Contributions by Hon. John Michael Sallu (7 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Namshukuru Mwenyezi Mungu, namshukuru Mwenyekiti wa Chama chetu cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, nashukuru Chama chetu cha Mapinduzi, nashukuru wananchi wa Handeni Vijijini na wadau wote walionifanya niwepo hapa ili kuwatumikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli napongeza sana juhudi zilizofanywa katika kuandaa Mpango huu. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kuandaa Mpango mkakati utakaotutoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Ndugu zangu si dhambi kushukuru na kupongeza juhudi zilizofanywa katika kuanzisha miradi mikubwa katika nchi hii ambapo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache wa muda, nitaanzia na bwawa kubwa la Stigler’s Gorge. Bwawa hili la Mwalimu Nyerere litazalisha umeme wa maji megawatt 2,115 ambapo ndiyo rahisi duniani kote. Kwa hiyo, utachagiza maendeleo makubwa kwa viwanda vyetu vikubwa, vya kati na vidogo. Hivyo, itatusaidia sana sisi wananchi wa Handeni Vijijini kuongeza thamani ya mazao yetu kwani sisi ni wakulima wazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kuanzisha viwanda hivyo ambavyo tayari vimeshaanza na tuna mikakati ya kuvutia wawekezaji, vilevile maji na barabara ni muhimu. Ili mazao hayo yaweze kufika kwenye viwanda, ndugu zangu lazima tufanye mpango mkakati bajeti ya TARURA iongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viwanda vinaendana na maji. Naomba Wizara yetu ya Maji tukitoka hapa tuwe na mpango mkakati ili tuongeze pesa ili wananchi wetu wa vijijini wapate maji safi na salama na kuweza kuendesha mitambo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni upanuzi mkubwa wa bandari zetu. Bandari zetu zimepanuliwa sasa lazima tutafute mbinu chochezi ziweze kufanya kazi zituingizie pato. Kwa mfano, wananchi wa Mkoa wa Tanga tumeshuhudia meli kubwa ya mita 200 ambayo ilibeba tani 55,000 za Clinker kwa ajili ya kwenda Rwanda. Meli hiyo iliondoka pale Tanga ikiwa tupu, sasa lazima tutafute mbinu chochezi ili bandari zetu ziweze kubeba mizigo kuingiza na kutoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Madini iweze kusaidia wachimbaji wetu wadogo wa chuma na madini ya viwandani kwani Handeni Vijijini tuna madini ya chuma na madini ya viwandani kwa wingi sana. Wachimbaji wadogo wamejitahidi, pale tuna takribani tani zaidi 50,000 imelala pale chini ambapo waliingia mkataba na Dangote lakini kwa bahati mbaya haijachukuliwa. Kama tungeweka mbinu chochezi basi tani hizo zingeondoka na meli hiyo na bandari yetu ingefanya kazi, Halmashauri ingepata siyo chini ya shilingi milioni 600, bandari yenyewe ingepata mapato siyo chini ya dola milioni 150 kwa sababu mzigo huo wa tani takribani 50,000 gharama yake ununuzi (FOB) huwa ni dola milioni 4. Kwa hiyo, ndugu zangu naomba tutafute namna chochezi Wizara ya Madini ikitusaidia ili tuweze kuwahudumia wachimbaji wetu hawa wadogo tuweze kuhamasisha uingizaji wa pesa kwa kutumia bandari yetu ya Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara hii ya Kilimo. Kwanza niwape hongera sana Waziri, Naibu Waziri, Makatibu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya kusukuma gurudumu letu la kilimo. Nikija upande wa mbegu, mbegu ni kitu muhimu sana katika kilimo, kwa bahati nzuri uzalishaji wa mbegu wa ndani sasa unaanza kupanda kulinganisha na miaka ya nyuma ambako zaidi ya asilimia 70 ya mbegu ilikuwa inaagizwa kutoka nje, hapo niwape hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri ameainisha kwamba ataipa nguvu kubwa ASA ili iweze kuzalisha mbegu kwa wingi. Lakini hapo hapo naishauri Serikali isiwasahau wazalishaji binafsi kwa kuwawekea mazingira rafiki ili waweze kuzalisha kwa wingi kwani mpaka sasa hivi wazalishaji binafsi wanazalisha asilimia 90 ya mbegu. Kwa hiyo, hatutakiwi tuwaache nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watafiti wetu wa mbegu wanafanya juhudi kubwa kutengeneza mbegu zenye tija lakini mara nyingi zinaishia kwenye makabati, hazipati kutangazwa vya kutosha ili wananchi wakazifahamu. Ushauri wangu hapa, turudishe lile zoezi la kugawa mbegu kwa ruzuku. Wananchi wakipewa mbegu kwa ruzuku wakulima wadogo wadogo wataanza kutambua zile mbegu mpya zilizokuja na hivyo ikifikia kununua watakuwa wanazitafuta kwa majina zile mbegu mpya watalaam wetu walizozitengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukija kwa upande wa umwagiliaji. Sisi wa Handeni vijijini tuna mto mkubwa unapita pale mto wa Pangani ambao haukauki mwaka mzima. Tuna mabonde mazuri ya umwagiliaji ambayo nilikuwa naomba Serikali iyatolee macho. Bonde la Masatu lililoko Kata ya Segera na Bonde la Jambe lililoko Kwamgwe. Kwa kutumia umwagiliaji, tunaweza kutengeneza mazao ya mbogamboga ambayo yanaweza kusaidia sana kiuchumi pamoja na ku-export nje ya nchi tukapata hela za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile kwenye mazao ya matunda, kwenye matunda, sisi wa Handeni Vijijini tunazalisha sana matunda ya maembe pamoja na michungwa. Lakini kwa bahati mbaya tumevamiwa sana na wadudu waharibifu wa matunda hayo. Nzi weupe, kwa hiyo, naomba Wizara itoe macho itusaidie janga hili ambalo linadhuru sana machungwa na miembe iliyoko kwenye kata takriban 10. Nikizitaja kata ambazo zimeathirika sana ni Kata ya Kwedizinga, Segera, Mgambo, Kabuku, Kabukundani na Kwamgwe. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itoe macho ili iweze kutusaidia janga hili la wadudu waharibifu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa muda niliopata. Naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Vilevile, naipongeza sana Wizara kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuifikisha sekta yetu ya madini hapa tulipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natajikita zaidi kwa wachimbaji wadogo. Wachimbaji hawa wana mchango mkubwa sana kwenye sekta ya madini na kwenye pato la Serikali kwa jumla. Kama ilivyoelezwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukiangalia upande wa madini ya dhahabu, wachimbaji wadogo wamechangia asilimia 30; kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nawapongeza sana wachimbaji wadogo kwani ndiyo wagunduzi wakubwa wa madini ndani ya nchi yetu, pamoja na kwamba hawana vifaa. Migodi yote inayochimbwa karibuni wamegundua wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji hawa wadogo tunatakiwa tuwashike mkono, Serikali pamoja na Wizara tutafute namna sahihi ya kupata mikopo yenye riba nafuu. Napenda kuyashauri mabenki yatafute namna ya kuzungumza na wachimbaji ili wajue hasa sekta inakwendaje, kwa sababu inaonekana hawaamini kuwakopesha wachimbaji wadogo, lakini nina imani wakikaa kwa pamoja watakuja na namna sahihi ya wachimbaji hawa kuweza kupata mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawakaribisha mabenki kwenye Jimbo langu la Handeni Vijijini, tuna vijiji zaidi ya kumi ambavyo vinachimba dhahabu; vijiji zaidi ya saba vinachimba feldspars; vijiji viwili vinachimba dolomite. Kwa hiyo, tuna vijiji zaidi ya 30 ambavyo vina madini mbalimbali, mabenki waje tukae nao tutafute namna sahihi ya kuweza kuwakopesha wachimbaji wadogowadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwa upande wa GST. GST inatakiwa itoe mchango mkubwa kwenye kuangalia wapi pana madini na kwa kiasi gani. Katika Jimbo langu la Handeni Vijijini, tuna madini ya chuma, graphite na dhahabu lakini wachimbaji wale hawawezi kujua chuma kile tulichokuwa nacho pale kiko kingi kiasi gani au graphite ile iko nyingi kiasi gani. Vilevile hii ni faida kwa Serikali kwani tukijua tuna graphite kiasi gani na tuna madini ya chuma kiasi gani, tunaweza kujipanga tuone tufanyeje kwa sababu kupanga ni kuchangua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la uongezaji thamani madini. Jambo hili tukilitumia vizuri litatusaidia sana kwenye upande wa ajira za vijana wetu, kwani uongezaji thamani madini siyo lazima madini ya dhahabu au almasi peke yake, kuna madini ya viwandani ambayo yanaweza kutumika kutengeneza vitu mbalimbali. Kwa mfano, insulators za umeme na vito mbalimbali, nina maana vipuri vya akina mama vinaweza kutengenezwa kutokana na madini ya feldspars.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa mfano nchi ya China, utakuta insulators zinatengenezwa na viwanda vidogo sana, ni kama SIDO type. Kwa hiyo, tukiweza kutafuta ujuzi tukawapa watu wetu ujuzi, kama vile ambavyo imefanyka kwenye vikundi vya akina mama na vijana kupewa ujuzi wa kutengeneza sabuni na batiki, basi tukatengeneza namna vijana wakapata ujuzi wa kutumia malighafi hii ya madini ya viwanda, itatusaidia sana kuongeza ajira kwa vijana wetu na kuongeza pato la madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze na shukrani. Naishukuru sana Serikali yetu sikivu. Namshukuru sana mama kwa kuja na bajeti hii bajeti sikivu. Hapa nipende kumpongeza ndugu yangu Waziri, Mheshimiwa Mwigulu, Naibu wake na watendaji wote walioko chini yake kwa kuandaa bajeti hii Sikivu, iliyosikiliza mawazo mengi ya Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli namshukuru sana mama kwa jinsi ambavyo ametukumbuka kwenye barabara. Sisi wa vijijini kwa kutuongezea zile hela za TARURA zimetusaidia sana na zitasaidia sana kusisimua maendeleo ya kilimo kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najikita zaidi kwenye kilimo kwa sababu Jimbo langu linashughulika zaidi na kilimo, kwa hiyo, katika ile asilimia 65 ya watu wanaoshughulika na kilimo na jimbo langu tumo. Kwa kweli asilimia moja ya bajeti ni ndogo sana kwa kilimo, kwa sababu kilimo kwa sababu kilimo kimebeba asilimia 65 ya wananchi. Ili tuweze kupata maendeleo kwenye nchi yetu, tunahitaji asilimia 65 ya wananchi kuisisimua ili iweze kulima kwa tija. Ili iweze kulima kwa tija tunahitaji Maafisa Ugani wa kutosha pamoja na mbinu za kuwaelimisha ili waweze kulima kwa tija kwani mazao yanayopatikana sasa hivi ndani ya heka moja yako chini sana hayana tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile katika kusisimua wakulima hawa soko ni muhimu sana la ndani na nje. Soko la ndani linaweza kusisimuliwa zaidi kwa kuwa na mbinu za kutengeneza viwanda vidogo vidogo ambavyo vitaleta tija ya ku-add value, kuongeza thamani mazao yetu. Kwa hiyo, taasisi husika zinatakiwa hapa Serikali iziangalie kama alivyosema mwongeaji aliyepita, kuna hizi CAMARTEC watakiwa waje na mbinu ya kuhakikisha kwamba tunapata viwanda vidogo vidogo ambavyo vitasaidia kusisimua uchumi kule vijijini. Uzuri ni kwamba ndugu zetu wa REA wamejitahidi umeme unaenda kila mahali, kwa hiyo sasa ni jukumu la viwanda hivi kusisimuliwa ili viweze kuleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, soko la nje ndugu zetu wa TANTRADE wanajitahidi, naomba na sisi wafanyabiashara tujitahidi kutafuta soko la nje kwa kadri iwezekanavyo kwa sababu ukiangalia wenzetu jirani wanauza sana nje mazao yetu sisi. Mazao yetu mengi yanapitia Kenya. Kwa hiyo hapa kuna jambo la kujifunza. Kwa mfano, kilimo cha mbogamboga na matunda ambapo kwenye jimbo langu tuna eneo kubwa sana wanalima machungwa na maembe pamoja na mbogamboga, kata takribani 14. Hapa nashauri lijengwe soko la matunda pale Segera ili liweze kurahisisha matunda haya kukusanywa na kuweka soko la Kimataifa pale ambapo litakuwa na majokofu ya baridi kwa ajili ya matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa napo pana kitu cha kujifunza kwa sababu baada ya kukusanya na kununua mazao haya ya matunda na mbogamboga tunatakiwa tuyapeleke nje, lakini bandari zetu bado hazijawa imara kusafirisha mazao haya. Maana ukiangalia kwa sasa hivi mazao mengi ya mbogamboga na matunda yanapitia Bandari ya Mombasa, hata yale maparachichi ya Njombe mengi yanapitia Mombasa badala ya kupitia Bandari ya Dar es Salaam au ya Tanga. Sasa hapa tuna kitu cha kujifunza. Serikali ikae na wafanyabiashara ili iweze kuona tuna upungufu gani ambao bandari zetu ya Tanga na Dar es Salaam haiwezi kusafirisha mbogamboga na matunda kwa urahisi kiasi ambacho kinawafanya wakapitie kwenye bandari nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuongelea suala la umwagiliaji, kwa sababu umwagiliaji utaongeza sana tija kwa wakulima wetu. Sisi wa Handeni Vijijini tunapitiwa na Mto mkubwa wa Pangani ambapo tungeweza kutumia vizuri Bonde ya Masatu na Bonde la Kwamgwe ambapo maji yameshafanya kazi ya kuzalisha umeme sasa yanaenda kutupwa tu baharini. Kwa kutumia mabonde haya tungeweza kusisimua sana kilimo kwa wananchi na kuleta tija na hatimaye kuongeza kipato cha wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mito ya msimu ambayo wakati wa mvua inaleta tafrani kubwa kwenye madaraja yetu. Sasa hii mito ya msimu tungeweza kuyakinga maji na tukayatumia kwa ajili ya umwagiliaji wa mbogamboga na matunda, tungeongeza tija kubwa kwa wananchi wetu. Mito hiyo ni kama vile Mto Msangazi na Mto Mnyuzi ambayo inakatiza katika eneo kubwa la Jimbo la Handeni Vijijini ambapo tukiitumia vizuri, basi tutatengeneza mazingira bora ya wakulima na hivyo kuongeza tija na kipato kwa ujumla na hatimaye kuongeza pato la halmashauri na nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije kwenye suala la zile mashine za kukusanyia kodi. Mashine zile zinahitaji mtandao wa simu (network) na eneo kubwa la Jimbo la Handeni Vijijini hatuna network ya kutosha. Hivyo tunatumia mashine ambazo zinaweza kukusanya kodi offline lakini inabidi lazima mkusanyaji huyo wa kodi atoke aende kutafuta mtandao ili aweze ku-reconcile data zake. Sasa hicho kipindi cha kwenda kutafuta mtandao na kupanda kwenye mti kupata mtandao ina maana kuna malori ya mizigo yanapita pale, kwa hiyo kuna mapato tunakosa. Hivyo, Wizara husika naomba itusaidie, mtandao upatikane katika maeneo yote ili tuweze kukusanya mapato ya halmashauri kadri inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kushukuru upatikanaji wa mbinu mbadala ya kupata hela ya kuchangia TARURA kwa sababu tukiimarisha TARURA tutaweza kutoa mazao yetu kwenda sokoni na bei itakuwa nzuri kwani sasa hivi kuna mazao yanaharibika na kuozea mashambani kwa kukosa barabara nzuri. Hivyo, nasihi ule ukusanyaji wa vyanzo ambavyo tumevipanga hapa ufanyike vizuri na Fungu lilindwe vizuri ili kweli lipelekwe kutengeneza barabara zetu za TARURA zipitike mwaka mzima ili tuweze kutoa mazao na tupate maendeleo tarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii. Kwanza nikushukuru sana kwa jinsi unavyotuongoza na unavyotulea, na jambo lako ni jambo letu na Insha Allah Mwenyezi Mungu ataliwekea mkono litakwenda kwa kheri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kumshukuru sana Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha nyingi ambazo zimeendesha miradi mingi katika majimbo yetu hususan Jimbo langu la Handeni Vijijini. Kwa kweli tunamshukuru sana kwenye Jimbo letu la Handeni Vijijini ameleta fedha ambazo zimeendesha miradi mingi sana ya maendeleo kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kumshukuru ndugu yangu January Makamba, Naibu wake Byabato, Katibu Mkuu Ndugu yangu Mramba na timu yote ya Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha umeme na mambo yote ya mafuta ambayo yapo chini ya Wizara yao yanakwenda vizuri kabisa na nchi yetu inaimarika; kwa kweli hongereni hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na speed inavyokwenda sasa hivi ya umeme vijijini kwenye Jimbo letu la Handeni Vijijini mpaka ikifika mwezi Desemba vijiji vyote 91 vitakuwa vimeshapata umeme. Kwa kweli tunashukuru, tunashukuru sana kwa sababu heka heka na speed ya mkandarasi inaenda vizuri kwa hiyo tuna imani ikifika mwezi Desemba hali ya vijiji vyetu kupata umeme itakuwa imefika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nitoe ombi kwenye vitongoji. Jimbo letu la Handeni Vijijini lina vitongoji 770, kwa hiyo naomba tuangalie kwa jicho la huruma kwa sababu vitongoji ni vingi sana na shida ya umeme vitongojini ni kubwa na tayari vitongoji vile vina idadi kubwa ya watu kwa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kumshukuru sana Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mara ya pili kwa kuridhia kutoa fedha ambazo zinaleta mwarobaini ambao ulikuwa unasababishwa na tatizo la kukatika umeme zaidi ya mara 20 kwa siku kwenye Jimbo langu la Handeni Vijijini. Sasa ameridhia kutoa fedha bilioni 77.5 kwa ajili ya kujenga sub station kubwa ya MVA 120 pale Mkata, na line ya double circuit itatoka Mkata kuelekea upande wa Kwa Msisi, Mkalamo mpaka Pangani kwenye migodi ya graphite na chuma, na line nyingine itatoka pale Mkata itaelekea Kabuku Mzundu mpaka kwa Bojo kwenye migodi ya dolomite, calcite pamoja na chuma. Line nyingine itakwenda upande wa Manga – Madebe – Sua mpaka Kang’ata kwenye migodi ya dhahabu. Kwa kweli umeme huo utatukomboa sana hata kiuchumi kwenye eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama haitoshi Mama huyu vile vile ameridhia kutoa fedha kwa ajili ya line nyingine kubwa itakayotokea pale Mkata kuelekea Handeni Mji mpaka kwa ndugu zetu wa kule Kilindi. Kwa kweli tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara kwa kuzama zaidi kwenye vyanzo vya nishati jadidifu. Hivi karibuni tumeshuhudia wakisaini umeme wa umemejua. Na mimi napenda kusisitiza hapo kwenye nishati jadidifu kwa sababu kwanza ni nishati salama lakini vile vile itatuongezea nguvu kwenye Gridi yetu ya Taifa. Kwenye masterplan inatakiwa ikifika mwaka 2030 masterplan ya umeme tunatakiwa tuwe na megawatt zisizopungua 10,000. Sasa nilikuwa nashauri tuzame zaidi kwenye Umeme wa Jotoardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Umeme wa Jotoardhi Tanzania tuna viashiria 50 vya umeme wa joto ardhi ambavyo tukivitumia vizuri tutaweza kupata megawatt zisizopungua 5,000 ambazo zitakuwa ni mchango mkubwa sana kwenye Gridi yetu ya Taifa. Lakini kwa kuanzia kuna maeneo matano ambayo tayari yamekaa vizuri, na ninaishukuru Wizara imeweza kununua ridge kwa ajili ya kuchimba ili tupate mvuke ule wa kuendesha zile turbines.
Mheshimiwa Spika, katika hayo maeneo matano ambayo yanatarajiwa kutota megawatt 200 naomba Wizara ipeleke fedha kuhakikisha jambo hili linatokea. Lakini vile vile niombe Serikali kwa ujumla kukamilisha Sheria ya Umeme wa Jotoardhi kwa sababu bila sheria hatutakwenda vizuri kwenye eneo hilo; kwa sababu kwenye jotoardhi inatakiwa kuwe na sheria madhubuti itakayowawezesha hata wawekezaji kuweza kuvutiwa kuja kuwekeza kwenye umeme wa jotoardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na ndugu zangu hii joto ardhi huwa pamoja na kuzalisha umeme lakini lina vitu vingi unaweza kuvuna ndani yake. Kwa mfano mvuke ule ukishatumika kutengeneza umeme utaweza kutusaidia kukausha mazao, kukausha mbegu zetu, kwa yale maeneo yanayolimwa mbegu za kuzalisha mbegu. Pia itatusaidia kukausha vitu kama samaki, lakini vile vile inazalisha vitu kama hydrogen na sulphur ambazo zitatumika hospitalini, vile vile tunaweza tukapata Carbon dioxide ambayo huwa inatumika kwenye vinywaji baridi bia na soda. Kwa hiyo jotoardhi hili lina faida kubwa sana, kwa hiyo nilikuwa naomba tuwekee mkazo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa haya machache nashukuru sana naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza ninatoa shukrani nyingi kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa na political will kwenye kilimo, hii inatusababisha wakulima sasa tuwe na imani kwamba kilimo kitakuwa ndiyo mkombozi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninashukuru sana Mheshimiwa Bashe Waziri wa Kilimo, Naibu wake, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa jinsi ambavyo wanachapa kazi. Kwa mfano, katika Bunge hili niliwahi kuongelea inzi weupe wanaosumbua matunda hususani machungwa kwenye Jimbo langu, kwa kweli timu hii ilifanya kazi kwa haraka sana na wakaleta viuatilifu katika awamu mbili, kwa kweli wakulima wangu wamenufaika sana na hivyo viuatilifu na Kata zote zinazolima machungwa sasa hivi wanakamata wale inzi na machungwa yanaendele kuwa bora, nashukuru sana timu yote ya Wizara ya Kilimo kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninashukuru Watafiti, kwetu zao la muhogo liliingia kama zao la kuokoa njaa lakini baada ya muda limekuwa ni zao la uchumi. Watafiti pale walituunga mkono wakaja kutukomboa kutoka kwenye kilo tatu mpaka tano kwa shina, mpaka kilo 10 hadi 15 kwa shina na sasa muhogo umeendelea kuwa na tija. Uzalishaji baada ya kuhamasika umekuwa mkubwa sana, sasa hivi hekta zipatazo 70,135 zina muhogo ambazo tuna makisio ya kuvuna takribani tani Milioni Kumi lakini tatizo kubwa linalotukabili sasa ni masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANTRADE wamejitahidi kututafutia masoko ya nje lakini bado yanasuasua, kuna soko la ndani ambalo hatujaligusa kabisa, kwa utafiti nilioufanya tuna makampuni takribani 20 yanayoagiza starch kutoka nje lakini hawanunui kabisa starch yetu ya ndani. Namuomba Mheshimiwa Waziri Bashe akishirikiana na Wizara ya viwanda tuweze kuli-tap hili soko kwa sababu soko la ndani ni soko la uhakika zaidi ambalo linaweza kuleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Viwanda tuhakikishe kwamba waagizaji hawa wa starch waweze kutumia starch yetu ya ndani. Kweli kuna ambao wanaweza kutumia hii starch moja kwa moja kama raw ilivyo, lakini wapo wanaotumia modified starch, kwa hiyo Wizara hizi zishirikiane kuona kwamba hiyo modified starch inayotakiwa ni ya mtindo gani ili viwanda vyetu viweze kuelimishwa na hata wale ambao wanataka kuwekeza sasa wanaweza kujua wawekeze kwenye viwanda vya namna gani ili kukidhi soko hilo la ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwenye muhogo niende kwenye alizeti, napenda kumshauri Waziri ana mikakati mizuri ya kukomboa nchi yetu kwa zao la alizeti lakini katika ile Mikoa aliyoweka ya kimkakati Mikoa ambayo ina mvua mbili kwa mwaka hawakuiweka. Kuna Mikoa ambayo ina mvua mbili kwa mwaka ambapo na Jimbo langu lipo kwenye eneo hilo, ambalo unaweza kulima alizeti mara mbili kwa mwaka na ukavuna mara mbili kwa mwaka. Hii ingeweza kutatua tatizo la mafuta tulilonalo kwa haraka Zaidi. Ardhi tunayo ya kutosha, wananchi wapo tayari kabisa, tunaomba hizo ruzuku za alizeti nazo zije kwetu tuweze kukomboa shida iliyopo kwenye nchi yetu kwa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la umwagiliaji nchi yetu ina mabonde mengi ya umwagiliaji na vilevile kwenye Jimbo langu kuna Mabonde ya mto Pangani na mabonde ya mto Msangazi, ninaomba Idara ya umwagiliaji ifuatilie mabonde haya na kuweza kuweka mbinu sahihi ya kutumia mabonde haya ili tuweze kuzalisha mbogamboga kwa wingi ambazo zinaweza kutuletea tija kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache nashukuru sana naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara hii nyeti ya Nishati.
Kwanza naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo anatupambania na kuhakikisha tunapata fedha za kuendesha miradi ili kuimarisha nchi yetu. (Makofi)
Pili, nimpongeze ndugu yangu Waziri wa Nishati Mheshimiwa January Makamba pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na timu yote ya Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kupambania nchi yetu iweze kuwa na nishati bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba nijikite kwenye Power Master Plan. Kwenye Power Master Plan tunatakiwa ikifika mwaka 2025 tuwe na megawati zipatazo 5,000 sasa ukiangalia ni lazima tupate vyanzo vingi vya kujazia pale. Katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri ametaja vyanzo vingi, lakini mimi nilikuwa napenda sana kusisitizia chanzo cha umeme joto. Umeme joto ni umeme unaopatikana chini ya ardhi, Tanzania tuna vyanzo vingi. Katika hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati amevitaja vyanzo vinne na katika vyanzo hivi vinne tunapata megawati 200. Lakini mpaka sasa mpangilio wa umeme joto bado uko nyuma sana, sasa hapa nilikuwa nataka kutoa ushauri kwamba umeme joto huu kinachosababisha ile mitambo ifanye kazi ni ule mvuke unaotoka chini ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mvuke ule kwa jinsi ilivyo sasa hivi uko chini ya Wizara ya Madini. Sasa unakuta wale wadau wa maendeleo ambao wao ni rahisi sana kuchangia kwenye miundombinu, wanakuwa hawawezi kutupa misaada ya fedha kuendeleza joto ardhi hili. (Makofi)
Kwa hiyo, nilikuwa nashauri kwenye sheria zetu za nchi tubadilishe sheria iwe kama vile kwenye mafuta na gesi, mvuke huu uwe nao chini ya Wizara ya Nishati isiwe chini ya Wizara ya Madini. Kwa hiyo huo ulikuwa ni ushauri wangu. Lakini vilevile naomba kushauri tujipange vizuri kwa hizi rare mineral stones ambazo zenyewe zinatengeneza umeme jadidifu. Sasa hivi dunia inakwenda zaidi kwenye umeme jadidifu, umeme ambao unatumika kwenye magari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nchini tuna madini mengi yakiwemo madini ya nickel, niobium pamoja na graphite na kwenye jimbo langu kuna graphite nyingi ya kutosha. Sasa nilikuwa nafikiri kwamba ni wakati muafaka Serikali kuja na mbinu sahihi ya kuangalia mwenendo wa madini haya na kuangalia sheria zetu zilivyokaa ili tuweze kujipanga, tuingie kwenye ushindani wa dunia wa huu umme jadidifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kwenda kuongelea suala la REA. Kwa kweli nashukuru sana kwa mipangilio mizuri ambayo Mheshimiwa Waziri ameitangaza hapa ya kuweza kutafuta mbinu sahihi ya kufanya umeme vijijini kwa mara moja ili wananchi wetu waweze kupata manufaa mengi. Kwa hiyo, namuomba kwenye area hiyo ambayo amekuja na hiyo mbinu ambazo amezitaja kwamba, kuna makampuni yatapewa yafanye engineering, construction na finance hilo ni jambo bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba juhudi hizo ziongezwe kwa sababu kwa kweli vijijini tuna vitongoji vingi sana, ni vikubwa ambavyo bado havina umeme. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu kuna takribani ya vitongoji 400 ambavyo vimeshakuwa vikubwa na vinahitaji umeme na havina umeme. Vingine viko katika maeneo ambayo viongozi wakubwa wanapita, kwa hiyo mara nyingi vinatoa picha mbaya. Wananchi wakifika pale wanalalamika hawana umeme na umeme unawekwa kwenye kila kijiji, lakini vile vitongoji havina umeme. Kwa hiyo, ni jambo ambalo nilikuwa naomba tulifanyie nguvu ili tuweze kuiboresha nchi yetu vijiji vyote vipate umeme, kwani kule itavutia maendeleo na viwanda vidogo vidogo ambavyo vitasababisha maendeleo kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni TANESCO; kwa kweli wananchi wanajitahidi sana kutaka kujiunga na umeme. Nikichukulia mimi kwenye Jimbo langu kwenye hizi center kubwa za Mkata, Kabuku na Segera kuna wananchi wengi wameshaweza kuweka umeme kwenye nyumba zao na wameomba, lakini vifaa havijakuwa vya kutosha vya kuwaunganishia umeme. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Wizara yetu hii ya Nishati ifanye mbinu ya haraka kuhakikisha wananchi hawa ambao wako tayari na ni wateja ambao wataongeza pato kwenye TANESCO na nchi yetu kwa ujumla waweze kupatiwa umeme haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache nashukuru sana ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)