Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Santiel Eric Kirumba (10 total)

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunganisha mifuko ya mikopo iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwezesha makundi maalum kupatiwa mikopo kwa urahisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelekezo yako, lakini pia kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishaona umuhimu na kupitia Mheshimiwa Rais iliagiza na kuelekeza mifuko kuweza kuunganishwa na kufuatia maelekezo hayo, Serikali iliunda kamati ya pamoja iliyohusisha Wizara zote zinazosimamia mifuko hiyo, kwa ajili ya kufanya tathmini ya utendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kupima utendaji wa mifuko na programu hizo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, mapendekezo mbalimbali yametolewa kwa ajili ya kuboresha utendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji wananchi ikiwa ni pamoja kuunganisha baadhi ya mifuko yenye majukumu na malengo yanayoshabihiana. Taarifa ya tathmini hiyo inaendelea kufanyiwa kazi ndani ya Serikali kwa hatua zaidi ili hatimaye kuiunganisha na kuongeza tija na ufanisi.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu imekwishatekeleza agizo hilo kwa kukamilisha tathmini ya mfumo wa kiutendaji wa mifuko hiyo na baada ya kuunganishwa, mtazamo mpya wa muunganiko wa programu na mifuko husika na utekelezaji wake utaanza baada ya mamlaka kuridhia, asante.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaboresha Bandari Kavu ya Isaka?

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kwa maana ya TPA, imenunua na kupeleka vifaa vya kuhudumia mizigo ambavyo ni forklift moja na reach stacker moja ambavyo vinatumiwa na Shirika la Reli Tanzania kwa maana TRC kuendesha Bandari Kavu ya Isaka, Shinyanga kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kununua na kupeleka vifaa hivyo katika Bandari Kavu ya Isaka ni kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za usafirishaji mizigo kati ya Dar es Salaam, mikoa ya Jirani na Shinyanga na Nchi jirani za Rwanda, Congo na Burundi. Bandari Kavu ya Isaka imekuwa ikitumika japo kwa kiwango kidogo kutokana na changamoto ya mabehewa ya kubeba makasha na injini inayoikabili. TRC mwaka jana Disemba, 2021, imepokea mabehewa 44 na injini tatu za treni kwa ajili ya kuhudumia mizigo kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu ya Isaka. Aidha, Serikali kupitia TPA na TRC inaendelea kufanya ushawishi kwa wateja wa bandari na wasafirishaji wakiwemo wale wa kutoka Nchi jirani za Rwanda, Congo na Burundi kutumia zaidi Bandari Kavu ya Isaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kujenga vyoo maalum kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika madarasa mapya yanayojengwa ili wanafunzi hawa wasikose masomo pindi wanapokuwa kwenye siku zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa matundu ya vyoo unazingatia mahitaji ya wamafunzi wote wakiwemo wavulana na wasichana pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuzingatia hili Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kuzisimamia na kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa pindi wanapojenga shule
mpya wazingatie kujenga matundu ya vyoo kulingana na michoro na ramani zote zinazotumwa kwao kwa kuwa ndani ya michoro hiyo imejumuisha chumba maalum cha wasichana kwa ajili ya kujisitiri wanapokuwa katika hedhi.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuhimiza mashirika mengine ya simu kujiunga na mpango wa M-Mama kwani umekuwa msaada kwa wajawazito wengi?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mfumo wa M-mama unatekelezwa na kusimamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Vodacom, USAID, Vodafone Foundation, Pathfinder International na Touch Foundation. Mfumo huu unalenga kusaidia upatikanaji wa usafiri wa dharura kwa mama mjamzito, mama aliyejifungua na mtoto mchanga kote nchini.

Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya mfumo kwa haraka na kwa kuwafikia walengwa wengi zaidi, kuna haja ya wadau mbalimbali kuongeza nguvu kwa kushirikiana katika utekelezaji wakiwemo watoa huduma wengine wa mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kuwaalika mashirika binafsi wakiwemo watoa huduma wengine wa mawasiliano pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo wajitokeze kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mfumo wa M-mama hapa nchini.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Uwanja wa Ndege katika Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga kitajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfadhili wa mradi huu tayari ameshaleta fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi. Aidha, Serikali imekwishafanya marekebisho ya mkataba na kuwasilisha kwa Mfadhili ili atoe idhini (no objection) kwani kutakuwa na mabadiliko ya gharama ikilinganishwa na wakati mkataba huo uliposainiwa mwaka 2017. Kazi za ujenzi wa mradi huu zitaanza mara moja tutakapopata no objection kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha Kitengo cha Watoto Njiti katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa sasa ina sehemu maalum yenye uwezo wa kulaza Watoto Njiti 18 kwa wakati mmoja. Hata hivyo, ujenzi unaendelea wa Bilioni 1.2 utakaowezesha hospitali kuwa na vitanda 42. Kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 zimetengwa Shilingi Bilioni Sita kwa ajili ya ujenzi.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaboresha Kitengo cha Watoto Njiti katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa sasa ina sehemu maalum yenye uwezo wa kulaza Watoto Njiti 18 kwa wakati mmoja. Hata hivyo, ujenzi unaendelea wa Bilioni 1.2 utakaowezesha hospitali kuwa na vitanda 42. Kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 zimetengwa Shilingi Bilioni Sita kwa ajili ya ujenzi.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuwapa Likizo ya uzazi zaidi ya siku 120 wanaojifungua watoto njiti ili kuwa na muda wa kutosha kuwatunza watoto hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa tuwatendee haki Wananchi wa Shinyanga waliyomchagua Mbunge Santiel Eric Kirumba, kwa kujibu swali Na. 176 kama lilivyoelekezwa kwenye Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali Na. 176 lililoulizwa na Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Utumishi wa Umma, likizo ni miongoni mwa haki za watumishi wa umma ambazo wanastahili kupewa na waajiri wao kwa mujibu wa Kanuni H.12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma mwaka 2009, kanuni hiyo ikisomwa pamoja na Kanuni ya 97 ya Kanuni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la likizo ya mtumishi aliyejifungua mtoto njiti halijaelezwa bayana katika Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni ya 135 ya Kanuni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2022, linapotokea suala ambalo halikuelezwa bayana katika Kanuni ya Utumishi wa Umma, mtumishi atamtaarifu mwajiri kuhusu suala hilo. Mwajiri anaweza kutumia busara kulitatua pale inapobidi na anaweza kutumia sheria nyingine au kushauriana na Katibu Mkuu Utumishi kwa ufafanuzi wa suala hilo ikiwemo nyongeza ya siku katika likizo.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Sekta Binafsi ili kutoa chakula mashuleni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina wadau mbalimbali wanaounga mkono jitihada za Serikali katika utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni. Baadhi ya wadau hao ni kama vile Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), United Nations Children's Fund (UNICEF), World Vision, Feed the Children, SANKU, GAIN Tanzania, Project Concern International (PCI), CiC, Save the Children.

Mheshimiwa Spika, wadau hao hufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika kuzijengea uwezo Kamati za Shule namna ya ushirikishwaji wa wazazi/walezi katika upatikanaji wa chakula cha wanafunzi shuleni, kutoa elimu ya uongezaji wa virutubisho katika chakula cha wanafunzi shuleni (fortified foods); kuhamasisha upatikanaji wa matumizi ya mazao lishe (biofortified) yakiwemo maharage, mahindi ya njano, kwa ajili ya uji wa wanafunzi; kushirikiana na shule zenye utayari wa kuendesha shughuli za kilimo cha mazao ya chakula kwa kugawa mbegu za mahindi na maharage shuleni; na kuandaa miongozo ya utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni.

Mheshimiwa Spika, mpango upo na unatekelezwa kwa kushirikisha wadau ili kuendelea na mpango wa kutoa chakula.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -

Je, lini Serikali itarudisha mikopo ya asilimia 10 kwa Makundi Maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ilisitishwa tarehe 13 Aprili, 2023 ili kupitia na kuboresha utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo kutokana na changamoto zilizobainishwa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, Serikali imesharekebisha sheria na imepitisha Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2019 na 2021 na kutoa Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2024.

Mheshimiwa Spika, shughuli zilizoanza kutekelezwa ni kutoa mafunzo kuhusu mfumo mpya wa utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo kwa wasimamizi 862 katika ngazi za mikoa na halmashauri. Aidha, mafunzo yanaendelea kutolewa kwa Kamati za Usimamizi za Huduma za Mikopo ngazi za kata, halmashauri, wilaya pamoja na vikundi.

Mheshimiwa Spika, kufuatia mafunzo yaliyotolewa, uchambuzi wa awali wa mikopo umeshaanza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na mikopo hiyo inatarajiwa kuanza kutolewa kabla au ifikapo tarehe 30 Novemba, 2024, ahsante.