Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tumaini Bryceson Magessa (27 total)

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile mradi huu wa Chankorongo ulioko Ziwa Victoria unaweza tu kupita katika vijiji alivyovitaja; je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba maji kutoka Ziwa Victoria yanaweza kufika kwenye maeneo ya Nyarugusu, Bukoli na Kata ya Nyakamwaga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magessa, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa eneo la Nyarugusu, maeneo ya machimbo haya Serikali tayari tuko kwenye mpango wa kupitisha mradi mkubwa pale wa maji kutoka Geita na utapita eneo hilo maji yanayotoka Ziwa Victoria na eneo lile pia, watapata extension kwa maana ya mtandao wa mabomba, maji yatafikia hapo na vilevile nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge namna ambavyo waliweza kuzungumza na Mheshimiwa Waziri alipokuwa ziara katika eneo lake, basi yale mazungumzo yamezingatiwa kama ambavyo umeona tayari Meneja yule aliweza kubadilishwa na sasa hivi yupo Meneja mwingine ambaye yupo tayari kuendana na kasi ya Wizara hivyo, eneo la Nyarugusu pia litapata maji.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa vile Wizara ya Ardhi kupitia Tume ya Mipango ya Ardhi inasimamia na kuratibu shughuli za matumizi bora ya ardhi; na kutokana na kwamba Tume hii imeshafanya matumizi bora ya ardhi kwenye hatua tofauti tofauti, lakini maeneo mengi nchini hayajafikishwa kwenye hatua ya mwisho na hivyo kuwachanganya wananchi kwamba, matumizi bora ya ardhi yaanze kutumika au yasitumike: Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kukamilisha matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo ambayo wamekwishaanza kuyapanga sasa?

Swali la pili; inaonekana wazi kwamba Wizara inahamasisha Halmashauri zitenge fedha: kwa kuwa Tume hii ambayo sasa inaonekana wanaendelea na huku Wizara inahamasisha tu; na kuhamasisha siyo kumlazimisha mtu, inakuwa siyo wajibu, yaani Halmashauri haiwajibiki moja kwa moja: Je, Serikali haioni kwamba sasa itoe nyaraka ambayo inaweza kuifanya kila Halmashauri itenge fedha hizi kila mwaka kwa ajili ya kutenga matumizi bora ya ardhi katika maeneo waliyonayo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza Mheshimiwa Tumaini anasema: Je, Wizara haioni umuhimu wa kukamilisha mpango wa matumizi katika yale maeneo ambayo yamekwishaanza?

Mheshimiwa Spika, ni kweli swali lake ni la msingi. Changamoto tunayoipata ni kwamba katika suala zima la uanzishwaji maeneo mapya, unaweza ukawa na kijiji ambacho tayari kilishafanyiwa mpango wa matumizi na wakaanza kuutumia, lakini baadaye tunapogawa maeneo unakuta tena kile kijiji kinakatwa. Kwa hiyo, ule utekelezaji wa ile mipango ya awali inashindikana kufanyika, inabidi kuanza upya.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai tu kwa Halmashauri zote nchini ambazo ndiyo mamlaka za upangaji, pale ambapo vijiji tayari vinakuwa vimeshawekewa mpango wa matumizi, tunaomba sana sana sana visifanyiwe mgawanyiko wowote. Kwa sababu, kitendo cha kugawanya kijiji kile kinaharibu mpango mzima, inabidi kuanza upya. Kwa hiyo, tumejikuta kuna vijiji tayari vilishafanyiwa mpango, lakini matumizi yake sasa yanashindikana kwa sababu kumezaliwa kijiji kingine ndani ya kijiji kingine. Kwa hiyo, naomba hilo liangaliwe katika Mamlaka zetu za Upangaji, nasi Wizara tutakuwa makini katika kufanya ufuatiliaji wa karibu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anauliza kuhusu kuzitaka Halmashauri zitenge bajeti; pengine wanajivutavuta katika suala hilo, lakini nataka nimtie tu shime kwamba Wizara haijanyamaza katika hilo. Katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi 1,500,000,000/=, kwa ajili ya kusaidia katika shughuli hiyo ya upangaji wa matumizi, lakini hii haiondolei Mamlaka husika za Upangaji kutotimiza wajibu wake. Kwa hiyo, bado tunasisitiza kila Halmashauri ya Wilaya ihakikishe katika vitengo vyake, inapopanga bajeti za maendeleo, waikumbuke sekta ya ardhi kuitengea bajeti ya kutosha. Kwa sababu ardhi usipoipangia matumizi ndiko huko ambako migogoro inaanzia.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara tunaingia katikati kuweza kusukuma hili jukumu liende, kwa sababu tunasimamia miongozo na nyaraka mbalimbali ambazo zinasukuma uendelezaji wa sekta ya ardhi. Kwa hiyo, ninachotaka au tunachoelekeza, Halmashauri zenye mamlaka, hili ni jukumu lao la msingi kuhakikisha upangaji, upimaji na umilikishaji unafanyika, kuhakikisha vijiji vyote vinakuwa na mpango wa matumizi ya ardhi, kwa kutenga bajeti stahiki na Wizara tutakuwa tayari kuendelea kuwasaidia. Kama ambavyo sasa hivi tunatoa fedha kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha katika maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa ridhaa yako unipe nafasi tu kidogo niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara imeweka mikakati, mbali na mpango wa matumizi ya ardhi katika maeneo ya vijiji, sasa tunakwenda kufanya zoezi la urasimishaji kwa nchi nzima. Zoezi hili litafanyika kwa nchi nzima bila kuacha mtaa wowote, tukisaidiana na wenzetu wa benki ambao watakwenda kutoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja kuanzia kwenye kupima mpaka kumilikishwa. Mwananchi atakabidhiwa hati yake baada ya kuwa amemaliza kulipa mkopo. Mikopo siyo mikubwa kwa viwanja vya urasimishaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana tutakapokuwa tunaendelea kuhamasisha kwenye Halmashauri zetu, kwenye Wilaya zetu, tulipe kipaumbele ili tuwawezeshe wananchi wetu. Mheshimiwa Rais amesharidhia zoezi hilo lifanyike na tayari makubaliano na NMB Benki, Wizara imeshaingia nao. Tumeshaanza kama pilot area eneo la Mbarali. Kwa hiyo, tutafuata wapi, ni jitihada za Halmashauri wenyewe kuweza kuwawezesha. Ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa vile sasa Kituo cha Geita sasa kitakuwa kinahudumia mkoa mzima, nami ninachojua ni kwamba pale Geita hata gari la zimamoto halipo: Je, ni lini Geita itapata gari la Zimamoto ili iweze kuhudumia mkoa mzima kutoka kwenye center moja ya Geita? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa vile kutoka Geita ni mbali na Katoro, ni lini sasa Kituo cha Polisi cha Geita kitapewa gari la Polisi ili liweze kuwahudumia wananchi wakati wakisubiri huduma ya gari la zimamoto kutoka Geita ili mali zao zisiporwe wala kuharibika baada ya moto kutokea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Geita kuna jumla ya magari manne ya zimamoto. Magari haya ni mazima na yanafanya kazi katika mkoa huo. Kwa bahati nzuri, pia sasa Serikali imeshafikiria kupeleka gari la zimamoto katika mji mdogo wa Katoro. Kitu cha msingi ambacho namwomba Mheshimiwa Mbunge, aendelee kustahimili kidogo, Serikali tumo mbioni kupeleka gari la zimamoto katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba wakati wao wanaendelea kustahimili, zipo njia mbadala ambazo tunazitumia kuhakikisha kwamba itakapotokea majanga hasa ya moto na mengine, wananchi hawa wanaweza kupata msaada wa haraka. Hivi karibuni tulifunga mkataba ama makubaliano na wale skauti, kwamba watusaidie kuendelea kutoa taaluma, washirikiane na Jeshi la Zimamoto ili kuhakikisha kwamba taaluma inaenea na majanga yanapotokea wanaweza kupata msaada wa haraka. Sisi kama Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto pia tunaendelea kutoa taaluma. Kikubwa ambacho tumesisitiza hasa kwa Jeshi la Zimamoto, waweze kuwahi kwenye matukio kwa haraka panapotokea majanga haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa, ni lini sasa tutapata gari la Polisi ambalo litakwenda angalau kuweza kutoa huduma? Katika Mji Mdogo wa Katoro, Kituo cha Polisi cha Katoro tayari gari la Polisi lipo, ipo gari ya One Ten, ambayo inatumika, sema tu, kwa kweli gari ni ya muda mrefu, limechakaa. Tunachowapongeza Jeshi la Polisi, Geita wameshaomba magari katika Jeshi la Polisi ili waweze kupelekewa magari hayo yaweze kuwasaidia katika harakati mbalimbali za ku-serve maisha ya jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, majibu haya yaliyotoka ni ya Wilaya ya Geita, nami maswali yangu yalikuwa yanaelekea Jimbo la Busanda. Kwa hiyo, nilipokee tu kwa sababu Jimbo la Busanda liko ndani ya Wilaya ya Geita, lakini mgawanyo wake inawezekana Wilaya ya Geita usiwe ule ambao tunautarajia kuupata kule Busanda.

Swali langu la kwanza la nyongeza: Je, Serikali ina mpango gani; kwa sababu sasa hivi kuna ramani mpya ya vituo vya afya na vituo vingi vinavyotajwa vina ramani ya zamani ikionekana wazi kwamba kuna upungufu mkubwa wa wodi za wanaume na wodi za wanawake: Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya hivi vituo vya afya vijengwe kwa ramani hii mpya ya sasa? (Makofi)

Swali la pili; pamoja na vituo vilivyotajwa, kuna upungufu mkubwa sana wa uimarishaji wa upatikanaji wa dawa kwenye vituo hivyo: Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba vituo hivi sasa vinaweza kuwahudumia wananchi na upatikanaji wa dawa ukawa kama uliokuwa unapatikana awali; kwa sababu, kwa miaka miwili sasa wananchi wana vituo vya afya lakini hawapati dawa kwa ajili ya kuwahudumia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza Mheshimiwa Mbunge alilokuwa anahitaji kufahamu ni juu ya ramani ambazo zimekuwa zikitolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye ujenzi wa vituo vya afya kwamba, wakati mwingine haziendani na mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikubwa ambacho naweza nikamwambia Mheshimiwa Mbunge, zile ramani zilizoletwa katika maeneo husika ni minimum standards. Maboresho yanaweza yakafanyika kulingana na maeneo husikwa. Kwa hiyo, endapo kutakuwa na hitaji fulani, watu wa eneo husika wanaweza kufanya maboresho pamoja ikiwemo kuijulisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nasi tutawapa ruhusa hiyo ili kuhakikisha hivyo vituo vinajengwa kulingana na mahitaji husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amezungumzia kwamba, tumekuwa na vituo lakini bado mahitaji ya dawa hayapatikani vya kutosha. Jambo hili nafikiri karibu Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto tumekuwa tukilijadili hili kila wakati na tumekuwa tukilitolea ufafanuzi. Kikubwa, wote tunafahamu kwamba, mahitaji kama bima za afya, fedha ambazo wananchi wanatoa pale pale, lakini kwa hivi karibuni Serikali imeongeza bajeti kubwa kwenye madawa na usimamizi wake mzuri. Kwa hiyo, tutaendelea kuongeza dawa katika vituo vyetu na tutaongeza vile vile usimamizi ili ziweze kuwafikia walengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu yale yale ambayo alinipatia mwaka 2021 leo yamejirudia tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwenye swali hili. Kwa vile mazungumzo ya ahadi yaliyotolewa na Barrick yamechukua muda sasa na hayana mafanikio: Nini kauli ya Serikali kwa ujenzi wa barabara hii bila kuhusisha Barrick ili iweze kufanyika? Kwa sababu wale waliotoa ahadi wanaonekana kama hawapo tayari kutekeleza ahadi hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa vile upembuzi yakinifu wa barabara hii umeshafanyika toka mwaka 2017, lakini nasikitika kwamba nyumba zilizoko barabarani zote hazina alama: -

Je, nini mpango wa Serikali kuonyesha wananchi kwamba nyumba hizi zitabomolewa kama barabara itajengwa hivi karibuni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Magessa, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, bado mazungumzo yanaendelea na yako kwenye hatua nzuri. Kama yangekuwa yamekwama, tungeacha na kutafuta utaratibu mwingine. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya Barrick na hizo Wizara ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; tunapoweka alama za kuanza kubomoa, ni pale ambapo taratibu zote za kuanza ujenzi zimeanza na fedha ya kutoa fidia imeshapatikana. Tukishafikia hatua hiyo, basi tutaanza kuweka alama kuonesha wananchi ambao watapisha barabara hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya swali hili ambayo yanaonekana yanatia moyo kwamba kuna majadiliano. Lakini niiombe Serikali majadiliano hayo yasichukue muda mrefu sana. Pamoja na majibu haya mazuri na swali moja la nyongeza.

Katika kuchochea uchumi shirikishi na shindani kuna barabara ndani ya Jimbo la Busanda kutoka Katoro kupita Kaseme kwenda Ushirombo, Jimboni Bukombe; je ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo ambayo imeishafanyiwa upembuzi yakinifu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Tumaini Magessa, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Katoro hadi Ushirombo imeishafanyiwa usanifu na sehemu ya barabara hii inatekelezwa na Mpango ama Mradi wa RAIS, lakini sehemu iliyobaki itaendelea kuhudumiwa na TANROADS na Serikali ina mpango wa kutafuta fedha kukamilisha barabara yote kipande kitakachobaki baada ya kile kipande kitakachojengwa na Mpango wa RAIS kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Ni dhahiri kwamba ndani ya nchi hii nzima wameshahamasisha shule 39 tu, sasa unaweza ukajua nchi hii ina shule ngapi na sasa zimehamasisha shule 39 tu kunywa maziwa na watu waliohamasisha ni 90,000. Sasa swali langu la nyongeza ni hili.

Mheshimiwa Spika, kwakuwa Mikoa yote iliyotajwa bahati mbaya sana ni kama Mikoa mitatu, minne na Mikoa tunayo mingi tu na hasa Mkoa ninaotoka mimi Mkoa wa Geita haukutajwa.

Ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha maziwa mengi yanayopotea huko vijijini kwa sababu yamekosa hifadhi yanaweza kupata hifadhi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili nini mkakati wa Serikali kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata maziwa ili tuwe na uelewa kwamba wafugaji ambao wanafuga sasa wana uwezo wa kufuga kwa tija zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bryceson Tumaini Magessa Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mikakati yetu kama Wizara ni pamoja na kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa maana ya TAMISEMI ili kuweza kutanua wigo zaidi wa kuongeza idadi ya shule. Ni kweli kwamba shule hizi tulizozisema ni chache na kwa hiyo kwa kushirikiana na wenzetu tunayo imani ya kwamba tutaongeza idadi ya shule.

Mheshimiwa Spika, namna gani ya mkakati wa kuweza kuyakusanya maziwa ya vijijini, ukitazama katika bajeti yetu ya mwaka 2021/2022 tunayoimaliza, Serikali iliondoa kodi ya vikusanyio kwa maana ya cans zile za stainless steel ambazo zilikuwa zikiuzwa takribani Shilingi 260,000, hivi sasa zinauzwa Shilingi 219,000. Hii imerahisisha kuongeza idadi ya cans za kukusanyia maziwa.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine ni juu ya nini tulichonacho sasa kwa ajili ya kuongeza viwanda vidogo vya kutengeneza maziwa na kukusanyia maziwa kule vijijini. Katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 katika vitu vikubwa tutakavyokwenda kuvifanya ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunatatua zile changamoto zinazowakabili wafugaji wetu na kupelekea kushindwa kusindika maziwa yao, ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo zile ambazo ni kikwazo.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo naomba nimuahidi Mheshimiwa Magessa yeye na Wabunge wengine wakereketwa wa viwanda vidogo wakae tayari katika kutushauri na kuweza kufikia lengo hili.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa uboreshaji huu ni kazi ambayo imepangwa (planned activity): Je, Serikali imepanga kukamilisha lini hii kazi ya uboreshaji wa maeneo ambayo iliyaanzisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Jimbo la Busanda lina wananchi takribani zaidi ya 700,000; ina kata 22, lakini ina tarafa mbili tu: Ni lini Serikali itaongeza idadi ya tarafa ili wananchi waweze kufikiwa kwa urahisi zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa miundombinu katika Halmashauri zetu ni zoezi ambalo sasa linaendelea na Serikali imeshajenga majengo mapya ya Halmashauri zaidi ya 115 na inaendelea na ujenzi wa majengo ya Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, na pia tutakwenda kwenye ngazi za kata. Kwa hiyo, zoezi hili ambalo linaendelea kutekelezwa ni la muda, na mara litakapokamilika kutokana na upatikanaji wa fedha, basi tutakwenda kwenye hatua nyingine ya kuona uwezekano wa kuanzisha mamlaka nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusiana na kuanzisha tarafa katika Jimbo hili la Busanda, namwomba Mheshimiwa Mbunge na pia nielekeze Halmashauri kufuata taratibu za uanzishwaji wa tarafa, kwa maana ya kufanya vikao kwenye ngazi ya DCC, RCC na kuwasilisha kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tathmini ifanyike na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa, ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; je, nini upi mpango wa Serikali katika ujenzi wa barabara ya Katoro – Kaseme – Magenge hadi Ushirombo?

Swali la pili; ni lini Serikali itapandisha kiwango cha barabara kutoka Geita – Buyagu – Kamena hadi Bukoli ili iweze kuhudumiwa na TANROADS ukizingatia kwamba maombi yake yamekwishafikishwa Wizarani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Katoro – Ushirombo imeshakamilishwa kufanyiwa usanifu, sehemu ya barabara hii pia tunao mradi wa RISE ambao kipande fulani kitatekelezwa kwenye mradi wa RISE ambao taratibu za manunuzi zinaendelea wakati Serikali inatafuta fedha kukamilisha barabara yote ya Katoro – Nyikonga hadi Ushirombo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la barabara ya Geita – Nyankumbu – Kamena hadi Bukoli nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama imeshaletwa kwenye Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya kupandishwa hadhi, Serikali itaangalia kama inakidhi vigezo ili barabara hii iweze kupandishwa hadhi na iweze kusimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yanayoonesha kwamba kikundi kimoja Jimboni Busanda kitapata shilingi milioni 69.4 hivi, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Jimbo la Busanda katika maeneo ya Ziwa Viktoria yana vikundi vingine katika Kata ya Nyamwilolelwa, Kata ya Bukondo na Kata ya Nyachiluluma: Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba, inaweza kuongeza vikundi vinavyokopesheka kwenye maeneo hayo ili huduma hii iweze kuwasaidia wananchi wengi kwa ajili ya maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Nini mkakati wa Serikali kuhamasisha ufugaji wa samaki kwenye maeneo ambayo yako mbali na Ziwa Victoria? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza Mheshimiwa
Mbunge amezungumzia kuhusu kuongeza idadi ya vikundi katika jimbo lake. Bahati nzuri katika mwaka wa fedha tutaongeza idadi ya vikundi kufikia 893. Kwa hiyo, katika mwaka huu unaokuja basi na jimbo lake tutaongeza hivyo vikundi ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kuhusu maeneo ambayo yako mbali na Ziwa Viktoria, ni kwamba, tumeanzisha programu maalum ya ufugaji wa samaki kwa njia ya mabwawa ambayo sasa hivi katika mwaka uliopita tulikuwa na mashamba darasa kumi. Kwa hiyo, matarajio yetu ni kwamba mwaka wa fedha unaokuja, tutafanya hivyo. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati wa sasa na tutaendelea kuhimiza. Mfano mzuri, hata hapa Chamwino tunafanya shamba darasa katika maeneo ambayo ni kame. Kwa hiyo, huo ni mkakati ambao upo na ni endelevu, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hali iliyoko Kalenga ni sawa sawa na hali iliyoko Busanda tunavyo vituo viwili vya Chikobe na Bukori. Nini mkakati wa Serikali wa kuviboresha vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali lake la nyongeza la lini Serikali itatenga fedha za katika Vituo vya Afya vya Chikobe na Bukoli. Ni lengo la Serikali kuhakikisha inajenga vituo vya afya vya kimkakati kote nchini; na ndiyo maana katika mwaka wa fedha huu ambao unamalizika tarehe 30 Juni mwaka huu Serikali ilitenga bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini. Hivyo basi tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pale ambapo fedha zitapatikana tutavitenga vituo hivi vya afya vya Chikobe na Bukoli.
MHE. TUMAINI B. MAGESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, mitaro na madaraja katika Mji Mdogo wa Katoro ni mibovu, katika Kata tatu za Ludete, Nyamigota na Katoro yenyewe. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba miundombinu hiyo inatengenezwa ili wananchi waweze kuhudumiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba, taasisi yetu ya TARURA ambayo inasimamia barabara za Mijini na Vijijini inakuwa na fedha ya kutosha kwa ajili ya kutengeneza barabara hizi, zikiwemo za Mji Mdogo wa Katoro, ndiyo maana Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeiongezea fedha TARURA mara tatu ya bajeti iliyokuwepo 2021. Hivyo, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona katika barabara hizi za Mji Mdogo wa Katoro kama zimetengewa fedha kwenye mwaka huu wa fedha tunaoenda kuuanza Julai na kama hazijatengewa fedha basi tutahakikisha zinatengewa fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza kwa vile taarifa za TAMISEMI hazikuwa sahihi je, Serikali iko tayari kuwarejeshea wananchi pesa ambazo zimezidi kutoka shilingi 27,000 hadi 321,000 baada ya taarifa yetu kujulikana kwamba siyo sahihi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, zoezi la kubaini vijiji mji ambavyo vimetajwa hapa kwenye swali la msingi litakamilika lini ili wananchi wenye uwezo mdogo kwenye vijiji vyetu waweze kupata umeme ikiwemo Kaduda, Chibingo, Ibondo na vingine vingi? Naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Tumaini Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niweke taarifa sahihi kwamba tunaamini kabisa taarifa za TAMISEMI zilikuwa sawa kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji. Isipokuwa kinachogomba ni ile hali ya kwamba watu wanatambuliwa kuwa wako mjini lakini wao wanajiona hawako Mjini na kwa sababu tumelibaini hilo tumeona ni vema sasa sisi Wizara ya Nishati twende site na kubaini hata kama eneo ni la mji, lakini je, uhalisia wa maisha ya wakazi wa maeneo yale ni wa namna gani? kwa sababu Sheria ya Mipango Miji imeweka maeneo na mazingira ya masharti kama kuna maduka, kama kuna vituo vya afya, kama kuna barabara za lami na nini hayo ndiyo maeneo ya mji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu taarifa ya TAMISEMI kwa mujibu wa sheria ilikuwa sawa. Lakini maeneo hayo yanawakazi wenye vipato tofauti na hivyo sisi tunafanya utafiti na upembuzi yakinifu kuona ni kiasi gani kilipwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo niseme kwamba anaposema turudishwe kwa wananchi namuomba asielekee huko. Kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita inaweka ruzuku kwenye gharama za kuunganisha umeme kwa kulingana na maeneo mbalimbali yalivyo. Kwa hiyo Serikali iliweka ruzuku hata hii 320,000 bado ni ruzuku imewekwa ili wananchi waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shughuli ikikamilika ambayo ameuliza kwenye eneo la pili ni lini? Tunaendele, tunafanya kazi hii ni kubwa tulimaliza awamu ya kwanza tukaona kuna maeneo hatukufika tumerudi. Tunaomba yeye na Waheshimiwa Wabunge wawe wavumilivu ili zoezi litakapokamilika tuweze kuja kutoa taarifa sahihi na kuweza kutangaza gharama sahihi kila eneo.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, lini Serikali itajenga vituo vya afya kwenye Kata za Rwamgasa, Nyakagomba na Magenge tulizoziomba mwaka 2021?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itajenga vituo vya afya hivi alivyovitaja Mheshimiwa Magessa kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuzingatia idadi kubwa ya wananchi katika Jimbo la Busanda ambayo ni takribani laki saba.

Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kujenga Chuo cha VETA kwenye maeneo hayo?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, kwa vile jibu la msingi linathibitisha kwamba Chuo hicho kimejengwa Geita Mji na sisi tuko Geita Vijijini.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga Chuo cha VETA Geita vijijini badala ya Geita Mji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tumaini Magessa kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha eleza kwenye maswali ya msingi kwamba tuna chuo ambacho tumejenga pale Geita; lakini ni sera ya Serikali kwa Awamu hii ya Kwanza kujenga vyuo hivi katika ngazi za Wilaya, na tutakapokuwa tumekamilisha ujenzi huu katika ngazi za Wilaya ambapo mnafahamu Waheshimiwa Wabunge wote katika mwaka huu Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo katika zile Wilaya ambazo tumekosa na katika Mkoa mmoja wa Songwe ambao ulikuwa hauna chuo hiki.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya kukamilisha awamu hii, tutafanya tathmini na kuona maeneo yapi yana idadi kubwa ya wananchi au ya wakazi na kuweza kuangalia namna gani tunaweza tukasogeza huduma hii karibu na maeneo hayo likiwemo na hili eneo la Busanda. Vile vile tunaweza kuzingatia katika Halmashauri au Wilaya ambazo zina Majimbo au Halmashauri zaidi ya moja kuweza kuwafikishia huduma hii katika Halmashauri hizo kulingana na upatikanaji wa fedha lakini vile vile na kukidhi kwa sifa za maeneo hayo.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali kwamba tunae Mkandarasi CRJE ambaye anatakiwa kufanya kazi maeneo yetu. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali moja ni kwamba nini mpango wa Serikali kuwaunganishia umeme wananchi ambao wamekwishalipia umeme na wamekwishakuwa surveyed na wanasubiri umeme huu zaidi ya mwezi mmoja kuunganishiwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba taasisi zote kwenye vijiji ambavyo vimeshawekewa umeme zinaunganishiwa umeme ili wananchi na taasisi zile ziweze kutumika vizuri zaidi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza kwa ufuatiliaji mzuri wa maeneo ya vijiji katika jimbo lake ambayo hayajapatiwa umeme. Kuhusu suala la ambao wamekwishalipia na hawajaunganishiwa, Serikali imeanzisha programu maalum na kutafuta fedha na kutenga fungu la fedha maalum kwa ajili ya kununua vifaa ambavyo vilikuwa vinakosekana kwa ajili ya kuwaunganishia wateja wote takribani 100,000 ambao hawajaunganishiwa umeme na bahati nzuri kadri siku zinavyoenda tunapunguza hiyo back log. Kwa hiyo, kwa wananchi wa Busanda kazi inaendelea na watafungiwa umeme haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu taasisi kama unavyofahamu katika bajeti ya Wizara kwa mwaka ujao wa fedha tumetenga fedha mahususi kwa ajili ya kuunganisha umeme katika taasisi mbalimbali za umma ikiwemo shule na vituo vya afya.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali kwamba kuna fedha imetengwa. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, uboreshaji wa vituo hivi ulihitaji vile vile uongezaji wa idadi wa askari. Nini kauli ya Serikali juu ya uongezaji wa askari kwenye vituo hivi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Uboreshaji wa vituo hivi vile vile ulihitaji kujenga nyumba za askari kwenye maeneo ya vituo hivi. Nini kauli ya Serikali kwenye ujenzi wa nyumba hizo? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la upungufu wa askari, hivi karibuni tunaendelea na mchakato wa kuajiri askari wapya. Wako askari ambao wanakamilisha mafunzo yao hivi karibuni na wengine tumetangaza hivi karibuni askari wapya. Kwa hiyo, miongoni mwa askari hao watakapomaliza mafunzo yao tutawapeleka ili kukabiliana na upungufu wa askari kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika tunatambua pia changamoto ya makazi ya askari katika maeneo hayo. Namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira tukikamilisha ukarabati katika bajeti ijayo tutaangalia vile vile uwezekano wa kutatua changamoto au kupunguza changamoto ya makazi ya askari katika eneo hilo.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Je, ni lini Serikali itakarabati Shule chakavu za Msingi katika Jimbo la Busanda ikiwemo Lubanda, Lulama na nyinginezo nyingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua katika Jimbo la Busanda pia kuna shule chakavu. Tayari Serikali imeshaanza kuwaainisha shule chakavu zaidi katika majimbo yote kote nchini na fedha zinatafutwa kwa ajili ya kuanza ukarabati kwa awamu. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Jimbo la Busanda pia litapewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Je, ni lini Serikali itakarabati Shule chakavu za Msingi katika Jimbo la Busanda ikiwemo Lubanda, Lulama na nyinginezo nyingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua katika Jimbo la Busanda pia kuna shule chakavu. Tayari Serikali imeshaanza kuwaainisha shule chakavu zaidi katika majimbo yote kote nchini na fedha zinatafutwa kwa ajili ya kuanza ukarabati kwa awamu. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Jimbo la Busanda pia litapewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Je, ni lini zoezi la uboreshaji maeneo yaliyopo litakamilika, ukizingatia jibu kama hili lilitolewa mwaka wa fedha uliopita?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Katika Jimbo la Busanda tuna Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro ambapo wakati tunapewa mamlaka mwaka 2014 kulikuwa na watu 86,231, lakini leo hii tunavyozungumza baada ya sensa, tuna watu 231,332 ikiwa ni ongezeko la watu 144,000. Tunakusanya mapato kama shilingi bilioni 1.3, tuna shule za msingi 24 na shule za sekondari 16. Je, nini mkakati wa Serikali kuipandisha hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo ya Katoro kuwa Halmashauri ya Mji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua sana umuhimu wa kuanzisha mamlaka mpya katika maeneo mbalimbali kote nchini ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele kuboresha kwanza miundombinu, majengo ya Utawala, ofisi na majengo mengine ya huduma za kijamii katika mamlaka ambazo zipo ili ziweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baada ya kukamilisha zoezi hilo la kuwezesha miundombinu, tutakwenda kuanzisha mamlaka nyingine. Kwa hiyo, tamko la Serikali litatolewa muda ukifika kwa ajili ya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusiana na kuanzisha Halmashauri ya Mji wa Katoro ambayo ni mamlaka ya mji, hili nalo linaenda sambamba na jibu langu la msingi kwamba baada ya kukamilisha taratibu hizo, basi tutaona namna ya kufanya kama itakidhi vigezo. Ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, je, katika utekelezaji wa bajeti mwaka huu wa fedha, ni lini Serikali itaanza mchakato wa miradi ya umwagiliaji katika maeneo yaliyo pembezoni mwa Ziwa Victoria Jimboni Busanda ukizingatia imebaki miezi miwili kwenye hii bajeti? Nashukuru sana,
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Miradi mingi ambayo ipo katika mwaka wa fedha wa bajeti uliopo sasa hivi, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kuitangaza kila wakati na ninaamini kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha tutakuwa tumeshatangaza na kupata mkandarasi.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, ni lini Kituo cha Chikobe kitafanyiwa uboreshaji kwa sababu miundombinu yake ni mibovu sana? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Chikobe, kitafanyiwa ukarabati mara tutakapoanza kukarabati vituo vya afya baada ya kukamilisha ukarabati wa hospitali za halmashauri.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wananchi takribani 400,000 kutoka kata sita za Jimbo la Busanda wanaofanya shughuli za kiuchumi kwenye maeneo haya kwa sababu hayana miti, lakini Serikali imesema wazi kwamba inakwenda kuanza kupanda hekta 100 kati ya hekta 50,000. Kwa hiyo, hekta karibu 50,000 zinabaki hazijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili. Kwa nini Serikali isiruhusu eneo fulani litumiwe na wananchi kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo kwa sababu hekta 50,000 zitakuwa zimebaki?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa nini wananchi wasigaiwe miche na TFS ili waanze kupanda miche hiyo wakati wakiendelea na shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge yote kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la msitu lililoharibika ni hekta 2,000 na siyo hekta 50,000 kama Mheshimiwa alivyokuwa anasema, lakini kwa sababu jambo analolishauri lipo katika taratibu zetu, pale ambapo tuna mpango wa kupanda miti huwa tunatoa ridhaa kwa wananchi kushiriki kwenye kupanda miti kwenye maeneo hayo, lakini vilevile kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo yale ambayo yamepandwa miti. Pale inapotokea kwamba miti hiyo imeshakua mikubwa, wananchi wanaacha kufanya shughuli hiyo ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili tunalichukua, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane ili tuweze kuweka mkakati utakaokuwa jumuishi kwa wananchi wote wanaohitaji kufanya shughuli hii na kuona mahitaji ya miche ya miti inayohitajika ili tuweze kujipanga na kuweza kutoa ridhaa na kuwasaidia.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, ni lini Serikali itaboresha skimu ya umwagiliaji Nyamalulu Jimboni Busanda?

Swali la pili, ni upi mkakati wa Serikali kutumia Ziwa Victoria kuhakikisha kwamba skimu za umwagiliaji zinajengwa na tunaweza kuboresha uzalishaji wa mazao ya chakula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kuhusu maboresho katika skimu ya Nyamalulu katika Jimbo la Busanda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili lipo katika mpango na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, mkakati kuhusu Ziwa Victoria tunaendelea nao kwa sababu tuna mkakati wa pamoja kati ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji pamoja na Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha maji yale tutakayoyatumia yaweze kuwanufaisha wananchi katika maeneo hayo yote matatu ambayo nimeyataja. Kwa hiyo, lipo katika mipango ya Serikali na litatekelezeka, ahsante. (Makofi)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni lini Serikali itaanza uboreshaji wa miundombinu ya barabara za Mji Mdogo wa Katoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akipambania maendeleo katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba Serikali kila mwaka wa bajeti inatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara. Mathalani katika Serikali ya Awamu ya Sita, bajeti ya TARURA imeongezeka kutoka bilioni 275 mpaka kufikia bilioni 710.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote hiyo ni dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba inafikia mtandao mkubwa zaidi wa barabara hizi kwa kuwa zina manufaa makubwa kwa wananchi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kila mwaka wa fedha itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha inazifikia barabara nyingi zaidi ikiwemo barabara katika Mji wa Katoro.(Makofi)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa vituo 898 hadi Septemba, 2024. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya kwenye Kata ya Nyakagomba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya kwenye Kata ya Lwamgasa na Magenge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akifuatilia sana kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inafika katika jimbo lake na inanufaisha wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba niyajibu maswali yake yote mawili kwa pamoja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya uwekezaji mkubwa sana katika kuimarisha huduma za afya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu, jumla ya shilingi trilioni 1.18 zimetumika katika kuhakikisha kunajengwa miundombinu mizuri kwa ajili ya kutoa huduma ya afya msingi, lakini pia kununua vifaa na vifaatiba. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika Kituo hiki cha Afya cha Nyakagomba ambacho ameomba na ninaamini ni kipaumbele kabisa katika jimbo lake, basi katika mwaka huu wa fedha zitatoka fedha kwa ajili ya kuja kuanza kujenga kituo cha afya cha kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kuwatangazia Wabunge wote kwamba, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu na uhitaji wa kuimarisha huduma za afya msingi, basi na kwa kusikia vilio vya Waheshimiwa Wabunge vya uhitaji wa vituo vya afya katika majimbo yao, katika huu mwaka wa fedha naomba mfahamu na mpokee taarifa kwamba nyote mtapata fedha kwa ajili ya kuanza kujenga vituo vya afya vya kimkakati. (Makofi)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana nini mkakati wa Serikali kupitia Ushirika kukarabati maghala yaliyokuwa yakitumika kuhifadhi pamba na pembejeo yaliyochakaa sana Jimboni Busanda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, moja ya mkakati tulionao ni pamoja na maghala ambayo yako katika eneo la Jimbo la Busanda katika mwaka wa fedha unaokuja tutayakarabati, ahsante. (Makofi)