Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Latifa Khamis Juwakali (14 total)

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, ni lini vijana wa Tanzania watapewa stadi mbalimbali za kuwaongezea ujuzi wa maarifa kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Wananchi Kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum, Tanzania Zanzibar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwapatia vijana ujuzi wa stadi za kazi na maarifa kama hatua mojawapo ya kuwawezesha vijana kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi, Serikali kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi imetoa stadi mbalimbali za kazi kuongeza ujuzi kwa vijana kama ifuatavyo:-

(i) Jumla ya vijana 5,538 wamepatiwa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi (Apprenticeship) katika fani za ufundi stadi katika nyanja mbalimbali kupitia Taasisi ya Don Bosco na Vyuo vilivyoko chini ya VETA;

(ii) Serikali imeingia mikataba na VETA kwa kushirikisha ujuzi kwa vijana katika Mikoa yote nchini katika fani za ufundi wa magari, useremala, uashi, upishi, huduma za vyakula na vinywaji, ufundi umeme, uchomeleaji vyuma, ufundi bomba, uchongaji wa vipuri na ushonaji wa nguo. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 kufikia Februari, 2021 jumla ya vijana 10,178 walikuwa wamerasimishwa na kati ya hao vijana 28 ni watu wenye ulemavu; na

(iii) Vijana wanaohitimu elimu ya juu wanaendelea kupata mafunzo ya uzoefu kazini ambapo Serikali imeendelea na zoezi la kuwashikiza wahitimu kwa waajiri. Kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Februari, 2021, wahitimu 1,203 wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Kati wamekamilisha mafunzo ya uzoefu kazini kupitia viwanda, taasisi na makampuni mbalimbali ya sekta binafsi na umma nchini. Wahitimu 2,037 wanaendelea kupata ujuzi na uzoefu katika taasisi mbalimbali ambazo ni za binafsi na za umma na kati yao, wahitimu 92 ni watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, programu zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinashauriwa kuhakikisha zinawajengea wadau wake stadi za ujuzi mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya programu husika.
MHE. BAKARI HAMAD BAKARI - K.n.y. MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuwapatia Bima ya Afya wanafunzi wa elimu ya juu na wanaosubiri kupata ajira?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za bima ya afya kwa kuongeza kitita cha huduma na upatikanaji wa huduma kwa wanachama kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuwawezesha wananchi wengi kujiunga katika mfumo wa bima ya afya na hivyo kuwa na uhakika wa kumudu gharama za matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati inayotekelezwa ni pamoja na utekelezaji wa bima ya afya kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao hujiunga kwa kuchangia na kunufaika na huduma za bima ya afya kwa mwaka mzima. Vilevile kwa wale wanaosubiri kupata ajira, Mfuko wa Maendeleo wa Bima ya Afya una utaratibu wa umeandaa utaratibu wa vifurushi ambavyo vimezingatia uhitaji wa aina ya huduma, umri na ukubwa wa familia kwa kuwapatia wanachama wigo na kuchagua aina ya kifurushi kwa kulinganisha na mahitaji yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa kutambua umuhimu wa kila mwananchi kuwa na Bima ya Afya, Serikali inakamilisha rasimu ya muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao utawasilishwa Bungeni mwezi Juni, 2021. (Makofi)
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mashindano ya michezo mbalimbali kwa kila mwaka wakati wa sherehe za Muungano ili kudumisha hamasa za Muungano kwa vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninakubaliana na Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, kuwa mashindano ya michezo kuelekea maadhimisho ya Muungano yalikuwa yanaleta hamasa kubwa kwa wananchi kila ifikapo Aprili kila mwaka. Kwa kutambua hilo, Serikali italifanyia kazi suala hili na Ofisi ya Makamu wa Rais itaratibu utekelezaji wake kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwani ni ukweli usiopingika kuwa michezo ina umuhimu mkubwa sana katika kudumisha Muungano wetu huu adimu na adhimu. Baada ya utekelezaji huo, Serikali itatoa taarifa, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. LATIFA K. JUAKALI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwahamasisha Vijana kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juakali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha mazingira yatakayoleta tija kwa vijana na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali. Mikakati hiyo ni pamoja na ifuatayo:-

(i) Kutoa mikopo yenye riba nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana, ambapo hadi kufikia Oktoba, 2021 jumla ya vikundi vya vijana 957 vimewezeshwa kupata mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 6.7 ambayo imechochea ufanyaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi;

(ii) Kutoa mikopo isiyo na riba kupitia asilimia nne ya mapato ya ndani ya Halmashauri, ambapo hadi kufikia Juni, 2021 zaidi ya vikundi vya vijana 15,349 vimewezeshwa kupata mikopo yenye thamani ya Shillingi Bilioni 54.7;

(iii) Tumeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali, ambapo hadi sasa Halmashauri 111 zimetenga maeneo yenye ukubwa wa ekari 217,802 ambayo yamewanufaisha vijana 3,232; na

(iv) Tunaendelea kuendesha programu za mafunzo katika fani mbalimbali ikiwemo za ukuzaji ujuzi, Uanagenzi, Urasimishaji ujuzi pamoja na mafunzo ya kilimo cha kisasa. Kupitia mafunzo hayo, vijana 43,881 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi, Vijana 20,334 wamepata mafunzo ya kurasimisha ujuzi na Vijana 12,580 wamewezeshwa kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mikakati hii vijana wameweza kujipatia ajira pamoja na kujikita kwenye miradi ya uzalishaji mali ambayo imeendelea kuchangia ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. LATIFA KHAMISI JUWAKALI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo ya Jeshi kama Chejuu na Dunga, Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA
K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamisi Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Kundi la Vijana kutoka Mkoa wa Kusini Unguja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uthamini na upimaji wa maeneo ya Chejuu, na Dunga huko Zanzibar umekamilika, vitabu vya uthamini vipo Kamisheni ya Ardhi Zanzibar. Aidha, kukamilika kwa zoezi hili kunasubiri kukakamilika majadiliano yanayoendelea kati ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Mara majadiliano hayo yatakapokamilika, Wizara itawasilisha maombi ya fedha kwa ajili ya fidia kwa kutumia kiasi cha fedha kilichotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, aendelee kuwaomba wananchi wa maeneo hayo ya Chejuu, Dunga na maeneo mengine waendelee kuwa na subira wakati tukikamilisha majadiliano hayo. Nakushukuru.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya masomo ya dini kutokuwa principal pass ya kujiunga na Stashahada na Shahada?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu wa uendeshaji wa elimu ya Chuo Kikuu hapa nchini na katika nchi nyingine duniani, Mabaraza ya Vyuo Vikuu (Seneti) yamepewa mamlaka ya kisheria kuweka vigezo mahsusi vya udahili kwa kila programu ya masomo kwa ngazi husika (Specific Program Requirements).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hapa nchini, principal passes za masomo ya dini zinatambuliwa kama vigezo mahsusi vya kujiunga na baadhi ya program za masomo kwa ngazi ya Stashahada na Shahada ya kwanza. Mfano, baadhi ya Vyuo Vikuu ambavyo vimekuwa vikitumia masomo ya dini kama kigezo kimojawapo cha kujiunga na program za masomo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro; Chuo Kikuu cha Zanzibar; Chuo Kikuu cha Arusha; Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania; Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi; Chuo Kikuu Huria cha Tanzania; Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -

Je, ni vikundi vingapi vya vijana wa Zanzibar vimenufaika na mikopo au uwekezaji kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umeanzishwa kwa Sheria ya Fedha Namba 6 ya 2001 (The Public Finance Act, 2001) chini ya kifungu namba 45, ikisomwa sambamba na kifungu namba 12 cha sheria hiyo, ambapo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana hutoa huduma ya mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana Tanzania Bara tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar upo Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao pia unahudumia vijana na wana mpango maalum unaowahudumia vijana wa Zanzibar chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, na Michezo na unaendeshwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivyo, kwa pande zote mbili za Muungano tuna ushirikiano wa karibu katika masuala yote ya maendeleo ya vijana na kubadilishana uzoefu, lakini pia masuala ya utatuzi wa changamoto kwa ajili ya kuwajenga vijana katika kuweza kupata fursa za ajira na mitaji. Ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. LATIFA K. JUWAKALI aliuliza: -

Je, upi mkakati wa Serikali wa kukuza ujuzi na stadi kwa vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifah Khamis Juakali Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukuza ujuzi na stadi za kazi kwa vijana, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kukuza Ujuzi wa miaka 10 (2016/2017 na 2025/2026) ambapo umelenga kuhakikisha nguvu kazi ya vijana inashiriki katika kujenga uchumi wa Taifa. Mkakati huu unatekelezwa kupitia program na mipango mbalimbali ya kukuza ujuzi na stadi kwa vijana inayotekelezwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Baadhi ya programu na mipango hiyo ni pamoja Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambayo tangu kuanza kutekelezwa mwaka 2016/2017 imetoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kwa jumla ya vijana 118,415 na Mpango wa Mafunzo na Uwezeshaji wa Vijana kushiriki kilimo unaotekelezwa na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu lakini kutekelezwa na Wizara ya Kilimo, ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -

Je, zimebaki changamoto ngapi za Muungano kutatuliwa baada ya kufanyika jitihada za kuzipunguza?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, changamoto au hoja Muungano zilizobaki na ambazo zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi ni nne (4). Hoja hizo ni Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Usajili wa Vyombo vya Moto, Uingizaji wa sukari inayozalishwa Zanzibar katika Soko la Tanzania Bara, na Mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu.

Mheshimiwa Spika, changamoto hizo zipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na ni matumaini ya Serikali zetu mbili kuwa changamoto zote zitapatiwa ufumbuzi.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, ni mafunzo ya aina gani yanatolewa kwa vijana wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inatoa mafunzo ya ujuzi Stadi na stadi za kazi kwa nguvu kazi ya vijana iliyopo katika soko la ajira, yaani kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo yanayotolewa ni: -

(i) Mafunzo ya kukuza ujuzi wa ufundi katika fani mbalimbali kwa njia ya Uanagenzi yaani Apprenticeship training ambapo kijana anatumia zaidi ya 60% ya muda wa mafunzo katika maeneo ya kazi;

(ii) Mafunzo ya kurasimisha ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo yaani Recognition of Prior Learning Skills ambapo vijana wanafanyiwa tathmini ya mapungufu waliyonayo, kupatiwa mafunzo na hatimaye kupatiwa vyeti ambavyo vitawasaidia kuendelea na mafunzo ngazi zinazofuata kwa ajili ya kuajiriwa au kujiajiri;

(iii) Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi kwa wahitimu yaani Internship Training ambapo wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu wanapelekwa maeneo ya kazi kujifunza kazi;

(iv) Mafunzo ya kukuza ujuzi kwa wafanyakazi waliopo makazini yaani Skills Updating and Upgrading ili kuziba mapengo ya ujuzi yanayotokana na mabadiliko ya teknolojia na utendaji wa kazi na utoaji wa huduma;

(v) Mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara, miradi, Urasimishaji na Uendelezaji. Mafunzo haya huenda sambamba na utoaji mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana;

(vi) Mafunzo ya Stadi za Maisha kwa Vijana hasa wale walio nje ya mfumo wa shule ili kuwawezesha kujitambua, kuwa na uzalendo na kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao, ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Bodi ya Mitaji kwa wahitimu wa elimu ya juu kama ilivyo kwa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilianzishwa mwaka 2004 ili kuweka utaratibu wa kisheria unaowawezesha wanafunzi wahitaji wenye sifa ya kujiunga na vyuo vikuu kumudu gharama za elimu ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, hata hivyo, Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa vijana kupitia halmashauri kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani. Nashauri wahitimu wa elimu ya juu kutumia fursa hiyo kupata mitaji. Nakushukuru sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, Serikali imefanya tathmini ya mafunzo wanayopatiwa vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza mafunzo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Rashid Shangazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo iliandaliwa baada ya kufanya utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 ambapo ulionesha kiwango cha ujuzi wa nguvu kazi ya Taifa ni asilimia 3.6 kwa ujuzi wa juu, asilimia 16.4 kwa ujuzi wa kati na asilimia 79.9 ujuzi wa kiwango cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022 Serikali ilifanya tena utafiti wa nguvukazi na kuonesha kiwango cha ujuzi wa nguvukazi kimeanza kuwa bora na nguvukazi yenye kiwango cha chini cha ujuzi ilifikia asilimia 76.9 ya nguvu kazi kutoka asilimia 79.9 na kiwango cha kati kimefikia asilimia 19.9 ya nguvukazi kutoka asilimia 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kujiridhisha na ubora wa mafunzo yanayotolewa kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Serikali imepanga kufanya tathmini ya mafunzo yanayotelewa kwa kufanya tracer study katika mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, Serikali imefanya tathmini ya mafunzo wanayopatiwa vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza mafunzo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Rashid Shangazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo iliandaliwa baada ya kufanya utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 ambapo ulionesha kiwango cha ujuzi wa nguvu kazi ya Taifa ni asilimia 3.6 kwa ujuzi wa juu, asilimia 16.4 kwa ujuzi wa kati na asilimia 79.9 ujuzi wa kiwango cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022 Serikali ilifanya tena utafiti wa nguvukazi na kuonesha kiwango cha ujuzi wa nguvukazi kimeanza kuwa bora na nguvukazi yenye kiwango cha chini cha ujuzi ilifikia asilimia 76.9 ya nguvu kazi kutoka asilimia 79.9 na kiwango cha kati kimefikia asilimia 19.9 ya nguvukazi kutoka asilimia 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kujiridhisha na ubora wa mafunzo yanayotolewa kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Serikali imepanga kufanya tathmini ya mafunzo yanayotelewa kwa kufanya tracer study katika mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kutenga walau asilimia tano kwa kila mradi wa kisekta ili kuwagusa vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na kuthamini umuhimu wa kuwawezesha vijana katika kila sekta. Kwa sasa, Serikali inawezesha makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na: -

(i) Kutenga 30% ya zabuni itakayotekelezwa katika Halmashauri zote nchini;

(ii) Kupitia mapato ya ndani ya halmashauri zote nchini, Serikali imeendelea kutenga 10% ya mapato; asilimia nne kwa ajili ya vijana, asilimia nne kwa ajili ya wanawake, na asilimia mbili kwa ajili ya watu wenye ulemavu kwa masharti nafuu; na

(iii) Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana inawezesha miradi ya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kutathmini na kuboresha sera na miongozo yake ili kuhakikisha kuwa vijana wanaendelea kutengewa fedha kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza miradi pamoja na kuwekewa sera rafiki zaidi kuwawezesha kujipatia mitaji, ahsante.