Answers to supplementary Questions by Hon. Mwanaidi Ali Khamis (58 total)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha kwa majibu yake mazuri na amenipa mwongozo na yametoa matumaini, lakini nina maswali mawili mdogo ya nyongeza: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa ni wengi walioweka amana zao pale walitumia viinua mgongo vyao kuweka amana katika Benki ya FBME, hasa kule kwetu Zanzibar nilikotoka. Amesema wamelipwa wateja nusu na waliobakia bado hawajalipwa na watakaolipwa watalipwa kutokana na fedha ambazo watapata amount ambayo haitazidi 1,500,000/=; na kwa kuwa hii benki ni ya nje; na kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Financial Institutions, BOT ndio wenye dhamana ya kukaribisha mabenki ndani, swali langu;’ je, ni lini watalipwa fedha zao zote kwa sababu, benki hii haijafilisika FBME?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Benki Kuu ya Tanzania itaacha kuingiza benki hovyo hovyo kama hizi za kutoka nje zikaleta madhara katika nchi yetu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Hassan King kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza alilouliza Mheshimiwa King amesema kwamba, lini wateja hao ambao wana amana zao katika benki ya FBME watapatiwa fedha zao. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, wateja waliokuwa na amana zaidi ya shilingi 1,500,000 watalipwa kiasi kitakachobaki chini ya zoezi la ufilisi wa benki ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za benki husika. Suala hili liko chini ya mujibu wa sheria, kwa hivyo sheria zitakapomalizika Mheshimiwa King basi, wateja wote wenye amana katika benki hiyo watalipwa pesa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; anaulizia lini benki zitatoa ukomo wa kuchukua benki ambazo hazina faida katika nchi yetu. Mheshimiwa King jibu lako la pili naomba nilichukue ili nikalifanyie kazi na nitakujibu kwa barua ili uelewe maelezo zaidi katika Serikali yetu, uweze kupata ufafanuzi zaidi wa kupata jibu lako sahihi. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Nataka tu niongezee kakipengele kadogo kale ambako kanaongelea lini hawa watu watapata fedha. Kwa benki hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameuliza utaratibu huu ambao ameuelezea Mheshimiwa Naibu Waziri umekuwa mrefu kwa sababu benki hii ilikuwa ina-operate katika nchi mbili. Kwa maana hiyo, ule utaratibu wa mufilisi kuweza kukusanya madeni na kukusanya na mali zote ili azibadilishe ziwe fedha ili aweze kuwalipa wale wateja ambao amana zao zilikuwa zinazidi kile kiwango cha awali ambacho wanapewa pale benki inapokuwa kwenye mufilisi, kikamilike. Kwa hiyo, hicho kikishakamilika hapo ndipo ambapo mufilisi ataweza kufanya hiyo kazi ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameisema na hawa wateja waweze kupata hizo fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la pili ambalo Mheshimiwa muuliza swali ndugu yangu King amesema ni lini Benki Kuu itaacha kuruhusu mabenki yaingine hovyo hovyo. Nimhakikishie kwamba, mabenki hayaingii hovyo hovyo na Serikali inafanya due diligence kwa kila benki inapotaka kufanya kazi hapa nchini na ndio maana Benki Kuu iliingilia kati ilipoona baadhi ya mabenki hawaendi sawasawa na vile ambavyo yanatakiwa yafanye kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai tu kwa wananchi wetu kwa sababu, huwa kuna report zinazotolewa kila miezi mitatu na kunakuwepo na mkutano mkuu wa wadau wa benki na sisi tuwe tunafuatilia ili tuweze kuona mienendo ya benki. Tusisubirie tu Benki Kuu ambaye ni msimamizi aweze kufanya jukumu hilo ambalo linawahusu pia, wadau wadau wa benki ambao wanatakiwa watoe muongozo kwa benki yao. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wewe ni miongoni mwa watu waliofika Jimboni kwetu na kuona namna ambavyo tunalima miwa kwa bidii kwa kufuata kauli ya Mheshimiwa Rais ya nchi kujitegemea katika suala zima la sukari; na kwa kuwa hao wenye viwanda ndio waliopewa vibali vya kuingiza sukari inayopungua katika nchi yetu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka mwekezaji mwingine wa kiwanda ili kuondoa monopolism ya kiwanda ambacho kipo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri na Mawaziri husika katika sekta hii ya kilimo na viwanda na biashara, watakuwa tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili, kwenda kuwasikiliza wananchi hasa wakulima wa miwa Jimboni kwangu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, Serikali inaona umuhimu wa kuongeza uwekezaji wa viwanda vya sukari nchini hasa katika Kiwanda cha Kilombero ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini. Kwa upande wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Serikali na mbia mwenza, iko katika majadiliano ya kupanua kiwanda hiki na hatimaye kuongeza uzalishaji wa sukari ili miwa yote inayolimwa iweze kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, napenda kumwahidi Mheshimiwa Abubakari kwamba niko tayari kuongozana naye pamoja na wataalam wangu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kujionea hali halisi ya uzalishaji katika kiwanda hicho, pale tutakapopata nafasi mara baada ya mkutano huu wa Bunge kuahirishwa. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuongezea majibu kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali iko kwenye mazungumzo na wawekezaji kadhaa angalau watatu ambao wana nia ya kuwekeza katika kujenga viwanda vipya vya sukari. Naamini kwa mazungumzo hayo, tukiwapata tutapunguza sana tatizo la sukari na nia ya Serikali ni kuona kwamba katika mwaka mmoja ujao tunajitosheleza kwa mahitaji ya sukari hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba, wiki ijayo baada ya Bunge hili mimi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tuna ziara katika Mkoa wa Morogoro na tutajitahidi tufike pia jimboni kwa Mheshimiwa ili kuweza kuona changamoto. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini Lukumbule ni lango kubwa ambalo wafanyabiashara wanapita kupeleka bidhaa zao Msumbiji na wale wanaotoka Msumbiji wanapita Lukumbule kuleta Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekubali kufanya tathmini na kwa kuwa wananchi wa Tanzania wanaopeleka bidhaa Msumbiji mara nyingi hunyang’anywa mali zao kwa kukosa documents za kusafirisha mizigo yao kwenda Msumbiji.
Je, Serikali haioni haja ya haraka kufanya tathmini hiyo ili kuhakikisha wananchi wetu wa Tanzania wanaoenda Msumbiji hawanyang’anywi mali zao mara kwa mara? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini lina miji mitano mikubwa; Nalasi, Mchoteka, Malumba, Lukumbule pamoja na Misechela ambayo ina wafanyabiashara wengi na miji hiyo iko zaidi ya kilometa 80 kutoka ilipo Ofisi ya TRA Tunduru Mjini.
Je, Serikali haioni haja ya kupeleka agencies katika maeneo hayo ili wafanyabiashara wale waweze kulipa kodi zao wakiwa katika maeneo yao ya biashara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeona umuhimu wa ushauri wa Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, ushauri tumeupokea na tutaufanyia kazi kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyowekwa na pale tutakapopata majibu basi tutamfikishia majibu kwa haraka sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri lakini naomba niulize maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza; ni dhahiri kuwa Taifa letu linahitaji wawekezaji wengi kutoka Mataifa mengine, lakini naamini itakuwa ni ngumu kupata wawekezaji ikiwa hawa tu tulionao wanashindwa kuwekeza kutokana na mrundikano mkubwa wa kodi zilizoko ndani ya Taifa letu.
Sasa nataka kujua je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kulichukua jambo hili na kufanya marekebisho ya sheria za kodi ili wananchi wetu waweze kufanya biashara kwa uhuru? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa TRA wamekuwa na utaratibu wa kufanya makadirio ya kodi wanapofika kwenye biashara za watu; ni nini tamko la Serikali katika hili maana TRA wamekuwa wakiwakadiria watu kodi kubwa ambazo zinazidi mitaji yao na kusababisha watu wengi kufilisika na kufunga biashara. Ni nini tamko la Serikali kwa hiki kinachoendelea leo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Fiyao kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kutokana na mazingira mazuri na rafiki hakuna ukandamizaji wa kodi kwa wananchi/wafanyabiashara atakayekimbia kwa kufanya biashara kwa sababu ya kulipa kodi kubwa ambazo Serikali imeziweka kiurafiki na kulipa kodi kwa sheria na utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la pili la Mheshimiwa Stella Fiyao kuwa kama Mheshimiwa anaona kuna kodi kandamizi ambazo wafanyabiashara wanapatiwa basi tungemuomba atuletee changamoto hizo na Serikali itazifanyia kazi kwa mujibu wa sheria na mipango yote iliyowekwa katika Serikali. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sheria inawaruhusu wachezesha bonanza kulipa asilimia 0.03 ya mapato yao, nataka kumuuliza Waziri, je, ni nani anayejumlisha mapato yao kwa mwaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Wachina hawa wanaochezesha mabonanza wanarundika pesa zao nyumbani wala hawapeleki benki. Mfano mzuri ilitokea Morogoro, ulipofanyika msako Morogoro walikutwa na bilioni 2.5, ukafanyika msako Arusha wakakutwa na bilioni 5.0 ndani. Sasa sisi kama Halmashauri kupata ile asilimia tunayoitaka kwenye levy tunaipataje? Je, Serikali wako tayari kuruhusu kwamba, kule Halmashauri tuweke makufuli pamoja pale kwenye zile slot machine, ili wanapoenda kufungua watendaji wetu tujumuike nao ili tuweze kupata hesabu vizuri kwa ajili ya kukusanya hiyo service levy? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato ya service levy ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa wenyewe kwa mujibu wa sheria iliyowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, naomba kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Musukuma kwamba, anajali na anaijali Serikali kwa kuangalia uchumi wa nchi unavyokwenda. Hata hivyo, Mheshimiwa Musukuma ushauri wake tumeuchukua na tutaufanyia kazi kwa mujibu wa sheria kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama ilivyo sheria. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakubaliana na Serikali kwamba kifungu cha 9 (1)(j) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kinaipa mamlaka PPRA kufanya kazi nyingine ikiwemo ya kuandaa mifumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakubaliana kwamba mfumo huu wa TANePS umeandaliwa na wataalam wa nje kupitia mradi uliofadhiliwa na Benki ya Dunia; lakini atakubaliana na mimi, kwamba Serikali kupitia wataalam wa ndani kupitia Wizara ya Fedha imeandaa mifumo ambayo inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa ukiwepo huu wa GPG, MUSE na GSPP.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Juzi tumeona Mheshimiwa Rais wakati anapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, ameonesha nia ya kuitaka serikali kuwa na mifumo michache ili kuongeza ufanisi.
(i) Je, Serikali haioni kwamba kuendelea kuwa na mifumo mingi kwenye taasisi nyingi itaendeleza urasimu badala ya ufanisi?
(ii) Kwa kuwa mfumo huu ukiuangalia na kwa language iliyoandikwa na wataalam hao wa nje haikuzingatia business concept ya nchi, yetu na mfumo huu umekuwa na matatizo mengi, hata siku mbili zilizopita mfumo huu ulikuwa chini na kuleta matatizo makubwa kwenye manunuzi.
Je, haoni kwamba ni wakati muafaka sasa kupitia kurugenzi yetu ya taarifa za mifumo ya fedha pale Hazina tutapunguza gharama kwa ku-integrate mfumo huu na mifumo ambayo nimeitaja hapo juu? (Makofi).
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Silaa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mfumo wa TANePS tayari umeshaunganishwa na mifumo mingine ya GPS na taratibu zinaendelea ili kuunganisha na mifumo mingine ya serikali ikiwemo mifumo ya MUSE nakadhalika ili kupunguza gharama za uendeshaji Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Slaa, ni kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya juzi alipokuwa akipokea taarifa za CAG; kuhusu kuunganisha mifumo ya malipo yote ya Serikali ili kubaki na mifumo michache ili kupunguza gharama za uendeshaji. Kwa hivyo, Mheshimiwa Rais amesema kwamba tuwe na mifumo michache ambayo inaweza kuendesha Serikali na kupunguza gharama za Serikali ili kuondoa usumbufu na upotevu wa fedha za Serikali. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali bado kuna tatizo. Wengi wa wateja waliokuwa wa benki hii ambayo ilifutiwa leseni pamoja na wanahisa ni wanyonge, ni watu ambao wasingeweza kusubiri kwa muda mrefu wakisubiri amana zao zilipwe. Pamoja na kwamba kuna ambao walilipwa 1,500,000/= kwa kupitia DIB naona kwamba suala la muda ni changamoto. Wateja wengi hawataweza kusubiri kwa muda mrefu kiasi hiki, sasa hivi ni miaka mitatu na miezi mitatu tangu benki hii ifutiwe leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itamke bayana, je, ni lini itamaliza tatizo hili kwa kulipa amana zote kwa wana hisa na wateja ambao walikuwa wa benki hii?
Mheshimiwa Naibu Spika na ninaomba hapa ni- declare interest, kwamba mimi mwenye nilikuwa mwanahisa wa benki hii nasubiri hiyo pesa kwa miaka mitatu sasa, ningeipata ningenunua hata ng’ombe. Naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa John kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, Bodi ya Bima ya Amana bado inaendelea na zoezi la ufilisi wa mabenki na itakapokamilisha ufilisi wateja wote waliozidi zaidi ya shilingi 1,500,000/= watalipwa fedha zao kulingana na mapato yaliyokusanywa na kupatikana kutokana na benki husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge, changamoto ambazo wanazipata katika benki ya amana mpaka sasa hivi ni wale ambao waliokopeshwa fedha hizo bado wanaendelea kuwa na ugumu wa kulipa. Hata hivyo Serikali inaendelea kutafuta taratibu nyingine ili kuhimiza wale waliokopeshwa kulipa madeni hayo ili wateja wanaodai fedha zao katika benki hiyo waweze kulipwa kwa haraka. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, akina mama wa Mkoa wa Tanga ni watafutaji na wachapakazi, wamejiunda kwenye vikundi lakini wanakosa tija kwa kukosa elimu ya kuandaa maandiko ya miradi na namna ambavyo wanaweza kuunganishwa kwenye taasisi za fedha ili waweze kupata mikopo. Je, ni lini Serikali italeta makongamano hayo ambayo Serikali imeyafanya katika mikoa mingine kwenye Mkoa wa Tanga ili akina mama hawa na wenyewe waweze kupata ujuzi huo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za ujasiliamali?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, elimu ni kitu endelevu; makongamano pekee yanaweza yasikidhi ile haja ya akina mama wa Mkoa wa Tanga. Je, ni kwa namna gani sasa Serikali inajipanga kuimarisha Ofisi za Maendeleo ya Jamii kwenye Halmashauri zetu ili ziweze kutoa elimu hii ya uandishi wa maandiko ya miradi pamoja na kuwasaidia akina mama na taasisi za kifedha badala ya kutegemea zile za Halmashauri peke yake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, hadi sasa Serikali imeshafanya makongamano katika mikoa mitano kati ya mikoa 26 nchini. Katika mikoa hiyo 26 Tanga ni mkoa mmojawapo kati ya mikoa 21 ambayo haijapata mafunzo hadi sasa. Tunategemea kupata rasilimali fedha na baada ya kupata rasilimali fedha hizo tutafanya makongamano hayo katika mikoa iliyobaki. Nimuombe tu Mheshimiwa Husna awe mstahamilivu kwa hili, Serikali tumeshajipanga kuendesha makongamano hayo wakati wowote tutakapopata fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Husna amesema vipi tutawezesha halmashauri ili wanawake waweze kupata elimu. Serikali imeshaanza kuweza halmashauri nchini na katika mwaka 2000 imeandaa miongozo ya utoaji mikopo kwa ajili ya vikundi mbalimbali vya wanawake ikiwemo kuwapatia elimu ya ujasiliamali na mafunzo ya uendeshaji wa biashara kabla na baada ya kupata mikopo. Hata hivyo, mwongozo huo umeambatanishwa na mfano rahisi wa andiko la miradi ulioandikwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kutoa elimu kuhusu namna ya kuandaa andiko hilo.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Husna kwa kuwapigania wanawake wa mkoa wake ili waweze kupata elimu ya kiuchumi kwa ajili ya kuondoa umaskini.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, sheria zilizopo bado kuna changamoto kubwa sana katika eneo hili na ndiyo maana hata Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kimeliona hili na kimeahidi kwamba kitaelekeza Serikali kwenye ukurasa wake wa 145 inasema hivi; “Chama cha Mapinduzi kitaelekeza Serikali kuimarisha huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na matunzo kwa watoto.” Kwa msingi huu naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, je, Serikali haioni saa ipo haja ya kurekebisha sheria zilizopo ili gharama ya matunzo ya watoto iendane na hali ya uchumi wa sasa na maisha ya sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili kwa kuwa vitendo vya masuala ya familia vimezidi kushamiri; je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuanzisha Mahakama ya Familia (Family Court) kama walivyofanya kwenye Mahakama ya Ardhi ili masuala haya ya matunzo ya watoto yaweze kubebwa kwa uzito unaostahili na kupanua wigo wa haki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaungana na Mheshimiwa Mbunge kuwa kuna haja ya chombo maalum kitakachokuwa kinashughulikia masuala ya familia. Ushauri wake tumeupokea na tutaufanyia kazi kulingana na sheria zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali iweke kiwango cha matunzo kitakachozingatia hali ya uchumi ya sasa kusaidia matunzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi kuwa huduma za matunzo ya watoto umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kifungu cha 44(a) na (e) sheria hii imeipa mamlaka Mahakama kufanya maamuzi ya kuzingatia mambo yafuatayo; kuangalia kipato cha wazazi wote wawili, ulemavu wowote na uwezo wa kipato cha mzazi katika jukumu la kutunza mtoto, wajibu wa majukumu ya mzazi katika kutoa matunzo kulinganisha na majukumu ya kutoa matunzo kwa watoto, gharama za maisha katika eneo ambalo mtoto anaishi na haki nyingine za kisheria ambazo mtoto anahitaji kupatiwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, changamoto ya wanawake kutelekezewa watoto imekuwa kubwa sana; je, Serikali haioni umuhimu wa kubadilisha kuleta mabadiliko ya Sheria ya Ustawi wa Jamii Bungeni ili iendane na hali halisi ya maisha ya sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutalifanyia kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo ili wanawake waweze kupata haki zao kikamilifu. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri kwanza niipongeza Serikali kwa kuona kuna haja ya kuwa na mpango mkakati wa Taifa wa kutokemeza ukatili. Hata hivyo, inashangaza kuona Serikali yenyewe imejiwekea asilimia 50 tu kutokomeza matendo haya, ifikapo 2022.
Mheshimiwa Spika, malengo haya bado yako chini na tunawapa mwanya…
SPIKA: Mheshimiwa Zaytun nenda kwenye kuuliza swali.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali haioni kama kuna haja ya kujiwekea malengo ya juu ambayo yatadhibiti matendo haya na kukomesha?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa vitendo hivi vingi vinafanyika kwenye ngazi za kata na za vitongoji lakini madawati ya kijinsia mengi yapo kwenye ngazi za wilaya. Je, Serikali haioni kama kuna haja ya kushusha huduma hii kwenye ngazi za chini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nilieleza kuwa, mpaka sasa Serikali imeshaanzisha madawati 420 ya jinsia ya watoto kwa vituo mbalimbali nchini. Aidha, ningependa kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa huduma za wahanga wa ukatili zinafanyika katika kila Kituo cha Polisi na kila Kituo cha Polisi kimewekwa chumba maalum kwa ajili ya kuwahudumia wahanga hao.
Mheshimiwa Spika, vilevile wahanga hao wa ukatili uhudumiwa na Polisi ambao masuala yao yote huanzia katika Vituo Vidogo vya Polisi na kumalizia Vituo Vikubwa vya Polisi kwa ajili ya kushughulikiwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Zaytun, ni kweli kuwa kuna sababu ambazo zinasababisha vitendo vya ukatili wa kijinsia ni uwepo wa imani za ushirikina. Serikali ishaanza kushughulikia suala hili ili kutekeleza mpango wa Taifa na kutokomeza ukatili dhini ya wanawake na watoto. Aidha, nimuahidi kuwa nitalifuatilia suala hili na kuhakikisha wanawake wote wa Arumeru na Monduli wanakuwa salama pasipo na kunyanyaswa. Pia ni watake Maafisa wa Maendeleo ya Jamii Arumeru na Monduli kupanga mpango kazi maalum ili kuwaendeleza wananchi wa Arumeru kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na majibu ya Serikali kwamba nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali. Swali la kwanza; kwa kuwa sheria hizi huwa zinafanyiwa marekebisho kadri uhitaji unavyotokea au wakati. Je ni lini sasa Serikali italeta marekebisho ya sheria hii ili kuwapa nafasi nzuri zaidi waathirika kuripoti haya matukio?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Vituo hivi vya Mkono kwa Mkono ni vichache, vinakadiriwa kuwa
14 nchini na uhitaji ni mkubwa kwa sababu tunahitaji kuwatunza wale waathirika kwenye vituo hivyo kabla ya mashauri kukamilika ili kulinda uchunguzi. Je Serikali ina mpango gani sasa kwa ajili ya kuongeza vituo hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza kwa nini dawati hilo halishirikishwi na vituo vya hospitali; kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi dawati hili hushirikiana na Vituo vya Mkono kwa Mkono na pia hushirikiana na Jeshi la Polisi, huduma za afya pamoja na wanasheria ili kuhakikisha kwamba waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia hupata huduma stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuongezea kwamba, sio kila wahanga waathirika wa vitendo vya ukatili wa jinsia, wanahitaji huduma za afya; waathirika wengine wanahitaji huduma za kisheria, unasihi, na msaada wa kisheria ili kuona kwamba wanapatiwa huduma stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, je ni lini sasa Serikali litaleta marekebisho hayo Bungeni. Napenda kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba, hadi sasa hatujapata ugumu wa marekebisho ya sheria ya masuala ya ukatili wa kijinsia. Kwa hivyo nimwombe Mheshimiwa Husna atuletee marekebisho au maboresho ya dawati hili ili Serikali iweze kuangalia zaidi maboresho hayo na muathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia aweze kupata huduma na kuweza kuleta malalamiko yake bila ya kuwa na hofu kwa kutumia sheria ambazo zimewekwa. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kutokana na majibu yaliyotolewa na Serikali, inaonyesha ni dhahiri ni Halmashauri mbili tu kati ya Halmashauri 184 nchi nzima ambazo zimepatiwa pikipiki. Hali hii inaonyesha jinsi ambavyo upo uhitaji mkubwa katika Halmashauri nyingine. Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuhakikisha kitengo hicho kinawezeshwa kibajeti katika Halmashauri zote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Josephine kwa kufuatilia Maafisa hawa na kuona umuhimu wa kazi zao wanazozifanya.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Maafisa hawa wana changamoto kubwa ya vitendea kazi. Mimi mwenyewe binafsi baada ya kumalizika Bunge la Bajeti niliweza kutembelea mikoa mitatu pamoja na Wilaya zake, yaani Mkoa wa Tabora, Iringa na Ruvuma na nimekutana na Maafisa hawa wa Ustawi wa Jamii wakanielezea changamoto zao.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Wizara inaendelea na mikakati ya kuwasiliana na wadau wa Maendeleo ya Jamii ili pamoja na miradi ambayo wanaitekeleza na wadau hao, kuwawezesha Maafisa hawa wa Jamii kuendelea kupata vifaa vya kufanyia kazi kulingana na mazingira yao waliyokuwa nayo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inawajali sana wafanyakazi pamoja na wananchi wake. Kwa hili tumelipokea na tutaendelea kulifanyia kazi suala hili la upatikanaji wa vitendea kazi kwa mikoa yote nchini Tanzania. Ahsante, napenda kuwasilisha.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uhalisia kwamba halmashauri zetu nyingi nchini zina changamoto sana ya miundombinu. Serikali haioni kuna haja ya kubadilisha usafiri kutoka kwenye pikipiki na kuwapatia magari maafisa maendeleo ya jamii hawa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na kwa uwanda mkubwa? Kwa mfano, kipindi cha mvua mtu huyo atatumiaje pikipiki maana yake atakuwa analowa, hawezi kutekeleza majukumu yake. Serikali haioni umuhimu wa kuwanunulia magari maafisa maendeleo ya jamii ikiwa ni pamoja na Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMIS): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyogeza la Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli, maafisa hawa wanatembea kwa pikipiki kwa ajili ya kufuatilia wafanyakazi hawa au vitendo mbalimbali vinavyotokea katika jamii. Serikali kama nilivyoeleza imejipanga kuzungumza na wadau ambao wanaendeleza maendeleo haya ya jamii ili kuhakikisha kwamba maafisa hawa hawatopata tabu katika kazi zao katika mazingira yao ya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo, ahsante nashukuru. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nilikuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kutokana na tafiti ambazo zinaendelea inaonyesha kwamba kutakuwa kuna ongezeko kubwa la wazee duniani ikiwemo na Tanzania. Sasa Wizara inajipangaje kuhakikisha inaongeza vituo vya kulelea wazee, aidha kutoka mikoa angalau basi twende hata kwenye Wilaya.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na ukarabati ambao unaendelea kwenye hivyo vituo: -
Je, Serikali imejipangaje kuweka vifaa tiba na mahitaji muhimu kwa ajili ya wazee wetu ndani ya hivyo vituo?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bahati kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Bahati na kumpongeza kwa kujali wazee, kwani wazee ni tunu ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake na mwanzo Mheshimiwa Bahati Mbunge, ushauri wake umepokelewa na kuzingatiwa katika mapendekezo ya bajeti katika kipindi cha mwaka 2022/2023. Hata hivyo kila mwaka tunaboresha mahitaji ya wazee kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji muhimu kama vile mavazi, chakula, malazi na afya bora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo linasema kwamba wazee wapewe msaada wa kisaikolojia. Makazi ya wazee yanaongozwa na kusimamiwa na Maafisa wa Ustawi wa Jamii, wataalam ambao wanatoa msaada wa kisaikolojia kwa wazee wetu. Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anawajali sana wazee, anawapenda na kuhakikisha kwamba wanapata haki zao za msingi kila wakati na pale inapohitajika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Wizara hii tayari inaona ina changamoto sana ya kupata fedha kwa ajili ya kundi hili la wazee, lakini bado wazee hawa wana changamoto sana ya uwezo.
Je, Wizara ya ina mkakati gani sasa wa kutumia ile sera ya asilimia 10 kuweza kuwaweka na wazee kupata kama asilimia mbili ili ziwasaidie?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Issa tunakuomba kwamba sheria bado zinafanya kazi na zitakapokamilika basi wazee hawa watapewa haki zao na watapewa msaada wa kuongezewa kiasi cha fedha kwa ajili ya mahitaji ya maisha yao. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, watoto hawa wa mitaani ndio watoto ambao wanazalisha makundi kama panya road, damu chafu na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Serikali inazo nyumba za kulelea hawa Watoto. Ningeomba kujua Serikali ina vituo vingaapi vya kulelea watoto wa mitaani.
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Nchi yetu ya Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu Watoto. Kwa mfano The UN Convention on the Right of the Child na mkataba wa Afrika wa The African Charter on the Right of the Child. Swali langu; je, Serikali inamkakati gani wa kuhakikisha kwamba watoto wa Tanzania ambao wako mitaani wanapata elimu ambayo ni haki yao pamoja na kujua haki zao za msingi?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inavituo viwili vya kulea Watoto ambavyo inavimiliki. Vituo hivyo ni Kurasini ambacho kipo Dar es Salaam na Kikombo ambacho kipo Dodoma. Vituo hivyo vina idadi ya Watoto 142 ambapo 88 wakiwa ni wakiume na 54 ni wa kike.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, watoto wote ambao wanalelewa katika vituo vya watoto ambavyo vinamilikiwa na Serikali wanapata haki zote za msingi ikiwemo elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu na elimu ya ufundi (VETA). Wanapomaliza wanapewa vifaa maalum vya kujiendeleza ili waweze kujiajiri wenyewe. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kumekuwa na wimbi kubwa la wazazi kuwafanyia vitendo vya kikatili watoto. Je, Serikali inampango gani wa kuwajengea watoto uwezo au uelewa mashuleni wa kujitetea pindi wanapopitia ukatili wa kijjinsia?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kukubaliana na hili, Serikali inatekeleza afua mbalimbali za kutoa elimu za malezi na makuzi, pamoja na elimu ambayo inakabiliana na ukatili dhidi ya watoto. Aidha, kuimarisha Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wanawake na watoto zilizopo ngazi zote nchini kwa ajili ya kuwa elimu wananchi wa jamii yetu.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Watoto wa mitaani hususani watoto wa kiume wamekuwa wakipitia unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia hususan suala la kulawitiwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchukua hatua za haraka ikiwemo mabadiliko ya sheria ili kuweka sheria kali na za mfano kwa watu wanaotenda vitendo vya ulawiti kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na ukatili kwa watoto ambao wanalawitiwa. Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na maafisa wetu wa maendeleo na ustawi wa jamii, tunahakikisha kwamba, watuhumiwa wote ambao wanafanya vitendo vya ukatili kwa watoto wetu wanachukuliwa hatua kali pale inapostahiki. Ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Je, kuna katazo lolote la watu hawa (wamachinga) kupangwa katika maeneo ya wazi katika halmashauri na maeneo ya taasisi?
Pili; je, Serikali inaweza kutoa ruhusa kwa ajili ya wamachinga, hasa waliokuwa wanauza mananasi, kuweza kujipanga eneo la Railway na wale wa samaki kurudi eneo la Manyema? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inawajali sana wananchi wake, hasa wafanyabiashara wadogowadogo. Rais ametoa shilingi milioni 10 kwa kila mkoa kwa ajili ya kujengwa ofisi za wafanyabiashara wadogowadogo.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tayari imeshachora michoro hiyo kwa ajili ya ujenzi huo. Wafanyabiashara hawaruhusiwi kufanya biashara zao katika maeneo ya wazi na ya taasisi. Wafuate maelekezo ya viongozi wao wafanye biashara katika maeneo waliyopangiwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, eneo la wazi la Manyema, Moshi limetengwa kwa ajili ya shughuli za reli. Wafanyabiashara hawaruhusiwi kufanya biashara kwa ajili ya usalama wao, lakini pia kuzuia shughuli za shirika la reli hiyo.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Moshi tayari imeshawatengea wafanyabiashara hao walioondoshwa katika eneo la Reli la Manyema kufanya biashara zao katika maeneo mengine. Ahsante. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri alisema kuna ngazi mbalimbali ambazo zinashughulika na hayo, lakini wanaonaje sasa wakati huu wasianzishe jeshi la jamii kama lilivyo Jeshi USU kwa upande wa Maliasili, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba jamii inalinda watoto wetu dhidi ya ukatili pamoja na wanawake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Ni kwa nini sasa Serikali isiende kwenye shule zetu kwa ajili ya kuanzisha klabu za stadi za maisha na majukwaa ya stadi za maisha kwa ajili ya kuwajengea watoto wetu uwezo wa kujilinda wenyewe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nusrat kama ifuatavyo. Swali lake la kwanza kuhusu Jeshi Jamii; Wizara imejipanga na mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) ili kuhakikisha kwamba wanakuwa na usalama. Mpango huu umejielekeza kuanzia ngazi ya vijiji hadi mkoa na kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama katika kila eneo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu jukwaa la watoto; Wizara yetu ina majukwaa ya watoto ambayo yanahimiza ulinzi na usalama. Pia yapo mabaraza na clubs za watoto kuanzia shule za msingi, sekondari hadi Vyuo. Klabu hizi zinawafunza watoto na kuwaelimisha waweze kujitambua, kujielewa, kujiamini na kujieleza wakati wowote katika kujikinga na ukatili dhidi ya watoto. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Manyara umeonekana kuwa ni mbili mbili katika ukatili wa jinsia na sababu kubwa ni kwamba waathirika bado hawana elimu ya kutosha kuhusu hatua za kuchukua: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza ukatili wa jinsia katika Mkoa wa Manyara? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
kuhusu swali la ukatili wa jinsia kwa watoto katika mkoa wako, Wizara kama nilivyoeleza imejipanga katika mpango wa Taifa kutokomeza ukatili wa jinsia (MTAKUWWA). Mpango huu unahusisha vijiji hadi mkoa.
Kwa hiyo, kuna Kamati katika kila mkoa ambazo zinahusisha usalama wa watoto na wanawake katika kuhakikisha tunatokomeza ukatili kwa watoto na tunapinga ukatili wa jinsia kwa wanawake na wananchi.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru sana kwa majibu ya Serikali amefafanua vizuri kabisa madhara yanayotokana na wenza kutokuwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, ukiangalia athari ambazo zinatokana na wenza kutokupata nafasi ya kufanya kazi wakiwa wako pamoja, ni kubwa sana na zinaathiri jamii; na sisi tunajua kwamba familia bora ndiyo inajenga jamii bora. (Makofi)
Sasa ni nini mkakati wa Serikali wa kukabiriana na hili suala lililopo mbele yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, ni nini kauli ya Serikali kwa waajiri wale ambao hawatoi fursa ya kuhakikisha kwamba wafanyakazi wao wanapata haki ya kufanya kazi wakiwa karibu na wenza wao?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zainab kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza linahusu madhara ambayo yanawapata watoto wakati wenza wao mbalimbali. Serikali kupitia MTAKUWWA imeunda Kamati Maalum za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake kwa ngazi zote. Maafisa wetu wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wanapita kuelimisha kwa njia za vyombo vya habari, mikutano na makongamano mbalimbali pamoja na midahalo ya kitaifa ambayo inaendelea kila mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nini tamko la Serikali kuhusu wenza ambao wanakatazwa kuwafuata wenza wao walipo. Kanuni na sheria zipo ambazo zinaeleza kila kitu katika Serikali. Serikali yetu imeunda sera, kanuni na miongozo ambayo inawaelemisha wananchi kufuata sheria zitakazowafanya wapate vibali vya kwenda kukaa na wenza wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo zaidi napenda kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge tujifunze kukaa na watoto wetu wakati wowote ule kuwapa muda maalum ambao tunaweza kuwaelimisha elimu ambayo Serikali yetu na utamaduni wetu. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo yameonesha msingi wa hoja hii muhimu sana ya kuhakikisha kwamba ustawi wa familia kwa maana ya wenza na watoto kuishi pamoja ili kuweka makuzi bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako tukufu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma inadhamana ya kuangalia ustawi wa watumishi wote nchini. Baada ya kutambua tatizo hili la wenza kukaa maeneo tofauti tofauti na kusababisha kuwa na athari kubwa katika malezi ya familia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ameshatoa Waraka Namba 452501 kifungu cha 6(b) kimetoa masharti ya kumhakikishia mtumishi ana uwezo wa kuomba kibali cha kuhamia kwa mwenza wake endapo eneo husika litakuwa na nafasi na atakuwa na uthibitisho wa vyeti vya ndoa na nyaraka nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe wito kwa waajiri wote kuhakikisha wanazingatia kifungu cha waraka huo ili kusaidia ustawi wa familia, malezi ya watoto na kuhakikisha kwamba wafanyakazi wetu wanakuwa na fursa ya kuishi na wenza kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nasikitika kwa majibu ya Serikali, kwa sababu tunatambua kwamba ukatili wa kijinsia umeongezeka, sasa mpaka leo wanatuambia madawati ya kijinsia yako 420 na tuna kata takribani 4000. Ina maana takribani asilimia 10 tu ndio watu wanaopata hii huduma ambao wana athirika. Hata hivyo madawati ambayo wanasema wanatarajia kuanzisha Mashuleni wameanzisha so far, Madawati 1,300 na tuna shule zaidi ya 30,000 kwa Sekondari na Msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati hizi anazodai kuamzishwa kwa asilimia 88, aidha hazijaanza kazi labda kwa sababu ya changamoto ya kimuundo au kibajeti. Nataka kujua sasa, ni lini Serikali itazielekeza halmashauri ziweze kutenga bajeti ili kuhakikisha kwamba zinazipatia hizi kamati ambazo zimeanzishwa kwenye hivi vijiji ili ziweze kutekeleza kwa tija na kupunguza au kuzuia kabisa matukio ya ukatili wa kijinsia ambayo yamekithiri katika jamii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa sasa matukio haya ukatili wa kijinsia yanakuwa hayachukuliwi hatua mpaka pale labda vyombo vya habari au mitandao ya kijamii inapo ripoti kwenye jamii ndipo tunaona viongozi wa ngazi za juu wanafuatilia na kuchukua hatua. Nilitaka kujua Serikali imeweka utaratibu upi ambao utawezesha utolewaji wa taarifa na ufuatiliaji wa matukio ambayo yameripotiwa kwenye hizi kamati ambazo mmesema zimeanzishwa kwa asilimia 88 ili kuhakikisha…
MWENYEKITI: Mheshimiwa uliza swalo sasa.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Ndilo swali lenyewe, ili kuhakikisha sasa waathirika wa vitendo vya ukatili wanapata huduma na haki staki kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther ifuatvyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha kamati. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Esther kwa wazo zuri ambalo amelitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe waheshimiwa Wabunge ambao wanaingia katika Mabaraza ya Madiwani walipe kipaumbele suala hili ili Kamati hizi ziweze kujiwezesha na baadaye kufanya kazi kwake kwa makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifumo na utoaji wa taarifa. Kwa suala hili kwa kuwa utekelezaji wa MTAKUWWA ni mtambuka, Serikali itaendelea kutumia mifumo iliyopo kisheria. Kuhusu swali la Jeshi la polisi ndio muamala ambao unaweza kutoa taarifa za ukatili wakati upelelezi unapo kamailika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Mwananchi aweze kuhukumiwa, Mahakama ndiyo itakayo toa hukumu katika vifungu ambavyo vilivyowekwa. Hata hivyo kesi ili iende haraka tunawaomba waathirika wote wawe na ushirikiano na vyombo vya sheria na pia kuwa wawazi katika kuleta maelekezo yao. Ahsante. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba asilimia 88 ndio wameunda katika vijiji, kata na kwenye mitaa yetu. Hata hivyo Kamati hizi zimekuwa hazitekelezi majukumu yake ama hazifahamiki ipasavyo. Mimi nilitaka kujua, je, kamati hizi za ulinzi na usalama wa watoto zimeundwa na wajumbe gani ili tuwatatmbue tuweze kuwafuatilia?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swal la nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo wa Kuanzishwa Madawati ya Ulinzi na Usalama kwa Watoto ulianzishwa Juni, 2022 na kuanzishwa madawati hayo machache. Hata hivyo wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Elimu pamoja na Mamlaka ya Jeshi la polisi tutaendelea kuimarisha Kamati hizi ifikapo mwaka 2023 basi tutahakikisha shule zote zina madawati. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia yameendelea kukithiri hapa nchini, je, ni lini Serikali italeta Muswada wa Sheria ya Ukatili wa Kijinsia hapa Bungeni kama ambavyo Tanzania iliridhia katika Mkutano wa 44 wa Bunge la SADC (SADC Parliamentary Forum)?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, tutajipanga Wizara pamoja na Wizara mtambuka ambazo tunatengeneza miamala hii ya miswada kwa pamoja ili kuweza kuifikisha pale panapohitajika, ahsante sana.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Taarifa za Polisi na mambo tunayoyaona kila siku kwenye jamii yanaonesha kwamba ukatili wa kijinsia unaendelea kuongezeka; je, nini sababu ya ongezeko hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeweka mikakati mingi ya kudhibiti ukatili wa kijinsia ikiwemo Mabaraza ya Watoto, Madawati ya Jinsia, Kamati za Ulinzi, nani anaratibu afua hizi zote? Kwa nini basi tunapata taarifa tu kutoka kwenye Dawati la Polisi, lakini kwenye hizi afua mlizoweka hatupati taarifa zake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bernadeta, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli taarifa za Jeshi la Polisi zinaonesha kwamba ukatili umeongezeka. Sababu ya kuongezeka vitendo vya ukatili ni mmomonyoko wa maadili wa malezi na makuzi kwa Watoto; wazazi na walezi kutowajibika kumlinda mtoto; matumizi mabaya ya kieletroniki, na pia kuiga maadili ambayo siyo utamaduni wa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanapokuwa katika majukwaa yao kutoa elimu hii ya kutokomeza ukatili wa jinsia kwa wananchi wao. Vilevile tunaambiwa mtoto wa mwenzio ni wako, kwa hivyo tuwajibike sote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Swali lake la pili, afua zote zinatekelezwa na Wizara tukishirikiana na wadau mbalimbali hasa Jeshi la Polisi ambalo lina mamlaka ya kutoa taarifa zote za ukatili wa kijinsia katika nchi yetu, ahsante. (Makofi)
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali imefanya utafiti na tathmini na kujua kama elimu inayotolewa inatija na inaleta mabadiliko katika jamii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali haioni haja sasa kutumia taasisi za dini kuiandalia programu maalum kwa ajili ya kutoa elimu kusaidia kukinga vitendo hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tamima, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza; kupitia MTAKUWA uliomaliza muda wake 2020/2021 uliotolewa kwenye Kikao cha Mawaziri wa Wizara mtambuka kilichofanyika tarehe 26 Januari, 2023 inaonesha kuwa jamii iliyopewa elimu inapata tija kwa jamii na inaendelea kuripoti taarifa za vitendo vya ukatili katika vyombo vya usalama.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Serikali kwa kushirikiana na madhehebu ya dini nchini itaendelea kutekeleza programu ya malezi kwa ajili ya kutoa elimu ya kujikinga na vitendo vya ukatili katika taasisi zote za dini, ahsante.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Je, Serikali haioni iko ya haja ya udhalilishaji na ukatili wa wanawake na watoto kuwa ajenda ya kitaifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Maryam, ushauri wake tumeupokea na tutaufanyia kazi kwa sababu vitendo vya ukatili ni vya jamii na jamii yote tunatakiwa tushirikiane kwa pamoja ili kuungana na kupinga vitendo vya ukatili nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; niulize hivi, je, Serikali haioni haja sasa ya kutoa tamko la kuondoa udhalilishaji wa watoto wa kike wanaoolewa chini ya miaka 18 badala ya kusubiri maoni ya wadau kwa kitu ambacho kiko wazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kutoa jibu kwa Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ina taratibu zake na mtoto wa kike anaruhusiwa kuwa na umiliki wa kitu cha peke yake kuanzia miaka 18. Kwa hiyo, ushauri huo tunaomba tuendelee na kuwapa Serikali majukumu haya ili kuhakikisha nini tunakifanya katika nchi yetu, ahsante. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Moja ya vichocheo vikubwa vya udhalilishaji wa wanawake na watoto ni picha za ngono zilizoko katika mitandao, nchi za Uarabuni zimefanikiwa kuzuia kitu wanachoita Uniform Resource Locators (URL) ili picha za ngono zisionekane katika nchi ile.
Je, Serikali haichukui hatua sasa kuzuia picha za ngono kuonekana katika mitandao yetu ya simu ili kuokoa vijana wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa ajili ya kujikinga na vitendo vya ukatili kwa watoto wote kupitia vijarida mbalimbali na pia Serikali inakataza kutoa picha za ngono katika mitandao. Mtu yeyote ambaye atafanya vitendo hivyo na akagundulika, basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA
HABARI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niongezee maelezo kidogo kwenye swali lililoulizwa na Ndugu Tarimba Abbas, Mbunge wa Kinondoni.
Mheshimiwa Spika, katika maendeleo ya TEHAMA, moja ya changamoto kubwa tunayoipata ni udhibiti huo wa baadhi ya taarifa ambazo kwa kweli zinamomonyoa utamaduni na maadili ya nchi yetu, lakini kupitia TCRA tumeongeza uwekezaji mkubwa na sasa tuko katika hatua za mwisho za kuongeza nguvu ya kudhibiti movement ya picha kama hizo kwa kuweka gateways. Uwekezaji huu ukikamilika na ufungaji wa mifumo hii ukikamilika, hili jambo tutakuwa tumelidhibiti kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilithibitishie Bunge lako, tunao uwezo mpaka sasa wa kufuatilia na kujua nani anasambaza picha chafu. (Makofi)
Kwa hiyo, nitoe tahadhari kwa watu ambao wanatumiwa picha, njia rahisi ukitumiwa picha chafu usimtumie mtu, ni bora ukaifuata kwa sababu ukimtumia mtu mamlaka zina uwezo wa kujua nani kamtumia nani.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ashante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali kupitia vyuo vikuu hapa nchini inatoa mafunzo ya saikolojia. Kwa nini basi isiajiri wataalamu wa saikolojia ili kupunguza tatizo hili kwa sababu kumekuwa kukiongezeka kesi za mauaji na ukatili kila kukicha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa nini Serikali isiwe na mpango wa kusajili chama cha wataalamu wa saikolojia kama ilivyo kwa taaluma nyingine nchini kama udaktari? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza ni ajira; Serikali inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kupata kibali kwa kuajiri wataalamu hao kadri bajeti inavyoruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili kuunda bodi ya wataalamu; Serikali ipo kwenye mchakato wa kukamilisha utungaji wa Sheria ya Wataalamu wa Ustawi wa Jamii ili kuona kwamba itakapomalizika basi bodi hiyo itaundwa ili kusajili wataalamu hao wa ustawi wa jamii ikiwemo wanasaikolojia. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuwa sera ya Wizara ya Elimu inatambua umuhimu wa kuwa na walimu wanaotoa ushauri wa nasaha kwenye shule zetu.
Je, Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii ina mpango gani wa kuhakikisha ya kwamba jambo hili linatekelezeka na kwenye shule zetu kunakuwa na walimu wanaotoa ushauri nasaha kwa watoto wetu hususan ukizingatia kwamba kuna wanafunzi wengi wanaohitimu masomo ya saikolojia na kwa kuanzia wanaweza kuanza kwa njia ya kujitolea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa wanasaikolojia hao. Kwa hiyo Serikali ipo katika kujipanga na kuhakikisha kwamba pale tunapopata nafasi za ajira basi wataalamu hao tutawaajiri na kushirikiana na Afisa wa Maendeleo ya Jamii kuwapa elimu wananchi wetu. Ahsante. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wataalamu wa saikolojia na unasihi bado ni tatizo; je, Serikali haioni imefikia wakati wakaanza kliniki tembezi ili kuweza kutembea katika maeneo mbalimbali na kutoa huduma hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wapo wataalamu hao katika kila mikoa na wanafanya kazi katika Halmashauri hadi vijijini. Pale wananchi ambapo wanapata tatizo katika vijiji vyao basi wamfuate mkuu wa Kijiji. Mkuu wa Kijiji atatoa taarifa katika Halmashauri kuhakikisha wataalamu wale wanakuja kuwapa elimu ya saikolojia watoto hao. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, tatizo hili ni kubwa kiasi ambacho sasa hivi watu wanaishia Mirembe badala ya kutibiwa wakiwemo wanaume wanaopigwa na wake zao, wakiwepo watoto wa shule ambao wanajeruhiwa na wenzao au na walimu.
Je, ni lini hasa Serikali itaona ni wakati muafaka wa kutoa hata mafunzo hadharani wakati wanaposhughulikia hizo ajira?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu kama nilivyoeleza Wizara imejipanga kuhakikisha tunatoa elimu kwa wananchi wote hasa wale ambao wanakuja katika sehemu zetu husika wana matatizo ya saikolojia basi tunawapa elimu na tumejipanga kwamba tutakapopa wafanyakazi wengi basi elimu hiyo tutaitoa kwa kila mikoa na kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata elimu hii ili kuondokana na matatizo ya saikolojia na kuondokana na msongo wa mawazo. (Makofi)
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; baada ya kutambua sababu za uwepo wa watoto hao, Je, Serikali ina mpango gani? Swali la pili kwa kuwa mikoa iliyofanyiwa utafiti huo ni michache; Je, Serikali ina mpango wa kuendelea na utafiti kama huo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika,napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tamima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na mikakati endelevu kutoa malezi bora kwa wazazi na mafunzo ili kuwatunza watoto katika ngazio ya familia lakini itafanya iwakutanishe watoto hao na wazazi wao. Watoto wasio na wazazi watapata huduma na haki zote stahiki katika vituo vyetu vya watoto tunavyolelea watoto yaani, Kikombo – Dodoma na Kurasini – Dar es Salaam lakini pia tutaimarisha ulinzi na usalama kwa watoto hao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali itaendelea kufanya tafiti mbalimbali katika mikoa ambayo inachangamoto za mitaani ili kuhakikisha usalama wao. Lakini pia nitoe rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanakaa na familia yao familia za watoto wao ili kuhakikisha wanapata malezi bora. Pia mtoto wa mwenzio ni wako, na watoto wote wanastahili kupewa haki muhimu kwa vile mtoto wa leo ni Taifa la kesho, ahsante. (Makofi)
MHE: SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, umezungumzia suala la kusaidia program nyingi zinazoendelea mikoani. Ni kweli mmeweka ada ndogo nyingine hadi shilingi 10,000 lakini mahitaji ya wasichana hawa kwenda kusoma ni zaidi ya 400,000; kwamba, aje na godoro na mambo mengine mengi, hamuoni kwamba mnawaonea wasichana wa vijijini na wanakosa haki ya kuweza kuhudhuria mafunzo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la pili la Mheshimiwa Hawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafanya jitihada mbalimbali ya kuwapa mafunzo walengwa kwa kuwakwamua mabinti wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na kuwafikia katika vijiji vyao ili kuondokana na madhila na kujikwamua kiuchumi ili waweze kuimarika na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Pia hadi kufikia Februari, 2023, jumla ya vikundi 6,127 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu wameunganishwa na kupewa mikopo midogo midogo ambayo inawawezesha kuwainua kiuchumi ili waondokane na mashaka ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza asilimia 10 za Miradi ya Maendeleo zipelekwe katika mifumo ya kibenki kuwakwamua wananchi wote ili waweze kupata fedha hizo kwa ajili ya kujijengea uchumi na kuimarisha uchumi wao kwa maendeleo ya maisha yao, ahsante. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Hali ya ukatili nchini hapa ni mbaya bado hususani kwa wanawake na watoto. Kwanza niwapongeze umoja wa wanawake Tanzania kwa kuweza kufatilia ufanisi wa madawati ya kijinsia nchi nzima. Lakini vilevile madawati haya bado yanachangamoto kubwa sana ikiwemo ukosefu ya miundombinu rafiki ya kuhudumia wahanga hawa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mazingira rafiki ya kuboresha miundombinu hii ili kuulinda usiri wa wahanga hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni juzi tu kuna kesi ya ulawiti mzazi kamlawiti mtoto wake Mkoani Shinyanga na kesi hii imepelekwa Mahakani juzi. Tukio hili limetokea Januari lakini kesi imepekwa juzi, mtuhumiwa huyu amepewa dhamani.
Je, Serikali haioni licha ya ushahidi wote uliyopelekwa Mahakani lakini mtuhumiwa huyu kapewa dhamani; je, Serikali haioni kwamba kwenye kulegeza mazingira haya ya kesi hizi inachochea mazingara haya kwenye jamii zetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, madawati mengi yalianzishwa kwa kutumia majengo ya zamani ndani ya vituo vya polisi. Hata hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jensi la Polisi ili kuboresha madawati hayo lakini hata hivyo hadi sasa madawati 79 yenye viwango yameisha jengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; kosa la ubakaji na ulawiti ni makosa ambayo yanadhaminika kisheria hivyo watuhumiwa kuachiwa huru na kupewa dhamana haimanishi Serikali ina halalisha na kuchochea ongezeko na vitendo vya ukatili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako Tukufu kama kuna vifungu vya sheria ambavyo mnahisi vinaleta msongamano kwa wananchi ama vinaleta tatizo basi Waheshimiwa Wabunge mlete maoni yenu ili Wizara ya Katiba na Sheria iweze Kutunga Sheria na kutafuta…
NAIBU SPIKA: Ahsante kwa majibu mazuri, ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na mikakati hiyo mizuri ya Serikali, wanawake wa Tanzania wanataka kusikia: Je, ifikapo mwaka 2025 asilimia hii 50 kwa 50 itakuwa imefikiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Hivi sasa tumeshuhudia jinsi wanawake waliopo kwenye nafasi mbalimbali wanavyofanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa. Kwa mfano tu, Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Spika wetu, Mheshimiwa Dkt. Tulia: Je, Serikali ina mikakati gani sasa ya kuwainua kiuongozi wanawake hasa kwenye ngazi ya chini ili basi wainuke kiongozi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mtekelezaji mzuri wa ilani. Katika kipindi chake cha miaka miwili ameshafikia asilimia 31 ya uteuzi wa wanawake viongozi. Kwa vile mamlaka ya uteuzi ni yake, tuendelee kumwamini katika majukumu yake na kufikia 50 kwa 50. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, Serikali imeridhia na inatekeleza mikataba ya Kimataifa na kikanda kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, lengo ni kukuza ushiriki wa wanawake katika nyanja zote za maendeleo ikiwemo kuhakikisha usawa katika ngazi nyeti na nafasi nyeti za uongozi na maamuzi nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Vikundi vingi vya Majukwaa bado havina uelewa wa pamoja wa lengo mahsusi la uanzishaji wa majukwaa haya. Sasa nini kauli ya Serikali kuhusu hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni utaratibu upi unatumika kahakikisha waratibu wa majukwaa haya wanashuka kutoa elimu ya mwongozo wa uratibu wa majukwaa haya katika ngazi ya kata na mitaa?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunaendelea kutoa mafunzo kwa lengo la kukuza uelewa kwa majukwaa haya ya kuendeleza uchumi kwa ajili ya wanawake. Napenda kutoa rai kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii, kuhakikisha kwamba wanatoa mafunzo kwa lengo la kuwaelewesha wananchi ni nini cha kufanya katika majukwaa haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wizara yangu inafuatilia na kufanya tathmini mbalimbali katika vikundi vyote vya majukwaa ya wanawake kiuchumi na kuhakikisha kwamba tunawatembelea kila baada ya robo ya mwaka wa fedha kuhakikisha vikundi vile vinafanya kazi vizuri na kuhakikisha wanafuata sera, sheria, kanuni na miongozo yote ambayo tumeipanga, ahsante. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naishukuru sana Serikali kutupongeza Mkoa wa Pwani kwa kufanya vizuri, lakini pia kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 161 kwa kuanza hayo mafunzo. Maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, je, ni lini hasa mafunzo hayo yataanza kwa kuwa majukwaa yale yameundwa muda mrefu na tumefanya jitihada mpaka Kitongoji, Vijiji, Wilaya mpaka na Mkoa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika jibu lake la msingi amesema zimetengwa hizo fedha shilingi milioni 161 na ndani yake kutakuwa na za Mkoa wa Pwani, lakini nataka niulize, je, Serikali inaipa wajibu gani Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia Katibu Tawala wa Mkoa na Halmashauri zetu za Mkoa wa Pwani katika kulea majukwaa haya ili yalete tija iliyokusudiwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, swali lake la kwanza kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, Serikali imetenga shilingi milioni 161 kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kuwajengea uwezo wanawake ili kuinuka kiuchumi ambapo Mkoa wa Pwani umetengewa shilingi milioni 58.5 kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo.
Niwaombe tu Maafisa Tawala wa Mikoa wote nchini waanze kuandaa programu hizo za mafunzo na mwaka wa fedha ukiingia mafunzo hayo yaanze. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, zipo taasisi mbalimbali za binafsi ambazo zinawezesha wananchi kutoa mikopo mmoja-mmoja na vikundi. Kwa hiyo, niwaombe wananchi waendelee kutumia fursa hizo kuhakikisha uchumi wao unakua, ahsante. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ziko baadhi ya Halmashauri hapa nchini ambazo mapato yake sio toshelevu hivyo hawawezi kutosheleza kutoa mikopo ya asilimia 10.
Je, ni upi mkakati wa Wizara hii kuwawezesha wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya kitongoji na vijiji?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inawaagiza Maafisa Tawala wa Mikoa na Maafisa Ustawi wa Jamii waendelee kutoa elimu kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu, ili kuweza kujiinua kiuchumi na kuhakikisha wanakuwa vizuri katika maisha yao na maendeleo yao. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza nishukuru majibu yake ni mazuri sana, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, nina matarajio kwamba sasa kila Mkoa utapata kituo hiki cha One Stop Center. Swali langu, ni lini vituo hivi vitaanza?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Maafisa Ustawi wa Jamii ndio wanaotoa huduma za kisaikolojia; nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba mnaajiri Maafisa Ustawi wa Jamii wa kutosha ili waweze kutoa huduma hii?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Tendega kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuratibu uanzishaji wa vituo vya mkono kwa mkono hadi kufikia lengo la kuwa na angalau kituo kimoja kwa kila Mkoa. Hii ni kwa sababu ya kuwasaidia wananchi wetu pale wanapopata matatizo au changamoto ili waweze kwenda mahali ambapo watafanikiwa na kutatuliwa matatizo yao.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Serikali itaendelea kuwaajiri Maafisa Ustawi wa Jamii kila tunapopata kibali ili waweze kusambazwa nchi nzima na kuhakikisha matatizo yote yanaondoka kwa wananchi na kupata elimu ambayo itawasaidia ili wasiathirike na msongo wa mawazo, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa hivi vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka nchini, na tumetambua huo mkakati wa Serikali kuhakikisha vituo na kuajiri ustawi wa jamii, lakini nataka nijue sasa mkakati kabisa wa kuhakikisha kwamba tunaondoa kabisa huu ukatili wa kijinsia. Mkakati gani ambao Serikali inao kuhakikisha kwamba, yani kunakuwa na zero ukatili wa kijinsia Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, natambua kuwa kuna vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini. Jukumu letu ni kuhakikisha wanawake na watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili kuwapatia huduma muhimu ikiwemo ushauri nasaha ili wasiathirike kiakili pale wanapopata vitendo vya ukatili, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kuhakikisha jamii nzima inashirikiana katika jambo hili la kutokomeza ukatili wa watoto, wanawake na makundi maalum nchini, lakini nadhani Bunge lako tukufu linafahamu kwamba Serikali inao mpango mkakati wa kitaifa wa kutokomeza unyanyasaji wa makundi haya maalum ambao ni jumuishi kwa sekta zote, na kila Wizara imeshirikishwa katika kuhakikisha mkakati huo maarufu kwa MTAKUWA unafanikiwa na unazaa matunda ya kuhakikisha Taifa hili la Tanzania linakuwa mstari wa mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo tumeshuhudia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan yeye mwenyewe kwa kuzingatia matakwa ya kimataifa amekuwa mstari wa mbele kutengeneza afua ambazo zitasaidia mapambano hayo dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia katika Taifa letu. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini sambamba na hilo nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; naomba kupata commitment ya Serikali kuhusiana na kutunga sheria hii. Je, sheria hii itaweza kutungwa ndani ya uhai wa Bunge hili?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa, sheria imechukua muda mrefu kutungwa. Je, Serikali haioni sababu ya kutengeneza mkakati au mpango maalum wa kuona jinsi ya kuweza kuwaangalia hawa Maafisa Ustawi ambao wanakiuka taratibu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Toufiq, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, inaona umuhimu wa sheria hii. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi Serikali itasimamia sheria hii ili iweze kuwasilishwa mapema katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kuhusu Maafisa Ustawi kuwa na maadili. Ushauri umepokelewa. Hata hivyo, Wizara inafuata kanuni za utumishi wa umma kwa wafanyakazi wote na wafanyakazi wote wanaokiuka maadili, hatua za kisheria zinachukuliwa pale wanapofanya makosa. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante, na kwa niaba ya Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali. Pamoja na hayo majibu ya Serikali, katika chuo hiki, wanafunzi wanapata taabu sana maeneo ya kuishi ili kupata taaluma pale. Ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha inajenga mabweni kwenye eneo hili na chuo hiki ili wanafunzi wapate sehemu ya kukaa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Katika Kanda ya Kaskazini, mikoa yote hakuna Chuo cha Maendeleo ya Jamii; je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha Maendeleo ya Jamii katika Jimbo la Hai ambapo tayari tumeshapanga eneo la kujenga lipo tayari?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunatambua kuwa umuhimu wa miundombinu ya utoshelevu katika kujenga mabweni ya wanafunzi katika vyuo, Serikali itaendelea kutenga rasilimali fedha ili kuweza kuendelea kujenga mabweni hayo katika kila sehemu ya vyuo ili wanafunzi wapate kuwa na maendeleo mazuri na kuwa karibu na kuishi maeneo ya shule.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ushauri wake tumeupokea na tunawapongeza Wanajimbo la Hai kwa kuwa na kiwanja cha kujenga Chuo cha Maendeleo ya Jamii. Wameona umuhimu wa vyuo hivi. Wizara itaendelea kutenga fedha kadiri bajeti itakavyoruhusu, katika mwaka wa fedha 2025, kuona vipi Chuo hiki tunakijenga ili wananchi waweze kuwa na chuo katika Mkoa wao, ahsante. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza: Kwa kuwa Muswada huu una muda mrefu takribani miaka 20 sasa na lilikuwa ni tegemeo la wazee wengi kupokea sheria hii: Je, Serikali inaweza ikatueleza vikwazo vilivyosababisha kuichelewesha sheria hii kutungwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa wazee hawa wamelitumikia Taifa hili kwa muda mrefu: Je, Serikali ina mipango gani ya haraka ya kuwahudumia wazee hawa ili waweze kupata huduma zinazostahili kwenye ofisi za Serikali wakati wakiwa wanasubiri sheria hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili Muswada ukamilike na ufikishwe Bungeni kuna taratibu na sheria na miongozo ambayo iliyowekwa na sasa inafanyiwa kazi. Mara baada ya kumalizika Muswada huo, utawasilishwa Bungeni kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajali sana wazee; na katika Sheria mpya ambayo imetungwa tumeweka kipengele cha ulinzi na usalama kwa wazee. Kwa hiyo, kupitia Bunge lako tukufu naelekeza kwamba taasisi zote za Serikali na binafsi ziweze kuweka utaratibu maalum wa kuwasaidia wazee katika huduma za jamii pale wanapofika sehemu hizo, kwani Serikali inawapenda wazee na wazee ni tunu ya Taifa letu, ahsante. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naipongeza Serikali kwa kufanya zoezi la kuhakiki na kubaini wazee hao ambao hawana uwezo. Pia, pamoja na kuwabaini, Serikali ikawapatia vitambulisho vya ICHF kwa ajili ya kupata matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo ni kwamba pamoja na kupewa hivyo vitambulisho, wakienda kwenye maeneo ya kupata huduma za afya wanaishia kutangatanga kwa sababu hawapati dawa.
Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba wazee hawa sasa watapata dawa bila matatizo?
Swali la pili; huko nyuma kulikuwa na slogan ilikuwa inasema” Mpishe Mzee Kwanza” sasa hivi slogan hiyo imeanza kupotea, wazee wanahangaika, wakienda kupata huduma sehemu nyingine hata hospitali na maeneo mengine, hakuna anayejali.
Ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunarudi kwenye mkakati ule wa mwanzo wa kuhakikisha wazee wanapishwa ili kupata huduma kwanza ili wakaendelee na mambo yao mengine? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hawa wazee kwenda kwenye vituo vya huduma za afya pamoja na vitambulisho vyao wanakuwa hawapati huduma, tutafanya ufuatiliaji kwa sababu huenda wako watu ambao hawawathamini wazee hawa waliotambuliwa kuwa hawana uwezo kwa mujibu wa mwongozo uliowekwa na Wizara Mama ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tutashirikiana na Mabaraza ya Wazee yaliyopo nchini kote ili kufuatilia na kupata maoni ya wazee hawa wasiopata hizo huduma ni kwenye maeneo gani hasa, kwa sababu vipo vituo vya afya vingine vinafanya vizuri sana. Huenda ni baadhi ya maeneo ambayo tutayafuatilia tuyaibue na tushirikiane na Mheshimiwa Waziri wa Afya kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala hili la kampeni ya “Mpishe Mzee, Mzee ni Tunu Apate Huduma”, kama kuna mahala pameanza kusinzia pia tutafanya ufuatiliaji maana kampeni hii ni endelevu na tuliianzisha mwaka 2021 na imeendelea vizuri mwaka 2022. Sasa kama kuna mahala panalegalega, napeleka tu salamu kwa wale wanaotakiwa kufanya kazi hiyo wakiwemo Maafisa Ustawi wa Jamii wakishirikiana na Wakuu wa Vituo kupitia Waziri mwenye dhamana ya afya, tutafanya ufuatiliaji ili kuiinua tena kampeni hiyo. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nini mkakati wa Serikali kushirikisha taasisi mbalimbali zinazojihusisha na elimu ya masuala ya afya ya uzazi. Je, Serikali haioni haja ya taasisi hii kupata vipindi kwenye mashule mbalimbali ili kutoa elimu kwa watoto wa kike?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile mimba za utotoni zinaenda sambamba na ndoa za utotoni. Nini sasa baada ya Serikali kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali. Lini Serikali italeta Muswada wa ndoa za utotoni?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau tunaimarisha mikakati ya uratibu za afua na kutoa huduma za afya shuleni kwa kushirikiana na majukwaa ya watoto walioko shuleni, vitabu vya watoto, madawati, ulinzi na usalama, mabaraza ya watoto, na kutumika katika elimu ya afya shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili. Wizara ya Maendeleo ya Jamii ikishirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea na mchakato wa kukusanya maoni juu ya kujua umri wa kuolewa kwa mtoto wa kike. Pia, mchakato huo ukimalizika Muswada huu utaletwa katika Bunge lako Tukufu na kujadiliwa na kupitishwa sheria ya kuthibiti ndoa za utotoni.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza. ukiacha mikoa 12 ya Tanzania Bara ambayo imefanikiwa kupata haya Mabaraza ya Watoto, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mikoa 14 iliyobaki nayo inapata mabaraza haya? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; suala la vitendo vya ukatili kwa watoto limekuwa likiendelea siku hadi siku kwenye jamii yetu. Je, Serikali haioni haja sasa yakuja na sheria kali itakayo komesha vitendo hivi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuanzisha mabaraza haya katika shule zote za vijijini na mitaani nchi nzima. Serikali pia imeshasambaza Mwongozo wa Taifa wa uwaandaaji na uendeshaji wa Mabaraza ya Watoto katika halmashauri zote nchini, ambapo utawasaidia kuendesha mabaraza hayo kwa kushirikiana na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Bunge lako Tukufu limeshapitisha sheria na adhabu kali za kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto. Niwaombe wananchi, waendelee kutoa ushirikiano kwa Maafisa Mahakama na kutoa ukweli pale wanapofika katika sheria. Niwasisitize kuwa, mahakama itaendelea kufanya kazi yake pale ukweli watakapoutoa katika sehemu za sheria, ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; kwa kuwa mimba zinazotokana na ubakaji, ni mimba zisizotarajiwa hasa kwa walengwa; je, Serikali imeweka adhabu gani kwa wanaofanya kitendo hiki? (Makofi)
Swali langu la pili; je, Serikali ina mkakati gani wa kuwabaini watoto wote wanaozaliwa kutokana na mama zao kubakwa ili kuwapa huduma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAUME NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza Serikali imeweka adhabu kali ikiwemo kifungo kwa ajili ya udhalilishaji, ukatili na ubakaji, kwa lengo la kupunguza vitendo vya ukatili katika jamii na mimba za utotoni. Pia inaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha kwamba vitendo hivi vya ukatili vinakwisha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, Serikali itaendelea kutoa huduma za kijamii kwa wahanga waliofanyiwa vitendo vya ukatili na ubakaji ili kuwabaini watoto hawa, wale waathirika wa vitendo vya ukatili na waliobakwa, tunawaomba wanapokwenda kuripoti katika vituo vya afya, basi kesi zao jinsi zinavyokwenda ndipo tutakapojua jumla ya watoto ambao wamezaliwa kutokana na ubakaji na kuwapa huduma zinazostahiki. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza. swali la kwanza; tumekuwa na kampeni kwa miaka mingi iliyopita, kuelimisha na kuwezesha mtoto wa kike, tukasahau mtoto wa kiume. Sasa je, Serikali ina mikakati gani kuwapa upendeleo maalum watoto wa kiume ili waweze kupata elimu nzuri na kujiamini ili baadaye waweze kuoa wanawake waliosoma?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kumekuwa na kuvunjika kwa ndoa, siku hizi ndoa zinavunjika sana na watu wanaachana sana kiasi ambacho kunakuwa na watoto ambao hawana wazazi wawili wa kuwalea. Je, Serikali ina mikakati gani katika kuelimisha, kutoa elimu kwa Watanzania hasa kuonesha majukumu ya akina mama na majukumu ya akina baba katika ndoa ili watoto hawa waweze kulelewa na wazazi wawili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Serikali kupitia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 inatoa haki sawa kwa watoto wote wa kike na wa kiume wakiwemo wenye ulemavu. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi kujenga madarasa katika kila mkoa kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata elimu na waweze kufikia malengo ambayo wamekusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023 inatambua umuhimu wa ushiriki wa wanawake na wanaume akiwemo mtoto wa kiume kama wakala muhimu wa kuleta mabadiliko na kuimarisha maendeleo ya familia nchini. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuku kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nashukuru kwa majibu hayo, japo naamini kwamba Mheshimiwa Waziri ama Serikali itakubaliana nami kwamba tatizo hili la mmomonyoko wa maadili nchini ni kubwa kuliko hatua ambazo tunachukua. Sasa naomba kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi za kuhakikisha tunachukua hatua dhidi ya watu wanaojihusisha na masuala haya ya mapenzi ya jinsia moja pamoja na mashirika ama watu wanao-support ama wanaosaidia kuenea kwa jambo hili hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuleta Muswada hapa Bungeni ili tuweze kutunga sheria ya kudhibiti masuala ya mapenzi ya jinsia moja hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja ni kosa la jinai kwa Kifungu Na. 154 cha Sheria, na Kanuni za Adhabu Sura ya 16 inatambua mtu yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kosa hilo ataadhibiwa kifungo cha miaka 30. Ikithibitika na mtendewa aliridhia kufanyiwa kitendo, basi atahusika na kosa hilo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, sheria na kanuni na adhabu zipo. Kinachotakiwa ni kufanyiwa marekebisho. Bunge la Kumi na Mbili, Mkutano wa Kumi na Moja, Kikao cha Sita aliagiza Serikali kushirikiana na Tume ya Sheria kuhakikisha kwamba tunafanya utafiti kwa kushirikiana na Tume ya Sheria ambayo mabadiliko yatakayofanyika yafikishwe katika Bunge lako Tukufu. Tume inaendelea na kazi hiyo, na mara baada ya kumalizika, Muswada huo utaletwa Bungeni ili kujadiliwa na kupitishwa. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, Serikali ina mkakati gani wa kushirikiana na taasisi za kidini na wataalam ili kuwasaidia wale walioathirika na mapenzi ya jinsia moja?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina malezi, makuzi na utamaduni wa Mtanzania. Kwa hiyo, Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dini tunahakikisha kwamba tunatoa elimu ambayo itawasaidia wananchi ili kujikinga na vitendo hivyo vya jinsia moja na kuondoa mmomonyoko wa maadili ili nchi yetu iendelee kuwa salama, ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nitumie fursa hii kuipongeza Serikali kwa namna ambavyo inajitahidi kutenga bajeti kwa ajili ya kulinda watoto wetu, lakini hata hivyo vitendo hivi vinazidi kwenda kwa kasi hasa ukatili wa watoto wadogo kwa ubakaji na ulawiti ni jambo baya sana.
Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, swali langu la kwanza; je, mpango kazi wa kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa awamu ya pili mmekadiria kuweka kiasi gani cha bajeti?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; pamoja na jitihada za Serikali kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali ikiwemo Polisi, Mahakama na wengine, je, Serikali haioni umuhimu kushirikiana na wadau muhimu sana katika Taifa hili ambao ni viongozi wa dini ambao wana majumba ya ibada katika maeneo yote tunayoishi kufanya nao makongamano kwa sababu wao ndio wadau wakubwa wanaokataza mabaya na kuamrisha mema? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Najma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga fedha 983,778,118,850 kwa ajili ya mpango wa pili wa MTAKUWWA ili kupingana na vitendo hivi vya kuatili ikishirikiana na Wizara za Kisekta pamoja na fedha za wadau.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, viongozi wa dini ni wadau na Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa MTAKUWWA ili kuendeleza kufanya makongamano na kuhamasisha majukwaa mbalimbali ili kupinga janga hili la ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ahsante.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa, kumekuwa na matukio ya kupiga picha za watu ambao wamepata athari za ukatili pamoja na udhalilishaji, nini kauli ya Serikali kuhusiana na kadhia hii?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Toufiq kuwa ni kweli kumekuwa na masuala ya kupiga picha kwa waathirika wa vitendo vya ukatili, Serikali inatoa kauli kali kwa wale wote ambao wanapiga picha vitendo vya ukatili na kuvirusha katika ma-group ya whatsApp au mitandao ya kijamii, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa sababu sheria, taratibu na miongozo ipo yote kwa ajili ya kuhakikisha mtu analindwa na kupata haki zake katika ukatili wa kijinsia, ahsante. (Makofi)
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini kadri siku zinavyokwenda vitendo hivi vya ukatili vinazidi kuongezeka siku hadi siku nchini nchini na kumekuwa na mikakati mingi, mipango mingi, lakini bado vitendo hivi vinaongezeka kwa kasi. Je, ni upi mpango wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na mpango wa maendeleo ya Wizara ya Mambo ya Ndani upi mpango jumuishi wa kuhakikisha wanapambana na vitendo hivi vya ukatili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, ni lini sasa vitendo hivi vitakoma? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la mwanzo, Mpango jumuishi unaohusisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni dawati la watoto la kijinsia, lakini pia Polisi ni moja ya Kamati ya Kudumu ya Kutokomeza Ukatili wa Wanawake na Watoto ambapo tunashirikiana pamoja kuwa kuhakikisha MTAKUWWA unatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, 60% ya vitendo vya ukatili vinatokana na jamii. Kwa hiyo niwaombe wananchi au Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane kwa pamoja, tukiona ishara ya vitendo vya ukatili basi tushirikiane na kamati za kisekta; tutashirikiana ili kuhakikisha kwamba vitendo hivyo vinachukuliwa hatua mara moja. Ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vitendo hivi vinakithiri kila siku na sheria iliyopo ni ya kifungo cha Maisha. Je, Wizara hawaoni kwamba kuna umuhimu wa kuleta Muswada ili kubadilisha kutoka kifungo cha maisha na kuwa adhabu ya kifo?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, vitendo hivi tunajua vimekithiri katika nchi yetu na Wizara hivi sasa imeleta Muswada wa Sheria kuhakikisha tunarekebisha sheria hizo na kuhakikisha kwamba wale wote wanaohusika na vitendo hivi vya ukatili basi hatua kali zinachukuliwa dhidi yao. Ahsante.