Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jacquline Andrew Kainja (18 total)

MHE. JACKLINE K. ANDREA Aliuliza:-

Je, Serikali imeweka mpango gani wa elimu ya sheria ya usalama barabarani kwa madereva wa bodaboda ili waendeshe kwa kutii sheria na kuepusha ajali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jackline Kainja Andrew, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limekuwa likitoa elimu kuhusu Sheria ya Usalama Barabarani kwa madereva, bodaboda na watumiaji wengine wa barabara na vyombo vya moto kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani (The Road Traffic Act No.68/1973).

Mheshimiwa Spika, elimu hiyo hutolewa kwa kupitia Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, televisheni, radio, magazeti, vipeperushi mbalimbali, Maadhimisho ya Saba Saba na Nane Nane, matamasha mashuleni na kwenye vijiwe na maskani ya bodaboda. Aidha, katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Desemba, 2020 jumla ya vipindi 399 vya Elimu ya Usalama Barabarani vimerushwa hewani na kuoneshwa mubashara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na vituo 89 vya radio na televisheni. Pia elimu imetolewa kwa madereva wa bodaboda 638,275 na kwenye vijiwe vya bodaboda 7,760 nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, Wizara inashukuru sana wadau mbalimbali katika kutoa elimu hiyo ambayo ni TRA, PUMA, AAT, APEC, Future World Training College na Amend. Lengo ni kujenga ufahamu wa sheria na kuepusha ajali kwa madereva wa bodaboda na watumiaji wengine wa barabara. Ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italiangalia zao la asali na kulitafutia soko la uhakika ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, asali ni mojawapo ya mazao yanayozalishwa na nyuki, mazao mengine ni pamoja na nta, gundi ya nyuki, sumu ya nyuki, chavua na maziwa ya nyuki. Wizara imeendelea na jitihada za kutangaza mazao ya nyuki ya Tanzania kwa kushirikiana na TANTRADE kwenye mikutano mbalimbali ya kibiashara, maonyesho, warsha na makongamano yanayofanyika ndani na nje ya nchi pamoja na Balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa uzalishaji wa asili nchini ni wastani wa tani 30,400; sehemu kubwa ya asali hiyo zaidi ya asilimia 95 huuzwa katika soko la hapa nchini na asilimia tano huuzwa kwenye soko la nje kwenye nchi za Rwanda, Kenya, Burundi, Umoja wa Jumuiya ya Ulaya na Umoja wa Nchi za Kiarabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ukarabati pamoja na ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki katika Mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma na Geita ambavyo vitatumika kama soko la mazao ya nyuki. Serikali pia imeweka mfumo wa ufuatiliaji wa mazao ya nyuki katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao hayo kwa lengo la kuthibiti viwango vya ubora wa mazao ya nyuki pamoja na kufufua, kuendeleza na kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika wa ufugaji nyuki ili kuunganisha nguvu za uzalishaji pamoja na soko la uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa soko la mazao ya nyuki kupitia mradi mpya wa kusaidia mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki utakaotekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022. Naomba kuwasilisha.
MHE. JACQUELINE K. ANDREW aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya ardhi katika mikoa ya Tabora na Singida ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa utulivu na amani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrew, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, natambua kuwa imekuwepo migogoro ambayo kwa muda mrefu haikuwa imepatiwa ufumbuzi. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara iliagiza Ofisi zote za Ardhi za Mikoa nchini ikiwemo Singida na Tabora kuanzisha jedwali la migogoro ya ardhi ili kuibainisha na kuitatua. Kwa Mkoa wa Tabora, jumla ya migogoro 211 iliorodheshwa na kati ya hiyo migogoro 102 ilipatiwa ufumbuzi. Aidha, kwa Mkoa wa Singida jumla ya migogoro 226 imetambuliwa na kati ya hiyo migogoro 34 imetatuliwa na iliyobaki asilimia 85 inatokana na madai ya fidia ambayo wananchi wanadai Halmashauri na taasisi mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Wizara katika kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la migogoro ya ardhi nchini ni pamoja na kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi kwa wananchi, kuzitaka taasisi za umma kulipa fidia kwa wananchi kwa wakati, kuendelea kutoa elimu kwa umma, kushirikiana na Serikali za mitaa kudhibiti ujenzi kwenye miundombinu ya umma kama shule, viwanja vya michezo, maeneo ya wazi, Wizara za Kisekta kushughulikia kero za makundi mbalimbali ya watumiaji ardhi kama wafugaji na wakulima na maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wadau wote hasa taasisi za umma ambazo zinadaiwa fidia na wananchi inayochangia asilimia 39 migogoro yote nchini kuacha kuchukua ardhi za wananchi bila kilipa fidia na taasisi zinazodaiwa fidia kulipa mara moja vinginevyo maeneo hayo yatarejeshwa kwa wananchi, ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango wa kuwajengea miundombinu ya kisasa akina mama wa Tabora itakayoweza kukausha mboga kama uyoga, mchicha na majani ya maboga kwa njia ya kisasa zaidi ili kuongeza kipato?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha masoko ya ndani na nje ya nchi ilia kina mama wa Tabora wanaokausha mboga waweze kuuza mboga hizo kwa faida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrew Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tabora kama ifuatavyo kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa kilimo wakiwemo USAID-kupitia mradi wa Lishe, Shirika la Mpango wa Chakula Dunia (WFP) na JICA kupitia mradi wa TANSHEP imekuwa ikijenga uwezo wa wadau kuhusu matumizi ya teknolojia mbalimbali ikiwemo usindikaji wa mazao ya bustani. Serikali pia inahamasisha matumizi ya teknolojia ya ukaushaji wa mboga kwa kutumia nishati ya jua kwa kuwa teknolojia hiyo ni nafuu na rahisi kutumika ikilinganishwa na teknolojia nyingine.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na FAO inatarajia kutekeleza Mradi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 7.3 utakaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia ili kuwasaidia kina mama wa Mkoani Tabora na Katavi kuimarisha masoko na kusaidia katika teknolojia ya uhifadhi mazao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na SIDO na miradi na TANSHEP katika sekta horticulture kuunganisha wakulima na masoko ili kuboresha masoko ya ndani na nje ya nchi. Serikali kwa kupitia SIDO imekuwa ikiwapatia akinamama mafunzo ya ukaushaji wa mazao ili yawe na ubora unaotakiwa. Mafunzo yanalenga kufikia viwango vya bidhaa vinavyotambuliwa katika viwango vya TBS. Aidha, wasindikaji hao watakuwa wakipelekwa kwenye maonesho ya aina mbalimbali kama vilevile nanenane ili kutangaza bidhaa zao. Serikali pamoja na Wizara ya Viwanda kupitia SIDO, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Umoja wa Wajasiriamali Mkoa wa Tabora wanaendelea kuwatafutia majengo wakinamama ambayo yatatumika katika kusindika na kama display centres. Aidha, SIDO imeandaa mkakati wa kuwaingiza wasindikaji watakaokidhi vigezo katika portal ya SIDO.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Zahanati katika Kata ya Ng’ambo iliyopo Tabora Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Andrea Kainja Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma ya zahanati kwa fedha kutoka Serikali kuu na fedha za makusanyo ya ndani ya Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetoa fedha shilingi bilioni 27.75, kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati 555. Ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ilipokea fedha ya shilingi milioni 150, kwa ajili ya ukamilishaji wa Zahanati ya Ituru, Igosha na Igombe.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 35.15, kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 758 nchi nzima. Ambapo Halmashauri ya Manispaa Tabora imetengewa shilingi milioni 100 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya Zahanati ya Zaire na Zahanati ya Kapunze kila moja shilingi milioni 50. Aidha, kupitia mapato ya ndani Manispaa ya Tabora imetenga fedha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kukamilisha zahanati ya Mtendeni na Zahanati ya Igambilo, kila moja kwa shilingi milioni 50.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati yaliyojengwa na wananchi kote nchini. Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora inashauriwa kutenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa zahanati katika Kata ya Ng’ambo ili kusogeza huduma kwa wananchi.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Kanda ya Magharibi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga fedha za ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Magharibi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na tayari kazi ya kuandaa michoro ya hospitali hiyo imeshaanza na upembuzi yakinifu wa eneo ambalo itajengwa kwa kuzingatia ukaribu wa wananchi wote katika mikoa inayounda Kanda ya Magharibi. Ahsante. (Makofi)
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza majengo katika Kituo cha Afya Itobo Wilayani Nzega?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza kuongeza majengo katika Kituo cha Afya Itobo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Shilingi milioni 500 zilipelekwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje, jengo la maabara, kichomea taka, jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji na jengo la kufulia nguo. Ujenzi wa majengo haya upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA K. n. y. MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Shule nyingine ya Msingi katika Kata ya Ng’ambo Tabora Mjini kwani Kata hiyo ni kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Andrea Kainja Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli shule nyingi za msingi hapa nchini zina wanafunzi wengi wanaozidi kiwango katika shule. Hali hiyo pia ni matokeo ya utekelezaji wa Sera ya Elimu Msingi bila malipo iliyoanza utekelezaji wake mwaka 2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata Ng’ambo ina shule moja ya msingi yenye madarasa 17 ambayo yanahudumia wanafunzi 2,408. Aidha, ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi katika Kata hiyo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga Shilingi Milioni 50 za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi madarasa mawili ya shule mpya ya msingi inayotarajiwa kujengwa katika eneo la Kilimani katika Kata hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 itatenga fedha ya ujenzi wa madarasa katika shule mpya ya msingi eneo la Kilimani kupitia programu ya EP4R.
MHE. JACQUELINE K. ANDREW aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga bajeti kwa Hifadhi changa za utalii ili kukuza utalii katika hifadhi hizo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrew, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, tayari ilishaanza mchakato wa kuboresha hifadhi changa 17 za utalii ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara, huduma za malazi na chakula na maeneo ya uwekezaji ambapo tayari wawekezaji wameonesha nia ya kuwekeza. Hifadhi za Taifa changa zilizopo katika mkakati huo ni Burigi-Chato, Gombe, Ibanda-Kyerwa, Katavi, Kigosi, Kisiwa cha Rubondo, Kisiwa cha Saanane, Kitulo, Milima ya Mahale, Milima ya Udzungwa, Mikumi, Mkomazi, Mto Ugalla, Nyerere, Ruaha, Rumanyika-Karagwe na Saadani.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha hifadhi hizo kwa lengo la kukuza utalii na kuongeza mapato. Maboresho hayo yanaenda sambamba na utekelezaji wa Programu ya Tanzania, the Royal Tour ambapo kwa sasa Serikali imejikita zaidi kwenye maeneo mapya ya utalii zikiwemo hifadhi hizo.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti katika maeneo yanayoonekana kuwa na madini ili wananchi wanufaike?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini nijibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inaandaa mpango wa kufanya utafiti kwenye maeneo yanayoonekana kuwa na viashiria vya madini ikiwemo madini ya kimkakati. GST imepewa mamlaka ya kisheria kufanya utafiti wa madini nchini kwa lengo la kupata taarifa za kina za uwepo wa madini katika maeneo husika. Wizara ya Madini imeshaielekeza GST kuandaa mpango wa utafiti wa madini wa nchi kwenye maeneo ya kipaumbele ili kuombea bajeti ya kufanya kazi hiyo. Nashukuru.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuwapatia vyombo vya usafiri Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kufuatilia Mikopo inayotolewa na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa vyombo vya usafiri kwa ajili ya Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha kwa kuwawezesha usafiri na kutenga pesa kati ya 500,000 mpaka 5,000,000 kwa ajili ya ufatiliaji kama ilivyoelekezwa kwa mujibu wa kanuni ya ufatiliaji wa mikopo ya makundi haya yakiwemo ya wanawake, vijana na walemavu.

Mheshimiwa Spika, katika Mwezi Februari, 2023, Serikali iligawa pikipiki 916 kwa Watendaji wa Kata, pikipiki 85 kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii, pikipiki 5, 889 kwa Maafisa Ugani wa Kilimo na pikipiki 1,200 kwa Maafisa Ugani wa Mifugo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusisitiza kwamba utumiaji wa vyombo hivyo kwa pamoja ndiyo utatuletea tija katika kufikia maendeleo ya kufuatilia vikundi vyetu na misaada inayoendelea kupelekwa katika zile asilimia 10. Nashukuru. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kabla zahanati haijafunguliwa inawekewa vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 15.15 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye zahanati ambazo zimekamilika ambapo tayari Serikali imekwishatoa fedha shilingi bilioni 12.90.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 18.4 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye zahanati zote zinazoendelea kukamilishwa na itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya zahanati zinazoendelea kukamilishwa kwa kadri fedha zinavyopatikana.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA K.n.y MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kukamilisha ujenzi wa Shule katika Kijiji cha Izengabatogilwe, Kata ya Ugalla - Urambo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaqueline Andrea Kainja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 imepeleka Shilingi Milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika kitongoji cha Gimagi kwenye shule shikizi ya shule Mama ya Izengabatogile.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga Shilingi Milioni 220 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya madarasa ikiwemo ya shule katika Kijiji cha Izengabatogile, Kata ya Ugalla, Wilayani Urambo.
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Mahakama ya Wilaya ya Urambo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza mpango wa kuboresha majengo katika ngazi mbalimbali kwa kujenga majengo mapya na kukarabati baadhi ya majengo ya zamani. Aidha, katika mpango huu, jengo la Mahakama ya Wilaya ya Urambo limepangwa kufanyiwa ukarabati mkubwa mwaka wa fedha 2024/2025. Ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari kadri ya upatikanaji wa fedha. Kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2021/2022 jumla ya walimu wa Sekondari 7,799 na walimu 8,950 wa msingi waliajiriwa. Aidha, katika mwaka 2022/2023, walimu wa Sekondari 5,329 na walimu 7,801 wa Msingi wameajiriwa na kupangwa moja kwa moja katika shule kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uwiano wa idadi ya wanafunzi kwa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa walimu hao katika ufundishaji na ujifunzaji bora na kujenga nguvu kazi yenye maadili mema. Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaendelea kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari kulingana na mahitaji kwa shule zote nchini na uwezo wa kifedha wa Serikali. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREW aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga uzio kwenye Shule zote za Bweni za Wasichana Wilayani Urambo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa uzio kwenye shule za bweni za wasichana nchini kwa ajili ya usalama wa mali na wanafunzi zikiwemo shule za Halmashauri ya Wilaya ya Urambo. Aidha, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni ujenzi wa miundombinu ya msingi inayowezesha wanafunzi wote kupata fursa ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali itapeleka shilingi bilioni 2.4 katika Jimbo la Urambo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali yakiwemo madarasa 16, mabweni nane na matundu ya vyoo 20 katika shule mbili za sekondari mpya za kata katika Kata ya Nsenda Kijiji cha Mtakuja na Kata ya Ukandamoyo Kijiji cha Tumaini. Aidha, kwa mwaka 2024/2025 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 110 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu (two in one) ambayo itajengwa katika Kata ya Uyogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, itaendelea kutenga na kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari kulingana na vipaumbele vyake.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali kuwezesha upatikanaji wa vitabu Shule za Msingi ambazo zimeanza mtaala mpya wa Kingereza kuanzia darasa la kwanza?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, katika kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi kwa madarasa yaliyoanza kutumia mtaala ulioboreshwa yaani darasa la awali, darasa la kwanza na darasa la tatu. Serikali imechapa na kusambaza nakala 9,818,251 za mihtasari, vitabu vya kiada na kiongozi cha mwalimu kwa mchanganuo ufuatao:-

(i) Nakala 509,582 za mihtasari na mtaala ulioboreshwa wa elimu ya awali, msingi na sekondari;

(ii) Nakala 8,000,000 za vitabu vya kiada vya kimacho (maandishi ya kawaida) kwa darasa la awali, darasa la kwanza na darasa la tatu kwa shule zinazotumia Kiswahili na Kiingereza kama lugha za kufundishia;

(iii) Nakala 43,785 za vitabu vya maandishi yaliyokuzwa;

(iv) Nakala 6,990 za vitabu vya Breli; na

(v) Nakala 1,183,568 za viongozi vya mwalimu.

Mheshimiwa Spika, vitabu hivi vimesambazwa kwa uwiano kati ya 1:2 - 1:4 (kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili mpaka kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne), nakushukuru.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Viwanja vya Michezo nchini katika ngazi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la ujenzi wa miundombinu ya michezo ni la Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Michezo zikiwemo taasisi, mashirika, watu binafsi na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika kuhakikisha kuwa kila Wilaya inakuwa na viwanja vya michezo, hivi karibuni Serikali itazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga mafungu katika bajeti zao ili kutekeleza miradi ya ujenzi wa viwanja vya michezo kwa maeneo yao. Tayari kuna halmashauri zimeanza utekelezaji huu ambazo ni:-

Halmashauri za Wilaya za Kinondoni (Uwanja wa KMC), Bukoba Mjini (Uwanja wa Kaitaba), Nyamagana (Uwanja wa Nyamagana) na Namungo (Majaliwa Stadium). Aidha, Halmashauri ya Wang’ing’ombe inajenga Kijiji cha Michezo ambacho kitakapokamilika kitakuwa na viwanja vya michezo ya soka, volleyball, Netball na Basketball. Pia, Halmashauri ya Sengerema, Mkoani Geita imeandaa ‘Concept Design’ kwa ajili ya kituo cha michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali ipo kwenye ukarabati mkubwa wa viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa. Hata hivyo, Serikali inaendelea na ujenzi wa Uwanja wa Arusha (Arusha Stadium) na ukarabati wa viwanja vingine vitano vya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027. Hivyo basi, nitoe rai kwa halmashauri, wilaya na mikoa ambayo haijaguswa na miradi ya AFCON 2027 kuanza kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kujenga viwanja vya kisasa vya michezo ili pia wapate vyanzo vipya vya makusanyo ya maduhuli katika maeneo yao. Nashukuru. (Makofi)