Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Cosato David Chumi (4 total)

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Kiswahili kinatambulika kama lugha ya nne kwa nchi za Afrika, lakini Bunge la Afrika linatumia Lugha ya Kiswahili katika vikao vyake. Nini kigugumizi cha kuzungumza Kiswahili katika Jukwaa la SADC?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; changamoto kubwa ya Kiswahili katika Jukwaa la SADC inaonekana ni ufinyu wa bajeti kwa ajili ya wakalimani. Je, Serikali haioni sasa ni wakati mzuri wa kutumia jukwaa hilo ili kuweka wakalimani ili kuweza kuzungumza Kiswahili ambacho tutaweze kukitangaza katika Nchi za SADC kwa ukubwa wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ninapenda kumhakikishia na kulihakikishia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi kwa ujumla kwamba hapakuwa na kigugumizi na ndiyo maana kumekuwepo na jitihada mpaka sasa. Pamoja na kuwa Kiswahili siyo lugha rasmi kati ya zile lugha rasmi za SADC, lakini kinatumika katika Mikutano ya Wakuu wa Nchi na Wakuu wa Serikali na ngazi ya Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, jitihada zinafanyika na kwa sasa, ili lugha iwe rasmi, lazima mabadiliko ya kanuni na miongozo ndani ya SADC yaweze kufanyiwa kazi ambayo Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba kipengele kile kinafanyiwa marekebisho ili kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya nne rasmi katika shughuli zote za SADC.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wakalimani, ni kweli kuna gharama kubwa sana za kugharamia masuala mazima ya kufanya ukalimani. Hata hivyo, kwa ushawishi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshawishi na kujenga hoja ili kusudi mzigo ule uweze kubebwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na SADC. Kwa sasa SADC katika mikutano inayoendelea, wamekubali kugharamia wakalimani katika shughuli zote zinazoendelea. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, bado tunakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa wakalimani. Kwa uzoefu nimeona, inafikia wakati wanaletwa Wakalimani wa Kenya katika Bunge la Afrika ambao wakati mwingine hata lafudhi yao siyo nzuri. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanaweza kusomesha wakalimani wa kutosha siyo tu kwa ajili ya kupelekwa kufanya ukalimani, lakini pia kuwapeleka dunia nzima ili waweze kufanya kazi ya kutangaza na kufundisha Kiswahili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anatropia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ndani ya Serikali kumekuwa na jitihada za kuhakikisha kwamba, Kiswahili pamoja na kuwa ni lugha yetu ya Taifa, lakini tunaifanya kama bidhaa, kwamba, tuwe na wakalimani wa kutosha katika maeneo mbalimbali kwa sababu, kwa kufanya hivyo wao pia, watatuingizia mapato kupitia fedha za kigeni. Mojawapo ya jitihada ni kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, kushirikiana na wenzetu wa BAKITA, kushirikiana na vyuo kwa sababu, ukalimani nao ni taaluma. Watu wengi hudhani kwamba, kwa kujua tu Kiswahili na Kingereza au Kiswahili na Kifaransa, basi automatically utakuwa mkalimani.

Mheshimiwa Spika, ukalimani ni taaluma. Kwa hiyo, tunatoa wito kwa vyuo vyetu chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu ya Juu kuhakikisha kwamba, wanatoa mafunzo ya ukalimani kama taaluma, ili na sisi tunapotembea katika mikutano mbalimbali duniani tukutane na wakalimani ambao ni Watanzania.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, katika hatua za kueneza Kiswahili duniani, Bunge liliwahi kuazimia na kuishauri Serikali kuweka madawati ya Kiswahili kwenye Balozi zetu. Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa azimio hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Ninachoweza kumjibu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, jitihada zinafanyika siyo tu katika Balozi zetu kuwa na Madawati ya Kiswahili, lakini pia, hata kushawishi Balozi nyingine za nje zinazowakilishwa hapa nchini ziwe na taratibu mbalimbali za kuhakikisha kuwa, zinakuwa na kitu kama Madawati ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo pia na jitihada mbalimbali kwa mfano hivi karibuni kutakuwa na shughuli kubwa sana kule Havana, Cuba ambayo ni mojawapo ya jitihada za kukuza Kiswahili siyo tu katika ukanda wa Afrika Mashariki na katika Bara letu la Afrika, bali duniani kwa ujumla. Kwa hiyo, jitihada hizo zinafanyika kwa ushirikiano ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na wizara nyingine za kisekta, ikiwemo kama nilivyosema, Wizara ya Elimu pamoja na wenzetu wanaosimamia utamaduni kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa pamoja na Baraza la Kiswahili la Zanzibar.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, Tanzania ndiyo waasisi wa Lugha ya Kiswahili na kwenye suala la Kiswahili huko duniani watu wengi wangependa kujua kusoma na kuandika. Ni kwa nini tusiwe na mikakati ya kuhakikisha kwamba, tunatoa walimu wengi kuwapeleka duniani, ili waweze kufundisha hiyo Lugha ya Kiswahili iweze kusambaa kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na nashukuru kwa swali. Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi na majibu mengine ya nyongeza, jitihada zinaendelea kufanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara pamoja na Wizara za Kisekta, ili kuhakikisha kwamba, kama nilivyosema vyuo vyetu pia, vifundishe ukalimani kama taaluma. Kwa sababu, kujua tu Kiswahili kama lugha na kujua Kiingereza kama lugha haitoshi sisi kuwafanya wakalimani.

Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe nakumbuka wakati nafanya masomo yangu Amsterdam niliwahi kuombwa kuwa mkalimani, lakini ile nilikuwa nafanya kama ukalimani kwa sababu, najua Kiingereza na Kiswahili, lakini, ili tuwe na wanataaluma kabisa wa ukalimani ni lazima kama Serikali na kama nchi, tuwekeze katika kuhakikisha kwamba, tunakuwa na wanataaluma hao na kwa kweli, jitihada zinafanyika na ndiyo maana makongamano maeneo mbalimbali yanafanyika. Pia kilishakuwa katika mikutano mingi ya Kimataifa, hasa inayofanyikia hapa nchini, lugha inayotumika inakuwa Kiswahili na kuwa na vitendea kazi ambavyo vinatumika kama vile kufanya ukalimani kwa wale ambao hawajui Lugha ya Kiswahili.