Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Cosato David Chumi (129 total)

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii, lakini pia ningependa kufanya masahisho ya jina langu, naitwa Cosato David Chumi, sio Chumu kama ulivyokuwa umesema na hilo la kwanza ni Cosato siyo Cosota. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuishukuru Wizara, lakini pia kuishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuja na Wizara ambayo siyo tu ita-deal na michezo na habari lakini pia ita-deal na sanaa. Naipongeza sana na ninawapongeza watendaji wote kwa hotuba hii na maandalizi yote ya bajeti yao. Najua ndiyo tunaanza; mwanzo ni mgumu lakini pia mwanzo ni muhimu, lazima tuanze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Waziri Kivuli Mheshimiwa Sugu. Huyu bwana, ndugu yangu, nashangaa hajanitaja katika watu waliochangia mafanikio yake, kwa sababu toka akiitwa II Proud, baadaye Mr. II; halafu Sugu na sasa hivi Mheshimiwa. Tumefanya naye kazi Arusha kule, mvua ikanyesha, onyesho likabuma; lakini namshukuru kama promoter niliyekuwa nimeandaa onesho lile hakunidai, maana yake mvua ilinyesha, onesho likabuma. Kwa hiyo, nakupongeza brother, tumetoka mbali. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesikia kwamba kutakuwa na mechi ya Wabunge wa Simba na Yanga; na mimi nakubali. Huko nje tumetaabika sana, lakini kwenye mechi hiyo napenda kuwahakikishia wapenzi na mashabiki wa Simba tutahakikisha kwamba tunawafuta machozi. Timu yetu kabambe, yupo Mheshimiwa Godfrey Mgimwa hapa, yupo Mheshimiwa Nassari, tafadhari uanze kuja mazoezini tuwafute mashabiki machozi humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi, nianze kwa kuzungumzia mchezo unaopendwa sana kama wenzangu walivyosema mchezo wa mpira wa miguu (soka). Mimi nasema hii soka yetu bila vifaa na viwanja vya michezo ni bure. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwa kushirikiana na TAMISEMI, kwanza tuanze kulinda viwanja katika shule zetu maana huko ndiko ambako vipaji vinatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila vifaa, bila viwanja, hatuwezi kwenda kokote. Pia kodi ya vifaa vya michezo; leo hii kijana anayecheza mpira, kiatu chake siyo chini ya shilingi 40,000. Hata hawa TFF nina taarifa kwamba wameleta mipira size mbili, tatu na nne ambayo ilikusudiwa kwa ajili ya kugawa kwenye shule kama kifaa cha kufundishia kwa sababu nacho ni kifaa; wameshindwa kuigomboa kwa sababu wanadaiwa kodi karibu dola 18,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri tunapokusudia kuinua michezo, hebu tuangalie viwanja shuleni, viwanja mitaani kwa kushirikiana pia na Wizara ya Ardhi. Watu wa Mipango Miji wanapopanga mipango, watenge pia maeneo ya viwanja; lakini pia Serikali za Mitaa kwa maana ya TAMISEMI, wavilinde viwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niulize, hivi sisi football yetu, hii soka yetu Mheshimiwa Waziri ni ya ridhaa au ni ya kulipwa? Kwa ufahamu wangu naambiwa ni ya ridhaa, lakini ndani yake humo humo tunaambiwa kuna wachezaji ma-pro; wako akina Ngoma, akina Kiiza, wanalipwa madolali ya pesa. Sasa hebu tuirasimishe ieleweke moja, iwe ya kulipwa, tui-commercialize ili ituongezee mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hiyo timu yetu ya Taifa sijui kama Charles Boniface Mkwasa analipwa marupurupu kama waliyokuwa wanalipwa wale makocha wa kigeni. Tafadhali, hebu tujaribu kuwajengea uwezo makocha wetu wazawa, lakini pia tuwalipe kama tunavyowalipa wageni. Sasa kama sisi timu ya Taifa makocha wetu hatuwajali, je, vilabu, vitawajali akina Jamhuri Kiwelu? Vitaanzia wapi? Hebu tuoneshe mfano katika hili. Kocha wa timu ya Taifa alipwe kama tunavyowalipa wale wageni. Nina hakika akilipwa vizuri tutayaona matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusu mchezo wa riadha; wenzetu nchi jirani Kenya na Ethiopia mchezo huu umewasaidia sana kutangaza utalii wa nchi zao. Leo hii New York Marathon, Tokyo Marathon humkosi Mkenya wala Mhabeshi. Hebu tuuone huu mchezo; nina hakika kuna ndugu zangu kule kwa akina Mheshimiwa Massay Flatei wanaweza kabisa, wako hata Singida kwa jirani yangu hapa Mheshimiwa Mama Mlata. Hebu tuwekeze pia nguvu katika mchezo huu kwa sababu itatusaidia kututangazia utalii na utalii unaongoza katika kutupa mapato ya fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye sanaa. Napenda kuwapongeza wasanii wa Jimbo langu la Mafinga Mjini. Nafahamu wanaishi kama watoto yatima, lakini wanajikongoja. Ninaamini kwa mipango mizuri, tutafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, hivi hii BASATA kazi yake kubwa ni kuwafungia tu wasanii? Kama ikiwa katika filamu, tuna Bodi ya Filamu, inakagua filamu ndipo inatoa kibali ziendelee; kwanini pia katika suala la muziki, video tusiwe na utaratibu huo? Kwa sababu moja, video imeshaingia mtaani, imeshafanya damage katika jamii kimaadili, lakini pia kuna damage ya msanii, ameingia gharama. Leo hii unakuja unamfungia, ulikuwa wapi BASATA? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, hata COSOTA na Bodi ya Filamu, kazi zao namna wanavyofanya wamejielekeza tu pale Dar es Salaam, usiwaone hawa akina Singo Mtambalike hawa, akina Richie hawa; toka wameanza kufanya hizi kazi, utaratibu wa kutunza kazi za ndani kwa kweli siyo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna kitu kinaitwa zaga zaga; ukienda Kariakoo pale watu wametandika chini hizi filamu za kutoka nje za series, zinauzwa shilingi 1,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msanii wetu unamtaka aweke sticker, lakini pia hata hiyo sticker yenyewe kuipata mpaka uende Dar es Salaam. Sisi tunataka mapato, sticker ya TRA mpaka uende Dar es Salaam. Kwa nini tusiweke utaraibu sticker zipatikane pia mikoani na katika ofisi za TRA kuwarahisishia hawa wasanii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, hata hizi ada, COSOTA na BASATA, kama unataka kuandikisha filamu, dakika moja ni shilingi 1,000; kwa ujumla ukitaka kuandikisha masuala haya, uwe registered na BASATA na COSOTA na Bodi ya Filamu, sio chini ya shilingi 340,000 na msanii atoke mkoani ajigharamie nauli, malazi na bado hata akifika hapo ofisini ushirikiano anaoupata ni wa hali duni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ielekeze BASATA pia katika kutoa elimu kwa wasanii kupitia Maofisa Utamaduni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema tayari nina kitambaa cheupe, ndugu yangu Waitara baadaye twende kwa King Kiki tukapeperushe kitambaa. Jamani kazi na dawa. Pia, tunawaunga mkono hawa wasanii, huyu mzee ametoka mbali. Kwenda kwetu pale kama Waheshimiwa Wabunge, tunamtia moyo.
MHE. COSATO D. CHUMI: Hata kama hatumpi chochote ndugu zangu, nadhani Sugu utawashawishi wenzako huko, hebu twende tukamtie moyo huyu mzee na kama hauna kitambaa, mimi nitakuazima; kama huna kitambaa, wewe chukua hata karatasi tukapeperushe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pia na mimi kwa kupata nafasi hii ya kuchangia. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maandalizi ya bajeti waliyotuletea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kupongeza, nimeona katika bajeti kuna suala la kuanzisha industrial clusters, nashauri hapa Halmashauri zipewe kama agizo kutenga maeneo hayo, lakini pia katika hotuba nimeona kuna suala la kufanya tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa. Hii ni muhimu kwa sababu itatusaidia kuonyesha jinsi gani ya kwenda mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati tunafanya tathmini hii nimuombe Mheshimiwa Waziri pia afanye tathmini ya mashirika ambayo tunaambiwa kwamba yalikuwa ni ya Serikali lakini kwa namna za ajabu ajabu yameangukia mikononi mwa watu binafsi. Mfano wa shirika hili ni kama PRIDE. (Makofi)
Katika pongezi zangu pia nipongeze kwa kuwepo ushuru kwenye bidhaa za samani kwa maana ya furniture. Nasema hivi kwa sababu mimi natoka Mufindi (Mafinga) tuna viwanda kule vya mazao ya misitu naona itakuwa ni chachu ya kuvisaidia kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mimi binafsi nipongeze kwa kuongeza ushuru kwenye industrial sugar. Suala hili litasaidia wawekezaji wa ndani kupanua viwanda vyao na hivyo wakulima wetu wa miwa hasa wale wakulima wa nje (out growers) watahamasika kuendelea kulima, wao watapata mapato, lakini pia na Serikali itaendelea kupata mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi sasa nije kwenye maoni. Nimehangaika sana na nimebahatisha nimepata ile ripoti ya timu ya Mheshimiwa Chenge (Chenge One) ambayo ilikuwa inaainisha maeneo mbalimbali ya kuboresha mapato. Nashangaa sana labda ni kukosa ufahamu au uzoefu. Hao wenzetu wa TCRA kuanzia tarehe 16 watazima simu fake maana yake ni kwamba wana mitambo ya kuweza kung’amua simu fake. Mimi najiuliza, wanawezaje kukosa kuwa na mitambo ya ku-track mapato na makusanyo yatokanayo na makampuni ya simu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwe wa kweli, makampuni ya simu sisi hatuja-exhaust ipasavyo mapato kutoka kwenye hayo makampuni na ndiyo maana hata Waheshimiwa Wabunge wanapolia kwenye gratuity na kuelekeza vyanzo vitizamwe maeneo mengine mojawapo ni kwenye makampuni ya simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata competition iliyopo na mwenendo mzima wa haya makampuni ya simu yaani kuna unfairness kubwa sana. Ukiweka vocha ukilala ukiamka balance imeliwa. Ukinunua bando kwa mfano ni mkataba kwamba unanua bando mpaka itakapoisha ununue nyingine, lakini ikiisha unachajiwa direct kwenye ile pesa yako ya kuzungumza, yaani ni madude mengi sana yanafanyika kwenye makampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mapato yatokanayo na makampuni ya simu Mheshimiwa Waziri anapowasilisha hotuba yake ya watu wa mawasiliano alisema tuna around simcard milioni 40; je, kweli sisi Serikali kupitia TCRA wakishirikiana na TRA tumepata makusanyo ya kutosha kutoka kwenye makampuni ya simu?
Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho, hebu jaribu kutueleza Serikali ina mikakati gani katika kuhakikisha kwamba tunapata mapato ipasavyo kutoka kwenye makampuni ya simu kama ambavyo mnakusudia kupata mapato kutoka kwenye maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu misamaha ya kodi kwa taasisi za dini na watumishi wa umma. Mheshimiwa Dkt. Kafumu ameeleza pale kuhusu haja ya kuwapa watumishi wa umma morali.
Mheshimiwa Waziri hata hawa watumishi tunasema kwamba ikiwa mtumishi anataka kununua gari itabidi ule msamaha wake wa kodi aliokuwa anapewa kwanza alipie halafu baadaye aje a-claim. Mheshimiwa Waziri watumishi wa nchi hii hali zao ni duni sana, haka ni ka-privilege kadogo walikonako. Hebu mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye hili tuwaache. Kama mtu anadunduliza anataka apate kausafiri tafadhali tumtie moyo kwenye suala hili la msamaha wa vyombo vya usafiri kwa watumishi. Namuomba Mheshimiwa Waziri kwa kweli tusiwawaguse, haka ni ka-privilege, ni sehemu ya kupandisha morali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri amesema jambo hili pia litagusa hata mashirika ya dini, mashirika ya dini katika nchi hii yana-supplement sehemu kubwa sana huduma mbalimbali za elimu na afya. Sasa tunasema kwamba kama watakuwa wananunua bidhaa au masuala yoyote itabidi kwanza walipe kodi halafu baadaye waje wa-claim, vitu vingine Mheshimiwa Waziri ni misaada.
Mimi kwa mfano juzi nimepata msaada wa ambulance sikuwa na bajeti hiyo ya kulipia. Sasa hawa watu vitu vingine wanaletewa kama misaada tukisema kwamba walipie halafu ndipo warejeshewe naona tutakuwa tunawavunja nguvu, ni jambo tunalopaswa tuliangalie mara mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia suala la bodaboda, tumesema usajili utoke shilingi 45,000 mpaka shilingi 95,000, hii ni sehemu mojawapo ambayo watu na vijana wamejiajiri. Kama vijana wa bodaboda wamejiajiri na wanatusaidia sisi usafiri katika maeneo mengi maana yake ni kwamba kuwaongezea gharama ni kuongeza gharama kwa mtumiaji wa ule usafiri, napenda tuwatizame watu hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo napenda kuongelea suala la mitumba, mitumba mbali ya kuwa ni biashara kubwa hata mimi hapa nimevaa hii suti yangu hapa ni ahsante JK wakati ule nasafiri ndiyo nilinunua hii suti, lakini nina hakika nusu ya watu humu ndani tunavaa mitumba. Sasa tunapoongeza hiyo kodi kutoka 0.2 cent mpaka 0.4 cent ndugu zangu, tunawateketeza vijana waliojiajiri katika biashara hiyo. Kweli leo hii tunafuta mitumba baada ya miaka mitatu kulingana na makubaliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, je, viwanda vyetu viko tayari kweli kutuzalishia sisi nguo za kututosheleza humu au baadaye tunageuka kuwa soko la Wachina katika bidhaa zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja na haraka haraka kwenye suala la VAT kwenye sekta ya utalii. Sisi wenyewe tunakiri kwamba sekta hii imechangia mapato ya fedha za kigeni kwa asilimia 25. Nilisema wakati nachangia Wizara ya Maliasili na Utalii hata fedha tunayoweka kwa ajili ya ku-promote utalii wetu bado ni ndogo. Sasa kama tunakusudia sekta itupe mapato ya kutosha kama ambavyo imekuwa inatupa hayo mapato kwa asilimia 25, tuna kila sababu ya kuendelea kuilea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi leo promotion tu tunawekeza chini ya dola milioni mbili, wenzetu wa Kenya kwa mujibu wa takwimu nilizonazo karibu milioni 80 USD, Rwanda milioni 11 USD na Uganda milioni 8 ambayo tunadhani siyo washindani wetu. Badala ya kuielea hii sekta bado tunaiongezea mzigo wa VAT, wenzetu wamefuta VAT na ndiyo maana mimi nasema pamoja na hizi integration blocks katika uchumi wa dunia ya leo tuwe wanjanja. Maana Mheshimiwa Waziri ametuambia kwamba hilo wamekubaliana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini wenzetu katika bajeti yao wameliondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana kila siku nasema tuwe tunajiongeza na sisi tusikubaliane kila kitu kwa tu spirit ya East Africa, tukubaliane lakini na sisi turudi je, kwetu tumejipanga vipi kutumia hiyo fursa ipasavyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba naomba misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini na watumishi wa umma tafadhali Waziri atakapokuja kuhitimisha azungumzie hili, haka ndiko kadude pekee watumishi walikobaki nako kakurejesha morali yao, tuwatizame tuwaache kwa sababu mtu anaweza akalipa lakini marejesho kuyapata kwa kweli ikawa ni kazi sana.
Kwa hiyo, niombe kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hayo ni baadhi ya mambo napenda ayasisitize namna gani tutahakikisha tunapata mapato kutoka kwenye makampuni ya simu, namna gani tutaweza kuona kwamba hii VAT tunaiondoa kuvutia utalii na kuunyanyua lakini pia kwa ujumla namna gani suala la mitumba tuliache kama lilivyokuwa tusubiri kwanza tujipange hapa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nashukuru sana kwa nafasi pia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuipongeza Serikali kwa usikivu wake wa kusikiliza kilio cha wananchi na kutoa agizo la kukubali kuagiza sukari. Huo ni uthibitisho kwamba hii ni Serikali tulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo napenda pia kuwashukuru Mawaziri. Kuna mjumbe mmoja alipokuwa anachangia alisema Mawaziri hawa wako reachable, kwa kweli na mimi nawapongeza kwamba ni kama simu ukipiga inakuwa reachable. Wakati mwingine hawa hata kama hujapiga wako reachable.
Nasema hivi kwa sababu nilifanya ziara katika Jimbo langu na Mheshimiwa Jafo, Naibu Waziri alipoona taarifa ya ziara ile na yeye akaenda kutembelea pale mahali ambapo mimi nilikwenda kutembelea ili kujionea mwenyewe zile changamoto. Kwa hiyo, hii ni uthibitisho wa usikivu pia wa Mawaziri hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo nianze kwanza kwa kusema kwamba tumesema tunapokusudia kujenga uchumi wa viwanda sekta binafsi ni injini ya kujenga uchumi huo. Mimi napenda kuongeza kwamba injini hii bila oil, ambapo kwangu mimi oil ni utumishi wa umma (public service) maana yake ni kwamba injini hii inaweza ika-knock. Kwa sababu hiyo basi, niiombe Serikali kupitia Wizara husika iwatazame watumishi wa umma walau kwa baadhi ya mambo kwa mfano fedha zao za likizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetokea kwenye utumishi wa umma ambapo ikiwa mwaka huu utakwenda likizo basi utalipwa fedha yako ya nauli mwaka unaofuata hulipwi, unalipwa alternatively. Sasa naomba wakati Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza makusanyo na kubana matumizi basi iwatazame watumishi wa umma katika suala hili. Pia iwatazame katika fedha zao za uhamisho kwa mfano walimu. Hata katika hii nauli unakuta mtu anakwenda likizo halafu anaambiwa fedha yako utakuja kulipwa ukirejea na inaweza kumchukua hata miaka mitatu, mwingine anakata tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie nauli kwa watumishi wa umma wanaokaa maeneo ya mijini. Mnafahamu kwa mfano Jiji la Dar es Salaam Serikali ina utaratibu wa kutoa mabasi lakini kuna maeneo mengine ya mikoani ambako watumishi wanatoka umbali mrefu kwenda kwenye maeneo ya kazi. Sasa kama sehemu ya kuwaongezea morale na kuwapunguzia ukali wa maisha, nashauri Serikali ilitazame jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusiana na Waraka huu wa Serikali, labda niusome. Kuna Waraka wa TAMISEMI Na.CFB/173/355/0 wa tarehe 06/06/2011 wenye kichwa cha habari kinachosema Majukumu ya Maafisa Biashara na namna bora ya utoaji taarifa. Mojawapo ya majukumu katika waraka huu ni kuhamasisha shughuli zilizo chini ya viwanda, biashara na masoko na uwekezaji pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali ili kuongeza kipato cha wananchi na kuongeza wigo wa kodi katika Serikali za Mitaa na Serikali Kuu.
Sasa ukienda katika halmashauri zetu ofisi za biashara si kitengo wala si idara isipokuwa ziko ndani ya Idara ya Fedha. Naziomba Wizara hizi mbili zijaribu kuangalia muundo wa Maafisa Biashara ili kusudi hata hizi shilingi milioni 50 ambazo tunatarajia zitatoka kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais basi zikawe na tija ili Maafisa Biashara wasibaki tu kuwa watu wa kukagua leseni bali wawe watu ambao wanaweza kusaidia wananchi katika kung’amua fursa mbalimbali za kijasiriamali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu nijielekeze katika Sekretarieti ya Ajira. Napenda kuipongeza kwa sababu kweli tuna changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira lakini jinsi ambavyo imejitengeneza kimtandao, jinsi ambavyo watu wana-apply online na maombi yao yanaendelea kutunzwa online ni jambo la kupongeza kwa sababu pia linapunguza malalamiko katika ajira ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niombe pengine ingeanza kwenda kwenye zones ili kuwapunguzia waombaji wa nafasi za kazi gharama zile za nauli na malazi kwa sababu mpaka sasa hivi pamoja na kuwa kuna nyakati inafanya interview kwenye maeneo ya nje ya Dar es Salaam lakini asilimia kubwa ni Dar es Salaam. Sasa uwezo utakapoongezeka basi tuanze walau na zone kwa ajili ya kuwasaidia watafuta ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, nijikite sasa kwenye Jimbo langu. Namshukuru tena Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea katika shule ya msingi Mchanganyiko Makalala. Shule hii ina watoto wenye mahitaji maalum. Kwa sababu shule hii iko katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga lakini ni kama shule ya kitaifa kwa sababu inachukua watoto kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu basi Serikali iitazame kwa macho mawili. Nampongeza Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla kwa hatua ile ya kutembelea shule ile, naamini changamoto zile alizojionea zitamsaidia katika kuona umuhimu wa kuitazama shule hii kwa macho mawili katika uwiano wa walimu lakini pia miundombinu ambayo kwa kweli siyo rafiki sana kwa watoto wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la elimu naiomba Wizara, Mheshimiwa Rais alipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam tarehe 13/02/2016 aliahidi kwamba ataupa Mkoa wa Dar es Salaam shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kukabiliana na ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza.
Niiombe Serikali hata sisi tunaotoka kwenye Halmashauri za Miji changamoto hii tumekutana nayo. Mafinga pale kuna ongezeko la watoto kwa asilimia 135. Serikali itutazame kwa sababu kwanza ni Halmashauri mpya bado haina makusanyo lakini pia iko mjini. Sasa sisemi kwamba na sisi tupewe shilingi bilioni mbili lakini tutazamwe kwa chochote kitakachoweza kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na suala la pampu. Pale tuna pampu ilipaswa iwe imefungwa toka mwezi wa kumi na moja lakini mpaka wakati huu yule aliyepewa kazi ya ku-supply amekuwa anapiga chenga. Kwangu naona hili ni jipu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa sababu wao ndiyo walitakiwa wanunue pampu na kutufungia sisi kwenye Halmashauri ya Mji. Ametuletea pampu haina TBS certification, haina manual, maana hata ukinunua simu Kariakoo ya shilingi 18,000 unapewa manual, lakini pampu hii hata manual haina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie katika suala la utawala bora. Wenzetu upande wa pili kule wanalialia Rais apunguze kasi ya kutumbua majipu. Mimi nasema tumuunge mkono Mheshimiwa Rais. Kuwa opposition sio kupinga kila kitu. Madawati kupinga, ujenzi wa maabara kupinga, hapana, kuna mambo tumuunge mkono Mheshimiwa Rais. Mimi naamini ninyi huko si majipu kwa hiyo mpunguze kulialia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, nimalizie kuzungumzia wastaafu ambao wanahudumiwa na LAPF wanalalamika kwamba wenzao wa central government tayari wameongezewa lakini wao bado. Kwa hiyo, niombe pia suala hilo litazamwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, niwahakikishie wana Mafinga kwamba nitaendelea kuwatumikia bila kuangalia rangi wala itikadi zao, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na laiti ningejua Mheshimiwa Mapunda angekuwa na maneno mazito hivi, ningeridhia kumpa muda wangu, lakini kwa sababu ameshamaliza ngoja niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuunga mkono hoja na kwa sababu muda unaweza ukaniwia mchache, nina mambo machache ya kuzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuzungumza kuhusu mchezo wa mpira ambao ndiyo unapendwa kuliko mchezo wowote. Katika kuzungumzia suala la mchezo wa mpira, napenda kuzungumzia umuhimu wa timu yetu ya Taifa kujiweka katika mazingira ambayo inaweza ikawa inapata nafasi za kushiriki katika mashindano ya Kombe la Dunia na mashindano ya AFCON.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina takwimu, katika takwimu za viwango vya FIFA mpaka mwezi Machi sisi Tanzania tulikuwa wa 157 wakati Afghanistan walikuwa wa 156, unaweza kupata picha ina maana hata Afghanistan wametuzidi sisi. Kwa nini inatokea hivi? Viwango vya FIFA vinapangwa kulingana na idadi ya mechi unazocheza zilizopo kwenye kalenda ya FIFA.



Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo letu sisi, wasimamizi wa mpira ambao ni TFF hawalizingatii hilo na matokeo yake tunacheza mechi chache sana kufuatana na kalenda ya FIFA kitu ambacho kingeweza kutupa sisi points za kupanda kwenye viwango vya FIFA. Sasa unapokuwa chini ya viwango vya FIFA maana yake ni nini? Hata unapopangiwa kwenye mashindano ya ku-qualify kwenda AFCON au kwenda World Cup unajikuta kwamba uko kwenye pot four, maana yake ni kwamba pot one wanaingia wale ambao ni vigogo kadhalika pot two na pot three. Sasa kila mara utakuta wewe unapangiwa na timu ambazo ni vigogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mashindano ya ku- qualify kwenda Kombe la Dunia, sisi mechi ya kwanza tulipangiwa na Malawi tukashinda, lakini mechi ya pili tukajikuta tunaangukia kwa Algeria. Kilichotupata wote mnajua, goli saba kwa mbili. Kwa sababu gani? Kwa sababu sisi hatushiriki ipasavyo mechi za Kimataifa kulingana na kalenda ya FIFA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, katika mwaka 2016 Tanzania imeshiriki mechi tatu tu ambazo ziko kwenye kalenda ya FIFA ukilinganisha na wenzetu, kwa mfano Rwanda wamecheza mechi 11, Uganda mechi 13, Kenya mechi 10, hata hao Afghanistan wenye matatizo, walicheza mechi sita; sisi tumecheza mechi tatu tu, utawezaje kupanda kwenye viwango vya FIFA?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, nimechukua takwimu za miaka mitatu iliyopita na miaka mitatu tuliyomo; katika kipindi cha miaka mitatu kutoka mwaka 2014 mpaka 2016 sisi tumecheza mechi za FIFA 24 tu ukilinganisha na Rwanda mechi 26, Uganda mechi 43, Kenya mechi 27, hata Afghanistan mechi 29. Sasa kuna watu hapa wanamkumbuka Leodgar Tenga, ni kwa sababu ya mambo kama haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha uongozi wa TFF ya sasa hivi tumecheza takribani mechi 24 tu; kwa kipindi kama hicho, wakati wa Tenga tumecheza mechi 47.

Sasa takwimu hizi ndiyo zitakupeleka kwenye viwango bora vya FIFA na ili ujihakikishie kuwa kwenye ushindani unaoweza kukupeleka kushiriki Kombe la Dunia au AFCON, lazima uwe kwenye viwango bora vya FIFA angalau namba moja mpaka 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutoshiriki mechi hizi athari yake ni nini? Athari yake kama nilivyosema, unajikuta unapangiwa na vigogo kama Algeria. Kuonesha kwamba ushiriki wa mechi za FIFA ni muhimu, baada ya kucheza mechi zilizopo kwenye kalenda ya FIFA na Burundi na Botswana, ukienda kwenye takwimu za FIFA World Rankings zilizotoka jana, tarehe 4 Mei, sasa hivi kutoka 157 tumefika 135. Kwa hiyo, kuna umuhimu sana wa TFF kujikita katika kuhakikisha kwamba inahakikisha kuwa Timu ya Taifa inacheza mechi nyingi kulingana na kalenda ya FIFA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mmoja tunataniana hapa, tulikuwa tunaangalia kirefu cha TFF - Tanzania Football Federation, lakini inaanza kugeuka sasa inakuwa Tanzania Football Fungiafungia. Maana yake sasa tazama watu wanafungiwa, hata hapa Bungeni mtu akikosea anaitwa anapata haki ya kusikilizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 kutokana na ile waliyosema kupanga matokeo, kuna wachezaji wamefungiwa miaka kumi katika soka. Hata dunia ya akina Messi na akina Ronaldo, huwezi ukacheza maximum of more than ten years. Unapomfungia mtu miaka kumi, si umeua kipaji chake. Maana yake ni nini? Lazima tuwe considerately. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa TFF isijikite tu kwenye mambo haya ya usimamizi wa nidhamu ikajikuta inaacha kusimamia mambo ambayo yangetufanya sisi tupande katika viwango vya FIFA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nizungumzie soka letu. Nilisema hata mwaka 2016, kwa nini tusi- commercialize mpira wetu? Uingereza timu yao ya Taifa inasuasua, lakini hakuna mahali ambapo kuna biashara kama katika soka ya EPL. Je, Serikali, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, wewe ni mwanasheria, naamini unaweza ukatusaidia, kwa nini tusi-commercialize mpira wetu na sisi ikawa ni chanzo kikubwa cha kutupa mapato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya sasa hivi, soka ni uchumi ndugu zangu. Usione watu wanamnunua Ronaldo au Messi kwa mamilioni ya pesa, yanarudi kwa namna nyingi tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaishauri Serikali, hebu tufikirie, kama sisi sasa hivi tuna soko huria, kwa nini pia katika soka tusi-commercialize hii ikawa professional football? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi pia katika vilabu; siwezi kuisema tu TFF peke yake, hata vilabu vyetu vikubwa Simba na Yanga; hivi wewe unajiita Rais wa Klabu, majengo toka walivyojenga akina Marehemu Tabu Mangala, mnashindwa hata kujenga viwanja vya michezo vya mazoezi? Unaenda kila siku kuazima uwanja Boko Veteran! Wewe Rais wa Simba au Rais wa Yanga, unaacha legacy gani katika klabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyakati hizi kuna fursa nyingi sana za kuweza kupata wadhamini, watu wa kuwekeza; Azam wamekuja juzi tu tumeona. Sasa lazima tujisifu kwamba ni viongozi wa vilabu ambao kweli tunaacha legacy katika vilabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nkamia amesema lazima soka ianzie kwenye timu za vijana, lakini mimi nataka niende mbele zaidi, hata Serikali Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe peke yako huwezi, lazima ushirikiane na Wizara ya Elimu, lazima ushirikiane na TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kutenga maeneo na kuyapima kwa ajili ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimesoma Malangali sekondari, ilikuwa ni shule yenye mchepuo wa kilimo. Tulikuwa tuna shule kama Shycom cha mchepuo wa biashara, lazima kama tuko serious tunataka tuvune kutoka michezo tuanzishe shule ambazo zitakuwa na michepuo ya michezo, tutaziwekea miundombinu ya kimichezo, lakini lazima pia ziwe na walimu kutoka Chuo cha Walimu wa Michezo kule Malya, otherwise Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe tutakuja tuta- table hapa bajeti tutachangia, tutaondoka 2020 itafika, World Cup tutaishia kuiona kwenye tv, AFCON tutaishia kuiona kwenye tv. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, kama seriously tunataka kuwekeza kwenye michezo, ni lazima tufanye mambo hayo. Kwa sababu gani? In connection na michezo, moja, kwanza unatangaza Taifa. Tumeona Alphonce Simbu amekwenda kule London Marathon. Kitendo cha kuwa mtu wa tano tu, tayari sisi umeshavutia idadi kadhaa ya watalii, umeongeza mapato katika Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapopiga kelele kuhusu michezo, siyo kwa ajili ya kuburudika, hapana, ni kwa sababu michezo ni chanzo kikubwa sana cha mapato na hivyo itakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu. Marekani leo hii, entertainment and sports industry mchango wake katika Pato la Taifa la uchumi wa Marekani siyo chini ya asilimia saba. Kwa hiyo, hatuzungumzii kuhusu tu kuji-entertain. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, lazima nizungumzie pia wasanii. Juzi hapa kumetokea mvutano kwamba Serikali izuie picha kutoka nje, hapana. Ninachosema Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, filamu zinazotoka nje ikiwa msanii wa ndani lazima alipie COSOTA, lazima alipie BASATA, lazima alipie Bodi ya Filamu kukaguliwa picha zake; ni lazima pia na hizi filamu zinazotoka nje tuweke utaratibu ziweze kulipia mapato katika Taifa hili. Sasa filamu kutoka nje inanunuliwa shilingi 1,000, filamu ya ndani inanunuliwa shilingi 2,500 lakini hii ya nje haijapitia mfumo wowote ambao utahakikisha kwamba inalipia kodi. Kwa hiyo, tunaposema haya tunazungumzia mapato katika Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nizungumze pia kuhusu wasanii na wenyewe wafanye kazi ambazo zina mvuto, isiwe kama tunavyoona kwenye mitandao ya kijamii, dhihaka imejaa sana. Kwa hiyo, nao wafanye kazi kadri inavyotakiwa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema pale mwanzo, naunga mkono hoja lakini lazima tuoneshe seriousness kwa vitendo katika suala zima la michezo kwa sababu za kiuchumi na kimapato. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusu madai ya mtumishi aitwaye Ndugu Charles Kanyika. Naomba kuleta suala hili kwa maandishi kama ambavyo tayari nimewasilisha kwa Mheshimiwa Waziri. Mtumishi huyu anatarajia kustaafu tarehe 15/06/2017 mpaka sasa hajapelekewa michango yake PSPF kwa miezi 18 suala ambalo litaathiri mafao yake. Nimeambatanisha maelekezo yake baada ya jitihada zake kuomba ufumbuzi wa suala hili kutofanikiwa. Pamoja na kuwa huyu ni mtumishi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, ajira yake toka awali kwa mtiririko wa barua zake, mwajiri ni Wizaraya Elimu, naomba tumsaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo ya elimu ya juu, hii dhana ya kwamba mwanafunzi aliyesoma O-level mpaka A-level katika shule zinazoitwa za bei mbaya kwa hiyo hastahili mkopo kwa kigezo kuwa wazazi/walezi wana uwezo wa kulipia sio sahihi. Wapo watoto ambao wamesomeshwa na wafadhili baada ya A-level wafadhili sera zao au uwezo hauwapi nafasi ya kuwalipia elimu ya juu. Naomba wanafunzi wa aina hiyo watizamwe. Katika mchango wangu huu nimeambatanisha maombi kutoka kwa Padri Stephen wa Selesian of Don Bosco ambao watoto waliowafadhili wamekosa mikopo. Naomba ikiwa wana sifa Bodi ione uwezekano wa kuwasaidia. Nimeambatanisha barua pepe ambayo Padri Stephen aliniandikia na barua yangu kwa Waziri ambayo nakala nitaikabidhi Bodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu NACTE vs St. Bakhita. Kumekuwa na mkanganyiko wa namba za usajili ambazo wanafunzi wa St. Bakhita ambacho ni Chuo cha Uuguzi, wamepewa namba mbili tofauti na hawajui ipi ni namba yao ya usajili. Kila wanafunzi wanapohoji wanapokea vitisho kiasi cha hata kupewa supplematary au discontinuation. Naomba NACTE itizame suala hili ili wanafunzi wawe na amani, pia nimemjulisha Mheshimiwa Waziri suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu NACTE kuingiliwa na Serikali kuliko kawaida, kwa mfano, Kurugenzi ya Mafunzo ya Wizara ya Afya ni kama iko juu ya NACTE naona kuna namna ya kudhoofisha NACTE. Nashauri NACTE ipewe nafasi ya kufanya kazi kwa mazingira bora ya ku-regulate vyuo vya kati. Aidha, ijengewe uwezo wa rasilimali watu na nyenzo ili ifanye kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, NACTE ijitazame hasa katika kukagua vyuo, unakuta watoto wanasoma, wanamaliza vyuo, wakienda kwenye ajira ghafla wanaambiwa chuo alichosoma hakijasajiliwa na cha kusikitisha chuo kipo Dar es Salaam. Hili halikubaliki, ni uzembe wa hali ya juu. Pili, tozo mbalimbali wanazolipisha vyuo binafsi zimegeuka mzigo kwa wazazi. Ni kweli lazima kuwepo na tozo hizo ili kuiwezesha NACTE itekeleze majukumu yake ipasavyo lakini ziwe fair and affordable maana kinyume chake ni kuwabebesha mzigo kwa wazazi na walezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndoto ya uchumi wa viwanda bila kuweka nguvu kwenye elimu ya ufundi ni ngumu. Kwa ilivyo sasa Wizara ijikite (it has to take lead) kuhakikisha kuwa tunahuisha elimu ya ufundi katika maana halisi na sio kwenye maneno ya makaratasi. Tunahitaji ma- technician, ma-artisan kuliko hata graduates. Tunazungumzia uchumi wa mafuta na gesi lakini hata focus iko kwenye Post- graduate level (masters) na kuendelea. Nashauri sana, hata hii VETA isiwe bora VETA bali iwe na michepuo kulingana na mazingira na mahitaji ya maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo kwa kada za afya ngazi za chini. Naamini kama Taifa kila kada ina umuhimu wake lakini uzito na mahitaji yako tofauti. Nimelisemea hili katika mchango wangu wa Wizara ya Afya. Mahitaji ya kada za afya kuanzia Labaratory Technicians, Wauguzi, Maafisa Afya ni kada ambazo huko vijijini wanafanya kazi kama madaktari na ni tumaini kubwa la wananchi. Hata hivyo, gharama za ada kwa vyuo vya uuguzi ni wastani wa shilingi milioni 3.5 kwa mwaka. Kwa kuwa vyuo vya Serikali havina uwezo mkubwa wa kudahili (kwa takwimu uwezo ni around 5,000 vyuo vyote kati ya maombi 13,000), nashauri Serikali ifikirie uwezekano wa kutoa mikopo kwa kada hizo. Kwa mfano, Peramiho wanamsaidia mwanafunzi kumlipia 50% ya ada na akimaliza anafanya kazi mwaka mmoja huku akikatwa sehemu ya mshahara kufidia mkopo/ile 50% ya ada. Tunaweza kuwa na utaratibu kama huo kusaidia kuongeza idadi ya watumishi wa kada ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maslahi ya walimu, ni kweli kuwa Wizara hii ina deal na sera, lakini imekuwa kama kukwepa majukumu, kila ukimzungumzia mwalimu utaambiwa mara ni suala la TAMISEMI au Utumishi na kadhalika. Mwalimu ni dereva, hata kama gari ni new model, ni Benz, Vogue na kadhalika kama dereva yuko demoralized hasa katika welfare, gari haliwezi kufika. Walimu wamegeuka kama second citizen, Maafisa Utumishi kauli zao kwa walimu wanapofuatilia haki zao ni vitisho mwanzo mwisho. Walimu wakitumika kwenye kazi za mitihani, vitambulisho, kura hawalipwi ipasavyo eti mtu anadanganywa na chai na keki kisha anapewa shilingi 10,000, is totally unfair.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi ni mdau muhimu katika elimu, kumeanza kujengeka dhana kama private sector ni mshindani wa public sector katika elimu kuanzia utoaji wa miongozo, vitabu na usimamizi. Kwa mfano, public schools zimepewa vitabu lakini private school siyo wapewe bure lakini vipatikane sokoni. Tulihimiza watu wajenge shule na vyuo vikuu, leo hii kauli zetu kama viongozi is like nani aliwaambia muwekeze kwenye elimu. Cha muhimu uwepo usimamizi bora, tuione private sector kama ni partner kwenye suala la elimu na sio washindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tanzania Institute of Education, wengi wamesema kuhusu suala hili, taasisi hii ama iongezewe nguvu kiutendaji ama kuwepo chombo cha ku- regulate maana as of now ni mchapaji, muidhinishaji na msambazaji jambo ambalo siyo sawa kitaalam. Pia makosa kwenye vitabu yamekithiri na vitabu havifiki kwa wakati, kimsingi wamezidiwa. Nashauri wajengewe uwezo both kitaaluma na nyenzo. Vilevile kama tutarejea kurudisha Bodi ya EMAC na sekta binafsi, tuongeze umakini kwenye usimamizi. Katika uchumi wa soko ni vizuri tujikite kwenye udhibiti kuliko kuhodhi suala la vitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye matokeo ya darasa la saba Mafinga Mjini pamoja na kuwa ni Halmashauri mpya tumekuwa nafasi ya nne kitaifa. Idara ya Ukaguzi hawana magari wala ofisi na vitendea kazi. Nafahamu jibu litakuwa hili ni suala la TAMISEMI lakini naamini ukaguzi uko Wizara ya Elimu, kwa hiyo, naomba ipatiwe gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na usumbufu wa michango ya chakula cha mchana, nashauri Halmashauri za mjini kama ilivyo Mafinga Town Council pawepo na utaratibu wa shule za msingi kusoma mpaka saa nane mchana siyo kama ilivyo sasa ambapo ama watoto wanarudia mchana au wazazi wanaombwa michango ya chakula. Kwa hali ilivyo na kwa mjini walimu wanatoka Kitongoji A mpaka B au C, sasa kwenda na kurudi ni gharama. Nashauri mliangalie kitaalam na kitaaluma ikifaa shule za mjini waishie saa nane mchana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi ni moyo wa elimu. Ukaguzi ni kama CAG kwa Serikali lakini level ya uhuru (independent) iko chini. Ukaguzi hii ya sasa inaikagua Serikali na walimu, je, sio muda muafaka sasa kuifanya iwe agency?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukufahamisha kuwa shule ya msingi ya mahitaji maalum Makalala ipo katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga na si katika Halmashauri ya Mufindi kama ilivyo kwenye kitabu Ukurasa wa 272 kuhusu nukta nundu, ukurasa wa 296 kuhusu usambazaji wa vifaa maalum. Hoja yangu, kwa kuitaja Mufindi DC badala ya Mafinga TC ina mkangayiko, hili limejitokeza kwenye maeneo mengi, hivyo kuchelewesha utekelezaji, kwa mfano kiutawala (administratively) vifaa hivyo vikifika Mufindi DC kuwe na taratibu za kuandikiana kwenda Mafinga TC ambako ipo shule ya mahitaji maalum Makalala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi/ushauri, naomba kwenye taarifa zenu muitambue shule ya mahitaji maalumu ya Makalala kwamba ipo kwenye Halmashauri ya Mji wa Mafinga na si Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. Ninaelewa kwa nini watu wengi wanachanganya, ni kwa sababu awali ilikuwa Halmashauri moja kabla ya kugawanywa Julai, 2017 na kupata Mafinga na Mufindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ikiwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia, siyo tu katika Bunge hili la Kumi na Moja, lakini katika Bunge kwa ujumla wake. Nipende kuchukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mungu kwa uzima na afya zetu wote humu ndani maana uzima na zetu zinatoka kwake. Pia nipende kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini na niwahakikishie kwamba, nitakuwa mtumishi wao bila kujali itikadi zao, nitawatumikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kuwa sikupata fursa kuchangia katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais nipende pia kumshukuru na kumpongeza na pia kuwapongeza Mawaziri na Serikali kwa ujumla kwa jinsi ambavyo wameanza kazi kwa kasi inayotia moyo wananchi. Nafahamu kutakuwepo na kukatishwa tamaa kwingi lakini niwatie moyo, tusonge mbele, katika lolote jema unalolifanya mtu lazima hapakosekani mtu wa kukukatisha tamaa. Sisi tuchape kazi tuwatumikie Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi na mimi nijikite katika suala zima la Mapendekezo ya Mpango. Kwanza kabisa nikubaliane na nimuunge mkono Profesa Muhongo kwa sababu bila nishati ya umeme hata hii ndoto ya viwanda hatutaweza kuifanikisha. Pia nimuombe Profesa, kwa ujuzi na utaalam wake twende mbele zaidi kwa sababu kwa kuwa na gesi haitoshi tu kuwa na umeme, kama ulivyokuwa umesema megawatt 10,000 kwa malengo, sawa itatusaidia, lakini hebu kwa kutumia utaalam wako na wataalam mbalimbali wa masuala ya jiolojia tu-extend namna gani tutanufaika na gesi. Kwa mfano, kitaalam gesi ni kitu ambacho kinahitajika sana duniani. Tunaweza kusafirisha gesi siyo kwa kujenga bomba lakini kwa kufanya liquidfaction na tuka-export gesi kwa nchi jiraji kama vile China na India ambazo kutokana na geographical location yetu tunaweza kusafirisha gesi kwa kutumia meli kubwa.
Kwa hiyo, nikuombe Profesa kwa utalaam wako tu-extend ili kusudi gesi hii, tunapokwenda katika uchumi wa kati tuweze kunufaika zaidi kama ambavyo nchi kama Russia zinavyoweza kunufaika na gesi, siyo kwa kutumia tu katika kuzalisha ndani lakini pia kwa kuza nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pilli, nipende kuzungumzia sekta ya utalii. Hata katika taarifa ya utekelezaji wa Mpango ambao umepita Sekta ya Utalii imethibitika kwamba ilikua kwa kasi na mchango wake katika pato la taifa ulikuwa ni mkubwa sana. Niombe tu, katika mpango kwa kuwa hii ni sekta ambayo ilionesha wazi imekua kwa kasi hebu tuendelee kuipa nguvu. Pia tutanue wigo wake. Tunaweza kutanua sekta ya utalii kwa kuitangaza kupitia michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu nchi jirani wanatangaza sana utalii kupitia michezo hasa mchezo wa riadha. Hebu tujaribu pia kuona namna gani tunaweza kuwekeza. Nafahamu geographically, kama ambavyo nchi jirani kuna wanariadha wanatoka maeneo fulani fulani, na sisi pia tuna maeneo hayo ambayo tungeweza kutengeneza wanariadha wa kutosha ambao wangetumika siyo tu kwa kuongeza kipato lakini pia kuitangaza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwona Mheshimiwa Massay juzi alikuwepo kwenye riadha pale kutoka huko Hanang Mbulu. Tunaweza kutenganeza wanariadha wazuri ikawa siyo tu source of income kwa nchi lakini kwa kuitangaza nchi. Kupitia michezo tumeona tumeona mchezaji Mbwana Samata pamoja na kuwa baadhi ya vyombo vya habari vilipotosha na kuonyesha kama anatoka DRC au anatoka Botswana na kadhalika, lakini ni sehemu ambayo inatosha kabisa kutangaza utalii na hivyo kukuza utalii na mwishowe kukuza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nizungumzie suala la miundombinu. Ni kweli kabisa naona Waheshimiwa Wabunge wengi wakisimama wanazungumza kuhusu reli ya kati ni vizuri, lakini pia tusiisahau reli ya TAZARA. Sisi watu tunaotoka Nyanda za Juu Kusini tunalima vizuri mazao ya nafaka. Reli hii ingeweza kutosha kabisa kusafirisha siyo tu mazao ya chakula kama mpunga na mahindi, lakini hata mazao mengine ya biashara na hasa zao la mbao kutoka huko Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala zima la miundombinu, nashauri Mpango pia ujaribu kuelekeza au kutazama miundombinu kuelekea maeneo ambayo tayari ni ya uzalishaji. Kwa mfano, sisi katika Wilaya ya Mufindi barabara ya kutoka kiwanda cha Mgololo unakutana na semi-trailers kila siku, ni uchumi mkubwa kama tutaijenga barabara hii kwa kiwango cha lami maana yake ni kwamba tuta- stimulate uchumi wa watu wa maeneo ya jirani na mikoa ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wakisimama, na hata mpango unaeleza ambavyo sekta binafsi ni engine ya ukuaji wa uchumi. Pia, hebu tujaribu kujiuliza hii sekta binafsi inafanya kazi na nani? Nakubaliana nanyi kwamba ni engine ya uchumi; lakini engine ambayo huweki oil kwa wakati, engine ambayo huweki maji kwa wakati bila shaka ita-nock. Sasa maji na oil ni Utalii imethibitika kwamba ilikua kwa kasi na mchango wake katika pato la taifa ulikuwa ni mkubwa sana. Niombe tu, katika mpango kwa kuwa hii ni sekta ambayo ilionesha wazi imekua kwa kasi hebu tuendelee kuipa nguvu. Pia tutanue wigo wake. Tunaweza kutanua sekta ya utalii kwa kuitangaza kupitia michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu nchi jirani wanatangaza sana utalii kupitia michezo hasa mchezo wa riadha. Hebu tujaribu pia kuona namna gani tunaweza kuwekeza. Nafahamu geographically, kama ambavyo nchi jirani kuna wanariadha wanatoka maeneo fulani fulani, na sisi pia tuna maeneo hayo ambayo tungeweza kutengeneza wanariadha wa kutosha ambao wangetumika siyo tu kwa kuongeza kipato lakini pia kuitangaza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwona Mheshimiwa Massay juzi alikuwepo kwenye riadha pale kutoka huko Hanang Mbulu. Tunaweza kutenganeza wanariadha wazuri ikawa siyo tu source of income kwa nchi lakini kwa kuitangaza nchi. Kupitia michezo tumeona tumeona mchezaji Mbwana Samata pamoja na kuwa baadhi ya vyombo vya habari vilipotosha na kuonyesha kama anatoka DRC au anatoka Botswana na kadhalika, lakini ni sehemu ambayo inatosha kabisa kutangaza utalii na hivyo kukuza utalii na mwishowe kukuza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nizungumzie suala la miundombinu. Ni kweli kabisa naona Waheshimiwa Wabunge wengi wakisimama wanazungumza kuhusu reli ya kati ni vizuri, lakini pia tusiisahau reli ya TAZARA. Sisi watu tunaotoka Nyanda za Juu Kusini tunalima vizuri mazao ya nafaka. Reli hii ingeweza kutosha kabisa kusafirisha siyo tu mazao ya chakula kama mpunga na mahindi, lakini hata mazao mengine ya biashara na hasa zao la mbao kutoka huko Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala zima la miundombinu, nashauri Mpango pia ujaribu kuelekeza au kutazama miundombinu kuelekea maeneo ambayo tayari ni ya uzalishaji. Kwa mfano, sisi katika Wilaya ya Mufindi barabara ya kutoka kiwanda cha Mgololo unakutana na semi-trailers kila siku, ni uchumi mkubwa kama tutaijenga barabara hii kwa kiwango cha lami maana yake ni kwamba tuta- stimulate uchumi wa watu wa maeneo ya jirani na mikoa ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wakisimama, na hata mpango unaeleza ambavyo sekta binafsi ni engine ya ukuaji wa uchumi. Pia, hebu tujaribu kujiuliza hii sekta binafsi inafanya kazi na nani? Nakubaliana nanyi kwamba ni engine ya uchumi; lakini engine ambayo huweki oil kwa wakati, engine ambayo huweki maji kwa wakati bila shaka ita-nock. Sasa maji na oil ni nani? Maji na oil ni Watumishi wa Umma wa nchi hii. Mimi ni-declare interest nilikuwa Mtumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Mpango pia ujielekeze kwa Watumishi wa Umma, uwatazame katika maslahi yao, kuanzia mishahara yao, wakati wanapokwenda likizo; utakuta kwamba mwaka huu watapewa nauli mwaka mwingine hapewi nauli, lakini pia hata nauli ya kwenda kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwa Dar es salaam kuna Wizara zina gari za kuwapeleka wafanyakazi kazini na kuwarudisha, lakini kuna maeneo mengine mfanyakazi kwa mfano anatoka Kongowe anafanya kazi katikati ya mji, je, tunategemea mfanyakazi huyu atakuwa na moyo wa kuchapa kazi ipasavyo wakati maslahi yake uki-compare na hao wa private sector yako chini kwa kiwango cha kupindukia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nishauri; katika mpango hebu tutazame pia Watumishi wa Umma kwa sababu kama tunasema private sector ni engine, basi wao tuwachukulie kama vile ni oil. Ndiyo maana katika ofisi za umma survival ya watu wengi ni kusubiri safari za kikazi kwa sababu ule mshahara hautoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimalizie kwa kusema kwamba, kama ambavyo Profesa Muhongo amesema watahakikisha wanamalizia vipoto vya REA awamu ya kwanza na ya pili. Nashauri kabla ya kutekeleza Mpango unaokuja hebu tukamilishe viporo, kama kuna viporo vya zahanati, kama kuna viporo vya miradi mbalimbali tuvikamilishe, hiyo itatupa nafasi ya kuweza kusonga mbele na kutekeleza ipasavyo mpango unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie pia kwa kusema, katika kumalizia viporo hivyo niombe hasa katika sekta ya afya. Hebu tuangalie maeneno kulingana na population na namna ambavyo tunahudumia. Naomba kuunga mkono mapendekezo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 80 ya mbao laini (soft wood) inatoka kwenye viwanda vilivyoko Mafinga, ambapo kuna kiwanda cha SAO-Hill na viwanda vya wajasiriamali wa kati ambao wanaajiri kati ya wafanyakazi 100 - 200 kwa kila mwenye kiwanda, hii ni direct employments, achilia mbali indirect employment. Kwa ufupi, uchumi Mafinga, Makambako, Iringa na maeneo yote ya jirani unategemea sana suala la uvunaji wa misitu kwa nia ya kuvuna mbao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika kitabu chako Mheshimiwa Waziri, sijaona ukigusia viwanda vya mazao ya misitu, hususan viwanda vilivyopo katika Mji wa Mafinga. Kitakwimu, Mafinga na Mufindi inachangia pato la Taifa kwa kiwango cha juu. Mara kadhaa kama Wilaya imekuwa ranked No.3 katika kuchangia pato la Taifa, mchango mkubwa ukitoka katika uzalishaji wa mbao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Serikali iwasaidie wenye viwanda vya kati kwa kuwadhamini ili wapate mashine za kisasa za kuchania mbao. Ilivyo sasa, hata kama mtu ana shamba la miti, mabenki yanaogopa kukopesha kwa dhana ya risk ya moto. Hawa wajasiriamali wakipata mashine za kisasa wataweza kutumia mabaki kuzalisha vitu vingine kama ulivyosema tooth pick, chip board na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu umeme. Kiasi cha asilimia 30 ya muda wa kufanya kazi unapotea kutokana na kukatika kwa umeme. Nashauri Wizara ya Nishati TANESCO wafunge sub-station Mafinga ili kuondokana na tatizo la umeme. Kwa sasa umeme unaotumika unatoka Mgololo; na kwa kuwa Mji wa Mafinga umekua na viwanda vya kuchana mbao vimeongezeka, umeme unapofika, unakuwa umepungua nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nitashukuru kusikia kutoka kwako kuhusu namna gani viwanda vya mbao vya wajasiriamali wa kati vitakuwa incorporated kwenye michango ya Wizara na siku ufike na kuhakikishia hatutaagiza tenda tooth pick nje. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. COSATO D.CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda kuongelea kuhusu nguzo za umeme kutoka nje. Viwanda vya Sao Hill (Mafinga) na TANWAT (Njombe) waungwe mkono katika suala la tenda ya nguzo hasa kwa ajili ya REA phase III na TANESCO. Nguzo kutoka nje zinapata msamaha wa import duty na pia malipo yanafanyika kwa wakati. Pia Serikali (TANESCO) inawasaidia kwa mfumo wa Letter of Credit (LC). Favour hii inayotolewa kwa kampuni za nje haitolewi kwa wazalishaji wakubwa kama Sao Hill na TANWAT.
Viwanda nilivyovitaja vina uwezo kwa sababu vina misitu, lakini pia hata wananchi wamepanda miti ya kutosha. Nashauri tuunge mkono wazalishaji wa nguzo wa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni REA. Pongezi zangu kwa watendaji wa REA, hiki ni chombo cha kupigiwa mfano siyo kwa sababu wanapewa fedha la hasha, bali utendaji bora wa watumishi wote wa REA. Tumeona taasisi ngapi za Serikali zinapewa fedha lakini bado hakuna tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mkubwa kuhusu REA, Serikali ione uwezekano kupitia TAMISEMI/Wizara ya Fedha kuzisaidia Halmashauri gharama za wiring kwenye maeneo ya huduma (shule na zahanati) ambazo REA wamefikisha umeme lakini wananchi (vijijini) wameshindwa kuuingiza kwenye shule, mabweni na zahanati kwa kuwa hawana uwezo. Nafahamu ni jukumu la REA kufikisha umeme na siyo kugharamia kuingiza ndani, hata hivyo Serikali kwa pamoja mnaweza kuona tunawasaidiaje.
Tatu, katika Jimbo langu Mafinga Mjini kuna kijiji kinaitwa Sao Hill huko ambako nguzo za umeme zinazalishwa. Kijiji hicho naomba tukiwekee umeme kuenzi japo mchango wa kijiji hiki katika suala zima la nguzo. Tuwaonee imani yaani wao nguzo zitoke kwao lakini umeme wausikie. Pia vijiji vya Mtule, Matanana, Kisada, Bumilayinga, Ulole, Itimbo, Maduma na Kikombo na pia maeneo ya pembezoni mwa Mji wa Mafinga, nashauri TANESCO wafunge sub-station maana matumizi yameongezeka kutokana na kuongezeka kwa viwanda vya kuchana mbao na kukua kwa mji.
Nne ni kuhusu mafuta na gesi. Pamoja na wafanyabiashara kupiga vita EWURA, nashauri Wizara iwe makini na wafanyabiashara wanjanja wanaojenga hoja dhaifu za kuondoa “marker” ili kudhibiti wanaokwepa kodi. Pia tumejipanga vipi kuhakikisha haturudii makosa ya kwenye madini katika suala zima la kuhakikisha kuwa tunanufaika na sekta ya mafuta na gesi?
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nipende kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini na Halmashauri ya Mji wa Mafinga, kwamba ni Halmashauri mpya tuna mwaka wa pili tu lakini katika matokeo ya darasa la saba tumeshika nafasi ya tano katika halmashauri zaidi ya 150. Ni jambo ambalo tunajivunia, ni kutokana na ushirikiano kati ya wananchi, mimi Mbunge wao, Waheshimiwa Madiwani, watumishi, walimu na wananchi kwa ujumla na ninaomba tuendelee kushirikiana ili ikiwezekana mwakani tufike tatu bora

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda pia kuishukuru Serikali; tulikuwa na kilio kwa ajili ya bweni la Shule ya Msingi Maalum Makalala; ilituletea fedha milioni mia moja. Na kwa kutumia muundo wa force account tumejenga bweni zuri, Mheshimiwa Profesa Ndalichako alifika pale, tena tumetumia shilingi milioni 76 na fedha iliyobaki tutanunua samani kwa ajili ya bweni lile. Haya yote ni ushirikiano kati ya sisi viongozi na wananchi wa Mafinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuishukuru Serikali kwa ajili ya ujenzi unaondelea wa tanki la maji la ujazo wa lita 500,000 pale Kinyanambo. Pia Serikali imetupa kibali tayari mkandarasia atakwenda site kuanza kujenga tanki la lita 90,000 pale Kijiji cha Maduma na mradi wa maji kule Bumilayinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imetupatia shilingi milioni 500 ambazo tutaendelea na ujenzi kuimarisha kituo cha afya pale Ihongole. Haya ni mambo ambayo lazima tuyapongeze na kama hiyo haitoshi jana katika taarifa nimeona TAMISEMI inatuletea watumishi wa kada ya afya asiopungua saba ili kuendelea kuimarisha huduma za afya katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga na Hospitali ya Mafinga ambayo inahudumia Wilaya nzima ya Mufindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika Road Fund niiombe Serikali, tuna viporo, wakandarasi wamefanyakazi na wanatudai takribani shilingi milioni 212 fedha za mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwashukuru wahisani na marafiki mbalimbali ambao wanashirikiana na Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga katika kuimarisha huduma za afya na elimu. Napenda kuushukuru Ubalozi wa Japan wametupatia fedha tunajenga pale theatre ya kisasa kabisa. Sasa niiombe Serikali hususani Wizar ya Fedha; kwa kuwa fedha zile zilikuwa centralized sasa TBA ambao tumewapa ile kazi speed yao inakuwa ndogo kwa sababu bado hawajpelekewa fedha na yule mhisani angependa kuona maendeleo ya ile kazi.

Kwa hiyo, ningeomba Hazina watusaidie TBA wapate fedha hizo ili speed ya kazi iende sambamba na jinsi ambavyo mhisani yule alikuwa ametuelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Jenista Mhagama kwamba vikundi vya wajasiriamali, kama ulivyokuja ukatuelekeza tuvipike, tumevipika vimeiva, tunakusubiri kwa hamu sana uje utuletee ile mikopo ya riba nafuu.

Sambamba na hilo, wakati tunajadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa, mara zote nimesema, engine ya ufanikishaji wa utekelezaji wa mpango ni utumishi wa umma. Kama morale ya watumishi wa umma iko chini kama wanavyotumia lugha ya siku hizi kwamba vyuma vimekaza ni wazi kuwa mafanikio ya kufanikisha Mpango yatakuwa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo niipongeze Serikali, kwamba hatimaye baada ya uhakiki wa muda mrefu sasa imeangalia welfare ya watumishi, na ninaamini morale itapanda kwa sababu nimeona kumetengwa kiasi cha shilingi bilioni 159 kulipa malimbikizo kwa ajili ya watumishi mbalimbali ambao walishapanda vyeo na madaraja, lakini walikuwa hawajalipwa kile ambacho kinastahili kuwalipa. Kwa hiyo, naamini kwamba morale ya kazi itaendelea kupanda na kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wengine wanabeza uchumi haukui; ukiangalia takwimu za juzi za World Bank yule Mwakilishi Mkazi wa World Bank anasema kwamba; wao kama World Bank wali-project uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.9 lakini umekuwa kwa asilimia 6.8, ni jambo ambalo la kujivunia, ni jambo ala kujipongeza. Hata makusanyo kutoka kukusanya wastani wa asilimia 11 sasa Serikali inakusanya wastani wa asilimia 12.8 na mafanikio haya ni ndani ya miaka miwili. Lengo ni kufikia mwaka 2020/2025 tufikie makusanyo ya asilimia 19 kama ambavyo nchi zingine wameweza kufanikiwa, ni mambo ya kupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile uthubutu wa kuanza ujenzi wa reli tena kwa gharama nafuu. Tumeona wenzetu majirani, kilometa moja ni wastani wa dola milioni 8.5, sisi kilometa moja ni chini ya dola milioni 3.5. Ni jambo ambalo unaweza kuona kwamba Serikali iko makini katika kufaya majadiliano ya kufikia makubaliano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukuaji wa bandari. Sasa hivi tunaona wale waliokuwa wamekimbia wameanza kurejesha imani. Kwa hiyo, ni matarajio kwamba ufanisi katika bandari yetu ambao umeanza kuongezeka utachochea utendaji wa kazi na hivyo kuongeza mapato kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, Tulipitisha hapa Sheria ya Madini, kulikuwa na malalmiko kwanini imekuja under certificate of urgency, lakini manufaa yake wote tunayaona. Kile kitakachopatikana maana yake ni kwamba kitakwenda kusaidia kuboresha aya, huduma za jamii kama elimu, ujenzi wa barabara na miundombinu mingineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma katika mpango na ninapongeza jitihada za ujenzi wa Kiwanda kule Mkulazi ambazo zinafanywa kwa ushirikiano wa Mifuko ya Jamii. Lakini nitoe ushauri, sisi mahitaji yetu kwa mwaka ni wastani wa tani 590,000. Katika hizi tani 300,000 ni matumizi domestic na tani 170,000 ni ile sugar for industrial.

Sasa pamoja na jitihada za uwekezaji huu ambazo zinaendelea, mimi nishauri kwamba tujaribu kuangalia katika yale mabonde muhimu tuwekeze pia kwa mfumo wa small- medium size kwamba unakuwa na kiwanda kinaweza kuzalisha tani 5,000 pale Kilombero, kiwanda kinakuwepo Rufiji hata vitatu au vinne, kwa sababu gharama zake za uwekezaji ukizi-split unaweza kuvutia wawekezaji wadogo wadogo wengi na hivyo kuongeza uzalishaji lakini pia kuongeza mapato kwa Seriakli pamoja na kupanua wigo wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema hivi? Brazil wenzetu wanazalisha tani milioni thelathini na sita kwa mwaka na kwa takwimu hizo, Brazil globaly uzalishaji wao ni asilimia 20, lakini katika Soko la Dunia wao wanashika kwa asilimia 40.

Kwa hiyo, unaweza kuona kwamba sukali bado inahitajika kwa kiwango kikubwa na sisi ili kuimarisha shilingi yetu maana yake ni lazima tuuze nje. Kwa hiyo, licha ya kwamba tuna soko la ndani, lakini pia tuna soko ambalo lipo, limejaa tele katika global market.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ukienda katika takwimu inaonesha kwamba nchi kama Nigeria yenyewe inaagiza sukari ya thamani ya milioni 500 kwa mwaka, hilo ni soko lipo. Ukienda South Africa inaagiza sukari ya thamani ya dola milioni mia tatu na sita, maana yake ni soko lipo, ukienda Ethiopia wanagiza sukari ya dola milioni 188 kwa mwaka, maana yake ni soko lipo. Kwa hiyo pamoja na jitihada za Mkulazi tutafute pia mbinu nyingine ambayo inaweza ikachochea small-medium size factories ili tujitosheleze kama soko la ndani lakini pia tupeleke nje kusudi tuweze kuiimarisha shilingi yetu. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nizungumzie pia umuhimu wa kufufua viwanda hususani mradi wa kielelezo hasa wa Mchuchuma na Liganga. Mradi huu kila mara unakuja kwenye vitabu. Sisi watu wa Nyanda za juu Kusini tunadhani kwamba kufanikiwa na kuanza kutekelezwa kwa mradi huu utasaidia sana kuchochea uchumi katika eneo hilo na hivyo si tu kuongeza mapato ya Serikali lakini pia kupanua wigo wa ajira sambamba pia na kuimarisha shilingi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kufufua viwanda tuangalie pia jinsi ya kuwasaidia wawekezaji wa ndani. Kwa mfano mimi kule Mafinga, suala la mazao ya mistu ni jambo ambalo nimekuwa nikilisema mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali hasa Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii wanahusika kutupa sisi wawekezaji malighafi, lakini nimesema mara nyingi MPM kile wanachopewa wanavuna tu kama theluthi mbili. Sasa ile theluthi moja inayobaki wapewe wawekezaji wetu wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu; bei imeshuka sana. Sisi hapa mbao zetu hauwezi kushindana na mbao inayotoka Malawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu Serikali ijaribu kuangalia bei za misitu kusudi tuone namna gani tunaweza kuwapa wawekezaji wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa; kama nilivyosema wakati Maliasili wanahusika kutoa malighafi, Wizara ya Viwanda na Biashara moja kwa moja inahusika katika kulea hii sekta ya mzao ya misitu. Kuna potential kubwa kwenye mzao ya misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mwijage na Naibu wake, katika miaka mwili nimemwambia sana Mheshimiwa Mwijage uje Mafinga na Mufindi. Minimum mtu kawekeza shilingi milioni 500 na tuna viwanda siyo chini ya 40, kuna watu sasa wameanza kuongeza thamani katika mazao wakitengeneza mkaa kutokana na zile pumba zinazotokana na mazao ya misitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ile kwanza itatusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Vilevile hawa watu kuna fursa nyingi wangependa kuzifahamu kutoka TAB, wangeweza kufahamu mambo mengi kutokana na tozo za OSHA, NEMC, TBS na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote tukifanya kongamano la pamoja itatuwezesha sisi kujua ni changamoto gani wanazokabiliana nazo ili tui-raise hii sekta iweze kukua, ikuze ajira lakini pia iongeze pato; kwa sababu sasa wanaongeza thamani katika mazao tuuze nje ili tuendelee kuimarisha shilingi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naendelea tena kuiomba Serikali katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 tunaomba kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika Mji wa Mafinga bado hatujapokea fedha kutoka Road Fund. Tuna viporo vingi vya kuimarisha barabara ule ni mji unaokuwa kwa kasi tungependa tuwe japo na kilometa mbili, tatu za lami lakini kama hatutapata fedha itatuwia vigumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali sambamba na kuomba fedha ambazo zinatakiwa ziende TBA kwa ajili ya mradi ule wa ujenzi wa theatre, pia ituangalie katika suala la barabara za pale Mjini Mafinga. Pia kwa ajili ya ujenzi wa tanki la mita milioni moja ambalo Mheshimiwa Waziri wa Maji namshukuru sana, ameniahidi kwamba kesho tutaonana naye ili kuweza kujua maendeleo ya kupata kibali cha kutangaza hiyo kazi yamefikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, nakushukuru na niwaambie wananchi wa Mafinga nawapenda sana, ushirikiano wetu ndiyo silaha na moto wetu na slogan yetu tunasema Mafinga kazi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa kupata nafasi na kama mdau wa michezo napenda kuishukuru Wizara na Watendaji wake wote kwa maandalizi ya hii hotuba yao. Pia napenda kushukuru vyombo vya habari vya Serikali, hasa Daily News kwa sababu sasa hivi wamekwenda digital, wanatusaidia kueneza Kiswahili kwa kuchapisha lile jarida lao linalotoka kwa ajili ya nchi za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kupongeza Idara ya Habari Maelezo kwa wepesi wake wa kutoa taarifa mara kwa mara kwa Umma wa Watanzania. Nawaomba waendelee kwa sababu hii ndiyo idara ambayo inategemewa kutoa matamko na maelezo mbalimbali, kinyume chake kutakuwa na vacuum ambayo inaweza kujazwa na taarifa ambazo zinaweza zikapotosha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, niende kwa haraka sasa katika mchezo unaopendwa na watu wengi duniani, mchezo wa mpira wa miguu. Hapa naipongeza TFF, angalau baada ya mwaka 2017 kuchangia na kutoa takwimu za ushiriki wa Timu ya Taifa katika michezo ile kulingana na kalenda ya FIFA, naona TFF angalau walizingatia ule ushauri na sasa hivi Timu ya Taifa inashiriki kadri ya kalenda ya FIFA katika mechi za majaribio au za kujipima nguvu au za kirafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesaidia mpaka wiki iliyopita angalau tumepanda kutoka nafasi ya 146 mpaka 137. Hata hivyo, bado kuna kazi inatakiwa ifanyike, tuendelee kukutana na timu ambazo angalau ziko kwenye viwango vya hamsini bora kwenye FIFA ranking maana yake ile inatusaidia sisi kupata angalau points nyingi na hivyo kuisogeza Timu yetu ya Taifa katika viwango bora vya FIFA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mojawapo ya vitu vilivyotusaidia ni kuwafunga Congo DRC ambao wako nafasi ya 38 katika FIFA World Rankings. Kwa hiyo, tusiandae mechi kucheza tu na ambao niseme ni kama wachovu wenzetu, hapana. Tukabiliane na hao ma-giant kama tulivyofanya kwa Algeria, hata kama tulipoteza. Maana yake ni kwamba tunaendelea kuijengea uwezo Timu yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Timu ya Ngorongoro, Timu ya Serengeti na Timu za Wanawake. Kimsingi TFF naona inajitahidi kuhakikisha kwamba timu zetu zinashiriki katika michuano ya Kimataifa kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, la pili ambalo linaweza kusaidia Timu yetu ya Taifa iwe na ushindani, ni ligi yetu kuwa na ushindani. Sasa hivi kanuni inasema timu inaweza ikaajiri wachezaji saba wa kigeni, lakini je, ni wachezaji wa kiwango gani? Kwa hiyo, napenda kushauri TFF, mfano Ligi Kuu ya Uingereza ili ucheze, lazima uwe umethibitisha ubora yaani lazima uwe timu yako iko katika viwango.

Kwa mfano, kiwango cha kwanza mpaka nafasi ya kumi mchezaji lazima awe amecheza angalau asilimia thelathini (30) ya mechi za Timu ya Taifa kwa miaka miwili. La, kama unatoka katika timu ambayo kwenye FIFA Ranking iko nafasi ya 21 mpaka 30, lazima mchezaji uwe umecheza angalau asilimia 60 katika timu yako ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi inawezekana kuna wachezaji wanatoka nchi za Afrika Magharibi kweli kiasi fulani zimepiga hatua, lakini hata wachezaji wanaotoka kwenye Ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati hebu basi TFF iweke vigezo, isiwe tu bora mchezaji. Maana yake nimefuatilia kalenda ya FIFA, hakuna wachezaji walioitwa kwenda kuchezea timu zao za Taifa lakini hapa tunawaita ma- professional. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha Juuko Murushid, Emmanuel Okwi, ukiacha Dany Usengimana na yule wa Singida United na ukiacha, siku za nyuma, Haruna Niyonzima, hakuna mchezaji yeyote ameitwa kwenye timu yake ya Taifa, lakini sisi hapa tunamlipa fedha nyingi. Kwa hiyo, naiomba TFF i-set standard kwamba ili mchezaji acheze Ligi Kuu hapa nyumbani, lazima kuwe na vigezo fulani, hatuwezi kuwa na vigezo kama vya Spain au vya England au vya Italy, lakini lazima tu-set standard ili hapa isiwe soka ambayo imekuwa kama vile ni soka holela holela tu, kwamba watu wanakuja kujifunzia mpira hapa. Hilo litasaidia kuleta ligi yenye ushindani, lakini kutokana na ligi yenye ushindani maana yake tutakuwa na timu ya Taifa ambayo ni bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, Uingereza sasa hivi kuelekea Kombe la Dunia 2022 wameamua kuongeza kwamba kila timu lazima iwe na wachezaji wa ndani kutoka nane mpaka 12. Sisi tunasema wachezaji wa kigeni wawe saba; ni vizuri, hatuwezi kuiga kila kitu kutoka kwa wenzetu waliopiga hatua sana, lakini angalau tu-set hizo standards. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Kamati imezungumzia hapa kuhusu Timu ya Taifa kwamba maandalizi yanakuwa ni duni; naiomba Serikali, pamoja na kwamba mambo haya yanasimamiwa na TFF, lakini hakuna namna. Kama tunataka kufanya kweli michezo ni biashara, tutangaze utalii kama Mheshimiwa Waziri alivyosema, kwamba Serikali ikakaa pembeni katika uandalizi wa timu za Taifa. Tumeona tumeenda juzi Jumuiya ya Madola imeendelea kuwa vichekesho vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tufanye hivyo hakuna namna, ni lazima Serikali kwa kushirikiana na wadau kwa namna yoyote, ni lazima i-take lead, tusiviachie Vyama vya Michezo, lazima Serikali i-take lead ndiyo tutavuna matunda mema. Vinginevyo tutajadili hapa, tutapiga madongo vyama vya michezo, bila Serikali kuweka mkono wake hakuna namna tutapiga hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, napenda kuhoji Mheshimiwa Waziri, wakati Serikali ikijibu swali Na. 62 hapa, ilieleza masuala ya udhamini ambao inaupata TFF kutoka kwa vyombo mbalimbali hapa nchini. Kama hii taarifa ni kweli na naiamini, kwa sababu ni ya Serikali, katika sehemu ya jibu ilisema; “aidha, TFF iliingia mkataba na Kampuni ya Bia ya TBL mwaka 2013 - 2017 kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni kumi kwa ajili ya Taifa. Mkataba huo ulishamalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TFF imeingia mkataba wa ufadhili na Kampuni ya Bia ya Serengeti kwa miaka mitatu; 2017 - 2019, wenye thamani ya shilingi milioni 700 na milioni 450 kwa ajili ya Ligi Kuu ya Wanawake. Maana yake kimahesabu kati ya 2013 - 2017 ilikuwa dola milioni kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya 2017-2019 ni dola milioni moja. Hivi gharama za maisha zinapanda au zinashuka? Maana yake hii nimeitoa kwenye Hansard, kwamba mwaka 2013 - 2017 unaingia udhamini wa dola milioni kumi, 2017 - 2019 unaingia udhamini wa dola milioni moja. Sijui, yaani najaribu kufikiri, kwa kweli sipati picha na ningependa kwenye majumuisho Mheshimiwa Waziri atusaidie kutueleza jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, entertainment and media industry, kwa mujibu wa PWC, Tanzania ni kati ya nchi tano ambazo entertainment industry inakuwa kwa kasi sana. 2016 mapato yalikuwa dola milioni 504, sawa na shilingi trilioni 1.1. Kufikia 2021 inatarajiwa mapato yatakuwa dola bilioni 1.1, sawa na shilingi trilioni 2.4. Where is our stake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasanii wetu wananufaikaje katika hizi trilioni zinazoingia? Au ni fedha tu zinaishia kwenye makampuni ya kuuza data, kwenye makampuni ya promosheni? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hii vacuum ambayo inatokea kwenye media and entertainment industry naomba atakapokuja ku-wind up, atusaidie, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba wasanii wanaendelea kunufaika na hizi trilioni ambazo Taifa linaingiza? Kwa sababu katika 2.4 trillion mpaka mwaka 2021 hapa wasanii wakipata japo asilimia 20 tu, maana yake ni kwamba utakuwa umeongeza ajira ngapi katika Taifa? Wengi wanaofanya shughuli hii ni vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, this entertainment and media industry is very potential. Hebu tutazame, tukae na hawa wasanii, tuwaelekeze tamaduni zetu, tuwape miongozo ili waendane na tamaduni na mila zetu lakini at the same time waweze kunufaika na kile kinachopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya, napenda kuunga mkono hoja na nawatakia wapenzi wote na mashabiki wote wa Simba na Yanga mchezo bora Siku ya Jumapili. Ahsante sana.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, misitu; (kwa nini ni muhimu kuwa na Chuo cha Misitu Mufindi) Pamoja na mchango huu, naomba kuwasilisha nakala ya kwa nini tuwe na Chuo kama Tawi la Chuo cha Misitu cha Olmotonyi. Nakala yangu imejieleza vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, mgao wa malighafi, ninashukuru Wakala wa Misitu kwa kuitikia kilio changu cha kukutana na wadau wa mazao ya misitu kabla ya msimu kuanza. Hata hivyo kama sehemu ya maoni ya wadau tulipokea tarehe 30 Aprili, 2018 mgao uzingatie pia kiwango cha uwekezaji na hivyo kwa waliowekeza mitaji mikubwa wepewe mikataba ya malighafi, mfano watu kama kina CF (Makambako), Hongwei International just mention some few ukiacha MPM na Sao Hill (ambao kiasi fulani wameyumba) kuna watu wanapewa kwa mkataba wakati wao hawavuni, hawana viwanda isipokuwa wanauza malighafi zao kwa wenzao, sio haki kabisa.

Ninashauri timu inayopita kukagua, itende haki na itoe maoni ya wanaostahili kupewa mikataba ya malighafi. Ikiwa mtu anatoa ajira direct employment ya watu 200 na kuendelea kwa nini asipewe mkataba? Mgao wa cubic meter 90,000 za Sao Hill ambao wameyumba mngefanya review ili walau one third ya mgao huo uende kwa wavunaji wadogo waliowekeza.

Mheshimiwa Spika, ushauri, ili kupunguza malumbano na mivutano isiyo na sababu Wizara itoe maelekezo kuwa na chama kimoja tu ambacho kitafanya kazi na Serikali pasipo mivutano maana mwisho wa siku wote ni wadau hivyo kuwa na chama kimoja ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, napongeza uongozi wa shamba la Sao Hill kwa ushirikiano na Mafinga Town Council.

Mheshimiwa Spika, why a need for a forestry college in the Southern Highlands of Tanzania and preferably in Mufindi District?

Mheshimiwa Spika, historia/background, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania imejaaliwa kuwa na hali ya hewa nzuri na udongo wenye rutuba, vyote kwa pamoja ni muhimu kwa kilimo cha miti ya misindano na mikaratusi. Wananchi wanaoishi katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa na Katavi wanajishughulisha kwa kiasi kikubwa na upandaji miti. Wilaya ya Mufindi iliyoyo katika Mkoa wa Iringa inaongoza kwa upandaji miti kitaifa. Wilaya hii pia ni nyumbani (is a home of) misitu ya Sao-Hill, msitu mkubwa wa pili Barani Afrika na wa kwanza nchini Tanzania. Ukubwa wa msitu huu ni zaidi ya nusu ya misitu yote inayomilikiwa na Serikali ya Tanzania iliyopo sehemu mbalimbali kama Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Tabora, Mbeya na kwingineko. Msitu una eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 135,903. Msitu huu umesambaa katika tarafa nne kati ya tano za Wilaya ya Mufindi. Umesambaa katika tarafa za Kibengu, Ifwagi, Kasanga na Malangali.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1937 Waingereza walianzisha Chuo cha Misitu Mkoani Arusha kiitwacho Olmotonyi. Chuo hiki kililenga kuzalisha wataalam wa misitu katika fani mbalimbali. Wakati Chuo cha Olmotonyi kikifunguliwa msitu wa Sao-Hill ulikuwa katika hatua ya majaribio. Kuanzishwa chuo mikoa ya Kaskazini ilikuwa ni muhimu kwa sababu tayari kulikuwa na misitu kadhaa iliyokuwa imepandwa na Wajerumani na Waingereza kwa nyakati tofauti. Chuo hiki kiliwapa fursa Watanzania toka sehemu mbalimbali ya nchi kupata elimu ya misitu na hivyo kuajiriwa katika mashamba mbalimbali ya Serikali na katika Wizara ya Maliasili. Hata hivyo, kwa kuwa Serikali ya kikoloni ilikuwa inaona shida kuwagharamia watu wa mbali usafiri, kipaumbele kikubwa ilikuwa ni kuwasomesha watu wa Kaskazini ambao walikuwa karibu na chuo. Hivyo, tangu kipindi cha ukoloni Watanzania wengi wanaoishi mbali na Chuo cha Olmotonyi walikosa fursa ya kupata elimu ya misitu.

Mheshimiwa Spika, baada ya uhuru Serikali ilirithi chuo hicho na kukiendeleza ikiwa ni pamoja na kuanzisha elimu ya misitu Sokoine University of Agriculture (SUA). Baada ya Serikali kupanua shughuli za upandaji miti katika msitu wa Sao-Hill baada ya uhuru ilitambua kwamba haikuwa na maafisa misitu wa kutosha hasa wazawa.

Mheshimiwa Spika, miaka ya 1980 ikaanzisha chuo cha kutoa mafunzo ya elimu ya misitu ya muda mfupi katika makao makuu ya Sao-Hill (majengo bado yapo hadi leo) (Sao-Hill Forestry College). Kwa sababu ambazo hata hazifahamiki chuo kilihudumu kwa muda wa miaka saba tu hivyo hakikuendelea kutoa tena mafunzo. Kutoendelea kwa chuo hicho kimewanyima wananchi wengi wa maeneo yanayozunguka misitu na Mkoa ya jirani ya nyanda za juu kujipatia elimu ya misitu na hivyo kuwafanya wategemezi kwa NGOs chache zinazotoa huduma hiyo. Pia vijana wengi wa nyanda za juu wamekosa exposure ya elimu ya misitu na hivyo kuishia kufanya unskilled jobs ambao zinawafanya kulipwa ujira mdogo sana.

Mheshimiwa Spika, kwa nini tuwe na Chuo cha Misitu Mufindi (Mufindi/Sao-Hill Forestry College, a Constituent College of Olmotonyi Forestry College). Tayari kuna majengo (madarasa, ofisi za walimu na mabweni) pale makao makuu ya Sao-Hill ambayo yalijengwa tangu miaka ya 1980 hivyo haitatumika gharama kubwa ya kuanzisha chuo kwa kuwa majengo ya kuanzia yapo. Kwa sasa majengo hayo wanaishi wafanyakazi na mengine wanafugia tu kuku na kuhifadhia mahindi.

Natambua jitihada za Serikali katika kuyafufua majengo hayo kwa msaada wa watu wa Finland ili yatumike kutoa mafunzo kwa wakulima wa miti wadogo wadogo. Hata hivyo, hii haizuii majengo hayo kutumika kama chuo kishiriki cha Chuo cha Misitu cha Olmotonyi kwa sababu wananchi wanaopata mafunzo yatakuwa yanatolewa kwa muda mfupi tu (kwa uelewa wangu). Hivyo, kuwa na chuo kitakuwa ni msaada mkubwa hasa kwa vijana wengi wanaotoka maeneo yanayozunguka msitu na hata nyanda za juu katika mikoa tajwa hapo juu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi tarafa zake nne kati ya tano zimezungukwa na misitu na hivyo hii ndio shughuli yao kubwa ya kiuchumi kwa sasa. Kuwa na chuo kitavutia vijana wengi kusoma ili kupata elimu ya misitu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi ina wawekezaji wengi wakubwa kwa wadogo waliowekeza katika kilimo cha miti. Wawekezaji hawa wanatakiwa kuajiri watu wenye weledi katika mashamba yao. Pia wanahitaji wavunaji wenye elimu ya kuvuna misitu kitaalamu zaidi. Kuwa na chuo Mufindi kutafungua fursa mpya za ajira kwa vijana wengi ambao watapata mafunzo kwa ngazi mbalimbali za cheti na diploma.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi ndio mwenyeji wa msitu mkubwa zaidi nchini na wa pili Afrika. Eneo kubwa la ardhi ya wananchi lilichukuliwa ili kupisha uwekezaji huu. Kuwa na chuo Mufindi ni njia mojawapo ya Serikali kutoa fadhila na kudumisha mahusiano mema kati ya wananchi wa Mufundi na Sao-Hill/Serikali kwa kuwa vijana wao watapata elimu ya misitu inatakayoinufaisha jamii nzima inayozunguka mradi na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, vijana wengi wa Mufindi hawaajiriki katika mashamba ya miti na viwanda vya kupasua mbao. Wengi wao wanaajiriwa katika kazi ambazo sio za kutumia utaalam kama kusukuma magogo, kuzima moto, kupanda miti na kusafisha mashamba. Hii imejenga matabaka kati ya wenyeji wengine na hivyo kujiona kama hawathaminiwi ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, ni moja ya ahadi zilizowahi kuahidiwa tangu kipindi cha mkoloni wa kiingereza na kurudiwa tena na Serikali yetu baada ya uhuru. Wakati wanawashawishi wananchi kuhama ili kupisha mradi wa Sao- Hill wananchi waliahidiwa vitu vingi ikiwa ni pamoja na ajira, chuo cha misitu na mengine. Ahadi hiyo ilianza kutekelezwa miaka ya 1980 baada ya kuanzisha chuo pale Sao-Hill lakini hakikudumu hadi leo hii yamebaki majengo tu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi ina eneo la kutosha na hali ya hewa nzuri. Vilevile uwepo wa msitu mkubwa, viwanda vya kuchakata magogo vikubwa na vidogo pamoja na kiwanda cha karatasi vinaifanya Wilaya kuwa sehemu nzuri hasa kwa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, relevance ya kuwa na chuo eneo tofauti na Mufindi kama ilivyo sasa Arusha kwa sasa haipo kwa kuwa hakuna viwanda vya karatasi, wala viwanda vya kutosha kwa mafunzo ya vitendo na pia eneo hilo sio rafiki kwa kilimo cha miti kwa sasa kwa kuwa hawana ardhi ya kutosha hivyo manufaa yake kwa jamii inayokizunguka chuo ni ndogo ukilinganisha na manufaa ambayo wanaweza kuyapata wakulima wa miti wa Mufindi pamoja na wa Nyanda za Juu kwa ujumla ambao ndio wadau wakubwa wa misitu kwa sasa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa na mimi kuchangia Wizara hii na kwa haraka kabisa napenda kuipongeza Wizara kuanzia Mheshimiwa Waziri, Naibu, Makatibu Wakuu pamoja na Mabalozi ambao ni Wakurugenzi wanaoongoza idara mbalimbali katika Wizara ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi hizi haziwezi kwenda tu hivi hivi zitaendana na ukurasa wa 25 ambao unaelezea misamaha ya madeni ya nje. Hii yote ni jitihada za kazi nzuri ambao Wizara pamoja na Wakurugenzi na Mabalozi kote waliko wanaifanya na ndiyo maana tumeweza kusamehewa baadhi ya madeni katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia na mimi nichukue nafasi hii kuwapongeza wenzangu Mheshimiwa Masele na Mheshimiwa Mboni Mhita kwa nafasi walizochaguliwa. Hii inaendelea kuthibitisha kwamba Taifa bado linaendelea ku- maintain heshima yake katika nyanja za kidiplomasia Afrika na dunia kwa ujumla. Kwa hiyo tuendelee kusonga mbele na kuchapa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa sababu si haba niseme kidogo, sina nia ya kumjibu ndugu yangu Mheshimiwa Mbilinyi lakini niseme tu kwamba, katika nyanja za kidiplomasia nchi kama Algeria nitawapa mfano ndiye supporter mkubwa wa POLISARIO Chama cha Ukombozi wa Sahara. Hata hivyo, Algeria hii ambao POLISALIO Makao yake Makuu yako Algeria ina mahusiano (bilateral) na Morocco. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kum-support mtu fulani haikuzuii wewe kufanya mahusiano na yule mtu mwingine as far as you have interest in that particular mahusiano. Kwa hiyo si jambo geni, hata South Afrika ni supporter mkubwa wa POLISARIO, ndio wanao finance POLISARIO, lakini wana mahusiano bilateraly na Morocco. Kwa hiyo, unaangalia wewe una interest gani na misimamo yako inabaki vile vile; niliona ni muhimu kulisema hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nipende pia kupongeza kwa kufunguliwa hizi balozi zetu nyingine, sita na Mheshimiwa Waziri amesema mabalozi wamesha kwenda. Pia kama ambavyo Kamati ilikuwa imeshauri kuwa na umuhimu wa kufungua zile tunaita General Consulate katika Miji ya Lubumbashi na Guangzhou. Nimeona kwamba Serikali imezingatia ushauri wa Kamati na Wabunge kwa ujumla na kwamba sasa tunakwenda kufungua General Consulate katika hiyo miji ambayo iko strategically kibiashara kwa Taifa letu, kama hiyo Lubumbashi na Guangzhou.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mambo ambayo ya kupongeza na yanaonesha kwamba Serikali inachukua mawazo yetu Wabunge na kuyafanyia kazi. Kwa hiyo niwasihi tu kama Serikali twende kwa haraka katika kulitekeleza kwa vitendo jambo hili ambalo mmelichukua kutokana na ushauri wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie; Mheshimiwa Waziri amekuwa kwenye nyanja hii ya diplomasia, atakuwa anafahamu kwamba sasa hivi kuna reform inaendelea UN Security Council, kwamba na sisi kama Afrika tungependa tupate nafasi katika sehemu ile ya zile kura tano za veto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Taifa nimwombe Mheshimiwa Waziri tujipange vizuri na hatua mojawapo ya kujipanga ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunapeleka maafisa katika vituo vyetu vya ubalozi. Tukiwa na maafisa wa kutosha maana yake ni kwamba ushiriki wetu utakuwa ni madhubuti. Kuna vituo ambavyo ni multilateral stations, Mheshimiwa Waziri anafahamu, kama New York, anafahamu pale kuna Kamati sita ambazo kila Kamati inapaswa iwe na afisa kwa ajili ya kutetea maslahi mbalimbali ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano wa Kamati ya tano, Mheshimiwa Waziri anafahamu kabisa kwamba baada ya kufunga ICTR tuko kwenye transition kupitia ile Mechanism For International Criminal Tribunala. Katika bajeti ya 2018/2019 mapendekezo yalikuwa kwamba tupate nadhani dola milioni mia mbili kumi na tano. Hata hivyo, kutokana na kukosa ushawishi wa kutosha, Waziri anafahamu mataifa makubwa yamepunguza tumepata dola milioni 88.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jitihada za baadhi ya mataifa kuhakikisha kwamba hata ikiwezekana ile iliyokuwa ICTR ifungwe ihamie The Hague. Sasa jambo hili likifanyika ni hasara kwa Taifa letu kwa sababu, imagine kama mahakama ile inapangiwa dola milioni 215 maana yake ni kwamba hata kiuchumi zitaongoza mzunguko katika Taifa letu, siyo tu pale Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Nanibu Spika, pia jitihada hizi inabidi tujipange kikamilifu kuweka kukabiliana nazo; kwa nini; kwa sababu wa uwepo wa ICTR pale Arusha ni legacy kubwa kwa Taifa letu katika dunia. Sasa jitihada hizi kama hatutahakikisha tunapeleka watumishi wa kutosha katika balozi zetu, maana yake ni kwamba hata ushiriki wetu katika vyombo mbalimbali especial hizi Kamati utakuwa ni minimum. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri tu speed up hii process ya kupeleka maafisa kwani umuhimu wake uko wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama vile haitoshi, kwa nini mimi nasema nasema masuala haya, watu wengi tunapozungumza masuala ya peace keeping wanazungumzia chapter six na chapter seven; lakini ukweli UN imeendelea kupunguza fedha za kulinda amani katika maeneo ya migogoro Afrika. Hii ni kwa sababu ama tunapunguziwa ushawishi kutoka labda na understaffing.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimwmbe Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye ni nguli katika nyanja hii, katika hii reform inayoendelea ya UN Security Council hebu sisi kama watu ambao tunaaminika kiplomasia na kimataifa, kwamba tuna ushawishi mkubwa Kusini mwa Afrika, tuna ushawishi mkubwa katika bara la Afrika, tuna ushawishi mpaka katika South East Asia, hebu tu-play role yetu ili kusudi ushawishi kama Taifa katika Umoja wa Mataifa uendelee kuwa mkubwa ili kusudi hata yanapokuja masuala ya bajeti kwa mfano za peace keeping tuweze kushawishi pesa itengwe ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu madhara yake ni nini, tumeona tumepoteza wanajeshi pale Congo. Ingekuwa UN inapeleka bajeti ya kutosha ya peace keeping; maana tumeambiwa mapigano yalidumu masaa 14, maana kama vingekuwa vifaa vya kisasa, tuna ndege za rescure maana yake tungeweza kuokoa wanajeshi wetu wale. Haya yote hayafanyiki kwa sababu ndani ya mfumo wa UN wakubwa wa dunia wanajitahidi kuhakikisha ile keki inapelekwa katika mambo ambayo wao wanaona yatakuwa yanawasaidia lakini sisi hayatusaidii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niishauri Serikali kwamba tuendelee kuthibitisha kwa vitendo kwamba sisi ni taifa kubwa katika ushawishi wa diplomasia kimataifa Afrika na duniani kwa ujumla; na ushiriki huu utathibishwa kwa sisi kuendelea kuwa na staff wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia sitakuwa nimetenda haki kama sitawashukuru Wizara katika ujumla wake. Nimeona hapa wametuletea kijitabu kinasema find about us; ndani yake kina anuani za Balozi zetu. Maana yake ni kwamba sisi hapa ama tuna ndugu zetu ama tuna watu wanaenda katika matibabu au watu wanaenda kutafuta fursa za kibiashara au kuna wanafunzi. Sasa kijitabu hiki kitarahisisha yale mawasiliano ya kidiplomasia kujua nchi gani balozi ni nani na anuani yake ni ipi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi wametupa pia kijitabu ambacho kinaonesha anuani za Balozi za nje ambazo ziko hapa nchini. Vile vile wametupa kijitabu hiki kinachoonesha diplomasia ya Tanzania ambapo ndani yake wametuonesha picha, wameandika na caption ya utekelezaji mbalimbali wa Diplomasia Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli niwashukuru sana na naamini Mheshimiwa Masoud, Mzee wangu wa Matambile pale atakuwa leo amefurahi na atacheka mpaka jino la mwisho kwa sababu ni kitu ambacho tumekuwa pia tukizungumza katika Kamati na Serikali imeweza kuthibitisha. Niongeze tu wakati ujao wanaweza kutuboreshea pia kwa kutuletea kijitabu ambacho kinaeleza kila nchi ina fursa gani na watu wanaweza kuzipata fursa zile kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya, napende kushukuru na naunga mkono hoja. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Naomba moja kwa moja nianze kwanza kwa kushukuru Mamlaka ya TRA hususani Kamishna Mkuu na Kamishna wa Kodi za Ndani, lakini pia na Waziri kwa sababu wakati fulani niliwasilisha kwao malalamiko, licha ya kuwa niliwasilisha kwa meseji juu ya wananchi wangu wanaofanya biashara ya mbao na matatizo wanayokutana nayo. Kwa kweli hatua zilichukuliwa, Kamishana wa Kodi za Ndani akaja Mafinga akafanya mkutano karibu saa sita kuwasikiliza wale wadau. Kwa sababu ilifika wakati ilikuwa kama vile kufanya biashara ya mbao ni laana. Ukipakia mzigo mtu mwenye lori anaulizwa mashine ya EFD aliyokulipa mwenye mzigo ya transport iko wapi, hana, faini milioni nne. Kwa hiyo, tulikuwa tuna paralyse sekta ya mazao ya misitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa hili napenda kupongeza lakini pia napenda kushauri. Kumekuwa na malalamiko sana ya wafanyabiashara hususani wafanyabiashara wadogo wa Mji wa Mafinga. Ushauri wangu kwa Serikali na kwa TRA, naomba kupitia Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi kwa mwaka walau mara mbili iwe inatoa elimu lakini pia ikutane na wafanyabiashara na kujua ni changamoto gani wanakutana nazo ili kwa pamoja waweze kuwa on the same boat. Kwa sababu tunachotaka watu walipe kodi sustainably siyo mwaka huu mtu alipe kodi Sh.1,000,000, mwaka unaofuatia Sh.800,000, mwaka unaofuata Sh.500,000, mwaka unaofuatia ame-collapse. Lazima tuwekeane mazingira Serikali ipate chake lakini pia na wafanyabiashara wa-survive progressively. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, mimi nilishika shilingi hapa wakati wa bajeti ya Wizara kuhusiana na fedha za miradi viporo. Mheshimiwa Jitu jana amezungumza, kwamba fedha hizi Serikali imekubali itatoa kwa awamu nne, itaanza na shilingi bilioni 32 kwa 29 kwa miradi ya elimu na afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mimi kwa Serikali fedha hizi Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana zikawa ni reflected kwenye hiki kitabu cha matumizi. Naiamini Serikali yangu lakini wasiwasi wangu Waheshimiwa kama tutapewa hizi fedha awamu hii ya mwezi wa sita na ambazo Mheshimiwa Waziri nikuombe, tumebakisha siku tisa kumaliza mwaka wa fedha, ni matarajio yangu kwamba ya kufanya majumuisho fedha hizi zitakuwa zimeshaenda kwenye halmashauri ili michakato ya manunuzi kupitia force account iweze kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema zile reflected humu Waheshimiwa Wabunge, tukianza mwaka 2018/2019 kama hazipo humu, pamoja na kuwa naiamini Serikali yangu tunaweza tukapigwa changa la macho. Kwa sababu baadaye tutaambiwa haipo katika vitabu. Nawaomba sana muangalie suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, Serikali hapa imesema kuhusu asilimia kumi ya wanawake na vijana na kwa mujibu wa Kamati imependekeza kuwa iwe 4, 4, 2 kwa maana wanawake, vijana na walemavu. Hata hivyo, lazima tukubaliane, halmashauri hazifafani uwezo. Mimi napendekeza hii asilimia kumi ilenge maeneo ambayo ni majiji au manispaa. Kuna halmashauri baada ya Serikali ku- centralize vyanzo vingi hii ten per cent inakuwa kama maigizo unless otherwise tunafanya politics.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tuko serious kabisa tumehamasisha wananchi wajiunge katika vikundi Serikali itusaidie katika baadhi ya maeneo ambako vyanzo viko chini iweze kupeleka asilimia kumi ya vikundi kama ruzuku. Otherwise kama halmashauri kwa vyanzo vya ndani inakusanya shilingi milioni 500 asilimia kumi unazungumzia shilingi milioni 50, hivi ukiwapa vikundi Sh.100,000 na vikundi viko vingi tumewasaidia au tumefanya politics?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, usahuri mimi kwa Serikali kwenye ten percent hii katika baadhi ya maeneo tusifanye unform. Majiji kama Arusha, Dar es Salam, Mwanza na Manispaa unaweza ukasema waende kwa utaratibu huo, lakini kuna maeneo kwa kweli vyanzo ni dhoofu. Kwa hiyo, Serikali iangalie uwezekano wa kupeleka ruzuku ili hamasa tuliyowapa wananchi kwamba wajiunge katika vikundi iwe ni kweli kwa vitendo isiwe tu katika makaratasi ten percent. Ten percent yenyewe imekuwa ngumu kwa sababu hata OC haiendi ipasavyo; halmashauri zinajikuta kwamba zinachukua fedha matokeo yake inakua ten percent katika makaratasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia challenge mbalimbali ambazo Serikali imesema inakabiliana nazo katika masuala ya kuongeza makusanyo. Mheshimiwa Waziri tuna fedha tunapoteza kwenye suala la fuel levy kwa sababu hatujui mpaka leo mafuta kiasi gani yanaingia katika Taifa hili. Ameenda Mheshimiwa Rais pale bandarini, ameenda Waziri Mkuu tena Waziri Mkuu nadhani ameenda hata tatu kuhusiana na suala la flow meter lakini mpaka leo hatufahamu suala la flow meter limefikia wapi. Flow meter yenyewe iliyopo watu wana tamper nayo wakati mwingine wanacheza nayo isipige alamu lakini hata ule mchakato wa kupata flow meter nyingine hatujui umeishia wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Waziri anataka pesa, kuna pesa zingine ziko nje nje lakini tutaweza kuzipata kama tutadhibiti baadhi ya mianya moja wapo likiwa ni suala zima la kudhibiti tuweze kujua idadi ya mafuta yanayoingia katika taifa letu. Otherwise tutawakamua Wamachinga, tutawapa sijui hiyo TIN namba that’s is very peanut, kuna pesa mamilioni kwa mabilioni katika suala zima la mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la ETS, yaani I am very layman linapokuja suala la mambo ya uchumi lakini na u-layman wangu nashindwa kuelewa hivi sisi kweli Mheshimiwa Mpango katika zama hizi za digital tunashindwa kuwa na control mechanism ya sisi kama sisi ili kuokoa yale mabilioni badala ya kwenda kwenye kampuni tu bora kampuni yakabaki hapa yakatusaidia na tumesomesha vijana. Nadhani Mheshimiwa Waziri hili jambo kama Serikali mnatakiwa mlitafakari mara mbili. Hatuwezi tukawa tunahangaika kwamba hatuna vyanzo lakini kuna pesa tunazipoteza tu. Naamini katika mifumo ya kisasa Serikali ina uwezo kabisa wa kujua na ku-cotrol uzalishaji uwe wa maji, soda au wa vinywaji vyovyote hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la Mheshimiwa Waziri kurejeshewa mamlaka ya kusamehe, kuna watu wengine hapa tunapata miradi ambayo ni misaada kutoka kwa wafadhili marafiki, kutoka kwa NGO’s na Balozi mbalimbali, niombe sehemu ile ya msamaha Mheshimiwa Waziri hebu iwe extended iende mpaka kwenye miradi ya namna hii ambayo tunaipata katika kuangaika kwa ajili ya wananchi wetu. Mimi nina mradi pale Ubalozi wa Japan unatujengea theater ya kisasa, Halmashauri imelazimika kulipa zaidi ya shilingi milioni 30 kama sehemu ya VAT. Niombe pamoja na mipango hii ambayo umeileta hebu huo msamaha tukupe nguvu uweze kusamehe hata misamaha ambayo sisi tumehangaika kwa marafiki zetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ukurasa 59 wa hotuba na Waheshimiwa Wabunge naomba mnisikilize sana, amekuja hapa na hizi HS Codes kwa ajili ya makaratasi ya kuzalishia madaftari na vitabu. Mheshimiwa Waziri hizi HS Codes, unless ama mmejua au hamjajua, Waheshimiwa Wabunge niwafahamishe kilichosamehewa kwenye daftari kwa mujibu wa hizi HS Codes ni cover, hili hapa, kama ni kitabu ni cover. Hizi HS Codes Mheshimiwa Waziri ni za makaratasi magumu. Kama kweli tunataka tusamehe kwa ajili ya uzalishaji wa madaftari, muende mkazi-review hizi HS Codes. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge tujitahidi kujifahamisha na kuhabarishana. Kwa sababu ukienda tu ukiona hizi HS Codes hapa tumepiga makofi; lakini sisi kama Wabunge wa Bunge Tukufu tupigie makofi hii cover? Katika daftari cover na hiki cha ndani kipi kingi? Kina Mwalimu Mulugo wanajua mambo ya madaftari. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri muende mka-review kitu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za LGDG, mimi naendelea kuomba mmesema kuna miradi mikakati; siyo kila halmashauri inaweza kuwa na mradi mkakati, hapa ndiyo sisi pakutokea kama Wabunge na kama halmashauri. Kwa hiyo, mimi naomba tusijifiche kwenye kichaka cha miradi mikakati, fedha hizi zinazokwenda kwenye maendeleo na ku-stimulate wananchi kuchangia na kuhamasisha na kufyatua matofali kwa kutumia nguvu zao Serikali iendelee kuzitenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, sports betting, hatuwezi kukwepa duniani sasa hivi hicho ni chanzo kikubwa sana cha mapato. Sheria imetoka asilimia 6 mpaka 10 ya mauzo ghafi, napendekeza na kushauri ili kuleta fairness kwa mchezaji na mchezeshaji na ili kuvutia wachezaji wengi wasikwepe waendee kwenye online sports betting, Serikali iweze kuangalia kusudi tupanue wigo wa mapato. Kwa sababu ukiweka mazingira ambayo yanavutia kwa mchezaji na mchezeshaji maana yake tutapata fedha nyingi lakini sehemu ya fedha tutenge iende kwenye michezo. Kama ni kugharamia timu ya taifa, timu za riadha , kuboresha viwanja kwa sababu michezo nayo ni sehemu ya kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa ujumla, Naibu Waziri na Watendaji wote kwa maandalizi ya Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwanza kwa pongezi. Nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watoto wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nawapongeza watoto? Wakati Mheshimiwa Rais alipoingia madarakani alikuwa anapenda kutueleza Watanzania kwamba iko siku mtanielewa. Msemo huo aliupenda kuusema mara kwa mara, “iko siku mtanielewa.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza watoto kwa sababu gani? kati ya watu wa kwanza kumwelewa Mheshimiwa Rais, walikuwa ni watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Mheshimiwa Rais alipoingia alisisitiza sana umuhimu wa kulipa kodi lakini pia kudai risiti. Sisi Watanzania hatukuwa na huo utamaduni. Ukinunua bidhaa, ilikuwa ukipewa risiti unaona kama usumbufu, unamwambia mwenye duka, kaa na makaratasi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto walimwelewa na hapa nitatoa mfano. Mimi nikiwa na wanangu, nimeenda Petrol Station, nikijaza mafuta nikitaka kuondoka, wanangu wananiambia Baba risiti, risiti! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba watoto wa Taifa hili walikuwa wa kwanza kumwelewa Mheshimiwa Rais, lakini baadaye with time Watanzania tumeendelea kumwelewa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema sisi tufanye kazi. Watanzania wanachotaka ni kazi na mambo yanayoonekana, maana wanasema acha kupiga mayowe, wacha wayaone wenyewe na Watanzania wanayaona wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huu, nina hii karatasi. Nimesoma Mpango kwa utulivu na ninapenda pia kumpongeza Mheshimiwa Spika na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kutuletea hivi vitendea kazi. Maana yake hapa nabofya tu, nasukuma tu maandishi yanashuka yanapanda, nachangia kwa wepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachotaka nikiseme katika sura ya 4 ya Mpango ambapo umeeleza mipango ambayo tutaielekeza kwa nguvu kubwa kuifanyia kazi. Yapo mambo mengi, nami nataka niseme jambo moja; namwomba Mheshimiwa Waziri kama kuna Msaidizi katika Bunge aje achukue hii document ambayo inaeleza small and medium scale sugar plant. Hii nyaraka kila mwaka nimekuwa nikichangia kwa maandishi na kuiwasilisha kwenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tunapozungumza hapa, India sasa hivi wanazalisha sukari tani milioni 35, wamewapita Brazil ambao walikuwa wanazalisha tani milioni 32. Ukitaja mahitaji ya sukari kwa mwaka katika dunia hii, yanaingiza kiasi cha dola bilioni 22 za Kimarekani. Maana yake kwanza uhitaji wa sukari ni mkubwa, lakini hata sisi katika Taifa letu sukari ni kitu ambacho uhitaji wake ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzetu Brazil wamefanikiwa vipi? Pamoja na Miradi kama hii ya Mkulazi ambayo ni Miradi mikubwa, bado Mheshimiwa Waziri tunaweza tukawekeza katika viwanda vidogo vidogo vya kuzalisha sukari ambavyo kwanza moja, havihitaji mtaji mkubwa, lakini pili, havichukui muda mrefu kuweza kujengwa na tatu, vinaweza vikawa viwanda shirikishi. Viwanda shirikishi kwa namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano. Tuna maeneo katika nchi yetu yana mabonde ambayo tungeweza kuzalisha sukari. Kwa mfano, maeneo potential, kuna Bagamoyo, kuna hiyo Mkulazi ambayo tunaenda nayo, kuna Lwipa Ifakara, Rufiji Pwani, Mkongo Mara na Kasulu Kigoma, kote huku tunaweza tukajihakikishia kuzalisha sukari ambayo itatosheleza Taifa letu, lakini kwa sababu pia sukari inahitajika kwa wingi katika dunia tukapata fedha za Kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kufupisha tu katika hili, naomba nimkabidhi Mheshimiwa Waziri hii nyaraka kwa sababu nimeichangia kwa maandishi kwa muda wa miaka mitatu, huu ni mwaka wa nne, pengine ikija kwa maandishi haipati. Sasa niikabidhi kabisa mkononi mwake nikimaliza hapa nitaenda kumpelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo ambalo msisitizo wake kwanza tuzalishe sukari ya kutosha, tujitosheleze kwenye soko la ndani lakini tuuze nje kwa sababu itatuletea fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ningependa kuzungumza kuhusu utalii. Napongeza kuhusu ununuzi wa ndege ambao unaendelea. Watu wengi, nikienda kule kwetu Bumilayinga, Matanana, Ndolezi kuna watu wanapita wanawaambia wananchi wewe utapanda lini hiyo ndege? Nawaelimisha wananchi kwamba kwa uwepo wa ndege, maana yake tunarahisisha suala zima la utalii ambapo tutapata fedha za kigeni, kesho tutapata umeme, maji, Vituo vya Afya na dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina ushauri katika ndege. La kwanza, mimi siyo mtaalam wa mambo hayo, lakini ukweli usemwe na tuambizane humu ndani. Kumekuwa na delays kwenye Shirika la Ndege zisizoelezeka. Mbaya zaidi handling yake imekuwa siyo nzuri. Siku moja mimi nasafiri kuja Dodoma, nimekutana na mzee pale Airport Dar es Salaam anaenda Mwanza, ndege yake ilikuwa ya saa kumi 12.00, anafika kwenye ku-check in, ndipo anapoambiwa bwana ndege itakuwa ina-delay mpaka saa 3.00.

Mheshimiwa Mwenyekiti, worse enough mtu huyu hata hakuna namna ya kumjali. Utaratibu wa Mashirika mengi ya Ndege unaweza ukampa voucher hata ya thamani ya shilingi 10,000/= kwamba bwana nenda pale Canteen kwamba nenda upate japo kikombe cha kahawa. Kwa hiyo, nawaomba tusijisahau kwa sababu demand iko kubwa. Tuwajali abiria wetu na kadri tunavyoweza hizi delays inawezekana ni mambo technical, lakini tujitahidi kuzipunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nashauri, baada ya kuwa na hizi ndege, sasa tu-focus kwenye ndege za kubeba capacity ya abiria 14 labda mpaka 32. Hizi sasa zitatusaidia kuwa-fetch abiria kwa mfano katika utalii. Kama tunavyosema, nia ni kupanua wigo katika utalii. Inaweza kubeba abiria kutoka Dar es Salaam ikawamwaga Mikumi, ikaenda ikawamwaga Ruaha National Park, ikaenda ikawamwaga Selou, Manyara na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ilivyo, kutoka Dar es Salaam kwenda Ruaha kwa mfano, gharama yake kwa hizi ndege za private tulizonazo, unaweza kukuta ni sawa sawa na kutoka Dar es Salaam kwenda Johanesburg au kwenda Dubai. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali ione uwezekano wa kupata ndege ndogo ambazo zitakuwa zina-shuttle hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia mazingira ya wezeshi katika suala zima la Uwekezaji. TIC na Waziri katika Uwekezaji wanafanya kazi nzuri, lakini jamani lazima tuseme ukweli, tutoke kwenye digit tatu. Sasa hivi tuko 141, hebu twende tukawe hata 99. Sasa kuwa hivyo maana yake nini? Tumeona miundombinu inajengwa, umeme shughuli inafanyika, barabara zinajengwa, lakini Mheshimiwa Waziri bado kuna mambo yanatakiwa yaendelee kufanyika katika kupunguza ule urasimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kuna blueprint, operational itakuwa lini? Hii blue print iwe operational. Pamoja na hayo, napenda kusema baadhi ya maeneo naomba yatazamwe kwa macho mawili. Kwa mfano, mimi natoka Mafinga, nimeona Mheshimiwa Waziri hapa kuna zile Kanda maalum za Kiuwekezaji, nashauri tuwe na Kanda maalum ya Kiuwekezaji kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini maalum kwa ajili ya mazao ya misitu. Huu nao ni uchumi ambao ni mkubwa sana, (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nafahamu suala la umeme ni huduma, lakini ni biashara, lakini kuna maeneo yatizamwe kwamacho mawili. Katika Wilaya Mufindi tuna-consume Megawatt 14, kuna maeneo Mkoa una-consume Megawatt 4. Sasa maeneo kama sisi ambao demand ni kubwa, tuna Viwanda vya Mbao, tunaomba tutazamwe kwa sababu tutazalisha, tutalipa bili kubwa ambazo zitasaidia TANESCO na REA kupanua umeme katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii pale Matanana, Mwongozo Mafinga na Ifingo watu wana viwanda, wana mashine lakini umeme haujafika. Kwa hiyo, naomba hata kama tunapeleka katika nchi nzima, yale maeneo ambayo kuna uzalishaji, tuyatizame kwa macho mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niseme kuhusu TARURA. Tunajenga kweli barabara za kuunganisha Mikoa, lakini kwa mfano, mimi pale Mafinga, Mtula tuna scheme ya umwagiliaji, tutafikishaje bidhaa sokoni ikiwa TARURA wanapewa fedha ndogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naendelea kusisitiza, kwa sababu TARURA ndiyo inatuhudumia kwa kiwango kikubwa, natoa ushauri kwa Serikali, tutafute chanzo maalum ambacho kitaiwezesha TARURA ili iweze kuzihudumia barabara ambazo ndiyo backbone ya nchi kwa maana ya kwamba, mbali ya kubeba mazao, lakini pia zinabeba bidhaa, wakati mwingine zinabeba mbolea kuwafikishia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumejenga Kituo cha Afya, Ihongole, lakini barabara haipitiki kwa mwaka mzima. Sisi Mafinga tunahitaji shilingi bilioni 4.8 kwa mwaka, tunapata shilingi bilioni moja, tunajua ni kwa sababu ya ukomo wa Bajeti. Kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali, tuone pia TARURA tutaijengea vipi uwezo ili kusudi tuimarishe barabara zetu kwa ajili ya kusafirisha mazao, bidhaa na mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Timu ya Simba Sports Club kwa ku-qualify kuingia robo fainali ya Club Bingwa Afrika, lakini pia niwapongeze waliokuja na lile wazo la visit Tanzania kwasababu pia inasaidia katika kutangaza utalii. Niwashukuru pia wenzetu wa Yanga sasa hivi wanatushangilia kwasababu pia wao mwakani, kwa namna moja au nyingine Tanzania itapata nafasi nne, kwa hiyo nao watapata nafasi ya kushiriki. Kwa hiyo nawashukuru sana; lakini pia nawatahadharisha Simba, kwamba hawa hawa wanaotushangilia leo kesho wanaweza wakatuzomea, kwa hiyo tuwe carefully.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi, tumeona katika Taifa letu wapo watu ambao; jana Mheshimiwa Kibajaji alisema vizuri sana, Mheshimiwa Msukuma alipendekeza; kwamba ikimpendeza mamlaka Mheshimiwa Lusinde apate doctorate ya heshima. Mimi kwa binafsi yangu na kwa mamlaka yangu mimi mwenyewe binafsi tayari Mheshimiwa Kibajaji huwa ninamwita professor, nilishampa professorial kwasababu zangu binafsi na pia kwasababu katika uwanda wa siasa na ujengaji wa hoja kwakweli yupo vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupata msiba wa mpendwa wetu Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli nilikuwa naongea na Mheshimiwa Kibajaji, kwamba tuombe sana Mungu; kibajaji akaniambia maana; yeye huniita mimi tena professor sijui kwa nini, kwasabau zake binafsi. Lakini akasema utakuwa unakosea yako ya Mungu halafu yako ambayo sisi lazima tuwajibike kwamba hatuwezi kufanya mambo ya kijinga kijinga alafu tunasema tuombe Mungu, hapana. Yapo ambayo tunatakiwa tuombe Mungu, na yapo ambayo sisi kama binadamu tuna sehemu yetu ya kuyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tulimuona juzi kwenye ziara kule kwenye mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere, lakini pia kumpongeza Mheshimiwa Rais Amini Jeshi Mkuu tulimuona Uganda akishuhudia kutia saini kwa makubaliano yale na kuanza kutekeleza kwa bomba la mafuta. Yote yale ni katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na kwamba kazi iendelee. Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake amezungumza mambo mengi lakini moja wapo ni jambo la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali langu namba 16 kwenye Bunge lililopita niliuliza kuhusu lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara za lami katika Mji wa Mafinga. Ili kuendeleza sekta nzima ya uchumi wa viwanda ili kupiga hatua na kukuza ajira zaidi ya milioni saba ambazo tumeahidi katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi Ukurasa wa 29 moja wapo ya nyenzo muhimu ni ujenzi wa miundombinu hususan ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninatoka Mafinga, mara zote nimesema, na Mheshimiwa Pacha wangu David Mwakiposa Kihenzile amesema juzi, kwamba bila ujenzi wa miundombinu ya barabara hasa maeneo ambayo yanauzalishaji mkubwa kiuchumi hatua yetu ya kupiga kasi ya uchumi itakuwa ndogo. Kwa hivyo mimi ninapendekeza na kuishauri Serikali, tutakapokuja kujadili suala la TARURA tuone namna ambavyo tutaiwezesha TARURA ili kusudi tuweze kuweka misingi imara katika ujenzi wa miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninapozungumza kuna watu wanasema ukiongeza labda shilingi 50 kwenye lita moja ya mafuta utaongeza gharama za usafiri. Gharama za usafiri haziongezeki kutokana na gharama za mafuta isipokuwa kutokana na barabara mbovu ambazo hazipitiki mwaka mzima. Ikiwa tuna barabara zinapitika mwaka mzima hata gharama za nauli haziwezi kuwa kubwa na wala gharama za usafirishaji haziwezi kuwa kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kutoka Mafinga kwenda Sawala umbali wa kilometa kama 40 nauli kipindi cha mvua inafika mpaka elfu 10,000 - 15,000, lakini umbali huo huo kutoka Dodoma kwenda Iringa ambao ni umbali wa kilometa zaidi ya 260 nauli haizidi elfu 10,000. Kwahiyo gharama za usafirishaji zinaendana sana na hali yetu ya miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kutoka Mafinga kwenda Mtwango kwenda Ifupila baadhi ya magari yamepaki hayawezi kwenda kwasababu mbali ya ubovu wa barabara lakini pia inachangia gharama kubwa za matengenezo ya magari. Kwa hiyo mimi niombe sana, pamoja na kuutazama Mji wa Mafinga tuangalie Barabara ya Mafinga kwenda Mgololo, Barabara ya Mtwango kwenda Nyororo kwasababu inabeba uchumi mkubwa wa Wilaya ya Mfindi Mkoa wa Iringa na nyanda za juu kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema haya si kwamba tunazungumza kama luxuriously, hapana, tunasema hivi ili kusudi ku-bust kasi ya ukuaji wa uchumi. Leo hii ukienda Barabara ya Mafinga - Mgololo unakuta semi- trailer 10 zimepaki kwa muda wa wiki, haziwezi ku-move; maana yake ni kwamba tuna slow speed ya ukuaji wa uchumi na hata zile ajira milioni nane tulizozisema katika Ilani hatuwezi kuzi-realize kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilio changu kikubwa mimi leo ni kuhusu barabara. Kama tutaweza kuwekeza nguvu katika ujenzi wa barabara hususan maeneo hayo ambayo yana uchumi mkubwa maana yake tuta-speedup ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili napenda kusema, dunia leo hii ndugu zangu inafanya kazi 24/7 saa 24 siku saba. Jana nilikuwa na swali lini Serikali itaruhusu baadhi ya miji hasa ambayo iko kando ya barabara kuu kama vile Mlandizi, Chalinze, Morogoro, Mikumi, Ruaha Mbuyuni, Ilula, Ifunda, Mafinga, Makambako watu hawa wajiachie wafanye biashara saa 24, ajira ziko rasmi za Serikali lakini ziko za vijana kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi Mafinga pale inapofika saa nne Polisi wanapofika na kutaka vijana wafunge biashara wakati vijana hawa mchana kutwa walikuwa msituni wakiitafuta shilingi, tutakuza vipi uchumi? Kwa hiyo, nashawishi Bunge hili na Serikali tuangalie baadhi ya maeneo ya miji kama hiyo niliyoitaja na mingine miji kama Korogwe na Mombo kwa shemeji zangu, watu wajiachie wafanye biashara. Duniani kote kazi ya dola ni ulinzi na usalama, wao wa-guarantee vijana wajiachie wafanye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini masuala ya saa tano kuanza kukimbizana na vijana wafunge biashara zao ambao mchana kubwa walikuwa wanatafuta kipato chao, mimi kwangu naona siyo sahihi na hili kwa kweli siwezi kukubaliana nalo. Ndiyo maana nikasema kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali ziletwe hapa sheria tuweze kuwezesha maana kazi ya Serikali ni ku-facilitate.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake amezungumzia kuhusu sekta ya michezo na amesema contribution ya sekta ya michezo kwenye pato la Taifa ni 3% tu kati ya 2013 mpaka 2019. Pia ameeleza kwamba sekta hii inaajiri vijana wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina mambo mawili; kwanza ili tunufaike na Media Entertainment and Sports Industry kama siku zote ambavyo huwa nasema hatuna namna lazima tukiangalie kwa macho mawili Chuo cha Michezo cha Mallya na Taasisi ya Sanaa ya Bagamoyo - TaSUBa, ili kusudi tuweze kuwezesha vijana na nyenzo mbalimbali za masuala haya ya michezo, burudani na utamaduni.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili lazima tuangalie pia viwanja. Sasa hivi unakuta kwamba kiwanja kama cha Jamhuri kama tuna tamasha labda la Fiesta sijui Mziki Mnene la Wasafi au Mtikisiko unakuta matamasha haya yanafanyika katika viwanja vya mpira. Ni ushauri wangu kwa Serikali tujenge uwanja wa Standard Olympic ambao utakuwa kama One Stop Center; viwanja vya kuogelea, table tennis na kila aina ya michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia lazima tufike wakati tuhamasishe wawekezaji wawekeze katika majumba makubwa na viwanja maalum ambavyo ni kwa ajili ya masuala ya burudani. Kwa sababu as it is leo utakuta uwanja pale wa Taifa kuna tamasha iwe la muziki wa injili, iwe la muziki wa kimataifa yote yanafanyikia pale. Kwa hiyo, ama kupitia wawekezaji ama namna yoyote ambayo Serikali itaona inafaa kama tunataka tunufaike na sekta ya michezo na burudani lazima tuangalie Chuo cha Michezo cha Mallya na Taasisi ya Sanaa ya Bagamoyo lakini lazima tuwekeze katika miundombinu wezeshi ya kuwezesha vijana hawa kuwa na maeneo ya kufanyia hizi kazi zao. Michezo sanaa na burudani inaajiri vijana katika ajira isiyo rasmi siyo chini ya milioni 2 na huu ukuaji wa teknolojia ya sayansi na teknolojia kwa maana ya matumizi ya internet, inaleta sana ukuaji wa uchumi katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja nikisisitiza tufanye kazi saa 24 siku saba, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. CASATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi na ninapenda kuchukuwa nafasi hii, kwanza kuwa shukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake, lakini pia shukrani za pekee kwa Mamlaka ya Mawasiliano kwa maana ya TCRA ambapo miaka miwili iliyopita walitusaidia watu wa Mafinga katika Shule ya Msingi Mchanganyiko ya Makalala hii ni shule ya watoto wenye mahitaji maalumu siku hizi tunaita watoto wenye uono hafifu zamani tulikuwa naita watoto vipofu, wale wanamahitaji maalumu kwa maana vifaa wanavyotumia katika kujifundishia na kujifunzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo TCRA walitusaidia lakini pia walitusaidia pale shule ya Sekondari Luganga kuwapa vifaa ili kuwawezesha wanafunzi kupata masomo katika namna ambayo kidogo inawepesi kwa hiyo, napenda kuwashukuru sana kwa ushirikiano huo na kwa kazi nzuri ambayo wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na shukrani hizo ninayo maombi machache na mchango mdogo kwa wizara na kwa Serikali kwa ujumla. Asubuhi nilikuwa nina swali kwa Wizara ya Nishati kuhusu masuala ya umeme na sehemu ya majibu ya Mheshimiwa Waziri akijibu swali lake, alikiri kwamba Mji wa Mafinga unakuwa kwa kasi na kunaviwanda vikubwa 80, maana yake ni kwamba huu ni mji wenye mchango mkubwa sana katika uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili Mafinga na Wilaya ya Mufindi kwa ujumla kama alivyosema pacha wangu David Kihenzile iendelee kuwa na mchango mkubwa na kama alivyosema Waheshimiwa wengine katika michango yao masuala haya ya matumizi ya simu yanaumuhimu wake. Kwa hiyo, niiombe Serikali kuna maeneo kwa mfano; Kijiji cha Mtula, Itimbo, Buliainga, Kisada, Ulole, na Maduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivi viko umbali wa kama kilometa zisizozidi tano kutoka katikati wa mji wa Mafinga, lakini mawasiliano yake hayana huhakika. Sasa kama nilivyosema kama ni huu mji wenye viwanja vikubwa 80 maana yake kwanza kwa kukosa mawasiliano inachelewesha mchango wa hawa watu katika ukuwaji wa uchumi wa Taifa na wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namba mbili pia inacheleweza mapato ya Serikali kwa sababu wangekuwa na mawasiliano inamaana kwamba wangetumia simu wangenunua data, wangenunua muda wa maongezi lakini pia wangefanya miamala ya fedha kwa hiyo katika mzunguko mzima ule Serikali ingepata kitu ambacho inastahili kupitia kodi na tozo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana kwa Serikali kwenye yale maeneo ambayo yanashughuli kubwa za kiuchumi ni kweli hii ni huduma lakini pia ni biashara. Sasa unapowekeza lazima pia kama ni huduma maana yake kila mmoja itabidi imfikie ile huduma, lakini ukilingalia kwa jicho la kibiashara elekeza nguvu maeneo ambapo itakupa faida kwa haraka ili uweze kuwapelekea huduma wale ambao kwao mzunguko ni mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwangu na hususani na watu wa Mafinga na Mufundi kwa ujumla kutokana na uchumi wetu kutokana na mazao ya misitu na bidii namna watu wanavyofanya kazi, naishauri Serikali sana itupie jicho kule wanaweza wakawekeza kule shilingi milioni 10 ikakupatia wewe milioni 100 ambayo ikaweza kupeleka huduma maeneo mengine. Kwa hiyo, nashauri namna hii ya kupeleka hizi huduma uziangalie pia katika jicho la kibiashara, kwamba unaweza ukanicheleweshea A ukamuwahishia B ili kusudi kesho uweze kumhudumia C na D na F kwa hiyo naomba sana hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma sana ripoti ya mara kadhaa PWC inaitwa Entertainment and Media Outlook 2018/2022 yaani African Perspective hawa mabwana wameelezea kwa matumizi ya internet kama Wabunge wengine walivyosema siyo tu katika suala nzima Media and Entertainment Industry, lakini pia katika mchango wake wa uchumi katika mataifa mbalimbali kwa mfano; mchana watu wengi wamesema sisi hapa Tanzania kweli tunanufaika na matumizi ya data na uwelewa umekuwa mkubwa tumeona juzi TCRA wametupa workshop na imetusaidia sana kupanua wigo wa mawasiliano na ufahamu wa suala nzima la internet katika maisha yetu ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe wito kwa Mheshimiwa Waziri na Wizara yako kwa ujumla na vyombo vyake Mfuko wa Mawasiliano na TCRA najua inawezekana huwa mna-platform, lakini niombe muwe na platform za watu ambao ni wasanii tuseme watu wa entertainment ili waweze kuwaambia ni changamoto gani ambazo wanakutana nazo inapokuja suala nzima la suala la matumizi mawasiliano katika ujumla wake. Kwa sababu tunaweza tukadhani kwamba tume exhaust hii potential lakini kumbe bado kwa sababu sisi pengine tumejifungia tuko na makaratasi na na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, semina ya juzi ya TCRA sisi wengine imetufungua sana kwa mfano mimi nilikua najua kwamba gharama za simu katika Tanzania ni kubwa sana, lakini kutokana na Takwimu ambazo tumepewa kwenye ile semina nimebaina kwamba kumbe sisi katika Afrika Mashariki na katika SADC sisi ndiyo the cheapest. Sasa unaweza ukawa unatengeneza manunguniko na lawama kutoka kwa wananchi au kwa wadau kumbe simple because hawako informed. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, kutana na jamii ya Media and Entertainment Industry, fahamu changamoto wanazokutana nazo, fahamu na wenyewe fursa gani wameziona katika jicho la Media and Entertainment Industry, bila shaka kwa pamoja mnaweza kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini usiishie hapo tu ningeomba katika hiyo platform kadri itakavyo kupendeza washirikishe pia na watu wa izara ya habari na utamaduni kwa sababu wao pia wanawasimamia wasanii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano leo hii mtu akitengeneza filamu yake inatakiwa ikaguliwe na bodi ya filamu, lakini hiyo bodi ya filamu ofisi yao ipo Dar es Salaam tu. Hili jambo nimelisema sana TCRA nadhani wapo level ya kanda, NEMC wapo level ya kanda, lakini kwanini bodi ya filamu, BASATA na COSOTA wao wakae tu pale Dar es Salaam na siku moja nilisema hapa. Msanii ametoka Mafiga Bumilahinga au ametoka Tandahimba au ametoka Kigoma, kwanza ameingia gharama au Shinyanga kwa dada yangu Lucy, ameingia gharama za kusafiri, anaingia gharama za malazi anafika katika zile ofisi anaambiwa bwana printer imearibika. Sasa katika dhama hizi unamwingizia huyu mtu gharama za kile kitu anachokifanya, lakini wakati mwingine unakuwa ume-discourage. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana kuna potion kubwa sana katika suala nzima la Media and Entertainment Industry, Mheshimiwa Waziri kaa na hawa wasanii, kaa pia na wizara inayohusika na hilo jambo kwa pamoja naamini na wataalamu wako walivyokuwa wasikivu kwa jinsi nilivyowaona TCRA juzi mtajuwa tu kuna potential kubwa kiasi gani wapi watu hawa muweze kuwasaidia wapi muweze kuwa-guide. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mtu mwingine alikua analalamika kwamba wakati mwingine sheria zetu yaani haziko ku-facilitate zimejiongoza sana kwenye kudhibiti kuliko ku-facilitate. Kwa hiyo, ukikaa na hawa wadau wataweza kukupa mawazo na kueleza kwamba jamani hapa rekebisheni hili hapa lina-potential hii, hapa sisi kama wasanii tutanufaika moja mbili ta, hapa kama Serikali tutanufaika moja, mbili, tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni siku ya tatu na asubuhi nilisema nimepita pale TANESCO kuna foleni unawakuta hadi watu wazima wamesimama pale, watu hawawezi kununua LUKU online mpaka sasa hivi. Nimeona Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwa maana Waziri wa Nishati ameshaanza kuchukuwa hatua, lakini that one is not enough na nimesema hii mambo ya kuombana excuse kutupa tahadhari na kutuomba radhi kwamba kutakuwa na 1,2,3 kweli haya mamifumo pengine siyo ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwenye wizara yako na TCRA ukishirikiana na vyuo, kampasi zinazohusika na hayo mambo ya IT, DIT, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDOM mnaweza mkawa na mifumo ambayo itakuwa na backup system, kwamba mfumo A ukifa kuna weza ukawepo mfumo wa dharura ambao unaweza kusaidia lile tatizo kwa muda ule ili kusudi kupata suluhisho la kudumu katika tatizo kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa mimi hapa ninajitolea mfano; naomba ku- declare interest, nina hotel Mikumi toka jana tunawasha generator siyo kwamba hatuna fedha ya kununulia Luku, tunayo fedha ya kununulia luku lakini you can’t buy online kweli Waziri amesema twende ofisi ya TANESCO hivi mtu leo hii atoke Mkonze kwa hapa Dodoma kwa mfano aje akasongamane pale TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwanza TANESCO yenyewe inajikosesha mapato ambayo ni Serikali, lakini pili unapararaize shughuli za uzalishaji sisi wenye viwanda 80 Mafinga kama leo viwanda 30 vimekosa kuwa na LUKU toka juzi. Hivi ni ajira kiasi gani umeziathiri, pay as you n kiasi gani umeathiri, SDL kiasi gani, umeathiri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaweza kuona Mheshimiwa Waziri nakuomba sana hii sekta na hii wizara nikwambie kitu yaani wewe ndiyo kila kitu, ukienda kwenye umeme ni wewe, nimesema Media and Entertainment Industry ni wewe, ukienda kwa Mheshimiwa Lukuvi unataka kulipa hizo kodi za ardhi itakuwa ni wewe, ukienda kwenye kulipa mishahara utakuwa ni wewe. Kwa hiyo, ninaomba uiangalie hii wizara na wataalamu wako kwa jicho ambalo ni pana kweli kweli ili kusudi changamoto unazokutana nazo kwenye mambo ya online tuweze kuondokana nayo kwa sababu tunaenda kwenye uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, kwanza tupate mapato lakini pia tu-speed up uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na pole sana nimekusumbua sana kuku-remind kwa sababu ilikuwa nichangie asubuhi na nilifunga safari kutoka Jimboni kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara hii kwa sababu wiki iliyopita alifanya ziara na alifika kwenye Jimbo letu ambako kuna msitu mkubwa wa Sao Hill. Waheshimiwa Wabunge, huu ni msitu mkubwa katika Afrika Mashariki na Kati. Pia nipende kupongeza TANAPA kwa kutoa madawati, naamini na kule Mafinga yatafika. Lakini pia napenda kupongeza uongozi wa shamba la misitu ya Sao Hill kwa jinsi ambavyo tunashirikiana vizuri katika shughuli mbalimbali za kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, sasa nijielekeze kuchangia. Kuna msemo kaa karibu na waridi na wewe uweze kunukia kama waridi. Sasa kule Mafinga bahati mbaya sana na Wilaya ya Mufindi kwa ujumla, tuko karibu na waridi ambao ni msitu wa Sao Hill lakini hatunukii kama waridi, kama alivyosema Mheshimiwa Kigola, tuko kwenye msitu lakini watoto wanakaa chini, sijui ni laana ya namna gani.
Kwanza ningependa kuzungumzia kuhusu vibali. Kuna mgao wa namna tofauti katika kutoa vibali, lakini utoaji wa vibali umegubikwa na ujanja ujanja usiokuwa na mfano. Niseme kabisa mwanzoni, kama sitapata maelezo mazuri wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha nitakusudia kutoa shilingi. Katika suala la vibali, kwanza kabisa kweli msitu huu ni wa Kitaifa lazima unufaishe Watanzania wote, lakini kama nilivyosema, kama unakaa karibu na waridi lazima unukie kama waridi. Msitu huu lazima kwanza uanze kuwanufaisha wale waliozungukwa na msitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi babu yangu alikuwa Sub Chief wakati wa ukoloni. Sisi watu wa Mufindi, watu wa Mafinga tumetoa maeneo, tumepanda miti…
MWENYEKITI: Waheshimiwa naomba utulivu ndani ya ukumbi.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa maeneo, tumepanda miti, lakini pia sisi ndiyo tunaolinda ule msitu. Kwa hiyo, ninaomba Serikali, ninaomba Wizara katika mgawao wa vibali kwenye shamba la msitu wa Sao Hill lazima watu wanaozunguka msitu wapate, lazima wavunaji wadogo wadogo watizamwe, vijiji vitizamwe, makundi maalum hata under privilege kama vile akina mama wajane wapate, vikundi vya walemavu wasioona, walemavu wa ngozi, wasiosikia wapate vibali kupitia jumuiya zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huu namuomba Mheshimiwa Waziri na timu yake tunataka by name and by location tujue watu wa kule wangapi wamepata vibali? Hatutaki kukaa karibu na waridi tusinukie kama waridi. Leo hii tuko karibu na waridi lakini wanaonukia waridi wako Tanga, wako Mwanza wako Zanzibar. Wakati huu Mheshimiwa Waziri hatuwezi kukubaliana hata kidogo kwenye suala la vibali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na suala la vibali ukienda kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, wachimbaji wadogo wanapewa ruzuku na Serikali. Mwaka jana Serikali imewapa ruzuku wachimbaji wadogo kiasi cha bilioni saba point something, mwaka huu wametengewa billion six point something. Je, kwa nini tusiwatengee pia ruzuku wavunaji wadogo ili waweze kununua mashine za kisasa. Kwa sababu zile mashine walizonazo tunazoita ding dong tunazotaka kuzipiga vita uwezo wake ni mdogo kiasi kwamba katika gogo the recovery percentage ni only 25, asilimia 75 inakuwa ni waste product. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ije na utaratibu tutoe ruzuku kwa wavunaji wadogo waweze kununua mashine za kisasa ili kusudi hata wakivuna msitu basi tuweze kupata mazao yenye tija na siyo mabaki mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo la vibali kuna suala la MPM zamani tukiita SPM (Kiwanda cha Karatasi cha Mgololo). Kiwanda cha karatasi kinapewa cubic meter laki mbili kwa mwaka, lakini cha kusikitisha MPM wanauziwa nusu ya bei wavunaji wetu wanauziwa cubic mita moja shiligi 28,000, MPM shilingo 14,000 lakini worse enough hawa MPM wamepewa kiwanda wazalishe karatasi, wanachofanya wanazalisha at a certain stage wanasafirisha raw material inaenda Kenya zinazalishwa karatasi tunaletewa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, hata watu walioajiriwa pale kuna foreigners wako pale, wengine kazi yao wengine ni kuhesabu magogo kazi ambayo hata mtu ambaye ameishia darasa la pili anaweza kuifanya. Ninaomba Mheshimiwa Waziri na AG ningeomba upitie mkataba wa MPM kwa nini wao wanunue nusu bei, halafu watu wetu tununue kwa bei kubwa lakini pia tusinufaike na kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda unakimbia ningependa pia kuzungumzia sekta ya utalii, tunakiri kwamba hii ndiyo sekta ambayo inaingiza mapato ya fedha za kigeni kwa wingi. Je, Tanzania Tourist Board (TTB) ambao wanawajibu wa kufanya promotion wameachwa kama watoto yatima, ukienda leo hii Kenya bajeti ya promotion na advertisement ni zaidi ya dola milioni 85, Uganda hapa ambao tunaona siyo washindani wetu wanatenga milioni nane USD, Rwanda milioni 11, sisi TTB tunaitengea chini ya milioni mbili, je, tutaweza kutangaza? Tunabaki tu kusema sisi ni wa pili kwa vivutio inatusaidia nini kuwa wa pili kama hatunufaiki na tutanufaika vipi kama hatuwekezi ? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tourism Development Levy (TDL) kulingana na sheria Ngorongoro na TANAPA wanatakiwa wawape TTB asilimia tatu kuchangia katika masuala ya promotion, lakini fedha zile zinaenda kwanza Wizarani zinaingia kwenye mambo mengine. Miaka mitatu, minne kabla ya sheria hii TTB walikuwa wanapewa 1.5 na TANAPA 0.5 na Ngorongoro ilitusaidia tukatangaza mpaka kwenye premier league, hivi leo hii tungekuwa tukiitangaza kwenye Leicester City unadhani tungekuwa tumenyanyua utalii kwa kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba tunaposema utalii unachangia tuwekeze pia katika kuhakikisha kwamba tunajitangaza ipasavyo. Haiwezekani leo hii eti tumewatengea TTB wafanye ziara za maonyesho ziara tano unataka uvutie utalii! Haiwezekani hata kidogo tukatoka. Hata suala la vitanda kwamba ni 1.5 US dollar mimi nashauri tu-charge kwa asilimia kwa sababu mtu anayelaza kwa shilingi 30,000 unam-charge 1.5 USD, anayechajisha laki vivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi na kwa haraka kabisa napenda kutumia nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan alipokuja kulihutubia Bunge alieleza sasa nia ya Serikali kuanza kutenga fedha kidogo kidogo kugharamia timu zetu za Taifa na hata timu za wanawake napenda kutoa pongezi sana, lakini pia napenda kutoa pongezi kwa Azam kwa uwekezaji waliouweka ambao kwa kweli unasaidia tu sio sisi kuangalia mpira, lakini pia ni sehemu ya ajira. Ukienda huko kwa wananchi wetu kuna kitu kinaitwa vibanda umiza, unakuta mtu ana banda lake anaonesha mpira, anauza vinywaji, anapata kipato na maisha yanaendelea, kwa hiyo ninawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nitoe wito kwa vilabu wasibweteke tu na uwekezaji huu na wenyewe pia watafuta wadhamini wengine, lakini pia napenda kutoa pongezi wa wachambuzi wote wa michezo hususan zamani tulikuwa tumezoea vipindi vya michezo unasubiri jioni, lakini siku hizi kuna vipindi vya michezo hata katika stesheni za redio kama Wasafi, EFM TBC Fm unapata habari za michezo muda wowote, kwa hiyo nao napenda kuwapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya pongezi hizi watu wengi wamesema kuhusu michezo kweli michezo pamoja na kuwa ni burudani inatuondolea stress na kadhalika lakini kama ambavyo siku zote mimi nimesema michezo ni sehemu ya ajira ni mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, michezo, sanaa na burudani ni kitu kikubwa katika uchumi wa nchi na hasa kwa kuendelea katika uchumi wa kutumia sayansi na teknolojia, digital economy michezo ina nafasi kubwa sana, lakini sasa michezo ili uweze kukupa hiyo tija sasa lazima kuwe na usimamizi bora, nitatoa mfano hapa tarehe 5 Mei, 2017 nilitoa mchango wangu hapa nikasema TFF ambao ni Tanzania Football Federation imegeuka sasa kuwa Tanzania Football fungia fungia kwa sababu ya kufungia fungia yaani jambo dogo tu unamfungia mtu, yawezekana kweli ni kanuni, mimi ninashauri, unajua unapomfungia mtu kama Mwakalebela ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa TFF ile ya Tenga ambayo ndio imejenga msingi wa mpira huu tulionao leo kwa kweli you have to think twice mimi kwa mawazo yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo yawezekana ni kanuni ni taratibu zao lakini wajaribu kuziangalia kuwe na adhabu ambao kidogo ni friendly ambao unaweza kumjengea mtu kurekebika kuliko kumfungia, unamfungia Mwakalebela miaka mitano, huyu mtu ambaye katika football, katika michezo ni mtu ambaye amekuwa na mchango mkubwa sana kwa hiyo ndio maana kunakuwa na lawama nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Leo hii sisi katika FIFA ranking Tanzania tupo wa 137 hata Libya ambao wako kwenye kupigana wako wa 119 sasa hata Mama alipokuja hapa kwenye Bunge alisema tumechoka na mimi nasema tumechoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa sababu tumechoka mimi ninashauri unawezekana ukawa ushauri sio mzuri na haitakuwa mara ya kwanza, sisi kwanza timu yetu ya Taifa kwanza ipumzike, tujipange, tujipange hata miaka mitano. Ghana wamefanya hivyo, Cameroon wamefanya hivyo, Comoro wamefanya hivyo, wamejipanga, leo hii tunajua Cameroon wako wapi, Ghana wako wapi, hata Comoro ambao vilabu vyao vilikuwa vikija hapa tunawafunga 12 kwa sifuri sasa hivi wameshatuacha katika list ya Afrika, yaani kama ile ambayo easy way of doing business sisi wa 141 katika East Africa Uganda ya 84; Kenya ya 102; Sudan ya 123; kwa kwa maana ya ile CECAFA Rwanda ya 129 yaani tuliowazidi sisi ni Burundi tu kwenye mazingira ya kufanya biashara pia tuliowazidi sisi ni Burundi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unaweza ukaangalia hivi vitu ni kama vile sijui kama vinashabihiana, sasa ukienda katika mpira wa Uingereza, Spain na Ujerumani wale wote ukienda Man U wawekezaji wametoka Amerika ukienda Chelsea - Abramovich ametoka Russia, ukienda Arsenal kwa nini wale watu wanakuja? Kwa sababu kuna mazingira bora ya kuwekeza katika mpira. Man City wanatoka Arabuni Leicester City wanatoka Singapore kwa sababu gani? Kwa sababu kuna mazingira bora ya nini ya kuwekeza, sasa mazingira bora yanatoka wapi, yanatoka kuanzia kwenye usimamizi wa watu wenye mpira ambao ni TFF.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi huwa ninasema maisha ni ujanja, sio ujanja ujanja, lakini TFF inavyoendeshwa ni full ujanja ujanja ndio maana tunakosa nini uwekezaji, kweli leo hii wamekuja hao wa Azam, Azam wamewekeza pia nao kwa sababu watapata faida kwa kuuza ving’amuzi na kadhalika. Lakini kama tunataka serious watu wawafuate Azam ni lazima kwakweli mazingira ya uwekezaji kama yale tunayosema kwenye biashara katika mpira wetu yaboreshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa watu wanazungumzia kujenga viwanja Serikali hii bajeti iliyokuja hapa bilioni 54, uwanja tu kama wa Abuja National Stadium bilioni 800 ambao unaweza kufanya mambo ya mpira na mambo hayo aliyokuwa anasema Mheshimiwa Babu Tale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hiyo hapo Serikali haiwezi, Serikali iwe facilitator na vyombo vyake vya michezo, wawekezaji waje wawekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitapenda kuzungumzia kuhusu COSOTA, BASATA na Bodi ya Filamu; hii mimi nimelisema miaka minne tunawashukuru wameviunganisha wamesema One Stop Centre. Ukienda EWURA ukienda NEMC hivi regulator authority unazikuta hadi ngazi ya kanda, ninashauri Serikali, ione uwezekano tuache kumsumbua msanii kutoka Kongwa, kutoka Itimbo Mafinga kutoka Tandahimba kuja Dar es Salaam akae siku tatu gharama za usafiri na kadhalika, haya siyo mazingira bora ya kuwawezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninakuomba Mheshimiwa Waziri jaribu kama utaona ni gharama tumia Maafisa Utamaduni uwe japo na ngazi ya Kanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakuja Shirika la Magazeti ya Serikali; kama ambavyo tunasema tuwe na national career kwa maana lazima kama Taifa uwe na shirika la Ndege kama Taifa uwe na Shirika la Utangazaji, Shirika la Magazeti ya Serikali ni chombo muhimu sana katika dunia ya sasa.

Mheshimiwa Spika, magazeti yale ya Daily News, Habari Leo ndiyo chanzo kikuu ukitaka kusema cha taarifa za Serikali, lakini TSN mimi nimekaa newsroom, nimefanya kazi ya uandishi wa habari kwa miaka nane hali ya TSN siyo nzuri, wameomba bilioni 16 wanunue mtambo ambao utachapisha siyo magazeti yao tu, lakini utafanya uchapishaji mpaka kutoka watu wa Congo ita-generate income leo hii ukibeba gazeti la Daily News tunasema washindani, hawawezi kwasababu watu hawa hawana nguvu hiyo, hatujawawekezea. Sasa kama tumeweza kuweka nguvu kwenye Shirika la Ndege la Serikali, TBC mmeona kazi waliyofanya wakati wa mazishi ya Mheshimiwa JPM ni kwa sababu wamewezeshwa.

Mheshimiwa Spika, Leo hii TBC wamepewa shilingi bilioni tano; ninashauri tuiangalie sana Shirika la Magazeti ya Serikali ili liweze kushindana na akina The Guardian, liweze kushindana na akina Mwananchi, kwa sababu hiki ndiyo kisemeo cha Serikali. Tufumbe macho tuiwezeshe TSN ili kusudi hili gazeti la Daily News, diplomatic community kabla hajasoma chombo chochote cha habari anaanza kusoma Daily News, sasa Daily News haina uwezo tena wa kujichapisha kushindana na The Guardian matokeo yake hata mtangazaji anayepeleka matangazo hawezi kupeleka kwasababu halina mvuto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hawa watu TSN wanaidai Serikali nadhani almost shilingi bilioni 11 lakini na wao wanadaiwa na suppliers mbalimbali pesa nyingi tu. Kwa hiyo, mimi naomba Serikali na baadaye naweza nikashika shilingi inakuja na mkakati gani kuisaidia kitu ambacho ndiyo kisemeo cha Serikali, ili wasaidiane na TBC, wasaidiane na TBC Radio wasaidiane na vyombo vingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuhitimisha tu, mimi narudia tena, ili tuvutie wawekezaji katika sekta ya michezo, burudani na sanaa ni lazima tugeuke kuwa facilitators, wala tusiwaze sisi kama Serikali tutawekeza leo hii kama nilivyosema tulienda nakushukuru sana katika miaka mitano ulijitahidi sana Bunge Sports Club imeshiriki kwenye michezo ya Mabunge ya Afrika Mashariki tumeenda pale Burundi, tumekuta unaenda asubuhi uwanja wa mazoezi, kuna timu ina wachezaji 31 ni magoli kipa tu wana-train ugolikipa tu, na leo hii tunaona kuanzia Namungo kule golikipa ni Mrundi yule wako makipa wengi tu ni Warundi.

Mheshimiwa Spika, leo hii ligi yetu ina wachezaji kutoka Burundi wako wengi tu. Tumeenda pale Kampala watu wamewekeza sasa ili ukisimamia bora nitakwambia kwa kumalizia kitu kidogo tu, hata waamuzi sisi hapa hatupeleki waamuzi kwenye michezo, hawapati nafasi kwa sababu usimamizi siyo mzuri nitakwambia katika CHAN hii ambayo tulienda kushiriki hii katika waamuzi 47, 19 wa kati, wasaidizi walikuwa 20 na wale wa VAR (Video Assistant) walikuwa nane miongoni mwao wakiwepo akinamama wawili Lydia Abebe kutoka Ethiopia na Bernadeta Kwimbila kutoka Malawi. Sisi hapa kama hauna menejimenti nzuri ya mpira utakosa hata waamuzi.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais nikiwa kama mtu ambaye nimekulia sehemu ya maisha yangu Wizara ya Mambo ya Nje. Mheshimiwa Rais ndiye mwanadiplomasia namba moja. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amethibitisha kwa vitendo kuwa mwanadiplomasia namba moja; kwanza, kwa ziara zake za Kenya na Uganda. Nilishasema hapa, kule Kenya imesaidia sana ziara ile kufungua milango hasa kwa sisi ambao tunalima mahindi, lakini pia Kenya nasi tunafanya biashara nyingi mbalimbali. Nampongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Mheshimiwa Rais pia ameendelea kuzungumza na kushiriki mikutano mbalimbali online ya Kimataifa. Ameshazungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani, pia amezungumza na Rais wa Benki ya Dunia, amezungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, hayo ni sehemu ya ule udiplomasia namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa nini? Kwa sababu ukienda katika bajeti yetu, katika “C” na “D”, ambayo inaelezea kwamba sehemu ya bajeti yetu itatokana pia na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo na mikopo ya ndani na nje. Takribani shilingi trilioni saba itatokana na mikopo pamoja na misaada. Sasa ili upate mikopo hii na misaada ambayo inatengeneza asilimia 20 ya bajeti yetu, ni lazima uaminiwe na uaminike Kimataifa. Vinginevyo huwezi kupata. Hili Mheshimiwa Rais amelithibitisha kwa vitendo kwa haya ambayo nimeyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, Tanzania imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba. Katika kuchaguliwa huku, ilipita bila ya kupingwa. Kwa kuweka record sawa, mara ya mwisho Tanzania ilikuwa Makamu wa Rais mwaka 1991 na pia imewahi kuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika Mkutano wake wa 34 Mwaka 1979 wakati wa Salim Ahmed Salim.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu gani? Kama nilivyosema bajeti yetu asilimia 20 inategemea misaada na mikopo ya riba nafuu. Sasa katika hili, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yako kwa ujumla katika Serikali. Bajeti mliyotuletea kama walivyosema wenzangu ni bajeti kweli ya wananchi, lakini katika haya Mheshimiwa Rais, ambayo anayafanya kama mwanadiplomasia namba moja, yako ambao sisi kama watendaji katika Serikali tunao wajibu ya kuyafanya ili tusimwangushe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika maelezo yako ya bajeti Mheshimiwa Waziri, umeelezea masuala ya mikopo ya riba nafuu na misaada. Masuala haya

Mheshimiwa Waziri yanakwenda na terms and conditions; masharti na vigezo lazima vizingatiwe. Sasa nakuomba na timu yako ya wataalam, katika kufanya majadiliano, tuzingatie sana terms and conditions. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana ambapo tumekusumbua sana mimi na wenzangu wa miji 45, wakiwemo akina Mheshimiwa Kanyasu na Mheshimiwa Mabula. Kwa kweli umekuwa msikivu na umelielewa lile jambo na umetuahidi hapo upo katika mazungumzo ya hatua za mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile jambo litakwenda kusaidia miji 45, siyo katika ujenzi tu wa miundombinu kwa maana ya barabara, pia unaenda kuisaidia miji hii na Halmashauri hizi katika kujenga vitega uchumi ambavyo vitakuwa ni vyanzo vya mapato. Kwa mfano, sisi Mafinga, mojawapo ya mradi ambao tumeuainisha ni kujenga soko kubwa la mazao ya misitu. Kwa maana ya kwamba katika SADC Kusini mwa Afrika, soko kubwa la mbao, milunda na nguzo, liwe pale Mafinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri na timu yake, tuharakishe jambo hili ili liweze kuanza kwa wakati. Pia kwa kutoa mfano tu, mradi wa maji wa miji 28 ambao ni mkopo wa fedha wa riba nafuu kutoka India is not a grant ni mkopo ambao tutaulipa. Tunapozungumza hapa ni mwaka wa sita haujaanza kutekelezwa.

Mheshimwa Mwenyekiti, pamoja na ule udiplomasia namba moja wa Mheshimiwa Rais, yeye anatufungulia njia, nasi sasa ni wajibu wetu katika kufanya majadiliano, tuhakikishe hayo majadiliano yanazingatia terms and conditions. Kwa sababu tukimbana Mheshimiwa Waziri wa maji katika mradi wa miji 28, anasema kwamba bwana, kuna masharti ambayo kwa kweli ilibidi tukae upya na kuanza kuyafikiria upya.

Mheshimwia Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tusimwangushe Mheshimiwa Rais, kama mwanadiplomasia namba moja. Ameshatutengenezea njia, sisi wataalam tunapokaa kujadiliana katika kuhitimisha hayo masuala ya mikopo na misaada, basi tuzingatie sana terms and conditions ambazo zitakuwa in our favor kama Taifa. Nitazungumzia pia kuhusu TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na timu yake kwa kutushirikisha sisi Wabunge (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za usafirishaji katika nchi hii hazitokani na kuwa na bei ya mafuta, gharama za usafirishaji zinatokana na ubovu wa barabara. Tukienda kukabiliana na kuhakikisha kwamba tunaondokana na ubovu wa barabara, gharama za usafirishaji zitapungua. Nitatoa mfano, kutoka Mafinga kwenda Mdaburo wakati wa mvua ambapo ni kilomita zisizozidi 50, nauli ni shilingi 10,000, lakini kutoka Dodoma kwenda Iringa ambako ni kilometa 260 nauli ni shilingi 10,000. Kwa nini kilomita 50 nauli ni shilingi 10,000 sawa sawa na kilomita 260? Ni kwa sababu barabara ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokuja na huu mpango wa TARURA, tukimshukuru Mheshimiwa Rais na hizo shilingi milioni 500 ambazo mmetushirikisha Wabunge kwa kiasi kikubwa, na hii fedha ambayo tunaipendekeza kwenye tozo za mafuta, ushauri wangu na ombi kwa Serikali, ikawe ring- fenced ili ikatuondolee kero ya barabara. Kutoka Mafinga kwenda Mgololo kilomita 80, sana sana unachoweza kufanya ni kukodi gari ya shilingi 100,000 ili ikupeleke, kwa sababu basi likienda na kurudi hizo gharama za matengenezo ni kubwa kupindukia.

Mheshimwa Mwenyekiti na waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, tukubaliane hii tozo ipite, lakini iwe ring-fenced kwa sababu inaenda kuwa mkombozi wa barabara. Gharama za nauli toka naingia hapa Bungeni; kutoka Iringa kwenda Dodoma, nauli ya basi imebaki ile ile kwa sababu barabara inapitika throughout. Kwa hiyo, ubovu wa barabara ndiyo chanzo cha gharama kubwa za usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, juzi amesema kuhusu Mchuchuma na Liganga. Hivi Rais akishasema, nini kinafuata? Ni utekelezaji. Kama tungeweza kupata kile chuma, hata hii reli ya SGR tunayojenga, wataalamu wanasema gharama zake zingepungua kwa asilimia 50. Siyo tu chuma na makaa ya mawe, kuna madini mengine. Naomba Mheshimwa Waziri na timu yako jambo hili Mheshimiwa Rais ameshasema, sisi watu wa nyanda za juu kusini, itakuwa ni mkombozi mkubwa wa uchumi, italeta speed of effect, katika uchumi siyo tu Mikoa ya nyanda za juu Kusini na Taifa zima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ukisoma bajeti, maeneo yote Mheshimiwa Waziri anasema, “napendekeza.” Kwa hiyo, niwatoe shaka wananchi. Wengi wamesema kuhusu Luku kwamba wapangaji watalipa; wengi wamesema kuhusu tozo zilizopendekezwa kwenye miamala ya simu na namna ya kulipa gharama za simu; niwatoe hofu wananchi, kazi yetu Wabunge ni kuishauri Serikali na baadaye masuala haya kabla ya kutekelezwa, yatakuja kwenye Sheria ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasi kama ambavyo bajeti ikisomwa tunapewa siku moja ya kuitafakari, pia na wananchi nao wanaitafakari. Nasi humu ndani tunatoa maoni yetu kutokana na feelings za wanachi ambao tumeshaanza kuziona. Lengo ni mwisho wa siku kukusanya mapato. Kukusanya kwa namna gani? Ndiyo wajibu wetu na wataalamu wetu wa uchumi waweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, napongeza sana suala la nyasi bandia. Nakuomba Waziri, wewe ni mwana michezo, isiishie level ya Jiji. Nakuomba pia Mheshimiwa Waziri ile 5% ambayo itapatikana Sports Betting, umesema kwamba itaenda kukuza sekta ya michezo. Hata hivyo, nina angalizo, kusema kwamba nani ata-determine, kwamba TFF ndio ata-determine mtu atakavyokuwa ameomba nyasi bandia zije kwamba ana-qualify au asi- qualify, hapana. Nashauri jambo hili liachiwe BMT. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, kiwango cha kuaminika cha TFF siyo kikubwa kama unavyodhania. Mheshimiwa Waziri kwenye hili naomba BMT ndio wapewe hiyo mandate ya kwamba kama ni Halmashauri imeomba, kama ni Jiji limeomba au kama ni taasisi au shule fulani imeomba, Baraza la Michezo la Taifa ndiyo liseme kwamba huyu apewe ama asipewe, lakini hii ambayo katika uchaguzi tu unaenda kila Mkoa, wadhamini washachukuliwa ndiyo uwape dhamana ya kwamba watupendekezee kiwanja gani kijengwe au kisijengwe, hapana. Napendekeza hiyo ibaki kwa Baraza la Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nasema nawasalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Kazi iendelee.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mungu awabariki sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha ushauri na maoni yangu kuhusu mbolea ya ruzuku kwa Mafinga na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwamba kwa kuwa sisi tunalima mwaka mzima, basi mbolea ipatikane mwaka mzima na kwa ujazo tofauti. Ukienda mpaka wa Namanga utaona bidhaa zinazovuka, kati ya bidhaa kubwa inayovuka ni pamoja na viazi ambavyo asilimia kubwa vinalimwa mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.

Mheshimiwa Spika, tunazungumza kuhusu kuongeza ajira, eneo hili linatoa ajira kuanzia wakulima, wauzaji wa pembejeo lakini pia sekta ya usafirishaji kuanzia kufikisha pembejeo shambani na kusafirisha viazi. Yawezekana ni gharama kubwa na yawezekana mwelekeo ni kutoa ruzuku kwa ajili ya mazao ya chakula, kama hivyo ndivyo, basi walau hata kama haitakuwa 50%, basi iwe ruzuku hata ya 25%, kwa mfano mbolea ya shilingi 150,000 basi ipatikane japo kwa shilingi 100,000.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujazo, wapo wakulima wanalima kilimo cha kumwagilia na cha mabondeni kwa maana ya vinyungu, hawa wanahitaji mbolea kwa matumizi ya awamu tofauti, kuna wakati anahitaji mbolea ya ujazo wa kilo tano, kilo kumi, kilo 20 na kadhalika. Hii itawapunguzia usumbufu ambapo kwa sasa wakulima wetu wanalazimika kuchanga fedha na kununua mfuko mmoja na baadae kuanza kugawana kwa kupima kwenye visadolini.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Wizara kwa wasilisho la bajeti na ninaomba kuchangia kama ifuatavyo; kwanza tuokoe zao la mkonge na viwanda vyake.

Mheshimiwa Spika, katika kitabu cha hotuba ya Waziri ukurasa wa 11-14 imetaja mchango wa kilimo katika pato la Taifa kuwa ni 26.1% na kwamba kilimo kinachangia 65% ya malighafi za viwanda. Zao la mkonge ni moja ya zao ambalo linaweza kuchangia asilimia za mchango wa kilimo katika pato la Taifa. Mawazo ya aina hii nimeyawasilisha pia katika bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Spika, katika ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 imetaja kuzalisha ajira milioni nane, ni wazi kuwa ajira hizi kwa kiasi kikubwa zitatokana na mnyororo wa thamani kuanzia katika malighafi za kutoka mashambani/kilimo hadi viwandani (agro-processing industry). Ajira hizi pamoja na viwandani itaendelea hadi sokoni. Ni masikitiko makubwa sana kwamba wakati tumeamua kufanya zao la mkonge kuwa zao la kimkakati, hakuna jitihada za makusudi za kulinda viwanda vya kuchakata zao la mkonge kwa maana ya kulinda soko. Ndani ya Serikali hakuna ufuatiliaji wa maagizo na maelekezo ya Waziri Mkuu ya Septemba, 2021 na rejea yake Novemba, 2021 kwamba Wizara inayohusika na mazingira kwa maana ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira izuie importation ya kamba za plastic ambazo kwa kiasi kikubwa mbali ya kuvuruga soko la kamba za kitani, lakini pia zinaathiri mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo ni matarajio yangu kwamba ikiwa Wizara ya Kilimo mnayo dhamana ya kukuza kilimo na kuongeza mchango wa malighafi za viwandani, basi pia mnao wajibu wa kuwa kiongozi wa kulinda viwanda ambavyo vinatumia malighafi za kilimo. Hivyo kama Wizara ya Kilimo mnayo nafasi kubwa ya kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira kuhakikisha kuwa zuio hilo linasimamiwa ili kuwalinda wakulima na kulinda viwanda na ajira za Watanzania kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Pili ni kuhusu vijana waliohudhuria mafunzo ya kilimo nchini Israel, je, wamesahaulika, tumewatelekeza au hawana tija? Kwa miaka kadhaa kama Taifa tumekuwa tukiwapeleka baadhi ya vijana waliomaliza SUA kwenda kuhudhuria mafunzo ya miezi takribani kumi na moja, hata hivyo wakirudi hatuwatumii, hatujui wako wapi? Kwa nini vijana hawa tusingeanza nao kwenye BBT hata kuwafanya ndio viongozi wa wengine? Katika hotuba ya Waziri ukurasa wa 75 amezungumzia mpango wa mashamba makubwa ya pamoja, nashauri kwa kuwa tayari tuna vijana waliopata maarifa ya hali ya juu ya kilimo huko Israel tuone kwa namna gani tutawatumia, sio sahihi na ni kupoteza rasilimali watu na fedha kuwaaacha hawa vijana wanaelea tu.

Mheshimiwa Spika, swali dogo, je, Wizara inawatambua, wako wangapi, wako wapi na wanafanya nini? Ndio maana baadhi ya watu wanaona BBT ni siasa, haya siwezi kuyasema Bungeni live bali nawaletea kwa maandishi, je, kama BBT sio siasa? Kwa nini hatuwatumii hawa vijana, wako idle wakati skills wanazo, kwa nini tutafute wapya ambao pengine kujiunga kwao na BBT ni kwa sababu wako desperate, hawana kazi, kwa sababu wamekosa ajira, hawana mbadala ndio maana wakakimbilia BBT.

Mheshimiwa Spika, je, BBT ni siasa au business as usual kama tulivyoshuhudia ya Kilimo Kwanza na kadhalika? Kama sio siasa basi ni matarajio yangu kwamba tuta-make maximum use of the available resources wakiwemo hawa vijana waliopata mafunzo Israel. Na ninatamani sana Waziri katika majumuisho aseme jambo kuhusu hawa vijana. Labda hii programu haikuwa na baraka za Wizara, labda kwa utaalam wenu mnaona haiwahusu, lakini iwe ni kilimo au yeyote aliyeratibu programu hii, bado mwisho wa siku ni Serikali katika ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ushauri wangu kwa Wizara, Waziri atuambie hatma ya hawa vijana, vinginevyo kwangu mimi nitaona hata BBT it is business as usual, it is politics. Na kuthibitisha kwamba kama Serikali tunawatambua hawa vijana soma hii meseji; “Kwanza Waziri wa Kilimo Josephat Hasunga wa Songwe aliwahi kuja Israel na akaahidi mambo mengi tu endapo tutarudi Tanzania, pili, Naibu Waziri Anthony Mavunde mwaka jana alihudhuria mahafali. Tatu kuna siku alikuwa Dodoma Mavunde alisema BBT itakuchua wanafunzi waliotoka Israel sijui wamemsaliti akina nani huko juu! Nne, Naibu Waziri Katambi aliwakaribisha Bungeni kama wageni wake siku fulani Bunge lililopita."

Mheshimiwa Spika, kuhitimisha suala hili, ni wazi Wizara na Serikali kwa ujumla inawatambua vijana hao, basi tuone namna ya kufanya, kuwatumia ili wawe na mchango katika kilimo chetu.

Mheshimiwa Spika, mafuta ya kula na kuondolewa kwa ushuru kutoka 35% hadi 0% je imesaidia kukua kwa kilimo cha mbegu za uzalishaji mafuta ya kula au tumenufaisha ma- tycoon wa biashara ya mafuta ya kula?

Mheshimiwa Spika, suala hili pamoja na kuwa ni la Viwanda na Biashara pamoja na Hazina, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba wenzetu wa Kilimo wanao wajibu wa kwanza kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa mafuta ya kula na hata kuuza nje. Lakini kwa mshangao na masikitiko makubwa mwaka wa fedha tunaoumaliza huu wa 2022/2023, Serikali iliondoa ushuru wa the so called mafuta ghafi kutoka 35% hadi 0% kwa mwaka mmoja kwa waagizaji kutoka nje. Maamuzi haya baadhi yetu tuliyapinga na kushauri kwamba hata kama ni ahueni basi walau iende kwa hatua na kwa awamu, kwa kupunguza hata hadi 15%.

Mheshimiwa Spika, ilitolewa hoja kwamba ingesaidia kupunguza bei ya mafuta ya kula, tukiwa honest wala haikuwa na mashiko, sana sana tumewanufaisha wafanyabiashara wakubwa, kwa sababu kwanza hawaingizi crude kama walivyodai, wanaingiza refined na kufanya packaging, matokeo yake tumewaumiza wakulima wetu wa alizeti, je, sisi kama Wizara ya Kilimo tumekuza kilimo au tumekirudisha nyuma?

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa azma ya Taifa hili kujitosheleza kwa mafuta ya kula ina safari ndefu sana kwa sababu wafanya maamuzi wanaangalia maslahi binafsi na sio maslahi ya walio wengi ambao ni wakulima wetu. Leo hii morale ya kulima alizeti imeshuka mno kutokana na bei ya alizeti kuwa ndogo. Kuna kichaka watu wanajificha ooh tumeondoa ili kupunguza makali ya bei, makali ya bei yamekuja kupungua baada ya wananchi kuanza kuvuna alizeti zao, kwa hiyo kuondoa ushuru kutoka 35% hadi 0% hakujawa na faida sio kwa mlaji wa mwisho wala mkulima wa alizeti. Kama Wizara mnapaswa kuwa na wivu na kutetea kilimo na hasa kwa mazao ambayo yatalisaidia Taifa kuondokana na kuagiza baadhi ya bidhaa kutoka nje kama ilivyo kwa mafuta ya kula. Yafaa sote kwa pamoja tuwe na dhamira moja na tuone aibu kuendelea kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi, na ndio maana mwaka jana nilishauri, washirikisheni JKT, mtaona matokeo in just two years.

Mheshimiwa Spika, napongeza jitihada za Mheshimiwa Waziri Mkuu zinazoendelea kule Kigoma za kilimo cha michikichi. Ninaamini tukiwawezesha JKT tutavuka, lazima tufike wakati tuwe na uthubutu, tuwe wakweli wa nafsi, sio sawa kama Taifa kuendelea kutumia zaidi ya USD milioni 300 kuagiza mafuta ya kule, tuone aibu kama Taifa. Tukiwekeza katika JKT sio tu kwamba tutaokoa fedha za kigeni, lakini pia tutauza mafuta katika nchi jirani za DRC, Malawi, Zambia na hata Burundi na Rwanda. Nchi hizi zinategemea mafuta ya kula kutoka Malaysia, tukizalisha tunalo soko la ndani lakini pia soko hata ndani ya EAC na baadhi ya nchi za SADC.

Mheshimiwa Spika, kule Chita, nashauri Serikali ikajifunze kilimo cha mpunga chini ya JKT, ni aibu sisi kutoa vibali eti kuagiza mchele tani 90,000; haya ni mambo tunapaswa kuyakataa kwa vitendo, hata programu ya BBT awamu ya pili, kama tuna dhamira njema na ya dhati, nashauri mngehusisha vijana waliopata mafunzo JKT na usimamizi ungefanywa kwa ushirikiano wa ofisi hizi tatu, Kilimo, Kazi na Ajira na JKT.

Mheshimiwa Spika, usalama wa mbegu na mbegu bora; katika ukurasa wa 119 wa hotuba ya Waziri ameeleza kuhusu suala la utafiti wa mbegu bora, ninashauri tuwe na mpango maalum wa kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa mbegu bora na salama. Mfumo uliopo kwa hakika sio salama katika suala la usalama wa chakula na usalama wa Taifa. Nashauri pia tuhusishe vyombo vyetu hasa JKT katika kufanya tafiti za mbegu bora, mimi naamini kwamba innovation mara nyingine inatokea kwenye vyombo vya ulinzi na usalama hasa majeshi, simaanishi kwamba tuwaachie wao, hapana, tuwashirikishe, tushirikiane na ndio maana nawasihi ndugu zangu wa Kilimo mkatembelee Chita, kipo kitu mtajifunza.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naanza pia kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa mawili. Kwanza, kama ambavyo tumesema siku zote, nampongeza sana kwa matokeo chanya yanayotokana na ile Royal Tour. Tumeona ongezeko la utalii na katika taarifa imeonesha kwamba kuna ongezeko la utalii kwa asilimia 123. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anaendelea kuidhinisha fedha kwenda katika miradi ambayo itaendelea kuchochea na kusisimua sekta ya utalii. Kwa mfano, watu wa Iringa tunamshukuru na kumpongeza sana kwa sababu ameendelea kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa pale Iringa ambapo utakapokamilika utachochea sana utalii hasa kusini kwa maana ya Mbuga ya Mikumi na Mbuga ya Ruaha. Kwa hiyo, kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake na vyombo vyao vyote. Watu wengi wamempongeza sana Mheshimiwa Waziri alivyokuwa amefanya vizuri kwenye Wizara ya Michezo, nami napenda tu niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, alifanya vizuri kwa sababu pia ni mwanamichezo, pamoja na kuwa sasa hivi ametukimbia kwenye Bunge Sports Club, ndiye aliyekuwa namba tisa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michezo ya pale Mombasa ya Mabunge ya Afrika Mashariki, yeye ndiye alichukua kiatu cha dhahabu pale Mombasa, lakini baada ya kuja mdogo wake, Mheshimiwa Sanga, naona amerithi ile nafasi kutokana na majukumu mengi aliyonayo Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana. Kwa kutumia michezo, ninapenda kushauri kwamba tuendelee kutumia michezo katika kutangaza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia nafasi hii kuwapongeza sana chama cha wanaosimamia uratibu wa mshindano ya magari. Tarehe 14, Mei walifanya mashindano ya magari katika Msitu wa Sao Hill kama sehemu pia ya kutangaza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza sana waandaaji wa Great Ruaha Marathon. Hii ni mbio ambayo itakimbiwa Julai, 08. Yaani marathon hii itafanyika ndani ya Mbuga ya Wanyama ya Ruaha, maana yake ni katika kushirikisha michezo kuendelea kutangaza utalii. Pia Mheshimiwa Waziri na timu yako, nikuombe, kwa kutumia wataalamu wako, wako baadhi ya watu wanapendekeza na kushauri kwamba kama inawezekana na kama taratibu za kitaalamu zinaruhusu, basi kule kwenye mbuga zetu kuwe hata na viwanja vidogo vya michezo kama mpira wa kikapu, mpira wa volleyball, mpira wa pete, na hata viwanja vidogo vya kucheza mpira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watalii wanakuja wanatamani baada ya kutembea waende kufanya michezo ya namna hiyo. Kwa hiyo, kama taratibu za kiikolojia zinaruhusu, naomba Mheshimiwa Waziri uweze kulichukua jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuwa, kwa kutumia michezo, naipongeza sana Timu yetu ya Wanawake ya Under 17, nawapongeza Tembo Warriors, wewe mwenyewe ulikuwepo kule Uturuki, pia nawapongeza wanariadha, nitawataja baadhi tu, akiwemo Alphonce Simbu na Gabriel Geay ambao wamekuwa wakishiriki katika mashindano mbalimbali ya marathon. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na mimi nikushauri na timu yako na kupitia TTB, sina shaka kabisa na Damasi Mfugale, ni mtu ambaye ni open-minded, hebu tujaribu pia kuwekeza katika michezo kama sehemu ya kutangaza utalii. Kwa mfano, ukiwekeza kwa mwanariadha ukamsaidia vifaa, ukamsaidia training, kuweka kambi, ukamsaidia na walimu wa kuwasaidia kama timu ya watu watano, anapokwenda kushiriki kama Boston Marathon, ile tu kushiriki ni mvuto kwa Taifa letu, inaongeza kuchochea kuvutia watalii katika Taifa hili. Kwa hiyo, naomba nikuombe pia utumie michezo katika kutangaza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda nijielekeze kwenye sekta ya misitu. Watu wengi wanadhani kwamba misitu ni mbao tu, lakini mimi na wenzangu kutoka kwenye maeneo ya misitu tunapenda kutumia neno mazao ya misitu. Kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu pamoja na mbao, juzi tumepitisha hapa Bajeti ya Wizara ya Nishati, wamesema watatupa vitongoji 15 kila Jimbo, maana yake ni vitongoji kama 3,000 hivi. Katika kufanikisha ndoto hiyo ya kufikisha umeme tutatumia nguzo, ni mazao ya misitu. Lakini tuna ujenzi katika Mji wetu wa Serikali, katika kujenga pale tunatumia milunda, mbao, marine board, hayo ni mazao ya misitu. Kwa hiyo hii sekta ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mafinga, Mufindi na Njombe, kuna wawekezaji wakubwa ambao wametoa ajira kubwa sana kwenye viwanda vya plywood. Waheshimiwa Wabunge, niwafahamishe kwamba katika miti pia kuna utomvu, kuna makampuni yanagema utomvu, hayo ni mazao ya misitu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba wanasema kwamba sekta ya mazao ya misitu inachangia asilimia tatu tu ya Pato la Taifa, siyo kweli, kwa sababu wao wanangalia tu ule mti ukishatoka kuwa mti basi wamemaliza mchango wa sekta ya mazao ya misitu. Lakini sekta ya misitu ni pana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri kutembelea uone uwekezaji uliofanywa na Serikali, lakini na makampuni na watu binafsi. Halafu nikuombe tembelea viwanda vya mazao ya misitu na baada ya hapo kutana na wadau wa sekta ya mazao ya misitu. Hapa yapo mambo ambayo mimi ninakuomba Mheshimiwa Waziri na timu yako kuweza kuyasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni suala la kurejesha kile ambacho makampuni yanakipata kwa jamii. Kwa kweli, napenda kuwapongeza sana TFS, wamekuwa wakishirikiana nasi, wametujengea mabweni, wameshiriki nasi kuboresha mazingira ya soko letu pale Mafinga, lakini makampuni ambayo yananufaika na sekta ya mazao ya misitu, bado hatujaiona Corporate Social Responsibility.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri na timu yako, mimi nawaamini sana, kama ambavyo tumefanya kwenye sekta ya madini na akina Mheshimiwa Doto, hebu tuje na utaratibu ambao hii sekta pia ya mazao ya misitu kile inachopata sehemu irejeshe kwa jamii, siyo tu wabaki TFS ndiyo warejeshe kwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwaombe mshirikiane na Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Kuna hiki kitu wananchi wetu wanatuuliza mambo ya hewa ya ukaa, tunaambiwa kwamba kuna fedha nyingi duniani zimetengwa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, sasa sisi tumepanda miti ya kutosha, wananchi wamehamasika. Nitatoa pongezi hapa kwa wenzetu wa FDT, kwa wenzetu wapanda miti kibiashara, wamekuwa wanatoa elimu na miche kwa wananchi kama ambavyo wanatoa TFS. Wananchi wameitikia, lakini tunauliza, je, katika suala zima la hewa ya ukaa, nafasi yetu Wanamafinga, Wanamufindi, Wanairinga, Wananjome, iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuombe ushirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), je, na sisi, kwa sababu tunachangia sana ku-regulate haya mabadiliko ya tabianchi. Kwa kupanda miti maana yake tunachangia sana, kwenye mambo haya mazima ya kuleta oxygen na hewa safi, lakini pia tunatunza vyanzo vya maji. Kwa hiyo, nikuombe sisi kwenye kipengele hicho tutanufaika kwa namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nitumie pia nafasi hii kuwapongeza watu wa Ebony FM Radio, katika kutimiza miaka yao 17 wamejitolea kuhamasisha kupanda miti 1,500,000. Kwa hiyo, unaweza kuona jinsi ambavyo hamasa iko juu sana. Tuendelee kuwaunga mkono lakini tuone wananufaika vipi na hewa ya ukaa, wananufaika vipi na hiyo CSR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la REGROW, Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu nilikaa naye, nashukuru alinipa muda wa kutosha, nilimweleza. Ninaomba tumtendee haki Mheshimiwa Rais. Mradi huu wa REGROW sasa ni mwaka wa tano. Mradi huu aliuzindua Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais Tarehe 12 Februari, 2018 wadau wote na sisi watu wa Iringa na Mikoa yote ya kusini tulikuwepo katika shughuli hiyo, lakini lazima tukubaliane kumekuwa na kusuasua kwenye utekelezaji wa huu mradi. Mimi nakuamini na timu yako mkijipanga tutakavyouboresha huu mradi yako mambo ambayo yataendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya kufanya biashara ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona umeeleza mambo ambayo yanatarajiwa kufanyika hebu yafanyike kwa haraka. Nasi tunasema watu wa utalii Kusini, kwamba kama ambavyo tumesema Iringa ni kitovu cha utalii na Mkuu wa Mkoa wa Iringa na timu yake, nawapongeza sana, wameendelea kuhamasisha lile tukio la kila mwaka la utalii kusini. Hivyo, Mheshimiwa Waziri kwa hiyo hii REGROW hebu ifike wakati, narudia kusema, tumtendee haki Mheshimiwa Rais ambaye alizindua mradi huu lakini utekelezaji umekuwa wa kusuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kama ambavyo tunafanya katika masuala mengine ya utalii, kwa mfano wageni wanavyolipa leseni ni tofauti na wanavyolipa wenyeji. Hata tunapokwenda kwenye mbuga za utalii unapoingia pale getini kama ni Mikumi, Ruaha au Ngorongoro, anavyolipa mgeni tofauti na anavyolipa mwenyeji. Kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri, kwenye suala la uwindaji, mimi nashauri sana wawindaji wazawa ambao wengine wanawinda for fun, wengine wanawinda kwa sababu mbalimbali, ziwe za kibiashara, hebu tuweke utaratibu kwamba kwa mfano makampuni makubwa giant tuyatengee labda asilimia 70, hawa wawindaji wazawa na wenyeji tuwatengee asilimia 30. Wao washindane kama wao na haya makampuni yashindane kama wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kiukweli wawindaji wetu ambao ni wazawa kwamba wataweza kushindana na haya makampuni ya ma-giant kutoka America, Urabuni, Ulaya na Asia? Itakuwa ni ngumu. Kwa hiyo mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri, hawa nao wanahitaji kama Watanzania ku-enjoy na kufurahia hii nature ambayo tunayo, hii ambayo Mungu ametujalia. Kwa hiyo, ili wenyewe pia wa-enjoy, wape asilimia 30 washindane wenyewe na makampuni makubwa yape asilimia 70. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napongeza tena Timu ya Yanga kwa sababu ilichofanya pia imetangaza Taifa letu, imetangaza utalii, ndiyo maana nasisitiza kwamba kupitia michezo tunaweza kutangaza sana Taifa letu na kutangaza sana utalii. Wenyewe mmeona Algeria Waarabu wamelala na viatu na wameijua Yanga, wameijua Tanzania, wamelijua Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mungu atubariki sana, awabariki Watanzania, ambariki Mheshimiwa Rais, abariki kila kilicho chema kwa ajili ya Taifa letu na maendeleo ya wananchi wetu wakiwemo wananchi wa Mafinga. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii, kuna mengine sikupanga kuyasema lakini kutokana na maelezo ya Waziri Kivuli, nimejikuta kwamba nawajibika kuyasema. Sisi wengine background zetu zinatuongoza kusema hivi ambavyo nitasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme moja tu kwamba tujifunze kua-appreciate, the way Waziri Kivuli amewasema Mabalozi, kwa kweli kwanza kitendo cha kuwafananisha na Mabalozi wa Nyumba Kumi, maana yake ni kwamba ni kama vile Mabalozi wa Nyumba Kumi wao sio watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninaamini Mheshimiwa Msigwa, ili atambulike popote lazima aende kwa Balozi wa Nyumba Kumi. Lakini pia Mabalozi hawa wameisha fanyakazi nzuri ya kuwakilisha Taifa letu, hii ni nchi ambayo hakuna kiongozi mkubwa duniani hajafika katika nchi hii, haya ni matokeo ya kazi nzuri ya hawa Mabalozi. Clinton ameisha fika hapa, Obama katika utawala wake mpaka sasa hivi amefanya jumla ya ziara 46, katika nchi zaidi ya 150 duniani, katika hizo 46 amefika hapa, ni kutokana na kazi nzuri ya hawa Mabalozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Marais wa nchi kubwa kama China, Hu Jintao ameondoka alikuja hapa, ni kazi nzuri ya hawa hata huyu wa sasa. Sasa ndio maana nasema tujifunze ku-appreciate na kutiana moyo kuliko kusemana semana kwa namna ambayo haitusaidii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme tu kama alivyosema Mheshimiwa Lusinde, yaani kweli kuna time ya kupinga lakini sio kupinga tu. Mheshimiwa Dkt. Jakaya alikuwa anasafiri anapingwa, huyu sasa hivi hasafiri ameamua kutanua wigo kwa Mabalozi unapinga, where are you standing you guys? Anyway niendelee kujilinda na background yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite sasa kwenye Sera ya Mambo ya Nje, hii economic diplomacy. Nimshauri Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla, hebu tujaribu kuona je, sera hii inaendana na current situation? Wakati sera hii inapoanzishwa mwaka wa 2001, je, changamoto kwa mfano kama mambo ya global warming, mambo kama ya vikundi vya kigaidi, mambo ya kuibuka kwa jumuiya nyingine mpya za kiuchumi, kama the BRICS yalikuwepo, na kama hayakuwepo sera imejipanga vipi, au Wizara imejipanga vipi ku-accommodate hali kama hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeshauri Wizara iwe na kitengo au na idara maalum ambayo kazi yake itakuwa ni kusimamia utekelezaji na kufanya tathmini ya diplomasia ya kiuchumi. Nijikite katika suala la EAC, ni kweli kwamba katika siasa za kimataifa za sasa hivi you can‟t work alone, lazima uwe katika economic integration, katika economic blocks. Lakini pia na sisi kwenye hizi blocks tujitizame, hebu tuangalie pia ni namna gani tunaweza ku-benefit nje ya EAC. Nitatoa mfano kwa mfano, DRC trade wise mizigo ambayo tunasafirisha kwenda DRC volume wise inazidi ya Rwanda, Burundi na Uganda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hata kama tutajenga reli, tutaimarisha bandari, kama hatutailinda DRC, strategically kama huyu ni partner wetu kibiashara, kwa sababu ya kwenda na mkumbo wa Single Custom Territory nawaambia tutapoteza na ili tufanikiwe na kulinda soko la DRC kibiashara, lazima Lubumbashi tufungue ubalozi mdogo, hili halikwepeki, kusudi tulinde maslahi ya Kongo.
Lakini pia sisi tunashiriki Congo Peace Keeping na kadhalika, we are not going there kama shopping hapana, nchi zote duniani Amerika unaona wanaenda Iraq, na kadhalika baada ya pale ni kuulinda na kung‟amua fursa za kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa zilizoko Kongo, hebu tujaribu kuzilinda. Lakini pia Mheshimiwa Waziri hata hii Single Custom Territory, leo hii nasikia kwamba tumekubaliana na wenzetu kwamba after sometimes tutapiga marufuku mitumba. Je, ndani hapa viwanda vya nguo tumejipanga sisi, au tutakuwa soko la wa Kenya, kama ambavyo leo hii maziwa ukienda kwenye maduka yanatoka Kenya, ukienda walimu katika kila shule tano, tatu unakuta ni walimu kutoka nje. Sawa tunaonesha spirit ya EAC lakini pia na sisi kama hii Wizara ya ku-coordinate mambo kama hayo, tunajipanga vipi, Mheshimiwa Waziri ningependa katika kujumuisha, uje na masuala kama hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine la muhimu JPC. JPC zetu kwa kweli zimekuwa tu za kinadhalia. JPC ni muhimu katika kutatua changamoto na kuchochea uhusiano hasa uhusiano wa kiuchumi. Hebu tutenge fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafanya hizi JPC (Joint Permanent Commission) maana yake ndio mwanzo na chemchem ya mahusiano. Lakini hayo yote Mheshimiwa Waziri utakapoyajumuisha, ili haya yote tuweze kuyafanikisha vizuri lazima tuangalie staff welfare. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanadhani wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje wanalipwa mishahara in terms of dollar, Kumbe maskini ya Mungu wanalipwa ni terms of TGS shillings. Lakini sio hivyo tu hata Balozi zetu Mheshimiwa Rais katika kubana matumizi, amesema kwamba kazi nyingi zitafanywa na Balozi zetu, tumezi-equip kwa kiasi gani na tunazi-facilitate kwa kiasi gani? Je, zina staff wa kutosha? Sio mtumishi yuko nje ughaibuni, lakini nyumba kila mwisho wa mwezi unapofika, roho yake iko juu kwamba mwenye nyumba atakuja kudai pango, unategemea huyu mtu ata-deriver? Unategemea huyu mtu ata-perform? Maendeleo ni gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuje na mipango ambayo pia itaangalia staff welfare. Hata pale Makao Makuu Wizara ya Mambo ya Nje, mimi nimetoka pale nafahamu, watu wanafanya kazi usiku na mchana, Mheshimiwa Waziri hili unalifahamu, kwa hiyo tuangalie ni kwa namna gani tutaenda, lakini pia katika diplomacy ili uwe a good diplomatic person, lazima pia u-save abroad. Sasa huwezi kuwa a good diplomat unakaa headquarter miaka kumi, kumi na tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie pia suala la posting, kwa sababu kama tunakusudia watu hawa wafanye kazi ipasavyo lazima tuwa-expose. Lazima tuangalie welfare yao, lazima tuwatafutie short training za mambo ya diplomasia ya kiuchumi ili kweli tuendane na kasi ya mambo ya dunia ya sasa inavyokwenda. Namshukuru Mheshimiwa Rais, amempa Wizara mtu ambaye ni nguli wa mambo haya, huyu mtu ameongoza ushauri katika mgogoro wa Somalia mpaka leo hii Somalia ina Serikali, jambo ambalo hata wa Marekani walishindwa. Leo hii mnawasema eti Mabalozi hawafanyi kazi, maana yake huyu katoka katika kitu cha aina hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe utakapokuwa unajumuisha, tafadhali ili tuenende sambamba na demokrasia ya kiuchumi, tuzingatie kufufua JPC kivitendo sio kwa maneno. Lakini tuangalie welfare ya watumishi katika Balozi zetu, lakini pia na watumishi pale headquarter, lakini kuhakikisha pia watumishi wanakwenda posting.
Napenda kuishukuru Wizara, Katibu Mkuu, Wakurugenzi wote, kwa kazi inayofanyika nzuri na tunaendelea kuwatia moyo, msikatishwe tamaa na maneno ya kukatisha tamaa. Sisi tusonge mbele Mungu awabariki sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Natumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kutoa mawazo yangu katika siku ya leo tunapochangia Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza napenda kabisa kwanza kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake. Pongezi hizi nazitoa kwa niaba ya wananchi ya Mafinga, kwa niaba ya wananchi wa Mufindi Kusini ambao wewe umekalia hicho kiti na kwa niaba ya wananchi wa Mufindi Kaskazini kwa kaka yetu Exaud Kigahe ambaye ni Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini natoa pongezi hizi? Nampongeza Mheshishimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwanza kwa ule mpango wa EPC+F, watu wengi walikuwa na mashaka kwamba unaweza mpango ule usije ukawa ni kitu cha kikweli kweli, lakini wiki iliyopita tumeshuhudia kusainiwa kwa Mikataba na ujenzi wa Barabara ya Mafinga Mgololo kilomita 81 unaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa sababu pia jana wameweka saini mkataba wa Barabara ya kutoka Mtiri kwenda Ifwagi mpaka maeneo ya Mkuta kilomita 14 ambako ni Jimbo la Mufindi Kaskazini, lakini wakati huo huo Nyororo–Mtwango ambako ni kwako wewe Mwenyekiti wameshaanza. Hapa naomba niweke na kaombi kidogo pamoja na kuwa umesema tuki–address kiti hapa naki–address kiti na naomba pia nim–address na Waziri wa Fedha. Tunaomba pale Nyororo – Mtwango tumeshaanza, lakini kwa sababu tunafanya kwa fedha za ndani, tunaomba Serikali itupie jicho, ipeleke fedha ili ujenzi wa ile barabara uende kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, katika hiyo Wilaya ya Mufindi ambao ni tajiri wa mazao ya misitu, maana tumezungumza hapa kuhusu vitongoji 15 kila jimbo kupatiwa umeme, nguzo zitatoka kule. Kwa hiyo itaimarisha miundombinu kutoka Sawala – Iyegeya mpaka Lulanda, jumla kilomita 40.7. Nafahamu ziko zile thelathini na ngapi na zile kumi ambazo tumeongezewa. Kwa hiyo haya yote mimi binafsi kama nimetoka Mafinga na Mufindi ambako Mheshimiwa Mwenyekiti wewe ni shahidi, sisi kama Wabunge watatu tumesimangwa sana, tumesemwa sana, lakini wananchi walikuwa hawajui, yako mengine tunaweza tukayasema hadharani lakini mengine tunayaficha chini ya meza, hatimaye yamekuwa, barabara zinaanza kujengwa. Kwa hiyo naipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi specific kwa Wanamufindi, nakuja na pongezi kama mbili, maana pongezi ni nyingi. La kwanza, ni hili la kuondoa ada kwa watoto wetu watakaokwenda kwenye Vyuo vya Ufundi, DIT, Dar Tech na ile zamani tulikuwa tunaita Mbeya Tech siku hizi inaitwa MUST.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mikubwa ya umeme, tuna Mradi wa SGR yote hii itahitaji mafundi wa kuihudumia kama sehemu ya maintenance. Kwa hiyo wazo hili ambalo Mheshimiwa Rais amelileta ni jambo jema, kwa sababu tutapata watoto wetu ambao watakuwa na ujuzi, watahudumia miundombinu ya reli yetu, lakini pia na miundombinu itakayotokana na umeme tutakaozalisha kwenye bwawa wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasilishe ombi na ushauri kwa Serikali kwa maana ya Waziri wa Fedha. Naomba sisi tunaotoka kwenye mazao ya misitu, ukienda kwenye msamaha wa VAT sana sana unapata kwenye vitendea kazi kama vile matrekta ya kuvuta magogo kutoka shambani kupeleka site au kupeleka barabarani. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, ili tuwe na connectivity, baada ya kuwa tumetoa ada kwenye hivi Vyuo vya Ufundi, tutoe pia VAT kwenye equipment hasa hasa za mazao ya misitu ili hawa watoto tukishawasomesha wawe na mahali pa kuanzia. Kwa hiyo hili ni jambo muhimu sana katika ku–add value. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napongeza ni ambalo linaenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Mheshimiwa Nape. Mara nyingi tunalalamika kuhusu mambo haya ya bundle na kadhalika, napongeza kwa sababu Mheshimiwa Waziri Nape na Serikali kwa ujumla wamekuwa wasikivu na wananchi wengi wanaweza wakawa hawajui, ile kupitisha miundombinu kwa ajili ya masuala ya mawasiliano ilikuwa kwa kilomita moja ukipitisha labda kwenye barabara za TARURA au za TANROAD kwa kilomita moja walikuwa wanatozwa dola 1,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limesemwa sana na mimi nilichangia kwenye Mpango na Serikali imekuwa Sikivu, sasa imepungua kutoka dola 1,000 ile kupata leeway mpaka dola 200 na ile annual fee imetoka 1,000 mpaka 100. Kwa hiyo matarajio yetu kwamba punguzo hili linaenda kuchochea uchumi wa kidigitali. Kwa hiyo, hili hapa napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zinaweza zikawa nyingi, lingine ni hili la kuwa na dirisha la kutoa huduma kwa wawekezaji. Napongeza kwamba kutakuwa na mfumo wa pamoja ambapo Taasisi kama NEMC, OSHA, BRELLA, TRA, TBS na kadhalika, zitakuwa zinapata kwa pamoja. Hapa napo nitoe angalizo, unakuta mfanyabiashara au mwekezaji amejaza kila kitu, litakapofika suala la control number, that’s a big problem, mara mtandao uko chini, mara njoo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu kwamba Serikali wakiongozwa na Wizara ya Mawasiliano ya Mheshimiwa Nape, hebu turahisishe maana yake yale ni mapato. Mtu ameshajaza kila kitu siku tatu kupata control number, anaambiwa mtandao sijui uko chini, mtandao uko taratibu, mtandao sijui umesimama. Naomba kama tunafanya huu muunganisho wa mifumo tuendane pia na kuimarisha na kuboresha miundombinu ya kuwezesha sasa huu uchumi wa kidijitali uende vizuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hili suala ambalo kwenye ukurasa nadhani wa 50 hadi 51, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na ningeomba Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, naona unazungumzishwa hapo hili unisikilize vizuri sana pamoja na kwamba Mwenyekiti umesema tuelekeze kwako. Kwenye suala hili la kukosekana au kuwa na upungufu wa dola, Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesema jitihada tunazofanya mojawapo ni kuhakikisha tunazalisha, tuuze nje kuliko kuagiza, sasa hapa nakuja wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuamue suala moja, tunaamua kuwa Taifa la wazalishaji au Taifa la wachuuzi, mimi Cosato Chumi na wanamafinga sisi tunataka tuwe Taifa la wazalishaji na hayo ndiyo maono ya Mheshimiwa Rais na ndiyo maana tukapewa ruzuku ya mbolea, ndiyo maana tunapewa ruzuku kwenye mbegu. Kwa hiyo, mimi ushauri wangu kwenye suala la mafuta na mimi hili nasema na sitoacha niliseme mpaka litokee, hebu Mheshimiwa Waziri tuende na mfumo wa kwenye sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari viwanda vilikata tamaa kuwekaza kwa sababu tulikuwa tunatoa vibali hovyo hovyo sukari inakuwa flooded hapa lakini baada ya kudhibiti na kuweka utaratibu mzuri tunaona uwekezaji na upanuzi kwenye viwanda vya sukari umeongozeka na sasa hivi deficit ni kama tani 15,000. Kwa hiyo, naomba kwenye ngano na mafuta ya kula na watu wa Serikali kuna mahali wanataka kutuchonganisha Wabunge na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikiliza juzi Mheshimiwa Waziri vizuri sana kwamba basi tutapandisha, kana kwamba huo ushuru wa asilimia 35 kana kwamba ukipandishwa bei itakuwa kubwa, hata ulipopungua, ulipokuwa zero rated Waheshimiwa Wabunge, bei ya mafuta ya kula haikupungua huo ndiyo ukweli, mlaji wa mwisho hakunufaika, yamenufaika ma–tycoon lazima tuseme ukweli. Bei ya mafuta imepata ahueni kidogo juzi baada ya kuanza kuvuna alizeti. Kwa hiyo, naomba na wataalam wake Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili la Kamati naunga mkono mapendekezo ya Kamati kwa ujumla imeenda vizuri, isipokuwa kwenye suala la cement ile shilingi 20 ambayo ni sawa na mfuko 1,000 Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais ameshiriki mikutano sasa mfululizo mara mbili, ule wa dunia wa mabadiliko ya tabianchi, kuna fedha nyingi kwenye mifuko ya mabadiliko ya tabianchi, na kuna mahali Kamati imempongeza Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, kuliko tutwishane mzigo Watanzania bado ziko fedha nyingi. Mheshimiwa Kakoso amesema hapa jana, hii biashara tu ya hewa ya ukaa kama sisi tunaotoka Mufindi, Iringa, Njombe Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inaweza ku subsidize kuliko kumtwisha mwananchi hii shilingi 20 sawa na 1,000 kwa mfuko wa cement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kutoka mwisho, nina barua umoja wa wastaafu Halmashauri ya Mji wa Mafinga wanaomba ile pensheni ya iongezwe. Mapendekezo yao wanasema lile dirisha kwamba wazee kwanza wanapokwenda kupata afya, hapana tuwe na dirisha lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo la mwisho kwa Mheshimiwa Bashe, nimekutumia meseji kuhusu mahindi. Mimi naomba niwatoe wasiwasi Serikali, mmesema tu – apply na asubuhi umesema watu wana – apply lakini mtandano uko chini. Hii dhana kwamba eti wakulima tutauza hadi tusahau kujiwekea chakula siyo kweli. Sisi tuna akili timamu kwa miaka yote. Kwa hiyo, ni mambo mawili, ama mrahisishe upatikanaji wa vibali kwenye huo mfumo wenu tuuze nje, pili kama hamuwezi NFRA nunueni kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Mungu Ibariki Mafinga, Mungu Ibariki Mufindi, Mungu bariki viongozi wetu, mmbariki sana Mama Samia Suluhu Hassan. Ahsanteni sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DAVID C. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo. Yameshasemwa mengi sana na Wajumbe ambao wametangulia kwa hiyo nisingependa kurudia ningeenda kwenye some specific issues.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ambalo ninapenda kuliweka wazi na kulisemea ni suala la watu kulipa kodi. Kodi katika Taifa lolote ni kama vile nerves za fahamu za mwanadamu. Kwa hiyo, kodi kwa kweli lazima kodi ilipwe, hilo halina mjadala, hata mataifa makubwa ambayo wakati mwingine yanatusaidia kama wahisani au kwa mikopo zile ni kodi za wale wananchi, kwa hiyo, linapokuja suala la kodi kwa kweli kusiwe na mjadala kodi lazima zilipwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuje namna gani sasa ya huo ulipaji wa kodi, nitaanza kwa kusema katika hali ya kawaida kabisa ukusanyaji wa kodi lazima uendane sambamba na elimu kwa walipa kodi. Leo hii wananchi wetu kwa kukosa ufahamu pale Mafinga mwananchi amedunduliza, ameuza gobo (mahindi yale ya kuchoma ambayo yanavunwa bado mabichi), amepata kibali amevuna mbao ameuza, amenunua gari lake labda kwa mtu “A”, keshokutwa TRA wanamkamata kwamba wewe bwana ulinunua hili gari hukulipa kodi, hukulipa capital gain, sawa ni sheria lakini mtu huyu kumbe hana ufahamu wa lile jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye akinunua gari, akaandikishana mkataba na aliyemuuzia akampa kadi yeye anaona ameshamaliza, sasa kumbe hata hawa walipa kodi wadogo wadogo hebu TRA sambamba na ukusanyaji twende na elimu pia ya ulipa kodi kwa sababu hata sisi wenyewe Wabunge wengi tunapotaka kama unafanya biashara masuala ya kodi lazima utatafuta mshauri wa kukuelekeza katika suala zima la kodi.
Kwa hiyo, tupeleke elimu kwa watu hawa sasa mtu huyu kama nilivyosema amenunua gari lake, ameamua kufanyabiashara ya kusafirisha watu, kumbe hajui ukitaka iwe gari ya biashara kuna taratibu zake pia za kikodi gari inakamatwa, ameshajimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TRA the way wanakuja yaani hawaji kwa ile elimu kwamba you are supposed to do this ili uwe katika njia hii hapa. Yaani wanakuja kwa namna ambayo ni ya ambush. Kwa hiyo, kama nilivyosema sipingani, kodi lazima ilipwe, lakini pia jitihada za kukusanya kodi ziende sambamba na elimu ya kuwaelimisha wananchi kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili hizi machine za EFD kwanza hazijasambazwa vya kutosha, lakini leo nilikuwa nasoma kwenye gazeti, Sheria ambayo sisi wenyewe of course tulipitisha kama hujadai risiti kuna fine utapigwa pale lakini mashine nyingi ninyi wote mashahidi unaenda, oh, mtandao uko chini mashine haifanyi kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri hebu tusaidie hii ilikuwa ni deal ya watu au kweli wenye biashara mashine ni mbovu? Lakini shaka yangu kwamba hizi mashine yawezekana toka mwanzo hazikuwa mashine madhubuti. Sasa hawa wanao-supply tumejiridhisha kweli wana-supply mashine za EFD zinazotakiwa? Kwa hiyo, tunaweza tukajikuta siku tunashurutisha watu kumbe mashine yenyewe hatujazisimamia ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie, elimu ya kulipa kodi ina umuhimu wananchi toka lile tangazo la Mheshimiwa Magufuli na tangazo la kale katoto nipe na risiti, imewaingia watu mpaka watoto wangu nikinunua gazeti tu wananiambia baba mbona hujadai risiti? Lakini sasa kama elimu imeanza kuwaingia hivyo ya kudai risiti na mashine hazifanyi kazi kwa wakati, mtandao uko chini, je, tutafikia malengo ya Mpango? Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri ulitazame hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la Liganga na Mchuchuma, amesema hapa ndugu yangu asubuhi, Mheshimiwa Sixtus Mapunda. Mimi hujizuia sana kuleta mambo ya Ukanda, lakini katika hili naungana naye au kwa sababu liko Kusini?
Mimi natoka Nyanda za Juu Kusini, bahati mbaya inaweza kuwa bahati mbaya au nzuri nilifanya mazungumzo na Balozi wa China kwa ajili ya mambo ya jimbo langu. Kati ya kitu ambacho hata Ubalozi wa China unasikitika mojawapo ni suala kulegalega suala la Mchuchuma, kulegalega suala la Bagamoyo na Mheshimiwa Waziri katika kitabu chako umesema hii ni miradi ya vielelezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yawezekana kuna watu wengine wamesoma zaidi, wanaufahamu wa mambo haya lakini pia ni vizuri sana kutumia elimu yetu kuhakikisha kwamba tunalisaidia Taifa kusonga mbele pale ambapo tumekwama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano naambiwa katika suala hili, yule mbia ambaye ana ubia pamoja na NDC fedha za kulipa fidia wananchi wa Ludewa kule kwa ndugu yangu zimeshapatikana na zipo. Lakini mgogoro unaambiwa upo kwenye power purchasing agreement, sisi tunataka tununue kwa senti saba za dola wao kwa senti 13; lakini ukiangalia mradi ule katika ujumla wake, lengo lake zile megawatt 600 ni katika kutusaidia sisi tupate umeme. Lakini mradi wenyewe katika ujumla wake kama alivyosema Mheshimiwa Mama Nagu unaenda kusaidia ku-stimulate viwanda vingine. Tunataka sisi kujenga reli hapa, hayo mavyuma tutayatoa kule. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nikuombe kwenye suala la Mchuchuma tulipokwama tuone tunatoka wapi tuweze kufanikisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine kwa kushirikiana na Wizara ya Mamboya Nje, tusiwe nchi ya kusaini tu ma-MoU, alikuja hapa Rais wa China mara baada ya kuapishwa ni nchi ya kwanza duniani kuitembelea tumesaini mikataba 16, juzi tumesaini na Morocco, je, follow up iko wapi ya kila mkataba tuliosaini utakuwa na tija kiasi gani, tumekwama wapi, nani amekwamisha? Ili kusudi dhamiraya mpango huu iweze kutimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie muda wangu naona unaniishia kuhusu suala la kilimo, katika Mpango huu hakuna mahali popote palipo reflect suala la kilimo kama ambavyo Mpango wenyewe wa Miaka Mitano unasema. Sasa niombe tujaribu kuwekeza katika kilimo hiki na tusaidie pia Shirika la Maendeleo ya Viwanda vidogovidogo SIDO kwa ajili ya kitu kinaitwa knock down technology. Juzi tumeona wakulima wa nyanya wanauza nyanya ndoo mpaka shilingi 800. Sasa wakati tuna-deal na mamiradi makubwa hebu pia tuone namna gani tunaweza kukinyanyua kilimo kwa namna ya kawaida, tukashirikiana na SIDO, tukajenga viwanda vya kawaida, tuka-add value katika mazao ya wakulima ili kusudi hawa wakulima kweli waonekane ni uti wa mgongo wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni single custom territory watu wengi wamesema; na mimi kwa ufahamu wangu ningeshauri sana Congo DRC tuwape special treatment ndugu zangu. Sisi single custom territory tu-deal nayo na sisi hapa EAC. Lakini hawa watu ambao volume yao kibiashara ni kubwa hebu wao tuwape special treatment.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya nimalizie kwa kusema wako watu wanaosema pengine Mawaziri wanaogopa kumshauri Rais, sidhani kama kuna kitu cha namna hiyo. Hawa ni watu wenye confidence, wenye kujiamini katika kazi, tuwape nafasi…
MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kupongeza hotuba nzuri ya bajeti ikiwa ni pamoja na hatua kadhaa ambazo zimeelezwa kama vile kurejesha retention ya 20% ya kodi za ardhi na majengo kwa Halmashauri zetu, kuanzishwa kwa Single Window Payments System pamoja na Taarifa ya Kamati ya Bajeti ikiwa ni pamoja na maoni, mapendekezo.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya mchango wangu baadhi nimerejea mchango wangu wa Bunge la Novemba wakati Kamati zikiwasilisha taarifa za Kamati na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya ninayorejea ni umuhimu wa Taifa letu kuhusu namna ambavyo itanufaika na fedha za mifuko ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani. Zipo fedha kwa ajili ya grants ku-support nchi zinazoendelea katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Fedha hizi zingeweza kusaidia katika kujenga miundombinu ambayo itasaidia wakulima kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Mifuko kama Green Climate Fund, Climate Investment Funds, Adaptation Fund na Global Environment Fund baadhi ya hii mifuko inatoa mikopo ya riba nafuu au ku-support miradi ambayo inasaidia kupunguza ongezeko la carbon. Kwa mfano Rwanda wamepata pound milioni 24.5 ambazo zilisaidia kuanzisha Rwanda Green Fund ambayo imewezesha kutoa renewable energy kwa kaya 57,500 na ilizalisha so called Green jobs 137,500.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo nashauri mapendekezo ya kutoza shilingi 20 kwenye cement iondolewe na mbadala wake iwe ni hizi fedha za mifuko niliyotaja kwa sababu nyingi kati ya fedha hizo ni grants.

Kuhusu ATCL, napongeza jitihada zote za kuongeza ndege, nashauri yafuatayo; pawepo route ya kutoka Dodoma kwenda kwenye Kanda Kuu kama vile kwenda Mwanza kwa maana ya Lake Zone, kwenda Mtwara kwa maana ya Southern, kwenda Mbeya kwa maana ya Southern Highlands, kwenda KIA na pia kwenda Kigoma. Ilivyo sasa kama abiria atatoka Dodoma anataka kwenda Mbeya, lazima kwanza aende Dar, akifika Dar anaanza upya safari na tiketi mpya kwenda Mbeya, hii sio sawa, tutafute namna ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, niliwasilisha mchango wangu wa kwanza kwa Maandishi na pia nilipata nafasi ya kuchangia kwa kuongea tarehe 21 Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango wangu wa awali, naomba kuwasilisha tena mchango wangu wa maandishi kwa masuala kadhaa, kwanza ni kuhusu Mradi wa REGROW; Mradi huu wa kuimarisha utalii Kusini ulisainiwa Februari, 2018 na Mheshimiwa Rais wakati huo akiwa Makamu wa Rais. Lengo la mradi huu ambao ni mkopo wa Benki ya Dunia wa USD milioni 150 ni kuboresha utalii Kusini, ikihusisha kuimarisha miundombinu ya kuwezesha kuinua utalii kama vile upgrading of 14 airstrips, barabara kama kilometa 2000 ndani ya mbuga, njia za kutembea kwa miguu kilometa 350, ujenzi wa Kituo cha Taarifa za Kitalii pale Kihesa, Kilolo na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ni mradi ambao ulipaswa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano, lakini utekelezaji wake kwa kweli ni wa kusuasua. Nafahamu suala hili lipo Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini Wizara ya Fedha ndio mshiriki mkuu wa mijadala ya masuala yote ya mikopo na misaada, na mpaka kupatikana kwa fedha hizi USD milioni 150. Kwa hiyo inao wajibu wa kujua je, fedha hizi zinatumika kadri ya malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu; kwa kuzingatia kwamba jitihada za kutangaza utalii kuanzia filamu ya Royal Tour zinaendelea kuongeza idadi ya watalii, ni muhimu sana mradi wa REGROW kasi ya utekelezaji ikaongezeka na kwa kuwa kupatikana kwa fedha hizi Hazina ilihusika, ni vizuri pakawepo mfumo wa kuitaka Wizara ya Kisekta kutoa taarifa ya utekelezaji ya miradi husika. Kwa hiyo, natamani kuona Serikali ikitueleza suala hili linaendeleaje.

Kuhusu suala la kodi kwa magari ya abiria; katika ukurasa wa 101 wa hotuba ya bajeti, imependekezwa kuwa magari ya abiria yatozwe viwango kadri ya idadi ya abiria. Hata hivyo nashauri kodi hii itizame pia umbali ambao gari inasafiri. Kwa mfano yapo mabasi makuukuu yanayosafiri mikoani ndani ya Wilaya, kwa mfano hapa Dodoma, yapo mabasi yanatoka mjini yanaenda vijijini kama vile Mvumi, Mlowa Bahi na kadhalika. Yapo mabasi huko mikoani ambayo yanatoka makao makuu ya Wilaya yanaenda vijijini umbali usiozidi kilometa 100 na yanapita katika barabara ambazo wakati wa masika hazipitiki kwa wepesi, kwa hakika basi la aina hii linaweza kusafiri wiki moja, wiki ya pili lifikie gereji, ni yale mabasi tunayoyaita spana mkononi.

Mheshimiwa Spika, sasa basi kama hili ambalo nauli kutokana na umbali unaweza kukuta nauli ni shilingi 5000 kwa kiwango cha juu. Kwa mabasi ya abiria 65 ni sawa na makusanyo ghafi shilingi 325,000, hapo bado mafuta na gharama nyingine za uendeshaji kama vile spare na tozo mbalimbali, je ni sawa basi kama hili kutozwa shilingi 2,200,000 kwa mwaka?

Mheshimiwa Spika, nashauri viwango hivi vitizamwe upya na ikibidi vizingatie masuala kama uchakavu wa gari na umbali linalosafiri, na suala hili lizingatiwe pia kwenye magari ya mizigo.

Mheshimiwa Spika, magari ambayo yameanza kuchoka, kodi isiwe sawa na magari ambayo bado hayajachoka. Kwa mfano tuangalie umri wa gari kama moja ya kigezo, kwa sababu gari ambayo imeanza kuchoka, kwanza inatumia mafuta mengi hii inafanya gari hilo kununua mafuta mengi na hivyo Serikali inapata fuel levy, na pia gari la aina hiyo ambalo ni spana mkononi pia linatumia spare mara kwa mara ambapo pia Serikali inapata kodi kupitia kodi mbalimbali kutokea kwa wauza spare.

Kwa hiyo ushauri wangu kodi hii itazamwe na ikibidi izingatie umri wa gari na umbali inaosafiri kwa upande wa mabasi ya abiria.

Mheshimiwa Spika, kuhusu sewa ya ukaa, naomba Serikali irejee mchango wa Mheshimiwa Kakoso siku ya tarehe 20 Juni, 2023 kuhusu namna ambavyo tunaweza kunufaika kama Taifa na utajiri wa misitu kupitia biashara ya hewa ya ukaa. Hii ni biashara kubwa, lakini inayohitaji utaalam wa juu sana kwa sababu inataka sio tu umakini, lakini imejaa ulaghai mkubwa miongoni mwa makampuni. Kwa mfano sisi watu wa Mufindi, Kampuni ya Green Resources Limited-GRL walinunua maeneo mengi ya vijiji na wananchi katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Njombe, wamepanda miti na wanalipwa fedha za hewa ya ukaa, lakini wananchi na wanavijiji hawapati kitu.

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu kwa Wizara ya Makamu wa Rais-Mazingira nimeshauri kwamba tuliwekee mkazo eneo hili kwa kushirikisha sekta binafsi na NGOs, hili ni eneo ambalo Serikali hatujalitizama kwa kina, kuna fedha nyingi sana na Mheshimiwa Rais ushiriki wake kwenye COP 26 Glasgow ulithibitika kwa sababu alikuwa jasiri akayaeleza mataifa makubwa kwamba yanapaswa kuheshimu ahadi zao za kutoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwa sababu mataifa makubwa yanaongoza kuchafua mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, nashauri ndani ya Serikali tuweke mkakati maalum, tuwe na timu ya wataalam hata kwa kulipia, tuijue habari hii ya biashara ya hewa ya ukaa na masuala mazima yanayohusu mabadiliko ya tabia nchi, fursa zilizopo na kadhalika. Tusiwaze kupanda tu miti, zipo fursa nyingi, tujifunze Wilaya ya Tanganyika kwa kuanzia lakini tutumie Balozi zetu kama Ubalozi wetu wa Brasilia kujua nchi kama Brazil imefanikiwa vipi kunufaika na biashara ya ukaa na msisitizo wangu ni kushirikisha sekta binafsi, tusijifungie ndani kwa sababu ukweli ni kwamba utaalam wa suala hili ni wa kipekee, kwa hiyo, wakati huu tufanye ushirikishwaji, pia wakati huo huo kama ambavyo tuliwahi kuwa na mipango mahususi wa kuzalisha vijana wetu kwa ajili ya sekta ya oil and gas basi tutumie mfumo ule kuwekeza katika elimu kwa vijana wetu kwa ajili ya suala zima la mabadiliko ya tabia nchi na yatokanayo ikiwemo biashara ya hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Spika, naamini Serikali ikikaa na Mheshimiwa Kakoso na baadhi ya wataalam itaona wapi pa kuanzia.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana nami kupata nafasi hii ya kuchangia jambo hili.
Awali ya yote, pamoja na kuwa muda ni mchache nitumie pia fursa hii kuwapa pole wananchi wa Mafinga hasa pale Jambeki kutokana na lile janga la moto na pia janga la moto lililowakumba pale stand ya Mafinga, nawapa pole sana! Na ninawatia moyo kwamba Serikali itaendelea na jitihada za kututafutia gari la zimamoto.
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, baadhi ya wachangiaji wamesema kwamba tunalalamika tu, tumekuwa watu wa ku-complain. Mwingine amesema tunagombana na EU, tunagombana Kenya, tunagombana na Uganda. Mimi niseme jambo moja kwanza, hatulalamiki, pili, hatugombani na yeyote isipokuwa tunalinda maslahi ya Taifa letu. Mwingine amesema kwamba tumechukua muda mrefu sana ku-negotiate jambo hili, ndiyo negotiation zilivyo za Kimataifa. Kuchukua muda mrefu wala siyo tatizo leo hii Uturuki bado inaendelea ku-negotiate na EU ili iweze kuingia. Pia kushiriki negotiation na kutosaini ni mambo ya kawaida katika masuala ya Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, Mkataba wa Roma huu ulioleta ICC, Marekani alishiriki lakini hakusaini, kwa hiyo, siyo dhambi kutosaini, wala sisi siyo watu kwanza. Pia hata katika negotiation kwanza kuna stage ya kwanza una-negotiate, pili, unarudi je, tume-achieve katika ile negotiation? Baada ya pale ndiyo unaamua usaini au usisaini. Sasa watalaam wame-negotiate wamekaa chini wameona kwamba katika mkataba huu hatujakidhi matarajio ya yale ambao tunajarajia ku-achieve, wameshauri tusisaini. Haya ni mambo ya kawaida kabisa katika taaluma za mambo ya Kimataifa na mambo ya mikataba ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, pia kuna kitu kingine ambacho watu wengi wameshindwa kukitazama; kuna kitu kinaitwa EBA, kirefu cha EBA ni Everything But Arms. Sasa Everything But Arms ni nini? Kwa lugha nyepesi katika EU-EBA inasema kwamba The EU will offer quarter and duty free market access to all products originating from the LDCs with the exceptional of arms, everything but arms. Sisi ni LDCs - Less Developed Country. Maana yake ni kwamba with EU-EBA mpaka hapa tulipo tunaweza kuingiza chochote katika Soko la EU, isipokuwa silaha, lakini free of duty. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzetu Kenya, wao tayari wameji-pronounce kwamba ni middle income country, chochote wanachofanya kule wanachoingiza kule katika Soko la EU lazima wachajiwe ushuru usiyo pungua asilimia 10, sisi with EPA, without EPA kwa yule EU-EBA tayari tunayo hiyo haki ya kuingiza chochote kule bila ushuru. Sasa ndiyo maana tujiulize kwa nini wenzetu wamesaini? (Makofi)
Mheshimiwa Zitto amesema hapa kuhusu maua. Kenya wanauza maua yasiyopungua thamani ya dola 500,000 kwa mwaka, pia export ya Kenya katika EU pamoja na UK ambayo imejitoa kwa mwaka ni wastani wa 1.5 billion USD. Sasa kwa kuwa wanalazimika kulipa ile asilimia 10 wanalipa siyo chini ya milioni 100 kwa mwaka kama ushuru wanapoingiza zile bidhaa. Lakini ni nani anayemiliki maua, ile industry ya maua katika nchi ya Kenya? Kenya tofauti na Tanzania hapa hata mimi Mtoto wa Mama Cosata leo hii ni Mbunge, in Kenya that cannot be possible. Mtoto wa malalahoi ukaja kuwa Mbuge kama tulivyokuwa sisi humu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, industry ya maua ya Kenya wanao-dominate ni ma-giant ambayo ni ma-ruling class na ndiyo maana haraka haraka wame-ratify huu Mkataba ili kusudi uwape hiyo favour. Kwa hiyo, haya mambo ndugu zangu tunapojadili kama alivyosema Ndugu yangu Khatib maslahi ya kitaifa tuyatazame mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili kwa nini tunakataa kusaini? Mimi nampongeza Mheshimiwa Rais na ninaipongeza Serikali kwa kuitika wito wa kuleta jambo hili hapa na sisi tuseme lolote. Kwa nini tunakataa? Madhara yake moja, tutapoteza ushuru,ambao mpaka sasa tunatoza hizo bidhaa wanazotuletea. Tukipoteza ushuru maana yake ni nini? Kupitia ushuru huo ndiyo tunatarajia tujenge nchi yetu, tuhudumie watu wetu, tufanye elimu bure, tulipe mikopo ya wanafunzi, tujenge zahanati na kadhalika, sasa hicho tunakiondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, tukikubali jambo hili ita-damage jitihada zetu za kujenga uchumi wa viwanda. Kwa sababu tutakubali sasa tuwe tu ni soko.
Mwisho, tujiulize kwa nini wenzetu tunasema jambo hili lazima tusaini as block wao wamesaini, tumeshasema mfano huo wa maua Mheshimiwa Zitto amesema. Pia tuendelee kutafakari kwa kina tunapojadiliana na wenzetu ndani ya East Africa, unafiki huu mwisho wake nini na nini hatima ya East Africa Community na kwa mwenendo na trend ya unafiki wa namna hii?
Kuna watu wamekuwa na mashaka kwamba kwa kutusaini ita-damage mambo mengi, mojawapo wanasema Foreign Direct Investment (FDI) kwamba tutakosa kupata kuvutia mitaji kutoka EU, siyo kweli. Mheshimiwa Hawa Ghasia ametoa takwimu hapa katika FDI nchi ambazo zinaongoza mpaka sasa hivi kuwekeza mitaji yao hapa kwetu ni China, India, Kenya ikifuatia na nyinginezo. Katika nchi 10 ni mbili tu ndizo zinatoka EU, huu mkataba ukisaini maana yake ni kwamba una-discourage FDI kutoka kwingine. Je, tuna uhakika gani hawa watu tukisaini nao kweli wataendelea kutuletea mitaji, ambapo hadi sasa hivi ni nchi mbili tu kati ya 10 ambazo zinaleta hapa hiyo FDI? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine watu wengine wana mashaka kwamba ita-damage mahusiano yetu ya kidiplomasia, siyo kweli. Hii siyo dhambi kutosaini. Leo hii Norway haiko katika EU kwa sababu inalinda maslahi yake. Uturuki inataka kuingia kwa sababu inadhani itanufaika zaidi, Norway haitaki kuingia kwa sababu inalinda maslahi yake, hata Sweden imeingia mwaka 1995 pia kwenye ile Euro Zone kwa maana ya currency hawapo kwa sababu wanalinda maslahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nini way forward, katika biashara yoyote kitu muhimu ni soko na ndiyo maana tumeleta Jumuiya ya Afrika Masharika, ndiyo maana tuna SADC, lakini pia ndiyo maana tunafikiria kuangalia namna gani tutaunganisha COMESA, SADC na Afrika Mashariki ili tuwe na soko kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia hata katika Afrika tunajadili sasa hivi kuwa na continental free trade area ili tupanue soko. Kwa hiyo, ushauri wangu wakati tunajadili haya naipongeza Serikali, lakini naendelea pia kushauri wakati tunakataa kusaini Mkataba huu na tuendelee kuboresha mazingira yetu ya kuwezesha kuvutia mitaji ili dhana ya kujenga uchumi wa viwanda iweze kutimia.
Mheshimiwa Spika, mwisho, ninashauri, tupende kujihabarisha Waheshimiwa Wabunge. Mkasome ile article ya Mzee Mkapa, ina some details kwa lugha nyepesi sana. Tutaweza kujifunza na kuona, lakini na kuwaelimisha watu wetu huko nje, kwa nini tumekataa kusaini, madhara yake ni nini?(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na kuipongeza Serikali kwa kutosaini. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa haraka napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza viongozi wenzetu walioteuliwa Mama Anjelina pamoja na ndugu yangu Ridhiwan ambaye kule kwenye Bunge Sports Club huwa tunamwita super sub yaani yule mchezaji anayeingia kipindi cha pili akishasoma mchezo, akiingia basi mambo yanakuwa vizuri magori yanatililika na ndiyo maana tukawa mabingwa kwenye michezo ya Mabunge ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo, naamini hata huko kwenye ardhi, ataendeleza mazuri anayoyafanya tukiwa uwanjani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Katibu Mkuu, mzee Kijazi, ni mtu rahimu pamoja na timu yake na Naibu Katibu Mkuu wake. Pia napenda kuipongeza Wizara hasa ambavyo imeshusha huduma mpaka ngazi ya mikoa. Kwa mfano sisi watu wa Mafinga zamani ilikuwa lazima twende kwenye Ofisi ya Kanda kule Mbeya lakini sasa ofisi iko palepale Iringa, napongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imetokea nimepata huduma kwa baadhi ya Makamishna akiwemo Kamishna wetu wa pale Iringa ndugu Mtui, Kamishna Msaidizi wa hapa Dodoma ndugu Kabonge na Kamishna wa Dar es Salaam ndugu Kayela. Ni watu ambao wanafanya kazi vizuri na ni wasikivu, naamini na Makamishna wengine wote wanafanya kazi vizuri chini ya Kamishna wao ndugu Mathew ambaye kwa kweli ni mtu ambaye kama una jambo la wananchi wako anakusikiliza vizuri. Hivi ndivyo ambavyo inatakiwa tufanye kazi katika kuwahudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi napenda kusema kwamba migogoro mingi ambayo watu wengi wameisema tunaweza tukaitatua tukiwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi na tukiiwezesha ipasavyo Tume yetu ya Matumizi Bora ya Ardhi lakini na hizo ofisi zetu ipasavyo, kwa sababu bila kupanga kupima na kumilikisha bado migogoro itaendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Tanzania tuna square km 945,087 wakati nchi kama Vietnam wao wana square km 391,690 lakini hawana migogoro, maana yake ni kwamba ardhi tunayo bwerere lakini kitu kinachotushinda pengine ni kuipangia matumizi bora ambayo itatuwezesha kupunguza migogoro. Ndiyo maana sisi Halmashauri ya Mji wa Mafinga tumejielekeza pamoja na kupima viwanja lakini tumeona ya kwamba tujielekeze katika kuwa na maeneo kwa ajili ya uwekezaji, kwa ajili ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenga sasa eneo karibu heka 700 kwa ajili ya Industrial Park, maana yake ni kwamba sasa tunakuja mbele ya Wizara kuomba mtuwezeshe tuweze kupima, kupanga na kumilikisha, tukishakuwa na hii industrial park maana yake ni kwamba Wawekezaji watakuja, vijana wetu watapata ajira, Halmashauri itapata mapato lakini na Serikali nayo itapata mapato katika ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kwa nini tumeamua hivyo, kwa sababu Mafinga na Mufindi ni Miji ambayo inakua kwa kasi, kuna viwanda vingi, lakini baadhi ya Wawekezaji wamejikuta wakati mwingine wanaingia katika mikono ya watu ambao sio waaminifu, pia wakati mwingine viwanda vinawekwa maeneo ambayo siyo vizuri kiusalama kwa sababu ni maeneo ya karibu na makazi ya watu, ni maeneo kwa sababu hayakupangwa kuwa ni maeneo ya viwanda kama Halmashauri tunashindwa kufikisha huduma muhimu kama za maji, barabara na hata wenzetu wa TANESCO inawawia vigumu kufikisha huduma ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Wizara ituangalie Mafinga kwa macho mawili, katika suala hili la Industrial Park na kwa kweli tumedhamiria, hapa ninapozungumza Mkuu wangu wa Wilaya Ndugu Saada Mtambule pamoja na timu ya Mkurugenzi wapo EPZA kuweza kujifunza, kwa sababu tunataka kuwa modal ambao tutakuwa na Industrial Park ambayo itakuwa suluhisho pia kwa ajira za vijana wetu. Kwa hiyo ninawaomba sana Wizara ituangalie kama itakuwa ni grant, ama utaratibu wowote ambao utaona inaweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga, kupima na kumilikisha kunasaidia mambo mengi, kwa mfano kunaipunguzia Serikali gharama wakati ambapo ingekuwa imepanga hatuwezi kuingia kwenye gharama za kujipa hizi fidia, pia mara nyingi inapunguza migogoro, tukipanga pia tunakuwa na maeneo kwa ajili ya huduma mbalimbali. Kwa mfano, hapa katika eneo letu la Bunge, utaona ya kwamba eneo hili kadri huduma zinavyohitajika unaona kabisa tunahitaji eneo kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukijadili hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo hili lilijitokeza kwamba tuone umuhimu wa kuongeza au kupanua eneo hili la Viwanja vya Bunge, jambo hili kwa mujibu wa maelezo ilielezwa ya kwamba linapelekwa Wizara ya Ardhi ili wenzetu watusaidie kufanya uthamini ili kuona uwezekano kwa mujibu wa taratibu za Serikali kama wanaotuzunguka tunaweza tukawalipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo, maeneo haya ya Bunge humu ndani tuna Muhimili wa Bunge, tuna Mheshimiwa Spika ambae ni Kiongozi wa Muhimili, pia yupo Mheshimiwa Waziri Mkuu ambae ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali pamoja na Mawaziri wake, yupo Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Watumishi wa Serikali, kwa mfano leo hii wako Makamishna, wako watu wa Wizara ya Ardhi. Vilevile wakati Mheshimiwa Rais akija hapa kuhutubia Bunge au wakati wa Bajeti Kuu, Viongozi wengi wa Taifa letu huwa wanakuwepo hapa katika Viwanja vya Bunge kwa maana ya kwamba Serikali huwa iko hapa. Wanakuwepo viongozi wastaafu, wanakuwepo viongozi wa vyombo vya dola, wanakuwepo Viongozi Wakuu wa Chama cha Mapinduzi sasa mimi nalitazama hili katika jicho la kiusalama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa jinsi ilivyo ndiyo maana nashauri kwamba mchakato huu wa kuongeza eneo la Bunge uende kwa haraka kwa sababu gani, tufikirie Serikali yote iko hapa, kama mtu ana nia ya kufanya jambo baya just ukitoka tu hapa mlango wa geti la Waziri Mkuu tayari unakuta pale ni maeneo ambayo ni maghala, kwa mfano mbele pale kuna maeneo ambayo ni bohari ya mafuta ambayo hata kiusalama kama limetokea jambo, is high risk na katika usalama wanasema, katika security huwezi ku-compromise mambo ya gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ninaomba wenzetu wa Wizara ya Ardhi pale ambapo wana wajibu wa kutusaidia kufanya tathimini na kufanya uthaminishaji basi wakamilishe hilo zoezi ili kusudi Bunge yale maeneo ambayo yanayotuzunguka yaweze kuchukuliwa kwa mukhtadha wa hilo jicho ambalo nasema ni jicho la kiusalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata jicho la kihuduma wananchi wetu wanakuja hapa kutaka kupata huduma mara nyingi the most you can do wakipata kibali wataingia watakusubiri kule kantini. Nakumbuka wakati wa mgogoro wetu wa nguzo na Serikali walipokuja watu wa nguzo ilibidi tukae pale kantini, lakini tukamuomba OS wa Bunge akatusaidia tupate ofisi tujadili lile jambo na Mheshimiwa Waziri wa Nishati na baadaye likapata suhuhisho. Kwa hiyo, hata kihuduma vinginevyo utakuta tunakutana na wananchi wetu kule nje kwenye magari ili tusikilize hoja zao, kama wanataka kumwona Waziri kwa hiyo pia kihuduma na kiusalama ninashauri sana kile kipengele au ile section ambayo wenzetu wa Wizara ya Ardhi wanalifanyia kazi walifanyie kazi kwa haraka na tuende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kutoka mwisho ni suala la Baraza la Ardhi. Wananchi wa Mufindi wanalazimika kusafiri kwenda Iringa wanapokuwa na shughuli zao za masuluhisho ya masuala ya ardhi, nimwombe Mheshimiwa Waziri na Serikali, imefika wakati sasa tuwe na Baraza la Ardhi pale Mafinga ambalo litahudumia Wilaya ya Mufindi, kwa sababu mtu kutoka Mgololo, Kitasengwa, Bumilahinga, Itimbo kwenda Iringa ni mbali, kwa hiyo ninaomba wizara ione na sisi kama Wilaya tuko tayari kutoa jengo kwa ajili ya huduma hiyo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kwa dakika moja ninaomba Serikali ingalie watu wanapouziana ardhi, zile gharama tunazolipa ili kufanya transfer kwa kweli watu wengi wananunua ardhi, kama mimi nikiuziana na Mheshimiwa Bonnah hapa, kwa sababu tunaaminiana naogopa kuhamisha ule umiliki kwa sababu ya zile gharama, hebu tuziangalie ili watu wafanye transfer na baadae weweze kulipa kodi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nasisitiza tena kama nilivyosema asubuhi Mungu abariki viongozi wetu, Mungu abariki Taifa letu Mungu abariki Mafinga pia. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ambayo pia mimi ni mjumbe wa Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema lolote kwanza nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na timu yake pamoja na maafisa wote ambao kwa namna moja au nyingine wameshiriki katika kufanikisha hotuba hii ya bajeti. Lakini pia wanafanya kazi nzuri sana ya kupokea wageni, ya kuratibu ziara za Mheshimiwa Rais na viongozi mbalimbali katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi niseme jambo moja nimeona katika michango yetu baadhi yetu Wabunge na mimi kama Mbunge, lakini hasa kama Mjumbe wa Kamati ningependa kuliweka sawa kwa sababu wananchi wanatusikia sasa tusije tukaenda nje ya mjadala katika suala zima la uraia pacha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri sana tukaelewa kama Wabunge kwamba suala la uraia pacha pamoja na kuwa ni jambo la Kikatiba, lakini jambo linalokuja kwenye masuala ya uraia Wizara inayohusika ni Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwa hiyo, tusije tukawabebesha mzigo Wizara ya Mambo ya Nje katika jambo hili ambalo kwa kweli tumeshalisema mara nyingi lakini bado linarudi kule kule kwamba ni suala la Kikatiba lakini ni suala la Wizara ya Mambo ya Ndani kama linaamua kufanyiwa kazi katika mifumo ya Kiserikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende pia kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kama mwanadiplomasia namba moja, nimelisema hili mara kadhaa jinsi ambavyo anakuwa mwanadiplomasia namba moja kwa vitendo na kuitangaza diplomasia yetu ya uchumi. Tunaposema diplomasia ya uchumi maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba vile ambavyo tunaweza, tukatumia mbinu zote za kidiplomasia kama Taifa katika kutafuta maslahi mapana ya Kitaifa kama vile kutafuta wawekezaji, kama vile kufungua fursa za kibiashara, kama vile kutafuta masoko ya bidhaa zetu. Kwa mfano, sisi tunaotoka Iringa na Njombe tumeona kabisa kwamba tumefungua fursa za mazao kama vile mazao ya misitu lakini pia na zao la parachichi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hiyo ni kazi kubwa sana inayofanywa na mwanadiplomasia namba moja ambaye ni Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan, lakini pia kuvutia wawekezaji na mimi ninasema haya ni mmoja wa wanufaika wa diplomasia hii ya uchumi ambao Mheshimiwa Rais kama mwanadiplomasia namba moja anaitendea haki. Sisi katika Jimbo la Mafinga tuna wawekezaji wengi ambao wamekuja kutokana na Taifa letu kutangazwa kupitia hii diplomasia ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hivyo tu kupitia mwanadiplomasia namba moja kama Taifa pia tunanufaika, tunapata mikopo ya riba nafuu, yako maeneo tunapata misaada au kama grants lakini pia tunapata fursa za kimasomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa uniruhusu nitoe mfano, sisi watu wa Iringa tukiongozwa na Mheshimiwa William Lukuvi kwa miaka mingi sana tumesema kuhusu barabara ya kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park, hivi juzi tumeona Benki ya Dunia imetoa mkopo wa riba nafuu wa trilioni 1.2 ambao mkopo huu sio tu kwamba utatunufaisha sisi watu wa Iringa kwa kujenga barabara ile ya kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park, lakini pia yako maeneo yatakayonufaika na ungeniruhusu niyataje machache kuonesha jinsi ambavyo mwanadiplomasia namba moja kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje kazi inavyofanyika inatuletea manufaa katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkopo huu wa trilioni 1.2 kutoka Benki ya Dunia, pamoja na mambo mengine utaenda kujenga barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi ya urefu wa kilometa 201; utajenga barabara ya Rusahunga – Rusumo kilometa 92; utajenga barabara ya Songea – Rutukila kilometa 111; lakini pia utaenda kujenga hiyo barabara ya Iringa kwenda Ruaha National Park pamoja na kujenga viwanja vya ndege vya Lake Manyara, Iringa na Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii ndio maana halisi ya diplomasia ya uchumi kwamba, kupitia ziara hizi mbalimbali, kupitia makubaliano mbalimbali tunafungua fursa za kibiashara, lakini pia fursa za kimikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Mheshimiwa Rais alipoenda Dubai Expo 2020 kule, tumeona mikataba na hati za makubaliano 37 zilisainiwa ambazo pamoja na mambo mengine zitaendelea kufungua hizo fursa na hapa mimi kama zao la Wizara ya Mambo ya Nje nipate kupata ufafanuzi kidogo kwamba tunaposema hati na makubaliano watu wengine walikuwa wanajaribu kubeza kwamba hayo si ni makubaliano tu, kumbe katika nyanja ya kidiplomasia huwezi kufanya jambo lolote kabla kwanza hujafanya makubaliano yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndio maana nitumie nafasi hii kupongeza Ubalozi wa Abudhabi pamoja na Dubai kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali kufanikisha maonesho hayo ya Dubai Expo, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza Balozi Mbelwa Kairuki ambaye kupitia majadiliano na makubaliano mbalimbali Taifa letu limekubaliwa kuingiza muhogo na soya katika soko la China. Huwezi tu ukaingiza hizo bidhaa bila kufanya makubaliano mbalimbali, yote haya yanatokana na kazi nzuri inayofanywa katika dilpomasia ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uniruhusu pia kupongeza kwa kufunguliwa Ubalozi wa Lubumbashi, nakumbuka toka nimekuwa Mbunge hapa mwaka 2016 na wewe ukiwa Mwenyekiti wetu kuanzia kwenye Kamati, tumeshauri sana na hatimaye Ubalozi mdogo Lubumbashi umefunguliwa. Hii ni manufaa kwetu ikiwemo watu wa Iringa ambao pale Lubumbashi kwenye mpaka wa Mokambo zaidi ya malori 400 kwa siku yanaingia katika nchi ya Congo. Kwa hiyo, tumefungua masoko mbao zetu kutoka Mafinga zimepata soko Lubumbashi. Na sasahivi DRC imekuwa sehemu ya Afrika Mashariki, tuna imani kwamba, tutaendelea kunufaika na soko hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nitoe ushauri, kazi yetu ni pamoja na kushauri; pamoja na changamoto za kidunia baadhi yetu wamesema iko sasa sababu ya kufikiria kama Serikali na mifumo mingine ya Kiserikali kuona umuhimu wa kufungua ubalozi katika nchi ya Iran. Iran imepiga hatua sana katika suala la textile industry na sisi hapa tunalima pamba, tunaweza tukajikuta kwamba tunafungua fursa sio tu za kibiashara, lakini pia fursa za kugawana uzoefu katika eneo kubwa la viwanda, hasa hususan viwanda vya nguo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa pili; niishauri sana Wizara mambo mengi tukitaka tufanikiwe tupitie zile tume za ushirikiano za pamoja kwa maana ya kwamba tume za kudumu kwa maana ya zile JPC. Kupitia hizi mambo mengi yatanufaisha nchi yetu na Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa tatu; kama Wizara ningeshauri sana Wizara i-take lead katika kuhakikisha kwamba kama Taifa tunanufaika na mifuko mbalimbali katika dunia inayotoa fedha katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki kule Glasgow kwenye mkutano wa mazingira na aliwaambia wakubwa wa dunia ambao kwa sehemu kubwa wanaongoza katika kuchafua mazingira kwamba waheshimu zile ahadi zao na kwa uchache nitaje, kuna mifuko kama Green Climate Fund, Africa Climate Change Fund ambao uko chini ya Benki ya Maendeleo ya Afrika, kuna Adaptation Fund, kuna mifuko kama Climate Investment Fund, na kadhalika iko mifuko mingi.

Kwa hiyo, niiombe Wizara, Rais wetu ameshiriki kule kikamilifu na kwa kweli alikuwa ni miongoni mwa viongozi waliohutubia. Sasa Wizara itusaidie katika kuratibu kama Taifa tunaweza tukanufaika vipi na fedha hizi za mifuko ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Iringa, watu wa Mafinga, watu wa Njombe, tunalima, kwa mfano mwaka huu kutokana na matatizo ya mvua tutaelekeza kilimo chetu kwenye kilimo cha mabondeni, kilimo cha vinyungu kwa hiyo, tukinufaika na mifuko hii itakuwa ni fursa kwetu nzuri...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Chumi kwa mchango mzuri.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya naunga mkono hoja na kama kawaida nasema Mungu atubariki sote na Taifa letu. (Makofi)
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi japo nilikuwa najua nina dakika kumi, nimeshtukiziwa ziko tano, anyway nitajaribu kuzitumia hivyohivyo. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuunga mkono na kupongeza Serikali kwa maamuzi yake ya kufungua Balozi katika nchi sita ikiwemo Israel, Korea, Algeria na nyinginezo pamoja na Uturuki. Itakumbukwa wakati fulani hapa alipofanya ziara Mfalme wa Morocco ilitokea hali kama ya sintofahamu kwamba kwa kuwa sisi tunaunga mkono Polisario inakuwaje tunapokea ugeni kutoka Morocco, lakini nieleze tu kwa uzoefu wangu kwamba misimamo mbalimbali haikuzuii kuwa na bilateral relations ndiyo maana hata Polisario headquarters yao ipo Algeria, lakini bado wana uhusiano Algeria na Morocco. Vivyo hivyo sisi msimamo wetu kuhusu PLOunajulikana lakini ndiyo maana tunafungua Ubalozi Israel kwa sababu tunapokwenda kujenga uchumi wa viwanda lazima tufungue milango zaidi ya kiushirikiano na nchi ambazo zimepiga hatua katika nyanja mbalimbali, mfano nchi ya Israel wako mbali katika teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji, kwa hiyo naunga mkono sana jitihada hizo za Serikali. Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema kwenye Kamati na mimi ni Mjumbe wa Kamati, kuchanganya fedha za ziara za viongozi na fedha za Wizara zinaonyesha picha kubwa kwamba Wizara hii ina fedha nyingi, lakini kumbe fedha zile siyo za kwake, matokeo yake Wizara inashindwa kufanya kazi nyingi za msingi. Mfano mmojawapo ni ukarabati wa majengo ya Kibalozi, tuna eneo kule Maputo ambalo tumepewa na Serikali ya Msumbiji toka mwaka 1978, liko eneo ambalo ni prime, lakini mpaka leo halijajengwa. Sasa ni muhimu sana Serikali ikaanza kuangalia maeneo kama hayo ambayo ni prime lakini tumepewa zaidi ya miaka karibu 40 sasa hivi, tuone tunayafanyaje ili hata wale waliotupa wasije wakajatua kutupa. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu mikataba; ukiangalia katika ripoti ya Kamati mikataba zaidi ya 43 bado haijaridhiwa na Bunge na hapa niseme jambo moja, Wizara ya Mambo ya Nje kazi yake ni kuratibu masuala haya, ninaishauri Serikali tuwe na kitengo maalum kama kitakuwa chini ya Waziri Mkuu au Ofisi ya Rais ambacho kitakuwa kinafuatilia masuala yote kama haya. Tumeona mikataba mingi inasainiwa, lakini Wizara za kisekta zinashindwa ku-finalize kuifanya ile mikataba ifikie hatua ya kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuifikisha kwenye Bunge letu kwa ajili ya kuridhia. Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuondokane na jambo hilo pengine tungekuwa na kitengo maalum, kwa sababu ninavyofahamu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje hawezi kumuagiza Katibu Mkuu wa Kilimo au Viwanda na Biashara kwamba jambo hili mbona halijatekelezwa, lakini tukiwa na kitengo maalum cha kufuatilia masuala kama haya inaweza ikatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo pia linagusa Wizara ya Fedha, wawekezaji wengi ukizungumza wanalalamika sana kuhusu double taxation na protection of investment. Ukizungumza na Jumuiya za Kibalozi zinasema kwamba wawekezaji wao wangependa kuja kuwekeza lakini kwa sababu hatuna mikataba ambayo inaruhusu double taxation kuondolewa na protection of investment inawa-discourage. Kwa hiyo, niombe Wizara ya Fedha ishirikiane na Wizara ya Mambo ya Nje kwa ukaribu kwa sababu hata kama tunataka kukusanya pesa tu bila kujenga misingi imara ya wapi tutakusanya tutakuwa hatuwezi kufikia malengo tunayokusudia. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho au la pili kutoka mwisho kutokana na dakika chache nilizonazo ni kuhusu wahamiaji hasa wale ambao tumewapa uraia kule Ulyankulu. Kwa kweli Serikali ya Mkoa wa Tabora na Serikali ya Wilaya ya Kaliua inatumia muda mwingi na resources nyingi katika kuhangaika na masuala yaliyopo kwenye maeneo yaliyokuwa ya wakimbizi ya Ulyankulu. Kwa jinsi tulivyotembelea Kamati wanasema, sijui kama lugha hii itakuwa nadhifu, lakini jambo lile ni kama vile kumbemenda mtoto, sasa ku-deal nalo its very delicate. Tumewapa watu uraia, wanataka kuwa na nchi ndani ya nchi, sasa jambo hili tujifunze wakati ujao, sisi tulikuwa nchi ya kwanza kutoa uraia kwa watu wengi duniani kwa wakati mmoja, tutizame jambo hilo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ruzuku kwa wananchi wanaokuza miche ya miti na wanaopanda miti Mafinga. Wananchi wa Mafinga na Mufindi kwa ujumla wamekuwa hodari katika kupanda miti na kutunza mazingira kwa ujumla. Hata hivyo, wananchi hawa kwa kiasi kikubwa wameachwa kama yatima hasa kutoka katika Wizara hii. Angalau Maliasili na Utalii kupitia Shamba la Sao Hill wamekuwa wakitoa mbegu (miche) kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuunga mkono juhudi za wananchi wa Mafinga na Mufindi kwa ujumla, Wizara hii ije na mpango wa kutoa ruzuku kwa wananchi wanaojishughulisha na upandaji wa miti. Suala hili linaweza kuwa kichocheo kwa wananchi wa maeneo mengine hapa nchini kuona umuhimu sio tu wa kupanda miti kwa mazoea kama ilivyo hivi sasa. Ruzuku kwa wakulima/wananchi wanaopanda miti itakuwa kichocheo kikubwa cha lengo la kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya kijani (ukurasa wa tisa (9)).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Usimamizi wa Mazingira; kutokana na ongezeko la majukumu, ni wazi kuwa NEMC imezidiwa kutokana na uhaba wa watumishi. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana hata elimu ya mazingira kwa umma imekuwa haifanyiki ipasavyo. Naishauri Serikali ione haja sasa ya kuongeza watumishi katika ofisi hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upandaji miti bila kuitunza ni bure; nchi yetu imekuwa na kampeni kubwa ya upandaji miti, tukiwa realistic ni asilimia ndogo mno ya miti iliyopandwa ambayo inaendelea kuwepo. Nashauri Wizara ibadilishe mikakati ili tusiishie tu kuwa tunapanda miti bila kuitunza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwa siku ya leo pamoja na kuwa sauti yangu haipo vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali kwa sababu ya kupokea maoni ya Wabunge na maoni ya wadau; na kurejesha Tume ya Mipango lakini kuja pia na hii Wizara ambayo inaongozwa na Profesa Kitila Mkumbo ambaye wakati naanza Chuo Kikuu cha Dar es salaam alikuwa Rais wangu wa DARUSO na mimi nikawa Mbunge kwenye Bunge la Wanafunzi. Tulikuwa tunachuana sana pale USRC nadhani unakumbuka Makamu wako wa Rais akiwa Dkt. Francis. Kwa hiyo, nakufahamu kwa utendaji toka siku zile tukiwa pale Chuo Kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa na Mheshimiwa Kibajaji, Mheshimiwa Lusinde tulikuwa tunaenda Iringa, Mafinga kwenye shughuli pale Bwawani kwa Mchungaji Mahimbi na wachungaji wale walisema wao kama viongozi wa dini wapo na Serikali na mojawapo ya kazi wanayoifanya ni kuombea Serikali lakini pia kumuombea Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tupo na watu wanatuombea katika nchi hii sisi kama viongozi kwa hiyo ni wajibu wetu kutenda yaliyo mema kwa manufaa ya nchi hii. Siku ile ninapoongozana na Mheshimiwa Lusinde, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu akaniambia naona mmejichagua, sikumwelewa. Baadaye akaniambia si naona mnaenda wote simba huko Mafinga mmechagua, wewe simba Mheshimiwa Kibajaji nae simba. Sasa mimi baadaye nikakaa nikaona alah! Kumbe Waziri wa Mipango naye yanga, Waziri wa Fedha naye yanga, of course mmeteuliwa lakini imetokea nyinyi nyote yanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni simba inaeleweka niwaombe kabisa fanyeni kama yale ambayo wanafanya Max Nzegeli na Pacome katika utendaji wa kazi ndani ya Serikali, nadhani mtakuwa mmenielewa vizuri najua wana simba wenzangu hawawezi kunikubali katika hilo lakini kuna hatua tukifika lazima tukubali ili tujipaange kwa hiyo, tumekubali yote tunajipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili. Kuna mtu juzi alikuwa ananiambia naona Wabunge Bunge hili mmechachamaa nikamwambia kwa nini? Akasema ingekuwa wakati wote mko hivi hivi, nikamwambia hapana inategemeana na agenda ya wakati huo. Kwa mfano, wakati ambapo yamefanyika mambo ya kupongeza tutapongeza, wakati mambo ya kusahihisha tutasahihisha, ndiyo wajibu wetu kama Wabunge. Kwa hiyo, kwa wakati huu kwanza mimi nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake na yakupongeza yapo mengi lakini mimi kwa niaba ya Wanamafinga nitasema moja tu maana yake naweza nikamaliza muda wangu kabla sijaenda kwenye hoja ya kuchangia mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja la kupongeza ni suala katika elimu, sisi pale Mafinga tuna shule ya msingi Mwongozo; ilikuwa na watoto kama 1800. Tumepata fedha tumejenga pembeni Shule ya Msingi Muungano, tumepunguza msongamano kwa watoto lakini Kata ya Boma ambayo ina watu wengi kuliko watu wote katika Mkoa wa Iringa kwa mujibu wa sensa na hapa pia nitumie nafasi hii kuwashukuru watu wa takwimu, walikuja kutujengea uwezo watu wetu namna ya kutumia takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alisema jana Mheshimiwa Profesa Shukrani nadhani hapo, kwamba ile sensa ikatusaidie katika kutumia takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo; na kuna kitu wale watu wa sensa walitufundisha pale tulikuwa na viongozi wa dini na wazee na wakaanisha kata gani ina vijana wengi, kata gani ina wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tulijifunza kwamba hii kata yenye vijana wengi maana yake inabidi mipango mingi ya kuweka shule nyingi ielekezwe kule kwa sababu hao ni vijana ambao population wise wao wapo kwenye stage ya kuongeza idadi ya watu duniani. Lakini viongozi wa dini mmoja aliniambia; Mbunge nimejifunza hapa kwamba lazima nijue waumini wangu wazee ni wangapi, vijana ni wangapi, watoto ni wangapi hata tunapopanga mipango ya maendeleo ya kanisa letu au ya msikiti wetu basi tunaendana na ile takwimu na mtawanyo wa idadi ya watu katika eneo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza pia watu wa sensa. Kwa hiyo, nampongeza pia Mhehimiwa Rais katika elimu tumeona madarasa, ukienda Itimo pale kwetu Mafinga, ukienda Ndolezi, sabasaba na pale Ndolezi Kata ya Boma tuna shule mpya ya sekondari ambayo ita-accommodate sasa hawa watoto wanaotoka kwenye shule hizi za msingi. Kwa hiyo, itoshe kusema kwamba sisi kama Wabunge na hasa Wabunge wa CCM pale pa kukosoa na kusahihisha tutasema na pale pa kupongeza tutasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye mpango. Mimi nimesoma mpango na kwa jinsi ya mpango ulivyo maana yake ni kwamba ni wajibu wangu kama Mbunge kutoa maoni na mapendekezo kama ambavyo umesema mpango. Sasa yapo mambo nitashauri kwa maana katika hii matarajio au maoteo ya bajeti ya trilioni 47 ina mtawanyo wake kuna deni la Taifa kuna mishahara kuna OC na kuna mambo ya maendeleo; na fedha hizi tutazitoa wapi? Tutatoa mapato ya ndani ya kodi na yasiyo ya kikodi, ninawapongeza TRA wamekuwa wakikusanya vizuri unaona yale maoteo wakati mwingine wanavuka zile asilimia, kuna fedha ni mikopo na misaada kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe ushauri. La kwanza katika ukurasa wa 11 wa paper ile ya Mheshimiwa Mwingulu ukurasa wa nane amesema kwamba, Mikakati. Amesema baadhi ya mikakati ni ile kuwa na one stop center ili kuboresha mifumo ya ukusanyaji pamoja na kutoa namba ya malipo jumuishi. Sasa hapa nimuombe Waziri wa Maliasili na Utalii na Waziri wa TAMISEMI, sisi Mafinga Mufindi tunategemea misitu na tunategemea msitu wa Sao Hill. Sasa wakati mipango ya Serikali ni kuwa na one stop center maeneo ya kukusanya mapato kwa jumuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi utaratibu uliokuwepo, kama mimi nikipewa ile bili na TFS kwa maana ya shamba la Sao Hill ninakwenda kulipa mle mle ndani nalipa na fedha za Cess na fedha zingine katika ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa TFS wamekuja na utaratibu kwamba ile Cess awepo mtu wa halmashauri ya Mufindi wa Halmashauri ya Mafinga pale kwenye shamba la Sao Hill awe anakusanya. Sasa tunasema makusanyo jumuishi, one stop center kwanza tunatawanya nguvu na resource; lakini pili hatuwezi kukusanya ipasavyo. Kwa hiyo, mimi naomba na ninashauri TFS na Waziri na Wizara ya TAMISEMI tuendelee na ule utaratibu kwa sababu ndiyo maona ya Serikali lakini ndiyo utaratibu ambao una ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina ugomvi na TFS na wala sijawahi kuwa na ugomvi nao naamini katika hili tukishauriana vizuri tuendelee na ule utaratibu mtu akipewa bili alipe na kwanza hata yule mlipaji unampunguzia usumbufu. Sambamba na hilo ili tuboreshe na kuongeza makusanyo, ninashauri ndugu zangu tuangalie pia kwenye VAT sio tu kwenye mambo ya misitu hata katika upana wake tujaribu kuona je, hatuwezi kupunguza ikawa user friendly watu wakalipa kwa wingi wakalipa kwa hiari kama ambavyo tumesema hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kutoka mwisho. Wapi fedha nyingine tutapata, amesema hapa Mheshimiwa Kakoso, ninawashauri watu wa Serikali, nendeni kwenye Hansard kasomeni haya mambo ya hewa ya ukaa aliyosema Mheshimiwa Kakoso. Labda watu hawaelewi hewa ya ukaa maana yake ni nini? Sisi wenye misitu, kuna kitu ukanda wa bahari kinaitwa blue carbon, ile pale misitu kila inachopumua wale wenzetu wenye viwanda ndiyo inasaidia at least kwenye mambo ya climate change ku-regulate hii hali ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna fedha na Mheshimiwa Rais kila mwaka anaenda kwenye mkutano wa mazingira. Kwa hiyo, tayari kama mkuu wa nchi tayari ameshatoa hiyo sapoti. Kwa hiyo, wenzetu tushirikiane kwenye hewa ya ukaa kuna fedha kwenye mikopo, kuna fedha kwenye misaada lakini kuna fedha kwenye biashara hiyo ya mkaa. Ninaomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho. Timu yetu ya JKT Queens mimi ni mwanamichezo jana imeshinda ipo kule Adjan wakiwa na Masau yule msemaji na ikifanikiwa kwenye mchezo ujao ikatoka sare itaingia nusu fainali. Kwa hiyo, tunavyounga mikono michezo, tuangalie Simba na Yanga lakini tuunge pia mkono JKT Queens ambao wachezaji asilimia mia moja ni wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na kama mwanasimba nasema tumekubali tunajipanga. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na napenda kutumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya tulizonazo humu ndani. Pia kwa niaba ya wananchi wa Mafinga, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru Serikali na Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake wote kwa jinsi ambavyo tunaendelea kuijenga Mafinga. Hivi karibuni tulikabidhi gari la kubebea wagonjwa pale kwenye Kituo cha Afya cha Ifingo, kama hatua za kuboresha huduma za afya kwa wananchi wetu wa Jimbo la Mafinga Mjini ambalo pamoja na kuwa lina hospitali ambayo ni kama vile inahudumia Wilaya nzima na wilaya za jirani, lakini pia ipo kando ya barabara kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kupata ambulance ile maana yake ni kwamba inaenda kutusaidia kurahisisha utendaji. Hata hivyo, natumia nafasi hii kuomba gari kwa ajili ya kufanya tathmini. Nilizungumza na Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Festo Dugange, alinihakikishia kwamba tutapata wasaa wa kulijadili jambo hilo na kuona ni kwa namna gani watatusaidia watu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga kupata gari kwa lengo lilelile la kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia pia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake kwa Hotuba nzuri ya Bajeti. Naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla, kwa kuja na hii Idara inaitwa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali. Idara hii nimeona hapa kulikuwa na watu wa CAG, kwa namna fulani Idara hii inaisaidia Serikali kufanya monitoring ya utendaji wa kila siku wa shughuli za Serikali, hususan katika kufuatilia utekelezaji wa miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, tofauti na siku za nyuma ambapo tungesubiri pengine mpaka mwisho ndiyo mradi uje ufanyiwe tathmini, lakini idara hii inafanya ufuatiliaji wa kazi kadri zinavyoendelea. Kwa hiyo, kama kuna mapungufu maana yake ni kwamba yatafanyiwa kazi wakati ile kazi inaendelea ili kuipunguzia Serikali hasara ambayo pengine ingekuwa imejitokeza. Kwa maana nyingine, hii ni kama vile tunasema prevention is better than cure, yaani kwamba hii badala usubiri kutibu, basi yenyewe inaanza kuchukua tahadhari mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo naomba kuishauri Serikali. Kwa sababu hii ni Idara muhimu sana ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji wa Shughuli za Serikali, naomba mambo mawili muhimu. Kwanza, ili itimize wajibu wake kiufasaha na malengo yaweze kutimia, lazima tuiongezee nguvu kazi. Nguvukazi ya watu kwa maana ya watendaji, nguvukazi ya vitendea kazi na nguvukazi ya rasilimali fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kusisitiza jambo hili kwamba, ili iwe na thamani na maana halisi ya kuanzisha Idara hii, basi tuifanye kwa vitendo kwa maana ya kuiongezea watendaji, kuiongezea vitendea kazi na kuiongezea nguvu ya fedha. Kwa sababu, kazi inayofanya ni kuokoa mamilioni na mabilioni ya fedha za Serikali ambazo kama isingekuwepo, kama ingekuwa haifuatilii na kama itashindwa kufuatilia kama lengo lilivyo, maana yake ni kwamba tutashindwa kuokoa hizo fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo ningependa kushauri na kulizungumzia ni kuhusu kazi na ajira. Mojawapo ya kitu muhimu ambacho kinaweza kuimarisha suala zima la upatikanaji wa ajira ambazo ni rasmi na za kujiajiri, ni pamoja na uwepo wa miundombinu madhubuti. Kwa hiyo, nashauri sana, pamoja na kazi nzuri ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu imeifanya katika hizi siku za karibuni kukabiliana na maafa kutokana na mafuriko, kutokana na miundombinu ya maeneo mbalimbali ya barabara kuharibika, naomba na kushauri, hili liwe kama funzo na fundisho kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba huwa tunakuwa na fedha ya dharura na inawezekana bajeti yetu ikawa ni finyu kiasi kwamba tusiwe na fungu kubwa la dharura, lakini maafa yaliyojitokeza mwaka huu, yawe funzo kwetu na tujielekeze kwa kiwango kikubwa kuwa na fedha za dharura especially kwa ajili ya miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Sasa hivi ilivyo kama sehemu ya watu kujiajiri, nchi yetu asilimia kubwa ni wakulima. Leo hii miundombinu maeneo mengi hakuna mawasiliano. Nitatoa mfano tu, pale Mafinga Barabara ndogo tu ya kutoka Uguta kwenda Kikombo kalavati limezolewa na maji. Maana yake ni nini; wananchi kutoka Mafinga kwenda Kikombo kupeleka bidhaa watashindwa kwenda ama itabidi watumie safari ndefu kuzunguka maeneo ya Rungemba na Kitelewasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, wananchi hawa kutoa mazao yao kuyapeleka sokoni Mafinga Mjini, ama watashindwa kama mazao yao ni mali mbichi zitawaharibikia au itabidi wazunguke kwenda Rungemba ili wafike sokoni, maana yake tunawaongezea gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, maeneo kama kwenda Bumilayinga, maeneo kama ya Mtula ambako kuna Skimu ya Umwagiliaji, kama hakuna miundombinu ya uhakika maana yake ni kwamba kuhusu kipengele kizima cha kazi na ajira, hakitakuwepo kwa sababu hakuna movement, kutakuwa hakuna ajira kwa sababu hakuna movement.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, hata matengenezo ya magari leo hii watu wa vibasi kama hiace wanaokwenda Mufindi kwa pale Mafinga, anatumia masaa mengi kufika kwenye kituo anachokwenda, lakini akienda akirudi atakuwa na gharama kubwa sana za ku-service chombo chake. Kwa hiyo, hata kile alichokipata kama sehemu ya kujiajiri na chenyewe chote kinapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu; tuwekeze katika miundombinu na ikiwezekana sijui kama nitaeleweka, lakini katika bajeti ya mwaka huu, kama kuna kitu ambacho inabidi tukiwekee macho mawili ni sehemu ya kuimarisha miundombinu. Leo hii Mafinga, Mufindi hata maeneo ya Njombe, watu wanaofanya shughuli zao za msitu hawawezi kwenda msituni kusomba magogo au kufanya shughuli zao kwa sababu miundombinu na barabara hazipitiki kwa namna inayotakiwa. Kwa hiyo nguvu yetu na akili yetu kama Taifa tuwekeze sana katika miundombinu kwa sababu kwa kuwepo miundombinu imara maana yake ni kwamba tutakuwa tumejitengenezea ajira kwa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, yawezekana kabisa huu ukawa ni mzigo mkubwa sana kwa Serikali; ushauri wangu, tulipitisha hapa Sheria ya PPP, hebu tujaribu kuitumia sheria hiyo kuona kwa namna gani tuta-engage private sector katika kuimarisha na kujenga miundombinu. Nchi yetu ni kubwa, Serikali kwa hakika kama tutasema ijenge peke yake itachukua miaka mingi kuweza kuwa na miundombinu ya uhakika. Kwa hiyo tutumie utaratibu shirikishi wa kutumia sekta binafsi kujenga miundombinu katika baadhi ya maeneo. Naamini ni salama zaidi kwa wananchi kuongeza gharama kidogo, lakini wakafika kwa wakati na kwa usafiri wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho kwa kumalizia katika hili hili la ajira na kazi, naomba kuishauri na kuipongeza Serikali kwa mpango wa BBT. Sasa, kwa sababu hii ni programu, ushauri wangu bado naendelea kusisitiza ndani ya Serikali kushirikiana, JKT, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo tuone kwa namna gani tunaweza tukawashirikisha vijana ambao wanaenda JKT kwa nia ya kujitolea, wanapata mafunzo ya uzalishaji mali, mafunzo ya nidhamu na kwa namna gani tutawa-incorporate kwenye mpango wa BBT, naamini watakuwa na tija kwao kama sehemu ya kujiajiri, lakini pia watakuwa na tija kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni kuhusu Mradi wa TACTIC. Huu ni mradi wa kuboresha miji, manispaa na majiji kama ilivyo DMDP katika Jiji lako la Dar es Salaam. Mimi Mafinga na baadhi ya miji tupo awamu ya tatu. Ushauri wangu na ambao nimeutoa na nimeusema kila siku, kwa sababu mpango huu upo chini ya Benki ya Dunia na kwa sababu ni mkopo nashauri kwa kushirikiana na TAMISEMI Wabunge ambao tunatoka awamu ya tatu na ya pili tukutane ili tuweze kushauri kusudi mradi huu uweze kwenda kwa mapema na kwa haraka. Hii ni kwa sababu mradi huu pamoja na ujenzi wa barabara, lakini pia tunakwenda kujenga vitega uchumi ambavyo vitakuwa vyanzo vya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sisi Mafinga tunaenda kujenga Stendi pale Kinyanambo, tunakusudia kujenga soko kubwa la mazao ya misitu na pia tunakusudia kuimarisha na kuboresha soko letu. Hivi vyote vinakuwa ni vyanzo vya mapato ambavyo hatimaye vitaipunguzia Serikali mzigo. Kwa mfano, zile fedha ambazo zingeenda TARURA kama miradi itatekelezwa hii ya DMDP II na TACTIC maana yake kuna portion itatoka TARURA itaenda kufanya kazi sehemu nyingine kwa sababu miradi hii itakuwa tayari imetekelezwa chini ya mpango wa Benki ya Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, Mungu atubariki wote, Mungu aibariki Mafinga, Mungu aibariki Tanzania na nawatakiwa wote mchezo mwema siku ya Jumapili kati ya Simba na Yanga. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na pia namshukuru Mungu kuwa mchangiaji wa kwanza kwa siku hii ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya mchango wangu, nina mambo machache ya kusema ambayo ni ya kuipongeza Serikali na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu, mambo haya pamoja na kuwa ni ya kitaifa, lakini yanagusa maisha ya wananchi wenzangu wa mafinga. Baadhi ya mambo haya nitayataja kwa haraka kwa sababu ya muda na ni mambo yanayostahili kupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kiti kilishaongoza hapa ndani kwamba, vyovyote iwavyo hatutaruhusiwa kuruka sarakasi au kupiga magoti, kwa hiyo, mimi na wananchi wenzangu wa Mafinga, kesho saa 4:00 tumeamua kwa dhati ya mioyo yetu kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa haya ambayo nitaenda kuyasema hapa ambayo ametufanyia watu wa Mafinga. Sisi watu wa Mafinga maisha yetu ni misitu. Tumeona katika bajeti ya Serikali, baada ya kilio cha muda mrefu, hatimaye sasa VAT imeondolewa kwenye mti, jambo ambalo zamani hata mti ulikuwa unatozwa VAT. Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini kwa wananchi wetu wa Mafinga? (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, pale watakapoenda kwenye shamba la Sao Hill, kama ana bill ya kulipa shilingi milioni moja ambapo angelazimika kulipa 1,180,000, sasa 180,000 ni ahueni, itaenda kuongezeka kwenye mtaji. Pia, hata cess, kadhalika tumeondoa kutoka tano hadi tatu. Maana yake ni kwamba tumempunguzia mzigo pia mfanyabiashara wa mazao ya misitu, na Halmashauri nayo tumeibakizia kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la kilimo, sisi ni wakulima. Tumeona katika hotuba ya Mheshimiwa Bashe, zaidi ya shilingi bilioni 150 zitaenda kutolewa kama ruzuku kwa ajili ya wakulima wetu. Hili ni jambo la kupongeza sana kwa sababu linagusa maisha yetu na uhai wa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa pia niombe kwa Mheshimiwa Bashe, sisi watu wa Mufindi, pamoja na kilimo ambacho tutaenda kuanza mwezi wa Kumi na Moja, sasa hivi tukishavuna tu mwezi wa Saba, tunarudi mabondeni kwenye kilimo maarufu tunakiita kilimo cha vinyungu. Nacho tutaomba hiyo mbolea ya ruzuku, pale mwaka wa fedha utakapoanza basi taratibu zianze kwa haraka ili nasi tunapoenda kulima kile kilimo cha vinyunguni, ambacho kinasaidia sana kujazia kama kunakuwa na upungufu wa chakula, basi tuanze kunufaika na kufaidika na matunda mema ya Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, tumepata mradi wa miji 28, ambao ni mradi wa maji ambao tulizungumza hapa Bungeni zaidi ya miaka saba. Wiki mbili zilizopita nasi Wabunge wa miji 28 tulialikwa pale Ikulu, wakandarasi wameshapatikana, wameshasaini, wanaingia kazini. Maana yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupata mradi huu, maana yake ni kwamba, akina mama wa Rungemba, Kitelewasi na Matanana, muda ambao walikuwa wanaupoteza kwenda kutafuta maji, sasa watatumia muda ule kufanya shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, yako mambo mengi ya kusema pale Mafinga, ndiyo maana nimesema tumeamua kwa sababu ya muda, sisi wana-Mafinga kesho pale Mafinga tutafanya shughuli maalum ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake. Yako masuala ya nguzo ambayo ilikuja taharuki kwamba zitanunuliwa nje ya nchi, lakini baadaye tumekaa na Mheshimiwa January Makamba, tumekubaliana na Serikali, nguzo zitanunuliwa hapa hapa nchini na maisha ya wananchi wetu yataenda kupata ahueni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama vile haitoshi, katika miundombinu, naipongeza sana Serikali, tumeona Barabara ya Mafinga – Mgololo. Pamoja na Serikali kuwa na sera ya kuunganisha mikoa kwa mikoa, lakini Serikali imeona umuhimu wa barabara hii kwa sababu za kiuchumi; barabara ya Mafinga kwenda Mgololo na Nyololo mpaka Mtwango ambayo itasaidia sana kusisimua uchumi wa Taifa letu, na pia uchumi wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 35, ameeleza umuhimu wa kuwa na viwanda na vijana wafanye kazi saa 24. Nami naiomba Serikali, nimesema kwa miaka mitatu, minne, watu wa Mafinga tunaomba, watu ambao tunaishi kandokando ya barabara kuu kama Ruaha Mbuyuni, Tunduma, Mikumi, na Korogwe kwa shemeji zangu, turuhusiwe kufanya biashara saa 24. Hii Mheshimiwa Waziri nakuomba iwe kama ni sheria au kanuni au mwongozo. Kwa sababu, as it is now, tunafanya biashara saa 24 kwa kudra za kiongozi aliyepo eneo linalohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi tuna Mkuu wa Mkoa, Queen Sendiga, mwelewa sana, tuna Mkuu wa Wilaya, Saad Mtambule, mwelewa sana, tuna OCD mwelewa sana, walau anasema, jamani kusiwe na vurugu watu wafanye biashara wajiachie. Akija kiongozi ambaye sio mwelewa, kwa sababu hakuna sheria wala kanuni wala mwongozo, inakuwa tafrani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali itoe kama ni mwongozo au kanuni kwamba, baadhi ya maeneo watu wafanye biashara saa 24. Duniani kote watu wanafanya kazi kwa shift. Kama ulivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye viwanda unataka watu wafanye biashara saa 24. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais kupitia ile Royal Tour tunaamini kwamba kutaongezeka watalii wengi sana. Bajeti yetu asilimia 11.2 inategemea mikopo na misaada. Sasa kuna huu mradi wa Regrow, huu mradi wa kuendeleza utalii Kusini. Mradi huu ni fedha za mikopo kutoka Benki ya Dunia. Ni mradi ambao Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais, tarehe 12/2/2018 tuliuzindua pale Iringa. Mojawapo ya manufaa ya mradi huu ni kuboresha sekta nzima ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumza sasa mradi huu una miaka mitano, utekelezaji wake unaenda ukisuasua. Kwa mujibu wa kalenda ya utekelezaji, ilitakiwa kufikia sasa hivi iwe imeshatumika wastani wa Dola milioni 111, lakini mpaka sasa hivi kuna maeneo ya kuboresha. Kwa mfano, ku-upgrade viwanja vya ndege, kujenga barabara na kuimarisha mafunzo. Sasa katika mbuga zetu ikiwemo Mbuga ya Ruaha National Park, haya mambo yote yakifanyika, hata mimi wananchi wangu wa Mafinga watauza mbao, watauza milunda, watauza nguzo kwa watu wanaojenga mabanda kule kwenye National parks. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kwa miaka mitano unaenda ukisuasua, lakini bad enough huu ni mkopo. Kwa hiyo, tunapochelewa kuutendea haki maana yake hatupati returns kwa wakati, maana yake tutakuja kulipa mkopo ambao tumejichelewesha sisi wenyewe. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Maliasili na Utalii inayohusika na jambo hili, sasa lifanyike kwa speed. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kengele imelia, nimelisema sana suala ambalo kama Taifa tunaweza kunufaika na mifuko inayotoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mheshimiwa Rais alienda Glasgow akashiriki ule Mkutano wa Mazingira na akapata nafasi ya kuzungumza, akayaambia Mataifa makubwa kwamba tunaomba muheshimu ahadi zenu. Kwa sababu, Mataifa makubwa ndiyo wanaoongoza kwa kuharibu mazingira. Sisi huku tukipanda miti Mafinga, Mufindi na kwingineko, tunasaidia katika haya mambo ya carbon emission. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kifuko ambayo inatoa fedha. Sisi kama Taifa, juzi alisema Mbunge wa Kiteto, ni taasisi mbili tu, nami nazipongeza; NEMC na CRDB ndizo ambazo zinanufaika na hizi fedha. Hizi fedha nyingi ni grants wala siyo mikopo. Tupate hizi fedha, tunaweza kujengea miradi ya umwagiliaji kule Mafinga. Wananchi wetu tunaweza tukawapa miche zaidi ya kupanda tukakabiliana kwa namna moja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho au la pili kutoka mwisho ni hizi mamlaka za udhibiti. Kuna hizi taasisi, regulatory authorities; Mheshimiwa Mkapa Mungu amlaze mahali pema; Serikali ya Awamu ya Tatu iliona kuna umuhimu sana, nchi inayoendelea huwezi ukaacha mambo yawe holela holela, lazima uwe na vyombo vya ku-regulate hali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa vyombo hivi vingi unavikuta viko chini ya Wizara ambazo vyenyewe vinahusika kuzi-regulate. Tuna SUMATRA, LATRA, EWURA, TASAC, naomba mkasome literature za mambo ya regulatory authority. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, hivi vyombo vinapaswa viwe independent. Kama haviwi chini ya Ofisi ya Rais, basi viwe chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili vipate ile nguvu kweli ya ku-regulate. Leo hii huyu regulatory authority, huyu huyu anawajibika kwa Katibu Mkuu fulani au kwa Waziri fulani. Kama tuko open minded, tunataka kuisaidia nchi, hebu tutengeneze utaratibu hizi regulatory authorities zipate uhuru unaotosheleza ili kweli ziweze kufanya kazi hiyo ya ku-regulate uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, nawashukuru sana wote na wale ambao watakuwa wako tayari kuungana nami kesho Mafinga, karibuni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mungu awabariki na Mungu abariki Taifa letu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushukuru kwa kupata nafasi na pia nipende kuwapongeza Mawaziri wanaofanya kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Mheshimiwa Jenista alifika mpaka kule Jimboni Mafinga akazungumza na wajasiriamali na akina mama kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia Baraza la Uwezeshaji, pia ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde hakuwa na ziara rasmi lakini alivyopita pale akasimama stand akaongea na vijana kuwatia moyo, kwa hiyo, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunajadili hotuba ya Waziri Mkuu ambayo ndani yake kuna Bunge, moja kwa moja nizungumzie kuhusiana na ufanisi wa ufanyaji kazi wa Bunge. Tumeshuhudia siku zilizopita badala ya kukutana wiki tatu tumekutana wiki mbili. Kwa mujibu wa Katiba, wajibu wa Bunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali na sehemu mojawapo ya kuisimamia ni kupitia tunavyokutana kwenye
Kamati, lakini pia tunavyokagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali. Niombe bajeti hii pamoja na jinsi ambavyo tumeambiwa imeongezwa, iliangalie Bunge katika namna ambayo italiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aeshi amezungumza hapa kuhusu Bunge Sports Club, sisi tulioenda Mombasa kwenye mashindano ya Bunge tunajua kilichotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumechagua Wabunge wa EALA ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika masuala mazima ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo suala la michezo. Tumekwenda kule kuna watu tulikuwa tunapanda kwenye karandinga, huu ni ukweli mpaka kuna watu
wametuuliza ninyi ni Wabunge kweli maana we were seen like a second citizen wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niombe kwa nia ya kufanya kazi kwa ufanisi, tumeona hapa wakati wa kukagua miradi Wabunge wanasafiri na double coaster zinaharibika njiani. Hata security yao, pamoja na kuwa wanakuwa na maaskari mle ndani lakini kuna healthy
security, afya yao katika kusafiri kwenye mazingira ya magari ambayo basically yamejengwa kwa ajili kuwa school bus sio jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba ili Bunge lifanye kazi kwa ufanisi hebu kile kinachotengwa kipatikane. Kwa sababu sisi hatufanyi kwa kujipendekeza, tunafanya kazi kwa mujibu wa Katiba iliyowekwa. Naomba hilo tulitizame sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu pembejeo. Wamezungumza Waheshimiwa hapa na kaka yangu Mgimwa amesema. Tumesikia kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu amekutana na watu waliokopesha pembejeo, ni kweli matajiri wakubwa walikataa kuwahudumia
wakulima wetu, wafanyabiashara wadogo wadogo wakajitokeza. Kwa hiyo, mimi niombe baada ya uhakiki watu hawa walipwe pesa zao. Kwa sababu ni kupitia kilimo watu wetu kwa mfano mimi kule Mafinga kuanzia Bumilainga mpaka Itimbo watu wale hawana shida, wewe wape
mbolea tu ni wapiga kazi wazuri. Vijiji vyote Isalamanu na Kitelewasi watu wanalima mwaka mzima lakini wapete tu mbolea kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hawa ambao wamekopeshwa wapewe fedha zao kwa wakati ili kusudi wakati ujao waweze kuwa na moyo wa kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi wetu. Kwa hiyo, niombe sana Ofisi zinazohusika, najua itakuja Wizara ya Kilimo tutalisemea, lakini suala la pembejeo ni suala linalogusa maisha ya watu.
Kwanza, mbolea zifike kwa wakati kwa sababu msimu unajulikana. Sasa mbolea ya kupandia iende mwezi wa pili sio jambo zuri, wananchi wanaona kama tumewatelekeza.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa nadhani wa 16 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu umezungumzia kuhusu kutenga maeneo kwa ajili ya biashara. Mimi niombe mamlaka zinazohusika, Halmashauri zetu kwa hali ilivyo baada ya kutoa ule utaratibu wa retention haziwezi kuwa
na fedha kwa ajili ya kutenga maeneo, kwa sababu tunaposema kutenga haiishii tu kutenga ni pamoja na kuyapima maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa Halmashauri hazina nguvu hii tena tuje na utaratibu ambao tunaweza tukazisaidia, zikatenga maeneo yakapimwa yakajulikana haya ni maeneo ya biashara, haya ni maeneo ya wafanyabiashara wadogo wadogo na yakajengewa
miundombinu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake amempongeza Alphonce Simbu, huyu ni mwana michezo.
Sasa katika kutenga maeneo pia tuzisaidie Halmashauri zitenge maeneo kwa ajili ya michezo. Kwa sababu ni kupitia michezo vijana wanapata ajira na kupitia michezo tunapata akina Samatta na hawa akina Simbu. Bila kuwa na miundombinu kwa maana ya viwanja hatuwezi kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia michezo tumeona hapa utalii umeongezeka kwa asilimia 12 lakini kupitia michezo tunaweza tukafanya promotion kwa wepesi zaidi. Leo hii Simbu ameshinda Mumbai Marathon ni Wahindi wangapi India wameweza kuifahamu Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba Halmashauri bado hazijaweza kuwa na nguvu especially kama ya Mji wa Mafinga. Wananchi wamejitahidi wamejenga zahanati, juzi tunashukuru Ubalozi wa Japan umetusaidia tujenge theatre. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwenye Halmashauri kama hizi ambazo ni mpya na wananchi wamejenga maboma itie nguvu yake katika kuhakikisha kwamba zahanati zinakamilika. Vilevile kama ambavyo Serikali imefanya kwenye utaratibu wa kuwapata walimu wa sayansi na hesabu pia tuweke utaratibu na tupate vibali ili
kusudi watumishi wa kada ya afya nao waweze kuongezwa katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa haya yote tunayoyasema na kuyatekeleza na tutakayoyatekeleza yatafanikiwa tu ikiwa Serikali kwa macho mawili itaangalia welfare ya watumishi wa umma. Chochote tutakachofanya kama watumishi wa umma morale wako chini nadhani
kwamba hatuwezi kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa tutazungumza kwenye Wizara husika lakini Serikali iangalie kama wamepata promotion, waweze kulipwa zile haki zao zinazoendana na promotion zao na welfare yao kwa ujumla watumishi wa umma. Kwa sababu hawa pamoja na
rasilimali fedha ni watu muhimu kuhakikisha kwamba tumefanikisha mipango tuliyoipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia pia, katika hoja hii na namshukuru Mungu kwa uzima na afya zetu. Mimi nitakuwa na mambo kadhaa, lakini kwanza naanza na pongezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia, kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali na Mheshimiwa Rais kwa mambo ambayo yanafanyika katika Jimbo la Mafinga Mjini. Kwanza sisi, kama watu ambao tunajishukughulisha na kilimo, tunapongeza sana suala la mbolea. Tulishauri hapa Bungeni, kweli Serikali ikaleta ruzuku ya mbolea na baadae kulikuwa na changamoto za hapa na pale, tumeendelea kushauri na maboresho yameendelea kufanyika. Kwa hiyo hili ni jambo linalostahili pongezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, naishukuru na kuipongeza Serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kijamii. Tuna kituo cha afya pale Ifingo, tunashukuru sana kimekamilika na tumepata gari la kubebea wagonjwa (ambulance), tunachosubiri kutoka kwa wenzetu wa TAMISEMI ni gari, kwa ajili ya ufuatiliaji kwa wenzetu wa Idara ya Afya. kituo hiki pamoja na kusaidia watu wa Kinyanambo, lakini pia, kinasaidia watu kutoka hadi Ihalimba, watu wa Kata ya Rungemba na watu wa kutoka Jimbo jirani la Kalenga wanakuja pale kupata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika elimu, tumesogeza elimu kwa kujenga Shule ya Sekondari pale Ndolezi na sasa tunaendelea kwa kushirikiana na wananchi kujenga shule nyingine ya msingi, ili kupunguza umbali wa wale watoto wanaotoka kule Ndolezi kwenda Mafinga au kwenda Mwongozo au kwenda Mkombwe Shule ya Msingi. Kwa hiyo, tunapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, nawapongeza wananchi wote wa Jimbo la Mafinga Mjini kwa sababu, haya yote tunayofanya tunashirikiana kutoka Kata zote na Vijiji na Mitaa yote kwa sababu na wenyewe pamoja na jitihada na nguvu ya Serikali na nguvu ya halmashauri, lakini yapo maeneo kama wale wa Ndolezi na wale wa Kikombo walitoa nguvu zao kwa kushirikiana na jitihada za Serikali kufanikisha miradi ikamilike. Wale wa Kituo cha Afya cha Lufingo, wale wa Bumilayinga wote tunafanya kazi kwa kushirikiana, lakini pia, yote yanafanikiwa kwa sababu, tunashirikiana na uongozi wa Serikali kwa maana ya Mkuu wa Mkoa, Ndugu yangu Peter Serukamba na uongozi wake wa Mkoa, lakini na Mkuu wetu wa Wilaya Dkt. Linda pamoja na Madiwani, wote tunashirikiana na wataalamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanafanikiwa chini ya usimamizi wa Chama chetu Cha Mapinduzi chini ya Comrade Yassin Daudi, MNEC wetu Ndugu Asas na Katibu wetu wa Mkoa Ndugu Goma, lakini kwa pale Wilayani tuna Mwenyekiti wetu jembe Ndugu George Magelasa Kavenuke na Katibu wetu Ndugu Clement Bakuli pamoja na viongozi wa ngazi zote za chama. Hawa wote ninawapongeza kwa sababu, tunashirikiana kuleta maendeleo pamoja na wadau wa maendeleo muhimu sana wenzetu wa Water for Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wametuchimbia visima virefu vya maji kwenye shule zote za sekondari, kwenye zahanati zote, kwenye hospitali yetu ya Mafinga na kwenye vituo vyetu vyote vya afya vya Ifingo, Ihongole pamoja na kule Bumilayinga. Kwa hiyo, ninawapongeza sana na wadau wengine tunaoshirikiana nao kwa maana ya TARURA, TANESCO, RUWASA, MAUWASA, TFS na Shamba la Saohill pamoja na JKT Mafinga katika kufanikisha maendeleo ya wananchi wa Mafinga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi, sasa ninakuja katika mchango wangu. Jana kuna mtu alichangia hapa na alisema Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Mheshimiwa Prof. Mkumbo ni Singida Boys na mimi nasema nawa-consider wao kama wachezaji wa Yanga Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua kwamba, ule ushirikiano wao umeleta heshima kwa klabu ya Yanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama ingekuwa ni Simba ningesema hawa ni Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute. Kwa hiyo, ule ushirikiano umeiwezesha Simba kwenda robo fainali Klabu Bingwa, lakini ushirikiano ule ndani ya Yanga, wa Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua, umeiwezesha Yanga kwenda kuchukua ubingwa na kwenda robo fainali. Sasa ninawaomba ushirikiano huu ambao nimetoa mfano, sasa na ninyi mshirikiane kama Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango kuhakikisha kwamba, uchumi wa nchi na maisha ya Wananchi wa Tanzania yanakuwa ni maisha ambayo yameboreshwa na yanakuwa na affordability. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili hayo yafanikiwe, tunapozungumzia bajeti, maana yake ni mapato na matumizi. Sasa yapo mapato unaweza kuyapata kwa kutoka jasho, lazima ufanye uzalishaji, lakini yapo mapato yanaweza kupatikana katika nchi yetu bila kutoka jasho. Ninawaomba Mheshimiwa Waziri, nendeni mkarejee mchango wa Mheshimiwa Kakoso wa mwaka jana wakati wa bajeti kuhusu namna gani Taifa linaweza likanufaika kutokana na hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi watu wa Gazeti la Mwananchi waliandaa kongamano la kuzungumzia mambo ya mabadiliko ya tabianchi na kwa namna gani hii changamoto inaweza kugeuzwa kuwa fursa. Inaonekana nchi yetu kwa kutumia misitu tuliyonayo, tunaweza tukapata takribani shilingi trilioni mbili na nusu zikachangia katika Pato la Taifa. Hebu wekezeni nguvu katika jambo hili na kuna dhana inajengeka kwamba, hiyo hewa ya ukaa watapata fedha watu ambao wametunza misitu asilia, lakini mimi naomba muende mbele, hata misitu ya kupandwa, hata chai, hata parachichi, hata mikorosho, unaweza kupata fedha katika suala zima la hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili. Ili tuweze kupata fedha maana yake ni lazima tuzalishe. Sasa nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Kilimo, kumekuwa na kilio kikubwa katika suala zima la kilimo cha chai. Kule Mufindi wawekezaji waliochukua hawafanyi chochote, wafanyakazi kwa miezi minne hawajalipwa mishahara, ukienda Rungwe kilio hichohicho, ukienda Lupembe kule kwa mwenzangu Mheshimiwa Swalle kilio hicho hicho, ukienda Korogwe, ukienda Lushoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu jamani tuone tunaokoa vipi sekta ya uzalishaji ya chai, ili kuona kupitia chai tunaendeleaje kupata fedha za kigeni kama alivyosema Mheshimiwa Mrisho Gambo. Mwisho wa siku tunahitaji dola, tutapataje dola kama hatujaboresha mazingira ya kuzalisha, tukauza hiyo chai tukapata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninawaomba hebu tujaribu kuliangalia katika muktadha mzima wa kuongeza mapato ya nchi yetu, lakini, ili haya mambo yaweze kwenda vizuri ni lazima miundombinu wezeshi iwepo. Sisi watu wa Mufindi maisha yetu ni kilimo hicho cha chai, mazao ya misuti na kilimo katika ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kufanya majumuisho, utueleze hatma ya Barabara ya Mafinga kwenda Mgololo, tumesaini mkataba mwaka jana, Mwezi wa Sita, Tarehe 16, mpaka sasa mkandarasi hajaingia kazini. Ninawaomba, ile barabara ni uchumi sio tu wa Mafinga, Mufindi na Iringa, bali ni uchumi wa Taifa hili kwa sababu, kule kunatoka mazao ya misitu; nguzo, mirunda na mbao zinatoka kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unakuta pale malori, ma-semi trailers yame-park wiki nzima, hayawezi ku-move. Wakati wa mvua umesimamisha uchumi kwa sababu, yale magari yaki-move, nilishawahi kusema hapa, yatajaza mafuta, utapata fuel levy, Serikali itapata mapato. Kwa hiyo, hata gharama za uzalishaji zinakuwa kubwa, nawaomba sana, Mheshimiwa Waziri tuliangalie hili, lakini katika suala hilohilo ambalo ninalizungumzia tena la uzalishaji, Mheshimiwa Waziri tuliteta na wewe pale nje, sisi watu wa Mufindi ndiyo watu wa kwanza kuanzisha Benki ya Wananchi, ilikuwa inaitwa Mufindi Community Bank (MUCOBA).

Mheshimiwa Naibu Spika, benki nyingine za wananchi mnazoziona nchi hii, walikuja kujifunza MUCOBA, lakini benki hii kutokana na mtikisiko wa kiuchumi wakati fulani tuliyumba kiasi kwamba, ninamshukuru sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, na Mzee Yassin Daudi alikuwa Mwenyekiti wa Chama wa Wilaya. Tulikaa wakatusaidia, wenzetu wa Benki ya Zanzibar wakaja na wakaongeza mtaji, lakini all over a sudden mwaka jana, Mwaka 2022, TRA wamekuja kuchukua katika akaunti ambayo iliwekewa fedha za wananchi za mikopo ya asilimia 10 shilingi 681,000,000. Sasa mimi nashindwa kuelewa Mheshimiwa Waziri, benki ambayo inachechemea inawezaje ikadaiwa fedha kiasi cha shilingi 681,000,000?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mawasilisho kadhaa, nitayaleta mezani kwako unisaidie, barua imeandikwa kwa Kamishna kuomba jambo hili lifanyiwe kazi. Matokeo yake sasa Benki ya Wananchi wa Zanzibar imeona kwamba, hapa hakuna biashara na imeondoka, lakini Benki hii ya Wananchi wa Mufindi ilikuwa ni msaada kuondokana na ile mikopo tuliyosema hapa siku moja ni mikopo ya kausha damu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri, hebu iangalie hii benki ambayo ni mkombozi kwa wananchi wa kawaida wa Mufindi, wanachukua mikopo katika gharama nafuu na pasipokutakiwa kuweka dhamana kubwa. Mimi naamini unaliweza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la miradi. Nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sisi tuna mradi, katika Mradi wa Miji 28 Mafinga tupo, lakini mpaka sasa hivi mkandarasi hajalipwa certificate nne, kaondoa watu wake site. Sasa tulijinadi tukasema kwamba, lazima kufikia Mwaka 2025 mradi utakamilika, sasa imebaki miezi saba, mkandarasi hayupo site. Nakuomba, wewe kama Waziri wa Fedha, Fedha zipatikane.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho na Mheshimiwa Rais kwenye hili ninampongeza sana, ameshiriki mikutano yote ya mazingira duniani akiendelea na hii slogan yake ya clean energy, sasa clean energy haipo tu kwenye kupikia. Mheshimiwa Waziri hebu kwanza tufanye incentives kwa watu wanaowekeza kwenye masuala mazima ya gesi, watu wanaowekeza kubadilisha magari yatoke mifumo ya mafuta kuwa ya gesi, sisi hapohapo tumekuja kuweka tena tozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaomba katika kipindi cha miaka mitano hebu kwanza tusahau, twende na slogan ya Mheshimiwa Rais ya clean energy. Sasa huku Rais anasema clean energy, sisi tunaweka tozo juu yake, hatuta-achieve hilo jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho. Mheshimiwa Waziri umesema kwamba, mafuta yakipanda, ile ikiwa imeshuka ile bei utakuwa unai-maintain, ili fedha iende kwenye barabara...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa Chumi.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba kuhitimisha, naunga mkono hoja. Naomba haya niliyoyasema, hasa hili la MUCOBA na Barabara ya Mafinga – Mgololo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitilie mkazo.
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu Benki ya Wananchi wa Mufindi (MUCOBA) kuchukuliwa fedha zake shilingi milioni 681 na TRA.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango huu wa maandishi naomba Waheshimiwa Mawaziri warejee mchango wangu kuhusu Benki ya Wananchi Mufindi (Mufindi Community Bank-MUCOBA).

Mheshimiwa Spika, benki hii ni benki ya kwanza ya wananchi hapa nchini, kama nilivyoeleza katika mchango wangu. Benki hii ilipitia kipindi kigumu sana kiasi kwamba BOT ilitishia kuifunga kama ilivyotokea katika baadhi ya Benki za Wananchi. Benki hii ni mkombozi wa wananchi wa Mufindi hasa katika mikopo ya masharti nafuu. Benki hii imesaidia kwa miaka mingi kuchangia uchumi wa wananchi wa Mufindi kuanzia kutoa ajira na kutoa support kwa wafanyabiashara wadogo hususani wafanyabiashara wa sekta ya mazao ya misitu, vikundi vya wajasiriamali vya vijana na wanawake. Ni benki ambayo ni mkombozi wa wananchi wa Mufindi na Iringa kwa sababu benki ilijitanua mpaka kufungua Tawi Iringa Mjini, Ilula na kufungua Ofisi za Mawakala katika maeneo ya Igowole mpaka Madibira ambako ni Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya. MUCOBA ni nembo ya Mufindi.

Mheshimiwa Spika, ilikuwa ni matarajio yetu wana Mufindi kuona kuwa baada ya kupitia kipindi kigumu hata kufikia Benki ya Watu wa Zanzibar - PBZ kuongeza mtaji, Serikali ingekuwa mlezi mwema wa kuhakikisha kuwa benki inastawi na kushamiri kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi. Kiuwekezaji benki hii imesaidia wawekezaji wengi wa ndani ya Mkoa wa Iringa kwa kuwapa mikopo na huduma mbalimbali za kifedha. Katika nyakati ambazo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuunda Wizara ya Mipango na Uwekezaji, ni matarajio yetu Wana-Mufindi kuwa uwekezaji wa taasisi local za wananchi unapaswa kulindwa na kulelewa ipasavyo. Huu ni mfano halisi wa local content katika sekta ya kibenki. Benki hii ni mfano wa nguvu ya wananchi siyo tu kushiriki bali kumiliki uchumi wao.

Mheshimiwa Spika, haikuwa kazi rahisi kwa benki hii kusimama tulifanya jitihada kubwa sana na vikao visivyokuwa na hesabu mpaka kufikia hatua ya wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukubali Benki ya Watu wa Zanzibar - PBZ kuingiza mtaji wake. Tulikaa vikao vya kutosha kati yetu na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, sisi tukiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mufindi Mzee Yassin Daud ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Mzee Mizengo Pinda - Waziri Mkuu Mstaafu akiwa wakati huo mlezi wa CCM wa Mkoa wa Iringa alishirikiana nasi katika kuhakikisha kuwa benki hii inajikwamua kutoka hatari ya kufungwa na BOT.

Mheshimiwa Spika, vikao hivyo na majadiliano ya mara kwa mara na Maafisa wa BOT ambao walifikia hatua ya kuweka afisa mahususi kushirikiana na benki isifilisike, vilizaa matunda kwa Benki ya Watu wa Zanzibar kuona potential iliyopo ndani ya MUCOBA na kuamua kuongeza mtaji.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo hatua za TRA kuchukua fedha kiasi cha shilingi milioni 681 kwa nguvu imeturudisha nyuma sana kama benki na kama wananchi wa Mufindi na kwa ufupi, pamoja na kuwa mimi siyo mchumi, inashangaza benki ambayo inasuasua kiuchumi, haitengenezi faida, inawezaje kuwa na malimbikizo ya kodi ya shilingi milioni 681?

Mheshimiwa Spika, shida ilianza pale ambapo TRA ilipokadiria kodi kama vile hii ni benki kubwa za kiwango cha NMB au CRDB, hii ni benki ndogo isiyozidi mtaji wa shilingi tano, matokeo yake PBZ wameondoa fedha zao na sasa benki inakaribia kushindwa kufikisha ile minimum requirement ya BOT, hili jambo limewashangaza hata wenzetu wa PBZ kwamba wao wameweka fedha kama mtaji, sisi (TRA) tunatoa fedha za mtaji shilingi milioni 681.

Mheshimiwa Spika, athari za hatua hii ni kuwarejesha wananchi kwenye mikopo tunayoita kausha damu, yawezekana siyo wote wanapata mikopo MUCOBA, lakini hata hao waliokuwa wanapata hivi sasa hawapati, hakuna gawio kwa wanahisa, lakini zaidi ya yote linafifisha jitihada za benki kuendelea kupanua wigo wa kukua, mwisho PBZ imeamua kuondoa mtaji wake na matokeo yake hata kisiasa hili suala litaathiri sana Chama Cha Mapinduzi kwa sababu hii ni benki ya wananchi ambayo sehemu ya mtaji wake ulitoka kwa wananchi kupitia michango yao ya kukatwa kiasi fulani cha fedha kupitia IMUCU na pia halmashauri zote mbili za Mufindi na Mafinga ni wanahisa na wananchi walinunua hisa.

Mheshimiwa Spika, je, hatuoni kuwa tunatengeneza chuki kwa Serikali? Sina maana kwamba sheria zisifuatwe, hapana, naomba tuangalie kiasi hiko cha shilingi milioni 681, ni kiwango sahihi, je, tunaenda nyuma au tunaenda mbele?

Mheshimiwa Spika, kwangu mimi na kwa wananchi wa Mufindi na Iringa kwa ujumla tunawarudisha nyuma kijamii, kiuchumi hata kisiasa wanakuwa na hasira na Serikali. Haiwezekani wananchi hawapati gawio, hawapati mikopo, utarajie wawe na furaha. Tutafakari suala hili kwa umakini na hekima ya Mungu ituongoze.

Mheshimiwa Spika, ushauri/ombi, ninashauri Serikali kwa maana ya Wizara, BOT na TRA kuona uhalali wa jambo hili na kulitafakari upya sio tu kwa mustakabali wa MUCOBA, bali sekta nzima ya benki. Nasema hivi kwa sababu sisi Mufindi tumekuwa shule kwa benki nyingine zote za wananchi (community banks).

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili lilikuwa bado katika majadiliano, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa mamlaka aliyonayo, aamuru TRA irejeshe fedha hizo ili benki iendelee kuzungusha mpaka hapo mwafaka utakapofikia, kwangu mimi ni ubabe kwa Serikali/TRA kuchukua fedha katika jambo ambalo liko kwenye majadiliano.

Mheshimiwa Spika, ninaamini Mheshimiwa Waziri na wataalamu wake wa Wizara, BOT na TRA mtaona kilio hiki cha Wana-Mufindi na kama kuna mapungufu yoyote ninyi kama walezi mnaweza kuona namna njema ya kulifanyia kazi suala hili kuliko hali ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28, Mji wa Mafinga ni sehemu ya Mradi wa Maji wa Miji 28 ambapo ndani ya Serikali ilikubalika kuwa kwa kuwa fedha za mkopo nafuu kutoka India USD milioni 500 hazitaweza ku-cover miji yote 28 iliamriwa kuwa miji minne ikiwemo Mafinga itagharamiwa kwa fedha za ndani, lakini kwa nia njema ibaki ikitambulika kuwa ni mradi wa miji 28. Mradi huu sisi Wabunge na viongozi wa chama kutoka maeneo ambayo ni wanufaika wa mradi tulialikwa kwenye signing ceremonies pale Ikulu mbele ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, Jandu Plumbers ni kampuni inayotekeleza mradi huu, hata hivyo ikiwa imebaki miezi minne muda wa miezi 20 ukamilike mradi umefikia only 22%, shida kubwa ni fedha, mpaka sasa mkandarasi ametoa certificates nne hajalipwa, matokeo yake amewaondoa wafanyakazi site. Ninawaomba sana kama sehemu ya kumheshimisha Mheshimiwa Rais tutoe fedha ili mradi huu ukamilike, shida kubwa ni fedha, isije ikaonekana sisi ambao mradi unatekelezwa kwa fedha za ndani ni kama tumefanya dhambi maana miji 28 mambo yanaenda vizuri, najua hali ya fedha ilivyo kutokana na miradi mikubwa, hata hivyo ninaomba mtuangalie Mafinga kwa macho mawili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Barabara ya Mafinga - Mgololo kwa Mfumo wa EPC+F, suala hili limeleta mkanganyiko sana ndani ya Bunge na ndani ya nchi, siyo tu kwa sababu ya mfumo wenyewe, bali kutokana na shauku ya uhitaji wa kuwa na barabara kwa ajili ya kuchochea shughuli za uzalishaji na uchumi kwa ujumla. Barabara ya Mafinga - Mgololo ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa mazao ya misitu, mazao ya chai, mazao ya chakula na shughuli nyingine za kiuchumi. Ni catalyst kwa uchumi wa Mufindi, Iringa na Taifa zima.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, nawaomba Serikali kwa namna yoyote itakayofaa, ujenzi uanze katika Barabara ya Mafinga - Mgololo na nina hakika takwimu ziko wazi hasa katika suala zima la mchango wa Mufindi katika pato la Taifa. Takwimu za TRA za larger taxpayers mtaona, hoja yangu.

Mheshimiwa Spika, kujengwa kwa barabara hii kutasaidia na kupanua wigo wa mchango wa Mufindi katika pato la Taifa, nawaomba sana fursa hii isipotee ili Mufindi tuendelee kuwa na mchango madhubuti katika uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusu fedha za Busket Fund- Mafinga Town Council. Suala hili nimelizungumzia mara kadhaa katika jitihada za kutafuta ufumbuzi. Tulitembelea TAMISEMI tukaonana na viongozi wa Wizara akiwemo NKM na Mkurugenzi wa Huduma za Afya. Ombi letu, Serikali itoe maelekezo mahsusi kwa Halmashauri Wilaya ya Mufindi sehemu ya fedha wanayopokea iende kwenye Hospitali ya Mafinga ambayo inahudumia Wilaya nzima (Mafinga TC na Mufindi DC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, mwaka 2016/2017, Mafinga TC tulipangiwa shilingi milioni 101, Mufindi DC walipangiwa around shilingi milioni 700. Kwa mwongozo, inatakiwa 30% ya fedha hiyo iende ikahudumie hospitali. Kabla hatujawa Halmashauri mbili tulipokea around shilingi milioni 800 ambapo 30% yake sawa na shilingi milioni 240 ilienda kuhudumia Hospitali ya Wilaya lakini ilivyo sasa Mafinga TC tunapokea around shilingi milioni 100 ambapo 30% yake ni around shilingi milioni 30 ndiyo inayoenda kuhudumia hospitali. Kwa hiyo, utaona upungufu kutoka shilingi milioni 240 mpaka shilingi milioni 30, ni punguzo kubwa, tunapokea 12.5% tu ya kuhudumia hospitali suala ambalo linaathiri mno utendaji wa kazi na kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu, kwa kuwa Hospitali ya Mafinga inahudumiwa na Mafinga TC lakini function wise hospitali inahudumia Halmashauri zetu mbili, Serikali kwa maana ya Wizara ya Afya na TAMISEMI, itoe maelekezo kwa Halmashauri ya Mufindi ili sehemu ya fedha za Busket Fund zipelekwe Mafinga TC kwa nia ya kuhudumia hospitali ya Mafinga inayohudumia Wilaya nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni fedha za Mfuko wa Wanawake (5%). Nimepitia kitabu na Mafinga TC ni kati ya Halmashauri chache sana ambazo hazijawapa vikundi vya wanawake fedha zao. Hii ni kutokana na conflicting interests. Nashauri na naomba Wizara izitake Halmashauri hizo zitoe maelezo kwa nini mpaka sasa tupo robo ya mwisho ya mwaka fedha hizo hazijatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ukiangalia katika Jedwali hata Halmashauri ambazo zimetoa fedha, percentage wise ni kasi kidogo sana. Hali hii inatokana na ukweli kwamba Halmashauri zinachukulia suala la 5% ya fedha ya Mfuko wa Wanawake kimzaha. Nitatoa mfano, kwa mujibu wa mwongozo wa matumizi ya fedha za makusanyo ya ndani 5% + 5%= 10% ni ya wanawake na vijana, 50% ya kuendeshea ofisi na 40% kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, haijawahi kutokea ile 50% ya kuendeshea ofisi ikakosekana. Halmashauri zinatumia kila kinachokusanywa kwa ajili ya kuendeshea ofisi na kupuuza kutenga fedha za Mfuko wa Wanawake. Je, Serikali imejipanga vipi katika kuhakikisha kuwa suala hili haliendelei kujirudia kwa sababu hata Kamati ya LAAC suala hili limekuwa likirudia kila mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni kuhusu kutoa ruzuku/ mkopo kwa wanafunzi wa kozi za uuguzi. Nimekuwa nikipendekeza kuwa kwa kuwa mahitaji ya kada hizi kuanzia AMO, Laboratory Technician na kadhalika ni makubwa na wazazi wengi wanashindwa kumudu gharama za kuwalipia, je, kwa nini Serikali isifikie hatua ikaunda utaratibu wa kutoa ruzuku/mkopo kwa wanafunzi wenye nia na sifa za kusomea fani hizo? Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kuhusu zuio la kulima vinyungu. Kilimo cha mabondeni (vinyungu) ni mkombozi wa wananchi wa Mafinga, Mufindi, Iringa na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Hata hivyo, Serikali mmezuia kilimo cha vinyungu bila kufanya tathmini ya kina. Watendaji wa Serikali wameshindwa kutafsiri maagizo na kupanikisha (make panic) wananchi kwa kutishia kufyeka mazao yao, kuweka alama za ‘X’ na kuwapa notice ya siku tisini. Ndugu zangu lazima kuwe na tafsiri pana kuhusu mabondeni na vyanzo vya maji. Kuna maeneo ambayo kwa vigezo vyovyote wananchi hata wakilima haiathiri suala la mtiririko wa maji au vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kigezo cha mita sitini kisiwe uniform, kuna maeneo ingeweza kuwa mita kumi au ishirini. Nashauri very strongly tafsiri ya Sheria isipotoshwe. Kilimo cha mabondeni yapo maeneo hayahusiani na hayana connection na Mto Ruaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ziara ya Makamu wa Rais Mkoani Iringa kuhusiana na kuhuisha na kufufua vyanzo vya maji imetafsiriwa tofauti, sasa imekuwa ni vitisho, wananchi hawana amani. Nashauri na naomba suala hili lizingatie pia kuwa bado hatuna miundombinu ya kumwagilia, hivyo si kila eneo tuweke zuio la mita sitini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mafinga Mjini. Mji wa Mafinga pamoja na kuwa ni Halmashauri ya Mji bado kuna vijiji kumi na moja, naomba mipango ya Wizara izingatie kuwa pamoja na kuwa ni mji tuna maeneo ni vijiji, hivyo tusisahauliane katika mipango ya maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, pamoja na kuwa suala la utumishi ni la TAMISEMI na Utumishi, ikama ya watumishi wa mamlaka ya maji ni wachache, Mhandisi wa Maji wa Halmashauri hana msaidizi, yuko peke yake. Naomba tuongezewe watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na pia niishukuru Wizara, watendaji kwa ujumla na niwashukuru zaidi kwa huu mzigo, nimeukuta pale kwenye pigeon hole yangu, una documents za kutosha, utaendelea kuniongezea ufahamu na kujihabarisha zaidi kuhusu Sekta hizi za Maliasili na Utalii, kwa hiyo, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi, napenda mchango wangu u-base kwenye statement ifuatayo; kwamba conservation has to take into consideration the livelihood of the people, so it is conservation with development. Katika thinking za zamani ilikuwa inaonekana kwamba binadamu katika viumbe hai ndiye anayeongoza kwa uharibifu wa mazingira na masuala mazima ya hifadhi.

Baadaye thinking hizi zimeendelea kubadilika na kumfanya binadamu awe part and parcel ya kutunza mazingira na hifadhi zetu kwa namna ambayo itamfanya awe shirikishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini binadamu alikuwa destructive? Kwa sababu kimazingira, kimahitaji, alikuwa analazimika kutafuta namna ya kujikimu lakini katika kutafuta namna ya kujikimu ikawa inamsababishia awe ni mharibifu wa mazingira. Ndiyo maana conservation ya sasa tunasema conservation with development, maana yake ni kwamba utunzaji wa mazingira lazima uendane na uzingatie pia maisha ya watu. Huwezi ukasema unatunza mazingira halafu maisha ya watu yanaendelea kuteketea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Juzi nilitoa kilio cha vinyungu hapa, huwezi ukasema maisha ya watu halafu unawazuia wasilime kitu ambacho ndiyo maisha yao au unawazuia wasifuge kitu ambacho ndiyo maisha yao. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema conservation lazima iwe with development, tusi-focus tu kwenye conservation tukaacha watu wanaanza kuangamia. Sasa tutakuwa tuna-conserve kwa ajili ya nani ili aweze kuishi? Kwa hiyo, msingi wa mchango wangu ningependa usimame katika msimamo au falsafa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naanza na naanza kwa masikitiko kwa sababu mambo mengine ni ya kushangaza, lakini unashangaa halafu unaendelea mbele na safari na maisha. Mimi yanapokuja ya kusikitisha kutoka kwa wananchi wangu wa Mafinga hakika siwezi kukaa kimya, lazima niyasemee. Watu wa Iringa, Mafinga, Mufindi, Njombe na Kilolo, wanaongoza na wana mwamko mkubwa wa kupanda miti, ndiyo hiyo tunasema conservation with development, lakini kutoka kusikojulikana Serikali inakuja inaanza kutoa maelekezo ambayo kimsingi yanakwenda kinyume kabisa na hii tunayosema conservation with development. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nina karatasi hapa na bahati nzuri Mheshimiwa Profesa Maghembe nilionana naye, inaelezea uvunaji katika misitu ya jamii, watu binafsi na taasisi. Kipengele (b) kinasema, uvunaji utaruhusiwa mara baada ya ukaguzi wa miti kufanyika na kuthibitishwa na Afisa Misitu kuwa miti hiyo imefika kiwango cha kuvunwa. Afisa Misitu wa Wilaya au Meneja Misitu wa Wilaya atapima kipenyo cha mti kabla haujaangushwa. Mwananchi huyu ambaye amejipandia miti yake, ametafuta miche yeye kusikojulikana, leo hii anapangiwa lini avune mti wake. This cannot be accepted at all!

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mtu anapokwenda kuvuna miti yake ana shida zake, mwingine mtoto amekosa mkopo anataka aende shule, mwingine ana mgonjwa hospitali anataka akamhudumie, wewe unamwambia kwamba eti kwanza mpaka Afisa Misitu aridhie. Kwanza hiyo capacity ya hao Maafisa Misitu, hata juzi tumelalamika hapa, je, hao Maafisa Misitu tunao wa kutosha wa kuweza kufanya hiyo kazi? Mtu yuko Mapanda, Usokani, Luhunga, Bumilayinga, Luganga, Afisa Misitu ataweza saa ngapi kwenda kufanya kazi hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo kama hili naomba baadaye Waziri anapohitimisha atupe msimamo wa Serikali. Hatuko tayari kupangiwa lini tuvune miti ambayo tumeipanda kwa nguvu yetu, sio miti ya Serikali, ile ni miti yetu na tunavuna sisi kwa shida zetu wenyewe. Juzi ilikuwa vinyungu, leo kwenye miti, yaani mnataka mpaka nione kazi ya Ubunge ni ngumu, hapana, sitakubali, jambo linalohusu maslahi ya wananchi wangu nawahakikishia nitawatetea mpaka mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye bei ya magogo, kwa nini sisi Taifa letu linawajali wawekezaji wa nje kuliko wa ndani? MPM wanauziwa magogo nusu ya bei, sisi wawekezaji wetu wa ndani wanauziwa kwa bei ya juu. Mheshimiwa Waziri mwaka jana ametoa maelezo ambayo bado hajani-convince, naomba mwaka huu anipe sababu, kwa sababu kama point ni investor na huyu wa ndani naye ni investor, naye anunue kwa nusu ya bei kama yule ambaye ametoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nizungumzie kuhusu utalii. Mimi nimesema mara nyingi, utalii bila matangazo ni bure, nina takwimu hapa. Uganda ambao sisi tunaona kwamba si washindani wetu kwa sababu tu sisi tuna vivutio vingi kuliko watu wengine duniani baada ya Brazili, katika bajeti yao ya kutangaza mwaka jana wameweka dola milioni nane, Rwanda dola milioni 11, sisi dola milioni mbili, tutavuna kweli kutoka kwenye sekta hii? Kama hiyo haitoshi, maana nimelinganisha na Rwanda na Uganda, Kenya mwaka jana kwenye Expo - Italy, yale maonesho ya barabarani ya miezi sita, bajeti waliotenga ni 3.9 million dollar, onesho hili moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bila kuwekeza kwenye kutangaza hatuwezi kuvuna, tutabaki tunajisifia sisi wa pili baada ya Brazil. Ni lazima tuiwezeshe TTB kwa vitendo. Kwa sababu ukienda hata kwenye TDL inasema kwamba kulingana na GN.218, TANAPA na Ngorongoro wataipa TTB asilimia tatu ya mapato au makusanyo yao, lakini sijui kama inaenda na kama inaenda sijui kama inafanya kilichokusudiwa. Naomba tuongeze nguvu katika jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya utalii lazima kwa namna yoyote i-take into consideration maoni ya wadau wengine na hasa sekta binafsi, vinginevyo itakuwa lawama hizi za VAT. Serikali inasema kwamba VAT haijakuwa na athari, wadau wanasema imekuwa na athari lakini kama wangehusishwa kutoka mwanzo maana yake ni kwamba wote tungekuwa on the same boat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mpango wa matumizi bora ya ardhi. Haya yote tunayoyasema ndugu zangu, Serikali peke yake haiwezi, katika kila jambo lazima ifanye ushirikishaji na inapogusa maisha ya watu lazima sisi viongozi wa kuchaguliwa tushirikishwe. Bila kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi tutakuja wa vinyungu tutalalamika, atakuja Mheshimiwa Doto Biteko wa wafugaji atalalamika, atakuja mtu wa tembo atalalamika. Kwa hiyo, kwa vyovyote lazima tuwekeze katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Menyekiti, tumeambiwa juzi population ya Vietnam ni milioni 91, eneo lao ni 360,000 square kilometers, population density watu 255, sisi per square kilometer watu 57, Singapore per square kilometer watu 7,987 hawajawahi kugombana wala hawajawahi kudhuriana kwa sababu wamekuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi. Sasa ili hili lifanyike siyo tu la Mheshimiwa Profesa Maghembe peke yake, ni la Wizara ya Ardhi, ni la TAMISEMI, ni la Wizara karibu tatu au nne, tano. Kwa kufanya hivyo, tutaondokana na haya matatizo kwa sababu square kilometers ni zilezile lakini idadi ya watu inaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumuuliza Mheshimiwa Profesa Maghembe, hivi ile Embassy Hotel ni gofu tu hatuna mpango wowote? Namba mbili, yule mjusi aliyeko Ujerumani hatusemi kwamba arudi, je, hakuna namna ambayo sisi tunaweza tuka-benefit kutokana na yule Mjusi? Wajerumani naambiwa wako tayari kushirikiana na sisi kujenga historical site na hoteli pale mjusi alipotoka lakini je hatuwezi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu wa kuzungumza, ninayo yafuatayo; TDL - Sekta ya Utalii kutoza 1.5 USD Bed Night Levy siyo nzuri kimapato. Utaratibu ungewekwa tozo hii iwe kwa asilimia kwa sababu it is unfair kwa anayelaza kwa shilingi 30,000/= anatozwa 1.5 USD sawa naye anayelaza kwa dola 50 na kuendelea, hata kiuchumi siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa takwimu za watalii ni 1.2 million na kwa kuwa utalii wetu ni ule tunaitwa Low Volume High Yield. Hivi hata kwa hesabu za common citizen, kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu katika kitabu cha bajeti ukurasa wa 136 jedwali Na. 9 wastani wa siku za kukaa watalii hotelini ni siku 10. Sasa kwa mahesabu ya haraka tuchukulie wageni 1.2 million wamelala siku tano, maana yake hizo ni a total of 6,000,000 nights ambazo ukifanya ile Bed Night Levy ya USD 1.5 per bed ambayo ni kama shilingi 3,000/=; maana yake ni 6,000,000 x 3000 = 18 billion ambayo ingeweza kabisa kutusaidia katika kuutangaza utalii, kuimarisha mafunzo hasa kupitia Chuo cha Utalii na hata kutoa ruzuku kwa wajasiriamali wa miradi ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba tuanzishe chombo maalum cha kuratibu TDL, chombo hiki kitabainisha njia mbalimbali za namna ya kuimarisha makusanyo kupitia TDL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi sambamba na kuanzisha One Stop Centre, ni wazi kuwa Serikali haiwezi kujenga mahoteli zaidi ya kujishirikisha na ujenzi wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege. Kwa sababu hiyo, ushirikishwaji wa sekta binafsi haukwepeki. Tufike wakati sekta binafsi tuione kama mdau na siyo adui/mwizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 23 wa kitabu, umeelezea kuhusu VAT, kuna confusion. Wadau wanasema imeathiri Sekta ya Utalii, lakini Serikali inaonesha kuwa hakuna athari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kama ilivyoshauriwa na Kamati, Wizara ikae na wadau kupitia na kujiridhisha kuhusu suala hili. Nasisitiza pia pawepo na One Stop Centre kwa ajili ya masuala ya ku-facilitate masuala ya utafiti kama ambavyo TIC; ukifika unakutana na Idara zote kuanzia BRELA, TRA na kadhalika. Tufanye hivyo katika utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani nikiwa Afisa Mambo ya Nje, Mama Blandina Nyoni akiwa Katibu Mkuu Maliasili alitoa USD 10,000 (dola 10,000) kwa baadhi ya Balozi zetu kutumia kutangaza utalii, na ilisaidia sana. Kila Balozi ilitumia kadri ya mazingira. Wapo walionunua TV na kila mgeni akija kufuatilia visa, wakati anasubiri anaangalia filamu mbalimbali kuhusu utalii wa Tanzania. Nashauri tupanue wigo wa kutangaza utalii kwa kuendelea kuhusisha taasisi nje ya Wizara kulingana na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli kama tunasema katika sera kuwa jamii zinazozunguka mbuga na hifadhi zitakuwa sehemu ya kunufaika, mbona hii single entry inaenda kuua kuliko kunufaika? Hoja kwamba kuna ukwepaji wa mapato bado inaweza kutazamwa hasa katika baadhi ya maeneo. Hili suala ni kama vile kuwalinda wawekezaji wakubwa na kuwamaliza wawekezaji wadogo na hasa wanavijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Ryoba ni ya msingi na muitazame. Leo hii ufugaji unaongezeka badala ya ng’ombe 500 kama ilivyokuwa awali. Kuna ng’ombe 8,000 matokeo yake ni nini? Wataanza kuingia kwenye hifadhi, dhana ya conservation kama matokeo ya WMA. Hii itazamwe upya, tuwe open minded, tufikirie zaidi namna bora ya kudhibiti upotevu wa mapato lakini kwa kuzingatia ustawi wa jamii zinazozunguka hifadhi.

Kuhusu misitu vs vibali; kwanza nashukuru ushirikiano ambao Mafinga tunapata kutoka Sao Hill na TFS. Tumepokea madawati na Halmashauri yetu iko tayari kutoa eneo kwa ajili ya Ofisi ndogo na parking kama sehemu ya ushirikiano. Nimesoma kijitabu na niliitwa na Kamati kuhusu utaratibu wa upatikanaji malighafi Sao Hill, hata hivyo nashauri kuwa pamoja na utaratibu huo, usawa na uwazi (fairness na transparency) ni muhimu sana. Siyo sawa mtu mmoja (sitamtaja) alijidai kuwa eti ana mkataba na Serikali (TFS) apewe ujazo mkubwa kisha awauzie wengine tena kwa majigambo makubwa kwamba wataendelea kumtegemea yeye. Hili halikubaliki! Ni vizuri mgao wa malighafi uzingatie uwezo wa kiwanda na sio umaarufu wa mtu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutotoa mgao kwa vikundi, pamoja na kuwa ni sheria/kanuni, nashauri suala hili litizamwe upya. Ni muhimu sana kutenga kiasi kidogo kwa ajili ya makundi ya mahitaji maalum kama wenye ualbino na vikundi vya wajane as CSR (Corporate Social Responsibility).

Suala la wanachi kupata vibali ndipo wavune miti yao sio sawa na litatuletea mgogoro na wananchi bila sababu yoyote. Nimechangia kwa kuzungumza, lakini nasisitiza maamuzi kama haya yawe shirikishi kuliko ku-impose tu. Mtu ana shida, anataka kuuza msitu wake atatue shida yake, why tumwekee mlololongo? Je, capacity hiyo mnayo? Tutafakari upya na nakuletea tangazo hilo, barua Na. TFS/ SH2/MUF/MSC/VOL.1/113 ya tarehe 9 Mei, 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa hatuwezi kumrejesha mjusi aliyeko Ujerumani. Ushauri wangu ni kwamba shirikianeni na Wizara ya Mambo ya Nje, Wajerumani walishaonesha nia kwamba pale kwenye shimo alipotoka yule mjusi pajengwe reception na hoteli ambayo itatumika na wageni watakaopenda kuona lile shimo alipotoka mjusi. Jambo hili linataka utashi tu na linawezekana na litaongeza idadi ya watalii na hivyo kuongeza mapato.

Pili, Wajerumani pia wako tayari kutoa funds lakini specifically kwa ajili ya kuimarisha masuala ya archeology na conservation. Yote hayo ni in connection na huyu mjusi. Aidha, Mheshimiwa Dkt. Mwekyembe anaweza kuwa msaada katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, iwe ni kwenye misitu, uwindaji au utalii kwa ujumla ni vizuri viongozi wa kuchaguliwa kuanzia Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa, Madiwani na Wabunge washirikishwe ipasavyo hasa katika maamuzi yanayokusudiwa kufanywa, yanaathiri maisha ya wananchi kwa asilimia 50. Mfano, suala la mkaa, vinyungu, single entry na kadhalika. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu kuyapa uwezo wa kifedha mashirika ya Nyumbu, Mzinga na SUMA JKT. Nikiwa mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama nilitembelea Nyumbu na wajumbe wenzangu na kujionea kazi nzuri inayofanywa na shirika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Shirika lingeweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kama lingekuwa huru hasa kwa mujibu wa sheria. Ilivyo sasa shirika hili kwa mujibu wa sheria liko chini ya Msajili wa Hazina hali hii inasababisha si tu mgongano wa kimaagizo, lakini pia utekelezaji wa mipango na maono (vision) ya shirika unachelewa kwa sababu ya mlolongo wa kiutawala, kwa mfano kuna nchi zilionesha nia ya kushirikiana na Shirika la Nyumbu tangu mwaka 2007, hata hivyo uamuzi haukutolewa kwa wakati kutokana na sababu za kisheria na kiutawala na hivyo kupoteza fursa hiyo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nashauri Serikali ione uwezekana wa kuleta mabadiliko ya sheria ili Shirika la Nyumbu liwe chini ya Wizara/Jeshi kwa asilimia moja. Ninaamini uchambuzi wa kina ulifanyika, itathibitika kuwa mabadiliko ya sheria yataleta tija kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikufanikiwa kutembelea Mzinga kama ilivyokuwa kwa wenzangu, lakini uhalisia ni kuwa kuna fursa za wazi za kiuchumi na kimapato ikiwa Mzinga itawezeshwa, ninaamini kuna soko kubwa nje ya nchi kutokana na bidhaa zitakazozalishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu SUMA JKT, binafsi nimetembelea kila mwaka maonesho na huwa sikosi kutembelea mabanda ya SUMA JKT. Pia nimefanya ziara binafsi ya mafunzo katika Kambi ya Ruvu nikiwa na baadhi ya vijana kutoka Jimboni. Hakika iwe ni katika kilimo,ufugaji, ufundi na kadhalika, SUMA JKT inafanya kazi nzuri mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulinzi tumeshauri mara kadhaa kuwa maeneo yote ya Serikali na taasisi za umma ulinzi ufanywe na SUMA JKT, lakini pia Serikali ihakikishe wote wanaodaiwa wanalipa kwa wakati, ikibidi fedha zao za OC zikatwe zikalipe deni. SUMA JKT ipewe wigo mpana katika kushiriki suala la kuelekea uchumi wa viwanda hasa viwanda vidogo vidogo. Hili litawezekana tu ikiwa itawezeshwa kifedha kwa namna (mechanism) ambayo Serikali itaona inafaa; kwa mfano kuidhamini kwa mikopo ya riba nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mafunzo ya vijana - JKT; katika ukurasa wa tano wa kitabu cha Taarifa ya Kamati imeeleza kuwa ikiwa fedha kiasi cha shilingi bilioni nane zitatolewa JKT itaweza kukarabati makambi na hivyo kuongeza vijana wa kujiunga na JKT. Mpaka tunajadili bajeti
hii ni kiasi kidogo cha shilingi bilioni moja tu kimetolewa. Suala la mafunzo ya JKT kwa vijana wetu ni muhimu sana kwa sababu linaongeza uzalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo wengi wao wanaingia katika ajira na kujiajiri. Ushauri wangu, katika wakati huu ambapo matumizi ya mitandao yamekuwa yakichangia kumomonyoa maadili ya vijana, mafunzo haya ni muhimu katika kujenga Taifa la kesho linalojitambua. Ninaamini kila kijana anayepitia JKT anajenga ushawishi (influence) kwa vijana wengine na wasiopungua 100 katika kijiji au mtaa anaoishi na kwa ushawishi huo wapo vijana waliohamasisha vijana wenzao kujiunga katika vikundi vya kuzalisha mali. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa haraka haraka, napenda kukushukuru. Naishukuru Wizara na Watendaji wote kwa ujumla kwa mawasilisho ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nateta na mwenzangu hapa, nikawa najiuliza kuna kila sababu sisi kama Bunge kwa nafasi yetu Kikatiba kuna mambo bila kujali itikadi lazima tuwe kitu kimoja kwa maslahi ya Taifa. Sasa hata kama uzalendo wako ni wa mashaka, kwenye suala hili la mchanga mimi matarajio yangu kuna mambo tunaweza tukabishana kwa kutafuta kiki na kadhalika, lakini kwenye masuala kama haya ya mchanga wa dhahabu my dear friends, brothers and sisters hili jambo ushauri wangu, nawaomba tuwe kitu kimoja, tuwe nyuma ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tuwape mileage, mtu anazungumza eti atashitakiwa kwenye Mahakama za Kimataifa, si zipo! Kazi yake ni nini? Tutaenda, tutakutana huko. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge kuna mambo hebu tuweni kitu kimoja; tunaweza kujijengea huko nje kwa wananchi, ni aibu kubwa sana especially kwa jambo hili. Jambo hili hata mtu ambaye ni layman analiona kwamba ni jambo la thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna Tume nyingine ambayo inafiti ni namna gani tumeibiwa sisi na kuhujumiwa kiuchumi katika suala la mchanga. Sitarajii kwamba suala hili tuwe against kwa mipango mizuri hii ya Serikali, kwa sababu tunalia maji, tunalia dawa, sasa tunalia majengo. Juzi tumesema zahanati hazijakamilika, tunalia hapa majengo huko Ubalozini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo kama haya tushirikiane kuunga mkono jitihada hizi. Nami ningetegemea hata ambao ni Wanasheria nguli wa nchi hii, sasa wajipange kwamba kama Serikali itapelekwa kwenye hizo mahakama wao watakuwa msitari wa mbele kushirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba wanatetea maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kuna mambo hebu sisi tuwe united, tuwe kitu kimoja. Tusipinge tu simply because itikadi zipo tofauti. Haya ni mambo yanagusa maisha yetu, ni mambo yanagusa maisha ya vizazi vyetu. Kama kuna makosa yalifanyika, hatuwezi kukaa macho tukasema sasa tuache tuendelee tu kukosea, hiyo haiwezekani kwa sababu kulifanyika makosa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu dakika pia ni chache, ningependa kuzungumzia pia umuhimu wa Wizara kuhakikisha kwamba inapeleka Maafisa katika Balozi zetu. Maafisa wapo wachache, kuna baadhi ya Balozi unakuta Balozi yupo mmoja, hana Afisa wa kumsaidia kufanya kazi na Balozi huyu ni mgeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu MPM - Kiwanda cha Karatasi Mgololo. Mara kadhaa nimeongea na Mheshimiwa Waziri kuhusu kiwanda hiki na hata nimefikia kumwandikia, kuomba ridhaa ya kuuona na kuupitia mkataba wa ubinafsishaji wa kiwanda hicho ambacho awali kilijulikana kwa jina la SPM.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoenda uchumi wa viwanda jambo ambalo Serikali ilisisitiza ni kuhakikisha kuwa wote waliopewa viwanda kuhakikisha vinazalisha katika uwepo na malengo yaliyokusudiwa. Hata hivyo, MPM wanazalisha katika stage fulani kisha wanasafirisha material kwenda kufanya finishing Kenya, kisha karatasi zinarejeshwa kuja kuuzwa hapa nchini, hapa kuna double loss.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, hawazalishi end product kwa maana ya karatasi, tunapoteza sehemu ya ajira kwa sehemu ya finishing kwenda kufanyiwa Kenya, lakini pia tunapoteza mapato maana tungeweza kupata fedha za ndani na kigeni kwa kuuza ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya masuala ya East Africa Community kuhusu rules of origin, MPM inatuletea karatasi kutoka Kenya na ushuru unaolipiwa is only 10% na siyo 25% maana sote tupo ndani ya EAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri, kiwanda hiki kinauziwa magogo nusu ya bei 14,300/= kwa cubic meter, inapewa magogo hayo na Serikali (Sao Hill Forest). Je, kina sababu gani ya kutozalisha finished product kwa maana ya karatasi? Kusimamia na kuhakikisha kuwa ile machine Na.1 inafanya kazi italeta tija na kuipa Serikali heshima kuwa inamaanisha ilichosema kuwa, itahakikisha wote waliopewa viwanda wanatenda kadri ya malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, One Stop Centre, Uanzishwaji biashara za kati na za chini ni suala lenye malengo marefu kiasi kwamba inasababisha biashara nyingi kutokuwa rasmi. Ushauri, tuwe na one stop centre, mfano wa TIC kila Mkoa, kuliko ilivyo sasa mara BRELA, mara TIN, mara OSHA. Tuki-centralize katika level ya mkoa itarahisisha suala zima la kuanzishwa biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya masuala ambayo ukizungumza na Jumuiya ya Kibalozi (Diplomatic Community) ni suala la Double Taxation na Protection of Investments, wanasema mahusiano katika dunia ya sasa ni kuhusu kuimarisha fursa za kibiashara (Trade Opportunities) na ili kuzifaidi fursa hizo ni lazima pawepo mazingira bora ya kufanyia biashara na uwekezaji. Mazingira hayo mojawapo ni hili la double taxation na protection of investments.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nchi nyingi mfano Oman, Kuwait na za South East Asia, kama Korea, Japan na hata China ziko tayari kushawishi watu wao kuja kuwekeza hapa nchini, lakini ukakasi upo kwenye assurance yao hususani katika masuala hayo ya double taxation na protection of investments.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba tupunguze woga, tupo na mashaka mno, kila jambo tunahisi tutaibiwa au kudhulumiwa, naamini tunao wataalam ambao watatufanya tufikie ile tunaita win win agreement. Hivyo ili yafanikiwe ni lazima Wizara ishirikiane na Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Fedha, ambao focus yao ni kukusanya tu pasipo kuangalia kuwa bila ushiriki wao katika suala zima la double taxation, itakuwa haileti tija iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Maafisa Biashara. Katika mchango wangu bajeti iliyopita niligusia suala hili, kuwa tunapoenda uchumi wa viwanda na reflection yake kiuwekezaji kama lilivyo jina la Wizara, Muundo wa Kada hii kuendelea kufichwa ndani ya Idara ya Fedha katika Halmashauri zetu sio sahihi. Ikiwa Nyuki tu ni Kitengo kwa nini hii isifanywe Idara au angalau Kitengo?

Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Biashara wamebaki kufanya kazi ya kukagua leseni, wapo vijana ni wasomi wazuri lakini wako under utilization, kwa sababu hata Wakurugenzi wanajikuta wanawapangia kazi ambazo sio za utaalam wao. Ni wakati sasa kada hii, ninyi Wizara muongee na Utumishi na TAMISEMI muweze kuipa nguvu kimuundo ili watumike ipasavyo hasa katika suala zima la biashara na uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mafinga Mjini na Uchumi wa Mazao ya Misitu (Mbao). Mji wa Mafinga ni kitovu cha shughuli za kiuchumi na uzalishaji katika Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa. Hata hivyo watu hawa hawajapata fursa ya kupata huduma mbalimbali na changamoto wanazokutana nazo hasa katika sekta ya mbao, uzalishaji wa nguzo na milunda. Ombi langu, naomba waje hapa Dodoma kutokana na Waziri na Watendaji ili msikie maoni na ushauri wao kwa namna gani mnaweza kuwasaidia kushiriki ipasavyo katika suala zima la kuelekea uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu SIDO, inafanya kazi vizuri lakini SIDO wamejikita level ya Mkoani tu, Mafinga ina fursa yingi, tungependa SIDO ishirikiane na Halmashauri ya Mji wa Mafinga katika suala zima la kuwepo ama kutenga Industrial clusters kama walivyofanya Mkoa wa Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Industrial Cluster’s, jambo hili lilijitokeza mwaka 2016/2017, hata hivyo nikifanya tathmini ni Halmashauri chache zimelitekeleza. Nashauri, kwa kushirikiana na TAMISEMI, Halmashauri zipewe maelekezo maalum kutenga maeneo hayo na ikibidi wapewe deadline maana hatuwezi kuwa na viwanda pasipo kutenga hizo Industrial Cluster’s.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Vinyungu na Mita 60 Kutoka kwenye Vyanzo vya Maji. Suala hili nalipeleka kwa Mheshimiwa Waziri kwa kuwa linagusa kilimo moja kwa moja japo usimamizi wa sheria ya mita 60 inasimamiwa na watu wa mazingira kupitia NEMC

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha vinyungu kwa lugha nyepesi tunaweza kusema ni kilimo cha mabondeni. Sasa tafsiri hii ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji au kingo za mito ni tofauti sana na kilimo cha vinyungu. Vinyungu (Iringa na Njombe) au masebula (Kigoma, Katavi, Rukwa na Kagera) ni kilimo cha muda mrefu ambacho ni sawa na asilimia 50 ya maisha ya wananchi wanaoishi kwa kutegemea vinyungu miaka nenda miaka rudi na hakijawahi kuathiri mtiririko wa maji; na ndiyo maana mpaka leo ni mikoa hiyo pekee ambayo vyanzo vya maji vimeendelea kuwepo. Wananchi wanaheshimu vyanzo vya maji, wanatunza maji tena kwa njia ya asili; hivyo vinyungu si tatizo wala chanzo cha kuvuruga vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari; Mkoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, na Ruvuma/Rukwa imeendelea kuwa kimbilio la chakula miaka yote kwa sababu pamoja na mashamba ya kawaida vinyungu vimekuwa na mchango wa zaidi ya asilimia 40 ya chakula katika mikoa hiyo kuanzia mahindi, viazi na mazao ya mbogamboga kwa hiyo kuibuka na kusema tunazuia kilimo cha vivyungu maana yake tunaandaa mazingira ya kuleta njaa kwenye maeneo hayo. Jambo hili litazamwe upya na maamuzi yanayohusu kilimo cha vivyungu, wananchi na sisi viongozi wao tushirikishwe ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Suala la Mbolea. Ukweli ni kuwa mfumo wa ruzuku ulinufaisha watu at individual level wakiwemo wafanyabiashara na baadhi ya watendaji wa Serikali. Uamuzi wa kuagiza kwa mkupuo (bulk) utasaidia. Angalizo ni kama ifuatavyo:-

(a) Haitakuwa na maana ikiwa mbolea itachelewa kuwafikia wakulima wa mbolea vijijini. Kwa mfano kwetu Iringa msimu unaanza Oktoba kuandaa mashamba na kufikia Novemba tarehe 15 wanakuwa wameshapanda bila kujali mvua zipo au hazipo, mbegu hutangulia ardhini. Sasa katika hali hiyo ni vyema mbolea iwafikie mapema Oktoba

(b) Kuhusu upatikanaji, jambo hili ni kubwa sana na mtego kwa Serikali hasa kama upatikanaji na usambazaji utakuwa duni. Ushauri wangu, maandalizi kwa kila msimu yafanywe mapema Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanasiasa VS Ushirika. Serikali imedhamiria sana kutusaidia kupitia ushirika na hasa SACCOS. Baadhi ya maeneo Halmashauri zimeshapokea fedha kwa ajili ya SACCOS za vijana na hata zile milioni 50 kwa kila kijiji, matarajio ni kuwa zitapitia ushirika na SACCOS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na uwepo wa Sheria bado wanasiasa directly or indirectly wanajihusisha kwenye SACCOS na ushirika na wengine ni viongozi. Hili ni bomu mbele ya safari kwa sababu linaweza kuibua chuki, upendeleo na baadaye kuvuruga ushirika na SACCOS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri. Pamoja na uwepo wa sheria ni vizuri Wizara ikasimamia utekelezaji wa sheria na kupitia TAMISEMI mwongozo/waraka ukatolewa kuwaeleza Mamlaka za Mikoa (Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri) kuwa wanasiasa hawaruhusiwi kuwa sehemu ya ushirika/SACCOS ili kuepusha migongano na hatari ya kuvuruga ushirika/SACCOS, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi, nilichangia katika hotuba ya Utumishi na Utawala Bora, kwamba mabaraza haya tuyajengee uwezo japo hata kutembelewa na Mwanasheria as an observer ili tu kujionea proceedings kusudi upungufu
utakaobainika, itafutwe namna ya kuupunguza kwa kutumia ama semina au mafunzo ya muda mfupi kadri ya mazingira yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Diaspora vs Umiliki wa Ardhi; lililoko tamko ambalo limeleta mkanganyiko hasa kwa Watanzania ambao wanaishi nje ya nchi lakini wamebaki na utaifa/uraia wao kama Watanzania. Tafsiri ya watu wengi walioko nje ni kwamba kwa Mtanzania anayeishi nje hastahili kumiliki ardhi kumbe iwekwe wazi kwamba ni haki kwa Mtanzania kumiliki ardhi hata kama anaishi nje ilimradi tu ni raia wa Tanzania kwa wale waliobadilisha uraia diaspora per se, utaratibu mbele ya safari uje utazamwe ilimradi kufungua fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafinga Mjini vs upimaji wa ardhi na uwepo wa Master Plan. Mji wa Mafinga unakua kwa kasi sana kutokana na biashara ya mazao ya misitu (mbao, nguzo, milunda na kadhalika.) Ukuaji huu umeleta mahitaji ya ardhi iliyopimwa kwa kasi, hata hivyo uwezo (capacity) wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga kuendana na speed hiyo umekuwa mdogo kutokana na uhaba wa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi/ushauri, Wizara ifikirie kuwezesha upimaji/uandaaji wa Master Plan kwa Mji wa Mafinga na maeneo mengine ambayo ni miji ili kuepukana na ujenzi holela/squatters. Kwa jitihada zangu nilionana na Profesa Lupala ambaye kwa ushirikiano na ushauri wake, wanafunzi wa field wa Ardhi University watatusaidia kukusanya data ili baadaye Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri yetu tutakamilisha Master Plan. Nimewasilisha ombi la kupewa baadhi ya watumishi wa ilivyokuwa CDA hasa Maafisa Ardhi, Mipango Miji na Wapimaji kama jitihada za kukabiliana na uhaba wa watumishi wa kada ya ardhi ili kufanikisha azma ya kupanga Mji wa Mafinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi; naamini ni jambo la gharama kubwa lakini kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kukabiliana na migogoro ya wakulima na wafugaji, hatuna namna zaidi ya Wizara hii ku-take lead kwenye suala hili ambalo linagusa kilimo, maliasili na hata usalama wa nchi. Tukifanikisha jambo hili tutaondokana na malalamiko mengi ya kila mmoja katika Taifa kuanzia kilimo, kufuga, hifadhi na hata uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutengwa maeneo ya Industrial Clusters; wakati tunapoelekea uchumi wa viwanda ni muhimu kila Halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya viwanda na kwa kuwa uwezo wa kupima maeneo yote ni mdogo, basi angalau tuanze na jambo hili kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambayo imekuwa ikilisema jambo hili mara kwa mara katika kulitekeleza. Nashauri utolewe Waraka kwa kushirikiana na TAMISEMI kuziagiza Halmashauri kutenga hizo Industrial clusters.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mazao ya Misitu Mafinga/Mufindi vs TRA Mkoa ni kubwa na inakua kwa kasi hasa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hususan Iringa na Njombe. Ni Sekta ambayo tulishirikisha wadau katika masuala yanayohusu sekta hii. Serikali itapata mapato na sekta ita-grow. Hata hivyo, hali ilivyo ni kinyume kabisa na hapa naomba niwe open.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hulka yangu kama Mbunge niliyetokea kwenye Utumishi wa Umma, siyo mtu wa kupiga mayowe, lakini ninakoelekea nahisi nitaanza kupiga kelele na mayowe jambo ambalo siyo jema, kwa jitihada zangu kufuatia usumbufu uliokithiri kwenye check point ya Iringa. Niliwasiliana na Waziri na Kamishna Mkuu akiwa Kidatu kuhusu usumbufu na manyanyaso wanayopata wavunaji na wasafirishaji wa mazao ya misitu/mbao pale kwenye check point ya Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nifafanue kidogo. Uvunaji wa mbao uko wa aina kama mbili. Kwenye msitu wa Serikali ule wa Sao Hill ambao mfumo wake uko very clear kwenye misitu na mashamba ya watu binafsi ambapo nako kuna mashamba makubwa kama kuanzia ekari hamsini na kuendelea. Ni wenye mashamba madogo kama ekari moja, mbili mpaka kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inatokea mvunaji mdogo ananunua kwa kuungaunga mpaka kujaza semitrailer au Scania ile tunaita kipisi, mtu huyu anasafirisha mbao lakini akifika check point ya Iringa anadaiwa risiti ya mashine ya EFD. Sasa mtu huyu aliyenunua kwa mwanakijiji ambaye hajui chochote kuhusu EFD, itatoka wapi? Maana nimenunua kijijini kwa mkulima na hana mashine, maana yeye kauza nusu ekari ili apate fedha ziende kumlipia ada mtoto au matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mjasiriamali huyu anatozwa faini kati ya Sh.250,000/= mpaka Sh.750,000/= wakati mzigo wake hauzidi Sh.3,000,000/= kabla ya gharama za usafiri. Mbaya zaidi watu wanatishwa, wanalipa fedha na hawapewi risiti. Fedha inaingia mfukoni mwa individual. Mtu huyo huyo akifika Kibaha anabugudhiwa kwa kuwa ni syndicate, wanapigiana simu na wale wa check point ya Iringa kisha wanamruhusu huyo mjasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifanya nini? Baada ya mawasiliano na Mheshimiwa Waziri na Kamishna wa Kidatu, nilipewa mawasiliano na Kamishna anaitwa Yusufu tukashauriana TRA Mkoa ikae na wadau tujadili muktadha mzima wa biashara hii ili Serikali ipate chake na wajasiriamali walipe bila kufilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha (lazima niwe wazi) Meneja wa Mkoa akiwa ana shaka lakini nikawasihi kuwa mkutano nitausimamia na utakuwa wa amani na wa kujenga. Nashukuru tulikaa na tukaafikiana kuunda Task Force ikihusisha TRA na wafanyabiashara wa mbao. Hata hivyo bado uonevu unaendelea. Juzi hapa malori yamezuiliwa siku tatu. Kiuchumi hii ni hasara kubwa mno. Sitetei kuwa wasilipe, hapana tuwe na utaratibu ambao utazingatia mazingira halisi ya biashara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina kawaida ya ku- personalize issues, lakini kuna mtu anaitwa Onyango ana damage Serikali kwa vitisho, kauli na hata matusi. He is not coorperative at all. Amegeuka kero kuliko kuwa facilitator, labda kwa kuwa amekaa miaka mingi Iringa watu wa Iringa, Mafinga, Kilolo na Mufindi are very humble hawahitaji vitisho zaidi ya kuelekezwa tu, Mawakala wanawatisha watu, wanachukua rushwa, Onyango akipigiwa simu ni vitisho tu. Please naomba mtushirikishe mtusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza hivi nakisi ya bajeti ni 3.9% au ni 11.9%? Kwa sababu mikopo na misaada ni around trilioni 11 lakini deni la Taifa ni trilioni tisa na mikopo siyo uhakika. Kwa nini tusisimame kwenye kilio chetu? Naona kama we are not realistic.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia zaidi kwenye bajeti; lakini hili la mbao mlitazame. Hii sekta ni uchumi mkubwa na angalieni Mufindi inavyochangia pato la Taifa, one of the source ni mbao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kuhusu Maafisa kupelekwa Ubalozini. Napendekeza kuwa kwa kuanzia Serikali ingepeleka Maafisa maeneo ya kimkakati hasa nchi za South-East Asia kama Korea, China na pia nchi au vituo ambavyo ni multiple kama Sweden au Ujerumani ambako Ubalozi unafanya kazi nchi zaidi ya tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kupendekeza umuhimu wa kufungua ubalozi mdogo kwa kuanzia Lubumbashi na Guangzhou. Jambo hili ni muhimu hasa ukizingatia biashara iliyopo katika ya nchi yetu na maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza mara kadhaa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, lakini bado nahisi hakuna uelewa wa pamoja kuhusu suala hili na hasa kuhusu umuhimu wake katika suala zima la FDI. Nashauri Wizara i-take lead hata kwa kuishauri mamlaka kuu kuhusu nafasi ya suala hili hasa katika dhana nzima ya kuelekea uchumi wa viwanda ambao kwa hakika tunategemea pia wawekezaji kutoka nje ambao wangependa kuhakikishiwa masuala muhimu kama Avoidance of Double Taxation na hili la Promotion and Protection of Investments.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada za kutenga fedha za kukarabati majengo, upo umuhimu wa kutafuta mbinu mpya hata kwa utaratibu wa PPP, kadri taratibu zinavyoelekeza ili tujenge kwenye viwanja ambavyo viko maeneo ambayo ni prime, lakini pia hata kimahusiano, viwanja kama pale Maputo, tumepewa zaidi ya miaka 30 iliyopita, hatujaweza kujenga. Nchi husika pamoja na mengine mengi inaweza kuona kuwa hatujali au hatuthamini mchango wao wa sisi kupewa viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posting (downsizing ni sawa na downgrading); ninafahamu kwamba kuna maafisa wamerejeshwa, lakini hatujapeleka Maafisa Balozini. Kuna nchi Balozi yupo peke yake bila maafisa, suala ambalo linaathiri sana utendaji. Nchi kama China, Belgium (EU), France, Italy, Uganda, Sweden, Ujerumani na kadhalika, kimajukumu Balozi kukosa Afisa inadumaza jitihada zote za kuelekea uchumi wa viwanda.

Mhashimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wamekua vituoni, hivyo nina imani wanapata feeling ni kwa namna gani utendaji wa kazi unakuwa mgumu kwa Mabalozi wasiokuwa na Maafisa. Kuna dhana kuwa posting ni kama privilege, ninashauri kama suala hili liko juu ya uwezo wa Wizara, kwa uzoefu wao Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu waieleze mamlaka kuna athari za Mabalozi kutokuwa na Maafisa vituoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo Mabalozi ambao kitaalam na kitaaluma siyo wanadiplomasia, tunajaribu kufikiria Balozi wa aina hiyo awe hana Afisa, atafanya kazi katika mazingira gani? Hata nchi husika zinapata shahada kuwa ni kama tunapunguza mahusianao kwa ku-down size staff.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Honorary Consul Lubumbashi limezungumzwa sana kutokana na umuhimu wa DRC Congo katika uchumi wetu lakini pia halina gharama za kifedha. Je, limefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la malalamiko kuhusu unyanyasaji wa house girls Arabuni limejitokeza mara kadhaa na hata Kamati yetu imelijadili kwa kukutana na baadhi ya wadau na Waheshimiwa Wabunge wenye familia zao Arabuni na hususan Oman.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni vizuri Wizara ikashinikiza ipasavyo na Wizara ya Kazi na Ajira ili kuwepo utaratibu ambao utaondoa ukakasi unaoanza kujitokeza kiasi kwamba suala hili linaweza kuathiri mahusiano yetu na nchi hizo. Uganda wamefanikiwa sana katika suala hili, wapo wanaotaka wasichana wazuiwe kwenda kufanya kazi Arabuni, lakini kwa upande mwingine watu wanataka fursa kufanya kazi nje. Wafilipino wamefanikiwa katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini Serikali ikiweka utaratibu mzuri, jambo hili ni la manufaa kwa Taifa kiuchumi, lakini pia kimahusiano. Ni matarajio kuwa baada ya michango ya Wabunge Mheshimiwa Waziri kwenye majumuisho atasema lolote hasa kushauri wanaofanya kazi ya uwakala wa kupeleka wafanyakazi wa ndani Arabuni kuwasiliana pia na Balozi zetu kwa taarifa tu. Kimsingi suala limejadiliwa sana katika social media na kwa hisia kali sana, ni muhimu Serikali/Wizara kulisemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba mtumishi wa umma anafanya kazi sehemu yoyote ndani ya Serikali. Hata hivyo ni faida zaidi kuwatumia watumishi pale ambapo wanakuwa na tija zaidi. Kwa mfano, maafisa waliorejea hasa watu wa uchumi ambao wamejengewa uwezo kwa kufanya kazi nje, baadhi yao wamepata mafunzo kuhusu diplomasia ya uchumi. Ni matarajio kuwa kuelekea uchumi wa viwanda, maafisa hao kwa uzoefu na taaluma yao wangeweza kuwa msaada mkubwa kwa Wizara. Hata hivyo, waliporejea wamehamishiwa Wizara, bado ninashawishika kuamini kuwa ilikuwa ni tija kuwa-retain watumishi hao kwa kuangalia pia waliingiaje Wizarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, waliokuwepo enzi Mheshimiwa Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Wizara hii watakumbuka alivyotoa wazo la Wizara kupata maafisa wa fani ya uchumi. Good enough wamekaa na kupikwa katika nyanja hii hapo Wizarani na Balozini, lakini ghafla kumeingia uoga kwa kuwahamishia kwenye Wizara nyingine, sijui uoga huu unasababishwa na kitu gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uteuzi wa baadhi ya Wakurugenzi kuwa Mabalozi nje ya nchi, waliopo wanakaimu, nashauri Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu, pamoja na kuwa uteuzi ni suala la mamlaka kuu, ipo nafasi ya kushauri ili Wizara kupata watendaji ambao siyo makaimu kwa nia ya kuleta ufanisi zaidi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu kwa kuzungumza nina mawazo katika kuimarisha sekta ya sukari kutokana na potential ya soko la ndani na nje. Mfano sisi tunaagiza sukari yenye thamani dola za Kimarekani milioni 60.9 (shilingi bilioni 123 za Kitanzania), majirani zetu kama Angola ambao ni member wa SADC wanaagiza sukari kwa thamani ya dola za Kimarekani milioni 161.1, Ethiopia dola za Kimarekani milioni 188, haya ni masoko wazi lakini ili tuyafaidi. Pamoja na mradi wa Mkulazi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, tufikirie kuwezesha wawekezaji wa ndani kupitia benki za TIB na ile ya kilimo TAB ambayo mpaka sasa ina around shilingi bilioni 164 lakini imekopesha shilingi bilioni 3.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwekeza kiwanda cha kuzalisha tani 150,000 inahitaji wastani wa dola za Kimarekani milioni 80 bila kujenga facilities nyingine. Pamoja na mashamba utahitaji jumla ya dola za Kimarekani milioni 150, hapo tayari una miundombinu ya nishati na barabara. Sasa kumbe tutumie mfumo wa small scale growers ambapo tunakuwa na factory nyingi maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na Halmashauri na sekta binafsi. Maeneo potential ya kuzalisha sukari ni pamoja na Bagamoyo tani 120,000; Mkulazi tani 200,000; Ruipa tani 60,000; Rufiji tani 60,000; Kasulu tani 30,000 na Mkongo – Mara tani 30,000, jumla tani 500,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kutumia small scale sugar plants ni kama ifuatavyo:-

(i) Inahitaji eneo dogo kama five acres.

(ii) Inahitaji kama shamba la miwa la ekari 3,000 ili kulisha kiwanda.

(iii) Inapunguza gharama za kusafirisha miwa kwenda kiwandani mfano leo hii pale Kilombero kuna miwa inasafirishwa umbali hadi wa kilometa 60 lakini ikiwa ndani ya shamba la eka 3,000 huwezi kuwa na gharama kubwa ya kusafirisha.

(iv) Inachukua wastani wa miezi kumi kujenga kiwanda cha small scale.

(v) Inahitaji mwaka mmoja kuwaendeleza wakulima wadogo (small scale farms).

(vi) Ina promotes ushiriki wa small holder farmers.

(vii) Ni rahisi kutoa extension service na pia mwekezaji hahitaji kugombania ardhi maana yeye atasaidia small holder kwa mbegu na pia huduma nyingine muhimu kuwezesha kupata miwa yenye content kubwa ya sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muundo huu umewasaidia sana Brazil ambao wanazalisha 20% ya sukari (tani milioni 36) na wanahodhi 40% ya soko la dunia. Hivyo, potential ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Benki ya Kilimo. Nimeona juzi hapa benki ikiwa imepata fedha zaidi. Hata hivyo, kuna matatizo makubwa kwenye hii benki kuanzia Mtendaji Mkuu mpaka Bodi. Mfano, hivi Zanzibar State Trading Corporation (ZSTC) waliomba mkopo wa shilingi bilioni 10 ili wanunue karafuu, Bodi ikapitisha lakini kwa uzembe wa Mtendaji Mkuu mkopo ukacheleweshwa, msimu ukapita baadaye ZSTC wakaukataa mkopo. Tujiulize with a capital of over 164 billion, how come wametoa mkopo wa less than five billion? And this is a bank na main core/function of the bank ni kukopesha. Mliangalie hili jambo ili benki hii iwe nyenzo kuelekea uchumi wa viwnada. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kazi na Ajira (Workers Welfare Viwanda vya Mafinga). Mafinga ina Viwanda vingi vya mazao ya misitu, lakini hali za wafanyakazi ni duni (welfare). Mbaya zaidi wafanyakazi wakipeleka malalamiko Ofisi ya Mkuu wa Wilaya taarifa
zinarudi kwa mwekezaji kumsemea mlalamikaji kuwa ni mtu mbaya, matokeo yake, mfanyakazi anatafutiwa visa anafukuzwa kazi na kwa lugha ya kejeli anaambiwa nenda popote. Naomba na kushauri, Mheshimiwa Waziri afanye ziara ya kushtukiza na akifika aongee na wafanyakazi, asiishie kupokea taarifa ya menejimenti au ya uongozi wa wilaya tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wanapaswa kuwathamini wafanyakazi, OSHA wasiishie tu kuchukua tozo bali wafanye serious ukaguzi, mazingira ya kufanyia kazi ni mabaya, is completely against labour rights. Kwa mfano, kuna kazi ya kupanga magogo, wafanyakazi hawana gloves, hawana mabuti, wamevaa kandambili, hawana kofia, ni mazingira hatarishi. Hawana usafiri, mtu anatembea kilometa nne hadi tano kwenda kazini a total of eight to ten kilometers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa viwanda uendane na hali bora za wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kuongelea kuhusu madeni ya matangazo kwenye magazeti ya Serikali. Sikuona busara kulisema hili hadharani, kiukweli Wizara na Taasisi za Umma zinadaiwa mamilioni ya fedha za matangazo kwenye magazeti ya Daily News na Habari Leo. Je, huko kwenye private media kama Mwananchi, The Guardian, The East African ni kweli kuwa Wizara na Taasisi hazilipii hayo matangazo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyakati hizi ambazo social media imekuwa fast kueneza na kusambaza taarifa ipo sababu kuyawezesha magazeti ya Serikali kwa kulipa madeni ya matangazo ili vyombo hivyo viweze kuendelea kuwekeza na kukabiliana na private media ambazo kwa nguvu ya fedha zinaweza kuwa chanzo cha upotoshaji wa taarifa. Nyote mnajua nguvu ya media, hatuwezi kukwepa kuwezesha vyombo vyetu japo kwa kulipa madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ving’amuzi Vs free channel. Kwa nini wenye ving’amuzi hawaachii free channel tano kama miongozo inavyoelekeza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kupata nafasi. Napenda kuipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa jinsi ambavyo tulishirikiana wakati watu wa Halmashauri wa Mji wa Mafinga tulipopata msaada kutoka Ubalozi wa Japan. Kulikuwa na some complications, lakini kwa ushirikiano mkubwa tuliweza kufanikiwa kiasi kwamba tukafanikiwa kupata huo msaada baada ya Wizara kufanya marekebisho ya kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichangie katika bajeti hii kwa kuanza kusema yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema ni wizi katika Sekta ya Madini, nilikuwa najaribu kupitia nyaraka mbalimbali, mojawapo, ni hii inasema protecting your community against mining companies. Katika document hii imeeleza kwa ufasaha namna gani makampuni makubwa ya madini yanavyofanya mbinu mbalimbali ambayo hitimisho lake ndiyo tunaita wizi. Katika utangulizi wa document hii anasema:

“The company may deliberately try to disrupt and weaken a community’s ability to organize effectively against them.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maana yake ni nini? makampuni yanaweza yakatumia mbinu mbalimbali yakatugawa sisi ili tusiweze kushikamana katika kukabiliana na wizi mbalimbali ambao wanaufanya. Wizi huu unafanyikaje? Kwa sababu wenzetu wako mbali kwa teknolojia na mbinu mbalimbali za kufanya international trading. Moja, wanafanya kitu tunaita trade mispricing. Ndiyo ile wakileta machinery wanakuza bei baadaye wanadai tax refund. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, wanafanya kitu kinaitwa payment between parent companies and their subsidiaries, ndiyo maana tulikuwa tunagombana na Acacia lakini amekuja kuibuka Mwenyekiti wa Barrick ambayo ndiyo Kampuni Kuu. Pia wanafanya wizi huo kwa kutumia profit shifting mechanism ambayo imekuwa designed ku-hide revenue, ndiyo maana tunaita wizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, watatumia mbinu nyingi kutu-divide. Gazeti la The East African la wiki hii limeandika, “Magufuli Fight for Mineral Revenue Splits Parliament.” Hiki siyo kitu kizuri kwetu kama Taifa. Lazima sisi tubaki kitu kama kimoja. Kama Bunge, kama Taifa, lazima tuwe nyuma ya Mheshimiwa Rais ambaye ameamua kuthubutu kukabiliana na huu wizi mkubwa wa Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Director wa Global Justice anasema kuwa Afrika siyo maskini na ukipitia ripoti mbalimbali za Taasisi za Kimataifa, zinasema kwamba kupitia makampuni haya, fedha inayoondoka ni zaidi ya mara kumi ya fedha wanayotupa sisi kama misaada. Maana yake ni nini? Ukienda kwenye bajeti yetu, karibu shilingi trilioni saba ni mikopo, misaada na fedha kutoka kwa wahisani; lakini inayoondoka kupitia wizi huu niliousema, maana yake ni mara kumi ya shilingi trilioni saba. Kwa hiyo, zinazoondoka hapa nchini kwetu ni shilingi trilioni 70, ndiyo maana tunasema wizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa hizi zinazoondoka kwa mbinu hizi mbalimbali ambazo Mheshimiwa Rais ameamua kuwa na uthubutu ili tuweze kukabiliana na multinational companies, lazima sisi kama Taifa na kama Bunge tuwe united, tusigawanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa nini ameweza kuwa na uthubutu? Ukisoma gazeti la Sunday Nation la Jumapili linasema, “Uhuru tycoons raise millions in two hours” kwa ajili ya kampeni, lakini we are lucky Rais wetu ameingia pale hakuwa na backing ya watu wenye hela chafu, kwa hiyo, tunapopata kiongozi wa namna hii, lazima tuwe united kumuunga mkono, kwa sababu tunachozungumzia ni upotevu wa mapato ambayo yakipatikana wote tutafaidika. Wote hapa tunalia, nami nalia kuhusu kukosekana maji, umeme, huduma bora za afya, kuanzia Lumwago, Bumilanyinga, Isalavanu mpaka Itimbo na Mafinga kwa ujumla. Sasa anapotokea kiongozi mwenye uthubutu ni lazima sisi tushikamane kumuunga mkono kukabiliana na multinational companies. Haya madude ni hatari sana, nitawaambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hugo Chaves alipoingia madarakani tarehe 11 Aprili, 2002, alifurumua mikataba kama anavyojaribu kufanya Mheshimiwa Rais. Madude haya (multinational companies) yaliji-organise yakafanya hujuma kumwondoa madarakani lakini kwa sababu Bunge na wananchi wa Venezuela walikuwa united, baada ya masaa 47 alirudi Ofisini. Ndiyo maana nasisitiza ndugu zangu tuwe kitu kimoja kukabiliana na madude haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu siyo wakati wa kutafuta personal recognition. Kila mtu kwa nafasi yake alipaza sauti kuhusiana na hujuma na wizi huu. Wapo waliokuwa wanaharakati wakati huo kama Mheshimiwa Tundu Lissu, wapo waliokuwa Wabunge kama Mheshimiwa Peter Serukamba na Mheshimiwa Kigwangalla ametajwa hapa, wapo akina Rugemeleza na Nshema wale wa LEAT wote walipaza sauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwaka 2008 Mawaziri wanaohusika na Sekta ya Madini walikutana kujadili katika Afrika namna gani tutanufaika kutokana na madini. AU Summit 2009 ilipitisha azimio ni kwa namna gani tutaendelea kunufaika na madini na kuachana na wizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 Mawaziri wa madini katika Afrika walikutana na kujadili na kuja kitu kinaitwa “From Mission to Vision”; na hiki ndicho Mheshimiwa Rais anachofanya. Ametoka from mission to vision to action. Sasa ameingia kwenye action. Anapoingia kwenye action, sisi tuna kila sababu ya kumuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka ujue wizi huu, nenda kasome kitabu hiki cha Nicolaus Shakson; (Treasure Island), “Uncovering the Damage of Offshore Banking and Tax Havens.” Yote haya ni wizi unatumika. Vile vile kasome kitabu cha Mwandishi the same; “Poisoned Worse; The Dirty Politics of African Oil.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kaangalie document inaitwa “Stealing Africa.” Why is Africa so rich in resources, yet so poor? Ni kwa sababu ya wizi wa namna hii ambao lazima tukubaliane tuwe united kama Taifa, tuwe pamoja kama Bunge na kwa maana hiyo, tutaweza sana kufanikiwa. Vinginevyo tukitafuta muda wa recognition, kila mtu played his/her own part. Viongozi wa dini walisema, wananchi wa kawaida walisema, wanaharakati walisema, Wabunge walisema. Kwa hiyo, ni wakati ambao tunatakiwa tukwepe sana kugawanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, wakati anaapishwa Commisioner wa TRA, Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema, “Maafisa wako na Mameneja wa Mikoa waache kutoa kauli za kuigombanisha Serikali na wafanyabiashara, wakusanye kodi kwa kufuata sheria na taratibu na pia wawe na lugha nzuri.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa Mawakala wa TRA, lugha yao na operation namna wanafanya, ni kuigombanisha Serikali na wananchi. Naiomba TRA, pamoja na kutoa elimu ya mlipa kodi, ijaribu kukaa na hawa Mawakala wao iwe inawapa hata training ya namna gani ya kufanya customer care. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda umeniishia naona unanikimbia; katika makinikia haya, yako mengi. Sisi kule Mufindi suala la misitu, nimeshaandika hata katika mchango wangu; MPM wanauziwa magogo mpaka leo nusu ya bei pasipo sababu. Hayo nayo ni makinikia. Kwa hiyo, naiomba Serikali, kama ilivyoanza katika dhahabu, kuna makinikia kwenye misitu, kuna makinikia kwenye fishing industry kutoka bahari kuu, kuna makinikia kwenye mambo mengi, hata kwenye mchezo wetu wa soka kuna makinikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na kwa sababu muda mchache napenda kuanza kwa kuunga mkono hoja na napenda kuwafahamisha Mheshimiwa Mwamoto, Mheshimiwa Mchengerwa, Mheshimiwa King na Mheshimiwa Kitandula na wenzenu Simba moja, Mtibwa sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo kwa haraka kabisa napenda niende moja kwa moja kwenye ukurasa wa 31 wa hotuba ya Waziri Mkuu kuhusiana na upatikanaji wa mbolea. Kitabu kimeeleza kwamba upatikanaji wa mbolea ni asilimia 64 maana yake ni kwamba asilimia 36 wananchi wetu hawapati mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tumeona changamoto nyingi za usambazaji wa mbolea. Ninapenda kuishauri Serikali kutokana na changamoto zilizojitokeza mwaka huu hebu ijaribu kuangalia ili wakulima wetu waweze kupata mbolea sio tu kwa bei nafuu, lakini kwa wakati. Inasikitisha sana kuona mkulima wa Isalavanu, kule Itimbo, kule Kitelewasi anapata mbolea ya kupandia mwezi wa pili wakati uandaaji wa mashamba unaanza mwezi wa kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali kwa changamoto ambayo wamekutana mwaka huu kwenye usambazaji wa mbolea, hebu wazipitie na kuona kwamba kwa namna gani tutamsaidia mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama vile haitoshi tumeona kwenye ukurasa wa 27 unaozungumzia upatikanaji wa chakula tumekuwa na ziada ya chakula tani milioni 2.6. Lakini wale wanunuzi wa chakula NFRA wamenunua tani 26,000 tu za mahindi maana yake ni kwamba mazao yale ambayo ni ziada yameenda wapi? Yamekosa soko, sasa mwananchi huyu mkulima wa Itimbo, wa Bumilainga mbolea tunamcheleweshea lakini anafanya jitihada anazalisha ziada bado tunamzuia kuuza mazao yake. Kwa kweli tunakuwa tunawafanya wakulima kama second citizen katika nchi yetu.

Kwa hiyo, napenda kushauri maana yake Bunge ni kuishauri Serikali hebu iweze kuona upatikanaji wa mbolea kwa wakati, lakini pia kunapokuwa na ziada ya chakula tuwasaidie wananchi hao kupata soko tusifunge kuwazuia kwamba wasiuze nje kama ilivyotokea kwenye mazao ya mahindi tunawakatisha tamaa, muda ni mchache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili naomba sana Mheshimiwa Mama Jenista Mhagama, Kaka yangu Antony Mavunde nadhani ni mdogo wangu kuhusiana na suala zima la uchumi wa viwanda. Ni kweli tunasisitiza na Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla imekuwa mstari wa mbele tunamuona Rais amekutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara amesikiliza kero zao, ameelekeza Mawaziri wazitatue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, rai yangu tunapoita wawekezaji na uchumi wa viwanda lazima twende sambasamba na kuangalia walfare ya wafanyakazi wanaofanya kazi katika viwanda hivyo, itakuwa haina maana leo hii kama mimi mfano pale Mafinga tuna wawekezaji lakini unakuta mama anatoka Changarawe anaenda Kinyanambo C kibaruani anatembea almost kilometa sita mpaka tano mpaka saba; mfanyakazi huyu analazimika kuamka saa kumi alfajiri, ana-risk maisha yake anaenda kazini, mshahara mdogo, hakuna NSSF, hakuna matibabu.

Sasa mambo haya nikuombe Mheshimiwa Mavunde kwa sababu ndio unahusika moja kwa moja Kazi, Ajira na Vijana, tembelea Mafinga, toa maelekezo kwa wawekezaji ili kusudi uchumi wa viwanda uende sambasamba na kuangalia walfare ya wafanyakazi, vinginevyo tutaleta viwanda, lakini hali za wananchi wetu zitaendelea kuwa duni itakuwa haina maana kweli Serikali itapata kodi lakini pia lazima wananchi wetu wafurahie uchumi wa viwanda kwa wao kupata kazi ambazo watalipwa vizuri, lakini pia haki zao zitakuwa zinazingatiwa ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia maana muda ni mchache sana naomba niende haraka kwenye point yangu ya mwisho kuhusiana na sekta binafsi. Nimepongeza jitihada za Mheshimiwa Rais lakini mimi naomba na kupendekeza kwa Serikali kwa mikono miwili kabisa baada ya kukutana na wafanyabiashara wale tumeona kabisa concerns zao na tumeona muda ulikuwa ni mchache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwa Serikali na naomna Mheshimiwa Rais akiweza akutane pia na sekta kwa sekta mfano sekta mojawapo sekta ya usafirishaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhitaji mkubwa wa sukari na mafuta hapa nchini. Kinachohitajika ni kutengeneza mazingira bora ya kuzalisha miwa na oil seed (alizeti, ufuta na kadhalika). Naamini Serikali ikifanya kazi kwa pamoja kati ya Wizara za Kilimo, Wizara ya Viwanda na Wizara ya Fedha, kwa mfano, Brazil imefanikiwa kutokana na kuwekeza katika viwanda vidogo na vya kati, hii ni kwa sababu kuwekeza katika viwanda vikubwa inahitaji fedha nyingi lakini pia huchukua muda mrefu mpaka hata miaka mitano na ndiyo maana Wizara inayo kila sababu kutengeneza mazingira ya kuibua maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa na uwekezaji wa viwanda vya sukari. Tujifunze kutoka Brazil, potential ipo kubwa na ya wazi. The same can be applied kwenye suala la mafuta ya kula. Ninaamini hata kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi (JKT) tunaweza kuibua maeneo yanayofaa kulima oil seeds (alizeti) na kadhalika ili kuwa na malighafi ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini Wizara ya Kilimo iki-take lead, Taifa hili litapiga hatua na dhana hii ya uchumi wa viwanda itakuwa ya vitendo na yenye kuleta tija. Pamoja na mchango huu, naambatanisha nakala yenye kuonesha maeneo potential kwa uwekezaji wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wamesema sana kuhusu mbolea. Ushauri wangu ni kwamba hiyo inayoitwa ruzuku, afadhali fedha yake ingetumika kufanya distribution, kwa maana kuwa isaidie ku-cover gharama za usafirishaji. Hii ni kwa sababu wakulima wanachohitaji ni mbolea kuwafikia kwa wakati. Suala la bei kwao siyo issue sana, issue ni mbolea iwafikie kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengi nchini ambayo tunaweza kujenga viwanda vidogo na vya kati (tani 10,000 mpaka tani 30,000 kwa mwaka). Kila mkoa una maeneo kama haya, kwa mfano, Kilosa tani 10,000; Manyara tani 10,000; Mara tani 30,000; Ruvuma tani 10,000; Dodoma – Chamwino tani 10,000; Kigoma – Bonde la Malagarasi tani 30,000; Pwani – Rufiji tani 30,000 na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendelezaji wa viwanda vidogo unachukua muda mfupi, kama miezi minane hadi kumi. Gharama zake ni za chini USD milioni tatu hadi USD milioni 10 ukilinganisha na vile vikubwa USD milioni 100 hadi USD milioni 300 ambavyo huchukua miaka miwili mpaka mitano. Viwanda vidogo viko karibu na wananchi. Bei ya sukari yake ni nafuu kutokana na gharama kuwa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri za Wilaya husika zinaweza kuingia ubia na wawekezaji wazalendo katika maeneo yao na miradi hii inaweza kuingizia mapato Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hizi muhimu. Awali ya yote ninapenda kusema mambo mawili nimemuona Mheshimiwa Mwigulu pale Simba tatu Mbeya City moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa niliseme katika kazi nyepesi duniani ni kazi ya kukosoa hata kama unatazama mpira ni rahisi sana kusema pale Okwi angefanya hivi au Chirwa angefanya hivi lakini ukiingia mambo yanakuwa ni tofauti kabisa. Kwa hiyo, this is the easiest job in the world! Hawa wenzetu wanapokosoa Waheshimiwa Mawaziri niwatie moyo tu kwa sababu wanafanya easiest job in the world wewe take easy tu chapa kazi kanyaga twende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nami kama wenzangu ninapenda kuwashukuru Mawaziri na watendaji katika Wizara hizi, Mheshimiwa Selemani Jafo Waziri wa TAMISEMI, Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Gorge Kakunda na Mheshimiwa Josephat Kandege, Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa George Mkuchika. Pia hata Makatibu Wakuu wa Wizara hizi ukienda pale TAMISEMI kwa Mhandisi Mussa Iyombe au kwa mama yangu Dkt. Zainab Chaula na kwa Dkt. Ndumbaro pale Utumishi bado sijapata nafasi ya kukutana na wale Manaibu wengine. Kiongozi yule anatoka kwenye Kiti anakuja huku anakusikiliza, mnajidiliana mnashauriana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la namana hiyo ndiyo uongozi ni jambo la kupongezwa unashida za wananchi wako wanakusikiliza mnashauriana the way forward. Kwa hiyo, ufanyaji wa kazi wa namna hii mimi niwapongeze. Hii ndiyo namna pekee ya kumuunga Mheshimiwa Rais mkono katika ndoto zake za kuendelea kuisogeza nchi yetu mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi niseme pia pongezi za jumla kwa Serikali kwa watu wa Mafinga, tunapenda kuishukuru sana Serikali katika masuala ya afya, maji na elimu kwa sababu usipokuwa mtu wa kushukuru maana yake ni kwamba wewe pia hustahili kuwepo kwa maoni yangu. Mpaka sasa tumepokea shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, fedha hizi zitaongeza mzunguko katika Mji wa Mafinga. Mwenye kusomba kokoto mwenye kusomba tofali, mama lishe, wote hawa wanatakuwa ni wanufaika wa fedha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imetusaidia katika maji nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji tuna tanki pale la lita laki tano na sasa tumeanza ujenzi wa tanki lingine la lita milioni moja. Hizi ni hatua changamoto bado zipo, haziwezi kumalizika siku moja lakini ni vizuri kushukuru pale ambapo inastahili kushukuru. Kama haitoshi tuna mradi kule Maduma wa ujenzi wa tanki la lita 100,000 pia tuna mradi kule Bumilainga unaendelea, yote ni kusogeza huduma karibu na wananchi, hata katika elimu tumepata takribani shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuboresha miundombinu kwenye shule ya sekondari Changarawe, shule ya msingi Maalum Makalala ambapo Mheshimiwa Jafo ukiwa Naibu Waziri baada ya kutembelea tu immediately tukapata shilingi milioni 100 tukajenga bweni na bado tena tumepata karibuni shilingi milioni 220 kuendelea kuboresha miundombinu katika shule ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi katika afya tumepata shilingi milioni 500 nawashukuru sana Mawaziri, Mheshimiwa Waziri wa Afya tumepata ambulance shughuli zinaendelea, yaani ni kwamba kwa lugha nyingine pamoja na kuwa changamoto hazijaisha unaweza kusema Mafinga mambo ni moto. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye changamoto Mheshimiwa Waziri niwaombe, mlituomba tulete taarifa za miradi viporo kutokana na zile fedha za LDG, sisi tunasubiri pesa zile kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya cha Bumilainga, ukamilishaji wa zahanati tatu za Kitelewasi, Kisada na Ulole pamoja na nyumba za watumishi. Pia kukamilisha hostel ya wasichana ya Mnyigumba katika kata ya Lungemba na pia kukamilisha ukarabati wa shule ya msingi Kikombo jumla ni milioni 859 ambazo kama Serikali mliona kwamba tuainishe maeneo ambayo katika kuunga mkono juhudi za wananchi basi, ninyi mtatupa pesa tumalizie miradi viporo. Niombe Serikali kama ni Wizara ya Fedha kama ni TAMISEMI basi fedha hizi tuletewe ili tupate kukamilisha miradi ile ambayo wananchi kwa nguvu zao walikuwa wa kwanza kuianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la TARURA, tunashukuru kwamba Mafinga tumepata fedha milioni 500 tumeboresha kituo cha afya cha Ihongole, lakini tunashida kubwa ya barabara unafikaje katika kituo cha Ihongole. Kati ya mahitaji ya Mafinga kwa ajili ya barabara kwa kweli kama siyo changamoto ya barabara kama nilivyosema, katika mambo mengine kwa jinsi tunavyokwenda mpaka kufika mwaka 2020 Mafinga mambo yatakuwa ni moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni fire kabisa. Shida kubwa iko katika barabara, kati ya mahitaji bilioni 8.2 kwa mfano kwaka huu 2018 tumetengewa kutokana na ukomo wa bajeti shilingi milioni 830 hii ni kama asilimia kumi ya bajeti, kwa nini.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ninasema katika suala la TARURA ndugu zangu hata tukiwa na TARURA kumi, kama hatutabadilisha kanuni ya mgao wa fedha za Mfuko wa Barabara maana yake ni kwamba hatuwezi kupiga hatua yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati shughuli hizi zingine za maendeleo zinaenda ni muhimu sana kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine katika kuhakikisha kwamba mazao yanasafirishwa kwenda sokoni. Kwa mfano, Mafinga katika barabara tulizonazo only asilimia 24 ndiyo zile tunaita good and fair kwamba zinapitika, lakini barabara nyingine kiasi cha takribani kilometa 288 ambayo ni asilimia 88 ya barabara ni za udongo. Kwa mfano, hii barabara ya kutoka Mashine ya Mpunga kwenda mpaka Kituo cha Afya Ihongole kwa kuwa ni ya udongo na ile wanaita average daily traffic ni 4,030 maana yake ni kwamba hata ukitengeneza kila wiki kwa sababu ina traffic kubwa itaharibika tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suluhisho na ushauri wetu Wabunge tutakapoleta Finance Bill hebu katika hizi fedha pamoja na kazi nzuri ambayo TANROADS wamekwishafanya tupeleke mgao kutoka asilimia 30 mpaka walau asilimia 50, kwa sababu TARURA wenye barabara zaidi ya kilometa laki moja wanapata asilimia 30, TANROADS wenye barabara takribani kilometa 30,000 wanapata asilimia 70 ya fedha. Hata tuwe na TARURA bado wananchi wa Mafinga, wa kutoka Changarawe kwenda kule Mtula ambako kuna irrigation scheme hawataweza kunufaika na ku-feel matunda mema ya Serikali ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli. (Makofi)

Kwa hiyo, suluhisho pekee, kwa sababu kazi yetu Wabunge ni kushauri, tushauri kwa pamoja ili kanuni ya mgao wa fedha za barabara iweze kubadilika ili TARURA isibakie kuwa TARURA jina bali iwe TARURA ambayo ina resources za kuweza kufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia napenda kuipongeza Serikali, wenzetu wa Mufindi kwa jitihada zetu pamoja na Mheshimiwa Kigola, Mheshimiwa Dada Rose Tweve, Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa sasa wanakwenda kupata shilingi 1.5 bilioni ili wawe na hospitali yao na hivyo kupunguza msongamano katika hospitali ya Mafinga. Hata hivyo, kwa kuwa hospitali hii haitajengwa overnight ndiyo maana nasisitiza tupate fedha zile za miradi viporo ili tukamilishe zile zahanati na Vituo vya Afya vya Bumilainga kusudi kupunguza msongamano kwenye Hospitali ya Mafinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja na Mungu aibariki Mafinga, abariki watu wa Mafinga na aibariki Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, zuio la mifuko ya plastic; nchi jirani zote katika kutekeleza the so called EAC Polytene Material Control Bill ilipitishwa baada ya muda wa karibu miaka mitano, zimezuia kabisa uzalishaji, usambazaji na matumzi ya mifuko ya plastic. Sisi Tanzania mpaka sasa tumeendelea kuzalisha mifuko ya plastic kwa namna ambayo imejaa ujanja mtupu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Kenya na Uganda kuzuia, sasa sisi tumegeuzwa soko. Kati ya tani zaidi ya 1,500 zinazosambazwa kwa mwaka ni tani 100 tu ndo zinazalishwa hapa nchini, maana yake ni kuwa chini ya asilimia kumi ndio inazalishwa hapa nchini. Hivyo hoja ya kuwa tunalinda viwanda sio kweli kwa sababu asilimia 90 ya mifuko inatoka nje na zaidi nchi jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira wanasema Viwanda, Biashara na Uwekezaji ndio kikwazo, wao hawana tatizo. Ni matumaini yangu kuwa kwenye hitimisho, Wizara itakuja na maelezo ni kwa nini mpaka sasa haijazuia uzalishaji kama inavyodaiwa wa mifuko ya plastic?

Mheshimiwa Mwenyekiti, BRELA na usajili wa kimtandao; wananchi wengi siku za nyuma waliliwa fedha zao na middle men, lakini toka usajili kuanza kufanyika kwa njia mtandao (online) kumekuwa na ufanisi wa hali ya juu, ni suala la kupongeza, ushauri, BRELA ifanye semina nyingi kadri iwezavyo ili elimu hii ienee maeneo mengi hasa yenye uzalishaji, kwa mfano Mafinga ina shughuli nyingi za mazao ya misitu, kuna mbao lakini wengi wa wafanyabiashara bado hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuwa na kampuni na faida zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ya kubahatisha; hii ni biashara inayokuwa kwa kasi sana. Hata hivyo taratibu zinazotawala biashara hii hazileti matunda bora, kwa mfano ilivyo sasa katika Sports Betting, mchezeshaji analipa asilimia sita ya mauzo ghafi. Hii iliwekwa kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, baada ya kukua kwa hii biashara, ni wakati sasa kuzingatia yafuatayo:-

(i) Kuonesha uhuru/kodi ya mauzo kutoka asilimia sita hadi asilimia 20. Maana yake katika kila shilingi 100 Serikali itapata shilingi 20 badala ya shilingi sita ilivyo sasa.

(ii) Ili kuvutia wachezaji wengi ambao sasa baadhi yao wameanza kupendelea kucheza Sports Betting za nje kwa hoja kuwa makato ya asilimia 14 ya zawadi ya mshindi ina-discourage. Ni afadhali kanuni ikawa kwa mfumo wa capital gain asilimia kumi. Hii itachochea wengi kucheza na Serikali kupata nyingi katika ile asilimia 20 ya mauzo ghafi maana washindi ambao hutupatia asilimia 18 ni wachache kuliko wachezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vilivyobinafsishwa; ushauri wangu kama ambayo Serikali inatutajia idadi ya viwanda, ituambie status ya viwanda vilivyokuwa vimebinafsisha ikoje, vingapi vinazalisha na kwa capacity gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya mazao ya misitu; nimeshaiomba Wizara na Waziri tufanye kongamano tukihusisha vyombo vyote muhimu kama vile BRELA, OSHA, TIC, TIB, TRA, TFS, NEMC na Wizara ili wawekezaji wa mazao ya misitu waweze kuelezwa fursa zilizopo, lakini pia kueleza changamoto wanazokabiliana nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya mazao ya misitu ni eneo lenye potential kubwa. Ni masikitiko yangu kuwa jitihada za kumuomba Waziri kutembelea Mafinga ili kujione uwekezaji lakini pia kujionea changamoto zinazowakabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, fedha za CDG, maombi haya tuliyaleta baada ya Serikali kutuandikia kuwa tutambue na kubainisha miradi viporo ambayo Halmashauri na wananchi waliibua na baadhi ya miradi wananchi wamejikongoja zaidi ya miaka kumi. Tulipopokea barua hiyo tuliona ni ukombozi mkubwa. Mfano sisi Mafinga tulipanga kukamilisha Kituo cha Afya cha Bumilyinga (shilingi milioni 413); kukamilisha Zahanati tatu za Kitelewaji, Kisada na Ulole na nyumba tatu za wauguzi (shilingi milioni 203); kukamilisha hostel katika shule ya sekondari ya Kata Mnyigumba katika Kata ya Rungemba (shilingi milioni 19) na ukarabati wa shule ya msingi Kikombo kujenga madarasa nane (shilingi milioni 179) na jumla shilingi milioni 859. Naomba sana Hazina watusaidie fedha hizi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu gaming/sports betting, kuna dhana kuwa watoto wanaharibika kwa ku-bet,, sio hoja ya msingi, hili ni suala la maadili, tujiulize mbona watu na Taifa tunategemea kodi kwenye vileo? Sports betting imeshakuwa kwa kasi sana, kwa mwaka 2017 iliingiza shilingi bilioni 28.2 ambayo ni sawa na bajeti ya Wizara ya Habari.

Mheshimiwa Spika, kuna potential kubwa sana kwenye sports betting, kitu muhimu ni usimamizi bora na kuweka mazingira bora ya kuvutia wachezaji wengi, kwa sababu kinyume chake watu wanakimbilia kucheza online nje ya nchi. Hivyo basi ushauri wangu:-

Mheshimiwa Spika,tulipoanza ili kuvutia wawekezaji tuliweka kodi asilimia sita ya GGR, hivi sasa kwa kuwa industry imekua, tuongeze kutoka asilimia sita hadi asilimia 20 ya GGR. Lakini wakati huo huo tuvutie zaidi wachezaji wawe wengi ili tufanikiwe.

Mheshimiwa Spika, tupunguze kodi kwa mshindi kutoka asilimia 18 ambayo ni VAT tuifanye asilimia kumi as a capital gain. Kwa kufanya hivyo itavutia wachezaji wengi na Serikali itapata zaidi kutoka asilimia sita hadi asilimia 20 ya GGR. Mfano mchezeshaji akikusanya shilingi milioni 100 maana yake Serikali itapata shilingi milioni 20 kama asilimia 20 badala ya shilingi milioni sita ya sasa ambayo ni asilimia sita.

Sasa katika hiyo shilingi milioni 100 ikiwa jumla ya washindi wakawa wamepata shilingi milioni 15 maana yake asilimia 18 ni shilingi milioni 2.7 ukijumlisha na ile shilingi milioni sita ya asilimia sita jumla Serikali itapata shilingi milioni 8.7, lakini ingekuwa ni GGR ya asilimia 20 Serikali ingepata shilingi milioni 20 na pia ingepata asilimia kumi ya shilingi milioni 15 as capital gain ya shilingi milioni 1.5 hivyo jumla Serikali ingepata shilingi milioni 21.5 badala ya shilingi milioni 8.7. Huu ni mfano mdogo tu lakini ambao unaihakikishia Serikali mapato kutoka kwenye GGR.

Mheshimiwa Spika, hali ilivyo sasa watu wengi wana- opt kucheza online kwenye makampuni ya nje na Serikali inakosa fedha. Sio dhambi kabisa kuvutia wachezaji wengi hasa kwenye sports betting. Mfano Australia kati ya watu kumi, watu saba wanacheza sports betting, so tuvutie wachezaji wengi tupate GGR. Ahsante
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata nafasi. Nianze tu kwa kuipongeza Wizara, Mawaziri pamoja na taasisi zilizopo chini yake. Pia nitoe pongezi za pekee na niseme labda ni shukrani kwa Wakala wa Misitu Tanzania kwa sababu mara ya kwanza nilipoingia hapa Bungeni nilizungumza sana juu ya umuhimu wa Wakala wa Misitu kukutana na wadau wa sekta ya misitu hasa walioko katika Jimbo la Mafinga Mjini na Wilaya ya Mufindi. Nawapongeza kwa sababu mwaka jana kabla ya msimu tumefanya kikao na mwaka huu alikuja Mtendaji Mkuu Profesa, tarehe 30 Aprili. Tumesikilizana na wadau, naamini Wakala wamechukua mawazo yao na watayafanyia kazi. Hivi ndivyo inavyotakiwa kufanya kazi kwamba tunapotoa ushauri kwa Serikali ikiuchukua na kuufanyia kazi inakuwa ni kwa manufaa yetu sisi na wananchi wetu kwa ujumla wake katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nizungumzie changamoto chache ambazo ziko kwenye sekta ya mazao ya misitu. Moja, tulipokutana na wadau walizungumzia lile suala ambapo ukishafanya malipo ili uingie msituni kuvuna unapewa siku zisizozidi 30 uwe umeshamaliza kuvuna na zile siku 30 zinahesabia Jumamosi na Jumapili. Sasa nitoe mfano, kama huo mwezi tarehe 1 imeanza ni Jumamosi maana yake kuna siku takribani 10 zitakuwa Jumamosi na Jumapili. Maana yake ni kwamba huyu mdau anakuwa ana siku 20 tu, zile 30 zinakuwa ni kwa maneno. Kwa hiyo, niiombe Serikali hususani Wakala wa Misitu, hebu tuangalie, mtu akishalipia zile tunazoita siku 30 basi ziwe siku 30 za kikazi, tusijumuishe Jumamosi na Jumapili na pia tuondoe kama hapo katikati kutakuwa na siku za sikukuu ili kumpa huyu mtu nafasi ya kufanya kazi kwa ufanisi na kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni changamoto katika check points. Watu wa mazao ya misitu hususani mbao, nguzo na mirunda kuna zaidi ya check point karibu 10 na nitazitaja kwa haraka. Kwa mfano, mtu akitoka kule Mufindi anakutana check point Mtiri, Makwave, Lungemba, Tanangozi pale kwenye kaburi la Kiyeyeu, Igumbilo, Ruaha Mbuyuni, Sangasanga pale kwenye njiapanda ya kwenda Mzumbe, Chalinze, Vigwaza na Kiluvya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi tunapoelekea uchumi wa viwanda watu wanaosafirisha mazao ya misitu hususani mbao, mirunda na nguzo hawaruhusiwi kusafiri mara baada ya saa 12.00 jioni. Sasa imagine mtu anatoka Mafinga anakwenda Mwanza atatumia wiki nzima kufika Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kwa kuwa tayari tuna check point na kuna magari yanafanya patrol hebu turuhusu watu wasafiri usiku, kwa sababu tuna slow down speed ya kukuza uchumi katika Taifa. Sehemu ya kutumia siku mbili, kwa mfano, mtu akitoka Mafinga kufika Dar es Salaam sanasana ni siku moja lakini analazimika kutumia siku tatu. Maana yake ni nini? Kwanza umeongeza gharama za uendeshaji kwa mwenye gari na matokeo yake yule mtu ataziongeza zile gharama kwa mwenye mzigo matokeo yake mlaji wa mwisho atajikuta anapata mzigo kwa bei kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, kwa kuwa tuna check point na tuna magari ambayo yanafanya patrol hebu turuhusu hili kusudi tukimbize uchumi. Kwa sababu hawa watu, kwa mfano, wenye magari wanaosafirisha mizigo hii wanajaza mafuta; maana yake ni kwamba kama akienda akirudi mara nyingi tayari pia Serikali itakuwa imepata fuel levy. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweze kulitazama suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ambalo napenda kulizungumzia pia ni kwenye sekta hii ya misitu. Pale Mufindi, Mafinga kulikuwa na majengo ambayo yalikuwa ni madarasa, ofisi za walimu na mabweni kwa ajili ya chuo kidogo cha masuala ya mazao ya misitu. Sisi watu wa Mafinga, Mufindi na Nyanda za Juu Kusini tunaomba tuwe na chuo ambacho kitafundisha masuala haya ya mazao ya misitu. Kwa nini nasema hivi? Sisi ndiyo wenye msitu mkubwa Afrika ya Mashariki na Kati maana yake ni kwamba hata mazoezi kwa vitendo lakini pia hata wale ambao watakuwa wamejifunza iwe rasmi au kwa mafunzo ya muda mfupi watatumika katika viwanda mbalimbali ambavyo wawekezaji wamewekeza katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika kikao cha wadau tulizungumzia umuhimu wa wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo kuhakikishiwa malighafi. Wawekezaji hawa wanachukua mikopo iwe ya ndani ya nchi, nje ya nchi, benki za ndani au kwa namna nyingine yoyote wenye mabenki wanasita kuwapa mikopo kwa sababu hana guarantee ya kupata material. Kwa hiyo, niombe Wakala wa Misitu, kama walivyosema katika ukurasa wa 38, Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa kwamba ameunda kikosi kazi ambacho kitapitia hali ya upatikanaji wa material katika Kiwanda cha Mgololo. Hawa wawekezaji kuanzia Mgololo, Sao Hill na wawekezaji wengine siwezi kuwataja kwa majina pale Mafinga Mjini wanahitaji kuwa guaranteed kupata material ili kusudi waweze kuwa na uhakika wa kuchukua mikopo ambapo kweli wenye mabenki wataweza kuwadhamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, hawa wawekezaji, nisome kipengele kimoja katika Biblia, 1 Timotheo 5:8 inasema, mtu yeyote asiyewatunza na kuwathamini wale wa nyumbani kwake hasa, ameikana imani tena ni mbaya kuliko asiyeamini. Sasa mimi wa nyumbani kwangu ni nani? Mimi wangu ni pamoja na wapiga kura lakini na hawa wawekezaji ambao wakiwa guaranteed material mimi siasa zangu zinakuwa nyepesi kwa sababu ni kazi sana kuongozo mwenye njaa lakini hawa watu wakiwa na material maana yake watu wangu watapata vibarua, watapata kazi, watapata kipato chao na watakuwa na mchango wa uchumi katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hapa kuhusu TANAPA kutozwa kodi. Mara kadha hata Mheshimiwa Rais amesema na mimi nilikuwa wa kwanza kusema humu ndani, nchi yetu ina vivutio vingi, lakini hata makampuni ya soda, jiulize Coca Cola, Pepsi kila siku wanatangaza, nani asiyeijua Coca Cola au Pespi? Kila mtu anaijua. Kwa hiyo, mimi nashauri hizi gharama ambazo mnaikata TANAPA bora mngewaachia kwa kiwango fulani ili kuwaongezea nguvu TANAPA na Ngorongoro ya kujitangaza na pia kuiwezesha TTB ili kusudi vivutio hivi viweze kweli kuleta watu. Biashara yoyote ni matangazo, sasa utatangaza wakati bajeti yenyewe ni ndogo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, katika Mkoa wa Iringa kuna maeneo mengi ambapo wapigania uhuru akiwemo Mandela na Sam Nujoma wamepita. Niiombe Serikali, kwa mfano, kuana eneo la Kihesa Mgagao, sisi tumelifanya gereza lakini kumbe lile eneo tungelifanya la makumbusho hata watu wengi kutoka Kusini mwa Afrika wangeweza kwenda pale na kuona kwamba, ala, kumbe Mandela alipita hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo Sam Nujoma alitumia jina kama Sam Mwakangale ili aweze kupata passport ya Kitanzania kuendesha harakati zake za uhuru wa Namibia. Hebu tuyang’amue hayo maeneo nayo tuongeze katika sekta yetu ya utalii, yatatupa mapato kuliko ambavyo tumeyafanya yapo chini. Hizi Serengeti na kadhalika pamoja na kuwa tunazitangaza lakini tuyatambue maeneo hayo tuwekeze katika utangazaji ili kusudi mapato yaweze kuongezeka katika utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, niishauri Serikali, hebu ijaribu kufikiria kuhusu single entry. Single entry inaumiza wadau ambao wako kandokando ya mbuga za wanyama. Hawa ni part na parcel wa kunufaika na mbuga lakini kutokana na single entry matokeo yake watu hawa wanakuwa idle, vijiji havizalishi na hatimaye wanajiingiza katika shughuli ambazo si salama na ni illegal katika mustakabali mzima wa sekta yetu ya maliasili na utalii. Kwa hiyo, hebu Serikali ijiridhishe, mimi naamini ina mbinu za kutosha kuweza kudhibiti ile sababu iliyosababisha kuwepo na single entry ili kufanya pia vijiji vinavyozunguka mbuga viweze kuwekeza navyo viweze kupata watalii lakini pia watalii waweze ku-enjoy mbuga zetu na tamaduni za wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuchangia kuhusu wafanyakazi wanaolipwa kwa kifungu 5000 (mapato ya ndani) katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga (Mafinga TC). Kufuatia kugawanywa kwa Halmashauri ya Mufindi na kupatikana Mafinga TC, wafanyakazi wengi wanaolipwa kwa mapato ya ndani walipelekwa Mafinga TC. Mafinga TC tunatumia around Sh.12,000,000 kila mwezi kulipa wafanyakazi hao ambao miongoni mwao wako ngazi ya uandamizi. Hali hii imekuwa na changamoto kubwa mbili kwa Halmashauri ya Mafinga Mji na kwa watumishi.

(i) Kwa halmashauri, tunajikuta tunatumia kiasi cha Sh.120,000,000 kwa mwaka kulipa mishahara ya watumishi. Kama watumishi hao wataingizwa katika mfumo wa Hazina, fedha hiyo itasaidia katika shughuli za maendeleo.

(ii) Kwa watumishi, kutokana na mishahara yao kutegemea makusanyo ya ndani, wafanyakazi hawa wamekuwa wakichelewa kupata mishahara, hali hii imekuwa ikiathiri hata huduma zao za afya. Mara mbili mfanyakazi ameshindwa kupata huduma Hospitali ya Ikonde kwa sababu ilionekana kuwa michango ya bima ya afya haijawasilishwa. Baadhi yao waliokopa benki, marejesho yanacheleweshwa na kujikuta wakipigwa penati. Hali hii inawaathiri sana wafanyakazi hao, wanajihisi ni second citizen.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itusaidie kuwaingiza watumishi hawa ili walipwe na Serikali Kuu. Yawezekana ni jambo ambalo lipo katika halmashauri nyingi, lakini naomba Mafinga TC tutazamwe kwa macho mawili. Kuna hoja kuwa Mafinga tuna mapato ya Msitu wa Sao Hill, lakini ukweli ni kuwa beneficiary wa Msitu wa Sao Hill ni Mufindi DC, hivyo, naomba mtusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu kupandishwa madaraja/vyeo watumishi. Kuna manung’uniko makubwa sana kuhusu kubadilishwa kwa tarehe za wao kupanda vyeo, baadhi yao walipanda mwaka 2015. Ni kweli kuwa maelekezo ya kuhakiki vyeti na suala zima la watumishi hewa, suala hili lilisitishwa, aidha, mishahara yao haikubadilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, waraka ulitoka kuwa barua au kupanda vyeo kusomeke kuanzia 1/11/2017 na wengine kuanzia tarehe 1/4/2018. Nafahamu yawezekana kutokana na suala la kibajeti Serikali inaona kuwa itakuwa na mzigo mkubwa wa kulipa malimbikizo. Hali hii inaweza kushusha morali ya watumishi. Kama Serikali haitawalipa malimbikizo ni miaka almost mitatu itapotea na hivyo kuathiri hata pension zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hekaheka nyingi za kuweka sawa masuala ya watumishi wa umma, nashauri na kupendekeza kuwa watumishi hao waangaliwe upya na vyeo vyao vizingatie tarehe ya awali ya kupanda vyeo. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji dhidi ya kazi/ajira; pamoja na jitihada za Serikali kuifanya TIC kuwa chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, bado kuna jitihada inapaswa zitazamwe katika suala zima la welfare ya wafanyakazi katika maeneo yaliyowekezwa. Wafanyakazi hawalipwi ipasavyo, hakuna social security, hakuna utaratibu wa bima za afya, kimsingi ustawi wa wafanyakazi katika sekta binafsi ni eneo linalopaswa kutazamwa kwa ukaribu na wenzetu wa kazi na ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa umma wakati wa uhakiki wa watumishi, wako ambao kimakosa waliondolewa kwenye mfumo na baadaye walirejeshwa. Hata hivyo hawajalipwa malimbikizo yao ambayo kimsingi mamlaka husika zimeshayathibitisha, isipokuwa ni Hazina kufanya malipo. Suala hili hakika linashusha morali ya watumishi, nashauri na kupendekeza Hazina walipe malimbikizo hayo kwa kuwa ni makosa ya kibinadamu ambayo yamerekebisha ni muafaka sasa wa kulipa malimbikizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme; Mafinga kutokana na viwanda vingi Mji wa Mafinga nimeshauri mara kadhaa nishati (TANESCO) watazame kwa macho mawili pawepo na Wilaya ya ki-TANESCO ya Mafinga maana pia Mufindi kama Wilaya ina Viwanda vingi vya Chai, Karatasi Mgololo, hivyo uhitaji wa umeme ni mkubwa sana kutokana na mazao ya misitu. Nashauri kuwa uwekezaji tunaovutia uendane na upatikanaji wa umeme wa viwandani maana kadri uzalishaji unavyoongezeka ndivyo na ajira na mapato zaidi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kuhusu malipo ya watumishi waliorejeshwa kwenye mfumo. Kuna watumishi ambao waliondolewa kimakosa kwenye payrollna baadaye wakarejeshwa, hata hivyo, hawajalipwa malimbikizo yao. Mfano, Mafinga wapo watumishi 51 na jumla ya madai ni Sh.118,164,330na mpaka sasa hawajalipwa. Hali hii pia iko kwanchi nzima, naomba Serikali itusaidie watumishi hawa walipwe madai yao hayo.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kuanza kwa mambo mawili. Kuna mtu anaitwa Beno Kakolanya na kuna mtu anaitwa Cletus Chota Chama au sisi watu wa Simba tunamwita triple C, kwamba mtu anapofanya jambo jema anastahili kupongezwa, wala si dhambi kupongeza. Ndiyo maana mashabiki na wapenzi wa Yanga na hata wa Simba siku ya Simba na Yanga tulimpongeza Beno Kakolanya kwa sababu aliokoa magoli mengi ya wazi. Ndiyo maana hata wapenzi wa mashabiki wa Yanga wanampenda na kumpongeza Cletus Chota Chama kwa kwa sababu anafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Kuna mambo yamefanyika ni wajibu wetu kama Wabunge kupongeza na kuitia moyo Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaenda kwenye mengi nitaenda kwenye afya tu ukurasa wa 30, ukarabati wa hospitali za wilaya 10, vituo vya afya 295 na nyumba za watumishi 306. Kama hiyo haitoshi nikienda ukurasa wa 33 kwenye suala la elimu tumeona ongezeko la watoto kutoka milioni 1.5 mpaka milioni 2 kutokana na elimu bila malipo. Hawa watoto laki tano maana yake ni kwamba wangekosa masomo, wangekosa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hatua hizi tunazopiga kuna tabia inataka izuke katika taifa letu la kuzua taharuki, ni lazima tuikemee. Kuna watu wapo tayari wao kuzua sura ya hofu. Nitatoa mfano, watu wanatoa hoja hapa, hivi mimi kwa mfano kwetu Mafinga familia yangu imemuita mke wangu Mafinga, hivi wewe nyumba ya tatu


unaanza kuperuzi kwa nini ameitwa kwenda mafinga kujadili mambo yao ya familia? Watu wamemuita Balozi wao wanaenda ku-discuss issue zao why do you speculate wanaenda kujadili nini, uitake Serikali ikuambie eti ameitwa kwa nini? Thus is none of your business. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge hii hali ya kupenda kuzua hofu, jambo dogo tu kulikuza na kuleta hofu hofu; na ndiyo maana na mpongeza sana Katibu Mkuu Dkt. Bashiru katika mdahalo mmoja alipoeleza kuhusu hofu, alisema wenye hofu ni mafisadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unafanya kazi zako, unawakikilisha wananchi wako kama Chumi hapa, kwa nini usiringe?


Kwa hiyo, lazima sisi kama viongozi tuwe mstari wa mbele kueleza yaliyo mema na kuonesha mstakabali kwa lugha njema na zaidi ya yote sisi kama Bunge kushauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu hapa wamesema hapa FDI (Foreign Direct Investment) zimeshuka.


Nataka niwaambie globally zimeshuka kwa asilimia 23 siyo sisi tu, kutoka trilioni za Kimarekani 1.37 mpaka trilioni 1.43.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Afrika zimeshuka kwa asilimia 21, katika East Africa zimeshuka kwa asilimia 25.3 kutoka dola za Kimarekani bilioni 8.8 mpaka bilioni 6.6 na hapa anguko hilo katika East Africa sisi tuna nafuu. Ukienda Kenya ndiyo ime-record the highest anguko ni asilimia 60.6 yaani kutoka bilioni 1.8 mpaka dola milioni 717.7, Uganda anguko ni asilimia 14.2 sisi Tanzania asilimia 7 yaani ni Rwanda na Burundi tu ndiyo ambao wamekuwa na afadhali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Rwanda kutoka dola za Kimarekani milioni 600 mpaka dola milioni 1.2, hata Burundi kutoka dola za Kimarekani milioni 65 mpaka dola milioni 146. Kama una akili timamu unaweza kulinganisha dola milioni 186 ambazo zimeingia Burundi na sisi ambao tumeingiza hapa nchini dola bilioni 3.3 kama FDI? Kuna nchi zimepongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi si takwimu za Cosato Chumi, nenda kwenye ripoti ya UNCTAD (United National Conference on Trade and Development), The World Investment Report ya 2018. Katika FDI zilizokuja hapa East Africa sisi ndiyo the highest. Katika dola bilioni 4 zilizokuja katika East Africa sisi tumepata share ya 1.2 bilioni FDI, Uganda 0.7 bilioni dola za Kimarekani na Kenya 0.67 bilioni. Kwa hiyo, hata katika East Afrika yaani sisi tume-attract the highest. Sasa haya mambo pamoja na mapungufu yake lazima tupongeze halafu tuangalie sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye Easy of Doing Business bado hatupo vizuri, maana yake tukiwa vizuri tutavutia zaidi ya hii tumevutia. Kwanza kabla sijaenda kwenye hiyo, hizo FDI maana nisiseme tu FDI zimeleta nini? Katika East Africa sisi zimezalisha ajira zaidi ya 20,000 sawa na asilimia 20 waliotuzidi ni Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nachotaka kushauri, tumesema Bunge kazi yetu ni kushauri, katika ile Easy of Doing


Business Index sisi tume-fall, tupo namba 147 ukilinganisha na Rwanda ambao ni 29 na ni kwa nini tumeanguka? Kuna mambo mengi, Mheshimiwa Dkt. Mpango pamoja na jitihada hizi za kujenga mazingira wezeshi, miundombinu, nishati na kadhalika tunalo jambo moja kama Serikali kuchelewa kufanya maamuzi. Kwa hiyo, ni lazima tuambizane ukweli Serikali kuchelewa kufanya maamuzi na kwa wakati ni tatizo. Mtu amepata work permit Labour akienda Immigration anachelewa kupata residence permit. Kuna contradiction ya maamuzi katika maeneo mbalimbali ya mamlaka, tukiweza hili maana yake ni kwamba tutavutia uwekezaji. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuboresha mazingira tuangalie pia na ndani. Haiwezekani umetoa mbao Mafinga unapeleka Mwanza unaambiwa usafiri mchana tu ikifika saa
12.00 umesimamishwa, uta-run vipi uchumi? Gari kwenda Mwanza inatumia siku nne ingetumia siku mbili au siku moja maana yake kwanza hiyo gari ingejaza mafuta mengi na Serikali ingepata fuel levy. Kwa hiyo, haya ndiyo mambo ya kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa kumalizia, lazima nimpongeze Mheshimiwa Kangi Lugola. Hata ukienda nchi za watu kuna maeneo wanafanya biashara saa 24. Huwezi ukazuia biashara za watu saa tano, hivi wewe uende pale Mikumi uwaambie wale akina mama ikifika saa tano wafunge biashara wakati wao biashara yao wanategemea watu ambao wako on transit. Uje Mafiga uwaambie kina mama ntilie wafunge biashara saa nne wakati wao client wao wanategemea vijana waliotoka msituni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna maeneo tujaribu kuboresha na wala si sheria, ni kanuni ambazo Mawaziri wanaweza wakazirekebisha ile Easy of Doing Business ikawa nzuri tukavutia foreign investment, tukapata mapato mengi ili huu mpango tukaugharamie ipasavyo kwa sababu tumeona mikopo kutoka nje na misaada haiji kwa ile pace tuliyotarajia. Kwa hiyo, kikubwa lazima kitoke ndani, kitatoka ndani vipi ni kwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu awabariki kwa kunisikiliza, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nitatumia vizuri dakika tano. Awali ya yote, kwa niaba ya wananchi wa Mafinga, niseme napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, niliposimama hapa 2017 kutetea suala la vinyungu kuna baadhi ya watu hawakunielewa lakini kwa watu wa Mafinga, Mufindi, Iringa, Kilolo, Njombe na maeneo yanayofanana kwetu vinyungu ni maisha na maisha ni vinyungu kwa sababu ndiyo uchumi wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nijielekeze kwenye jambo ambalo nimekuwa nikilisema na sitaacha kulisema, suala la Serikali kufikiria na kuona umuhimu wa kuruhusu kusafirisha mazao ya misitu saa 24. Hapa ninapozungumza saa 11.00 hii umepakia mbao zako pale Mafinga huwezi kuondoka mpaka kesho saa 12.00 asubuhi, hii tunachelewesha uchumi. Naomba Serikali na hasa Wizara ya Maliasili na Utalii waliangalie jambo hili na bahati nzuri nime-peruse naamini sijakosea nimegundua ni kanuni siyo sheria. Kwa hiyo, bado Mheshimiwa Waziri anaweza akakaa na wadau akalifanyia kazi tukaruhusu malori yasafiri saa 24 kusafirisha mazao ya misitu ili tu first track uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa nina hesabu ndogo tu, ukichukua mzigo kutoka Mafinga mpaka Mwanza unatumia mafuta takribani lita 880. Kwa maana kwenda kwa sababu una mzigo utatumia 530 kurudi kwa sababu huna mzigo utatumia 350 na katika kila lita moja Serikali inapata fuel levy 313. Kwa wiki moja gari inaenda mara moja lakini the same, lori kwa wiki moja ingeweza kwenda mara tatu na ikienda mara moja Serikali inapata fuel levy Sh.274,400 ikienda mara tatu kwa wiki Serikali itapata fuel levy Sh.826,200. Maana yake ni kwamba kwa wiki moja kama Serikali itapata fedha hiyo basi kwa mwezi itapata Sh.3,304,800 na fedha hizi zinaenda kwenye Road Fund. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba yaani sisi wenyewe kwa kutoruhusu magari yasafiri usiku tumejipunja kama Serikali. Maana yake ni nini, gari moja Serikali badala ya kupata shilingi milioni tatu point something kutokana na fuel levy inaishia kupata milioni moja inapata loss ya shilingi milioni mbili. Wote tunalia na umeme wa REA, Sh.100 kwa kila lita inaenda kwenye REA. Kwa hiyo, gari zikisafiri kwa haraka na usiku maana yake Serikali nayo itapata mapato na wale wananchi uchumi wao utakuwa umezunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutoka Mafinga mpaka Dar es Salaam tuna checkpoint siyo chini ya 10 at the same time tuna magari ya patrol, hii sheria yenyewe ukii-trace ni ya 1959 wakati Serikali ya wakoloni haina vitendea kazi vya kutosha ndiko uliko originate. Kwa hiyo, naomba kama Serikali ina wawasi na mbao pori sisi ambao miti yetu tunapanda wenyewe ituruhusu tusafirishe saa 24. Haiwezekani mchana ukutane na roli, basi na gari za Wabunge, malori hata Ulaya traditionally yanasafiri usiku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hilo nizungumzie suala la utalii ambao unachangia fedha nyingi za kigeni. Ukienda katika utalii kuna tozo na kodi 33 yaani kama unataka kufanya kazi kwenye industry hii inabidi ujipange na tozo 33 na hizo 33 zenyewe leo unaenda kushoto, kesho kulia, kesho kutwa nyuma, siku nyingine mbele. Hii ni sekta inayochangia sana mapato kuwa na One Stop Center ili kurahisisha facilitation kuhakikisha kwamba utalii na hizi ndege tulizoleta unaendelea kuchangia pato la Taifa kutoka asilimia 17 kwenda zaidi ya hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Serikali iliondoa maduka ya duty free yaliyokuwa yakitumika kutoa huduma kwa watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwepo Polisi, Magereza, Zimamoto na kadhalika na imeleta utaratibu wa kulipa kiasi cha fedha kama mbadala wa duty free.

Hata hivyo, watumishi wa Uhamiaji wamekuwa hawalipwi licha ya kuwa nao ni sehemu ya vyombo vya ulinzi na usalama. Hali hii inaleta hali ya unyonge hasa kwa kuzingatia kuwa kazi zao ni za ulinzi na usalama. Nashauri Serikali ione umuhimu wa kuwajumuisha Uhamiaji ili na wao wapate huu unafuu.

Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa gari ya polisi kati ya Dodoma na Iringa. Barabara ya Dodoma – Iringa hivi sasa inatumiwa na magari mengi ya mizigo, abiria na binafsi. Hata magari ambayo ni transit kati ya Tanzania na nchi za jirani yanatumia barabara hii ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Cairo-Johanesburg. Pamoja na umuhimu huu, hakuna huduma ya gari la polisi hali ambayo ni hatari sana, hasa inapotokea ajali ambayo ina majeruhi wanaohitaji huduma ya haraka. Pamoja na kuwa siyo jukumu la Jeshi la Polisi kubeba majeruhi lakini uwepo wa gari unasaidia kufika eneo la tukio kutoa msaada wa kiusalama.

Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 19/4/2019 (Ijumaa Kuu) nilipata ajali kati ya Chipogolo na Mtera. Nawashukuru sana Askari wa Kituo cha Chipogolo, pamoja na usafiri wa kuunga-unga walifika kutoa msaada. Nikiwa eneo la ajali, nilishuhudia magari ya viongozi wakiwemo Wabunge, Mawaziri na mengine ya Serikali yakipita na ndipo nilipobaini kuwa barabara hii inahitaji kuwezeshwa hasa kwa vyombo vya usafiri walau katika Kituo cha Chipogolo (upande wa Dodoma) na Migori (upande wa Iringa).

Mheshimiwa Spika, naamini aina yoyote ya gari itawasaidia. Nasema haya nikiwa ni mhanga wa hali halisi kwa sababu baada ya ajali ambayo haikuwa na madhara kwa maana ya majeruhi, ilituchukua zaidi ya saa zima kupata msaada wa lifti ya gari. Sasa nilijiuliza ingekuwaje au inakuwaje pale ambapo kumetokea majeruhi wanaohitaji msaada wa haraka? Naamini hata kupitia wadau, Jeshi la Polisi wanaweza kupata msaada wa gari.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na nilikuwa nateta hapa na dada yangu Mheshimiwa Rita, tukasema kwamba, kuna siri katika mafanikio ya hii ofisi. Siri yenyewe nimeona katika watendaji wakuu wa hii ofisi wako hapa saba na ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde, lakini katika hawa saba watano ni akinamama, kwa hiyo, kweli, akinamama wanaweza. Mimi ni mtoto wa mama, nalelewa na sasa hivi na mke wangu ni mama, kwa hiyo, akinamama wanaweza. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Umeona, una mabinti wangapi?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina binti mmoja na yeye najua atanilea wakati ukifika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, kwa haraka kabisa kwanza napenda kupongeza jambo moja kubwa ambalo Serikali na Mheshimiwa Rais amelifanya, nalo ni kutupa Waziri ambaye maalum kabisa atahusika na masuala mazima ya uwekezaji. Pia, napongeza hatua za Serikali kuamua chombo kinachohusika na uwekezaji kwa maana ya TIC kukiweka chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nadhani hii itarahisisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ambayo Serikali imejiwekea katika kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hivyo tu, naona pia jitihada nyingi ambazo Serikali inazifanya ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundombinu wezeshi. Tunaona kuna mradi mkubwa utakaokuja wa umeme, yote hii ni kuhakikisha kwamba, uchumi wa viwanda kwa sababu, uchumi wa viwanda bila kuwa na nishati ya uhakika hatuwezi kuufikia. Kwa hiyo, jitihada hizi bila shaka kila mmoja anayo sababu ya kuzipongeza, tunasema kwamba, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Naamini kabisa kwa Serikali kuamua kuwa na Waziri maalum ambaye atahusika na mambo ya uwekezaji, changamoto nyingi ambazo wawekezaji wale ambao tunawavutia wanakutana nazo, lakini pia na wawekezaji wa ndani, zitaenda kupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ninao ushauri kwa Serikali; suala la kwanza nashauri kwamba, pia tuweze kuangalia magumu gani au vitu gani ambavyo ni changamoto katika ku-slow down masuala mazima ya uwekezaji. Kwa mfano, naona kabisa tunayo hii Wizara na tunaye Waziri na tunacho hiki chombo cha TIC, lakini kuna maeneo chombo hiki hakina mamlaka ya kufanya maamuzi. Kwa hiyo, niiombe na kuishauri Serikali tuamue kwa wakati, tumekuwa na shida ya kuamua kwa wakati na hata Mheshimiwa Rais mara kadhaa amesema ni afadhali uamue ukosee ufanye marekebisho mbele ya safari kuliko kutoamua kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano; kule kwetu Mafinga tuna kampuni ambayo imekusudia kuajiri vijana 1,000 kwa ajili ya kuvuna gundi kwenye Msitu wa Sao Hill. Pengine watu mnaweza mkashangaa kwamba, watu wengi wanadhani kwamba, miti ni kwa ajili tu ya mbao, lakini katika miti pia unaweza ukavuna gundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hii inavuna gundi ma-container kwa ma-container na inasafisirisha kupeleka China, lakini sasa wanataka wajenge kiwanda ili ile processing iweze kufanyikia pale Mafinga. Maana yake ni kwamba, ajira zitaongezeka, lakini ninapozungumza sasa hivi kuna kitu kinaitwa National Land Allocation Committee, ni miezi nane wale wawekezaji bado hawajapata hati ili kuwawezesha kuanza kufanya kazi. Huu natoa ni mfano mmoja tu, lakini unaweza kuona kuna mambo mengi ambayo jitihada hizi zote ambazo zinafanywa na Serikali, kama vyombo mbalimbali ambavyo kwa namna moja au nyingine vina-cut across kwenye suala la uwekezaji, hatuwezi kupiga hatua mbele. Maana yake ni kwamba, Mheshimiwa Mama Angella Kairuki na vyombo vyake watabaki tu kuratibu, lakini kama vyombo vingine havifanyi maamuzi kwa wakati hatuwezi kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa pengine ningependa kabisa kuzungumza kuhusu taasisi mbalimbali ambazo zinafanya kazi ya udhibiti, yaani hizi regulatory authorities. Nitatoa tu mfano vyombo kama OSHA, NEMC, TBS, WMA nikiwa na maana wale Wakala wa Vipimo, SUMATRA na
kadhalika. Ningeshauri vyombo hivi ifike wakati vijielekeze katika kufanya kazi ya ku-facilitate kuliko ku-ambush wawekezaji. Vijielekeze katika kutoa elimu kabla ya kufanya ambush na kufanya masuala ya kupiga ma-penalt. Kwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba tutakuwa kweli yale mazingira bora ya uwekezaji ambayo yanaendana na uwekezaji katika miundombinu kama umeme, barabara na kadhalika yataweza kufanya wawekezaji kweli waje na wawe wenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba tutakuwa kweli yale mazingira bora ya uwekezaji ambayo yanaendana na uwekezaji katika miundombinu kama umeme, barabara na kadhalika yataweza kufanya wawekezaji kweli waje na wawe wenye tija. Kama hiyo haitoshi, niombe na kushauri pia wakati tuna- focus kuvutia wawekezaji kutoka nje tuangalie pia na wale ambao tayari wameshawekeza wanakutana na changamoto gani wanakutana nazo ambazo pengine tukiweza kuwaondolea zitawasaidia wao kupiga hatua na hivyo kuongeza ajira lakini kuongeza pato la uchumi katika taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, natoa rai kwa Serikali na hasa kwa wenzetu wa Kazi na Ajira, uwekezaji huu lazima uendane na ku-reflect welfare ya wafanyakazi katika maeneo yale ambayo wanafanya kazi. Hapa nazungumzia kulipwa kwao, masuala mazima ya hifadhi ya jamii na bima za afya. Nitatoa mfano na hili nimelisema mara nyingi, pale Mafinga tuna wawekezaji hasa wa kigeni hawajali na ku- observe na ku-comply kwenye sheria za kazi. Hawaruhusu vyama vya wafanyakazi, hawalipi bima za afya na hawatoi michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kutoa rai kwa Mheshimiwa Mavunde naomba ufanye ziara katika Mji wa Mafinga ambako viwanda vipo kwa wingi sana uweze kujionea hali halisi. Pamoja na Mheshimiwa DC na RC kufanya ziara lakini bado nashauri wewe pia ufanye ziara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kutoka mwisho ni chakula. Natoa ushauri, kutokana na bei ya mahindi kushuka sana, wakulima wa maeneo ambayo chakula kinalimwa kwa wingi kidogo walikata tamaa, hawajalima kama inavyotakiwa na tunaona una hali kidogo ya ukame katika baadhi ya maeneo. Kwa hiyo, nishauri Serikali kupitia Hifadhi ya Chakula inunue chakula cha kutosha iweze kuhifadhi ambapo baadaye itakuja kuuza kwa bei nafuu kwenye maeneo ambayo yatakuwa hayana chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki kama sitazungumzia barabara. Tuna chombo tumeanzisha kinaitwa TARURA, Waheshimiwa Wabunge na Serikali kwa ujumla, kama hatutaiwezesha TARURA kuwa na fedha za kutosha, nilisema mwaka jana tunaweza tukawa na TARURA hata 100, bila fedha za kutosha katika chombo hiki barabara hazitajengwa kama tulivyokusudia. Kweli Serikali imejielekeza katika barabara za kuunganisha mikoa na imefanya kazi nzuri sana lakini sasa nashauri wakati umefika tujielekeze kwenye hizi barabara ambazo zinabeba mazao kutoka vijijini na kuleta kwenye barabara kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mimi pale Mafinga kwa kweli barabara wakati huu wa mvua yaani ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, naona suluhisho pekee ni TARURA kuwezeshwa kuwa na fedha za kutosha ili kuweza kutengeneza barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, napongeza kwa Tanzania ku-qualify kwenda AFCON. Nimesema mara kadhaa, michezo ni biashara, uchumi na ni ajira. Tutumie fursa hii tunapokwenda Egypt lakini pia tutumie fursa na Waziri Mkuu amesema ya U-17, wenzetu wa TFF na Baraza la Michezo watusaidie kuratibu katika namna ambayo kufanyika kwa mashindano hayo hapa nchini kutakuwa ni neema kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwe na management nzuri ya namna ya kuingia pale uwanjani hasa Uwanja wa Taifa kwa sababu hamasa ni kubwa, watu wanajitolea kwa wingi kuja uwanjani lakini mtu anafika uwanjani anapoteza saa nzima anaingia uwanjani bado dakika kumi. Ni suala tu la ku-manage ili kusudi watu wanapokuja uwanjani viingilio vinapatikana lakini pia hamasa inakuwa kubwa na wananchi wananufaika. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kupata nafasi. Nianze kwa pongezi kwa hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri. Pia niipongeze kama walivyosema wenzangu wengine; Mheshimiwa Mwamoto, na Mheshimiwa Ngeleja, kwamba umekuwa ni mwaka wenye mafanikio katika soka letu na katika michezo kwa ujumla. Tukianza na Taifa Stars kufuzu kwenda AFCON, hatujawahi kufanya hivyo karibu miaka 40. Ni jambo la kujipongeza na sasa tuelekeze nguvu katika maandalizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama vile haitoshi, tumekuwa waandaaji wa Under Seventeen ya AFCON. Ile kuandaa, pamoja na matokeo ambayo hayaridhishi katika Timu yetu ya Serengeti, lakini kule kuweza kuandaa mashindano haya maana yake ni kwamba kama tunavyosema michezo ni ajira, michezo ni biashara, wakati ujao tunaweza tukaandaa pia mashindano makubwa zaidi. Kwa hiyo, ni kama lesson ya sisi kujiandaa katika kufanya maandalizi ya kufanya mashindano haya makubwa ya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitakuwa siyo mwingi wa fadhila kama sitapongeza Bunge Sports Club, tulikwenda pale Burundi wote kuanzia wavuta kamba, soka, riadha, wavu na netball. Kwa kweli kwa sababu mimi nacheza soka kama kiungo mchezeshaji, napenda pia kutoa pongezi za pekee kwa Walimu wetu Mheshimiwa Venance Mwamoto na Mheshimiwa Ahmed Ngwali, walitufundisha na tulicheza mchezo wa kuvutia mpaka walikuwa wanashangaa, ninyi kweli ni Wabunge? Kwa hiyo, pongezi sana kwao na kwa timu nzima ya Bunge Sports Club, lakini kwa uongozi mzima kuanzia Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na Sekretarieti kwa maana ya Katibu wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima niseme kuhusu Simba Sports Club, wamefika robo fainali, ni hatua kubwa katika mashindano ya Vilabu katika Bara la Afrika, nayo imetusaidia sisi kutubeba kama ambavyo wamesema wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo mara zote nimesema michezo inaenda na hamasa. Pia nitakuwa siyo mwingi wa fadhila nisipowataja baadhi ya wasemaji wa Vilabu ambao kwa kweli wanatia chachu na hamasa kubwa sana. Mtu kama Masau Bwire, nadhani kuna watu hawamjui kwa sura lakini wanamjua kwa kumsikia; mtu kama Thobias Kifaru wa Mtibwa, Masau Bwire yuko Ruvu; mtu kama Haji Manara; watu kama kina Jafar Idd Maganga; watu hawa wanaleta hamasa ya kuwezesha watu kwenda viwanjani, lakini kama ambavyo tuliona tulipokwenda Burundi, Bunge tulikuwa kitu kimoja. Michezo inaweza kuleta umoja, michezo inaweza kuleta mshikamano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema pongezi hizi, niseme kwamba michezo, sanaa na burudani ni biashara. Kwa takwimu nilizonazo, nchi kama kama Nigeria na Marekani, yaani baada ya ajira inayotolewa na Serikali, inayofuatia ni ile inayotolewa na Sekta ya Michezo, Sanaa na Burudani. Watafiti wamekadiria kwamba, kufikia mwaka 2020, mapato katika Sekta hizi za Michezo, Sanaa na Burudani yatafikia shilingi trilioni 2.2 dola za Kimarekani. Unaweza ukaona ni fedha kiasi gani. Kwa hiyo, nasi hapa nchini ili tuweze kunufaika, vyombo vinavyohusika kama walivyosema wenzangu, viweze kusimamia ipasavyo kutengeneza mazingira bora ili sanaa, michezo na burudani iweze kuwa chanzo cha mapato lakini kama ambavyo sasa ni chanzo cha ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo hivi ni pamoja na BASATA, TFF, Bodi ya Filamu, Shirikisho la Riadha na kadhalika, wajielekze kutengeneza mazingira bora ya kuvutia pia hata wadhamini. Kwa sababu, kwa mfano mchezo wa soka leo hii hatujapata wadhamini kwenye ligi kuu yetu. Kwa sababu gani? Inawezekana mdhamini anakuja mahali ambapo anaona kuna umakini na usimamizi bora. Leo hii ligi yetu ukianzia waamuzi, ni mambo ambayo kwa kweli yako shaghalabaghala.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilienda kuangalia mchezo wa Panama na Baobab hapa katika uwanja wa Jamhuri, hakuna hata huduma ya kwanza. Kuna mambo yanahitaji fedha. Mchezaji kaumia, nimeona amebebwa mgongoni. Kuna mambo ni management, ni usimamizi tu wa kawaida ambao unaongea na Mganga Mkuu wa eneo husika, tunaomba huduma ya kwanza, anawasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bila kuwa na usimamizi ambao ni madhubuti katika michezo, naamini kabisa hatuwezi kuvutia wadhamini; na ile dhana ya kwamba michezo, sanaa na burudani ni sehemu ya ajira na ni chanzo cha mapato, hatutaweza kuifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati tunajielekeza kutafuta fedha, lakini wale wanaohusika na dhamana ya michezo tuhakikishe kwamba tunasimamia kwa ufasaha ili kusudi makampuni yaweze kuwekeza fedha zao. Leo hii tunapozungumza ligi kama ya Uingereza, Champions Leage, inakuwa na mvuto. Wadhamini wanapigana vikumbo kutia fedha zao, kwa sababu iko well organized. Kwa hiyo, kuna mambo yanataka tu usimamizi, kuna mambo tu yanataka management.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, nami nimpongeze pia mwamuzi pekee anayechezesha kwenye AFCON ambaye ni mwana mama Jonesia Rukyaa Kabakama. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule AFCON Mheshimiwa Waziri kati ya waamuzi 56, hakuna hata mmoja ambaye anatoka Tanzania. Hii nayo ni sekta ambayo tunatakiwa kuiangalia, tulee waamuzi, tuwasaidie, walipwe vizuri. Kwa sababu kama tunasema ni chanzo cha ajiria, pia tunapopata waamuzi wanaokwenda kuchezesha michezo ya Kimataifa, kwanza tunatangaza Taifa letu, lakini wanachopata wanakuja kuwekeza hapa nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, nami naomba kuunga mkono hoja. Naomba tujielekeze sasa kuishangilia Serengeti. Pamoja na yanayotukuta, lakini tusikate tamaa, hakuna mwanzo mwepesi, mwanzo daima ni mgumu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kazi nzuri sana inayofanywa na Bodi ya Mikopo hasa ufuatiliaji wa madeni, lakini pia na huduma nzuri hasa ofisi yenu ya Dodoma watumishi na meneja wao wanasikiliza hongera sana. Hata hivyo, wapo walipaji ambao wameshamaliza mikopo ambayo walikatwa zaidi ya walichokuwa wanadaiwa ambapo sasa ile fedha kurejeshwa inasumbua sana. Nashauri sana inapotokea hivyo wahusika warejeshewe zaidi yao ili waendelee kuwa Mabalozi wema wa Bodi ya Mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kuna suala la majina kufanana pamoja na kuwa marejesho hufanywa kwa kutumia check number, zipo cases ambazo kutokana na majina kufanana kunatokea nyakati makato ya mtu A anakatwa mtu B na yale ya B anakatwa A and vice versa. Nashauri Bodi iliangalie hili ili kuondoa mtu kukatwa mara mbili na mwingine kutokatwa marejesho. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya vifaa vya upasuaji. Naishukuru Wizara kwa kuelewa hali halisi ya Hospitali ya Mafinga ambayo inahudumia Halmashauri ya Mafinga Mji, Mufindi DC na Wilaya za jirani ikiwemo Mbarali (Madibira), Mlimba, Iringa Vijijini na Makambako na hivyo Serikali kutupatia fedha za kujenga na kuboresha Kituo cha Afya cha Ihongole angalau imeleta nafuu kwa Hospitali ya Mafinga ambayo pia ipo kandokando ya barabara kuu ya Tanzania-Zambia (TANZAM I).

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na huduma kuendelea kuboreshwa, tumejikuta idadi ya watu wanaohudumiwa ikiongezeka hasa akina mama wajawazito ambao theluthi moja hufanyiwa upasuaji. Kutokana na hali hiyo, tulipata msaada kutoka Ubalozi wa Japan ambapo tumejenga jengo la upasuaji. Hata hivyo, msaada huo ulihusu jengo tu na siyo vifaa. Halmashauri tumejipanga na tumenunua baadhi ya vifaa. Naomba Wizara ione uwezekano wa kutusaidia baadhi ya vifaa ili tufungue na tuanze kutoa huduma kwa baadhi ya vyumba kwa kuwa jengo lina vyumba vitatu vya upasuaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango huu wa maandishi, naambatanisha barua ambayo niliwasilisha kwako na maelezo ya ziada kuhusu mradi huu. Naamini chochote kitu, anything can make a difference. Nafahamu mna jukumu kubwa kupitia MSD, tunaomba sehemu ya vifaa tusaidiwe kwa kiwango chochote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, barabara, maeneo ya uzalishaji. Pamoja na jitihada za kuunganisha mikoa kwa mikoa, nashauri na kupendekeza Serikali iongeze nguvu kwenye maeneo ya uzalishaji kiuchumi ili kuchochea shughuli za uzalishaji na hivyo kuongeza Pato la Taifa. Mfano, Wilaya ya Mufindi, Barabara ya Mafinga kwenda Mgololo ni uti wa mgongo wa uchumi kuelekea kwenye Viwanda vya Chai, Karatasi na Mazao ya Misitu. Wakati wa mvua unakuta malori yamekwama kwa wiki nzima, hii maana yake ni ku-slow down speed ya uzalishaji na hasa usafirishaji.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi inachangia Pato la Taifa kwa kuwa miongoni mwa wilaya tano bora kimapato. Pamoja na hali hii, bado inaweza kuchangia zaidi ikiwa barabara hii itapitika mwaka mzima. Hivyo, nia yangu hapa ni kuishauri Serikali kuwa itazame maeneo ya kimkakati kiuchumi hata kama maeneo haya hayaunganishi mkoa kwa mkoa.

Mheshimiwa Spika, mawasiliano; Mji wa Mafinga ni mji wa kibiashara na unakuwa kwa kasi sana kutokana na uwepo wa shughuli za viwanda vya mazao ya misitu. Hata hivyo, kuna maeneo ambayo ni just about or less than 15 kilometres from Mafinga Town, hakuna mawasiliano. Mawasiliano ni component muhimu kwenye shughuli za kiuchumi na purchasing power iko juu, wakipata mawasiliano yatachangia uchumi kwa kununua data na muda wa maongezi. Hivyo naomba mawasiliano katika Vijiji vya Kisada, Bumilayinga, Ulole, Kikombo, Maduma na Itimbo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kufanya ziara/kongamano la wawekezaji na wafanyabiashara Mafinga. Wakati tunaelekea uchumi wa viwanda, Mafinga tumepiga hatua kubwa hasa katika suala zima la mazao ya misitu. Hata hivyo, tuna changamoto nyingi sana kuanzia masuala ya Regulatory Authorities lakini pia kuna fursa kutoka TIB, TADB na kadhalika. Nimeomba mwaka wa nne sasa Serikali (Wizara) kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri tufanye kongamano Mafinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la PVOC, binafsi baada ya kuhudhuria semina ya TANTRADE ambapo TBS na WMA walitoa mada kati ya hizo niliuliza suala la PVOC ambalo kwangu mimi naona ni kuwanufaisha watu kati (the so called agents). Maana kazi kubwa inafanywa na TBS za nchi husika, mfano ukitoa mzigo China lazima pawepo TBS ya kule itoe certificate lakini tena mtu analipa dola 800 ili upate COC, inapotea bure. Afadhali ingelipwa hapa, kwa sababu pamoja na yote hayo bidhaa ambazo ni fake na substandard zinaingia nchini. Makusudio yangu ni kushika shilingi hasa ikiwa hapatatolewa maelezo ya kutosha.
Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (The East Africa Community Protocol on Information and Communication Technology)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, nitaenda haraka haraka na niseme tu kwamba sisi kama Tanzania kwa namna moja au nyingine ni Mhimili wa Jumuiya hii ya Afrika Mashariki, kwa hiyo kuridhia Itifaki hii ya Masuala ya Kinga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kunathibitisha kwamba tuna maslahi mapana lakini tutaendelea kuwa Mhimili wa kuhakikisha kwamba Jumuiya hii inaendelea kuwepo na inaleta matunda mema tofauti na mawazo ya baadhi ya watu wengine wamekuwa na mashaka kwamba pengine siku ikivunjika Vyombo vya Usuluhishi kama vilivyotajwa vitakuwa havipo tutafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tungekuwa na mawazo chanya tukiwa na matarajio kwamba Jumuiya itaenda kutuletea mambo yaliyo mema, lakini kwa haraka niseme kuhusu Ibara ya 6 ambayo inaeleza kwamba nchi pamoja na ile hali ambayo ilikuwa katika Jumuiya iliyopita Itifaki hii ina masuala mazima kwa namna moja au nyingine yanaenda kuzuia nchi kujinufaisha binafsi isipokuwa kwa makubaliano na hakuna nchi itanufaika na mali za Jumuiya kama ilivyotokea mwaka 1977.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona kabisa ni mambo ambayo yanaendelea kutuweka pamoja, lakini Ibara ya 10 inaonyesha kuwa Afrika tunaweza sasa na tunathibitisha kwamba tunaweza kujiamulia mambo yetu na hii ni heshima kwa wananchi wa Afrika Mashariki kwamba inapotokea mgogoro ni wajibu wetu sisi kutafuta ufumbuzi na hata itakapolazimu kwenda katika Vyombo vya Sheria, kwenda katika Vyombo vya Kimahakama basi tutakwenda kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na wakati ule ambapo baada ya yale matatizo ilibidi watu Commonwealth waje watusaidie, kwa hiyo hii inaendelea kuthibitisha kama ambavyo sisi katika Tanzania tunaionyesha Dunia chini ya Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwamba kuna mambo tunaweza tukayasimamia na tukayafanikisha na hii Ibara ya 10 inaonyesha kwamba sisi kama wana Afrika Mashariki tumejidhatiti kwamba kama kutatokea matatizo, kama kutatokea migogoro sisi wenyewe tutakaa chini tutasuluhishana, tutawekana sawa na ikilazimu kwenda Mahakamani hatutakwenda The Hague, bali tutabaki katika Mahakama ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Ibara ya 11 inatoa room ya marekebisho kama kutaonekana kuna jambo tunadhani tuliongeze basi tuweke marekebisho, baada ya kusema hayo naunga mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Mradi wa Scheme ya Umwagiliaji ya Mtula. Baada ya umwagiliaji kuhamishiwa Wizara ya Kilimo, ninaomba Serikali ione uwezekano wa kukamilisha Scheme ya Umwagiliaji ya Kijiji cha Mtula ambayo ni msaada mkubwa kwa kilimo na uchumi wa wananchi wa Mafinga.

Mheshimiwa Spika, uchumi wa viwanda, msingi wake ni kilimo; jitihada za kujikwamua na uhaba wa sukari, zitafanikiwa ikiwa tu Wizara ya Kilimo itaongeza jitihada za kilimo cha miwa hasa kwa small scale na hasa kwa kufanya ubia kati ya Serikali (halmashauri na sekta binafsi).

Mheshimiwa Spika, naambatisha haya maelezo ya Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Miwa, Dkt. George Mlingwa, na wenzake. Pamoja na kuwa andiko hili ni la mwaka 2016/2017 bado ninaamini module hii ambayo wenzetu Brazil wametumia inaweza kuwa suluhisho la uhaba wa sukari ambao msingi wake ni kilimo cha uhakika cha miwa.

Mheshimiwa Spika, maelezo kwa ufupi kuhusu sukari, kuna maeneo mengi nchini ambayo tunaweza kujenga viwanda vidogo na vya kati, (tani 10,000 mpaka tani 30,000 kwa mwaka). Kila mkoa una maeneo kama haya. Kwa mfano Kilosa tani 10,000, Manyara tani 10,000, Mara tani 30,000, Ruvuma tani 10,000, Dodoma Chamwino tani 10,000, Kigoma Bonde la Malagarasi tani 30,000, Pwani – Rufiji tani 30,000 na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, uendelezaji wa viwanda vidogo unachukua muda mfupi, miezi nane mpaka kumi. Gharama zake ni za chini USD milioni tatu hadi kumi ukilinganisha na vile vikubwa USD milioni 100 hadi milioni 300 ambavyo huchukua miaka miwili hadi mitano. Viwanda vidogo viko karibu na wananchi, bei ya sukari yake ni nafuu kutokana na gharama kuwa chini. halmashauri za wilaya husika zinaweza kuingia ubia na wawekezaji wazalendo katika maeneo yao. Miradi hii inaweza kuziingizia mapato halmashauri zetu.
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashukuru kupata nafasi na kama wenzangu walivyosema na mimi naunga mkono maazimio haya ya Bunge ya kuridhia ubadilishaji na kuongeza hadhi haya mapori kama ilivyokuwa imetajwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nipende kusema mambo machache. La kwanza kama ambavyo pia Kamati imesema sasa hivi tunaenda na kitu kinaitwa conservation with sustainable development, maana yake ni nini kwamba kwa kuyapa hadhi hii mapori haya moja itaimarisha ulinzi, lakini pili itajenga mazingira bora ya kuendeleza utalii. Sasa ili hayo yaweze kufanyika na kufanikiwa kuna kitu sisi katika nchi yetu tunasema ni ya pili kwa vivutio vya utalii baada ya Brazil, maana yake tukizungumza katika ile tunaita comparative advantage sisi tuko vizuri katika dunia baada ya Brazil, lakini tukizungumzia competitive advantage bado kuna mambo ya kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nijielekezee katika kutoa ushauri sasa kwa Serikali pamoja na kupongeza jitihada hizi basi kuongeza nguvu ili tuweze kuwa competitive katika suala zima la utalii kusudi kuongeza mapato kutoka asilimia 17 iliyoko sasa hivi na kuendelea.

Sasa ili tuwe competitive maana yake ni nini, lazima tuboreshe mazingira ya kuwekeza katika shughuli za utalii, lakini pili kuiongezea ngu TANAPA na TTB katika kujitangaza. Lakini la tatu pia kupunguza vikwazo ambavyo kwa namna moja au nyingine vimekuwa kizuizi katika kuhakikisha kwamba sekta hii ya utalii pamoja na kuongeza hadhi hizo hatufikii malengo ambayo yanaweza kutufanya tukawa competitive katika masuala mazima ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine na la muhimu ambalo Mheshimiwa Masele alilisema pale ni kujengea uwezo vyuo vyetu vya mafunzo ya utalii ikiwa ni pamoja na kuviongezea nguvu katika mafunzo ya lugha, kwa sababu tunatarajia watalii waje kutoka maeneo mbalimbali pamoja na lugha yetu ya Kiswahili pamoja na lugha ya Kiingereza, lakini vyuo hivi vipewe msisitizo wa kuongeza mafunzo ya lugha nyingine za ziada ili watalii wanapokuja basi kunakuwa na mawasiliano ambayo ni mepesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho napenda kuipongeza Serikali na hasa Mheshimiwa Kigwangalla na timu yake na Naibu wake na watendaji wake kwa kweli kama ambavyo niliwahi kusema wakati fulani mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, wanafanya kazi nzuri, katika utendaji wao kazi nzuri basi wasisite pia kutazama na kutupia jicho katika suala zima la historical sites. Nimewahi kutoa mfano pale Kihesa Mgagao ambayo ilikuwa ni kambi ya wapigania uhuru….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. COSATO D. CHUMI: ...tungeitazama na tungeweza kuongeza mapato zaidi. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, utalii na fursa ya watalii ambao ni askari wa UN wanaolinda amani kupitia UN – Mission; kuna kundi kubwa la askari ambao wako kwenye UN – Mission mbalimbali katika eneo la Maziwa Makuu na pia pembe ya Afrika. Nitafafanua kidogo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, DRC kuna Mission ya MONUSCO na Central Africa kuna MINUSCA. MONUSCO tu ina takribani watumishi 16,000, wengi wao askari kutoka Mataifa kama Pakstani, Bangladesh na Nepal. MINUSCA ina wafanyakazi zaidi ya 12,000, kutokana na mazingira ya kazi kila baada ya kipindi fulani hupewa likizo. Kwa sababu ya umbali wa kwenda makwao wengi hupendelea kwenda maeneo jirani kupumzika ikiwemo Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto; kwa sababu ya utaratibu wa Visa Rejea (Referred Visa) ambayo maombi yake huchukua muda mrefu na wakati mwingine hakuna majibu. Tunawapoteza watu hao ambao sasa wanakwenda Rwanda, Kenya na Uganda. Hili soko kubwa ikiwa mtu huyo ameshafanyiwa vetting katika level ya UN na ana passport ya UN, tunakosaje kuwa na utaratibu maalum. Tufikirie kwa mwaka tukiwapata japo 5,000 tu ni mapato kiasi gani. Ikizingatia kuwa hawa ni wale ambao High Value Tourism na ni long stay kwa sababu watakaa muda mrefu mpaka likizo yao itakapokwisha ambayo huwa ni wastani wa siku 14 mpaka 21.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri; Serikali kupitia Wizara husika ya Mambo ya Ndani (Uhamiaji) na Mambo ya Nje na wao washirikiane kuona kuwa tunafaidi fursa hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Niseme wazi na pengine naweza nisieleweke lakini ndiyo ukweli; kama kuna Wizara zilikuwa pasua kichwa, basi Maliasili na Utalii, Nishati na Madini siku za nyuma, lakini mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni; toka Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ameingia hapo kwa kweli, tuwe wakweli wa nafsi za ukweli; Wizara imetulia, Wizara imekuwa ina mwelekeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ana timu nzuri. Nikiona Katibu Mkuu Profesa, Naibu Katibu Mkuu Dokta, TFS yuko Profesa, lakini pia hata Wenyeviti wake wa Bodi wengi ni Mabrigedia, ni Majenerali. Kwa hiyo bila shaka kazi hii, pamoja na msaidizi wake, Mheshimiwa Kanyasu, wataendelea kuifanya ili Watanzania waweze kupata neema na pato linalotokana na utalii liweze kuongezeka. Napongeza hili kwa dhati ya moyo wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, nipende kupongeza pia uongozi wa TFS, lakini pia na uongozi wa Shamba la Sao Hill pale Mafinga na Wilaya ya Mufindi kwa jinsi ambavyo tunashirikiana. Zamani kulikuwa na shida sana ya mambo ya vibali, ujanja ujanja ulikuwa mwingi, lakini taratibu tumekuwa na vikao vya pamoja, tumekuwa na vikao vya wadau na mambo kiasi fulani yamekwenda katika mstari ambao unastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, katika Sekta ya Misitu na mimi niseme mambo makubwa mawili; kwanza, sisi tunaotoka ambako misitu inatuongozea maisha kwa asilimia siyo chini ya 50 mpaka 70, tulikuwa tumependekeza na kuishauri Serikali iweze kuondoa lile zuio la kusafirisha mazao ya misitu saa 24. Nilitarajia Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo namwamini, toka tukiwa DARUSO, mimi niko Mlimani yeye yuko Muhimbili, tukiendesha gurudumu la kuhakikisha kwamba mambo ya cost sharing yanakaa vizuri, namwamini katika hili na naamini atalitekeleza na wananchi wa Mafinga na maeneo mengine watalisikia katika hotuba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu gani? Nime-peruse kitabu hiki kutoka ukurasa wa kwanza mpaka ukurasa wa 97, nilitarajia nitaikuta kauli inayohusiana na jambo la kuruhusu mazao ya misitu kusafiri saa 24, kwa hiyo natarajia Mheshimiwa Waziri atakapokuja katika kujumuisha atatueleza lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kama nilivyosema, sisi wananchi wa Mufindi, Mafinga, Iringa, Njombe na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini tunaendesha maisha yetu kwa kutegemea mazao ya misitu. Sasa kuna watu ambao wanavuna katika Msitu wa Sao Hill. Nimwomba Mheshimiwa Waziri, wakati umefika sasa, kama ambavyo walifanya katika Sekta ya Madini ambapo kuna mikopo kwa wale wachimbaji wadogowadogo, hebu sasa tuwe na utaratibu wa kuwapa mikataba hata ya miaka mitatu mitatu wavunaji wetu ili waweze kukopesheka katika mabenki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ya kutoa kibali ni utaratibu mzuri, lakini tunawomba Mheshimiwa Waziri tunakoelekea sasa watu hawa wapate mikataba ili kwa mikataba ile kwanza, watakuwa na uhakika wa kuajiri watu, lakini pia watakuwa na uhakika wa kupata mikopo na mwisho watakuwa na uhakika wa kuchangia Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia kusema katika suala zima la Chuo cha Misitu Olmotonyi; Mheshimiwa Waziri, tumekuwa tukiomba na hiki ni kilio chetu watu wa Mafinga na maeneo yale, kwamba walau tungekuwa hata na campus kwa ajili ya chuo cha misitu katika Nyanda za Juu Kusini na bahati nzuri pale Sao hill majengo yapo. Jambo hili ni mwaka wa tatu sasa nalisema. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa jinsi ambavyo anajituma katika kufanya kazi na wasaidizi wake; hebu waone kwamba sasa ni wakati wa Chuo cha Misitu kuwepo Nyanda za Juu Kusini na pale Mafinga, Sao Hill, tayari majengo yapo. Hii yote itakuja kuleta tija katika uvunaji wa misitu, lakini katika kuchakata mazao yanayotokana na misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie utalii; sisi hapa Tanzania tunasema ni wa pili baada ya Brazil, hii hapa tunaita ni comparative advantage, lakini Mheshimiwa Waziri ili tunufaike na utalii lazima tufanye kitu kinaitwa competitive advantage. Kwa sababu kama ni wa pili tayari ni wa pili, sasa kuwa kwetu wa pili tunanufaika vipi? Kweli nimeona hapa katika takwimu za Mheshimiwa Waziri ameonesha ambavyo ongezeko la watalii kwa mwaka huu tunapoelekea ni watalii milioni 1.5. Kwa ongezeko hili tumepata fedha za kigeni dola bilioni 2.5 mwaka 2017 na sasa imeongezeka mpaka Dola za Kimarekani bilioni 2.4. Sasa tukisema dola pengine mwingine haelewi, hizi fedha kwa Kitanzania ni zaidi ya trilioni 5.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipunguza vikwazo katika Sekta ya Utalii tunaweza sisi tukahakikisha ndani ya miaka michache tuna watalii wasiopungua milioni tano. Tukipata watalii milioni tano maana yake ni nini; ikiwa sasa kwa watalii milioni moja na laki tano tunapata walau trilioni 5.2 kwa mwaka, maana yake ni kwamba tutakuwa tunakadiria kupata mapato yasiyopungua trilioni 15, hiyo ni nusu ya bajeti yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tufike huko tusibaki tu kusema kwamba sisi ni wa pili, sasa sisi kuwa kwetu wa pili tufanye nini? Tumeona kuna vikwazo mbalimbali katika kuhakikisha kwamba biashara ya utalii inakua. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kama walivyofanya wenzetu wa madini, aitishe kongamano, nampongeza, alipoingia tu katika Wizara hii aliita mkutano wa wadau, lakini ulikuwa ni wa wadau wa Sekta nzima ya Maliasili na Utalii, namwomba waitishe mkutano maalum tu kwa ajili ya mambo ya utalii. Ikiwa hii ni sekta inayotupa fedha za kigeni zaidi ya asilimia 20, kwa nini tusiilee ili tuweze kuongezea pesa za kigeni na hivyo kuendelea kujenga uchumi wetu imara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia kuzungumza kuhusu maeneo mahususi, historical sites; Mheshimiwa Waziri amesema ambavyo wameongeza maeneo na mazao mapya ya utalii, lakini nitatoa tu mfano, pale Kilolo kwa kaka yangu, Mheshimiwa Mwamoto, kuna Gereza la Mgagao, gereza hili walikuwa wanakaa, Walter Sisulu amekaa pale, Mandela amekaa pale na watu wa South Africa wangependa kuja kutembelea pale kama sehemu ya makumbusho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Balozi alipofika pale na kukuta tumefanya gereza akasikitika kwamba ninyi mnatukumbusha enzi za apartheid. Namwomba Mheshimiwa Waziri akae katika Serikali waangalie mambo ya historical sites, kule Iringa kuna maeneo ya Isimila, kule Kalenga kuna kaburi la Bismarck; haya yote kwa pamoja yanaweza kutuongezea sisi kuleta idadi kubwa ya watalii, lakini tukiendana pia na kuondoa vikwazo ambavyo kwa namna moja au nyingine vinarudisha sekta nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, wakati Simba inacheza, Klabu Bingwa Afrika, Haji Manara anasifika kwa kuhamasisha na watu kujaa Uwanja wa Taifa, zaidi ya 60,00; Taifa Stars ilipocheza na Uganda, zaidi ya watu 60,000 wameingia pale Uwanja wa Taifa. Mheshimiwa Waziri, aje na mkakati wa kuhakikisha tunahamasisha pia utalii wa ndani… (Makofi)

MWENYEKITI: Hebu rudia tena, klabu gani hiyo?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la michezo, kuna msemaji anaitwa Haji Manara wa Simba Sports Club…

MBUNGE FULANI: Bodaboda!

MHE. COSATO D. CHUMI: …kuna msemaji anaitwa Thobias Kifaru, kuna msemaji anaitwa Masau Bwire; hawa watu wanaleta hamasa watu wanaenda viwanjani. Je, sisi kama Taifa kwa nini tusihamasishe watu wetu waweze kwenda kwenye mbuga ili tuwe na…

MBUNGE FULANI: Bodaboda!

MHE. COSATO D. CHUMI: ...tupate fedha za kigeni. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, Mheshimiwa Rais juzi amesema Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, wawe na laini za TTCL. Nami nitoe wito; familia zetu sisi viongozi ziwe za kwanza kwenda kufanya utalii wa ndani ili kuhamasisha na hivyo kujipatia fedha kwa sababu utalii wa ndani unaingiza fedha, mama anauza bagia, mama anauza sambusa, fedha inakwenda moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya, naunga mkono hoja na Mungu atubariki sote. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Misitu. Kwa dhati ya moyo wangu nawapongeza sana mmejitahidi sana kuiinua sekta na kuleta utulivu katika sekta na hasa suala zima la upatikanaji wa malighafi katika Shamba la Sao Hill. TFS na uongozi wa Shamba la Sao Hill wamekuwa na ushirikiano mzuri na Halmashauri ya Mji wa Mafinga hasa katika Corporate Social Responsibility na suala la ushirikishwaji wa wadau. Naomba suala hili la kushirikiana wadau na sisi viongozi wa kuchaguliwa liwe sustainable, na ni vizuri kila mara kabla ya mgao kuanza vikao viwepo ili wadau na sisi viongozi wao tuwe na uelewa mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pamoja na hayo nina hoja kadhaa; Kuhusu Kuruhusu Mazao ya Misitu Kusafirishwa Masaa 24. Hili suala tumeshalileta na wakati wa kujibu swali langu la msingi na nyongeza tarehe 04 Aprili, 2019 Serikali Waziri na Naibu Waziri walilieleza Bunge kwamba jambo hilo liko katika hatua ya mwisho, nilitarajia suala hilo liwemo kwenye hotuba yako. Ombi langu ni kuwa tusikie kuhusu jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Mikataba kwa Wavunaji. Pamoja na mchango wangu wa maelezo ya mdomo bado ninawasilisha suala hili na pia natahadharisha badhi ya viongozi wa vyama vya wavunaji wanatumia fursa vibaya kwa kuendelea kujilimbikizia vibali. Yapo malalamiko mengi, ni muhimu kadiri tunavyoingia kwenye uwazi hali na ujanja ujanja huu umalizwe ili sekta iendelee kuwa na utulivu. Hata mtakapofikia hatua ya kuwapa wavunaji mikataba iwe ni wale ambao ni genuine na wavipate kwa uhakika na uwazi. Suala hili litafanikisha na kuongeza mapato kwa kuwa itawapa uhakika wa kukopa na kuajiri ipasavyo wafanyakazi ambao watachangia kupitia PAYE, SDL nakadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Single Entry. Katika zama hizi za eGovernment – TEHAMA ni muhimu sasa kuliangaia suala hili kwa umakini ili kuziwezesha jamii zinazozunguka mbuga zetu kunufaika na utalii. Vilevile pia kuwapa uhakika wa kipato wananchi ambao ni sehemu ya ulinzi dhidi ya ujangiri. Mimi ni mdau wa utalii na familia inaendesha VAMOs Hotel Mikumi na Mafinga, pale Mikumi, Tungamalenga na maeneo ya aina hiyo uchumi umelala kwa sababu watalii wanapita juu kwa juu na hivyo kuondoa fursa ya kipato cha wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Chuo cha Misitu – Olmotonyi Kuwa na Campus ndogo Mafinga. Naomba kuwasilisha tena ombi hili ambalo mkirejea michango yangu ya nyuma, nilishawasilisha; naomba mlitafakari.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuruhusu Baadhi ya Miji kufanya Biashara Saa 24; nafahamu ni suala la biashara kwa maana ya leseni inaeleza muda wa kufanya biashara, Hata hivyo, kama tunataka mapato (kupanua wigo) Wizara iongeze (take lead) kuhakikisha kuwa, baadhi ya miji kama vile Mikumi, Ruaha Mbuyuni, Ilulu, Mafinga, Makambako, Igawa na kadhalika iwe designated kama miji ya kibiashara saa 24 sambamba na miji mikubwa kama Dar-es-Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na miji ya mipakani yote kufanya biashara saa 24.

Mheshimiwa Naibu Spika, Soko la DRC Congo hasa kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Kuna soko kubwa la mazao Kongo Mashariki. Hata hivyo, ili kunufaika na soko hilo lazima upitishe bidhaa kwa njia mbili:-

(i) Tunduma – Kasulambesa – Lubumbashi

(ii) Dar-es-Salaam – Rusumo – Kigali – Bukavu mpaka Kigoma

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2018 wakulima wa Njombe walipoteza tani 600,000 za mahindi na mchele baada ya Zambia kuleta vikwazo maana na wao wanategemea Soko la DRC Mashariki. Hivyo, njia sahihi na isiyo na vikwazo ni kutumia Bandari ya Karema ambayo upande wa pili ni Momba au Kigoma – Kalamie na kuna soko kubwa mno, hivyo tukiimarisha bandari zetu tutaongeza tija na trade volume itaongezeka maradufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, yapo ya kufanyika kwa mfano kupitia JPC – Joint Permanent Commission ambayo haijafanyika since 2002. Kupitia JPC au mikutano ya ujirani mwema itafanikisha kuondolewa kwa vikwazo kadhaa. Kwa mfano, suala la visa ambayo ni dola 50 kwa dola 200, visa ya kibiashara, lakini pia SUMATRA kwa sheria na kanuni hairuhusu meli kubeba mizigo na abiria, lakini kwa DRC – Congo kutokana na hali yao meli za mizigo zinaruhusiwa na abiria, sasa wakivuka Lake Tanganyika wanapigwa faini dola 500, next week hawaji. Kwa mujibu wa World Bank, mwaka 2017 wafanyabiashara wadogo waliuza mchele DRC wa thamani ya dola 1.5m almost Tshs 3.5b. Hivyo, kuna fursa ya kuongeza trade volume kati ya Tanzania na DRC.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Sukari; pamoja na mchango huu naambatanisha mawazo haya japo ni ya 2016. Kipo cha kujifunza, ili kuondokana na uhaba wa sukari hapa nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kuhusu kutoa mwongozo rasmi kuwezesha TANESCO kuendeleza pale REA III inapoishia kabla ya kukabidhi mradi. Niwapongeze kwa kazi na hasa kwa kuanza kutuelewa watu wa Mafinga kwamba kutokana na uwepo wa viwanda vya mazao ya misitu, uhitaji wa umeme ni mkubwa, hivyo tunahitaji transfoma zenye capacity kubwa. Tayari tumepokea transoma mbili kati ya tano ambazo Mheshimiwa Waziri alituahidi wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais, hata hivyo, kuna jambo ambalo nashauri litolewe mwongozo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano sisi Mafinga baada ya wananchi kuona umeme unakuja, walijiandaa kuongeza shughuli za uzalishaji kwa kununua mashine kubwa za kuchana mbao, hata hivyo kutokana na scope kuwa ndogo, REA III haijawafikia wananchi wa aina hiyo ambao wapo tayari kujigharamia kwa kujiwekea nguzo kutoka pale ambapo scope ya REA III awamu ya kwanza imeisha. Hata hivyo, kwa kuwa utaratibu wa kiukandarasi na mikataba, TANESCO hawawezi kuendeleza pale mkandarasi alipoishia kwa kuwa mradi bado haujakabidhiwa rasmi kwa TANESCO na hasa ukizingatia kuwa kuna miezi kumi na miwili ya matazamanio.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, naomba Wizara itoe mwongozo rasmi wa kuruhusu hasa maeneo mahususi ambayo wananchi wapo tayari kujigharamia kwa nguzo kama ilivyo katika baadhi ya maeneo ya Mafinga. Naamini kwamba nimeeleweka, maana kuna maelezo lakini hayajanyooka kwa maana kwamba kanuni na taratibu zinataka TANESCO aendelee baada ya kukabidhiwa mradi na ndiyo maana nashauri kuwa patolewe mwongozo rasmi kuhusu suala hilo.

Mheshimiwa Spika, Mafinga kuwa na wilaya ya ki- TANESCO; suala hili nimelileta mara kadhaa, hata hivyo sijui kama naeleweka. Mufindi ni wilaya ambayo ina viwanda vingi vya chai, karatasi na viwanda vya mazao ya misitu. Hata makusanyo (revenue) inayokusanya ni makubwa kushinda hata baadhi ya mikoa. Hivyo, hili ni eneo ambalo lina potential kubwa sana. Hata hivyo, shughuli za viwandani zinapoteza wastani wa 30% ya muda wa kufanya kazi kutokana na ama kukatika umeme au hitilafu hasa nyakati za mvua. Kwa kuwa tunategemea connection iliyopo Mgololo, ikitokea fault yoyote, umeme unakatwa ili kurekebisha hizo faults.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi letu, tuwe na TANESCO Mafinga (kama ilivyo Dar ambapo kuna wilaya za TANESCO nje ya wilaya za kiutawala mfano Tabata, Mikocheni na kadhalika). Tunaomba hivi kutokana na hali halisi ya uhitaji na pia kusogeza huduma karibu kwa wateja, lakini pia kwa kuwa eneo hili lina potential kubwa maana yake ni kuwa tutaongeza revenue ya TANESCO.

Mheshimiwa Spika, pia hii itawezesha TANESCO Mafinga kuhudumia viwanda vya mazao ya misitu na wakazi wa maeneo jirani wakati TANESCO Mufindi itahudumia viwanda vya chai na wakazi wa Mufindi. Mimi siyo mtaalam lakini naamini nimeeleweka, na rejea zangu za maandishi kwa barua zipo katika ofisi za TANESCO na REA.

Mheshimiwa Spika, densification hasa Kitelewasi, Shule ya Sekondari Mnyigumba na kadhalika. baadhi ya vijiji kama vile Kitelewasi ambapo kuna Shule ya Sekondari Mnyigumba walipata umeme REA II ambapo scope haikufika maeneo yote ikiwemo Shule ya Sekondari Mnyigumba ambapo tulihitajika kulipia milioni 78. Suala hili nimeshalifikisha kwa maandishi na barua Wizarani na REA, hivyo naomba densification iweze kujumuisha maeneo ya Kitelewasi na Kijiji cha Kikombo.

Mheshimiwa Spika, vijiji mbadala na upatikanaji wa materials kwa ajili ya TANESCO; kuna maeneo ambayo tumewasilisha REA kupitia TANESCO kwa ajili ya reviewed scope ambapo kuna eneo Ifingo, Kinyanambo Sekondari, Banda Beach, Lumwago na Isalavanu Primary School. Pia kuna maeneo ambako line kubwa ilipaswa kujengwa na mkandarasi lakini tayari maeneo hayo yalishajengwa line kubwa na hivyo tunaomba gharama zilizokuwa zijenge line kubwa, basi mkandarasi aelekezwe kupeleka umeme maeneo ya nyongeza ya Lumwago, Zanzibar na Banda Beach. Haya yote hasa kuhusu vijiji mbadala yapo tayari REA.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa materials; kama nilivyosema awali, yapo maeneo TANESCO wanaendelea kwa mfano Mwongozo, Ifungo na Makamadoresi ambako kuna shule ya watoto wadogo inayoendeshwa na Masista. Tunaomba TANESCO wapelekewe materials kwa wakati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya, lakini zaidi usikivu wenu. Binafsi kila nilipoomba kuonana na Mawaziri au Watendaji kuanzia Katibu Mkuu, DG wa REA na TANESCO kwa kweli nimepata nafasi na nimesikilizwa na shida za wananchi wa Mafinga zimepata walau suluhisho,

Mheshimiwa Spika, hata hivyo nina ushauri na mambo kadhaa kwa Wizara. Hoja yangu ya siku zote ni kuhusu kuona uwezekano wa kuwa na Wilaya mbili za Kitanesco katika Wilaya ya Mufindi kutokana na umuhimu wake, hasa katika dhana nzima ya uchumi wa viwanda.

Ushauri wangu ni kwamba tuwe na ofisi kwa ajili ya Mafinga ambako kuna viwanda vingi vya mazao ya misitu na tuwe na Ofisi Mufindi ambako kuna viwanda vingi vya chai pamoja na Kiwanda cha Karatasi Mgololo. Ninaamini hata mapato, Mufindi inazidi baadhi ya mikoa. Hivyo kusogeza huduma hii haitakuwa mara ya kwanza. Kwa mfano, Ilala ina zaidi ya Wilaya moja ya Kitanesco.

Mheshimiwa Spika, transfoma zinazofungwa Mafinga za KV 50 ni ndogo ukilinganisha na uhitaji hasa wa viwanda vya mazao ya misitu. Maombi yangu; umeme ni huduma na ni biashara/mapato, ni kwa ajili ya uzalishaji, hivyo kuwekeza nguvu kwenye maeneo kama Mafinga itasaidia kuongeza mapato ambayo yatatumika kusambaza umeme maeneo ambayo umeme ni kwa ajili ya huduma zaidi. Kwa hiyo, iwe ni ujazilizi au REA III awamu ya pili, ipo kila sababu maeneo kama Mafinga kuyaangalia kwa macho mawili na kwa jicho la uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu taa za barabarani. Tayari Halmashauri ya Mafinga Mji, imeshawasilisha andiko kadri ambavyo DG wa REA alituelekeza. Hivyo kwa umuhimu ule ule ambao Serikali ilikubali mazao ya biashara ikiwa ni pamoja na nguzo za umeme kusafirishwa masaa 24, tunaomba taa za barabarani katika maeneo ambayo ni junction za kibiashara.

Mheshimiwa Spika, lingine ni Luku. Sina utaalam wa masuala ya IT, lakini nashauri kwamba kama teknolojia inaruhusu, basi mtu anaponunua umeme asilazimike tena kwenda kwenye mita kuingiza token. Iwe kama ving’amuzi ambapo ukinunua tu inaji-update. Naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nawashukuru wananchi wa Mafinga na kila mmoja ambaye kwa namna moja ama nyingine amefanikisha mimi kurejea hapa na mimi kama ulivyosisitiza suala la TARURA, tumelisema sana, ni wakati sasa kama walivyosema watu wengine, tuje na ubunifu wa kutafuta chanzo ambacho kitasaidia TARURA kupata fedha ya kutosha ili angalau watu tuwe na uhakika wa kurudi hapa mwaka 2025. Kwa sababu pale Mafinga bila kuwa na barabara za lami maana yake ni kwamba wakati huo ukifika bora nisiende. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiunganisha na jambo hili, jana nilikuwa na swali nikiuliza Serikali, ni lini wataanza ujenzi wa barabara za lami? Majibu kutoka TAMISEMI ni kwamba Serikali iko katika hatua za mwisho za kuhakikisha kwamba ile miji 45 chini ya utaratibu wa uendelezaji miji, itakwenda kuanza kunufaika muda siyo mrefu ujao kwa sababu wako katika mazungumzo ya hatua za mwisho. Kwa hiyo, naisihi Serikali na kuiomba basi mazungumzo hayo yaende kwa haraka ili kusudi miji hiyo 45 ianze kunufaika na hivyo kupunguza mzigo kiasi fulani wa TARURA katika kuhudumia barabara zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mimi ni mwanamichezo, najielekeza moja kwa moja katika ukurasa wa 37 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais ambaye wamesema, katika miaka mitano ijayo tutakuza sanaa, michezo na utamaduni.

Mheshimiwa Spika, sanaa, michezo na utamaduni imekuwa chanzo kikubwa cha mapato katika dunia ya sasa ambapo matumizi ya internet yamekuwa makubwa sana. Nina takwimu hapa, projection ya PWC inasema kwamba mwaka 2017 mapato yaliyotokana na media and entertainment industry katika Tanzania yalikuwa takribani dola milioni 496. Projection kufikia 2022 itakuwa bilioni 1.1 ambayo ni sawa trilioni 2.5. Kwa hiyo, hii ni sekta ambayo ni chanzo kikubwa cha mapato, lakini pia ni chanzo kikubwa cha kuchangia ajira, katika zile ajira milioni nane ambazo Mheshimiwa Rais amepanga tuzizalishe katika mwaka 2020 – 2025.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza TCRA, baada ya kuwa wamewafungia Wasafi Tv, sasa wamesema kwamba adhabu imepungua. Najielekeza katika COSOTA na BASATA. Mheshimiwa Rais alielekeza nami nimezungumza karibu miaka mitano, imekuwa sasa under one roof, lakini haitoshi. Ikiwa TCRA, NEMC wako mpaka level ya kanda, kwa nini BASATA na COSOTA wasirudi hadi level ya kanda kuwapunguzia wasanii safari na gharama za kusafiri mpaka Dar es Salaam?

Mheshimiwa Spika, tazama msanii atoke Kongwa, aende Dar es Salaam, anaingia gharama nyingi. Atoke Tandahimba, Ilemela au Mafinga, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba kama hii ni sekta ambayo inazalisha mapato ya kiasi cha shilingi trilioni 2.2 na ni chanzo cha ajira, ukiangalia hapa matamasha mbalimbali ambayo huwa yanafanywa hapa nchini kwetu, yamekuwa ni chanzo kikubwa cha ajira.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, nawapongeza Wizara ya Habari, wana tamasha hili la Serengeti Festival, ukienda pale Jamhuri kuanzia mama ntilie, muuza mahindi, muuza Big G atapata pesa. Matamasha mbalimbali kama muziki mnene EFM, kama tamasha la Tunawasha la Wasafi, matamasha kama Fiesta la Clouds, mtikisiko la Redio Ebony kule Iringa, yaani wakati ule wa tamasha, mzunguko wa fedha unakuwa umeongezeka sana.

Mheshimiwa Spika, sasa tunaposema tumsaidie Mheshimiwa Rais, taasisi ambazo zinalea sekta hii, ninashauri zishuke mpaka ngazi ya chini, BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu waende mpaka kiwango cha angalau ngazi ya kanda ili ku-facilitate wasanii, kusudi lile lengo la kuzalisha ajira milioni nane na kuongeza mapato katika Serikali na mtu mmoja mmoja yapate kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaposema easy way of doing business maana yake ni kupeleka zile huduma karibu na wale ambao wana contribution na mapato na kuzalisha ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, naunga mkono hoja, nitachangia ipasavyo na kikamilifu katika Mpango. Mungu atubariki sote. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kuhamisha Gereza la Mgagao Kilolo na kuifanya sehemu ya makumbusho; kama Mjumbe wa Kamati napongeza jitihada za vyombo katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Lakini pia viongozi wa Wizara hasa kwa ushirikiano na Kamati na wepesi wenu katika kupokea ushauri na ambavyo mko accessible.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa ushauri ambao nimekuwa nikiutoa na kuuleta karibu kila mwaka, nawaomba sana mfikirie sana kuhusu kuhamisha gereza hili ambalo kwa mujibu wa historia, viongozi waliokuwa wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika walipata kuishi hapo kiasi kwamba watu wengi wakiwemo Mabalozi wa Afrika Kusini hapa nchini wametamani sana kupafanya eneo la kukumbuka historia yao, jambo hili tukiunganisha na jitihada za Mheshimiwa Rais kupitia Royal Tour, litasaidia kuvutia watalii.

Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba jambo hili linagusa Wizara zaidi ya moja ikiwemo Maliasili na Utalii na pia Wizara ya Ardhi, hivyo nashauri Wizara ya Mambo ya Ndani iwe kiongozi katika hili ili lifikie mwisho.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa dakika tano kwa kweli kuchangia ni chache nitakwenda moja kwa moja katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajielekeza katika Sehemu ya Tatu ya Mpango huu wa Tatu inayozungumzia kukuza ushiriki wa sekta binafsi kwenye maendeleo ya kiuchumi. Mipango yetu ni kutengeneza ajira milioni 8 na katika kutengeneza hizi ajira asilimia karibu 80 tunategemea zitoke katika sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika Taarifa ya World Bank na ambayo imo katika Mpango huu ambao Serikali imeuwasilisha, hiyo Ripoti ya Easy Way of Doing Business, sisi Tanzania tuko nafasi ya 141. Pamoja na kuwa kuna kasentensi pale kanasema kwamba tumefanya vizuri kutoka 144, lakini kwangu mimi if we are serious kutengeneza ajira milioni nane mimi naona hatujafanya vizuri, lazima ilenge kwenda katika digits mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika East Africa sisi tumeshindana tu na Burundi. Katika SADC sisi tunashindana tu na Zimbabwe. Sasa katika hii hali ya kuvutia uwekezaji na kutengeneza ajira milioni nane bila kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara, naona ajira milioni nane zitakuwa ni ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yako mambo ambayo lazima tufanye. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba amesema tutengeneze mabilionea na tusiogope. Jambo la kwanza ambalo tunatakiwa tusiogope ni kusema uhalisia sahihi lakini suala la pili tusiogope hata sisi wenyewe kuthubutu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya kutengeneza mabilionea mimi nasikitika sana, kule Mafinga unakuta mtu kauza miti yake, milioni 300, 400, sisi kule uchumi tunamshukuru Mungu, inakuja sijui Task Force, I don’t know whatever you call it, akaunti inafungwa. Mimi nilitarajia niulizwe kwamba wewe Cosato Chumi mfanyabiashara, kwa nini unafanya biashara akaunti haina hata milioni tano, lakini don’t ask me kwa nini nina milioni 500. Wewe tafuta mbinu zako za Kiserikali, angalia je, hii milioni 500 ya Chumi ni safi au siyo safi? Ukinifungia akaunti you cripple me down, tutatengenezaje mabilionea na hizo ajira milioni nane? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii pale Mafinga tozo katika Sekta ya Mazao ya Misitu ziko 13, viwanda vitano vimefungwa. Imagine kama kiwanda kimoja kinaajiri watu 300, tayari watu 1,500 hawana ajira. Pia umekosa SBL na PAYE; tutatengeneza kweli ajira milioni nane katika mazingira haya? (Makofi)

Kwa hiyo, katika kumsaidia Mheshimiwa Rais na Serikali, ni lazima kwanza tuwe wakweli wa nafsi. Ukweli wa nafsi ni lazima kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara. Mimi nasema ni wajibu wetu Wabunge na Serikali kwa ujumla kwa sababu wakati mwingine kweli tutasema TRA lakini mimi nimekwenda TRA wananiambia hii SBL ukiwa hujalipa zaidi ya tarehe 07, penati yake kwa kampuni ni 225,000, kwa individual 75,000. Pia hata kama umelipa ila hujafanya online filing kuna penati yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa angalia nimelipa lakini bado kuna penati, namuuliza Afisa wa TRA anasema bwana, Mkuu hii ni sheria tena na wewe ni Mbunge mlipitisha wenyewe. Kwa hiyo, wao at some point wanatekeleza sheria. Kwa hiyo, kuelekea blueprint na kutengeneza mazingira bora ya biashara yako mambo ni kisheria yaleteni humu turekebishe. Yako mambo ni Kanuni, Mawaziri wenye dhamana elekeeni huko ili lengo la kutengeneza ajira milioni nane iwezekane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuelekea huko, pamoja na kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara yako masuala ya miundombinu. Pale Mafinga kwenda Mgololo wakati wa mvua unakuta semitrailer kumi zimepaki wiki nzima zimekufa barabarani haziwezi ku-move; umesimamisha uchumi. Yale malori yangesafiri kwenda na kurudi ungejaza mafuta, Serikali ingepata fuel levy maisha yangeendelea, lakini zipo zimesimama siku tano. Sasa kati ya mambo ambayo tunatakiwa tufanye ni pamoja na suala zima la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa Mafinga ukishajenga barabara ya Mafinga – Mgololo kama alivyosema asubuhi ndugu yangu Mheshimiwa Kihenzile na barabara ya Mtwango – Nyololo, una-speed up uchumi. Kama Serikali ilikuwa inapata shilingi bilioni 10 matokeo yake utapata shilingi bilioni 50 mambo mengine yataendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho katika suala hili la kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara ni suala la umeme. Nampongeza Mheshimiwa Dkt. Kalemani, anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kazi nzuri angalieni umeme ni huduma, at some point ni biashara. Kule ambako kuna viwanda vingi watu wanataka kuzalisha mtapata pesa kama Mafinga, leta huo umeme. Leta umeme watu wawekeze, tulipe bili zikawapelekee watu umeme sehemu nyingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nakuomba kwa ridhaa yako…

NAIBU SPIKA: Muda umeshaisha Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naunga mkono hoja, naomba tuwe wakweli wa nafsi na Mungu atusaidie. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na ningependa kuanza kwa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, nampongeza Mheshimiwa Rais hasa kwa ile ziara yake ya majirani zetu Kenya. Ziara ile Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi imeendelea kufungua fursa za kibiashara sio tu kwa sisi ambao tunatoka tunakolima mahindi kama mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na hususani Mafinga, lakini kwa maeneo mengi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napongeza jitihada hizi kwa sababu katika maisha huwezi kuchagua jirani, lakini jirani ndio ndugu yako. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na hii kama yeye diplomat namba moja, hii ndio maana halisi ya diplomasia ya uchumi. Lakini pia naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wa Mabalozi ambao miongoni mwao watakuwa ni Wakurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje kwa sababu kwa muda mrefu Wizara ilikuwa ukiacha Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha na Chief Accountant na mtu wa PMU, the rest walikuwa wanakaimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kitendo hiki cha kuteua kwa kweli ni jambo la kupongeza sana na linawapa watumishi wale confidence katika kufanya kazi. Lakini pia nitumie nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri kwa uteuzi na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa kweli, yaani ninyi ni wanadiplomasia wabobevu na nikuambie tu Mheshimiwa Waziri, matumaini aliyonayo Mheshimiwa Rais kwenu ninyi na sisi Wabunge na Watanzania kwa ujumla, ni makubwa sana na sisi tunawaombea mfanye kazi kwa bidii na Mungu atawaongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha sasa diplomasia ya uchumi yapo mambo ni muhimu katika kuwezesha jambo hili lifanikiwe kama alivyosema Mheshimiwa Zungu Mwenyekiti wetu wa Kamati. Baadhi ya mambo muhimu ni pamoja na watumishi katika Balozi zetu, lakini pamoja na vitendea kazi kama magari pamoja na nyumba kama ofisi, lakini pia nyumba kama makazi. Sasa katika suala la makazi na ofisi kama alivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti pale. Nianze kwanza na yale maeneo ambayo ni muhimu kwa Serikali kutenga fedha, ili kuendana na mpango wa Serikali wa mwaka 2018/2019 mpaka 2030/2031; mpango kama wa miaka 10 hivi. Mpango huu lengo lake ni ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo na makazi na ofisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema mjumbe aliyetangulia, tunatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya ofisi na makazi na haikwepeki kwa sababu lazima tuwe na ofisi na lazima tuwe na makazi. Lakini hili pia ni eneo moja ambalo Serikali inaweza ikawekeza ikapata fedha. Nitatoa mfano, kwa mfano, Nairobi tuna kiwanja pale ambacho pakijengwa kitega uchumi, projection yake kwa mwaka tunaweza tukapata 2.3 bilion na hivyo tutakuwa tumeokoa pango ambalo tunalipa kwa sasa 1.4 billion.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kujenga kwanza tuta-generate income, lakini pili, tutapunguza gharama ambazo sasa tunaziingia katika kukodi majengo ya ofisi na makazi. Tukienda Congo DRC tuna kiwanja pale ambapo tunaweza tukajenga jengo la ofisi na kitega uchumi ambapo tunaweza tukapata karibu bilioni 13 kwa mwaka na tukaokoa gharama ambazo ni milioni 540 tunazotumia kwa sasa. Lakini vivyo hivyo tukijenga Comoro tunaweza tukapata mapato milioni 520, lakini tukawa tumeokoa milioni 420. Kwa hiyo, kiujumla kama unapata 520 na umeokoa milioni 420 umepata kama bilioni moja. Kwa hiyo, niombe kwa Serikali na hasa hususani Wizara ya Fedha kujenga majengo nje ya nchi sio luxurious, ndio uchumi wenyewe kwa sababu tutaokoa fedha lakini pia, tutakuwa tumeingiza fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika taarifa yetu ya Kamati, unaweza ukaona yako maeneo ambako mpaka sasa hivi yanatuingizia fedha nyingi sana mojawapo ni hiyo New York. Lakini katika mwaka huu wa fedha huu ambao tunaumaliza, tunatumia karibu shilingi bilioni 22 kwa makazi na ofisi. Bajeti hii tunayoenda nayo tutatumia bilioni 24 kwa makazi na ofisi, masuala ambayo kama tutajielekeza katika ule mkakati wetu wa miaka 10 kwamba tujenge na tukarabati baadhi ya maeneo na bahati nzuri viwanja vyetu viko maeneo ambayo ni prime, kwa hiyo, tutaokoa hizi gharama lakini pia tuta-generate income, lakini diplomatically unapokuwa na jengo lako mwenyewe nayo inaongeza hadhi ya heshima katika Taifa lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni suala la watendaji na maafisa katika Balozi zetu, ni muhimu sana Balozi hizi ili kuleta tija katika diplomasia ya uchumi zikawezeshwa kwa kupeleka maafisa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumezungumza hapa ndani nadhani ni miaka minne na kuna mwaka mimi nilishika mpaka shilingi, lakini mara zote Serikali ilisema watapeleka, watapeleka na mbaya zaidi maafisa wengi wamerudi. Nchi kama Marekani ina tofauti ya masaa baina ya West na East masaa matatu, sasa unakuwa na afisa pale mmoja au unakuwa na Balozi tu. Nchi kuna vituo nitatoa mfano hapa. Vituo ambavyo ni multirateral kwa mfano, Kituo kama Geneva pale kuna Mashirika makubwa ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Kazi, Shirika la Afya, WTO wako pale, lakini sasa unapokuwa tu na Balozi bila maafisa wa kumsaidia tija ya diplomasia ya kiuchumi haiwezi kupatikana. (Makofi)

Maeneo kama Rome kuna mashirika pale ya Kimataifa, lakini hata pale New York kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa unafanya kazi kwa kutumia Kamati zake zile sita ni kama hili Bunge Waheshimiwa Wabunge, tunakutana kwenye Kamati tunakubaliana tunakuja hapa tunayahitimisha, vivyo hivyo Umoja wa Mataifa ndivyo unavyofanya kazi, kwa hiyo, kama huna staffing ya kutosha ina maana kuna Kamati itakaa, itajadili mambo, itayapitisha, wewe utakuwa umekosa mchango wako ama kwa namna nyingine utakosa kitu ambacho kingeweza kukunufaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, masuala ya peace keeping, Umoja wa Mataifa umeendelea kupunguza budget ya peace keeping, lakini sisi ni moja ya nchi ambayo inashiriki sana katika masuala ya peace keeping.

Sasa kama hukuwepo kwenye ile Kamati ina maana ile bajeti itapita, lakini kama ungekuwepo au masuala kama ya wakimbizi kama ungekuwepo ungejenga hoja kwamba jamani jambo hili ni la muhimu lisipite, tulirekebishe kwa mtindo moja, mbili, tatu. Kwa hiyo, huu ni umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba tunapeleka maafisa ili kusudi hiyo diplomasia ya uchumi iweze kutimilika na iweze kuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi kama China unakuta Balozi yuko peke yake na wale waambata tu, hana maafisa wale ambao ni foreign service officer wa kumsaidia na ni nchi kubwa, lakini ni rafiki na ina uchumi mkubwa. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali kama ni Wizara ya Fedha kama ni Wizara yenyewe ilione hilo.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, baada ya kuwa nimepongeza uteuzi wa Wakurugenzi niombe pia Wizara, tuweze kushirikiana na Utumishi wapatikane Wakurugenzi Wasaidizi ambao ndio wanakuwa head of section ili kusudi kuwe na succession plan isiwe kama sasa hivi ambapo watu wamekaimu karibu miaka minne. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe na hii Mheshimiwa Waziri ni jukumu ambalo liko ndani yenu ninyi kama Wizara, kisha mnashirikiana na Utumishi mnawapandisha watu na Mheshimiwa Balozi Mulamula wewe watu wengi pale ni matunda yako.

Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe ni sehemu ya matunda yako, kwa hiyo, unawajua nani ana weledi, wana uwezo kiasi gani, wapatieni watu hizo fursa wawe Wakurugenzi Wasaidizi, diplomasia ya uchumi iweze kuthibitika kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno haya Mungu atubariki sote, Mungu aibariki Tanzania, kazi iendelee, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nami kwa kuanza, naunga kabisa mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Wakala wa Misitu Tanzania kwa niaba ya watu wa Mafinga kwa ushirikiano wao chini ya usimamizi wa Chama cha Mapinduzi tumeweza kujengewa mabweni mawili. Hivi ninavyozungumza tutapewa fedha kiasi cha shilingi milioni 130 kwa ajili ya kutengeneza lami nyepesi pale kwenye eneo letu la soko kubwa katika Wilaya ya Mufindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kutoa shukrani zangu za dhati, lakini yale mabweni tuliyojenga ni ya girls. Sasa boys wanatuuliza, pale Luganga Secondary na Changarawe Secondary wanasema mbona sisi mmetusahau? Kwa hiyo, natumia fursa hii pia kuwasilisha kama ombi kwa Serikali kwamba kama tumeanza na girls, which is good, kwa sababu, wako kwenye higher risk, basi tuwaangalie pia na boys. Nitumie nafasi hii pia kutoa wito kwa wawekezaji wengine waige Wakala wa Misitu Tanzania kwa sababu, tunashirikiana nao vizuri sana katika suala zima la CSR.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumekuwa tukishirikiana nao, wakati mwingine tunaazima ma-grader kutoka Sao Hill sisi Halmashauri tunajaza mafuta tunatengeneza barabara zetu. Japokuwa mwaka huu walikuwa wametingwa sana, sasa naomba wakipunguza kutingwa kidogo, watusaidie ma- grader sisi tutajaza mafuta, tutapunguza kidogo kero ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, napenda nifahamishe Bunge lako na Watanzania kwa ujumla kwamba, msitu wa Sao Hill, kutokana na mapato yake, Serikali katika misitu inapata asilimia 35 kutoka katika Msitu wa Sao Hill tu ambapo Makao Makuu yake yako pale Mafinga. Nitumie nafasi hii kuwashukuru sana kamati, walifanya pale ziara na hata katika taarifa yao wameandika na wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na campus ya Chuo cha Misitu pale Mafinga, kwa sababu, itasaidia hata wanafunzi kwenda kupata mafunzo kwa vitendo katika ule msitu ambao ni mkubwa katika Afrika Mashariki na Kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na ukubwa wa msitu huu ambao kwa mujibu wa takwimu kwa mwaka tunapata karibu takribani shilingi bilioni 42. Kati ya mwaka 2015 hadi 2020 tumepata kama shilingi bilioni 216 kwa maana Serikali imepata hizo fedha. Hata hivyo, kasi ya wavunaji kwenda msituni imeendelea kupungua kutokana na wingi wa tozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumza hapa, kuna tozo 13 katika sekta ya misitu. Tozo mojawapo ni LMDA. Tozo hii ilianzishwa ili kuisaidia Serikali kupanda miti kwa sababu kwa muda mwingi lile shamba halikupanda miti. Sasa hivi miti imepandwa kwa wingi, naishauri Serikali ingetoa tozo hii ili kusudi kupunguza gharama za watu kwenda msituni.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni tozo katika VAT. Najua tutakwenda kwenye Muswada wa Fedha. VAT ni Kodi ya Ongezeko la Thamani, lakini wananchi wa Mafinga na Mufindi anapoenda kukata tu ule mti nao anatozwa VAT. Ni ongezeko gani la thamani limeongezeka katika ule mti? Sasa matokeo yake wavunaji hawaendi kuvuna msituni, Serikali haipati mapato. Of course wanaenda kuvuna kwa wananchi ambao miti haitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kuna vitu amesema hapa Mheshimiwa Nape, hata katika wanyamapori, ziko tozo ambazo nadhani tuziangalie kwa macho mawili, kwa sababu, inavyokuwa sasa, yaani msitu unao, fedha hauna. Sasa unakosa shilingi kumi ambayo bora uikose shilingi kumi ambayo ingekuzalishia wewe shilingi 100 katika mtiririko mzima wa Ongezeko la Thamani. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, suala la VAT litazamwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ipo katika masuala ya wanyamapori, vitalu vingi sasa vimekaa idle. Vikikaa idle madhara yake wale watu wanaokuwa wanakodishwa vitalu, mojawapo ya masharti ni pamoja na kufanya uhifadhi katika vile vitalu. Sasa vikikaa idle maana yake kwamba uhifadhi unakuwa haifanyiki, vinashuka thamani. Kwa hiyo, Serikali ifike wakati tuangalie, kuna wakati bora ukose shilingi kumi ukapata shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni migogoro ya wakulima na wafugaji. Nasema hapa, bila kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, tutaendelea kila mwaka kuongeza maeneo. Nina takwimu hapa kidogo tu; katika Tanzania sisi, nchi yetu, population wise, yaani population density, sisi ni watu 67 per kilometer square. Nchi kama Rwanda ni watu 525 per kilometer square. Burundi 463 per kilometer square. Malawi 205 per kilometer square. Kwa hiyo, ukiangalia population density sisi siyo kwamba tuko over populated, ila tunachotakiwa kufanya ni kitu kimoja; tunaanza kwenye kilimo. Lazima tulime kilimo chenye tija. Hiki kilimo cha kudhani kwamba ukilima ekari nyingi ndiyo utapata mahindi mengi, hakitatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ufugaji lazima tufuge ufugaji wenye tija. Siyo kwamba ukiwa na ng’ombe 10,000 ndiyo utapata maziwa mengi. Sasa kutokana na kwamba hatujawekeza tija katika kilimo kwamba, ekari moja inakupa gunia tatu, sasa kumbe eka moja ingekupa gunia 20 usingelima eka kumi. Sasa matokeo yake ili upate magunia 30 unalima ekari kumi; ili upate nyama nyingi, unafuga ng’ombe wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa wito kwa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wawasaidie wakulima na wafugaji wa nchi hii wafuge na kulima kwa tija. Vinginevyo ardhi ya nchi hii haitakaa itoshe. Watakuja watu wa Maliasili na Utalii hapa mtawasulubu. Hao ng’ombe hawataacha kwenda kwenye hifadhi na migogoro ya wakulima na wafugaji haitakaa iishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suluhisho, ni lazima tulime kwa tija, eneo dogo lizalishe sana; tufuge kwa tija, eneo dogo upate mifugo inayokupa tija. Kinyume chake, nchi hii tutakuwa kila siku tuna-declare kuongeza maeneo ya wakulima na wafugaji wakati we are not overpopulated kama nchi nyingine ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge. Bila kufanya hivyo, migogoro haitakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Nashukuru. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha mchango wa maandishi kama ifuatavyo; kwanza sekta ya maliasili na utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na utalii; kwa miaka mingi sekta ya utalii imekuwa na mchango wa takribani 25% katika kuingiza fedha za kigeni, hata hivyo baada ya shida ya Covid-19 sekta hii imetetereka kwa hali ya juu sana, katika ajira sekta hii kwa ujumla inaajiri takribani Watanzania milioni nne. Baadhi ya nchi na hata mashirika makubwa ya fedha duniani yamekuwa yakitoa stimulus package ili walau kukabiliana na janga la Covid-19. Sisi Taifa letu bado haliwezi kubeba mzigo wa kuwa na stimulus package na ndio maana hata TANAPA imebidi kuisaidia. Kwa sababu hiyo nashauri tusiongeze tozo katika sekta ya utalii, tuache zilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wanyama pori/TAWA; naunga mkono suala la kugawa vitalu kwa njia ya mnada, hata hivyo ili tupate fedha lazima tuuze kwa bei rafiki kuliko ilivyo sasa ambapo vitalu vingi vinakosa wapangaji na tunakosa sio fedha tu lakini tunaviweka vitalu katika uhatari wa kukosa kuhifadhiwa kwa sababu masharti ya anayepewa kitalu ni pamoja na uhifadhi. Wenzetu Zimbabwe wana maeneo 40 tu lakini kwa mwaka wanapata around USD 130 million, mbali ya kupata fedha kwa kukodisha vitalu kuna faida mbalimbali kama vile ajira kwa rangers, fuel levy kutokana na magari yanayotumika na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kwanza Serikali ijiridhishe kuhusu vitalu itabaini kuwa tunakosa fedha kwa sababu ya bei ya kuanzia, hivyo Serikali ipange bei za kuanzia ambazo zitavutia wateja, bei za USD 80,000 hazijaweza kutusaidia, tushuke walau hata nusu, haina maana tuna vitalu lakini hatuvikodishi, ni kama una nyumba unataka kuipangisha kwa shilingi laki moja kwa mwezi, hupati wapangaji kwa miaka mitatu, wakati ungepangisha kwa nusu ya bei, ungeweza kupata mapato lakini pia nyumba ikikaa bila kuishi mtu inachakaa. Nimetoa mfano wa kawaida kabisa wa ki-layman ili walau nieleweke, ninaamini vitalu vya uwindaji vinaweza kutuongezea mapato ya kutosha hata kuvuka bilioni 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni misitu/TFS; asilimia 60 ya ardhi ya Mafinga/Mufindi ni misitu, tuna msitu mkubwa wa Sao Hill, ni msitu mkubwa Afrika Mashariki na Kati. Hata hivyo wingi wa tozo umeendelea kupunguza wavunaji katika msitu na hivyo kukosesha Serikali mapato, wavunaji wana opt kwenda kuvuna miti ya wananchi ambayo haitoshelezi, nashauri VAT na LMDA ziondoshwe, duniani kote hakuna anayetoza VAT kwenye mti. Kwa mfano bei ya soko kwa cubic meter moja ni shilingi 320,000 kwa hiyo mvunaji ambaye anauza 320,000 anaingia gharama zifuatazo; ili upate cubic meter moja ya mbao unahitaji miti ya ujazo wa cubic meter tatu ambapo ni 3x64,940=194,820 hii royalty; kuna VAT 18% shilingi 35,068; kuna cess 5%= shilingi 9,741; kuna LMDA 17,000x3= shilingi 51,000 kwa sababu kama nilivyosema ili kupata cubic meter moja ya mbao unahitaji cubic meter tatu za miti na kuna TP yaani transit pass ya miti 7000x3= shilingi 21,000. Kwa hiyo jumla ya tozo ni shilingi 311,629. Ukichukua 320,000 ukatoa 311,629 mvunaji anabakiwa na shilingi 8,371. Hapa sijataja gharama nyingine za uendeshaji kama mafuta, vibarua wa kusogeza magogo na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hii tozo tu ni 97% ndio maana wavunaji wanakimbia kuvuna katika msitu wa Serikali tunakosa fedha lakini pia ni double taxation kutoza VAT kwenye mti, halafu tena kwenye mbao, kadhalika cess inatozwa mara mbili, sio tu ni uonevu lakini pia ni kinyume cha sheria lakini pia hotuba inasema Serikali haitaki mapato ya dhuluma, haya pia ni ya dhuluma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tozo kwenye mafuta ya kula; ndugu zangu lazima tuwe honest, hatuwezi kulinda ambacho hakipo, mwaka wa nne sasa hatujaanza kuzalisha mafuta kutokana na mawese, lakini pia jitihada za kulima alizeti na ufuta hazijaimarika ipasavyo, kuongeza tozo ni kumtesa mwananchi, bei ya mafuta ya imekuwa ikiongezeka mwaka hata mwaka kwa zaidi ya 100%. Hivyo nashauri sana tuitazame hii tozo, tusilinde ambacho hakipo, Wizara ya Kilimo iongoze mbio kuhakikisha suala aliloanzisha Mheshimiwa Waziri Mkuu katika michikichi na alizeti ili tujikwamue kwa vitendo suala la mafuta ya kula, tusilinde ambacho hakipo.

Kuhusu uchukuzi/bandari/TAZARA; nashauri, kwa kuwa bandari ni chanzo cha mapato, yapo maeneo tuyaimarishe ili kupunguza muda wa kusafirisha mizigo; TAZARA iimarishwe ili ifikishe mizigo mpaka Makambako na Mbeya ambapo nchi jirani watakuja kuchukua cargo zao Makambako au Mbeya, tuta-fast track uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Tunduma malori yanatumia mpaka wiki kuvuka, suala hili linapunguza ufanisi, ndio maana Bandari kama Beira zinakuwa washindani wetu wakati hawastahili, hivyo maeneo yanayotupa mapato tuyalee, tuweke mageti hata Mbozi, suala kwamba transit cargo itarudi nchini, sio sawa labda kama hatuna nia njema kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fuel levy/vinasaba; kwa muda wa miezi karibu miwili TBS wanaifanya kazi hii, jambo hili ni jambo jema kuvijengea uwezo vyombo vyetu, hata hivyo katika wakati wa mpito yaani transition period naomba tuwe makini, EWURA wawezeshwe katika kufanya kaguzi kwa kupewa vifaa vya kukagulia ili tusipoteze fuel levy, as it is tunapoteza mamilioni kwa sababu mafuta ambayo ni transit yanabakizwa nchini, tunapoteza mapato, ushauri wangu Serikali ichukue hatua za haraka na kuthibitisha hilo Serikali ifanye mahesabu ya fuel levy ya mwezi Mei.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulinda viwanda vya ndani/ Kiwanda cha Pareto Mafinga; hiki ni kiwanda cha pili duniani na Tanzania ni ya pili kwa kuzalisha pareto baada ya Tasmania-Australia na kwa taarifa tu, pareto ni zaidi ya data ya kuulia wadudu kama inavyojulikana, bali ni final product ni component muhimu katika masuala ya military. Sasa Kiwanda cha Pareto Mafinga kimekuwa kikitoa mbegu na huduma za ughani kwa wakulima wa zao la pareto, lakini sasa ikifika wakati wa mavuno, wanatokea walanguzi wanaongeza bei kidogo wananunua maua ya pareto, kiwanda kinakosa malighafi, ajira zinakuwa hatarini kupotea, Serikali itakosa kodi na kadhalika. Ninaomba sana maelekezo yaliyotolewa na Serikali yawe kwa vitendo ili sio tu kulinda kiwanda hiki lakini pia kusimamia vitu kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mabenki ya Serikali TADB, TIB, TPB; ninaandika kama layman wa Banking Industry lakini kama mfuatiliaji wa masuala ya kitaifa, je, benki hizi zinapata faida? Kama hazipati faida ni kwa nini?

Nafahamu jitihada za kuunganisha benki ambazo zimeshaanza na tayari TIB Corporate na TPB, hata hivyo ninashauri benki hizi zote ziwe benki moja tu ambayo itajihusisha na kilimo/mifugo/uvuvi na uwekezaji, lakini lazima tukubali kuwa banking industry sio huduma, ni biashara, kama tunataka tupige hatua basi benki hizi zizae faida ili ikopeshe wengine, kwa nini zije benki kutoka nje zipate faida halafu sisi benki zetu Serikali zisipate faida, labda tuamue kuwa ni vyombo vya kutoa ruzuku.

Mwisho, je Benki ya Kilimo toka imeanza imekuwa na tija kwa kiasi gani? Vinginevyo tutalalamika mtaji mdogo, je, hata huo mtaji mdogo umeleta tija gani hata kama ni kidogo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, tutazame mwenendo mzima wa hii benki, vinginevyo itakuwa political bank of agriculture, tuwe makini, huu ni uchumi though kila kitu ni siasa lakini uchumi usizidiwe na siasa. Naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. CASATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami nianze mchango wangu kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais. Niliwahi kusema hapa wakati wa Bunge la Bajeti kwamba Mheshimiwa Rais kama Mkuu wa Nchi na Mkuu wa Dola, ndiye Diplomat namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ametendea haki ile kuwa Diplomat namba moja, kwanza ambavyo mmemwona anashiriki katika shughuli mbalimbali Kimataifa na matunda yake tumeyaona ikiwemo pamoja na huu mkopo ambao tumetoka kuzungumza na mchangiaji aliyepita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi kwa Mheshimiwa Rais kama Diplomat namba moja, nilikuwa napenda kutoa changamoto au wito kwa wataalamu wetu; kwa mfano nitanukuu hapa, wakati Mheshimiwa Rais akiwa kwenye Mkutano wa Mazingira kule Scotland, amesema kwamba tunapimwa kwa vitendo vyetu na siyo kwa ahadi kubwa kubwa. Mheshimiwa Rais alikuwa na uthubutu wa kuyaambia Mataifa makubwa ambayo yamekuwa yaki- pledge katika kuchangia masuala mazima ya madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi; na amesema, naomba kunukuu.

“Mabadiliko ya tabia nchi ni suala la dunia nzima na hivyo majawabu yake ni lazima yawe ya Kimataifa na hivyo tunatoa wito kwa nchi zilizoendelea ambazo ndiyo zinazoongoza kwa uchafuzi, zitekeleze kwa vitendo ahadi zao za kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa fedha za kutosha kutuwezesha sisi nchi za kipato cha chini kufanikisha malengo yetu kwenye michango ya Kitaifa ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa uendelevu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa nilikuwa napenda kushauri wataalam, kuna fedha ambazo pamoja na kuwa nchi zilizoendelea hazitoi kwa kiwango kinachotakiwa, lakini kuna fedha zinazotolewa katika mifuko mbalimbali, nitaitaja baadhi kama vile Climate Investment Funds, Green Climate Funds, Adaptation Fund na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mifuko hii ili uweze kupata zile fedha ambazo kwa namna moja au nyingine zitawezesha Taifa lako kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, zitawezesha nchi kama Tanzania, watu kama wa Iringa, watu kama wa Mufindi na Njombe ambao wanapanda miti kwa wingi na hivyo kusaidia dunia kupunguza hewa ya ukaa ili uweze ku-access zile funds, lazima kuna vigezo kama Taifa uwe umepitia na umefikia. Baadhi ya vigezo lazima uwe na taasisi ambazo zimekuwa accredited au zimepata ithibati ambapo ndani ya ule utaratibu utaeleza zile fedha utatumiaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Rais ameshafungua mlango. Kwa hiyo, pamoja na kwamba nchi hazijatoa fedha kwa kiwango kikubwa, lakini kile kiwango ambacho kipo kwa Taifa letu mpaka ninapozungumza sasa, ni taasisi mbili tu; ni NEMC na CRDB ambao wamekidhi hivyo vigezo, wanaweza ku-access hizo Fund. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Mpango kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira) tuwezeshe taasisi nyingi ziweze kujengewa uwezo. Sisi watu wa Mafinga na Mufindi ambao tunachangia kupunguza shida katika mabadiliko ya tabianchi tuweze ku-access zile funds ili kusudi ziweze kutusaidia katika kukabiliana na madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nchi kama Kenya, Rwanda na Morocco, wanapata mabilioni ya pesa kila mwaka, kwa sababu tu wameweza kukidhi vigezo ambalo ni jambo la kawaida. Hapa nitoe wito kwa wenzetu wa Vyuo Vikuu, Taasisi za Elimu ya Juu, hebu zitusaidie katika kuona zinaweza kujengeaje uwezo taasisi mbalimbali; za Serikali na za binafsi ili tuweze ku-access hizo funds kusudi siyo tu watu wa Mufindi, Mafinga, Iringa na Njombe wanufaike, lakini Taifa zima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ambalo napenda kushauri kwenye Mpango, tunatumia pesa nyingi sana kuagiza sukari na mafuta ya kula. Kwa mfano, katika mafuta ya kula, tunatumia karibu shilingi bilioni 500 kuagiza mafuta kula. Kwenye sukari vivyo hivyo; kila mwaka tunakuwa na uhaba wa sukari na sukari inapanda bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuwaandikia Mawaziri kadhaa kuhusiana na ushauri kwamba pamoja na ule mradi mkubwa wa Mkulazi, bado kama Taifa tuna maeneo ambayo tunaweza tukawekeza katika small scale industry na Taifa likajitosheleza kwa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala zima la mafuta ya kula, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, namwona kila mara anaenda Kigoma kwa ajili ya masuala mazima ya Mchikichi. Yaani kama Taifa, ninashauri sana Mpango kama ulivyosema katika kilimo, hebu tujielekeze katika kupunguza kutumia fedha za kigeni kuagiza bidhaa ambazo hapa hapa nchini tunaweza tukazizalisha ikiwemo sukari na mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 126 wa Mpango, umesema mambo mbalimbali ikiwemo kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuboresha uwezeshaji wananchi kiuchumi, kukuza sekta binafsi na mwisho wa yote ni kuchochea maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa napenda kuishauri Serikali na Mpango kwa ujumla, wakati tunatengeneza mazingira ya uwekezaji kuvutia wawekezaji, ninashauri pia wawekezaji hawa tunaowavutia katika kule kuwekeza kwao kuwe na mantiki na kusaidie kunyanyua maisha ya wananchi. Kwa nini nasema hivi? Ukija pale Mafinga tuna wawekezaji wengi sana kutoka China wamewekeza kwenye mazao ya misitu, lakini ile biashara namna wanavyofanya, pamoja na kuwa tunasema tupo kwenye soko huria, lakini soko huria ambalo haliwi regulated litakuwa soko holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninapozungumza, pamoja na Serikali ya Mkoa naya Wilaya kuwasaidia watu wanaouza magogo kwa Wachina, kuna kitu kinaitwa betting; yaani unaenda pale na gari lako, umepakia magogo, unamuuzia Mchina mwenye kiwanda, mnaanza kubishana. Anakwambia hii ni shilingi 700,000/=, wewe unamwambia hapana ni shilingi 900,000, laki saba na nusu, laki nane na nusu, inaitwa betting.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naishauri Serikali watusaidie kuweka bei elekezi ili wale watu wanaouza magogo kwa wale wawekezaji waweze kuuza kwa bei ambayo itarejesha gharama zao na pia watapata faida ili kwenye ule ukurasa wa 26 tunaposema kuchochea maendeleo ya watu, basi tuweze kuwa tumechochea maendeleo ya haya watu kesho waweze ku-afford huduma za afya, waweze ku-afford huduma za elimu na kadhilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, nimalizie na suala la mbolea. Mimi nilifanya ziara katika baadhi ya maeneo, mwananchi mmoja alinishika hivi ananitingisha, ananiuliza, nijibu Mbunge; niuze madebe mangapi nipate mfuko mmoja wa mbolea? Kwamba debe la mahindi ni shilingi 5,000/=; mfuko wa mbolea shilingi 100,000/=. Yaani auze madebe 20 apate mfuko mmoja wa mbolea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nami naungana na wewe na Mheshimiwa Nape, lazima Mpango ujielekeze kwenye suala zima la kilimo ambacho kinachangia pato la Taifa kwa asilimia 26.6; bidhaa zote zinazouzwa nje kilimo kinachangia asilimia 26; lakini zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wamejiajiri kwenye kilimo; lakini leo hii mfuko wa mbolea ni shilingi 100,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali na kwa Mpango kwa ujumla, pamoja na kujenga viwanda, lakini pawe na uwezekano wa kuweka ruzuku kwenye mbolea.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru na ninasema, Bwana asipoulinda Mji, waulindao wakesha bure. Mungu ailinde nchi yetu. (Makofi/Kicheko)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa hoja ambayo imewasilishwa mezani. Nitajielekeza kwenye hoja ya Kamati ya Ulinzi, Mambo ya Nje na Usalama.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza napenda kutumia nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Mafinga Mjini, kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge letu. Mwenyezi Mungu akusimamie na kukuongoza; hizi ni salamu ambazo nimetumwa na Wanamafinga nizifikishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya salamu hizo, kama mara zote ambavyo huwa nasema kwamba, Mheshimiwa Rais ndio mwanadiplomasia namba moja. Pale anapokuwa amefanya kazi ametimiza majukumu yake kama mwanadiplomasia namba moja, tunao wajibu wa kumpongeza na kumtia moyo. Mimi sitaishia tu kumpongeza na kumtia moyo, lakini nitafanya na takwimu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na kazi nzuri ya diplomasia, kama mwanadiplomasia namba moja ambayo Mheshimiwa Rais anaifanya, nchi yetu imeendelea kupata fursa mbalimbali za kibiashara, hasa katika eneo letu la afrika Mashariki, lakini na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, hapa unipe ruhusa nitoe takwimu kidogo tu; kutokana na kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais, biashara kwa maana ya trade balance kati yetu sisi na kenya, kwa mara ya kwanza tumefanya vizuri sana katika kipindi cha Januari mpaka Septemba, 2021. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa takwimu kibiashara, mauzo yetu katika nchi Jirani ya Kenya, kama wenzetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na hii naitoa kulingana na takwimu za ile Kenya National Bureau of Statistics kwamba, mauzo yetu yameongezeka kutoka dola za kimarekani milioni 347 sawasawa na bilioni za Kitanzania 802 mpaka dola za kimarekani milioni 396, sawasawa na fedha za Kitanzania bilioni 915.

Mheshimiwa Spika, hili ni ongezeko kubwa na ni ongezeko ambalo mara nyingi, trade balance kati yetu sisi na wenzetu, wenzetu wamekuwa wakituzidi, lakini kutokana na kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais, kama mwanadiplomasia namba moja ameifanya, tunaona sasa kama Taifa letu na sisi trade balance kati yetu sisi na majirani zetu sasa inaendelea kukua. Kwa hiyo, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu, kama Kamati tulikuwa na kilio cha muda mrefu na kuishauri Serikali kupeleka maafisa katika balozi zetu, ili waendelee kutafuta fursa za kiuwekezaji, fursa za biashara na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya Taifa letu. Ninapozungumza hapa Wizara imefanikiwa kupeleka maafisa 137 katika balozi zetu 44 ambao ni sawa na wastani wa asilimia 63% kati ya maafisa 215 wanaohitajika. Hii ni hatua kubwa ambayo itaenda kuongeza ufanisi katika balozi zetu, itaenda kuongeza utendaji na zaidi ya yote kung’amua zaidi fursa za kiuwekezaji na hivyo kuliongezea Taifa letu mapato zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kama ambavyo tumesema katika Kamati yetu, bado kuna shida kubwa ya uchakavu wa majengo na uhaba wa majengo katika balozi zetu. Kama taarifa yetu ilivyojionesha ni Balozi nne tu za Cairo, Lusaka, Maputo na Harare ndizo ambazo maafisa wetu au Serikali yetu ina majengo kwa maana ya ofisi na ina majengo kwa maana ya makazi ya maafisa wetu wa ubalozi.

Mheshimiwa Spika, jambo hili linaifanya Serikali kubeba mzigo mkubwa sana wa kugharamia pango kwa ajili ya ofisi na pango kwa ajili ya makazi ya maafisa wetu na hivyo kuwa ni mzigo mzito sana kwa Serikali. Ndio maana Kamati yetu imekuwa ikishauri na inaendelea kushauri kwamba, Serikali kwa maana ya Hazina, waweze kutoa fedha ili ule mpango mkakati ambao Wizara ya Mambo ya Nje imejijengea au imejiwekea wa miaka 15 wa kuondokana na kupangisha na kukodi majengo ya ofisi na makazi ambayo hata kiusalama sio nzuri sana, basi uweze kutimia, lakini utatimia ikiwa tu wenzetu hawa watapatiwa fedha kama ambavyo Kamati imeelekeza.

Mheshimiwa Spika, hapa nitatoa mfano mdogo. Kwa mfano, katika Ubalozi wetu wa Marekani, pale Washington DC, tuna jengo ambalo ikiwa Serikali itatoa fedha kiasi cha bilioni 3.8 likakarabatiwa, maana yake ni kwamba, lile jengo ambalo tunalitumia sasa hivi tutahama na hivyo, lile jengo tunalolitumia sasa hivi tutalipangisha na kwa mwaka tutapata wastani wa bilioni 2.4. Kwa hiyo nitoe wito na ushauri kama Kamati ambavyo imesema tukitoa fedha hizi kwa Wizara tukakarabati majengo maana yake kwanza tutaokoa fedha ambazo tunapanga sasa, lakini pili, tutazalisha mapato zaidi kwa ajili ya kuendeshea shughuli zingine za Serikali.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano mdogo. Kwa mfano, katika Ubalozi wetu wa Marekani, pale Washington DC, tuna jengo ambalo, ikiwa Serikali itatoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.8 likakarabatiwa, maana yake ni kwamba, lile jengo ambalo tunalitumia sasa hivi tutahama na kulipangisha na kwa mwaka tutapata wastani wa shilingi bilioni 2.4.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo natoa wito na ushauri ushauri kama Kamati ambavyo imesema, tukitoa fedha hizi kwa Wizara, tukakarabati majengo, maana yake kwanza tutaokoa fedha ambazo tunapanga sasa, lakini pili, tutazalisha mapato zaidi kwa ajili ya kuendeshea shughuli nyingine za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili katika Kamati yetu ambalo tumeliona, tulikuwa tumeshauri kwamba Magereza wajitosheleze kwa chakula. Tunapozungumza hivi sasa, Magereza kutokana na kazi nzuri wanayofanya, wameokoa takribani shilingi bilioni 11 ambazo zilitokana na kuwalipa wazabuni kwa ajili ya chakula kwa wafungwa na mahabusu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wetu kama Kamati na mimi kama Mjumbe wa Kamati, ninashauri ili Magereza iweze kujilisha na kuzalisha ziada, basi kile ambacho kinakuwa kimepangwa na Serikali katika bajeti, fedha zile ziende. Sambamba na kuwapa fedha ambazo zitawasaidia kuwa na uwezo katika kujenga miundombinu ya umwagiliaji, pia Jeshi la Magereza tunapozungumza hivi sasa ukiacha yule Mkuu wa Magereza (Commissioner General of Prison) ambaye kimuundo anatakiwa kuwa na wasaidizi wanne, hana hata msaidizi mmoja. Pia kimuundo kuna ma- Deputy ambao wanatakiwa kuwa kama 17, lakini yuko mmoja tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni wakati wa Serikali sasa kuliwezesha Jeshi la Magereza kifedha na nyenzo ili liweze kuzalisha kwa ajili ya kujilisha kama ambavyo wameokoa hizo shilingi bilioni 11, lakini pia waweze kuzalisha kwa ajili ya ziada. Haya yatawezekana ikiwa tu tutawapa fedha, na ile ikama yao kwa maana ya muundo wao yule Mkuu wa Magereza, apatiwe wasaidizi wake.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kutokana na muda, naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Ninapenda kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Masauni Naibu wake na timu yake nzima ambao tumekutana kwenye Kamati kwa takriban wiki nzima kupitia Azimio hili la Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi za Afrika kuzuia na kupambana na ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekitti, lakini pia nitumie nafasi hii kuwapongeza wajumbe wenzangu wa Kamati, kama alivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti wetu Vita Kawawa, kwa utulivu na umakini wa hali ya juu katika kuhakikisha kwamba tunafikia siku hii ya leo kuwasilisha hili azimio humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwenye masuala mengi mbalimbali kimataifa, jambo la kupambana na ugaidi ni jambo ambalo sisi kama Taifa na kama nchi ambayo hatuishi katika kisiwa tunapaswa kushirikiana katika kukabiliana na uhalifu mbalimbali ukiwemo vitendo hivi vya kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa na kwa jinsi ambavyo vitendo vya ugaidi vyenyewe jinsi vilivyo; kwanza mpambano wa kigaidi si kama vita ya kawaida ambayo pengine nchi A inaweza ikawa inapambana na nchi B, au kikundi cha mataifa kadhaa kikawa kinapambana na kikundi cha mataifa kadhaa, kwamba kitu ambacho kinaonekana. Tatizo la ugaidi ni vita ambayo adui kwanza humuoni na wala hujui yuko wapi na wala hujui anaishi wapi. Kwa hiyo, kwa ugumu huo maana yake ni muhimu sana kufanya jambo hili ili kukabiliana nalo katika namna ya kushirikiana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa tumekuwa tukishiriki katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya uratibu wa Umoja wa Mataifa na wakati mwingine chini ya utaratibu wa Jumuiya zetu za kikanda kama vile SADC. Kwa hiyo hata katika jambo hili ni muhimu sana kuhakikisha kwamba tunaendeleza utamaduni wetu wa kushirikiana na wengine duniani na kikanda katika muktadha mzima wa kuhakikisha kwamba tunakabiliana ipasavyo si tu na vitendo lakini ikibidi hata na viashiria vya masuala ya kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mbalimbali chini ya utaratibu wa Umoja wa Mataifa au Umoja wa Kikanda kama nilivyosema tumeshiriki katika masuala ya ulinzi wa amani, ama katika eneo letu hili la maziwa yetu makuu ama hata katika nchi mbalimbali kama huko Lebanon nchi za Afrika za Kati, kote huko kuna majeshi yetu ambayo yanashiriki katika ulinzi wa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi zote ni taratibu ambazo tunaziweka kimataifa ili kukabiliana na matukio au na vitendo mbalimbali ambavyo vinaweza vikahatarisha usalama si wa nchi yetu tu bali usalama wa eneo la kikanda na usalama wa dunia katika ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuridhia azimio hili la Bunge na Itifaki hii, sisi sasa pia tunaweza tukanufaika. Kama nilivyosema, suala lenyewe hili ni gumu kwa sababu napambana na adui ambaye kwanza umuoni na hujui yuko wapi. Kwa hiyo miongoni mwa faida ambazo tutanufaika nazo ni pamoja na ku-share taarifa. Kwa mfano tunacho hiki kituo cha kanzidata ambacho kipo pale Algeria, maana yake tukiwa sehemu ya hii Itifaki, sehemu ya hili azimio kuna taarifa sisi kama taifa tunaweza tukapewa ambazo tukazitumia katika kuhakikisha kwamba tunakabiliana si tu na vitendo lakini hata na viashiria vya ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, kwa wanasheria wanaweza wakanisaidia; katika sheria, hasa sheria za kimataifa, kuna kitu kinaitwa extradition ambapo ni makubaliano baina ya nchi na nchi kubadilishana wafungwa. Lakini kupitia suala hili na azimio hili bado tunaweza kubadilishana wahalifu, tukawa na utaratibu maalum ambao unaweza kutuwezesha sisi kama taifa kubadilishana na wahalifu ambao kwa namna moja ama nyingine wanashiriki katika vitendo au kwa namna moja au nyingine kuna viashiria kutokana na watu wao na masuala ya kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia taifa letu tumekuwa tukifanya juhudi kubwa za kujenga uchumi wa nchi yetu, tunajenga miundombinu kama vile viwanja vya ndege; na kwa mfano sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa SGR. Hii ni miundombinu ambayo kwa namna moja au nyingine inasaidia katika kuvutia wawekezaji, inasaidia katika katika kuhakikisha kwamba tunapanua shughuli zetu za kiuchumi na kukuza biashara baina yetu na mataifa mengine, pia na baina yetu na majirani. Sasa, ili uweze kuwavutia wawekezaji, pamoja na miundombinu hii kama ya ujenzi wa barababara, kama nilivyosema ujenzi wa SGR, miundombinu ya nishati kama vile bwawa la umeme; lakini pia mwekezaji ili aje anataka awe na uhakika na usalama katika ile nchi au taifa analoenda kujiwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa moja wapo ya mambo ambayo ni muhimu kama taifa ni pamoja na kuhakikisha tuishi kama kisiwa, tunashiriki katika itifaki hizi ambazo ni za kimataifa au taratibu mbalimbali za kikanda. Kwa hiyo wanaangalia katika list na kuona kwamba hawa kumbe ni washirki katika jumuiya ya kimataifa na ni washiriki katika kikanda kuhakikisha kwamba kama taifa lao wanakuwa salama. Si wao tu lakini pia na majirani zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la utalii, kama nilivyosema tunaendelea na ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege. Kama sisi kule Iringa tunaendelea na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa. Pia hivi karibuni tutaanza ujenzi wa barabara kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park. Hivi vyote kwa namna moja au nyingine vitavutia watalii, pamoja na kutumia fursa ya kutangaza ile filamu ya Royal Tour ambayo inavutia watalii. Sasa, ili nao, watalii, waweze kuja katika nchi yetu yapo mambo ambayo ni ya msingi ambayo wanatazama. Wanaangalia, je, Tanzania kama Taifa inashirikiana kimataifa kwa kiwango gani na kikanda kwa kiwango gani katika kuhakikisha kwamba inakuwa tu si yenyewe salama lakini salama na watu na majirani wanaotuzunguka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mtu anapoangalia katika check list anaona kama taifa tumeridhia azimio kama hili, kama taifa tunashirikiana na jumuiya za kimataifa katika kuhakikisha usalama wa taifa letu na majirani kwa hiyo inampa yule mtu confidence ya kuja kutembelea kama mtalii, lakini pia nakuja Tanzania kama mwekezaji. Kwa hiyo, itoshe kusema kwamba, jambo hili ni muhimu na limeletwa wakati ambao ni sahihi, na kama kamati ambavyo imeshauri, na ile sheria yetu ya kukabiliana na ugaidi pia tuifanyie mabadiliko ili iweze kuendana na suala hili kama ambavyo tumesema iwe combat and abrogation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nawashukuru sana. (Makofi)
Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nami naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Ezra. Kwanza napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuwa na scholarship maalum kwa ajili ya watoto ambao wanaenda kusoma sayansi.

Mheshimiwa Spika, kuna scholarship zimetolewa kwa ajili ya watoto zaidi ya 600, ni jambo jema nami kwa mawazo yangu na uelewa wangu nimeona kwamba kama Taifa tuna miradi mingi inayoendelea. Tuna mradi wa SGR, tuna mradi wa Bwawa la Umeme na juzi tumeona uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanja kikubwa sana cha Kimataifa cha Msalato na viwanja vingi vinaendelea kujengwa kikiwemo kiwanja cha Iringa pale ambacho kitapanua wigo sana wa utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi vitu vyote ambavyo tunavijenga, hii miundombinu yote baada ya kuwa imekamilika, itahitaji huduma katika kuiendesha miundombinu hii. Vile vile itahitaji wataalamu na utaalamu na nadhani kwa sababu hiyo ndiyo maana Mheshimiwa Rais akaona atoe scholarship kwa ajili ya watoto ambao baadaye watakuja kutumika katika kusimamia miundombinu na miradi mbalimbali ambayo tunaijenga sasa hivi kwa fedha nyingi ambazo ni za Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo basi, suala la mikopo ni suala ambalo siyo la hiari tena kwa Taifa letu, ni suala la lazima. Tukitoka huko nje kwa wananchi sisi kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi, katika mikutano yetu ya hadhara, katika vikao vyetu vya ndani tumekuwa tukijinasibu kwamba tumeongeza fedha kwa ajili ya mikopo ya watoto wetu. Sasa inapotokea kwamba watoto na waliokuwa na ufaulu wamekosa, maana yake ni kwamba tunajichanganya sisi wenyewe na wananchi, kwamba tumeongeza fedha kama alivyosema Mheshimiwa Kanyasu, kijana anauliza hiyo shilingi milioni 570 sasa iko wapi?

Mheshimiwa Spika, sasa kama tumeongeza fedha na watoto hawapati, kwa kadri ya matarajio na kwa kadri ambavyo tumewaaminisha kwamba tumeongeza fedha, maana yake ni kwamba tunakuwa tunawachanganya wananchi.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi niseme jambo moja, maana tayari hii ni crisis, hili ni tatizo. Sasa je, tatizo hili ni namba moja, ni tatizo kama hivyo walivyokuwa wanasema wenzangu namna ya kuwatambua wanaostahili mikopo au tatizo ni ufinyu wa bajeti?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kuwa tumetambua shida ni nini, tatizo ni nini, basi kama Bunge ambao tunaishauri na kuisimamia Serikali, ni wajibu wetu kuona tunatoka na suluhisho gani?

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tulipokuwa tuna shida ya ongezeko la bei ya mafuta kutokana na ongezeko la bei ya mafuta duniani, Serikali yetu tunaipongeza sana ilikaa chini, ikaona kuna umuhimu wa kutoa ruzuku kupunguza makali ya bei ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipokuwa na kilio hapa cha mbolea, Serikali yetu ikafuata ushauri wa Wabunge, imekuja imetoa ruzuku ya mbolea. Mwaka 2021 au mwaka 2020 wakati tulipokuwa na crisis ya bei ya mahindi, tulikaa na Serikali; Wabunge wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Serikali ikatafuta fedha ikawezesha hifadhi ya chakula, ikatoa fedha mahindi yakanunuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu, kama hili ni tatizo basi kama ni la kibajeti, hebu tukae chini tuone tunafanyeje, fedha ipatikane watoto wapate mikopo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuwapongeza kwa kuimarisha suala la udhibiti ubora kwa kutoa mafunzo kwa Walimu na Maafisa Elimu Kata, kwa sababu ubora wa elimu yetu hasa kuanzia ngazi ya msingi na sekondari ni jambo muhimu sana.

Pili ni kuhusu elimu jumuishi; napongeza hatua zinazochukuliwa na pia shukrani kwa Wizara kuisaidia Shule ya Msingi Mchanganyiko/Jumuishi ya Makalala ambayo iko katika Halmashauri ya Mafinga Mji, mazingira ya shule hii sasa yanavutia na pia kupitia wahisani wa Water for Africa, shule imepata kisima kirefu na kufungiwa mfumo wa maji ya moto. Nawashukuru sana.

Hata hivyo, ninawasilisha maombi ya gari kwa ajili ya shule hii ambayo ipo umbali wa kama kilometa tano kutoka Mafinga Mjini. Hii ni kwa sababu shule hii inahudumia watoto wenye ulemavu wa akili, wenye uono hafifu na wenye ualbino ambao wengi wao familia zao zimewatekeleza kiasi kwamba hata shule ikifungwa watoto wanabaki shuleni. Aidha, watoto hawa wakiugua inawapa walezi wakati mgumu kuwahudumia kwa sababu hospitali iko umbali wa kama kilometa saba. Kwa ufupi naomba mtusaidie kuitazama shule hii kwa macho mawili kwa sababu pia inahudumia watoto kutoka nje ya Mafinga, kwa mfano kuna watoto kutoka Makambako (Njombe) na Rujewa (Mbeya).

Mheshimiwa Spika, shukrani kwa Shule ya Sekondari ya Nyamala kupata kibali na kupokelewa kuwa shule ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mafinga Mji ilinunua Shule ya Sekondari ya Nyamalala ambayo ilikuwa shule binafsi. Tuliwasiliana na Ofisi ya Waziri na kupata usaidizi wa haraka na ushirikiano mkubwa na kukubaliwa ombi letu la shule hii kuwa ya Serikali. Pamoja na shukrani hizi naomba kukumbusha ili iingie katika mipango ya mwaka ujao wa fedha wa 2022/2023. Nafahamu kuwa shule hizi zinasimamiwa na TAMISEMI, hata hivyo kwa yale ambayo yako chini ya Wizara ya Elimu basi naomba ikumbukwe. N5aomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Napongeza maandalizi yote ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika hotuba hii ya bajeti utekelezaji na makadirio ya mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuanza kwa nukuu ya baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyeitoa katika speech yake, ilikuwa kwenye Kiingereza ikisema the situation and challenges of education in Tanzania tarehe 22 Oktoba, 1984. Katika nukuu hii alisema; not being selected to enter form one does not imply that they have failed yaani hao wanafunzi it is result of the very few form one places which exist.

Mheshimiwa Spika, hii maana yake ni nini? Nataka nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwamba nyakati hizo tulikuwa tunakosa nafasi za kwenda kidato cha kwanza, sio sababu labda tulifeli, ni kwa sababu nafasi zilikuwa chache. Sasa napongeza Serikali kwa sababu tumejionea mwaka huu fedha tulizopata ambazo ni mkopo ambao of course tutalipa sisi wenyewe Watanzania, jinsi mgawanyo umeelekeza hadi kugusa maeneo ya elimu na hivyo watoto wetu kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu moja bila kusubiri second or third selection. Napenda kupongeza sana Serikali katika jambo hili.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kupongeza Serikali kwa shughuli ambazo zinaendelea katika majimbo mbalimbali ikiwemo Jimbo la Mafinga Mjini ambapo napongeza pia utaratibu wa kutujulisha Wabunge, hapa nina barua kutoka TAMISEMI ikinieleza kuhusu milioni 500 za ujenzi wa barabara katika Jimbo la Mafinga Mjini na kazi inayoendelea. Kwa hiyo sisi watu wa Mafinga tunaona pamoja na changamoto zingine zote, kazi iendelee tunaiona kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nijielekeze katika jambo hili ambalo hata mwaka jana nilisema. Kama Taifa, viko vitu lazima tujitosheleze ndani, nilisema kuhusu sukari, mafuta ya kula, bidhaa mbalimbali ambazo katika nyakati ngumu kama hizi ambazo zinazoendelea huko kwa wenzetu, maana yake kama tunajitosheleza hata kama ni kupanda kwa bei hakuwezi kupanda kwa bei kama unavyotegemea kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kazi ya Bunge mojawapo ni kushauri, sasa nashauri. Ukienda katika ukurasa wa 57 wa kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu anazungumza ambavyo Jeshi la Kujenga Taifa linafanya kazi nzuri ya ujenzi, kandarasi mbalimbali, nataka nishauri wakati wa amani duniani kote, wakati wa utulivu majeshi ya ulinzi kazi yake ni uzalishaji. Kwa hiyo nataka kushauri tuwape JKT hii kazi, nilikwenda na Kamati Chita nimejionea kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, tuna maeneo mengi yana rutuba, tuthubutu, for two years hatutaagiza mafuta kutoka nje, unless tutake wenyewe. Tulime alizeti za kutosha, tuwape kazi ya kutafiti mbegu zinazotakiwa, tulime ufuta, tutaondokana na kutumia mabilioni ya fedha kuagiza hizi bidhaa nje na bei kupanda. Tukifanya hivi, tutawapa wananchi wetu unafuu mkubwa sana katika Maisha. Kwa hiyo naomba na nashauri jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, ukienda pia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 80 unatoa msisitizo wa mambo muhimu katika mwaka wa fedha tunaoelekea, ni kutoa msukumo katika kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na vipaumbele hivyo vinajumuisha kuchochea uchumi shindani na shirikishi. Pia kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ninapozungumza hapa watu wa Mufindi, Mafinga, Njombe na Kilolo tuko katika hali ya taharuki baada ya kuambiwa kwamba Serikali sasa ina mpango wa kuanza kuagiza nguzo kutoka nje. Sasa sijajua kama kuagiza nguzo kutoka nje ina-reflect Mpango wetu wa Maendeleo wa Taifa kama ambavyo hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inaeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa miaka sita saba Serikali imetuamini tume-supply nguzo katika miradi ya REA, TANESCO. Hapa napenda nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa January Makamba, tulipopata taarifa hii nilimwendea na immediately akaitisha kikao baina ya wazalishaji, TANESCO na yeye, kutaka kujua ni sababu gani zinaifanya TANESCO ifikirie kuanza kuagiza nguzo kutoka nje, wakati hapa tunasema kwamba vipaumbele vya mpango wetu ni kuchochea uchumi shirikishi. Huu ni ushirikishwaji gani, nguzo tunazo unaagiza nguzo kutoka nje, ni kwa sababu gani.

Mheshimiwa Spika, katika kikao kile TANESCO wanasema kwamba ni suala la uwezo. Kwa mwaka uzalishaji wa nguzo ni zaidi ya milioni tatu, consumption ni milioni moja unawezaje kusema kwamba ni uwezo. Pili wanawema ubora, narejea hotuba ya Waziri Mkuu kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani, sasa kama ni suala la ubora uki-supply nguzo laki moja ukakuta nguzo 500 hazina ubora ni jambo la kawaida, hata viwandani soda kuna nyingine unakuta ziko flat. Kwa hiyo kama tuko serious kupunguza makali ya wananchi wetu, yako mambo ni lazima tuyasimamie kwa nia ya ile dhana tunayosema local content. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi ninapozungumza, kwa mfano, katika nguzo kuna chain kubwa ya uchumi. Yuko mtu ambaye anazalisha, ana shamba, yuko mtu anakuja kununua kwa mwenye shamba, yuko mtu atapewa kibarua cha kuangusha nguzo na kuzimenya, yuko mtu atapakia kwenye fuso, yuko mtu atasafirisha kwenda kiwandani, yuko mwenye kiwanda ata-treat atanunua dawa, yuko mwenye semi-trailer atasafirisha kwenda Mwanza, Kigoma na kadhalika. Hawa wote katika utendaji wao wa kazi pako sehemu wananunua mafuta. Wakinunua mafuta Serikali inapata fuel levy. Sasa chain yote hiyo all of a sudden tunataka tuiondoe. Je, tunaondokana na hili jambo la kujenga uchumi shirikishi na shindani?

T A A R I F A

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka tu kumtaarifu Mheshimiwa Cosato anapoendelea kuchangia kwamba katika Wilaya ya Kilolo tu peke yake kuna kiwanda cha nguzo kikubwa na kina wawekezaji wanatoka nje ya nchi, ambazo hizo hizo ndio nchi ambazo zinatarajiwa kuagizwa hizo nguzo na wanatumia mashine kama hizo hizo zilizoko kwenye hizo nchi. Kwa hiyo afahamu tu kwamba na wana nguzo za kutosha, hata hivi tunapozungumza ambazo hazijachukuliwa na Serikali. Nilitaka tu kumfahamisha hilo. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa David Cosato Chumi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hii na naongeza, Halmashauri zetu asilimia 60 ya own source zinategemea mazao ya misitu. Ninaposema mazao ya misitu ni nguzo, mirunda, mbao na mazao mengine kama plywood. Nguzo tu peke yake zina-make one third ya mapato yetu. Kwa mfano sisi Mafinga mapato ya ndani ni karibu bilioni 4.5. Maana yake unapoanza kuagiza nguzo kutoka nje unatuondolea mapato ya bilioni 1.5, ndio maana narejea hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, huku ndio kuchochea uchumi shirikishi na shindani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachotaka nikiseme, kuwajengea wananchi wetu uwezo ni pamoja na local content kuifanya kwa vitendo, lakini kinyume chake huku kama tunavyosema, bei za mafuta zinapanda, bei za sukari zinapanda, lakini tena yale mazingira machache yanayowaongezea kipato nayo tunataka tuwanyang’anye, je tutajenga uchumi shindani na shirikishi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, itoshe tu kusema kwamba jambo hili Serikali ijitafakari na iliangalie mara mbili.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Na mimi napenda kutumia nafasi hii kupongeza maandalizi ya mpango pamoja na Taarifa ya Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu, mimi ni mwanamichezo nitumie nafasi hii kuwapongeza Wananchi, jana wametuheshimisha, wamefuata nyayo na wameweza kuuthibitishia umma kwamba kumbe hata sisi ugenini tunaweza na hivyo wameenda hatua ya makundi. Nawapongeza sana. (Makofi/vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na pongezi hizi zinzendana na kama siku zote ambavyo nasema michezo ni uchumi, michezo ni biashara; kwa sababu kwa Yanga kuingia
katika makundi sambamba na Simba maana yake ni kwamba, timu hizi zinapocheza kwa mfano hapa Dar-es- Salaam tunaona watu wanafanya biashara, magari yanasafiri yanajaza mafuta tunapata fuel levy, akinamamantilie wanauza chakula, n.k. Kwa hiyo michezo ni biashara tuendelee kuwekeza katika michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuseme hayo napenda kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali, hasa kwa suala la ruzuku ya mbolea. Kwa kweli sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini tulikuwa na kilio kikubwa. Pamoja na changamoto ndogondogo ambazo wananchi wanakabiliananazo huko site lakini kwa kweli ni jambo ambalo linaenda kuinua kilimo chetu, linaenda kuongeza mapato kwa sababu, kutokana na kilimo ambacho ni takriban asilimia 60 wananchi wetu wataongeza kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa ujenzi wa barabara ya Mafinga kwenda Mgololo, Iringa kwenda Ruaha National Park na Uwanja wa Ndege wa Iringa. Hivi vyote vikikamilika kwa sisi watu wa Iringa vitaenda kusisimua sana uchumi kwa sababu utalii ukiongezeka sisi watu wa Mafinga, pamoja na kwamba, tutauza mbao na mirunda lakini pia wakulima wetu watauza mbogamboga, wakulima wa parachichi watauza matunda. Ni jambo la kupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na pongezi hizi nitoe tahadhari. Nimeona katika Taarifa ya Kamati, Ukurasa wa 34, kwamba wana mashaka na EPC+ Financing. Sasa na sisi tuliambiwa barabara ya Mafinga – Mgololo itajengwa kwa EPC+Financing kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri anapokuja ku-wind up tuweze kupata ufafanuzi kutokana nah ii hoja ya kamati, tunaendaje mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la Tanzania ya Kidijitali. Ukienda katika Ukurasa wa 14 na 15 wa Kamati, uchambuzi unasema kwamba, Kamati imebaini kwamba mapato mengi ya Halmashauri hasa yale yanayokusanywa nje ya mfumo hupotea bila kuingizwa kwenye akaunti za Serikali. Lakini pia Kamati inasema kwamba pamoja na jitihada na kazi inayofanywa na Mfuko wa Mawasiliano imebaini kuwa kuna ugumu wa kuyafikia baadhi ya maeneo kimtandao kutokana na uwezo wa kifedha au kutokana na kwamba, yale maeneo hayana vivutio vya kibiashara kwa hiyo, kampuni za kibinafsi haziwezi kujenga minara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunataka tuongeze mapato. Kwamba hoja ya kwanza, ili tudhibiti upotevu wa mapato lazima tuwe na mifumo ya kidijitali lakini at the same time hatuwezi kuwanayo kwa wakati kwa sababu, gharama za kujenga minara na hiyo miundombinu ni kubwa mfuko tu peke yake hautoshi. Kwa hiyo, kamati imesema nini? Kamati imeshauri kwamba, pawepo na vivutio maalum vya ki-kodi kwa ajili ya ujenzi wa minara na uendeshaji kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, wakati kamati inashauri hivyo nataka nikupe contradiction iliyopo. Kwa mfano kwa wenzetu nchi jirani hapa East Africa, kwa mfano Kenya ukijenga huo mkongo kwa urefu wa kilometa moja Serikali ina-charge dola 50, yaani ukipitisha katika ile road reserve au ile open space ambayo ni ya jiji, wenzetu Uganda wanatoza dola 30, Rwanda kwa sababu wanavutia zaidi wanatoza dola 0, sisi tunatoza dola 1,000 kwa kilometa moja ukitaka kujenga ile fibre.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaweza ukaona, wakati huku tunapendekeza nafuu ya kikodi kumbe sisi wenyewe bado kuna baadhi ya charges zinaweza kutusaidia kupunguza hizi gharama ambapo mwisho wa siku itasaidia kupunguza hata haya malalamiko ambayo kila siku tunamlilia Mheshimiwa Nape kwamba, “punguza bando, gharama ni kubwa.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, unapopitisha miundombinu ya maji kwa Kilometa moja, unalipa wastani wa Dola 50. Ukipitisha Sewage system Dola 50, ukipitisha wire overhead Dola mbili, ukipitisha cable Dola 50, ukipitisha miundombinu ya gesi na oil Dola 50, lakini ukipitisha fibre unatozwa Dola 1,000. Kwa hiyo, kama unataka tuwezeshe hii mifumo ili kudhibiti upotevu wa mapato na kwenda online na hii Tanzania ya kidijitali, maana yake ziko taratibu, sheria na kanuni, na ni lazima kwanza tuweze kuzipitia hata kabla hatujaanza kufanya unafuu wa kikodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuoneshe faida; kwa mfano, BRELA toka walipoenda digital, makusanyo yao mwanzoni yalikuwa Shilingi bilioni 11 kwa mwaka. Mwaka uliofuatia wakakusanya Shilingi bilioni 18, sasa hivi wanakusanya mpaka Shilingi bilioni 29. Nikufahamishe, leseni hizi za biashara za halmashauri, kimsingi vile vitabu vinatolewa na BRELA. Halmashauri A inaweza kupewa vitabu viwili, ikaenda kutengeneza vitano, ndiyo maana kunakuwa na upotevu ambao Kamati imesema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwisho wa siku ni lazima tuiwezeshe Serikali na Wizara ya Mheshimiwa Nape ili kusudi huu mkongo wa Taifa ujengwe hata kwenye maeneo ambayo hayana vivutio kibiashara, tuweze kuwa na miundombinu ambayo itatuwezesha kukusanya mapato kwa njia ya kidijitali ili hayo mapato yatusaidie kujenga miundombinu ya elimu, madarasa, vituo vya afya na gharama nyingine kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baada ya kusema hayo naona kengele imelia, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza kwa maandalizi ya hotuba nzuri ambayo imegusa maeneo mengi ya maisha ya wananchi. Nina ushauri/mchango katika baadhi ya masuala kama ifuatavyo: -

Kwanza, ujuzi kazi ukurasa wa 62-63; kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Elimu, katika nchi yetu asilimia 79.9 ya nguvu kazi yetu ni low skilled labour ambao majority ni wale waliomaliza darasa la saba. Asilimia 16.6 ni middle skilled labour wakati asilimia 3.6 ni high skilled.

Hata hivyo kazi kubwa ya shughuli za uzalishaji zinafanywa na hawa asilimia 79.9 ambao tukiwapa ujuzi kazi kama ambavyo inafanyika kupitia ile programu ya kukuza ujuzi tutakuwa tumewasaidia na tumelisaidia Taifa. Nafahamu juu ya ile national skills development through green house ambayo inajielekeza zaidi kwenye ujuzi kazi wa kilimo.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu tupanue wigo wa mafunzo na hapa nawasilisha ombi mahususi kwa ajili ya mafunzo ya ujuzi kazi kwa vijana wa maeneo ya Kilolo, Mafinga, Mufindi na Njombe ambako uchumi wetu unategemea sana mazao ya misitu. Vijana wetu katika maeneo hayo wakipata mafunzo ya ujuzi kazi katika suala la kuongeza thamani katika mazao ya misitu wanaweza kupata ajira rasmi katika viwanda na hivyo wakawa na mchango kupitia PAYE/SDL, lakini pia wanaweza kujiajiri wakajijengea uwezo hata wa kuajiri wenzao.

Mheshimiwa Spika, mafunzo haya yanaweza kufanywa kwa kushirikiana na TFS na asasi za kijamii kwa maana ya NGOs zinazojishughulisha na masuala ya misitu kama vile Panda Miti Kibiashara na Forestry Development Trust of Tanzania. Aidha, kupitia mifuko mbalimbali ya uwezeshaji kwa vijana, tunaweza kuwasaidia vijana hao kwa kuwapa mikopo ya vitendea kazi ili kusaidia ushiriki wao katika uchumi wa mazao ya misitu kwa kuongeza thamani. Kwa mfano hivi sasa zaidi ya asilimia 60 ya mti unapotea kama waste, lakini wakipata ujuzi kazi na vitendea kazi tunaweza kuhakikisha kuwa recovery rate kwa kila mti inapanda kutoka asilimia 40 ya sasa hadi asilimia 90 kwa sababu katika mti ukiacha mbao kuna bidhaa nyingine kama MDF, Plywood na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nimeona benki za CRDB na NMB zimetenga fedha kwa ajili ya kilimo kwa mikopo ya riba kati ya asilimia tisa hadi kumi mikopo ambayo tungeweza pia kuelekeza katika sekta ya mazao ya misitu.

Pili ni kuhusu kushirikisha JKT katika uzalishaji wa bidhaa muhimu kama mafuta ya kula na sukari. Wakati wa usalama ni vema vyombo vyetu vikawezeshwa ili kushiriki katika shughuli za uzalishaji. Ninaamini mabilioni tunayotumia kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi tunaweza kuepuka na kujitosheleza kwa chakula ikiwa tu tutawezesha JKT na Magereza kuzalisha alizeti na ufuta kwa ajili ya viwanda vya ndani. Tukiwa wakweli wa nafsi ni aibu kama Taifa kushindwa kujitosheleza kwa mafuta ya kula wakati ardhi yenye rutaba tunayo bali ni suala la kuamua tu, tunahitaji political will katika suala hili, kama ambavyo tumewashirikisha JKT katika miradi ya ujenzi na tukiwakabidhi jukumu hili ndani ya muda mfupi tutakuwa tumejikwamua na tunaweza kuuza nje na pia kukabiliana na kilio cha kupanda bei kiasi ambacho we have less control na yawezekana ni mchezo wa waagizaji. Naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kusimamia masuala ya kazi sehemu za kazi kama vile masuala ya OSHA na kadhalika, ninaamini Ofisi ya Waziri ni kichocheo cha uongezekaji wa ajira.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni TANESCO wanasema wataanza kuagiza nguzo za umeme kutoka nje ya nchi, suala hili litaathiri sana ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Sekta ya mazao ya misitu ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Mazao ya Misitu mwezi Novemba 2021 ni sekta ambayo imeajiri watu wengi vijana kwa wanawake.

Kwa hiyo, hatua ya kuamua kuagiza nguzo za umeme nje ya nchi itaathiri ajira za vijana na wanawake wa mikoa ya Njombe na Iringa na maeneo mengine ya nchi, kuna mnyororo mkubwa wa ajira na kipato, kuna wenye mashamba ya nguzo ambao ni wananchi lakini pia kuna Shamba la Serikali la Sao Hill ambalo ndio muuzaji mkubwa wa nguzo. Suala hili litaathiri kipato cha wafuatao; wenye mashamba ambao ni wananchi, Wakala wa Misitu (TFS) ambao wanamiliki Shamba la Serikali la Sao Hill, wakataji na wanaomenya nguzo, wanaopakia kwenye malori madogo, wanaosafirisha nguzo kutoka mashambani kufikisha kwa wenye viwanda, walioajiriwa na wenye viwanda, Halmashauri kwa sababu asilimia 30 ya mapato yetu ya own source ni kutokana na nguzo na pia Serikali kwa sababu katika shughuli za nguzo kuna sekta ya usafirishaji ambapo Serikali inapata fedha kupitia fuel levy.

Mheshimiwa Spika, ushauri; hoja za TANESCO/Serikali kwamba wazalishaji hawana uwezo sio sahihi kwa sababu kutoka viwanda vitano sasa kuna viwanda 18 ambapo uzalishaji kwa mwaka ni mpaka nguzo milioni tatu wakati uhitaji kwa mwaka ni wastani wa nguzo milioni moja, maana yake kuna ziada ya nguzo milioni mbili.

Suala la ubora, sio kweli kwa sababu kuna mfumo wa kupima ubora wa kwanza ukiwa ni moisture content ambapo haipaswi izidi asilimia 25 lakini pia suala la treatment, viwanda vina mitambo ya kisasa ambayo hata Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembela moja ya viwanda hivyo cha Sao Hill Industries.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo na kama kweli tuko serious na uchumi wa viwanda, nashauri Serikali iondokane na wazo la kuagiza nje ya nchi nguzo za umeme, nimetaja hapo juu mnyororo wa mapato ya sekta hii, kama Taifa kuanza kuagiza nguzo nje sio tu tunarudi nyuma bali pia tunaathiri suala zima la kazi na ajira. Katika hotuba ya Waziri Mkuu mmezungumzia ujuzi kazi kama kuna mapungufu ndio maana nmeshauri kuwa pamoja na vitalu shamba kwa maana ya ujuzi kazi katika kilimo, Serikali itusaidie kuwa na programu maalum ya mafunzo ya ujuzi kazi kwa ajili ya sekta ya mazao ya misitu. Naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nami napongeza Kamati zote mbili, nami ni Mjumbe wa Kamati ya NUU. Hili ninalolisema mara zote nimelisema na sitaacha kulisema kwamba, Mheshimiwa Rais, kama mwanadiplomasia namba moja, ameendelea kuitendea haki nafasi yake, ameendelea kufanya ziara, ameendelea kutafuta wawekezaji, ameendelea kufanya shughuli zote ambazo zinathibitisha kwamba Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ni mwanadiplomasia namba moja katika Taifa letu. Hizi shughuli anazozifanya zitakuwa na thamani na manufaa kwa Taifa letu kama kutakuwa na connection na kama kutakuwa na link kati ya shughuli ambazo zinaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara nyingine za kisekta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa yetu, mojawapo ya jambo ambalo limejitokeza ni kukosekana kwa mkakati maalum wa kiushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje katika kutekeleza diplomasia ya uchumi na Wizara nyingine za kisekta. Ni kweli kwamba ushirikiano upo, lakini tunachokitaka ni ushirikiano wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitatoa mfano. Kwa takribani miaka minne, na bahati nzuri Waziri wa Kilimo yuko hapa; Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa ikiratibu vijana takribani 100 kwenda nchini Israel kujifunza masuala ya kilimo kwa muda wa miezi 11. Hapa ninalo tangazo la 2019 ambalo limeandikwa, “Tangazo la Mafunzo ya Kilimo Nchini Israel.” Tangazo hili linaalika vijana waliomaliza SUA waende Israel wakajifunze kilimo kwa muda wa miezi 11. Sasa wakisharudi wale vijana ni wa nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale vijana sio tena wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Wale ni vijana wa Kilimo; lakini mpaka hapa tunavyozungumza sijui kama Wizara hata ina takwimu vijana hawa ni wangapi in total na wako wapi? As far as I know, majority wamerudi. Sana sana the best they can do, wanajiajiri katika biashara ya boda boda. Sasa tumewapeleka vijana miezi 11 wamejifunza very advanced skills za mambo ya kilimo, lakini kwa sababu hakuna mkakati mahususi wa kuonesha hiyo link, Wizara ya Mambo ya Nje imeshatimiza wajibu wao, lakini wale ambao wangepaswa kuwalea wanakuwa hawajatimiza lile ambalo lingekuwa ni endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri. Katika maazimio ya Kamati ya Bajeti, maoni na mapendekezo mahususi, ukurasa wa 68, imeeleza ya kwamba, katika huu mpango ambao Mheshimiwa Bashe anakujanao wa block farming Serikali ianze na vijana wa JKT. Naomba kulishawishi Bunge lako, kama sehemu ya hayo maazimio ambayo kwa namna moja au nyingine yatakuja kulisaidia Taifa letu kukabiliana na mfumuko wa bei, hususan katika kipengele cha mafuta ya kula. Katika bajeti iliyopita, katika Muswada wa fedha, tulisema hapa tumetoa ahueni kwa waagizaji wa mafuta, lakini tuwe honest katika nafsi zetu, je, mafuta ya kula yamepungua bei kutokana na hilo punguzo ambalo tumewapa waingizaji wa mafuta? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli tukiwa wakweli wa nafsi, hakuna punguzo ambalo linamfikia mlaji, isipokuwa ni manufaa wanayojinufaisha wafanyabiashara wakubwa wanaoagiza mafuta hayo. Kwa sababu hiyo, nashawishi Bunge lako, tuongeze azimio kwamba, katika hii hoja mahususi ambayo wenzetu wa bajeti wamesema, tuseme kwamba, Bunge liazimie tuwape kazi na nyenzo wenzetu wa JKT na SUMA-JKT ya kuhakikisha kwamba Taifa hili ndani ya miaka miwili, litajitosheleza kwa mafuta ya kula na litaweza kusafirisha mafuta ya kula kwenda nje. That is the only way ya kuhakikisha tunakabilana na mfumuko wa bei katika baadhi ya vitu ambavyo tunaweza tukazalisha hapa nchini. Vinginevyo tutabaki na taarifa za UVICO, na taarifa za vita ya Ukraine na Urusi. Lazima tuje na mikakati, tubuni namna ambayo tutaondokana na shida hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tumesema kwamba, lazima tu-link. Kuna hawa vijana wa JKT, hawa waliotoka Israel wangeweza kuwa ndio wasaidizi wao katika hiyo block farming. Katika ku-link, nakushukuru wewe unatoka Mufindi, sisi tunazalisha mazao ya kilimo. Katika diplomasia ya uchumi tunasema kwamba, pawepo na mkakati kwamba hii elimu ifike mpaka kule chini. Sisi watu wetu wa Mafinga, Mufindi, Iringa, Kilolo na Njombe waweze ku-access masoko ya mbao, milunda na mazao ya misitu kwenye soko la Congo. Waweze ku-access soko la nafaka kwenye soko la Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri bashe shahidi, wale Bodi ya Mazao Mchanganyiko walipeleka kule mazao yamekaa miezi mitatu yanashindwa kuingia kwa sababu tu kumekosa link kuwashirikisha watu wa mambo ya nje kushirikiana na Kilimo na Viwanda na Biashara kujua je, soko la Congo limekaaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe soko la Congo kule Lubumbashi ni lazima ushirikiane na wale tycoon ujue wanapita njia gani ndio uweze ku access lile soko, sasa kama hakuna hiyo link tutabaki tu tunalaumiana, hivyo itoshe tu kusema kwamba tunahitaji kuwa na link kati ya diplomasia yetu ya uchumi, uzalishaji wetu na Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze umetusomea hapo tangazo, nimeona kutakuwa na Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo itakuwa ni mojawapo ya link nzuri sana kwa sababu bila viwanda, bila mazao huwezi kuwa na Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhitimisho niende kwenye suala la NIDA kwa haraka sana, pamoja na maazimio ya jumla. Katika suala la NIDA kwenye taarifa yetu tumesema ya kwamba NIDA inafanya kazi nzuri so far inafanya kazi nzuri, lakini wananchi wanataka vitambulisho. Mpaka hapa tunapozungumza NIDA wanafanya kazi mbili utambuzi, usajili na kutoa vitambulisho. Mpaka sasa wameshatambua wananchi takribani milioni 23 kati ya wananchi milioni 34 mpaka kufikia 2025/2026 wanaenda vizuri kwa sababu ni asilimia 68.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hao waliotambuliwa ambao ni milioni 23 ni milioni 19 sawa na asilimia 84 tayari wana ile namba ya NIDA, lakini wenye vitambulisho ni milioni 10 tu sawa na asilimia 56. Maana yake kila watu 100, 56 wana kitambulisho cha NIDA 44 hawana kitambulisho cha NIDA. Kwa hiyo, pale Serikali inayo wajibu wa kuisaidia NIDA kama ni Fedha au namna nyingine isaidie ili mwananchi apate kitambulisho, kwa sababu baadhi ya huduma zinataka siyo uwe na namba bali uwe na kitambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maazimio ya jumla naomba kuhitimisha ipasavyo tuzisaidie Wizara hizi za Fedha, kwa sababu tumeona utekelezaji wa maazimio na tumesema kwamba Bunge linapoazimia siyo Mheshimiwa Chumi au Siyo Mwenyekiti wala siyo Mheshimiwa Vita Kawawa, sisi tunaazimia kwa niaba ya Wananchi. Kwa hiyo, matarajio yetu ni kwamba yale tunayoyaazimia ni kutatua changamoto na kero za wananchi, sasa yasipotekelezwa maazimio, maana yake ni kwamba hatujatatua na kupunguza kero za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu na ushauri wangu kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha pamoja na changamoto za kibajeti tuhakikishe kwamba yale tunayoazimia ambayo yanahitaji fedha kuyatekeleza basi wenzetu wapewe fedha. Kwa kuhitimisha Wizara ya Mambo ya Nje tu kwa mfano, kwa miaka mitano walitakiwa wapewe bilioni 48 za kuweza kujenga majengo na kuyaboresha ambayo majengo haya tungeweza kuyapangisha yangetupa mapato lakini mpaka ninavyozungumza ndani ya miaka mitano wamepewa tu bajeti ambayo haizidi asilimia 19. Kwa hiyo, katika kutekeleza maazimio ambayo yanahitaji fedha wenzetu wa fedha wajitahidi kutoa fedha ili tutekeleze, tupunguze kero za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja zote, Mungu atubariki wote, abariki wananchi wa Mafinga na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza sana kwa mchanganuo mzuri wa bajeti unajieleza kwa kila sekta. Pia napenda kuwapongeza viongozi wote, Waheshimiwa Mawaziri wote kuanzia Waziri Bashungwa, Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dkt. Dugange nawapongeza hasa kwa prompt action kila ambapo kuna suala la kushughulikia. Ninawiwa pia kuwapongeza Watendaji Wakuu na wa chini, wako very cooperative. Kwa kweli katika hali ya kawaida huwezi kutarajia Katibu Mkuu au Naibu Katibu Mkuu umuandikie message na akujibu, lakini kwa hakika kuanzia Profesa Shemdoe, Dkt. Grace, Dkt. Mkama na Ndugu Gerald Mweli na Mzee Cheyo kwa kweli binafsi ninapata ushirikiano mkubwa sana. Nimewiwa kuwapongeza na muendelee hivyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 mlitoa maelekezo kwa LGAs zote kuwa na mradi mmoja wa kimkakati, kwa mfano Mafinga tunaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya Ifingo, ni jambo jema ambalo linawafanya wananchi kunufaika na own source. Nashauri pamoja na kuwa tunaanzia mipango katika vikao vyetu vya Kamaka, Kamati ya Fedha hadi Baraza la Madiwani, nimebaini kuwa kama Wizara iki-set lengo LGAs zinabanwa kutekeleza, kwa mwendo huu kila baada ya miaka mitano ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo unapokamilika tutakuwa na miradi ambayo sio tu ina tija kwa wananchi lakini ambayo inaonekana kwa macho ya kawaida. Kwa sababu hiyo, nashauri na mwaka huu wa fedha Wizara itoe maelekezo mahsusi kwa kila LGAs zenye mapato ya kiwango fulani kutekeleza mradi mmoja wa kimkakati usiopungua shilingi milioni 400.

Kuhusu wamachinga, imekuwepo dhana kwamba ni maeneo ya Majiji na Manispaa tu ndizo zina changamoto ya wamachinga, kumbe hata TCs kama Mafinga TC au Makambako TC au Korogwe TC na kadhalika. Nimeona katika mipango ya Serikali kiasi fulani cha fedha kitapelekwa katika baadhi ya Majiji kama Dodoma kwa ajili ya miundombinu ya wamachinga, nashauri fedha hizi hata kwa kiwango kidogo, LGAs ambazo ni Town Council pia ziweze kutazamwa. Kwa mfano Mafinga TC ni Mji ambao upo kando ya highway ya Dar - Malawi/Zambia mpaka South Africa, ni mji wa kibiashara kutokana pia na sekta ya mazao ya misitu, hivyo changamoto ya miundombinu ya wamachinga ni kubwa hivyo ni muhimu kupewa fedha kwa ajili ya jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TARURA/Tactic; kwanza napongeza utararibu ambao ni shirikishi, hususani kutujulisha fedha za ujenzi wa barabara, lakini pia semina ya Wabunge kuhusu ambavyo TARURA imejipanga kuanza kutangaza zabuni mapema kusudi miradi kuanza kabla mvua hazijaanza. Pili napongeza watendaji wa TARURA kuanzia CEO wao Engineer Seif na watendaji wake mkoani Iringa na Mufindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,ushauri wangu na maombi; wakati tunapewa fedha za barabara, Mafinga tumepata bilioni moja kwa sababu ya maelezo kuwa tupo kwenye Mradi wa Tactic, ninavyoona mradi huu wa Tactic utatekelezwa kwa awamu na kwamba sasa katika miji 12 tayari wataalam wameshaenda kufanya kazi za awali, ninaomba na kushauri kwanza wakati ambao bado mradi wa TACTIC haujaanza tutengewe fedha kama maeneo mengine ambako walipata shilingi bilioni 1.5; pili, nashauri kama ambavyo Serikali ilijenga heshima na kuchochea ukuaji wa shughuli za uzalishaji katika mradi wa TSCP, mradi huu wa Tactic ni vema ukianza kwa pamoja kwa sababu kwa maelezo utatekelezwa kwa awamu, tukianza pamoja tutaokoa baadhi ya gharama hasa kwa sababu gharama ya vifaa vya ujenzi zinapanda kila kukicha, mradi utakaotekelezwa mwaka 2022 gharama zake sio sawa na wale ambao tutaanza miaka ijayo na tatu, Dromas nashauri TARURA watusaidie kuharakisha mchakato wa kuingiza barabara katika mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Mafinga mimi binafsi kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa/ Vijiji, Madiwani na TARURA tulitembea jimbo zima kubaini barabara ambazo zinapaswa kufunguliwa na ambazo zinapaswa kuingia katika mfumo. Ilikuwa ni kazi ngumu ya wiki mbili, baadhi ya maeneo tuliwashirikisha mpaka Mabalozi. Naomba kwa msisitizo mtusaidie barabara za Mafinga ziingie katika Dromas, na hii itasaidia sana kuendana na zoezi zima la anuani za makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uharaka katika maombi ya kubadilisha matumizi ya fedha; ninashauri, Halmashauri tukiwasilisha maombi ya kubadilisha matumizi ya fedha basi tupate mrejesho kwa wakati. Ninao mfano hai, Mafinga TC kwa mujibu wa utaratibu tuliwasilisha maombi ya kubadilisha matumizi ya fedha kwa kuandika kwa RAS na baadae RAS akawasilisha Wizarani, lakini imetuchukua miezi almost sita maana kutoka Septemba mpaka Machi na hii baada ya mimi Mbunge kuanza kufuatilia in personal kwa sababu Madiwani katika vikao walianza kuhoji na kuniomba nifuatilie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, alimradi taxation zote na sababu za kubadilisha matumizi tunakuwa tumekidhi basi tujibiwe kwa wakati na kama kuna maelekezo tofauti basi pia tujulishwe. Nadhani katika jambo hili hakuna ambaye sikumtafuta kuanzia Mheshimiwa Waziri mpaka Mzee Cheyo na ndio maana pale mwanzo nimewapongeza kwa sababu wote walikuwa wana-respond kwa haraka mpaka likafanikiwa, lakini it took too long.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa kukamilisha mpango kabambe wa hifadhi ya mazingira kama ilivyojionesha katika ukurasa wa 36 wa hotuba ya bajeti. Pamoja na pongezi hizi ninaomba kutoa ushauri kama ifuatavyo: -

Kwanza ni kuhusu kukijanisha Dodoma; ninashauri kushirikisha vyuo vya elimu ya juu na kati katika kukijanisha Dodoma. Kwa mfano, tunaweza kusema kila wanafunzi wawili wapande mti na kuulea katika muda wote wa masomo. Tuna vyuo kama vile UDOM, St. John, Mipango-IRDP, CBE, Hombolo na baadhi ya vyuo binafsi kama vile DECA. Ikiwa wanafunzi wanakaa almost miezi tisa katika mwaka, ninaamini wakipewa mche na kukawa ni sehemu kwa mfano ya kigezo cha kupata mkopo, tunaweza kusaidia kukijanisha maeneo ya vyuo na maeneo yanayozunguka.

Pili, COP26 na namna ya kunufaika na fedha za mifuko ya GCF, GEF, Adaptation Fund n a kadhalika, nilifuatilia mkutano wa Glasgow, niliona ambavyo Mheshimiwa Rais alivyoyasihi mataifa makubwa kuheshimu pledge zao katika kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi. Tumeona CRDB wamepata fedha kwa mfumo huu.

Mheshimiwa Spika, nashauri tuzisaidie taasisi nyingi zaidi kama vile vyuo vikuu, NGOs na kadhalika ziweze kupata fedha hizi ambazo nyingi ni grants. Ukifuatilia kwa ukaribu utafahamu kwamba ili ku-access hizi funds kuna vigezo kama vile kupata accreditation. Nchi kama Kenya, Rwanda na Morocco wamekuwa wanufaika wa hizi funds na zimesaidia katika miradi ambayo inasaidia kuinua maisha ya wananchi wa kawaida. Kwa mfano kama ilivyo katika mikoa ya Iringa na Njombe ninaamini funds hizi zingeweza kuhamasisha zaidi suala la kupanda miti katika mikoa mingine kadri ya species ambazo zitafaa.

Mheshimiwa Spika, tatu ni kuhusu hewa ukaa/carbon credit; wananchi wengi wa Mafinga/Mufindi wamekuwa wakiomba kupata elimu kuhusu suala hili. Tunawashukuru sana Wakala wa Misitu Tanzania-TFS ambao waliwezesha ziara ya mafunzo kwa Madiwani wa Mafinga na Mufindi kutembelea Wilaya ya Tanganyika kuhusu manufaa ya hewa ukaa.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mufindi ama kwa kutojua au kwa shida zao waliuza maeneo yao kwa makampuni makubwa kama vile green resources ambapo kuna maelezo yasiyo rasmi kwamba waliahidiwa kwamba waachie maeneo yao na kwamba watanufaika na malipo ya hewa ukaa. Kwa sababu suala hili naweza kusema ni complicated, nashauri itolewe elimu kwa kuanza na semina kwa Wabunge na baadae kwa Wenyeviti wa Halmashauri na wadau wengine kadri mtakavyoona inafaa ili tuweze kufahamu ni vigezo gani vinapaswa kuzingatiwa ili taasisi au mwananchi apate kunufaika na masuala ya hewa ukaa. Kwa mfano ilivyo sasa, wananchi wa Mufindi na maeneo ya Morogoro kama vile Uchindile wanadai kuwa fedha za hewa ukaa zinatolewa, lakini wanufaika ni makampuni makubwa yaliyopanda miti katika ardhi ya vijiji.

Mheshimiwa Spika, nne ni kuhusu kupanda miti milioni 1.5 kwa kila Halmashauri; kama nilivyoshauri katika kukijakinisha Dodoma, nashauri ushiriki wa shule za msingi, sekondari na vyuo, sio katika kupanda tu bali katika kuitunza miti. Kwa sababu hakika tumekuwa tunapanda miti kila mwaka lakini inayo-survive ni michache mno.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza kuwapongeza kwa mtiririko na mpangilio mzuri wa hotuba ya bajeti hasa katika viambatisho vinavyoonesha miradi iliyokamilika, inayotekelezwa na ile ambayo itatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, aidha nawashukuru kwamba baada ya mkandarasi wa kwanza wa kuchimba visima katika Vijiji vya Itimbo na Matanana kutokomea, leo kwa maelekezo ya juzi ya Waziri Mheshimiwa Aweso na Katibu Mkuu Engineer Sanga, magari ya kuchimba visima yamewasili leo tarehe 12 Mei, 2022 katika Kijiji cha Matanana na baadae wataenda Itimbo.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha maombi kwenu, kwamba baada ya kuchimba na kwa kurejea mazungumzo yetu kwamba Mafinga as of now ukiacha mradi wa UVIKO katika Kijiji cha Ulole, hakuna mradi ambao unatekelezwa au umetekelezwa. Utakumbuka hata Mradi wa Vijiji vya Ugute na Ulete wanasema vilikuwa vimesahaulika, mmetumia neno oversight. Kwa sababu hiyo, naomba mtusaidie baada ya kuchimba visima hivi vya Matanana na Itimbo, design ifuatie ili tukamilishe katika mwaka wa fedha 2022/2023. Kwa kifupi ninaomba mradi au mwendelezo uingie katika bajeti hii tunayoipitisha sasa. Mkitusaidia maana yake tutakuwa tumemaliza vijiji hivi kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, suala la pili; baada ya mazungumzo yetu katika Kikao (Mheshimiwa Aweso, Mheshimiwa Chumi, Katibu Mkuu - Engineer Sanga, Ndugu Bwire na RM Joyce), nilifahamishwa kwamba kwa kuwa kulikuwa na oversight Wizara iko katika hatua mwisho kutangaza na jana nashukuru sana kupitia Ndugu Bwire nimefahamishwa kuwa tangazo la tender tayari. Hata hivyo, katika kitabu chenu vijiji hivi viwili vya Ugute na Ulete havipo, ninapata shaka kuwa isije ikafika wakati wa utekelezaji ikaonekana vijiji havipo katika kitabu cha bajeti, hivyo nashauri izingatiwe ili vijiji hivi ambavyo kimsingi ni mwendelezo wa miradi ya mwaka huu wa fedha wa 2021/ 2022 viweze kuwa reflected kwenye kitabu cha bajeti ya mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, ombi la gari; nafahamu kwamba kuna uhaba mkubwa wa magari, hata hivyo ninaomba kwa jicho la kipekee, mtusaidie kupata gari la uhakika ambalo litaweza kusaidia RUWASA na MAUWASA, kwa sasa gari la RUWASA Mufindi ni kuukuu na MAUWASA hakuna gari kabisa. Kwa kasi ya ukuaji wa Mji wa Mafinga ikiwa ni pamoja na viwanda vya mazao ya misitu na vijiji vinavyozunguka, upo umuhimu mkubwa sana kutusaidia kupata gari.

Mheshimiwa Spika, mwisho, kwa dhati ya moyo wangu nawapongeza sana kwa namna ambavyo miradi inafuatiliwa kwa ukaribu na ushirikishwaji sisi Wabunge, walau sasa miradi inafanyika kwa speed, naamini hata Mradi wa Miji 28 utatekelezwa kwa speed na ufanisi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi; na napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maandalizi ya Bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitazungumza mambo mengi, mimi najielekeza kwenye jambo moja tu, ambalo linagusa viwanda pamoja na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Neema na mimi kwa miaka kadhaa sasa nimekuwa nikishauri kuhusiana na suala la sukari; na wakati wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu nilisema kuhusiana na mafuta ya kula; na juzi Mheshimiwa Injinia Ezra amesema, Mheshimiwa Kingu na Wabunge wengine wamesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama taifa lazima tufike mahali kuna mambo tuyakatae, na kama Bunge lazima mahali tufike kuna mambo tuyakatae. Sasa tunayakataa mambo gani? Na tunayakataaje? Kati ya mambo ambayo tunatakiwa tuyakatae moja wapo ni hili la kuagiza bidhaa kutoka nje ambazo tunaweza kama taifa kuzalisha hapa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tukawa tunaagiza mafuta ya kula, tunaagiza ngano, tunaagiza sukari. Mjumbe mmoja alisema hapa. Kwa mfano tunategemea mafuta ya kula kutoka Malaysia kwa asilimia kubwa, what if siku ikitokezea soko kubwa liko Marekani wakaelekeza mafuta yao yote kwenda Marekani, na sisi tutafanya nini kama taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yako mambo lazima kama taifa tuyakatae, kwa sababu haiwezekani kama Taifa sisi ni kuagiza tu, ni kuagiza tu, ni kuagiza tu vitu ambavyo tunaweza kuzalisha hapa nchini. Hii mifumuko ya bei, ugumu wa maisha tunaosema ni kwa sababu pia takriban kila kitu tunaagiza. Yaani ukiangalia sisi kama taifa kitu ambacho ambacho hatuagizi ni hewa tu ya Mwenyezi Mungu ambayo ametugaia lakini a lot of things sisi ni kuagiza! ni kuagiza! ni kuagiza!. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashauri jambo hili tulikatae kama taifa. Tutakataaje? Mwaka 2019 tarehe 15 mimi baada ya kuchangia, pamoja na mchango wangu wa maandishi niliandika barua kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Kilimo, Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Fedha. Niliandika barua kuwaambia namna ambavyo kama taifa tunaweza tukaondokana na shida ya kuagiza sukari kila mwaka. sasa kwa nini niliandika barua hiyo kwa Mawaziri hawa? Ni kwa sababu sukari ni biashara lakini ni viwanda; lakini kabla hujapata sukari lazima mtu wa kilimo awe amehusika katika kulima miwa.

Pia ili aweze kulima miwa lazima Waziri wa Fedha kwa namna moja ahusike katika masaula mazima ya financing. Yuko Waziri mmoja sitamtaja alinijibu na haikuwa lazima ile barua wanijibu, hapana, ulikuwa ni ushauri tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama taifa, wenzetu Brazili na India wamefanikiwaje katika sukari? Wametumia small scale industries. Kwamba unakuwa na maeneo ambayo yako suitable kulima miwa, lakini pia gharama zake si kubwa katika kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nashauri tuwekeze kwenye small and medium scale sugar plantations? Kwanza kiwanda hakihitaji eneo kubwa, kina hitaji kama heka tano tu, na pia unahitaji kama heka 3,000 za kuzalisha miwa. Lakini pia ukishazalisha miwa hiyo heka 3,000 ambayo niliwaandikia watu wa Kilimo na TAMISEMI; unaweza kushirikiana na Halmashauri za maeneo husika zenyewe zikatoa ardhi, Wizara ya Fedha wana-finance kupitia hata Benki ya Kilimo na uwekezaji wake hauzidi dola kati ya milioni 3.5 hadi milioni 5. Maana yake hapo unazungumzia bilioni nane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hata ukiwa na wale wakulima wa nje (out growers) inakuwa ni rahisi kuwapa extension services. Lakini pia ukijenga viwanda hivi vidogo vidogo hata gharama za usafirishaji wa miwa kutoka shamba kwenda kwenye hiyo factory hauwi mkubwa kama ilivyo sasa. Tunazungumza mradi wa Mkulazi, huu nadhani ni mwaka wa sita. Mradi wa Dola milioni 150 lakini sisi hapa tukiwa na Dola milioni 100 kwa miaka miwili hatutaagiza sukari nje na tutauza sukari nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yapo. Kuna Manyara, Mfilisi, Kibelege Ifakara, Luembe, Wami, Kasulu na Lufiji. Kwa sababu nchi yetu imejaliwa hali tofauti tofauti. Kwa hiyo, mimi nashauri sana Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ikae kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Mheshimiwa Rais ameunda kikosi kazi chini ya Profesa Mkandala kwa ajili ya kuzungumza na kujadili namna gani mustakabali wa kuendesha siasa zetu katika hali iliyo njema na bora. Mheshimiwa Waziri…

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kumpa mchangiaji kaka yangu Mheshimiwa Cosato Chumi kwamba mikakati ya kuwekeza katika viwanda vya TCD ndogo vyenye uwezo wa kuzalisha kuanzia tani 100 na kuendelea aliyekuwa Mkurugenzi wa NSSF wakati huo ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Uwekezaji na Viwanda alishakuja na mipango mikakati kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo lakini mipango hiyo masikini ya Mungu sijui imepotelea wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa taarifa hii anachokisema Mheshimiwa Cosato Chumi tunauwezo wa kujenga viwanda vya TCD ndogo ndogo tukaeupukana na uagizaji wa sukari na kuliokoa Taifa letu katika kutumia fedha za kigeni kwa ajili ya uagizaji wa sukari. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Cosato Chumi, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa na Mheshimiwa Kingu ninaamini ni miongoni mwa walionielewa ninacho kimaanisha. Naamini ataungana na mimi ninaposema kama taifa kuna mambo tukatae. Kwa muundo huo wa kuwa na viwanda vidogo vidogo ambavyo tunaweza kushirikisha, kama nilivyosema, Halmashauri zikatoa ardhi, Benki ya Kilimo ikatoa mitaji, Wizara ya Kilimo ikasaidia katika namna ya kuhakikisha kwamba tunakuza hiyo miwa. Mimi ndugu zangu nimekaa Kilombero, miwa ukipanda ni miezi 12 unaanza kuvuna na baada ya hapo kila baada ya miezi sita utavuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaposema tukatae ndiyo mambo kama haya kwamba anasema hapa Mheshimiwa Kingu. Bahati nzuri Profesa mko nae huko sasa aliyekuwa NSSF ndiye Katibu Mkuu; na ndiyo maana nasema Mheshimiwa Waziri pamoja na ile timu yako unaweza ukawa na kitu kinaitwa kitchen cabinet...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia muda wangu kidogo. Kitchen cabinet ni nini?

MWENYEKITI: Malizia kidogo.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na timu yako unaweza ukawa na timu ya wataalam kutoka SUA. Kama tumeunda kikosi kazi kwa ajili ya mambo ya siasa, kwa nini tusiunde kikosi kazi kwa ajili ya mambo ya uchumi? Ili tukatae mambo ya kuagiza, ukachukua wataalam kutoka SUA, ukachukua wataalam kutoka UDSM pale, kutoka Mzumbe, kutoka hapa Chuo cha Mipango wakasaidia nao kama kitchen cabinet. Simaanishi kwamba wataalam ulionao hawana uwezo, hapana, ili wakushauri ipasavyo ili kusudi dhana ya kwamba tukatae, tukatae, tukatae baadhi ya mambo iweze kuthibitika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nakushukuru. Nilisema siku moja, katika baadhi ya maeneo along the high way naomba Serikai itusaidie. Watu kama wa Mafinga, Mikumi, Makambako, Mombo – Korogwe na kwingineko turuhusiwe kufanya biashara masaa 24. Tujiongezee kipato na Halmshauri zipate kipato, kwa sababu sheria as it is now mwisho kufanya biashara ni saa nne. Lakini hata dunia zingine watu wanafanya shughuli saa 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono na Mungu atubariki. Mungu abairiki taifa letu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nawapongeza sana kwa kazi nzuri, hii inathibitisha kuwa mnafanya kazi kama timu.

Mheshimiwa Spika, nina ushauri na mawazo machache; kwanza ni kuhusu udhibiti wa Malaria; nafahamu kuhusu Kiwanda cha Kibaha ambacho ni ubia kati ya Serikali yetu na Serikali ya Cuba, nafahamu kiwanda hiki ni muhimu sana, ikiwa tutaamua kwa dhati kutumia dawa inayozalishwa ili kutokomeza mazalia ya mbu, tutapiga hatua kubwa.

Mheshimiwa Spika, ushauri, jipeni muda kujua uhalisia na mwenendo wa Kiwanda hiki, nani anakisimamia na kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu damu salama, napongeza hatua ya Wizara kugawa mifuko ya kukusanyia damu kwa Halmashauri zote, hata hivyo nashauri suala la hamasa ya wananchi kuchangia damu iongezeke, kwa namna gani. Nashauri namna bora ni kutoa kits kama point ambazo hizo zinaweza kumpa unafuu katika kupata huduma mbalimbali, kwa mfano tunaweza kusema kuwa wanafunzi wakiomba mkopo wa elimu ya juu, ambaye amewahi kuchangia damu anakuwa na better chance ya kupata mkopo kwa asilimia fulani zaidi kuliko mwingine.

Mheshimiwa Spika, nimetoa kama mfano lakini wataalam wetu wanaweza kutusaidia best practice ambayo italeta hamasa kuchangia damu, kwa mfano baadhi ya nchi mwenye point nyingi anakuwa considered katika nafasi kama za ajira, za jeshi na kadhalika. Hii itasaidia sana kukuza hamasa ya watu au makundi katika jamii kama vile wanafunzi kuchangia damu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ajira kwa wanaojitolea hasa pale Benjamin Mkapa, nilikuwa na mgonjwa Hospitali ya Benjamin Mkapa, mzazi. Ndugu zangu wiki mbili ambazo nimekaa pale hospitali na mzazi ambaye alijifungua wiki tatu Kayla na hivyo kulazimika kukaa kwa muda hospitali, nimeshuhudia ambavyo kwanza madaktari na wauguzi wakifanya kazi kwa bidii na moyo wa kujituma. Kwa kweli nimeona pia nilivoenda kuwaona wagonjwa ndugu zangu kwa kweli watu wanafanya kazi sana.

Ushauri wangu kuhusu ajira kwa wanaojitolea, Mheshimiwa Waziri nafahamu kwamba zipo taratibu za kiutumishi lakini zipo exceptional cases, pale Benjamin Mkapa wauguzi wa kike kwa kiume wanakesha na wale watoto waliozaliwa wakiwa na matatizo kama vile kuzaliwa kabla ya siku, wanafanya kazi, wanawabembeleza kwa moyo tena kuna wakati unakuta hata mama mzazi hawezi kumhudumia mtoto wa aina hiyo kwa kiwango cha hawa wauguzi.

Mheshimiwa Spika, ninaomba watizamwe kwa jicho la kipekee. Suala hili nimeshauri hata katika mchango wangu kwa Wizara ya Utumishi.

Kuhusu Mafinga Hospital; kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy wakati ule kabla hajahamishiwa TAMISEMI, lakini pia Katibu Mkuu alipita Mafinga. Nafahamu kuwa hospitali hii iko chini ya TAMISEMI, hata hivyo ninaomba kama ambavyo Serikali imefanyia ukarabati shule kongwe, ione uwezekano wa kuzifanyia ukarabati mkubwa hospitali kongwe kama ya Mafinga ambayo inahudumia zaidi ya Halmashauri tano. Tunashukuru kupitia fedha za UVIKO tunajenga jengo la dharura, hata hivyo kwa kuwa iko kando ya highway inazidiwa sana kwa huduma. Kwa mfano katika suala la watumishi, bado nasisitiza pamoja na kuwa ni suala la TAMISEMI, Mafinga itizamwe kwa macho mawili kwa sababu ya location. Kwa mfano Mafinga inahudumia wagonjwa kutoka Ihalimba - Mkoa wa Morogoro, Mbalari - Mkoa wa Mbeya, Nyigo - Mkoa wa Njombe na pia Mufindi DC na Iringa DC. Hivyo kwa namna ambayo itawapendeza na kwa fursa zitakazojitokeza kuitizama kwa macho mawili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza kwa maandalizi ya hotuba iliyojaa ufafanuzi wa sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha yafuatayo; kwanza kazi na ajira, kupitia kilimo tunaweza kupanua wigo wa ajira, lakini pia tunaweza kujitosheleza kwa baadhi ya bidhaa ambazo kutokana na kilimo tutazizalisha na tukapunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa kama mafuta ya kula. Ushauri wangu wa mara zote, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ulinzi na JKT, tuwekeni nguvu kama Taifa katika kuzalisha mbegu ambazo tutazalisha mafuta ya kula.

Mheshimiwa Spika, napongeza jitihada za Mheshimiwa Waziri Mkuu zinazoendelea kule Kigoma za kilimo cha michikichi. Ninaamini tukiwawezesha JKT tutavuka, lazima tufike wakati tuwe na uthubutu, tuwe wakweli wa nafsi, sio sawa kama Taifa kuendelea kutumia zaidi ya USD milioni 300 kuagiza mafuta ya kula, tuone aibu kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, hata jitihada za kupunguza VAT kwa waagizaji mafuta ya kula hazijawa na nafuu iliyokusudiwa, zaidi imenufaisha wafanyabiashara waagizaji wa mafuta ya kula, matokeo yake bei ya alizeti imeshuka kwa wakulima wetu na wakati huo huo bei ya mafuta ya kula haina ahueni yoyote.

Mheshimiwa Spika, tukiwekeza katika JKT sio tu kwamba tutaokoa fedha za kigeni lakini pia tutauza mafuta katika nchi jirani za DRC, Malawi, Zambia na hata Burundi na Rwanda. Nchi hizi zinategemea mafuta ya kula kutoka Malaysia, tukizalisha tunalo soko la ndani, lakini pia soko hata ndani ya EAC na baadhi ya nchi za SADC.

Kule Chita, nashauri Serikali ikajifunze kilimo cha mpunga chini ya JKT, ni aibu sisi kutoa vibali na kuagiza michele tani 90,000; haya ni mambo tunapaswa kuyakataa kwa vitendo, hizi programu za Block Farming zingehusisha vijana waliopata mafunzo JKT na usimamizi ungefanywa kwa ushirikiano wa ofisi hizi tatu, Kilimo, Kazi na Ajira na JKT.

Mheshimiwa Spika, pili, usalama wa mbegu na mbegu bora; pia ninashauri tuwe na mpango maalum wa kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa mbegu bora na salama. Mfumo uliopo kwa hakika sio salama katika suala la usalama wa chakula na usalama wa Taifa. Nashauri pia tuhusishe vyombo vyetu hasa JKT.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi japo sijafahamu ni dakika ngapi natakiwa kuchangia lakini itoshe tu kusema kwamba nami napongeza Ofisi ya Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri na kwa utendaji mzuri, pia kwa kwake Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi alivyokuwa mtu rahimu na mtu ambae anafikika hata ukiwa na jambo kwa ajili ya wananchi wako anakusikiliza na linapata ufumbuzi pale ambapo kuna changamoto. Kwa hiyo nawapongeza sana yeye na Mawaziri wanaofanya kazi katika Ofisi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa siyo mwingi wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo inafanyika katika sekta zote muhimu za afya, elimu maji na barabara, kama alivyosema Mheshimiwa Seif kweli kabisa Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi. Anaupiga mwingi kama Mayele lakini pia anaupiga mwingi kama Clatous Chota Chama. Sasa ukichanganya hapo unaweza kuona ni jinsi gani mambo, yaani unajaribu ku-imagine Chama na Mayele mambo yanavyoweza kuwa mazuri. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa sababu mimi ni mwanamichezo naomba pia nitumie nafasi hii kuwapongeza Simba na Yanga kwa kufika hatua ya robo fainali, kwa sababu tumesema kwamba mpira na michezo kwa ujumla ni ajira ni biashara ni uchumi. Ninapenda pia nitumie nafasi hii kuwakumbusha tu Watanzania kwamba Simba hii ambayo imepangiwa na mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika ilishawahi kupangiwa na mabingwa watetezi Zamalek mwaka 2003 na ikawatoa pale pale Cairo – Misri kwa mikwaju ya penati tatu kwa mbili baada ya kuwa wametoka moja bila Simba wameshinda kwa goli lililofungwa na Ndugu Emmanuel Gabriel dakika ya 56 lakini walipoenda kule Simba wakafungwa moja ikabidi waende kwenye changamoto ya mikwaju ya penati na Simba wakawang’oa Zamalek. Kwa hiyo, kama ambavyo tumepangiwa Mabingwa Watetezi vilevile watu waweze kujua kwamba tumejipanga vizuri tunaweza tukalitangaza Taifa na tukatangaza utalii wa nchi yetu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nampa taarifa mchangiaji anatueleza historia sana lakini ninataka kumwambia ukizungumzia kikosi bora ni cha Young Africa na nimhakikishie kwenye mechi tunayokutana na Simba tutawafunga nasi kama tunaongoza group Nigeria tunaenda kushinda. Tunaenda kuwaonesha, tunaenda kushinda ugenini. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chumi taarifa unaikubali?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa muktadha ufuatao, kwamba maisha ni historia, leo yetu imetengenezwa na jana na kesho yetu itatengenezwa na leo kwa hiyo nakubaliana nae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo napenda kutumia nafasi hii kuipongeza sana Serikali katika suala zima la mbolea na ruzuku ya mbolea, kwa kweli Serikali imetusaidia sana. Serikali ilikuwa sikivu tulijenga hoja na kwa kweli wakatuwekea ruzuku. Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto ya hapa na pale katika upatikanaji wa mbolea ile ya ruzuku. Kwa mfano, mbolea kutofika vijijini kwa wakati, pia changamoto za stika watu wanaenda stika zinakuwa bado, wakati mwingine wanaenda wanaambiwa kwamba stock haijasoma na kadhalika, lakini ni changamoto ambazo ni manageable tunaamini kwamba msimu ujao tutafanya vizuri zaidi. Kwa hiyo, ili tuboreshe suala zima la upatikanaji wa mbolea nina mambo machache ya kushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nashauri ule usambazaji walau uende mpaka ngazi ya Kata. Pili, ninashauri ujazo wa mbolea iwe na ujazo tofauti tofauti. Wapo wakulima wengine wanahitaji ujazo wa kilo tano, wengine kilo 10, wengine kilo 20. Isiwe tu mbolea ya ruzuku mifuko iwe ni ya kilo 50 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba upatikanaji wa mbolea uwe ni kwa mwaka mzima. Nikisoma hapa katika taarifa ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 31, kiasi cha takribani shilingi bilioni 284 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa scheme za umwagiliaji. Maana yake ni kwamba, sasa tunaenda kujidhatiti katika kilimo ikiwemo kule Mtula kwamba tutalima mwaka mzima. Kwa hiyo, kama tutalima mwaka mzima maana yake ni kwamba nashauri mbolea ya ruzuku pia ipatikane mwaka mzima, tusisubiri tu wakati ule ambao msimu unaanza, kwa sababu tume- encourage wananchi wetu walime mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, watu wa Iringa, Njombe tunalima kile kilimo cha mabondeni, kilimo cha vinyungu ni mwaka mzima. Tukimaliza sasa hivi kulima hichi kilimo cha kawaida tutarudi kilimo cha mabondeni pamoja na kuwa tunazingatia kutunza vyanzo vya maji. Kwa hiyo, ushauri wangu mbolea ipatikane mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama ambavyo tumetoa ruzuku kwenye mbolea, Wananchi wa Mafinga nilipofanya ziara wameshauri kwamba pia mbegu nazo zipatikane mbegu za ruzuku ili kusudi vyote hivi viweze kusisimua kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine tumeelezwa hapa kuhusu usalama wa chakula, lakini usalama wa chakula unaendana pia na usalama wa upatikanaji wa mbegu. Mimi nilikuwa nashauri hebu pamoja na taasisi yetu ya utafiti wa mbegu tuvishirikishe vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Kujenga Taifa katika kufanya tafiti za mbegu. Kwa sababu baadhi ya mbegu ambazo tunaletewa ni zile mbegu ambazo mwaka huu ukipanda mwakani haiwi kama zamani ambavyo tulikuwa tunatumia lilelile zao umepanda mwaka huu mwakani ukivuna baadhi ya sehemu ya mazao unatumia kama mbegu. Kwa hiyo, nilikuwa napenda kushauri hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa sababu ya muda ni suala la TARURA. Kweli tunawapongeza kabisa kunatengwa bajeti, kama mimi hapa Mafinga mwaka 2021 tulikuwa tunapata shilingi milioni kama 900 lakini 2022/2023 tunapata mpaka shilingi bilioni 2.3 na tunatarajia itaenda kuongezeka. Kama alivyosema Mheshimiwa Iddi kumekuwa na shida kubwa sana na changamoto ya Wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mafinga kwa mfano, kuna barabara ambayo Mkandarasi ilikuwa atukabidhi Tarehe 04 mwezi Machi lakini mpaka hapa ninapozungumza ameshakamatwa na TAKUKURU, ameshahojiwa na Mkuu wa Wilaya, ameshaitwa kwa Mkuu wa Mkoa, ameshaitwa mpaka kwa viongozi wa chama, nothing is going on. Kwa hiyo, nashauri wakati Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla inatenga fedha kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo, wako watu au baadhi ya Wakandarasi ambao siyo waaminifu wanapewa kazi lakini hawazifanyi kwa wakati, ambapo kimsingi wanakwamisha au kuchelewesha maendeleo ya wananchi. Kwa hiyo, ninashauri Serikali tutafute namna ikiwezekana tuwe na Wakandarasi wachache au kama hawana nguvu ya kifedha basi tuwatafutie mechanism ya kuwapa mikopo kwa namna ambayo itawezesha wao kufanya kazi kwa wakati na kwa ufanisi ili kusudi zile fedha na zile shughuli ambazo zimepangwa ziweze kufanyika, kwa sababu it is very embarrassing kwamba mtu kapewa kazi anatakiwa akabidhi Tarehe 04, Machi, mpaka leo ninavyozungumza tarehe 06 Aprili, amefanya kazi asilimia 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo vyote vya Kiserikali including Chama cha Mapinduzi kimechukua kila hatua, nothing is going on. Sijui tunafanyaje maana sasa tunasema tusije tukawa tu Taifa la kulalamika ndiyo maana nashauri tutafute namna ambayo Wakandarasi wa namna hii pamoja na kuwachukulia hatua, tuone Je, kuna namna gani kama Taifa tunaweza kuwajengea uwezo Wakandarasi wetu wanaopewa kazi za ndani ili fedha ile tunayopitisha hapa Bungeni ikafanye kazi ambayo imekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo naomba kuunga mkono hoja, nikisisitiza na kurudia kwamba kuhusu suala la mafuta ya kula bado nasisitiza na kushauri tufanyeni kama trial tuwape JKT miaka miwili tuwawezeshe, tuone kama hatujajitosheleza kwa mafuta ya kula tukaokoa fedha za kigeni hizi ambazo kila mwaka tunatuma kununua mafuta ya kula hapa nchini, huo ndiyo ushauri wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu atubariki wote, aibariki Simba na Yanga na awabariki Watanzania kwa ujumla. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa wasilisho lenu, napongeza ubunifu wa Waziri na timu yako kukutana na sisi Wabunge, napongeza kwa sababu mawazo yetu/yangu yamezingatiwa, pamoja na kwamba siyo yote ambayo bila shaka ni kutokana na ufinyu/ukomo wa bajeti. Nawashukuru sana kwa kukubali wazo na ombi langu la kuitizama hospitali kongwe ya Mafinga ambayo inahudumia Halmashauri tano za jirani kwa maana ya Mufindi DC, Mbalari, Mlimba, Iringa DC na sehemu ya Makambako. Hospitali hii pia iko kando ya barabara ya TANZAM 1 ambayo ndio corridor kuu kuelekea nchi za ukanda wa SADC kwa maana ya Malawi, Zambia, DRC na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza kututengea shilingi milioni 900 kwa ajili ya hospitali hii na nawaahidi mimi na Madiwani wenzangu kwa ushirikiano na CMT tutasimamia kwa ukaribu kuhakikisha kuwa lengo linatimia kwa viwango na kwa wakati. Ombi langu fedha iletwe kwa wakati na utekelezaji uwe kwa force account.

Kuhusu TARURA, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri na walau bajeti imeongezeka Mafinga kutoka around 900 million mpaka around 2.3 billion. Hii ni hatua kubwa, hata hivyo zipo changamoto hasa ya wakandarasi. Nitatoa mfano, Mkandarasi Rahda Investment wa Mbeya anayejenga barabara ya kuelekea katika Kituo cha Afya cha Ihongole, ndugu zangu sijui niseme nini, barabara hii mkandarasi alikuwa atukabidhi barabara tarehe 4 Machi, 2023 lakini mpaka nawasilisha mchango wangu huu, kazi haijafika hata 20%. Mkandarasi huyu ameitwa kwa DC, amekamatwa na TAKUKURU, wenzetu wa Chama cha Mapinduzi wamepiga kelele weeeee hakuna kinachoendelea, ilifika wakati wananchi waliandamana wakaamua kuondosha mawe ambayo mkandarasi aliyamwaga, kusambaza na kuondoka zake, siku moja kabla ya kikao cha Road Board akarejea site, in short anatufanyia mchezo, mkiwa wakali anaonekana siku mbili, siku ya tatu anaondoka, kwa ufupi ametugombanisha na wananchi na Mbunge, wananchi na Serikali, wananchi na chama, sote tunaonekana ametuweka mfukoni.

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana, namna mtakayoona inafaa kuchukua hatua sio tu kwa kumuondoa lakini kwa kutafuta namna ambayo itatuondolea hii aibu, nawaomba. Kuna jitihada zimefanyika kwamba labda kazi hii afanye mwingine kwa internal arrangement, hii ni kwa sababu kiushauri wanasema kuvunja mkataba italeta more complications, naomba na naona aibu kuwasilisha jambo la ujenzi wa barabara ya kilometa moja kwenu.

Mheshimiwa Spika, nina ushauri kwamba pamoja na kuwa fedha haitoshi, lakini hii ambayo inatengwa walau inasaidia kupunguza kadhia ya barabara, hata hivyo nilichojifunza, inaonekana kazi ni nyingi kuliko uwezo wa wakandarasi au uwepo wa mitambo. Kwa sababu hiyo mkandarasi anashika kazi nyingi kwa sababu zipo, lakini anakuwa hana vifaa, ninashauri tuchukue hatua za makusudi na kuona uwezekano wa kuwasaidia kwa kuwajengea uwezo ama kuwadhamini kupata mkopo wa mitambo au TARURA kila kanda kuwa na mitambo ambayo itakuwa inakodishwa kwa wakandarasi na baadae wanakatwa katika malipo yao. Huu ni ushauri ambao wataalam wanaweza kudadavua na kuona the best practice ambayo inaweza ikawa sehemu ya suluhisho la kukabiliana na wakandarasi ambao hawatekelezi kazi kwa wakati na kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu TACTIC, kwanza naendelea kushauri tuendelee na vikao kati ya Wabunge wa miji 45, pili ninashauri kwa kuwa mradi huu utasaidia pia kujenga miradi ambayo itakuwa sehemu ya chanzo cha mapato, hii Tier 2 na 3 zingeunganishwa ili utekelezaji wake 2024/24. Kuchelewa kuanza utekelezaji kwa jambo ambalo ni mkopo wa WB ambayo nafahamu ina vigezo vingi vya kufuatwa lakini naamini majadiliano yakifanyika tunaweza kutekeleza tier hizi 2 na 3 kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, pia naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi katika maeneo mahususi; kwanza naomba tusome huu ujumbe kuhusu madai ya huyu mwalimu; "Pole na majukumu Mheshimiwa, mimi ni Mwalimu Pascal Canisio wa Mnyigumba Sekondari. Ninaidai Serikali shilingi 2,770,000 (mishahara ya miezi mitatu), ni miaka mitatu sasa na jina langu linaonekana liko kwenye mfumo. Ninaomba msaada niweze kulipwa mapema ili nitatue matatizo yangu. check no. 11178565."

Nimemshauri awasiliane na Afisa Utumishi wa Halmashauri, majibu yake; "Wanasisitiza Serikali inalipa taratibu kulingana na bajeti, Mheshimiwa. Tatizo wapo watu wamedai baada ya mimi na wamelipwa."

Mheshimiwa Spika, naomba tumsaidie ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, maombi maalum; tuliwasilisha maombi ya Shule ya JJ Mungai kupewa fedha za ukarabati mkubwa. Tunashukuru shule ya A-Level ya Changarawe sasa imekaa vizuri. Shule ya JJ Mungai ni kati ya shule ambazo zilikuwa shule za wananchi chini ya MET - Mufindi Education Trust ambazo zilijengwa kwa nguvu ya wananchi na baadae zikachukuliwa na Serikali. Toka wakati huo na hasa baada ya kuanzisha kidato cha sita, hatujawahi kupata usaidizi kutoka Serikalini, tumewasilisha andiko fupi kuelezea hali halisi ya shule na tumetaja maeneo yanayopaswa kufanyiwa ukarabati.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya; kama ambavyo nimeeleza mara kadhaa, na ninashukuru mmetusikia na kututengea fedha shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa hospitali kongwe ya Mafinga. Hata hivyo Kata ya Upendo tumeanzisha ujenzi wa kituo cha afya na tayari tumeshajenga OPD na hivi karibuni tutaanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje. Hivyo ombi letu kutokana na ukuaji wa ongezeko la watu na uchumi wa mazao ya misitu, uhitaji wa huduma katika kata hii ni muhimu sana, baada ya Kata ya Boma, Kata ya Upendo ni ya pili kwa idadi ya watu katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, ina watu 25,000 hivyo Serikali ikishirikiana nasi tutaendeleza ujenzi wa Kituo cha Afya Upendo tutasaidia sana kuboresha huduma.

Mheshimiwa Spika, kuhusu TACTIC; bado nashauri, Tier 2 na Tier 3 ziunganishwe ili utekelezaji wake uende kwa pamoja na kwa haraka. Mradi huu pamoja na kuboresha miundombinu, itasaidia hizi Halmashauri kuwa na vyanzo vya mapato, kwa mfano Mafinga moja ya miradi ambayo tumeainisha ni stendi ya malori ambayo tayari kwa mapato ya ndani tumeweka fence wire na tayari malori ya safari ndefu maarufu kama transit yana- park na kidogo tunapata mapato. Mradi mwingine ni stendi ya mabasi Mafinga ipo kando ya TANZAM 1, highway ya kwenda nchi za SADC, aidha, kutokana na kuimarika kwa sekta ya mazao ya misitu, Mji wa Mafinga unakua kwa kasi kama kitovu cha biashara katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hivyo mradi huu utakuwa viable na hautakuwa white elephant kama ambavyo imejitokeza katika baadhi ya maeneo.

Mwisho, nawapongeza sana utaratibu wa kutujulisha wajumbe kuhusu fedha zilizopelekwa katika Halmashauri zetu, ninaomba uwe ni utaratibu wa mara zote. Tupo Wabunge wa aina nyingi, tupo ambao tunafanya kazi kwa ukaribu na CMT/Mkurugenzi, hivyo kujua kila kinachoendelea, lakini wapo Wabunge ambao hata fedha za Mfuko wa Jimbo zikiingia anasikia kupitia group letu la whatsapp. Kwa hiyo, kwa kutoa taarifa mnatusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, angalizo; pamoja na miongozo ya wapi fedha zikatumike, nashauri, pale ambapo kutakuwa na maboresho kwa maana ya baadhi ya Halmashauri kuwa na maombi mbadala, basi pawepo utaratibu wa kuyapokea ikiwa tu maombi hayo yatapata baraka za Kamati ya Fedha ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu hapa turuhusu flexibility lakini kwa kuweka mechanism ambayo baadae haitakuwa vurugu kwamba sasa kila mtu anataka kubadilisha kutoka shule A na kwenda shule B au C.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa utendaji mwema, pamoja na changamoto kadhaa kama vile rasilimali watu na fedha kwa ujumla mnafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, nina mchango katika maeneo yafuatayo; kwanza ni kuhusu kulegeza masharti kwa watumishi wanaokaimu.

Mheshimiwa Spika, wapo watumishi ambao wanakaimu kwa dokezo na sio kwa barua ile ambayo inatoka Utumishi. Kwa mfano nina mwanasheria katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, yeye alikuwa mwalimu akasoma sheria, na amekuwa msaada katika Halmashauri. Kwa mfano Mafinga TC imetokana na kugawanywa kwa Halmashauri mama ya Mufindi, bahati mbaya sana japo ndio utaratibu katika kugawana mali na madeni, Mafinga TC ilirithi migogoro mingi ya ardhi kutoka Halmashauri mama ya Mufindi ambayo ilikuwa migumu sana. Ni kweli kwamba ni wajibu wa mwanasheria kutetea kesi za Serikali/Halmashauri, hata hivyo ameshiriki kuokoa Halmashauri kulipa mamilioni ya fedha ambayo ni kutokana na kesi za madai ya migogoro ya ardhi ambayo tulirithi kutoka Halmashauri mama ya Mufindi. Mwanasheria huyu alifanya kazi bega kwa bega na mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kesi za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, kwa vipindi vifupi tuliletewa mwanasheria kamili kuwa Mkuu wa Idara lakini hakukaa sana, kwa hiyo katika kipindi cha miaka takribani nane kutoka Julai, 2015 mwanasheria huyu amefanya kazi kwa miaka zaidi ya sita akiwa ni Mwanasheria Daraja la II.

Mheshimiwa Spika, ninaleta hoja hii kama case study ya suala la watumishi wanaokaimu kwa madokezo na hususani wale ambao wametokea katika kubadilishwa kada kwa maana ya recategorization.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa kuwa mtumishi wa aina hii na wote wa aina, wamethibitisha uwezo katika kazi na kwa kuwa walishakuwa watumishi, napendekeza moja; wafanyiwe mserereko ili kuwasogeza kwenye ngazi ambayo wanaweza walau wakawa wanakaimu sio kwa dokezo bali kwa barua rasmi kutoka Utumishi, nasisitiza hili la Mwanasheria wa Mafinga TC nimelitumia kama mfano.

Mheshimiwa Spika, pili, kuwaachia mshahara binafsi watumishi waliofanyiwa recategorization; ninashauri, pale ambapo mtumishi amekidhi vigezo na kufanyiwa recategorization, nashauri ikiwa alikuwa amefikia TGS F kwa mfano lakini baada ya recategorization akarudi katika kada mpya kwa kuanzia daraja la kuingilia ambapo mara nyingi ni daraja la pili la kada husika, mshahara wake ubakie TGS F kuliko kurudi TGS D. Hii itasaidia sana kuwapa morali watumishi.

Mheshimiwa Spika, tatu, wastaafu kulipwa kwa wakati; lipo tatizo kubwa kwa watumishi wanapokaribia kustaafu au wakishastaafu hasa walimu. Kuna hali fulani kama ya kuwa desperate mtu anapoingia hatua ya kustaafu, wanakuwa na hofu kubwa, stress na mashaka kwamba je, nitalipwa kwa wakati au nitacheleweshewa kama mwenzangu fulani.

Mheshimiwa Spika, suala hili lipo zaidi kwa walimu, kiasi Mbunge kila mara unapokea simu au ghafla mwalimu mstaafu anakupigia anakuambia nipo Dodoma naomba nikuone nimekuja kufuatilia suala la mafao. Mara nyingi wakienda kwenye mifuko hupewa majibu mapokezi kwamba jambo lako linashughulikiwa, hii anaweza kujibiwa mara kadhaa na baadae anakata tamaa, anafunga safari anakuja Dodoma. Hili hujitokeza mara nyingi kama kwa mfano, kuna michango haikuwasilishwa kwa wakati, hufikia hatua mstaafu kuamua kujilipia ile tofauti kusudi tu mafao yake yawe processed. Nashauri tuwe na utaratibu mzuri zaidi wa kuandaa mafao ya wastaafu wetu kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Spika, angalizo; nashauri suala la ajira libakie huko huko na kwa mfumo huu, suala la kusema mnagawa nafasi kwenda kwenye majimbo ni hatari, ni ugomvi kwetu Wabunge, fikiria jimbo lipate nafasi 20, wahitaji wako 200, wakikosa 180 lawama kwa Mbunge, sisi tubaki na kazi ya kushauri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Serikali iokoe viwanda vya mkonge, okoeni ajira.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Wizara kwa wasilisho la bajeti na ninaomba kuchangia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tuokoe zao la mkonge na viwanda vyake. Katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025 imetaja kuzalisha ajira milioni nane, ni wazi kuwa ajira hizi kwa kiasi kikubwa zitatokana na mnyororo wa thamani kuanzia katika malighafi za kutoka mashambani/kilimo hadi viwandani (agro-processing industry). Ajira hizi pamoja na viwandani itaendelea hadi sokoni.

Mheshimiwa Spika, ni masikitiko makubwa sana kwamba wakati tumeamua kufanya zao la mkonge kuwa zao la kimkakati, hakuna jitihada za makusudi za kulinda viwanda vya kuchakata zao la mkonge kwa maana ya kulinda soko. Ndani ya Serikali hakuna ufuatiliaji wa maagizo na maelekezo ya Waziri Mkuu Septemba, 2021 na rejea yake Novemba, 2021 kwamba Wizara inayohusika na Mazingira kwa maana ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira izuie importation ya kamba za plastic ambazo kwa kiasi kikubwa mbali ya kuvuruga soko la kamba za kitani, lakini pia zinaathiri mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, ni matarajio yangu wenzetu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara wanayo nafasi kubwa ya kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira kuhakikisha kuwa zuio hilo linasimamiwa ili kuwalinda wakulima na kulinda viwanda na ajira za Watanzania kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Mheshimiwa Spika, industrial park Mafinga Mjini; tumetenga ekari 750 kwa ajili ya industrial park na kupitia Mradi wa TACTIC tutajenga miundombinu wezeshi na tayari EPZA walitembelea eneo hilo na kutoa ushauri, pamoja na kuwa tuko katika hatua za awali za kupanga, kupima na kumilikisha, nawaomba Wizara tufanye kazi kwa ushirikiano ili tuweze kufanikisha suala hili kwa lengo like lile la kuzalisha ajira hasa kupitia fursa ya mazao ya misitu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza katika siku hii ya leo. Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, pia kwa sababu mimi ni mwanamichezo napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza Simba na Yanga kwa ushindi walioupata weekend hii katika michezo yao ya robo fainali na tunawaombea katika mechi zijazo waweze kushinda ili kusudi Taifa letu liweze kuingia katika hatua ya nusu fainali ambayo itakuwa rekodi kwa Taifa letu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaomba nijielekeze kwenye hoja. Mimi nina mambo kama matatu hivi. Kwanza, kumekuwa na jitihada kubwa sana za kuhamasisha upandaji wa miti, ni jambo jema na jambo zuri lakini lazima ifike wakati tujiulize je, kupanda huku kunaendana na utunzaji? Kweli tumeweka malengo ya kupanda nadhani miti 1,000,000 kwa kila Halmashauri, tunapanda vizuri sawa lakini je, miti mingapi inapona? Kwa hiyo pamoja na kupanda tujielekeze pia katika utunzaji wa miti hii ili tusije tu tukawa na takwimu za kwamba tumepanda miti kadhaa lakini miti ambayo inaendelea kuishi na kuwepo kwa nia ya kutunza mazingira inakuwa ni michache. Kwa hiyo, nguvu zielekezwe kwenye kupanda lakini pia na kwenye kutunza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ninalopenda kuchangia ni kwa namna gani kama Taifa tumejipanga kunufaika na Mifuko ya Umoja wa Mataifa ambayo ina jukumu la kusaidia nchi maskini kukabiliana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru na napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais katika mkutano wa mazingira kule Scotland – Glasgow, alikuwa jasiri na aliyaeleza mataifa makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa yana mchango mkubwa katika kuharibu mazingira na kuchangia madhara haya ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuahidi kuchangia ile mifuko takribani Dola Bilioni Mia Moja ambayo fedha hizi zitasaidia nchi maskini ambazo kimsingi hazichangii sana mabadiliko ya tabianchi, hazichangii sana kuharibika kwa mazingira, sasa hizi nchi kubwa zinao wajibu wa kuzi–support hizi nchi ndogo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais alikuwa jasiri na aliyaambia Mataifa makubwa kwamba pamoja na ahadi zenu ifike wakati muweze kuheshimu ahadi zenu na kutoa hizi fedha. Sasa kama Taifa tumejipangaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza Wizara na Serikali walikuja na huo mwongozo pamoja na kanuni za udhibiti na usimamizi wa biashara ya carbon au hiyo tunaiita hewa ya ukaa. Mifuko hii iko mingi na katika Mkutano wa mwaka jana maarufu kama COP27 kumeanzishwa Mfuko unaitwa Loss and Damage Fund. Mfuko huu malengo yake ni kusaidia katika kutibu majanga mbalimbali ambayo nchi hizi maskini zinapata kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu na hoja yangu kwa Mheshimiwa Waziri na kwa Serikali kwa ujumla, tumejipangaje katika kuhakikisha kwamba tunanufaika na fedha hizo na tunaweza kukabiliana na majanga yanapotokea. Kwa mfano, jambo la muhimu la kwanza sana inatakiwa lazima uwe na orodha ya majanga yanayotokea katika Taifa lako ili mfuko ule utakapoanza kutekelezwa basi walau unapoenda kuwasilisha yale maombi tayari unakuwa na ile orodha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, pamoja na Kanuni hizi, natumia nafasi hii kuwapongeza sana Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania walifadhili Halmashauri ya Mji wa Mafinga tukaenda kujifunza kule Wilaya ya Tanganyika kwa Mheshimiwa Kakoso. Wenzetu wamepiga hatua sana. Nimeona Serikali Mheshimiwa Jafo amesema kufikia 2024 Januari, hakutakuwa na matumizi ya mkaa kwa Taasisi za Umma na Binafsi ambazo zinahudumia watu kuanzia mia moja. Je, kama Taifa tumejipangaje katika kutumia nishati mbadala?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mafinga tunavyo viwanda vya mkaa ambao unatokana na mabaki yanayotokana na uzalishaji wa mazao ya misitu. Sasa yale mabaki ni kwamba tungeweza kuyachoma kwa kuyachoma maana yake tungeendelea kuharibu mazingira, sasa viwanda kama hivi vilikuwa vitatu,viwili vimeshafungwa, kimoja kinaendelea lakini hata hiki kimoja mkaa kinauza nje ya nchi kwa sababu hapa nchini hawawezi kuuza kwa sababu bei inakuwa ni kubwa kutokana na mazingira yale ya uwekezaji siyo rafiki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona pia Mheshimiwa Waziri Mkuu alipiga marufuku matumizi ya kamba hizi za nylon, kwamba ili tuweze kufufua zao la mkonge, tuweze kutengeneza ajira lakini kwa ajili hiyo ya kulinda mazingira tupige marufuku uingizaji wa kamba za plastic lakini kamba bado pia zinaingia. Je, tunajipangeje katika haya yote, kwa mfano kuhakikisha kwamba hawa watu wanaozalisha nishati mbadala kama nilivyosema viwanda hivi vya Mafinga, tunaviwekea mazingira gani ili vizalishe ule mkaa ambao kama mtu hana uwezo wa kugharamia gesi basi aweze kuwa na ule mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, watu wa Mufindi, Iringa na Njombe tumepanda miti kwa wingi, niliposoma kanuni sijui kama nimeelewa vizuri na kwa kuwa inawezekana hata mimi Mwakilishi naweza nikawa sijaelewa vizuri, nilikuwa naiomba Wizara iwe na mpango mkakati maalum, waje watuletee elimu na kutuwezesha kufahamu je, hata hii miti ya kupanda nayo tunanufaika katika hii biashara ya hewa ya ukaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru kwa kunipa nafasi na Mungu atubariki wote na awabariki Simba na Yanga katika mechi zijazo. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana kwa kuja na Mwongozo na kanuni za biashara ya carbon. Hamasa ya kupanda miti ni kubwa, napongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo na ufinyu wa bajeti yapo masuala ambayo kwa kushirikiana na sekta binafsi na asasi za kiraia tunaweza kufanikisha mengi. Na hapa nina ushauri ufutao: -

Kwanza, tukumbuke kwamba tumechelewa sana kama Taifa kunufaika na mifuko ambayo ninahitaja mara kadhaa, kama GCF, GEF, AP na kadhalika; na hii tukiwa honest inatokana na ukweli kwamba ndani ya Serikali tuna tabia na hulka ya kujifungia, yapo mambo lazima tufanye engagement, tuwe na partnership, ikiwa Mheshimiwa Rais ameonesha njia katika kushirikiana na sekta binafsi na asasi za kiraia na sisi tunao wajibu wa kufuata nyayo hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika COP 27 baadhi ya asasi na NGOs zilifanya jitihada za kukutana na Mfuko wa GCF, na tayari kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Climate Action Network wanayo concept note ya USD 380M jointly with ambayo fedha ikipatikana utekelezaji wa mradi utafanywa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji, Mifugo na Mamlaka ya Hali ya Hewa. Mradi huu utatekelezwa katika mikoa 22 na mradi utawafikia karibu 70% ya wakulima wadogo, wafugaji na jamii za wavuvi na fedha hii zaidi ya 65% itakwenda Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa nilizonazo GCF walithibitisha kupokea andiko wakashauri ili kukidhi vigezo, linapaswa andiko liwe kwenye luggage za kitaaluma kadri ya mwongozo vya GCF. Moja ya ushauri ni Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira wafanye mawasiliano na GCF kuomba support ya kupata Mshauri Mwelekezi na GCF wako tayari kulipia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba suala hili lipo kwenu toka mwaka jana mwishoni na uzuri linafanywa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, hata hivyo hakuna kinachoendelea. Huu ndio msingi wa hoja yangu kwamba tunachelewa sana kufanya maamuzi, tupunguze kujifungia, ninawasilisha kwa maandishi kwa sababu kwa maadili nisingependa kuyazungumza kwa kuongea, lakini nitashukuru ikiwa ushauri huu Serikali itaufanyia kazi kwa kuwa wepesi katika kushirikiana na sekta binafsi na kuwa wepesi kimawasiliano, tupunguze urasimu.

Pili ni kuhusu biashara ya carbon; napongeza sana kuja kwa kanuni na mwongozo, hata hivyo bado tunahitaji kuwekeza katika utaaalam na ushawishi. Suala hili linahitaji utaalam wa hali ya juu sana hasa katika kupiga mahesabu husika.Ninaamini kuwa tukijipanga vema, tunaweza tukapunguza kukata miti, kwa sababu wananchi ikiwa watanufaika na biashara ya carbon, watapanda miti zaidi na iliyopo, wataitunza kwa umakini mkubwa sana. Kwa hiyo, narudia tena ushirikishwaji wa sekta binafsi na NGOs ni jambo muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, zuio la matumizi ya mkaa 2024 vs uwekezaji kwenye nishati mbadala; Mafinga tulikuwa na viwanda vitatu vya kuzalisha mkaa (Briquettes charcoal) ambao ni bora na rafiki kimazingira. Hata hivyo katika viwanda hivyo, viwili vimefungwa, kimebaki cha Briquettes Energy Solution ambacho hata hivyo kinauza mkaa nje mpaka Ujerumani na uhitaji ni mkubwa sana. Ushauri wangu, viwanda vya aina hii tuwe na mpango mkakati wa kuvijengea mazingira rafiki ya kiuwekezaji, lakini kwa kuwa pia zinashiriki kukabiliana na uharibifu wa mazingira kwa sababu zinatumia mabaki ya mazao ya misitu, zinastahili kupata fedha kutoka mifuko husika, lakini pia kuna mkanganyiko kwamba fedha za carbon ni kwa ajili ya misitu ya asili, je, ukweli ni upi?

Mheshimiwa Naibu Spika, utaalam vs ushawishi wa kisiasa hasa kikanda; ili kupata fedha hizi kunahitajika utaalam lakini ushawishi wa kisiasa, hasa kikanda, kwa mfano kupitia EAC, SADC na hata AU, kwa sababu kutengwa fedha ni jambo moja, lakini kuzipata ni jambo la kipekee. Mfano mzuri ni Mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi kule Simiyu, nyote mnafahamu mzunguko uliotumika kuzipata fedha hizo, nashauri ushirikiano ndani ya Serikali na nje ya Serikali na ndio maana nasisitiza lazima ndani ya Serikali tuwe open, tuwe sharp, tukubali ushauri na tuwe wepesi kufanya engagement, hii itasaidia sana kupata fedha kutoka mifuko niliyoitaja lakini pia tukijipanga na suala zima la Loss and Dama Fund kwa sababu majanga ni makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana Wizara kwa hotuba ya Bajeti, lakini zaidi kwa ile programu ya mentorship ambapo tuliwaona madaktari ambao wataenda kila Wilaya kufanya mafunzo kwa mwezi mmoja.

Pili Mheshimiwa Waziri ameeleza kuhusu wahudumu wa ngazi ya jamii (CHWs), hata hivyo naomba awaondoe shaka wahudumu waliopo, na hii ni kwa kuzingatia message hii ambayo nimetumiwa na mmoja wa CHWs.

"Habari za kazi! Naomba mnisaidie kwa Wizara ya Afya, Aaziri alitangaza kuwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii watatangaza kwa vijana waliofika kidato cha nne, na watawalipa. Sasa wahudumu waliojitolea tangu mwaka 1986 na wapo je, hawa Wizara inawafanyia nini inapowastaafisha, mimi mwenyewe nimefanya tangu 1992 kwa kujitolea, na Wilaya ya Mufindi wapo kila Kijiji."

Mheshimiwa Spika, nadhani ipo sababu ya kuwaondoa shaka hawa waliopo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwapongeza Wizara kwa kazi nzuri lakini kubwa kwa ushirikishwaji wa sisi Wabunge kuanzia ngazi ya Wizara mpaka Mameneja wa RUWASA Mikoa na Wilaya na pia kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji. Tunaona team work na kwa mwendo huu sekta hii itaendelea kuimarika, tuendelee ushirikishaji wa sisi Wabunge, lakini pia katika ngazi za Wilaya kwa maAna ya Halmashauri, Madiwani na Ofisi za ma-DC wote wawe wanaelewa katika maeneo yao kuna miradi gani, itatekelezwa kwa namna gani na kwa muda gani. Hii itatusaidia kuwa wamoja. Na kwa kuwa tunatekeleza Ilani ya CCM basi ni muhimu sana viongozi wa chama katika maeneo ambako mradi unatekelezwa kuwa na ufahamu kwa maana ya ownership, vivyo hivyo viongozi wa ngazi za chini kwa maana ya Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji. Nasema hivi kwa sababu kazi kubwa inafanyika, kwa hiyo, tusipokuwa na muunganiko wa taarifa hakika watu wengi na hasa wapotoshaji watazungumza tofauti.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi wa Miji 28 Mafinga; tunashukuru sana kazi imeanza japo wananchi wanatamani sana kuona physical works kama uchimbwaji wa mitaro na kadhalika. Tunawaelimisha kuwa mradi huu ni miezi 20 na kwamba ni design and construction, tunawafafanulia.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, matarajio ya wananchi ni kwamba mradi huu ni mkombozi wa kero ya maji, lakini kwa upande mwingine, scope ya utekelezaji kwa maana ya distribution ni kilometa 20 tu. Kwa ukuaji wa Mji wa Mafinga kutokana na viwanda vya mazao ya misitu, nashauri Serikali ianze kufikiria awamu ya pili ya mradi ambayo itajielekeza katika ujenzi wa matanki na usambazaji, nawapongeza timu yangu ya MAUWASA wanajituma sana hasa katika kuwasiliana na Wizara kuhusu fursa mbalimbali zinazojitokeza. Mradi huu wa miji 28 ni mkubwa sana, haitaleta picha nzuri ikiwa baada ya kukamilika maeneo mengi ya mji yafikiwe na huduma, sote tunatambua ambavyo signing ceremony sio tu ilihudhuriwa na Mheshimiwa Rais, lakini pia wananchi walishuhudia live, na hivyo wamejenga matumaini makubwa sana, lakini wanaposikia kuwa kuna maeneo mradi hautafika inawakatisha tamaa, ndio maana nashauri mapema, tuanze kuona kwa namna gani tutapata phase two kama mwendelezo wa mradi huu.

Mheshimiwa Spika, nafahamu kuimarisha chanzo ndio jambo kubwa, distribution na matanki sio kazi kubwa sana, tukitengewa around shilingi bilioni 10 yaani bilioni kumi kuanzia mwaka ujao wa fedha, tutaweza kufikisha maji eneo kubwa la mji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu RUWASA; nawapongeza kwa maeneo ya vijijini, hata hivyo kilio kikubwa ni kukamilisha Mradi wa Matanana na Itimbo ambao ni wa visima, lakini kilio zaidi ni Kijiji cha Kisada, nilitaraji kuwa kitakuwepo katika mpango wa mwaka wa fedha ujao, lakini sijaona Kisada kwa hiyo naomba iwepo, lakini la pili pamoja na kuwa RUWASA ipo kiwilaya. Nashauri miradi kati ya Halmashauri mbili isichaganywe, kwa mfano kuweka vijiji vya Mafinga TC katika orodha ya vijiji vya Mufindi DC inaleta mkanganyiko, na hili lilishajitokeza mwaka jana, mradi wangu wa Kitelwasi Ugute ukaachwa kwa kile kilichotajwa kama oversight, hivyo ushauri wangu tupange mipango kwa kuzingatia kijiji kipo Halmashauri gani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maandalizi ya hotuba nzuri, lakini zaidi kwa kuwa open minded, nimepata wasaa wa kuzungumza na Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu kuhusu sekta ya misitu na kwa kweli walinisikiliza na kupokea mawazo yangu.

Mheshimiwa Spika, sekta ya misitu ni mtambuka kwa kiasi fulani, jana tumepitisha bajeti ya Wizara ya Nishati, moja ya mkakati wao ni kufikisha umeme vitongoji 15 kwa kila jimbo, lakini pia kuna miradi ya REA III, Awamu ya Pili, miradi ya ujazilizi wao wanaita 2A, 2B,2C na kadhalika na miradi ya TANESCO, yote hii inategemea kwa sehemu kutumia nguzo zinazotoka katika sekta ya misitu, lakini pia ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali kuanzia majengo ya shule, zahanati, vituo vya afya na hospital za wilaya, ujenzi wake kwa sehemu unatumia mazao ya misitu kuanzia milunda, mbao, plywood na kadhalika. Hata Mji wa Serikali Mtumba, majengo mengi kama sio yote yanatumia bidhaa zinazotokana na misitu.

Kwa hiyo, sekta hii ni muhimu sana katika kuchangia pato la Taifa, hata takwimu kwamba sekta hii inachangia 3% sio sahihi kwa sababu takwimu hii inaangalia tu mti/gogo, mara baada ya kuvunwa, bidhaa inayofuatia inaonekana sio msitu tena. Kwa hiyo, kwa ufupi sekta hii ni muhimu na tuendelee kuitizama na hasa katika suala zima la EWP, nashauri kongamano tulilofanya mwaka 2021 tuendelee nalo kila mwaka kwa nia ya kunyanyua sekta hii na hasa suala zima la EWP.

Mheshimiwa Spika, kuhusu REGROW mradi huu ambao ni mkopo wa Benki ya Dunia umekuwa unatekelezwa kwa kusuasua sana, huu ndio ukweli, mradi huu ukitekelezwa kwa kasi utasaidia sana kukuza utalii Kusini, utaboresha mazingira ya utalii na hivyo kuvutia wawekezaji zaidi. Mheshimiwa Rais ametufanyia kazi kubwa katika kututangazia utalii kupitia Royal Tour, kwa hiyo REGROW itasaidia sana kuendana na kasi ya kuongezeka kwa watalii.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mmoja wa watu ambao nimeusemea sana mradi huu, nashauri tuongeze kasi ya kuutekeleza, ninaamini kwa kasi ambayo Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu wake walionesha kwenye sekta ya michezo, wataitumia kusukuma mradi huu, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba mzigo mzito mtwishe Mndengereko, basi mimi namtwisha mzigo huu ili twende kwa kasi.

Mheshimiwa Spika, ndege ndogo; kuna gharama kubwa sana ya usafiri wa anga kutembelea mbuga zetu, ushauri, kaeni ndani ya Serikali tupate ndege za ability ya kati ya watu nane hadi 14 ambazo zitaweza kutua mbugani, na hizi ziwe za ATC, kwa kuanza hata mbili zitafaa kuwa zina shuttle kati ya Dar es Salaam, KIA na mbuga zetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, napenda kupongeza hotuba ya Wizara na kwa ujumla wanavyofanya kazi kwa ushirikishwaji, napongeza sana hili linaloendelea la kuhuisha mitaala na sera, ushiriki mpana wa wadau bila shaka utasaidia kupata mawazo mapana ambayo hatimaye tutapata kile tunachokusudia.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia Watendaji wa Bodi ya Mikopo kuanzia Meneja wa hapa Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Bodi Ndugu Badru na wasaidizi wake, wamekuwa msaada sana hasa wakati wa changamoto za mikopo, wapo watoto wa wapiga kura wetu wakiwa na changamoto kwa kweli watu wa Bodi ya Mikopo wako very cooperative katika kutusaidia nini cha kufanya, nawashukuru, nawapongeza na endeleeni na moyo huo huo wa kuwa solution oriented.

Mheshimiwa Spika, sasa katika vyuo, baada ya mtoto kupata mkopo kumekuwa na changamoto, mara fedha hazijaingia au zitaingia kwa awamu, nashauri vyuoni, vitengo vinavyohusika na disbursement ya funds kuwafikia wanafunzi vifanye kazi kwa speed kama wanavyofanya Bodi.

Pili, nawapongeza kwa ujenzi wa Vyuo vya VETA, hata hivyo nina ushauri na maombi maalum kwa ajili ya Halmashauri ya Mji Mafinga.

Mheshimiwa Spika, eneo hili linakua kwa kasi na hii ni kutokana na sekta ya mazao ya misitu, nafahamu kwamba kunajengwa Chuo cha VETA Mufindi, hata hivyo kwa ombi maalum, naomba katika mpango ujao kujumuisha Mafinga TC kutokana na umuhimu wake hasa kwa kuwa ni centre ya uzalishaji wa mazao ya misitu.

Kuhusu elimu ya awali; nafahamu kuna muingiliano wa majukumu katika baadhi ya maeneo ya usimamizi wa elimu kati ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI, hata hivyo kuimarika au kuporomoka kwa elimu, mwenye dhamana ni Wizara ya Elimu, kwa sababu hiyo bado tunao wajibu wa kuyatazama kwa macho mawili baadhi ya maeneo hasa eneo la elimu ya awali. Kwa mfano, kwa ufahamu wangu ukiacha courses za early childhood katika baadhi ya vyuo vikuu, kuna vyuo maarufu kwa muundo wa ki-montesory ambavyo ni mahususi kuwaandaa walimu wa kufundisha watoto wadogo. Lakini kama Serikali tunapoajiri walimu ni nadra kabisa kuona ajira mahsusi kwa ajili ya walimu wa kufundisha watoto wadogo kwa maana ya madaraja ya awali.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu tusichukulie elimu ya awali kama ziada bali tuchukulie kuwa ndio msingi wa kuanza kumjenga mtoto kujiamini, kujitambua, kushirikiana na wenzake na hivyo kumjengea msingi wa kuanza kuwa raia bora na mwema.

Mheshimiwa Spika, kuna kama woga wa ku-declare kuwa elimu ya awali itambulike kama sehemu ya elimu ya msingi na izingatiwe na kupewa uzito katika mipango yetu kama Taifa. Ushauri wangu, tusitawaliwe na woga wa gharama na tukumbuke kauli ya Mwalimu if you think education is expensive, try ignorance. Kwa hiyo, kama tumefikia hatua ya kuhuisha mtaala na sera, ni muhimu kuifanya elimu ya awali kuwa ni jumuishi. Tusiogope maana wakati ni sasa.

Mheshimiwa Spika, wakati tunaendelea na mijadala na mashauriano kuhusu kuhuisha mitaala na sera yetu, ni muhimu tukawa makini hasa katika kuangalia wapi tulikosea na wapi tuparekebishe na kwa kiwango gani. Nasema hivi kwa sababu wapo baadhi yetu ambao tunaona kama mfumo wetu umefeli kabisa which is not, mfumo huu umewezesha baadhi ya Watanzania kufanya kazi duniani kote, wapo madaktari wanaofanya kazi nchi za Kusini mwa Afrika na wanategemewa, wapo wahadhiri wanafanya kazi katika vyuo mbalimbali duniani, lakini pia vijana wetu wanaosoma katika mfumo wa elimu yetu wanapata udahili katika vyuo mbalimbali duniani iwe ni Amerika, Ulaya, Asia, Arabuni na kadhalika hawajawahi kukataliwa kwa hoja kwamba mfumo wa elimu yetu ni mbovu au haukidhi vigezo vya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapofanya mapitio haya tusije tukafikia hatua kuona kama vile mfumo wetu wa elimu uliopo ni kama haufai, ni zero; hapana, lazima tujivunie mfumo wetu ulikotutoa mpaka hapa tulipo, na kwa hiyo tufanyie marekebisho baadhi ya maeneo muhimu na kwa uzito wake.

Mheshimiwa Spika, mwisho nimekuwa nikijiuliza, hivi hatuwezi kuja na utaratibu wa kidato cha tano kuanza mapema kuliko ilivyo sasa ambapo kijana anamaliza shule kwa maana ya kidato cha nne Novemba, kwenda kidato cha tano anasubiri mpaka Julai jambo ambalo ni risk sana hasa kwa watoto wa kike kukaa idle miezi almost sita. Kwa kuwa kuna maendeleo ambayo yamewezesha matokeo kutoka mapema, je, hatuoni ni wakati sasa watoto wanaojiunga kidato cha tano kuanza mapema kadri wataalam watakavyolidadavua. Nafahamu linaweza kuleta ukakasi na kuvurugika kwa mihula ya shule/vyuo lakini kwa kuwa tuna wataalam tujaribu kuwaza nje ya box kuona kama linaweza kufanyika.
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa kazi nzuri lakini zaidi ushirikiano kuanzia Wizarani hadi watu wa Mfuko wa Mawasiliano na TCRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafinga tumekuwa wanufaika wa TCRA, wameshatusaidia katika shule ya msingi mchanganyiko ya Makalala yenye watoto wenye mahitaji maalum na pia shule ya sekondari Luganga tumeshapata vitendea kazi kutoka TCRA. Lakini pia nimeona kwenye bajeti Kata za Wambi na Bumilayinga zitapata minara. Ni kata muhimu kwa sababu Wambi ndipo yapo Makao Makuu ya Halmashauri na Bumilayinga tumejenga Kituo cha Afya, hivyo ni muhimu kupata mawasiliano. Aidha, TTCL wamekamilisha mnara katika Kijiji cha Itimbo, bado kuwasha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nina maombi TCRA kwa ajili ya shule mpya ya sekondari ya Upendo ili tuwasaidie vitendea kazi vya TEHAMA.

Pia ninashauri kulitizama kwa ukaribu Shirika la Magazeti ya Serikali kwa kuwawezesha mtambo ili waweze kuchapa magazeti yao kwa rangi na hivyo kuwawezesha kushindana katika soko. Aidha, Managingi Editor anakaimu nadhani toka ambaye sasa ni Katibu Mkuu aondoke, Bi. Tuma Abdallah amekulia TSN, nadhani ni wakati sasa kumthibitisha ili kumpa morali na ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TBC Radio, wananchi wa Mafinga wanatamani mno kupata matangazo ya TBC lakini inasikika kwa taabu mno, hata redio nyingine hazisikiki, wananchi wa mji huu wa kibiashara kutokana na biashara ya mazao ya misitu wanaomba basi hata redio nyingine zisikike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC Tv kwa kweli kazi nzuri, ubunifu wa hali ya juu wa vipindi, nawapongeza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nawapongeza Waziri na timu yake kwa bajeti ambayo imefafanuliwa vema sana. Nina mawazo ambayo naomba kuyawasilisha kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, nianze na EPC+F; napongeza hatua hii ambayo kwa mujibu wa hotuba ya Waziri mikataba itasainiwa kabla ya mwezi Juni. Jambo hili linaonekana kama ndoto na wananchi wamekuwa bado gizani, nadhani wataamini pale watakapoona kweli mkataba unasainiwa. Hizi ndio feelings za wananchi wanaosubiri kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Mafinga - Mgololo.

Mheshimiwa Spika, tunachokifanya ni maendeleo lakini pia ni kujenga na kuimarisha siasa na uelewa wa wananchi. Wananchi wakiwa na mashaka ni muhimu Serikali kuwaondolea mashaka, tunaita political management kwamba hiki kilichoandikwa ndicho kitakachotendeka. Nasema hivi kwa sababu kwa uelewa wa wananchi kutokana na Bajeti ya Ujenzi hii tunayoendelea nayo kwa maana ya mwaka 2022/2023, matarajio yao ni kwamba ujenzi ulikuwa unaanza mwaka huu, kwa hiyo wanaposikia kwamba mkataba wa EPC+F utasainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, wanatuambia mbona kila mwaka mnaitaja tu hii barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo na kwa kuwa siasa ni perception, nashauri shughuli ya kusaini mikataba na wakandarasi iwe shughuli nzito ili kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali yao. Barabara hii imesubiriwa miaka mingi, ni ukombozi kwa uchumi wa Mufindi, Iringa na Taifa kwa ujumla hasa kutokana na umuhimu wa mazao ya misitu na zao la parachichi.

Mheshimiwa Spika, nashauri shughuli iwe shirikishi kwa maana ya Chama, Serikali na Halmashauri (Madiwani) washiriki katika signing ceremonies.

Mheshimiwa Spika suala la pili ni ufafanuzi, wananchi wanafuatilia sana hizi hotuba katika mitandao, wanauliza kuwa hii barabara Kasma 4037 imeandikwa kilometa 78 na imetengewa shilingi 50.00? (ukurasa wa 248), na kwamba chanzo cha fedha ni GoT kwa maana Serikali ya Tanzania, na mbona kwenye hotuba Waziri ametaja hiyo EPC+F, je, kipi ni kipi, nami nauliza kwa lugha ya wananchi.

Mheshimiwa Spika ushauri wangu, kwa kuwa jambo hili ni geni na ili kuwapa wananchi comfort na uelewa Mheshimiwa Waziri anapojumuisha atolee ufafanuzi ni nini hii EPC+F. Ni muhimu sana wananchi kuelewa na sehemu sahihi ya kueleweshwa ni wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ATCL; napongeza jitihada za Serikali kununua ndege na hasa ya mizigo. Hata hivyo nina ushauri kuhusu ATCL hasa katika suala la delays na kukosekana kwa connections. Ilivyo kama unatoka Dodoma kwenda Mbeya lazima ukate tiketi mbili, yaani Dodoma-Dar, kisha Dar-Mbeya. Nimeshauri suala hili mara kadhaa, sasa sijui ni masuala ya kitaalam au ni kitu gani. Kwa nini tusiwe na connecting routes?

Mheshimiwa Spika, nimeshauri pia mara kadhaa kwamba pawepo na routes za kuanzia Dodoma kwenda pande kuu za nchi hata kama itakuwa kupitia Dar. Kwa mfano kwa nini tusiwe na routes Dodoma to KIA, Dodoma to Mbeya, Dodoma to Mtwara via Dar. Dodoma to Mwanza na Dodoma to Kigoma via Tabora. Ikiwa juzi tumezindua Ikulu yetu maana yake ni kwamba sasa Dodoma ni real capital city ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nashauri pia ili kuendana na kasi ya kupokea watalii kama matokeo ya Royal Tour, tufikirie kuwa na ndege ambazo zitakuwa zinabeba abiria kwenda kwenye mbuga za wanyama. Tukiwa na ndege za kubeba abiria kati ya nane hadi 14, zitabeba watalii kutoka KIA to Manyara, Serengeti, Mikumi, Ruaha na kadhalika. Tukiwa na ndege za aina hiyo zitasaidia kupunguza gharama za kufikisha watalii mbugani lakini pia watafika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, taa za barabara katika Mji wa Mafinga; naomba kukumbusha uwekaji wa taa za barabarani kando ya barabara ya TANZAM eneo la Mafinga Mjini hasa Kinyanambo hadi Hospitali ya Mafinga. Suala hili linakumbushwa sana na wananchi kwa kuwa hata wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais lilizungumzwa na Mheshimiwa Waziri mbele ya wananchi na mbele ya Mheshimiwa Rais alieleza umma wa Wana-Mafinga kwamba kutawekwa taa za barabarani umbali wa kilometa mbili, naona mwaka wa fedha uko mwishoni na taa hizi bado hatujaanza kujenga. Ni ombi langu kwa niaba ya wananachi wa Mafinga kutekeleza ahadi hii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara Iringa-Msembe; barabara hii ambayo ni kiungo muhimu katika biashara ya utalii, katika bajeti hii ya mwaka 2022/2023 kwa uelewa wa wananchi na sisi Wana-Iringa ni kwamba inaanza kujengwa mwaka huu, hata hivyo nimeona kwamba huenda ikatangazwa mwezi Juni, kwa wananchi wanashindwa kuelewa na hata mimi nilitarajia kwamba tutakuwa tumeanza kujenga au walau mkataba kuwa umeshasainiwa. Kwa hiyo, rai yangu ufafanuzi ufanyike, kwa sababu uelewa ni kwamba hata hii kutangaza mwaka huu pengine ujenzi hautaanza mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuboresha utendaji wa bandari kupitia mwekezaji; kwanza nawapongeza sana bandari kwa ubunifu, lakini zaidi kwa ushirikishwaji. Sisi Wabunge tumepata semina kuhusu nini kinakusudiwa kufanyika na kitakuwa na manufaa gani kwa nchi yetu. Yapo mashaka na maoni tofauti, tuyapokee lakini kama Taifa lazima tuamue kwenda mbele, haiwezekani tuendelee kuchekwa na nchi majirani kwamba tumekalia uchumi. Tuamue sasa, twende mbele.

Mheshimiwa Spika, mimi kwa bahati nzuri nimetembea duniani nikiwa mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje, mfano mdogo nchi ndogo kwa eneo kama Singapore, bandari yao inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na ni chanzo cha mapato kwa nchi yao. Katika kufanya maamuzi tukishajiridhisha ni kwa manufaa ya Taifa letu, basi mengineyo tuweke pamba masikio, tufanye maamuzi sasa, tusirudi nyuma.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia siku ya leo katika Wizara yetu. Nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ambaye ndiye Amir Jeshi Mkuu wa Taifa letu na mara kadhaa nimesema hapa Mheshimiwa Rais kama mwanadiplomasia namba moja amekuwa akiitendea haki nafasi yake kwa sababu tumeendelea kuwa Taifa ambalo linaaminika katika ulinzi wa amani duniani, katika ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali za kiafrika. Hii ni kutokana na kazi nzuri ambazo Mheshimiwa Rais anazifanya kuendelea kutuheshimisha katika Jumuiya ya kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kama jina lake lilivyo Innocent yuko very innocent, msikivu na Kamati tunafanya nae kazi vizuri sana pamoja na Katibu Mkuu Faraji Mnyepe na viongozi wa Jeshi kwa maana Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Salum Haji Othuman ambae mara nyingi tumekuwa nae kwenye vikao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiona nchi imetulia kama alivyosema Mheshimiwa Ngasa, tunafanya shughuli zetu, tunashiriki kazi za Bunge, wakulima wanaenda mashambani, wananchi wangu Mafinga wanaenda kuchana mbao na kadhalika, maana yake wako watu hawalali usingizi. Kati ya watu ambao hawalali usingizi ni pamoja na wenzetu wa Jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwa namwambia mtu, ukimwona Mwanajeshi vyovyote alivyo wewe mheshimu tu, awe na maji ya kunde kama mimi, kimo cha kati kama mimi vyovyote alivyo mheshimu tu, kwa sababu wanafanya kazi ya kutukuka ya kukesha. Sisi hatuwezi kujua tutakwenda huko masokoni, tutakwenda kunywa soda na kadhalika, tutakwenda kwenye ibada tutakwenda kufanya kila kitu lakini kuna watu ambao wanakesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hii kama alivyosema Mheshimiwa Fakharia, kazi ambayo imefanyika pale Ikulu ni mojawapo wa mfano kwamba, vyombo vyetu vikiaminiwa na kuwezeshwa vinaweza vikafanya maajabu makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe ushauri ambao nimetoa nadhani kama mara tatu mfululizo. Kama ambavyo umeona ile kazi ya Ikulu ya kuheshimisha, nenda Chita utaenda kuona maajabu, kwa wale ambao wamefika wanaweza kujionea jinsi ambavyo kilimo cha mpunga kinafanyika kwa weledi mkubwa sana. Ndiyo maana mara nyingi nashauri na nimesema hata mwaka jana, hii nchi yetu mimi nilisikitika na lazima niseme ukweli, Waziri wa Viwanda na Biashara anatoa vibali tuagize mchele tani 90,000 Tanzania, kuna vitu Hapana! Sasa, namna ya kusema hapana ni nini? Tuwekeze JKT, nilisema mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwezesheni JKT na kupitia SUMA JKT, wape target tu miaka miwili uone kama utaagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi hii, uone kama utatoa vibali vya kuagiza mchele kutoka nje. Tumefanya mambo mangapi kwa majaribio? Hebu tufumbe macho tukipe mkopo, tukiwezeshe, tuone maajabu.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Cosato Chumi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Felista Njau.

TAARIFA

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka nimpe mchangiaji taarifa kwamba kwa ukosefu wa fedha JKT wana hekari 12,500 lakini mwaka huu imekuwa ni pori na miundombinu iko ardhini, kwa hiyo wamekosa fedha wangekuwa na fedha wangeweza kwenda mbele. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Cosato Chumi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili na huyu kama Mjumbe wa Kamati nadhani amenielewa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachotaka niseme ni nini? Kama Taifa kijiografia tunayo nafasi ya kunufaika na kuneemeka kutokana na geographical position, sasa miongoni mwa watu wanaoweza kutusaidia ni hivi vyombo, lakini hawawezi kutusaidia kama hatuviwezeshi ipasavyo. Ushauri wangu ni kwamba tuviwezeshe hivi vyombo na tuwape fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili na hili napenda kwa dhati ya moyo wangu nikushukuru wewe binafsi. Mimi na baadhi ya wenzangu tulienda JKT mwaka jana, hapa ndipo ambapo nataka nitoe ushauri na nisisitize. Kumekuwepo nafasi haba za vijana kwenda JKT wanaomaliza Kidato cha Sita, mara nyingi pengine kwa kukosa uelewa tunaona kama vile JKT imewanyima nafasi vijana, Hapana! Hawana vitendeakazi, hawana facilities. Kwa hiyo, nashauri Wizara ya Fedha tuwawezeshe JKT wajenge mahanga ya kutosha ili kusudi vijana wengi waende JKT.

Mheshimiwa Spika, zamani nilidhani JKT ni maguvu tu, lakini tulienda pale unakaa darasni wakati mwingine mpaka saa nne usiku, unafundishwa uzalendo, kuna vitu vingi. Kwa nafasi hii ninashauri na pengine ushauri huu unaweza usipokelewe vizuri sana, hata Watumishi wa Umma wanapoajiriwa kama ambavyo tunafanya semina elekezi, waende JKT hata mwezi mmoja. mimi nakwambia tutaona mabadiliko makubwa sana katika nchi yetu, kwa maana ya mindset, tabia, utendaji na uzalendo kwa ujumla. Simaanishi waliopo kwamba siyo wazalendo lakini itawaongezea uzalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia yapo mambo mawili. Jana tumejadili Wizara ya Uchukuzi hapa na tumesema mambo muhimu ambayo tunatakiwa tufanye katika kuboresha bandari yetu. Wenzetu hawa wakileta vifaa tayari wamekwisha jenga bonded warehouse, tunaomba na tunaishauri Serikali waruhusiwe wakishachukua vifaa vyao vya Jeshi wakavihifadhi kwenye bonded warehouse wakati taratibu zingine zinaendelea, tusivi – expose pale.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni la kisheria, tuniomba Serikali ilete sheria ili kusidi vile vifaa vya wenzetu visitozwe kodi. Kwa sababu kama alivyosema Mheshimiwa Zahor, ukisema tu ni military equipment mwingine anadhani ni vile vifaru tu hata buti ni kifaa cha Jeshi. Kwa hiyo, niombe sana kama naeleweka hii tuone haya mambo mawili. Moja, hili la kwanza nadhani ni administrative tu kwamba bonded warehouse zao wanazo zitumike kuhifadhia vifaa vyao na hilo la TRA.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni la wastaafu. Mimi napokea maombi kutoka Mafinga, sasa kidogo inanichanganya maana ni Mjumbe wa Kamati, nimepokea recently wakati tumeshamaliza Vikao vya Kamati, nikiwauliza wastaafu waliokuwa Wanajeshi kwanza wanaomba kwamba ile pensheni yao wanadhani kwa kuwa walistaafu wakiwa katika vyeo vya chini na wengine walilazimika kustaafu labda kutokana na maradhi kwa hiyo ile pesheni yao ni nyembamba kidogo. Kwa hiyo, wana ombi Serikali iwaangalie wastaafu pia kuwafikishia kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia niliona hapa timu ya JKT, imepanda Ligi Kuu, mimi ni mwanamichezo nampongeza sana Kocha Ndugu Malale Hamsini pia na JKT Queen ya wanawake Kocha Ali Ali kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana, naunga mkono hoja na Mungu akubariki sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwapongeza Wizara kwa hotuba, lakini pia kwa ushirikishwaji, tulipata semina kama Bunge, lakini mimi binafsi kama mmoja wa Wabunge ambao Halmashauri zetu zitanufaika na Mradi wa Kuboresha Umiliki wa Ardhi maarufu kama hakimiliki salama, nilishiriki pia katika semina ya kujengewa uwezo kuhusu mradi huu. Napongeza pia uwepo wa banda la Wizara hapa Bungeni, imekuwa ni fursa nzuri kupata huduma binafsi lakini pia kupata huduma kwa niaba ya wananchi na hata ndugu, jamaa na marafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masuala machache ya kuchangia kama ifuatavyo; kwanza ni kuhusu Mradi wa Miliki Salama; nilipohudhuria semina ya kwanza kuhusu mradi huu, niliona hoja kutoka kwa Wajumbe wa Kamati kwamba fedha nyingi inaenda kwenye masuala ambayo it is more of administrative badala ya kupanga, kupima na kumilikisha maeneo mengi zaidi, kwamba ujenzi wa majengo, uimarishaji wa mifumo na kadhalika sio masuala ya muhimu kuliko kupima vijiji vingi zaidi na kutoa hati nyingi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo napongeza kwamba sasa vijiji vimeongezeka kutoka 250 hadi 500 na pia hati na leseni za makazi kutoka laki tano hadi milioni moja kwa kila kipengele. Kwa hiyo, yapo maeneo ambayo mawazo yamezingatiwa. Hata hivyo bado kuna maoni na malalamiko kwamba ilibidi tuongeze zaidi eneo la kupimwa, maoni ni kwamba kwa nini fedha nyingi ziende kwenye majengo na kuimarisha mifumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, suala hili ni muhimu sana, ujenzi wa ofisi na kuimarisha mifumo utakuwa ni jambo la kudumu, itatumika kwa ajili ya mradi na pia hata baada ya mradi kukamilika majengo kwa maana ya ofisi na mifumo itaendelea kutumika, kwa hiyo ni wajibu wa Serikali kufanya ushirikishwaji kuanzia ngazi za Mitaa/Vijiji, Kata na Halmashauri ili kuleta uelewa wa pamoja na ownership ya mradi. Nafahamu kwamba kutafanyika vikao kuanzia ngazi ya CMT katika Halmashauri, lakini nashauri kuwashirikisha Waheshimiwa Madiwani katika kila ngazi. Vikao vya ngazi za chini katika Mitaa/Vijiji, ni muhimu ushiriki wa Madiwani uwepo. Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo pamoja na kuwa jambo hili ni la Serikali, nashauri ushirikishwaji wa viongozi wa CCM kama observers, kwa mfano katika vikao vya ngazi ya Halmashauri kwa maana ya Madiwani ni muhimu Mwenyekiti na Katibu wa Chama katika Wilaya/Halmashauri husika wakaalikwa kama watazamaji ili tu kujua from the horses mouth maana na faida ya mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia kupunguza upotoshwaji katika level zote. Kuhusu gharama za ujenzi wa majengo ya ofisi na kuimarisha mifumo, nadhani ni suala ambalo Wizara inabidi ifafanue kwamba huu ni msingi imara katika kuboresha na kuimarisha sekta ya ardhi kama sehemu ya kufikia hatua sio tu ya kumaliza migogoro, lakini pia kuhakikisha mipango ya matumizi bora ya ardhi inakuwa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango kabambe katika Mji wa Mafinga/industrial park; kama ilivyoelezwa katika ukurasa wa 37, Mji wa Mafinga uko katika hatua za mwisho kukamilishwa, nashauri na kupendekeza jambo hili ambalo mimi binafsi nimelisukuma sana toka nilipochaguliwa mara ya kwanza mwaka 2015 wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Mipango Miji Profesa Lupala, kwa kushirikiana na Ndugu Mahenge na Dean of Students wa Chuo Kikuu cha Ardhi tulianza kushirikiana na Wizara katika hatua za mwanzo za kukusanya data. Ninaomba Wizara itusaidie tukamilishe suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili ninaomba Wizara kama ambavyo imekuwa ikiniahidi katika mazungumzo ya siyo rasmi na viongozi wa Wizara, tusaidiwe kukamilisha ndoto ya Wana-Mafinga kuwa na industrial park, tayari tuna eneo tumetenga ekari 750 kwa ajili ya industrial park na mara kadhaa tumezungumza na Kamishna Mathew juu ya jambo hili. Namshukuru Kamishna Mtui tulianza naye lakini pia hata alipokuja Kamishna Minja amelipokea vizuri sana. Ushauri wangu, kama ni kwa utaratibu wa revolving fund au kwa namna Wizara itakavyoona inafaa basi tulitekeleze suala hili kwa kuzingatia kuwa kuna potential kubwa ya viwanda vya mazao ya misitu, na kama sehemu ya jitihada za kufanikisha suala hili, wenzetu wa EPZA walitembelea kuona potential hiyo na hasa kwa kuzingatia pia kuwa tupo kando ya highway ya TANZAM ambayo ni kiungo muhimu sana katika biashara kati ya Tanzania na nchi za SADC na hasa DRC, hivyo industrial park inaweza pia ikatumika kama logistics center.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Wizara tulipe suala hili uzito. Huko kwingine mnakosema kuwa fedha za revolving fund zimetumika sivyo, it won't be in Mafinga.

Kuhusu Baraza la Ardhi Mufindi, wanasema haki iliyocheleshwa ni sawa na haki iliyokoseshwa, wananchi wa Mafinga/Mufindi kilio chao ni huduma ya Baraza la Ardhi, issue ilikuwa ni majengo na sasa issue naambiwa wajumbe wameshapatikana, tatizo ni Mwenyekiti. Kwa hiyo, wananchi wanalazimika kwenda Iringa Mjini, naomba na nashauri tupate Baraza la Ardhi kwa ajili ya wananchi wa Mafinga/Mufindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuipongeza Wizara kwa ushirikiano wao mzuri na pia kwa kusogeza huduma hasa za Taasisi kama vile REA na TANESCO hapa Bungeni, hii imetusaidia sana Wabunge kupata ufafanuzi wa papo kwa papo katika masuala ya majimbo yetu.

Mheshimiwa Spika, nina masuala mawili tu; moja ni kuhusu bei hasa maeneo ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji yanasomeka kuwa yapo mjini, lakini uhalisia wa maisha na kipato ni maisha ya kijijini. Kwa mfano Halmashauri ya Mji wa Mafinga, ni mji lakini ina vijiji kumi na moja rasmi katika kata tatu. Lakini pia yapo maeneo ya pembeni mwa mji ambako maisha na kipato ni ya kijijini. Mfano wa maeneo haya ni mengi, hapa Dodoma ni Jiji lakini katika kata 41 ni kata kama 20 tu ndizo maisha ya mjini, kata nyingine 21 maisha na kipato ni ya kijijini. Kwa sababu hiyo mara kadhaa kupitia maswali na majibu nimeshauri kwamba tutizame upya bei ile ya shilingi 340,000 ndani ya mita 30.

Mheshimiwa Spika, nafahamu kwa maeneo ya vijiji yanayohudumiwa na REA bei ni shilingi 27,000. Naomba nieleweke vema, simaanishi kwamba maeneo ya vijiji lakini ambayo kwa mujibu wa sheria yanasomeka kuwa ni miji yatozwe shilingi 27,000, hapana, ushauri wangu ni kwamba tuwe na makundi kwa mfano ziwepo bei tofauti tofauti, tunaweza kusema kwa mfano maeneo ya pembezoni ya mji ikawa Kundi A bei shilingi 150,000; Kundi B ikawa ni vijiji ambavyo kwa mujibu wa sheria viko mjini lakini kimaisha na kipato ni kijiji, mfano pale Mafinga maeneo kama Ndolezi, Luganga, Mkanzaule na kadhalika maisha yao ni kijiji, kundi hili tukasema walipe shilingi 97,000.

Mheshimiwa Spika, hizi bei ni mfano tu lakini ninyi kupitia wataalam wenu mnaweza kuchakata mkaona namna bora ya kulifanikisha suala hili ambalo kwa mujibu wa majibu hapa Bungeni, mara kadhaa tumeelezwa na Wizara kwamba suala hili liko katika hatua za mwisho za kufanyiwa kazi. Naomba kama litawezekana basi tupate majibu kamilifu na kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni kuhusu nguzo; Kamati ya kupitia sekta ya uzalishaji na upatikanaji wa nguzo za umeme; kwanza nawapongeza Serikali kwa ushirikishwaji pale ilipokuja taharuki kwamba Serikali itaanza kuagiza nguzo kutoka nje ya nchi. Tulikaa na Waziri na timu yake pamoja na viongozi wa Serikali na Chama wa Mikoa ya Iringa na Njombe, kikao hiki kilihusisha Waziri, Katibu Mkuu, Kamishna wa Nishati na watendaji wa TANESCO na REA kwa upande wa Wizara na kwa upande wa mikoa ilihusisha Wenyeviti wa CCM wa Mikoa ya Iringa na Njombe na Wenyeviti wa Wilaya zote, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, baadhi ya Waheshimiwa Madiwani na wadau wa sekta kwa mana ya wazalishaji na wasambazaji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uzito wa suala hilo na jinsi ambavyo linagusa maisha ya watu na uchumi wao, ilishauriwa paundwe Kamati ya Wizara na wadau ili kupitia mnyororo mzima wa suala la nguzo kuanzia upatikanaji wake na suala zima la ubora. Kamati hiyo iliundwa kwa nia njema yq kupata muafaka kuhusu suala la nguzo kuhusu upatikanaji, masuala ya manunuzi, ubora na kadhalika. Nia miradi ipate nguzo kwa wakati na kwa ubora na wakati huo huo wananchi waendelee kunufaika kama ilivyo katika suala zima la local content.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu Kamati hiyo ikamilishe kazi yake ili mapendekezo ya Kamati yawafikie wadau na Serikali kwa nia ile njema ya kuhakikisha nguzo zinapatikana kwa wakati na kwa ubora. Bado naamini tunaweza kuzalisha nguzo hapa nchini, kwa hiyo, Kamati hiyo kuhitimisha kazi yake ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, naomba.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi napenda kutumia nafasi hii kwa niaba yangu mwenyewe na kwaniaba ya wananchi wa Mafinga kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa tuzo hii ambayo anaipata, akiwa ni kiongozi wa 12 katika Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuzo hii haitolewei tolewi tu, inatolewa kwa mtu ambaye kwanza amethibitisha dhamira yake katika kuendeleza miundombinu ya usafirishaji, hili si jambo dogo. Miundombinu ya usafirishaji na kuaminika huku kwa Mheshimiwa Rais kwanza kunalijengea taifa letu heshima lakini pia kunalijingea taifa letu kuaminika na kuaminiwa na vyombo vikubwa vya kimataifa duniani. Kama ambavyo tumeona, tuzo hii imetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, na tunafahamu mchango wa Benki ya Maendeleo ya Afrika katika ujenzi wa miundombinu katika taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwakutoa tuzo hii kwa Mheshimiwa Rais wetu si tu kwamba tunaendelea kuaminika katika Benki ya Maendeleo ya Afrika lakini pia tunaendelea kuaminika katika vyombo vingine vya fedha duniani. Kwasababu kama ambavyo tumeona kwenye bajeti yetu juzi kila Mbunge aliyesimama kilio kikubwa kilikuwa ujenzi wa barabara na kikubwa kilikuwa resource hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuaminika na kwa kupata tuzo hii kwa kuheshimishwa kiasi hiki maana yake ni kwamba sasa kama taifa hata tunapoenda kuomba kama ni grants hata kama ni mikopo ya riba nafuu kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya taifa letu tutaweza kuaminiwa na kuaminika. Na hivyo, kwa kujenga miundombinu hiyo maana yake ni kwamba tutaweza kusafirisha bidhaa zetu kwa namna nyepesi, tutaweza kusafirisha mbolea zetu kuwafikia wakulima kwa namna nyepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, itoshe kusema kabisa kwamba kama taifa, kama wabunge na kama Watanzania tujionee sifa kwa kuwa na kiongozi ambaye katika Afrika pekee mwaka huu ameenda kupewa tuzo hiyo. Ninaamini kabisa hata wana-Mafinga hapa ninapozungumza kuna ujenzi wa barabara zinaendelea pale Mafinga ni matokeo ya heshima hii ambayo tumepewa. Kwa hiyo, naunga mkono azimio hili na Mungu ambariki Rais wetu Mungu abariki Taifa letu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nitakuwa na sehemu kama tatu. Kwanza, pongezi; pili, nitazungumzia Baraza la Kiswahili la Taifa; na tatu, soka letu na nne, nitazungumzia uingiaji salama katika Uwanja wa Taifa na mwisho utawala bora katika michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameongeza hamasa katika michezo. Zile shilingi milioni tano, tano alizokuwa anazitoa kwa magoli yanayofungwa kwenye club bingwa na kwenye shirikisho, imeleta heshima sana na ikaleta hamasa kubwa sana. Kwa hiyo, tunampongeza sana na tunapongeza vilabu vyote ambavyo vimeshiriki kimataifa, Simba pamoja na Yanga ambao walituheshimisha kwa kufika fainali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza utajielekeza kwenye Baraza la Kiswahili la Taifa. Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza sana. Tumesema kwamba tutafanya Kiswahili kuwa bidhaa na watu wengi wanadhani kwamba ukijua tu Kiswahili kama hivi ambavyo tunaongea, basi unaweza ukawa Mwalimu wa Kiswahili au mkalimani. Kumbe sivyo, lazima ujifunze Kiswahili kama lugha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka pia kukifanya Kiswahili bidhaa kwa maana ya kwamba kikafundishwe huko nje, lazima pia tujifunze na lugha za mataifa mengine. Kwa hiyo, nawapongeza sana BAKITA, wana kitabu hapa English, Kiswahili na Portuguese cha mtu ambaye anajifunza Kiswahili ambaye ni Mreno. Sasa ili aweze kufundishika vizuri, ndani yake pia kuna sehemu ya Kiingereza. Pia wamekuja na Mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni hatua ya awali, kati na juu. Hii kweli wanathibitisha kwamba BAKITA wapo kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, wana kitabu kinaitwa furahia Kiswahili, Kiswahili kwa wageni. Kwa hiyo, tunaona jitihada ambazo BAKITA wanazifanya katika kuhakikisha kwamba Kiswahili kweli kinakuwa ni bidhaa kama ambavyo tumesema. Sasa nami nitoe wito kwa Wizara ya Elimu na Vyuo Vyetu Vikuu, navyo viwekeze nguvu katika kufundisha siyo tu Kiswahili, lakini kufundisha Kiswahili kama lugha ambayo baadaye inakuwa bidhaa, kufundisha wakalimani wa kutosha, na kufundisha katika namna ile ambayo kweli watu watapata nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tulisikia South Africa wanataka walimu 1,000 lakini huwezi kwenda South Africa kufundisha Kiswahili kwa sababu tu unajua Kiswahili, lazima ujue Kiswahili kama lugha, lazima ujue Kiingereza, lakini ikibidi lazima ujue lugha za wenyeji wa maeneo yale. Kwa hiyo, nawapongeza sana BAKITA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nilisema kwamba suala la pili nitazungumzia kuhusu soka letu. Katika timu nne ambazo zimeingia fainali ya shirikirikisho na fainali ya club bingwa Afrika, Al Ahly wao katika timu yao first eleven walikuwa wana wachezaji wa kigeni watatu tu. Wale Wydad ambao waliwatoa Simba walikuwa na wachezaji wawili tu. Hawa USM Alger, walikuwa na wachezaji wawili tu. Yanga walikuwa na wachezaji wazawa sita. Maana yake ni nini? Hatusemi kwamba vilabu visiwe na wachezaji wa kigeni, lakini hii ni kwa sababu hatuwekezi kwenye soka la vijana kuanzia under seventeen, under twenty, under twenty-three. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ushiriki World Cup au Afcon kila mwaka, uwe na uhakika, ni lazima tuwekeze kwenye soka la vijana. Hapa kuna mambo mawili; kuna Serikali na wadau. Kwa hiyo, Serikali wajibu wake: moja, kujenga miundombinu ya viwanja; pili, kupitia sera za kikodi kuhakikisha kwamba tunapunguza kodi katika vifaa vya michezo. Leo hii ukimpeleka mtoto kama pale Fountain Gate au Magnet au Kambiyaso, ile kit yake tu, kwamba vifaa kwa maana ya viatu, soksi, jezi na mpira wa kuchezea, minimum labda unazungumzia Shilingi laki moja na nusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tuweze kuwa na Timu ya Taifa itakayokuwa shindani, lazima tuwe na wachezaji wazawa wa kutosha, lakini ili tuwe na wazawa wa kutosha, lazima tuwekeze kuanzia hiyo under seventeen na kuendelea. Kwa hiyo, hilo nimeona niliseme vizuri. Kwa hiyo, kuna wajibu wa Serikali na wajibu wa wadau. (Makofi)

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo ni muhimu niliseme ni kuhusu uingiajia wa pale uwanjani. Mmeona juzi tunatoa pole kwa ile familia, lakini lazima tufike wakati tujifunze wakati wa mechi kubwa management ya namna ya kuingia uwanjani iwe ni salama. Haiwezekani mechi inachezwa saa 10.00, unatakiwa uende uwanjani saa 12.00 asubuhi. Tuwekeni utaratibu mwema wa jinsi ya kuingia pale uwanjani.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Cosato, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kapinga.

TAARIFA

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji juu ya uingiaji salama katika Uwanja wetu wa Taifa. Kwa utaratibu wa uwanja ule, una mageti, lakini kwa bahati mbaya sana utaratibu uliozoeleka, mageti yanayofunguliwa ni matatu tu; lile la Simba, lile la Yanga, na lile kubwa, lakini uwanja ule wote umezungukwa na mageti, lakini sasa wananchi wanasongamana kiasi kwamba wanasababisha ile hali inayotokea pale na mauaji.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Cosato, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa sababu inaboresha namna ya kuingia katika uwanja na kwa usalama na kwenda uwanjani isiwe kama kero, isiwe kama adha. Maana yake tunasema kuna kitu Mheshimiwa Jesca huwa anasema afya ya akili. Michezo na burudani ni mojawapo ya tiba nzuri sana ya hiyo mnayoita afya ya akili. Kwa hiyo, mtu kwenda uwanjani ni kutaka kupata entertainment. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema lingine nitazungumzia utawala bora katika soka. Nilisema mwaka 2022, Chama cha Mpira cha Wanawake mpaka leo hawajafanya uchaguzi. Walipofanya uchaguzi, ulivurigika, walisema kwamba wapigakura wamekuwa wengi, wakasema watafanya baada ya miezi mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, wewe kama mama kwa kukosekana ule uchaguzi maana yake tunakosa uwakilishi wa wanawake kwenye Kamati ya Utendaji wa TFF. Kwa hiyo, nawaomba Baraza la Michezo, Msajili wa Vyama za Michezo na Wizara kwa ujumla, jambo hili ni muhimu. Kama tunazungumzia kunyanyua wanawake, na timu zetu za wanawake zinafanya vizuri, tufanye uchaguzi wa chama cha soka cha wanawake hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuwapongeza kwa hotuba ya bajeti ambayo iko well detailed, aidha, nawapongeza kwa ubunifu wa kutuletea maonesho hapa kwenye viwanja vya Bunge. Ilitusaidia sana kupata uelewa sio tu wa masuala ya umeme lakini nishati kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla utendaji wenu kuanzia TANESCO hadi REA ni wa kuvutia na shirikishi. Aidha, kwa niaba ya wananchi wa Mafinga, Mufindi na Mikoa yote ya Iringa na Njombe tunawapongeza na kuwashukuru ambavyo tumeshirikiana katika suala la Serikali kukubali kuendelea kununua nguzo za umeme hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu; ninatambua kwamba ni haki ya kila Mtanzania kufikishiwa umeme. Hata hivyo pamoja na kuwa umeme ni huduma, lakini pia ni biashara, kwa sababu hiyo nashauri baadhi ya maeneo kama Mafinga na Mufindi ambako kuna viwanda vingi tuanze kuelekeza nguvu huko ambako umeme ni biashara ili TANESCO ipate returns ambayo itaenda kugharamia umeme kule ambako wao ni huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri huu ni pamoja na kutufungia transfoma zenye KV kubwa na kuwapa TANESCO bajeti kubwa. Hili linaweza kufanyika kwa kuangalia tu mapato katika maeneo hayo kama Mufindi, mtabaini wazi kwamba TANESCO inapata mapato makubwa, kwa hiyo, hapa tunapopata mapato makubwa tuongezewe nguvu ili mapato yaongezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa muktadha huo nawasilisha maombi ya Mradi wa Ujazilizi kuwa na wigo mpana hasa katika vijiji vya Halmashauri ya Mafinga Mji ambayo administratively ni mji lakini una vijiji kumi na moja, ambapo Kijiji kama Matanana wananchi wana mashine za kuchana mbao lakini wamezifungia ndani kama ambavyo wananchi wa Kata ya Sao Hill ambapo kuna ujenzi wa shule ya sekondari chini ya mradi wa SEQUIP wamefungia ndani mashine zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali iko sawa katika Kijiji cha Ndolezi na pia Mitaa ya Luganga, Mtangani, Majengo mapya katika Kata ya Wambi. Hali hii pia iko katika Mtaa wa Lumwago ambao wanaishi vijana wengi wanaojenga kwa kasi sana, kama ambavyo hali hii ipo Ifingo, Miami na Kijiji cha Rungemba na Itimbo ambako kuna eneo kubwa la viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu hiyo nashauri kwamba densification na bajeti ya TANESCO walau iongezeke kuendana na kasi ya ukuaji wa Mji wa Mafinga na hasa kuelekea katika maeneo ya uzalishaji kwa maana ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa nimeshatuma mchango wangu kwa maandishi, nimewiwa kushauri jambo kuhusu LUKU, je, hatuwezi kutumia mifumo ya kisasa kama tunavyofanya katika huduma za ving'amuzi ambapo ukinunua tu inaji-update yenyewe automatic? Nashauri tuje na mfumo huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nawapongeza Wizara kwa maandalizi ya hotuba nzuri ya bajeti, Mawaziri wa Wizara hii wana bahati ya kuwa na watendaji wenye weledi, namfahamu Katibu Mkuu Dkt. Abbas toka tukiwa naye kwenye media, akiwa newsroom ya Business Times-Majira, kadhalika Ndugu Yakubu ambaye pia amekaa newsroom za kimataifa, Ndugu Singo Mkurugenzi wa Michezo ni mtu open minded, kwa hiyo Wizara ina kila sababu ya kuacha alama (legacy).

Mheshimiwa Spika, nawapongeza TFF kwa kuwezesha na kufanikisha ushiriki wa timu zetu za Taifa zote kuanzia za vijana, wanawake na wakubwa. Tunajua ni mzigo mkubwa sana, lakini wanajitahidi sana,

Ushauri wangu kwanza ni kuhusu kufungia fungia, nashauri pamoja na kuwa ni kanuni ambazo vilabu vimejitungia kwa kushiriki katika kuzitunga, TFF wasaidieni ili tuwe na adhabu mbadala, kumfungia mtu miaka mitano ndugu zangu put yourself in such a position!

Mheshimiwa Spika, tulipitisha sheria kwamba 5% ya zawadi ya mshindi iende kuimarisha michezo, nashauri fedha hii kwa kuanza tuutupie jicho mchezo wa riadha.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye mchango wangu wa kuzungumza, tuepuke kuingilia uchaguzi wa TWF na hapa kwa nia njema nawashauri TFF, waacheni wanawake wachaguane kwa huru na haki, hakuna asiyejua kuwa TFF kwa ujanja ujanja walivuruga uchaguzi wa TWF, matokeo yake mpaka sasa TWF haina mwakilishi katika Kamati ya Utendaji ya TFF, hili suala tukilitizama katika jicho la jinsia, linaleta tafsri ambayo sio nzuri. Wizara kama kiongozi na msimamizi mkuu naishauri suala hili liishe, hakuna jambo ambalo linasemwa lisiwafikie familia ya michezo. Baadhi ya viongozi wa TFF kauli zao katika suala hili sio jema, tujitafakari.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa maendeleo yote yanayoendelea katika sekta ya elimu. Nina mchango mdogo tu, kama mtu ambaye nimetokea Wizara ya Mambo ya Nje na kwa kuzingatia nafasi ya Tanzania katika kupigania ukombozi wa Kusini mwa Afrika, nashauri kama sehemu ya kuendelea kujenga ushawishi katika ukanda wa SADC, Maziwa Makuu na ndani ya EAC kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje, tuje na kitu kinaitwa education diplomacy. Kwa mfano, kwa kutumia Bodi ya Mikopo, tunaweza kutenga 10% kwa ajili ya education diplomacy ambapo tunatoa scholarship kwa baadhi ya nchi ndani ya eneo letu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tukiwa na programu ya kuchukua wanafunzi 100 kutoka Comoro kwa miaka kumi mfululizo, maana yake ni kuwa ndani ya miaka mitano utakuwa na wanafunzi 500, lakini tayari utakuwa na wanafunzi kama 200 ndani ya Comoro ambao wamehitimu Tanzania, kwa miaka kumi unaweza kuwa na idadi fulani ndani ya Serikali ya Comoro katika sekta binafsi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, tukifanya hivi kwa nchi kama DRC, Zambia, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini na kadhalika tutajenga ushawishi katika nchi hizo na hivyo kunufaika na watu ambao watakuwa na unasaba na Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, ninaamini economic diplomacy inaweza kufanikiwa zaidi kwa kuunganisha nguvu mbalimbali iwe elimu, michezo, sanaa na kadhalika; ndiyo maana tutakuwa wenyeji wa AFCON, ni sehemu ya sports diplomacy kama sehemu ya economic diplomacy. Kwa hiyo, pamoja na exchange program, naamini Wizara ya Elimu inayo nafasi ya kushiriki economic diplomacy zaidi ya kuwaandaa wanafunzi wetu kupitia elimu, bali pia kupitia education diplomacy.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwapongeza kwa hotuba ya bajeti ambayo itafungua fursa zaidi. Hata hivyo nina ushauri na hoja kadhaa ambazo nisipopata majibu ya kuridhisha nitashika shilingi kwa nia njema ya kupata ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni Mradi wa REGROW; mradi huu ulizinduliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 12 Desemba, 2018 wakati huo akiwa Makamu wa Rais. Hata hivyo kumekuwa na kusuasua sana katika kutekeleza mradi huu ambao ni mkopo wa Benki ya Dunia wa kiasi cha dola milioni 150 za Kimarekani.

Mheshimiwa Spika, matarajio ya mradi huu pamoja na mambo mengine ni kuboresha mazingira ya shughuli za utalii ikiwa ni pamoja na ku-upgrade existing roads, airstrips lakini pia kujenga kituo kikubwa cha habari kwa maana ya information centre pale Kihesa, Kilolo. Aidha, mradi huu unatarajiwa kuboresha ushiriki wa wananchi wanaozunguka hifadhi ama kwa mafunzo ya uhifadhi au kwa kupata ajira ndani ya sekta.

Mheshimiwa Spika, mradi huu ambao narudia kusema kuwa utekelezaji wake ni wa mwendo wa kinyonga ungeweza kunufaisha kaya zaidi ya 20,000 na wakulima wanaozunguka Hifadhi ya Ruaha.

Mheshimiwa Spika, mradi huu kwa mujibu wa maelezo ulipaswa kwa mtiririko uwe umeanza na kukamilika mwaka 2024 ambapo ilipaswa mpaka kufikia mwaka huu wa 2022 kiasi cha fedha dola milioni 111 ziwe zimeshatumika kutekeleza hayo niliyoyataja hapo juu. Kwa mtiririko ilipaswa baada ya uzinduzi by 2020 kiasi cha dola milioni 41 kilipaswa kiwe kimetumika; by 2021 kiasi cha dola milioni 76 kiwe kimetumika; by 2022 kama nilivyosema kiasi cha dola milioni 111 kilipaswa kiwe kimetumika; by 2023 kiasi cha dola milioni 141 kilipaswa kiwe kimetumika; na by 2024 kiasi chote cha dola milioni 150 kiwe kimetumika, na hapa tuelewane hoja sio tu kutumika bali kutumika katika shughuli zilizopangwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya utalii na ushiriki wa wananchi katika uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada kubwa kufungua milango kwa kushiriki mikutano ya Kimataifa ikiwemo Royal Tour ambako anaitangaza nchi na utalii wetu, kwa kufanya hivi watalii watakuja, je, kama tumekuwa na mwendo wa kinyonga kutekeleza mradi wa REGROW hatuoni kuwa tunajikwamisha na kumkwamisha Mheshimiwa Rais?

Mheshimiwa Spika, pili, fedha hizi sio grant, ni mkopo ambao inafaa matunda yake yaanze kuonekana, lakini sasa tunajivuta, mara ilikuwa sijui GN kutoka ardhi ili kufidia na eneo, sijui muda wa mradi tumeongeza, for whose interest. Kwa hiyo, kama mtu ninayejali utalii kama sehemu ya kuongeza mapato ya Taifa na wananchi, jambo hili sio sahihi, ndio maana pasipo majibu ya kutekelezeka nitashika shilingi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu misitu; tunashukuru sana sekta imetulia sana, nawapongeza sana TFS kwa ushirikiano na pia kwa kupokea mawazo ya wadau. Nawashukuru pia kwa CSR, wanatupa support kubwa sana watu wa Mafinga na Mufindi, nawashukuru mno.

Mheshimiwa Spika, nina ushauri katika mambo mawili; kwanza ni kuhusu tozo; ninashauri baadhi ya tozo sasa umefika wakati tuziondoe, kwa mfano LMDA, tayari sasa maeneo mengi yamepandwa miti, tozo hii ambayo ililenga kuirudisha shambani kupanda miti, ni wakati sasa tukaiondoa sambamba na kuangalia suala la bei na tozo nyingine ili kusisimua biashara.

Pili, Kituo cha Panda Miti Kibiashara chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland; sisi Halmashauri ya Mafinga Mji kwa kushirikiana na Seikali tunaomba tufanye jitihada za pamoja ili baada ya phase ya sasa kumalizika, Finland watusaidie kwa phase nyingine zaidi ili kuendana na muda wa uvunaji wa miti toka mradi ulipoanza. Hii itasaidia kufanya tathmini ya uhakika na kupima matokeo ya mradi umekuwa na msaada kwa kiasi gani katika Taifa na jamii. Hata hivyo ili jambo hili lifanikiwe ni muhimu sana sote kwa pamoja tukashirikiana kushawishi GRL kutuachia lile eneo na baadae mradi ukiwa umemalizika kwa ukamilifu kituo kirithiwe na Halmashauri ya Mafinga Mji.

Mheshimiwa Spika, CSR kwa makampuni; jambo hili ni la hiyari lakini makampuni makubwa yaliyowekeza katika maeneo yetu yanao wajibu wa kutoa CSR, kwa sababu sisi tumewapa maeneo lakini moto ukitokea wananchi wanashiriki kuuzima, ikiwa TFS kupitia Shamba la Sao Hill wanatoa CSR, why not haya makampuni? Ushauri, naomba tuwe na forum nao na ikibidi watoe taarifa zao za CSR.

Mheshimiwa Spika, mimi ndio champion wa kushauri na kusukuma ajenda ya kwamba kama tunataka kujenga uchumi wa viwanda tuzuie kusafirisha veneer, na mimi ndiye pia nilishauri kuwa kwa kuwa kiwanda sio kama kwenda kununua nyanya sokoni ambapo utazikuta tu, basi tuwape muda, hata hivyo imethibitika kuwa muda huo ni mfupi na ndio maana kama mshika au mtoa hoja ninashauri, pafanyike extension hata ya miaka miwili ili watu hawa wajipange.

Mheshimiwa Spika, ni mjinga tu ndiye ambaye huwa habadilishi mawazo, jambo hili limeathiri pia mapato ya mtu mmoja mmoja, lakini pia own source kwa Halmashauri zetu ikiwemo Mafinga Mjini. Ni kwa muktadha huo nashauri kuwa tufaye extension pasipo masharti na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri pamoja na ugeni wake katika Wizara nilimueleza kwa kina jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nasema kwamba ushauri huu wa kufanya extension ya ban uwe huru pasipo masharti kwa sababu kwa msisitizo kabisa wapo watu walitumia mwanya huu kujineemesha jambo ambalo sio sawa.

Mheshimiwa Spika, tunachosisitiza mara zote ni welfare ya wafanyakazi katika viwanda na pia ulipaji wa kodi na tozo za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu utomvu maarufu kama gundi, imethibitika kuwa hakuna athari hasa kwa miti iliyokaribia kuvunwa, ushari wangu makampuni yanayovuna ambayo hayazidi mawili, moja linavuna katika shamba la Serikali na moja katika mashamba ya GRL, wapewe miti ya kutosha ili kusudi wananchi wapate ajira, Halmashauri ipate cess na Serikali iongeze mapato. Suala hili lina faida sana hasa katika ulinzi shirikishi dhidi ya majanga ya moto. Kazi ya kuvuna gundi ilikuwa inaajiri zaidi ya watu 1000 na wengi wao wanawake, na ni kazi ambayo mtu anaweza kufanya sanbamba na kazi zingine, kwa mfano mtu akitoka shamba anajiongezea kipato kwa kwenda kuvuna gundi, analipwa kulingana na kiwango alichovuna, mimi kama mtu niliyekulia kwenye misitu, nawapa ushauri ambao ni genuine sana ambao tija yake ni kubwa kwa ustawi wa misitu na jamii zetu.

Mheshimiwa Spika, bei elekezi ya vigogo; katika vikao tulivyokaa tumejadili sana suala la bei elekezi ya vigogo kwa Wachina, ninashauri tufikie mwisho, nakambuka Kamati ya Profesa Felister ilikuwa tayari na ripoti ya nini kifanyike ili kuwa na win win situation, kwa hiyo pamoja na kuwa biashara ni huria lakini lazima tuwe na mechanism za kuona kuwa wananchi wetu wananufaika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza jioni hii, sauti yangu haipo vizuri sana kwasababu ya furaha tuliyokuwa nayo kule tulikotoka, furaha ya kupata miradi ile ya maji kama tulivyosema kule leo Waheshimiwa Wabunge tumetoka kusaini ile Miji 28 tumeisemea sana. Kwa hiyo, tumekuwa na furaha sana tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Bunge kwa ujumla kwa sababu limesukuma sana ajenda hii, na kwakuwa maji ni kila kitu tunaamini sasa hata kama viwanja vilikuwa vikavu sasa vitakuwa vinamwagiliwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nipongeze Wizara kwa kazi nzuri inayofanya, pia nitumie nafasi hii kuwapongeza mabinti zetu ambao wamefuzu kwenda World Cup, pia niweze kupongeza Simba Sports Club kwa kuendelea kutubeba katika michezo ya Afrika mwakani tena msimu ujao tutakuwa na timu nne, tutakuwa na timu nne kutokana na performance ambayo Simba imekuwa ikiifanya kwenye michuano ya Kimataifa na ninaona kuna dalili wenzetu pia wanaweza mwakani tukawa nao sasa waje kujifunza kutokana na uzoefu ambao Simba tumekuwa tukiupata mpaka kuwezesha kupata nafasi nne. (Makofi/Vigelegele)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa David Cosato Chumi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Amos Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, wanasema wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani, nakubaliana na performance yao lakini unapozungumzia timu iliyojiandaa kuiwakilisha vema Taifa letu ni Dar Young African kwa kuanza kuchukua ubingwa mapema kwa gap kubwa zaidi ya point 10 mpaka sasa hivi, hamna namna na hii haijaja tu ni maandalizi mazuri ambayo tumejipanga wanayanga kuhakikisha tunaenda kuipeperusha bendera yetu vizuri. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa David Cosato Chumi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, mimi nataka nijielekeze kwenye mambo ya msingi na kwa sababu hiyo siipokei. Waheshimiwa Wabunge naomba mnisikilize vizuri. (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, kweli.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, ninataka nitoe ushauri wa muhimu sana, mwakani tutakuwa na timu nne, tulishakuwa na timu nne lakini yaliyowakuta wale tunawaita wanajeshi wa mpakani biashara wakaishia njiani kutokana pengine na kukosa uzoefu wa namna gani unatakiwa ujipange unapokwenda Kimataifa. Pamoja na kucheza na kadhalika nikufahamishe kwamba kushiriki Kimataifa kuna mambo mengi na hapa niwaombe TFF watusaidie sana zile timu ambazo zitakuwa zimepata nafasi kwenda kushiriki Kimataifa ikiwezekana wawape hata rehearsal. Kwa mfano; nakumbuka Biashara walienda Djibouti siku hiyo hiyo wakashindwa kwenda Libya kwa sababu unapoenda nje lazima ujue je, ile nchi unayoenda je, unahitaji visa? Je, kama unahitaji visa ni ile refereed visa ambayo inabidi uombe in advance au unahitaji visa ambayo ni visa on arrival, haya mambo yote ya logistics haya lazima uwe na weledi nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana natoa wito kwa TFF hizo timu nne zitakazoshiriki michuano hiyo ya Kimataifa wawape hayo mafunzo, hapa natoa wito kwa vilabu vyetu kama ambavyo tunao wasemaji katika vilabu vyetu, kama ambavyo tunao Madaktari katika timu zetu ifike wakati sasa tuwe na ma-protocol officer kwenye vilabu vyetu. Mimi nimefanyakazi Foreign Affairs, nimefanyakazi Idara ya Protocol mtu wa itifaki ni muhimu sana kwa sababu ndiyo anashughulika na logistic zote. Je, timu ina passport, wachezaji wana passport, masuala ya visa, mambo ya Airline kwamba je, hii route tunayoenda tuunganishe wapi au tufanye vipi iwe route fupi timu isifike imechoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo maana naendelea kutoa wito kwa TFF na Serikali maana tunaweza tukawa tunapata timu nne, nafasi nne kila mwaka, Simba wanatoka jasho wanatubeba tunakuwa na timu nne lakini zikifika kule zinaishia njiani. Naomba hilo Waheshimiwa Wabunge tulichukulie kwa uzito sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili mchezo wa riadha. Huu ni mchezo ambao unaweza kusaidia sana kututangaza tena si kwa gharama kubwa sana. Kwa mfano, katika marathon kubwa duniani New York Marathon, Tokyo Marathon, Boston Marathon, London Marathon, Chicago Marathon. Kwa mfano, New York Marathon tu wakati wale wakimbiaji wanakimbia kuna zaidi ya watu milioni mbili along the road wanafuatilia. Sasa kama pale una wanariadha wa Tanzania watatu, wanne wamevaa ile nguo ya kukimbilia imeandikwa Tanzania unakuwa umetangaza Taifa kwa gharama bure kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi ya watu milioni 300 wanafuatilia kwenye tv hizi marathon, sasa sioni sababu gani sisi watushinde Wahabesh, watushinde Eritrea, watushinde Kenya ambao mazingira tunafanana. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali hebu tuwekeze pia katika mchezo huu tuwe very serious ili kusudi tuweze kuitangaza nchi yetu kupitia mchezo wa riadha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajipanga sana kwenda Kombe la Dunia, tunaenda na hii timu ya mabinti zetu, je, tumejiandaaje? Mheshimiwa Waziri lazima tujue kama Taifa tunao makocha wangapi wa leseni gani na wako wapi, je, tunao matabibu wa michezo, tunao sports psychologist wangapi, wale watoto wameenda Cameroon kuna mazongezonge wamekutana nayo nani kulikuwa na psychologist ambaye anakuwa sports psychologist wa kuwaandaa hawa watoto kukabiliana na kwenda ugenini? Waamuzi ni mambo ambayo kama tunakataka tuwe serious, ndugu zangu kitu kama mpira wa miguu hakina muujiza it needs serious preparation. Preparation kubwa kwa watanzania hamasa jamani tumeshafika mbali, hamasa ya mpira ipo juu tunashida ya mambo mawili, miundombinu ya viwanja na suala la waamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kama unataka uache legacy jielekeze kwenye hayo mambo mawili. Viwanja Mheshimiwa Waziri bahati nzuri tunaweza kushirikiana na Chama cha Mapinduzi vile viwanja tayari miundombinu ya msingi ipo, lakini pia viwanja hivi tukivitengeneza viwe kwa ajili ya mchezo wa mpira wa miguu labda na riadha. Siyo sahihi sana kiwanja hicho hicho leo ikija sijui tamasha la muziki humo humo, tamasha la muziki wa injili humohumo, tamasha sijui la nini humohumo haiwezekani. Ndiyo maana tunaendelea kushauri kujenga Sports Arena na kujenga facilities kwa ajili ya mambo ya entertainment na burudani kwa sababu ni kitu ambacho kinapeleka sana Taifa mbele.

Mheshimiwa Spika, mwisho; mchezo wa netball; nashukuru sana umerudi mikononi mwa watu wenye mpira wao, kina Shyrose Banji nakumbuka miaka mitatu iliyopita tumeshinda kwenye South Africa kushiriki wakati nafasi tumeipata. Tunaomba nao tuupe support.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho kabisa Mheshimiwa Waziri Chama cha Mpira wa Miguu wanawake, kwa kweli kwenye soccer kimataifa sasa hivi wanawake wanatubeba. Uchaguzi Mheshimiwa Waziri unajua ulisitishwa kimazongezonge na mimi huwa ni mtu honest niwaombe TFF, TFW muilee, msiiletee mazongezonge acheni wafanye uchaguzi wao. Figisu kwenye kile kitu si vizuri kama ningepata nafasi kwenye Maendeleo ya Jamii ningechangia hebu tuwanyanyue na wenyewe wanawake kwa sababu Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Mpira wa Wanawake pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, lakini saa hizi karibia mwaka wanakosa kule uwakilishi na sisi tunasema tuwawezeshe wanawake tutawawezesha nini kama hatutengenezi hiyo platform? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, itoshe kusema kwamba michezo ni zaidi ya burudani, nikazi, ni ajira but we have to be very serious Mama ametusaidia Royal Tour imetangaza nchi yetu na kupitia michezo, kupitia riadha, kupitia hawa watoto juzi, kupitia hawa watakaokwenda timu nne kimataifa tutaendelea kulitangaza Taifa letu lakini lazima tusaidie katika kutengeneza logistic, mambo ya protocol, mambo ya viwanja na mambo ya waamuzi na haya yote tukidhamiria inawezekana. Mungu Ibariki Tanzania, Mungi Ibariki Nchi yetu, Mungu wabariki viongozi wetu. Ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwapongeza nyote, Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Mkuu mwenyewe, Mawaziri wote wanaomsaidia Mama Jenista Mhagama, Kaka Ndejembi, Dada Ummy na Kaka Katambi pamoja na wataalam wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni pamoja na Makatibu Wakuu wote wawili, Wakurugenzi, Maafisa na watumishi wote; ikiwa ni pamoja na Private Office ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Baada ya pongezi, naomba kutoa maoni na ushauri kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na kazi na ajira, ushauri wangu hususani kuhusu kukuza na kulinda ajira chache hasa katika sekta binafsi, nashauri taratibu za vibali vya kazi ziweze kuzingatiwa. Kwa ilivyo sasa kuna wimbi kubwa la raia kutoka China ambao wamegeuka wachuuzi, siyo Kariakoo tu, bali hata katika miji midogo kama Mafinga, Makambako na kadhalika. Suala hili tusipokuwa makini iko siku litazua tafrani kati ya jamii ya Wachina na Watanzania wazawa japo ni neno lisilopendwa kusikika, kuna kitu kitatokea siyo tu katika nyanja ya uchumi lakini hata kijamii na kidplomasia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa kunajengeka chuki siyo dhidi ya jamii ya Wachina bali wananchi dhidi ya Serikali, wanasema kuwa Serikali kwa nini inaachia Wachina kushindana na Watanzania kwenye ajira za chini ambazo kimsingi zinapaswa kufanywa na wazawa. Ushauri wangu, tukiliacha jambo hili bila kulidhibiti iko siku litaleta mgongano ambao utatuingiza katika shida ya kimahusiano ya kidplomasia na marafiki zetu wa muda mrefu China.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu BBT; programu hii ambayo inasimamiwa na Wizara ya Kilimo inaweza kuwa msaada mkubwa katika kuongeza ajira kwa vijana. Napongeza hatua zote za awali ambazo zimeanza kuchukuliwa, ushauri wangu, washirikiane na Kilimo na JKT katika kuhakikisha kuwa vijana wanaojitolea JKT wanakuwa sehemu ya wanufaika wa BBT. Naamini watakuwa na mchango mkubwa sana si kwao binafsi tu, lakini na kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuimarisha Idara ya Tathmini na Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali; kwanza napongeza uamuzi wa Serikali katika kuanzishwa kwa Idara hii muhimu ambayo itasaidia sana hata katika kupunguza hoja za CAG, lakini zaidi katika kuimarisha utendaji Serikalini hususani katika kukamilika miradi kwa wakati. Hata hivyo ili kuwa na matokeo chanya na kutimia kwa malengo ya kuanzishwa kwa Idara hii muhimu, rasilimali fedha na rasilimali watu ni muhimu sana. Katika kipindi kifupi toka kuanzishwa kwa Idara hii imethibitika kuongezeka kwa umakini wa kiutendaji ndani ya Serikali kwa sababu Idara imekuwa kama watch dog ndani ya Mawizara na Taasisi zetu za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na manufaa haya na kwa faida ya kuokoa gharama kama vile miradi kuchelewa kukamilika ambapo mara kadhaa Serikali imelazimika kuongeza fedha kwa miradi ambayo ilichelewa kukamilika kutokana na kushindwa kufuatilia utendaji wakati miradi inaendelea. Kwa hiyo kuimarisha Idara hii ni sawa na ile tunasema prevention is better than cure kwa maana kwamba kupitia Idara ya Tathmini na Ufuatiliaji tunaweza kuzuia kabla madhara makubwa hayajatokea, ushauri wangu Idara hii itazamwe kwa macho mawili kwa maana ya financing na human resources.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu EPC+F; Serikali ilisaini mikataba kadhaa na wakandarasi wa kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwa Mfumo wa EPC+F. Mikataba hii ilisainiwa Juni, 2023 na ni zaidi ya kilometa 2,000, mpaka sasa bado hatujaanza hata kilometa moja. Tatizo tunaambiwa wakandarasi wanaomba kulipwa angalau advance payment ya 10%.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu Serikali ifanye kila linalowezekana ili walau wakandarasi walipwe hii 10% kwa kuwa pamoja na sababu za kiuchumi suala hili kisiasa linaweza kuwa na shida kutokana na ukweli kwamba kama Serikali tulilitangaza sana na kuwapa matumaini wananchi, hivyo kutokuanza kwa miradi italeta ugumu katika chaguzi zijazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kuwapongeza kwa kazi nzuri hasa kuhakikisha kuwa baada ya muda mrefu watumishi wanapanda madaraja na kulipwa stahiki zao. Pamoja na changamoto za hapa na pale, lakini kwa ujumla kazi nzuri imefanyika, nawapongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nina ushauri mahususi hasa kuhusu nafasi za Watanzania kufanya kazi katika Taasisi na Mashirika ya Kimataifa. Kumekuwepo na manung'uniko kwamba watumishi wanaopata nafasi za kwenda kufanya kazi katika Taasisi na Mashirika ya Kimataifa baada ya kumaliza mikataba wakirejea wanarudi katika ngazi ile ile aliyoondoka nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba, kwa kuwa mtumishi huyu alienda kufanya kazi kwa mfano kwa miaka mitatu, mitano au nane, akapata exposure na uzoefu zaidi, basi akirejea na akakuta wenzake wamepanda ngazi na yeye aendelee katika ngazi ile ambayo wenzake pia wameshapanda. Kwa kufanya hivi, itawamotisha wengi kuomba nafasi hizo katika Taasisi na Mashirika ya Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, naambiwa kwamba kuna nyakati hata zile nafasi ambazo ni kama share yetu katika baadhi ya taasisi ambazo nchi yetu ni wanachama kama vile SADC na kadhalika zinakosa watu (Watanzania) kwa kuwa tu ama watumishi wetu hawajaomba au kwa kukosa mwamko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa jumla ni kwamba Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje iwe na mkakati maalum wa kuwahamasisha watumishi wetu kuomba nafasi katika taasisi na mashirika ya Kimataifa, na ikibidi hata kuwajengea uwezo wa namna ya kupata nafasi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nina watumishi katika Halmashauri ya Mafinga Mji ambao wamekuwa wakikaimu, mmoja mwanasheria ambaye amekuwa akifanya kazi kama Mkuu wa Kitengo cha Sheria toka Halmashauri inaanzishwa mwaka 2015, kuna wakati aliletwa Mkuu wa Kitengo lakini hakukaa sana akaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kanuni na taratibu za kiutumishi, nashauri watumishi wa aina hii wawe rewarded kwa kuzingatia uwezo wake kikazi na muda ambao amekaimu. Kwa mfano, mwanasheria huyu ametusaidia sana kuokoa mamilioni ya fedha kutokana na kushinda kesi za ardhi na za madai ambazo nyingi tulirithi kutoka Halmashauri mama ya Mufindi DC.

Mheshimiwa Naibu Spika, wa pili ni Kaimu Mweka Hazina wa Mafinga Mji, ambaye kupitia barua yenye Kumb. Na. HM/MAF/CS.20/PF.140/14 ya tarehe 04 Januari, 2024 aliombewa kuthibitishwa/kupandishiwa mshahara. Mtumishi huyu nilipomwuliza shida ni nini, alinifahamisha ana CPA, lakini hana masters.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufahamu wangu, akiwa na CPA kwa mhasibu ni sifa muhimu kuliko hata masters. Ushauri wangu, naomba watumishi wa aina hii Serikali iwatazame kwa macho mawili hasa kwa kuzingatia kwamba baadhi ya wenzao wenye sifa kama wao wanakuwa wamethibitishwa katika nafasi kama hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni suala la recategorization. Ushauri wangu wa kila mwaka kwenu ni kwamba mtumishi akifanyiwa recategorization, basi walau abakie na mshahara wake. Kwa mfano, mwalimu ambaye yuko kwenye TGTS F, akasoma na akafanyiwa recategorization akawa HR, ni wazi lazima aanzie HR Daraja la Pili, lakini mshahara wake abakie nao ule ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuongea na Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete akafafanua kwamba mwajiri anaweza kumwombea mtumishi aliyefanyiwa recategorization mshahara binafsi, lakini mimi naliona gumu kiutekelezaji. Hivyo ni vyema ikawekwa openly kuwa mtumishi akifanyiwa recategorization automatically mshahara wake utabakia ule ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza tena maana katika lolote linalofanyika hapa nchini, engine ni utumishi wa umma. Mmebeba dhamana kubwa na Mwenyezi Mungu awasimamie katika utendaji wenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza kwanza kwa ushirikishwaji na wepesi katika ku-respond kwenye changamoto kila zinapojitokeza.

Mheshimiwa Spika, pili nawapongeza sana REA ambao tarehe 17 Aprili, 2024 walitoa mafunzo ya nishati safi ya kupikia kwa viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga ambapo pia mafunzo hayo yalihudhuriwa na viongozi wa dini na wazee maarufu wa Mji wa Mafinga. Katika mafunzo hayo Mkurugenzi wa Nishati Mbadala kutoka REA Bi. Advera Mwijage alitoa taarifa kuhusu hali ya umeme na hatua za utekelezaji wa hatua ya Ujazilizi 2C na pia alieleza fursa ya mkopo wa vituo vidogo vya mafuta somo ambalo liliwavutia wengi. Kwa ufupi mafunzo hayo sambamba na kugawa mitungi 350 ilifanikiwa sana na tunawashukuru sana REA.

Pili, naomba kushukuru utendaji mzuri wa Meneja wetu wa Tanesco Mhandisi Modest na timu yake, amekuwa very sharp hasa katika mawasiliano, sote kuanzia Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Madiwani tunashirikiana naye vizuri mno na kwa wakati. Ni kawaida yetu binadamu hasa sisi wanasiasa kutoa taarifa za kulalamika tu, lakini mtu akifanya vema tuna-mute. Hivyo nimeona ni vyema niseme kuhusu utendaji mwema na wa ushirikiano kutoka kwa Mhandisi Modest. Tunaomba kama anahama basi iwe vertical kwamba anapanda, lakini kama ni horizontal basi ni afadhali abakie Mufindi/Mafinga.

Tatu, suala la bei kwa sisi ambao kwa mujibu wa ile Sheria ya Mipango Miji inayosema kwamba eneo kutambulika kuwa mji kuna vigezo ambavyo kimsingi kuna maeneo bado ni vijiji, kwa sheria hiyo vijiji, hivyo vinakosa sifa ya kupata umeme kwa bei ya vijijini; mfano Mafinga ni mjini, lakini kuna maeneo ni vijiji kijamii na hata kiuchumi, kwa hiyo, bei ile ya shilingi 360,000 ni kubwa mno, nimeuliza maswali mara kadhaa, majibu ni kwamba kuna timu imeundwa kupitia maeneo hayo ili kuja na majibu ya way forward.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo suala hili sasa ni mwaka wa pili hakuna majibu, inawezekana kabisa hii bei ya shilingi 27,000 ikawa ni mzigo mzito kwa Serikali, hata hivyo mnaweza kuja na bei tofauti tofauti kulingana na maeneo, kwa mfano vijijini kabisa inaweza kubakia shilingi 27,000, lakini baadhi ya maeneo ambako ni kama peri-urban pawepo bei ambayo kidogo ni nafuu. Kwa mfano Mafinga kuna maeneo kama Ndolezi, Luganga, Mtura, Sao Hill na kadhalika inasomeka kuwa ni Mafinga Mjini lakini uhalisia wa kipato kwa maana ya uchumi na hata kijamii maisha ni ya kijijini, kwa sababu hiyo maeneo ya aina hiyo iwepo bei elekezi ambayo sio shilingi 27,000 na wala sio shilingi 360,000 lakini inaweza kuwa hata shilingi 100,000 kulingana na namna ambavyo hiyo timu ambayo tuliambiwa kuwa imeenda kufanya mapitio imejionea.

Mheshimiwa Spika, hitimisho; katika ujazilizi yapo maeneo imeonekana kuwa yapo mbali na HT hivyo vitongoji kadhaa Mafinga vitakosa fursa kwa sababu hiyo, hivyo naomba tuone uwezekano kupitia TANESCO kupata HT ili kuwezesha REA kupitia mkandarasi wa ujazilizi waweze kuendelea.

Mwisho, ni lini utekelezaji wa ahadi ya vitongoji 15 kila jimbo utaanza? Hii ni kwa sababu suala hili limo kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 na bado kama mwezi mwaka wa fedha kumalizika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kama Mbunge wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini naendelea kuishukuru Serikali kwa suala la mbolea ya ruzuku, tunaishukuru mno Serikali. Hatua hii imesaidia mambo kadhaa:-

(i) Kupunguza makali ya bei;

(ii) Kuhamasisha wananchi kuongeza mashamba kwa maana ya eneo la kulima; na

(iii) Kuongeza uzalishaji/mavuno kwa maana ya high productivity.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna changamoto kadhaa kwa mawakala, makampuni, TRA na namna ya usambazaji wa mbolea za kufika vijijini japo hadi ngazi ya kata.

Mheshimiwa Spika, mawakala wanakabiliana na changamoto ya kwanza kutoka kwa baadhi ya makampuni, kwa mfano kwa Kampuni ya Yara inamtaka wakala kulipa fedha yetu pamoja na ile ya ruzuku hali ambayo inamnyima wakala nguvu ya kimtaji kuweza kusambaza kwa haraka na kwa ukubwa. Baadhi ya makampuni hayana masharti magumu, wapo ambao wanataka tu commitment ya wakala kwa kutaka tu aweke deposit ya kiasi fulani cha fedha baada ya hapo wanaendelea kufanya kazi na wakala na mbolea inafika kwa mkulima kwa wakati. Kwa nini Yara wasiwe flexible, Yara ni giant company, ni matarajio yangu kuwa ingeunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwa na masharti rafiki kwa mawakala. Binafsi nawaona Yara kama wahujumu wa jitihada za Serikali.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu Serikali iwape maelekezo Yara, wawe na masharti nafuu kwa mawakala, wao Yara ni wanufaika wa mfumo wa mbolea ya ruzuku, lakini pia ni wanufaika kibiashara ndani ya Tanzania, kwa nini wasiwe na moyo mwema wa kui-support Serikali katika suala hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu issue ya TRA, wakati waingizaji wa mbolea kwa maana ya makampuni wanauza mbolea kwa bei ya soko na mawakala wa pembejeo wanauza kwa bei ya ruzuku, TRA imekuwa ikiwasumbua linapokuja suala la kodi. Hii inatokana na ukweli kwamba kunakuwa changamoto za kimahesabu baina ya mawakala na maafisa wa TRA, kwa maafisa wa TRA kutokutambua mfumo wa dijitali wa TFRA Agro-dealer Tools na hivyo mawakala kujikuta wakipigwa faini na TRA kwa kuonekana kuwa wana manunuzi makubwa kuliko mauzo.

Mheshimiwa Spika, shida ni kwamba Maafisa wa TRA hawatambui kwamba wafanyabiashara hao wananunua mbolea kwa bei ya juu kwa maana bei ya soko na kuuza kwa bei ya ruzuku ambayo ni bei ya chini, hali ambayo inasababisha kuonekana wana manunuzi makubwa na mauzo kuwa madogo. Kwa sababu hiyo kuna kila sababu Serikali kwa maana Wizara ya Kilimo kukaa na Wizara ya Fedha ili kuweza ku-harmonize suala hili. Wote tunamtumikia mwananchi mmoja, tuwe na uelewa wa pamoja. Tusiwaumize mawakala licha ya kuwa hii ni biashara, lakini kwa kiasi fulani ni huduma.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa mbolea inafika ngazi walau ya kata, kumekuwa na changamoto ya gharama za bei ya nauli ya mbolea kukosa uhalisia kwenye kufika ngazi ya kata, kwa mfano umbali wa kilometa 40 gharama za kusafirisha mfuko mmoja wa mbolea ya kilo 50 ni shilingi 300 hali inayosababisha mawakala kufanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwingine kushidwa kupeleka mbolea vijijini na wakulima kulazimika kufuata mbolea maeneo ya mjini kwa umbali mrefu na hivyo kuongeza gharama. Nashauri wataalam watusaidie namna ya kukabiliana na changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu maghala, kutokana na uwepo wa mbolea ya ruzuku na kutokana na ukweli kwamba bado hatujawa na maghala makubwa na ya kisasa, nashauri ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula na hasa nafaka tutumie sekta binafsi katika kujenga maghala makubwa na ya kisasa, Serikali peke yake haitakaa iweze na kama itaweza basi itachukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kilimo cha parachichi; Kata za Wambi, Rungemba, Bumilayinga, Sao Hill na Isalavanu wananchi wameitikia wito wa kulima parachichi na wenzetu wa Kibidula wamekuwa msaada sana ku-support huduma za ugani na kuwatafutia soko wakulima wa nje yaani out growers. Nashauri Serikali kuwaunga mkono wananchi na Kibidula hata kwa kuwasaidia kufanya kilimo cha mkataba ili kulinda haki za pande zote mbili.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mara kadhaa suala la soko limekuwa changamoto, nashauri watu kama hawa wa Kibidula kupewa kila aina ya support na ushauri kwa sababu walau hawa ni mkombozi linapokuja suala la soko kuyumba.

Mheshimiwa Spika, pili, nafahamu kuwa kuna miradi ya RISE na Agro-connect, naomba awamu ijayo tuitazame barabara ya changarawe kupitia Skimu ya Umwagiliaji ya Mtula, Matanana, Kisada kutokezea Nyololo, eneo lote inakopita kuna shughuli za uzalishaji wa mazao ya mbogamboga na matunda kwa maana ya parachichi, itasaidia sana kufikisha mazao sokoni kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, tatu, Mheshimiwa Waziri Bashe na timu yake wamekuwa wakifanya kazi kubwa kiasi wamefanya Watanzania kuona kuwa kilimo is no longer a theory issue, but real. Hata hivyo, yako maeneo ni kikwazo, kwa mfano wenzetu wa TRA, Bandari na TANROADS/mizani, hasa kwa mazao ya mbogamboga na matunda, pamekuwepo na ucheleweshaji wa mizigo kwa sababu zisizo za msingi, huwezi kumsimamisha mtu ambaye amebeba kontena la parachichi kisa tu sijui risiti ya EFD ya transport, sisemi kwamba sheria zivunjwe la hasha, bali kuna maeneo tutumie common sense, gari limesajiliwa, dereva ana leseni, kwa nini usiache gari liwaishe mzigo sokoni na huyu dereva au mwenye gari umpige faini hata online kama ambavyo wamekuwa wakifanya Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu bandari, nashauri pamoja na maboresho yanayoendelea katika kuimarisha bandari yetu, pawepo jitihada za makusudi kuwa na eneo maalum kwa ajili ya kusafirishia mazao ya mboga mboga. Hivi sasa wasafirishaji kwa mfano wa parachichi wanategemea Bandari ya Mombasa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu BBT na visima 67,000; jambo hili limekuwa na mixed feelings kwa sababu ya uelewa, nashauri Serikali isichoke kuelimisha kuwa hii ni program up to 2030 maana kuna watu wanadhani hii ni one year project, nashauri Wabunge na Watanzania kwa ujumla waelimishwe kwa lugha rafiki, in humble manner, maana wapo watu wanaamini kuwa tayari Wizara ina mabilioni ya fedha kumbe so far ni pledges.

Mheshimiwa Spika, napongeza pia kupanua wigo wa BBT kupitia ile programu ya visima 67,000, nayo ni muhimu sana ifahamike kuwa ni programu ya kutoka sasa hadi 2030, vinginevyo ama kwa kutoelewa au kwa nia ya kupotosha watadhani kwamba programu hii ni kwa this financial hii ya 2024/2025. Kwa hiyo nashauri maelezo yajitosheleze na Serikali wasichoke kufafanua.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nawashukuru sana kwa Mradi wa Umwagiliaji wa Mtula.

Mheshimiwa Spika, namalizia kwa kusema kilimo chetu, maisha yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Ninapenda kutumia nafasi hii kumshukuru Mungu kwa afya na uzima wetu. Pia ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ile Royal Tour na nitasema kwa nini pongezi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu pamoja na pongezi nitazungumzia suala la misitu na umuhimu wa kuzingatia local content katika misitu. Nitazungumzia pia suala la bomu baridi hilo la kufukuza tembo, nitazungumzia utalii wa matukio na mwisho kama nafasi itatosha nitazungumzia sekta ya wanyamapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyosema, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa ile Royal Tour na kwa bajeti hii pamoja na maandalizi yake napenda kupongeza Waziri Mheshimiwa Kairuki, kaka yangu Bwana Dunstan Kitandula, huyu ni mtu rahimu na mpole sana, lakini pia Katibu Mkuu Dkt. Abbas na Naibu Katibu Mkuu Kamishna Wakulyamba pamoja na watumishi, wafanyakazi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza kwanza kwenye sekta ya misitu. Kwa bahati nzuri na wewe unatoka kwenye misitu na unafahamu kwa namna gani sekta ya misitu ina mchango mkubwa katika uchumi wa watu wa Iringa na Mkoa wa Njombe mpaka maeneo ya Madaba. Sisi Mafinga tumejaliwa kuwa na msitu mkubwa ambao unakwenda katika Wilaya ya Mufindi mpaka maeneo ya Kilombero huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa na jambo moja kwa Mheshimiwa Waziri, timu yake na wenzetu wa TFS, tunapozungumzia local content wakati mwingine nadhani kwamba ile local content ni mambo tu ya Kimataifa na mambo ya kwetu hapa Kitaifa. Kumbe local content maana yake ni kwmaba hata wale wenyeji walioko kwenye yale maeneo kama ni ya utalii au ni ya misitu wawe beneficiary wa uwepo wa ile neema ambayo Mwenyezi Mungu amewajalia watu wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwangu hapa nasema nini, nimwombe Mheshimiwa Waziri na watu wa TFS wanapotoa ajira za muda mfupi, zile temporary, hakikisheni pia wanazingatia wenyeji wanaozunguka msitu wa Sao Hili. Wananchi wanaotoka kwenye vijiji vile nao wawe sehemu wa kupata vile vibarua. Wakati fulani tulikuwa tunatoa vibarua ikiwa inaeleweka kabisa kwamba msimu huu kijiji hiki kitapata vibarua labda watoto kumi au vijana kumi au akina mama kumi. Kwa hiyo, ninawaomba kuwepo na clear information ili wananchi wa Mufindi na Mafinga waweze kunufaika kama ambavyo wanasema siku zote kwamba ukiwa karibu na uaridi lazima unukie uaridi. Kwa hiyo, sisi watu wa Mafinga na Mufindi kunukia kwetu uaridi la kwanza na sisi kuwa sehemu ya washiriki katika ajira za muda mfupi zinazotokea kwenye mashamba ya Sao Hill. Ninaomba hili tulizingatie sana kwa muktadha ule niliosema wa local content.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili tuliwaomba Mheshimiwa Waziri na hii mimi tumewaomba Mkoa wa Iringa kwa nia njema. Tumewaomba kwamba jamani pale kwenye shamba la Sao Hill tutengeeni sehemu tujenge soko kubwa la mazao ya misitu la kimataifa, this is good for both of us. Nimewaambia, nimeongea na Mheshimiwa Waziri personal, nimeongea na Katibu Mkuu na pia nimeongea na Profesa Dos Santos. Sasa nikasema je, kweli jambo hili nina haja au sisi watu wa Mufindi tuna haja ya kumwandikia Waziri Mkuu kumuomba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kitu ambacho tumewaomba Mheshimiwa Waziri ni kwa manufaa yetu sisi sote, Wana-Mafinga, Wana-Mufindi, Wana-Iringa, Wana-Njombe, lakini pia wao ili tuikuze sekta. Tutakapokuwa na soko kubwa la mazao ya misitu tutakuwa pia tumeikuza hii sekta yetu. Tulisema, Profesa anajua, tumezungumza sana kuhusu percentage recovery kwenye mti, kwamba ule mti unakuta kwa jinsi ilivyo sasa hivi labda ni 40% tu ule mti ndio unatumika, 60% ni waste.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiwa na eneo la namna hiyo maana yake ni kwamba katika mti tunaweza tukafanya ile recovery percentage ikawa hata 90%, kwamba huyu hapa atafanya mambo ambayo huyu hapa kama ana mambo ya sawdust atafanya. Kwa hiyo niwaombe, pamoja na kuwa Mheshimiwa Waziri alisema watalamu wamemweleza tofauti, mimi nawaombe, ninawaombeni kwa niaba ya wananchi wa Mafinga na Mufindi hebu mkalitafakari upya jambo hili, ni kwa manufaa ya sisi na sekta ya misitu, hili nimewasilisha kama ombi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu katika misitu, tuliwaomba na mwaka jana nilisema pia kwamba makusanyo yale ya cess, zamani ilikuwa kwamba yule mtu anayepata kibali cha kuvuna analipa malipo yote kwa mkupuo mmoja, halafu baadaye mnatenganisha ile ambayo ni cess wanatupatia sisi halmashauri. Wakaja na utaratibu kwamba tujikusanyie wenyewe. Ile pale kama nilivyosema, kama tuko karibu na uaridi na tunukie uaridi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba utaratibu ule tuufikirie upya. Mtu anapokwenda kulipia na sisi kama Serikali tumesema tunataka twende na utaratibu wa one point katika masuala ya malipo. Sasa kwa nini mtu asilipe, halafu baadaye mtugawie ile ambayo ni sehemu yetu ya cess. Watu wa TFS wanasema sijui kuna gharama za bank charges na kadhalika. Sisi tuko tayari ku-share hizo costs, lakini ilivyo sasa sisi kama tunategemea cess maana yake makusanyo sasa yanaendelea kushuka. Nawaomba wakae na local government, kwa maana ya TAMISEMI, tuone na tuje na huo mfumo ambao utatuwezesha sisi kukusanya cess pasipo kutumia mabavu wala nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ambalo ninataka niliseme na nipongeze ni suala la bomu baridi kwa ajili ya kufukuza hao tembo na hapa ni lazima kama Serikali na kama Wabunge tuzipongeze Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa ushirikiano na kitaasisi ambao umewezesha kuja na hili bomu baridi ambalo litasaidia sana maeneo ambayo wenzetu wanapata matatizo ya tembo kuingia kwenye makazi ya wananchi.

Kwa hiyo, napongeza vyombo, na nawapongeza nimeona wamekwishatoa order, wamenunua, na watu wengine tuunge mkono jitihada, vyombo vinapokuja na ugunduzi fulani fulani basi sisi kama Taifa, wale watu wa Mzinga wana mazao mbalimbali tuwaunge mkono, tununue mazao yale kwa ajili ya manufaa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kuhusu Royal Tour kwamba utalii wetu uendane na kitu kinaitwa utalii wa matukio. Mtu akija kupanda Mlima Kilimanjaro, akija Serengeti, akija Ruaha mwakani aweze kupata hamu ya kuja ten ana ili aweze kupata hamu ya kuja tena maana yake ni kwamba tuwe na matukio ambayo yanasindikiza hivi vituo vyetu. Kwa mfano kuna maeneo wenzetu kama Brazil wana kitu kinaitwa Rio Festival. Hizi festival hata hapa Tanzania wenzetu Sauti za Busara Zanzibar watu wanakuja kwa ajili ya utalii, lakini pia anakuja kwa ajili ya lile tukio. Kwa hiyo, tupanue wigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninaamini ndugu yangu Mafuru ni brain, atakuja kupitia TTB tukawa na utalii wa matukio. Leo hii tulikuwa na wageni hapa wa waratibu wa The Great Ruaha Marathon. Wamebuni kitu kizuri kwamba unakimbia Marathon ndani ya Mbuga za Ruaha. Kwa hiyo, tubuni, tuwe na matukio mbalimbali ambayo yataongoza vile vivutio vya utalii. Kuna kitu kinaitwa Nyama Choma Festival, yule mtu kama alikuja mwaka jana apate hamu tena ya kuja mwakani kwa ajili ya lile jambo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele imelia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huo utalii wa matukio kuna huu utalii wa michezo. Nilitoa mfano ile Simba ilivyoshiriki African League, yale ndiyo matukio ambayo pia yanaleta utalii. Tunavyokuja kufanya AFCON tunaleta utalii. Kwa hiyo, tupanue wigo pamoja na hii traditional utalii lakini tuongozane na utalii wa matukio…

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nawapongeza tena Mzinga kwa kuja na bomu la baridi kwa ajili ya tembo na Wizara kwa kushirikiana na Mzinga kwenye jambo hilo muhimu Mungu atubariki sote. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kupata nafasi hii na pia nitumie fursa hii kuishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuona haja na umuhimu wa kuja na muswada wa sheria hii ambao utatuongoza katika kuilinda na kuifanya hii taaluma iwe na sheria ambayo inaisimamia. Kwa sababu ni miongoni mwa taaluma zile tunazoita rare professional, lakini hii ni kati ya hizo rare professionals ambapo peke yake haikuwa na sheria, haikuwa na masuala yoyote yaliyoletwa kama mambo ya kuwa na bodi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba kuna sheria zinazo-govern Bodi za Wahandisi, sheria zinazo-govern masuala ya Wafamasia, Wapima, Wahasibu na kadhalika. Kwa hiyo, ni jambo la kupongeza kwamba sasa tunakuja kuwa na sheria ambayo siyo tu itasimamia taaluma hii ya uthamini, lakini pia sheria hii jambo lingine la kupongeza na la muhimu sana imekuja sasa na muda specifically hasa kuhusu toka mtu alivyofanyiwa uthamini mpaka lini atatakiwa kulipwa fidia yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshashuhudia mara nyingi uthamini ukifanyika na fidia kuja kulipwa hata baada ya miaka 10. Katika sheria hii, inabainisha wazi kwamba baada tu ya uthamini kufanyika na baada ya huyu Chief Valuer (CV) kuwa amesha-approve ile taarifa ya uthamini maana yake katika kipindi cha miaka miwili waliofanyiwa uthamini watapata kile ambacho kinawastahili. Kwa hiyo, hii ni hatua mojawapo ya kuthibitisha kwamba Serikali inajali na inawathamini wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nina some observation hapa kutoka katika hii sheria. Kwa mfano, tukienda na suala zima la observation ya codeof conduct, nadhani ni Ibara ya 20 na ile ya 21, inasema kuhusu malalamiko, lakini haisemi specifically hatua gani au adhabu gani yule ambaye atakiuka maadili ya taaluma hii atapewa. Nilikuwa nadhani kwamba pamoja na maelezo ambayo yapo katika kipengele hiki, ingekuwa vizuri kama sheria ingeeleza specifically kwamba yule ambaye atakuwa amekiuka maadili, basi kuna adhabu fulani ipo categorically kabisa itamkumba yule mtu. Sambamba na hii, katika hiki kipengele pia cha yule atakayekuwa analalamikiwa, pamoja na kutosema waziwazi kwamba adhabu gani atapewa katika msingi wa natural justice, haijasema waziwazi kwamba itampa nafasi ya kusikilizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba haya ni kati ya mambo ambayo pengine baadaye kwenye majumuisho kitaalam ingeweza kutazamwa mara mbili zaidi, kwamba iseme wazi yule atakayelalamikiwa, yale malalamiko kama yatathibitishwa ni adhabu gani itamkumba yule mtu. Pia wakati huo huo iwe imetoa room ya yule mlalamikiwa kusikilizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, ukienda katika Ibara ya 8 ya Wathamini Wasaidizi, na mimi napenda niungane na baadhi ya wachangiaji kwamba ikiwa yule Mthamini Mkuu elimu yake na uzoefu wake kwamba Shahada ya Pili ina uzoefu wa miaka mitano; kwangu, kwa sababu hii ni rareprofessional ambayo watu wanasoma miaka minne kama sikosei, lakini pia hata wale watakaokuwa wamesajiliwa, ukienda huko mbele utaona kwamba lazima iwe baada ya uzoefu wa miaka mitatu. Kwa hiyo, napendekeza iwe ni shahada moja ambayo ni Shahada ya Kwanza na angalau miaka mitano isiwe sawa na yule ambaye atakuwa Mthamini Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Ibara ya 14, tukizingatia kwamba jana tumepitisha hapa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa (Access to Information) kwa nia ya kupanua wigo wa upatikanaji taarifa, nashauri iseme clearly kwamba itatangazwa kwenye magazeti yasiyopungua mawili yanayosambazwa kwa wingi, kwa sababu hapa imeeleza kwamba ile orodha itatangazwa katika Gazeti la Serikali lakini pia katika gazeti moja ambalo linasambazwa kwa wingi. Sasa linaweza kuwa hilo moja likaangukia kuwa ni Daily News mathalani au Mwananchi. Sasa tukawa tume-limit ile access to information ya masuala haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mapendekezo yangu, sheria ingesema angalau magazeti yasiyopungua mawili yanayosambazwa kwa wingi pamoja na ile ya Gazeti la Serikali. Hii pia ya upatikanaji wa hii taarifa unaweza kuiona katika Ibara ya 17 na Ibara ya 34 kama kuna masuala ya uchunguzi na kadhalika. Yale yote yanayohusiana na haya ya watu kupata taarifa, napendekeza isiishie tu kwenye Gazeti la Serikali na gazeti moja linalosambazwa kwa wingi, bali angalau hata magazeti mawili kwa maana ya kwamba kama liko moja la Kiingereza, basi moja la Kiswahili ili kupanua ule wigo wa access to information. Kwa hiyo, vipengele vyote ambavyo vinahusiana na kutoa hii taarifa, mapendekezo yangu tungepanua huo wigo wa taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika usajili imeeleza hapa kwamba inabidi kuwe na uzoefu wa miaka mitatu. Napendekeza kwa yale yale niliyosema, kama hii ni rare profession na ambayo wanataaluma hii katika mafunzo yao wanafanya, nadhani kila mwaka practical training, basi angalau tungesema miaka miwili, yaani sifa mojawapo ya mtu kupata usajili isiwe miaka mitatu, iwe ni miaka miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika kipengele cha 68 Mthamini Mkuu ni kama sheria inampa haki fulani tu ya kuwa yeye ni mtu wa kukaa ofisini tu, kwamba mthamini yeyote aliyesajiliwa ambaye ripoti yake itakuwa na maelezo au taarifa yenye makisio ya juu au ya chini, ule uzembe utamkumba mwanataaluma mwenyewe, yaani mthamini atakuwa tu ame-relax tu na tayari ile report pengine ameshai-approve.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba hapa aende miles away, kwamba kama atakuwa na shaka, basi kwa gharama zozote pafanyike au atume timu au mthamini mwingine apate kwenda kujiridhisha juu ya lile jambo kwa sababu otherwise naona kwamba yeye atakuwa tu amekaa ame-relax kwa sababu aliyekosea ni mtu mwingine basi yeye hawajibiki popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kwa kuwa kengele imeshanipigia, nazungumzia hili la ukomo wa muda. Kwa mfano, tutakapokuwa na uthamini ambao una-cover eneo kubwa, kuna ujenzi wa barabara kutoka hapa let‟s say mpaka Iringa. Sasa ule uthamini, hii cut-off date itahesabika wapi? Kwa mfano, uthamini huu unaweza kuchukua hata miezi sita, je, wale watakaoanziwa Dodoma, watakaokutwa Mtera, Isimani, Nyang‟oro na kadhalika, wao ile cut-off date itasubiri mpaka siku ya approval ya ripoti ama tuwe na utaratibu ambao itahesabika ile siku ya kwanza anajaza tu ile fomu ya kufanyiwa uthamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya, napenda kwenda kwenye kipengele cha 55 kama muda utaniruhusu, ile inayosema kwamba mthamini ataingia tu kwenye eneo; nashauri kwamba pawepo na prior information au hata notice in advance kwa sababu the way ilivyo inaonekana kwamba huyu mthamini ana access kubwa ya kuingia kwenye eneo na kufanya kazi yake na kama hatapata ushirikiano, yule ambaye hatatoa ushirikiano, kuna adhabu ambayo itamkumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kuwe na advance information kwamba kuna hili linakuja kufanyika ili kumwondoa huyu mtu kwenye tahadhari ya kutokuwa na ushirikiano, sasa akiwa kama amekuwa ambushed, maana yake ni kwamba atakosa kutoa ushirikiano na akikosa kutoa ushirikiano, huku mbele unakuta kwamba kuna adhabu ya faini au kifungo kisichopungua miezi 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya napenda kushukuru na mimi wananchi wangu wa Lungemba ambao wanasubiri malipo ya fidia, nadhani sheria hii sasa inaenda kuwa-accommodate ipasavyo na fedha zile zitalipwa kwa wakati kama ambavyo sheria inaenda kuelekeza. Nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. COSATO D. CHUMI: Bahati nzuri mimi huwa I don’t care makelele ya wengine, niko focused. Kwa hiyo, I will never lose my focus. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojadili kitu ambacho ni mhimili wa nne wa dola, kama ambavyo tunasema, unless otherwise tuna-pretend kwamba huu ni mhimili wa nne wa dola. Kama kweli huu ni mhimili wa nne wa dola, haiwezi kukwepeka kusema kwamba inapokuja umiliki lazima Watanzania wawe na asilimia nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuufanya mhimili wa nne wa dola umilikiwe kwa asilimia 100 na watu wa nje; that is very dangerous. Ndugu zangu, hilo napenda tulielewe vizuri sana kwamba tunajadili mhimili wa nne. Kwa hiyo, lazima katika kujadili sheria hii au muswada huu tuzingatie kwamba kuna mambo kwa kweli ni lazima tuyape uzito. Mojawapo likiwa hili la kuhakikisha ya kwamba katika zile shareholder asilimia nyingi ziwe za sisi Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wamesema hapa, pia ni namna ya kuwawezesha Watanzania wenyewe. Nami nampongeza Mheshimiwa Kubenea, ana asilimia 100. Kumbe it is possible; amesema hapa. Kwa hiyo, ndugu zangu hilo napenda sana twende nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo niende kwenye muswada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe nilikuwa mwandishi wa habari, nimekaa newsroom almost miaka minane. Nimefanya kazi; sikwenda kusoma kama taaluma, lakini nimefanya in house training, nikawa mwandishi wa habari mzuri tu. Sasa tasnia hii kwa miaka nenda, rudi; labda sisi humu, baadhi yetu Wabunge tunataka tuendelee kuifanya ambavyo ilivyo kwa maana labda tunaitumia kwa malengo yetu. Kama tunataka tukifanye chombo hiki kweli kiwe muhimili wa nne ambacho kinatusaidia na sisi tukisaidie, naamini kuna mambo mazuri mengi katika muswada huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo, kuna suala la kuwa na Bodi ya Ithibati na hapa lazima niseme kidogo kwa uchungu; kama alivyosema mwingine. Mimi sikutarajia mtu kama Mheshimiwa Zitto, ndugu yangu, tumefanya harakati Chuo Kikuu pamoja, mimi nilinusurika kufukuzwa, wewe ukafukuzwa; nadhani unakumbuka; kuja kusema kwamba hatuhitaji Baraza la Ithibati la kulinda taaluma hii, that should not come from a person like Zitto. Mimi sikutarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Tuna wahasibu, wafamasia, waandishi, madaktari na juzi hapa tumepitisha muswada wa sheria kwa ajili ya surveyors na wakemia. Kwa hiyo, kwangu mimi naona kuwa na Baraza la Ithibati ni jambo muhimu katika kuijengea taaluma hii, kweli kuipa ile hadhi ya taaluma, siyo kuibana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda tuseme, twende mbele, kwa maoni yangu mimi nilivyokuwa ninaona, hii Bodi ya Ithibati, nimeenda pale kwenye composition, maana kuna amendments hapa, baadhi nimechelewa kuzipitia, sijui kama imekuwa accommodated au laa. Kama itakuwa iko tayari imeingia humo, nitawiwa radhi, lakini nilikuwa nashauri kwenye composition ile, kwa sababu hii ni taaluma ya habari, tumesema pale kutakuwa na seven members na katika wale, wawili watakuwa ni wana taaluma wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kisheria sasa, tungeongeza kwa sababu nia ni kuilinda na kuipa hadhi taaluma hii, badala ya kutoka wale wawili, basi tuende japo watatu mpaka wanne kwenye composition. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa nashauri, pengine sheria kilaalam, mimi siyo mwanasheria, ingeenda mbali zaidi. Mlio wanasheria mnaweza kusaidia namna ya kuitengeneza kwamba ika-define who is the accredited journalist? Kwa nini nasema hivi? Kuna watu wamesema hapa, uandishi wa habari ili sasa kulinda watu ambao wameshakuwepo kwenye taaluma hii, tunaweza tukasema katika hizo sifa za huyo accredited journalist pawepo na sifa za kitaaluma kwa maana ya labda elimu ya kidato cha nne au elimu ya diploma au elimu ya certificate, lakini pia tuka-take into consideration kwamba kuna watu ni waandishi nguli, hawakwenda darasani katika taaluma ile ya uandishi wa habari. Tukatafuta namna ya ku-equate kwamba huyu mtu by experience anaweza kuwa kwa experience yake akawa sawa na mtu mwenye stashahada au mwenye degree, ndiyo mapendekezo yangu. (Makofi)
Mhehimiwa Mwenyekiti, nasema hivi ili kusudi tuendelee kuilinda taaluma especially kwa wale ambao wamekuwepo kwenye fani by experience na wamethibitisha uwezo wa kufanya kazi kwa ufasaha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ni lazima tukiunge mkono kwenye muswada huu ni kuwepo kwa Media Training Fund. Waandishi wengi wangependa sana kujiendeleza kitaaluma, lakini kipato duni kimewakwamisha. Sasa sheria inapokuja na mfuko wa namna hii ni sehemu mojawapo ya kuwakwamua hawa waandishi wa habari waweze kupata mafunzo. Naamini kuna waandishi wengi wangependa kupata mafunzo lakini kipato duni kimewakwamisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala zima la Baraza la Habari, nimeona pale haijaeleza sifa za yule Katibu wa Baraza la Habari kama ambavyo imeeleza kwa yule atakayekuwa Mkurugenzi. Kwa hiyo, ushauri wangu pengine pamoja na mengine yote ingeenda clearly kusema awe na sifa gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kugharamia, nilivyosoma kwenye muswada, hakuna mahali ambapo Baraza chanzo chake cha fedha kitakuwa ni kipi kama ambavyo imeeleza kwenye Mfuko wa Mafunzo. Nashauri kwamba kitaalam itazamwe ni namna gani inaweza ikaingia pale? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 58 ni ukombozi wa hali ya juu kwa waandishi wa habari na wote wanaofanya kazi. Ndugu zangu Wabunge, katika tasnia hii kuna unyonyaji uliokithiri na usioelezeka kutoka kwa wamiliki, ndiyo maana wakati mwingine ndugu yangu Mheshimiwa Kubenea nikiona anatetea sana, pengine anatetea kwa upande wa umiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu waandishi katika nchi hii wanafanya kazi kwa kukopwa. Mtu mpaka leo hajalipwa mshahara wa mwezi uliopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, mwingine analipwa kwa story. Muswada huu hasa katika kipengele cha 58, nchi hii ina vyombo vingi sana vya habari, lakini wote waliopo kwenye fani hii watakubaliana nami, asilimia 60 ya waandishi ni wale tunaowaita wa kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu haujasema sana kuhusu asilimia hii inayokaribia 60 kwa sababu umeeleza kwamba mwajiri ni lazima amtengenezee mwandishi mazingira yakiwemo ya kinga ya bima, lakini waandishi wa kujitegemea ambao ndio wengi katika tasnia hii, umebaki kama uko silent. Nashauri kitaalam tuone namna gani tunaweza tukafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Kwa sababu kwa kufanya hivyo, tutaondokana na mambo mengi. Pengine mwandishi welfare yake ikiwa iko vizuri, tutapunguza mambo mengi hata ya rushwa ndogo ndogo, ndiyo maana nasisitiza hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona kifungu cha 50, bahati nzuri nimeona kwenye amendment kuhusiana na ile mitambo kwamba mchapishaji naye anaweza kuingia kwenye matatizo na mitambo pengine ikachukuliwa. Bahati nzuri nimeona imeondolewa, ni jambo la kupongeza kwa sababu mchapishaji anachapisha magazeti lakini pia ana kazi nyingine, anachapisha vitabu ana watu amewaajiri. Sasa kwa kufanya kosa hilo kwamba mitambo ichukuliwe, ilikuwa ni kuleta damage siyo kwake tu lakini kwa chain kubwa ya watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema vyanzo vya mapato kwa maana ya wamiliki ni jambo ambalo tulizingatie tukizingatia kwamba huu ni mhimili wa nne wa dola kama ambavyo tunasema. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri, utakapokuja kuunda kanuni, sijui kisheria utaiwekaje, lakini kuna kila sababu ya kuangalia namna ya kulinda welfare ya waandishi wa habari dhidi ya wamiliki wa vyombo vya habari. Hapo kwa kweli kumekuwa na unyanyasanyi na unyonyaji uliopitiliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana.