Contributions by Hon. Priscus Jacob Tarimo (30 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nisikitike tu kwamba nilikuwa nimejiandaa kuongea dakika 10 na sasa tumeambiwa ni tano tano, nitajaribu kwenda kwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii adhimu ya kuwatumikia Watanzania katika chombo hiki kitukufu cha Bunge.
Nikishukuru chama changu cha Mapinduzi lakini zaidi niwashukuru wazazi wangu baba na mama Tarimo pamoja na familia yangu, mke wangu Eveline na watoto wangu watatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda mbali niseme tu kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Nasema hivyo nikiwa nimechukua reference ya kwanza kwenye hotuba ile ya Bunge la Kumi na Moja ambayo aliitoa Mheshimiwa Rais hapa na baadaye yale aliyoyafanya kwa miaka mitano ambayo yalisababisha sasa Watanzania kutuelewa na tukapata ushindi wa kishindo kwa mwaka huu wa 2021 kwa Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais yako mambo mengi ambayo nataka niyaongelee. Nianze na maslahi ya watumishi wa umma kama yalivyo kwenye ukurasa wa 8 na wa 9 wa hotuba ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba watumishi wa umma wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu haswa walimu. Wanalalamikia madeni yao ya muda mrefu, kupandishwa kwa madaraja pamoja na mfumo mpya huu ambao umeshakuja lakini hata wastaafu wamekuwa na malalamiko ya kucheleweshewa mafao yao. Naomba Serikali iliangalie suala hili vizuri na kwa sababu liko kwenye hotuba hii basi liweze kushughulikiwa kwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee mikopo ya halmashauri hasa ile asilimia 10 kwa ajili ya akina mama, vijana na walemavu. Niishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuamua kuibadilisha sheria ile na kuzifanya fedha zile sasa ni revolving kwa maana ya kwamba fedha zinazokopeshwa sasa zinaweza zikawekwa kwenye mfuko ambao ni revolving fund na kukopeshwa kwa vijana na akina mama wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ya kuishauri Serikali kuhusiana na mikopo hii. Wangalie uwezekano wa kukopesha fedha hizi kwa mtu mmoja mmoja na kwa sababu sasa tuna mfumo mzuri kwa kupitia vitambulisho vya NIDA, hata kama ikibidi kuwakopesha vifaa kama bodaboda ili basi ilete tija zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni katika ile sheria iliyobadilishwa na kusema kuwe na mradi wa pamoja. Nakubaliana kabisa na mawazo ya Serikali lakini nishauri pia kukopeshwa kikundi ili wakopeshane kama zamani iendelee kuruhusiwa kwa sababu iliwajenga akina mama wengi katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la viwanda limeelezewa vizuri na nimshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa kutuwekea kiwanda kiwanda kikubwa sana pale Moshi mjini lakini bado nina ombi kwa Serikali. Viko viwanda vilivyobinafsishwa ili viendelezwe vitoe ajira na kodi mfano ni kiwnada cha viberiti cha Kibo Match na kiwanda cha magunia. Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ya Bunge la Kumi na Moja, ukurasa wa 21, alielezea dhamira yake ya kuwanyang’anya viwanda wale walioshindwa kukidhi vigezo vile. Moshi tuko tayari, tunaomba aje awanyang’anye wale waliofanya viwanda vile ni mago-down.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa wa 95 kuna marekebisho ya viwanja vya ndege 11. Naomba niikumbushe Serikali kiwanja cha ndege cha Moshi nacho kimetajwa lakini kinahitaji matengenezo ya haraka. Kiwanja hiki kina umuhimu mkubwa sana, kitabibu, kibiashara na kiutalii. Naomba kipewe kipaumbele katika viwanja vya ndege vinavyorekebishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 32 umeongelea masuala ya afya na niipongeze Serikali kwa hatua kubwa ya kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya pamoja na za mikoa na za rufaa zile za kanda. Nawaomba katika hizi 98 zinazotarajiwa kujengwa katika awamu hii tafadhali sana wawakumbuke wananchi wa Moshi Mjini na Vijijini, pote pale hakuna hospitali ya wilaya ya Serikali, tunaomba sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la elimu nililizungumzia jana kwenye swali langu na limezungumziwa sana. Hoja yangu kubwa itajikita kwenye mikopo kama nilivyosema na niendelee kusisitiza, wapo watu wanaokidhi vigezo vyote lakini hawapati mikopo ile pengine kwa sababu walisomeshwa kwa ufadhili kwenye shule za binafsi au kwa sababu nyingine zozote. Kama Mawaziri watahitaji kuniona nitawapa mifano halisi ambayo ipo na naifahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba msisitizo upelekwe kwenye kidato cha tano na cha sita hasa kwenye shule za kata kwenye Taifa hili. Kuna shule ambazo zina nafasi tuweke mkazo zaidi kwenye elimu inayoendelea kwa kujenga madarasa mapema badala ya kujenga mwisho baada ya watoto kumaliza shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 36 wa hotuba ile umeongelea wafanyabiashara wadogo. Niipongeze sana Serikali namna ambavyo imewaweka vizuri na niombe uangalizi uwekwe katika kuwapanga vizuri. Yapo maeneo wamezuia kabisa kutumia miundombinu ambayo imewekwa kama barabara. Halmashauri zinayo nafasi kubwa na sisi tunaendelea kuzishauri lakini tuweke namna bora ya kuwapanga wafanyabiashara hawa wadogo ili basi waweze kushirikiana na watumiaji wengine wa miundombinu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 37 Mheshimiwa Rais ameongelea umuhimu wa kuboresha michezo. Mimi naona eneo bora zaidi la kuanzia ni kuboresha viwanja vya michezo ambavyo vinasimamiwa na halmashauri kwenye majimbo mbalimbali. Moshi Mjini tunacho kiwanja cha majengo, naomba Serikali iangalie namna ya kutusaidia na kukiboresha.
Mheshimiwa Naibu Spika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia na eneo la watalii ambalo kaka yangu na baba yangu Mheshimiwa Dkt. Kimei ameliongelea lakini pia madereva…
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami niungane na wachangiaji waliotangulia kuipongeza Serikali ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu, kwa namna ambavyo wameweza kuweka ule mpango, hasa matumizi ya ile hela trilioni 1.3. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa namna ambavyo waliendelea kumshauri Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi kuanzia kwenye hela ile ambayo kimsingi ni hela ya stimulus yapo maeneo ambayo ningeomba tuyafanyie kazi. Kunapokuwa na mdororo wa uchumi kwa sababu yoyote ile fedha kama hii inatusaidia kurudi, ku-bounce back, kwenye kuendeleza uchumi. Tunayo bahati hatukufunga biashara zetu, hatukujifungia na ndiyo maana katika record hata kwenye taarifa hii sisi ndiyo pekee tulikuwa tuna ukuaji chanya mwaka 2019, wenzetu walikuwa na 0.3, 0.8, wengine -3.4, sisi tulikuwa tuna 4.6 kwa sababu hatukujifungia tuliendelea na kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hatujapeleka kwenye ku-stimulate biashara kama stimulus, ningeomba sana tuziangalie biashara zile zilizodhurika sana moja kwa moja na kuwepo kwa UVIKO-19 hasa kwenye utalii na hoteli. Kwa sababu, hatuwezi kuwapa hela na kwa sababu Wabunge wengi wameongelea riba za benki kwa ujumla, mimi ningesema tuwe na kipengele sasa cha kuzisaidia kabla hatujaja kwenye riba za ujumla. Kwamba, kampuni zile nyingi zina mikopo benki, zimefanyiwa restructuring, zinalipa interest bado na baadaye watatakiwa walipe na ile principle, tuweke restructuring ambayo tutaziangalia zile sekta na zile biashara tuzielekeze benki ziwapunguzie riba, ikiwezekana zisimamishe riba mpaka watakapokuwa wame-stabilize ili kuweza kuimarisha uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ushauri huo niende kwenye mpango wetu huu. Watu wengi wameongelea kilimo na mimi sitaacha kuongelea kilimo. Kuna vitu bado tunaendelea kuchanganya, kuna suala la mchango wa sekta ya kilimo kwenye GDP, hiyo ndiyo asilimia 29.1, lakini kuna suala la mchango wa kilimo katika ukuaji wa uchumi, ile asilimia Nne tuliyoitaja ambayo inaonekana ndiyo tulikuwanayo 2019 ilichangiwa sana na sekta ya kilimo ambayo kwa kipindi kile ilichangia kwa asilimia 26.1. Sasa kwenye kilimo kuna nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa sababu wewe ulitoa mwongozo kwenye bajeti iliyopita. Katika bajeti iliyopita ya trilioni 36 kwenye kilimo ilienda bilioni 294, it is less than 1%, wakati imeajiri directly zaidi ya asilimia 55 ya Watanzania, lakini kwenye mnyororo wake, usafirishaji, usindikaji, na adhalika ni asilimia 70 ya watu wameajiriwa pale, lakini tumewapa less than one percent ya bajeti yetu, hatuwezi kusonga mbele kwa namna hiyo. Kwa hiyo, ninashauri sana hata ikiwezekana bajeti ijayo hata asilimia 10 ikiwezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea umwagiliaji siyo vitu vya kutoka mbinguni. Bwawa la Nyumba ya Mungu limetengenezwa miaka ya 70, siyo ziwa ni bwawa lilitengenezwa na ni baada ya uhuru. Tunaweza kutengeneza mabwawa ya namna hiyo maeneo mbalimbali yakasaidia umwagiliaji pamoja na kilimo cha uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba bajeti ijayo iangalie sana hii sekta ya kilimo. Tungetamani yale maeneo ambayo yamefanyiwa research yanaonekana mazao fulani yanafaa tu-substitute, hawa vijana wa bodaboda, bodaboda inauzwa milioni mbili na laki tano, ukiangalia tukiweka maeneo ya ardhi yenye rutuba ambayo yana tija hawa vijana tunawahamishia kule wanalima na pato letu linaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na sekta ya kilimo ni kwenye mifugo. Wafugaji wetu ni wafugaji wa kitamaduni, hawafugi kwa ajili ya kuuza kwa sababu, wao wanaamini wale ng’ombe ndiyo hela yao. Inahitajika elimu tujitoe hapo. Hapo Kongo soko la nyama lina thamani ya bilioni 70 kwa sasa au zaidi na wananunua nyama kutoka Belgium, Netherlands, Ujerumani, South Africa na India, lakini sisi hatuuzi nyama hapo na wako jirani tu. Tuwafunze wale wakulima wetu kwamba, hawa ng’ombe unaweza kuwaweka benki kwa kuwafuga vizuri, kwa kuzingatia njia za kisasa tukauza nyama tukapata hela za kigeni tena kuanzia hapa jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali, imefanya kazi kubwa sana kwenye sekta ya afya. Tatizo kubwa sasa baada ya kuboresha hospitali za Wilaya na kutengeneza vituo vya afya na hospitali za Mikoa ni watumishi na kila tukiuliza tunaambiwa kuna utaratibu unaitwa wage bill kwamba, hatuwezi kuajiri tena tusubiri. Sasa kama chanzo cha mapato hospitali za Kanda ziwezeshwe kwa sababu, tumeshaweka vifaa. Tuangalie namna ya kutumia wataalam hata kwa contracts siyo kwa kuwaajiri ili tuangalie soko la medical value tourism ambayo India mwaka 2020 walikuwa wanatabiriwa kuwa na kipato cha kama Nine billion dollars kutokana na watu wanaoingia pale kwa ajili ya kutibiwa, ikifika 2022 wanasema itakuwa na thamani ya 13 billion dollars. Kwa hiyo, hizi hospitali za Kanda tukishaimarisha hizi za chini zile tuziwekee utaratibu ambao tutaweza kuzitumia kama sehemu ya kipato nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano ni rahisi mtu anayetoka Mombasa kutibiwa KCMC kwa distance na gharama kuliko kwenda Nairobi na imekuwa ikitokea hivyo hata katika level hii tuliyopo. Tukiangalia na Kanda nyingine za Mwanza na huko Kusini tunaweza tukaingiza hela kupitia kwenye medical value tourism. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo kingine cha mapato ni upimaji wa ardhi yetu. Ukishapima ardhi kinachofuata ni kodi. Ikiwezekana, ingewezekana tungepima nchi nzima kila mahali kuwe na hati, lakini mimi maeneo haya nina special interest, miji mingi ukiangalia tunafanya kazi sasa hivi ya kurasimisha makazi kwa sababu, hatukupima kule ambako Mji unapanukia kwa hiyo watu wakajenga kiholela. Tunarasimisha makazi ambayo siyo mazuri ni holela na hayawezi kuboreshwa kwa namna yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini miji yote katika fedha ambazo tutazipata karibuni tuweke vifaa kwenye Halmashauri au kila Mkoa vya kupima ardhi kila Mji unaonekana unakua kuelekea wapi, tupime maeneo yale, tutoe hati, watu walipe kodi, hicho ni chanzo cha mapato kizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa kukuza uchumi wetu. Miradi mikubwa yote wanapewa Wakandarasi wa kutoka nje, siyo jambo baya ni mahusiano, lakini ikumbukwe kwamba, wakishamaliza fedha kubwa au sehemu kubwa ya fedha ile inaenda nje. Sasa kama fedha tayari tunazo na tunaogopa kuwapa wakandarasi wetu tunaona kama hawatafanya vizuri, kwa nini tusitengeneze utaratibu ambao tutawasimamia vizuri zaidi fedha zile zibaki hapa? Hao mabilionea tunaongelea 5,000 wawe 10,000 keshokutwa wafike 1,000,000 kwa kuwasimamia vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakuwa na miradi mikubwa unaona hela yote inaenda kwa wakandarasi kutoka nje. Yaani kwa mfano sasa hivi hata hao mabilionea ukiwaita, nadhani ukiwaangalia wazawa hasa utaona ni wachache tu watakuwa hapo, lakini hawa waswahili wa kawaida…
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Priscus pokea Taarifa.
T A A R I F A
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba, anachosema ni kweli, mbaya zaidi tuna bodi…
MWENYEKITI: Anachokisema kipi?
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la kuwapa kazi kubwa wakandarasi wa nje, uhakika ni kwamba, tuna Bodi ambayo inasajili Wakandarasi wa ndani na tuna fedha nyingi Serikali inawalipa waajiriwa wa bodi ile, lakini tuna-entertain kufanya kazi kwa kutumia force account wakati tunajua value ya private sector katika nchi yoyote ya maendeleo duniani.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Priscus unapokea Taarifa hiyo?
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante kengele imeshalia. Mheshimiwa Priscus unadhani kuna mabilionea wangapi Moshi pale?
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ngumu kusema maana hatuna access ya kujua. (Kicheko)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia ripoti ya CAG pamoja na ripoti ya Kamati Tatu ambazo zimeletwa mbele yetu. Nitajielekeza kwenye maeneo manne, nianze na PIC kwenye taarifa yao ya uchambuzi wa taarifa hii ya CAG, katika ukurasa wao wa 24 kipengele cha Mbili, Nne na cha Tano kuhusiana na mikopo chechefu.
Mheshimiwa Spika, hili ni tatizo na pamoja na kwamba tunaangalia benki hizi za Serikali hasa TADB na TCD ni vizuri tulifungamanishe na suala la interest rate ambalo tunalipigia kelele kila siku, ukiongea na Commercial Banks kwa nini interest rate haiwezi kushuka wanasema ni kwa sababu ni risk kubwa kwa mikopo ya kwetu, ambayo inaonekana hata kwenye benki zetu kwamba mikopo, kwa mfano ukiangalia kwenye ile taarifa mpaka asilimia 58 ya mikopo inaonekana ni mikopo chechefu.
Mheshimiwa Spika, nadhani kuna mahali tunakwama hasa kwenye eneo la uhasibu, mimi nadhani kwa ukiangalia SME biashara hizi za kati na biashara ndogo nyingi zinapopeleka mahesabu hata kwenye commercial Bank kunakuwa na mahesabu ya benki ambayo yanaonyesha yanafanya biashara kubwa na anapata faida kubwa, lakini kuna mahesabu ya pili yanakuwa ni ya TRA ya kuonesha kwamba hawatengenezi faida au faida kidogo na haya yote yanakuwa certified na hawa watu wanaitwa CPA ninajua na huku wapo. nadhani ni suala la kuweka mfumo ambao utafungamanisha ili tuweze kwanza tutoe mikopo ambayo itawasaidia wafanyabiashara na taasisi zinazofanya biashara, lakini tutoe mikopo ambayo italeta tija pia kwenye Serikali.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani tunaweza kufanya jambo moja tukapitisha Sheria ambayo inaifungamanisha NBAA taasisi za fedha pamoja na wafanyabiashara waliopo. Maana yake ni nini, taasisi inataka kutoa mkopo kwa mfanyabiashara fulani au kwa kampuni fulani ni rahisi tu, inatakiwa kuwe na sehemu ambapo financial institution ikienda inaona mahesabu yake ambayo yana uhalisia na yana-reflect kodi yanayolipa. Kwa sababu kama yanapata faida kwa nini asilipe kodi, kama halipi ina maana atakuwa na sababu gani asilipe.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa tunaenda unakuta mtu anapeleka mahesabu makubwa kwenye taasisi za fedha, inaonekana faida ni kubwa, anapewa fedha ambayo pengine hana hata uwezo nayo ndiyo tunaingia kwenye mikopo hii ambayo ni mikopo isiyolipika au ni mikopo chechefu.
Mheshimiwa Spika, nafikiri tuangalie sheria ya namna ya kufungamanisha, kama kulivyotengenezwa credit bureau kuwe kuna sehemu ambapo financial institution ikienda ikichukua mahesabu ya biashara fulani inayotaka kukopeshwa anaweza akaona pia output ya kodi ambayo inaendana na mahesabu aliyoletewa na ikawa haina mawaa. Hilo ni wazo la kwanza kwa PIC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili kwenye taarifa ya PIC ni kwenye uwekezaji wa fedha hizi za umma, mitaji kwenye hasa shughuli hizi za kibiashara. Katika ukurasa wa saba waripoti yao wameeleza vizuri namna kile kipengele cha 22.1 na 22.2 wameeleza ni namna gani fedha za umma zinawekezwa na zinakusanywa vipi na zinategemea zilete faida gani? Ninaomba niende sehemu moja tu ya mfano, Serikali inawekeza fedha nyingi sana pale Moshi Mjini kwenye Kiwanda cha Karanga Leather, nia yake ni nzuri na tunategemea kupata ajira labda 3,000 au zaidi, ukiangalia kwenye mnyororo wa faida, faida ni kubwa zaidi, lakini ukiangalia ule uwekezaji na namna ambavyo tunazi-manage ni dhahiri kabisa kwamba matokeo yake mwisho mtakuja kuiona Karanga Leather kwenye vitabu vya CAG tena! Kwa nini?
Mheshimiwa Spika, uwekezaji ni mkubwa mpaka sasa hivi ni zaidi ya Bilioni 156 lakini namna unavyokuwa managed ni jinsi mnavyoona sasa kwamba, tunasubiri matamasha tulete pair tatu za viatu hapa, tunasubiri warsha tulete viatu na mabegi, wakati investment hii inatakiwa itoe production kubwa ambayo inaweza ikatuelekeza kwenye export. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi sioni shida kwa sababu ukiangalia structure ya Dubai Port ambayo ni mali ya UAE wako wataalam kutoka nje wabobezi kwenye mambo ya bandari ambao wanafanyakazi na faida inakuja pale, kwa hiyo nafikiri kiwanda kikubwa kama hiki sasa hivi kimeajiri watu 253 tu na kiko miaka tayari imeshafika minne hakijamaliziwa, ninafikiri kuna haja ya kuwatafuta wabobezi wa biashara wa ndani na nje, na wabobezi wa masoko watusaidie kuendesha tuwalipe tupate faida, lakini tukiendelea kuviendesha kwa utaratibu wa teuzi na hizi Bodi ambazo PIC nao wameelezea matatizo yake, ni dhahiri kwamba matokeo ya kiwanda kama hiki hayataonekana na baadae itakuwa hasara na tutarudi kwenye vitabu kuonesha kwamba hela hii imepotea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine naomba niende kwenye taarifa ya LAAC na hapa nianze na ile mikopo ya vikundi, ni dhahiri kabisa tunaipenda ile mikopo inawaidia watu wetu, lakini ukiangalia hii taarifa ya CAG, ukiangalia uwezo wa kurejesha wa hiyo mokopo ni dhahiri hizi hela tumezitoa kama ruzuku. Hii iitwe TASAF part two kwa sababu hizi hela kuna maeneo mimi nilifanya ziara Jimboni, kuna maeneo vikundi vimekopeshwa 45 kinarudisha kikundi kimoja tu, maana yake ni nini? Kwamba ni hela tumetoa za kwenda ku-boost uchumi siyo za kuzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivi? Ukiangalia structure ya ule Mfuko hasa baada ya kupitisha Sheria kwamba uwe wa mzunguko, ni kwamba fedha hizi za kila mwaka, kwa kila Halmashauri maana yake zikiwa zinarejeshwa na bado tunatenga ule mfuko utakuwa mkubwa, utaweza hata kuwafikia mtu mmoja mmoja. Lakini kwa sababu hazirejeshwi ule Mfuko haukui.
Mheshimiwa Spika, kwenye ule ukurasa wa 11 wamesema mwaka huu kwa mapato ya Halmashauri zote asilimia 10 inaweza ikafika Bilioni 75, hizi ni hela nyingi sana, lakini tunaenda kuitoa halafu haitarejeshwa, mwaka unaofuata tutatenga tena na tena, maana yake ni nini? Badala ya kuwasaidia watu wajikomboe kwenye umaskini au kuwasaidia wananchi kiuchumi, tunaenda kuwasababishia umaskini kwa sababu tunajua ni hela ya kwenda kufanyia shughuli ambayo siyo serious, hela hizi hazina riba na huweki collateral.
Mheshimiwa Spika, ninaungana na Mbunge aliyesema ni vizuri tuzi-contract kwa benki. Mimi nilishawahi kufanya field Benki ya Akiba Manzese, kuna hela ya kuwasaidia akina mama walio na uwezo wa chini sana kutoka ILO walikuwa contracted Akiba Commercial Bank ndiyo wakawapelekea wale watu, mabenki wana uwezo wa kufuatilia kutathmini biashara ya mtu, kuishauri na wakaweza kutoa ule mkopo na kufuatilia kwa njia ambayo itakuwa haina matatizo kwetu, nasi tutakachofanya ni kuiongezea ile benki mtaji kwenye hizi hela, tunakubaliana kwamba wao watabaki na percent kiasi Fulani, siyo kwamba waongeze gharama ili waweze kuwachaji wale wanufaika, lakini kwa Afisa Maendeleo ya Jamii kwenda kukopesha hela, kutathmini biashara na akasema inatoa faida hii biashara na akafuatilia akusanye hiyo hela, tunajidanganya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni vizuri tutafute mfumo mbadala, sijajua mfumo ambao TAMISEMI wameuanzisha kama utaleta majibu lakini tukikubaliana na benki zetu tukatangaza tenda, Bilioni 75 kwenye mfuko wa benki yoyote ni hela nyingi, tukawaelekeza, utaratibu ule wa kukopesha tukaufanya sisi wao wakaenda kumalizia kwa ku-verify na kutoa ushauri fedha hizi zinaweza zikaleta tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye hizi fedha bado kuna matatizo, uwiano ni asilimia Nne kwa vijana, Asilimia Nne akina mama na asilimia Mbili kwa walemavu. Sasa Serikali inataka kulazimisha kwamba hata mahali ambapo walemavu hawataki mkopo tulazimisha hizo hiyo asilimia Mbili wapewe, sasa hawataki au hawapo lakini inakuja ni kweli kwamba kwa nini mmekopesha akina mama zaidi? walemavu hawajakopeshwa? wapo hawataki kufanya biashara, maana yake sasa wanalazimishwa Afisa Maendeleo ya Jamii ili wasipate hiyo kero wanawalazimishia watu mkopo, wewe chukua tu! Sitaweza kurudisha, wewe chukua tu utarudisha utaangaliaangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa huu uwiano uwepo lakini maeneo ambayo kwa mfano, maeneo mengi nimejifunza vijana hawawezi kukaa pamoja kwa muda mrefu kwa sababu bado ni watu wanaotafuta wanaenda sana, kwa hiyo ni wachache sana wanakuwa kwenye makundi lakini akina mama ni watu walio-settle wapo kwenye lile eneo, kwa hiyo tusilazimishe kwamba huu uwuiano ufuatwe kama inaonekana wana uwezo zaidi au vijana wana uwezo zaidi hilo eneo wapewe fedha zirudi lakini kubwa zaidi ziweze kusimamiwa vizuri watu wapate. Isitokee kwamba kuna kundi linahitaji likakosa na share yake imetoka lakini kama halipo na mwaka unaisha wa fedha wapewe wale kundi ambalo liko tayari liweze kufanyia kazi hizo fedha (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende eneo la mwisho ni eneo ambalo kwenye taarifa ya LAAC ukurasa ule wa Saba kipengele 2.2.3 udhaifu wa manunuzi na usimamizi wa miradi. Watu wengi wameliongelea, ni kweli kabisa kuna udhaifu mkubwa kwenye manunuzi ambayo nafikiri kila mtu atasema ifumuliwe lakini ikifumuliwa sijui itawekwa kwa namna gani ili manunuzi yaweze kuleta tija, kwa sababu kalamu ya Shilingi 1,000 ambayo wewe unaweza kununua, ikinunua Serikali itanunua 2,000 mpaka 3,000 wataalam watashauri namna ya kurekebisha mfumo wa manunuzi.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye force account. Hili ni janga force account by design ilitakiwa iende sehemu ambayo tunao wataalam wanaojitosheleza. Halmashauri iwe na Injinia wa ujenzi anayejua, iwe na Mthamini anayejua, iwe na watu wote wa technical wanaojua ili ile hela waisimamie kama ilivyo kwenye kampuni.
Mheshimiwa Spika hela, zinapelekwa kwenye halmashauri zinaambiwa zifanye kazi kwa force account, hiyo Halmashauri haina hata Injinia tunachotegemea ni nini? Tunakwenda kutengeneza matatizo makubwa, iko miradi ambayo baada ya muda haitafaa. Nitolee mfano kwenye Halmashauri moja juzi wamepelekana TAKUKURU, mradi unavyoonekana ukiangalia kwa sababu hela tunapeleka sehemu moja, tunapeleka hela za kufanana maeneo yote, lakini ukija kuangalia hela sehemu moja imefanya vizuri tena Halmashauri zilizoko karibu, sehemu nyingine hakuna kitu kabisa, lakini kuna maeneo mengine inaenda hela kwa ajili ya force account lakini unakuta hata eneo la labor wamem-contract mtu, kwa hiyo contractor anapewa tena labor kampuni kabisa inapewa kazi ya labor. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu huu wa force account ni lazima tukubaliane aidha hiyo sijui kuajiri tunaweza au hatuwezi ziende sehemu ambazo wataalam wapo wa kutosha ndiyo fedha zipelekwe kwa utaratibu wa force account, vinginevyo tuwape Wakandarasi kwa sababu bahati nzuri tunapata mpaka retention kule na baada ya muda kama huo mradi haujakaa sawa tunauwezo wa kuwaambia warudie, lakini kwenye force account ikishakuwa imeharibika inaharibika na ni ya kwako. Ninashauri force account…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Niendelee kuwashukuru wapiga kura wangu wa Moshi Mjini kwa namna wanavyoendelea kuniunga mkono na kunitia moyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajaribu kwenda kwa harakaharaka kutokana na muda, lakini nianzie kwenye kilimo. Kwenye kilimo mpango ulioletwa ni mzuri lakini unahitaji kujaziwa mambo mengi ambayo mengi wameyataja Wabunge wenzangu lakini na mimi niongezee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tunaweka nguvu kwenye kilimo na tunaendelea kutegemea kilimo cha maji ya mvua, tutakuwa tunapoteza muda. Wakati tatizo la mabadiliko ya tabianchi linaendelea kuwa kubwa, tukitegemea kilimo bila kuwa na mpango madhubuti wa umwagiliaji tutakuwa tunapoteza muda. Bwawa la Nyumba ya Mungu lililoko kwenye Mkoa wa Kilimanjaro lilijengwa miaka ya 67, lina faida kubwa pamoja na kuzalisha umeme, kuna samaki lakini mabwawa kama haya yanaweza kutengenezwa ili kusaidia umwagiliaji ili kilimo chetu kiwe chenye tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona mpango wa kilimo cha large scale. Block farming kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wadogo ni kizuri lakini kama tunataka kilimo kilete tija ni vizuri tuwe na sera pia ambazo zitasaidia wakulima wakubwa waweze kuwekeza katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna eneo ambalo nadhani Wizara inabidi ilifanyie kazi zaidi. Nadhani suala hili Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo alishaliongelea siku za nyuma kwamba ni lazima Sera ya Viwanda iwe na mwingiliano wa karibu na Sera ya Kilimo. Kwa mfano, sasa hivi tuna matatizo ya mafuta ya kula lakini tunaona tumefeli kwenye alizeti kwa maana ya kwamba demand yetu imekuwa kubwa kuliko supply. Hata hivyo, Kigoma kuna mawese huoni kinachofanyika ambacho kitaleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunaagiza sukari lakini mwenzetu wa Kilombero amesema wanatupa sijui tani za miwa 40 kila msimu. Juzi tu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alikuwa na kikao na wakulima wa ngano kwa maana ya kwamba tunaagiza ngano nyingi. Kwenye haya mazao ambayo demand yake ndani tayari ni kubwa kwa nini kusiwe na mpango wa muda mfupi na wa muda mrefu mpaka miaka 20 kuhakikisha tunakidhi soko la ndani la mazao haya ikiwa ni pamoja na kuweka viwanda vyake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miradi ambayo inaenda kukamilika. Nimejaribu kuangalia sijaona mpango ulionyooka wa ku-support SGR kwa mfano. Ningefurahi sana kama ningeona tayari kuna juhudi za kuongea na nchi kama Congo kuhakikisha kwamba watatumia SGR kwa ajili ya kusafirishia mizigo yao itakapokamilika. Hii ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuunganisha Bandari ya Dar-Es-Salaam kwenye viwango vyake, kuna mtu amesema hapa na kuitangaza ili kwenye hii miradi ambayo inaenda kuiva karibuni tuone ni namna gani itaingiza fedha ili kusaidia mipango hiyo, sijaliona. Mimi nilitegemea sasa hivi kuwe kuna economic diplomacy ya kuangalia nchi kama za Rwanda, Burundi, Congo, tunatafuta njia gani watapitisha mizigo yao yote hapa kwetu, hiyo ni pamoja na ATCL. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utalii nako bado kuna matatizo. Kwanza niseme tu wale wafanyabiashara wa utalii na Mkoa wa Kilimanjaro ni mmoja wa maeneo hayo, wana kilio kutokana na janga hili la corona. Biashara zao zimekwenda chini sana, wanaomba Serikali iwaangalie japo hata kwenye tozo ili kuwapunguzia makali. Hata hivyo, kuwepo kwa ATCL nilitegemea kuwepo kabisa na mkakati wa kuunganisha na baadhi ya mashirika ya kimataifa, ili i- promote utalii kwa ndani ili sasa tuanze kupata fedha kutika kwenye mashirika haya ya kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mikopo hasa kuwainua wafanyabiashara wadogo, nilishasema kwenye kuchangia hoja mwanzo kwamba tuangalie uwezekano wa kumkopesha mtu mmoja-mmoja. Pia hapa kwenye umri tuliojiwekea hasa kwa vijana, sina shida sana na akina mama, tumesema vijana ni miaka 18 mpaka 35, lakini vijana wa Kitanzania wenye miaka mpaka 45 wana nguvu ya kuweza kufanya kazi na kuzalisha. Tujaribu kuangalia sheria zetu kwa nini vijana sasa miaka 36 mpaka 45 hawakopesheki kwenye fedha hizi ili kuchangia kwenye pato la Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TARURA, huwezi kusema kilimo bila kuwa na miundobinu iliyo sawa. TARURA wamepewa jukumu, najikita kwenye kuishauri Serikali itafute namna bora ya kuipatia TARURA chanzo cha mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa katika ujenzi wa barabara nchini ni fedha. Tunayo mahitaji mengi kuliko uwezo wetu kifedha na hasa uwezo wa ndani.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu juu ya namna ya kupambana na hali hii hasa kwa kuongeza mapaato kwenye Mfuko wa Barabara:-
(i) Kuongeza tozo ya mafuta kutoka shilingi 263 ya mwaka 2013 na kupunguzwa hadi shilingi 158 ya sasa mpaka angalau shilingi 300 kwa lita ya petroli na dizeli;
(ii) Kurejesha tozo ya angalau shilingi 100 kwa kila laini moja ya simu kwa mwaka na angalau shilingi 50 kwa mwezi ili kuongeza urari kwenye mfuko;
(iii) Kuweka asilimia kidogo ya nyongeza kwenye CIF ili kupata fedha angalau kama ile ya reli;
(iv) Kutengeneza barabara za kimkakati kwa ushirikiano na sekta binafsi kwa kuweka Road Tolls na kuingia mikataba kama ile ya EPC+F; na
(v) Infrastructure bond.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote ni muhimu sana kwa mapato husika kulindwa kisheria na Serikali kuweka discipline ya kukusanya na kulinda vyanzo husika na mapato yake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kwanza kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara hii ya Ardhi siku hii ya leo ili niweze kufikisha masuala mbalimbali ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyoisimamia Wizara yake akisaidiana na Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kweli wameleta chachu kubwa kwenye usimamizi wa masuala ya ardhi najua mfupa huu ni mfupa mgumu, lakini sina wasiwasi Mheshimiwa Waziri alikuwa Diwani, lakini ameshawahi kuwa Meya, kwa hiyo, anajua kule chini ambako hasa ndio kunakotengenezewa haya matatizo namna ambavyo kupo, kwa hiyo, nimtie moyo na nimwambie tu, tuna imani kwamba atatufikisha mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze moja kwa moja kupongeza baadhi ya maeneo ambayo amefanya vizuri mpaka sasa. Majengo ya National Housing Tanzania nzima yapo maeneo ambayo ni prime, maeneo muhimu ambayo ndiyo yanabeba taswira. Majengo haya kwa muda mrefu yalikuwa hayafanyiwi ukarabati, yanakuwa yamebaki yamechakaachakaa, yana sura mbaya na kusababisha maeneo kama Mji wa Moshi kuonekana na sura chakavu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri lakini na Mkurugenzi wa National Housing kwa kuleta zaidi ya shilingi milioni 300 kwenye mkoa wetu wa Kilimanjaro na kurekebisha au kufanya ukarabati kwenye majengo yale ya National Housing ambayo yapo katikati ya mji hasa barabara ya Double Road. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeze kazi ya Kliniki za Ardhi ambazo anazifanya Mheshimiwa Waziri ambazo zinaleta majibu ya moja kwa moja na kumuonesha uhalisia kwenye maeneo yale ambayo anafanyia kazi. Pia nimpongeze kwenye hati hizi za kielektroniki, unakuta sehemu moja watu watatu wana hati na zote zinafanana. Kwa kuleta hati hizi za kielektroniki ambazo zina serial number ina zina tarehe ina maana itapunguza kwa kiasi kikubwa sana migogoro, lakini italeta urahisi katika utatuzi kwa sababu itajulikana ni nani mwenye hati zile za mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pale kwenye ukarabati nilete ombi Mheshimiwa Waziri, pamoja na kukarabati zile nyumba hasa kwenye maeneo ya biashara ninaomba waangalie namna ya kurekebisha maeneo ya pedestrian, maeneo ya watembea kwa miguu yawekwe angalau pavement ili sasa uzuri huo ambao umeonekana katika ukarabati wa majengo u-reflect kwenye maeneo ya watembea kwa miguu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa muhimu sana leo unakwenda kwenye ukurasa wa nane wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini naangalia tena kwenye ukurasa wa 47 alipoorodhesha vile vipaumbele vya Wizara katika bajeti hii alisema ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishwaji wa ardhi mijini na vijijini, sasa hapa ndio ninapotaka kuweka point yangu ya muhimu.
Mheshimiwa Spika, miji inakua, wakati Dar es Salaam inaanza enzi hizo pale Manzese palikuwa panaonekana ni nje ya mji, kwa hiyo, wakati inakua pale pakaachwa, pakajengwa kiholela, slum, hivyo hivyo pakaja Kimara. Sasa maeneo mengi ya miji yanayokua, watu wamekuwa na tendency ya kununua maeneo ya pembezoni, moja ni kwa sababu ya kasi ya ukuaji, lakini pili ni kwa sababu ya gharama kwenye yale maeneo yanayohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili linasababisha maeneo ya pembezoni ya maeneo yale ambayo yameshatambulika kama ni maeneo ya miji kununuliwa kwa kasi na kujengwa kiholela maana yake ni nini? Kwa mfano, natolea mfano halisi wa Moshi Mjini, Moshi Mjini ndio mji mdogo zaidi Tanzania, una kilometa za mraba 58, ulipokuwa unapanuka, maeneo ambayo yalitambulika kuanzia na Baraza la Madiwani, yameshapita kwenye DCC, yamekwishapita kwenye RCC na yakaletwa Wizarani kwa ajili ya kupanua mji mwaka 2016. Mpaka leo tangu hayajapata baraka hiyo, yalishakwenda mbali sana mpaka tukapata GN Na. 219 ya terehe 15 Julai, 2016, lakini tangazo hilo lilitiwa saini na Mheshimiwa Lukuvi akiwa Waziri wa Ardhi tarehe 26 Juni, 2016.
Mheshimiwa Spika, ombi la msingi ni kupanua maeneo yale ya kiutawala kwa sababu eneo lile limeshajaa kabisa, hatuna maeneo ya makaburi, makaburi yamejaa, eneo la dampo tumenunua Moshi Vijijini na ni umbali mrefu, lakini adha kubwa zaidi ni kwamba barabara ya kwenda pale kwenye dampo hatuwezi kukarabati na maeneo mengine ya kiutawala. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu eneo la Moshi Mjini linapakana na eneo la Hai, linapakana na Moshi Vijijini ilikuwa ni vigumu kulifanyia maamuzi mara moja, lakini vikao vyote vimeshafanyika na wakati huo mimi nilikuwa Diwani nilishiriki, tukapitisha hayo, lakini mpaka leo tumeshindwa kuongezewa eneo hilo ili tuweze kupanga eneo hilo vizuri na kwa bahati mbaya waliokuwa wanapinga mwanzo walionesha eneo hilo ni eneo la kulima, lakini Mheshimiwa Waziri ninaomba ufanye ziara, uje nikutembeze, maeneo hayo yanauzwa kiholela, yanapangika kiholela na yanajengeka kiholela, nyumba kubwa na za kifahari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Mnavyochelewa kuja kulifanyia maamuzi maana yake tutakuwa kila mara miji yetu badala ya kuipanga vizuri kazi yetu itakuwa ni kuirasimisha tu ambayo imeshapangika vibaya, barabara haziwezi kupelekwa, huduma za jamii haziwezi kupelekwa. Kwa hiyo, ninamwomba sana Waziri, sina nia ya kuja kukamata shilingi, nilikuwa ninaweza hapa na ndio ningekamatia, lakini ninaomba nimwelezee, naomba walifikishe mwisho suala la upanuzi na ninaelewa kuna matatizo ya kibajeti tunaposema liwe jiji, tuachane na jiji kwanza, turuhusuni yale maeneo ambayo tayari yameshapita kwenye vikao ya upanuzi yaingie, tupanue mji wetu ili suala la jiji lije baadaye, hilo ndio suala langu la kwanza ambalo nimeona ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni eneo la urasimishaji makazi, limekuwa na phases mbalimbali, kuna mwanzo ilikuwa inafanyika na Serikali, baadaye wakaleta sekta binafsi ifanye, watu wakachanga hela, likaishia njiani. Tuna maeneo mengi kwenye baadhi ya kata hasa pale Moshi Mjini ambazo watu walishatoa hela kwenye makampuni ya urasimishaji, idadi haikufika ile inayotakiwa, makampuni mengine yakawa yameshaondoka na hela watu wameshatoa, urasimishaji haujakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha alete hoja ambayo itaonesha namna ya kufunga suala la urasimishaji hasa kwenye maeneo ya miji ambayo tayari yanahitaji sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna eneo linahitaji sana kuangaliwa na Wizara, kwa mfano Wizara ya Ardhi haina wataalamu kabisa, Mkoa wa Kilimanjaro nafikiri mkoa mzima surveyor ni mmoja, Moshi Mjini tulikuwa na surveyor tena msomi mwenye PhD wakamchukua, wakampeleka UDOM, hawajatuletea surveyor mpaka leo, ma-QS hali kadhalika.
Mheshimiwa Spika, sasa unajitahidi sana kutatua migogoro, lakini moja ya maeneo yanayokusababishia migogoro ni kutokuwa na wataalamu kule chini ambao watasimamia na kuhakikisha wanakupa taarifa za uhakika za kila siku kwenye maeneo yake, lakini pamoja na wataalam hata kwenye ofisi, sisi Moshi Mjini tulitoa eneo la ofisi kwa ajili ya Wizara ya Ardhi nimeona pale umeandika kwamba unaweka mkazo katika kujenga ofisi, lakini mpaka sasa hivi hamna kilichoendelea, eneo lipo pale kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Wizara yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine la muhimu sana ni eneo la maeneo ya wazi na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri alikuwa Diwani, anafahamu jinsi maeneo ya wazi yanauzwa, yanauzwa kwa kasi sana na yanauzwa kwa watu binafsi, hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi Manispaa ya Moshi katika baadhi ya maeneo ya Kata ya Rau, Ng’ambo na Mji Mpya yalipata mafuriko, tumechukua watu tukawapeleka kwenye hizi shule mpya wakae pale kwa sababu gani? Hatuna maeneo ya wazi, yameuzwa, watu wanamilikishwa pamoja na mazuri yote ambayo yanaendelea kwenye Wizara yako naomba tutafute namna ya kuweka sheria kali kwenye maeneo ya wazi hata ikibidi hati yake iwe tofauti, lakini tuhakikishe kwamba inakuwa ni kosa la jinai mtu kununua eneo la wazi hata akiwa na hati shida hii ya kusema lazima afute Rais kwenye eneo la wazi hata kama ni miaka 20 mtu analo, tuweze kulirudisha kwa wananchi kwa sababu tunayahitaji sana maeneo ya wazi na maeneo ya wazi yanauzwa sana... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Haya kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi wa Moshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa salam zangu za pole kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu na Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa kumpoteza Rais wetu Hayati Dkt. Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pole hizo, nitoe pongezi kwake Rais sasa Mheshimiwa Mama Samia kwa kuchukua nafasi yake kama Rais. Vile vile nawapongeza Mawaziri wote na viongozi wote ambao wengine wamebaki kwenye nafasi zao, wengine wamebadilika na wengine wameingia ili kuweza kulisongesha gurudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyo vipengele kama kumi ambavyo nitaviongelea kama muda utaruhusu. Naomba nianze na kilimo. Tumeshakubaliana kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu. Yako maeneo ya kufanyia kazi na mengine ya meshatajwa au kusemewa na viongozi wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni eneo la utafiti. Nafikiri ni muda muafaka sasa Wizara itumie nguvu kubwa kwenye maeneo yote, wajue ni mazao gani yanalimika kirahisi wapi na kwa njia ipi. Nchi ambazo zinaweza kutusaidia sana kwenye hili tukichanganya na wataalam wa ndani kutoka kwenye vyuo vyetu pamoja na SUA ni pamoja na Egypt, Israel na Netherland ambao wamefanikiwa sana kwenye kilimo pamoja na mazingira yao kuwa magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine muhimu sana kwenye kilimo ni la umwagiliaji. Bwawa la Nyumba ya Mungu lilijengwa na Serikali yetu miaka ya 1960, nafikiri ni mwaka 1967. Eneo lile lilipojengwa limekuwa ni kichocheo kikubwa. Mzungumzaji aliyepita ameongelea mafuriko huko kwao Kyela. Serikali ikiweka nguvu katika namna ya kuyachukua haya maji na kutengeneza mabwawa kwenye maeneo yenye kilimo, itasaidia sana kuondoa utegemezi wa kilimo hiki ambacho kinategemea mvua na ambavho hakina tija sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo, nafikiri kuna vitu ambavyo tuna uwezo navyo, ambavyo tuna mahitaji navyo sana hapa ndani. Tuna upungufu wa mafuta ya kula. Kwa hiyo, tukiwekeza kwenye alizeti, tayari soko lipo, la ziada litakuja tu baadaye. Tuna upungufu wa ngano; tukiwekeza hapo maana yake soko la ndani lenyewe linaanza na linatosheleza. Hata sukari, tuna upungufu na tunatumia fedha nyingi sana kuagiza kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa na mpango wa muda mrefu wa kuhakikisha miaka kama ni mitano au kumi hili tatizo linaisha, tunaweza kabisa na tutakapofanikiwa hilo, basi nyongeza itakayopatikana, itaweza kuuzwa nje na kutupatia fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kugawa maeneo ya kimkakati, yaani block zone pamoja na kuwashirikisha wakulima wadogo. Ningependa sana kama ningeona mkakati wa kuwavutia wakulima wakubwa wa ndani na wa nje kwa kuwatengea maeneo na kuweka sera ambazo zitawavutia waje walime hapa kwetu. Wakilima, watatusaidia kwenye soko la ndani na vile vile kwenye kuuza nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa ambalo linawezekana hapa na ninalitolea mfano kwenye taasisi ile ya TAHA ni kutumia hii block zone. Ukishawaweka watu kwenye block ni rahisi kuwafuatilia na kuwapelekea wataalam wanaowashauri kama inavyofanya Taasisi ya TAHA kwenye mboga mboga pamoja na matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishaweza kuwekeza vizuri tukaweka hizi sera vizuri kwenye kilimo, tunahamia kwenye viwanda. Viwanda vitakuwa ndiyo watumiaji wa bidhaa zinazotokana na kilimo. Hapa ndiyo sera tunayokwenda nayo, lakini sijaona sera au incentives zinazosababisha watu watoke maeneo mengine waje waweke viwanda vyao hapa. Sijaona. Ni muda muafaka sasa Wizara ione namna ya kuendelea kutafuta na kuweka mazingira yatakayovutia wawekezaji wa nje na wa ndani kwenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia, tukiweka viwanda vya vile vitu ambavyo tuna upungufu navyo ndani, maana yake tunahakikishia wawekezaji kwamba soko lipo; hivyo ambavyo nimetaja hapo juu kwenye kilimo; suala la mafuta, sukari na vitu vingine ambavyo tayari tuna uhitaji navyo sana ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengine yanatia hasira. Nami nilisema mara ya kwanza na ninarudia tena. Naunga mkono wale waliobinafsishiwa viwanda kwa nia ya kuviendeleza ili vitoe ajira na viingize kodi wakashindwa, wanyang’anywe tuvitangaze tena upya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Moshi kuna Kiwanda cha Magunia, kimefungwa, hakifanyi kazi; kuna Kiwanda cha Viberiti, Kibo Match, kimefungwa na wana nyumba pale zimefungiwa chini, hazifanyi kazi. Ili kulitilia nguvu hili, ni muda muafaka sasa tuvichukue, halafu tutangaze upya viwanda hivi viweze kuanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la afya. Hili kidogo niliongelee kwa choyo kwa kuangalia Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa huu una Hospitali ya Rufaa moja, inajulikana kama Mawenzi, imejengwa miaka mingi iliyopita, 2022. Hospitali ile imekuwa ya kizamani sana na miundombinu yake iko kwenye hali mbaya sana. Kinachosikitisha zaidi, kuna Jengo la Mama na Mtoto ambalo lingekuwa na huduma nyingine za kisasa katika design yake kama IMR, X-Ray za kisasa na vitu kama hivyo; lakini imeanza kujengwa 2008 mpaka leo haijamalizika na ni jengo moja na sijaiona kwenye ripoti ya CAG kwamba ni nini kilisababisha inachukua muda mrefu namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara iende ikaangalie pale Mawezi kuna nini? Tangu mwaka 2008 jengo moja halimaliziki. Naomba sana kwa sababu Mkoa wa Kilimanjaro hatuna Hospitali ya Rufaa inayoendana na mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Moshi Mjini au Moshi kama Wilaya hatuna Hospitali ya Wilaya, tunatumia hospitali za binafsi sasa hivi. Mheshimiwa Rais aliyetangulia mbele za haki, Hayati Dkt. Magufuli alituahidi. Nami naomba ahadi hiyo iendelee kuhamishiwa kwa viongozi waliopo na sisi tupate Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya suala la afya, nakwenda kwenye miundombinu. Kwanza naipongeza Serikali kwa mafanikio iliyopata. Kwenye SGR, ATCL, Bandari zinazoendelea kuboreshwa ikiwa ni pamoja na barabara nyingi zinazojengwa. Natamani sana nione Wizara zinazohusika zikifanya juhudi ya kuhakikisha tunakuwa na economic diplomacy ya kuwashawishi kwa mfano watu wa Kongo. Kwamba ni kwa nini wapitishie mizigo yao kwa barabara kupitia Zambia badala ya sisi kuboresha bandari ile ya Kigoma na Rukwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliongelee kidogo. Upande huu wa Mashariki wa nchi yetu tayari kumeshafunguka, lakini upande wa Ziwa Tanganyika pale ambapo tunapakana na Kongo ambapo ni milking cow, inatakiwa zile bandari ziboreshwe. Pale Rukwa reli iende mpaka pale bandarini, ziwekwe meli za kuweza kuvusha vitu viende kule Kongo. Balozi wetu pale atusaidie kuongea na watu wa Kongo nao wafungue barabara kwa upande ule wa kwao mambo yaende. Hakuna sababu ya mizigo kutoka kwenye bandari ya Dar es Salaam, ipitie Zambia ndiyo iende Kongo. Ni hela tumezikalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba hilo tuliwekee nguvu kidogo liweze kuleta…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha. Ahsante sana.
MBUNGE FULANI: Unga mkono hoja.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi. Niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote kwa kutuletea bajeti nzuri, lakini ombi langu tuweze kuweka nguvu katika kutafuta fedha ili mipango hii iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kupongeza, nimeiona barabara ya Tengeru – Moshi – Himo ipo kwenye bajeti ambayo inasababisha msongamano mkubwa sana pale Moshi. Pia nimeuona Uwanja wa Ndege wa Moshi ambao ni muhimu sana katika utalii na biashara, niwapongeze sana Wizara. Vilevile katika bajeti nimeona barabara za Chuo cha Polisi au Shule ya Polisi Moshi, nipongeze sana na kushukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ni kuhusu barabara kuu hizi zinazojengwa na TANROADS, haswa barabara ya Moshi – Arusha, katika maeneo mengi haziwi na mitaro. Sasa maji yale ambayo wanayajengea makalvati na madaraja na kwa sababu ya nature ya Mkoa wetu wa Kilimanjaro na Manispaa ya Moshi huwa ni mteremko, kuna Kata za Ng’ambo, Msaranga, Mji Mpya na Miembeni zinaathirika sana na maji haya ambayo yametengenezewa makalvati lakini hayajawekewa mitaro kuyaelekeza katika mito. Niombe sana Serikali iangalie uwezekano wa kutengeneza mitaro ili maji haya yasiendelee kuleta maafa kwenye makazi ya watu (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara ambayo kwa muda mrefu tumeiombea upgrade na tulishaipanua na tayari watu walishavunja nyumba zao kupisha upanuzi wa barabara hiyo. Barabara hiyo ni ya Sokoine ambayo inaanzia katika roundabout ya YMCA kwenda mpaka KCMC inaenda kuungana na barabara ya Mwika. Barabara ile inaunganisha barabara mbili za TANROADS, kwa sababu tulishaiombea ije TANROADS ili iweze kuunganishwa na kupanuliwa basi tunaomba tafadhali sana Serikali iangalie umuhimu wa kui- upgrade barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara nyingine ambayo haipo moja kwa moja kwenye Jimbo langu lakini ni ya muhimu sana kwenye Jimbo la Moshi Mjini. Barabara ya TPC – Mabogini – Kahe na baadaye itaenda kuungana mpaka Chekereni. Barabara hii ina umuhimu kwanza kwa sababu ndiyo inayoleta chakula katika eneo la mjini, lakini pia hatuna maeneo kwa ajili ya bypass. Barabara hii ikiweza kutengenezwa inaweza kutusaidia ili iwe ndiyo bypass kwa ajili ya kuhamisha malori na kuondoa msongamano mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara iliyokuwa ya Arusha ya zamani inaitwa Old Arusha Road barabara hiyo ilikuwa ya TANROADS lakini baada ya TANROADS kuhamisha barabara kupeleka kwenye barabara hii mpya ya Arusha barabara ile imetekelezwa, lakini ina umuhimu sana iwapo lolote linatokea kwenye barabara kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iangalie uwezekano wa kuitengeneza barabara ya Old Arusha Road ambayo inaanzia Moshi inakwenda Moshi Vijijini mpaka Jimbo la Hai. Barabara hii inaumuhimu sana katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisimalize bila kuongelea kidogo kuhusu TARURA ambayo ni sehemu ya bajeti hii. Tunayo matatizo mengi sana katika maeneo yetu na yalizungumziwa sana. Lipo lile suala la kupata fedha, mimi niendelee kusisitiza ni muhimu sana TARURA waongezewe fedha ili angalau waweze kusimamia barabara za mijini na vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uzoefu wangu wakati fedha hizi zilipokuwa zinaletwa, halmashauri tulikuwa tunanunua mitambo, magreda na mashindilia kwa hiyo gharama za kurekebisha barabara haswa hizi ambazo siyo za lami inakuwa ni rahisi. Nitoe ushauri TARURA wawezeshwe kununua mitambo ili kazi iwe rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, mchango wangu ni kuhusu Benki ya Nyumba ya Taifa. Watanzania asilimia kubwa wanajenga nyumba kwa fedha taslimu, hali hii inasababisha rushwa makazini, kwenye biashara na jamii kwa ujumla. Nyumba ni hitaji muhimu na la lazima, lakini ni ulinzi pia kwa familia. Ni vyema kuhakikisha kuwepo kwa benki ya nyumba au mfumo wa kibenki wa kutatua suala hili. Hapa ushauri wangu si kwa kuwapa fedha bali ni kwa kuwakopesha wenye viwanja vifaa vya ujenzi; kwa kutumia nyumba na kiwanja hicho kama dhamana na iwe ya muda mrefu kuanzia miaka 10 hadi 30 kwa wananchi. Hii itasaidia kuwapa amani Watanzania, lakini pia itasaidia kuongeza urari mifukoni mwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa kifupi kabisa mambo machache kwenye hotuba hii ambayo imewasilishwa. Naomba nianzie suala la makampuni ya kimataifa ambayo yanafanya kazi katika nchi yetu. Yapo makampuni mengi yanafanya kazi na makampuni au biashara ndogo ndogo, zipo kampuni za tax kama Uber, Taxify na pamoja na nyingine za namna hiyo. Zipo kampuni za booking kwenye mahotel mbalimbali zipo hoteli.com, booking.com na nyingine za namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba wakati Mheshimiwa Waziri atakua anaenda kuhitimisha atufahamishe ni namna gani wanaweza kupata kodi kupitia makampuni haya haswa yale ambayo hayana ofisi locally ambayo yanafanya biashara na yanakusanya fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba pia nigusie kwenye suala la wizi, watu wengi wamegusia suala la wizi ninaomba niligusie kwa sehemu mbili, kuna wizi kwa maana wizi wa software na wizi kwa maana hard ware. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi mtu akiibiwa simu ambayo imeshasajiliwa na IMEI yake hipo kuweza kufuatilia inaonekana ni jambo kubwa sana, wakati teknolojia imeshakwenda mbali sana, simu hizo zinaweza kuzimwa na zisiweze kutumika na kwa bahati mbaya sijaelewa shida inakuwa wapi kwa sababu inabidi uende kwa subscriber wako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nadhani wizara inaweza kuweka utaratibu kukawa kuna call center moja ambyo ukiibiwa simu regardless na matandao wako ukipeleka taarifa zako pale wanaweza ku-share kwa mitandao yote na wakai-block hiyo simu. Lakini hiyo ya kui- block ni hatua ya mbele zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa nadhani njia rahisi ya kukomesha kwa haraka ni kwamba ikishaibiwa simu ikisetiwa call center ya namna hiyo basi hizi IMEI number ikiweza kuwa shared kwenye hiyo mitandao basi waweze ku-trace line nyingine itakayowekwa hata kama ni ya mtandao mwingine anayetumia akamatwe vitendo vya namna hiyo vikiendelea vinakomesha wizi wa simu na baadaye laptop pamoja na vyombo vingine hivi vinavyotumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili niwashauri Serikali kama wanaona ni gharama ku-run kitu cha namna hiyo, mimi nadhani kuna vijana wa kitanzania wengi baadhi ni watu nawafahamu wanaweza kufanya kazi hiyo kwa niaba ya Serikali na wengine walishapeleka mpaka maombi wakaambiwa ni mpaka tubadili policy. Sasa unaibiwa simu unaenda kutoa taarifa polisi inabidi kusubiri siku tatu nne na hapo ikishafikia hivyo uwezi kuokoa kitu chochote haswa information zinazokuwa kwenye vyombo vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba hili lifanyiwe kazi tunacho chuo cha Cyber Crime pale CCP kimeanzishwa, ninadhani ni muda sasa kama wataona ni gharama kufanya hivyo tunaweza kupitisha sheria kwamba mtu anaibiwa kifaa cha umeme hicho, kama simu computer au tablet aweze kupewa huduma ndani ya masaa 24, ndani ya masaa 24 maana yake mtu anaweza aka-trace watu walioiba na kupata kifaa chake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende upande wa software na huu nadhani kidogo watu wengi wamegusia na Mheshimiwa Rais alipokuwa anaongea naye aligusia, kwamba inawezekanaje mpaka sasa tunasajili mpaka line zetu kwa kutumia fingerprint lakini wale wezi wa kwenye mtandao bado wapo na bahati mbaya fedha hizi zinamlolongo au zina cheni kama ukimtumia hawezi kuzitumia bila kwenda kwenye wakala na kuzitoa au kulipia huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inaonekana bado wizi huu unashamiri na watu tunao na teknolojia, walizima zile simu za kichina ndani ya siku kadhaa tu wakaweza kuzizima, lakini kwa sasa hivi hawa watu wanaiba kwa mtandao kila siku wanaweza kuwasha laini hatujui wanasajilije bila kuwa na fingerprint na hatujui kwanini hawawezi kukamatwa mpaka viongozi wa nchi atoe rai kwenye jambo dogo kama hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani ni vizuri wizara wajipange kwa ajili ya hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kuunga mkono hoja ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi ya kuweza kuchangia lakini pia nianze kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa uwasilishaji mzuri na uandaaji mzuri wa bajeti ya Wizara yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaenda haraka haraka ili niweze kuongelea mambo mengi zaidi. Nianze kwa kuunganishwa kwa TBS na TFDA pamoja na marekebisho ambayo yametajwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wa 18. Nia ya kuunganisha taasisi hizi za TBS na TFDA ilikuwa nzuri sana ili kuboresha utendaji. Lakini badala yake imeleta vikwazo, shida katika utendaji. TBS sasa imekuwa ndiyo mamlaka ya ku-standardize na ku-regulate majukumu ambayo kikawaida yasingetakiwa yafanyike na taasisi moja. Badala yake sasa kumesababisha kuwepo kwa bidhaa fake sokoni, hasa bidhaa zinazotoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaweza kutoa mfano; kwa mfano, maziwa ya watoto wachanga, sheria inasema yale ambayo yameshakubaliwa sasa ambayo yamepiwa yanaonekana yana vigezo yawe na maelezo kwa Kiswahili kwa maana ya kwamba ingredients na vitu kama hivyo. Lakini sasa hivi ukitoka tu hapo nje ukienda supermarket yamejaa maziwa ambayo hayana vigezo na yapo sokoni.
Kwa hiyo, TBS ilipounganishwa na TFDA, badala ya kuleta kheri imeleta tatizo. Ni vizuri sheria ile iliyopitishwa basi iweze kutofautisha majukumu ndani ya TBS kwamba yale ya ku-standardize yasimamiwaje na haya ya ku-regulate yaweje kwa sababu ya kuiunganisha…
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Neema.
T A A R I F A
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ningependa kumpa Taarifa mzungumzaji hiki anachokisema cha jukumu la kuangalia ubora na usalama wa chakula ilivyoondolewa kutoka TFDA kwenda TBS inahatarisha sana maisha ya Watanzania. Unakuta wengi wetu tunanunua labda boksi ya juice ya machungwa tukijua kwamba lile ni chungwa halisi, lakini kihalisia ndani yake kunakuwa na concentrate, ladha na rangi. Kitu ambacho ni hatarishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kumpa taarifa kwamba TBS na Wizara lazima iangalie namna gani ya kuandaa kanuni zitakazomlinda mlaji na kutoendelea kuweka maisha ya Mtanzania rehani. Ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Priscus.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea na ni ufafanuzi mzuri wa hiki nilichokuwa nasema kwamba haya majukumu yalivyopelekwa pamoja yameleta matatizo badala ya kuleta heri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye viwanda. Wakati viwanda, hasa vile vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali vinabinafsishwa kulikuwa kuna taasisi mbili zinahusika; viwanda vilivyopitishwa kwenye LAT na vile vilivyopitishwa kwenye PSRC. Vile vilivyopitishwa kwenye LAT ni vile ambavyo vilikuwa liquidated. Yaani vilikuwa vinauzwa, na ile ilikuwa ni discretion ya mnunuaji afanye nini. Lakini vile vilivyopitishwa PSCR ilikuwa ili viweze kuboreshwa, viongezewe mtaji, teknolojia, vitoe ajira na vilipe kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Moshi Mjini vipo viwanda vingi amevitaja Mheshimiwa Ndakidemi sasa hivi. Kiwanda cha Kibo Match, Kibo Paper na viwanda vingine. Vile vilibinafsishwa ili viendelezwe, lakini vimefungwa havifanyi chochote. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia. Nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti yao. Nianze kwa kuwaomba sana Wizara waanze kuyafanyia kazi mambo ambayo yalifanyiwa mjadala kati yao na Washika Dau kwa maana ya Wafanyabiashara wa Utalii, lakini na mawasilisho ya Vyama vya Wafanyakazi wanaojihusisha kwenye biashara hii ya utalii kama ma-guide, ma-porter na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na maslahi ya wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye utalii, ma-porter, ma-guide na wapishi. Kundi hili ni kundi kubwa la vijana lililojiajiri kwenye kazi ngumu hii ya utalii, lakini hawana mikataba wengi wao, lakini pia hawana bima za afya, wanakwenda kule kwenye baridi sana. Ningeiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuandaa hata mfumo wa kuwa na pensheni kwa watu ambao hawako kwenye sekta rasmi, lakini wanaopata kipato kama hawa ambao wanajihusisha na biashara ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia hao watu wanahitaji elimu kubwa, kwa nature ya biashara ya utalii, mfanyabiashara yule akishawapokea wageni huwa mara nyingi wanakabidhiwa kwa hawa waongoza utalii. Sio wote wana utashi wa kutosha, naomba sana Wizara iangalie uwezekano wa kuwapa elimu ya mara kwa mara na semina za mara kwa mara hasa kuhusu mambo muhimu ya nchi yetu ikiwa na takwimu, kwa sababu hawa ni mabalozi muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kilio cha muda mrefu sana kuhusiana na ada zetu kwenye mbuga zetu na maeneo yetu ya utalii pamoja na viwanja vyetu vya ndege. Kama kichocheo muhimu cha utalii naomba Wizara ifanye utafiti wa kutosha kulinganisha bei hizi pamoja na maeneo mengine ili kuweza kufanya maamuzi sahihi. Kama ilivyo kwenye halmashauri zilizopo kule Geita zinapata CSR kutoka kwenye machimbo yale, katika Mkoa wa Kilimanjaro halmashauri zinazozunguka kwa mfano Mlima Kilimanjaro, tungependa sana na sisi tuwe tunapata kipato fulani kwa ajili ya kusaidia halmashauri zile ambazo zinazunguka mlima ule na ambazo zinafanya kazi kubwa ya kulinda mazingira maeneo yale. Nimeona wenzetu wa Geita wanapata kipato kizuri sana, lakini kwetu naona suala hilo halipo. Tunaomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba suala hili liliwasilishwa na wafanyabiashara suala la sera hasa kwenye suala la kodi, naomba Serikali ifanyie kazi hasa kwenye eneo la kukata rufaa hasa wafanyabiashara wanapokuwa wana matatizo kwenye kodi. Katika sheria ile kuna kifungu cha 16 ambacho kinapingana kabisa ambacho kinasema ukikata rufaa kwa Kamishna lazima iwe suala linalohusu Civil Concern. Sasa kipengele hiki kinapingana kabisa na kipengere kifungu cha 7 na kifungu cha 53 ambacho kinatoa haki ya rufaa. Wafanyabiashara waliwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri, naomba nilitilie msisitizo ili basi marekebisho yaweze kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Utalii imepigwa sana kipindi hiki cha Corona, lakini imetupa mafunzo mawili. Funzo la kwanza ni kuweza kuweka record zetu sawa ili baadaye tuweze kutoa stimulus ikiwezekana na stimulus siyo lazima iwe kwa kutoa fedha hata kwa kuwapunguzia gharama kwa kipindi ambacho kitakuja cha utalii. Hata kuhuisha leseni zao kwa sababu walikata leseni kipindi ambacho hawakufanya biashara. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana hilo liweze kuzingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuangalia masoko mapya, kipindi cha Corona tumeweza kupata soko jipya la Urusi, lakini kikwazo kikubwa kimekuwa ni lugha, wenzangu wameshataja. Ni vizuri tuanze kuchunguza masoko mapya na tuhakikishe tunafanya kazi ya kujua lugha hizo za Kichina, Kirusi na za maeneo mengine ili tuweze kupata masoko hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la helicopter ya Uokozi, Rescue helicopter. Pale Kilimanjaro ilikuwa inafanyika na mfanyabiashara binafsi. Ilikuwa ina tija sana na ni chanzo cha mapato, lakini kutokana na hali hii ya COVID yule bwana ameshindwa kujiendesha. Ni vizuri Wizara iangalie chanzo hiki cha mapato, iweze kununua helicopter ya uokozi ambayo itakuwa inalipiwa kwa wale ambao wanakwenda kupanda mlima ili mtu akipata tatizo basi huduma ile ambayo imeshazoeleka, imeshatangazwa iweze kuwepo na ni chanzo cha mapato kwa ndugu zetu wa Wizara ya Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi kabisa naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia hutuba hii ya Wizara yetu ya Fedha. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, wote ni ndugu zangu. Nawashukuru Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Watendaji wote kwa shughuli hii nzito. Naipongeza Serikali kwa kweli, tayari tumeshaona mwanga mbele, tunawashukuru sana, tunawapongeza. Kazi ya muhimili huu huwa ni kuwakumbiza nyie, lakini ninyi wenyewe mmetuonesha njia na tutawaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na miradi ya kimkakati. Nimeshawahi kuteta na Mheshimiwa Waziri. Kule Moshi katika miradi ile ya kimkakati, Halmashauri yetu tulipewa Stendi ya Kimataifa pale. Stendi ile imeshameza shilingi bilioni saba za Serikali Kuu. Serikali ya Halmashauri imetengeneza barabara za kuzunguka na kutokea eneo lile na kuzamisha pale zaidi ya shilingi milioni 500, lakini miradi ile imesimama, mwenzangu juzi alitoa mpaka takwimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali tumeishaianza kazi, ile fedha tusiifukie. Nasi tuna maombi mawili; tunaomba aidha Serikali itusaidie tumalizie, mradi ule una kama shilingi bilioni 17 au 19, lakini kama Serikali itaona imebanwa, itusaidie kusaini kibali cha kuturuhusu sisi Halmashauri iweze kukopa. Original plan ndiyo hiyo. Kwa hiyo, tunaomba hayo yaweze kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na madhara ya UVIKO-19. Dunia nzima hayo madhara yameonekana na kumekuwa na utaratibu wa kutoa kitu kinaitwa stimulus na kiukweli katika nchi yetu, kila mahali wamedhurika, lakini zaidi kwenye utalii na usafirishaji na hoteli. Sasa naiomba Serikali, kama itashindwa kutoa stimulus kwa maana ya kupeleka fedha, maana naona baada ya ile Kamati aliyoiunda mama yetu, naona Benki ya Dunia kama siyo IMF wamesema watatoa dola milioni 400 na kitu. Sijajua mpango wa Serikali na hizo fedha ni vipi kama tutapewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba stimulus iwe katika maeneo haya. Kama Serikali itashindwa kabisa kutusaidia fedha, basi itusaidie hata kwenye kuhuisha zile leseni bila gharama, lakini ikishindikana hiyo, basi kuna zile charges ambazo zimepanda ndugu yangu wa Arusha jana alilalamika sana, basi zibaki zile za mwaka jana na zile nyingine mpya hasa zile za ardhi zisimamishwe kabisa mpaka hao watu watakapo-recover kwa sababu kuna muda mrefu sana mpaka wa-recover. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande huo huo, wafanyabiashara wengi hasa wakubwa na wa kati wanafanya biashara kwa mikopo na wengi wamekopa kwenye mabenki ya ndani. Sasa hatua za mwanzo, zile benki zimepunguza au zimeondoa principal, zimebakiza interest. Sasa kwa kawaida unajua, ile interest ikiendelea kuchajiwa ni umesogeza tu na mzigo mbele unazidi kuwa mkubwa. Naomba Benki Kuu kama inaweza, kama njia ya stimulus, iondoe interest pamoja na principal mpaka angalau mwakani mwezi wa Sita au mwezi wa Kumi na Mbili, hali hii ikishatulia, basi wale wafanyabishara waweze kurudi kwenye biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina lingine la kuishauri Serikali, hasa kwenye sera za uwekezaji. Hatujawa na sera za wazi kabisa ambazo zinaweza kum-support mtu anayetaka kuja kuwekeza hapa. Kwa majarida ya Kimataifa yanasema, katika nchi ambazo hazitabiriki ni pamoja na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitatoa mifano michache tu, moja ya sera ambazo zinaweza kuvutia watu ni pamoja na interest za benki na watu wengi wameziongelea. Hiyo ni positive, lakini negative ya sera ambazo zinatukosti ni kipindi ambacho Serikali ilizivamia biashara zenye leseni, tena leseni kutoka za mamlaka tofauti tofauti, viwanda na biashara na BoT zile bureau de change na kuzifunga bila ya maelezo mengi na kunyang’anya zile hela. Sasa hizo sera za namna hiyo ndio zinasababisha tunakuwa nchi ambayo haivutii sana wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana kuishauri Serikali. Na sehemu nyengine ambazo tunaweza kusaidia kwenye sera za uwekezaji ni kwenye kodi, sheria zetu za kodi zinamatatizo kidogo. Nilishawahi kutoa mfano hapa kuhusiana na kodi kwenye ile Tanzania Revenue Appeals Act. Ile sura ya saba inatoa haki ya ku-appeal, sura ya 16 wanaku- limit kwamba mambo haya na haya na haya, yaani kwamba ni kama tu ukiwa umeonewa na Kamishna na una-appeal kwenye board. Lakini hiyo pia inaenda kinyume pia na Tanzania Appeal Act sura ya 53 ambayo inatoa haki ya appeal kwa lolote. Sasa hizi ni moja ya vitu vichache ambavyo vinasababisha tuwe hatuna mazingira mazuri ya kuwekeza, kwa hiyo, ningeshauri hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali, imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kuangalia na kupandisha madaraja kwa watumishi wa Serikali, lakini kwenye hili peke yake halitoshi, lazima tukumbeke wale watumishi ule mshahara wao ni factor ya kodi ya Serikali kwa sababu inakatwa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeshauri, pamoja na hizo juhudi zilizofanyika zote kipo kitu amabacho inabidi tukiangalie, watanzania wote walioajiriwa na waliojiajiri tunajenga nyumba zetu kwa cash hii ni gharama kubwa ukija kuangalia, yaani unapokuta barabarani mtu anaendesha mkokoteni amepakia geti ni mjasiriamali anapambana, ninajua Serikali imeweka mazingira mazuri kupita Watumishi Housing lakini bado. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie uwezekano wa kuitumia benki kama TIB, maana sitaki kurudi nyuma tuiofufue Tanzania Housing Bank, lakini TIB iwe na mfumo wa kuhakikisha tunawezesha wafanyakazi kujenga nyumba zao, iwe ni security kwao na ni security pia kwenye maeneo yetu ya kazi. Haya mambo ya uwajibikaji na rushwa hayataweza kuisha kwa sababu kila mtu atataka kujenga na nyumba leo imeonekana ni moja ya vitu vitakavyo msaidia kama retirement. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo mazuri ningeshauri hilo, pia kwa Polisi wamekuwa wakihoji, Polisi peke yao ndio ambao hasa kuanzia Inspector, wanatakiwa kustaafu wakiwa na miaka 55, Magereza na Immigration wao wanaenda mpaka miaka 60, sasa wanasema kunini, na wao ni watu wanaofanya mazoezi wako fiti, wanaomba liangaliwe hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la viwanja vya michezo, mimi nina mambo mawili pale, kwanza niipongeze Serikali pamoja na masuala ya nyasi bandia, kwa mfano wa viwanja vya Halmashauri, tunavitumia kama chanzo cha mapato na mambo mengine mengi yanafanyika pale, vikiwekwa viwanja vya nyasi kidogo vinakuwa haviwezi kutumika kwa michezo mengine na vitu vyengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ile mliyosema kwa majiji sita haya majiji ndio yenye viwanja. Hebu tuangalieni halmashauri zenye maeneo kama Moshi, tunauwanja wa majengo, Waziri Mkuu alifika pale akasema atatusaidia, sisi tuko tayari tumeshachimba maji na tumshafanya grading na tumeshaanza juhudi za kuweka majani na tumetenda milioni 300, hebu njooni muanze na sisi, na sisi wenyewe tutakuwa jiji karibuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana eneo la madini wamefanya vizuri sana, na nimeona kuondoa VAT kwenye kwenye yale madini ambayo yatakuja kubusti viwanda vyetu vile vya uchenjuaji ni hatua nzuri sana. Niongezee tu Serikali iunde kamati ya kwenda kushawishi sasa zile nchi ambazo hayo madini yapo ili yeje yachenjuliwe hapa, ili kubust export yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazo ambalo nimeona litatusaidia kuhakikisha vile viwanda vya uchenjuaji vinafanya kazi vizuri. Mwisho kabisa nilishaongelea tena suala la kuangalia kuunganisha bandari, reli na yale maeneo ya muhimu ya kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona mda umeisha nashkuru sana naunga mkoni hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia kwenye taarifa hii ya Kamati ya Sheria Ndogo nanikushukuru sana kwa nafasi ya kuniteua kuwa katika Kamati hii, na nikiri imekuwa ya manufaa sana kwangu hasa ukilinganisha kwamba mimi nilikuwa Diwani miaka 10; kwa hiyo, chini kule niliona sheria hizi zinapoanza, na namna zinakuja kuhitimishwa huku juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nitakwenda kwenye ujumla tu; la kwanza ambalo limeongolewa na watu wengi ni lile suala la ushirikishwaji wa wadau. Kuna upungufu mkubwa sana, yapo mambo mengi ambayo Kamati inafanyia kazi lakini wadau wangeshirikishwa tangu awali wala hayo mambo yasingetakiwa yatufikirishe sana kwenye hizi ngazi za juu. Kwa hiyo ninaomba sana sheria ndogo hizi hasa za Halmashauri ushirikishwaji wa wananchi usiangalie tu ile ya kutoa matangazo kwenye mbao za matangazo, lakini viko vikao vya chini kama vikao vya mitaa ambavyo sheria hizi zikipelekwa na wataalam wakitoa elimu kule basi mambo mengi yanaweza yakajaziwa nyama na mengine yakarekebishwa kabla ya kuja ngazi za juu na kuja kwenye Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sura nyingine ambayo inaonekana kwa haraka katika kodi nyingi ambazo tumeziona hasa za Halmashauri ni position ya watu wawili ambao wanahusika na utungaji.
Mheshimiwa Spika, wataalam inaonekana wao wanakuwa na pressure ile ya kuongeza mapato kwa hiyo wanakuwa wanazijazia tu mapato unakuta kuna mahali tuliona sheria imeletwa eti kuuza dawa za kienyeji kuwe na tozo kwa siku shilingi 1,000/shilingi 5,000; hizo dawa za kienyeji ukiangalia zingine hata hayo makusanyo ya siku hayafiki hiyo shilingi 5,000. Kwa hiyo, kunakuwa na ile presha tu ya kuhakikisha kwamba watendaji wanataka kukidhi kiu ya kupandisha mapato na inapoenda kwa pressure na kwa viongozi kama Madiwani nayo inapita basi ikija huku uhalisia unaonekana hauwezekani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nadhani inahitajika wakati makundi haya mawili kwa maana ya kwamba watendaji pamoja na wawakilishi waangalie uhalisia wa ukusanyaji wa kodi kwa sababu baadhi ya kodi ilionekana, hata gharama yake ya kukusanya ni kubwa kuliko kile ambacho kinahitajika kuja kuwa kinakusanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini lipo suala lingine ambalo limekuwa linaleta matatizo sana kwenye Sheria Ndogo za Halmashauri, baada ya vile vitambulisho vya ujasiriamali wapo watu ambao wanakuwa excluded kabisa kutokana na ile definition kwamba turnover yao haizidi shilingi milioni nne. Lakini unakuta halmashauri nyingine wamewaleta hawa na kuwatungia sheria ambayo inawatambua katika kutozwa tozo mbalimbali. Sasa ukiangalia inakinzana na ile sheria au definition ya vile vitambulisho vya wajasiriamali wadogo. Kwa hiyo unakuta kuna muingiliano wa sheria mbili katika sehemu moja.
Mheshimiwa Spika, niongelee kidogo suala la filamu; tumepata matatizo sana kwenye sheria ile. Pamoja na mambo mengine, inasemekana waigizaji wetu wakitaka kuigiza kwa mfano kama polisi, wakaombe kibali polisi ili kuvaa zile nguo zinazofanana na polisi au jeshi. Lakini hata kutumia maeneo yanayofanana na ya Serikali wanasema inakinzana na usalama.
Mheshimiwa Spika, sasa wenzetu wanatengeneza mpaka maeneo ya bandia, hawa wa kwetu hawana uwezo huo, lakini sheria na kanuni unakuta zimewanyima kuingia huko na kama unavyofahamu, filamu ni jambo la kimataifa, zinakwenda kushindana na filamu nyingine. Sasa unakuta filamu zetu watu wanakuwa ni polisi lakini amevaa kama mwanamichezo, kwa hiyo uhaliasia unakuwa hauwezi kuonekana kwa sababu ya masharti ambayo tunaweka ambayo hayawasaidii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata kwenye mavazi, wadau walipokuja walituuliza swali ambalo pengine nafikiri hata Wabunge watashangaa; walisema masharti yamekuwa magumu kana kwamba inabidi hata mtu anayekwenda kuogelea kwenye filamu ya Kitanzania aogelee na hijabu. Sasa inaleta shida, ushindani kwenye soko la kimataifa, filamu zetu haziwezi kushindana na zile nyingine kwa sababu ya masharti ambayo tunajiwekea wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa kifupi kabisa huo ndiyo mchango wangu, na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, na mimi nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mjadala huu wa Kamati ya Sheria Ndogo, lakini kabla sijaenda mbele na mimi pamoja na kwamba ulishakataza kuendelea kukupongeza, basi nichukue nafasi hii kukupongeza wewe pamoja na Naibu Spika kwa ushindi ambao mliupata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeze Kamati nzima lakini kipekee nimpongeze sana Katibu wetu wa Kamati ambaye amekuwa, akitengeneza majedwali ambayo yanatusaidia sana katika uchambuaji wa Sheria hizi Ndogo. Niwapongeze Serikali haswa Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao walikuja mbele ya Kamati pamoja na watendaji wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakwenda moja kwa moja kwenye maeneo machache; nianze na la wadau. Ni muhimu sana kwa upande wa Serikali wanapokuwa wanaanza huu mchakato wawashirikishe kwa karibu wadau. Wadau hawa ambao wako field wanakuwa na uzoefu mkubwa na wamejawa maarifa ya kile ambacho kinaweza kufanyika kule kwenye field. Naweza kutoa mifano michache ilipokuja Tume ya Taaluma kwa Walimu (Teachers Professional Board), tuligundua kuna wadau wa muhimu sana ambao walikuwa hawajashirikishwa. Wengine ni wale walioko on the ground, lakini wengine ni Taasisi, ambazo zinawasaidia sana waalimu kama vile HakiElimu na nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini umuhimu wa wadau uliendelea kuonekana wakati tunapitisha sheria na kanuni za wavuvi ilionekana kwamba sheria iliyochukua usawia katika maeneo yote kuna tofauti kubwa sana kutekeleza sheria hiyo katika water bodies zetu. Kwa mfano, sheria iliyokuwa inataja urefu ambao aina fulani ya samaki wavuliwe ilionekana inafaa Ziwa Victoria, lakini Ziwa Tanganyika lenye kina kirefu katika urefu huo hupati hata samaki hao. Kwa hiyo, ni muhimu kuwashirikisha wadau kwa upana wao ili waweze kuleta ule utaalam na uzoefu wao pale uweze kuleta tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna wakati wadau ni Wizara nyingine na wakati Wizara moja inatunga sheria hizi au kanuni hailazimiki kuwasiliana na Wizara nyingine. Mfano, wakati Bodi ya Filamu wanaleta tozo zao kwa ajili ya maeneo ambayo yanaonyeshwa filamu kwa sababu tulikuwa tumeshapitisha sheria za Halmashauri mbalimbali ambazo nazo zilikuwa zimeweka tozo hizo tuliwashauri Wizara hizi mbili kukutana ili kuleta uwiano, kwa sababu mwisho wa siku mzigo mzito ulikuwa unakwenda kumdondokea yule mwananchi wa chini, lakini vilevile tumeelezea suala la umuhimu wa kuangalia uzoefu au uwezekano wa utekelezaji wa sheria.
Mheshimiwa Spika, zipo Halmashauri zilileta Sheria ya kuwatoza kwa mfano ma-mc kwenye sherehe na wanatoza kwa tukio. Tulipoangalia sheria kama hizi tukaona ni vigumu kwa watekelezaji wa sheria hii kuzunguka usiku kwenye kumbi za starehe/sherehe kuhakikisha kwamba ma-mc hao wamelipa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, badala yake tukaishauri waweze kufanya tozo moja kwa mwaka inakusanyika na haimlazimishi kwenda kuzunguka usiku kwenye kumbi za sherehe na pengine watu wanaweza wakawa wanafurahi wakawaletea matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala la utekelezaji wa makubaliano tunayokuwa tumekubaliana na urejeshaji wa kilichofanyika. Wizara nyingi zimekuwa zikichelewa kuleta utekelezaji, nyingine kutokuleta kabisa lakini nyingine kuchelewa. Ikumbukwe baadhi ya sheria unakuta zimeshaanza kutumika kabla hazijaletwa kwenye Kamati yetu. Sasa tunapotoa maoni na yanachelewa kuletewa marejesho au kufanyika na mengine kutokufanyika kabisa yanaleta matatizo makubwa sana katika utekelezaji wa sheria hizi ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nikomee hapo na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia. Nami leo sitahangaika na mambo makubwa sana ya Kitaifa, bali nitaenda kwenye mambo ya kawaida ambayo yatatusaidia kusonga mbele kama jamii. Nakubali na naipongeza Serikali, na ninajua kinachoisukuma Serikali kwa sababu tunayo matatizo mengi, kwa hiyo, kila hatua inayofanyika ina ahueni upande fulani. Katika mpango, yale maeneo matano ya kujikita, kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na mwisho kabisa kuendeleza rasilimali watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa upana wake, huo ndiyo uhalisia wa yale ambayo tunayahitaji kama nchi. Tunachokikosa ndani, ni namna tunavyoweka vipaumbele. Hii nikawaida, ukiwa na matatizo mengi; kwa mfano, una njaa, wakati huo huo una kiu, wakati huo huo kichwa kinauma, wakati huo huo hujaoga, kila solution unaiona ni ya maana, lakini kuna solution ambayo ikija itasaidia hizo nyingine kuweza kushughulikiwa. Yaani kuna vile vipaumbele. Kuna mzungumzaji mmoja alisema tunakosa ufungamanishaji wa mipango ya Wizara moja na Wizara nyingine. Wengine wakaja mpaka na mpango wa kurudisha ile Big Result wengine wakasema tuwe na Tume ya Rais ya ufuatiliaji wa matokeo, lakini mimi naona haya yote ni mle mle.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa namba 19 wa hotuba ya Waziri, ameongelea sekta binafsi ameweka na takwimu. Sote tunajua kwa hawa watu wote milioni 61 Serikali haijaajiri hata milioni moja. Kitu kinachoweza kuajiri watu wengi ni sekta binafsi. Sasa ni nini kifanyike kwenye sekta binafsi ili iajiri? (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, sasa kwenye sekta binafsi, ukiangalia leseni unazotakiwa kuwa nazo kufungua biashara, mfano biashara ya hoteli; kuna leseni sijui, kuna TALA kuna OSHA, kuna TRA hapo, kuna fire kuna NEMC, TFDA, TBS sijui huko halmashauri ukiacha leseni, kuna leseni za vileo, halafu zote unakuta mtu amezi-frame, ameziweka kwenye ukuta, hata nafasi ya kuweka decoration hakuna. Kwa nini usiwe na mfumo ambao unapoenda Manispaa, hivi vitu vingine vyote vimeunganishwa? Kwa hiyo, unalipia tu una-tick na inakuwa ndiyo precondition ya leseni kutoka badala ya kila mamlaka kujichukulia jinsi inavyotaka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa zaidi ni procedure ya kuzipata hizo leseni. Kwa mfano, NEMC yenyewe, process yake na gharama za ile Certificate ni shughuli hasa! Kuna baadhi ya Taasisi huelewi; wanakuja watu wa OSHA na Fire kwa pamoja, na wote wanaangalia mfumo wa umeme, wote wanaangalia uokozi kama ikitokea dharura, wote wanachukua hela na wote wanaongozwa na sheria tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, OSHA inatoa namna ya kupata leseni yao. Ukipata inasema, ulipe baada ya siku 30. Ila ukienda kwenye kanuni iliyotungwa na Waziri ni kwamba baada ya siku 30 kama hujalipa unachajiwa asilimia tano ya lile deni kila siku. Maana yake ni nini? Huyu mtu anayejipanga amechelewa kulipa unam-discourage kabisa hata kulipa, lakini je, hizi shughuli za OSHA zinafungamana moja kwa moja na uzalishaji wa hizi biashara tunazoziongelea, jibu ni hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha huu usumbufu kwenye biashara, ukienda kwenye Deni la Taifa ambalo tumeambiwa limefanyiwa auditing limeonekana tuna uwezo nalo, ni nini kinaelekeza Serikali ikope kiasi gani na kwa ajili gani? Hatuna, kwa sababu hatuna yale maeneo ambayo tumeyatenga. Kwa mfano, hivi kweli katika nchi hii ambayo tunataka wafanyabiashara, tunataka wawekezaji wa nje, bado maji ya kunywa ni shida kwa watu, maji ya kuoga ni shida kwa watu, bado umeme ni shida kwa watu huyu mwekezaji anakuja kufanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni nchi ambayo tuko katika Maziwa Makuu, tuna mito ya kutosha, tuna kila resource iliyoko karibu na sisi. Kwa nini hili Deni la Taifa tusiweke dheria ambayo inasema kwa miaka mitano mkopo wowote ambao tutachukua uelekezwe asilimia fulani kwenye maji na umeme kwa miaka mitano mpaka hilo tatizo liishe. Tujue kabisa kwamba umeme na maji sio tatizo tena kwetu ili tuwaite hao wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Ardhi, ni kweli tuna rasilimali nzuri sana ya Ardhi, nafikiri sisi tuko vizuri sana uki- compare na wenzetu wa Afrika Mashariki ukiacha Congo. Hata hivyo kwa jinsi tunavyotumia hii ardhi hatuna maeneo tuliyotenga kuendana na advantage za kijiografia kwa ajili ya matumizi fulani. Sehemu ya makazi iwe makazi, kilimo iwe kilimo, kila mahali wanafanya jinsi wanavyoona. Nitatoa Mfano Mkoa wa Kilimanjaro, eneo lililokuwa zuri zaidi kwa kulima kahawa ni kule chini pembezoni ya mlima lakini huko ndiko tumejenga zaidi. Eneo lile la tambarare ambalo hakuna mvua, hamna udongo wa volcanic tumepaacha ndiyo kwa ajili ya mashamba ambayo yatanyeshewa na nini? Kwa hiyo hakuna Mpango wa Serikali unaosema maeneo haya yatakuwa ni ya kilimo tu, maeneo haya yatakuwa ni ya kazi hii tu na mwisho wake tumebaki na EPZ zile ambazo tumeziweka kati kati ya miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna solution niliiongelea juzi, mikopo chechefu ndani ya nchi. Ile mikopo chechefu tunavyoiangalia sio kwa ajili tu ya zile biashara au zile benki kukosa hela, lakini inawapa watu umaskini. Mtu anakuwa na access ya kukopa kuliko uwezo wake wa kurudisha, maana yake ni kwamba atashindwa kui- manage ile hela, ataingia kwenye madeni, ndio unaona kila siku mikopo yetu hailipiki. Nilisema ni rahisi kuwa na system ambayo itai-connect TRA, mahesabu ya wafanyabiashara, lakini ita-connect NBAA kama Msimamizi Mkuu wa Mahesabu lakini na hizo benki, yaani kwamba ukiangalia tu mtu anataka kukopa bilioni moja, ukiangalia kodi zake anazolipa kwenye biashara zake ina- justify, ukiangalia mahesabu ambayo amepeleka NBAA yana-justify.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi tunakuwa na vitabu vingi, yaani NBAA hao ambao ni certified account anatengeneza kitabu anaki-certify hicho ni kwa ajili ya TRA, anatengeneza kingine anaki-certify hicho ni kwa ajili ya benki na kingine hata ukitaka cha kwako cha nyumbani anakutengenezea. Sasa sio mfumo, hatuendeshi uchumi kwa namna inyotakiwa. Kwa hiyo nashauri sana hiyo mifumo iunganishwe ili iweze kuleta tija kwa hawa wafanyabiashara na hata hizo taasisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni huduma za uokozi, hii lazima tukubaliane. Ni kichocheo pia kwenye uchumi hasa kwa wawekezaji wa nje. Nakumbuka at one time Dubai waliendelea sana wakiwa na maghorofa makubwa, wakawa challenged na fire and rescue services waliyokuwa nayo. Hawakuwa na fire ambayo inaweza ikafika ghorofa ya 100 wakati wakiwa na hayo majengo. Sina hakika hata sasa hivi kama Dar es Salaam tuna gari la fire ambalo katika zile ghorofa tulizonazo pale, moto ukitokea juu kuna mechanism ya kuuuzima. Hiyo ni kichocheo cha namna ya kuwakaribisha wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda wangu umeisha, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya mimi pia kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kusema kwamba ninaunga mkono hoja, ikiwa ni pamoja na haya nitakayokwenda kuyasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuchangia mimi nitakwenda kwenye mfumo wa kurasa ili niweze Kwenda haraka. Ninaanza ukurasa wa 13, ambapo kwenye hotuba wameongelea Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi. Napongeza sana hatua hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna matatizo. Mashirika haya ya Serikali ambayo yanafanya biashara yamekuwa hayafanyi vizuri. Mfano mzuri ni pamoja na kile Kiwanda cha Ngozi ambacho kipo pale Moshi Mjini, ambacho kilitakiwa kiwe kinaajiri angalau watu 3,000; na kwenye mnyororo wake wa faid ampaka watu 10,000. Hata hivyo mpaka sasa kimeajiri watu 250 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili hizi taasisi za kibiashara za Serikali zifanye vizuri ni vizuri namna ya kuwapata viongozi wake isiwe kwa namna ya uteuzi na badala yake tuwe tunawatafuta kutokana na merits, uwezo na competence yao kwenye hizo fields. Kwa kufanya hivyo viwanda hivi vitafanya kazi vizuri. Kwa hiyo kwenye hiki kiwanda kinachoanzishwa, ikiwa ni pamoja na vingine watu wapatikane kwa merits ili waweze kuviendesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende ukurasa wa 14 na ukurasa wa 45 ambao umeongelea viwanja vya ndege. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Yetu Samia Suluhu Hassan. Moshi Mjini tunarekebisha kiwanja chetu cha ndege ambacho ni muhimu sana kwa Moshi Mjini, Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na nyanja mbalimbali ikiwemo utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilete ombi; kuna nyumba ambazo zilivamia eneo lile; baadhi zina hati na nyingine hazina hati. Niombe, ili kuleta tija zaidi kwenye ule uwanja vile viwanja tutafute namna ya kuvifidia wakati huu ambapo mradi unaendelea ili kiwanja kile kiweze kupanuliwa katika kiwango kinachotakiwa kuwezesha mpaka hizi ndege hizi za bombardier kutua pale na kuleta tija zaidi. Kwa hiyo, kwa sababu ujenzi unaendelea ni rahisi kwa Wizara kuweka fidia pale kwa baadhi ya zile nyumba ili kuweka sura ile inayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendele ukurasa wa 41, na hili linaendana sana na swali ambali nimeliuliza asubuhi kwenye maswali ya nyongeza. Kwenye matumizi bora ya ardhi, pale kwenye ukurasa wa 41, hotuba imeelezea vizuri sana; lakini kuna maeneo ambayo yanahitaji kupewa kipaumbele zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Moshi Mjini ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 58. Tulishaleta maombi yaliyopita kwenye michakato yote, ya kuongeza eneo eneo mpaka kufikia kilometa za mraba 142, na tulishapata GN No. 219 ya tarehe 15 Julai, 2016. Mchakato ule ulisimama. Nimeshaandika barua nimepeleka kwa Waziri Mkuu, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI ili kuomba huo mchakato tu kwanza wa kupanua ile mipaka ukamilike. Tunaomba hivi kwa sababu ninavyoongea hapa sasa hivi Moshi Mjini tumekosa eneo la dampo, tumekwenda kununua eneo Moshi Vijijini ndiko dampo letu liliko. Pia makaburi yetu yanajaa, tutalazimika Kwenda kununua tena maeneo mengine ya makaburi na huduma nyingine za wananchi ilhali tayari kuna mchakato ulishafikia sehemu nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme, kwa pale tulipo sasa, kwa sababu ni padogo sana hata pato letu haliwezi kuongezeka, hata eneo la viwanda haliwezekani kwa sababu viwanja vinakwenda pembezoni. Hata hivyo, zaidi ni kwamba yale maeneo ambayo tuliyaweka kwenye master plan ya kipindi cha nyuma, kwa ajili ya kupanua, tayari yanaendelea kuvamiwa na kujengwa kiholela. Si tu kuvamiwa, watu wanauza na yanajengwa kiholela. Maana yake ni kwamba hata mtakapokuja kuturuhusu kupanuka tutapanuka kuendana na maeneo ambayo hayajapangika vizuri. Kwa hiyo ninaomba sana hili la Moshi Mjini mlichukulie kwa uzito wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende ukurasa wa 51, umeeleza vizuri sana juu ya elimu, na mimi hapa nitagusa Wizara zote mbili, Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI kwa sababu ni suala ambalo linagusa kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Moshi Mjini tuna Shule ya Sekondari ya Mawenzi, ni shule nzuri, ina miundombinu mizuri na ina eneo kubwa. Shule hii ina mchanganyiko. O-Level wako day lakini A-Level wako boarding. Ninaleta ombi, Wizara ionge namna ya kuifanya shule hii iwe na boarding kuanzia O-Level mpaka A-Level. Hii ni kwa sababu kuna eneo kubwa hivyo itakuwa miongoni mwa shule nzuri kama zilivyo Shule ya Moshi na Shule Moshi Tech. Kwa hiyo tunaomba sana watuwekee mabweni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini shule mpya tuliyoijenga, shule ya Msandaka ambayo iko pembezoni kidogo, nayo Halmashauri tumetenga zaidi ya milioni 150 kwa ajili ya mabweni. Tunaomba Wizara sasa nayo iangalie ili tuongeze shule hizi za mabweni katika manispaa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye ukurasa wa 61 na 62, kumeongelewa masuala ya kazi, wafanyakazi na mifuko ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vya Serikali vilibinafsishwa. Kiwanda cha magunia, Kiwanda cha Moshi Leather, kiwanda cha utilization; wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi kwenye hivi viwanda wakati vikiwa vya Serikali hawajawahi kulipwa mafao yao na wanaendelea kudai. Wanasumbuka kuja ofisini kwangu kwa makundi kila siku, na wengine mpaka wameshaaga dunia wakiendelea kudai. Naomba Serikali ifanye mpango, iangalie namna ya kutafuta fedha ili kuwalipa waliokuwa watumishi wa mashirika ya umma yaliyobinafsishwa ambao wanatangatanga, hawapewi hatima yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 62 ni kuhusu mifuko ya jamii, nako kumekuwa kuna usumbufu mkubwa usio wa lazima. Baadhi ya watu wanapokuwa wamemaliza muda wao wa utumishi, wengine ni watumishi wa Serikali, kama walimu, unakuta amestaafu kabla hajapandishwa daraja. Anapokwenda kutafuta daraja lililokuwa haki yake anazungushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, wastaafu hawa ambao wameshaitumikia Serikali wanapopata huu usumbufu kwa kweli wanatupa picha mbaya sana kw ahata hawa wanaotumika sasa hivi kuona kwamba unaweza ukatumikia kwa moyo lakini mwishowe ukaja ukapata mateso.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 65 ni kuhusu uwezeshaji wa wananchi kiuchumi; nilishaliongea mara nyingi na ninashukuru sana Mheshimiwa Rais ameona twende kwa njia hiyo. Hii mikopo ambayo hairejeshwi ni kwa sababu ya watu tuliowapa kazi hiyo, Maafisa Maendeleo ya Jamii hawana utaalam wa ku-assess mradi, kukopesha na kwenda kuchukua mkopo huo. Ninaungana moja kwa moja na wazo la Mheshimiwa Rais kwamba tutafute benki ambazo tutawapa hizi kazi na sisi tuendelee kuwa wasimamiaji wakuu na kusiwe na interest wala collateral kama ilivyo, ni jambo linalowezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 69 na 73, kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na mapambano dhidi ya dawa za kulevya; kwa bahati mbaya hapa nitatumia lugha ambayo si rafiki sana. Kwa hii rushwa tunayoona, kwa haya mazingira tunayoyasikia kutokana na taarifa ya CAG suala ya rushwa tuchukue njia waliyoichukua China, tutoe adhabu kali zaidi, miaka 30, 40, 50, hata ikibidi adhabu za kunyongwa, kwani tunachoogopa ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku tulikuwa na mjadala kuhusiana na adhabu ile ya kubaka. Mtu akibakwa afanywe nini miaka 30, mmoja wa watu waliokuwa wameshiriki ile washa akasema hapana ni kubwa mno tukamwambia basi wewe umejiandaa kubaka. Kama wewe unaona adhabu hiyo ni kubwa umejiandaa kufanya hilo tukio. Hili suala la rushwa, suala la madawa ya kulevya tupitishe sheria hapa itakayoweka adhabu kali, miaka 30, 40 na ikibidi kunyongwa kwa wale wanaoshiriki ili tukomeshe, kwa sababu tunapoona aibu kusema hivyo maana yake hawa wanaokosa hizo haki nao wanateseka na wengine wanakufa kwenye mahospitali na kwenye maeneo yetu ya haki. Kwa hiyo, mimi nimeona nichukue njia hiyo ngumu kuishauri Serikali tufikirie suala hilo kwa njia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 83, kuna ukatili dhidi ya watoto. Nashukuru sana kwa sababu maazimisho ya Dawati la Jinsia Kitaifa yalikuja kuzinduliwa Moshi Mjini na taarifa iliyosomwa na Waziri wa Kisekta Dkt. Gwajima, ilionesha katika asilimia 100 ya watoto wanaofanyiwa ukatili, asilimia 60 wanafanyiwa nyumbani na kwa sababu nyumbani wanafanyiwa na ndugu na kama ni ndugu maana yake kesi haziendi mahali. Sasa tuna kitu cha kufanya, ni lazima tutafute namna bora hata ikibidi tuwe na namba maalum ya watoto kuweza kuifikia, wakifanyiwa ukatili waweze kutoa taarifa na inapoonekana ni ndugu, sisi Serikali tuichukue sisi na sio ndugu, maana ndugu wanaombana msamaha, wanamaliza wakati mtoto anakuwa ameshaharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe na njia ya kuhakikisha tunawalinda hawa watoto. Haya madhara ambayo tunayaongelea ya hii tabia inayokuja pengine wengine wanalazimika kwenda kwa sababu walishafanyiwa ukatili, wakaona ile ndio njia. Kwa hiyo nashauri sana kwenye ukatili huu wa Watoto, tuwe na namba maalum ambayo watoto wanaweza kuipiga lakini tuwe na uwezekano wa kubadilisha sheria nazo ziwe kali na hata ikibidi tunaweza tukafanya vitu ambavyo kimsingi vitaonekana sio vizuri. Kwa mfano, hakuna sababu ya ndugu ambao wameshafikia umri wa mature kuendelea kukaa na kulala chumba kimoja na watoto wetu, tunaamini kwamba ni ndugu hawatawadhuru lakini taarifa ndio hiyo imetoka asilimia 60 wame…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa mwisho na nitajitahidi niende kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Wizara kwa juhudi zao hasa Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri wake kwa kweli wako field muda wote na nimekuwa nikiwafikia mara kwa mara. Niwashukuru pia watendaji, ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu na Dkt. Ntuli ambaye anashughulikia masuala ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee yale ambayo tumeshafanya hasa kwenye barabara ambapo sisi tuna mradi wa TACTIC kwenye Jimbo la Moshi Mjini ambayo ilichelewa kwa mwaka mmoja lakini tunategemea watalisukuma ili mwaka huu basi liweze kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye hospitali ya wilaya kuendana na jiografia yetu tulishapewa milioni 500, lakini kutokana na ufinyu wa maeneo sisi tunajenga gorofa, tumeleta ramani kwao wameshapitisha, tuliomba watuongezee ili fedha ya kuanza ili ile fedha ya kwanza kitu kitachowekwa pale kiweze kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye kituo cha afya wametupa milioni 250, Naibu Waziri Mheshimiwa Silinde alikuja aliona namna tunavyokwenda kwa kasi, tunaomba basi ile 250 ya kumalizia nayo iweze kufika ili tuweze kukamilisha kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kwenye shule, ambayo tunaijenga kwenye Kata ya Msalanga, ile milioni 470 tumeifanyia kazi vizuri, tunaomba sana sisi tumejipanga kwa kutumia nguvu za wananchi, tuanze kuongeza mabweni. Sasa tunaomba juhudi hizo za wananchi zikianza, kwa sababu kati ile iko pembezoni, basi Serikali iangalie namna ya kutuongezea, ili basi tuweze kuwa na mabweni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeenda kwenye suala la Wamachinga, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hatua aliyochukua kwa ile incident ya Mwanza. Nimwambie maeneo yote yenye Wamachinga kumekuwa na tabia hiyo ya kuwanyang’anya watu vitu na sidhani kama ni njia nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, kule Moshi, kuna watu walikuwa wanauza mabegi, walinyang’anywa na wanapofanya ile operation wananchukua maeneo yote. Sasa inapokuja kwenda kuwarudisha, vile vitu wanavyovichukua hawaandiki vitu gani ni vya nani? Tunawasababishia wale Wamachinga umaskini na sioni sababu ya kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu au mawazo yangu, ni vizuri wawatumie wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwenye hizo operation, wanawafahamu wale watu na vitu vyao ili vinapochukuliwa, baadaye itakapobidi kuwarudishia basi warudishiwe vitu vyao, lakini kuvichukua na kupotea, ni sawasawa kabisa na kusema Serikali inawanyang’anya wananchi mali zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye kuwapanga, naamini tukiweza kuwatumia Wenyeviti wa Serikali za Mtaa tunaweza kuwapanga vizuri badala ya kuwa na zile operation za kuwanyemelea kuvunja na kuchukua vitu na kuvipoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masoko mbalimbali, tumekuwa na incident za kuwaka moto masoko. Ninawazo ambalo nadhani linaweza likasaidia, kwa nini tusibadilishe mtindo wa ujengaji kwenye masoko haya ambayo siyo rasmi, badala ya kutumia mbao tutumie chuma ili kupunguza haya matatizo yanayotokana na moto ambao unajitokeza mara kwa mara. Kule Moshi umetokea lakini bado watu wanarudia kujenga kwa kutumia mbao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba hilo mliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mradi wa kimkakati wa stendi pale Moshi, mradi ule umesimama kwa muda mrefu, ningeomba Mheshimiwa Waziri anapohitimisha aangalie namna ya kusaidia miradi hii ya kimkakati ambayo ilikuwa kwenye halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, stendi yetu ya Ngaka – Mfumuni imesimama na hakuna kinachoendelea.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa Mtemvu, taarifa.
T A A R I F A
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji wakati anamalizia kuzungumzia juu ya masoko ya kimkakati, pamoja na stendi. Tunalo soko ambalo ni sambamba na stendi pale Mbezi Louis ya Magufuli, mpaka sasa tunatambua stendi ile inaingiza takribani bilioni 50 za Watanzania za ndani lakini bado haijakamilika, kwa sababu ya VAT na kadhalika baada ya kutokea kwenye jiji kuja ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo. Tunawaomba sana ili ile fedha za Watanzania zikatumike, zikawe na tija, basi ni vizuri mhakikishe stendi ile inakamilika ili iweze kuleta tija ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea tu kwa sababu ni ndugu yangu huyu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba niende pia kwenye suala kupanga miji, hili linahusisha Wizara mbili, mfano wa Moshi, tulishafanya vikao na Wilaya ya Hai, pamoja na Moshi Vijijini kupanua maeneo. Sasa kwa sababu inahusisha TAMISEMI pamoja na Wizara ya Ardhi, imeendelea kuwa na mkwamo mkubwa na matokeo yake ni nini yale maeneo ambayo tulikuwa tupanukie yameendelea kujengwa bila mpangilio, kwa sababu kule hakujawa mjini, kwa hiyo, kumekuwa na slums zinatokea kule na baadaye tukija kupanua mji, basi tunaenda kurasimisha maeneo ambayo hayatakuwa na miundombinu wowote. Sioni ugumu wa kuongeza yale maeneo ya kiutawala na iwe hivyo kwa miji yote ambayo inakuwa, tuwe tuna plan ahead, bada ya kuwa ya slum ambazo kila mara tunazirasimisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala ambalo liko TAMISEMI, lakini linahusisha pia ajira, watu wa bodaboda. Bodaboda ni ajira rasmi na kama ni ajira rasmi ni vizuri wale watu waendeshaji ambao sio wamiliki na wale ambao ni wamiliki wanaendesha waweze kuingizwa kwenye mfumo wa WCF kwa kuwatumia TAMISEMI, kwa nini nasema hivyo? Hawa watu ndio wanapata ajali sana na wakipata ajali, wamekuwa ni mzigo kwenye matibabu yao, wangeweza kurasimishwa wakawekwa kwenye Mfuko ule wa WCF, wanaweza kutibiwa na kupata fidia pale wanapopata ajali badala ya hali ilivyo sasa ambao wanakuwa mzigo kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, pamoja na watu wengi kuongelea kuwaongezea posho Madiwani pamoja na Wenyeviti, hili ni la muhimu sana, lakini tuangalie kwa upana. Isipokuwa ningeomba pia suala la ajira hizi mpya tuangalie zile kada za Walimu pamoja na watumishi wa afya, hasa wale ambao tayari wanajitolea kule ili waweze kupewa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Maliasili na Utalii. Nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuitangaza nchi yetu katika eneo hili la utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alifanya vizuri sana kwenye michezo, lakini kwa historia ya zile Wizara tano ngumu (mifupa migumu) ni pamoja na Maliasili na Utalii. Sisi tunakutakia kila la heri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nianze na janga la moto kwenye Mlima Kilimanjaro ambalo linatokea mara kwa mara. Kwanza, sasa niwape Wizara habari njema kwamba Mheshimiwa Rais ameleta fedha za kukarabati Uwanja wa Ndege wa Moshi, kazi inaendelea, utakuwa ni uwanja wa Kisasa. Sasa ni jukumu lenu kuona ni namna gani mnaweza kuweka huduma za zimamoto kwa kutumia ndege mkishirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ili kupambana na janga lile la moto linapotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri pia mfanye juhudi ya kujua ni nini huwa kinasababisha na ni namna gani mnaweza kuwa mnazuia moto huo kutokea mara kwa mara? Ni muhimu sana mfanye hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii unahitaji investment na ukiangalia nchi kumi bora ambazo zinafanya vizuri sana kwenye utalii, sisi tuko hapo katikati. Ukiangalia gap kati ya nchi ya kwanza inayoongoza kwa watalii wengi ambayo ni Egypt, ukija ya pili ni Morocco ,halafu South Africa na Tunisia ambazo mapato yake yanaanzia dola milioni 13 mpaka Nane hapo kwa Tunisia. Uwekezaji wao kwenye tourism ni mkubwa sana. Tunahitaji katika miaka hii ya Bunge hili Mheshimiwa Waziri uje na mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuna mchangiaji asubuhi alisema kuweka matangazo kwenye timu za mpira. Mimi nadhani wakati mwingine siyo lazima tu-copy kila kitu. Kwa mfano, hapa nchini nafikiri kuna tangazo ukiliweka kwenye jezi ya Yanga unapoteza hata baadhi ya washabiki wa Simba. Tutafute njia ambayo ni inclusive itakayoleta watu wengi kwenye matangazo yetu ambayo tutafanya. Siyo lazima kwenye timu za mpira kwa maana ya jezi lakini angalau uwanjani ili tuvute watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji hauishii kwenye kutangaza. Hapo kwenye kutangaza nitakuja na mawazo mbadala hapo baadaye. Kuna suala la miundombinu, hili sisi tunafeli sana. Barabara ya kutoka Ngorongoro kwenda Serengeti kupitia geti la Nabi, barabara ile hata kama mzungu amekuja hapa kwa ajili ya adventure, pale utakwenda kumvunjavunja, magari yanaumia na fedha hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna project ya kuweka lami kwenye ile barabara ilisimamishwa kipindi cha nyuma, siamini Wazungu wanakuja ili waishi kwenye maisha ya barabara ngumu ya kutingishika na kuumiza magari kama ile ya kutoka Ngorongoro kwenda Serengeti. Hebu liangalieni upya kwa sasa. Wakati mwingine siyo lazima msikilize watu. Hata watu waliosema tusijenge bwawa letu hili walisema ni kwa sababu za kimazingira, lakini hatuwezi kufa kwa njaa kwa sababu eti tunasubiri mbunga ambayo ni world heritage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ile barabara tuangalie, tunaweza kuitengeneza vizuri hata kama siyo kwa lami, bali kwa teknolojia nyingine ambayo haitaleta shida na usumbufu mkubwa. Kwa barabara ilivyo ni hasara kwa magari na kwa wageni wale wanaokwenda pale. Kwa hiyo, kwenye miundombinu ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye Mlima Kilimanjaro miundombinu ni pamoja na zile camp. Camp zile ziboreshwe bila kuharibu mazingira, ziwe na mazingira mazuri. Siyo lazima mtu akipanda mlima basi vyoo anavyotumia vionekane ni vyoo vya hali hafifu, hapana. Tuboreshe mazingira ya Mlima Kilimanjaro kwenye zile camp na tuhakikishe kwamba tunapata wateja wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miundombinu mliongelea suala la vitanda kwenye presentation yenu kwenye semina. Mheshimiwa Waziri, mimi nina ushahidi. Kuna baadhi ya watu wanataka kuwekeza kule kwenye mbuga, kuweka hivyo vitanda tena vya gharama kubwa, lakini kuna baadhi ya makampuni yameshika maeneo miaka mitatu, minne kwa ajili ya kuwekeza na hawajawekeza na hayo maeneo ni potential. Kwa nini msiwafutie hao walioshikilia hata kama ni matajiri ili tuwape hao wawekezaji ambao wapo tayari kuwekeza hata sasa hivi? Hata ukinifuata, nitakuonesha baadhi ya maeneo na hao watu ambao wako tayari. Wenzetu wanakuja mpaka na coordinates. Ukiuliza unaambiwa hili ni la mwekezaji fulani, miaka mitano hajawekeza. Basi tuangalie namna ya kuwekeza hivyo vitanda ili tuwe na vitanda vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye hoteli, ni moja ya kitu kinachosababisha tuwe hatuna wageni wengi. Ninatoa tu mfano wa jumla, ule mkutano wa wanashheria ule wa (TLS) unafanyika kwenye miji michache sana Tanzania kwa sababu gani? Haufanyiki Dar es Salaam kwa sababu wengi wanaishi pale, unafanyioka Arusha kwa sababu kuna vitanda vingi na accommodation ya kutosha. Wakija hapa Dodoma, tayari tuna ukumbi mzuri wa ku-accommodate watu 2000, 3000 lakini watalala wapi kwa hapa Dodoma? Kwa hiyo, suala la hoteli ni muhimu sana katika uwekezaji au ukuzaji wa utalii kama sehemu ya miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, nafikiri Serikali yetu inatakiwa iwe na macho na maamuzi ambayo yamekwenda mbele zaidi. Kwa mfano, kuna hoteli ile ya Ngurdoto Mountain Lodge ambao ni uwekezaji mkubwa wa mzawa, bahati mbaya ameondoka, biashara imekwenda vibaya, Serikali imeacha pale, ajira za watu zimekufa, eneo lile limekufa. Kwa nini Serikali isi-intervene kwa kununua share au kuingia makubaliano na wawekezaji ili tuwekeze eneo kama lile na tuwe na maeneo haya ya utalii ambayo tunayahitaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kwenye miundombinu kuna kazi kubwa sana ya kufanya na siyo lazima wafanye Serikali. Wanaweza kuweka mpango mzuri na wa kuwavutia wawekezaji wakawekeza kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la gharama. Moja ya matatizo ambayo yanaukumba utalii wa Tanzania ni kwamba watalii wanasema destination yetu imekuwa ni ghali sana. Mimi najua moja ya maeneo yenye gharama kubwa ni pamoja na landing fees za viwanja vyetu vya ndege. Hebu tuangalie namna ya ku-harmonize. Tunaweza tukatoa hata holiday ya miaka kadhaa, tukaangalia namna ya kupata hayo mapato kupitia sehemu nyingine ili utalii uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye gharama hizi ni pamoja na mikopo. Wakati ule tumepayta janga la UVIKO niliwahi kutoa wazo, nikasema ni vizuri Serikali iongee na mabenki kwa watu wa utalii iwe kama wakulima, wanakopeshwa lakini wanalipa kwa wakati, kwenye kipindi cha high season. Kipindi cha low season, zile interest na principle zisimamishwe ili waweze kujiweka sawa na season inapoanza waende. Kama wakulima wanavyokopeshwa kwamba kipindi cha mavuno kinajulikana ndipo wanaanza kulipa mikopo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuwapunguzia gharama wawekezaji, maana yake tutaweza kuwasaidia sasa nao wawaajiri wale wafanyakazi wadogo kwa muda mrefu na tukakuza ajira kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilishaliongelea mara mbili tatu ni suala la park fees. Haiwezekani tukawa na park fees ambazo ni uniform tu. Mbunga ambazo zinafanya vizuri, hazina tofauti kubwa na mbuga ambzo hazina watu kabisa. Sasa ni nini tutatoa incentives kwa watu kupeleka watalii kwenye mbunga hizi ambazo hazifanyi vizuri? Tuangalie, kuwe na tofauti kubwa kiasi kwamba mtu ataona nita-save ili aende kwenye mbuga hizi ambazo hazifanyi vizuri. Kwa hiyo, nafikiri hayo ni maeneo ambayo tunaweza tukawekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, manpower ni tatizo kubwa kwa nchi yetu ya Tanzania. Mtu yeyote anaweza akaenda kwenye hoteli zilizopo Zanzibar; asilimia kubwa ya wale wafanyakazi active Zanzibar na porini, ni wale wanaotoka nje kwa nchi jirani. Waswahili unakuja kuwakuta huku chini kwenye kazi ambazo hawa-interact na wageni. Kwa nini tusiwekeze? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, VETA, kwa kweli kwenye kuwaandaa wafanyakazi wa utalii hawafanyi vizuri. Tena kuna mtu aliniambia, Tanzania ndiyo nchi pekee unakuta mpaka mfanyakazi wa ndege ana-attitude, yaani hawezi kukuchekea hata kama ana stress zake. Sasa industry hii inahitaji watu kwanza manpower iende kwenye lugha, wapishi wazuri na hata supporting staff. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Airport zetu na entry point, kwa mfano mtu wa immigration ni vizuri achaguliwe yule mtu ambaye anaweza kuongea lugha vizuri, anawasiliana kwa ukarimu na yuko sharp. Hivyo hivyo, ukienda TRA kwenye entry points kwa maana ya Airport na baadhi ya zile border ambazo zinapitisha watalii. Sasa ukifika kwenye hizi border zetu, watu wenyewe waliopo wana attitude tayari hata kabla hujaingia, hawakaribishi watu vizuri, hawaongei vizuri, lugha inawagonga. Hapo hatujaenda kwa ma-guide, wapishi na hata wahudumu wa hoteli. Kwa hiyo, kwenye manpower ni lazima tuwe na mpango wa muda mrefu wa kuhakikisha tunakuwa na manpower ambayo inaweza ika-support ukuaji wa utalii. Baadhi ya maeneo watu wanakwenda kwa sababu ya manpower tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kidogo mambo ambayo nafikiri yanaweza kusaidia kukuza utalii. Kwenye presentation ya Wizara walisema tuna-deal tu na maliasili, tumeacha uwekezaji. Ni kweli, kwa sababu baadhi ya uwekezaji unahitaji hela, na kama siyo nguvu ya wwekezaji wenyewe, basi Serikali i-intervene. Kuna vitu havihitaji nguvu, vinahitaji advocacy. Kwa mfano, nikimwuliza mtu yeyote hapa ni kwa nini ile cable car ilisimamishwa na nini implication za kusimamishwa na ni namna gani tunaweza kuwa na kitu mbadala pale kwenye Mlima Kilimanjaro ambacho haki-intervene lakini kinaongeza mapato? Hakuna. Hata hivyo, watu wamezuia cable car na wanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo tunaweza kuewekeza. Michezo ya golf, kuna game ilikuwa ifanyike kule Kili Golf, uendeshaji wa baiskeli kama Toure Kilimanjaro tuka-boost kama ilivyo Kilimanjaro Marathon…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hii Bajeti Kuu pamoja na Mpango wa Taifa. Kwa kuanza tu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake, lakini shukrani za dhati kwa Mama Samia kwa suala ambalo tumelipigia kelele, lile suala la bureau de change ambalo wamelifanyia kazi nimeona kwenye ukurasa wa 53 na 54 wa Hotuba ya Bajeti Kuu, lakini inaonekana wamefanyia kazi Arusha peke yake na ameahidi kuendelea kuondoa au kurekebisha vile vigezo ili na maeneo mengine basi waweze kufanya hii biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaipongeza Serikali kwa namna inavyoendelea kusimamia uchumi wetu, uchumi wetu umekua sasa karibu bilioni 85 ikilinganishwa na bilioni 69, ni hatua kubwa na mengine mazuri yanakuja mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mapendekezo maeneo matatu kabla sijaendelea na maeneo yale ambayo nafikiria kuyachangia. Kwenye eneo la mazao nimeielewe vizuri sana nia ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo Mheshimiwa Bashe, nia yake ni njema kabisa na tukimsikiliza tutaona haya ambayo anakusudia ili mazao haya yaje kuonekana kwenye export zetu kwa maana ya thamani zake. Niendelee kumshauri yale masoko ya ukanda huu wa pembezoni wayawekee nguvu sasa, ina maana upande ule wa Namanga upande huu wa kila maeneo yenye mpaka ambayo kunapitisha mazao waimarishe yale masoko na kule Kilimanjaro tulikuwa tuna eneo lile la Lokolova ili haya mambo ambayo ambayo amekusudia ambayo Mheshimiwa Rais amekusudia yaweze kufanyika kwa uzuri zaidi bila kuleta usumbufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa pili ni kwenye kodi inayotaka kuwekwa kwenye cement. Mimi nadhani ukiangalia sensa yetu inaonesha uwiano wa watu na umiliki wa makazi, kwa sababu kwenye dodoso kulikuwa kuna umiliki wa makazi pale, sasa na makazi yaliyoandikwa pale ni makazi ya aina gani, sidhani tumefikia mahali pa kuweka kodi kwenye cement, watu bado wanalala nyumba za tembe ni viizuri tuangalie chanzo kingine hii ya cement tena ilitakiwa tu-subsidies ili watu waendelee kujenga nyumba tutoke kwenye nyumba za Tembe tuwe tunalala kwenye nyumba za cement. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mafuta pia natoa ushauri, sioni kuweka shilingi 100 kwa wote inaleta tija. Hebu Wizara ikae na wataalam waangalie ni namna gani tunaweza tukawa na bei uniform ya mafuta nchi nzima. Kwa sababu kule Kigoma wanalipa bei ghali sana mafuta na wanakipato kidogo, wakati Dar es Salaam wanalipa kidogo sana na Tanga kwa sababu wapo karibu na bahari. Ni vizuri tuangalie uwezekano wa kuzifufua zile depot za maeneo kule Moshi kulikuwa kuna depot, sijui huko Mwanza depot na Serikali iangalie uwezekano wa kuisimamia tuwe na bei moja kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama CocaCola na kampuni za maji wanaweza, kwamba nchi nzima kuna bei moja na kama bei ya usafiri ndiyo inaleta shida Mheshimiwa Bashe alitoa zile pikipiki kwa Maafisa Ugani zimewekwa GPS zote tunaweza kufunga magari yote yanayosafirisha mafuta GPS kuhakikisha kwamba ile gharama haiwezi kutuletea utofauti mkubwa wa bei, tukawa na bei moja ya mafuta nchi nzima ninaamini linawezekana badala ya kuongeza shilingi 100 kwa watu wote wakati watu wa Dar es Salaam mafuta ni bei rahisi, huku Kigoma Mikoani Arusha huko tunapata mafuta ni bei ya juu. Kwa hiyo, nimesema hayo masuala matatu nitoe ushauri ili tuweze kusonga mbele tuone namna ambavyo tunaweza kuboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la utalii. Ninakumbuka kwenye semina ambayo tulifapewa na Wizara ya Utalii walisema Tanzania inategemea maliasili tu kwenye utalii. Pamoja na maliasili ambayo inaleta mpaka conflict kwa baadhi ya maeneo kwa maana ya wakulima sijui na wafugaji na maeneo ya hifadhi maana yake bado tuna nafasi ya kuweka vivutio ambavyo ni man-made. Dubai vivutio vyake asilimia kubwa karibu vyote ni man-made na wanapata watalii milioni 14, 16 kwa mwaka. Sisi na hii Maliasili pamoja na zile changamoto ambazo zimetajwa tunapata 1,400,000 ambayo ndiyo the highest tumepata mwaka 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kwa yale maeneo ambayo tunaweza kuongeza vivutio ambavyo ni man-made ambavyo havina madhara negative kwa jamii yawekwe na ndipo hapo niliposema kwa mfano suala la cable car kuna argument kwamba haina madhara na kuna argument kwamba ina madhara, msimamo wangu na msimamo wa wananchi ni kwamba kama cable car haipunguzi mapato ya Serikali, haiharibu mazingira, haipunguzi ajira, haina madhara negatively kwa mapato ya Serikali wanaihitaji ili iongeze mapato. Kwa hiyo, kama negative impact hazipo tunaihitaji lakini kama zipo basi hilo tunaona haina tija kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kidogo ambacho ninadhani Wizara inatakiwa ikifanyie kazi na ni Wizara ya Viwanda na Biashara, inaingia Wizara ya Afya tuliondoa TFDA tukaweka TMDA lakini aspect ya chakula hasa kwenye import na export TBS hawawezi kuifanya lakini ukiacha TBS hawawezi kuifanya pia siyo international practice, ni vizuri suala dogo kama hili ni suala la uamuzi leteni sheria hapa turudishe TFDA watu wakiweka miguu chini nje kwenye vyakula tunavyo-export hatuwezi kabisa kusimama kwa sababu hatuna TFDA. TMDA hifanyi ile kazi ilikuwa inafanya TFDA na badala yake TBS pia hawawezi kupima vitu kama maziwa haya ya watoto hizi formula, kwa hiyo tufanye tu mara moja siyo kila kitu mpaka Rais aseme ndiyo tufanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mitumba ya nguo viatu ambavyo ni second hand kwenye nchi yetu. Kwa hali ya sasa mitumba inayokuja Tanzania ni ya hali ya chini sana, kwanza wale wafanyabiashara wanapoteza fedha kwa sababu wanafungua mtumba wanakuta nguo zinazouzika ni chache lakini wananchi wetu wananunua nguo nza mitumba za bei kubwa ambazo hazina ubora. Kuna watu wananunua mitumba Kenya wanaileta mpaka Tanzania Mikoa mingi tu, tumeona wana-advertise ni mtumba wa Kenya una ubora zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu katika usimamizi wa eneo hili, hebu Serikali iende iangalie namna ya kulisimamia ikiwa ni pamoja na hizo hatua ambazo mnazifikiria mbele za kuondoa hii, lakini wakati mnai-ban mitumba mhakikishe kuna nguo zinazotoka kwenye hizi nchi zinazo-import zina quality, kwa sababu sasa hivi tuna-import vitu kutoka baadhi ya nchi, zikija hapa tunaambiwa ni Ngozi lakini vikivaliwa siku mbili vimechanika huwezi kulinganisha na vile vya mtumba ambavyo vipo, kwa hiyo hatua ya ku-ban mitumba iangaliwe sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Moshi kuna Kiwanda cha Karanga Leather. Serikali ime-invest billions of moneys zaidi ya bilioni mia moja lakini Serikali haijaweza kusimamia kile kiwanda, kiwanda kinategemea kiajiri watu 10,000 wale wa moja kwa moja 3,000 lakini mpaka sasa hivi kimeajiri watu 250 na hela imeenda pale. Rais kila siku anasema mumwambie Mashirika na Makampuni ya Serikali ambayo hayafanyi vizuri sasa tusiendelee kutengeneza matatizo, kama kuna hao Wabia waletwe waingie kwenye kile Kiwanda cha leather pale Moshi kiweze kuleta ajira, tulete Pato la Taifa na kodi iweze kukusanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kodi ambayo bado sijaweza kupata mantiki yake, kodi tunazotoza kwenye magari chakavu. Ukiangalia dumping ya kwetu haiakisi kusudio la kuanzishwa kwake. Maana ya dumping ilikuwa magari ambayo ni ya zamani sana yasiingie nchini na kwa bahati mbaya dumping yetu ina-charge percentage ya value. Sasa gari linavyozidi kuwa la zamani zaidi, value yake kule inazidi kuwa ndogo kwa hiyo hata kukata percentage maana yake gari ya zamani utaikuta bei ya kufika hapa ni rahisi kuliko gari ya mwaka jana. Hebu tuangalie tutafute dumping ambayo itasaidia magari ya karibuni yawe na bei nafuu kuliko magari ya zamani sana ili ilete tija. Kwa hiyo, magari hapa Tanzania yamekuwa aghari bila sababu na maana yake ni kwamba hatumsaidii Mtanzania, lakini gari lina faida lina mafuta, kuna mambo ya gereji, kuna udereva hapo leseni zinakatwa, kwa hiyo ni vizuri mliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ambayo nimepata ili na mimi niweze kuchangia kwenye mpango wetu huu wa maendeleo wa Taifa. Nami nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, Naibu Mawaziri na wataalam wote walioshiriki kuandaa mpango huu, bila kuisahau Kamati nzima ya bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kabisa kwamba, naunga mkono hoja maana kuna msemaji amesifia vizuri, ametoa mchango wake, amemsifia Rais na akawasifia Mawaziri wanatoka kwake, akashindwa kuunga mkono hoja hii. Nami nikajua ndiyo maana Mawaziri wote wawili wameoa Mkoa wa Kilimanjaro, maana sasa kama huungi mkono hoja kidogo anasababisha waje kule kwetu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kupongeza Serikali kwa namna ambavyo inasimamia mpango huu. Nianze kwa kusema kwamba, kuna maneno ambayo ningetamani sana tuyaone kwenye mpango wetu. Sijayaona moja kwa moja kwenye hotuba na pengine yapo kwenye tafsiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona mahali ambapo tumeonesha nia thabiti ya kwenda kuwa na bajeti ambayo tunaweza kui-fund wenyewe kwa 100%. Sijaona mahali kwenye huu mpango ambapo tunayo nia ya kwenda kuhakikisha bajeti yetu kwa miaka hii ya hivi karibuni, mwaka 2025 tutatoa utegemezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua sasa hivi tuko kwenye 70%, lakini ni lini tutafikia 80%, 90% na 100%? Pia, hata kwenye mapendekezo ya Kamati wamesema na wamelitaja hilo kwamba, ni eneo ambalo na wenyewe wanategemea kuliona, kwamba, angalau sasa katika kila mpango tuseme mpango huu pamoja na mambo yetu yote tuliyoweka, tunategemea utegemezi wa bajeti yetu kwenye mikopo, misaada, mikopo ya nje tutaisogeza kutoka kwenye hii 30%, tutabaki na 10% na kuendelea. Kwa hiyo, hilo nategemea tuanze kuliona kwa siku ambazo zinakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nilitegemea pia kuona ni namna gani mpango huu unakwenda kuongeza tax base. Mheshimiwa Rais wakati anaongea na ile Kamati ya kwenda kumshauri kuhusiana na mambo ya kodi alisema kabisa kwamba, Tanzania wanaolipa kodi moja moja wanaonekana ni milioni mbili tu, sasa nilitegemea kwenye mpango utuoneshe ni namna gani tumekusudia kwenda kuongeza tax base, badala ya kwamba ni watu milioni mbili au taasisi milioni mbili, tunatoka milioni mbili, tunakwenda milioni mbili na laki tano, milioni tatu na kuendelea ili Tax base ikiongezeka, maana yake mzigo wa tax kwa wale wachache ambao wanatambulika utakuwa umepungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye miradi ya kimkakati. Ninaipongeza sana Serikali na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwamba, miradi hii ya kimkakati imeshaonekana tayari inaleta tija. Leo tunaongelea SGR tayari inafanya kazi, leo tunaongelea bandari, wameelezea mafanikio ambayo yalikuwepo kwenye yale maono na tayari yameshaanza kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea Bwawa la Mwalimu Nyerere, juzi nimeona nadhani wale ni songas, mkataba wao umeisha na wala hatuna haraka wala wasiwasi wa kuwaongezea Mkataba kwa sababu umeme tayari tunajitosheleza. Vilevile, naona jinsi ambavyo shirika letu la ndege linavyoendelea kupambana, kwanza, kutoa usafiri ndani ya nchi, lakini kuendelea kupambana kimataifa. Tumeanza safari za Afrika Kusini, Marekani, Uarabuni na nyingine zinakwenda Zanzibar na kadhalika, kwa maana ya kwamba kutoka nje na kuja Zanzibar moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, juhudi za Serikali kuhakikisha Dodoma kama Makao Makuu inaendelea kuwa ndiyo makao makuu ya nchi, inapendeza na tunaona kabisa Serikali inafanya juhudi. Airport inaendelea na miradi inaendelea, kwa hiyo, ninaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii miradi imetupima sana uwezo wetu wa kutekeleza mambo, ili sasa tuendelee tusikate tamaa na tusiridhike ni vizuri sasa ile miradi mingine ambayo inazungumziwa sana LNG, Liganga na Mchuchuma, tuweke timeframe kwamba, ni lini na hii inaingia kuongeza nguvu katika pato letu la Taifa, miradi mikubwa na kuonesha kwamba uchumi wetu unakua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la utalii, kwa sababu Moshi Mjini ni moja ya vituo vya utalii katika Kanda ya Kaskazini, ni eneo la muhimu sana. Nimeona nia ya Serikali kuhakikisha kwamba utalii wa mikutano, utalii wa michezo na utalii wa kimatibabu, unakwenda kujumuishwa katika kutangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye takwimu, kwenye yale majedwali pale, naona kama kuna tatizo. Tumesema tunategemea kutoka watalii milioni mbili kwenda milioni tano, lakini mchango wao kwenye Pato la Taifa, milioni mbili kwenda milioni tano ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya watalii tunaowapata. Pia, expenditure ya kila mtalii kutoka dola 230 kwenda dola mia tano hamsini na kitu kwa mwaka 2026, mchango ni kama mara mbili, lakini mchango wake kwenye pato la Taifa tunasema utatoka 17.5% kwenda 18.9%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa wakati watoa hoja wanaenda kuhitimisha hili wanifafanulie vizuri, kwa sababu kimapato tumesema expenditure ya mtalii mmoja itatoka zaidi ya dola 200 na kwenda zaidi ya 500, tumesema idadi ya watalii tunategemea itoke milioni mbili kwenda milioni tano. Sasa inakuwaje kwenye mchango tumesogea asilimia moja tu? Nadhani kuna kitu hapa nitaomba watufafanulie ili na sisi tuweze kufahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza kwamba, pia kwenye eneo la utalii tuangalie namna ya kuongeza utalii unaotokana na manmade attractions, vitu tunavyovitengeneza. Nilishasema tena Dubai ina utalii maradufu ya sisi na vitu vyao vingi ni man made. Kwa hiyo, tuendelee kuangalia vitu ambavyo ni man made ambavyo vinaweza kutusaidia kwenye utalii wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo lingine, sijaona mahali ambapo wameelezea au tumeonesha namna makusudi kwamba, sasa hivi hawa watalii milioni mbili tulionao, tuna vitanda kiasi gani na tutakapopata watalii milioni tano, tunao uwezo wa kuwa-accommodate? Tunavyo hivyo vitanda? Tuna sera ambayo itasababisha hivyo vitanda vijengwe? Tuwe na hoteli za kutosha na kuwa-accommodate hawa watu ambao ni mara mbili pamoja na miundombinu mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wameelezea vizuri hali ya uchumi kwa regional integration zote. Wameonesha SADC na position yetu, wameonesha East African Community na position yetu. Sijaona mahali ambapo wameonesha uchumi wetu utawezaje kunufaika kwa kuwa kwenye hizi regional integrations, kwamba, ni kitu gani cha kimkakati cha kuhakikisha kwamba tunahakikisha tunakipata mapema. Kwa mfano, tunakuwa supplier wa chakula kwenye regional integration (SADC pamoja na EAC).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tuna position gani katika manufacturing katika hizo jumuiya mbili? Ilitakiwa mpango utuelekeze moja kwa moja. Hapa nikumbushe kwamba wakati tunapambana na SGR kwa haraka kuhakikisha inakwenda nchi kama Congo, tukumbuke pia kuna mpango wa kutoa treni kutoa Afrika ya Kusini kuja Angola mpaka Congo. Ni namna gani sisi tutahakikisha ya kwetu inafika mapema na benefits tunaanza kuzipata kabla ya hiyo nyingine haijaja? Kwa sababu dunia ni ushindani, sasa hatuwezi kutengeneza reli yetu taratibu wakati competitor wameanzia kule Afrika Kusini na wakafika kabla yetu. wakifika kabla yetu watakuwa wamesha-cement position yao kwenye hiyo na sisi tutapata shida ya kupata return kwenye uwekezaji wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye sekta za muhimu za Kilimo na Uvuvi. Ninaelewa kabisa juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha haya maeneo ambayo ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu, yanaendelea kuwa imara na yanaendelea kusaidia uchumi. Hata hivyo, kuna eneo ambalo ningetaka kuliona kwenye mpango; kwa mfano, ni namna gani haya mafuriko yanayotokea tunaya-capitalize ili kuhakikisha tunajenga mabwawa ya umwagiliaji yatakayosaidia kilimo, maeneo yote ambayo yana umwagiliaji. Pia, kwa mfano, ni namna gani Sekta ya Ngozi ambayo nimeiongelea juzi kwamba, 95% ya ngozi inayotoka kwetu inauzwa West Africa kama chakula. Kwa hiyo, maana yake bei yake siyo nzuri kama ingeenda kwenye manufacturing. Ni namna gani kwenye uvuvi nako tunahaikisha inakwenda kwenye manufacturing?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pamoja na mambo mengine ambayo nitachangia kwa kuyaandika, niunge mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia katika Hotuba ya Kamati hizi mbili, lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda, nitachangia kwenye Kamati ya Bajeti peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna suala geni ninaliongea, ni masuala ambayo tumeshayaongea hapa kuanzia wakati mpango wa Serikali unaletwa, wakati wa bajeti tunayaongea na bado hayajapata majibu ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kwenye kipengele 2:1:4 cha Taarifa ya Bajeti ambacho kinapatikana ukurasa wa 10 ambacho msemaji aliyetoka kuongea amekigusia au ndio amemalizia kinachohusiana na akiba ya fedha za kigeni, lakini nitaongelea pia au nitafungamanisha na kipengele 2:4:1 kilichopo ukurasa wa 25 kinachosema kutotabirika kwa Sera za Kodi na namna mambo haya yanavyoweza kusababisha biashara kudorora nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku mbili, tatu zilizopita kuna mchangiaji alisema humu kwamba kuna uhaba mkubwa wa fedha za kigeni hasa dola kwenye mabenki yetu. Wako wafanyabiashara na kuna Wabunge wafanyabiashara wamekwenda benki inachukulia hata wiki mbili kwa Dola laki moja na hili limeendelea na maeneo mengine unashawishiwa angalau mteja wako unayetaka kufanya naye biashara kwa Dola umshawishi aweze kuchukua fedha nyingine kama Euro na kadhalika. Sasa hatujapata majibu ya kutosha kwamba huu upungufu wa fedha za kigeni huku kwa wafanyabiashara unatokana na nini? Kwenye taarifa hapa inaonekana tuna fedha za kigeni za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naifunganisha na kipengele 2:4:1, kutokutabilika kwa Sera za Kodi. Nataka kusema kwamba siyo Sera za Kodi tu lakini ni sera za uendeshaji katika nchi hii. Tulifanya operation ya kuondoa Bureau De Change, tukafunga Bureau De Change na kunyang’anya watu hela na nyaraka nyingine zilichukuliwa na tukasema kwamba sasa benki ndio zitafanya hiyo biashara na watu wakakubali, lakini kumekuwepo na utaratibu wa watu wachache kupewa leseni za bureau de change. Wako watu wengi wamekidhi vigezo vipya lakini hawapewi leseni za bureau de change.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siko tena kule kwenye kuuliza warudishiwe leseni, kule nimeshaona kwamba haiwezekani kwamba warudishiwe fedha zao, lakini wako ambao aidha walikuwa katika lile kundi la mwanzo au wengine wapya wamekidhi vigezo vyote vilivyowekwa kwenye maandishi lakini hawajapata. Nina uhakika na ushahidi wa watu saba, wanapojibiwa kwamba do not meet seat and proper test, yaani unajibiwa hivyo tu, mtu ana hela, mtu anafanya biashara nyingine, mtu analipa kodi, mtu amewekeza kwenye maeneo kedekede, lakini kwenye Bureau De Change anajibiwa hivyo tu au wengine wanaambiwa wana integrity issues, haielezwi. Sasa sijaelewa ipo kwenye kanuni, ni utashi wa Wizara au ni utashi gani, lakini tunaleta usumbufu mkubwa, watu wanahangaika na hatujui twende kwa nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoongelea suala la Bureau De Change nikiongelea Moshi Mjini na Arusha hatuongelei tu hawa wafanyabiashara wakubwa, tunaongalea Porter and Tour Guider aliyetoka porini au mlimani ameingia pale mjini saa kumi amelipwa tip yake kwa Dola anataka kubadilisha anunue nyama aende nyumbani hana mahali pa kubadilisha hiyo hela na ni kwa nini? Kwa sababu Bureau De Change zimezuiwa na benki hazifungui baada ya ule muda wa kawaida wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa Waziri atuambie, Serikali ituambie, kuna siri gani kwenye issue ya Bureau De Change? Kwa nini leseni wamepewa watu wachache? Watu wengine wanakwenda wanajibiwa kirahisi na hakuna majibu na watu wanateseka na dola hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa zaidi, Bureau De Change walikuwa wana-change currency mpaka 20, lakini kwenye mabenki wana-change currency chache sana, Kenyan money ni baadhi ya benki kama KCB, Euro, dola, paund currency nyingine hawabadilishi, lakini tunajua kwamba kuna watu wetu wanakwenda hija wanahitaji hela, kuna watu wetu wanakwenda Dubai, wanahitaji hela ya Dubai, kuna watu wetu wanakwenda South africa wanahitaji hela ya South Africa, lakini mabenki yamejikita kwenye currency chache. Kwa hiyo ningependa sana Serikali itoe wingu kwenye suala la Bureau De Change kwa sababu linasababisha hasara kubwa, linasababisha usumbufu kwa wananchi na linawasababisha wafanyabiashara kushindwa kufanya biashara zao kwa uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ningependa kuiongelea ni kipengele 2:1:2 ambacho kiko ukurasa wa saba, linalohusiana na mfumko wa bei. Nataka nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hela anayotoa kwa ajili ya ku-subsidize mafuta. Nimeona taarifa juzi Wizara ya Kilimo nayo imesema italeta mahindi mtaani kwa Sh.700 kwa kilo. Kwa kweli hizo ni juhudi kubwa sana za Serikali, lakini ukiangalia kwenye jedwali lililoko hapa katika mfumko wa bei, jedwali namba moja kwenye Taarifa ya Bajeti, inaonyesha chakula ndio kimekwenda asilimia 9.7 kwenye mfumko na chakula siyo mahindi peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunathamini sana mchango wa Serikali kupunguza hayo makali, lakini jicho zaidi litupiwe kwenye chakula, ni dhahiri kabisa purchasing power ya chakula Tanzania na Kenya zinatofautiana kwa sababu uchumi wake ni mkubwa. Kenya wana demand kubwa kwa sababu chakula chao hakiendi kwenda kuliwa, kinaenda kulisha viwanda na wana-export. Kwa hiyo wanaweza kununua kwa bei kubwa, tukiachia uhuru asilimia mia moja watu wetu watakufa njaa, lazima kuwe na control mechanism ya kuhakikisha chakula kinapata bei nzuri kwa namna ambavyo Serikali itaona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapa. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Fedha pamoja na Mpango wa Taifa na mimi nigusie pale alipomalizia Kamani hapa kwenye dollarization.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeshauri najua Wizara ya Fedha imefanya kazi nzuri sana na inaendelea kupambana sana na inflation na inaonekana lakini ijitahidi zaidi ipambane na black market. Huku benki tunasema ni 2,690, elfu mbili mia sita na ngapi, wanakuambia hakuna chukua 500, 300 huko nje ni 2,800 mpaka 2,850 ili tu-stabilize zaidi, tunao uwezo huo kwa sababu ni kitu kidogo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe kuwe na special consideration kwa watu ambao bidhaa zao zote wanazo-deal nazo zinatoka nje. Mathalani watu wanaochukua tenda Serikalini halafu wana-order vitu nje, halafu vinachukua muda kufika, vilevile Serikali inachukua tena muda kuwalipa, sasa waki-deal na hela ya ndani tu bado wataenda kupata shida. Kwa hiyo hayo maeneo mawili matatu yakiwekewa mkazo hapo kwenye dola tutakuwa tumekaa vizuri lakini nakubaliana kabisa na lile wazo la Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana Wizara zote mbili kwa ujumla kwa eneo la wakandarasi. Nimeona ule ukurasa wa 54 wameonesha nia ya kuhakikisha wakandarasi wazawa ambao wanapata sub contract, inapotoka interest na wale wazawa nao wanapata ile interest, hilo ni jambo zuri sana. Ameongeza stake ya wakandarasi wazawa kwenye kazi ni jambo zuri sana tumelipigia kelele mara nyingi niwapongeze sana, niombe tu sasa tuangalie pia namna ya kuweka interest hata kidogo kwa wakandarasi wazawa kwa malipo yanayochelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba maeneo mengi yamekaa vizuri yako maeneo ambayo ninashauri Serikali i-consider kuyarekebisha. Eneo la kwanza ni ile faini ya kutokutoa risiti ambayo iko ukurasa wa 100 pale ambayo ni ile Sheria Namba 86(1). Unajua jinsi unavyoweka ile kodi ya juu au faini ya juu unatoa mwanya wa wale wanapiga ile kodi ku-negotiate ili walipe ile ya chini halafu wapate hapo cha juu. Kwa hiyo, mwisho mzigo utaenda kumdondokea mfanyabiasara wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuliangalie milioni 15 ni nyingi sana kuna maduka ambayo yanatumia EFD na milioni 15 ni almost mtaji wake hata kama turn over ni kubwa, sasa ukimwambia faini ni milioni 15, TRA wana mtindo wa kwenda kwenye ile ya juu ili mrudi mezani muongee na mkiongea pale unaona kabisa wana chochote ili warudi kwenye ile ya chini naomba tuliangalie sana hilo na ninaongea kama mtu ninayetoka kwenye jamii ya wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ninapowashauri Serikali waiangalie ni eneo la ile tozo kwa magari yanayotumia gesi. Haya magari bado ni machache, motive yetu ni kutia nguvu au kuwasaidia magari yawe mengi, haya magari wanafanya modification kule nyuma unakuta wameweka mtungi wa gesi hakuna hata sehemu ya kuweka begi, sasa ikiwekea tozo ya shilingi 382 kwa kilo tayari unaanza ku-discourage, kwa sababu menzake yeye ana nafasi huko nyuma na huu mzigo ukimwangukia hawataona ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa sababu Rais anataka clean energy kwenye kupika definitely tunaenda kwenye clean energy kwenye magari pia. Ni afadhali ihamishiwe kwa sababu kwa sasa hivi miaka mitano ijayo magari ya umeme yatakuwa mengi, ni heri tuihamishie kwenye magari ambayo tunayaagiza ya umeme na hybrid ili tuweze kulinda hawa wa gesi kwanza, watakapokuwa wengi hiki chanzo kitakuwa na tija, lakini kwa hawa wachache ambao wako Dar tu ukawarundikia shilingi 382 naona ni nyingi sana, tuangalie hata 150 ili na wao waweze kupambana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nirudi eneo la road fund, barabara ni siasa, barabara ni maisha, barabara ni maendeleo. Tumekuwa tunawalalamikia sisi hapa wote Wabunge Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi kwamba barabara hazijengwi na nini lakii tunajua kile kikapu chetu kikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaushauri kwamba ni vizuri tuangalie namna ya kuimarisha mfuko ule, ndiyo sehemu ya kwanza ya kuanza, kwanza tuanze tuhakikishe ile hela yote inayokatwa kwenye maeneo yote iende yote kama ilivyo isiguswe. Wanasema sijui ni ring fencing kuna kiingereza chake, sasa ni vizuri yaende kwa sababu barabara kwa kweli itatusaidia sana kuharakisha maendeleo na tu aim juu zaidi siyo two trillion ambayo wamependekeza twende mpaka 2.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zipo barabara za muhimu na zina maslahi kwa uchumi na zitapata watu. Tuende kwenye PPP na zile road toll kwa mfano ile barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ya njia sita tukaweka road toll hatujamzuia mtu kutumia hii ya kawaida kama ana haraka lakini maana yake tunamsaidia yule mwenye haraka kama kenya walivyoweka ile barabara ya haraka kutoka Mlolongo kwenda mpaka Westland, inakusanya hela na ile hela inaendelea kuingia kwenye Mfuko wa Barabara. Kwa hiyo ningeomba sana toll roads na PPP inaweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la kuangalia kwa hara, hela inayokatwa kwa ajili ya REA tumeshapiga hatua kiasi gani kwenye REA? Si karibu tunamaliza vijiji vyote? Hatuwezi kuipunguza pale kwenye REA tukaongezea hapo kile kipande kilekile bila kuongeza kwa wananchi kikaenda kusaidia kwenye mafuta? Kwa hiyo nadhani kitasaidia kwenye barabara Road Fund ikawa ina hela hii itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo ambalo ninapenda niishauri Wizara ya Ardhi na hii ishirikiane na Wizara ya Fedha. Watanzania wote hata mwenye kupata kipato cha shilingi laki moja wanajenga nyumba cash na kama wanajenga nyumba cash na nyumba ni security akiingia kazini akipata mwanya wa rushwa atakula, mwanya wa kuiba atakula kwa sababu security ya kwanza ni kupata nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusirejeshe ile housing bank? Mtu akiingia kazini asaini mkataba kama ana kiwanja apate mkopo wa miaka 20, 30 wa kujenga nyumba apate amani na aheshimu kazi yake kwa sababu akiacha hiyo kazi tayari nyumba itauzwa, tuingize pale ili hiyo hela inayobaki mkononi kwa mtu kama tuna housing bank itumike kwenye maeneo mengine, ifanye uchumi wetu uchangamke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujenga nyumba cash kwa kweli ni gharama sana na hela nyingi inaenda karibu vitu vyote ambavyo vinatoka nje. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri sana tufikirie namna ya kuwa na Tanzania housing bank hasa kwa wale ambao wana maeneo yaliyopimwa na wana hati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iachane na biashara haiwezi, iachane kabisa na biashara, iendelee kutoa huduma. Kuna kiwanda kimejengwa pale Moshi cha Karanga Leather imeingizwa bilioni zaidi ya 100 na ni hela hiyo hiyo ya wastaafu NSSF sijui PPF Serikali ilikuwa inaleta viatu hapa pea moja moja imeshashindwa hata ile pea moja moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi kuwekeza Kiwanda cha Ngozi cha namna ile uendeshe kwa mtu ambaye anateuliwa hajawahi kuona Ngozi inatengenezwaje zile mashine ni za kisasa kabisa. Tuuze share 51% tubaki na 49%, kama ilivyo TBL kama ilivyo TPC na mashirika mengine walete hela wafanye kazi na tena iwe ni export kwa sababu kiatu kitakachotengenezwa pale kwa sababu mashine zile ni za leo za Italy za dunia ya leo kile kiatu hakiwezi kuwa bei rahisi sawa na mtumba unaotoka pale Kiboriloni road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutengeneze au kama tukiamua kama hatutaki kukitoa tena kwa watu ili kilete hela za kigeni basi tuanze kupitisha sheria ya kwamba majeshi yote ya ndani yatumie viatu kutoka pale ambao sasa tunavunja tena ile nia halisi ya kuwa na soko la ushindani na hii ni kwa viwanda vyote Serikali haiwezi kusimamia kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kile kiwanda ukiuliza matatizo waliyonayo sasa hivi wanataka bilioni 10 working capital kwa nini? Mshahara wao hautokani na kazi wanayoifanya, hela ya NSSF imekaa pale, Magereza wamekaa pale, tuwape watu wenye uwezo watengeneze viatu kama inavyotengenezwa pale EPZ export sisi tupate hela na tuweze kutoa soko la ngozi na ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni hata kile kiwanda cha sukari cha Mkulazi hatuwezi mimi najua, kile kiwanda cha TPC kilikuwa cha kwetu tukatengeneza wenyewe mwisho wa siku tukaanza kubadilisha kila kitu, tukashindwa! Tumerudisha mpaka sasa hivi kinatoa gawio kwa Serikali. Kwa hiyo, nashauri hata kile cha Mkulazi tutafute wadau tuwauzie share, tubaki na share zetu za maana, ajira itokee na ufanisi uwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la SGR, sijasikia kabisa SGR inakuja lini Kaskazini. Sasa purchasing power ya Kaskazini ni kubwa. Purchasing power ya Kaskazini hata hizo za luxury ni kubwa sana. Tuleteeni SGR, ianzie Dar es Salaam – Tanga – Kilimanjaro iende Arusha – Manyara mpaka Musoma iende itokee huko. Kule kuna purchasing power kubwa. Nina uhakika tutaweza kufanya marejesho kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo ambalo linahusu utumishi na nilishaliwasilisha mara kadhaa. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kwa kuboresha huduma za afya. Pale Moshi tuna KCMC ambayo ndiyo hospitali ya kanda, super specialist. Sasa hivi tuna deal na kansa, tutaenda kwenye kitengo cha moyo wameshakipatia fedha na tunaenda kwenye kufungua ubongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shida tunayopata, salary scale yake haifanani na Bugando na haifanani na Muhimbili. Maana yake ni nini? Mfanyakazi kuliko abaki pale, super specialist, anaona mazingira mazuri zaidi aende Bugando au aende wapi. Hilo ni suala la kurekebisha tu ili hizi huduma zitolewe kote kwa usawa na sisi tuendelee kuwahudumia wananchi wetu vizuri. Tayari uwekezaji ni mkubwa, naomba sana Serikali ifikirie namna ya kuweka salary scale ambayo inafanana kwa hizi super specialist hospitals.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni vizuri Wizara hii ya Mipango ifanye kazi kwa uchungu kama mtu binafsi, kama mchaga au kama mpare kwa maana ya kwamba, haiwekzekani kuna mradi Serikali imepeleka shilingi bilioni saba ujenzi wa stendi ya Mfumuni. Halmashauri imeshindwa ku-negotiate. Shilingi bilioni saba imekaa pale chini na kile ni chanzo cha mapato kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuwafata CRJE. Hawa watu wakubwa walioko hapa, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Professor Kitila wakienda CRJE ambao mnawalipa kwa miradi mingine mkawaambia, bwana tuna interest na hili eneo kwa sababu hela imekaa chini muda mrefu tunaihitaji ili iongeze mapato Moshi na iingie Serikalini warudi site wamalizie ile stendi imebaki kiasi kidogo sana. Tunatenga fedha, lakini tunashindwa kupata wakandarasi kurudi.
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante muda wako umeisha.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi kabisa naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia. Na mimi niungane na wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na viongozi wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi lakini bajeti ni ndogo, mambo ni mengi na muda nao ni mdogo, nitajaribu kwenda kwa harakaharaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na wazo la Mheshimiwa Sanga la kuangalia namna ya kutumia CSR za makampuni kuwekeza katika michezo. Kwa kifupi tu bajeti wanayopewa leo ya milioni 35 haiwezi kujenga moja ya tatu ya ule Uwanja wa Mkapa. Nimeangalia kwenye dodoso hapa ule uwanja ni dola milioni 56, ni kama bilioni 133. Kwa hiyo hiyo bajeti yenyewe hata kiwanja kama kile haiwezi, ukiacha mambo ya watumishi huko na vitu vingine. Kwa hiyo ninaomba sana tuangalie namna ya kuiwezesha Wizara iwe na hela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitoe mfano; Moshi tuna Uwanja wetu wa Majengo, kila mwaka tunatenga bajeti ikinyesha mvua kubwa barabara zikiharibika wakiangalia mahali pa kutoa tunasema toa kule kwenye michezo, yaani michezo nchi hii imeendelea kuwa nayo ni mchezo, yaani michezo ni mchezo. Lakini kwenye Baraza la Madiwani lililopo sasa Moshi Mjini, mwaka jana tumetenga milioni 300 na mwaka huu milioni 300 na Uwanja ule wa Majengo tayari tunakwenda kuutengeneza, tayari pitch imeshawekwa, tunaweka uzio na kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Wizara; na kwa sababu sasa hakuna hela ya kusiadia kule Majengo nashindwa niioombeje, lakini hata kama mtatembeza bakuli mkipata chochote kwenye Halmashauri kama ya Moshi ambayo tumepeleka milioni 600 kwenye uwanja na sisi tunakuwa wa mfano, basi mtusaidie kutuongezea hela ili uwanja wetu ukamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna mpango wa kujenga viwanja viwili (arenas). Naona mmoja unajengwa Dar es Salaam, mwingine walisema ni Dodoma. Mimi naomba niwaambie, ili michezo iendelee kukua ni lazima tu-diversify. Ni vizuri mmoja ukijengwa Dodoma huo mwingine ujengwe ama Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini au kule kusini Mbeya, maeneo ambayo yanafikika, ili tuweze kupanua huu mchezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Moshi Mjini sisi tuna eneo pale, lina ukubwa wa mita za mraba 157,000, unaweza kuweka arena pale. Kanda ya Kaskazini tuna Uwanja wa Ndege wa Kimataifa pale Hai, Moshi Mjini tuna uwanja mdogo, ule uwanja unafikika. Kwa hiyo ni vizuri tu-diversify, siyo viwanja vyote vijengwe Dar na Dodoma halafu kwingine kusiwe na viwanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aspect ya kwamba michezo ni utalii, na nilikuwa nataka kulichangia hili katika Wizara ya Utalii lakini ni vizuri nililete hapa. Sisi Moshi Mjini tuna mashindano makubwa ya kukimbia, Kilimanjaro Marathon, inaleta watu karibu 8,000 kutoka nchi zaidi ya 51. Wale watu wakishamaliza kukimbia huwa wanakwenda mbugani, wanapanda mlima, wanakwenda Zanzibar, wanaingiza fedha kwenye utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yapo maeneo Wizara ya Michezo ikiwekeza vizuri inaweza kusaidia sekta nyingine na ili hizi sekta sasa na zenyewe zichangie kwenye michezo. Hii Kilimanjaro Marathon ni mfano, lakini tunaweza kuwa na Mchezo wa Golf wa kimataifa, tunakwenda ku-lobby na PGA. Kuna moja ilikuwa ifanyike kule Kili Golf, kuna kiwanja ambacho kipo katikati ya Mlima Meru na Mlima Kilimajaro, Kilimanjaro Golf, unaitwa Kili Golf; unaweza ukaleta yale mashindano pale, yatatangazwa dunia nzima lakini wale washiriki pia watapata nafasi ya kwenda kwenye mbuga za wanyama kwenda kutalii ili watuingizie fedha. Hiyo ni pamoja na cycling tour.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote hayaji tu. Kule Rwanda kuna Tour De Kigali; hayaji tu, lazima ukafanye lobbying na vile vyama vya cycling vya kimataifa. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri mkitushirikisha sisi tunaweza kuungana kuweza kufanya hiyo lobbying. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanja vya golf, na ninasema golf kama mchezo mmoja, lakini kwa michezo mingine yote. Tume-concentrate sana kwenye mpira wa miguu, ni vizuri tukumbuke kwamba ndondi nayo sasa hivi imeanza kutupia kimataifa, muziki unatuaisha kimataifa, riadha juzi kuna mkimbiaji wetu amemshinda mpaka Kipchoge. Kwa hiyo ni vizuri tuangalie namna ya kukuza hii michezo yote kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye golf Moshi pale tuna uwanja wetu wa golf, Uwanja wa kwanza golf Tanzania, Moshi Club, tuna denii kubwa sana la land rent. Sisi hatutaki tusamehewe, tunaomba Mheshimiwa Waziri uongee na Waziri wa Ardhi waondoe interest, sisi tuko tayari kulipa ile land rent yote ili kuweza kusimamia ule Uwanja wa kihistoria wa Moshi Club.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la riadha. Kuna ulazima wa kutengeneza kambi maeneo ya nyanda za juu, maeneo ya Rift Valley kama kule Karatu, na maeneo ya West Kilimanjaro ili watu waje wa-train. Kule Kenya kuna eneo linaitwa Iten ambalo mpaka wakimbiaji wa nje wanakuja ku-train wiki mbili, wiki tatu kabla ya mashindano makubwa. Sisi tuna maeneo yanafaa, kule West Kilimanjaro kunafaa, kule Karatu kunafaa, itengenezwe kambi watu waje wawekeze nyumba za kulala ili wakimbiaji waje washiriki huku, na ni utalii pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye incentives, kampuni ambazo zimeshasaidia michezo mpaka sasa, sijajua Serikali inazisaidiaje; Azam kama mfano mzuri, GSM, Mohamed Enterprises, CRDB ambao wana-sponsor Mchezo wa Basketball wa Taifa, NMB; ni namna gani Serikali inatia chachu kwa kampuni hizi ili kampuni nyingine nazo ziwekeze kwenye michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Moshi tulikuwa na mashindano makubwa sana ya volley ball. Yalikuwa yanakuwa sponsored na Bonite Bottlers. Sijaona ni namna gani Serikali inasaidia makampuni binafsi ambayo yanawekeza kwenye michezo ili kuvutia makampuni mengine nayo yapate hamu ya kuwekeza kwenye michezo. Kwa hiyo nadhani kuna kitu cha kufanya ili tuweze kusukuma gurudumu hili mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, na mimi nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia azimio hili muhimu na kipekee kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, niliomba kuchangia kwa sababu wakati wa bajeti hii ambayo tunaendelea nayo tarehe 23 Juni, 2022 nikiwa nachangia hapa niliiomba Serikali ifikirie namna ya kutafuta wabia wa uendeshaji wa bandari hii na kwa bahati nzuri niliwataja hawa hawa ambao wamekuja kubahatika kuwa wabia wetu ambao DP World. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niliwajuaje DP World nikawataja kwenye mchango wangu mwaka jana, mwezi wa sita? Mwaka 2006 nilikuwa nafuatilia mwenendo wa mijadala ya Bunge la Marekani. Alipokuwepo Rais George W. Bush alileta muswada kwenye Bunge la Marekani waridhie DP World wachukue management ya bandari zao sita za Marekani (USA). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mjadala ukawa mkali sana na ulienda ukagusa kila eneo na mjadala ulikuja kusimama kwa sababu waliokuwa wanaendesha bandari za Marekani walikuwa ni P&O wa Uingereza, lakini walinunuliwa na DP World ambapo DP World walikuwa na kila kigezo cha kuendesha, isipokuwa mjadala ule ulikwama Bungeni Marekani kwa sababu za kiusalama kwa upande wao.
Mheshimiwa Spika, hawa DP World ambao Serikali yetu imewachagua uwezo wao sio wa kutilia mashaka hata kidogo. Hata hivyo, tunarudi ni nini tufanye kwa upande wetu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Priscus, amekwenda vizuri ila hakumalizia vizuri. Baada ya pale kilichotokea; baada ya DP World kukataliwa na Congress ya Marekani, kilichoendelea pale ilichukua kampuni nyingine ambayo sio ya Marekani na ilikuwa ni kampuni ya Uingereza ambayo ndiyo inaendesha zile bandari sita mpaka sasa. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Priscus Tarimo.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naendela kusema jambo moja, kuna kipindi katika nchi yetu tulikwama kwenye mambo ya msingi kwa sababu ya baadhi ya viongozi kushindwa kufanya maamuzi. Leo hatuwezi kuacha Mheshimiwa Rais ametuongoza kwenye kufanya maamuzi ya busara, sisi tuikwamishe Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, uamuzi ambao tumekwishaanza kuufanyia kazi, azimio lililopo mbele yetu ni azimio la ukombozi kwa kila namna unavyolitazama. Mikutano ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea mambo wanayotuhoji juu ya maamuzi yetu ya ndani ni kwa sababu ya uwezo wetu wa kibajeti, ni kwa sababu tunaendelea kuwa tegemezi.
Mheshimiwa Spika, huu mpango kwa kila angle unayoiangalia unakwenda kutukwamua kwenye bajeti tegemezi. Kama tunakwenda kuitoa bandari kwenye mchango wa trilioni saba kwenda kwenye mchango wa trilioni 26 mpaka 30 kwenye pato letu, tunakwenda kupata uhuru wa kiuchumi na tunakwenda kuyasimamia mambo yetu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni lazima kwa pamoja tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha azimio hili linapita. Tunapokwenda kumuunga mkono Mheshimiwa Rais ni lazima pia tuwasikilize hao wanaotukosoa, ni wananchi wetu, wana hoja, lakini ningeomba sana Kitengo cha Mawasiliano cha Serikali kiwe kimetangulia mbele, kwa sababu kwenye hoja hizo, kuna hoja za kuzifanyia kazi, lakini kuna hoja zinahitaji ufafanuzi tu. Kwa nini tuache upotofu utangulie, baadae tuje tufanye kazi ya kusafisha? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni vizuri sisi tuwatangulie katika kutoa ufafanuzi kwenye zile hoja ambazo zimpotoshwa. Hata hivyo, kwenye hoja ambazo ni za msingi zipo ambazo tumezichukua tutazifanyia kazi kwenye hatua zinazofuata, kwenye HGA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukirudi kwenye hadithi za Biblia katika busara za Mzee Suleiman, tunakumbuka hoja za wanawake wawili waliokuwa wanagombania mtoto. Busara za Mfalme Suleiman ilikuja pale ili kujua ni yupi mzazi kweli wa yule mtoto aliposema mtoto huyu akatwe nusu wagawanywe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanaopinga hili azimio hawaongelei hizi ajira 72,000 watazipata wapi kama tusipopitia hili suala? Hawaongelei haya mapato tutakayoenda kuyapata tutayapata wapi kwa ajili ya Watanzania na maendeleo ya yetu? Hawaongelei kabisa kukua kwa uchumi wetu kutokana na haya. Maana yake wanataka kulizuia na hawana mbadala wa kututoa hapa tulipo kutupeleka mbele. Tukiangalia kiuhalisia namna halisi ni sisi ambao tunaona ni namna gani tunakwenda kusimamia hili azimio. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia ushauri wa Kamati katika kila angle wamepita mle mle ambapo wananchi ndipo wanapolilia. Ni kwa nini watu wengine waendelee kupotosha wakati uhalisia uko mbele? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba niwashawishi Wabunge wenzangu tuliunge mkono kama ambavyo tumkwishaonesha ili tuweze kupata manufaa haya yanayokuja na hili na mimi siku zote nilikuwa ninasema tunajenga reli ya kisasa hivi reli hiyo itabeba abiria tu? Hiyo hela ambayo tumewekeza au huo mkopo utarudi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuja hawa DP World, wakaweza kuongeza mizigo kwenye bandari yetu kama inavyoonekana hapa kutoka tani milioni 18 mpaka tani milioni 48 maana yake bandari zetu, reli yetu na bandari za kwenye maziwa zitafanya kazi na tutarudisha mikopo na hela tutapata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ahsante sana nimesema nigusie maeneo hayo na ninaunga hoja mkono. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii, nianze kwanza kwa kumpongeza Rais kwa kazi anazoendelea kulifanyia Taifa hili. Nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake kwa kazi wanazoendelea kuifanyia Wizara yao, kazi za muhimu sana kwa Taifa hili. Lakini pia nimpongeze…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ungekuja kiti cha mbele uonekane vizuri ili wananchi wako wakuone. Hebu njoo ukae mbele hapa, fanya haraka lakini. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaomba unilindie dakika zangu. Basi naendelea kuwapongeza watendaji wa Wizara, nilimtaja Katibu Mkuu, Injinia na Balozi Aisha, Erick Hamis - Bandari, TRC - Kadogosa, Mr. Matindi – ATCL na wengine wote kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache nitajaribu kwenda kwa haraka. La kwanza kabisa ni barabara ya Tengeru – Moshi – Himo na baadae mpaka Holili ambayo ni kilomita 105. Barabara hii kutoka Moshi kwenda Arusha ilikuwa ni muda wa dakika 45 mpaka saa moja. Lakini kutokana na msongamano mkubwa wa magari sasa hivi ni masaa mawili mpaka mawili na nusu. Huu ni upotevu mkubwa wa hela na upotevu mkubwa wa muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ahadi ya kuipanua barabara hii imekuwepo kwa muda mrefu sana. Sasa nimeangalia kwenye Hotuba kwenye ukurasa wa 17 nimeona imetengwa Bilioni 8.4 lakini ni kilomita 105. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri wakati unapokuja kuhitimisha, watu wa upande ule wafahamu ni barabara yote inatengenezwa au ni vipande vipande. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye Mji wa Moshi peke yake naona mmeelekeza kwamba itatengenezwa kilomita 8.4. Lakini pale kwenye daraja la Kikavu mita 560. Pia nikaona kuna mkopo kutoka Japani kipande cha kutoka Tengeru mpaka USA. Sasa tunatengeneza vipande vipande au mtatusaidia tupate fedha itengenezwe yote ili hilo tatizo liweze kuisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo ya Arusha pamoja na wingi wa watu pia tunahitaji bypass baadhi ya maeneo. Moshi ni Jiji linalotegemewa kukua muda wowote, sasa hatuna bypass pale. Tumekuwa tukiipigia kelele sana barabara ya Getifonga ambayo sasa iko chini ya TARURA inayokwenda mpaka Maboginikahe na baadae mpaka Chekereni. Nawaomba ni vizuri sana TARURA na TANROADS wakae pamoja. Kama Majiji yanatengenezewa bypass ile ni moja ya sehemu muhimu sana ya kutengeneza bypass waone ni nani ataifanyia kazi hiyo barabara. Lakini hata hivyo kwa sasa barabara hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo ya watu wa Moshi Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la airport. Tulipewa airport mwaka jana, Moshi Airport kurekebishwa na nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba hiyo ilikuwa ni ahadi ya Rais pia alipokuwa kwenye Royal Tour aliondokea pale akaona ile hali ya uwanja. Lakini mpaka leo pamoja na kwamba tulipewa bajeti iliyopita kazi haijaanza, tunaomba kujua shida ni nini maana ikipita tena kwenye bajeti hii haipo, kwenye bajeti iliyopita mpaka sasa tunaenda mwezi wa sita haijaanza matokeo yake tuataambiwa hela zilirudi na kazi imeshindikana kufanyika. Naomba wakati wa kuhitimisha atufahamishe ni nini kinaendelea kwenye Moshi Airport. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye utengenezaji wa barabara kwenye Taasisi za Serikali, mwaka jana palikuwa pamewekwa Moshi Police School (Chuo cha Polisi Moshi) barabara zake za ndani mpaka sasa hazijatengenezwa, nimejaribu kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye wakati ule alikuwa Naibu Waziri wa Fedha, hazijaweza kutengenezwa na kwenye ile randama eneo hilo sasa imewekwa Taasisi nyingine, sina haja ya kuitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha utufahamishe kama ile ya mwaka jana haijafanyika hii mpya inafanya nini pale ili ikiwezekana itolewe turudishe Chuo cha Polisi Moshi ili barabara zake za ndani zitengenezwe. Na nimejitahidi sana, nilikuwa Diwani wa Kata ile ya Kilimanjaro miaka 10 lakini kwa kutumia fedha za Halmashauri na za TARURA barabara za Taasisi hazitengenezwi. Sasa Chuo cha Polisi barabara zake ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la kuiwezesha Wizara. Ninaangalia haswa kwenye suala la bandari na position ya Tanzania kwa nchi hizi za Afrika Mashariki lakini na majirani wengine wengi wameongelea. Mimi nadhani tuna kazi ya kufanya na hatutakiwi kuogopa. Kuna nchi zingine wameweza kuwatumia DP World. DP World ni kampuni ya Dubai ya bandari ambayo imejiweka kibiashara na inaendesha bandari kwenye nchi nyingine. Hata Uingereza wanaendeshewa bandari zao baadhi, India, Australia, Argentina. Kama hatuna hela za ku-invest ili bandari zetu zifanye kazi vizuri tuweze kufanya majadiliano na watu kama hao wenye uwezo lakini pia wana connection ambazo zinaweza kutusaidia kuboresha bandari lakini tukaunganisha na reli ili tuweze kupata fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo mengine ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la wakandarasi wazawa, niseme tu tumeelezwa kwamba wakandarasi wa nje wanapokuwa na miradi na zile deadline wanakuwa wanapewa interest wakicheleweshewa malipo, wakandarasi wa ndani haiko hivyo. Sasa mfumo huu unasababisha Serikali inakuwa kama inaenda kuwaua wakandarasi wazawa, hawalipwi kwa wakati, wakicheleweshewa hawapewi interest lakini pia upataji wao wa kazi haswa hizi kubwa hata kwa kushirikiana unakuwa wa kusuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kama tunataka kujenga Taifa imara lazima tuwawezeshe wakandarasi wa ndani, waweze kutumia hizi hela ndani na wakizitumia ndani multiplication yake inaendelea kuwa kubwa kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie hapo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishukuru kwa nafasi hii ya kuichangia Wizara hii ya Utalii, Wizara ambayo tuna interest nayo sana kwenye Mkoa wetu wa Kilimanjaro, lakini nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa lile tukio la Royal Tour. Wapo watu wengi ambao bado wanabeza, lakini na mimi niungane na wale wanaomtia moyo Rais kwa sababu tayari amethubutu na amefanya na matokeo yameshaanza kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu kwa kazi ambazo wanaendelea kufanya katika Wizara yao ambazo zinaleta matokeo chanya kwa nchi yetu. Mimi nina mambo machache ya kuchangia, nianze na jambo ambalo nilishalileta kwenye swali, la CSR.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale yenye migodi zile halmashauri zinazozunguka ile migodi zinapata kiasi cha fedha asilimia fulani ambayo ni CSR kwa ajili ya maendeleo yao pale pembeni kwa wale wanaozunguka ile migodi. Sasa maeneo yanayozunguka haya mapori pamoja na vivutio vya utalii ni muhimu sana na wao waweze kupata kiasi fulani katika yale mapato ambayo yanapatikana kwenye utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano, Mkoa wa Kilimanjaro kuotesha mti ni hiyari, lakini kukata mti ni mpaka uwe na kibali cha Mkuu wa Wilaya na ni kwa nini tunafanya hivyo? Ni kwa sababu miti kule inahitajika sana kwa ajili ya kutunza uoto ule wa asili na kutunza mazingira ya ule mlima ikiwa ni pamoja na theluji yake. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema asilimia 85 ya nishati inayotumika nchini inatokana na mazao ya misitu ikiwa ni mkaa, kuni na vinginevyo. Sasa kule Kilimanjaro haturuhusiwi kukata hiyo miti hata kama unataka kuangukia nyumba, process yake ni ndefu. Sasa mkitusaidia CSR itawasaidia halmashauri kuangalia namna mbadala ya ku-subsidize maisha ya hawa watu ili wasitumie hiyo nishauti na badala yake watumie nishati mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie maneno ambayo wameyaongelea Waheshimiwa wawili, Mheshimiwa Neema Mgaya pamoja na Mheshimiwa Swai kuhusiana na kodi nyingi na mimi hili silifunganishi tu kwa kuwaongezea faida wale wadau wa utalii, lakini zaidi ninafikiria kwamba tukiwapunguzia mzigo na biashara hii ya utalii ni seasonal, ina maana na wao wataongeza maslahi kwa wale watumishi wao kwa mfano wapagazi ili waweze kwa sababu, watu hawa wamekuwa wakipata mishahara kipindi ambacho ni high season, kipindi ambacho ni low season wanakuwa wanatangatanga na maisha yao yanakuwa magumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ili hawa wanaojihusisha na kazi hizi za utalii kama wapagazi, waongoza watalii, waweze kupata kipato hasa kipindi cha low season ni vizuri tuwapunguzie mzigo hawa wafanyabiashara ya utalii ili na wao waweze kuishusha hiyo faida chini na wale watu waweze kupata mafao yao bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na debate kali kwenye mitandao na mengine makongamano yamefanyika mpaka kule Moshi kuhusiana na cable car. Na mimi niwasilishe mawazo ya pande zote mbili, upo upande unaosema cable car ije na wao wanasema ni aina mpya ya utalii na inahusiana na watu ambao hawapandi mlima na nia yake sio kupeleka watu kileleni, bali ni kuwapeleka eneo ambalo wanaona mandhari nzuri na kuwarudisha. Kwa hiyo, kwao wao ni nyongeza kwenye pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini upande wa pili wapo ambao wanasema cable car inatakiwa ipandishe watu mpaka kileleni, itapunguza ajira, itapunguza siku ambazo mtalii anakaa kule mlimani, itapunguza kipato cha Serikali; na mimi nasema kama ni cable car ya namna hiyo basi hatuna budi kuisimamisha, lakini ninaomba Wizara ifanye tathmini nzuri, ifanye mawasiliano na makongamano pamoja na wafanyabiashara na wadau wengine tuone ni kitu chenye tija, hata ikibidi sio lazima aje mtu kutoka nje kuwekeza kwenye cable car, kama haidhuru mazingira yetu na kama ni kitu ambacho kitatuongezea kipato badala ya kupunguza, kitaongeza ajira badala ya kupunguza, Serikali inaweza kufanya yenyewe badala ya kuachia mtu binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaweza kujenga reli ya SGR, kale ka-cable car sidhani kama ni kitu ambacho tunashindwa. Na mifano iko maeneo mengi duniani ambapo calbe cars zimekuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongelee park fees ambazo nimeziongelea pia kidogo hapo nyuma. Inashangaza kwamba park fees zetu upande ambao uko busy kama ile Northern Circuit bado hazitofautiani sana nah uku Southern Circuit. Mimi naishauri Wizara ili kuongea idadi ya watu kule maeneo ambayo watalii hawaendi kwa wingi kule Southern Circuit na maeneo mengine kile kiingilio (park fees) kingeshushwa sana ili kuvutia watu wengine; kipandishwe pale ambapo tutaona watalii wamekuwa wengi ili kifanane nah uku kwingine. Kwa hiyo, kuna haja ya kuangalia yale maeneo yaliyoko busy warekebishe kidogo, lakini maeneo ambayo hayako busy washushe kabisa kiingilio. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niishauri Wizara suala la conference tourism, inajulikana kama MICE, ni sekta ya tourism ambayo basically inafungamanishwa na sekta nyingine, ni utalii wa mikutano. Sasa najua wao kama Wizara hawahangaiki na suala la mikutano, lakini wanaweza wakafungamana na Wizara nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano NSSF wanajenga majengo makubwa tu, lakini ni dhahiri wakijenga kumbi za kisasa za mikutano kwa mfano pale Moshi itaongeza idadi ya watu wanaokuja kwenye mikutano na huo ni utalii, lakini watu hao wakimaliza mikutano wanaenda kwenye vivutio vyetu kutalii. Ni sehemu ambayo inakua sana, utalii wa mikutano unahitaji kufungamanishwa. Ni vizuri sana Wizara ianze kuangalia namna ya kuwasiliana na Wizara nyingine kuiwekea hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili haliwahusu utalii peke yao, suala la intellectual property na copyrights. Magari haya ya utalii ambayo yamekuwa modified yalianzia Moshi kwenye kampuni ambayo inaitwa Rajinda Motors na walitaka wapewe copyright na intellectual properties za ubunifu wao, lakini Serikali imekuwa ikiwapiga chenga, sasa hivi yanakuwa duplicated kila mahali na sisi hatupati kitu chochote cha ziada. Nilikuwa nashauri inapotokea mtu amebuni kitu, hata kama sio kwenye utalii, lakini kwenye idara yoyote, aweze kupewa nguvu na Serikali, alinde ule ubunifu wake kama ilivyo kwa wale Rajinda Motors ambao walibuni haya magari ambayo ni extended kwa ajili ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la rescue services kwenye Mlima Kilimanjaro. Kuna wafanyabiashara walikuwa na helicopter pale Moshi Airport na ilifanya vizuri sana kwa sababu watu wakija wanachangia, incase akipata shida ile helicopter inafanya rescue. Sasa hivi haipo kwa sababu, baada ya uvico mfanyabiashara yule ilibidi ashindwe ile biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa nashauri Serikali, kama inaweza inaweza kuifanya hii huduma kwa kushirikiana na NHIF pamoja na kampuni nyingine ambazo zinaweza zikafanya ile huduma. Ni huduma muhimu inaweza ikatumika hata nje ya huo utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa namna ambavyo umeendelea kuusimamia mjadala huu na mimi ninachukua nafasi hii kuwashukuru wale wote waliochangia na wote waliochangia wameendelea kuboresha hoja hii na kutuwekea mazingira mazuri ya namna ya kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitagusia baadhi ya maeneo, hakuna ubishi kwamba tunahitaji manpower eneo hili, hilo halina ubishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la zimamoto na uokoaji, baadhi ya watu wamekimbilia kwenye moto tu, lakini mtoto akitumbukia kwenye shimo la choo kunahitajika utaalamu wa kumtoa. Kwa hiyo, ndiyo maana ninasema kuna vitu vingi vya kufanya kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo maana mimi kuna hoja zinazokuja, kwa mfano ile Tume ya Haki Jinai inataka kurudishwa kwenye halmashauri, mimi hilo siliungi mkono kwa sababu badi ninajua halmashauri nyingi hazina uwezo wa kulisimamia hilo.
Mheshimiwa Spika, siyo kwamba halmashauri tu hazina uwezo, hii shughuli ya uokoaji ni shughuli inayohitaji amri za kijeshi, kutumia amri za kiraia moto unawake watu waende siyo rahisi.
Kwa hiyo, kuna baadhi ya vitu vilivyoko kwenye Haki Jinai, mimi sitaki hata kuvigusa. Kwa hiyo, ndiyo maana bado ninasisitiza jeshi libaki kuwa jeshi na hii kazi ifanyike kijeshi, lakini halmashauri tusiondolewe wajibu wetu au namna ya kushiriki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru mchangiaji mmoja amesema hawajazuiwa lakini ninajua kabisa, sisi Moshi Mjini tulikuwa na magari tuliyopewa na miji dada (miji marafiki), lakini lilipokuwa jeshi tuliwapa na jeshi waliamua iende wapi.
Mheshimiwa Spika, mimi kwenye hoja yangu ninamaanisha, kama Moshi Mjini tukishirikiana na ninyi kununua gari au tumepewa na wadau, libaki pale kwa matumizi yetu, jeshi mwendelee kulisimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri, hata pale Moshi Mjini kabla ya gari mpya ambayo tumeipata, gari iliyokuwepo ilikuwa inahitaji service, jeshi halikuwa na hela na halmashauri hawana kifungu cha kwenda kutengeneza gari la Jeshi la Zimamoto. Kwa hiyo, ndiyo maana ninasema kuwe na ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwakumbushe, ushirikiano huu hautakuwa mpya, viwanja vya ndege viliingia makubaliano na jeshi, vyenyewe vinanunua yale magari vinayasimamia, vina-service lakini wanaoyafanyia kazi ni Jeshi la Zimamoto. Kwa hiyo, nilikuwa ninasema hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo ninahitaji ufafanuzi, sikusema iwe lazima kwa sababu siyo kila mahali kuna maghorofa. Ninasema kwa halmashauri zenye uwezo na kuna uhitaji huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Moshi Mjini tumeunguliwa Soko la Mbuyuni, ndani ya mwaka mmoja tumeunguliwa mara mbili. Mara ya kwanza tulilizima likiwa nusu, mara ya pili liliisha lote. Sasa shida iko wapi? Wale wafanyabiashara wadogo hawana insurance. Mtaji wake ukiungua pale na vitu vyake maana yake ndiyo ameanza zero, zero kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wale ni wananchi wetu tunahitaji kuwahudumia na ndiyo maana nikasema halmashauri zenye uwezo na kwa nini nimesema kwenye uwezo, gari itakayohitajika Dodoma kwa jinsi ya majengo yaliyoko Dodoma, siyo sawa na Dar es Salaam. Sisi tunaweza tukanunua ya kufanana nchi nzima, lakini Dar es Salaam wana majengo ya ghorofa 36. Gari yao itahitajika ambayo labda ina lift zaidi na uwezo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, halmashauri ikiona ina sababu ya kuwekeza pale kuokoa maisha na uhai wa wananchi wake, basi iweze kufanya hivyo, lakini kuna maeneo kwa mfano, ninakubaliana kabisa na mawazo yaliyoletwa ya kusema kwamba hili suala linahusisha Wizara nyingi, kwa hiyo ni suala mtambuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli, Wizara ya Ardhi, TAMISEMI, Wizara ya Maji, lazima zikae pamoja katika kupanga kwenye kushughulikia hili jambo. Hilo mimi ninakubaliana nalo 100% kwa sababu fire hydrant nyingi zimefukiwa na barabara na barabara zinajengwa either na TARURA au na TANROADS, lakini fire hydrant ni za Wizara ya Maji na Mamlaka za Maji. Ni lazima wakae pamoja ili kuweza kufanya hayo mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna haja pia ya kuangalia namna ya kuweka ulazima. Kwa mfano, kila mtu anafikiria gari ya fire ni ile ya shilingi bilioni kwa ajili ya kuzima moto, kwenye miji ambayo iko kwenye highway magari yanagongana, mtu yuko hai gari limemminya, kuna vifaa vinahitajika vya kuvunja yale machuma, kukata, kuvuta ili kumtoa, watu wanakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna clips tunazo, mtu alikufa pale Mbeya kwenye Mlima nadhani sijui ni Sekenke, watu wanamwangalia hawawezi kumwokoa. Kwa hiyo, kuna magari madogo labda yanahitajika na vifaa vidogo ambavyo halmashauri inaweza kutokana na eneo lake, basi iweze kufanya hivyo, siyo kuliondoa jukumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jukumu la Serikali na mimi niseme hapa tunasaidiana, ndiyo maana ya ugatuzi, kwa sababu Serikali itaendelea kuwekeza, hata leo ikiwekeza mara mbili ya hela mliyosema, bado mahitaji yapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuseme kwa Dar es Salaam, kwa mfano hata kama mna magari matano, yametokea majanga mawili/matatu, lazima mtahitaji manpower zaidi na magari zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nimeitoa hoja hii ili Serikali iangalie namna ya kuboresha na kushirikiana, lakini halmashauri pia tunaona tuna wajibu wa kuwahudumia wananchi wetu na kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba Serikali ichukue hoja hii na iifanyie kazi pamoja na mapendekezo yaliyotolewa na Wabunge na yale ambayo nilitoa mwanzo ili basi tuweze kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja hiyo. (Makofi)
SPIKA: Wabunge hawajasikia vizuri. Ili niweze kuwahoji, unatoa hoja tena. Kwa hiyo, hiyo sehemu ya mwisho hawajasikia.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, mawazo niliyoyaleta pamoja na mawazo yaliyoletwa na Wabunge, yale yote ambayo yana tija, ninaomba yachukuliwe na Serikali yafanyiwe kazi ili tuweze kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara hii nyeti sana ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ninampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Makamu wake na Wanakamati wote, kwa kweli wamefanya kazi nzuri ambayo inaonesha kule ambako wananchi wameelekea. Pamoja na pongezi hizo nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dada yangu Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Waziri Kaka yangu Mheshimiwa Dunstan Kitandula, Katibu Mkuu Dkt. Abbas pamoja na Naibu Katibu Mkuu CP. Benedict Wakulyamba kwa sababu kwa kweli pamoja na changamoto nyingi zilizopo kwenye Wizara yao, nao wamefanya kazi kubwa, bado tunaendelea kuona namna ambavyo wanapambana, ujangili umepungua, uhifadhi umekuwa bora haya mapungufu kwa pamoja tunaona namna ya kuyarekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwapongeza kwa hatua zao za kusudi kabisa za kuinua utalii. Niliona kwenye habari wiki mbili zilizopita kwamba waliamua kupunguza gharama za leseni zile za utalii kutoka dola 2,000 kwenda dola 1,000 nawapongeza sana na hii ndiyo itakachowasaidia kupata idadi ya watalii. Kwa mfano, Mlima Kilimanjaro target mmeonesha ni kutoka watalii 56,000 kwenda watalii 200,000 hongereni sana na naomba tuwaombee kwamba haya yakazae matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze zaidi pale mlipoona umuhimu wa kupunguza fee au leseni ile ya u-guide kutoka dola 50 kwa kila mwaka mkaweka shilingi 100,000 kwa miaka mitatu. Hii itaongeza kipato cha wale watumishi kabisa ambao ni ma-guide ambao tunawahitaji sana katika kuwaongoza watalii lakini niwaombe mkaangalie sasa maslahi ya hao wengine huko chini, wale wapishi, ma-porter na kadhalika. Hawa wanaweza kupata faida zaidi kama mtaweza kuwaangalia hawa wafanyabiashara wa utalii kuwapunguzia zile kodi ambazo zinaonekana nyingi ni za kujirudia rudia ili basi na wao waweze kuwaangalia wale makuli - porters na wapishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungumzaji waliotangulia walishaongea, moja ya eneo la kuangalia ni barabara. Pamoja na kwamba mmesema fedha zile zitarudishwa kukusanywa kule, hili suala la barabara mimi nadhani, mbona ni kazi ndogo tu, mkiwa na vifaa ninyi mnaweza mkawa mnatumia wale wataalam wa TARURA. Kwa nini katika kila Wizara ama kama Wizara yenyewe msiwe na vifaa kuendana na zone kwa ajili ya kurekebisha zile barabara hasa zile za kwenye mbuga kama Serengeti, Ngorongoro ili kupunguza gharama lakini ili kuweza kuzifanya ziwe nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi watalii, teknolojia inakwenda mbali watalii hawataki tena kurushwa rushwa, vumbi iliyozidi, barabara ni vizuri ziwe nzuri zaidi kwa sababu hata magari yanayokuja model mpya hayastahimili hizi barabara mbovu sana. Kwa hiyo naomba ma-tour operators wanapata hasara sana kwenye gharama ya kurekebisha yale magari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona kwenye habari, wanahabari walienda kutembelea hoteli ya Burigi kule Chato, nimeona inaendelea kutengenezwa taratibu, wasiwasi wangu ni kwamba, kasi ya kuweka hela pale naona ni ndogo, ile hoteli nimeisikia muda mrefu. Ni vizuri tupeleke fedha ya kutosha miradi kama hiyo ikamilike lakini iweze kuleta tija haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho, Serikali haitaweza kuziendesha, nimesikia mchangiaji mmoja amesema na zile hoteli za Serikali zirudishwe, Hapana! hata kama zitarudishwa tutafute wabia. Kuna watu wame-specialize kwenye management, makampuni makubwa tufanye nayo na hii tunaweza kuangalia hata ile Hoteli ya Ngurdoto ambayo nasikia ilikuwa inakufa lakini juzi juzi naona tumefanikiwa kurudisha tena mikutano ya Afrika Mashariki. Namna ya Serikali kulipa lile deni na kununua share na kutafuta management companies hasa hizi za nje ili kuendesha hoteli kama hizo ziweze kuleta tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa Wizara ya Mipango kunatakiwa kulete tija ya haraka sana kwenye Wizara mbalimbali. Kwa mfano tu, Wizara ya Utalii kuna component ya conference tourism naona ipo Mambo ya Nje, AICC ipo pale lakini na ile Julius Nyerere Convection Centre sasa ule ni utalii mkubwa kwa sababu kwanza unaleta biashara kwenye hoteli na baadae wanaenda kutembelea vivutio. Nilikuwa naomba hii Wizara ya Mipango ione namna ya ku-link, vitu kama AICC wanapoenda kwenye utalii hawa TTB wanapoenda kutangaza wana- incorporate vipi? Wanaangalia vipi namna ambavyo inaweza ikaunganishwa pamoja na utalii wetu huu wa wanyama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sehemu kama ATCL linawezaje kusaidia utalii nchini maana kwa mfano tu, kumekuwa na shida kubwa sana ya cancellation kwenye ATCL lakini tulitegemea ATCL ndiyo i-compliment utaliii. Ni namna gani Wizara ile ya Mipango itafanya kazi na Wizara hii ifanye na Uchukuzi ili kuleta tija.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye mahoteli, uwekezaji pamoja na kuweza kupata man power. Kwa hiyo kuna mahali pa kuweza kufanya hizi Wizara ziongee. Wameelezea namna ambavyo wanaangalia man power lakini nataka nikuambie, kwenye man power Tanzania tuna shida kubwa ya customer care, tuna shida kubwa ya kiingereza na lugha nyingine, masoko mapya, Kirusi, Kichina, Kituruki. Ni vyuo gani vinafundisha hayo masomo vizuri ili hao watalii tunaotaka milioni tano watakaotoka kwenye masoko mapya wapate watu ambao wataongea nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuhimu sana hayo mambo yaweze kuunganishwa. Nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia. Pia niungane na wenzangu na hasa Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Sheria Ndogo kuanza kabisa kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wenzangu wamekwenda kwenye case specific, mimi nitakwenda kwenye mambo ya jumla ambayo tunafikiri yataweza kusaidia katika utungaji wa sheria hasa kwenye halmashauri zetu na kwa kuanza kabisa najua Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Ofisi ya Mwandishi wa Sheria pamoja na Wizara wanafanya juhudi kubwa sana kuhakikisha hizi kanuni au hizi sheria ndogo zinaleta tija. Sasa kwa sababu ya makosa ambayo tumeshayaona mara nyingi, nitoe ushauri wa jumla kwanza. Ni vizuri sheria zote za halmashauri zinazokuja hapa kabla hazijaingia kwenye Kamati Ndogo au wakati zinaingia Wabunge wa maeneo husika pamoja na kwamba ni Madiwani wapewe zile sheria na wao wazipitie.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivi kwa sababu zipo sheria ambazo either kwenye mchakato wake wa kutengenezwa kuna maneno yameingia katikati ambayo yanaenda kusababisha kero kwa wananchi; na Mheshimiwa Mbunge anaonekana yeye tayari ni Diwani na amezijadili wakati kiuhalisia Mheshimiwa Mbunge anakuwa hapa Bungeni kwa zaidi ya miezi saba kwa mwaka mzima na hivyo huenda kikao kilichopitisha sheria hizo yeye hakuwepo. Zikienda kuleta kero kule tayari na yeye zinamgusa moja kwa moja
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeyaona hayo kwa sababu baadhi ya Waheshimiwa Wabunge tuliowa-consult kwamba kuna sheria hii inataka kupita kwenye halmashauri yako tunaona iko hivi, unaona kabisa kwamba Mheshimiwa Mbunge hana taarifa. Kwa hiyo huo ni ushauri wa jumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa pili ni halmashauri ambazo zina mchanganyiko wa maeneo yenye miji pamoja na maeneo yenye asili au yanayokuwa yana asili kama ya vijiji. Tumeona kwenye sheria za mifugo, sheria za kilimo pamoja na sheria za mazingira. Unakuta kuna halmashauri, hata Dar es Salaam, kwa mfano Temeke, kuna sheria ambayo ilikuwa inaelezea kuwa na limit ya mifugo na mifugo iwe na kitambulisho nadhani; lakini kuna maeneo katika halmashauri hiyo hiyo yana asili ya kijiji ambayo sheria hiyo ikienda, inaenda kusababisha matatizo. Kwa hiyo, ni vizuri sheria zisiwe generous hivyo ili ziweze kuleta tija zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wameongelea ile sheria iliyokuwa inatoza kodi kwa wapaa samaki, wale wanaokwarua, wanakwangua au, wapaa samaki, sijui Kiswahili sahihi; ambapo walikuwa wanawa-charge shilingi 200 kwa kila mtu. Sasa ukiangalia zipo sheria zinazoelezea asilimia ya gharama za ukusanyaji wa kodi yoyote. Ukiangalia tu hawa hapa wa samaki ambao walikuwa wanatakiwa walipe shilingi 200 ukiangalia kale ka-rim kakuweka kwenye mashine ya EFD kale kashilingi 2,000 kanatoa risiti 100, kwa hiyo risiti mia moja kwa shilingi elfu mbili ukigawanya kale kakaratasi peke yake katakula shilingi ishirini. Hapa hatujapiga mahesabu ya wino, hatujapiga mahesabu ya mkusanyaji, hatujapiga mahesabu mengine yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona kabisa hii kodi ambayo wenzetu walikuwa wanataka kuileta si tu wanaleta usumbufu kwa wale watu wa chini bali pia gharama yake ya ukusanyaji inaweza ikapita hata hiyo shilingi 100, shilingi 200, kwa hiyo, itakuwa haina hata tija kwenye makusanyo ya halmashauri hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na makosa ya jumla; kwa mfano, halmashauri inaleta kodi kwenye eneo ambalo haihusiki tena katika kusimamia. Kwa mfano, sheria ile iliyoletwa na halmashauri ya Mtwara Mikindani ya ku-charge lori kubwa kuingia mjini, si tu kwamba ilikuwa inaleta usumbufu zaidi kuliko wao walivyokuwa wanafikiria kupunguza msongamano, lakini ni dhahiri kwamba barabara za mijini nyingi ni tani 10, haya malori wanayoongelea ni tani 30, wao wanatoa tozo kwenda kukusanya hiyo hela wakati barabara ziko chini ya TARURA. Kwa hiyo, unaona kwamba wanakusanya kwenye eneo ambalo si lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ni kuhusu sheria ya ukataji barabara kwa ajili ya kupitisha miundombinu. Halmashauri inataka kukusanya lakini barabara ni mali ya TARURA. Kwenye hilo la lori kubwa ni kwamba wanakusanya kodi kwenye uvunjaji wa sheria na wala si faini. Maana yake ni kwamba mtu mwenye lori la tani 30 atalipa hiyo hela wanayotaka aingize lori lenye tani 30 likaumize barabara wakati sio mamlaka yao na barabara zimeshahama.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine, kuna halmashauri zinaleta sheria za ukusanyaji ushuru wa mauzo kwa mfano ya nafaka halafu wanasema bei itakayokuwa inatumika ni bei ya soko bila kuonesha ni bei ipi; ya soko, inayotolewa na Wizara, inayotolewa na Benki Kuu au inayotolewa na halmashauri yenyewe. Wanasema tutakusanya asilimia tatu kwa kilo kwa bei ya soko, lakini bei ipi ya soko inayopatikana kupitia chanzo gani. Kwa hiyo, haya yote yanaenda kuleta mkanganyiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho lililokuwa na mkanganyiko; halmashauri nyingi zimeleta sheria ya ukamataji mifugo na wanasema mifugo itakamatwa kwa siku kadhaa na kama fine haitalipwa watapiga mnada. Hata hivyo, kwa huo muda ambao wanakuwa na hiyo mifugo, hawakuonesha wajibu wa halmashauri kwenye kuhudumia hiyo mifugo, chakula, maji na baada ya hizo siku sita kama watakwenda kwenye mnada na mnada ukashindwa kufanyika kwa sababu bei ya soko haikufikiwa, ni nani ataendelea kusimamia hali ya hiyo mifugo kwa kipindi chote. Kwa hiyo, hayo ni mapungufu ambayo kiujumla yameonekana na yatakapoendelea kuboreshwa yatasaidia hizi sheria ndogo zije zikiwa na uhalisia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)