Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. John Michael Sallu (8 total)

MHE. JOHN M. SALLU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Kwamsisi mpaka Mkata kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kwamsisi hadi Mkata yenye urefu wa kilometa 35 ni sehemu ya barabara ya Mkalamo Junction hadi Mkata yenye urefu wa kilometa 73.1. Barabara hii ni ya mkoa na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, sehemu ya barabara hii kutoka Mkalamo Junction hadi Kwamsisi yenye urefu wa kilometa 38.51 iliingizwa katika mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Pangani – Tungamaa – Mkwaja hadi Mkange yenye urefu wa kilometa 95.2. Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami amepatikana ambaye ni China Railway 15 Group na Mkataba umesainiwa tarehe 6 Septemba, 2021. Gharama za ujenzi ni shilingi bilioni 94.539 na muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miezi 48.

Mheshimiwa Spika, sehemu iliyobaki ya Kwamsisi hadi Mkata iliingizwa katika mpango wa RISE (Roads to Inclusion and Socioeconomic Opportunities) ambao inafadhiliwa na Benki ya Dunia. Mradi huu upo katika hatua ya manunuzi ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOHN M. SALLU aliuliza: -

Je, ni lini minara ya simu itajengwa katika maeneo ambayo hayana mawasiliano katika Jimbo la Handeni Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma ya mawasilianao katika Jimbo la Handeni Vijijini katika Kata za Kwamatuku ambapo umejengwa mnara wa Tigo katika Kijiji cha Kwamatuku; Kwamkonje ambapo umejengwa mnara wa Tigo katika Kijiji cha Kwamkonje; na Misima ambapo imejengwa minara miwili ya TTCL katika Vijiji vya Kibaya na Msomera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya tathmini ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika Jimbo la Handeni Vijijini katika Kata za Kang’ata, Kwamgwe, Kwamkonje, Kwaruguru, Kwasunga, Mazingara, Mgambo, Misima, Ndolwa na Sindeni pamoja na vijiji vyake vyote. Ilibainika uwepo wa changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano ambapo utatuzi wake unahitaji ujenzi wa minara ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia matokeo ya tathmini hiyo, Serikali imeziingiza kata hizi katika zabuni ya mradi wa Tanzania ya kidigitali iliyotangazwa na imefunguliwa tarehe 31 Januari, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JOHN M. SALLU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga daraja la Kwasunga – Handeni Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa John Marko Sallu Mbunge wa Jimbo la Handeni Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Handeni na Wilaya ya Bagamoyo inatenganishwa na Mto Mligazi. Mto huu umekuwa changamoto kubwa kwa watumiaji wa barabara ya Kwasunga inayotoka Mkata kuelekea Kwasunga kuunganisha vijijni vya Miyono katika Wilaya ya Bagamoyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA Mkoa wa Tanga imeingia mkataba Na. AE/092/2021-2022/TAG/C/01 na Mkandarasi Mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kampuni ya BICO wenye gharama ya Shilingi milioni 42.98 kwa ajili ya uchunguzi wa miamba. Kazi ya uchunguzi imeshafanyika na kwa sasa mkandarasi huyo yupo katika hatua ya mwisho ya kuwasilisha taarifa ya matokeo ya uchunguzi ambapo baada ya kazi ya usanifu wa daraja pamoja na uandaaji wa michoro na gharama za ujenzi Serikali itatenga fedha za ujenzi wa daraja hilo.
MHE. JOHN M. SALLU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi kwa kiwango cha lami kipande cha barabara ya Turiani hadi Handeni kilometa 104?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii inayoanzia Magole, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya kuanzia Magole hadi Turiani yenye urefu wa kilometa 45.27, katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa sehemu iliyobaki kati ya Turiani – Mziha hadi Handeni kilometa 104 kwa awamu, ahsante.
MHE. JOHN M. SALLU aliuliza: -

Je, ni lini Kituo cha Afya katika Kata ya Segera, Tarafa ya Mkumbulu kitajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA YA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga fedha shilingi bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati katika kata 234 kote nchini. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ilipewa shilingi milioni 500 ya ujenzi wa Kituo cha Afya Sindeni.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye Kata za kimkakati nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Segera katika Tarafa ya Mkumbulu.
MHE. JOHN M. SALLU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kipoza umeme transfoma kutoka kwenye umeme wa msongo wa kV 132 pale Mkata?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 imetenga jumla ya shilingi bilioni 16.94 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme chenye uwezo wa MVA 120 kilichopo katika eneo la Mkata, Wilaya ya Handeni Vijijini. Ujenzi wa kituo hicho unatarajia kuanza mwezi Agosti, 2022 na kukamilika mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kituo hiki utaenda sambamba na ujenzi wa njia ya kusambaza umeme ya msongo wa kV 33 yenye urefu wa kilometa 40 kutoka Mkata hadi Kwamsisi kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa umeme katika machimbo graphite yaliyopo katika eneo la Kwamsisi. Pia Mradi huu ni sehemu ya mradi mzima wa Kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Projects) ambao umetengewa jumla ya shilingi bilioni 500 katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
MHE. JOHN M. SALLU aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza kupanua barabara ya kutoka Segera – Manga hadi Chalinze?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetangaza zabuni kwa ajili ya kupata Mhandisi Mshauri wa kufanyakazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa Kina wa barabara ya Segera - Manga - Chalinze yenye urefu wa kilomita 175 na zitafunguliwa tarehe 14 Febuari, 2024. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inatarajiwa kukamilika Agosti, 2025. Baada ya kazi hiyo kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa barabara hiyo. Aidha, Serikali imekuwa ikipanua maeneo hatarishi kama kwenye milima na miinuko ili kupunguza ajali za barabarani. Ahsante.
MHE. JOHN M. SALLU K.n.y MHE. REUBEN N. KWAGILWA aliuliza:-

Je, lini Serikali itazipandisha hadhi zahanati za Mkwajuni Chanika na Hedi Kwamagome kuwa Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati ya Hedi Kwamagome ina eneo la ekari 10 na inahudumia takribani wakazi 15,138. Zahanati hii ipo umbali wa kilometa 17 kutoka hospitali ya Halmashauri, hivyo inakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na kuipandisha hadhi zahanati hiyo kuwa kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Zahanati ya Mkwajuni Chanika ina eneo la ukubwa wa ekari Saba na ipo umbali wa kilometa mbili kutoka Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Handeni na hivyo haikidhi vigezo vya kuwa kituo cha afya. Aidha, zahanati hiyo itaendelea kuboreshwa kadri ya mahitaji ili iweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi. Ahsante.