Supplementary Questions from Hon. Anton Albert Mwantona (19 total)
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Kabla ya yote nipongeze sana Wizara ya Maji. Napongeza Wizara ya Maji, Naibu Waziri alikuja kwetu Rungwe Jimboni, ametembelea miradi, ameona matatizo ya maji kwa wananchi wa Rungwe. Naomba sasa niulize swali langu; je, ni lini mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Tukuyu utaanza kutekelezwa hasa baada ya Naibu Spika kutembelea na kutuahidi pale. Lakini pia upembuzi yakinifu ulishafanyika…
NAIBU SPIKA: Umeshauliza swali.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantona Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji mdogo wa Tukuyu tunafahamu kabisa miundombinu yake ni chakavu na idadi ya watu imeongezeka, tayari maelekezo yapo kwa Meneja wa Maji Mkoa wa Mbeya na ameshaanza manunuzi ya vifaa vya kazi na kufikia mwezi Machi kazi zitaanza kufanyika pale Tukuyu na upatikanaji wa maji unakwenda kuboreshwa. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Wizara ya Maji. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwenye Mradi wa Maji Tukuyu nimeridhika, lakini kuna mradi mwingine ambao unaendelea katika Mji wa Ushirika, Kata ya Mpuguso. Tenki tayari limeshajengwa, mabomba tayari yameshafika kwenye tenki, usambazaji wa maji bado kwa wananchi kwa muda mrefu. Naomba Wizara ituambie wananchi wa Rungwe lini itaanza kusambaza maji kwa wananchi wa Rungwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tuna Kituo cha Afya cha Ikuti ambacho kina matatizo makubwa sana ya maji. Nilikuwa naomba Wizara iwaambie wananchi wa Ikuti, Jimbo la Rungwe, ni lini maji yatasambazwa hasa baada ya upembuzi yakinifu wa mradi ule kuonekana kwamba, ni milioni 100 tu ambayo itapeleka maji kutoka kwenye chanzo cha maji mpaka kwenye Kituo cha Afya cha Ikuti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unaoendelea pale miundombinu yake imeshakamilika, imebaki tu usambazaji wa maji. Mheshimiwa Mbunge mradi ule unakwenda kukamilika wiki chache zijazo na maji yatafika mabombani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Kituo cha Afya cha Ikuti kupata maji, Mheshimiwa Mbunge Serikali tutalifanyia kazi na namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, ndani ya muda mfupi utekelezaji wake utakuja kufanyika.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nilikuwa naomba Serikali itoe kauli, hasa kwa kutumia Sheria Na. 5 ambako halmashauri nyingi zipo huko kupima ardhi kwa kutumia hati za kimila; kwa sababu ukiangalia kwenye statement nyingi za halmashauri zetu inaonekana hoja kubwa ya migogoro ni kutokuwa na hati za kumiliki ardhi.
Je, Serikali ina mpango gani kwa kutumia hati miliki za kimila kuhakikisha maeneo yote ya umma, shule na vituo vya afya yanapimwa kama inavyotakiwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa; ya kwamba hoja yake ni ya msingi na ni nzuri, lakini, shule ambazo zinamilikiwa na halmashauri haziwezi kupimwa kwa hati ya kimila, zile zinapimwa chini ya Sheria Na. 4; kwa maana ya kwenda kwenye general land. Kwa hiyo kama hitaji hilo lipo ni kwamba ni halmashauri pia, tuone namna ya kuhakikisha, na Wizara ilishaelekeza, kwamba taasisi zote za umma zipimwe. Huwezi kuipima kwa kutumia Sheria Na. 4.
Mheshimiwa Spika, niombe tu kwamba halmashauri zijipange katika kutumia Sheria Na. 5 kwasababu ile imeshaingia kwenye general land na haiwezekani tena kukaribisha kwenye umiliki wa kijiji. (Makofi)
SPIKA: Kwa hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri zikishapimwa zitapewa hati each na hati ile inalipiwa kodi ya ardhi, au inakuwaje?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, watapewa, na kodi inayolipwa sasa hivi; tulibadilisha sheria hapa mwaka 2019, wanalipa token tu, shilingi 5,000 kwa mwaka badala ya kutumia ukubwa wa eneo. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Wizara. Hii barabara ni muhimu sana kwa upande wa Rungwe lakini pia kwa upande wa Ileje. Ni barabara kwa upande wa Rungwe inapita kwenye Kata ya Kyimo, Iponjola pamoja na Ikuti ambapo kuna milima mikali, barabara muda mwingi inakuwa sio nzuri. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ituambie exactly ni lini hii barabara itaanza kufanyiwa upembuzi yakinifu ili ijengwe kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini barabara ambayo pia ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 - 2025 kutoka Kiwira kupitia Kata ya Kinyala, Igogwe mpaka Mbalizi itafanyiwa pia upembuzi yakinifu na kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Anton Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Ibungu –Kalembo – Katengele - Sange - Luswisi – Kafwafwa - Ikuti hadi King’o ni kweli ni barabara ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Ileje na Rungwe. Nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutahakikisha kwamba katika awamu hii ya miaka mitano barabara hii inafanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu na mimi ni mnufaika kwa sababu inapita kwenye Jimbo langu na kwenye Kijiji changu pia cha Kalembo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mbunge kwamba barabara hii itafanyika kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi. Pia, barabara hii ya Kiwira – Kinyala - Igogwe hadi Mbalizi nayo pia iko kwenye Ilani ambayo nayo pia imeainishwa kati ya barabara zile ambazo zitafanyiwa usanifu wa kina. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Rungwe na wa Ileje kwamba barabara hizi tutahakikisha kwamba zinafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa lami kadri fedha zitakavyopatikana. Ahsante.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni nini kauli ya Serikali kwenye Jimbo letu la Rungwe kuna vijiji 24 ambavyo vilikuwa kwenye REA II havijapatiwa umeme, lakini pia kwenye REA III, round ya pili vijiji tisa haviko kwenye orodha ya kupatiwa umeme katika hii REA III, round ya pili. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantona, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali la maeneo ambayo yalisahaulika. Tumeshatoa maelekezo na taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge, naomba tena nirudie tu. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge na kama kuna vijiji sita au tisa au vingapi ambavyo vilisahaulika tunaomba atuletee.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya utaratibu baada ya wiki mbili zilizopita, kupitia maeneo yote ya nchi nzima katika vijiji vilivyosahaulika na viko vingi. Kwa Mheshimiwa Lukuvi vilisahaulika vijiji viwili na maeneo mengine, tumepata vijiji 610 na vyote tumeviingiza kwenye mpango wa kutekelezwa na tuna shilingi bilioni 150 na wakandarasi tayari wameshapewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwape tu uhakikisho wananchi kupitia Bunge letu Tukufu kwamba kama kuna Mbunge yeyote, kijiji chake kimesahaulika tunaomba sana atuletee, Mradi wa REA III, round ya pili ni mradi wa kumbakumba wa vijiji vyote. Kwa hiyo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge watuletee vijiji vyao vilivyosahaulika ili visisahaulike ili utekelezaji uende pamoja na maeneo yanayotekelezwa. Ahsante sana.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza katika Wizara hii ya Nishati. Jimbo la Rungwe lina vijiji 99. Katika vijiji 99, vijiji 66 vilikuwa kwenye mradi wa REA II na vijiji 33 viko kwenye mradi wa REA III; lakini katika vijiji 66 ni vijiji 41 tu ndiyo vilikamilishiwa umeme, lakini vijiji 25 havikukamilishiwa umeme katika awamu ya pili ya REA.
Mheshimiwa Spika, Waziri alikuja kufanya ziara kule kwetu kwenye ufunguzi wa REA III tarehe 28 mwezi wa Nane akasema kuna fedha ilibaki kwenye REA II, shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya kupeleka umeme kukamilisha mradi wa umeme kwenye REA II. Akasema, ndani ya miezi miwili huo mradi utakamilika na wananchi watapata umeme.
Mheshimiwa Spika, la kusikitisha, mpaka leo umeme bado haujafika na kazi bado haijaanza. Nilikuwa naomba Waziri atoe kauli hapa, ni lini mradi wa umeme REA II vijiji 25 katika Jimbo la Rungwe utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mbunge wa Rungwe kwa swali lake. Naomba kutoa majibu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye mradi wa REA III round ya kwanza zilikuwepo lots 29 na lots 8 bado hazijakamilika katika eneo hilo la Rungwe na maeneo mengine. Kama tulivyosema, kulikuwa na kuchelewa kwa sababu ya kuchelewa kupatikana kwa vifaa na maeneo kama hayo, lakini Serikali tayari imeiagiza REA kuhakikisha inakamilisha miradi hiyo na wakandarasi kabla ya mwezi wa tatu mwaka huu. Kwa hiyo, vile viporo vyote ambavyo vilibakia kwenye mradi wa REA II, REA III round one, vyote tunatarajia viwe vimekamilika kabla ya kwisha kwa mwezi wa Tatu mwaka huu 2022 eneo la Rungwe likiwemo. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza private sector ni mdau kutoa ajira kwa wananchi ya wananchi wa Tanzania kwa kushirikiana pamoja na Serikali. Tukiangalia katika nyanja mbalimbali private sector imeathirika kwa kiasi fulani especially ukiangalia kwenye mambo ya shule na taasisi nyingine; uendeshwaji wa shule umekuwa ni mgumu kwa kiasi fulani kiasi kwamba utoaji wa ajira kwa vijana wetu umekuwa ni mgumu kwa kiasi kikubwa. Labda kutokana na UVIKO 19 na mambo mengine ambayo yako: Je, Serikali ina mpango gani kusaidia private sector na kufanya tathmini ya kina kwenye private sector kwa lengo la kuisaidia ili iweze kusaidia kutoa ajira kwa vijana wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye swali langu la msingi nimesema vijana ambao wamehitimu Vyuo Vikuu zaidi ya 100 wamejiunga pamoja na wapo tayari; na wameweka utaratibu wao, wamesema wenyewe ni kilimo cha makambi; kwamba wanaweza wakakaa sehemu wakaweka kambi, wakafanya kilimo. Walikuwa wanaomba Serikali iweze kuwasaidia mtaji wa pembejeo pamoja na soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza, Serikali ina kauli gani kutokana na hao vijana ambao tayari wameshajitoa, wako tayari kufanya kilimo cha makambi kuweza kuwasaidia ili waweze kupata ajira? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBASS P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, kama ifuatavyo katika maswali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyooleza kwenye swali la msingi katika swali lake la pili ambapo amesema vijana tutawasaidia vipi ambao tayari wameshaji-mobilize ili waweze kupata fedha au kuwekewa mtaji waweze kuendelea na shughuli zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kama nilivyolieleza kwenye jibu la msingi ni kwamba tunashirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha kwanza tunatenga maeneo, na hapo kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge tayari kuna ekari 88.9 ambazo zinaweza kuwasaidia hawa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Wizara ya Kilimo itaweka miundombinu na jukumu la mafunzo litabaki kuwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu; na tatu, tutaenda sasa katika kuhakikisha mpaka kwenye hatua ya mwisho ya kutafuta masoko kwenye zao la kilimo au zao biashara ambalo watakuwa nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hapa tuwasiliane, tuweke mpango mzuri kwa ajili ya kuwasaidia hao vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza Serikali ina mpango gani wa kusaidia private sector kwa kuwa ndiyo mdau mkuu pia katika kutoa ajira? Tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kubadilisha sera mbalimbali hasa zile ambazo zinahusiana na masuala yanayogusa ajira. Katika sera nyingi ambazo ziko katika Wizara za kisekta tumeshaanza kufanya mapitio mapya kuweza kuhakikisha sera hizo zinaendana na usasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mabadiliko mbalimbali ya sheria ili kuweza kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwezekano mkubwa wa private sector kukua kama jinsi ambavyo tumerekebisha sheria ya kuajiri au kuratibu ajira za wageni. Tumeenda pia kwenye mabadiliko ya sheria na sera na mipango ya masuala ya uwekezaji na uchumi. Kwa hiyo, kwenye eneo hilo Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake, tunaona sasa ameendelea kuweza kuhakikisha kwamba private sector inaweza kufanya kazi kwa ukubwa zaidi na upana ili iweze kuajiri watu wengi zaidi. Nakushukuru.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwamba imetujengea vituo vitatu vya afya kwa mwaka uliopita, ambapo kuna Kituo cha Ndanto, Kituo cha Kiimo pamoja na Kituo cha Ikinjola ambavyo viko mwishoni kabisa kukamilika na watumishi wameshapelekwa; je, ni lini vifaa tiba katika vituo hivyo vya afya vitapelekwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye Kituo cha Afya cha Masukuru, jengo la X-Ra, liko tayari, pia na jengo la mortuary liko tayari, lakini kwa bahati mbaya sana x-ray hatuna na mtumishi wa mortuary pale katika Kituo cha Afya Masukuru hakuna. Ni lini x-ray pamoja na mtumishi wa mortuary katika Kituo cha Afya cha Masukuru watapelekwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipokee shukrani za Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali hii Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga Vituo vya Afya vitatu ndani ya mwaka mmoja. Nimhakikishie kwamba mipango ya ujenzi wa Vituo vya Afya inakwenda sambamba na mipango ya ununuzi wa vifaa tiba. Katika bajeti ya mwaka huu Serikali imetenga jumla shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya vifaa tiba kwenye vituo vya afya 530. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia tutatoa kipaumbele kwenye vituo vya afya ambavyo vimekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na ukosefu wa mashine ya x-ray na mtumishi wa mortuary, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kununua vifaa tiba hivi kwa awamu. Kwa hiyo, mara pale tutakaponunua x-ray za kutosha basi kituo hiki cha afya pia kitatazamwa pamoja na kupelekewa mtumishi wa mortuary, ahsante. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Rungwe wakulima wa parachichi wako kwenye kilio kikubwa sana ambapo wameambiwa wanunuzi watanunua maparachichi kupitia AMCOS, AMCOS yenyewe Rungwe iko moja, masharti yamekuwa ni magumu kwamba lazima pesa wapeleke kwenye AMCOS ndio watatununulia maparachichi hao wanunuzi wa parachichi. Ni jambo la kusikitisha sana wananchi wanalia wanunuzi wote wamekimbia wameenda maeneo ya Njombe, Mbozi na maeneo mengine, pale Rungwe maparachichi yanaozea shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kupata kauli ya Serikali; Je, wapotayari kuwalipa fidia wananchi ambao maparachichi yao yanaozea shambani sasa hivi? Pia tupate kauli ya Serikali wanasema nini kuhusu kilimo cha parachichi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantona Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akilifuatilia hili jambo, tumeongea na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya na tumekubaliana.
Mheshimiwa Spika, avocado siyo korosho, avocado sio pamba, avocado siyo kahawa, hauwezi kulazimisha kununua avocado kwa kukusanya kwenye Chama cha Msingi, hauwezi kulazimisha avocado kuipeleka kwenye Chama cha Msingi kwa sababu ni perishable. Kwa hiyo, tumekubaliana na Mkuu wa Mkoa waufute huo utaratibu na wameshaanza kuufuta, wawaache wakulima wenye contract na wanunuzi wauze moja kwa moja kwa wanunuzi wao. Wahakikishe tu Serikali inapata ushuru wake stahiki katika njia halali na wafute tozo zote walizoziweka ambazo hazijaidhinishwa na Wizara ya Kilimo kwenye zao la avocado. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri hilo katazo linafanywa lini, kwa sababu maparachichi yanaoza. Mkuu wa Mkoa hilo katazo atalifanya lini?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, katazo hili nimeongea na Mkuu wa Mkoa siku Mbili zilizopita na tumeshakubaliana na Wizara ya Kilimo imemwandikia barua Mkuu wa Mkoa siku ya jana kumueleza haya ambayo ninayasema. Kwamba, avocado haiwezi kuuzwa kwenye mfumo ambao unataka kufanyika Rungwe.
SPIKA: Hilo limeshaeleweka mmempa maelekezo ya hilo katazo lini, kwa sababu haya mazao yanaharibika. Kwa hiyo, kama atakuja kutoa hilo katazo baada ya miezi mitatu hiyo ndiyo hoja. Katazo linatoka lini? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, katazo limetoka juzi kwa simu jana limekwenda kwa barua. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi kuuliza swali la nyongeza. Serikali ilianzisha ujenzi wa hosteli kwenye Chuo cha Uuguzi pale Tukuyu mwaka 2008. Ujenzi umekamilika, umefikia hatua ya kufanya finishing tu yaani kuweka madirisha na milango, wanafunzi 150 wanakaa nje ya chuo. Je, ni mpango gani wa Serikali kuhakikisha kwamba majengo yale yanakamilika na wanafunzi wale 150 wanaingia kukaa chuoni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantona kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mbunge labda nimwambie tu kwa mwaka huu kwa ajili ya umaliziaji vyuo kama hivi ambavyo vimekaribia kufanyiwa finishing ili watoto waingie ndani, zimetengwa around bilioni 2.7 kumalizia vyuo ambavyo viko 17 vinavyotakiwa kumaliziwa nchi nzima. Kwa hiyo kitamaliziwa kabla ya mwezi wa 12 kila kitu kitakuwa kimekaa vizuri.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe masikitiko yangu makubwa, nimekuja mara nyingi hapa kwa mradi wa REA II ambao ni Vijiji 25, ukizingatia huu mradi ulikuwa ni mradi wa mwaka 2014 ndiyo ulianza, hivi vijiji 25 vilitelekezwa. Nilikuja hapa mwaka jana mwezi wa Februari Bunge, Naibu Waziri mwenyewe hapa alisema kwamba Mwezi April mradi utakuwa umeshakamilika. Nimekuja Bunge la Mwezi wa Sita akaniambia mwezi wa Tisa mradi utakuwa umeshakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekutana na Waziri mwenyewe amekuja kufanya ziara kule nyumbani Jimboni kwangu, amefanya mkutano na wananchi pale Tukuyu akawaambia mpaka Disemba mradi utakuwa umeshakamilika. Leo hii naambiwa hapa kwamba mradi huu umechanganywa na REA Namba III Awamu ya Pili na utaisha Disemba, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda Wizara haikuelewa vizuri swali langu. Huu ni mradi REA II ambao ni wa muda mrefu, nilikuwa naomba nipate majibu. Ni lini mradi wa REA II vijiji 25 utakamilika?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, REA III Awamu ya Pili nilikuwa na Vijiji 36, mpaka ninavyoongea hapa ni Vijiji Vitatu tu ndiyo vimeshawashiwa umeme, kuna Kijiji cha Mboyo Kata ya Isongole, Kijiji cha Ndwati na Kijiji cha Lienje Kata ya Ikuti na deadline ilikuwa ni Disemba mwaka 2022. Leo naambiwa hapa kwenye swali la msingi kwamba tunapeleka tena mpaka Disemba 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri ni lazima tuwe serious kwa sababu wananchi wetu wanatusikiliza, ahadi Serikali wanazotoa nasi tunawaambia, leo naambiwa 2023 ndiyo mradi utakamilika. Naomba nipate ufafanuzi wa Serikali, mambo gani yaliyopelekea kubadilisha deadline kutoka Disemba 2022 mpaka Disemba 2023?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anton Albert Mwantona kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama swali lilivyoulizwa ilikuwa ni kwamba ni lini Vijiji vilivyobaki katika REA II vitakamilishwa. Kule mwanzo vilipochukuliwa hivi Vijiji 25 vilitakiwa vifanyike katika REA II lakini havikufanyika vilibaki. Kwa sababu maelekezo ya Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kwamba hii Awamu ya REA III mzunguko wa pili usiache kijiji hata kimoja bila kupelekewa Umeme. Kwa hiyo, Vijiji hivi 25 vimeunganishwa kwenye Mkataba wa REA III Round II ili navyo vifanyiwe kazi na vikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua tutawaelekeza wenzetu wanaotekeleza mradi kwenye maeneo haya ili wahakikishe kwanza katika scope hii wanashughulika na vile Vijiji ambavyo ni vya muda mrefu halafu hivi ambavyo vilikuwa ni vya REA III Round II waje wavimalizie kwa kadri tunavyosogea mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine ambalo ni la msingi ameuliza kuhusu kubadilika kwa muda wa kumaliza mkataba wa REA III Round II kutoka Disemba mwaka jana kwenda Disemba mwaka huu. Sababu kubwa ziko mbili, kwanza ni ile ambayo tulikwisha ieleza ya matatizo tuliyoyapata ya kuongezeka kwa bei na changamoto zilizotokana na UVIKO, tatizo jingine ni tatizo chanya ambalo ni kuongezeka kwa Kilometa Mbili kwa kila Kijiji katika mradi huu ambao unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kwa scope ile ya zamani ambayo ilitakiwa iishe Disemba, baada ya kuongeza zaidi ya nusu ya ile scope imekwenda sasa kufikia mpaka Disemba mwaka huu, tutahakikisha kwamba tutavutana na kukabana na Wakandarasi ili hizi kilometa mbili ambazo zinaongezeka kwenye Vijiji vyetu Disemba mwaka huu kazi yote iweze kukamilika katika maeneo yetu.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi lakini pia namshukuru Rais wa Jamhuri wa Tanzania alipofanya ziara katika Jimbo langu la Rungwe aliahidi kuweka taa katika Mji Kiwila, Mji mdogo wa Tukuyu pamoja na Ushirika.
Je, ni lini sasa taa hizo zitawekwa katika miji hiyo ambayo nimeitaja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi tunavyoongea miji ya Kiwila, Tukuyu na Ushirika itawekewa taa; na sasa hivi Mkandarasi ameshapatikana, wako kwenye hatua za mobilization, ahsante.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, mradi unasuasua hauendi vizuri sana kwa sababu ni mwezi wa Nane sasa hivi hakuna kinachoendelea kule kwenye mradi, ukiuliza kwanini unasuasua wanatuambia kwamba ni kwa sababu unatekelezwa kwa force account na watumishi wapo busy na mambo mengine.
Je, Serikali ipo tayari kutafuta Mkandarasi badala ya kutumia force account ili mradi uweze kwenda haraka na wananchi wapate huduma ya maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza na Mheshimiwa Mwantona kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nipende kukupongeza kwa ufuatiliaji mzuri wa hili suala la maji la Tukuyu Mjini na hata jitihada ambazo zimefikiwa kwa kilometa tatu ni kwa sababu ya ushirikiano, hivyo ninapende kukuondoa hofu.
Mheshimiwa Spika, force account ni moja ya namna ambavyo inasaidia katika Wizara na miradi inakuwa vizuri, lakini suala la kuweka Mkandarasi kwa baadhi ya maeneo naomba tuseme tumeipokea na tutaweza kushauriana namna bora ya kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANATONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini maana yangu hasa ilikuwa mgawanyo wa fedha za TARURA kwa kuzingatia mtandao wa barabara katika Halmashauri zetu. Kwa mfano, ukichukua Mbeya peke yake, Rungwe ni ya pili. Mbeya Vijiji ya kwanza, mtandao mkubwa kama kilometa 1,000 na Rungwe inafuata, lakini bajeti tunayopata ni ndogo kuliko Halmashauri nyingine. Kwa hiyo, naomba Serikali ituambie ni vigezo gani vinatumika kugawanya hizi pesa za barabara katika Halmashauri zetu, kwa mfano, utakuta Halmashauri ina kilometa nyingi zaidi, lakini inapata fedha chache?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mwaka jana 2022 Mheshimiwa Rais alitembelea Rungwe akaahidi kutoa kilometa mbili za lami pale Mji wa Tukuyu: Je, ni lini fedha hizo zitakuja ili mradi huo wa barabara ya kilometa mbili za lami uweze kutekelezwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwantona, la kwanza hili la vigezo vya mgawanyo. TARURA ilipokea vigezo vilevile vilivyokuwepo awali kabla ya taasisi hii kuanzishwa ambapo vilikuwa vimetengenezwa na Road Fund nchini kuweza kuwapelekea fedha Halmashauri mbalimbali. Baada ya TARURA kuanzishwa, changamoto hii Serikali imeiona na tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Angellah Kairuki alielekeza TARURA kufanya tathmini na kuona ni namna gani fedha inaweza ikapelekwa kulingana na barabara ambazo zipo na ukubwa wa maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari kazi hiyo ilikuwa imeshafanyika na baada ya kazi hiyo kufanyika, sasa kuna independent team ambayo imepewa ku-verify tu, kuona. Vigezo ambavyo vitatumika sasa, ni kuona urefu wa barabara, kuangalia ukubwa wa eneo husika, vilevile kuangalia milima, wingi wa mvua, agri-connect katika maeneo hayo shughuli za kilimo zinafanyika kiasi gani, na kadhalika kuweza kutoa fedha ya kwenda kwenye barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la pili la nyongeza la kilomita mbili ambazo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan hii tutaendana kadiri ya upatikanaji wa fedha kuweza kukamilisha ahadi hii. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za Dkt. Samia Suluhu Hassan huwa zinatekelezeka kwa wakati, na tayari tutaangalia katika bajeti ya mwaka huu kupitia Taasisi ya TARURA kuona ni nini kinaweza kikatengwa ili ahadi hii ianze kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi; je, ni lini barabara ya kutoka Kimo – Iponjola – Ikuti – Ibungu mpaka Kafwafwa itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantona, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hiyo ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Mbeya kwa maana ya Wilaya ya Rungwe na Wilaya ya Ileje na katika mwaka huu wa fedha tunaouendea imetengewa Bajeti kwa ajili ya kuanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kutoka Ibungu – Katengele – Kafwafwa hadi Kimo, ahsante. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nipate ufafanuzi zaidi kwenye jibu la msingi. Mkandarasi anayetekeleza mradi sasa hivi kule Rungwe ni ETDCO siyo State Grid Limited. Kwa hiyo, nilikuwa naomba nipate ufafanuzi zaidi kwamba, huyu State Grid Limited ameingiaje hapo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwenye REA II kuna vijiji 25 viliachwa, vilitelekezwa, yaani kama viporo; napenda nijue kwamba ni lini huu Mradi wa REA II vijiji 25 utaanza kutekelezwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mkandarasi ETDCO ndio yuko site na Mkandarasi ETDCO anatekeleza Mradi wa REA III Round II. Ndiyo mradi unaoendelea ambao ni mkubwa ambao ETDCO anautekeleza na tunatarajia itakapofika Desemba atakuwa amemaliza kwa sababu, ni katika ile azma ya kuhakikisha vijiji vyote vinapata umeme ifikapo Desemba.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili sasa lililosema la vijiji 25 ambavyo vilikuwa vimeachwa na REA Awamu ya Pili tulikuwa tuna mabishano na mkandarasi kuhusu wigo wa utekelezaji na namna ya utekelezaji. Kuna maeneo alisimamisha nguzo, kuna maeneo aliweka waya halafu akaondoka, baada ya mvutano wa muda mrefu, ndiyo sasa tumemrudisha yeye mwenyewe, huyu huyu State Grid, ili aje kukamilisha vile vijiji vyake 25 ambavyo alikuwa ameviacha. Ndiyo maana tunasema ataanza Julai na atamaliza mwezi wa Kumi wakati ETDCO alianza tangu mwaka juzi, atamaliza Desemba mwaka huu.
MHE. ANTHONY A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini barabara inayoanzia KK Kata ya Kimo ikipitia Ikwenjola, Ikuti, Ibungu mpaka Kafwafwa ambayo iko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY KASEKENYA MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantona Mbunge wa Rungwe Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Kimo, Kafwafwa, Luswiswi, Katengele hadi Ibunge kwenye bajeti ya mwaka huu tunaokwenda kuitekeleza imepangwa ifanyiwe upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa na maandalizi ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami baada ya kukamilisha hizo taratibu za awali, ahsante.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nifanye marekebisho kidogo, siyo Halmashauri ya Mji wa Tukuyu ni Mji wa Tukuyu, kwa mujibu wa taratibu na sheria nataka nijue majukumu hasa miji midogo ni nini? Wale watumishi wa miji midogo wanatakiwa wafanye majukumu gani hasa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na matumizi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niiombe Serikali kama ingeweza ikaandaa mwongozo ambao utasaidia hii miji midogo kuweza kujitegemea na kukua ili hatimaye baadae wawe na uwezo kuwahudumia wananchi katika maeneo yao ya kiutawala hasa katika ukusanyaji wa mapato na matumizi na kuyasimamia matumizi hayo, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka za miji midogo zilianzishwa kwa mujibu wa sheria na zina majukumu yake na zina Baraza la Madiwani wa Mamlaka ya Mji Mdogo. Pia zina mtendaji wa mamlaka lakini pia zina mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo. Kazi zao pamoja na majukumu mengine ni pamoja na kuhakikisha kwamba zinakusanya mapato katika eneo lao la utawala katika mitaa yao. Pia kuwasilisha mapato hayo katika account ya halmashauri mama ambapo mkurugenzi wa halmashauri ndiye accounting officer wa halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa katika mitaa ambayo inaunda mamlaka ya mji mdogo, Mamlaka ya Mji Mdogo ni hatua ya kwanza ya kuelekea kupata kibali au kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji. Kwa hiyo, hii ni hatua ya mwanzo wakati wanajenga uwezo wao kujiendesha kuelekea kwenye Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swala la pili; kuhusu mwongozo wa miji hii kujitegemea, kwa sababu hii ni hatua ya kukua kuelekea kwenye Halmashauri ya Mji maana yake ukishafika hatua ya Halmashauri ya Mji wanakuwa na mkurugenzi ambaye ndiye accounting officer na inakuwa ni Baraza la Madiwani la halmashauri ya mji mambalo lina majukumu yote kwa mujibu wa sheria za Serikali za Mitaa, ahsante.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kutoka KK – Iponjola – Ikuti - Kafwafwa hadi Ibungu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ni barabara ambayo ipo kwenye Ilani kuhakikisha kwamba katika kipindi hiki tunafanya usanifu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunavyoongea sasa hivi, kutoka Kimwa hadi Kafwafwa Mkandarasi Mshauri yuko site kwa ajili ya usanifu na upande wa Kafwafwa hadi Ibungu tayari wako kwenye hatua za manunuzi kwa ajili ya kufanya usanifu ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.