Supplementary Questions from Hon. Ghati Zephania Chomete (23 total)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na Sera ya Matibabu Bure kuendelea kutekelezeka, lakini bado kuna wazee wengi hawajapatiwa vitambulisho hivyo vya kuwawezesha kupata matibabu hayo:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wazee wote wenye sifa wanapata vitambulisho hivyo ili waweze kunufaika na Sera ya Matibabu Bure? (Makofi)
(b) Kuna malalamiko hata kwa wale wazee wachache wenye vitambulisho hivyo; wanapofika hospitalini wanaambiwa hakuna dawa: Je, ni lini Serikali itahakikisha ukosefu wa madawa huu unakwisha ili kuwaondolea wazee wetu kero hiyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Sera ya Wazee inatambua kwamba tunahitaji kuainisha wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo ili waweze kupata matibabu bila malipo. Serikali imeendelea kuweka utaratibu kupitia Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauti zetu kupita katika vijiji kwa kushirikiana na Watendaji katika Vijiji na Kata kuwatambua wazee hao wenye sifa, lakini pia kuhakikisha wanapata vitambulisho kwa ajili ya matibabu bila malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba bado hatujafikia asilimia 100 kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, lakini jiitihada za kuhakikisha tunafikia hapo zinaendea. Naomba nichukue nafasi hii kuwaelekeza Watendaji Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mitaa wote kote nchi kuhakikisha wanaweka mpango kazi wa kuwatambua wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, wasio na uwezo na kuweka mipango ya kuwapatia vitambulisho ili waweze kupata matibabu bila malipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni endelevu, haliwezi kwisha kwa sababu kila siku kuna mtu anafikisha miaka 60. Kwa hiyo, hatuwezi kusema tumemaliza wazee wote, kwa sababu ni suala endelevu, kila mwaka kuna watu ambao wata-turn miaka 60 na Serikali itaendelea kuwatafutia vitambulisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika vituo vyetu kumekuwa kuna malalamiko kwa baadhi ya vituo na baadhi ya Halmashauri kwamba wazee wetu wakifika kwa ajili ya matibabu pamoja na vitambulisho vyao, wanakosa baadhi ya dawa muhimu. Kuna sababu mbili; sababu ya kwanza ni kwamba magonjwa mengi ambayo yanawapata wazee wa miaka 60 na kuendelea mara nyingi baadhi ya dawa zao hazipatikani katika ngazi ya vituo. Kwa hiyo, mara nyingine kunakuwa na changamoto ya magonjwa yale kwa ajili ya advanced cases, lakini wanahitaji kupata labda kwenye ngazi ya wilaya na ngazi ya rufaa, wakienda kwenye vituo vyetu mara nyingine hawapati zile dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka utaratibu wa kuendelea kwanza kuwaelimisha wananchi hao, lakini pia kuweka utaratibu wa kuona namna gani zile dawa muhimu katika maeneo husika zitapatikana ili kuwarahisishia wazee wetu kupata matibabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya pili ni ile ambayo nimeelezea kwa ujumla wake kwamba Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba katika vituo vyetu kote nchini ili kuhakikisha wazee wetu na wananchi kwa ujumla wanapata dawa kama ambavyo imekusudiwa.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali machache ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imesema kwenye majibu yake ya msingi kuwa teknolojia mbadala itakayotumika sasa ni ujenzi wa zege kwa kutumia nondo. Je, ni lini teknolojia hii itawafikia wachimbaji wale wadogo wa Nyamongo, Butiama, Tarime na Buhemba ili waweze kufanya uchimbaji wenye tija kwao na kwa Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali imekiri kuwa kinachopelekea kutumia miti, mitimba na magogo kwenye mashimo ni ufinyu wa mitaji waliyonayo wale wachimbaji. Je, ni lini Serikali itawawezesha kwa kuwapa mitaji wachimbaji hao ili waweze kukidhi mahitaji hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena niweze kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linazungumza juu ya lini teknolojia hii itafikishwa kwa wachimbaji wadogo. Nimpe taarifa tu, Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mojawapo ya Migodi ya Wachimbaji Wadogo ya Kalende katika eneo la Tarime tayari mgodi mmojawapo wa Mara Mine umekwishaanza kutumia teknolojia hii kuashiria kwamba kumbe teknolojia imefika. Kwa sababu inahitaji kusambazwa kwa wengi nitumie nafasi hii, kumuagiza Afisa Madini Mkaazi wa Mkoa wa Mara, Ofisi yetu ya Musoma, aanzishe mafunzo kwa wachimbaji wote wa maeneo hayo ili waweze kuipokea teknolojia hii.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kuhusu uwezeshaji. Itakumbukwa hapa kwamba, mwaka jana 2020 Tume ya Madini ilianza kutoa semina kwa mabenki yetu nchini ili kujenga awareness ya kwamba, uchimbaji madini ni biashara inayolipa kama biashara nyingine. Tulipokuwa tukisoma bajeti yetu hapa, tulithibitisha jinsi ambavyo mabenki yamepokea kwamba, biashara ya madini inawezekana na ni kweli kwamba tayari mabenki yameanza kuwezesha wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakachokifanya ni kuendelea kutoa elimu hii kwa mabenki ili kwamba, watambue maeneo ambayo yanapata tija katika uchimbaji na kwa jinsi hiyo waweze kuelekeza fedha katika kuwezesha wachimbaji wadogo. Ahsante sana.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali madogo tu ya nyongeza: -
(a) Serikali imetangaza tarehe 4 Juni zabuni je, ni lini sasa kilometa 76 zilizobaki zitafanyiwa kazi? (Makofi)
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha barabara hii inaendelea kupitika wakati wote. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Zephania Ghati Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwamba ametoa kibali barabara hii imetangazwa inajengwa kwa awamu, kwa kuanzia na kilometa 25 tuna bilioni Sita za kulipa advance payment baada ya kumpata mkandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali lake la pili kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Mkoa wa Mara kupitia TANROADS imetenga shilingi milioni 411 kwa ajili ya kuendelea kufanyia maboresho barabara hii hadi hapo itakapokuwa imekamilika. Ahsante.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kulikuwa na mpango wa ujenzi wa barabara ya Tarime kupitia Nyamwaga, Nyamongo mpaka Serengeti lakini kuna taarifa kuwa mpango huo haupo. Je, ni nini tamko la Serikali juu ya barabara hiyo kwa wananchi wale? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ghati Chomete, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Mara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni swali lingine tena naulizwa, siku mbili zilizopita liliulizwa swali kwenye barabara hii hii. Naomba nimjibu Mheshimiwa Ghati Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mara kwa kumhakikishia tu kwamba, Mheshimiwa Mwita Waitara, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, jana amekuja ofisini akiwa na madai haya haya, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo na wananchi wa Tarime, mpango huu unaosemwa hakuna mpango uliofutwa. Nataka nimhakikishie kwamba tayari tuko kwenye hatua za kusaini mkataba kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kuanzia Tarime hadi Nyamwaga, kilometa 25 na zabuni inaandaliwa kuanzia Nyamwaga hadi Mugumu kilometa 61. Jumla kilometa hizo 82, kwa hiyo hakuna mpango uliofutwa na iko kwenye mpango.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa inafanana kabisa na changamoto iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara. Je, ni lini Serikali itakwenda kutatua changamoto hii ya uhaba wa madaktari, hasa kwa magonjwa ya wanawake na watoto katika hospitali hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyofuatilia mambo ya mkoa wake, na nakumbuka alikuja Wizarani kwa ajili ya hilo. Ninamuomba Mheshimiwa Mbunge tukutane wakati wa haya mapitio ya kuwahamisha tuone tunaweza kufanya nini kwenye eneo la mkoa wake.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa nakushukuru sana lakini pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya vifaa tiba ikiwemo vitanda vya kujifungulia akina mama katika Mkoa wa Mara.
Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi na akina mama wa Mkoa wa Mara kwamba endapo italeta vifaa tiba hivyo hospitali pamoja na Vituo vya Afya vya Mkoa wa Mara vitapata vitanda kwa ajili ya kuondoa tatizo hilo?
Swali la pili; je, Serikali imejipanga vipi kuthibiti wizi wa dawa nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu siyo mara ya kwanza kufika Wizarani akizungumzia Hospitali yake ya Mkoa wa Mara. Lakini nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwa sababu yeye anajua kwa sasa tayari vifaa vyenye thamani ya bilioni tatu zimeshapelekwa Mkoa wa Mara na hapa tunapoongea tayari CT Scan ipo pale Mkoani Mara na Digital Xray inangojea tu jengo liishe ili kazi ianze.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kuwa hospitali ya Mkoa wa Mara tumeshakubaliana ndani ya Wizara na Waziri wa Afya ameshatoa maelekezo tarehe 12 na Mkoa wamekubaliana na maelekezo ya tarehe 12 Disemba hospitali hiyo inaenda kuanza na watumishi watahama kwenye hospitali waliokuwepo ili wahamie kwenye hospitali ya Mkoa.
Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili la suala kuwa tumejipangaje kudhibiti wizi wa dawa. Moja, tumetengeneza mfumo ambao MSD sasa wataweza ku- track dawa kuanzia zinapotoka Taifani mpaka zinapofika kituoni. Wakati huo huo kama Wabunge mnakumbuka tulikuja hapa kwenu na kuwaonesha mianya ambayo inapotea dawa zinapofika kwenye Wilaya zetu na Mikoa yetu. Ushirikishwaji huo sio kwamba tulikuwa tunasema wizi wa dawa, lakini tulitaka kumleta kila mtu on board tujue wote ili tuweze kushirikiana kusimamia na sasa kule kwenye zahanati zetu, vituo vyetu vya afya, hospitali zetu za Wilaya tunashirikisha jamii na Waziri wa Afya ameshatoa maelekezo kwamba dawa ikitoka MSD inapofika Wilayani, Mkuu wa Wilaya ajue, Mkurugenzi ajue, lakini Mbunge apewe copy ili wote pamoja na zile Kamati za Afya za zahanati, za vituo vya afya na Wilaya wajue dawa iliyoingia ili kwa pamoja tushirikiane kulinda huu ubadhirifu ambao umekuwa ukitokea kwenye nchi yetu.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Shule nyingi za sekondari na primary Mkoani Mara hazina miundombinu ya maji. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha miundombinu hiyo inawafikia ili kuepuka magonjwa ya milipuko? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ghati Chomete, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Ghati amekuwa ni mlezi mzuri sana wa watoto mashuleni na amefuatilia sana hili suala la huduma ya maji mashuleni. Naomba nitumie Bunge lako Tukufu kuwaagiza Viongozi wa Mkoa wa Mara kwa maana ya MD na RM wahakikishe wanapeleka maji mashuleni, hili tulishaagiza, ni ufuatiliaji na utekelezaji tu, hivyo waweze kufanya kuanzia sasa na mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali madogo ya nyongeza.
Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi wa Tarime, Rorya, Sirari, Nyamwaga, Nyamongo na Serengeti kwamba, mradi huu wa kutoka Ziwa Victoria utaenda kuanza mwaka huu wa fedha 2022/2023?
Swali la pili, wananchi wa Mji wa Tarime kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia chanzo cha maji kutoka Mto Nyanduruma, lakini maji yale ni machafu na yana rangi ya tope.
Je, Serikali ni lini itaweka chujio la maji ili kuwawezesha wananchi wale kupata maji safi na salama? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ghati Chomete kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Ghati Chomete kwa maswali mazuri na amekuwa akifuatilia sana hii miradi, kwa sababu ya mashirikiano katika suala la lini maji ya Ziwa Victoria yatatumika, tayari tumeshafikia hatua zote ziko sawa na sasa tunasubiri tu idhini ya kupata nafasi ya Mheshimiwa Rais ili aweze kushiriki katika kusaini ili mradi wa Miji 28 uanze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la chujio pia tayari ni moja ya mikakati ya Wizara na tunatarajia kufikia mwaka ujao wa fedha nalo pia litapewa kipaumbele.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Serikali ilikuwa na mpango wa Bima za Afya kwa wote, je, ni hatua ipi imefikiwa ili kupata Bima hizo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, hatua zilizofikiwa. Kwanza zimefikiwa hatua zote za kitaalam, tuko kwenye hatua ambayo nafikiri uliona Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Waziri wa Afya alileta ushauri wake na akawaleza Wabunge hatua tuliyofikia ambavyo Wabunge mmetoa input muhimu na mmeturuhusu tuendelee na mchakato.
Kwa hiyo, hatua ambayo tunaendelea sasa ni zile hatua ambazo kwa kweli inatakiwa maoni yenu Wabunge nasi pamoja Serikali na Wabunge tuweze kulisukuma na Muswada huo uje mapema Bungeni. Kikubwa tunategemea mchango wenu mzuri ili mwisho wa siku tukishapitisha basi pasiwepo na kasoro ambazo tutaziona baadae.(Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na uwekezaji mzuri kufanyika wa kujenga Kiwanda cha Nguo cha MUTEX Musoma, lakini mpaka sasa kiwanda kile hakifanyi kazi. Je, ni upi mkakati wa Serikali kufufua kiwanda hicho?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja ya mikakati tunayoifanya Serikali ni kuona namna gani tunafufua viwanda ambavyo havifanyi kazi na sisi kama Serikali tumeshaanza kuona vile viwanda ambavyo vilikuwa vimepewa watu binafsi na hawaviendelezi kuvirudisha Serikalini na hatua ya pili sasa ni kuvitafutia wawekezaji ili waweze kuwekeza katika viwanda hivyo na kimojawapo ni kiwanda hiki cha MUTEX kilichopo kule Musoma, nakushukuru.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Naishukuru Serikali kwa kutuletea walimu wa sayansi 197, lakini bado tuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa masomo ya sayansi 889; je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Mkoa wa Mara ili waweze kutatua changamoto hii iliyowakabili na watoto wao waweze kufaulu vizuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa walimu wengi wa masomo ya sayansi ni walimu wa jinsia ya kiume: Je, Serikali haioni haja ya kuwa na program maalum ya kuwawezesha watoto wa kike kufundisha masomo ya sayansi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Chomete, la kwanza la upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi katika Mkoa wa Mara; kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba tunaajiri walimu 13,130 na tutazingatia maeneo yenye upungufu mkubwa hapa nchini ikiwemo Mkoa wa Mara. Hivyo nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Mkoa wa Mara nao upo katika mikoa ya kipaumbele kupata walimu hawa wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali la pili, nitoe rai kwa watoto wa kike waweze kwenda kwenye vyuo hivi vya ualimu na kusomea kufundisha masomo ya sayansi, ili tuweze kupata pool kubwa ya maombi ya watoto wa kike wanaoenda kufundisha masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tena kwamba katika ajira hizi mpya, tutahakikisha wale walimu ambao wanakidhi vigezo na ni walimu wa sayansi wanaajiriwa katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa maeneo haya wananchi walikuwa wanalima na wanayatumia kwa ajili ya kujipatia chakula. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwarudishia maeneo haya na ikawasimamia ili waendelee kulima na kuendelea kujipatia chakula?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Ghati, anayetetea wananchi wake wa Tarime, lakini nimweleze kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu la msingi ni kwamba, eneo lile limechukuliwa ili kutunza mazingira, lakini pia na kutunza shughuli za usalama ambazo wengine walikuwa wanatumia maeneo yale kulima kilimo cha mazao haramu ya bangi, kwa hiyo, uwepo wa magereza umesaidia kudhibiti hali ile ili isitokee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, mlima ule uko karibu sana na mjini. Nadhani shughuli za kilimo mijini zinaruhusiwa, lakini huwezi ukasema pale kwa namna mji unavyoendelea kukua patakuwa na maeneo mengi ya kulima zaidi ya kutunza usalama uliopo. Hata hivyo, tutaongea na Mamlaka ya Mji wa Tarime ili kuona kama kweli yako maeneo pembeni ya mlima yanaweza kutumika na wananchi basi wananchi waruhusiwe kuendelea na shughuli zao. (Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa, changamoto hii ya miundombinu ya maji mashuleni bado ni kubwa sana hasa katika Mkoa wa Mara. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha ina peleka miundombinu hii ya maji katika shule za Mkoa wa Mara?
Swali la pili, kwa kuwa sasa Serikali inatekeleza miradi ya ujenzi wa madarasa, ujenzi wa mabweni katika shule zetu. Je, haioni haja sasa ya kutenga fungu maalum wakati ikitekeleza miradi hiyo, inaweka na fungu la utekelezaji wa miundombinu hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Chomete, swali la kwanza juu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha changamoto hii inaisha.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, mradi huu wa SRWSS ni wa miaka mitano na utaisha mwaka wa fedha 2024/2025 na value yake jumla ni shilingi bilioni 119.6, hivyo basi Serikali inaendelea kadri siku zinavyokwenda kupunguza changamoto kwenye mashule kupitia mradi huu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la miradi yote inayotekelezwa sasa ya ujenzi wa madarasa na ujenzi wa shule mpya, katika shule zinazojengwa hivi sasa, shule mpya lakini katika ukarabati wa vyumba vya madarasa kwenye shule mbalimbali nchini kupitia miradi ambayo ipo ya EP4R, SEQUIP, BOOST na LANES na mingineyo, component ya matundu ya vyoo vilevile na maeneo ya kuoshea mikono ipo, kwa hiyo sasa hivi Serikali inapopeleka fedha katika maeneo mbalimbali inahakikisha na hizi facilities zinakuwepo.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naishukuru Serikali kwa jitihada zake ambazo inazifanya kuhakikisha huduma hii imefika mijini. Swali langu ni kwamba: Je, ni upi mkakati wa kutoa elimu ya kutosha kwa akina mama hasa walioko vijijini ili waweze kujua nini maana ya huduma ya M-mama ili kupunguza vifo vya mama na mtoto hasa kwa maeneo ya vijijini? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza lengo la huduma hii kwa kweli siyo mijini sana, kwa sababu mijini huduma ziko karibu na watu. Lengo letu ni kupeleka vijijini ambako tatizo la upatikanaji wa huduma ni kubwa na hasa pale mama mjamzito au mtoto mchanga anapokosa huduma ya ziada baada ya kusaidiwa kwenye zahanati. Kwa hiyo, lengo letu ni kuwafikia walioko vijijini. Tukipeleka kwenye mkoa, tunataka iende vijijini ambako ndiko mahitaji yalipo.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu, lakini kama nilivyosema wakati najibu maswali ya nyongeza, nawaomba Wabunge wa Viti Maalum, tushirikiane tuzungumze tuone namna ya kuifikisha elimu hii kwa akina mama kwenye maeneo yetu ili waweze kuitumia huduma hii kwa sababu ipo, ni bure na inapatikana masaa 24 na inaokoa maisha ya mama na mtoto. (Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Kivuko cha MV Musoma kilitolewa na Serikali na kivuko kilichopo hakikidhi mahitaji na kina changamoto nyingi sana, kinaweza kusababisha matatizo: Je, ni lini Serikali itarejesha Kivuko kile? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa miundombinu ya ujenzi kule Kinesi inahusisha maeneo waliyokuwa wanamiliki wananchi pale Kinesi: Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wale ili waweze kupisha mradi huo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kivuko cha MV Musoma ambacho kilikuwa kinafanya kati ya Mwigobero na Kinesi kilihamishwa kwenda kutoa huduma katika Kivuko cha Kisorya na Rugezi kwa sababu ya ukubwa wake. Kivuko cha Totuu kilitolewa Chato kwenda Musoma kufanya kazi kwa sababu kituo kilichokuwa kinafanya kazi kati ya Nansio kwa maana ya Kisiwa cha Ukerewe na Kisorya kilikuwa kimeharibika na kilikuwa kinahitaji matengenezo makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba Kivuko cha MV Ujenzi ambacho kinafanya kazi kati ya Rugezi na Kisorya tuko kwenye hatua za mwisho kabisa. Kilichokuwa kinafanyika ni kubadilisha engine, sasa tunapaka rangi. Tunaamini mwishoni mwa mwezi wa Saba, kivuko hicho kitakuwa kimekamilika ili MV Musoma iweze kurudi kwenda kufanya kazi kati ya Mwigobero na Kinesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu matengenezo au ujenzi katika eneo la Kinesi, tayari tumeshafanya tathmini na tumeshaainisha wananchi watakaopisha ujenzi wa maegesho. Hivi tunavyoongea sasa hivi, taratibu za kuandaa majedwali ya kuwalipa zinaendelea ili mwakani tunapoanza tuweze kujenga maegesho upande wa Kinesi pamoja na miundombinu yake, ahsante.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi, kama ilivyo katika zao la mpunga, kahawa aina ya Arabica inalimwa Mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime na hasa Tarime Vijijini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wakulima wale ili waweze kuongeza uzalishaji katika zao hilo ili kuinua uchumi wao na uchumi wa nchi yetu.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya mikakati tuliyonayo na kukuza zao la kahawa mojawapo ni uzalishaji na usambazaji wa miche bora ya kuwafanya wakulima wengi waweze kuzalisha kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu tumejipanga kuzalisha miche milioni 20 kuwafikia wakulima wengi kadri iweekanavyo na hivyo pia tutawagusa wakulima wa Mkoa wa Mara.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Wilaya ya Butiama haina Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ghati Chomete, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Butiama ni moja ya Wilaya mpya ambazo hazina Vituo vya Polisi ngazi ya Wilaya na Kata zake mbalimbali hazina vituo hivyo. Kama nilivyokwishasema kwenye jibu langu la msingi, kipaumbele katika ujenzi wa Vituo vya Polisi utazingatia Mikoa, Wilaya na Kata ambazo hazina kabisa vituo lakini msisitizo utawekwa kwa wale ambao tayari wana maeneo na wameanza kujitolea. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya ya Butiama ni moja ya eneo litakalozingatiwa katika bajeti ijayo. (Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa miradi ya TACTIC, imeshaanza na Halmashauri ya Manispaa ya Mji wa Musoma haimo kwenye miradi hiyo kwa sasa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mradi huo unaanza? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Stendi ya Mabasi ya Mji wa Musoma ina hudumia wananchi kutoka Tarime, Serengeti, Rorya, Butiama, Musoma Vijijini na maeneo mengine yanayozunguka Mkoa wa Mara. Kwa sasa stendi ile ni chakavu sana na haipitiki hasa mvua ikinyesha. Je, Serikali ina mkakati upi wa muda mfupi, kuhakikisha stendi ile inaendelea kuingilika ili kusubiri mkakati wa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Miradi ya TACTIC, itaanza utekelezaji wake rasmi mwaka wa fedha 2022/2023, lakini Halmashauri hii ya Musoma pia ipo kati ya zile lot ya kwanza, ya pili na ya tatu ambapo tutakwenda kutekeleza. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba itapokuwa inaanza mwaka ujao wa fedha, basi Manispaa hii ya Musoma hii stendi itakuwa miongoni mwa zile lot tatu ambazo zipo kwenye TACTIC.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Stendi ya Mabasi ya Musoma Mjini kuwa ni chakavu sana na inahudumia wananchi wengi. Natoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma kuhakikisha wanatenga fedha za mapato ya ndani, kwa sababu stendi ni kipaumbele lakini ni chanzo cha mapato. Kwa hiyo, lazima mapato ya ndani yaanze kuboresha stendi ile wakati wanaandaa andiko la kuomba fedha kama mradi wa mkakati kwa ajili ya kukamilisha. Ahsante.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Wilaya ya Butiama haina Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ghati Chomete, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Butiama ni moja ya Wilaya mpya ambazo hazina Vituo vya Polisi ngazi ya Wilaya na Kata zake mbalimbali hazina vituo hivyo. Kama nilivyokwishasema kwenye jibu langu la msingi, kipaumbele katika ujenzi wa Vituo vya Polisi utazingatia Mikoa, Wilaya na Kata ambazo hazina kabisa vituo lakini msisitizo utawekwa kwa wale ambao tayari wana maeneo na wameanza kujitolea. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya ya Butiama ni moja ya eneo litakalozingatiwa katika bajeti ijayo. (Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali iliahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kilometa tano katika Halmashauri ya Mji wa Tarime. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa ili mradi huo uanze?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ili barabara hiyo ya kilometa tano ambayo imeahidiwa na Serikali Tarime iweze kuanza kujengwa, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge kuweza kuona ni nini kinaweza kikafanyika na fedha ikipatikana basi ahadi hii iweze kutekelezwa mara moja.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo taarifa kwamba Mheshimiwa Rais amenunua mashine za kusafisha figo 171. Je, hospitali hii ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere maarufu kwa jina la Kwangwa itapata mgao huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Rais wetu Samia Suluhu Hassan amenunua mashine 171 na mashine 110 zimeshasambazwa kwenye hospitali 11 na sasa Waziri wetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu ameshaelekeza mashine 11 ziende kwenye hospitali aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia jengo la zahanati lililojengwa katika Kata ya Mkoma, Wilaya ya Rorya kwa nguvu za wananchi mpaka kufikia hatua ya kupaua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati ambayo imejengwa katika Kata ya Mkoma katika Jimbo la Rorya, ni kweli, kwanza nichue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete kwa namna ambavyo amefuatilia kuhusiana na jambo hili, pia niwapongeze sana wananchi wa kijiji hiki kwa kutoa nguvu zao na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua jitihada za wananchi na itaingiza kwenye mpango wa kuweka fedha mapato ya ndani au Serikali Kuu kwa ajili ya kuunga mkono nguvu za wananchi na kukamilisha zahanati hiyo, ahsante. (Makofi)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kumekuwa na tatizo la MSD kupeleka madawa kwenye hospitali, vituo vya afya yanayokaribia kwisha muda wake. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha tatizo hili au jambo hili linamalizika kabisa ili lisilete madhara kwa wananchi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Kituo cha Afya cha Muriba katika Jimbo la Tarime Vijijini kinahudumia wananchi wa Kata tano ambao idadi yao ni 73,000 na zaidi, lakini idadi ya dawa zinazopelekwa ni za kuhudumia wananchi wa Kata moja yaani wananchi 14,000. Je, ni kwa nini Serikali isipeleke dawa kulingana na idadi ya watu wanaohudumiwa pale? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishakubaliana Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Afya kuhusiana na dawa zinazopelekwa kwenye vituo vyetu kuwa na muda mrefu kabla hazijafikia expiring date yake. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tangu Mwaka wa Fedha 2021/2022, tayari kwa kiasi kikubwa sana dawa zinazopelekwa kwenye vituo vyetu angalau zina miezi 12 kabla ya ku-expire na tutaendelea kuhakikisha kwamba suala hili linasimamiwa hivyo ili wananchi wetu wapate dawa salama pia ziweze kutumika badala ya kuharibika zikiwa vituoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wakati tunapeleka dawa kwenye vituo vya afya, hatuangalii kituo cha afya kiko katika Kata ipi kwa maana kwamba hatuweki mipaka kwamba wananchi wa kata ile tu ndiyo watapata huduma, tunaangalia catchment population ya wananchi wote hata kama ni kata tano, sita zinapata huduma katika kituo kile basi tunahakikisha tunapeleka fedha kwa ajili ya dawa zinazotosha wananchi wote ambao wanapata huduma ile. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutakiangalia kituo hicho cha afya ili tuweze kukiongezea pia bajeti ili kihudumie vizuri wananchi wa kata za Jirani. Ahsante.