Contributions by Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi (83 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii. Kwa kuwa ni mara yangu kwanza kuchangia katika Bunge lako Tukufu, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na kunipa nafasi ya kuongea hapa nikiwa mwakilishi wa watu wa Jimbo la Moshi Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya. Nataka niwashukuru watu wengi ambao wamenisaidia nikawa Mbunge, nianze kuishukuru familia yangu, namshukuru sana mama pamoja na watoto, nakishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua nigombee ubunge, nawashukuru wapiga kura wa Moshi Vijijini kata zote 16 walinipa kura za kutosha kuhakikisha nimeshinda kwa kishindo na Mheshimiwa Rais na Madiwani wote 16. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo ameifanya toka mwaka 2015 tangu achaguliwe kuwa Rais na kwa hutoba nzuri sana ya kulizindua Bunge hili. Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais aliongea mambo mengi makubwa ambayo sisi kama Wabunge endapo tutayazingatia na kama tutaisimamia Serikali vizuri nina hakika tutaacha alama kama moja ya Mabunge bora katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye mchango, nitachangia eneo la kilimo mifugo na uvuvi na nafasi ikipatikana nitaongelea miundombinu na sekta ya afya. Tukubaliane Wabunge wenzangu wote waliopo huku ni matunda ya watoto wa wakulima, kama siyo mtoto wa mkulima ni mtoto wa mfugaji, kama siyo mtoto wa mfugaji ni mtoto wa mvuvi. Tukubaliane tu Rais ana nia nzuri ya kuhakikisha kwamba katika miaka mitano ijayo anaboresha sekta hii ambayo nimeitaja ambapo sote sisi ndiyo tumetoka huko. Niombe tu kwamba ni wakati wetu sisi kama Wabunge tumuunge mkono Rais, tuhakikishe kwamba tunarudi kule nyumbani tulikotoka kwa kuziunga mkono hizi sekta ili nao waweze kuongeza kipato na kuchangia katika pato la Taifa na katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu sekta hii ina changomoto nyingi sana, changamoto mojawapo ni kwamba wakulima wengi wafugaji na wavuvi ni wazee, vijana wetu ambao ndiyo wanategemewa warithi hii kazi hawana interest na hizi kazi za kilimo ama ufugaji ama uvuvi. Niishauri Serikali ikiwezekana tuchukue hatua muhimu kabisa ya kuhakikisha tunawashawishi vijana wetu ili waweze kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa kwanza wa Serikali ni kwa Wizara ya Elimu ikiwezekana wabadilishe zile shule zote za kata ambazo ziko karibu na vijijini zifundishe somo la kilimo na Vyuo vya MATI, LITA, VETA, Chuo Kikuu cha Sokoine na Chuo Kikuu cha Mandela ambacho vinafundisha kilimo kwenye mitaala yao waweke component ya ubunifu na ujasiriamali. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawaandaa hawa vijana ili waje wawe waajiriwa kwenye hii sekta ya mifugo kilimo na uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme tu kwa kuwa Rais amedhamiria kusaidia hii sekta ya uzalishaji ambayo ni kilimo, mifugo na uvuvi, nishauri Serikali iweke pesa za kutosha kwenye utafiti wa kilimo, mifugo na uvuvi ili waweze kuzalisha mbegu za kutosha na teknolojia ambazo zitatumika kuongeza tija katika kilimo. Tukishazalisha mbegu bora na tukiziwezesha zile taasisi zinazozalisha mbegu kama vile ASA kama vile NIKE pale Arusha watazalisha mbegu bora za kilimo za mifugo na zamaki ambazo zitatumika kuongeza tija na kuwaongezea wakulima wetu kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo jingine muhimu ni eneo la umwagiliaji; Serikali ina nia nzuri ya kuboresha sekta ya umwagiliaji na tukitaka tuzalishe vizuri naishauri Serikali pia iiongezee Wizara ya Kilimo pesa za kutosha ili sekta ya umwagiliaji iweze kupata mshiko. Tukishapata maji ya kutosha nina uhakika tunaweza tukalima mbogamboga. Mbogamboga ni eneo ambalo linaweza likasaidia sana nchi yetu nitatoa mifano na figure kidogo. Ukilima nyanya inayoitwa tanya kwa space ya 60 kwa 60 unapata miche 11,111 kwa hekari moja na mche mmoja wa nyanya unauzwa Sh.1,000, kilo mbili unaweza ukauza kwa Sh.1,000 na ukiuza kwa hekari moja utapata Sh.22,000,000. Ukiuza kwa Sh.500 unaweza ukapata Sh.11,000,000; ukiuza kwa Sh.250 kwa kilo hiyz nyanya unaweza kupata zaidi ya milioni tano. Sasa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuwa-support wakulima wenzetu. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja ili tuwaajiri vijana wakulima na watu wengine. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri na Naibu Waziri pamoja na wataalamu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi ni hitaji muhimu la binadamu wote. Kumnyima binadamu haki ya kumiliki, kutunza na kutumia ardhi ni kuvunja haki za binaadamu. Katika jimbo langu la Moshi Vijijini, kuna migogoro mikubwa baina ya wakulima na wafugaji katika Kata za Mabogini (Kijiji cha Mserekie) na Arusha Chini (Mikocheni na Chemchem) zilizoko maeneo ya tambarare. Migogoro hii inahusiana na matumizi ya ardhi. Migogoro hii imeshasababisha madhara makubwa ikiwemo vifo na uharibifu mkubwa wa mali. Mpaka sasa Serikali ya Wilaya na Mkoa haijaweza kupambana na changamoto hii, kwani tatizo hili linajirudia mara kwa mara. Kwa mfano, katika Kata ya Arusha Chini, Kijiji cha Mikocheni migogoro hii imesababisha shule ya sekondari isijengwe, kwani mmiliki halali wa haya maeneo hajaainishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya wakulima na wafugaji jimboni kwangu inasababishwa na uhaba unaoendelea kukua wa rasilimali ardhi. Vilevile, migogoro hii inakuwa kwa sababu pande hizi mbili zina maadili ya kimila yanayotofautiana sana yanayohusisha makabila ya Wamasai (wafugaji) na Wachaga na Wapare (wakulima).
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro hii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na haya yafuatayo; kupanuka kwa shughuli za kilimo na makazi ya watu; kubadilika kwa tabia nchi kunakopelekea malisho kukauka na kusababisha uhaba wa chakula cha mifugo na pia Serikali haijayapima haya maeneo na kuyamilikisha kwa wahusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali; kwanza kutokana na migogoro inayoendelea, kuna umuhimu wa Serikali kuingilia jambo hili na kuhakikisha kuwa maeneo husika yamepimwa na kumilikishwa rasmi kwa wahusika, ili utatuzi wa migogoro hii kupitia mifumo ya kimila na ile ya kitaifa iweze kutumika kwa usahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kutokana na mazingira ya Kitanzania, ninaishauri Serikali ipitie sera za umiliki wa ardhi zenye utata zinazoweza kuchochea migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Sera nzuri na rafiki itasaidia kutoa haki bila malalamiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa fursa ya kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano na ule wa Mwaka Mmoja wa 2021/2022. Kutokana na uhaba wa muda, nitachangia kwenye eneo la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni sekta muhimu sana. Karibu kila Mbunge aliyesimama hapa na hata Mabunge yaliyopita; nimekuwa nafuatilia kwenye runinga, hii ni mara yangu ya kwanza, Wabunge wengi walikuwa wanaonyesha hisia zao kwamba kilimo ni muhimu. Pamoja na huo umuhimu, bado kilimo kina changamoto kubwa kwamba hatujawekeza kikamilifu kwenye miradi ya kilimo. Bado hatujawa serious sana kwenye kilimo kama ambavyo Wabunge wengi wameonyesha hisia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wasilisho alilotoa Waziri wa Fedha na Mipango, miaka mitano iliyopita tuliwekeza vizuri sana kwenye miradi mikubwa ya maendeleo na nitaitaja hapa. Tuliwekeza vizuri sana trillions of money kwenye SGR, tulitoa 3.79 trillion, tukawekeza kwenye barabara 8.6 trillion, tukawekeza kwenye elimu 3.15 trillion, tukawekeza kwenye ndege 1.24 trillion, kwenye maji 2.03 trillion, kwenye umeme na nishati 2.83 trillion. Ni kitu kizuri na hii miradi imetupa heshima kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo sasa, miaka mitano iliyopita fedha iliyokwenda Wizara ya Kilimo ilikuwa ni shilingi bilioni 189.9 tu. Niseme tu, kwa mawazo yangu, nafikiria kiasi hiki kilikuwa ni kidogo sana kwa miaka mitano. Hebu tujiulize, sote tunakiri kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa hili, ni nini kinatukwaza tusiwekeze fedha za kutosha kwenye sekta ya kilimo? Nina hakika tukijitoa kikamilifu tukawekeza kwenye kilimo, tutamkwamua mkulima, tutalikwamua Taifa hili na sote tutaingia kwenye uchumi wa kati tukiwa pamoja na wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba sasa ni wakati wa kufanya maamuzi magumu tuwekeze trillions kwenye kilimo na siyo billions kama ilivyokuwa kwenye miaka mitano iliyopita. Tuwekeze trillions kwenye kilimo ili tuweze kusaidia nchi yetu kwa Pamoja kwa sababu kilimo ndiyo kinachoajiri watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwekeza fedha za kutosha kwenye kilimo, zitatusaidia mambo mengi sana. Sitaki kuyarudia lakini machache ambayo wenzangu wameshayasema, tutasaidia vituo vya utafiti na huduma za ugani. Namshukuru sana Waziri wa Kilimo, amesimamisha Maonyesho ya Nane Nane, ameshaona kuna shida kwenye ugani, amesema fedha zielekezwe kwenye Ugani. Kwa hiyo, tutasaidia huduma za Ugani na uzalishaji mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiachana na hilo, tukiwekeza fedha nyingi kwenye kilimo, hizo trilioni ambazo nashauri, zitasaidia sana kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, tutachimba mabwawa ya kutosha, tutachimba visima mahali popote palipo na maji kwenye nchi hii, tutarekebisha ile miundombinu ya mifereji ya asili ambayo ipo nchi nzima na tumeiacha haijafanyiwa kazi sana. Tukisharekebisha hii mifereji tutakuwa na maji ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini kitatokea tukishakuwa na maji ya kutosha? Maji yatasambaa nchi nzima kwa ajili ya kilimo kama tulivyosambaza umeme na barabara. Tukishafikia hapo, maji yakishapatikana, tutalima kwa uhakika na kuvuna zaidi ya mara mbili kwa mwaka. Kile kitu ambacho Mheshimiwa Bashe na Wizara ya Kilimo walikuwa wanasema block farming, kitafanyika kwa uhakika, kwa sababu tutakuwa na maji ya kupeleka kwenye hizi blocks ili tuweze ku-irrigate na watu wazalishe mazao ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yakishapatikana, wakulima wetu hawatasita kwenda kuchukua mikopo benki. Watakuwa na uhakika wa kuzalisha na kupata kitu. Watakwenda kukopa TIB na Benki ya Kilimo na maisha yataanzia hapo, watu watafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda umeisha lakini niseme tu, ni vyema pia tuwezeshe hizi benki; TIB na Benki ya Kilimo, wapewe mitaji ya kutosha na waelekezwe kuwa na window maalum ya kuwasaidia wakulima wadogo wadogo, siyo wakulima wakubwa tu. Kwa hiyo, tukifanya hivyo, tutakuwa tumewasaidia wakulima na watazalisha vya kutosha. Wakishazalisha vya kutosha, tutaanzisha viwanda na tutafanya mambo mengi ambayo yataleta maendeleo kwa Taifa letu, tutamkwamua mkulima kutoka kwenye umasikini na tutakuwa tunakwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa. Nakushukuru sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Mpango huu wa Tatu wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa mwaka 2021/2022 – 2025/2026. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa wasilisho zuri sana walilotoa hapo jana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Maendeleo ambao Waziri aliwasilisha jana, una vipengele vitano ambavyo wanalenga kuvitekeleza. Nami nitajikita kwenye eneo la tano katika ule mpango na eneo hili ni lile linalozungumzia kuendeleza rasilimali watu ambapo Serikali inategemea kuanzisha Program za kuendeleza maarifa na ujuzi kwa kuwasaidia vijana wetu kuanzia ngazi ya Elimu ya Awali mpaka Vyuo Vikuu. Kuna tatizo hapo. Kwa hiyo, nitalenga kwenye hili na nitaangalia mchango wa vijana kwenye kuchangia pato la Taifa, kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiojificha kwamba kilimo ni kitu muhimu sana; mifugo na uvuvi ni sekta muhimu katika maendeleo ya nchi yetu na karibia kila Mbunge aliyesimama hapa leo hii amelisema hilo. Nafasi ya vijana kwenye kilimo sasa hivi siyo nzuri sana, vijana wengi hawashiriki kwenye kilimo. Wanaoshiriki kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni wazee ambao wameshachoka na hawajaacha urithi mzuri kwa vijana wetu kushiriki katika hizi sekta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, program hii ya Serikali nilitaka nishauri kwamba ni program muhimu sana kama tutashirikisha vijana na kama tutasaidia vijana, tuwafunze vizuri ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye kuboresha Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi waweze kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wanaomaliza Darasa la Saba, Kidato cha Nne, sekondari Kitado cha Sita, Vyuo vya Kati na Vyuo vya Juu, wengi wao pamoja na kwamba ni watoto wa wakulima, wafugaji na wavuvi wakimaliza masomo hawaendi kwenye kilimo. Wanakimbilia mijini, wanakwenda kuendesha bodaboda, wanakwenda kuwa machinga, wanakwenda kuajiriwa. Kwa nini wanafanya hivyo? Wanafikiria kabisa kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi ni kazi duni kitu ambacho sio sawa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali itawekeza na kufuata ushauri ambao nitatoa leo hii hapa, nina hakika tunaweza kuwahusisha vijana wetu katika hizi sekta ambazo nimezitaja na watatoa mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Sasa nitoe ushauri kwa Wizara ya Elimu na TAMISEMI ikiwezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais alivyokuwa anawaapisha Makatibu Wakuu na Viongozi wa Taasisi za Serikali alielekeza tubadilishe mitaala. Alisema mitaala ibadilishwe, tuwafundishe vijana wetu, tuwape stadi ambazo watakwenda wakitoka pale wajiajiri, wafanye vitu vinavyoonekana, yaani mtu akimaliza Darasa la Saba awe na skills za kumsaidia kwenda kuzalisha. Akimaliza Form Four iwe hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niishauri Wizara ya Elimu ibadilishe mitaala ifanye kilimo; kikijumuisha, kilimo, mifugo na uvuvi; liwe ni somo la lazima kuanzia Darasa la Kwanza mpaka Kidato cha Nne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivi tutawafundisha hawa vijana kwa vitendo, tutaweka components nyingi. Nimesema kwenye hiki kilimo kitakuwa na hivyo vitu ambavyo nimevitaja, tutawafundisha ujasiriamali na ubunifu wa miradi ya kilimo kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mtaalam wa kilimo. Ni kwa nini nilienda kilimo? Hiki kitu nilikipata Shule ya Msingi. Kuna siku tulikwenda kwenye study tour, kwenye Kituo kimoja cha Utafiti wa Kahawa kule Lyamungo, nikaona walivyopanda kahawa kwenye mistari, mahindi kwenye mistari, maharage kwenye mistari, nikasema hapa hapa, mimi nakwenda kusoma kilimo. Leo hii nami ni mtaalam wa kilimo na nimeshatoa mchango mkubwa sana kwenye nchi hii, kwenye hiyo sekta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama tutabadilisha mitaala yetu tuhakikishe kuanzia Elimu za Awali, hii program ya Serikali ambayo Mheshimiwa Waziri ame- present hapa; kuanzia zile programs za awali tunafundisha vijana wetu kilimo, nakuhakikishia watakapotoka pale watakwenda kujiajiri na watafanya vizuri, watachukua urithi wa wazee ambao sasa hivi wengi wamechoka na hawawezi kulima tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo masoko yapo. Mahali pa kuanzia; kijana akijiingiza kwenye kilimo, akilima mahindi, mboga, mpunga, akazalisha mchele, Fuso huwa zinakwenda mpaka kijijini kuchukua haya mazao kule. Kwa hiyo, mahali pa kuuza kwa kuanzia sidhani kama ni shida kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni ushauri wangu kwa Wizara ya Elimu mlizingatie hili, tuwafundishe vijana wetu kilimo, ambapo nimeshasema kinabeba vitu vingi tu, ili waweze kujiajiri watakapomaliza Darasa la Saba na waachane na yale mambo ya kwenda kufanya umachinga, kuendesha bodaboda ama kuajiriwa kwa watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, nafikiri ni wakati sasa wa Serikali kuanzisha program maalum kila Wilaya kwa ajili ya vijana wetu na hizi Wilaya zitenge maeneo ya kutosha kwa ajili ya vijana. Haya maeneo yatatumika kama block farm zile ambazo Mheshimiwa Bashe amekuwa anasema, tuwapatie maeneo ya kulima, kufuga, maeneo ya kuanzisha visima vya kufugia Samaki. Kwa kufanya hivyo, watakuwa wamejiajiri baada ya kupata study hizi kule Shule ya Msingi na Sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishatengeneza hizi block farms, kwa mfano tukienda kule Kilimanjaro, wale wazee wangu kule kuna mashamba mengi yametaifinishwa, mashamba ya ushirika, nawashauri ikiwezekana yale mashamba badala ya kupiga kelele wanayatumia vibaya tuwape vijana walime kwenye hizi block farms, vijana walime kwenye haya mashamba ili wazalishe na waweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hizi block farms zitakuwa, tukishakuwa nazo itakuwa ni rahisi kuweka miundombinu ya umwagiliaji, kitakuwa ni kitu kirahisi sana, tutaweka miundombinu ya umwagiliaji na vijana wanaweza wakavuna mara mbili hadi tatu kwa mwaka. Nitatoa mfano kidogo tu, kijana akilima mboga ekari moja, tuseme amelima nyanya ana uhakika wa kupata milioni 22 kama amewekeza. Nisikilizeni vizuri jamani, ekari moja ya nyanya unaweza ukapata milioni 22 na hapo ukitoa milioni moja ya kununua pembejeo, mbegu na vitu vingine unabaki na milioni 21. Kuna kijana atakayekwenda kuwa Mmachinga kweli, huo ni msimu mmoja na ukilima misimu miwili, ni pesa nyingi zimekaa, zimelala ambazo naomba tusaidiane ili vijana wetu wajiingize kwenye hii miradi ya kilimo na waweze kujipatia pesa ili waoe. Vijana wengi sasa hivi ukimwambia aoe anakwambia hapana maisha magumu bwana, nioe nitampa nini, lakini pesa zipo kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wakiwa kwenye hizi block farms wanaweza wakapatiwa huduma za ugani, watafundishwa namna ya kuzalisha vizuri, wanaweza wakapatiwa mitaji na mikopo itakuwa ni rahisi sana kuwasaidia hawa vijana wapatiwe mitaji na mikopo. Nitatoa mfano tu, kuna maeneo mengi ambayo yana pesa ambazo vijana wanaweza wakazi-access na wakafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ule Mfuko wa Halmashauri, asilimia nne ambazo huwa zinatolewa, vijana wanaweza wakazipata. Kuna Benki ya Kilimo ya Taifa inaweza ikawasaidia hawa vijana, kuna mfuko wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo, unaitwa SELF Microfinance Fund, kuna Mfuko wa Pembejeo wa Taifa, wenzangu wameshausemea hapa, kuna Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali, kuna Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (Youth Development Fund), kuna Mfuko wa Mheshimiwa Rais wa Kujitegemea (Presidential Trust Fund). Tukiweza kuwaunganisha vijana wetu na hii Mifuko, tukiwapa maeneo Mungu atupe nini? Nina hakika vijana watazalisha kwa hakika na tutawatoa kutoka hatua moja waende hatua nyingine, haya mambo ya kwenda kuwa Wamachinga, bodaboda yatakuwa ni historia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishafanikisha hilo, pia ni rahisi kuwaunganisha na masoko ya ndani. Tumeshaona jitihada za Wizara ya Kilimo kwenye kutafuta masoko kwa mfano sasa hivi wanaotaka kulima soya soko lipo China, wanaotaka kulima mihogo Serikali imeshatafuta soko China. Kwa hiyo sidhani kama kutakuwa na shida kubwa sana ya soko na wakishaanza kuzalisha ni rahisi kuwaelekeza pia wafungue viwanda vidogo vidogo, waongeze thamani kwenye mazao watakayolima pale, kwa mfano wanaolima mpunga, wakishakoboa mchele badala ya kuuza raw rice wanaweza wakafanya packaging; wanaolima mahindi wanaweza wakasaga wakapaki; wanaolima nyanya wanaweza wakasaga wakakausha wakapaki, wakawa wameongeza thamani; TBS ikawasaidia vijana watakuwa wameanzisha viwanda vidogo vidogo kwa kusaidiana na SIDO na tutachangia kikamilifu kwenye uchumi wa Taifa hili.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro; Naibu Waziri, Mheshimiwa Mary F. Masanja na wataalamu wa Wizara na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa sana kwenye Sekta ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye suala la Half Mile na umuhimu wa kufungua njia mpya za kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia maeneo ya kata za mpakani za Uru na Old Moshi; na uwepo wa mti mrefu kuliko yote Afrika katika Kijiji cha Tema Kata ya Mbokomu, Jimbo la Moshi Vijijini. Huu ni mti wenye miaka mingi zaidi duniani. Una miaka 600. Pia nitachangia kuhusiana na ongezeko la watu na wanyama wa kufuga linavyotishia hifadhi ya Ngorongoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Half Mile ni eneo lenye upana wa kati ya 0.5 -0.8 ya mile. Eneo hili lilikuwa linatenganisha Mlima Kilimanjaro na makazi ya watu. Eneo hili kwa upande wa Majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo linajumuisha vijiji 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia inaeleza kwamba watu walianzisha makazi katika maeneo ya Mlima Kilimanjaro takribani zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Pamoja na wachaga kuwepo kwenye makazi yao miaka niliyotaja hapo juu, Mkoa wa Kilimanjaro una historia ngumu inayohusisha uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro na umiliki wa rasilimali ya ardhi ambavyo walivirithi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1921, wakoloni walipitisha Sheria ya Kuhifadhi Viumbe wa Porini (Wildlife Conservation) ambapo misitu ya Kilimanjaro ilihusika. Sheria hii iliwanyima haki wenyeji wa Kilimanjaro wasiingie msituni. Aliyeingia alionekana mharibifu na mhalifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1922, Sera za Ukoloni zilimpa nguvu Gavana kuwa mmiliki wa ardhi yote. Mwaka wa 1923 wakoloni walianzisha programu ya kuwanyang’anya wananchi kwenye ardhi yao yenye rutuba na kuanzisha mashamba ya Masetla ya Wazungu. Mashamba haya yalitaifishwa kwa Azimia la Arusha la Mwaka 1967, na bado hayako mkononi mwa wananchi moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, Wakoloni walitumia sheria kandamizi kujimilikisha ardhi ya wana Kilimanjaro na rasilimali za msitu wa Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sheria ya Wildlife Conservation ya 1921 na ile ya kuwanyang’anya mashamba ya 1923, wakoloni waliingiwa na huruma na kuanzisha Sheria ya Half Mile Strip mwaka wa 1941 kwa lengo la kuwapatia majirani wa Msitu Kilimanjaro huduma za mazao ya misitu kama vile dawa za asili (ngesi), mboga za majani (mnafu) miti ya kujenga nyumba, kuni na majani ya ngombe. Kiuhalisia, eneo hili liko kwenye Forest Reserve na siyo kwenye National Park.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na malengo ya kuanzishwa kwa eneo la Half Mile, tokea enzi za ukoloni, kazi za kibinaadamu zilisababisha uharibifu wa mazingira katika Half Mile na yale maeneo ya hifadhi kwa kukata miti, kupasua mbao, kuchoma misitu, kuchunga mifugo na kuendesha shughuli za kilimo ndani ya hifadhi. Hii ilitokana na kukosekana kwa usimamizi mahiri kutoka katika mamlaka husika Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uharibifu huu, Serikali ilisimamisha vijiji vyote 40 kutokutumia Half Mile Strip tokea 2004, kwa sheria iliyoanza kutumika 2005. Hii ilitokana kusainiwa kwa sheria ya kuziingiza Half Mile Strip za maeneo ya Moshi Vijijini na Rombo iliyotiwa sahihi na Marehemu Rais Mkapa 18/7/2005 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 16/9/2005.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya zuio hili, Serikali yetu iliondoa ile huruma ya Wakoloni kwa Wana Kilimanjaro ya kutumia ile Buffer Zone ya Half Mile. Siku hizi hakuna cha Half Mile tena na ukikamatwa na maaskari wa KINAPA utakuwa na bahati mbaya sana. Wapiga kura wangu wameniambia kuwa wengi wamepigwa na wameambulia vilema, wamebakwa, na wengi wamedhalilishwa kwa namna mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kunyima watu matumizi ya Half Mile, hii imesababisha umasikini mkubwa, ikiwa ni pamoja na wanyama waharibifu (needed; kama, nyani, Tembo) kuingia kwenye mashamba ya wanakijiji na kuharibu mazao. Kabla ya mwaka 2005, shughuli za wananchi kwenye Half Mile zilizuia wanyama kuingia vijiji vya mpakani na ilikuwa hakuna uharibifu wa mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Makamu wa Rais Dkt. Ali Mohammed Shein alipotembelea Mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2008 akiambatana na Waziri wa Maliasili Mheshimiwa Prof. Jumanne Maghembe wananchi walimweleza matatizo yaliyojitokeza baada ya Serikali kuunganisha eneo la hifadhi la KINAPA na misitu ya hifadhi za asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ziara hiyo, Wizara ilikaa na kuiagiza TANAPA (kwa barua Kumb Na. CAB. 315/ 484/01/A ya tarehe 22/1/2008 ya Waziri, Mheshimiwa Prof. Maghembe kwenda kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, na barua kumb na CJA.246/374/01/42 ya tarehe 27/2/2009 ya Katibu Mkuu Dkt. Ladislaus Komba kwenda kwa Mkurugenzi wa TANAPA) wachore ramani upya na kutenga eneo la nusu mile liwe nje ya Hifadhi ya KINAPA kama ilivyokuwa awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelekezo hayo hapo juu na kukumbushwa mara kwa mara na wadau wa maendeleo wa mlima Kilimanjaro, hadi leo ramani hiyo haijatoka na sheria hii kandamizi kwa wananchi wa vijiji 40 vya mpaka na mlima Kilimanjaro bado inawanyanyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria kandamizi kama hii siyo nzuri na zinasababisha migogoro isiyo ya lazima baina ya wananchi na Serikali yao. Kama mwakilishi wa wananchi, hata mimi naikataa kabisa sheria kandamizi kwa wapiga kura wangu. Namwomba Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan aliangalie jambo hili kwa jicho la huruma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wetu ambaye ni msikivu sana afuatilie pale wenzake walipoachia ili haki itendeke. Wana Moshi Vijijini, Vunjo na Rombo tunaomba maeneo yote ya vijiji vya mpakani vipewe fursa ya kuulinda na kuutunza mlima wao kama ilivyokuwa zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ikibadilishwa, Half Mile Strip inaweza kutumika kwa mafanikio makubwa chini ya usimamizi wa Serikali Kuu, Serikali ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji na kusaidia wananchi wa vijiji husika:-
(a) Kuutunza mlima;
(b) Kuwapatia wananchi huduma;
(c) Kuinua uchumi wa wananchi, Wilaya, Mkoa na Taifa; na
(d) Kukuza utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ikibadilishwa, tunatarajia kupanda miti ya muda mfupi kama Cyprus, Pine, Mikaratusi na aina nyinginezo zinazokua haraka kwa ajili ya nguzo za umeme, nguzo za ujenzi wa nyumba zikiwemo ghorofa. Miradi kama hii iko Iringa. Rais akiruhusu hili, nchi nzima itanufaika kwani Kilimanjaro ina miundombinu bora ya kusafirisha hizi bidhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni ule wa kuiomba Wizara ifanye utafiti na kufungua njia mpya za kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia kata za mpakani huko Uru na Old Moshi. Njia hizi zinaweza kuwa fupi, na baadhi ya watalii wanaweza kuzifurahia sana. Kwa kufanya hivyo, tutaongeza uwekezaji kwenye maeneo haya, ajira na mzunguko wa pesa utaboreka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu ni kuhusu mti mrefu Afrika. Wagunduzi kutoka Chuo Kikuu cha Beyreuth Ujerumani wakiongozwa na Dkt. Andrew Hemp wamegundua kwamba mti mrefu (81.5m) kuliko yote Afrika uko katika Kijiji cha Tema, Kata ya Mbokomu, Jimbo la Moshi Vijijini. Mti huo unaitwa Entandrophragma Excelsum (Mkusu). Inasemekana kuwa mti huo ndiyo ulio na miaka mingi zaidi duniani (600 years).
Mheshimiwa Mwenyekiti, watafiti wa Kijerumani wameshauri kuwa mti huo unaweza kuishi zaidi kama utatunzwa na kuhifadhiwa vizuri. Ninaiomba Serikali iboreshe uhifadhi wa mti huu na kuboresha miundombinu ya barabara kuufikia, kwani hiki ni kivutio kipya cha utalii ndani na nje ya Tanzania. Barabara ya kwenda eneo hili ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa nne ni kuhusu hatari inayoikabili Hifadhi ya Ngorongoro. Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lilianza mwaka 1959 likiwa na wakazi 8,000. Ripoti inaonyesha kwamba sasa hivi kuna wakazi zaidi ya 100,000 na ongezeko kubwa la mifugo kama ngombe, mbuzi na kondoo katika eneo la hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli za uhifadhi kule Ngorongoro zimekuwa ngumu kutokana na migogoro baina ya binadamu wanaoishi eneo la hifadhi na wanyamapori. Wanyamapori huvamia maboma ya wafugaji na kula wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo. Vilevile kuna baadhi ya wananchi wanaolima katika eneo la hifadhi. Hii imesababisha eneo hili kushambuliwa na magugu vamizi na kuishia kupunguza eneo la malisho kwa wanyamapori na wale wa kufugwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi cha mifugo kimeongezeka sana na hii imesababisha kuongezeka kwa magonjwa ya kuambukiza toka kwenye wanyama wanaofugwa kwenda kwa wanyamapori na kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa wanaofugwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatua stahiki hazitachukuliwa mapema, hali itakuwa tete sana miaka michache ijayo. Naishauri Serikali ichukue hatua stahiki kwa kuirekebisha Sheria ya Kuanzisha Hifadhi ya Ngorongoro. Maboresho ya sheria yalenge kulinda wanyamapori, kwani Ngorongoro ni mahsusi kwa wanyamapori. Wakazi na wanyama wa kufugwa waondolewe eneo la hifadhi na wapelekwe kwenye maeneo yao ambayo yako ya kutosha nje ya eneo la hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri Mheshimiwa Juma Aweso na Naibu wake Engineer Maryprisca Mahundi pamoja na wataalamu wa Wizara ya Maji kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, Waziri na timu yake wamekuwa mfano wa kuigwa kwenye kutatua changamoto za maji na kuwatua akinamama ndoo kichwani, kwani maji ni haki ya msingi kwa binadamu wote. Kwa ujumla, inatia faraja kuona upatikanaji wa maji vijijini unaongezeka, kama alivyoonesha kwa kina katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka huu wa 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu la Moshi Vijijini kuna changamoto ya upatikanaji wa maji ya bomba katika maeneo yafuatayo; Kata ya Kibosho Kirima yenye vijiji vya Kirima Juu, Kirima Kati na Boro ina wakazi 10709 na kaya 2,332. Kata hii inahudumiwa na RUWASA. Miradi ya Maji ya Boro na Kirima ina changamoto kubwa ya upungufu wa maji kwenye mifumo. Upungufu huu umeleta usumbufu mkubwa sana kwa wananchi na taasisi zikiwemo Chuo Kikuu cha Kilutheri cha Masoka, shule za sekondari zenye mabweni (Kirima na Masoka), shule za msingi na taasisi za dini zilizopo kwenye kata.
Mheshimiwa Spika, kwenye taasisi hasa zile zenye mabweni, wanafunzi wameishia kutumia maji yasiyo salama kutoka miferejini na mtoni na kusababisha magonjwa mbalimbali ya tumbo na ngozi. Tunaishukuru Serikali kwa kutenga fedha za kuboresha mradi huu.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya kata za Kibosho Kati na Okaoni zenye jumla ya vijiji 14 zinahudumiwa na Mradi wa Maji Otaruni ambao ulijengwa miaka ya 1980. Eneo hili linahudumiwa na RUWASA. Kwa sasa watu wameongezeka sana na mifumo ya usambazaji maji imechakaa. Kwa hiyo, kuna uhitaji wa kuupanua na kuukarabati. Tunaishukuru Serikali kwa kutenga shilingi 200,000 katika mwaka huu wa fedha unaoishia ili kufanya ukarabati. Tunaomba Serikali iangalie miundombinu ya eneo hili kwa jicho la pekee na kuongeza bajeti ili mradi huu ukamilike.
Mheshimiwa Spika, kuna changamoto ya upatikanaji maji ya uhakika katika baadhi ya vijiji kumi vya kata ya Kibosho Magharibi. Vijiji hivyo ni Manushi Sinde, Manushi Ndoo, Mkomongo, Kifuni, Umbwe Onana, Umbwe Sinde, Manushi Sinde, Manushi Mashariki, Manushi Kati na Umbwe Kati. Kata hii ina wakazi 20,291 na baadhi ya maeneo haya yanaunganishwa na chanzo cha maji toka Jimbo la Hai, kwenye mradi wa Makeresho - Lyamungo - Umbwe na inahudumiwa na RUWASA.
Mheshimiwa Spika, maji ya mradi huu huelekezwa zaidi kwenye Jimbo la Hai. Ili kutatua kero hii, kuna umuhimu wa Wizara kutenga fedha za kusaidia kununua mambomba na kuunganisha wananchi wa maeneo haya na chanzo kingine cha maji kilicho karibu katika eneo la Moshi DC na kuachana na kile cha Jimbo la Hai.
Mheshimiwa Spika, katika kata ya Mabogini kuna mradi unaoitwa mradi wa vijiji vitano; vijiji hivyo ni Muungano, Chekereni, Maendeleo, Mtakuja na Mserekia. Mradi huu umeanza na umekwishaombewa fedha na MUWSA na unangoja utekelezaji na kukamilisha.
Mheshimiwa Spika, kero nyingine kubwa iko katika kijiji cha Mabogini. Tunaomba miradi hii ipewe kipaumbele, kwani wakazi wa Kata ya Mabogini ni wengi (28,992) na kuna changamoto kubwa ya maji ya kunywa. Hili ni eneo la kimkakati ambalo wahamiaji wengi toka mlimani wameanzisha makazi huko na hawana vyanzo mbadala vya maji. Tunashukuru kwa kupatiwa shilingi milioni 500 ili kutekeleza mradi huu.
Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali itutengee pesa za kutosha ili maji yafike mpaka Remiti Umasaini kwani maeneo haya yana uhaba mkubwa wa maji. Tunashukuru kwa kupatiwa shilingi milioni 500 ili kutekeleza mradi huu. Tunashukuru kwa kupatiwa shilingi milioni 500 ili kutekeleza mradi huu. Tunaiomba Serikali itutengee pesa za kutosha ili maji yafike mpaka Remiti Umasaini kwani maeneo haya yana uhaba mkubwa wa maji.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Old Moshi Mashariki, MUWSA ilikabidhiwa mradi wa maji ya kunywa wa Old Moshi Mashariki unaohudumia vijiji vinne vya Kikarara, Tsuduni, Mahoma na Kidia takribani miaka miwili iliyopita. Eneo hili lina wakazi wapatao 9,528. Tunaishukuru Serikali kwani wameanza kuweka mabomba ambayo hayajasambaa kata nzima. Tunaiomba Wizara iwawezeshe MUWSA wakamilishe huu mradi.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Uru Shimbwe yenye vijiji vya Shimbwe Juu na Shimbwe Chini, wananchi wana changamoto kubwa ya maji na wamejiongeza na kuanza kujenga miundombinu katika vyanzo vyao vya maji vilivyoko mlimani kwa kutumia nguvu za wananchi. Kuna Mradi wa Maji Kimangara (kilometa nne) na mradi wa maji Mofuni (kilometa nne).
Mheshimiwa Spika, baada ya ujenzi, wana Shimbwe wanakabiliwa na changamoto ya mabomba ya kusafirisha maji kwenye kila mradi kwenda vijiji husika.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kimochi ina zaidi ya wakazi 13,000. Kata hii ina vijiji vya Mowo, Sango, Shia, Miami, Lyakombila na Kisaseni. Eneo lote linahudumiwa na MUWSA. Tunaishukuru Serikali kwa jitihada za awali kuwafikishia wakazi wa eneo hili maji. Ila bado kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji maji katika maeneo mengi hasa Kijiji cha Sango. Tunaiomba Serikali itutengee pesa za kutosha ili maji yafike maeneo yote ya kata hii vikiwepo vijiji vya maeneo ya tambarare.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Uru Kusini yenye vijiji saba (Okaseni, Kimanganuni, Rua, Kariwa, Longuo A, Kitandu na Shinga) ina takribani wakazi 22,904 na ina miradi mitatu ya Mang’ana, Kisimeni na Mbora. Changamoto ya miradi hii ni maji kidogo katika mifumo ambayo hayatoshelezi na mara kwa mara huwa ni machafu sana. Hata ripoti ya Mkaguzi Mkuu yam waka huu imeeleza kwamba maji hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Arusha Chini katika vijiji vya Mikocheni yenye wakazi 4,378 na Chemchem yenye wakazi 2,140 kuna uhaba wa maji. Sasa hivi ni watu wa Kirua Kahe wanatoa huduma ya maji ya kuuza katika maeneo haya. Maji huuzwa kwa bei ya juu na si salama kwa matumizi ya binadamu. Kata hii inahudumiwa na RUWASA.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kujenga mradi wa Ochai Ngoma katika Kata ya Uru Mashariki unaohudumia vijiji vinne kati ya saba, tenki lililopo ni dogo na halitoshelezi. Kuna umuhimu wa kujenga tenki kubwa la kuhifadhi maji ili lihudumie vijiji vyote saba (Materuni, Mruia, Mwasi Kaskazini, Kishumundu, Mwasi Kusini, Mnini na Kyaseni) yenye wakazi 14,78. Kata hii inahudumiwa na MUWSA.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Uru Kaskazini, MUWSA haijatekeleza ahadi ya kuunganisha vijiji vya Msuni (wakazi 2,272) na Njari (wakazi 3,327). Chanzo cha maji haya kiko Uru Kaskazini na maji haya yamepita maeneo ya Uru Kaskazini na kwenda Kata ya Uru Kusini na Kata ya Pasua ya Jimbo la Moshi Mjini.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Old Moshi Magharibi kuna mradi wa maji wa Tela Mande ambao umekamilika. Mradi huu una maji mengi sana na ya ziada ambayo kwa sasa yanahudumia wananchi wa ukanda wa milimani. Vijiji na vitongoji vya kata hii vilivyopo ukanda wa tambarare kama kile cha Mandaka Mnono havina maji ya bomba.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuelezea changamoto zilizopo hapo juu, naishauri Wizara ya Maji itekeleze yafuatayo; kwanza naishauri Serikali itenge fedha za kutosha ili watafute na kujenga vyanzo vipya vya maji na kuyapeleka kwenye miundombinu ya miradi ya maji ya Boro na Kirima Kata ya Kibosho Kirima ili kutatua changamoto ya uhaba wa maji.
Mheshimiwa Spika, pili naishauri Serikali itenge fedha za kutosha kukarabati, kupanua na kujenga upya mradi uliopo katika Kata za Kibosho Kati na Okaoni kwa kutumia vyanzo vilivyojengewa tokea miaka ya 1980.
Mheshimiwa Spika, tatu naishauri Serikali kupitia Wizara ya Maji itenge rasilimali pesa ya kutosha ili kujenga miundombinu mipya kwa ajili wa wananchi wa Kata ya Kibosho Magharibi yenye vijiji 14 kwani maji kutoka mradi wa Lyamungo - Umbwe kutoka Jimbo la Hai hayafiki kwa uhakika katika Jimbo la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, nne, naishauri Serikali ipeleke fedha za kutosha kukamilisha mradi ulioanza na kuhakikisha maji yanafika Umasaini, eneo lenye uhaba mkubwa wa maji.
Mheshimiwa Spika, tano naishauri Serikali itenge rasilimali fedha ya kutosha kukamilisha mradi wa maji uliopo Kata ya Old Moshi Mashariki.
Mheshimiwa Spika, sita naishauri Serikali kupitia Wizara ya Maji isaidie juhudi zilizoanzishwa na wananchi wa Kata ya Uru Shimbwe kwa kuwanunulia mabomba ya kusafirisha maji na kuyafikisha kweye vijiji vya Uru Shimbwe Juu na Chini.
Mheshimiwa Spika, saba naishauri Serikali kupitia Wizara ya Maji iwekeze vya kutosha na kuhakikisha wakazi wa Kata ya Kimochi wanapata maji ya kutosha kuanzia ukanda wa juu na tambarare.
Nane, naishauri Serikali kupitia Wizara ya Maji iwekeze na kutatua kero ya maji kidogo kwenye mifumo ya miradi na ile ya maji machafu iliyolalamikiwa katika kata ya uru kusini, kwani mkaguzi mkuu ameeleza hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Mheshimiwa Spika, tisa ninaishauri Serikali iangalie kwa jicho la pili na kuwapatia maji wananchi wa vijiji vya Mikocheni na Chemchem vilivyoko Kata ya Arusha Chini.
Mheshimiwa Spika, pia kumi ninaishauri Serikali ije na mkakati wa kujenga tenki kubwa la kuhifadhi maji na litumike kuhudumia Kata saba za Uru Mashariki.
Kumi na moja, nanaishauri Serikali iwaunganishe kwenye mfumo wa maji wananchi wa vijiji vya Msuni na Njari vilivyopo Kata ya Uru Kaskazini kwani vyanzo vya mradi huu viko kwenye kata yao. Kwa kufanya hivyo, wananchi watakuwa walinzi bora wa miundominu na vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Spika, mwisho ninaishauri Serikali ipeleke maji ya mradi wa Tela Mande uliopo Old Moshi Magharibi katika maeneo ya tambarare huko Mandaka Mnono na vitongoji vyake.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mohammed Mchengerwa, Naibu Waziri Mheshimiwa Mary Francis Masanja na wataalam wa Wizara, taasisi zilizo chini ya Wizara na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa sana kwenye sekta ya maliasili na utalii.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye changamoto ya magugu vamizi katika mbuga zetu za wanyamapori na maeneo ya akiba, udahili wa wanafunzi kutoka nje katika Chuo cha Wanyamapori Mweka na fursa za utalii zilizopo katika jimbo la Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, ripoti za kiutafiti zilizofanyika katika Mbuga za Serengeti, Ngorongoro, Mapori Tengefu zimeonesha kwamba magugu vamizi yamesambaa katika maeneo mengi ya hifadhi za wanyamapori na mapori ya akiba yaliyoko nchini.
Mheshimiwa Spika, aina ya magugu vamizi hayo yaliyoko katika baadhi ya maeneo nimeayaorodhesha. Magugu vamizi yaliyoko Ngorongoro ni Azolla filiculoides (red water fern), Argemone mexicana (Mexican poppy), Datura stramonium (jimsonweed), Gutenbergia cordifolia, Acacia mearsii na Parthenium hysterophorus (famine weed); huko Serengeti magugu vamizi yaliyoonekana huko ni Parthenium hysterophorus, Opuntia stricta, Tithonia diversifolia, Lantana camara, Chromolaena odorata na Prosopis juliflora; huko mbuga ya wanyama ya Burigi Chato magugu vamizi yaliyopo ni Tegetes minuta na Argemone Mexicana; na huko Mahale Mountains National Park mmea uitwao Senna spectabilis (Caesalpiniaceae) umekuwa ni gugu vamizi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uvamizi wa magugu yaliyotajwa hapo juu, maisha ya wanyamapori katika maeneo mengi ya Hifadhi za Taifa yapo hatarini kwani uwepo wa magugu haya umesababisha athari nyingi, kubwa ikiwa ni kuua majani na mimea mingine inayoota karibu yake.
Mheshimiwa Spika, magugu vamizi hayo yana tabia inayoonesha kwamba yanapoota hakustawi kitu kingine kwa kuwa hufunika eneo lote na kusababisha kutoweka kwa nyasi na kuathiri malisho ya wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, hata ripoti moja ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali (CAG) ilionesha kuwepo kwa magugu vamizi katika Hifadhi ya Ngorongoro ambayo inahatarisha uwepo wa wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo hivi sasa kunatakiwa kuwe na mikakati dhabiti ili kudhibiti magugu haya kwani yanasambaa kwa kasi kubwa sana katika mbuga mbalimbali na maeneo ya akiba hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali iwe na mpango kazi maalum na iwekeze kikamilifu kwenye kudhibiti magugu vamizi ili kulinda ikolojia ya mbuga zetu ziweze kutoa huduma ya kuwapatia wanyama chakula.
Mheshimiwa Spika, Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka hutoa mafunzo ya usimamizi wa wanyamapori na utalii. Ni chuo kimojawapo pekee chenye hadhi kubwa hapa Barani Afrika. Chuo hiki hutoa Shahada, Stashahada na Astashahada katika nyanja mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, chuo hiki hupokea idadi kubwa ya wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na changamoto ya kupokea wanafunzi kutoka katika baadhi ya mataifa ya Afrika kama Kenya na Msumbiji. Vigezo vilivyowekwa na NACTE vimekuwa vinazuia wanafunzi kutoka mataifa haya kujiunga na Chuo cha Mweka.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Wizara ikae na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na NACTE ili waangalie upya vigezo vya kujiunga na Chuo cha Mweka ili tuwe na muundo wa kuwasaidia wanafunzi kutoka nchi hizi wapate elimu kama walivyotumwa na nchi zao. Haifurahishi kuona mtu anatumwa na nchi yake kusoma shahada, na akifika ananyimwa fursa na kuambiwa asome stashahada. Jambo hili limekuwa siyo rafiki, na limepunguza idadi ya wanafunzi kutoka nje na kutunyima fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kilimanjaro ni mdau muhimu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Ninasema hivyo kwa sababu Mlima Kilimanjaro na viunga vyake ni moja ya vivutio muhimu vya utalii ambavyo vimeipatia Tanzania heshima kubwa kimataifa. Ndani ya Mlima Kilimanjaro na maeneo yanayouzunguka mlima kuna vivutio vya aina mbalimbali vya kitalii.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, Rais wetu alishiriki kikamilifu kwenye filamu ya Royal Tour iliyokuwa na kipengele cha kutangaza utalii ukiwepo Mlima Kilimanjaro. Kutokana na hili, ni vyema tukachukua tahadhari mapema ili watalii watakapoanza kumiminika kuja kutalii Kilimanjaro kama ambavyo imeanza kujitokeza wakutane na mazingira mazuri. Tusipofanya hivyo, watalii wakija wakikumbana na changamoto watapeleka sifa mbaya kuhusiana na eneo letu, na kuathiri idadi ya wageni watakaotembelea Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kwenye suala la vivutio vya Mlima Kilimanjaro na umuhimu wa kutatua changamoto za vivutio hivyo ili kuwezesha watalii kufika maeneo hayo kirahisi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni imegundulika kwamba mti mrefu kuliko yote Barani Afrika ujulikanao kama Mkukusi umepatikana katika Kijiji cha Tema, Kata ya Mbokomu, Jimbo la Moshi Vijijini, Mkoani Kilimanjaro. Mti huo ambao una urefu wa mita 81.5 upo ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA). Ugunduzi huo umeonesha pia huu ni mti wenye miaka mingi zaidi duniani kwa aina hii ya mti kwani una miaka 600.
Mheshimiwa Spika, mti huu umeupa heshima Mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa jumla. Kugundulika kwa mti huo kumeongeza chachu ya watalii kupanda Mlima Kilimanjaro na wengine kwenda kushuhudia mti huo. Licha ya mti huu kuwa kivutio ambacho kinaweza kuiingizia Serikali fedha za kigeni, lakini changamoto iliyopo ni ugumu wa kuufikia mti huo. Ili kufika katika eneo la Mrusungu ambapo ndipo ulipo mti huo mrefu zaidi, ni safari ya kutembea kwa mguu kwa takribani muda wa saa nne kwenda na kurudi kwa kupita katika milima, mabonde, mito na makorongo.
Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto hii, ninaishauri Serikali iboreshe miundombinu ya barabara ili kuweza kuufikia mti huo iwapo watalii watataka kwenda kuuona. Barabara ya kufika kwenye mti huu ni mbaya sana, na hii ni changamoto inayowafanya watalii wasitembelee eneo hili. Tunaiomba TANAPA isaidie ujenzi wa hii barabara katika mipango yao ya mwaka 2023/2024. Katika mwaka ujao wa fedha, TANAPA ina programu ya kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilometa 500, na kukarabati kilometa 10,500. Katika hizo barabara, tunaomba tusisahau barabara inayokwenda kwenye huu mti mrefu.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ihakikishe kuwa eneo hili linaendelezwa ili liwe na hadhi ya kuwa sehemu ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro. Vilevile ninaishauri Serikali itengeneze utaratibu wa kuhakikisha wanaokwenda kuuona mti wanalipa ada.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili utahusu maporomoko ya maji Materuni au kwa jina lingine Mnambe Waterfalls. Maporomoko haya ni moja ya maporomoko ya maji katika Mto Mware, Kata ya Uru Mashariki, Jimbo la Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro. Maporomoko haya yanapatikana katika Kijiji cha Materuni pembezoni mwa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Maporomoko haya yana urefu wa zaidi ya mita 100.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kivutio cha maporomoko ya maji, eneo hili la utalii limekuwa maarufu kwani watalii wanaokwenda kuona maporomoko hupata fursa ya kutembelea shamba la kahawa na kujifunza jinsi kahawa inakuzwa, kuvunwa na kusindikwa. Watalii hupata fursa ya kujaribu kwa mkono yao kuchoma na kuandaa kikombe cha kahawa kwa kutumia njia asili ya Wachagga.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayokabili eneo hili ni ubovu wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 15 kutoka Mjini Moshi. Kutokana na ubovu wa barabara, watalii hupata shida kufika katika eneo hili. Changamoto za barabara katika maeneo yanayopeleka watalii kwenye vivutio vya Mlima Kilimanjaro zinatakiwa zipewe kipaumbele cha pekee na Wizara ya Maliasili na Utalii kwani wao ni wanufaika wakuu.
Ninaishauri Serikali iachane na kuzitegemea TARURA na TANROADS kwani mitandao yao ya barabara ni mingi, na hawajatoa kipaumbele kikubwa kwa barabara za jimbo langu kama zile za kupeleka watalii kupitia Umbwe Gate, Kidia VIP Route, Materuni Waterfalls, Mti Mtefu Kijiji cha Tema huko Mbokomu, Kanisa la Kibosho Singa, na maeneo mengine muhimu.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali, huu ni wakati wa kutumia michango ya Corporate Social Responsibility (CSR) unaotokana na mapato ya Mlima Kilimanjaro kutengeneza miundombinu ya barabara katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, baada ya michango yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa. Nikiwa kama Mjumbe wa Kamati, nianze moja kwa moja kwa kuiunga mkono hoja na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo pamoja na msaidizi wake na Watendaji wote wa Wizara ya Kilimo na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayoifanya kwenye kukiendeleza kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa ushuhuda. Kwenye utoto wangu ilikuwa ni miaka ya 1960, lakini kuanzia miaka ya 1970 nilikuwa kijana. Kuanzia miaka hiyo ya 1970 nimekuwa natoa huduma katika Wizara ya Kilimo hadi leo hii. Kwa hiyo, kuna ushuhuda nataka niseme kwamba, kwa miaka hii ambayo tumeingia huku Bungeni, Bajeti ya Kilimo kwa nia njema ya Mheshimiwa Rais wetu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294 na mpaka sasa hivi tuna bajeti hii ambayo Mheshimiwa Waziri anatuomba pesa ni shilingi trilioni 1.2. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natoa ushuhuda hapa kwamba mara hii maendeleo na mwenendo wa Wizara ya Kilimo ni mzuri sana. Tumejionea wenyewe kwamba kilimo kinachangia vizuri kwenye Pato la Taifa na kilimo cha sasa hivi kimeleta tija. Mheshimiwa Waziri anapeleka mbolea kule na tija inaonekana ikiwemo kujitosheleza kwa chakula ndani ya nchi yetu na kuna ajira, na vijana wa BBT wapo pale. Pia taasisi zote maendeleo yao ni mazuri sana na zinafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Umwagiliaji pia inafanya kazi nzuri sana, tunaona miradi mingi ya umwagiliaji. Hapa namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwenye Jimbo langu nimeshapata miradi ya umwagiliaji kiasi. Ukanda wa tambarare kule Mandaka Mnono kuna mradi unajengwa. Pale Mabogini kuna mradi ambao ulikuwa ni wa Wajapani, lakini ukanda wa Arusha Chini tunahitaji mradi pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni mengi, ni ya kuua mtu kabisa na sasa hivi wananchi wa Arusha Chini, kwenye vijiji vya Chemchem na Mikocheni kuna mafuriko, watu wapo kambini. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba twende tukawekeze mradi wa umwagiliaji pale Mikocheni na Chemchem maji ni mengi. Haya maji sasa badala ya kutusaidia kuzalisha chakula yanaumiza wananchi na wapo makambini kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utahusu zao la kahawa. Nikiwa kama mtu niliyetoka kwenye eneo linalolima kahawa nitachangia kwenye hili eneo na ndicho kitu ambacho wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wale wanaolima kahawa watapenda wakisikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa ni zao muhimu sana, tunaliita ni dhahabu ya kijani. Zao hili ni bidhaa ya pili kwa umaarufu hapa duniani. Baada ya mafuta ya petrol na diesel kahawa ndiyo zao la pili maarufu hapa duniani. Pia ni kinywaji cha pili kinachotumika duniani baada ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi kama Mwanakilimanjaro naringa sana kwamba tunazalisha kinywaji cha pili kwa matumizi duniani. Inakadiriwa kwamba watu wanaokunywa kahawa duniani wanatumia kama vikombe bilioni 2.6 kwa siku. Wanywaji hawa wa kahawa wanaipenda kahawa kwa sababu ina mambo mengi mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, wataalamu wanasema kwamba kahawa inaondoa msongo wa mawazo, kahawa inaweza ikazuia usipate kisukari (type two diabetes), inaweza ikazuia ugonjwa wa moyo, inaweza ikapunguza maumivu na pia inaweza ikarefusha Maisha. Watafiti wameshaona haya mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaringa kwamba mikoa inayozalisha kahawa hapa duniani inachangia kwenye haya mambo kwenye dunia yetu hii. Mikoa hii ni mingi, ipo zaidi ya 12 ikiwepo Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Ruvuma, Lushoto na kule kwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa katika maeneo yetu hapa nchini inazalishwa na wakulima wadogo wadogo ambapo duniani kuna wakulima milioni 25 wanaoshiriki kwenye kuzalisha kahawa. Pia sisi Tanzania ni sehemu ya hawa wakulima wadogo wadogo wanaozalisha 80% ya kahawa hapa duniani. Kwa hiyo, tunashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa kama mzawa wa eneo linalozalisha kahawa, niseme hapa kwamba wakulima wa kahawa kwa ujumla wake wana maisha magumu, siyo jinsi tunavyofikiria ilivyokuwa kule nyuma. Bei wanazopata ni ndogo, hazitoshelezi ukilinganisha na kazi kubwa ambayo ipo kwenye uzalishaji wa kahawa. Zao la kahawa lina kazi ngumu sana na zina gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kahawa ya Arabica, kuna kukata matawi, kuna kufanyia palizi, kuna kuweka mbolea, kuna kupiga dawa, kuna kupukuchua kahawa, kuna kuvuna kahawa, kuna kuchagua na kuondoa zile kahawa mbovu, kuna kukausha na kuisafirisha kuipeleka sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ugumu wa uzalishaji wa hii kahawa kutokana na hivyo vitu ambavyo nimesema wanavifanya wakulima wetu, bei ya kahawa ni ndogo. Kwa mfano, taarifa tulizozipata kutoka kwenye Bodi ya Kahawa kwa mwaka 2022/2023 zimeonyesha kwamba bei ya kahawa ilikuwa shilingi 3,000 kwa kilo kwa kahawa aina ya Arabica na shilingi 2,000 kwa kahawa aina ya Robusta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kilo ya kahawa ambayo tumeuza kwa shilingi 2,000 mpaka shilingi 3,000 huwa ikienda kule nje huzalisha vikombe 120 hadi 140 vya kahawa. Kahawa kilo moja ya kwetu hapa huzalisha vikombe 120 mpaka vikombe 140 vya kahawa na bei ya kikombe kimoja cha kahawa huko wanakoitumia ni sawa na dola 3.5 mpaka dola 3.7. Tukija kwenye pesa za Kitanzania, hiki kikombe kimoja cha kahawa kinauzwa shilingi 8,750 mpaka shilingi 9,300. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima kama nilivyoeleza hapo awali, hupata shilingi 2,000 mpaka shilingi 3,000 kwa kilo moja ambapo hawa wanaokwenda kuinywa kule, mtu anayeuza yule wa mwisho ukizidisha hivyo vikombe 120 mpaka 140 anapata kati ya shilingi 1,050,000 mpaka shilingi 1,300,000. Kwa hiyo, hebu linganisha shilingi 2,000 na shilingi 3,000 mpaka shilingi 1,000,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachoonekana hapa ni kwamba mwananchi anayezalisha kahawa anapata chini ya bei ya nusu kikombe cha kahawa. Kwa hiyo, pamoja na hii bei kuwa ndogo, wananchi hawa wamechangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023/2024, Bodi ya Kahawa imeonyesha kwamba tumeuza tani 81,000 na kuiingizia nchi yetu kiasi cha shilingi bilioni 440.4. Hii inaonyesha kwamba tumevunja rekodi ya mauzo ya kahawa kwenda nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia njema ambayo tunayo, naomba niishauri Serikali kitu kimoja, ili kahawa iweze kuleta tija na wananchi wafurahie hii kazi ya kuzalisha hili zao la kahawa, cha kwanza ambacho ninaishauri Serikali, kwa mfano kwenye Mkoa wa Kilimanjaro, sisi ni wazalishaji wakubwa wa kahawa ya Arabica ambayo ndiyo inapendwa duniani kote. Sasa, shida moja kubwa tuliyonayo kule ni maji. Kahawa inahitaji maji ya kutosha. Muda wote kahawa inahitaji ipate maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma tulikuwa na miradi kama ya traditional irrigation project, ilikuwa inahudumia ile mifereji ya asili. Watu wanapata maji wanazalisha kahawa na mazao mengine. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, mimi fedha za Mfuko wa Jimbo nilipeleka kusaidia mifereji ya asili, naomba nao waje waniunge mkono ili turekebishe ile mifereji tupate maji ya kutosha ili wananchi wapate kahawa ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, tumeona disparity iliyopo kati ya bei wanayopata wananchi na kule duniani watu wanavyopata faida kutokana na hii kahawa. Naomba Serikali isaidie wananchi kupata masoko ya uhakika, na tusiwe na ukiritimba ili yule mlaji wa mwisho apate fedha ya kutosha na aweze kunufaika na hili zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitashauri, ninajua Mheshimiwa Bashe ni mtu makini sana, apambane na wale wanaozalisha end products za kahawa, tusindike kahawa yetu hapa hapa nchini. Wakamate wale ma-tycoon wakubwa watano wanaotengeneza products za kahawa, waje waweke viwanda hapa ili tusindike kahawa yetu hapa na tuiuzie hapa hapa ili zile fedha ziweze kubaki hapa nchini na wananchi wetu watapata bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwingine ni kuhusu usambazaji wa miche bora ya kahawa. Tumeona kwamba mwaka huu wanategemea kusambaza miche milioni 20. Namwomba Mheshimiwa Waziri, bado tunahitaji miche. Watu wamehamasika, kwa hiyo, miche iongezwe, kwani miche milioni 20 haitoshi. Mikoa inayolima kahawa ni mingi na kwa hiyo, ikiwezekana tushirikishe wadau wengine ili tuweze kuzalisha miche ya kutosha.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Profesa, hitimisha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho ni kuboresha huduma za ugani kwa wakulima ili wapate pembejeo kama dawa, kama ilivyokuwa zamani, ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye uzalishaji wa hili zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa na Naibu wake Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye kusimamia Wizara ya Uchukuzi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa leo utahusu changamoto za mdau muhimu wa uchukuzi hapa nchini ya bodaboda na ushauri wa nini kifanyike kuwasaidia. Kundi hili ni muhimu, lakini limesahaulika sana.
Mheshimiwa Spika, usafiri wa pikipiki maarufu bodaboda sasa ni kimbilio la Watanzania walio wengi bila kujali ukubwa wa kipato chao. Kwa kutumia bodaboda mtumiaji hutumia muda mfupi kufika anapoenda. Kwenye miji mikubwa yenye misongamano, bodaboda hutumika ili kuokoa muda wa kusafiri. Sehemu nyingi vijijini huwa hakuna magari na barabara za kupitisha magari, hivyo basi bodaboda hutegemewa sana.
Mheshimiwa Spika, biashara ya bodaboada ni biashara inayokua kwa kasi sana hapa nchini Tanzania. Hii ni kwa sababu vijana wengi kutokana na ukosefu wa ajira wameamua kuingia kwenye biashara ya bodaboda. Hivyo basi, kazi ya uchukuzi kwa kutumia bodaboda imekuwa ni fursa kwa vijana kutokana na ukosefu wa usafiri wa magari kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Ni muhimu kundi hili liangaliwe kwa jicho la pekee ili wasaidiwe kuboresha huduma zao kwa raia.
Mheshimiwa Spika, katika sehemu karibu zote nchini Tanzania, usafiri kwa kutumia huduma ya bodaboda imekuwa kitu cha kawaida. Kutokana na changamoto ya barabara, kwenye maeneo mengine ya makazi hii ndiyo njia pekee ya watu kufika makwao. Bodaboda hutumika pia kwenye shughuli za kisiasa, zimekuwa zikinogesha misafara ya wanasiasa wetu wakiwa katika majukumu yao ya kutembelea maeneo mbalimbali, lakini pia bodaboda zimekuwa usafiri mbadala ikiwa mtu ana haraka na hataki kukwama katika changamoto ya msafara wa magari barabarani. Vilevile wafanyabiashara pia wanatumia bodaboda kuwachukulia wateja wao bidhaa za aina mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu huu wa bodaboda, waendeshaji wa vyombo hivi hukabiliana na changamoto nyingi. Hivyo basi Wizara ya Uchukuzi ikishirikiana na wadau wengine wa uchukuzi wanahitaji kuja na mikakati ya kitaifa ili kukabiliana nazo. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na:-
Kwanza, baadhi ya waendesha magari huwadharau sana bodaboda. Utakuta bodaboda ipo barabarani gari inaipigia honi kwa fujo itoke au utakuta gari inataka kuingia barabara kuu wakiona bodaboda hawasubiri wanaingia tu na kusababisha ajali. Ikumbukwe vyote ni vyombo vya moto, vina haki ya kutumia barabara na vinalipia mapato ya Serikali. Aidha, bodaboda inakuwa imebeba roho za watu pia. Hilo nalo linahitaji kuangaliwa, kwani vitendo hivi husababisha ajali na vifo.
Pili, waajiri walio wengi hawawapi mikataba madereva wa bodaboda inayowapa haki zao kimkataba. Wale wenye mikataba, sehemu kubwa haina haki ya kupata bima za afya na kuweza kujiwekea akiba. Mikataba inaonesha kulinda maslahi ya mwenye chombo badala ya maslahi ya dereva wa bodaboda.
Tatu, hapa nchini hakuna mfumo rasmi na rafiki wa kuwakagua madereva wa bodaboda kama wamekidhi vigezo vya kufanya hiyo kazi.
Mheshimiwa Spika, nne, baadhi ya abiria wanaowapa huduma huwa wanakuwa wezi na sio abiria wa kweli. Katika maeneo mengi hapa nchini waendesha bodaboda wengi wameibiwa na kuporwa pikipiki na watu wanaojifanya kuwa abiria, lakini baadaye wanawageuka na kuwapora kwa kuwatishia kuwafanyia mambo mabaya ikiwa ni pamoja na kuwatoa uhai.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ya tano ni ajali kuongezeka; hii inasababishwa na vijana wengi kutokujua sheria za barabara. Kuna vijana wanaamini ukishajua kuendesha bodaboda mtaani unaweza pia kuendesha barabarani. Hii hupelekea waendeshe pikipiki barabarani bila kuwa na uelewa kuhusu sheria za barabara. Ajali nyingi zimepelekea vifo na ulemavu wa kudumu kuongezeka. Taarifa zinaonesha kwamba asilimia 70 wa majeruhi wa ajali za barabarani wanaopokelewa MOI wanatokana na ajali za bodaboda.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ya sita ni ya waendesha bodaboda kupata vishawishi vya ngono. Kuna abiria ambao ni wanawake wakipanda pikipiki hawataki kulipa na kuwaambia waendesha bodaboda kuwa wanaweza kulipa kwa kufanya ngono hasa abiria ambao wanawachukua usiku kutoka sehemu za starehe.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya saba ni kwamba waendesha bodaboda wanaugua ugonjwa wa pneumonia kutokana na upepo mkali na baridi kwa wale wasiovaa kinga za baridi.
Mheshimiwa Spika, nane ni kuhusu faini za barabarani; waendesha bodaboda wengi huwa wanakamatwa na polisi na kuandikiwa faini kwa kutofuata sheria za usalama barabarani na kuhatarisha maisha yao na ya watumia njia kwa miguu na hata kusabaisha mtafaruku na usumbufu kwa waendesha magari.
Mheshimwa Spika, kutokana na changamoto zilizotajwa hapo juu, ni vyema Wizara ya Uchukuzi ikaweka umuhimu mkubwa kwenye sekta hii ambayo kwa mawazo yangu ndiyo inayosafirisha watu wengi kuliko vyombo vingine vyote vya usafiri hapa nchini na kutoa ajira za vijana wetu wengi na huchangia kwenye pato letu la Taifa.
Mheshimia Spika, ili kukabiliana na changamoto ya bodaboda hapa chini, ninaishauri Serikali ifanye tafuatayo:-
Kwanza kuwe na usajili wa vituo rasmi vya bodaboda katika maeneo yote nchini (vijijini na mijini). Kwenye hivi vituo kuwe na ukaguzi wa madereva pamoja na pikipiki mara kwa mara na kwa yule asiyekidhi vigezo asiruhusiwe kupakia abiria hadi pale atakaporekebisha kasoro zake. Ni vyema madereva wa bodaboda waende kupata mafunzo maalumu ya uendeshaji salama.
Pili, nguvu na uwezo wa pikipiki uangaliwe; pikipiki nyingi za bodaboda kwa sasa zina cc125-150. Pikipiki hizi hukimbia sana na hiki ndicho chanzo cha ajali nyingi. Napendekeza Serikali iweke sheria kwa pikipiki za kusafirishia abiria zisiwe na nguvu zaidi ya cc100.
Tatu, sheria iweke adhabu kali kwa waendeshaji wanaopakia abiria zaidi ya mmoja (mishikaki); nan ne, Serikali ihamasishe raia kukataa kupanda abiria zaidi ya mmoja (mishikaki) kwa sababu udhibiti wa chombo (control) hupungua kwa dereva akipakia abiria zaidi ya mmoja, hivyo ni rahisi kupata ajali ukiwa uko kwenye mshikaki endapo itatokea dharura yoyote.
Mheshimiwa Spika, katika barabara zote kuu za nchi, kuwe na eneo muhimu la waendesha pikipiki kama ilivyo kwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli.
Aidha, bodaboda hufika katika maeneo yote ya vijijini na mijini. Kama kuna sera yoyote itakayotungwa kuzuia bodaboda zisifike maeneo fulani, hili inabidi liangaliwe kwa umakini mkubwa kwani inaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa kuyafikia maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo pikipiki zinahitajika sana, sera zizingatie kwenye kutoa kipaumbele kwa usafiri wa bodaboda dhidi ya magari binafsi kwa kuboresha usafiri wa umma.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naishauri Serikali pia ifanye yafuatayo ili kuwasaidia watoa huduma katika sekta hii kukabiliana na changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na wadau wengine ianzishe clinics za kutoa elimu na katika clinics hizo, yafuatayo yapewe kipaumbele:-
(i) Clinic hizi zitoe elimu mara kwa mara kwa waendesha bodaboda kuhusu usalama barabarani;
(ii) Clinic kwa wamiliki wa bodaboda ziwaelekeze kwamba mtu wanayempa chombo cha usafiri awe ana leseni;
(iii) Waendesha bodaboda wazingatie sheria za barabarani na kutotumia kilevi chochote muda wa kazi;
(iv) Vijana wafundishwe kujihami ili wasiambukizwe au kuambukiza VVU;
(v) Kwa kuwa changamoto kubwa ya kazi ya bodaboda ni ajali, clinic hizi ziwafundishe umuhimu na namna ya kupata bima za afya na kujiunga na mifuko ya pensheni ili akiba hizi zije kuwasaidia uzeeni. Bima za afya zitakuwa msaada mkubwa katika usalama wao pale inapotokea changamoto ya ajali au kuugua; na
(vi) Clinic hizi zitoe elimu kwa madereva bodaboda ili waweze kuepukana na kundi la kulaumiwa. Bodaboda linafahamika kama kundi linalovunja sheria za barabarani na kufanya vurugu, hasa pale mwenzao anapopata ajali. Wengi hujichukulia sheria mkononi ikiwa ni pamoja na kuua watu na kuchoma magari hata kama kosa ni la bodaboda.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri wetu wa Elimu Profesa Adolf Mkenda na Naibu wake Mheshimiwa Omari Kipanga, Katibu Mkuu, Watumishi wote wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara kwa kazi kubwa sana wanayoifanya kwenye Sekta yetu ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa hii Wizara kusema ukweli ni mzuri sana, tunaona kuna mambo mengi mazuri yanafanyika, kuna mageuzi makubwa ambayo wamefanya na wanasimamia vizuri sana Sekta ya Elimu kuanzia shule ya msingi, sekondari na vyuo na taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara, kwa hiyo, nawapongeza sana kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana pia Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ya bajeti ambayo amekuja na mikakati mitano ambayo anataka afanikishe mambo katika Wizara hii. Kikubwa pale kwenye Bodi ya Mikopo nimeona wana programu ya kufuatilia ile mikopo ambayo wameitoa, naomba waongeze nguvu pale, Bodi ya Mikopo iongeze nguvu pesa zirudi ili wanafunzi wengi zaidi wasomeshwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutoa mikopo pia turudi nyuma tuangalie zile program ambazo zamani tulikuwa tunawapa mikopo, kama vile madaktari, watu wa sayansi na mahesabu tusiache mtu pale kwa sababu hao ndiyo watakuja kutusaidia kujenga nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla Wizara yetu imepata kiongozi bora sana, ni mchapa kazi, msikivu sana, mnyenyekevu, ana upendo na mshikamano wa hali juu sana kwa Wabunge wenzake, hivyo Profesa Mkenda tunampa maua yake katika majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye kuboresha viwango vya vyuo vikuu hapa nchini. Nianze kwa kusema kwamba lengo la mzazi au mlezi yeyote anapompeleka mtoto wake chuoni ni kuhakikisha kwamba anapata elimu bora, ujuzi, uzoefu na mwishoni anakuwa na mafanikio kwa kuajiriwa kwenye sekta binafsi, sekta za Serikali au kwa kuwa mjasiriamali kwa kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili hili lifanyike ni vema kabisa zile taasisi zote ambazo zimepewa dhamana ya kuwapa vijana wetu elimu zikawa zimekamilika kikamilifu. Pia, takwimu tulizonazo zinaonesha kwamba taasisi zetu nyingi hasa zile za Serikali na binafsi hapa nchini, hazijakamilika na zina upungufu wa hali ya juu, sitaki kurudia data alizotoa jana Dkt. Oscar Kikoyo, lakini alichosema ni ukweli na alitoa mfano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kutokukamilika kwa taasisi zetu hizi na kwamba kuna upungufu mkubwa sana wa wahadhiri, ufundishaji, utafiti na kutoa huduma kwa jamii umeathirika kwa kiwango kikubwa. Hii inathibitishwa na ukweli kwamba kuna ranking ambazo wenzetu kule duniani huwa wanafanya kutuangalia vyuo vyetu tukoje. Kwa hiyo, vyuo vyetu havifanyi vizuri kwenye ranking katika ukanda wa Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano hapa, katika vyuo 100 bora hapa Afrika, chuo cha kwanza bora ni University of Cape Town, ni cha kwanza Afrika na cha 328 duniani. Nitaruka, Chuo Kikuu cha Nairobi ambaye ni jirani yetu, ni cha saba Afrika na ni cha 855 duniani. UNISA - University of South Africa ambayo ni kama Open University ya hapa kwetu, ni cha kumi Afrika na ni cha 1,074 duniani. Jirani yetu Makerere University ni chuo cha 13 Afrika na 1,613 duniani. Chuo chetu pendwa kikubwa cha University of Dar es Salaam ni cha 37 Afrika na ni chuo cha 2,475 duniani. Chuo chetu cha SUA ni cha 86 Afrika na cha 4,244 duniani, Chuo cha Afya cha Muhimbili ni cha 95 na cha 4,642 duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi niliofanya hawa ni weber metric ndiyo wamefanya hii evaluation na ndiyo huwa wana evaluate vyuo vyetu, imeonesha kwamba katika top ten vyuo 10 bora Afrika, saba vimetoka Afrika Kusini na kimoja kimetoka Afrika Mashariki ambacho ni Chuo Kikuu cha Nairobi. Kwa hiyo, angalau tunaringa East Africa tumewakilishwa na Chuo Kikuu cha Nairobi. Kwenye vyuo 100 bora duniani, 10 vimetoka East Africa, (saba vimetoka Kenya na Uganda na vitatu vya kwetu ambavyo ni UDSM, SUA na MUHAS) viko kwenye 100 bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape angalizo kidogo ili tuelewane hapa tunapokwenda. University of Dar es Salaam ya kwetu ilianzishwa mwaka1961 na ilikuwa ni Campus ya Chuo Kikuu cha London. Mwaka 1963, University of Dar es Salaam wakarekebisha mambo tukawa na University of East Africa tukawa na vyuo vya Makerere, Dar es Salaam na Nairobi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo vilikuwa vinaendeshwa pamoja na vilipokuwa vinaendeshwa pamoja vilikuwa vinafanya vizuri kwa sababu mdhibiti alikuwa mmoja na vilikuwa vinafanya vizuri. Mwaka 1971, University of Dar es Salaam ilianzishwa kama Chuo Kikuu kinachojitegemea na kikawa kina campus nyingine Morogoro na kadhalika hapa nchini. Tangu wakati huo, tangu tutoke kule hatujawahi kuwa tunafanya vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii ranking unaona kabisa University of Nairobi ni ya 10, Makerere ni ya 13; hawako mbali sana bado wanaendelea kufanya vizuri, hatuwezi kuwalaumu. Kwenye ranking ya vyuo vya Afrika sisi ni wa 37, mwingine ni wa themanini na ngapi na wa 95. Hapa tunaona kwamba kuna vitu vimeshuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, niishauri Serikali iwekeze kikamilifu kwenye uendeshaji wa vyuo vyetu vikuu, vipewe pesa ya kutosha ili wahitimu wa vyuo vyetu hivyo wanaotoka kule wawe bora na siyo bora tu wahitimu, hapana. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunatoa taswira ya wasomi wetu kwamba tuna-produce wasomi wa uhakika ambao watakapokwenda kwenye labor market mahali pengine popote watakuwa na ushindani wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tuna fursa nyingi kama walivyosema wenzangu. Tuna fursa za kupokea wanafunzi kutoka nchi ambazo haziongei Kiingereza; kwa mfano Rwanda huwa wanaleta wanafunzi huku Tanzania kusoma. Sasa Rwanda, Burundi, Mozambique na Sudan wanatuletea wanafunzi. Sasa tuboreshe ili wale jamaa wanapokuja hapa watoke na kitu siyo waone kwamba wamekuja kusoma hapa Tanzania hawajatoka na kitu. Kwa hiyo, napendekeza kabisa tuwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba tunaboresha hivi vyuo ili wasomi wetu wawe wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali. Ushauri wa kwanza; tuwe na program ya kuwasomesha vijana wetu kuanzia assistant lecturers mpaka postdoc, tuwe na program nzuri ya kuwaendeleza vijana wetu. Niishukuru sana Wizara kwamba walitenga hela ya kutosha kusomesha wafanyakazi 189 na 207 wa PhD au 189 wa masters ambapo hapo 27 walikuwa ni wa vyuo binafsi; wamefanya vizuri. Sasa hili fungu liongezewe pesa ili tuboreshe hawa vijana tuwe na PhD za uhakika na wapelekwe nje wasisomeshwe hapa, tusifanye in breeding ya kuzalisha wataalam ambao Degree ya kwanza wamesoma SUA, ya pili SUA na ya tatu SUA; hii ni in breeding ya hali ya juu. Wapelekwe nje wakasome wapate uzoefu wa kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye zile campus mpya ambazo tumefungua, nitatoa mfano wa Campus ya Musoma ya Mwalimu Nyerere. Tuliifungua mapema hatukupeleka walimu pale sasa walichelewa sana kudahili wanafunzi kwa sababu ilikuwa hamna walimu. Ushauri wangu; Serikali isifungue campus mpya hadi isomeshe vijana wa kutosha na kuwapeleka kule. Ukishakuwa na pool ya kufundisha ndiyo tupeleke wanafunzi otherwise tutakuwa tunafungua campus unamlipa VC, watu wote, watumishi wote na hakuna kitu kinachoendelea. Kwa hiyo tuhakikishe kwanza tumefungua, tumesomesha vijana kabla ya…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umewasha. TCU wapambane, wahakiki ubora. Pale ambapo wanaona program haitolewi vizuri, basi wafungie zile program ambazo tunajua hazina walimu wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, sekunde moja tu. Ile publication incentive ambayo wametoa ni kitu chema sana wamewapa watafiti 47. Naomba sasa wasimpe mtu binafsi zile pesa. Hizi hela ikiwezekana zipelekwe kwenye account ya chuo, mtu asiende kunywa bia na zile pesa. Zipelekwe kwenye account ya chuo huyu mtu azitumie hizo hela kufanya utafiti, kununua vifaa vya utafiti, kusomesha vijana wengine, kuhudhuria makongamano ili apate uzoefu wa kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, nami nianze kukushukuru kwa kunipa fursa hii. Kwa namna ya pekee kabisa, nimshukuru Waziri na Mwenyekiti wa Kamati kwa hotuba nzuri ambayo tumeielewa vizuri sana.
Mheshimiwa Spika, nitachangia kwenye eneo la changamoto zinazowakabili walimu wa shule za Serikali za msingi na za sekondari hapa nchini. Wote tunakubaliana kimsingi kabisa kwamba walimu kwenye jamii yetu ni watu muhimu sana, wanafanya kazi ya wito kutoka kwa Mungu kabisa. Wanatusaidia sana kufundisha watoto wetu kuanzia elimu ya awali mpaka kufika sekondari form five na form six. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wabunge tuliomo humu ndani tutakubaliana kwamba wote tumepitia kwenye mikono ya walimu kwa namna moja au nyingine. Hata hivyo, nasikitika kusema pamoja na hawa watu kuwa muhimu sana, Serikali tumewasahau, kuna vitu ambavyo haviko sawasawa na kuna malalamiko makubwa sana kutoka kwa walimu wetu.
Mheshimiwa Spika, niseme tu zamani walimu walikuwa wanatamba Rais wa Awamu ya Kwanza alikuwa mwalimu; Awamu ya Pili alikuwa mwalimu; Awamu ya Nne walikuwa wanamuita shemeji yetu; Awamu ya Tano alikuwa ni mwalimu na mama alikuwa mwalimu. Hata hivyo, pamoja na kuwa na bahati ya kuwa na viongozi wakuu wa Serikali waliokuwa walimu wamebaki kama yatima, stahiki zao kama Serikali hatujaziangalia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali kuwasahau kwa kiasi kikubwa, nitaeleza tu machache ambayo yanatoka rohoni kwangu, kumewafanya walimu wetu wafundishe wakiwa na msongo mkubwa sana wa mawazo. Walimu wengi hawafurahii kazi kwa sababu wanaona kama vile tumewasahau. Walimu wetu wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana. Nitatoa mfano tu; mwaka 2016 Serikali ilipunguza wafanyakazi na idadi ya walimu ilipungua kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya hii idadi kupungua Serikali ni kweli imeshafanya jitihada za kuongeza walimu lakini haijaenda na idadi ambayo inatakiwa ambapo mwalimu anatakiwa afundishe wanafunzi 45 kwenye darasa moja ukilinganisha na walimu 33 ambao ni idadi ambayo iko kwenye shule za private. Jambo hili limeshasababisha tukawa na ufaulu ambao sio mzuri sana. Wanajitahidi na tunawalaumu kwamba wakati mwingine labda hawafanyi kazi vizuri ni kwa sababu ya changamoto ambazo nitazitaja.
Mheshimiwa Spika, walimu wetu wana changamoto nyingi na niende harakaharaka, changamoto ya kwanza ni mishahara midogo. Walimu wanaingia kazini kuanzia saa moja asubuhi, wanafunzi wanashika namba wanatoka jioni, akirudi nyumbani hana hata muda wa kufanya vitu vingine, anaanza kusahihisha kazi ambazo amewapa wanafunzi na baada ya kusahihisha anaanza kuandaa somo la kesho. Kesho yake ni hivyo hivyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maisha yao kusema kweli ni kazini, ni wito, muda wote wanautumia kufanya hii kazi. Wao siyo kama sekta nyingine ambazo huwa wanasafiri wanapata per diem. Hawa watu huwa ni kwenye kituo chake cha kazi kuanzia mwaka wa kwanza mpaka wa mwisho kama hajapata fursa ya kwenda kusahihisha mitihani.
Mheshimiwa Spika, mshahara wa shilingi 420,000/= kwa mwalimu wa Shule ya Msingi au shilingi 560,000/= wanaopata hivyo, alipie nyumba, avae vizuri ili aonekane ni kioo kwenye jamii, ale vizuri, achangie kwenye shughuli za kijamii kama wananchi wengine, hizi fedha ni ndogo sana, hazitoshi. Kwa hiyo, nitapendekeza baadaye ni nini kifanyike.
Mheshimwa Spika, changamoto ya pili ambayo walimu wetu wanakumbana nayo ni madaraja. Wengi wao hawapandishwi madaraja kwa muda unaostahili. Mwalimu anaweza akawa amekaa miaka 10 hajapanda daraja; na hii ina effect kubwa sana kwenye maisha yao wanapostaafu. Kwa hiyo, hili nalo ni jambo muhimu ambalo ningependa tuliangalie kwa pamoja ili tuwasaidie wapande madaraja kama sekta nyingine ambazo zinapanda madaraja.
Mheshimiwa Spika, ni takwa la kisheria kila baada ya mwaka mmoja watumishi wanaenda likizo na wanalipwa na Serikali. Walimu wengi waliopo kule vijijini hawalipwi zile fedha za kwenda likizo. Hii ni shida! Mishahara ni midogo, mwisho wa mwaka ukifika hawezi kujisafirisha kwenda nyumbani. Kwa hiyo, naomba tuwaangalie kwa mazingira ambayo tunafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kitu kingine ni uhamisho. Kuna walimu wameshahamishwa kwenye maeneo ya kazi, lakini kwa bahati mbaya kutokana na ufinyu wa fedha, hawajalipwa fedha za uhamisho. Kuna madeni ya posho za kuhama, fedha ya kujikimu na fedha za kufunga mizigo. Kwa hiyo, naomba hii changamoto nayo tuiangalie kwa namna ya pekee ili tuweze kuwapa moyo walimu wetu kule walipo.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya tano ni madeni ya kwenda kwenye masomo. Walimu wengi wanakwenda kwenye masomo na kuna wachache wanaopata fursa ya kwenda kusoma na wanapokwenda kusoma kuna sheria inaruhusu wapate fedha ya kwenda kwenye masomo. Kuna madeni makubwa sana kwenye Halmashauri zetu na hawajalipwa hizi fedha.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine kubwa ni madeni ya posho za madaraka kwa Maafisa Elimu wa Kata na pia kuna posho ya madaraka pia kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu, hii ni changamoto. Ili kuwapa motisha walimu wetu ambapo ndugu zangu wote tumepitia kule, tuwasaidie hawa watu nao wajisikie ni sehemu ya ajira katika nchi hii.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya saba ni nyumba za kuishi walimu wanaoajiriwa kule vijijini. Wenzangu wameshalisemea hili, nami ninasisitiza kabisa kwamba ni muhimu tuwajengee walimu hasa wale wanaokwenda kwenye mazingira magumu kule vijijini wapate nyumba za kuishi, otherwise wanaishia kuwa na maisha magumu sana. Utakuta wanaishi kwa namna ambayo siyo maadili ya Kitanzania kutokana na shida ambazo zipo kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto zote ambazo walimu wanapambana nazo, mimi nawashukuru sana na ninawapongeza kwamba wameendelea kufanya hii kazi kwa upendo, hawajagoma. Wakishirikiana na vyama vyao vya taaluma, wamekuwa watiifu sana na wameendelea kufundisha watoto wetu. Baada ya kusema hayo naomba niishauri Serikali mambo machache yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa hii sekta na specifically hapa nazungumzia walimu, naishauri Serikali itafute fedha mahali popote zilipo, kama ni huku ndani ama nje ya nchi, tuhakikishe tumetatua hizi changamoto ambazo zimewakabili walimu wetu. Changamoto ambazo nashauri tuzitatue kwanza, tuwalipe mishahara mizuri ikiwezekana. Dada yangu Mheshimiwa Ummy tujipige pige tupate fedha ili hawa watu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu sana walipwe mishahara mizuri, angalau ifanane fanane na wale wanaofundisha shule za private. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa pili, napendekeza wapandishwe madaraja. Kwa wale waliochelewa ikiwezekana tuwapandishe. Kuna kitu wanakiita mserereko. Tuwapandishe madaraja kwa kutumia ule mtindo wa mserereko, kama mtu miaka 10 alitakiwa awe kwenye daraja fulani, sasa hivi ufanyike utaratibu kuhakikisha wamepata hayo madaraja yao kwa sababu watakapostaafu ule mshahara wa mwisho unamsaidia sana kwenye maisha yake ya uzeeni. (Makofi)
Mheshmiwa Spika, ushauri mwingine, ninapendekeza tutafute fedha kama wenzangu walivyosema, tuwajengee walimu shule kule walipo. Kama tumeweza kujenga barabara, ni nini kinatushinda kuwajengea walimu hasa wale wa vijijini wakapata nyumba za kuishi wasidhalilike kule walipo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wa nne ni madeni ambayo yapo. Napendekeza Serikali ijitahidi ilipe likizo kwa wale ambao hawajalipwa, walipwe posho za madaraka wale ambao hawajalipwa na zile za uhamisho na za kwenda masomoni. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Profesa.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mifugo na Uvuvi na wataalamu wa Wizara na wadau wa sekta hizi kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, sekta ya mifugo na uvuvi inatoa mchango kidogo sana katika uchumi wa Tanzania pamoja na ukweli usiofichika kwamba tuna idadi kubwa sana ya mifugo na tunalo eneo la Bahari Kuu ya Hindi, Maziwa Makuu Matatu na Mito mingi iliyosambaa nchi nzima ambayo ina utajiri mkubwa wa samaki.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kilimanjaro una uhaba mkubwa wa ardhi. Pamoja na hilo, Kilimanjaro kuna fursa nyingi za kufuga aina fulani ya wanyama na samaki kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uhaba wa malisho, maeneo ya mlimani (Kilimanjaro) yanaweza kutumika vizuri sana kwa ufugaji wa ndani (zero grazing) wa mfugo ya kimkakati kama vile ng’ombe na mbuzi wa maziwa, nguruwe, sungura, kuku na bata. Hali ya hewa ya mkoa inaruhusu ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wenye tija kubwa kama ilivyo kwenye nchi za Ulaya. Vilevile eneo la Ukanda wa Chini (Kata za Arusha Chini na Mabogini) lenye wafugaji wa nje, lina uwezekano wa kuzalisha kwa tija ng’ombe, mbuzi na kondoo wa nyama.
Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za wafugaji wa Jimbo la Moshi Vijijini, aina za kienyeji za wanyama (ng’ombe, mbuzi, nguruwe, kuku) wanaofugwa ni kikwazo kikubwa kwenye maendeleo ya sekta ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uvuvi, kwa kuwa Mkoani Kilimanjaro kuna maji mengi ya kutosha, kuna uwezekano mkubwa sana wa kuwapatia wananchi kipato kizuri kupitia sekta ya uvuvi kwa kuboresha aina ya samaki waliopo kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu, na kuanzisha ufugaji mpya wa samaki kwa kuchimba mabwawa na kufuga samaki wa aina mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, hili litawezekana ikiwa wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini watapatiwa mafunzo ya kitaalamu ya jinsi ya kufuga na kukuza samaki kwa kutumia teknolojia ya maji kidogo yanayozunguka. Ufugaji wa samaki hauna gharama kubwa ikiwa mfugaji atachimba bwawa.
Mheshimiwa Spika, ufugaji endelevu wa samaki unaweza kutatua changamoto za umaskini kwa kuwaongezea kipato na kuchangia kikamilifu kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Arusha Chini kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu, wavuvi wanaweza kusaidiwa na Maafisa Ugani wa uvuvi mbinu bora za ufugaji wa samaki, ikiwepo matumizi ya vizimba.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji wa vizimba ulioko Ziwa Victoria na kwenye mabwawa machache Tanzania unaweza kufanyiwa majaribio kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha ufugaji wa samaki na mifugo ya kimkakati katika Jimbo la Moshi Vijijini, ninaishauri Wizara itusaidie yafuatayo; kwanza, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa mifugo na uvuvi wafanye utafiti na kuangalia changamoto na fursa zilizopo katika Jimbo la Moshi Vijijini, ili wajue pa kusaidia.
Pili, Wizara ipeleke wataalamu wa mifugo kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa mifugo ya kimkakati yenye tija katika Jimbo la Moshi; tatu, kuwe na programu maalum ya kuzalisha mitamba wa maziwa wenye sifa zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na mifugo mingine kama mbuzi wa maziwa, ng’ombe wa nyama, nguruwe na kuku. Wafugaji wengi hawana mbegu bora za ng’ombe wa maziwa, kwa ujumla huwa wanabahatisha.
Mheshimiwa Spika, nne, Wizara ihamasishe kuanzishwa kwa vikundi vya ushirika wa wafugaji mifugo na samaki ambavyo itakuwa rahisi kuwapatia huduma za mitaji na utaalamu.
Mheshimiwa Spika, pia Wizara itupatie wataalamu wa kuchimba mabwawa; Wizara ianzishe vituo vya kanda vya kuzalisha vifaranga wa samaki ili wafugaji wavipate kwa urahisi kwani vipo tu kwenye Mikoa ya Morogoro, Tabora, Ruvuma, Lindi, Tanga na Geita.
Mheshimiwa Spika, Wizara iwezeshe wazalishaji vifaranga binafsi ili wasaidie juhudi za serikali kwenye kukuza hii sekta; Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Moshi, wawezeshe kupandikiza vifaranga bora vya samaki katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, kwani wavuvi waliniambia kwenye kampeni kuwa samaki wamehama, ikiwa na maana kuwa wamepungua.
Mheshimiwa Spika, Wizara iwe na huduma za uhakika za ugani zikizingatia lishe ya samaki; Serikali iwekeze kwenye kuanzisha mashamba darasa ya ufugaji bora wa mifugo ya kimkakati na samaki jimboni kwangu Moshi Vijijini ili wajifunze kwa vitendo (kama ilivyowasilishwa kwenye hotuba ya bajeti 2021/2022).
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko na Naibu wake Dkt. Stephen Kiruswa na watendaji wote wa Serikali kwa kazi nzuri wanazofanya kwenye sekta ya madini na mimi nitachangia kwenye changamoto za wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya Tanzanite nchini.
Mheshimiwa Spika, sekta ya madini ni moja ya sekta kubwa nchini inayoinua uchumi wa nchi. Tanzanite ni kati ya madini yanayolipatia Taifa pesa za kigeni na kuliingizia Taifa kipato. Madini ya Tanzanite hupatikana nchini Tanzania tu.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wa kigeni wamefanikiwa sana kunufaika na rasilimali hii ya Taifa letu. Kampuni ya nje ya Tanzanite One ni moja ya kampuni iliyofanikiwa kwa kuwa na vifaa vyenye ubora kwa wachimbaji wake.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ambazo Serikali inapaswa kuzitatua ili kuwanufaisha na rasilimali hii ya Taifa lao.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayowasumbua wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya Tanzanite ni matumizi ya teknolojia za kizamani, upatikanaji wa zana za kisasa za uchimbaji na mitaji midogo kwa kundi hili.
Mheshimiwa Spika, bei ya zana za uchimbani ni kubwa na vilevile hutozwa kodi kubwa. Hapa nchini Tanzania ni wafanyabiashara wachache wanajihusisha na biashara ya zana za uchimbaji kama vile vifaa vya kuchoronga miamba, vilipuzi miamba na kadhalika kutokana na kodi nyingi kwenye bidhaa hizi. Kwa hali ilivyo sasa hivi, vifaa hivi vikiingizwa nchini wachimbaji wadogo hushindwa kumudu gharama.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto nilizotaja hapo juu, naishauri Serikali yafuatayo; kwanza Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Waziri wa Fedha washauriane na kuondoa kodi kwa wazawa wanaoagiza na kufanya biashara ya vifaa ili viingie kwa wingi, madini yachimbwe na wengi na kodi iongezeke kutoka kwenye mauzo ya Tanzanite badala ya ile ya kwenye vifaa.
Pili, Wizara ijadiliane na benki za biashara nchini ili zitoe mikopo ya mitaji na ya kununulia vifaa vya kuchimba Tanzanite kwa wachimbaji wadogo wadogo.
Tatu, Serikali kupitia taasisi zake iwasaidie wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite kupata wataalamu na teknolojia za kisasa za kuchimba madini.
Mheshimiwa Spika, nne, Serikali ifanye tafiti za kina katika maeneo ya Mererani ili kujua maeneo yenye madini na kujua yapo umbali gani ili kurahisisha uchimbaji kwa wachimbaji wadogo wadogo. Kwa kufanya hivi, itarahisisha uwekezaji na uchimbani na kuipatia Serikali kipato cha uhakika.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante nianze kwa kumpongeza sana Waziri wa Kilimo na naibu wake pamoja na timu ya wataalam kwa kazi nzuri wanayoifanya Wizara yetu ya kilimo. Nitachangia kwenye sehemu mbili ya kwanza ni umuhimu wa kuongeza bajeti ya kilimo nataka niiombe Serikali kitu hapa na cha pili ni fursa zilizopo Mkoani Kilimanjaro kwenye sekta ya umwagiliaji hasahasa kwenye jimbo langu la Moshi Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wote tunakubaliana kabisa kimsingi kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu na muhimili mkuu kwenye kukuza uchumi wa Tanzania. Kilimo inachangia vitu vingi sana asilimia 65 ya watanzania wako kwenye kilimo inachangia asilimia 27.5 kwenye pato la Taifa asilimia 24.7 kwenye fedha za kigeni asilimia 60 kwenye malighafi za viwanda na asilimia 100 kwenye chakula cha nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na umuhimu huo wa kilimo hawa watu wanapewa hela ndogo sana, Serikali inatenga pesa ndogo sana kwenye hii Wizara na tunamlaumu waziri na timu yake lakini kusema ukweli shida haiku kwa hawa watu. Kwa sababu hata wewe Mheshimiwa Spika jana uliongea nikafurahi sana, ni mtoto wa mkulima unaguswa na kuna kitu kizuri hakiko sawa sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pesa ambayo Wizara ya Kilimo imetengewa kwenye bajeti ambayo waziri ameaomba ni asilimia 0.08 haijafika hata one percent, mnataka waziri afanye nini na timu yake jamani, sisi kama Serikali, hela hii ni kidogo na haitoshi tukilinganisha bajeti za nchi zingine za nchi za Afrika Mashariki ambazo Kenya Uganda na Rwanda hawa wanawekeza vizuri sana kwenye kilimo ukilinganisha na sisi watanzania ambao tunalima kwa uhakika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika niishauri Serikali ni muhimu kabisa tuongeze bajeti ya kilimo tukisema tumewapa pesa tuwape hili wafanye kazi, bila hivyo tutakuwa tunalalamika na hatuwatendei haki wakulima wetu. Niseme kwamba kuna declaration ya Malabo ambayo Serikali yetu iliingia mwaka 2014 tarehe 26 mpaka tarehe 27 Juni. Viongozi wa nchi wakakubaliana kwamba tutatenga angalau asilimia 10 ya bajeti iende kwenye kilimo kwenye haya mataifa maraisi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini naona hatujafika hata one percent jamani tunakwenda wapi niombe tu angalau tungekubaliana na hiyo ten percent kilimo leo tungukuwa tunawapa kitu kama tirioni 3.6 ambayo wangeweza wakafanya kiti kidogo, wakaboresha utafiti wakaboresha ugani, na vitu vinginevyo ambavyo wameweka kwenya mpango wao. Kwa hiyo, ombi langu kwa Serikali na Waziri Mkuu wetu yupo hapa baba yetu Waziri Mkuu tunaomba kabisa Wizara ya Kilimo iangaliwe kwa jicho la huruma kwa sababu tunavyokwenda sio sawa kabisa nakubaliana na Mheshimiwa Joseph Kandege bajeti ya kilimo ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo niende kwenye jimbo langu sasa Mkoa wa Kilimanjaro una fursa nyingi sana za kilimo cha umwagiliaji eti tumebarikiwa kuwa na ule mlima unatiririsha maji mengi sana kutoka mlimani na yanaishia bahari ya Hindi. Bahati mbaya sana maji haya hayajatumika vizuri, nina naishauri wizara itumie hii fursa ya yale maji badala ya kuishia baharini na kuuwa watu kwenye mafuriko tuwekeze tujenge skimu za kutosha tuboreshe ile mifereji ili kilimo kule Kilimanjaro tutoe mchango kama tulivyokuwa tunafanya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna maeneo ya ukanda wa tambarare kule jimboni kwangu, eneo la Mabogini tunaweza tukajenga skimu mpya, kuna kama hekta 1,350. Kata ya Arusha Chini tunaweza tukajenga skimu mpya kwenye vijiji viwili, kuna hekta kama 2,000. Kuna eneo la Old Moshi Mashariki kwenye Kijiji cha Mandaka Mnono kuna hekta 1,250. Tukiwekeza katika maeneo haya, nina uhakika tutachangia kikamilifu katika zile hekta ambazo Serikali inategemea kuboresha kwenye kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono hoja. Naomba sana tuifikirie Wizara ya Kilimo kwenye funding. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na nianze moja kwamoja kwa kumpongeza sana Waziri wetu wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa ripoti nzuri aliyowasilishwa. Ile ripoti ilikuwa imejaa kila kitu nami nimepata uelewa mkubwa sana wa vitu ambavyo Wizara ya Afya inafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nirudie kumpongeza Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Naibu wake Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu Dkt. Shekalaghe, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Tumaini Nagu, Taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Afya, Madaktari wote nchini na manesi na wafamasia kwa kazi nzuri wanayofanya. Kusema ukweli Udaktari ni kazi ya wito na hawa watu wanatutendea haki sana. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nisitoke hapa bila kumpongeza Rais wetu, Rais wetu ameona umuhimu wa hii Sekta ya Afya na ametoa pesa za kutosha kabisa kusaidia Watanzania ili wapate huduma. Nampongeza Rais kwa sababu kwenye bajeti hii ambayo wanatuomba tuwapitishie, Mheshimiwa Rais ametenga shilingi 1,235,000,000,000 ikiwa ni nyongeza. Mwaka jana hii bajeti ilikuwa ni trilioni…
(Hapa umeme ulikatika)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Kilimo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Uvuvi na Maji kwa kuwasilisha vizuri hotuba ya bajeti na Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge. Pia niwapongeze sana wataalamu wa Wizara pamoja na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa sana kwenye sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa umeainisha nafasi ya sekta ya kilimo katika uchumi wa Tanzania kwani sekta hiyo inaajiri asilimia 65 ya nguvu kazi ya Watanzania, huchangia asilimia 27.5 kwenye pato la Taifa, asilimia 24.7 fedha za kigeni na asilimia 60 ya malighafi ya viwanda hapa nchini. Kilimo huchangia asilimia 100 ya chakula kinachotumika hapa nchini. Kwa bahati mbaya sana, umuhimu huu wa sekta ya kilimo haujaonekana kabisa kwenye bajeti ya Wizara. Kwa mfano, bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2021/2022 ni shilingi 294,162,071,000, hii ikiwa ni asilimia 0.08 ya bajeti ya Taifa ambayo ni trilioni 36.260.
Mheshimiwa Spika, Rais wa Awamu ya Sita alipohutubia Bunge alieleza kuwa Serikali yake itatoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo ili kuwakwamua wakulima wetu. Kwenye hili, Serikali haijazingatia ahadi ya Rais wetu. Asilimia 0.08 ya bajeti ya kilimo katika bajeti yote ya Taifa ni kidogo sana na haiendani kabisa na ahadi ya Rais ambaye ni kiongozi wetu mkuu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilimo ndio roho ya uchumi wa nchi yetu, ni vyema Serikali ikaiwezesha kikamilifu Wizara ya Kilimo ili waweze kutatua changamoto za wakulima.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali itekeleze lile Azimio la Malabo lililoazimiwa Equatorial Guinea na wakuu wa nchi za Afrika tarehe 26-27 Juni, 2014 ambapo waliazimia kuwekeza asilimia 10 ya bajeti zao za Taifa kwenye kilimo. Kwa mantiki hiyo, bajeti ya kilimo ingekuwa takribani shilingi trilioni 3.626.
Mheshimiwa Spika, kama Serikali itawekeza kikamilifu kwenye kilimo, naishauri Wizara ya Kilimo iwekeze kwenye mambo makuu muhimu yafuatayo:-
(a) Utafiti wa mazao ya chakula na biashara (uzalishaji wa mbegu bora na mbinu za kuongeza tija); taasisi za utafiti wa kilimo ziwezeshwe.
(b) Utafiti wa udongo kwenye kila eneo linalolimwa ili kujua changamoto za rutuba ya udongo.
(c) Utafiti wa mabadiliko ya tabianchi.
(d) Utafiti wa masoko ya kilimo na kuzingatia intelejensia ya masoko.
(e) Kuboresha ushirika kwa kubadilisha sheria kandamizi za ushirika na kusaidia kwenye eneo la uongozi wa ushirika.
(f) Uboreshaji wa shughuli za ugani.
(g) Uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya kimkakati kupitia Wakala wa Mbegu (ASA).
(h) Uwekezaji wa kutosha kwenye kilimo cha umwagiliaji, kwa kuelekeza fedha kwenye maeneo yenye maji ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili ni kuhusu fursa za kilimo cha umwagiliaji katika Jimbo la Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kilimanjaro una fursa kubwa sana za kilimo cha umwagiliaji. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Kilimanjaro kuna mito mingi inayoanzia mlimani na kuishia Bahari ya Hindi bila kutumika kikamilifu kwenye kilimo.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ijenge skimu mpya na kukarabati ile mifereji ya asili ili haya maji yatumike kuzalisha mazao badala ya kuishia baharini.
Katika jimbo langu la Moshi Vijijini, ninaishauri Serikali ifanye yafuatayo:-
Mosi, Serikali iwekeze kikamilifu kwenye kuboresha na kujenga upya mifereji ya asili. Miundombinu hii imechoka, na ni muhimu sana kwenye kilimo cha kahawa, ndizi, mbogamboga na matunda. Mifereji hii ikiboreshwa kikamilifu itasaidia katika block farms za asili za mazao hayo katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Pili, Serikali ijenge skimu mpya za umwagiliaji katika maeneo ya tambarare ambayo hukumbwa na mafuriko makubwa kila mwaka. Maji ya mafuriko yaelekezwe shambani kuzalisha chakula (mpunga na mazao mengine). Mafuriko ya mwaka huu yamesababisha maafa makubwa, na Wizara ya Kilimo ilipeleka misaada ya chakula na ya kibinadamu katika Kijiji cha Mandaka Mnono kilichopo Kata ya Oldmoshi Magharibi.
Mheshimiwa Spika, pia Wizara ijenge skimu mpya Kata ya Oldmoshi Magharibi katika kijiji cha Mandaka mnono ambapo kuna 1250 ha. Pia Wizara ijenge skimu mpya Kata ya Arusha Chini katika Vijiji vya Mikocheni na Chemchem ambako kuna 2000 ha. Wizara pia ijenge skimu mpya Kata ya Mabogini ambapo kuna 1350 ha.
Mheshimiwa Spika, skimu hizi mpya zikijengwa, zitaongeza 4600 ha kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa chakula na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa wananchi na Taifa.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima na Naibu wake Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi 74,223,193,000 kutekeleza shughuli za Wizara.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kuhusu hali ya wazee hapa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika vipaumbele 10 vya Wizara kwa mwaka wa 2023/2024, kipaumbele namba nane kinasema; "kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa haki za watoto na huduma za ustawi wa jamii kwa wazee."
Mheshimiwa Spika, kutokana na kipaumbele hicho cha Wizara hapo juu, ni dhahiri kwamba masuala ya wazee yanahitaji msukumo wa kipekee. Tunaishukuru Wizara kwa kutenga shilingi bilioni 1.8 kusaidia wazee kwa mwaka huu wa pesa wa 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, wazee ni watu muhimu ambao wengi wametulea. Wazee wengi huko vijijini wamechoka, hawana uwezo na inalilazimu Taifa kuwatazama.
Mheshimiwa Spika, wazee wengi wanachukuliwa kama tabaka lililotengwa, hivyo ni vyema wakahudumiwa na kupatiwa matibabu, makazi, vyakula, kuwasaidia fedha za kujikimu kama ilivyo kwenye mataifa mengine na majirani zetu wa Zanzibar kupitia Pension Jamii.
Mheshimiwa Spika, kuna sera inayosema matibabu ni bure kwa wazee, lakini wakienda hospitali wanaambiwa ni wale wasiojiweza na wanakosa dawa na matibabu.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine inayowakabili wazee wetu ni ukatili dhidi yao. Ukatili huu umekuwepo kwenye baadhi ya jamii yetu kwa miaka mingi. Jambo hili halijatiliwa mkazo unaostahili katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Spika, ukatili huu unafanywa katika ngazi ya kaya na vijiji na watu wa karibu ambao ndiyo hutambulika kama wasaidizi wa karibu wa wazee katika ngazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu, ninaishauri Serikali ifanye yafuatayo: -
Kwanza, Serikali ishiriki kwenye kujengea uwezo mashirika yanayojihusisha na masuala ya wazee, mabaraza ya wazee ngazi ya mikoa na wilaya, asasi za kutetea haki za binadamu na kuchukua juhudi za kuielimisha jamii juu ya haki za wazee na umuhimu wa kumlinda mzee.
Pili, Serikali ipange bajeti ya kutosha ya kuwahudumia wazee wasiojiweza na kuhakikisha wanapata tiba, makazi na chakula. Kiasi cha shilingi bilioni 1.8 zilizotengwa kwa mwaka 2023/2024, hazitoshi.
Tatu, Serikali iwalipe wazee Pension Jamii kama ilivyo huko Zanzibar.
Nne, Serikali itenge fungu maalumu kuwasaidia wazee waanzishe miradi ya kujiongezea kipato kama vile ufugaji wa kuku, nyuki, mbuzi na ng’ombe.
Tano, Serikali ifikirie kuwa na wawakilishi wa wazee huku Bungeni kama kundi maalumu kwani makundi ya vijana na akina mama wana uwakilishi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi nianze kumpongeza sana Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa kuwasilisha hotuba zao za bajeti na ile ya Kamati ya Kudumu ya Bunge vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye kuangalia mchango wa Mkoa wa Kilimanjaro kwenye sekta ya viwanda na biashara. Historia inaonesha kwamba Mkoa wa Kilimanjaro kwa muda mrefu umekuwa na historia ya kuwa na viwanda vikubwa ambavyo vimeshachangia sana kwenye kulipatia Taifa letu kipato kikubwa na mkoa wetu pamoja na watu ajira za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Moshi Vijijini kiwanda ambacho kinafanya kazi vizuri sana sasa hivi ni kiwanda cha TPC ambacho kinaajiri watu kwa wingi sana na kinachangia kikamilifu kwenye pato la Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla. Kuna viwanda ambavyo vimefungwa havifanyi kazi na viwanda hivi ambavyo vimefungwa vimeshasababisha matatizo makubwa sana kwenye mkoa wetu wa Kilimanjaro kiuchumi na kijamii kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, orodha ya viwanda ambavyo vimefungwa kule Kilimanjaro na vimetuletea matatizo makubwa sana ni kama ifuatavyo; kiwanda cha kwanza ni kiwanda ambacho kiko jimboni kwangu, Kiwanda cha Kukoboa Mpunga kilichoko Kijiji cha Chekereni, Kata ya Mabogini; hiki ni kiwanda cha kukoboa Mpunga. Kiwanda cha pili, ambacho kipo jimboni kwangu ni kiwanda cha viatu cha Uru Kaskazini kinaitwa Kiwanda cha Viatu cha Msuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingine ambavyo ni vya Moshi DC vya jirani yangu ni Kibo Match Corporation Limited, kiwanda cha kutengeneza viberiti; kuna Kiliwood Product ambacho hata Mheshimiwa Musukuma amekitaja, kuna Kibo Papers Limited, kuna Kiwanda cha Maguni Moshi, kuna Kiwanda cha Twiga Chemicals ambacho kinazalisha bidhaa za kilimo na vipo vingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya viwanda hivi kufa, mimi niseme tu sababu zingine ni za ajabu ajabu na sikubaliani nazo sana. Mojawapo ni kwamba wawekezaji ambao walipewa viwanda hivi hawakuwa na nia thabiti ya kuviendeleza hivi viwanda kwa maana nyingine hawakuweza kwenye kuendeleza hivi viwanda. Sababu ya pili ni kwamba teknolojia zimebadilika na hao wenye hivi viwanda hawakuwekeza kwenye teknolojia mpya na sababu ya tatu, ambayo ninayoomba Serikali iliangalie hili, ni kuruhusu bidhaa za nje. Nitatoa mfano, Kiwanda cha Magunia kilishindwa kuzalisha kwasababu Serikali iliruhusu kuingiza jute bags ambazo zilikuwa na bei rahisi na yule mtu wa magunia akashindwa kuzalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na viwanda hivi kufa, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita kwa juhudi kubwa ya kuanzisha tena upya viwanda kule Kilimanjaro. Kuanzia mwezi Disemba, 2017 mpaka mwezi Machi, 2020 Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na viwanda 113 vipya ambavyo vilianzishwa kwa juhudi ya Serikali. Katika viwanda hivi, viwanda 80 vilikuwa viwanda vidogo sana, viwanda 26 vilikuwa viwanda vidogo, viwanda vinne vilikuwa vya kati na viwanda vitatu vilikuwa ni viwanda vikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa viwanda, ninaushauri kwa Serikali kwamba kwanza kabisa tufufue tuwe na programu maalum ya kufufua viwanda ambavyo nitavielezea hapa chini kwasababu vinatija kubwa sana kwa mkoa wetu wa Kilimanjaro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naiomba Serikali ihamasishe wawekezaji hasa wazawa wa Kilimanjaro najua mko huko mliko, rudini nyumbani mje tuijenge Kilimanjaro yetu, tuweke viwanda ili hadhi ya mkoa wetu iwe kama zamani. Nasema haya kwa sababu Mkoa wa Kilimanjaro kuna miundombinu rafiki sana ya kufanya biashara na kuwekeza viwanda. Viwanda muhimu vyenye tija ambavyo vimeshafungwa ni kama vifuatavyo; cha kwanza, kinaitwa Kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Kilimanjaro ambacho kipo Mabogini. Kiwanda hiki Serikali iliwapa KNCU (Chama cha Wakulima wa Kahawa) nafikiri hapa kulikuwa na kosa kidogo badala ya kuwapa CHAWAMPU (Chama cha Wakulima wa Mpunga) kule Mabogini ili wakiendeshe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuanzia Septemba, 2014 kiwanda hiki hakijawahi kufanya kazi. Mimi naishauri Serikali nakuomba waziri kwasababu kiwanda kimesharudishwa Serikalini kupitia kwa Msajili wa Hazina naomba ikiwezekana tuwape CHAWAMPU wale watu wa Mabogini ndio wanaolima mpunga tuwawezeshe ili waweze kuendesha kiwanda chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha pili, Kiwanda cha Viatu Msuni, hiki pia kipo jimboni kwangu na kinamilikiwa na Kata ya Uru Kaskazini, kilifunguliwa miaka ya 1970 na Baba yetu wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa sasa kimekufa. Tunaiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri upeleke wataalam wa TRDO pale wakawape utaalam namna ya kufufua hiki kiwanda ili tuunge juhudi za hawa watu wanaokimiliki. Ni kata tu inamiliki hiki kiwanda. Tunaomba sana, tuwaunge mkono wana Kata ya Uru Kaskazini ili kiwanda hiki kifufuliwe.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kingine ni Kiwanda cha Magunia ambacho kipo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Patrick, muda wako umeisha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi baada ya kusema hayo nimeshayapeleka kwa maandishi naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Viwanda na Biashara na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa kuwasilisha vizuri hotuba ya bajeti na ripoti ya Kamati. Pia niwapongeze sana wataalamu na wadau kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye kuipeleka nchi yetu kwenye Tanzania ya viwanda, ndoto iloyobebwa kikamilifu na Serikali ya Awamu ya Tano na Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa una historia ya kuwa na viwanda vingi ambavyo vilichangia sana kwenye ajira na mapato ya mkoa na Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingi vya zamani vilivyokuwa na majina makubwa kimkoa na kitaifa kwa sasa vimefungwa. Baadhi ya viwanda maarufu ambavyo havifanyi kazi ni Kilimanjaro Machine Tools Manufacturers Ltd., Twiga Chemicals Ltd. cha kuzalisha madawa ya kilimo, Kiliwood Products Ltd. cha kuzalisha bidhaa za mbao, Kibo Paper Ltd. cha kuzalisha karatasi, Tanzania Packaging Manufacturers (1998) Ltd. cha kuzalisha magunia, Kiwanda cha Viatu Msuni kilichofunguliwa miaka ya 1970 na Baba wa Taifa, Kibo Match Ltd. cha viberiti na Kilimanjaro Paddy Hulling Co. Ltd. cha kukoboa mpunga kilichopo Chekereni, Kata ya Mabogini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufa kwa viwanda hivi kwa kiasi kikubwa kumesababishwa na baadhi ya wawekezaji kutokuwa na nia thabiti ya kuviendeleza, kubadilika kwa teknolojia za uzalishaji na ushindani wa bidhaa kutoka nje kama vile mifuko ya jute iliyoua soko la magunia ya katani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vipya mkoani Kilimanjaro kama ilivyo kwenye mikoa mingine hapa Tanzania. Kuanzia Disemba, 2017 hadi kufikia Machi, 2020 mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na viwanda vipya 113; kati ya hivi, viwanda 80 ni vidogo sana, viwanda 26 ni vidogo, viwanda vinne ni vya kati, na viwanda vitatu ni vikubwa. Viwanda hivi vinachangia kikamilifu kwenye pato la mkoa na Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa viwanda katika kujenga uchumi wa nchi yetu na kutoa ajira, ninaishauri Serikali iwe na programu maalumu ya kufufua viwanda vya zamani vilivyowahi kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi na iendelee kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vipya mkoani Kilimanjaro kwani kuna miundombinu rafiki na hii itaboresha uchumi wa mkoa na Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda muhimu vyenye tija na ninavyopendekeza vifufuliwe ni kwanza Kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Kilimanjaro (Kilimanjaro Paddy Hulling Company Ltd.) kilichopo Kata ya Mabogini. Serikali ilikabidhi kiwanda hiki kwa Chama Kikuu cha Ushirika (KNCU) kinachojishughulisha na biashara ya kahawa na tokea mwezi wa Septemba, 2014 kimekuwa hakifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili lilikuwa kosa kubwa sana na KNCU, walishindwa kukiendesha, na ulikuwepo mgogoro mkubwa sana wa umiliki wa kiwanda hicho na Umoja wa Wakulima wa Mpunga wa CHAWAMPU ambao ni wakereketwa wa mpunga. Msajili wa Hazina amekirudisha kiwanda hiki Serikalini toka mwezi Oktoba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali iwasiliane na wadau mbalimbali ikiwemo CHAWAMPU ili apatikane mwekezaji atakayekifufua na kukiendesha kiwanda hiki kwa tija. Kiwanda hiki kimezungukwa na wakulima wa mpunga wanaozalisha mara mbili kwa mwaka.
Pili ni Kiwanda cha Viatu Msuni kilichopo Kata ya Uru Kaskazini; kiwanda hiki kinamilikiwa na Kamati ya Maendeleo Kata ya Uru Kaskazini (WDC). Kina uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali za ngozi. Ninaiomba Serikali itume wataalamu wa TiRDO kwenye kiwanda hiki ili ushauri wa kitaalamu upatikane na kiwanda hiki kifufuliwe na kuunga juhudi za wana ushirika huu kwenye kukuza uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni Kiwanda cha Magunia; kiwanda hiki kinamilikiwa na Mohamed Enterprises Ltd. Kiwanda hiki hakijafanya kazi toka kinunuliwe miaka 14 iliyopita (2006). Tunaishauri Serikali ifuatilie utekelezaji wa mwekezaji wa kuanzisha uzalishaji wa magunia. Ikibainika kuwa safari ya uzalishaji kama bado ni ndefu, Serikali ichukue hatua stahiki kwa manufaa ya Taifa.
Nne, ni Kiwanda cha Madawa ya Kilimo cha Twiga Chemicals; kiwanda hiki kinamilikiwa na Twiga Chemicals Ltd. na bado miundombinu yake ni mizuri. Kwa kuwa kiwanda hiki kimerudishwa Serikalini kupitia kwa Msajili wa Hazina toka Oktoba, 2018, ninaishauri Serikali iharakishe kumtafuta mwekezaji ili dawa za kilimo zizalishwe hapa nchini na kuokoa fedha zetu za kigeni ambazo hutumika kuagiza madawa ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano niKiwanda cha bidhaa za Mbao (Kiliwood Products Ltd.); kiwanda hiki kilikuwa kinamilikiwa na Hans Industries na kwa kuwa alishindwa kukifufua, kupitia kwa Msajili wa Hazina kimerudishwa Serikalini. Ninaishauri Serikali iharakishe kumtafuta mwekezeji ili uzalishaji urejee na kuliwezesha Taifa kuzalisha bidhaa za mbao na kuachana na utaratibu wa kuagiza bidhaa kutoka nje. Malighafi za mbao zinapatikana kwa wingi hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita ni Kilimanjaro Machine Tools; kiwanda hiki kinamilikiwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Kiwanda hiki kinaweza kutoa mchango mkubwa sana kwenye kuzalisha vipuri vya mashine za aina mbalimbali na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni za kuagiza vipuri kutoka nje ya Tanzania. Ninaiomba Serikali iisaidie NDC kwenye kuingia ubia na wadau mbalimbali na kukifufua kiwanda hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoa wa Kilimanjaro una fursa nyingi sana za kuanzisha viwanda vipya. Mkoa huu una fursa kubwa za kilimo cha mboga, kahawa, ndizi, mahindi, maharage, mpunga, matunda na maziwa. Bidhaa hizi zinaweza kutumika kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kuongeza thamani ya mazao yetu yanayozalishwa mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha hili ninaishauri Serikali ianzishe programu maalumu itakayowashirikisha wadau muhimu wa viwanda kama vile TiRDO, SIDO, TCCIA, VETA na CTI ili watoe mafunzo ya kuhamasisha ujasiriamali wa viwanda mkoani Kilimanjaro. Mkazo uwe kwenye kusindika matunda, mbogamboga, maziwa, unga wa mahindi, michele na maharage. Kuna uwezekano mkubwa sana wa kuanzisha viwanda vya usindikaji wa kahawa na kutengeneza juice au mivinyo ya ndizi mbivu. Serikali ikiweka mazingira wezeshi, wajasiriamali wengi wa Kitanzania watatumia fursa hii kutengeneza ajira na kuingizia mkoa na Taifa mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza sana Waziri wa Nishati na Naibu wake pamoja na jopo la wataalamu wa Wizara kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye kuipeleka nchi yetu kwenye Tanzania ya Wiwanda kwa mchango wao mkubwa kwenye sekta ya umeme.
Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali, bado wananchi wengi wa Jimbo la Moshi Vijijini hawajapatiwa nishati ya umeme kupitia mradi wa umeme vijijini (REA).
Mheshimiwa Spika, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 inaelekeza kwamba kufikia 2025, vijiji vyote Tanzania vitakuwa vimeunganishiwa umeme. Upatikanaji wa umeme vijijini utachochea kuboreka kwa maisha, ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kama zile za kuchomelea vyuma, gereji, maduka, salon za kunyoa na kutengeneza nywele na mabanda ya kuonyesha mpira.
Mheshimiwa Spika, ni kutokana na ahadi hii, ninaiomba Wizara ya Nishati isaidie kutatua changamoto za nishati ya umeme katika Jimbo langu la Moshi Vijijini. Kukosekana kwa umeme katika baadhi ya vijiji na vitongoji jimboni kwangu kunawafanya wananchi kuingia gharama kubwa ya kununua mafuta ya taa kila siku ili waweze kupata mwanga nyakati za usiku.
Mheshimiwa Spika, maeneo yenye changamoto ya umeme Jimbo la Moshi Vijijini ni katika Kata ya Kindi, Kijiji cha Chekereni Weruweru, Vitongoji vya Miembeni, na Kisiwani havina umeme kabisa. Mbunge ametokea Kata ya Kibosho Kirima. Katika Kijiji cha Boro kwenye Vitongoji vya Boro Kati na Boro Juu (anakotokea Mbunge), voltage za umeme ni ndogo sana na hupelekea kushindwa kuendesha vifaa vya ndani kama friji na vyombo mbalimbali vya ndani. Mashine za Welding (kwenye vitongoji hivi) na pump ya kuvuta Maji Masoka Sekondari hushindwa kufanya kazi kutokana na umeme mdogo. Shule hii ina wanafunzi zaidi ya 800.
Mheshimiwa Spika, wajasiriamali wameshindwa kuweka mashine za kusaga unga, mashine za kutengeneza matofali na miradi mingine midogo inayohitaji umeme wa uhakika. Wanafunzi wa bweni wa Sekondari ya Masoka hushindwa kupata huduma ya umeme ili wajisomee usiku kutokana na umeme mdogo. Umeme huwaka kuanzia saa
5.1 usiku. Naomba Wizara isaidie kutatua changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Okaoni, Vijiji vya Sisamaro, Omarini na Mkomilo vinahitaji kuunganishwa japo baadhi ya maeneo nguzo zimepita ila bado kuunganishwa. Kata ya Kibosho Mashariki inahitaji huduma. Katika Kijiji cha Sungum Vitongoji vya Kyareni na Nkoitiko havijaunganishwa. Katika Kijiji cha Singa, Kitongoji cha Singa Juu hakijaunganishwa. Katika Kijiji cha Mweka, Kitongoji cha Mweka Juu na Omi havijaunganishwa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Kibosho Kati, baadhi ya maeneo ya Kijiji cha Uri hakijaunganishwa. Kwa ujumla, katika vijiji vya Otaruni na Uri, kuna changamoto ya ukosefu wa umeme kwenye baadhi ya Vitongoji. Pia kuna tatizo la umeme kidogo (low voltage) kwenye vijiji hivyo. Tunaiomba Serikali iweke Transfoma za kutosha ili kukabiliana na tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Uru Mashariki, Kijiji cha Materuni, Kitongoji cha Wondo hakijaunganishwa. Walichimba mashimo kwenye baadhi ya maeneo na kuleta nguzo tokea mwezi wa Tisa mwaka 2020 na hawajarudi tena. Katika Kata ya Mbokomu, Kitongoji cha Mmbede Kyaroni, Tema na Masanga na baadhi ya maeneo ya Korini Kati havijaunganishwa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Mabogini sehemu ambazo hazijapata umeme hadi sasa ni kama ifuatavyo:-
(1) Vitongoji vya Sanya “Line A” na Mjohoroni vilivyopo katika Kijiji cha Mabogini.
(2) Kitongoji cha Uru, katika Kijiji cha Muungano;
(3) Katika Kijiji cha Maendeleo, Vitongoji vya Mshikamano na Uarushani;
(4) Mgungani katika Kijiji cha Mtakuja;
(5) Katika Kijiji cha Mserekia, hakuna umeme katika Vitongoji vya Mbeya kubwa, Mbeya ndogo, Remit, Mkwajuni na Mafuriko. Vilevile Kijiji cha Mji mpya, Kitongoji cha Utamaduni hakijaunganishwa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Mabogini wapo wananchi waliofanya wiring lakini surveyor hawaji kukagua ili waruhusiwe kulipia; pili, wapo wananchi ambao wamesharudisha form na hawajaitwa kwenda kulipa ili wawashiwe umeme. Tunaiomba Wizara ifuatilie jambo hili.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Old Moshi Magharibi Kitongoji cha Saningo katika Kijiji cha Mandaka mnono hakina umeme kabisa. Kata ya Kimochi Kitongoji cha cha Kiwalaa kilichopo Kijiji cha Sango, Kitongoji cha Iryaroho kilichopo katika Kijiji cha Mowo na Kitongoji cha Maryaseli katika Kijiji cha Lyakombila havina umeme.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo niliyotaja hapo juu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha umeme wa kutosha unapatikana katika maeneo yote ya Jimbo la Moshi Vijijini. Hili litafanikiwa ikiwa Wakandarasi watalipwa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, vilevile, naishauri Serikali iwe na programu ya kuwaelimisha wajasiriamali wa vijijini kuhusu fursa zilizopo vijijini, na ni kwa namna gani wanakijiji wanaweza kutumia nishati hii kujiajiri na kuongeza thamani ya bidhaa zao?
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nianze kwa kumpongeza sana Rafiki yangu Waziri pamoja na Naibu wake; timu nzima ya Wizara pamoja na wadau wa utalii na maliasili kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye maeneo kama manne hivi. Kama muda hautaniruhusu, nitapeleka kwa maandishi. Nitachagia suala la Half Mile, wapigakura wangu wamenituma kule Moshi kwamba niombe kitu kuhusu Half Mile. Halafu nitatoa ombi la Wizara ikiwezekana wafungue route mpya za kupanda mlima Kilimanjaro kupitia Kata za Mpakani za Uru na za Old Moshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda tutambue uwepo wa mti mrefu kuliko yote Barani Afrika wenye mita 81.5; na huu ndiyo mti mzee kuliko miti yote duniani, uko Kilimanjaro kwenye Kijiji cha Tema kwenye Kata ya Mbokomu. Pia nitazungumzia mgogoro uliopo wa kwenye hifadhi ya Ngorongoro kama muda utaruhusu kwa sababu watu wameongezeka kama alivyosema Mheshimiwa Paresso na kuna tatizo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa half mile. Half mile ni nini? Half mile ili ni eneo linalotenganisha Mlima Kilimanjaro eneo la hifadhi na makazi ya wananchi. Kwa hiyo, ni eneo lenye upana wa nusu maili ambalo linatengenisha watu na Mlima Kilimanjaro. Historia ya watu Kilimanjaro inaonesha kwamba tulianza kuishi pale karibia miaka 2,000 iliyopita. Kwa hiyo, tumekaa pale muda mrefu tu. Pamoja na kukaa huko kwa muda mrefu, lakini tuna experience mbaya sana watu wa Kilimanjaro kuhusiana na umiliki wa ardhi kule kwetu na hizi hifadhi za asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vitu tumevirithi, lakini niseme tu mwaka 1921 tulipata shida kidogo na Wakoloni, walipitisha sheria ya kusema kwamba watu wasiende kule Kilimanjaro kule mlimani, iliwekwa sheria kabisa kwamba mtu akienda kule ni kosa. Mwaka wa 22 Gavana aliyekuwa anatawala nchi yetu alisema ardhi yote ni yake; na mwaka 23 wakaanza program mbaya kabisa ya kuwanyang’anya watu ardhi yao na kujimilikisha na kuanza mashamba ya masetla. Mashamba hayo tuna bahati kwamba yalitaifishwa mwaka 1967 kupitia Azimio la Arusha, lakini bado hayajawa mikononi mwa wananchi moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla Wakoloni wametuletea matatizo makubwa sana kwa sheria kandamizi za umiliki wa ardhi pamoja na zile maliasili zetu. Pamoja na ukatili wa Wakoloni, niseme kwamba mwaka 1941 walianzisha kitu kinachoitwa half mail. Walituonea huruma wakasema ruksa sasa nusu maili wananchi mwingie mpate huduma za misitu kama kuni, mboga kama mnavu za kwenda kupika kitalolo, kuna chakula cha kienyeji kule nyumbani, mkajipatie mbao za kujenga na vitu vingine. Kwa hiyo, walituruhusu, walikuwa na huruma kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliendelea hivyo mpaka mwaka wa 2004. Matumizi yalikuwa mabaya kwenye hii half mail, Serikali yetu ya Tanzania ikasimamisha ule utaratibu ambao wakoloni walituonea huruma Serikali ikasema sasa basi kwa sababu mmeshaharibu sana; ni ukweli kulikuwa kuna uharibifu kwa sababu usimamizi haukuwa mzuri sana kwenye hii half mail, Serikali ikasimamisha, kwa hiyo, ikawa tena hakuna half mail na lile eneo likawa declared ni eneo la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zuio hili la Serikali liliondoa ile huruma ya wakoloni ambao walituhurumia watu wa Kilimanjaro. Eneo hili sasa hivi linalindwa na maaskari wa KINAPA (Kilimanjaro National Park). Jamani, hawa watu ni wakorofi, wapiga kura wangu wameniambia kwamba wakati naomba kura watu wamepigwa, wameuawa na akina mama wamebakwa. Kwa hiyo, kuna mambo yanaendelea kule ambayo siyo mazuri sana. Wakati Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein alipotembelea Kilimanjaro mwaka 2008 kwenye safari ya kikazi, wananchi walimweleza hii kero na alikuwa na Mheshimiwa Prof. Jumanne Maghembe kwenye hiyo ziara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara ilikaa ikaelekeza TANAPA wachore ramani mpya. Kwa hiyo, Wizara ilipelekewa barua ambayo iliandikwa na Mheshimiwa Waziri Maghembe na Katibu Mkuu, Dkt. Ladislaus Komba kwamba wachore ramani ili eneo lirudishwe kwa wananchi. Bahati mbaya mpaka leo hakuna kitu ambacho kimeshafanyika na bado half mail strip hatujaipata. Kwa hiyo, tunamwomba Waziri achukulie pale walipoachia wenzake ili atusaidie. Hizi sheria ni kandamizi na zinafanya wananchi waichukie Serikali yao bila sababu. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa Muda wa Mzungumzaji)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, chonde chonde, nakuomba ulibele hili na hii mtakapopeleka kwa Mheshimiwa Mama Samia tunamwomba sana alifanyie kazi mara moja, nasi tupate haki ya kumiliki na kutunza ule mlima ambao ni wa kwetu. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Prof. Ndakideni.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa fursa hii, kuchangia kwenye bajeti hii ya Serikali ambayo imeongezeka kutoka trilioni 34.88 hadi trilioni 36.33, ikiwa ni ongezeko la asilimia nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Waziri na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, kwa kuwasilisha vizuri sana hii bajeti yao na ninaomba kabisa nikiri kwamba, bajeti hii imeandaliwa vizuri sana kimkakati. Na inaleta matumaini makubwa sana kwa watanzania kwenye makundi mbalimbali ambao niseme, wafanyakazi, wafanyabiashara, wakulima, wakinamama, vijana, walemavu, watu wa viwanda, bodaboda na hata wastaafu wameipokea vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyoletwa ni nzuri na kusema ukweli inategemea kwenda kulegeza vyuma. Kule mitaani watu walikuwa wanasema kwamba, vyuma vimekaza. Bajeti hii nategemea kwamba, itakwenda kulegeza vyuma na itatupeleka mbele kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii inategemea kuongeza pato la Taifa kutoka asilimia 4.8 hadi asilimia 5.6, inategemea kudhibiti mfumko wa bei ibakie kati ya asilimia
3 na asilimia 5. Inategemea mapato ya ndani yatafikia asilimia 15.9 ya pato la Taifa na makusanyo ya kodi yanategemea kuongezeka kutoka asilimia 12.9 hadi asilimia 13.5 ya pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii pia, inategemea kama tutaipitisha Waheshimiwa Wabunge, naomba wote tuiunge mkono inategemea kuwa na akiba ya fedha za kigeni za kutusaidia kuagiza bidhaa za nje kwa miezi minne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri wanayofanya. Nianze kwa zile shilingi milioni 500 ambazo mama yetu ametupatia/Rais wetu, kwangu ni fursa kubwa sana. Kwamba, barabara zinakwenda kurekebishwa nchi nzima na niwapi tumeshaona tu Rais anaingia tu na kutupa zawadi kubwa kama hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu, hii fedha inakwenda kusaidia sana kwenye ujenzi wa barabara ya TPC, Mabogini mpaka Chekereni. Na kuna fedha ya ujenzi wa shule za Sekondari za Kata nina hakika wananchi wangu kule Moshi, Kata ya Kindi, Kijiji cha Chekereni, Weruweru tunakwenda kujenga shule pale kwa hiyo, ni jambo lenye heri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii pia, inakwenda kupunguza mzigo kwa mfanyakazi, ambapo kodi ya ajira inakwenda kupungua kutoka asilimia 9 mpaka asilimia 8 na hii itaongeza maslahi ya wafanyakazi na pia, kwa wafanyakazi pia kuna bilioni 449 inayokwenda kupandisha watu karibu 92,000 madaraja. Pia niipongeze Serikali kwa kupunguza faini kwa watu wa bodaboda, kutoka shilingi 30,000 hadi shilingi 10,000 ni kitu kizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na pia Serikali inakwenda kubadilisha mabadiliko ya Kanuni ya Sheria ya Bajeti, ambapo kama tutapitisha hakuna tena kurudisha fedha Hazina zitakuwa zinabakia kule na hii ni kitu kizuri. Kuna mambo mengi sana ambayo kutokana na muda sitaweza kuyasema nitawasilisha kwa maandishi. Lakini Serikali vilevile imepania kikamilifu kulinda viwanda vya ndani kwa kuondoa tozo za ushuru wa forodha, katika malighafi za aina mbalimbali ambazo zitaingizwa na zitasaidia kuboresha viwanda vya ndani. Kwa mfano, kwenye kilimo vile vifungashio vya maziwa, mbegu, kahawa, korosho, pamba wameondoa ushuru wa forodha na hii itachochea watu kufungua viwanda na kufanya biashara hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nina ushauri kwa Serikali. Ushauri wangu wa kwanza ni kwamba, katika bajeti ya Taifa ya trilioni 36.3 asilimia 29.3, ambayo ni sawa na shilingi trilioni 10.66 zitatumika kulipa deni la Taifa. Hizi ni fedha nyingi karibia one third itatumika kulipa deni la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali ikiwezekana tutafute vyanzo vingine vya fedha, ili tukusanye fedha nyingi na zitumike kwenye kudhamini miradi mbalimbali. Vile vile ninaishauri Serikali ibuni mbinu mbalimbali za kukusanya kodi kwenye biashara ndogo ndogo. Hizi biashara ndogo ndogo zimepanuka sana ni wengi lakini wengi wao hawalipi kodi. Kwa hiyo, mjipange muangalie namna ya kuwakata kodi hawa wafanyabiashara wadogo wadogo, ambao wanaweza wakachangia sana katika pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaishauri Serikali iendelee kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na wawekezaji wa nje. Ii tupanue wigo wa kuwaajiri watu wengi zaidi na tukishapanua wigo wa kuajiri watu wengi vile vile tutapata kodi na tutaongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inategemea kukopa ili ku-support miradi ya maendeleo na inategemea kukopa shilingi trilioni 7.34 ili kugharamia miradi ya maendeleo. Katika hizi shilingi trilioni 4.99, zitatoka kwenye Taasisi za ndani kwenye Mabenki ya ndani au Taasisi nyingine za ndani na shilingi trilioni 2.35 zitatoka nje.
Nilifikiri ilitakiwa iwe the opposite kwamba, nyingi tukope kutoka nje na kidogo tukope ndani, Ili tuwaachie wafanyabiashara wa ndani waweze kukopa kutoka kwenye Mabenki yetu. Kwa sababu tunawaminya wafanyabiashara wa ndani hawana mahali pa kukopa na hiyo inasababisha wasiweze kuwekeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa pili, ni kuhusu ushirikishaji wa sekta binafsi katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo. Kwenye ule Mpango wa Pili, ni ukweli usiopingika kwamba, Serikali haikuishirikisha sekta binafsi sana kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo. Kazi nyingi zilikuwa zinafanywa na Serikali, Taasisi za Serikali kwa mfano, mikutano ya Kiserikali tulikuwa tunaambiwa twende VETA tusiende kwenye hoteli nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu ya aina mbalimbali walikuwa wanafanya Taasisi za Serikali. Kwa hiyo, sekta binafsi ilipwaya sana walikuwa hawaajiri. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali kwenye Mpango wa Tatu huu, sekta binafsi wameshajifunza kwamba, kama kuna kitu walifanya makosa sasa hivi watarekebisha na tuwashirikishe ili waweze nao kushiriki kwenye ujenzi wa Taifa lao na kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa mwisho na ushauri wangu wa mwisho kwa Serikali ni kwenye sekta ya kilimo. Wabunge wengi hapa walilia sana kwamba, kilimo hakijatendewa haki. Lakini mawazo mengi yalichukuliwa ila la kilimo pamoja na kwamba, karibu kila Mbunge alisema bajeti ya kilimo ni ndogo halikubebwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri, ikiwezekana kwenye ile bajeti ijayo tunajua hili hatuwezi kulifanyia kitu kikubwa lakini kwenye ile bajeti ijayo tujitahidi kilimo, mifugo, wapate fedha za kutosha kwa sababu sehemu kubwa ya watanzania ni wakulima na wanahitaji kusaidiwa. Tukishapanua kilimo tunauhakika kabisa kwamba tuta-improve productivity na watu watapata kipato cha kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Mipango na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa kuwasilisha vizuri sana hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali na maoni ya Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imeelezea mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyowasilishwa ni nzuri na inalenga kulipeleka Taifa letu hatua moja mbele. Kwa mantiki hiyo, ninaiunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kiasi kikubwa bajeti hii imeheshimu mawazo ya Wabunge katika michango yao toka Bunge la Kumi na Mbili lianze, isipokuwa kilio cha kuongeza bajeti ya kilimo na mifugo hakikuzingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii, Serikali imebainisha maeneo muhimu ya kipaumbele kwa mwaka 2021/2022. Kwa upande wa wafanyakazi, ninaipongeza Serikali kwa kupunguza kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kwa wafanyakazi kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane. Hatua hii kwa kiasi imewapunguzia wafanyakazi mzigo mkubwa wa kodi na kuboresha maslahi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuipongeze Serikali kwa kuboresha mazingira ya kazi kwa Madiwani na Watendaji wetu wa Kata. Serikali imeonesha nia njema sana ya kuzijali kada hizi zinazofanya kazi na wananchi katika ngazi ya vitongoji na vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Serikali kwa kutenga shilingi bilioni 328.2 kwa ajili ya kugharamia Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Zoezi hili ni muhimu sana kwenye kupanga maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika michango mbalimbali, tuliwasikia Wabunge wengi wakilalamikia tozo mbalimbali zilizokuwa zinawaumiza vijana wa Kitanzania waliokopa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Naipongeza Serikali kwa kufuta tozo ya asilimia sita iliyokuwa ikitozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya mkopo wa elimu ya juu kwa wanufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine lililolalamikiwa na Wabunge ni watumishi kutokupandishwa madaraja kwa kipindi cha miaka mitano na zaidi iliyopita. Ninaipongeza Serikali kwa kutenga jumla ya shilingi bilioni 449 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 92,619. Hatua hii itawapa motisha na kuboresha maisha ya wafanyakazi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu kumekuwepo na changamoto za muda mrefu za ulipaji wa mafao kwa wastaafu kutokana na ufanisi mdogo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika kuhudumia wastaafu wetu. Ninaipongeza Serikali kwa kuja na mkakati wa kulipa madeni yanayodaiwa na mifuko kwa kutenga fedha kwenye bajeti na kutumia utaratibu wa kutoa hatifungani maalum isiyo taslimu zitakazoiva kwa nyakati tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo ya Waziri hatua hii inakwenda kumaliza kabisa tatizo hilo la wazee wetu kudai haki yao. Katika bajeti hii Serikali imependekeza kuwa kuanzia sasa wanataka kuanza kulipa michango hiyo moja kwa moja kutokea Hazina kwa taasisi zote ambazo watumishi wanalipwa na Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Wizara kwa nia njema ya kufanya mabadiliko katika Kanuni ya 21 ya Sheria ya Bajeti ili kuondoa changamoto iliyopo ya fedha ambazo hazijatumika hadi tarehe 30 Juni ya kila mwaka kurejeshwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali. Mabadiliko haya yamekuja wakati muafaka na yatasaidia sana kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika idara mbalimbali za Serikali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Waziri kwa kuja na mapendekezo ya vyanzo vipya vya mapato. Mimi naunga mkono mapendekezo yake na niwaombe Watanzania wote waelewe kwamba Taifa letu litajengwa na sisi wenyewe. Pendekezo la kulipia kodi ya majengo kupitia matumizi ya umeme (LUKU), tozo za simu na tozo za kutumia miamala ya fedha ni ubunifu mzuri. Hapa Serikali itaongeza idadi ya walipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ilithibitika kuwa kulikuwa na ushiriki kidogo wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Mpango wa Pili. Kwa kiasi kikubwa utekelezaji ulifanywa na taasisi za Serikali. Hii ilitokana na tabia mbaya iliyokuwa imejengeka kwenye sekta binafsi ya kuuza huduma kwa bei kubwa. Kazi hiyo hiyo ilifanyika kwa bei ya chini sana na kwa kiwango kizuri kwa kuzitumia taasisi za Serikali. Katika Mpango wa Tatu, ninaishauri Serikali ishirikishe sekta binafsi kwenye utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaishauri Serikali katika maeneo machache yafuatayo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninaishauri Serikali ishirikishe sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi ya Serikali iliyopo kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa. Katika hili, sekta binafsi wahamasishwe na kuelekezwa wawe waaminifu kwenye kutoa gharama halisia za utekelezaji kwani wameshajifunza makosa waliyofanya siku za nyuma. Wakishirikishwa kikamilifu, watazalisha ajira, wigo wa walipa kodi utapanuka na mapato yataongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, katika Bajeti Kuu ya Serikali ya shilingi trilioni 36.33; asilimia 29.3 (trilioni 10.66) zitatumika kulipia Deni la Taifa. Kiasi hiki ni kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali ibuni vyanzo vipya vya mapato kwani wigo wa kukusanya bado ni finyu sana. Napendekeza ianzishwe tozo mpya kupitia malipo kwenye mita za maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, biashara ndogo ndogo zimepanuka sana na wengi huwa hawalipi kodi. Ninaishauri Serikali ibuni mikakati madhubuti ya kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, ninaishauri Serikali iendelee na kuboresha mazingira kwa wawekezaji wa ndani na nje. Tukipata wawekezaji wengi, ajira, wigo wa kulipa kodi na mapato ya nchi vitaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tano, Serikali inategemea kukopa shilingi trilioni 7.34 kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati ya hizo, shilingi trilioni 4.99 zitakopwa ndani na shilingi trilioni 2.35 zitakopwa nje. Katika hili Serikali inapochukua mikopo mikubwa kutoka ndani (mabenki yetu), itakuwa inaminya sekta binafsi kukopa na kuziyumbisha. Sekta binafsi zikiyumba, ajira zitakosekana na wigo wa kulipa kodi na mapato kuathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sita, Wabunge wengi waliotoa mawazo katika michango yao, walishauri ufanyike uwekezaji wa kutosha katika sekta za uzalishaji (kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda) na walipendekeza bajeti ya sekta hizi ziangaliwe kwa jicho la pili. Bahati mbaya, Serikali haikuzingatia maoni ya Wabunge wengi. Ninaishauri Serikali kwenye bajeti itakayofuata ya mwaka 2022/2023 iongeze Bajeti ya Kilimo na Mifugo kwani inaajiri asilimia 65 ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, saba, Serikali imelimbikiza madeni mbalimbali ambayo wazabuni wameshatoa huduma. Ninaishauri Serikali ilipe madeni ambayo uhakiki umekamilika. Kwa mfano, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NMAIST) iliyoko Arusha ina deni (shilingi 6,007,562,000) lililohakikiwa muda mrefu, lakini malipo hayajafanyika. Ninaiomba Serikali isaidie kwenye hili ili shughuli za kukuza hii taasisi zisikwame.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo na ushauri wangu, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami nikushukuru mno kwa kunipa nafasi ya kuchangia katioka hoja hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Itifaki hii ambayo tunaijadili hapa ni makubaliano ambayo yameingiwa kati ya Tanzania na nchi wanachama wenzetu ikiwa na lengo moja kubwa ambalo ni kuhakikisha kwamba tuna-harmonize na kutumia sheria, kanuni ambazo zipo ili kumsaidia Mtanzania ashiriki kikamilifu katika biashara mbalimbali ambazo zinafanyika katika Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo, ni kitu muhimu na Wizara husika imefanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwa-summon wakatuletea maelezo mengi marefu tu kuanzia Wizara ya Kilimo, Waziri pamoja na wataalamu wake wamejitahidi sana, Waziri wa Mifugo naye alikuja. Tuliiita Wizara ya Mambo ya Nje nao wakaja wakatuelezea mambo ya ki-protokali na Wizara ya Biashara vilevile walikuja. Kwa hiyo, ni kitu muhimu ambacho tunaliomba Bunge kwa umoja wetu tupitishe Itifaki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Itifaki hii ni muhimu sana na itatusaidia kwa kiasi kikubwa kufanya biashara na wenzetu kama ambavyo Waziri ameeleza. Sisi kama nchi ya Tanzania wote tunakubali kwamba kwa sekta ya kilimo tuko vizuri, tuna uwanda mpana sana wa kulima na bidhaa zetu kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ni nyingi ukianzia mahindi, mbogamboga, maua, maparachichi, matunda, kila kitu tunacho hapa. Vilevile ukija upande wa Wanyama, tunao ng’ombe wengi sana kushinda wenzetu, tunao kuku na samaki wengi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mbele ya safari Wabunge wenzangu nawahakikishia tukipitisha Itifaki hii sisi ndio tutakuwa wanufaika wakubwa kuliko hata wenzetu. Kwa hiyo, kwa umoja wetu naomba tukubaliane tuipitishe, ili tuende mbele, pesa ziingie kwenye mifuko ya raia wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaambia hivyo kwa sababu sisi kama nchi tumechukua muda mrefu sana kujiandaa kuingia kwenye Itifaki hii. Kwa hiyo, kwa mawasilisho waliyofanya Mawaziri ambao nimewataja tuko tayari kabisa. Niombe tu tuliwa-grill sana Mawaziri kuna wakati ambapo tulikuwa hatujajiridhisha na maelezo tulikuwa tunawaambia nendeni mkatuletee ili tujiridhishe tukawa- convince Wabunge wenzetu wakubali Itifaki hii na hilo limefanyika. Kwa hiyo, sisi kama wajumbe wa Kamati tumeridhika kabisa na maelezo ambayo yametoka Serikalini kwamba Itifaki hii ni muhimu na nawaomba tena kwa umoja wetu turidhie ili tuende mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, faida ambazo zitapatikana kwa kuridhia Itifaki hii ni nyingi sana, wenzangu wameshataja na sipendi kurudia lakini mimi kama Mchaga nizungumzie ile ya biashara. Tukiridhia Itifaki hii biashara yetu itaongezeka vizuri, tutafanya biashara ya uhakika ya mazao, mifugo, samaki na tutapata kipato cha kutosha kabisa. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tuko tayari kusema ukweli kwa maelezo ambayo Waziri ametoa. Nitaeleza vitu vichache tu, tayari wamesha-identify taasisi nyeti ambazo zitasimamia afya ya mimea ambapo wameshaunda taasisi inayoitwa Tanzania Plant Health and Pesticide Authority, itakuwa inashiriki kikamilifu, tuta-compete vizuri na wenzetu wa nchi za jumuiya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya ya wanyama kuna taasisi ambazo zipo, mfano Tanzania Veterinary Laboratory Agency, hawa wanashughulikia ng’ombe na wanyama wengine. Kuna TAFIRI kwenye mambo ya samaki na kwenye usalama wa chakula tuna Shirika letu la TBS, wapo tayari kuhakikisha kwamba viwango ambavyo vinahitajika kutekeleza itifaki hii vinatekelezwa vizuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niseme kwamba sera mbalimbali zipo tayari. Tumemuelekeza Waziri pale ambapo sera hazipo waende chap watengeze sera ili tuendane na wenzetu na tuweze kutekeleza Itifaki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kuna ushauri ambao pia tuliutoa naomba nirudie; tunaiomba Serikali chondechonde wahakikishe kwamba tunawajengea uwezo wataalamu wetu ambao watashiriki kwenye Itifaki hii. Tuwe na watafiti waliosoma sawasawa watakaokuwa wanashiriki kwenye utekelezaji wa Itifaki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunaomba tuwe na uwekezaji wa kimkakati. Tuwe na maabara ambazo ni advanced zinazoweza kupima na kutoa majibu sahihi ambapo hatutakinzana na wenzetu wa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ule ugonjwa wa kutokuipatia Wizara pesa ya kutosha. Tunaomba kwenye utekelezaji wa Itifaki hii kwa sababu tutakuwa tunashirikiana na nchi nyingine, Serikali itenge pesa za kutosha ili Profesa Mkenda na wenzake wasikwame kwenye kutekeleza Itifaki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kimoja kwenye udhibiti wa usalama wa chakula. Zamani tulikuwa na taasisi iliyokuwa inaitwa TFDA, haya ni maoni yangu hayajatoka kwenye Kamati; tulii-dissolve ile tukawa na TMDA na sasa hivi TBS ndiye anayekagua kuanzia ukaguzi wa magari kule Japan mpaka huku, ana kazi nyingi sana. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ifikirie uwezekano wa kuwa na chombo ambacho kitakuwa kinaangalia usalama wa chakula. Ikiwezekana kwa mfumo mwingine tuwe na TFA nyingine ambayo itakuwa inashugulika na masuala ya kudhibiti ubora wa vyakula ambavyo vitakuwa vinauzwa huko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Naomba Wabunge wenzangu tu-support Azimio hili, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kuchaguliwa na Wabunge kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye utekelezaji wa bajeti ambao umefanyika katika Wizara zetu tatu tunazozisimamia kuanzia mwezi Julai hadi Disemba mwaka huu wa fedha. Nianze kwa kuipongeza Serikali na Wizara ya Maji kwa kazi nzuri ambazo zinaendelea katika Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunakubaliana kama Wabunge kwamba Wizara ya Maji inafanya kazi nzuri na kuna miradi ya kutosha kabisa kwa kila Mbunge katika kila Jimbo, miradi inayogharamiwa na Serikali Kuu, Mfuko wa Maji na zile hela ambazo Mama yetu Rais Samia ametoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano katika pongezi zangu hizi kwamba kwenye bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Maji Serikali ilikuwa imetenga shilingi 646,630,000,000 na katika pesa hizi Serikali imeshapeleka shilingi 413,950,671,097.95 ambayo ni sawa na asilimia 61. Kutokana na hili Mheshimiwa Juma Aweso na timu yake wanang’ara, wameendelea kung’ara kusema ukweli. Kwa hiyo, tunaipongea Serikali kwa kazi nzuri na kwa jinsi wanavyoisapoti hii Wizara ambayo tunaisimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeona kwamba kama Kamati kuna changamoto kwenye hii Wizara kidogo na ninaomba muichukulie seriously Waziri na watendaji wako, kwamba kwenye manunuzi kila kitu kinafanyika makao makuu na hizi Mamlaka za Maji na RUWASA kuna saa wanakwama kwamba, vifaa havifiki kwa wakati. Kwa hiyo, ni maoni yetu kama Kamati kwamba, hili lifanyiwe marekebisho ili ununuzi uende haraka na Waziri aendelee kuchapa kazi kama ambavyo anachapa pamoja na watendaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Wizara hizi kama Wizara, viongozi wa Wizara hizi wanajitahidi sana kutekeleza miradi mbalimbali, lakini wana changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa fedha kama ilivyokuwa kwa Wizara ya Maji; kwa mfano, katika bajeti ya maendeleo Tume ya Umwagiliaji imepangiwa shilingi bilioni 35 kama pesa za ndani na shilingi bilioni 11.5 kama pesa za maendeleo kwa pesa kutoka nje, lakini hadi mwezi Disemba, 2021 Tume hii ilikuwa imepokea shilingi milioni 349 tu ambayo ni 1% tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tuko serious tunakubaliana kwamba, Wabunge wote huku kila aliyekuwa anasimama alikuwa anasema kilimo, maji, umwagiliaji, lakini kweli kwa hii trend ya kutoa 1% kwa miezi sita tutafika kweli? Tutatekeleza vile vitu ambavyo tulikuwa tume-plan na tumewaahidi watu kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hapa tunaona kuna tatizo na tunaiomba Serikali iiangalie hii Wizara kwa jicho la huruma na wawape pesa, ili watengeneze miradi ya maji na mambo yaendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya uvuvi mambo ni yaleyale katika pesa za maendeleo zilizotengwa ambazo ni shilingi bilioni 99 wameshapokea shilingi bilioni tatu tu ambayo ni sawa na 5.1% katika sekta ya uvuvi. Katika sekta ya mifugo walitengewa shilingi bilioni 16.8 na wameshapokea shilingi 2.4 ambayo ni sawa na 14.6%.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hizi sekta ambazo zinaajiri wakulima wengi, wafugaji na wavuvi, sidhani kama tunazitendea haki. Kwa hiyo, ni mawazo ya kamati kwamba, pesa zilizopelekwa kutekeleza miradi ya aina mbalimbali ni ndogo na tukumbuke Rais alivyokuja kufungua Bunge letu, kutuhutubia hapa, alitoa ahadi kwamba, sekta hizi za uzalishaji kilimo, mifugo na uvuvi zitapewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tutii lile agizo la Rais ili tufike mbele, bila hivyo ninaona tunakwenda ambako siko, tutahukumiwa na wale wapigakura.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niseme tu naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na watendaji wake kwa kazi nzuri wanazofanya kuilinda nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966 Sura 192 na Sheria ya JKT ya mwaka 1963 Sura 193, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekabidhiwa jukumu la kusimamia Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa katika kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, Wizara hii ina wajibu wa kuvipatia vyombo hivi mahitaji yake ya kimsingi ili kuviwezesha kutekeleza majukumu hayo. Katika hili, bado baadhi ya wanajeshi wetu hawajapatiwa huduma ya msingi ya kupatiwa nyumba za kuishi na walio wengi kuishi uraiani.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo mengi duniani huwezi kumkuta mwanjeshi akipanga kwenye nyumba uraiani. Hii imewasaidia kuwajenga kisaikolojia askari wao na kutanguliza utaifa kwanza kutokana na Serikali zao kuwawekea mazingira bora ya kuishi pamoja.
Mheshimiwa Spika, ninapendekeza wanajeshi wetu wote wajengewe mazingira bora na familia zao kwa kujengewa makazi na kuishi kambini. Kwa kufanya hivi, hii itarahisisha kufuatilia nyendo zao na kusimamia maadili yao ya kazi za kijeshi. Vilivile, wakikaa pamoja kambini itarahisisha kuwapatia huduma muhimu kama maji, umeme, tiba na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ina majukumu ya kulinda mipaka ya nchi yetu na kuandaa umma wa Watanzania kushiriki katika shughuli za ulinzi wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha azma hii, ninapendekeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania lieendelee kutoa mafunzo ya ulinzi ya kimkakati wa mgambo kama sehemu muhimu ya jeshi la akiba. Napendekeza mafunzo haya yawe ni lazima kwenye mikoa yote inayopakana na nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, uzoefu tulioupata kwenye vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine imeonesha kwamba jeshi la akiba linalohusisha wananchi wa rika mbalimbali huko Ukrane limetoa mchango kubwa kukabiliana na Taifa kubwa la Urusi lenye uwezo mkubwa wa kivita na silaha za kisasa.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti,nashukuru sana. Nami nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuwasilisha vizuri Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2023/2024. Nianze pia kwa kutambua juhudi za Serikali ambazo inafanya kwa kuhakikisha kwamba miradi mbalimbali inatekelezeka ikiwepo miradi michache tu ambayo nitaitaja:
Tunajenga barabara, tunaboresha viwanja vya ndege, tunaboresha ununuzi wa ndege, kuna shule tunajenga, maji, barabara za vijini, ya Mikoani vyote hivyo ni kazi nzuri ambayo Serikali yetu inafanya. Kwa hiyo, niipongeze sana Serikali na niombe waendelee kukusanya fedha ili hii miradi iishe ikamilike kama tulivyopanga kwenye mpango wa 2022/2023 tupate heshima yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye sekta ya kilimo mifugo na uvuvi. Nianze kwa kuipongeza Serikali na Bunge hili lako Tukufu kwa kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Shilingi Bilioni 294 mpaka Bilioni 954 na ile ya Wizara ya Mifugo kutoka shilingi bilioni 168 mpaka Shilingi Bilioni 268 ijapokuwa imeongezea Haba na haba hujaza kibaba siyo mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali, huu ulikuwa ni uthubutu wa hali ya juu kabisa kuongeza hizi bajeti za hizi sekta mbili tuendelee kuhakikisha kwamba wanapokea hizi pesa ili yale mafanikio ambayo tunategemea wakulima wetu wayaone kule yaweze kuwafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kwenye mpango nitaanza na kuongelea suala la utafiti kwenye vituo vyetu vya utafiti wa kilimo, ngoja nianze na kilimo. Tumekuwa na mikutano mingi na watafiti wa TARI na pia tumetembelea vituo vya utafiti TARI, tulichokiona kule kunasikitisha, miundombinu ya hivi vituo vya utafiti iko taabani. Tanzania tuna vituo vya utafiti 17 ambavyo miundombinu ya ofisi haijakaa vizuri, ukienda kwenye maabara ni almost hazipo kabisa, ukija kwenye nyumba za kulala za watumishi haziko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali angalau kwa TARI wamewatengea Shilingi Bilioni 39 kwenye mpango huu wa mwaka huu na mambo yanakwenda vizuri. Wameongeza kutoka Bilioni 11 mpaka Bilioni 39. Kwa hiyo tunaishukuru sana Serikali. Niombe kwenye huu mpango kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara kwamba bila utafiti hakuna mahali tutakapokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi zimefanikiwa Duniani kupitia utafiti. Kwa hiyo, tukiwaongezea kwenye huu mpango Watafiti wetu pesa ya kutosha ili waweze kufanya utafiti wa kuzalisha mbegu. Utafiti wa kubuni mbinu bora za kuongeza tija kwenye kilimo tutafika mahali ambapo na sisi tutanufaika na utafiti wetu. Kwa hiyo, kwenye huu mpango niombe ikiwezekana walikuwa wanasema wakipata Shilingi Bilioni 75 watu wa TARI wangefika mahali ambapo watafanya kitu ambacho kinaonekana. Kwa hiyo niombe tufikirie kuwasaidia watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kwenye mpango wa pembejeo. Tunaishukuru sana Serikali yetu ambayo imeshawekeza pesa karibu Shilingi Bilioni 100 kwenye pembejeo za ruzuku hasa ya mbolea. Tunaweza tukatoa mbolea kwa wakulima wetu lakini kama hujawapa mbegu na viuatilifu anaweza asizalishe akafikia pale tunapotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kwenye huu mpango mpya wahakikishe kwamba tunaweka pesa ya kutosha ili tuwapatie wakulima wetu mbegu, mbolea na viuatilifu ili uzalishaji uweze kukamilika kwa sababu bila hivi vyote vitatu kwenda pamoja nafikiri hatutafika mahali pazuri na kama pesa haitoshi ya ruzuku ninapendekeza kwamba tuwe na Mfuko maalumu tuipatie Benki yetu ya kilimo pesa ya kutosha ili waweze kupatia wakulima wetu mikopo nafuu, waweze kununua hivi vitu ambavyo haviwezi kutoka kwenye ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu kwenye kilimo ni Kilimo cha Umwagiliaji. Kama sote tunavyoona mabadiliko ya tabianchi yamesababisha shida kubwa sana na kuna upungufu wa chakula karibia dunia nzima. Kwa hiyo, sisi kama Taifa tuna bahati nzuri kwamba tuna maeneo mengi na maji ya kutosha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara ya Kilimo kwamba ina miradi karibia 36 ambayo ipo inaendelea wanajenga skimu mpya. Niwaombe katika mpango huu tuhakikishe kwamba tunajenga miradi ya umwagiliaji kwenye maeneo ambayo kuna maji ya kutosha ili tuweze kunufaika na hiki kilimo cha umwagiliaji, kikubwa napendekeza pia kwenye huu mpango waongezewe pesa za umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la Nne ni kilimo cha bustani, hivi karibuni tumezindua Mpango wa Taifa wa Kilimo cha Bustani, niombe kilimo cha mboga mboga ndiyo kitu ambacho kinaweza kikalikwamua Taifa letu kwa sababu mboga mboga zina bei mahali pote. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwenye huu mpango wahakikishe wanafuatilia ule mpango ambao umezinduliwa, mpango wa Kitaifa ili tuweze kutekeleza pamoja na tuhakikishe kwamba wananchi wanazalisha mboga na matunda ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa nne ni kwenye sekta ya mifugo na uvuvi. Nitazungumzia pia suala la utafiti kwenye hii sekta ya mifugo na uvuvi. Pale mifugo shirika linalo-deal na utafiti pale linaitwa TALIRI, kwenye mwaka wa 2021 walipokea Shilingi Milioni 522.5. Hizi pesa ni ndogo sana kwa watafiti wa mifugo kwamba hii pesa Milioni 500 na tunategemea tupate kitu kikubwa kwa hawa watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAFIRI, watafiti wa samaki walipokea Shilingi Bilioni 1.7 mwaka huohuo ambao nimeutaja, angalau siyo mbaya sana lakini wenzao wa TARI mwaka huohuo walipokea Shilingi Bilion 11. Nashauri kwenye mpango huu Serikali ihakikishe kwamba hizi taasisi za utafiti za mifugo na uvuvi zinapatiwa fedha za kutosha ili waweze kutekeleza azma yao ya kuzalisha nyama ya kutosha, waweze kuzalisha ngozi za kutosha, maziwa ya kutosha, kuku wa broiler wa kutosha na samaki wa kutosha. Tusipofanya hivyo tutakuwa hatuwatendei haki na tutakuwa tunawalaumu bure tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kwenye hii sekta ya uvuvi ni meli ya kufanya utafiti. Tuseme ukweli hawa watu wana-operate katika hali ngumu sana. Meli ya kufanya utafiti hawajanunuliwa ilishaagizwa lakini mpaka sasa hivi haijapatikana. Ninaiomba Serikali tujitahidi angalau tuwapatie hawa watu meli moja ili waweze kufanya utafiti kwenye Bahari Kuu, kule nina hakika kuna fedha nyingi sana ambazo Taifa linaweza kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri walio kwenye Ofisi yake kwa jinsi wanavyotekeleza majukumu yao. Nimpongeze yeye binafsi kwa kuwasilisha vyema hotuba ya bajeti na kwa usimamizi mzuri wa shughuli zote za Serikali.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye hatma ya wavulana kielimu kutokana na uwepo wa shule chache zilizojengwa maalumu na mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wavulana.
Mheshimiwa Spika, hapa nchini Tanzania mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha za kujenga shule moja maalumu ya sayansi kwa ajili ya wasichana katika kila mkoa. Ujenzi huu haujafanyika kwa wavulana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na upendeleo nilioeleza hapo juu, hapa nchini kuna uwekezaji mkubwa sana kwenye shule bora za wasichana. Uwekezaji mkubwa umefanywa na taasisi za dini na watu binafsi. Kutokana na uwekezaji huu, shule hizi za wasichana zina ufaulu mzuri sana kwenye matokeo ya kidato cha nne na sita. Mfano wa shule bora binafsi zenye ufaulu mkubwa ni pamoja na St. Fransis Girls - Mbeya, Barbo Johansson Model Girls - Dar es Salaam, St. Christian Girls - Tanga, Loretto Girls - Mwanza, Samaritan Girls Secondary School - Shinyanga, Anwarite Girls Secondary- Kilimanjaro, Precious Blood - Arusha, Bethel Sabbs Girls Secondary School, St. Theresa of Avila Girls Secondary, Hekima Girls Secondary School - Kagera, Visitation Girls School - Kilimanjaro, Kandoto Science Girls Secondary - Kilimanjaro, Marian Girls - Pwani, Feza Girls - Dar es Salaam, Kibosho Girls Secondary - Kilimanjaro, Mazinde Girls - Tanga, Kifungilo Girls - Tanga, St Mary’s High School - Dar es Salaam, John the Baptist Girls Secondary School - Dar es Salaam, Kunduchi Girls Islamic High School - Dar es Salaam, Bethsaida Girl’s Secondary School - Dar es Salaam, St. Marie Eugenie Girls Secondary School - Kilimanjaro, Joyland Girls Secondary School - Kilimanjaro, St. Christina Girls Secondary School - Tanga na St. Clara Girls Secondary School - Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, idadi ya shule binafsi za wasichana ni kubwa, na hapo juu nimetoa mifano michache.
Kwa upande wa wavulana, uwekezaji wa kimkakati ni mdogo sana. Shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na taasisi na watu binafsi zenye majina makubwa ni chache. Ninazoweza kuzitaja ni zile za seminari, Marian Boys, Feza Boys, Tengeru Boys na nyingine chache ambazo sijazitaja.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, idadi kubwa ya wasichana wanaosoma katika hizi shule binafsi nilizotaja hapo juu hufaulu vizuri na wengi wao hufanikiwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini. Kwa kifupi, mazingira ya kuwasaidia wasichana kujiendeleza zaidi ni mazuri kuliko ya wavulana.
Mheshimiwa Spika, tusipochukua hatua za kimakusudi kusaidia watoto wa kiume kwa kuwajengea shule maalumu, huko mbele ya safari uwepo wao katika vyuo vya elimu ya juu utakuwa na walakini. Dalili za awali zinaonesha kuwa idadi ya wavulana wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu inapungua na ya wasichana inaongezeka.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo ya hapo juu, ninaishauri Serikali yafuatayo; kwanza ijenge shule maalumu za sayansi za wavulana kila mkoa kama walivyofanya kwa wasichana na pili, iwasiliane na wadau wa maendeleo na kuwashawishi wajenge shule maalumu zenye hadhi kubwa kwa ajili ya wavulana.
Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo, wavulana watakuwa wametendewa haki kama ilivyofanyika kuwajengea watoto wa kike shule maalumu katika kila mkoa.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula na Naibu Waziri Ndugu Ridhiwani Kikwete pamoja na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitachangia kuhusu migogoro ya umiliki ardhi katika Jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu la Moshi Vijijini kuna migogoro ya umiliki wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji katika Kata za Mabogini (Kijiji cha Mserekie) na Arusha Chini (Mikocheni na Chemchem) zilizoko maeneo ya tambarare.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro hii imeshasababisha madhara makubwa ikiwemo vifo na uharibifu mkubwa wa mali kama mazao ya wakulima. Mpaka sasa Serikali ya Wilaya na Mkoa haijaweza kupambana na changamoto hii, kwani tatizo hili linajirudia mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya wakulima na wafugaji jimboni kwangu inasababishwa na uhaba unaoendelea kukua wa rasilimali ardhi. Kutokana na hali hii, wakulima wamekuwa wanafungua mashamba kwenye maeneo ya wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro hii kwa kiasi kikubwa husababishwa na yafuatayo; kwanza Serikali haijayapima maeneo ya wafugaji na wakulima na kuyamilikisha kwa wahusika kwa kutoa hati za kimila na za Serikali.
Pili, kubadilika kwa tabia nchi kunakopelekea malisho kukauka na kusababisha uhaba wa chakula cha mifugo na kuwafanya wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima; na tatu, kupanuka kwa shughuli za kilimo na makazi ya watu ambapo maeneo ya ufugaji yamepungua.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hii ninaishauri Serikali kama ifuatavyo; kutokana na migogoro inayoendelea, kuna umuhimu wa Serikali kuingilia jambo hili na kuhakikisha kuwa maeneo husika yamepimwa na kumilikishwa rasmi kwa wahusika. Pia Serikali iharakishe zoezi hili kwa kutumia mifumo ya hati za kimila zinazotambuliwa kisheria na baadaye wapewe hati za Serikali za kumiliki ardhi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mazingira ya Kitanzania, ninaishauri Serikali ipitie sera za umiliki wa ardhi zenye utata zinazoweza kuchochea migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Sera nzuri na rafiki itasaidia kutoa haki bila malalamiko.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali, Wizara za sekta husika (Ardhi, Kilimo na Mifugo na Uvuvi) zishiriki kikamilifu kwenye zoezi hili na kila Wizara itenge bajeti ya kusaidia kupima ardhi na kushughulikia changamoto hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia katika ripoti hii na ninachangia kama Mjumbe wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo ni siku ya mwisho ya mwezi Januari, na kuna Waheshimiwa Wabunge hatujaonana, naomba kwanza niwatakie Heri ya Mwaka Mpya kwa sababu najua sijachelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitachangia kwa uchungu sana suala moja nyeti ambalo ni uharibifu wa vyanzo vya maji na athari zake. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameshachangia mambo mengine kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, mimi ngoja nijikite kwenye uharibifu wa vyanzo vya maji na athari zake.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja ya ushauri wote ambao kamati imetoa. Nchi yetu ya Tanzania tuna baraka kubwa sana, tumejaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji. Tuna mito mingi, maziwa, chem chem na tuna maji mengi ambayo tumeambiwa na Wizara ya Maji kwamba yako chini ya ardhi. Rasilimali maji hizi ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku. Tusipokuwa waangalifu kuhakikisha kwamba tuna tunza na kuchunga rasilimali maji hizi, huko mbele ya safari tutapata shida kubwa sana kwa sababu hatutaweza kuzalisha chakula, hatutapata maji ya kunywa na kadhalika na kadhalika, athari ziko nyingi sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kutokana na umuhimu wa maji kwenye hizi sekta ambazo tunazisimamia ni umuhimu sana sana kutunza vyanzo vya maji ili tuhakikishe tunapata maji na hasa tukizingatia kwamba sasa hivi kuna mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea. Uharibifu wa vyanzo vya maji umekithiri katika maeneo mengi nchini kwetu na uharibifu huu umeshasababisha matatizo makubwa kwenye mambo mbalimbali kama vile uzalishaji wa umeme, wote ni mashahidi kwamba kulikuwa na katakata ya umeme hapa nyuma, ni kutokana na upungufu wa maji katika vyanzo vyetu vya maji.
Mheshimiwa Spika, uharibifu huu unatokana na nini hasa? Uharibifu huu tunafanya sisi wenyewe binadamu. Binadamu sisi ndiyo vyanzo vya uharibifu wa hivi vyanzo vyetu vya maji ambapo watu kwa kujua kabisa au kwa makusudi wanakata miti bila kuzingatia sheria. Baada ya kukata hii miti, tunapata athari kubwa sana za upungufu wa maji ambayo tungeyatumia kwenye shughuli nyingine kama vile za kilimo, kuwapa ng’ombe maji wanywe, kupata maji ya kunywa majumbani pamoja na shughuli za uvuvi.
Mheshimiwa Spika, huku kukata miti ambako kunaendelea katika maeneo mengi ya nchi hii kumeshasababisha mabadiliko ya tabianchi ambapo tunajionea wote. Ukienda kwa mfano kule Kilimanjaro, ule mlima sasa hivi uko uchi kabisa. Theluji imekwisha pale mlimani na kama nilivyosema awali kwenye maeneo mengi kwa kuwa tunakata kata miti sana, maji yamepungua na nimeshasema athari ambazo tumeshajionea hivi karibuni. Ni sasa hivi tu mvua zimeanza ndiyo tumeanza kujinasua na matatizo ya ambayo yapo.
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, kule Dar es Salaam mliona wenyewe crisis ambayo ilitokea. Jiji la Dar es Salaam ambalo ndiyo jiji letu kuu la biashara, ilikuwa hamna maji na watu walipata shida kubwa sana. Tukubaliane Waheshimiwa Wabunge wote huko tulikotoka tulikuwa na crisis ya maji hata kule Kilimanjaro pamoja na kwamba tuna maji mengi kwenye mito lakini kulikuwa na mgao wa maji na hii ilitokana na kuharibu vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pale Dar es Salaam shida kubwa ilikuwa ni matumizi mabaya yaani utunzaji mbaya wa Bonde letu la Mto Ruvu. Kumekuwa na activities za binadamu ambazo zimeharibu Bonde la Mto Ruvu na Pangani na maji hayakufika Dar es Salaam na tumeona shida ambayo ilitokea pale. Kama tunataka tuwe salama, niiombe Serikali chonde chonde tuhakikishe tunatunza vyanzo vya maji na kwenye kamati yetu tumesema mambo mengi ya kufanya lakini nitashauri vitu vichache.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali kitu cha kwanza cha kufanya, tumeshapitisha Sheria ya Kutunza Vyanzo vya Maji ya Mwaka 2022. Niiombe Serikali iajiri wanasheria wa kutosha katika mabonde yote tisa, tuwapatie zana zote muhimu waende wakapambane na huu uharibifu wa kukata miti ili ile sheria itekelezwe. Mtu yeyote anayeharibu vyanzo vya maji achukuliwe sheria kwa hiyo, ushauri wangu wa kwanza ni kwamba Serikali iboreshe vitengo vya sheria kwenye mabonde yote ili hawa wanasheria waweze kufanya kazi na vyanzo vyetu vya maji viwe salama na sisi wote tuwe salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa pili kwa Serikali, Serikali za Wilaya na Serikali za Mikoa, maji ni suala la Usalama wa Taifa na tusicheze na suala la maji kabisa. Ninashauri hizi Serikali za Wilaya na za Mikoa na za Kata ikiwezekana, zile Kamati za Usalama za haya maeneo zijihusishe kikamilifu kuhakikisha kwamba tunatunza vyanzo vya maji. Wawe wanafanya inspection from time- to-time wahakikishe kwamba vyanzo haviharibiwi na mahali ambapo wameharibu, zichukuliwe hatua za kisheria za kuwapeleka hawa watu mahakamani.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa pili waswahili wanasema mtoto wako ukitaka asife kama kuna mchawi karibu mpe yule mchawi akusaidie kumtunza yule mtoto. Mimi nashauri Serikali ianzishe program muhimu kabisa ya kufundisha wananchi ambao wako kwenye vile vyanzo vya maji, umuhimu wa kutunza hivi vyanzo na washirikishwe kikamilifu. Kwa hiyo, elimu itolewe na Serikali ili wananchi watunze hivi vyanzo vya maji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele imeshagonga ya pili Mheshimiwa.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kwa kumpongeza sana Waziri wetu Mheshimiwa Innocent Bashungwa pamoja na Manaibu wake wawili Mheshimiwa Ernest Silinde na Mheshimiwa Dkt. Dugange kwa kazi nzuri na kubwa wanaoifanyia hii nchi yetu. Ofisi ya Rais TAMISEMI hii Wizara wanayoiongoza hawa ndugu zetu ni ofisi ambayo inatoa huduma kubwa sana katika nchi yetu, inafanya kazi ambazo zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo sababu wamepata bajeti kubwa kwenye bajeti hii ya 2022/2023 watapata trilioni 8.77 ambayo ni sawa na asilimia 21 ya bajeti yote ya nchi hii. Kwa hiyo, ukweli vijana chapeni kazi. Niwapongeze pia Katibu Mkuu, na Manaibu Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye hoja zangu za leo na nitachangia kwenye sekta ya afya kwenye Jimbo langu barabara na elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Bungeni nimekuwa ninasimama mara nyingi nikiwa na agenda ya kuiomba Serikali tujengewe hospitali ya Wilaya na nichukue fursa hii rasmi kuishukuru sana Serikali kwa sababu tayari wameshatenga shilingi milioni 500 na kazi ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya kule kwenye Jimbo langu Moshi DC imeshaanza, kwa hiyo naishukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nimshukuru sana Mkurugenzi wa Maendeleo wa Moshi DC huyu alikuwa very fair alipeleka barua Kata zote 32 za Halmashauri yetu walioleta barua yenye vigezo wamechagua Kata mbili ambazo zilikidhi vigezo vya kujenga Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hospitali hii inajengwa kwenye Kata ya Mabogini na tunaishukuru sana Serikali. Pamoja na shukrani zangu kwa Serikali bado niseme tu kwenye Jimbo la Moshi Vijijini tunachangamoto kubwa sana ya miundombinu ya vituo vya afya. Katika Kata zangu 16 ni Kata Tatu tu zina vituo vya afya na kuna upungufu kama asilimia 81 hivi kwamba asilimia 81 ya maeneo hayana vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-summarize hapa, nimeomba vituo vya afya vya kimkakati, nilikuwa nimeomba nijengewe kituo cha afya kwenye Kata ya Arusha Chini, Kata ya Old Moshi Mashariki na Kata ya Kibosho Kirima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vituo 252 ambavyo unajenga nchi nzima Mheshimiwa Waziri haukunipa hata kimoja kwa hiyo naomba unifikirie kama kutakuwepo na namna hizi Kata zangu za kimkakati hii asilimia 81 ili ipungue kidogo na sisi tupandepande wananchi wangu wafurahi. Katika Jimbo langu pia kuna zahanati ambazo zimeshakidhi vigezo vya kuwa vituo vya afya niombe kuna zahanati ya Lima ambayo ipo Kibosho kati, hii ilijengwa na msamaria mwema akaweka karibia kila kitu kipo kwa hiyo tunaomba ipandishwe hadhi iwe kituo cha afya ili kupunguza huu ukakasi wa vituo vya afya ambao uko kwenye Jimbo langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna zahanati nyingine kwenye Kata nyingine kwa mfano zahanati ya Shiha katika Kata ya Kimochi, zahanati ya Kindi au tunaita Mary Bennett Clinic na zahanati ya Uru Kaskazini katika Kata ya Uru kaskazini hizi zipo tayari kupandishwa kuwa vituo vya afya, tunaomba Wizara itusaidie ili haya maeneo nayo yapandishwe hadhi tupate vituo vya afya vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kuhusu barabara. Kwanza niishukuru sana Serikali ya Mama Samia kwa kutupatia Bilioni 1.5 kufanya marekebisho ya barabara za Moshi Vijijini ambazo zina changamoto kubwa sana wakati wa mvua, pamoja na kupata fedha hizi lakini bado kuna changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri na timu yote kwamba waangalie kwa namna ya pekee zile pesa ambazo mmeleta mpaka sasa hivi mikataba ilisainiwa tangu Desemba lakini mpaka sasa hivi wamefanya grading tu katika barabara kama sita hivi ambazo tulipangiwa zitengenezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba mfuatilie tuhakikishe kwamba zinakamilika kwa kiwango cha changarawe kama tulivyopewa ahadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Noah Lemburis…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Prof. Patrick Alois Ndakidemi kwa mchango wako.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza sana Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda na Naibu wake Mheshimiwa Omari Kipanga na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya kwenye kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, nitachangia kuhusu mkanganyiko uliopo kwenye matumizi ya GPA ya 3.8 katika vyuo vikuu vya Serikali vilivyo chini ya TCU.
Mheshimiwa Spika, kwenye kuajiri walimu wa vyuo vikuu, vigezo vinavyotumika ni vya kutumia GPA za waombaji. Mwongozo uliotolewa na TCU umeelekeza kwamba mtu anayeomba kazi ya kufundisha ni lazima awe na minimum GPA ya 3.5 kwenye degree ya kwanza, na minimum GPA ya 4.0 kwenye degree ya pili.
Mheshimiwa Spika, ninavishukuru vyuo binafsi kwani vinafuata mwongozo huo wa TCU, lakini inasikitisha kuona kwamba kwenye vyuo vya Serikali, kuna utaratibu unaokiuka maelekezo ya TCU na kuwanyima Watanzania haki ya kuajiriwa katika vyuo hivi.
Mheshimiwa Spika, katika vyuo vya Serikali, mtu anayeomba kazi ya kufundisha ni lazima awe na minimum GPA ya 3.8 kwenye degree ya kwanza na minimum GPA ya 4.0 kwenye degree ya pili. Mwongozo wa TCU umepanga, first class 4.4 – 5.0, upper second 3.5 – 4.3, lower second 2.7 – 3.4, na pass 2.0 – 2.6.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu hapa ni kwamba hii GPA ya 3.8 inayotumiwa na vyuo vya Serikali imetoka wapi? Kwa grading system ya TCU iliyoko hapo juu, GPA inayoanza na GPA 3.5 ni cut off point ya upper second, ndiyo maana TCU wakaelekeza hiyo itumike.
Mheshimiwa Spika, kwenye hiyo GPA 3.8, hii wameiweka kwa vigezo gani? Kwa nini isiwe GPA 3.6, 3.7 au 3.9. Kwangu mimi naona huu ni ukiritimba na tunawanyima nafasi za ajira vijana wetu wanaotaka kuajiriwa Serikalini.
Mheshimiwa Spika, mtu aliyesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, SUA, Mzumbe vyenye walimu wabobevu na miundombinu bora ya ufundishaji na akapata GPA ya 3.5 anaweza akawa na uwezo mkubwa kuliko aliyetoka chuo “x” na “y” aliyepata GPA ya 3.8 chenye uhaba wa walimu.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ifanye marekebisho na kutumia GPA ya 3.5 kwa vyuo vyote ili kutoa haki sawa za kuajiriwa katika vyuo vikuu vya Serikali na binafsi. Hii itafanya wanaotaka kuhama kutoka vyuo binafsi wakiwa na GPA ya 3.5 hadi 3.7 kwenye degree ya kwanza wapate nafasi za kufundisha. Kwa kufanya hivi, tutaondoa ubaguzi unaojitokeza kwenye vyuo vya Serikali.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora na Naibu wake pamoja na watendaji wa Serikali katika Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye; kwanza umuhimu wa Serikali kuanzisha mfuko maalumu wa pension kwa sekta isiyo rasmi ya wakulima, wafugaji na wavuvi; pili umuhimu wa Serikali kupitia upya sheria inayowafanya maprofesa kustaafu wakiwa na miaka 65 na kutokupata mikataba maalumu ya kuendelea kufundisha; na tatu, wakuu wa idara na taasisi mbalimbali kukataa kupitisha barua za watumishi wanaoomba kuhamishwa kutoka vituo vyao vya kazi kwa sababu maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu asilimia 65 ya Watanzania wako kwenye sekta za uzalishaji za kilimo, mifugo na uvuvi. Kundi hili huishi maisha ya shida sana wanapofikia uzee na kukosa nguvu za kuendelea kujipatia kipato. Kwa kuwa watu hawa wako kwenye mifumo ya uzalishaji na hujipatia kipato, ni vyema Serikali ikafikiria namna ya kuanzisha mfuko maalum wa pension ukisaidiwa na makato maalum kutoka kwenye mauzo ya mazao kwa makundi haya ili yaingie kwenye mfuko wao maalum wa pension.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili likiratibiwa vyema litakuja kusaidia makundi haya katika maisha yao ya uzeeni watakapokuwa hawana tena nguvu ya kufanya kazi na kujipatia kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo hili likifanikiwa na likisimamiwa vizuri, huko mbele ya safari wazee wetu waliostaafu katika kazi za kilimo, ufugaji na uvuvi hawatakuwa tegemezi wala ombaomba kwenye jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vyuo vyetu vikuu vya Serikali, kuna changamoto kubwa ya tatizo la rasilimali watu likiwa limesababishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha Serikali kubadilisha utaratibu wa maprofesa kuendelea kufundisha kwa mikataba maalum hadi wanapofikisha umri wa miaka 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa miaka michache iliyopita, zaidi ya maprofesa 91 waliondoka katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kati ya Januari, 2016 na Desemba, 2020; maprofesa 111 waliondoka kwenye utumishi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, hakuna profesa hata mmoja wa somo la hisabati tangu aliyekuwepo alipoondoka, hapajakuwepo na mrithi wa kusaidia kusimamia research za mahesabu katika ngazi ya uzamivu. Hata kwenye soko la ajira si rahisi kuwapata wataalam wenye vipaji hivi na vyuo vyote vya Serikali nchini vinakabiliana na changamoto kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya rasilimali watu vyuo vikuu Tanzania inasababishwa pia na masharti magumu ya kuajiri wataalam kutoka nje ya Tanzania. Kuajiri wataalam kutoka nje kwenye maeneo ya kimkakati ni muhimu ili kutusaidia kwenye kukuza rasilimali yetu, na kutuunganisha na mifumo ya kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa vibali huchukua muda mrefu na husababisha walengwa kutoka nje kubadili mawazo na kuacha kuja kufanya kazi Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imejitokeza tabia ya wakuu wa idara na taasisi mbalimbali za Serikali kukataa kupitisha barua za watumishi wanaoomba kuhama na kwenda kufanya kazi kwenye sehemu tofauti kwa manufaa ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya mtumishi kuomba kuhama na kwenda kulihudumia Taifa sehemu yoyote hapa nchini anapoona ataongeza tija na maendeleo ya Taifa. Uamuzi wa mwisho wa kutoa ruhusa ya kuhama hutolewa na Katibu Mkuu - Utumishi na Utawala Bora. Wajibu wa mkuu wa idara au taasisi ni kupitisha barua ikiwa na mapendekezo yake na si kuzuia barua isifike ngazi za juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuelezea changamoto za hapo juu, naishauri Wizara yafuatayo;
kwanza Serikali ianzishe mfuko maalum wa pension kwa sekta zisizo rasmi za wakulima, wafugaji na wavuvi.
Pili, Wizara ya Utumishi na Utawala Bora itoe vibali vya kuajiri wanataaluma wa kutosha kuendana na idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa. Hii ni pamoja na kuajiri wataalam kutoka nje katika maeneo ya kimkakati kama yale ya sayansi, uhandisi na hesabu.
Tatu, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora wapitie sheria na kuongeza umri wa maprofesa kutumika kwa mikataba uanzie pale wanapostaafu wakiwa na miaka 65 na waendelee hadi wanapofikisha umri wa miaka 75. Hii haina hasara kwa Serikali kwani wanapostaafu mishahara yao inakuwa bado iko kwenye ikama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwaandaa hawa wataalam, Serikali hutumia gharama kubwa sana. Tunapositisha huduma zao, vyuo binafsi huwachukua bila gharama na kuwatumia kuwajengea sifa, ilihali vile vya Serikali vinadorora.
Nne, Waziri wa Utumishi na Utawala Bora atoe maelekezo kwa wakuu wa idara na taasisi za Serikali watende haki ya kupitisha barua za watumishi wanaoomba kuhama kwenye vituo vyao ili wampe fursa Katibu Mkuu mhusika kutoa uamuzi wa mwisho. Napendekeza watakaokaidi hili wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, Naibu Waziri na wataalamu wa Wizara na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa sana kwenye kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kwenye suala la umuhimu wa kubadilisha sheria na kurudisha eneo la Half Mile kwa wakazi wa vijiji vilivyomo katika mipaka ya Mlima Kilimanjaro ili washiriki kikamilifu kutunza mazingira ya Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, Half Mile ni eneo lenye upana wa kati ya 0.5-0.8 ya mile. Eneo hili lilikuwa linatenganisha Mlima Kilimanjaro na makazi ya watu. Eneo hili kwa upande wa majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo linajumuisha vijiji 40.
Mheshimiwa Spika, wakoloni wa Tanganyika walitumia sheria kandamizi kujimilikisha ardhi ya wana Kilimanjaro na rasilimali za msitu wa Mlima Kilimanjaro na kuwapora wana Kilimanjaro haki yao ya kufaidi rasilimali zao za asili.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa 1941 wakoloni walianzisha Sheria ya Half Mile Strip kwa lengo la kuwapatia majirani wa msitu Kilimanjaro huduma za mazao ya misitu kama vile dawa za asili (ngesi), mboga za majani (mnafu) miti ya kujenga nyumba, kuni na majani ya ng’ombe.
Mheshimiwa Spika, tofauti na malengo ya kuanzishwa kwa eneo la Half Mile, kazi za kibinadamu zilisababisha uharibifu wa mazingira katika Half Mile na yale maeneo ya hifadhi kwa kukata miti, kupasua mbao, kuchoma misitu, kuchunga mifugo na kuendesha shughuli za kilimo ndani ya hifadhi. Hii ilitokana na kukosekana kwa usimamizi mahiri kutoka katika mamlaka husika Serikalini.Mheshimiwa Spika, baada ya uharibifu huu, Serikali ilisimamisha vijiji vyote 40 kutokutumia Half Mile Strip toka mwaka 2004, kwa sheria iliyoanza kutumika mwaka 2005. Hii ilitokana na kusainiwa kwa sheria ya kuziingiza Half Mile Strip za maeneo ya Moshi Vijijini na Rombo iliyotiwa sahihi na Marehemu Rais Mkapa tarehe 18/7/2005 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali tarehe 16.9.2005.
Mheshimiwa Spika, baada ya zuio hili, Serikali yetu iliondoa ile huruma ya wakoloni kwa Wana Kilimanjaro ya kutumia ile buffer zone ya Half Mile. Siku hizi hakuna cha Half Mile tena na ukikamatwa na maaskari wa KINAPA utakuwa na bahati mbaya sana.
Mheshimiwa Spika, wapiga kura wangu wamenituma niiombe Serikali ibadilishe sheria hii kwani baada ya kunyima watu wasitumie Half Mile, hii imesababisha matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira ya msituni Kilimanjaro kwa kupanuka kwa shughuli za kukata miti ndani ya msitu ikifanywa na maharamia; kuongezeka kwa wanyama waharibifu wa mazao kwenye mashamba ya wakulima kama nyani, ngedere na kima kuingia kwenye mashamba ya wanakijiji na kuharibu mazao.
Mheshimiwa Spika, kabla ya mwaka 2005 shughuli za wananchi kwenye Half Mile zilizuia wanyama kuingia vijiji vya mpakani na ilikuwa hakuna uharibifu wa mazao.
Mheshimiwa Spika, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Ali Mohamed Shein alipotembelea Mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2008 akiambatana na Waziri wa Maliasili Profesa Jumanne Maghembe wananchi walimweleza matatizo yaliyojitokeza baada ya Serikali kuunganisha eneo la Hifadhi la KINAPA na misitu ya hifadhi za asili.
Mheshimiwa Spika, baada ya ziara hiyo, Wizara ilikaa na kuiagiza TANAPA (kwa barua yenye Kumb Na. CAB. 315/ 484/01/A ya tarehe 22.1.2008 ya Waziri Profesa Maghembe kwenda kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, na barua Kumb Na. CJA.246/374/01/42 ya tarehe 27.2.2009 ya Katibu Mkuu Dkt. Ladislaus Komba kwenda kwa Mkurugenzi wa TANAPA) wachore ramani upya na kutenga eneo la Half Mile liwe nje ya Hifadhi ya KINAPA kama ilivyokuwa awali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maelekezo hayo hapo juu na kukumbushwa mara kwa mara na wadau wa maendeleo wa Mlima Kilimanjaro hadi leo ramani hiyo haijatoka na sheria hii kandamizi kwa wananchi wa vijiji 40 vya mpaka na Mlima Kilimanjaro bado inawanyanyasa.
Mheshimiwa Spika, sheria kandamizi kama hii si nzuri na zinasababisha migogoro isiyo ya lazima baina ya wananchi na Serikali yao na uhifadhi wa mlima unawatenga wananchi wa vijiji jirani.
Mheshimiwa Spika, kama mwakilishi wa wananchi, hata mimi naikataa kabisa sheria kandamizi kwa wapiga kura wangu na ninamwomba Waziri Jafo amshauri Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan aliangalie jambo hili kwa jicho la huruma kama alivyoelekeza Makamu wa Rais mwaka 2008 ili wananchi wawe sehemu ya kutunza mlima na kuzuia majangili wasiingie mlimani kukata miti na kuharibu mazingira ya Mlima Kilimanjaro. Wananchi wanaoishi vijiji vya mpakani wakielekezwa na kukabidhiwa maeneo ya kulinda, wanaweza wakawa walinzi bora bila hata kutumia bunduki.
Mheshimiwa Spika, sheria ikibadilishwa, Half Mile Strip inaweza kutumika kwa mafanikio makubwa chini ya usimamizi wa Serikali Kuu, Serikali ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji na kusaidia wananchi wa vijiji husika kuutunza mlima na kuboresha mazingira yake; kuwapatia wananchi huduma na kuinua uchumi wa wananchi, Wilaya, Mkoa na Taifa.
Mheshimiwa Spika, sheria ikibadilishwa, wananchi washauriwe kupanda miti ya muda mfupi kama cyprus, pine na mikaratusi na aina nyinginezo zinazokua haraka kwa ajili ya nguzo za umeme, nguzo za ujenzi wa nyumba zikiwemo ghorofa, miradi kama hii iko Iringa. Rais akiruhusu hili, nchi nzima itanufaika kwani Kilimanjaro ina miundombinu bora ya kusafirisha hizi bidhaa na kuzisambaza zinakohitajika.
Mheshimiwa Spika, kama hatua stahiki hazitachukuliwa mapema, hali itakuwa tete sana miaka michache ijayo, na mazingira ya Mlima Kilimanjaro huenda yakaharibika zaidi.
Mheshimiwa Spika, KINAPA hawana watumishi wa kutosha wa kuulinda mlima na kupanda miti mingi ya kutosheleza kulinda mazingira ya mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro na Naibu wake Mheshimiwa Godfrey Pinda na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kuhusu uwepo wa sheria iliyo kwenye GN. 269 ya Aprili, 2020. Sheria ilitoa kipindi cha mpito cha miaka miwili kuitekeleza na sasa iko kwenye hatua za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, sheria hii inayokataza uwepo wa maduka ya dawa mita 500 kuzunguka Hospitali za Serikali kwa hisia kwamba baadhi ya wataalamu wa Wizara ya Afya wanaihujumu Serikali kwa kuiba dawa na kuziuza maduka ya karibu au kuwa na maduka karibu na hospitali za Serikali na huishia kuyakuza maduka yao.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu alitoa agizo la kuondolewa kwa maduka yote ya dawa ambayo yapo mita 500 ndani ya eneo la hospitali za Serikali kwa kile kinachodaiwa kuhujumu upatikanaji wa dawa katika hospitali hizo. Tangazo hili lilisababisha taharuki kubwa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa mawazo yangu, sheria hii ilipotungwa haikuzingatia maslahi ya wagonjwa wa Kitanzania na wamiliki wa maduka binafsi ya dawa yaliyo karibu na hospitali. Maduka haya yapo kusaidia upatikanaji wa dawa kwani Serikali yenyewe bado haina uwezo wa kusambaza dawa zote na vifaa tiba kwa wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, hii sheria ina mapungufu makubwa sana. Mimi naona hakuna mwananchi anayependa kwenda nje ya hospitali kutafuta dawa au vifaa tiba bali changamoto za uhaba wa madawa na vifaa tiba zilizopo ndani ya hizo hospitali ndio zinafanya waende nje.
Mheshimiwa Spika, madhumuni ya kuanzisha sheria hii yanakinzana kabisa na uhalisia uliopo. Tatizo kubwa lililopo Wizara ya Afya ni katika mfumo mzima wa ugavi, usambazaji na usimamizi wa dawa, na si uwepo wa maduka ya watu binafsi ya dawa karibu na hospitali za Serikali.
Mheshimiwa Spika, watumishi wasio waaminifu wakiiba na kutoa dawa nje ya hospitali, dawa inaweza kwenda popote nje ya hospitali na hata mikoa ya mbali kwa haraka kwa kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo bodaboda.
Mheshimiwa Spika, ninachokiona, si kweli kwamba maduka yaliyo karibu na hospitali ndio wateja wa wizi wa dawa kutoka hospitali za Serikali. Kutokana na ukweli huu napendekeza kwa Waziri wa Katiba na Sheria kwa kushauriana na Waziri wa Afya sheria hii ifutwe kwani kwa kufanya hivyo tutawapunguzia wananchi adha ya kutafuta dawa na vifaa tiba wanazoandikiwa kwenda kununua nje ya hospitali za Serikali; Wizara ya ya Katiba na Sheria itambue kwamba Wizara ya Afya ilitoa vibali mbalimbali vya kuanzisha maduka ya dawa. Kufunga biashara zao kutasababisha hasara kubwa kwa hawa wawekezaji wazalendo na kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na kodi wanazolipa; maduka ya watu binafsi ya dawa hasa yale yaliyo karibu na hospitali husaidia upatikanaji wa dawa kirahisi kwani Serikali yetu yenyewe bado haina uwezo wa kutoa dawa zote na vifaa tib ana kufuta hii sheria kutaonesha hawajali wafanyabiashara na wawekezaji wa biashara ya dawa na vifaa tiba hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya kulinda usalama wa raia.
Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu utalenga kwenye zoezi la kusitisha ubandikaji wa bima katika vioo vya magari ambayo ililetwa na kanuni ya mwaka 1979 ikiitwa The Display of Road License and Evidence of Motor Vehicle Insurance Regulation, GN 79 of 1979.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ilielekeza kwamba kuanzia Aprili Mosi, 2021 ukataji wa bima kwa vyombo vya moto ufanyike bila mteja kubandika stika kwenye kioo cha gari kama ilivyozoeleka na badala yake mteja hupewa namba ya stika ya kielektroniki (e- sticker).
Mheshimiwa Spika, mteja anakapokata bima hupewa namba ya stika ya kielektroniki, risiti ya malipo EFD, hati ya bima pamoja na mkataba wa bima.
Mheshimiwa, lengo la uboreshaji huu ilikuwa na nia ya kupata huduma haraka, kudhibiti upotevu wa mapato na uhalifu unaoweza kufanywa na watu wasio waaminifu.
Mheshimiwa Spika, kabla ya mabadiliko haya, hapo zamani kabla ya mambo ya teknolojia, njia pekee ya kujua uhai wa bima ilikuwa ni kupitia hiyo sticker iliyokuwa inabandikwa kwenye kioo cha gari. Askari akisimamisha gari hukagua uwepo wa sticker iliyo hai na kumruhusu asiye na kosa kuendelea au kumkamata aliyevunja sheria.
Mheshimiwa Spika, ujio wa matumizi ya bima mtandao ilitokana na uwepo wa makampuni yaliyokuwa yanatengeneza sticker fake na kuikosesha Serikali mapato na kuhatarisha usalama wa raia.
Mheshimiwa Spika, sticker hizi ilikuwa zinarahisisha ukaguzi wa trafiki na kumsaidia kiurahisi mwenye gari kujua bima yake inamaliza muda wake lini.
Mheshimiwa Spika, katika matumizi ya njia hii mpya ya kimtandao, madereva katika maeneo mengi ya nchi wamepata changamoto kwa sababu trafiki wa barabarani na TIRA hawajapeana mwongozo wa kutosha juu ya utaratibu mpya wa kutokubandika sticker, na ndio maana wanaoendelea kuumia ni baadhi ya wateja wenye magari.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu ninaishauri Serikali chini ya Mamlaka ya Bima na Polisi Tanzania wakae na kufanya yafuatayo; kwanza warudishe utaratibu wa zamani wa kubandika sticker za Bima ya Taifa kwenye vioo vya magari. Maeneo ambayo mifumo ya ukaguzi ya kielektroniki haisomi, madereva hupata bughudha na kusimama barabarani muda mrefu. Mara nyingine wameandikiwa faini pamoja na kwamba wamelipia bima kwa mfumo mpya.
Mheshiiwa Spika, pili, sheria za nchi zitumike kutoa adhabu kali kwa makampuni au watu binafsi watakaojihusisha na utengenezaji wa sticker fake.
Tatu, busara itumike ili usajili wa kielektroniki uwepo na pia iruhusiwe anayetaka sticker apewe na abandike kwenye gari lake. Mfumo wa kielektroniki ni muhimu sana kwenye kuhifadhi kumbukumbu sahihi za walipa bima.
Mheshimiwa Spika, nne, mafunzo maalumu ya namna ya kutumia mifumo hii ifanyike ili mabadiliko yaliyotokea yaeleweke pande zote na mwisho wa siku watumiaji wa chombo kama kalipia bima yake asipate usumbufu wa aina yoyote barabarani.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara (Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji) na Naibu wake (Mheshimiwa Exaud Kigahe) na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye sekta ya uwekezaji kwenye viwanda katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoa wa Kilimanjaro kihistoria ni mkoa ambao ulikuwa na viwanda vingi ambavyo vilichangia sana kuinua pato la wananchi wa mkoa huu na pato la Taifa kwa ujumla. Viwanda hivyo kwa sasa vingi vimefungwa kutokana na sababu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kiwanda kilichokuwa kimepata mafanikio makubwa sana ni kile kiwanda cha kukoboa mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Co. Ltd kilichopo Chekereni – Moshi, katika Kata ya Mabogini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki kiko kwenye eneo ambalo linazalisha mpunga mara mbili hadi tatu kwa mwaka. Kiwanda hiki hakifanyi kazi tangu Septemba, 2014. Kiwanda cha kukoboa mpunga kilikodishwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahawa (KNCU) na baada ya kushindwa kukiendesha, mkoa ulimshauri Msajili wa Hazina kukirudisha Serikalini ili atafutwe mwekezaji mwingine anayeweza kukiendesha. Tayari Msajili wa Hazina amerejesha kiwanda hiki Serikali tangu tarehe 18/10/2018, lakini bado hajapatikana mwekezaji na shughuli zimelala. Kutokuwepo kwa kiwanda hiki kumeondoa fursa ya wakulima kupata bei nzuri ya mpunga na ajira kiwandani kwa wana Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha pili kilichopo jimboni kwangu na hakifanyi vizuri ni kiwanda cha bidhaa za ngozi Msuni kilichopo Kata ya Uru Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki kinamilikiwa na Kamati ya Maendeleo Kata ya Uru Kaskazini (WDC). Kina uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali za ngozi kama viatu, mikoba na mikanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoomba mwaka jana, narudia tena kuiomba Serikali itume wataalamu wa TiRDO kwenye kiwanda hiki ili ushauri wa kitaalamu upatikane na kiwanda hiki kifufuliwe na kuunga juhudi za wana ushirika huu kwenye kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Moshi Vijijini ni maarufu sana katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Kama Serikali itakuwa na mikakati ya kuhamasisha uwekezajj wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao ya kilimo na mifugo, hii itasaidia kutengeneza ajira na kuongeza kipato cha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naishauri Serikali ifanye yafuatayo: -
Kwanza, Wizara itafute mwekezaji katika Kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Co. Ltd kilichopo Chekereni – Moshi, katika Kata ya Mabogini. Kiwanda hiki kinaweza kuwa ni chanzo cha kusafirisha nje mchele ulioongezwa thamani na kuwapatia wakulima kipato na Taifa kwa ujumla.
Pili, Vyama vya Ushirika vilivyopo Jimbo la Moshi Vijijini vihimizwe na kuhamasishwa kuwa na viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali ya kilimo na mifugo na kuyaongezea thamani ili kuzalisha bidhaa zinazotokana na kahawa, ndizi, mbogamboga, nafaka, mikunde, maziwa, asali, alizeti na mengine mengi.
Tatu, kama nilivyoomba mwaka jana, naomba tena Shirika la Utafiti wa Viwanda Tanzania (TiRDO) lishiriki kikamilifu kwenye kutoa ushauri wa kitaalamu kukifufua kiwanda cha bidhaa za ngozi Msuni kilichopo Kata ya Uru Kaskazini.
Nne, Serikali ianzishe programu maalumu itakayowashirikisha wadau muhimu wa viwanda kama vile TiRDO, SIDO, TCCIA, VETA na CTI ili watoe mafunzo ya kuhamasisha ujasiriamali wa viwanda Mkoani Kilimanjaro na hususani katika Jimbo la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda na Naibu wake Mheshimiwa Omary Kipanga pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara Profesa Eliamani Sedoyeka na Naibu Makatibu Wakuu Profesa James Mdoe na Profesa Carolyne Nombo na watendaji wengine wa Serikali katika Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye umuhimu wa Serikali kupitia upya sheria inayowafanya maprofesa kustaafu wakiwa na miaka 65 na kutokupata mikataba maalumu ya kuendelea kufundisha na pili, changamoto za utoaji wa mikopo kwa wanafunzi waliosoma shule binafsi wanaojiunga na vyuo vikuu Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika vyuo vyetu vikuu vya Serikali, kuna changamoto kubwa ya tatizo la rasilimali watu likiwa limesababishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha Serikali kubadilisha utaratibu wa maprofesa kuendelea kufundisha kwa mikataba maalumu hadi wanapofikisha umri wa miaka 70.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa miaka michache iliyopita, zaidi ya maprofesa 91 waliondoka katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine. Kati ya Januari 2016 na Desemba, 2020 maprofesa 111 waliondoka kwenye utumishi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela hakuna profesa hata mmoja wa somo la Hisabati tangu aliyekuwepo alipoondoka, hapajakuwepo na mrithi wa kusaidia kusimamia research za mahesabu katika ngazi ya uzamivu. Hata kwenye soko la ajira si rahisi kuwapata wataalamu wenye vipaji hivi na vyuo vyote vya Serikali nchini vinakabiliana na changamoto kama hii.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya rasilimali watu vyuo vikuu Tanzania inasababishwa pia na masharti magumu ya kuajiri wataalamu kutoka nje ya Tanzania. Kuajiri wataalamu kutoka nje kwenye maeneo ya kimkakati ni muhimu ili kutusaidia kwenye kukuza rasilimali yetu na kutuunganisha na mifumo ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa vibali huchukua muda mrefu na husababisha walengwa kutoka nje kubadili mawazo na kuacha kuja kufanya kazi Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika nchi za jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki, maprofesa wa Kenya na Uganda hustaafu wakiwa na miaka 70. Kutokana na uwepo wa maprofesa hawa kwenye mifumo ya ufundishaji na utafiti, vyuo vikuu vya Kenya na Uganda vina ubora wa kuzidi vile vya Tanzania katika orodha ya vyuo bora duniani.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ubaguzi wa kupata mikopo kwa wanafunzi wanaoomba mikopo kwa vyuo vikuu kutokana na shule walizosoma hata kama ufaulu wao unafanana. Wanafunzi waliosoma shule binafsi wamekuwa wakinyimwa mikopo kwa kigezo kwamba wana uwezo wa kifedha. Jambo hili ni la kibaguzi na sii halali.
Mheshimiwa Spika, wazazi wanaosomesha watoto wao shule binafsi si kwamba wana uwezo mkubwa wa kifedha bali hujinyima ili watoto wapate elimu bora.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuelezea changamoto za hapo juu, naishauri Serikali kufanya yafuatayo; kwanza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora wapitie sheria na kuongeza umri wa maprofesa kutumika kwa mikataba uanzie pale wanapostaafu wakiwa na miaka miaka 65 na waendelee hadi wanapofikisha miaka 75. Hii haina hasara kwa Serikali kwani wanapostaafu mishahara yao inakuwa bado iko kwenye ikama. Nchini Kenya maprofesa hustaafu wakiwa na miaka 70.
Mheshimiwa Spika, kuwaandaa hawa wataalamu, Serikali hutumia gharama kubwa sana. Tunapositisha huduma zao, vyuo binafsi huwachukua bila gharama na kuwatumia kuwajengea sifa, ilhali vile vya Serikali vinadorora.
Pili, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iwasiliane na Wizara ya Utumishi na Utawala Bora itoe vibali vya kuajiri wanataaluma wa kutosha kuendana na idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa. Hii ni pamoja na kuajiri wataalamu kutoka nje katika maeneo ya kimkakati kama yale ya sayansi, uhandisi na hesabu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Bodi ya Mikopo hutoa mikopo na si zawadi, naishauri Serikali kuondoa ubaguzi kwa wanafunzi wanaojiunga vyuo vikuu bila kuangalia shule alikosoma.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niungane na wenzangu kumpongeza sana Waziri wetu wa maji ndugu yetu Jumaa Aweso na Engineer Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, viongozi wa mamlaka za maji, RUWASA na wale wa mabonde kusema ukweli hawa watu wanafanyakazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa jinsi inavyoiangalia kwa jicho la huruma hii Wizara yetu ya Maji. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba vijiji wanapata maji kwa asilimia 85 na mijini asilimia 95. Mpaka sasa hivi vijijini tumeshafikisha asilimia 74.5 na mijini tumeshafikisha asilimia 86.5. Kwa hiyo naipongeza Serikali kwa jinsi inavyopeleka fedha za kutosha katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ilikuwa imetenga Shilingi Bilioni 785.9, na hadi kufikia mwezi Machi tulishapeleka asilimia takriban 77, bado asilimia 23 tu. Kwa hiyo, najua Serikali ikimalizia hii asilimia 23 iliyobakia Wizara itaendelea kufanyakazi nzuri; na kutokana na upatikanaji huu wa fedha, Jumaa Aweso na wenzake wanafanyakazi nzuri wanang’ara vizuri kabisa. Wamejitahidi kuhakikisha kwamba ile kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani wanaitekeleza kwa vitendo kwa sababu kuna fedha za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukubaliane kwamba takriban kila Mbunge hapa ana mradi mmoja au miwili ya maji. Kwa hiyo nitashangaa tunapopitisha bajeti ya Wizara hii; mimi ninawaomba kwa sababu mimi ni Mbunge wa Kamati inayoisimamia hii Wizara tupitishe ili Jumaa na wenzake wakafanye kazi vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusimamia Wizara hii tulitembelea miradi ya maji kukagua kama wanafanyakazi vizuri. Tukaenda katika mradi wa Kimbiji – Mpera huko Dar es Salaam tukatembelea mradi wa Mlandizi – Chalinze, tumeona maajabu, DAWASA wanafanyakazi nzuri; na tulipendekeza, Mameneja wengine waende kwenye maeneo hayo wakajifunze jinsi ya kufanyakazi kama yule wa DAWASA, nampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutembelea hii miradi lakini pia, katika hotuba ya Waziri ameonesha miradi ambayo imekamilika. Kwa mfano, kufikia mwezi wa Aprili miradi 303 ya vijijini ilikamilika, kuna miradi 127 iliyokuwa chechefu ameshakamilisha. Kuna miradi ya mijini 40 ambayo pia imeshakamilika. Yote hii ni kazi nzuri anayofanya Waziri pamoja na wenzake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka huu ameomba kupatiwa kiasi cha Shilingi Bilioni 657.9, na anategemea kukamilisha miradi na kutekeleza miradi mingi mipya ambayo kwa ujumla wake vijijini kuna miradi kama 1,029 yenye fedha nyingi ambazo ameonesha; mabwawa 15 na miradi ya mijini 175. Hii yote ni kazi nzuri ambayo Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inataka ifanyike ili akina mama wasipate shida ya maji. Kwa hiyo, nirudie tena kuwaomba Waheshimiwa Wabunge tupitishe bajeti ili Jumaa aendelee akafanye kazi pamoja na wenzake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nirudi kwenye Jimbo langu la Moshi Vijijini kwa sababu kuna changamoto kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata ambayo ninatoka ya Kibosho Kirima nikiri hapa kwamba Mbunge wenu huwa ninakwenda Jimboni kila nikitoka hapa, lakini mwaka mzima uliopita mwaka wote kwenye bomba langu pale nyumbani hakuna maji. Kwa hiyo najua una mipango mizuri naomba mtusaidie, ili mimi Mbunge wenu na wale wananchi wangu wapate maji ya kunywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Kibosho Kati ambaayo ina vijiji 14 kati ya Kibosho kati na Kibosho Okaoni watu wameongezeka sana na mradi wa zamani hautoshelezi mahitaji ya watu pale. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri uangalie hizi Kata mbili vijiji 14 ni watu wengi, ili tuboreshe ile miundombinu wapate maji ya kunywa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Kibosho Magharibi hapa kuna vijiji nane ambavyo havijapata maji. Kata hii kwa sasa hivi ilikuwa inapata maji kutoka eneo la Mheshimiwa Saashisha. Tunaiomba Wizara kwa jicho la huruma tutafute chanzo kwenye DC yetu, ili tuwaletee hawa watu maji ya kunywa nao wanufaike kama watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Mabogini kuna vijiji ambavyo tangu tupate uhuru vilikuwa havina hata maji ya mfereji kwa mfano, kule Umasaini. Niliuliza swali la nyongeza hapa bado narudia kukuomba Mheshimiwa Waziri kule Umasaini kule Remiti tuhakikishe tumepeleka maji ili wale wafugaji na wananchi wengine wapate maji ya kunywa.
Katika Kata ya Old Moshi Mashariki nakushukuru sana umenipa Shilingi milioni 400, Engineer Kija Limbe anajitahidi, lakini ninaomba, ikiwa ni pamoja na pale Kata ya Mbokomu, manunuzi myaboreshe ili hawa watu wapate maji ya kunywa na tuendelee kuisifia Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. Katika Kata ya Kimochi pia nashukuru tulipata Shilingi 500,000,000 kazi imeshaanza naomba tuchakarike ili hii miradi ionekane na watu wanufaike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Uru Kusini katika ripoti ya CAG alisema kwamba yale maji ni machafu na hayafai kwa matumizi ya binadamu. Mheshimiwa Waziri watu wameshaogopa kwa sababu CAG ameshaandika kwamba yale maji yana matatizo. Naomba mje muangalie ili tuangalie tutakavyowasaidia hawa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaushauri kidogo; mambo ni mengi nitapeleka kwa maandishi. Kwa kuwa changamoto kubwa kule Kilimanjaro imekuwa ni upatikanaji wa vifaa ninashauri muwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba, procurement inafanyika mapema miradi inasainiwa mapema ile ambayo haihitaji Force Account. Kwa hiyo, manunuzi yafanyike ili hao Mameneja wetu wa RUWASA na yule Mkurugenzi wa MUWASA apate vifaa kwa wakati kwa sababu shida kubwa tumeona ni kwenye ununuzi wa vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Afya Ndugu Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Godwin Mollel na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kuhusu changamoto zifuatazo nikianza na changamoto ya matibabu kwa wazee wenye ugonjwa wa kisukari na kuishia kukatwa viungo kama miguu. Pia sheria inayokataza uwepo wa maduka ya dawa mita 500 kuzunguka Hospitali za Serikali
Mheshimiwa Spika, wazee wanaougua ugonjwa wa kisukari na kukatwa miguu hupitia changamoto kubwa ya gharama kwa kutakiwa kulipia fedha nyingi kununua miguu ya bandia. Gharama za miguu miwili ni kubwa. Kuna mgonjwa amenilalamikia kuwa mwaka wa 2019 alinunua miguu bandia kwa thamani ya shilingi milioni tano ikiwa na silicone liner. Mgonjwa huyu huyu mwenye umri wa miaka 68 ameniambia kuwa mwaka huu wa 2022 anatakiwa alipe shilingi milioni tatu kuikarabati.
Mheshimiwa Spika, wazee waliokumbwa na ugonjwa huu na kukatwa miguu wanakuwa hawana uwezo wa kushiriki tena katika shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato. Kwa gharama hizi, huu ni mzigo mkubwa kwa wagonjwa wa kisukari na wanaoshindwa kulipia huishia kufa kwa mateso.
Mheshimiwa Spika, kuna sheria inayokataza uwepo wa maduka ya dawa mita 500 kuzunguka hospitali za Serikali. Uwepo wa sheria iliyo kwenye GN 269 ya Aprili, 2020 ulitoa kipindi cha mpito cha miaka miwili kuitekeleza, na sasa iko kwenye hatua za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, sheria hii inayokataza uwepo wa maduka ya dawa mita 500 kuzunguka hospitali za Serikali kwa hisia kwamba baadhi ya wataalamu wa Wizara ya Afya wanaihujumu Serikali kwa kuiba dawa na kuziuza maduka ya karibu au huwa na maduka karibu na hospitali za Serikali na huishia kuyakuza maduka yao.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu alitoa agizo la kuondolewa kwa maduka yote ya dawa ambayo yapo mita 500 ndani ya eneo la hospitali za Serikali kwa kile kinachodaiwa kuhujumu upatikanaji wa dawa katika hospitali hizo. Tangazo hili lilisababisha taharuki kubwa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa mawazo yangu, sheria hii ilipotungwa haikuzingatia maslahi ya wagonjwa wa Kitanzania na wamiliki wa maduka binafsi ya dawa yaliyo karibu na hospitali. Maduka haya yapo kusaidia upatikanaji wa dawa na vifaa vya tiba kwani Serikali yenyewe bado haina uwezo wa kusambaza dawa zote na vifaa tiba kwa wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, hii sheria ina mapungufu, mimi naona hakuna mwananchi anayependa kwenda nje ya hospitali kutafuta dawa au vifaa tiba bali changamoto za uhaba wa dawa na vifaa tiba zilizopo ndani ya hizo hospitali ndio zinafanya waende nje.
Mheshimiwa Spika, madhumuni ya kuanzisha sheria hii yanakinzana kabisa na uhalisia uliopo. Tatizo kubwa lililopo Wizara ya Afya ni katika mfumo mzima wa ugavi, usambazaji na usimamizi wa dawa na si uwepo wa maduka ya watu binafsi ya dawa karibu na hospitali za Serikali. Watumishi wasio waaminifu wakiiba na kutoa dawa nje ya hospitali, dawa inaweza kwenda popote nje ya hospitali na hata mikoa ya mbali kwa haraka kwa kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo bodaboda. Ninachokiona si kweli kwamba maduka yaliyo karibu na hospitali ndio wateja wa wizi wa dawa kutoka hospitali za Serikali.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu, napenda kuishauri Serikali yafuatayo; Serikali igharamie viungo bandia (kama miguu bandia) pamoja na ukarabati wake kwa wahanga wa kisukari waliokatwa miguu hususan wazee; gharama za viungo bandia kwa wagonjwa wa kisukari viingizwe kwenye bima ya afya; na Waziri wa Afya kwa kushauriana na Waziri wa Katiba na Sheria wafute sheria inayokataza uwepo wa maduka ya dawa mita 500 kuzunguka hospitali za Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo tutawapunguzia wananchi adha ya kutafuta dawa na vifaa tiba wanazoandikiwa kwenda kununua nje ya hospitali za Serikali; Wizara ya Afya itambue kwamba ilitoa vibali mbalimbali vya kuanzisha maduka ya dawa. Kufunga biashara zao kutasababisha hasara kubwa kwa hawa wawekezaji wazalendo na kuikosesha Serikali mapato; maduka ya watu binafsi ya dawa hasa yale yaliyo karibu na hospitali husaidia upatikanaji wa dawa kirahisi kwani Serikali yetu yenyewe bado haina uwezo wa kutoa dawa zote na vifaa tiba; na kufuta hii sheria kutaonesha hawajali wafanyabiashara na wawekezaji wa biashara ya dawa na vifaa tiba hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nianze moja kwa moja kwa kumpongeza sana Waziri wetu wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe na Naibu Waziri Mheshimiwa Antony Mavunde pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayoifanya. Watendaji hawa ni watu wenye busara kubwa sana wamekwenda kwenye meza ya majadiliano, wamekaa na Wizara ya fedha na wadau wengine wa maendeleo, wakashawishi mpaka bajeti ya kilimo ikaongezeka kutoka Shilingi 294,000,000,000 hadi Shilingi 751,000,000,000 sawa na ongezeko la takribani asilimia 155 na hii ni 1.8 percent ya bajeti yote ya Taifa, hongereni sana Waziri na wenzako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Wabunge wote, Wabunge wote huku ndani tulipiga kelele kwamba bajeti iongezeke na kwa namna ya pekee pia nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa kusikiliza kilio cha Wabunge wote na kwa sababu tumeona kabisa alikuwa na nia nzuri na bajeti imeongezeka, tunashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naendelea kuishauri Serikali kwamba tukienda na Azimio la Malabo tulitakiwa tuwe na angalau asilimia 10 ya Bajeti ya Taifa iende kwenye kilimo lakini hii 1.8 ni bado tungefurahi sana 4.1 trillion ambayo ndiyo asilimia 10 kufuatana na Azimio la Malabo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaendelea kusema kwamba bado ni muhimu Serikali iongeze hii bajeti kwasababu Kilimo kinaajiri asilimia 65 ya Watanzania wote, kilimo kinachangia asilimia 27 kwenye Pato la Taifa, kilimo kinachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni, kilimo kinatulisha watu wote nchi hii. Kwa hiyo naomba sana Serikali ifikirie kuongeza hii bajeti kama walivyokubaliana Marais kwenye lile Azimio la Malabo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo matatu ambayo ni suala la mbolea, maparachichi na nitaongelea changamoto za Jimboni kwangu ikishindikana nitaishia nitakapoishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu kitunguu na nyanya ilivyo ni muhimu sana katika kukaanga chakula na kuandaa chakula kizuri, mbolea ni component muhimu sana kwenye kuongeza tija uzalishaji kwenye Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu uliopita wote tumeona kwamba bei za mbolea zilikuwa kubwa kidogo, Wabunge wengi wamesema zilipanda kutoka Shilingi 50,000 kwa mfuko wa kilo 50 hadi kufikia Shilingi 150,000 kwenye baadhi ya maeneo, hili lilikuwa ongezeka kubwa kusema kweli karibia asilimia 200 ya nyongeza ya bei ya mbolea. Wakulima wengi walishindwa kununua mbolea na msimu huu hali ya kilimo sidhani kama itakuwa kama tulivyozoea kwasababu ya wakulima wengi watakuwa wamekwazika kwenye bei ya mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zipo sababu ni nyingi ambazo zimesababisha mbolea ikapanda bei, tunaona kule China waliweka lock down na Urusi wana vikwazo vya uchumi kwasababu ya vita wanavyopigana na Ukraine kwa hiyo vitu vingine ni nje ya uwezo wetu na hii imesababishia bei ya mbolea katika soko la dunia ikapanda na hata hapa Tanzania sisi hatujawa insolated tuna-face the same problem. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo pamoja na kwamba tuna matatizo lakini kama nchi ninashauri Serikali lazima ifanye vitu fulani ili tuondokane na hii changamoto. Ushauri wangu wa kwanza kwa Serikali Waziri katika hotuba yake amesema wana-plan kuwasiliana na Wizara ya Nishati ili kile kiwanda cha kutengeneza urea kiwepo, hili ni jambo muhimu sana. Kama intercom wame-invest Dola Bilioni 180 wakaweka kiwanda, jamani mbolea ni suala la usalama wa Taifa letu. Kama hakuna chakula hakuna usalama hapa, mimi ninaishauri Serikali kabisa kwa nia nzuri wakae chini waangalie namna ya ku-invest, gesi yetu ya asili tunayo tutumie ile gesi tutengeneze mbolea yetu wenyewe ili tujihakikishie usalama wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama China huwa zina-plan wanaweza wakawekeza hapa au tukanunua kutoka China tukatengeneza mbolea yetu wenyewe, kwa hiyo ushauri wangu wa kwanza kwa Serikali ni kuwekeza kwenye kutengeneza mbolea yetu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa pili, ninaishauri Serikali ihamasishe Vyama vya Ushirika wanunue mbolea kwa pamoja, (bulk procurement) kwa kufanya hivyo tutapunguza gharama za kuingiza mbolea nchini na bei inaweza ikashuka ikawa afadhali kidogo, tunaona kule kwenye Tumbaku wanafanya hivyo na mambo yanakwenda vizuri. Ushauri wangu wa tatu ni kuishauri Serikali ikiwezekana watoe bei elekezi ya mbolea ili kila mtu asiwe anajipangia tu bei ya mbolea lakini tuwe na bei elekezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa Nne ni kuishauri Serikali ikiwezekana kupitia utafiti tuwahamasishe wakulima wetu watumie mbolea za asili ili wale ambao hawataweza kununua mbolea watumie mbolea za samadi, mboji na kadhalika. Na ushauri wa mwisho kwenye hili suala la mbolea ni…
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Cherehani taarifa.
T A A R I F A
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninampa taarifa mzungumzaji kwamba kwenye upande wa tumbaku tunao umoja wa wakulima wa Tumbaku unaitwa TSJE ndio maana tunanunua mbolea kwa mfumo wa Pamoja, basi tungeomba na mazao mengine waweze kuunganisha umoja wao ili waweze kuagiza mbolea kwa pamoja na bei inapungua, ahsante sana.
MWENYEKITI: Unaipokea taarifa hiyo Mheshimiwa Profesa.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea kwa moyo mmoja. Ushauri wangu wa mwisho ni kuishauri Serikali ikiwezekana wakae wapunguze tozo ambazo siyo muhimu kwa wakati huu. Kwa mfano, tozo za ushuru za usafirishaji na uingizaji wa mbolea zikipunguzwa zinaweza zikatoa nafuu kwa wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kwenye zao la Maparachichi. Kama tulivyosikia watu wengi wanazungumzia maparachichi yanalimwa kwenye maeneo mengi hapa nchini, hii ni hanging fruits tukiitumia hii fursa vizuri ile target ya Mheshimiwa Waziri ya kuhakikisha kwamba mboga mboga na matunda yanachangia Dola Bilioni Mbili kwenye Pato la Taifa tutaifikia vizuri. Kwa hiyo ninaendelea kuishauri Serikali isimamie na isukume wahakikishe kwamba angalau tunaunda vikundi vya kupanda parachichi pamoja, wauze pamoja, tuvune pamoja ili tuweze kulijaza soko na kwa kufanya hivyo nawaomba wananchi wangu kwenye Jimbo la Moshi vijijini maeneo ya Uru, Old Moshi, Kibosho, mpaka Mabogini kule, tuingie kwenye hii biashara kwasababu Waziri ameshasema hapa kwamba kuna miche 20,000 atakayotoa ili na sisi tunufaike na hili jambo lenye heri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni changamoto kwenye Jimbo langu. Mheshimiwa Waziri tuna changamoto ya miche ya kahawa, wachaga kule sasa hivi tumechacharika tunataka kupanda kahawa tuchangie kwenye Pato la Taifa, kwa hiyo nikuombe ile miche ambayo unatoa usitusahau. Kuna maeneo yangu ya Uru, Kibosho na Old Moshi tupo tayari kulima kahawa na ndizi, ile miche utakayoleta tunaomba utusaidie ili na sisi tuchangie kwenye Pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni miundombinu ya …
MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa Ndakidemi nilikuongeza muda wako umalizie changamoto za Jimboni, naona umeshaielezea vizuri au kuna kitu unadhani umekisahau.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia.
MWENYEKITI: Sawa.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mifereji ya asili na miundombinu ya umwagiliaji tuna eneo kama hekta 4,060 kwenye eneo la Mabogini, Arusha Chini, na Mandagamnono kwa hiyo tukiboreshewa mifereji ya asili na miundombinu ya umwagiliaji tutachangia vya kutosha katika Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri Mkuu Mheshiliwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa hotuba nzuri kutoka katika ofisi yake. Pia niwapongeze Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako pamoja na Naibu Mawaziri wao. Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake hawa wanaupiga mwingi.
Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu utajikita kwenye Kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) cha Kibaha mkoani Pwani kilicho chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC). Kiwanda hiki kimeshaanza uzalishaji wa viuatilifu vya kuangamiza mbu na wadudu wa mazao na vilevile kina uwezo wa kuzalisha mbolea.
Mheshimwa Spika, bidhaa za kiwanda hiki ni za kibaiolojia. Kiwanda hiki kimejengwa kutokana na mahusiano mazuri ya kidiplomasia baina ya Tanzania na Cuba. Ni kiwanda bora na cha mfano Barani Afrika.
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki cha viuadudu kilianza uzalishaji rasmi mwaka 2017 ambapo uwezo wa uzalishaji wa kiwanda ni lita milioni sita kwa mwaka na kinatumia malighafi inayopatikana ndani ya nchi kwa asilimia 98. Pamoja na uwezo wa kiwanda hiki, pamekuwa na changamoto kubwa ya soko la bidhaa kutoka kiwandani, hali iliyopelekea watumishi wa kiwanda kutokulipwa stahiki zao kutokana na ukosefu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, lengo la ujenzi wa kiwanda hiki lilikuwa ni kuchangia kutokomeza malaria nchini na Afrika kwa ujumla kwa kuzalisha viuatilifu visivyo vya kemikali. Lengo la pili ni kuzalisha viuatilifu na mbolea zisizo na kemikali. Mbolea hizi zitaendeleza kilimo hai ambacho kina soko kubwa duniani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa kiwanda hiki bora na cha kisasa, pamekuwepo na matumizi mabaya ya rasilimali hii kutokana na ukosefu wa soko la bidhaa zinazozalishwa. Mpango wa awali ulizitaka Halmashauri zote nchini kununua bidhaa hizo ili kuangamiza mbu waenezao malaria kwa pamoja kama nchi. Cha kusikitisha ni kwamba Halmashauri nyingi nchini hazijashiriki kununua dawa katika kiwanda hiki.
Mheshimiwa Spika, utokomezaji wa malaria hapa nchini utafanikiwa tu ikiwa nchi yetu itaanzisha programu maalum ya kununua na kutumia dawa hizi kwa wakati mmoja katika maeneo yote hapa nchini Tanzania. Huko Zanzibar matumizi sahihi ya dawa kutoka katika kiwanda hiki kumepunguza ugonjwa wa malaria kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Spika, hapa Tanzania kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa watu wengi kwani asilimia kubwa ya wakazi hujishughulisha na shughuli za kilimo. Lakini kilimo hukabiliwa na changamoto kubwa ya wadudu wa mazao na uchakavu wa ardhi. Pamoja na changamoto hizi, Tanzania inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mbolea na viuatilifu na hata zile zilizopo kutokidhi mahitaji ya soko. Uwepo wa kiwanda hiki unaweza kuwa mkombozi wa wakulima wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa kiwanda hiki, ninaishauri Serikali kufanya yafuatayo; kwanza Wizara ya Afya ihusike kikamilifu na ichukue jukumu la hukakikisha kuwa dawa kutoka kiwandani zinanunuliwa na kusambazwa nchi nzima.
Pili, ikiwezekana, Bohari ya Madawa (MSD) ihusishwe kununua dawa ya viuadudu vya mazalia ya mbu kutoka Kiwanda cha Biotech kilichopo Kibaha ili kuzuia malaria badala ya ilivyozoeleka kupoteza mamilioni ya fedha kununua madawa kutoka nje kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa malaria.
Mheshimiwa Spika tatu, kwa kuwa kiwanda hiki kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja chini ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), ninashauri Serikali itenge fedha na kuwalipa wafanyakazi wanaodai stahiki zao.
Nne, Serikali ijikite kikamilifu kwenye uzalishaji wa mbolea na viuatilifu hai ili vitumike kikamilifu kwenye sekta ya kilimo kwani kuna changamoto kubwa nchini ya bidhaa hizi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Nianze moja kwa moja kwa kumpongeza sana Waziri wetu, Mheshimiwa Angellah Kairuki na wasaidizi wake wawili, Mheshimiwa Dkt. Dugange na Mheshimiwa Ndejembi na Mkuu wangu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mkuu wangu wa Wilaya Makori Kisare na DED wangu, kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Jimbo langu la Moshi Vijijini. Ukweli watatutendea haki na tunashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ni Wizara mama ambayo ni muhimu sana kwenye maendeleo ya watu wetu, kwa sababu utaona bajeti yake imeongezeka kutoka trilioni
8.7 mpaka trilioni 9.0, karibu asilimia 20 ya bajeti yetu ya Taifa. Ni kutokana na umuhimu wa hii Wizara. Kwa hiyo niwaombe waende wakasimamie hii Wizara vizuri ili hizi fedha zinazotolewa na Rais wetu zitumike vizuri na ziletee wananchi wetu maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais haraka sana; kwamba mama anaupiga mwingi, ametusaidia sana kwenye kuboresha ajira. Tumeona juzi ametoa ajira 21,200. Miundombinu ya afya ni nchi nzima kuanzia hospitali za rufaa, za mkoa, za wilaya, vituo vya afya, zahanati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye elimu; Mama amefanya makubwa sana, madarasa usiseme kitu, nami nimepata hospitali ya wilaya kule, kwa hiyo tunashukuru sana. Mambo ni mengi ambayo Mama amefanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na muda, naona leo umebana sana, hivyo, niende moja kwa moja kwenye mchango wangu. Katika mchango wangu ntaongelea tatizo la miundombinu ya barabara Jimboni kwangu Moshi Vijijini na pia ntaongelea mambo ya afya kama muda utaruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Moshi Vijijini changamoto yetu kubwa ni barabara, ndiyo changamoto kubwa na kule Moshi Vijijini tuna bahati nzuri kwamba tuko milimani na mvua huwa zinanyesha. Hii mvua ni agent mkubwa wa kuharibu barabara zetu kule Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, tunaishukuru Serikali kupitia TARURA walitutengenezea barabara nyingi, Barabara ya Gate Fonga - Mabogini mpaka Kahe; Barabara ya Boro – Sangiti; Barabara ya Kiboriloni kwenda Mbokomu; Barabara ya Mandaka – Mnono; Barabara ya Uru Madukani – Materuni; Barabara ya Mweka Junction – Singa Hospitali; Barabara ya Samanga – Chemchem. Nina masikitiko kidogo, barabara hizi zimejengwa kwa kiwango cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakandarasi ambao wamepewa pesa nyingi kutengeneza hizi barabara kuacha ile ya Samanga – Chemchem, barabara hizi zipo kwenye kiwango cha chini kabisa. Kitu kikubwa ambacho kimetokea nilivyosema mvua ni agent wa kuharibu barabara, ni kwamba hakuna mitaro. Barabara zimejengwa, zimechongwa vizuri, wameweka moramu. Kwa mfano ile ya Mabogini, tumewekeza shilingi milioni mia tatu na hamsini na kitu pale, lakini hata kabla haijaanza kutumika mvua ilivyonyesha imesafisha ile moram yote kwa sababu hatukuweka mitaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe huu ujenzi ambao umefanyika nimwombe Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake, Engineer Seif, hii itawaharibia. Fedha za Serikali zinatumika vibaya na haijakaa vizuri. Tuwatumie ma- Internal Auditors wa kwetu wa Wizarani waende wakakague hizi barabara, siyo za kwenye jimbo langu tu, naona Wabunge wengi wanalalamika kwamba barabara hazijajengwa kwa viwango. Tutumie Internal Auditors wa TAMISEMI au ikibidi pia CAG aende kule aangalie, akague aone kama zile hela zimetumika vizuri. Ombi langu ni hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ombi lingine; katika barabara inayokwenda kwenye Kijiji cha Chemchem kupitia Samanga kule Jimbo la Moshi Vijijini, Kata ya Arusha Chini, tulikuwa tumeomba kujengewa daraja linalounganisha hivi vijiji viwili kupita pale Mto Ronga. Bahati mbaya hela zilikuwa ndogo tulitengewa shilingi milioni 475, na pesa hizi zimetumika kutengeneza ile barabara, lakini lile daraja bado haliko kwenye mpango. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, ikimpendeza tunaomba lile daraja litengenezwe ili tuweze kuunganisha Vijiji vyetu vya Chemchem na Samanga ili watu waweze kupita na kwenda kufanya shughuli za uzalishaji kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la pili, ni kuhusu kuiongezea TARURA fedha. Kama nilivyosema Jimbo la Moshi Vijijini tuna tatizo kubwa la barabara. Yaani sisi changamoto yetu kubwa ni barabara. Na kuna barabara nyingi ambazo hazijatengenezwa. Niombe kwenye zile hela za tozo, mimi sijatendewa haki pia kwenye hizi hela za tozo; mwanzo ule mgao wa kwanza ulikuwa sawasawa, lakini huu mgao wa pili nimepata shilingi milioni 700 tu na wengine wamepata bilioni moja, bilioni ngapi. Kwa hiyo niombe zile pesa za tozo tuzigawe vizuri ili niweze kufanya ukarabati wa barabara ambazo nitazitaja hapa kwenye jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ambazo ziko kwenye mfumo wa TARURA na hali ni mbaya. Barabara inayotoka pale Weruweru Sekondari kupanda Manushi mpaka pale Mrama Estate; barabara ya kule Mabogini eneo la Shabaha kwenda Newland; barabara ya kule Bonite Relini kwenda Chekereni, Weruweru; barabara ya Kisawio – Uru Seminari – Molangi; hizi ni barabara muhimu chache tu pamoja na nyinginezo. Naomba chonde chonde tusaidiane ili wananchi katika maeneo haya waweze kutengenezewa hizi barabara na wapite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la tatu ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Kuna barabara ambazo zilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi mara tatu, nne, lakini bado hazijakamilika. Kule Moshi wanatuangalia wanasema tusipojengewa hizi barabara kama mlivyoahidi kwenye Ilani yenu ya Chama cha Mapinduzi tutakuwa kwenye matatizo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, barabara ya Gate Fonga – Mabogini – Kahe iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hii ni mara ya tatu haijatengenezwa. Tunaomba Wizara iitengee pesa itengenezwe kwa kiwango cha lami kwani kule ndiko inakojengwa hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya pili, ni Barabara ya Uru – Mamboleo – Materuni na Uru – Mamboleo – Shingwe; ziko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, zimejengwa kwa mita 300, 400 tu. Niombe sana watufikirie na hizo barabara zijengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni ile ya Kibosho Shine…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Profesa, muda wako umekwisha. Unga mkono hoja.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Angellah Kairuki na Naibu Mawaziri wake (Dkt. Festo Dugange na Deogatius Ndejembi) pamoja na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya kutatua changamoto za wananchi hapa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Moshi Vijijini, tuna changamoto za kimsingi zinazohusiana na uwepo wa vituo vichache vya afya. Pia kuna uhaba wa kidato cha tano katika shule zetu za kata za sekondari.
Mheshimiwa Spika, jimbo langu la Moshi Vijijini kuna uhaba mkubwa wa vituo vya afya. Katika kata 16 za Moshi Vijijini, ni kata tatu tu zina vituo vya afya vya Serikali vilivyosajiliwa. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, TAMISEMI iliagiza tupendekeze maeneo matatu ya kujengewa vituo vya afya vya kimkakati. Mimi nilipendekeza nijengewe katika kata za Oldmoshi Mashariki; Kibosho Kirima; na Arusha Chini. Cha kusikitisha ni kwamba mimi sijapewa hata kituo kimoja kwenye maeneo nyeti na ya kimkakati niliyowasilisha Wizarani ambayo nimeyataja hapo juu.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Oldmoshi Mashariki ina eneo kubwa ambalo lilikuwa ni makao makuu ya Halmashauri. Majengo hayo yako wazi, kwani halmashauri imehamishiwa eneo lingine. Tunapendekeza, yafanyike maboresho katika baadhi ya majengo ili kituo cha afya kipatikane kwa gharama ndogo kutoka katika eneo hili. Vilevile Serikali inashauriwa kujenga chuo cha afya katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, kipaombele namba mbili na tatu ilikuwa ni kujengewa vituo vya afya katika Kata za Kibosho Kirima na Arusha Chini. Kwa kuwa vituo pendekezwa ni vya kimkakati, tunaiomba Serikali itekeleze azma ya kutujengea vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, katika kukagua miradi ya maendeleo jimboni, nilipokea maombi toka kwa wananchi ya kupandisha hadhi baadhi ya maeneo yanayotoa huduma za tiba kuwa vituo vya afya. Katika Kata ya Kibosho Kati, kuna msamaria mmoja aitwaye Barnabas Mallya amejenga zahanati ya kisasa yenye vifaa vyote muhimu; na inaitwa Zahanati ya Lima. Alikabidhi zahanati hii Serikalini, bahati mbaya sana rasilimali hii ya majitoleo haitumiki kikamilifu kwa sababu ya ukosefu wa wataalamu. Kuna haja kubwa ya kuipandisha hadhi hii zahanati na kuifanya kituo cha afya kwani imekidhi vigezo.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kindi haina kituo cha afya, ila kuna kliniki (Mary Bennet) ambayo imeshakarabatiwa kwa msaada wa Wajerumani na kuwekwa vifaa tiba vya kisasa toka Ujerumani vya aina mbalimbali. Ninapendekeza kliniki hii ipandishwe hadhi na kuwa kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kimochi haina kituo cha afya. WDC ilikaa na kupendekeza Zahanati ya Shia iboreshwe iwe kituo cha afya kwani wana eneo la kutosha, naiomba TAMISEMI ifikirie ombi hili.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kibosho Magharibi ina Kituo cha Afya Umbwe kilichojengwa miaka ya 1977 na kuzinduliwa na Baba wa Taifa. Kituo hiki ni kituo pekee katika Tarafa ya Kibosho yenye kata sita. Vilevile hutoa huduma kwa wananchi na Wilaya ya Hai hasa Kata ya Machame Mashariki.
Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa kituo hiki cha afya, wanakabiliwa na changamoto zifuatazo: -
(a) Kituo cha Afya Umbwe kinahitaji kupanuliwa ili kukidhi hadhi ya kuwa kituo cha afya ikiwa ni pamoja na kuongeza majengo, wahudumu, vifaa tiba na dawa za kutosha.
(b) Kituo cha Afya Umbwe hakina gari la kubeba wagonjwa. Kuna uhitaji wa gari jipya ili liweze kuhudumia wajawazito na wagojwa wengine.
(c) Kituo cha Afya Umbwe hakina jengo la upasuaji, maabara ya kukidhi mahitaji ya sasa, jengo la mortuary na jokofu.
(d) Kituo cha Afya Umbwe hakina uzio.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali kwa kuboresha shule za kata katika jimbo langu la Moshi Vijijini. Ninaiomba Serikali ipandishe hadhi ya kuwa na kidato cha tano na sita shule za sekondari za kata zifuatazo: -
(i) Shule ya Sekondari Masoka iliyo Kata ya Kibosho Kirima. Shule hii ina eneo la kutosha na imekuwa inafanya vizuri sana kitaaluma.
(ii) Shule ya Sekondari Kimochi iliyoko Kata ya Kimochi.
(iii) Shule ya Sekondari Mpirani au Mabogini. Shule hizi ziko Kata ya Mabogini.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, pamoja na kuishauri Serikali, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa George Simbachawene na Naibu wake Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete pamoja na watendaji wa Serikali katika Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye utaratibu uliotumika mwaka 2020 kuhitimisha ajira na kusimamisha mishahara kwa watumishi wa Serikali Watanzania waliogombea nafasi za kisiasa (Ubunge) na madhara yake; na umuhimu wa Serikali kupitia upya sheria inayowafanya maprofesa kustaafu wakiwa na miaka 65 na kutokupata mikataba maalumu ya kuendelea kufundisha.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuhitimisha utumishi wa umma kwa kugombea nafasi za kisiasa umeanishwa kwenye Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa tarehe 2 Januari, 2015 unaohusu utaratibu kwa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa nchini. Waraka huo umefafanua utaratibu wa watumishi wote wa umma wenye nia ya kugombea nyadhifa za kisiasa kama ifuatavyo: -
Kwanza, mtumishi wa umma atakayeamua kugombea nafasi ya Ubunge wa kuchaguliwa, Viti Maalumu vya Ubunge au nyadhifa nyingine za kisiasa ataruhusiwa kufanya hivyo, baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza kuwa mgombea wa Ubunge na atalazimika kuacha kazi na kulipwa mafao yake.
Mheshimiwa Spika, utaratibu uliotumika ulikuwa tofauti na waraka ulivyoelekeza hapo juu. Serikali iliiagiza Hazina kutowalipa mshahara wa kuanzia mwezi Julai watumishi wake wote waliochukua fomu ya kugombea nafasi ya uongozi wa kisiasa kupitia vyama vya siasa. Siyo tu kuwa mishahara ilisimamishwa, bali baadhi ya waajiri walichukua hatua ya kuwaondoa kazini watumishi waliochukua fomu za kugombea uongozi wa kisiasa mara walipobainika kuchukua fomu za kugombea Ubunge.
Mheshimiwa Spika, watumishi wengi sana wenye uwezo walichukua fomu za kugombea Ubunge, na baada ya kunyimwa mishahara kwa kipindi cha kuchakata majina ya wagombea, hii ilisababisha hofu na usumbufu mkubwa. Watumishi wengi walichukua fomu wakijua kuwa kisheria hakuna shida kutia nia. Kitendo hiki kitatia hofu watumishi wa Serikali (hasa vijana) wenye uwezo wa kugombea katika chaguzi zijazo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyochangia kwa maandishi katika bajeti ya mwaka 2022/2023, katika vyuo vyetu vikuu vya Serikali, kuna changamoto kubwa ya tatizo la rasilimali watu likiwa limesababishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha Serikali kubadilisha utaratibu wa maprofesa kuendelea kufundisha kwa mikataba maalumu hadi wanapofikisha umri wa miaka 70.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa miaka michache iliyopita, maprofesa wengi katika vyuo vya Serikali wamestaafu katika umri wa miaka 65 kwa mujibu wa sheria. Katika vyuo vikuu vya Serikali kuna uhaba mkubwa wa walimu katika ngazi ya maprofesa na kwenye soko la ajira si rahisi kuwapata wataalamu wenye vipaji hivi.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya rasilimali watu vyuo vikuu Tanzania inasababishwa pia na masharti magumu ya kuajiri wataalamu kutoka nje ya Tanzania. Kuajiri wataalamu kutoka nje kwenye maeneo ya kimkakati ni muhimu ili kutusaidia kwenye kukuza rasilimali yetu, na kutuunganisha na mifumo ya kimataifa. Upatikanaji wa vibali huchukua muda mrefu na husababisha walengwa kutoka nje kubadili mawazo na kuacha kuja kufanya kazi Tanzania.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuelezea changamoto za hapo juu, naishauri Wizara yafuatayo: -
Kwanza, Serikali ifuate sheria na kanuni za kiutumishi kwenye masuala mbalimbali. Naishauri Serikali iwalipe mishahara iliyosimamishwa watumishi wote wa Serikali waliotia nia ya kugombea kama ilivyoainishwa kwenye Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa tarehe 2 Januari, 2015 unaohusu utaratibu kwa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa nchini kwani hawakuvunja sheria wala kanuni kutia nia.
Pili, Wizara ya Utumishi na Utawala Bora itoe vibali vya kuajiri wanataaluma wa kutosha kuendana na idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa. Hii ni pamoja na kuajiri wataalamu kutoka nje katika maeneo ya kimkakati kama yale ya sayansi, uhandisi na hesabu.
Tatu, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora wapitie sheria na kuongeza umri wa maprofesa kutumika kwa mikataba uanzie pale wanapostaafu wakiwa na miaka miaka 65 na waendelee hadi wanapofikisha miaka 75 au watakapokuwa hawana uwezo wa kufanya majukumu yao.
Hii haina hasara kwa Serikali kwani wanapostaafu mishahara yao inakuwa bado iko kwenye ikama.
Mheshimiwa Spika, kuwaandaa hawa wataalamu, Serikali hutumia gharama kubwa sana. Tunapositisha huduma zao, vyuo binafsi huwachukua bila gharama na kuwatumia kuwajengea sifa, ilhali vile vya Serikali vinadorora.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko na Naibu wake Dkt. Stephen Kiruswa na watendaji wote wa Wizara na taasisi zinazosimamiwa na Wizara na wadau wa sekta ya madini kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kwenye uchimbaji wa mawe ya kutengeneza saruji (gypsum), na bidhaa nyingine huko Makanya, Mkoani Kilimanjaro, na maeneo mengine hapa Tanzania. Madini haya ni muhimu kwani hugusa maisha ya Mtanzania moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, saruji itokanayo na madini haya hutumiwa na idadi kubwa ya Watanzania kwenye ujenzi wa nyumba, miundombinu ya maji ya kunywa na umwagiliaji, barabara na maghala.
Mheshimiwa Spika, mawe ya kutengeneza saruji, chaki, gypsum powder, Plaster of Paris (P.O.P) na mbolea ya kilimo ya kupambana na magadi hupatikana katika eneo la Makanya na maeneo mengine ya Tanzania kama Kilwa (Cement ya Dangote), Dodoma, Tanga, Singida na maeneo mengine. Katika maeneo haya kuna kiasi kikubwa cha rasilimali ya mawe ambayo hutumika kutengeneza saruji (sementi) viwandani. Kwa maoni yangu, bado uchimbaji huu haujawa na tija tarajiwa.
Mheshimiwa Spika, wapo watu wengi ambao wameibukia kuwa matajiri wakubwa kutokana na kujihusisha na kazi hii ya uchimbaji wa mawe haya ya kutengenezea saruji (cement) katika eneo la Makanya na maeneo mengine yaliyotajwa hapo juu. Kwa maoni yangu, madini haya hayajapewa kipaumbele kikubwa, kwani bidhaa zake kama saruji ina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Idadi ndogo ya wachimbaji wazawa hushiriki katika biashara hii muhimu kutokana na changamoto mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kuchimba mawe haya ni ngumu na sasa ni wakati muafaka wa kuwashirikisha wachimbaji wazawa kwa kuwawezesha kushiriki katika shughuli hii ili kujiongezea kipato na kuchangia katika pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, changamoto inayowakabili wachimbaji wazawa ni matumizi ya teknolojia za kizamani, upatikanaji wa zana za kisasa za uchimbaji, na mitaji midogo kwa kundi hili.
Mheshimiwa Spika, bei ya zana za uchimbaji ni kubwa, na vilevile hutozwa kodi kubwa. Hapa nchini Tanzania ni wafanyabiashara wachache wanajihusisha na biashara ya zana za uchimbaji kutokana na kodi nyingi kwenye bidhaa hizi. Kwa hali ilivyo sasa hivi vifaa hivi vikiingizwa nchini wachimbaji wadogo wadogo wazawa hushindwa kumudu gharama.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto nilizotaja hapo juu, naishauri Serikali yafuatayo; kwanza, Serikali ihamasishe wazawa kuwekeza katika uchimbaji wa haya madini ya gypsum; pili, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Waziri wa Fedha washauriane na kuondoa kodi kwa wazawa wanaoagiza na kufanya biashara ya vifaa ili viingie kwa wingi, madini yachimbwe na wengi na kodi iongezeke kutoka kwenye mauzo ya gypsum na cement badala ya ile ya kwenye vifaa.
Tatu, tunazishukuru benki za biashara kwani zimeongeza mikopo kwa wachimbaji wa madini wadogo wadogo kutoka shilingi bilioni 36 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 145 kufikia mwezi Machi, 2023. Hata hivyo, ninaishauri Serikali iendelee kujadiliana na benki za biashara nchini ili ziendelee kutoa mikopo ya mitaji ya kuchimba na ya kununulia vifaa vya kuchimba mawe ya kutengeneza cement kwa wachimbaji wadogo wadogo kwenye maeneo yote husika nchini.
Nne, Serikali ifanye tafiti za kina katika maeneo mengine Mkoani Kilimanjaro na maeneo mengine hapa nchini ili kujua maeneo mengine yenye madini ya gypsum. Utafiti huu uoneshe madini yako maeneo gani ili kurahisisha uchimbaji kwa wachimbaji wazawa. Kwa kufanya hivi, kanzidata hiyo itatumika kurahisisha uwekezaji na uchimbani na kuipatia Serikali kipato cha uhakika.
Mheshimiwa Spika, tano, Serikali ihamasishe wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vya kuzalisha vifaa na mitambo ya kutumika migodini hapa nchini; na sita, Serikali ihamasishe wawekezaji wajenge viwanda vya saruji katika maeneo yaliyo karibu na machimbo ili kupunguza gharama za kusafirisha mawe.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Abdallah Ulega, Naibu wake Mheshimiwa Ernest Silinde, taasisi zilizopo chini ya Wizara na wataalam wa Wizara na wadau wa sekta hizi kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyochangia mwaka jana kwenye kipindi cha bajeti, Mkoa wa Kilimanjaro una fursa nyingi za kufuga aina mbalimbali za wanyama kama vile ng’ombe na mbuzi wa maziwa na nyama, kondoo, nguruwe, sungura, kuku, bata na samaki kwa kutumia rasilimali zilizopo. Tunaiomba Serikali ipeleke teknolojia bora za ufugaji wa wanyama hawa katika Jimbo la Moshi Vijijini, kwani kwa kufanya hivyo tutaongeza tija katika uzalishaji na kuwaongezea wafugaji kipato na kulisaidia Taifa kupata fedha.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya mlimani (Kilimanjaro) yanaweza kutumika kwa ufugaji wa ndani (zero grazing) kwa ng’ombe wachache na mbuzi wa maziwa, nguruwe, sungura, kuku na bata. Katika maeneo haya, tunaiomba Wizara ifikirie kupeleka mbegu bora za wanyama wanaofugwa na wafugaji.
Mheshimiwa Spika, eneo la ukanda wa tambarare kwenye Kata za Arusha Chini na Mabogini lina wafugaji wa Kimasai na lina uwezekano wa kuzalisha kwa tija ng’ombe, mbuzi na kondoo wa nyama.
Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za wafugaji wa Jimbo la Moshi Vijijini, aina za kienyeji za wanyama (ng’ombe, mbuzi, nguruwe, kuku) wanaofugwa ni kikwazo kikubwa kwenye maendeleo ya sekta ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, sekta ya uvuvi inaweza kuwapatia wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini kipato kikubwa iwapo itaendelezwa. Hili litawezekana ikiwa wananchi watapatiwa mafunzo ya kitaalamu ya jinsi ya kufuga na kukuza samaki kwa kutumia teknolojia ya mabwawa. Ufugaji endelevu wa samaki unaweza kutatua changamoto za umaskini kwa kuwaongezea kipato na kuchangia kikamilifu kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Arusha Chini kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu, wavuvi wanaweza kusaidiwa na Maafisa Ugani wa Uvuvi mbinu bora za ufugaji wa samaki, ikiwepo matumizi ya vizimba. Uwekezaji wa vizimba unaweza kufanyiwa majaribio kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha ufugaji wa ng’ombe na mbuzi wa maziwa na nyama, kondoo, nguruwe, sungura, kuku, bata na samaki katika Jimbo la Moshi Vijijini, ninaishauri Wizara itusaidie yafuatayo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza naishauri Serikali iwe na programu maalumu ya kuzalisha mitamba wa maziwa wenye sifa zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na mifugo mingine kama mbuzi wa maziwa, ng’ombe wa nyama, nguruwe na kuku. Wafugaji wengi hawana mbegu bora za ng’ombe na mbuzi wa maziwa. Kwa ujumla, huwa wanabahatisha.
Mheshimiwa Spika, pili, naishauri Serikali ihamasishe kuanzishwa kwa vikundi vya ushirika wa wafugaji mifugo na samaki ambavyo itakuwa rahisi kuwapatia huduma za mitaji na utaalamu.
Mheshimiwa Spika, tatu, naishauri Wizara ianzishe mashamba darasa ya samaki Jimboni Moshi Vijijini kwani kuna rasilimali nyingi za maji katika maeneo yote jimboni. Hii ni pamoja na kuanzisha kituo cha kuzalisha vifaranga wa samaki ili wafugaji wavipate kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, nne, naishauri Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Moshi, wawezeshe kupandikiza vifaranga bora vya samaki katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, kwani wavuvi waliniambia kwenye kampeni kuwa samaki wamehama, ikiwa na maana kuwa wamepungua.
Mheshimiwa Spika, tano, napendekeza Serikali ifanye majaribio ya kuweka vizimba kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ili kuongeza tija kwenye ufugaji wa Samaki; na sita, naishauri Serikali iwekeze kwenye kujenga majosho ya kuogesha mifugo katika maeneo ya Kata za Arusha Chini na Mabogini zenye uhitaji mkubwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu wake Mheshimiwa Exaud Kigahe na watendaji wote wa Wizara na taasisi zote zilizo chini ya Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye umuhimu wa uwekezaji kwenye sekta ya viwanda hapa nchini kwa kuliwezesha Shirika la Maendeleo la Taifa (The National Development Corporation (NDC) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO). Pia nitagusia changamoto za viwanda katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu, chini ya Mwalimu Julius Nyerere tangu kujipatia uhuru na baada ya kutangaza Azimio la Arusha mwaka 1967 iliandaa mpango wa kutuletea maendeleo kwa falsafa ya ujamaa na kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, kupitia falsafa hiyo, viwanda vingi vilijengwa nchi nzima ili kusindika mazao karibu yote ya kilimo na mifugo. Kwa mfano, viwanda vya nguo vya Kilitex, Mwatex, Urafiki, Mutex viwanda vya korosho, kahawa, magunia, viatu, maziwa, nyama, Tanzania Cigarette Company, Tanzania Breweries na kadhalika. Vilevile mwaka 1965 serikali ilianzisha Shirika la Maendeleo la Taifa (The National Development Corporation (NDC). Shirika hili lilianzishwa kusimamia viwanda nchini.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali iliboresha elimu za ufundi katika vyuo vyetu vikuu na kati ili kuzalisha wataalam wa kuhudumia viwanda vyetu. Ili kuimarisha uchumi wetu, Serikali ilianzisha taasisi za kiufundi kama CAMARTEC, SIDO, TEMDO na taasisi ya utafiti wa viwanda TIRDO.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kama ilivyoelezwa hapo juu, nchi yetu ilibadilika na kukumbatia sera ya kubinafsisha viwanda na mashirika yetu ya umma kama ilivyoelekezwa na Benki ya Dunia kwa masharti ya kupatiwa mikopo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia utekelezaji wa sera hiyo, ramani yetu ya maendeleo ya Taifa ilivurugika na kudhoofisha sekta ya viwanda nchini.
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya viwanda katika miaka ya mwanzo baada ya Uhuru yalipatikana tukiwa na wasomi wachache sana waliobobea katika nyanja mbalimbali, leo hii tunaingia miaka 62 toka tupate uhuru. Kwa sasa tunao Watanzania wengi wenye elimu, ujuzi, uzoefu na maarifa ya namna ya kusimamia viwanda vilivyoko na vitakavyojengwa nchini. Kwa mantiki hiyo, ni wakati muafaka kuchukua hatua ya kuwatumia wataalam wetu wazawa na rasilimali zetu kusaidia kwenye kuwekeza na viwanda vipya hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kama Taifa, sasa ni wakati muafaka wa kutafakari na kufanya maamuzi ya kuliwezesha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ili kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya kuendeleza na kusimamia uwekezaji wa viwanda hapa Tanzania kwa kutumia wataalam wetu wazawa. Hii inawezekana ikiwa watapatiwa rasilimali pesa ya kutosha na wataalam watakaohitajika kwani katika uongozi wa awamu ya kwanza, NDC iliendesha shughuli zake kwa mafanikio makubwa. Shirika la NDC inatekeleza miradi inayogusa sekta zote muhimu kama kilimo, madini, afya, viwanda, nishati na biashara. Baadhi ya miradi hiyo ni Kiwanda cha Viuadudu Kibaha, Migodi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma, Mradi wa Chuma cha Pua, Liganga, Mradi wa Magadi Soda, Monduli, Arusha.
Vilevile NDC inasimamia Bandari Kavu ya Nafaka, ETC Cargo, Dar es Salaam na mashamba ya zao la mpira yaliyopo Tanga na Morogoro. Pia NDC inamiliki kiwanda cha kuzalisha vipuli vya mashine na mitambo mbalimbali kilichopo mkoani Kilimanjaro cha KMTC. Kwa mantiki hii, NDC wanatekeleza majukumu makubwa sana kwenye sekta ya viwanda na uwepo wao ni muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TIRDO liliundwa ili kufanya utafiti na kutoa huduma za kitaalam ili kuendeleza viwanda nchini. Shirika hili ni muhimu sana kwani miundo na ujenzi wa viwanda umebadilika sana kutokana na kuwepo kwa teknolojia mpya sehemu nyingi duniani.
Mheshimiwa Spika, hapa Tanzania viwanda vingi vilivyojengwa miaka ya nyuma vimefungwa kutokana na sababu mbalimbali. Kutokana na ukweli huu, huduma ya utafiti ya TIRDO inahitajika ili kutoa ushauri elekezi wa ni nini kifanyike kufufua viwanda hivi.
Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu la Moshi Vijijini, moja ya kiwanda kilichokuwa kimepata mafanikio makubwa sana ni kile kiwanda cha kukoboa mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Co. Ltd kilichopo Chekereni – Moshi katika Kata ya Mabogini.
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki kilikuwa kimejengwa kwenye eneo ambalo linazalisha mpunga mara mbili hadi tatu kwa mwaka. Kiwanda hiki hakifanyi kazi tangu Septemba. 2014. Kiwanda cha kukoboa mpunga kilikodishwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahawa (KNCU) na baada ya kushindwa kukiendesha, mkoa ulimshauri Msajili wa Hazina kukirudisha Serikalini ili atafutwe mwekezaji mwingine anayeweza kukiendesha. Tayari Msajili wa Hazina amerejesha kiwanda hiki Serikalini tangu tarehe 18 Oktoba, 2018 lakini bado hajapatikana mwekezaji na shughuli zimelala. Kutokuwepo kwa kiwanda hiki kimeondoa fursa ya wakulima kupata bei nzuri ya mpunga na ajira kiwandani kwa wana Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, kiwanda cha pili kilichopo jimboni kwangu na hakifanyi vizuri ni kiwanda cha bidhaa za ngozi Msuni kilichopo Kata ya Uru Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki kinamilikiwa na Kamati ya Maendeleo Kata ya Uru Kaskazini (WDC). Kina uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali za ngozi kama viatu, mikoba na mikanda.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoomba katika bajeti ya mwaka juzi na mwaka jana, narudia tena kuiomba Serikali itume wataalam wa TiRDO kwenye kiwanda hiki ili ushauri wa kitaalamu upatikane na kiwanda hiki kifufuliwe na kuunga juhudi za wana ushirika huu kwenye kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, jimbo la Moshi Vijijini ni maarufu sana katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Kama Serikali itakuwa na mikakati ya kuhamasisha uwekezajj wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuzindika mazao ya kilimo na mifugo, hii itasaidia kutengeneza ajira na kuongeza kipato cha wananchi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naishauri Serikali ifanye yafuatayo: -
Kwanza, Serikali ichukue hatua haraka na kuliwezesha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ili litekeleza kikamilifu majukumu yake ya kuendeleza na kusimamia uwekezaji wa viwanda hapa Tanzania. Hii itawezekana ikiwa wataongezewa raslimali pesa na wataalamu wa kutosha.
Pili, kwa kuwa huduma ya TiRDO inahitajika sana kwenye kutoa ushauri elekezi wa ujenzi wa viwanda nchini, ninaishauri Serikali itenge fedha za kutosha na kupeleka wataalam wa kutosha kwenye fani zote ili kuliwezesha shirika hili kutekeleza majukumu yake.
Tatu, Wizara itafute mwekezaji katika kiwanda cha kukoboa mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Co. Ltd kilichopo Chekereni - Moshi, katika Kata ya Mabogini. Kiwanda hiki kinaweza kuwa ni chanzo cha kusafirisha nje mchele ulioongezwa thamani na kuwapatia wakulima kipato na Taifa kwa ujumla.
Nne, Vyama vya Ushirika vilivyopo Jimbo la Moshi Vijijini vihimizwe na kuhamasishwa kuwa na viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali ya kilimo na mifugo na kuyaongezea thamani ili kuzalisha bidhaa zinazotokana na kahawa, ndizi, mboga mboga, nafaka, mikunde, maziwa, asali, alizeti na mengine mengi. SIDO na TEMDO wanaweza kusaidia sana kwenye hili.
Mheshimiwa Spika, tano, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka juzi na mwaka jana, bado naliomba tena Shirika la Utafiti wa Viwanda Tanzania (TiRDO) lishiriki kikamilifu kwenye kutoa ushauri wa kitaalam kukifufua Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi Msuni kilichopo Kata ya Uru Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia katika bajeti hii tunayoiita ni bajeti yetu, bajeti ya wakulima. Nasema ni bajeti yetu au bajeti ya wakulima kwa sababu karibia kila Mbunge hapa amezaliwa na mkulima, hata kama hujazaliwa na mkulima unakula chakula ambacho amelima mkulima. Kwa hiyo, nianze kwa kuwaomba Wabunge wote tupitishe bajeti hii kwa sababu ni bajeti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri kwa kazi nzuri anayofanya pamoja na timu yake yote. Jamani, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni; Mheshimiwa Bashe na timu yake, Naibu wake pale, Katibu Mkuu na viongozi wote wa taasisi wanaitendea haki sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja pia kumpongeza Rais wetu kwa maono yake. Wakati ameingia madarakani bajeti yake ya kwanza ilikuwa shilingi bilioni 294, lakini kwa kuwa anajali sana wakulima akaipandisha kufikia shilingi bilioni 954 kwenye hii bajeti tunayoimalizia sasa hivi, na hiyo inayokuja amepandisha tena imekuwa shilingi bilioni 970, sawa na asilimia 2.2 ya shilingi trilioni 44.4 ya bajeti yetu ya Taifa. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Rais kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuomba kwamba ikiwezekana, bado bajeti hii haijakidhi matakwa ya wakulima, tunaomba iongezwe, ikiwezekana ifikie shilingi trilioni mbili ili Mheshimiwa Bashe na timu yake waweze kufanya kazi ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivyo kwa sababu wakulima ndiyo sehemu kubwa ya uchumi wetu, kama tutawawezesha, sasa hivi wanachangia 29.1 percent kwenye GDP ya nchi yetu, tukiiongeza hii bajeti najua tutaonesha maajabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo, fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya miradi kwa mwaka huu ni shilingi bilioni 731 ambapo ni karibia asilimia 85 ya bajeti yote ya Wizara ya Kilimo. Kwa hiyo pesa yote kwenye ile 900, 700 na kitu iko kwenye miradi ya maendeleo ya kilimo, kwa hiyo pesa yote iko site na tunawapongeza sana Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka huu ambayo tunaiombea ni shilingi bilioni 767 kwa bajeti ya maendeleo. Kwa hiyo niwaombe ikiwezekana hii bajeti iongezeke ili hawa ndugu zetu waweze kufanya mambo ya maana. Kuna miradi ya kielelezo mingi ambayo Wizara imeshatekeleza na nitai- discuss kwa ufupi sana. Mradi wa ruzuku ya mbolea wamefanya vizuri lakini niwaombe, pamoja na kwamba mmefanya vizuri, tulishatumia karibu shilingi bilioni 342, zile changamoto za usambazaji ambazo tulikumbana nazo naomba mzi-address ili isije ikaleta shida tena. Mwaka wa kwanza ulikuwa ni wa kujifunza, tunategemea kwa kuwa zoezi bado ni endelevu, waboreshe pale ili tuweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa harakaharaka nitachangia kuhusu utafiti na uzalishaji wa mbegu kwa wakala wa mbegu. Ninaomba, mbegu ndiyo msingi wa maendeleo katika sekta ya kilimo. Watafiti na wale wazalishaji wapewe pesa ya kutosha ili tuwe na mbegu bora ambayo wakulima wataitumia kule mashambani waweze kupata tija kutokana na kilimo chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, hapa niombe kitu ile sheria ya mbegu tunaomba iboreshwe. Kuna watu wanazalisha mbegu za asili, ile sheria inawakataza watu kuuza mbegu ambazo hazijapitia kwenye mfumo rasmi. Tunaomba ile sheria iboreshwe ili mbegu za asili kama zile za mpunga wa Kyela kama wakikidhi vigezo nao waweze kuuza hizo mbegu za asili ziwafikie walaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haraka haraka nitakwenda kwenye Tume ya Ushirika. Naishukuru Serikali imeongeza bajeti ya Tume ya Ushirika kutoka shilingi bilioni 1.1 hadi shilingi bilioni mbili sawa na ongezeko la asilimia 109. Hawa wameongezewa pesa ili kuimarisha vyama vya ushirika hapa nchini. Naomba kama Mbunge mwenzangu kutoka Kilimanjaro alivyosema asubuhi, kuna tatizo kwenye Tume ya Ushirika, kwenye vyama vya ushirika kuna matatizo makubwa sana. Nendeni mkasimamie ushirika tuhakikishe kwamba tunaboresha ushirika, wananchi wasiibiwe pesa yao kule waliko. Kuna wizi mkubwa sana unaendelea, hata kule Kilimanjario kwangu. Naomba kabisa Tume ya Ushirika iende COASCO wasimamie wahakikishe kwamba tunafanya kitu ambacho kitawapendeza wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka naomba niongelee mambo ya jimboni kwangu. Katika Jimbo la Moshi Vijijini tuna changamoto kubwa moja. Changamoto ya kwanza kubwa kabisa ni maji ya kumwagilia. Zile skimu za umwagiliaji za asili zimeshachoka. Nami Mbunge nilivyopata pesa ya Mfuko wa Jimbo, katika kata 16, kata 14 zote nimepeleka kwenye skimu ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, mimi pesa yangu ya Mfuko wa Jimbo nimepeleka kusaidia wakulima wapate maji. Sasa jamani ni wakati wenu na ninyi mnisaidie. Kuna skimu za asili ambazo tunaomba zijengwe, Kibosho Magharibi, kuna skimu ya Shumeli; Kibosho Mashariki, skimu ya Lyalenga, Shumbe ya Kimangara; Kaskazini, skimu ya Tumbo, Kusini skimu ya Kisarika; Mbokomu skimu ya Ondou; Kibosho Magharibi, Makeresho; Kibosho Kilima Lengurutu; na Old Moshi Skimu ya Muu. Naomba Mheshimiwa Waziri mtusaidie ili watu wapate maji tuweze kuchangia kwenye pato la Taifa. Tukishapata maji, tutazalisha kitu ambacho tunataka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, tunaomba tujengewe skimu mpya kwenye kata ya Arusha chini ambapo kuna hekta 2000 ambazo zipo pale zinangojea zijengewe skimu na tukishapata hiyo skimu, nina uhakika tutachangia vizuri kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe kwa kusema hivi, hapa Afrika Mashariki, Tanzania tuna mazingira mazuri sana ya ku-practice kilimo. Tuna eneo kubwa ambalo tunaweza tuka transform nchi yetu ikazalisha chakula kingi sana. Waziri leo hapa asubuhi amesema karibu hekta milioni 44 zinaweza zikatumika kuzalisha kilimo. Tumezipita nchi zote, hata Kongo tumeipita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo maziwa makuu matatu na mito mingi. Nimalizie kwa kusema, hii Wizara ya Kilimo ina wasomi wengi; ina maprofesa ina madaktari ina watu wenye masters, degree ya kwanza, diploma na certificates. Naiomba Wizara iwatumie hao wataalam vizuri. Mkiwasikiliza watachangia kwenye pato la Taifa na tutatoka kwenye ile low-income country ya Dola 1,080 na tutakwenda juu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe, Naibu Waziri Mheshimiwa Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Ndugu Gerald Mweli, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Hussein Mohamed, wataalam wa Wizara, wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa sana kwenye sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu fursa za kilimo cha umwagiliaji katika jimbo la Moshi Vijijini, hali ya Vyama vya Ushirika na Kiwanda cha Kukoboa Mpunga kilichopo Kijiji cha Chekereni, Kata ya Mabogini jimbo la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, mkoa wa Kilimanjaro una fursa kubwa sana za kilimo cha umwagiliaji. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Kilimanjaro kuna mito mingi inayoanzia mlimani na kuishia bahari ya Hindi bila kutumika kikamilifu kwenye kilimo.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ijenge skimu mpya na kukarabati zile skimu za asili ili haya maji yatumike kuzalisha mazao badala ya kuishia baharini.
Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu la Moshi Vijijini ninaishauri Serikali ifanye yafuatayo; kwanza Serikali iwekeze kikamilifu kwenye kuboresha na kujenga upya skimu za asili. Kule Kilimanjaro kulikuwa na mradi wa Rehabilitation of Traditional Irrigation Schemes. Tangu mradi huu ufungwe, miundombinu ya skimu hizi imekuwa kwenye hali mbaya. Kwa ujumla miundombinu hii imechoka na maji hayawafikii tena wakulima wa kahawa, ndizi, mbogamboga na matunda kama maparachichi. Skimu hizi za asili zikiboreshwa (Kata za Kibosho, Kirima, Kibosho Kati, Kibosho Mashariki, Kibosho Magharibi, Kindi, Okaoni, Uru Shimbwe, Uru Mashariki, Uru Kaskazini, Uru Kusini, Kimochi, Oldmoshi Mashariki, Old Moshi Magharibi na Mbokomu) zitasaidia sana kuongeza tija kwa wakulima wangu wa Jimbo la Moshi Vijijini.
Pili, Serikali ijenge skimu mpya za umwagiliaji katika maeneo ya tambarare ambayo hukumbwa na mafuriko makubwa kila mwaka. Maji ya mafuriko yaelekezwe shambani kuzalisha chakula (mpunga na mazao mengine). Maeneo ya kuzingatia ni: -
a) Wizara ijenge skimu mpya Kata ya Arusha Chini katika Mto Ronga itakayohusisha vijiji vya Mikocheni na Chemchem ambako kuna takribani 2000 ha.
b) Wizara ijenge skimu mpya ya ziada Kata ya Mabogini ambapo kuna 1350 ha.
Mheshimiwa Spika, skimu hizi mpya zikijengwa, zitaongeza 3350 ha kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa chakula na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa wananchi na Taifa.
Mheshimiwa Spika, mchango mwingine ni kuhusu mashamba ya ushirika na vyama vya SACCOS zilizopo kwenye maeneo mbalimbali ya Jimbo la Moshi Vijijini. Uongozi wa mashamba na baadhi ya SACCOS ni changamoto kubwa sana. Viongozi wengi wa ushirika hawana taaluma za kuongoza ushirika.
Mheshimiwa Spika, katika baadhi ya vyama jimboni kwangu kuna matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za mashamba mengi ya ushirika. Katika mikutano yangu ya hadhara, wakulima wametoa malalamiko kuwa wanaibiwa na viongozi wa ushirika.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa fedha za kutosha zimetengwa kwenye idara ya ushirika, ninaishauri Serikali ifanye ukaguzi maalum katika mashamba na SACCOS zote na watakaobainika wamefuja mali za ushirika, wachukuliwe hatua za kisheria na vyombo husika. Hii ni pamoja na kurekebisha sheria na sera za ushirika Tanzania ili tuwabane wabadhirifu wa mali za ushirika.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa mwisho ni kuhusu Kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Co. Ltd.
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki kimesimamisha shughuli zake na kabla ya kufungwa, kiwanda hiki kilikuwa moja ya kiwanda kilichokuwa kimepata mafanikio makubwa sana. Kiwanda hiki kipo Chekereni – Moshi katika Kata ya Mabogini.
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki kiko kwenye eneo ambalo huzalisha mpunga mara mbili hadi tatu kwa mwaka. Kiwanda hiki hakifanyi kazi tangu Septemba, 2014. Kiwanda cha Kukoboa Mpunga kilikodishwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahawa (KNCU) na baada ya kushindwa kukiendesha, mkoa ulimshauri Msajili wa Hazina kukirudisha Serikalini ili atafutwe mwekezaji mwingine anayeweza kukiendesha. Tayari Msajili wa Hazina amerejesha kiwanda hiki Serikali tangu tarehe 18 Oktoba, 2018 lakini bado hajapatikana mwekezaji, na shughuli zimelala. Kutokuwepo kwa kiwanda hiki kumeondoa fursa ya wakulima kupata bei nzuri ya mpunga na ajira kiwandani kwa wana Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki kinaweza kuwa ni chanzo cha kuongeza thamani na kusafirisha mchele wetu nje na kuwapatia wakulima kipato na taifa kwa ujumla. Naiomba Wizara isaidie kumpata mwekezaji.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa; na nianze moja kwa moja kwa kumpongeza sana Waziri wetu wa Maji Mheshimiwa Engineer Jumaa Aweso, Mheshimiwa Engineer Mahundi, Katibu Mkuu Kemikimba na nisiwasahau wale watendaji wetu kule mkoani Engineer Munishi, Kija Limbe, Mussa Msangi wa Wilaya, na kwa namna ya pekee Engineer Mussa wa Mfuko wa Maji. Ninawashukuru sana kwa jinsi ambavyo mnatusaidia kule Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, pongezi zangu za pili kwa Rais wetu. Mama ana nia thabiti ya kuwatua akina mama wenzake ndoo kichwani. Nasema hivyo kwa sababu tunaona bajeti ya Wizara ya maji imeongezeka kutoka shilingi bilioni 705 kwenda shilingi bilioni 756 kwenye bajeti inayokuja. Na ile ya maendeleo imeongezeka kutoka bilioni 657 mpaka 695. Hizi zote ni Juhudi za Mama, juhudi nzuri, moyo mzuri, nia njema ya kuwasaidia akina mama.
Mheshimiwa Spika, katika miradi ambayo Wizara ya Maji itatekeleza, nitachangia zaidi kwenye mradi ya maji vijijini. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu wametenga pesa ya kutosha kabisa. Asilimia 72 ya fedha zote za maenedeleo ambazo ni shilingi bilioni mia tano na, zinakwenda kujenga miradi 1,546 vijijini, kuhudumia zaidi ya wananchi milioni 13. Hili ni jambo zuri kusema ukweli. Sasa baada ya kusema hayo, katika bajeti hii, ukienda kwenye ukurasa wa 262, kule moshi vijijini Mheshimiwa Waziri na timu yake wametukumbuka vizuri. Tunakwenda kujengewa chanzo cha maji na kuweka mitandao ya bomba kwenye mradi wa Kilema-Okaoni ambapo wametenga shilingi bilioni 204, tunashukuru. Mnakwenda kupanua mradi wa Tema, Shishamaro na Uru Shimbe ambako mmetenga shilingi milioni 699. Mnakwenda kuboresha mfumo wa mradi wa maji katika chanzo cha Urunduma ambao utapeleka maji katika Kata za Okaoni na Kibosho Kati, mmetenga shilingi milioni 300, tunashukuru; na mmetenga shilingi 69,000,000 kwa ajili ya kufanya usanifu na kugundua vyanzo vipya vya maji katika maeneo ya Tema, Shishamaro na Uru Shimbwe, tunashukuru kwa hili.
Mheshimiwa Spika, sasa, ili tufikie ile azma na sisi watu wa Moshi Vijijini tuwe na asilimia 85 naiomba Wizara inisikilize na inisaidie kwenye mambo yafuatayo. Katika kata ya Uru Kusini kuna wakazi 31,000, na kuna miradi mitatu ya maji ambayo ni mradi wa Mang’ana, Kisimeni na Mbora. Kwenye kata hii zipo taasisi nyingi za Serikali ikiwemo Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge. Katika miradi hii niliyoitaja maji ni kidogo na mabomba mara nyingi yako tupu. Tunamuomba Mheshimiwa Waziri na timu yake watuletee mradi wa kuongeza maji kwenye hii miradi mitatu ili hii kata ambayo ina watu wengi sana kule kwenye jimbo langu wapate maji ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, kata ya pili ni Kata ya Arusha Chini ambako ina wakazi kama 13,900 hivi, na kwenye kata hii Vijiji vya Mikocheni na Chemchem hakuna maji, badala yake wanahudumiwa na mradi wa Kirua Kahe ambapo watu wanapeleka maji kwa punda, kwa trekta kusaidia hivi vijiji. Ni kweli hawa watu wa Chemchem na Mikocheni wana shida. Kutokana na uhaba huu kuna mito inapita pale karibu, tunamuomba Waziri ikiwezekana mtujengee miradi hata kutoa kule mtoni tuje tutibu yale maji tuwape watu wa hii kata wapate maji kama Watanzania wengine.
Mheshimiwa Spika, kata ya Old Moshi Magharibi kuna mradi mkubwa wa Tellamande ambao namshukuru Waziri mkuu alikuja akaufungua. Maji ni mengi na yanapasua mabomba. Lakini eneo la Old Moshi Magharibi katika vijiji vya Mandaka Munono na vitongoji vya Sanindo hakuna maji. Tunaomba tu MUWSA wapeleke maji kwa kutumia chanzo hiki hiki au RUWASA watusaidie kutumia chanzo hiki ili hawa watu na wao wapate maji ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, katika kata ya Uru Kaskazini ambako kuna watu elfu kumi mia nane naa kuna chanzo kizuri cha maji ambacho kinatoa maji Uru Kaskazini kuyapeleka Uru Kusini na Kata ya Pasua kwenye Manispaa ya Moshi Mjini. Lakini wale watu wa Uru Kusini Vijijni vya Njari na Msumi hawajaunganishwa kwenye huu mfumo wa maji na maji yanataoka kwao. Nikuombe chonde chonde Mheshimiwa Waziri tuangalie hawa watu kwa sababu maji yanatoka kwao, watakuwa walinzi wazuri wa hii miradi, na wao waunganishwe katika huu maradi.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kimochi, ina watu 16,000. Tunaishukuru Serikali ilitupa milioni 500 na MUWASA bado wametupa ili kuboresha mfumo wa maji katika maeneo haya. Lakini bado vijiji vya Sango, Shiha na Kisaseni havijapata maji. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie katika hili.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ni Kata ya Mabogini ambayo ina watu kama 56,000, na ndiyo kata kubwa kabisa na yenye watu wengi kuliko zote katika Mkoa wa Kilimanjaro. Niombe sana, nashukuru Serikali mlitupa shiling milioni 500 tukawajengea miradi ya maji, maana kuna vijiji vilikuwa havijapata maji tangu tupate uhuru. Niombe, kwenye Viijiji vya Mabogini kwenye Kitongoji cha Sanya Line D, Vijiji vya Muungano, Vitongoji vya Mwamko, Umoja, Uru, Relini, Kijiji cha Chekereni, Kitongoji cha Chekereni, Kijiji cha Maendeleo, Kitongoji cha Uarushani na Kijiji cha Mtakuja kitongoji cha Upareni, Kijiji cha Mserekia, Kitongoji cha Remiti, wanahitaji maji.
Mheshimiwa Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri ni kijana mchapakazi Pamoja na timu yako. Mimi ukinitendea haya utakuwa umewatendea watu wa Jimbo la Moshi Vijijini haki, na tutaendelea kuwaombea daima.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri Jumaa Aweso na Naibu wake Engineer Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu Engineer Kemikimba pamoja na wataalam wa Wizara ya Maji kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, Waziri na timu yake wamekuwa mfano wa kuigwa kwenye kutatua changamoto za maji na kuwatua akinamama ndoo kichwani, kwani maji ni haki ya msingi kwa binadamu wote.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla inatia faraja kuona upatikanaji wa maji vijijini unaongezeka kama alivyoonesha kwa kina katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka huu wa 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu la Moshi Vijijini kuna changamoto ya upatikanaji wa maji ya bomba katika maeneo yafuatayo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza, Kata ya Mabogini ina wakazi wengi wapatao 57,231 na kuna changamoto kubwa ya maji ya kunywa. Katika Kata ya Mabogini kuna changamoto ya maji katika vijiji vya Mabogini, Muungano, Chekereni, Maendeleo, Mtakuja na Mserekia. Ninaomba Wizara ipeleke maji katika vitongojj ambavyo havijapata maji katika vijiji vilivyotajwa.
Mheshimiwa Spika, pili, Kata ya Kimochi ina zaidi ya wakazi 16,046. Kata hii ina vijiji vya Mowo, Sango, Shia, Miami, Lyakombila na Kisaseni. Eneo lote linahudumiwa na MUWSA.
Tunaishukuru Serikali kwa jitihada za awali kuwafikishia wakazi wa eneo hili maji, ila bado kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji maji katika maeneo mengi hasa Kijiji cha Sango, Shia na Kisaseni. Ninaiomba Serikali itutengee pesa za kutosha ili maji yafike maeneo yote ya kata hii vikiwepo vijiji vya maeneo ya tambarare.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Uru Kusini yenye vijiji saba vya Okaseni, Kimanganuni, Rua, Kariwa, Longuo A, Kitandu na Shinga ina takribani wakazi 31,557 na ina miradi mitatu ya Mang'ana, Kisimeni na Mbora. Changamoto ya miradi hii ni maji kidogo katika mifumo ambayo hayatoshelezi. Naiomba Serikali isaidie, kwani mbali na hivyo vijiji kuna taasisi ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Kuna shida kubwa sana ya maji hapo chuoni. Ninaiomba Wizara iangalie namna ya kusaidia.
Mheshimiwa Spika, nne, Kata ya Arusha Chini yenye wakazi 13,977 kuna shida ya maji katika Vijiji vya Mikocheni na Chemchem. Sasa hivi ni watu wa Kirua Kahe wanatoa huduma ya maji ya kuuza katika maeneo haya. Maji huuzwa kwa bei ya juu na si salama kwa matumizi ya binadamu. Kata hii inahudumiwa na RUWASA. Ninaiomba Wizara ijenge mradi kwa kutumia maji ya kutoka Mto Ronga na Kikuletwa.
Mheshimiwa Spika, tano, katika Kata ya Uru Kaskazini yenye wakazi 10,817 MUWSA haijatekeleza ahadi ya kuunganisha vijiji vya Msuni na Njari. Kuna chanzo cha maji Uru Kaskazini ambacho hupeleka maji Kata ya Uru Kusini na Kata ya Pasua ya Manispaa ya Moshi Mjini. Wananchi wananyanyasika sana kwani maji ya eneo lao hayawasaidii. Ninaiomba Wizara iunganishe Vijiji vya Msuni na Njari ili wananchi wapate maji.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Old Moshi Magharibi, kuna wakazi 8,431 na kuna mradi wa maji wa Tela Mande ambao umekamilika. Mradi huu una maji mengi sana na ya ziada ambayo kwa sasa yanahudumia wananchi wa ukanda wa milimani.
Mheshimiwa Spika, vijiji na vitongoji vya kata hii vilivyopo ukanda wa tambarare kama kile cha Mandaka Mnono na Saningo havina maji ya bomba. Ninaiomba Wizara iwapelekee maji wananchi hawa walioko ukanda wa tambarare.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa, na ninaomba niendelee pale nilipoachia.
Mheshimiwa Spika, kwa pesa ambazo Serikali imetoa katika Wizara hii ya Afya, tumeona Wizara imefanya mambo mengi makubwa ambayo ni faraja kwa Watanzania wote. Kuna huduma za kinga ambapo tunapata chanjo za pepopunda, kifaduro, kupooza, surua mpaka UVIKO. Kuna huduma za lishe, huduma za usafi wa afya na mazingira, huduma za afya mipakani kwa wasafiri wanaoingia Tanzania kuzuia ujio wa magonjwa mapya na huduma za kibingwa ambazo zimefanywa na vijana wetu wa Kitanzania.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Waziri, juzi niliguswa hasa nilipomwona yule mtoto aliyekuwa na Selimundu mkamleta hapa, mkatuambia dada yake, Esther, ndiye aliyetoa uroto akamsaidia kaka yake, na yule mtoto amepona, Waziri na wataalam wetu, tunawapa big up, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, hawa mabingwa wetu wa figo, wa kupasua ubongo bila kupasua fuvu, moyo na Selimundu tuendelee kuwapa nguvu ili waendelee kuwahudumia Watanzania. Chonde chonde, najua mmeshaanza, lakini tuongeze nguvu zaidi, kwa sababu ukienda kwenye Kliniki za Selimundu, utaona ule huruma vile vitoto vinavyoteseka. Kama tiba tayari imeshapatikana, naomba sana tuendelee kuwapa nguvu Wizara ili watekeleze hilo.
Mheshimiwa Spika, niongee kwa kifupi kuhusu Hospitali ya KCMC, ni hospitali bingwa inayofanya vitu vingi. Pale kuna uhaba wa madaktari na watumishi wengine. Wana-operate at fifty percent capacity. Kwa hiyo, naomba mwaongezee watumishi ili waendelee kutoa huduma kwa Watanzania ambao wanaopelekwa pale kupata tiba.
Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie masuala machache kwenye jimbo langu kabla sijachangia kitu ambacho nilitaka kusema. Naishukuru Serikali, imetujengea Hospitali ya Wilaya pale Mabogini. Ni eneo ambalo lina watu wengi, karibu 20.3 percent ya wakazi wa jimbo langu wametoka pale. Kwa hiyo, tunashukuru sana, hospitali ile imekamilika. Naendelea kuomba Wizara itupelekee vifaa, dawa na vitu vingine ili wananchi waanze kupata huduma. Katika Hospitali ya Kibosho, nilikuwa nimemwomba Waziri anipatie digital x-ray, bado wanangojea kule Kibosho Hospital. Chonde chonde, dada yangu Mheshimiwa Ummy, hii ni ahadi, wananchi wanaingojea, mwendelee kutusaidia.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa leo utajikita kwenye changamoto ya watu wenye ulemavu na wanaohitaji viungo bandia. Hapa Tanzania kuna wenzetu wengi ambao wana ulemavu na wanahitaji viungo bandia kwenye miguu na mikono. Kinachosababisha hao watu wawe na ulemavu ni nyingi. Kwanza, wanaweza wakawa wamezaliwa hivyo; ya pili, wanaweza kuwa wamepata ajali; wengine wameugua saratani na kisukari wakaishia kukatwa mikono na miguu; na sasa hivi hali ilivyo, vijana wetu wa bodaboda wamejiajiri kule, wanaendesha boda boda na bahati mbaya tunawagonga, yeye na abiria wanaishia kukatwa mguu au mkono.
Mheshimiwa Spika, sasa idadi ya hawa wagonjwa imekuwa kubwa na ninaomba Serikali iangalie kwa jicho la pekee kwa sababu hili kundi hatujaliangalia vizuri. Linahitaji viungo bandia na hawa watu wanahitaji warudie maisha yao ya zamani ili waweze kuchangia kwenye uchumi wa Taifa, lakini kwa kuwa hakuna hivi viungo, basi wanakuwa na mateso makubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini watu wachache ndio wamepata hii huduma? Ni kwamba, kwanza kabisa hospitali zilizopo zinazotoa huduma ya viungo bandia ni chache hapa nchini. Kwa haraka haraka ninajua kuna KCMC, kuna Bugando Hospital, kuna MOI na Dodoma General Hospital. Hiyo ni sababu ya kwanza. Kwa hiyo, tunaomba huduma hii isambae kwenye hospitali za mikoa ili watu watibiwe kwenye hospitali zao za mikoa huko huko.
Mheshimiwa Spika, sababu ya pili ni gharama za viungo kuwa ni kubwa sana. Viungo bandia, kumwekea mtu mguu, kwa utafiti nilioufanya mimi ni kati ya shilingi milioni 1.5 mpaka shilingi milioni 3.5; na mkono ni kati ya shilingi milioni mbili mpaka shilingi milioni 4.5. Sasa kwa Mtanzania wa kawaida, hao wenye saratani waliokatwa mikono na miguu, ni wazee ambao hawajiwezi kabisa. Kwa Mtanzania wa kawaida, hii gharama ni kubwa sana. Naomba Serikali iwaangalie hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine kikubwa ni kwamba Mfuko wetu wa Taifa wa Bima ya Afya, mfuko wetu pendwa, hautoi huduma kwa viungo bandia. Yaani wewe ukiugua, kama ukikatwa mguu, unatakiwa ujilipie mwenyewe. Namwomba Waziri atakapo kuja ku-wind-up hapa atusaidie kwa sababu kuna watu wanateseka huko, ni wengi kweli kweli.
Mheshimiwa Spika, sasa nitoe ushauri kwa Serikali kwamba, chonde chonde, ijumuishe viungo bandia kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima yetu ya Afya. Watu wanapopata ajali akikatwa mguu, kama anahitaji kiungo bandia, basi iwe kwenye huduma ambazo zinaweza zikatolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima yetu ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu cha pili, naishauri Serikali, ikiwezekana tufanye utafiti. Kuna watu wengi sana wako huko ambao, akishaenda hospitali akiambiwa gharama ni kubwa, anarudi nyumbani kwenda kufa peke yake tu. Tufanye utafiti, tupate kanzidata ya wagonjwa ni wangapi ambao wana hili tatizo ili tuweze kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa tatu kwa Serikali ni kwamba Vyuo vyetu Vikuu vya Afya ambavyo vipo vingi, vimetapakaa nchi nzima, vifundishe wataalam wa hii fani ili waweze kuwahudumia Watanzania wenzao ambao wana hili tatizo. Kama nilivyosema awali, napendekeza pia hii huduma isiishie kwenye zile hospiatli nne tu ambazo zipo sasa hivi, iende kwenye hospitali zote za mkoa. Kila mkoa uwe na kitengo ambacho kitakuwa kinasaidia hawa wagonjwa ambao wana hili tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu mwingine kwa Serikali, ikiwezekana ihamasishe wadau wa maendeleo au Serikali yenyewe, kila mahali penye hii huduma pawe na Unit ya kutengeneza hivi viungo bandia ili watu waweze kupata huduma hapo kwa hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho ni kwamba, wahitimu ambao wameshahitimu hapa nchini, tunao ambao wamesoma KCMC, Serikali iwape ajira na iwapeleke huko mikoani ili waweze kutoa huduma kwa watu ambao wana hili tatizo la viungo bandia.
Mheshimiwa Spika, kingine muhimu, elimu itolewe kwa watu ambao wameshapata hili tatizo kwamba ukikatika mkono au mguu siyo mwisho wa maisha. Unaweza ukavaa kiungo bandia ukaendelea na shughuli zako kama ilivyokuwa awali. Ikiwapendeza, mbadilishe sera itakayotoa umuhimu wa kutatua tatizo hili katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niseme kwamba wagonjwa wengi ambao wana hili tatizo la kukatwa miguu na mikono, hukwazika kwa kiwango kikubwa cha gharama ambazo nimezitaja hapa. Naiomba Serikali, chonde chonde, tuangalie namna ya kuweka kwenye mifumo yetu ili ndugu zetu ambao wamepata haya matatizo waweze kuhudumia na Serikali yao pendwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Afya Ndugu Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Godwin Mollel na wataalam wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanazofanya kwenye kutekeleza wa Ilani ya CCM.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kuhusu changamoto ya watu wenye ulemavu na kuhitaji viungo bandia.
Mheshimiwa Spika, hapa nchini kuna wenzetu waliopatwa na matatizo yaliyosababisha kukatwa viungo vya mwili kama miguu na mikono. Watu hawa wamekuwa wakipambana kuirudisha furaha ya awali ili angalau waweze kushiriki mambo mbalimbali katika jamii ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli zao walizokuwa wakifanya awali.
Mheshimiwa Spika, Mtanzania yeyote anaweza kupatwa na ulemavu wa kiungo kutokana na sababu nyingi ikiwamo kuzaliwa na kilema, ajali na kuugua saratani au kisukari. Kutokana na hilo, idadi ya walemavu wa viungo vya miguu na mikono imekuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, viungo bandia vina nafasi kubwa katika kutatua tatizo hilo. Hapa Tanzania ni watu wachache wameweza kupata huduma na idadi ya waliopo nyumbani ni kubwa zaidi kuliko wanaopata huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, naomba ieleweke kwamba kukatwa kiungo siyo mwisho wa maisha au kushiriki katika shughuli za kimaendeleo. Elimu ikitolewa, tafsiri inaweza kuwa tofauti kabisa na kuwarudishia matumaini ya kuishi Watanzania wenzetu waliokata tamaa.
Mheshimiwa Spika, uhitaji wa viungo bandia hapa nchini umeongezeka sana kutokana na ajali zitokanazo na matumizi ya vyombo vya usafiri kama pikipiki ambapo kumesababisha mrundikano wa wahitaji wa viungo bandia vya miguu na mikono.
Mheshimiwa Spika, waathirika wengi hufika hospitali, lakini wagonjwa hao wanapotajiwa kiwango cha fedha zinazohitajika ili wapatiwe huduma, idadi kubwa huondoka na hawarudi tena kutokana na gharama kubwa.
Mheshimiwa Spika, hospitali chache zenye huduma hizi ni pamoja na KCMC, Bugando, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Dodoma General Hospital.
Mheshimiwa Spika, gharama za huduma hii huwa ni kubwa kutokana na bei ya malighafi ambazo huagizwa kutoka nje ya nchi. Kwa mfano, utafiti niliofanya nimebaini kuwa gharama za kuweka mguu (kutegemea na hospitali) ni kati ya shilingi milioni 1.5 hadi 3.5. Mkono ni takribani shilingi milioni mbili hadi 4.5. Gharama hizi ni kubwa sana kwa Mtanzania wa kawaida.
Mheshimiwa Spika, pamoja na bei kuwa juu, Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) hautoi malipo kwa watu wenye matatizo ya kuwekewa viungo bandia. Hii imekuwa ni changamoto kubwa hasa kwa watoto wanaokua, kwani huhitaji kabadilishiwa viungo mara kwa mara kila maumbile yao yanapobadilika.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naishauri Serikali yafuatayo; kwanza naishauri Serikali kuandaa sera zitakazowezesha upatikanaji wa viungo hivyo kwa urahisi kutokana na hali ya uhitaji kuongezeka.
Pili, naishauri Serikali ijumuishe huduma hizi katika Bima za Afya (NHIF) ili watu waweze kupata huduma hiyo kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika, tatu, naishauri Serikali ifanye tafiti ili kuwa na kanzidata ya waathirika na wahitaki wa viungo bandia.
Nne, naishauri Serikali kupitia vyuo vyetu hapa nchini izalishe idadi ya wataalamu watakaokidhi hitaji la kutoa huduma kwa wahitaji wa viungo bandia hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, tano, naishauri Serikali ipeleke huduma ya viungo katika hospitali zote za mikoa hapa nchini.
Sita, naishauri Serikali ihamasishe wadau kuanzisha vituo vya kutengeneza viungo bandia katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Saba, naishauri Serikali iwapatie ajira vijana wahitimu wa fani ya viungo katika maeneo mbalimbali hapa nchini; na nane, nishauri Serikali itoe elimu kwa uMma kuhusu uwepo wa viungo bandia ili wanufaike na huduma hii.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninakushukuru kwa kunipa fursa na nianze kwa kumpongeza sana Waziri wetu Profesa Adolf Mkenda, Naibu wake Omari Kipanga na Katibu Mkuu Profesa Carolyne Nombo na Wakuu wote wa taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanzia pale alipomalizia mwenzangu, nimpongeze sana Rais kwa kuboresha shughuli za elimu katika nchi yetu kwa sababu anajaribu ku-address, kutatua kero kubwa ambazo ni ujinga, umaskini na magonjwa na Wizara hii inahusika moja kwa moja kwenye kupambana na hivi vitu. Ninaanzia pale Mheshimiwa Sekiboko aliposema kwamba ubora na mimi nitaongelea ubora wa vyuo vikuu. Nataka tulinganishe vyuo vyetu vikuu vya Tanzania na vyuo vya Afrika na duniani kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Tanzania na Afrika Mashariki, Tanzania tunakweda vizuri. Nchi yetu inakua vizuri sana na sisi kama nchi Taifa letu lina miundombinu bora sana ya elimu. Tunatoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita na tunatoa mikopo kwa vijana wetu waweze kusoma. Kwa hiyo suala la kusoma hapa nchini siyo shida. Nchi yetu inajitahidi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilisikiliza taarifa ya habari ya BBC, wakasema kwamba kule Afrika Kusini kati ya watoto 10, nane hawajui kusoma vizuri na kuandika, lakini nchi ya Afrika Kusini katika Bara letu la Afrika ndiyo nchi yenye vyuo bora kuliko nchi zote kwenye Bara la Afrika. Sasa hapa kwetu Tanzania kwenye ubora wa vyuo vikuu tuko vibaya sana, hatuko vizuri. Ni kwa nini, ni nini kinatokea kwamba hata wale ambao asilimia kubwa hawajui kusoma na kuandika wanatupita?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ranking iliyofanyika kuangalia vyuo vikuu bora 200 duniani, Afrika Kusini nafasi ya kwanza mpaka ya tano ilichukuliwa na Afrika Kusini. Chuo Kikuu cha Nairobi kilikuwa cha sita, Chuo Kikuu cha Makerere Uganda kilikuwa cha 16. Chuo Kikuu cha Kenyatta kilikuwa cha 24. Chuo chetu Kikuu cha Dar es Salaam kilikuja cha 34, Chuo Kikuu cha SUA kikawa cha 67, Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili cha 94, State University of Zanzibar cha 163 na UDOM ikawa ya 184. Tunawashukuru hivi vyuo angalau vimetupeleka juu kidogo lakini bado kuna kitu hakiko sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini South Africa wanatushinda na ukiangalia kwa ujumla wake katika hii ranking, vyuo vya Kenya na Uganda vimetupita vibaya sana. Sisi tuko chini kusema ukweli kwenye hii aspect.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wenzetu wamefanikiwa sana kwa sababu wamewekeza kikamilifu kwenye sekta ya elimu na hapa sawa tunakwenda vizuri lakini bado kuna haja ya kuendelea kuwekeza pesa za kutosha kwenye sekta ya elimu ili vyuo vyetu navyo vionekane vizuri kwenye uso wa Kimataifa. Vigezo vinavyotumika kwenye ku-rank hivi vyuo ni vitu vya kwenye mtandao tu, mambo ya kwenye mtandao na sisi kama nchi Tanzania iko vizuri sana kwenye mambo ya mtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wanaangalia kwenye mtandao kama kuna machapisho ya kisayansi yaliyofanywa na wasomi wetu. Kitu cha pili wanachoangalia ni shughuli za kitafiti kwenye mitandao ya vyuo vyetu. Je, kuna shughuli zinazoendelea za kitafiti? Je, chuo kimesajiliwa na mamlaka husika kama TCU? Je, chuo kinatoa degree za kwanza, Master na Ph.D? Hiyo tunafanya. Je, vyuo vinatoa elimu kwa kuwasiliana, wananfunzi wanakaa darasani na kusoma? Vyote hivyo tunafanya lakini bado hatuonekani kwamba tunafanya vizuri kama vyuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili wanachoangalia ni shughuli za kitafiti kwenye mitandao ya vyuo vyetu. Je, kuna shughuli zinazoendelea za kitafiti? Je, Chuo kimesajiliwa na mamlaka husika kama TCU? Je, Chuo kinatoa degree ya kwanza, masters na Ph.D? Je, vyuo vinatoa elimu kwa kuwasiliana, na wanafunzi wanakaa darasani na kusoma? Yote hiyo tunafanya,a lakini bado hatuonekana kwamba tunafanya vizuri kama vyuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanya huku vibaya kunasababishwa na viongozi wetu wa vyuo kukosa ubunifu kuonesha vitu vizuri ambavyo wamefanya. Ubunifu hamna, hiyo ndiyo sababu yangu ya kwanza. Sababu ya pili ni uvivu wa wanasayansi wetu wa Kitanzania kuchapisha, kuandika kwenye majarida ya Kimataifa ili sisi kama Taifa tuweze pia kutamba na kwenda kifua mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya tatu ni tovuti zetu za vyuo vikuu haziweki vitu, hazina taarifa ya vyuo vyetu vikuu. Hakuna taarifa za mambo mazuri tunayofanya. Matokeo mengi ya utafiti ambayo wenzetu wanafanya, yanabakia kwenye makabati na kwenye kuta nne za vyuo vikuu, hayatoki nje ya pale. Hizi ni sababu kubwa ambazo zinatufanya tusionekane tuko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini athari za kupata low rank ya Universities zetu? Athari ya kwanza ni heshima hakuna. Tunakosa heshimia tukijilinganisha na wenzetu wa nchi nyingine. Athari ya pili, ni umaarufu wa Maprofesa wetu na Wahadhiri wetu. Huwezi kujilinganisha kwamba na wewe ni Profesa ukatamba kabisa kama chuo chako hakipo pale, yaani your nowhere, huwezi kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakosa nafasi ya kupata washirika wa kusaidiana nao kufanya utafiti. Huwezi kwenda kwa watu ambao labda ni vilaza ukafanya nao kazi, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kwamba wasomi wetu wanakosa nafasi. Kama hatuko vizuri, tunakosa nafasi kwenye masoko ya Kimataifa. Ushauri wangu nini kifanyike? Cha kwanza namwomba Mheshimiwa Waziri asimamie hili, Wahadhiri wote na wanafunzi wanaofanya Masters na Ph.D wajisajili kwenye Google Scholar, kwani mchakato wa kupata vyuo bora unatokea kwenye Google Scholar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili, watafiti wetu wachapishe kwenye majarida ya kimataifa, tusiende kwenye zile journal za ajabu ajabu ambazo hata hazipo kwenye mifumo. Twende kwenye majarida ya kimataifa kama wanaume na wanawake wenye nguvu pia. (Makofi/Kicheko)
MBUNGE FULANI: Naam!
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia tuwe na sera ya kuweka machapisho yetu kwenye depository vyuo vyote, kwenye library zetu ziweze kuonekana online. Cha nne, tuoneshe abstract, hata tukishindwa kuonesha zile Ph.D na Masters ambazo vijana wetu wameandika, tuziweke online ili wanapochakata na sisi tuonekane tupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha tano, matukio yanayotokea kwenye vyuo vyetu kama mikutano, tukienda kwenye makongamano, wanaangalia vitu vyote hivi viwekwe online ili wanapochakata na sisi tuonekane kwamba huwa tunashiriki kwenye hivyo vitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, pia tukienda kufanya presentations kwenye Mikutano ya Kimataifa tuyaweke kwenye mitandao ya vyuo vyetu. La muhimu hapa niwaombe Wakuu wa Vyuo na Wakuu wa Mabaraza ya Vyuo wasimamie hili kwa sababu kabisa sioni sababu ya sisi kuwa na low ranking. Nchi yetu inawekeza pesa nyingi sana kwenye elimu lakini kweli kabisa hatuko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mimi najua nilitoa mchango wangu na ndiyo sababu nimesimama hapa kwa nguvu kabisa, siogopi kuchangia kwamba tukaze viatu, tukaze uzi, twende vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe kwa kusema kwamba hili suala la kuwa na nafasi za chini kwa vyuo vyetu siyo kitu chema, inatupunguzia heshima ya nchi yetu. Namwomba Waziri achukue hatua makini kabisa mapema kukabiliana na tatizo hili ambalo tukishakabiliana nalo mtatujengea heshima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda na Naibu wake Mheshimiwa Omari Kipanga na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya kwenye kutekeleza Ilani ya CCM.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kuhusu nafasi ya vyuo vikuu vya Tanzania kimataifa, na uhitaji wa kuboresha website za vyuo vyetu ili vionekane kimataifa na kukamata nafasi za juu Barani Afrika na duniani.
Mheshimiwa Spika, Tanzania yetu ni nchi inayokua kwa kasi hapa Afrika Mashariki na kwa kuwa nchi yetu ina muundo bora wa elimu, ni vyema ubora huo ukaonekana katika vyuo vyetu vikuu.
Mheshimiwa Spika, kwenye mpangilio wa vyuo vikuu 200 bora Barani Afrika, kwa kutumia mtandao wa uniRank kwa mwaka huu wa 2023, Chuo Kikuu cha Nairobi ni cha sita kwa ubora, na cha Makerere ni cha 16 kwa ubora na Kenyatta University ni cha 24.
Mheshimiwa Spika, Chuo chetu Kikuu cha Dar es Salaam kimeshika namba ya 34, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ni cha 67, Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili ni cha 94, State University of Zanzibar ni ya 163 na University of Dodoma ni ya 184.
Mheshimiwa Spika, katika vyuo vikuu bora 200, Kenya na Uganda wametuzidi kwa mbali kwenye Ubora.
Mheshimiwa Spika, vyuo vya Afrika Kusini vimeshika nafasi za juu na nyingi Barani Afrika kwa sababu nchi yao imewekeza kikamilifu kwenye elimu ya vyuo vikuu, na vimefanikiwa kwa sababu vina mahusiano mazuri na vyuo vikuu bora duniani ambapo wamekuwa wanajifunza kutoka kwa wenzao kwa kushirikiana katika shughuli za utafiti na programu za kubadilishana uzoefu.
Mheshimiwa Spika, uniRank inatumia vigezo vya kimtandao kuorodhesha vyuo bora Afrika na duniani kwa ujumla. Ubora huo hutegemea machapisho ya kisayansi yaliyofanywa na chou; shughuli za kiutafiti za chou; uwepo wa cheti cha usajili wa chuo na kutambuliwa na Mamlaka za nchi (TCU); chuo kutoa mafunzo ya shahada ya kwanza au za juu (Masters na Ph.D); na chuo kutoa elimu kwa njia ya kawaida ya kuingia darasani na kukutana ana kwa ana na waadhiri.
Mheshimiwa Spika, kufanya vibaya kwa vyuo vikuu vya Tanzania kumesababishwa na viongozi wa vyuo vyetu kukosa ubunifu wa kuonyesha mambo mazuri yanayofanyika vyuoni kwenye mitandao. Pia changamoto ingine kubwa ni kwamba wasomi na watafiti wa Kitanzania katika vyuo vyetu wamekuwa wavivu kuchangia machapisho yao katikaa jukwaa la wasomi duniani. Vilevile website nyingi za vyuo vyetu zinakosa taarifa muhimu za chuo na matokeo ya utafiti hubakia kwenye kuta za chuo.
Mheshimiwa Spika, ubaya wa kushika nafasi za chini kwa vyuo vyetu vikuu inaondoa heshima ya chuo na wafanyakazi katika macho ya wadau, kama vile wanafunzi na wafadhili; umaarufu kidogo wa wafanyakazi wa chuo kwenye wasomi wa vyuo vingine vya ndani na nje; kuathiri ushirikiano na vyuo vingine vikubwa duniani kwenye kufundisha na utafiti. Hawatashirikiana na vilaza; na kukosekana nafasi kwa wasomi wetu katika soko la dunia.
Mheshimiwa Spika, ushauri kwa Wizara na vyuo ni kama ifuatavyo; iwe ni lazima kwa wahadhiri wote wa chuo kujisajili na google scholar (point huchakatwa kutoka huko); walimu na wanafunzi wote wahimizwe kuandika tafiti zao katika majarida ya kimataifa. Tafiti mpya tu ndio hutumika kutoa alama; iwepo sera ya kuweka machapisho yote kwenye repository ya maktaba kuu ya chuo, ni iweze kuonekana kwenye mtandao; walimu wote wahimizwe kuweka machapisho yao kwenye sehemu ya wazi (open source research repository); benki ya machapisho ya chuo kikuu iwe na mfumo wa kuonesha kwenye mtandao vitabu vya degree za Masters na Ph.D; kuwe na mfumo wa online kuonesha abstracts zote za kazi za wanafunzi za Masters na Ph.D; matukio yote muhimu ya chuo yapigwe picha na kuwekwa mtandaoni; wekeni mtandaoni nyaraka za mawasilisho yaliyofanyika katika mikutano au makongamano mbalimbali yaliyofanywa na walimu au wanafunzi katika sehemu duniani.
Mheshimiwa Spika, nihitimishe kwa kusema kwamba nafasi za chini kwa vyuo vyetu vikuu vya Tanzania siyo kitu chema kwani kinapunguza heshima ya nchi yetu kwenye macho ya wadau mbalimbali kama vile wanafunzi watarajiwa, watafiti, wasomi na wafadhili. Ni vyema Wizara ikachukua hatua mapema kukabiliana na tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa na Naibu Mawaziri wake wawili; Mheshimiwa Atupele Mwakibete na Mheshimiwa Godfrey Kasekenya kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye kutengeneza mitandao ya barabara na ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu umuhimu wa kujenga kwa lami barabara ya zamani ya Moshi - Arusha (Old Moshi Road) na changamoto za barabara katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa kwanza ni kuhusu umuhimu wa barabara ya zamani ya Moshi - Arusha (Old Moshi - Arusha Road). Hii ni barabara iliyokuwa imejengwa kwa lami toka wakati wa mkoloni. Kwa upande wa Arusha, kipande cha Mkoa wa Arusha kimeshajengwa na kinaendelea kukarabatiwa kwa kiwango cha lami (Kijenge hadi USA River). Kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro, hakuna ambacho kimefanyika; kwa upande wa Moshi, barabara hii inaanzia keep left inakoanzia barabara ya Arusha kuelekea barabara ya International School kuelekea Daraja la Muitaliano, Magereza, Kwa Akwilini, Weruweru Sekondari kutokea Lambo Estate.
Mheshimiwa Spika, barabara hii ikitengenezwa, itakuwa ni ya mchepuko (bypass) kuingia na kutoka Mjini Moshi kama ilivyo ile ya USA River. Vilevile itakuwa ni ya msaada mkubwa kama kutatokea kikwazo cha aina yoyote ile cha magari kupita kwenye ile barabara kuu ya Arusha - Moshi.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili utahusu changamoto za barabara zinazojengwa na TANROADS Jimboni kwangu.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Moshi Vijijini, barabara ya Kibosho Shine - Mto Sere inahudumiwa na TANROADS. Wameshaweka mitaro katika baadhi ya maeneo, na haijajengwa hata kidogo kwa kiwango cha lami. Barabara hii ni muhimu kwani ni sehemu ya kusafirisha watalii kwenda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Umbwe. Tunaishukuru Serikali kwani kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali wamepanga kukarabati kilometa 2.1 za barabara hii kwa shilingi milioni 119.79.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuendeleza ujenzi wa barabara ya Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni - Kidia kwa kiwango cha lami. Barabara hii inajengwa na TANROADS na bado haijakamilika. Mwaka 2023/2024 barabara hii imetengewa shilingi milioni 160.00 kutoka kwenye Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibosho Shine - Kwa Raphael - International School ilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2005 na inajengwa na TANROADS lakini hadi leo haijakamilika. Bado kipande cha kama kilometa nane. Tunaishukuru Serikali kwani kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kujega kwa kiwango cha lami kipande cha kilometa 0.9 kwa kutumia shillingi milioni 266.2 kwa kutumia Mfuko Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Rau - Uru - Shimbwe yenye urefu wa zaidi ya kilometa 13 ilikuwa kwenye ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Tunaishukuru Serikali kwani ujenzi umeanza na mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 Mfuko Mkuu wa Serikali utajenga kwa kiwango cha lami urefu wa kilometa 1.1 kwa kiasi cha shilingi milioni 325.05, na Road Fund watakarabati kilometa 2.9 kwa kutumia shilingi milioni 105.00.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Uru - Kishumundu Parish - Materuni iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami. Tunaishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Lakini mwaka huu wa 2023/2024 zimetengwa shilingi milioni 79.86 kukarabati kilometa 1.4, na mfuko wa barabara wametenga shilingi milioni 150.00 kuweka lami.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Mabogini inakojengwa Hospitali ya Wilaya kuna changamoto kubwa ya ubovu wa miundombinu ya barabara. Hii inajumuisha barabara ya TPC - Mabogini - Kahe yenye urefu wa kilometa 11.4. Barabara hii imekuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2010 ambapo waliahidi kuitengeneza kwa kiwango cha lami, lakini hadi leo ujenzi haujatekelezwa. Kwa kuwa iko chini ya TARURA na kwa kuzingatia bajeti finyu ya TARURA hadi leo ahadi hiyo haijatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, ni kutokana na hali hiyo, nikiwa kama mwakilishi wa wananchi hawa nilipeleka ombi kwa Baraza la Maendeleo la Mkoa wa Kilimanjaro (RCC) kuipandisha hadhi na kuiombea ihudumiwe na Wakala wa Barabara (TANROADS). Ombi hili liliridhiwa na RCC na bodi toka mwaka 2021.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo ya hapo juu, naishauri Serikali ifanye yafuatayo; kwanza, naishauri Serikali iweke kwenye mipango kujenga barabara ya mchepuo (bypass) kwenye ilikokuwa barabara ya zamani ya Moshi - Arusha. Upande wa Moshi barabara hii inaanzia keep left ya Arusha kuelekea barabara ya International School kuelekea Daraja la Muitaliano, Magereza, Kijiji cha Eka, Kwa Akwilini, Weruweru Sekondari kutokea Lambo Estate.
Mheshimiwa Spika, pili, ninaiomba Serikali itenge fedha za kutosha na ianze kujenga kwa kiwango cha lami kipande cha barabara ya Kibosho Shine - Mto Sere kinachojengwa na TANROADS. Vilevile ninaishauri Serikali ifikirie kujenga kwa kiwango cha lami kipande cha Sere hadi gate la Umbwe la kupanda Mlima Kilimanjaro. Barabara hii ni mbovu mno pamoja na kwamba hutumika kusafirisha watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Umbwe na kuingizia Serikali kipato kupitia sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, tatu, ninaiomba Serikali itenge kiasi cha fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni - Kidia kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, nne, ninaiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa barabara ya Kibosho Shine - Kwa Raphael - International School kwa kiwango cha lami kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2005. Ujenzi wa barabara hii umechukua zaidi ya miaka 13.
Mheshimiwa Spika, tano, ninaishauri Serikali itenge fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Rau - Uru - Shimbwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa zaidi ya kilometa 13 kama wananchi walivyoahidiwa wakati wa kampeni.
Sita, ninaishauri Serikali itenge fedha na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Uru - Kishumundu - Materuni.
Mheshimiwa Spika, saba, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iingize barabara ya TPC - Mabogini - Kahe yenye urefu wa kilometa 11.4 kwenye mtandao wa TANROADS kwani RCC na bodi walikubaliana na ombi hili toka mwaka wa 2021. Ninaiomba Serikali itenge fedha za kutosha na ujenzi wa barabara hii uanze mara moja kwani Hospitali ya Wilaya inajengwa eneo hili.
Mheshimiwa Spika, baada ya ushauri nilioutoa hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na nianze kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Waziri wetu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Majeshi Generali Jacob John Mkunda na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Salim Haji Othman pamoja na Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajab Mabele na Makamanda wote nchi hii kwa kazi nzuri mnayofanya, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu kwa jinsi alivyoipa kipaumbele sekta ya ulinzi kwenye Taifa letu. Tunamshukuru sana Rais wetu kwa hilo kwa sababu, tunaona hata bajeti ya Wizara ya Ulinzi imeongezeka kwa 6.9 percent. Hiyo inaonesha dhamiri njema ya Rais wetu kwenye kuboresha ulinzi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jeshi letu la Wananchi ni Jeshi imara sana na ni Jeshi bora, linaongozwa kwa misingi ya uzalendo, utii na nidhamu ya hali ya juu. Amani tunayoringia hapa nchini kama Watanzania inatokana na uimara wa Jeshi letu. Jeshi letu liko imara na sisi Watanzania tunafurahia sana uwepo wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama Taifa nchi yetu imeshafanya mambo mengi sana ambayo nitataja kwa haraka haraka mambo machache. Kwanza kabisa ilishiriki kwenye vita vya kukomboa Mataifa ya Kusini mwa Afrika. Pili, ikafundisha Majeshi ya Vyama vya Ukombozi katika nchi hizi ambazo tulizikomboa. Tatu, kikubwa kuliko vyote, tulimtandika nduli Iddi Amini na kumsambaratisha moja kwa moja, ile vita ilikuwa nzuri na ni nchi ambayo iliweza kuliondoa Jeshi la nchi nyingine madarakani moja kwa moja na kulisambaratisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile Jeshi letu limeshiriki katika operations mbalimbali hapa duniani kwenye kulinda amani, kikubwa pia, limeshiriki katika shughuli mbalimbali za kuokoa watu, kwa mfano, Mheshimiwa Waziri amesema juzi walikuwa huko Malawi, hapa nchini wala hatusemi. Kule kwangu Kilimanjaro walikuja wakazima ule moto kule mlimani, sisi tunawshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla Jeshi letu ni la Wananchi kwelikweli na siyo mchezo. Ukiangalia kona zote nilizotaja wanafanya mambo ambayo yanaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa katika mchango wangu leo nitajikita kwenye vijana wanaojiunga na JKT, wale wa kujitolea, kwa miaka miwili na wanapoondoka ni nini kinatokea, nitashauri ni nini kifanyike kama makamanda mtanisikiliza.
Mheshimiwa Spika, Jeshi letu la Kujenga Taifa lina lengo la kulea vijana wetu na wanawafundisha vitu vingi sana, ikiwepo umoja, uzalendo, mbinu za kuzalisha mali na mafunzo ya ulinzi, hawa vijana wamepatiwa hivyo vitu, vijana hawa huchaguliwa kwa kuangalia walivyofaulu, kwa mfano, kama wewe ni darasa la saba una cheti, unachaguliwa, wanaenda mpaka form six na ukishinda masuala ya ukakamavu unaingia Jeshini.
Mheshimiwa Spika, wanapoingia kambini vina wetu huwa wanafundishwa na makamanda ambao wamesoma, Jeshi letu lina wasomi wazuri sana kwenye sekta mbalimbali, wanafundishwa na watu wenye degree na diploma. Mafunzo wanayopata kule Jeshini yanakwenda kwenye ulinzi wa Taifa, uzalendo, kilimo, ufugaji, ujenzi, useremala, ufugaji nyuki, ufugaji mifugo na ujasiriamali kwa ujumla hata biashara wanafundishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa katika stadi nilizotaja hapo juu huwa zinatolewa kwa nadharia na vitendo kwa hiyo, hawa vijana wanafundishwa darasani na kwa vitendo na wakitoka pale wanakuwa wameiva vizuri kabisa, lakini baada ya mafunzo ya miaka miwili vijana wetu hawa hurudi uraiani, niwe mkweli, wengi wao huwa hawafanikiwi kuendelea, kwa mfano walivyokuwa kwenye kilimo hawaajiriwi kwenye sekta za kilimo, hawaendi kwenye sekta za mifugo na kwenye ajira za Serikali. Tunalishukuru sana Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto, Uhamiaji na Jeshi la Wananchi Tanzania, huwachukua hawa vijana walio na cheti cha Jeshi na kuwapa kazi. Huwapa kipaumbele cha kuwaajiri, lakini wale waliosoma kilimo na vitu vingine haiwasaidii, haionekani inawasaidia mahali popote pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninafikiria sasa ni wakati ambapo jeshi letu lichukue ushauri wa kushirikiana na mamlaka zinazotoa vyeti vingine. Kwa mfano, nimeona Waziri amesema wana ushirikiano mzuri sana na Wizara ya Kilimo na Mifugo. Washirikianenao sasa watangeneze mitaala inayofaa iwe kwenye National Qualification Framework ili hawa vijana wanapotoka pale wanapofundishwa na Wanajeshi wetu ambao wamesoma, amefundishwa uzalendo yuko vizuri, apate diploma au cheti. Ni kitu kirahisi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule Jeshini kuna kitu ambacho kimeshatokea kwenye Kambi yetu ya Monduli, pale Arusha. Wanashirikiana vizuri sana na chuo cha, taasisi ya Accounts ya Arusha (Institute of Accounts Arusha) na wanatoa degree ya Shahada ya Kwanza ya Sayansi za Kijeshi, hapo wamefanikiwa. Sasa ninashauri JKT ibadilike tuwatafute hawa watu kama ni VETA, mtu wa darasa la saba apate cheti, kama ni mtu wa NACTE apate diploma, na kadhaika hata ikiwezekana degree wapate. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanapotoka hawa vijana wetu wakimaliza haya mafunzo ambayo nimeyataja kwenye hizi sekta ambazo wanawafundisha kule, wakiwa na cheti cha diploma au certificate au degree kutoka Jeshini, nakuhakikishia tutawapigania kama mpira wa kona kuwapa kazi. Kwa sababu watakuwa wamefundishwa ukakamavu, uzalendo na hakuna mtu atakayemkimbia mtu ambaye amepata mafunzo kupitia kwa hawa makamanda wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nihitimishe kwa kusema kwamba naomba hili jambo lipewe kipaumbele ili hii effort ambayo vijana wanatumia miaka miwili isiishie pale ambapo wamepata vile vyeti tu vya Jeshi, wapewe na hizi qualifications nyingine ili waweze kusaidia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi - Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula na Naibu Waziri Mheshimiwa Geofrey Pinda, Katibu Mkuu - Ndugu Anthony Damian Sanga pamoja na wataalam wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia kuhusu umuhimu wa kupima ardhi yote hapa Tanzania, na migogoro ya umiliki ardhi katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kuwa sehemu iliyopimwa na kupatiwa hati hapa Tanzania haijafikia asilimia 30. Hali hii imesababisha Taifa letu kushindwa kuweka mipango thabiti ya maendeleo katika maeneo mbalimbali, na kulinyima Taifa fedha ya kodi ya viwanja vilivyopimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupima ardhi ya Tanzania ni ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Jukumu hili hutekelezwa kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ilivyo sasa hivi kuna umuhimu wa hii tume kupiga kambi kwenye maeneo yote nchini na kusaidia kupima maeneo yote na kuyapatia hati. Watumishi wa tume hii watoke maofisini waende mashambani kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria za Ardhi upimaji wa mipaka ya vijiji ni lazima uwe shirikishi kwa kuwahusisha Halmashauri za Vijiji kwani wao ndio wasimamizi wa ardhi za vijiji. Ni muhimu sana kuwashirikisha ili kuondoa migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili zoezi la upimaji liwe na mafanikio, baada ya makubaliano ya mipaka, ni muhimu kuwekwe alama za kudumu (beacon) au zikatumika alama za kudumu kama vile maumbile ya asili ya kudumu ikiwemo mito au milima. Ni vyema kwenye kuweka kumbukumbu vizuri, muhtasari wa makubaliano yakawekwa kama kumbukumbu ili zitumike kama rejea ikiwa litajitokeza tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu la Moshi Vijijini kuna migogoro ya umiliki wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji katika Kata za Mabogini (Kijiji cha Mserekie) na Arusha Chini (Mikocheni na Chemchem) zilizoko maeneo ya tambarare.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii imeshasababisha madhara makubwa ikiwemo vifo na uharibifu mkubwa wa mali kama mazao ya wakulima. Mpaka sasa Serikali ya Wilaya na Mkoa haijaweza kupambana na changamoto hii, kwani tatizo hili linajirudia mara kwa mara. Migogoro ya wakulima na wafugaji jimboni kwangu inasababishwa na uhaba unaoendelea kukua wa rasilimali ardhi. Kutokana na hali hii, wakulima wamekuwa wanafungua mashamba kwenye maeneo ya wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii kwa kiasi kikubwa husababishwa na yafuatayo; kwanza, Serikali haijayapima maeneo ya wafugaji na wakulima na kuyamilikisha kwa wahusika kwa kutoa hati za kimila na za Serikali.
Pili, kubadilika kwa tabia nchi kunakopelekea malisho kukauka na kusababisha uhaba wa chakula cha mifugo na kuwafanya wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima; na tatu, kupanuka kwa shughuli za kilimo na makazi ya watu ambapo maeneo ya ufugaji yamepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hii ninaishauri Serikali kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri fedha za ndani za Serikali na zile za mikopo kutoka nje zitumike vizuri kuwezesha Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kukamilisha jukumu lake la kupima ardhi yote ya Tanzania. Idadi kubwa iende kazini na si kwenye makongamano, mafunzo na semina.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na migogoro inayoendelea jimboni kwangu, kuna umuhimu wa Serikali kuingilia jambo hili na kuhakikisha kuwa maeneo husika yamepimwa na kumilikishwa rasmi kwa wahusika. Pa kuanzia Serikali iharakishe zoezi hili kwa kutumia mifumo ya hati za kimila zinazotambuliwa kisheria na baadaye wapewe hati za Serikali za kumiliki ardhi.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mazingira ya Kitanzania, ninaishauri Serikali ipitie sera za umiliki wa ardhi zenye utata zinazoweza kuchochea migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Sera nzuri na rafiki itasaidia kutoa haki bila malalamiko.
d) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali, Wizara za sekta husika (Ardhi, Kilimo na Mifugo na Uvuvi) zishiriki kikamilifu kwenye zoezi hili, na kila Wizara itenge bajeti ya kusaidia kupima ardhi na kushughulikia changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax na Naibu wake Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbaroruk na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya na mchango wangu utajikita kwenye suala la uraia pacha hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Watanzania wenzetu ambao wamezaliwa hapa nchini wakiwa na uraia wa asili wa kuzaliwa hapa Tanzania. Wenzetu hawa wengi waliondoka wakiwa watu wazima na uraia wetu wa kuzaliwa kwenda nje ya nchi na kupata uraia wa nchi nyingine kama sharti la kupata ajira huko ughaibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia tukitafakari kwa undani, hawa ndugu zetu waliomba uraia wa nchi hizo kwa sababu za kiuchumi na ustawi wao wa kijamii na hii haiondoi ukweli kwamba wao ni Watanzania kwa kuzaliwa na kwa damu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria yetu ya Tanzania hairuhusu uraia pacha. Mtanzania akishapata uraia wa nchi nyingine, moja kwa moja sheria yetu inamnyang'anya uraia wa Tanzania. Baada ya kuukosa uraia wa Tanzania, miongoni mwa haki wanazozikosa nchini walikozaliwa ni pamoja na kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi na kutokuchagua viongozi wala kushiriki kugombea nafasi ya umma katika uchaguzi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uraia wa Tanzania unaongozwa na Sheria ya Uraia Sura ya 357 Toleo la mwaka 2002 ambapo Serikali hairuhusu uraia pacha kwa watu wazima isipokuwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 ambao wanakuwa na uraia wa Tanzania na uraia wa nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na kilio cha kuomba uraia pacha kutoka kwa wenzetu waliozaliwa Tanzania kiasili na kupata uraia wa nchi nyingine, wakati sasa umewadia kwa Serikali yetu kuangalia muswada huo wa sheria na kuruhusu uraia pacha nchini kwa kuyaangalia maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia, inafaa uraia pacha utolewe kwa wale ambao walizaliwa Tanzania na kupata uraia wa nchi nyingine. Tumeona sehemu zilizoruhusu uraia pacha kwenye baadhi ya nchi kumewezesha kupata viongozi wa juu wanaoongoza mataifa makubwa na mfano mzuri ni Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ambaye ana asili ya Taifa la India.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uraia pacha utaruhusu yafuatayo; kwanza Watanzania wanaoishi nje ya nchi watapata haki za kumiliki mali na ardhi, kufanya biashara, kupata huduma za afya, na kushiriki katika shughuli za kisiasa; pili, itawawezesha diaspora kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiutamaduni ya nchi yao. Diaspora hawa huko waliko tayari wameshasaidia kudumisha na kukuza utambulisho wa Kitanzania; na tatu uraia pacha utawawezesha Watanzania wenzetu kushiriki kikamilifu na kuleta miradi ya maendeleo ya jamii, elimu, afya na mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, diaspora inayokuwa na uraia pacha inaweza kuleta ujuzi, maarifa na mtaji wa kiuchumi kutoka nchi wanazoishi kuja Tanzania. Hii inaweza kusaidia katika kukuza sekta mbalimbali za uchumi kama vile viwanda, kilimo, utalii na huduma za kitaalamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, raia kutoka nchi jirani za Afrika Mashariki kama vile Kenya, Rwanda na Uganda zimeruhusu uraia pacha. Ni vyema ikiipendeza Serikali yetu kujifunza kutoka kwa majirani zetu na kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, kuna umuhimu wa kuangalia sheria yetu ya uraia wa Tanzania na ikiipendeza Serikali ifanye mabadiliko ya sheria ili kuruhusu kuwezesha uraia pacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Nishati Mheshimiwa January Makamba na Naibu wake Mheshimiwa Stephen Byabato pamoja na jopo la wataalam wa Wizara kwa kazi kubwa wanazofanya kupeleka umeme na nishati nyingine muhimu kwa wananchi wetu hapa nchini Tanzania.
Mheshimwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuongeza bajeti ya Wizara hii kutoka shilingi trilioni 2.91 kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 hadi shilingi 3,048,632,519,000 kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu kukosekana umeme katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Moshi Vijijini ambayo hayajaunganishwa.
Mheshimwa Spika, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupeleka umeme vijijini, bado wananchi wengi wa Jimbo la Moshi Vijijini hawajapatiwa nishati ya umeme.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi ninaiomba Wizara ya Nishati isaidie kutatua changamoto za nishati ya umeme katika Jimbo langu la Moshi Vijijini kwani bajeti iliyotengwa ni kubwa na Wanamoshi Vijijini watafurahia kufikiwa.
Mheshimiwa Spika, maeneo yenye changamoto ya umeme katika Jimbo la Moshi Vijijini ni kama ifuatavyo; Kata ya Mabogini; kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, katika Kata ya Mabogini sehemu ambazo hazijapata umeme hadi sasa ni Vitongoji vya Sanya "Line A" na Mjohoroni vilivyopo katika kijiji cha Mabogini.
Pia katika Kitongoji cha Uru - katika Kijiji cha Muungano; katika Kijiji cha Maendeleo, Vitongoji vya Mshikamano na Uarushani; Mgungani - katika Kijiji cha Mtakuja; katika Kijiji cha Mserekia, hakuna umeme katika Vitongoji vya Mbeya Kubwa, Mbeya Ndogo, Remit, Mkwajuni na Mafuriko. Kijiji cha Mji Mpya, Kitongoji cha Utamaduni hakijaunganishwa. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye maeneo yaliyotajwa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Arusha Chini kwenye Kijiji cha Mikocheni, Vitongoji vya Masaini na Mashimo ya Mchanga hakuna umeme. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye maeneo haya.
Aidha katika Kata ya Kimochi, Kitongoji cha Kiwalaa kilichopo Kijiji cha Sango; Kitongoji cha Iryaroho kilichopo katika Kijiji cha Mowo; na Kitongoji cha Maryaseli katika Kijiji cha Lyakombila havina umeme. Ninaiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo niliyotaja hapo juu.
Katika Kata ya Kibosho Mashariki kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, Kata ya Kibosho Mashariki inahitaji huduma katika Kijiji cha Sungu Vitongoji vya Kyareni na Nkoitiko havijaunganishwa; katika Kijiji cha Singa, Kitongoji cha Singa Juu hakijaunganishwa; katika Kijiji cha Mweka, Kitongoji cha Mweka Juu na Omi havijaunganishwa. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vijiji na vitongoji vilivyotajwa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Kibosho Kati kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, katika Kata ya Kibosho Kati, vijiji vya Uri na Otaruni umeme una nguvu kidogo (low voltage) na kunahitajika transfoma. Katika Kijiji cha Otaruni, Kitongoji cha Ngoroshi hakuna umeme, na tunaomba wananchi wapatiwe huduma.
Katika Kata ya Okaoni - Vijiji vya Sisamaro, Omarini na Mkomilo vinahitaji kuunganishwa japo baadhi ya maeneo nguzo zimepita ila bado kuunganishwa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Kindi, Kijiji cha Chekereni Weruweru, Vitongoji vya Miembeni na Kisiwani havina umeme kabisa. Pia baadhi vitongoji vya vijiji vya Kindi Juu na Kindi Kati havijapata umeme, ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vijiji na vitongoji hivi.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Uru Mashariki, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, Kijiji cha Materuni, Kitongoji cha Wondo hakijaunganishwa. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye kitongoji hiki.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Mbokomu ni kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, Kitongoji cha Mmbede Kyaroni, Tema na Masanga na baadhi ya maeneo ya Korini Kati havijaunganishwa. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana (Mb) na Naibu wake Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma (Mb), Katibu Mkuu Bwana Saidi Yakubu, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Nicholaus Mkapa pamoja na timu ya wataalam kutoka Wizarani kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye utekelezaji wa agizo la Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kujadiliana na mamlaka husika kurudisha mafuvu ya vichwa vya machifu wetu na vyombo vya sanaa vilivyochukuliwa kikatili na kupelekwa Ujerumani na wakoloni. Agizo hili alilitoa kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni Kilimanjaro lililoandaliwa na uongozi wa machifu wa mkoa huo tarehe 22 Januari, 2022. Suala hili linazihusu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mamia ya mafuvu ya binadamu yaliyochukuliwa na Wajerumani kutoka makoloni yake ya zamani ikiwemo Tanzania. Inakadiriwa kuwa kuna mafuvu zaidi ya 200 kutoka Tanzania ambayo yako Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mafuvu ya watu maarufu ni pamoja na majemedari wa kabila la Wangoni wajulikanao kama Nduna na Mbano kutoka Songea. Wengine ni Machifu maarufu kama Mkwawa wa Iringa, Sina wa Kibosho, Meli wa Old Moshi na wengine wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuvu hayo yalichukuliwa na Wajerumani kutoka kwenye maeneo ya maziko hasa makaburi. Mengine yalichukuliwa kutoka kwenye maeneo ya kunyongea watu yaliyokuwa yameasisiwa na Wajerumani hapa Tanzania. Kwa mfano, eneo alikonyongewa Mangi Meli wa Old Moshi katika Jimbo la Moshi Vijijini limehifadhiwa kama sehemu ya makumbusho kule Moshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mangi Meli aliuawa mwaka 1900 kwa kupambana dhidi ya utawala wa ukoloni wa Ujerumani. Baada ya kuuawa mwili wake ulikatwakatwa na kichwa chake kikasafirishwa kwenda nchini Ujerumani. Pia kichwa cha Chifu Mkwawa kilikatwa na kupelekwa Ujerumani akiwa kwenye mapambano na wakoloni wa Kijerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kilio kikubwa hapa nchini Tanzania kutoka kwa makabila yenye mashujaa hawa kutaka masalia ya mafuvu ya wapendwa wao kurudishwa nchini. Kilio hiki ni pamoja na kurudisha mafuvu wa Machifu Sina wa Kibosho na Meli wa Old Moshi ambao wametokea Jimbo la Moshi Vijijini, hili ni jimbo langu la uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hili, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika tamasha la Utamaduni, Kilimanjaro lililoandaliwa na uongozi wa machifu wa mkoa huo tarehe 22 Januari, 2022 aliagiza majadiliano ya kurudisha mafuvu ya vichwa vya machifu wetu yafanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakfu wa urithi wa kitamaduni wa Prussia huko Berlin, Ujerumani umeridhia kurejesha mabaki kadhaa ya binadamu na kazi za sanaa ambazo ziliibwa na Wajerumani walipokuwa wanatawala baadhi ya nchi za Kiafrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa zinazoeleza kuwa watafiti wa Ujerumani wameshafanya utafiti wa kuyatambua mafuvu kutoka Tanzania. Kwa mfano, katika utafiti huo, mjukuu wa Mangi Meli kutoka Old Moshi alifanyiwa vipimo vya kinasaba (DNA) ili kusaidia kusaka fuvu la babu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana, wawakilishi kutoka Ujerumani walilitembelea Bunge letu hapa Dodoma na wanashauku kubwa ya kukamilisha zoezi hili. Ninaishauri Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Maliasili na Utalii walivalie njuga jambo hili kwa pamoja na kukamilisha zoezi la kurudisha mafuvu ya mashujaa wetu nchini Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) na Naibu wake Mheshimiwa Hamad Hassan Chande (Mb), Katibu Mkuu Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Naibu Makatibu Wakuu Lawrence Mafuru, Jenifa Omolo na Amina Shaaban na wataalamu wa Wizara, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na wadau wa maendeleo wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya katika sekta ya fedha na uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni ulizuka mzozo kati ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo na Serikali ambapo wafanyabiashara walifunga biashara zao kwa takribani siku mbili. Mambo makubwa waliyolalamikia wafanyabiashara wa soko hili ni usajili wa store zao za mizigo wasioutaka, tuhuma za rushwa kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wasio waaminifu, kamatakamata na kunyanyaswa na kikosi kazi (Task Force) cha TRA, viwango vikubwa vya makadirio ya kodi na utitiri wa kodi. Mpaka wafanyabiashara walipogoma, walijihisi kuwa Serikali iliwakamua sana na walikuwa na hofu ya kumaliza mitaji yao na biashara zao kufilisika kwani wakusanya kodi na ushuru walikuwa wanachukua zaidi ya kile walichokuwa wanazalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kwa busara zake na kuutatua huu mgogoro kisiasa. Soko la Kariakoo linahudumia wafanyabiashara kutoka mikoa yote Tanzania na nchi za nje kama Demokrasia ya Watu wa Congo (DRC), Burundi, Malawi, Zambia, Rwanda na Uganda likiwa linaendeshwa na wafanyabiashara wakubwa, wadogo na wachuuzi. Wote hawa huliingizia Taifa letu kipato cha kutosha. Inakadiriwa kwamba soko la Kariakoo linaweza kuiingizia Serikali mpaka zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa mwezi kama malipo ya kodi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, soko la Kariakoo likitetereka, matokeo yake ni mabaya kwani kwani litaathiri biashara nchi nzima na nchi za jirani ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato hapa nchini. Kutokana na umuhimu wa soko hili kwa uchumi wa Taifa letu, ni vyema Serikali ikajipanga na kukwepesha mgogoro wa aina yoyote ule na hiki chanzo kikubwa cha mapato. Tujikumbushe kwamba ni mara ya kwanza toka tupate uhuru kuona tukio baya la mgomo katika soko letu la Kariakoo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna umuhimu mkubwa wa kuipa moyo na kuisaidia hii sekta binafsi ili waendeshe shughuli zao wakiwa na utulivu. Wakikatishwa tamaa na kuziacha biashara zao, madhara yake yatakuwa makubwa kwa Taifa letu. Kutokana na fundisho tulilolipata huko Kariakoo, naishauri Serikali ipeleke Bungeni sheria zinazolalamikiwa na wafanyabiashara na kuzifanyia marekebisho ili ukusanyaji ufanyike kwa kutumia sheria na kanuni rafiki za kikodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla, ni vyema kupitia upya na kuangalia baadhi ya vipengele vya Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Tozo za Huduma ya Bandari, Sheria ya Magari (kodi katika usajili na kuhamisha umiliki), Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sheria ya Forodha (Usimamizi na Ushuru) Sheria ya Rufaa ya Mapato ya Kodi, Sheria ya Serikali za Mitaa (Ukadiriaji) na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema Waziri akaja na mapendekezo yake katika kipindi hiki cha bajeti ili kuhakikisha Serikali inazikabili changamoto za kibiashara kwa wafanyabiashara wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, napendekeza utafiti unaofanywa na Wizara uwe endelevu na ulenge kuibua fursa mpya za mapato ya kodi na yasiyo ya kikodi ili kuongeza wigo wa walipakodi na kuondokana na kuwategemea walipakodi wachache kuiendesha nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa hotuba nzuri ya Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ile ya Bajeti Kuu ya mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, michango yangu itajikita kwenye mambo yafuatayo nikianza na migogoro ya Ushirika Mkoani Kilimanjaro; kumekuwepo na migogoro mingi inayohusisha uporaji wa mashamba au matumizi mabaya ya mashamba yanayomilikiwa na vyama vingi vya ushirika mkoani Kilimanjaro. Mengi ya mashamba haya ni yale yaliyotaifishwa na Serikali kufuatilia kuanzishwa ka Azimio la Arusha na kukabidhiwa vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Spika, migogoro hii inasababishwa na viongozi wa ushirika na imezidi kutafuna wananchi masikini hususani wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro. Kwa kiasi kikubwa migogoro hii husababishwa na viongozi wa bodi za vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Spika, utafiti niliofanya unaonesha kuwa katika Wilaya za Siha, Hai, Rombo na Moshi kuna migogoro ambayo Serikali inapaswa kuweka jicho ili kulinda mali za wakulima maskini ambao wanatapeliwa mashamba yao na wajanja wachache. Kwa mfano, katika Wilaya ya Siha upande wa West Kilimanjaro kuna shida kubwa na wananchi wanaishi kama wakimbizi kwa sababu ardhi imehodhiwa na watu wachache kinyume cha matakwa ya wanaushiriia wengi.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ichukue hatua ya makusudi kuyanusuru mashamba haya kwa manufaa ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu ukataji holela wa miti ya asili na uharibifu wa vyanzo vya maji mkoani Kilimanjaro; huku mkoani Kilimanjaro katika Wilaya za Siha, Hai, Moshi na Rombo kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa kukata miti ya asili kama vile Mikufi katika maeneo ya mtoni ambako kuna vyanzo vya maji. Majangili hutumia chainsaw kuangamiza rasilimali za asili za Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, jambo hili limekuwa ni changamoto inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na tayari limesababisha mito kukauka na kuathiri upatikanaji wa maji ya kunywa na ya kumwagilia mashamba. Ninaishauri Serikali ichukue hatua kali mapema za kulinda maeneo haya. Katika jambo hili kubwa sheria za nchi zizingatiwe ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika kusababisha uharibifu kwa kuzishirikisha idara za misitu, mamlaka za maji na jeshi kulinda na kutunza vyanzo hivyo.
Kuhusu migogoro katika vyanzo vya maji mkoani Kilimanjaro; baadhi ya maeneo ya Jimbo la Moshi Vijijini yanakabiliwa na shida kubwa ya majisafi na salama ya kunywa. Juhudi kubwa zimefanywa na mamlaka husika kuwapelekea wananchi maji kupitia miradi inayofadhiliwa na Serikali mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, inasikitisha kuona kwamba baadhi ya wananchi walio karibu na vyanzo vya maji katika maeneo ya Moshi Vijijini (Kimochi, Oldmoshi Mashariki, Kibosho Kati) wanapinga miradi hiyo isijengwe pamoja na wenzao kukabiliwa na shida kubwa ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana kuhusu umiliki wa rasilimali hizi za maji. Kuna wanaofikiria hizo rasilimali ni mali zao binafsi na si za Taifa kama sheria inavyotamka.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii, kumekuwepo na changamoto kwenye ujenzi wa miradi ya maji. Kwa makusudi, baadhi ya wananchi wenye nia ovu wamekuwa wa kuzuia na kuhujumu ujenzi wa miradi katika maeneo niliyotaja. Kwa mantiki hii, ninaishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu rasilimali za maji na umuhimu wa kushirikiana ili kulinda na kupeleka huduma ya maji kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, changamoto zinazokikabili Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka; kuna changamoto zinazokikabili Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka ambazo kwa kiwango kikubwa zimeshusha hadhi yake ya kuwa Chuo cha Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto hiyo ni kupungua kwa idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaojiunga na Chuo hicho kila mwaka. Changamoto iliyopo ni ile ya masharti magumu kwenye mfumo wetu yanayosababisha baadhi ya masomo yanayotolewa na nchi nyingine yasitambuliwe chuoni hapo kwa wanafunzi wanaotoka nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hili, ni vyema vyombo vyetu vya udhibiti na usimamizi wa elimu hapa nchini (TCU na NACTE) viangalie namna ya kurekebisha kanuni ili kuruhusu wanafunzi kutoka mataifa ya nje kuja na kupata elimu hapa nchini. Hii ni pamoja na kutambua sifa, vyeti na masomo yanayotolewa na nchi nyingine katika udahili hapo chuoni Mweka.
Mheshimiwa Spika, baada ya mchango yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari - Ndugu Nape Nnauye na Naibu wake Engineer Kundo Mathew na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu la Moshi Vijijini kuna maeneo ambayo yana changamoto kubwa ya mawasiliano kutokana na kutokuwa na mvuto wa kibiashara na mashirika ya kibiashara (Tigo, Vodacom, Ttcl, Halotel, Airtel) hayajawekeza kwenye maeneo haya. Maeneo haya yanahusisha vijiji vilivyopakana na Mlima Kilimanjaro katika kata za Kibosho Magharibi, Kibosho Okaoni, Uru Kaskazini na Oldmoshi Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishauri Serikali kupitia kwenye Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iwekeze na kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo haya. Kata hizi ni za kimkakati kwani baadhi zina njia za kitalii za kupeleka watalii katika Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa UVIKO-19, mikutano ya ana kwa ana ilisitishwa kwa kuwa nchi nyingi zilijifungia ili kulinda raia wao na maambukizi ya UVIKO-19. Majukwaa maarufu ya Zoom, Skype, GoToMeetings, Microsoft Teams, na Google Hangouts yalitumika kwenye mikutano kwa njia ya mtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukwaa haya yamesaidia sana nchi yetu kwa kiasi kikubwa, hata hivyo, haikua rahisi kuandaa na kushiriki matukio mbalimbali kwa njia hii. Moja ya changamoto kubwa zaidi ni gharama kubwa za mtandao wa internet na uwezo hafifu wa mitandao. Pia ni kawaida kwenye maeneo yetu kuona upatikanaji wa huduma ya internet ikibadilika mara kwa mara kutegemeana na mahali mtumiaji alipo. Kwa mfano, wakati mtu akiwa kwenye mawasiliano, mitandao hukatika mara kwa mara wakati shughuli zikiendelea na kuwaaacha washiriki njia panda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hizi, ninaishauri Serikali iboreshe miundombinu ya mawasiliano katika maeneo yote muhimu hapa Tanzania. Maboresho haya yatasaidia kuifungua nchi hasa kwa kuzingatia kuwa tunategemea kupata watalii wengi baada ya kampeni ya Rais ya Royal Tour.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili unahusiana na huduma za habari na mawasiliano kwa watu wenye ulemavu wa usikivu (viziwi) nchini Tanzania. Kwenye hili bado kuna changamoto licha ya juhudi za Serikali za kulisaidia kundi hilo lipatiwe huduma. Viziwi ni moja kati ya makundi ya watu wenye ulemavu wanaohitaji huduma maalumu kupata habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo waliyonayo viziwi huwakwaza katika mawasiliano katika mazingira wanayoishi na hivyo kuwaathiri kwa njia nyingine mbalimbali katika nyanja za elimu, mahusiano na maendeleo ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya viziwi ni ya kimawasiliano na kwa hiyo hayaonekani kwa macho, viziwi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kusahaulika katika utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali iwekeze kikamilifu na kuweka miundombinu na rasilimali watu ya kutosha ili kundi hili lipate haki yao ya msingi ya kupata habari na kuwasiliana na jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezuka tabia mbaya ya kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya YouTube na matapeli wa mitandao ya simu kwa kutumia majina ya watu maarufu. Baadhi ya taarifa zimesababisha kero, usumbufu na kuvunja heshima na haki za kibinadamu kwa wahusika kwa kuwasingizia mambo yasiyo na ukweli. Suala hili linasababisha taharuki na kuvuruga haki za kibinadamu kwa walengwa. Video hizi za YouTube husababisha hasara kwa watumiaji kwani watu hugharamia kununua bundle na kuishia kupata habari potofu. Matapeli wa simu wanaotumia majina ya watu maarufu hutapeli watu na kuomba fedha haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali ichukue hatua za haraka kukabiliana na tatizo la taarifa za uongo za waandishi wa YouTube na matapeli wa simu kwa mtazamo wa kulinda haki za binadamu kwa waathirika ikizingatia misingi ya kisheria na kisera inayosimamia tasnia ya habari Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na TCRA iweke utaratibu wa kuwabaini na kuwachukulia hatua waandishi wanaokiuka maadili kwenye mtandao wa YouTube na matapeli wa simu. Adhabu kali zikitolewa, mambo haya yatapotea kwenye jamii yetu ya Kitanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa na Naibu Mawaziri wake wawili; Mheshimiwa Atupele Mwakibete na Mheshimiwa Godfrey Kasekenya kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye kutengeneza mitandao ya barabara na ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kuhusu reli ya TAZARA na changamoto za barabara katika Jimbo la Moshi Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa kwanza ni kuhusu umuhimu wa reli ya uhuru ya TAZARA. Reli hii inayomilikiwa na Serikali ya Tanzania (50%) na Zambia (50%) ilianza kazi yake mwaka 1976 ikiwa na mashine 102. Lakini taarifa za hivi karibuni zinaonesha kwamba hivi sasa ziko engine 14 tu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii, changamoto kubwa ya TAZARA kwa sasa hivi ni vitendea kazi duni. Reli hii ilianzishwa ikilenga kusafirisha shaba ya Zambia pamoja na kuingiza bidhaa Zambia kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba reli hii ni kitega uchumi muhimu, katika miaka ya hivi karibuni matumizi ya reli hii yamedorora sana. Mizigo mingi kwenda nchi jirani husafirishwa kwa malori jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa barabara. Kama hatua stahiki zingechukuliwa kuboresha miundombinu ya reli hii, mizigo kwenda Zambia, Malawi na eneo la Kusini ya Congo ingesafirishwa kutokea bandari ya Dar es Salaam na kuipatia Serikali kipato cha uhakika.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili ni kuhusu changamoto za barabara katika Jimbo langu la Moshi Vijijini. Kata ya Mabogini inakojengwa Hospitali ya Wilaya kuna changamoto kubwa ya ubovu wa miundombinu ya barabara. Hii inajumuisha barabara ya TPC - Mabogini - Kahe yenye urefu wa kilometa 11.4. Barabara hii imekuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2010 ambapo waliahidi kuitengeneza kwa kiwango cha lami, lakini hadi leo ujenzi haujatekelezwa. Kwa kuwa iko chini ya TARURA, na kwa kuzingatia bajeti finyu ya TARURA, hadi leo ahadi hiyo haijatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, ni kutokana na hali hiyo, nikiwa kama mwakilishi wa wananchi hawa, nilipeleka ombi kwa Baraza la Maendeleo la Mkoa wa Kilimanjaro (RCC) kuipandisha hadhi na kuiombea ihudumiwe na Wakala wa Barabara (TANROADS). Ombi hili liliridhiwa na RCC na bodi toka mwaka wa 2021.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Moshi Vijijini, barabara ya Umbwe - Sere inahudumiwa na TANROADS. Wameshaweka mitaro katika baadhi ya maeneo na haijajengwa hata kidogo kwa kiwango cha lami. Barabara hii ni muhimu kwani ni sehemu ya kusafirisha watalii kwenda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Umbwe.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuendeleza ujenzi wa barabara ya Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni - Kidia ambayo itaunganisha makao makuu ya Halmashauri ya Moshi kwa kiwango cha lami. Barabara hii inajengwa na TANROADS na bado haijakamilika.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibosho Shine - Kwa Raphael - International School ilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2005 na inajengwa na TANROADS lakini hadi leo haijakamilika. Bado kipande cha kama kilometa nane.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Rau - Uru - Shimbwe yenye urefu wa zaidi ya kilometa 13 ilikuwa kwenye ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahadi hii ilitolewa na Rais. Pamoja na kuikumbusha Serikali kwa kuuliza swali Bungeni, bado ujenzi wa barabara hii haujapewa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Uru - Kishumundu - Materuni iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami. Lakini hadi sasa hatujaona nia ya Serikali kutekeleza ahadi hii.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo ya hapo juu, naishauri Serikali ifanye yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ninaishauri Serikali za Tanzania na Zambia wakae na kuangalia uwezekano wa kuiboresha reli ya Uhuru. Hii ni pamoja na kufanya maboresho ya ile mikataba na sheria ya awali ya kuanzishwa mradi huu ili viendane na hali halisi ya sasa hivi tofauti na ilivyoanzishwa mwaka 1976.
Mheshimiwa Spika, pili, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iingize barabara ya TPC - Mabogini - Kahe yenye urefu wa kilometa 11.4 kwenye mtandao wa TANROADS kwani RCC na bodi walikubaliana na ombi hili tangu mwaka wa 2021. Ninaiomba Serikali itenge fedha za kutosha na ujenzi wa barabara hii uanze mara moja kwani Hospitali ya Wilaya inajengwa eneo hili.
Mheshimiwa Spika, tatu, ninaiomba Serikali itenge fedha za kutosha na ikamilishe kipande cha barabara ya Kibosho Shine - Mto Sere kinachojengwa na TANROADS. Vilevile ninaishauri Serikali ifikirie kujenga kwa kiwango cha lami kipande cha Sere hadi geti la Umbwe la kupanda Mlima Kilimanjaro. Barabara hii ni mbovu mno pamoja na kwamba hutumika kusafirisha watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Umbwe na kuingizia Serikali kipato kupitia sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, nne, ninaiomba Serikali itenge kiasi cha fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni - Kidia kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, tano, ninaiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa barabara ya Kibosho Shine - Kwa Raphael - International School kwa kiwango cha lami kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2005. Ujenzi wa barabara hii umechukua zaidi ya miaka 12.
Mheshimiwa Spika, sita, ninaishauri Serikali itekeleze ahadi ya kujenga barabara ya Rau - Uru - Shimbwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa zaidi ya kilometa 13 kama wananchi walivyoahidiwa wakati wa kampeni.
Saba, ninaishauri Serikali itenge fedha na kuanza ujenzi wa barabara ya Uru - Kishumundu - Materuni.
Mheshimiwa Spika, baada ya ushauri niliotoa hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mifugo na Uvuvi Ndugu Mashimba Ndaki, Naibu wake Ndugu Abdalah Ulega, wataalamu wa Wizara na wadau wa sekta hizi kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kilimanjaro una fursa nyingi za kufuga aina mbalimbali za wanyama kama vile ng’ombe na mbuzi wa maziwa na nyama, kondoo, nguruwe, sungura, kuku, bata na samaki kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya mlimani (Kilimanjaro) yanaweza kutumika kwa ufugaji wa ndani (zero grazing) kwa ng’ombe wachache na mbuzi wa maziwa, nguruwe, sungura, kuku na bata.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la ukanda wa tambarare kwenye Kata za Arusha Chini na Mabogini lina wafugaji wa Kimasai na lina uwezekano wa kuzalisha kwa tija ng’ombe, mbuzi na kondoo wa nyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi za wafugaji wa Jimbo la Moshi Vijijini, aina za kienyeji za wanyama (ng’ombe, mbuzi, nguruwe na kuku) wanaofugwa ni kikwazo kikubwa kwenye maendeleo ya sekta ya mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya uvuvi inaweza kuwapatia wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini kipato kikubwa iwapo itaendelezwa. Hili litawezekana ikiwa wananchi watapatiwa mafunzo ya kitaalamu ya jinsi ya kufuga na kukuza samaki kwa kutumia teknolojia ya mabwawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufugaji endelevu wa samaki unaweza kutatua changamoto za umaskini kwa kuwaongezea kipato na kuchangia kikamilifu kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Arusha Chini kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu, wavuvi wanaweza kusaidiwa na Maafisa Ugani wa uvuvi mbinu bora za ufugaji wa samaki, ikiwepo matumizi ya vizimba. Uwekezaji wa vizimba unaweza kufanyiwa majaribio kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha ufugaji wa ng’ombe, mbuzi wa maziwa na nyama, kondoo, nguruwe, sungura, kuku, bata na samaki katika Jimbo la Moshi Vijijini, ninaishauri Wizara itusaidie yafuatayo:-
Kwanza, naishauri Serikali kwa kushirikiana na wadau wa mifugo na uvuvi wafanye utafiti na kuangalia changamoto na fursa zilizopo katika Jimbo la Moshi Vijijini ili wajue pa kusaidia.
Pili, naishauri Serikali ipeleke wataalamu wa mifugo kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa mifugo ya kimkakati yenye tija katika Jimbo la Moshi vijijini.
Tatu, naishauri Serikali iwe na programu maalumu ya kuzalisha mitamba wa maziwa wenye sifa zinazohitajika ikiwa ni pamoja na mifugo mingine kama mbuzi wa maziwa, ng’ombe wa nyama, nguruwe na kuku. Wafugaji wengi katika Jimbo la Moshi Vijijini hawana mbegu bora za ng’ombe wa maziwa. Kwa ujumla huwa wanabahatisha.
Nne, naishauri Serikali ihamasishe kuanzishwa kwa vikundi vya ushirika wa wafugaji mifugo na samaki katika Jimbo la Moshi Vijijini ambavyo itakuwa rahisi kuwapatia huduma za mitaji na utaalamu.
Tano, naishauri Serikali itupatie wataalamu wa kuchimba mabwawa katika Jimbo la Moshi Vijijini.
Sita, naishauri Serikali ianzishe Kituo cha Kanda cha kuzalisha vifaranga wa samaki jimboni kwangu ili wafugaji wavipate kwa urahisi kama vile vilivyopo kwenye Mikoa ya Morogoro, Tabora, Ruvuma, Lindi, Tanga na Geita.
Saba, naishauri Serikali iwezeshe wazalishaji vifaranga binafsi katika Jimbo la Moshi Vijijini ili wasaidie juhudi za Serikali kwenye kukuza hii sekta.
Nane, naishauri Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Moshi, wawezeshe kupandikiza vifaranga bora vya samaki katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, kwani wavuvi waliniambia kwenye kampeni kuwa samaki wamehama ikiwa na maana kuwa wamepungua. Hii ni pamoja na kuanzisha uvuvi wa vizimba.
Tisa, naishauri Serikali iwe na huduma za uhakika za ugani katika Jimbo la Moshi Vijijini ikizingatia lishe ya samaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumi, napendekeza Serikali ifanye majaribio ya kutumia vizimba kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ili kuongeza tija kwenye ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishauri Serikali iwekeze kwenye kuanzisha mashamba darasa ya ufugaji bora wa mifugo ya kimkakati na samaki jimboni kwangu Moshi Vijijini ili wajifunze kwa vitendo kama ilivyowasilishwa kwenye hotuba ya bajeti yam waka 2022/2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. PROF. PATRICK A. NDEKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nami nitoe shukrani zangu za pekee kwa kunipa fursa mwanamme wa pili kuchangia katika hoja hii muhimu.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu kwa kuona umuhimu wa kuiondoa idara hii kutoka Wizara ya Afya na kuifanya idara kamili na niendelee kwa kumpongeza sana Waziri wetu Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima na Naibu wake Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis kwa kazi nzuri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, mimi nitaanzia pale alipomalizia mwenzangu Profesa Manya kwamba wazee, nataka nichangie kuhusu wazee. Wazee wako kwenye kundi maalum katika hii Wizara lile kundi maalum linajumuisha wazee, vijana, machinga na watu wenye ulemavu. Sasa mimi ngoja niongelee wazee kwa sababu na mimi ni mzee na hawa wazee hawajapata mtu wa kuwasemea kwa sauti kubwa huku Bungeni kwa sababu moja kubwa muhimu kwamba labda sisi Wabunge wazee ambao tuko huku tunakimbizana kutetea hoja za kwenye Jimbo, akinamama wanatetea hoja zao, kwa hiyo hawana mwakilishi huku lakini leo ngoja niwaongelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wazee ni watu muhimu sana kwenye jamii yetu, tuki-define wazee ni mtu mwenye miaka kuanzia 60, 70 na hata kwenye vitabu vitakatifu vya Qurani na vya kikristu wanasema wazee tuwaangalie ni kundi muhimu sana. Wazee ni amana kubwa na ni utajiri katika Taifa letu, hawa wazee wameshirikiana na Mwenyezi Mungu kwenye kuhakikisha kwamba sote tuliopo hapa tumeumbwa tukawa watu na tuko huku duniani, kwa hiyo hii ni kazi nzuri ambayo wazee wetu wamefanya.
Mheshimiwa Spika, pamoja na haya wazee kwenye nchi yetu ya Tanzania wamekuwa na busara kubwa sana. Rais wetu wa kwanza aliyetuletea uhuru Mwalimu Nyerere aliwashirikisha wazee, walimpa busara na kuhakikisha kwamba wanamshauri mpaka tukapata uhuru. Kwa hiyo, kile chochote tunachoringia nchi hii sasa hivi, majivuno yetu naomba tuwahusishe wazee kwamba wamefanya contribution kubwa sana kwenye mafaniko ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, katika sensa ya mwaka 2012 idadi ya wazee hapa nchini ilikuwa takribani milioni 2.5 ambapo wakinamama walikuwa milioni 1.3 na wazee wanaume walikuwa milioni 1.2. Idadi hii ni ndogo ukilinganisha kwamba Tanzania yetu ina watu karibu milioni 45 wakati wanahesabiwa mwaka 2012. Kwa hiyo, idadi ya wazee ni kama 5.6% tu; kwa nini idadi hii ni ndogo? Idadi hii ni ndogo kwa sababu zifuatazo; kwanza kabisa wazee wengi kule vijijini na mijini ambapo tumeshaona vijana wengi hawana kazi siku hizi wana umaskini mkubwa wa hali ya juu na wengi wao hawana hata pesa ya kununua chakula.
Mheshimiwa Spika, pia wazee wengi kule vijijini wanakumbwa na magonjwa ya uzee kama tezi dume kwa wanaume, kansa za matiti kwa akinamama, kansa za vizazi, magonjwa ya pressure na magonjwa mengine kisukari na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, namshukuru Waziri amesema kwamba wameshatambua wazee kama milioni 1.5 kwenye hotuba yake na wameshawapatia bima za afya, hiyo tunashukuru sana, lakini kusema ukweli hizi huduma wazee hawazipati kama ambavyo tungependa iwe na kutokana na hali hii mbaya ya kwamba wazee hawapati huduma wameishia kuuza rasilimali zao. Kwa mfano mzee anaona niuze shamba au niuze nyumba niliyokuwa nayo kwa sababu watoto wengi hawana uwezo wa kuangalia wazee, anauza shamba, anauza gari, anauza nyumba ili aokoe maisha yake asife, kwa hiyo hiyo ni changamato.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine kubwa ni kwamba wazee wengi wameshatelekezwa kule kwenye jamii, watu wengi siku hizi hawawaangalii sana wazee na hatumlaumu mtu, labda ni kwa sababu za kiuchumi na kipato sio cha kueleweka. Pia kwenye maeneo mengine kuna mauaji ya ukatili kwa wazee wetu, mtu ameshalitumikia Taifa letu hili lakini anaishia kuuawa kikatili kabisa kwa mambo ya kishirikina na kandalika.
Mheshimiwa Spika, changamoto hizi ambazo nimezitaja hapo juu zimesababisha hawa wazee wetu wafe mapema, wanakufa mapema kabla ya wakati wao. Sisi kama Watanzania na Taifa la Kitanzania nimuombe Waziri wetu ni jukumu letu sasa kuhakikisha tunawaangalia hawa wazee wapate huduma zao ili wasife mapema kama ambavyo imezoeleka huko.
Mheshimiwa Spika, wajibu wa kuwalea wazee uko kwenye vitabu vitakatifu, Qurani inasema tuwaangalie wazee na hata Biblia zinasema tuwaangalie wazee kwa hiyo ni wajibu wetu. Mimi niipongeze sana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wao wameshaanza kuwapa pensheni wazee kule. Kule wazee wanapata pensheni kidogo na mzee hahitaji kitu kikubwa ukienda kule kijijini anakuomba naomba pesa kidogo ninunue sukari. Kwa hiyo, tukianza hata na kuwapa kilo mbili za sukari hawa wazee wetu najua tutafika mahali na mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi nyingine kama za Botswana, Swaziland, Seychelles, Mauritius, Afrika Kusini zimeshaanza kutoa pensheni kwa wazee kuwatunza wazee wao na nchi kama Kenya, Uganda na Zambia ziko kwenye mchakato wa kuhakikisha pia wanawapa wazee wao pensheni kwa nini sisi watanzania tusifanye hicho kitu jamani na siyo wengi watu milioni 2.5 tushindwe kuwapa kilo moja au mbili ya sukari.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba nitoe ushauri wangu kwa Serikali. Ushauri wa kwanza kuna sera ya wazee iliwekwa tangu mwaka 2003 naiomba Serikali ishirikiane na wadau wengine ikiwepo Help Age ni Shirika la Kimataifa linalosaidia sana mambo ya wazee warekebishe ile sera iendeane na wakati wa sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, kitu cha pili ninaishauri Serikali mwarobaini wa hii kitu sera tumeshaitunga tutunge sheria ya wazee mtu ambaye hatatekeleza sheria basi atachukuliwa hatua. Kwa hiyo namuomba Waziri uhakikishe kwamba sheria ya wazee ipo kwa sababu tangu hii sera itoke mwaka 2003 mpaka leo bado hamna sheria ya wazee.
Mheshimiwa Spika, kitu kingine ushauri wangu naomba chonde chonde huku Bungeni wazee hatuna wawakilishi ikiwezekana zile nafasi wazee kwa sababu ni kundi maalum nao wapatiwe wawakilishi wao waje huku Bungeni waje waongelee mambo ya wazee. Mimi hapa napambana na Jimbo, wale wengine wanapambana na mambo ya akinamama na kadhalika, vijana wanapambana na mambo ya vijana kwa hiyo wazee ingependeza nao wapate uwakilishi huku Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ikiwezekana naishauri Serikali kama ikiwezekana tupawe pensheni hawa wazee hela kidogo tu ya kununua sukari nao ili maisha yaende mbele; na ushauri wangu mwingine ni kuhusiana na Bima ya Afya napendekeza iwe bima itakayoweza kuwasaidia hawa wazee wapate huduma zote bure, siyo anakwenda anaambiwa hii dawa haipo kwenye bima, hapana, bima kama tunasema wazee hawa milioni 2.5 wanapata bima basi wapate huduma zote za kiafya.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali watokomeze kabisa hii tabia ya kumaliza vizee vyetu, wazee unakuta tu labda ana pressure ya macho yamekuwa mekundu anaambiwa ni mchawi wanamuua. Kwa hiyo naomba kabisa Serikali isimame kidedea ihakikishe tunawalinda wazee wetu. Wazee ni utajiri, wazee ni tunu ya Taifa letu naomba tuwaheshimu, tuwahudumie kama Taifa na kwa kufanya hivyo tutapata baraka kwa Mungu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima na Naibu wake Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, wazee ni amana na utajiri wa jamii; wazee ni wadau wa kwanza walioshirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji. Wazee ni wadau muhimu wa malezi na makuzi ya watoto na vijana na Taifa letu kwa ujumla. Wazee ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo misingi ya jamii na mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana.
Mheshimiwa Spika, wazee ni walezi kwa watoto na vijana; wazee ni urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii kwa siku hizi.
Mheshimiwa Spika, wazee ni sehemu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii.
Mheshimiwa Spika, wazee wa Kitanzania wamelitumikia Taifa kwa muda mrefu tena kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwaletea na kuhakikisha wanapata mafanikio ambayo tunajivunia sasa. Tanapaswa tutambue kwamba wazee hao wamelitumikia Taifa kwa muda mrefu. Tena wamechangia mafanikio makubwa ambayo Tanzania inajivua kwa wakati huu!
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto mbalimbali za maisha ya uzeeni bado wazee wa Tanzania wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Tanzania ilikuwa na jumla ya watu 44,929,002 ambapo wazee walikuwa 2,507,508 (ambapo wanawake walikuwa 1,307,358 na wanaume 1,200,210) sawa na asilimia 5.6%. Kwa idadi hii Tanzania ina wazee wachache.
Mheshimiwa Spika, sababu za uchache wa wazee katika jamii yetu ni kama zifuatazo; hapa nchini Tanzania katika maeneo mengi hasa yale ya vijijini, uzee umeambatana na umaskini, magonjwa na unyanyapaa unaohusishwa na uchawi. Vitu hivi vimekuwa ni sababu ya kuwatenga na kuwakosea heshima wazee katika baadhi ya jamii zetu za Kitanzania.
Mheshimiwa Spika, wazee wa Tanzania wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo; wengi wanakabiliwa na umaskini wa hali na kipato vijijini na mijini, na baadhi hukosa hata fedha za kununua chakula; wazee katika umri wao, wengi wao wanakumbana na changamoto za magonjwa ya wazee (tezi dume, kisukari, kansa ya kizazi na aina nyinginezo za kansa, shinikizo la damu); upatikanaji duni wa madawa na vifaa tiba kwa wazee na wanapokumbana na changamoto hizi na kukosa msaada, wazee huishia kuuza rasilimali zao kama mashamba na nyumba ili kupata huduma muhimu ambazo hawana uwezo kuzigharamia.
Mheshimiwa Spika, pia baadhi yao kutelekezwa na jamii inayowazunguka na mauaji ya kikatili kwa kisingizio cha imani za kishirikina.
Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa wazee pamoja na uchache wao, kunaashiria uhitaji wa ongezeko la huduma mbalimbali kwa wazee. Kutokana na ukweli huu, tunahitaji kuzingatia sana jinsi nchi yetu itakavyoshughulikia matatizo ya watu wetu kuzeeka.
Mheshimiwa Spika, hii ni kutokana na ukweli kwamba hata muumba wetu alionesha kuwajali wazee na hata dini zetu mbili kubwa hapa nchini za uislamu na ukristo zinatuelekeza kuwapenda, kuwajali na kuwatunza wazee.
Mheshimiwa Spika, wajibu wa kuwahudumia au kuwasaidia wazee ni wa kila mmoja. Tuna jukumu kama Taifa au kila mmoja wetu katika jamii kuwashukuru, kuwaenzi na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi wa Taifa letu. Hii ni pamoja na kuwapatia kipato kila mwisho wa mwezi ili wewezi kujikimu.
Mheshimiwa Spika, jambo kama hili linafanyika huko Zanzibar na nchi nyingine Kusini mwa Jangwa la Sahara kama vile Botswana, Lesotho, Mauritius, Namibia, Seychelles, South Africa na Swaziland. Mataifa haya yamefanikiwa kuwapatia wazee wao pensheni, na nchi nyingine kama Kenya, Uganda na Zambia ziko kwenye mchakato.
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali isikwepe jukumu la kuwatunza wazee kwa sababu nguvu zao za uzalishaji mali zimepungua kutokana na kazi waliyoifanya wakiwa vijana kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa familia zao na Taifa kwa ujumla. Tunao wajibu wa kuwajali wazee wetu kwa hali na mali ikiwa ni sehemu ya matunda ya uwajibikaji wao kwetu na kwa Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, hivyo, ninatoa ushauri ufuatao kwa Serikali; kwanza, Serikali iboreshe Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 kwa kushirikiana na wadau; sheria inayosimamia masuala yote ya wazee iaandaliwe na kuanza kutumika mara moja; kama ilivyo kwa makundi yote maalumu (vijana, walemavu na akina mama), wazee wapatiwe nafasi za uwakilishi kutetea maslahi yao katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ianze mchakato wa kuwalipa pension wazee wetu ambao hawana msaada wa aina yoyote ule wa kipato. Jambo hili jema na lenye baraka linatekelezwa huko Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, pia wazee wapatiwe bima ya afya inayoweza kupambana na changamoto zote za kupambana na magonjwa ya uzeeni ili wazee wafaidi huduma hizo kama ilivyokusudiwa kwenye sera wa kuwapatia huduma za afya ya mwaka 2007; Serikali ihakikishe mafao ya wastaafu yanalipwa kwa wakati ili kuwaondolea wazee usumbufu wa kufuatilia; Serikali na wananchi wote kwa ujumla kulinda na kutetea haki za wazee, ikiwemo kuthamini mchango, uzoefu na ushiriki wao kwa maendeleo ya Taifa; Serikali iendelee kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza mauaji ya wazee na kuhakikisha wazee wanalindwa dhidi ya ubaguzi, uonevu, ukatili na mila potofu na wasiokuwa na msaada, Serikali na wadau mbalimbali waangalie jinsi ya kuwasaidia wale wasiokuwa na makazi, tiba na msaada wa mahitaji ya msingi.
Mheshimiwa Spika, nchini Tanzania kuna Sera ya Wazee iliyotungwa mwaka 2003 lakini hadi sasa haijatungwa sheria ya kusimamia utekelezaji wa sera hiyo. Sheria ya kuwalinda wazee ndio itakuwa muarobaoni wa changamoto za maisha wanazokabiliana nayo hasa ya kiuchumi na afya kwani wanapoishiwa nguvu za uzalishaji, hukosa mahitaji ya msingi anayostahili binadamu.
Mheshimiwa Spika, licha ya Tanzania kuwa na sera ya Taifa inayotaka wazee wasiojiweza kupatiwa matibabu bure, lakini utekelezaji wake bado ni wa kiwango cha chini na baadhi ya maeneo, wazee wamelazimika kuingia mifukoni kwa ajili ya kununua dawa. Wengi ya wazee hao wanasema Sera ya Taifa ya mwaka 2007 inayofungua milango kwa wazee wasiojiweza kupatiwa matibabu bure haitekelezwi ipasavyo na kwamba baadhi ya Waganga Wafawidhi wa Mikoa na hata wale wa Wilaya wamekuwa wakiwatoza fedha licha ya sera hiyo kueleza bayana.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee niipongeze Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutunga Sheria ya Masuala ya Wazee Na. 2 ya mwaka 2000; kuweka utaratibu wa kuwapatia pensheni jamii na vitambulisho vya kupatiwa huduma mbalimbali wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70.
Mheshimiwa Spika, hapa kwetu Tanzania wazee ni utajiri, hatutakiwi kuwatenga wala kuwadharau bali wanabaki kama miamba na walezi wakuu wa mila, desturi na tamaduni njema katika jamii yetu. Katika harakati za kupigania Uhuru wa Taifa letu, Mwalimu Nyerere alielekezwa na wazee mbinu za kutumia na hatimaye tukapata uhuru. Kutokana na umuhimu wa wazee, hata Maraisi wa awamu zote zilizopita wakiwa na jambo huwaita wazee na kuteta nao. Pamoja na umuhimu wao, inasikitisha kuona kwamba wazee hawajaangaliwa kama kundi maalumu kwenye Taifa letu na wanasahauliwa katika maslahi yao.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Naibu wake Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa kwanza utahusiana na umuhimu wa diplomasia ya uchumi katika kipindi hiki hapa Tanzania. Kutokana na hali ya kudorora kwa uchumi wa dunia na Tanzania yetu kunakochangiwa na ugonjwa wa UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi na vita vya Urusi na Ukraine, Tanzania inatakiwa kutumia mbinu za kidplomasia ili kujinasua na athari hizi. Kwenye hili, nchi yetu inatakiwa kujielekeza katika kujenga uchumi wa kujitegemea na kutafuta fursa za uwekezaji ili kukuza uchumi wetu kupitia diplomasia ya uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Rais wetu kwa juhudi zake za kuifungua nchi yetu kimataifa. Kwa kipindi kifupi, Rais wetu amefanikiwa kurejesha heshima ya nchi yetu Barani Afrika na nje ya Afrika kama ilivyokuwa kipindi cha awamu za kwanza, pili, tatu na nne. Rais wetu ametembelea mataifa mbalimbali Barani Afrika na nje ya Bara letu pamoja na kushiriki mikutano ya kimataifa kama njia na mbinu ya kuongeza ushirikiano na mataifa mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi zetu waelekeze nguvu kwenye kusaidia juhudi za Rais wetu kuitangaza vyema Tanzania ili tufanikiwe kuipaisha nchi yetu kiuchumi na kisiasa. Juhudi zifanyike kushawishi kupitia diplomasia ya kiuchumi kuvutia uwekezaji, biashara za kimataifa na utalii. Tukiongeza nguvu, Tanzania yetu itakuwa na ushawishi Barani Afrika kama zilivyo nchi za Nigeria, Afrika Kusini na Misri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha hili, ninaishauri Serikali itoe mafunzo maalumu kwa Mabalozi wetu pamoja na wasaidizi wao ili wawe na uelewa wa diplomasia ya uchumi pamoja na mbinu na mikakati ya kuitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili ni kuhusu malalamiko niliyopokea kutoka kwa mwanafunzi wa Sudan aliyemaliza Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyoko Arusha, Tanzania. Msomi huyu ni mwalimu wa chuo kikuu huko Sudan. Alipowasilisha vyeti vyake chuoni Sudan ili abadilishiwe cheo, alielekezwa na uongozi wa chuo apeleke vyeti vyake vikathibitishwe kuwa ni halali na ubalozi wa Tanzania huko Khartoum. Alipokwenda kwenye ubalozi, alikuwa na nakala halisi za cheti chake cha PhD, pasi yake ya kusafiria iliyokuwa na kibali cha kuishi Tanzania, kadi ya kitambulisho cha uanafunzi kutoka Chuoni Mandela, barua iliyomsajili chuoni Mandela, na nakala ya dissertation yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwasilisha ushahidi wote huu, Ubalozi wa Tanzania hawajamsaidia na imechukua muda mrefu sana kupata huduma hii na analalamika huenda akachelewa kupandishwa daraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mteja huyu analalamika kuwa atajisikia vibaya sana kama itamlazimu kutuma vyeti vyake Tanzania kuthibitishwa ili hali kuna ubalozi unaoiwakilisha nchi yetu Sudan.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali iwaelekeze mabalozi wetu watekeleze majukumu yao kwa wakati ili kuepuka kero za kulalamikiwa kwani hali kama hizi zinaharibu taswira nzuri ya nchi yetu kwenye uso wa kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa tatu ni kwenye eneo la umuhimu wa Wizara kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani. Lugha ya Kiswahili imetumika kwa mafanikio makubwa sana kuliunganisha Taifa letu. Kiswahili ni lugha ya Taifa na hutumika katika shughuli zote za Serikali likiwemo Bunge. Hivi karibuni sheria imepitishwa na kuelekeza Kiswahili kitumike mahakamani. Kenya inatumia Kiswahili kama lugha ya Taifa, Uganda wanatumia Kiswahili kama lugha ya Jeshi na Polisi. Kiswahili kinatumika Mashariki mwa Congo, Rwanda, Burundi, Visiwa vya Ngazija, baadhi ya maeneo ya Malawi, Zambia, Msumbiji na Somalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lugha hii imekuwa inatumiwa katika kusambaza habari katika vituo mbalimbali ulimwenguni kama vile Sauti ya Amerika, BBC, Deutsche Welle, Monte Carlo, RFI na nchi nyinginezo kama vile Uchina, Urusi na Iran. Aidha, imekuwa ni mojawapo ya lugha muhimu zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini Marekani Uingereza, Ulaya bara, Urusi, Uchina na Barani Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchini Afrika Kusini Baraza la Mawaziri limeidhinisha Kiswahili kifunzwe katika shule za umma na za kibinafsi. Kwenye hili, Kiswahili imekuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika inayotoka nje ya Afrika Kusini kufunzwa katika nchi hiyo. Vilevile Umoja wa Afrika na Jumuiya ya SADC imeidhinisha Kiswahili kitumike kama mojawapo ya lugha za kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki itatekeleza azma hii kwa kushirikiana na wadau wengine, Kiswahili kina nguvu ya kupanuka katika nchi ambazo hazijawahi kukizungumza na kina nguvu ya kuliunganisha Bara la Afrika na nchi nyingine duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kasi ya ukuaji wa Kiswahili, ninaishauri Serikali kupitia kwenye Wizara hii iwe na mkakati mahsusi wa kueneza lugha ya Kiswahili kupitia Balozi zilizo katika nchi mbalimbali duniani ili Kiswahili kiwe moja ya lugha kuu duniani. Naishauri Wizara iendeleze kwa nguvu zote kuendeleza na kutangaza kiswahili pale alipoachia Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Nishati Ndugu January Makamba na Naibu wake Engineer Stephen Byabato pamoja na jopo la wataalamu wa Wizara kwa kazi kubwa wanazofanya kupeleka umeme na nishati nyingine muhimu kwa wananchi wetu hapa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utahusu umuhimu wa kupeleka huduma ya gesi asilia katika Jimbo la Moshi Vijijini na huduma ya umeme katika maeneo ambayo hayajaunganishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya bajeti Waziri ameeleza kwamba kuna mradi wa gesi asilia utakaojengwa kupeleka huduma hii Mombasa nchini Kenya. Katika hotuba yake, ameeleza kuwa mikoa ya Pwani, Tanga Kilimanjaro na Arusha itanufaika na mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Moshi Vijijini limepakana na Mlima Kilimanjaro, wananchi wengi hutegemea nishati ya kuni kutoka katika misitu ya Mlima Kilimanjaro na maeneo mengine ya jirani. Wanasayansi wamesema kwamba matumizi ya kuni kwa kiasi kikubwa yamesababisha uharibifu wa mazingira na nishati mbadala inahitajika kukabiliana na changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ujio tarajiwa wa mradi wa gesi asilia Mkoani Kilimanjaro, ninaishauri Serikali ianze kwa kusambaza miundombinu ya gesi hii katika vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro ili kuunusuru mlima na ukataji wa nishati ya kuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupeleka umeme vijijini, bado wananchi wengi wa Jimbo la Moshi Vijijini hawajapatiwa nishati ya umeme. Hivyo basi ninaiomba Wizara ya Nishati isaidie kutatua changamoto za nishati ya umeme katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yenye changamoto ya umeme Jimbo la Moshi Vijijini ni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kimochi, Kitongoji cha Kiwalaa kilichopo Kijiji cha Sango, Kitongoji cha Iryaroho kilichopo katika Kijiji cha Mowo na Kitongoji cha Maryaseli katika Kijiji cha Lyakombila havina umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo niliyotaja hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Okaoni, vijiji vya Sisamaro, Omarini na Mkomilo vinahitaji kuunganishwa japo baadhi ya maeneo nguzo zimepita ila bado kuunganishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Kindi, Kijiji cha Chekereni Weruweru, Vitongoji vya Miembeni, na Kisiwani havina umeme kabisa, ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vijiji hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kayta ya Kibosho Kirima, Mbunge ametokea kata hii. Kama nilivyoomba mwaka jana katika Kijiji cha Boro kwenye vitongoji vya Boro Kati na Boro Juu (anakotokea Mbunge), voltage za umeme ni kidogo sana na hupelekea kushindwa kuendesha vifaa vya ndani kama friji na vyombo mbalimbali vya ndani. Mashine za welding (kwenye vitongoji hivi) na pump ya kuvuta maji katika shule ya sekondari Masoka hushindwa kufanya kazi kutokana na umeme kidogo. Wajasiriamali wameshindwa kuweka mashine za kusaga unga, mashine za kutengeneza matofali na miradi mingine midogo inayohitaji umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wa bweni wa sekondari ya Masoka hushindwa kupata huduma ya umeme ili wajisomee usiku kutokana na umeme kidogo. Umeme huwaka kuanzia saa tano usiku. Ninaiomba Wizara isaidie kutatua changamoto hii, kwani pamoja na maombi yangu mwaka jana, bado Wizara haijatusaidia kutatua changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kibosho Mashariki, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana inahitaji huduma katika Kijiji cha Sungu Vitongoji vya Kyareni na Nkoitiko havijaunganishwa; katika Kijiji cha Singa, Kitongoji cha Singa Juu hakijaunganishwa; na katika Kijiji cha Mweka, kitongoji cha Mweka Juu na Omi havijaunganishwa. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vijiji na vitongoji vilivyotajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Kibosho Kati, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana, Vijiji vya Uri na Otaruni umeme una nguvu kidogo (low voltage) na kunahitajika transfoma. Katika Kijiji cha Otaruni, Kitongoji cha Ngoroshi hakuna umeme na tunaomba wananchi wapatiwe huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana, katika Kata ya Uru Mashariki, Kijiji cha Materuni, Kitongoji cha Wondo hakijaunganishwa, ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye kitongoji hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Mbokomu kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana, Kitongoji cha Mmbede Kyaroni, Tema na Masanga na baadhi ya maeneo ya Korini Kati havijaunganishwa, pia ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana, katika Kata ya Mabogini sehemu ambazo hazijapata umeme hadi sasa ni Vitongoji vya Sanya "Line A" na Mjohoroni vilivyopo katika kijiji cha Mabogini; Kitongoji cha Uru - katika Kijiji cha Muungano; katika Kijiji cha Maendeleo, Vitongoji vya Mshikamano na Uarushani; Mgungani - katika Kijiji cha Mtakuja, na katika Kijiji cha Mserekia hakuna umeme katika Vitongoji vya Mbeya kubwa, Mbeya ndogo, Remit, Mkwajuni, na Mafuriko. Kijiji cha Mji mpya, Kitongoji cha Utamaduni hakijaunganishwa. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye maeneo yaliyotajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri Mheshimiwa Mary F. Masanja na wataalamu wa Wizara na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa sana kwenye sekta ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, Mlima Kilimanjaro na viunga vyake ni moja ya vivutio muhimu vya utalii ambavyo vimeipatia Tanzania heshima kubwa kimataifa. Ndani ya Mlima Kilimanjaro na maeneo yanayouzunguka mlima kuna vivutio vya aina mbalimbali vya kitalii.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, Rais wetu alishiriki kikamilifu kwenye filamu ya Royal Tour iliyokuwa na kipengele cha kutangaza utalii ukiwepo Mlima Kilimanjaro. Kutokana na hili, ni vyema tukachukua tahadhari mapema ili watalii watakapoanza kumiminika kuja kutalii Kilimanjaro wakutane na mazingira mazuri. Tusipofanya hivyo, watalii wakija wakikumbana na changamoto watapeleka sifa mbaya kuhusiana na eneo letu na kuathiri idadi ya wageni watakaotembelea Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kwenye suala la vivutio vya Mlima Kilimanjaro na umuhimu wa kutatua changamoto za vivutio hivyo ili kuwezesha watalii kufika maeneo hayo kirahisi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni imegundulika kwamba mti mrefu kuliko yote Barani Afrika umepatikana katika Kijiji cha Tema, Kata ya Mbokomu, Jimbo la Moshi Vijijini, Mkoani Kilimanjaro. Mti huo ambao una urefu wa mita 81.5 upo ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA). Ugunduzi huo umeonesha pia huu ni mti wenye miaka mingi zaidi duniani kwani una miaka 600. Mti huu umeupa heshima Mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa jumla. Kugundulika kwa mti huo kumeongeza chachu ya watalii kupanda Mlima Kilimanjaro na wengine kwenda kushuhudia mti huo.
Mheshimiwa Spika, licha ya mti huu kuwa kivutio ambacho kinaweza kuiingizia Serikali fedha za kigeni, lakini changamoto iliopo ni ugumu wa kuufikia mti huo. Ili kufika katika eneo la Mrusungu ambapo ndipo ulipo mti huo mrefu zaidi, ni safari ya kutembea kwa mguu kwa takribani muda wa saa nne kwenda na kurudi kwa kupita katika milima, mabonde, mito na makorongo.
Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto hii, ninaishauri Serikali iboreshe miundombinu ya barabara ili kuweza kuufikia mti huo iwapo watalii watataka kwenda kuuona. Barabara ya kufika kwenye mti huu ni mbaya sana na hii ni changamoto inayowafanya watalii wasitembelee eneo hili.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ihakikishe kuwa eneo hili linaendelezwa ili liwe na hadhi ya kuwa sehemu ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro. Vilivile ninaishauri Serikali itengeneze utaratibu wa kuhakikisha wanaokwenda kuuona mti wanalipa ada.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili utahusu maporomoko ya maji Materuni. Maporomoko haya ni moja ya maporomoko ya maji katika Mto Mware, Kata ya Uru Mashariki, Jimbo la Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro. Maporomoko haya yanapatikana katika Kijiji cha Materuni pembezoni mwa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Maporomoko haya yana urefu wa zaidi ya mita 100. Pamoja na kivutio cha maporomoko ya maji, eneo hili la utalii limekuwa maarufu kwani watalii wanaokwenda kuona maporomoko hupata fursa ya kutembelea shamba la kahawa na kujifunza jinsi kahawa inakuzwa, kuvunwa na kusindikwa. Watalii hupata fursa ya kujaribu kwa mkono yao kuchoma na kuandaa kikombe cha kahawa kwa kutumia njia asili ya Wachagga.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayokabili eneo hili ni ubovu wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 15 kutoka mjini Moshi. Kutokana na ubovu wa barabara, watalii hupata shida kufika katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, changamoto za barabara katika maeneo yanayopeleka watalii kwenye vivutio vya Mlima Kilimanjaro zinatakiwa zipewe kipaumbele cha pekee na Wizara ya Maliasili na Utalii kwani wao ni wanufaika wakuu. Ninaishauri Serikali iachane na kuzitegemea TARURA na TANROADS kwani mitandao yao ya barabara ni mingi, na hawajatoa kipaumbele kikubwa kwa barabara za jimbo langu kama zile za kupeleka watalii kupitia Umbwe Gate, Kidia VIP Route, Materuni Waterfalls, Mti Mrefu Kijiii cha Tema huko Mbokomu, Kanisa la Kibosho Singa na maeneo mengine muhimu.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali, huu ni wakati wa kutumia michango ya Corporate Social Responsibility (CSR) unaotokana na mapato ya Mlima Kilimanjaro kutengeneza miundombinu ya barabara katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, baada ya michango yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndugu Mohamed Mchengerwa na Naibu wake Mheshimiwa Pauline Gekul pamoja na timu ya wataalamu Wizarani kwa kazi nzuri wanayofanya.
Mheshimwa Spika, nianze mchango wangu kwa kuipongeza timu yetu ya soka ya wasichana ya Serengeti Girls kwa hatua kubwa ya kuingia fainali ya kombe la dunia itakayofanyika huko India kuanzia tarehe 11.10.2022 hadi 30.10.2022.
Mheshimiwa Spika, soka la wanawake nchini Tanzania linakua kwa kasi ya ajabu na timu hizi zimeonesha mafanikio makubwa ukilinganisha na zile zinazotoka ukanda wa CECAFA, COSAFA na zile za Kanda za Afrika Magharibi.
Mheshimiwa Spika, timu hii imetupa heshima kubwa kwa hiki kilichotokea, soka hili la wanawake Tanzania limefanikiwa kuitangaza vyema nchi kupitia timu ya Taifa ya Twiga Stars na Serengeti Girls ambazo zimeweza kutwaa vikombe mbalimbali, kushinda katika mechi kubwa za kimataifa na kuipaisha nchi yetu katika viwango vya soka Barani Afrika na duniani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio ya kubeba makombe mbalimbali na kuingia fainali ya kombe la dunia kwa wasichana wenye umri wa chini ya miaka 17, soka la wanawake nchini linakabiliwa na changamoto kubwa za aina mbalimbali, na ninazitaja kama ifuatavyo; kwanza kuna wakati maandalizi ya timu za taifa za wanawake kushiriki katika mashindano huwa duni sana; pili, kumekuwa kuna tatizo la kuibua vipaji vya wachezaji kutoka ngazi za vijiji, kata, wilaya na mikoa na tatu, kuna tatizo la uhaba wa makocha na waamuzi wa kike hapa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nne, kuna tabia ya wasichana wanaocheza soka kuiga tabia za kiume na hivyo kupoteza uhalisia wao kama wasichana. Tabia hiyo imehusisha uvaaji wa suruali, pensi, fulana na kofia za kiume. Vilevile wachezaji wengi wameiga kutembea kitemi kama watoto wa kiume. Kwa mawazo yangu, kitendo hiki kimesababisha wasichana wetu wakadhalilishwa huko Cameroon kwa kuhisiwa kuwa walikuwa wavulana.
Mheshimiwa Spika, tano, changamoto nyingine kubwa ya kukua kwa soka la wanawake ni kukosekana kwa wadhamini wengi wa kueleweka
Mheshimiwa Spika, baada ya kuainisha changamoto hapo juu, ninaishauri Serikali ichukue hatua zifuatazo; kwanza Serikali itenge bajeti ya kutosha kuhudumia kambi ya Taifa ya timu za wanawake; pili, ili kuibua vipaji, soka la wasichana lianze kuchezwa katika ngazi za shule za msingi na sekondari. Hii ni pamoja na kuwa na mashindano ya aina mbalimbali kwa watoto hawa katika ngazi ya wilaya, mikoa, UMITASHUMTA na UMISETA.
Mheshimiwa Spika, Serikali iandae mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa walimu na waamuzi wa soka la wanawake na pia Serikali kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liwekeze kikamilifu katika soka la wanawake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ihamasishe makampuni ya udhamini yawekeze kwenye soka na ligi za akina dada kwani wamefanya vizuri kimataifa ukilinganisha na zile soka na ligi za wanaume. Ushiriki wa wanawake katika soka utakuwa zaidi kama wadau zaidi watajitokeza na kuwainua na kutoa sapoti kwa wanamama ambao wanajitoa kwa ajili ya maendeleo ya soka la wanawake.
Mheshimiwa Spika, ninashauri mamlaka husika ziwahimize wachezaji wa kike kuvaa mavazi ya kike na matendo yao yawe kama ya watoto wa kike kwani huko Ulaya na kwingineko, wanasoka wanawake huwa na kila sifa anayostahili kuwa naye mtoto wa kike.
Mheshimiwa Spika, baada ya mchango wangu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake Mheshimiwa Hamad Hassan Chande na wataalamu wa Wizara pamoja na wadau kwa kazi nzuri wanayofanya katika sekta ya fedha na uchumi.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalo jukumu kubwa la kuwapatia wananchi huduma bora za umma. Ili Serikali iweze kutimiza wajibu wake kwa umma, inahitaji kuwa na rasilimali fedha ya kutosha inayotokana kwa kiasi kikubwa na makusanyo ya kodi kutoka vyanzo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, jukumu hili limeainishwa vizuri sana katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025. Kama Serikali itashindwa kukusanya mapato ya kutosha kupitia mamlaka husika, uwezo wake wa kutoa huduma bora kwa Watanzania utakuwa kidogo.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu inakabiliwa na tatizo la kupoteza sehemu ya mapato yanayotokana na kodi kutokana na sababu mbalimbali. Upotevu wa mapato ya Serikali husababishwa na yafuatayo: -
Moja, asilimia kubwa ya wafanyabiashara wadogo (SME's na Wamachinga) hawajadhibitiwa na kuwekwa rasmi kwenye mifumo wa kulipa kodi. Idadi yao ni kubwa lakini mchango wao kwenye kulipa kodi ni mdogo sana.
Pili, ukwepaji wa kodi; katika hili imejidhihirisha kwamba watu wachache sana, hasa hasa walio kwenye ajira na sekta rasmi ndio wanaolipa kodi, hivyo kubeba mzigo wa wale wasiolipa kodi, ambao bado wanafaidi bidhaa na huduma za umma sawasawa na wale wanaolipa kodi. Walipakodi waliosajiliwa kukusanya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni walipakodi wachache na hawa ndio wanaotumia mashine za EFD.
Tatu, kwa kiasi kikubwa, wafanyakazi wa Halmashauri nyingi nchini wenye majukumu ya kukusanya kodi pamoja na sehemu kubwa ya wafanyabiashara walio rasmi na wasio rasmi hawana mashine za kukusanyia kodi. Hii imesababisha Serikali kupoteza kiasi kikubwa cha mapato.
Nne, upotevu kwenye misamaha ya kodi; baadhi ya misamaha ya kodi iliyotolewa na Serikali kwa nia nzuri imekuwa ikitumika visivyo kuwanufaisha watu au makampuni yasiyostahili. Hali hii imekuwa ikisababisha upotevu wa fedha za Serikali.
Tano, utoroshwaji wa mali na fedha nje ya nchi; viwango vipya vya upotevu wa mapato yatokanayo na utoroshwaji wa fedha nchini kwenda nje ya nchi ni dola za Kimarekani milioni 464 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu, natoa mapendekezo yafuatayo kwa Serikali; kwanza naishauri Serikali iwe na mkakati wa kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo na wale wasio rasmi, iwasajili kwenye maeneo yao na kuweka mifumo rasmi ya kuwalipisha kodi kutokana na shughuli wanazofanya. Kufanikisha hili, Serikali inashauriwa kuajiri watumishi wa kutosha ili wasaidie kufanikisha azma hii.
Pili, naishauri Serikali ipunguze misamaha ya kodi na hii itolewe kwa wanaostahili baada ya kufanya tathmini ya kutosha kubainisha wahitaji sahihi; tatu, naishauri Serikali iboreshe uwazi katika utoaji wa misamaha ya kodi; nne, naishauri Serikali iendelee kuelimisha wananchi na kuwajibisha wale wote wanaohusika na ubadhirifu au wanaokiuka sheria zinazosimamia fedha za umma.
Tano, naishauri Serikali isambaze kwa wafanyabiashara wote mashine za kukusanya kodi (EFD), na izidi kuwekeza katika mifumo ya kielektronki ya ukusanyaji kodi, hata katika ngazi ya Halmashauri na wafanyabiashara wadogo wadogo; sita, naishauri Serikali itekeleze kwa makini suala la mapitio ya sheria mbalimbali ili makampuni yote yalipe kodi stahiki; na saba, naishauri Serikali itoe elimu kwa wananchi wote ili watambue kuwa ni wajibu wao kulipa kodi kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya nchi yao.
Mheshimiwa Spika, kwa kufanya haya, mapato mengi yataweza kukusanywa na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kupata huduma muhimu na kwa ubora zaidi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kushukuru kwa kunipa fursa kuchangia katika hoja hii ambayo iko mbele yako. Nianze moja kwa moja kwa kumpongeza Shemeji yangu Waziri Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba kwa wasilisho zuri alilofanya, kuwasilisha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo na ile Bajeti Kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze sana Serikali yangu CCM inayoongozwa na Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutekeleza vyema sana ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Serikali yetu inatekeleza miradi mingi sana katika Majimbo yetu yote Serikali ya Awamu ya Sita na pamoja na miradi inayotekelezwa katika Majimbo yote, Serikali inatekeleza miradi ya mikakati ambayo ni miradi mikubwa ikiwepo ile ya reli ya SGR, mradi wa Julius Nyerere, Daraja la Busisi na miradi mingine mikubwa, kwa hiyo tunaipongeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sintokuwa na shukrani kama sitasema ahsante kwa kidogo ambacho Serikali imetupatia katika Jimbo langu la Moshi Vijijini. Naishukuru sana Serikali kwa sababu tumepata miradi ya kutosha kusema ukweli, tuna daraja la pale Rau, Rais wetu alikuja akalizindua ambalo liligharimu Shilingi Milioni 910, kuna Mradi wa Maji wa Telamande Waziri Mkuu alikuja akauzindua uligharimu shilingi milioni 905, kuna ujenzi wa madarasa 53 ya mradi wa UVIKO ambayo yamegharimu shilingi bilioni moja na milioni sitini, kuna mradi wa maji wa mradi wa UVIKO pia uko katika Kata za Kimochi na Mabogini ambazo ni bilioni moja, kuna ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo tumeshapata shilingi 500. Zahanati ya Uru Kusini ambayo tumeshapata shilingi milioni 500, ukarabati wa barabara saba kwa kiwango cha moramu ambapo tumepata shilingi bilioni 1.5 tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na utaalam wangu mimi nitachangia kwenye Sekta ya Kilimo na nianze kwa kumpongeza sana Waziri wetu na Serikali yetu kwa kupandisha bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mpaka shilingi bilioni 954 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 308.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa pesa hizi ambazo zimepeleka Wizara ya Kilimo nina hakika zinakwenda kuhudumia wakulima ambao ni karibia asilimia 65 na wataenda kunufaikia vizuri sana. Ushauri wangu kwenye hili kwamba nitaongelea kilimo cha kahawa, kilimo cha mbogamboga, nafaka na mikunde kama muda utabaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kahawa tunaiita ni dhahabu ya kijani na bei ya kahawa ya Arabica kwenye soko la dunia sasa hivi ni dola 4.2 na ile ya Robusta ni dola mbili, na mwaka ulioishia wa fedha ni kwamba kule Moshi wakulima walipata mpaka shilingi 7,000 kwa kilo moja na leo asubuhi George alisema kule Bukoba wakulima walipata shilingi 3000.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji wa zao la kahawa hapa nchini kwa ujumla umeongezeka kutoka tani 60,651 mpaka tani 73,027 ikiwa ni ongezeko la asilimia 20.4 na ongezeko hili kwa mwaka huu ulioishia data za TRA zinasema kwamba nchi yetu mwaka 2021 ilipata kiasi cha pesa dola milioni 155 ikiwa ni zao la pili kutoka kwenye korosho ambayo ilipata dola milioni 159.
Mheshimiwa Naibu Spika, kahawa inazalishwa kwenye Mikoa mingi hapa nchini, kahawa inazalishwa Kilimanjaro, Kagera, Arusha, Ruvuma, Mbeya, Mara, Songwe na Kigoma. Sasa pamoja na umuhimu wa kahawa katika uchumi wa nchi yetu tumeshaona ni zao la pili ambalo linaliingizia Taifa letu pesa nyingi, lakini kuna changamoto ambazo zipo na ningependa tuzijadili hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote haya yanayozalisha kahawa changamoto yao kubwa ni upatikanaji wa maji ya kumwagilia ili wakulima waweze kuvuna kwa wingi hiyo ndiyo changamoto ya kwanza, changamoto ya pili ni miche bora, na changamoto ya tatu ni pembejeo. Kama wenzetu wa korosho na tumbaku wanavyopata pembejea wakulima wa kahawa walikuwa hawapati pembejeo na hii ilisababisha tusiende vizuri sana. Kwa hiyo ninaishauri Serikali kwamba zile pesa za umwagiliaji ambazo zimetoka, tuwekeze kwenye mifereko ya asili ili tuwafikikishie wakulima maji na wakishapata maji watazalisha kahawa nyingi na tutaipatia Taifa letu pesa za kutosha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili ni miche. Kuna ile miche Milioni 20 ambayo Mheshimiwa Waziri Bashe amesema kwamba atategemea kwenye bajeti hii tunaomba miche na pembejeo wapelekewe wakulima ili tuweze kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili ni kwenye zao la mbogomboga. Mbogomboga ni zao la thamani sana na sekta hii ikiandaliwa vizuri kama tutapanga vizuri tukiwa na mikakati ya kutosha, tukiwapa vijana kazi ya kutuzalishia mbogamboga, nina uhakika kama Taifa tutawatoa vijana na Taifa litapata pesa nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka uliopita, ulioishia 2021 sekta ya mbogamboga iliingizia nchi yetu dola za Kimarekani milioni 373 na mwaka huu tunategemea mbogamboga zitaingiza dola milioni 750 na kufikia 2030 mbogamboga tunategemea zitaliingizia Taifa dola milioni mbili. Sasa niombe ukienda kwenye maeneo kama Mji wa Karatu, ule Mji umejengwa pale kutokana na zao la vitunguu. Karatu tunayoiona leo imetokana na zao la vitunguu, kwa hiyo tukiwekeza tukiwapata vijana kazi ya kuzalisha mbogamboga, tukiwawekea miundombinu ya kutosha kwanza, tuwaandae wawe kwenye vikundi, wakishakuwa kwenye vikundi tuwahamasishe wazalishe mbogamboga kwa wingi ili zile ndege tumenunua ziweze kupeleka nje na kuliingizia Taifa pesa za kigeni. Tukiboresha huduma za ugani kwa hawa vijana ambao tutakuwa tumewaandaa tunaweza tukaanzisha viwanda vidogovidogo ambavyo pamoja na kupeleka mbogomboga nje pia tutaliingizia Taifa letu pesa za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa mwisho ni kwenye nafaka na mikunde. Tanzania yetu hii inajitosheleza kwa chakula, mwaka wa 2021 nafaka na mikunde uzalishaji uliongeza kutoka tani milioni 18 toka tani 18,196,733 hadi tani 18,665,065. Mafanikio haya ya uzalishaji mzuri wa nafaka ulitokana na uwepo wa mvua ya kutosha, lakini mwaka huu kama tunavyojua wote mvua ni kidogo sana, huenda tukapata matatizo na tukawa na uhaba wa nafaka na chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Waziri wa Kilimo na kwa Serikali kwa ujumla wake ni kwamba zile scheme mpya ambazo tunazianzisha sasa hivi, zilenge Mikoa ambayo ina maji mengi ya kutosha ili tusije tukaanzisha scheme kwenye maeneo ambayo hakutakuwa na maji na hazitakuwa sustainable tunaweza tukapata hasara. Kwa hiyo mchango wangu ni kwamba scheme hizi ziwekwe kwenye maeneo ambayo yana maji ya kutosha ili hii miradi iwe endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa hotuba nzuri kutoka katika ofisi yake. Pia niwapongeze Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mheshimiwa Jenista Mhagama; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi; pamoja na Manaibu wao Mheshimiwa Ummy Nderiananga na Mheshimiwa Patrobass Katambi kwa kazi kubwa wanazofanya kulijenga Taifa letu. Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake wanafanya kazi kubwa kwenye majukumu yao ya kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita kwenye tatizo la ulevi kwa vijana na mchezo wa kamari katika sehemu nyingi hapa nchini Tanzania na hususan Mkoani Kilimanjaro. Vijana ni nguzo ya Taifa katika nyanja za uchumi, michezo, maadili na uongozi na wakiachwa kujitumbukiza katika ulevi na utumiaji wa dawa za kulevya kama ilivyo sasa hivi tutalifanya Taifa letu kuangamia siku za mbeleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la ulevi kwa vijana na kuongezeka kwa mchezo wa kamari Mkoani Kilimanjaro katika maeneo ya vijijini limekuwa kubwa na linaua kabisa uwezo wa kundi hili kuchangia kuijenga nchi yetu kupitia nguvu kazi yao kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukosefu wa ajira rasmi Serikalini kwa vijana wetu, sehemu kubwa ya vijana wamejiingiza katika ulevi wa pombe kali zilizotapakaa mitaani na kuvuta bangi na kutumia dawa za kulevya za aina mbalimbali. Kudhihirisha tatizo hili, akiongea katika hafla ya kuzindua Mbio za Mwenge tarehe 2 Aprili, 2024 katika Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa alisema: “Siku za hivi karibuni imeibuka aina mpya ya bangi inayotumiwa na vijana wetu yenye kiasi kikubwa cha kilevi inayofahamika kama 'cha Arusha' na 'Skanka'.” Alieleza kuwa aina hii ya bangi yenye sumu nyingi huchanganywa kwenye sigara na wanaoitumia hubadilika na kuwa kichaa na kupoteza mwelekeo kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, huko Mkoani Kilimanjaro, viongozi wa dini mbalimbali wamelalamikia tabia ya vijana wengi wa kiume vijijini kubugia pombe kali, dawa za kulevya na bangi kitu ambacho kimesababisha athari mbalimbali. Vilevile, vijana wengi hushiriki kwenye kucheza kamari. Matokeo ya kamari hizi ni kwamba hela zote huishia kwenye kamari. Mabonanza ya Wachina yako hadi huko vijijini, mabonanza haya yamefilisi vijana wetu huko vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla pombe kwa vijana wetu hawa ni sumu. Hatari zake hujumuisha vijana wetu kukosa nguvu za kiume na kushindwa kushiriki tendo la ndoa na kushindwa kuzaa watoto. Kasoro hii imelalamikiwa na viongozi wa dini na wale wa Serikali kwenye Mkoa wetu wa Kilimanjaro katika maeneo ya Rombo, Vunjo na Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, athari nyingine kubwa za pombe, dawa za kulevya na bangi ni ajali mbaya zinazosababishwa na ulevi, magonjwa ya ini, UKIMWI na aina nyingine nyingi za saratani. Pombe, bangi na dawa za kulevya husababisha umaskini na vinapelekea vifo vya haraka kwani vijana waathirika, kuwa maskini na huishi katika mazingira magumu na mara nyingi hushindwa kumudu matibabu. Vilevile, vilevi huwa ni chanzo cha magomvi yasiyo na msingi, ajali za uzembe, kujeruhiwa na kuuawa na vibaka na msongo wa mawazo. Tabia hii ya vijana wetu kujiingiza katika vilevi ni ya kusikitisha kwani nchi isipokabiliana nalo kwa nguvu zote, sote tutaathirika kwa namna mbalimbali ikiwemo usalama wa Taifa na familia zetu na mali tulizonazo huku nyumbani na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hii, zinahitajika jitihada za pamoja kati ya wazazi, viongozi wa mila, jamii, vitongoji, vijiji, kata, wilaya mkoa na madhehebu ya dini na Serikali kwa ujumla katika kulishughulikia na kulimaliza tatizo hili la ulevi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la wazazi kuhakikisha kwamba katika umri wa kijana kuna mambo ya msingi yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini na kwa ungalifu mkubwa. Vijana wafundishwe na kutayarishwa namna ya kuishi katika jamii, namna ya kupambana na umaskini kwa kufanya kazi na mfano mzuri wa malezi ya vijana uko kwenye jamii ya Kimasai. Mpaka sasa vijana wa kabila hili ni mfano wa kuigwa kwani wamedumisha mila zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla tatizo la ulevi kwa vijana wetu vijijini (Mkoani Kilimanjaro na maeneo mengine nchini) ni kubwa sana na jambo hili ni letu sote. Ni vyema tukaweka nguvu pamoja ili kuitokomeza shida hii na kunusuru maisha yao kwani linatishia nguvu kazi ya Taifa letu ambayo inatokana na kundi la vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kupitia Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, iwasaidie vijana wa Kitanzania wawe na programu za kuweka vipaumbele katika mambo makuu matatu katika maisha yao ya kila siku ambayo ni utaifa, uchumi na kushiriki katika fani mbalimbali za kujipatia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie mchango wangu kwa kusema kwamba Tanzania yetu ya leo na kesho inawategemea sana vijana. Hivyo basi ni vyema nchi yetu ikawekeza nguvu kubwa katika malezi ya vijana kwa kuhakikisha kuwa wanaachana kabisa na ulevi wa aina yoyote ile kwa sababu vijana ni tunu, hazina na thamani katika Taifa letu. Ni vyema jambo hili likasaidiwa na michakato ya kisheria katika ngazi za vijiji, kata, wilaya na Taifa. Uwepo wa sheria kali katika maeneo hayo kutasaidia sana kukabiliana na ulevi uliokithiri kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kwa hotuba nzuri ya bajeti. Pia niwapongeze wasaidizi wake Wizarani kwa jinsi ambavyo wanasukuma ajenda za uwekezaji hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye masuala yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naishauri Serikali isimamie vyema utekelezaji wa Sera ya Uwekezaji ili kuisaidia nchi yetu kuzalisha kwa kutumia rasilimali tulizonazo na kutuletea maendeleo makubwa na kuongeza pato la Taifa. Pa kuanzia ni vyema Serikali ikabiliane na vikwazo vinavyoikabili Sekta ya Uwekezaji ambavyo baadhi ni vikwazo vya kikodi, vikwazo visivyo vya kikodi, vikwazo vinavyohusiana na utaratibu wa masuala ya uwekezaji na vikwazo vya wezeshaji uwekezaji hasa wale wa ndani. Kama Serikali itaangalia kwa makini vikwazo hivi, itakuwa imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kuwawezesha wadau kushiriki kwa mafanikio na kufurahia matunda ya kuwekeza.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili, utahusu maeneo ya kimkakati ambayo Serikali inatakiwa kufungua fursa za uwekezaji kwa wadau mbalimbali. Nchi yetu imebarikiwa kuwa na maeneo makubwa yanayoweza kutumika kuzalisha mazao mbalimbali ya kimkakati. Maeneo mengi ya Tanzania hupokea mvua za kutosha na pia yana maji yanayoweza kutumika kumwagilia na kuzalisha mazao, kwa mfano, maeneo ya Iringa, Mbeya, Njombe na West Kilimanjaro yana maeneo makubwa yanayofaa kuzalisha mazao ya kimkakati ya ngano na shayiri ambayo yana soko kubwa la ndani na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kwenye Sekta ya Mafuta ya Kupikia, nchi yetu ina uwezo mkubwa wa kuwekeza kwenye kilimo cha mazao ya mafuta ya kupikia kama vile alizeti, michikichi, karanga, ufuta na nazi. Uwekezaji huu kwenye kilimo ni vyema ukaenda sambamba na uanzishaji wa viwanda vya kuyaongezea thamani mazao hayo ili tuzalishe mafuta yetu na kuyauza ndani na nje. Kuna uwezekano mkubwa sana wa kuvutia wawekezaji wa sekta ya mafuta ya kula katika Mikoa ya Singida, Tabora, Dodoma, Simiyu, Kigoma, Manyara, Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo uwekezaji wake utakuwa na tija kubwa ni kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya mbolea na viuatilifu. Nchi yetu ni nchi ya kilimo na Serikali yetu inatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mbolea na viuatilifu vya viwandani. Soko la bidhaa hizi ni kubwa hapa nchini na kwa majirani zetu. Naishauri Serikali ihamasishe na kuweka mazingira rafiki ya kuwekeza katika maeneo haya ili kulisaidia Taifa na wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Serikali kwa kuboresha huduma za afya kwani hospitali, vituo vya afya na zahanati zimetapakaa nchi nzima. Kutokana na hili, ni wakati muafaka sasa Serikali ikahamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya dawa kwani soko la ndani lipo na ziada itapelekwa nje. Kwa kufanya hivi, nchi yetu itakuwa imejinasua kwenye tabia ya kuwa mwagizaji wa dawa kutoka nchi ya India na nyinginezo za nje.
Mheshimiwa Spika, fursa nyingine ni kuwekeza katika utengenezaji wa pikipiki hapa nchini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna matumizi makubwa ya pikipiki hapa nchini. Vijana wengi wamejiajiri kwenye biashara ya pikipiki. Hivyo basi, kuna umuhimu wa kuwa na viwanda vya pikipiki na ni vyema Serikali ikaweka mazingira mazuri na kuvutia wawekezaji katika eneo hili. Tukiwa na mwekezaji wa kimkakati, bei za pikipiki zitakuwa chini na vijana wataweza kuzimudu.
Mheshimiwa Spika, kama Serikali itahamasisha uwekezaji kwenye maeneo haya machache niliyoainisha, hii italisaidia Taifa katika safari yake ya kukuza uchumi na kutuletea maendeleo.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko na Naibu wake Mheshimiwa Judith Kapinga pamoja na wataalam wa Wizara kwa kazi kubwa ya kusimamia sekta ya nishati hapa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niipongeze Serikali kwani hadi kufikia mwezi Machi, 2024 jumla ya vijiji 11,837 sawa na 96.37% ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishiwa huduma ya umeme. Hii ni hatua kubwa na ni rai yangu kwamba zoezi la kuunganisha umeme katika maeneo yaliyobaki katika Jimbo la Moshi Vijijini litakamilika ili wananchi wanufaike.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye maeneo mawili; kwanza ni umuhimu wa Serikali kuwekeza kikamilifu kwenye umemejua, na pili ni changamoto ya umeme katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Moshi Vijijini ambayo hayajaunganishwa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya tabianchi, huenda huko mbele ya safari tutakumbana na tatizo kubwa la kupata umeme unaozalishwa na maji. Hivyo basi, ninaishauri Serikali iwekeze kikamilifu kwenye matumizi ya nishati safi na salama itakayotumia jua.
Mheshimiwa Spika, nishati ya jua huundwa kwa paneli zinazokusanya nishati ya mwanga na baadaye hubadilishwa kuwa nishati ya umeme. Umemejua ni chanzo cha uhakika cha nishati ya umeme na kama Serikali itahamasisha uwekezaji katika Umemejua hasa katika maeneo ya vijijini, hii inaweza kuwa suluhisho la kuwapatia watumiaji umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ishirikiane na wadau wa nishati ya jua ili teknolojia hii iweze kuwafikia watumiaji kirahisi. Hii ni pamoja na kuondoa kodi mbalimbali kwenye vifaa vya Umemejua vinavyoagizwa kutoka nje ili kuwapunguzia wananchi bei.
Mheshimiwa Spika, kwenye changamoto za umeme jimboni kwangu, ninaiomba Serikali itusaidie katika maeneo yafuatayo:-
Kwanza katika Kata ya Arusha Chini, kwenye Kijiji cha Mikocheni, Vitongoji vya Masaini na Mashimo ya Mchanga hakuna umeme. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vitongoji hivi.
Pili, katika Kata ya Okaoni, vitongoji vingi katika Vijiji vya Sisamaro, Omarini na Mkomilo vinahitaji kuunganishwa kwani wananchi wamesubiri kwa muda mrefu.
Tatu, kata ya Kindi, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana, katika Kata ya Kindi, Kijiji cha Chekereni Weruweru, Vitongoji vya Miembeni na Kisiwani havina umeme kabisa. Pia baadhi vitongoji vya Vijiji vya Kindi Juu na Kindi Kati havijapata umeme. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vijiji na vitongoji hivi.
Nne, katika kata ya Mbokomu, kama nilivyoomba kwenye bajeti za miaka mitatu iliyopita, katika Kata ya Mbokomu, Vitongoji vya Mmbede Kyaroni, Tema na Masanga na baadhi ya maeneo ya Korini Kati havijaunganishwa. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vitongoji hivi.
Mheshimiwa Spika, tano katika Kaya ya Mabogini, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, katika Kata ya Mabogini sehemu ambazo hazijapata umeme hadi sasa ni Vitongoji vya Sanya "Line A" na Mjohoroni vilivyopo katika Kijiji cha Mabogini; pia Kitongoji cha Uru katika Kijiji cha Muungano; katika Kijiji cha Maendeleo, Vitongoji vya Mshikamano na Uarushani; Mgungani katika Kijiji cha Mtakuja; katika Kijiji cha Mserekia, hakuna umeme katika Vitongoji vya Mbeya Kubwa, Mbeya Ndogo, Remit, Mkwajuni na Mafuriko.
Mheshimiwa Spika, aidha Kijiji cha Mji Mpya, Kitongoji cha Utamaduni hakijaunganishwa. Ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye maeneo yaliyotajwa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Kimochi, Kitongoji cha Kiwalaa kilichopo Kijiji cha Sango, Kitongoji cha Iryaroho kilichopo katika Kijiji cha Mowo, na Kitongoji cha Maryaseli katika Kijiji cha Lyakombila havina umeme, ninaiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo niliyotaja hapo juu.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kibosho Mashariki; kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, Kata ya Kibosho Mashariki inahitaji huduma katika Kijiji cha Sungu, Vitongoji vya Kyareni na Nkoitiko havijaunganishwa; katika Kijiji cha Singa, Kitongoji cha Singa Juu hakijaunganishwa; katika Kijiji cha Mweka, Vitongoji vya Mweka Juu na Omi havijaunganishwa, hivyo ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vijiji na vitongoji vilivyotajwa.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Kibosho Kati, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, Vijiji vya Uri na Otaruni umeme una nguvu kidogo (low voltage) na kunahitajika transifoma, na katika Kijiji cha Otaruni, Kitongoji cha Ngoroshi hakuna umeme, na tunaomba wananchi wapatiwe huduma.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Uru Mashariki; kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi, katika Kijiji cha Materuni, Kitongoji cha Wondo hakijaunganishwa, hivyo ninaiomba Serikali ipeleke huduma kwenye kitongoji hiki.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe na Naibu wake Mheshimiwa David Silinde na wataalam wa Wizara na taasisi zote zinazosimamiwa na Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye zao la kahawa. Hapa duniani kahawa ni moja kati ya vinywaji maarufu vinavyopendwa na vinavyotumika. Baada ya maji ya kunywa, kahawa ni kinywaji cha pili kinachotumika zaidi duniani. Kahawa inapendwa kuliko vinywaji vingine kama chai na kakao, kutokana na uwepo wa caffeine kubwa.
Mheshimiwa Spika, wanasayansi wanasema kwamba unywaji wa kahawa mara kwa mara una faida nyingi kiafya kama vile kuzuia uwezekano wa kupata kisukari type 2, alzheimer's disease, msongo wa mawazo, ugonjwa wa moyo, kurefusha maisha, kupunguza maumivu mwilini na kuongeza hamu ya kula - fiber intake. Kutokana na umaarufu huu, kahawa ya kijani ni bidhaa ya pili kibiashara duniani baada ya mafuta ya petroli na dizeli.
Mheshimiwa Spika, inakadiriwa kwamba wanywaji wa kahawa duniani hutumia wastani wa vikombe bilioni 2.6 kila siku. Huko Amerika na Australia kikombe cha kahawa kinauzwa dola 3.72 na dola 3.50 (shilingi 9,300 – 8,750). Aidha, kilo moja ya kahawa iliyokaangwa inaweza kuzalisha vikombe 120 - 140 Amerika 1,116,000 - 1,302,000) na Australia (1,050,000 - 1,225,000).
Mheshimiwa Spika, takwimu kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania zimeonesha kwamba kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 bei ya kilo moja ya Arabica ilikuwa shilingi 3,000 na bei ya kilo moja ya Robusta iliuzwa shilingi 2,000. Bei hii haijafika hata bei ya nusu kikombe cha kahawa iliyoelezwa hapo juu.
Mheshimiwa Spika, ukilinganisha bei hii na na kazi ngumu za kuzalisha zao la kahawa, pesa anayopata mkulima ni ndogo sana na kilimo cha kahawa hakimlipi mkulima wa kahawa ya Arabica. Kwa ujumla uzalishaji wa kahawa ni mgumu.
Mheshimiwa Spika, kazi muhimu na zenye gharama kwenye kahawa ni pamoja na kukata matawi, kupalilia, kuweka mbolea, kupiga dawa, kuvuna, kupukuchua, kuchagua na kuondoa kahawa mbovu, kuikausha na kuisafirisha kuipeleka sokoni.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ugumu wa kuzalisha kahawa, bei wanayopewa wakulima wetu huwa ni ndogo sana. Kwenye mnyonyoro wa masoko mkulima huuza kwenye vyama vya ushirika, bodi ya kahawa na baadaye hupelekwa nje na kwenye mfumo huu mkulima hupata bei ndogo.
Mheshimiwa Spika, takwimu kutoka Bodi ya Kahawa zinaonesha kwamba tani 81,498 za kahawa ziliuzwa nje ya nchi kwa msimu wa 2022/2023 na kutupatia dola milioni 231 (shilingi bilioni 440.4) na kuweka rekodi ya mauzo toka tupate Uhuru, jambo hili ni jema. Ili nchi ifikie lengo la kuzalisha kahawa nyingi kama ilivyo kwenye mipango ya kitaifa na mkulima kupata bei nzuri kwa kahawa wanayozalisha, naishauri Serikali ifanye haya yafuatayo:-
(i) Kwa kuwa kahawa inahitaji maji mengi muda wa msimu wote, ni vyema miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya wakulima wadogo ikarekebishwe (mifereji ya asili). Serikali itenge fedha za kutosha kuboresha mifereji ya asili kwenye maeneo yanayozalisha kahawa, kwani maji ni hitaji kubwa kwenye uzalishaji wa kahawa.
(ii) Serikali iendelee kutoa miche bora ya kahawa kwa njia ya ruzuku kwa wakulima. Miche 20,000,000 haitoshelezi mahitaji ya wakulima.
(iii) Serikali ihamasishe wawekezaji watakaofanya usindikaji wa bidhaa za kahawa hapa nchini. Serikali ishawishi makampuni makubwa ya kusindika kahawa wafungue viwanda hapa nchini. Ni vyema makampuni kama Nestle, Starbucks Corporation, Matthew Algie & Company Limited, Kraft Foods Inc., Tata Consumer Products Limited, Strauss Group Limited, Jacobs Douwe Egberts na Tchibo Coffee International Limited yakashawishiwa kuwekeza hapa nchini.
(iv) Serikali iimarishe uwezo wa makampuni ya ndani kuongeza thamani kwenye zao la kahawa kwa kuikaanga na kusindika kahawa hapa nchini. Tuwe na viwanda vingi kama kile cha instant coffee cha Bukoba.
(v) Pembejeo muhimu za kahawa kama vile mbolea na dawa za wadudu na magonjwa zitolewe kama ilivyo kwenye zao la korosho.
(vi) Serikali isaidie wakulima wa kahawa kupata soko la uhakika watakakouza kahawa yao kwa bei nzuri na ya kuridhisha. Ni vyema vyama vya ushirika vikapatiwa taarifa za uhakika za soko na vikaruhusiwa kushiriki kwenye kutafuta bei nzuri ya kahawa popote soko lilipo duniani.
(vii) Serikali isaidie wakulima kuzalisha kahawa yenye ubora ili kukidhi viwango vya soko la kimataifa.
(viii) Serikali isaidie kuwapatia wakulima wa kahawa hapa Tanzania huduma muhimu za ugani.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Hamad Masauni na Naibu wake Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye majukumu ya ulinzi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa leo utahusu changamoto za mdau muhimu wa kusafirisha abiria ambao ni bodaboda na ushauri wa nini kifanyike kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya bodaboada ni biashara inayokuwa kwa kasi sana hapa nchini Tanzania. Hii ni kwa sababu vijana wengi wameamua kuingia kwenye biashara ya bodaboda kutokana na ukosefu wa ajira. Hivyo basi, kazi ya kusafirisha abiria kwa kutumia bodaboda imekuwa ni fursa kwa vijana kutokana na ukosefu wa usafiri wa magari kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto ya barabara, kwenye maeneo mengine ya makazi, hii ndiyo njia pekee ya watu kufika makwao. Bodaboda hutumika pia kwenye shughuli za kisiasa kwani zimekuwa zikinogesha misafara ya wanasiasa wetu wakiwa katika majukumu yao ya kutembelea maeneo mbalimbali, lakini pia bodaboda zimekuwa usafiri mbadala ikiwa mtu ana haraka na hataki kukwama katika changamoto ya msafara wa magari barabarani. Vilevile wafanyabiashara pia wanatumia bodaboda kuwachukulia wateja wao bidhaa za aina mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukweli huu, ni vyema kundi hili liangaliwe kwa jicho la pekee ili wasaidiwe kuboresha huduma zao kwa raia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na umuhimu huu wa bodaboda, waendeshaji wa vyombo hivi hukabiliana na changamoto nyingi. Hivyo basi Wizara ya Mambo ya Ndani ikishirikiana na wadau wengine wanahitaji kuja na mikakati ya kitaifa ili kukabiliana nazo. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na:-
(i) Baadhi ya waendesha magari huwadharau sana bodaboda. Utakuta bodaboda ipo barabarani, gari inaipigia honi kwa fujo itoke au utakuta gari inataka kuingia barabara kuu wakiona bodaboda hawasubiri, wanaingia tu na kusababisha ajali. Ikumbukwe vyote ni vyombo vya moto, vina haki ya kutumia barabara na vinalipia mapato ya Serikali. Aidha, bodaboda inakuwa imebeba roho za watu pia. Hilo nalo linahitaji kuangaliwa, kwani vitendo hivi husababisha ajali na vifo.
(ii) Waendesha bodaboda wengi huwa wanakamatwa na polisi na kuandikiwa faini kwa kutofuata sheria za usalama barabarani na kuhatarisha maisha yao na ya watumia njia kwa miguu na hata kusabaisha mtafaruku na usumbufu kwa waendesha magari.
(iii) Waajiri walio wengi hawawapi mikataba madereva wa bodaboda inayowapa haki zao kimkataba. Wale wenye mikataba, sehemu kubwa haina haki ya kupata bima za afya na kuweza kujiwekea akiba. Mikataba inaonesha kulinda maslahi ya mwenye chombo badala ya maslahi ya dereva wa bodaboda.
(iv) Hapa nchini hakuna mfumo rasmi na rafiki wa kuwakagua madereva wa bodaboda kama wamekidhi vigezo vya kufanya hiyo kazi.
(v) Baadhi ya abiria wanaowapa huduma huwa wanakuwa wezi na sio abiria wa kweli. Katika maeneo mengi hapa nchini, waendesha bodaboda wengi wameibiwa na kuporwa pikipiki na watu wanaojifanya kuwa abiria, lakini baadaye wanawageuka na kuwapora kwa kuwatishia kuwafanyia mambo mabaya ikiwa ni pamoja na kuwatoa uhai.
(vi) Changamoto nyingine ni ajali kuongezeka. Hii inasababishwa na vijana wengi kutokujua sheria za barabara. Kuna vijana wanaamini ukishajua kuendesha bodaboda mtaani unaweza pia kuendesha barabarani. Hii hupelekea waendeshe pikipiki barabarani bila kuwa na uelewa kuhusu sheria za barabara. Ajali nyingi zimepelekea vifo na ulemavu wa kudumu kuongezeka. Taarifa zinaonesha kwamba 70% ya majeruhi wa ajali za barabarani wanaopokelewa MOI wanatokana na ajali za bodaboda.
(vii) Changamoto nyingine ni ya waendesha bodaboda kupata vishawishi vya ngono. Kuna abiria ambao ni wanawake wakipanda pikipiki hawataki kulipa na kuwaambia waendesha bodaboda kuwa wanaweza kulipa kwa kufanya ngono hasa abiria ambao wanawachukua usiku kutoka sehemu za starehe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto zilizotajwa hapo juu, ni vyema Wizara ya Mambo ya Ndani ikaweka umuhimu mkubwa kwenye watoa huduma hawa ambao kwa mawazo yangu ndiyo inayosafirisha watu wengi kuliko vyombo vingine vyote vya usafiri hapa nchini na kutoa ajira za vijana wetu wengi na huchangia kwenye pato letu la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto ya bodaboda hapa chini, ninaishauri Serikali ifanye yafuatayo:-
(i) Idara ya Usalama Barabarani ishirikiane na LATRA ili kuwe na usajili wa vituo rasmi vya bodaboda katika maeneo yote nchini (vijijini na mijini). Kwenye hivi vituo, kuwe na ukaguzi wa madereva pamoja na pikipiki mara kwa mara na kwa yule asiyekidhi vigezo asiruhusiwe kupakia abiria hadi pale atakaporekebisha kasoro zake. Ni vyema Idara ya Usalama Barabarani itoe mafunzo maalumu ya uendeshaji salama wa bodaboda.
(ii) Bodaboda hufika katika maeneo yote ya vijijini na mijini. Kuna maeneo mengine askari huzuia bodaboda kuingia sehemu za miji mikuu. Hivyo basi, kama kuna sera yoyote itakayotungwa kuzuia bodaboda zisifike maeneo fulani, hili inabidi liangaliwe kwa umakini mkubwa kwani inaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa kuyafikia maeneo hayo.
(iii) Pikipiki nyingi za bodaboda kwa sasa zina cc125-150. Pikipiki hizi hukimbia sana na hiki ndicho chanzo cha ajali nyingi. Napendekeza Serikali iweke sheria kwa pikipiki za kusafirishia abiria zisiwe na nguvu zaidi ya cc100.
(iv) Askari wa Usalama Barabarani wahamasishe raia kukataa kupanda abiria zaidi ya mmoja (mishikaki) kwa sababu udhibiti wa chombo (control) hupungua kwa dereva akipakia abiria zaidi ya mmoja, hivyo ni rahisi kupata ajali ukiwa uko kwenye mshikaki endapo itatokea dharura yoyote.
(v) Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na ile ya Uchukuzi na wadau wengine ianzishe clinics za kutoa elimu. Katika clinic hizo, yafuatayo yapewe kipaumbele:-
(a) Clinic hizi zitoe elimu mara kwa mara kwa waendesha bodaboda kuhusu usalama barabarani.
(b) Clinic kwa wamiliki wa bodaboda ziwaelekeze kwamba mtu wanayempa chombo cha usafiri ana leseni.
(c) Waendesha bodaboda wazingatie sheria za barabarani na kutotumia kilevi chochote muda wa kazi.
(d) Vijana wafundishwe kujihami ili wasiambukizwe au kuambukiza VVU.
(e) Kwa kuwa changamoto kubwa ya kazi ya bodaboda ni ajali, clinic hizi ziwafundishe umuhimu na namna ya kupata bima za afya na kujiunga na Mifuko ya Pensheni ili akiba hizi zije kuwasaidia uzeeni. Bima za Afya zitakuwa msaada mkubwa katika usalama wao pale inapotokea changamoto ya ajali au kuugua.
(f) Clinic hizi zitoe elimu kwa madereva bodaboda ili waweze kuepukana na kundi la kulaumiwa. Kundi bodaboda linafahamika kama linalovunja sheria za barabarani na kufanya vurugu, hasa pale mwenzao anapopata ajali. Wengi hujichukulia sheria mkononi ikiwa ni pamoja na kuua watu na kuchoma magari hata kama kosa ni la bodaboda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Mipango na Uwekeza, Profesa Kitila Mkumbo kwa hotuba nzuri ya Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka wa 2023 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo kuongoza Wizara mpya ya Mipango na Uwekezaji ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais. Kuanzishwa kwa Wizara hii kulikuwa ni muhimu sana kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu. Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo ni mwanazuoni mahiri na nina uhakika ataitendea haki nafasi yake.
Mheshimiwa Spika, tangu tulipopata uhuru nchi yetu ilikuwa inakabiliwa na maadui wakuu watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini. Nchi imepiga hatua kupambana na maradhi na ujinga ila bado tuna njia ndefu ya kupambana na umaskini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii, nchi yetu inahitaji mipango madhubuti ya kuondoa umaskini unaowakabili wananchi wa Tanzania, kwani Mungu ametujalia rasilimali nyingi za kimkakati ambazo kama zitatumika vizuri zitasaidia sana kuondoa umaskini unaowakabili Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Tanzania inasifika kwa kuwa na rasilimali nyingi yakiwemo madini ya aina nyingi, ardhi nzuri ya kilimo, mifugo, mbuga za wanyama katika kila kanda, maziwa, mito, bahari, bandari na vitu vingine vingi. Pamoja na baraka hii kubwa nchi yetu imekosa mipango madhubuti ya kuzitumia rasilimali zilizopo kutuletea maendeleo. Bado watu wetu ni maskini sana.
Mheshimiwa Spika, toka tupate uhuru maendeleo tuliyofikia ni kidogo. Kuna nchi nyingi hapa duniani zilikuwa na uchumi sawa au kidogo kuliko sisi, lakini kutokana na mipango mizuri ya maendeleo na usimamizi wa utekelezaji mipango, nchi hizo zimefikia uchumi wa juu. Ni maoni yangu kwamba Tanzania hatustahili kuwa katika kiwango hiki cha maendeleo (cha uchumi wa kati kiwango cha chini) tukilinganisha na utajiri mkubwa wa rasilimali tulizonazo ambazo nimezitaja hapo juu.
Mheshimiwa Spika, ni vyema Serikali ikaja na mpango bora wa kuboresha uchumi na kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu yatakayohakikisha upatikanaji wa mahitaji ya kizazi cha sasa pasipo kuathiri upatikanaji wa hayo mahitaji kwa kizazi cha baadaye. Nashauri mpango huo ulindwe kisheria ili pasiwepo mabadiliko katika utekelezaji na usiwe unatekelezwa kwa matakwa mengine yoyote nje ya utaifa.
Mheshimiwa Spika, naishauri Wizara ya Mipango na Uwekezaji ije na mpango madhubuti utakaohakikisha miundombinu ya uchukuzi na mawasiliano inajitosheleza kwenye Taifa letu. Tuwe na uhakika kwamba reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari na mtawanyiko wa mikongo ya njia za mawasiliano ni imara, kwani hivi ni vitu vya msingi kwenye kutuletea maendeleo kwani vinahitajika sana kurahisisha biashara na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, ili kutupatia maendeleo ya haraka, sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zinahitaji kipaumbele cha kipekee katika mpango wa Serikali, kwani sekta hizi zinaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania. Kwenye sekta ya viwanda ni muhimu sana mipango madhubuti itengenezwe ili tuwe na viwanda vya aina mbalimbali (vidogo, vya kati na vikubwa) ili vitumike kikamilifu kwenye kuchakata malighafi za kilimo na madini. Mipango ikifanikisha hili ni kwamba viwanda vitasaidia kupunguza tatizo la ajira nchini kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa maendeleo, ninaishauri Serikali iwekeze kimkakati katika madini mapya ya kimkakati ya lithium, chuma, makaa ya mawe na helium ili viwanda vijengwe hapa nchini badala ya kuyapeleka madini haya nje ya nchi kama malighafi kwa nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika, ni vyema sana kuhakikisha mipango yetu inasimamiwa na kuhakikisha huduma za elimu nchini zinaimarishwa. Ni muhimu mpango uzingatie kuwa kuna vitendea kazi vya kutosha na miundombinu mingine yote pamoja na rasilimali watu ya kutosha ili kwa pamoja vitoe elimu bora kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, mipango yetu ya maendeleo iweke vipaumbele na kuhakikisha kuwa huduma za umeme wa uhakika, maji safi na salama na zile za afya nchini zimeimarika.
Mheshimiwa Spika, nahitimisha mchango wangu kwa kushauri kwamba ni vyema mpango na dira ya Taifa letu ijumuishe mambo muhimu yenye maslahi mapana kwa Taifa letu na utekelezaji wake ulindwe kisheria.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu wake na Katibu Mkuu na timu yake na Wizara ya Mifugo kwa kazi kubwa mnayofanya kuna mageuzi makubwa mmeyaleta na tunayaona kusema ukweli kwenye maziwa, Ngozi, kuku, mbuzi, samaki na mengine mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa mradi wa shamba darasa la kuku ambalo lilipatiwa kwenye Kata ya Uru Kaskazini na Kibosho Magharibi nashukuru sana, tunaomba tuje tumalizie ile kazi. Pia nashukuru kwa majosho ambayo tumejengewa kule lakini bado nahitaji josho kwenye Kata ya Arusha Chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anaongeza bajeti ya Wizara hii. Miaka michache iliyopita bajeti ilikuwa ndogo sana lakini sasa hivi tumeona increase ya 63% ambapo tunaona wanapata shilingi bilioni 460, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Hii pesa ni muhimu na mimi niseme hapa pesa hii haiwatoshi hawa watu, wanahitaji pesa nyingi ili waje na mageuzi ambayo wametarajia kwenye kuongeza utafiti, kutuletea chanjo, huduma za ugani, mbari za mifugo, malisho, vizimba, BBT na mambo mengi. Wana mambo mengi wanataka kufanya kwa hiyo wanahitaji pesa. Niombe Serikali kama Kamati tulivyo-recommend iwaongezee hawa watu pesa ili waweze kufanya mageuzi wanayotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie pale alipomalizia Mheshimiwa Rahhi kwamba tunaomba kama Kamati tulivyoshauri tuwe na Wakala wa Mifugo na Wakala wa Uvuvi ili waweze kusimamia hii sekta kwa uhakika zaidi kwa sababu sasa hivi usimamizi nao unaonekana ni shida. Kwa hiyo tukianzisha hizi wakala zitamsaidia Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla kwenye kuwupa output. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite kwenye jimbo langu, Mkoa wa Kilimanjaro umebarikiwa sana, una mazingira yanayoweza kufuga kama Ulaya hivi. Upande wa milimani tunaweza tukafuga ng’ombe wa maziwa wanaoweza kutoa mpaka lita 40 kwa siku na upande wa tambarare Mabogini na Arusha Chini kule tunaweza tukazalisha nyama nyingi sana. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri sisi kule Kilimanjaro tunaomba utusaidie, tupe mbegu bora za mitamba inayoweza kutoa lita 20 hadi 40 kwa siku, uone Mchaga atakavyopambana na Wapare kule. Sisi utatudai maziwa na nyama na kila kitu. Pia, mbegu bora za malisho ili tupeleke kwenye haya maeneo kwa mfano ile Mbegu ya Juncao ni mbegu bora na zile nyingine. Sisi tunakuomba utukopeshe tutakulipa maziwa na nyama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni samaki, najua Mkoa wa Kilimanjaro una maji mengi na tuna potential ya ku-contribute kwenye uchumi wa Samaki. Sasa tuna Nyumba ya Mungu pale na wale wavuvi wetu wa Nyumba ya Mungu wangependa sana wawe kwenye program ya vizimba. Nimwombe Mheshimiwa Waziri vile vizimba 497 ambavyo ameviweka kwenye program hii, sisi tukopeshe vizimba na awafundishe vijana wetu namna ya kufuga samaki kwa kutumia teknolojia ya vizimba. Tusiende tu kwenye maziwa hata Nyuma ya Mungu tunajua tutazalisha samaki wengi halafu sisi atudai samaki na mchango wetu kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, kwenye samaki kuna eneo ambalo lina-potential kubwa sana, ukanda wa tambarale tunalima mpunga eneo la Mandaka Mnono, Mabogini na kule Arusha Chini tunalima mpunga, hebu leteni mbegu, anzisheni kuzalisha vifaranga tuwapelekee wakulima wa mpunga, tuwape samaki watupe kule kwenye majaruba uone tutakavyozalisha samaki wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Wizara iajiri Maafisa Ugani wakutosha wawafundishe watu namna ya kufuga samaki kwenye majaruba ya mpunga, siyo Kilimanjaro tu hata maeneo mengine ambayo yanalima mpunga tunaweza tukasaidia sana uchumi wa samaki na ile 1.8 ikaruka ikawa juu ya hapo, tukachangia vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kilimanjaro tunayo maji mengi, mifugo ina potential ya kukusaidia, samaki ina potential ya kusaidia Wizara, kwa hiyo tunaomba watukopeshe miradi sisi tutawalipa nyama na samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Innocent Bashungwa na Naibu wake Mheshimiwa Engineer Godfrey Kasekenya, watendaji wote walio chini ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye kutengeneza mitandao ya barabara na madaraja maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu changamoto za barabara zinazojengwa na TANROADS katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Kiboriloni - Tsuduni - Kidia kwa kiwango cha lami. Barabara hii inajengwa na TANROADS na bado haijakamilika. Tuliwahi kutembelea barabara hii na Kamati ya Siasa ya Wilaya baada ya chama kupokea malalamiko kwamba ujenzi ulikuwa umelegalega. Pamoja na maelekezo na ahadi kwamba ujenzi ungeendelea, hadi leo ujenzi umekwama na mkandarasi hajaonekana site.
Mheshimiwa Spika, kuna sehemu mbaya sana kwenye barabara hii na wananchi wanailaumu sana Serikali.
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Uru - Kishumundu - Materuni inajengwa kwa kiwango cha lami. TANROADS inajenga barabara hii kwa niaba ya TARURA. Kero kubwa ni kwamba kasi ya ujenzi ni ndogo sana.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Moshi Vijijini, Barabara ya Kwa Rafaeli - Mto Sere inahudumiwa na TANROADS. Wameshaweka mitaro katika baadhi ya maeneo, na haijajengwa hata kidogo kwa kiwango cha lami. Barabara hii ni muhimu kwani ni sehemu ya kusafirisha watalii kwenda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Umbwe.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibosho Shine - Kwa Rafaeli ilikuwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi toka mwaka 2005 na inajengwa na TANROADS lakini hadi leo haijakamilika.
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Rau - Uru - Shimbwe yenye urefu wa zaidi ya kilometa 13 ilikuwa kwenye ahadi za viongozi wa Kitaifa kujengwa kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara hii umeanza kwa kasi ndogo sana.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo ya hapo juu, naishauri Serikali ifanye yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, ninaiomba Serikali itenge kiasi cha fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni - Kidia kwa kiwango cha lami, kwani wananchi wanalalamika sana.
Mheshimiwa Spika, pili, ninaishauri Serikali itenge fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Uru - Kishumundu - Materuni.
Mheshimiwa Spika, tatu, ninaiomba Serikali itenge fedha za kutosha na kukamilisha kwa kiwango cha lami kipande cha Barabara ya Kwa Rafaeli - Mto Sere. Vilevile ninaishauri Serikali ifikirie kujenga kwa kiwango cha lami kipande cha Sere hadi Geti la Umbwe la kupanda Mlima Kilimanjaro. Barabara hii ni mbovu mno pamoja na kwamba hutumika kusafirisha watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Umbwe na kuiingizia Serikali kipato kupitia sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, nne, ninaiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa Barabara ya Kibosho Shine - Kwa Rafaeli - International School kwa kiwango cha lami kama ilivyoanishwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi toka mwaka 2005. Ujenzi wa barabara hii umechukua zaidi ya miaka 13.
Mheshimiwa Spika, tano, ninaishauri Serikali itenge fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Rau - Uru - Shimbwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa zaidi ya kilometa 13 kama wananchi walivyoahidiwa na wagombea Urais wakati wa kampeni.
Mheshimiwa Spika, baada ya ushauri niliotoa hapo juu, naunga mkono hoja.