Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Boniphace Nyangindu Butondo (1 total)

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Sote tunatambua jitihada kubwa inayofanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa katika eneo la kuhakikisha kwamba miundombinu hasa ya barabara inaimarishwa mijini na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi hiki tumekuwa na wakati mgumu wa mvua hasa katika baadhi ya mikoa, mfano Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Pwani Kaskazini, hali ambayo imekuwa ikisababisha kwa hali ya juu sana uharibifu wa miundombinu hii ambayo tumeijenga na kutumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka na wa dharura wa kibajeti ilimradi kuhakikisha kwamba tunanusuru hali ya mawasiliano kwa maana ya barabara ambayo sasa imekuwa ni mbaya sana; katika maeneo ya vijijini na mjini, ili wananchi waendelee kutoa huduma na kusafirisha na kusafiri kama ilivyokuwa kawaida na kama ilivyo azma ya Serikali ya CCM? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa maelezo yake, anataka kujua mpango wa Serikali wa kibajeti wa kuwezesha kurudisha miundombinu iliyoharibiwa kutokana na mvua nyingi. Kwanza nikiri kwamba mvua ni nyingi na mvua inaendelea kunyesha kote nchini. Tumeendelea kushuhudia maafa mbalimbali ikiwemo na miundombinu zetu barabara, madaraja na makalavati yanabomoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu kwa barabara pia hata maisha ya watu. Kuna maeneo imesababisha mafuriko; nyumba, mali mbalimbali zimepotea, hata maisha ya Watanzania wengine hawapo, wametutangulia mbele ya haki kutokana na kusombwa na maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niungane na Waheshimiwa Wabunge kuwapa pole wale wote waliofikwa na maafa hayo. Wale ambao wametutangulia mbele za haki, Mwenyezi Mungu aweke roho zao mahali pema Peponi, Amina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali umeelezwa vizuri sana hapa. Kulikuwa na maswali kadhaa kwa Waziri wa Ujenzi ambaye aliulizwa swali la namna Serikali inavyoweza kukabiliana na jambo hili. Mtakumbuka pia Waheshimiwa Wabunge kwamba hata Mheshimiwa Spika alitoa nafasi nyingi kwa Wabunge kuuliza kwenye eneo hili na kuitaka Serikali itoe maelezo ya nini Serikali tumekifanya mpaka sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, maafa hayo na kuharibika kwa miundombinu ya barabara na makalavati, tumezipa jukumu zile taasisi zetu mbili; TANROADS pamoja na TARURA inayosimamia barabara zilizoko wilayani na vijijini, kuhakikisha wakati wote wanafuatilia mwenendo wa mvua zinazoendelea kunyesha nchini na kama kuna eneo limeharibiwa, kulirudisha kwa haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila taasisi kupitia Wizara zake; TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi, kibajeti zimejiweka vizuri na hata Mheshimiwa Waziri alipokuja hapa Waheshimiwa Wabunge waliouliza swali hili, kila mmoja aliambiwa fedha iliyopelekwa kwenye eneo lake. Kwingine tumeleta shilingi milioni 500, shilingi milioni 300. Kwa hiyo, Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa, tunarudisha miundombuinu ili huduma za wananchi kwenye maeneo hayo ziendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua hatutarudisha kwa viwango vya awali, lakini muhimu ni kuwafanya watu waendelee kupita na kutumia miundombinu hiyo vizuri. Pia, tukiwa tunaendelea kuona mvua zinanyesha, nitoe tahadhari kwa Watanzania hasa walio kwenye maeneo hatarishi, kuondoka kwenye maeneo hayo hatarishi na kukaa kwenye maeneo ambayo yapo kwenye miinuko ili tuweze kupunguza maafa haya hasa pale ambapo maji yanazidi kiasi na kufika kwenye nyumba zilizo kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwahakikishia Watanzania kwamba Serikali tupo macho kupitia Taasisi zetu za TARURA na TANROADS pale ambako kuna uharibifu tunaanza na halmashauri yenyewe ambako TARURA ipo. Pia, kwenye TANROADS, Ofisi zipo kwenye mikoa, jukumu lao sasa ni kupita maeneo yote na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kila mvua zinaponyesha kuona kama je, miundombinu yote imebaki salama au kuna tatizo limejitokeza, na kuhakikisha kwamba tunarudisha huduma hiyo kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mpango wetu ndani ya Serikali, ahsante sana. (Makofi)