Questions to the Prime Minister from Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe (3 total)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la kwanza. Tangu mwaka 2019, Serikali ilisitisha kutunga na kutoa mitihani kwa wanafunzi ambao walikuwa wanasoma masomo ya ufundi kwenye zile shule za msingi za ufundi na kusababisha miundombinu ya Serikali, vifaa vya kujifunzia, Walimu na samani nyingine ambazo zilikuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kutoa mafunzo haya ambayo ni muhimu sana. Je, Serikali ina mpango gani sasa kufufua shule hizi za msingi za ufundi ambazo pia ni mahitaji sana kwa Tanzania. Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali iliona umuhimu wa kutoa elimu ya ufundi kwa vijana wetu kuanzia umri mdogo na Serikali ikaanzisha mafunzo hayo kuanzia ngazi ya shule ya msingi. Hata hivyo, kwa kuwa tunazo shule nyingi za msingi, Serikali haikumudu kutoa vifaa vya ufundi kwa kada zote, kwa sababu ufundi upo maeneo mengi. Hapa ndipo Serikali ikaona ni muhimu kuanzisha mfumo wa kuwa na vyuo maalum vinavyoweza kuwapata vijana wale na kuwapeleka maalum kwenye chuo ambacho kimeandaliwa, kina vifaa na Walimu ili kuweza kuwapatia mafunzo na baadaye mafunzo hayo kuyaweka kwenye level ambayo pia inaweza kumsaidia kwenda kwenye level au ngazi nyingine. Kwa hiyo, Serikali iliamua kuimarisha VETA na ikaiondoa VETA kutoka Wizara ya Kazi na kuileta kuwa chini ya Wizara ya Elimu ambayo inasimamia sera ya elimu yote nchini.
Mheshimiwa Spika, VETA hiyo imeendelea kuchukua vijana wetu, mwanzo ilikuwa inachukua vijana waliomaliza kidato cha nne, lakini baadaye tukapanua wigo tukajenga vyuo kwenye ngazi ya mikoa yote nchini; ni zoezi ambalo limekamilika kwa sasa. Baadaye tukaona tupanue wigo huu tuweze kutoa fursa nyingi kwa vijana wetu na Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa VETA kila Wilaya, ni zoezi ambalo linaendelea sasa kwa lengo la kuwapatia vijana hawa fursa ya kwenda kusoma ufundi katika nyanja mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, wanaokwenda VETA ni wa kuanzia waliomaliza elimu ya msingi, kidato cha nne na kule sasa tumeweka level mbalimbali; hatua ya kwanza, ya pili, ya tatu na hatua zote wanafanya mitihani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali iliona ni busara kuanzisha vyuo maalum ambavyo tutaweza kuweka vifaa vya kutosha na Walimu wa kutosha ili kuweza kutoa elimu hiyo kwa urahisi na kwa uhakika zaidi, ndilo zoezi ambalo kwa sasa linaendelea nchini kote. Hata hivyo, tuliamua kutumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) navyo pia vikahamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii vikaletwa Wizara ya Elimu ili tuweze kusimamia sera ile ile ya kuwezesha vijana kuwa na ujuzi kuwa na utaalam kwenye sekta mbalimbali ili iweze pia kuchukua wanafunzi mbalimbali. FDCs pia inachukua hata wale ambao hawajamaliza darasa la saba wanajifunza uashi, useremala, sasa hivi TEHAMA, lakini pia ushonaji na karibu sekta zote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuuimarisha utaratibu huu na kutoa fursa zaidi kwa watoto wetu nchini kupata ujuzi mbalimbali. Programu hizi zinaendelea Wizarani hata Ofisi ya Waziri Mkuu nayo pia imeanzisha programu inayowachukua wote waliomaliza darasa la saba hata chuo kikuu kuwapa uwezo wa kufanya ujuzi. Wakimaliza kozi yao kwa muda huo waliopangiwa wanaweza kufanya shughuli nyingine za kujiajiri, wanaweza pia kuajirika na kuanzisha kazi ambazo zinaweza kuwasaidia wao ikiwemo na kilimo pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuliona kule chini uwezo wa kupeleka vifaa vyote katika kila shule ya msingi kwenye shule zetu 12,000 isingewezekana. Kwa hiyo, hivi vyuo sasa vinakuwa na nafasi nzuri na ndivyo hivyo ambavyo tunavijenga kwenye ngazi ya Wilaya. Hayo ndiyo malengo ya Serikali. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa nyakati mbalimbali wakati ugonjwa wa Covid 19 umeshamiri wananchi wengi waliokuwa wanaishi nje ya nchi walirejea nchini, ikiwemo wanafunzi waliokuwa wanaendelea na masomo kwenye kada mbalimbali.
Pia hivi karibuni wakati vita ya Ukraine na Urusi inaendelea hali kadhalika wananchi wakiwemo wanafunzi wamerejea nchini. Wanafunzi ambao walikuwa wanaendelea na masomo kwenye kada mbalimbali na kwenye vyuo mbalimbali nchini sasa hivi wako hapa nchini wengine wamesitisha masomo kabisa, wengine wanasoma kwa njia ya mtandao kwa mazingira magumu sana. Ni nini kauli ya Serikali kwa wanafunzi hawa ambao wamekosa masomo? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mbunge Hai Mkoani Kilimanjaro kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna vijana wa kitanzania wanasoma kwenye vyuo mbalimbali nje ya nchi na ugonjwa huu wa Covid 19 ulipoingia nchi kadhaa ziliamua kuwarudisha vijana kwenye nchi zao wakiwemo vijana wetu wa kitanzania ambao walikuwa wanasoma huko na wamerudi. Na si tu Covid 19 hata hii vita inayoendelea nchini Urusi na Ukraine tunaona vijana wetu wengi wamerudi hapa nchini. Nini kinafanyika hapa ndani ya nchi kuokoa miaka waliyoipoteza kwenye masomo?
Mheshimiwa Spika, tulitoa tangazo kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu kwamba vijana wote wa kitanzania waliorudi kutoka nje waliokuwa wanasoma nje kuja nchini waripoti Wizara ya Elimu ambako pia Taasisi ya TCU inayoshughulikia vyuo vya elimu ya juu kwa sababu wengi wanasoma vyuo vya elimu ya juu waende wakieleza elimu yao walikuwa wanasoma course gani, wamefikia kipindi gani halafu tuone ufaulu wake huo kutoka hapo alipo mpaka alipoishia ili sasa Taasisi yetu ya TCU iweze kuchukua zile alama. Wanavyo vigezo vyao ambavyo vinatumika katika kurasimisha taaluma waliokuwa wanasoma nje na taaluma iliyoko ndani ili waweze kuendelea na vyuo vya ndani, utaratibu huo ndio tumeutumia.
Mheshimiwa Spika, sasa kama wako vijana ambao wamerudi utaratibu huu haujawapitia kuna mambo mawili. Moja atakuwa hajaenda kuripoti ili apate huduma hiyo; lakini mbili course anayoisoma kama inafanana na course ya Tanzania, course zetu zina vigezo vya kimataifa. Anaweza kuwa alikuwa anasoma chou ambacho hakifikii viwango vya vyuo tulivyonavyo nchini hawa watakuwa bado hawajapata nafasi hiyo mpaka pale ambapo watapewa ushauri wa course gani sasa anaweza kuianza hapa nchini ili aweze kuisoma.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna hayo mambo mawili ambayo Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua ya kwa nini vijana wengine ambao hawajarasimishwa kuingia kwenye vyuo mpaka leo wako nje ya vyuo.
Kwa hiyo, nitoe wito kwa watanzania wale ambao wameenda kusoma nje wamerudi nchini kwa matukio yote mawili covid 19 na vita ya Ukraine na Urusi waripoti TCU wapeleke taarifa za course aliyokuwa anazisoma chuo ili TCU ifanye ulinganisho wa course aliyokuwa anasoma na course zilizopo nchini kwenye vyuo vyetu, baada ya hapo atapata maelekezo ili kuondoa tatizo hilo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza ninaipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo inaratibu zoezi la utoaji wa mikopo ya 10% ya mapato yote ya halmashauri ambapo akina mama wanapewa asilimia nne, asilimia nne - vijana na asilimia mbili wanapewa watu wenye ulemavu. Hivi karibuni yamefanyika maboresho ya kanuni na kuruhusu kundi la vijana umri wake kuongezwa kutoka miaka 35 mpaka 45.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kundi la akina baba limeachwa nyuma, Serikali haioni ni wakati sahihi kuruhusu kundi la akina baba na wao linufaike na mikopo hii, kwa sababu kumekuwa na malalamiko makubwa ya akina baba kukosa fursa hii na wao ndiyo wakuu wa kaya, wao ndiyo wakuu wa familia hizi.
Je, Serikali haioni ni wakati sahihi sasa kufanya marekebisho ya kikanuni ili kundi la wanaume (akina baba) na wao wanufaike kwa mikopo hii bila kigezo cha umri? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa fursa za mikopo kwenye maeneo mbalimbali zilifanyiwa tathmini, tukagundua kwamba yapo makundi hayana fursa nzuri, yana fursa ndogo sana kupata mikopo hii. Makundi haya ni yale ambayo baadaye tulianzisha mikopo maalumu ile kupitia halmashauri zetu nao ni walemavu, wanawake na vijana. Hili kundi tuliamua kuanzisha mfuko maalumu kwenye halmashauri zetu ili wapate nafasi ya wazi kupata mikopo kwenye haya maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala la wanaume kupata nafasi. Hao ndio walikuwa wanapata nafasi ya wazi ya kunufaika na hata baada ya kubadilisha umri, bado ninaona wana nafasi kubwa. Wakati huo vijana wakiwa wanafikia umri wa miaka 35, wanaume ambao ni vijana wanapata nafasi ya kukopa wakiwa vijana, lakini baada ya miaka 35 kwa wakati huo walikuwa pia na fursa za kwenda kwenye taasisi za kifedha na ndiyo fursa ambayo tulifanya tathmini tukagundua kwamba wengi wanaopata mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha ni wanaume kuliko akina mama baada ya kufanya tathmini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata baada ya kuwa tumebadilisha kigezo cha kijana kutoka miaka 35 mpaka 45, bado kijana huyu huyu sasa tumemuongezea muda na bado akizidi muda wa miaka 45 anakuwa mtu mzima, vilevile anaweza kupata mikopo.
Kwa hiyo, utakuta kundi hili pia bado lina nafasi ya kupata mikopo kwenye taasisi yoyote ya fedha, lakini pia wana nafasi ya kupata mikopo kwenye halmashauri. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba kundi hili lina fursa ile ya awali ya kuingia kwenye taasisi baada ya miaka 45, chini ya miaka 45 anapata kwenye taasisi na vilevile kwenye mikopo ya halmashauri. Kwa hiyo, fursa hii tumeigawa hivyo, tunajua kabisa haya makundi yote yanaweza kupata nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini Serikali imefanya, tumeshazungumza na taasisi zote za fedha ambazo zinajishughulisha na utoaji wa mikopo, kufungua dirisha la mikopo kwa wajasiriamali wote na kuhakikisha kwamba kila anayefika pale anapata fursa sawa na mwingine ili kuboresha, kuwafanya Watanzania kubuni miradi na kuweza kupata mikopo ili waweze kujiongezea uchumi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kufatilia hilo, tunaendelea kufanya tathmini, pale ambako tutagundua bado kuna kundi ambalo halipati fursa tutaendelea kuweka utaratibu kupitia mifuko tuliyonayo hata pia ndani ya Serikali. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha utoaji mikopo kwa makundi yote, ili yeyote kutoka kwenye makundi hayo aweze kupata fursa ya kupata mitaji na kuendesha shughuli za kiuchumi, ahsante. (Makofi)