MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia ningeomba niende mbele zaidi kwa sababu uhalisia unaonesha wanafunzi wanaosoma shule za binafsi hawapati mkopo either wote au kiasi, lakini pia kwa sababu ya umuhimu wa baadhi ya fani kama udaktari na gharama kubwa ya kusomesha watoto kwenye fani hizo, Serikali inaonaje kuwa na mpango wa muda mrefu ili wanafunzi wote wameweze kupata mikopo kwa asilimia mia moja?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kama ilivyotokana na jibu langu la msingi, Serikali inaendelea kupanua wigo wa bajeti katika Bodi yetu ya Mikopo. Kwa hiyo naomba nilichukue suala la Mheshimiwa Mbunge kwa vile kutoka mwaka 2017, Serikali imeweza kuongeza bajeti katika bodi ya mikopo kutoka bilioni 427 mpaka hivi sasa tuna bilioni 460. Kutokana na hivyo basi, wanufaika ni wengi na wanaendelea kuongezeka kutoka wale laki moja katika kipindi cha mwaka 2015 mpaka kufikia laki moja na arobaini mwaka 2021.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapoongeza bajeti hii tuna hakika tunaweza kufanya coverage kubwa ya wanafunzi. Naomba kutoa taarifa katika waombaji wa mwaka huu wale wa mwaka wa kwanza maombi yote yalikuwa 66,000, lakini waliopata jumla karibu walikuwa 55,000. Kwa hiyo tunaendelea kuongeza ule wigo kwa lengo kuhakikisha kwamba wanufaika wanakuwa wengi zaidi.