Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Simon Songe Lusengekile (29 total)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali na niipongeze Serikali kwa namna inavyochukua hatua juu ya mradi ule. Pamoja na hayo mradi ule katika Kijiji cha Mwagulanja umeacha sehemu kubwa sana ya wananchi wa Isuka takriban kilometa nne kufikia point ambapo maji yamewekwa.

SPIKA: Mheshimiwa swali lako ni Nyashimo…

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, ni Kata ya Nyashimo sasa hicho Kijiji nilichokisema. Naomba tu kuuliza Serikali nini mpango sasa wa kufanya extension kutoka kwenye ule mradi kwenda kwenye Kijiji cha Mwagulanje kule Isuka ili wananchi wa kule nao waweze kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Simon Lusengekile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huu mradi unaendelea kutekelezwa. Extension ni kazi ambayo hata yule Meneja aliyeko pale anaweza kufanya, kwa hiyo nimwaminishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kufika mwezi Machi, tutaanza kuzitekeleza extension, lakini kwa kutumia wataalam wetu ambao wako kule.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kuniona na mimi niulize swali la nyongeza kwa Wizara hii yetu ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Mahakama ya Wilaya ya Uyui ni sawasawa na tatizo lililoko pale kwetu Wilaya ya Busega na kesi za Mahakama ya Wilaya zimekuwa zikienda kusikilizwa Wilaya jirani ya Bariadi.

Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kutumia jengo lililopo la Mahakama ya Mwanzo ili litumike kusikiliza kesi za Mahakama ya Wilaya, lakini hivyo hivyo ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa…

NAIBU SPIKA: Swali ni moja Mheshimiwa, swali la nyongeza ni moja.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba Waziri wa Katiba na Sheria nipende kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutumia jengo la Mahakama ya Mwanzo inategemea sana sifa ya hilo jengo kwa sababu vingine ni vyumba vidogo ambavyo haviwezi kuhimili huduma ambazo zinatakiwa kutolewa kwenye ngazi ya Wilaya, lakini tutalichukua na kulifanyia utafiti ili kuona kama hiyo Mahakama ya Mwanzo ina sifa zinazostahili kuwa kwenye kiwango cha matumizi ya Wilaya na tukijiridhisha huduma itaanzishwa mara moja kwenye eneo husika, ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Niishukuru Serikali kwa majibu mazuri ambayo Naibu Waziri amewasilisha, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; wananchi wa Kata hii ya Imalamate yenye vijiji vitatu, kwa maana ya Mahwenge, Imalamate pamoja na Jisesa, wamejitolea sana kwa kujenga maboma ya kisasa ya zahanati. Je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuifanya kata hii kuwa moja ya kata za mfano ambazo wananchi wamejitolea kwa kujenga maboma haya ili waipatie kipaumbele cha kukamilisha maboma haya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Naibu Waziri yuko tayari sasa baada ya Bunge baada ya Bunge hili la Bajeti kuambatana pamoja nami ili kwenda kuwatembelea wananchi wa Kata ya Imalamate kuona kazi kubwa ambayo wameifanya ambayo itakuwa ya kuigwa katika nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega, kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kuhakikisha anawasemea wananchi wake na kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya huduma za afya. Pia niwapongeze sana wananchi wa Kata hii ya Imalamate na wananchi wa Busega kwa ujumla kwa kuendelea kuchangia nguvu zao katika ujenzi wa miundombinu ya kutoa huduma za afya kwa maana ya zahanati na vtuo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua na inathamini kwamba wananchi hawa wameendelea kutoa nguvu zao. Na ni kweli, ni moja ya kata ambazo zimefanya vizuri katika ujenzi wa vituo vya afya na hivyo katika mwaka ujao wa fedha, tumetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya maboma matatu katika Jimbo la Busega. Kwa hiyo bila shaka fedha hizi zitakwenda kukamilisha majengo haya katika Kata ya Imalamate.

Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kushirikiana naye kuwahudumia wananchi wa Busega, lakini pia kutambua michango yao. Hivyo baada ya kikao hiki, tutapanga na Mheshimiwa Simon Songe tuweze kuona lini muda muafaka tutaambatana kwenda Jimboni kwake Busega.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali katika Jimbo la Busega imeanzisha vituo vya afya viwili ambavyo mpaka sasa vimeshaanza lakini bado vinakosa wodi ya wazazi, wanaume pamoja na wodi ya wanawake. Nini kauli ya Serikali ili kupeleka fedha kwa ajili ya kumalizia vituo hivyo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lusengekile, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imejenga vituo vya afya viwili katika Jimbo la Busega na ujenzi ule unaendelea kwa awamu. Tumejenga awamu ya kwanza lakini tunafahamu kwamba kunakosekana wodi ya wazazi, lakini pia wodi ya wanaume na baadhi ya miundombinu mingine ambayo bajeti ijayo tutatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali tayari imemaliza kushauriana na wenzetu wa KFW na tayari kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali imetenga bilioni 19 za ndani kwa ajili ya kuanza mradi huu. Je, ni kiasi gani kimetengwa kwa kutoka kwa hawa marafiki zetu wa KFW kwa ajili ya mradi huu kwa mwaka wa fedha 2021/2022?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa, miradi mingi ya maji imekuwa ikitengenezwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu tu na Mkoa wetu wa Simiyu wananchi walio wengi ni wakulima na wafugaji. Je, Waziri anawahakikishiaje wananchi wa Mkoa wa Simiyu kwamba, mradi huu utaenda kuwasaidia katika zoezi zima la umwagiliaji na matumizi ya mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simon Lusengekile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anahitaji kufahamu ni kiasi gani kimetengwa na hawa wenzetu wa Serikali ya Ujerumani:-

Mheshimiwa Spika, kwa majibu ya rahisi ni kwamba, sisi tumetenga hiyo milioni 19 ambavyo imesomeka kwenye bajeti yetu na kwa Serikali ya Ujerumani wametenga bilioni 55 kwa ajili ya mradi huu. Na huu mradi ni mradi mkubwa ambao utakwenda kugharimu zaidi ya bilioni 444, fedha za ndani zitakazotumika zitakuwa ni bilioni 124 na fedha za KFW 320.

Mheshimiwa Spika, kwa suala la kuzingatia umwagiliaji na ufugaji, sisi kama Wizara tumezingatia na tumeweza kuona kwamba tunaenda kuhakikisha kukabiliana na mabadiliko ya tabia-nchi katika Mkoa wa Simiyu. Na shughuli kubwa ambazo zitaendelea kufanyika ni ujenzi wa mabwawa ambayo yatatumika katika umwagiliaji, lakini vilevile malambo katika namna ambavyo tutaendelea kupata fedha katika miaka ya fedha ya mwaka 2021/2022 pia malambo kwa ajili ya mifugo yatajengwa.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Kwa kuwa uhitaji wa uwanja wa ndege Mkoa wa Singida ni sawa na uhitaji wa uwanja wa ndege Mkoa wa Simiyu na tumekuwa tukipata majibu kwamba Serikali iko kwenye mchakato.

Sasa na mimi nataka tu commitment kwamba je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa uwanja wa ndege Mkoa wa Simiyu pale Igegu ili wananchi waweze nao kupanda ndege nikiwemo na mimi?
NAIBU WAZIRI, UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye swali la Mheshimiwa King una kwa kuwa mkoa huu ni mkoa mpya, Mkoa wa Simiyu na usanifu wa kina na upembuzi yakinifu umeshafanyika, gharama zimeshajulikana, Serikali inatafuta vyanzo mbalimbali, tukipata fedha Mheshimiwa Mbunge wa Busega naomba nikuhakikishie kwamba utapata uwanja katika Mkoa wa Simiyu. Kama ambavyo ameanza mapema lakini wanafanya kubwa sana. Hongereni sana kwa kazi nzuri ambayo mnafanya katika mkoa huo. Ahsante sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nikupongeze wewe kwa kutaja jina langu vizuri na nimkumbushe tu Naibu Waziri, naitwa Simon Songe Lusengekile.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa barabara hii inachochea sana uchumi wa wananchi wa Jimbo la Busega na Jimbo la Bariadi, kwa maana ya Ngasamo, Shigara, Dutwa pamoja na Mariri.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu sana wa kuipa kipaombele barabara hii ili iweze kutengeneza kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tunaelekea sasa mwisho wa Bunge letu la Bajeti; je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kutembelea Jimbo la Busega ili aone umuhimu wa hii barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lusengekile, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana na ndiyo maana kwanza Mheshimiwa Mbunge tayari kuna fedha zipo anajengewa madaraja mawili hapa kama nilivyoyataja katika jimbo lake. Lakini, la pili tumeahidi kwenye jibu langu la msingi kwamba barabara hii inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka huu wa fedha ambao unaanza Julai ambayo ni keshokutwa. Kwa hiyo, hii ikikamilika tutajenga barabara hii kwa kiwango cha lami tunajua umuhimu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili mimi niko tayari kufanya ziara kule Busega. Kwanza kuna shemeji yangu pale kwa hiyo nitaenda kumsalimia. Tuko tayari, tutaambatana. Ahsante sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, niishukuru sana Serikali kwa hatua za haraka ilizochukua. Ninavyozungumza sasa tayari msingi wameshaanza kuchimba. Pamoja na hayo, kwa kuwa kutoka Busega kwenda Bariadi ambako sasa kesi hizi zinaendeshwa za Kiwilaya ni kilometa takriban 70 na pale Makao Makuu ya Wilaya tuna jengo la Mahakama ya Mwanzo.

Je, Serikali sasa haioni haja ya kuturuhusu kutumia jengo lile angalau kwa hiki kipindi ambapo bado tunasubiri jengo letu kukamilika, kusikiliza kesi za kiwilaya ili kuondoa huu usumbufu wa wananchi kwenda Bariadi na kutumia gharama kubwa ambazo wakati mwingine wanashindwa kuzimudu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, pale kuna Mahakama ya Mwanzo, lakini vigezo vile vya kuitumia kama Mahakama ya Wilaya ndiyo kidogo vinakinzana, kwa hiyo waendelee kuvumilia ili tutakapokamilisha jengo lenye sifa, waweze kuanza kulitumia rasmi. Ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hospitali ya Halmashauri ya Busega inahudumia takribani wakazi 300,000 na hatuna kabisa X-ray inabidi wananchi wale kwenda kutafuta huduma za X-ray kwenye wilaya nyingine kama Bariadi, Bunda na Magu. Je, ni lini Serikali itaipatia X-ray Hospitali ya Halmashauri ya Busega ili iweze kuhudumia wananchi wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Hospitali hii ya Wilaya ya Busega haina mashine ya X-ray na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vipaumbele vya kupeleka mashine za X-ray, kipaumbele cha kwanza ni kupeleka katika hospitali za halmashauri.

Kwa hiyo, kadri ambavyo tunaendelea kuweka mipango yetu tutahakikisha hospitali zote za halmashauri zinakwenda kupata X-ray na ushahidi tumeona katika fedha hizi za UVIKO tunakwenda kununua digital X-ray zaidi ya 75 kwa ajili ya hospitali zetu za wilaya ambazo hazina, lakini pia vituo vya afya ambavyo vina idadi kubwa ya wananchi. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba tutaipa kipaumbele Hospitali ya Wilaya ya Busega. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nami naomba niulize swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inayotokea Duto kuelekea Nyashimo kupitia Shigala, Malili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Duto - Nyashimo itajengwa tu pale ambapo fedha na bajeti itaruhusu kwa sababu tayari ipo kwenye mpango kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa zoezi hili alilolisema Mheshimiwa Waziri hapo awali lilishawahi kufanyika na halikuwa na mafanikio na barabara hii ni muhimu sana kwa Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Mwanza. Je, nini maelekezo yake ya haraka kwa wafanyakazi wa TARURA ili zoezi lifanyike haraka ili tuweze kuunganisha barabara hii katika mikoa hii miwili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimeshatoa maelekezo kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Busega kupitia TARURA waanze mara moja mchakato huo ili nia ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka huduma kwa wananchi na nia ya Mbunge wa jimbo lile kuhakikisha barabara hiyo inapitika muda wote ifikiwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maelekezo haya nimeshayatoa na nayarudia tena na nitakuwa wa kwanza kuyafuatilia maelekezo hayo ili yaweze kutekelezeka.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Kituo hiki cha Afya Kiloleli kinahudumia zaidi ya Kata tatu kwa maana ya Kiloleli, Nyaruhande pamoja na Rubugu, lakini kina kituo cha afya kimoja: Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa wodi ya wanawake, watoto pamoja na wanaume ili kukidhi mahitaji ya kituo cha afya hiki?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Waziri yuko tayari kutembelea Kituo cha Afya Kiloleli ili kuona mahitaji ya wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, alichoomba Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, pamoja na kwamba kituo hiki cha afya kinafanya kazi, ameomba tu tuongeze fedha kwa ajili ya wodi tatu ili kuhakikisha kwamba kiwe full kwenye matumizi yake.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu sasa hivi tumekuwa tukipata fedha karibu kila mwezi na zile fedha tumekuwa tukizielekeza kule, kwa hiyo, fedha nyingine tutatenga kwa ajili ya kuhakikisha tunapata wodi tatu katika kituo hiki ili kiwe full katika matumizi yake.

Mheshimiwa Spika, la pili, ameomba kwenda kutembelea. Najua ni rafiki yangu na anaelewa kwamba nikitembelea pale atapata mambo mengi na mema. Nimhakikishie tu kwamba tutakwenda pamoja, tutatafuta moja ya weekend tukiwa katika kipindi cha Bunge hili refu tufike ili tuone hizo kero ambazo amezizungumza. Ahsante sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais mwaka jana alipotembelea Mji wa Lamadi aliahidi ujenzi wa stendi. Je, ni lini ujenzi huu sasa utaanza ili kuokoa maisha ya watu kwa sababu ya msongamano mkubwa ulioko pale?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe Lusongekile, Mbunge wa Jimbo la Busega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais Daktari Samia Suluhu Hassan alielekeza mamlaka za Halmashauri ya Busega kuanza mpango wa kujenga stendi katika eneo la Lamadi. Ofisi ya Rais TAMISEMI tumekwishamwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busega kufanya tathmini na kuandaa makadirio ya gharama kwa ajili ya kuanza ujenzi huo. Kazi hiyo inaendelea watawasilisha Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya hatua zaidi, ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niishukuru sana Serikali kwa mpango iliyoweka, tuiombe sasa tu zabuni iwahi na mkandarasi apatikane ili wanachi wanufaike na taa hizi za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja tu la nyongeza mahali hapa. Ni nini sasa Mkakati wa Serikali ya uwekaji wa taa za barabarani kwenye miji iliyoendelea ikiwemo Magu, Busega pale Masanza pamoja na Nasa Ginnery lakini pamoja na Itilima Mkoani Simiyu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nitoe tu maelezo kwa ajili ya swali hili. Kwamba kwa sasa Serikali imetoa mamlaka kwa Mameneja wa Mikoa wote wa TANROADS kupitia mikutano ya mifuko ya barabara pamoja na RCC kuanisha miji yote mikubwa ambayo imekua na inahitaji taa ili waweze kuziombea hela kwa ajili ya kuweka barabara kwenye miji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa kwa barabara zote ambazo zinajengwa kwa sasa imekuwa ni sehemu ambapo tunapoanza kujenga barabara miji yote inawekewa taa. Kwa hiyo inakuwa ni sehemu ya gharama ya zile barabara. Kwa hiyo ni pamoja na hiyo miji aliyoisema Mheshimiwa Simon Songe, ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kupeleka fedha wilayani kama alivyotuhakikishua Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Serikali sasa imesema miradi hii ya ujenzi wa vyuo vya VETA itaanza mwaka huu kwa Wilaya 63 ikiwemo na wilaya ya Busega. Je, nini mpango wa Serikali wa kumaliza vyuo hivyo kwamba itamaliza lini ili Watanzania waweze kunufaika katika hizi Wilaya 63?

Swali la pili, je Naibu Waziri yuko tayari sasa kutembelea Busega ili tuje tumuoneshe eneo ambalo tayari tumeshatenga kwa ajili ya ujenzi wa VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simon Songe, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaeleza kwenye majibu ya msingi kwamba Serikali imetenga fedha na tunaenda kuanza ujenzi huu baada ya taratibu za manunuzi, lakini topographical survey, geo-technical survey pamoja na environment impact assessment kuweza kukamilika. Kwa hiyo nimuondoe hofu na wasiwasi kwamba tunaenda kuanza ujenzi huu.

Mheshimiwa Spika, lakini lini tutamaliza? Kwanza naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi huu tutajenga kwa awamu, kwa hiyo katika awamu ya kwanza tunakwenda kujenga majengo tisa ikiwemo na karakana tatu, lakini katika awmu ya pili tunakwenda kujenga majengo nane ili kuweza kukamilisha yale majengo 17.

Kwa hiyo, katika mwaka huu wa fedha tutakadiria kwamba au tunaazimia tutakamilisha yale majengo tisa na katika mwaka ujao wa fedha tutamalizia yale majengo manane yaliyobaki. Kwa hiyo, matarajio ya kumaliza ni mpaka mwaka ujao wa fedha tutakapokamilisha majengo yote 17.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ameulizia kuhusu suala la kwenda. Hili ni jukumu letu, ni kazi yetu kwa vile tunapeleka fedha kule, fedha nyingi, ni lazima tufanye usimamizi wa karibu na ufuatiliaji wa karibu. Kwa hiyo tuko tayari kama Wizara kwenda kuona maeneo haya ya ujenzi, lakini vilevile kwenda kuratibu taratibu za ujenzi kuhakikisha kwamba unakamilika kwa viwango vinavyohitajika, nakushukuru sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Nyashimo Wilayani Busega kuelekea Dutwa Wilayani Bariadi imekuwa ikiahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami yenye takribani kilometa 47 kupitia Malili, Dutwa na pale Shigara.

Leo nataka commitment ya Serikali Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya kutoka Nyashimo kwenda Dutwa sasa hivi inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na itakapokuwa imekamilika barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukipata ahadi ya Serikali kupitia Waziri Aweso kuanza kwa mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria kutoka Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu. Lakini mpaka sasa haujaanza na tuliahidiwa kwamba ungeanza mwezi wa nane mwaka jana. Nini commitment ya Serikali juu ya mradi huu kuanza kwa ajili ya kunufaisha wananchi wote hao niliowataja?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, nikiri maelekezo ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ni kutumia rasilimali toshelevu ikiwemo mito pamoja na maziwa kuhakikisha kuwa tunatatua matatizo ya maji. Tumepata fedha zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa ajili ya kutumia Ziwa Victoria na kutatua tatizo la maji katika Mkoa wa Simiyu ikiwemo Bariadi, Busega na Itilima.

Kwa hiyo, mkakati wa Serikali sasa hivi tupo hatua ya kumpata mkandarasi na tupo hatua za mwisho. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mkandarasi atapatikana kwa wakati na utekelezaji wake tunaenda kuanza mara moja. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara ya kutoka pale Nyashimo kwenda Dutwa yenye kilometa 47 tumekuwa tukiahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami zaidi ya miaka 10 sasa na kila nikiuliza toka nimekuja hapa Bungeni nimekuwa nikiambiwa kwamba itaanza kujengwa mwaka wa fedha ujao. Sasa naomba kuuliza ni mwaka wa fedha upi barabara hii sasa itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lusengekile, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema lakini kujenga kwa barabara pia kunategemea kwa kweli na upatikanaji wa fedha na mpango wa Serikali kwa kweli ni kuzijenga hizi barabara kwa kiwango cha lami ikiwepo na barabara ya Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, tunakwenda kwenye bajeti naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, kadiri muda unavyokwenda na kadiri tutakapoendelea kupata fedha barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali, tunatambua kwamba nchi hii hujengwa na wafanyakazi ambao wameajiriwa na wafanyakazi ambao hawajaajiriwa kwa mfano wakulima na wafugaji.

Je, sasa Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia hawa watu ambao wameijenga nchi yetu kwa muda mrefu wakiwa hawajaajiriwa kwa kazi za Serikali kwa maana ya wakulima na wafugaji ili kuwasaidia wanapofikia umri ambao hawawezi kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali inapaswa kuzingatia Watanzania wote wanaojenga nchi yao katika kufanya kazi mbalimbali. Moja ya mikakati ya Serikali ambayo iliona suala hilo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema, ni pamoja na kubadilisha skimu za utoaji wa pensheni katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kuzingatia kwamba yapo makundi ambayo siyo ya wafanyakazi, wanafanya kazi zisizo rasmi, lakini wanafanya kazi kwa mfano kwenye maeneo ya viwanda, kilimo, biashara na wajasiriamali wadogo wadogo. Tayari Mfuko wa NSSF ambao unashughulika na sekta isiyo rasmi umeanza kukusanya michango kwa kuwatambua hawa walio kwenye makundi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, bado Serikali pia kwa kutambua kwamba wapo ambao ni wajenzi wa Taifa na wakifikia katika hatua ya uzee wanahitaji msaada. Serikali imekwisha kuandaa vituo vya wazee ambao wanakuwa wanahitaji msaada wa Serikali kwa mfano wa matibabu na maisha, kuna mpango maalum wa TASAF ambapo zaidi ya wazee 647,512 ni wanufaika wa mfuko huo. Lakini zaidi ya hapo pia vipo vituo maalum zaidi ya 14 katika mikoa 26 nchini ambavyo Serikali imeviweka kwa ajili ya kuwasaidia wazee, ahsante sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ahsante kwa majibu ya Serikali.

Kwa kuwa, ufanisi wa Mabaraza umekuwa mdogo sana kwa sababu hayapo kila Wilaya, ukilinganisha kwa mfano Itilima wanapata huduma Maswa, Meatu wanapata huduma Maswa na tumefanya wanachi kuingia gharama kubwa bila sababu za msingi. Ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 74(1) ukurasa wa 179, imeeleza kwamba Mabaraza haya sasa yahamishiwe kwenye Muhimili wa Mahakama.

Je, ni lini Serikali itaanza mchakato huo na kuukamilisha mapema?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ninakushukuru na naomba nijbu swali moja la Mheshimiwa Simon Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Simon kwa kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Wizara yetu ya Katiba na Sheria pamoja na Wizara ya Ardhi pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama na mfumo mzima wa Mahakama wako kwenye hatua za mwisho za kukamilisha mjadala huu wa kuhamishia Mabaraza haya kwenye Muhimili wa Mahakama kama ambavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeeleza. Ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga minara katika Kata ya Shigala, Nyaruhande na Kijiji cha Kijereshi ili kuboresha mawasiliano kwa sababu kata hizi zinashida kubwa ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niwajulishe watanzania, Waheshimiwa Wabunge, tarehe 13 Mei, 2023 tunakwenda kusaini Mkataba wa kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata 713 ambayo ni wilaya 127 mikoa yote, ambapo ni Vijiji takribani 1407. Watanzania takribani milioni 8.5 wanakwenda kupata huduma ya mawasiliano, ambapo Mheshimiwa Rais, ameidhinisha kiasi cha bilioni 125.9 kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeno hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wahudhurie katika hafla ya utiaji Saini wa mikataba hii ambayo inakwenda kufikisha huduma ya mawasiliano kote Tanzania.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kituo cha Afya cha Kiloreli kilipandishwa hadhi, kutoka zahanati na baadaye kikawa kituo cha afya, lakini bado hakina majengo yoyote yenye kukidhi kuwa kituo cha afya;

Je, Serikali ina mpango wowote kuleta fedha kwa ajili ya kuongeza majengo pale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba inajenga majengo yote ambayo yanahitajika kwenye vituo vya afya hapa nchini, kikiwemo ambacho amekitaja Mheshimiwa Songe cha kule Wilayani Busega. Hivyo basi kadri ya upatikanaji wa fedha tutahakikisha tunapeleka fedha katika kituo hiki cha afya ili kiweze kuapata majengo yanayohitajika.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu lakini pia na swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Busega wamejenga maboma ya madarasa 69 na nyumba za walimu 11. Je, Serikali sasa iko tayari kupelekea fedha kwa ajili ya kumalizia maboma ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala hili la maboma kama nilivyotoka kusema hapa awali, tayari kuna timu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maelekezo yake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki ambayo inafanya tathmini kujua maboma ya nyumba za walimu lakini vilevile maboma ya madarasa, pale tutakapopata idadi kamili kutoka kwenye Halmashauri hizi ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Busega tukaa na kutafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma haya. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Barabara ya kutoka pale Nyasho kupitia Mwanangi – Badugu kwenda Busami imekuwa ikiharibika mara kwa mara na ni ya muhimu sana katika uchumi wa Jimbo la Busega: Je, lini Serikali iko tayari kujenga barabara hii kwa kiwango cha changarawe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la Mheshimiwa Songe la barabara zake kule Jimboni Busega, wote ni mashahidi kwamba TARURA sasa imeongezewa fedha mara tatu na Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani, na bajeti ile imebaki pale pale katika kiwango cha juu cha zaidi ya Shilingi bilioni 776 ambayo Bunge hili lilipitisha. Hivyo basi, niwatoe hofu Wabunge wengi kwamba sasa tunakwenda kufungua barabara nyingi zaidi za mijini na vijijini na vile vile kukarabati barabara nyingi zaidi zikiwemo za kule kwa Mheshimiwa Songe Wilayani Busega.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sheria za uandaaji wa hesabu zimekuwa zimekubadilika mara kwa mara kulingana na mahitaji ya kimataifa; je, sasa Serikali haioni ni wakati sahihi sasa wa kutenga fungu rasmi kwa ajili ya hawa wahasibu ili wakaweze kuhudhuria classes za NBAA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe, Mbunge wa Jimbo la Busega kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali tutaendelea kutenga fedha kadri inavyopatikana lakini kwa sasa tutaendelea na mafunzo ili kuhakikisha kwamba haya yanayotokea sasa hayaendelei. Ahsante sana.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE; Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, Kata hizi mbili ambazo nimezitaja na vituo vya afya ambavyo nimevitaja vina wananchi wengi na vinahudumia wananchi wengi sana katika vituo hivi.

Je, Serikali sasa haioni sababu za kuwa na mpango wa haraka ili kuharakisha ujenzi wa wodi hizi ambazo nimezitaja ili wananchi waweze kupata huduma wasisafiri umbali mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kweli Kituo cha Afya cha Lukungu na Kiloleli ni miongoni mwa vituo vya afya ambavyo vinahudumia wananchi wengi sana na kwa kutambua hilo, tayari Serikali imekwishaainisha vituo vya afya vyote ambavyo vina miundombinu pungufu na vinahudumia wananchi wengi ili fedha iweze kutafutwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaongeza miundombinu ambayo inapungua.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Songe kwamba Kituo cha Afya cha Lukungu tayari kimeingizwa kwenye mpango huo na mara fedha ikipatikana tutahakikisha tunaenda kujenga miundombinu hiyo, ahsante
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa majibu yake awali, lakini nina swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Busega ni moja ya Halmashauri mpya hapa nchini na makusanyo yake ni kidogo sana.

Je, Serikali haioni sababu ya msingi ya kutenga fedha kutoka Serikali Kuu ili kuanza ujenzi wa miundombinu hii ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mkurugenzi afanye tathmini kubaini gharama zinazohitajika kujenga madarasa hayo na miundombinu hiyo na awasilishe rasmi Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili tuweze kuona kama Halmashauri inaweza kujenga sehemu ya miundombinu hiyo, lakini eneo lingine la miundombinu, Serikali Kuu iweze kuchukua. Ahsante.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwenye orodha ya masoko ya Samaki yatakayojengwa katika mpango ambao ameusema Mheshimiwa Naibu Waziri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni pamoja na Nyamikoma, Jimbo la Busega. Mpaka sasa soko hili halijaanza kujengwa na imebaki miezi minne kukamilika kwa mwaka wa fedha. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa soko hili la Nyamikoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaanza ujenzi wa Soko Nyamikoma mara tu fedha zitakapokuwa zimepatikana. Tayari Serikali imeshaanza ujenzi wa masoko katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tunduma, Muleba, Momba, Ludewa, Busega, Nkinga na Kalambo. Kwa hiyo, mara tu tutakapopata fedha Serikali itaanza ujenzi haraka sana iwezekenavyo katika Kijiji cha Nyamikoma. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Lamadi la kimkakati ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya mwaka 2022?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, ahadi za viongozi wakuu wa nchi ni kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge bila shaka tayari andiko hili lilishafika na limepita katika ngazi zote, kwa hiyo Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuja kutekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)