Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abdulhafar Idrissa Juma (11 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kutupa kibali cha kuwa hai na kutunusuru na mambo mbalimbali tunayoyaona na tusiyoyaona.

Mheshimiwa Spika, la pili, nikushukuru wewe, nami kwa mara ya kwanza leo nasimama katika Bunge lako Tukufu kwa ridhaa yako, nakushukuru sana. Kwa namna ya kipekee nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kilichonipa fursa ya kukiwakilisha katika nafasi ya kugombea Ubunge katika Jimbo la Mtoni; na hapohapo niunganishe kwa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mtoni Zanzibar kwa kunichagua mimi leo hii nikawa Mbunge katika Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza nikisimama leo hii nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Mtoni. Imani waliyoiwekeza kwangu sina mashaka yoyote kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nitailipa kwa kuwatumikia wao na Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja na kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini hapohapo naendelea kumpongeza kwa kuendelea kuwa Mwenyekiti mwema wa chama ambacho kinaiongoza Serikali hii.

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi kwa niaba ya wananchi wenzangu wa Jimbo la Mtoni, tulifarijika sana pale ambapo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliposema wazi ndani ya Bunge hili Tukufu akituhutubia sisi na akilihutubia Taifa hili kwamba katika awamu yake hii anaendelea kuahidi kuulinda Muungano wa Tanzania kwa gharama yoyote; tulifarijika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sisi kule Zanzibar Mapinduzi kwetu ni jambo la mbele yawezekana kuliko uhai wa mtu mmoja mmoja kwa maslahi ya Taifa hili, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kusema tena wazi kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yataendelea kulindwa na kuheshimiwa katika utawala wake; tunampongeza sana katika hotuba yake hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nizungumze kwa uchache sana lile ambalo pia nimedhamiria kulichangia kwa maslahi hasa ya wananchi walionituma katika Bunge hili, wananchi wa Jimbo letu la Mtoni. Jimbo letu nasi linapakana na bahari, moja ya mambo ambayo Mheshimiwa Rais ameyasema atayasimamia na Serikali hii ya Awamu ya Tano katika kipindi cha pili tutayaona ni kuimarika uvuvi wa Bahari Kuu.

Mheshimiwa Spika, Uvuvi wa Bahari Kuu ni moja kati ya Sekta za Muungano. Ni kweli bado kwa nguvu zetu za ndani hatujafanya vizuri sana katika uvuvi wa Bahari Kuu, lakini pia Bunge lako tukufu hili katika mwaka 2018 moja ya ripoti za Kamati zilisema wazi kwamba kama tukiwekeza vya kutosha katika Bahari Kuu, Taifa letu linao uwezo wa kupata takribani bilioni 350 kila mwaka kutokana na uvuvi wa Bahari Kuu. Sina mashaka yoyote kwa haya yaliyosemwa 2018 yalitoa dira kwa Chama Cha Mapinduzi kuweka katika Ilani yetu, lakini yalitoa dira kwa Rais wetu kuja kuyazungumza mbele ya Bunge hili Tukufu na hivyo kuwahakikishia Watanzania kwamba meli nane za uvuvi katika Bahari Kuu zitakuja katika awamu yake hii ya pili.

Mheshimiwa Spika, sisi kule Zanzibar, hasa wananchi wa Mtoni, tumefarijika sana kwa sababu meli nne katika hizo, bila kuficha maneno Rais amesema hizi zitakwenda kufanya uvuvi wa Bahari Kuu Zanzibar na sina mashaka yoyote itachochea uchumi wa Zanzibar na wananchi wenzetu katika majimbo yetu kwa kule Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Zanzibar sisi bahari ni kitu muhimu sana na eneo la bahari ni kubwa kuliko eneo la ardhi ambalo Mungu ametutunuku. Kwa hiyo kivyovyote Bahari Kuu ni kubwa kuliko bahari ndogo ambayo kwa sasa inatumika na inaleta maslahi kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa kule Mtoni wameniagiza niseme katika Bunge hili na nichangie hotuba hii kwamba ujio wa meli ile ama meli hizo zitakapofika hawaoni tu mabadiliko ya uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini wanaona mabadiliko ya kifikra kwa wawekezaji wetu na wao sasa kuanza kuwekeza kwa kuleta meli zenye uwezo wa kuvua Bahari Kuu na hivyo kuongeza ajira kwa wananchi wetu wa ndani lakini kuongeza pato la fedha za kigeni kupitia kuuza samaki hawa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo imejipambanua wazi kupambana na masuala ya kifisadi katika awamu hii ya pili. Ni kweli vijana wengi ama fursa nyingi za ajira zimejitokeza katika awamu iliyopita na tunatumai yale tuliyoahidi na yaliyoahidiwa na Ilani ya Chama chetu, Serikali yetu kupitia Rais wetu aliyo madarakani itayatizmiza kwa kuendelea kupambana na ufisadi.

Mheshimiwa Spika, tukipambana na ufisadi zile ajira milioni nane tulizowaahidi Watanzania katika ilani yetu, na chini ya usimamizi wa Dkt. John Magufuli, tuna uhakika zitatimia. Viongozi wenzetu katika Serikali mkimsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia mianya ya upotevu wa fedha, hali za wananchi wetu zitaendelea kuimarika, fursa za Taifa hili kwa vijana zitaendelea kuimarika na sisi viongozi tuko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali; na wananchi wa Jimbo la Mtoni wamenielekeza nimalizie kwa kusema wataendelea kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iyatende yale ya Muungano kwa maslahi ya Wazanzibari na Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ABDUL-HAFAR IDRASSA JUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na kuwa mchangiaji wa mwanzo katika hoja hizi zilizokuwa mezani.

Mheshimiwa Spika, ningeomba nijielekeze sana katika hoja iliyowasilishwa na Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali za Mitaa, kwa sababu ni sehemu ya Wajumbe wa Kamati hiyo.

Mheshimiwa Spika, Fedha za Maendeleo kwa kiwango kikubwa Serikali Kuu imekuwa ikitimiza wajibu wake. Hakuna halmashauri ambayo haijapelekewa kabisa Fedha za Maendeleo, lakini nini kilichopo katika halmashauri zetu kikubwa? Ni usimamizi usioridhisha wa Fedha za Maendeleo wa Wakurugenzi na wasaidizi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Samahani kidogo Mheshimiwa Mbunge.

Waheshimiwa Wabunge tunaposimama tutazame mchangiaji yuko wapi. Usimkate mchangiaji kwa sababu anapozungumza, anazungumza na mimi. Tuzingatie sana hilo ni la muhimu kwa sababu pia haitaleta picha nzuri kukwambia rudi kwenye kiti chako.

Mheshimiwa Juma.

MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa hiyo, fedha za maendeleo Serikali Kuu inapeleka, lakini usimamizi wa halmashauri zetu katika fedha za maendeleo hauridhishi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo wanaopelekewa takribani milioni 500 mfano. Halmashauri zote zikapelekewa milioni 500 zikafanye jambo fulani, labda kujenga kituo cha afya ama kiwango fulani cha fedha kwa ajili ya kujenga skuli mpya, lakini nini kinachotokea? Wapo wanaokamilisha, wapo wasio kamilisha, wapo ambao hawafanyi kabisa, wako wengine mpaka leo wamejenga robo na fedha imekwisha.

Mheshimiwa Spika, sasa usimamizi wa fedha zinazopelekwa kwa maafisa wetu masuuli bado hauridhishi, lakini fedha kwa maendeleo zinazotengwa na wao wenyewe kutoka fedha zao za ndani hizo ndizo kabisa. Wapo wengine fedha wanazipata, sheria inawataka wapeleke asilimia 40, wanapeleka kiwango wanachotaka. Sasa nini maana ya sheria zilizotungwa na Bunge?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani Halmashauri zetu Serikali iongeze umakini wa kuzisimamia ili ziweze kutimiza wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu asilimia 10. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza utaratibu mpya wa usimamizi wa fedha za asilimia 10 ya halmashauri. Lakini katika bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo taarifa yake ndio imewasilishwa hapa mbele bilioni tano haikupelekwa katika mfuko wa asilimia 10. Si kwamba ikatafutwe, fedha ilishakusanywa, lakini Wakurugenzi na maafisa masuuli wenzao waliamua tu kutokupeleka bilioni tano za vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii inamaanisha kwamba, kwa kutokupeleka bilioni tano katika mwaka 2021/2022 vijana katika Taifa hili wamenyimwa shilingi bilioni mbili ya kujiendeleza kiuchumi; wanawake katika Taifa hili wamenyimwa shilingi bilioni mbili ya kujiendeleza kiuchumi, na watu wenye ulemavu wamenyimwa shilingi bilioni moja ambayo ilipatikana na sheria tumeitunga Bunge ilitaka wakapewe.

Mheshimiwa Spika, kama tungeamua kuwa na vikundi 50 tu nchi nzima, kila kimoja kikapewa shilingi milioni 100, fedha ambayo ilikuwa imeshapatikana, leo tungekuwa tumesaidia Watanzania wangapi? Lakini Wakurugenzi na maafisa wao masuuli hawakupeleka fedha hizi.

Mheshimiwa Spika, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika mwaka huohuo amebainisha takribani bilioni 88.4 zimekopeshwa hazijarejeshwa. Hivi ni wazimu wa aina gani ukampe mtu fedha halafu ushindwe kurejesha fedha yako ilhali ulimpa ya mkopo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ni nini ambacho kamati tuliona? Na mimi kama Mbunge ninashauri kwamba, japo Mheshimiwa Rais ameelekeza mfumo mpya wa utoaji wa utoaji wa fedha hizi ambao Serikali inaendelea kuufanyia kazi lakini zile ambazo zimeshatoka lazima zipatikane kwa sababu, amewapa watu. Vikundi hewa vilikuwepo, wametengeneza vikundi hewa, kikundi kimepewa fedha eti mtu aliandika namba yake ya simu, leo simu haipatikani, ulimpaje mtu fedha kwa namba ya simu? Inawezekana vipi kama maafisa masuuli hawapo katika sehemu ya mchezo huu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini ushauri wangu wa jumla ni kwamba; pamoja na Maazimio ya Kamati, kuna umuhimu sasa wa kufanyika tathmini ya jumla ya Halmashauri moja baada ya nyingine kupima uwezo wake wa kifedha, kupima uwezo wake wa kutoa huduma kwa wananchi na kupima umuhimu wa uwepo ama kutokuwepo kwake.

Mheshimiwa Spika, ingekuwa biashara Serikali Kuu katika fedha za matumizi ya kawaida kwa mwaka 2021/2022 Halmashauri ya Kigoma, fedha za matumizi ya kawaida, mshahara, OC na mambo mengine, kununua stationaries, wamepewa shilingi bilioni 16.3. Fedha walizikusanya wao ni milioni 700. Japo wamezidi bajeti yao kwa asilimia 3, lakini ingekuwa biashara ya kawaida hebu tutathmini jamani; unachukua bilioni 16 unakwenda kukusanya bilioni tatu?

Mheshimiwa Spika, sasa narudia tena ushauri wangu, tufanye tathmini. Muundo huu wa Serikali za Mitaa tulionao ulikuwepo tangu hakujawa na WhatsApp, tangu Mheshimiwa Nape hajasambaza minara katika maeneo mengi ya nchi hii. Sasa tufanye tathmini basi tuone Halmashauri tulizonazo tuna umuhimu wa kuendelea kuwanazo katika muundo huu? Tuzibadilishe kulingana na mahitaji ya sasa ama tuone namna gani vizuri zaidi vya kufanya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningetamani pia kuona Serikali inaboresha hatua za kinidhamu kwa watu ambao wanakuwa wamehusika kabla ya kupeleka katika hatua za kisheria. Wanaosababisha upotevu wa fedha, wakishafanya utafiti wao wanawapeleka TAKUKURU. Kule TAKUKURU mambo yanakwenda yanaenda Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda tu nikwambie; yupo Mkurugenzi ana kesi ya jinai kwa matendo aliyoyafanya kutoka katika halmashauri moja. Sasa hivi ni Mkurugenzi katika Halmashauri nyingine anatoka na gari la Serikali anakwenda kuhudhuria katika kesi yake ambayo ametenda makosa katika halmashauri fulani.

Mheshimiwa Spika, sasa utaratibu wa kinidhamu nadhani pia Serikali iuboreshe kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, kwa wakuu wa idara na watumishi wengine kabla ya kufika katika utatuzi wa kisheria. Wapo Wakurugenzi wamebainika ndugu zao ndio walikuwa wana POS machine, wamekusanya fedha, fedha haijapelekwa, ndugu huyu hajulikani yuko wapi, Mkurugenzi yule kahamishwa, wanasema taratibu za kisheria zinaendelea, taratibu za kinidhamu ziko wapi?

Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni za Watanzania na ninaomba, pamoja na Maazimio ya Kamati, lakini Serikali ijiangalie katika uchukuaji wa hatua za kinidhamu kwa watu wanaohusika na ubadhirifu katika masuala ya halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kabisa katika hoja yangu ileile ya ushauri mkuu wa kufanya tathmini. Wenyeviti wa Halmashauri ni Madiwani na sisi Wabunge kwa wale ambao sheria inawaruhusu ni Madiwani katika halmashauri zetu. Tumebaini, yapo maeneo Madiwani ambao wengine ni Wenyeviti wa Halmashauri kwa kushirikiana na watendaji wetu katika Halmashauri wanafanya makusudi kumharibia Mbunge aliyekuwa madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nini ushauri wangu katika tathmini hiyo. Ningetamani tathmini hiyo pia, iangalie je, hakuna uwezekano Mbunge wa jimbo akawa ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali Kuu mwaka 2021/2022 imepeleka shilingi trilioni 5.9 katika Halmashauri, za maendeleo pamoja na masuala mengine ya matumizi, lakini Halmashauri zote zimekusanya bilioni 800. Kuna Mheshimiwa Diwani mmoja pale ambaye labda hamtaki na yeye anautaka Ubunge kwa sababu ndiye ameshika zile nafasi na labda kwa sababu mahusiano ya Mkurugenzi na Mbunge hayako vizuri, wanatumia nafasi hiyo kumuharibia.
Mheshimiwa Spika, sasa ile tathmini ikifanyika tuangalie nini kinachowezekana, kama mambo haya yalipitishwa muda mrefu, kama nilivyosema, tangu WhatsApp na Facebook tunatumia sana Yahoo, sasa tuko katika Gmail na mengine. Sasa tuangalie ikiwezekana basi tufuate utaratibu ambapo Mbunge wa jimbo ikiwa halmashauri ina Mbunge zaidi ya mmoja itafutwe namna, lakini Mbunge akawe Mwenyekiti wa Halmashauri, ili kujaribu kuunganisha uwajibikaji wa pamoja.

Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kukushukuru. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa anayoendelea kutupa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna ambavyo amekuja na hotuba ambayo ni dhahiri inakwenda kutimiza yale ambayo chama chetu kimeilekeza Serikali katika awamu hii kupitia ilani yetu ya mwaka 2020 - 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya sijasema niliyodhamiria, nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wangu kutoka Jimbo la Mtoni ambapo mvua zinazoendelea kunyesha kule Zanzibar, baadhi yao kupitia Shehia ya Sharifu Musa Zone ya Chemchem B, wamepata athari ya kingiliwa na maji katika majumba yao. Nitumie nafasi hii kuziomba mamlaka zenye dhamana katika Serikali ya Zanzibar na katika Jimbo letu la Mtoni waone namna gani watakwenda kuwasaidia wananchi wale ili tatizo lile liwaondoke na lisijirejee tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hii ya Waziri Mkuu, napenda nichangie suala la umeme. Ni vyema sana, nami nimefarijika kwa kweli nilipoona Serikali imeshalipa sehemu ya fedha za Mradi wa Bwawa la Umeme. Bwawa lile halina tija tu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania peke yake ama kwa wananchi wanayoishi Tanzania Bara, lakini bwawa lile pia litaleta faida kwa sisi tunaotokea upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nikumbushe, Kisiwa cha Unguja, kinapokea umeme kupitia waya uliotandikwa chini ya Bahari kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar na Kisiwa cha Pemba kinapokea umeme kutoka Tanga uliotandikwa chini ya Bahari hadi Pemba. Umeme ule unatoka katika Mamlaka ya Shirika la Umeme la upande wa Tanzania Bara, TANESCO.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bwawa likichimbwa, umeme ukizalishwa, bei ikishuka, wananchi wa Tanzania wakiwemo wananchi wa Zanzibar na Jimbo langu la Mtoni, watanufaika kwa bei ya umeme kushuka na kuboresha maisha yao. Naipongeza sana Serikali kwa hatua hii na ninawatia moyo, sisi wananchi wa Tanzania na sisi viongozi tuko nyuma yenu katika jambo hili na tutawaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipate fursa sasa ya kuzungumzia Mfuko wa Jimbo hasa kwa majimbo ya upande wa Zanzibar; mfuko ule wa kuchochea maendeleo ya jimbo katika Bunge la Muungano. Fedha hizi zimekuwa zikiandaliwa, zimekuwa zikitolewa, lakini mpaka jana majimbo takribani yote ya Zanzibar hayajapokea fedha za Mfuko wa Jimbo katika majimbo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Serikali yetu imeshatoa hizo fedha, lakini yawezekana fedha zile zimekwama Ubungo. Kwa kuwa kuna flyover, sidhani kama kuna foleni tena; yawezekana fedha zile zimechelewa kupata boti, lakini kwa kuwa boti ziko nyingi, sidhani tena; lakini yawezekana fedha zile zimeelekezwa kabla ya kufika katika Mfuko wa Mbunge wa Jimbo, zikamsalimie shangazi, zimsalimie na mjomba na ziangalie kidogo uzuri wa binamu, halafu ndiyo ziingie katika Mfuko wa Jimbo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ione namna bora fedha hizi zitatoka na kama zitapita kumsalimia mjomba, kumsalimia shangazi na kuangalia uzuri wa binamu, lakini zifike kwa wakati katika majimbo yetu. Maana wananchi wa Jimbo la Mtoni wanazisubiri fedha hizo zikasaidie kutatua changamoto zinazowakabili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zilivyoanza kuingia katika Majimbo yetu upande wa Tanzania Bara, nasi kwa kifua mbele tukaanza kujinasibu kwamba ile miradi ambayo imeibuliwa na wananchi; mfano katika Jimbo langu la Mtoni, wameibua mradi wa kujenga daraja ambao lingeweza kuwaunganisha watoto wavuke kwa haraka kutoka school, kutoka upande mmoja wa Shehia kwenda upande wa pili; wameibua mradi wa kujenga jaa la kukusanya taka kwa muda kabla ya Manispaa kuja kuzichukuwa, wanachosubiri ni fedha tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, wakati mambo haya yakiendelea kupangwa, jambo hili lizingatiwe sana. Hatuna tatizo na namna fedha zinavyopita, lakini zipite kwa haraka ili wananchi wa Jimbo la Mtoni na majimbo mengine ya Zanzibar waweze kujivunia hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuzungumzia suala la Muungano kwa namna ambavyo limezungumzwa katika hotuba ya Waziri Mkuu. Naipongeze sana Serikali yetu kwa namna ambavyo inaendelea kushughulikia masuala ya Muungano. Leo naomba nishauri pia namna nyingine ambayo labda ipo, lakini natamani iendelee kuboresha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za Muungano zipo nyingine kuzitatua kwake ni kuziondoa katika mambo ya Muungano; lakini zipo nyingine ambazo kuzitatua kwake ni kuziba mianya ile inayoleta changamoto na kuyaunganisha zaidi kwa mambo ya Muungano yaliyo imara zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa natolea mfano suala la mpira wa miguu. Natambua huko nyuma Zanzibar ilipata kuwa Mwanachama wa Mpira wa Miguu (CAF) Afrika. Baadaye kutokana na sheria za CAF na namna Muungano wetu ulivyo, ikashindikana. Sasa kwa nini tuendelee kufikiria kutenganisha baadhi ya mambo wakati ni muhimu tukaweza kuyaunganisha vizuri na yakaondoa changamoto hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naitaka Serikali iendeleze nguvu katika kujitapa na kuyasema wazi yale mafanikio ya kimuungano, kwa sababu changamoto huwa zinasemwa sana na wakati mwingine zinataka kutuamisha sisi tuliozaliwa baada ya Muungano, kama vile Muungano una matatizo mengi sana. Kumbe Muungano una raha nyingi sana. Muungano huu umetupa fursa Wazanzibari kutoka Zanzibar ambapo hakuna milima mikubwa mikubwa, tukafika Dar es Salaam, tukaona milima ya wastani ya Kisarawe, tukasogea Morogoro tukaona milima mikubwa mikubwa ya Ulugulu, tukasogea Kilimanjaro tukaona milima mikubwa sana ya Kilimanjaro. Hiyo ni moja ya raha na faida za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muungano huu umewapa fursa ninyi wenzetu wa Tanzania Bara kuvuka maji na kwenda kushuhudia neema za Zanzibar zikiwemo shadow na poda nzuri zinazopakwa na wanadada wa Zanzibar. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, neema na faida za Muungano ni nyingi. Basi naiomba Serikali yetu, katika bajeti yake inavyoendelea kusema, iyataje waziwazi mambo ya Muungano ambayo yanafanya vizuri kwa faida ya kizazi chetu na kizazi kijacho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtoni, nashukuru sana na mimi naunga mkono hoja hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika, naendelea kukushukuru na kumshukuru Mwenyezi Mungu kama desturi yangu kutokana na neema hii ya uhai na afya ambayo mara nyingi tunaendelea kupewa.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie haraka haraka katika hotuba hii ya bajeti kuhusiana na masuala haya ya utatuzi wa masuala ya Muungano. Niipongeze sana Ofisi ya Makamu wa Rais kwa namna ambavyo imeendelea kupambana na masuala ya Muungano na wakafanikiwa kutatua baadhi ya changamoto za Muungano hasa hizi tano ambazo zimesemwa katika bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nigusie hasa hii kuhusu gharama za kushusha mizigo bandarini. Muungano huu pamoja na faida zake kama walivyotangulia kusema wachangiaji wenzangu; changamoto zitakazokuja kujitokeza kwa umri wake ni namna ambavyo wananchi wa upande mmoja wanafaidi fursa za upande mwingine kwa usawa ama katika nafasi ya kupeana favour kwa sababu ni Muungano. Zanzibar ina watu wasiozidi 1,600,000 kwa makadirio; lakini Dar es Salaam tu peke yake ambayo ndiyo geti kubwa la watu kutoka Tanzania Zanzibar kuingia Tanzania Bara ina watu takribani 5,000,000 kuelekea 6,000,000.

Kwa hiyo, utaona namna gani potentiality ya soko la kibiashara ilivyo kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara, hasa kupitia geti la Dar es Salaam. Nipongeze sana kwa hatua hii, lakini iendelezwe haraka ika-reflect kwa wananchi wetu kama walivyosema wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utatuzi huu unaweza ukaleta ufumbuzi wa kurahisisha biashara lakini Muungano huu ni wa watu. Mimi nakuthibitishia sijafanya utafiti lakini ni uhakika zaidi ya asilimia 70 ya familia za wananchi Zanzibar tuna Ndugu zetu upande wa Tanzania Bara moja kwa moja. Mimi binafsi yangu, baba na mama yangu wanaishi Tanzania Bara, kwa hiyo, kuna mambo mengi sana nayahitaji katika kuunganisha. Kwa hiyo, wakati wakitatua masuala ya kibiashara na watatue masuala ya kiubinadamu moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haifurahishi hata kidogo mtu anatoka Zanzibar, amebeba sukari kilo tano tu kwa ajili ya kumpelekea mzazi wake au jamaa yake Tanzania Bara akifika pale bandarini anasumbuliwa. Sasa wakifanya utatuzi katika jambo hili isemwe wazi; Wizara ya Muungano ikaweke bango pale bandari ya Zanzibar, iweke bango pale bandari ya Dar es Salaam waseme sukari mwisho kilo moja ama usibebe kabisa ishia hukohuko; TV usibebe kabisa, ukibeba fuata tararibu hizi za kibiashara. Kwa hiyo, ningetamani waseme pamoja na kuwapongeza kwa haya waliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la TASAF. Zanzibar ina Shehia 338; mpaka sasa Shehia 204 ndizo ambazo zinapata ruzuku ile kwa watu wa kaya maskini. Natambua katika bajeti hii ilivyosomwa kuna mnyanyuko wa Shehia, miongoni mwa Shehia zitakazonufaika ambazo zilikuwa hazipati ni zile zilizopo katika Jimbo langu la Mtoni. Jimbo langu lina Shehia tano, Shehia tatu zilikuwa zinapata msaada wa kaya maskini; Shehia ya Sharif Musa na Shehia ya Kwagoa zilikuwa hazipati. Natambua katika bajeti hii Shehia hizo mbili zimekwenda kuonekana lakini natambua pia si Shehia zote 338 za Zanzibar zitakwenda kumulikwa na mradi wa TASAF katika awamu inayoendelea. Naomba sana Serikali yetu hii, iendelee kutunisha na kutafuta uwezo wa mfuko wa TASAF ili Shehia zote 338 katika Visiwa vya Unguja na Pemba vinufaike na mradi huu wa kunyanyua na kuziwezesha kaya maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge tulipewa semina kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema kuhusiana na Mfuko wa Jimbo kwa kule Zanzibar; natamani semina hiyo hiyo pia wakapewe wale wasimamizi wa fedha zetu kwa upande wa Zanzibar. Tujue, sisi tumeambiwa mipaka yetu ya fedha hizi na wale wakaambiwe kwamba mipaka ya fedha hizi za Mfuko wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni huu ili tukienda kuongoza vile vikao vya matumizi wasije wakaona labda tunawaingilia katika baadhi ya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, napongeza sana jitihada zinazochukuliwa katika kutoa elimu, lakini pia mfanye tathmini ya elimu mnayoitoa kuhusu Muungano; je, inakidhi mahitaji ya kisasa ya mabadiliko ya teknolojia? Mnaweza mkatoa elimu lakini bado ikawa haiwafikii watu wengi kwa sababu bado tunanung’unika sana kuhusu Muungano kuliko neema zake.

Mheshimiwa Spika, naomba nielezee Kiti chako na Bunge hili raha za Muungano, mimi ni mmoja wa wanufaika maana mke wangu ni Mchaga wa Rombo. Muungano una mambo mengi mazuri. Kama elimu inatolewa, taarifa zinakwenda, sasa fanyeni evaluation namna mnavyopeleka elimu na mabadiliko ya teknolojia. Ningetamani kila tunapopita tuone tunazungumzia raha za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaona changamoto zinazojitokeza visiwa kuanza kuliwa, hatutegemei visiwa vyetu vije vifutike, lakini kama mabadiliko ya tabianchi ulimwenguni yakiendelea ni lazima athari ya kupotea visiwa itatokea, tutakwenda wapi? Tuyaseme haya wazi sasa kama Muungano unatupa fursa ya kutembea, unatupa fursa ya kujenga na kujianda kama yale tunayotaka kuyazuia yakishindikana tuweze kuishi upande huu bila bughudha yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii, naipongeza Wizara hii lakini naendelea tu kuishajihisha, Shehia 338, tuko katika Shehia 204 sasa mmeongeza Jimbo la Mtoni, mkimaliza Shehia 2 sina kesi nanyi lakini Zanzibar zitimie Shehia zote 338; Zanzibar tuendelee kula raha na kufaidi Muungano. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia katika hoja hizi zilizokuwa mbele yetu. Pamoja na mambo mazuri na ushauri mzuri ulitolewa na Kamati uliowasilishwa na Mwenyekiti, ningependa niendelee kuzungumzia masuala mawili, jambo la kwanza, suala la UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejitahidi sana kama Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia katika kupambana na masuala ya UKIMWI. Afua za UKIMWI zimeendelea kupatikana, lakini ripoti ya Kamati na takwimu za Serikali zinaonesha kwamba, vijana hasa walio kati ya miaka 15 na miaka 24 ndio walioathirika zaidi na maradhi haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana 28,800 kwa mwaka, tena vijana hao ni kati ya miaka 15 na miaka 24, ndio ambao wanaongoza kwa kuathirika. Sasa mimi ningependa nishauri nini pamoja na haya; ningetamani sana Serikali yetu pamoja na Watanzania wote turejeshe nguvu ya kupambana na masuala ya UKIMWI katika ngazi ya familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi ya familia hatuzungumzi sana uwazi kuhusiana na namna ambavyo UKIMWI unaweza kuambukizwa. Ndio maana tunazungumza sana katika kuhakikisha watu wetu hawapati virusi vya UKIMWI kwenye familia kwa kuwashauri wasitende vitendo vile ambavyo vinasababisha kuambikiwa kwa UKIMWI. Moja ya njia kubwa ya kupata virusi vya UKIMWI ni kutenda ngono isiyokuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dini zote, dini ya Kiislamu, ngono kabla ya wakati ama ngono nje ya ndoa ni dhambi, Dini ya Kikristo, sina mashaka na dini zote. Ngazi ya familia tumekuwa tunawakataza sana watoto wetu kushiriki vitendo vya ngono kwa ku-refer tu maelekezo yale yaliyotoka katika vitabu vyetu vitukufu, lakini shetani yupo kwa ajili ya watu wema. Sasa hawa vijana wetu ambao tunawaambia kwamba, msishiriki ngono, mkishiriki ngono mtapata dhambi tu, shetani yupo kwa ajili yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani katika ngazi ya familia sasa tuwe wawazi kidogo. Tuwaeleze watoto wetu kwamba, ngono ni dhambi, lakini kwa sababu wengi wanashiriki tuwaambie basi siku ukishiriki ngono shiriki ukiwa umevaa condom, maana utakuwa umepata dhambi, lakini umelinda afya yako, kuliko akapata dhambi na asilinde afya yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaweza ikanusuru vijana wetu. Kwa siku moja vijana 80, kwa mwezi mmoja vijana 2,400, kwa mwaka mzima vijana 28,000 hali ni mbaya. Sasa tukiendelea kutumia dini peke yake katika kuwakataza vijana wasishiriki tukiamini itatosha peke yake kuwakinga, hapana haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, dini mpinzani wake mkubwa ni shetani. Jambo zuri sana kushiriki jambo la kimapenzi kwa mtu yeyote aliyekuwa juu ya miaka 18 kwa ridhaa yake sio kosa kwa mujibu wa sheria zetu. Sasa katika ngazi ya familia tuwe wawazi, tuwaambie ukitenda utapata dhambi, lakini shetani akikupitia ama kama ukimfuata shetani halafu mkaenda mkatenda, vaa mpira ili kuhakikisha kwamba, hujiambukizi virusi vya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia niongezee katika masuala ya maradhi yasiyoambukiza. Ningetamani niungane na Kamati katika kuishauri Serikali, umefika wakati sasa wa kuunda Tume Maalum ya Kupambana na Maradhi Yasiyoambukiza kama tulivyounda Tume Maalum ya Kupambana na UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote humu ndani na Watanzania karibu wote hakuna familia ambayo haijaathirika na maradhi yasiyoambukiza. Kama hakuna mtu mwenye maradhi ya moyo kuna mwenye maradhi ya kisukari, kuna mwenye uzito uliopitiliza. Sasa tuishauri Serikali ione sababu ya kuunda tume maalum kupambana na maradhi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maradhi yasiyoambukiza sio tu ni hatari, lakini ndio maradhi ghali zaidi kuyatibu katika familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza katika Bunge siku ya leo kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza bajeti hii. Bajeti hii imeakisi mwelekeo wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na inavyokwenda kutekelezeka kabla ya mwaka 2025. Ilani yetu imeelekeza kuendelea kutafuta ahueni katika kila nyanja katika Taifa letu. Yale ambayo yamesemwa na Waziri Mkuu, kuanzia yale yaliyotekelezwa na yale ambayo yamepangwa kutekelezwa katika bajeti hii, sina mashaka yoyote chini ya Mama Samia, mwaka 2025 Ilani ya Chama cha Mapinduzi itakuwa imetekelezeka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuyasema hayo, yaliyozungumzwa katika bajeti hii, naomba nichangie kuhusiana suala la TASAF. Katika Jimbo langu la Mtoni, mimi ni mnufaika wa TASAF katika Shehia zote. Hivi karibuni Shehia mbili ambazo zilikuwa hazipo; Shehia ya Kwagoa na Shehia ya Sharifu Mussa zimeingizwa katika mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niishauri Serikali. Zipo changamoto katika kupata wanufaika wa TASAF katika maeneo yetu kwa sababu ya kijiografia. Umaskini wa Zanzibar haufanani na umasikini wa mtu wa Kigoma. Umaskini wa Zanzibar haufanani na umasikini wa Tanga na maeneo mengine. Umasikini unapishana kutokana na mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wasaidizi wetu katika TASAF kama watatafsiri mtu kumiliki tv ya chogo kule Zanzibar hafai kuwa katika TASAF, wanaweza wakakuta Wazanzibar wengi hawana sifa hiyo, lakini ni watu masikini ambao wanastahiki kusaidiwa na Mfuko wa TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu, japo mchakato wa rufaa za TASAF unaendelea, lakini wapo ambao wameenguliwa kwa sababu vyoo vyao wamekuta kuna masinki.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niwakumbushe wenzetu, sisi kule Zanzibar unaweza ukanunua TV mpya, badala ya kuuza TV uliyokuwa nayo ukamgawia mtu ambaye unadhani anastahiki kugawiwa. Sasa mimi niwakumbushe wenzetu, umasikini huu unapishana. Nashauri wenzetu katika TASAF, wakiwa wanafanya tathmini ya kutafuta watu wenye kustahiki kusaidiwa na mfuko huu wa TASAF, waugawe umasikini kutokana na mazingira yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwetu Zanzibar hatulimi. Ukimkuta mtu masikini hasa katika jimbo langu ni masikini kweli kweli, anahitaji msaada wa Serikali. Hatuna ardhi ya kulima, jimbo langu kwa ardhi ni ndogo. Ukikuta hana uwezo wa kufanya biashara, huyo anastahiki na TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kushauri kwamba pamoja na mambo mazuri, wamechukuliwa baadhi yao, wanaendelea kupewa na wananufaika na msaada huu wa TASAF lakini mgawanyo wa masuala ya kuutafsiri umasikini, watafsiri umasikini kwa mazingira yake. Mazingira yanatofautisha umasikini wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nizungumzie suala la UKIMWI katika bajeti ya Waziri Mkuu. Kwanza naipongeza Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Mama Samia, wameendelea kuhakikisha upatikanaji wa ARV nchi nzima. Mimi ni Mjumbe wa Kamati inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, hakuna mahali tulipokwenda tumekuwa ARV hazipatikani, zinapatikana kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda katika bajeti hii tuendelee kuiboresha tuhakikishe zinapatikana mashine za kupima viral load katika maeneo yale ambayo yanatoa huduma CTC. Ili kupima ufanisi wa ARV katika mwili wa mtu ambaye anatumia vidonge hivi, ni lazima tupime virusi kwa kutumia viral load.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo tumeyaona hayana mashine zenye uwezo wa kupima viral load. Katika bajeti hii ya Waziri Mkuu, mambo yake mazuri sana, lakini yaongeze nyama kwa kuhakikisha mashine za viral load zinapatikana. Tunatambua Tanzania wapo waathirika wa virusi vya UKIMWI takribani milioni 1.7, sasa kwa nini tusihakikishe tunakuwa na viral load zitakazowafanya wasihame kutoka eneo moja kwenda eneo lingine ili kupata huduma hii kwa ajili ya kusaidia wananchi wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa dhamira ya kuongeza bajeti katika fungu la maendeleo kwa fedha za ndani. Hata hivyo naomba dhamira hii iendane na kutekelezwa. Mwaka wa fedha unaokwisha huu walitenge shilingi bilioni moja, mwaka huu wametenga shilingi 1,880,000,000, lakini shilingi bilioni moja iliyopita, changamoto ipo, hazijatoka zote. Sasa dhamira ni nzuri ya kuongeza bajeti, lakini dhamira iende ikatekelezeke ili wenzetu wa Tume ya Taifa ya Kupambana na Virusi vya UKIMWI wawe na uwezo wa kuhakikisha tunafikia zile 95 tano kufikia mwaka 2030. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuzungumzia maradhi yasiyoambukiza. Nashauri tena jambo hili kupitia bajeti ya Waziri Mkuu. Maradhi yasiyoambukiza kwa sasa ndiyo yanayoongoza kuua Watanzania. Maradhi yasiyoambukiza ndiyo maradhi ambayo yanafilisi familia zetu, maradhi yasiyoambukiza ndiyo yanayoleta unyonge kwa ndugu zetu. Sasa basi, ninaishauri sana Serikali yetu ione tunavyoweza kuanzisha Tume ya Kupambana na Maradhi Yasiyoambukiza kama ambavyo tumeanzisha Tume ya UKIMWI.

Mheshimiwa Naibu Spika, shilingi ngapi tunazipoteza kila siku kuhakikisha watu wenye maradhi ya figo wanasafishwa damu. Shilingi ngapi zinapotea kila siku watu kwa ajili ya kuchukua vidongo vya pressure? Maradhi yasiyoambukiza ni tabia zetu tu, namna tunavyoishi, namna tunavyokaa muda mrefu na kupigwa na viyoyozi mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweza kuanzisha Tume inaleta hamasa na kuleta uelewa mkubwa kama Tume ya Kupambana na UKIMWI. Leo wote humu ndani tunajua namna gani virusi ya UKIMWI vinaambukizwa, lakini tukibainika tuna virusi vya UKIMWI, tuna amani na tunatumaini kwa sababu tunajua Serikali imeandaa dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba Tume hii ianzishwe ili kuongeza hamasa na kutambua maradhi yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya, naunga mkono hoja hii. Nashukuru sana (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika mpango huu wa Serikali. Kabla ya kukushukuru wewe namshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeusikiliza mpango na nimeusoma kwa umakini na nimeurejea mara kadhaa. Naomba nijiridhishe kwamba Mpango huu umeakisi yale ambayo tuliyaelekeza katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2020/2025. Ni chama chetu ndicho ambacho kimemuweka Rais madarakani na sehemu kubwa ya Wabunge tuliomo humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo yale yaliyoandikwa kwenye mpango nimeona dhamira ya kuendelea kukamilisha madaraja yale ambayo tumeyaahidi, nimeona dhamira ya kuendelea kuboresha sekta ya afya, nimeona dhamira ya kuendelea kutoa ruzuku kwa wanufaika wa TASAF zaidi ya milioni moja nchi nzima. Kwa hiyo, yale yale ambayo tuliyaahidi kwenye Ilani yetu yanaendelea kutekelezwa na Mama Samia katika Awamu yake ya Sita na kweli kazi inaendelea. Kwa hiyo, hili nimejiridhisha na kwa nafasi hiyo naunga mkono mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja, mpango wowote ni kukusanya na kutumia. Mpango wa kutumia umekaa vizuri sana, mpango wa kukusanya unaelekea kukaa vizuri, lakini usimamizi wa yale yaliyokusudiwa kutumiwa bado tuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naweza nikarudia Taarifa za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali za miaka takribani miwili au mitatu iliyopita. Kila mwaka katika Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, fedha za wananchi zinapotea katika mazingira tofauti. Fedha hizo tukiweza kuzizuia, tunao uwezo wa kufanya mengi makubwa kwa ajili ya wananchi wetu na hivyo tukaisaidia Serikali yetu kuweza kufanya vizuri zaidi huko mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umetolewa mfano wa marejesho ya fedha zinazotolewa kama kukopesha wananchi 10% ile ambapo 4% kwa vijana, 4% kwa akina mama na 2% kwa walemavu zaidi ya shilingi bilioni 80 nchi nzima. Shilingi bilioni 80 kama ikisimamiwa vizuri inaweza Kwenda kwa vijana na ikaleta matokeo na kila mwaka fedha zinaongezwa. Lakini tumeona kwenye Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali namna fedha hizo wakayi mwingine zinakwenda, zinapotea na hazionekani nini zimefanya. Hatuwaoni vijana waliotajirika kwa fedha hizi katika Halmashauri zetu, hatuwaoni akina mama waliotajirika na wala wenzetu wenye ulemavu waliotajirika. Kuna umuhimu Wizara ya Fedha katika mpango huu mhakikishe mnakwenda kuweka macho katika nafasi hii na maeneo mengine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumze jambo lingine kuhusiana na Muungano. Taifa letu ni la Muungano, nchi hii ni Tanzania ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mpango huu umezungumza masuala ya kimuungano katika masuala ya tabianchi. Kuna manufaika na umeelekeza kwamba kutapelekwa fedha na sehemu nyingine iliyozungumzwa ni katika kujenga au kuboresha nyumba ya Makamu wa Rais, Tunguu, napongeza kwa haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna umuhimu wa kutenga fedha maalumu za kufanya utafiti za Muungano wetu mara kwa mara kutokana na mahitaji yake. Katika mpango huu tukiweka fedha maalumu, tukazitenga ambazo zitakuwa kazi zake ni kufanya tafiti tu ya Muungano wetu. Kuna watu wanahoji kwa nini kuna Muungano wa Serikali mbili mpaka leo? Lazima tuwe na tafiti ambazo zitasaidia kuboresha na kuondosha manung’uniko ya kimuungano. Kwa sababu bado wafanyabiashara wa Zanzibar wanaendelea kunung’unika kuhusiana na mambo wanayotengenezewa katika bandari. Sijaona mpango huu ukielekeza ni kipi kifanyike katika kuhakikisha manung’uniko ya wafanyabiashara hasa wadogo wadogo wa Zanzibar wamaweza wakaondolewa vikwazo ili wanufaike na fursa za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wakati akija kufanya majumuisho Mheshimiwa Waziri atambue kwamba miongoni mwa fursa ambazo wafanyabiashara wadogo…

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza kwa kukazia ukweli juu ya suala la manung’uniko ya wafanyabiashara kutoka Zanzibar hususani kwa kadhia wanazozipata katika bandari ya Dar es Salaam. Hata juzi kuna mfano wa haluwa ya shilingi laki moja tu raia amebanwa pale na kutakiwa kuilipia nusu ya ile bei aliyonunulia. Kwa kweli ni kilio na lazima liangaliwe kwa jicho pevu kabisa, ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Idrissa.

MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na nimeipokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya tunayaondoaje? Ni kwa kufanya tafiti tu, ndio maana nashauri Mheshimiwa Waziri akija kuleta majumuisho atuambie na aone umuhimu wa kuwa na fedha maalumu zitakazopelekwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano kufanya utafiti wa hali ya Muungano wetu kwa sasa, changamoto zilizopo na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi bado najiuliza labda kukiwa na utafiti utaniletea uthibisho mzuri. Kwa nini mpaka leo kama suala la afya sio suala la Muungano? Lakini tukiwa na utafiti unaweza ukatusaidia labda tukiendelea kuwa suala la afya sio suala la Muungano kunaweza kukawapa fursa nyingi zaidi Watanzania, lakini kama likiwa la Muungano litaleta fursa nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoshauri ni umuhimu wa uwepo wa fedha maalumu za utafiti juu ya Muungano wetu, wala tusione aibu kufanya hivyo kwa sababu ndio Muungano pekee, kielelezo cha umoja katika bara la Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na mimi katika hotuba hii ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali hasa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa yale ambayo amekuwa akiyatenda na haya ambayo yameelezwa katika bajeti ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhahiri kama ambavyo mara nyingi nimekuwa nikizungumza humu ndani. Mwaka 2025 Chama changu cha Mapinduzi hakitakuwa na kazi ya kumrejesha Mheshimiwa Dkt. Samia madarakani Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kufanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba nichangie katika masuala yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, katika sekta ya Miundombinu, napongeza kwa jitihada ambazo zinaendelea kufanyika. Ningeomba sasa Ofisi ya Waziri Mkuu katika bajeti yake hii ione umuhimu wa kuleta mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi ili kuruhusu Sekta ya Miundombinu iwe kama Sekta nyingine za kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sifurahishwi sana kuona mpaka leo bado tunajenga barabara mfano za Mwendokasi kupitia fedha ambazo zinatafutwa na Rais Samia na Serikali yetu. Kama tumetoa fursa kwa wafanyabiashara wakaweza kuja kujenga viwanda, tukawapa vivutio mbalimbali vya kodi, wakajenga viwanda wakazalisha ndani ya Tanzania, watanzania wakaajiriwa, Serikali ikapata kodi, kwa nini tunashindwa kutoa fursa kama hizo kwa wawekezaji wakajenga miundombinu hasa ile ya mwendokasi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu barabara ya mwendokasi inapojengwa sio watanzania wote na magari yao wanaruhusiwa kutumia ni magari maalumu. Kwa hiyo, ni magari maalumu ambayo yanapita na kufanya biashara katika barabara hiyo. Sasa kwa nini Serikali isitangaze kwa wenye fedha duniani wakaja wakajenga barabara za mwendokasi ili fedha ambazo zingekwenda kujenga barabara zikatumika kwa shughuli nyingine kama vile kuhudumia hospitali zetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo jambo sio geni na huko duniani lipo. Serikali yetu ilitupa nafasi sisi tulikwenda kujifunza nje. Huko duniani ziko bandari zimejengwa na watu kwa asilimia 100 na Serikali inakusanya kodi tu. Sasa kwa nini katika sekta ya miundombinu tusiende huko katika kuleta vivutio kama tulivyoleta vivutio katika sekta ya viwanda? Ningetamani kuona katika suala la bandari ya Bagamoyo linakwisha na kuanza kujengwa kupitia wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli inawezekana tumekosea sasa je, tumekosea ndio tuache ibaki hivyo hivyo? Tuache tusiwe na bandari kubwa Zaidi? Makosa yaondoshwe Sheria iletwe katika Bunge hili tuone namna inavyoweza kubadilishwa basi Bandari ya Bagamoyo na Bandari nyingine ziweze kujengwa kupitia sekta binafsi kwa maslahi ya taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba sasa pia nizungumzie suala katika Manispaa hasa zile asilimia 10 zinazohusu vijana wenzangu akina Mama pamoja na Watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwanza nikupe taarifa nina miaka 32 hivi karibuni nitatimiza miaka 33, kwa hiyo bado ni kijana na nina maslahi makubwa sana na vijana katika Taifa hili pamoja na Wananchi wangu wa jimbo la Mtoni. Fedha zile ambazo zinakopeshwa asilimia 10 mara nyingi ukopeshwaji wake hauleti matokeo mazuri. Nafasi hii niitumie kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuelekeza fedha hizi zianze kutolewa kupitia Mfumo wa Kibenki. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais amesema suala hilo litafanyika katika bajeti ya Serikali ijayo bajeti ya mwaka 2024/2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, fedha hizi katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo zimetengwa kuendelea kusimamiwa na Halmashauri. Nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Msimamizi Mkuu wa Serikali basi fedha hizi katika mwaka 2023/2024 zisije zikatumika kama kiinua mgongo kwa wale watu ambao wamekuwa wakigawana na vikundi vyao kwa sababu wanajua baada ya hapo zitaanza kutumika kupitia Benki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2020/2021 ilionesha kwamba takribani Shilingi bilioni 47 katika halmashauri 155 katika hizi fedha za asilimia 10 zimeshindwa kukusanywa kurejeshwa. Maana yake nini? Bilioni 47 zingekusanywa wangekopeshwa vijana kila mmoja mwenye uwezo wa kufanya Biashara Milioni 100 maana yake tungetengeneza Mamilionea 470 wakasimamiwa na halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri zote zina maafisa biashara. Laiti Maafisa biashara wangeweza kusimamia kuwasaidia wafanyabiashara sio tu kuwakimbiza pale wanapokuwa hawajakata leseni labda tungekuwa na wafanyabiashara wakubwa wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa fedha hizi katika bajeti hii ya mwaka 2023/2024 kwa sababu ndio itakuwa ya mwisho kusimamiwa moja kwa moja na halmashauri kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, basi Ofisi ya Waziri Mkuu ikazisimamie lasivyo nitakapokuja hesabu ya Maguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka huu 2023/2024 ambao tunapitisha bajeti yake itakuja na matatizo yale yale. Ningetamani kuona Ofisi ya Waziri Mkuu inakwenda kuzisimamia ili nione Mamilionea vijana kutokana na fedha ambazo zinatengwa na halmashauri yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa suala la vyama vya siasa. Nitumie nafasi hii kuomba bajeti ya Waziri Mkuu wale ambao wanasimamia masuala ya vyama vya siasa watenge muda zaidi kuvipa Elimu na kuvikumbusha vyama vya siasa umuhimu wa Demokrasia. Mheshimiwa Rais ametuonyesha njia umuhimu wa ustahimilivu, umuhimu wa kusikiliza sasa na wao wawe wastahimilivu na wawe wenye kusikiliza. Hata hivyo, hivi vyombo ambavyo vinasimamia vyama vya siasa vitimize wajibu huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda tukumbushane humu ndani, mwaka 2015 watanzania waliamua Kumchagua Dkt. John Pombe Magufuli na Rais Samia ambaye yuko sasa madarakani kama Makamu wake wa Rais. Watanzania hao hao waliamua kuchagua Wabunge wengi wa upinzani pia na waliamua kuchagua Wabunge wengi zaidi wa CCM lakini mwaka 2020 Watanzania waliamua Kuchagua Wabunge wa CCM wengi zaidi kwa sababu ya yale yaliyotendwa na Serikali iliyokuwa madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa vyama vya siasa kama ambavyo vilifurahia na hasa vya upinzani vilivyopata Wabunge wengi mwaka 2015 vijifunze kustahimili Watanzania wakiendelea kuiamini CCM.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema awali, kwa mwendo wa Rais Samia hakuna pahala katika Taifa hili ambapo hajaweka mkono. Dhahili, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi mwaka 2025 watatawala katika viti vyote vya Bunge hili kwa sababu watanzania watawaamini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale wenye kusimamia vyama vya siasa wakae watukumbushe viongozi wa Chama Tawala na vyama vingine kwamba kushindwa katika uchaguzi Mkuu ni matokeo na baada ya kushindwa wasije wakatumia nafasi hiyo kuwafitinisha watanzania maana baada ya uchaguzi watahitajika kuendelea kulijenga taifa lao. Hata hivyo, wakati wa kuwakumbusha pia wawasomee basi katiba ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 5 ili mioyo yao iwe na amani pale mambo yoyote yatakapotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo nakushukuru sana naunga mkono hoja hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii tuliyo nayo mezani. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali na Waziri mwenye dhamana, lakini kwa nafasi hiyo pia nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuhakikisha kuwa wawekezaji wanakuja Tanzania na matokeo ya uwekezaji yanatokea, tunaanza kuyaona. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuhakikisha anasimamia maono ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii tumeelezwa hapa na Waziri wakati anasoma bajeti yake kwamba mpaka sasa mpaka mwezi wa pili bajeti, fedha alizopokea kutoka Wizara ya Fedha hazijafika 60%, lakini Wizara hii ndio ambayo inaleta wawekezaji ambao ndio wanaolipa kodi na kulisaidia Taifa katika masuala mbalimbali. Nitumie nafasi hii basi kuiomba Wizara ya Fedha kwa sababu maziwa wanayoyakamua sehemu kubwa yanasababishwa na Wizara hii, basi Wizara hii waipe fedha kwa wakati hasa fedha za maendeleo ili waendelee kutoa yale ambayo yanategemewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza pia ipi dhamira ya uwekezaji katika Taifa letu. Michango mingi tumezungumza mambo mengi mazuri kwa ajili ya wananchi wetu, lakini naamini dhamira ya uwekezaji ni kuhakikisha tunakuza ajira katika Taifa letu, ni kuhakikisha tunaiongezea Serikali kipato kwa kodi, lakini ni kuhakikisha bidhaa zinapatikana bila usumbufu kwa wananchi wetu tena kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, bajeti ya Waziri imesema bidhaa ya cement au saruji tunazalisha kwa kiwango kikubwa kuliko mahitaji yaliyopo ndani ya nchi, hivyo tunauza nje ya nchi, lakini kwa nini bado bei ya cement kwa mujibu wa taarifa ya Waziri ni Sh.17,600. Hii Sh.17,600 sio fedha ndogo kwa wananchi wetu wanyonge. Najiuliza kama material ya cement yanapatikana ndani ya nchi, wanafanya kila kitu ndani ya nchi, kwa nini bado bei yake haijafika kama bei ambazo tukinunua cement nje ya nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako baadhi ya marafiki zangu ni wafanyabiashara wa cement, wanaagiza bidhaa ya cement kutoka Iran. Bei ya bidhaa ya cement wanayonunua Iran mpaka wakija kuuza katika soko la Zanzibar, bado bei ni nafuu kuliko bei hii ya cement inayozalishwa ndani ya Tanzania na tunauza nje ya Tanzania. Sasa nini dhamira ya uwekezaji kwa wananchi maskini katika Taifa hili? Kama dhamira ya uwekezaji ni kuhakikisha wanapata bidhaa kwa bei nafuu, nataka Mheshimiwa Waziri aje aniambie, kwa nini pamoja na cement kuuzwa nje ya nchi kutokana na uzalishaji kuwa mkubwa, lakini bado bei yake ni kubwa kuliko cement ambayo inazalishwa kutoka nchi nyingine za na ikafika Tanzania na ikaweza kufanana bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atueleze kwa nini bei yake isiwe ndogo? Kwa nini bei ambayo mfanyabiashara ataenda kununua Iran asiwe ananunua ndani ya Taifa letu na huyu anasafirisha, analipa kodi na bado mambo mbalimbali yanaendelea kuyafanya. Kwa hiyo nataka kuona dhamira ya uwekezaji itoe matunda kwa wananchi maskini, sio tu peke yake kwa kutoa matunda katika ajira na Serikali kupata kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo nizungumzie suala la ununuzi wa Tanga Cement kama ambavyo baadhi ya wenzangu wamezungumzia na ndio wajibu wetu kwa sababu tumechaguliwa tuje tuishauri Serikali na tusipoishauri tutakuwa hatujatenda wajibu wetu wa kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Mtoni na majimbo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu ya baadhi ya Wabunge ambao wameendelea kusimamia ama kuishauri Serikali iangalie mchakato wa Twiga Cement kuinunua Tanga Cement ni hofu ya kibiashara na ni hofu wazi kabisa. Hofu hiyo msingi wake ni sheria tuliyoitunga ndani ya Bunge hili, kama sheria tumeitunga ndani ya Bunge letu kwa dhamira ya kulinda hofu kama hiyo kitu gani kinatufanya Serikali ishindwe kusimamia sheria iliyotungwa na Bunge hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria imesema wazi katika masuala ya kuingia sokoni kama wakati wanafanya merge haitakiwi uzidi 35%. Mwenye mamlaka ya kusimamia hiyo sheria, watendaji kupitia Wizara hii FCC walikiri kwamba hili jambo likifanyika litazidi 35%, sasa leo kitu gani kilichotokea tena nyuma wakajisahaulisha yale waliyoyasema, tena hata wakajisahaulisha hukumu iliyotolewa na Mahakama ambayo haijatoa kwa kupenda, ni sisi wawakilishi wa wananchi ndio tulitunga sheria hii. Ni sisi wawakilishi wa wananchi ndio tulihakikisha panakuwepo na Mahakama, tulihakikisha panakuwepo na FCC kwa sababu tulijua yatatokea mambo ambayo tunataka kulinda maslahi ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sio dhambi mtu kuuza kitu chake, hata mimi naweza kuuza vitu vyangu, lakini katika Taifa hili kuna sheria, vipo vitu Mwenyezi Mungu amekutunuku wewe mwenyewe, ukivifanya katika Taifa letu ama ukivitumia katika Taifa letu ni makosa kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo kuuza kitu chake mtu sio dhambi, lakini utaratibu wa sheria zetu ufuatwe. Utaratibu uko wazi, wanunuzi wapo, kama vipi itangazwe, mbona tumeona makampuni mengi yaliyo-merge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijaribu kuanza kufuatilia masuala ya merging ya kampuni wakati Millicom anauza hisa zake kuelekea iliponunuliwa sasa hivi na kampuni ya Axian na nilifuatilia sana kwa maslahi ya kampuni ambayo Serikali ya Zanzibar ina hisa Kampuni ya Zantel. Pale ndipo wakati nafuatilia nikalikuta suala hili pia, nikasema acha nilifuatilie kwa maslahi ya Taifa letu. Nikafuatilia tangu mchakato ulivyoanza, nikajua taarifa za watu na wadau mbalimbali waliokwenda Mahakamani, nikajua hukumu iliyotoka ambayo ilishauri kwamba suala hili lisifanyike kwa maslahi ya Watanzania. Ni Mtanzania gani mwingine huko nyuma ambaye ana maslahi tofauti na maslahi ya Watanzania ambaye anaruhusu suala hili lifanyike tena? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kampuni hii ikachukua ikamiliki soko zaidi ya 42%, wakiamua kuangusha bei ya saruji, wataua viwanda vingine vidogo vya Watanzania na watu wengine mbalimbali, hapo tutakuwa tunasaidia uwekezaji au tunaua uwekezaji? Je, jambo hili likifanyika bei ya saruji ikapanda zaidi kuliko ilivyo sasa hivi, tunawasaidia Watanzania au tumewaua Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inawezekana sheria hii kwa maono ya hawa imeshapitwa na wakati, lakini ndio iliyopo, tufuate sheria iliyopo. Pia niishauri Serikali kupitia Wizara hii na Serikali nzima, suala hili la Tanga Cement kuuza hisa zake na interest ya Twiga kununua tulitumie kama visibility study ama kama maono basi, pana sheria nyingi sana ambazo haziko sahihi kwa mujibu wa mwenendo wa masuala ya kibiashara katika Taifa letu. Kuna sheria za manunuzi nyingi haziko sahihi kwa wakati huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili tulitumie kama mfano kwamba Serikali ilete mabadiliko ya sheria mbalimbali ambazo wanadhani yanaweza yakasaidia masuala ya kibiashara. Katika hatua ya sasa, kile ambacho kipo kwa mujibu wa sheria kiheshimiwe ili wafanyabiashara waendelee kuiheshimu Serikali, wawekezaji waiheshimu Serikali, lakini wananchi watambue yale tunayoyashauri na kupitisha katika Bunge ni kwa maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nikawa wa kwanza kuchangia katika bajeti hii muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Kwa sababu maendeleo yoyote ni usalama na hata matibabu mazuri yanatendeka vizuri pakiwa na usalama.

Mheshimiwa Spika, napongeza bajeti hii kwa namna ambavyo imesomwa na kwa namna ambavyo nayo imejielekeza pamoja ni masuala ya ulinzi lakini imejielekeza kutekeleza Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi ambayo inasimamiwa na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, napongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze pia kwa namna ambavyo Jeshi letu limeendelea kukabiliana na baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika mipaka yetu. Katika moja ya kazi ngumu sana ambazo zinahitaji kujitolea mno ni kazi ya kuwa mwanajeshi. Daktari tunamhitaji pale tunapokuwa tunaumwa tu, tukishapona hatumuhitaji tena daktari. Lakini mwanajeshi ama jeshi letu tunalihitaji tukiwa wazima, tunalihitaji tukiwa tunaumwa, tunalihitaji tukiwa na uchumi imara na tunalihitaji uchumi wetu ukitetereka ili liendelee kudhibiti mipaka yetu tuendelee kuwa salama. Nalipongeza sana kwa namna ambavyo limekuwa likifanya vizuri katika kutimiza wajibu wao huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nizungumzie kuhusiana na mahusiano baina ya majeshi yetu hasa Jeshi letu la Wananchi Tanzania na wananchi wanaokaa karibu na Kambi zao hasa zilizoko Mjini. Mimi hapa nataka nipongeze kupitia Kambi ya JWTZ ya Mwanyanya iliyokuwepo katika Jimbo langu la Mtoni. (Makofi)

Kambi ile imezungukwa yote na makazi ya watu, kambi ile ina mahusiano mazuri sana wananchi katika eneo lile na askari wetu katika Kambi ile wamekuwa ni mfano mzuri wa askari wengine katika Jeshi letu Tanzania nzima. Kambi ile imejitolea baadhi ya vitu ikachanga na wananchi ili watengeneze sehemu ya njia iliyoharibika. Jeshi pale lilitoa kokoto, jeshi lilitoa simenti, jeshi lilitoa mchanga wananchi na vijana wakajikusanya na sisi viongozi tukaongeza nguvu, wakamwaga zege katika eneo korofi ambalo linatumika na wananchi na wao askari wanalitumia kwa uchache sana. Napongeza sana nidhamu na uimara wa Jeshi letu katika kushirikiana na wananchi wetu katika kipengele hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukarimu huu wa Jeshi letu kushirikiana na wananchi umesababisha wananchi wengi katika Jimbo la Mtoni wanaoishi karibu na Kambi ile ya Mwanyanya kupenda kutumia Hospitali ya Jeshi iliyokuwepo katika Kambi ile. Sasa ombi langu kwa sababu ukarimu wao umetuvutia sana pamoja vituo vingine vya afya vilivyokuwepo, lakini tunapenda kutibiwa kwao, ukarimu na namna ambavyo wanatupokea basi naiomba Wizara hii katika fedha zake za kuboresha vituo vya afya vilivyopo katika majeshi na nyingine ipelekwe pale katika Kambi ya Mwanyanya ili pawe na vifaa vingi zaidi vya kuhudumia wananchi. Vifaa hivyo pale vikipelekwa vitahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nikwambie hatuendi pale pia kwa sababu hakuna Hospitali nyingine laa! lakini ni namna ambavyo Jeshi letu limekuwa na ukarimu na linawapa wananchi tiba sahihi. Kwa hiyo, naomba katika bajeti hii pamoja najua kuna mambo pale yanafanywa wakati mwingine linakarabatiwa taratibu naomba mtupelekee fedha katika kambi ile ikaboreshwe hospitali na katika hospitali nyingine zote. Hospitali zilizopo katika kambi zetu zinahudumia sana wananchi yawezekana kuliko majeshi tuliyokuwa nayo. Sasa mimi naomba hospitali ile iboreshwe, hospitali nyingine ziboreshwe na hospitali zote hasa ambazo Kambi zipo karibu na makazi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niendelee kulipongeza Jeshi letu, sisi tuko pamoja, bajeti yenu tutaipitisha kwa kishindo muendelee kulinda mipaka yetu, tuko pamoja nanyi na Mungu awajaalie kila kheri. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia katika hoja tuliyonayo mbele yetu. Mimi ninaomba nianze kwanza kwa kuipongeza Serikali kwa mambo mazuri yanayoendelea kupangwa na mambo mazuri yanayoendelea kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani na Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongeza Taifa letu, yote yaliyokuwa yameahidiwa wakati wa kampeni na yote ambayo yameandikwa katika Ilani ya Chama chetu yameendelea kutendeka na hayo dhamira yake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na ndiyo dhamira ya CCM na Serikali yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kulijenga Bwawa la Mwalimu Nyerere na tayari tumeona linatoa huduma kwa wananchi. Tuliahidi katika Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Mama Mheshimiwa Dkt. Samia amefanikisha na Serikali yake imesaidia hilo. Tuliahidi treni itatoa huduma, treni imeshaanza kutoa huduma kwa hiyo, tunaendelea kuipongeza Serikali kwa yale yote yanayoendelea kutendeka. Ni nini ambacho ningependa kuchangia katika bajeti yetu hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti imependekeza kuweka tozo ama kodi katika gesi inayotumika katika magari. Moja ya sehemu ambayo tunatumia fedha nyingi sana za kigeni, kama Taifa, ni katika kuagiza mafuta tena yanayotumika katika magari. Mheshimiwa Waziri hapa ametangaza amesema, kama tukifanikiwa kupitisha hiki ambacho tunaendelea kukijadili, basi baada ya kuanza kutumika kwake hakutakuwa na matumizi ya dola. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapendelea pasitumike dola katika matumizi ya kawaida, lakini kiuhalisia hata sisi sote tuliopo humu ndani tukitoka tu baada ya kuahirisha Bunge tutenda kutumia dola kwa sababu, tutapanda katika magari na magari haya yanatumia mafuta na mafuta haya tunayaagiza kwa kutumia dola za kimarekani. Fedha nyingi sana tunazitumia katika kuagiza mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza jitihada za kuhakikisha tunapunguza matumizi ya dola kwa kuongeza uzalishaji wa ndani katika mambo mbalimbali, mfano viwanda vya sukari, napongeza. Mfano, tunashadihisha sasa tuanze kutumia na kuzalisha mafuta ndani, lakini hatujaongeza nguvu katika kuacha kutumia mafuta ya petrol na diesel kwenye magari yetu na tumeweka kabisa tozo katika hili. Wenzangu wamesema na mimi narudia kusema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nzima hii ya Tanzania ina vituo vitatu tu ambavyo vinatoa huduma ya gesi kwa magari ambayo yanatumia gesi. Mimi nadhani kama tukiamua kuweka tozo, kama tukiamua kuweka kodi, isiwe kodi inayokwenda kutumika kama kodi nyingine zote. Kodi hii iwekewe mfuko maalumu wa kusaidia uwezekano wa wawekezaji kuwekeza katika vituo vya gesi, ili gesi ipatikane zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya sababu ambayo inasababisha vituo vya mafuta ya petrol na diesel kuwa vingi kuliko vituo vya gesi ni gharama ya uwekezaji. Gharama ya uwekezaji kuwekeza kituo cha kutoa huduma ya gesi ni kubwa sana kuliko vituo vya mafuta. Mimi nadhani kama tuliweza kutoa bilioni 100 kila mwezi kusaidia kupunguza bei ya mafuta, kama kodi hii tukiiweka na tutafute fedha nyingine kuhakikisha unapatikana urahisi wa kuwekeza vituo vya gesi, tukifanya hivyo tutapunguza matumizi ya dola katika kununua mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya dola yamesababisha dola ipande na kupanda kwa dola kumeathiri watu wengi sana. Sisi Wazanzibar tunapenda sana sikukuu, kule kwetu tunyime kila kitu usitunyime sikukuu; hivi leo tunavyozungumza nadhani ni Eid ya nne kule Zanzibar na baadhi ya wananchi wangu wameniambia wanataka kutoka wakasherehekee Eid. Kwa hiyo, sisi tunapenda sana sikukuu, lakini wananchi wamelalamikia ongezeko la bei ya kuwanunulia watoto nguo za sikukuu. Nguo iliyonunuliwa mfungo mosi, nguo ile ile katika mfungo tatu imepanda, tatizo ni dola tu imepanda. Pamoja na kupanda kwa gharama za usafirishaji baharini, lakini dola imepanda. Tunafanya nini kuhakikisha mafuta haiwi sababu ya kutumia dola zetu na tuzitumie katika mambo mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninashauri kama tutakubaliana humu ni lazima hiyo tozo ama hiyo kodi iwepo, isiende katika mfuko wa matumizi ya kikawaida, iwe ni fedha maalumu katika kusaidia upatikanaji wa vituo vya gesi na urahisi kwa wawekezaji, ili wananchi watumie gesi katika magari yao. Miongoni mwa mapato yasiyo ya kodi yanatokana na Shirika letu la Ndege la ATCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Mheshimiwa Dkt. Mama Samia, kwa kuhakikisha ndege zinaendelea kuwepo, ndege zinaendelea kupatikana na zimekuwa msaada, lakini ndege zinafanya biashara. Kumpata mteja kwa mara ya kwanza katika biashara ni jambo linalowezekana. Pamoja na usimamizi mzuri sana, kazi ngumu sana katika biashara ni kumfanya mteja arejee huduma yako. Sasa wahudumu wa kike na wakiume wa ndani ya ndege nadhani wanavutia, mambo ni mazuri, lakini kwa upande wa ATCL angalieni wahudumu wenu wanaokutana na abiria iwe wakati wa ku-check au iwe wakati wa kununua tiketi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kununua tiketi hakuna matatizo sana, pana matatizo katika nyakati za ku-check. Abiria ndiyo bosi wa ATCL sio Mkurugenzi wa ATCL, sasahivi bado watu wanakimbilia huduma za ATCL kwa sababu, hakuna mbadala, siku watakayopata mbadala wataacha kutumia ATCL; baadhi ya wahudumu wenu ndio wanaosababisha. Sasa waangalieni wahudumu wenu katika zile counter za ku-check, wana-treat vipi wateja? Wanasaidia vipi wateja? Wanawapa wateja mbadala upi wa huduma pale wanapokuwa wamechelewa kwa sababu, hii ni biashara na tunategemea fedha, ili bajeti hii tunayotaka kuipitisha sehemu ya fedha hizo tunazitegemea katika Shirika la Ndege? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipongeze Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA, kwa namna ambavyo wamekuwa wanajitahidi kuendeleza mahusiano. Siku moja nilikwenda Mamlaka ya Mapato, TRA, Temeke na sikupenda kujitambulisha kama Mbunge nikasema ngoja nipate huduma za kawaida na wananchi wenzangu. Mbele ya Bunge hili naomba nimpongeze sana Meneja wa TRA wa Mkoa wa Kodi wa Temeke, sikumbuki sana jina lake, lakini anaitwa Masau Malima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilivyofika nilikuta watu wengi katika foleni. Miongoni mwa watu waliokwenda kuomba msaada ni mtu ambaye alikuwa anatakiwa kulipa kodi ya shilingi 18,000; amekwenda anaomba msaada wa Meneja wa Mkoa na alitenga muda akamsikiliza mwananchi yule. Mwananchi aliondoka amefurahi na ninaamini Taifa letu limepata kodi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niipongeze TRA kwa kuendelea kujenga mahusiano na walipakodi. Waendelee kufanya hivyo na hapa nimemtaja huyu maalumu, awe mfano na chachu kwa wengine, ili tuendelee kulijenga taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)