Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Antipas Zeno Mgungusi (17 total)

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Lupiro – Malinyi – Londo – Namtumbo, yenye urefu wa kilometa 296 ambayo ipo katika Ilani ya CCM 2020?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Lupiro – Malinyi – Londo – Namtumbo yenye urefu wa kilometa 296 ni sehemu ya barabara kuu ya Mikumi – Kidatu – Ifakara – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha yenye kilometa 547 ambayo inaunganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii, Wizara kupitia TANRAODS, imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2018. Ujenzi wa sehemu ya Kidatu – Ifakara kilometa
66.9 kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Ruaha Mkuu unaendelea. Fedha kwa ajili ya ujenzi wa sehemu iliyobaki ikiwemo ya Lupiro – Malinyi – Londo – Namtumbo zinaendelea kutafutwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi, Serikali pia imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali ya barabara hii, ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 720 na shilingi milioni 377.2 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii katika mikoa ya Morogoro na Ruvuma mtawalia ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Sehemu kubwa iliyokuwa ikitumika kwa shughuli za uchumi katika Wilaya ya Malinyi imetwaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) mwaka 2017 ambapo waliweka mipaka maarufu kama “TUTA LA 2017” bila kushirikisha wananchi.

Je, Serikali haioni haja ya kurejea na kufanya upya mapitio shirikishi ya mipaka ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo yanayozungumziwa na Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya Pori Tengefu la Kilombero lililoanzishwa mwaka 1952 na kuhuishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 269 la mwaka 1974 likiwa na ukubwa wa Kilomita za mraba 6,500. Eneo hilo vile vile ni sehemu ya ardhi oevu yenye umuhimu kitaifa na kimataifa kutokana na kuhifadhi bioanuai mbalimbali na zilizo adimu duniani kama vile mnyama aina ya Puku. Aidha, Bonde hilo huchangia takriban asilimia 62.5 ya maji yote ya Mto Rufiji na hivyo kuwa chanzo muhimu cha maji kwa mradi tarajali wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere.

Mheshimiwa Spika, aidha tuta linalozungumziwa liliwekwa mwaka 2012 hadi 2013 kwa lengo la kuokoa kiini cha Bonde la Mto Kilombero kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira uliokuwa unaendelea.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2017 ilifanya mapitio ya mipaka ikiwa ni hatua mojawapo ya kuangalia uwezekano wa kurekebisha mipaka (GN) ili iendane na hali halisi kwani kwa asilimia kubwa eneo la hifadhi lilikuwa limeathiriwa na shughuli za kilimo na ufugaji. Suala hili lilipelekwa kwenye Kamati ya Mawaziri Nane iliyoundwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano. Utekelezaji wa mapendekezo hayo umeshafanyika na muda si mrefu wananchi watajulishwa maamuzi ya Kamati hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Wilaya ya Malinyi waendelee kuwa na subira wakati utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri ukiendelea kufanyiwa kazi, naomba kuwasilisha.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Sehemu kubwa ya maeneo ya Kilimo cha Mpunga Malinyi imemegwa na Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) kwa Mipaka mipya iliyowekwa Mwaka 2017 bila maridhiano na Wananchi wa sehemu ya bonde la Kilombero. Je, Serikali haioni kuwa ni vema kufanya upya mapitio shirikishi kwenye mipaka ya eneo la Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la Bonde la Kilombero ni sehemu ya ardhioevu yenye umuhimu kitaifa na kimataifa kutokana na kuhifadhi bioanuai mbalimbali na zilizo adimu duniani kama vile mnyama aina ya sheshe. Aidha, Bonde hilo huchangia takriban asilimia 62.5 ya maji yote ya Mto Rufiji na hivyo kuwa chanzo muhimu cha maji kwa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere.

Mheshimiwa Spika, uwekaji wa mipaka wa Bonde la Kilombero ulizingatia mfumo halisi wa kiikolojia wa Bonde hilo, ili uweze kukidhi matarajio ya uhifadhi wa ardhioevu. Hivyo basi, Pori Tengefu Kilombero lilianzishwa mwaka 1952 kwa GN. Na. 107/1952 na halijawahi kubadilishwa mipaka yake. Naomba kuwasilisha.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kutenga fedha za kuvunja Mlima Londo ili kuunganisha Wilaya ya Malinyi na Namtumbo hata kwa kiwango cha changarawe ili njia hii iweze kupitika huku Serikali ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya Lupiro – Malinyi – Kilosa –Kwa Mpepo – Namtumbo Lumecha ya kilomita 296?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Ifakara – Lupiro –Malinyi – Kilosa Kwa Mpepo – Londo – Lumecha mwaka 2018. Katika usanifu huo, barabara itakayojengwa imeukwepa Mlima Londo kutokana na gharama kubwa ya kuuvunja mlima itakapopita barabara hiyo. Hivyo, Serikali itajenga barabara kwa kiwango cha lami kupita katika maeneo yaliyoainishwa katika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, namsihi Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo barabara hii na kuendelea kuifungua kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Malinyi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi n a Teknolojia naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa vyuo vya mafunzo na ufundi stadi katika Mikoa na Wilaya kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 25 na Mikoa minne nchini kwa lengo la kuwapatia vijana ujuzi katika fani mbalimbali utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Malinyi na maeneo mengine, wananchi wa Malinyi wanashauriwa kutumia Vyuo vya VETA vilivyopo katika Mkoa wa Morogoro ambavyo ni Mikumi, Dakawa, Kihonda, Ulanga pamoja na vyuo vingine vya VETA vilivyopo nchini kwa ajili ya kupata elimu na mafunzo ya ufundi. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kutoa kipaumbele cha ajira kwa Majeshi yote nchini kwa Vijana waliohitimu JKT?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2013 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa maelekezo kwa Wizara zote pamoja na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa. Utaratibu huo umekuwa ukitekelezwa na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kuanzia mwaka 2013 yalipotolewa maelekezo hayo. Aidha, inakumbushwa kuwa lengo la mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwapatia vijana wa Tanzania elimu ya uzalendo, ujasiriamali na kujifunza stadi za kazi ili waweze kujiajiri mara wamalizapo mkataba. Ahsante sana.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga walau kilometa chache barabara ya Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo mpaka Lumecha kilometa 296?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na itaanza kujenga kilometa chache chache za barabara ya Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo hadi Londo mpaka Lumecha yenye urefu wa kilometa 296 hasa kwa kuanza na maeneo korofi ili barabara hii iweze kupitika kwa urahisi wakati wote wa mwaka. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE.ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kurekebisha utaratibu wa kuwaachia makusanyo ya fedha Jeshi la Uhifadhi hasa TANAPA?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kupongeza Serikali ya Awamu ya Tano na Sita kwa kuendelea kutekeleza takwa la kisheria la kuhakikisha makusanyo yote yanaingia kwenye kapu moja (Mfuko Mkuu wa Serikali). Katika kuendelea kutekeleza takwa hilo, Serikali ilibadili Sheria ya Fedha ya mwaka 2020 ambapo jukumu la kukusanya mapato yasiyo ya kodi ikiwemo ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lilikasimiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020, mapato ya Jeshi la Uhifadhi (TANAPA) yalishuka kutokana na kushuka kwa ukusanyaji wa mapato kulikosababishwa na kupungua kwa wageni kufuatia makatazo ya kusafiri na kufungiwa (lockdown) baada ya kuibuka kwa janga la UVIKO-19. Hii ilisababisha Jeshi la Uhifadhi (TANAPA) kushindwa kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hizo za kimapato, Serikali iliamua kugharamia shughuli zote za uhifadhi ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi na kutoa ruzuku ya kugharamia matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Aidha, katika kuhakikisha Jeshi la Uhifadhi (TANAPA) halikwami katika utekelezaji wa majukumu yake kwa wakati, Serikali imekuwa ikitoa fedha za matumizi kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) miezi miwili kabla yaani advance disbursement. Hata hivyo, Serikali itaendelea kufanyia kazi hoja ya Mheshimiwa Mbunge wakati ikiendelea na utaratibu huu hadi hapo itakapoona kama kuna uhitaji wa kubadilisha Sheria.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, lini Jeshi la Uhifadhi litapata Kamishna Jenerali na kuleta muunganiko katika divisheni za NCAA, TANAPA, TAWA na TFS?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu (The Wildlife and Forest Conservation Service) lilianzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Sura ya 283.

Mheshimiwa Spika, utendaji wa taasisi zinazounda Jeshi hilo upo chini ya Kamishna wa Uhifadhi wa kila taasisi nao watakuwa ndio makamanda wa taasisi zao. Muundo wa Jeshi la Uhifadhi unaotumika kwa sasa unafanya kazi vizuri. Endapo kutabainika kuwa na changamoto katika kutekeleza mfumo huo, Serikali itafanya marejeo ya Sheria ya

Wanyamapori ili kuwezesha kuwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali kupitia UCSAF itapeleka minara ya mawasiliano Wilaya ya Malinyi kwa kuwa maeneo mengi ya wilaya hiyo hayana usikivu wa mawasiliano na data?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Jimbo la Malinyi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka wa fedha 2015/2016 na 2020/2021 Kata za Biro, Sofi, Ngoheranga na eneo ilipo Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi zimenufaika na Miradi ya huduma za mawasiliano ya simu kupitia ruzuku ya Serikali. Aidha, ujenzi wa minara katika Kata ya Ngoheranga na eneo ilipo ofisi ya Mkurugenzi inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia mradi wa Tanzania ya kidigitali imeainisha Kata za Igawa na Njiwa ambazo tayari zimepata mtoa huduma wa kuzifikishia huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa minara hii ikikamilika itatoa huduma za mawasiliano katika teknolojia ya 3G na 4G.
MHE. DKT. THEA M. NTARA K.n.y. MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, mpango wa kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa ghala la Taifa la chakula umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kutekeleza mpango wa kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa Ghala la Taifa imeendelea na jitihada za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji ambapo mkoa una jumla ya skimu 233. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 zaidi ya shilingi bilioni 15 zilitengwa kwa ajili ya kuendeleza skimu za umwagiliaji ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, mkandarasi mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu wa Bonde la Kilombero na Ifakara amekwishapatikana ili kupitia taarifa hiyo ya miradi mipya ya umwagiliaji iweze kuanzishwa na kuongeza uzalishaji. Sambamba na hilo, Serikali inaendelea kuboresha huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo sahihi ikiwemo mbegu bora na mbolea na uimarishaji wa miundombinu ya uhifadhi wa mazao baada ya mavuno.
MHE. ANTIPAS Z. MAGUNGUSI aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuwatumia vijana waliopata mafunzo ya JKT kutumikia Jeshi la Uhifadhi kwa mkataba wa muda mfupi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Magungusi, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu imekuwa ikiajiri Askari wenye taaluma kuu tatu ambazo ni Askari waliohitimu Astashahada ya Wanyamapori, Astashahada ya Misitu na Askari waliohitimu Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi hususan Askari, SUMA JKT wamekuwa wakiingia mikataba ambayo inawezesha vijana waliohitimu JKT kupata kazi za mikataba kwa shughuli mbalimbali za ulinzi wa maliasili (wanyamapori na misitu). Mfano, kwa sasa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wameingia mkataba na SUMA JKT kwa ajili ya kuongeza nguvu ya ulinzi wa misitu kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa wa Askari.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Je, kwa nini Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania hawafundishi nje ya nchi hata katika Ukanda wa Afrika Mashariki au Nchi za SADC?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Tanzania ina makocha 19 wenye viwango vya CAF A Diploma ambao wanakidhi viwango vya kufundisha nje ya nchi. Hata hivyo, makocha hawa hawafanikiwi kupata fursa za kufundisha nje ya nchi kutokana na historia ya elimu walizonazo. Hivyo basi, Wizara kwa kushirikiana na TFF wanaratibu mpango wa kutoa mafunzo ya Ukocha kwa wanafunzi wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya michezo ikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Butimba na Vyuo Vikuu nchini ili kupata Makocha wenye sifa.
MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Je, lini Serikali itatoa idhini kwa Makampuni binafsi kutoa elimu ya kujikinga na majanga ya moto kwa Wananchi na Taasisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa makampuni binafsi kushiriki katika shughuli za huduma ya zimamoto na uokoaji nchini, kama vile ufungaji wa mifumo ya kuzima moto, usambazaji na matengenezo ya vifaa vya kuzima moto kwa wananchi na taasisi. Serikali itafanya marekebisho madogo ya kanuni ya ukaguzi, tozo na cheti ya mwaka 2008 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kutambua na kujumuisha makampuni binafsi katika utoaji wa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa masharti na vigezo vitakavyowekwa na Serikali, nashukuru.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Je, lini Mkandarasi wa Barabara ya Lupilo, Malinyi, Kilosa kwa Mpepo hadi Londo ataanza kazi kwa mtindo wa EPC + F?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara kwa utaratibu wa EPC+F unahusisha kufanya usanifu wa barabara kabla ya kuanza ujenzi. Kwa sasa Mkandarasi ameanza na anaendelea na usanifu wa kina. Aidha, Serikali na wakandarasi wanaendelea na taratibu za kupata fedha kwa ajili ya malipo ya awali kwa miradi yote ya EPC+F ukiwemo huu wa barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo hadi Lumecha Mkoani Ruvuma. Ahsante.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS K.n.y. MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza kulipa fidia wananchi wa Kijiji cha Ngombo waliopisha Hifadhi ya Pori Tengefu la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Ngombo kipo katikati ya eneo la ardhi oevu ndani ya Pori Tengefu Kilombero. Uwepo wa kijiji hiki pamoja na vijiji vingine ndani ya pori hilo ulifanya ukubwa wa eneo la pori kupungua kwa 61.5% kutoka kilometa za mraba 6,500 hadi kilometa za mraba 2,500. Hali hiyo ilipelekea Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri Nane kuelekeza Kijiji cha Ngombo kufutwa na wananchi wake kuhamishiwa maeneo mengine sambamba na eneo la Pori Tengefu Kilombero kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia hatua hiyo, Serikali imeshakamilisha zoezi la uthamini kwa wananchi wa Kijiji cha Ngombo kwa vitongoji vyote vitatu vinavyounda Kijiji hicho ambavyo ni Idenge, Ikwachu na Ifuru. Aidha, jumla ya shilingi 7,351,097,480.46 zimeainishwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi hao. Wizara inasubiri fedha kutoka Hazina ili iweze kulipa fidia kwa wananchi ili waweze kuondoka katika eneo la hifadhi na eneo hilo kuendelea kusimamiwa kama Pori la Akiba Kilombero kwa mujibu wa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura ya 283.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuondoa miradi chini ya shilingi milioni 100 katika Mfumo wa NeST ili kupunguza ucheleweshaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, Mfumo wa NeST unawezesha matumizi ya njia ya ununuzi wa thamani ndogo usiotumia fedha taslimu (Minor Value Procurement Method) kwa kazi za ujenzi hadi zenye thamani ya shilingi milioni 100. Kwa njia hii, taasisi nunuzi inaweza kununua moja kwa moja kutoka kwa muuzaji wa bidhaa, mkandarasi au mtoa huduma bila kuhitaji kuwashindanisha wazabuni zaidi ya mmoja. Kwa kupitia mfumo wa NeST, taasisi nunuzi itatumia siku zisizozidi tatu kukamilisha mchakato wote hasa kwa ununuzi wa miradi yenye thamani chini ya shilingi milioni 100.

Mheshimiwa Spika, hivyo taasisi nunuzi zinashauriwa kutumia mfumo wa NeST na kuchagua njia ya ununuzi inayoendana na thamani ya mradi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hasa hasa yenye thamani chini ya shilingi milioni 100, ahsante sana.