Contributions by Hon. George Natany Malima (18 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, na mimi niungane na wenzangu wote kukupongeza na kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia. Ni Mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili tukufu. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Malima tumefurahi kwa sababu kiti ulichokikalia ndio kilekile cha Mpwapwa. (Makofi/Kicheko)
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nilipoambiwa asubuhi nilifurahi sana. Nimeambiwa kiti hiki Senetor alikuwa analia sana kwa ajili ya barabara, barabara ya kutoka Kongwa kwenda Mpwapwa na mimi leo nimesimama mbele ya Bunge lako kushukuru sana kwa ajili ya nafasi hii, lakini pia nishukuru Chama changu cha Mapinduzi ambacho kilinipa ridhaa ya kugombea na nilishinda kwa kishindo, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais. Kusema kweli hotuba yake ndio imebeba mustakabali wa Taifa letu. Ni wajibu wetu sisi kama Wabunge, mawaziri tumasaidie Rais kutafsiri maono yake katika njia ya utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzangu wote wamesema habari ya TARURA na mimi ni muhanga wa TARURA. Kwenye jimbo langu la Mpwapwa barabara ni mbaya sana kwa sababu kwanza jiografia ya Mpwapwa ni eneo lenye vilima vingi, kwa hiyo, mvua zikinyesha maji yanaporomoka yanakata barabara, leo hali ya barabara za vijijini kule Mpwapwa ni mbaya sana na mimi nisiseme sana, ningependa tu kusema naomba sana bajeti ya TARURA iongezwe na niseme tu ifike hata asilimia 45 inaweza kusaidia kupunguza tatizo la barabara za vijijini.
Mheshimiwa Spika, lakini tatizo lingine kubwa ni la upande wa TANROADS. Barabara hii ya kutoka Kongwa kwenda Mpwapwa ni barabara yenye urefu mfupi sana, ni barabara yenye takribani kilometa 32, lakini barabara hii imedumaza sana uchumi wa Mji wa Mpwapwa na watu wake. Hakuna mtu angependa kwenda Mpwapwa leo kwa sababu ya ubaya wa barabara ile. Barabara hiyo Senator Lubeleje amelia sana miaka ya nyuma. Sasa naomba Serikali ifike wakati kilio chetu cha watu wa Mpwapwa kisikike ili barabara hii itengenezwe, ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi. Na mimi naamini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itasaidia barabara hii kujengwa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuzungumza ni wazo zuri la Mheshimiwa Rais kuamua kutoa elimu bure kwa watoto wetu wa kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Wazo hili ni jema sana, lakini wasiwasi wangu nimeona kwamba tusipomsaidia Rais sisi kama Serikali wazo hili mwisho wa siku tutakuwa na wanafunzi wengi wanamaliza shule darasa la saba na wengine wanamaliza kidato cha nne hawajui kusoma na kuandika kwa sababu idadi ya wanafunzi wanaoingia katika darasa la kwana na kidato cha kwanza haiendani na idadi ya walimu.
Mheshimiwa Spika, walimu hawatoshi kwa kipindi kifupi nilichokaa Jimboni nimegundua kuna upungufu mkubwa sana wa walimu karibu kila shule walimu hawatoshi naomba sana Wizara ya Elimu ijaribu kutafuta namna ya kuongeza walimu katika shule za msingi na shule za sekondari.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningeweza kuzungumza ni juu ya umeme, nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa kazi njema sana ambayo ameifanya kuleta umeme katika nchi hii. Lakini mimi naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri ukiangalia, ukipita kwenye vijiji umeme umepita kwenye centers za vijiji haujapanuka nimesikia asubuhi kwamba mpango wa Serikali ni kujenga mpaka kwenye vitongoji kuweka umeme, basi wanapoenda kuweka umeme kabla ya vitongoji, lakini vile vijiji vikamilike ukienda kila kijiji bado kuna kilio watu wanataka umeme umepita katika eneo la center lakini maeneo mengine bado hayajafikiwa. Kwa sababu ya kazi nzuri ya Waziri naamini mpaka miaka mitano itakapofika kazi hii itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Spika, tatizo la maji ni tatizo ambalo pia katika Jimbo langu linaendelea na ni kubwa naomba sana Serikali ushauri wangu ni kwamba wakati mwingine tunataka kupata miradi mikubwa sana kwenye vijiji ya maji, lakini hebu nishauri badala ya kushauri miradi mikubwa ya kuweka network ya maji kwenye vijiji tuchimbe angalau kisima kimoja tu wakati tunasubiri upembuzi yakinifu, tunasubiri tathmini watu wawe wanakunywa maji hata kwenye kisima pale tu peke yake, halafu hayo mengine yatafuata kuweka networking na nini sasa hivi maeneo mengi hakuna maji vijijini watu wanaendelea ku-suffer na Mheshimiwa Rais amezungumza kwamba inapofika 2025 kila kijiji kitakuwa na maji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga hoja 100%.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Kwanza kabisa, kabla sijachangia naomba kutoa pole kwa Watanzania wote kwa ajili ya msiba mkubwa ambao ulitupata tarehe 17 wa Mheshimiwa wetu Rais, Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli. Pia nitoe pole kwa Rais wetu wa sasa, Mheshimiwa Mama Samia Hassan Suluhu kwa ajili ya msiba huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie na nitaanza na kuzungumzia ukurasa wa 67 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Katika ukurasa huo wa 67,
Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza nia ya Serikali ya kuanza Awamu ya Pili ya ujenzi wa Mji wa Kiserikali wa Mtumba. Jambo hilo limenipa faraja sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dodoma ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na wafanyakazi wengi wamehama kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuwe na makazi ya kutosha ili wafanyakazi hawa wafanye kazi bila kuwa na shida ya upangaji wa nyumba na usumbufu wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ipo miradi ambayo Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakisaidiana na mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu ambaye ni Rais wetu wa sasa, walikuwa wameipanga. Naiomba sana Serikali izingatie sana jambo hilo. Kwanza, kuna Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato. Uwanja huu ni muhimu sana kwa Serikali yetu; kwa uchumi wetu na kwa sababu Dodoma ni Makao Makuu tutakuwa na wageni wengi ambao watatoka nje ya nchi watakuja na ndege kubwa ambazo zitahitaji kutua katika Mji wetu wa Dodoma. Vile vile kutakuwa na mwingiliano wa watu wengi, kwa hiyo, tutaweza kufanya biashara kupitia kiwanja hiki cha ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja huu wa ndege utakuza uchumi wa Jiji la Dodoma kwa sababu watu watafanya biashara mbalimbali. Walioko pembezoni mwa uwanja watafanya biashara kwa sababu kutakuwa na wageni wengi ambao watakuwa wanatua katika uwanja ule na kuondoka. Kwa hiyo, ni muhimu sana tukazingatia kwamba Mji Mkuu wa nchi yetu uwe na uwanja mkubwa wa ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine ni kwamba kuna mpango ule wa kujenga barabara ya kuzunguka Mji wa Dodoma (ring road). Barabara hii ni muhimu sana. Bado ina umuhimu mkubwa, nami nafarijika kwa sababu Serikali yetu imejipanga kutekeleza. Faida kubwa ambayo tutaipata kwenye barabara hii, itasaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji letu la Dodoma. Magari yale makubwa yenye mzigo, yakitoka Dar es Salaam na maeneo mengine, yakiona hayana haja ya kuingia mjini, yatazunguka kupitia hiyo barabara kuelekea Mwanza, Iringa au Arusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, barabara hiyo itatusaidia magari kama malori na wale wa usafiri wa kawaida ambao hawana nia ya kuingia mjini, waweze kwenda haraka na kuzunguka. Hiyo italeta mandhari nzuri sana ya Mji Mkuu wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mkuu hauwezi kukamilika kama hakuna maji ya kutosha. Mji huu watu wameongezeka sana, kwa hiyo, kile kiasi cha maji kilichokuwa kinatosheleza miaka ya nyuma sasa hivi hakitoshi. Tunahitaji kuwa na mkakati wa kuwa na maji ya kutosha katika Jiji la Dodoma. Mpango wa kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria, naomba sana Serikali izingatie; pia kuna Mpango wa kujenga Bwawa la Farkwa ambalo ni jirani sana hapa Chemba, hilo pia litasaidia kuongeza kiwango cha maji katika Jiji letu la Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali izingatie sana hayo. Ili Mji wetu uweze kuonekana kwamba ni Mji Mkuu unahitaji kuwa na mambo hayo muhimu sana. Lazima wageni wetu wakifika wasikutane na shida ya maji. Kwa kweli maji ndiyo sura ya Jiji lolote katika Dunia. Kama hakuna maji, hata wageni wetu watatushangaa, tumeletaje Mji Mkuu Dodoma hakuna maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuhakikishe kwamba tunatoa kipaumbele maji yaletwe Dodoma na yawe ya kutosha, yaendane na idadi ya watu wanaohamia katika Mji wa Dodoma. Baada ya miaka mitano kutakuwa na watu wengi zaidi. Kwa hiyo, suala la maji ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumzia Mji Mkuu wa nchi yetu, naomba kidogo sasa nizungumze katika eneo la kilimo hususan katika eneo la mbegu. Wakulima wetu wengi bado wanalima kilimo cha zamani, cha mazoea. Wanatumia mbegu za zamani ambazo hazina tija. Hii inatokana na ukweli kwamba, pamoja na nia njema na bidii ya Serikali kuendelea kufanya utafiti juu ya mbegu bora zenye tija lakini bado kiwango cha mbegu hakitoshelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kiwango hakitoshelezi, shida imekuwepo kwamba mbegu inayopatikana ni kidogo, kwa hiyo, bei inakuwa kubwa. Tuki- apply ile law of demand; supply ikiwa ndogo, demand kubwa automatically bei itakwenda juu. Mwaka huu wakulima wetu wamenunua mbegu ya mahindi, nami nimenunua pia. Nilikuwa nanunua kilo mbili kwa shilingi 15,000/= just imagine, kijijini nani anaweza kununua mbegu kilo mbili kwa shilingi 15,000/=? Kwa hiyo, unaweza kuona ni kwa kiasi gani bado tunahitaji mbegu bora za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Januari kule kwetu Mpwapwa tulitembelea kiwanda kimoja kimoja kiko kule Morogoro, kinaitwa Mahashree Agro-Processing Tanzania Limited. Kiwanda hiki ni cha watu kutoka India, wanakamua mafuta ya mbegu mbalimbali na tulikwenda baada ya wao kuja Mpwapwa kutafuta Soko la Karanga. Sasa kabla hatujawaunganisha na wakulima wetu tuliona ni vizuri sana tujiridhishe tuone kiwanda hiki kina-capacity ya kiasi gani kununua karanga kwetu. Kwa hiyo, tulienda mimi, Mkuu wa Wilaya na Watendaji wa Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipofika kwenye kile kiwanda tulikuta kweli wana capacity kubwa sana ya kununua mbegu mbalimbali pamoja na karanga. Alichotuambia yule mwenye kiwanda ni kwamba, shida iliyoko katika maeneo yetu ya Mpwapwa na Kongwa, zile mbegu siyo bora, hazitoi mafuta ya kutosha. Kwa hiyo, alikuwa ana-suggest kwamba ni vizuri sana tukapata mbegu ambazo zitakuwa bora, zitakuwa na tija kwa wakulima wetu na zitatoa mafuta ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la mbegu ni muhimu sana na tunaiomba sana Serikali yetu izingatie, pamoja na mambo mengine, ili kilimo hiki kiweze kuwasaidia wakulima, lazima tuwe na mbegu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni kwamba katika maeneo yote yenye kilimo kama ya kwetu huko kwenye karanga na kadhalika, haitasaidia hata tukipata mbegu bora kama barabara zile zinazotoka kwenye maeneo ya kilimo hazitatengenezwa. Hilo ni jukumu ambalo nataka niwa-assign TARURA. Ni muhimu sana watu wetu wakipata karanga au mazao ya kutosha kama alizeti na kadhalika, ni muhimu sana kukawa na njia za kuyaleta kwenye masoko. Wakati mwingine yameharibikia shambani kwa sababu hakuna namna ya kuyaleta kwenye masoko. Kwa hiyo, suala la barabara Serikali naomba iendelee kulitilia mkazo na hasa barabara za vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie hotuba hii ya bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kazi nyingi ambazo anaendelea kuzifanya katika nchi yetu lakini pia hata utengamano wa taifa, kuna utulivu wa kutosha. Naompongeza sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa ajili ya bajeti nzuri ambayo imetayarishwa na Wizara yake, Naibu Waziri pamoja na timu yake yote. Kwa kweli bajeti hii kila Mtanzania, kwa sisi tunaotoka huko nje kila mtu anaisifia. Imegusa karibu kila maeneo na matarajio ya watu; kwa hiyo watu wana matarajio makubwa sana na bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba, kutengeneza bajeti nzuri ni jambo moja lakini kutekeleza bajeti hii ni jambo lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yangu kwamba bajeti hii itatekelezwa kwa ukamilifu wake. Isipotekelezwa katika ukamilifu wake maana yake pongezi zote hizi zitakuwa za bure. Kwa hiyo nakusihi sana Mheshimiwa Waziri, bajeti hii ikitekelezwa vizuri Watanzania wanakwenda kukomboka kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia habari ya barabara za vijijini (TARURA). Ninaipongeza Serikali kwa kuamuzi wa kutoza tozo la shilingi 100 kwa ajili ya kuchangia mfuko wa TARURA. Nchi hii inashida kubwa sana, barabara za vijijini zina urefu wa kilomita zaidi ya 108,000; lakini katika hotuba yako umesema ni kilometa 2,250 tu ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami, kwa hiyo utaona kuna tofauti kubwa sana. Na mimi naamini kuongezeka kwa bajeti hii kutaongeza mtandao wa barabara za kiwango cha lami katika Mfuko huu wa TARURA; kwa hiyo nakupongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi hizi za vijijini zimedumaza uchumi wetu kwa sababu kule ambako zinakwenda ndiko kwenye uzalishaji wa kilimo. Na utaona kwamba hakuna mahusiano kati ya barabara na maeneo yanayozalisha mazao ya kilimo na maeneo yenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo. Kwa hiyo mazao mengi yanaozea porini kwa sababu hakuna barabara ya kupeleka mazao kwenye maeneo ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana barabara hizi fedha zitoke barabara zitengenezwe ili wananchi wanapofanya shughuli za kilimo na mazao yakipatikana yasafirishwe mara moja kwenda kwenye maeneo ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwenye upande wa kilimo. Tunaamini kabisa kama asilimia 65 ya uchumi wetu unategemea kilimo. Ningeshauri sana Serikali tujikite kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji kinaweza kutukomboa kwa sababu kama unafanya kilimo cha umwagiliaji unaweza kuvuna mara mbili au mara tatu kwa mwaka; Badala ya kutegemea kilimo cha mvua ambacho mnategemea kuvuna mara moja na huna uhakika kwa sababu mvua inaweza kuwa nyingi, kuna maeneo mengine mvua inakuwa hakuna. Kwa hiyo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ni lazima Serikali itenge maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na hapo ndipo kufanyike kilimo cha kutosha. Kwa hiyo naomba sana Serikali kupitia bajeti ya kilimo Wizara ya Kilimo basi tushughulike sana na kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, papo maeneo mengi yenye maji ya kutosha. Tulikuwa tunapita juzi kutoka Singida, kuna mabwawa yamezagaa huko njiani lakini maeneo yanayozunguka mabwawa hakuna hata mchicha, hakuna mtu anashughulika hata na mchicha tu pale. Sasa ni lazima tubadilishe mindset ya watu wetu, yale maji ya kwenye mabwawa yanayozagaa hovyo katika nchi yetu tuyatumie effectively. Kama ni elimu basi itolewe kupitia Wizara yetu ya Kilimo, watu wayatumie vizuri yale maji. Lakini matokeo yake yale maji mpaka yatakauka, yatatumiwa na Wanyama, hakuna mtu anayeshughulika hata kulima mboga maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo uchumi wetu hauwezi kuendelea kwa sababu hata maji yale machache tunayoyaona barabarani hayatumiki vizuri. Kwa hiyo naomba sana elimu itolewe ili wale watu wanaoishi katika maeneo yanayozunguka maeneo ya maji basi wafanya kilimo cha umwagiliaji. Lakini pia kwenye kilimo bado haitoshi kama hatutakuwa na mbegu bora. Shida kubwa ya nchi yetu hatuna mbegu za kutosha ambazo ni mbegu bora. Naomba tujikite sana kwenye utafiti, wataalam wetu watafiti sana habari za mbegu. Tunatakiwa kuwa na mbegu bora ili tuweze kupata kilimo chenye tija. Tunaweza kuwa na maji, tunaweza kuwa miundombinu mizuri ya umwagiliaji lakini kama tuna mbegu ambazo hazina tija tutaendelea kupiga mark time hatutapata mazao ya kutosha kwa ajili maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mbegu ni jambo ambalo Serikali lazima litoe kipaumbele. Mbegu inayopatikana sasa haitoshi, na hata hiyo kidogo inayopatikana inauzwa kwa bei ya juu sana ambayo watu wetu asilimia 90 hawawezi ku-afford kabisa. Kwa hiyo ni lazima tutafute mbegu za kutosha, mbegu bora, na ikiwezekana Serikali itoe subsidy ili watu wazipate katika bei ambayo wanaweza ku-afford, na hasa watu wetu ambao wako kwenye maeneo ya uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Serikali kwa ajili ya kuwakumbuka Waheshimiwa Madiwani. Sisi wote tunatoka kwenye halmashauri zetu, tunaona namna Madiwani wanavyohangaika. Wakiitwa kwenye vikao mbalimbali wanageuka kuwa ombaomba kwa sababu hawana fedha za kusafiria kwenda wilayani. Kwa hiyo lazima either wamuombe Mbunge au nani, hii kitu inawadhalilisha Madiwani. Madiwani ni watu waliochaguliwa kama sisi na wananchi, hivyo lazima Serikali ione umuhimu wa Waheshimiwa Madiwani. Na sisi Wabunge mara nyingi tunawatumia Madiwani kutusaidia kupita kwenye chaguzi zetu, kwa hiyo tuna kila sababu ya kuwatetea. Namimi nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya uamuzi wake wa kuamua kwamba sasa walipwe kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyojua zipo halmashauri ambazo zipo hoi kabisa katika nchi hii, na hazina vyanzo vya mapato vya kutosha. Kwa hiyo kila siku Waheshimiwa Madiwani wanakwenda vikao wanakopwa. Wengine wanamaliza muda wao wanakuwa hawajalipwa posho nyingi tu, na mpaka leo wanadai kwenye halmashauri. Lakini si kwa sababu labda ya ujeuri Mkurugenzi, kwa sababu halmashauri hazina vyanzo vya kutosha. Kwa hiyo jambo hilo naomba lizingatiwe vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia upande wa afya, kuna maboma ya Vituo vya Afya, Zahanati ambayo yamekaa zaidi ya miaka mitano mpaka 15. Wakati umefika sasa Serikali iende ikamalizie haya maboma. Tuna maboma ya zahanati zaidi ya 8,000, maboma ya vituo vya afya zaidi ya 1,500 katika nchi hii. Haya yote yangekuwa yanafanya kazi huduma za afya ingeboreka Zaidi, lakini yote yapo na haya yamejengwa kwa nguvu za wananchi. Wamefika mahali wameshindwa, sasa Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuboresha ama kumalizia haya majengo ili huduma za afya kwa wananchi ziweze kuwa za uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu, nataka nizungumzie eneo la Bodi ya Mikopo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, amezungumza vizuri sana, akasema mikopo wanayopewa wanafunzi si hisani, ni fedha ambayo baadaye wanatakiwa kuirudisha, na zipo taratibu za kuzirudisha fedha hizo, kwa hiyo siyo hisani. Hata hivyo idadi wanaonufaika na mfuko huu bado ni ndogo sana, idadi ya wanaobaki wanaoachwa bila ya kupewa mikopo na wakiwa na sifa ni wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana Bodi ya Mikopo ijaribu kupanua wigo. Mheshimiwa Waziri amezungumza habari ya kuwaongezea bajeti Bodi ya Mikopo, hii itasaida vijana wetu wengi kujiunga na elimu ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, utaratibu wa kuwatambua wanufaika bado mimi nauona una kasoro kubwa sana. Wapo vijana wengi ambao kweli wanahitaji na wanasifa za kupewa mikopo hiyo, lakini kwa sababu mbalimbali hawapewi mikopo. Kwa hiyo bajeti ikiongezeka kwa vyo vyote vile vijana wengi watapata mikopo na wataweza kujiunga na Elimu ya Juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nipongeze uamuzi wa bodaboda. Watu wengi wanaoishi mjini wanafanya biashara za bodaboda; na vijana wengi ndio wanaohusika. Anakuwa aidha amepewa bodaboda na mtu au yeye mwenyewe kajikusulu kanunua bodaboda. Na kwa sababu ya wingi wa bodaboda uliopo, biashara ya bodaboda bado hailipi sana. Kwa hiyo ilipokuwa inafikia hatua ya kumtoza faini ya Shilingi 30,000 kwa kosa la barabarani, sawa sawa na mtu aliyekosea anayeendesha lori haikuwa sawa kabisa. kwa hiyo nataka nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hilo na kuwapunguzia adhabu ili angalau tujaribu kuwasaidia waweze kujikwamua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa sababu ya kunipa nafasi na mimi nichangie katika hotuba ya Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Nataka niwapongeze sana kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia katika Taasisi ya TAKUKURU. Taasisi hii inafanya kazi nzuri kwa ajili ya kupambana na rushwa na mambo ya ufisadi katika nchi yetu. Lakini katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri alikuwa amesema Taasisi moja ya Transparency International ilitupa alama ya 38; hii ni ishara kwamba bado tuna kazi kubwa ya kufanya kwa ajili ya kupambana na vitendo hivi vya rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ninapenda kutoa ushauri kwa Serikali, TAKUKURU ijikite sana kwenye utafiti, tuangalie sana vyanzo vya rushwa viko maeneo gani na kusema kweli maeneo mengi ambayo yana shida ya rushwa ni yale ambayo yanatoa huduma kwa wananchi. Kwa hiyo, tufanye utafiti wa kutosha, tujue na kubaini maeneo ambayo yana mianya ya rushwa ili kabla ya kuanza kukimbizana na mla rushwa mmoja mmoja tupambane kwanza na kuziba hiyo mianya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wale wananchi wenye uzalendo ambao wanatoa taarifa sahihi zinazosaidia kupambana na vitendo vya rushwa. Najua taarifa hizi zinatolewa katika mazingira ya usiri mkubwa. Lakini ninashauri wawe motivated katika mazingira hayo hayo ya usiri ili waendelee kusaidia katika kupambana na vita ya rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze kuhusu TASAF - Mpango wa Kusaidia Kaya Maskini. Mpango huu pia umeendelea vizuri na hasa kule jimboni kwangu vijiji vingi vimepata mpango huu. Lakini naomba sana katika Jimbo la Mpwapwa bado kuna vijiji 22 havijaingia katika huu Mpango wa Kusaidia Kaya Maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nitoe ushauri, bado kuna malalamiko madogo madogo kwamba utaratibu mzima wa kutambua kaya maskini bado una kasoro ndogo ndogo. Wale walengwa wanaotakiwa kufaidika na mpango huu hawatambuliwi, matokeo yake unakuta kaya ambayo inapata huduma hii haina sifa ya kupata huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maana yake kuna wimbo la rushwa hapo limegubika, maana sioni mantiki ya mtu kwenda kuona kwa sababu utaratibu ni kwamba lazima maafisa wafike wakaone kaya ile ina hali gani ya kiuchumi. Sasa kama umekuta ina unafuu wa kiuchumi kwa nini uiandike katika orodha ya kaya maskini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hilo ni jambo ambalo tunaomba Wizara iendelee kupambana nalo. Tunapenda sana watu wetu wale ambao kwa kweli wanahitaji msaada huu basi wanufaike na msaada huu, badala ya kunufaika watu wasiohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze juu ya uongozi; katika bajeti ya TAMISEMI, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walichangia juu ya migogoro inayoendelea katika maeneo yetu. Unakuta DED hapatani na Mkuu wa Wilaya, hapatani na mwenyekiti wa Halmashauri. Mimi nafikiri haya yote yanatokana na ukweli kwamba wanapoteuliwa hawapewi semina ili wajue wajibu wao. Matokeo yake mtu ana-overlap mpaka kwenye kazi ya mtu mwingine halafu kunakuwa hakuna maelewano ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ule utaratibu wa semina elekezi mimi naomba urudishwe ili watu wakipata uteuzi au wakiajiriwa kwenye nafasi fulani basi apewe maelekezo namna ya kuenenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Wizara hii ya Elimu. Niwapongeze sana kwa kazi nzuri ambayo wanayoendelea kuifanya katika wizara hii. Napenda nichangie katika eneo la miundombinu. Sera yetu ya elimu bila malipo imepelekea kuwa na ongezeko kubwa sana la wanafunzi wanaojiunga darasa la kwanza, lakini hata wale wanaojiunga kidato cha kwanza. Kwa hiyo utaona kwamba miundombinu haitoshi kwa sababu ya wingi wa wanafunzi. Kwa hiyo, naishauri sana Serikali kupitia Wizara hii ya elimu iangalie eneo hili kwa jicho la karibu sana kwa sababu uwiano wa watoto wanaojiunga shule na uwiano wa miundombinu inayojengwa haufanani kabisa.
Mheshimiwa Spika, niongelee hasa hapa kwenye madawati. Naamini kabisa catalyst ya kufaulu watoto ni mazingira mazuri ya kusomea. Mtoto anayesoma amekaa chini au amesimama hawezi kufaulu sawa na yule anayekaa kwenye viti. Hata hivyo, ninachokiona, mara nyingi msisitizo wa kutengeneza madawati unafanyika mwezi Januari, wanapojiunga darasa la kwanza na kidato cha kwanza ndipo matamko yanatoka kwamba kufika tarehe Fulani madawati yaweshakamilika, watoto waanze shule. Baada ya hayo hakuna kitu kinaendelea na mimi katika Jimbo langu la Mpwapwa, watoto wameathirika, wapo waliosubiri madawati yatengenezwe ndipo wajiunge na shule wakati wengine walishaanza tayari kusoma; wao wanasubiri madawati yatengenezwe.
Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa naomba nishauri Serikali tuwe na Mpango endelevu wa kutengeneza madawati. Kwani kuna ubaya gani ikifika Januari tuna madawati store, lazima tuwe na utaratibu wa kutengeneza madawati kwa kutumia halmashauri zetu. Madawati yatengenezwe mwaka mzima ili tuwe na madawati ya kutosha, yawekwe stote. Tunapofungua shule mwezi Januari basi wanafunzi wapate mahali pa kusomea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni walimu, walimu kama tunavyojua wote hawatoshi na mimi ningeshauri Wizara ijitahidi sana kupata vibali kwa ajili ya kuajiri walimu. Lakini kuna tatizo moja dogo. Katika Jimbo langu nime-experience, walimu wanapangiwa vituo, wanaripoti halafu wakiondoka hawarudi tena. Hiyo sielewi kwa sababu unahesabika kama shule il eina walimu saba kumbe ina walimu sita au watano. Walimu wawili waliripoti halafu hawakurudi tena kwenye kazi, ni kwasababu ya mazingira ya namna hiyo. Sasa Wizara lazima ije na Mpango na ikiwezekana ikomeshe tabia hii ya walimu ambao wanaajiriwa na kupangiwa vituo halafu wanaondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia vijana wetu wengi wanaomaliza elimu ya vyuo vikuu hawarudi makwao, wanakaa mjini. Kwenye miji kama Dodoma, Dar es Salaam, Arusha na mahali pengine wamejazana na kila siku utakutana nao wana bahasha za kaki wakitafuta kazi za kuajiriwa. Ni kwasababu elimu waliyoisoma hawawezi kui-apply kule walikotoka. Hawawezi kui-apply kwenye mashamba, kwenye entrepreneurship kwasababu hawakujifunza hayo. Kwa hiyo, nataka nitoe wito kwa Wizara, Mheshimiwa rais katika hotuba yake juzi alizungumza habari ya kuboresha mitaala ili iendane na mazingira ya nchi yet una iendane na soko la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kilimo ndiyo sekta inayotoa ajira kwa wingi kuliko sekta nyingine yoyote lakini kwa bahati mbaya sana haifundishwi sasa shuleni. Kwa hiyo unategemea vijana wote ambao watamaliza shule hawawezi kwenda kufanya kilimo kwasababu hawajajifunza. Sasa tunapoiangalia mitaala hii kwa upya lazima iendane na mazingira yetu. Tuwafundishe katika sekta ambayo wataenda kufanya ajira, wanaenda kupata ajira ya kutosha. Wataenda kujiajiri wenyewe na ndiyo lengo letu. Elimu yetu i-focus kwenye kujiajiri wenywe. Vijana wetu wajiajiri wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze wamezungumza habari ya ukarabati wa vyuo vyetu vya ualimu. Ni muhimu sana walimu wetu wakafundishwa, wale wanaokuja kufundisha watoto wetu wakasoma katika mazingira mazuri katika Jimbo langu la Mpwapwa chuo chetu kinasaidika katika utaratibu huu. Bajeti inayoisha mwaka huu tulipata shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mipya pale chuoni. Kuna ujenzi wa bwalo, kuna ujenzi wa jengo la ghorofa moja kwa ajili ya computer lakini kuna ujenzi wa nyumba za watumishi ambao iko katika mtindo wa two in one. Lakini kinachonisikitisha ujenzi umesimama…
SPIKA: Tayari, muda umekwisha Mheshimiwa.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, naomba Wizara iangalie ili ujenzi huu uanze mapema. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu kuipongeza Wizara hii ya Afya kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika. Naomba nichangie katika eneo la upungufu wa dawa. Kama ambavyo wenzangu wengi wameeleza, kuna shida kubwa sana ya dawa katika hospitali zetu lakini hasa katika vituo vya afya na zahanati. Mara nyingi vituo vya afya na zahanati viko vijijini na kule vijijini ndiko watu wengi walipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu huu umesababisha kumekuwepo na mrundikano wa maduka ya dawa katika maeneo ya vijiji. Kusema kweli maduka mengi hayana sifa ya kuwepo. Hatari iliyopo ni kwamba hata wale wanaohudumia kuuza dawa zile, hawana utalaam wa kuuza dawa na kwa sababu wako vijijini hawafuatili. Kwa hiyo, watu wengi wanakunywa dawa ambazo wakati mwingine zimepitwa na wakati, zime-expire, lakini hakuna mtu anaweza kufuatilia mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wamechukua advantage kwa sababu ya upungufu wa dawa, wanajua kabisa kule kijijini hakuna dawa, kule kwenye zahanati hakuna dawa, kwa hiyo wanapeleka maduka na hawaweki hata watu professional. Anajua akimweka professional kwanza hatakaa kijijini lakini pia hawezi kumlipa mshahara, hivyo, anaweka mtu ni mtu. Kwa hiyo, yule anakuwepo pale, mtu akienda kutafuta dawa anachofanya anapiga ramli kwamba huyu anahitaji paracetamol lakini ukweli ni kwamba hajui na hiyo ni hatari tunaweza kujikuta tumeua watu wetu kwa sababu ya jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri Serikali maduka haya ya vijijini ya dawa yafuatiliwe. Kwanza kujua hawa watu wanaouza dawa wana utaalamu wa kuuza dawa hizo? Wanafahamu hizo dawa? Wana A, B, Cs za dawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wafuatilie waone hizo dawa hazijapitwa na wakati? Kwasababu kule mambo yanajiendea hivyo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni upungufu wa watumishi. Hili ni tatizo la nchi nzima, hospitali nyingi za wilaya, vituo vya afya, watumishi hawatoshi. Kwa mfano hospitali yangu ya Wilaya ya Mpwapwa ina upungufu mkubwa sana wa watu. Hospitali ile inatakiwa kuwa na wafanyakazi 310, lakini waliopo sasa hivi ni 152 ambayo ni sawa na asilimia 49. Ina upungufu wa wafanyakazi 158 ambayo ni sawa na asilimia 51; upungufu huu ni mkubwa sana na ndio maana unaona huduma hii pamoja na nia njema ya Serikali hakuna efficiency kwasababu, watumishi hawatoshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri sana Wizara hii iangalie uwezekano wa kupata watumishi wa kutosha. Na hasa katika hospitali zile ambazo watu wengi wanazitegemea kama hospitali za wilaya na mikoa na zile hospitali za rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni miundombinu chakavu katika hospitali zetu karibu zote. Ukienda katika hospitali za wilaya karibu nchi nzima, za mikoa, utakuta majengo mengi ni chakavu, lakini hakuna vifaa tiba. Kwa mfano ukienda katika hospitali ya Wilaya yangu ya Mpwapwa jengo lile la OPD limechakaa san ahata unasema hapa mazingira hayaruhusu kabisa kutoa huduma ya afya pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna majengo mengine, miundombinu ya maji-taka na maji-safi yote ni ya zamani na imeharibika, lakini pia umeme hakuna umeme wa uhakika, lakini hospitali ile ya Mpwapwa mpaka leo haina X-Ray, just imagine. Haina X-Ray wakati mwingine wanaazima kutoka kwenye kituo cha afya, X-Ray ya kizamani sana, lakini hospitali kama hadhi kama ya wilaya inahitaji kuwa na Digital X-Ray. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iangalie sana Mpwapwa hakuna X-Ray tunaazima kutoka kituo cha afya ndio inakuja kutumika na X-Ray ile haina efficiency yoyote ni mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huwezi kuhudumia watu wa wilaya nzima kwa kutumia vitu vya kubahatisha kama hivi. Kwa hiyo, Wizara nashauri sana hivi vitu vya miundombinu ni muhimu, hospitali zetu ziwe na vifaa tiba vya kisasa, ili tuweze kuendana na wakati, lakini pia huduma kwa watu wetu iweze kufanyika vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningetaka kuchangia ni juu ya bima ya afya kwa ajili ya wazee. Sera hii imetungwa siku nyingi, lakini sioni kama kweli Wizara inatoa hizi bima kwa wazee. Katika Wilaya yangu ya Mpwapwa nadhani ni katika wilaya chache ambazo hazina, wazee wengi hawana bima ya afya. Pamoja na bima ya afya, lakini pia wazee wetu hata wale wanaokwenda kwenye Dirisha la Wazee huduma haipo. Wazee wenye umri mkubwa unakuta wamesongamana msururu akifika kwenye dirisha anaambiwa dawa hii hamna kanunue mahali fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo pia la kuliangalia sana, kama hakuna dawa ni afadhali wasipange foleni. Kwa nini wapange foleni watu wenye umri mkubwa wanarudi wanaumwa na dawa hawakupata? Si ijulikane moja kwamba, hakuna dawa wazee wasiende kupanga foleni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wizi Mheshimiwa mmoja amezungumzia sana habari ya wizi wa dawa. Na nimeona ukienda katika vijiji utakuta maduka ya dawa ni ya baadhi ya watumishi wasio waaminifu. Yeye ndiye anayeandika dawa kwa hiyo, anaandika dawa na anaelekeza nenda kanunue mahali fulani, lakini kijijini ni watu wangapi wanaweza kununua dawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, wana bima ile iliyoboreshwa, lakini dawa pale hamna. Dawa zinaharibiwa na baadhi ya wahudumu ambao sio waaminifu kwa hiyo Serikali lazima iwe makini sana na wahudumu wa namna hii vinginevyo tutapigizana kelele hapa kila siku, huduma hazitakuwa nzuri, watu wetu wataendelea kuathirika na utaratibu huu ambao sio mzuri. Wizi wa dawa ni jambo kubwa sana linaloendelea sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia katika ripoti hizi tatu za Kamati za LAAC, PIC na PAC. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuleta maendeleo katika nchi yetu. Pia nikupongeze wewe binafsi kwa kazi nzuri ambayo unaendelea kutusimamia ndani ya Bunge hili. Tatu, niwapongeze Wenyeviti wa Kamati hizi tatu pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hizi tatu kwa ajili ya kazi njema ya kuandaa ripoti ambayo leo tunapata fursa ya kuichangia.
Mheshimiwa Spika, ukisikiliza hotuba nyingi hapa ndani, malalamiko makubwa sana yapo kwenye utendaji hafifu wa mashirika yetu ya Umma. Malalamiko haya yanakuja kwa sababu mashirika haya yanatumia mitaji ya Umma, yaani fedha za walipa kodi, lakini faida ambayo ilikuwa imetarajiwa kutoka kwenye mashirika haya, haipo. Kwa hiyo, ndiyo maana Wajumbe au Wabunge wanalalamika sana.
Mheshimiwa Spika, zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha mashirika haya yasifanye vizuri. Wabunge wengi wameeleza, lakini nami nitaeleza. Moja, ni mashirika haya mengi kuendeshwa bila Bodi za Wakurugenzi kwa kipindi kirefu sana.
Mheshimiwa Spika, majukumu ya bodi yanajulikana. Bodi ndiyo chombo pekee kinachosimamia kutoa maamuzi, usimamiaji wa utekelezaji wa majukumu yote ya taasisi, lakini unakuta mashirika mengi kwa kipindi kirefu yanaendeshwa bila bodi.
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nitoe mifano michache tu. Katika ripoti ya CAG ukurasa wa 62 ameorodhesha kwamba mwaka 2020/2021 kulikuwa na orodha ya mashirika 31 ambayo yalikuwa yameendeshwa bila bodi kwa kipindi kirefu sana. Mojawapo ni Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere; kimekaa bila bodi kuanza Julai, 2015 mpaka Februari, 2022. Muda huu ni wa miezi 80 ambao ni sawa na miaka sita, taasisi kama hii inakaa bila bodi.
Mheshimiwa Spika, lingine ni Shirika la Maendeleo na Utafiti wa Viwanda Tanzania, na lenyewe limekaa bila bodi kuanzia Oktoba, 2015 mpaka Februari, 2022, miezi 77 ambayo ni sawa pia na miaka sita na miezi kadhaa. Lingine ni Makumbusho ya Taifa, kuanzia Julai, 2015 mpaka Februari, 2022 sawa na miezi 38, nalo pia kwa miaka mitatu limekuwa halina bodi.
Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile uendeshaji huo wa mashirika yetu hauwezi kutarajia kupata tija kwa sababu menejimenti inajiendesha bila kuwa na mtu wa kumwangalia, matokeo yake ukiangalia mashirika yetu yote Kamati ya PAC ambayo tunashughulikia mashirika na tumepitia mashirika yote ama yana mzigo wa madeni, ama yanaendeshwa kwa hasara lakini ni kwa sababu hakuna chombo madhubuti, hakuna bodi ambayo inaweza ikasimamia utekelezaji wa majukumu yao na mwisho wa siku tuweze kushuhudia tija ambayo ilikuwa imekusudiwa.
Mheshimiwa Spika, pia kwenye ripoti ya CAG ukurasa wa 66 aya ya 47 na 48 ya Mwongozo wa Uhasibu (NBAA) ya mwaka 2021 zinaeleza umuhimu wa bodi, kwamba bodi lazima iidhinishe hesabu za taasisi yake. Kabla ya CAG kukagua, lazima bodi iidhinishe ndipo ikague; lakini CAG anasema, alishindwa kutoa maoni kwa mashirika Matano. Hakutoa maoni yake (opinions) kwa sababu hesabu zile zilikuwa hazijaidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi tunapoongea, hatuna uhakika; siyo Serikali na Umma kwa ujumla kwamba status ya mashirika haya ikoje? Maana jicho la Serikali au jicho la Umma ni CAG. Kwa hiyo, tunasubiri CAG akishakagua atoe maoni kuhusu shirika husika, lakini mpaka sasa hivi mashirika hayo matano ambayo CAG alishindwa kutoa maoni yake ni kwa sababu hayakuwa na bodi na sheria inataka hesabu zake ziidhinishwe na bodi, halafu ndipo afanye ukaguzi na atoe maoni yake.
Mheshimiwa Spika, mashirika hayo nitayataja machache. Mojawapo ni Shirika la Maendeleo na Utafiti wa Viwanda Tanzania, lingine ni Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere, na lingine ni Shirika la Utafiti wa Uvuvi. Haya mashirika CAG hajatoa maoni mpaka leo na hatujui yanaendeleaje mpaka sasa. Hilo ni eneo ambalo pia linaleta shida kwamba bila kuwa na bodi, kuna mambo mengi yanaweza kukwama kabisa.
Mheshimiwa Spika, pia kuna issue ambayo pia CAG amei-raise kwenye ripoti yake ukurasa wa 75 anasema; mashirika manne hayakukata michango ya kisheria ya kupeleka kwenye Mifuko ya Pensheni na Mfuko wa Fidia wa Wafanyakazi. Sasa hayo yote ni kwa sababu ya udhaifu wa usimamizi. Haiwezekani mashirika yakakata makato ya kisheria halafu yasipelekwe kunakotakiwa. Hasara yake ni kukosekana kwa mafao ya wafanyakazi wanaostaafu. Watapataje mafao kama haya yamekatwa, lakini hayajapelekwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo maana tunaona wazee wengi wanakufa mapema wakishastaafu, kwa sababu wanamangamanga, wanakwenda kufuatilia fedha hazipo. Kumbe taasisi hiyo waliyokuwa wanafanya kazi ilikuwa haipelekei ile michango. Kwa sababu menejimenti ilikuwa haipeleki, hakuna mtu wa kuangalia juu kuona kwamba wanapeleka au hawapeleki. Kwa hiyo, jambo hili ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo lingine au hasara nyingine ni kwamba kunakosekana na fidia kwa wafanyakazi inapohitajika. Mfanyakazi anaweza kuwa anahitaji fidia, lakini kwa sababu fedha hii haikuwepo kwenye ule mfuko, haitakuwepo, matokeo yake anapigwa danadana. Pia kushindwa kutuma hizo fedha kwenye taasisi hizi kuna hasara kubwa sana, kuna attract invoice penalty. Shirika linapigwa penalty kwa sababu halikupeleka michango kwa wakati au halikupeleka kabisa. Hii penalty inasababisha hasara na ndiyo maana tunaona mashirika mengi yanaendeshwa kwa hasara kwa sababu hizo; fedha nyingi zinalipwa kwa sababu ya penalty au adhabu, wakichelewa kupeleka kwenye mifuko ya kisheria.
Mheshimiwa Spika, jambo la kuwa na bodi tungeamua kabisa kusema kwamba ni jambo la kufa na kupona ili taasisi hizi tunazowekeza fedha nyingi za Serikali ziweze kuleta tija iliyokusudiwa ni lazima mashirika yote yaendeshwe chini ya bodi zake za Wakurugenzi.
Mheshimiwa Spika, nije kwenye kipengele cha matumizi mabaya ya fedha za Serikali; mashirika yote yameonekana yanashindwa kudhibiti matumizi yake na ndiyo maana hayafanyi vizuri, na mengi hayawezi hata kutoa gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Nichukue mfano mmoja tu wa taasisi moja eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Mheshimiwa Spika, eneo hili la Hifadhi ya Ngorongoro linamiliki ndege aina Cessna yenye namba ya usajili 5H-MPZ. Ndege hii ni ya zamani sana. Mpaka mwaka 2021 ilikuwa na umri wa miaka 47. Taasisi hii ilikuwa inatumia ndege hii kwa ajili ya doria, lakini CAG anasema katika ukurasa wa 59 Mamlaka hiyo ya Ngorongoro ilifanya matengenezo kwa gharama ya shilingi milioni 278.42, lakini plan yao ilikuwa ikishakamilika ifanye safari za saa 900, lakini cha kusikitisha sana ndege hii imefanya safari saa 18 tu.
Mheshimiwa Spika, sasa ukijiuliza, Shilingi milioni 278 zimetumika kukarabati ndege hii, lakini makusudio au matarajio waliyokuwa wametarajia kufanya safari au kuzunguka kuangalia doria kwa saa 900 inaishia kufanya doria kwa saa 18. Hasara hii ni kweli inafanyika na watu ambao wameenda shule? Je, hao watu tuliowaweka humo kufanya kazi hizo za kusimamia mamlaka yetu, wanao uwezo wa kufanya kazi kama hiyo? Ni kweli hawaoni kwamba hili lilikuwa ni kosa kubwa sana? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana hatua kali zichukuliwe kwa watu kama hao, kwa sababu hatuwezi kuendelea, hatuwezi kupata mafao, hatuwezi kupata tija kwenye mashirika kama haya kama tuna watu ambao wanaendelea kucheza na fedha za walipa kodi katika mazingira kama haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine, naomba kuzungumzia changamoto ya kupata vibali vya ajira na mfumo wa ununuzi kwa mashirika ya Umma na hasa yale yanayofanya biashara. Mashirika mengi yanapata mitaji ya Serikali ili kufanya biashara na kuleta tija na kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hata hivyo, kwa mazingira ya biashara ya leo, huwezi kushindana.
Mheshimiwa Spika, nashauri, tufanye biashara mashirika haya ya Umma, lakini tutumie private thinking. Maana yake ni kwamba, lazima tubadilike. Wenzetu wa private wana-enjoy flexibility ya maamuzi. Mfano, akipata bidhaa fulani kwenye soko kwamba ina-hit katika soko, wao wanafanya maamuzi overnight. Wanahitaji mtaalamu wa kutengeneza hiyo bidhaa, kesho wameshampata. Kesho kutwa wanaanza uzalishaji. Wanahitaji raw materials; kesho wameshatafuta raw materials zinapatikana, wananunua na kuanza uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, sisi tunaanza mchakato wa ajira, unachukua miezi mitatu ndiyo tumpate huyo mtaalamu kuja kutengeneza bidhaa hiyo ambayo wenzetu wameshaanza mara moja, lakini sisi hiyo kupata raw materials lazima mchakato pia uwepo wa manunuzi unaochukua zaidi ya miezi mitatu. Unaporudi, unaanza kutengeneza bidhaa, unakuta ama imeshatoka kwenye soko au lile soko limeshakuwa captured na private sector. Kwa hiyo, hatuwezi kushindana na ndiyo maana unaona pia hakuna tija kwenye mashirika yetu.
Mheshimiwa Spika, ningeshauri tukitaka kufanya bishara lazima tubadilike. Yale mashirika ambayo yanafanya biashara, tuwape uhuru wa kufanya maamuzi haraka. Tunaweza kukasimu madaraka kwenye bodi ili waweze kufanya maamuzi haraka ili wafanye biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, biashara haihitaji mchakato wa miezi mitatu na kuendelea, biashara haihitaji theories, biashara inahitaji maamuzi. Biashara ni maamuzi na biashara lazima uamue kwa sababu biashara ina- determine soko. Soko likipatikana leo, lazima upambane kulipata leo, huwezi kupambana kwa ajili ya kusubiri mchakato. (Makofi)
SPIKA: Muda wako ulishakuwa umeisha, nilikuacha kwa sababu ni wewe ni mtu wa mwisho ili umalizie mchango wako. Kwa hiyo, nakupa sekunde 30.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa na mengi lakini naomba basi, niunge mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia bajeti hii ya Serikali. Kwanza nianze na kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kazi nyingi zinazofanyika vizuri katika nchi yetu. Sisi kule watu wa Mpwapwa tumepata miradi mingi sana, haijawahi kutokea katika historia ya jimbo letu. Tumepata miradi upande wa barabara, tumejenga madaraja ambayo yalikuwa yanasumbua kwa kipindi cha miaka mingi. Vilevile tumepata madarasa mengi kama ambavyo Wabunge wengine wamepata, na hivi karibuni tumepata shilingi zaidi ya bilioni 735 kwa ajili ya upanuzi wa shule yetu ya wasichana pale Mpwapwa Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapanua shule yetu ya wavulana Mpwapwa Sekondari, tumepata milioni 295, tumeendelea, tumepata vituo vya afya. Kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya juhudi hizi ambazo amezifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nimpongeze sana Waziri wa Fedha. Bajeti hii amegusa karibu maeneo mengi sana yanayohusu wananchi, nawapongeza sana Waziri, Naibu Waziri na timu yake nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na bajeti nzuri kama hii mimi naona ni jambo moja lakini utekelezaji wake ni jambo lingine. Ninataka kumshauri Waziri waitekeleze katika mapana yake kama ambavyo wameileta. Haya mengine tuliokuwa na shida kwamba bajeti inakuwa nzuri lakini utekelezaji wake unakuwa haufikii malengo ambayo yale tulikuwa tumekusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuchangia upande wa ukusanyaji wa kodi kupitia ETS au Electronic Tax Stamps. Utaratibu huu mimi nauunga mkono sana uendelee kutumika kama ambavyo umekuwa ukitumika kwa kuwa unatusaidia kuongeza mapato, stamp hizi zinabandikwa kwenye bidhaa zinazozalishwa. Kwa hiyo kwanza tutajua ni bidhaa kiasi gani zilizozalishwa na inakuwa rahisi sasa kukata kodi. Ingawa kuna malalamiko machache yanaendelea dhidi ya mkandarasi anayetekeleza mradi huu. Naishauri Serikali mkae na huyu mkandarasi muweze ku-resolve matatizo yote ambayo yameonekana katika utekelezaji wake lakini utaratibu huu nauunga mkono ningeshauri Serikali iendelee naoi li kuongeza mapato ya Serikali yetu hivyo kufadhili miradi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni upande wa kilimo. Kilimo kama walivyosema wengine ndio uti wa mgongo, na tunajua kabisa zaidi ya asilimia 65 ya ajira za nchi hii zinapatikana kutokana na kilimo. Nimeona Wizara ya Kilimo; niwapongeze sana; wamekuja na mkakati wa kuhakikisha kwamba sasa tunaondokana na kilimo cha kutegemea sasa tutakuwa tunafanya kilimo cha umwagiliaji. Mabwawa yanajengwa sehemu nyingi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nishukuru kwa sababu kule Mpwapwa tuna bwawa kubwa lenye thamani ya shilingi bilioni 27.9 ni bwawa kubwa ambalo naamini litaleta ukombozi mkubwa sana kwa wananchi wa Mpwapwa. Sasa kitu ambacho ningeomba Serikali izingatie sana hapa ni kutengeneza miundimbinu tunaweza kuwa na maji mengi sana lakini kama miundombinu ya umwagiliaji haipo bado tutaendelea kukutana na shida nyingi za uhakika wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilimo hicho niwapongeze sana ile mamlaka ya kuhifadhi chakula NFRA mwaka huu kulikuwa na shida ya chakula katika maeneo mengi katika nchi yetu ni pamoja na Jimbo langu la Mpwapwa. Walifanya vizuri sana kutusaidia. Wakati wanaanza kusambaza chakula bei ya debe moja la mahindi ilikuwa imefikia shilingi 25,000 lakini wao walipoleta mahindi yakaanza kuuzwa kwa shilingi 16,000. Ulikuwa ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi lakini shida ambayo niliiona ni kwamba hawakuwa na uwezo wa kufika maeneo yote ya Wilaya ya Mpwapwa kwa sababu ya nguvu ndogo ya bajeti ama idadi ndogo ya wafanyakazi. Kwa hiyo, ningeomba sana Serikali izingatie hili jambo iwaongezee nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri umesema mna mpango wa kununua tani 400,000. Mimi nadhani hizo tani ni ndogo kwa sababu ya uhaba wa mvua iliyotokea mwaka huu bado tunafikiria kwamba kutakuwa na shida ya chakula mwaka unaokuja. Kwa hiyo hawa watu wawezeshwe wawe na chakula cha kutosha. Zinunuliwe hata tani 700,000 ili ikiwezekana basi shida hii ya chakula itakapotokea Serikali iwe na uwezo wa kupambana na hii shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kwa upande wa ardhi. Ardhi ni jambo moja kubwa sana ambalo linaleta maendeleo kwa watu wetu. Serikali mmezungumza habari ya kupunguza kodi na tozo mbalimbali kwa wamiliki wa ardhi na mimi naungana nao hilo jambo ni zuri ili watu wengi waweze ku-afford kumiliki ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo bado hatujafanya vizuri kwa upande wetu wa Serikali ni kupima ardhi kwenye miji ya wilaya na miji ambayo inakuwa kwa kasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akipimiwa ardhi yake akawa na hati ya kumiliki ardhi kwanza faida yake ni kwamba miji itajengwa kulingana na mipango miji. Kwa hiyo upimaji wa ardhi kwa kawaida unapendezesha miji, miji inaonekana imejengwa vizuri. Faida ya pili yule mwenye kumiliki ardhi ambaye ana hati ya kumiliki ardhi anaweza kuwa na access ya kupata mikopo kwenye vyombo vyetu vya fedha, na akishapata mikopo itamsaidia kujitafutia biashara na kufanya ujasiriamali. Kwa hiyo itakuwa ni ukombozi mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wengi hawawezi kupata mikopo katika vyombo vya fedha kwa sababu tu hawana dhamana na dhamana kubwa ambayo inatakiwa kwenye vyombo vingi vya fedha ni umiliki wa ardhi, yaani mtu lazima uwe na hati ya ardhi. Kwa hiyo ningeomba sana maelezo yaliyoelezwa kwenye bajeti ni mazuri na namwomba Mheshimiwa Waziri jambo hili Serikali ilitilie maanani. Watu wapimiwe ardhi waweze kumilikishwa ardhi ili waweze kufanya maendeleo ya maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia nimeona kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia mpango huu wa kunusuru kaya maskini (TASAF). Mpango huu ni mzuri na umeleta tija katika maeneo mengi ya nchi yetu, na kwamba sasa pia waweza kutambua maeneo kama 186 ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, ambalo ni jambo zuri. Malalamiko yangu, niliwahi kusema hata huko nyuma, utaratibu wa kutambua hizo kaya maskini bado hauko sahihi. Katika Jimbo langu la Mpwapwa wako watu ambao mimi nawajua ni maskini kabisa wana sifa zote lakini hawajaingia kwenye huu mpango wamekuwa wakilalamika. Kwa hiyo maana yake nni kwamba kuna kasoro katika utaratibu mzima wa kutambua nani ana sifa, kaya ipi ina sifa ya kuingia kwenye huo mpango na ipi haina sifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii imefanywa na watendaji wachache wasio waaminifu wamekwenda wamechukua watu wasio na sifa kuingia kwenye huu mpango wamewaingiza wameacha watu ambao kwa kweli wana sifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imefanywa na watendaji wachache wasio waaminifu, wamekwenda wamechukua watu wasio na sifa, wamewaingiza kwenye huu mpango, wamewaacha watu ambao kwa kweli wana sifa. Kwa hiyo Serikali ningeomba pia tunapotekeleza bajeti hii ya 2023/2024, Mpango huu wa TASAF ni mpango mzuri, kama hatuwezi kuusimamia vizuri tutanufaisha watu ambao hawastahili, tutaacha wale wanaostahili. Matokeo yake, lengo na madhumuni ya mpango huu yatakuwa hayajatimia kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo pia ningependa nichangie ni kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia nadhani amevunja rekodi ya kutoa fedha nyingi sana kuliko wakati mwingine wowote ambazo zimeenda katika ngazi zote za Serikali. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, lakini lengo lake na madhumuni yake bila shaka angetarajia kuona ustawi wa wananchi wake, angetarajia kuona yale ambayo tumekusudia, yale ambayo yeye mwenyewe anawaza mpaka anapeleka hizo fedha yanatokea katika uhalisia wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hii miradi mingi ambayo Mheshimiwa Rais ameipeleka katika maeneo yote ama haijakamilika ama imekamilika, lakini iko chini ya kiwango, kama ni majengo hayana ubora, ni kwa sababu ya usimamizi hafifu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri kama msimamizi wa bajeti, Waziri wa Fedha, fedha hizi anapozipeleka kwenye maeneo mbalimbali kuwe na mpango mahususi wa kusimamia fedha hizi. Maeneo mengi fedha hizi zinachezewa vibaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ujenzi wa madarasa, unakuta hayako kwenye kiwango. Fedha ile ambayo wengine wanakamilisha kabisa kwa kiwango bora, lakini wengine hawakamilishi kabisa. Vituo vya afya, ukifuatilia utakuta vingine havijakamilika kabisa, fedha ni ile ile ambayo wengine wamekamilisha. Hii ni kwa sababu ya usimamizi mbovu. Haitakuwa na maana yoyote kama Mheshimiwa Rais atatafuta fedha, ataleta katika maeneo ya wananchi akitarajia kujenga hospitali, kujenga zahanati, kujenga shule imara na bora, halafu yote hayo yasitokee. Pia wananchi wanatarajia sana kuona kwamba mambo yao yanaenda vizuri, kama ni miradi inaenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tusimamie fedha za Serikali...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa George Malima, ahsante sana kwa mchango wako. (Makofi)
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa ajili ya kunipa nafasi ya kuchangia hoja zote mbili. Mashirika mengi ya umma hayafanyi vizuri yote ambayo tumeyapitia hayafanyi vizuri kabisa na hasa katika maeneo yafuatayo. Kwanza mashirika mengi ya umma yanadaiwa yana mzigo mkubwa sana wa madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mashirika haya hayana uwezo wa kukusanya madeni yao, unakuta shirika linadaiwa lakini pia linawadai watu pesa nyingi sana na mimi nitatoa mfano hapa mmoja Shirika la SIDO. SIDO lina mzigo mkubwa sana wa madeni mwaka 2018/2019 ilikuwa inadaiwa bilioni 4.7 lakini 2019/2020 deni lake limefikia bilioni 8 ongezeko la 77% unaangalia unaona kwamba sasa hili deni wanadai bilioni 5 wao wangekusanya hizo bilioni 5 wangeweza ku- offset hili deni angalau lingekuwa limebaki kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hawana uwezo wa kukusanya madeni yao lakini vilevile hawana uwezo wa kulipa madeni yao, na Shirika hili tunalitarajia sana lingeweza kuwa mkombozi wa uchumi wa nchi hii kwa sababu kazi yake kubwa ni ku-support viwanda vidogo vidogo. Lakini kama linaendeshwa katika mtindo huu, haliwezi kuleta tija yoyoe inayokusudiwa. Serikali lazima iangalie sana kwa ukaribu uendeshaji wa shirika hili kupitia ofisi ya msajili. Bila hivyo hii SIDO haitokuwa na maana yoyote Serikali itaendelea kutoa ruzuku na itaendeshwa na itapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mwaka 2018/ 2019 Shirika lilitengeneza faida ya bilioni 1.56 lakini 2019/2020 limetengeneza hasara ya bilioni 2 sasa unaweza kuona uendeshaji wa namna hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nashauri sana Mashirika haya yajitahidi sana kwanza yawe na utamaduni wa kulipa madeni yao mara wanapopata huduma au wanapofanya biashara walipe madeni hata kama kwa kidogo kidogo. Pia wawe na mikakati mahsusi ya kukusanya madeni kwa wale wanaowadai hiyo itawasaidia kuendesha mashirika yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia matumizi sheria imewekwa ya fedha Na. 16 ya mwaka 2015 ambayo inaweka ukomo wa kutumia mwisho 60% kuna kitu gani mashirika mengi yamepita 60% kuna tatizo gani katika Serikali kuhakikisha kwamba inasimamia hii sheria kila shirika likaenda kama sheria inavyotaka. Kwa sababu kila shirika unaloliona utakuta limevuka hiyo sheria limevuka huo ukomo wa 60% kwa nini Serikali haisimamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nashauri sana Serikali kupitia Msajili wa Hazina mashirika haya yabanwe yaweze kutekeleza sheria hii ya fedha Na. 16 hii itasaidia hata matumizi yale yasiyo ya lazima yataweza kuepukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna shida ya miradi mingi kutokukamilika kwa wakati lakini ukiangalia sababu kubwa ziko moja kwanza ni michakato mingi kila wakati shirika liko kwenye mchakato mipango iko kwenye mchakato litaanza yako mashirika tumeyakuta wana miradi imepita hata miaka 10 haijakamilika. Mfano hata mradi wa Liganga na Mchuchuma kila wakati mnaambiwa michakato inaendelea, lakini pia Serikali haitoi maamuzi kwa wakati au haitoi maamuzi mapema kwamba mradi huu uanze wakati fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nayo ni shida nyingine kwamba maamuzi hayafanyiki halafu fedha zinaendelea kutumika mradi haujaanza na hizi fedha za wananchi walipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine hata ile iliyoanza kidogo Serikali haipeleki fedha ili miradi ile iendelee kutekelezwa kwa wakati. Kwa hiyo, tuna tatizo hilo kwamba mashirika yetu tusipokuwa waangalifu hayawezi kutuletea tija tunayoikusudia. Tunategemea kila shirika liwe na uwezo wa kutoa mchango katika mfuko mkuu wa Serikali. Lakini sasa hivi mengi hayana huo uwezo ama yanachangia kidogo sana ama mengine hayachangii kabisa lakini kwa sababu hatujawa serious katika maeneo haya. Mashirika haya lazima tuyasimamie vizuri tukitaka tukuze uchumi wa nchi hii tukitaka tupate tija, tukitaka Serikali ipate gawio ni lazima tuwe na utaratibu wa kuyasimamia kwa karibu. Serikali, TR lazima isimamie.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Lakini kabla sijachangia na mimi naomba kushiriki kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri sana ambayo amenza kuifanya tangu alipoingia madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa Mpwapwa, kama unavyojua Mpwapwa ina majimbo mawili, tumepata madarasa mengi, madarasa takriban 103. Madarasa 20 ya shule za msingi na madarasa 83 shule za sekondari, ni kitu ambacho hakijawahi kutokea, kwa hiyo tunamshukuru sana. Lakini pia kwa ujumla wetu kwenye haya majimbo mawili, ya Kibakwe na Mpwapwa, tumepata vituo vya afya vitatu, shule za sekondari zinazojengwa na nguvu ya Serikali ni tatu, na pia barabara zote za vijijini zimefunguka. Napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kufanya kazi hii nzuri. Naamini majimbo yote yamenufaika na fedha hii ambayo Mama Mheshimiwa Rais wetu ametoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimshukru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ajili ya uongozi wake mzuri sana hapa Bungeni. Mtu mnyenyekevu, ambaye ameongoza Bunge hili kwa kipindi kirefu akisimamia mambo ya Serikali katika Bunge hili, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa nianze kuchangia mambo matatu. Kwanza naomba nizungumzie habari ya barabara. Sera ya Serikali ni kuunganisha miji yote ya mikoa na wilaya kwa barabara za lami, lakini bahati mbaya sana katika Jimbo letu la Mpwapwa na Kibakwe sisi barabara haijaunganishwa kwa lami. Tuna kipande kinachotoka njia panda ya Kongwa kuelekea Mpwapwa Mjini, lakini pia kutoka Mpwapwa Mjini mpaka Chipogolo. Barabara hiyo ni kati ya ahadi za Mheshimiwa Rais Marehemu Magufuli, aliahidi kwamba ingejengwa katika kiwango la lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Mpwapwa ni mji mkongwe lakini umedumaa sana kimaendeleo kwasababu ya tatizo la barabara hii. Hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuthubutu kuja kuwekeza Mpwapwa kwasababu ya barabara mbaya. Na kutokuwa na wawekezaji wa kutosha katika mji wa Mpwapwa kiuchumi hatuwezi kukua. Kama mnavyojua uwekezaji ndio unazalisha ajira nyingi sana kwa vijana wetu, kwa hiyo suala la ajira kwa vijana wa Mpwapwa, kama ile barabara haitawekwa lami, itabaki kuwa historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana barabara hii Serikali mwaka huu wa fedha 2022/2023 basi tukumbuke, kutokee muujiza tupate barabara ya lami. Waheshimiwa Wabunge walionitangulia wote wamepiga kelele; tangu uhuru kipande hiki hakijawekwa lami, ni kama kilometa 40. Kwahiyo wananchi wa Mpwapwa wanaendelea kuteseka na hali ngumu ya uchumi kwasababu hawana interaction na watu. Ukiwa hauna barabara watu hawawezi kufika kwako.hata katika maisha ya kawaida nyumbani kwako kama hakuna njia safi ya watu kupita kuja kukusalimia hawatafika, kwa hiyo hautakuwa na interaction na watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo ningependa kuzungumza ni madaraja. Pale Mpwapwa tuna madaraja matatu ambayo yana umuhimu mkubwa sana, yote yanaunganisha majimbo yote mawili. Kuna daraja la Godegode, daraja la Gulwe na Daraja moja la TANESCO, lipo mjini. Mheshimiwa Waziri Simbachawene anashindwa kwenda kule kwenye Jimbo lake kwasababu madaraja yote yamevunjika. Ukipita njia hii ya Godegode daraja limevunjika, ukipita njia hii ya Gulwe daraja limevunjika. Sasa utasikia watu wanamtafuta hawamuoni, lakini atapita wapi? Kwa hiyo ninaomba sana madaraja haya pia yaangaliwe kwa karibu sana (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine nizungumzie sekta ya kilimo. Wengi tumezungumza; katika Wilaya ya Mpwapwa wilaya nzima ina maeneo mengi mazuri sana kwa ajili ya Kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano Kata za Chunyu, Mlembule, Lumuma, Mbuga pamoja na Nduga ni maeneo ambayo yana maji; lakini shida tunayoipata kule hata kilimo kile kinachofanywa na wakulima wetu pale hakina tija kwasababu hakuna miundombinu. Mimi ningeshauri Serikali; kwamba tukitaka ku-emphasize kilimo lazima tuangalie sana kilimo cha umwagiliaji, kilimo ambacho hakitegemei mvua za msimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka huu mvua hapa Dodoma haijamalizia, kwa hiyo mazao mengi yanakauka sasa. Lakini tungekuwa tunamwagilia maana yake tungekuwa na uhakika wa chakula. Kwa hiyo ninaomba sana Serikali iwatengenezee hawa watu miundombinu barabara zimefunguka lakini wakipata Kilimo wakalima kwa mfano kule tulilima vitunguu sana, vitunguu vile vinaweza kusafirishwa kutoka kwenye maeneo yao kwenda kwenye masoko, kwenda Dar es salaam ama kuja Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa hivi wanalima kidogo sana. Tumesema ajira kubwa katika nchi hii inapatokana kutokana na kilimo, asilimia 65 ya ajira inapatikana kutokana na kilimo, lakini je, ni asilimia ngapi ya hizi ajira? Hawa watu walioajiriwa na kilimo ni asilimia ngapi wanapata tija halisi inayotakiwa na Kilimo? Utakuta asilimia kubwa ni watu wanaolima kilimo cha kujikimu tu, hawapati mazao yanayotakiwa kwasababu ya ukweli kwamba miundombinu ya umwagiliaji haipo; na mimi ningependa sana Wizara ya Kilimo ijikite sana kwenye miundombinu ya umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la mazingira pale Mpwapwa Mjini. Mji wa Mpwapwa umepitiwa na korongo kubwa sana. Lile korongo limeleta athari nyingi kwa miaka mingi sasa. Maisha ya watu yamepotea na nyumba zimechukuliwa. Hata mwaka huu nilimletea picha za athari zilizotokea Mheshimiwa Waziri wa Mazingira. Tunaomba sana Serikali iangalie namna ya kutatua hilo tatizo la mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naona kengele ya pili imegongwa naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja iliyopo mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha nia ya dhati kabisa ya kufanya uwekezaji katika nchi yetu. Shilingi trilioni 73 ambayo yote imeenda kwa ajili ya uwekezaji si fedha kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma, nimepata nafasi ya kupitia mashirika mbalimbali. Zipo changamoto nyingi. Changamoto moja wapo ambayo ningependa kuizungumzia hapa ni mzigo mkubwa wa madeni ambayo taasisi hizi zinayo. Taasisi nyingi zinaendeshwa kwa hasara kwa sababu zina madeni mengi sana, lakini pia hata unapokutana nazo huwezi kuona mikakati ya dhati kabisa ya kulipa hayo madeni. Kwa hiyo taasisi kama hizi zinazoendeshwa kwa madeni huwezi kutegemea utapata tija ile iliyokusudiwa wakati wazo la uwekezaji lilipoanzishwa. Kwa hiyo ndiyo maana unaona Mashirika haya yanashindwa hata kutoa gawio katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa sababu wanadaiwa lakini pia hawana mikakati ya kulipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetoa mifano tu kidogo ya Mashirika kama mawili au matatu, kwa mfano Taasisi ya NSSSF mwaka 2019/2020 ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 239.58 lakini mwaka 2020/2021 ikawa inadaiwa shilingi bilioni 256.43 na 2021/2022 inadaiwa shilingi bilioni 306.29. Sasa taasisi kama hii inahusika na kulipa mafao ya watumishi wale wanaostaafu. Nataka kujiuliza taasisi yenye madeni kama haya inaweza kuendelea kuwa na uwezo wa kulipa michango ya wastaafu, au ndiyo kama zile tunazoona mtaani kila siku wastaafu wanazunguka mtaani Kwenda na kurudi kwa sababu mashirika haya hayafanyi vizuri? Mimi ningeshauri sana Serikali lazima tujikite kutafuta sababu kubwa ambayo inasababisha mashirika haya yasifanye vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hili la uendeshaji mbovu. Wale wanoendesha, kama ambavyo wamesema wengine, kuna wafanyakazi ambao siyo waaminifu, hawatumii vizuri michango hii ya watumishi; kwa hiyo lazima tuwamulike na tuwachukulie hatua. Nimeona baadhi ya Mawaziri wameonyesha commitment kwamba Serikali itaendelea kuchunguza wale wote ambao hawafanyi vizuri kwenye mashirika ya umma wachukuliwe hatua. Mimi ningependa sana kusikia siku moja watendaji wabovu wanachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye Shirika la Michezo ya Kubahatisha nalo kwa miaka mitatu mfululizo limeendelea kupata madeni huku madeni yakiendelea kukua. Kwa mfano, mwaka 2019/2020 lilikuwa na deni ya shilingi milioni 742.5, lakini mwaka 2020/2021 likawa linadaiwa shilingi bilioni 2.8. Hata wao tulipokutana nao hawaonyeshi nia ya dhati kwamba wana mikakati gani ya kuhakikisha kwamba deni hili linalipika na linapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi nyingine ni Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), nalo pia ni Shrika ambalo lina mzigo mkubwa sana wa madeni. Mwaka 2019/2020 lilikuwa linadaiwa shilingi bilioni 1.36, lakini hadi 2021/2022 likawa linadaiwa shilingi bilioni 5.9. Mashirika haya yote usitegemee kwamba yanaweza kutoa mchango katika Mfuko Mkuu wa Serikali, lengo ambalo kwa kweli ndilo kubwa. Unapowekeza hata kwenye biashara yako binafsi unategemea upate faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unawekeza halafu hupati faida kila mwaka, na kila unapokwenda kuangalia hesabu zake hazionyeshi matumaini maana yake huwezi kupata faida; na ndiyo maana tunashauri kwamba Serikali ijaribu kupita upya mashirika haya; hebu tuone yale ambayo yako kabisa yana dhamira ya kufanya biashara na kuleta tija iliyokusudiwa yaendelee na yapewe uwezo; lakini yale ambayo hayafanyi vizuri ama menejimenti zibadilishwe na bodi ama mashirika hayo yaunganishwe na mashirika mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ningependa kulizungumzia kidogo hapa ni utegemezi wa ruzuku. Yapo mashirika mengi yanategemea sana ruzuku; na ukishangaa shirika ambalo linapewa ruzuku ya Serikali bado linaendeshwa kwa hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeomba hapa kwamba Serikali iangalie vizuri, kwamba, kama shirika halifanyi vizuri hakuna sababu ya kupeleka fedha pale, ni afadhali tuwapeleke wale wanaofanya vizuri. Mashirika mengi yanategemea ruzuku, ni pamoja na NEMC pia. Mwaka 2022 ilipata shilingi bilioni nne zilikopwa kutoka Serikalini. Sasa ukiangalia bado halifanyi vizuri, bado lina mzigo wa madeni na bado Serikali inapeleka fedha nyingi mahali pale; nadhani tuangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia shirika lingine ni Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA), pia linapata ruzuku nyingi sana. Na hata ile ziada ambayo wana-register kila mwaka inatokana na fedha kutoka ruzuku ya Serikali sisi tungetegemea tuone ziada inayozalishwa na wao wenyewe na kwa ruzuku hii kwa mfano VETA mwaka 2020/2021 walipata ruzuku ya shilingi bilioni 62 kutoka Serikalini. Na ndiyo maana ukiangalia kwenye hesabu zao kuna ziada kwa miaka mitatu mfululizo, ni kwa sababu fedha nyingi inatoka Serikalini lakini wao wenyewe hatujaona kama kuna kitu wanajaribu kufanya…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuzungumza ni uzingatiaji wa vigezo vya Msajili wa Hazina; vigezo vinavyohusu utendaji wa kifedha na utendaji wa ujumla. Msajili wa Hazina amepewa mamlaka ya kuweka vigezo (KPIs) kwa ajili ya kuendesha mashirika, lakini yako mashirika ambayo hayafuati hata kimoja, je mfano tu Bodi ya Chai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Chai ni kati ya mashirika ambayo hayafuati vigezo vya Msajili wa Hazina. Kwa mfano ukiangalia kwenye gharama za watumishi kwa matumizi ukomo wa TR ni asilimia 40 lakini wao wanaendesha kwa asilimia 64. Kwa utegemezi wa ruzuku TR anazungumzia hoja ya kupunguza kutegemea ruzuku lakini wao wanategemea ruzuku kwa asilimia 86. Uwiano wa matumizi kwa mapato, ukomo wa TR ni asilimia 50 lakini Bodi ya Chai wao wanaendesha kwa asilimia 116 lakini unaona kwamba hawaendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na yapo mashirika mengine, kwa mfano Mfuko wa Pembejeo wa Taifa na NHIF; yote haya hayafuati vigezo vile ambavyo vimewekwa na Msajili wa Hazina lakini unaangalia unaona kwamba Msajili wa Hazina hana meno, hana namna ya kuwachukulia hatua watu kama hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri muswada uletwe turekebishe sheria. Msajili wa Hazina awe na Sheria, awe na nguvu ya kuyawajibisha Mashirika kama haya ambayo hayafuati taratibu hizi. Taratibu hizi zimewekwa maalum kwa ajili ya kusaidia mashirika yetu yaweze kufanya vizuri. Sasa kama hakuna kitu cha kuwasukuma wafanye hivyo ndiyo maana tunaona mashirika mengi sana hapa hayafuati na yanafanya yanavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni tatizo la kuchelewesha kuwalipa wakandarasi na wale watoa huduma. Tatizo hili limeleta hasara kubwa sana serikalini. Unapochelewesha kumlipa mkandarasi au mtoa huduma maana yake kunakuwa na penalty, kunakuwa riba, baadaye unapokuja kulipa lazima ulipe na riba. Tumeona kwenye ripoti kwamba kwenye mashirika 12 ambayo yalichelewesha kuwalipa wakandarasi na watoa huduma, walilazilika kulipa zaidi shilingi bilioni 63. Hizi fedha ni nyingi sana na zingeweza kufanya kazi nyingine ya kuwaletea wananchi Watanzania maendeleo lakini zinalipwa kwa ajili ya riba na wale waliofanya hivyo, waliochelewesha kuwalipa wakandarasi au watoa huduma wanaendelea kuwa ofisini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, jambo hili ni jambo ambalo linatia aibu, kwa nini tucheleweshe kuwalipa halafu tuingie kwenye penalty kubwa kama hii, shilingi bilioni 63.7. Mimi nadhani watu kama hawa Serikali lazima iwachukulie hatua, kwa sababu wanatuingiza kwenye hasara kubwa na fedha hizi ni za walipakodi na wakati mwingine walipakodi wa chini kabisa ndio wanaolipa hizi fedha. Sasa zinatumika vibaya na bado tunaendelea kusema waendelee kuwa ofisini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hatua lazima zichukuliwe, tumpe meno Msajili wa Hazina, anaposimamia mashirika haya awe na nguvu ya kumwajibisha Mtendaji au kuiwajibisha Bodi ya hiyo taasisi. Hii itatusaidia kupunguza gharama kama hizi ambazo zimekuwa zikitokea, ni kama hakuna mtu wa kuangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo na hii imetuletea shida pia. Unapochelewa kukamilisha mradi gharama zinapanda kwa sababu bei za vifaa zinabadilika, lakini pia kuna zile gharama za kimkataba. Mkandarasi mlikubaliana ujenzi kwa miaka mitatu, inafika miaka saba, lazima kuwe na penalty, ndio haya mambo ambayo tunayasema. Kwa nini tunachelewesha miradi ya maendeleo? Kwa nini haikamiliki kwa wakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna watu wanahusika, Serikali ichukue hatua kuliko kusubiri mpaka tulipe gharama hizi, tunasubiri mpaka vifaa vinapanda bei. Kwa hiyo, gharama iliyokuwa imekusudiwa kulipwa kwa huo mradi mmoja, unapokuja kukamilika tunalipa mara tatu zaidi, pamoja na penalty, pamoja na gharama za kimkataba. Kwa hiyo nafikiri na hili jambo ni muhimu sana, ningependa pia nilizungumzie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikubaliane na wenzangu wote kuunga mkono hoja. Tuendelee kum-support Mheshimiwa Rais kwa kumsaidia katika maeneo kama haya ambayo yameonekana yanaleta shida katika uwekezaji. Fedha hizi amezitoa kwa wingi, shilingi trillioni 73, sisi kumuonesha kwamba tunamuunga mkono lazima tusimamie haya mashirika kwa uhakika na kwa usahihi mkubwa sana. Bila hivyo hizo fedha zitakuwa zinatolewa, tija haipatikani na tunaendelea kusema tuna uwekezaji hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Wizara hii ya Kilimo. Kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye anaendelea kutulinda, kututunza na kutufanya tuendelee na shughuli zetu kama kawaida. Pili, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi nyingi sana katika Wizara hii ya Kilimo. Sisi kule Mpwapwa tumepata bwawa kubwa sana la umwagiliaji lenye thamani ya shilingi bilioni 27.8 ambalo ujenzi wake unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe. Yeye anajua jinsi nilivyofuatilia na hatimaye akakubali na sisi watu wa Mpwapwa tupate bwawa hili. Nakushukuru sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde, nawapongeza kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia bajeti ya Wizara hii. Mheshimiwa Waziri ameanza kueleza hali ya kilimo katika nchi yetu ya Tanzania. Ameeleza kwamba, kuna ukuaji wa Sekta hii ya Kilimo kwa 0.9% na kwamba, kulikuwa na ukuaji wa 3.3% mwaka 2022, lakini kwa ujumla mwaka 2023 kumekuwa na ukuaji wa 4.2%.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa jitihada hizi, lakini naamini kabisa nchi yetu inaweza kukua zaidi ya hapa. Ukuaji huu ni mdogo ukilinganisha na maeneo ya kilimo tuliyonayo katika nchi yetu, tunaona kwamba tungeweza kufika katika asilimia kubwa kuliko hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda niongelee kwenye eneo la umwagiliaji. Umwagiliaji ndicho kilimo cha uhakika kuliko kilimo kingine chochote na ripoti au bajeti imeeleza kwamba, mpaka sasa hivi nchi yetu ina hekta 727,000.3, ndilo eneo ambalo linafanyiwa kilimo cha umwagiliaji. Ukiangalia nchi yetu ni kubwa na pia maeneo ni mengi ambayo kama yangeweza kutambuliwa, kujengwa mabwawa na kuwekewa miundombinu ya umwagiliaji, ukuaji wa sekta hii ya kilimo ungeweza kuwa mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye pato la Taifa bado ni mdogo. Tofauti yake ni ndogo sana, kutoka mwaka 2022 mpaka mwaka 2023 imekua kwa asilimia 0.3, kwa hiyo, bado utaona mchango wake ni mdogo sana. Ni mdogo kwa sababu gani? Eneo tunalolitumia, kwa ajili ya umwagiliaji ni eneo dogo la hekta 727,000 tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule Mpwapwa tuna maeneo mengi, lakini naamini hata sehemu nyingine za nchi yetu pia, kuna maeneo mengi ambayo yana sifa ya kufanya kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano, kule Mpwapwa, Kata ya Chitemo kuna eneo zuri, Mlembule kuna eneo zuri, Godegode, ukienda kule Pwaga, ukienda Kitati, ukienda Lumuma, haya maeneo yote kama yangeweza kufanyiwa utafiti na Serikali yakaweza kujengewa miundombinu, kilimo hiki kingeweza kuwa na tija na kingeongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni ukosefu wa mbegu bora. Wakulima wengi wa Kitanzania wana juhudi sana ya kilimo, lakini shida ambayo wanakutana nayo ni kwamba, unapofika msimu wa kilimo wanapokwenda madukani kununua mbegu, wapo wafanyabiashara wengine ambao siyo waaminifu, wanauza mbegu ambazo ni fake. Mbegu ambazo hazijafanyiwa utafiti, hazina sifa ya kuitwa mbegu bora. Kwa hiyo, wakulima wanapokwenda kupanda zile mbegu, matokeo yake hawapati ile tija ambayo walikuwa wanaitarajia. Hili ni tatizo kubwa sana. Naishauri Wizara ya Kilimo, wakati msimu wa kilimo ukikaribia wafanye ufuatiliaji kwenye haya maduka yanayouza mbegu, watakutana na mbegu hizi fake ninazosema. Hii itatusaidia kupunguza athari hizi zinazotokea.
Mheshimiwa Spika, pia, nimeona wanasema wametenga fedha katika sekta hii kama shilingi bilioni 43 hivi. Fedha hizi wanasema kazi yake kubwa ni kujaribu kufanya utafiti ili kupata mbegu bora na kuzisambaza. Basi bajeti hii ingejikita sana kwenye utafiti ili tuwe na mbegu bora na lengo liwe ni kutosheleza nchi yetu yote ya Tanzania. Wananchi wetu wanaoshughulika sana na kilimo waweze kupata mbegu bora kwa wakati na kwa bei ambayo ni affordable ili waweze kuongeza kilimo na ikifika mwakani au angalau hata baada ya miaka miwili tuweze kuona matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bashe anachakarika sana kujaribu ku-transform kilimo katika nchi yetu, nampongeza sana. Tunaona mikakati mingi anayoifanya, lakini kama hawezi kujikita kwenye upatikanaji wa mbegu bora, juhudi zake zote zinaweza kuwa hewani. Kwa hiyo, naomba sana nimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba, mbegu ndiyo kitu muhimu sana katika kilimo. Ni lazima tupate mbegu zilizo bora ambazo watu wetu wanaweza kunufaika nazo. Kama tunavyosema, kilimo ndicho kinachangia asilimia kubwa ya ajira katika nchi yetu, lakini kwa miaka mitatu nimefuatilia hali ya asilimia ya ajira zinazotokana na kilimo iko katika range ya 65 mpaka 70, kwa nini haikui? Ni kwa sababu ya mambo kama haya madogomadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza, hatuja-utilize eneo letu lote la umwagiliaji, lakini pili, hata wakulima wetu hawatumii mbegu zile ambazo tunadhani ni bora ambazo zinaweza kuleta tija. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia sana suala la utafiti ili tuwe na mbegu bora.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo pia tunakutana nalo kwenye vijiji, ni wakulima wetu hawana elimu ya kilimo. Tunao Maafisa Ugani, lakini hawatoshelezi. Taarifa yake inasema mpaka sasa hivi tuna asilimia 35 tu ya Maafisa Ugani ambao wako kwenye maeneo yetu, lakini tuna upungufu wa Maafisa Ugani 20,000 na kuendelea, sasa hili ni tatizo. Kata moja inakuwa na Afisa Ugani mmoja, vijiji ni sita, anawezaje kufanya kazi katika mazingira hayo?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunadhani kwamba, Serikali ni lazima ichukue hatua muhimu na maamuzi magumu kuajiri Maafisa Ugani kwa wingi. Kama tunataka kupata matokeo, kama tunataka kuongeza pato la Taifa kupitia Sekta hii ya Kilimo ni lazima tuwe na wataalam wanaojua ambao watawasaidia wakulima wetu kulima kilimo cha kisasa. Pia, wawe wanaweza kutambua mbegu fake na mbegu bora kwa sababu ya utaalam watakaokuwa nao. Bila hao, wakulima wetu wataendelea kulima kama kawaida, watalima kilimo walichokizoea na matokeo yake hakutakuwa na tija.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuchangia na pengine litakuwa la mwisho ni kuhusu uhakika wa masoko kwa mazao yetu ya kilimo. Sasa hivi ukienda vijijini mazao mengi yameiva na yamekomaa, lakini walanguzi wameshavamia kule wananunua kwa bei ya chini kabisa. Kwa hiyo, mkulima anapomaliza msimu wa kilimo anakuwa haoni kitu alichopata. Ameuza mazao yote kwa bei ndogo, wanaofaidi ni wale middlemen wanaokuja kulangua na kwenda kuuza mahali pengine.
Mheshimiwa Spika, Serikali ingekuwa na mfumo wa kuwa na masoko rasmi ambayo mkulima anajua nikilima karanga, nikilima ufuta, nitakwenda kuuza mahali fulani na bei inaweza kuwa imetangazwa inajulikana. Hii itawasaidia kujikwamua kiuchumi, lakini pia, sekta itakuwa na itaongeza pato la Taifa. Kwa hiyo, masoko ni jambo la muhimu. Hatujawa na soko kamili katika nchi hii, wakulima wetu hawajui. Tunajaribu kuhangaika kutumia vyama vya ushirika, lakini bado kuna maeneo mengi vyama hivi havifiki. Kwa mfano, Wilaya yetu ya Mpwapwa, sidhani kama kuna chama cha ushirika pale. Wakulima wetu wanajihangaikia wenyewe, wakishapata mazao walanguzi wanakuja wanachukua mazao yao kwa bei ya chini, wale wanabaki maskini mwaka baada ya mwaka. Kwa hiyo, naomba sana jambo hili lichukuliwe.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, miaka miwili mitatu huko nyuma Kanda ya Kati tulipiga kelele sana juu ya kilimo cha alizeti na zabibu, lakini kuanzia mwaka jana na mwaka huu sisikii kitu. Ni kama hiki kitu kilikuwa ni mbio za sakafuni. Sasa hivi hakuna tena pressure ya kuhimiza watu walime alizeti, walime zabibu. Hii inawezekana ni kwa sababu ya bei za mafuta ambazo hazieleweki, lakini pia soko la zabibu ambazo zinalimwa hapa Dodoma bado halijulikani.
Mheshimiwa Spika, watu wanatengeneza michuzi ya zabibu, lakini mahali pa kuuza hakuna, matokeo yake inaharibika. Kwa hiyo, watu wanaacha wanakata tamaa. Wakulima wanakata tamaa kuendelea na kilimo kwa sababu hakilipi na wala hakijawa na mfumo rasmi wa kuwasaidia wakulima. Kwa hiyo, tukitaka wakulima wetu wafanye vizuri, ni lazima tuwawekee mazingira mazuri kwa maana ya masoko, mbegu na wataalam wawepo, hapo ndipo tutaona kilimo hiki kinakua. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bashe naunga mkono hoja, lakini zingatia haya mambo. Kilimo chetu kitakua na wananchi wetu watafaidika. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia Hotuba hii ya Waziri wa Maji. Kwanza naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa jinsi ambavyo sisi watu wa Mpwampwa ametugusa kwa upande wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunalo bwawa kubwa linajengwa pale Msagali lenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 27 lakini tunayo madarasa zaidi ya 80 tumejenga katika kipindi hiki lakini pia barabara upande wa TARURA tumefungua barabara karibu zote za vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni pia tumepewa fedha kwa ajili ya kujenga mabweni katika shule yetu ya Sekondari ya Mpwawa high school ili iweze kuchukua wanafunzi wengi. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu ni mara ya kwanza Mpwapwa kupata miradi mingi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru sana Waziri Maji ndugu yangu Aweso. Aweso anasifa moja ni msikuvu sana, Mpwapwa tuna miradi mingi ya maji, tuna mradi wa Kisokwe – Biro – Mazae lakini tuna mradi wa Mpwapwa Mjini ambao utahudumia Ving’hawe mpaka Mang’angu lakini tuna mradi mwingine ambao unatekelezwa pale katika Kata yetu ya Lupeta ambayo utaudumia vijiiji viwili Lupeta Namakutupa. Tuna mradi katika shule yetu ya Sekondari ya Berege unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, concern yangu kubwa nikwamba miradi hii haitekelezeki, haikamiliki dhamira njema ya Serikali ni kumtua ndoo kichwani mama wa kitanzania lakini jambo hili linaenda linachukua muda mrefu sana. Katika miradi hii niliyoitaja katika Wilaya ya Mpwapwa ina miaka zaidi ya miwili sasa. Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kwamba kuna siku moja nilikupeleka katika Shule ya Sekondari ya Berege ukaona shida ya watoto wale, watoto wako wengi zaidi ya 1,000 hawana maji ya kunywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukatoa maelekezo kwamba, kisima kichimbwe mara moja na kwamba kilichimbwa mara moja lakini baada ya pale watoto wale wamekuwa wakishuhudia mtambo ule. Hakuna pampu imewekwa, na shida ya maji inaendelea katika Shule ya Sekondari ya Berege. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri utoe maelekezo ya haraka kama ulivyotoa mara ya kwanza kuchimba, utoe maelekezo kisima kile kiwekwe pampu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, iko miradi ya kuchimba visima virefu katika jimbo langu la Mpwapwa iko katika vijiji vya namba thelathini Kata ya Mlembule kule, Nana, Ngaramiro, Katechitemo kuna Igojirani kuna mradi wa kusambaza maji unaendelea. Mheshimiwa Waziri miradi hii kila mwaka naiona kwenye bajeti inakuja bajeti inapita vijiji hivi maji hayachimbwi, na nilikuwa nategeamea kwamba miradi ya kuchimba visima ni miradi yenye gharama ndogo sana, lakini watu wanateseka sana kwa sababu ya miradi midogo kama ile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuwa nakuomba sana Mheshimiwa unapo wind up hotuba yako ningependa kusikia miradi hii ya Mpwapwa itatekelezwa lini? Naamini Mheshimiwa Rais angetaka kuona kweli wakinamama wakitanzania wametuliwa ndoo kichwani. Lakini naona kama tunasubiri mpaka wachoke sana ndiyo tutue hizo ndoo kichwani. Kwanini mpaka wachoke? Dhamira hii nadhani hii slogan ingekamilika haraka ili tutafute nyingine, tumekuwa kila mwaka tunazungumzia kumtua ndoo kichwani mama wa kitanzania lakini matokeo yake bado utekelezaji haupo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri tuwaongezee bajeti. Najua labda tatizo ni fedha ndiyo maana miradi hii aikamiliki tuongeze bajeti ili miradi hii ikamilike Waheshimiwa Wabunge siasa ya kwenye majimbo yetu ni maji piga uwa ni maji, maji lazima yapatikane. Sasa kama maji hayapatikani watu wanashuhudia mkandarasi yupo anazunguka tu hakamilishi mradi siasa ya kule kwenye majimbo inakaa vibaya. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri uliangalie sana jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizunguzia ni utaratibu wa kutoa bili za maji, kumekuwa na malalamiko sana kwa wananchi kwamba wanabambikiwa bili maana yake nini? Maana yake bili inayokwenda, inayomkuta mraji wa maji inakuwa kubwa kuliko maji ambayo ameyatumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani hii inatokana na ukweli kwamba wafanyakazi wa mamlaka zetu wengi hawafiki kwenye maeneo ambako wananchi wanatumia maji. Badala ya kusoma zile mita wanafanya hesabu za makadirio sasa katika kukadiria kuna impact mbili moja ni hasi kwamba Taasisi yetu ya Maji itapata hasara kwa sababu unaweza uka-under bill ukamuwekea bili ndogo kuliko maji anayotumia. Lakini nyingine ni kwamba mnunuaji unaweza ukamzishia bili akatakiwa kulima hela nyingi kuliko kiasi cha maji anachotumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri kwanini msi–shift kutoka kwenye current billing system mwende kama wanavyofanya watu wa TANESCO. Tufanye pre-paid system ili mtu akinunua unit ya maji anatumia ikiisha maji yanakatika, hili aweze kupata hiyo huduma tena lazima anunue kama tunavyonunua umeme na tunavyonunua simu hii itawasaidia kuondoa hizi lawama na kelele kwa ajili ya watumiaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia kuna hizi taasisi za watumiaji wa maji wanaita COWSOS, ideally it was good lakini utekelezaji wake nimeona kama umekuwa na matatizo makubwa ni changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, mfumo ni kwamba kunakuwa na kamati za maji kwenye vijiji lakini wale watendaji ambao wanafanya kazi technical wanaletwa na uongozi wa Wilaya wa Maji RUWASA. Sasa wakishwa letwa pale kinachotokea ni kwamba wale watendaji wanapo ajiriwa pale kamati ile ya wanakijiji inampa mkataba, lakini utakapompa maelekezo anapofanya vibaya hawezi kuwasilikiliza hawa anasikiliza wale waliyomleta.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kumekuwa na vurugu miradi haiendelei, matumizi mabaya ya fedha lakini wale wameletwa na mtu wa wilaya. Kwa hiyo, hawawezi kusikiliza Kamati, Kamati haiwezi kutoa ushauri kwa huyo mtu. Baadae kamati ya kijiji ambayo ndiyo wenye maji wanageuka kuwa watumwa wa mtendaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana jambo hili Mheshimiwa Waziri walipitie upya ili waone kama kuna namna nyingine ya kubadilisha.
Mheshimiwa Spika, wameharibu mambo mengi, mahali pengine niliona Mtendaji Mhasibu wa maji ana–paralyze mpaka system ya kijiji. Wakitaka kuitisha mkutano waulize mapato na matumizi ya mradi wa maji, anahonga wenyeviti wa vitongoji ili wasiitishe mkutano asije akaulizwa hayo maswali. Kwa hiyo unakuta hata Serikali ya Kijiji haiwezi kufanya functions zake kwa sababu anawa–paralyze kwa visenti (cent) vilevile vya mradi wao…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningeomba sana Mheshimiwa Waziri anaposimama basi atueleze kwa nini miradi haikamiliki, na ikiwezekana aniambie Mpwapwa miradi itakamilika lini?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango katika hotuba hii ya Wizara ya Afya. Kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, kwa ajili ya kazi nyingi nzuri ambazo zinaendelea kufanyika katika nchi yetu. Sisi watu wa Mpwapwa Mheshimiwa Rais, amefanya mambo mengi makubwa na hasa ktika sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Spika, tumeopata shilingi milioni 900 katika ukarabati wa hospitali yetu ya wilaya. Mtakumbuka huko nyuma nimezungumza sana habari ya uchakavu wa ile hospitali lakini nashukuru sana Wizara imepata tarifa na imesikia. Sasa hivi ukarabati unaendelea lakini tunajenga jengo jipya la huduma ya mama na mtoto. Kwa hiyo, nina mshukuru sana Rais, kwa ajili ya kutusaidia hilo.
Mheshimiwa Spika, sio hilo tu, tumejenga jengo la ICU kwa gharama ya shilingi milioni 250 na pia tumepata vifaa katika jengo hilo tayari vimefungwa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400 na huduma zinaendelea pale. Pia, kwa muda mrefu hospitali hii ya Mpwapwa haikuwa na x–ray lakini leo nina furaha kuwaambia Bunge lako Tukufu kwamba sasa tuna digital x–ray na wananchi wa Mpwapwa wanaendelea kufurahia huduma za Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha pia tumefanikiwa kujenga au kumalizia maboma ya zahanati nane na zingine kazi zinafanyika tayari zinaendelea kumaliziwa na nyingine tayari zinatoa huduma kwa wananchi. Pia, tumeopata vituo vya afya viwili, kituo cha Iwondo na kingine tumejenga Matomondo. Vituo hivi vimejengwa maeneo ya Kimkakati, maeneo ambayo yako mbali sana na mjini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri amesema katika mwaka huu wa fedha wamepanga kununua ambulance zaidi ya 700. Niombe Mheshimiwa Waziri, utukumbuke na sisi wa Mpwapwa, tuna vituo vitatu kwa ujumla, kituo cha Mima, Iwondo na Matomondo vituo ambavyo viko kwenye maeneo ya kimkakati. Lakini pia tuna hospitali yetu ya wilaya haina gari ya kubebea wagonjwa, kwa hiyo, tukumbuke kwa ajili ya kupata magari ya kubebea wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri nikushukuru wewe binafasi, umekuwa moja ya Mawaziri wanaofanya kazi zao kwa umakini sana. Nichukue fursa hii kukupongeza, na hata ukisoma ripoti yako unawea kuona umegusa kila eneo hata tunaposimama kuchangia tunasema kusema kweli tunataka kuweka mkazo tu lakini kwa kweli umejaribu kugusa kila eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia katika eneo la matibabu ya wazee, Mheshimiwa Waziri, umezungumza katika ukurasa wa 55 habari ya kuongeza dawa kwa ajili ya wazee. Lakini kuboresha huduma zao, lakini nikwambie kwamba bado hatujawa na mkakati thabiti wa namna ya kuwahudumia wazee kwa sababu wiki mbili zilizopita nilimpeleka mpiga kura wangu mmoja mwenye umri wa miaka zaidi ya 70. Nilipofika pale hospitali nilikuta kuna mabango yameandikwa mpishe mzee asipange foleni, kuna msamaha wa wazee. Mheshimiwa Waziri, lakini kusema kweli hayo mambo yameandikwa lakini practically hakuna kitu kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wazee wanateseka sana kwa sababu ya umri na uchumi wao mdogo basi wanateseka na wengi wanafariki kwa sababu ya kuteseka na kuchelewa kupata matibabu. Mheshimiwa Waziri, ningekushauri jambo hili mliangalie upya ikiwezekana mje na mpango mahususi au sera mahususi ya kuwatibu wazee wetu.
Mheshimiwa Spika, wazee wetu ni wengi wamefanya kazi katika Taifa hili kwa uaminifu mkubwa lakini leo inaonekana kama hatuwajali kabisa. Kwa hiyo, mzee yule hata tulipofika issue nyingine ikawa ni dawa ile aliyotakiwa kupata hakuna. Nikupongeze nimeona mmeongeza dawa tano kwa ajili ya wazee labda hilo litatusaidia. Pia shida iko pale kwamba dawa hazipo. Mheshimiwa Waziri, uje na sera maalum kwa ajili ya wazee hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, ambalo ningependa kukusisitiza pia ni uhaba wa dawa. Nimeona kwenye ripoti umezungumza mikakati ya kuongeza dawa hospitali lakini kwa kweli hospitalini bado kuna shida ya dawa. Kama nilivyosema watu wengi hawawezi kunua dawa nje ya maduka private. Kwa hiyo, mtu anakwenda hospitali na bima yake anaadikiwa dawa inakuwa hamna, akienda nje bima haiwezi kutumika, yako maduka ambayo hayakubali bima. Kwa hiyo, yule mtu anarudi nyumbani hana dawa kwa sababu tu hana hela ya kununua dawa.
Mheshimiwa Spika, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri, yale maduka ambayo yako ndani ya hospitali yapate dawa zote ili wananchi wetu wakifika pale waweze kuhudumiwa vizuri. Shida ya dawa bado ni kubwa pamoja na juhudi nyingi ambazo Serikali inafanya na wewe Mheshimiwa Waziri lakini dawa bado ni chache.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni huduma zisizolirisha katika hospitali zetu. Kuna wafanyakazi wachache ambao bado hawana lugha nzuri kwa wagonjwa. Mfano, hospitali yangu ya Wilaya ya Mpwapwa bado kuna malalamiko mengi kuhusiana na uhafifu wa huduma zinazotolewa pale. Watu wanajibiwa vibaya, watu hawatibiwi kwa wakati, kuna vurugu nyingi. Mheshimiwa Waziri ningeomba jambo hili ikiwezekana watumishi hawa wa afya wapate semina za mara kwa mara ili kuwafundisha maadili ya kazi zao. Kazi ya kuwatibu watu ni kazi ya wito inahitaji upendo, inahitaji mtu anaejitambua vizuri.
Mheshimiwa Spika, pamekuwa na watu ambao ni wajeuri, mtu anakwenda anaumwa anajibiwa vibaya wakati mwingine wanadaiwa rushwa, wanadaiwa fedha kwa mambo ambayo hayatakiwi kulipiwa. Kwa hiyo, kuna fujo nyingi kwenye maeneo haya ya kutolea huduma na kelele hizi zinachafua mahusiano bora au mahusiano mazuri na Serikali na wananchi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nirudie kumshukuru Mheshimiwa Waziri wetu wa Afya kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza jioni ya leo. Kwanza nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipa msukumo mkubwa Wizara hii ya Ardhi. Kusema kweli ardhi ndiyo maisha ya wanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamesema kuanzia asubuhi tulipoanza kuchangia, wamezungumza suala la kumilikisha ardhi kwa wananchi wetu wa Tanzania. Napenda nimpongeze sana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Mabula na Naibu Waziri, ndugu yangu, Mheshimiwa Pinda, wanafanya kazi nzuri katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni kati ya Wizara chache zenye changamoto nyingi. Interest kubwa ya wananchi iko kwenye ardhi na ndiyo maana kila anayesimama anazungumza habari ya wananchi kumilikishwa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu umuhimu wa kupima ardhi katika maeneo yote ya nchi yetu. Umuhimu wake uko hapa, mwananchi akipimiwa ardhi yake anaweza kupata hati, akipata hati ya kumiliki eneo lake anaweza kuitumia kupata mikopo katika vyombo vyetu vya fedha na hivyo kumwondolea umaskini. Wananchi wetu wengi ni maskini lakini wana maeneo ambayo hawana uhakika kwamba kesho wataishi pale au wataondolewa lini. Hiki ndicho kitu ambacho Wabunge wengi wamezungumza leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana wananchi wetu wakawa na uhakika na eneo wanapoishi. Kwamba akiwa na hati, eneo lake limepimwa, hata kama Serikali itataka kutwaa eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya umma, lazima fidia itakuwa nzuri, kutakuwa na utaratibu wa kisheria ambao utamsaidia yule anayeondoka eneo lile atakwenda kule anakokwenda akiwa amepata fidia nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ilivyo, mtu amekaa anaambiwa apishe labda bomba la mafuta au apishe nini, anaondoka hakuna cha fidia wala nini, anaendelea kuwa maskini kuliko aliokuwa nao wakati ule. Kwa hiyo nashauri sana Wizara hii ipime. Migogoro hii ya ardhi mnayoiona Waheshimiwa ni kwa sababu ardhi yetu haijapimwa, kwa hiyo wananchi kila siku wananyang’anyana ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika ofisi ya Mheshimiwa Waziri, bado katika idara nyingi, hasa kwenye halmashauri, kuna wafanyakazi wachache wasio waaminifu. Wanamilikisha ardhi kwa mtu zaidi ya mmoja, matokeo yake mtu anakaa anajua ana kiwanja mahali Fulani, kumbe kile kiwanja kina wamiliki zaidi ya mmoja au watatu. Matokeo yake kila siku wako mahakamani kwa ajili ya kesi ya kutafuta nani mwenye umiliki halali. Naomba Mheshimiwa Waziri jambo hili alichukulie kwa uzito sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wafanyakazi wanaofanya ubadhirifu wa namna hii wachukuliwe hatua kali, hata ikiwezekana waachishwe kazi. Huwezi kumilikisha ardhi watu wawili, watatu, ukatarajia kutakuwa na amani katika eneo hilo, haiwezekani kabisa. Kwa hiyo, hili jambo ni muhimu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mpwapwa tuna maeneo, tuna kata ambazo tayari zina sifa za kupimiwa ardhi. Katika hotuba ya Waziri, ukurasa wa 34, amezungumzia habari ya Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355, akatoa hata sifa za eneo kutangazwa kwamba linaweza kupimwa. Waziri amesema anaangalia uchumi wa eneo hilo, maendeleo ya eneo hilo, hata mazingira yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mpwapwa tuna maeneo mengi ambayo yanakidhi hizi sifa alizokuwa amezisema Mheshimiwa Waziri. Kwa mfano, kuna Kata za Chitemo, Chunyu, Mlembule, Lupeta, Godegode, Berege, Miima; haya ni maeneo ambayo yangepaswa kupimwa kwa sababu yana sifa zote. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo ili eneo letu lipimwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpwapwa Mjini pia hatujapima, yaani zoezi la kupima linasuasua sana. Tunaomba Mheshimiwa Waziri a-push maeneo haya yapimwe ili wananchi wetu waweze kuyatumia kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ambayo pia inaweza kufanyika vizuri ni kwamba Waziri akipima maeneo, Serikali itakusanya kodi kwa sababu wale wote watakaokuwa wamepimiwa maeneo na kupata hati, watapaswa kulipa kodi ya kila mwaka ya pango la ardhi. Ingawa utaratibu wa sasa Mheshimiwa Waziri, bado hauleti matumaini ya kukusanya fedha za kutosha, bado wananchi wetu hawajawa na hamasa ya kulipa kodi, walio wengi hawalipi kodi, lakini ni kwa sababu ya utaratibu ulioko sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ulioko sasa unamsubiri mlipakodi aende mwenyewe kulipa kwenye mamlaka inayohusika, lakini tungetumia utaratibu mwingine, hata wa kulipa kupitia simu, ili mtu apate unafuu wa kulipa. Leo tunakusanya kodi chache sana za pango la ardhi kwa sababu ya utaratibu ulioko sasa. Kwa hiyo naomba pia Mheshimiwa Waziri waliangalie sana hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia leo ni juu ya utoaji wa hati. Hili nalo ni tatizo lingine katika Wizara hii. Mtu akishapimiwa na kulipa kila kitu, hati inachukua muda mrefu sana kupatikana. Hii ndiyo inasababisha hata viwanja vinavamiwa, kwa sababu mtu amelipa anakaa mwaka au miaka miwili hajapewa hati yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kuna tatizo gani, kwa nini hati hazitoki? Kama mtu amekamilisha kila kitu kinachotakiwa kwa nini hapewi hati yake haraka ili aweze kufanya maendeleo, aweze kuendeleza, aweze kupata mikopo katika mabenki ili aendeleze maisha yake? Hati zinachelewa sana, naomba sana suala la hati waliangalie kwa ukaribu ili wananchi wetu waweze kujikwamua katika maisha haya ya sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ule mradi wa upimaji. Wamesema sana wenzangu, nami naomba sana fedha hizi nyingi zitumike kwenye mambo ya upimaji wa ardhi. Tumeona katika ripoti ya Waziri, fedha kidogo sana ndiyo inakwenda kwenye ile mamlaka ya kupima, lakini fedha nyingi zinatumika katika kazi ambazo kwa kweli hazina tija kwa wananchi wetu. Kwa hiyo kwa kauli za Wabunge wengi waliosema, naamini Mheshimiwa Waziri atakwenda kuangalia upya, fedha zile zifanye kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini akitumia fedha hizo kwa ajili ya kupima, kwanza kasi ya upimaji itakuwa kubwa, lakini mwakani hatakuja akasema tuna asilimia 25 ya upimaji mpaka sasa hivi. Ndiyo maana migogoro ni mingi, asilimia 25 ni sehemu ndogo sana iliyopimwa. Migogoro hii haitaisha ndugu zangu kama hatutapima maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninakushauri sana Mheshimiwa Waziri, fedha hizi zitumike vizuri, zipime maeneo mengi katika nchi yetu ili mwakani anaporudi hapa atuambie tumepima asilimia 75 na hiyo 75 itatuonesha kwa sababu tutaona migogoro ya ardhi imepungua, hasa ndilo lengo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasemaji wamesema hata nchi za wenzetu majirani migogoro yao ya ardhi siyo mingi kama ya kwetu, lakini ni kwa sababu hatujapima. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, anafanya kazi nzuri sana katika Wizara yake, nampongeza sana, lakini kwenye eneo hili la kupima, naomba sana alichukue kwa uzito wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, basi naomba niunge mkono hoja; ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika hotuba hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kufanya katika nchi yetu na hasa ile subsidy ambayo imetolewa kwenye bei ya mafuta na hata tumepunguziwa kidogo namshukuru sana. Pia niwapongeze Wizara ya Nishati, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa ambayo pia inaendelea kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri bado kuna changamoto katika Wizara hii na napenda kuzungumzia baadhi ya changamoto ambazo nimeziona. Changamoto ya kwanza ni huu Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini ambao unasimamiwa na REA. Umeme umesambaa katika vijiji vingi katika nchi hii, lakini ukienda katika hivyo vijiji utakuwa umeme umewekwa katika center ya kijiji, kijiji kimoja kinakuwa na nguzo 20 au chini ya 20, kwa hiyo unakuta sehemu kubwa ya kijiji hakuna umeme. Hii imesababisha malalamiko mengi sana kwa wananchi. Ningeshauri sana jambo hili walizingatie, haitakuwa na maana tukisema tumeweka umeme katika vijiji vyote katika nchi hii, wakati wanaonufaika katika vijiji ni asilimia ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni Mradi wa Kusambaza Gesi Majumbani. Mradi huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, lakini usambazaji wake unasuasua sana. Hadi sasa gesi hii imesambazwa katika Mikoa mitatu Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na katika viwanda ni viwanda 53 tu ambavyo vimesambaziwa gesi, lakini pia nyumba ambazo zimesambaziwa gesi ni 1,379, nadhani tunaweza kuona ambavyo speed yake ni ndogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya gesi kwenda majumbani ni kubwa sana, itatusaidia kutunza mazingira yetu. Watu wengi wakisambaziwa gesi majumbani wataepuka matumizi ya mkaa na kuni, hivyo tutalinda mazingira yetu. Kwa hiyo ningeomba sana Wizara hii iendelee kwa speed ile ambayo watu tulikuwa tunaitarajia, ikiwezekana miji yote au mikoa yote ya Tanzania ipate huduma hii ya gesi majumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye Jimbo langu la Mpwapwa, bado usambazaji wa umeme sio wa kuridhisha sana. Mpaka sasa hivi kuna zaidi ya vitongoji 50 ambavyo havina umeme, lakini vijiji ni zaidi ya 15 bado havina umeme. Nimesikia wengine wanasema kimebaki kijiji kimoja, lakini mimi ni zaidi ya vijiji 15. Kwa hiyo ningeomba sana speed ya usambazaji pia iongezeke, vitongoji zaidi ya 50 ni vingi mno, hata tunashindwa kuelewa kama kweli katika Jimbo la Mpwapwa tuna katika umeme vijiji vyote. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri na wenzake wazingatie sana jambo hili. Umeme ndio suluhisho la uchumi katika nchi yoyote duniani, kama nchi haina umeme maana yake hata uchumi wake utaendelea kudumaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni muhimu katika viwanda na tumesema viwanda vikubwa au vidogo ndio vinavyotoa ajira kwa wananchi wengi, sasa kama hatuna umeme wa uhakika maana yake viwanda havitakuwepo na hata tukiwa navyo havitafanya kazi kama inavyotakiwa. Kwa hiyo ni muhimu sana tukazingatia kwamba, tukiwa na umeme wa uhakika tutakuwa tumejitahidi kutoa ajira kwa vijana wetu na viwanda vitakuwepo, lakini vijana wa vijijini ambako pia hakuna viwanda watafungua viwanda vidogo vidogo. Watafungua viwanda vya kuchomelea vyuma, wengine watafungua saloon, kuna kazi nyingi sana ambazo zinategemea umeme. Kwa hiyo, Wizara hii ni muhimu inatakiwa iangalie sana na izingatie jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la bei ya kuunganisha umeme, jambo hili bado halijaeleweka vizuri, utasema kijijini ni Sh.27,000, lakini bado wananchi hatujaelewa vizuri au hawajaelewa vizuri wapi ni mjini na wapi ni kijijini. Kwa hiyo unakuta kamji kapo nje ya mkoa lakini kwa sababu kuna ka-centre kidogo, basi gharama ya kuunganisha umeme inakuwa ni kubwa. Nadhani jambo hili kama Wizara ingeweza kuli-address vizuri ili wananchi waelewe ni maeneo gani ambayo gharama ya kuunganisha umeme inatakiwa iwe Sh.27,000 na maeneo gani yanayotakiwa kuunganisha umeme kwa bei ya Sh.300,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila hivyo kumekuwa na migongano mingi sana, wananchi wa vijijni wakiambiwa hiyo bei ya Sh.300,000 hawawezi ku-afford, matokeo yake hawa watu wanaamua kuacha, kwa hiyo hakuna umeme vijijini. Kwa hiyo naomba hilo nalo liwekwe vizuri ili tuelewe ni maeneo gani yanaunganishwa kwa Sh.27,000 na maeneo gani yataunganshwa kwa bei ya Sh.300,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine au changamoto ambayo ipo kwenye Wizara hii ni kukatika katika kwa umeme hovyo na hii nadhani inasababishwa na uchakavu wa miundombinu. Wizara ingejikita sana kuboresha miundombinu kwasababu kukatika katika kwa umeme katika maeneo yetu kumesababisha hasara kubwa sana kwa wananchi, vifaa vyao vinavyotumia umeme vimeungua na taratibu za kupata compensation ni ngumu, kwa hiyo watu wamekutana na tatizo hili, umeme unakatikakatika kila wakati. Kwa hiyo tunaamini kwamba jambo hili wanalijua na watajitahidi sana kuimarisha miundombinu. Miundombinu iliyopo sasa katika maeneo mengi ya nchi yetu imechakaa sana na ndio maana umeme hauwezi ku-flow vizuri. Hivyo, tunawaomba sana kama Wizara wazingatie hili na ikiwezekana ule mradi wa kusambaza nguzo za zege uendelee katika maeneo yote ili umeme uwe stable, nchi iwe na umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia afya sote ya kuendelea kuwepo Bungeni tukihudumu.
Mheshimiwa Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu, na kwa kweli matunda yake tunaendelea kuyaona.
Mheshimiwa Spika, namshukuru kwa dhati Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika nchi yetu hasa ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na nishati ya kutosha. Vilevile namshukuru Naibu Waziri, Mheshimiwa Judith Kapinga ambaye naye anasaidia kazi na wanaendelea vizuri. Pia, naishukuru timu nzima ya Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Spika, ukitaka kuona nchi yoyote ambayo inaendelea kwa kasi, moja ya factor ambazo utaziona pale ni uhakika wa umeme katika nchi hiyo. Nadhani hilo ndilo jambo ambalo nasi tunatakiwa kujikita sana. Nchi yetu inahitaji kuwa na umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha nia ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba tatizo la umeme katika nchi yetu linatatulika. Ukitaka kujua hilo, utaona jinsi ambavyo miradi mingi ya kuzalisha umeme inaendelea kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano hapa umetolewa wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ambalo linatarajia kutoa Megawatt 2115. Vilevile kuna ile Kinyerezi I ambayo tunategemea itumie natural gas ambayo itatoa Megawatt 185, lakini ule Mto Kagera kule Rusumo tunategemea kutoa Megawatt 85 na miradi mingine ambayo inaendelea mahali pale.
Mheshimiwa Spika, kitu ambacho ningechukua fursa kuwashauri Wizara ya Nishati ni kuendelea kutafuta vyanzo vipya. Vyanzo vilivyopo bado havitoshi. Sisi kama nchi, tunatarajia tuwe na umeme wa kutosha, lakini pia tupate fursa ya kuuza katika nchi Jirani. Kwa namna hiyo tutahakikisha uchumi wetu utakuwa unaenda mbele.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini ambao unatekelezwa na REA. Mradi huu umekuwa mzuri sana, na kwa kweli ukienda vijijini, leo vile vijiji ambavyo tayari vina umeme, hata kama katika lile eneo dogo lakini vijana tayari wamejiajiri. Vijana wamejiajiri wanafanya biashara, wameanzisha viwanda vidogo vidogo na kwa kufanya hivyo wamekuza pato la familia zao na Pato la Taifa kwa ujumla. Kwa hiyo, jambo hili ni la muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, shida kubwa iliyoko sasa kwenye REA ni kasi ndogo ya kutekeleza mradi huu. Wamesema wengine kwamba ukienda kwenye kijiji utakuta kuna nguzo 20, 25. Kwa hiyo ni watu wachache ambao wamefikiwa na umeme huu, lakini asilimia kubwa ya wananchi wa vijijini kwenye kijiji husika utakuta hawana umeme. Kwa hiyo, hilo limekuwa tatizo na kumekuwa na kelele nyingi.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa upande wa vitongoji nilikuwa nafikiri tusianze kwenda kwenye vitongoji kwanza, tumalizie zile nyumba za kwenye kijiji. Zile nyumba zinazotakiwa kupata umeme katika Kijiji, zipate umeme ndipo twende kwenye vitongoji vyake. Hiyo itatusaidia sana kuliko kuruka kwenda kwenye kitongoji, wakati huku kwenye vijiji kuna watu kumi tu ndio wenye umeme.
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni muhimu kwa sababu umeme ukipatikana kwa maeneo yote, hata kelele za kuilaumu Serikali zitapungua sana. Kwa hiyo, nilikuwa nawashauri watu wa REA waongeze kasi ya utekelezaji wa mradi wenyewe.
Mheshimiwa Spika, pia nichukue fursa hii kuwashukuru Wizara ya Nishati katika Jimbo langu la Mpwapwa ambapo bado vijiji vitatu na mkandarasi yuko site. Vijiji vyote vimepata umeme isipokuwa shida ni ile kasi ya vile vijiji vitatu, mkandarasi haendi kwa kasi inayotakiwa. Hata hivyo ninaamini Wizara itaweka msukumo ili hivyo vijiji vitatu vilivyobaki viweze kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni huduma za TANESCO. Miaka ya nyuma kulikuwa na huduma ambazo hazikuwa nzuri na hivyo zilisababisha wananchi kuilaumu sana Serikali, lakini nawapongeza kwamba leo wamekuja na solution. Sasa wanatumia mifumo kwa ajili ya mawasiliano, na kuna call centers. Mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma nilipata fursa ya kutembelea hii miradi ninayoisema ya kuzalisha umeme.
Mheshimiwa Spika, pia tumetembelea Makao Makuu ya TANESCO na tumeona mifumo ambayo imewekwa, kuna call centers na mawasiliano yako vizuri na wateja. Zamani ilikuwa tukipata shida ya umeme tunaweza kusafiri kutoka nyumbani mpaka kwenye Ofisi ya TANESCO ndipo upate huduma. Leo unapiga simu mara moja na tatizo linatatulika ukiwa nyumbani kwako.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa hili nawapongeza, ni hatua kubwa, lakini bado tunataka kuendelea kuboresha huduma kwa wateja, hii itatusaidia sana. Kwanza shirika lenyewe litapata fedha kwa wingi kwa sababu litatoa huduma kwa haraka na watakusanya mapato kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni uchakavu wa miundombinu. Kule Mpwapwa tumekuwa na shida ya kukatikakatika umeme, nadhani ni maeneo mengi katika nchi hii. Umeme unakatikakatika sana katika Wilaya yetu ya Mpwapwa kwa sababu ile miundombinu inayosafirisha umeme kutoka kwenye kituo chetu cha zuzu imechakaa na kwa hiyo, unakuta kila siku umeme unakatika bila taarifa na mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, napenda sana Wizara ya Nishati iangalie jambo hili sana, tunahitaji umeme wa uhakika. Ili uweze kufanya shughuli zako za kiuchumi lazima umeme uwe wa uhakika, uwe na uhakika kwamba leo unataka kufanya kazi masaa 12, basi ufanye kazi masaa 12, lakini unapanga masaa 12 umeme unakatika, unafanya kazi masaa mawili. Kwa kufanya hivyo, hatuwezi kukua kiuchumi, tutaendelea kudidimia, tutakuwa maskini.
Mheshimiwa Spika, tunahitaji umeme kuliko kitu kingine chochote. Kwa hiyo, tatizo la kukatikakatika umeme bila sababu za msingi, naomba Wizara ishughulike nalo sana, kwa sababu vinginevyo hatuwezi kusonga mbele.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naunga mkono hoja, nashukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza, nianze na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa. Ameruhusu fedha nyingi sana kwa ajili ya uwekezaji kwenye Mashirika na Taasisi mbalimbali za Serikali. Kwa hesabu za Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 75.79 kwenye Mashirika mbalimbali ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na katika uchambuzi wa Kamati yetu tumeangalia sana mashirika mbalimbali ambayo Serikali imewekeza mitaji, lakini tumeona baadhi ya mashirika utendaji wake wa kazi au uendeshaji wa mashirika hayo umekuwa ukisuasua sana. Jambo ambalo limeondoa kabisa tija ambayo tulikuwa tumeitarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kutoa mfano wa mashirika hayo machache, yapo mengi lakini machache, mojawapo ni: Shirika la TANOIL hii ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC); Shirika lingine ni TTCL; na lingine ni Bodi ya Mkonge. Haya ni mashirika ambayo uendeshaji wake umekuwa wa kusuasua sana. Kwa miaka mitatu mfululizo Mashirika haya yamekuwa yakitengeneza hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mashirika ya namna hii hayatufikishi kule ambako tulikuwa tunatarajia. Hayana uwezo wa kutoa mchango katika kuinua uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina iweke usimamizi wa karibu sana kwa mashirika kama haya ili lile lengo tulilokusudia, lengo ambalo Serikali na lengo ambalo Mheshimiwa Rais angetarajia la kuongeza uchumi wa Taifa letu liweze kutimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tumeliona ni hali ya tegemezi wa ruzuku ya Serikali, Mashirika mengi bado yanategemea ruzuku hayawezi kujiendesha yenyewe. Hii inatokana na ukweli kwamba hayaendeshwi vizuri. Kuna udhaifu kwenye management, kuna udhaifu kwenye Bodi za Mashirika haya. Kwa hiyo, mashirika haya yameendelea kutegemea Serikali bila ruzuku ya Serikali hayawezi kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirika hayo ambayo nimeyataja ni kati ya hayo ambayo yanaendelea kutegemea ruzuku ya Serikali. Ukiangalia Ripoti ya Msajili wa Hazina ya mwaka 2022/2023 inasema kwamba utegemezi wa mashirika mbalimbali umeongezeka ambapo kwa miaka mitatu mfululizo umekuwa kwa 21.2% kutoka shilingi bilioni13.2 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 17.4 kwa mwaka 2022/2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kuwekeza kwenye mashirika kama haya lilikuwa ni kwamba yaendeshwe vizuri ili ule utegemezi wa ruzuku uendelee kupungua kila mwaka. Sasa jambo hili limeshindikana baadhi ya mashirika yameshindwa kabisa kutekeleza utaratibu huu. Kwa hiyo, yameenda yanaendelea kupokea ruzuku na kusababisha mzigo kwa Serikali. Fedha ambazo zingeenda kufanya majukumu mengine zinaendelea kupelekwa kwenye mashirika kama haya ambayo kimsingi hayafanyi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza ningeshauri Serikali iangalie mashirika kama haya kama hayawezi kujirekebisha, kama hayawezi kufanya vizuri basi hakuna sababu ya kuendelea kuyapa ruzuku. Fedha hizi ambazo zinatolewa kwenye mashirika haya ziweze kufanya kazi nyingine za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa niaba ya Serikali isimamie kwa karibu mashirika haya ikiwezekana baada ya muda mfupi yajikwamue yaweze kujiendesha yenyewe bila kutegemea ruzuku ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida nyingine ambayo tumeiona ni upungufu wa mitaji ya uendeshaji, yapo mashirika ambayo hayana fedha kabisa ya kujiendesha yanaendesha mashirika yao kwa madeni. Wanashindwa kabisa kulipa hata fedha za watoa huduma, fedha za wakandarasi wao ni kwa sababu hawana mitaji na ningeweza kushauri ikiwezekana watafute njia mbadala. Zipo Taasisi za kifedha ambazo zinatoa mikopo, lipo soko la hisa, wanaweza kutumia utaratibu wa PPP wakaweza kupata mitaji ili waweze kujiendesha wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirika kama hayo ambayo nimesema hayana pesa kabisa yanaendeshwa kwa shida na kwa madeni ni pamoja na TTCL, MSD (Bohari ya Dawa), Benki ya maendeleo (TIB) na kuendelea. Mashirika haya hayana fedha yanaendeshwa kwa madeni, matokeo yake hatuwezi kupata ile tija ya uwekezaji ambayo ilikuwa imekusudiwa. Kwa hiyo, tunashauri wazingatie sana ikiwezekana watafute fedha katika vyanzo ambavyo nimevitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hali mbaya ya ukwasi kwa baadhi ya Taasisi hizi, hazina fedha kabisa. Taasisi kama hizi kama Serikali haiwezi kuwasaidia basi tujue kabisa haziwezi kuendelea. Ukiangalia hesabu zao wana mizigo ya madeni, wao wenyewe wapo hoi. Kwa hiyo, nadhani tusiendelee kuweka fedha nyingi kwenye mashirika kama haya ama tubadilishe management yake, tuweke watu wengine ambao wanaweza kuwa na uwezo wa kuendesha mashirika haya vizuri badala ya kuendelea kuwatumia wale wale ambao hawafanyi vizuri hilo ni jambo muhimu sana. Kupitia Ofisi ya TR, Serikali itafute management yenye uwezo, bodi zenye uwezo ili kusimamia mashirika haya ili yajiendeshe kwa faida na ile tija tunayo kusudia tuweze kuiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu mashirika mengi ambayo yanaonekana kama yana mitaji mikubwa sana kwenye hesabu zao. Ukienda kuangalia hesabu kama ya TTCL utakuta ina mtaji mkubwa lakini kinazalishwa kutokana na hiyo mitaji ni kidogo sana. Unakuta ama wana majengo ambayo hayapangishwi, wana ardhi ambayo haijaendelezwa, wengine wana mitambo ambayo imepitwa na wakati kwa sababu ya mabadiliko ya teknolojia lakini imeendelea kuonekana kwenye hesabu zao kwamba hawa watu wana mtaji mkubwa, lakini mitaji hiyo haizalishi kile ambacho kilitarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo wanaingia gharama ya uendeshaji, gharama ya kutunza hayo majengo, gharama ya kutunza viwanja kulipia kodi, gharama ya kutunza mitambo ambayo haiwezi kuzalisha tena. Kwa hiyo, ninashauri hatua zichukuliwe na mashirika haya ikiwezekana watunze au watumie mitaji ambayo inazalisha badala ya kuendelea kuingia hasara ya uendeshaji wa mitaji ambayo haifanyi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri sana jambo hili Serikali iliangalie kwa karibu kupitia Msajili wa Hazina, yale mashirika ambayo yana mitaji mikubwa haizalishi chochote ile mitaji ama iuzwe ili tusiendelee kuingia gharama ya kutunza majengo ambayo hayawezi kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)