Answers to Primary Questions by Hon. Khamis Hamza Khamis (100 total)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kutoa fedha za matumizi mengineyo (OC) kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya kama inavyotoa kwa Wakuu wa vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nami kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mahali hapa, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa ametujalia tumekutana hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nichukue fursa hii niwashukuru na kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Uzini kwa uzalendo na mapenzi makubwa ya kunichagua kwa kura nyingi nikawa Mbunge. Maana wamenitoa kutoka kwenye mavumbi, wamenitoa kwenye majalala, wamenileta kwenye viti, nimekaa na wafalme. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, aidha, nichukue fursa hii nimshukuru na kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, maana baada ya Mungu kuweka baraka, naye ikampendeza akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. (Makofi)
SPIKA: Sasa jibu swali Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kama Taasisi ya Serikali hupokea fedha za matumizi (OC) toka Wizara ya Fedha na huzigawa fedha hizo kupitia Kamati Maalumu ya Fedha (Tanzania Police Force Resources Committee), ambayo huzigawa fedha hizo kwenda kwa Makamanda wa Polisi wa Kanda Maalum, Mikoa na Vikosi; na hao ndiyo wenye mamlaka ya kupata OC kisheria.
Mheshimiwa Spika, jukumu la kugawa fedha kwenda kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya hufanywa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa husika kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila Wilaya, kama vile ukubwa wa wilaya, Idadi ya vyombo vya usafiri ilivyonavyo, ikama ya Askari na takwimu za matukio ya kihalifu yaliyopo. Ahsante.
MHE. JACKLINE K. ANDREA Aliuliza:-
Je, Serikali imeweka mpango gani wa elimu ya sheria ya usalama barabarani kwa madereva wa bodaboda ili waendeshe kwa kutii sheria na kuepusha ajali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jackline Kainja Andrew, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limekuwa likitoa elimu kuhusu Sheria ya Usalama Barabarani kwa madereva, bodaboda na watumiaji wengine wa barabara na vyombo vya moto kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani (The Road Traffic Act No.68/1973).
Mheshimiwa Spika, elimu hiyo hutolewa kwa kupitia Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, televisheni, radio, magazeti, vipeperushi mbalimbali, Maadhimisho ya Saba Saba na Nane Nane, matamasha mashuleni na kwenye vijiwe na maskani ya bodaboda. Aidha, katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Desemba, 2020 jumla ya vipindi 399 vya Elimu ya Usalama Barabarani vimerushwa hewani na kuoneshwa mubashara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na vituo 89 vya radio na televisheni. Pia elimu imetolewa kwa madereva wa bodaboda 638,275 na kwenye vijiwe vya bodaboda 7,760 nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, Wizara inashukuru sana wadau mbalimbali katika kutoa elimu hiyo ambayo ni TRA, PUMA, AAT, APEC, Future World Training College na Amend. Lengo ni kujenga ufahamu wa sheria na kuepusha ajali kwa madereva wa bodaboda na watumiaji wengine wa barabara. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi ya kukabidhi kwa wananchi wa Vijiji vya Msanda, Muungano, Songambele na Sikaungu shamba lililokuwa limechukuliwa na Jeshi la Magereza Mollo Sumbawanga lenye ukubwa wa ekari 495?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza na wananchi wa vijiji vilivyotajwa walikuwa na mgogoro siku za nyuma ambapo mgogoro huo ulimalizwa mwaka 2019 kwa Serikali kutoa eneo la ekari 1,800 kwa lengo la kumaliza mgogoro kama ilivyohitajika.
Mheshimiwa Spika, hitaji la ekari 495 ni dai jipya ambalo Wizara kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza na Ofisi ya Mkoa wa Rukwa, tunaendelea kulifanyia kazi. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE Aliuliza :-
Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Nchi ya Msumbiji kwa upande wa Kusini.
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Uhamiaji na cha Polisi kuhudumia maeneo hayo ya mpakani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada za ujenzi wa Kituo cha Polisi daraja “C” unaofanywa na Halmashauri ya Tunduru umefikia katika hatua ya lenta. Aidha, ujenzi wa Kituo cha Uhamiaji utategemea makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji kama taratibu za ujenzi wa Vituo vya Uhamiaji mipakani unavyotaka. Kwa sasa makubaliano hayo bado hayajafanyika.
MHE. AGNESTA L. KAIZA Aliuliza:-
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshaji wa kupandisha vyeo kwa Askari wa Jeshi la Polisi katika ngazi ya Wakaguzi Wasaidizi na kwa Wakaguzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi ni Taasisi ya Serikali ambayo mfumo wake wa upandishwaji wa vyeo huzingatia sheria na kanuni za utumishi. Askari, Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi hupandishwa vyeo pamoja na watendaji wengine wa Jeshi la Polisi kwa kuzingatia ikama na bajeti ya mwaka husika.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 mpaka 2018 jumla ya askari 2,354 walipandishwa vyeo kuwa Wakaguzi Wasaidizi na kwa kipindi cha kuanzia 2015 mpaka 2020 jumla ya Wakaguzi Wasaidizi 1,163 walipandishwa vyeo kuwa Wakaguzi wa Polisi. Serikali itaendelea kuwapandisha vyeo Askari Wakaguzi na Maofisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi kulingana na taratibu zilizoelezwa hapo awali. Ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA Aliuliza:-
(a) Je, Serikali inasemaje kuhusiana na ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa watoto nchini?
(b) Je, kwa nini Serikali haifanyi tafiti kujua sababu za kesi nyingi kushindwa kuwatia hatiani wabakaji na kuja na mpango mpya wa kudhibiti vitendo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum yote mawili kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wa Serikali kuwalinda wananchi wakiwemo watoto dhidi ya makosa ya ubakaji na udhalilishaji. Ili kupambana na vitendo hivi Serikali imekuwa ikichukua hatua kali ikiwemo kifungo cha miaka 30 jela kwa wanaojihusisha au kusaidia kufanyika kwa vitendo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti nyingi zimefanywa na asasi mbalimbali za Serikali na zisizokuwa za Kiserikali na zimebaini kwamba kuna sababu mbalimbali ambazo zinasababisha. Sababu hizi zikiwemo sababu za muhali lakini pia kuna sababu za kumalizana nje ya Mahakam ana wahanga kuchelewa kuripoti vituo vya polisi. Kwa kipindi cha mwaka 2020 jumla ya washtakiwa 1,183 walihukumiwa vifungo jela.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako tukufu naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kutoyafumbia macho matukio ya udhaliliishaji na ubakaji ikiwemo kutoa taarifa kwa vyombo vya dola vinavyohusika. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA K.n.y. MHE. KHATIB SAID HAJI Aliuliza:-
Je, Serikali inachukua hatua gani ya dharura kukabiliana na mrundikano mkubwa wa mahabusu katika magereza nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia nichukue fursa hii kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwa na imani na sisi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Jimbo la Konde kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba, nalijibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2021 idadi ya wafungwa na mahabusu nchini ilikuwa ni 33,473 kati ya hao waliohukumiwa ni 16,735 na mahabusu ni 16,738 huku uwezo wa magereza yetu nchini ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na kutatua changamoto hizo Serikali imechukua baadhi ya hatua nyingi ambazo tunaamini kwa njia moja ama nyingine zinakwenda kutatua ama kuondoa kabisa tatizo hili la mlundikano wa mahabusu katika magereza.
Kwanza Serikali imeamua ama inaendeleza ushirikishwaji wa vyombo vya haki jinai, lakini kingine kufanya mabadiliko ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2009, lakini pia ushirikishwaji wa Mahakama na Jeshi la Magereza katika kutumia mfumo wa TEHAMA (video conference), lakini kingine kufanya upanuzi na kujenga magereza mapya ya Wilaya ambazo hazikuwa na Magereza kama vile Chato na Ruangwa, lakini kingine utoaji wa dhamana kwa masharti nafuu, lakini pia kuanzishwa kwa mahakama zinazotembea (mobile court) kwa mashauri madogo madogo yanayotolewa uamuzi pasipo watuhumiwa kupelekwa magerezani. Aidha, kutoa elimu kwa raia ili, kutojihusisha na vitendo vya kihalifu, jambo ambalo linaweza kwa kiasi kikubwa likapunguza mlundikano wa mahabusu katika magereza. Ahsante. (Makofi)
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO Aliuliza:-
Jeshi la Polisi linashikilia pikipiki nyingi katika Vituo vya Polisi kwa muda mrefu.
(a) Je, Serikali haioni fedha nyingi zinapotea kwa pikipiki nyingi kuchakaa zikiwa katika Vituo vya Polisi na hivyo kuleta hasara kwa Taifa?
(b) Je, kwa nini Serikali isiunde Kamati Maalum kila baada ya miaka mitatu kupitia sababu zilizosababisha pikipiki hizo zishikiliwe kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, pikipiki ni mojawapo ya chombo cha moto kinachotumika kufanya biashara ikiwemo kusafirisha watu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kuna sababu tatu zinazopelekea kushikiliwa kwa pikipiki hizo kwenye Vituo vya Polisi:-
(i) Kundi la kwanza, ni zile pikipiki zilizokamatwa kwenye makosa ya jinai ambazo zimetumika kwenye kutenda makosa au zilizoibiwa toka kwa watu;
(ii) Kundi la pili ni zile pikipiki zilizokamatwa baada ya kutenda makosa ya usalama barabarani; na
(iii) Kundi la tatu ni zile pikipiki zilizookotwa na hazina wenyewe na kuhifadhiwa vituoni. Hivyo pikipiki hizi zipo vituoni kama vielelezo vya kesi na vielelezo ambavyo havina mwenyewe na kuwepo kwake kituoni ni kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mashauri yote yaliyopo Mahakamani yanayohusu vielelezo vilivyopo Vituo vya Polisi yamalizike kwa wakati ili mashauri hayo yasikae muda mrefu. Aidha, Pikipiki na vyombo vingine vya moto kuondolewa kwake vituoni kunategemea na amri ya Mahakama na maamuzi ya kesi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa tatizo hili si kubwa linahimilika, lakini iwapo tathmini itaonyesha kuongezeka ukubwa wa tatizo hili, basi Serikali ipo tayari kuunda Kamati Maalum kama ilivyoshauriwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika asante.
MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawapatia Vitambulisho vya NIDA wananchi wote waliojiandikisha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saada Monsour Hussein, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Serikali ni kuhakikisha watu wote waliosajiliwa na kupata namba za utambulisho wanazalishiwa na kugawiwa vitambulisho vya Taifa.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Agosti, 2021, Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kuzalisha na kugawa kwa wananchi jumla ya vitambulisho 8,397,524. Aidha, Mamlaka inaendelea na mpango kazi wa uzalishaji ambapo wananchi wote wenye sifa watazalishiwa na kugawiwa vitambulisho vyao ifikapo tarehe 31 Desemba, 2021. Nakushukuru.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati Kituo cha Polisi Bububu ambacho ni chakavu sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Jimbo la Bububu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi Bububu na tayari tathmini kwa ajili ya ukarabati imefanyika mwezi Mei, 2021 na fedha kiasi cha shilingi 33,172,200 zinahitajika kwa ajili ya kubadilisha paa, mfumo wa umeme, mfumo wa maji taka na maji safi, pamoja na kupaka rangi. Aidha, Serikali inatafuta fedha za ukarabati wa kituo hicho ikiwa ni pamoja na vituo na makazi ya askari ya maeneo mengine ambayo yanafanyiwa tathmini kwa ajili ya ukarabati. Ahsante.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA Aliuliza:-
(a) Je, ni lini mahabusu wataruhusiwa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali wakiwa Gerezani?
(b) Je, ni nini kauli ya Serikali katika kuwezesha Magereza kwa chakula kwa kuwa mkakati wa kila Gereza kujitegemea kwa chakula umeshindwa kutekelezeka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Songwe, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kifungu cha 78(1) cha Sheria ya Magereza, Sura 58 iliyorejewa Mwaka 2002, kimeeleza kuwa, pamoja na mahabusu kulazimika kufanya kazi za usafi kwenye bweni analoishi na usafi wa mwili wake, vyombo anavyotumia, nguo na samani anazotumia, pia anaweza kufanya kazi za uzalishaji kwa ridhaa yake. Kifungu hiki kinasomwa sambamba na Kanuni Na. 421 ya Kanuni za Kudumu za Magereza, Toleo la Nne la Mwaka 2003.
(b) Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango wa kujitosheleza kwa chakula Magerezani umeanza kwa magereza nane (8) ya Songwe, Kitai, Kitengule, Mollo, Pawaga, Arusha, Ushora na Ubena kwa lengo la kuzalisha kwa wingi na kusambaza chakula katika magereza mengine ambayo hayapo kwenye mpango. Uwezo wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa umeongezeka na kufikia 54% kwa mwaka 2020/2021 ikilinganishwa na 23% kwa mwaka 2019/2020.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni sita kwa ajili ya kuongeza mashamba na kuimarisha miundombinu na zana za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuyafikia malengo ya kujitosheleza kwa chakula.
MHE. OMAR ALI OMAR Aliuliza:-
Je ni lini Serikali itatoa ajira kwa Jeshi la Polisi, hasa ikizingatiwa kuwa haijatoa ajira tangu mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Jimbo la Wete kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuajiri na kuongeza idadi ya askari polisi hapa nchini kwani idadi yao hupungua kutokana na askari kustaafu, kufariki dunia, kufukuzwa kazi na wengine kuacha kazi, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka 2021/2022 imetoa kibali cha ajira kwa askari polisi 3,103 ambapo mchakato wake unaendelea hivi sasa. Nakushukuru.
MHE. ANNE K. MALECELA Aliuliza:-
Je, Serikali ilishawahi kulifanyia matengenezo yoyote muhimu gari lililotolewa na Mbunge kutoka kwa wafadhili toka Japan na kupelekwa Kituo cha Polisi Gonja katika Jimbo la Same Mashariki mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba ama napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge wa Same Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi cha Gonja kilichopo Wilaya ya Same kina gari namba PT 1988 Toyota Land Cruiser, ambalo lililetwa hapo mnamo mwaka 2015 ili kuhudumia wananchi. Mnamo tarehe 22 Juni, 2021 gari hilo lilisimama kufanya kazi ili kulinda usalama wa watumiaji na katika kulifanyia ukaguzi gari hilo lilikutwa lina ubovu wa mfumo wa usukani, mfumo wa break, clutch plate, mfumo wa umeme, ball joints na kuisha kwa matairi na bush. Aidha, tathmini ya matengenezo ya gari hilo ni shilingi 4,500,000 na fedha za matengenezo zimeshaombwa kutoka Makao Makuu ya Polisi. Ninakushukuru.
MHE. ABDUL- HAFAR IDRISSA JUMA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukifungua Kituo cha Polisi cha Betrasi kilichopo katika Jimbo la Mtoni Zanzibar ambacho kimefungwa kwa zaidi ya mwaka sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrisa Juma Mbunge wa Mtoni Zanzibar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi cha Betrasi ni kituo kidogo cha polisi ambacho kilijengwa mwaka 1994 na kilikuwa kinafanya kazi kwa masaa 12, kutwa na kilikuwa kinawahudumia wananchi wa eneo la Mtoni na kilijengwa na mdau wa ulinzi kwa wakati ule Ndugu Noushad Mohamed. Kituo hiki kilifungwa mwaka 2018 kutokana na uhaba wa askari. Wananchi wa eneo hilo pia wanapata huduma za polisi katika Kituo cha Polisi cha Bububu na pindi pakipatikana ongezeko la askari kituo hicho pamoja na vituo vingine vya aina hiyo vitafunguliwa ili kuhudumia wananchi. Nakushukuru.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya Zimamoto katika Mji Mdogo wa Katoro ili kupunguza hatari ya moto iwapo utatokea ikizingatiwa kwamba kuna ongezeko kubwa la wafanyabiashara katika Mji huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nami kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Magessa Tumaini, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa huduma za uzimaji moto na uokoaji katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Kutokana na ufinyu wa bajeti na upungufu wa rasilimali watu na vifaa, Mji Mdogo wa Katoro utaendelea kupata huduma za zimamoto na uokoaji kutoka katika Kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilichopo Geita Mjini mpaka hapo Jeshi litakapopata rasilimali za kutosha kuweza kuwa na Kituo katika Mji Mdogo wa Katoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kutoa Elimu ya Kinga na Tahadhari ya Moto katika Mji Mdogo wa Katoro ili kupunguza majanga ya moto yanayoweza kutokea katika mji huo. Ahsante.
MHE. MWANTUM DAU HAJI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya Kusini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Unguja:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kusini Unguja ulianza mwaka 2008 na gharama ya ujenzi wa mradi ni shilingi 225,000,000/= mpaka kukamilika kwake. Mpaka sasa ujenzi huu uko kwenye hatua ya msingi na unagharamiwa na Serikali kupitia bajeti ya maendeleo, na ujenzi umekwama kwasababu ya kukosekana kwa fedha za kutekeleza mradi wa ujenzi kutokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imo katika kufanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wadau wa ulinzi na usalama pamoja na wananchi, ili kuchangia na kukamilisha mradi huo, ili uweze kuwasaidia wananchi na shughuli za ulinzi na usalama ziweze kupatikana katika eneo hilo la Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja. Ahsante sana.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza:-
Je, ni lini warithi wa askari E.152 (Makame Haji Kheir) aliyefariki tangu Mwaka 2003 akiwa mtumishi wa Jeshi la Polisi Kituo cha Madema watapewa mafao yake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge Lengelenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi Makao Makuu Dodoma na Ofisi ya Polisi Kamisheni ya Polisi Zanzibar hazijapata kumbukumbu za maombi ya mafao wala nyaraka za mirathi kumhusu Askari tajwa hapo juu kutoka kwa msimamizi wa mirathi. Aidha, kwa sasa Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar limeshafanya jitihada ya kufanya mawasilinao na msimamizi wa mirathi ndugu Mlenge Haji Kheir ili kupata nyaraka zinazohusiana na maombi ya malipo ya mafao ya mirathi ya askari huyo ili ziweze kushughulikiwa. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA K.n.y. MHE. AUGUSTINE V. HOLLE aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu na Kata ya Makere:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu ilianzishwa mwaka 1996 kwa ajili ya kupokea wakimbizi kutoka nchi ya DRC. Wakati wa uanzishwaji wa kambi hiyo hakukuwa na mgogoro wa ardhi kwa sababu lilikuwa ni eneo lisilotumika. Aidha, pamoja na eneo la kambi, Serikali ilitenga eneo lingine la kambi kwa ajili ya wakimbizi iwapo eneo la awali litazidiwa.
Mheshimiwa Spika, kadiri ya muda ulivyoenda, wananchi walianza kuvamia eneo la akiba kwa lengo la kuwatumia wakimbizi kama vibarua katika shughuli za kilimo katika eneo hilo. Kwa kuzingatia maelezo hayo, ni wazi kuwa hakuna mgogoro wa ardhi baina ya Kambi ya Nyarugusu na Kata ya Makere, bali ni suala la uelewa ambapo wananchi wanaendelea kuelimishwa juu ya matumizi sahihi ya eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kumaliza tatizo la wakimbizi nchini kwa kuwarejesha wakimbizi makwao kwa kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa na nchi wanazotoka wakimbizi hao. Baada ya wakimbizi hao kuondoka maeneo yote ya kambi za wakimbizi yatarejeshwa Serikalini ili mamlaka zinazohusika ziweze kuyapangia matumizi stahiki.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JAFAR SANYA JUSSA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itavipatia Vituo vya Polisi vya Paje na Jambiani samani za Ofisi pamoja na magari kwa ajili ya doria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaffar Sanya Jussa, Mbunge wa Paje, kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya ukosefu wa samani katika Vituo mbalimbali vya Polisi nchini, ikiwa ni pamoja na Vituo vya Paje na Jambiani kutoka Mkoa wa Kusini Unguja na hii ni kutokana na ufinyu wa bajeti. Aidha, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau werevu wa ulinzi na usalama ili kuhakikisha Vituo vya Polisi vinapata samani za kisasa ili kuongeza ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kituo cha Paje wadau werevu wamechangia meza sita, viti kumi na nne na makabati manne. Pia katika Kituo cha Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja wamechangia meza tatu, viti sita na mabenchi mawili na wameahidi kuchangia ama kuendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatambua pia umuhimu wa vyombo vya usafiri katika kutekeleza majukumu ya Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi linatarajia kupata magari kwa ajili ya kutendea kazi na pindi yatakapofika yatatengwa kwenye maeneo yenye uhitaji wa magari na Vituo vya Paje na Jambiani vitazingatiwa zaidi. Nashukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH (K.n.y. MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Askari wapya Pamoja na kuleta vitendea kazi vya kutosha kwa Polisi Zanzibar inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa Askari kutokana na wengi kufikia umri wa kustaafu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar, Mbunge wa Malindi kutoka Zanzibar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mgawanyo wa rasilimali watu na vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi pamoja na mambo mengine huzingatia hali ya uhalifu wa eneo husika, jiografia ya eneo, idadi ya watu wanaohudumiwa na Jeshi la Polisi na ikama ya watumishi sambamba na upatikanaji wa vitendea kazi kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Spika, uwiano wa askari wa Jeshi la Polisi kwa Raia kimataifa ni askari mmoja kwa raia mia nne hamsini (1:450) hata hivyo kwa upande wa Zanzibar takwimu zinaonesha kuwa uwiano ni askari mmoja kwa raia mia tatu na tisini na mbili (1:392). Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 hii inamaanisha kuwa idadi ya Polisi Zanzibar ni wengi ukilinganisha na mahitaji katika kuhudumia wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vitendea kazi, napenda kukiri kuwa kama ilivyo maeneo mengine ya nchi, kuna uhaba wa vitendea kazi. Serikali itaendelea kuongeza ikama ya watumishi na vitendea kazi kadri nafasi za ajira na fedha zitakavyokuwa zinapatikana. Nakushukuru.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
(a) Je, ni matukio mangapi ya moto yametokea kwenye Shule na masoko katika kipindi cha miaka mitano iliyopita?
(b) Je, uchunguzi uliofanyika ulibaini vyanzo vya moto huo ni nini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2016 hadi 2020 ilipokea taarifa 175 za matukio ya moto kwenye Shule na taarifa 55 za matukio ya moto kwenye masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika chunguzi na tafiti mbalimbali za vyanzo vya matukio ya moto katika masoko na mashuleni, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilibaini vyanzo vya moto kuwa ni migogoro baina ya wanafunzi na menejimenti za shule, lakini matumizi ya umeme yasiyo sahihi, uhalifu, uchomaji wa makusudi (hujuma), hitilafu za umeme, uchakavu wa mifumo ya umeme na uzembe wa kuacha moto kwenye majiko ya mkaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kudhibiti matukio hayo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na mikakati ya kuzuia majanga ya moto kwa kufanya ukaguzi wa majengo na kutoa ushauri na mapendekezo ya kitaalam, yakiambatana na utoaji wa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto na pia kusisitiza kuwepo kwa vifaa vya awali vya kuzimia moto yaani (fire extinguishers) na vifaa vya kung’amua moto yaani (fire detectors) na uwepo wa Walinzi katika maeneo husika. Nakushukuru.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA K.n.y. MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Je, Serikali inachukua hatua gani kukabiliana na Waganga wapiga ramli chonganishi na Manabii wa uongo wanaodanganya na kutapeli wananchi kila siku?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatibu Said Haji Mbunge wa Jimbo le Konde kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ina jukumu la kulinda watu na mali zao na kuleta amani na utulivu miongoni mwa jamii ikiwa ni pamoja na kuzuia na kupambana na uhalifu wa aina yoyote ile ili usitokee. Katika kutekeleza majukumu hayo operesheni na misako ya mara kwa mara imekuwa ikifanyika katika kuwakamata waganga wapiga ramli chonganishi na manabii wa uongo wanaodanganya na kuwatapeli wananchi na kuwaletea hasara kubwa na mfarakano katika jamii kwa kuwachukulia hatua mbalimbali kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2020 jumla ya wapiga ramli chonganishi 57 walikamatwa na kufikishwa Mahakamani na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nichukue fursa hii kuwatahadharisha wananchi kujiepusha na waganga wapiga ramli chonganishi na manabii wa uwongo kwani matendo yao husababisha hasara, mfarakano na vifo katika jamii. Pia tuendelee kujitokeza bila uoga kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu vitendo hivyo viovu ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-
Je, serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya huduma ya kipolisi katika maeneo ya pembezoni mwa miji ikiwemo na mkoa wa Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine tena kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga Mbunge Wa Viti Maalum kutoka mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatekeleza mpango wa Askari Polisi kata /shehia katika kata zote 3956 na shehia 335 za Tanzania, ambapo hadi kufikia mwezi Februari, 2021 jumla ya askari 3963 wameshapangwa kwenye kata/shehia zikiwemo kata zilizopo pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine kwa lengo la kutoa huduma za kipolisi pembezoni kuliko na idadi kubwa ya watu na huduma ya vituo vya polisi ipo mbali, lengo ni kushirikiana na wananchi katika ulinzi na kupunguza uhalifu katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa baadhi ya maeneo huduma za polisi ziko mbali, Jeshi la Polisi kupitia mpango wa askari kata limekuwa likishirikiana na walinzi wa jadi ikiwemo sungusungu ili kupambana na kutatua uhalifu huo. Nakushukuru.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Jeshi la Polisi linao uwezo wa kukomesha tatizo sugu la ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo nchini:-
Je, ni kwa nini Serikali isiunde Kikosi Maalum cha kuwashughulikia watu wanaojihusisha na vitendo vya ubakaji na ulawiti?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kupambana na tatizo sugu la ubakaji na ulawiti Jeshi la Polisi limejiwekea mikakati thabiti inayohusisha ufuatiliaji wa vyanzo vya makosa na kuyatafutia ufumbuzi. Moja miongoni mwa mikakati hiyo ni kutoa elimu kwa kushirikisha jamii kupitia madawati ya unyanyasaji wa jinsia yaliyopo kwenye vituo vya polisi. Aidha, hutoa elimu ya mapambano dhidi ya makosa ya aina hii katika shule za msingi na sekondari, maadhimisho pia ya kitaifa na matamasha mbalimbali. Aidha, wale wote wanaobainika kutenda makosa hayo huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Mheshimwa Spika, kwa sasa mikakakati ya jeshi la polisi inatosheleza kukabiliana na tatizo hilo bila ya kuhitaji kuanzishwa kwa kikosi maalum kwani yote ya jinai ikiwemo udhalilishaji yana adhabu zake kisheria. Aidha, makosa haya yanatendeka miongoni mwa jamii hivyo, ni lazima jamii nzima ishirikiane kuyapinga na kuyakataa kwa kutoa taarifa vituo vya polisi na kuwa tayari kwenda kutoa ushahidi mahakamani, ili adhabu stahiki zitolewe kwa wahalifu hao, ahsante.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Jengo la Utawala la Central Police Njombe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Njombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jengo la ofisi zinazotumika kwa sasa kama jengo la polisi la utawala (Central Police) Mkoa wa Njombe lipo katika hifadhi ya barabara kuu iendayo Mkoa wa Ruvuma. Kwa sasa Jeshi la Polisi limeshaomba eneo toka Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa ajili ya kujenga ofisi za utawala na makazi ya askari na Halmashauri imeshatoa hekari 40 eneo la Lunyunyu.
Mheshimiwa Spika, tathmini kwa ajili ya kulipa fidia wananchi walioko eneo hilo imeshafanyika kupitia Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe na kiasi cha shilingi 322,000,000 zinahitajika kwa ajili ya malipo ya fidia na kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia hii ili ujenzi uanze mara moja. Nakushukuru.
MHE. LAZARO J. NYAMOGA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua hitaji la ofisi ya Makao Makuu ya Polisi Wilaya ya Kilolo na eneo linalohitajika kujengwa ofisi limeshapatikana na ni eneo la Luganga na lina ukubwa wa hekari 16. Zoezi la kufanya tathmini ili kulipa fidia wananchi limeshafanyika tangu mwezi Julai 2020 kupitia wataalam toka Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na kupata makadirio ya shilingi 110,092,554.00 zinazohitajika kulipa fidia wananchi hao.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi na mara baada ya kuwalipa wananchi fidia kwa mujibu wa sheria na taratibu ujenzi utaanza mara moja.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Je, Serikali inachukua hatua gani kutatua mgogoro wa mipaka kati ya Jeshi la Magereza na wananchi wa Kata ya Ukondamayo hususan Kijiji cha Tumaini, Wilayani Urambo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kukujulisha kwamba kwa sasa hakuna mgogoro wa ardhi kati ya Kata ya Ukondamoyo hususani Kijiji cha Tumaini na Gereza la Kilimo Urambo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli hapo awali ulikuwepo mgogoro baina ya vijiji vinne mojawapo Kijiji cha Tumaini. Mgogoro huo ulitatuliwa na kuhitimishwa mwaka 2000 kwa kushirikishwa viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Ardhi, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Urambo na Serikali ya vijiji vyote vinne vilivyokuwa na mgogoro kikiwemo Kijiji cha Tumaini.
Mheshimiwa Spika, hitimisho la mgogoro huo ni baada ya Jeshi la Magereza kukubali kutoa eneo la jumla ya ekari 3,218 kwa vijiji vilivyokuwa na mgogoro mojawapo Kijiji cha Tumaini kupewa ekari 505, Kijiji cha Imalamakoye ekari 195, Kijiji cha Nsendakanoge ekari 1,655 na Kijiji cha Itebulanda ekari 860.
Mheshimiwa Spika, aidha, hati ya makubaliano ya hitimisho la mgogoro ilisainiwa na viongozi wa vijiji vyote vinne vilivyokuwa na mgogoro kikiwemo Kijiji cha Tumaini na mawe ya mipaka (beacons) yakawekwa upya kwa utambulisho wa Namba Uv 66, Uv 69, Uv 107, Uv 35 na Uv 108, nakushukuru.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Je, Serikali inachukua hatua gani kutatua mgogoro wa mipaka kati ya Jeshi la Magereza na wananchi wa Kata ya Ukondamayo hususan Kijiji cha Tumaini, Wilayani Urambo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kukujulisha kwamba kwa sasa hakuna mgogoro wa ardhi kati ya Kata ya Ukondamoyo hususani Kijiji cha Tumaini na Gereza la Kilimo Urambo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli hapo awali ulikuwepo mgogoro baina ya vijiji vinne mojawapo Kijiji cha Tumaini. Mgogoro huo ulitatuliwa na kuhitimishwa mwaka 2000 kwa kushirikishwa viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Ardhi, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Urambo na Serikali ya vijiji vyote vinne vilivyokuwa na mgogoro kikiwemo Kijiji cha Tumaini.
Mheshimiwa Spika, hitimisho la mgogoro huo ni baada ya Jeshi la Magereza kukubali kutoa eneo la jumla ya ekari 3,218 kwa vijiji vilivyokuwa na mgogoro mojawapo Kijiji cha Tumaini kupewa ekari 505, Kijiji cha Imalamakoye ekari 195, Kijiji cha Nsendakanoge ekari 1,655 na Kijiji cha Itebulanda ekari 860.
Mheshimiwa Spika, aidha, hati ya makubaliano ya hitimisho la mgogoro ilisainiwa na viongozi wa vijiji vyote vinne vilivyokuwa na mgogoro kikiwemo Kijiji cha Tumaini na mawe ya mipaka (beacons) yakawekwa upya kwa utambulisho wa Namba Uv 66, Uv 69, Uv 107, Uv 35 na Uv 108, nakushukuru.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA K.n.y. MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi wa Kigoma ambao wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara kwa kuitwa wakimbizi nchini mwao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupita Idara ya Uhamiaji imepewa jukumu la kudhibiti, kusimamia na kufuatilia uingiaji, ukaaji na utokaji wa wageni hapa nchini kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 12 (1) cha Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 rejeo la mwaka 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza jukumu hilo, Idara ya Uhamiaji imekuwa ikifanya operesheni, doria na misako mbalimbali kwa lengo la kuwabaini wageni wanaoingia na kuishi nchini kinyume cha sheria na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya mahojiano na uchunguzi wa kina ili kujiridhisha juu ya uraia wa watuhumiwa wanaokamatwa wakati wa operesheni husika na kwamba Idara ya Uhamiaji katika kushughulikia masuala ya uraia huzingatia matakwa ya Sheria ya Uraia Sura ya 357 rejeo la mwaka 2002. Operesheni, doria na misako hufanyika kwa mikoa yote na siyo Mkoa wa Kigoma pekee. Nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-
Je ni kwa nini askari polisi wasiwekewe utaratibu wa kusamehewa kodi katika vifaa vya ujenzi na kupewa viwanja kwa bei elekezi ili wawe na moyo wa kulitumikia Taifa bila kujiingiza katika njia za udanganyifu kwa lengo la kujiandaa na maisha baada ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa utoaji wa msamaha wa kodi kwa bidhaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya ujenzi kwa askari wa Jeshi la Polisi ulikuwa unatekelezwa kupitia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), na kutokana na changamoto za kimuundo na mfumo uliosababisha uvujaji wa mapato na utozaji kodi usio na usawa, Serikali ilifanya marekebisho yaliyopelekea kufutwa kwa baadhi ya misamaha ya kodi ikiwemo ya vifaa vya ujenzi kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua kazi kubwa na nzuri katika kulitumikia Taifa letu inayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi, ilianzisha utaratibu mwingine wa kibajeti wa kutoa nyongeza ya posho maalum kwa kila Askari ili kufidia gharama za kodi pale wanapofanya manunuzi ya vifaa vya ujenzi pamoja na mahitaji yao mengine. Nakushukuru.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Jimbo la Kiwani ili kuepusha wananchi kufuata huduma za Polisi masafa marefu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdalla Rashid, Mbunge wa Kiwani kutoka Mkoa wa Kusini Pemba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua hitajio la Kituo cha Polisi eneo la Kiwani na kwa sasa wananchi wa Kiwani wanapata huduma ya polisi kutoka katika Kituo cha Polisi Kengeja ambacho kipo umbali wa kilometa tano tokea Kiwani Central.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa sehemu ya Kiwani hakuna eneo lililotengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkoani kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi na nyumba za makazi ya askari.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya pamoja na wananchi ili kutoa eneo kwa Jeshi la Polisi litakalotosha kwa mahitaji ya ujenzi wa Kituo cha Polisi pamoja na makazi ya askari, ili Jeshi la Polisi liweze kutoa huduma karibu na wananchi katika eneo hilo la Kiwani, nashukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi kwa kuwa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inaendelea kutekeleza mpango kazi wa kuzalisha vitambulisho, na inatarajiwa ifikapo Agosti, 2021 wananchi wote waliotambuliwa na kupewa namba za usajili watakuwa wamepatiwa vitambulisho. Aidha, mpango huu unalenga kuzalisha vitambulisho kwa awamu kwa kila wilaya, ambapo kwa kipindi cha kuanzia tarehe 14 Januari 2021 hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2021 Mamlaka imefanikiwa kuzalisha na kusambaza vitambulisho 7,148,971 katika wilaya 73 nchini. Tanzania bara wilaya 63 na Zanzibar wilaya 10, na kazi ya uzalishaji inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Mei, 2021 Mamlaka imefanikiwa kugawa namba za utambulisho kwa wananchi 11,737,021 Kutokana na mfumo wa NIDA kuunganishwa na mifumo mingine ya taasisi za Serikali na binafsi. Aidha, wananchi wanaendelea kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kama vile huduma za kifedha, kufungua biashara, kupata namba ya mlipa kodi (TIN), kupata hati za kusafiria, umilikishaji ardhi na kusajili laini za simu kwa kutumia namba za utambulisho wakati wakisubiri kupatiwa vitambulisho vyao vya taifa. Nakushukuru.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Je ni chombo gani kinasaidia abiria kupata haki yake pindi abiria anapopata ajali safarini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge Wa Viti Maalumu kutoka Iringa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu au watu wanaopata ajali au madhara kutokana na chombo cha moto ambacho fidia yake inasimamiwa na Sheria ya Bima wanapaswa kulipwa fidia ya madhara waliyoyapata ama kwa kuumia au kifo kutoka kwenye kampuni ya bima ambayo chombo hicho cha moto kimekatia bima yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ajali kutokea tukio hukaguliwa na Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani na wahanga wa ajali hupatiwa fomu ya matibabu. Taarifa ya ajali fomu hii hupelekwa ofisi za bima husika na kwa mmiliki wa chombo cha moto kilichopata ajali. Kisha shauri la ajali hupelekwa mahakamani na kesi ikimalizika fomu namba 115 hutolewa kuonyesha matokeo ya kesi (Final Case Report). Ndipo wahanga wa ajali au ndugu huchukua nyaraka za ramani ya tukio la ajali, fomu ya matibabu, fomu ya taarifa ya ajali, fomu ya matokeo ya kesi, fomu ya ukaguzi wa chombo kilichofanya ajali, taarifa ya uchunguzi wa marehemu, kama mhanga amefariki na nakala ya bima ya gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyaraka zote hizo hupelekwa kwenye kampuni ya bima ambayo chombo cha moto kilichohusika na ajali kimekatia bima yake na wahanga hufidiwa kutokana na ukubwa wa madhara waliyoyapata. Kwa ufupi Jeshi la Polisi linathibitisha kutokea kwa ajali, Mahakama inatafsiri sheria kuhusu tukio, Daktari anathibitisha madhara waliyopata wahanga na kampuni ya bima inalipa fidia. Ninakushukuru.
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR aliuliza: -
Je, ni kwa nini wananchi wa Tanzania Bara wanatozwa na polisi faini za papo kwa papo kwa kutotumia mashine za EFD wakati Polisi wa Zanzibar hawatozi faini za papo kwa papo kwa wananchi wasiotumia mashine hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar, Mbunge wa Jimbo la Malindi kutoka Mkoa wa Mjini Zanzibar kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, sheria zinazotawala sekta ya usafiri wa barabarani nchini zipo chini ya mamlaka mbili tofauti huku msimamizi wa sheria zake ni Jeshi la Polisi Tanzania. Kwa upande wa Tanzania Bara sheria inayosimamia masuala ya barabarani ni Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 ya mwaka 1973 iliyorejewa mwaka 2002 na kanuni zake, na kwa upande wa Tanzania Visiwani sheria inayosimamia masuala ya barabarani ni Sheria ya Usafiri Barabarani Sura ya 7 ya mwaka 2003 na kanuni zake.
Mheshimiwa Spika, sheria zote mbili zinatambua adhabu ya tozo ya papo kwa papo kwa Tanzania Bara kifungu kinachotumika ni cha 95 Sura ya 168 ya 1973 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na kanuni namba 30 ya mwaka 2015 na kwa Tanzania Visiwani kifungu kinachotumika ni cha 183 Sura ya 7 ya mwaka 2003 na kanuni namba 64 ya mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti makosa ya usalama barabarani ambayo yanasababisha ajali zinazoleta vifo, ulemavu, majeraha na uharibifu wa mali. Serikali kupitia Jeshi la Polisi linahimiza sheria na kanuni zilizowekwa zifuatwe kama zilivyoelezwa kwa mamlaka zote zinazosimamia usalama barabarani na usafiri wa barabarani ili kuzuia ajali barabarani zisitokee. Nakushukuru.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Mwanakwerekwe ambacho kiliwekwa jiwe la msingi mwaka 2008 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe kama ifuatavyo: -
Mheshimwa Naibu Spika, Mwanakwerekwe kuna Kituo cha Polisi cha Daraja “C” ambacho kinatumika hadi sasa na kinafanya kazi kwa saa ishirini na nne, na eneo hilo lilitolewa na Serikali baada ya kuhamisha Idara ya Maonyesho Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo la Magogoni Amani kwa Mabata ndiko kuna jengo la kituo kidogo cha polisi, ambacho kinajengwa kwa nguvu za wananchi na jiwe la msingi liliwekwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka 2008 na ujenzi wake umefikia kwenye hatua ya renta. Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatafuta fedha ili kumalizia ujenzi wa kituo hicho kiweze kuhudumia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu usalama wa Askari ambao wakati mwingine huvamiwa na kujeruhiwa pamoja na kuporwa silaha wakati wakiwa kazini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge Viti Maalum kutoka Zanzibar, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Askari wa Jeshi la Polisi wapo imara katika kutimiza majukumu ya kazi zao za kila siku na wamepata mafunzo mbalimbali yakiwemo mafunzo ya mbinu za medani, matumizi ya silaha na mafunzo ya kujihami. Pia katika utendaji wa kazi wao hufuata utaratibu wa kujilinda na kulinda wengine, ila mazingira na maeneo ya utendaji kazi husababisha changamoto mbalimbali kutokea kama hizo za kuvamiwa na kujeruhiwa. Mara zote Jeshi la Polisi hudhibiti hali hiyo na kushughulikia kwa haraka matukio ya namna hiyo na kuimarisha amani na utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaweka Kituo cha Uhamiaji katika eneo la Chipingo ili kuondokana na vivuko bubu vilivyopo Mpakani mwa Tanzania na Msumbiji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Chipingo ni kipenyo kilichopo Wilaya ya Masasi katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji kandokando ya Mto Ruvuma umbali wa Kilomita 86 kutoka Masasi Mjini. Kwa upande wa Msumbiji hakuna ofisi za Uhamiaji wala huduma za Uhamiaji bali kuna walinzi wa mpaka wa nchi hiyo.
Mheshimiwa Spika, ufunguaji wa vituo vya mipakani hutegemea makubaliano baina ya nchi zinazochangia mpaka. Kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Msumbiji, kumebaki kituo kimoja cha mpakani kinachofanya kazi cha Mtambaswala kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ghasia na hali tete ya usalama.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelezo hayo, Serikali inaendelea kufuatilia hali ya usalama katika mpaka huo na hali itakapotengemaa mawasiliano na Msumbiji yatafanyika ili kufungua vituo zaidi kuhudumia wananchi wanaotumia mpaka huo. Ninakushukuru.
MHE. RAVIA IDARUS FAINA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Ofisi za NIDA katika Wilaya ya Kusini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ravia Idarus Faina, Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na Ofisi za Wilaya kwa ajili ya kuwafikishia wananchi huduma za usajili na utambuzi wa vitambulisho karibu na maeneo yao. Katika kutekeleza mpango huo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kufungua ofisi 150 katika Wilaya zote za Tanzania Bara na Visiwani.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya NIDA katika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja itajengwa katika Mwaka wa Fedha 2022/2023. Nakushukuru.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali imepanga kuanza kukarabati majengo ya Kituo cha Polisi Makunduchi.?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi Makunduchi pamoja na nyumba za makazi ya Askari ambayo ni jengo la ghorofa moja linaloishi familia nne na mahanga mawili ya familia kumi na sita. Tathmini kwa ajili ya ukarabati imeshafanyika na jumla ya Shilingi 110,093,400 zinahitajika. Ukarabati huo ni wa kubadilisha paa, dari, mfumo wa maji safi na taka pamoja na kupaka rangi. Jeshi la Polisi linatafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo ikiwa ni pamoja na majengo mengine ya vituo na makazi ya askari yaliyokwisha fanyiwa tathmini. Nakushukuru.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Vituo vya Polisi vilivyopo katika Kata za Kilema, Kirua Vunjo, Kahe na Marangu katika Jimbo la Vunjo vinapewa usafiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhitaji mkubwa wa magari katika vituo vya Polisi vilivyo katika Jimbo la Vunjo ambavyo ni Kilema, Kiruavunjo, Kahe na Marangu kama vyanzo muhimu katika kutendea kazi. Kwa kupitia mkataba wake wa kampuni ya Ashok Leyland ya nchini India, Jeshi la Polisi linategemea kupokea magari 369 na pindi magari hayo yatakapofika kipaumbele kitatolewa kwa vituo vya polisi vyenye uhitaji mkubwa ikiwemo kituo ama vituo vilivyo katika Jimbo la Vunjo. Nakushukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani ya kupunguza au kuondosha kabisa wizi wa mazao ya kilimo na mifugo katika maeneo ya Unguja na Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi nchini ndilo lenye jukumu la kulinda maisha na mali za wananchi na linatambua suala la uhalifu na wizi wa mifugo na wizi wa mazao ya kilimo unaosumbua wananchi wa Zanzibar, katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Septemba 2021 jumla ya matukio 72 ya wizi wa mifugo na 85 ya wizi wa mazao umeripotiwa katika vituo vya Polisi. Watuhumiwa 48 wa wizi wa mifugo na 52 wa wizi mazao wamekamatwa na kesi 22 za wizi wa mifugo na 36 za wizi wa mazao zinaendelea mahakamani na ziko kwenye hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuanzisha na kushiriki kwenye vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuzuia uhalifu na Jeshi la Polisi litaendelea kufanya doria kwenye maeneo yote ili kudhibiti na kutokomeza uhalifu hapa nchini. Nakushukuru.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kutenganisha Mahabusu/Magereza ya Watoto na Watu wazima ili kuwalinda Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono vinavyoweza kujitokeza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kulinda haki ya mtoto, Serikali ilitunga Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 ambayo inakataza kifungo kwa watoto na kuweka mahabusu magerezani na iwapo italazimu kuwekwa mahabusu sharti awe chini ya uangalizi wa Kamishna wa Ustawi wa Jamii au mahabusu za nyumbani au chini ya uangalizi wa taasisi yeyote itakayotamkwa katika amri ya Mahakama.
Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Jeshi la Magereza za Mwaka 2003 Toleo la 4, chini ya Kanuni 488 zimeweka utaratibu mzuri wa kuwatenga wafungwa na mahabusu katika sehemu maalum na vyumba maalum kwa kuzingatia umri ambapo wafungwa na mahabusu watoto hutengwa katika mabweni yao maalum pasipo kuchanganywa na wakubwa.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali inalo Gereza la Wami ambalo ni maalum kwa watoto ama vijana waliokatika ukinzani wa sheria na kuhukumiwa vifungo ambavyo huhamishiwa huko na kutumikia vifungo vyao wakiwa peke yao kama vijana bila ya kufungwa na watu wazima.
Mheshimiwa Spika, aidha Serikali inaendelea kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kingono na ukatili mwingine na kusimamia ipasavyo Sheria ya Watoto na Sheria zingine nchini zinazotoa ulinzi kwa watoto. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -
Je, Serikali imefikia hatua gani katika kutekeleza amri ya Mahakama ya kuwalipa fidia Wanakijiji wanaozunguka katika eneo la Gereza la Namajani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Napenda Kujibu Swali La Mheshimiwa David Cecil Mwambe Mbunge wa Jimbo la Ndanda lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwepo na mgogoro wa ardhi baina ya Gereza la Namajani na wanakijiji wa Kijiji cha Ngalole. Mgogoro huo ulitatuliwa na Mahakama kwa kuamuru Jeshi la Magereza kulipa fidia ya shilingi bilioni 2.4 kwa eneo la ukubwa wa ekari 2,064 lililokuwa na mgogoro.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza amri ya Mahakama ya kulipa fidia kwa wanakijiji wanaozunguka eneo la Gereza Namajani, Serikali kwa nia thabiti tayari imefanya utambuzi wa Wanakijiji wanaostahili kulipwa fidia kama hatua za awali na hivi sasa inaendelea na mchakato wa upatikanaji wa fedha za kulipa fidia hiyo na pindi fedha itakapopatikana italipwa haraka kwa wananchi hao.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Ukatili kwa watoto umekithiri nchini kama vile ubakaji, ulawiti, kuchomwa moto na mimba za utotoni.
(a) Je ni watoto wangapi wamefanyiwa ukatili huo kwa jinsia zao wa kike na wa kiume?
(b) Je kuna takwimu halisi ya hatua zilizo chukuliwa na Serikali dhidi ya matukio hayo nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko Mbunge Viti Maalum lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuanzia Januari hadi Septemba 2021 takwimu ya vitendo vya ukatili kwa watoto vilivyoripotiwa Vituo vya Polisi inaonyesha jumla ya watoto 6,168 wamefanyiwa ukatili na kati yao wanawake 5,287 na wanaume 881, waliobakwa ni 3,524, waliolawitiwa ni 637 kati yao wanaume 567 na wanawake 70, waliochomwa moto ni 130 kati yao wanaume 33 na wanawake 97, waliopata mimba ni 1,877.
Mheshimiwa Spika, kesi na watuhumiwa waliokamatwa na kufikishwa Mahakamani ni 3,800, kesi zilizo chini ya upelelezi ni 2,368 na kesi zilizohukumiwa ni 88 na nyingine ziko kwenye hatua mbalimbali Mahakamani. Nakushukuru.
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa wakulima wa mbogamboga ikiwemo pamoja na hatua za kuchukua ili kulinda mazingira katika Bonde la Mto Msimbazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imebaini uharibifu wa mazingira ya Mto Msimbazi unaofanywa na wananchi wanapofanya shughuli si za kilimo tu bali pia uchimbaji wa mchanga pamoja na umwagaji maji machafu kwenye Bonde la Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004, katika kuhakikisha kwamba wakulima wa mbogamboga pamoja na wadau wengine hawaharibu mazingira ya Mto Msimbazi, Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa programu maalum za kuelimisha na kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya mwongozo wa mita 60 kwa lengo la kunusuru mazingira ya vyanzo vya maji ikiwemo Mto Msimbazi.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rasi kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeelimisha watendaji wa Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha wananchi wanaofanya shughuli za kimaendeleo kwenye Bonde la Mto Msimbazi kuzingatia kanuni na miongozo ya hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia mabalozi wa mazingira imeanza utekelezaji wa kampeni kabambe ya hifadhi na usafi wa mazingira ambapo suala la hifadhi ya vyanzo vya maji ni moja ya eneo la kipaumbele katika utekelezaji wa kampeni hiyo. Nakushukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha usajili wa Taasisi ya NEMC katika Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Green Climate Fund (GCF) ili kuipatia nchi fursa za fedha za mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Donge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ni Ofisi kiungo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi Kitaifa ililiteua Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili liweze kuanza mchakato wa kupata Ithibati na kuwa mratibu wa fedha za Mfuko wa GCF.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Mei, 2021, NEMC iliwasilisha maombi rasmi kulingana na taratibu na baada ya GCF kujiridhisha mwezi Julai, 2021 walitoa invoice kwa ajili ya kulipa ada ya kufanyiwa Ithibati. Ada hiyo imelipwa mwezi Agosti, 2021 na hivi sasa GCF kwa barua ya tarehe 10 Januari, 2022 wameiarifu NEMC kwamba maombi yao yanafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kwa sasa suala hili liko GCF, naomba tuwe na subira wakati GCF wanaendelea na taratibu zao za mapitio. Aidha, nitoe wito kwa taasisi zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuata taratibu ili ziweze kupata ithibati kwenye Mfuko huo wa Green Climate Fund. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuunda Kikosi Kazi kuratibu Mikataba ya mazingira na mabadiliko ya Tabianchi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Kusini Pemba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa mikataba mbalimbali ya Kimataifa ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira ambayo inaratibiwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, utaratibu unaotumika katika kuratibu masuala ya mikataba ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wa kushirikiana katika majadiliano ya pamoja na kushiriki katika mikutano ya Kimataifa na utekelezaji wa Mikataba hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutekeleza program na miradi mbalimbali ya hifadhi na usimamizi wa mazingira inayotekelezwa chini ya mikataba husika.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -
Je, Serikali ina mikakati gani kuelimisha wananchi wanaozunguka Hifadhi za Misitu kuhusu biashara ya uuzaji/utunzaji wa hewa ukaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Maziringira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa Watanzania na Serikali inanufaika na biashara ya hewa ukaa. Serikali Kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara za kisekta pamoja na wadau inaandaa mwongozo na kanuni za usimamizi wa biashara ya hewa ukaa ambazo zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2022. Mwongozo na kanuni hizo zitaonesha namna ya utaratibu na kusimamia biashara hiyo ikiwemo mgawanyo wa manufaa kwa wadau watakaohusika katika mnyororo wa biashara ya hewa ukaa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, baada ya kukamilika kwa mwongozo na kanuni, Serikali imejipanga kuendelea kutoa elimu kuhusu biashara ya hewa ukaa kwa wadau mbalimbali wakiwemo wananchi ambao ni sehemu kubwa ya biashara hiyo inayofanyika katika maeneo yao. Nakushukuru.
MHE. REGINA N. QWARAY K.n.y. MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti wa kujua sababu za kusambaa kwa maji ya Ziwa Bassuto na kuhama kwa samaki kwenye Ziwa Eyasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujiibu swali la Mheshimiwa Samweli Hhayuma, Mbunge wa Hanang kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeona hakuna haja ya kufanya utafiti wakujua sababu ya kusambaa kwa maji na kuhama kwa samaki ziwa Bassuto. Sababu kuu ni kujaa maji wakati wa mvua nyingi, ziwa hilo ni dogo halina uwezo wa kuhifadhi maji mengi yanayosababishwa na mvua nyingi. Aidha, maji hayo hutawanyika na kuingia Ziwa Eyasi na kwa kuwa Ziwa Bassuto lina viumbe mbalimbali ikiwemo samaki, maji hayo yanapoingia kwenye Ziwa Eyasi huingiza na viumbe mbalimbali wanaoishi kwenye Ziwa Bassuto ikiwemo samaki. Hali hii inasababisha wananchi wanaotegemea samaki wa Ziwa Bassuto inawabidi kupata samaki hao kwenye Ziwa Eyasi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa viongozi wa Wilaya ya Hanang kuendelea kuhamasisha wananchi kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo Maziwa ya Bassuto na Ziwa Eyasi.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, kuna Mkakati gani wa kukabiliana na mafuriko katika Mto Mbezi yanayosababisha uharibifu wa miundombinu ya shule na makazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazotokana na mafuriko katika mito yetu nchini ukiwemo Mto Mbezi. Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali imeandaa Mwongozo wa usafishaji mchanga, tope na taka ngumu kwenye mito na mabonde katika Mkoa wa Dar es Salaam wa Mwaka 2021. Mwongozo huu unalengo la kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kusafisha tope na mchanga kwenye mito na mabonde ili kuruhusu uwepo wa mtiririko mzuri wa maji kuelekea baharini ili kuepuka athari za mafuriko.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kumhakikishia Mbunge kuwa, itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Mwongozo ili kutatua changamoto ya mafuriko katika mito na mabonde yaliyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam ili kukabiliana na madhara ya mafuriko na kuhakikisha miundombinu ya shule na makazi ya watu yanaendelea kuwa salama. Nakushukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -
Je, vikao vinavyopokea na kujadili changamoto za Muungano bado vipo na lini vilikaa mara ya mwisho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa kuwa vikao vya kupokea na kujadili changamoto za Muungano bado vipo na vitaendelea kuwepo kutokana na umuhimu wake kwa mustakabali wa Muungano wetu.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kulitaarifu Bunge kuwa, kwa mwaka 2021/2022 vikao hivyo vilifanyika kwa mujibu wa mwongozo huo ambapo kikao cha Kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya kushughulikia Masuala ya Muungano kilifanyika Tarehe 24 Agosti, 2021. Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
MHE. HASSAN SADIKI SIMAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya ucheleweshwaji wa fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo upande wa Tanzania Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Hassan Sadiki Simai Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua jitihada kuhakikisha kuwa fedha za Mfumo wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo zinawasilishwa kwenye majimbo ya Zanzibar kwa wakati. Mtiririko wa uwasilishwaji wa fedha hizo umekuwa wa kuridhisha. Kwa mwaka 2022/2023 shilingi bilioni 1,400,000,000 zimepelekwa Zanzibar mwezi Septemba, 2022. Aidha, fedha za mwaka 2021/2022 zilipelekwa Zanzibar mwezi Oktoba, 2021. Nakushukuru.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaviwezesha vikundi vya uhifadhi mazingira Vijiji vya Chwaka, Kiwani, Jundamiti, Mwambe, Nanguji na Kendwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kiwani. kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeshachukua hatua za kuvijengea uwezo vikundi vyote vilivyotajwa ili viweze kukua na kujiendesha vyenyewe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kuvipatia mafunzo ya awali yanayohusu taratibu za uendeshaji na uendelezaji wa vikundi vya ushirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali kupitia Idara ya Vyama vya Ushirika, Zanzibar imepanga kutoa mafunzo kwa Baraza la Wanaushirika la Wilaya ya Mkoani katika robo ya pili ya mwaka huu wa fedha (Oktoba – Disemba 2022).
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira kwa vikundi vya mazingira pamoja na kuwapatia tunzo ya mazingira na vifaa vya usafi kwa vikundi vinavyofanya vizuri katika uhifadhi wa mazingira, Unguja na Pemba.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -
Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na uharibifu unaotokana na ukataji mikoko na uvunaji wa matumbawe ili kuvinusuru visiwa visitoweke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto iliyoainishwa na Mheshimiwa Mbunge Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimekuwa zikichukua juhudi mbalimbali za kisera, kisheria pamoja na kuandaa miongozo mbalimbali ya utunzaji wa mazingira ya baharini ili kuhakikisha uharibifu wa mazingira ya bahari unadhibitiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa juhudi hizo ni kama zifuatazo: -
Kwanza, kujenga uelewa kwa wanajamii juu ya utunzaji wa mazingira na rasilimali za bahari ikiwemo uhifadhi wa mikoko na matumbawe.
Pili, upandaji wa mikoko na matumbawe katika maeneo yaliyoathirika kwa kutumia njia mbalimbali endelevu na za kitaalamu. Kwa mfano upandaji wa hekta Saba za mikoko Unguja na hekta 10 Pemba kwa mwaka 2020 – 2021 pamoja na kuweka matumbawe bandia 90 Unguja na Pemba.
Jambo lingine ni ushirikishwaji wa jamii katika kusimamia maeneo ya mikoko na matumbawe ikiwemo kuanzisha hifadhi ndogondogo za kijamii katika maeneo ya Kukuu, Fundo, Makoongwe kwa Kisiwa cha Pemba na maeneo ya Mtende, Tumbatu na Kizimkazi kwa upande wa Kisiwa cha Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru wananchi wa Manispaa ya Mtwara dhidi ya vumbi la makaa ya mawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshachukua jitihada za kuweka miundombinu ya kupunguza vumbi la makaa ya mawe ili kuwanusuru wananchi. Tayari Mamlaka ya Bandari Tanzania imefunga mfumo maalum wa dust suppression system unaotumia maji kupunguza vumbi. Pia, limetengwa eneo maalum kwa ajili ya kujenga conveyor belt itakayotumika kupakia makaa ya mawe katika meli. Aidha limetengwa eneo maalum nje ya mji takribani kilometa 34 katika Kijiji cha Kisiwa Mgwao kutoka Mtwara Mjini kwa ajili ya kuhifadhi mizigo ya namna hiyo. Hatua hii itasaidia kupunguza, kusambaa kwa vumbi katika mazingira.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia NEMC, kwa kushirikiana na Manispaa ya Mtwara na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kwa pamoja tunaendelea kufuatilia na kusimamia usafirishaji wa uhifadhi wa mazingira katika maeneo hayo, nakushukuru. (Makofi)
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN aliuliza: -
Je, ni kwa kiasi gani Taasisi za Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinashirikiana katika shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS,, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Haroub Suleiman, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Taasisi za SMT na SMZ zina ushirikiano wa kuridhisha katika shughuli za kiuchumi ambapo kupitia miradi na program mbalimbali, taasisi zetu za SMT na SMZ zimekuwa zikishirikiana katika shughuli za kiuchumi hasa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Mzunguko wa Pili, mradi wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga; mradi wa udhibiti uvuvi na maendeleo shirikishi Kusini Magharibi ya Bahari ya Hindi; mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini; Mkakati wa Kudhibiti Sumu Kuvu Tanzania; na Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru (Makofi)
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuanzisha mfuko wa mabadiliko ya tabianchi kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya Tabianchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge na mtumishi wa wananchi wa Jimbo la Donge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa vyanzo vya fedha vya uhakika ili kuimarisha jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kufuatia kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021, Serikali kwa sasa inafanya mapitio ya Sheria ya Mazingira, Sura ya 191 ikiwemo taratibu za kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira. Mfuko huu ukianzishwa, pamoja na mambo mengine utazingatia ufadhili wa shughuli za mabadiliko ya tabianchi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI K. n. y. MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuingia kwenye biashara ya Gesi Joto (Carbon Trading)?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, biashara ya gesijoto ilianzishwa chini ya Mkataba wa Kyoto unaozibana nchi zilizoendelea kutekeleza miradi ya kupunguza uzalishashaji wa gesijoto (Clean Development Mechanism – CDM) ili kusaidia nchi zinazoendelea kuleta maendeleo endelevu bila kuchafua mazingira.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaingia na inanufaika na biashara ya hewa ukaa, Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Mwongozo wa Taifa wa Biashara ya Hewa Ukaa kwa mwaka 2016. Tanzania inayo miradi mitatu ya biashara ya gesijoto inayotekelezwa nchini. Hadi sasa jumla ya tani 900,000 za gesijoto zimeshauzwa kupitia miradi ya uzingatiaji wa kupunguza gesijoto inayotekelezwa nchini.
Mheshimiwa Spika, aidha, miradi minne ya biashara ya soko hiari ya gesijoto imeelekezwa nchini tangu mwaka 2009 na jumla ya tani 1,456,600 za gesijoto zimepunguzwa na kuuzwa kupitia utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais inafanya mapitio Mwongozo wa Taifa wa Biashara ya Hewa ya Ukaa ili kuwezesha taifa na wananchi wake kushiriki kikamilifu na kunufaika na biashara hii. Aidha, katika kuboresha ushiriki, Wizara ya Maliasili na Utalii inaandaa mwongozo maalum wa usimamizi wa misitu ambayo itashiriki biashara ya gesijto nchini. Ninakushukuru.
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -
Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa kuzuia mafuriko katika Mto Msimbazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Lambert Kaizer, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mradi huu kwa sasa uko katika hatua za kufanya uhakiki wa taarifa na mali za wananchi wanaopaswa kupokea fidia na kusainiwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia. Mradi huo unategemewa kuanza rasmi mwezi Julai, 2022.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira inaamini kuwa utekelezaji wa mradi huu utawezesha kuondoa kabisa tatizo la mafuriko katika Bonde la Mto Msimbazi.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kurudisha uoto wa asili wa milima ya Iringa ili kuendelea kutunza mazingira yake na vyanzo vya maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Maiznigra, naomba Kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imebaini kuwepo kwa uharibifu wa mazingira unaotokana na uvamizi wa wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye milima na vyanzo vya maji katika Wilaya ya Iringa Mjini pamoja na Wilaya nyingine Mkoa wa Iringa. Kutokana na changamoto hiyo, Mkoa wa Iringa umeanzisha programu ya upandaji miti kwenye maeneo yaliyoharibiwa ambapo kila Kata imepanda miti 1,000 kwa mwaka ili kuokoa maeneo yaliyoharibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, programu hii imeimarishwa zaidi na uzinduzi wa kampeni ya ‘Soma na Mti’ iliyozinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mheshimiwa Dkt. Selemani Saidi Jafo tarehe 25 Januari, 2022 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iringa. Kampeni hii imehamasisha shule za Msingi na Sekondari za Mkoa wa Iringa kupanda miti takribani 27,656 katika maeneo mbalimbali ikiwemo shule vyanzo vya maji, mabonde, miteremko ya milima na kandokando ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha mazingira ya milima na vyanzo vya maji katika Mkoa wa Iringa yanastawi Ofisi ya Mkoa wa Iringa inaendelea kuotesha vitalu vya miche Laki Tatu kila mwaka na kuwapatia wananchi wa mkoa wa Iringa kuipanda katika maeneo yao. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha Miradi ya muda mrefu ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi inayotekelezwa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Usonge Hamad Juma, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaratibu miradi miwili kwa Upande wa Zanzibar. Mradi mmoja wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa kwenye Wilaya ya Kaskazini A, Unguja; na Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo Kame Nchini (LDFS) unaotekelezwa katika Wilaya ya Micheweni, Pemba.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati, tayari Serikali imechukua hatua za kiutendaji kuwataka waratibu na washughulikiaji wa miradi hii kitaifa kuhakikisha miradi inakamilika kikamilifu na kwa ubora. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar ili kusimamamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa upande wa Zanzibar ili miradi hii ikamilike kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti wa sababu za kuyeyuka kwa theluji ya Mlima Kilimanjaro na kukauka kwa vyanzo vya maji?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania inayo mipango na mikakati ya kuendelea kufanya utafiti wa sababu za kuyeyuka kwa theluji ya Mlima Kilimanjaro na kukauka kwa vyanzo vya maji. Kupitia Taasisi mbalimbali za ndani ya nchini, zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, vinaendelea kufanya tafiti kuhusu suala hili. Baadhi ya sababu zilizobainika kuchangia hali hiyo ni pamoja na kuongezeka kwa wastani wa joto duniani, shughuli za binadamu zinazoendelea, ukataji wa miti na uchomaji misitu ovyo.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuhimiza uongozi na wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuongeza jitihada za kutunza mazingira ya mlima huo kwa kudhibiti uchomaji moto ovyo na kuongeza jitihada za kuhifadhi mazingira na kupanda miti.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kudhibiti mafuriko katika Mto Mara kwa kuvuna maji kupitia Mabwawa na kujenga Skimu za Umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, tayari imezindua Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Environmental Master Plan for Strategic Intervention 2022-2032) ambao umeelekeza mikakati na shughuli endelevu zitakazoweza kufanyika katika maeneo hayo ni kama vile: kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha uwepo wa mtiririko wa uhakika katika mito ikiwemo Mto Mara, Mto Kagera, Mto Ruaha Mto Wami na Ruvuma; kuhamasisha matumizi sanifu kwa watumiaji wote wa Mto Mara, Kagera, Ruaha, Momba na Mto Ruvuma; na kuimarisha viwango vya maji katika vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Mto Mara ni moja ya miongoni ya Mito mikubwa muhimu nchini Tanzania. Hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara nyingine za kisekta zitakaa na kuona namna bora ya kuvuna maji ili kudhibiti mafuriko, nakushukuru.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -
Je, ni kero zipi za Muungano zimetatuliwa na zipi zimebaki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Serikali za pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimejadili na kuzipatia ufumbuzi jumla ya changamoto 22. Baadhi ya changamoto hizo ni: -
(i) Gharama za Kushusha Mizigo Bandari ya Dar es Salaam kwa Mizigo inayotoka Zanzibari;
(ii) Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia; na
(iii) Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Kushughulikia Masuala ya Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, changamoto zote zilizopatiwa ufumbuzi zimefafanuliwa kwa kina na zinapatikana katika tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zilizobakia kutatuliwa ni nne ambazo ni: -
(i) Mapendekezo ya Tume ya pamoja ya Fedha;
(ii) Usajili wa Vyombo vya Moto;
(iii) Uingizaji wa Sukari katika Soko la Tanzania Bara; na
(iv) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na Hisa za SMZ zitakazokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: -
Je, ni kero zipi za Muungano zilizoibuliwa na kutatuliwa toka kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa Mbunge wa Mtambwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali za pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimejadili na kuzipatia ufumbuzi jumla ya changamoto 22, ambapo baadhi ya
changamoto hizo ni gharama za kushusha mizigo Bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, utaratibu wa vikao vya kamati za pamoja za SJMT na SMZ vya kushughulikia masuala ya Muungano. Aidha, changamoto zote zilizopatiwa ufumbuzi zimefafanuliwa kwa kina na zinapatikana kupitia tovuti yetu ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zilizobakia kutatuliwa ni nne, ambazo ni Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Usajili wa Vyombo vya Moto, Uingizaji wa Sukari katika Soko la Tanzania Bara, na Mgawanyo wa Mapato Yatokanayo na Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na Faida ya Benki Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti mafuriko ambayo husababisha uchafuzi wa mazingira na kuongeza umaskini katika Jimbo la Mwera?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Jimbo la Mwera kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Magharibi A yakiwemo maeneo ya Jimbo la Mwera, hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni pamoja na hatua zifuatazo: -
(i) Kuunda Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Wilaya ya Magharibi A yenye jukumu kuu la kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Wilaya wa Kukabiliana na Maafa wa mwaka 2022; sambamba na kuwaelimisha wananchi.
(ii) Kuandaa mpango wa wilaya wa kukabiliana na maafa ambao umeainisha wadau, majukumu yao na mpango wa utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kufanya tathmini ya kina katika maeneo yote yanayokumbwa na mafuriko nchini ikiwemo maeneo ya Jimbo la Mwera.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -
Je, ni changamoto gani mpya za Muungano zimejitokeza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa hakuna changamoto za Muungano zilizojitokeza. Sote tunafahamu kuwa Muungano wetu umeendelea kuimarika ambapo wananchi wa pande zote mbili wameendelea kunufaika kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio ya kutokuwa na changamoto mpya ni kutokana na jitihada za serikali zetu mbili za Muungano kuweka Muongozo mzuri wa kushughulikia changamoto kwa haraka zinapojitokeza katika hatua za awali. Lengo la Serikali zote mbili ikiwa ni kuhakikisha changamoto zote zinazopitiwa zinapatiwa ufumbuzi na kuendelea kuimarisha Muungano ili kuepusha changamoto mpya kujitokeza, nakushukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -
Je, kwa nini Halmashauri ya Magharibi “A” imeweka Sheria ya Kodi na VAT kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Mfuko wa Jimbo hutolewa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Jimbo, Sura 96 ya mwaka 2009. Aidha, fedha hizi zinatumika kwa kuzingatia miongozo, kanuni na taratibu za usimamizi wa fedha za umma. Kila upande wa Serikali zetu mbili una utaratibu wa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzizar kufuatilia utaratibu unaotumika na Halmashauri ya Magharibi “A” kwenye Mfuko wa Jimbo. Aidha, dhamira ya Serikali ni kuendelea kutoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa pande zote mbili kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii na kuwaletea wananchi maendeleo.
MHE. AMINA DAUDI HASSAN aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kutenga fedha ya mabadiliko ya tabianchi kusaidia wananchi wenye visima vya maji chumvi Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daudi Hassan, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, inatekeleza miradi mbali mbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa pande mbili za Muungano ambayo inahusika na uchimbaji wa visima. Kwa upande wa Zanzibar, Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini (EBBAR) umechimba visima sita katika Wilaya ya Kaskazini “A”. Pia, Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) umechimba visima viwili katika Shehia ya Maziwa Ng’ombe na Shehia ya Kiuyu katika Kisiwa cha Pemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO K.n.y. MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inawapa elimu ya utunzaji mazingira wananchi wanaofanya shughuli za kilimo katika vyanzo na njia za mito ili wafanye kilimo bila kuleta athari za mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha mpango mkakati wa kutoa elimu kwa umma wa miaka mitano na lengo la mpango mkakati huu ni kuhamasisha umma wa Tanzania kuhusu maendeleo endelevu pamoja na uhifadhi wa mazingira. Mkakati huu umehusisha namna ya utoaji elimu kuhusu matumizi ya ardhi ndani ya mita 60 katika maeneo ya vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, licha ya Serikali kuruhusu wananchi kufanya shughuli za kilimo kwa umbali wa mita 60 katika maeneo ya vyanzo vya maji, bado kuna changamoto nyingi za uharibifu mkubwa wa mazingira. Hivyo, naomba nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wenzangu wa siasa tutumie uwezo wa kuwashawishi na kuhamasisha jamii zinazofanya shughuli za kiuchumi katika maeneo ya vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa dharura wa kunusuru athari za mabadiliko ya tabianchi - Nungwi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, Mbunge wa Jimbo la Nungwi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi zilizopo eneo la Nungwi. Tayari, Serikali kupita Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga kiasi cha shilingi milioni 650 kwa ajili ya kufanya tathmini ya awali ya kuzuia athari hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hatua hizo ni pamoja na kuelimisha wananchi kupanda mikoko pamoja na kuhamasisha ulimaji wa mwani usioharibu fukwe. Serikali zote mbili za JMT na SMZ zitashirikiana katika kutafuta fedha zaidi ili kudhibiti uharibifu unaotokea eneo la Nungwi, nakushukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -
Je, kwa miaka mitano iliyopita, Tanzania ilipata kiasi gani kutoka katika Mfuko wa Fedha za Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (LDCF) ?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge Wa Donge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi sasa imeweza kutekeleza miradi minne ambayo inatekelezwa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fedha tulizo pokea ndani ya miaka mitano kutoka Mfuko wa Nchi Zinazoendelea (Least Development Countries Climate Fund-LDCF) ni Kiasi cha Dola za Marekani Milioni 19,343,743.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za miradi yote minne kwa kina inapatikana katika tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais www.vpo.go.tz.
Aidha, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutafuta fedha zaidi kutoka kwenye Mfuko wa LDCF ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kadri fursa zinapopatikana kwa pande mbili za Muungano wetu.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza:¬-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kikundi maalum kuweza kutathmini hewa ukaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Pemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeshaweka mipango thabiti ya kusimamia na kutathimini hewa ukaa. Ofisi ya Makamu wa Rais, imetoa Mamlaka kwa Kituo cha Uratibu na Usimamizi wa Kaboni (NCMC) kilichopo Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kwa ajili kuratibu, kutathmini na kutoa utaalam wa masuala yote yanayohusu gesijoto na biashara ya hewa ukaa nchini. Aidha, katika kuhakikisha biashara ya hewa ukaa inakuwa biashara rasmi hapa nchini, Ofisi ya Makamu wa Rais, imeandaa kanuni na mwongozo wa kusimamia na kudhibiti biashara ya kaboni za mwaka 2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kushirikiana na wadau wengine kwa kuhakikisha kwamba masuala haya ya hewa ukaa yanaeleweka kwa kila mdau na Watanzania wote kwa ujumla. Nakushukuru.
MHE. KABULA E. SHITOBELA aliuliza:-
Je, nini mpango wa Serikali wa kuondoa magugu ambayo yanasababisha uchafuzi katika Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali wa Mheshimiwa Kabula Enock Shitobela, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti magugu maji yasiendelee kuleta athari katika Ziwa Victoria, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali tangu mwanzoni mwa miaka ya tisini. Hatua hizo ni pamoja na:-
(i) Kutekeleza Mradi wa Hifadhi ya Mazingira katika Ziwa Victoria (Lake Victoria Environmental Management Project) ambao pamoja na mambo mengine ulitekeleza shughuli zilizolenga kudhibiti magugu maji kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo za kibaiolojia;
(ii) Kutoa elimu na kuwajengea uwezo wananchi wanaoishi karibu na Ziwa namna ya kujitolea katika kazi za kutokomeza na kuenea kwa magugu maji kila yanapojitokeza Ziwani; na
(iii) Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa na inatekeleza Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Kukabiliana na Viumbe Vamizi wa mwaka 2019-2029 ambao unatoa mwongozo wa namna ya kuzuia kuingia na kuenea kwa viumbe vamizi na pia una mipango endelevu ya kushughulikia viumbe vamizi waliopo na wale wale wanaoweza kuingia.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na juhudi hizi za kupambana na magugu maji katika Ziwa Victoria ili kudhibiti uhabirifu wa mazingira na athari zitokanazo na uharibifu huo nchini, nakushukuru.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa tishio kwa usalama wa viumbe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge Wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa sera, mikakati na mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inatoa elimu na namna bora ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wadau wote muhimu wakiwemo wananchi katika maeneo yote nchini.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanahamasishwa kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira na kusababisha athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo kukata miti ovyo, kuepuka kilimo kisichoendelevu katika vyanzo vya maji, kuepuka ufugaji unaoharibu mazingira pamoja na uvuvi haramu. Vilevile, Serikali inachukua hatua kwa kuanzisha na kutekeleza miradi ya kuzuia madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali inaendelea kusimamia sera, mipango na mikakati ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (www.vpo.go.tz )
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kuhusu hewa ya ukaa ili wananchi waelewe na wanufaike na elimu hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, biashara ya kaboni (biashara ya hewa ukaa) ni moja ya mbinu za kupunguza uzalishaji wa gesijoto (mitigation) ambayo iliridhiwa katika Itifaki ya Kyoto ikizitaka nchi wanachama kupunguza uzalishaji wa gesijoto iliyorundikana angani. Biashara hii ipo katika masoko ya aina mbili ambayo ni Soko la Hiari/Huria (Voluntary Carbon Market) na Soko la Umoja wa Mataifa (Official Carbon Market).
Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mwongozo wa Biashara ya Kaboni pamoja na Kanuni zake za mwaka 2022. Aidha, elimu kuhusu biashara ya kaboni hadi sasa imetolewa kimakundi ikiwemo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Wizara zote za kisekta pamoja na taasisi zake, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mkoa na kwa wadau mbalimbali. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu ya mazingira kwa Umma ikiwemo ya biashara ya kaboni.
Mheshimiwa Spika, ni matumaini ya Serikali kwamba kupitia jitihada hizo wananchi watapata uelewa na kunufaika na biashara ya kaboni. Nakushukuru.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Je, ni lini Mradi wa Climate Change utawafikia wananchi wa Tarafa ya Chamriho wanaokabiliwa na tatizo la ukame?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linasimamia utekelezaji wa Mradi uitwao Bunda Climate Resilience and Adaptation Project wenye kiasi cha dola za Kimarekani 1,400,000 unaofadhiliwa na Adaptation Fund. Mradi huo unatekelezwa Wilayani Bunda katika maeneo ya Kata za Kasuguti, Namhura, Iramba, Neruma, Mahyolo, Igundu na Butimba. Kwa mujibu wa andiko lililoidhinishwa, Tarafa ya Chamriho kwa sasa iko nje ya mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kutafuta fursa mbalimbali za miradi ya Mazingira kwa kushirikiana na Halmashauri ya Bunda ili kukabiliana na changamoto iliyopo katika Tarafa ya Chamriho.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza:¬-
Je, sababu zipi zimekwamisha ujenzi wa ukuta maeneo yanayoathiriwa na Bahari Nungwi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-¬
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, Mbunge na Mtumishi wa Wananchi wa Jimbo la Nungwi, najibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa fukwe wa Bahari ya Hindi. Lakini kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha zoezi la ujenzi wa ukuta wa Nungwi umechelewa lakini kwa sasa Serikali imepata fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imetenga fedha jumla ya shilingi milioni mia sita na hamsini kwa ajili ya kufanya tathmini ya awali ili kuwa na usanifu wa miundombinu itakayosaidia kurudisha ufukwe katika hali ya awali.
Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kuwahimiza wananchi wa maeneo ya Pwani kuongeza jitihada za kupanda mikoko, kutofanya uchimbaji holela wa mchanga lakini pia kuhamasisha ulimaji na uvunaji wa mwani usiyoharibu fukwe. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar zitaendelea kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali, nakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: -
Je, sababu zipi zinasababisha eneo linaloathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kupewa kipaumbele cha utekelezaji wa Mradi ili kunusuru hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, Mbunge wa Jimbo la Nungwi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya tabianchi yanazidi kusababisha athari katika maeneo mbalimbali ya nchini yakiwemo maeneo ya ukanda wa pwani nchini. Katika kubainisha maeneo yaliyoathirika na kuyaweka katika kipaumbele, Serikali inafanya tathmini ya kiwango cha uharibifu na athari zilizojitokeza hii ni moja ya sababu mojawapo ya vigezo vinavyotumika katika kuweka kipaumbele maeneo yaliyoathirika katika mipango ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kubaini maeneo mbalimbali yenye changamoto kubwa ya uharibifu wa Mazingira na kuyaweka katika kipaumbele ili kuyatafutia rasilimali fedha, nashukuru.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -
Je, ni nini Mpango wa Serikali kudhibiti Mto Nakasangwe na Mto Tegeta na kadhalika inayopanuka kwa kasi na kutishia maisha ya watu na mali katika Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za kupanuka kwa Mto Nakasangwe na Mto Tegeta kama ifuatavyo:
i. Kuandaa Mwongozo wa usafishaji mchanga, tope na taka ngumu kwenye mito na mabonde kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
ii. Kutoa elimu kupitia vipindi vya redio, televisheni, maonesho na mikutano kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa vyanzo vya maji katika ngazi zote ili kuongeza kasi ya uhifadhi vya vyanzo vya maji na kingo za mito.
iii. Kuhamasisha Umma kuhusu upandaji wa miti rafiki kwa vyanzo vya maji ambavyo itasaidia katika kuzuia mmomonyoko wa kingo za mito na kuimarisha mtiririko wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kusisitiza utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 kuhusu uhifadhi ya eneo la mita 60 katika kingo za mito, fukwe za bahari na maziwa yanayozuia matumizi yeyote ya kibinadamu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kutambua kupanuka kwa kingo za mto Tegeta na Nakasangwe, Serikali itaangalia uwezekano wa kufanya tathmini katika maeneo hayo kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu kama ilivyofanyika katika maeneo mengine ambapo Serikali ilibuni na kutekeleza miradi ya ujenzi wa kuta, kama vile ujenzi wa ukuta wa Pangani na fukwe katika Barabara ya Barak Obama katika jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza:¬-
Je, lini Serikali itajenga ukuta wa Ikulu Ndogo ya Muungano Pemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Jimbo la Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaandaa mipango mahususi ya kutekeleza suala hilo ambapo tathmini ya kitaalamu ya kina imefanyika ili kupata gharama za ukarabati wa Jengo la Ikulu ndogo ya Muungano Pemba ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ukuta. Aidha, inategemewa kuwa, utekelezaji utaanza katika mwaka wa fedha 2024/2025, nakushukuru.
Manufaa yatokanayo na kero za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza:-
Je, kero 11 za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi zimeleta manufaa kiasi gani katika utekelezaji kwa pande zote mbili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Said Issa, Mbunge wa Jimbo la Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio yaliyotokana na ufumbuzi wa changamoto 11 za Muungano wa kiuchumi, kijamii na kisiasa hasa katika maeneo ya ajira kwa Watumishi wa Zanzibar wanaofanya kazi katika Taasisi za Muungano, wameendelea kunufaika na ajira hizo ikiwa ni 79% kwa Tanzania Bara na 21% kwa Zanzibar. Mgawanyo wa Fedha za Mapato yatokanayo na Misaada na Mikopo Nafuu ya Kibajeti (GBS) imeendelea kuongezeka tangu kupatiwa ufumbuzi kwa changamoto hii na kuendelea kuimarisha Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Kodi ya Mapato yatokanayo na mishahara ya watumishi wa Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.75 kimekuwa kikitolewa kwenda SMZ kila mwezi kuanzia mwaka 2012/2013 kama malipo ya PAYE; na Kampuni zilizosajiliwa Tanzania Bara na zenye matawi Zanzibar zimeanza kulipa Kodi ya Zuio (Withholding Tax) kwa upande wa Zanzibar. Aidha, mapato yanayotokana na Tozo za VISA kutumika pale yalipokusanywa kama ilivyo kwenye mapato mengine ya Muungano.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kwamba wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, suala hili limepatiwa ufumbuzi na sasa wafanyabiashara kulipa kodi inayostahiki kwa tathmini ya bidhaa inayotumika Tanzania Bara. Kwa muktadha huo, suala la ulipaji wa tofauti ya kodi kwa bidhaa zinazotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara imewekwa vizuri kwa wafanyabiashara wa Zanzibar, nakushukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-
Je, lini Serikali itafanyia kazi changamoto ya Kodi na Tozo kwenye Fedha za Mfuko wa Jimbo kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi na tozo hutozwa kwa mujibu wa Sheria pindi bidhaa au huduma zinapotolewa au kununuliwa. Aidha, bidhaa na huduma zinazotolewa hukatwa kodi ya zuio la kodi (withholding tax) kwa kuzingatia Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332, chini ya Kifungu cha 83(1)(c) kwa mujibu wa ada ya huduma kwa ajili ya utoaji wa huduma za kitaalam. Aidha, Kifungu cha 83A, malipo ya bidhaa zinazotolewa na mkazi wa uendeshaji biashara. Vilevile, kodi hutozwa kwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi iliyotumika Zanzibar inayojulikana kama Sheria zinazotolewa na mkazi wakati wa uendeshaji wa biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Mfuko wa Jimbo zinaendelea kuleta tija na matokeo chanya katika kuimarisha na kukuza uchumi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla na hivyo huleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano. Nakushukuru.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa dharura wa kudhibiti mito inayopanuka na kuhatarisha maisha na mali za wananchi katika Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za mito kupanuka kutokana na mvua kubwa zilizonyesha. Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali, kwanza, ni kutenga fedha katika bajeti. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, Ofisi ya Makamu wa Rais imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu utakaowezesha ujenzi kwa maeneo yatakayopendekezwa kwa Mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na Bonde la Wami-Ruvu tayari imeingia mkataba na kampuni ya Meg Business Solution Limited tokea tarehe 19 Aprili, 2024 kwa ajili ya kusafisha tope, taka ngumu na kudhibiti mmomonyoko wa kingo za Mto Mbezi eneo la Ukwamani, Mzimuni pamoja na ufukwe uliopo mtaa wa Mbezi A Kata ya Kawe. Hivyo, kwa kukamilika kwa kazi hizo kutachangia kudhibiti kupanuka kwa mto Mbezi katika kata ya Kawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa wito kwa Serikali za Mitaa kote nchini kusimamia kikamilifu Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 ili kuzuia shughuli za kibinadamu kama vile uchimbaji wa mchanga usiofuata utaratibu na kuelimisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira ili kudhibiti upanukaji wa mito na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, nakushukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, kuna ukweli kwamba kina cha maji ya Bahari ya Hindi hapa Tanzania kimeongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na nini athari zake?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba ni kweli kina cha maji ya Bahari ya Hindi hapa Tanzania kimeongezeka kutokana na kuendelea kuongezeka kwa joto la dunia linalosababisha kuendelea kuyeyuka kwa barafu katika maeno mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa utafiti na vipimo vilivyopo maji ya Bahari ya Hindi katika Pwani ya Dar es Salaam yanaongezeka kwa wastani wa kiasi cha milimita sita kwa mwaka tangu mwaka 2002.
Mheshimiwa Spika, athari za kuongezeka kwa kiwango cha maji ya bahari ni pamoja na:-
(i) Kuongezeka kwa mmomonyoko na upotevu za fukwe;
(ii) Uharibifu wa miundombinu kama vile gati za bahari, barabara, nyumba ofisi na masoko;
(iii) Upotevu wa bioanuwai muhimu ikiwemo mikoko na nyasi za bahari;
(iv) Upotevu wa ardhi ya kilimo, makazi na visima vya maji baridi kuingiwa na chumvi na mafuriko ya mara kwa mara. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutunza mazingira ya Bwawa la Zombo Kilosa ili litumike kwa shughuli za ufugaji wa samaki na kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kutunza mazingira ya Bwawa la Zombo. Hatua hizo ni pamoja na upandaji wa miti kuzunguka bwawa katika eneo la hifadhi ya bwawa ndani ya eneo la meta 60.
Mheshimiwa Spika, aidha katika kipindi cha msimu wa mvua 2024/2025 Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa kushirikiana na Bonde la Wami - Ruvu, imepanga kupanda miti 5,000 ili kuongeza uoto wa asili na kuzuia mmomonyoko wa udongo katika maeneo yanayozunguka bwawa, aidha kulinda eneo la hifadhi ya bwawa ndani ya meta 60, kuzunguka bwawa dhidi ya shughuli zisizoendelevu na kuendesha doria za mara kwa mara na utoaji wa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi katika vijiji vinavyonufaika na bwawa husika hususan kilimo na ufugaji, nakushukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, ni mikataba mingapi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambayo watumishi wake wanatoka Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imeridhia mikataba 12 ya kimataifa na kikanda kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Utekelezaji wa mikataba hii hufanyika kwa ushirikiano na uratibu baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira - Tanzania Bara pamoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Tanzania - Zanzibar. Hivyo, utekelezaji wa mikataba hii hujumuisha watumishi wote wa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi zetu mbili zimekuwa zikishirikiana kwa pamoja kwenye vikao vya maamuzi vya mikataba hii. Pia pande zote mbili za Muungano zinanufaika na utekelezaji wa mikataba hii hususani kupitia, programu na miradi inayoratibiwa kupitia mikataba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa maslahi mapana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kukabiliana na changamoto za kimazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika kuwakinga Wananchi na madhara yanayoweza kutokea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera (Zanzibar), kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuandaa nyenzo za kisera zinazosaidia kutoa dira, kuibua mikakati na kubuni miradi inayosaidia jamii katika maeneo mbalimbali kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Hii inajumuisha Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021, Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira 2022 -2032, na Mchango wa Taifa katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza mikakati hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini. Miradi hii inajumuisha upandaji miti, usambazaji wa maji safi kwa matumizi ya majumbani na mifugo, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, kuhimiza matumizi ya nishati mbadala na majiko banifu ili kupunguza kasi ya ukataji wa misitu, ujenzi wa kuta katika maeneo ya fukwe za bahari yanayokabiliwa na mmomonyoko wa ardhi, ujenzi wa matuta na mabwawa ya kudhibiti mafuriko, kuwezesha jamii kubuni miradi mbadala ya kuongeza kipato na iliyo rafiki kwa mazingira na urejeshaji wa maeneo ya ardhi yaliyoharibika, ahsante.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, lini Serikali itawasilisha Marekebisho ya Sheria ya Mazingira ili kuipa NEMC uwezo wa hadhi ya mamlaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Mwinyi Azan, Mbunge Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Pemba, najibu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Ofisi ya Makamu wa Rais ipo katika mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191. Katika marekebisho hayo, kubadili muundo wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) ni moja ya masuala yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho ili NEMC iweze kuwa Mamlaka.
Mheshimiwa Spika, ni matumaini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwamba hadi kufikia Juni 2024, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 uwasilishwe katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nakushukuru.
MHE. ZAHOR MAHAMMED HAJI aliuliza: -
Je, lini Serikali itautaarifu Umma kuhusu changamoto za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ili Wanasiasa wasipotoshe Wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea na programu za kutoa elimu kwa Umma kupitia hotuba za Viongozi Wakuu, makongamano, maonesho maalum, utayarishaji wa vipindi vya televisheni, redio, magazeti, uandishi na uchapishaji wa vitabu ikiwemo kitabu cha hoja zote zilizopatiwa ufumbuzi kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu changamoto zilizopatiwa ufumbuzi. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2024/2025 Ofisi imepanga kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa kutumia ipasavyo mitandao ya kijamii, vikao na makundi maalum, ziara za kimafunzo na makongamano.
Aidha, hoja zilizopatiwa ufumbuzi zimewekwa kwenye tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo ni www.vpo.go.tz
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa dharura wa kudhibiti Mito inayopanuka na kuhatarisha maisha na mali za wananchi katika Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na changamoto za kudhibiti mito kupanuka hususan kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali imechukua hatua ya dharura kwa kuandaa Mwongozo wa Usafishaji Mchanga, tope na taka ngumu kwenye mito na mabonde katika Mkoa wa Dar es Salaam 2021 ukiwa na lengo la kuelekeza aina ya mfumo wa usafishaji wa mito kwa kuchimba mchanga, tope na taka ngumu zinazohitaji kuondolewa ili kudhibiti mtiririko wa maji katika mito na mabonde.
Mheshimiwa Spika, aidha, mwongozo huu unatoa maelekezo ya hatua mbalimbali zitakazochukuliwa na wadau wa kuhifadhi na utunzaji wa mazingira katika kuhakikisha mazingira ya mito yanalindwa na kuhifadhiwa na kutumika katika njia sahihi ya uchimbaji mchanga ikiwa ni pamoja na kudhibiti uchimbaji wa michanga na ujenzi wa makazi ndani ya meta 60 kutoka kwenye kingo za mito.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Serikali za Mitaa kote nchini kusimamia kikamilifu Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 ili kuzuia shughuli za kibinadamu kama vile uchimbaji wa mchanga na kuendelea kuelimisha jamii juu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kupunguza athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, nakushukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza:-
Je, upi mkakati wa Serikali wa kukabiliana na matumizi ya mkaa na kuni nchini ili kulinda mazingira?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Mtemvu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kuanzia mwaka 2024 hadi 2034 ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. Mkakati huu unalenga kuhakikisha angalau 80% ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mkakati huu unalenga kupunguza gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia, kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika ya nishati safi ya kupikia, kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi ya kupikia, pamoja na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa Kingo za Mto Msuka Ilemela utakamilika ili kuepusha vifo vya mara kwa mara pindi mvua zinaponyesha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Kingo za Mto Msuka unaendelea ambapo hadi sasa ujenzi wa daraja na kingo zake zenye urefu wa takribani meta 500 umekamilika. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Manispaa ya Ilemela kupitia Mradi wa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia imeomba kiasi cha shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na kukamilisha ujenzi wa Kingo za Mto Msuka ambapo ujenzi wake utaendelea baada ya fedha hizo zilizoombwa kupatikana.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza:-
Je, fedha kiasi gani imepatikana Zanzibar kwa miaka mitatu iliyopita kupitia Mifuko ya Kimataifa ya Mazingira na mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikipokea fedha kutoka kwenye Mifuko ya Kimataifa ya Mazingira na mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCF). Fedha hizo zimekuwa zikitumika kutekeleza miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa upande wa Zanzibar, jumla ya shilingi bilioni 5.3 zimepelekwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya za Wete, Micheweni, Kaskazini Pemba, Kaskazini A, Kaskazini B na Kaskazini Unguja. Miradi iliyotekelezwa kupitia fedha hizo ni pamoja na Mradi wa kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula kwenye maeneo kame nchini yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2. Aidha, Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumoikolojia Vijijijini – EBARR (shilingi bilioni 1.4); na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Wakazi wa Pwani shilingi bilioni 2.7. Ninakushukuru.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA K.n.y. MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza:-
Je, lini tathmini ya athari za kimazingira zitokanazo na maji ya bahari kwenye mashamba ya Mpunga - Bonde la Tibirinzi Chakechake itafanyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chakechake kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya tathmini ya mazingira katika eneo la Tibirinzi ambapo matokeo ya tathmini hiyo yalibainisha kuwa jumla ya hekta tano zimeathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kukusanya taarifa za kina zitakazowezesha kubaini athari za kimazingira na kijamii katika maeneo yanayovamiwa na maji ya bahari ikiwemo eneo la Tibirinzi ili kubaini viwango vya athari na hatua za kuchukua katika kukabiliana na athari hizo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, mkakati wa kwanza, ulikuwa ni kutoa elimu kwa Umma kuhusu athari za matumizi ya mifuko ya plastiki; Pili, Serikali ilipiga marufuku uzalishaji, matumizi, uingizaji, usambazaji na usafirishaji nje ya nchi mifuko ya plastiki kuanzia tarehe 01 Juni, 2019 na tatu, Serikali ilitunga kanuni za kupiga marufuku mifuko ya plastiki za mwaka 2019 kupitia Tangazo la Serikali Na.394 la 2019 ili kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki isiyofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa mamlaka na taasisi zote za Serikali kuimarisha na kuwezesha vitengo vyake vinavyosimamia utekelezaji wa marufuku ya mifuko ya plastiki ili viweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 na kanuni zake. Aidha, naomba Asasi za Kiraia pamoja na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika kupambana na matumizi ya mifuko ya plastiki. (Makofi)
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN aliuliza:¬-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza fukwe za bahari zilizoathirika upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-¬
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imepanga kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa fukwe zilizoathirika kwa upande wa Zanzibar ambapo jumla ya shilingi 661,000,000 zimetengwa kwa ajili ya miradi hiyo. Kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi 300,000,000 zitatumika kukamilisha ujenzi wa matuta ya kuzuia maji ya bahari kuingia sehemu ya mashamba ya mpunga katika Shehiya ya Mgogoni, Mkoa wa Kusini Pemba, katika Ufukwe wa Sipwese na shilingi 361,000,000 ni kwa ajili ya kufanya tathmini katika Eneo la Nungwi, Visiwani Zanzibar ili kusanifu namna bora ya kudhibiti uharibifu unaoendelea. Nakushukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, ni mikataba mingapi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambayo watumishi wake wanatoka Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imeridhia mikataba 12 ya kimataifa na kikanda kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Utekelezaji wa mikataba hii hufanyika kwa ushirikiano na uratibu baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira - Tanzania Bara pamoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Tanzania - Zanzibar. Hivyo, utekelezaji wa mikataba hii hujumuisha watumishi wote wa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi zetu mbili zimekuwa zikishirikiana kwa pamoja kwenye vikao vya maamuzi vya mikataba hii. Pia pande zote mbili za Muungano zinanufaika na utekelezaji wa mikataba hii hususani kupitia, programu na miradi inayoratibiwa kupitia mikataba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa maslahi mapana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kukabiliana na changamoto za kimazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi, nakushukuru. (Makofi
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH K.n.y. MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani kunusuru vipando visivyohimili maji ya bahari katika Bonde la Tibirinzi Chakechake Pemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hatua hizo ni pamoja na ujenzi wa matuta ya kuzuia maji bahari yasiingie katika mabonde ya kilimo ikiwemo Kisiwa Panza, Kilimani, Msuka, Sipwese, Micheweni na Tovuni; na upandaji wa miti ya aina mbalimbali ikiwemo mikoko/mikandaa katika maeneo ya ufukwe ili kupunguza kasi ya uingiaji wa maji ya bahari katika maeneo ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutafuta fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kuendelea kuweka miundombinu wezeshi inayozuia maji ya bahari kuingia katika makazi na maeneo ya kilimo ikiwemo Bonde la Tibirinzi. Lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kutumia maeneo hayo kwa shughuli za kilimo na uchumi.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa Mpango wa Kuirithisha Zanzibar ya Kijani ambao unalenga kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa misitu, na miti iliyopo na upandaji na utunzaji wa miti hususani kwenye maeneo ya fukwe ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza:-
Je, utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kupitia mfumo ekolojia Wilaya ya Kaskazini “A” Zanzibar umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo ya Ekolojia Vijijini (Ecosystem-based Adaptation for Rural Resilience - EBARR) unaotekelezwa katika Wilaya za Mvomero, Simanjiro, Kishapu, Mpwapwa kwa upande wa Tanzania Bara na Kaskazini A - Unguja upande wa Zanzibar. Mradi huu unaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kaskazini A – Unguja, mradi huu unatekelezwa na umefikia katika 95% ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.4 zimetolewa. Shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika Shehia za Matemwe Kijini, Mbuyutende na Jugakuu; uchimbaji na ujenzi wa visima sita; ujenzi wa vitalunyumba (Greenhouse) vitatu kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga; ununuzi wa boti sita za kisasa na vifaa vya uvuvi; ujenzi wa vituo vitatu vya ufugaji, utengenezaji wa sabuni na ushonaji; ununuzi wa vyerehani 42 kwa ajili ya vikundi vya ushoni na upakasaji; ununuzi wa mizinga ya nyuki 200; mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vyote; kuanzishwa kwa vitalu vya miche 56,000; na utengezaji wa majiko banifu kwa kaya 125. Ninakushukuru.