Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rose Vicent Busiga (7 total)

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nami naomba niulize swali la nyongeza.

Je, katika hizo fedha shilingi bilioni 8.75 Kituo cha Afya cha Nkhomola kitakuwa ni miongoni mwa vituo vya kupatiwa hizo pesa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rose, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, fedha hizi ambazo zimetengwa shilingi 8,750,000,000 zitakwenda kuainisha vituo vya afya 20 vyenye uchakavu wa hali ya juu zaidi. Kwa sababu sina orodha hapa naomba kwa ridhaa yako baada ya kipindi hiki nitaangalia na kuona kama kituo hicho ambacho amekitaja Mheshimiwa kipo kwenye orodha hiyo, ahsante.
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza: -

Ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata ya Ng'homolwa, Kijiji cha Nkweni?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rose Busiga, Mbunge wa Viti Maalum Geita, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba naamini kijiji hicho na kata hiyo ipo katika mradi wetu wa REA III Round Two, na kabla ya mwaka huu kuisha kijiji hicho kitakuwa pia kimepata umeme kwenye baadhi ya vitongoji na sasa maendeleo yataendelea kwenye vitongoji ambavyo vitakuwa vimebaki.
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naomba niulize swali la nyongeza. Katika Mkoa wetu wa Geita kuna nyumba nyingi sana za Askari ambazo ni chakavu; je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kukarabati nyumba hizo za askari ili askari wetu wa Mkoa wa Geita waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hapo awali kwamba kwa sasa Serikali tunatafuta fedha na zitakapopatikana, pamoja na maeneo mengine yenye uchakavu wa nyumba na vituo, tutahakikisha kwamba Mkoa wa Geita nao tunautazama, lengo na madhumuni sasa wananchi waweze kupatiwa huduma hizo vizuri zaidi, nakushukuru.

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Nami naomba kuuliza swali la nyongeza.

Ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inatatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Geita.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali nyongeza la Mheshimiwa Rose Busiga. Ninakupongeza kwa swali zuri lakini unafahamu nimeshafika Geita kufanya ziara na tuna miradi mingi sana ndani ya Mkoa wa Geita na fedha nyingi zimeweza kuelekezwa. Kwa hiyo, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha miradi hii iliyoanza inakamilika lakini miradi mengine tutaendelea kuibua kadri ya mahitaji.
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itakamilisha Barabara ya Geita – Bukoli – Kakola mpaka Kahama kwa kiwango cha lami ili kusaidia kuunganisha Mkoa wa Geita na Shinyanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja Mheshimiwa Rose ni moja ya barabara ambayo Serikali imeipa kipaumbele kikubwa sana. Ni kweli kwamba Mkoa wa Geita na Mkoa wa Shinyanga ulikuwa haujaunganishwa kwa kiwango cha lami na hii ndiyo ajenda kubwa ya Mkoa wa Geita. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kuanzia Kahama hadi Ilogi – Kakola, kwa kushirikiana na wenzetu wa bajeti, tayari tumeshasaini mkataba, kwa hiyo, hiyo barabara itajengwa. Tunavyoongea sasa hivi barabara ya kutoka Ilogi – Bukoli – Nyaluyeya hadi Geita, ipo kwenye mpango wa manunuzi ambayo muda wowote itatangazwa ili tuweze kuunganisha Geita na Kahama kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ni lini Serikali Kuu itatenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo hicho cha Nhomolwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa huduma hizo zinazotolewa ni huduma ndogondogo kama vile upimaji wa watoto au upimaji wa malaria, ni lini sasa kituo hicho cha afya kitaenda kutoa huduma kulingana na hadhi ya vituo vya afya vingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo ameendelea kufuatilia ujenzi wa Kituo hiki cha Afya cha Nhomolwa kwa manufaa ya wananchi wa Mbogwe. Nimhakikishie kwamba Serikali kupitia mapato ya ndani inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo yaliyobaki zikiwemo wodi, maabara na majengo mengine ili kituo kianze kutoa huduma zote za level ya kituo cha afya. Kwa Serikali Kuu mwaka 2025/2026, tutatenga fedha pia kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kukamilisha majengo haya kwa ajili ya kukamilisha kituo hiki.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na huduma zote za msingi za kituo cha afya zitaanza kutolewa mara majengo mengine yatakapokamilika ambayo yatatengewa fedha katika Mwaka wa Fedha 2025/2026. Ahsante.