Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khamis Hamza Khamis (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, sasa nichukue fursa hii, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa Mbingu na Ardhi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nichukue fursa hii tena kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako hili Tukufu kwa kuwa wametoa michango mizuri, michango ambayo kitaalam tunaita very constructive ideas, michango ambayo ni michango jengefu. Michango ambayo sisi tutaichukua tunakwenda kuifanyia kazi ili kuona namna ambavyo tunaboresha utoaji wa huduma au tunaboresha Wizara yetu au tunaboresha vyombo vyetu katika kuhudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo sasa nianze kutoa majibu ya baadhi ya michango ambayo Waheshimiwa wameichangia lakini pia wameulizia ndani yake wametaka kujua baadhi ya mambo.

Mheshimiwa Spika, kuna michango mbalimbali ambayo imetolewa, kiujumla ni kwamba kuna Kituo cha Polisi cha Ng’ambo Station Zanzibar kimezungumzwa hiki, kiukweli kituo hiki ni cha zamani maana binafsi ninafungua macho yangu kile kituo nakiona vile vile. Kama Serikali tunao wajibu wa kukifanyia maboresho lakini kwa wanaokifahamu kituo kile hatuwezi kukipanua kwasababu ni kituo ambacho kimezungukwa na barabara. Pande zote ukizitazama kimezungukwa na barabara. Kwa hiyo, kikubwa ambacho tunakifanya ni kwamba kama Serikali tunakwenda kukiboresha zaidi katika utoaji wa huduma ili kiweze kutoa huduma zaidi lakini sio kukitanua na kukijenga upya kwa mazingira kilipo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna hoja nyingine ilikuja hapa Mheshimiwa Omar Ali Omar alizungumzia suala la nyumba za Polisi Finya. Ni kweli nyumba zile nimewahi kufika, nimetembelea pale, nimeona hatua ambayo nyumba zile zimefikia na nimeona waliniambia idadi ya fedha ambazo zinatakiwa ili kumaliza nyumba zile.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee Serikali ilitoa maelekezo na tukalichukua lile jambo na tayari tumeshatoa maelekezo kunakohusika kwamba tuweze kupatiwa zile fedha ili tukamalize kituo kile. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na wasiwasi nyumba zile zitamalizwa na askari wa eneo lile na maeneo ya Jirani watapata mahali pazuri pa kuweza kukaa na familia zao.

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Maida Hamad naye ameeleza suala zima la upungufu wa wafanyakazi wa Jeshi la Polisi hasa katika kisiwa cha Pemba. Ni kweli upuingufu upo lakini kama ambavyo mara nyingi huwa nazungumza hasa nikisimama hapa huwa naelekeza kwamba upatikanaji wa ajira una some procedures lazima zifuatwe, sio kwamba tukurupuke tu tuajiri kwasababu tuna uhitaji, kuna mambo lazima tuyafuate, lazima tupate kibali cha kuajiri ambacho tunakiendea mbio sasa hivi kukipata, lazima tuangalie bajeti tuliyonayo, lazima tuangalie uhitaji wa hawa wanaotaka kuajiriwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kikubwa nimuambie Mheshimiwa ndani ya bajeti hii tunategemea kuajiri askari wasiopungua 400 ambao hao sasa wataenda ku-cover hizo nafasi. Mheshimiwa asiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine, limezungumzwa suala la OC, amesema kwamba OC ziende moja kwa moja vituoni. Utaratibu umeshawekwa wazi hasa kwenye PGO kwamba fungu alinalo mwenye Fungu ni IGP na RPC. Kwa hiyo, hilo la kusema kwamba ziende vituoni moja kwa moja hapa inabidi tuje tukae tena tujue namna ya kufanya lakini utaratibu uko wazi hivyo kwamba linatoka kwa IGP, linakuja RPC, RPC ana-distribute kwenye OCD’s na vituoni.

Mheshimiwa Spika, kingine Mheshimiwa Ravia Idarus Faina na yeye amezungumzia suala la je, ni lini sasa Serikali itajenga ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Zanzibar? Hili tuseme kwamba tunalichukua kwa umuhimu wa kipekee sana. Ni jambo ambalo tumeliona na limetugusa na tumeona sasa tuna haja ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa asiwe na wasiwasi na hilo, tunakwenda kujenga ofisi nzuri ya kisasa ambayo itakuwa ni Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri akienda atafikia pale, Naibu Waziri na shughuli nyingine za Kiwizara zitafanyika hapo. Hilo asiwe na wasiwasi.

Mheshimiwa Spika, lakini akaja na hoja ya PGO, akasema kuna baadhi ya vipengele vinaepukwa, kuna baadhi ya taratibu hazifuatwi, maeneo hayafuatwi. Ni vyema Mheshimiwa angejaribu kueleza yale maeneo ambayo anahisi kwamba hayakufuatwa na sisi tukajua namna ya kuyaweka sawa kwasababu ukituambia haifuatwi na wakati taratibu zipo, zinafuatwa zote tunakuwa hatujui tufanye nini lakini vizuri tungepata kujua yale maeneo ambayo bwana kwenye maeneo fulani na fulani hapa PGO imekengeuka kidogo haikufuatwa.

Mheshimiwa Spika, kingine kulikuwa kuna jambo la zile tunaita fire clubs. Hapa nataka niseme katika suala hili la zimamoto hatuwezi kuzima moto kwa uzoefu tu kwamba tunauzima moto lazima kuna mambo automatic tuelezane. Kwanza tuwaeleze wananchi kwamba wachukue tahadhari katika suala la ku-control majanga.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, sisi tuna wajibu wa kutoa elimu kwa jamii kitu ambacho tunakifanya mara kwa mara katika Jeshi letu la Zimamoto lakini cha tatu ambacho tunakifanya na tayari tumeshakifanya, hivi karibuni tulifanya makubaliano pale, tulisaini makubaliano baina ya Jeshi hili la Zimamoto na wale watu wa scout ili sasa waweze kutufikishia ujumbe hata mashuleni na maeneo mengine ili hata likitokeza tatizo au janga lolote la moto waweze kuli- save wakati Jeshi la Zimamoto wanakuja kuhami hilo.


Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika hili tumejipanga vizuri na tuwaambie tu wananchi kwamba tutaendeleza kutoa elimu kwasababu kitu kimoja kikubwa ambacho kitawafanya watu waweze ku-control haya majanga ni taaluma ambayo tuanenda kuwapa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna jambo jingine ambalo limeulizwa. Mheshimiwa Faina ameuliza suala zima la Ofisi ya NIDA Wilaya ya Kusini. Ofisi ipo! Tunachokiangalia sisi ni utoaji wa huduma. Hatuangalii kuwepo kwa ofisi kwasababu inawezekana Ofisi ikawa ipo kubwa ya ghorofa lakini huduma zikawa hazipatikani. Lakini sisi huduma inatolewa, ukienda Makunduchi Ofisi ipo pamoja na kwamba ni ndogo lakini huduma zinatolewa na wananchi wanapata huduma kwa wakati uliopangwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kikubwa niwaambie tu kwamba Ofisi zinatoa lakini kikubwa ambacho tumeshakubaliana kwamba tunakwenda kujenga Ofisi ya Kisasa ya NIDA, Serikali itajenga pale Kusini Makunduchi ili wananchi waweze kupata huduma za upatikanaji wa vitambulisho kwa muda ambao umekusudiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwaambie tu kwamba wasiwe na wasiwasi tumeshajipanga vizuri, mwanzoni ama mwishoni mwa mwezi wa tano tunategemea maeneo mengi ya Tanzania watu watakuwa tayari wameshapata vitambulisho vya NIDA.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna changamoto nyingine zimeelezwa za magari ya Polisi, wengine hawana, wengine zipo lakini mbovu, wengine hazina maringi, wengine hawana kabisa. Pia kumezungumzwa masuala ya upandishwaji vyeo, hayo yote ni mambo ambayo tuko nayo na tunaenda kuyafanyia kazi. Kikubwa ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono bajeti hii ili ipite ikatatue changamoto zinazokabili baadhi ya vyombo vyetu ambavyo mmeviorodhesha.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nami naomba niseme machache kutokana na yale ambayo yamezungumzwa, lakini zaidi nitajikita kwenye hili jambo la NEMC, jambo la Mazingira kwa ujumla na jambo la Muungano ambalo ni sehemu ya zao lililotuleta hapa baadhi yetu wengi.

Mheshimiwa Spika, mchangiaji mmoja nadhani wa mwanzo aligusia suala na NEMC na akasema kwamba NEMC wamekwenda, wameshafanya assessment na wameshatoa vibali, lakini bado wameweka zuio; na kibaya zaidi wameweka zuio kwenye baadhi ya miradi hasa miradi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nataka niseme katika hili kwamba NEMC ni taasisi ambayo inasimamiwa na inafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na taratibu zote. Kama tutafika wakati NEMC tutaona mahali ambapo tutakwenda kuparuhusu pafanyike, ikiwa skuli, ikiwa kiwanda, ikiwa mgodi, ikiwa chochote kikiwa kinaelekea kuharibu mazingira, kuchafua mazingira ambayo baadaye yanakwenda kuathiri maisha ya watu. Hapa ni lazima kwanza tujue namna ya kufanya kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Mheshimiwa Spika, hatuwezi tu kuruhusu kwa sababu tu watu wanataka wafanye, kwa sababu mwisho wa siku mazingira yale yakiathirika, athari na lawama zinakuja kwa Serikali, hasa NEMC kama ambavyo imezungumzwa. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hili jambo tuwaachie NEMC waendelee kufanya harakati zilizopo kwa mujibu wa taratibu. Tukifika wakati tukaona sasa usalama wa wananchi upo vizuri, tutaruhusu tuone namna ambavyo itawezekana.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala la fedha za miradi ya mazingira hasa kwa upande wa Zanzibar. Fedha zinakwenda; na kwa sababu tunasema, kinachofanyika tunakiona katika pande zote mbili za Muungano. Kwa maana Zanzibar tunapokwenda kukagua tunaona miradi; na Bara pia tunapokwenda kukagua tunaona miradi, na utaratibu wa fedha unatoka kwa mujibu wa taratibu zote.

Mheshimiwa Spika, hapa nataka tutoe wito. Changamoto iliyopo ni kwenye usimamizi na utekelezaji wa miradi hii. Ni kweli sisi ni sehemu ya wajibu wa kusimamia miradi hiyo, lakini tunao wenzetu tunaoshirikiana nao wakiwemo Halmashauri na wenzetu wa upande wa pili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hapa tunataka tutoe wito kwa wenzetu wote ambao tunashirikiana nao, kwa sababu suala la uhifadhi wa mazingira, tunashirikiana Serikali zote mbili. Kwa hiyo, Halmashauri wafanye wajibu wao na wengine wanaosimamia hili watekeleze wajibu wao ili nasi tujue namna ya kufanya katika suala hili.

Mheshimiwa Spika, pia kuna suala la changamoto ya Muungano. Sidhani kama tunaweza tukadumu kwenye Muungano kwa zaidi ya miaka 50, halafu ikawa changamoto ni nyingi kuliko mafanikio. Nikiwa naamini kwamba Muungano huu una mafanikio mengi sana kuliko changamoto, na kwa sababu changamoto nyingi au hizo ambazo inaitwa kero, nyingi tayari zimeshasawazishwa, zimeshatatuliwa. Zilizobakia zote, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, niwaambie Watanzania wote kwa ujumla, sasa hivi tupo kwenye harakati za kuweka vikao katika pande zote mbili za Muungano ili lengo na madhumuni, tuhakikishe kwamba changamoto zinazotatiza katika Muungano zinamalizika na zinatatulika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi tukasema tunaenda katika Muungano huu tusiwe na changamoto. Lazima tutakuwa nazo kwa sababu tunaohusika na tunaokubaliana ni binadamu, lakini tunapoona kuna changamoto na tukiona hii inakwenda kutatiza na kuliweka Taifa mahali pabaya, tunakaa, tunakutana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaambie Waheshimiwa kwamba, hata hizo changamoto ambazo bado tunazo, Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tayari tumeshakaa, tunaendelea kukaa na tutakaa kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto zote ambazo zinagusia katika Muungano, ili katika miaka tunayokwenda, tukarithishe vizazi vijavyo Muungano ambao hauna changamoto.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini pia nichukue fursa hii nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kwenye upande huu wa kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini zaidi katika suala zima la mazingira. Tumekuwa tukiona mara kwa mara amekuwa akienda katika Mikutano mbalimbali ya Kimataifa kuiwakilisha nchi yetu hasa kwenye suala zima la mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliamua nisimame hapa nizungumze baadhi ya mambo ambayo yamezungumzwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kwamba mengine yalikuwa ni ushauri, lakini bahati nzuri mengine wanahitaji wapate ufafanuzi kuona kwamba kama Serikali ni jitihada gani ambazo tumezichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na jambo hili ambalo limezungumzwa na Profesa Manya, suala la mitetemo na suala la changamoto za uchafuzi wa mazingira hasa kwenye masuala ya viwanda. Niseme tu kwamba sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, zipo jitihada mbalimbali ambazo tumezichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tumeshatoa maelekezo kwa upande wa makelele, tumekaa na nyumba za ibada, wenzetu ambao wengi wao wanakuwa wanapiga hayo makelele, lakini tumekaa na wamiliki wa baa, tumekaa na wamiliki wa maeneo na vitu vingine ambavyo kwa njia moja au nyingine wanasababisha hili suala zima la uwepo wa makelele yanayosababisha mpaka watu kushindwa kupata usingizi kama alivyosema katika nchi ya wastaarabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyozungumza baada ya sisi kutoa maelekezo, Maafisa wetu wa NEMC tayari wapo field wanafuatilia na kusimamia yale maelekezo ambayo kama Wizara tumeyatoa. Kwa hiyo, niwaambie tu Wahemishimiwa Wabunge hili jambo sasa tunakwenda kulikomesha kulifanyia kazi kama ambavyo wananchi wantaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa viwanda tayari tulishatoa maelekezo. Kwanza tulishawaelekeza wamiliki wote wa viwanda nchini wahakikishe kwamba wanatengeneza na kuweka mifumo rafiki ambayo itakuwa iko salama kwao na kwa wananchi, mifumo ambayo inatirisha maji. Kwa sababu ni kweli tulishuhudia baadhi ya viwanda wanatiririsha maji kwenye vyanzo vingine vya maji na maeneo mengine ya makazi ya wananchi, kitu ambacho kimekuwa kero kwa wananchi. Kwa hiyo, tumekwishatoa maelekezo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwahi pia kutoa maelekezo na tunaendelea kusimamia maelekezo yetu kuhusu suala zima la utoaji wa moshi na sumu nyingine katika viwanda hivi. Lengo na madhumuni ni wananchi wetu waweze kuishi katika maisha ya furaha zaidi kwa hiyo, niwambie tu Waheshimiwa Wabunge, suala la kero ya makelele, moshi, maji machafu na kero nyingine katika viwanda vyetu tumeshalifanyia kazi na utekelezaji umeanza na hivi tunavyozungumza vijana wetu wako field wanasimamia suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuja hapa hoja ya visiwa. Ni kweli niseme kwamba hii ni changamoto na niwambie tu kwamba kwamba tayari Serikali kupitia Ofisi ya Makamau wa Rais, tumeshaanza kujenga kuta kwenye baadhi ya maeneo. Tumeanza kule Kwesekwese Pemba, tumeanza kule Mikindani, Mtwara na niwambie tu wale wote ambao wana changamoto hizi, tutakuja tufanye utafiti lakini pia tutahakikisha kuwa tunatenga fedha kwa ajili ya kujenga hizo kuta. Kwa sababu athari za haya maji kuingia kwenye vipando, kuingia kwenye maeneo ya makazi imekuwa ni changamoto. Jambo la Nungwi tumeliona na maeneo mengine tumeyaona tunaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wao waendelee kuwa na Subira, Serikali tunarafuta fedha kwa ajili ya kujenga hizo kuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuja hapa vile vile hoja ya kwamba tuongeze fedha zaidi katika fungu la Serikali rather than kukaa na kutegemea kutoka kwa wafadhili. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge tu kwamba, miradi hii ina sehemu nyingi, sio kwamba tunategemea eti kutoka kwa wafadhili tu. Kuna miradi ambayo inatekekelezwa na NEMC ambayo ni Serikali, kuna miradi ambayo inatekelewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo ni Serikali. Sasa hilo fungu ambalo linatoka nje sio kwamba tunakwenda tu, lakini ni kutokanana makubaliano ya Kimataifa ambayo tunakubaliana wakati tunapokwenda kukaa katika vikao vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi ni lazima fedha hizi wao wazitoe kwa sababu asilimia kubwa ya uchafuzi wa mazingira, ukiangalia na ndio maana wanakubali kutoa fedha hizi kwa sababu ni wao ndio wanatuchafulia mazingira ya anga na mazingira mengine. Kwa hiyo, niwambie tu Waheshimiwa kwamba wazo hili tunalichukua tunakwenda kulifanyia kazi, tutajitahidi tuongeze fedha kwenye hili fungu la Serikali ili tuimarishe miradi ile ambapo tutahisi fedha kutoka kwa wafadhili hazitoshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuendelea tumepata pia hili jambo la kulipa kodi lile ambalo Waheshimiwa wanalalamika kwa upande wa Muungano. Nataka niwambie Waheshimiwa kwamba, kwanza nataka watu wafahamu kwamba Muungano huu ndio wengi wetu umetuleta hapa, sisi wengi wetu ni wanufaika wa Muungano huu. Wakati tunajibu maswali pale tulieleza kwamba kero hizi zilikuwa nyingi, lakini leo tumekwishafika kero 22, zimebakia kero nne, kero ambazo tayari timu zetu ziko katika vikao vya majadiliano ili kuhakikisha kwamba tunachanganua kero hizi. Sidhani kama Muungano huu unaweza ukadumu kwa zaidi ya miaka 50 halafu ukawa una changamoto nyingi rather than mafanikio. Kwa hiyo, wakati tunahesabu changamoto za Muungano huu, basi tuhesabu zaidi mafanikio ya Muungano huu. Wapo waliosema kwamba wengine wana asili ya pande zote mbili kwa sababu ya umuhimu wa Muungano huu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niungane na wenzangu na kwanza nichukue fursa hii nimshukuru Mungu kwa kuwa ametujalia tuko hapa, lakini pia nichukue fursa hii nami kwanza niunge hoja mkono kwa Taarifa za Kamati ambazo zimewasilishwa hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nichukue fursa hii niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri waliyoichangia, lakini nichukue fursa hii nimshukuru sana Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye maeneo mbalimbali, lakini hasa kwenye jambo la kuuendeleza muungano wetu, lakini katika jambo la kuendeleza kutunza, kuhifadhi mazingira yetu na kupambana dhidi ya athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumezungumzwa mambo mengi, lakini miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa ni jambo la hoja ya muungano ambalo kwa upande wa hoja hii Waheshimiwa Wajumbe wamepongeza sana kwa hatua kubwa iliyofikiwa, lakini vilevile kumegusiwa jambo la mazingira hasa kwenye jambo la biashara ya hewa ya ukaa. Nataka niwaambie Waheshimiwa pongezi ambazo wamezitoa, hasa kwenye tasnia ama kwenye eneo hili la muungano ni kwa sababu, kwanza ya juhudi kubwa ambayo Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan anaifanya katika kuendeleza kutuunganisha Watanzania na kuhakikisha kwamba, tunaendelea kuwa kitu kimoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja za muungano zilikuwa nyingi ama changamoto zilikuwa nyingi, lakini ndani ya kipindi chake Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan zaidi ya hoja 14 amezitatua na leo muungano wetu uko salama na unakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa zaidi katika kuendeleza timu ambayo imeundwa. Timu hii ama Kamati hii ya majadiliano ya hoja za muungano imekuwa inafanya kazi kubwa na ndio maana umefika wakati sasa imetolewa maelekezo kamati hii iwe inakutana ndani ya kipindi cha miezi mitatu; kila miezi mitatu ikutane ili lengo na madhumuni tusiendeleze kulea changamoto za muungano kwa muda mrefu, maana yake zikitokea, tukae tutatue muungano usonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ni busara za viongozi wetu Dkt. Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais, lakini Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano nao wanafanya kazi kubwa katika kuuboresha na kuutunza Muungano huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamezungumzwa jambo hapa la biashara ya hewa ukaa, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tupo tayari na tumeendelea kuchukua hatua mbalimbali. Moja, tumeshaanzisha tumefungua kituo maalum, kituo ambacho kinatoa taarifa zote sokoine pale, kituo ambacho kinatoa taarifa zote, lakini kituo ambacho kinaendeleza kufanya utafiti. Kituo ambacho kinaendelea kusaidia wawekezaji na watu wengine ambao wako interested katika kutaka kujua juu ya suala zima la biashara hii ya hewa ya ukaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kutoa elimu, tumeanza kwa Halmashauri, tumekwenda kwa Wakuu wa Mikoa, tumekwenda kwa Wakuu wa Wilaya, tumewapa Wabunge, wawakilishi na sasa tunataka tushuke kwa wananchi mmoja-mmoja, ili waielewe biashara hii ili lengo na madhumuni wananchi waweze kufanya biashara hii, lakini wao wapate kipato na maendeleo kupitia huduma za jamii yapatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tunaendelea kuendelea kuwashauri wananchi kuwaambia kwamba, sisi kwanza tuko tayari kushirikiana nao. Muwekezaji yeyote ambaye yuko interested na biashara hii na yuko tayari kufuata sheria na taratibu zilizowekwa kwa sababu, tulishaandaa muongozo na muongozo umeshatoka wa biashara ya hewa ya ukaa maana kule nyuma tulikuwa tunakwenda, lakini tukasema tuandae muongozo maalum ambao utawapa wananchi dira na muelekeo katika kuendeleza biashara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muongozo upo, wawekezaji waje, ili lengo na madhumuni wananchi wapate, lakini na huduma za jamii ziendelee, na tayari iko Mikoa ambayo tumeshaanza kutoa hizo huduma, hospitali zipo, elimu zipo, maji safi yapo na huduma nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, mimi niendelee tu kuunga mkono hoja hii, ahsante sana. (Makofi