Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Cosato David Chumi (34 total)

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Hospitali ya Mji wa Mafinga inahudumia wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na pia Wilaya jirani za Mbarali na Iringa Vijjini lakini pia iko kandokando ya barabara kuu, hivyo kukabiliwa na mzigo mzito wa kuhudumia majeruhi wa ajali zinazotokea kwenye barabara hiyo kama ile ya Mafinga:-
Je, Serikali iko tayari kuiongezea hospitali hiyo fedha na watumishi mara mbili zaidi ya kiwango inachopata sasa iweze kuwa na uwezo wa kutosha kukabiliana na mzigo wa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiipatia hospitali hii fedha kwa ajili ya kuendesha huduma ambako kwa mwaka wa fedha 2016/2017, fedha zilizotengwa ni shilingi milioni 90 kwa ajili ya maendeleo na shilingi milioni 90 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za uboreshaji huduma za afya, Serikali imesisitiza umuhimu wa kila Halmashauri kuboresha makusanyo ya ndani kupitia mifumo ya afya ya jamii yaani CHF/TIKA na fedha za makusanyo mengine kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma katika hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu watumishi, Hospitali ya Wilaya ya Mafinga ina jumla ya watumishi 209, upungufu ikiwa ni watumishi 95 sawa na asilimia 31.3. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imeidhinishiwa kuajiri watumishi 18 na itaendelea kuongeza idadi hiyo kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya hospitali hiyo.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Wavunaji na watumishi wa msitu wa Taifa Sao Hill wanapata huduma za kijamii na mahitaji yao katika Jimbo la Mafinga Mjini na kwa kuwa msimu uliopita hakuna kijiji au mtaa hata mmoja uliopata kibali cha kuvuna msitu katika Jimbo hilo:-
(a) Je, Serikali iko tayari kutoa kibali cha kuvuna msitu kwa kila kijiji au mtaa ili fedha zitakazopatikana kutokana na vibali hivyo ziweze kusaidia shuguli za kuboresha huduma za jamii kama vile kuchonga madawati na kumalizia ujenzi wa zahanati?
(b) Je, Serikali iko tayari kutoa vibali vya kuvuna misitu kwa vikundi rasmi vya wajasiliamali ili kuwasaidia kukuza mitaji yao na kujipatia maendeleo ya kiuchumi?
(c) Je, ni kiasi gani cha fedha kimetolewa kama sehemu ya kurejesha hisani kwa jamii kutoka kwa kampuni ya misitu na viwanda vikubwa vya mazao ya misitu vilivyopo kwenye Jimbo la Mafinga na maeneo ya jirani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugawaji wa malighafi kutoka katika mashamba ya miti unaongozwa na Mwongozo wa Uvunaji wa mwaka 2007 uliofanyiwa mapitio mwaka 2015. Aidha, Wizara yangu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania imekuwa ikipokea na kuyafanyia kazi maombi mengi ya vibali vya uvunaji vyenye uhitaji wa mita za ujazo nyingi kuliko kiwango kinachoruhusiwa ikilinganishwa na uwezo wa mashamba wa kutoa malighafi kwa viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu kwa mwaka. Kwa mfano mwaka 2015/2016, jumla ya maombi 4,986 ambayo yalihitaji mita za ujazo 15,454,214 yalipokelewa na kufanyiwa kazi. Hata hivyo, ni maombi 1,030 pekee yenye jumla ya mita za ujazo 740,800 yaliidhinishwa, ambacho ndicho kiwango cha ukomo kulingana na uwezo wa mashamba katika mwaka huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uchache wa malighafi, Wizara imekuwa inatoa kipaumbele cha vibali vya uvunaji miti kwa viwanda vyenye mikataba na Serikali, miongoni mwao ni baadhi ya viwanda vya Serikali vilivyobinafsishwa, viwanda vingine vikubwa na vya kati, ikifuatiwa na wavunaji wadogo wadogo, vikundi na taasisi za watu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitoa vibali pia kwa wadau na vijiji vinavyopakana na misitu kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa madawati. Kwa mfano, katika shamba la miti la Sao Hill kati ya mwaka 2010/2011 na 2015/2016 vibali vya uvunaji kwa vijiji 183 vyenye thamani ya sh. 2,820,000,000 vilitolewa. Vile vile, shamba la Sao Hill lilihifadhili miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi milioni 880 ikiwemo utengenezaji wa madawati katika vijiji 23.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uzoefu wa hivi karibuni Wizara yangu imeona haja ya kupitia upya mwongozo wa uvunaji wa mwaka 2007 kwa namna ambayo itazingatia manufaa kwa jamii jirani na misitu hiyo kama ilani ya CCM inavyoelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu haina takwimu zinazohusu kiasi cha fedha zilizorejeshwa kama hisani kwa jamii kutoka kampuni na viwanda vikubwa vya mazao ya misitu vilivyopo kwenye Jimbo la Mafinga Mjini na maeneo ya jirani. Aidha, ushauri unatolewa kwa Mheshimiwa Mbunge awasiliane na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafinga ili aweze kupatiwa takwimu hizo.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Sudan Kusini imekubaliwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Je, ni lini Serikali itafungua Ubalozi katika nchi hiyo ili kutengeneza mazingira ya kunufaika na fursa zilizoko katika nchi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa la Sudan Kusini lilianzishwa mwezi Julai, 2011 baada ya kura za maoni za wananchi wa nchi hiyo kuamua kujitenga kutoka nchi ya Sudan na kuunda Taifa jipya ya Sudan Kusini. Aidha, mwezi Aprili, 2016 nchi ya Sudan Kusini ilijiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa sasa Tanzania haina Ofisi za Ubalozi nchini Sudan Kusini. Katika kipindi hiki ambacho Serikali haijafungua Ubalozi nchini Sudan Kusini, shughuli za Kibalozi kwa nchi hiyo zinafanywa na Ubalozi wetu, Nairobi nchini Kenya.
Malengo ya Wizara kwa mwaka 2016/2017 ni pamoja na kuongeza uwakilishi wetu nje ya nchi kwa kufungua Balozi mpya na Ofisi za Kikonseli hususan katika nchi ambazo Taifa linanufaika zaidi na fursa za kiuchumi kama vile soko la bidhaa zetu, biashara, uwekezaji, ajira pamoja na utalii.
Aidha, naomba ieleweke kuwa licha ya kuwepo kwa fursa hizo, maamuzi ya kufungua Ofisi za Ubalozi nchini Sudan Kusini pamoja na uendeshaji wa shughuli za Ofisi za Ubalozi zitakazofunguliwa zitategemea na Serikali itakapokuwa tayari Kibajeti.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapunguzia wasanii gharama
za ukaguzi wa filamu ambapo kwa hivi sasa gharama hizo ni shilingi elfu moja
kwa dakika?
(b) Je, Bodi ya Filamu imejipanga kwa kiasi gani kuhakikisha huduma
zake zinatambulika nchi nzima tofauti na sasa ambapo ni wasanii wachache wa
filamu ndiyo wanafahamu wajibu na majukumu wa Bodi hiyo ambayo hata ofisi
zake hazijulikani ipasavyo sehemu zilipo Jijini Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi,
Mbunge wa Mafinga Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ada za uhakiki kwa nchi yetu zipo kwa
mujibu wa sheria na kanuni. Gharama hizi hulipwa kwa nakala mama tu (master)
baada ya hapo mtayarishaji huzalisha nakala kwa idadi anayohitaji. Nchi yetu
hutoza ada ambazo ni rafiki ukilinganisha na nchi nyingine. Kwa mfano, Nigeria
ambayo ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwa upande wa filamu hutoza filamu
yenye urefu wa dakika 60 ambayo ni filamu ya lugha ya asili kwa naira 30,000
sawa na zaidi ya dola 150 ambayo ni sawa na Sh. 337,950 kwa viwango vya
ubadilishaji vya Sh. 2,253 kwa dola na Kenya ni sawa na Sh.190,000 za Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu hutoza filamu za Kitanzania zenye
urefu wa dakika 60 kwa Sh.60,000 sawa na Sh.1,000 kwa dakika. Gharama hizi ni
asilimia 18 ya zile za Nigeria na asilimia 32 ya zile za Kenya. Kwa maana hiyo, ni
wazi kwamba Tanzania hutoza ada ambayo ni nafuu na rafiki.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Filamu imeendelea kujitangaza
kwa wadau kupitia shughuli mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Mfano kushiriki
katika Maonesho ya Sabasaba, Nanenane, Wiki ya Vijana na Kilele cha Mbio za
Mwenge wa Uhuru na Jumuiya ya Afrika Mashariki Utamaduni Festivals. Vilevile
Bodi inatumia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo TBC1, E-FM, Clouds Media,
Gazeti la Mtanzania na kadhalika. Pia Bodi imekuwa ikifanya warsha za
kuwajengea wadau weledi katika masuala ya filamu sehemu mbalimbali
ikiwemo mikoa na wilaya ambapo ni sehemu ya kujitangaza. Aidha, Bodi
inakamilisha tovuti yake ambayo itasaidia kujitangaza na itaendelea kutumia
vyombo vya habari, machapisho na warsha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Bodi za Mikoa na Wilaya ambazo
zinafanya majukumu ya Bodi katika ngazi za Mikoa na Wilaya. Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI itaendelea kuimarisha Bodi za Mikoa na Wilaya ili ziweze
kutoa huduma kwa wigo mpana zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi za Bodi awali zilikuwa Barabara ya
Morogoro, Jengo la Textile ambapo hapakuwa rafiki kwa wadau. Mwaka 2012,
Wizara ilihamisha ofisi za Bodi kwenda Mtaa wa Samora, Jengo la Shirika la
Nyumba, Plot No. 2271/32 ambapo zipo Ofisi za Habari Maelezo mkabala na Tawi
la Benki ya NMB, ghorofa ya kwanza.
MHE. COSATO D. CHUMI Aliuliza:-
Serikali katika mwaka huu 2016 imeelekeza wazi kuwa haina mpango wa kununua magari ya wagonjwa na kwamba jukumu la kununua magari hayo limeachiwa Halmashauri za Wilaya ambazo hazimudu kununua magari hayo hali inayowafanya baadhi ya wahisani kujitolea kununua magari hayo.
Je, ni lini Serikali italeta mapendekezo ya kubadilisha sheria hiyo ili magari hayo yaingie kwenye Jedwali la Saba na hivyo kupata msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa haina mpango wa kuleta mapendekezo ya kubadilisha Sheria ya Ununuzi wa Magari ya Kubebea Wagonjwa. Jukumu la kununua magari hayo ni la Halmashauri husika ambao wanatakiwa kutenga fedha na kuhakikisha kuwa wananunua magari hayo kulingana na mahitaji. Wizara pindi inapopata misaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo imekuwa ikigawa magari hayo katika Halmashauri mbalimbali nchini kwa kuzingatia mahitaji.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Kodi ya mwaka 2014, Jedwali la Saba imeeleza kuwa ununuzi wa vifaa tiba utapatiwa msamaha baada ya kuridhiwa na Waziri mwenye dhamana ya afya. Magari ya kubebea wagonjwa ambayo yana vigezo ambavyo vimewekwa, huombewa msamaha wa kodi na Waziri wa Afya ambapo hupatiwa exemption certificate yaani hati ya msamaha na Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kujiridhisha kuwa yana vigezo stahiki. Niwasihi Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote wenye nia ya kusaidia kukabiliana na changamoto hii kwa kununua magari, kuwasiliana na Wizara ya Afya kuhusu vigezo
vinavyotakiwa kabla ya kuagiza magari hayo ili yaweze kustahili kupatiwa msamaha wa kodi.
Mheshimiwa Spika, sanjari na hilo, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuzihimiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga fedha za ununuzi wa magari haya kulingana na uhitaji halisi katika Halmashauri husika.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Serikali ilitoa Waraka Na.3 wa mwaka 2014 kuhusu Posho ya Madaraka kwa viongozi wa elimu wakiwemo Walimu Wakuu wa Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo na Waratibu Elimu Kata lakini tangu waraka huo utolewe yapata karibu miaka miwili sasa posho hiyo haijaanza kulipwa.
Je, ni lini Serikali itaanza kulipa posho hiyo ya viongozi wa elimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Viongozi kuanzia Julai, 2016. Walimu Wakuu wanalipwa kiwango cha shilingi 200,000 kila mwezi na Wakuu wa Shule na Warataibu wa Elimu Kata wanalipwa Posho ya Madaraka kwa kiwango cha shilingi 250,000 kwa mwezi. Kuanzia Julai, 2016 hadi Aprili, 2017, Serikali imelipa posho hiyo jumla ya shilingi bilioni 1.87. Posho hiyo inalipwa kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa elimu katika ngazi ya shule nchini.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA (K.n.y. MHE. COSATO D. CHUMI) aliuliza:-
Serikali ina utaratibu wa kuwalipa watumishi wa umma gharama za nauli ya likizo mara moja katika miaka miwili wakati wanaenda likizo.
Je, Serikali ipo tayari kuanzisha utaratibu wa kuwalipa gharama za nauli za likizo watumishi wa umma kila mwaka katika kuongeza, kupandisha morali ya kazi na pia kupunguza makali ya maisha?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, likizo ya mwaka ni haki ya kila mtumishi wa umma na haki hii imebainishwa katika kifungu cha 31 cha Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini Namba6 ya mwaka 2004 na Kanuni ya 97 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kulipa gharama za nauli kwa watumishi wa umma kwa ajili ya likizo umeainishwa katika Kanuni H. 5 (1) (a), (b) na (c) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009. Kwa mujibu wa kanuni hiyo, mtumishi wa umma anatakiwa kulipiwa gharama ya nauli kwa ajili yake, mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne kutoka kituo chake cha kazi hadi nyumbani kwake mara moja katika kipindi cha miaka miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuwapa motisha watumishi wa umma ili kuwaongezea morali ya kazi. Hata hivyo, motisha inayotolewa inapaswa kuzingatia hali ya uchumi wetu. Hali ya uchumi wetu kwa sasa inaruhusu utaratibu huu wa kulipa gharama za nauli ya likizo kwa watumishi wa umma mara moja katika kipindi cha miaka miwili. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha motisha kwa watumishi wa umma kadri uchumi unavyoimarika.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Kumekuwepo na matangazo mengi ya watu waliopoteza vyeti vya kitaaluma hasa vinavyotolewa na Baraza la Mitihani:-
(a) Je, ni utaratibu gani unaotumika pale mtu anapopoteza cheti ili aweze kupata cheti kingine?
(b) Je, anapata cheti halisi au nakala ya cheti?
(c) Baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa kwa Baraza la Mitihani wanapoombwa kuwasilisha cheti katika mamlaka fulani ambayo mtu ameomba kazi au nafasi ya masomo na hivyo kusababisha waombaji wengi kukosa nafasi kutokana na ucheleweshaji huo; je, ni taratibu gani mtu anatakiwa kuzifuata ili ombi lake lifanyiwe kazi ipasavyo na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mhitimu aliyepoteza cheti hupatiwa cheti mbadala au uthibitisho wa matokeo kwa kufuata utaratibu ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu upotevu wa cheti na kupata hati ya upotevu wa cheti na kupata hati ya upotevu. Lengo la kuripoti polisi ni kupata msaada wa kiuchunguzi ili kusaidia kukipata cheti kilichopotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kutangaza gazetini kuhusu upotevu wa cheti kwa lengo la kuutarifu umma ili kusaidia kukipata cheti kilichopotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, endapo hakikupatikana hata baada ya kutangazwa katika vyombo vya habari, mhitimu atajaza fomu ya ombi la cheti mbadala au uthibitisho wa matokeo na kuwasilisha Baraza la Mitihani la Tanzania. Fomu hiyo inapatikana kwenye Ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania na pia kwenye tovuti ya Baraza ambayo ni www.necta.go.tz.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne Baraza la Mitihani Tanzania hufanya uchunguzi wa uhalali wa umiliki wa cheti husika na kutoa huduma stahiki. Wahitimu waliofanya mtihani kuanzia mwaka 2008 ambao vyeti vyao vina picha, hupatiwa vyeti mbadala (Duplicate Certificate) na waliofanya mtihani kabla ya mwaka 2008 hupatiwa uthibitisho wa matokeo ambao hutumwa kwa waajiri wao au mahali pengine kwa mahitaji yaliyotolewa na mwombaji. Hivyo, kundi hili la pili hawapewi cheti mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cheti mbadala kinachotolewa ni cheti halisi. Hata hivyo, kinaongezewa maandishi yanayosomeka Duplicate kuonesha kuwa cheti hicho kimetolewa kwa mara ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwombaji wa cheti mbadala au uthibitisho wa matokeo hupatiwa huduma baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika na zilizowekwa.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Wanariadha wa baadhi ya nchi ambazo kijiografia mazingira yao yanafanana na baadhi ya maeneo katika nchi yetu wamekuwa wakishiriki katika mashindano ya riadha ya majiji makubwa duniani kama vile New York Marathon, Tokyo Marathon na kadhalika na hivyo kuzitangaza nchi zao ipasavyo.
Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa inafufua mchezo wa riadha ili kutumia kutangaza utalii wa nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa baadhi ya nchi zimekuwa zikifanya vizuri katika mashindano makubwa duniani na hivyo kuzitangaza nchi zao ipasavyo. Hata hivyo, nchi yetu imeanza kufanya vizuri katika mashindano ya riadha kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma kupitia kwa wanariadha wake kama vile Francis Naal, Samson Ramadhani, Gidamis Shahanga, Juma Ikangaa, Suleiman Nyambui na Filbert Bayi. Mathalani, nchi yetu imeweza kupata mafanikio katika riadha hivi karibuni kupitia wanariadha wake kama ifuatavyo:-
(a) Alphonce Simbu aliyekuwa mshindi wa kwanza na kupata medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Standard Chartered Mumbai Marathon, India tarehe 15 Januari, 2017;
(b) Cecilia Ginoka Panga aliyeshinda Beijing International Half Marathon yaliyofanyika tarehe 16 Aprili, 2017; na
(c) Emmanuel Giniki Gisamoda aliyeshinda Shanghai International Half Marathon yaliyofanyika tarehe 23 Aprili, 2017.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuleta maendeleo endelevu ya mchezo wa riadha na michezo yote kwa ujumla, pamoja na mambo mengine, Wizara inakamilisha mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 ili kuhakikisha inaendana na mahitaji ya sasa katika maendeleo ya michezo ikiwemo kuimarisha uendeshaji na usimamizi katika ngazi zote, ugharamiaji pamoja na uibuaji na uendelezaji wa vipaji katika ngazi mbalimbali.
Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeendesha mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA ambayo pamoja na mambo mengine, yanalenga kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wetu katika mchezo wa riadha. Aidha, hivi sasa Wizara yangu inakamilisha taratibu za kuandaa miongozo ya Kiserikali ili kuwezesha wadau wote kuendesha kuendesha shughuli zao katika mazingira ya weledi na stadi bora za michezo.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia kwa kushirikiana na wadau inatekeleza programu mbalimbali za kuendeleza mchezo wa riadha nchini ikiwemo Kilimanjaro Marathon, Bagamoyo Marathon, Tulia Marathon, Heart Marathon na kadhalika ambayo hushirikisha wanarisha kutoka ndani na nje ya nchi. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Mataifa makubwa duniani yanayoongoza kwa kuharibu mazingira, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa na mifuko kama vile Climate Investment Funds (CIF), Global Environment Facility (GEF), Green Climate Fund (GCF) na kadhalika wamekuwa wakitenga fedha kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Je, Taifa limejipangaje kunufaika na fedha za mifuko hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niombe radhi kwa sauti, lakini pia kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako tukufu naomba nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati.
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais kushughulikia Muungano na Mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimshukuru Makamu wa Rais Mama yetu mama Samia Suhulu na wafanya kazi wote wa Ofisi yetu ya Wizara yetu kwa ushirikiano mkubwa wanaouonesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri Mkuu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa ambao anauonesha kwetu. Lakini nisisahau kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Singida Mjini pamoja na familia yangu kwa ushirikiano wanaouonesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya shukrani hizo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira nijibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuendeleza kunufaika na fedha kutoka katika Mifuko ya Kitaifa ya Mabadiliko ya tabianchi, Serikali imejipanga kwa kuandaa mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2012 na inakamilisha Mpango wa Taifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi, kukamilika kwa mkakati huo kwa mpango huo utaiwezesha nchi kunufaika na fedha kutoka mifuko hiyo. Mkakati wa mpango huo umeainisha maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya kuandaa miradi ya kukabiliana na mabaliko ya tabianchi ambayo imeombewa fedha na utekelezaji kutoka katika mifuko hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutumia fursa hii kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Tanzania tayari imeanza kunufaika na fedha za mifuko hiyo kupitia mfuko wa GEF, tunatekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na miradi ya kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame ya Tanzania ambapo tumepata dola za Kimarekani 7,155,963 na mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kupitia mfumo ikolojia katika maeneo ya vijiji nchini Tanzania tuliopata dola za Kimarekani 7,571,233.
Aidha, kwenye mfuko wa GEF katika mzunguko wake wa sita zilitengwa dola za Kimarekani milioni mbili ambazo zinatumika kwa ajili ya kutekeleza miradi midogo midogo ya nchi. Mfuko wa GCF ulianzishwa mwaka 2011 na ulianza kutoa fedha mwaka 2015. Kwenye mfuko huo Tanzania ilitarajia kupata dola za Kimarekani 124 kwa ajili ya mradi wa maji wa Simiyu unaotekelezwa chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha Tanzania inakamilisha utaratibu wa kupata dola za Kimarekani 300,000 kutoka GCF; ambazo zinatumika kujenga uwezo kwa Taasisi zetu ili ziweze kuandaa miradi itakayofadhiliwa na mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Climate Investment Fund inajumuisha mifuko miwili iliyoanzishwa mwaka 2008, mifuko hiyo ni Clean Technology Fund na Strategic Climate Fund. Mdhamini wa mifuko hii ni Benki ya Dunia, mifuko hii hutoa mikopo yenye riba nafuu kwa nchi zinazoendelea na kwa ajili kutekeleza miradi ya kupunguza uzalishaji wa gesi joto ambayo siyo kipaumbele cha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kukuza uelewa na kuhamasisha sekta mbalimbali kutekeleza mkakati wa mabadiliko ya tabianchi kwa kuandaa miradi ambayo inakidhi vigezo vya vifuko hii ili Taifa liendelee kunufaika na fedha hizi. Aidha, Serikali kupitia taasisi zake mbalimbali imefanya tijihada za kujisajili yaani accreditation na Mfuko wa Mabadiliko wa Tabianchi ili taasisi hizi ziweze kuwasilisha maombi ya fedha hizo moja kwa moja kutoka mifuko hiyo. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Serikali kupitia Kanuni mbalimbali za Utumishi inatambua mtumishi wa mke au mume na watoto au wategemezi wanne. Hata hivyo, utumishi wa umma hautambui baba wala mama hasa linapotokea tatizo la msiba, mara zote huduma ya misiba ya wazazi imekuwa ni jukumu la mtumishi mwenyewe:-
Je, ni lini Serikali itawajumuisha wazazi wa mtumishi kama wanufaika wa huduma mbalimbali anazopata mtumishi wa umma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato Chumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma, Toleo la Mwaka 2009, huduma ya mazishi hutolewa kwa mtumishi mwenyewe na wategemezi wanne. Serikali haigharamii mazishi ya baba au mama wa mtumishi kutokana na ukweli kwamba wapo wazazi wenye watoto zaidi ya mmoja katika utumishi wa umma na katika maeneo tofauti nchini. Endapo kwa mfano wazazi wa mtoto zaidi ya mmoja ambao katika utumishi wa umma watafariki Serikali ingelazimika kulipa gharama pengine mara tatu au zaidi kwa kuwa hakuna mfumo madhubuti wa kutambua watu ili kubaini wazazi wenye watoto zaidi ya mmoja katika utumishi wa umma. Kwa kuwa sasa Serikali haina mfumo jumuishi wa utambuzi na udhibiti wa taarifa hizi ingelipa gharama kubwa za huduma za mazishi za mara nne au mara tano au mara tatu kwa mzazi mmoja aliyefariki.
Mheshimiwa Spika, ili kuziba pengo lililopo la kuhudumia mazishi ya wazazi, Serikali imeruhusu watumishi wenyewe kuchangiana kupitia vyama vya hiari ambapo michango yao hufunguliwa akaunti maalum ili inapotokea misiba ya wazazi waweze kupeana rambirambi katika Mifuko ya Kufa na Kuzikana. Kupitia mifuko hii, watumishi wanapofiwa na ndugu zao wa karibu wakiwepo wazazi huwa wanapewa rambirambi. Aidha, huwa kuna michango ya rambirambi ya papo kwa papo inayosaidia gharama za misiba ya watumishi na ndugu wa karibu wakiwemo wazazi, na endapo wazazi wapo mbali na vituo vya kazi watumishi hupewa ruhusa maalum ya siku 14 kushiriki katika misiba.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Tunapoelekea kujenga uchumi wa viwanda ni wazi kuwa fursa za kibiashara zinazojitokeza nyingi zitafanywa na wajasiriamali wadogo; hata hivyo muundo wa kazi kwa kada ya Maafisa Biashara katika Halmashauri zetu umefichwa ndani ya Idara ya Fedha, pamoja na kazi na uzito wa majukumu ya biashara siyo idara wala kitengo:-
Je, ni lini Wizara kwa kushirikiana na Utumishi itafanya kada hii kutambulika kwa uzito wake ili wanufaike na uwepo wa Maafisa Biashara kuliko ilivyo hivi sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika muundo wa sasa wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulioidhinishwa mwaka 2011 wenye Idara 13 na Vitengo Sita, kada ya Maafisa Biashara ipo ndani ya Idara ya Fedha na Biashara. Napenda kulialifu Bunge lako Tukufu kuwa hivi sasa Serikali inaufanyia mapitio ya kina muundo huo kwa kuzingatia uzito wa kazi kwa kila kada ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Cosato David Chumi kwa kuwa maudhui ya swali lake yamechangia mawazo mazuri katika mapitio ya muundo wa Serikali za Mitaa yanayoendelea.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali italeta mabadiliko katika sheria inayosimamia malipo ya fidia kwa askari anayejeruhiwa au kupoteza maisha akiwa anatekeleza majukumu ya kulinda usalama ndani au nje ya nchi kwenye vyombo vya UN au SADC Mission ili kuendana na mabadiliko ya kupanda kwa gharama za maisha?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, malipo ya fidia kwa askari aliyejeruhiwa au kufariki akiwa anatekeleza majukumu ya ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa hupangwa na kusimamiwa na Umoja wa Mataifa. Kwa kawaida, Umoja wa Mataifa hukaa vikao vya maamuzi na kutoa waraka ambao kwa ujumla hutekelezwa na nchi zote zilizopeleka majeshi katika Misheni za Umoja wa Mataifa unaofafanua stahiki mbalimbali za malipo kwa wanajeshi wanaoumia au kufariki wakati wa kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani. Waraka huo huzijulisha nchi wanachama zinazochangia vikosi, Maafisa wanadhimu na waangalizi wa amani stahiki ya malipo. Hivyo, siyo jukumu la nchi husika kuamua ilipwe fedha kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Misheni za SADC, hadi sasa hakuna Misheni inayomilikiwa na SADC pekee, bali iliyopo inaitwa Force International Brigade ambayo imeunganishwa na Misheni ya Umoja wa Mataifa nchini DRC ambayo taratibu za kulipa askari aliyeumia au kufariki bado inasimamiwa na Umoja wa Mataifa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa afisa au askari aliyeumia, utaratibu huo hufanyika kwa kuwasilisha nyaraka muhimu ambazo hutoa mwelekeo wa kiwango alichoumia ili alipwe kulingana na stahili.
Mheshimiwa Spika, kwa afisa au askari aliyefariki, Umoja wa Mataifa kwa sasa inalipa fidia ya dola za Kimarekani 70,000 kwa askari wa nchi yoyote aliyefariki akiwa anatekeleza majukumu ya ulinzi wa amani katika Misheni za Umoja wa Mataifa.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, Serikali iko tayari kubadilisha sheria/kanuni ili kuruhusu mazao ya misitu kusafishwa usiku na mchana (saa 24)?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Kuzuia Kusafirishwa kwa Mazao ya Misitu Na. 68 ya 2000, iliwekwa kutokana na changamoto za usafirishaji haramu wa mazao ya misitu ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni vigumu sana kudhibiti uhalifu huo wakati wa usiku. Ukaguzi wa kina wa mazao ya misitu hufanyika kwenye kituo cha mwanzo cha safari na vituo vya ukaguzi vilivyoko barabarani kwa kukagua nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na kibali cha usafirishaji na kuangalia aina ya mazao, jamii ya miti na kiasi kinachosafirishwa. Kutokana na ugumu wa ukaguzi nyakati za usiku Serikali ilitunga Sheria ya Kuzuia Usafirishaji wa Mazao ya Misitu Nyakati za Usiku.

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine iliyopelekea kuwepo kwa zuio la kusafirisha mazao ya misitu usiku wakati huo ni pamoja na uhaba wa watumishi, udanganyifu na ubadhirifu hali ambayo kwa sasa imeshughulikiwa. Hivyo, Wizara itaanza kutoa vibali maalum kwa wasafirishaji wa mazao ya misitu ya kupandwa kusafirishwa masaa 24. Mfano, mwaka 2018 kupitia Tangazo la Serikali Na. 478, Serikali imetoa kibali cha kusafirisha usiku nguzo za umeme kwa saa 24 ili kuharakisha usambazaji wa umeme vijijini.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Barabara za Mji Mafinga hazipitiki kwa mwaka mzima na kati ya kilomita 407 kwa mujibu wa DROMAS lami ni kilometa 5.58.

Je, Serikali ipo tayari kuongezea fedha TARURA ili ijenge barabara za kupitika kwa mwaka mzima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa DROMAS Mji wa Mafinga una Mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 325.67. Aidha, urefu wa mtandao wa barabara unatarajiwa kuongezeka pindi zoezi la uhakiki wa mtandao wa barabara linaloendelea litakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Mji wa Mafinga ili kuhakikisha zinapitika wakati wote na imeongeza bajeti ya matengenezo ya barabara kwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga kutoka Shilingi milioni 876.81 mwaka kwa fedha 2017/2018 hadi Shilingi bilioni 1.036 mwaka wa fedha 2019/2020. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini yaani (TARURA) unakamilisha zoezi la kuhakiki mtandao wa barabara zake na itaweka vipaumbele vya ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja kwa kuzingatia urefu na umuhimu wa barabara husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kupitia formula ya mgao wa fedha za Mfuko wa Babarara ili kuona namna bora ya kuiwezesha TARURA kwa kuiongezea fedha ili iweze kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika halmashauri mbalimbali nchini, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, ni lini Halmashauri ya Mji wa Mafinga itaingia katika mpango wa uendelezaji na uboreshaji wa Miji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) iliingia makubaliano ya mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha miji nchini. Programu hii ina maeneo mawili katika uboreshaji; uboreshaji wa miundombinu na kuzijengea uwezo Halmashauri hizi ili ziweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vigezo vilivyokuwa vimewekwa katika programu hii ni kuwa, ili Halmashauri iweze kuingia katika utekelezaji wa programu ni lazima iwe Manispaa au Mji. Hivyo, Mafinga ilikosa sifa za kuwa katika programu hii kwa wakati huo, ambapo ilianza kutekelezwa mwaka 2012, bado Mafianga haikuwa na hadhi ya Mji. Utekelezaji wa programu hii ulipaswa kukamilika Desemba, 2018. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali programu hii imeongezewa muda hadi Juni, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika utekelezaji wa programu hii, Serikali imeanza mazangumzo na Benki ya Dunia ili kuwa na programu nyingine ya uboreshaji na uendeshaji wa miji nchini itakayoanza baada ya kwisha kwa programu hii ya sasa. Serikali itatoa kipaumbele kwa Miji na Manispaa ambayo haikuwepo kwenye programu awamu ya kwanza ikiwemo Mafinga Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanzisha Wilaya ya TANESCO katika halmashauri ya Mji wa Mafinga ili kukabiliana na kasi ya ukuaji (kiviwanda na kimakazi) wa Mji wa Mafinga?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mufindi ina halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga. Katika halmashauri ya Mji wa Mafinga tayari ipo ofisi ya wilaya ya TANESCO inayotoa huduma kwa wananchi wa Mji wa Mafinga pamoja na wananchi wa Wilaya ya Mufindi. Kwa sasa, Ofisi ya TANESCO iliyopo Mafinga inakidhi mahitaji ya kutoa huduma kwa wananchi wote wa Mji wa Mafinga. Hata hivyo, Serikali kupitia TANESCO itaendelea kuboresha huduma za ofisi hiyo ili kukidhi ukuaji wa shughuli za biashara za wananchi wa Halmashauri ya Mafinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kusogeza huduma zaidi kwa wananchi, TANESCO ilifungua ofisi ndogo (sub office) katika maeneo ya Igowole, Kibao na Mgololo. Ofisi hizi ni kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa urahisi kwa wananchi wa maeneo husika. Katika hatua za muda mfupi za kukabiliana na kasi ya ukuaji wa viwanda na makazi katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Serikali kupitia TANESCO imeongeza njia ya pili ya umeme (Ifunda Feeder) ya msongo wa kilovoti 33 kutoka kituo cha kupooza umeme cha Tagamenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua nyingine, TANESCO ina mpango wa kujenga kituo kikubwa cha kupooza umeme (Grid substation) katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga na Kazi ya upembuzi yakinifu imekamilika mwezi Januari, 2019 na ujenzi wa kituo unatarajiwa kukamilika Mwaka wa Fedha 2019/2020.
MHE. COSATO D. CHUMI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi wa Barabara za lami na kufunga taa za barabarani katika Mji wa Mafinga chini ya Mpango wa Uendelezaji Miji nchini?
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia mimi na Waheshimiwa Wabunge wote afya njema na kutuwezesha kuwa wawakilishi wa wananchi kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa imani kubwa aliyonipa kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Wanging’ombe kwa kunichagua na kuchagua mafiga matatu ya Chama cha Mapinduzi na niwahakishie utumishi uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nijibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi,Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Miji ya Kimkakati (Tanzania Strategic Cities Projects -TSCP) umetekelezwa katika Halmashauri za Majiji ya Tanga, Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza na Halmashauri za Manispaa za Mtwara- Mikindani, Ilemela na Kigoma-Ujiji kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 355.5 sawa na shilingi bilioni 799.52.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Miji 18 (Urban Local Government Strengthening Programme - ULGSP) umetekelezwa katika Halmashauri za Manispaa za Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Iringa, Mpanda, Lindi, Singida, Musoma na Bukoba na Halmashauri za Miji Kibaha, Babati, Geita, Korogwe, Bariadi na Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Miji ya Kimkakati (TSCP) pamoja na Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Miji 18 (ULGSP) ilimalizika muda wake Mwezi Desemba, 2020. Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuanza kutekeleza Programu nyingine ya kuendeleza miundombinu itakayohusisha Halmashauri26 zilizokuwepo kwenye Programu zilizomalizika pamoja na Halmashauri nyingine 19 za Miji ikiwemo Mafinga.
MHE. COSATO D. CHUMI Aliuliza:-

Kituo cha Uwekezaji (TIC) kinampa haki mwekezaji kuajiri wataalam lakini upande wa pili sheria inampa mamlaka Kamishna wa Kazi kufanya maamuzi kuhusu maombi ya vibali vya kazi:-

Je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya sheria ili kuondoa mgongano huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili, naomba nichukue fursa hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Shinyanga ambao walinichagua kwa kishindo. Pia nikishukuru zaidi Chama cha Mapinduzi, wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa kishindo nchi nzima usio na mashaka yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pole kwa wananchi wa Shinyanga kwa kupotelewa na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, Ndugu Erasto Kwilasa. Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu, amina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kufungua milango kuwavutia wawekezaji kuwekeza nchini. Serikali kupitia Sheria ya Uwekezaji, Sura 38 kama ilivyofanyiwa marekebisho na marejeo yake mwaka 2015 inatoa motisha mbalimbali (incentives) kwa wawekezaji. Miongoni mwa motisha hizo ni kuwaruhusu wawekezaji kuajiri wataalam wa kigeni watano, kwa lugha ya kigeni inaitwa Immigration Quota wakati wa hatua za awali za utekelezaji wa miradi yao (startup period) inapoanza kufanyika chini ya kifungu cha 24 cha Sheria ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulinda uchumi wetu, ajira za wazawa, maslahi na usalama wa nchi yetu, Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Na.1 ya mwaka 2015 kupitia kifungu cha 5(1)(b) na 11 kinampa Kamishna wa Kazi mamlaka ya kusimamia ajira za raia wa kigeni nchini kwa lengo la kuhakikisha ajira zinazotolewa kwa wageni ni zile ambazo sifa za kielimu, ujuzi, uzoefu wa kazi ni adimu hapa nchini. Katika kutekeleza jukumu hili, Kamishna wa Kazi hupokea na kuchambua maombi ya vibali vya kazi vya raia wa kigeni kutoka kwenye kampuni/taasisi zinazohitaji kuajiri wageni wanaokidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria tajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamishna wa Kazi ameendelea kuzingatia sheria zote, taratibu, sera na kanuni katika kufikia maamuzi yake. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge katika kupokea maoni na mapendekezo yanayolenga mabadiliko ya sheria na sera ili kuimarisha zaidi uwekezaji nchini bila kuathiri matakwa ya sera, sheria, taratibu na kanuni na miongozo iliyowekwa nchini.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kuruhusu wananchi wanaoishi kwenye Miji ambayo ipo kando ya barabara kuu kama Mji wa Mafinga kufanya biashara kwa saa ishirini na nne?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kubuni mikakati mbalimbali katika kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo ikiwa ni pamoja na kuwatengea maeneo kwa ajili ya kuendesha biashara zao na kuwatambua kwa kuwapatia vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo na watoa huduma. Kutokana na uhaba wa maeneo ya kufanyia biashara kwenye baadhi ya Miji, yameanzishwa masoko ya usiku ambayo yanaendeshwa kwa kufunga baadhi ya Mitaa nyakati za jioni hadi usiku kwa ajili ya kupisha wafanyabiashara wadogo kuendesha biashara zao. Baadhi ya Halmashauri hizo ni Jiji la Dodoma, Jiji la Dar-es-Salaam na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mheshimiwa Spika, uendeshaji wa biashara nyakati za usiku umeonekana kuwa na changamoto nyingi za ulinzi na usalama wa wafanyabiashara, wateja pamoja na bidhaa zao. Uzoefu unaonesha kuwa maeneo zinakofanyika biashara kwa saa 24 kuna miundombinu yote muhimu ikiwemo taa, kamera, vyoo na maeneo ya kuhifadhia bidhaa za wafanyabiashara.

Aidha, ili kuwa na usalama wa uhakika katika masoko, kunahitajika ulinzi wa Polisi au Askari wa akiba kwa maana ya Mgambo, hususan nyakati za usiku. Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama itaendelea kutafuta namna bora ya kuwezesha wafanyabiashara waishio kwenye Miji kando ya barabara Kuu ikiwemo Mafinga kufanya biashara zao kwa saa 24 ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu ya msingi.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kuanzisha Wilaya ya TANESCO kwa ajili ya kuhudumia viwanda na wananchi katika Mji wa Mafinga ili kuendana na kasi ya uchumi wa viwanda?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mufindi ina Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga. Katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, ipo Ofisi ya Wilaya ya TANESCO inayotoa huduma kwa wananchi wa Mji wa Mafinga pamoja na wananchi wa Wilaya ya Mufindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, Ofisi ya TANESCO iliyopo Mafinga inakidhi mahitaji ya kutoa huduma kwa wananchi wote wa Mji wa Mafinga ikiwa ni pamoja na wateja wa viwanda vikubwa 80, wateja wa viwanda vidogo vidogo 445 na wateja wadogo 23,207. Hata hivyo, Serikali kwa kutambua ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Mji wa Mafinga, TANESCO imefungua Ofisi Ndogo (Sub Office) katika Kata ya Igowelo, Kibao na Mgololo katika Kata ya Makungu. Ofisi hizi zimeanzishwa ili kusogeza huduma karibu kwa wananchi walio mbali na Mji wa Mafinga ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa urahisi kwa wananchi wa maeneo hayo.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:

Je, mpaka sasa ni wawekezaji wangapi wamemilikishwa ardhi na kupata Hati kupitia Kituo cha Uwekezaji TIC?
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji wa kigeni wanamiliki ardhi kwa ajili ya uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999. Kifungu cha 20 cha Sheria hiyo kinaelekeza kwamba, Kamishna wa Ardhi atatoa hati ya umiliki wa ardhi (Certificate of Right of Occupancy) kwa jina la Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya uwekezaji endapo uwekezaji huo unafanywa na mwekezaji wa kigeni. Kwa kutumia hati hiyo, TIC hutoa Hati ya Umiliki Isiyo Asili (Derivative Right) kwa mwekezaji wa kigeni aliyewasilisha maombi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mwekezaji kupewa Hati ya Umiliki Isiyo Asili na TIC, hati hiyo inasajiliwa na Msajili wa Hati (Registrar of Titles) ambaye anatoa hati ya umiliki wa ardhi hiyo (Derivative Title) kwa jina la mwekezaji wa kigeni kulingana na masharti ya uwekezaji husika kama yalivyoainishwa kwenye mkataba wake na TIC.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia utaratibu huo, tangu mwaka 1999 hadi mwezi Mei, mwaka huu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimewezesha upatikanaji wa Hati za Umiliki Zisizo Asili (Derivative Rights) 401 kwa wawekezaji wa kigeni.
MHE.COSATO D. CHUMI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa GN kuwezesha Mradi wa Regrow kuanza rasmi katika eneo la Kihesa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa tangazo la awali la siku 90 la nia ya kubadilisha matumizi ya sehemu ya eneo la Msitu wa Kihesa Kilolo, tarehe 9 Julai, 2021. Siku 90 tayari zimekwisha, hivyo Serikali imepanga kutoa GN ya Msitu wa Kihesa, Kilolo mwezi Novemba, 2021. Naomba kuwasilisha.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, lini Serikali inafungua Ubalozi Mdogo katika Jiji la Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili, baada ya Mheshimiwa Rais kuniamini kuendelea na nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini. Nami namwahidi kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na uadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imefungua Konseli Kuu katika Jiji la Lubumbashi, Jimbo la Haut Katanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ofisi za Konseli Kuu hiyo kwa sasa zipo katika Kiwanja namba 1174 Avenue Ruwe, Quartier, Makutano, Jijini Lubumbashi. Ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu Kuwa Konseli Mkuu tayari amewasili Lubumbashi tarehe 7 Februari, 2022. Aidha watumishi wengine wanaendelea kuripoti katika Kituo hicho kwa awamu kulingana na mahitaji na taratibu za kidiplomasia, ahsante sana. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, Serikali inaweza kuongeza uhai wa paspoti za muda wanazopewa Madereva hadi kufikia Miezi sita?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Pasipoti za muda wanazopewa madereva ni hati za dharura za safari (Emergency Travel Documents) ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati za Safari ya Mwaka 2002, hutolewa kwa safari moja kwa muda ulioainishwa ndani ya hati husika. Aidha, hati hii ya safari hutolewa kwa waombaji wenye safari za dharura.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la kuongeza muda wa hati za dharura za safari litahitaji mabadiliko ya sheria endapo itaridhiwa, Serikali inawashauri madereva kuomba pasipoti ili kuepuka usumbufu wa kuomba hati za dharura za safari mara kwa mara kwa vile safari zao siyo za dharura. Nashukuru.
MHE. DAVID C. CHUMI aliuliza: -

Je, Serikali inakusanya kiasi gani cha asilimia Tano ya zawadi ya washindi wa mchezo wa kubashiri na kimechangia kiasi gani kukuza michezo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka mwezi Septemba mwaka 2022, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi za Tanzania Bilioni 3.4 ikiwa ni asilimia Tano ya mapato yatokanayo na michezo ya kubashiri. Kwa mujibu wa muongozo wa mfuko wa Maendeleo ya Michezo fedha hizi hutumika kuhudumia Timu za Taifa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa michezo na wanamichezo, kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Timu za Tembo Warriors na Serengeti Girls ni miongoni mwa wanufaika wa hivi karibuni wa fedha hizo katika maandalizi na ushiriki wao kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa Walemavu na Wanawake chini ya miaka 17 ambapo zilifanikiwa kufika hatua ya robo fainali na kuipandisha daraja nchi yetu katika nafasi za soka Duniani. Ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, Bodi za Parole za Mkoa na Kitaifa zinakaa vikao vingapi kwa mwaka na wafungwa wangapi wamepata msamaha kwa mwaka 2020/2021?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Parole ya Taifa na Mikoa iliundwa kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 1994 na ikafanyiwa marekebisho na Sheria Na. 5 ya nwaka 2002 kwa lengo la kutaka wafungwa wengi wanufaike na mpango huu. Bodi za Mikoa na Taifa kisheria zinatakiwa kufanya vikao vyake angalau mara nne kwa mwaka.

Aidha, katika kipindi cha mwaka 2020/2021 idadi ya wafungwa waliopata msamaha kupitia Bodi ya Parole nchini ni 70. Nashukuru.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, ni lini Mafinga itanufaika na Mradi wa Umeme wa Peri-Urban?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya maeneo na Mitaa ya Mji wa Mafinga yatanufaika na Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili C (Densification IIC) ambao upo katika hatua za ununuzi wa Wakandarasi. Aidha, Serikali imekamilisha uhakiki wa vitongoji visivyo na huduma ya umeme na kuandaa mradi kabambe wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote uitwao Hamlet Electrification Project ambapo Mafinga Mjini nayo itanufaika na mradi huu. Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kuanzia Mwaka wa fedha wa 2023/2024 kulingana na upatikanaji wa fedha, nakushukuru.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, kwa kiasi gani Taifa linanufaika na vijana wanaopelekwa kwenye mafunzo ya kilimo Israel?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Israel zilikubaliana kushirikiana kwa kuanzisha programu ya kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaomaliza Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati vya Mafunzo ya Kilimo na Mifugo nchini Israel. Lengo la programu hiyo ni kuongeza ujuzi na maarifa juu ya teknolojia za kisasa.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2015 hadi sasa, jumla ya vijana 261 wa Kitanzania wamenufaika na mafunzo ya kilimo kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Israel (Ministry of Foreign Affairs Israel’s Agency for International Develeopment Cooperation) kupitia Agrostudies.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kuwatumia vijana waliohitimu mafunzo kwa vitendo nchini Israel kupitia programu ya BBT na Block farm ambapo wanapata fursa ya kuwashirikisha na vijana wengine uzoefu wao kutoka nchini Israel. Hadi sasa jumla ya vijana 79 walioshiriki mafunzo nchini Israel ni miongoni mwa vijana 812 walio kwenye mafunzo ya kilimo biashara katika Vituo Atamizi. Baada ya kipindi cha mafunzo, watapata fursa ya kufanya kilimo biashara kupitia mashamba ya pamoja ya block farms chini ya BBT.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, Serikali ipo tayari kuandaa mazingira kuwezesha biashara kati ya China na Tanzania kufanyika kwa shilingi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chusmi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika biashara za Kimataifa, wafanyabiashara wanao uhuru wa kutumia sarafu yoyote inayorahisisha biashara na inayokubalika na nchi nyingine kwa lengo la kupunguza gharama za miamala na muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itafanyia kazi jambo hili ili kuona ni nini kinapaswa kufanyika kuwezesha wafanyabiashara wa nchi ya China kukubali matumizi ya sarafu ya Tanzania, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, kwa kiasi gani Mkongo wa Taifa umesaidia kuboresha na kupunguza gharama za mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano nchi nzima ambao unafanyika kwa awamu mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ni kweli uwepo wa muundombinu huu umeboresha huduma za mawasiliano na kusaidia kupunguza gharama za mawasiliano kwa kupunguza gharama za uwekezaji kwa watoa huduma za mawasiliano ambao wangepaswa kujenga muundombinu kama huu kuboresha miundombinu na huduma zao. Hii imesaidia kupunguza gharama za mawasiliano (cost of backhaul transport bandwidth) kwa asilimia 99 na kufanya gharama za maunganisho kwa watoa huduma kupungua kutoka shilingi 157 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi mbili mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kupungua kwa gharama hizi kumesaidia kushuka kwa gharama za huduma kwa mtumiaji wa mwisho kutoka shilingi 147 kwa dakika mwaka 2009 hadi shilingi 30 kwa dakika mwaka 2022, sawa na asilimia 79.6; hii ni pasipo kutumia vifurushi.

Mheshimiwa Spika, matokeo makuu ya kushuka kwa gharama hizi kupitia miundombinu wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni kuongezeka kwa matumizi ya huduma za mawasiliano kwa wananchi na Serikali kwa ujumla. Ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kuiwekea SUMA JKT mazingira rafiki ili iweze kukopa na kutekeleza miradi yake kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, SUMA JKT wanaruhusiwa kukopa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134 kama ilivyo kwa mashirika mengine ya Serikali. Hivyo shirika litatakiwa kuwa na hali nzuri ya kifedha inayothibitisha uwezo wa taasisi kukopa na kulipa.

Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Uandaaji, Utekelezaji na Usimamizi wa Miradi na Majadiliano ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 2020 umeelekeza hatua muhimu za kuzingatia kwa Wizara au Taasisi ya Serikali ikiwa inaomba mkopo, dhamana na msaada, kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kutenga fedha za dharura kwa ajili ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA imekuwa ikitenga fedha za dharura sawa na asilimia tano ya bajeti ya fedha za Mfuko wa Barabara. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 11.45 kwa ajili ya fedha za dharura za matengenezo ya barabara nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha ya dharura kwa ajili ya kufanya matengenezo na ujenzi wa miundombinu ya barabara kulingana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kuboresha mtandao wa barabara unaohudumiwa na TARURA.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, Taifa linanufaika kiasi gani katika uuzaji wa bidhaa na huduma katika maeneo ambayo Jeshi letu linafanya ulinzi wa amani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imekuwa mstari wa mbele kushiriki katika jitihada mbalimbali za kutafuta amani kama ilivyoainishwa katika Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001. Hivyo, ushiriki wa Tanzania katika Misheni za Ulinzi wa Amani umekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo walinda amani wetu kufaidika na mafunzo ya ziada ambayo yanawajenga na kuwaimarisha; pia ajira za kiraia kwa Watanzania na kudumisha utamaduni wetu kupitia kukua kwa lugha ya Kiswahili, kwani katika maeneo mengi ya DRC, Lebanon na Darfur, kumekuwa na ongezeko la matumizi ya Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na manufaa yaliyoainishwa, zipo fursa za kiuchumi zinazopatikana katika shughuli za ulinzi wa amani, ikiwa ni pamoja na biashara ya bidhaa zinazoweza kutumika katika vikosi vilivyopo katika misheni hizo, kama vile chakula, mavazi, vinywaji, vifaa tiba na madawa. Fursa nyingine ni usafirishaji wa mizigo, ujenzi wa majengo yanayohamishika, vifaa, huduma za TEHAMA na nyinginezo. Aidha, Tanzania inaweza pia kuuza teknolojia ya kutumia panya katika kubaini na kutegua mabomu ambayo yametegwa ardhini kama fursa za kiuchumi, ahsante sana.