Supplementary Questions from Hon. Latifa Khamis Juwakali (9 total)
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini ninaa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kati ya hao vijana 5,538 ambao wamepatiwa ufundi au mafunzo stadi ni wanufaika wangapi wanatoka Zanzibar?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, baada ya mafunzo hayo, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwatafutia miradi ama fursa mbalimbali ili waweze kujiajiri na kuajirika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kuhusu swali la kwanza, nikubaliane nawe lakini pia mbali na takwimu suala hili limekuwa likifanywa na Wizara ya Michezo, Vijana na Utamaduni kwa upande wa Zanzibar. Kwa hiyo, tutapata takwimu hizo na tutaziwakilisha kwa sababu suala hili kwa upande wa Bara na Zanzibar kuna parallel program lakini zaidi tunashirikiana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, ni kweli kwamba vijana hawa wanapomaliza kupewa mafunzo na stadi za kazi wanazopewa, Serikali imeweka mpango katika mifumo miwili.
Kwanza, kuna Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo vijana hawa baada ya kupewa stadi hizi za kazi wanaweza kuwezeshwa katika hatua ya pili baada ya kuwa wamebuni miradi ambayo ni endelevu na ambayo inaweza ikawasaidia vijana kuweza kujikimu katika maisha yao lakini pia kuweza kufanya biashara au kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye sekta za kilimo. Kwa mfano, kwa kipindi cha mwaka wa jana katika halmashauri 84 yalitolewa mafunzo na kampuni tatu hizi hizi za vijana waliopata mafunzo na wakapewa fedha zaidi ya shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kutengeneza vitalunyumba ambapo zoezi hilo limefanyika katika halmashauri 84. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili fedha hizi za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwenye halmashauri kwa maelekezo hayo hayo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wetu wa Nchi, Mheshimiwa Jenista Mhagama wamekuwa wakisimamia ambapo fedha zimekuwa zikitolewa na halmashauri kupitia 4:4:2 kwa maana ya asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu katika halmashauri zote. Fedha hizi zinakusudia kuwapa vijana mikopo au fursa ya kuweza kujiendeleza katika maeneo ambayo watakuwa wameendelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo katika eneo hilo hilo ni agizo la Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mpango ambao umewekwa kwamba katika Halmashauri zote yametengwa maeneo ya vijana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watakapotaka kujiingiza kwenye kilimo au fursa zozote wanaweza wakapewa. Mathalani ukiangalia Kahama kuna eneo la Zongomela ambapo vijana waliopata mafunzo ya ufundi stadi wameweza kupata eneo lile na wanatengeneza samani mbalimbali ikiwemo grill, vitanda lakini pia wanauza mbao. Ukienda eneo la Mvomero vilevile kuna garage ziko pale zimetengenezwa hata maeneo ya Misungwi na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kifupi tu nimwambie kwamba vijana hawa wanapopata stadi hizi za kazi bado hawaachwi hivi hivi tunaendelea tena kuwalea ili kuhakikisha kwamba zile stadi na skills walizozipata zinawasaidia katika kujikwamua kwenye maisha yao. Nashukuru.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mbali na majibu mazuri yaliyojibiwa na Mheshimiwa Waziri, lakini bado nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kama ni hivyo ndivyo, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha kwamba katika hayo mashindano ambayo mnaenda kuyaandaa yanaenda kuwaunganisha vijana wa kike na wa kiume moja moja kwa moja au asilimia 50 ya wanawake na asilimia 50 ya wanaume katika hayo mashindano? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kama hivyo ndivyo, Mheshimiwa Waziri ni lini mashindano hayo yataanzishwa kwa sababu tayari tulishaona katika mpango kazi mmetuambia kwamba hayo mashindano yataanza. Nahitaji commitment ya Serikali, ni mwaka gani hayo mashindano yataanza? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri wangu kwa majibu mazuri, lakini nimpongeze dada yangu Latifa kwa sababu miongoni mwa vijana ambao wamewakilisha Tanzania mwaka huu katika mjadala wa siku ya Muungano, Latifa alikuwa mmojawapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hilo, suala zima la kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki kwa uzuri zaidi, tutalifanyia kazi. Na bahati nzuri kama unavyofahamu Serikali ya Awamu ya Sita imejielekeza huko kuhakikisha mchanganyiko wa jinsia zote mbili zinashiriki vizuri. Wasiwasi wangu ni kwa wanaume tusijetukajikuta kwamba idadi ya wanaume ikawa ndogo kuliko idadi ya wanawake katika michezo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika upande wa commitment jambo hili kwa sababu suala zima la uratibu na Wizara ya Michezo kule Zanzibar na Wizara ya Michezo hapa Bara tutalifanya, baadae tutatoa taarifa rasmi katika suala zima la mchakato wa michezo hiyo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya maeneo yanayoweza kuongeza ajira kwa vijana ni eneo la kuongeza thamani kwenye bidhaa. Je, Serikali inamkakati gani wa kuja na programu zinazoweza kuwasaidia vikundi vya vijana vinavyopata mikopo ya halmashauri kuweza kuongeza thamani kwenye bidhaa ambazo inazalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; ni kutokana na mabadiliko mbalimbali ikiwemo ya Sayansi na Teknolojia zipo ajira mbalimbali zinazoweza kuzalishwa kutokana na mabadiliko hayo. Je, Serikali inamkakati gani wa kufanya maboresho ya sera ya vijana ili vijana waweze kupata ajira kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea hususani katika Sekta ya Sayansi na Teknolojia. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwanza kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Judith Kapinga amekuwa akifanya kazi kubwa ya kutushauri Serikali katika eneo hili hongera sana Mheshimiwa Judith. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la kwanza anauliza kuhusu kuongeza thamani, Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tunaendelea kuhakikisha kwamba tunawaunganisha vijana na fursa hizi mbalimbali tunashirikiana na wenzetu wa SIDO na UNIDO tuna mfano hai wa vijana wetu wa Kampuni ya JATU wanafanya vizuri kuongeza thamani, mazao.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna vijana wa Kiwanda cha Chaki kule Maswa, tuna vijana pia wa Kiwanda cha Mabegi Mwanza na vijana wengine na tunaendelea bado kuhakikisha kwamba vijana wetu wanaongeza thamani vitu wanavyozalisha badala ya kuuza raw material na tutaendelea kuendelea kutilia mkazo katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anataka kufahamu ni lini tutaleta sera hii; tupo katika hatua nzuri na tayari kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumeshakusanya maoni kwa wadau wote wanaohusika na masuala ya vijana na tumemaliza sasa tuna rasimu ya kwanza ambayo inafuata utaratibu wa kiserikali na baadaye tutaendelea kuwafahamisha kwamba tumefika hatua gani, lakini tunaweza kuahidi tu kwamba kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha tutakuwa tayari tuna sera ya vijana. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nikushukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanakwenda kuwatia moyo wananchi.
Kwa kuwa suala hili Wizara mmesema kwamba lipo katika mchakato na wananchi hawa bado sasa hivi wanaendelea kuwa na matumaini makubwa, lakini bado wanakosa kushiriki shughuli zao za kiuchumi ikiwa suala la kilimo, suala la ufugaji kwa sababu tayari walishafanyiwa tathmini.
Je, Serikali mnatoa kauli gani kwa wananchi hawa ili waendelee kuwa na matumaini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri wananchi hawa itakapokuwa imetoka hiyo fidia; je, muda huo ambao mtakuwa tayari mmeitoa hiyo fidia inakwenda kuendana na thamani ya fedha katika kipindi hicho yaani value for money? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, Mheshimiwa Latifa Khamisi Juakali kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika jibu la msingi tayari kuna majibu yanayowapa wananchi matumaini, niwaambie tu Mheshimiwa Mbunge wananchi waendelee kuwa na matumaini kwa sababu azma ya Serikali hii ni kuhakikisha kwamba tunaondosha migogoro yote ambayo inakabili baina ya vyombo vyetu vya ulinzi na wananchi; na ndiyo maana katika jibu la msingi tukasema kuna majadiliano yanaendelea baina ya SMZ na Jeshi la Wizara ya Ulinzi. Lakini pia tukasema kwamba tayari tumeshaomba fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa ahakikishe watu wake wanaendelea kuwa na matumaini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine kikubwa ni kwamba tutahakikisha kwamba thamani zitakwenda kwa mujibu wa mali zao, ikiwa vipando, ikiwa nyumba, lakini Serikali haitawadhulumu, itahakikisha kwamba wanapata kile ambacho wanastahiki. Nakushukuru.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa, sasa Serikali imetuelezea kwamba kuna vyuo mbalimbali ambavyo vinatoa elimu ya juu ambayo inazingatia hiyo principal pass. Je, hamuoni sasa Serikali kuandaa Mpango maalum kupitia TCU ambao ndiyo wadhibiti ubora wetu wa Elimu ili waweze kuwashauri sasa Vyuo Vikuu vyetu waweze kuliingiza ili somo la dini liwe kama ni miongoni mwa Principal pass?
Swali langu la pili, kwa kuwa masomo haya ya dini yanawajenga vijana wetu kimaadili lakini pia yanawajenga wanafunzi wetu wetu kimaadili lakini na kiimani. Je, hatuoni sasa kulitoa hili somo la dini kwamba siyo miongoni mwa principal pass ambazo zitamsaidia mwanafunzi kujiunga na Chuo Kikuu, hatuoni sasa tunawaandaa wanafunzi wengi ambao wakimaliza Vyuo Vikuu watakuwa hawana maadili mazuri kwa sababu wanafunzi hawatalisoma hili kama ni somo la msingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Latifa Juwakali kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha kueleza kwenye majibu ya msingi kwamba masomo haya ya dini yanatumika kwenye baadhi ya Vyuo na kwenye baadhi ya program. Hatuwezi program zote tukasema kwamba ziingize masomo ya dini, kwa sababu itategemea na program gani mwanafunzi anayokwenda kusoma. Kwa hiyo, tumebeba ushauri huo alioutoa lakini ninaomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba TCU jukumu lake ni kudhibiti, kufanya Ithibati ya ubora wa masomo yanayotolewa na siyo kupanga kwamba program gani iingizwe na kwa requirement zipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza zile Senate ndizo zenye wajibu wa kupanga namna gani requirements zinazotakiwa kwenye program husika. Kwa hiyo, tunalibeba suala hili la kuona namna gani masomo yetu ya dini yanaweza yakaingizwa kwenye baadhi ya hizo program kwa kadri tutakavyoona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; mfuko huu upo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali haioni haja sasa ya kuendelea kutoa fedha hizo kwa vijana wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, mbali na mikopo kuna fursa nyingine zipi zinaweza kupatikana katika Ofisi ya Waziri Mkuu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi la awali, suala hili linaongozwa kwa mujibu wa sheria ya fedha ambayo ni Sheria Namba 6 mwaka 2001, kwa masuala ambayo hayahusiana na Muungano. Lakini kwa kuwa tuna mashirikiano mazuri na upande wa Tanzania Zanzibar tutaendeleza ushirikiano huo katika masuala ya mafunzo kupeana fursa za mitaji na ajira kama jinsi ambavyo Wizara hizi zimekuwa zikishirikiana kwa karibu sana kwa kipindi chote.
Kwa hiyo, tutaendelea ushirikiano huo mzuri na tunashukuru kwa wazo hilo ambalo umelitoa na sisi tutalifanyia kazi tuone namna gani bora la kuweza kulirasimisha na pengine hata ikilazimisha kubadilisha sera au sheria tutalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine kusuasua kwa utekelezwaji wa changamoto inapelekea kuibuka kwa changamoto mpya za Muungano. Ni nini commitment ya Serikali kuweza kuzuia changamoto yoyote nyingine ya Muungano isijitokeze?
Swali langu la pili, Serikali inatoa commitment gani ya kutatua changamoto hizi nne zilizobakia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nikianza na swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge namna ya kuzuia changamoto nyingine mpya zisijitokeze, hili ni juhudi ya Serikali zote mbili kuhakikisha wakati wote mara baada ya maamuzi yale yanayojitokeza katika vikao vile vya majadiliano vilivyotatua ile migogoro kuanza utekelezaji mara moja wa yale makubaliano waliyofikia.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, hizi changamoto nne zilizobaki mkononi tunatarajia kwamba kikao chetu kitakuwa mwezi wa Agosti, ambapo katika mazingira ya kawaida hizi zilizobaki ni chache sana tunaweza tukafika mahali, Mungu jalia tutazimaliza zote nne na watu tutaanza kufaida matunda ya Muungano wetu. Ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nachukua nafasi hii kuipongeza Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya kwa vijana nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; je, Wizara mnampango gani au mnafanya utafiti kuona mafunzo haya jinsi gani yanawanufaisha vijana hao mara baada ya kumaliza mafunzo hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; nataka kujua kama Wizara mnamkakati gani sasa wa kuweza kuwaongezea au kuwapa mitaji mikubwa zaidi kwa vile vikundi ambavyo vinafanya vizuri zaidi ili kuweza kuzalisha bora zaidi na kuzalisha vitu vizuri zaidi ili kuendelea kujiajiri na kuajiriwa ili kuweza kuongeza mapato kwa nchi yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Latifa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunao mpango wa ufuatiliaji na tathmini ambao kila baada ya miezi mitatu tunafanya kupita kwenye maeneo ambayo vijana hawa wapo wakipata mafunzo lakini pia wale ambao wanapewa mitaji mbalimbali. Tumekuwa na utaratibu wa kufanya ufuatiliaji na tathmini ili kubaini na kuona kama kuna tija katika fedha ya nyingi ya Serikali ambayo inatolewa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweza kuwawezesha vijana kujikimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye hatua ya pili ambapo ameniuliza swali kama tunawapa mitaji? Ni kweli kwamba vijana hawa hatuwaachi tu kwa maana ya kuwatambua na kuwapeleka kwenye maeneo yao ya kupata mafunzo na wanapomaliza kupata mafunzo tunawaunganisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo ambao tunawapeleka VETA, wapo amabao tunawaunganisha kama wamefuzu vizuri kwenda kwenye maeneo ya ajira. Lakini pia tunwaratibu na kuwasaidia kuweza kupata ile mikopo ya 10% ya halmashauri ambapo mwongozo kwa sasa nikijibu swali la kwamba tuwape mitaji inayojitosheleza, tilikua tunatoa kwa vikundi vya watu 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hatua ya sasa na kwa Mwongozo mpya na kwa usikivu wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa vijana aliona ni vema aweze kubadilisha badala ya kuwapa vijana 10, sasa tunatoa mkopo kwa kuanzia shilingi milioni moja mpaka shilingi milioni 10 tumetoka sasa shilingi milioni 10 mpaka shilingi milioni 50 kwa kijana mmoja mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hatua nyingine tunawasaidia pia kuweza kupata mikopo kupitia benki. Zipo benki ambazo zimekwisha kuanza kuonesha mfano. Benki a Azania inatoa mikopo kwa single digit kwa sasa lakini zaidi ya hapo pia tunayo mifuko mingine, katika Wizara ya Kilimo tunao Mfuko wa Pembejeo za Kilimo ambapo vijana hawa nao pia wakimaliza kwenye mafunzo mbalimbali iwe VETA au kule kwenye programu za unenepeshaji ng’ombe au BBT tunawaendeleza kwenda mbali zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni ninayo furaha kukwambia tumepeleka vijana tena awamu nyigine ambao watafikia sasa 700 wanaoenda kupata mafunzo nchini Israel ili kuweza kuwatengeneza vijana na kuweza kuhakikisha kwamba kwa kweli wanatumia fursa za kiuchumi na kushiriki ujenzi wa Taifa lao, ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nikushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali nilikuwa na swali moja la nyongeza.
Je, Serikali inatoa tamko gani sasa kuhakikisha kila muhitimu anapewa kipaumbele anaporudi au anapomaliza au anapohitimu katika elimu yake ya elimu ya juu ili aweze kupata mikopo katika halmashauri waweze kujiajiri na ili kuweza kurejesha mikopo kwa wakati? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba halmashauri zetu zimekuwa zikitenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo ambayo ni kwa ratio ya 4:4:2 asilimia nne kwa vijana, asilimia nne kwa wanawake na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ile inatolewa kwa mujibu wa sheria na zipo kanuni ambazo tumekwenda kuzifanyia marekebisho mwanzoni ilikuwa vijana ni lazima wawe vijana 10 katika kikundi lakini hivi sasa ni vijana tano tu wanaunda kikundi wawe na shughuli maalum ya kufanya na mikopo ile wanaweza kupata.
Kwa hiyo, sisi kauli kama Serikali ni kuwahakikishia tu vijana kwamba wajiunge kwenye vikundi ambavyo ni vya ujasiriamali na sasa hivi haihitajiki kwamba iwe tayari umeshaanza kufanya shughuli hata kama una wazo tu lakufanyakazi fulani au shughuli fulani mikopo ile unaweza kupata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kauli yetu kwa vijana hawa wajiunge kwenye vikundi na kutumia kanuni zile zilizopo kuhakikisha kwamba halmashauri zetu zinawapata mikopo hii ili waweze kukidhi maisha yao, lakini waweze kurejesha mikopo ile elimu ya juu waliyoichukua. Nakushukuru sana.