Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Antipas Zeno Mgungusi (15 total)

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya barabara hiyo kutoka Kijiji cha Misegese kufika Malinyi Mjini huwa haifikiki kipindi chote, hata mvua ikinyesha siku moja tu, tunalazimika kutumia mitumbwi kufika Malinyi Mjini na magari hayafiki kabisa. Mkandarasi ambaye yuko site anaweka calavat moja badala ya yanayotakiwa kama sita au saba. Amepewa kazi ya kuinua tuta mita 200 badala ya kilometa moja ambayo ni uhitaji halisi. Je, Serikali haioni haja ya kumuongezea uwezo kujenga kulingana na uhitaji ambao nimeutaja?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda Malinyi baada ya Bunge hili ili kujionea hali halisi ya miundombinu na kutafuta suluhisho la pamoja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mgungusi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na swali la mwisho, naomba niseme kwamba barabara hii imekuwa inaulizwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengi ambao ni wanufaika wa barabara hiyo. Kwa hiyo, niwadhihirishie ama niwaaminishe kwamba mara baada ya kikao hiki nitahakikisha naitembelea barabara hiyo ili niweze kuifahamu vizuri kwa sababu kila mara Wabunge wa eneo hilo wananifuata kwa ajili ya kutafuta utatuzi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili alilouliza kuhusiana na tuta linalojengwa na mkandarasi, naomba Mheshimiwa Mbunge Mgungusi kwa sababu, bahati nzuri mkandarasi yuko site, tutaongea na Meneja wa TANROADS ambaye ndiye anamsimamia mkandarasi huyu ili kama kuna shida ya kitaalamu ama ya uwezo, Serikali tutahakikisha kwamba tunampa maelekezo ya afanye vile inavyotakiwa kama ambavyo ipo kwenye design. Ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Februari nilitoa ombi kutokana na majibu hayo kwamba Kijiji cha Ngombo ambacho kinatajwa kihame tuliomba tuko radhi kipunguziwe ukubwa wa mipaka na kupunguza mifugo Zaidi ya 90% ili wananchi waweze kubaki sehemu iliyobaki ichukuliwe kwa ajili ya uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia eneo kubwa la Jimbo huo mpaka wa 2017 tuliomba tupewe walau mita 700 kama siyo kilomita 1 kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kwa maana umbali sehemu ambayo tunafanya shughuli mpaka mto ni mrefu sana tofauti na ambavyo inasemwa kiujumla. Kwa hiyo, je Serikali iko radhi kuridhia maombi haya?

Mheshimiwa Spika, la pili, majibu ya Naibu Waziri kuhusu wanashughulikia hii Tume ya Mawaziri nane ni tangu mwaka jana wanasema tunashughulikia tutajibu tutajibu watu tuko pending hatufanyi shughuli za kilimo, hatujui hatma yetu. Lini hasa Serikali itatoa msimamo wa mwisho juu ya jambo hili ili tuendelee kuwaza mambo mengine tulimalize?

Mheshimiwa Spika, la tatu, kwa wale ambao tayari wameshalima Wizara inaridhia kipindi hiki tuweze kuvuna? Ahsante
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ningependa kutoa ufafanuzi kwa Mheshimiwa Antipas kwamba mipaka ya Bonde Tengefu la Kilombero iliwekwa mwaka 1952 kwa GN Namba 107 na ikarejewa mwaka 1997. Mipaka hiyo haijawahi kurekebishwa mpaka sasa kilichofanyika ni wananchi wa maeneo mbalimbali kuvamia maeneo hayo na kutokana na uvamizi huo Serikali ikachukua hatua ya kuunda kamati maalum ya Mawaziri ikiongozwa na Waziri Mwandamizi Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi ambapo taarifa yake imefikia hatua ya mwisho tunaenda kutoa tathimini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo maombi hayo yote tayari Mawaziri walishakwenda kule wamefanya tathmini ripoti iko tayari na watajulishwa wananchi. Kuhusiana na kulima hatuwezi kuendelea mtu kulima ndani ya hifadhi. Kwasababu mpaka unajulikana unaposema unaomba tulime maana yake unataka tulime ndani ya hifadhi madhara ya kulima ndani ya hifadhi hii ni kuhujumu mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, tusubiri maelekezo ya kamati maalum ya Baraza la Mawaziri tutajua hatma ya suala hili.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, wakati tunasubiri hatma ya mgogoro wa bonde hilo na mipaka hiyo kutoka kwa Kamati ya Mawaziri Wanane maisha yaliendelea na wananchi wa kule tulilima na sasa mpunga uko tayari kwa ajili ya kuvunwa. Je, Wizara haioni haja ya kutoa ushirikiano na wananchi tuweze kuvuna mpunga huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antipas, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli bonde hili kuna baadhi ya wananchi walikuwa wamevamia kwa ajili ya kilimo na sasa hivi ni kipindi cha mavuno. Kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inaweza ikawaruhusu na sisi kwa sababu, yale ni mazao na ili kuepuka njaa kwa wananchi wetu. Na kwa kuwa Serikali hii inawathamini wananchi, tutatoa vibali maalum ambavyo vitawasaidia kwenda kwenye maeneo hayo wavune kwa utaratibu ambao utasimamiwa na Serikali.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nilijitahidi kuwa specific kidogo; watu wa Malinyi na Namtumbo na Ruvuma yote tunahitaji kuona Mkoa wa Morogoro na Ruvuma unaunganishwa kwa maana ya kufunguliwa. Suala la lami tutavumilia kusubiria, tunajua gharama ni kubwa, kilometa ni nyingi, lakini kuunganisha tu hata kwa kiwango cha vumbi; je, Serikali iko tayari?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama inaridhia, iko tayari kuweka fedha kidogo kwa ajili ya barabara hiyo katika bajeti inayofuata? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antipas Mgungusi Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema, eneo analoliongelea lina milima mingi na linapita kwenye safu ya Mbuga ya Selous, ina urefu wa takribani kilometa zisizopungua kama kilometa 100. Ndiyo maana katika jibu letu la msingi tumesema tumeona tumefanya tathmini, kuvunja ule mlima ni gharama sana.

Kwa hiyo, kuna haja ya kutafuta fedha kubwa ili katika huo mradi tuweze kupindisha barabara kuzunguka hiyo milima ili tuweze kuwa na uhakika wa kuipitisha hiyo barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lake limechukuliwa, lakini ni wazi kwamba fedha inayohitajika ni eneo la zaidi ya kilometa 100. Kwa hiyo, ni bora tukaamua kabisa kuujenga huo mradi. Hata hivyo, bado tumeendelea kutoa fedha kidogo ili kufungua kulingana na fedha inavyopatikana kuunganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro kati ya Wilaya hizo mbili za Malinyi na Namtumbo. Ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi ambao wanamaliza kKidato cha nne Wilaya ya Malinyi ambao hawaendelei na masomo ya Kidato cha Tano wako zaidi ya 600 kila mwaka; na wengi wao kimbilio lao lilikuwa ni kilimo; na sasa kutokana na mgogoro kati ya Wizara ya Maliasili (TAWA na wananchi wa Malinyi) kuna uwezekano mkubwa tukapoteza maeneo ya kulima. Wanafunzi hao wanahitaji ujuzi wa ziada kwa ajili ya kujikwamua nje ya kilimo:-

Je, Serikali haioni haja ya kuiingiza Malinyi katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antipas kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, anayoyazungumza Mheshimiwa Mbunge ni kweli, uhitaji wa vyuo hivi ni mkubwa sana sio tu kwa Malinyi. Kama nilivyozungumza kwenye jibu langu la msingi kwamba tunamalizi ujenzi wa vyuo hivi 25 katika wilaya 25 pamoja na mikoa minne nimuondowe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge katika bajeti ijayo iwapo Serikali tutapata fedha kipaumbele cha kwanza itakuwa ni eneo hili la Malinyi na maeneo mengine ambayo yenye uhitaji mkubwa ukilinganisha na maeneo mengine tayari yanavyuo karibu.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini na maswali mawili la nyongeza.

Swali la kwanza; agizo la Serikali kwa Wizara nyingine kutoa kipaumbele cha ajira kwa Vijana wa JKT limetekelezeka kwa kiwango gani tangu 2013?

Swali la pili; inafahamika kuwa malengo ya mafunzo ya JKT siyo ajira, bali ni kufundisha ujasiriamali na uzalendo. Je, Serikali haioni haja sasa kuaajiri kutoka JKT kwa kufuata mtiririko ule wa first in first out? Kwa maana operesheni ya mwanzo wawahi kuajiriwa kuliko wale wanaofuata ili kutovunja moyo vijana wetu wazalendo. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Antipas Mgungusi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la first in first out, huu ndiyo utaratibu ambao unatumika, lakini wakati mwingine kunakuwa kuna uhitaji wa utaalam maalum au sifa maalum, kwa hiyo pamoja na kwamba mfumo wa first in first out unatumika, unaweza ukatumia mfumo huu lakini kundi la kwanza usipate watu wenye zile sifa maalum ambavyo Vyombo Vyetu vya Ulinzi na Usalama wanatafuta, kwa hiyo unalazimika kwenda kwenye kundi la pili.

Mheshimiwa Spika, hoja ya Mheshimiwa Mbunge nimeielewa na ndiyo maana hata Waheshimiwa Wabunge wengine wamepiga makofi wakiashiria kwamba ni swali la msingi. Kwa hiyo, tunachokifanya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, sasa hivi nimeunda Kamati ambayo tunashirikisha Wizara mbalimbali hasa Wizara ambazo ni productive sectors. Wizara ya Kilimo, tayari tunashirikiana nao ninamshukuru Mheshimiwa Bashe, upande wa Kilimo cha kimkakati, tunashirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, tunataka tupanue mawanda au scope ya JKT kwa kushirikisha sekta nyingine. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Viwanda na Biashara na taasisi ambazo zipo chini ya Wizara hizi. Kwa mfano, SIDO, VETA, TIRDO, TEMDO lakini benki yetu ya TADB. Asilimia 10 za vikundi kwenye Halmashauri tukae pamoja kama Serikali tuwe na mkakati wa pamoja ambao utashirikisha Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara hizi na Taasisi hizi ili kusaidia kutengeneza commitement ya ajira Milioni Nane ambazo tumeahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kupitia Jeshi la Kujenga Taifa kwa sababu tunaandaa vijana kwenye kujifunza stadi za kazi, basi kwa mawanda hayo tunaweza tuka-absorb vijana wengi zaidi ambao wanamaliza mafunzo ya kujitolea wanarudi nyumbani. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini barabara hiyo ambayo anaizungumzia kwa sasa kuna dharura kwa maana ya mawasiliano yamekatika baina ya Malinyi na Morogoro Mjini.

Je, Wizara iko tayari kuiongezea TANROADS Mkoa fedha na kuielekeza ku-attend dharura hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi Mbunge wa Malinyi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara ya Malinyi ni kati ya wilaya ambazo ziko chini na hii barabara mvua nyingi zinazonyesha milimani zinapita huko, kwa hiyo kuna changamoto kubwa ya mvua kupita juu ya barabara. Kwa kulitambua hilo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imeliona na mpango kwanza ni kuongeza fedha kwa maana ya bajeti ili tuweze kuinua hiyo barabara na kuongeza makalavati sehemu ambazo maji mengi yanapita. Ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali ambayo sijaridhika sana. Kimsingi nilitarajia nijibiwe swali na Wizara ya Fedha, lakini hamna shida kwa sababu Serikali ni moja. Ilikuwa ni nia njema ya Serikali kuokoa Jeshi la Uhifadhi kwa maana ya kufanya operesheni zake kutokana na uwezo wao mdogo wa kuingiza mapato kipindi cha COVID. Sasa hivi kuna jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na Serikali hasa Mheshimiwa Rais katika kuifungua nchi. Tunatarajia wageni watakuwa wengi na Jeshi la Uhifadhi litaweza kujiimarisha. Je, Serikali haioni haja sasa kubadilisha sheria ili TANAPA na TAWA waweze kukusanya fedha zao wenyewe na kuendelea kupeleka gawio Serikalini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antipas Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwenye jibu la msingi nimesema wazi kabisa kwamba ni vyema fedha yote inapokusanywa ikaingia kwenye kapu moja ili kuona hata vyanzo vyetu vya mapato tunapataje. Pamoja na yote hayo maelezo yangu yalikuwa ni kwamba kipindi hiki ambacho sasa tumeanza kuimarika, bado tunachechemea, nikimaanisha kwamba Serikali bado inalisaidia hili Shirika la Uhifadhi (TANAPA). Kwa hiyo tutakapofikia mahali ambapo tunasimama wenyewe basi Serikali itaona kama kuna haja ya kubadilisha sheria tutaleta ndani ya Bunge lako Tukufu na sheria itaendelea kurekebishwa. Ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ni standard ya kawaida kwa taasisi zote za Serikali, lakini hasa majeshi, kuwa na kiongozi mkuu wa taasisi husika kwa ajili ya chain of command, lakini Jeshi la Uhifadhi halina kiongozi mkuu kwa maana ya divisheni zile TFS, TAWA, TANAPA, kila mtu ana-operate mwenyewe anavyoona inafaa. Sasa ikitokea viongozi wakuu wa nchi wanataka kuongea na majeshi wao Jeshi la Uhifadhi wanampeleka nani kuwawakilisha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu kwamba wakiona changamoto wataanzisha mchakato wa kubadilisha sheria ili kupata kamishna. Anataka aone changamoto gani ilia one sasa kuna uhitaji wa kuwa na Commissioner General wa Jeshi la Uhifadhi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la msingi ni kwamba taasisi hizi zina majukumu tofauti. Ukiangalia utekelezaji wa majukumu yao unaendana sambamba na namna ambavyo majeshi haya yameundwa. Kwa mfano kwenye Taasisi za TANAPA na Ngorongoro, taasisi hizi zina baadhi ya vitu ambavyo vinaruhusiwa kutumika lakini kuna baadhi ya taasisi ambazo zinazuia kama TAWA na TFS.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye upande wa TAWA na TFS tunaruhusu masuala ya uvunaji na uwindaji wa kitalii. Kwa hiyo, utaona yale majukumu yenyewe ya taasisi yanatofautiana. Kwa hiyo, kila kamishna wa uhifadhi anatekeleza majukumu kulingana na muundo wa taasisi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa sasa hivi tunaona bado wanafanya kazi vizuri na wote wanaripoti kwa Katibu Mkuu, kwa hiyo mkuu wa nchi anapotaka kuzungumza na majeshi haya anazungumza na Katibu Mkuu ambaye ndio msemaji wa Wizara kwa upande wa utendaji.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa maoni yake, tunayapokea na pale ambapo tutaona kwamba kuna uhitaji sasa wa kuunda jeshi ambalo litakuwa na mwakilishi ambaye ni Kamishna Jenerali, basi tutafanya hivyo na tutapitia kanuni zetu ili tuendane sambamba na majeshi yaliyopo.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mpaka hivi ninavyozungumza Ofisi ya Halmashauri ya Malinyi bado hakuna mawasiliano na mkandarasi hajafika site. Hata hivyo ninafahamu kwamba mfuko wa mawasiliano kwa hiyo (UCSAF) walishatoa fedha ila TTCL ambao walipewa kazi hawajafanya mpaka sasa hivi;

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kuambatana na mimi weekend hii wewe au Mkurugenzi wa TTCL na UCSAF kwenda Malinyi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sehemu kubwa ya Jimbo la Malinyi hasa Kata ya Usangule, Sofi na Itete kwenye vijiji kama Dabadaba hakuna mawasiliano kabisa.

Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antipas, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali iliingia mkataba wa bilioni 10.88 na Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL, ambapo katika fedha hizo zingine zinaenda katika Halmashauri ya Malinyi ambayo ni milioni 320 kwa ajili ya kujenga mnara wa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano TTCL kuhakikisha kwamba, pamoja na Halmashauri ya Malinyi na halmashauri nyingine zote 33 ambazo tumeingia nao mkataba wahakikishe wanakamilisha miradi hii ndani ya wakati, kwani kwa kufanya hivyo tutawarahisishia halmashauri kukusanya mapato na vilevile wananchi wataweza kupata huduma ya mawasiliano bila kuwa na changamoto yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kipengele cha pili, kata ambazo Mheshimiwa amezitaja mimi nilifanya ziara na yeye tukiwa pamoja katika jimbo lake; Kata ya Itete katika eneo linaitwa Madabadaba na Usangule, Kilosa Mpepo, yote hayo yameepata watoa huduma katika mradi wetu wa Tanzania ya kidigitali. Kwa hiyo tunaamini kwamba kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambayo ameyatoa ni kwamba ni lazima mikataba hii ikatelezwe ndani ya muda ambao tumekubaliana. Kwa hiyo tunaamini kwamba ndani ya miezi tisa mkataba huu ukikamilika wananchi wa eneo la Malinyi watapata huduma ya mawasiliano.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na nia njema ya kutumia SUMA JKT kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye jeshi la uhifadhi na ninajua malipo yao kidogo ni makubwa ukilinganisha na watu ambao wana- volunteer; je, Wizara sasa haioni haja ya kutumia vijana ambao wapo kambini au mtaani lakini hawapo SUMA JKT? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, vijana wetu waliomaliza elimu ya wanyapori kwa maana ya Mweka, Pasiansi na Olmotonyi ambao wapo mtaani kwa sasa, Wizara haioni haja ya kuwapa mkataba wa muda mfupi na kuwalipa posho? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kuwa ni Mhifadhi Mkuu na amekuwa akitumikia Serikali kwa miaka ya nyuma akiwa Mhifadhi, lakini kwa sasa hivi Serikali ilishaanza kuwatumia hao vijana wa JKT. Hivi ninavyoongea, tayari taasisi zinaajiri. Pia tumeanzisha makampuni ambayo vijana ambao hawajapata ajira za Serikali wanaingizwa kule na taasisi zetu zinachukua vijana kutoka kwenye makampuni hayo. Kwa hiyo, utaratibu huu tunaendelea nao. Wale waliopo kambini tunawatumia pia kwa ajili ya doria za muda mfupi pale ambapo inapojitokeza changamoto za wanyama wakali na waharibifu.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki na mnafahamu kamati za kitaifa nyingi ni za wazi. Kwa mfano, ile Kamati ya Makinikia mnaikumbuka, kamati ya hamasa ya Taifa Stars inafahamika. Kwa nini, kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki? Je, Serikali wako tayari kuitangaza ili tuwafahamu?

Swali la pili, mchakato ni wa muda mrefu sana nadhani unafahamu. Serikali inahitaji muda gani wa ziada ili kuhitimisha jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Antipas Mgungusi kwamba, Kamati hii haikuwa ya siri. Kamati hii ilitangazwa tarehe 20 Julai, 2022 baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Mwenyekiti, wake alikuwa Profesa Hermas Mwansoko na Katibu wake alikuwa Dkt. Emmanuel Temu, ikiwa na Wajumbe tisa, wakiwamo Masoud Ali Kipanya, Mrisho Mpoto, Ndugu Khadija Mwanamboka, Ndugu Mwanajuma Ali na wengineo. Kamati hii ilishakamilisha kazi yake kwa hiyo, hili jambo limerudi kwa Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ndiyo inafanya hatua za mwishoni za kukamilisha mchakato huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hamu yetu kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuona kwamba, mchakato huu unakamilika kama ambavyo ni hamu ya Mheshimiwa Mbunge Antipas. Kwa hivyo, mahali ilipofika sasa hivi ni mwishoni kabisa. Hivyo, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni inafanya michakato wa kumalizia kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwaka huu wa 2024 hautakwisha kabla hatujajipatia vazi la Taifa, ahsante. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, hao makocha ambao amewataja, wamesoma Leseni A ya CAF mwaka 2016, mpaka leo TFF haijawapatia vyeti vyao, hali ambayo inawakwamisha kutafuta ajira nje ya nchi. Je, ni lini watapewa vyeti vyao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Ni utamaduni wa nchi yetu kulinda ajira za ndani dhidi ya wageni mpaka pale itakapothibitika taaluma hiyo haipo hapa ndani. Hapa tuna makocha wengi ambao wapo mtaani hawana kazi, lakini wageni wamekuwa wakija kwa wingi sana kufundisha vilabu vyetu hata vile vya daraja la kwanza. Wenzetu wa Zambia na Namibia wameweka utaratibu kuwalinda makocha wazawa kwa maana ya kwamba, kufundisha ligi kuu ya kwao, mpaka uwe umefundisha timu ya Taifa huko ulikotoka: Je, Serikali ya Tanzania ina mpango gani kulinda walimu wa mpira wa ndani?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Antipas Zeno, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Mheshimiwa Antipas amependa kufahamu hatima ya makocha hawa ambao walipewa mafunzo mwaka 2016 chini ya TFF pamoja na CAF. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba jambo hili limekuwa likifuatiliwa kwa karibu na wenzetu wa TFF, na bahati nzuri miongoni mwa watu ambao walikuwa kwenye mafunzo haya ni pamoja na Katibu Mkuu wa TFF Kidau na jambo hili wamekuwa wakiwasiliana ni jinsi gani walimalize ili hawa makocha waweze kupata haki yao.

Swali la pili, alipenda kufahamu mkakati wa Serikali wa kuweza kuwalinda makocha wa ndani kwa sababu sasa tumeshaanza kuwazalisha. Sisi kama Wizara tunafahamu kwamba vijana wetu wanapokuwa na sifa lazima tuwalinde. Tuna mkakati wa Wizara yetu wa kukuza michezo wa mwaka 2021 mpaka 2031, miongoni mwa vitu ambavyo tunakwenda kuzingatia ni kuhakikisha tunatoa kozi kwa makocha wetu. Ndiyo maana hata sasa kozi inaendelea, zaidi ya nchi tatu zinashiriki. Watakapofuzu vijana zaidi ya 20 wa Kitanzania, maana yake wataendelea kupewa fursa, ahsante. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini kwa sasa wakati tunasubiri mchakato huo, barabara ya Malinyi imefungwa, haipitiki kwa maana ya barabara ya TANROADS. Je, Serikali ipo tayari kupeleka fedha za dharura kwa Meneja wa TANROADS wa Mkoa kwa ajili ya kutatua dharura hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TANROADS tayari wanaendelea na shughuli za kuifungua barabara. Tulituma fedha za awali, na tayari Meneja wa Mkoa wa Morogoro, mkoa ambao umeathirika sana, ameishaingiziwa fedha tangu jana kwa ajili ya kuendelea kufungua barabara ambazo zimejifunga. Ahsante. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wakandarasi wengi wale ambao wana sifa za kuendana na mfumo kwenye miradi midogo hawapatikani vijijini, mara nyingi wanatoka mijini. Muda wao wa kuji-mobilize kufika site kutoa huduma unakuwa mwingi na kazi huwa zinachelewa. Je, Serikali haioni haja ya kuhakikisha kwamba inawapa upekee local fundi au wakandarasi wadogo kutotumia mfumo au kujengewa uwezo ili waweze kutosheleza vigezo vyao kusudi kazi ziweze kufanyika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antipas, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baadhi ya wakandarasi wale wadogo wadogo bado iko changamoto ya uelewa juu matumizi ya mfumo huu, lakini Serikali itaendelea kutoa elimu kwa local fundi na wale wote wenye mahitaji ya matumizi ya mfumo huu, ahsante.