Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Tumaini Bryceson Magessa (19 total)

MHE. TUMAINI B. MAGESSA Aliuliza:-

Je, ni lini Mradi wa Maji wa Chankorongo utawekewa vituo vya kuongeza kasi ya maji ili upate uwezo wa kutoa huduma katika maeneo mengi zaidi Jimboni Busanda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Chankorongo unatumia maji ya Ziwa Victoria ukiwa na pampu yenye uwezo wa kuzalisha lita 155,000 kwa saa ambapo kwa sasa unatoa huduma kwa wakazi wapatao 23,756 wa vijiji vitano vya Chankorongo, Chikobe, Nyakafulo, Chigunga na Kabugozo katika Jimbo la Busanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha mradi huu unanufaisha wakazi wengi wa Jimbo la Busanda, Serikali imeanza upanuzi wa mradi huo wa maji kwa kuanza utekelezaji wa Mradi wa Maji Katoro-Buseresere wenye thamani ya shilingi bilioni 4.2. Kupitia mradi huo wakazi wa vijiji vya Luhuha, Nyakagomba, Inyala na Mji Mdogo wa Katoro watanufaika na huduma ya maji. Kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 20 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2021.

Aidha, katika kuhakikisha wananchi wengi wananufaika na huduma ya maji, Serikali kupitia programu ya Mpango wa Malipo kwa Matokeo inaendelea na ujenzi wa miradi ya maji ya bomba katika vijiji vya Nyakagwe na Rwamgasa ambapo wakazi wapatao 14,315 wa vijiji hivyo watanufaika na huduma ya maji safi.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA Aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje katika kupanga matumizi bora ya ardhi kwa Vijiji vyote nchi nzima ili kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Magessa Tumaini, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya Mwaka, 2007 Sura ya 116 Kifungu cha18, kimebainisha Mamlaka za Upangaji kuwa ni Halmashauri za Vijiji, Wilaya na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ngazi ya Taifa na Mkoa. Jukumu la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji ni la Halmashauri za Vijiji na Wilaya. Wizara ya Ardhi kupitia Tume ya Mipango ina jukumu la kuwajengea uwezo, kusimamia na kuratibu Mamlaka za Upangaji na sekta mbalimbali katika utekelezaji wa mipango hiyo.

Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi, jitihada mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuhakikisha vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Jitihada hizo ni pamoja na zifuatazo: -

Kwanza, ni kutenga bajeti kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini, kupitia Mamlaka za Upangaji na hivyo kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi.

Pili, kushirikisha wadau mbalimbali wa kimkakati wa matumizi ya ardhi, kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji mbalimbali nchini.

Tatu, kuendelea kuhamasisha Halmashauri za Wilaya na Mikoa kutenga bajeti ya uandaaji wa mipango wa matumizi ya ardhi katika vijiji kwenye maeneo yao.

Nne, kushirikiana na vyuo vinavyofundisha masuala ya ardhi ikiwemo Chuo cha Ardhi, katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Tano, kubuni miradi ya kimkakati itakayowezesha uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi nchini.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya Zimamoto katika Mji Mdogo wa Katoro ili kupunguza hatari ya moto iwapo utatokea ikizingatiwa kwamba kuna ongezeko kubwa la wafanyabiashara katika Mji huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nami kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Magessa Tumaini, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa huduma za uzimaji moto na uokoaji katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Kutokana na ufinyu wa bajeti na upungufu wa rasilimali watu na vifaa, Mji Mdogo wa Katoro utaendelea kupata huduma za zimamoto na uokoaji kutoka katika Kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilichopo Geita Mjini mpaka hapo Jeshi litakapopata rasilimali za kutosha kuweza kuwa na Kituo katika Mji Mdogo wa Katoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kutoa Elimu ya Kinga na Tahadhari ya Moto katika Mji Mdogo wa Katoro ili kupunguza majanga ya moto yanayoweza kutokea katika mji huo. Ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italipatia Jimbo la Busanda Vituo vya Afya hususan Tarafa ya Butundu na Tarafa ya Busanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Busanda katika Wilaya ya Geita lina Vituo vya Afya vitano ambapo vituo vya Afya vitatu vya Nyarugusu, Kashishi na Bukoli vipo katika Tarafa ya Busanda na Vituo vya Afya viwili vya Chikobe na Katoro vipo katika Tarafa ya Butundwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendelea kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Geita kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 hadi 2019/2020 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Geita shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Geita; shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Katoro na shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nyarugusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Geita. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Geita na Hospitali ya Katoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetengewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma manne ya zahanati, yakiwemo maboma ya Zahanati za Lubanda na Bujura katika Jimbo la Busanda. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetengewa fedha shilingi milioni 375 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Isulwabutundwe na shilingi milioni 375 kwa ajili kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Butobela.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za afya katika Jimbo la Busanda, ikiwemo kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Geita kupitia Nyarugusu kwenda Bukoli hadi Kahama ambapo upembuzi yakinifu ulishafanyika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Magesa Tumaini, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kuandaa nyaraka za zabuni kwa barabara ya Geita – Nyarugusu – Kahama yenye urefu wa kilometa 133.9 imekamilika mwaka 2017. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Aidha, mwaka 2021, Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick ilionesha nia ya kufadhili ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Kwa sasa, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara ya Madini na Wizara ya Fedha na Mipango zinaendelea na mazungumzo na Kampuni ya Barrick kuhusu utaratibu wa ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 838.97 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali katika barabara hii. Aidha, Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Shinyanga kwa kutumia fedha za maendeleo inakamilisha ujenzi wa mita 600 kwa kiwango cha lami katika barabara hii kuanzia eneo la Busoka katika Manispaa ya Kahama. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU K.n.y. MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya maboresho ya ujenzi na ukarabati Vituo vya Afya Chikobe na Bukoli ili vitoe huduma stahiki kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Jimbo la Busanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa mwaka 2023/2024 itatenga kutoka mapato ya ndani shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Kituo cha Afya cha Bukoli. Aidha katika mwaka huo, Halmashauri ya Wilaya ya Geita itatenga shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati katika Kituo cha Afya Chikobe. Ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, nini hatma ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Geita – Nyarugusu hadi Kahama hususani kipande cha Geita – Nyarugusu – Bulyanhulu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika makubaliano ya msingi ya awali kati ya Serikali na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick, Kampuni ya Barrick ilikubali kutoa dola za Kimarekani milioni 40 kugharamia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Hivyo, Serikali na Kampuni ya Barrick zimekubaliana kuwa fedha hizo kiasi cha dola za Kimarekani milioni 40 zitumike kwa ujenzi wa barabara ya Kahama – Bulyanhulu junction – Geita yenye kilometa 120 na kipande cha Bulyanhulu junction hadi Kakola (kilometa 11.3). Kwa sasa Serikali iko katika hatua ya kukamilisha majadiliano hayo ili kuwezesha mradi huo kuanza kutekelezwa, ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia soko la ndani la maziwa kwa kuhimiza na kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni kabla ya kutafuta masoko ya nje?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Magessa Tumaini, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mkakati wa kukuza soko la maziwa nchini kwa kuimarisha na kuendeleza programu mbalimbali zinazochochea unywaji wa maziwa ikiwemo programu ya unywaji wa maziwa shuleni. Mpango wa unywaji maziwa shuleni umeweza kuwafikia watoto 90,000 wa shule za msingi 39 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Iringa, Mbeya, na Tanga.

Vilevile Serikali inaendelea kuhamasisha unywaji maziwa nchini, kwa kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, maonesho mbalimbali ya Wiki ya Maziwa Kitaifa inayoadhimishwa mwezi Mei kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itakutana na wadau mbalimbali wakiwemo wa tasnia ya maziwa ili kuandaa mikakati thabiti kwa lengo la kuongeza idadi ya shule zinazotoa huduma ya unywaji wa maziwa. (Makofi)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, lini Wananchi wa Busanda watapatiwa Wilaya ya Busanda kama ilivyopendekezwa na Baraza la Madiwani, DCC na RCC Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 24/02/2021 Mkoa wa Geita uliwasilisha mapendekezo ya kuanzisha Wilaya mpya ya Busanda kwa kugawa maeneo ya Wilaya za Geita na Chato. Kwa kuwa mamlaka nyingi zilizoanzishwa bado zina upungufu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya utawala na huduma za kijamii, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itakapokamilisha maboresho ya miundombinu na huduma kwenye mamlaka zilizoanzishwa, itaendelea na taratibu za uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala ambayo yatakakidhi vigezo, ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya kutoka Geita – Bukoli hadi Kahama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepata fedha kiasi cha dola za Marekani milioni 40 sawa na shilingi bilioni 92 kupitia Mkataba wa makubaliano na Kampuni ya Kuchimba Madini ya Barrick kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Kahama – Bulyanhulu hadi Kakola urefu wa kilometa 73. Kwa sasa kazi ya kupitia usanifu inafanyika kwa pamoja kati ya wataalam wa Serikali na Kampuni ya Barrick. Kazi zimepangwa kutangazwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023 na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali itatenga fedha katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kipande kilichobaki cha barabara kutoka Geita – Bukoli – Bulyanhulu Junction kilometa 57.4, ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Wavuvi ambao wameunda vikundi na kuanza ufugaji wa vizimba katika Jimbo la Busanda?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Magessa Tumaini, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2022/2023, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Maendelo ya Kilimo (TADB) inatekeleza mradi wa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba ya pembejeo za ufugaji samaki ikijumuisha vizimba, vifaranga vya samaki na chakula cha samaki kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba. Aidha, jumla ya wanufaika 3,154 wameainishwa kunufaika na mradi huo ikijumuishwa vikundi 93, kampuni 10, na watu binafsi 32. Kwa upande wa Geita DC vikundi vitatu vinatarajiwa kunufaika na program hiyo ikiwemo kikundi cha Tumaini chenye wanachama 10 kutoka Jimbo la Busanda. Vikundi hivi vitapatiwa mikopo ya pembejeo za ufugaji samaki kwenye vizimba yenye thamani ya Shilingi milioni 69.4 kwa kila kikundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba ya pembejeo za ufugaji samaki kwa kuwawezesha wafugaji samaki wenye vizimba 893. Hivyo, natoa wito kwa wafugaji samaki nchini wakiwemo wale wa Jimbo la Busanda kuendelea kuchangamkia fursa hii kwa kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika wa ufugaji samaki.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:-

Je, ni kwa nini bei ya kuunganisha umeme katika Kijiji cha Lwamgasa ni shilingi 321,000 tofauti na vijiji vingine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Magessa Tumaini, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa kutoka TAMISEMI, eneo la Lwamgasa linatambuliwa kama Mji Mdogo na hivyo malipo ya gharama ya kuunganisha umeme iliwekwa 320,960 kwa vile panakidhi mwonekano wa mji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepokea maombi mengi kutoka kwa wakazi wa maeneo ya vijiji miji wanaotozwa shilingi 320,960 kama gharama za kuunganisha umeme ndani ya mita 30 iwe 27,000. Kijiji cha Lwamgasa ni miongoni mwa vijiji miji hivi. Kwa sasa, uchambuzi bado unaendelea ili kubaini uhalisia wa maeneo hayo. Uchambuzi ukikamilika gharama halisi stahiki zitatolewa, nashukuru.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Busanda ili kiweze kutoa elimu ya uchimbaji madini na hatimaye kuongeza tija kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Vyuo vya Ufundi Stadi nchini ili kuwapatia ujuzi wananchi utakaowawezesha kutekeleza shughuli za kiuchumi katika maeneo yao. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilipeleka fedha kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 4.2 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Geita kilichojengwa katika Halmashauri ya Mji wa Geita. Ujenzi wa Chuo hiki upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Busanda ipo katika Wilaya ya Geita, Serikali inaomba wananchi wa Busanda kutumia chuo hicho cha Mkoa kilichojengwa katika Wilaya ya Geita ambapo elimu ya uchimbaji wa madini itatolewa.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA kwenye vijiji zaidi ya 40 Busanda?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Busanda lina jumla ya vijiji 83 ambapo kati ya vijiji hivyo vijiji 40 vimefikiwa na miundombinu ya umeme na vijiji 43 havina umeme hivyo vimeingizwa katika Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Geita ulikumbwa na changamoto iliyotokana na mkandarasi wa kwanza ambaye ni M/s Samheung Electric Power Company Limited aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi katika Wilaya za Nyang’hwale, Mbogwe na Geita, Mkoa wa Geita kushindwa kuwasilisha dhamana ya kutekeleza kazi yaani performance guarantee ndani ya siku 28 kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi.

Mheshimiwa Spika, hali hii ilipelekea wakala kuanza upya taratibu za ununuzi wa mkandarasi wa kutekeleza mradi huu katika Mkoa wa Geita ambapo kampuni ya M/S CRJE-CTCE Consortium ilishinda zabuni hiyo. REA na mkandarasi waliingia mkataba mpya mwezi Januari, 2022 wa kutekeleza mradi huu unaotarajia kukamilika mwezi Julai, 2023. Kwa sasa mkandarasi huyo anaendelea na utekelezaji wa mradi huo kwa gharama ya shilingi bilioni 25.4 katika Mkoa wa Geita na Busanda ikiwemo.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:-

Je, upi mpango wa kuboresha Vituo vya Polisi Busanda hususani Kituo cha Katoro na Chigunda?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama maandalizi ya kuboresha vituo vya Katoro na Chigunda, tathmini kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji wa mazingira ya vituo hivyo imeshafanyika na kubaini kuwa kiasi cha shilingi 37,265,000 zinahitajika. Fedha hizo tunatarajia kuzitenga kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/2025 ili kugharamia ukarabati wake.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, nini mkakati wa Serikali wa kulipatia Jimbo la Busanda Halmashauri, kwani michakato ya DCC na RCC iliwasilishwa TAMISEMI?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliwasilisha maombi ya kupandishwa hadhi Jimbo la Busanda kuwa halmashauri kwenda Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa barua ya tarehe 24 Machi, 2020. Maombi hayo yalifanyiwa kazi kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imetoa kipaumbele katika kuboresha na kukamilisha miundombinu kwenye maeneo ya kiutawala yaliyopo ili yaweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baadaye kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa. Ahsante.
MHE. EDWIN E. SWALLE K.n.y. MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, lini ujenzi wa Barabara ya Katoro hadi Ushirombo hususani kipande cha Katoro hadi Luhembero utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Katoro hadi Ushirombo yenye urefu wa kilometa 58.2 unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sasa maandalizi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Nyikonga hadi Kashelo kilometa 10.5 yanaendelea chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia ambapo mkataba kwa ajili ya kuanza ujenzi unatagemewa kusainiwa mwezi Agosti, 2024. Kwa sehemu zilizobaki za Katoro – Nyikonga kilometa 26.2 na Kashelo – Ushirombo kilometa 21.5, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:-

Je, lini TFS itawaruhusu Wananchi wa Busanda kufanya shughuli za kiuchumi katika hifadhi ya misitu iliyopo kati ya Geita na Katoro kwani haina miti?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Msitu Geita ilihifadhiwa rasmi mwaka 1953 na inasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa hekta 50,836.535 ilifanyiwa mapitio ya mipaka yake kupitia Tangazo la Serikali Na. 717 la Mwaka 2018 kwa lengo la kupunguza maeneo yaliyokuwa yamevamiwa na wananchi au kutoa maeneo yaliyoombwa kwa shughuli za maendeleo kwa vijiji na mitaa inayopakana na hifadhi hiyo. Mabadiliko hayo ya mipaka yalisababisha kupungua kwa eneo la hekta 4,522.95 kwa malengo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia uharibifu uliofanyika katika hifadhi ya msitu huo, Serikali imeweka mpango wa kurejesha uoto wa asili uliopotea na kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Serikali imetenga fedha za kupanda miti kwenye hekta 100. Hivyo kwa kipindi hiki ambacho Serikali inafanya jitihada za kurejesha uoto wa asili uliopotea, jitihada zozote za kuruhusu kufanyika shughuli za kibinadamu/kiuchumi zitafifisha jitihada za Serikali.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Vituo vya Afya Kata za Lwamgasa, Nyakagomba na Magenge – Busanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya katika kata za kimkakati. Hadi kufikia Septemba, 2024 Serikali ilikuwa imekamilisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya 898 ambavyo vinatoa huduma ngazi ya kituo cha afya ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji wa dharura vikiwemo Vituo vya Afya vya Bukoli na Nyakagwe kwa thamani ya shilingi milioni 400 katika Jimbo la Busanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kujenga vituo vya afya katika kata za kimkakati kote nchini, zikiwemo kata zitakazokidhi vigezo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kadiri ya upatikanaji wa fedha.