Supplementary Questions from Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge (28 total)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Hivi karibuni tumepata kuona kupitia mitandao, mwanafunzi aliyejulikana kwa jina Asia ambaye alifaulu vizuri masomo yake ya sayansi amepata division two ya point kumi na moja, lakini mwanafunzi huyu alikosa mikopo bila sababu ya kueleweka, ni mpaka baada ya kujiweka wazi mitandaoni na kulia sana ndipo Loan Board ikaweza kumpa mkopo mwanafunzi huyu.
Naomba kuiuliza Serikali; mwanafunzi huyu ambaye alifaulu vizuri, tena mtoto wa kike na masomo ya sayansi, imekuwaje akakosa mkopo na ni kigezo kipi walikitumia baadaye kumrudisha ili kuweza kupata mkopo? Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Swali lako ni zuri sana Mheshimiwa Mwanaisha lakini ni very specific, linahitaji muda. Mimi namuagiza tu Mheshimiwa Waziri afanye utaratibu wa kukutafutia jibu hilo halafu mtaongea kwa wakati wenu. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Hivi karibuni tumepata kuona kupitia mitandao, mwanafunzi aliyejulikana kwa jina Asia ambaye alifaulu vizuri masomo yake ya sayansi amepata division two ya point kumi na moja, lakini mwanafunzi huyu alikosa mikopo bila sababu ya kueleweka, ni mpaka baada ya kujiweka wazi mitandaoni na kulia sana ndipo Loan Board ikaweza kumpa mkopo mwanafunzi huyu.
Naomba kuiuliza Serikali; mwanafunzi huyu ambaye alifaulu vizuri, tena mtoto wa kike na masomo ya sayansi, imekuwaje akakosa mkopo na ni kigezo kipi walikitumia baadaye kumrudisha ili kuweza kupata mkopo? Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Swali lako ni zuri sana Mheshimiwa Mwanaisha lakini ni very specific, linahitaji muda. Mimi namuagiza tu Mheshimiwa Waziri afanye utaratibu wa kukutafutia jibu hilo halafu mtaongea kwa wakati wenu. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, wakati mimi nilipokuwa nasoma chuo tulikuwa tunapata ziara za mafunzo (study tours) mara kwa mara kwenye maeneo ambayo kazi zilikuwa zinatendwa kwa vitendo. Hata hivyo, utaratibu huo ulikoma na tukabakiwa tu na utaratibu wa mafunzo viwandani (industrial practical training) sasa ili kuzalisha vijana mahiri, wabunifu na wenye uwezo wa kuhamisha maarifa ya kisayansi katika uzalishaji. Je, Serikali haioni haja ya kuongeza utaratibu wa study tours pamoja na huu uliopo wa mafunzo viwandani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, niishukuru Serikali na niipongeze kwa kutambua mchango wa wataalam wanawake wa kisayansi mpaka wameamua kupanga kujenga shule za masomo ya kisayansi kila mkoa. Je, Serikali inaweka utaratibu gani sasa kuhakikisha wasichana waliofaulu vizuri masomo ya sayansi wanapata mikopo na fursa nyingine za elimu ya juu bila kuhangaika na usumbufu wowote kama ambavyo imetoa hivi karibuni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ulenge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika utaratibu wa kawaida vyuoni tunakuwa na program zile za practical training baada ya kumaliza mwaka husika wa masomo, lakini tumekuwa na utaratibu wa zamani ule wa kufanya study trip. Hata hivyo, kutokana na uhaba wa bajeti program hizi zilisimama.
Naomba kulithibitishia Bunge lako tukufu, hivi sasa tunakwenda kuimarisha na kuboresha bajeti yetu katika maeneo haya ya elimu, especially, katika vyuo vikuu na utaratibu huu sasa wa hizi study tour unaweza ukarejea.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili ambalo ni wasichana; kama mnavyofahamu Mheshimiwa Rais wakati anahutubia Bunge hili alizungumza hapa kwamba tunakwenda kujenga shule 26 katika kila mkoa kwa lengo la kuhakikisha kwamba wasichana wanakwenda kupata study za masomo ya sayansi katika maeneo haya. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wasichana hawa pindi watakapomaliza masomo yao haya tunakwenda kuwa-absorb kwenye vyuo ili sasa tuweze kupata wataalam wasichana na wanawake wengi katika masomo haya ya sayansi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipaumbele chetu kama Serikali na katika mikopo yetu ya elimu ya juu tutahakikisha kwamba masomo haya ya sayansi yanapewa kipaumbele, hasa kwa wasichana wetu hapa nchini. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Serikali inatekeleza Mpango wa peri-urban kuhakikisha vijiji vilivyopo ndani ya majiji navyo vinapatiwa umeme. Naomba kujua ni lini Serikali itaweka wazi ratiba yake ili na vijiji vilivyopo ndani ya Jiji la Tanga vitapelekewa umeme huo wa REA? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanaisha, Mbunge wa Tanga kwa kueleza kwanza kidogo kwamba Serikali yetu kupitia maelekezo yanayotolewa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, imekuwa ikipeleka umeme katika maeneo mbalimbali kwa taratibu tofauti tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Wakala wa Umeme TANESCO ambao una jukumu na wajibu wa kuhakikisha wanapeleka umeme katika maeneo yote ya mjini na vijijini kwa maana ya kwamba ile miradi inayowekwa katika mazingira fulani, ikishakamilika, basi TANESCO wanaendelea kupeleka umeme katika maeneo hayo. Hata hivyo, tumekuwa na hizo REA I, REA II na REA III; pia tumekuwa na kitu kinaitwa densification (Mradi wa Umeme Jazilizi); vile vile iko hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema ya peri- urban ambao ni mradi unaopeleka umeme katika maeneo ya mijini lakini yenye asili au uonekano wa vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa peri-urban ulianza kwa kupeleka umeme katika Majiji ya Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma na awamu ya kwanza imeelekea kukamilika, itakamilika mwezi wa nne mwaka huu na baada ya hapo sasa tutaingia katika awamu ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu ya pili itakapoanza basi Waheshimiwa Wabunge wote watafahamishwa na wale wote ambao ni wanufaika watapata nafasi hiyo. Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo ya peri- urban bado yanapelekewa umeme na Wakala wa Umeme TANESCO kwa kuzingatia kwamba ni jukumu lake kuhakikisha kwamba anapeleka umeme katika mazingira yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kuwa taarifa itapatikana na ratiba kamili itafahamika. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza na nitauliza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Shirika la Huduma za Mawasiliano Nchini, yaani TTCL inadai Taasisi za Serikali zaidi ya bilioni 82 za Kitanzania na Shirika la Posta linadai zaidi ya bilioni 1.5 kwa Taasisi za Serikali nchini.
Je, nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wadaiwa wote sugu wanalipa madeni yao haraka ili mashirika haya yaweze kujiendesha kiushindani? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kushukuru sana kwa kunipa fursa hii nikiunganisha na kadondoo ulikokasema nakushukuru sana kwa mwongozo huo, na ni washukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa jinsi ambavyo wamesimama na Serikali pamoja na Wizara ya Fedha katika kutoa elimu ya sheria tulizozipitisha na tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuzisaini.
Mheshimiwa Spika, nikirejea kwenye jambo alilokuwa ameliuliza Mheshimiwa Mbunge ni kweli tumeshapokea deni la TTCL na tuna hata baadhi ya wengine wanaoidai na wenyewe TTCL wamelazimika kufika hata Wizarani kwetu kusema tunaidai TTCL, lakini TTCL wanasema na wenyewe wanazidai Taasisi za Serikali, mnatusaidiaje.
Mheshimiwa Spika, nikiri mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba jambo hili tumelipokea na jambo ambalo ameleta Mheshimiwa Mbunge tumelipokea tunaendelea kufanyia kazi na uchambuzi na namna ya kushughulika na madeni haya madogo pamoja na haya makubwa na tutaziangalia hizi taasisi ambazo tutaongea ndani ya Serikali kuziangalia hizi taasisi za Serikali kwa sababu Serikali ni moja tuweze kuona ni namna gani tunalisaidia shirika letu hili ili na lenyewe liweze kufanya hizo commitment ambazo zimefanya katika hizo taasisi zingine.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza. Naomba kuuliza swali moja; Serikali imeweka mfumo wa kidigitali wa kulipa kodi za ardhi, lakini mfumo huo haumruhusu mwananchi kupata control number moja kwa moja, ni mpaka afike kwenye ofisi za ardhi ili kuhamasisha ulipaji kodi kwa haraka na kumwepushia mwananchi kulipa faini zisizo za lazima, je, Serikali haioni haja ya kuboresha mfumo huu ili kumwezesha mwananchi kulijua deni lake moja kwa moja kama wanavyofanya Wizara ya Maji? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanaisha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna changamoto katika suala zima la kuweza kupata zile bill kupitia mtandao, lakini bado kama Wizara tulirahisisha kwa kutumia simu zetu ukipiga *152*00# unafuata maelekezo kama ambavyo tunafanya katika masuala ya M-Pesa na mambo mengine. Suala la msingi unalotakiwa kujua wakati unatafuta kujua bill yako unatakiwa uwe unajua plot number yako ya kiwanja au namba ya hati yako kwa sababu itakuuliza na wakati huo itakuuliza kama kiwanja chako kiko Dar es Salaam au kiko mikoani. Kwa Dar es Salaam unaweka namba moja (1) lakini kwa mikoani unaweka namba mbili (2) halafu unafuata maelekezo. Kwa hiyo kuna wakati mwingine mitandao inasumbua, kweli inakuwa ni shida lakini ukiweza kupata mahali ambapo mfumo umekaa vizuri, bado unaweza ukapata bill yako, unaweza ukalipa kodi yako kwa kutumia simu yako hiyo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kama Wizara pia tunajaribu kuboresha mifumo kwa sababu kuna wakati mwingine unadaiwa 500,000 una 300,000 unataka kulipa. Ule mfumo mara nyingi hauruhusu kulipa part payment, inabidi uwasiliane na Afisa Ardhi ili aweze kukupa. Sasa hivi wataalam wetu wanafanyia kazi hiyo ili uweze kulipa hata kama una sehemu ndogo ya kuweza kulipa basi utalipa part payment na nyingine utakuja kumalizia na mfumo utapokea na Wizara ndiyo kazi inayoifanya sasa hivi. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, KFW Germany wamekuwa wakitoa huduma hiyo tangu mwaka 2013 mpaka 2018 mwishoni Mkoani Tanga, lakini 2019 mwanzoni ndipo walisitisha huduma zile na kuweza kupeleka mikoa mingine. Naomba kujua sababu gani imesababisha KFW Germany kuacha kutoa huduma ile ya mama na mtoto Mkoani Tanga na kuhamishia sehemu nyingine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Mwaka 2017 Serikali kwa mara ya kwanza ilianzisha upasuaji kwa watoto wenye upungufu wa usikivu nchini Tanzania, yaani wanafanyiwa upasuaji na wanapata mashine ambayo ni cochlear implant surgery machine, lakini accessories ama spare parts za mashine hizo zimekuwa ni ghali sana kwa wananchi wa kawaida kuweza kuzi-afford. Betri moja la mashine ile ambayo ni rechargeable ni zaidi ya laki tano, lakini ukienda kwenye…
NAIBU SPIKA: Swali Mheshimiwa.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, Serikali sasa ione haja ya kuvigiza vifaa hivyo nchini na wananchi waweze kununua kupitia Serikali, ili kuweza kushusha bei ya ununuzi kwasababu India ni rahisi sana. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali yake mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kwamba, kwa nini, sababu iliyofanya ule mkataba ukavunjika wa elfu mbili maana mkataba ule ulikuwa ni wa kipindi maalum 2012 ambao umeanza kama anavyosema 2013 na mpaka 2018, lakini nafikiri anauliza sababu iliyofanya:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kwanza ambayo sisi tunaijua ilikuwa ni mkataba wa wakati maalum, lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge tutafuatilia vizuri zaidi kwasababu inawezekana kulikuwa na uwezekano wa kuongeza mkataba na ukaweza kusitishwa. Tutaenda kufuatilia pamoja na yeye ili tujue na nitampa taarifa kwamba, ni nini kama kuna uwezekano wa kufanya lolote tuweze kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kufuatia hilo najua amekuwa akipata shida sana na umekuwa ukija wizarani kwa ajili ya akinamama wa Mkoa wa Tanga kuchajiwa hela. Mimi na wewe tutatafuta muda tuende tukaangalie tatizo liko wapi tulishughulikie haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili lilikuwa ni suala la upandikizaji wa viungo, watu wenye shida ya usikivu, upandikizaji ili waweze kusikia:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikwambie kwamba, Serikali yetu ukweli watu walikuwa wanapelekwa nchi za nje kwenda kuweza kupandikizwa hivyo viungo na walikuwa wanatumia zaidi ya milioni 100 kwa mtu mmoja. Lakini sasa Tanzania vimeshanunuliwa vifaa na upandikizaji huo umeanza kwenye hospitali yetu ya Muhimbili na ndicho anachozungumzia Mheshimiwa ambayo bado ni changamoto kwasababu, kununua tu vifaa vyenyewe ni zaidi ya milioni 40 ili kuweza kumpandikiza mtu huyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaenda vilevile kuja na Muswada wa kupanga gharama za vifaa tiba na dawa hatuna muongozo wa kudhibiti bei za vifaa hivyo, mtu anajiamulia tu kuuza bei anayoitaka. Lakini kwasababu Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alitoa bilioni 80 juzi kwa ajili ya kununua vifaa tiba tutaenda kuzingatia kwenye eneo hilo tuhakikishe Muhimbili wana vifaa hivyo kupitia MSD.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya swali la nyongeza; na nitauliza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mashine ya kupima kiwango cha usikivu kwa watoto mara wanapozaliwa (auditory brainstem response test) ipo Muhimbili peke yake hapa nchini. Hospitali zote za rufaa nchini hazina kifaa hiki, sasa ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuhudumia wanafunzi wenye ububu na uziwi na kuendesha kwa gharama kubwa shule hizo: Je, Serikali haioni haja ya kuhakikisha kwamba mashine hizo zinapatikana na inakuwa ni lazima kwa kila mtoto anayezaliwa kupimwa kiwango chake cha usikivu?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa swali zuri la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha, Mbunge, kuhusu masuala ya kuwapima watoto kiwango cha usikivu pale wanapozaliwa, kwamba ni gharama sana kwa sababu ni hadi uende Muhimbili. Nakubaliana kabisa na ninampongeza kwa kuliona hili.
Mheshimiwa Spika, niweze tu kusema haja ipo na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha miundombinu ya hospitali za kibingwa, hasa za kanda ili kusogeza siyo tu vifaa, pamoja na hawa wataalam wanaotakiwa kupima. Tuna hospitali yetu ya Mtwara imeshafikia asilimia 95, tuna ya Chato inakamilika, pia tuna Meta Mbeya inakamilika.
Mheshimiwa Spika, ni pendekezo la msingi na ni hoja ya msingi sana. Katika bajeti inayokuja tutaanza kuona kadri tunavyozindua, hata hawa wataalam wanaoshughulika na masuala ya usikivu, tuendelee kuwapa training tuwasogeze kwenye hospitali hizo. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa, miongoni mwa viumbe hai waliozuiliwa ni pamoja na vipepeo ambao sio maliasili, vipepeo wanaozalishwa na watu binafsi Wilayani Muheza, Mkoani Tanga. Je, Serikali iko tayari kutoa tamko rasmi kwamba, masharti waliyoyatoa yatawahusu viumbe hai ambao ni maliasili na vimbe hai wanaozalishwa na watu binafsi hayawahusu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Mto Zigi, Mkoani Tanga, una mamba wengi ambao wanaua watu wengi kwa muda mrefu sana. Tangu nikiwa binti mdogo watu wanafariki na juzi tu kuna mtu ameliwa na mamba na vilevile watu watatu wameshaliwa na mamba miezi miwili iliyopita. Je, Serikali haioni haja ya kwenda kuvuna mamba wale hata kama mto ule hauko ndani ya hifadhi, lakini mamba ni maliasili? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mwanaisha kwa maswali mazuri ambayo ameyaelekeza kwa Serikali, likiwemo hili la wanyamapori hai. Nataka nimwondoe wasiwasi, tunaposema wanyamapori hai ni wanyama wa aina yoyote iwe mdudu, nani, anaposafirishwa nje ya nchi sisi kama Maliasili na Utalii tunatambua kwamba, hiyo ni rasilimali ya nchi na haipaswi kuhamishwa kutoka eneo moja kwenda nje ya nchi. Kwa hiyo, nataka nimtoe wasiwasi na ndio maana hata hawa mamba pengine hawapo hata kwenye hifadhi, lakini kwa kuwa ni maliasili za Taifa lazima tuzilinde. Tunazilinda ili tuweze kuleta watalii ndani ya nchi waje kuona na tunapata mapato kutokana na vivutio hivi tulivyonavyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kifupi maswali yote nimeyajibu kwa pamoja, lakini hili la kuvunwa mamba nimtoe wasiwasi, mwezi uliopita tulikuwa tuna tathmini ya kukusanya data ya mamba wote ambao wamekuwa wakisumbua wananchi. Tayari tuko kwenye mkakati wa kwenda kuwavuna, hivyo muda wowote ninavyosema kuanzia sasa, tutatuma wataalam wa kwenda kuvuna mamba hao. Naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii ya swali la nyongeza. Licha ya Serikali kuleta Wizara hii maalum kabisa ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, naomba kufahamu ni nini mpango wa Serikali kuajiri Afisa Maendeleo Jamii Kata na Afisa Maendeleo Jamii wa Vijiji ambao ni wachache sana ili wanawake wetu waweze kufikiwa na kuweza kukua kiuchumi? (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Ulenge. Serikali inatambua upungufu wa watumishi hawa, Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii. Kadri ya asilimia 96 kwenye Kata zetu hazina hawa watu; na kwenye bajeti ya mwaka huu tutapanga kuanza kupunguza upungufu huo kwa kushirikiana na wadau wetu.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya swali la nyongeza. Kwa kuwa kanuni ya 10(3) ya kifungu 37A cha Sura ya 290 ya Fedha za Serikali za Mitaa inayohusu asilimia 10; imeitaka Mamlaka ya Serikali za Mitaa kukabiliana na mkopaji namna bora ya kurudisha fedha zile za mkopo. Je, Serikali haioni kwamba Kanuni hii inatoa loophole kwa Watendaji kuingiza mambo kinyume cha utaratibu na hawaoni haja kuweka muda wa marejesho kulingana na kiwango cha fedha ambacho kikundi kile kitakuwa kimekopa? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kanuni ya Fedha ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Kanuni ile inayoelekeza mikopo ya asilimia 10 imeweka nafasi ya Watendaji katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kukubaliana na vikundi vya ujasiriamali kuhusu utaratibu na muda wa marejesho ya mikopo hiyo. Dhamira yake ilikuwa, kwa kuwa mazingira haya ya wakopaji yanatofautiana sehemu moja na nyingine, lakini pia uwezo wa vikundi kurejesha unatofautiana kutoka kikundi kimoja na kikundi kingine, kwa hiyo, tunapokea ushauri wake. Tutafanya tathmini kuona uwezekano wa kuweka standard ya muda wa marejesho kwa kiasi fulani na pia tutaboresha njia hiyo kuhakikisha kwamba zile fedha hazipotei. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zoezi la fidia lilianza mwaka, 2012 mpaka 2013 kama sikosei na verification imekuja kufanyika mwaka 2015; na mpaka wananchi kulipwa, wamelipwa mwaka 2021 ambayo ni takribani miaka tisa: -
Je, Serikali haioni haja wale ambao hawakulipwa kwa mujibu wa Sheria yetu ya Barabara ya 2007, ukiwaacha pembeni kulingana na sheria ya awali ya masharti ya ADB kufutwa machozi kwa kuzingatia kwamba wamekaa miaka tisa bila kufanya maendeleo yoyote? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa malalamiko ya kupotezewa muda mwingi wananchi yapo Tanzania nzima kwenye suala zima la kulipwa fidia: -
Je, ni lini Serikali itaileta Sheria ya Barabara ya Mwaka, 2007 Act (No. 13) tukirekebishe kifungu Na. 16 ili kuweze kuongeza muda wa kuwalipa fidia wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Eng. Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuwapigania haki wananchi wa Mkoa wa Tanga ambao anawatetea.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika fidia za wananchi hawa wapo ambao waliridhika na wamechukua fidia, lakini wale ambao hawakuridhika, suala hili walilifikisha Mahakamani. Kwa hiyo, naomba nisiitolee maelezo zaidi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu mMarekebisho ya sheria, naomba niseme tumelichukua na tutakwenda kulifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mwani limekuwa ni zao ambalo linaingizia nchi nyingi fedha za kigeni na uzalishaji Tanzania kwa sasa ni tani 3,500 tu, lakini uhitaji uliopo kwa wanaotu-approach nchini kwetu ni tani zisizopungua 10,000. Swali langu ni kwamba ni upi mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji wa mwani nchini? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kutoka Tanga, ukanda huu wa mwambao wa bahari ya Hindi mpaka Mtwara, zaidi ya kilometa 1,084 kuna vikundi vya wanawake visivyopungua 8,000. Naomba kujua ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha masoko kwa wanawake hawa wanaozalisha mwani nchini na bei yenye tija?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa, Engineer Mwanaisha Ng’azi Ulunge, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, la kwanza katika jibu la msingi nimeeleza juu ya mkakati wa Serikali wa kuweka shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakopesha vikundi vya akina mama kamba na kitu tunaita taitai, na kitu tunaita mbegu ili waweze kuongeza uzalishaji. Na hiyo tutagawa katika vikundi vyote pamoja na hivi vikundi alivyovitaja Mheshimiwa Ulenge. Kwa hiyo, hilo litasababisha kuongezeka kwa uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, suala la bei na soko, nataka niwahakikishie kwamba kwa hali ilivyo na kwa uelekeo tunaouona, soko la mwani linazidi kukua siku hata siku na kwa msingi huo, tutakapokuwa na uzalishaji mkubwa, sasa uwezo wa kuweza kuliongoza soko katika bei utakuwa ni mkubwa, ni pamoja na kuweka mkakati wa bei elekezi ili zisishuke.
Mheshimiwa Spika, kama mwani aina ya spinosio uuzwe 800 kwenda juu, kama mwani wa aina ya kotonii uuzwe 2,000 kwenda juu. Huo ndiyo mkakati wetu tunaouelekea. Nashukuru.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, ni lini Serikali itajenga kituo cha kupozea umeme pale kwa Mbwembwele ili kuondosha tatizo la kukatikakatika katika Mji wa Handeni?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; mkandarasi anayesambaza umeme wa REA katika Wilaya ya Korogwe, anafanya kazi kwa kusuasua, tangu mkataba ulipoanza mwezi Mei, amesimamisha nguzo katika vijiji vitatu tu. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na mkandarasi huyu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Ulenge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la kwanza Serikali tayari imetoa pesa, shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa grid ya Taifa na Wilaya ya Handeni ni mojawapo ya eneo ambapo patajengwa kituo cha kupooza umeme katika eneo la Mkata kwa kuanzia na kinajengwa mwaka huu wa fedha wa 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili, mkandarasi anayepeleka umeme vijijini katika eneo la Korogwe, tutahakikisha kwamba kufikia Desemba mwaka huu anakamilisha kazi kwa sababu ndiyo mujibu wa mkataba. Tunaendelea pia kufuatilia kwa karibu kuondoa zile changamoto ndogo ndogo ambazo zilikuwa zimejitokeza za upungufu na ukosefu wa vifaa lakini kazi zitakamilika kwa wakati.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya jitihada kubwa kama ambavyo umeeleza za kuhakikisha inanunua vifaa vya TEHAMA nchini pamoja na kuwafundisha Walimu: Je, ni vipi jitihada hizi zinaunganishwa kuhakikisha kwamba tunaitumia TEHAMA kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali lake la msingi, Serikali bado inaendelea na jitihada ya kuzalisha walimu katika masomo ya sayansi nchini. Sambamba na hilo, kama nilivyozungumza ni kwamba tunaendelea na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na mahali tutakapoanzia ni kwenye vituo vyetu vya TRC na lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba vifaa vile tunaweza kwenda kuwafundisha walimu wetu.
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la kuanzisha vituo hivi ni kuhakikisha kwamba tuna-absorb walimu wengi zaidi kuweza kuwafundisha katika maeneo hayo ili watakaporudi kule shuleni waweze kufundisha, kwa sababu siyo lazima walimu wa TEHAMA watokane na wale walimu wa sayansi tu.
Tukishawafundisha walimu wetu, hata wale walimu wa masomo ya kawaida bado wanaweza kutumika katika kufundisha somo hili la TEHAMA.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa
Spika, ahsante sana kwa nafasi ya swali la nyongeza. Kwa kuwa Jiji la Tanga limetanuka na lina makazi mapya mengi, sasa ni lini Serikali itajenga vituo vya Polisi katika maeneo ya Kange Uzunguni, Kange Mbugani, Mwahako na Mwakidila? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunatambua ukubwa wa Jiji la Tanga na kwa kweli limepanuka sana na umuhimu wa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo ni mkubwa, kwa hiyo tutashauriana na uongozi wa Polisi wa Mkoa ili kuwajumuisha wadau akiwemo Mheshimiwa Ulenge na wengine wadau wema kuanza kujenga Vituo vya Polisi kwenye maeneo haya yaliyopanuka ili kuimarisha ulinzi kwenye maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba moja, upungufu wa damu unaotokana na kukosekana madini chuma unatajwa kuwa chanzo kikuu cha udumavu wa kimo na akili nchini, tatizo ambalo linapelekea Taifa kuwa na watu wasioweza kubuni na wasioweza kujifunza. Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kutatua changamoto hii kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, tafiti zinaonesha kwamba asilimia 47 ya wanawake walio katika umri wa kubeba ujauzito wana tatizo la upungufu wa damu na asilimia 57 kwa wanawake wajazito mtawalia. Sasa ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wasichana wanakuwa na damu sahihi ili kuandaliwa kuwa kinamama wenye afya imara na uwezo wa kuhimili kubeba ujauzito? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Engineer Ulenge, kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia afya ya watoto na mama na nimeona jinsi anavyoshirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Tanga katika kufuatilia mambo hayo katika Wilaya za Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu maswali yake mawili ambayo kimsingi kwa kweli ni kama swali moja limetenganishwa. Ninachoweza kusema, kwanza Rais wetu Dokta Samia Suluhu Hassan alishazindua Mkakati wa Lishe wa Taifa na kama mnakumbuka aliwasainisha Wakuu wa Mikoa yote kwa ajili ya masuala ya lishe na lishe hiyo sio kwa ajili ya watoto ni kwa ajili ya kila mtu na ambayo kinamama ni sehemu ya wanaotakiwa kufanya hivyo. Maana yake tukizingatia taratibu za lishe hatutakutana na mambo kama haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwamba wakinamama sasa ambao wamefika umri ambao ni wa kubeba mimba na ambao wanajitayarisha, tunafikiri Waheshimiwa Wabunge Mtusaidie kwamba suala la kubeba mimba lisiwe suala la dharura. Kama unataka kubeba mimba, basi unahitajika kujitayarisha na tunashauri waweze kuchukua folic acid. Tunawashauri watumie vidonge vya folic acid na mambo mengine, vitamin kimsingi ukijitayarisha namna hiyo ukibeba mimba hutakuna na upungufu wa damu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia amesema issue ya kimo, uzito na mambo mengine. Ni kweli kwamba suala hili linasababisha pia udumavu wa akili na inatuletea hasara kubwa kwa sababu lina uhusiano na maendeleo yetu, kwamba tusipozingatia haya tunaenda kuwa na kizazi ambacho hakiwezi ku - compete kwenye soko la ajira hakiwezi kuwa innovative na ndiyo maana unaweza kushangaa Tanzania tuna profesa mzuri wa uchumi anakuelezea kupata hela lakini yeye mwenyewe hana hela hayo ndiyo matatizo yanayotokana na mambo kama haya. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini hata hivyo swali hili naona halipaswi kujibiwa na Wizara hii. lakini nitauliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa kuna baadhi ya Wizara kama vile Wizara ya Ardhi na Wizara ya Afya imeweza kuhamisha wataalam wa kada zinazoendana na Wizara zile kutoka halmashauri kwenda kwenye Wizara mama zao. Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya tathmini ya kina ya Sera hii ya Ugatuaji ili kuendana na mahitaji halisi ya sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu namba mbili; kwa kuwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la upotofu wa maadili nchini, kama vile ukatili wa watoto na wanawake. Je, Serikali haioni haja katika Ofisi ya Sekretarieti ya Mkoa (RAS) kuwepo na RAS Msaidizi kwa ajili ya maendeleo ya jamii? Kwa sababu mpaka sasa hivi ofisi zote za mkoa hakuna RAS Mmsaidizi kwa ajili ya issues za maendeleo ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi kama nilivyosema kwamba Serikali sasa baada ya kuundwa kwa Wizara hii mpya inaendelea kuangalia utaratibu gani mzuri utaweza kuimarisha uratibu au mfumo wa ngazi ya mkoa mpaka kwenda kwenye halmashauri ili Wizara hii ambayo sasa hivi inakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii iweze kufanya kazi kwa uharaka na ufanisi kwa kuwatumia wale wataalam wake. Hivyo basi niseme kwamba nimepokea mchango wake na tunapoendelea na majadiliano haya ya kuimarisha hii mifumo tutawasilisha ili Serikali kwa ukubwa wake na upana wake iweze kuangalia.
Lengo letu ni kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa kule na wataalam hawa ziko vizuri wakati wote na za haraka na jamii inabadilishwa fikra zao ili kupokea maelekezo na matakwa ya utekelezaji wa sera zingine zote. Naweza nikaweka hivi kwa ujumla wake.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa, umaskini unatofautiana kutokana na mahali kwa mahali. Maskini wa jamii ya wafugaji, makazi siyo kitu cha msingi kwake, lakini maskini wa mahali pengine makazi inawezekana ikawa ni kitu cha msingi kwake. Kwa hiyo, ni lini Serikali itaona haja ku-standardize hivi vigezo vya kuzipata kaya maskini ili jamii ile iepukane na migogoro? (Makofi)
Swali langu la pili, nitazungumzia vile vipengele vinne vya Miradi ya TASAF na nitazungumzia suala zima la Public Work Program kwamba, kwa kuwa miradi hii inapokamilika inakabidhiwa katika mitaa au vijiji. Ni lini sasa Serikali itaweka utaratibu maalum kuhakikisha kwamba wanashirikishwa wanakijiji wote au jamii yote ili miradi ile iwe vipaumbele kwa jamii husika badala ya zile kaya zilizolengwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza juu ya ku - standardize vigezo. Utaratibu wa kupata wahusika au wafaidikaji ni utaratibu kwanza shirikishi. Wananchi wanashirikishwa katika ngazi ya kijiji, wanajadili juu ya taratibu zao, wanajadili juu ya vigezo na kutambua wapi ambao wanatakiwa kufaidika katika mradi huo. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie, tunapokwenda hata kwenye jamii ya wafugaji, wafugaji wenyewe wanashirikishwa ili kuweza kutambua na kutanabaisha vipaumbele vyao. Hivyo pia tunapokwenda kwenye jamii za wakulima na jamii mbalimbali. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba taratibu ziko wazi, vikao vinayokaa ni shirikishi na wanavyohitaji wananchi ndivyo ambavyo mradi wetu wa TASAF unakwenda kusimamia.
Swali la pili juu ya vipaumbele ambavyo vipo katika maeneo yetu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyokuwa nimejibu katika swali la msingi na maelezo ya ziada katika swali lake la kwanza la ziada, kwa uhakika kabisa nataka nimuhakikishie yeye na kulihakikishia Bunge lako kwamba tunapokwenda katika vijiji mambo yote yanayotakiwa na wanayohitaji wananchi ndiyo kipaumbele cha mradi huo wa TASAF na siyo vinginevyo.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa, barabara ile ni ya changarawe na magari yenye uzito mkubwa ndiyo yanapita kuelekea kule kwenye matanki ya mafuta yanapojengwa na gharama ya kurudishia changarawe imekuwa ni kila baada ya miezi miwili ambayo inapelekea maintenance cost kuwa kubwa. Je, hamuoni haja kuishauri EACOP barabara ile ijengwe kwa kiwango cha lami kupunguza maintenance cost na kuweza kutumika baada ya mradi kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Engineer Ulenge, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi kwamba barabara hii tayari baada ya utiwaji saini wa mkataba wa bomba la mafuta la Hoima tayari imehama kutoka TARURA na sasa inawahudumiwa na wao wenyewe EACOP. Tayari wameshaingia mkataba na mkandarasi wa kwao ambaye ataihudumia mpaka pale mradi huu utakapokamilika. Tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tutaufanyia kazi kupitia wenzetu wa TARURA, kuweza kukaa na wenzetu wale wa EACOP kuona ni namna gani wanaweza kuanza walau taratibu kui - upgrade barabara hii lakini haya yote yanategemeana na uwepo wa fedha.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja, kwa kuwa Bunge lilishazimia Kampuni ya KADCO kurejeshwa chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, sasa ni lini Serikali itafanya hivyo kutii Azimio la Bunge? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sawali la pili, ni lini sasa Serikali itakamilisha mchakato wa sheria kuipa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kusimamia kuendeleza viwanja vya ndege nchini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) : Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli mwezi Novemba, 2022 Bunge lako tukufu liliazimia KADCO kuwepo chini ya viwanja vya ndege nchini. Swali la pili, uanzishwaji wa Sheria ya Viwanja vya Ndege nchini. Ninaomba nijibu yote kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, mara baada ya Bunge lako tukufu kuazimia kwamba lazima KADCO iwe chini ya TAA, hatua ambayo Serikali tumefanya mpaka sasa, kwanza tuliielekeza TAA kuandaa draft kwa maana ya mapendekezo ya sheria, na tayari draft hiyo imeshakuja Wizarani na tuliyapitia, kuyaboresha na kuyapeleka kwa Mwanasheria Mkuu ili kupata idhini au kibali. Tayari Mwanasheria Mkuu alishatoa kibali na sasa ipo ngazi ya wataalamu kwa maana ya Makatibu Wakuu.
Mheshimiwa Spika, tunategemea tutaomba kibali kwenye Baraza la Mawaziri ambalo litafanyika mwezi wa saba na hatimaye matarajio ya Wizara mwezi wa tisa sheria hiyo iweze kuwasilishwa hapa Bungeni. Sheria hii itaweka msingi wa viwanja vyote vya ndege nchini kuwa chini ya TAA.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna viwanja vya ndege vilivyo chini ya TANAPA, kuna viwanja vingine viko chini ya mamlaka nyingine za Serikali. Sasa sheria hii itaweka msingi kwamba viwanja vyote vya Serikali hapa nchini viwe chini ya TAA, ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Licha ya juhudi kubwa za Serikali za kutatua changamoto ya maji Mkoani Tanga, bado Wilaya ya Muheza inapata maji kwa mgawo tena saa 8.00 za usiku. Je, ni lini Serikali itawezesha maji yale kutoka mapema ili wanawake wa Muheza waweze kupumzika usiku?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, eneo la Muheza kutoa maji ya mgawo usiku wa manane, huu sio utaratibu mzuri na tunataka kukomesha hili. Naomba wananchi wawe watulivu na subira, tutahakikisha huduma ya maji inapatikana saa zote na kama ni saa chache basi muda rafiki.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ninapozungumzia tiba ya macho, pua na koo, nazungumzia ongezeko la mabubu na viziwi nchini. Sasa kwa kuwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la mabubu na viziwi nchini ambalo limesababisha Serikali kupeleka ruzuku kwa wanafunzi kutoka bilioni 3.6 mwaka 2018/2019 mpaka bilioni 6.3 mwaka 2021/2022. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka vifaa vya kupima usikivu kwenye hospitali za wilaya ili kila mtoto anapozaliwa aweze kupimwa usikivu ili kupunguza tatizo la ububu na uziwi nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa, tangu mwaka 2016/2017, Serikali ilianzisha upasuaji wa kupandikiza vifaa vya usikivu nchini. Je, ni juhudi gani zimefanyika kuongeza vitengo vya speech therapy katika hospitali zetu, ili kuondosha tatizo la mabubu na viziwi nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, moja anaulizia ni kwa namna gani Serikali itajipanga kupeleka vifaa tiba kwenye level ya wilaya. Tunapokea ushauri wake na sio tu kwenye eneo la kupeleka vifaa kwa ajili ya kupima watu wenye matatizo hayo, lakini ni ku-include kwenye package ya mama anayejifungua, wakati anajifungua basi mtoto aweze kuhakikishwa kwamba amechunguzwa vitu vyote kiasi kwamba, hata wakati anahudhuria clinic kuna uchunguzi kama huo ili kuwatambua mapema na kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba, toka 2016 kulikuwa na operation za kuweka vipandikizi kwa wale watu ambao wana shida ya usikivu; tunapokea ushauri wake na bado tunasema hivyohivyo kama kwenye issue ya suala zima la watoto wadogo, vilevile tutapeleka kwa kuanzia kwenye level za mikoa kuhakikisha operations kama hizo zinaweza kufanyika na watu wao kupata huduma, lakini vilevile kwa watu ambao tayari wana tatizo hilo tunatengeneza utaratibu wa kuwasaidia hasa wanapokuja hospitali, watu wanaoweza kufafanua zile lugha za ishara na mambo mengine, ili waweze kupata huduma kama watu wengine. Ahsante sana.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Tanga ilifanya vizuri sana miaka ya 1980 na sababu kubwa ilikuliwa ni uwepo wa viwanda vingi ambavyo asilimia 90 sasa vimeshakufa. Kwa kuwa, meli kubwa na nyingi haziwezi kwenda mahali ambako zitapeleka tu mzigo bila kuchukua, yaani ile exchange of containers hakuna meli kubwa ambayo itakwenda bila kukutana na hali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, tunamini kabisa bandari ndiyo uti wa mgongo wa Taifa hili; Je, Wizara hii ya Uchukuzi haioni haja ya kushirikiana kwa karibu na Wizara zingine kuhakikisha kwamba meli kubwa zinakuja kwa kufufua viwanda ambavyo Tanga vimekufa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Bandari ya Mwambani ilipangwa kuendeshwa kwa ubia lakini kikwazo ilikuwa ni Sheria ya Ubia ambayo sasa imekwishafanyiwa marekebisho. Sasa Serikali itueleze wazi, mpaka sasa imeshachukua hatua gani kuhakikisha mpango ule wa kuendesha Bandari ya Mwambani kwa ubia unatekelezeka?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Eng. Mwanaisha kwa kazi yake kubwa anayofanya ya kufuatilia mchakato wa miundombinu katika Mkoa wa Tanga. Serikali imeshaanza kufanya mambo mengi katika eneo hilo, mojawapo ni ukarabati wa hiyo Bandari ya Tanga lakini pia uwepo wa fursa kama bomba la mafuta ni hatua muhimu kwenye kuelekea Tanga kuwa eneo muhimu sana la kiuwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kama je, tuko tayari kushirikiana na Wizara nyingine, ni kweli, tuko tayari kushirikiana na sekta nyingine ikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha kwamba viwanda vilivyokuwa vimefungwa na vimefanya vizuri miaka ya 1990 na huko nyuma vinafufuliwa ili angalau bandari hiyo iweze kupata mizigo. Mojawapo ya mambo ambayo tunayafanya ni pamoja na kufufua pia uwanja wa ndege wa Tanga ili ndege kubwa na za kati ziweze pengine kuanza kutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza kuhusu Bandari ya Mwambani, kwenye mpango wetu mkakati wa mwaka 2045 hiyo ni moja kati ya maeneo ambayo tunatazama kwa jicho la karibu zaidi. Kwa sasa hivi, moja tumeshakamilisha mabadiliko ya sheria ya PPP na hivyo tunakaribisha mtu yeyote anayetaka kuja kushirikiana nasi katika kuendeleza bandari hiyo ili kwa pamoja tuweze kuhakikisha kwamba Bandari ya Mwambani inafanya vizuri zaidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa ziara yake nzuri aliyoifanya katika Wilaya ya Lushoto na sasa maji yanatiririka pale kwenye Kata ya Kwai. Naomba kuuliza ule mradi mkubwa ambao uta-cover kata 13 za Wilaya ya Lushoto ni lini utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ulenge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kukushukuru kwa pongezi zako lakini kwa kazi kubwa na wewe unayoshiriki kuifanya katika Jimbo la Lushoto katika majimbo yale matatu ushiriki wako niliweza kuukuta na hongera sana pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mradi huu wa kata 15 ambao umeutaja tayari Serikali tunaendelea na hatua za mwisho kabisa ili tuweze kuja kuuanza mara moja na utekelezaji utaendelea mwaka ujao wa fedha.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza ni kwamba Sheria ya Kodi na Sheria za Uwekezaji hazisomani, kwa maana miradi mingi inafunguliwa lakini wawekezaji hawafanyi hivyo kwa sababu hakuna vivutio. Je, ni lini Serikali italeta hapa sheria hizo ili ziweze kupitiwa upya na ziweze kusomana? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Shirika la UNDP limewezesha mikoa mbalimbali kuanzisha miongozo ya uwekezaji, na kule Tanga tumeanzisha na tumeanza kuzindua miongozo ile ya uwekezaji. Ni nini sasa Serikali inafanya baada ya miongozo ile kuenea Tanzania nzima ili dhamira ile ya kuanzisha viwanda iweze kutimia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli bado kuna changamoto kwenye baadhi ya sheria na pia kwenye sera za uwekezaji. Serikali imeishaanza kupitia sheria mbalimbali za taasisi zetu, sheria za kodi, na vile vile tumeanza kuboresha au kuhuisha sera zetu mbalimbali ikiwemo Sera ya Uwekezaji, Sera ya Viwanda na Sera ya Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, haya niliyosema ndiyo ambayo Serikali tunafanya sasa ili kuhakikisha sera zetu na sheria zetu zinaendana na mahitaji sahihi kulingana na uhalisia wa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kama nilivyosema, tumeshaanza kutengeneza miongozo mbalimbali ya uwekezaji na miongozo hii au makongamano haya yamekuwa yakifanyika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Tanga. Matokeo haya katika Mkoa wa Tanga mahususi ni kutengwa kwa maeneo. Kwa mfano, maeneo yale kongwe ya maeneo ya uwekezaji 68, haya yamewekwa kwa ajili ya kujenga viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, miongozo hii sasa imeshaanza kuzaa matunda, na wawekezaji wengi wameshaanza kuonesha nia ya kuwekeza katika nchi yetu, na pia katika Mkoa wa Tanga ambako Mheshimiwa Mbunge ameuliza. Nakushukuru sana.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imesema inaweka vifaa kwenye vyuo vyetu, lakini je, haioni haja sasa ya kuhakikisha vyuo vyote nchini vinakuwa na database ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanafunzi kwa ajili ya matumizi ya baadaye? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ili kutengeneza mnyororo wa thamani wa matumizi bora ya tafiti na kuuchochea ubunifu na ugunduzi nchini.
Je, Serikali haioni haja sasa ya ku-pioneer kusimamia uanzishaji wa jamii za wanataaluma wa sekta mbalimbali na kuwaunganisha na wanafunzi wa vyuo ili kuchochea ubunifu na ugunduzi nchini? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na suala la kuanziasha kanzidata, tayari Serikali imeshafanya kazi hii. Hivi sasa tunavyozungumza vyuo vingi sana vya elimu ya juu pamoja na taasisi zetu za elimu ya juu tayari zimeanza kuwa na hizi database au kanzidata ambazo zitakuwa zinahifadhi hizi soft copy au nakala laini za utafiti na ubunifu. Hivi sasa tumeanza kwa ngazi ile ya Shahada zile za Umahiri (Masters) pamoja na zile za Uzamivu (Ph.D) na tumeziagiza taasisi zetu zote ziweze kuanzisha kanzidata hizi ili kuhakikisha kwamba zile tafiti na bunifu ninaweza kutunzwa siyo hizi tu za sasa hata zile za miaka ya nyuma tumeanza ku-digitalize ili kuweza kuzitunza katika kanzidata hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili ambalo anataka kufahamu kama Serikali ina mpango gani juu ya uendelezaji, lakini kutengeneza linkage baina ya wanataaluma na wale ambao wanafanya kazi kule viwandani. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu, Serikali tayari imetoa mwongozo kwanza wa uanzishwaji wa vikundi hivi au kampuni hivi tunaziita kampuni tanzu katika Taasisi zetu za Elimu ya Juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi wetu wa mageuzi makubwa ya kiuchumi (HEET) pamoja na ule wa EASTRIP tumenzisha makampuni tanzu kwenye taasisi zetu za elimu ya juu kwa lengo la kutengeneza wigo wa wanataaluma wetu na watafiti kuwa na linkage na viwanda na maeneo mengine ya sekta binafsi ili kuhakikisha zile tafiti na bunifu zao zinapelekwa kule, lakini zinaweza kutumika katika maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari ukienda kwenye Taasisi yetu ya DIT, Nelson Mandela pale Arusha, lakini University of Dar es Salaam hata ukienda MUST kule Mbeya wana Makampuni haya ambayo yanatengeneza linkage baina ya taasisi zetu za kitaaluma na viwanda vyetu. Nakushukuru sana.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Shule nyingi za Sekondari Mkoani Tanga zina maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo ambayo yangesaidia kupata chakula cha mchana kwa wanafunzi. Je, ni lini Serikali itatoa waraka maalum kwa walimu wa Mkoani Tanga, ili maeneo hayo yatumike vizuri, kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi? (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, nani anayepaswa kulima kati ya wanafunzi na walimu ili niwe nimeelewa swali lako vizuri?
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, swali la msingi la kwenye hili swali Namba 43 linazungumzia chakula ambacho...
SPIKA: Hilo limeeleweka, yaani muktadha wa swali lako, umesema walimu waelekezwe ili yale maeneo yatumike vizuri; kwa maana ya kutafuta wakulima wa kulima? Ama yale maeneo walime walimu ama walime wanafunzi?
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, vyovyote iwavyo, lakini maeneo yatumike vizuri. Yanakuwa ni kama vile sehemu ya elimu ya kujitegemea, lakini pia, shule ziwe na miradi ili kuepusha huu mzigo wa Serikali kuwalipa wazabuni. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa lishe na hasa katika ustawi wa wanafunzi wetu. Kwa hiyo, kwa muktadha wa swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba nichukue nafasi hii kuendelea kuwahamasisha Wakuu wa Shule waweze kuwa wabunifu, kuanzisha vibustani vidogo vya matunda, mbogamboga na mazao madogo ili waweze kuchangia katika lishe za wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Mbunge dhamira yake ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, shule zetu hizi na zenyewe kwenye maeneo yao wanaweza kuwa wabunifu na kuanzisha vimiradi vidogo ambavyo vitasaidia katika lishe za watoto ambazo ni muhimu sana katika makuzi yao katika kupata afya ambayo itawawezesha kupokea masomo vizuri.