Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Edwin Enosy Swalle (13 total)

MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza:-

Barabara ya kutoka Kibena (Stop Lupembe) mpaka Madeke C Mfiji, kilometa 125, imeshafanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu tangu mwaka 2015.

Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kibena - Lupembe – Taweta yenye urefu wa kilometa 125 ni Barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Njombe. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya taratibu za ununuzi wa Mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha huu wa 2020/2021, Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 5.96 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya barabara ya Kibena – Lupembe yenye urefu wa kilometa 50. Aidha, wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa vipande vingine, Wizara yangu inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia Wawekezaji katika kilimo cha Parachichi mkoani Njombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwaka 2020, thamani ya zao la parachichi katika Soko la Dunia inakadiriwa kuwa Dola za Kimarekani milioni 4,800. Kwa Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, soko la parachichi linakadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 254. Aidha, nchi yetu imeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji na uuzaji wa zao la parachichi katika masoko ya ndani na ya Kimataifa kama vile Umoja wa Ulaya, China, India na Kenya. Hivyo, mwaka 2020 kiasi cha Dola za Kimarekani milioni nane kilipatikana kutokana na wastani wa kiasi cha tani 4,000 zilizosafirishwa katika Soko la Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na ufanyaji wa biashara kwa kushughulikia kero zitokanazo na ukadiriaji na ukasanyaji wa kodi usio rafiki; upatikanaji mgumu wa ardhi unaochukua muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji; changamoto za upatikanaji wa vibali vya kazi na ukaazi; na kuondoa tozo mbalimbali ambazo ni kero katika Serikali za Mitaa. Hadi sasa, jumla ya tozo 273 ambazo zilikuwa kero kwa wawekezaji zimefutwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Sera ya Uwekezaji, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kutoa vivutio kama vile misamaha ya kodi kwenye makasha/majokofu (cold rooms) yanayotumika kuhifadhi mazao ya bustani ikiwemo zao la parachichi. Aidha, Serikali ina mpango wa kujenga chumba baridi katika uwanja wa ndege wa Songwe, ambapo ndege za Kimataifa zinazobeba mizigo zitaanza kusafirisha parachichi na mazao mengine ya matunda na mboga mboga moja kwa moja kwenda kwenye masoko ya Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, Serikali imepanga kujenga jengo lijulikanalo kama ukanda wa kijani katika bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa na mazao yanayoharibika mapema likiwemo zao la parachichi. Jitihada nyingine ni pamoja na kutafuta masoko ya nje, kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, uhifadhi, uchukuzi na usafirishaji. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote ikiwemo sekta binafsi katika kukuza uwekezaji wa zao la parachichi.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, upi mpango wa Serikali katika kukwamua zao la zhai ambalo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yenye changamoto nyingi nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa zao la chai kutokana na mchango wake katika Pato la Taifa, ajira kwa wadau wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa zao na kipato kwa wakulima wa chai. Katika kuongeza uzalishaji na tija ya zao la chai, Serikali inaendelea kuwekeza katika utafiti na uzalishaji wa miche bora ya chai ambapo hadi kufikia Mei, 2021, Taasisi ya Utafiti ya TRIT imefanikiwa kuzalisha aina mpya nane za miche za zao la chai zinazohimili ukame, ukinzani na magonjwa, zenye tija nzuri ya uzalishaji na ubora wa vionjo vya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Taasisi za TARI na TRIT kwa kushirikiana na Kampuni ya Mbolea ya Minjingu inaendelea na majaribio ya mbolea ya Minjingu kwenye mashamba ya chai. Hatua nyingine ni kutoa mafunzo ya vitendo kwa wakulima 2,000 wa chai kupitia mashamba darasa 97 katika Halmashauri za Wilaya za Njombe, Rungwe na Mufindi kwa lengo la kuongeza tija, ubora na ushindani wa chai ya Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kuhamasisha wakulima wa chai kutumia umwagiliaji katika na baadhi ya wakulima chini ya makampuni ya Uniliver na DL wameanza kufanya majaribio ya matumizi ya mifumo ya umwangiliaji kwenye kukuza chai. Vilevile kupitia Mradi wa Agri-connect Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa ajili ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya chai, kahawa na bustani katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe na Katavi ambapo barabara zilizojengwa hadi kufikia Mei, 2021 zina urefu wa jumla ya kilometa 87.

Aidha, Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) inaendelea kuhamasisha Vyama vya Ushirika katika zao la chai kutumia mfumo wa uagizaji wa mbolea bulk ambapo mwezi Februari Chama cha Ushirika wa Mazao na Masoko Mkonge kilifanikiwa kuagiza tani 500 mbolea aina ya NPK kwa ajili ya zao la chai.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa masoko ya chai na ifikapo Desemba, 2021 tutakuwa na mnada wa chai nchini Tanzania kwa mara ya kwanza ambao utafanyika Jijini Dar es Salaam na kutoa fursa kwa wazalishaji wakubwa na wadogo kushiriki kwenye uuzaji wa chai ndani ya nchi badala ya kupeleka chai kwenye mnada wa Mombasa nchini Kenya.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha zao la chai nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la chai linaingizia Taifa fedha za kigeni zaidi ya dola milioni 60 kwa mwaka na kutoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 50,000 viwandani na mashambani. Zao hili linalimwa katika Wilaya 12 na Mikoa sita ambayo ni Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga, Kagera na Mara ambapo wakulima wadogo wa chai wapatao 32,000 hujishugulisha na kilimo cha zao hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea na jitihada za kuendeleza zao la chai kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na ubora kwa kutenga fedha za kwa ajili ya utafiti, upatikanaji wa miche bora ya chai, kuimarisha miundombinu, kutoa mafunzo na masoko. Kwa mwaka 2021/ 2022, Serikali imetenga fedha za maendeleo jumla ya shilingi 400,000,000 kwa ajili ya kuzalisha miche 1,000,000; kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo na kuendeleza mashamba mama manne yanayosimamiwa na Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTDA) ya Korogwe na Lushoto.

Mhasimiwa Mwenyekiti, kupitia Mradi wa AGRICONECT jumla ya Euro milioni tano na laki tano zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza zao la chai katika mnyororo wa thamani katika kipindi cha miaka minne inayoishia 2023/2024 katika Wilaya za Rungwe Busokelo, Mufindi na Njombe. Mradi unaotekelezwa na Kampuni za IDH, TRITI na TSHTDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi 290,722,500 zimetengwa kwa ajili ya kuzalisha miche 750,000, kutoa mafunzo kwa wakulima hususani kanuni bora za kilimo, kuimarisha Vyama vya Ushirika vipatavyo 34 na kuimarisha huduma za ugani. Miche itakayozalishwa imelenga kutumika kuziba mapengo kwa kuanzisha mashamba mapya. Aidha, ufadhili wa AGRICONEC na kwa kushirikiana na sekta binafsi, Wizara inaratibu uanzishwaji wa mnada wa chai katika kuhakikisha kuwa chai ya wakulima inapata bei nzuri na soko la uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnada huo wa chai nchini unatarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa mwaka huu. Wizara kwa kushirikiana na wadau inakamilisha mkakati wa chai utakaoishia mwaka 2030. Wenye lengo mahususi ya kuongeza tija, uzalishaji wa ubora wa chai, ufanisi katika kutoa huduma za ugani pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji. Mkakati huu unalenga kuongeza uzalishaji wa chai kutoka tani 33,000 hadi kufikia tani 9,000 chai kavu, ifikapo mwaka 2030 na kuongeza matumizi ya teknolojia katika mnyororo wa thamani na kuimarisha mfumo wa masoko. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, tangu kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kuna changamoto gani katika kukuza na kuendeleza Mfuko wa Elimu ya Bodi ya Mikopo ili kukopesha wanafunzi wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kukuza na kuendeleza Mfuko wa Elimu ya Bodi ya Mikopo ili kukopesha wanafunzi wengi zaidi. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imekuwa ikiongeza fedha za bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 106 kutoka shilingi bilioni 464 ya mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali, kumekuwepo na changamoto kadhaa katika kukuza na kuendeleza Mfuko wa Elimu ya Bodi ya Mikopo ambazo zinazotokana na mambo yafuatayo; jambo la kwanza baadhi ya wanufaika wa mikopo iliyoiva kutojitokeza na kurejesha kwa hiari mara baada ya kumaliza masomo. Lakini kambo la pili baadhi ya waajiri kutowasilisha kwa wakati orodha ya waajiriwa wapya ambao ni wanufaika wa mikopo na wengine kuchelewa kuwasilisha makato ya fedha kwa wakati kutokana na wanufaika ambao ni waajiriwa wao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo imeendelea kutoa elimu kwa wanufaika na waajiri ili kuhamasisha urejeshaji wa mikopo kwa hiari na kwa kuzingatia matakwa ya kisheria. Vilevile imeendelea kuimarisha kaguzi kwa waajiri pamoja na kuwashirikisha wadau wa kimkakati kama BRELA na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kubaini wanufaika wapya na kuongeza kasi ya urejeshaji mikopo iliyoiva kwa lengo la kukuza na kuendeleza Mfuko wa Elimu ya Bodi ya Mikopo ili kukopesha wanafunzi wengi zaidi. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali isiteue Majaji wa muda mfupi (Acting Judges) ili kusikiliza kesi za mauaji zinazochukua muda mrefu Mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uteuzi wa Majaji upo Kikatiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haina ibara inayotambua au kuruhusu uteuzi wa Majaji wa muda mfupi (Acting Judges). Aidha, Ibara ya 117(3) ya Katiba inatambua uwepo wa Mahakimu wenye mamlaka ya nyongeza ya kusikiliza baadhi ya mashauri ya Mahakama Kuu yakiwemo kesi za mauaji.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta muswada wa sheria wa kuweka ukomo wa upelelezi kwenye kesi za mauaji nchini?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kesi za mauaji zinaangukia katika makosa makubwa (capital offences) zikiambatana na adhabu kubwa ambayo ni kunyongwa hadi kufa au kifungo cha maisha pale mtu anapopatikana na hatia. Hivyo upelelezi wake unahitaji muda na umakini mkubwa ndiyo maana kwa sasa upelelezi haujawekewa ukomo wa kisheria.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Mashtaka katika kuratibu na kusimamia upelelezi wa makosa ya jinai ametoa Mwongozo wa Mkurugenzi wa Mashtaka Na. 1 wa mwaka 2022 kuhusu ufunguaji wa mashtaka na ukamilishaji wa upelelezi wa kesi za jinai uliotolewa tarehe 30 Septemba, 2022 na kuanza kutumika tarehe 1 Oktoba, 2022. Mwongozo huo unataka upelelezi wa kesi za mauaji ambazo hazihitaji utaalam kutoka taasisi nyingine usichukue zaidi ya siku 60 na zile zinazohitaji utaalamu kutoka taasisi nyingine usichukue zaidi ya siku 90. Ahsante.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali katika kuharakisha kesi za mauaji ambazo huchukua muda mrefu kusikilizwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enossy Swalle, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeunda kikosi kazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai cha kupitia majalada ya kesi za mauaji zenye muda mrefu kuanzia miezi miwili na kuendelea. Majalada hayo yanafanyiwa mapitio na kutolewa uamuzi. Kikosi kazi hiki kinaendelea na kazi ya kupitia majalada ambapo kazi hii inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2022.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kuwa na subira ili kutoa muda hadi mwishoni mwa mwezi Mei, 2022; kesi zote za muda mrefu zitakuwa zimeshughulikiwa.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, lini ujenzi wa barabara ya Kibena Stop – Lupembe hadi Madeke kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuanza ujenzi wa Barabara ya Kibena – Lupembe hadi Madeke yenye km 126 kwa awamu, ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 itaanza ujenzi wa km 25 kwa sehemu ya kutoka Kibena hadi Nyombo. Kwa sasa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wanaendelea kuandaa nyaraka kwa ajili ya kutangaza zabuni. Zabuni zinatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha hadi ikamilike yote, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA K.n.y. MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya afya katika Jimbo la Lupembe ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka na imekwishaanza kutekeleza mpango wa kujenga vituo vya huduma za afya katika Jimbo la Lupembe.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya katika Jimbo la Lupembe. Aidha, hadi kufikia tarehe 30 Mei, 2022 imekwishapeleka shilingi bilioni 1.5 ambapo shilingi milioni 550 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya Ikondo na Kitiwa; shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati tatu za Ihang’ana, Maduma na Lyalalo; na shilingi milioni 800 kwa ajili ukarabati wa miundombinu ya Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Ahsante.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupeleka Watumishi, Vifaa Tiba na Tendanishi kwenye Vituo vya Afya na Zahanati katika Jimbo la Lupembe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi milioni 700 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023, Serikali imepeleka jumla ya watumishi 72 wa Kada mbalimbali za afya kwa ajili ya kutoa huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya kwa ajili ya kwenda kutoa huduma kwenye vituo kote nchini, ahsante.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga barabara ziendazo maeneo ya mazao ya kimkakati kama chai, kupitia mradi wa Agri-Connect - Lupembe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeainisha barabara zinazopita kwenye maeneo ya mazao ya kimkakati, ikiwemo zao la chai katika Jimbo la Lupembe, ambazo zina urefu wa jumla ya Kilometa 182.5. Kwa Mwaka wa fedha 2023/2024, usanifu wa Barabara ya Ukalawa – Kanikelele – Lupembe yenye urefu wa Kilometa 18.5, upo hatua za mwisho kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na mpango wake wa kutenga bajeti ili kuboresha barabara kwenye maeneo ya mazao ya kimkakati ikiwemo Jimbo la Lupembe. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza:-

Je, lini Serikali itarejesha Kiwanda cha Chai cha Wakulima wa Lupembe, Muvyulu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kuanzia Mwezi Januari, 2024, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ilianza kufanya tathmini ya mali za Kiwanda cha Chai cha Wakulima, Lupembe, kwa ajili ya kumlipa mwekezaji (Dhow Mercantile East Africa Limited) fidia kulingana na thamani halisi ya mali za kiwanda kabla ya kukirejesha kwa Wakulima wa Lupembe (MUVYULU). Kazi hiyo ya tathmini inatarajiwa kukamilika kabla ya Mwezi Juni, 2024.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa kazi hiyo kutawezesha mwekezaji huyo kulipwa fidia kulingana na makubaliano yaliyofikiwa baina ya mwekezaji huyo na Chama cha Ushirika cha Muvyulu ambapo Serikali itarejesha kiwanda hicho kwa wakulima wa zao la chai, Lupembe.