Primary Questions from Hon. Boniphace Nyangindu Butondo (19 total)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO Aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Kolandoto hadi Kishapu kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la na Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kolandoto hadi Kishapu inayojulikana kwa jina la Kolandoto – Mwangongo yenye urefu wa kilometa 53 ni sehemu ya barabara ya Kolandoto – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti – Oldeani B, yenye urefu wa kilometa 328 inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ili kuijenga kwa kiwango cha lami imekamilika. Kazi hii ilifanywa na Mhandisi Mshauri M/S. Intercontinental Consultants and Technocrats pvt Ltd ya India.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeanza maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami ambapo katika mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao, jumla ya hilingi milioni 2,500 (bilioni 2.5) zilitengwa. Aidha, wakati maandalizi ya kuanza ujenzi yakiendelea, Serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 443.31 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, ni kwa nini Mgodi wa Mwadui Williamson Diamond Limited umesimamisha shughuli za uzalishaji wa almasi kwa muda mrefu na ni lini mgodi huo utaanza uzalishaji tena?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa Mwadui unaomilikiwa na Kampuni ya Williamson Diamond Limited ulisimamisha shughuli za uzalishaji mwezi Aprili, 2020 na hii ni kutokana na kushindwa kumudu gharama za uzalishaji kufuatia anguko la bei ya madini ya almasi katika masoko ya dunia. Anguko la bei ya almasi katika soko la dunia lilisababishwa na athari za ugonjwa wa COVID-19 mwishoni mwa mwaka 2019. Athari ya kuanguka kwa bei hii ya almasi kulisababisha bei ya wastani ya almasi katika mauzo ya mgodi huo kwa mwezi Machi, 2020 kuanguka hadi kufikia Dola za Kimarekani 131.13 kwa karati, bei ambayo kimsingi haikidhi gharama za uzalishaji wa mgodi huo. Kwa mujibu wa makadirio ya mgodi huo wastani wa bei unapaswa kuwa angalau Dola za Kimarekani 208 kwa karati ili mgodi uweze kukidhi gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi huo utaanza tena uzalishaji baada ya maombi yao ya overdraft funds kukubalika na benki za hapa nchini. Hii ni kwa ajili ya kugharamia shughuli zao za uzalishaji angalau kwa kipindi cha miezi mitatu hadi kufikia awamu nyingine ya mauzo ya almasi. Hali ya bei ya almasi kwenye soko la dunia kwa sasa inatarajiwa kuwa bora zaidi ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2020.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Mwanholo na Nyenze dhidi ya Mwekezaji na Mchimbaji Madini Eli Hilal Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nyangindu Boniphace Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mgogoro wa mipaka kati ya Vijiji vya Mwanholo na Nyenze dhidi ya Mwekezaji na Mchimbaji wa Madini aitwaye Eli Hilal Wilayani Kishapu unaohusisha eneo lenye ukubwa wa hekta 2,872.4. Eneo hilo awali lililkuwa linamilikiwa na Mgodi wa Wiliamson Diamond Limited, kabla ya kugawiwa kwa Mchimbaji Eli Hilal ambaye alimilikishwa na Serikali. Baadhi ya wanakijiji wa Mwanholo na Nyenze hawaitambui mipaka ya eneo la mwekezaji wa uchimbaji wa madini na wengine wanalalamikia maeneo yao kutwaliwa na mwekezaji wa uchimbaji bila kulipa fidia.
Mheshimiwa Spika, mwezi Februari, 2021, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga iliunda Timu ya Wataalam kwa ajili kufanya uchunguzi wa mgogoro huo. Timu iliyoundwa imewasilisha taarifa yake na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga inaendelea kuifanyia kazi taarifa iliyowasilishwa ili kubaini masuala yanayoweza kushughulikiwa na Mkoa na yale yanayohitaji uamuzi wa ngazi za juu. Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga itashirikiana na wananchi na wadau wote muhimu katika kutatua mgogoro huu na kuhakikisha haki inatendeka.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro uliopo mpakani mwa Wilaya ya Kishapu Kata ya Mwamalasa Kijiji cha Magalata na Wilaya ya Iramba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa, upo mgogoro wa mipaka kati ya Wilaya ya Kishapu na Wilaya ya Iramba. Mgogoro huo upo katika eneo la Bonde la Mto Manonga katika Kijiji cha Magalata Wilaya ya Kishapu na Kijiji cha Mwasangata Wilaya ya Iramba.
Mheshimiwa Spika, Mgogoro huu unatokana na malisho ya mifugo na maji, ambapo kwa upande wa Wilaya ya Kishapu jamii ya wafugaji wanaoishi kijiji cha Magalata hutumia bonde la Mto Manonga kwa ajili ya malisho na maji na upande wa Wilaya ya Iramba jamii ya wafugaji wanaoishi kijiji cha Masangata hutumia pia bonde la mto Manonga kwa ajili ya malisho na maji. Mgogoro huu mara nyingi hutokea wakati wa kiangazi ambapo jamii za pande zote mbili hutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo ambayo hupatikana kwa wingi katika Bonde hilo.
Mheshimiwa Spika, vikao mbalimbali vya usuluhishi vimefanyika vikihusisha viongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Uongozi wa Mikoa, Wilaya na Wananchi wa Vijiji vinavyohusika. Aidha, vikao hivyo vimesaidia kurejesha amani, utulivu na usalama kati ya vijiji hivyo hususan Magalata na Mwasangata.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na jitihada za kuutatua mgogoro huu kwa njia shirikishi ili kudumisha amani na utulivu katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa utoaji wa mbegu bora za alizeti ili kuongeza uzalishaji wenye tija kwa Wakulima katika Wilaya ya Kishapu?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ni miongoni mwa Halmashauri zenye fursa ya uzalishaji wa zao la alizeti nchini. Kutokana na umuhimu wa nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatekeleza Kampeni ya Kitaifa yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti kwa kuimarisha utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, kutoa elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi yetu ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kutoka Shilingi bilioni 7.5 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 11.6 kwa mwaka 2021/2022 na bajeti ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kutoka Shilingi bilioni 5.42 kutoka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 10.8 kwa ajili ya utafiti na uzalishaji wa mbegu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mikakati hiyo upatikanaji wa mbegu bora za alizeti umeongezeka kutoka tani 587 mwaka 2021 hadi tani 2,124 mwezi Januari, 2022. Kati ya hizo ASA imesambaza tani 1,600 kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 3,500 kwa kilo, ambapo tani 48 za mbegu bora za alizeti zimesambazwa katika Mkoa wa Shinyanga na usambazaji wa mbegu unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na mahitaji. Aidha, katika msimu wa 2022/2023 Serikali inalenga kuzalisha na kusambaza tani 5,000 za mbegu bora za alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako tukufu, naomba kutoa wito kwa viongozi katika Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kuwa mbegu zinazosambazwa kwa wakulima zinatumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, ni lini barabara ya Kolandoto - Mhunze hadi Mwangongo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilishakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kolandoto – Mhunze hadi Mwangongo (kilometa 53) kwa lengo la kuijenga kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Zabuni kwa ajili ya kazi hiyo zitatangazwa mwezi Novemba, 2022. Ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawatafutia wakulima wa Kishapu Masoko ya Mazao ya Mtama na Uwele?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya zao la mtama na uwele kwa ajili ya matumizi ya viwanda vya ndani ya nje ya nchi. Kutokana na ongezeko la mahitaji hayo, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha wakulima wa mazao hayo wanapata masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuzalisha mbegu bora zinazokidhi mahitaji ya soko, kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wa ndani kama TBL ambao wameanza kununua mazao hayo katika Mikoa ya Dodoma na Manyara na kufungua Vituo vya Mauzo katika Mji wa Juba, Sudan Kusini na Lubumbashi Nchini Congo.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka maji ya Ziwa Victoria kwenye Kata 24 zilizopo katika Tarafa tatu Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha wananchi katika maeneo ya Mijini na Vijijini wanapata huduma ya uhakika ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/ 2023, kazi itaendelea kuhakikisha Kata 24 za Wilaya ya Kishapu zinapata huduma ya maji safi na salama na kufikia lengo la asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, ni lini Mradi wa Umeme wa Nguvu ya Jua utaanza kutekelezwa katika Kata ya Talaga Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Jua katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilayani Kishapu unalenga kuzalisha umeme kwa kutumia jua kiasi cha megawati 150 kwa gharama za Euro milioni 115.30 ambayo itakuwa ni megawatIi 50 na Euro milioni 42 kwa awamu ya kwanza na megawati 100 kwa Euro milioni 62 kwa awamu ya pili. Fedha za awamu ya kwanza tayari zimepatikana, taratibu za kumpata Mkandarasi Mshauri na Mjenzi zipo katika hatua za mwisho. Fedha ya awamu ya pili inaendelea kutafutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo kwa ajili ya fidia kwa wananchi wa Kijiji cha Ngunga watakaoathirika na mradi, kiasi cha shilingi bilioni 1,825 kitaanza kulipwa mwishoni mwa mwezi Aprili, 2023 na Ujenzi wa Mradi huu (awamu ya kwanza) utatekelezwa kwa kipindi cha miezi kumi na nne (14) kuanzia mwezi Juni, 2023, baada ya kukamilisha taratibu za manunuzi ya wakandarasi na malipo ya fidia.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila Kata inakuwa na Mahakama hasa maeneo ya Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma na dhamira ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi, hususan kwa kujenga na kukarabati majengo ya Mahakama. Katika kutekeleza azma hii, tunao mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, katika ngazi zote, kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama za Rufani.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mahakama za mwanzo, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa walau kila Tarafa inakuwa na Mahakama ya Mwanzo na baadaye tuweze kwenda hadi ngazi ya Kata kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, lini mabwawa ya mifugo yatachimbwa Kata za Lagama, Masanga Mwamalasa, Ngofila, Bunambiyu, Mwasubi na Somagedi – Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo katika Jimbo la Kishapu. Kazi ya ujenzi wa mabwawa hufanyika kwa hatua kuu tatu ambazo ni; kutafuta chanzo cha maji (water source), kufanya usanifu na kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa kutambua changamoto ya upatikanaji wa maji katika jimbo la Kishapu hususani katika kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge, naomba kutoa wito kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wataalam wa Wakala ya Huduma na Usafi wa Maji Vijijini (RUWASA), kuanza kazi ya kutafuta chanzo cha maji katika maeneo husika, kuandaa michoro (design) na mchanganuo wa gharama (BOQ) ili kuweza kupewa kipaumbele kwenye mpango na bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa wito kwa wafugaji na wadau wengine, kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya maji ya mifugo ili kusaidia kupunguza changamoto ya maji kwa ajili ya mifugo hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka umeme katika Kata za Lagana, Itilima na Bunambiyu Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mkandarasi M/S SUMA JKT anayetekeleza mradi wa REA III Round II katika Wilaya ya Kishapu ana jumla ya vijiji 51 katika mkataba wake, vikiwemo vijiji vya Kata za Lagana, Itilima na Bunambiyu Wilayani. Mkandarasi kwa sasa anaendelea na utekelezaji wa mradi ambapo ameshawasha umeme katika vijiji 13 kati ya 51 sawa na asilimia 25.5. Aidha, kati ya vijiji 13 vilivyowashwa, vijiji vitano ni vya Kata ya Itilima. Mkandarasi anaendelea na ujenzi katika vijiji 38 vilivyobakia vikiwemo vijiji vitano vya Kata ya Lagana, vijiji vitatu vya Kata ya Itilima na vijiji viwili vya Kata ya Bunambiyu ambavyo vinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2023.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, Serikali imemfungulia Mkandarasi Hati ya Muamana (LC) ili aweze kuhakikisha anaongeza kasi ya kufanya kazi na kuimaliza mwezi Desemba, 2023, nakushukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Wilaya ya Kishapu ni kituo cha Daraja B, na ujenzi wake umesimama ukiwa umefikia kwenye hatua ya umaliziaji. Tathmini kwa ajili ya kumalizia ujenzi imefanyika na kiasi cha shilingi 262,672,520 zinahitajika. Fedha hizo zimepangwa kutolewa kwenye mfuko wa tuzo na tozo katika mwaka wa fedha 2023/2024. Fedha zitakapotolewa ujenzi huo utakamilishwa, ili wananchi wa Kishapu waanze kunufaika na huduma za Polisi kupitia kituo hicho. Nakushukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu katika baadhi ya Kata Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imepanga kufikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Busangwa, Itilima, Masanga, Mwakiponya, Mwamalasa, Shagihilu na Talaga ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 ili kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu katika kata hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kata hizo zimejumuishwa katika zabuni inayotarajiwa kutangazwa kabla ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 kukamilika kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa wodi za wagonjwa, nyumba za Madaktari, maabara na mortuary katika Vituo vya Afya vya Mwanhalanga na Negezi utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilipeleka shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wazazi lenye huduma za upasuaji wa dharura katika Kituo cha Afya Mwanhalanga na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo matano katika Kituo cha Afya Negezi, ambapo ujenzi umekamilika na majengo yanatumika.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhitaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo wodi za kulaza wagonjwa, nyumba za watumishi, maabara na majengo ya kuhifadhia maiti katika vituo vya afya Mwanhalanga na Negezi, katika Halmashauri ya Kishapu.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, lini Kituo cha Afya cha Nhobola kitafanyiwa ukarabati baada ya kuwa chakavu kwa kipindi kirefu ikiwa ni pamoja na upanuzi wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Nhobola ni miongoni mwa Vituo vya Afya 202 kongwe ambavyo vinahitaji ukarabati mkubwa ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, Serikali itavifanyia ukarabati vituo hivyo kwa awamu kikiwemo Kituo cha Afya Nhobola katika Halmashauri ya Kishapu, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Tarafa ya Negezi ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi kwani tarafa hiyo ina kituo kimoja tu cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Negezi ina kata nane ambapo kata mbili kati ya hizo zina vituo vya afya. Vituo hivyo ni Kituo cha Afya Negezi kilichopo Kata ya Negezi ambacho kilipokea shilingi milioni 500 mwaka 2021/2022 na Kituo cha Afya Nhobola kilichopo Kata ya Talaga ambacho ni cha muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya kwenye kata za kimkakati kote nchini zikiwemo kata zitakazokidhi vigezo katika Tarafa ya Negezi.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, lini Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana wenye thamani ya shilingi bilioni 6.6 utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana kwa mujibu wa mkataba umekamilika. Kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa bomba kuu kwa umbali wa kilometa 33.65, ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 100,000 katika Kijiji cha Lagana, Ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji katika Kijiji cha Lagana na ulazaji wa bomba la usambazaji maji umbali wa kilomita 7.86 katika Kijiji cha Lagana ikijumuisha matoleo ya maji (offtake) sita katika Vijiji vya Igaga, Isagala, Mwamashele, Busongo/Mwamanota, Bubinza na Mwamadulu. Katika Vijiji vya Mwamashele na Mwamadulu, Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana unatoa huduma kwa wananchi wapatao 3,040 wa Kijiji cha Lagana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, lini fedha za kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Mji wa Mhunze Wilayani Kishapu kwa kiwango cha lami zitatolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuzifanyia usanifu barabara zote kuu na muhimu za Mji wa Mhunze kutoka tabaka la udongo na changarawe kwenda tabaka la lami ambapo kilometa mbili za Barabara za DED - DC kilometa moja na Madukani kilometa moja zimejengwa kwa tabaka la lami kwa gharama ya shilingi bilioni 1.07. Aidha, katika mwaka 2024/2025, Serikali imetenga bajeti ya shilingi milioni 680 kwa ajili ya ujenzi wa tabaka la lami kilometa moja Barabara ya Madukani.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka mpaka kukamilisha barabara muhimu za Mji wa Mhunze Wilayani Kishapu kwa kiwango cha lami.