa katika Hospitali ya Ilula mmoja na ya Kilolo mmoja.
Sasa, je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi katika kata hizi, kwanza ili kutoa pole kwa watu hao, lakini pili ili kuweza kuona yeye mwenyewe na nafahamu yeye ni mtu ambaye ametembelea maeneo mengi ili aweze kujionea hali halisi na kuweka msisitizo wa kuweka minara katika maeneo hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, maeneo yenye mitandao, yenye wananchi wenye matumiani makubwa sana yakutumia vifurushi vya bei ndogo, yalikatishwa tamaa na ongezeko la bei ya vifurushi ambapo ilitarajiwa vishuke. Tunaishukuru Serikali kwamba imerudisha katika ile hali ya kawaida, lakini matumaini ya wananchi ilikuwa ni kushushwa. Sasa je, ni lini Serikali itarudia ule mpango wake wa awali wa kushusha vifurushi, ili Watanzania wakiwemo wananchi wa Kilolo ambao wanataka sana kutumia vifurushi hivi katika shughuli zao za kibiashara, waweze kufurahia bei nafuu ya vifurushi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba maswali yangu hayo mawili madogo yajibiwe.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, nimesema kwamba Serikali tayari imeshaanza kufanya tathmini katika Kata ya Irole pamoja na Masisiwe ili tuweze kuingiza katika mpango wa awamu ya tano na ya sita katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la pili, nafahamu kabisa hili ni swali ambalo Waheshimiwa Wabunge wote wangeweza kuliuliza. Naweza kusema kwamba kazi ya Serikali ya kwanza ni kuhakikisha kwamba ina-stabilize bei iliyopo na hilo ndilo ambalo tumelifanya kwa sasa. Naona kwamba kulikuwa na changamoto ambapo makampuni yaliweza kuwa na bei tofauti tofauti ambazo ziliwaumiza sana wananchi, lakini Serikali ikatoa maelekezo ya kuhakikisha kwamba bei ya hapo awali inarejea kama ambavyo Watanzania walikuwa wanakusudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafahamu kwamba, katika kurejesha hizi gharama za vifurushi, kuna changamoto yake. Kupandisha kifurushi ni mchakato ambao unahusisha ujenzi wa mifumo ambayo itaweza ku-support hicho kifurushi kipya ambacho utakiingiza sokoni. Vile vile unaposema kwamba urudishe maana yake kwamba unaaanza kufanya reverse engineering maana yake unaanza kurudisha kwenye mfumo ule ulioko zamani, kama ulikuwa umeshautoa maana yake sasa inabidi uanze kuusuka tena ili uanze kutoa bei ambazo zilikuwa zinatolewa hapo kabla.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge pia ameongelea namna gani Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba bei hizi, zinashuka zaidi ya sasa ambavyo Watanzania wangetarajia. Changamoto ya biashara ya mawasiliano, kitu ambacho tunakiangalia Serikali ni kwamba hapa tunatakiwa kuangalia tuna-balance namna gani kati ya consumer, watumiaji wa huduma, Serikali pamoja na mtoa huduma. Ni lazima tuangalie ile production cost yake, ni lazima aweze kufanya biashara katika kiwango ambacho anaweza akapata faida ili Serikali pia iendelee kupata kodi lakini kodi hizohizo ziweze kurudi kujenga barabara na zahanati na hatimaye Wabunge katika Majimbo yao wanayotoka tuweze kushuhudia kuna mabadiliko ya barabara na zahanati ambazo zitakuwa zinajengwa. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza nafasi ya swali la nyongeza. Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unalenga kupeleka mawasiliano katika maeneo yote ya nchi yetu. Je, ni lini sasa Mfuko utawezesha upatikanaji wa mawasiliano katika kata na maeneo yasiyo na mawasiliano katika Mkoa wa Manyara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rahhi, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote jukumu lake la msingi ni kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano kwa Watanzania wote, hasa katika maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara. Maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara maana yake watoa huduma wengine hawatoweza kupeleka huduma hiyo kwa sababu wanaongozwa zaidi na business plan zao, business case zao na ndio maana kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, sasa Serikali inafanya tathmini katika maeneo yote ambayo yana changamoto ya mawasiliano katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie kwamba, tumeshaanza kufanya tathmini mipakani pamoja na maeneo maalum ambayo yalikuwa na changamoto kubwa sana ambapo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilalamika mara kwa mara, lakini mpaka sasa tathmini hiyo imeshakamilika. Kuanzia mwaka huu wa fedha, tayari tunatarajia kuanza kutangaza zabuni kwa ajili ya kupeleka mawasiliano katika maeneo hayo. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia swali la nyongeza. Changamoto iliyoko Jimbo la Kilolo ni sawa na changamoto iliyoko katika Hifadhi ya Same ambayo katika hifadhi hiyo barabara kuu inapita kuelekea katika Jimbo la Same Mashariki. Katikati ya Hifadhi hiyo, hakuna mawasiliano ya simu, jambo ambalo linapelekea vijana wengi kwenda kufanya mambo ya kiukorofi, kuteka baadhi ya magari na kuwapora wananchi mali zao. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba inajenga minara ya simu maeneo hayo ili endapo ukorofi kama huo vijana wataufanya, waweze kutoa mawasiliano kwa ajili ya kutetea haki yao? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Zuena Bushiri, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari ina mpango wa kuhakikisha kwamba tunapeleka mawasiliano katika maeneo ya mbuga na hifadhi ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yasiwe na changamoto tena kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema. (Makofi)
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Pamoja na kwamba kuna changamoto ya mitandao kupitia maeneo mbalimbali ya Tanzania, lakini halikadhalika kuna changamoto pia ya wizi wa kimitandao, tumekuwa tukipoteza fedha nyingi sana kupitia hii mitandao. Swali langu, je,ni lini Serikali itaweza kudhibiti wizi huu wa kimtandao unafanywa na simu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utapeli wa kimtandao viko chini ya makosa ya kimtandao na Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015. Hata hivyo watekelezaji wa sheria hii ni pamoja na vyombo vingine vya dola, ikiwemo na Jeshi la Polishi. Tunafanya juhudi za kutosha kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa umma, kwa sababu ndicho kitu ambacho ni cha msingi sana kwa Watanzania kuelewa namna gani wanaweza wakatumia simu zao za mkononi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia changamoto ambayo ilikuwepo ni pamoja na wale waliokuwa wanapewa majukumu ya kuandikisha au kuuza zile lines za simu, ambao walionekana kutokuwa na uaminifu na hatimaye kuwa wanawatapeli Watanzania badala ya kusajili line moja kwa mtu mmoja, matokeo yake anajikuta kwamba Mtanzania amesajili line tano kabla ya kuondoka katika kituo cha kusajili lines hizo. Matokeo yake hizi lines zitakapochukuliwa na watu ambao wanania ovu matokeo yake ndio zitakuja kutumika kwa ajili ya matatizo kama hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa umma lakini pia tunatumia teknolojia ambayo itaanza kudhibiti, matatizo ambayo yangesababishwa na watu ambao wamepewa majukumu ya kuuza hizi lines. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine, Serikali bado inayafanyia kazi na kufanya uchambuzi wa kutosha ili kujiridhisha kwamba tunatumia njia gani ambayo itakuwa rafiki zaidi kwa Watanzania bila kuwabugudhi katika maisha yao ya kila siku. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Changamoto ya mawasiliano iliyopo katika Jimbo la Kilolo inafanana kabisa na changamoto ya mawasiliano ambayo tunayo katika Jimbo la Handeni Mjini, hasa maeneo ya Kwa Magome, Malezi, Mlimani, Konje, Kwediyamba, Kwenjugo, Msasa, Kideleko na Mabanda. Je, ni lini, Serikali itapeleka mawasiliano katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema Serikali inabidi ifanye tathmini, ni kwa sababu tumekuwa na uelewa ambao unatofautiana kidogo. Kuna maeneo ambayo tayari unakuta kwamba kuna mnara mmoja, kuna minara miwili, lakini wananchi wetu wanatamani kuona kila kijiji kina minara mitatu au minne. Kazi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kupitia Serikali yetu, ni kuhakikisha pale ambapo hakuna kabisa mawasiliano na ndipo Serikali inapokwenda kufikisha mawasiliano kwa wananchi. Ndio maana tunasisitiza sana, Serikali tutaendelea kuhakikisha kwamba tunafika katika maeneo husika na kufanya tathmini na kujiridhisha kama tatizo ni kwamba hakuna mawasiliano ama mawasiliano yaliyopo hayana ubora unaotakiwa na kama hayana ubora unaotakiwa basi tutaelekeza TCRA kuhakikisha kwamba inawawajibisha watoa huduma katika maeneo husika kulingana na makubaliano ya utoaji wa huduma nchini. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba tufanye masahisho katika majina ya vijiji. Kata ya Mkonona ni Nambunda siyo Nambundu na siyo Waniku.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya masahisho hayo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dhumuni la uanzishaji Mfuko huu pamoja na madhumuni mengine ni kuziwezesha vile vijiji vya mpakani kuweza kupata mawasiliano ya simu hasa kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi yetu unakuwepo. Mfuko huu ulianzishwa mwaka 2007, vijiji vile bado vina matatizo makubwa ya mawasiliano. Hivi ninavyoongea hatuna mawasiliano ya simu ya Airtel wala mitandao mingine. Je, wakati mchakato huu wa kutangaza tenda unaandaliwa ni hatua gani za dharura zinachukuliwa hili kuhakikisha vijiji vile vinapata mawasiliano hasa kwa kipindi hiki kigumu ambacho usalama wetu na nchi ya Msumbiji ni mbaya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tatizo hili la mawasiliano linakwenda sambamba na usikuvu wa redio yetu ya TBC. Katika Wilaya yangu hatuna kabisa mawasiliano ya TBC. Je, ni hatua gani za dharura Mfuko huu unaweza kuisadia TBC ikasikika ndani ya Jimbo langu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuonyesha ukaribu na Wizara yetu kwa kuhakikisha kwamba anatupatia taarifa sahihi ili na sisi tuweze kuzifanyia kazi kadri inavyowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea vijiji ambavyo viko mipakani, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tayari imeshafanya utafiti na tathmini ya vijiji vyote Tanzania nzima siyo Nanyumbu peke yake ambapo maeneo yote ya mipakani tunatarajia kuutangaza tenda kwa ajili ya ujenzi na kuhakikisha kwamba tunalinda mipaka yetu yote. Mipaka ya Mtwara, Namanga, Sirari pamoja na maeneo mengine Serikali tunafahamu kabisa kwamba mawasiliano ni jukumu letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilisema katika jibu la msingi maeneo haya ni yale ambayo mara nyingine hayana mvuto wa kibishara. Ndio maana kupitia Mfuko huu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema ulianzishwa mwaka 2007 kazi yake mahsusi ni kuhakikisha tunafikisha mawasiliano katika maeneo ambayo watoa huduma wengine hawawezi kufikisha mawasiliano, hilo ni jukumu la Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Sasa hivi Ku-migrate kutoka 4G kwenda 5G service providers wengi duniani wamegundulika wanatumia multivendor badala ya kutumia system ambayo imewekwa. Multivendor inaongeza risk ya complicity ya 5G. Wanafanya hivyo kupunguza gharama zao na mteja anapoingia kwenye 5G anataka apate speed anayolipia. 5G inaweza ika-download kitabu cha kurasa 1,000 for 3 to 5 seconds. Serikali imejiandaa vipi ili risk hii ya complicity ya 5G isitokee Tanzania kama ilivyoanza kutoa kwenye nchi nyingine?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zungu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, teknolojia ya 5G na 4G vyote hivi vinaendana na uwekezaji. Tunaposema uwekezaji wa 3G, 4G na 5G kwanza lazima Serikali ijiridhishe watoa huduma waliopo wanapotumia hizi spectrum ambazo tumewapitia kwa ajili ya 3G na 4G wameweza ku-deploy vizuri kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoondoka kutoka teknolojia moja kwenda teknolojia nyingine pia inaathari ya moja kwa moja kwa watumiaji wa huduma hii. Kwa hiyo, ni lazima sasa tutengeneze mazingira ili pindi tutakoporuhusu sasa spectrum ya 5G kutumika basi watoa huduma pamoja na watumiaji wa huduma hii wawe tayari kwa ajili ya mabadiliko hayo. Nashukuru.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nitoe taarifa, katika Jimbo la Igalula kuna watoa huduma wamekwishafika baadhi ya maeneo ambayo wamekwishasainiana mikataba ikiwemo Maguliathi, Migongwa, Makoyesengi na Mbulumbulu lakini wameondoka mpaka sasa hivi hawajui nini hatima ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niulize maswali mawili ya nyongeza, Jimbo la Igalula ni miongoni mwa majimbo yenye changamoto kubwa ya mawasiliano na vijiji vingi vimekua, wananchi wana simu lakini hawana mawasiliano hasa katika Vijiji vya Songambele, Kawekapina, Nyauwanga na Simbozamalu. Sasa ni lini Serikali itaiwekea mpango wa kupelekea minara hasa vijiji hivi vilivyokuwa katika Jimbo la Igalula? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; tuna huduma ya mawasiliano katika kata alizozitoa katika jibu la msingi lakini, huduma hizi zimekuja miaka mingi iliyopita, sasa mitandao imekuwa ikisumbua na wananchi hawapati huduma. Je, ni lini Serikali itakwenda kwa watoa huduma kukagua kwa sababu idadi ya watu imekuwa kubwa, wananchi ikifika jioni haipatikani simu na huduma haipatikani. Serikali ina kauli gani kwa watoa huduma ili waweze kwenda kuipitia minara hii ili iweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Protas Daudi, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza ameongelea kuhusu watoa huduma ambao wamefika na kuanza kufanya utafiti ili waweze kuweka minara. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi ambayo anaifanya kwa niaba ya wananchi wake wa Jimbo la Igalula. Mheshimiwa Mbunge alishafika katika ofisi zetu na akatuomba tuweze kuhakikisha kwamba mawasiliano katika Jimbo lake yanapatikana na ndio maana mpaka sasa amesema kwamba, kuna watoa huduma tayari wameshafika katika eneo lake. Hii ni kwa sababu, Serikali imeenda kutekeleza ombi la Mheshimiwa Mbunge. Pia tufahamu kwamba, mikataba tunayowapatia watoa huduma ni mikataba ambayo inachukua takribani miezi tisa katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kama ambavyo amesema hatua ya kwanza watoa huduma wanayoifanya, ni kwenda kupata ile lease agreement pale ambapo mnara unatakiwa kwenda kujengwa. Hatua ya pili mtoa huduma anatakiwa kwenda kutafuta aviation permit ili aweze kuruhusiwa kujenga mnara. Hatua ya tatu ni kwenda kutafuta environmental impact assessment permit ili aweze kuruhusiwa na ndugu zetu wa mazingira. Baada ya hapo ndipo sasa apate building permit.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi process zote ni sequential process ambazo hatua moja ikitokea ndio inatoa nafasi ya hatua ya pili kufanyika. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge baada ya kukamilika kwa huu mchakato mzima wa kupata hivi vibali, basi utekelezaji wa ujenzi wa minara hii katika Jimbo lake utatekelezwa bila kuwa na changamoto yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la pili ambalo ameongelea kwamba, kuna minara ambayo ipo lakini haitoi huduma stahiki. Ni kweli kabisa tunatambua kwamba kuna minara mingine ambayo ilijengwa miaka ya nyuma ambapo population ya eneo husika ilikuwa kidogo, iliweza kuhudumia wananchi waliokuwepo kwa kipindi hicho, lakini kwa sababu wananchi wanaendelea kuongezeka maana yake sasa minara hii inaanza kuzidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo tumeshaelekeza watoa huduma wetu waende kufanya tathmini, ili wajiridhishe tatizo halisi ni lipi, kwa sababu kuna matatizo mengine ambayo yatahitaji kufanya treating tu ya antenna. Mengine itabidi kuongeza capacity, tatizo lingine itabidi kuongeza nguvu ya transmitter na tatizo lingine ambalo litatufanya tukaongeze antenna zingine ili ziweze kuhudumia wananchi wa eneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote ni lazima tathmini ifanyike kwa kina na kuna mengine ambayo yana budget implication, lakini kuna mengine ambayo ni matatizo ya kiufundi peke yake, tayari watoa huduma tumeshawaelekeza na tayari wameshaanza kufanya tathmini katika maeneo yote nchini ili kujiridhisha kwamba tatizo linalolalamikiwa linahusiana na nini hasa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Matatizo yanayowapata wananchi wa Igunga ni sawasawa kabisa na matatizo yanayowapata wananchi wa Jimbo la Buchosa hasa katika Visiwa vya Kome na Maisome. Naomba Mheshimiwa Waziri anieleze kwamba ni lini watajenga minara katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Eric Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Buchosa yameshaingizwa tayari kwenye mpango wa utekelezaji katika zabuni itakayotangazwa ya awamu ya sita ili eneo hilo sasa lipate mawasiliano kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Buchosa. Ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa mujibu wa taarifa ya TCRA asilimia 68 ya Watanzania wako kwenye maeneo yenye mtandao wa kuweza kutoa huduma ya internet, lakini ni asilimia 26 tu wenye simu janja ama vifaa vingine vyovyote vinavyoweza kuwapa access ya internet. Sasa na changamoto kubwa ni kwa sababu ya kodi na vitu vinavyofanania hivyo, sasa kwa kuzingatia kwamba Wizara inataka kuifanya Tanzania iwe katika utaratibu wa kidijitali, wana mkakati gani basi wa kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa gharama nafuu, ili Watanzania wengi waweze na kuwa na hivi vifaa na hatimaye kuweza kushiriki katika dunia ya TEHAMA na kidijitali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alivyosema tuna changamoto hiyo kwa sasa, lakini sasa Serikali tunafahamu kwamba tunaenda kwenye uchumi wa kidijitali, lakini tunapoenda kwenye mfumo wa kidijitali maana yake ni kwamba tunahitaji kuwa na internet penetration na mpaka 2025 tufikie tuwe tumeshafikia asilimia 80 kutoka asilimia 43 ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maendeleo ya dijitali yoyote yanaendana na vifaa ambavyo vita-support matumizi halisi ya teknolojia husika. Mheshimiwa Mbunge pia anafahamu kwamba, tuko kwenye mchakato wa kuangalia namna bora ambayo itasababisha vifaa hivi vitakapokuwa vinaingia nchini, basi viwe vina bei ambazo zitawavutia Watanzania wengi kununua hizi simu ili waweze kutumia teknolojia ambayo itakuwa inatumika. Ahsante. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, Kata ya Michenjele ambayo iko mpakani na Msumbiji nako kuna tatizo kubwa la usikivu wa mawasiliano ya simu hakuna hata mnara wa aina moja ambao unapatikana kule Michenjele: -
Je ni lini Serikali itapeleka huduma hii kwenye maeneo yale ya mpakani?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Katani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kata ya Michenjele ipo katika vijiji ambavyo vimeshafanyiwa tathmini kwa ajili ya Awamu ya Sita ya mipakani na border and special zone. Lakini kata hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja kwa mfano Kata ya Mihambwe tayari kuna mtoa huduma wa airtel ambao anaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa minara.
Mheshimiwa Spika, lakini pia Kata ya Mdimba kama ambavyo nilijibu katika swali langu la msingi kuna mtoa huduma tayari ambaye ni tigo ambaye anaendelea na utekelezaji lakini pia kina Kata ya Chaume ambapo tayari kuna mtoa huduma ambaye anaendelea na ujenzi wa mnara katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wilaya yetu ya Igunga hususan Jimbo la Manonga sisi ni wakulima wa pamba, mpunga, madini na mifugo kwa wingi. Katika vijiji kama hicho ambacho nimekitaja cha Ikombandulu, Mwakabuta, Ikungwi Ipina, Utuja na Shalamo ni katika maeneo yenye uzalishaji kwa wingi katika mazao niliyoyataja. Ipi mikakati ya Serikali kuhakikisha maeneo hayo yanapata mitandao ya simu kwa wakati?
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Mwisi, Simbo, Choma, Ibologelo na Indembezi wanapata mawasiliano ya simu lakini mitandao hii ipo chini sana hasa kwenye internet. Je, Serikali kupitia wadau wanaotoa huduma katika maeneo hayo ipi mikakati yao na hasa ukitambua sasa hivi Tanzania tuna- launch 5G, nini mikakati ya Serikali kuhakikisha maeneo hayo niliyoyataja tunapata angalau 4G kwa ajili ya kusaidia wataalam, watafiti na waandishi wa Habari…
SPIKA: Ahsante sana umeeleweka Mheshimiwa.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Hususan kwenye vijiji vilivyopo nchini Tanzania, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi kwamba Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tupo katika mkakati wa kufanyia tathmini Kijiji hicho sambamba na vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshavitaja ili kuhakikisha kwamba tujiridhishe ukubwa wa tatizo baada ya hapo vitaingizwa katika zabuni ya awamu zinazokuja katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, suala la pili kuhusu masuala ya internet. Tunafahamu kwamba kwa sasa hivi tunakoelekea katika uchumi wa kidigitali na tunaelewa kabisa kwamba internet coverage inahitajika ili Watanzania waweze kutumia vizuri katika shughuli zao za hapa na pale. Tumeshaelekeza watoa huduma wote wafanye tathmini katika minara ambayo bado inatumia teknolojia ya 2G ili waweze ku- upgrade na kuweza kutumia teknolojia ya 3G, 4G na hatimaye baada ya kujiridhisha kwamba tutakuwa tunahitaji 5G basi tutakuwa tumefikia huko.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, maeneo mengi ya Mkoani Songwe ikiwepo Kata Maalum ya Mbangala ambayo ni Kata maalum kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu yanakabiriwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Nataka kufahamu nini mkakati wa Serikali katika kupeleka mawasiliano katika maeneo haya ya Wilaya nzima ya Songwe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iko kwenye mchakato na katika hatua za awali kabisa katika kuhakikisha inafanyia tathmini Vijiji na Kata zote nchini ili kujiridhisha wapi tuna tatizo la mawasiliano ili tuhakikishe kwamba katika mwaka wa fedha ujao tuweze kuviingiza na kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata mawasiliano.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, changamoto ya wananchi wa Manonga inafanana sana na wananchi wa Jimbo la Kyerwa. Nimekuwa nikiongelea changamoto ya Kijiji cha Kitega, Kata ya Songambele ambacho kipo chini ya mlima na kipo karibu na Rwanda, hakuna mawasiliano ya Redio wala simu wala kitu chochote. Ni mpango gani wa Serikali na wa dharura kuhakikisha kile Kijiji tunakirudisha Tanzania kwa kukipa mawasiliano kwa sababu ni kama wapo gizani. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tayari Serikali kupitia Wizara yetu na kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote tayari tumeshafanya tathmini katika Vijiji na Kata zote zilizopo mipakani na katika maeneo ya mbuga na hifadhi. Tayari tunaenda kuviingiza katika mpango wa kuhakikisha kwamba mwaka huu tunaenda na utaratibu wa kuanza kwanza na maeneo ya mipakani.
Katika siku ambayo tunapitisha bajeti yetu tuliwaambia Waheshimiwa maeneo ya mipakani ndio ambayo tunaenda kuyapa kipaumbele yakiwepo maeneo ya Mheshimiwa Mbunge, ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Kintanula ni walinzi shirikishi wa hifadhi kubwa kabisa ya Rungo Mhesi Kizigo ambayo ipo pale na wanasaidia kupambana na majangili kwa njia ya mawasiliano. Sasa kupitia mnara huu, wananchi hawana mawasiliano sasa. Ili kuepusha ajali nyingi ambazo zinatokea za watu kuanguka juu ya miti na kuvunjika mgongo na wakati mwingine viuno; je, Serikali inasemaje? Ni lini itakwenda kukamilisha mradi huu ili wananchi hao pia wanufaike na mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna mnara ambao unajengwa pale katika Kijiji cha Mhanga, ulisimama Kitongoji cha Jirimli, ulikuwa unajengwa na Halotel. Sasa Serikali ipo tayari kuzungumza na Halotel ambao walisimamisha ujenzi wa mnara huu ili waendelee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, Kijiji hiki kitaingizwa katika utaratibu wa kufanyiwa tathmini ili tujiridhishe ukubwa wa tatizo na kujua kama tunahitaji kwenda kuweka mnara au tunaenda kuongeza tu nguvu ya mnara uliopo ili uweze kuhudumia wananchi wa pale.
Mheshimiwa Spika, pia lengo la Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ni kufikisha mawasiliano kwa wananchi wote. Kwa hiyo, hilo ni jukumu la Serikali, nasi Serikali tumejipanga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vijiji ambavyo vinahitaji mawasiliano kikiwemo na Kijiji ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, kitakuwepo ndani ya mkakati wa Kiserikali wa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, pia kuhusu masuala ya Halotel; katika ujenzi wa minara, wakandarasi wengi ambao wanapewa tender za ujenzi wa minara hii ni kwamba wamekumbana na changamoto nyingi katika kipindi hiki ambacho tulikuwa tuna Covid 19, lakini pia katika baadhi ya vibali ambavyo walikuwa wanaomba, vingine vilichelewa kwa sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wao. Sasa Serikali imejipanga kwamba katika vipengele ambavyo vinahusisha na vibali ambavyo Serikali moja kwa moja inahusika, tunaenda kuhakikisha kwamba tunashirikiana na wenzetu ambao wanatoa vibali ili vibali vile vinatoka kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake lakini bado ningeomba kwa kuwa maisha ya sasa yanategemea sana matumizi ya simu na wahusika wanaathirika kwa kiasi kikubwa naomba niyataje maeneo hasa ambayo yanahitaji kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo, Kata ya Itundu, hasa Katuli, Ilani, Kiloleni, Mwinyi, Kalembela, Jumbe na Kikwete Kata ya Muungano ni Muungano yenyewe, Magulungu, Isenda, Utenge na Kangeme, Kata ya Usisya ni Usisya Kati, Mabundulu, Katungulu na Majengo. Kata ya Uyogo ni Uyogo yenyewe, Igembesabo, Kasela, Igunguli na Mirambo, Kata ya Ugala ni Ugala yenyewe Izengamatogile na Isogwa, Songambele, Mlangale na Ukwanga na Kata ya Kapilula ni Kata yote, naomba lini wanapatiwa mawasiliano watu wa Urambo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Urambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli alichokiongea Mheshimiwa Mbunge ni kweli kabisa, kwasababu tayari tarehe 16 Machi 2021 nilifanya ziara katika Jimbo lake la Urambo, na kweli nikagundua kuna maeneo ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano. Lakini katika maeneo ambayo tuligundua yana changamoto ya mawasiliano, tulitoa maelekezo ili tathmini ifanyike na kuhakikisha kwamba wananchi wa Urambo hawapitwi mbali na huduma ya mawasiliano kwa ajili ya kujiletea maendeleo kupitia mtandao wa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Tabora Mjini lina kata 29 na
vijiji 41, na katika vijiji hivyo vingi havina mawasiliano ya simu na vijiji vingine vipo karibu kabisa, kilomita mbili tu kutoka mjini lakini bado ni vigumu kupata mawasiliano; mathalani kata ya Itetemya. Ninaomba kuuliza;
Je, ni lini Serikali itatufanyia mpango wa kuongeza angalau minara ili mawasiliano yaweze kuwa mazuri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA
HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mawasiliano ni takriban nchi nzima ina changamoto mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ambazo zinatokana na teknolojia iliyowekwa katika eneo husika, lakini pia mnara uliowekwa pale inategemea kwamba uliwekwa katika wakati upi, kwamba iawezekana kulikuwa na population ya watu wachache na sasa wameongezeka sasa mnara unaweza ukazidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunafahamu kabisa kwamba kuna maeneo ambayo kutokana na sababu za kijiografia unakuta kwamba katika kata moja mawasiliano yapo katika vijiji sita lakini Kijiji kimoja kinakuwa kinakosa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kupitia Wizara yetu imeanza kufanya utafiti wa kujiridhisha ili tuweze kupata teknolojia ambayo tutakuwa tunafikisha huduma ya mawasiliano katika zile sports ambapo unakuta kwamba ni Kijiji kimoja tu ambacho kimekosa mawasiliano lakini tufikishe kwa teknolojia ambayo ni nafuu na yenye gharama nafuu. Waheshimiwa Wabunge pia tuweze kusaidiana kuhakikisha kwamba tunawaelewesha wananchi wetu kujua kwamba mawasiliano yatafika kwasababu bahati nzuri mmetusaidia kupitisha bajeti ambayo itatufikishia mawasiliano katika vijiji vyetu.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Waziri kwa majibu mazuri, pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa asilimia 90 mpaka 95 ya wateja wapya kwenye mitandao ya simu wanapatikana kutokana na mfumo huu wa freelancer na Kampuni yetu ya TTCL imekuwa ikisuasua katika kuongeza wigo wake.
Je, lini sasa TTCL au Wizara itaagiza TTCL waweze kutumia mfumo huu ili waweze kuongeza wigo wao?
Swali langu la pili ni kwamba mfumo huu wa freelancer siyo ajira kamili, I mean vijana wamekuwa wakilipwa kwa njia ya commission na haya makampuni kwa mfano yana vijana kama laki moja hivi ambao wako kwenye mfumo huo. Sasa kutokana na kutokuwa na sheria inayotambua mfumo huu, hawa vijana wamekuwa wakitumia wakati mwingine loophole ya kuyashitaki haya makampuni kwamba wameajiriwa na hivyo kuleta hofu ya haya makampuni kuendelea kuajiri hawa vijana.
Je, Serikali italeta lini hapa sheria ili sasa itambue mfumo huu kwamba ni mfumo kamili ambao unasaidia kuajiri vijana wengi ambao hawana kazi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI MAWASILIANO TEKNOLOJIA NA HABARI:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga Gedion Mbunge wa Kalanga kama ifuatavyo: -
Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mbunge wa Kalenga Mheshimiwa Kiswaga kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya Jimbo na wananchi wake wa Kalenga. Haya ni matakwa ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kupitia ukurasa wetu wa 96, 97, 98 na ukurasa wa 113 kuongeza wigo wa mawasiliano kufikia asilimia 94. Sasa kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, tayari imeshatoa maelekezo kwa TTCL kuanza kutumia mfumo huu na mpaka sasa wana-agrigator watano na freelancer takribani 3000. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunasimamia hili ili waendelee kuongeza wigo mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini suala la kamisheni kati ya freelancer na watoa huduma ni suala ambalo Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba inaweka mfumo mzuri ambao utatumika katika kusimamia ili kuwepo na uwajibikaji kwa freelancer pamoja na watoa huduma ili kuhakikisha kwamba tunaondoa hili gap ambalo lilikuwa linasababisha na kutokana na uhalifu uliokuwa unatokea sababu ya freelancer kutumia hizi national ID kwa matakwa yao na si matakwa ambayo yamewekwa kisheria, ahsante.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Wizi wa kimtandao unaongezeka kila kukicha; kwa kuwa TCRA kwa maana ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania wana uwezo wa kujua namba fulani inayofanya wizi ipo mahali fulani: Je, kwa nini Serikali sasa haioni kwamba uwepo utaratibu maalumu wa Jeshi la Polisi pamoja na TCRA kuzuia watu kabla hawajaibiwa kwa sababu wana uwezo wa ku-trace hiyo namba? Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, pale namba inapotumika ambapo namba ile siyo ya kawaida kwa mfano hizi namba zinazoanzia 15000 na kuendelea ndiyo namba ambazo ni za mitandao yenyewe, unakuta zinatuma ujumbe kwa mfano umeshinda labda shilingi milioni 600, umeshinda shilingi milioni sita, umeshinda kiasi kadhaa; anatuma mtu anaendelea kukatwa fedha zake. Sasa nauliza je, pale mwananchi ambapo anakuwa hana kosa na kosa ni la hawa wenye mitandao wenyewe kwa mfano TiGO au Vodacom, kuna mkakati gani wa Serikali ili wananchi ambao hawakufanya makosa yoyote waweze kubanwa hizi kampuni za simu kulipa fedha zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa maslahi ya wananchi wa Jimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, naomba niwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kwa kushiriki katika michakato mbalimbali ya kuishauri Serikali ili tuweze kuboresha huduma kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo Mheshimiwa Mwakasaka ameliongelea ni kwamba Serikali inamkakati gani wa kujaribu kuzuia wizi kabla hata haujatokea? Sheria ya makosa ya Kimatandao ya Mwaka 2015 ambayo ilianzishwa mahususi kwanza kutambua makosa yenyewe ya kimtandao ni yapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kikubwa ni kwamba kupitia Kamati ambayo imeshaundwa, kwa nafasi hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuisimamia vizuri Kamati hiyo, kazi yake kubwa ni kwenda kutoa elimu kwa Umma. Inapotoa elimu kwa Umma ni pale ambapo sasa Mtanzania anajua kabisa kwamba ni kosa lipi ambalo linahusika na sheria hii na kulihalalisha kwamba nikilifanya basi hatua za kisheria zitachukuliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni kujenga uwezo kama ambavyo nimesema kwamba kuna kitengo maalum cha makosa ya kimtandao, ambayo ni Cybercrime Unit ambayo inashughulika na makosa haya. Lakini kuwajengea uwezo na kuleta vitendea kazi ambavyo…
NAIBU SPIKA: Elekea kwenye jibu la pili hilo ameshaelewa Mheshimiwa Mwakasaka. Jibu swali lake la pili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali la pili anaongelea kuhusu message ambazo wanakuwa wanatumiwa. Nalo hili linaangukia katika makosa yale yale ya kimtandao tunasema unsolicited messages. Hili tayari tumeshakaa na watoa huduma tumeshaanza kuweka mkakati wa kuhakikisha kwamba, tunawasaidia na kuelewa kwamba namna gani message hizi hazitakiwi kutumwa kwa watanzania ambao hawajaziomba. Matokeo yake wanakuwa na makosa ambayo hawajahusika moja kwa moja. Ahsante. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyoneza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kuuliza. Katika mkoa wetu wa Iringa bado kuna maeneo ambayo yanasuasua katika mawasiliano na hasa katika ya Nyazwa, pamoja na kuwa kuna mnara wa Halotel lakini bado kabisa maeneo mengi sana hakuna mawasiliano. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba Mkoa wote wa Iringa kata zote zinapatiwa mawasiliano ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati Mbunge wa Viti Maalum kutoka Iringa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba inafikisha mawasiliano kwa wananchi wote na kuhakikisha kwamba tunaimarisha upatikanaji wa mawasiliano. Lakini naomba kupokea changamoto hii ili tuweze kutuma wataalamu wetu wakafanya tathmini na ili wajiridhishe kchangamoto iko na ukubwa gani ili tuchukue hatua stahiki. Ahsante.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nikupongeze kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya katika Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ((Makofi)
Mheshimiwa Spika, mawasiliano ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu, bila mawsiliano kila kitu kinakuwa siyo sawasawa. Kwa muktadha huo; Jimbo la Mchinga lina tarafa nne ndani ya tarafa mbili angalau klidogo mawasiliano ya simu yanapatikana lakini ndani ya tarafa mbili nyingine, Tarafa ya Milola na Tarafa ya Mipingo hakuna kabisa mtandao. Kukosekana kwa mtandao unasababisha pale kuwa kama kisiwa.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itatuletea mtandao katika Tarafa ya Mpingo na Milola na hasa katika vijiji vya Mipingo, Namakwia, Namkongo, Matakwa na Kiwawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete Mbunge wa Mchinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Salma Kikwete kwa kuendelea kuwapigania wananchi wake ili wapate huduma ya mawasiliano ili waweze kufanya shughuli zao za kibiashara kama ambavyo Watanzania wangetamani.
Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunafiksiha mawasiliano kwa Watanzania wote. Hivyo basi changamoto kama hii inapotokea katika maeneo tofauti tofauti basi kama Serikali ni wajibu wetu kupokea changamoto hii ili tuhakikishe kwamba wataalamu wetu tuwatume katika maeneo specific ili wakapate ukubwa wa tatizo na namna ambavyo tutaenda kulishughulikia kulingana na eneo husika lenyewe. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge wa Mchinga amesema, yeye kwake ni tarafa mbili, mimi nina tarafa tano. Kati ya tarafa tano tarafa tatu hazina mawasiliano kabisa. Na utaona hapa sisi wa Lindi tunazungumzia Tarafa, siyo Kijiji, ni tarafa nzaima ambayo ina kata kadhaa na vijiji kadhaa.
Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Serikali, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuja kukomboa Mkoa wa Lindi na suala la mawasiliano kwa sababu pamekuwa na ahadi za miaka nenda, miaka rudi kulimaliza hili jambo?
Hii habari ya kusema tutakuja kutembea ndio majibu yamekuwa haya kila siku. Nataka commitment ya Serikali kuja kutusaidia Mkoa wa Lindi tuondokane na tatizo hili.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye Mbunge wa Mtama kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nape Nnauye kwa sababu amekuwa akitoa taarifa ya changamoto ya mawasiliano ya wananchi wake wa Jimbo la Mtama. Na kwa bahati nzuri nimekaa naye sana na tayari tumeshakubaliana mimi na yeye tutatoka hapa kwenda mpaka Mtama kwenda kujiridisha tukiwa na wataalamu wote kiasi kwamba sasa hili tatizo pindi ambapo tutajua kwamba tatizo lipo wapi ili tuweze sasa kuingiza katika mpango wa utekelezaji wa mwaka ujao. Ahsante sana.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa changamoto iliyopo Jimbo la Nsimbo linashabihiana kabisa na changamoto ya Jiji la Kitalii la Arusha; tunazo kata ambazo zilikuwa zamani Wilaya ya Arumeru kabla hatujawa jiji Kata kama ya Olmoti ambayo ina mitaa ya Nafco na Milongoine, Kata ya Terrat ambayo ina mitaa ya Ulepolosi, Masikilia na Engavunet na Kata ya Olasiti ambayo ina mtaa wa Oloesho bado zina changamoto kubwa ya mawasiliano ya simu.
Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu kwenye kata na mitaa hiyo ambayo nimeitaja?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mrisho Gambo Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mrisho Gambo kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo lake la Arusha.
Mheshimiwa Spika, nimeshafika Arusha, na maeneo ambayo ameyataja nayatambua kweli kabisa yana changamoto hiyo. Tayari tumeshaelekeza wataalamu wetu; kwa sababu changamoto ya Arusha si ujenzi wa mnara isipokuwa ni kuongeza nguvu katika minara iliyopo ili iweze kuhudumia wakazi wa Arusha kwa sababu wamekuwa wakiongezeka kwa kasi kubwa hivyo basi minara iliyokuwepo ilikuwa imeshazidiwa nguvu. Tayari wataalamu wetu wameshaanza kufanya kazi na pindi kazi hii itakapokamilika basi changamoto hii itakuwa imeweza kutatuliwa. Ahsante sana.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi pia.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Biharamulo tuna vijiji 75. Kati ya vijiji 75 vijiji 25 havina mawasiliano kabisa, kabisa, na bado tuna shida, ukiachilia mbali vitongoji. Sasa ni nini hatua ambayo Serikali imachukua kwa ajili kuweza kuboresha mawasiliano? Ukizingatia watu hawa nao inabidi washiriki mchango wa maendeleo wa nchi hii lakini wameachwa mbali kwa sababu wako katika maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa. Nataka kusikia kauli ya Serikali kuhusu vijiji 25 vya Biharamulo.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ezra Mbunge wa Biharamulo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ambayo imebahatika na ambayo itanufaika katika mpango wa utekelezaji mradi wa mipakani basi na Biharamulo inaenda kupata miradi takribani sita.
Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba kipindi kitakapofikia tena cha kuleta bajeti ili tuweze kuhakikisha kwamba maeneo mengi yanapata mawasiliano basi aweze kutuunga mkono kuhakikisha kwamba bajeti hii iweze kwenda kujibu mahitaji ya Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza:
Mheshimiwa Spika, changamoto ya mawasiliano iliyopo Kata ya Chilangala inafanana na Kata za Kitaya, Mnongodi na Namtumbuka ambazo zipo mpakani na Msumbiji na ambako kama utakuwa unafahamu sasa hivi kuna changamoto ya kiusalama kule. Naomba mpango mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba Kata hizi kwa sasa zinakuwa na mawasiliano ya uhakika ili isaidie katika…
SPIKA: Zipo kwenye Wilaya gani hizi Kata.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, zipo Wilaya za Mtwara Vijijini na Tandahimba ambazo zinapakana na jirani zetu wa Msumbiji. Kwa hiyo naomba mpango wa haraka wa Serikali wa kuhakikisha kwamba Kata hizi zote zinapata mawasiliano ya uhakika.
Swali langu la pili ni kwamba minara ambayo inajengwa vijijini sasa hivi ni kwa ajili ya mawasiliano ya sauti tu, kwa ajili ya voice, lakini kuna mahitaji makubwa ya internet sasa hivi vijijini na hata Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inasema tunataka kuboresha upatikanaji wa internet vijijini. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuboresha au ku-upgrade minara hii ili iweze kuhakikisha kwamba hata data zinapatikana vijijini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARl: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wabunge wote wa Mtwara kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia tunapofika katika maeneo yao ya kazi. Maeneo haya ya Kitaya pamoja na maeneo mengine ya Lulindi, Tandahimba pamoja na Newala tulishafika na kupitia fedha ambayo Serikali ilipitishiwa hapa Bungeni tayari kuna miradi ambayo imepangwa kwenda kutekelezwa kupitia miradi ya mipakani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi kabisa, kwa sababu dhamira ya Serikali ni ileile ya kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata mawasiliano. Maeneo ya mipakani tunayaangalia kwa umuhimu wake kwa sababu ni masuala ya kiusalama.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika Kata ya Kitaya, Mbunge anafahamu, mimi na yeye tulikwenda mpaka katika Kata ya Kitaya ambapo kuna mradi wetu ambao umeshakamilika na tayari umeshawashwa na huduma ya mawasiliano tayari imeshafika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala la uhitaji wa internet kwanza kabisa mpaka sasa Serikali inaboresha miundombinu ya Mkongo wa Taifa. Kwa upande wa Kusini mpaka sasa ukitoka pale Mangaka kwenda Mtambaswala takribani kilometa 72, tunajenga mkongo wa Taifa siku za hivi karibuni mradi huo utakamilika. Hivyo basi, hata ile miradi sasa ambayo itakuwa inahitaji data maana yake ni kwamba Serikali imeshaelekeza watoa huduma wote wahakikishe miradi yote ambayo itajengwa kuanzia sasa iwe inatoa huduma ya 3G na 4G na kuendelea. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na ya kuridhisha ya Serikali, nina swali fupi la nyongeza: -
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza wigo wa usikivu nchini, TBC haioni kwamba kuna haja ya kuwasiliana na redio za kijamii ili kuziwezesha kujiunga na TBC Taifa wakati wa matokeo makubwa kama vile taarifa ya habari na mengineyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Othman Hija kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Shirika la Utangazaji TBC linafanya mahusiano mazuri na Shirika la Utangazaji la Zanzibar. Baada ya kukamilisha katika miradi yetu ya awali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, tuna mpango wa kuja kushirikisha na redio zingine ili pale ambapo Shirika la Utangazaji Tanzania linapokuwa na changamoto ya miundombinu basi iweze kushirikisha redio nyingine ambazo zitakuwa zinasaidiana. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwanza kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini eneo la Bukiko ni kweli kupitia UCSAF, ulijengwa mnara wa Halotel lakini kuna shida kubwa; ule mnara unategemea umeme jua, kiasi kwamba nguvu ya umeme inapopungua kunakuwa hakuna mawasiliano, lakini vile vile kuna shida kubwa ya Internet kwa sababu mtandao ulioko pale ni wa 2G; Sasa naiomba Serikali niweze kujua, ni lini sasa Serikali itapeleka jenereta kwenye eneo lile? Vile vile iwasiliane na watu Halotel ili kuweka mtandao wa zaidi ya 2G kwa maana ya 3G na vyovyote itakavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwenye majibu, ni kweli kuna shida kubwa ya mawasiliano kwenye maeneo mengi, kwenye visiwa vya Ukerewe; na Serikali imejibu kwamba itaenda kupitia maeneo yote yenye shida: Ni lini sasa kazi hii itafanywa na Serikali ili timu iende kule, ifanye uchunguzi na hatimaye marekebisho yafanyike ili kuwe na mawasiliano mazuri kwenye eneo lile? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu jenereta; kwanza kabisa ile site ya mawasiliano iwe imekamilika, haijalishi kama ni umeme wa TANESCO au ni wa Solar, ni lazima site iwe na backup generator. Kwa vile Mheshimiwa Mbunge amelifikisha hili, basi Serikali inalipokea na tutalifanyia kazi ili kujiridhisha na changamoto ambayo ameiongea.
Mheshimiwa Spika, vilevile ni azma ya Serikali sasa kuhakikisha kwamba, maeneo mengi nchini yanapata huduma ya internet, yaani kutoka katika huduma ya zamani ya 2G kwenda 3G. Hapo kabla Wizara tayari ilishatoa maelekezo kwa watoa huduma ili kuhakikisha kwamba, minara inayojengwa kuanzia sasa basi iwe na huduma ya 3G.
Mheshimiwa Spika, tuna minara ya aina mbili; minara ambayo inatokana na ruzuku ya Serikali, lakini vilevile kuna minara ambayo inatokana na wawekezaji wenyewe. Ile ambayo inatokana na ruzuku ya Serikali tayari Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeshaanzisha mchakato wa ku-up grade minara yote ambayo itakuwa ina 2G kwenda kwenye 3G. Pia Serikali imeelekeza kwa watoa huduma wengine katika minara ambayo sio ya Serikali, ihakikishe kwamba, inaona umuhimu sasa wa kuelewa kwamba, sasa teknolojia ya 3G inahitajika kwa Watanzania wote. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hivi karibuni na katika Jimbo lote la Ndanda kuna matatizo sana ya network na hasa eneo la Ndanda ambako ndio Makao Makuu ya Jimbo na mtandao tunaotumia pale sana ni Vodacom pamoja na Airtel na Airtel kuna hisa za Serikali. Hata hivyo, wataalam walipopewa taarifa mpaka leo hawajaenda kufanya marekebisho. Sasa kwa nini Mheshimiwa Waziri asiwakumbushe watu wa Airtel kwenda kuufanyia marekebisho mnara ule ili mawasiliano yawe bora?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kimsingi ameomba Serikali tuongee na watu wa Airtel ili wakarekebishe changamoto iliyojitokeza. Tunaipokea changamoto hiyo na tutawasiliana na wenzetu wa Airtel ili kwenda kuifanyia kazi hiyo changamoto. Ahsante.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; pamoja na majimu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo amekiri Jimbo la Tabora Mjini lina sura mbili yaani Kata za Mjini na Kata za Vijijini; changamoto ya mawasiliano ni kubwa sana katika kata za mjini na kata za pembezoni. Kata za vijijini zina vijiji zaidi ya 41, asilimia 75 ya vijiji hivyo haina mawasiliano kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusema kwamba wamepeleka mawasiliano katika Kata za Kabila na maeneo mengine, lakini Kabila ni pale center ndipo ambapo unapata mawasiliano; lakini kwenye Vijiji vya Igosha, Umanda na vijiji vingine havina mawasiliano kabisa.
Je, Mheshimiwa Waziri ni kwa asilimia ngapi ya vijiji vya kata za pembezoni ambazo tayari mmeshapeleka mawasiliano hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata za Mjini ukiwa katika Kata za Malolo, Ng’ambo na Kidongo Chekundu hupati mawasiliano kabisa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Hawa uliza swali tafadhali.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti nimtajie kata ambazo zina changamoto na mawasiliano ili aweze kujibu vizuri. Katika kata hizi tatu za Kidongo Chekundu, Ng’ambo na malolo hakuna mawasiliano kabisa tunapokuwa katika kutembelea wananchi maeneo hayo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha pia mawasiliano katika Kata za Mjini ambazo hazina mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum - Tabora kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala la mawasiliano katika Mji wa Tabora na Serikali inakiri kabisa kwamba Mji wa Tabora ulikuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano. Lakini mpaka hapo anaposema Mheshimiwa Mbunge ni kweli kabisa kwamba vijiji vingi havikuwa na mawasiliano, lakini mpaka sasa kuna vijiji vingi ambavyo vimeshapata mawasiliano ambapo tunaamini kabisa kwamba katika utekelezaji wa mpango wa mwaka mmoja mmoja na katika utekelezaji wa miaka mitano tunaamini kabisa kwamba tutakuwa tumefikia katika hatua nzuri kabisa ya kutatua changamoto ya mawasiliano katika kata za pembezoni katika Jimbo la Tabora Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile upande wa kata za mjini; kata za mjini changamoto yake ni moja, ni kwamba kulikuwa na minara ambayo tayari ilikuwa imeshaanza kuzidiwa na tayari Serikali imeshatenga takribani shilingi bilioni 7.6 ambapo tunakwenda kufanya upgrade ya minara takribani 380 nchi nzima; na Tabora Mjini ikiwa sehemu mojawapo ya minara ambayo inakwenda kufanyiwa kazi. Lakini pamoja na hivyo kuna minara ambayo ilikuwa inatoa huduma ya 2G maana yake kwamba hapakuwa na uwezekano wa kupata internet lakini katika mpango huu huu Tabora Mjini tumeiweka katika mpango kabambe ambapo na Mheshimiwa Mbunge tutamshirikisha wakati tukifika Tabora kwa ajili ya kutatua hii changamoto ambayo wananchi wa Tabora wamekuwa wakilalamikia kwa siku nyingi. Ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, lakini pia na kwa kutoa fursa nyingi kwa Waheshimiwa Wabunge kuuliza maswali mengi ya nyongeza, tunakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga minara tisa ya mawasiliano kwenye Jimbo la Ngara. Naomba kuiuliza Serikali ni lini ujenzi huu wa minara tisa utaanza ili kutatua changamoto ya mawasiliano kwenye jimbo la Ngara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba, Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali ilitangaza kujenga minara tisa katika Jimbo la Ngara katika awamu iliyopita iliyokuwa imetangazwa. Lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, mwezi huu anakwenda kusaini mkataba wa ujenzi wa minara 90 ambayo ni pamoja na minara ambayo itakuwa hapo katikati Jimbo la Ngara.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na subira ili Mheshimiwa Waziri akishakamilisha jambo hili tayari utekelezaji utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia kwa utekelezaji wa changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Likawage.
Mheshimiwa Spika, maswali mawili ya nyongeza; moja, kwa kuwa changamoto ya mawasiliano Kata ya Likawage imedumu kwa muda mrefu na hivyo wana Likawage wanayo furaha sana kwa ambacho Serikali imewafanyia.
Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana kufuatana nami baada ya Bunge hili, ili kwenda kuzindua mnara huo?
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, changamoto hiyo iliyopo katika Kata ya Likawage bado pia ipo katika Kata ya Kikole. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba wanatatua changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Kikole? Ahsante.
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kipengele cha kwanza cha swali lake ni ombi la uzinduzi wa minara hiyo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kazi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na sisi tuko tayari kuambatananae na kuhakikisha kwamba, mnara huo unazinduliwa ili wananchi wa eneo husika waendelee kupata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili ni kuhusu kata ambayo inachangamoto ya mawasiliano. Ni jukumu la Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 61(j) ambapo inatakiwa kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano kwa wananchi wote, lakini kabla ya kufanya hivyo lazima tufanye tathmini na kujiridhisha ukubwa wa tatizo na baada ya hapo tutachukua hatua ili kutatua changamoto hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, hali ilivyo katika Jimbo la Kilwa inafanana kabisa na hali ilivyo kwenye Jimbo la Sumve ambapo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote wakiongozana na Naibu Waziri walikuja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa minara katika Kata za Bugando, Mwandu na Lyoma na ujenzi huo leo ni mwaka mzima haujakamilika.
Je, Wizara haioni sasa kuna umuhimu wa kuharakisha ujenzi huu ili watu wa kata hizo waanze kupata mawasiliano kama ilivyo kwenye kata zingine?
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, labda kwanza niongee kwamba ujenzi wa minara hii unahitaji vifaa ambayo tunaviingiza kutoka nje ya nchi na kwa sababu ya changamoto ambayo ilikuwepo ya UVIKO-19 uzalishaji wa vifaa hivi katika nchi ambazo tulikuwa tunaagiza ulipungua kwa kiasi kikubwa sana. Kwa hiyo, nina uhakika kabisa, na hii sio changamoto ya Sumve kuna maeneo mengi, na Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamelalamika minara katika maeneo yao bado haijasimama kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini naomba nitoe taarifa kuanzia sasa mpaka mwezi wa nne tunaenda kuhakikisha minara 288 inawashwa. Hivyo, baada ya kuwasha minara hii baadaye sasa ndio tutajua kwamba changamoto bado imebaki maeneo gani, ili tuweze kuchukua hatua. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba nishukuru pia kwa Serikali kutoa majibu mazuri lakini bado naomba niulize swali moja la nyongeza.
Katika Vijiji vya Ilalangulu, Chagu, Katumba na Songambele ni maeneo ambayo yanazungukwa na msitu wa Halmashauri na ambao msitu ule wakati mwingine wananchi wanapata shida ya kutekwa na hivyo kukosa mawasiliano.
Naomba Serikali itoe majibu kwamba ni lini hasa hawa wananchi nao wataweza kupata nafuu ya kupata mawasiliano kwenye vijiji vyao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema katika jibu langu la msingi na pia kwa maelekezo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara 61(j) ni haki ya msingi kwa kila wananchi wanaoishi ndani ya nchi yetu kupata mawasiliano; hivyo tunaamini kabisa kwamba baada ya kufanya tathmini na kujiridhisha ukubwa wa tatizo tutaenda kuchukua hatua na kuhakikisha kwamba wanafikishiwa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika maeneo ambayo yako pembezoni na maeneo ambayo ni ya mbuga tunaamini kwamba katika mkataba huu ambao Mheshimiwa Waziri anaenda kuusimamia ili usainiwe maeneo 90 yanaenda kupata utatuzi wa changamoto wa mawasiliano baada ya kukamilika kwa ujenzi wa minara 90. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira kipindi ambacho Serikali itakuwa tayari basi tutahakikisha kwamba mawasiliano katika eneo hilo itakuwa imetatuliwa ahsante sana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kata yangu ya Karitu ndiyo kata pekee ambayo bado haijapata mnara wa mawasiliano ya simu Jimboni kwangu. Zaidi ya mara mbili kata hii imekuwa kwenye orodha ya kata ambazo zinapaswa zijengewe minara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote lakini mwaka unaisha haujajengwa.
Sasa swali langu ni kwamba je, Wizara ina mpango gani au mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kata zote zinazokuwa kwenye mpango wa kujengewa minara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote basi inajengewa kwa mwaka huo husika wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusu kata ya Karitu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge alichokisema na hili limekuwa ni tatizo kwa muda mrefu ni kwamba katika zabuni ambazo zimepita tulitangaza ujenzi wa minara katika maeneo 199 lakini watoa huduma walijitokeza katika maeneo 90. Sisi kama Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tunatoa ruzuku, ruzuku ambayo tunayoitoa mtoa huduma anaenda kujiridhisha katika eneo ambalo anatakiwa kujenga mnara na baada ya kuona kwamba business case inaonesha kabisa kwamba baada ya muda mrefu kabisa hawezi kupata faida yoyote hivyo maeneo hayo wanayakwepa.
Mheshimiwa Spika, lakini sasa Serikali imeanzisha mazungumzo ili tuangalie namna bora ya kuhakikisha kwamba tunapotangaza maeneo haya basi maeneo yote yapate watoa huduma kulingana na market share ya kila mtoa huduma hapa nchini nakushukuru sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii, lakini nisikitike swali nimeulizia Itigi lakini wamejibiwa watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeuliza usikivu wa Itigi kwa sababu maalum, sisi Itigi hatusikii kabisa redio, ni kwa sababu redio Mwangaza waliweka mnara wao pale mtambo, kwa hivyo redio nyengine hazisikiki kabisa ikiwemo TBC, na swali hili ni mara ya 3 nauliza ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize Mheshimiwa Waziri aniambie Manyoni ni sehemu ya Itigi, Manyoni wanasikia TBC, Itigi hatusikii kabisa, sasa huo mtambo mtakaoufunga mwakani huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli mnatuahirishia miaka yote hii, Mheshimiwa Nape yupo hapa ulipokuwa Waziri wa Habari ulijibu swali hili ukatuambia mtatusaidia kutufungia mtambo pale sasa leo tunajibiwa tu watafunga na Manyoni na Ngara na wapi, hebu naomba comitment ya Serikali, sisi Itigi hatusikii kabisa redio, wananchi wetu hawana pesa ya kununua tv, hata Mheshimiwa Rais akihutumia hawamsikii kupitia viredio vyao.
Sasa ni lini mtatufungia kamtambo hako? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare Mbunge wa Manyoni Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya matangazo ya TBC, changamoto ni mbili ya kwanza ni uhafifu wa usikivu na pili inawezekana usikivu haupo kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto ya Manyoni kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, nimesema kwamba katika mwaka wa fedha ujao kuna Wilaya 14 ambapo Manyoni ikiwa moja ya Wilaya ambazo zinakwenda kutatuliwa changamoto za usikuvu wa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile nafahamu kabisa kwamba changamoto hii imekuwa ya muda mrefu lakini ni lazima pia tutume wataalamu wetu wakajiridhishe na ukubwa wa tatizo ili tujue tatizo ni kwamba hakuna mawasiliano au mawasiliano ni hafifu, ili tuweze kuchukuwa hatua stahiki ili kuhakikisha kwamba Itigi inapata mawasiliano ya TBC. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nitoe shukrani kwa majibu mazuri ya Serikali juu ya swali langu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza: -
Mheshimiwa Spika, kwani upo udanganyifu uliofanywa katika Kijiji cha Kibutuka na aliyekuwa mfanyakazi wa Tigo, alienda pale akadanganya wanakijiji kwamba, anahitaji eneo la kujenga mnara, baadaye wanakijiji walimpa bure wakitumia mukhtasari ule yule sasa hivi anekuwa ndio mnufaika wa kodi ya mnara ule badala ya kuwa wanakijiji waliopo katika kijiji kile.
Je, Serikali ina mkakati gani au ina kauli gani juu ya utapeli wa huyu mtumishi wa tiGO ambaye yeye anajifanya kwamba, ndio mmiliki wa lile eneo wakati aliliomba apewe bure?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; pamoja na kwamba, Vijiji vya Ndapata, Ndunyungu, Makata, Mtawatawa, Kipelele, Makinda na Nambinda havina mawasiliano ya kutosha. Nini mkakati wa Serikali wa kutuwashia ile minara ambayo tayari imeshawashwa kwenye baadhi ya vijiji hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kipengele cha kwanza. Ni kweli kabisa changamoto ya udanganyifu uliojitokeza tunaifahamu, lakini tayari suala hili lilikuwa limeshafika mahakamani na lilikuwa limeshatolewa maamuzi.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu pia migogoro ya ardhi inapotokea kwa Sheria Na.2 ya Mwaka 2002, tunafahamu kabisa kwamba, hili linahusisha Wizara ya Ardhi moja kwa moja, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa changamoto hii ambayo imejitokeza tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi, ili tuweze kujua namna gani tutatatua changamoto hii ambayo imejitokeza katika eneo husika.
Mheshimiwa Spika, vilevile swali la pili ni kuhusu minara ambayo haijawashwa. Ni kweli kabisa katika maeneo ya Jimbo la Liwale, kwanza kabisa labda tuseme kwamba, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana katika ujenzi wa minara ndani ya nchi yetu, likiwepo Jimbo la Liwale. Ni takribani bilioni 19.56 imewekezwa katika minara 161 ambapo tunatarajia katika kipindi cha miezi miwili mitatu minara hii ambayo tayari imeshasimama itahakikisha kwamba, itakuwa imeshawashwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imefanya uwekezaji mwingine wa minara 127 ambayo iko katika hatua za civil works. Katika kipindi cha miezi miwili mitatu, tunaamini kabisa kwamba, minara hii itakapokamilika, naamini maeneo mengi yatakuwa yamepata ufumbuzi wa changamoto hizi za mawasiliano, likiwepo Jimbo la Mheshimiwa Kuchauka ambalo ni Liwale. Nakushukuru sana.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri niliongozana naye mwaka jana kwenda Mtwara kuangalia maeneo ambayo yana matatizo ya mawasiliano ikiwepo bandarini pale Mtwara, pale Mitengo kwenye Hospitali ya Rufaa.
Sasa nahitaji commitment ya Serikali, kwa kuwa tulishawahi kwenda na mwenyewe ukaangalia uhalisia. Ni lini sasa minara hii itapatikana kwenye maeneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tuliongozana na Mheshimiwa Mbunge kuangalia changamoto ya mawasiliano katika maeneo haya. Lakini tulitoa maelekezo kwa operator wote ambao wanatoa huduma ya mawasiliano katika maeneo haya ili kuweza kufanya optimization ili kutatua changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, kwa vile Mheshimiwa Mbunge bado anaonesha kuna changamoto pale, basi tutatuma wataalam wetu ili waweze kufanya tathimini ili tujirizishe kama kuna uhitaji wa ujenzi wa minara katika maeneo hayo. Nakushukuru sana.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Naibu Waziri alifanya ziara jimboni Kata ya Jana na alipokuwa pale aliahidi ujenzi wa minara sita ambayo itajengwa Kata ya Mwakata, Kata ya Mwaluguru, Kata ya Chela, Kata ya Mega na Kata ya Runguya, Kijiji cha Nyangarata.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu ni lini utekelezaji huu utaanza?
Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika kata hizo tuliahidi na tayari zimeingizwa katika mpango wa utekelezaji wa miradi hiyo, na katika miradi ambayo inaongozwa na Mradi wa Tanzania Kidigitali ambao ni miradi 763 na katika minara hiyo 763 na maeneo ya Mheshimiwa Kassim Iddi yatakuwemo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aendelee kusubiri ilimradi tu mchakato wa utangazaji wa tender utakapokamilika, ujenzi wa minara utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuweza kuniona.
Kijiji cha Shoga kilichopo Kata ya Sangambi, Kijiji cha Sipa Kata ya Kambekatoto na maeneo karibu yote ya Kata ya Upendo yana changamoto kubwa sana ya mawasiliano ya simu za mkononi; je, ni lini sasa Serikali itapeleka minara ili kumaliza changamoto hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya msingi ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya mawasiliano ili Watanzania waendelee kutumia huduma ya mawasiliano katika biashara na mambo mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maeneo ya Mheshimiwa Masache ni kwamba yameingizwa pia katika utekelezaji wa Tanzania Kidigitali katika miradi 763. Nakushukuru.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hali ya kukosekana mawasiliano ya simu katika Kata ya Jangwani, Manispaa ya Mtwara Mikindani inafanana kabisa na hali ya Kata ya Dutumi na Kwala kwa Kijiji cha Kimalamisale, Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani.
Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri utafanya ziara katika maeneo hayo ili kujionea hali halisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu, Mbunge Viti Maalum - Pwani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alinijulisha siku mbili zilizopita kuhusu maeneo haya na mimi nikaenda kufuatilia katika utekelezaji wa miradi yetu kwa bahati nzuri maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge tayari yako kwenye utekelezaji katika ile miradi 763.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo, kama kutakuwa na uhitaji wa kwenda kufanya ziara basi sisi kama Serikali tuko tayari kufika katika maeneo yenye changamoto. Nakushukuru sana.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Ninaomba tu kufahamu kwa kuwa nilishamwandikia barua na tumezungumza, ni lini sasa atakuja Ludewa ili aweze kupokea shukrani za wananchi wa Ludewa kwa Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kamonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu na ombi la Mheshimiwa Mbunge tunalipokea na mimi nitaongoozana nae kwenda kuangalia changamoto za wananchi wa Ludewa. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Takribani wananchi Elfu Sita wa Kijiji cha Katurukira Kata ya Mkula na Kijiji cha Sururu Kata ya Signari hawana mawasiliano mazuri ya simu. Je ni lini Serikali itawasaidia wananchi miundombinu ili waweze kupata mawasiliano mazuri ya simu?
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mradi wa Tanzania ya Kidigitali (Digital Tanzania) na tayari mradi huu tenda yake imeshatangazwa tarehe 20 Oktoba na tarehe 2 Disemba tayari mradi utafunguliwa ambapo Kata na Vijiji vya Jimbo la Kilombero vimeingizwa katika mradi huo. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi pindi mchakato huu utakapokamilika basi ujenzi wa minara utaanza kufanyika rasmi katika Jimbo lake.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Lahoda iliyopo Wilaya ya Chemba ina mnara ambao hauna nguvu, hivyo kuleta shida katika mawasiliano. Je, ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba wanaimarisha mawasiliano ili wananchi wa Kata hii waweze kupata mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Chemba tayari tumeshatuma wataalamu wetu kwenda kuangalia changamoto iliyopo katika minara katika Jimbo la Chemba. Kikubwa tulichokuwa tunakiangalia ni aidha kuangalia kama kulikuwa na huduma ya 4G au haikuwepo, lakini kama ilikuwepo na changamoto ni mawasiliano hafifu basi tutahakikisha kwamba tunafanya namna ya kuongeza nguvu katika minara hiyo inayo lalamikiwa na wananchi. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Serikali itapeleka lini mawasilino ya uhakika ya simu kwa wananchi wa Ushetu hasa katika Kata ya Ulewe, Igwamanoni, Igunda pamoja na Bukomela ambapo wananchi hao bado wanapanda juu ya mti na milimani kutafuta mawasiliano ambayo ni hatari sana kwenye maisha yao.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata ambazo Mheshimiwa Cherehani amezitaja tayari katika bajeti ya Serikali ambayo ililetwa Bungeni hapa Kata hizo ziliwekwa katika bajeti. Bajeti hii ambayo inaunganisha minara 763 na kama ambavyo nimesema hapo mwanzoni tayari tumeshatangaza tenda tarehe 20 Oktoba na tarehe 2 Disemba itafunguliwa na baada ya hapo ujenzi wa minara hii utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wakati wenzetu wanakwenda kwenye mfumo wa 4G Jimboni kwangu baadhi ya Vijiji havina kabisa mawasiliano ikiwepo Kijiji cha Mhanga, Kintanula na Kijiji cha Lulanga.
Je, ni lini sasa Serikali itatimiza ahadi yake ya muda mrefu ya kupeleka minara katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masare kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge tunawasiliana mara kwa mara na hivi vijiji tayari kilichokuwa kinasubiriwa ni tenda kutangazwa na tenda tayari imeshatangazwa Tarehe 20 Oktoba. Hivyo, tunasubiri mchakato huu ukamilike ili utekelezaji wa mradi huu uanze mara moja. Mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge bahati nzuri tumeshafika katika eneo lake na vijiji ambavyo amevitaja mimi binafsi nimeshafika katika maeneo hayo, kwa hiyo nimhakikishie kwamba hilo ninalifahamu kabisa na Serikali itaenda kutekeleza. Ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itajenga Minara ya simu katika Kata ya Makame na Raiseli katika jimbo la Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halanga, Mbunge Viti Maalum Manyara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kwelli kabisa kuna changamoto ya Mawasiliano katika jimbo la Kiteto. Na bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, ndugu yangu wakili msomi Olelekaita pamoja na Mheshimiwa Asia, kwa kweli tunashirikiana vizuri sana na wao katika kuhakikisha tunatatua changamoto hii. Bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge anafahamu kabisa kuwa orodha ya vijiji vyake vyote vipo kwenye bajeti ya mwaka huu. Hivyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge wa Manyoni pamoja na Kiteto, tuhakikishe kwamba tunashirikiana katika kutoa maeneo ili kukamilisha ujenzi wa miradi hii. Ahsante sana.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina swali dogo la nyongeza kwamba nchi ya Uganda, siku ya jana tarehe 6 imekuwa ni nchi ya 12 katika Afrika kurusha Setilaiti yake angani. Setilaiti ile imeundwa kwa kupitia vijana ma- engineer wa Uganda wakishirikiana na nchi ya Japan na Kituo cha Anga cha Marekani: Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha program hii ya kuanza kufundisha vijana wetu kwa kushirikiana kama ilivyofanyika Uganda ili tuweze kupata setilaiti ambayo itaundwa na Watanzania halisi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nchi za Afrika mpaka sasa tuna setilaiti 41 na kuanzia mwaka 2016 ni setilaiti takribani 20 ambazo tayari zimekuwa angani. Katika hizo setilaiti 41 ni tisa tu ambazo zimekuwa designed, manufactured na baadaye kupelekwa angani ambazo zina asili ya Kiafrika.
Mheshimiwa Spika, bado tuna maeneo mengi ya kuendelea kujifunza, lakini kama nilivyojibu katika swali la msingi, Mheshimiwa Rais siku ya tarehe 8 Februari wakati akiwa na kikao kazi na Wakuu wa Mikoa, alielekeza Wizara yetu ili tuone umuhimu sasa wa kuwa na setilaiti yetu. Tayari Wizara yetu imeshaunda timu ya wataalam ambao watakuja kuishauri Serikali aina ya setilaiti itakayoendana na mahitaji ya Watanzania. Ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini nitumie nafasi hii kwanza kuipongeza Serikali, nimepitia taarifa yao ya miradi ya Tanzania ya Kidigitali, nimeona Kata za Gwata, Bokomnemela na Dutumi zimewekwa kwenye orodha ya Kata 763; nawashukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa swali la nyongeza; je, ni lini wakandarasi hawa ambao wameshapatikana watafika kwenye kata hizo na kuanza utekelezaji wa mradi husika? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni kwa kiwango gani huduma ya 3G inawasaidia Watanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Michael Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumejibu katika swali la msingi, tender ya upatikanaji wa mawasiliano katika miradi ya World Bank ambayo ilitangazwa tarehe 24 itafunguliwa tarehe 2 Desemba. Na baada ya kufunguliwa, mchakato wa upatikanaji wa vibali na hatimaye kuanza kwa hatua za ujenzi utakapokamilika ujenzi wa mawasiliano katika hizo kata utaanza mara moja.
Mheshimiwa Spika, katika kipande cha pili cha swali la Mheshimiwa Mwakamo, ni kwamba huduma ya 3G itawafikia lini Watanzania?
Mheshimiwa Spika, labda nitoe tu takwimu za harakaharaka; katika teknolojia ya 2G mpaka sasa kwa population coverage mpaka sasa Tanzania tumefikia asilimia 96; lakini kwa 3G tumeshafikia asilimia 72; 4G tumeshafikia asilimia 55. Internet penetration mpaka sasa kwa nchi yetu ni asilimia 50. ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa ya swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa katika orodha aliyotoa Mheshimiwa Waziri ya usambazaji wa minara vijijini kata zangu za Kaengesa, Mfinga, Izimba na Milepa hazimo; je, Serikali mna mpango gani wa kupeleka minara katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo uliagiza Wizara yetu tulete orodha hapa Bungeni, orodha hiyo ina segments mbalimbali; ina borders and special zone, phase six, miradi 763, vijiji ambavyo vimeshafanyiwa tathmini 2,116. Kama ukiangalia kwenye kata 763 haupo, basi tunaamini kabisa katika vijiji 2,116 unaweza ukawemo. Na kama utakuwa haupo basi tunaamini kwamba katika hatua za kuendelea kufanya tathmini tutaviingiza vijiji hivyo ili vipate mawasiliano, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, nimepokea majibu ya Serikali na ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ufafanuzi. Swali langu la kwanza lipo katika mfumo wa ombi, je, Naibu Waziri anaonaje kama atatafuta siku ya weekend katikati ya Bunge hili la Bajeti aongozane nami kwenda Jimboni Momba, kunisaidia kutoa ufafanuzi kwa wananchi wa Kijiji cha Namchinga ili waweze kuelewa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, Serikali inaonaje kama itatoa mwongozo kwa makampuni haya ya simu ili kuhakikisha wanapolipa pango la ardhi kwa Mmiliki lakini watoe na percent kwenye Serikali ya Mamlaka husika, aidha, Serikali ya Mtaa au Kijiji ili kutoa mgongano wa maslahi kwenye jamii.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya. Siku mbili tatu hizi tumekuwa tukiongea na Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Mtaa na Mwenyekiti wa Kata katika Kijiji hiki cha Namchinga. Kwa kweli anafanya kazi kubwa sana na hakika Jimbo la Momba wamepata Mbunge kwelikweli.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusu suala la kwenda kutoa elimu, naomba nilipokee na tutakaa tutajadili kadri nafasi itakavyoweza kupatikana tutaweza kufanya hivyo. Nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutafanya kulinganana na nafasi itakayopatikana.
Mheshimiwa Spika, jambo jingine kuhusu suala la kutoa percent kwa wananchi wetu na dhana kubwa ambayo inasababisha kwamba wananchi wanahitaji kupewa percent kuna dhana imejengeka kwamba minara hii iliyopo katika maeneo ya wananchi ina mionzi ambayo inawaathiri sana wananchi kiasi kwamba wanataka hii percent kama fidia.
Mheshimiwa Spika, Wabunge na wananchi wote, nikuhakikishie kwamba minara hii kiwango ambacho kimewekwa katika minara yetu, kiwango cha chini ni Volt Saba per meter, lakini minara yetu nchi nzima iko chini ya Volt Saba maana yake ipo kati ya Tatu mpaka Nne. Kwa hiyo, suala la mionzi naomba huu mtazamo tuutolee elimu ya kutosha ili wananchi wafahamu.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa Sheria ya Mwaka 2009, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2020 inasema kabisa kwamba makampuni ya simu yatatoa asilimia 0.3 kwenye Halmashauri kulingana na minara inayotumika katika Halmashauri husika. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Je, Serikali haioni haja ya kuimarisha mawasiliano hususan kwenye Wilaya za Mipakani kama Longido na Ngorongoro ambazo bado zina mawasiliano hafifu na muda mwingine wanatumia mawasiliano ya nchi jirani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Arusha, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi wa Special Zone and Borders ambao tayari unaendelea katika utekelezaji wake, labda tutajiridhisha katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amesema. Tutatuma wataalam wetu kwenda kuangalia kama halipo ndani ya mpango unaoendelea wa utekelezaji wa miradi ya Special Zone and Borders. Ahsante sana.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naomba kujua ni lini Wizara itajenga minara katika Kata ya Kikonda, Kinampundu na Mwangeza, ukizingatia Mwangeza wanavamiwa na tembo kila wakati, kwa hiyo wanahitaji mawasiliano kwa ajili ya kuomba msaada? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema hapa awali katika majibu yangu ya msingi ni kwamba kuna miradi mbalimbali inayoendelea. Niwaombe Wabunge, kuna miradi 763 ambayo imeshaletwa Bungeni, lakini pia tuna hayo maeneo ambayo ni 216 ambayo yameshafanyiwa tathmini.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliombe Bunge lako Tukufu, wajaribu kupitia katika ile miradi pale ambapo Mheshimiwa Mbunge atagundua kwamba maeneo anayoyasema bado hayajaingizwa katika mpango wa utekelezaji, basi Serikali tutayapokea kwa ajili ya kufanya hatua stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri Kata ya Kinyamsindo, Lahoda pamoja na Sanzawa zilishafanyiwa tathmini kwa ajili ya kujengewa minara. Je, ni lini sasa wataziingiza kata hizi kwenye zabuni ili zitangazwe na hatimaye wananchi wetu waweze kupata mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Kunti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tuna miradi ambayo inaendelea na pili kuna miradi 763 ambayo tayari Serikali imeshatangza zabuni, lakini vile vile tuna vijiji 216 ambavyo Serikali tayari imeshavifanyia tathmini. Kwa hiyo, tunaamini kwamba kwa kadri fedha itakapokuwa inapatikana, tunaamini kwamba vijiji hivyo, ikiwa pamoja na kata hiyo itaingizwa katika utekelezaji ili kuhakikisha kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi ianendelea kutekelezwa kwa niaba ya Rais wa Tanzania. Ahsante sana.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ujenzi wa Mnara katika Kata ya Itetemia uliokuwa umeanza umesimama kwa takribani miezi mitatu sasa, hakuna mwendelezo wowote. Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa mnara huo ili wananchi wa Kata ya Itetemia waweze kupata mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa, Mbunge wa Tabora, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Itetemia na eneo la Itetemia, mradi unaojengwa pale unajengwa na kampuni ya Halotel na kwa sababu tulikuwa na changamoto ya vifaa ambavyo vilikuwa vimeletwa lakini vilikuwa vime-miss baadhi ya vipuri. Tumehakikishiwa kwamba vipuri sasa vipo njiani na pindi vitakapofika Kata hii ya Itetemia na mnara wake wa Halotel utakuwa kamili na utawashwa kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Vijiji vya Katesh, Endagulda pamoja na Yaeda Jimbo la Mbulu Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Manyara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Katesh, Endagulda pamoja na Hhayeda ambayo yanatoka katika Jimbo la Mheshimiwa Flatei Massay, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Asia Halamga kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kufuatilia katika Mkoa wa Manyara, kuhakikisha kwamba huduma ya mawasiliano inaimarishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, maeneo yote haya yote matatu ambayo ameyataja Mheshimiwa Asia Halamga tayari tumeyaingiza katika mradi wetu wa minara 763.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa kuiweka Kata ya Ikindwa kwenye mpango wa kujenga mnara katika zabuni iliyopitishwa mwezi Oktoba, lakini nina swali la nyongeza kuhusu Kata ya Karitu. Miaka miwili, mitatu iliyopita, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulifanya tathmini kwenye Kata hii ya Karitu na ukabaini kuna upungufu wa mawasiliano na ukaingizwa kwenye zabuni. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kinachotakiwa kufanywa ni kutangaza upya, kuingiza upya Kata hii ya Karitu kwenye zabuni, badala ya kwenda kufanya tathmini upya kwa sababu kazi ya tathmini ilishafanyika na ndio maana kata hii iliingizwa kwenye zabuni miaka miwili, mitatu iliyopita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Serikali ilifanya tathmini katika maeneo haya, lakini kulingana na uwekezaji mbalimbali wa makampuni ambayo ni tofauti kabisa na uwekezaji wa Serikali, inawezekana kabisa mahitaji yanayohusika yanaweza kubadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo, kama nilivyojibu katika swali la msingi ni kwamba maeneo ambayo yalikuwa yameshafanyiwa tathmini katika Jimbo la Bukene yalikuwa ni mengi lakini tunaenda hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Tayari Kata ya Ikindo imeshaingizwa katika mradi ambao umeshatangazwa tarehe 22 Oktoba. Tunaamini kwamba kulingana na fedha zinavyozidi kupatikana basi na hii Kata ya Karitu na yenyewe itaingizwa katika utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Nyaruhande, Shigala, Wilaya ya Busega hazina minara ya mawasiliano, je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika kata hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Mkoa wa Simiyu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Nyarukande tayari imeingizwa katika utekelezwaji wa miradi 763. Kwa hiyo tuombe tu kwamba utaratibu utakapofika katika maeneo hayo, basi wananchi waandaliwe kwa ajili ya kutoa maeno kwa ajili ya ujenzi wa minara hiyo. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali moja; je, ni lini Serikali itaweka minara ya mawasiliano kati ya Manyoni na Tabora?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Genzabuke, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba eneo la Manyoni - Tabora bado lina changamoto ya mawasiliano na kwa sababu tunatekeleza kwa kadri fedha inavyopatikana, tunaamini kabisa kwamba katika eneo hili, tunalichukua na tunahakikisha kwamba tunaenda kulifanyia tathmini na tuangalie upana wa tatizo jinsi lilivyo ili tukachukue hatua ya kuhakikisha kwamba mawasiliano katika eneo hilo yanapatikana.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Mamba Kusini iliyopo katika Jimbo la Vunjo, kuna shida kubwa ya mawasiliano.
Je, ni lini Serikali inaweza kurekebisha tatizo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupokea changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Vunjo ili tukaifanyie tathmini ili sasa tuweze kufikisha mawasiliano katika eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na juhudi nzuri za Serikali za kujenga minara, badala ya kuijaza Tanzania na utitiri wa minara, ni lini sasa itakuja na teknolojia ya kutumia mnara mmoja ili kuepusha nchi nzima kuwa na utitiri wa minara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari teknolojia ya kutumia mnara mmoja inatumika hapa nchini. Tunaita core location, core location maana yake kwamba Tigo inakuwepo pale pale, Airtel inakuwepo pale pale, Voda inakuwepo pale pale, kampuni zote zinakuwepo pale pale. Changamoto inayokuwepo ni katika maslahi ya hizo kampuni wanapo- share wanaona kama vile wananyang’anyana wateja. Kwa hiyo, hii ni changamoto ambayo inawahusu mobile network operator moja kwa moja, ambapo wao ndio wanaweza kuamua kwamba waende ku-share ama kutoku-share, kulingana na maslahi ya kibiashara zaidi. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongezaa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe masikitiko yangu, Kata ya Ukata haina mnara wa Vodacom. Watu wa Vodacom walikuja wakajenga mnara kata ya Ukata ukakamilika lakini baadae wakauporomosha waliko upeleka hatujui. Pia hiyo minara ya Halotel ya Kata ya Kipololo Kijiji cha Lunoro na kijiji cha Litoho kweli imejengwa lakini haijawashwa tangu mwaka 2017 hadi leo sasa niombe Serikali itueleze itatupa lini mawasiliano katika hivi vijiji nilivyo vitaja?
Mheshimiwa Spika, la pili, Kata hii ya Kihangimahuka iko kilometa 25 kutoka Mbinga Mjini lakini hadi leo haina mawasiliano. Niombe ule mchakato uharakishwe ili wananchi hawa nao wapate mawasiliano, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, minara hii ilijengwa na inapojengwa baada ya hapo tunafanya technical auditing na baada ya kukamilisha technical auditing maana yake kwamba wanawasha; lakini kuna scenario mbili ambazo huwa zinatokea, ya kwanza wanaweza wakawasha baadaye kukawa na changamoto ya vifaa ambavyo wametumia. Shoti hizo huwa zinatokea lakini baada ya hapo huwa tunatoa maelekezo ya namna ambavyo wanatakiwa kwenda kurekebisha.
Mheshimiwa Spika, changamoto ilikuwepo hapa katikati ni changamoto ya uzalishaji wa vifaa, ambayo tumekuwa nayo kutokana na janga ambalo lilikuwa limetoka katikati. Nchi zote Afrika inawezekana kabisa supplier anakuwa ni yule yule kiasi kwamba tunajikuta tunakuwa kwenye queue ya kusubiri vifaa hivyo viweze kuzalishwa na ili waweze kununua na kulete kwa ajili ya kurekebisha katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, lakini vile vile suala la Kata ya Hukata, ni kweli kabisa nakiri, Kata ya Hukata ambayo nafahamu kabisa ndipo ambapo Mheshimiwa Mbunge anatoka. Nalijua tatizo hili kwa upana huo lakini kilichofanyika ni kwamba baada ya kujenga mnara katika kata ile na scope ya eneo ambalo ilitakiwa kupata mawasiliano haikuwezekana ikabidi tuhamishe mnara uende sehemu nyingine ili kuweza kufikisha mawasiliano katika eneo la Hukata.
Mheshimiwa Spika, changamoto iliyokuwepo; changamoto iliyopo ni kwamba mawasiliano yaliyopo pale kwa sasa bado ni hafifu, kwa hiyo sasa tunaandaa timu yetu iende ikajiridhishe na kuona namna gani sasa tutaenda kulitatua kwa ukubwa wake, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Ni kweli kabisa Kampuni za Vodacom na Tigo zinatoa huduma katika kata hii, lakini kutokana ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kata hii, maeneo mengi yamekuwa na changamoto ya mawasiliano. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha inashughulikia changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kuweza kuwezesha Kampuni ya Airtel na yenyewe inaweka minara katika kata hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Serikali kupitia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha kwamba inaboresha mazingira ya mawasiliano nchini kote. Vile vile kwa kuangalia katika jibu langu la msingi hasa hasa katika Kata hii ya Mamba tayari kuna mnara mwingine ambao unajengwa katika kata hii ambapo naamini kabisa utakapokamilika suala la mawasiliano litakuwa limeboreka kabisa, ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Naipongeza Serikali na hasa katika Jimbo langu la Nkenge wilaya ya Misenyi. Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja nimejengewa minara minne na hivyo kupunguza tatizo la mawasiliano. Hata hivyo, kama tunavyojua Jimbo la Nkenge linapakana na nchi ya Uganda muda mwingi tunapata mawasiliano ya simu na redio kutoka nchi Jirani. Je, ni lini sasa Serikali itaendelea kumaliza changamoto ya minara katika kata nyingine zilizobaki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nakumbuka tulifanya ziara mpakani kule, tukatembea wote, tukajionea hali halisi. Baada ya kuona hiyo hali ya changamoto ya mawasiliano, Serikali iliamua kumpelekea minara minne ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja. Kwa hiyo tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa minara katika Jimbo la Misenyi. Ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Katika Jimbo la Kilwa Kaskazini Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga minara 37 katika vijiji 37 vya Jimbo letu la Kilwa Kaskazini na hivyo vijiji 16 vimebaki vikiwa havina mawasiliano ya simu za mkononi.
Je, ni lini Serikali itajenga mitandao ya mawasiliano ya simu ya mkononi katika vijiji hivyo 16 vilivyobaki?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika jimbo hili ni zaidi ya asilimia 70 na sasa Wizara yetu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeandaa timu ya kuzunguka nchi nzima na kufanya tathimini na kuangalia maeneo yote ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano ili yaweze kuingizwa kwenye utaratibu wa utekelezaji. Kwa hiyo, naamini kabisa timu hii itakapokamilisha kazi yake, basi tunaamini kwamba bajeti tutakayoileta hapa itakuwa inatazama kwa mapana kulingana na matatizo ya changamoto ambazo zitakuwa zimetokea katika Jimbo la Kilwa Kaskazini. Ahsante.
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Kata ya Sindeni pana Kituo cha Afya cha Tarafa ambako mawasiliano ni shida kabisa. Vilevile katika Mji wa Mkata ambako ni Makao Makuu ya Halmashauri, imejengwa Hospitali ya Halmashauri pamoja na Makao Makuu ya Halmashauri kilometa nne tu kutoka katikati ya mji, lakini mawasiliano yanasuasua: Je, ni lini Serikali itafanya hatua za makusudi kabisa kuhakikisha taasisi hizo za kiserikali zinapata mawasiliano ili mifumo ifanye kazi na wananchi kupata huduma stahiki haraka iwezekanavyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ushirikiano wake mzuri ambao ametupatia hasa pale nilipofanya ziara katika Jimbo lake. Katika eneo hili ambalo ni la Sindeni, natambua kabisa kwamba kuna changamoto ya mawasiliano ambapo kulikuwa na mnara uliokuwa umejengwa kilometa 21 kutoka Makao Makuu ya Kata ambao haukuweza kufikisha huduma ya mawasiliano maeneo ambapo hiki Kituo cha Afya kilipojengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuahidi kwamba wataalamu wetu wataenda pale, watafanya tathmini, watakapojiridhisha ni namna gani tufanye, basi tutaingiza katika mpango wa utekelezaji. Kwa upande wa Kata ya Mkata ni kilometa nne. Kwa aina ya spectrum ambazo tunatumia nine hundred na eighteen hundred, ukiangalia hapa bado iko katika range. Kikubwa hapa, tutaenda kuliangalia tatizo ili tuweze kuongeza nguvu ya minara iliyopo katika Kata hii ya Mkata ili kuhakikisha kwamba Halmashauri na Hospitali zilizopo katika maeneo haya ambayo ni kilometa nne, zinapata huduma ya mawasiliano bila kuwa na changamoto yoyote, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naipongeza Serikali na ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika Jimbo la Mbulu Mji. Swali langu ni dogo: Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutekeleza mpango wake wa bajeti wa miaka miwili wa Kata za Gunyoda, Silaloda na Marang kuweka minara kwa kuwa alijionea hali halisi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Vijijini kuwa kata hizo ambazo amezitaja tayari ziko katika mchakato wa zabuni ambayo imefunguliwa jana. Kwa hiyo, tunaamini kwamba mchakato wa evaluation utakapokamilika, tutaelewa kwamba ni mtoa huduma gani ambaye amepatikana kwa ajili ya Mbulu Vijijini? Ahsante. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kakonko au Jimbo la Buyungu lina Kata 13. Kata zenye uhakika wa mawasiliano ni tano tu. Kutokana na hali hii, ndiyo imepelekea kuleta swali hapa Bungeni.
Je, Serikali inatoa kauli gani kwa kata nane ambazo ni Nyamutukuza, Nyabibuye, Gwarama, Kasoga, Rugenge, Gwanombo, Katanga na Mgunzu ambazo bado zina matatizo ya mawasiliano ya simu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana nami Buyungu ili aweze kuliona na kubaini tatizo hili ambalo nalitaja sasa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Aloyce kwa kazi kubwa anayoifanya, na kwa kweli ameendelea kushirikiana na Wizara kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za mawasiliano ndani ya jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo ambalo lina Kata 13, Kata tano zina uhakika lakini vile vile kuna Kata karibia tano nyingine ambazo mawasiliano yapo lakini bado kuna changamoto mbalimbali ambazo naamini baada ya kuzifanyia kazi tatizo lake litaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitumie fursa hii, kwa sababu kwa uwepo wa TCRA kwa mujibu wa Sheria Na. 12 ya mwaka 2003, inaipa TCRA mamlaka ya kuhakikisha huduma ya mawasiliano inatolewa kwa ubora unaotakiwa. Sasa niwatake waende katika Jimbo la Buyungu wahakikishe kwamba wanaenda kufuatilia na kuangalia quality of service kama inaridhisha katika jimbo hili ili wananchi wa Buyungu waweze kupata huduma ya mawasiliano ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile jambo lingine, Kata ya Katanga, Kasuga pamoja na Kata ya Gorama ambapo Mheshimwa Mbunge ndipo anapotoka; Gwarama ni kweli kabisa hakuna kabisa mawasiliano, lakini hii Kata imeingizwa katika mradi wa Special Zone and Boarders ambapo utaanza kutekelezwa muda siyo mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine Kata ya Katanga, Kasuga pamoja na Kata ya Gwarama ambapo Mheshimwa Mbunge ndiyo anapotoka. Gwarama ni kweli kabisa hakuna kabisa mawasiliano lakini hii Kata imeingizwa katika mradi wa Special Zone and Boarders ambapo utaanza muda si mrefu katika kutekelezwa. Mkandarasi katika eneo hilo amepatikana (Vodacom) na kwa hiyo tunaamini ndani ya miezi miwili, mitatu, ujenzi wa minara katika maeneo haya utakuwa umeshaanza na kwa hakika vijiji ambavyo viko katika Kata ya Katanga ambavyo ni vijiji viwili, Kata ya Kasuga vijiji vinne na Gwarama vijiji vitatu, tunaamini kwamba, wananchi wa maeneo haya watanufaika na huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Bukura kwa maana ya Kirongwe, Roche, Goribe na Ikoma ni Kata zilizoko mpakani na Mheshimiwa Waziri nafikiri unazifahamu hizi, lakini ni Kata ambazo hazina huduma yoyote ya mawasiliano. Pamoja na kwamba, Mkandarasi amepatikana ninataka nijue commitment yenu ni lini Mkandarasi huyu ataanza ujenzi wa minara kwenye maeneo haya ya mpakani kati ya Tanzania na Kenya?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Mheshimiwa Mbunge jana tuliwasiliana na nikamhakikishia ndani ya miezi miwili mitatu tayari ujenzi utaanza. Ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana kwenye mitandao ya simu, hasa Vodacom, ukiwa unaongea ina-stuck au inakoroma huku inaendelea ku-charge. Ningependa kujua nini tatizo katika mitandao hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Mkoa wa Kagera, vilevile suala hili Mheshimiwa Waziri tayari ameshaunda timu ya kuzunguka nchi nzima kujiridhisha na huduma za mawasiliano nchini. Ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto kama hizo, lakini tunaamini timu hii itakapokamilisha kazi yake basi tutachukua hatua stahiki ili wanchi wapate mawasiliano ya uhakika. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Jimbo la Babati Vijijini kwenye Kata za Gidas na Ufana na kuahidi kwamba, ataleta minara ya mawasiliano. Je, ni lini ahadi hii itatimizwa ili wananchi wapate mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa nimeshafika katika Jimbo la Babati Vijijini na katika Kata ambazo Mheshimiwa Sillo ameziongelea, tayari zimeingizwa kwenye mradi wa Tanzania kidijitali, tenda hiyo ilifunguliwa Tarehe 31 Januari, hivyo tunasubiri majibu ili tujue kwamba, ni Mkandarasi gani anapatikana kwa ajili ya vijiji hivyo. Ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali linguine la nyongeza. Pamoja na mjibu mazuri ya serikali lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa minara ya simu au huduma za simu zinafanywa kibiashara, na mwananchi anaponunua vocha yake au internet anadhamiria apate huduma kulingana na pesa aliyoweka. Hata hivyo, cha ajabu kutokana na kasi ndogo ya hii minara au hizi huduma za simu, wananchi wanafikia mwisho wa muda wa kutumia ile fedha yake ilhali hajapata huduma aliyokusudia. Sasa swali langu: -
Je, kwa kuwa hizi fedha za hawa wananchi wangu zinazokuwa zimetumika ilhali hawajapata huduma, je hizi kampuni za simu ziko tayari kuwafidia hao wananchi wetu ambao pesa zao zimetumika bila kupata huduma kwa sababu inaonekana huu ni wizi kama wizi mwingine?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa labda niseme kuwa minara amabayo imejengwa katika hizi kata 4 ambapo Mheshimiwa Mbunge ameonesha kulalamikia huduma inayotolewa pale, inatoa huduma ya 2G peke yake, haijaanza kutoa huduma ya 3G. Sasa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaenda ku-upgrade minara hii amabyo ilikuwa inatoa huduma ya 2G kwenda kwenye 3G, ambapo tukishafikia kwenye 3G na 4G maana yake kwamba Mtanzania na mwananchi wa Ulyankulu ataweza kutumia huduma ya internet bila kuwa na changamoto yoyote ile, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kata ya Masisiwe haijawahi kuwa na mnara wala mawasiliano tangu uhuru wa nchi yetu.
Je, ni lini Serikali itajenga mnara katika kata hiyo ili wananchi waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali ilileta vijiji ambavyo vinaenda kupatiwa mawasiliano ikiwemo kata ya Masisiwe. Mheshimiwa Mbunge tayari tushawasiliana na iliingizwa kwenye mradi wa Tanzania ya Kidigitali, mradi amabao umefunguliwa tarehe 31 Januari, 2023. Hivyo basi mchakato wa tenda utakapokamilika tutajua kwamba ni mtoa huduma gani ambaye amepatikana kwa ajili ya kufikisha mawasiliano katika kata ya Masisiwe.
Mheshimiwa mwenyekiti, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Tumbakose na kata ya Kimaha mawasiliano ni hafifu sana, naomba kujua commitment ya Serikali kwenda kujenga mnara maeneo hayo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Monni, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo hayana kabisa huduma ya mawasiliano tunatumia Sheria yetu Namba 11 ya mwaka 2006 iliyoanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwenda kufikisha mawasiliano kwenye eneo hilo. Lakini kama mawasiliano ni hafifu na kuna changamoto ya ubora wa mawasiliano kwa Sheria yetu Namba 12 ya mwaka 2003 iliyoanzisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, tunaielekeza Mamlaka ya Mawasiliano TCRA iende ikapime ubora wa mawsiliano ili tujiridhishe changamoto ipo wapi, ili tuhakikishe kwamba wananchi wa Chemba wanapata mawasiliano ya hakika na ubora unaotakiwa, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Katika Jimbo la Newala Vijijini kuna changamoto kubwa ya mawasiliano hasa katika kata za Chitekete, Makukwe na baadhi ya vijiji vya Nambali na Mkomatu.
Je, ni lini Serikali italeta mawasiliano katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa jimbo la Newala Vijijini lina changamoto, na mimi nilishafika kule; lakini Jimbo hili baadhi ya kata tuliziingiza katika utekelezaji wa miradi wa Special Zones and Border,s lakini vile vile baadhi ya kata tumeziingiza kwenye Mradi wa Tanzania ya Kidigitali. Pamoja na hayo yote Mheshimiwa Waziri pia amepanga timu moja ya kuzunguka na kujiridhisha katika maeneo ambayo yana changamoto kubwa ili tuyapatie kipaumbele, tunaamini kwamba timu hiyo itakapoleta majibu ya tathmini Waheshimiwa Wabunge tutaweza kuwahudumia kwa sababu ni dhamira ya Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata huduma ya mawasiliano, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Katika Jimbo la Kilwa Kusini Kata za Kikole, Kata za Kiranjeranje hususani Kijiji cha Makangaga, Kata ya Nanjilinji hususani Kijiji cha Nakiu na Kata ya Lihimalyao hususani Kijji cha Mangisani na Kisongo hakuna kabisa mawasiliano. Je, ni nini mpango wa Serikali kwenda kujenga minara kwa ajili ya mawasiliano katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali dhamira yake ni kuhakikisha kwamba inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 – 2025. Sisi kama Serikali maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja naomba niyapokee ili twende tukayatazame kwa upana, tutume Timu Maalum ikafanye utafiti na tathmini ili tujiridhishe kwamba tatizo kubwa ni mawasiliano hafifu au hakuna kabisa ili tuweze kuona kwamba ni njia ipi itaenda kutatua tatizo hili, ahsante sana.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ninaishukuru Serikali kwa kutuwekea mpango mzuri wa kutuletea minara katika Jimbo letu. Hata hivyo, Jimbo la Muhambwe lina mnara mmoja tu wa TTCL ambao umelemewa na badala yake inatumia kufanya roaming kwa minara ya kampuni nyingine.
Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuweka minara mingi ya TTCL ili tuweze kupata usikivu lakini pia mawasiliano ya bei nafuu?
(b) Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali pia kwa kutuletea kifaa hicho ambacho kitaenda kuboresha usikivu wa TBC Redio katika Jimbo letu, hata hivyo usikivu wa TBC Redio katika Jimbo letu ni hafifu sana inayopelekea wananchi wa Muhambwe kusikiliza zaidi Redio ya Burundi kuliko ya TBC Redio.
Je, nini mkakati wa Serikali kuboresha zaidi usikivu wa Radio katika Jimbo zima la Muhambwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, hivi leo nimejulishwa na Mheshimiwa Waziri amekuwa akiwasiliana nae kukumbushia kuhusu zile ahadi zake katika kipindi cha kampeni, Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo na ahadi hizo ambazo zinalenga katika Wizara yetu zitafanyiwa kazi zote. Vilevile suala la usikivu kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi ni kwamba kifaa hiki kitakaporejeshwa na kufanyiwa majaribio nina uhakika kabisa kwamba tatizo la usikivu katika Jimbo la Muhambwe litakuwa limemalizika kabisa. Ahsante. (Makofi)
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana changamoto za mawasiliano kwa Jimbo la Muhambwe zinafanana sana na changamoto za mawasiliano kwa Jimbo letu la Muheza katika Tarafa ya Amani ambayo ni Kata ya Amani Kisiwani Mbomole, Misalai, Zirai na Kwezitu: -
Je, ni lini sasa Serikali inakwenda kujenga minara ya simu ili kutatua changamoto ya mawasiliano kwa wananchi wa Tarafa ya Amani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwekeza kuhakikisha kwamba inatatua changamoto ya mawasiliano kulingana na maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Jimbo la Muheza tumeliingiza katika mpango wa utekelezaji wa mradi wa Tanzania kidigitali, hivyo tunaamini kwamba kabla ya mwaka wa fedha huu haujaisha zabuni hii itakuwa imeshatangazwa na hatimaye mtoa huduma atapatikana kwa ajili ya Jimbo la Muheza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru sana Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nawuye na Naibu wake Mheshimiwa Kundo, kwa ushirikiano mkubwa walionipatia kuhusu hili suala la mawasiliano ya mitandao na kwa majibu mazuri haya ya Serikali sina swali la nyongeza ila niwaambie wana Igunga subiri neema ya mitandao ya simu. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kupokea shukrani na pongezi kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wangu kwa ushirikiano ambao tunawapatia Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu kazi yao ni kuwawakilisha wananchi wao, ahsante.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika,
ahsante sana kwa kunipa fursa; je, Serikali ina mpango gani kuboresha mawasiliano ya simu ya katika Kata za Urushimbwe, Kibosho Kati na Mabogini, zilizopo katika Jimbo la Moshi Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya katika wananchi wake wa Jimbo la Moshi, lakini vilevile katika kata ambazo amezitaja Urushimbwe, Kibosho Kati pamoja na Mabogini, tayari tumeziingiza kwenye mradi wa Tanzania kidigitali. Vilevile Mheshimiwa Mbunge wiki mbili zilizopita alifika ofisini kwetu tukakaa tukaongelea kuhusu suala la kata hizi tatu na alihakikisha kabisa kwamba tayari tumeshaziweka kwenye utekelezaji wa mradi wa Tanzania kidigitali. Nakushukuru sana.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pia niipongeze Wizara na Mheshimiwa Naibu Waziri aliyetembelea Wilaya ya Misenyi na kuahidi kufunga minara katika kata kumi na mpaka sasa ameongea kata tatu zimeshafungiwa minara bado kata saba. Je, ni lini sasa kata hizo zitamaliziwa kufungiwa minara ili wananchi wapate mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kuna kata ambazo tuliziingiza katika utekelezaji wetu na tayari hatua za awali za ujenzi huo zimeshaanza. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira wakati utekelezaji huu ukiendelea kufanyika kwa wakandarasi wetu wa ndani.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza la nyongeza. Kata ya Suruke imeshajengwa mnara wa TTCL, lakini leo una mwaka mzima haufanyi kazi. Je, ni lini Serikali itawasha mnara ule wananchi waweze kupata huduma ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa minara una hatua, hatua ya kwanza ni kuhakikisha kwamba tunajenga ile passive equipment maana yake kusimamisha ule mnara. Hatua ya pili ni kuweka vile vifaa vya kurusha mawimbi maana yake active equipment. Hatua ya kwanza katika minara yote ya TTCL nchi nzima tumeshamaliza na hatua inayofuatia ni kuhakikisha kwamba sasa tunaweka zile active equipment. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira, kazi hiyo imeshaanza na vifaa vimeshaingia, nina uhakika kwamba kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha hatua zitakuwa zimeshakamilika za utekelezaji katika kusimika hizo acturial equipment. Ahsante sana.
MHE. ALYOCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Kakonko, zipo Kata za Nyamtukuza, Nyabiboye, Gwarama, Kasuga, Lugenge, Gwanubu, Katanga Namguzu, zina tatizo kubwa sana la mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika kata hizo. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamamba, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kakonko, ni jimbo ambalo liko mpakani na tayari tumeshaliingiza katika utaratibu wa miradi ya mipakani. Tayari tumeshawasiliana na Mheshimiwa Mbunge na kata hizo ambazo amezitaja, zimeshaingizwa katika mpango huo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge asubiri utekelezaji kulingana na taratibu za kimanunuzi ukamilike na baada ya hapo changamoto ya mawasiliano katika Jimbo la Kakonko itakuwa imepungua kama sio kwisha kabisa.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, changamoto ya mawasiliano kwa maeneo ya Kwekivu, Kimbe, Namkindi katika Jimbo la Kilindi ni kubwa na usikivu ni mdogo sana. Je, ni lini mtakwenda kutujengea minara kwa ajili ya kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kilindi, tumeshaliweka katika utekelezaji wa Tanzania ya Kidigitali, kwa hiyo, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana ili kuhakikisha kwamba wataalam wetu watakapofika katika maeneo yao, watoe ushirikiano na kutoa maeneo kwa ajili ya kusimika miradi hii ya minara.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Maeneo mengi ya Wilaya ya Nyang’hwale, hayana mawasiliano kabisa ya simu kama Nyamtukuza, Nyalubele, Ligembe na sehemu zote ambazo ziko maeneo yale ambayo yako karibu na Nyang’hwale. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka mawasiliano ili wananchi wale waweze kupata mawasiliano mazuri?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kujibu hili. Kwa mujibu wa matakwa ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 97 Ibara ya 61(j) inatutaka Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Tanzania wanapata huduma ya mawasiliano. Hivyo basi, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu najua Mheshimiwa Mbunge wa jimbo tayari tunaendelea kuwasiliana kuhusu changamoto hizo, naamini kabisa mpango wa mwaka mmoja utakapokamilika na mpango wa miaka mitano tunaamini kwamba maeneo mengi yatakuwa yameshapata mawasiliano nchi nzima. Nakushukuru sana.
MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kumekuwa na malalamiko makubwa ya kukoseshwa fursa ZIC kama fursa inayopatikana na NIC huku Tanzania Bara: -
Je, Serikali inatuhakikishia vipi kwamba kuna mchakato sasa kuweza kuondoa malalamiko haya ili sasa Zanzibar insurance kwa sababu ipo katika mikoa zaidi ya mitano huku Tanzania Bara inaweza ikapewa fursa sawa kuweza kuingia katika miradi mikubwa ya Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Omar Salim, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba ZIC ni kampuni kama makampuni mengine. Kazi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira rafiki ya kiushindani na kuhakikisha kwamba wanaweza kufanya biashara bila kuwa na changamoto yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa kwamba Serikali ikishaweka mazingira hayo, basi hata wao watajipima kulingana na mazingira ya kiushindani, kwa sababu kwa mujibu wa Sheria Serikali haiwezi kuingilia biashara ambazo wadau wanaweza kushiriki kwa pamoja. Ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami nilikuwa na swali la nyongeza. Kumekuwa na matangazo kwa ajili ya kulifagilia Shirika la Bima la Taifa kwamba mashirika mengi ya Umma yatumie shirika hili kwa sababu ni la Umma. Hata hivyo, tukizingatia pia Shirika la Bima la Zanzibar ni Shirika la Umma pia, na tumeambiwa kwamba ni biashara huria: Kwanini na ZIC nayo isitangazwe kama ambavyo inatangazwa NIC ili iweze kufanya kazi sawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Najma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba mashirika ambayo yanasajiliwa kwa mfumo ya kampuni yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria za kikampuni na sheria za kiushindani.
Kwa hiyo, sisi kama Serikali, iwapo kunakuwa na changamoto yoyote ile, basi tutaendelea kufanya utafiti na kujiridhisha ili njia stahiki sichukuliwe kuhakikisha kwamba mashirika haya ambayo ni moja ya Mashirika ya Umma pia tuweze kuona kwamba ni mazingira yapi yatawezesha kujiendesha kibiashara zaidi. Ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Lakini yeye mwenyewe anaelewa kwamba kuna kata tisa. Kwa hiyo ukiangalia idadi ya kata ambazo zinashughulikiwa bado nyingi zitakuwa na matatizo yale yale ambayo yanaendelea na kuwapa shida wananchi.
Je, Serikali, kutokana na umuhimu wa mawasiliano kwa upande wa kiuchumi na kijamii, inatoa tamko gani la kuwapa matumaini kata zile ambazo bado zina matatizo ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Urambo, na kwa kweli ameonesha ushirikiano mkubwa pale ambapo Serikali inapohitaji msaada wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba tunatambua kabisa kwamba kuna changamoto ya mawasiliano katika Jimbo hili la Urambo ambapo jimbo hili lenye kata 18; na katika hizo kata 18 kata tisa ndizo ambazo zina changamoto, si kwamba hazina mawasiliano, zina changamoto. Kata hizo ni; Kata ya Uyumbu, Muungano, Vumilia, Busoke pamoja na Songambele. Kata zote hizo tunafahamu kabisa kwamba zina changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigital tayari tumeanza na kata tatu. kwa hiyo tunaamini kabisa kwamba tunapoenda katika utekelezaji wetu tukishakamilisha kata hizi tatu tunaamini hata zile kata sita ambazo zimebaki tutazifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto kubwa inayokabili wananchi wa Ngara ya mawasiliano ya simu ni kuingiliana na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Ninataka kujua, ni nini mkakati wa Serikali ili kutatua changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka Mbunge wa Viti Maalum Kagera kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kabisa kwamba ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge huyu ameendelea kuwa msumbufu kweli kweli kwa ajili ya kuhakikisha maeneo hayo yanatafutiwa ufumbuzi. Lakini vilevile natambua pia usumbufu ambao nimeendelea kuupata kutoka Mbunge wa Jimbo la Ngara Mheshimiwa Ndaisaba kwa sababu haya maeneo tuliyatembelea na tukagundua kabisa kuna changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo; ya kwanza, si kwamba hatuna minara, kuna maeneo ambayo tuna minara lakini nguvu yake haikuwa inatosha. Hivyo tulitoa maelekezo kwa watoa huduma kuhakikisha kwamba minara yao inakuwa na nguvu ili huu mwingiliano usitokee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna maeneo mengine ambayo hatukuwa na minara ndiyo maana mwaka jana sasa kupitia mradi wa special zone na borders, yaani mipakani na maeneo maalum, tulihakikisha kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo tunaenda kujenga minara yakiwemo maeneo ya Ngara ambapo kuna miradi tisa ambayo inaenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya changamoto ya mawasiliano ambayo Mheshimiwa Waziri anakiri watu wamekuwa wakinunua bando, kwa sababu ya kuingia na kutoka kwa internet mtu anajikuta bando lake lina-expire kabla wakati hajalitumia. Sasa, kwa sababu hiyo, Je, Serikali haioni ipo haja ya kutengeneza utaratibu bando liwe linachajiwa kwa matumizi kwamba linaisha kwa sababu umetumia badala ya kuchajiwa kwa sababu muda wa lile bando umekwisha?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salome Makamba Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kulikuwa na changamoto hiyo lakini Serikali ikalitambua hilo na njia pekee ya kutatua changamoto hiyo ni Serikali tulitoa maelekezo ya kuhakikisha miradi yote inayojengwa nchini sasa inajengwa ikiwa na uwezo wa kutoa huduma ya internet hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tulibadilisha kanuni zetu pale ambapo unaona kabisa kwamba muda wako unaelekea kuisha lakini bando lako bado linatosha inawezekana ulikuwa umesafiri ukaenda sehemu ambayo haina internet basi utapata fursa ya kuhamisha au kujiunga na kifurushi kingine lakini na ile balance uliyokuwa nayo unai- carry forward.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kupitia hizi njia ambazo Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba inaboresha huduma ya mawasiliano tunaamini kabisa kwamba kupitia njia hizi na mabadiliko ya kanuni zetu itawezesha wananchi kutumia bando lao na mpaka linaisha. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kata ya Roche, Ikoma, Bukura pamoja na Goribe ni miongoni mwa kata ambazo ziko mpakani kati ya Tanzania na Kenya. Mheshimiwa Waziri nafikiri ulipata ridhaa ya kuzitembelea kata hizi ukaona hazina mnara na hakuna mawasiliano yote katika kata hizi. Nilitaka nijue katika zile minara ambayo umesema wanaitangaza mwezi Juni kama kata hizi nazo zinapata nafasi ya kutangaziwa ili waweze kupata mnara kuboresha na kuweka mawasiliano kwenye maeneo haya ya mpakani na kimkakati?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana Mheshimiwa Chege kwa sababu tumekuwa tukishirikiana vizuri sana; na maeneo na kata ambazo amezitaja Mheshimiwa chege tulishafika katika maeneo hayo. Vilevile katika mpango wa utekelezaji wa Tanzania Kidigitali tayari maeneo haya tumeyaingiza na Mheshimiwa Chege tayari anafahamu hilo. Kwa hiyo. kilichobaki sasa ni utekelezaji tu na tayari mkandarasi yuko tayari kwa ajili ya kuanza kazi mara moja kwa ajili ya maeneo hayo katika Jimbo la Rorya. Ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwa kweli ni matumaini yangu kwamba wananchi wa Micheweni watafarajika pindi watakaposikia majibu haya ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo nina swali moja la nyongeza. Mara nyingi imezoeleka katika Shirika la Posta wakati wanapotoa ajira wanachukua waajiriwa kutoka katika maeneo mengine. Je, Mheshimiwa Waziri ananihakikishiaje, pindi watakapofungua ofisi hii katika ajira ambazo watatoa watazingatia kipaumbele au wataweka kipaumbele kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi ambayo anaifanya kwa ajili ya wananchi wa Wingwi. Lakini vilevile ameendelea kuhakikisha kwamba anatupatia changamoto zinazoendelea ndani ya jimbo lake. Sisi kama Serikali tunaendelea kuzipokea na kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, lakini pili suala la ajira linafahamika kabisa kwamba mashirika yetu haya yanaajiri kwa kupitia utaratibu wa utumishi wa umma. Hivyo basi, tunaamini kabisa kwamba mfanyakazi yeyote, au yeyote ambaye ni Mtanzania ana haki sawa kuomba kazi na kupatiwa kazi kulingana na vigezo ambavyo vitakuwa vimewekwa.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Baada ya uzinduzi wa Royal Tour kumekuwa na ongezeko kubwa sana la watalii ndani ya Jimbo la Hai, lakini moja ya changamoto inayoikumba sekta hii ni mawasiliano. Hoteli za kitalii zilizoko kwenye geti la kuingia Machame ambapo Naibu Waziri ameshafika hazina mawasiliano kabisa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta mawasiliano ndani ya Jimbo la Hai?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni jukumu la Serikali kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 61(j) inatuelekeza kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano kwa Watanzania wote. Vilevile specifically kwa maeneo ya Jimbo la Hai mimi binafsi nimeshafika katika maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge na kweli kabisa tayari tumeshayachukua na tayari wataalam wameshafanya tathmini na tunayaingiza kwenye mpango wa utekelezaji wa Tanzania ya Kidigitali. Kwa hiyo naomba tuendelee kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba mawasiliano tunayafikisha huko, lakini tuwaandae wananchi wetu tutakapohitaji maeneo kwa ajili ya ujenzi wa minara hiyo, watupatie ushirikiano ili mawasiliano yaweze kufika. Ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Katika Jimbo langu la Donge kuna majengo ambayo yamejengwa zaidi ya miaka 20 iliyopita na wenzetu hawa wa Posta na Simu. Majengo yale mpaka leo hayakutumika na yanaendelea kuzeeka na kuchakaa hivi sasa. Sasa namwomba tu Mheshimiwa Waziri kama yuko tayari aidha tufuatane na kumwomba awaachie wananchi wa Jimbo la Donge watumie yale majengo kwa shughuli zingine za maendeleo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Soud, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania majengo yake mengi ni ya siku nyingi, lakini mpango wa uliopo ndani ya shirika letu ni kuhakikisha kwamba tunaboresha vituo vyetu vya mikoani. Kwa majengo yetu yaliyoko katika upande wa wilaya baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ambayo ni mikoa baadaye tutashuka mpaka kwenye wilaya na hatimaye majengo yote yataanza kufanya kazi iliyotajiwa na Watanzania. Ahsante.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna changamoto kubwa sana ya mawasiliano katika Jimbo la Babati Vijijini hasa Tarafa za Bashnet na Goroa na pia Mheshimiwa Naibu Waziri alishafika. Je, ni lini Serilkali itaanza kujenga minara ili wananchi wetu waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Sillo kwa sababu nilifanya ziara katika jimbo lake na tulitembea wote na tulijionea hali halisi, lakini habari njema kwa ajili ya wananchi wa Babati ni kwamba kata ambazo amezitaja tayari zipo kwenye mpango wa utekelezaji wetu. Hivyo basi, wananchi wa Babati wasubiri tu hatua za manunuzi zikamilike. Hatua hizo zikishakamilika basi nimwombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanatupa maeneo ambayo hayana migogoro kiasi kwamba tukiweka minara yetu isiingie kwenye migogoro ya ardhi. Ahsante sana.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hamasa kubwa iliyofanywa na Serikali kuhusu matumizi ya teknolojia iliyosababisha wananchi wengi kutumia mtandao wa internet: Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwa na bundle maalum kwa ajili ya wajasiriamali wadogo litakalowasaidia kutafuta masoko kwa njia ya mtandao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Ni lini sasa Serikali itahakikisha taasisi zote za elimu zinakuwa na huduma ya Wi- Fi itayaowasaidia walimu na wanafunzi kuongeza maarifa, na vilevile kutoa mchango wao katika ulimwengu wa elimu duniani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge alishaleta maombi yake kuhusu vikundi na vikoba kwa ajili ya kupata bundle maalum. Ni kweli kabisa kwamba, huwa tuna utaratibu kama maeneo ya vyuoni, na maeneo mbalimbali ambayo huwa yanapata special offer. Hilo tumeshalipokea na Serikali bado inalifanyia kazi, na pale ambapo tutakuwa tumekamilisha, basi tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele cha pili; ni wazi kabisa kwamba huu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 61 (h), inayotutaka kuanzisha huduma ya mawasiliano ya internet ya kasi katika maeneo yote ya umma (Public Place) ikiwemo maeneo ya hospitali, taasisi za elimu na vituo vya usafiri hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshaanza. Kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi, tumeshajenga vituo sita, na mwaka huu tayari kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, tumejipanga kwa ajili ya kwenda kufikisha huduma ya internet ya Wi-Fi katika maeneo 20 na tutaendelea kufanya hivyo mpaka tutakapofikia katika lengo la Serikali ambalo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kufikia asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna double standard baadhi ya makampuni yameondoa utaratibu wa kutumia salio la kawaida unapoingia kwenye menu za kibenki na makampuni mengine bado yanataka utumie salio la kawaida badala ya bando ulilonalo kwenye simu. Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha makampuni yote yanatoa huduma hii kwa usawa kwa kuondoa utaratibu wa kutumia salio la kawaida ili Watanzania wote waweze kunufaika na kurahisisha matumizi yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Pamoja na Serikali kusitisha gharama ya ongezeko la bando tokea Oktoba mwaka jana, kwa sasa hivi tatizo kubwa tulilokuwa nalo ni bando za kwenye simu zetu tunazoweka kuisha kwa kasi ya haraka sana. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha inaweka utaratibu maalum kwa ajili ya ku-regulate matumizi ya kasi za bando kwenye simu kama ilivyo limit kupanda gharama za matumizi ya bando kwenye simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala la kibiashara ni kama ambavyo nimejibu kwenye swali langu la msingi. Ni makubaliano kati ya mtoa huduma na benki na pale ambapo watoa huduma wanabadilisha wengine wanakuwa hawatozi ni masuala ya kiushindani ambapo sisi kama Serikali kazi yetu ni kuweka mazingira wezeshi ili ushindani uweze kutokea.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo unapotumia USSD, USSD maana yake si suala la kutuma meseji na kupokea, ni suala ambalo linakuwa linatoa options zingine ambazo mtumiaji anaweza kuona, na kuna hatua nyingi ambazo zinafanyika. Kwa hiyo, suala la kutumia bando ili uweze kukata huduma ya USSD inakuwa ni ngumu ni sawasawa na pale unapojiunga na bando halafu ukajaribu kupiga simu nje ya nchi. Hilo ni jambo haliwezekani, labda kama itawezekana tutakaa na watoa huduma ili tuangalie kama kuna uwezekano wa kuwepo na bando la USSD ili liweze kuhudumia huduma maalum.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili suala la kasi katika matumizi ya bando, kasi ni matumizi ya mtumiaji husika. Kama ana vitu vingi vya ku-download na kuna vitu vingi vya ku- upload matokeo yake ni kwamba kasi ya bando ambalo atakuwa amejiunga litaisha mapema. Kwa hiyo, naendelea kushauri kwamba watumiaji wa bando waweze kuangalia matumizi halisi katika simu zao na pale ambapo wanakuwa hawatumii basi waweze kuzima data ili data isiweze kuisha, ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali kwa kuanza kutekeleza mradi wa kujenga mnara katika Kata ya Kitanda, kupitia mradi wa Tanzania ya Kidigitali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali imetoa maelezo kwamba, Kata za Kikolo, Mbangamao na Kagugu zitafanyiwa tathmini; na maeneo hayo watu wakati mwingine wanapanda kwenye miti kutafuta mawasiliano: Nataka nijue sasa ni lini tathmini hiyo itaanza kufanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Kata ya Mpepai ulijengwa mnara ambao unaendeshwa na Kampuni ya Airtel, na wakati mwingine kunakuwa na changamoto ya mawasiliano, mtandao huwa haupatikani. Ninataka nijue ni lini sasa Serikali itafanya marekebisho katika eneo hilo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa fedha kwa ajili ya kufanya tathmini katika vijiji 2,116. Na katika upande wa Mbinga, Vijiji vya Luanda, Muhongozi, Matili na Kitanda zilifanyiwa tathmini hiyo.
Mheshimiwa Spika, lakini katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024, Kata za Kikolo na Kagugu zitaingizwa katika utaratibu wa kufanyiwa tathmini na baada ya hapo fedha zitakapopatikana zitaweza kufikishiwa huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kwa kipengele cha pili kuhusu mnara wa Airtel uliopo katika Kata ya Mpepai; changamoto ya mnara huu ni kwamba unatumia nguvu ya jua (solar energy) na tumeshakubaliana na watoa huduma kufanya mambo mawili yafuatayo; la kwanza ni kwamba pale ambapo umeme wa Gridi ya Taifa umeshafika wafanye juhudi za kuhakikisha kwamba wanaunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, na pale ambapo umeme wa Gridi ya Taifa haujafika basi wahakikishe kwamba wanaweka jenereta ili iwe njia mbadala pale ambapo solar inakuwa imezidiwa. Na hayo tayari tumeshakubaliana na hatua zimeshaanza kuchukuliwa, ni pamoja na katika eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kata za Kijirishi na Nyaruhande, Wilaya ya Busega, kuna changamoto sana ya mawasiliano ya simu.
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika kata hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, eneo ambalo amelitaja Mheshimiwa Esther Midimu ni katika vijiji 2,116 ambavyo tayari vimeshafanyiwa tathmini. Hivyo, Serikali iko katika mchakato wa kutafuta fedha ili kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Wilaya ya Ngorongoro bado ina changamoto kubwa ya mawasiliano, na Mheshimiwa Naibu Waziri analifahamu hili suala vizuri.
Je, ni lini sasa mnara wa Simu wa Jema utawashwa ili basi wananchi wa Oldonyosambu na maeneo jirani waweze kupata mawasiliano ya kutosha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Zaytun alishalifikisha jambo hili katika Wizara yetu na tayari tumeshachukua hatua. Jambo ambalo linafanyika sasa hivi ni technical audit na ikishakamilika mnara utawashwa. Ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kuna changamoto ya mawasiliano kwenye Kata za Makanya, Malibwi, Kwai na maeneo mengine katika Jimbo la Lushoto: -
Je, ni lini mawasiliano yatapelekwa katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shabani Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba inafikisha huduma ya mawasiliano nchini kote na tunakwenda kwa awamu. Hivyo, nalipokea ili wataalam wetu waende wakafanye tathmini katika maeneo hayo na tujiridhishe changamoto yenyewe iko katika upande upi ili tuweze kuchukua hatua stahiki.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itapeleka wakandarasi kwenye Vijiji vya Bokomnemera, Kimalamisale na Mpiji ambapo wana shida ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Michael Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mwakamo tayari ameshalifikisha jambo hili na tulishaongea na tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa ili kufikisha huduma ya mawasiliano katika eneo hilo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kuna matatizo makubwa na ya muda mrefu ya mawasiliano katika Mapori ya Kasindaga na Kimisi Mkoa wa Kagera: -
Je, ni lini Serikali itamaliza matatizo hayo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Conchesta kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba nipokee changamoto hii ili tukaifanyie kazi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, viko Vijiji vya Mtawatawa, Ndapata, Ndunyungu na Ndinda, ambavyo havina mawasiliano kabisa. Ni lini Serikali itaona umuhimu wa kupeleka mawasiliano kwenye vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, wataalam wetu wameshafika katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, na tayari katika orodha ya vijiji 2,116 tukitoka hapa Mheshimiwa Kuchauka tuonane ili niweze kukuonesha maeneo ambayo tayari umeyataja, yamo tayari kwenye utaratibu.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika Jimbo la Bagamoyo, Kata ya Magomeni, maeneo ya Sanzale, Kata ya Makurunge, Kamata ya Fukayosi maeneo ya Kijiji cha Mkenge, hakuna kabisa mawasiliano, ni ya shida sana. Ni lini sasa Serikali itapeleka wataalam kule kwenda kuweka minara mawasiliano yapatikane?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Muharami Mkenge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwamba tulianza na vijiji 2,116 ambapo ni katika mwaka wa fedha 2022/2023 na sasa katika awamu inayofwatia ambayo ni 2023/2024 vijiji na kata za Jimbo la Bagamoyo zitaingizwa katika utaratibu wa kufanyiwa tathmini na baadaye Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kwenda kufikisha huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. MAULID SALEH ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Nitakuwa na swali moja la nyongeza.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha mfumo wa TEHAMA na kudhibiti usalama wa mawasiliano nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maulid Saleh Ali, Mbunge wa Welezo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita inaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari imeshatoa mkakati (National Cyber Security Strategy) ya mwaka 2018, mwaka 2023 ambao ni kuhakikisha kwamba kuna usalama katika huduma zote zinazofanyika katika mtandao. Vilevile tunayo timu ambayo inaitwa Mwitikio wa Kukabiliana na Majanga ya Kompyuta (TZ-CERT) ambayo yenyewe kazi yake ni kuhakikisha kwamba pale changamoto kama hizi zinapotokea basi tunahakikisha tunaenda kuchukua hatua ili kuzuia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine tunao mfumo wetu ambao unaitwa Tele Traffic Management System ambao kazi yake ni kuhakikisha kwamba inadhibiti mambo mawili, kwanza kabisa ni kufatilia miendendo ya mawasiliano yote yanayoingia ndani ya nchi, vilevile ni kuangalia namna mapato yanavyotokea na namna ambavyo tunaweza tukaya–contrive.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utapeli hata hapa kwetu Tanzania unafanyika kwa kuomba michango na kadhalika. Je, Serikali ina mkakati gani wa kushirikiana na TCRA ili kuweza kuwaelewa wahalifu hawa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA
YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi. Ni kwamba Serikali ina mkakati maalum na zaidi ya hapo Serikali kwa kushirikiana na Vyombo vya Dola vinaendelea kuratibu na kufatilia mienendo yote ya matumizi ya simu na zile ambazo zinahusika katika utapeli basi huwa zinakamatwa na baadae tunazifungia, sambamba na hilo tunaendelea kutoa elimu kwa Watanzania ili kuelewa pale ambapo simu za namna hii zinapowafikia ili wajue kwamba ni hatua gani waweze kuchukua kwa kuwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania - TCRA.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, kwamba siyo utapeli wa simu za nje tu lakini pia kuna utapeli wa kiholela wa kuongezewa au kupandishwa vyeo humu nchini. Utapigiwa simu umeambiwa umepandishwa cheo kwa hiyo usubiri barua yako. Kwa hiyo na hili pia linatumika katika njia za simu. Je, Serikali ina mpango gani kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA
YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, utapeli unakuja kwenye picha tofauti tofauti. Kuna picha ya kutafutiwa kazi, picha ya kupandishwa vyeo kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, lakini sana sana tunachokiomba tu kwa Watanzania ni kwamba pale wanapopokea changamoto kama hizi basi waweze kuwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ili tuweze kuchukua hatua stahiki nasi tukiwa tunaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia kitengo chao cha Cyber Crimes Act. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwa ushirikiano huu basi tutaweza kuhakikisha kwamba changamoto hizi zinadhibitiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vita dhidi ya matapeli siyo vita dhidi ya Serikali peke yake, ni vita dhidi ya umma na kwa pamoja tukifanya kazi kwa pamoja tutahakikisha kweli tumetokomeza changamoto kama hii. Nakushukuru sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, Serikali inachukua hatua gani kwa matapeli wanaotumia lane za ndani ambazo zimesajiliwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA
YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema tuna mfumo unaoitwa Tele Traffic Management System, kwanza kabisa tunabaini simu ambazo zinafanya mambo ambayo hayastahiki na mpaka sasa tunatumia mfumo huo ambao unatumia simu za majaribio (Test Calls) na tukitumia baadae tunabaini na tangu Julai mwaka 2022 mpaka sasa ni takribani simu 826,951 zilibainika kufanya mambo ambayo yasiyostahili lakini kati ya hizo tayari tumeshachukua hatua na bahati mbaya sana tunapochukua hatua katika mambo haya huwa hatuyatangazi kwa sababu tunakuwa tumepeleka kwenye mamlaka ambayo yanatakiwa kutoa hukumu na katika mchakato huo bado kunakuwa na ukusanyaji wa taarifa na evidences ambazo zitafanya kwamba hukumu iweze kutoka vizuri, ndiyo maana huwa hatutangazi lakini Serikali imejizatiti kuhakikisha kwamba jambo hili linaendelea kukomeshwa, ahsante sana.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Serikali ilianzisha mfumo wa usajili wa biometric tukawa tunatumia vile vile finger prints kwa lugha nyingine ili kuweza kuwa–track ama kuwe na database ya kila mtu ambaye ana namba ya simu. Lakini ukweli ni kwamba watu wanatapeliwa kwa namba za simu ambazo zimesajiliwa. Sasa swali kwenu Serikali, unataka kukiri mbele yetu kwamba wizi wa kwenye mitandao ya simu unafanyika kwa makusudi baina ya makampuni ya simu na matapeli na mfumo wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA
YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema, changamoto ya utapeli kwanza kabisa ni jukumu letu sisi sote kushirikiana, lakini Serikali tunaendelea kutoa elimu kwa umma ili waweze kujua namna ya kujidhatiti na kupambana na changamoto kama hii. Pamoja na hivyo Serikali sasa imeendelea kuwekeza Zaidi katika mifumo ya TEHAMA ili iweze kudhibiti katika picha ya ki–technical zaidi kuhakikisha kwamba mambo haya yanaendelea kupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ki ukweli hasa kipindi cha pandemic, mambo kama haya ndiyo yanakuwa mengi zaidi, kwa sababu mawasiliano yanakuwa siyo ya moja kwa moja, simu ndiyo zinakuwa medium of communication. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA tutaendelea kuhakikisha kwamba changamoto hii inaendelea kupungua katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro kuna kata ambazo hazina mawasiliano mpaka wananchi wapande juu ya miti ndio wapate mawasiliano ; na kata hizo zina changamoto ya kuvamiwa na Tembo mara kwa mara.
a) Je, nini kauli ya Serikali ya kuwasaidia wananchi hao kupata mawasiliano ili wanapopata matatizo waweze kutoa taarifa?
b) Je,ni lini Serikali itadhibiti Wizi wa fedha za wananchi kwa kupitia simu kwa kuwa tatizo hili limekuwa ni changamoto kubwa sana katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika,napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuwena Athuman Bushiri, Mbunge Viti Maalumu Kilimanjaro kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zuwena kwa kazi kubwa ya kuwatetea wana Kilimanjaro katika masuala ya mawasiliano. Mheshimiwa Zuwena alifanya Ziara katika Tarafa ya Jipendae, na akatujulisha Serikali na tukapokea malalamiko hayo ambayo ni changamoto, na Serikali tukayafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kata ambazo Mheshimiwa Zuwena amezitaja, Kata ya Kwakoa, Kilya, Tohora pamoja na kata ya Kibisini tayari zimeingizwa kwenye utaratibu wa kupatiwa huduma za mawasiliano. Lakini katika eneo ambalo linaenda katika lango la Hifadhi ya Mkomazi pia nalo Serikali inatarajia kuingia mkataba na TTCL ili iweze kufikisha huduma ya mawasiliano katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwas wali la pili, Serikali haiwezi kupuuza malalamiko ya wananchi. Suala la wizi kwenye masuala ya simu na fedha za wananchi katika mitandao ya simu, nipende kusema jambo moja. Huduma ya mawasiliano ina wadau watatu, kuna watoa huduma, kuna watumiaji wa huduma na kuna Serikali. Serikali kazi yake ni kuhakikisha kwamba watoa huduma wanatoa huduma katika mazingira rafiki, lakini na watumiaji wa huduma wanapata huduma ambayo inaendana na haki ambazo wanazitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa maelekezo kwa TCRA kufanyia kazi malalamiko ya wananchi ili kujiridhisha na changamoto jinsi ambavyo ilivyo na kuhakikisha kwamba tunatoa majibu kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ni lini kata ya Mkindi, Kata za Masagaru, Kwekivu na Kimbe vijiji hivi vitapitiwa na minara kwa ajili ya masiliano kwa ajili ya wanachi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika,napenda kujibu swali la Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi huu wa tano Serikali inatarajia kuingia mkataba na watoa huduma ili kuweza kufikisha huduma ya masiliano katika maeneo 763. Vile vile Serikali imeshaanza kufanya tathmini katika vijiji 2116 vitakavyokamilika. Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano vikiwemo vijiji na kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amevitaja, ahsante sana.
Ahsante, Waheshimiwa tunaendelea Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Ngasa.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kumuuliza maswali mawili kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ni lini ulikwenda kukikagua kituo hiki cha Kengeja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa imepangiwa mwaka 2024/2025, je, kwa nini tusiachane na ukarabati na badala yake tukakijenga upya kutokana na hali ya kituo hiki ilivyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza, kwamba ni lini nitaenda kukagua. Ukaguzi unafanyika kila mara, naa tuna vituo nchi nzima na tunakwenda hatua kwa hatua. Tulifanya ukaguzi Shangani, Chakechake, na tayari tumeshafanya ukarabati katika maeneo hayo na fedha zitakapopatikana tutatenga muda wa kwenda kukagua ili tuweze kukarabati kutokana na mpango wa ndani unavyoendelea.
Mheshimiwa Spika, vilevile swali la pili, badala ya kujenga tunaanza na utaratibu wa kukarabati kwanza maeneo ambayo tunayo kwa sababu tayari mahali palipo ni kwamba ndiyo maeneo ambayo yanamilikiwa na Shirika la Posta Tanzania. Baada ya kuona kwamba sasa uhitaji utabadilika na mahitaji ya watu yakawa mengi tofauti na eneo lililopo, basi tutaangalia uwezekano wa kutafuta eneo lingine ili tuhakikishe kwamba tunakidhi mahitaji ya utoaji wa huduma za posta, ahsante.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Posta cha Dodoma ni kituo ambacho kimejengwa muda mrefu sana na hakiendani na hadhi ya makao makuu, nini mkakati wa Serikali wa kujenga kituo kipya cha posta cha kisasa ili kiendane na hadhi ya makao makuu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tumefanya ukarabati nchi nzima na kituo cha posta kikiwaki moja wapo. Pamoja na hivyo, tunaendelea na kutafuta maeneo ya kujenga vituo vingine vipya kulingana na Serikali kuingia makubaliano na Posta ya Oman. Tunaamini kabisa kwamba katika mradi huo ambao takribani milioni 100 USD zinaenda kutumika kujenga zile logistic park. Naamini kwamba kwa sababu Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi tutaitazama na kuhakikisha kwamba inakuwa na posta ya kisasa na yenye kutoa huduma ambazo zinaendana na mahitaji ya Watanzania.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na niipongeze baada ya kipindi cha miaka miwili baada ya ziara ya Naibu Waziri, katika jimbo langu tumekwishapata minara Minne mipya. Pia, nashukuru katika bajeti mpya sasa hiyo minara mipya minne ikienda kujengwa tutaielekeza katika maeneo yanayohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Misenyi, kama ilivyo mpakani mwa Nchi ya Uganda imekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano. Sasa ni lini minara mingine itajengwa katika Kata za Bugandika, Kilimilile, Buyango, Kitobo, Bwanjai na Mabale ili kuweza kufanya wananchi wa maeno hayo waweze kupata mawasiliano mazuri katika jimbo letu?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, wananchi wa Wilaya ya Misenyi, wamekuwa wakipata mawimbi ya redio ya nchi jirani ya Uganda. Ni lini sasa Serikali itaweka nia ya dhati kuhakikiasha kwamba wananchi wanafaidi mawasiliano ya mawimbi ya radio ya nchi yetu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunafanya feasibility study kwa ajili ya kupeleka huduma ya mawasiliano katika Kata ya Bugorora na Kakunyu hapakuwa na minara imejengwa. Lakini kwa sasa tumegundua watoa huduma kwa kutumia uwekezaji wao wamekwisha jenga minara katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa minara ambayo tulikuwa tumepanga kupeleka pale sasa tutaihamishia na kupeleka Kata ya Minzilo na tutapeleka katika eneo la Kashenye. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, wananchi wa eneo hilo pamoja na maeneo ya Kitobo na Kanyigo wote tutawaweka katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipengele cha pili, eneo la Misenyi lina changamoto ya huduma ya usikivu wa redio. Pia, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa fedha kwa ajili ya kwenda kujenga kituo katika eneo la Kyerwa ambapo tukishafunga mtambo wetu pale utaweza kufikisha huduma ya redio katika maeneo ya Misenyi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Katika bajeti hii tunayomalizia ya 2022/2023 Serikali ilikuwa imepanga kujenga minara ya mawasiliano katika Kata za Urushimbwe, Mabogini na Kibosho Kati. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na ujenzi wa minara hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Profesa Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kulikuwa na changamoto hii na Mheshimiwa Mbunge, aliwasilisha changamoto hii mara kwa mara lakini Serikali ilijitahidi sana kutafuta fedha na hatimae Mheshimiwa Rais, ametoa fedha na tunakwenda kuingia mkataba na kampuni ya Vodacom na TIGO kwa ajili ya Urushimbwe, Mabogini pamoja na eneo la Kibosho kati. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge hili tuna uhakika kwamba kati ya Mwezi wa Sita au wa Saba tayari ujenzi wa mnara huo utaanza rasmi.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga minara katika Kata ya Shigala, Nyaruhande na Kijiji cha Kijereshi ili kuboresha mawasiliano kwa sababu kata hizi zinashida kubwa ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niwajulishe watanzania, Waheshimiwa Wabunge, tarehe 13 Mei, 2023 tunakwenda kusaini Mkataba wa kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata 713 ambayo ni wilaya 127 mikoa yote, ambapo ni Vijiji takribani 1407. Watanzania takribani milioni 8.5 wanakwenda kupata huduma ya mawasiliano, ambapo Mheshimiwa Rais, ameidhinisha kiasi cha bilioni 125.9 kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeno hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wahudhurie katika hafla ya utiaji Saini wa mikataba hii ambayo inakwenda kufikisha huduma ya mawasiliano kote Tanzania.
MHE BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; Kata ya Mpui, Ikozi na Lusaka hayana kabisa minara ya simu. Ni lini sasa Serikali itajenga minara ya simu kwenye kata hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; minara iliyopo Kata ya Milepa, Zimba, Mfinga na Lusaka minara hiyo haina kabisa internet. Ni lini sasa Serikali itaweza kuweka internet kwenye minara hiyo hili wananchi wasiweze tena kupanda kwenye miti kutafuta internet? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kuhusu kata ya Mpui pamoja na Ikoze Serikali iko katika utaratibu wa kufanya tathimini na tathimini hiyo itakapokamilika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili maeneo ya Milepa pamoja na Zimba ni azima ya Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa matumizi ya internet kutoka asilimia 45 mpaka 80 Serikali imeshaanza na minara 488 katika awamu ya kwanza na katika awamu ya pili tutajumuisha Kata ya Milepa na Zimba ili wananchi wa maeneo hayo wapata huduma ya internet, ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo la Arumeru Magharibi kuna kata kama tano ambazo hazina mawasiliano Kata ya Bwawani yenye vijiji vinne, Olonyowase yenye vijiji vinne, Oljoro yenye vijiji vitatu, Laroi vijiji vitatu na Mwande vijiji vitatu.
Je, ni lini sasa Serikali itapeleka minara na kuhakikisha kwamba wananchi wale ambao wanateseka kupanda juu ya miti na juu ya milima na vigongo kwa ajili ya kupata mawasiliano ya kuwasiliana?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupokea changamoto ya mawasiliano katika kata ambao Mheshimiwa Mbunge, amezitaja. Tutazifanyia kazi na baadae tutamrejea kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma ya mawasiliano.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru napenda kujua ni lini wananchi wa Kata ya Masisile, Udekwa, Ilole na Nyanzwa katika Wilaya ya Kilolo watapata mawasilino ya simu na kuacha kupanda miti? (Makofi)
NAIBU WAZARI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya
Masisiwe, Udekwa, Mahenge, Kimara, Kilolo pamoja na Ebomu tayari Serikali inaenda kuingia mikataba na watoa huduma kesho tarehe 13 kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika Jimbo la Kilolo. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano kwenye Kata ya Jana, Mwalugulu, Kashishi, Chela na maeneo mengine je, ni lini sasa Serikali itaanza rasmi ujenzi wa minara hii katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshmiwa Naibu Spika, kwa Kata ya Jana tayari tumepata mtoa huduma Vodacom, Kata ya Mwalugulu tumepa mtoa huduma tigo na kata zingine na uhakika kwamba Mheshimiwa Mbunge akishatoka hapa tutawasiliana ili ajue watoa huduma gani wanaenda kutoa huduma katika maeneo hayo.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Kata ya Kapele pamoja na Kata ya Mkomba katika Jimbo la Momba ni miongoni mwa kata ambazo zenye shida kubwa sana ya mawasiliano. Naomba kufahamu ni lini Serikali itapeleka mawasilino katika kata hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge zipo katika vijiji 2,116 ambavyo tunasubiri Serikali ipate fedha ili tuweze kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mpaka hivi ninavyozungumza Ofisi ya Halmashauri ya Malinyi bado hakuna mawasiliano na mkandarasi hajafika site. Hata hivyo ninafahamu kwamba mfuko wa mawasiliano kwa hiyo (UCSAF) walishatoa fedha ila TTCL ambao walipewa kazi hawajafanya mpaka sasa hivi;
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kuambatana na mimi weekend hii wewe au Mkurugenzi wa TTCL na UCSAF kwenda Malinyi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sehemu kubwa ya Jimbo la Malinyi hasa Kata ya Usangule, Sofi na Itete kwenye vijiji kama Dabadaba hakuna mawasiliano kabisa.
Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antipas, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali iliingia mkataba wa bilioni 10.88 na Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL, ambapo katika fedha hizo zingine zinaenda katika Halmashauri ya Malinyi ambayo ni milioni 320 kwa ajili ya kujenga mnara wa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano TTCL kuhakikisha kwamba, pamoja na Halmashauri ya Malinyi na halmashauri nyingine zote 33 ambazo tumeingia nao mkataba wahakikishe wanakamilisha miradi hii ndani ya wakati, kwani kwa kufanya hivyo tutawarahisishia halmashauri kukusanya mapato na vilevile wananchi wataweza kupata huduma ya mawasiliano bila kuwa na changamoto yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kipengele cha pili, kata ambazo Mheshimiwa amezitaja mimi nilifanya ziara na yeye tukiwa pamoja katika jimbo lake; Kata ya Itete katika eneo linaitwa Madabadaba na Usangule, Kilosa Mpepo, yote hayo yameepata watoa huduma katika mradi wetu wa Tanzania ya kidigitali. Kwa hiyo tunaamini kwamba kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambayo ameyatoa ni kwamba ni lazima mikataba hii ikatelezwe ndani ya muda ambao tumekubaliana. Kwa hiyo tunaamini kwamba ndani ya miezi tisa mkataba huu ukikamilika wananchi wa eneo la Malinyi watapata huduma ya mawasiliano.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza: -
Je, Serikali iko tayari kufanya tathmini kwa vijana hao ambao wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi katika Mkoa wa Mtwara na nchi nzima ili kuona kama hiyo programu ina tija?
Swali la pili, hao vijana ambao hawajapatiwa vyeti kwa maana ya kutambuliwa ama kurasimishwa, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba vijana hao wamepatiwa vyeti na kutambulika katika elimu isiyo na mfumo rasmi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali iko tayari kufanya tathmini na siyo kwa Mkoa wa Mtwara pekee, ni nchi nzima kwa sababu sera hii ni kwa ajili ya wananchi wote.
Mheshimiwa Spika, kwa kipengele cha pili, wale ambao wamekidhi vigezo vya kupatiwa vyeti, utaratibu utafwatwa na watapatiwa vyeti vyao. Ahsante. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, tunafahamu kwamba, Serikali inatumia e-Government na TEHAMA kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii kiserikali, lakini mara kadhaa wananchi wamekuwa wakikosa huduma kwenye ofisi za Serikali kwa sababu ya kwamba, mtandao uko chini. Ni kwa nini sasa Serikali isije na mkakati mahususi wa kuhakikisha kwamba, utolewaji wa huduma kwa kutumia e-Government na TEHAMA kwenye ofisi za Serikali unatengenezewa upekee na kuhakikisha kwamba, wananchi hawakosi huduma kwa sababu za mtandao uko chini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, tumekuwa tunaona Serikali inafanya udhibiti wa mitandao, hususan katika kipindi cha uchaguzi, lakini pia tunafahamu kwamba, sasa hivi Serikali inachagiza uchumi wa kidijitali na wananchi wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya shughuli zao za kiuchumi. Ni kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kuhakikisha kwamba, majukwaa haya ya mitandaoni hayakosi mawasiliano, hususan kipindi ambacho Serikali inafanya udhibiti wa kasi hususan kipindi cha uchaguzi?
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza kuhusu matumizi ya internet katika ofisi za Serikali. Serikali imewekeza katika miundombinu, Ujenzi wa Mkongo wa Taifa. Katika ujenzi huo tuna capacity mbalimbali, tuna kitu kinaitwa Synchronize Transport Module maana yake STMA. Hizi STM kuna 1, 2 na 3; 1, 2, 3, 4 maana yake kwamba, ni capacity na speed ambapo kwa mfano STM 1 ambayo ina MBPS 155 maana yake hiyo ni capacity yake, lakini kuna ya 491, kuna ya 2488, lakini sasa niombe na kuwashauri wataalam wa eGA na wataalam ambao wako katika Wizara mbalimbali, wafanye tathmini ya mahitaji halisi ili waweze kujua kwamba, wanaweza wakapata capacity ipi itakayoendana na traffic wakati wanapokuwa wanahudumia wananchi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele cha pili cha udhibiti. Kuna Profesa mmoja anaitwa Tim Wu kutoka Colombia Law School alisema kwamba, ili ubunifu uendelee na ili tuwe na freedom ya access to information na ili business na innovation zizidi kukua ni lazima tusiweke restrictions katika aina gani ya mtandao tuweze ku-access na aina gani ya contents tuweze ku- access.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali yetu kupitia TCRA tumeweka utaratibu kwa watoa huduma kuhakikisha kwamba hakuna restriction ya aina ya content ambayo mwananchi anaweza kui-access.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, baadhi ya maeneo yale wamesharudishiwa wananchi kwa matumizi yao. Sasa ni lini Serikali itayaratibu na kuyapanga upya maeneo yale kwa maana ya vijiji, vitongoji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ikitokea wananchi wamechoka jina la mtaa, je, wanaweza wakabadilisha jina? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la kwanza; eneo ambalo limerudishwa katika vijiji tutashirikiana kwa sababu yanagusa Wizara mbalimbali, tutashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, tutashirikiana na Wizara ya Ardhi, lakini vilevile tutashirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kuona jinsi ya kulifanyia kazi na pale ambapo tutajiridhisha kwamba limesharejeshwa kweli, basi anuani za makazi zitawekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa pili, swali la pili, pale ambapo wananchi au Serikali inataka kubadilisha jina la mtaa au jina la barabara; kuna utaratibu ambao unapitiwa. Lazima vikao vifanyike kwa ngazi ya chini na wananchi washirikishwe na pale ambapo Serikali itajiridhisha kwamba ndani ya kata moja kuna jina la mtaa linalofanana na mtaa mwingine basi Serikali itawashirikisha wananchi ili kubadilisha, lakini hata pale ambapo wananchi wanalalamika katika maeneo hayo yote hayo yatafanywa kulingana na utaratibu uliowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kesi iko pale Goba, kwenye utaratibu ambao walishirikishwa mwanzoni waliamua kwamba jina lao liitwe Maghorofani, lakini baada ya kuwa wanatumia ile anuani wakajikuta kwamba jina lile linaitwa Janguo. Sasa tumeshatuma timu yetu kwenda kuhakikisha kwamba ni nani mefanya ujanja huo wa kubadilisha jina la mtaa bila wananchi wenyewe kujua kwamba utaratibu upi umetumika katika kubadilisha hilo jina.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwanza ili kuweka kumbukumbu sawa naomba nirekebishe jina langu kama lilivyotajwa na Mheshimiwa Waziri, mimi ninaitwa Mheshimiwa Kasalali na sio Kasasali.
Mheshimiwa Spika, baada ya marekebisho hayo, naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa utayari wake alipokuja kwenye Jimbo la Sumve kusikiliza changamoto zetu.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa kumeibuka aina mpya ya kangomba katika sekta ya mawasiliano ambapo kampuni za simu mara baada ya kufanya utafiti wa maeneo ambayo wataweka minara wamekuwa wakishirikiana na wajanja wachache wanaokwenda kuyatwaa maeneo haya kwa kuwalaghai wamiliki na hatimaye wao kuingia kwenye orodha ya watu wanaopangishwa na minara hiyo ya simu.
Je, nini tamko la Serikali juu ya ulaghai huu ambao umekuwa ukifanywa kupitia makampuni ya simu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Kata za Wala, Mwabomba na Maligisu hali ya mawasiliano ni mbaya sana na Serikali imesema inao mpango wa kupeleka mawasiliano katika maeneo hayo. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kupeleka mawasiliano haraka sana katika kata hizo ili kurahisisha mawasiliano kwa watu hawa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kuomba radhi kwa kukosea jina la Mheshimiwa Mbunge. Napenda sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya msingi, kuna maeneo ndani ya jimbo hili bado kuna changamoto na ndio maana Serikali tunaenda kufanya tathmini ili tujiridhishe ni hatua gani ambazo tunazichukua aidha kama ni kujenga mnara au kuongeza nguvu. Lengo ni kwamba mawasiliano ndani ya Jimbo hilo la Sumve yaweze kuimarishwa.
Mheshimiwa Spika, kwa swali la ulaghai. Nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa picha ambayo nimeiona nikiwa nafanya ziara. Kumekuwa na maeneo ambayo yamekuwa na changamoto kweli, watoa huduma kuhusishwa na jambo kama hili.
Mheshimiwa Spika, lazima nikiri kwamba sina uhakika na uthibitisho wa namna ambavyo watoa huduma wanashiriki, isipokuwa naamini kwamba kuna wajanja ambao wanahisi kwamba eneo fulani linakwenda kujengwa mnara basi wao wanawahi kwenda kulinunua ili baadaye wao ndio waweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, pia ninaamini kwamba kwa kushirikiana na Ofisi ya Halmashauri kwa sababu tulishatoa maelekezo, ujenzi wa minara ni lazima Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ihusishwe katika hatua zote ili kuhakikisha kwamba tumeondokana na migogoro ambayo inaweza ikatokea kwa sababu ya ujenzi wa minara.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa hii. Nina swali la nyongeza. Jimbo la Newala vijijini maeneo yake mengi yanakosa mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali itakuja kujenga minara katika jimbo lile ili mawasiliano yaweze kuboreshwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri, mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge tumeshafanya ziara katika jimbo lake na maeneo ambayo yalikuwa na changamoto, Serikali iliyachukua na tayari yameingizwa kwenye utekelezaji wa miradi 758 ambapo kata 713 zinaenda kuguswa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi bali awe na subira wakati utekelezaji ukiwa unaanza, ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kata za Masanga na Ngofia katika Jimbo la Kishapu hazina mawasiliano kabisa ya simu. Je, ni lini Serikali itapeleka minara katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kati ya majimbo ambayo yamepata minara mingi sana, minara zaidi ya tisa ni katika Jimbo la Kishapu na utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali na umeshaanza. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na watoa huduma ili miradi hii ikamilike kwa wakati, ahsante sana.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo la mawasiliano katika Kata ya Mchuki pamoja na Mbuchi kwenye Jimbo la Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kibiti kuna maeneo ambayo yana changamoto ya mawasiliano. Vilevile kuna maeneo ambayo tayari Serikali imeyaingiza katika ile miradi 758. Kama kuna maeneo ambayo yatabaki kuwa na changamoto Serikali inayapokea ili iwatume wataalam wake wakafanye tathmini na tujiridhishe ukubwa wa matatizo yaliyopo pale then tupate fursa ya kupeleka huduma ya mawasiliano, ahsante.
MHE. NASHONI W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza Serikali. Ni lini itapeleka mawasiliano katika Kijiji cha Songambele, Kalilani, Mkanga pamoja na Chagu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge wote. Miradi ya Mawasiliano ambayo tumesaini mwezi wa tano iko katika hatua za awali za utekelezaji wake. Ninaamini kabisa kwamba kwa sababu Waheshimiwa Wabunge hawajaanza kuona minara ikiwa ina simama katika maeneo yao, wavute subira ili tutakapoanza utekelezaji wake na baadaye minara itakapoanza kuonekana basi tutaweza kubaini maeneo ambayo yatakuwa bado yanahitaji kupelekewa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Songambele, tayari imeingizwa katika vijiji 2116 ambavyo vinafanyiwa tathmini na tayari Serikali imeshaanza kutafuta fedha ambapo Mheshimiwa Rais alishapata fedha ya kufikisha minara 600 mingine. Ninaamini Mheshimiwa Mbunge, atakuwa mmoja wa wanufaika katika minara hiyo 600, ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano katika Kata ya Makanya, Mbwei na Maibwi; je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tayari tulishawasiliana na Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi na amekuwa akinijulisha kuhusu changamoto hiyo. Maeneo na kata ambazo zina changamoto hizo tayari Serikali imeshazipokea na imeziingiza kwenye mpango wa utekelezaji wa miradi ambayo inakuja kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu, ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Ipande Kijiji cha Mhanga, Kata ya Sanjalanda Kijiji cha Gurungu, Kata ya Mgandu Kijiji cha Itagata na Kata ya Wamagande Kijiji cha Kitanura hakuna mawasiliano kabisa. Nini kauli ya Serikali kuwapelekea wananchi hawa minara ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Tanzania ya sasa ni Tanzania ya Kidigitali, hatutahitaji mtanzania yeyote aachwe nyuma, kwa hiyo naomba nipokee changamoto hizi ili tupeleke wataalam wakaangalie ukubwa wa tatizo ili tupeleke huduma ya mawasiliano na watanzania wote washiriki katika uchumi wa kidigitali, ahsante sana.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali iliahidi kujenga minara ya mawasiliano kwenye Kata ya Bugarama na Kata ya Kibogora lakini kazi haijaanza hadi sasa. Ni lini Serikali itakuja Ngara kwenye Kata hizo kujenga minara ya mawasiliano? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mwenyewe na Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro tulishatembelea jimbo lake na tulizunguka katika maeneo yote ambayo yana changamoto ya mawasiliano na baada ya kugundua changamoto hiyo Serikali ikaingiza katika mpango wa utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, katika mpango huo wa utekelezaji, tayari watoa huduma wameshapatikana lakini utoaji wa huduma hii una mchakato kidogo unaposaini, lakini kuna masuala ya vibali kwenda kupata ardhi kuingia mikataba na wenye ardhi, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo haya kwa kuwa Serikali imeshaahidi hakuna eneo ambalo litaachwa bila kujengwa mnara, ahsante sana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na Serikali imetoa majibu mazuri sana, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; Kata ya Ibili ilikuwepo katika mradi wa kwanza ambao ulikuwa ujengewe mnara, je, imeondolewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wategemee lini mradi huu wa kata tano utaanza?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Ibili imo katika Mradi wa Tanzania ya Kidigitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha pili, kama ambavyo nimesema katika jibu langu la msingi, Serikali kupitia UCSAF tunamtafuta mtoa huduma na mchakato utakapokamilika basi mtoa huduma atafika maeneo hayo kwa ajili ya kupata eneo na baadaye atapata vibali na kuanza shughuli ya ujenzi wa mnara huo kwa ajili ya wananchi wa Tabora Kaskazini. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Naibu Waziri amefika kwenye jimbo langu. Je, minara ya Kata za Eshkesh, Endahagichan, Geterer, Maretadu, Gidarudagaw na Endamiley lini inajengwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mbulu Vijijini lipo katika minara 758 na tayari watoa huduma wapo katika hatua mbalimbali, hivyo nwmwomba Mheshimiwa Mbunge, wanapofika katika maeneo yake wananchi watoe ushirikiano kwa ajili ya kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa minara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, akishirikiana na watoa huduma, basi ujenzi wa minara utaanza mara moja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza. Kata ya Lihimalyao na Vijiji vyake vya Mangesani pamoja na Kisongo katika Jimbo la Kilwa Kusini, hakuna kabisa mawasiliano ya simu na katika awamu hii ya ujenzi wa minara 758 haijafikiriwa au haijapata nafasi. Nini mpango wa Serikali kwenda kujenga minara katika Kata ya Lihimalyao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaongea na inawezekana kuna maeneo mengine ndani ya nchi yetu bado hayajapa mawasiliano. Serikali inaendelea kutekeleza miradi hii kwa awamu. Awamu ya kwanza tumemaliza minara 758, kuna awamu inayokuja ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha kwa ajili ya kuleta minara 600.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge, tukitoka hapa tukutane ili niweze kuchukua taarifa za uhakika kuhusu maeneo hayo ili tuwatume wataalam wetu, wakajiridhishe ili tuweze kuchukua hatua za kufikisha mawasiliano ndani ya kata hizo. Ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Maswali yangu ni kwamba;
a) Je, ni lini Serikali itafanya tathmini katika kata ambazo hazina mawasiliano ya uhakika ili changamoto ziondolewe nao wapate mawasiliano kama wenzao?
b) Je, ni lini Serikali itaachana na teknolojia ya 2G ili nao waende kisasa 4G na 5G?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote nchini yanapata huduma ya mawasiliano. Kwa upande wa kata ambazo, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, Serikali inatafuta fedha na fedha zikipatikana tutaenda kufanya tathmini ili kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili, kuhusu suala la kuondokana na huduma ya 2G; tunapokuwa na 3G ndani yake 2G imo. Tunapokuwa na 4G ndani yake 2G imo, tunapokuwa na 5G kwa sababu ile ni specific kwa ajili ya voice na hizi zingine ni kwa ajili ya data. Hizi zote zitakuwa zinaenda sambamba na kuhakikisha pamoja na kwamba kuna advancement ya teknolojia lakini hatuwezi kuachana na huduma ya sauti.
Mheshimiwa Spika, huduma ya sauti itaendelea kuwepo hivyo, hatutaweza kuachana kwa sasa kwa sababu ulimwenguni kote huduma ya 2G inaendelea kutumika na sisi kama nchi tutaendelea kuhakikisha kwamba kuna wananchi ambao watakuwa wanaendelea kutumia huduma hiyo basi tutahakikisha kwamba miundombinu ya huduma hiyo itaendelea kuwepo. Ahsante sana.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, sehemu ya pili ya swali la Mheshimiwa Mbunge, nadhani alitaka kujua hiyo huduma ambayo inatolewa sasa, ukiacha hiyo ya voice kama ulivyosema ya 2G, hizo nyingine zitawafikia lini hao wananchi? Ndilo lililokuwa swali la Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, Serikali kuanzia mwaka 2021 tulitoa maelekezo, miundombinu yetu yote ya minara ya mawasiliano inayojengwa, lazima iwe na huduma ya 2G na 3G. Hakuna mnara kuanzia mwaka 2021 ambao umejengwa ukiwa na huduma ya 2G pekeyake.
Mheshimiwa Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, katika jimbo lake la Urambo ambalo hata mimi nimepata kutembelea katika kata zake 12, katika kila mnara unaojengwa sasa hivi Urambo una huduma ya kutoa internet. Nakushukuru sana.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Katika Halmashauri ya Mlimba, Kata ya Uchinjile hakuna kabisa mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu katika kata hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimeshafika Mlimba na katika kata ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja ni kwamba tayari imeingizwa katika miradi 758. Zaidi ya hapo, Jimbo la Mlimba tumewapelekea minara saba ambapo tunaamini kwamba itakapojengwa basi utatuzi wa changamoto za mawasiliano utakuwa umefikia ukomo. Ahsante sana.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itafikisha Mkongo wa Taifa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ni Mkoa wa Simiyu pekee ambao haukuwa umeunganishwa na Mkongo wa Taifa lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha zimeshapatikana na tayari Mradi wa Ujenzi wa Mkongo wa Taifa kutoka Shinyanga kupita Bariadi kuelekea Bunda umeshaanza.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kupeleka mawasiliano ya simu katika Vijiji vya Mgema, Mtelamwai, Mtonya na Masuguru, Wilayani Namtumbo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Vita Kawawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba kumekuwa na changamoto ya namna gani Serikali inaenda kutekeleza Mradi wa Tanzania kidigitali hasa katika Miradi ya Minara 758 ambayo imesainiwa.
Mheshimiwa Spika, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, tayari utekelezaji umeshaanza lakini ni kwamba kinachofanyika sasa hivi ni upatikanaji wa maeneo yale ambayo yanaenda kujengwa minara na baadaye vibali vipatikane kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, utekelezaji huo unafanyika. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi na nimtoe wasiwasi kabisa. Pindi miradi hiyo itakapoanza kujengwa kwa haraka na itakamilika kwa wakati bila kuwa na shida yoyote. Tumewapatia miezi 18 kuhakikisha kwamba wanakamilisha miradi yote, ahsante sana.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Serikali ilishatupa taarifa Wabunge juu ya uwepo wa minara hiyo 758; je, ni lini sasa Wabunge tutapata taarifa rasmi na kuzirudisha kwa wananchi kwamba kazi hiyo inaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, tumeingia mikataba na mikataba ya utekelezaji wa miradi hii ni kuanzia miezi tisa mpaka miezi 20. Kwa sababu muda wa mkataba ndio ambao Serikali tunaosimamia, tunahakikisha kwamba ndani ya muda wa makubaliano watoa huduma wote, kulingana na idadi ya minara ambayo waliipata, miradi hiyo iwe imekamilika ndani ya muda wa mkataba, ahsante sana.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kule Sikonge tunayo minara kama mitano hivi ambayo ina nguvu ndogo sana yaani coverage yake ni eneo dogo sana. Je, ni lini Serikali itaelekeza haya makampuni waboreshe coverage ya minara yao hasa kwenye Kijiji cha Ibumba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakunda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kuna timu ambayo iliundwa na Mheshimiwa Waziri na inazunguka kufanya tathmini ili kujiridhisha na changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Spika, kuna minara ambayo ilijengwa miaka ya nyuma ambapo mahitaji yake ilikuwa watu labda 2,000 au 3,000. Sasa unakuta kwamba katika eneo fulani kuna ongezeko la wakazi 5,000 mpaka 6,000 kiasi kwamba inazidiwa. Kuna miradi mingine ambayo changamoto yake ni masafa, lakini kuna miradi mingine changamoto yake ni teknolojia iliyotumika. Kwa hiyo timu hii inapopita na kujiridhisha chanzo cha tatizo ni nini, ili Serikali ikachukue hatua stahiki kulingana na tatizo la eneo husika. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Kakunda eneo lake tayari alishanijulisha na tayari tumeshaliweka katika utekelezaji wa utafiti huo. Watakaporudi wataalam wetu tutajua kwamba tunaenda kuchukua hatua gani ili tutatue tatizo kulingana na hali halisi iliyopo katika eneo husika, nakushukuru sana.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali italeta mawasiliano katika Kata ya Gwata, Tununguo na Tomondo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kata ya Gwata ipo katika utekelezaji na tusubiri Mheshimiwa Mbunge mradi huu ambapo ukiwa unaendelea kutekelezwa ndani ya kipindi cha mkataba, tunaamini Kata ya Gwata itakuwa imefikishiwa huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itaiondoa Wilaya ya Kyela kwenye adha ya mawasiliano yake kuingiliwa na Mtandao wa Malawi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tunafahamu kwamba mawasiliano ni uchumi, mawasiliano ni usalama na mawasiliano ni huduma ya msingi ya kila Mtanzania. Sasa wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha tunaona ni busara kuwaacha kwanza wananchi wetu waishi katika mazingira ambayo wanaweza kuwasiliana. Pindi fedha zitakapopatikana, ndipo sasa tutakapoenda kuweka miundombinu yetu na kuhakikisha kwamba sasa mitandao ya nchi jirani tunaiondoa ili waweze kutumia mitandao ya nchi yetu, ili waweze kuchangia uchumi ndani ya Taifa letu na vilevile wawe na usalama ambao unajitosheleza katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali ina mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba tunakuja na mradi maalum wa borders and special zone kuhakikisha kwamba changamoto hii inaisha ili Watanzania wawe na amani ndani ya nchi yao.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Katika mikataba iliyosainiwa ya wakandarasi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya minara, nina minara tisa katika Wilaya ya Kishapu, lakini hadi sasa minara hiyo haijaanza kufanyiwa kazi; je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Butondo Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa, kwanza Mheshimiwa Butondo alikuwa na tatizo kubwa sana, akaleta na Serikali ikaipokea maombi yake na tukampelekea minara tisa9 kama ambavyo ametaja. Sasa kusaini mkataba ni jambo la kwanza. Jambo la pili, watoa huduma wanaenda ndani ya Jimbo la Mheshimiwa Butondo ili kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga hiyo minara. Wakishapata eneo wanakuja kutafuta vibali kwa mfano kibali cha mazingira (environmental impact assessment permit), kibali cha anga (aviation permit) vilevile wanatafuta kibali cha kutoka halmashauri kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo mlolongo wa vibali hivi, kila sehemu ukikuta kwamba wanatoa kwa uharaka basi mkandarasi ataweza kuanza ujenzi kwa haraka, lakini kukiwa na delay katika baadhi ya maeneo, ndipo inatokea kwamba tunasaini mkataba lakini miezi mitano unakuta kwamba mradi haujaanza.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeshaliona hilo, tunawaomba wote ambao wanahusika katika mnyororo mzima wa utoaji wa vibali, watoe kwa wakati ili kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati kwa sababu Watanzania wanahitaji huduma ya mawasiliano ili washiriki katika uchumi wa kidigitali. Ahsante sana.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kwenye Wilaya yangu ya Nanyumbu tulipatiwa minara tisa, lakini kuna kata ambayo ina changamoto kubwa haipo ndani ya minara hiyo tisa.
Je, Serikali haioni haja kuleta mnara mmoja kwenye Kata ya Likokona ambayo kuna changamoto ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nafahamu kabisa kwamba, Kata ya Likokona ina changamoto hiyo, mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge tulishafika katika maeneo hayo, lakini Serikali ilipokea kata hiyo na katika miradi inayotarajiwa kuja katika ile minara 600, kata hiyo tumeiingiza. Kwa hiyo tumwombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuiombea Serikali iweze kuendelea kupata fedha kwa ajili ya kuboresha huduma ya mawasiliano nchini, ahsante sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, Kata ya Kirogo wananchi wa Kata hii ili kufanya mawasiliano wakati mwingine huwalazimu kupanda juu ya milima, na kwa kuwa Kata hii ipo kwenye ile miradi ya kidigitali, ninataka nijue commitment ya Serikali, ni lini miradi hii itaanza ya ujenzi wa minara kwenye Kata hii ya Kirogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, mradi huu umeshaanza na upo katika hatua mbalimbali. Tunaamini kwamba Jimbo la Rorya watafika kwa ajili ya utekelezaji huo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kiteto ilikuwa na vijiji vingi sana, sasa kwa mujibu wa mikataba indication ni lini, walikubaliana watamaliza kwa kipindi gani? Kwa sababu kesho nina mkutano wa hadhara na haya maswali yatakuwa mengi sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Advocate Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye baadhi ya maswali ni kwamba utekelezaji wa miradi hii ya minara 758 kuna hatua kadhaa ambazo zinafanyika na mkataba wetu ukamilishaji wake utaanzia kwenye miezi tisa. Kuna maeneo ndani ya miezi tisa minara itakuwa imeshakamilika na kuna maeneo katika miezi 10, 11 mpaka mwisho wa mkataba wetu itakuwa ni miezi 20 tutakuwa tumehakikisha kwamba minara imeshasimama katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kikubwa sana ili kuhakikisha kwamba Serikali inaendelea ku-monitor utekelezaji, tumehakikisha kwamba tumewapatia utaratibu maalum, kila baada ya miezi mitatu wanatoa taarifa ya utekelezaji walipofikia na mpaka sasa watoa huduma wengi wameshatupatia utekelezaji wao, wengine wameshapata vibali, wengine wameshapata benki guarantee, kuna wengine bado hawajapata benki guarantee.
Kwa hiyo, watoa huduma mbalimbali wako katika hatua mbalimbali, lakini wako ndani ya muda ambao tumekubaliana. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Watanzania kwamba utekelezaji huu utaenda kama ambavyo umepangwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, ni lini Serikali itapeleka minara katika Kijiji cha Misyaje, Kata ya Malumba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kwanza kabisa nipokee changamoto hii ya mawasiliano kutoka kwenye hiyo kata, lakini nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwa sababu sina taarifa za kina kuhusu kata hiyo ili tuweze kuitazama na kwenda kuchukua hatua stahiki, nakushukuru sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano katika Kata ya Sirop, Wilaya ya Hanang?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Manyara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kata ya Sirop ina changamoto ya mawasiliano. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki cha Bunge tukutane ili nimuunganishe na watalam wetu ili waweze kumpa tarehe ya kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya tathmini, nakushukuru sana.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, swalil a kwanza; kwa kuwa wananchi katika karne hii ya leo wanateseka kupanda juu ya vichuguu na vilima kutafuta mawasiliano; je, tathimini hii itafanyika ili wananchi hawa wapate huduma? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwapa Wizara hii minara mia saba na hamsini na nane.
Je, sasa Wizara haioni ni wakati muafaka Kata za Oldonyowas, Oldonyosambu, Mwandet, Laroi, Oljoro na Bwawani kupata mgao wa minara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Noah, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba Watanzania hawapandi kwenye miti, hawapandi kwenye vichuguu ili kupata huduma ya mawasiliano na ndiyo maana Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inajitahidi sana kutafuta fedha ili kuhakikisha kwamba inatatua changamoto hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili cha swali la Mheshimiwa Mbunge, ili kufikia kwenye miradi kutangazwa na zabuni kupatikana hatua ya kwanza tunaanza na kufanya tathmini ili kujiridhisha tatizo likoje, tunafanya feasibility study, baada ya hapo tunafanya detailed design na baada ya hapo tunakuja kutangaza tender, sasa hatua ambayo imefikiwa ambayo Mheshimiwa Mbunge ameiongelea ni hatua ya kusaini Mkataba ambapo tayari pesa zimeshaelekezwa katika maeneo maalum.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge jambo moja kwamba, Serikali tayari imeshapata fedha kwa ajili ya kufanya tathmini katika maeneo yake na tukishakamilisha na fedha zikapatikana, basi tutatangaza tender kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasilino kwa ajili ya wananchi wa Arumeru Magharibi, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, napenda kuuliza swali; katika Jimbo la Kaliua kuna Kata ambazo ziko kwenye programu ya kupata mawasiliano ya simu hususani Iyagala, Isawima pamoja na Ugunga; je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa kuweka minara katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa ujenzi wa minara katika maeneo mbalimbali nchini unaendelea na uko katika hatua mbalimbali. Nimhakikishie kabisa Mheshimiwa Mbunge kwamba, tumetoa maelekezo kwa watoa huduma, ndani ya Mkataba ambao tumekubaliana nao, hatutowaacha ifike miezi ishirini ndiyo tuseme kwamba umekamilisha au haujakamilisha. Tumepeana kwamba kila baada ya muda fulani watupatie taarifa ya utekelezaji wamefikia wapi ili tuweze ku-monitor na ku-evaluate kadri mradi wa utekelezaji unavyoenda. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuhusu Jimbo la Kaliua utekelezaji utaendelea na sisi Serikali tunalitazama kwa makini sana ili wananchi wa Kaliua waendelee kupata huduma ya mawasiliano, nakushukuru sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Changamoto za mawasiliano zilizopo Arumeru Magharibi zinafanana sana na hali ilivyo kule kwetu Mashariki.
Je, ni lini Serikali itaondoa kabisa changamoto za mawasiliano katika Kata za pembezoni Ngarenanyuki, Leguruki, Maruvango, King’ori na Malula? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inawapenda Watanzania na kwa sababu inataka Watanzania wote washiriki katika uchumi wao wa kidigitali na ni lazima wawasiliane kwa kutumia mifumo ya TEHAMA na sisi kama Serikali ambao ni wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, najitolea kuhakikisha kwamba nitaenda katika Jimbo la Arumeru Mashariki ili tukajionee changamoto ilivyo na tuchukue hatua na hakuna cha kwamba ni kata moja tu, tutahakikisha maeneo yote ambayo yana changamoto kulingana na upatikanaji wa fedha tutafikisha mawasiliano, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu Kata ya Mapanda na Kibengu katika Jimbo la Mufindi - Kaskazini kwa sababu wananchi wanapata shida sana ya mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, maeneo ya Kibengu hayapo katika minara 758 lakini tunayaingiza kwenye tathmini ya minara kwenye vijiji 2,116. Kwa hiyo, tukishakamilisha na fedha zikapatikana, tutafikisha mawasiliano katika Kata hiyo, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, Kata ya Ilolanguru, Kata ya Ikobe, Kata ya Iponya na Lubembela zinakabiliwa na changamoto ya mawasiliano. Waziri lini utapeleka mawasiliano Wilaya ya Mbogwe katika Kata hizo nilizozitaja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyotajwa na Mheshimiwa Maganga kuna maeneo ambayo yanafanyiwa tathmini lakini kuna maeneo ambayo yapo ndani ya miradi 758. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge miradi hii itakapokamilika lakini na yale ambayo tumeyaingiza kwenye tathmini na fedha zikapatikana tutafikisha mawasiliano ndani ya Jimbo la Mbogwe. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu Jimbo la Ngara, Kata ya Murukulazo kwa sababu mawasiliano yanasuasua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa eneo hilo lina changamoto kwa sababu liko mpakani kule na linapata huduma kutoka maeneo ya ndani ambapo minara yake haina nguvu sana. Tulishatuma wataalam wetu katika maeneo haya kwa sababu yapo katika miji ambayo ni ya kimkakati na Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba, maeneo yote ya kimkakati tunahakikisha tunaimarisha huduma ya mawasiliano. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge tunalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itaanza kujenga minara 15 iliyopangwa kujengwa katika Wilaya ya Kilwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, tayari mradi wa Tanzania ya kidigitali minara 755 kwenda kwenye kata 713, Wilaya 112. Ninakuhakikishia kwamba iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Hivyo ninamuomba Mheshimiwa Mbunge tuwe na subira kwa sababu ujenzi wa minara ni hatua, hatua hizo zikishakamilika kusimamisha mnara wenyewe hauchukui hata miezi miwili. Kwa hiyo, ninamuomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kutoa ushirikiano katika maeneo ambapo wataalamu wetu watakapofika kwa ajili ya kupata maeneo na vibali basi awe sehemu ya ufanikishaji huo. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninataka niulize swali moja la nyongeza kwa Serikali: -
Jimbo la Songwe ni jimbo ambalo liko kijijini sana, na Kata za Magamba, Mpona, Ifwenkenya, Manda, Mkukwe, Ngwara na Gua hazina mawasiliano kabisa;
Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Jimbo la Songwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema, ili vijiji viingizwe katika utekelezaji ni lazima kwanza vifanyiwe tathmini, na tayari katika vile vijiji 2,116, vijiji vya Mkoa wote wa Songwe vipo. Na juzi tumesaini mikataba ya kupeleka minara 758 lakini Mheshimiwa Rais ametafuta fedha kwa ajili ya minara mingine 600. Kwa hiyo naamini kwamba katika vijiji ambavyo tayari vimeshafanyiwa tathmini, tutapeleka minara hiyo 600 ili kuhakikisha kwamba huduma ya mawasiliano inaimarika kwa wananchi.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninataka kujua tu, kwanza ni lini vijiji hivyo vitafanyiwa tathmini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; pale Singida Mjini, Kata ya Unyamikumbi ndiyo kata pekee ambayo mawasiliano yanasumbua sana: -
Je, ni lini Serikali itatuletea mnara kwa ajili ya kutatua tatizo la mawasiliano katika kata ile?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima kwa niaba ya Mheshimiwa Katani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tathmini tayari imeshaanza kufanyika na awamu ya kwanza tumekamilisha vijiji 2,116. Kwa hiyo naamini kwamba katika awamu ijayo vijiji na kata za Litehu, Ngonja na Mkwiti zitaingizwa katika utekelezaji huo, na baada ya hapo, fedha zitakapopatikana tutafikisha huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili kuhusu Kata ya Singida Mjini pale, tutatuma wataalam wetu wakaangalie tatizo ni lipi hasa. Kama ni kuongeza nguvu tutafanya hivyo, na kama itahitaji kupeleka mnara tutafanya hivyo. Ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Vijiji vya Kapewa na Mtetezi vilivyopo Kata ya Mpui vina changamoto kubwa ya mawasiliano. Nataka kujua ni lini Serikali mtapeleka minara katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja vipo katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania Kidigitali. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza; je, ni lini Serikali itapeleka mtandao katika Vijiji vya Hunyali, Kihumbu na Sarakwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge tayari ameshafika ofisini kwetu na mimi nimekuwa nikiwasiliana naye mara kwa mara na tayari vijiji ambavyo ameshavileta ofisini viko kwenye mchakato wa kuingizwa katika utekelezaji. Pindi fedha zitakapopatikana tutafikisha huduma ya mawasiliano katika vijiji ambavyo Mheshimiwa Getere amevitaja.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata ambazo Jimbo la Tabora Kaskazini hakuna mawasiliano; Igulungu, Chitage, Bukumbi na Chese?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa, tunakiri kwamba Tabora Kaskazini ina changamoto kubwa sana ya mawasiliano; na katika mradi wetu huu kwa bahati mbaya sana haikuwezekana. Hata hivyo, tayari tumeshachukua kata tano za Tabora Kaskazini ambazo tunakwenda kuzifikishia huduma ya mawasiliano ndani ya mwaka huu wa fedha, ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli kabisa Dar es Salaam, hasa Dar es Salaam Vijijini, Kibamba kule, mawasiliano ni shida. Maeneo ya Mabwepande eneo la Kibesa na maeneo ya Kata ya Saranga, maeneo ya mpakani na Ilala hakuna kabisa mawasiliano: -
Je, Serikali mko tayari kwa minara 600 hii kupeleka na maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge wiki jana alinifikishia changamoto hii, na tayari Serikali tumeshaipokea na tunaifanyia kazi. Tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge hatua ambayo tutakuwa tumefikia kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, ili upitishe miundombinu ya mawasiliano kwa kila kilometa moja watu wa mawasiliano wanachajiwa dola 1,000, lakini ukipitisha miundombinu kama ya maji au umeme kando ya barabara kuu za TANROADS au za TARURA, charge yake ni kama dola 50 kwa kilometa moja.
Je, Serikali haioni ni wakati sasa wa kuzungumza ndani kwa ndani ya Serikali ili kupunguza hiyo gharama ya dola 1,000 ili kupunguza hizo gharama za mawasiliano?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; maeneo ya Mtula, Kisada na Kata nzima ya Bumilayinga, kuna masiliano ya kusuasua: -
Je, ni lini Serikali itaboresha na kuimarisha mawasiliano katika kata hizo za Mji wa Mafinga?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweIi kabisa kuna gharama za kupitisha mkongo wa Taifa ambazo ni dola 1,000 ambazo tunaziita right of ways na Mheshimiwa Rais tayari ameshaelekeza tuhakikishe kwamba tunalifanyia kazi kwa sababu gharama hizi mwisho wa siku zinaingia kwenye capex na mwisho wa siku zinaenda kwa mtumiaji wa mwisho.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ili tuhakikishe kwamba mtumiaji wa mwisho anapata huduma ya mawasiliano kwa gharama nafuu ni kuhakikisha kwamba gharama ambazo zilizopo katikati hapa ambazo zitamsababishia mtumiaji wa mwisho kuwa na gharama kubwa ya kutumia huduma ya mawasiliano tumeshaanza kazi nzuri ya kushirikiana na wenzetu TANROADS, TARURA na kadhalika ili kuhakikisha kwamba hizi gharama tumezitazama kwa namna ambayo zitasaidia zaidi wananchi badala ya kuwaumiza wananchi, ahsante sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Je, ni lini Serikali itatupatia minara ya mawasiliano katika Kata ya Tangazo na Kijiji cha Namgogori hakuna kabisa mnara wa mawasiliano ili wananchi wangu waweze kufurahia huduma hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, maeneo ambayo ameyataja baada ya Bunge lako Tukufu tukutane ili tuweze kuyaweka vizuri na tutume wataalam wetu wakafanye kazi na baada ya hapo tuhakikishe kwamba tunafikisha huduma ya mawailiano, ahsante sana.(Makofi)
MHE. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Same Magharibi, Kata za Milimani kuna shida sana ya mitandao. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kuziangalia Kata hizo za milimani vilevile, ziletewe huduma ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mathayo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Same Mashariki pamoja na Magharibi nilifanya ziara katika maeneo yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Ni kweli kuna changamoto lakini habari njema kwa wananchi wa Same ni kwamba, Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika Kata zaidi ya 12 katika Wilaya nzima ya Same. Kwa hiyo, naamini kwamba katika maeneo ambayo yatakuwa bado yana changamoto tutatuma wataalam wetu waende wakajiridhishe. Kama tutahitaji kuongeza nguvu ya minara iliyopo tutafanya hivyo, kama tutahitaji kuweka minara mipya basi tutafanya hivyo, lengo likiwa ni kutatua changamoto ya mawasiliano kwa wananchi. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Jimbo langu la Manyoni Mgharibi Halmashauri ya Itigi kuna vijiji vya Mhanga, Tulieni, Mnazi na Vijiji Itagata na Vijiji vya Lulanga havina mawasiliano kabisa. Je, Serikali iko tayari sasa kuingiza katika mpango ujao wa bajeti vijiji hivi navyo vipate huduma ya minara.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira kuu ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inafikisha huduma ya mawasiliano. Kwa sababu ameiomba Serikali kama iko tayari, Serikali tuko tayari kuhakikisha kwamba tunaingiza katika mpango ujao wa kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma ya mawasiliano, nakushukuru sana.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa kila Mbunge anayesimama anaomba minara na maeneo mengi hata Mjini mtandao unasumbua. Ni upi mkakati wa Serikali kutumia satellite ili kuondokana na changamoto hii ya mawasiliano ambayo hata maeneo ya Mijini yenye mabonde na miteremko kumekuwa na vurugu sana za kukosekana kwa mawasiliano. Ni upi mkakati wa Serikali wa kutumia satellite ili mawasiliano yapatikane nchi nzima?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mikakati mingi. Serikali iliingia kwenye utatatibu wa Ujenzi wa Mkongo wa Taifa ili tuondokane na matumizi ya microwave ambayo ilikuwa na changamoto kubwa sana, ni ya gharama lakini kulingana na jiografia ya nchi yetu ilivyo ilileta changamoto kubwa. Vilevile, kuna maeneo ambayo tunatumia satellite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa maelekezo mahsusi ili tuanze mchakato wa kupata satellite yetu kama nchi. Tunaamini kwamba kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetatua chanagamoto nyingi sana za mawasiliano ambayo ni mchango mkubwa sana katika uchumi wa sasa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaji–engage na kila teknolojia inayoibukia ili kuhakikisha kwamba kwanza kabisa tuwe na teknolojia rahisi na inayoweza kwenda kutatua matatizo katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mara nyingine unakuta kuna mnara hapa lakini sehemu ya pili mawasiliano hauwezi ukapata, kunakuwa na dark sports za kutosha. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tumejipanga na tunaendelea na uchambuzi wa kina kuangalia ni teknolojia ipi ambayo itakuja kutupa majibu sahihi kwa ajili ya kutatua changamoto ya mawasiliano kwa wananchi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba na mimi niulize swali. Ni lini mawasiliano yatafika Ilolanguru, Chagu, Songambele, Ubanda na Mumbala? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa bado tuna changamoto baadhi ya maeneo katika nchi yetu lakini tunakwenda awamu kwa awamu. Tunapeleka minara 758 vilevile tumefanya tathmini ya vijiji 2116, baada ya hapo tunapeleka minara 600 na baada ya hapo tutapeleka minara 1000. Ninamuomba Mheshimiwa Mbunge aniletee maeneo hayo kwa maandishi ili niyaweke katika mpango wa utekelezaji wa awamu inayokuja, ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri naomba niweke kumbukumbu sawa ya majina haya. Miqaw, Aidurdagawa, Qamtananat, Endahagichan.
Swali langu la nyongeza, Je, ni lini sasa minara hii unakwenda kuijenga hasa vijiji nilivyotaja na Endahagichan?
Swali la pili, kwa kuwa umefika Jimbo la Mbulu Vijijini na wewe mwenyewe umeona kabisa. Ninaimani hakuna sababu ya kufanya tathmini kwa kuwa umefika mwenyewe na minara haipo katika vijiji nilivyovitaja na iko mbalimbali. Je, ni lini sasa unaweka kwenye mpango huu unaokuja ili vijiji hivi vikapata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana na namna ambavyo amesahihisha majina namna anavyoyatamka lakini pia nakubaliana na hali halisi ya changamoto ya mawasiliano katika Jimbo la Mbulu Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifanya ziara na Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake na tulipita meneo mengi. Maeneo mengi yalikuwa na changamoto ya mawasiliano lakini ukubwa wa tatizo tumeupunguza. Mheshimiwa Rais amekubali kutoa fedha kwa ajili ya kupeleka huduma ya mawasiliano katika Kata zifuatazo:-
Kata ya Endahagichan yenyewe ambapo tumepata mtoa huduma wa Airtel pia kuna Kata ya Eshkesh ambayo pia tumepata Artel, kuna Kata ya Geterer ambayo imepata Tigo, kuna Kata ya Masqaroda wamepata TTCL, Kata za Yaeda Ampa na Yaeda Chini wote wamepata Halotel na TTCL. Kwa hiyo, tunaendelea kupunguza ukubwa wa tatizo la changamoto ya mawasiliano ndani ya Jimbo la Mbulu Vijijini. Hivyo tunaamini kwamba awamu ijayo vijiji ambavyo tumesema tutavifanyia tathmini vitakapokamilika tutafikisha huduma ya mawasiliano. Ahsante.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, moja ya kata ulizotaja, kata ya Mundarara haipo Wilaya ya Ngorongoro, ipo wilaya ya Longido. Je, mpo tayari kubadilisha mnara ambao ulikuwa uende Kata ya Mundarara Kwenda moja kati ya wilaya za Ngorongoro?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali, itapeleka mawasiliano katika vijiji vya Kinaga, Loswashi, Nan pamoja na Osorosapia?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Shangai kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, napokea mabadiliko haya lakini itabidi tukutane ili tuweze kulifanyia uchunguzi wa kina ili tuweze kuona kwamba tunafanya nini. Tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba tatizo hili linatatuliwa.
Mheshimiwa Spika, suala la pili ni kwamba katika kata ambazo amezitaja Serikali iko katika tathmini. Tathmini mpaka sasa tumeshafikisha vijiji 2,224 na tunaamini kwamba tathmini ikishakamilika na Mheshimiwa Rais tayari ameshapata fedha kwa ajili ya kujenga minara mingine 600. Kwa hiyo, tunaamini katika hizo kata zitaingizwa katika ya utekelezaji wa minara ambayo itakuja kwa awamu inayokuja, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itapeleka na kujenga minara ya simu katika kata zenye shida kubwa ya mawasiliano ya simu yaani Serengeti ikiwemo Busawe, Issenye, Kenyamonta, Manchira, Mbalibalim Nagusi, Natta, Nyamatare, Nyambureti, Nyamoko na Uwanja wa Ndege?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amsabi Mrimi, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kbisa Mheshimiwa Mbunge ameshaleta changamoto ya maeneo ambayo yana changamoto ya mawasiliano, lakini katika kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge isipokuwa Kata ya Uwanja wa Ndege na ndio ambayo hatutaiingiza katika mpango huo wa utekelezaji. Zingine zote tutaziingiza katika utekelezaji, ahsante sana.
SPIKA: Sasa hiyo ambayo hamuiingizi ni kwamba mnao mpango wa baadaye ama? Maana wananchi sasa wakisikia kwamba hii ndio haiingizwi kwenye mpango?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ameshaleta changamoto hizo na tayari tulizipokea, ametaja hizo Kata nazikumbuka isipokuwa ya Uwanja wa Ndege ambayo hakuileta, sasa hiyo itabidi isubiri mpango wa awamu ijayo ili iweze kuingizwa, ahsante sana.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ningependa kujua ni lini Serikali itajenga minara katika maeneo ya Mkoa wa Kagera ambayo ni pori la Kimisi lakini pia Pori la Biharamulo, ni mapori hatarishi na wakati mwingine mtu akipata ajali au..
SPIKA: Unatoa mchango Mheshimiwa?
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, sawa, naomba kujua ni ni lini maeneo haya hatarishi yatawekewa mawasiliano kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANONA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kati ya mikoa ambayo imepata minara mingi sana katika minara 758 ni Mkoa wa Kagera, lakini kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ameonyesha changamoto iliyopo katika maeneo ya mabonde, mapori pamoja na maeneo mengine, tutatuma timu yetu ya wataalam wetu, wataenda kujiridhisha na ukubwa wa changamoto hizo ili tujue hatua gani tutachukua kutatua changamoto hiyo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH. G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, maeneo kama Mwamayunga, Isongwa, Ipembe, lini nayo yatapata minara ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANONA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kata ambazo amezitaja tayari tumeziweka kwenye tathmini katika vijiji 2224 na tayari Mheshimiwa Rais ameshapata fedha kwa ajili ya minara 600 na baada ya 600, kuna minara mingine 1,000 inakuja, kwa hiyo tukitoka hapa leo tukae Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuyapanga vizuri kwa ajili ya wananchi wa Jimbo lake ili waweze kupata huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. ISSA ALLY MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hali hiyo inafanana pia katika Kata za Lipumbulu, Sinano, Lupaso na Mchauru katika Jimbo la Lulindi, ni lini zitapatiwa minara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANONA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mheshimiwa Mchungahela pamoja na Kata ambazo amezitaja, zipo katika minara 758 ambayo tayari utekelezaji wake umeshaanza, ahsante.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi; ni lini Serikali itaiongezea nguvu minara ya TTCL iliyoko katika Kata ya Maguliwa, Jimbo la Kalenga, Kata ya Wasa na minara ya Airtel ambayo iko Kata ya Ulanda?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama iifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuelewa kuwa kuna haja ya kuongeza nguvu katika minara kadhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa tuna zaidi ya minara 800 ambayo inahitaji kuongezewa nguvu. Serikali imeanza na awamu ya kwanza ya kuongeza minara 408 na mpaka sasa kwenye mradi wetu wa Tanzania ya Kidigitali ni minara 302 inakwenda kuingizwa katika utekelezaji na kuhakikisha kwamba minara hiyo inapata nguvu ya kutosha na kupata huduma za internet.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo wakati Serikali inatafuta fedha ili tuhakikishe kwamba Tanzania yetu yote inakuwa ya kidigitali.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; sasa licha ya Serikali kutoa namba ya kuwaripoti matapeli wa mitandaoni, je, Serikali ina mpango gani wa kuona sasa waathirika wanapata mrejesho badala ya kutegemea majibu ya automatic yale mifumo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ntara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa swali zuri ambalo linatarajia kutoa elimu kwa watu wote. Kwanza kabisa, tuna namba 15040 ambapo ukikutanaa na namba za kitapeli basi unaweza ukatuma ujumbe na ujumbe huu utafika TCRA, baada ya hapo TCRA wataendelea kuufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nipokee ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kuona ni namna gani baada ya tatizo kufanyiwa kazi basi mtoa malalamiko aweze kupatiwa mrejesho.
Mheshimiwa Spika, tutalifanyia kazi, lakini vilevile napenda kuwaomba watanzania pale ambapo wanapigiwa simu na mtu akajitambulisha kwamba natoka Vodacom, Tigo na kadhalika basi naomba sana wapokee namba ambayo ni huduma kwa wateja ambayo ni namba 100. Tofauti na namba hiyo basi tuelewe kwamba hao sio watumishi wa Vodacom, Tigo wala kampuni yoyote ya mawasiliano, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; Vijiji vya Nsumba na Mboga, Kata ya Semembela na Kijiji cha Idubula na Burunde, Kata ya Karitu vimekuwa vikiwekwa kwenye mpango wa kujengewa minara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote lakini karibu miaka miwili sasa inapita na minara haijengwi.
Je, sasa Serikali inatoa kauli gani au commitment gani kwamba safari hii vijiji hivi vya Nsumba, Mboga, Idubula na Burunde vitajengewa minara ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya kuhakikisha kwamba utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kutekelezwa kwa kiwango kikubwa. Ni kweli kabisa nchi yetu ina vijiji zaidi ya 12,300; tunakwenda hatua kwa hatua na tayari tunapeleka minara 758, tumefanya tathimini katika vijiji 2,224 lakini vilevile tunakwenda kupeleka minara 600 kwa ajili ya huduma ya mawasiliano katika vijiji vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwamba katika awamu ijayo vijiji vya Idubula, Burunde pamoja na vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja tutaviweka katika hatua hizo za utekelezaji ili wananchi wa Bukene wapate huduma ya mawasiliano bila kuwa na changamoto yoyote.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Wilaya ya Kilolo imekuwa na changamoto nyingi sana na katika Wilaya hiyo hiyo kuna Kata ya Mahenge, Ukwega, Lugalo na Ihimbo wananchi wanapata shida sana ya mawasiliano.
Je, ni lini sasa Serikali itaondoa changamoto hizo ili wananchi wa Kilolo waweze kupata mawasiliano ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Iringa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kilolo walileta maeneo takribani 12 ambayo yalikuwa na changamoto ya mawasiliano, lakini eneo la Ilambo, Itimbo, Lugalo, Udekwa, Ukwega tayari tumeweka minara ya mawasiliano na huduma zinaendela.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kata nyingine ambazo tumezipelekea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo takribani shilingi bilioni 1.28 imekwishapelekwa kwa ajili ya kujenga minara nane katika Kata saba za Jimbo la Kilolo, nakushukuru sana.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, baadhi ya maeneo ya Kata za Rungemba, Bumilayinga na Isalavanu na Kata ya Sao Hill hazina mawasiliano ya uhakika.
Je, ni lini Serikali itafunga japo mnara mmoja kuzunguka maeneo hayo ili wananchi hawa wapate mawasiliano ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nipokee changamoto ya Mheshimiwa Chumi ili Serikali ikafanyie kazi na pale fedha zitakapopatikana tutafikisha huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; kwa kuwa kama wateja tumekuwa tunaripoti hao wanaotutapeli kwa makampuni ya simu, lakini hatupati mrejesho.
Nini kauli ya Serikali kwa Makampuni ya Simu ambayo hayatupi mrejesho wa namna gani wana-deal na matapeli hawa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii katika Bunge lako tukufu kuwaelekeza TCRA wakae na watoa huduma wote ili waone njia iliyosahihi zaidi ya kuhakikisha kwamba malalamiko yanayofikishwa basi Watanzania wanastahili kupata mrejesho wa malalamiko yao ili iwe rahisi kuweza kupima utekelezaji unakwenda kwa kipimo gani kulingana na malamiko yanayotumwa na mrejesho unaokuja. Hivyo, namwelekeza Mkurugenzi Mkuu na timu yake yote walifanyie kazi na sisi kama Serikali tutaendelea kufuatilia kwa karibu sana, ahsante sana.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni suala la kawaida kuona sehemu “A” ina mtandao mmoja na sehemu “B” haina mtandao mwingine kwa maana hapa kuna Tigo, hapa kuna Vodacom.
Sasa ningetaka kujua ni utafiti gani ambao umefanyika na kuonesha mnara mmoja hauwezi kutoa mawasiliano ya mtandao zaidi ya mmoja? Moja, tukifanikisha hilo tutaweza kupunguza gharama, lakini pia tutaweza kupunguza madhara yanayotokana na hiyo mitandao au minara kwenye maeneo ya watu.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kagera kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nitakuwa nimemuelewa vizuri anaongelea co–location; kama anaongelea co-location tunafanya cost benefit analysis ya watoa huduma anapoona kwamba hapa atakwenda kupata faida na pale atakapoona kwamba hawezi kupata faida hatoweza kufika pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana sasa Bunge lako tukufu lilipitisha Sheria Na. 11 ya mwaka 2006 kwa kuanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ili kuhakikisha kwamba Serikali inakwenda kutoa ruzuku na kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ambayo hayana mvuto wa kibishara ili Watanzania wote wapate huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa upande mwingine napokea ushauri wake na sisi tutaendelea kufanya utafiti ili kuboresha zaidi huduma ya mawasiliano nchini.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naipongeza Serikali kwa kunipa kandarasi ya utengenezaji wa minara tisa katika Wilaya yangu ya Kishapu, lakini kuna kata ya Ngofila, Kata ya Bunambiu na Mwasubi haziko kwenye orodha hiyo ya vijiji ambavyo vitakwenda kupata huduma hizo. Nini tamko la Serikali katika maeneo haya kuhakikisha kwamba huduma hiyo inapatikana?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru kwa kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpelekea minara tisa aliyoipata katika kipindi cha miaka miwili. Kwa hiyo, tunaamini kwamba hiyo ni hatua nzuri kabisa ambayo tunatakiwa kuendelea kuishukuru Serikali hii, lakini vilevile hatutakomea hapo na awamu zinazokuja tutajiridhisha na changamoto iliyopo katika kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja ili tuziingize katika utekelezaji. Aidha, kama ni kuongeza nguvu ama kupeleka mnara, wataalam wetu watuambia ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. DKT, CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, je, Serikali itakuwa tayari kuweka wazi mkeka wa mgawanyo wa minara 758 na hiyo mingine 600 tuliyoahidiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kimei, Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko tayari.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kumuuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasilano na Teknolojia ya Habari, unakumbuka mwaka 2021 ulifanya ziara kwenye Jimbo langu ukawaahidi wananchi wa Mbogwe minara mitano, lakini mpaka sasa hivi haujatimiza ahadi yako.
Je, ni lini unakwenda kutekeleza ahadi yako ambayo mimi na wewe tulifanya mkutano kule Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa nilifanya ziara katika Wilaya na Jimbo la Mbogwe na Serikali iliahidi kufikisha huduma ya mawasiliano, na mwezi wa saba wakandarasi wataingia field kwa ajili ya kuanza utekelezaji mara moja, ahsante sana.
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, hususan katika kata hizi tatu, lakini nina swali dogo la nyongeza: Je, Serikali iko tayari kupeleka mawasilino katika maeneo mengine yenye shida kama vile Ihahi, Azimio Mswiswi, Mapula, Ilaji, Igalako, Uhambule, Chamoto, Mbaliro na Matebete? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja zina mitandao isipokuwa jambo ambalo lipo kwa sasa ni kwamba, unakuta kata moja ina mtandao wa Halotel lakini wananchi wanahitaji Airtel, na kata nyingine wana Airtel lakini wananchi wanahitaji Vodacom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Na. 11 ya Mwaka 2006 lengo lake lilikuwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya mawasiliano, hata angalau kwa mnara mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Sheria yetu ya EPOCA Na. 3 inampa Mheshimiwa Waziri mamlaka ya kutunga kanuni. Sasa ili tutatue changamoto ya kuwa na minara mingi ndani ya eneo moja na kuwa na utitiri ndani ya eneo moja, tumeamua sasa kuingia kwenye kanuni ambayo inaelekeza watoa huduma; cha kwanza tuwe na infrastructure sharing, maana yake tukiwa na mnara mmoja watoa huduma wote watakwenda kuweka huduma ya mawasiliano pale ili Watanzania wote waweze kupata huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumeliongeza kuhakikisha kwamba tuna-share ile spectrum (masafa), badala ya kila mtoa huduma kuja na masafa yake, basi tumeruhusu ambapo sheria hapo kabla ilikuwa inazuia, sasa tumeruhusu ili kuhakikisha kwamba Waheshimiwa wote wenye changamoto za mawasiliano tuweze kuwapatia huduma kwa urahisi bila kuleta utitiri wa minara ndani ya nchi yetu, ahsante sana.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Iliwahi kuahidiwa hapa Bungeni juu ya kutupatia minara kwenye Kata za Maduma, Kitasengwa, Kasanga na Makungu na Kasanga kuna kituo cha afya: Je, lini Serikali itatimiza ahadi hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa David Kihenzile, ameshaleta changamoto hii na tunafahamu kwamba eneo la Kasanga kuna kituo cha afya, na ili kuhakikisha kwamba kituo kile kinafanya kazi kwa kutumia mifumo ya TEHAMA, ni lazima tufikishe huduma ya mawasiliano. Maeneo haya ya Maduma, Makungu pamoja na Kasanga tumeshaingiza kuhakikisha kwamba yanatekelezwa ili wananchi wa maeneo hayo wapate huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kata za Busale, Ibanda na Itope zipo mpakani sana mwa Malawi, na siku zote unapopita kwenye kata hizo mawasiliano yanapokwa na Wamalawi. Hata juzi Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Josephine Keenja, ameshuhudia hoteli zote zilizopo mpakani zilivyokosa wateja kwa kukosa mawasiliano: Je, ni lini sasa Serikali itatuondoa kwenye utumwa huo wa kubaki kama Wamalawi wakati sisi ni Watanzania?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuwa na Mradi wa Tanzania ya Kidigitali, tulikuwa na mradi wa special zones and boarders. Mradi huu ulikuwa mahususi kwa maeneo ya mipakani, hasa kule ambapo kuna mwingiliano wa mawasiliano na nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba mawasiliano ni uchumi katika maeneo ya mpakani, tunafahamu mawasiliano ni usalama, lakini ni haki ya msingi ya kila Mtanzania kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kuhakikisha kwamba wanapata mawasiliano. Kwa vile Mheshimiwa Mbunge amesema, basi tutatuma timu yetu tukajiridhishe tena kuona ni maeneo yapi ambayo yamebaki kuwa na changamoto hizo ili tuweze kuchukua hatua, ahsante sana.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Kwa kuwa Serikali katika Jimbo la Kisesa ilishaahidi kujenga mnara katika Kata za Isengwa, Mbugabanya, Mwabusalu, Mwakisandu, Lingeka na Mwabuma: Ni lini Serikali itatimiza azma yake hiyo ili kuboresha mawasiliano katika kata hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Jimbo la Kisesa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge alileta kata sita ambazo zilikuwa na changamoto, na kweli nasi tukajiridhisha kuna changamoto hiyo. Baada ya kupitia na kuangalia bajeti yetu, Mheshimiwa Rais ameridhia kupeleka fedha za ujenzi wa minara katika Kata za Mwabuma, Isengwa pamoja na Mwabusalu ambapo watoa huduma wa Airtel na TTCL watakwenda kujenga. Kata nyingine ambazo zimebaki, tunazipokea kama Serikali, fedha zitakapopatikana tutahakikisha kwamba tunafikisha huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kata za Mwabayanda, Kulimi na Kata ya Mwangonoli zote hazina kabisa mawasiliano ya simu. Je, Serikali ina mpango gani kuzipatia kata hizi mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kata hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, tumeziingiza kwenye awamu ya kufanya tathmini. Tumeshafanya awamu ya kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya kutoka hapa hizi kata kwa ustadi kabisa tuzipitie ili tukaziingize katika utaratibu wa kuzifanyia tathmini na pale fedha zitakapopatikana tuhakikishe tunafikisha huduma ya mawasiliano katika kata hizi, ahsante sana.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tuna Mkongo wa Taifa. Sasa Serikali haioni kuna haja ya kufunga minara hii hasa pembezoni ili kupunguza mahangaiko ya watumishi wawe na utulivu huko pembezoni wafanye shughuli zao kule kule hata kama kusoma wasome online?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliingia kwenye mpango wa kujenga Mkongo wa Taifa. Mkongo wa Taifa faida yake ni kwamba unaweza kupitisha traffic kwa wingi tena kwa kasi ya mwanga lakini vilevile lengo la kujenga Mkongo wa Taifa ni kuondokana na mifumo tuliyokuwa tunatumia zamani ya microwave lakini japo microwave kuna maeneo ambayo bado tunatumia. Lengo la kuwa na Mkongo wa Taifa ni kwamba baadae tutaunganisha minara ili kuhakikisha kwamba huduma inaweza kupatikana popote pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo makubwa ambayo tayari yameshafanyika, ambayo ni faida kubwa inayotokana na mkongo wa Taifa. Kwa sasa tuna vitu tunaita telecentre, telecentre hizi maana yake kuna maeneo ambapo mgonjwa haitaji kufika Muhimbili anaweza akapatiwa huduma akiwa Bukoba, akiwa Kagera, akiwa Mtwara lakini ile taarifa yake ikasomwa Muhimbili kule kwa sababu ya uwepo wa Mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunaomba pia tupokee ushauri wako tutaendelea kuboresha kuhakikisha kwamba nchi yetu inazidi kuhakikisha kwamba mifumo yote na huduma zote zinatolewa kwa kidigitali kwani ndio msingi halisi wa uchumi wa sasa, ahsante sana.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Kalenga Kata za Masaka pamoja na Kianga zina changamoto ya mawasiliano kwa muda mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipokee changamoto ya mawasiliano hayo ili tuweze kukaa na kuweza kuyapitia vizuri lakini naamini kwamba katika kata zake, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna minara tumempelekea katika jimbo lake na tunaamini kwamba kwa kiasi hicho kikubwa ni zaidi ya asilimia 70 ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hizi kata ambazo amezitaja tunazipokea kwa ajili ya utekelezaji, ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba yako Chitete na kwa bahati mbaya eneo hili halijapitiwa na Mkongo wa Taifa hivyo kusababisha changamoto ya mawasiliano kwenye tarafa ya Kamsamba na tarafa yote ya Msangano. Je, ni lini tutachepushiwa Mkongo wa Taifa kwenye Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna njia tatu za kufikisha mawasiliano pale ambapo hatujafikisha Mkongo wa Taifa. Tunatumia microwave na pale ambapo microwave haiwezi kufikisha tunatumia Virtual Satellite lakini kwa sababu ni nia na dhamira ya Serikali kuhakikisha nchi yetu yote inafikiwa na Mkongo wa Taifa. Mpaka sasa tumeshafikia Mikoa 25 lakini baada ya kufika Mikoa 25 tutaenda sasa Wilaya kwa Wilaya na mpaka sasa tumeshajenga kilometa 8319 lakini vilevile katika bajeti ya miaka miwili iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu. Mheshimiwa Rais aliridhia fedha takribani bilioni 345 kwa ajili ya kufikisha Mkongo wa Taifa katika maeneo mbalimbali ambapo ni kilometa 4442 zinaenda kujengwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaamini kwamba zikisha kamilika tutakuwa tumefikisha kilometa 12314 ambapo ni sawasawa na asilimia 85 ya utekelezaji na lengo la Ilani ya Chama cha Mapinduzi kufikia mwaka 2025, nakushukuru.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa, Malabo convection inaweka msingi wa Makosa ya Mtandao, Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na Biashara ya Mtandao, na kwa kutambua fursa zinazotokana na Soko Huru la Afrika la Biashara ya Mtandao; Je, ni lili sasa Serikali italeta azimio hapa Bungeni la kuridhia mkataba huu wa Malabo ili Tanzania isiendelee kuchelewa kupata fursa zinazotokana na soko huru hili la biashara Barani Afrika.
Swali la pili, kwa kuwa tayari Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi imeanza kutumika. Je, ni lini sasa Serikali itatunga kanuni kwa ajili ya sheria hiyo ili kuendelea kulinda Ulinzi wa Taarifa Binafsi ikiwemo changamoto kubwa ya ukatili wa kijinsia mtandaoni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Lugangira kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Neema Lugangira ambaye amekuwa mdau mkubwa sana katika sekta yetu hii ya mawasiliano.
Kwanza kabisa nianze na swali dogo la pili kuhusiana na Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Mheshimiwa Waziri tarehe 6 Mei, 2023 alisaini kanuni hizo ambazo ziko tayari kwa ajili ya kutumika. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge anaweza akapata fursa ya kuzipitia na kuona namna gani zinaenda kujibu hoja baadhi ya maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge ameligusia kuhusu maazimio kuletwa Bungeni. Tayari tuko kwenye mchakato huo na mchakato una hatua kadhaa lakini katika hizo hatua kuna hatua ya kuleta Bungeni. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tuko katika hatua nzuri kabisa na zikishakamilika hatua hizo za awali pale ambapo itahitaji sasa kuileta Bungeni tutaileta kulingana na utaratibu unavyotuelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana. (Makofi)
MHE JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini kanuni za MSA (Media Service Act) zitahuishwa na wadau kushirikishwa ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Mahawanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita tumepitisha marekebisho ya Media Service Act ambapo tunatarajia Mheshimiwa Rais akishasaini baada ya hapo Mheshimiwa Waziri atatangaza siku ya kuanza kutumika kwake, vilevile tutaanza mchakato wa kuhakikisha kwamba kanuni hizo ambazo zinaendana sambamba na mabadiliko hayo basi zitakuwa zimetungwa na zitapitia katika utaratibu uleule wa kuhakikisha kwamba tunahusisha wadau ili waweze kushiriki katika mchakato mzima na baada ya hapo kanuni zitakuwa tayari kwa ajili ya matumizi. Ahsante.
MHE. AMINA ALLY MZEE: Mheshimiwa Spika, asante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuharakisha juu ya mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Taifa uenee nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum - Zanzibar kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nilishukuru Bunge lako tukufu kwa kutupitishia bajeti ambayo inaenda kuhakikisha kwamba ujenzi wa Mkongo wa Taifa unakamilika. Lakini kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kwamba tayari tuna Wilaya 43 ambazo zimeshakamilika lakini katika bajeti ya mwaka jana Wilaya 23 tena zinaenda kukamilishwa. Lakini katika bajeti ambayo imepitishwa Ijumaa Wilaya 15 zingine zinaenda kukamilika kufikisha jumla ya Wilaya 81. Hivyo tunaomba kabisa kwamba kufikia mwaka 2025 wilaya zote nchini zitakuwa zimepata huduma ya mkongo wa mawasiliano wa Taifa. Nakushukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tatizo la Mkongo wa Mawasiliano lilipo Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja halitofautiani na tatizo la Kaskazini Pemba na Kusini Pemba. Nini kauli ya Serikali kuhusu mawasiliano katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa kwa upande wa Zanzibar umeshafika katika Wilaya zote kwa upande wa Zanzibar. Kwa hiyo labda tu tutaendelea kutoa elimu na ili kuwajulisha namna gani Mkongo wa Taifa huu unatoa huduma na kuwaonyesha vituo ambavyo vinatoa huduma hiyo. Nakushukuru sana.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Malinyi na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi haina mawasiliano ya simu; je, Serikali ina mkakati gani kumaliza adha hiyo katika Wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aleksia Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa bajeti ambayo Bunge lako tukufu limetupitishia jana katika kata ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziongelea na makao makuu ya Halmashauri zote zipo katika mpango wa utekelezaji. Hivyo tuombe tu kwamba tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba tutakapofikisha huduma hii basi tupate ushirikiano kutoka kwa wananchi katika maeneo yetu, ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, mkandarasi aliyejenga Mkongo wa Taifa kutoka Mangaka kwenda Mtambaswala kwenye kituo cha Mtambaswala imegundulika ameweka vifaa vya zamani na alitakiwa ajenge tank la maji jambo ambalo hakufanya hivyo. Nini kauli ya Serikali juu ya mkandarasi huyu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tumejenga kilometa 72 kutoka Mangaka mpaka Mtambaswala na Mheshimiwa Mbunge tulikuwepo wote wakati tunafika katika kituo kile ambacho ndio kinaenda kuunganisha na Msumbiji. Changamoto ambazo zimejitokeza katika kile kituo tayari Serikali inachukua hatua ili kujiridhisha ni wapi tatizo lilianzia ili kuhakikisha kwamba kituo hiki kinaanza kufanya kazi mara moja, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja na kwamba kata nyingi kutokuwa na mawasiliano ziko kata nne minara imekamilika sasa hivi zaidi ya miaka minne; Kata ya Muhongozi, Kipololo, Kijiji cha Lunolo, Kata ya Ukata Kijiji cha Litoho, kata hizi zimekamilisha minara. Ni lini itawashwa hii minara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mbinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, changamoto ya minara iliyopo katika Jimbo la Mbinga tayari Mheshimiwa Mbunge tumeshawasiliana na tayari hatua tumeshaanza kuchukua. Changamoto iliyokuwepo kwa kipindi kile ni kwamba mnara ukishasimama hiyo ni hatua ya kwanza ambayo ndio passive equipment. Lakini kuna hatua ya pili ambayo ni kuweka vile vifaa vya kurusha mawimbi ambayo ndio active equipment. Hapa katikati tumekuwa na changamoto kubwa sana ya covid-19, sasa hii changamoto imesababisha production ya vifaa kutoka katika nchi ambazo tunaagiza ndio imekuwa changamoto katika ukamilishaji wa vifaa hivi.
Mheshimiwa Spika, lakini mpaka sasa tayari TTCL wameshaagiza vifaa na vingine vimeshaingia nchini. Hivyo Mheshimiwa Mbunge atarajie kwamba minara hiyo ambayo tayari imeshasimama itawashwa hivi karibuni na mawasiliano yataanza kupatikana katika Jimbo la Mbinga. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze Serikali na hasa Engineer Kundo kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Lakini nimpongeze pia kwa namna ambavyo amefanya ziara katika Jimbo langu na kuiona changamoto hii kubwa katika eneo langu. Sasa kwa kuwa kata saba kati ya kata tisa ambazo zilikuwa na changamoto na sasa Kata ya Somagedi na Mwasubi bado zina changamoto ya aina hiyo hiyo. Je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba maeneo haya yaliyo na changamoto ya mawasiliano ya simu na yenyewe yanafanyiwa kazi kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo Mbunge wa Kishapu Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge zina changamoto ya mawasiliano lakini kati ya kata tisa kata saba anaenda kupata mawasiliano. Na haya maeneo katika hizi kata saba zote yanapatikana katika kitabu chetu cha bajeti ukurasa wa 153 ukianzia namba 578 mpaka namba 584 zote ni Kata za Kishapu ambazo zinaenda kupata huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa kwamba baada ya kukamilisha kata hizi saba basi kwa sababu utekelezaji hauwezi ukaenda kwa pamoja baada ya kukamilisha hizi basi tutaangalia uwezekano namna ambavyo tunaweza kuleta mawasiliano katika kata mbili ambazo zitakuwa zimebaki, nakushukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kumekuwepo na mwingiliano mkubwa wa mawasiliano na minara ya Safaricom kwenye kata ambazo ziko mpakani kwa upande wa Tarime na Rorya. Na hii inapelekea gharama kubwa kwa watumiaji kwa maana inaingia kwenye roming lakini pia uhafifu wa mawasiliano. Sasa nilitaka kujua ni lini Serikali itahakikisha inapeleka minara toshelezi ili wananchi wa kule waweze kupata mawasiliano bila kuingia upande wa Kenya wanakuwa kama wako Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko Mbunge wa Viti Maalum Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika maeneo ya Wilaya ya Rorya pamoja na Tarime kuna changamoto ya mawasiliano na changamoto yenyewe ni kuingiliana. Vilevile Serikali kupitia mradi wetu wa special zone and boarders tayari maeneo hayo tumeyazingatia kuhakikisha kwamba mawasiliano yanaenda kuimarishwa ili kusiwepo na mwingiliano wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na tunaelewa kabisa mwingiliano unasumbua na unaingilia hata masuala ya kiuchumi na kiusalama. Serikali inajua hilo na inachukua juhudi mahususi kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hiyo.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Jimbo la Mpwapwa lina changamoto kubwa sana ya mawasiliano na hasa katika Kata za Luhambi, Lupeta, Mlembule, chitemo na Ihondo. Je, ni lini Serikali itaweka minara ya mawasiliano ili kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mpwapwa Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa maeneo mengi nchini bado yana changamoto ya mawasiliano. Lakini kwa maelekezo ya Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ni kweli maeneo ni makubwa lakini hatuwezi kuyatekeleza ndani ya mwaka mmoja. Na ndio maana tunapanga mpango wa mwaka mmoja, tunapanga na mpango wa miaka mitano tunaamini kabisa kwa kipindi ambacho kuanzia sasa mpaka 2025 maeneo mengi yatakuwa yamepata suluhisho la mawasiliano kwa ajili ya wananchi wetu, nakushukuru sana.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela Kata ya Sangabuye Kituo cha Afya hakuna mawasiliano. Kata ya Kayenze Kisiwa cha Bezi hakuna mawasiliano. Ni zaidi ya miaka minne sasa Serikali iliahidi kupeleka minara katika kata hizo. Je, ni lini Serikali itapeleka minara katika kata hizo ili wananchi wa kata hizo waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Furaha Mbunge wa Viti Maalum Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Sangabuye ni eneo ambalo liko pembezoni mwa Ziwa Victoria ambapo mwaka huu mwezi wa pili nilifanya ziara na nikajionea hali halisi. Na Serikali ilichukua juhudi mahususi za kuhakikisha kwamba tunatafuta mtoa huduma akajenge mnara. Na tayari mkandarasi wa kwenda kujenga mnara katika eneo la Sangabuye tayari ameshapatikana. Hivyo tunasubiri tu muda wa utekelezaji ukamilike na wananchi wa Kata ya Sangabuye na Kituo cha Afya kilichopo pale waendelee kupata mawasiliano na vilevile wakinamama ambao wanatakiwa kulipa kwa kutumia M-pesa na Tigo-pesa basi haya mambo yote yaweze kwenda bila kuwa na shida yoyote, ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye Wilaya Kyerwa mwaka 2020/2021 kwenye bajeti tulitengewa minara saba na Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika Kyerwa ukatuahidi minara hiyo itajengwa lakini mpaka leo minara hiyo haijajengwa na wananchi wanaendelea kupata adha?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Bilakwate Mbunge wa Kyerwa Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa nilifika katika kata hizo na katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Vilevile labda nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tunapotangaza tender na mtoa huduma akapatikana maana yake yeye anaingia sasa kwenye kutafuta mkandarasi ambaye anaenda kumjengea minara hiyo. Na sasa tayari watoa huduma washatujulisha kwamba wako katika mchakato wa kuhakikisha kwamba mkandarasi anapatikana kwa ajili ya kwenda kujenga ile minara. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo lakini utekelezaji wa Serikali pale inapoahidi ni lazima ahadi yake itatimizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, niishukuru Serikali kwa majibu mazuri; lakini swali moja la nyongeza. Kuna hasara gani kwa Serikali yetu au kwa nchi yetu kujiunga na Mkataba wa Budapest ambao upo leo tukisubiri huo wa Umoja wa Mataifa ambao bado na una matatizo makubwa ambao haujakamilika? tujiunge na wa Budapest kusudi ikitokea tatizo hapa kati kati tuwe salama.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita ingependa kujiunga na Mikataba ya Kimataifa kama nchi zingine zinavyofanya lakini tunachokiangalia ni kutazama kwa kina huu Mkataba tunapoenda kujiunga nao una tija gani kwa Watanzania. Kwa hasara ambayo inaweza ikapatikana, kwanza kabisa katika Mkataba huu tulitamani kwamba tujiunge lakini Budapest Convention wameongeza itifaki, wanasema additional protocol of disclosure of electronic evidence. Maana yake kwamba inaruhusu mataifa mengine kuingilia mifumo yenu na kupata evidence on real time, hii ni hasara kubwa sana kwa nchi ambazo bado tuko nyuma kiteknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, mkataba huu wakati unaanzishwa umejengwa katika hiyo pin context haukuwa na ushirikishwaji wa mataifa mengine; kwa hiyo ni ngumu sana kama Taifa kwenda kujiunga na Mkataba huu. Lakini tunafanya nini kuhakikisha kwamba hasara kama hizi hatuwezi kuzipata? Ni kweli kabisa kutojiunga nao inawezekana tunapohitaji kupata ushirikiano inapotokea mtu amefanya kosa yupo katika nchi za kwao hatuwezi kupata ushirikiano; na tunafanya nini kama Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunaenda kujiunga na Mkataba na Malabo Convention. Mkataba huu umeongelea maudhui ya kuhakikisha kwamba tuwe na electronic transaction act, ambayo tayari Tanzania tunayo, tuwe na cyber security act ambayo Tanzania tunayo, tuwe na personal data protection act, Tanzania tayari tunayo; na sasa tayari tumeishapokea maoni kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tukamilishe ili tuweze ku-ratify kama nchi; na huu ni Mkataba ambao umetokana na African Union. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na huo sasa, tukishakamilisha kujiunga na Mkataba wa African Union maana yake sasa tutaenda kujiunga na ule mkataba, kama nilivyojibu katika jibu la msingi, tutajiunga na ule Umoja wa Mataifa. Ambapo maana yake European, African Union wote kwa pamoja tutakuwa tunauwezo wa kupata ushirikiano pale ambapo tunakuwa tunashughulikia makosa ya kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru, na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri mafupi yenye time frame, kwa kweli wananchi wa Kiteto wamesikia na tangu uhuru hawakuwahi kusikia Redio Tanzania. Lakini pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto ni kubwa sana, nataka kujua; Je, mnara huu wa Redio mnaojenga uta-cover eneo kubwa kiasi gani? Swali la pili; mwaka wa fedha 2023/2024 kuna vijiji takriba 20 na zaidi mlikuwa mmepanga kwamba mtajenga minara ya simu kwenye Kata za Dosidosi, Laiseri, Loolera, Magungu, Namelock, Ndirgishi, Njoro, Olboloti, Partimbo na Songambele. Nataka mniambie lini hasa miradi hii itaanza ili wananchi wa kiteto wapate mitandao ya simu.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Olelekaita kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa mtambo huu utakapokamilika utaweza kuhakikisha kwamba huduma hii inapatikana katika Wilaya nzima ya Kiteto na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mwenyekiti tunamtambo mwingine upo pale Kilindi, ule mtambo utaweza kusaidiana vizuri kabisa na mtambo ambao tutaukamilisha pale Kiteto, na Wilaya nzima ya Kiteto haitokuwa na changamoto yoyote ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ametaja Kata za Dosidosi, Laiseri, Lengatei nafikiri majina kama hayo lakini katika kata zote 12 kata moja ndiyo inaenda kuhudumiwa na Halotel, kata saba zinaenda kuhudumiwa na Airtel, kata tatu zinaenda kuhudumiwa na Tigo na kata moja ambayo ni ya Songambele inaenda kuhudumiwa na Vodacom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu uko katika hatua nzuri kabisa kwa sababu nafikiri mmeshaanza kuona wanapita huko kwa ajili ya kutafuta maeneo kwa ajili ya kuingia mikataba ili ujenzi uanze rasmi. Nakuhakikishia Mheshimwa Mbunge tuendelee kushirikiana ili maendeleo kutokana na mawasiliano yaweze kupatikana. Ahsante sana.
MHE. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa.
Je, wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga minara katika Kata za Uru Shimbwe, Kibosho Kati na Mabogini wako katika hatua gani? Kwani wananchi wanashauku kubwa kuona minara hii ikijengwa na ikianza kufanya kazi.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Ndakidemi Patrick Mbunge wa Moshi vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi wetu wa Tanzania ya Kidijitali Mheshimiwa Ndakidemi alipata kata tatu ambayo ni Uru Shimbwe ambapo mtoa huduma Tigo anaenda kuweka huduma ya mawasiliano. Pia na Kibosho Kati ni Tigo vilevile, na Mabogini tutakuwa na Vodacom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita, watoa huduma wako katika hatua mbalimbali; nafikiri Waheshimiwa wengi tayari wameshanipa mrejesho kwamba wameanza kuwaona wanapita kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanapata maeneo kwa ajili ya kuingia mikataba ya ujenzi wa minara yetu ya mawasiliano. Ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Waziri nakuja kwako tena leo kwa mara ya saba, naomba commitment yako. Je, ni lini utatuboreshea mawasiliano kwenye Kata ya Mkomba, Kata ya Kapele na Ming’ong’o Chitete na maeneo mengine yote ambaypo kuna changamoto ya mawasiliano ndani ya Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe kwa niaba ya wananchi wake wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba anawatetea wananchi wake wa Jimbo la Momba; lakini kwa bahati mbaya katika Mradi wetu wa Tanzania Kidijitali haikuweza kuchukua kata zote kwa sababu tunaelewa kwamba changamoto ya mawasiliano bado ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini habari njema sasa ni kwamba Mheshimiwa Rais ameshapata fedha na tayari Wizara yetu iko katika mchakato wa kukamilisha mambo ya mikataba ili tupate fedha kwa ajili ya kwenda kujenga minara mingine Zaidi. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kata ambazo amezitaja tutahakikisha kwamba zinakuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huo, ahsante sana.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je, ni lini Serikali itajenga minara ya kutosha kwa ajili ya Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kajege Mbunge wa Mwibara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kajege tayari ameshanijulisha changamoto ya mawasiliano katika jimbo lake na tayari maeneo yake nimeshayachukua tutawatuma wataalamu wetu wakafanye tathmini ili tujiridhishe na ukubwa wa tatizo ili tupeleke ufumbuzi wa tatizo kulingana na changamoto iliyoko kule, ninakushukuru sana.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni lini sasa mtaanza ujenzi wa minara hii kwenye maeneo ambayo umeyataja?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwenye maeneo ambayo huduma ya 5G, naomba nirudie.
Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo ambayo huduma ya 5G inapatikana kumekuwa na malalamiko mengi ya juu ya uwekaji wa bundle kwisha haraka. Sasa nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanatatua tatizo hili la kwisha bundle mapema? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kipengele cha kwanza, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi kwamba tayari Vodacom wako katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa ujenzi wa mnara huo.
Mheshimiwa Spika, kwa kipengele cha pili, naomba nielezee kidogo; ni kweli kabisa, kwanza niseme jambo moja, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake inawapenda sana Watanzania, na kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambayo ndio mlezi wa sekta ya mawasiliano nchini, kazi yetu ni kuhakikisha kwamba tunalinda na kutetea maslahi ya watoa huduma na watumiaji wa huduma. Hivyo, hatutapuuzia wala Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan haijawahi kupuuzia malalamiko ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaagiza taasisi zetu mbili, taasisi ya kwanza ambayo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyoanzishwa kwa Sheria Namba 12 ya mwaka 2003 kwa kutumia kifungu cha 40 wakashughulikie malalamiko haya ya wananchi kuhusu changamoto za kuongezeka kwa malalmiko ya uongezaji wa bundle, lakini linaisha bila kuwa na taarifa rasmi.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine, tuna TCRA CCC; hii ilianzishwa pia kwa Sheria Namba 12 ya mwaka 2003 ambapo kupitia kifungu cha 37 inampa mamlaka ya kuhakikisha kwamba inalinda haki na maslahi ya watumiaji kwa huduma ya mawasiliano. Hivyo, wakalifanyie kazi hili na watoe ripoti Wizarani, ili sasa kama kutagundulika kwamba kuna changamoto za kiufundi, basi TCRA wakafanye kazi kwa mujibu wa sheria.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Kata ya Kikonda, Kinampundu na maeneo ya Kata ya Ilunda yana shida sana ya mtandao. Ni lini Serikali inaenda kujenga mnara katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, changamoto katika jimbo lake ilikuwa kubwa sana, lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo tunayaingiza kwenye utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, lakini katika kata hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja, naomba niipokee ili tukaiingize katika utaratibu wa hatua zinazofuata kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, kuuliza maswali ya nyongeza. Nina maswali mawili, kama Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, nimewauliza wenzangu kule Kondoa, kwamba yapo majengo yaliyokamilika na mitambo na vitu vingine kama hivi vimejengwa Kondoa, lakini sifahamu huo mradi mkubwa namna hiyo umefanywa halafu Mwakilishi wa Wananchi na hata Mkuu wa Wilaya hana habari. Sasa ninataka kujua, je, majengo haya yamejengwa wapi? Na mitambo hii imejengwa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, majibu ya kusema tathmini itaanza, ninapenda kufahamu hapa nyuma tumeambiwa Serikali imetoa minara mingi sana kwenye nchi hii karibu wilaya zote. Hapa ninapokuambia jimbo langu si vijiji ni mitaa, kwenye minara mitano iliyokwenda Kondoa hakuna mnara hata mmoja ambao unakwenda kwenye Mtaa wa Jimbo la Kondoa Mjini. Wewe ni shahidi ukitoka Dodoma kilomita 30 tu, kuelekea huko tayari mawasiliano yote yanakatika barabara hii ni kubwa. Sasa ninataka nijue Serikali inawaambia nini Wananchi wa Kondoa Mjini na Mitaa yake ambayo haina mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli alivyoingia tu Bungeni hoja yake ya kwanza ilikuwa nikuhakikisha kwamba Kondoa wana Mtambo ambao utaenda kuhudumia Wananchi wa Kondoa, ili TBC iweze kusikika kwa ajili ya wananchi wake. Serikali ilipokea ombi lake na tayari Serikali imeshajenga, imejenga mnara imejenga jengo na pia, imeshaweka jenereta. Eneo gani mtambo huu umejengwa? Ukiwa unaelekea Arusha upande wa kulia pale ambapo majengo ya halmashauri yanapojengwa pale, kwenye kona pale na ndio mtambo wetu upo na mnara wetu upo pale. Mimi mwenyewe ninaufahamu na nilishafika pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoweza kusema ni jambo moja kwamba ninawaomba TBC wanapoenda kutekeleza miradi ya maendeleo ndani ya Majimbo ya Waheshimiwa Wabunge wahakikishe wanawashirikisha Waheshimiwa Wabunge pamoja na Madiwani na Ofisi za Halmashauri ili kuhakikisha kwamba miradi hii inakuwa nishirikishi. Kwa hiyo, hayo ni maelekezo yangu kwa TBC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kweli tumeshafanya tathmini. Tunapofanya tathmini hatua ya pili nikupata fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano. Maeneo yetu bado ni mengi ambayo bado yana changamoto. Kipaumbele cha Mheshimiwa Rais, ilikuwa ni kuhakikisha maeneo ya mipakani, kuhakikisha maeneo ambayo yapo vijijini. Vile vile, kuhakikisha tunawashawishi watoa huduma wakawekeze katika maeneo ya mjini ili kuhakikisha kwamba haya maeneo yote yana huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninampa matumaini Mheshimiwa Mbunge, kwamba jambo lake la Kondoa ni jambo la Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na tunalipokea tutaenda kulifanyia kazi na kuchukua hatua stahiki ili wananchi wa Kondao wapate huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize Serikali swali moja. Usikivu wa TBC ndani ya Mkoa wa Rukwa ni wa taabu na hususani katika Wilaya ya Kalambo hakuna kabisa, najua kuna juhudi za Serikali kujenga mtambo pale Kijiji cha Mkoi. Je, ujenzi huo utaanza lini ili Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wapate usikivu wa TBC? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa amekuwa mstari wa mbele kuwatetea sana wananchi wake na anahitaji wasikilize TBC Taifa. Sisi kama Serikali tulilipokea ombi lake na tulishaliingiza kwenye bajeti. Hivyo, ninamuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati utekelezaji utakapoanza basi tunashirikisha kwa hatua zaidi, ahsante sana. (Makofi
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Maeneo mengi ya Wilaya ya Ileje, kuna changamoto kubwa ya mawasiliano ni upi mpango wa Serikali kupeleka miundombinu ya mawasiliano ya kutosha ili kurahishisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu na kwa bahati nzuri amekuwa mshauri mzuri sana katika Wizara yetu kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za mawasiliano. Jambo jema kabisa ni kwamba katika minara ile 758, kati ya Majimbo ambayo yamebahatika sana ni Jimbo la Ileje ambalo limepata minara mitano. Kwa hiyo, ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, hivyo, tumuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kutupatia ushirikiano kuhakikisha kwamba wananchi wanatoa maeneo bila kuwa na masharti magumu ili tuhakikishe kwamba miradi hii inaanza kwa wakati na kukamilika kwa wakati, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, niishukuru Serikali kwa majibu mazuri; lakini swali moja la nyongeza. Kuna hasara gani kwa Serikali yetu au kwa nchi yetu kujiunga na Mkataba wa Budapest ambao upo leo tukisubiri huo wa Umoja wa Mataifa ambao bado na una matatizo makubwa ambao haujakamilika? tujiunge na wa Budapest kusudi ikitokea tatizo hapa kati kati tuwe salama.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita ingependa kujiunga na Mikataba ya Kimataifa kama nchi zingine zinavyofanya lakini tunachokiangalia ni kutazama kwa kina huu Mkataba tunapoenda kujiunga nao una tija gani kwa Watanzania. Kwa hasara ambayo inaweza ikapatikana, kwanza kabisa katika Mkataba huu tulitamani kwamba tujiunge lakini Budapest Convention wameongeza itifaki, wanasema additional protocol of disclosure of electronic evidence. Maana yake kwamba inaruhusu mataifa mengine kuingilia mifumo yenu na kupata evidence on real time, hii ni hasara kubwa sana kwa nchi ambazo bado tuko nyuma kiteknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, mkataba huu wakati unaanzishwa umejengwa katika hiyo pin context haukuwa na ushirikishwaji wa mataifa mengine; kwa hiyo ni ngumu sana kama Taifa kwenda kujiunga na Mkataba huu. Lakini tunafanya nini kuhakikisha kwamba hasara kama hizi hatuwezi kuzipata? Ni kweli kabisa kutojiunga nao inawezekana tunapohitaji kupata ushirikiano inapotokea mtu amefanya kosa yupo katika nchi za kwao hatuwezi kupata ushirikiano; na tunafanya nini kama Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunaenda kujiunga na Mkataba na Malabo Convention. Mkataba huu umeongelea maudhui ya kuhakikisha kwamba tuwe na electronic transaction act, ambayo tayari Tanzania tunayo, tuwe na cyber security act ambayo Tanzania tunayo, tuwe na personal data protection act, Tanzania tayari tunayo; na sasa tayari tumeishapokea maoni kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tukamilishe ili tuweze ku-ratify kama nchi; na huu ni Mkataba ambao umetokana na African Union. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na huo sasa, tukishakamilisha kujiunga na Mkataba wa African Union maana yake sasa tutaenda kujiunga na ule mkataba, kama nilivyojibu katika jibu la msingi, tutajiunga na ule Umoja wa Mataifa. Ambapo maana yake European, African Union wote kwa pamoja tutakuwa tunauwezo wa kupata ushirikiano pale ambapo tunakuwa tunashughulikia makosa ya kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali haioni sasa ipo haja ya kuharakisha utungaji wa sheria hiyo, Ili shirika liweze kujiendesha kibiashara?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali haioni haja ya kuhakikisha inalipatia magari shirika liweze kujiendesha na liweze kujitegemea ili liendane na soko nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza la Mheshimiwa Amina, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Shirika la Utangazaji (TBC) ambalo linaongozwa kwa notice ya Serikali 186 ya mwaka 2007 kutokana na Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 2002. Serikali ipo katika mchakato huo wa kuhakikisha kwamba utungaji wa sheria ya mwaka 2003 unafanyika kwa haraka. Sasa tayari tupo katika hatua ya pili ya uchambuzi, baada ya kuwa tumepata maoni mahususi kutoka Wizara ya Fedha. Hivyo, utungaji wa sheria huu upo katika hatua nzuri na baada ya hapo tutafikisha katika Bunge lako tukufu kwa ajili ya utaratibu unaotakiwa.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tayari Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuboresha vitendea kazi. Vitendea kazi ni pamoja na magari, ni kweli kabisa tunahitaji kuwa na OB Van za kutosha katika kanda zetu, lakini katika mikoa kulingana na ukubwa wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa fedha kwa ajili ya kuboresha studio zetu za TBC kwa kiwango ambacho kinaendana na teknolojia ya sasa. Tayari ametoa Shilingi bilioni 3.235 kwa ajili ya studio iliyopo Barabara ya Nyerere, kwa ajili ya TBC Taifa na TBC FM. Vile vile alitoa Shilingi milioni 601.8 kwa ajili ya kuboresha studio yetu ya hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa anayoifanya, kwa sababu hiki ni chombo cha umma ambacho kipo kwa ajili ya kuelimisha, kuburudisha na kutoa huduma kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kukushukuru sana.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, jana Tarehe 06 Novemba, 2023 kulikuwa na tatizo kubwa la mtandao wa Vodacom. Shughuli nyingi za kutuma fedha zilikwama, mambo mengi yalikwama kabisa, mawasiliano hata kutuma miamala ya fedha kwenye benki na kwenye simu.
Je, Vodacom jana ilipatwa na changamoto gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Kata hizi ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja zimefikia hatua gani, katika utekelezaji wake, maana wameshazipitia tayari, zimefikia hatua gani ili wananchi wa Kata hizi za Ruvu, Msindo, Mshewa, Vudee, Mhezi na Suji waweze kupata mitandao ya simu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na kipengele cha kwanza ni kweli kabisa, jana kumekuwa na changamoto kupitia mtandao wa Vodacom, tunasema kwamba kulikuwa na technical hiccups. Technical hiccups maana yake kwamba, ilitokea katika network service ambapo iliathiri masuala ya kupiga, sms, pamoja na kutuma pesa kwa mtandao wa M-Pesa, lakini wenzetu wametoa taarifa wanaendelea kuifanyia kazi na leo tumeona kuna improvement, pia wateja ambao waliathirika ni Watanzania milioni 1.8. Kwa hiyo, tunaamini kwamba wanaendelea kulifanyia kazi na baadae watatupatia mrejesho wa hatua ambayo wameifikia na tunaamini kwamba hili tatizo litakuwa limeisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kata za Ruvu, Msindo, Mshewa, Vudee, Mhezi pamoja na Suji ukiachilia hili suala la Kata ya Tae ambayo tutaiingiza katika mpango wa utekelezaji wa minara mingine inayokuja, hizi Kata ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza naomba uniruhusu nitoe ufafanuzi kidogo hapa. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla tumekuwa na maswali mengi sana kuhusiana na minara hii 758, tulichokifanya pale mwanzoni ni kubainisha Kata ambazo zina changamoto ya mawasiliano, lakini hatukubainisha maeneo ya kwenda kujenga minara hii. Kwa hiyo, tunachokifaya ni kuhakiksha kwamba tunaenda kubainisha maeneo sasa ambapo tunaenda kujenga minara na baada ya kufanya hivyo tunaenda kuhakikisha kwamba sasa tunaomba vibali. Wakati haya yote yanaendelea labda nikupe takwimu kidogo kwamba, mpaka sasa Airtel kati ya maeneo 188 mpaka sasa ameshaainisha maeneo 140 ambayo ni zaidi ya asilimia 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna TTCL yeye ameshamaliza maeneo yote pia ameshaingia mikataba na wahusika wa maeneo. Tigo kati ya maeneo 137 tayari maeneo 133 yameshakamilika. Halotel maeneo 22 yote ameshakamilisha kulingana na mkataba wake lakini Vodacom maeneo 133 kati ya 137. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba kuna hatua ambazo Waheshimiwa Wabunge hawatoziona kule zinatokea katika Majimbo yao ni kwa sababu kuna hatua ambazo ni za kiufundi na ni lazima tuzifuate na ni lazima zikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tunahitaji minara hii ijengwe kwa kasi, lakini ni lazima tuhakikishe kwamba, tunafuata utaratibu ambao hautakuja kuingiza Taifa katika janga la minara ambayo itajengwa halafu idondoke. Kwa hiyo ni lazima haya yafanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba, kampuni zote mpaka sasa zimeshaandika kuomba vibali na wakati wanaandika kuomba vibali bado wameagiza vifaa kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo, kuna hatua mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyika kuhakikisha kwamba minara hii itakapokuja kuanza kusimamishwa, nakuhakikishia kwamba inaweza ikasimama kwa pamoja na Watanzania, Waheshimiwa Wabunge, wote tutashangilia kazi kubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini kwa ndugu yangu wa Same, bahati nzuri yeye yuko katika minara ya Halotel ambapo wao kazi kubwa imeshafanyika, Halotel wameshaanza kujenga minara mitano. Katika minara hiyo mitano kuna mmoja ambao unajengwa katika Kata ya Mheshimiwa David Mathayo David. Nakushukuru sana.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru sana Serikali kwa kuwahakikishia wananchi wa Masaka kwamba sasa unapeleka mawasiliano. Pamoja na majibu mazuri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Kalenga lilipewa minara kumi: Je, hizo Kata nyingine za Kihanga pamoja na Ulanda nazo zitajengwa kwa pamoja? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimetoa ufafanuzi, miradi yote ambayo imeshaainishwa katika Mradi wa Tanzania ya Kidigitali upo katika hatua ambazo nimemaliza kuzielezea na tuwe na subira Waheshimiwa Wabunge. Naamini kabisa kwamba, hatua zote ambazo ni za ndani zikishakamilika, sasa tukishahamia site na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kusimamisha ile passive structure haimalizi hata wiki tatu na ukija kuhakikisha kwamba unafunga zile active equipment haimalizi hata wiki moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukishamaliza process za ndani hizi, tukahamia site nina uhakika ndani ya mwezi mmoja au miwili minara hiyo itakuwa inakamilika katika kila eneo ambalo tutakuwa tunapeleka huduma ya mawasiliano, ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Nilikuwa nataka niulize swali la nyongeza. Ni lini Serikali itakwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa mawasiliano kwa wananchi wa Kata ya Igombwe pamoja na Ihanja ambapo kuna minara inasuasua sana ikizingatiwa kwamba Kata ya Igombwe ndiyo Kata inayochangia kwa kiwango kikubwa pato la Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Elibariki Kingu, Mbunge kuhusiana na changamoto ya Kata ya Igombwe pamoja na Ihanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu minara tayari imejengwa, ipo. Changamoto ni kwamba Mheshimiwa Mbunge, amesema inasuasua. Tutawaelekeza TCRA kwa sababu kwa mujibu wa sheria, wao wana dhamana ya kuhakikisha kwamba watoa huduma wote wanazingatia quality of service. Kwa hiyo, tutahakikisha tunawatuma watalamu wetu wakajiridhishe, tatizo liko wapi? Kama mnara umezidiwa, basi tujue kwamba tunaongeza nguvu na kama mnara una changamoto ya kiufundi, basi wachukue hatua kuhakikisha kwamba wananchi wa Igombwe na Ihanja ambao ni wananchi wa Mheshimiwa Kingu na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wanapata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa kuwa Naibu Waziri amesema upembuzi yakinifu wa ujenzi wa minara umeshafanyika na katika Kata ya Iseke tayari walishafika: Je, ni lini sasa ujenzi wa mnara wa mawasiliano utaanza katika Kata ya Iseke? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Dkt. Chaya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Iseke kama ambavyo nimejibu katika majibu mengine ni kwamba, vifaa vikishaingia nchini na hatua za kiufundi na za kiutaratibu na za kisheria zikishakamilika, tutahakikisha kwamba Kata ya Iseke tunaanza ujenzi mara moja na kuhakikisha kwamba Wananchi wa maeneo hayo wanaendelea kufurahia matunda ya nchi yao, ahsante sana.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kata ya Mlowo ni Kata ambayo iko katikati ya Mji ndani ya Wilaya Mbozi, lakini kuna baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto kubwa ya mawaliano ikiwepo eneo la Saganoti na maeneo mengine ya Forest. Serikali ina mkakati gani wa kurekebisha mawasiliano katika maeneo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kupitia utekelekezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya mawasiliano. Kwa sababu hiyo, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunajiridhisha kila sehemu ambayo ina changamoto ya mawasiliano, basi tunafika na kuchukua hatua stahiki ili Watanzania wote waweze kupata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Stella, baada ya Bunge hili tuweze kuwasiliana ili tuweze kuchukua taarifa kamili kuhusiana na maeneo husika ili sasa tutume watalamu wetu wakajiridhishe ni nini kikafanyike katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya mawasiliano, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata ya Masisiwe katika Wilaya ya Kilolo? Kwa sababu wananchi wamekuwa wakipata mateso makubwa sana, hawana mawasiliano kwa muda mrefu sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Iringa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyeki, hii Kata ya Masisiwe Mheshimiwa Mbunge alishaiongea zaidi ya mara tatu mwaka 2022. Baada ya kuongea, tukaiingiza kwenye utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidigitali na sasa tunasubiri katika hatua mbalimbali za utekelezaji zikishakamilika Kata ya Masisiwe itapata mawasiliano, ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Kikolo katika Jimbo la Mbinga Mjini ina changamoto kubwa sana ya mawasiliano: Ni lini Serikali itapeleka huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilipokee na nilichukue kama changamoto ambayo tutaenda kuifanyia kazi, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwenye majibu Serikali imesema itavifanyia tathimini vijiji vilivyobakia je ni lini tathimini hii itaanza?
Mheshimiwa Spika, vilevile asilimia kubwa ya wananchi wa Wilaya ya Micheweni hutumia mitandao ya simu ya halotel na tigo lakini huduma zake zimekuwa ni hafifu mitandao hii. Je, Serikali inachukua jitihada gani kuwaondolea usumbufu wananchi wa maeneo ya vijiji hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kipengele cha kwanza ni lini tutafanya tathimini? Tayari tumeishamaliza kufanya tathimini katika vijiji 2,116 na hivyo naelekeza timu ya wataalam kutoka Wizarani kwetu wakishirikiana na UCSAF waende wakafanye tathimini mara moja katika kata ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziomba.
Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili ni cha kiufundi na kibiashara, pia ni cha kisheria, kwa sababu kinaangukia katika upande wa sheria kwa mujibu wa Sheria Namba 12 ya Mwaka 2003, na kwa kanuni zetu za mwaka 2018 inampatia TCRA mamlaka ya kuhakikisha kwamba inaangalia ubora wa huduma ya mawasiliano. Hivyo, basi nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri kuwaelekeza TCRA kwenda kufanya tathmini na kujiridhisha na quality of service katika maeneo hayo ili tujue ni hatua gani tunazichukua kulingana na majibu ambayo watayaleta, nakushukuru.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la mawasiliano katika Wilaya ya Ukerewe, Kata ya Bukiko ambayo inatumia Mnara wa Halotel 2G na mawasiliano ni ya kusua sua sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kupandisha hadhi minara ambayo inatoa huduma ya 2G kwenda kwenye 3G mpaka 4G. Tayari Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali tumepandisha hadhi minara 304. Hivyo tunaamini kwamba itakapokamilika tutaangalia baadhi ya meaeneo ambayo bado yana uhitaji huo. Kwa Kata ya Lukiko ambayo ipo katika Jimbo la Ukerewe tumeiingiza kwenye utekelezaji kwa kuhakikisha kwamba tunakwenda kupeleka mnara pale, nakushukuru. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri, katika jibu lake kwa Mbunge wa Wingwi, ameeleza kwamba atapeleka wataalamu katika maeneo ambayo ameyataja.
Je, wataalamu hao watafika katika Kijiji cha Mkia wa Ng’ombe ambao upo katika Jimbo la Konde, ambako pia tatizo ni sawa na la huko?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Said, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hili ni ombi, na Serikali ya Chama cha Mapinduzi dhamira yake ni kuhakikisha kwamba inawahudumia Watanzania katika maeneo mbalimbali. Hivyo Wizara tunapokea ombi hilo na tutahakikisha kwamba, wataalamu wetu wanafika katika eneo hilo.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwenye Kata ya Kilindi Asilia na Kata ya Luhande kwenye Vijiji vya Misufini kuna changamoto kubwa ya minara, kwa maana ya mawasiliano yanakatika mara kwa mara.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kutuma timu yako kuangalia namna ambavyo mawasiliano yanavyopatikana muda wote?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Kigua, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tuko tayari kama Wizara kutuma wataalamu wetu kwenda kufanya tathmini ili tujiridhishe na uhalisia wa tatizo na kuchukua hatua stahiki, ahsante.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, tarehe 9 Januari nilituma message kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na kwa Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF kuhusu minara 12 ya 2G katika Jimbo la Sikonge na wote mlijibu kwamba tumepokea.
Je, sasa ni lini itapandishwa hadhi ili kuwasaidia watu wa Sikonge upande wa internet?
SPIKA: Sasa hizo message tutajuaje sisi kama umetuma, maana ni suala la ushahidi, uliza tu swali lako Mheshimiwa Kakunda.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nilishawasilisha tayari taarifa ya minara 12. Sasa ni lini…
SPIKA: Bunge halitakuwa na ushahidi wa hayo mawasiliano yenu. Kwa hiyo uliza swali unalotaka ujibiwe na Mheshimiwa Naibu Waziri.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, swali ni lini minara 12 ya 2G katika Jimbo la Sikonge itapandishwa hadhi? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, binafsi naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Kakunda anaendelea kuwasiliana na mimi katika changamoto hiyo. Tayari, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri timu yetu inaendelea kufanya tathmini na kujiridhisha namna gani tutaweza kwenda kuanza hatua kwa hatua. Hatuwezi kupandisha yote kwa pamoja kwa sababu miradi hii ina budget implication na inategemea na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Kakunda taarifa yake hiyo tunaendelea kuifanyia kazi na wananchi wake watapata huduma hiyo ya internet.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuuliza Serikali ni lini itakuja kukamilisha mawasiliano katika Kata ya Gwata, ukizingatia ipo barabarani karibu Morogoro, kwaheri Morogoro na bado watu hawapatikani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Taletale, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika minara 758 bahati mbaya Kata hii hatukuiingiza, na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutafuta fedha na kuna minara takribani 636 ambapo katika hiyo, minara 15 inaenda kwenye upande wa TBC.
Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Kata yake tutaiingiza kwenye minara hiyo 636, ahsante sana.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali kwa hatua hizi ambazo imeanza kuzichukua kwa ajili ya kufanikisha kupata watumishi lakini kupata vyuo ambavyo vitasaidia kwenye kuhakikisha kwamba suala la artificial intelligence kwa maana ya akili mnemba linapewa nafasi yake na umakini wake katika nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni moja tu, kwa wakati huu ambao Taifa letu na dunia imekuwa ikipitia changamoto zinazotokana na mambo ya artificial intelligence, tumeona kuna viongozi na tumeona kuna watumishi na watanzania na watu mbalimbali wakichafuliwa kwa kutumia teknolojia hii. Ni upi mkakati wa Serikali wa haraka ili watanzania wengi wapate elimu kuhusu hili jambo kabla ya madhara makubwa hayajawa especial kwa wakati huu ambapo Taifa linaelekea kwenye uchaguzi watu wasije wakatumia kitu hiki kuendelea kuchafua watu na baadaye wakakosa haki zao za kimsingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni upi mkakati wa Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sanga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kama ambavyo nimejibu katika majibu ya msingi ni suala la kisera na la kisheria. Hata nchi za G7 mwaka 2018 kule Quebec walikaa na kutathmini kuona madhara makubwa yatakayo sababishwa na artificial intelligence kwa Kiswahili akili mnemba au unaweza ukasema akili bandia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili mwaka 2018 walipitisha baada ya IMF kutoa taarifa ya madhara makubwa katika upande wa cyber financial analysis ambayo ilisababisha upotevu wa fedha takribani dola bilioni 100 mpaka dola bilioni 250. Sasa baada ya kugundua hilo ikabidi wapitie sera zao na sheria ili wajue kwamba hili kosa litatambulika vipi na ili tuchukuwe hatua gani za kisheria kwa sababu huwezi ukachukua, huwezi ukasema kwamba hili ni kosa bila ya kuliweka kwenye sera na bila kuliweka kwenye sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zipi ambazo tunazichukua kama Serikali za dharura kuhakikisha kwamba Watanzania wanajua ili wasiingie kwenye changamoto hizo. Kazi kubwa ambayo inafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaanzisha mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili waweze kutambua madhara ambayo yanaweza yakatokana na akili mnemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akili mnemba ina offensive na ina defensive. Tunachokifanya ni kuhakikisha kwamba tunawapa elimu kuhusiana na offensive side isije ikaleta madhara kwao. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati mkubwa ambao lakini unaenda sambamba sasa na kuhakikisha kwamba tunaisuka sera yetu ya TEHAMA ya mwaka 2016 ikiunganisha na teknolojia zingine zinazoibukia ikiwemo akili mnemba. Kuna internet offence, kuna big data analysis lakini pia kuna cyber security haya yote lazima tuyaweke kwenye sera yetu ili tukaweke sheria ambazo zitatusaidia kuchukua hatua stahiki. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Serikali ina mpango gani wakupunguza upotevu wa fedha za mitandaoni kwa kutumia akili mnemba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi, katika jibu langu la msingi. Serikali ipo katika mkakati wa kuboresha sera yake pia tunatengeneza miongozo ambayo itasaidia kwa sababu artificial intelligence inaweza ikatumika kwenye cyber security, artificial intelligence inaweza ikatumika kwenye big data analysis, artificial intelligence inategemea ni matumizi gani ambayo wewe unayahitaji. Serikali tunaenda kuyaangalia katika upana wake na kuyaweka kwa pamoja ili tuhakikishe kwamba artificial intelligence ikatumike kwa faida na siyo kwa kuleta madhara. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote niishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri na kwa ahadi iliyotolewa ya kujenga mnara kwa ajili ya TBC. Niwapongeze pia kwa minara mingi ya simu ambayo inaendelea kujengwa katika Wilaya ya Kilolo, ambayo inatatua changamoto ya mawasiliano. Nawapongeza sana Waziri pamoja na Naibu Waziri, kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu madogo ya ngongeza, kwa kuwa mawasiliano yanaendana na uwekaji wa Mkongo wa Taifa. Je, ni lini Serikali itaweka Mkongo wa Taifa kufika katika Wilaya ya Kilolo?
Swali dogo la pili, Kwa kuwa tayari huu ujenzi wa mnara wa TBC process imeanza, nijue ni lini unatarajia kukamilika ili wananchi pia waweze kupata matumaini ya kupata matangazo ya TBC kwa uhakika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kazi kubwa anayoifanya katika Jimbo la Kilolo na kwa kazi anayoifanya katika kushirikiana na Serikali pale ambapo tunafika katika Jimbo, lake ili kuhakikisha kwamba tunaweka miundombinu ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika swali lake la pili kwamba ni lini sasa TBC itaanza kufanya kazi pale. Kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi umepangwa kukamilika ifikapo Juni, 2024. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, itakapofika Juni, 2024 naamini kwamba kazi itakuwa imeanza kwa wananchi wa Kilolo kupata huduma ya mawasiliano ya utangazaji ya TBC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba Wilaya zote nchini, Wilaya 139 ifikapo Disemba, 2024 wote tutakuwa tumefikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Ifikapo Juni, mwaka huu tutakuwa tumekamilisha kufikisha Mkongo wa Mawasiliano katika Kata 99. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu pale Mafinga tayari tuna pop yetu, pale Iringa Mjini tuna pop na kutoka Iringa Mjini mpaka Kilolo kuna kilometa 33, kwa hiyo tutahakikisha kwamba tumefikisha na tutajenga Kituo cha Mkongo katika eneo lake la Wilaya ya Kilolo. Nakushukuru sana.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itajenga mtambo kwa ajili ya usikivu wa TBC, katika Tarafa ya Kilimarondo, Jimbo la Nachingwea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali la Mheshimiwa Justin, tunao ujenzi wa vituo takribani 14 ambavyo vinaendelea, vilevile katika bajeti ijayo tunatarajia kuongeza vituo vingine nimuombe sasa Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu ni eneo specific ambalo sikutarajia angeweza kuligusia, akitoka hapa tukutane ili niangalie kama lipo katika vile vituo 14 ama vile vituo ambavyo tunaenda kuviongeza ili tuhakikishe kwamba tunakuwa na majibu ya uhakika kwa ajili ya wananchi wake wa Jimbo la Nachingwea. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Maeneo mengi katika Wilaya ya Simanjiro, hakuna kabisa mawasiliano ya simu.
Je, ni lini sasa Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata ya Ruvu Remit, Kata ya Loiborsiret, Kata ya Oljoro No. 5, Kata ya Komolo, Kata ya Kitwai, Kata ya Msitu wa Tembo, Kata ya Naberera na Kata ya Loiborsoit? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti kuna maeneo mengi ambayo bado yana changamoto lakini kwa Jimbo la Simanjiro, katika miradi yetu 758 kuna Kata takribani nne ambazo tunazipelekea huduma ya mawasiliano. Katika Kata hizo kuna zingine ambazo amezitaja sina uhakika kama zitakuwemo lakini namuomba tukitoka hapa tuweze kuonana nizijue specific ni Kata zipi na tuone kama kutakuwa na uwezekano wa kupata fedha ili na zenyewe tuziingize katika utekelezaji na wananchi wote wa Simanjiro ambao ni wananchi na wapiga kura wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Wabunge wote waweze kupata huduma ya mawasiliano, nakushukuru sana.
MHE. OMARI ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. changamoto iliyopo kwenye Jimbo la Kilolo, ni sawa na changamoto iliyopo Mkoa wa Kaskazini Pemba, juu ya usikivu wa TBC. Je, Serikali inatoa kauli gani kuwatolea wananchi changamoto hii, ukizingatia TBC ni Redio ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupokea changamoto ya Mheshimiwa Mbunge ili Serikali tukaifanyie kazi na baada ya hapo tutamshirikisha Mheshimiwa Mbunge ili atupatie ushirikiano specific katika maeneo ambayo ameyataja. Nakushukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri na tuendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kututekelezea miradi hiyo mitatu katika kipindi chake cha miaka mitatu. Pamoja na majibu hayo, naomba niulize maswali ya mawili (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ukamilishaji wa miradi iliyotamkwa kwenye majibu ya msingi ni ukamilishaji wa matanki au vihifadhia maji, lakini ili mradi ukamilike ni lazima usambazaji wa mabomba kwenda kwa wananchi ukamilike ili thamani ya fedha itimie. Sasa yapo maeneo kama CCM ya zamani Mpijimagohe, Torino kwa Mvungi, kwa Mzee Kadope na maeneo ya kwa Yusuph Michungwani.
Ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya muda mrefu kupeleka mabomba hapa katika maeneo hayo?
(b) Mheshimiwa Spika, Mtaa wa Msumi hasa Msumi Center na Darajani ni muda mrefu hawajawahi kuyaona maji safi na salama, lakini tayari Serikali imefanya utafiti wake na kutekeleza mradi au ina nia ya kutekeleza mradi wa shilingi bilioni 13.9. Je, ni lini sasa Serikali inatoa commitment kwa wananchi wa Kibamba ya kuanza kutekeleza mradi huo ambao mmeshaufanyia tathmini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia miradi hii kwa niaba ya wananchi wake wa Jimbo la Kibamba na kwa kweli anaendelea kufanya kazi nzuri. Sasa kupitia mradi wa kuboresha huduma za maji katika Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali imepenga kiasi cha shilingi bilioni 33 ambapo ndani ya fedha hizo kuna shilingi bilioni 13.9 kwa ajili ya kutekeleza mradi katika maeneo ya Msakuzi, Makobe, Msumi A, B, C, Tegeta, Mpindi na Magohe. Maeneo yote hayo yatakuwa ndani ya mradi huo wa kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, mradi huu utakapokamilika pamoja na maeneo ya Tegeta, utaweza kunufaisha wakazi takribani 166,548. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira katika bajeti hii itakapopitishwa, basi mradi huo utaanza mara moja. Katika maeneo ya usambazaji wa mabomba, yote hayo yapo ndani ya mradi huu wa kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam. Nakushukuru sana.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nini kauli ya Serikali kuhusiana na Mradi wa Maji Igongwi wa kupeleka maji kwenye kata tatu ambao umekamilika lakini bado maji hayawafikii walengwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanyika kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa mradi huu umeshakamilika, lakini ni katika hatua ya kwanza. Hatua ya pili ni kuhakikisha sasa maji yanawafikia wananchi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi kusudi mkandarasi aendelee na hatua ya mwisho ili wananchi wapate maji. Ahsante sana.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, wananchi waishio katika Visiwa vya Besi na Tefu hawana maji safi na salama kwa maana ya maji ya bomba. Ni lini Serikali itawapelekea maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula, Mbunge wa Ilemela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kisiwa cha Base ni moja ya visiwa vidogo vidogo ambavyo viko katika Ziwa Victoria, lakini Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria walifanya tathmini na kugundua kwamba hakuna maji ardhini. Tunachokifanya kwa sasa kupitia Mamlaka ya Maji Mwanza, MWAWASA wanaenda kuanzisha mradi mdogo ili waweze kuchakata maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika kisiwa hicho ambacho zaidi kinakaliwa na wavuvi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na Serikali kuhakikisha katika mwaka huu wa fedha 2024 tutaanza mradi huo na hatimaye wananchi wa kisiwa hicho watapata maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, lini Serikali itatatua changamoto ya maji iliyopo ndani ya Wilaya ya Makete kule Mfumbi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Njombe, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba baada ya kikao chako hiki cha Bunge, kwa sababu ni eneo specific ambalo amelitaja, tuweze kuonana ili niweze kujua na kuona kama limetengwa. Kama halijatengwa, basi tuone Serikali tunafanya nini ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wananufaika. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri kuwa wananchi wa Gairo watapata maji Desemba, 2024. Hata hivyo nina maswali mawili. Manispaa ya Morogoro mpaka wapate maji safi na salama ya kutosha, wanategemea Bwawa la Mindu. Bwawa hili limechukua muda mrefu. Je, ni lini Bwawa hili litaanza ukarabati wake, kwani limechukua miaka mingi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wananchi wanaozunguka Bwawa la Mindu wameshafanyiwa tathmini kusudi waondoke, na ni muda wa miezi minane hawafanyi kazi yoyote. Je, ni lini watapata fedha zao za fidia ili waweze kupisha bwawa hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, mradi huu wa uboreshaji wa bwawa hili tunatarajia kuingia mkataba na mkandarasi ifikapo Septemba, 2024. Vilevile, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.37 kwa ajili ya kuwalipa wananchi wanaozunguka katika lile bwawa ili waweze kupisha mradi kuendelea.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari hizo fedha zipo kwa ajili ya mchakato, kwa ajili ya malipo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba wananchi wake wa eneo hilo tayari watakuwa wamenufaika na mradi huo. Ahsante sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Kisondela katika Wilaya ya Rungwe hawana maji safi na salama. Ni lini Serikali italeta na ukizingatia kata hii Mheshimiwa Spika ni mdau mkubwa wa maendeleo na ni mlezi wa kata hiyo? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kata hiyo wewe ndiye mlezi, basi Serikali inalichukua. Vilevile tunatambua mchango wa Mheshimiwa Mbunge kwa kuisemea kata hiyo kwa umuhimu huo, naomba tutoke hapa tuonane ili tuweze kulichambua na kuona limekwama wapi ili tuweze kuwasiliana na RUWASA walioko katika eneo husika tuone kama iko kwenye mpango ili tuweze kutekeleza kwa haraka. Kama haiko kwenye mpango, basi Serikali ina njia nyingi za kutafuta vyanzo vya fedha ili kuhakikisha tunatekeleza miradi hiyo ya maji na wananchi waweze kunufaika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji katika Kata ya Nyakonga, Magoto na Mradi wa Maji Itiryo ni mradi wa mserereko, lakini hauna chujio wala dawa. Kwa hiyo, wakati wa mvua, maji ni machafu. Ni lini watapeleka chujio katika maeneo hayo ili maji yawe safi na salama kwa wananchi wangu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba inafikisha maji safi na salama. Kwa hiyo, kwa sababu ya changamoto hiyo, Serikali inalichukulia hatua moja kwa moja na tutakwenda kuona kwamba eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliongelea lina changamoto ipi ili wataalamu wetu waweze kuchukua hatua stahiki, ahsante, (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa miradi mingi ya maji inayoendelea ukiwemo Mradi wa Maji Ukara unasuasua kwa sababu ya wakandarasi kutolipwa pesa zao, ni lini sasa Serikali itakwamua miradi hii ili iweze kuleta tija kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imetenga kiasi cha shilingi bilioni 60, pia fedha ambazo zinatokana na mfuko wetu wa maji shilingi bilioni 18, vilevile RUWASA kuna fedha ambazo wamepata shilingi bilioni 30. Kwa hiyo, niamini kabisa kwamba wakandarasi ambao hawajalipwa na wale ambao tayari wameshawasilisha hati za madai, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan lengo lake ni kuwalipa wakamilishe miradi kwa wakati na Watanzania wapate maji. Ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, Mradi wa kutoa maji kwenye Kijiji cha Turuki kuyapeleka Liwale Mjini ni lini utaanza?
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mradi wa kuyatoa maji Kijiji cha Turuki...
SPIKA: Mheshimiwa umeshasikika, kwani nani amesema urejee?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, anasema hajasikia.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nilipokee kwa ajili ya hatua stahiki. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sensa iliyopita, wanufaika wameongezeka katika kijiji hicho na wananchi wamekuwa wanatarajia mradi huu ukamilike kwa wakati kwa sababu umekuwa ni mradi wa muda mrefu sana
Je, ni lini kwa uhakika, kwa sababu kilichopo site na unachokisema kina tofauti kidogo, ni lini kwa uhakika wananchi hawa watarajie kupata mradi huu wa maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna wananchi wa vijiji vya jirani ikiwemo Rhotia Juu pamoja na Kilimatembo Juu, ni lini na wananchi hawa wataweza kupata maji kwa sababu vijiji hivyo havina maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli natambua na Serikali inatambua uwepo wa changamoto hii katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analiongelea na ni kiu ya Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji. Ni kweli mradi huu umechukua muda mrefu, ni kweli kabisa kwa sababu ya hatua mbalimbali ambazo zilikuwa zinachukuliwa na Serikali ikiwemo utafutaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba kwa mujibu wa majibu yangu ya msingi, mradi huu unaenda kukamilika Juni, 2024. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika eneo la Kilimatembo pamoja na Rhotia, kuna mradi ambao unaendelea pale, lakini Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kupanua miundombinu ili tufikishe huduma ya maji katika maeneo yanayozunguka katika mradi ule na Kijiji cha Kilimatembo pamoja na Rhotia wataweza kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Kata za Kimyaki, Siwandeti, Kiranyi, ambayo ni maeneo yenye wananchi wengi zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba watu wanapata accessibility ya maji safi na salama na tuna mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba vijiji ambavyo vimebaki havina maji, lakini kulingana na programu ya kila Mbunge kupata vijiji vitano ambavyo vitapata huduma ya maji. Tutaangalia sasa kwamba ni vijiji vingapi ambavyo vitakuwa vimebaki havina huduma ya maji ili Serikali iweke mkakati maalum kwa ajili ya kuhakikisha tunafikisha huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambako miradi ya maji bado haijakamilika, tuna maelekezo mahsusi kutoka kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo imekwama basi tunaikwamua ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua ni lini Serikali itapeleka fedha katika Mradi wa Maji Itumba - Isongole ulioko Wilaya ya Ileje ili wananchi waweze kunufaika na maji hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Stella kwa kupitisha bajeti yetu ya maji kwa kishindo kabisa, alikuwa anapitisha huduma ya maji kwa wananchi wa Ileje. Kwa kupitisha bajeti hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapoingia sasa kwenye utekelezaji, tutapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huo unaenda kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; je, ni lini Mradi wa Maji wa Kata ya Ruaha Mbuyuni katika Wilaya ya Kilolo utakarabatiwa? Kwa sababu Mto wa Lukosi ulipochepuka uliondoa mabomba yote kwa hiyo, wananchi wa Ruaha Mbuyuni wanapata shida sana kupata maji safi na salama. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia changamoto ambayo imejitokeza katika mto ule. Ni kweli kabisa Serikali inatambua kuna mabomba ambayo yalipitiwa kulingana na mto jinsi ulivyokuwa umechepuka, lakini pia wakati tunajaribu kuweka jitihada za kurejesha huduma, bado mabomba yalipata changamoto. Serikali imeshatenga fedha na tayari tunanunua mabomba kwa ajili ya kwenda kurekebisha eneo lile ili kurudisha huduma haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5.56 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu yote ya maji ndani ya Jimbo la Kilolo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kabla sijauliza maswali ya nyongeza, ninaomba nitoe pole kwa Wana-Kyerwa na Wizara ya Maji kwa kumpoteza Meneja wetu wa Wilaya, ndugu yangu Tungaraza, tunawapa pole sana Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza; pamoja na Serikali kuweka mpango wa kuchimba visima vya maji, kuna visima ambavyo vimechimbwa zaidi ya miezi sita na mpaka sasa hivi visima hivi bado havijajengewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini visima hivi vitajengewa kwenye Kata ya Kibale, Kijiji cha Kigologolo, lakini pia kwenye Kata ya Businde, Kijiji cha Omuchwenkano?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna mradi wa maji katika Kata ya Songambele, Kijiji cha Songambele, ni zaidi ya mwaka sasa tumepitisha kwenye bajeti mradi huu haujaanza. Ni lini mradi mradi huu utaanza ili kuwapatia wananchi wa Songambele maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kwa niaba ya RUWASA na Wizara ya Maji na sekta ya maji kwa ujumla tunapokea pole hizo kwa kuondokewa na DM wetu kutoka kule Kyerwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu Kigologolo pamoja na Omuchwenkano, katika jibu langu la msingi nimeitaja Omuchwenkano, lakini vilevile katika Kigologolo, Serikali itaanza kwanza ukarabati kwa sababu ni kweli kabisa kisima kipo kimechimbwa, lakini bado ile miundombinu ya kusambazia maji haijakamilika na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inafanya ukarabati wa miundombinu ili wananchi waweze kufikishiwa huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, katika mradi wa Songambele, kwanza nimpongeze sana kwa ufuatiliaji mzuri sana Mheshimiwa Innocent Bilakwate kwa ajili ya mradi huu na kwa ushirikiano ambao anaendeea kutupatia na sisi Serikali hatutamuangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huu fedha ambazo zilitengwa kwa bahati mbaya au nzuri hatukuweza kuzipata kwa wakati. Nimhakikishie katika mwaka wa fedha 2024/2025 mkandarasi anaenda kupatikana na mradi huu utaanza mara moja, ahsante sana. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona, mwaka 2023/2024 Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya mradi wa maji wa Kata za Itandula na Mbalamaziwa, Jimbo la Mufindi Kusini, lakini mpaka sasa fedha hizo hazijaenda. Ni lini Serikali itapeleka fedha hizo kukarabati mradi huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua changamoto ya kucheleweshwa kufikishwa fedha katika mradi huo lakini nikuhakikishie kwamba kabla ya mwaka wa fedha haujaisha fedha hizo zitakuwa zimepelekwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa, kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, mradi huu ndio kwanza, upo 12.5% kwa maana yake upo nyuma kulingana na muda wa kimkataba mpaka sasa na sisi wananchi wa Rorya huu ndio mradi ambao ni suluhisho kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nipate commitment ya Serikali, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri mradi huu utakamilika na kuanza kutoa maji Halmashauri ya Wilaya ya Rorya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Mradi wa Bukura, Gabimori, Sakawa pamoja na Nyihara ni miradi ambayo imesimama kwa muda mrefu. Ninataka nijue, Mheshimiwa Waziri na imesimama, kwa sababu ya changamoto ya kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini fedha zitakwenda kwa ajili ya uendelezaji na ukamilifu wa miradi hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi mradi huu utakamilika Julai, 2025 na mpaka sasa tuna takribani miezi 12 ambayo imebaki. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa sababu najua kwamba mradi huu ni wa kimkakati katika eneo lake na kwa kisiasa na kwa afya ya wananchi wake. Tunamhakikishia kwamba pesa zitaendelea kupelekwa ili mradi huu uweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, maeneo ya Bukura, Sakawa, Nyihara ambapo najua Nyihara ndio Mheshimiwa Mbunge anapotoka, tunatambua kwamba miradi hii inaenda kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, tumwombe Mheshimiwa Mbunge atupatie ushirikiano na wananchi wake kipindi ambacho tutaanza utekelezaji ambapo ni baada ya mwezi Julai, maana yake kwamba sasa wananchi wataendelea kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini sasa Serikali au mna mkakati gani wa kubadilisha mabomba ya zamani kuweka mapya katika Jimbo la Temeke, kwa sababu mabomba haya yanapopasuka kunakuwa na upotevu mkubwa wa maji, lakini pia uharibifu wa nyumba za watu katika eneo ambalo mabomba hayo yamepasuka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa mabomba chakavu yanatusababishia Serikali upotevu wa maji. Tunapozalisha maji kwa mfano lita 1,000,000 na unakuta kwamba upotevu ni 40% maana yake kwamba ile production cost inaishia kwenye gharama ambazo anapelekewa mwananchi wakati maji yanayofika yanakuwa hayatoshi. Kwa hiyo, Serikali ina mkakati wa kuhakisha kwamba tunaendelea kupitia miundombinu yetu ambayo tayari imeshakuwa chakavu ili kuhakikisha kwamba tumeendelea kuibadilisha kwa kadiri fedha ambavyo tunakuwa tunapata ili kuhakikisha kwamba, upotevu wa maji angalau tunaendana na upotevu unaokubalika Kimataifa ambayo ni 15%.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutalifanyia kazi katika maeneo ya Temeke kuhakikisha kwamba wananchi wa Temeke hawapati changamoto ya maji kusambaa mitaani na wanapata maji ya uhakika ambayo ni toshelezi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nikushukuru Naibu Waziri kwa ziara ya kibabe uliyoifanya katika Jimbo la Kilolo. (Makofi)
Sasa swali langu la nyongeza Mradi wa Maji wa Masege, Masalali na Kihesa Mgagao umeanza kusua sua kutokana na mkandarasi kutokulipwa kwa wakati; je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi ili mradi ule uweze kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya na kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwa kuendelea kutupatia ushirikiano na sisi tunajiona kwamba tuna mwakilishi wa wananchi ambaye anahitaji kuwasemea wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge katika mradi huo ambao kama ambavyo umedai unasuasua Serikali kupitia Wizara ya Maji tumekaa na wenzetu Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba, sasa wakandarasi wetu ambao wanatekeleza mradi huo walipwe pesa ili wahakikishe kwamba mradi huo unakamilika kwa wakati na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi; Mheshimiwa Naibu Waziri upatikanaji wa maji Mamlaka ya Mji Mdogo Namanyere ni 52% na upotevu wa maji ni 47%, tunahitaji shilingi milioni 400 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini watatupatia hizo fedha tuweze kukarabati miundombinu iliyoharibika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwia Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni swali ambalo tayari Serikali tulilijibu hapa Bungeni na tayari Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso alielekeza fedha shilingi milioni 400 zipelekwe kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, mradi huu unakamilika. Mradi huo unapokamilika wananchi wa Namanyere wanapata huduma ya maji safi na salama, lakini vilevile unaenda kusaidia kuhakikisha kwamba, miundombinu yetu inaboreshwa na kuepusha upotevu wa maji ambao ni hasara kubwa kwa Serikali.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, tuendelee kushirikiana na tutahakikisha kwamba, fedha hizo zinafika kwa wakati na mradi uendelee kutekelezwa. Tunakupongeza kwa kuendelea kufanya kazi vizuri na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na utekelezaji wa Ilani ya CCM inaendelea kutekelezwa vizuri sana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kuhusiana na suala la Mtila nawatakia heri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza yanayohusiana na mradi mwingine wa Igongwi. Mradi muhimu sana wa kimkakati.
Swali la kwanza, mradi huu ambao utapeleka maji kwenye kata tatu na vijiji zaidi ya nane umekuwa ukisuasua, lakini tunajua umefikia 80% na kilichosababisha usikamilike kwa miaka saba ni fedha kutolewa kidogo kidogo. Swali, Serikali haioni sasa ni muda mwafaka wa kutoa fedha zote ili angalau hii 20% iliyobakia ikamilike? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi huu hata fedha zote zikitolewa unaweza usikamilike kwa sababu maji yanatoka kwenye Milima ya Madope katika Wilaya ya Ludewa na yanapita Kijiji cha Luvuyo ambapo wananchi nao wanataka mradi wao ukamilike ili waruhusu maji haya yaende Njombe.
Sasa Serikali ina mkakati gani kuhakikisha maji kwenye Kijiji cha Luvuyo ambapo wananchi wamezuia yasipite wanapata fedha ili mradi wao nao ukamilike?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali kama ifuatavyo; natambua Mheshimiwa Mwanyika mradi huu kwake ni mradi wa kimkakati lakini napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba mradi huu ni mradi wa kimkakati wa Chama Cha Mapinduzi na ni mradi wa kimkakati wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi ya kimkakati zaidi ya nane na miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, nyingine ipo katika 15%, 50% na 60% lakini kwa bahati nzuri kabisa mradi huu umeshafika katika 80% na bado 20%. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya na sisi tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaendelea kupeleka fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapeleka fedha kulingana na upatikanaji wake kwa sababu miradi hii yote mikubwa inahitaji fedha nyingi sana na tunatamani sana Watanzania wote katika miradi hii ambayo tunaitekeleza, yote iweze kukamilika waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kupeleka fedha kulingana na namna ambavyo mkandarasi atakuwa analeta hati za madai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili naomba nilipokee kwa ajili ya kuwaelekeza wataalamu ili wakafanye tathmini na kujiridhisha kwamba kijiji hicho kitapata maji kutoka kwenye chanzo kipi na tukishajiridhisha basi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaweza kupeleka fedha kama ambavyo ameomba kwa sababu yeye ndiyo msemaji, yeye ndiye mwakilishi wa Mheshimiwa Rais katika jimbo lake, sisi tutahakikisha kwamba tunamuunga mkono kwa kuhakikisha tunapeleka pesa kulingana na tathmini ambayo itakuwa imefanywa na wataalamu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kuna ahadi ya muda mrefu ya kupeleka maji katika Kata ya Mnazi katika Vijiji vya Langoni A, Langoni B, Kwemkwazu pamoja na Kiwanja. Ni lini Serikali itakamilisha usanifu na ujenzi wa mradi huu wa maji katika kata hii ya kimkakati kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo, Mheshimiwa Shangazi huu mradi na hasa Kata ya Mnazi natambua kabisa kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maji tuna ahadi ya kufika katika kata hii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutafika katika kata hii na kuhakikisha kwamba tunasukuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tayari Serikali imeshapata mtaalamu mshauri na gharama ya mradi ya takribani shilingi milioni 800 na tayari mtaalamu mshauri huyu ameshakabidhiwa site kwa ajili ya kuanza kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mtaalamu wetu atakapokamilika basi tunaamini kwamba mkandarasi atapatikana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa kwa haraka iwezekanavyo, ahsante sana.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, tunashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zimeendelea kuwepo Mkoa wa Pwani kwenye suala la maji, je, lini Serikali itaanza kujenga Mradi wa Maji uliopo Pangani ukizingatia toka mwaka jana mwishoni tulisaini mkataba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maji nchini kote. Vilevile kwa upande wa Mradi huu wa Pangani, Serikali tayari ipo katika hatua nzauri kabisa za kuendelea na utekelezaji wa mradi huu. Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge atupatie nafasi Serikali ili tuhakikishe kwamba mradi huu unakamilika na wananchi wa Pwani na maeneo maeneo yote yanayozunguka mradi huo wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la nyongeza. Ikiwa Serikali imefanya tathmini na maandalizi ya mchakato wa fidia ulishafanyika, maana yake ni kwamba, fedha ilitengwa kwa ajili ya mradi huo. Sasa nataka kujua, mradi huu umekwama wapi na fedha iliyotengwa tokea mwaka 2015 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu imepelekwa wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Shamsia kwa namna ambavyo anaendelea kupambana na kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika. Mradi huu haujakwama kwa sababu, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, fedha zilitengwa mwaka 2015. Katika upande wa engineering, unapofanya usanifu na baada ya usanifu mradi ukakaa kwa muda mrefu kabla ya kutekelezwa, maana yake ni kwamba inawezekana kuna mabadiliko ya mahitaji ya eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachofanya sasa kama Serikali ni kufanya mapitio ya usanifu ili tujiridhishe kama mahitaji ambayo yalikuwepo 2015 ni sawa na mahitaji ya sasa au tunapobadilisha ule usanifu maana yake ni kwamba, maeneo ambayo mradi utapita inawezekana kukawa na mabadiliko, ili tujiridhishe kwamba watakaolipwa watalipwa fedha kulingana na njia kuu ya bomba ambapo litapita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu haujakwama na tumeshaanza tayari kuhakikisha kwamba wananchi wa Mtwara wanapata maji, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa kujenga mtambo wa kusafisha maji chanzo cha Mbukwa, Wilaya wa Wanging’ombe wenye thamani ya shilingi bilioni 3.5 mkandarasi alikabidhiwa tangu Oktoba, 2023. Wananchi wa Wanging’ombe wanataka kujua, ni lini mradi huu utaanza kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Njombe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mradi huu upo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 154 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba upatikanaji wa maji vijijini unaendelea kutekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea juzi hapa kwamba wakandarasi wamekuwa wakijifichia kwenye kivuli cha kwamba Serikali haijalipa. Serikali imetoa shilingi bilioni 154 kwa ajili ya maji vijijini na shilingi bilioni 69 kwa ajili ya Mamlaka ya Maji Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kupeana taarifa, nasi kama Serikali tuweze kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi ambao wameonekana wanasuasua katika miradi ya Serikali, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naipongeza Serikali kwa Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria kwenda Kata ya Seng’wa, Jimbo la Maswa Magharibi. Nataka kuuliza, je, ni lini sasa vijiji viwili vilivyobaki vya Mwanundi na Manawa, navyo vitapata maji hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mashimba Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Mashimba Ndaki kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya wananchi wake wa Maswa. Vilevile tunaipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba mradi ambao ulikwama kwa takribani miaka 10 na kitu, kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kuja mpaka Busega, Bariadi hadi Itilima na awamu ya pili Maswa, Meatu, tayari mkandarasi ameshasaini mkataba na tayari yuko site ameshaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba wananchi wetu wa Mkoa wa Simiyu wanaendelea kupata maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kutoa maji katika Mji wa Kilwa Masoko kupeleka Kilwa Kisiwani ambao ulitengewa shilingi bilioni 1.6, kwa zaidi ya miaka mitatu sasa umekwama. Nini maelezo ya Serikali kuhakikisha kwamba wanatatua tatizo la mradi huu na hatimaye wananchi wa Kilwa Kisiwani wanapata maji kama ilivyotarajiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri, jana tulikuwa wote na Mheshimiwa Mbunge na tulijadili sana kuhusu huu mradi. Baada ya kukaa naye na kujadili kwa kina kuhusu mradi huu, nikachukua hatua ya kuwashirikisha wataalam, na hivi tunavyoongea, tayari RM ameshaanza kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi ambaye bado hajatekeleza mradi huu kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunajiridhisha kama anadai ili tuone kama ameshaleta hati ya madai ili aweze kulipwa na mradi uweze kuendelea bila kuwa na changamoto yoyote, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itarekebisha Bwawa la Maliwanda ambalo maji yake wanatiririka tu saa hizi kwa sababu ya mafuriko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto iliyopo Bunda, na changamoto hii Mheshimiwa Getere ameshanitaarifu na kuna wananchi ambao wamepata changamoto kule. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kutoka hapa tutaonana ili tukaangalie namna ya kuchukua hatua za dharura ili kuanza kutatua changamoto iliyojitokeza katika jimbo lake, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Maji wa Kata ya Igunda umekuwa wa kusuasua kwa muda mrefu. Ni nini kauli ya Serikali ili kuweza kukamilisha mradi huu ili kuondoa adha kwa wananchi wa Kata ya Igunda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba wilaya zilizoko katika Mkoa wa Shinyanga, zote zinapata maji kutoka Ziwa Victoria isipokuwa tu Ushetu. Tayari tumeshakaa na Mheshimiwa Mbunge na bahati nzuri jana tulijadili sana hili suala na hivyo vijiji tayari nimeshaviripoti kwa wataalamu wetu ili wakajiridhishe tuvute maji kutoka Kahama Mjini au tuvute maji kutoka Shinyanga ilimradi tu wananchi wa vijiji hivyo waweze kupata maji, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na ninaipongeza, kama imemaliza kutengeneza mradi huo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan amenunua magari/mitambo ya kuchimbia visima kila mkoa. Napenda kujua ni kwa nini sasa Mji Mdogo wa Namanyere bado hawajachimbiwa visima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Bwawa la Maji la Mji Mdogo wa Namanyere ni muhimu sana kwa Wilaya ya Nkasi. RUWASA wamejipangaje kumaliza ujenzi wa Bwawa la Maji la Mji Mdogo wa Namanyere? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Rukwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, ameendelea kuwa msemaji mkuu wa wanawake wa Mkoa wa Rukwa kuhusiana na suala la maji, nakupongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hili swali inawezekana likaulizwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kuhusu mitambo ambayo Mheshimiwa Rais ameinunua. Mitambo hii iliponunuliwa ni kwamba hatukuwa tumejiandaa na wataalamu wa kuiendesha, matokeo yake mitambo hii imejikuta kwamba ikienda katika maeneo ya porini inakwama na wataalamu wetu wakawa bado hawajaiva kiutaalamu kiasi kwamba ikawa inaleta changamoto sana, lakini kwa sababu hiyo, Mheshimiwa Waziri, Juma Aweso, alielekeza wataalamu wetu wapatiwe mafunzo toshelezi ili waweze kuiendesha mitambo hii na kufanya kazi kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuhakikishia na Bunge lako Tukufu kwamba tayari Mheshimiwa Waziri ametoa mwongozo na kwa mwongozo huo sasa tunaenda kuanza uchimbaji wa visima kwa kutumia hii mitambo ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi sana kuinunua. Sasa inaenda kuanza kufanya kazi kwenye vile visima vitano vitano vya kila Mbunge ambavyo ni visima 900. Kwa hiyo, nakuhakikishia na Bunge lako kwamba mitambo hii sasa iko tayari kuingia kazini na kuweza kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusu Bwawa la Namanyere, Mheshimiwa Waziri ametoa maelekezo ya kutoa fedha takribani shilingi milioni 400 mwishoni mwa mwezi wa nne na tayari kweli, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema zimeshatolewa na zimeshafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaelekeza RUWASA kuhakikisha kwamba bwawa hili sasa linaanza kufanyiwa kazi kwa uharaka zaidi ili liweze kutoa mahitaji ambayo yametarajiwa na kutatua changamoto ya maji katika maeneo ya Namanyere, ahsante sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa furs ana naishukuru Serikali kwa shilingi milioni 500 ambazo zilikwenda kujenga mradi kwenye Kata ya Kimochi katika Vijiji vya Mdawi, Shia, Sango na Kisaseni, lakini havijapata maji. Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia kupata maji katika vijiji hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali ilitenga shilingi milioni 500 na hasa katika bajeti hii ya mwaka 2024/2025 tumetenga fedha nyingine za kwenda kuhakikisha kwamba tunaenda kumalizia vijiji ambavyo vimebaki kufikishiwa huduma ya maji ambavyo ni Vijiji vya Sango, Mdawi pamoja na Shia. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa sababu imekuwa ni ndoto yake kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinapata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Waziri hilo Bwawa la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyere bajeti iliyotengwa ni shilingi bilioni 6.7, fedha iliyoenda ni shilingi milioni 950, leo tunazungumza ni tarehe 12 Juni, tunaenda kumaliza mwaka wa bajeti na mpaka sasa mkataba tu haujasainiwa. Ni upi mkakati wa Serikali ambao upo kuhakikisha hizi fedha zinakwenda na huu mradi unakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto ya bwawa hili na ninatambua kwamba wananchi wake wanasuburi kuona nini kinafanyika na kwa bahati nzuri pia Mheshimiwa Mbunge uliuliza kuhusu hili swali na nikakupa mkakati wa namna gani tunaenda kufanya. Naomba uwe na subira kwa sababu miradi hii inafanyika kwa hatua na mkandarasi akishapewa mkataba maana yake ni kwamba tutaanza kwa kumlipa advance, hatumlipi pesa yote, maana yake ni kwamba pesa nyingine itakayofuatia ni kulingana na ambavyo atakuwa ana raise certificate kulingana na progress ya kazi ambayo atakuwa anaifanya. Kwa hiyo, nakutoa wasiwasi, Serikali inatambua na tunaenda kulifanyia kazi kwa ukamilifu, ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika Kata ya Soya, Kijiji cha Mbarada na ukakutana na wananchi na wakakueleza kilio chao cha uhaba wa maji, ukawaahidi upatikanaji wa maji haraka iwezekanavyo. Ni lini unapeleka mitambo hiyo Kijiji cha Mbarada ili waweze kupata maji safi na salama kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kunti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sikosei Kijiji cha Mbarada kiko Wilaya ya Chemba na katika maeneo ambayo tulisikitishwa sana kama Serikali, baada ya kukuta hali ya upatikanaji wa maji ambayo wanayatumia wananchi wa pale yalikuwa mabaya sana, lakini napenda nimpe taarifa kwamba baada ya ile ziara na mpaka sasa, tukimaliza kipindi cha Bunge hapa, naweza nikakuonesha mitambo imeshafika pale na maji tayari wameshaanza kuona namna ambavyo yanatoka. Tunaamini kwamba uchimbaji na usambazaji wa miradi ya maji una hatua, kwanza kupata chanzo, kutengeneza tenki, kujenga mtandao na baadae kutengeneza maeneo ya kuchotea maji. Kwa hiyo, mradi huu utakamilika na wananchi watapata huduma ya maji, ahsante sana.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika Wilaya ya Serengeti Miradi ya Maji ya Gesaria, Nyamitita, Rigicha na Nyiberekera imekwama kabisa. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serengeti katika eneo la Nyamitita, tayari mkandarasi wetu yuko site, yuko kwenye utengenezaji wa line ya umeme ya kilometa sita. Pia katika eneo la Rigicha mkandarasi tayari yuko katika eneo na anaendelea kurekebisha line ya umeme, lakini katika kijiji ambacho amekitaja, jina lake naomba liingie kwenye Hansard kama alivyolitaja, kuna visima, vituo 30 vya kuchotea maji tayari vimekamilika na asubuhi hii DM alikuwa katika eneo hilo na amenipatia mrejesho wa kazi ambayo imeshafanyika.
Kwa hiyo, namtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kazi inaendelea na tutahakikisha kwamba maji yanapatikana kwa usahihi zaidi, ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pale Bunda tuna mradi wa maji kutoka Nyabihu umekamilika, lakini kuna changamoto ya miundombinu na ninyi Serikali moja ya changamoto ambayo mnakabiliana nayo ni upotevu wa maji. Kuna bomba kubwa kutoka Butakale, Kata ya Bunda Stoo, unaenda Kasakwa kule kwenye tenki, Mlima Balili, inahitajika shilingi bilioni 1.7 kujenga lile bomba ambalo ni chakavu kuokoa maji yasipotee ili wananchi wa Bunda Mjini wapate maji safi na salama. Lini sasa mtatoa hizo shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa bomba kuu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Bulaya kama Serikali tukushukuru kwa kutupatia taarifa kama hiyo. Ni mkakati wa Serikali kuendelea kuboresha miundombinu chakavu yote ambayo inatusababishia kuwa na upotevu wa maji kwa sababu tunayazalisha kwa gharama na yanapokuwa yanapotea maana yake ni kwamba Serikali inaingia kwenye hasara kubwa.
Kwa hiyo, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge nalipokea hilo na nitaenda kulifuatilia ili tuone tunafanya nini kuhakikisha kwamba bomba hilo linaenda kujengwa, ahsante sana.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga. Wananchi wa Itimbo wanauliza, mkandarasi ameshapatikana, ni lini anaenda kuanza kazi katika Kijiji cha Itimbo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali zuri. Mheshimiwa Mbunge kwa kweli tunaendelea kushirikiana vizuri na mkandarasi na ataingia site baada ya mwaka wa fedha kuanza, ahsante sana.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nanyumbu kwenye Kata ya Maratane mwaka jana, mwezi Julai tuliingia mkataba na mkandarasi wa kusambaza maji katika kata hiyo. Hadi sasa hivi mkandarasi hajaanza kazi, sababu kubwa hajapata down payment.
MWENYEKITI: Swali.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, ni lini atapata advance ili aanze kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee kidogo kwenye suala hili.
MWENYEKITI: Kwa kifupi kwa sababu majibu unaweza kuwa umeyasema.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na changamoto na wakandarasi, ni kweli kabisa kuna wengine hawajapata advance payment, lakini wengine hata kufanya ile mobilization hawajafanya, kwa hiyo, inatutia wasiwasi kuanza kuwalipa wakati hata mobilization ambayo iko kwa mujibu wa sheria kwamba tayari ukishapata mkataba unatakiwa kuanza kufanya mobilization. Kazi ambayo tunaifanya sasa hivi ni kuwasisitiza wakandarasi wote ambao tumeingia nao mikataba kuanza kufanya mobilization, tuone commitment yao na Serikali itatoa fedha kwa ajili ya advance payment kuhakikisha kwamba miradi inaanza kutekelezwa, ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Boko, pale Mnemela, Jimboni Kibaha Vijijini kuna tatizo la maji la muda mrefu na wananchi wamechoka kuona mabomba ambayo watu wa DAWASA wanashindwa kuyafanyia kazi. Je, Waziri unatoa agizo gani kwa Meneja wa DAWASA ili aweze kukamilisha mradi ule na watu wa Boko wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa changamoto hii naomba nitumie fursa hii na Bunge lako Tukufu kumwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa DAWASA kwenda kulifanyia kazi eneo hili na kuweza kufanya tathmini, kujiridhisha ukubwa wa tatizo ili Serikali iweze kuchukua hatua na wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali na nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kwa juhudi kubwa ambayo tunaiona jimboni ya kutaka kumaliza kabisa tatizo la maji. Tunavyozungumza sasa hivi mtambo wa kuchimba maji visima virefu kwa ajili ya kufuata maji ya ardhini huko jimboni na kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna shida kubwa sana ya maji katika Tarafa ya King’ori ambayo imebeba Kata za Kikatiti, Majengo, Malula, King’ori, Maruvango, Leguruki, Ngarenanyuki, Uwiro na Ngabobo. Pia eneo hilo maji yana- fluoride...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, swali.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza changamoto hizi za maji eneo hilo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi kuona Mheshimiwa Mbunge anatambua kazi kubwa ambayo inafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kweli mtambo upo na kama ambavyo nilijibu katika majibu mengine, mitambo hii sasa wataalamu tayari wameshapatikana wanaingia site kuhakikisha kwamba visima vinaanza kuchimbwa. Pamoja na hilo, Skimu ya Makilenga inahudumia takribani 50% ya Tarafa ya King’ori. Kwa hiyo, tumwombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba changamoto hii inaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa pia Serikali inashirikiana na mdau wa maendeleo kutoka Korea kuhakikisha kwamba kuna madini ya fluoride katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameongelea na madini hayo sasa tunaenda kufanya mchakato wa kuyaondoa na kuchuja na kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo lile wanapata maji ambayo hayatokuja kuwa na madhara katika afya zao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Serikali tayari imeshaanza kufanya kazi hiyo, nakushukuru sana.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza kwamba, Mheshimiwa Waziri wanasema uhondo wa ngoma uingie ucheze. Naomba, kama itawezekana, Wizara ije kwenye Tarafa ya Ngerengere. Kiukweli kabisa, sisi wakazi wa Kata ya Tununguo tuna changamoto kubwa sana ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kusikia kwamba kwamba tutapata visima sita, lakini hayo maji hayanyweki kabisa. Je, Serikali ni lini itaweza kutoka kwenda kwenye Tarafa nzima ya Ngerengere ili kuona hatima ya sisi Wanangerengere kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto iliyopo katika Tarafa hii ya Ngerengere. Vilevile nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa kushirikiana na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kubainisha maeneo yenye changamoto ya maji ili Serikali ikachukue hatua na wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sekta ya Maji iko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kujionea hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ili nasi tuingize katika mipango yetu ya muda mfupi na kati ili kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Je, ni lini Mradi wa Maji wa kutoka Mto Kiwira kwenda Jijini Mbeya utakamilika ukizingatia Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 117, na mpaka sasa ni fedha kiasi cha shilingi bilioni 14.3 tu ndizo zilizopelekwa na hili jambo tumeanza kuongea tangu mwaka 2020? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma ya maji katika vijiji vyote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya vijiji 12,318 Serikali tayari imeshafikisha huduma ya maji katika vijiji takribani elfu tisa mia saba na kitu. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira kwa sababu Serikali tayari imeshatoa fedha kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) ambao tayari wameshapokea takribani shilingi bilioni 154. Vilevile Mamlaka za Maji Mjini wameshapokea takribani bilioni 69.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakandarasi ambao wako site waendelee kufanya kazi kwa weledi na maarifa na kuhakikisha kwamba wanawasilisha hati za madai ili waweze kulipwa na kuendelea na kazi ili Watanzania wapate huduma ya maji, ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, mwaka 2023 Serikali iliahidi kuchimba visima 12 katika Jimbo la Same Magharibi kwenye Kata ya Ruvu, Station, Makanya, Mabilioni, Hedaru na Bangalala, lakini gari la Mkoa wa Kilimanjaro lilikuja likachimba visima viwili tu.
Je, hilo gari la Mkoa wa Kilimanjaro lililotolewa na Mama Samia Suluhu Hassan, litarudi lini Same ili kukamilisha visima 10 vilivyobaki ?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba Mheshimiwa Rais alitoa fedha kwa ajili ya kununua gari hizi. Shida iliyopo ni kwamba bajeti yake kidogo ilikuwa na changamoto. Sasa mwongozo umeshatolewa, kwamba magari haya yatarudi katika maeneo husika na kuendelea na uchimbaji wa visima vya maji ili wananchi wapate huduma ya maji. Ahsante sana.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mradi wa Oldonyosambu wenye vijiji takribani tisa ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli; na kwa kuwa ni mradi wenye athari kubwa kwa sababu ya floride na wananchi wanateseka na floride: Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi huo ambao sasa umechukua zaidi ya miaka minne ikitekelezwa kidogo kidogo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza miradi yote inayotokana na ahadi za Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi 2020/2025. Vilevile inaendelea kutekeleza ahadi za viongozi wa kitaifa akiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu. Kwa, hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kuiangalia changamoto hiyo na kutafuta fedha za kutosha ili kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika kwa wakati, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa kuwa Wizara ya Maji inalo jukumu la kufikisha huduma ya maji kwenye taasisi ambazo zinatoa huduma kwenye jamii: Je, Serikali itafikisha lini huduma ya maji kwenye shule ya sekondari iliyopo Kata ya Kagondo, Bukoba Mjini, shule ya msingi iliyopo Kata Kaharoro, Shule ya Msingi Kibeta, Shule ya Msingi Rwamishenye, Shule ya Sekondari Nyanga, Kituo cha Afya Nyanga pamoja na Kituo cha Afya Ijuganyondo ili wananchi na watoto wetu wa Jimbo la Bukoba Mjini waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua maji ni msingi wa uhai wa binadamu na engine ya maendeleo kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameiongelea, kwa sababu iko ndani ya mipango ya Serikali. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, na kwa namna ambavyo anaendelea kuisemea, nasi Serikali tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba wanafunzi, vituo vya afya na taasisi nyingine zote zinapata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huu mradi wa vijiji 14 Nchinila – Engusero umechukua muda mrefu sana: Je, Serikali ina kauli gani ya kusukuma mradi huu ili umalizike na wananchi wapate maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kiteto ni kame sana, je, Serikali ina kauli gani kuhusu kutupatia kipaumbele cha mabwawa ili wananchi wa Kiteto wanufaike na maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, nikiri na Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele kupigania mradi huu ili uweze kukamilika. Sasa kwa sababu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu kupitia kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nasi sekta ya maji Mheshimiwa Waziri tayari ameshaingiza kwenye mpango wa utekelezaji katika mwaka huu wa fedha, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kusoma bajeti tarehe tisa, utaona tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kwenda kusukuma mradi huu ili ukamilike kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira tu, siku bajeti ya Wizara ya Maji itakapofika hapa, basi makofi yake yatasaidia kupitisha bajeti hiyo ili wananchi wa eneo lake wakapate huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; ni kweli kabisa kwamba Wilaya ya Kiteto ina changamoto ya ukame. Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali na inaendelea kujiridhisha na vyanzo vya maji ili kuhakikisha kwamba wilaya hii inapata huduma ya maji safi na salama. Kwa hiyo, kwa kuanzia ni kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri, kwamba kwenda kujenga mabwawa pamoja na malambo, ambapo mpaka sasa kuna malambo ya Dongo, huko tunaendelea na utekelezaji. Kuna Dosidosi, Bwawani, Kijungu pamoja na Lambo la Makame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba tutakapoona maji bado hayajawa toshelezi, tutaendelea kwenda kuongeza miundombinu na kuhakikisha kwamba maji yanatosha katika eneo la Kiteto, ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Wananchi wa Kata ya Nhati bado wana changamoto kubwa ya maji, je, ni lini Mradi wa Darakuta - Minjingu utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini. Namwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kikao hiki cha Bunge tuonane ili tuweze kupata taarifa za kina kuhusu mradi wake kwamba umefikia katika hatua gani, ahsante sana.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mradi wa Matamba – Kinyika umeanza kujengwa mwaka 2019, lakini hadi leo umekuwa ni mradi unaosuasua, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mradi huu ili wananchi wa Matamba na vijiji vinavyozunguka Matamba viweze kupata maji kwa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Deo Sanga. Kwa kweli Wizara tunampongeza kwa sababu ya usimamizi mzuri wa miradi ndani ya jimbo lake; na katika ile miradi ya P4R Makete ni kati ya majimbo ambayo yamefanya vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba mradi huu wa Matimba – Kinyika upo katika zile hatua ambazo tunaamini wakandarasi wanasubiri fedha. Watakapo-rise zile certificate, basi watakapolipwa wataendelea na utekelezaji wake. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana ili kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata maji safi na salama.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kuipongeza Wizara ya Maji kwa kazi nzuri sana kwa sababu kata hii ilikuwa ina changamoto kubwa sana ya maji. Sasa, nina swali moja tu la nyongeza. Je, Serikali iko tayari baada ya kukamilisha mradi huu kuhakikisha kwamba wananchi ambao wako pembezoni na kata hii pia wanapata maji? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omari Kigua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa takribani shilingi bilioni 39 katika kufanya miradi 13 katika Jimbo la Kilindi. Katika jimbo hili, miradi tisa inafanywa kwa Mfumo wa Wakandarasi na miradi minne wanafanya kwa Mfumo wa Force Account.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwamba miradi hii 13 itakapokamilika, vijiji 78 vinaenda kunufaika na wakazi takribani 239,810 watanufaika na mradi huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pindi miradi hii itakapokamilika Serikali itaenda kuanza kupanua wigo wa upatikanaji wa maji vitongojini kulingana na upatikanaji wa fedha. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Kata ya Mishamo una zaidi ya miaka miwili haujakamilika. Je, ni lini mradi huo utaweza kukamilika katika kipindi hiki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso. kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba miradi yote ya maji inakamilika. Pia tunaendelea kuhakikisha kwamba tunakuwa na mawasiliano ya karibu sana na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuhakikisha kwamba, wakandarasi ambao watakuwa wamewasilisha hati za madai, walipwe na kuendelea na miradi mingine ili Watanzania wapate huduma ya maji bila…
Mheshimiwa Naibu Spika, lini utakamilika? Itategemea sasa na namna gani wakandarasi wameji-align kuhakikisha kwamba wanakamilisha miradi yao na kuweza kuwasilisha kazi za baadaye.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Tunaishukuru Serikali kwa kuchimba visima nane katika Jimbo la Mbulu Mjini na hadi sasa hakuna kisima kilicho tayari kwa ajili ya kujengewa miundombinu. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya visima vyote nane katika Jimbo la Mbulu Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko kwenye mkakati wa kuhakikisha kwamba miundombinu ya maji inajengwa ili huduma ya maji iweze kutolewa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika bajeti yetu ya mwaka huu, tutahakikisha tunazingatia hayo mahitaji ili wananchi wa Mbulu waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji katika Kata ya Kimochi, Moshi Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipokee changamoto hii kwanza nikaielewe kwa kina ili tuweze kuifanyia kazi kulingana na uhitaji wake. Nakushukuru sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji wa Mwanga – Same – Korogwe ili kuzisaidia Kata za Mkomazi na Mkumbara ambazo ziko mwishoni mwa mradi huo? Nakushukuru (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso alikuwepo Kilimanjaro na alikuwa kule kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miradi ya maji iliyoko katika Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Tanga inakamilika kwa wakati. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wake, miradi hii itakamilika ndani ya mwaka huu wa fedha.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, gari lililonunuliwa na Serikali na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuchimba maji katika mikoa yote ikiwemo Mkoa wa Singida, magari hata hayatulii sehemu moja na usimamizi wake umekuwa haueleweki. Je, Serikali imejipangaje ili miradi ya maji katika vijiji na katika maeneo yetu iweze kufanyika vizuri?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Massare, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Suluhu Hassan aliagiza magari ya kuchimbia visima na hii ilikuwa ni fursa kubwa sana kwa Watanzania. Kwa hiyo nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, kuwaelekeza ma-RM wote nchini kuhakikisha kwamba haya magari hayakupelekwa kwa ajili ya kwenda ku-park, yamepelekwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi ili Watanzania wapate maji na nitafuatilia ili kuona utekelezaji unaendaje. Ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Matwiga, awamu ya pili ambao ulianza toka 2012 unaenda kwa kusuasua sana. Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kutosha ili Vijiji vya Mazimbo, Mtanila, Ifuma na Lupa viweze kupata maji haya? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa mradi huu ulianza mwaka 2012, lakini unaenda kwa awamu. Awamu ya kwanza unahusisha vijiji viwili vya Matwiga pamoja na Isagawana na awamu hiyo ishakamilika tayari, wananchi wanapata maji. Awamu ya pili ambayo inahusisha vijiji sita, upo katika asilimia 90. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira, mradi huu utakamilika mwaka huu wa fedha na wananchi watapata maji.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini ujenzi wa Tanki la Maji la Tukuyu Mjini Wilayani Rungwe utakamilika ukizingatia tanki lile ni la muhimu sana linahudumu Kata ya Bulyaga, Makandana, Bagamoyo, Tukuyu Mjini, Kawetele na Ibighi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ni mkubwa na ni wa muhimu sana kwa Watanzania. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge anipe nafasi, nikaufanyie kazi, lakini pia nitampa mrejesho kwamba mradi huu upo katika hatua gani na wapi umekwama na chanzo ni nini ili tuweze kuufanyia kazi kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji. Nakushukuru sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nimepokea majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika mwaka wa fedha ambao tunaumaliza mwezi ujao, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga Mradi wa Mji wa Namanyere wenye gharama ya bilioni 6.75. Mpaka sasa hapa ninapozungumza bado mwezi mmoja tu na wamepeleka milioni 950. Je, ni lini watapeleka fedha iliyobaki kwa muda huu uliobakia na mkandarasi aende site kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri hapa kwamba upatikanaji wa maji ni 50%, lakini upotevu wa maji ni 47%. Je, Serikali hawaoni kwamba kuna haja sasa ya kupeleka fedha haraka ili tuanze ukarabati, kwa sababu hata kwenye hicho kiasi kidogo kinapotea?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, anafanya kazi kubwa sana kwa wananchi wake wa Nkasi Kaskazini na kwa kweli anaendelea kushirikiana vizuri sana na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba anashiriki katika utekelezaji wa miradi inayopatikana katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba tuna mradi wa bilioni 6.75 na mwisho wa mwezi huu Serikali tunakwenda kusaini mkataba na mkandarasi ili aweze kuingia. Hizo fedha ambazo zilitengwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024 ni fedha ambazo ni kwa ajili ya malipo ya awali. Kwa hiyo, mkandarasi akishasaini mkataba basi fedha hizo atalipwa na ataingia site kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu upotevu wa maji. Ni kweli kabisa, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, kwamba upotevu ni 47% ilhali upatikanaji wa maji ni 52.9%. Kikubwa ambacho naweza kukisema hapa ni kwamba, upotevu wa maji unaweza ukatokana na miundombinu, usimamizi na teknolojia tunayoitumia. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo. Tunaondoka kwenye mechanical meters tunakwenda kwenye smart prepaid water meters.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni katika kuhakikisha pia kuwa tuna-reduce upotevu wa maji na vile vile kuhakikisha kwamba tunapeleka. Mwezi Aprili Mheshimiwa Mbunge tumempelekea shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa Mji wa Namanyere. Hii ni katika kuhakikisha kwamba ule uharibifu na upotevu ambao ulikuwa unatokea, basi wananchi waweze kurejeshewa huduma na waweze kupata maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuwasaidia wananchi wa Mji wa Karatu, ambao wamepata changamoto ya kujaa bwawa pale Mji wa Karatu na pampu mbili kushindwa kufanya kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali daima imekuwa na utaratibu wa kuchukua hatua za dharura pale ambapo panatokea matukio ya dharura. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, naomba nilipokee na tuwaagize wataalam wetu wakafanye tathmini ili tuone kwamba tunatakiwa kuchukua hatua gani ili kutatua changamoto hiyo. Ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dodoma bado linakumbwa na adha kubwa ya upatikanaji wa maji. Pamoja na jitihada kubwa za DUWASA kuchimba visima Nzuguni lakini maji bado ni shida kwa wakazi wa Dodoma. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuiongezea fedha DUWASA ili iweze kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Jiji la Dodoma? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua na Serikali inatambua changamoto ya maji. Tunatambua umuhimu wa kuwa na maji ya kutosha kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kwa sababu ndiyo Makao Makuu ya Nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mkakati wa muda mfupi wa kuchimba visima vya Nzuguni pamoja na Nala vile vile tuna mpango wa kati na muda mrefu. Juzi hapa tumetangaza tender ya Bwawa la Farkwa ambapo tunaamini kwamba Bwawa hilo likishapata mkandarasi na kuanza kujengwa litatatua. Huo ni mpango wa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imejipanga kuhakikisha kwamba DUWASA inaongezewa nguvu ili iweze kutatua changamoto ambazo zinajitokeza kila mara. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Bajeti ya mwaka huu tulipangiwa kuchimbwa visima Mbulu Vijijini. Je, ni lini watachimba visima hivi ili wananchi wapate maji?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kifupi.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijasikia vizuri.
MWENYEKITI: Anasema hajasikia vizuri.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka huu ambayo inakwisha mwezi ujao kuna visima vitano tulikuwa tuchimbe Mbulu Vijijini. Je, ni lini tunachimba visima hivi ili wananchi wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpomgeze Mheshimiwa Flatei Massay kwa kazi nzuri anayoifanya. Serikali na Sekta ya Maji tuna maelekezo mahsusi kutoka kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupitia miradi yote ya 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024 ili kuhakikisha kwamba kule ambako tumeshafanya mkataba na wananchi kwamba tunawapelekea maji basi miradi hiyo tukaikamilishe kwa wakati ili Watanzania wapate maji safi na salama. Ahsante
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nyasa ni miongoni mwa Wilaya ambazo zina changamoto kubwa sana kutokana na ukubwa wa jiografia yake lakini pia hata maumbile yake, milima, mabonde na barabara nyingine ni mbaya za vumbi. Kwa hiyo, unakuta miradi mingi ya maji haikaguliwi vizuri kutokana na kutokuwa na gari. Je, Mheshimiwa Waziri haya majibu yako ya leo yatakuwa ni ya ukweli? Kwa sababu hata mwaka juzi ulinijibu hivyo hivyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na changamoto hizo na ucheleweshaji mkubwa wa kuagiza magari, ni namna gani mtafanya huduma ya haraka hasa katika maeneo hayo ambayo yanachangamoto kubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu haya ya Serikali ni majibu ya kweli, lakini ni kweli kabisa kwamba vitendea kazi vimechelewa na kwa sababu ya utaratibu wa mchakato wa manunuzi sisi kama Wizara, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha shilingi bilioni 6.14 kwa ajili ya ununuzi wa hayo magari 35 lakini yakiwa yanazingatia mahitaji ya maeneo mbalimbali na jiografia ya maeneo mbalimbali na ndiyo maana tuna magari aina ya Hardtop, tuna Double Cabin, na pia tuna Nissan ambayo yanaenda kugawanywa kulingana na hali halisi ya maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, majibu ya swali la pili, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ina azma ya kuhakikisha kwamba ina harakisha upatikanaji wa miundombinu safi ili kuweza kutoa huduma ya maji kwa wananchi. Hivyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, na ni kweli kabisa amekuwa akiongelea changamoto hii. Sisi kama Serikali tunaendelea kuipokea lakini pia Serikali ina mkakati wa kuhakikisha kwamba miradi ambayo imechelewa kukamilika tunaenda kuikamilisha ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na niishukuru Serikali kwa majibu ya uhakika yanayotia moyo na nina hakika kwamba wananchi wa kule Kalambo wameyasikia.
Kwa kuwa tatizo lililopo kule Kalambo mMoani Rukwa, linafanana kabisa na tatizo lililopo katika tambarare ya Mkoa wa Kilimanjaro Wilaya ya Rombo na Wilaya ile tuna Ziwa Chala, ni lini sasa Serikali hii itatumia Ziwa Chala kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Wilaya ya Tambarare ya Rombo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, Serikali ipo tayari kutumia vyanzo vya maji vya uhakika katika kuhakikisha kwamba tunawasogezea huduma ya maji wananchi katika maeneo mbalimbali wenye maeneo ya kijiografia yanayofanana na Kalambo kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge mama yangu alivyopendekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ziwa Chala tunapokea ushauri huo kama Serikali tutaenda kulifanyia kazi tuone urahisi zaidi kwa namna ambayo maji yataweza kuwafikia kwa gharama ambayo itakuwa inakubalika kwa wananchi wa eneo husika, ahsante sana.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Vijiji vingi vya Wilaya ya Kyerwa havina maji safi na salama licha ya kwamba tuna vyanzo vya kuaminika vya Mto Kagera lakini pia na Ziwa Victoria. Kata za Songambele, Lwabwele, Nyakatuntu, Businde, Bugara kuna changamoto kubwa ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua ni lini Serikali itatumia hivi vyanzo vya uhakika vya mto Kagera na Ziwa Victoria kuwapatia wananchi wa Wilaya ya Kyerwa maji safi na salama? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri kwa ajiri ya wananchi wa Kyerwa lakini pia Serikali imeshatoa kibali cha kutangazwa kwa Mradi wa Songambele wa shilingi bilioni 1.9 lakini vilevile Mradi wa Kigologolo kisima kimeshachimbwa. Nawapongeza sana waheshimiwa wabunge wote kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo, Mheshimiwa Bilakwate, mmefuatilia kwa ukaribu sana mradi huu na sisi kama Serikali tutaendelea kuhakikisha kwamba tunawaunga mkono... (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kifupi, kwa kifupi sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Lihilimaliyao katika Jimbo la Kilwa Kusini ndiyo kata yenye changamoto ya ukosefu wa maji iliyokithiri zaidi. Hapa Bungeni uliahidi kwamba...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali lako.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nauliza swali, lini Mheshimiwa Naibu Waziri atatekeleza ahadi ya kwenda Lihilimaliyao, Kilwa Kusini ili tukatatue changamoto ya maji katika kata hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea wito wa Mheshimiwa Mbunge na baada ya Bunge lako Tukufu kuahirishwa tutapanga ratiba kwa ajili ya kufika katika eneo hilo na kujionea hali halisi.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufuatilia kwangu hali ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, nimekuta kwamba Mradi huu wa Makonde ulikuwa ukamilike mwaka 2024, lakini mkandarasi ameongezewa muda na ni kutokana na hali ya ucheleweshaji wa malipo.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba sasa mradi huu unatekelezwa na unakamilika Disemba, 2025 kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa nifahamu kwamba je, Serikali imeweka utaratibu gani kuhakikisha kwamba miradi mingine ikiwa ni pamoja na ule wa Mto Ruvuma yote inakamilika kwa wakati? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu sana utekelezaji wa miradi hii kwa faida ya wananchi wa eneo lake. Ni kweli kabisa mradi huu unaenda kukamilika Disemba, 2025 na Mheshimiwa Mbunge amegusia namna ambavyo ulitakiwa kukamilika mwaka 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu nature yake ni design and build. Maana yake kwamba tunakuwa tunafanya design na ndiyo tunaendelea kujenga, kwa hiyo, muda ambao ulikuwa umetolewa wa kwanza wa kufanya feasibility study na kuja kufanyia mapitio ulisababisha tufanye extension ambapo mradi huu tunauhakika utaenda kukamilika mwaka 2025...
Kwa upande wa swali la pili ni kwamba miradi yote nchini tumeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba fedha zinapelekwa katika miradi mbalimbali ili iweze kukamilika kwa wakati, ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Wilaya ya Kyerwa tunamradi wa vijiji 37 wenye thamani ya shilingi bilioni 58. Mradi huu unaenda kuhudumia Kata ya Kyerwa, Yaluzumbula, Nyakatuntu mpaka Kamuli. Mradi huu ni lini utatangazwa ili wananchi waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mradi muhimu sana tunatambua na Wizara imeshaandika kuomba kibali ili uweze kutangazwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba unaanza kujengwa kwa ajili ya maslahi ya wananchi wa Kyerwa, ahsante sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa sababu Mradi wa Maji wa Makonde ni mradi ambao ni wa muda mrefu, Serikali mwaka 2022 ilituchimbia visima kwenye Kijiji cha Mpalu na Lochinu kwenye Jimbo la Newala Vijijini, lakini visima vile havijasambaza maji mpaka kwa wananchi. Je, ni lini Serikali itapeleka miundombinu ili yale maji kwenye visima yafike kwa wananchi? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, visima vyote ambavyo tumeshavichimba na tumesha-test, tumeshafanya pump test, tunaenda kuhakikisha kwamba sasa tunaenda kujenga a point source kwa ajili ya wananchi kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri, lakini je, kutokana na wananchi wa Jimbo la Temeke, kuna malalamiko ya kwamba wananlipa maji ambavyo hawatumii kihalali.
Je, ni lini sasa ndani ya Jimbo letu la Temeke mtaanza kufunga hizi pre paid meters?
Swali langu la pili, ni lini sasa mtafunga nyumba hizi ambazo zinamilikiwa na taasisi za Serikali, mfano TBA, wapangaji wanapoanza kupanga nyumba wanakuta kuna bili zile za nyuma, je, ni lini sasa mtafunga hizi meter katika hizi nyumba za Serikali ili anayepanga asikute ile bili inayotokana na aliyepanga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua changamoto ya bili kwa wananchi lakini vile vile kwa kufuatia maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kupunguza malalamiko kwa kufunga pre paid water meters ili kusaidia wananchi wasiwe wanawekewa bili ambazo haziendani na matumizi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari kupitia Wizara imeshaandika andiko dhana kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi na tayari kuna maeneo ambayo tayari tumeshaanza kufunga kama ambavyo nimetaja, lakini kwenye taasisi na siyo TBA peke yake, taasisi nyingi ambazo tunaamini kwamba namna ya kudaiana inakuwa na changamoto, sisi huko ndiyo kipaumbele chetu ili kuhakikisha kwamba hata yale mapato ambayo yanatokana na malipo yao yatatusaidia katika uendeshaji wa miradi yetu ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Temeke nikuhakikishie kwamba mfumo huu utakapokamilika hatutaki tuwe na mifumo mingi ndani ya nchi moja, ndani ya mamlaka mbalimbali, tunataka tuwe na mfumo mmoja ambapo kama Moshi, Mwanza, Dar es Salaam wote watatumia mfumo mmoja ili kuhakikisha kwamba tuna uwezo wa ku-regulate pre paid water meter zote ambazo tunaweza kuzifunga kwa wananchi na kuweza ku-monitor utumiaji na upatikanaji wa mapato kulingana na matumizi ya wananchi husika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji ya Chimala pamoja na Ruiwa, pamoja na kwamba utekelezaji wake umeanza, lakini unakwenda kwa kusuasua. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ya kutosha ili miradi hii iweze kukamilika kwa wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye Wilaya ya Chunya Serikali iliweza kuchimba visima 16 na tunashukuru kwa hilo. Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwenye Vijiji vya STAMICO, Upendo, Lualaje, Supermarket, Sipa na Nkwangu ili miradi hii iweze kutekelezeka na wananchi hawa waweze kunufaika na mradi wa maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Kasaka kwa swali ambalo ameuliza, lakini pia kuhusu upande wa Chunya amekuwa akifuatilia sana maeneo haya kuhakikisha kwamba katika vile visima 16, basi vinaendelea kutoa maji lakini katika vijiji ambavyo amevitaja, tunaendelea kuviweka katika mpango kuhakikisha kwamba vinapata huduma safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Chimala, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, Serikali inaendelea kupeleka fedha kwa kadiri zinavyopatikana ili kuhakikisha kwamba miradi yote nchini ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji inakamilika na kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi mkubwa wa kisima kirefu cha maji cha Alailalai Kata ya Gelai Lubwa Wilayani Longido ulitengewa fedha tangu mwaka 2023 na mkandarasi alipatikana, lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea. Je, nini mpango wa Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Catherine alishaulizia huu Mradi wa Longido na maeneo mengine ya Mkoa wa Arusha. Nampongeza sana kwa kuwa karibu na kufuatilia kwa ukaribu miradi ya maji katika Mkoa wa Arusha. Ni kweli kabisa mkandarasi hajaingia na sasa tupo katika hatua za mwisho kabisa kuhakikisha kwamba mkandarasi anaingia site na kuanza utekelezaji wa mradi huo, nakushukuru sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Kumuyange na Ntobeye Wilaya ya Ngara hadi leo mkandarasi hajafika site. Je, ni lini utekelezaji wa mradi huo utaanza ili kuwatua ndoo wakina mama wa Kata ya Ntobeye na Kata ya Kigina?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Kagera, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Kagera akiwemo Mheshimiwa Oliver kwa kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kwa kutetea miradi hii ambayo inaendelea kutekelezwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upekee kabisa Mheshimiwa Semuguruka amekuwa karibu sana na kutusaidia mpaka kuainisha maeneo ambayo yanaweza yakawa na vyanzo vya maji ambavyo vinaweza kutusaidia kuhakikisha kwamba wananchi wa Ngara na Mkoa wa Kagera wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama. Mkandarasi huyu yupo katika hatua za mwisho za mobilization ili kuhakikisha kwamba anaingia site na kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mradi unaanza mara moja, ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kijiji cha Sambaru Kata ya Mang’onyi Jimbo la Singida Mashariki ni miongoni mwa vijiji ambavyo ni vikubwa sana na kimsingi kilitakiwa hata kiwe kata, lakini akina mama wa Sambaru wanatumia muda mrefu sana na wanateseka sana kutafuta maji. Je, ni lini Serikali itapeleka mradi wa maji katika Kijiji cha Sambaru Kata ya Mang’onyi Jimbo la Singida Mashariki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba tunamtua mama ndoo kichwani. Nampongeza sana Mheshimiwa Nusrat kwa taarifa hii, na nimhakikishie tu kwamba baada ya Bunge lako hili, tutaonana ili anipe taarifa ya kina ili tuweze kuona ni sehemu gani hasa ambayo inahitaji huduma hiyo, nasi tutume wataalam wetu wakafanye usanifu na kujiridhisha kwamba mradi huo utahitaji kiasi gani, tuweze kuingiza kwenye mpango kwa ajili ya kutekeleza mradi huo. Nakushukuru sana.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali aliyoyatoa, nitakuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna miradi ya maji katika Kata za Oldonyosambu, Oldonyowas, Kimnyaki, Tarakwa, Siwandeki, Kiranyi, Oljoro na Naroi wakandarasi hawajalipwa fedha, ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi hao ili miradi hiyo iweze kukamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, kwa kuwa miradi mingi ya maji hapa nchini imekwama kwa muda mrefu, kuna mingine yenye miaka miwili mpaka mitano, Serikali haioni ni wakati muafaka kuweka mkakati mahsusi kupata vyanzo vya uhakika vya fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saputu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Saputu kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya na aliweza kufuatilia kwa ukaribu sana maeneo ya Oldonyosambu na Siwandeti pamoja na Tarakwa. Napenda kutumia fursa hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imepeleka kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya hii Kata ya Oldonyosambu. Vilevile fedha hizi baada ya kupelekwa, tayari kuna mabomba ya chuma ambayo yamepelekwa pale kwa ajili ya kutandaza karibia kilomita tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Siwandeti, mzabuni anaendelea kuleta mabomba ya plastic na tunaratajia katika hizi Kata za Siwandeti pamoja na Tarakwa mradi utakamilika ifikapo Desemba 2024, na kwa upande wa Olmuro RUWASA, mradi huu tayari umeshafikia asilimia 28 na tunaamini kabisa kwamba madai yale ambayo mkandarasi anaitwa Help Desk tayari amelipwa hati ya madai tarehe 28 mwezi wa Sita na tunaamini kabisa kwamba tayari amesharudi site na tunamwomba ahakikishe mradi huu unakamilika kwa wakati kama ulivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upande wa miradi ambayo imekwama. Ni kweli kabisa tunatambua kuna miradi mingi ambayo ilianzishwa nchini na haijakamilika. Serikali kupitia Wizara ya Maji, na kwa kupitia Waziri wetu, tumeelekeza kuwa hakuna haja ya kuanza kutangaza miradi mipya na kupeleka pesa wakati kuna miradi ambayo imeshafikia 70% au 80% ama 90% inaachwa ina-hang halafu tunaanzisha mradi mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeelekeza Mameneja wote wa Mikoa wa RUWASA na Mameneja wote wa mamlaka mbalimbali wahakikishe miradi yote ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji inapelekewa fedha na kukamilika kwanza kabla ya kuanza kutangaza miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mkakati wa sasa ambao tunahakikisha kwamba tunaufuatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha kwamba tunakamilisha miradi yote.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itaanza kuweka miundombinu katika visima ambavyo vimejengwa katika Kijiji cha Mtandika na Kituo cha Afya cha Ruaha Mbuyuni, kwa sababu muda mrefu vimechimbwa lakini hakuna miundombinu yoyote ya mabomba wala usambazaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Kijiji cha Mtandika kuna hii changamoto na tunatambua kwamba kuna kisima Serikali imeshakichimba pale. Nimhakikishie kwamba Serikali tayari imeshajipanga kwenda kuhakikisha kwamba miradi yote inaenda kuwekewa miundombinu ili kuhakikisha kwamba inatoa maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ila niseme tu nasikitishwa na majibu ya Mheshimiwa Waziri. Ni kweli kabisa kwamba mradi huu wa Mang’ola Juu umeanza ni takribani miaka mitatu sasa na umekuwa ukisuasua, umefikia 30% tu. Je, Serikali haioni kwamba mradi huu unakosa value for money? Serikali inachukua hatua gani za dharura kuhakikisha kwamba wananchi wa Mang’ola Juu wanapata maji kwa wakati kama ilivyokusudiwa hapo awali?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, tuna mradi wa maji wa Ziwa Victoria ambao unatoka kwa wananchi wa Rorya, Tarime Mjini na baadhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, lakini mradi huu nao utekelezaji wake umekuwa ukisuasua na ulitarajiwa kukamilika mwaka 2025, lakini mpaka sasa hivi ni 12.5% tu zimetekelezeka na mkandarasi ameondoka site kwa sababu ame-rise certificate ya 4.3 billion, hajalipwa mpaka sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua, ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inakuwa na uhalisia wa utekelezaji wa miradi hii ya maji ili wananchi wa Tarime wajue kwamba kufikia 2025 ni kweli mradi huu unaenda kutekelezeka?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ambavyo limeulizwa na Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unapoanza, tunaanza na feasibility study na baada ya hapo tunafanya usanifu na baada ya hatua zote hizo ni utekelezaji wa mradi. Unapoanza kwenye upembuzi yakinifu, usanifu, hizo zote ni hatua, lakini sasa tunapokuja kwenye execution ya mradi ndipo sasa tunapoona kwamba zile asilimia zinapofikia tunaelewa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, nakiri kwamba mradi huu ulianza miaka mitatu iliyopita, lakini kuanza rasmi ujenzi wenyewe hauna muda mrefu kama ambavyo Mheshimiwa ameugusia. Ninachotaka kusema ni kwamba Serikali imejidhatiti kuhakikisha kwamba miradi hii, kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaendelea na falsafa ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani, tutahakikisha mradi huu wa Mang’ola Juu unakamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo linaenda sambamba na suala la mradi wa Ziwa Victoria kutokea kule Rorya. Ni kweli nakiri kabisa kwamba tulipata changamoto na mkandarasi hapa katikati, lakini tayari tuko kwenye mazungumzo naye ili kuhakikisha kwamba anarudi site na kuhakikisha kwamba mradi unaendelea wakati mahitaji yake na madai yake yanaendelea kufanyiwa kazi na Serikali, kwa sababu tunajua kabisa kwamba Tanzania hii tutaijenga sisi wote na wakandarasi ni Watanzania wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Je, ni lini mradi unaoendelea katika Kata ya Mwika Kusini utakamilika? Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari tuongozane mguu kwa mguu kwenda kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa sababu wananchi hawa wanateseka sana kwa shida ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuongozana mguu kwa mguu, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa Wilaya ya Nkasi ina changamoto kubwa ya maji. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kupeleka mpango wa dharura ikiwemo kuchimba visima na mabwawa?
Swali la pili, ni lini mradi wa Isale utakamilika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe nelson Mwakang’ata, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwapigania wananchi wa Mkoa wa Rukwa katika miradi yetu ya maji na hakika kweli tunaendelea kushirikiana nae kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za maji.
Mheshimiwa Spika, Serikali tunao mpango wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu lakini mradi unaoendelea ni mpango wa muda mrefu. Ni kweli bado kuna changamoto ambapo Serikali tumeamua kuchimba visima vitatu ambavyo vinaenda kutatua changamoto ya maji na kuna visima vingine vitatu tunaenda kuvichimba katika mwaka huu wa fedha lakini visima hivyo vitakamilika katika mwaka wa fedha ujao. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, vilevile swali la pili, mradi wa Isale mpaka sasa umefikia asilimia 75 ya utekelezaji wake, mradi huo unagharimu takribani shilingi milioni 643, mpaka sasa Serikali imeshamlipa mkandarasi takribani shilingi milioni 262. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba mkandarasi ataendelea kwa kasi ile ile ili akamilishe mradi huu na tunaamini kwamba kwa sababu mkandarasi mwenyewe anaitwa Vibe International tunaamini kwamba atakuwa site ili akamilishe miradi hii kwa wakati na wananchi wapate maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.
Je, ni lini Serikali itamaliza kero ya maji katika Kata ya Malili, Ngasamo na Shigala Wilayani Busega? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunao mradi mkubwa wa Ziwa Victoria ambapo Serikali tayari imeshaingia mkataba na mkandarasi, tayari yuko site. Mradi huo utapita katika Wilaya ya Busega, Bariadi mpaka Itilima na kwa awamu ya pili utapita Maswa na Meatu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tunaendelea na miradi midogo midogo, tunavyo visima ambavyo vinaendelea kuchimbwa katika Wilaya ya Busega na Wilaya nyingine lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kwani miradi hiyo itakapokamilika basi tukaendelee kuisemea Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwani utekelezaji wake ni kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Mto Ruvuma kumaliza kabisa tatizo la maji katika Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa mradi huu ni mradi wa kimkakati kwa Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi, kwa kutambua umuhimu huo na Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakifuatilia sana akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea, Serikali inaendelea na mapitio ya usanifu wa mradi huu wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma ili yafike mpaka Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Serikali imeshafikia katika hatua nzuri na tuombe tu kwamba pindi tutakapoenda katika hatua ya utekelezaji Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba waweze kutoa ushauri, michango na maoni yao tutayapokea na kuyaingiza katika utekelezaji halisi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali inaweza kuharakisha kutoa kibali cha ujenzi wa uboreshaji wa maji Mjini Namtumbo, kwani ipo katika Bajeti hii ya 2023/2024?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimwa Vita Kawawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jana nimekutana na Mheshimiwa Vita Kawawa na akawasilisha changamoto hii. Nimhakikishie kwamba suala hili nililifikisha kwenye mamlaka husika na tayari kibali kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wetu anasema, Wizara ya Maji lengo letu ni kufikisha huduma ya maji safi na salama, hatutakuwa kikwazo. Kwa hiyo, kibali hicho kitatoka mara moja na mradi huo utaanza mara moja bila kuwa na kikwazo chochote, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa majibu ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa mradi huu utaanza Agosti, 2024 na sasa ni wakati wa bajeti, Serikali imejiandaa kutenga kiasi gani cha kuanza kutekeleza mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniventura Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya. Serikali kupitia yeye imefikisha miradi takribani nane katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024. Miradi hiyo inaenda kutoa huduma katika vijiji 39 ambavyo vina wakazi takribani 30,350, ambapo zaidi ya bilioni 18 zimetengwa kwa ajili ya maeneo yake. Hii ni kazi kubwa ambayo anaifanya kwa kushirikiana na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mradi huu ambao una gharama ya bilioni 25 na katika zoezi la usanifu ilitenga kiasi cha milioni 25 tumeshakamilisha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itatenga fedha za kutosha kukamilisha mradi ndani ya kipindi cha miezi 24. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Je, ni lini Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria ambao umeanza Jimbo la Nkenge katika Kata za Kashenye, Kanyigo na Bwanjai utakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mbunge Oliver pamoja na Mbunge wa Nkenge Mheshimiwa Kyombo, kwa kweli wanashirikiana vizuri sana kuhakikisha kwamba, wanatua akinamama ndoo kichwani lakini na kuwafikishia maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huu mradi uko katika hatua nzuri sana za utekelezaji. Nimhakikishie tu kwamba, wakandarasi walioko katika mradi huo na pesa ambazo wamekuwa wakidai tayari wameshaanza kulipwa. Naamini kwamba mradi huu utakamilika ndani ya wakati. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, miradi aliyoeleza inayoendelea Wilayani Kyerwa, wakandarasi wanadai zaidi ya shilingi bilioni sita. Je, ni lini wakandarasi hawa watalipwa ili miradi hii iweze kukamilika na kuwapa wananchi majisafi na salama?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mradi wa Kirera – Isingiro unajengwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza imeshakamilika. Je, ni lini Serikali itatoa kibali ili mradi huu uanze ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli, nikianza na swali la kwanza ambapo wakandarasi wanadai shilingi bilioni sita, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Fedha, tayari Wizara ya Fedha imetupatia exchequer ya shilingi bilioni 140. Pia kwenye miradi ile EP4R tayari wafadhili wameshaleta shilingi bilioni 150 na hivyo tayari Katibu Mkuu, leo nimeongea naye, ameshaanza kukusanya madai ya wakandarasi ili waweze kuwasilisha Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ya wakandarasi wanaodai.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kabisa na ninatambua kwamba Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiupigania sana. Mradi huu una zaidi ya shilingi bilioni hamsini na kitu. Tunapotoa kibali, lazima tuwe tumejiridhisha kwamba tuna fedha za kwenda kumlipa advance payment mkandarasi huyu ili aweze kuingia site.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Serikali iko kwenye utafutaji wa fedha, na itakapopatikana, kibali kitatolewa kwa ajili ya kutangaza tenda na mkandarasi atapatikana kwa ajili ya kwenda kutekeleza mradi huu ndani ya jimbo la Mheshimiwa Bilakwate,ahsante sana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kufahamu, je, ni lini mradi wa kutoa maji katika Mto Momba na kuyasambaza katika Miji ya Tunduma, Vwawa pamoja na Mji wa Mlowo utaanza kutekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, mradi wa kutoa maji kutoka Mto Momba tayari Serikali imeshaanza kuufanyia kazi. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana nasi ili tukamilishe hatua ambazo tuko nazo na baada ya hapo tutakwenda kuukamilisha mradi huo. Ahsante sana.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali kuhusu Mradi wa Maji wa Tukuyu Mjini ambapo hili swali ninauliza ni mara ya tano sasa. Je, ni lini Serikali itakamilisha tenki la maji la Tukuyu Mjini ukizingatia wananchi wa Tukuyu Mjini wanasumbuka sana na maji hasa wanawake? Naomba majibu hayo ambayo ni ya kuridhisha kwa leo ili wananchi wa Tukuyu waweze kusikia na kuelewa, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nafahamu changamoto ya mradi huu kuchelewa kukamilika. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tukitoka hapa tuonane ili tuweze kupitia changamoto ambazo zimesababisha kuchelewa kwa mradi huo na hatua ambazo Serikali tunaweza kuzichukua ili kuhakikisha kwamba wananchi wanaosubiri kwa hamu sana maji haya kutokana na tenki hilo litakapokamilika waweze kupata maji yaliyo safi na salama, ahsante sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nampongeza Naibu Waziri kwa ziara yake aliyoifanya miezi mitatu katika Jimbo la Kishapu. Wakati huo huo naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kishapu kata zaidi ya 20 zilikuwa na changamoto kubwa sana ya maji, lakini kata nne zina taabu sana. Usanifu ulishafanyika katika Kata za Seke-Bugoro, Mundo na Nyasamba ambapo takribani shilingi bilioni 15 zinahitajika. Old Shinyanga, Busangwa, Nyamtengela, Seke-Bugoro, shilingi bilioni nane; Iselamagazi, Mwanhili na Itongoitale shilingi bilioni tatu; na Mwamashele, Ngofila hadi Kiloleli shilingi bilioni 5.9. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Butondo kwa kushirikiana na Serikali vizuri sana na kukamilisha ule mradi wa bomba kutoka Ziwa Victoria. Amefanya kazi nzuri sana na tunamshukuru sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika mradi ambao katika vijiji ambavyo amevitaja na kata hizi, kwa gharama za jumla utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 33.5. Ni mradi ambao tunatarajia katika mwaka wa fedha 2025/2026 ndiyo tutakaouingiza ili kuutafutia fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba tunaandaa mazingira rafiki ya kwamba mradi huu unaenda kuwezekana kufanyika ndani ya Jimbo lake la Kishapu.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali lakini nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza; uchimbaji wa visima katika Halmashauri yangu ya Itigi katika Wilaya ya Manyoni, maeneo ya Kayui na Mtakuja wamechimba, lakini maji hamna kabisa. Je, Serikali iko tayari sasa kuajiri wataalam wazuri wa surveyors ambao kabla ya uchimbaji waweze kutuainishia kabisa kwamba hapa tukichimba tutapata maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ipo tayari sasa kwenda kuchimba kisima katika eneo la Kalangali ambapo kuna shida kubwa na tunajenga sasa hivi Sekondari ya Ufundi ya Amali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Massare kwa kazi kubwa anayoifanya na ufuatiliaji wa miradi ndani ya Jimbo lake. Kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, baada ya kuchimba visima tunaanza kupima wingi wa maji kwa maana ya pumping test na baada ya kujiridhisha maji hayo hayatokuwa yanatosha, basi tutaangalia eneo lingine. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Wizara ya Maji inao wataalam na vifaa vya kutosha kuhakikisha kwamba kazi hii tunaifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande swali la pili kuhusu Kalangali, ninatumia fursa hii kumwelekeza RM Mkoa wa Singida, ahakikishe anaangalia kipaumbele cha Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba, akaanze na eneo hili ili liweze kuhakikisha kwamba lina upatikanaji wa maji ambapo itaweza kusaidia katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, uchimbaji wa kisima kwenye Kata ya Mwika Kusini ulikumbwa na matatizo na maji hayakupatikana kwenye kina kinachokubalika. Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kufikisha maji kwenye eneo la Kata hii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Dkt. Kimei kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji na hasa wananchi wa Mwika ambapo Serikali ikiona eneo fulani halina maji, inaangalia chanzo kingine ambacho kinaweza kusaidia kufikisha maji katika eneo lingine. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali tutalifanyia kazi, ili kubainisha chanzo kingine ambacho kitakuwa na wingi wa maji ambao utaweza kusaidia katika Kata ya Mwika. Ninakushukuru sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu, lakini hali halisi ni kwamba, wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi wapo katika adha kubwa ya maji. Swali la kwanza; sasa, Naibu Waziri anasema nini kuhusiana na hali hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; upo tayari kuongozana na mimi kwenda kujionea hali halisi ilivyo kule kwa sababu hayo majibu pamoja na kwamba ni majibu sahihi, hayakidhi hali ya changamoto waliyonayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri kwanza kabisa tumekuwa na mjadala mrefu na Mheshimiwa Mchungahela kuhusu mradi huu. Kwa kweli kati ya watu ambao wanaufuatilia kwa karibu sana, Mchungahela amekuwa kinara katika kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ya Serikali ni kwamba, kwanza kabisa natumia fursa hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Mheshimiwa Waziri ameandika special request ya mradi huu Wizara ya Fedha ili uweze kutangazwa na kuhakikisha kwamba mradi huu unaenda kuanza mara moja kwa ajili ya wananchi wa Lilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge mradi huu sisi kama Serikali tunafahamu kwamba, tunaendelea kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais ya Kumtua Mama Ndoo Kichwani na tunafahamu kwamba, ahadi ni deni na Serikali itatimiza ahadi hiyo. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mbunge tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni majukumu yetu Serikali kuhakikisha kwamba, tunaitikia wito wa Waheshimiwa Wawakilishi wa Wananchi pale ambapo wanatuomba. Mheshimiwa Mchungahela nipo tayari kuongozana na wewe kwenda kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji ndani ya Jimbo la Lulindi. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ziara yake aliyoifanya Wilayani Nyang’hwale na kuacha maagizo pale Kata ya Nyijundu kwamba, kufikia tarahe 19 maji yawe yanatiririka na tayari maji yanatirirka Kata ya Nyijundu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuzisukuma zile milioni 286 kwa ajili ya kukamilisha usambazaji wa maji kwenye Kijiji cha Iseni, Kabiga, Nyangaramila, Nyamikonze, Kasubuya, Kaboha, Shibuha na Shibumba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge wa Nyang’hwale ameuliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna hizo pesa ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziongelea na kwa kweli nampongeza sana kwa sababu tuliweza kuzunguka katika Jimbo lake karibu Kata kwa Kata tulijionea hali halisi. Kweli mradi huu ambao ameutaja unahitaji hizi fedha ili uweze kukamilika kwa haraka. Ninakuahidi kwamba Mheshimiwa Mbunge tutasukuma hizo fedha zitoke haraka ili mradi uweze kukamilika kwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mradi wa Maji unaogusa Kata za Imbaseni, Maji ya Chai, Kikatiti hadi Samaria umesimama na mkandarasi amekimbia site kwa ukosefu wa fedha. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kule kwa ajili ya kukamilisha mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Pallangyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa na tayari Serikali kupitia Wizara ya Maji tumeanza ku-engage na mkandarasi. Pia, tumeshakaa na wenzetu Wizara ya Fedha sasa tuweze kuanza kutoa fedha. Tayari kwa kipindi hiki tumepokea bilioni 16 kutoka National Water Fund na jana tumepokea bilioni tisa. Pia, tumeanza kupokea kutoka Serikali Kuu, tumepokea exchequer ya bilioni 105. Kwa hiyo, tunaamini kabisa miradi ambayo ilikuwa imekwamba pamoja na wakandarasi ambao walikuwa bado wanadai sasa wakati umefika wa kuanza kuwalipa ili warudi site na kuendeleza miradi ambayo ipo katika hatua mbalimbali.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ipo Miradi ya Maji ya Kijiji cha Mwakizega, Buhingu na Kandaga. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; vipo Vijiji vilichimbiwa visima Basanza, Msebehi na Lemseni. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha sasa kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza sana Mheshimiwa Nashon kwa kazi kubwa ambayo unaifanya kwa wananchi wa Uvinza, mimi ni shahidi kabisa kwamba, tulizunguka kijiji kwa kijiji, Kazuramimba, Uvinza yenyewe na maeneo mengine kujionea hali halisi. Ninamhakikishia Mbunge kwamba, maeneo ya Basanza pamoja na maeneo mengine aliyoyataja, hatua ya kwanza tumechimba visima, hatua ya pili tunapima wingi wa maji na hatua ya tatu sasa tunaanza kufunga mitambo na kuhakikisha kwamba mtandao wa maji unakuwa unapatikana kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ambayo imesimama, Serikali kupitia Wizara ya Maji tumeshafanya tathmini ya miradi yote nchi nzima ambayo ipo katika hatua mbalimbali, tumeelekeza namna gani ya kwenda kuikamilisha. Kwa hiyo, kuanzia Mwezi wa Kumi mpaka wa Kumi na Mbili kuna baadhi ya miradi itakuwa imeshakamilika katika Mkoa wa Kigoma. Ahsante sana.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa mmesikia miradi yote ambayo ina changamoto mwezi wa Kumi na Mbili imekwisha. Kama mna maswali ya nyongeza swali hilo msiulize. (Kicheko)
MHE. STEPHEN L. BYABATO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nimshukuru Dkt. Samia kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa upanuzi mtandao wa Maji Bukoba Mjini unaogharimu shilingi 3,300,000,000 na Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja kukagua na akatoa maelekezo. Kama alivyosema itaisha Desemba, lakini niliomba kujua ni lini 207,000,000 iliyobakia ya kuleta mabomba kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji zitaletwa Bukoba Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Byabato, Mbunge wa Bukoba Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa tulifika Bukoba tukafanya ziara pia tukajionea hali ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na hakika Bukoba kwa upande wa maji hali ni nzuri sana, lakini tunatambua kwamba uhitaji wa fedha hizo katika eneo hilo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutazisukuma haraka iwezekanavyo kuhakikisha kwamba, zinafika na mradi unakamilika kwa wakati.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, je ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa kimkakati katika Tarafa ya Nambisi, Halmashauri ya Mji wa Mbulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima kabisa naomba nilipokee swali la Mheshimiwa, ili nikawe na majibu ya uhakika ya Serikali.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutuletea Miradi ya Maji Bukoba Vijijini, kwa kweli jitihada zinaonekana lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; miradi ya maji ya Bukoba Vijijini inajengwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA). Je, Wizara ya Maji ina maslahi gani kwa kutaka kuhamisha miradi hii ambayo imekamilika ili iendeshwe na Mamlaka ya Maji ya Bukoba Mjini (BUWASA) kinyume na matakwa ya wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pale Kemondo kuna mradi mkubwa sana wa maji ambao Serikali imejenga kupitia RUWASA hiyo hiyo (Wakala wa Maji Vijijini) wa shilingi bilioni 16 na sasa hivi umekamilika kwa 100% awamu ya kwanza. Ni kwa nini maji hayajaanza kutoka? Ni kweli kwamba kuna figisu za kutaka kuhamishia mradi huu Bukoba Mjini (BUWASA)? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa labda niseme hivi, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira na RUWASA kwa upande wa vijijini, vyote viko chini ya Wizara ya Maji. Ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kujikita kwenye utoaji wa huduma bora zaidi pamoja na kuhakikisha kwamba tunatoa maji safi na salama bila kujali kwamba yatatolewa na RUWASA ama yatatolewa na mamlaka yoyote. Lengo ni kwamba, kwanza yawe na bei ambayo haitamuumiza mwananchi; hilo ndilo ambalo tunaliangalia kwa ukubwa wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha kuuchukua mradi mwingine kutoka RUWASA kwenda mamlaka tunaangalia ufanisi, hilo la kwanza. La pili, tunaangalia mahitaji ya wananchi wa eneo husika wanahitaji kuhudumiwa na nani; na la tatu tunaangalia utekelezaji jinsi ambavyo mradi ulianzishwa. Ninaomba kabisa kwamba kwenye hili lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawaletea wananchi huduma iliyo bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la Kemondo, ni kweli kabisa nimefika pale Kemondo na nilipofika nilikuta kwamba kulikuwa na mitambo na pump zilikuwa hazijaletwa, nikatoa maelekezo. Tayari sasa hivi pumps zimeshaletwa na kilichobaki tunaongea na wenzetu wa TANESCO. Kuna mita fulani ambayo wanatakiwa kutufungia na baada ya kukamilisha; na mkandarasi wetu alikuwa anatudai pesa Fulani, wiki iliyopita tumemlipa hiyo pesa na anarudi site. Tutahakikisha kwamba mradi huo unakamilika na kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. SILYVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninampongeza Mheshimiwa Aweso, Waziri wa Maji kwa ziara aliyoifanya Disemba, 2023, ambapo tulisaini mikataba hii ya ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa baada ya kusaini mikataba hii ya utekelezaji wa mradi huu ni takribani sasa mwaka mmoja na ahadi ya Serikali ni mwezi wa 10. Je, Waziri yuko tayari mwezi Oktoba kufika Pangani ili kuzindua ujenzi wa mradi huu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika kusaini ile mikataba, Mheshimiwa Waziri kupitia Mtendaji Mkuu wa DAWASA aliahidi kuwa ndani ya miezi mitatu utafanyika utaratibu wa kutekeleza mradi mdogo wa kuhakikisha kwamba wananchi wa Kata ya Viziwaziwa na hususan Sagale Magengeni na Sagale Kambini na Viziwaziwa yenyewe wanapata maji; na ahadi iliyotoka pale ni kwamba kazi ile ilikuwa iko ndani ya uwezo wa Mtendaji Mkuu wa DAWASA na itafanyika ndani ya miezi mitatu na hadi sasa hivi ile kazi haijakamilika. Je, ni lini itafanyika ili wananchi wale wapate huduma kama ilivyoahidiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Koka, kama ifuatavyo -
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wizara ya Maji hatupendezwi na hatutaki kuwa kikwazo kwa Watanzania kupata huduma ya maji safi na salama na sisi wenyewe hatuhitaji kuona miradi inasuasua. Kwa sababu ameliongea, ni suala specific sana, ninaomba niipokee changamoto hii ya Mheshimiwa Mbunge ili tukaifanyie kazi, tuone wapi mradi umekwama na tuweze kuchukua hatua stahiki. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina swali moja muhimu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Kijiji cha Igunga tumechimba maji mara tatu lakini hatujapata maji ardhini. Tumeomba shilingi 300,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kuyatoa Ntomoko kuyaleta kwenye Kijiji cha Igunga. Nini kauli ya Serikali juu ya kuleta fedha hizo ili Watu wa Igunga waweze kupata maji? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kijiji cha Igunga baada ya kufanya utafiti na kuchimba maeneo kadhaa tukajiridhisha kwamba hakuna maji. Sasa, Serikali ikaangalia chanzo kilichopo Ntomoko na tayari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekubali kutoa kiasi cha shilingi 350,000,000 kwa ajili ya kuyaleta maji kutoka Ntomoko kuja katika Kijiji cha Igunga. Nakushukuru sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Wananchi wa Kijiji cha Boma la Ng’ombe ambapo mwenge umepita juzi, walitoa malalamiko makubwa kuhusu upungufu wa maji kwenye Kijiji cha Boma la Ng’ombe. Je, ni lini Serikali itataua changamoto ya maji kwenye Kijiji cha Boma la Ng’ombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Justin Nyamoga kwa kazi kubwa anayoifanya Kilolo.
Mheshimiwa Spika, nimeshafika Kilolo na kujionea changamoto hiyo lakini tunafahamu kwamba Serikali iko katika juhudi mbalimbali za kuboresha na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa maji unaendelea kuboreshwa. Tayari tumeshasaini mkataba katika baadhi ya kata, tunaamini kwamba baada ya kukamilika mikataba hiyo na kutekelezwa, basi tutaangalia uhitaji katika maeneo mengine na tutahakikisha kwamba tunapeleka huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni lini Mradi wa Maji wa Lema katika Kata ya Busale wilayani Kyela utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, eneo la Busale – Lema, Serikali imetoa kiasi cha shilingi 223,000,000 na mradi umefika 67%. Kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika na kutoa huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Namtumbo kwenye Kata ya Mgombasi, Serikali imefanya kazi nzuri sana ya kujenga mradi wa maji wa shilingi 2,700,000,000. Imejenga vizimba, chanzo cha maji na tanki la maji lakini kuna bomba la nchi nane ambalo halijapatikana…
SPIKA: Swali Mheshimiwa…
MHE. VITA R. KAWAWA: …mpaka sasa karibu miezi 10.
Je, Serikali itanunua lini bomba hili la nchi nane ili sasa watu waweze kupata hayo maji? Zaidi ya miezi 10 sasa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge alichokiongea na amekuwa akifuatilia na sisi (Serikali) tumeshachukua hatua. Tayari tumeshaelekeza ununuzi wa bomba la nchi nane ufanyike haraka ili liweze kwenda kulazwa kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kijiji cha Mtonya Kata ya Likuyuseka Halmashauri ya Namtumbo bado inatumia visima vya pampu ya mkono. Kati ya visima hivyo, 13 viko sawa lakini vitatu ni vibovu. Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati kwenye visima hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kutumia Bunge lako Tukufu, katika visima hivi 13 na vitatu ambavyo havitoi huduma kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu. Nawaelekeza RUWASA-Namtumbo kuhakikisha kwamba ukarabati huu unaanza mara moja na kwa sababu hatuna changamoto sana ya pampu, ili waweze kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo hili la Mtonya waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni lini mradi wa Mwakaleli 1 na Mwakaleli 2 unaohudumia vijiji nane utaanza kutoa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nipokee swali la Mheshimiwa Mwakibete ili nikatafute kuona status yake imefikia wapi na baada ya hapo tutakutana kwa ajili ya kupeana taarifa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeza Wizara ya Maji kwa kunikumbuka kwenye hoja hii ya kutoa maji Butiama kwenda Nyamuswa.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa usanifu umekamilika na kwa kuwa Bajeti 2024/2025 imetaja kwamba itatekeleza mradi huo. Je, ni bajeti kiasi gani imetengwa ya kutekeleza mradi huo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna mradi wa vijiji 33 ambapo Serikali imetumia shilingi 800,000,000 kufanya usanifu. Ni hatua gani imefikiwa katika mradi huo wa kupeleka maji katika vijiji 33 kwenye Jimbo la Bunda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Getere amekuwa kinara wa kupambana kuhakikisha kwamba maji yanapatikana kwa ajili ya wananchi wake. Katika bajeti yetu, usanifu umeshakamilika na utekelezaji utaanza katika bajeti yetu ya 2024/2025. Tayari Serikali imetenga kiasi cha shilingi 2,000,000,000 kwa kuanzia ili kuhakikisha kwamba shughuli ziendelee.
Mheshimiwa Spika, katika suala la pili katika vijiji 33, Mtaalamu Mshauri ameshawasilisha rasimu ya usanifu. Sasa Wizara ipo katika mchakato wa kuipitia rasimu hiyo ili tujiridhishe na hali halisi na baada ya hapo, tutatangaza zabuni za kumpata mkandarasi ili aweze kwenda kutekeleza mradi huo. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kushirikiana naye, kama yeye anavyoendelea kushirikiana na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa kutupa visima vidogo vidogo vya maji. Swali langu la msingi, je, Serikali lini itapeleka mradi mkubwa wa maji Wilaya ya Mbogwe ili tukomeshe kabisa suala la uhaba wa maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, wakati tukisoma Bajeti ya Serikali na upande wa RUWASA, Mheshimiwa Waziri alielekeza tuchimbe visima 900 nchi nzima tukizingatia kwamba kila Mheshimiwa Mbunge atapata visima vitano. Nitumie Bunge lako Tukufu kuwaelekeza, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri yapo clear, waanze kuhakikisha kwamba mitambo ambayo ilinunuliwa na Serikal, ianze kufanya kazi mara moja ili visima hivi vitano vitano, kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa viwe vimekamilika. Ahsante sana.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri atakumbuka kwamba mradi wa zaidi ya shilingi 500,000,000,000 wa maji Arusha, ulilenga kupeleka maji katika Kata ya Mererani, Endiamutu, Shambarai na Naisinyai. Je, ni lini sasa maji yatapelekwa katika Kata ya Shambarai na Naisinyai baada ya kwamba yamepelekwa katika Mji wa Mererani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhitaji wa maji katika kata ambazo Mheshimiwa Ole-Sendeka amezitaja. Nakuomba Mheshimiwa Ole-Sendeka baada yakutoka hapa tuonane ili niweze kupata majibu sahihi ya Serikali kwako Mheshimiwa Mbunge. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ni upi mpango wa Serikali kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 ili Kata za Mswaha na Mji wa Korogwe na maeneo mengine, yatatue changamoto kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, Mradi wa Miji 28 kwa upande wa Mkoa wa Tanga, unaojumlisha Handeni, Muheza, Korogwe pamoja na Pangani wenye jumla ya shilingi 170,000,000,000 umefikia wastani wa 32%. Juzi nilikuwepo kule nimetoa maelekezo kwa wakandarasi kuharakisha mradi huu kwa sababu hakuna changamoto ya kifedha. Kwa hiyo sisi kama Serikali tumeelekeza mradi huu usiwe nyuma ya wakati ili wananchi wa maeneo hayo wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Wilaya ya Meatu ni miongoni mwa wilaya ambazo ni kame sana, kule maji ni tatizo kubwa. Je, ni lini visima hivi vitano vitachimbwa katika Wilaya ya Meatu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, Meatu ipo kati ya wilaya tano ambazo zitafikiwa na maji ya kutoka Ziwa Victoria na tayari mradi umeshaanza kwa awamu ya kwanza kwa kujumuisha Wilaya ya Busega, Bariadi pamoja na Maswa lakini katika awamu ya pili, tutaenda katika Wilaya ya Meatu pamoja na Itilima. Tunafahamu kwamba huo ni mradi wa muda mrefu lakini tuna miradi ya muda mfupi ambapo tumeelekeza wataalamu wetu kufanya usanifu wa kupata vyanzo vya maji ili tuchimbe visima na kuhakikisha kwamba wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, je, ni lini mtarekebisha mabomba chakavu katika Kata ya Kilakala – Kigunga ili uhaba wa maji uweze kupotea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, uchakavu wa miundombinu unatusababishia hasara hata sisi Serikali tunapozalisha maji lakini yanafika machache na mengine yanapotea, hivyo kututia hasara kubwa sana. Nilikuwepo Dar es salaam katika Majimbo ya Kibamba lakini nafahamu, natambua kwamba uwepo wa Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo la Temeke pia tatizo bado lipo lile lile. Nimeishatoa maelekezo lazima sasa tufanye ukarabati wa miundombinu yetu yote ili kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata maji safi na salama lakini pia tunajiepusha na upotevu wa maji ambayo yanasababisha hasara sana katika mamlaka zetu, ahsante. (Makofi)
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwenye maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba kwa miaka mitatu toka 2021 mpaka 2024 wameweza kukamilisha kiwango cha 40%, lakini anatuambia kwamba kufikia Desemba mwaka huu ambayo imebaki miezi sita tu na kiwango kilichobaki cha kazi ni 60%, je, Serikali ina mpango gani wa ziada kuhakikisha kwamba wanakamilisha 60%?
Swali langu la pili la nyongeza je, kiasi gani cha fedha kimebaki cha kukamilisha mradi huo na Serikali mmejipangaje kupeleka fedha hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, natambua wasiwasi wa Mheshimiwa Mrisho Gambo na natambua wasiwasi huo kwa wananchi wake. Nimtoe hofu Serikali kama ambavyo nimejibu katika majibu ya msingi kufikia 2024 Desemba, mradi huo utakuwa umekamilika na fedha ambazo zitakuwa zimebaki kwa ajili ya kukamilisha mradi huo zitapelekwa kwa wakati sahihi ili kuhakikisha kwamba mradi unakamilika kwa wakati, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, nina maswali mawili tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyojibu kwenye jibu lake la msingi kwamba kuna mpango wa kuongeza usambazaji wa maji katika Kitongoji cha Kilemela, je, ni lini mpango huo utaanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kata ya Makulunge pamoja na Kata ya Fukayosi zinapata maji kutoka katika mtambo wa Wami. Vitongoji vya Engero, Mkwama, Kijiji cha Mkenge pamoja na Kitongoji cha Kalimeni wananchi wake hawajapata maji mwezi mmoja sasa, je, ni lini Serikali itarekebisha huo mtambo wa Wami ili wananchi hawa waweze kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri sana ambayo anaendelea kuifanya katika jimbo lake na kwa kuwasemea wananchi wake hasa katika sekta ya maji ameendelea kutupatia ushirikiano mzuri sana pale ambapo changamoto zinapotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa upande wa Kibaha na Bagamoyo tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kupanua wigo wa kufikisha huduma ya maji safi na salama katika vitongoji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, vitongoji ambavyo amevileta tutavifanyia kazi na tutaangalia namna ambavyo tutaenda kuvifanyia utafiti na kupata gharama halisi ili mradi uweze kuwafikia wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la mtambo ambao una changamoto, Serikali kupitia Wizara ya Maji tumeendelea kuhakikisha kwamba tunachukua hatua stahiki pale ambapo panatokea tatizo lolote lile katika mitambo yetu ili tuwe na uhakika wananchi wetu wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama na hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hayo ni maelekezo ya Ilani yetu ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha watu wanapata maji ya kutosha katika wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni lini Serikali itatatua shida ya maji Tarafa ya Wanging’ombe katika Jimbo la Wanging’ombe maeneo ya Saja, Kijombe na Kata ya Wanging’ombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na pia nimshukuru sana Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Njombe Viti Maalum kwa kuendelea na kazi yake kubwa ya kuwasemea akina mama ambao ndio tunawapa kipaumbele katika kutatua changamoto za maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaaomba nilipokee suala hili twende tukalifanyie kazi kwa sababu bado tunaenda kwenye bajeti ijayo ili tuone kwamba ni namna gani tutaweza kuliweka kwenye mpango wa bajeti ili tuweze kwenda kuchukua hatua ya kuwafikishia huduma ya maji safi na salama kwa kujenga miradi ambayo itawasaidia kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ningependa kufahamu, je, Serikali kupitia Wizara ya Maji haioni kuna uhitaji na sababu kubwa ya kuweka bei pungufu ya kuunganisha maji kama ilivyofanyika kwenye umeme kwa sababu nikitolea mfano kwenye Jimbo la Bukoba Mjini, Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kuna upatikanaji wa maji, lakini gharama ya kuunganisha wakazi ili waweze kunufaika na maji hayo bado ni kubwa sana.
Je, Serikali haioni ipo haja ya kuweka bei elekezi ambayo itakuwa ni gharama nafuu ili kuhakikisha kwamba kaya zote zinanufaika na maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Neema Lugangira, anaendelea kuwasemea wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ina mambo matatu ambayo imejikita nayo; la kwanza, upatikanaji wa huduma bora, lakini pia muda wa upatikanaji wa huduma yenyewe, lakini na gharama ambayo mwananchi anatakiwa kununua huduma hiyo ya maji. Kikubwa ni kwamba Wizara yetu kupitia Mheshimiwa Waziri, alishatoa mwongozo na mwongozo huo ni kulingana na aina ya uzalishaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aina ya maji ambayo tunayapata kwa njia ya mserereko, kuna aina ya maji tunayopata kwa njia ya umeme wa solar na kuna aina ya maji ambayo uzalishaji wake unatokana na umeme wa TANESCO. Kwa hiyo, ukiangalia uzalishaji wake na gharama zake zitakuwa tofauti. Kwa mfano, kwa sasa umeme wa TANESCO ndiyo umeme ambao uzalishaji wake unakuwa na gharama kubwa hivyo hata mtumiaji wa mwisho atapata kwa gharama kidogo ambayo imechangamka, lakini umeme wa solar kidogo inashuka kidogo, mserereko unakuwa chini kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ni nini? Kikubwa ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kupeana elimu ya kujua kwamba maji haya kuna gharama fulani ambazo zimehusishwa mpaka mtumiaji wa mwisho anaenda kuyapata hayo maji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tutaendelea kulitazama kama Serikali pale ambapo tutaona kwamba inaruhusu kupunguza gharama tutafanya hivyo kwa manufaa ya Watanzania, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, Wilaya ya Ileje ina changamoto kubwa ya maji ikiwemo Kata ya Isongole na Itumba. Ninataka kujua ni lini mtapeleka fedha ili kumalizia Mradi wa Maji wa Isongole - Itumba na wananchi waweze kunufaika na maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa swali jema na zuri kwa ajili ya wananchi wa Ileje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea exchequer kutoka Wizara ya Fedha na tumeelekezwa kuleta madai ya wakandarasi mbalimbali ili waweze kulipwa ili miradi yetu iendelee kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, Kata yetu ya Mapogoro, Wilaya ya Mbarali ina uhaba mkubwa sana wa maji, nini mkakati wa Serikali wa kutanua Mradi wa Maji wa Nyaugenge na pia mkakati wa muda mfupi ili wananchi wa kata ile waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, ninakumbuka juzi alikuwa na mkutano wa hadhara katika jimbo lake na hoja hii iliibuka na sisi Serikali tumeshaipokea na tunaifanyia kazi. Wenzetu wapo kwenye hatua za manunuzi kumpata mkandarasi kwa ajili ya kwenda kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hii ambayo imewakumba wananchi wake. Tuna jambo ambalo tunaenda kulifanya la dharura, tumeagiza RUWASA Mkoa wa Mbeya kwenda kufanya tathmini na kujiridhisha kama tunaweza kuchimba kisima cha dharura wakati tunasubiri mradi mkubwa wananchi wa pale waendelee kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali kwa kweli hayana uhalisia kwa kutuaminisha wananchi wa Tarime na Rorya kwamba mradi huu utakamilika Julai, 2025. Mradi huu ulikuwa ni wa miaka mitatu, sasa hivi tunavyoongea imepita miaka miwili na nusu, fedha zimetolewa shilingi bilioni 21.9 tu out of shilingi bilioni 134 ambayo ni 16% tu, utekelezaji 13%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kujua mkandarasi huyo ali-raise certificate mbili; ya 1.9 billion na 2.3 billion nahisi wameshakuuliza hapa, zaidi ya miezi sita lakini mmetoa 1.9 billion tu ndiyo maana amerudi site na hajarudi kikamilifu. Ni lini Serikali itamaliza kulipa ile 2.4 billion ambayo certificate hii amei-raise zaidi ya miezi sita iliyopita?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa sababu Serikali imeji-commit kumaliza huu mradi Julai, 2025 kwa hizo 86% kwa maana ya shilingi bilioni 112 zilizobaki na kwa sababu wamesema mradi huu unaenda kuwasaidia wananchi takribani 730,000, inatoa picha ni wananchi kiasi gani wanateseka hawana maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kupata commitment ya Serikali ni kwa jinsi gani wanaenda kutimiza ahadi hii kwa kutoa hizo shilingi bilioni 112 ndani ya muda wa miezi sita ili mkandarasi huyu CCECC aweze kumaliza na kukamilisha mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na pia nimshukuru Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge ambaye amekuwa mstari wa mbele kuusemea sana huu mradi na ni hakika kabisa kwamba Serikali inasikia sauti ya Watanzania kupitia kwa Wabunge na inatambua kabisa kwamba mradi huu ni wa kimkakati. Ni kati ya miradi ya miji 28 ambayo Mheshimiwa Rais anaendelea kutuelekeza sisi Wizara ya Maji kuisimamia kwa weledi mkubwa na maarifa yetu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi kwamba ni lini italipa, kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya msingi mkandarasi yupo 13%, alishalipwa takribani shilingi bilioni 22 na amesha-raise hiyo certificate. Tumemwomba arudi site wakati Serikali ikiendelea kuhakikisha kwamba ile certificate yake nyingine ambayo haijalipwa alipwe ili kuhakikisha kwamba mradi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu kwamba ahadi yetu ikoje kuhusu kulipa bilioni zote ambazo zimebaki, sisi kama Serikali tunalipa kwa mujibu wa hati za madai ambazo zitakuwa zinawasilishwa. Mkandarasi kila atakapokuwa anafikia hatua fulani na sisi Serikali tutakuwa tunahakikisha kwamba tunamlipa ili aweze kuendelea na mradi huo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika na lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wa Tarime - Rorya wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie ndani ya muda wa mkataba tuna uhakika kwamba mradi huu utakuwa umekamilika bila ya kuwa na changamoto yoyote, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Dajameda pamoja na Kijiji cha Muungano, Kata ya Laghanga Jimbo la Hanang hakuna maji kabisa na wananchi wanatumia umbali wa kilometa 30 kwenda kata nyingine ya Bassotu kufuata maji, je, ni lini Serikali itawapelekea wananchi hawa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Hanang ni kweli kabisa kwamba kuna changamoto katika vijiji hivyo pamoja na cha Muungano, lakini Serikali kupitia RUWASA tayari wameshafanya utafiti na wataanza kufanya usanifu wa kuvuta maji kutoka Bassotu kuja katika vijiji saba na katika hivyo vijiji saba ni pamoja na Kijiji cha Muungano na kijiji kingine ambacho amekitaja ambacho sijakisikia vizuri. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, suala la Tarime na Rorya linafanana na la Makao Makuu ya nchi. Je, ni lini Serikali italeta maji ya Ziwa Victoria Makao Makuu ya nchi Dodoma ili kuondoa adha ya ukosekanaji wa maji iliyopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, katika mipango yetu ya kudumu ya kutatua tatizo la maji la Dodoma ni kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria, tayari Serikali imeshafanya feasibility study na sasa tupo kwenye detailed design, tukishakamilisha tunatafuta fedha na mradi huo unajengwa na Jiji la Dodoma linapata suluhisho la kudumu la changamoto ya maji, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali imetupatia Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kwa vijiji vyote vya Kata ya Kashenye na Kanyigo awamu ya kwanza na awamu ya pili itaenda Kata ya Bwanjai. Mradi huo mpaka sasa upo 92% lakini sasa hivi ni takribani miezi minne mradi huo umesimama.
Je, ni lini sasa Serikali itatupatia fedha ili kumalizia mradi huo na hiyo kiu ya wananchi wa Kata Kashenye na Kanyigo iweze kutimia mwaka huu wapate maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba wakandarasi ambao wanasimamia miradi yote ya kimkakati wanalipwa ili waendelee na utaratibu wa kukamilisha miradi, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ilitupa heshima Siku ya Wanamke Duniani kuchimba baadhi ya visima katika mikoa yetu na katika Mkoa wa Iringa ilichimba katika Kijiji cha Mtandika Sokoni na Kituo cha Afya cha Ruaha Mbuyuni, lakini mpaka leo hii hakijawekewa miundombinu yoyote.
Je, Mheshimiwa Waziri sasa upo tayari tukimaliza Bunge hili ukaweke miundombinu ili heshima ya mwanamke iwepo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Iringa nafikiri hili eneo lipo Kilolo, upande wa Mtandika visima vilichimbwa mwishoni mwa mwaka 2023, visima hivi kimojawapo kiligundulika kuwa na chumvi nyingi sana. Mtandika tumetenga kiasi cha shilingi milioni 100, kwa ajili ya kwenda kumalizia, lakini kwa upande wa Ruaha Mbuyuni tuna mradi wetu wa mserereko ambao tunaandaa kufanya usanifu, ili twende kuhakikisha kwamba tunavuta maji, ili waweze kuhudumiwa na mradi mkubwa tofauti na mradi wa kisima ambacho kina chumvi nyingi, ahsante. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi ili aweze kukamilisha Mradi wa Maji wa Vijiji Nane, Ukara katika Jimbo la Ukerewe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu - Wizara ya Maji, ameshawaelekeza Regional Managers, Wakurugenzi wa Mamlaka ambao wote wana madai ya wakandarasi kuyawasilisha Wizarani ili yaweze kuwasilishwa Wizara ya Fedha kwa malipo, ili waendelee na miradi ikamilike kwa wakati, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi kuweza kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza natumia fursa hii kuishukuru Serikali kwa fedha nyingi ambazo wametupatia kwa miradi mikubwa ya maji ya Ziwa Victoria kwa maana tumeona wakandarasi. Tumepokea wakandarasi wawili ambao mmoja anafanya extension ya mradi ule pale Ziba-Nkinga lakini pia tumepata mkandarasi mwingine anautoa Ziba kwenda Simbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na wakandarasi hawa kuwa tayari wapo site wameshaingia kwa ajili ya kuanza kufanya hii kazi, na Mheshimiwa Waziri alikuja na ugeni wa Mheshimiwa Makamu wa Rais, sasa ni lini Mheshimiwa Waziri mwenyewe atapata nafasi ya kuja kuitembelea hii miradi kujionea kazi kubwa na nzuri ya kupeleka maji katika hayo maeneo ambayo inafanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, alipokuja alitupatia fedha kwa ajili ya kupeleka maji pale kwenye Kijiji cha Ntogo. Wakandarasi sasa hivi wameanza kuchimba mtaro kwa ajili ya kupeleka maji. Sasa, kwa sababu tulikuwa tunataka vijiji viwili; kimoja cha Ntogo pale Kaselya tumepata mkandarasi, na kwa kuwa tulikuwa tunataka tupeleke na Kijiji kile kingine cha pili cha Mwamloli, je, Mheshimiwa Waziri hawezi kutupatia shilingi milioni 300 kukamilisha hii kazi nzuri ambayo inafanywa na Chama Cha Mapinduzi ili twende vizuri kwenye mambo yetu yale mengine ya uchaguzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mbunge. Utekelezaji wa miradi hii unatokana na kazi kubwa sana ambayo Mheshimiwa Mbunge ameifanya kwa ajili ya kuwasemea wananchi wake wa jimbo lake. Matokeo haya ni kwa sababu ya kazi kubwa sana ya ushirikiano wake mzuri sana na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali ni wajibu wetu kuhakikisha tunafuatilia utekelezaji wa miradi ili iweze kukamilika kwa wakati. Vilevile, kuhakikisha sehemu ambayo hatujafika, tunaona njia ya kuhakikisha tunafanya utafiti na tathmini ya namna gani tupeleke huduma ya maji kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alivyoomba. Sasa Mheshimiwa Mbunge kama alivyoomba shilingi milioni 300, naomba nilipokee ili tuweke katika Mpango wa Serikali wa utekelezaji katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Je, lini Serikali itaharakisha ujenzi wa Bwawa la Farkwa ili kuweza kukabiliana na tatizo la maji katika Jiji la Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq kama ifuatavyo. Ni kilio cha Wanadodoma, na ni kilio cha Waheshimiwa Wabunge wa Dodoma, na ni kilio cha Watanzania kwa sababu hapa ndipo Makao Makuu ya Nchi yetu. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari alipata fedha kwa ajili ya kufanya mapitio ya mradi huu wa Farkwa ambao unakamilika. Sasa tumeanza mchakato wa kumtafuta mkandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka Desemba itakapofika, tuna uhakika mkandarasi atakapopatikana, ataingia kazini kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa kuvuta maji kutoka Bwawa la Farkwa ili iwe solution ya kati kwa kutatua changamoto ya maji ambayo tumeendelea kukutana nayo katika Jiji lla Dodoma. Kama ambavyo nilisema, uzalishaji wetu wa maji hapa Dodoma ni lita 79,000,000 lakini mahitaji yake ni lita 149,000,000. Sasa visima pekee havitaweza kutupatia maji ya kutosha kulingana na mahitaji na ndiyo maana kunakuwa na hii changamoto ya mgao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili Bwawa la Farkwa halitakuwa suluhisho la kudumu. Jambo ambalo liko katika Mpango wa Serikali ni kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria ili kuhakikisha kwamba sasa Jiji la Dodoma linaendelea kupendeza na wananchi wa Dodoma wapate maji ya uhakika na toshelevu kwa wakati wote, ahsante.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza. Katika awamu ya kwanza kuna madeni makubwa sana ya zaidi ya shilingi bilioni tatu ambayo ndicho chanzo cha sababu ya mradi kuchelewa. Je, ni lini madeni haya yatalipwa na Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya pili ya kupeleka maji Kanyangereko na Maruku mkandarasi mmoja alifukuzwa, alishindwa kazi na akaondolewa, mpaka leo ni karibu mwaka mzima tangu ameondolewa. Je, ni lini tutapata mkandarasi wa pili ili kazi iendelee?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Rweikiza kwa kazi kubwa aliyoifanya na kwa kuomba hii miradi. Aliiomba mbele ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais akaridhia kuanzishwa kwa miradi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madai. Serikali inatambua kuwa kuna madai ambayo mkandarasi anadai na ni takribani shilingi bilioni 2.971, ambapo tayari Serikali kupitia Wizara ya Maji tumeshawasilisha Wizara ya Fedha kwa ajili ya kufanyika haya malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipengele cha pili, ni kweli kabisa mkandarasi aliyekuwepo hakuweza kufanya ule mradi kwa ubora uliokuwa unatakiwa, lakini vilevile alikuwa nje ya muda. Kwa sababu hiyo Serikali ilichukua hatua ya kuhakikisha kwamba, tunawasilisha taarifa hii PPRA ili kuanza hatua ya pili na sisi Serikali tumeuingiza tena mradi huu katika Bajeti ya 2024/2025. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, hatua za manunuzi zitakapokamilika, basi mkandarasi atapatikana na kazi ya ujenzi wa mradi huo itaendelea. Ahsante sana.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nataka kujua ni lini Mradi wa Maji wa Kintinku, Lusilile, katika Wilaya ya Manyoni ambao unahudumia vijiji 11 utakamilika ili wanawake wa Tarafa ya Kintinku wapate huduma ya maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni maelekezo ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba, miradi yote ambayo imekwama kwa muda mrefu inafanyika na kukamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anaendelea kupambana kuhusu mradi huu aendelee kutupatia ushirikiano ili sisi tuweze kutimiza majukumu yetu na kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata maji. Ahsante sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba kuuliza, Miradi ya Maji ya Kijiji cha Kitundueta, Kata ya Muhenda, Mikumi na Kidodi ni lini inaaenda kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilipokee na baada ya kutoka hapa nikutane na Mheshimiwa Londo, ili tuweze kuangalia mradi wake umefikia hatua gani. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri aliahidi kutoa kiasi cha shilingi bilioni nne, kwa ajili ya Mradi wa Maji katika Wilaya ya Karatu. Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, jiandae Mheshimiwa Kilave.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani, naomba nipate maswali.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Paresso rudia swali lako.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri, kwa maana ya Serikali, alitoa ahadi ya kutoa kiasi cha shilingi bilioni nne, kwa ajili ya mradi wa maji katika Wilaya ya Karatu. Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia kwa sababu, lengo ni wananchi wapate maji. Namwahidi kwamba, hili nalipokea na nakwenda kulishughulikia ili kujua ahadi hiyo imefikia katika hatua gani ili kuhakikisha kwamba miradi inaendelea.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa DAWASA wameshindwa kuendeleza visima ambavyo vimechimbwa hasa katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Temeke. Kwa nini sasa msivirudishe kwa wananchi ili waviendeleze na kuvifanyia kazi kama mwanzoni kwa sababu, DAWASA wameshindwa kabisa kuvifanyia kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nasema mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba, DAWASA kwa maana ya Wizara ya Maji hatujashindwa, isipokuwa tutaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba, tunatatua changamoto ambazo zinaendelea kujitokeza, lakini tunaamini kwa ushirikiano na Mheshimiwa Mbunge, akiwa ni mdau namba moja katika Jimbo la Temeke, tutahakikisha tunatafuta njia ambayo itarahisisha zaidi kutatua changamoto hiyo. Ahsante sana.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, visima vitatu vilivyochimbwa na visima 10 vitakavyochimbwa vitajengewa vioski ili kutoa huduma ya maji kwa wananchi wakati Serikali inajipanga kujenga miradi mikubwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, ni hatua gani imefikiwa kuhakikisha visima 10 vitakavyochimbwa vinakamilika kabla ya mwezi Disemba kwa kuwa mwezi Disemba tayari mvua zinakuwa zimeshanyesha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge anaendelea kufuatilia miradi hii na tunashirikiana vizuri sana. Ni ukweli usiopingika kwamba Wizara yetu ya Maji inaendelea kuhakikisha kwamba inatoa huduma inayozingatia ubora unaotakiwa na katika hivyo visima vitatu na vile 10 vingine ambavyo vitakuja kujengwa tutahakikisha vyote vinajengewa vioski ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipengele cha pili, ni kweli kabisa Serikali imeanza mchakato wa kumpata mzabuni kwa ajili ya mradi unaofuatia wa visima 10 kwa sababu tunatambua kwamba itakapofika Disemba na mvua ikianza tutashindwa kuchimba. Kwa hiyo, sasa tumeshajipanga kuhakikisha kwamba zoezi hilo linakamilika kabla ya Disemba. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji katika Vijiji vya Kisimamkika na Zinga Kibaoni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kukamilisha miradi yote inayoendelea nchini ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata fursa ya kupata maji safi na salama. Kwa hiyo, pamoja na nchi nzima maana yake pamoja na vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja tutahakikisha kwamba katika Jimbo lake tunafuatilia kwa ukaribu na wananchi wapate maji safi na salama na kujiepusha na magonjwa ambayo yanaweza yakatokana na maji. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, tunashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zimeendelea kuwepo Mkoa wa Pwani kwenye suala la maji, je, lini Serikali itaanza kujenga Mradi wa Maji uliopo Pangani ukizingatia toka mwaka jana mwishoni tulisaini mkataba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maji nchini kote. Vilevile kwa upande wa Mradi huu wa Pangani, Serikali tayari ipo katika hatua nzauri kabisa za kuendelea na utekelezaji wa mradi huu. Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge atupatie nafasi Serikali ili tuhakikishe kwamba mradi huu unakamilika na wananchi wa Pwani na maeneo maeneo yote yanayozunguka mradi huo wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali na naishukuru sana Serikali kwa kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutuletea bilioni 3.39 na mradi umezinduliwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kuna Mradi wa Visima 18 unapeleka maji Arusha na Sera ya Maji inasema kwenye chanzo cha maji chochote, wananchi wanaozunguka eneo lile wanatakiwa wapate maji. Je, ni lini sasa Serikali itaanza utaratibu wa kuwapatia wananchi wale walioko kwenye ule mradi wa visima vya maji ili na wao waweze kupata maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo na changamoto kubwa sana, wananchi wa Mkalama, Shirimatunda, Shiri Muungano, Shiri Njoro, Mijongweni, Longoi na Kikavu Chini, kutokana na kwamba mradi wa maji kwenye maeneo haya unasimamiwa na Mamlaka ya Maji Moshi Mjini; je, ni lini Serikali itaondoa Mamlaka ya Usimamizi wa Maji Moshi Mjini na kurejesha kwenye RUWASA, Wilaya ya Hai ili Wilaya ya Hai iweze kusimamia yenyewe, Mamlaka ya RUWASA isimamie maeneo haya ili wananchi waweze kutatuliwa matatizo yao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kila mradi unaokuwepo katika jimbo lake, lakini siyo hivyo tu na kufuatilia utekelezaji wake. Nakupongeza sana Mheshimiwa Mbunge. Vilevile Mheshimiwa Mbunge ameongelea kuhusu Sera ya Maji. Ni kweli kabisa Sera yetu ya mwaka 2002 inaelekeza kuhakikisha kwamba pale palipo na vyanzo vya maji ni lazima vijiji vinavyozunguka pale wapate maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika ile miradi mikubwa, bomba kuu la maji linapopita, at least kilometa 12 upande wa kushoto na kulia, wananchi wanaoishi katika maeneo hayo waweze kunufaika. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, changamoto ambayo imebainika pale baada ya Wizara kufanya tathmini; kwa kutumia ule mradi wa visima 18 ili tuweke pump na kusukuma maji kuwafikia wananchi walioko pale, tumegundua kwamba pump itahitaji kusukuma maji kilometa 30, maana yake ni kwamba gharama ya maji ambayo yanawafikia wananchi yatakuwa yana gharama kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri ameelekeza RUWASA Kilimanjaro kufanya tathmini na usanifu ili twende kutumia maji ya kutoka Njoro Bluu kwenye chanzo ambacho ni maji mserereko, ambapo itakuwa na gharama rahisi zaidi kuwafikia wananchi na kupata maji ambayo yana gharama ndogo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba hilo linakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kweli kabisa kama ambavyo ameomba, kwamba mamlaka ya maji anahitaji isimamiwe na CBWSOs; naamini kwamba alikuwa anamaanisha CBWSOs; of cause CBWSOs iko kisheria; na sisi Wizara ya Maji, kupitia maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wetu, Mheshimiwa Jumaa Aweso, hatutaki kuwa kikwazo kwa wananchi kupata maji.
Mheshimiwa Spika, sisi pale ambapo tunaamini kwamba maji yenye ubora, toshelezi na salama yatafikishwa basi tutatumia mfumo huo ambao utaweza kuwarahisishia wananchi kupata maji ambayo ni safi na salama zaidi. Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mvua zinazoendelea nchini sasa hivi zimeharibu sana miundombinu ya maji, hasa kule ambako mafuriko yametokea, ikiwemo Mabogini, Chekereni na Chemchem kule Mkoani Kilimanjaro ambayo ni tambarare ya mlima. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya haraka kwenda kuwapatia wananchi hao maji safi na salama ili wasije wakapata kipindupindu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji ina mikakati ya kuhakikisha kwamba inaweza ku-manage maji mengi. Maji mengi maana yake ni mafuriko na maji machache, maana yake ni ukame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoweza kukifanya pale ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza catchments za maji ya kutosha na baadaye tunafanya treatment ili wananchi ambao wako katika maji machache ambao ni ukame waweze kupata maji na wale ambao wanaweza kuathiriwa basi tuweze kuya-control na kuhakikisha kwamba tunayatumia kama resource ambayo itawasaidia wananchi kupata maji safi na salama. Kwa hiyo, niwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kushirikiana kwa sababu sisi hatutakuwa kikwazo kwa wananchi ambao amewataja kupata maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, ni lini Mradi wa Sinyanga Group Wilayani Kyela utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge amekuwa akipambana nao tangu mwaka 2023. Natambua kwamba kulikuwa na changamoto ya malipo na mkandarasi GOPA contractors ambaye bado anatudai takriban milioni 122. Serikali tayari tumeshawasiliana na wenzetu Wizara ya Fedha, wameshaanza kuandaa kwa ajili ya kumlipa. Mradi tayari umeshafikia asilimia tano kwa sababu tayari kuna jengo la CBWSOs limeshajengwa na limefikia kwenye lintel. Tunaamini kwamba fedha zikishaingia na mkandarasi atarudi site. Tunaamini kwamba ndani ya mwaka wa fedha litakuwa limekamilika. Ahsante sana.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Bukene wanapata maji safi na salama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri Jimbo la Bukene linapitiwa na Mradi wa Ziwa Victoria. Tayari tunakwenda kuunganisha Jimbo la Bukene ili waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Takriban wananchi 80,000 wanakwenda kupata huduma ya maji na vijiji 20 vitanufaika na mradi huu kutoka Ziwa Victoria. Vilevile tuna takriban vitongoji 100 vinakwenda kupata huduma ya maji. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, mradi huu uko kwenye utekelezaji, tayari umeshaanza na muda siyo mrefu ukikamilika wananchi wake watapata maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na kwamba tayari imeshafanya kazi kubwa sana ya kuweka minara katika Jimbo la Mbulu Mjini, Kata ya Gunyoda na Silaloda zina jiografia ya milima. Minara hii itakayojengwa katika Kata ya Gunyoda na Kata ya Marang haitaweza kuhudumia Kata ya Gunyoda. Swali la kwanza; je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kujenga mnara katika Kata ya Silaloda kwa ajili ya jiografia ya milima? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa tumekuwa na minara mingi sana katika maeneo yetu. Je, Serikali haioni utashi wa kukaa meza moja na Makampuni ya Simu ili kuunganisha minara na kuweza kutoa huduma kwa pamoja ili kuleta ufanisi zaidi katika mawasiliano? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI K.n.y WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kata hii na kwa jiografia yake, ina milima sana kiasi kwamba line of sight inajikuta kwamba haiwezi kuhudumia katika maeneo ambayo yako mabondeni na hivyo changamoto bado inaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Spika, Serikali itatuma wataalam wake kwenda kufanya kazi ya kiufundi na kufanya tathmini. Tuchukue hatua ipi ambayo itaendana na aina ya tatizo ambalo litakuwa limeonekana pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni kuangalia namna ambavyo mitandao inaweza ikaunganishwa. Kwanza kabisa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tulikwishatengeneza kanuni. Kwanza ni Kanuni ya Roaming. Maana yake ni kwamba, mtoa huduma mmoja anaweza akatumia huduma ya mtoa huduma mwingine. Pili, ni infrastructure sharing, hii ni pamoja na hayo mambo ya co-location; maana yake ni kwamba Vodacom, Airtel, Tigo, wanaweza wakapatikana kwenye mnara mmoja ili kuhakikisha kwamba tunapunguza gharama za uwekezaji, lakini huduma iendelee kupatikana.
Mheshimiwa Spika, tumekwenda zaidi ya hapo, tumekwenda kwenye eneo la spectrum (masafa). Napo tumetengeneza kanuni ya kuruhusu sasa, kwamba tunaweza tukawa na spectrum sharing ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kupunguza gharama za uwekezaji na za uendeshaji, wakati huo huo huduma iendelee kuboreshwa na wananchi waendelee kupata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Katika Kijiji cha Uliwa Kata ya Uliwa kumekuwa na ahadi ya muda mrefu sana kuhusu huo mnara na hata na yeye alipokuwa Naibu Waziri aliahidi. Je, ni lini sasa mnara huo ambao umeahidiwa utajengwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI K.n.y WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mradi wetu wa Tanzania ya Kidijitali wenye minara 758, minara takribani 295 ambayo ni sawasawa na 40% imekwishakamilika, lakini kuna minara mingine ambayo inaendelea katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji huo tumekutana na changamoto mbalimbali kiasi kwamba tumejikuta tunahama katika eneo moja kwenda kutafuta eneo lingine. Vilevile tumekutana na migogoro katika maeneo ambayo minara inataka kujengwa. Hii yote imesababisha ucheleweshaji wa maeneo mbalimbali kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, kingine ambacho Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inakifanya, Mheshimiwa Waziri Jerry Silaa ameandaa kitabu chenye taarifa ya utekelezaji wa minara 758, ambapo kila mnara unakojengwa namba ya mtoa huduma ambaye atakuwa anatoa taarifa ya progress ya utekelezaji kila eneo. Katika taarifa hizo kuna namba za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao watakuwa wanaweza kutoa update ya hatua ambazo zinaendelea katika eneo husika. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwamba eneo la Mheshimiwa Mwanyika liko katika ile miradi ambayo iko katika hatua mbalimbali. Ninaamini kabisa kwamba, mpaka Mei, 2025 yote itakuwa imekamilika kama ambavyo Serikali imeelekeza. Ahsante sana.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, Kata ya Ikondo Jimbo la Lupembe ina changamoto kubwa ya mawasiliano, hasa maeneo ya Nyave, Idyadya, Itova na kadhalika. Je, ni lini mnara wa simu utajengwa Ikondo kwa ajili ya wananchi wangu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI K.n.y WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Advocate Edwin Swalle, Mbunge wa Lupembe kwa kazi kubwa na kwa namna ambavyo amepambania kuhusu hii Kata ya Ikondo. Ninaikumbuka vizuri sana. Kwa bahati nzuri na salamu njema kwake, leo nimepatiwa taarifa na Mheshimiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; katika maeneo ambayo nilikuwa ninajua kabisa kwamba yalikuwa na changamoto ya muda mrefu, Kata ya Ikondo, wakandarasi wameshafika site na wako tayari kwa kuanza kujenga mnara wa mawasiliano katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Ukiwa Sitalike kama unaelekea Namanyere, unapita Hifadhi ya Taifa ya Katavi, umbali wa zaidi ya kilometa 70 hakuna mawasiliano kabisa. Je, Serikali ina mpango gani, ukizingatia pale kuna wanyama wakali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI K.n.y WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto ambazo nimeongelea wakati wa kucheleweshwa kwa baadhi ya maeneo ya kujengwa minara nimeongelea migogoro; lakini kuna maeneo mengine tunapata changamoto ya kupata vibali. Kwa eneo lile tumepata changamoto ya kupata vibali kwa wakati kutoka TSF.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba tunaendelea kuwa-engage wenzetu na watakapoweza kutoa kibali hicho tuna uhakika kabisa kwamba tutakwenda kujenga minara katika maeneo hayo, ili kuhakikisha kwamba tunaondoa hatari ambayo inaweza ikatokana na wanyama wakali ambao Mheshimiwa Mbunge ametaja. Ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Kiteto tangu tupate uhuru hatusikilizi Redio Tanzania, na kauli ya mwisho walisema kwamba wangejenga mnara mwezi wa pili mwaka huu. Sasa, nini kauli ya mwisho kabisa kwa wananchi wa Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA MAJI K.n.y WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu kama ambavyo Mheshimiwa Advocate Olelekaita, Mbunge wa Kiteto alivyouliza.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa nimekwishafika Kiteto, na Mheshimiwa Mbunge tulizunguka katika jimbo lake takriban siku nzima ili nilijione changamoto. Tulifanya mkutano wa hadhara, wananchi waliongelea kuhusu changamoto hii. Ninamhakikishia kwamba, jambo hili ambalo ni ahadi ya Serikali kwa Watanzania, hasa wananchi wa jimbo lake, ahadi ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itatekelezwa na itatimia. Nimwombe, atupatie muda kidogo ili tuendelee kufanyia kazi baadhi ya changamoto ambazo zinaendelea kutokana na mambo ya kiufundi. Ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa majibu mazuri ya Serikali. Pia, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kutekeleza miradi hiyo ya maji katika Jimbo la Mbinga Mjini, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Serikali imejenga miradi katika Kijiji cha Mbagamao, Kijiji cha Tanga na Kijiji cha Ruvuma chini ambayo ni miradi mikubwa. Nilikuwa nataka nijue sasa ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kusambaza maji kwenye vitongoji ambavyo vipo jirani na miradi hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Kata ya Kikolo, Kijiji cha Kikolo pamoja na Kitongoji cha Kitete kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga mradi katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika maeneo haya Mbagamao, Mheshimiwa Mbunge amekuwa akituomba sana Serikali kwenda kuhakikisha kwamba tunaendelea kupanua na kusambaza mtandao wa maji katika vijiji alivyovitaja. Serikali inatafuta fedha na kuhakikisha kwamba tutaenda kufanya upanuzi huo katika vijiji na vitongoji ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviomba.
Mheshimiwa Spika, upande wa Kijiji cha Kikolo tayari tumekamilisha usanifu na tutaingiza katika bajeti yetu ya 2025/2026, kuhakikisha kwamba eneo hilo linaenda kupata huduma ya maji safi na salama. Kwa eneo la Kitete, bado Serikali kupitia Wizara ya Maji, tunaendelea kutafuta chanzo. Tutakapokipata chanzo, ndipo tutaanza usanifu wa mradi ili tujue kwamba itahitaji gharama ya shilingi ngapi kwenda kuutekeleza mradi huo. Baada ya hapo, Serikali itachukua hatua stahiki kwa wakati sahihi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sensa iliyopita, wanufaika wameongezeka katika kijiji hicho na wananchi wamekuwa wanatarajia mradi huu ukamilike kwa wakati kwa sababu umekuwa ni mradi wa muda mrefu sana
Je, ni lini kwa uhakika, kwa sababu kilichopo site na unachokisema kina tofauti kidogo, ni lini kwa uhakika wananchi hawa watarajie kupata mradi huu wa maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna wananchi wa vijiji vya jirani ikiwemo Rhotia Juu pamoja na Kilimatembo Juu, ni lini na wananchi hawa wataweza kupata maji kwa sababu vijiji hivyo havina maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli natambua na Serikali inatambua uwepo wa changamoto hii katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analiongelea na ni kiu ya Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji. Ni kweli mradi huu umechukua muda mrefu, ni kweli kabisa kwa sababu ya hatua mbalimbali ambazo zilikuwa zinachukuliwa na Serikali ikiwemo utafutaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba kwa mujibu wa majibu yangu ya msingi, mradi huu unaenda kukamilika Juni, 2024. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika eneo la Kilimatembo pamoja na Rhotia, kuna mradi ambao unaendelea pale, lakini Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kupanua miundombinu ili tufikishe huduma ya maji katika maeneo yanayozunguka katika mradi ule na Kijiji cha Kilimatembo pamoja na Rhotia wataweza kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Kata za Kimyaki, Siwandeti, Kiranyi, ambayo ni maeneo yenye wananchi wengi zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba watu wanapata accessibility ya maji safi na salama na tuna mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba vijiji ambavyo vimebaki havina maji, lakini kulingana na programu ya kila Mbunge kupata vijiji vitano ambavyo vitapata huduma ya maji. Tutaangalia sasa kwamba ni vijiji vingapi ambavyo vitakuwa vimebaki havina huduma ya maji ili Serikali iweke mkakati maalum kwa ajili ya kuhakikisha tunafikisha huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambako miradi ya maji bado haijakamilika, tuna maelekezo mahsusi kutoka kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo imekwama basi tunaikwamua ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua ni lini Serikali itapeleka fedha katika Mradi wa Maji Itumba - Isongole ulioko Wilaya ya Ileje ili wananchi waweze kunufaika na maji hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Stella kwa kupitisha bajeti yetu ya maji kwa kishindo kabisa, alikuwa anapitisha huduma ya maji kwa wananchi wa Ileje. Kwa kupitisha bajeti hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapoingia sasa kwenye utekelezaji, tutapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huo unaenda kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; je, ni lini Mradi wa Maji wa Kata ya Ruaha Mbuyuni katika Wilaya ya Kilolo utakarabatiwa? Kwa sababu Mto wa Lukosi ulipochepuka uliondoa mabomba yote kwa hiyo, wananchi wa Ruaha Mbuyuni wanapata shida sana kupata maji safi na salama. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia changamoto ambayo imejitokeza katika mto ule. Ni kweli kabisa Serikali inatambua kuna mabomba ambayo yalipitiwa kulingana na mto jinsi ulivyokuwa umechepuka, lakini pia wakati tunajaribu kuweka jitihada za kurejesha huduma, bado mabomba yalipata changamoto. Serikali imeshatenga fedha na tayari tunanunua mabomba kwa ajili ya kwenda kurekebisha eneo lile ili kurudisha huduma haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5.56 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu yote ya maji ndani ya Jimbo la Kilolo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kabla sijauliza maswali ya nyongeza, ninaomba nitoe pole kwa Wana-Kyerwa na Wizara ya Maji kwa kumpoteza Meneja wetu wa Wilaya, ndugu yangu Tungaraza, tunawapa pole sana Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza; pamoja na Serikali kuweka mpango wa kuchimba visima vya maji, kuna visima ambavyo vimechimbwa zaidi ya miezi sita na mpaka sasa hivi visima hivi bado havijajengewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini visima hivi vitajengewa kwenye Kata ya Kibale, Kijiji cha Kigologolo, lakini pia kwenye Kata ya Businde, Kijiji cha Omuchwenkano?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna mradi wa maji katika Kata ya Songambele, Kijiji cha Songambele, ni zaidi ya mwaka sasa tumepitisha kwenye bajeti mradi huu haujaanza. Ni lini mradi mradi huu utaanza ili kuwapatia wananchi wa Songambele maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kwa niaba ya RUWASA na Wizara ya Maji na sekta ya maji kwa ujumla tunapokea pole hizo kwa kuondokewa na DM wetu kutoka kule Kyerwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu Kigologolo pamoja na Omuchwenkano, katika jibu langu la msingi nimeitaja Omuchwenkano, lakini vilevile katika Kigologolo, Serikali itaanza kwanza ukarabati kwa sababu ni kweli kabisa kisima kipo kimechimbwa, lakini bado ile miundombinu ya kusambazia maji haijakamilika na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inafanya ukarabati wa miundombinu ili wananchi waweze kufikishiwa huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, katika mradi wa Songambele, kwanza nimpongeze sana kwa ufuatiliaji mzuri sana Mheshimiwa Innocent Bilakwate kwa ajili ya mradi huu na kwa ushirikiano ambao anaendeea kutupatia na sisi Serikali hatutamuangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huu fedha ambazo zilitengwa kwa bahati mbaya au nzuri hatukuweza kuzipata kwa wakati. Nimhakikishie katika mwaka wa fedha 2024/2025 mkandarasi anaenda kupatikana na mradi huu utaanza mara moja, ahsante sana. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona, mwaka 2023/2024 Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya mradi wa maji wa Kata za Itandula na Mbalamaziwa, Jimbo la Mufindi Kusini, lakini mpaka sasa fedha hizo hazijaenda. Ni lini Serikali itapeleka fedha hizo kukarabati mradi huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua changamoto ya kucheleweshwa kufikishwa fedha katika mradi huo lakini nikuhakikishie kwamba kabla ya mwaka wa fedha haujaisha fedha hizo zitakuwa zimepelekwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina mambo mawili. Jambo la kwanza, naiomba Serikali iendelee na hilo zoezi la kufanya tathmini ya awali kama ilivyoji-commit leo ili wananchi wa mikoa tajwa wapate hizo huduma za maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwa kuwa zoezi la usanifu wa kuchukua maji kutoka Mto Ruvuma kwenda Mtwara limehusisha uchukuaji wa maeneo ya watu wa maeneo ya Nanyamba, Mtwara DC na Mtwara Manispaa na linahitaji fidia, je, mkakati wa Serikali wa kulipa fidia kwa wananchi wale ambao maeneo yao yamechukuliwa ni upi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Maimuna na aliyeuliza swali kwa niaba pamoja na Wabunge wa Mikoa ya Kusini. Hii imekuwa ni ajenda yao kuu ya kuhakikisha kwamba mradi huu wa kutoka Mto Ruvuma unaharakishwa ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari Serikali imeshaanza kufanya tathmini ya awali ya usanifu na Mheshimiwa Mbunge ametuomba tuendelee nayo, sisi tutaharakisha zoezi hili likamilike ili tuweze kujua kwamba mradi huu utagharimu shilingi ngapi ili tuweze kuchukua hatua za kupata fedha kwa ajili ya kuutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili. Kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya msingi, Serikali inaendelea kufanya mapitio ya usanifu ili kuendelea kujiridhisha na pale ambapo bomba kuu litapita na watakaoathirika tuweze kulipa kwa pamoja badala ya kuanza kulipa nusu nusu wakati mapitio yanaendelea. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali italipa fidia pale ambapo mapitio ya usanifu yatakamilika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu hayo ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Bwawa la Mihingo ilikuwa lichimbwe na mkataba wake ulikuwa ni mwaka mmoja, sasa ni miaka mitano toka limeanza kuchimbwa, hali yake bahati nzuri viongozi wote wa Wizara wameshafika pale wameona hali yake. Sasa walisema miezi sita ijayo litakuwa limemalizika na miezi sita imepita. Sasa ni lini watamaliza hilo Bwawa la Mihingo ili kuondoa kero kwa wananchi wa Mihingo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mabwawa ya Rakana, Salama A, Tingirima, Kambubu na Nyaburundu yalishafanyiwa usanifu muda mrefu tu na michoro yote mnayo na kwa kuwa tunayo mitambo Mkoa wa Mara, ni lini sasa watapeleka mitambo kumaliza mabwawa haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Bwawa la Mihingo kama ambavyo nimejibu katika majibu ya msingi ni kweli limefikia katika 95% na Serikali imejipanga kwenda kuhakikisha kwamba bwawa hili linaisha.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Mabwawa ya Rakana vilevile kama ambavyo nimejibu katika majibu ya msingi kuwa usanifu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge kweli amekiri ulifanyika siku nyingi, kawaida katika mambo ya ujenzi wa mabwawa ukishafanya usanifu na muda mrefu ukapita hamjatekeleza maana yake mnaanza kupitia kuona kwamba mahitaji kama bado yapo vilevile na kama yamebadilika basi na kuhusiana na masuala ya fidia ili waweze kulipwa watu wanaostahili kulipwa fidia na ili mradi uweze kuanza. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge eneo hili tumejikita, tumejizatiti kuhakikisha kwamba mradi huu utaanza baada ya mapitio ya usanifu, ahsante sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na sheria iliyopo ambayo inataka wananchi kushirikishwa katika kupanga bei, hali halisi ni tofauti, maeneo mengi wananchi hawashirikishwi. Mfano, Wilaya ya Lushoto, Lukozi na Kata ya Lukozi, Kata ya Shume na Manolo, bei zilipelekwa kubwa ikamlazimu Mkuu wa Wilaya kwenda kushusha bei za maji kwa wananchi, nini hatua ya Serikali kudhibiti hali hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa gharama hizi zinasababishwa na wananchi kugharamia mafundi wa local fundi wanaokwenda kukarabati miradi hiyo. Je, Serikali haioni imefika muda muafaka kuwaajiri na kuwalipa mishahara local fundi na kuondoa mzigo huo kwa wananchi? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za huduma ya maji zinapangwa kutokana na sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kwanza; uzalishaji, eneo ilipo skimu husika, aina ya utoaji wa huduma, lakini vilevile na aina ya jamii inayozunguka eneo husika, lakini kwa mujibu wa sheria na EWURA anaingia katika upangaji wa bei ya maji. Kwa kuzingatia factor hizo zote, Serikali imekuwa ikiingilia kati pale ambapo tunaona kwamba kuna changamoto na ndiyo maana Mkuu wa Wilaya ni sehemu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo Waziri wetu wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, katika bajeti yetu tumepanga kuwepo na fedha za monitoring and evaluation kwa ajili ya wakuu wa wilaya pale ambapo kunakuwa na changamoto ya utekelezaji wa mradi au uendeshaji wa miradi, Mkuu wa Wilaya aweze kufika eneo husika na kutoa maelekezo ya Serikali, hilo tutaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linatokana na uzembe wa uendeshaji wa wataalam ambao wamekabidhiwa jukumu la kuendesha na hayo yote tumekuwa tukiyafuatilia na kuchukua hatua stahiki. Sote tutakubaliana, sheria kuwepo ni jambo moja, utekelezaji wa sheria ni jambo lingine, kwa hiyo, tumejitahidi sana kuhakikisha watu wetu wanaendelea kusimamia na kuhakikisha sheria haivunjwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu ajira kwa mafundi, ni kweli kabisa changamoto hii tumeanza kuiona baada ya kugundua kwamba kuna CBWSOs wameshindwa kujiendesha na wale local fundi wanashindwa kuwalipa, inasababisha hata ile miundombinu yetu kuendelea kuchakaa na kuharibika. Kwa sasa tayari tumeshaanza kukusanya maoni, namna bora zaidi ya kwenda kuendesha CBWSOs bila kuleta mzigo mkubwa kwa wananchi ambao wanatarajia kutumia huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, katika kufanya tathmini yetu na yeye tutamfikia kwa ajili ya kuomba maoni yake ili tuweze kuboresha zaidi na hatimaye gharama kwa wananchi iwe reasonable, lakini uendeshaji wa miradi yetu na miundombinu isiweze kuharibika kwa kukosa fedha ambazo zingesaidia sana.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Mradi wa kutoa Maji Ziwa Victoria ulianza kama siyo mwaka 2009 mpaka leo haujaanza kutekelezwa na mwaka jana Serikali ilitenga shilingi milioni 850 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huu hatua kwa hatua. Je, ni kitu gani kimefanyika mpaka leo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba Muleba Magharibi ambayo ina tatizo kubwa la maji inapata maji na wananchi wake wanatokana na adha ya ukosefu wa maji? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali inatambua ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge alichokiongelea kwamba mradi huu ulianza mwaka 2009 na kweli kabisa katika bajeti iliyopita shilingi milioni 850 ilitengwa. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia kwa faida ya wananchi wake wa Muleba Kusini nampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali inatenga fedha, lakini pia inaendana na upatikanaji wa fedha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa mradi huu, Serikali imejizatiti kwa sababu inatambua umuhimu mkubwa sana kwa ajili ya wananchi wa Muleba Kusini kupata maji ya kutoka Ziwa Victoria. Ni jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiliongelea, kama Tabora wanapata maji ya Ziwa Victoria lakini wao wapo karibu pale na kweli Serikali imelitambua hilo na inaliangalia kwa kina vizuri kabisa na tunaendelea kutafuta fedha ili zikishapatikana tu mradi huu uanze mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna miradi mikubwa, miradi ya kati na miradi ya muda mfupi, tumeanza na maeneo mengine kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi, tumeanza na zile kata zingine ambazo tunaenda kutoa huduma kwa watu wapatao 2,780, lakini pia tunachukua maombi ya Mheshimiwa Mbunge kwa eneo la Muleba Magharibi ili kuhakikisha kwamba tunaliingiza katika utaratibu wa utekelezaji wa miradi yetu ya muda mfupi ili wananchi wa Muleba Magharibi na wao wapate huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaanza kusambaza maji yanayotoka Kisarawe II katika Kata ya Mbagala Kuu, Kijichi, Toangoma, Kiburugwa na Mbagala?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kuwasemea vizuri sana wananchi wa Mbagala. Vilevile tunampongeza sana kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa katika kuibua changamoto ambazo zinahusiana na Sekta ya Maji ndani ya jimbo lake na sisi Serikali tunaendelea kuzichukua na kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie katika bajeti yetu ambayo tumeipitisha mwezi uliopita tunaamini kabisa kwamba pindi dirisha la utekelezaji wa bajeti hiyo litakapofunguliwa na tutaanza, siyo kwa upande wa Mbagala peke yake, ni upande wote wa Dar es Salaam ambao umekuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama. Kwa hiyo, upande wa Mbagala tutapata fursa hiyo ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza miradi hiyo ya kusambaza maji safi na salama. Ahsante sana.