MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kunipa nafasi kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la vituo vya afya na zahanati nchini baada ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa fedha za UVIKO-19. Palipo na mafanikio changamoto hazikosekani. Kumekuwa na uhaba mkubwa wa watumishi wa kada ya afya.
Mheshimiwa Spika, je, ni nini mkakati wa Serikali kukabiliana na changamoto hii?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mnzava, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba Serikali, na kwa maelekezo ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuboresha huduma za afya Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye maeneo ya kutolea huduma, zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa na hospitali za kanda, lakini pia hospitali kuu kama vile Benjamini Mkapa na maeneo mengine tumepanua maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, tunatambua uwekezaji huu ni mkubwa. Tumeanza na kuweka miundombinu, tumepeleka vifaa na maeneo mengine bado vifaa vinapelekwa, na mimi nimefanya ziara maeneo mengi, nimekuta vituo vya afya, zahanati hata hospitali bado tunaendelea kupeleka vifaa. Hata hivyo, vifaa hivi lazima viende sambamba na watumishi wa kada hii ya afya ambayo umesema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi wakati wa bajeti ya Wizara ya Afya hapa tumepata taarifa kwamba Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali cha ajira, na kibali hiki kiko kwenye sekta za afya, elimu, kilimo, fedha na utawala. Kwa hiyo, tunatarajia baada ya kibali hiki kuwa kimeshakamilika taratibu zake tutapeleka watumishi wa afya kwenye maeneo haya yote mapya ili huduma ianze kutolewa kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niungane na Watanzania wote wanamshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye sekta ya afya. Anataka kuona jamii ya Watanzania ikipata huduma kwenye maeneo yao kwa ukaribu, anataka kuona Watanzania wanatumia gharama ndogo kwa kupata huduma karibu na maeneo yao, na sisi tuendelee kumuunga mkono kama ambavyo tunamuunga mkono na tuamine kwamba mkakati huu wa Serikali wa kupeleka watumishi wa umma utakamilika katika kipindi kifupi sana kijacho. Hii ni kwa sababu tayari fedha ipo (Hapa ilikata) kwa sababu tayari fedha ipo na Waheshimiwa Wabunge mmeridhia. Jukumu letu kuanzia tarehe mwezi wa saba na kutoa fedha na ajira ipatikane na watumishi waanze kazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu imekuwa ikiwanufaisha wakulima kwa kuwapa ruzuku kwa baadhi ya mazao ikiwemo korosho. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwa mazao yote ya biashara ikiwemo pamba? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu inaendelea kusimamia kilimo na kuhamasisha wakulima kujitokeza kulima mazao yote ya biashara na chakula. Upo mpango mkakati wa kuwawezesha wakulima kuweza kulima kwa urahisi zaidi, lakini kupata zile huduma kwa gharama nafuu. Tunazo huduma za kilimo au mahitaji ya kuendeleza kilimo, tunaagiza kutoka nje na kwa gharama kubwa kama vile mbolea ambayo tunaagiza kutoka nje, tena kwa gharama kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu inao mpango wa kuwawezesha wakulima kwa kuwapunguzia gharama ya kupatikana kwa mbolea, lakini pia dawa na hata zana za kilimo na hiyo ndiyo inaitwa ruzuku. Si tu kwa zao la korosho kama ulivyosema, tunazungumzia mazao yote. Tunapotoa ruzuku kwa mbolea, mkulima anaweza akaamua kulima mahindi, choroko, pamba, chai, kahawa, anaweza kutumia vyovyote vile. Kwa hiyo ruzuku inayotolewa na Serikali inakwenda kwenye mazao yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili, nataka kumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye toka ameingia madarakani ameonesha nia ya kuwasaidia wakulima kwa kutoa ruzuku. Mwaka wa kwanza alitoa ruzuku ya shilingi 50,000,000,000 kununua pembejeo za kilimo na zimewasaidia sana wakulima na kiwango cha kilimo kimepanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana pia ameweza kuongeza na kutoa shilingi 50,000,000,000 nyingine kwa ajili ya ruzuku ya mazao yote. Tumenunua mbolea na dawa ambazo zimesaidia wakulima kulima mazao na kupata mbolea pamoja na dawa kwa ajili ya mazao yote. Pia, tumepunguza kodi kwenye vifaa vya kilimo, hiyo nayo pia ni ruzuku. Kwa hiyo utakuta ruzuku inakwenda kwenye mazao yote si tu korosho na pamba kama ambavyo imeelezwa, lakini pia na mazao ya chakula kama mahindi na mazao mengine, yote haya yanapata ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mpango huu utaendelea kila mwaka kulingana na uwezo wa kifedha. Pia, tunaendelea kuhamasisha wakulima kuwa na utaratibu wa kujiwekea fedha ili kuweza kumudu kuratibu kilimo cha msimu ujao. Mpango huu tunao ndani ya Serikali, muhimu wananchi tunapotoa ruzuku, kuthamini ruzuku hii kuwa hii ni kodi ya wananchi, badala ya kutumia kwa kuuza tena nje ya nchi. Tunatamani kuona ruzuku hii inatumika kwa wakulima wa Kitanzania ili kilimo chetu kiweze kupanda kwa uzalishaji wa hali ya juu. Ahsante sana.