Primary Questions from Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi (15 total)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano ya simu katika Kata ya Uru Shimbwe Jimbo la Moshi Vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote inatambua changamoto ya ukosefu wa huduma za mawasiliano katika Kata ya Uru Shimbwe yenye Vijiji vya Shimbwe Chini na Shimbwe Juu. Tathmini katika Kata hii ilifanyika mwezi Machi mwaka 2021 na kubainika kuwa vijiji hivi vina changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano. Hivyo, Vijiji hivi vya Kata ya Uru Shimbwe vitaingizwa katika zabuni zijazo za kupata mtoa huduma wa kuvifikishia huduma za mawasiliano. Nashukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara yenye kilometa 13 kuanzia Rau Madukani – Mamboleo – Shimbwe Juu katika Jimbo la Moshi Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza ahadi zilizotolewa na Waheshimiwa Marais walizozitoa katika Awamu zote. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 na 2019/ 2020 Serikali imeendelea kujenga kipande cha barabara chenye urefu wa mita 288 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi milioni 190 kwa barabara ya Rau Madukani – Mamboleo - Shimbwe Juu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, barabara hi iilifanyiwa matengenezo ya muda maalum yenye urefu wa kilometa 9 kwa kiwango cha changarawe ambayo iligharimu shilingi milioni 148.85. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 barabara hii imetengewa bajeti ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi yenye urefu wa kilometa 2.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi na matengenezo ya barabara nchini ikiwemo Moshi Vijijini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itarejesha utoaji wa ruzuku ya pembejeo za dawa kwa wakulima wa kahawa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kutokana na kukua kwa teknolojia ambako kumewezesha kugunduliwa kwa miche chotara ya kahawa ambayo ina ukinzani na magonjwa makuu ya kahawa ya kutu ya majani na Chole Buni, Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuzalisha miche bora ya kahawa milioni 20 yenye ukinzani mkubwa wa magonjwa na ambayo hutolewa kwa ruzuku kupitia Taasisi ya Utafiti TaCRI na Bodi ya Kahawa Tanzania.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kujenga Daraja Kata ya Arusha chini litakalounganisha Vijiji vya Muungano, Mikocheni na Chemchem?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 barabara hii imetengewa fedha kiasi cha Shilingi milioni 475.00 kwa ajili ya kuanza kujenga daraja katika Mto Ronga ili kuweza kuunganisha Vijiji vya Muungano, Mikocheni na Chemchem. Mradi huu upo katika hatua za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TARURA itaendelea kuweka katika vipaumbele vyake ujenzi wa barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuhakikisha inaweza kupitika katika kipindi chote cha mwaka.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha barabara zinazowapeleka Watalii Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka kipaumbele na jitihada katika ukarabati wa barabara zinazotumika kupeleka watalii katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau na mamlaka zinazohusika na utengenezaji na ukarabati wa barabara hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa jitihada hizo zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa barabara za Machame, Mweka na Marangu kwa kiwango cha lami na ukarabati wa mara kwa mara wa barabara za changarawe zinazoelekea lango la Rongai, Lemosho, Kilema, Londorosi na Umbwe. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali itafanya
ukarabati kwa kiwango cha changarawe kwa barabara inayoelekea kwenye lango la Umbwe.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua kero ya nyani, kima, tumbili na ngedere kwa Wananchi wanaopakana na Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu suali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ina vituo vya askari wanyamapori kwenye Wilaya zote zinazopakana na Hifadhi, ambapo Moshi kuna vituo vinne, Rombo kuna vituo vitatu, Hai kuna kituo kimoja, Siha kuna kituo kimoja na Longido kuna vituo viwili. Vituo hivyo vina askari wa Jeshi la Uhifadhi ambao kwa kushirikiana na maafisa wa wanyamapori kutoka wilaya husika wamekuwa wakifanya kazi ya kuwafukuza wanyamapori wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi ya wananchi au mashamba yao.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini wanaopatwa na madhara ya wanyamapori, wakiwemo nyani, kima, tumbili na ngedere na kadhalika kutoa taarifa kwa askari wa uhifadhi wa vituo hivyo pale wanyamapori hao wanapoingia kwenye maeneo yao ili waweze kudhibiti wanyamapori hao.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, lini Serikali itarejesha utoaji ruzuku ya pembejeo za dawa kwa Wakulima wa Kahawa ili wazalishe zaidi kama awali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya viuatilifu katika zao la kahawa ni njia ya udhibiti wa visumbufu vya zao la kahawa ili kulinda ubora wa mazao yanayozalishwa dhidi ya magonjwa ya Kutu ya Majani na Chole Buni. Aidha, utafiti wa zao la kahawa umebaini kuwa upandaji wa miche bora ya kahawa ni njia pekee inayowezesha kuzalisha mazao yenye tija nzuri, ukinzani dhidi ya wadudu waharibifu na magonjwa ya zao la kahawa na kupunguza matumizi ya viuatilifu kwenye kahawa kwa takriban asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kutoa ruzuku ya viuatilifu vya kahawa bali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) na Bodi ya Kahawa Tanzania imeendelea kuzalisha, kusambaza na kuhamasisha wakulima kubadilisha mikahawa ya zamani kwa kupanda miche mipya ambayo ina ukinzani dhidi ya magonjwa ambapo katika kipindi cha mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 jumla ya miche 41,348,628 imezalishwa na kugawiwa bure kwa wakulima.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kutatua changamoto za wakulima waliowekeza kwenye SACCOS na fedha zao kupotea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa upotevu wa fedha za wanachama wa SACCOS nchini unadhibitiwa ipasavyo, Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika inayo mikakati mbalimbali, ikiwemo kutoa miongozo ya uendeshaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchi zikiwemo SACCOS, kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU), ambao utasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Vyama vya Ushirika, zikiwemo SACCOS, kuendelea kutoa elimu ya ushirika kuhusu namna bora ya uendeshaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika kwa wananchi wote, wakiwemo wanachama, viongozi na watendaji wa SACCOS kupitia njia mbalimbali.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga kwa Kiwango cha lami barabara ya Getifonga – Mabogini – Kahe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 kuijenga kwa kiwango cha lami ambapo hadi sasa TARURA – Mkoa wa Kilimanjaro wamekamilisha usanifu kwa kiwango cha lami na inahitaji shilingi bilioni 28.59 ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 TARURA imetenga shilingi milioni 158.85 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kwa urefu wa kilomita 12 katika barabara hiyo na kazi imekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilometa 1.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kupeleka nishati ya gesi asilia katika vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro ili kupunguza matumizi ya kuni?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi asilia inaweza kusafirishwa kwa njia ya mabomba au kwa njia ya mitungi/tanki inayobebwa na malori/treni/meli ambapo gesi asilia inakuwa katika hali ya gesi iliyogandamizwa (Compressed Natural Gas – CNG) ama kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG). Hadi sasa, gesi asilia inachimbwa Mtwara na hivyo maeneo yaliyounganishwa na kuweza kutumia nishati ya gesi asilia ni yale yanayopitiwa na miundombinu ya mabomba ya kusafirishia gesi ambayo ni Mikoa wa Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kwenda Mombasa Nchini Kenya kupitia Mkoani Tanga, ni moja ya miradi inayotoa fursa ya kuunganisha Mikoa ya Kaskazini na gesi asilia ikiwemo Kilimanjaro kwa kuweka toleo katika eneo la Segera (Tanga). Mradi huu wa bomba bado unafanyiwa kazi Serikalini, utakapokamilika gesi asilia itaweza kufikishwa Mkoani Kilimanjaro, vikiwemo vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro na katika maeneo mengine mkoani humo na mikoa ya jirani, nakushukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa msaada wa kitaalamu kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ili kuongeza idadi ya samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha samaki wanaendelea kuwepo na wanaongezeka katika maeneo yote ya maji, ikiwemo Bwawa la Nyumba ya Mungu. Mikakati hiyo ni pamoja na kufanya tafiti na kuimarisha ushirikishwaji wa jamii na taasisi zisizo za kiserikali katika kusimamia na kulinda rasilimali za uvuvi kupitia Halmashauri, Serikali za Vijiji na Vikundi vya kijamii vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU).
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kufanya tafiti za kujua wingi na mtawanyiko wa samaki katika maziwa makuu na imejipanga kutanua wigo wa kufanya tafiti (frame survey) kwa maziwa madogo ili kutambua hali halisi ya uvuvi katika maziwa hayo. Aidha, tafiti hizo zinatoa taarifa sahihi ili kuiwezesha Wizara kutekeleza mikakati ya kuongeza wingi wa samaki ikiwemo uwezekano wa kupandikiza samaki.
Mheshimiwa Spika, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa, Wizara itaendelea na utoaji wa elimu ya Huduma za Ugani kuhusu athari za uvuvi haramu ili kulinda mazalia ya samaki na kuruhusu samaki kukua na kuongezeka kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, kuna ukweli kwamba kina cha maji ya Bahari ya Hindi hapa Tanzania kimeongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na nini athari zake?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba ni kweli kina cha maji ya Bahari ya Hindi hapa Tanzania kimeongezeka kutokana na kuendelea kuongezeka kwa joto la dunia linalosababisha kuendelea kuyeyuka kwa barafu katika maeno mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa utafiti na vipimo vilivyopo maji ya Bahari ya Hindi katika Pwani ya Dar es Salaam yanaongezeka kwa wastani wa kiasi cha milimita sita kwa mwaka tangu mwaka 2002.
Mheshimiwa Spika, athari za kuongezeka kwa kiwango cha maji ya bahari ni pamoja na:-
(i) Kuongezeka kwa mmomonyoko na upotevu za fukwe;
(ii) Uharibifu wa miundombinu kama vile gati za bahari, barabara, nyumba ofisi na masoko;
(iii) Upotevu wa bioanuwai muhimu ikiwemo mikoko na nyasi za bahari;
(iv) Upotevu wa ardhi ya kilimo, makazi na visima vya maji baridi kuingiwa na chumvi na mafuriko ya mara kwa mara. Ahsante.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:-
Je, Serikali imechukua hatua gani za muda mfupi wa kati na muda mrefu kunusuru theluji inayotoweka Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Profesa Ndakidemi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya kupungua kwa barafu katika Mlima Kilimanjaro ni kuongezeka kwa joto la dunia kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu hususan ukataji wa miti, kilimo, uchomaji wa moto katika maeneo yanayozunguka mlima, uwepo wa mvua chache na vipindi vya ukame na upepo mkavu kutoka Bahari ya Hindi.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mikakati ya muda mfupi Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kupanda miti takriban milioni nane kwa mwaka katika Mkoa wa Kilimanjaro, sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kupitia vipindi vya redio, televisheni, matamasha na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na wadau imezindua kampeni ya kupanda miti zaidi ya bilioni moja katika Mikoa ya Kaskazini ili kunusuru barafu ya Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, mikakati ya muda wa kati ni pamoja na kuhimiza matumizi bora ya ardhi na kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na kutekeleza mipango ya kudhibiti na kupambana na uchomaji moto mlimani. Aidha, katika kutekeleza mikakati ya muda mrefu, Serikali inaendelea kushirikiana na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuboresha teknolojia za kilimo, kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji, kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kurejesha mifumo ya ikolojia kwenye mlima na maeneo yanayozunguka.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:-
Je, Serikali imechukua hatua gani za muda mfupi wa kati na muda mrefu kunusuru theluji inayotoweka Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Profesa Ndakidemi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya kupungua kwa barafu katika Mlima Kilimanjaro ni kuongezeka kwa joto la dunia kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu hususan ukataji wa miti, kilimo, uchomaji wa moto katika maeneo yanayozunguka mlima, uwepo wa mvua chache na vipindi vya ukame na upepo mkavu kutoka Bahari ya Hindi.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mikakati ya muda mfupi Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kupanda miti takriban milioni nane kwa mwaka katika Mkoa wa Kilimanjaro, sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kupitia vipindi vya redio, televisheni, matamasha na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na wadau imezindua kampeni ya kupanda miti zaidi ya bilioni moja katika Mikoa ya Kaskazini ili kunusuru barafu ya Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, mikakati ya muda wa kati ni pamoja na kuhimiza matumizi bora ya ardhi na kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na kutekeleza mipango ya kudhibiti na kupambana na uchomaji moto mlimani. Aidha, katika kutekeleza mikakati ya muda mrefu, Serikali inaendelea kushirikiana na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuboresha teknolojia za kilimo, kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji, kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kurejesha mifumo ya ikolojia kwenye mlima na maeneo yanayozunguka.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itarejesha utoaji wa ruzuku ya pembejeo za dawa kwa wakulima wa kahawa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya soko la kahawa inayozalishwa kwa teknolojia ya kilimo hai, kwa maana ya organic coffee, ambayo husababisha wakulima kupata bei nzuri katika soko, Serikali inahamasisha wakulima kutumia njia mbadala ya matumizi ya dawa kwenye uzalishaji wa kahawa ikiwa ni pamoja na kupanda miche chotara ambayo inazalishwa na kusambazwa bure na Bodi ya Kahawa Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI). Aidha, miche ambayo inazalishwa na kusambazwa kwa wakulima ina ukinzani na magojwa makuu ya kahawa ya chole buni na kutu ya majani ambayo ndiyo yaliyokuwa yanasababisha mahitaji ya matumizi makubwa ya dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa 2023/2024, jumla ya miche 21,899,560 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima wa kahawa katika mikoa yote inayozalisha kahawa hapa nchini. Kati ya miche hiyo, Mkoa wa Kilimanjaro ulipata miche 1,664,635 ambayo imesambazwa kwa wakulima ambapo Wilaya ya Moshi imepata jumla ya miche 328,110 na kusambazwa kwa wakulima kupitia Vyama vya Ushirika. (Makofi)