Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdulhafar Idrissa Juma (7 total)

MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya kuridhisha kiasi ya Naibu Waziri, lakini vitendo vya udhalilishaji na uhalifu katika Wilaya ya Magharibi “A” ambapo Jimbo langu la Mtoni lipo, lakini pia na kituo hicho cha polisi tunachokizungumzia kipo, vimekuwa vikiongezeka sana.

Sasa je, nini kauli ya Serikali katika wakati huu wa vitendo vikiongezeka na kituo kimefungwa nini kauli ya Serikali juu ya mapambano yake ama inafanya nini kuhakikisha kwamba vitendo hivi vya uhalifu na udhalilishaji unapungua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrissa Juma, Mbunge wa Jimbo la Mtoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimuambie Mheshimiwa Abdul kwamba nipo tayari kufuatana na yeye kwanza kwenda kukiona kituo hicho, lakini pia nipo tayari kwenda kukaa na uongozi wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Mjini ili lengo na madhumuni kuweza kufanya nao mazungumzo, ili ikiwezekana baada ya kujiridhisha tuone namna ambavyo tunaweza tukakifungua kituo hiki na kikaendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nipo tayari kwenda kukaa na wananchi kuweza kuwaambia maneno mazuri ambayo yatawapa imani ya kuendelea kuwa amani na salama na utulivu katika Jimbo lao. Lakini kikubwa nimuambie kwamba hili suala lake aliloliuliza la kuongezeka kwa matukio haya ya udhalilishaji katika Mkoa huu, katika Jimbo lake na katika Wilaya hii, Serikali tuna mipango mingi ambayo tumeshaanza kuifanya. Lakini kubwa nimuambie kwamba kwanza tunakwenda kuongeza nguvu kwenye masuala mazima ya ulinzi shirikishi. Ulinzi ambao unawapa nafasi wananchi wenyewe kushiriki katika ulinzi huu wa wananchi wao binafsi na hapa nataka nichukue fursa hii, nimpongeze sana Mheshimiwa Abdul-Hafar amekuwa anafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza amewatafutia kituo hawa walinzi shirikishi, lakini kubwa amewatafutia vifaa vya ulinzi kwa ajili ya kufanya doria zao. Lakini pia anafika wakati anawagawia hata posho ili lengo na madhumuni shughuli za ulinzi katika Jimbo lake ziendelee. Lakini kingine ni doria, misako na operesheni mbalimbali tunaziendesha katika Jimbo hili, ili lengo na madhumuni wananchi waishi kwa amani. Lakini kikubwa ziara za Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa tutajitahidi tuziongeze katika Jimbo hili na maeneo mengine ili lengo na madhumuni wananchi waweze kujua wajibu wao na waishi kwa ulinzi, amani na utulivu. Nashukuru.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini ni lini hasa Serikali itaanza kugawa vitambulisho vya Taifa kwa wale ambao wameshasajiliwa hasa waliosajiliwa zaidi ya miezi sita ama zaidi ya miaka miwili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Ninafahamu Bungeni hapa tumesema tumejadili changamoto ya Vitambulisho vya Taifa tukaeleza, lakini tukasema changamoto ile imeshakwamuliwa baada ya ku-review ule mkataba na kuuhuisha, tukasema kinachosubiriwa ni mzalishaji kuanza kutengeneza vitambulisho hivi. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge ni kweli wananchi ambao kwa miezi Sita iliyopita wamesajiliwa na kutambuliwa na wakapewa namba baada ya Mkandarasi kuanza kuzalisha vitambulisho hivyo watapewa kipaumbele watu hawa ambao wamekaa muda mrefu bila kupewa kadi zile za vitambulisho. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. IDRISSA JUMA ABDUL-HAFAR: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu haya ya Mheshimiwa Waziri, lakini kumekuwa na ongezeko la malazi ya kisukari, malazi ya moyo pamoja na kansa kwa watoto walio chini ya miaka mitano na hata watoto kwa mujibu sheria za nchi zetu walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Je, Serikali haioni sasa iwe na utaratibu maalum wa kuhudumia kwa asilimia mia moja matibabu ya malazi yasiyoambukiza kwa watoto wote walio chini ya miaka 18? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli suala la kuhudumia watoto chini ya miaka mitano ni suala ambalo kiutaratibu wanatakiwa kupata huduma bure, bila malipo yoyote. Ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya kwamba wanahitaji huduma lakini baadhi ya dawa zinakosekana. Pia, tuna mzigo mkubwa kweli wa magonjwa hayo yasiyoambukiza, ndiyo maana tunaleta Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote wenye lengo la kusababisha sasa matatizo anayoyataja Mheshimiwa Mbunge yaweze kusuluhishwa.

Mheshimiwa Spika, ukiona uwekezaji mkubwa ambavyo umewekezwa kwenye miundombinu, vifaa tiba na tunaona mwaka huu kuna bilioni 10.7 zinaenda kutumika ni kwa ajili ya kuhakikisha wale wasiojiweza pia wanapata huduma bila malipo.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningetamani pia kujua kwa niaba ya muuliza swali Je, ni Balozi ngapi ambazo walau zimeshakuwa na viwanja japokuwa hazijafungua ofisi rasmi kuelekea kuwa na Ofisi rasmi katika Makao Makuu ya nchi?

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Balozi zote nchini zimegawiwa viwanja Dodoma na Taasisi zake na kila Ubalozi ulitengewa karibu heka tano tano kwa ajili ya kuwekeza makazi yake pale. (Makofi)
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri. Kwa niaba ya Mheshimiwa Kassim sasa mawasiliano haya ya Serikali yatakwisha lini, ikizingatiwa Serikali yote ipo Dodoma, ili mchakato huu uanze kufanya kazi. Ninashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdul-hafar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali ipo Dodoma lakini taasisi zenye kutoa vitambulisho siyo zote ziko Dodoma, ambacho tunaweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba mazungumzo yanaendelea Wizara itafuatilia na ple ambapo kutakuwa na mkwamo basi ngazi za Wizara tutazungumza kwa sababu imeonekana nia ya Watanzania ni kupunguza idadi ya vitambulisho ambavyo mtu anabeba ili kuwa na kitambulisho kimoja chenye taarifa zote. Ninakushukuru.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika nashukuru, nina swali moja la nyongeza.

Je, Serikali imeshapeleka elimu kwa Wakuu wa Shule na Kamati za Shule hasa shule za Serikali zilizoko vijijini kwamba ipo huduma hii ya afya kwa watoto na inaweza kupatikana kupitia shule? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, anasema kama Serikali imeshapeleka. Ni kweli tumeshaanza kupeleka na kwa sababu suala la elimu ni endelevu, tunaendelea kupeleka, lakini pia nilitumie Bunge lako tukufu, nawaomba Wabunge kwenye mikutano yetu ya kwenye Wilaya zetu, tuendelee kuwasisitiza wananchi na watu wengine na Serikali ya Wilaya na watu wengine kuhakikisha wanahamasisha hili na kuwapa taarifa wazazi, tufanye hilo kwa pamoja.

MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini ningependa kujua: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na Maafisa Maalum walio chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakaokuwa wanasimamia fedha hizi kwa upande wa Zanzibar badala ya kutegemea Maafisa wa Serikali ya Mapinduzi ambao hawawajibiki moja kwa moja katika Bunge letu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdul-hafar Idrissa Juma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali hilo, kwa ruhusa yako naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Abdul-hafar kwa namna anavyopigania Mfuko wa Jimbo kwa Jimbo lake na majimbo mengine ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Sheikh Abdul-hafar swali lako kama ushauri tumelichukua tunakwenda kushauriana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tuone kama ufanisi utapatikana zaidi kwa kuweka Maafisa kule basi Serikali yako ni sikivu na inaweza ikafanya hivyo. (Makofi)