Supplementary Questions from Hon. Justin Lazaro Nyamoga (71 total)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa ni zaidi ya miaka 30 sasa tangu wakulima wa chai wa Kilolo wapande chai yao na kujengewa kiwanda ambacho hakijawahi kufanya kazi; na kwa kuwa katika muda huo wako Mawaziri kadhaa na Manaibu wameenda kule wakapiga picha kwenye mandhari nzuri za mashamba yale na kuahidi wananchi wale kwamba shughuli hiyo itakamilika mapema iwezekanavyo na hawakurejea tena. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wananchi wa Kilolo kwamba sasa kiwanda kile kilichojengwa na hakikuwahi kufanya kazi, kitafanya kazi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa michakato mingi imepita ya kumpata mwekezaji na mchakato wa mwisho ulikuwa mwaka 2019 na wawekezaji walijitokeza na wakapatikana na wako tayari, na kwa kuwa uwekezaji huu haukukamilika kutokana na urasimu wa Serikali. Je, Serikali iko tayari kuwawezesha wale wawekezaji kwenda kuwekeza badala ya kuanza mchakato mwingine ambao unaweza ukachukua miaka mingine 30?Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Serikali imefanya jitihada nyingi sana kuhakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi. Kwa taarifa tu ni kwamba katika miaka ya nyuma tayari kuna wawekezaji walikuwa wamejitokeza kwa ajili ya kuwekeza katika kiwanda hicho na mmojawapo ni Mufindi Tea and Coffee Company chini ya DL Group. Hata hivyo, baada ya kupitia mchakato wa upatikanaji wa mwekezaji huyo ilionekana kwamba kuna baadhi ya vipengele vilirukwa lakini pia baada ya kuwa na due diligence ya kutosha ilionekana kwamba mwekezaji huyo alikuwa hana uwezo wa kuwekeza katika kiwanda hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, juhudi hizo bado zinaendelea na kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba sasa tunaandaa andiko maalum ambalo litaangalia namna bora ya uendeshaji wa kiwanda/shamba lile likihusisha ushirikishwaji wa wadau wote kwa maana ya wakulima wadogo, halmashauri ya Kilolo lakini pia na Msajili wa Hazina ambaye ndiye anasimamia kiwanda hicho. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Kilolo inafanana kabisa na Wilaya ya Mufindi; na kwa kuwa vyanzo vya mito kama Mto Mtitu na Mto Lukosi vinachangia kwa kiwango kikubwa kwenye vyanzo vikubwa vya mabwawa na pia ni vyanzo ambavyo vinasaidia katika nchi yetu. Je, ni lini Wizara itajibu kiu ya wananchi kwa kutatua tatizo la maji kwa kutoa fedha kwenye Mradi wa Mto Mtitu ambapo tayari RUWASA walishatoa na maji hayo yatafika hadi Iringa Mjini lakini pia yatahudumia kata zaidi ya 15 za Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge alivyokiri kwamba tayari shughuli zinaendelea pale kupitia Wakala wetu wa Maji Vijijini (RUWASA). Kadiri tunavyopata fedha tunahakikisha tunagawa katika maeneo yote ambayo miradi ipo kwenye utekelezaji.
Kwa hiyo, pamoja na mradi huu ambao upo katika Jimbo lake na ni Jimbo ambalo tumelitendea haki kwa sehemu kubwa sana, tutaendelea kupeleka fedha kadiri tunavyopata ili kuhakikisha mito yote ambayo mmebarikiwa watu wa Kilolo na maeneo mengine yote tunashughulikia kwa wakati. Lengo la Wizara ni kuhakikisha wananchi wanapata maji bombani na si vinginevyo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri ambayo yanatoa matumaini kwenye maeneo yale ambayo kumewekwa ahadi za kuweka minara. Hata hivyo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Kata ya Masisiwe na Kata ya Udekwa hakuna mawasiliano kabisa na tayari watu wawili wameanguka kutoka kwenye miti wakijaribu kutafuta mtandao na kuumia na kulazwa katika Hospitali ya Ilula mmoja na ya Kilolo mmoja.
Sasa, je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi katika kata hizi, kwanza ili kutoa pole kwa watu hao, lakini pili ili kuweza kuona yeye mwenyewe na nafahamu yeye ni mtu ambaye ametembelea maeneo mengi ili aweze kujionea hali halisi na kuweka msisitizo wa kuweka minara katika maeneo hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, maeneo yenye mitandao, yenye wananchi wenye matumiani makubwa sana yakutumia vifurushi vya bei ndogo, yalikatishwa tamaa na ongezeko la bei ya vifurushi ambapo ilitarajiwa vishuke. Tunaishukuru Serikali kwamba imerudisha katika ile hali ya kawaida, lakini matumaini ya wananchi ilikuwa ni kushushwa. Sasa je, ni lini Serikali itarudia ule mpango wake wa awali wa kushusha vifurushi, ili Watanzania wakiwemo wananchi wa Kilolo ambao wanataka sana kutumia vifurushi hivi katika shughuli zao za kibiashara, waweze kufurahia bei nafuu ya vifurushi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba maswali yangu hayo mawili madogo yajibiwe.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, nimesema kwamba Serikali tayari imeshaanza kufanya tathmini katika Kata ya Irole pamoja na Masisiwe ili tuweze kuingiza katika mpango wa awamu ya tano na ya sita katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la pili, nafahamu kabisa hili ni swali ambalo Waheshimiwa Wabunge wote wangeweza kuliuliza. Naweza kusema kwamba kazi ya Serikali ya kwanza ni kuhakikisha kwamba ina-stabilize bei iliyopo na hilo ndilo ambalo tumelifanya kwa sasa. Naona kwamba kulikuwa na changamoto ambapo makampuni yaliweza kuwa na bei tofauti tofauti ambazo ziliwaumiza sana wananchi, lakini Serikali ikatoa maelekezo ya kuhakikisha kwamba bei ya hapo awali inarejea kama ambavyo Watanzania walikuwa wanakusudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafahamu kwamba, katika kurejesha hizi gharama za vifurushi, kuna changamoto yake. Kupandisha kifurushi ni mchakato ambao unahusisha ujenzi wa mifumo ambayo itaweza ku-support hicho kifurushi kipya ambacho utakiingiza sokoni. Vile vile unaposema kwamba urudishe maana yake kwamba unaaanza kufanya reverse engineering maana yake unaanza kurudisha kwenye mfumo ule ulioko zamani, kama ulikuwa umeshautoa maana yake sasa inabidi uanze kuusuka tena ili uanze kutoa bei ambazo zilikuwa zinatolewa hapo kabla.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge pia ameongelea namna gani Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba bei hizi, zinashuka zaidi ya sasa ambavyo Watanzania wangetarajia. Changamoto ya biashara ya mawasiliano, kitu ambacho tunakiangalia Serikali ni kwamba hapa tunatakiwa kuangalia tuna-balance namna gani kati ya consumer, watumiaji wa huduma, Serikali pamoja na mtoa huduma. Ni lazima tuangalie ile production cost yake, ni lazima aweze kufanya biashara katika kiwango ambacho anaweza akapata faida ili Serikali pia iendelee kupata kodi lakini kodi hizohizo ziweze kurudi kujenga barabara na zahanati na hatimaye Wabunge katika Majimbo yao wanayotoka tuweze kushuhudia kuna mabadiliko ya barabara na zahanati ambazo zitakuwa zinajengwa. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Wilaya ya Kilolo haina majengo ya Mahakama na hivi sasa majengo yanayotumika ni ya Mahakama ya Mwanzo. Je, ni lini Serikali itajenga majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Kilolo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Tarafa ya Mazombe kuna Mahakama ambayo ilijengwa enzi za mkoloni na haijawahi kufanyiwa ukarabati wowote. Je, ni lini Serikali itakarabati majengo hayo ili yaweze kuendana na hadhi ya sasa na haki iweze kutolewa katika mazingira mazuri?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Wilaya ya Kilolo itaingizwa kwenye mpango wa ujenzi Kwa kipindi cha mwaka 2022/2023. katika kipindi kijacho cha fedha tunajenga ile Mahakama ya Mwanzo ambayo ipo Tarafa ya Mahenge na kwa ile ya Wilaya tutaanza kuiweka kwenye mpango nilioutaja.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu ukarabati wa ile Mahakama ya Mazombe, hii nayo tutaiweka kwenye mpango wa 2022/2023. Hii itaendana na ukarabati wa maeneo mengine yote ambayo tumeendelea kuweka mikakati kwa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, napenda tu kusema, katika kipindi cha mwaka 2021/2022 baadhi ya miradi yetu ambayo itaendeshwa katika kipindi hicho tumeiainisha tayari na katika ngazi ya wilaya tutakuwa na Mahakama nyingi sana ingawa kwenye mpango huo wilaya yake haipo. Kutokana na muda ningeweza kuziorodhesha wilaya hizi lakini kwa sasa inatosha kusema hivyo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kata ya Udekwa, Kata ya Ukwega, Kata ya Kimara na Kata ya Idete hazina mawasiliano kabisa kutokana na mvua ambazo zimeharibu kabisa barabara.
Je, Serikali ipo tayari kutoa fedha za dharura kwa ajili ya barabara ya kata hizi ambazo zina mazao mengi ili ziweze kutengenezwa na wananchi waweze kuendelea na shughuli zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba fedha za dharura katika barabara ambazo ameziainisha hapa. Nimwambie tu moja ya kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na TARURA katika kipindi hiki ni pamoja na kupeleka fedha za dharura katika maeneo yote ambayo yalikuwa yemeathirika sana na mvua kubwa ambazo zilikuwa zimenyesha. Pamoja na fedha ndogo ambayo tunayo kwa sababu katika fedha za dharura ambayo tunayo kwa mwaka huu ambayo unakwisha ni kama bilioni 12 ambazo tulikwenda kuziainisha katika yale maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ameainisha maeneo hayo, niseme tu kabisa Ofisi ya Rais, TAMISEMI itapitia hayo maeneo na ione kama kuna udharura wa haraka kabisa ili tuweze kupeleka fedha na hizo barabara ziweze kupitika. Ahsante sana.
MHE. LAZARO J. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali inatarajia kupata fedha hizo lini ili wale wananchi waweze kulipwa fidia badala ya kuendelea kusubiri kwa muda mrefu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na umbali uliopo kati ya Makao Makuu ya Wilaya na Kituo cha Polisi ambacho kinatumika kama Makao Makuu ya Polisi, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha za OC ili ofisi ile ya Polisi ya Wilaya iweze kujiendesha bila karaha wala kuombaomba fedha kwa wadau wengine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ameuliza, je, lini Serikali italipa fidia? Nataka nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inao mpango na italipa fidia wananchi hao kwa ajili ya eneo hilo kwa sababu inatambua umuhimu wa uwepo wa Kituo hicho cha Polisi ili wananchi waweze kupata huduma hizo. Kubwa zaidi tayari tumeshatoa maelekezo na wameshafanya tathmini wataalam kutoka Halmshauri ya Wilaya ya Kilolo inayohitajika kwa ajili ya fidia hiyo na tayari tumeshaelekeza pa kwenda kupata fedha hizo kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hao. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kufanya juhudi kuona namna bora ya kuwalipa fidia wananchi hao. Kubwa Mheshimiwa Mbunge aendelee kuzungumza na wananchi wake ili waendelee kuwa na subra jambo hilo limo mbioni kushughulikiwa.
Mheshimiwa Spika, swali la pili anauliza kama Serikali ipo tayari kuongeza OC. Niseme tu kwamba Serikali ipo tayari kuongeza OC lakini ni pale ambapo tutakuwa na fedha ya kutosha kufanya hivyo. Kwa hiyo, kwa sasa waendelee kuwa na subra hivyo hivyo tubananebanane lakini tunao mpango huo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo upo mbadala ambao tumeshauchukua, kwanza tumeongeza operesheni ama doria za mara kwa mara katika maeneo ambayo wananchi wako mbali na vituo vya polisi ili waweze kupata hizo huduma za ulinzi. Vilevile tunaendelea kusisitiza ulinzi shirikishi ambapo inasaidia huduma za ulinzi kufika mpaka maeneo ya vijijini kwenye kata. Lengo na madhumuni ni wananchi waendelee kupata huduma za ulinzi na waishi kwa amani.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JUSTINE L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, aHsante kwa nafasi hii.
Kwanza nashukuru sana kwamba Waziri wa Kilimo ametembelea shamba la chai pale Kilolo Jumamosi wiki iliyopita na kujionea mwenyewe lile pori ambalo nimekuwa nikilisema hapa. Na kwa kuwa Benki ya Kilimo iko tayari na ina fedha tayari kwa ajili ya kukopesha mwekezaji yeyote, sasa je, ni lini ule mchakato wa kutafuta mwekezaji utaanza tena bada ya kuwa ulisimama katika kipindi hiki cha mwaka karibu mmoja uliopita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza Waziri wa Kilimo Profesa Mkenda amekuwepo huko wiki iliyopita akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Tanzania Agricultural Development Bank. Baada ya muda mrefu kuhangaika kutafuta mwekezaji, position ambayo tunayo kama Wizara ya Kilimo na ambayo tutaenda kuitekeleza ni kuanzisha special purpose vehicle ambayo shareholding structure itawahusisha wakulima wadogo na Tanzania Agricultural Development Bank kwa sababu wao ndio wanaleta mtaji na wao wataleta menejimenti.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba ule mpango wa kuhangaika kutafuta mwekezaji wa nje tumeachana nao, tutatumia our own resources kufufua hilo shamba na tutaweka menejimenti ambayo ita- run, kwa sababu tumefanya majaribio kwenye Vyama vya Ushirika vya KAKU, Mbogwe na Chato tumefanikiwa.
Kwa hiyo, huu ndio utakuwa mwelekeo kwenye maeneo ambayo tutaweka mitaji, tutaanzisha special purpose vehicle, halafu tutaendelea kufanya biashara na ushirika utashindana. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika ahsante sana, kwanza nishukuru sana kwamba wakati wa kuchangia Mpango nilielezea kutokurudhishwa kuhusu mkandarasi aliyekuwa anaweka ile lami ya kilometa 10 na amebadiliswa na speed yake sasa yule anaeendelea kwa kweli ni nzuri na inaridhisha.
Sasa maswali yangu, kwa sababu ukiangalia kuna Project ya World Bank ambayo barabara hii kilometa zote 33.6 zilikuwemo na ninafahamu kwamba Waziri wa Fedha alisaini mkataba na hawa watu wa World Bank kwa ajili ya hiyo project. Je, upatikanaji wa fedha hizo utaondoa huo ujenzi wa awamu na kufanya barabara hii iweze kujengwa yote na kukamilika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Waziri atakuwa tayari kuambatana pamoja na mimi kwenda kuangalia hasa maeneo ya milimani kwa barabara hii ambayo hayapitiki ili tuweze kupata ufumbuzi na wananchi waweze kupita vizuri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru kwa kutambua jitihada za Serikali na kwamba ni sikivu, alichokiomba tumeshakitekeleza kama Wizara. Pia nimpongeze kwa kuwapigania sana watu wa Kilolo kuhusu hii barabara, sasa majibu yangu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema kwamba Waziri wa Fedha amesha saini mkataba huu na labda tu nielezee kwamba mkataba huu unafadhiliwa na Benki ya Dunia ambao umechukua muda kutokana na ukweli kwamba mradi huu ulikuwa una cover mikoa michache, kwa hiyo Serikali iliona huu mradi utanuliwe, pia ulikuwa unalenga sana barabara za changarawe, kwa hiyo, Serikali ikaona hatuwezi tukachukua fedha World Bank kwa ajili ya changarawe, kwa hiyo, kukawa na majadiliano ili kuuboresha, kwanza uchukue mikoa mingi pia uwe ni kwa kiwango cha lami ambapo ni barabara za kutoka vijijini kuunganisha na barabara za mikoa na barabara kuu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya kusaini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii kilometa zote 33 zipo kwenye mpango, na zitajengwa ndio maana tunafanya design upya kuhuisha ile design iliyokuwepo ili iendani na kiwango cha sasa cha barabara.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mimi Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba nipo tayari kuambatana naye kwa ajili ya kwenda kuangalia hizi barabara na kuhakiki jinsi ujenzi unavyoendelea, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa moja kati ya vigezo vilivyopo katika mwongozo ni halmashauri iwe na hati safi kwa miaka mitatu mfululizo; na kwa kuwa kigezo hiki ni kandamizi kwa wananchi kwa sababu wanaosababisha hati kuwa chafu au safi siyo wananchi bali ni watumishi wa halmashauri.
Je, Serikali haioni kwamba hata kama kuna marekebisho yanafanywa kigezo hiki kiondolewe mara moja ili halmashauri zote zipate haki ya kuomba miradi hii ya kimkakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapoandaa miradi hii ya kimkakati moja katika dhamira zake kubwa ni kuhakikisha kwamba miradi hii inakuwa na tija kwa ujumla wake. Ndiyo maana miongoni mwa vigezo, ukiachilia mbali hicho ambacho Mheshimiwa Mbunge amekizungumza, ni kuangalia mtiririko mzima wa fedha katika mradi ili kuona kwamba mradi ule utaweza kujiendesha kwa faida na baadaye uweze kuwa na tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hati chafu inapokuja inatoa kiashiria hasi juu ya ufanisi wa mradi husika. Hata hivyo kwa kuwa jambo hili ni la kitaalam, naomba nilichukue halafu tukaiwasilishe hoja yake kwa wataalam, tuone jinsi gani inaweza ikafanyika bila kuathiri lengo halisi la kuona tija inapatikana katika mradi ule, lakini wakati huohuo isiathiri dhamira njema ya wananchi kwa makosa ambayo hayawahusu.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ningependa tu kujua ni lini Serikali sasa itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Kilolo ambayo tayari ina ongezeko la vijana na chuo kinahitajika ili nao waweze kujiendeleza kama ilivyo kwenye maeneo mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba sasa kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa Serikali inaendelea na ukamilishaji wa vyuo vile vya VETA katika wilaya 29 ambazo sasa zinakwenda kukamilisha, lakini siyo tu kukamilisha na kuhakikisha vile vile vifaa kwa ajili ya mafunzo vinaweza kupatikana. Kwa hiyo katika mwaka huu wa fedha, juhudi za Serikali tunajikita kwenye eneo hilo, kukamilisha vyuo hivi vya wilaya 29, lakini na vile vya mikoa vinne. Kwa hiyo, nimhakikishie, baada ya ukamilishaji wa vyuo hivi, Serikali sasa tunajipanga vizuri kutafuta fedha ili kuweza kufikia wilaya zote kama sera yetu inavyosema kwamba kila wilaya ni lazima iwe na Chuo cha Ufundi cha VETA. Ahsante sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nakiri ni kweli nimeona kazi hiyo inaendelea katika kata hizo zilizotajwa. Pamoja na hayo nina maswali yangu mawili madogo ya nyongeza: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; katika utekelezaji wa miradi hii maeneo mengi ya huduma za jamii, hasa shule za msingi, shule za sekondari, makanisa na misikiti, hasa maeneo ambayo yako mbali kidogo na katikati ya miji, haziwekewi kipaumbele sana kupata umeme. Je, Serikali haioni kwamba ni vizuri kutenga bajeti maalum kwa ajili ya huduma za jamii, hasa sehemu ambazo watoto wetu wanasoma kwa sababu ni muhimu sana kuwa na umeme?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika miji mbalimbali midogo kwa mfano Mji wa Ilula uliopo Kata ya Nyalumbu, lakini pia Mji Mdogo wa Boma la Ng’ombe pamoja na Mji Mdogo wa Kidabaga, kumekuwa na kero kubwa ya kukatika umeme mara kwa mara. Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza kero hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyamoga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwenye utekelezaji wa Mradi wa REA III, Mzunguko wa Pili, tuliwaelekeza wakandarasi wanaopeleka umeme katika maeneo yetu pamoja na wale wanaoshirikiana nao, wenzetu wa TANESCO, kuhakikisha kwamba maeneo ya taasisi na miundombinu mingine kama elimu, afya na taasisi za dini yanakuwa ni maeneo ya kipaumbele. Kama alivyosema Mheshimiwa Nyamoga, ni kweli maeneo yale ambayo tayari umeme umeanza kwenda kwenye maeneo ya makao makuu ya vijiji tayari tunapeleka.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Nyamoga pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba kadri tunavyozidi kupeleka umeme kwenye maeneo ya pembeni kwa maana ya vitongoji, tutazidi pia kufika katika taasisi hizo na ni maelekezo ya Serikali kwamba umeme ufike katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la kufurahisha zaidi ni kwamba, sisi Wizara ya Nishati pia tumepewa kipande kidogo cha bajeti katika ile 1,300,000,000 za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan zinazopeleka maeneo ya UVIKO tunaopambana nao na sisi katika miundombinu hiyo mipya ambayo inajengwa tumepatiwa pesa kiasi fulani ambapo tutaweza kuongeza kasi ya kupeleka umeme katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili, ni kweli kwamba kumekuwa kuna makatizo ya umeme kwenye maeneo mbalimbali, lakini ni jambo ambalo lililopangwa kwa ajili ya kufanya marekebisho ya miundombinu. TANESCO katika mwaka huu wa fedha inazo bilioni karibu zaidi ya 200 kwa ajili ya marekebisho ya miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge waendelee kutuvumilia kidogo tukiwa katika hatua hizi na harakati za kuhakikisha tunaboresha miundombinu yetu. Na kwa Iringa tuna takribani bilioni moja na milioni 500 kwa ajili ya marekebisho ya miundombinu. Tutaendelea kuwahimiza wenzetu watoe taarifa sahihi na kwa wakati sahihi ili Waheshimiwa umeme unapokatika, basi wananchi waweze kufahamu nini kinaendelea. Nakushukuru.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika uendelezaji wa sekta ya afya pamoja na sekta nyingine kuna watumishi ambao wanahitajika sana sasa hivi, kwa mfano clinical officers, wafamasia na hawa hawasomi vyuo vikuu. Kumekuwa na pendekezo la muda mrefu sana la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati ambalo ni hitaji kubwa sana katika nchi yetu kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali sasa ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati pia wanapata mikopo kwa sababu, ndio mahitaji makubwa katika nchi yetu kulingana na miundombinu tunayoijenga kwenye maeneo ya vijijini ambayo yanahitaji sana hiyo kada ya kati kulitumikia Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli analozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba, uhitaji uko mkubwa sana kwenye vyuo vyetu vya kati, lakini kama tunavyofahamu na kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi, jambo kubwa hapa ni suala la bajeti. Iwapo kama bajeti yetu inaruhusu tunaweza tukavifikia vyuo vikuu vyote, lakini vilevile pamoja na vyuo vya kati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, bajeti itakaporuhusu tutahakikisha tume-cover kwanza eneo lote la vyuo vikuu halafu tutaangalia namna gani sasa mikopo hii inaweza kwenda kuwafaidisha au kuwanufaisha wenzetu wale ambao wako katika vyuo vya kati. Ahsante sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ni zaidi ya miaka 10 sasa tangu Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula imeanzishwa, ningependa kujua ni tathmini gani au ni utaratibu gani unatumika ili kupandisha hadhi kutoka kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo kwenda kuwa Halmashauri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ningependa kujua katika ugawaji wa halmashauri kipo kigezo cha idadi ya watu na katika maeneo yenye hifadhi kubwa ya misitu na maeneo yaliyohifadhiwa na mbuga kama Kilolo kigezo hiki kinakuwa tishio kusababisha kuchelewa kugawa kwa halmashauri pamoja na ukubwa wake. Je Serikali iko tayari kuangalia kigezo hiki na kuangalia zaidi ukubwa ili wananchi waweze kufikiwa na huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa mamlaka mpya zikiwepo halmashauri za miji zinategemea kukidhi vigezo vilivyowekwa ili halmashauri iweze kupewa mamlaka halisi ya kuwa halmashauri kutoka malmaka ya mji mdogo. Ni kweli kwamba Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula ina zaidi ya miaka 10 lakini taratibu za kuomba kuwa Halmashauri ya Mji ni zilezile ambazo zinatumika kuomba Halmashauri ya Wilaya. Kwa maana vikao vya kisheria katika vijiji na mitaa, kata ngazi ya wilaya pamoja na DCC na RCC. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na kuomba Wilaya igawiwe kuwa wilaya mbili lakini pia wafuate utaratibu huo kwa Halmashauri ya Mji wa Ilula ili tathmini ifanyike kuona kama kama inakidhi vigezo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na ukubwa wa kijografia wa Wilaya ambayo ina misitu mingi lakini wananchi wachache. Kigezo cha wananchi ni kigezo muhimu sana kwa sababu tunapeleka mamlaka mpya kuhudumia wananchi kwa hiyo idadi ya wananchi ndio sababu ya msingi zaidi ya kutenga halmashauri mpya badala ya eneo la misitu, lakini pia kwa maana ya ukubwa ambao hakuna idadi ya watu. Kwa hiyo, suala hilo ni muhimu na tutaendelea kuhakikisha kwamba, tunalizingatia katika kugawa mamlaka mpya. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Huu ukanda wa Milima ya Udzungwa unaelekea kwa kiwango kikubwa kwenye Wilaya ya Kilolo na huu ukanda unaungana na Kata ya Udekwa na Kata ya Ukwega ambayo pia, inaaminika kuwa na madini. Je, Wizara iko tayari kutuma wataalam kufanya utafiti ili kama madini hayo ya dhahabu yapo, kama ilivyo kule Ulanga, yaweze pia kuchimbwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nyamoga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama nilivyotangulia kusema, kama Wizara ya Madini, kupitia taasisi zake GST na hata STAMICO, tuko katika mpango mahususi wa kuendelea kufanya utafiti wa kubaini maeneo yote yenye madini nchini na itahusisha pia, eneo lake na sehemu alizozitaja kwa sababu, lengo letu kama Taifa ni kuhakikisha kwamba, rasilimali madini inakwenda kuzalishwa ili iletee Taifa letu tija. Nimhakikishie kwamba na nitumie pia nafasi hii kuiagiza taasisi yetu ya GST katika mpango kazi wao wa mwaka huu waweke katika utaratibu na ratiba safari ya kuelekea kule kufanya utafiti kwenye eneo la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali la kwanza; katika Kijiji cha Mgowelo ambacho kiko katika Kata hiyo hiyo ya Nyanzwa, kumetengwa zaidi ya hekta 3000 kwa ajili ya block farming. Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti kwenye eneo hilo na kuona umuhimu wa kuweka skimu pia kwenye hilo eneo kwa sababu ni hekta nyingi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwenye Bunge lililopita, niliomba Naibu Waziri au Waziri kutembelea eneo hili na kuangalia changamoto tunazopata za skimu mbalimbali, lakini mpaka sasa ziara hiyo haijafanyika. Je, Waziri ananiahidi lini atafika Jimboni Kilolo kwa ajili ya kutembelea na kuona tunaweza tukashauriana vipi? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, maswali yake mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kufika jimboni kwake naomba nimuahidi yeye na wananchi, nitakwenda mwenyewe baada ya Bunge hili kwa ajili ya kwenda kufanya kazi hiyo pamoja na kuangalia mwendelezo wa mradi wetu wa pamoja wa chai ambao yeye mwenyewe alikuwa muasisi wa kuanzisha huo mradi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hii block farm, naomba nimwombe baada ya kikao cha Bunge tukutane ofisini ili nimkabidhi timu ya watu ambao wataenda kufanya soil analysis na kuchukua mipaka ili tuiweke kwenye mipango ya Wizara.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hospitali ya DDH ya Ilula, bado inategemewa sana wananchi wa Tarafa ya Mazombe na Tarafa ya Mahenge. Je, Serikali ina mpango gani wa kuendelea kuipelekea fedha hospitali ili iweze kutoa huduma bora kama ilivyokuwa ikitoa mwanzo ilivyokuwa DDH kabla ya kujengwa hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justine Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha inawezesha hospitali zetu hizi za DDH kuendelea kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo hayo. Kwanza kwa kuhakikisha kwamba fedha za mfuko wa pamoja health center basket fund zinaendelea kupelekwa, Hospitali hii ni moja ya hospitali zinazoendelea kupewa fedha hizo ili kuziwezesha kujiendesha na kutoa huduma bora, lakini pia kuangalia uwezekano wa kuendelea kuwapatia watumishi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuiunga mkono hospitali hii ili iendelee kutoa huduma kwa wananchi wa Mazombe na Tarafa zingine za karibu.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, kwa miaka 20 sasa Wilaya ya Kilolo haina Makao Makuu ya Polisi na wala kwenye Wilaya penyewe hakuna Kituo cha Polisi.
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi za viongozi mbalimbali kujenga Makao Makuu ya Polisi katika Wilaya ya Kilolo kwenye Mji wa Kilolo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba Mheshimiwa kwenye Jimbo lake la Kilolo kama ambavyo Wilaya kadhaa zimekuwa zina ukosefu wa Vituo vya Polisi vya Wilaya na hii ni moja kati ya mambo ambayo jana niliyazungumza na mikakati ya Kiserikali ya kiujumla ya kukabiliana na tatizo hili, hivyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute Subira, lakini suala hili tumelichukua kwa uzito wake.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa TANROADS Mkoa wa Iringa walitii agizo la kwenda kuangalia barabara ya Mchepuko wa Mlima Kitonga, na tayari wameshafanya maandalizi ya awali. Je, Serikali inasemaje kuhusu kuanza usanifu na kuijenga barabara hiyo ya Mchepuko wa Mlima Kitonga ili wananchi waweze kupita kwa urahisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama alivyokiri kwamba tayari tumeshatoa maelekezo na baada ya kuipitia barabara sasa kinachofuata ni kuanza kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, suala hilo litafanyika kwa sababu ndiyo barabara itakayotuokoa ikitokea changamoto yoyote katika Mlima kitonga. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru: -
Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa chuo cha ufundi VETA kwa Wilaya ya Kilolo kitajengwa kama ambavyo zimekuwa ahadi za Serikali kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni sera ya Wizara ya Elimu kwamba, katika kila wilaya tunakwenda kujenga chuo cha VETA. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa vile sasa tumekamilisha ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 29 na vile vinne vya Mikoa ambavyo tunakadiria kunako mwezi Mei tutakwenda kumaliza katika mwaka ujao wa fedha tutaendelea na ujenzi katika maeneo ambayo bado vyuo havijaweza kujengwa. Ninakushukuru sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kata ya Masisiwe haijawahi kuwa na mnara wala mawasiliano tangu uhuru wa nchi yetu.
Je, ni lini Serikali itajenga mnara katika kata hiyo ili wananchi waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali ilileta vijiji ambavyo vinaenda kupatiwa mawasiliano ikiwemo kata ya Masisiwe. Mheshimiwa Mbunge tayari tushawasiliana na iliingizwa kwenye mradi wa Tanzania ya Kidigitali, mradi amabao umefunguliwa tarehe 31 Januari, 2023. Hivyo basi mchakato wa tenda utakapokamilika tutajua kwamba ni mtoa huduma gani ambaye amepatikana kwa ajili ya kufikisha mawasiliano katika kata ya Masisiwe.
Mheshimiwa mwenyekiti, ahsante.
MHE. JUSTINE L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, ninataka kujua ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba na watumishi katika zahanati za Lugalo, Masege na Mbawi pia katika vituo vya afya vya Ruaha Mbuyuni, Ilula na Mluhe.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justin Nyamoga Mbunge wa Jimbo la Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, vituo vyote ambavyo amevitaja ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha vinapelekewa vifaa tiba na watumishi na ndiyo maana tunakwenda kuajiri watumishi 7,600 mwaka huu wa fedha pia tumetenga Shilingi Bilioni 69.95 kwa ajili ya vifaa tiba. Nimhakikishie kwamba tutatoa kipaumbele katika vituo hivyo. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pale Ruaha Mbuyuni kuna mradi wa umwagiliaji ulikarabatiwa na Wizara kwa force account, lakini sasa mto ule umeanza kuchepuka tena: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari tuongozane ili tuweze kuangalia tunafanyaje katika kuukarabati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, namwahidi tu kwamba Mheshimiwa Mbunge, kabla mimi na yeye hatujaongozana Jumatatu, Afisa wetu wa Tume ya Umwagiliaji walioko pale Iringa atakwenda kuukagua kwanza na kutupa taarifa, nami na yeye pia tutakwenda pamoja.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kilolo yupo mwekezaji anaitwa Udzungwa Corridor na tayari anapanda mashamba makubwa ya miti kwa ajili ya biashara hiyo. Kwenye vivjiji vinavyozunguka kuna misitu mingi ya asili inayofanana na hiyo hiyo inayopandwa.
Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuhakikisha ile misitu ambayo wanavijiji wameitunza na yenyewe inaingia kwenye huo mfumo wa biashara badala ya kutegemea tu ile ambayo Mwekezaji anawekeza na anapanda miti ile ile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Nyamonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza katika kitu ambacho tunakithamini sana ni upandaji wa miti. Pili tunashughulika na suala zima la kuishughulikia miti. Kwa hiyo, kikubwa nimwambie misitu yote ya asili kama ambavyo nimeeleza katika jibu la msingi kwamba sasa hivi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, tumeshaandaa muongozo wa usimamizi wa misitu yote ili lengo na madhumuni tuingize kwenye mpango huo pia tuweze kunufaisha vijiji vilivyozunguka na pia tunufaishe Serikali, pia tutunze na tuhifadhi mazingira. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ninayo maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza katika skimu hizi ikiwemo hii ya Mgambalenga lakini pia skimu za Ruaha Mbuyuni na nyingine gharama za ulipiaji wa vibali katika bonde zilipanda kutoka Shilingi 70,000 hadi Shilingi 150,000 zaidi ya asilimia 100. Sasa ningependa kujua ni mpango gani wa Serikali wa kupunguza hizi gharama maana gharama za kilimo zimeongezeka kwa hiyo inakuwa ni vigumu wakulima wale wa kujikimu kuweza kumudu kulipia vibali kwa ajili ya umwagiliaji? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili katika Kata ya Nyanzwa skimu ya umwagiliaji iliyoko pale ambayo ni ahadi ya Mawaziri Wakuu kadhaa bado haijatekelezwa, pamoja na juhudi kubwa za kuifatilia zilizofanywa na mimi mwenyewe hata Diwani wa kule amekuja kufuatilia. Sasa ningependa kujua kwa sababu ndiyo uhai wa watu wa kule kwenye kilimo cha vitunguu.
Je, ni lini Serikali itajenga ile skimu kwa kuzingatia pia mwaka huu hali ya umwagiliaji imekuwa ngumu na hali ni mbaya, ni lini Serikali itafanya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Nyanzwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza kuhusu gharama ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge gharama zimekuwa juu tofauti na ile gharama ya awali ambayo ilikuwepo. Tumeielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kukutana na mamlaka ya bonde husika kukaa na kuangalia uhalali wa gharama hizo ili tumpunguzie adha mkulima.
Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu mradi wa Nyanzwa ni kweli mradi huu Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiufuatilia sana na ninampongeza sana kwa hili. Tayari pale tuna miundombinu ya hekta 300 na tunachangamoto kubwa ya uhaba wa maji ya umwagiliaji, katika bajeti ya mwaka 2022/ 2023 Tume itafanya usanifu wa kina wa bwawa kuvuna maji ya mvua na usanifu huo pia utahusisha eneo la hekta 9,000 ili kuwahudumia wakulima wengi zaidi na baadae tutajenga kama ambavyo usanifu utakuwa umeelekeza.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya kutoka Ilula – Mlafu – Mkalanga – Kising’a hadi Kilolo kwa sasa haipitiki kutokana na uharibufu mkubwa wa mvua.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuiagiza TANROADS kufanya marekebisho ya haraka ili barabara hii muhimu iweze kuendelea kupitika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa ahakikishe kwamba anakwenda kwenye hii barabara ndani ya siku mbili ili kwenda kufanya tathmini na kufanya marekebisho ya sehemu zote ambazo hazipitiki ili wananchi wa Kilolo waweze kuendelea kupata huduma ya barabara hii.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Kituo cha Afya cha Kata ya Ukumbi pamoja na Zahanati ya Kijiji cha Ilutila ni miaka 16 sasa ni maboma. Je, ni lini Serikali itamalizia kituo hicho cha afya pamoja na hiyo zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishaweka utaratibu na tulishawaelekeza Wakurugenzi wa halmashauri kuleta vipaumbele vya maboma hasa ya vituo vya afya lakini pia na zahanati ambazo zinauhitaji mkubwa katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nimwelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilolo kuwasilisha rasmi Ofisi ya Rais, TAMISEMI maombi ya vituo hivi ili Serikali iweze kuona namna ambavyo Serikali itatafuta fedha lakini pia na mapato ya ndani yatachangia kukamilisha vituo hivyo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza: Serikali haioni haja ya kufanya tathmini ya mashamba yote yaliyotelekezwa na kupata orodha yake ili taratibu za kubatilisha ziweze kufanyika katika Wilaya ya Kilolo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, hili shamba limetelekezwa tangu mwaka 1980, lakini hadi sasa halijaweza kubatilishwa: Je, Serikali haioni umuhimu wa kulibatilisha kwa haraka ili liweze kukabidhiwa kwa Halmashauri na kupangiwa matumizi mengine ili wananchi waweze kunufaika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mashamba ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu ni mamlaka za Halmashauri kubaini hayo maeneo na kuyaanzia michakato ya kuomba yabatilishwe. Hivyo, nitoe wito kwenye Halmashauri zote hapa nchini, kupitia maeneo ambayo yamesahauliwa na wale ambao walimilikishwa huko nyuma ili sasa hii michakato ya haraka iweze kufanyika na kubadili yale matumizi ya maeneo kupitia hizi mamlaka za juu.
Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la pili, kwa kuwa jambo hili lilichukua muda mrefu, kama nilivyosema mwanzo, inawezekana Halmashauri ilikuwa haijabainisha na kuanza ile michakato, lakini kwa sasa kwa hatua tulipofikia, hili jambo linakwenda kukamilika kwa sababu mwenye maamuzi ya mwisho katika ubatilishaji wa maeneo haya ya ardhi ni Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, tutakapomfikishia, tunaamini wazi kwamba atalitolea maamuzi ya haraka kadri inavyowezekana, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, ni lini bima ya afya watasajili vituo vipya vya afya kikiwemo cha Ng’uluhe, Ruaha Mbuyuni, Ilula pamoja na Nyalungu ili waweze kuanza kupata huduma watu kupitia mfuko wa bima ya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ninachoweza kukwambia ni kwamba ninakuomba tukae chini leta vituo vyako ambavyo havijasajiliwa tutizame vigezo, vikikidhi vigezo zianze kusajiliwa na huduma itolewe.
MHE. JUSTINE L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Ujenzi wa chuo hiki pamoja na kwamba umefikia hatua hizo lakini kuna shida ya huduma ya maji na gharama yake ni shilingi milioni 90. Je, ni lini Wizara itapeleka fedha milioni 90 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hicho na ili huduma ziweze kutolewa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tunaishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kujenga chuo katika Wilaya ya Kilolo. Je, ni lini ujenzi huo utaanza katika Wilaya ya Kilolo ili wananchi waweze kunufaika na huduma za chuo cha VETA.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza anataka kufahamu swala la maji katika Chuo cha Ngudu. Ni kweli tumepeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji kwa maana ya majengo lakini kwa maana ya uunganishwaji wa maji bajeti ile iliyokuja baada ya kuifanyia tathmini tuliona kwamba iko kubwa sana, ilikuwa inflated kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, tumeifanyia maboresho na sasa fedha zimekuja kama milioni 57 hivi kipindi kifupi kijacho tutapeleka fedha hiyo kwa ajili ya ukatishaji wa maji katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika swali lake la pili anataka kufahamu ujenzi wa chuo cha VETA Kilolo. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge tayari timu ya wataalam imeshafika Kilolo na tumeshafanya topographical survey, geotechnical survey pamoja na environmental and social impact assessment na baada sasa ya matokeo haya ya vipimo hivi tutakwenda kuanza ujenzi mara moja, nakushukuru sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Kutokana na mvua zinazoendelea barabara ya kutoka Kitoho kwenda Mwatasi inayounganisha na Masisiwe kwa sasa imepata madhara makubwa na haipitiki.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha za dharura ili barabara hii iweze kupitika vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, natoa tena maelekezo tena hapa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa Meneja wa TARURA Mkoa wa Iringa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilolo kuweza kwenda kuifanyia tathmini barabara hii ya Mwatasi - Kilolo na kuona maeneo ambayo yameathirika sana ili waweze kuyafanyia kazi kwa haraka.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kijiji cha Idunda kata ya Kimara wamekarabati jengo lao wenyewe ili liwe zahanati na limekamilika.
Je, Waziri yuko tayari kuagiza Serikali kupeleka watumishi na vifaa tiba mara moja kwa sababu wanatembea zaidi ya kilometa 40 kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwenye zahanati hii ya Idunda katika ajira hizi ambazo Serikali imetangaza za elimu na afya tutahakikisha kwamba zahanati hii inapata watumishi. Lakini vilevile kuhusu vifaa tiba naomba nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako hili kumuelekeza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilolo kuhakikisha anaanza kuweka fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba na sisi huku Wizarani tutaona ni lipi ambalo linaweza likafanyika ku-complement jitihada za Mkurugenzi wa Halmashauri.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru napenda kujua ni lini wananchi wa Kata ya Masisile, Udekwa, Ilole na Nyanzwa katika Wilaya ya Kilolo watapata mawasilino ya simu na kuacha kupanda miti? (Makofi)
NAIBU WAZARI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya
Masisiwe, Udekwa, Mahenge, Kimara, Kilolo pamoja na Ebomu tayari Serikali inaenda kuingia mikataba na watoa huduma kesho tarehe 13 kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika Jimbo la Kilolo. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni lini mkandarasi wa kujenga Barabara ya kutoka Iringa Mjini kwenda Kilolo ataweka saini mkataba na kuanza ujenzi? Kwa sababu limekuwa ni jambo la muda mrefu na wananchi wanasubiri kwa hamu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii kwanza inafadhiliwa na World Bank, na fedha zipo. Kinachoendelea sasa hivi ni kukamilisha tu taratibu kati ya Serikali na mkandarasi ambaye tayari alishapatikana ili aweze kukabidhiwa hiyo site kujenga hizo kilomita 33 za Iringa kwenda Kilolo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la kitunguu linalolimwa sana Wilayani Kilolo limekumbwa na ugonjwa unaoitwa kaukau kwa lugha ya mtaani ambao haujulikani na vitunguu vinakauka mara tu vinapokuwa vimepandwa.
Je, Serikali iko tayari kutuma wataalamu ili kufanya uchunguzi na kutafuta suluhisho katika ugonjwa huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa taarifa hii, Jumatatu wataalam kutoka Wizara ya Kilimo watakuwepo jimboni kwake kwa ajili ya kushughulikia tatizo hilo. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Ilula kwenda Image - Igumu ipo katika mpango wa kujengwa lami kupitia mradi wa RISE. Je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa ili wananchi wapate barabara bora, kwa sababu barabara hiyo sasa hivi ipo katika hali mbaya sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Mpango wa RISE unaendelea kutekelezwa, ni kweli kwamba barabara hii ya Ilula - Image na Igumu ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge ziko kwenye mpango huu wa RISE, nimhakikishie kwamba mpango ule unaendelea kutekelezwa na muda utakapofika tutahakikisha kwamba barabara hizo kwa kadri tulivyojipangia mpangokazi, zinatekelezwa kwa kiwango hicho ambacho kimepangwa kwenye mpango wetu. Ahsante sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Kijiji cha Luganga na Kijiji cha Kilolo ndipo yalipo Makao Makuu ya Wilaya lakini hivi ni vijiji vilivyosajili. Je, Serikali ipo pia tayari kuangalia hivi vijiji kwa sababu wamepewa kulipa zaidi ya shilingi 300,000 ambayo ni tofauti na 27,000 kwenye vijiji vingine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuhakikishie Mheshimiwa Nyamoga kwamba maeneo yote yatafikiwa na upembuzi huu unafanyika nchi nzima kwenye maeneo yote ili kuweza kubaini uhalisia wa kila eneo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika harakati za kuimarisha doria, Kituo cha Polisi cha Ruaha Mbuyuni hakina gari: Je, Serikali ina mpango gani wa kukipatia kituo hicho gari ili kuimarisha doria katika eneo hilo lililotajwa ili kupunguza ajali pia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli siyo vituo vyote vya Polisi vina magari. Tulichokifanya ni kuimarisha uwezo wa Makamanda wa Mikoa na wasaidizi wao kuwa na magari, lakini awamu inayofuata ni kuimarisha ngazi za Wilaya. Mheshimiwa Nyamoga Wilaya yako itapata gari kama haikuwa na gari la uhakika na tutakapoimarisha kwenye ngazi ya Wilaya tutaenda kwenye vituo vikubwa kama vya Ruaha Mbuyuni ili tuviimarishe. Kwa hatua za dharura tunaweza tukawapatia pikipiki za kuweza kuwawezesha wao kufanya ufatiliaji, nashukuru sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, Serikali itazingatia kuongeza umri wa vijana kutoka ile miaka ya awali 30 mpaka kufikia 45 kama tulivyopendekeza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, umri ule wa vijana uliowekwa pale ni kwa mujibu wa miongozo ya kimataifa ambayo inataja umri wa vijana ni upi. Kwa hiyo sisi tunaendana na convention zile za kimataifa na mikataba ya kimataifa. Kwa hiyo umri wa vijana utabaki vilevile.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Barabara ya kutoka Ipogolo kwenda Kilolo imekuwa ikiendelea kutafutiwa mkandarasi kwa muda mrefu. Napenda kujua ni hatua gani zimefikiwa na ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Barabara ya kutoka Ilula hadi Kilolo ambayo kipindi cha mvua huwa inakuwa imeharibika na Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye majibu yake aliahidi kwamba itafanyiwa matengenezo, hadi sasa kuna maeneo bado: je, ni lini matengenezo hayo yatafanywa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ipogolo – Kilolo yenye urefu usiopungua kilometa 33 ipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kwa Mradi wa Rise. Tunapoongea sasa hivi Mbunge atakuwa na wananchi wa Kilolo wanafahamu kwamba, iko kwenye hatua ya manunuzi kwa ajili ya kuanza kujengwa barabara yote kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya pili aliyoitaja ya Ilula – Kilolo ambayo anasema mara nyingi inaharibika, ni kweli, eneo hili lina mvua nyingi, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya kipindi hiki cha mvua kwisha wakandarasi wapo, watakuwa muda wote wanaingia site kwa ajili ya kuikarabati hii barabara kwa kiwango ambacho itapitika bila matatizo, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kata ya Ruaha Mbuyuni ambayo iko tu barabarani kabisa pale kwenye lami, Kijiji cha Msosa, Kijiji cha Ruaha Mbuyuni chenyewe na Kijiji cha Ikula kuna madhara makubwa sana yanayosababishwa na tembo kiasi cha kusababisha chakula kuwa pungufu. Serikali inachukua hatua gani katika kudhibiti tembo hao hasa kuongeza askari katika Kambi ya Mtandika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea maswali tisa ya nyongeza kwa Waheshimiwa mbalimbali na naomba niyajibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Londo; ameuliza ni nini kauli ya Serikali? Kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi. Ni kwamba sasa hivi tunaangalia njia mbadala wakati huo huo tunaendelea kutatua migogoro hii ya wanyama wakali na waharibifu. Tunajenga vituo, tunaajiri VGS, lakini wakati huo huo tumeshaweka sasa mipango kwenye baadhi ya maeneo tuanze kuweka fence ya umeme ili kupunguza hii athari ya wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la Mheshimiwa Anne Malecela, naomba niahidi mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba baada ya Bunge hili tutaongozana naye katika maeneo yale. Lakini pia tumeshaanza kuongeza nguvu kwake, tumepeleka askari na tutaendelea kuajiri VGS katika maeneo hayo ili tuweze kushirikiana pamoja. Kwa hiyo, wananchi wa Same kilio chenu kimeshasikika Bungeni na tutaongozana na Mheshimiwa Mbunge (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la Mheshimiwa Vita Kawawa, ni kweli Mheshimiwa Waziri alitoa ahadi ya ujenzi wa madarasa katika jimbo lake, na huu ulikuwa ni mpango wa CSR si kwa ajili ya fidia ya wanyama wakali na waharibifu. Ni kwamba Mheshimiwa Waziri alifanya ziara katika jimbo hilo na akatoa ahadi ya ujenzi wa madarasa ili kuwafanya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo tushirikiane pamoja katika uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee tu kuahidi kwamba ahadi ni deni, Wizara itatekeleza. Na kwa kuwa ilikuwa ni kauli ya Mheshimiwa Waziri basi tutafuatilia ili ahadi hii iweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dunstan, Mbunge wa Mkinga, yeye ameongelea kuhusu kituo; niahidi tu kwamba katika mpango wa fedha wa 2023/2024 uliopitishwa katika Bunge lako hili, tutapeleka kituo katika Jimbo la Mkinga ili tuongeze nguvu ya kudhibiti wanyama wakati na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Justin Nyamoga, madhara makubwa; naomba niahidi tu kwamba tutaendelea kufuatilia katika maeneo haya ili wananchi waweze kulipwa fidia inayotokana na wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Grace Tendega; naomba tu nilitaarifu Bunge lako, na kwa ridhaa yako, nipe tu nafasi kidogo nitoe ufafanuzi. Tumekuwa na changamoto nyingine imejitokeza katika Mkoa wa Iringa; kuna uvamizi wa simba kwenye baadhi ya maeneo, lakini naomba niwataarifu wananchi, nadhani wameona juhudi za Serikali toka uvamizi huu umejitikeza tumekuwa karibu na wananchi, tunatoa elimu.
Mheshimiwa Spika, naniendelee kutoa elimu kupitia Bunge lako hili, kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa simba, wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku. Lakini pia wenye mifugo wawashe moto kuzunguka maeneo yale ya mifugo ili kuepusha simba wasisogee katika maeneo hayo tunajitahidi sana kulinda maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Wanairinga, Serikali iko kazini na tumeshapeleka helikopta inazunguka usiku na mchana kuhakikisha tunawasaka hawa simba. Tuendelee kushirikiana pamoja ili kuhakikisha zoezi hili tunalikamilisha na simba hawa tunawachukua na kuwarudisha katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mheshimiwa Charles, Mbunge wa Mwibara; kumekuwa na changamoto ya viboko na tembo. Naomba niendelee tu kuahidi, nakumbuka tuliwasiliana na Mheshimiwa Mbunge na tukaongeza nguvu ya askari katika maeneo hayo. Tuendelee tu kuwasiliana, nguvu tutaongeza lakini pia tutaendelea kuajiri VGS ili waweze kusaidia pale inapotokea dharura katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ombi la Mheshimiwa Jimbo la Tunduru kwamba tuongeze VGS (askari wa vijiji). Tunaomba tulipokee hili na tutaweka priority katika eneo hili, tunajua hii changamoto ya wanyama wakali.
Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna shida moja ya mratibu ambaye alihamishwa. Nadhani maelekezo yameshatoka, atarudishwa katika eneo hilo ili aweze kushirikiana na wananchi kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Matiko tayari nimeshalijibu, kwamba tuko kwenye process ya ku-review hizi sheria na kanuni kuangalia sasa angalau tusogeze kiwango fulani ili wananchi nao waweze kuona umuhimu wa namna ya uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, kata tatu za Kilolo yaani Ukwega, Nyanzwa na Udekwa, hazina umeme, na mkandarasi alikuja akachomeka nguzo, sasa ni miezi sita haonekani.
Je, Serikali iko tayari kumuita na kumtafuta huko aliko ili aende akamalizie ile kazi kule? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo moja na eneo lingine hatua za utekelezaji zinatofautiana kulingana na mkandarasi alianza lini na amepata vifaa wapi na mambo kama hayo na kama nilivyoelekeza wakandarasi wote waendelee na kazi zisizohusiana na mazungumzo tunayoyafanya kuhusiana na bei.
Mheshimiwa Spika, naomba nikitoka hapa niwasiliane na Mheshimiwa Nyamoga ili nione hasa kwake kuna changamoto gani mahususi ili kama ni kuitatua mara moja tuitatue, kama ni ile ambayo inaendelea kwenye taratibu nyingine basi namhakikishia kwamba kazi itaendelea na itakamilika kwa wakati.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kwa kuwa mikopo hii mara inapotolewa wakopaji uanza kulipa mara moja, lakini wapo wakulima wa mazao ya muda mrefu kama parachichi na mazao mengine yanayochukua muda mrefu.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa kipindi cha kusubiria yaani grace period kabla hawajaanza? Uko tayari kutoa agizo hilo Mheshimiwa Naibu Waziri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hii inaongozwa kwa kanuni na sheria iliyotungwa na Bunge. Kwa hiyo, mpaka muda huu ninapozungumza bado kanuni zinazotumika ni zile ambazo zimetungwa. Kwa hiyo, ili kuongeza grace period maana yake tunahitaji mabadiliko ya kisheria ili tuweze ku-accomadate. Kwa hiyo, Bunge lako tukufu litakavyoona wakati unafaa basi mnaweza kufanya marekebisho na sisi tutatekeleza.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; katika Kata ya Kimara na Kata ya Idete yupo mwekezaji ambaye ni Kampuni inaitwa Odzungwa Corridor na yeye anafanyakazi ya kupanda miti kwa ajili kuja kuvuna hewa ya ukaa miaka ijayo.
Sasa je, Serikali haioni umuhimu wa kuzungumza naye ili aweze pia kushirikisha misitu iliyopo tayari ili huo uvunaji uweze kuanza na malipo yaweze kufanywa kwa sababu ipo miti ambayo iko tayari?
Lakini swali la pili; moja kati ya lengo la kuwepo kwa misitu kimsingi ni hifadhi ya mazingira na hivi karibuni bei za mazao ya misitu hususan mbao imeshuka sana na kama inakatisha tamaa wakulima kuendelea kulima miti na baadaye tutapata madhara makubwa.
Ni nini kauli ya Serikali kuhusu tatizo hili ambalo linaweza likawa na matatizo makubwa baadaye? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI. OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la ndugu yangu, Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kwa mara kadhaa alikuwa akizungumzia hoja ya upandaji wa miti wa kibiashara hususan katika wilaya yake ya Kilolo na Mkoa mzima wa Iringa pamoja na Mkoa wa Njombe wanavyojihusisha na upandaji wa miti.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ajenda ya huyu mkulima ambayo analima hii miti ni kama tunavyosema kwamba tumeandaa mwongozo sasa, mwongozo huu uta-address suala zima la uhifadhi wa mazingira na watu mmoja mmoja mara baada ya mwongozo huu watapewa maelekezo jinsi gani ya kushiriki vyema kwa ajili ya kupata utajiri mkubwa kupitia suala la misitu. Kwa hiyo, afanye subira tu nadhani kwa malengo yake yanaendana pamoja na mkakati wa Serikali tunaoendelea nao.
Mheshimiwa Spika, lakini suala zima misitu, thamani ya miti inashuka, basi niseme kwamba katika hilo kwetu sisi upande wa Mazingira tuseme kwamba hiyo ni fursa sasa kwa wale ambao wanaopanda miti ambao kesho na keshokutwa biashara hii hewa ya ukaa itapokuwa kubwa tutaenda kufanya mambo mawili; kwanza kutunza mazingira, lakini jambo la pili vilevile kuhakikisha kwamba tunakabiliana na mabadiliko ya tabianchi lakini kikubwa zaidi kuhakikisha tunapeleka utajiri wa mtu mmoja mmoja kupitia ajira ya misitu, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 Waziri wa TAMISEMI aliahidi kujenga kituo cha afya katika Kata ya Ikuna; je, Serikali ni lini itatimiza ahadi hiyo? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Wilaya ya Kilolo, Kata ya Ukumbi, wananchi wamejenga jingo la kituo cha afya kwa nguvu zao wenyewe na OPD imekamilika; je, Serikali iko tayari kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika Kata ya Ukumbi ili majengo yale ya vituo vya afya yaweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo kwa niaba ya Mheshimiwa Enosy Swalle Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali tunatambua tuna commitment ya kupeleka fedha kujenga kituo cha afya cha Kata ya Ikuna, na Mheshimiwa Mbunge wa Lupembe, Mheshimiwa Edwin Swalle, amekuwa akifuatilia mara kwa mara kwa bidii sana kuhusiana na miradi ya maendeleo kwa ujumla, lakini Kituo cha Afya cha Ikuna. Nimhakikishie kwamba Serikali tayari tunatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kujenga Kituo cha Afya cha Ikuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na Kituo cha Afya cha Kilolo ambacho wananchi wamejenga niwapongeze sana wananchi wa Kilolo kwa kutoa nguvu zao na niwahakikishie kwamba Serikali imeweka mpango wa kuchangia nguvu za wananchi kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya na tutafanya hivyo, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mradi wa Maji wa Uhambi Ngeto ambao umetengewa fedha kwa mwaka huu umekuwa ukitafutiwa mkandarasi tangu mwaka umeanza na mpaka sasa mkandarasi hajaanza kazi.
Je, ni lini mkandarasi huyu atapata mkataba ili aweze kufanyakazi kukamilisha mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli mradi huu bado haujapatiwa mkandarasi lakini taratibu zipo mwishoni kabisa. Mheshimiwa Mbunge naomba tuwasiliane baada ya hapa tuliweke sawa suala hili.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, barabara ya kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya eneo la Mlima Kitonga limekuwa na ajali nyingi na mara nyingi kuziba barabara hiyo na kusimamisha shughuli za kiuchumi kwenye nchi yetu. (Makofi)
Ni lini sasa Serikali itafanya utaratibu au kuipanua barabara ile au kuangalia njia mbadala ili shughuli za kiuchumi zisisimame wakati kunapotokea ajali kwenye eneo lile?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli eneo la Kitonga ni eneo lenye barabara ambayo ina miinuko na kona kali na Serikali imeendelea kulifanyia matengenezo ikiwa ni pamoja na kujenga zege, kuondoa kona na kuipanua ile barabara ili kuhakikisha kwamba magari mengi na hasa ambayo ni malori yanapishana kwa urahisi.
Suala lingine ambalo sasa tunafikiria ni kuimarisha barabara ambayo ni ya bypass ili kunapotokea changamoto na barabara ikiziba basi magari hayo yaweze kupita njia ya bypass, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kupitia Mradi wa Agri-Connect tulikuwa tumeomba Kilometa 15 ambazo zimo tayari kwenye bajeti ya Agri-Connect zijengwe kutoka Kilolo hadi Kidabaga ambapo ndiko shamba la chai lilipo. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kupitia Mradi wa Agri-Connect tulikuwa tumeomba Kilometa 15 ambazo zimo tayari kwenye bajeti ya Agri-Connect zijengwe kutoka Kilolo hadi Kidabaga ambapo ndiko shamba la chai lilipo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Nyamoga kwamba, mradi huu ulipoanza (Agri-Connect) Mkoa wa Iringa ulikuwa ni Mkoa wa kwanza kabisa kuanza utekelezaji. Vilevile, niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mheshimiwa Nyamoga alikuwa beneficiary wa kwanza kabisa wa ujenzi wa barabara hizi za Agri-Connect katika Jimbo lake. Hivyo basi, Serikali pia italiangalia hili la barabara ya Kilolo kwenda Kidabaga ambapo kuna uzalishaji mkubwa wa chai katika awamu ambayo inafuata kama nilivyomjibu Mheshimiwa Swalle ili kuziweka katika mpango na barabara hizi ziweze kujengwa. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa tayari daraja lipo kule Mbeya; na kwa kuwa Wizara tayari ilishabaini mahitaji kwamba kuna mahitaji ya daraja hilo.
Je, ni lini tutafanya hicho kikao na Wizara ya Ulinzi kwa sababu sisi Kilolo tuko tayari ili utekelezaji uanze kufanyika? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya haraka kwa sababu kipindi cha msimu wa mvua ambacho ndiyo huwa kina matatizo makubwa kimekaribia na ikiwa tutachelewa, madhara makubwa yanaweza kutokea, kwa sababu kila mwaka tunapoteza watu kama hatutaweza kujenga hilo daraja?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge juu ya umuhimu na uharaka wa ujenzi wa daraja hili, lakini nampongeza pia kwa utayari wake. Kama nilivyomjibu katika swali la msingi kwamba Wizara iko tayari kukutana naye pamoja na TARURA, hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki niweze kukutananaye na pale ambapo atakuja Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, nimfikishie ujumbe huu waweze kufanya kikao hicho kwa haraka na suala hilo liweze kupatiwa ufumbuzi.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Image na Kata ya Ibumu, Kijiji cha Ilambo na Iyai kuna changamoto kubwa ya mipaka na kusababisha wananchi mara nyingi kugongana kwenye malisho.
Je, Wizara ina mpango gani wa kufika katika maeneo hayo na kutatua mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justin Lazaro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake kwamba nitaenda mimi mwenyewe kufanya ziara na kuzungumza na wananchi na kutatua changamoto hii.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote niishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri na kwa ahadi iliyotolewa ya kujenga mnara kwa ajili ya TBC. Niwapongeze pia kwa minara mingi ya simu ambayo inaendelea kujengwa katika Wilaya ya Kilolo, ambayo inatatua changamoto ya mawasiliano. Nawapongeza sana Waziri pamoja na Naibu Waziri, kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu madogo ya ngongeza, kwa kuwa mawasiliano yanaendana na uwekaji wa Mkongo wa Taifa. Je, ni lini Serikali itaweka Mkongo wa Taifa kufika katika Wilaya ya Kilolo?
Swali dogo la pili, Kwa kuwa tayari huu ujenzi wa mnara wa TBC process imeanza, nijue ni lini unatarajia kukamilika ili wananchi pia waweze kupata matumaini ya kupata matangazo ya TBC kwa uhakika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kazi kubwa anayoifanya katika Jimbo la Kilolo na kwa kazi anayoifanya katika kushirikiana na Serikali pale ambapo tunafika katika Jimbo, lake ili kuhakikisha kwamba tunaweka miundombinu ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika swali lake la pili kwamba ni lini sasa TBC itaanza kufanya kazi pale. Kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi umepangwa kukamilika ifikapo Juni, 2024. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, itakapofika Juni, 2024 naamini kwamba kazi itakuwa imeanza kwa wananchi wa Kilolo kupata huduma ya mawasiliano ya utangazaji ya TBC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba Wilaya zote nchini, Wilaya 139 ifikapo Disemba, 2024 wote tutakuwa tumefikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Ifikapo Juni, mwaka huu tutakuwa tumekamilisha kufikisha Mkongo wa Mawasiliano katika Kata 99. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu pale Mafinga tayari tuna pop yetu, pale Iringa Mjini tuna pop na kutoka Iringa Mjini mpaka Kilolo kuna kilometa 33, kwa hiyo tutahakikisha kwamba tumefikisha na tutajenga Kituo cha Mkongo katika eneo lake la Wilaya ya Kilolo. Nakushukuru sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; shule hii ilitembelewa na Mheshimiwa Rais wakati akiwa Makamu wa Rais na kuahidi kuipandisha hadhi mbele ya wadau na wadau hao tayari wameshakamilisha ujenzi wa madarasa. Je, Serikali wakati inaendelea kutafuta fedha haioni sababu ya kuwaomba wadau hao hao kukamilisha ujenzi wa mabweni ili shule hiyo iweze kuanza kwa sababu wako wadau ambao tayari wamejenga madarasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Shule ya Sekondari Ilula iliyotajwa kama yenye kidato cha tano na sita, mabweni yake yametitia kutokana na mvua na kuwa hatarishi kwa watoto wanaosoma pale. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kujionea hali hiyo na kuchukua hatua za dharura?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa natambua jitihada anazozifanya Mheshimiwa Mbunge kuwapigania wananchi wake. Kuhusu swali lake la kwanza ambapo anasema Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya ujenzi wa mabweni basi na yeye ameweza kutoa maoni kwamba Serikali itazame namna ya kushirikiana na wadau katika kukamilisha mabweni hayo. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge mawazo yake ni mazuri na Serikali imeyapokea na tutayachakata na kufanya mawasiliano na wadau ili tuone kwamba kwa pamoja Serikali na wadau tunaweza kujenga mabweni hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu bweni kuzama na nipo tayari kuambatana naye kwenda kuona hali halisi na kuchukua hatua za dharura. Nakubali Mheshimiwa Mbunge kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, ahsante
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, licha ya kutengewa fedha za ukarabati hivi sasa tunavyozungumza kata sita za Wilaya ya Kilolo hazina mawasiliano kutokana na Daraja la Kidabaga kutopitika kabisa kwa ajili ya uharibifu wa mvua zinazoendelea.
Je, Serikali ipo tayari kuagiza hatua za dharura zichukuliwe ili magari yale yaweze kupita na shughuli ziendelee?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nitoe pole kwa wananchi ambao sasa hivi wamekosa mawasiliano; lakini tu nimjibu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge mvua zinazoendelea nchi nzima zimeleta athari kubwa sana kwenye miundombinu yetu ikiwa ni barabara pamoja na madaraja.
Mheshimiwa Spika, tayari tulishawaelekeza Mameneja, pale ambapo kumekatika mawasiliano tumeshatengeneza timu katika kila barabara. Mvua inapokuwa imekatika basi waweze kufanya jitihada za haraka ili kurejesha mawasiliano wakati tukisubiri kuja kuijenga hiyo barabara wakati mvua itakapokuwa imekatika; lakini kwa sasa tunarejesha mawasiliano kwa sababu hatuwezi kuzijenga kwa kiwango kizuri kwa sababu mvua zinaendelea. Baada ya mvua kukatika tutahakikisha kwamba tunarudisha mawasiliano ya kudumu.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Kilolo kupitia Kidabaga kwenda Idete hadi sasa haipitiki kutokana na maporomoko. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za dharura kwa ajili ya kuifanya ile barabara iweze kupitika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge alifika ofisini na tayari Mheshimiwa Rais ameshatoa fedha za dharura. Kwa hiyo, Meneja wa Mkoa wa Iringa ameshapewa maelekezo aende akafungue hiyo barabara ambayo imejifunga. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kabla ya swali Mheshimiwa Deo Sanga anashukuru sana kwamba malipo ya fidia ile yamefanyika na swali lake namba moja ni kwa sababu malipo yameshafanyika na lile eneo la makaburi siyo kubwa, Serikali haioni umuhimu wa kulipa haraka ili ipate uhuru wa kuendelea na ujenzi wa One Stop Centre pale Makambako?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pale Kilolo ambapo Makao Makuu ya Wilaya yamejengwa, kuna madai ya fidia ya muda mrefu na yalikwishawasilishwa Hazina mara kadhaa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuyaharakisha malipo yale ili wale wananchi pia waweze kupata haki yao? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyamoga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kuhusu ulipaji wa fidia kule Idefu, Makambako, kwa kuwa tumeshalipa fedha nyingi sana shilingi bilioni 4.6 kilichobakia ni kidogo tu ni shilingi milioni 100. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya mwaka huu wa fedha tunaenda kulipa fidia iliyobakia. Upande wa Kilolo Serikali ipo tayari kufanya haraka, tunasubiri tu Mthamini Mkuu aweke idhini, akishatoa idhini yake tunaenda kulipa hiyo. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nikushukuru Naibu Waziri kwa ziara ya kibabe uliyoifanya katika Jimbo la Kilolo. (Makofi)
Sasa swali langu la nyongeza Mradi wa Maji wa Masege, Masalali na Kihesa Mgagao umeanza kusua sua kutokana na mkandarasi kutokulipwa kwa wakati; je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi ili mradi ule uweze kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya na kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwa kuendelea kutupatia ushirikiano na sisi tunajiona kwamba tuna mwakilishi wa wananchi ambaye anahitaji kuwasemea wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge katika mradi huo ambao kama ambavyo umedai unasuasua Serikali kupitia Wizara ya Maji tumekaa na wenzetu Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba, sasa wakandarasi wetu ambao wanatekeleza mradi huo walipwe pesa ili wahakikishe kwamba mradi huo unakamilika kwa wakati na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ni lini Serikali itamalizia majengo ya zahanati katika Kijiji cha Iyayi, Uhominyi Nyawegete, Kitoho na Winome ambayo tayari yameshapauliwa na yako katika hatua za umaliziaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu sana wa huduma ya afya msingi na imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inajenga miundombinu kwa ajili ya kutoa huduma hii ya afya msingi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutafuta fedha ili iweze kukamilisha miradi ambayo tayari imeanza ikiwemo mradi alioutaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Skimu ya Umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni imebomoka kwa muda mrefu sasa na inawahudumia wananchi zaidi ya 10,000 pale. Ni mpango gani wa Serikali kuhakikisha kwamba ukarabati wa haraka unafanyika ili wale wananchi waendelee kunufaika na shughuli zao za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua changamoto ya Skimu ya Ruaha Mbuyuni na tutairekebisha haraka iwezekanavyo. Changamoto kubwa zilikuwa ni hizi mvua ambazo zilikuwa zinaendelea. Kwa hiyo, hatuwezi kuiacha kwa sababu tunajua umuhimu wa hii skimu, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, katika Kata ya Ukwega yaani Vijiji vya Mkalanga, Makungu, Lulindi na Ukwega yenyewe kuna kilimo cha kahawa, lakini wanakatishwa tamaa na ukosefu wa soko, kwa hiyo zao lile linaelekea kuondoka katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ipo tayari kupeleka wataalamu na kuangalia njia bora ya kwanza kukiimarisha kilimo kile, lakini pili kupata soko ili waendelee na kilimo cha kahawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Nyamoga kwamba Serikali tupo tayari, moja tutaleta wataalamu na hili lipo ndani ya uwezo wetu, lakini pili tutaendelea kutafuta masoko, lakini soko kubwa sasa hivi tunatumia mnada, lakini vilevile tunazungumza na balozi zetu kuleta wawekezaji zaidi kwa ajili ya kutengeneza viwanda ndani vya kuongeza thamani ya zao ambayo ndiyo yatakuwa moja ya sehemu ya masoko makuu ya kahawa ambayo inazalishwa nchini, kwa hiyo, hilo lipo na tunaliweza, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, swali la kwanza ni kwamba ni kweli kuna utaratibu wa shule za SEQUIP kujengwa na mojawapo ikiwa ni katika Jimbo la Mheshimiwa Kasalali, je, ni lini kwa mwaka huu wa fedha shule hizo zitaanza kujengwa kwenye jimbo hili na majimbo mengine? (Makofi)
Swali la pili, kuna shule za SEQUIP za awamu ya kwanza ambazo hazikuwa zimekamilika, je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha shule hizo kwenye majimbo yote ikiwemo Jimbo la Sumve na Jimbo la Kilolo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitafuta fedha na akapata fedha jumla ya shilingi trilioni 1.2 katika mradi tunaouita Mradi wa SEQUIP ambao lengo lake ni kuongeza shule zetu za sekondari kwenye kata na kuhakikisha zinafika, tunaongeza idadi ya shule kwa ajili ya kupunguza kwanza umbali wa wanafunzi kusafiri ili kufika kwenye shule, lakini pia kupunguza msongamano katika baadhi ya maeneo ambayo kuna msongamano kwenye shule hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa lengo la Serikali na lengo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anaboresha sekta ya elimu na hasa elimu hii ya shule za sekondari na shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mbunge ameuliza kwamba ni lini awamu hii au mwaka huu fedha zitatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule hizi katika mwaka huu wa fedha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imeshafanya uhakiki wa maeneo yote yaliyoainishwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hizi za kata katika mwaka huu na ninamhakikishia, wakati wowote fedha zitatolewa kwa ajili ya kuhakikisha tunatekeleza mradi huu kwa kadiri vile tulivyokuwa tumepanga kwa maana ya awamu ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu kwamba zile shule za awamu ya nyuma ambazo hazikukamilika, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha inakamilisha shule hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali ilishaanza kutoa fedha na itahakikisha inapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu ya shule hizi za kata ili wanafunzi waweze kuanza kuzitumia. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa sasa Kata nne za Jimbo la Kilolo hazipitiki kabisa kutokana na madhara ya mvua. Kata hizo ni Masisiwe, Ukwega, Kimara na Idete. Je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha upelekaji wa fedha za dharura ili Kata hizi ziweze kuunganishwa na barabara na huduma ziweze kuendelea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameeleza barabara hizi hazipitiki, namwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki cha Maswali na Majibu tukae ili tuweze kufuatilia kujua mustakabali mzima wa kuleta fedha kwa ajili ya kurekebisha barabara hizi.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula ina zaidi ya miaka 20 sasa; je ni mpango Serikali inao wa kuhakikisha kwamba inakuwa halmashauri kamili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kweli Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula ina umri mrefu haijapanda kuwa Halmashauri ya Mji, lakini zipo mamlaka nyingi ndogo katika nchi yetu ambazo pia zina umri mrefu. Zipo mamlaka ambazo hazikidhi vigezo vya kuwa halmashauri, Serikali inaendelea kufanya uchambuzi, lakini zipo ambazo zinakidhi kuwa Halmashauri za Miji. Kwa hiyo, naomba nilichukue suala hili ili muda ukifika tutakuwa tumeshafanya tathmini kama Mamlaka ya Ilula inakidhi haja ya kuwa halmashauri basi itapata sifa hizo baada ya Serikali kuamua kuanza kupandisha hadhi, ahsante.
MHE. JUSTINE L NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa barabara ya kutoka Ipogolo hadi Kilolo inajengwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuiunganisha barabara hiyo pale Kilolo kwenda Kibaoni – Kitowo ili iweze kutoka kwenye Wilaya ya Iringa Vijijini kwa sababu ya umuhimu wake, kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunajenga kwa kiwango cha lami kilometa 33 ambazo tayari Mkandarasi yuko site. Lengo ni kuhakikisha kwamba, tunaendelea kwa kadiri fedha zinavyopatikana kuweza kuiunganisha Kilolo na Iringa Vijijini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira, kadiri fedha inavyopatikana barabara hiyo tutaijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mradi huu Mradi wa Magubike umechukua muda mrefu kidogo, je, Serikali haioni umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa mradi huu ili wananchi wapate huduma?
Swali la pili, Mradi wa Umwagiliaji wa Mgambalenga ambao ujenzi wake umekuwa ukisuasua, je, Serikali inampango gani wakumwambia mkandarasi yule kuharakisha ujenzi kwa sababu tayari ana mkataba na analipwa. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mradi huu umekuwa wa muda mrefu lakini nataka niwahakikishie kwamba mwaka huu unatangazwa na mwaka huu utaanza kutekelezwa, lakini kuhusu Mgambalenga kulikuwa kuna matatizo ya kifedha nashukuru Wizara ya Fedha wameshatuandalia utaratibu wa kutupatia fedha, mkandarasi atarudi kuwa effective kufanya kazi yake. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru Wizara kuingiza kwenye bajeti Bwawa la Nyanzwa, kwa ajili ya umwagiliaji, lakini swali langu ni Scheme ya Ruaha Mbuyuni, bwawa lilibomoka muda mrefu na Mheshimiwa Waziri unafahamu. Ni lini sasa tutawasaidia wale wananchi kwa sababu, hali inazidi kuwa mbaya na mvua inakaribia? Nakushukuru.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Kamonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Scheme ya Ruaha Mbuyuni kila mwaka imekuwa ikibomoka na kila wakati tumekuwa tukienda kufanya rehabilitation ndogondogo kufanya watu wafanye kazi. Kwa hiyo kama Wizara tumeamua tu kufanya usanifu wa kina, kwa ajili ya ile scheme yote na pale pana maji mengi, ili tuweze kuijenga complete, kama ambavyo tumefanya mkombozi badala ya kuendelea kupoteza fedha kufanya repair ndogondogo. Kwa hiyo, nawaomba wananchi wa eneo lile na wananchi wa Mkoa wa Iringa watuvumilie, usanifu unaendelea, ukikamilika tu itatangazwa, ili ijengwe properly tuondokane na hili tatizo la kujirudia kila wakati.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Wananchi wa Kijiji cha Boma la Ng’ombe ambapo mwenge umepita juzi, walitoa malalamiko makubwa kuhusu upungufu wa maji kwenye Kijiji cha Boma la Ng’ombe. Je, ni lini Serikali itataua changamoto ya maji kwenye Kijiji cha Boma la Ng’ombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Justin Nyamoga kwa kazi kubwa anayoifanya Kilolo.
Mheshimiwa Spika, nimeshafika Kilolo na kujionea changamoto hiyo lakini tunafahamu kwamba Serikali iko katika juhudi mbalimbali za kuboresha na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa maji unaendelea kuboreshwa. Tayari tumeshasaini mkataba katika baadhi ya kata, tunaamini kwamba baada ya kukamilika mikataba hiyo na kutekelezwa, basi tutaangalia uhitaji katika maeneo mengine na tutahakikisha kwamba tunapeleka huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya cha Kata ya Ukumbi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Kata ya Ukumbi kimepokea fedha awamu ya kwanza na kinaendelea na ujenzi na nafahamu kwamba, kinahitaji fedha nyingine takriban shilingi milioni 250, kwa ajili ya ukamilishaji na Mheshimiwa Nyamoga amefuatilia mara kwa mara. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kipo kwenye mpango wa vituo ambavyo vinahitaji fedha, kwa ajili ya ukamilishaji na mara fedha zikipatikana tutahakikisha tunapeleka ili kituo kile kiweze kukamilishwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara ninayo maswali mawili. Swali la kwanza; ziko barabara ambazo zimekatika kata tatu ambazo nimekuwa nikizitaja hapa mara kwa mara. Barabara ya Kimala – Msonza – Masisiwe - Boma la Ng’ombe na Barabara ya Ukwega - Lulindi. Barabara hizi hazipitiki na zimesababisha changamoto kubwa. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za dharura kwa haraka ili matengenezo yaweze kufanyika wananchi wapate mawasiliano?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Barabara ya kutoka Mngeta - Idete ilijibiwa swali ni barabara inayounganisha na Mlimba, Mkoa wa Morogoro na ni barabara muhimu, imetengewa shilingi milioni 100 na haziwezi kutosha. Je, kwenye mipango ya bajeti ijayo ni kiasi gani cha fedha kimetengwa ili barabara hii iweze kukamilika na wananchi waendelee kupita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizozitaja Mheshimiwa Mbunge katika kata tatu Barabara ya Boma la Ng’ombe - Masisiwe barabara hii imeombewa fedha za dharura na nimhakikishie barabara hii itajengwa. Barabara ya Msonza - Kimala yenyewe imetengewa milioni 51.3 katika bajeti ya mwaka huu wa fedha na tayari mkandarasi amepatikana, baada tu ya mvua kukatika kazi ya ujenzi wa barabara hii itaanza. Barabara yake ya Idete - Mngeta na yenyewe ni sehemu ya Barabara ya Mhanga - Mngeta ambayo imeidhinishiwa milioni 100 na ujenzi utaanza wiki ijayo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara zake hizi alizozitaja na amekuwa akizizungumzia mara kwa mara, lakini hata mimi na yeye tulikaa kuzijadili, nimhakikishie barabara zake hizi zitajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kuhusiana na hii Barabara ya Idete - Mngeta ambayo imetengewa shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi anasema kwamba fedha hii anaona haitoshelezi. Nimhakikishie tayari Serikali imeanza kwa awamu hii tumetenga milioni 100, katika mwaka mwingine wa fedha tutatenga fedha zaidi ili kuhakikisha barabara hii inajengwa kwa viwango na inaweza kuwasaidia wananchi.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Mji wa Makambako unakuwa na idadi ya watu inaongezeka na kutokana na hivyo maeneo yamekuwa madogo kwa hiyo upimaji wa viwanja na maeneo kwa ajili ya makazi na shughuli nyingine yanakosenaka.
Je, ni lini Serikali itafanya mpango wa kuongeza lile eneo ili wananchi wa Makambako waendelee kupata makazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna maeneo mengi sana kwenye nchi hii ambayo ugawaji wake haukuzingatia jiografia na kwa hiyo huwa ni shida sana kwenye utoaji wa huduma, kwa mfano mtu wa kutoka Tarafa ya Mazombe na Mahenge Ilula, maeneo ya Ilula kwenda Kilolo kupata huduma inabidi apite Iringa Mjini. (Makofi)
Je, Serikali ina mpango gani wakupitia maeneo haya na kuona jinsi nzuri ya kuyafanya yawe katika uwiano wa kijiografia ili kurahisisha huduma za wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya halmashauri au majimbo ambayo yana changamoto ya kimipaka, lakini kwa Jimbo la Makambako Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga amefuatilia mara kadhaa kuongeza mipaka ya Jimbo la Makambako, Halmashauri ya Mji wa Makambako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niitumie nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, lakini pia Mheshimiwa DC kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kufuata utaratibu wa kupata maoni kwa wananchi wa maeneo hayo ili waweze kupeleka kwenye vikao vyao vya DCC na vikao vya RCC na kukubaliana kama wilaya, lakini kama mkoa na kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuchukua hatua na hili linakwenda sambamba na ile hoja ya baadhi ya mipaka kutozingatia hali za kijiografia za maeneo hayo na kuleta changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itapokea maoni kutoka kwa wadau na wadau hao ni wananchi wa maeneo hayo kwa maana ya DCC pamoja na RCC kwa ajili ya kuchukua hatua hizo, ahsante. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, katika Kata ya Ukwega yaani Vijiji vya Mkalanga, Makungu, Lulindi na Ukwega yenyewe kuna kilimo cha kahawa, lakini wanakatishwa tamaa na ukosefu wa soko, kwa hiyo zao lile linaelekea kuondoka katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ipo tayari kupeleka wataalamu na kuangalia njia bora ya kwanza kukiimarisha kilimo kile, lakini pili kupata soko ili waendelee na kilimo cha kahawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Nyamoga kwamba Serikali tupo tayari, moja tutaleta wataalamu na hili lipo ndani ya uwezo wetu, lakini pili tutaendelea kutafuta masoko, lakini soko kubwa sasa hivi tunatumia mnada, lakini vilevile tunazungumza na balozi zetu kuleta wawekezaji zaidi kwa ajili ya kutengeneza viwanda ndani vya kuongeza thamani ya zao ambayo ndiyo yatakuwa moja ya sehemu ya masoko makuu ya kahawa ambayo inazalishwa nchini, kwa hiyo, hilo lipo na tunaliweza, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, barabara ya kutoka Boma la Ng’ombe – Masisiwe – Idegenda iliharibiwa na mvua na haipitiki mpaka sasa; je, Serikali ina neno gani la matumaini kwa wananchi wa maeneo hayo kwa sababu mawasiliano hayakurudi tangu ilivyoharibiwa na mvua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Justin Nyamoga kwa kuendelea kuwapambania wananchi wake kuhakikisha wanapata miundombinu bora ya barabara katika jimbo lake. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akipaza sauti kuhusiana na barabara hii na nimhakikishie kwamba Serikali itaifikia barabara hii ili iweze kuhakikisha mawasiliano yanapatikana, iweze kuwanufaisha wananchi wake kiuchumi na kijamii.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru Serikali kwa majibu mazuri, pamoja na hayo ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia TEMDO wanatengeneza mtambo wa kuchakata sukari ambapo tayari wameshatembelea Kata hiyo ya Mahenge na Nyanzwa na wameonesha nia ya kufunga mtambo huo kwa majaribio. Je, Wizara ya Kilimo ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili mtambo huo ufungwe Mahenge ili kiwanda kile kiweze kuanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa ulimaji wa miwa unaenda sambamba na Bwawa la Bonde la Nyanzwa ambalo usanifu wake umekamilika. Je, Serikali inatoa commitment gani kwa bajeti ya mwaka ujao bwawa lile kujengwa ili kilimo cha miwa kiweze kufanyika na kuunga mkono kile kiwanda cha sukari? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ni moja, sisi kama Wizara ya Kilimo tupo tayari kushirikiana na kufanya kazi na Wizara ya Viwanda na biashara ili kuhakikisha kwamba tunaongeza tija kwa wakulima hususani wa eneo la Kata ya Mhenge. Kwa hiyo jambo hilo tupo nalo tayari na tutafanya nao kazi kwa ukaribu. Kuhusu commitment ya Serikali kwenye Bwawa la Nyanzwa ambalo tayari usanifu wake umeshakamilika hatua ya sasa inayofuata ni kutangazwa kwa tender hiyo na baada ya hapo ni kwamba tutapata mkandarasi na mwisho tutamleta katika eneo husika ili aanze kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu letu kama Wizara ni kuhakikisha maeneo yote tutakayotangaza tender yatafunguliwa na tutahakikisha kwamba miradi hii inaanza kabla ya mwaka wa fedha ujao. Ahsante. (Makofi)