Supplementary Questions from Hon. Boniphace Nyangindu Butondo (62 total)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweka maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napongeza kwa majibu mazuri Serikali kwa namna ambavyo wameweza kutolea majibu katika swali hili lakini barabara hii ya Kolandoto kwenda Mwangongo - Kishapu ikiwa na kilometa 53 imekuwepo katika mpango wa utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2015/2020 lakini barabara hii haikuweza kutekelezwa katika kipindi hicho.
Swali, je, Serikali haioni umuhimu sasa pamoja na Ilani kuainisha kuwa barabara hii sasa itakwenda kutekelezwa katika mpango wa miaka mitano kwa maana ya 2020/2025 imeweka umuhimu wa kuhakikisha kwamba barabara hii sasa inatekelezwa tofauti na kipindi cha miaka mitano ambacho haikuweza kutekelezwa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; barabara hii ni barabara ambayo ni trunk road ambayo kimsingi uchumi wake na uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Kishapu unaitegemea sana na hasa katika kusafirisha mazao kama pamba, mtama na mazo mengine, lakini barabara hii ni barabara ambayo itaenda kuunganisha takribani mikoa mitatu mpaka minne; Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Singida, hadi Mkoa wa Arusha ambako itapita Sibiti na Oldeani huko Arusha.
Naiomba Serikali itoe tamko na kuipa umuhimu barabara hii ili mradi iweze kuchochea na kuharakisha maendeleo katika mikoa hii. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Butondo, lakini pia Wabunge wote ambao barabara hii inawahusu. Barabara hii ya Kolandoto – Mwingogo hadi Oldeani B ni kweli ni trunk road, kwa hiyo, Serikali inatambua umuhimu wake na ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha kwamba barabara zote ambazo ni trunk roads zinakuwepo kwa kiwango cha lami. Katika jibu langu la msingi ambalo ni la utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2015/2020 barabara hii iko kwenye mpango na tumesema maandalizi yanaendelea. Kwa hiyo, naamini kabla ya mwezi Juni tutakuwa tumeshaanza utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye Ilani ya mwaka 2020/2025 na kwenye mipango yetu naamini barabara hiyo bado itapata fedha kwa ajili ya kwenda kutekelezwa ili kuweza kurahisisha usafiri na usafirishaji kati ya mikoa hiyo ya Shinyanga, Simiyu, Singida na Arusha. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kishapu na wananchi wa Kishapu kwa ujumla wameweza kujenga health centers tatu; Health Center za Dulisi, Mwigumbi na Mwang’halanga. Hata hivyo, health centers hizi zina upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba lakini pia lipo tatizo la upungufu mkubwa wa wafanyakazi (watumishi). Je, Serikali inasema nini kuhusiana na suala zima la kutatua tatizo hili katika Wilaya ya Kishapu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza wananchi wa Jimbo la Kishapu kwa kuchangia nguvu zao katika ujenzi wa vituo vya afya vitatu, lakini kwa kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinaanza kutoa huduma ili kuweza kuboresha huduma za afya katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kujibu katika swali la msingi, lakini katika maswali ya nyongeza yaliyofuata ni kwamba hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu imeendelea kuimarika. Hata hivyo, tunafahamu bado kuna changamoto katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika kata hizi ambazo zipo katika Jimbo la Kishapu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la muhimu ambalo Serikali inaendelea kulitekeleza; moja, ni kuhakikisha tunaendelea kupeleka dawa katika vituo hivyo kutoka Bohari Kuu ya Dawa kwa wakati na kuendelea kuboresha bajeti ya dawa katika vituo hivyo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na fedha zinazotoka Serikali Kuu. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Boniphace Butondo kwamba tutaendelea kushirikiana kwa karibu sana kuhakikisha vituo hivi vinapata dawa na vitendanishi vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba baada ya ujenzi wa vituo vingi vya afya, automatically tunakuwa na upungufu wa watumishi. Hiyo ni hatua moja. Serikali imeanza na hatua ya ujenzi wa Vituo vya Afya, nasi sote ni mashahidi, tumejenga vituo vingi kwa wakati mmoja, lakini tunaendelea na hatua ya pili ya kuajiri watumishi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuomba kibali cha ajira na kadri watumishi watakavyopatikana, tutahakikisha tunawapeleka katika Vituo hivi vya Afya katika Jimbo la Kishapu na pia katika majimbo mengine kote nchini. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mji wa Munze katika Wilaya ya Kishapu ni mji ambao umepata maji ya Ziwa Viktoria. Kumekuwepo na tatizo kubwa sana la maji kukatika katika Mji wetu wa Kishapu, wa Munze. Je, ni tatizo gani linalosababisha maji haya kukatika huku tukitambua kwamba maji ya Ziwa Viktoria yamekuwepo kwa wingi sana na halipo tatizo la maji, lakini changamoto kubwa ni kukatika kwa haya maji? Naomba majibu.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Kishapu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna mradi ambao tumepeleka maji ya Ziwa Viktoria katika Jimbo lake la Kishapu. Kukatika kwa haya maji changamoto kubwa ilikuwa ni deni la umeme. Sisi kama Wizara ya Maji tumeshatoa milioni 600 kuwapa wenzetu wa KASHWASA kuhakikisha wanalipa deni lile TANESCO ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana kwa majibu ya Serikali yaliyotolewa na Naibu Waziri. Kwanza nipongeze kwa jitihada hizi ambazo zinaendelea, lakini bado lipo tatizo kubwa la hizi benki ambazo Mgodi wa Mwadui umekwenda kwa ajili ya kuomba mkopo huu ilimradi uanze uzalishaji kwa mara nyingine. Jambo kubwa linalohitajika hapa ni hii corporate guarantee ambayo inatakiwa itolewe na Petra ambaye ndiye kimsingi mwekezaji wa Mgodi huo wa Mwadui, lakini jambo ambalo nadhani ni zuri zaidi kwa Serikali ni kuhakikisha inazungumza ama inakaa kwa karibu na Petra, ilimradi suala hili la corporate guarantee liweze kutolewa na Petra na badaye utaratibu wa kutolewa fedha na ili mgodi uweze kuzalisha ufanyike haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia…
NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali, liko tatizo kubwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Serikali yenyewe, lakini pia na suala zima la Service Levy pamoja na CSR ambayo imekuwa ni msaada mkubwa kwa shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Kishapu. Ni lini sasa Serikali itakwenda kusimamia na kushirikiana na hawa ma-banker ilimradi benki hizi ziweze kutoa fedha na kuweza kuzalisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa swali la pili nenda moja kwa moja kwenye swali.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, wako watumishi zaidi ya 1,200 pale katika Mgodi wa Mwadui na changamoto kubwa ya hawa watumishi ni mishahara yao kusimama kwa muda mrefu. Sasa ipo sababu ya Serikali kuona umuhimu wa mgodi huu kuhakikisha unaanza uzalishaji, ili adha na matatizo makubwa ya watumishi hawa waliopo katika Mgodi wa Mwadui waondokane na adha hii kubwa. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mbunge pia kwa kutambua kwamba, Wizara inafanya kila linalowezekana kuona kwamba, mgodi huu unarejea katika hali ya uzalishaji. Kwa swali lake la kwanza, lakini pia ni kweli kwamba, natambua Wizara itafanya kila linalowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza uzalishaji wa almasi Tanzania tunaongea habari ya Mgodi wa WDL ndio kiini kikubwa cha uzalishaji wetu wa almasi. Pia, tunatambua adha ambayo watumishi wanapata kwa kushindwa kulipwa mishahara, lakini pia tunatambua kwamba, kama uzalishaji hautafanyika kwa muda mrefu maana yake ni kwamba, hata shimo lile tunapochimba litaanza ku-cave in na kwa hiyo, gharama ya kuja kuanzisha mgodi mara nyingine itakuwa ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Madini itafanya kila linalowezekana, iwe ni kuongea na watoa huduma, iwe ni kuendelea kufanya ushawishi wake kwa ajili ya benki za hapa nchini na hata kuongea na Petra, ili ikiwezekana basi turejee katika uzalishaji. Mara tutakapoanza uzalishaji maana yake ni kwamba, matatizo yote aliyoyaainisha Mbunge ya adha ya watumishi kutolipwa pamoja na service levy vyote vitakuwa vinapatiwa suluhisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara itafanya kila njia inayowezekana; yaweza kuwa ni ushawishi kwa benki zetu, hilo moja, au kukaa na watoa huduma ili kwamba, wakubali kufanya hata kwa kukopwa ili baadaye tuzalishe halafu tuuze. Njia zozote ambazo zinaweza zikarejesha uzalishaji katika Mgodi wa WDL tutazi-pursue ili kwamba, tuweze kurejesha hali ya uzalishaji katika Mgodi wetu wa Almasi Tanzania. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika majibu haya, inaonesha kwamba maelekezo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa yametolewa tangu mwezi Februari, lakini unaweza ukaona ni miezi takribani minne lakini hakuna hatua ya majibu ama ya utekelezaji juu ya suala hili la mgogoro.
Je, Serikali ipo tayari kuhakikisha kwamba inaweka msukumo wa haraka ili mradi utatuzi huu uweze kufanyika haraka na wananchi waendelee na majukumu yao kama kawaida? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuambatana na mimi ili kwa pamoja tuweze kwenda kuona maeneo ya mipaka na kuona njia bora ya kuweza kutatua tatizo hili kwa haraka? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Butondo kwamba mwezi Februari ni kipindi ambacho Kamati Maalum ya Wataalam ilipoundwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kufanya tathmini na kuangalia chanzo na pia kupendekeza njia muafaka za kwenda kutatua changamoto ya mgogoro kati ya vijiji hivi viwili na mwekezaji. Walipewa miezi mitatu, wameshakamilisha mwezi Mei mwaka huu, 2021, kwa hiyo, hivi sasa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ipo katika hatua za kufanya tathmini na kutoa maelekezo ambayo yatakuwa yanaleta tija katika mgogoro huu. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba Serikali imelichukulia kwa uzito sana suala hili na inalipeleka kwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali kwa maana Ofisi ya Rais, TAMISEMI na mimi nipo tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge mpaka kule Jimboni Kishapu ili tuweze kuona maeneo hayo na pia kwa kushirikiana na uongozi uliopo tuweze kupata suluhu ya mgogoro huo. Nakushukuru sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, kumekuwepo na tatizo kubwa la kukatika sana kwa maji katika Mji wa Munze, Kishapu, Kata ya Mwadui Lohumbo, na Maganzo. Lakini Mheshimiwa Waziri aliwahi kujibu kwamba tatizo kubwa ni malipo ya madeni ya muda mrefu ya wateja, lakini wateja wamelipia madeni yao kwa wakati. na hili nimefuatilia mwenyewe nimeona kwamba kweli hawadaiwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufika katika Jimbo la Kishapu kujionea na kutoa utatuzi wa kudumu juu ya tatizo la kukatika kwa maji katika Mji wa Munze na maeneo mengine?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kaka yangu, Mbunge wa Kishapu; kwa kweli unafanya kazi kubwa na nzuri sana katika jimbo lako.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke wazi kabisa maeneo ambapo Serikali imewekeza miradi mikubwa kwa
ajili ya wananchi waweze kupata huduma ya maji, na wananchi wanalipia bili za maji ili kuhakikisha kwamba mamlaka inajiendesha, maeneo ambayo wananchi wanalipia bili zile za maji lakini wakurugenzi ama watendaji ambao wanashindwa kuendesha mamlaka hizo, hakuna neno lingine zaidi ya kutupisha. Tutaweka watu ambao wataweza kutuendesha ili mamlaka zetu ziweze kwenda na Watanzania waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na ahadi za viongozi wetu Wakuu wa Serikali na ahadi hizi zimekuwa zikitolewa tangu Awamu ya Nne, Awamu ya Tano na sasa Awamu ya Sita na ahadi hizo zimekuwa hazipo katika mkakati mzuri wa kuziratibu na pengine kuweka bajeti kwa ajili ya kuzitekeleza: Nini mpango mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba sasa ahadi zile zote zinaratibiwa nchi nzima na kuwekewa mkakati wa kibajeti ili mradi ahadi hizi ziwe ni ahadi zinazotekelezeka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Boniphace Butondo kwamba ahadi zote zinazotolewa na viongozi wa kitaifa zimeratibiwa na kwa kweli tunazifahamu na ndiyo maana tunakuwa tunazitambua kwamba zinatakiwa zitekelezwe. Zikishatolewa ahadi zinakuwa ni kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba kinachogomba hapa wakati fulani huwa ni bajeti kwamba unapanga, lakini hutegemea na bajeti ya Serikali. Kwa hiyo, ahadi zote ambazo zimetolewa zikiwepo na ahadi ambazo zimetolewa katika Jimbo lake, tunazifahamu na tumeziratibu na nyingine tumezipangia bajeti.
Kwa hiyo, ndiyo maana tunasema kulingana na upatikanaji wa fedha zikipatikana, miradi yote ambayo Waheshimiwa Viongozi wetu wa Kitaifa wamezitoa tutaitekeleza. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Kishapu na wadau wa maendeleo katika Wilaya ya Kishapu wameanzisha jengo kwa maana ya Ofisi ya OCD ya Wilaya ya Kishapu na jumla ya shilingi milioni 60 zimetumika na jengo hilo lipo hatua ya renter. Sasa je, Seikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba ina-suport nguvu za wananchi na wadau ili mradi huduma za kipolisi ziweze kwenda sawasawa katika Wilaya ya Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniface nalo naomba nilijibu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana kwa kuwa ni moja ya miongoni mwa watu ambao wanahamasisha sana wananchi ili kuweza kuanza ile miradi halafu Serikali kwa kupitia wafadhili tuje tuone namna ambavyo tunaweza tukamalizia. Kikubwa nimwambie kwanza, tutajitahidi baada ya Bunge hili tuje tuone hatua hiyo ambayo imefikia hicho kituo ili sasa tuone na sisi tathmini ya kuweza kujenga.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumwambie kwamba sasa tunakwenda kutafuta fedha, popote zilipo ili tuhakikishe kwamba kituo hiki tunakimaliza na wananchi waweze kupata hizo huduma katika maeneo hayo. Nakushukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, mimi naomba nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza siyo peke yake mgogoro huu umekuwepo nyakati za kiangazi mgogoro huu umekuwepo nyakati zote masika na kiangazi na sasa hivi tunapozungumza habari za shughuli za kilimo maana yake zinapoenda kutekelezwa na wananchi wa maeneo haya kipindi hiki pia mgogoro huu unaweza ukaibuka. Kwa hiyo siyo sahihi kwamba ni nyakati za kiangazi peke yake na hata masika kwa sababu shughuli za kibinadamu zinafanyika nyakati zote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mgogoro huu umekuwa ukichangia sehemu kubwa sana uvunjifu wa amani wa wananchi wetu nataka nipate commitment ya kutosha ya Serikali kwamba ni lini sasa watakwenda kutatua mgogoro huu ikiwa ni pamoja na kuijumlisha Wizara ya Ardhi kuhakikisha wanaenda kuainisha na kuweka beacon ili mipaka ya maeneo ya kiutawala yaweze kuainishwa sawasawa. (Makofi)
Swali la pili Wizara ya Ardhi mwaka 2019 walifika katika eneo hili la mgogoro na kwa bahati mbaya kwa sababu walifika nyakati za masika maji yalikuwa yametapakaa katika maeneo hayo ya mipaka na kwa hali hiyo walishindwa kufanya suala zima la kuainisha lakini pia na kuweka beacon na waliahidi wangeweza kutekeleza na kuumaliza mgogoro huu uliokuwepo katika maeneo haya ya Iramba na Kishapu.
Je, ni lini Wizara ya Ardhi watafika na kuhakikisha wanaweka beacon kuainisha maeneo ya kiutawala lakini na kuweka beacon ili mgogoro huu sasa usiendelee na wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI naomba nichangie kidogo nyongeza ya swali hili, nafikiri nilikutana na huyu Mheshimiwa Mbunge nalijua hili tatizo lakini mimi sijawahi kushiriki vizuri, lakini niliwaahidi kwamba tungeweza tukakutana na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI tukazungumza kwanza kiutawala kati ya Wakuu wa Mikoa hawa wawili lakini mimi Wizara yangu kazi ya kutafsiri mipaka ndiyo kazi yake kwa GN zilizoandikwa.
Mheshimiwa Spika, hivyo nataka kumuahidi Mheshimiwa Mbunge nitalisimamia mwenyewe hilo la kuweka mipaka ili wananchi wa Wilaya hizi waweze kujua mipaka yao iliyoainishwa na mwenye mamlaka kwa sababu mamlaka ya kugawa mipaka ya utawala ni ya Mheshimiwa Rais, sasa wakati mwingine huwa inatokea wananchi wanasema nilikuwa hapa nilikuwa hapa nawakumbusha tu mwenye mamlaka ya kugawa mipaka ya utawala ni Mheshimiwa Rais na mipaka hii huwa inaandikwa kwenye Kanuni zinaitwa GN na GN tunazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mbunge wananchi waambie Wizara yangu itakuja kutafsiri ardhini mipaka iliyoainishwa kama nia ya Mheshimiwa Rais ya kupanga na kuunda hizo Wilaya mipaka ya ardhini itakuja kuainishwa na kutafsiriwa na Wizara yangu na jambo hili litafanyika mara moja. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kilimo cha zao la pamba msimu wake ni kipindi hiki na wakulima katika Wilaya ya Kishapu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla wameshaanza kulima. Lakini Wizara ninaishukuru kwa sababu wamesaidia usambazaji wa mbegu japokuwa siyo kwa wakati. Je, ni aina gani ya mbegu inayotumika sasa hivi katika msimu huu, kwa ajili ya kilimo cha pamba, kwa maana msimu uliopita mbegu tuliyokuwa tunalima haikuwa na tija kwa maana ya uzalishaji wa kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia haikuwa himilivu kwa magonjwa mbalimbali. Kwa hiyo, ninataka nipate majibu Wizara inasema ni aina gani ya mbegu ambayo sasa, ni mbegu rasmi na ndio mbegu inayotumika katika kilimo cha msimu wa mwaka 2021/2022? Pia, ni nini mpango wa kuhakikisha kwamba viuatilifu vinasambazwa kwa wakati? Kwa sababu, kumekuwepo wa ucheleweshwaji wa viuatilifu ili mradi kupambana na aina mbalimbali ya magonjwa katika zao la pamba. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza aina ya mbegu tunayopeleka ni UK08 ambayo tumekuwa nayo kwa kipindi cha kama miaka mitatu, miaka minne sasa hivi. Changamoto iliyojitokeza mwaka jana tumeitatua kwa kuhakikisha kwamba, mbegu tunazozisambaza safari hii zimeshakuwa treated na wakati zinaenda kupandwa tayari mbegu zile zina dawa. Tatizo lililojitokeza mwaka jana ni tatizo ambalo halihusiani sana na mbegu ni tatizo ambalo lilitokana na mambo makubwa mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, mbegu zilizoenda zilikuwa hazina dawa ya kupandia ambalo tumelitatua mwaka huu. Jambo la pili ambalo lilijitokeza mwaka jana kule kwenye ukanda wa pamba kuna wale machinga, mbegu ambazo sisi tulizihakikisha zinaenda shambani zikalimwe ziliuzwa na wajanja halafu wakulima waka-replace kwa mbegu yoyote anayoipata barabarani. Kwa hiyo, tumeamua kutengeneza utaratibu upya, tume-control mfumo wa usambazaji na mbegu tumeshaziwekea dawa za awali.
Meshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viuatilifu huu ndiyo mwaka wa kwanza tunaanza na open stock ya milioni 2.5. Kwa hiyo, wakulima watakapopanda tunawapelekea na dawa immediately ili wasiweze kupata matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa maelekezo kuhusu pamba. Tuliamua mwaka huu wakulima wanunue mbegu kwa kujinunulia lakini tumeiona changamoto. Nataka niwaambie wakulima wa pamba na wadau wa pamba, tunafanya jitihada kama Wizara kutafuta fedha ku-finance mbegu hizi ili zao la pamba tuweze kuwagawia wakulima dawa na mbegu bure kama tulivyofanya mwaka jana. (Makofi)
MHE.BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, Shirika la COASCO ambalo linashughulika na suala la ukaguzi wa Vyama vya Ushirika nchini limeonekana kuwa na upungufu wa staffs ambao kimsingi ndido wanaosimamia masuala haya ya ukaguzi. Sasa je, Serikali inasema nini kuhusiana na suala hili la kuimarisha COASCO ili suala zima la ukaguzi wa Vyama vya Ushirika ikiwemo vyama vya msingi liweze kufanyika ipasavyo?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Butondo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza tunakiri kumekuwepo na udhaifu kwenye COASCO. Hatua tuliyoamua kuchukua kama Wizara na mwelekeo wa Serikali kuanzia mwaka kesho COASCO bajeti yake ya kwenda kukagua Vyama vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika itabebwa moja kwa moja na Serikali na hawatoishi kwa kupewa fedha na Vyama vya Ushirika ambao wanakwenda kuwakagua.
Lakini la pili, sasa hivi tunafanya capacity analysis ili tuweze kufikia malengo ambayo tunatakiwa kuyafikia.
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba ule utaratibu wa COASCO kwenda kukagua Chama cha Msingi ama Chama Kikuu na kuhudumiwa na chama, utaratibu huo kuanzia mwaka ujao wa fedha unakufa, bajeti yote ya ukaguzi ambayo ni ya wastani wa bilioni nne itabebwa na Wizara, nao watafanya kazi kama ambavyo tunamtengea fedha CAG.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kutokana na suala la zao muhimu la alizeti katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo tani ambazo zimetajwa hapa tani 48 zilizosambazwa katika Mkoa wa Shinyanga na tani hizi za mbegu hazijaainishwa katika Wilaya ya Kishapu ni kiasi gani cha tani za mbegu ambazo zimesambazwa katika Wilaya ya Kishapu peke yake. Pengine katika maswali yangu ya nyongeza ni kwamba ASA ambaye ni Wakala aliyekuwa anashughulikia usambazaji wa mbegu katika Mkoa wa Shinyanga Wilaya ya Kishapu peke yake ni Wilaya ambayo ilibidi wakulima wapate huduma kutoka Kishapu kwenda Manispaa ya Mjini Shinyanga Makao Makuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, Serikali haioni haja ya kusogeza huduma hii ili ASA aweze kusambaza ama kutoa huduma katika Wilaya per se? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; lipo eneo katika Wilaya yetu ya Kishapu ambalo linamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ambayo ni zaidi ya ekari mia tatu. Je, Serikali ipo tayari kuja kuliona eneo hilo na ikiwezekana kuanzisha kilimo maalum cha zao la pamba kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu hizi za kisasa ili tuongeze tija na upatikanaji wa karibu zaidi kwa wananchi wa Kishapu kwa ajili la suala zima la mbegu za alizeti?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa eneo la ekari 300 Serikali tupo tayari kushirikiana na Halmashauri husika ili tuweze kuona ni namna gani hilo eneo linaweza kutumika na kwa maslahi ya wananchi wa Kishapu, hivyo, milango ya Wizara ya Kilimo iko wazi karibu wewe na Mkurugenzi wako tuweze kujadiliana ni namna gani tunaweza kulitumia hilo eneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kusogeza huduma za ASA katika Halmashauri ya Kishapu. Ninataka tu nimuombe Mheshimiwa Mbunge na niwaombe Wabunge wote, siyo rahisi kuweka ofisi ya ASA katika kila Wilaya kwa wakati mmoja, gharama za uendeshaji zitakuwa kubwa na hazina economic value. Kama Halmashauri husika ina mahitaji specific ya mbegu, tupo tayari watuletee mahitaji yao, tuya- aggregate pamoja na tuwapelee katika ngazi ya Halmashauri ama Mkoa halafu wao wenyewe waweze kusambaza katika maeneo yao na wakulima wao kama tulivyofanya katika Mkoa wa Singida na Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawa-encourage Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, mahitaji ya mbegu za alizeti za Halmashauri yake wayalete kimaandishi ili sisi tuwapelekee katika ofisi zao za Halmashauri badala ya kufungua ofisi katika eneo hilo linalohusika.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza.
Swali hili ni kuhusiana na habari ya shilingi bilioni moja ambayo imetengwa. Unaweza kuona ni kiasi kidogo sana cha fedha, nilitaka nipate majibu na wananchi wa Jimbo la Kishapu wapate majibu kwamba kiasi hiki cha fedha tafsiri yake ni nini kwa sababu bilioni moja ni kiasi kidogo sana ili na matumini wawe wananchi wa Kishapu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa ukubwa wa barabara hii, hii fedha ambayo imetengwa haiwezi kuikamilisha, lakini nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni utaratibu kwamba barabara hizi hazijengwi kwa siku moja wala kwa mwaka mmoja na ndiyo maana mpango ambao tunautumia kwa kujenga barabara ni ku-raise certificate. Kwa hiyo, wakishaanza kila watakapokuwa wamefika hatua nyingine wanaandika certificate, wanalipwa na ndiyo utaratibu ambayo tumekuwa nao katika ujenzi wa barabara zetu baada kazi ana-raise certificate na Serikali inalipa hizo fedha. Kwa hiyo, ni barabara kuu tunalijua hilo na ndiyo maana tayari tumeanza kuandaa taratibu za kutangaza hiyo barabara. Ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, barabara ya Kolandoto Munze Mwingunge yenye kilometa 63 imekuwepo kwenye mpango wa utekelezaji kwa maana ya ujenzi katika kiwango cha lami kwa mwaka 2021/2022. Mwaka 2021/2022 haikuweza kutekelezwa. Je, nini mpango wa Serikali kwa mwaka 2022/2023 kuhakikisha kwamba unatekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kolandoto hadi Lalago kama alivyotaja hizo kilometa 62 imepewa Bajeti kwa ajili ya kuanza kujenga kwa kiwango hiki; kwa hiyo tusubiri tutakapoanza utekelezaji wa bajeti. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; changamoto bado ni kubwa sana hususani soko la ndani kwa wakulima wa zao la mtama na uwele. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba yenyewe inashughulika kununua mazao haya kupitia NFRA ili mradi kupunguza tatizo la changamoto ya soko la ndani?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna tatizo kubwa la ndege aina ya kwelea kwelea ambao wamekuwa wakishambulia sana mazao haya ya mtama pamoja na uwele na Serikali yetu ina tatizo la kutokuwa na ndege ambayo ni maalum kwa ajili ya kushughulikia ndege hawa waharibifu wa mazao haya. Je, Serikali haioni haja ya kuhakikisha kwamba inanunua ndege yake ili mradi iweze kushughulika kwa karibu na ndege hawa waharibifu ambao wanashambulia mazao haya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyangindu Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, la kwanza, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa akiwapambania na kuwasemea wakulima wa mtama pamoja na uwele kutoka Mkoa wa Shinyanga.
Mheshimiwa Spika, kuhusu uhakika wa soko la ndani, maelekezo tayari NFRA wanayo ya kununua mazao hayo ikiwemo mtama pamoja na uwele. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba NFRA anaendelea na zoezi la kununua mtama hivyo wakulima wa Shinyanga ni sehemu ya wanufaika wa soko hili la ndani kupitia NFRA.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusiana na ndege. Katika bajeti yetu ya mwaka huu tumetenga Shilingi bilioni tatu ya kununua ndege mpya kwa ajili ya kunyunyizia wadudu kwenye sehemu ya kukuza kilimo anga. Ninavyozungumza hivi sasa tuko katika due diligence, tunazo kampuni tatu, mbili kutoka Marekani na moja kutoka Afrika ya Kusini ambako baadaye sasa tutafanya maamuzi ni wapi tununue ndege hiyo.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunayo ndege yetu pia ya survey ambayo iko Nairobi Kenya, imekamilishwa matengenezo yake na yenyewe pia itakuja kuungana kuimarisha kilimo anga ili kuondokana na changamoto hii ya wadudu waharibifu.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kishapu ina jumla ya kata 29 na ina vijiji 128 na Wilaya hii sasa haina gari hata moja, magari yote ni mabovu na kwa sasa hivi tumekuwa tukitumia gari moja ambayo tumeazimwa na Mgodi wa Williamson Diamond Limited.
Sasa Serikali inafanya jitihada gani za haraka kuhakikisha kwamba inapeleka angalau gari moja ya dharura kwa ajili ya kuokoa wananchi kupata huduma za msingi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Kishapu inayochangamoto ya magari kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, gari walilonalo ni chakavu, linahitaji matengenezo ya mara kwa mara. Nimpe matumaini Mheshimiwa Mbunge pale ambapo tutapata magari yanayotokana na bajeti hii tunayoitekeleza kipaumbele kitawekwa kule ambako hawana magari kabisa.
Kwa hiyo, kama Kishapu watakuwa hawana gari tutaelekeza IGP aipe Kishapu kipaumbele katika ugawaji wa magari hayo. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. barabara Kolandoto - Munze - Mwangungo yenye kilometa 63 ni barabara ambayo imo katika mpango wa Ilani ya Utekelezaji ya Chama cha Mapinduzi na pia ipo katika mpango wa bajeti ya 2021/2022: Ni lini utekelezaji wa mradi huu utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara Kolandoto - Mwangungo kwenda Lalago ni barabara ambayo iko kwenye ilani na imekuwa ikipangiwa bajeti. Barabara hii ni ndefu inayokwenda mpaka Sibiti - Mbulu, kwa maana ya Hyadom – Mbulu. Barabara hii imeanza kutekelezwa kwa vipande na kwa sasa tutaanza ujenzi wa kipande cha Mbulu – Hyadom kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Wilaya ya Kishapu ni moja kati ya wilaya ambazo zinatekeleza ujenzi wa miradi hii ya VETA; na mpaka sasa hivi mradi huu una zaidi ya miaka mitatu uko katika ujenzi, lakini bado kuna upungufu wa ukamilishaji wa umeme, furniture, maji, na baadhi ya miundombinu katika maeneo hayo. Ni zaidi ya Shilingi milioni 400 zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha mradi huu. Ni lini Serikali itakamilisha suala la kuleta fedha kwa ajili ya kukamlisha mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge wa Kishapu na Waheshimiwa Wabunge wengine ambao maeneo yao tayari tumeweza kujenga vile vyuo 25. Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mwaka huu tayari ameshatoa jumla ya Shilingi bilioni 10.3 kwa ajili ya kukamilisha maeneo yale katika vile vyuo vyote 25. Katika zile kazi ambazo bado hatujakamilisha, na tayari tumeshaanza kuzipeleka kwenye maeneo yale kwa lengo la kukamilisha kazi hizo. Kwa hiyo, muda mfupi ujao tutakuwa tumekamilisha. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni lini utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Kolandoto kwenda Kishapu katika kiwango cha lami utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, barabara hii ipo kwenye mpango wa bajeti kwa ajili ya kuijenga mwaka huu na tutaendelea na mwaka ujao. (Makofi/Kicheko)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana Wilaya ya Kishapu ina vituo vya afya vitatu ambavyo vimekamilika na vimeanza kufanyakazi lakini kuna tatizo kubwa la upungufu wa watumishi katika vituo hivyo vya Dulisi, Mwangalanga pamoja na Mwigumbi.
Je, ni lini Serikali italeta watumishi wa kutosha pamoja na tatizo zima la vifaa tiba kushughulikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli vituo ambavyo amevitaja vina upungufu wa vifaa tiba lakini pia upungufu wa watumishi. Kama ambavyo nimejibu kwenye maswali mengine ya nyongeza na swali la msingi kwamba Serikali imeweka kipaumbele cha kuajiri watumishi na kuwapeleka kwenye vituo hivyo lakini pia kuhakikisha tunanunua vifaa tiba na kupeleka kwenye vituo hivyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Butondo kwamba Jimbo lake la Kishapu nalo litapewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mafupi na mazuri. Pia naipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo inashughulika na changamoto kubwa ya maji na wananchi wa Jimbo la Kishapu kwa ujumla. Tangu mwezi wa pili tarehe 11 mkataba baina ya Emirates Builders wenye thamani ya Shilingi bilioni 6.5 umesainiwa kwa ajili ya usambazaji wa maji ya Ziwa Victoria katika Kata nne; Kata ya Laghana, Mwamashare, Igaga, na Ngofila.
Swali: Je, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba inatoa ile 20% kama advance payment ili mradi huu uanze kutekelezwa kwa wakati kwa maana Mkandarasi mpaka sasa yuko site?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuambatana nami kwenda Jimboni kuona changamoto zilizoko katika Jimbo la Kishapu na kuhakikisha kwamba atasukuma kazi hii kwa haraka ili mradi maji yaanze kutoka katika Jimbo la Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Butondo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, advance payment tayari zimeanza kutolewa kwa Wakandarasi wote, naamini Emirates naye atakuwa katika list. Suala la kuambatana naye ni moja ya majukumu yangu, hakuna shaka. Nitafika kuhakikisha mradi unatekelezwa. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Wananchi wa Kishapu, Mfuko wa Jimbo wa Mbunge wa Jimbo la Kishapu, lakini pia na wadau wa maendeleo kama Mwadui na wengine wameweza kuchangia jumla ya Sh.53,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaunga mkono nguvu na jitihada za wananchi na wadau wa maendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza tumpongeze Mheshimiwa Butondo kwa kufuatilia kwa karibu masuala yanayohusu usalama wa raia na mali zao na uhamasishaji wa wadau kuchangia hizi fedha. Nimwahidi tu kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi tuna mpango mkakati wa kuimarisha ujenzi wa Vituo vya Polisi vya Mikoa na Wilaya ambazo hazina kabisa. Kwa hiyo hali ya fedha itakaporuhusu, Wilaya ya Kishapu ni moja ya maeneo yatakayopewa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. BONIPHANCE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Kishapu ni moja kati ya Wilaya ambazo zipo katika mkakati na mapambano ama kampeni za mabadiliko ya tabia nchi katika Kata ya Alagana pamoja na Kata ya Kiloleli, ipo miradi iliyotekelezwa hasa ya mabwawa ya mifugo ambayo kimsingi miradi hiyo imetekezwa chini ya kiwango.
Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kuambatana na mimi kwenda Jimboni kwangu kujenga miradi hiyo na kushauri namna bora amna namna gani ya kuweza kuirudia na kuitekeleza upya? (Makofi)
WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kumshukuru kaka yangu Mbunge wa Kishapu, nadhani swali lake lilikuwa linaendena na lile swali la kwanza la EBA, kwa sababu tuna Mradi wa EBA umetekelezwa katika halmashauri tano ikiwepo na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu sasa kwa vile swali hili lilikuwa linaenda katika upande ule wa Saasisha swali la Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, kiufupi niseme ni kwamba Mheshimiwa Mbunge nitaambatana na wewe tuende tukafanye kuangalia kama kuna mapungufu ya aina yoyote kuweza kuyafanyia kazi kama Serikali, ni jukumu letu kulifanya. Lakini binafsi naomba niwashukuru hawa Wabunge wa Kishapu, Wabunge wa Nzega, Wabunge wa Mkalama, Wabunge wa Mvomero na Mpwapwa katika mradi huo wameutendea haki sana kusimamia vizuri katika maeneo mbali mbali tumepata mafanikio makubwa. Kwa hiyo, Mbunge this is my commitment kwamba tutaenda pamoja kutembelea. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napongeza Serikali kwa majibu mazuri juu ya hatua ya mwendelezo wa Mradi huu muhimu wa uzalishaji wa umeme wa jua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni moja tu la nyongeza, kwamba ni kwa namna gani zana ya ushirikishwaji wa jamii inayohusika na hasa juu ya masuala ya fidia, imekuwa ikizingatiwa lakini pia suala zima la uongozi hasa wa ngazi za chini Serikali za Mitaa umekuwa ukihusishwa hili kuona kwamba michakato ya haki na tathmini iliyo halali kwa ajili ya malipo kwa wananchi inazingatiwa? Naomba kujibiwa.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Butondo kwa kulifuatilia jambo hili mara kwa mara, lakini namhakikishia kwamba kama anavyofahamu na anavyoona limefikia mwisho na mambo yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu la msingi nimesema malipo ya fidia yataanza kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, lakini taratibu zote zote za fidia zimepitiwa kama ambavyo zinaelekezwa na sheria. Kwa hiyo wale wataoathirika wote tayari wamebainishwa na wameshirikishwa katika mchakato huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo jambo zuri sana ambalo naomba kulisema kwa sababu ya uhitaji mkubwa wa umeme tuliokuwanao tumekubaliana na wenzetu wa TANESCO na Serikali imewaagiza watoe pesa zao kwanza kuanza kulipa fidia haraka kama mkopo, halafu badae Wizara ya Fedha itakapokuwa imelipwa watarudishiwa kwenye eneo lao. Kwa hiyo wiki hii ambayo tumeianza jana wananchi kule wataanza kulipwa fidia katika mazingira yao ili kuhakikisha kwamba mradi hii unakimbizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaelekeza wenzetu wa TANESCO watakapoenda kulipa fidia kupitia halmashauri, kupitia Serikali za Vijiji na Viongozi wetu wa Serikali waliokuwa nao washirikiane hili kuwabaini wale ambao ni waathirika halisi na waweze kupewa haki yao stahiki kwa mujibu wa sheria hili mradi uweze kutekelezwa bila tatizo lolote.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kituo cha Afya cha Negezi na Mwang’alanga ni moja kati ya vituo vya afya ambavyo vimeanza kufanya kazi katika kipindi hiki lakini bado vina mapungufu ya wodi za kawaida za wagonjwa, mapungufu ya mochwari na walk ways. Ni lini Serikali itakwenda kukamilisha vituo hivi vianze kufanya kazi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Negezi na hivyo vingine ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja ni miongoni mwa vituo ambavyo Serikali imeweka mpango wa kuhakikisha vinakamilishwa kwanza kabla ya kuanza vituo vingine vipya, ndiyo maana katika mwaka uliopita wa fedha na mwaka huu hatujajenga vituo vingi sana vya afya vipya kwa sababu lengo ni kukamilisha kwanza vituo ambavyo vimeanza kwa sehemu ili vitoe huduma kwa upana wake na baadae tuende kwenye vituo vingine.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ipo kwenye kipaumbele. Ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Barabara ya Kolandoto kwenda Kishapu - Mwangongo yenye kilometa 63 ni barabara ambayo sasa imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Kishapu; na barabara hii iko kwenye Mpango wa Bajeti 2022/2023; na iko kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi; ni lini sasa barabara hii itaanza kutekelezwa rasmi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nakubaliana naye, lakini hii barabara ni sehemu ya barabara ndefu ambayo tumeitengea bajeti na atakubaliana nami, kwa ajili ya kuanza maandalizi kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, tuna uhakika barabara hii kwa kuwa iko kwenye mpango na pia ni barabara kuu, Serikali itaijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Jimbo la Kishapu lina jumla ya kata 29, lina square kilometers 48,000; lina vijiji 117. Eneo hili kiutawala ni kubwa sana; ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba jimbo hili linagawanywa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA
URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatambua uwepo wa maeneo makubwa, kama alivyosema huku Kishapu kata 26 na vijiji 117. Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao, muda utakapofika tutaangalia vigezo na masharti ili kuona kama jimbo hili linafaa kugawanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa niaba ya Serikali niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge wote, kwenye eneo hili yapo majimbo mengi, kwa hiyo tutayafanyia kazi Waheshimiwa Wabunge. Karibu tuungane pamoja na wadau wengine wa Uchaguzi tutoe maoni na nina imani tutafanya vizuri tu, ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Wananchi wa Kata ya Busangwa, Kijiji cha Mwanima, wameshaandaa eneo la ekari 15 kwa ajili ya ujenzi wa health center na tayari wameshaanza ufyatuaji: Nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wana-support kwa ajili ya kukamilisha mradi huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunajenga vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati. Tayari kuna fedha ambayo imeshatengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivi vya afya kwenye maeneo kama anavyotaja Mheshimiwa Mbunge hapa. Kwa Busangwa, tutaangalia kama eneo hili pia limetengewa kwenye mwaka wa fedha huu ambao tunaenda kuuanza.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninapongeza kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunda hii Tume ya Hakijinai lakini moja kati ya mambo ya msingi ambayo Hakijinai itakwenda kuyafuatilia na kuyaona ni kuhakikisha kwamba huduma za kimahakama kwa maana ya huduma za kisheria kwa wananchi zinasogezwa.
Swali la kwanza, Kata ya Mwakipoya, Masanga, Lagana, Bunambiyu na Mwasuge ni Kata ambazo ziko pembezoni na ziko mbali na maeneo ya huduma ya kisheria. Sasa ni nini mpango wa Serikali walau wa kusogeza huduma hizi kujenga katika Kata hizi muhimu hizi Nne? (Makofi)
Swali la pili, huduma hizi za kisheria ni za muhimu sana na Halmashauri ama Wilaya ya Kishapu haina Mahakama ya Wilaya. Ni lini Serikali inakwenda kujenga Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Kishapu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru kwa kunipa nafasi nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge amependa kufahamu mpango wa Serikali katika kujenga Mahakama katika kata ambazo amezitaja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Butondo kwamba tumeshaanza kama Serikali, na mwaka huu wa fedha tumetenga Shilingi bilioni 57 kwa ajili ya kujenga Mahakama 60 za mwanzo nchini. Kwa hiyo, kata zake alizozitaja Mhehsimiwa Butondo zitafikiwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake pili ametaka kufahamu kama tuna mpango wa kujenga Mahakama katika Wilaya ya Kishapu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia, katika mwaka huu wa fedha, bajeti hii ambayo tulileta katika Bunge hili, kati ya Mahakama 24 za Wilaya ambazo tunazijenga kwa zaidi ya shilingi bilioni 31 na Mahakama ya Kishapu ipo, kwa hiyo itajengwa. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Upo Mradi wa Mwabusiga katika Kata ya Kishapu wenye thamani ya shilingi milioni 314, mradi wa maji ya Ziwa Victoria. Mradi huu unatekelezwa chini ya mpango wa force account na uko katika Mfuko ule wa Maji na bahati mbaya kabisa fedha sasa hazijaja. Ziko taratibu za ununuzi wa mabomba na vifaa vingine ambavyo vinahitaji fedha. Sasa lini Serikali itakwenda kuleta fedha na ukizingatia mwaka wa fedha sasa tunakwenda kuumalizia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi huu suala la fedha kila mwezi tunakuwa na mgao. Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa naomba tuonane ili mgao unaofuata mwanzoni mwa mwezi Juni tuweze kuupatia fedha.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kituo cha Afya cha Nobola kilichopo katika Tarafa ya Negezi, kimejengwa miaka mingi miaka ya 1970 na kituo hiki kimechakaa sana: Nini mpango wa Serikali wa kukarabati kituo hiki ikiwa ni pamoja na kufanya upanuzi kwa ajili ya kituo hiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini ya vituo vyote vya afya, hospitali kongwe na kuweka mpango kazi wa ukarabati kila mwaka wa fedha. Ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha pia katika bajeti yetu tuna fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo hivi vikongwe. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaelekeza Halmashauri ya Kishapu kuleta taarifa ili timu iweze kufanya tathmini na kuona mahitaji ya ukarabati na upanuzi wa kituo hicho, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na tunakupongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo na tunatarajia kwamba wana Mvomero watapata huduma hiyo mara moja baada ya ushirikiano kutoka Serikali Kuu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, je, ni lini sasa mradi huu utaanza kupewa support na Serikali ili kuonesha jitihada za wananchi wa Mvomero walizozianzisha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nakumbuka mwezi Julai Mheshimiwa Naibu Waziri ulitembelea katika Jimbo la Kishapu na Wilaya ya Kishapu, ukaona jitihada za ujenzi wa Ofisi ya OCD pale Kishapu; na jumla ya shilingi milioni 275 zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo; na uliahidi utapeleka fedha hizo kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika;
Je, ni lini fedha hizi zitafika ili ukamilishaji wa mradi huo wa Ofisi ya OCD uweze kukamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusu hili la mradi wa ujenzi wa kituo kule Mvomero, ni ahadi yetu kwamba katika mwaka wa fedha 2024/2025 kituo hiki kimeingizwa kwenye mpango na fedha zinazopungua zaidi ya shilingi milioni 60 zitatolewa na Jeshi la Polisi ili mradi huo utekelezwe na kukamilika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Kishapu, kwanza nawapongeza wananchi waliojitolea pamoja na Halmashauri yao na Mheshimiwa Mbunge kujenga kituo bora kabisa, kinachohitaji ni umaliziaji. Tumeahidi, katika bajeti ya mwaka huu zimetengwa shilingi milioni 275 kwa ajili ya ukamilishaji huo.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge hili nimhimize IGP kuhakikisha kwamba anapeleka fedha hizi mapema iwezekanavyo ili ukamilishaji ule ufanyike na hatimaye huduma za kipolisi ngazi ya Wilaya ziweze kutolewa, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yaliyotolewa. Ninaomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo jitihada kubwa ambazo zilishafanywa huko nyuma na wananchi kupitia utaratibu wa Vijiji vya Ujamaa na nguvu za wananchi kuhakikisha kwamba wanachimba mabwawa katika kipindi cha nyuma. Hapa miaka ya 90 mpaka 2000, Serikali iliweza kuchiba baadhi ya mabwawa, lakini mabwawa yale ni kama yalitelekezwa na baadaye yakawa yameharibika. Kuna uhitaji ama umuhimu wa kuyafufua yale mabwawa ambayo yalichibwa nyakati hizo, kabla ya kuweka mkakati wa muda mrefu ule wa kujenga mabwawa haya.
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mabwawa yaliyopo katika maeneo hayo yanafufuliwa kwanza?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natumia nafasi hii kumpongeza sana Mbunge wa Kishapu, Mheshimiwa Boniphace Nyangindu, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufatilia namna ambavyo wafugaji wake wanatakiwa wawe na maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyouliza swali lake la msingi, ni kweli kwamba Serikali ipo na mipango mingi ya kufufua mabwawa yote yaliyokufa. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge hili tutatuma wataalam kuja kufanya tathmini katika jimbo lake. Tujue tathmini hiyo, mabwawa yako mangapi na yanahitaji nini ili Wizara kamaSerikali Wizara iweze kutuma namna ya kuyafufua haya mabwawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua mabwawa ambayo yanahitaji kufufuliwa na Serikali yapo maeneo mengi. Serikali tunamuahidi Mheshimiwa Mbunge Serikali imejipanga vizuri. Tukishapata kujua gharama za shilingi ngapi inatakiwa kwenda kuyafufua hayo mabwawa tupo tayari kwenda kuyafufua mabwawa hayo kwenye Jimbo la Kishapu. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Katika mikataba iliyosainiwa ya wakandarasi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya minara, nina minara tisa katika Wilaya ya Kishapu, lakini hadi sasa minara hiyo haijaanza kufanyiwa kazi; je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Butondo Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa, kwanza Mheshimiwa Butondo alikuwa na tatizo kubwa sana, akaleta na Serikali ikaipokea maombi yake na tukampelekea minara tisa9 kama ambavyo ametaja. Sasa kusaini mkataba ni jambo la kwanza. Jambo la pili, watoa huduma wanaenda ndani ya Jimbo la Mheshimiwa Butondo ili kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga hiyo minara. Wakishapata eneo wanakuja kutafuta vibali kwa mfano kibali cha mazingira (environmental impact assessment permit), kibali cha anga (aviation permit) vilevile wanatafuta kibali cha kutoka halmashauri kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo mlolongo wa vibali hivi, kila sehemu ukikuta kwamba wanatoa kwa uharaka basi mkandarasi ataweza kuanza ujenzi kwa haraka, lakini kukiwa na delay katika baadhi ya maeneo, ndipo inatokea kwamba tunasaini mkataba lakini miezi mitano unakuta kwamba mradi haujaanza.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeshaliona hilo, tunawaomba wote ambao wanahusika katika mnyororo mzima wa utoaji wa vibali, watoe kwa wakati ili kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati kwa sababu Watanzania wanahitaji huduma ya mawasiliano ili washiriki katika uchumi wa kidigitali. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na ukiukwaji wa kikanuni na hasa kuhusiana na suala zima la ziara ya Kamati za Kudumu za Madiwani na kwamba kila robo ya mwaka Kamati za Kudumu zinatakiwa kutembelea na kuona miradi iliyotekelezwa katika kipindi hicho, ili kuona kwamba fedha zinazotumwa na Serikali chini ya Mama Samia Suluhu Hassan zinasimamiwa na kuona ile value for money. Sasa Finance Committee peke yake imekuwa ikienda kwenye ziara hii kinyume na kanuni na Kamati nyingine za kudumu zisiende…
SPIKA: Swali lako.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nini tamko la Serikali kuhusiana na changamoto hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ziara za Kamati za Kudumu za Waheshimiwa Madiwani katika Baraza la Madiwani zimewekwa kwa mujibu wa mwongozo ambao umeelekeza Kamati ya Fedha kutembelea miradi, lakini pia Kamati za Kudumu nyingine kama Huduma za Elimu, Afya na Maji na nyingine kutembelea miradi pia kuona utekelezaji wa miradi ile.
Kwa hiyo, nitumie fursa hii pia kuwasisitiza Wakurugenzi na Mabaraza kuzingatia Mwongozo wa Serikali ambao umetolewa ili kuweza kuwa na ufatiliaji wa karibu wa thamani ya fedha katika miradi ambayo inatekelezwa, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wilaya ya Kishapu na Mkoa wa Shinyanga unajihusisha sana na kilimo cha zao la kimkakati la pamba, lakini zao hili katika msimu huu limeshuka sana bei, kutoka shilingi 2,200 hadi shilingi 1060. Wakati huo gharama kubwa za uendeshaji ama uzalishaji wa zao hili umekuwa ukiongezeka ikiwemo pembejeo na gharama zingine;
Je, ni nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inafanya kila jitihada kuona kwamba bei hii inapanda ili kumtia moyo na kumhamasisha mkulima ilimradi aweze kuondokana na gharama ya uendeshaji wa zao hili na hivyo kupata manufaa kutokana na zao hili la pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya bei ya mazao mengi hapa nchini inatokana na kwamba wakulima wetu wanatumia nguvu kubwa ya wanachokiingiza shambani na wanachokipata havilingani. Sisi kama Serikali tumekuja na mkakati ufuatao. Tunaamini kabisa mkulima wa Tanzania akilima kwa tija suala la bei halitakuwa changamoto kubwa sana. Kwa hiyo mkakati wetu wa kwanza kabisa wa kuanzia ni kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanalima kwa tija na hivyo tumefanya yafuatayo;
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza tunasaidia kuendelea kufanya utafiti kwa ajili ya kuwapatia mbegu bora, cha pili ni kuwasaidia pia katika teknolojia ambayo itamsaidia mkulima aweze kulima kwa tija, na cha tatu ni usambazaji wa pembejeo kwa wakati ili mkulima aweze kufikia malengo yake. Hii itatusaidia sana kwenye kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanalima kwa tija na hatimaye hata akienda sokoni bei ikiwa imeporomoka lakini atakuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kufidia changamoto ambayo anaipata katika uwekezaji alioufanya shambani.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri, lakini bado kasi ya utekelezaji wa miradi inakwenda taratibu sana. Swali la kwanza: Je, Mheshimiwa Waziri, uko tayari kuambatana nami ili twende jimboni ili tukasukume kwa pamoja utekelezaji wa miradi hii katika jimbo langu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kata ya Bunambiyu pamoja na Mwasubi ni maeneo ambayo zikinyesha mvua huwa hayapitiki ni maeneo ambayo yanapata maji kwa wingi sana. Sasa, mko tayari kuhakikisha kwamba mnaweka msukumo mkubwa ili maeneo hayo yapewe kipaumbele, wakati huo huo maeneo hayo niliyoyataja na yenyewe yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Boniphace, amekuwa akifuatilia sana haya maeneo na mradi ule mkubwa wa umeme wa kutumia solar ambao tumeufanikisha juzi kuusaini, na katika Jimbo lake, mkoa wote wa Shinyanga na nchi nzima itakuwa ni faraja kubwa.
Mheshimiwa Spika, namuahidi kwamba niko tayari kuambatana naye kwenda kuhakikisha tunaendelea kumsimamia mkandarasi huyu kama tulivyoahidi katika bajeti. Vile vile, mbinu za kufungua LC, kuongeza wasimamizi na kuwawezesha, zitatusaidia kuhakikisha kwamba ndani ya muda tunakamilisha kazi hii. Hilo jambo la maeneo ambayo yana changamoto, tutalichukua kwa ukubwa wake ili kuhakikisha tunamaliza kazi hii mapema kwa mujibu wa mkataba. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hiyo. Barabara ya Kolandoto kwenda Kishapu ina kero kubwa kwa wasafiri na wasafirishaji. Ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi huu katika kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Kolandoto - Kishapu – Lalago, ni moja ya barabara kuu na Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba katika mpango huu wa fedha kwa maana ya bajeti ambayo tumepitishiwa, tayari tumeshatenga fedha kwa ajili ya kuanza kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naipongeza Serikali kwa kunipa kandarasi ya utengenezaji wa minara tisa katika Wilaya yangu ya Kishapu, lakini kuna kata ya Ngofila, Kata ya Bunambiu na Mwasubi haziko kwenye orodha hiyo ya vijiji ambavyo vitakwenda kupata huduma hizo. Nini tamko la Serikali katika maeneo haya kuhakikisha kwamba huduma hiyo inapatikana?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru kwa kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpelekea minara tisa aliyoipata katika kipindi cha miaka miwili. Kwa hiyo, tunaamini kwamba hiyo ni hatua nzuri kabisa ambayo tunatakiwa kuendelea kuishukuru Serikali hii, lakini vilevile hatutakomea hapo na awamu zinazokuja tutajiridhisha na changamoto iliyopo katika kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja ili tuziingize katika utekelezaji. Aidha, kama ni kuongeza nguvu ama kupeleka mnara, wataalam wetu watuambia ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Serikali kwa jitihada hizi ambazo imeweka mipango ya kuhakikisha kwamba, mwaka 2023/2024 ujenzi huu unakamilika.
Swali langu la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kuambatana na mimi ili kwenda kuona jitihada zilizofanywa na Mfuko wa Jimbo wa kwangu kama Mbunge, lakini nguvu za wananchi, wadau wa maendeleo kama Mgodi wa Mwadui Williamson?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari pia kwenda kuona jitihada kubwa zinazofanyika za kupata eneo katika Mji Mdogo wa Maganzo, ili tuweze kujenga kituo kingine kwa sababu Kituo kile cha Maganzo ni chakavu na bado kinahudumia Kata tano, Kata ya Mwadui Luhumbo, Kata ya Mondo, Kata ya Songwa na Kata ya Maganzo yenyewe ili kwamba, tuone namna ya kuweza kuwapa huduma kwa usahihi na katika hali ya ubora wananchi wanaozunguka maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi anazofanya na wadau walioko Kishapu katika ujenzi wa vituo vya Polisi kwa ajili ya usalama wa mali za wananchi na wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utayari wangu kuongozana nae, Mheshimiwa nimeshakuahidi na hapa ninathibitisha kwamba, baada ya kumaliza Bunge letu hili mwezi Julai nitakuwa tayari kwenda Kishapu, pamoja na mambo mengine, kuona jitihada za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini njambo la pili, tunatambua kweli katika Mji Mdogo wa Maganzo kuna shughuli nyingi za kibiashara na huko kwenye Mgodi muhimu wa Mwadui wa madini ya Almasi. Tunatambua uchakavu wa kituo kilichopo na kwamba kimebanwa sana na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo naweza nikashauri mapema kabla sijaja huko, ni kupata eneo ili tukiona kwamba eneo hilo linatosha tuliingize kwenye mpango wetu wa kujenga kituo kinachostahili kwenye eneo hilo la Maganzo. Nashukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Vituo vya Afya vya Mwang’aranga, Mwigumbi na Ukenyenge ni vituo ambavyo vina upungufu mkubwa sana wa watumishi;
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inapeleka watumishi kwenye vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, katika Vituo hivi vya Afya vya Mwang’aranga, Mwigumbi na hicho kingine alichokitaja Mheshimiwa Butondo, muda sio mrefu Serikali imetoka kuajiri watumishi wa kad ya afya, hivyo tutakwenda kuangalia na kuona ni wangapi wamepangiwa kwenda katika Halmashauri ya Shinyanga DC na kuweza kuona ni namna gani wanaweza wakapelekwa katika vituo vya afya alivyovitaja Mheshimiwa Butondo.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Katika Kata ya Tarada, Kijiji cha Ngunga upo mradi wa nguvu za jua ambao ni wa gharama ya shilingi bilioni 275. Zoezi la kulipa fidia kwa waathirika bado limeanza kusuasua kutokana na changamoto ya migogoro ya maeneo.
Je, Waziri yuko tayari kufika katika eneo hilo ilimradi kutatua kwa haraka tatizo hilo na mradi huu uanze kutekelezwa kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ameuliza kama Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufika katika eneo hilo, ninayo hakika kwamba dhati ya moyo wake, lakini na sisi wasaidizi wake Wizarani tutafika na kuweza kuona tatizo ni nini kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi ili tuweze kulitatua. Kwa kuonesha nia ya dhati, tayari na mkataba wa utekelezaji wa mradi ule umeshasainiwa. Hivyo, hizi changamoto nyingine ambazo zitazuia utekelezaji hatuwezi kukubaliana nazo. Tutafika ili tutatue tatizo na mradi uanze mara moja.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa jitihada kubwa ilizozifanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi hawa wa Kata ya Mnanje, Wilayani Nanyumbu, wanapata ukombozi kwa kupata hii consent ambayo itaweza kupunguza pakubwa sana adha na changamoto katika Kata hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali iko tayari kufanya jitihada za haraka kuleta hizi Milioni 250 ili kukamilisha ujenzi huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali itakuwa tayari kuleta watumishi wa kutosha ikiwa ni pamoja na vifaatiba ili kituo hiki kiweze kuanza kufanyakazi haraka na kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia tu kwamba hizi fedha Milioni 250, kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha huu Kata zote, maeneo yote ambayo tulipeleka fedha nusu, yatakuwa yamefikiwa ikiwemo katika Jimbo la Nanyumbu la Mheshimiwa Mhata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mara baada ya kukamilika moja ya lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunanunua vifaatiba pamoja na kupeleka watumishi katika vituo vyote ambavyo Serikali imeanzisha, ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii yakuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Jimbo la Kishapu, wadau wa maendeleo pamoja na Mfuko wa Jimbo tumechangia zaidi ya Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na mimi kwenda kuona jitihada za wananchi na kuweka mchango wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubali kuongozana na Mheshimiwa Butondo ili kwanza kutambua juhudi zilizofanywa na wananchi, wadau pamoja na yeye mwenyewe kupitia Mfuko wake wa Jimbo. Pili ni kuona namna ambavyo Serikali inaweza kuchangia kukamilisha kituo hiki cha ngazi ya Wilaya. Nashukuru sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze Serikali na hasa Engineer Kundo kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Lakini nimpongeze pia kwa namna ambavyo amefanya ziara katika Jimbo langu na kuiona changamoto hii kubwa katika eneo langu. Sasa kwa kuwa kata saba kati ya kata tisa ambazo zilikuwa na changamoto na sasa Kata ya Somagedi na Mwasubi bado zina changamoto ya aina hiyo hiyo. Je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba maeneo haya yaliyo na changamoto ya mawasiliano ya simu na yenyewe yanafanyiwa kazi kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo Mbunge wa Kishapu Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge zina changamoto ya mawasiliano lakini kati ya kata tisa kata saba anaenda kupata mawasiliano. Na haya maeneo katika hizi kata saba zote yanapatikana katika kitabu chetu cha bajeti ukurasa wa 153 ukianzia namba 578 mpaka namba 584 zote ni Kata za Kishapu ambazo zinaenda kupata huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa kwamba baada ya kukamilisha kata hizi saba basi kwa sababu utekelezaji hauwezi ukaenda kwa pamoja baada ya kukamilisha hizi basi tutaangalia uwezekano namna ambavyo tunaweza kuleta mawasiliano katika kata mbili ambazo zitakuwa zimebaki, nakushukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuuliza ni lini barabara ya Kolandoto kwenda Mwangongo yenye kilometa 63 itaanza utekelezaji kwasababu mwaka huu wa fedha imetengewa bajeti ya fedha shilingi 2,000,000,000? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii tumeiweka kwenye mpango kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango la lami kuanzia Kolandoto hadi Lalago na Lalago hadi Mwanuzi kilometa hizi 62 na kilometa 60 katika mwaka huu wa fedha, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, msimu wa kilimo cha mazao ya choroko pamoja na dengu wa mwaka 2021/2022 katika Mkoa wa Shinyanga wakulima wa dengu walipata changamoto kubwa ya kupatiwa fedha kwa wakati; na hii ni kutokana na mfumo mzima kutokuwa na maandalizi mazuri ya ulipaji wa fedha katika Vyama vya Msingi ambavyo vilinunua mazao haya kupitia Vyama hivyo vya Msingi; je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba fedha ziwe zinafika kwa wakati kupitia Vyama vya Msingi vilivyopo katika ngazi hiyo ya ushirika ili mradi kuondoa hata na changamoto hii ya wakulima wa dengu na choroko katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Butondo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya awali, kwa kutambua changamoto hizi tumeamua kuja na mwongozo maalum ambao utawajumuisha wadau wote. Lengo la mwisho ni kuhakikisha ya kwamba mkulima anafaidika na mazao yake na tunaondoa changamoto hasa za ucheleweshaji wa malipo. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani mwongozo huu tutakwenda kutatua changamoto zote zilizopo katika mfumo wa stakabadhi za ghala.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inajumla ya vituo vya afya nane lakini vituo vitatu tu ambavyo vinamagari haya ambulance na jiografia ya wilaya yangu ni ngumu kweli kweli. Nilikuwa nataka niombe pamoja na mpango wa wizara kuhakikisha kwamba inatoa..
SPIKA: Mheshimiwa Butondo uliza swali unataka gari iletwe/ipelekwe wapi?
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, ninaomba kuletewa gari na lipelekwe katika Tarafa ya Mondo ambayo itaongeza uwepo wa magari katika Tarafa hiyo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie kwamba katika tathimini ambayo tutafanya kubaini uhitaji wa magari ya wagonjwa na vigezo kama vinafikiwa tutafanya pia katika vituo vya afya ya Kishapu ili tuweze kufanya maamuzi hayo, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii yakuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Jimbo la Kishapu, wadau wa maendeleo pamoja na Mfuko wa Jimbo tumechangia zaidi ya Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na mimi kwenda kuona jitihada za wananchi na kuweka mchango wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nakubali kuongozana na Mheshimiwa Butondo ili kwanza kutambua juhudi zilizofanywa na wananchi, wadau pamoja na yeye mwenyewe kupitia Mfuko wake wa Jimbo. Pili ni kuona namna ambavyo Serikali inaweza kuchangia kukamilisha kituo hiki cha ngazi ya Wilaya. Nashukuru sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Wilaya ya Kishapu haina Mahakama yenye hadhi na kwa bahati nzuri jitihada zimefanyika za kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo: Je, Serikali inaahidi nini kumaliza tatizo hili la Mahakama yenye hadhi katika Wilaya ya Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Butondo swali lake la lini Mahakama itakwenda kujengwa kwenye eneo lake?
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tumeshaweka programu ya Mahakama zote za Wilaya ambazo katika mazingira ya kawaida mpaka kufikia 2025 tutakuwa tumekamilisha nchi nzima ujenzi wa Mahakama zetu. Sasa ni lini? Ninaomba tu Mheshimiwa baada ya majibu haya, kwa sababu programu hii ninayo, tuweze kumpitisha kwenye eneo lini tunakwenda kuanza ujenzi? Ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kuipongeza Serikali kwa majibu mazuri kuhusiana na miradi hii miwili Mwanhalanga na Ukenyenge.
Mheshimiwa Spika, ninaomba tu kushukuru kwamba shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Ukenyenge zilijenga yale majengo matano lakini upungufu bado ni mkubwa sana na hivyo kupelekea Kituo hiki kuendelea kubaki na kutokuwa na hadhi kama Kituo cha Afya. Tunahitaji majengo kwa ajili ya wodi za akina mama na akina baba lakini tunahitaji pia walkways kwa baadhi ya Wodi ambazo zitakuwa zinaunganishwa na hizi njia za kuwafikisha Madaktari na wagonjwa maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusiana na Kituo cha Afya cha Mwanhalanga. Kituo hiki cha afya kina majengo mawili tu na bado wagonjwa ni wengi sana. Ni lini Serikali itakwenda kujenga majengo maalum kwa ajili ya wodi za akina mama, wodi za akina baba, mortuary pamoja na nyumba za watumishi ili tuongeze ari ya watumishi kutenda kazi katika maeneo haya? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza napokea pongezi zake kwa Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli imefanyika katika Sekta ya Afya kwa ujenzi wa Vituo vya Afya kikiwemo hiki Kituo cha Afya cha Negezi ambacho kimepokea shilingi milioni 500. Ninamhakishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunatambua majengo haya bado hayatoshi, hayajakidhi mahitaji, bado tunahitaji wodi, bado tunahitaji mortuary na majengo mengine.
Mheshimiwa Spika, safari ni hatua Mheshimiwa Mbunge, Serikali inaendelea kutenga fedha kwenye bajeti, tuhakikishe kwamba fedha hizi zinapelekwa kwa ajili ya kukamilisha miundombinu hiyo.
Mheshimiwa Spika, pia kuhusiana na Kituo cha Afya cha Mwanhalanga, tunafahamu, tulishapeleka fedha lakini bado kuna majengo ambayo tumeshaweka mpango mkakati kwa ajili ya kutenga fedha ya ukamilishaji. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kishapu ni moja kati ya Wilaya ambazo hazina magari kabisa na sasa hivi tunatumia gari moja la kuazimwa na Mgodi wa Williamson Diamond Limited; ni lini magari haya mapya yaliyotolewa na Serikali yataletwa katika Wilaya ya Kishapu ili kutatua tatizo kubwa lililopo katika Wilaya hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshajibu kwenye maswali ya nyongeza yanayofanana na hili, labda niongeze maelezo ya ziada kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizi shilingi bilioni 15 zilizotolewa na Mheshimiwa Rais, tayari Hazina wameshatupatia shilingi bilioni 10.1 na tumenunua magari 30 kwa ajili ya OCDs lakini tumenunua magari kwa ajili ya RPCs wa mikoa 12 na mengine ya kuongozea misafara. Mara magari haya yatakapotolewa, nataka niwahakikishe Waheshimiwa Wabunge, Wilaya zote ambazo hazina magari, zitapata magari. Nashukuru. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nitoe shukrani kwa Serikali kwa taratibu na mipango iliyoiandaa kwa ajili ya kuhakikisha vituo hivi vinakarabatiwa ikiwa ni pamoja na kufanya upanuzi. Swali la kwanza; nataka tu nipate commitment ya Serikali, je, kwa huu mwaka wa fedha 2024/2025 unaokuja kituo hiki ni moja kati ya vituo ambavyo vitapewa kipaumbele na kukarabatiwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Kituo cha Afya cha Dulisi, Mwigumbi na Ng’wang’halanga ni moja kati ya vituo ambavyo vina upungufu mkubwa wa miundombinu japokuwa vina sifa ya kituo. Je, Serikali iko tayari kuvitazama vituo hivi na kuhakikisha kwamba miundombinu muhimu iwekwe pale ikiwa ni pamoja na wodi kwa ajili ya wagonjwa, nyumba za watumishi na mochwari katika hivi vituo vya afya vitatu nilivyovitaja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Serikali wa ukarabati wa vituo hivi vya afya tumeanza kwanza na kipaumbele cha ukarabati wa hospitali za halmashauri. Katika hospitali za halmashauri zilizoainishwa 50 tayari hospitali 39 zimeshafanyiwa ukarabati na bado hospitali 11 ambazo tunatarajia kuzikamilisha. Baada ya hapo tutakwenda kwenye ukarabati na upanuzi wa vituo vya afya vikongwe. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutakapoanza ukarabati wa vituo vya afya tutahakikisha pia hiki nacho kinapewa kipaumbele, kinakarabatiwa ili kiweze kutoa huduma vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na baadhi ya vituo vya afya ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja vyenye upungufu wa baadhi ya majengo. Serikali inatambua na tumeshaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote Nchini kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu unaopungua kwa awamu. Hata hivyo, Serikali Kuu itatafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono kuhahakikisha majengo hayo yanakamilishwa, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Negezi ambacho kimeanza kufanya kazi sasa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Kituo cha Afya cha Mwanhakanga, Kituo cha Afya cha Mwamigumbi na Kituo cha Afya cha Dulisi, ni vituo vya afya ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi na michango iliyotokana na mapato ya halmashauri.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inakamilisha miundombinu iliyosalia ikiwemo wodi za akinamama, akinababa na watoto, walkways, fence na mambo mengine yanayoendana na sifa za vituo vya afya ili mradi vituo vile vianze kufanya kazi kikamilifu na ipasavyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Zahanati ya Lagana ni moja kati ya zahanati ambazo zinahudumia kata tatu zinazozunguka katika maeneo hayo na moja kati ya mambo ambayo tulielekezwa na Serikali kama Waheshimiwa Wabunge ni kutoa mapendekezo ya kuhakikisha maeneo ambayo ni ya kimkakati na yaliyopembezoni yaweze kupewa kipaumbele cha kuwekewa vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha zahanati hii inapandishwa hadhi kuwa health center ili kiweze kuhudumia maeneo haya yanayozunguka kata jirani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ya kuwatetea wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu kuhusu Kituo cha Afya cha Mwanhakanga, Kituo cha Afya cha Dulisi na Mwagimbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Mwanhakanga tayari kimekamilika na kimeanza kutoa huduma, lakini Kituo cha Afya cha Dulisi na Kituo cha Afya cha Mwagimbi ni vituo vya afya ambavyo pia vimejengwa kwa nguvu za wananchi na vina majengo ya OPD pekee. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya miradi viporo ya hospitali, lakini mahsusi pia kwa ajili ya miradi viporo ya vituo vya afya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali itakuja kukamilisha ujenzi wa vituo vyake hivi muhimu vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu Zahanati hii ya Lagana, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanya jitihada ya kupata fedha ili Zahanati hii ya Lagana iweze kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya kutokana na umuhimu wake na kutokana na hoja ya msingi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza kuhusiana na kupatikana kwa kituo cha afya kwenye eneo alilolitaja. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika mwaka wa fedha 2023/2024 inaonesha kwamba Wilaya ya Kishapu itajengewa Mahakama ya Wilaya; ni lini ujenzi huo utaanza katika Wilaya ya Kishapu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kimsingi Mahakama ya Wilaya ya Kishapu ni miongoni mwa zile Mahakama ambazo ziko katika mpango mkakati wa kujengwa mwaka 2024/2025. Tunaishukuru sana Kamati ya Katiba na Sheria imepitisha pesa na hatua ya Mahakama ya Kishapu na yenyewe ipo katika maandalizi ya mchoro na Maandalizi hayo yameshakamilika na mzabuni ameshatangazwa ili kupata mkandarasi wa ujenzi.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali. Ofisi ya OCD Wilaya ya Kishapu imejengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na wadau wa maendeleo, ukiwepo Mgodi wa Mwadui, mpaka kufikia katika hatua ya upauaji. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri alifika na kuahidi kwamba, watahakikisha wanatoa shilingi milioni 271, kwa ajili ya kukamilisha mradi huo...
NAIBU SPIKA: Uliza swali.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: ...Mradi huo wa Kituo cha Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza wananchi wa jimbo lake kwa kazi kubwa walioifanya ya kujenga Kituo cha Polisi hadi hatua ya linter. Pia, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatenga fedha kama alivyoahidi Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ajili ya kumalizia kituo hicho kilichojengwa kwa nguvu za wananchi, ahsante sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nampongeza Naibu Waziri kwa ziara yake aliyoifanya miezi mitatu katika Jimbo la Kishapu. Wakati huo huo naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kishapu kata zaidi ya 20 zilikuwa na changamoto kubwa sana ya maji, lakini kata nne zina taabu sana. Usanifu ulishafanyika katika Kata za Seke-Bugoro, Mundo na Nyasamba ambapo takribani shilingi bilioni 15 zinahitajika. Old Shinyanga, Busangwa, Nyamtengela, Seke-Bugoro, shilingi bilioni nane; Iselamagazi, Mwanhili na Itongoitale shilingi bilioni tatu; na Mwamashele, Ngofila hadi Kiloleli shilingi bilioni 5.9. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Butondo kwa kushirikiana na Serikali vizuri sana na kukamilisha ule mradi wa bomba kutoka Ziwa Victoria. Amefanya kazi nzuri sana na tunamshukuru sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika mradi ambao katika vijiji ambavyo amevitaja na kata hizi, kwa gharama za jumla utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 33.5. Ni mradi ambao tunatarajia katika mwaka wa fedha 2025/2026 ndiyo tutakaouingiza ili kuutafutia fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba tunaandaa mazingira rafiki ya kwamba mradi huu unaenda kuwezekana kufanyika ndani ya Jimbo lake la Kishapu.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mwaka wa 2024 ulikuwa ni mwaka wa mvua nyingi za El-Nino na bahati mbaya sana zimeathiri barabara nyingi na madaraja mengi yamevunjika; zaidi ya kilomita 50 zimeathirika katika Wilaya ya Kishapu na Serikali imefanya tathmini na kugundua kwamba zaidi ya bilioni 2.7 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo. Je, ni lini Serikali itatekeleza uletaji wa fedha wa haraka na wa dharura ilimradi urudishaji wa miundombinu hiyo uweze kufanyika haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba mvua zilizonyesha, mvua za El-Nino, zimefanya uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara zetu na hasa hizi barabara za wilaya zinazosimamiwa na TARURA. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka wa bajeti ili kuhakikisha kwamba inafanya matengenezo ya barabara hizi ambazo zimeharibika. Nimhakikishie kwamba katika jimbo lake pia Serikali itaendelea kupeleka fedha kuhakikisha tunaziweka hizi barabara katika hadhi nzuri.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Wilaya ya Kishapu ina kata 29, lakini ina idadi ya watu 355,000 na ukubwa wa eneo ni kilometa za mraba 45,333; eneo hili ni kubwa sana na kimsingi Serikali ni lazima irahisishe kupeleka huduma kwa wananchi kwa kupunguza eneo la kitawala na hasa kijimbo.
Je, Serikali inasema nini ili kupunguza eneo hili na kuwa na majimbo mawili walau kuwarahisishia wananchi huduma za kimaendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie nafasi hii kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Butondo kwamba Serikali inatambua kwamba, Halmashauri ya Kishapu na Jimbo la Kishapu, ni miongoni wa majimbo makubwa na ameshawasilisha hoja hiyo mara kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee kumhakikishia tu kwamba, Serikali itachukua hatua hizo baada ya kupata taarifa rasmi kupitia vikao vya DCC na RCC na kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na pale ambapo utaona sasa kuna sababu ya kufanya hivyo na muda mwafaka basi hatua hizo zitachukuliwa. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba Serikali inatambua na tutachukua hatua hizo kadri itakavyowezekana, ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru, wananchi wa Jimbo la Kishapu bado wanahangaika kuhusiana na kituo cha afya cha wilaya. Tumejenga kwa kutumia nguvu za wananchi, Mfuko wa Jimbo pamoja na Mgodi wa Williamson Diamond Limited. Mradi huu unahitaji jumla ya shilingi 175 kwa ajili ya kukamilisha, Mheshimiwa Naibu Waziri aliyepita kipindi kilichopita, alifika katika kituo hicho na akaahidi mwaka huu wa fedha watakamilisha kituo hicho cha wilaya...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakwenda kukamilisha mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninajibu swali la Mheshimiwa Butondo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Serikali imeahidi kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2024/2025 kuwa inamalizia maboma 77 na imetenga takribani shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge pia boma lake la Kishapu tutaweka kwenye mpango na kumtengea fedha ili kuweza kukamilisha. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Kishapu wamechangia jumla ya shilingi milioni 250, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Wilaya. Ni lini Serikali itatimiza ahadi iliyoahidi kwa ajili ya kuwachangia ili wakamilishe mradi huo na uweze kufanya kazi? Nakushukuru sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hebu rudia tena swali lako.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Wilaya ya Kishapu wameshapata eneo, kwa ajili ya ujenzi wa magereza na tayari taratibu zote za fidia zimeshafanyika na Serikali ilishaahidi kwamba, itakwenda kutekeleza ujenzi huo kuanzia Mwaka wa Fedha 2024/2025. Je, ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa? Ninashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshatenga fedha kwenye Mwaka huu wa Fedha 2024/2025. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, as long as tumeshatenga fedha na bado mwaka wa fedha unaendelea, basi tutatekeleza mradi huo kwa ujenzi wa magereza katika jimbo lake. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niulize maswali maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; mwaka 2015 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Magufuli aliahidi kilometa nne katika Mji wa Mhunze na mpaka sasa kilometa moja imetekelezwa katika ujenzi. Serikali inasema nini juu ya kilometa tatu zilizobaki kwa ajili ya kuzitekeleza?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; tumekuwa tukipokea fedha za mfuko wa jimbo, tozo na road fund katika usawa sahihi kwa pamoja kwa maana ya kwamba, zimekuwa zikitolewa katika kila halmashauri kwa usawa lakini kiukweli mitandao ya barabara inatofautiana wilaya hadi wilaya. Kwa nini Serikali isije na formula mpya ya kutoa mgao wa fedha kulingana na ukubwa wa mtandao wa barabara katika kila wilaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifanya kazi kubwa sana ya kuwatumikia wananchi wake.
Kuhusiana na swali la kwanza, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha ahadi za Viongozi Wakuu zinatekelezwa. Kama alivyosema yeye mwenyewe tayari katika barabara hii ya Mji wa Mhunze ambayo iliahidiwa kilometa nne tayari kilometa moja imeshajengwa kwa lami. Nimhakikishie katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 shilingi milioni 688 zimetengwa kwa ajili ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami lakini na kuweka taa. Kwa hiyo, nikuhakikishie ahadi ile iliyotolewa na Hayati Magufuli ya kilometa nne inaendelea kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili; kusema kweli Mheshimiwa Mbunge hoja yako ni ya msingi na Serikali imelitambua hilo na tayari Serikali inafanya mchakato ili kutengeneza formula mpya ambayo itazingatia mambo kadha wa kadha ikiwemo urefu wa mtandao wa barabara katika jimbo husika katika mgao wa fedha hizi kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika kila jimbo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge, hoja yake ni ya msingi Serikali inaendelea nayo na katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, utaratibu mpya wa kutoa fedha hizi utaanza kutumika.